Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Mapenzi & Pesa! - PART 3 - SEHEMU YA 9 - Naomi Simulizi

Mapenzi & Pesa! - PART 3 - SEHEMU YA 9

James akabaki akifikiria. Mke amembadilikia haswa. Akabaki akiwaza na hukumu 
ikiendelea nafsini mwake akimfikiria Vai, kisha akawa kama amepata jibu. Akamfuata Jema jikoni akajaribishe wazo lake. “Au labda uwakaribishe hapa nyumbani?” Jema akamgeukia. “Kwamba mimi ndio niwakaribishe, baada ya wewe kuwafukuza!?” “Si kama Naya tu.” Akajua anajitoa. “Sasa, hivi ndio utafanya James.” Akaanza Jema kwa amri, James mtulivu na mwanae kabeba.

“Na naomba uzingatie. Kuanzia kesho, anza kutafuta dada zako kwa zamu, kuwajulia hali. Una dada wazuri sana na bado wadogo, wanazagaa mtaani wakiwa hawana uangalizi maalumu, na wewe ukiwepo hapa mjini, ukimuangalia Nanaa tu, wakati Nanaa amezungukwa na watu kibao.” Hapo akajua akijitetea ataharibu. Kimya.

“Pili, katika kumtafuta Vai, kwa upande wake, usigusie chochote juu ya mazungumzo yake na Joshua, ila kuonyesha unamjali. Inamaana ujirudi kwake.” “Jema!” “Hakika James. Ukizungumza naye, mpe sababu ya wasiwasi wako siku ile, mwambie ni kwakuwa hukutaka…” Akasita.

“Hapana. Ukisema ni kwa kuwa unamjali. Atajua unamdanganya maana ulimfukuza kwako na kumuacha aende na huyo Bale unaye muona mbaya, ila kwa Nanaa ndio ulitaka uwekewe ulinzi asifikiwe na Bale, yeye ambaye ni bora kuliko kina Vai.” “Jema umeniamualia mama.” “Kwani ni uongo?” “Nakulinda mke wangu. Wewe na mtoto.” “Basi endelea kunilinda mimi na JJ kwa kurekebisha.” “Kwani nimekataa? Si ndio nasikiliza maelekezo!” “Tengeneza na Vai kwanza. Ndio wewe mwenyewe uwakaribishe nyumbani.” “Au labda tuwe wote.” “Hapana James. Wadogo zako wanakuhitaji wewe. Na naomba uwe mwema kwao kama unavyokuwa mwema kwa Nanaa.” Akazidi kumkaba, James hawezi kujitetea.

“Wadogo zako wamepitia ujana kama Nanaa tu. Viola amezaa kabla ya ndoa kama Nanaa tu.” Akataka kusema lakini Nanaa aliolewa, lakini akaona usiku huo ameamuliwa yeye, bora awe bigger person. Apokee dozi yake, paishe. “Wewe umezaliwa na dada warembo kwenye ulimwengu huu wa wanaume waliojawa uchu, halafu ukajitenga nao, ukamkazania Nanaa tu, ulitegemea nini? Nanaa ameishia hapo sababu hata Geb mwenyewe aliona yupo mwanaume mwenye msimamo kwenye maisha ya Nanaa, unamlinda na kumjali, ndio maana na yeye akaongeza umakini kwa Nanaa. Sasa unafikiri kwa Vai na Viola ingekuwa hivyohivyo?” Kimya.

“Ndio maana mama Jema anakua mkali kwa mtu anayetuonea. Wakati wote anasema wanaume wakiona binti yupo yupo tu, hamna baba au mwanaume wa kumlinda, ndio na wao wanawachezea. Sasa wewe ukaweka ulinzi upande mmoja, ukajisahau kwa dada zako. Ndio ujirudi.” “Sawa.” James akatoka hapo na mwanae kimya kimya. Usiku huo ukaisha kwa kujihami haswa, hakutaka hata kuomba penzi, akawa mpole. Mume mwema.

Kulikoungua Mpini.

Sasa huko kanisani, akatokea kijana, mtanashati, jina Ezra, akaonekana anayo aghueni ya maisha, akawa anamtaka Jelini. Alipowasalimia siku hiyo ya jumapili, alikuwa akifahamiana na Jema zaidi, akamsoma Jelini kwa haraka, akajua ni wa kumuendea taratibu sana tena kwa tahadhari. Akajaribu kuwakaribisha waungane kwa chakula cha mchana siku hiyo kwenye hoteli aliyosema wanapika vyakula vizuri sana. Kumbe James alishamsoma, kwa haraka sana akakataa mpaka Jema akashangaa. “Tuna ratiba ingine.” Ezra akawa muungwana. “Basi wakati mwingine.” Akaondoka. Jema akamtizama James, James akachukua mwanae na kwenda kumfunga kwenye gari, wengine wakafuata nyuma. Jelini hata hana mpango.

Wakati wanakula Jema akaanza. “Ezra ni kijana mzuri! Mcha Mungu na ametulia.” “Na mimi nimemuona. Ni wale vijana wanaonekana wanajielewa.” Mama Jema akaongeza bila kufikiria mbali, au asijue kinachoendelea, wakila. “Muonekano unaweza ukadanganya.” Akadakia James na kuongeza. “Maana mtu anaweza akajionyesha kwa nje ni mzuri, kumbe anamakando mengi.” “Kwa jinsi nilivyomuona kwa pale kanisani, anaonekana ni mtu mzuri.” Jema naye akaongeza. “Kanisani kila mtu ni mtu mzuri, mtakatifu. Maana pale kila mtu anavaa sura ya kitauwa.” Mumewe alivyojibu hivyo, Jema akaona anyamaze. Wakala na kutawanyika.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Njiani wakiwa wanarudi kwao Jema akaanza. “Mbona kama nakuhisi unampinga sana Ezra?” “Mimi sijampinga, ila nimeongea ukweli.” Jema akacheka kwa masikitiko. “Nini sasa?” “Nisikilize James, najua Colins amefanyika kama ndugu, unaona kutoa baraka zako kwa mtu mwingine ili awe na Jelini, unaona ni kama usaliti. Lakini wote tunajua, maisha ya Colins yanaendelea kama kawaida. Hatakaa akarudiana tena na Jelini. Kwa nini tusimpe nafasi na Ezra naye tukaona. Pengine anaweza akageuka akawa mtu mzuri kwa Jelini.” “Hilo huwezi jua.” “Basi niombe tumpe nafasi.” “Kwani wewe Jelini amekwambia anatafuta kuwa na mahusiano?!” Hapo akawa mkali kidogo. “Hajasema, ila sio mbaya akaanza kufikiria mwanaume mwingine ili maisha yaendelee.” Akanyamaza.

James kwa Vai.

Kabla jumapili hiyo haijaisha, akampigia simu Vai. Alimshusha Jema na mtoto nyumbani, akaenda kwenye biashara zake, akiwa anarudi usiku nyumbani ndipo akampigia. Vai akiwa na Bale na wenyewe ndio walikuwa wamefika tu nyumbani baada ya jumapili ndefu, aliingia ndani na kujitupa kwenye kochi. Alipoona simu ya kaka yake alishituka mpaka akakaa.

Akamuonyesha Bale. “Usiogope. Pokea.” “Naogopa Bale!” “Alishakugombesha mpaka akatosheka. Unafikiri sasahivi atakwambia nini kingine? Na uzuri alikufukuzia kwangu. Huna chakuficha. Usiogope, pokea tu.” Bale akamtia moyo.

Kabla haijakatika, Vai akapokea. “Halo.” Akaanza kwa upole. “Hujambo?” James akasikika. “Tunaendelea vizuri. Shikamoo kaka.” James akajua inamaana ni yeye na Bale. Vai hapapendi nyumbani kwa mama yake. Kwanza mama yao huwa hashindi nyumbani. Anatoka asubuhi nakurudi usiku mwingi. Ni kama hapo kwa mama yake anaishi Viola, na mtoto wake tu. Mahali baba yake Nanaa alimjengea mama yao nyumba ilikuwa mbali kidogo na makazi ya watu. Kutembea parefu kufikia usafiri. Ni mara chache sana Vai anakwenda huko. Kwa hiyo akajua moja kwa moja anamzungumzia Bale.

“Vai?” “Nipo kaka.” James akaona ajishushe. “Nisiongee mengi, nikaharibu zaidi. Naomba radhi kwa jinsi nilivyokupokea ukiwa na mgeni wako.” Vai hakutegemea. Alilia sana. “Sikufanya vizuri, nisamehe dada yangu. Nilipaniki nikashindwa kufikiria. Niliongea maneno mabaya. Si sawa kwako. Naomba radhi.” Vai alikuwa akilia sana. Hakika hakutegemea. Akasimama kuelekea chumbani ili akazungumze vizuri na kaka yake.

“Nashukuru kaka. Na samahani kwa kumleta Bale kwako. Ila yeye binafsi amekuelewa kaka. Na aliniambia ilimuongezea heshima kwako. Unalinda familia yako wakati yeye aliangamiza yake. Ila kaka, binafsi imeniumiza sana. Nilifikiria na mimi ungenichukulia kama vile Nanaa!” Hapo akakumbuka maneno ya Jema.

“Nakumbuka jinsi ulivyohangaika naye kuhakikisha mchumba wake na wakwe zake wanapokelewa nyumbani, japo mama alikusumbua sana. Nakumbuka uliweza kuwaleta mpaka nyumbani Moshi. Moyoni mwangu na mimi niliamini kwa asilimia zote ungenichukulia japo inaweza isiwe kama Nanaa, lakini angalau hata kunifungulia mlango kaka yangu! Lakini ulinifukuza kikatili sana.” James akaumia sana.

“Inawezekana Bale asiwe kama mume wa Nanaa. Lakini Bale anajua amekosa kaka. Anajutia kosa. Ametubu. Ananijali sana. Ananitunza na kunifanya nitulie shuleni. Ananiongoza vizuri. Najua ubaya aliotenda zamani, kwa kunisimulia yeye mwenyewe mwanzoni tu tulipokutana. Alijitambulisha kwangu kwa historia yake mbaya, bila kunificha. Lakini kaka, Bale amebadilika.”

“Leo tumetoka kanisani, hajapumzika, tumeenda mpaka kwa mama, kumuangalia Nelson. Viola alikuwa hajui chakufanya. Bale alituchukua wote na Viola akiwa na mtoto wake. Akatusindikiza hospitalini.” James akaumia sana na kujilaumu.

“Nelson anaumwa nini tena!? Mbona mama hajaniambia!?” “Wewe unamjua mama. Hana muda na yeyote isipokuwa biashara zake. Viola anasema hii ni siku ya tatu mtoto anapandisha joto, anaharisha na kutapika pia. Wote wawili yeye na Nelson wameshindwa kwenda shule ijumaa. Mama hashindi nyumbani, alipompigia simu, amemwambia ampe dawa ya kushusha homa na kuzuia kuharisha, mpaka Bale alipoona ni lazima tumpeleke mtoto hospitalini. Si sawa kwa mtoto kama huyo kuendelea kuharisha kwa zaidi ya siku tatu. Tumemkuta mtoto amedhoofu, na Viola hana hela kabisa, mama amemkatalia kumpa, amemwambia ampigie simu baba yake Nelson, amdai na kumtisha atampeleka polisi.” “Na wakati wote tunajua alishagoma kumtunza mtoto wake!” James akashangaa sana.

“Wewe unamjua mama linapofika kwenye swala la kutoa pesa yake. Alikuwa tu akimtoa barabarani.” “Sasa hospitalini wamesema ni nini?” “Wamempima, amekutwa na Amoeba. Bale akaomba angalau awekewe maji, maana alikuwa amedhoofu sana kwa kuharisha na kutapika. Tumekaa hapo hospitalini wakimuwekea maji na kumpa glucose mpaka amepata nafuu. Bale mwenyewe amelipia na kuhakikisha anawarudisha nyumbani wakiwa na dawa na matumizi kwakuwa Viola alikuwa ameishiwa kabisa.”

“Ninachotaka kusema, Bale wa zamani sikubahatika kumfahamu, kaka yangu. Na nasikitika alikuumiza na wewe pia. Lakini huyu Bale wa sasa, sijawahi pata mtu akatujali kama yeye. Ameweka heshima katikati yangu na Viola, sio kama wanaume wengine walikuwa wakitufanya tujione tunashindana. Ananijali mimi na Viola ambaye yupo kama ametelekezwa na kila mtu, akihangaika na malezi ya mtoto peke yake. Bale anajali kaka, na makosa yake ya zamani, yamempa hofu ya Mungu.” Akajikuta machozi yakimtoka tena.

“Ananiheshimu, hanichezei au kunitumia vibaya kama wanaume wengine. Ananifikiria bila kuchoka. Ananitunza mpaka apate baraka zenu. Sijawahi pata mimi mwanaume kama Bale, kaka. Ndio maana nikapata ujasiri na mimi kumtambulisha kwako kama Nanaa. Najua na mimi nimekua mtoto mbaya. Nimekua na maisha machafu, lakini nimebadilika. Bale ananiongoza katika njia sahihi. Akili imetulia. Nafikiria mambo mazuri sio mabaya kama zamani. Ni hilo tu kaka yangu.” Vai akapata jukwaa kutoa dukuduku lake

“Nafikiri na mimi nilitakiwa kumpa nafasi. Nitazungumza naye, nimuombe radhi na kumshukuru kumsaidia Viola na Nelson pia.” “Nashukuru kaka. JJ na wifi wanaendeleaje?” Vai akawa muungwana kubadili mazungumzo. Mtu mzima ameomba msamaha, akaona asibakie kwenye hilo. Hawakuzungumza muda mrefu, wakakata simu.

Nyumbani.

Jema akamuona mumewe amerudi amepoa kweli. Akaona amuache kwanza. Wakiwa chumbani peke yao akaanza yeye mwenyewe. “Nashukuru kuzungumza na mimi jana. Kweli nimezembea kwa kina Viola. Wamekua ni mabinti waliozungukwa na watu, lakini wapo peke yao kabisa, wakiteseka.” James akazungumza kwa majuto kidogo.

“Nimezungumza na Vai, nimeumia sana. Kumbe Bale ndio anawasaidia wote wawili na mtoto wa Viola!” “Hujachelewa James.” “Naona na wenyewe hawana shida. Wapo tayari na mimi muda wowote. Nimezungumza na Viola naye baada ya kujua mtoto wake ni mgonjwa. Hakuwa na mengi ila shukurani tu, kwa msaada wa Vai na Bale. Anasema alikwama, akajua atampoteza mtoto wake.” “Kwa nini hakututafuta sisi?” “Nilitamani kumuuliza hivyo, ila nikajisuta. Nimemwambia asiache kunitafuta kwa lolote, hata kama analiona halina muhimu. Mimi ni kaka yake. Nahusika na Nelson kama vile yeye. Hakutegemea. Alilia sana.”

“Imeniuma sana Jema. Sana. Nimejilaumu sana kuona Mungu amenibariki mali zote hizi, halafu dada zangu wanateseka na kusaidiwa na mtu baki tu! Tena ambaye mimi nilimuona hafai, kumbe ndiye anafanya vizuri kuliko hata mimi! Ni kweli lazima kusimama kwenye nafasi yangu kwa ndugu zangu na kufanya mabadiliko ya makusudi. Nashukuru kwa kunifungua macho jana.” “Na Bale?” Jema akaona pasipoe. Kimya kidogo.

“Utanisamehe James. Usione kama nakuwekea pressure.” “Hapana. Ni sawa. Nimepanga kumuomba nipate naye muda wa chakula cha mchana kwenye mapumziko ya kazini. Nizungumze naye ana kwa ana. Sikutaka kuzungumza naye kwa simu. Naona anastahili heshima anayowapa dada zangu.” Jema alifurahi huyo, James akaona anavamiwa. Akapewa dozi ya kiutuuzima, akabaki akihema na kucheka. Akajua Jema amefurahi.

“Nashauri aina hii ya pongezi iwe ya mara kwa mara. Niwe nabakwa hovyohovyo tu.” Jema alicheka mpaka machozi. “James, umebakwa?” “Hakika huku ni kubakwa. Ila mimi sina neno. Na hivi jana nilinyimwa! Wewe ukijisikia kunibaka, ruksa.” Jema akambusu na kuelekea bafuni akicheka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Akiwa ofisini akapokea ujumbe, ‘Kama utakuwa na nafasi leo, tafadhali tukutane kwa chakula cha mchana. James.’ Bale alibaki akiitizama simu yake, asijue chakufanya. Akautuma ule ujumbe kama ulivyo kwa Joshua. Hapo hapo akajibu. ‘Milango imefunguliwa, ni wewe kupata ujasiri wa kuingia. Usiogope.’ Joshua akajibu, eti Bale akapata ujasiri kusoma hayo majibu ya Joshua. Hapo hapo akamjibu Joshua. ‘Asante.’ ‘Anytime.’ Joshua akajibu kwa haraka kama aliyekuwa na simu mkononi. Kisha akamjibu James muda na mahali anapoona pangefaa kwa kukutania.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Walipokutana, James akawa muungwana. Hakutaka mengi, ila kuomba radhi. “Binafsi nakuelewa James, nilikosa sana. Na najua wazi neno samahani, au nimebadilika halitoshi ila muda kuthibitisha najutia nilichotenda. Nilijawa na haraka ya maisha. Nikaona taratibu za baba zinachelewesha. Alibaki akiomba bila kuona mafanikio ambayo kwa sasa najua kwa hakika mimi na mama tulikosa kuona majibu ya Mungu kwa sababu tulipima mafanikio kwa namna yetu.”

“Tumekosa wakati wa Mungu na familia iliyokuwa imebarikiwa kwa namna ya ajabu sana. Kwa wakati ule ungeniambia haya, nisingeamini mpaka nilipoishi kwenye uhalisia. Kuwa na kila kitu bila Mungu. Ni kweli ni kama kukimbiza upepo tu. Havina raha! Nilikuwa na pesa nyingi sana, bila utulivu. Ilifika kipindi, nilitamani maisha ya nyumbani na sikujua jinsi ya kujirudi. Mungu alihakikisha ananipa kila nilichodhani ni muhimu, ilimradi tu nimtambue YEYE na nguvu zake anapokuwa kwenye maisha ya mtu. Nimeharibu sana, na siwezi kurekebisha nyuma. Tafadhali nipe muda na nafasi. Naomba Mungu anijalie niwe kile alichokusudia kwangu mpaka kunileta hapa duniani.” James kimya akisikiliza.

“Na kingine James, nampenda sana Vai. Sina nia naye mbaya, kumtumia sababu ya uzuri wake tu. Vai kama Vaileth mbali na muonekano wake, yeye ni mtu mzuri sana. Mpaka nahisi watu wengi wamemkosa au wanamkosa yule mtu wake wa ndani wakibakiwa kuhangaika na mtu wa nje tu, uzuri wake.” James kimya akimsikiliza maana na yeye ndio kwa mara nyingine tena ni kama anatambulishwa huyo dada yake.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Tokea wanakua, wapo nyumbani kwao, alikerwa na tabia za hao dada zake, mama yao akiwakingia kifua hata kwa makosa ya waziwazi. Alipoona wamejiunga wote wakimtesa Nanaa, ndipo akawekeza nguvu za makusudi kwa Nanaa, na kuwaacha hao mabinti mkononi kwa mama yao. Hakujihusisha nao mpaka walipotaka tena kujaribu maisha.

Bila shida James aliwaleta mjini. Akaishi nao mmoja baada ya mwingine. Wakawa ni kama usiku na mchana kuwalingalisha na Nanaa. Wakawa wavivu wakupitiliza. Yeye ndio anawatumikia hapo nyumbani kwake japo ndiye aliyekuwa akifanya kazi, wao wakishinda tu nyumbani, tofauti na Nanaa aliyekuwa yeye ndio akimtumikia na kumshukuru kumtunza. Nanaa alimtunza kaka yake akihakikisha akirudi nyumbani baada ya kazi ni mapumziko tu, kinyume na hao wawili. Vai na Viola.

Akaja kumpa Nanaa nafasi kama aliyompa Viola. Kuishi kwa kina Magesa. Viola akaishia kumuingilia Danny chumbani akiwa uchi, alipodhani mkewe hayupo. Likatokea la kutokea, kumbe Danny wa wakati ule akiwa chini ya ulinzi wa maombi ya kina mama G, alikuwa mwaminifu sana kwa Grace, mpaka alipotoka nje ya ulinzi wa Mungu, na kukuta shetani alikuwa akimsubiria kwa hamu zote. Shetani akiwa hana zawadi ya bure, alimpokea kwa mikono miwili, akampa mrembo aliyekuja kumuachia ubachela, kuua watoto na gonjwa analoishi nalo mpaka sasa.

James aliomba radhi kwa kina Magesa na kumtoa Viola hapo kwao, moja kwa moja kituo cha mabasi kumrudisha kwao Moshi. Kuanzia wakati huo, akanawa mikono kwa hao dada zake. Akawaacha mikononi kwa mama yao. Akahamisha akili na juhudi kwa Nanaa. Akampa nafasi kama yao. Nanaa wa wakati ule alikuwa yatima, hana kimbilio ila kila nafasi aliyokuwa akipewa kuitumia kwa makini. Akaishia kusoma mpaka shahada ya kwanza. Na nyumba ileile aliyotia aibu Viola, mabinti hao wanaofanana karibia sawa tu kasoro tabia, Nanaa akatoka na mume. Geb. Nanaa akawa fahari ya James. Kuonyesha juhudi zake si bure, ila dada zake wakibakia kumfedhehesha na mengine mengi. Ndio James kuwaacha kabisa mpaka wakati Jema alipotaka warudi shule. Napo ni kama alisaidia kidogo tu. Alipohakikisha wamerudi shuleni, akaachana nao.

Visa na mikasa ya hao mabinti Viola, Vai na Nanaa, vinapatikana kwenye Simulizi ya ….Ni Wangu!

https://www.naomisimulizi.com/2022/11/utambulisho-wa-simulizi-ya-ni-wangu.html

ITAKUPELEKA KWENYE VIDEO YouTube

https://www.naomisimulizi.com/2022/11/ni-wangu-sehemu-ya-1.html

~~~~~~~~~~~~~~~~~

“Vai ameleta maana nzima ya maisha kwangu.” Bale aliendelea. “Mungu alimleta kwangu kunikamilisha. Nilikuwa nikimwambia Joshua, kila upungufu nilio nao mimi, ukamilifu wake upo kwa Vai.” James akamwangalia akihisi anasikiliza habari za mtu mwingine, si Vai, mdogo wake. Vai! James akaona aendelee kusikiliza tu akiamini kuwa kweli watu hubadilika!

“Ninaishi na Vai,” “Kwa nini unaishi naye na amelipiwa chuo aishi hosteli?” James akauliza kiiungwana tu akimkatisha. Lakini hata Bale aliweza kugundua hapakuwa na ukali kwenye swali lake, ni kama anayetaka kufahamu zaidi. Ikamtuliza kueleza ukweli.

“Cha kwanza, siishi naye kama mke, kwa sababu siwezi kufanya hivyo bila baraka zenu au mpaka ndoa. Mazingira ya chuo huwa yanamfanya hatulii. Kuna aina ya ushindani ulitokea hapo katikati baina yake na waliokuwa rafiki zake. Kukatokea uadui na lawama, inamuwia ngumu Vai kuishi pale na kutuliza mawazo chuoni. Sasa kwa kuwa nina usafiri, naona ni bora aishi kwangu, atulie ili shule iishe. Asichanganywe.”

“Kwangu kuna utulivu. Hawazi swala lolote hata chakula, kwa kuwa mimi mwenyewe nampikia, nahakikisha anakua na chakula wakati wote, mawazo yake ni shule tu. Akishasoma na wenzie na madarasa yakiisha, nampitia kurudi naye nyumbani. Asubuhi nahakikisha yupo chuoni kwa wakati. Kukiwa na mtihani, na wenzie wakakataa kusoma naye mchana, hapo inamlazimu kulala hosteli. Anajitahidi kwakweli. Anafanya vizuri na Mungu amempa kibali huko hata kwa walimu wake na matron. Nipo naye nyumbani ili kumfanya atulie ila si kwa nia mbaya.” “Nashukuru Bale.” Bale akavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu.

“Na naomba pia nikushukuru kwa ajili ya Viola. Alihitaji msaada.” “Karibu. Ila naomba baraka zako James. Nampenda Vai, nataka kumuoa.” “Bale! Kabla hajamaliza chuo!?” “Hatutaanzisha familia, mpaka amalize chuo. Hilo nakuahidi James. Sitaki kumtenda Mungu dhambi, na siwezi kuendelea kuishi naye kwa jinsi ninavyoishi naye hivi. Tafadhali naomba baraka zako, nimuoe, awe mke wangu kihalali.” “Labda nikuulize, Joshua anajua hili?” “Ndiyo.” James akachoka kabisa.

“Kwamba yeye anaona sawa mfunge ndoa sasahivi?!” “Kipindi Vai yupo likizo baada ya kumaliza huu mwaka. Mwaka wapili anasoma akiwa mke wangu. Na yeye Joshua amesema nilazima nihakikishe anamaliza chuo kwa muda wazazi wake au nyinyi mmelipia bila kuzembea. Na ameahidi na yeye kulisimamia hilo.” James akabaki hoi. Inamaana hapo anazungumza na Bale, alishapata baraka kutoka kwa Joshua na Geb!

“Tafadhali James. Namtunza Vai vizuri, nipe baraka zako awe mke wangu, hicho kipengele tukimalize, tuendelee na mengine.” “Aisee nipe muda Bale. Nifikirie. Kisha nizungumze na Joshua pamoja na Geb, ndipo nikazungumze na mzee. Nimsikie na yeye.” “Nitasubiri bila kukubugudhi James. Utakapokuwa tayari, nijulishe tu, tuanze taratibu za mahari. Joshua ameniahidi atasimamia, nioe kwa heshima.” James hakuamini. Akacheka akitingisha kichwa.

“Nini?” “Aisee Joshua nimemnyanyulia mikono! Yupo na mimi kana kwamba hajui chochote kinachoendelea kabisa!” “Yeye mwenyewe aliniambia hajui jinsi ya kufanya, amemuachia Mungu atende mwenyewe. Ila ukweli anatuombea sana mimi na Vai. Anatubeba magotini bila kuchoka.” “Aisee huyo Mungu wake naona anatenda kwa ajabu! Acha mimi niwahi kazini. Tutazungumza zaidi.” James akamalizia chakula na kuondoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Sasa imekua akizungumza Bale popote, ni Joshua. Na Joshua akizungumza popote, lazima umsikilize kwa jinsi alivyoheshimishwa na Mungu. Sasa Bale naye amekua Kumu. Akamtumia ujumbe Joshua kumwambia kilichoendelea kati yake na James mpaka kutaka kumuoa Vai. ‘Amesema atafikiria na kuzungumza na wewe.’ Joshua akacheka mwenyewe. ‘Wewe ni Mungu, na badala yako SITAKI mwingine. Umepigana vita yote, unaniletea tu mateka!’ Akamwambia hivyo Mungu wake  akicheka, na kumjibu Bale. ‘Acha Simba wa Kabila ya Yuda angurume mpaka pakae sawa. Hajawahi kuongopa, na hataanzia kwako.’ Bale akacheka aliposoma hivyo. Akajua kwa hakika mwaka huo ataoa, na yeye apate starehe ya mwanamke.

Kwa Jelini

Jumapili inayofuata baada ya ibada, Ezra aliwasalimia na kucheza kidogo tu JJ akaondoka bila kutaka mengi maana na yeye alishaanza kumuogopa James. Wakarudi nyumbani kama kawaida, Jema akamwambia mumewe anataka kumkaribisha Ezra kwa chakula cha mchana jumapili inayofuata. “Taratibu Jema bwana! Mbona hivyo!?” “Hivi unajua ni miezi mingapi tokea Colins aondoke?” “Miezi 6, na siku 15 tu! Tayari tunafanya mapinduzi!” Jema akabaki ametoa macho. “Kwamba wewe mwenzangu unahesabu!” “Sasa si kama umri wa JJ tu. Unawezaje kusahau!?” Akaondoka kabisa hapo nyumbani kwenda kwenye biashara zake.

Lakini akajua itamuwia vigumu sana kukaribisha mtu mwingine kwenye maisha yao mbali na Colins. Hata huyo kijana aliyeshika nafasi ya Colins, hakuacha kumlalamikia, na hakuthubutu hata kumkaribisha hapo nyumbani. Jema akajua anapata naye shida kwa sababu si Colins.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Mungu Wa Wakati Ameanza Kutenda Yake.

Mwisho Wa Yote Ni Nini?

Inaendelea.


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment