~~~~~~~~~~~~~~~~~
Akiwa njiani kurudi
nyumbani kwake ndipo akampigia simu Bale. Ilishakuwa saa 12 jioni. “Unaendeleaje?” “Aisee mimi na Vai tupo wazima kabisa. Vipi
wewe na familia?” “Tunamshukuru Mungu kila kitu kipo sawa. Kesho mnaratiba
gani?” Bale akafikiria kwa haraka na kujibu kwa swali. “Mida gani? Maana asubuhi sana, nampeleka Vai kusuka kisha
nitaelekea kazini. Inavyoonekana itachukua muda mrefu mpaka mchana wa kwenye
saa saba hivi. Lakini najua wakisema saa saba, inaweza kuwa saa kumi.”
Wakacheka.
“Kwa hiyo
nitakuwa maeneo hayohayo yakaribu nikimsubiria mpaka amalize. Kwema lakini?”
“Naya anaandaa mazingira ya nyinyi kujumuika na sisi kwa chakula cha kesho
jioni.”
Gafla Bale akahisi ganzi mwili mzima. Akabaki akitetemeka na machozi yakaanza
kumtoka mfululizo, akashindwa kuzungumza kabisa. Akakata simu. Joshua
alitegemea. Si habari nyepesi kwake.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Vai alishituka sana
kutoka chumbani na kumkuta Bale akilia huku ameinamisha kichwa, simu kashika
mkononi. Alikuwa akilia kama amefiwa. Akaingiwa hofu ya ajabu. “Asije kuwa
Joshua kafa! Bale hatabaki kama alivyo.” Ndicho alichokifikiria kwa haraka
kinachoweza mliza Bale kwa kiasi kile. Akachukua simu mkononi mwake kuangalia
mtu wa mwisho aliyezungumza naye.
Wakati anafungua simu
yake, ujumbe ukaingia. ‘Naamini huu ni wakati wa Bwana,
Bale. Tutakuwa na wakati mzuri. Karibuni saa moja kamili usiku. Naamini bado
unapakumbuka nyumbani kwetu. Ukitaka maelekezo zaidi ya jinsi ya kufika,
usisite kunipigia. We are looking forwad to see you and Vai. Usiku
mwema.’ Vai alipogundua ni ujumbe kutoka kwa Joshua, na yeye akapatwa na
hali. Akapigwa na butwaa.
Kwa Mungu wa Yasiyowezekana kwa Wanadamu.
Wawili hao kama
vitoto vinavyojikomba, bila kuchelewa, saa 6:50 jioni walikuwa wameshawasili
kwenye hekali la Kumu, mlinzi aliwafungulia geti, Vai hakuwa amefika hapo,
akabaki mdomo wazi. “Sasa hapa unatakiwa kujikaza. Lasivyo mate yatakudondoka.
Maana huko ndani kwenyewe si mchezo.” “Acha masihara Bale!” “Sasa wewe
nilipokwambia Joshua amefanikiwa ulifikiria nini?” “Kubadili mboga.” Acha Bale
aangue kicheko.
“Kama unafikiri mimi
amenipa aina hii ya gari, na hata hawakumbushii kulidai, wewe ulifikiri mkewe atakuwa
akiendesha aina gani ya gari au anaishi kwenye mazingira gani?” “Nalo hilo
neno! Na ndio mcha Mungu hivyo!” “Mwenyewe anasema ndio chanzo cha
mafanikio yake na siri ya kuendelea kufanikiwa.” Wakamuona Joshua
anatoka mlangoni akionekana nadhifu haswa, hata ukiambiwa ndio mwenye nyumba
utaamini.
Alivaa nyeupe tupu.
Juu mpaka chini. Safi. Kinyumbani. Wote kimya kama watoto wa darasa la kwanza,
mwalimu ameingia darasani gafla wakiwa wanapiga kelele. Akawaonyeshea sehemu ya
kuegesha gari yao, wakaelewa. Wakavuta gari mpaka hapo, wakashuka.
Ukweli Vai
alitengenezwa nywele vizuri, akapendeza sana. Akafanania kualikwa kwenye nyumba
kama ile. Bale naye alivaa raba nzuri sana nyeupe, kama tsheti aliyovaa ila
akavaa jinsi nyeusi. Yeye alijua anapokwenda, kwa hiyo hakutaka awe out of
place, alikusudia kujiwakilisha pia.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Karibuni sana.”
Joshua akashuka ngazi kabisa kuwakaribisha. Wote mapigo ya moyo yakiwaenda
kasi, kama wasio stahili kuwepo hapo. “Asante.” Wakajibu kwa pamoja
wakipokezana kumshika mkono. Akaongoza njia, wakawa wakimfuata nyuma. Kufika
mlangoni Bale akaanza kutetemeka miguu, akijua ndani yupo Naya. Hofu ya ajabu
ikamuingia. Akasimama.
Wote wakamgeukia.
“Vipi?” Vai akamuuliza taratibu kwa sauti ya chini ili Joshua aliyekuwepo mbele
yao asiwasikie, ila na yeye akageuka. “Nahitaji kama dakika moja hivi.
Tangulieni tu.” “Usiogope Bale!” Akamsihi kwa upendo, Joshua akiwasikiliza. Wakamuona
machozi yakimtoka. Joshua akarudi pale alipokuwa amesimama. Akaegemea nguzo ya
ngazi na kuinama akilia.
“Nisikilize Bale.
Unakumbuka tulizungumza juu ya wakati wa Mungu?” Bale akaitika kwa kichwa.
“Basi huu ndio wakati wake. Maji yameshatibuliwa, ni wewe kuingia tu.
Sio rahisi, lakini huna jinsi. Nikikombe chako, lazima ukinywee. Twende.” Vai
alishaingiwa baridi, anatetemeka kwa hofu akimuhurumia Bale.
Mara mlango
ukafunguliwa. Wote wakageuka. Naya! Bwana alipendezea na hiyo nyumba, ungejua
tu ni yake. “Karibuni.” Akaongea akimwangalia Bale. Akagundua alikuwa akilia,
anajikausha machozi, mumewe ndiye aliyekuwa karibu yake. Akajua wazi alikuwa
akizungumza naye.
Akatulia akiwatizama, mwishoe akamgeukia Vai.
“Karibu ndani, Bale ni mwenyeji hapa. Twende.” Akarudi ndani, Vai akamtizama
Bale. “Twende wote Bale!” Bale akajifuta machozi na kujibu, “Tangulia nakuja.” Vai akaingia na kuwaacha hapo
nje.
Kuingia tu ndani
akabaki katikati ameduaa. Naya akaanza kucheka. “We Vai?” “Mimi sijawahi
kuingia kwenye nyumba nzuri hivi! Kumbe nyinyi wenzetu ndio wale wanao ishi!”
Ilibidi tu Naya acheke. “Ni pazuri sana. Pamepoa haswa. Kuna kijihali fulani
hivi cha utulivu. Mimi nimepapenda sana.” Maneno mengi, akashindwa kujizuia. “Karibu
sana.” Akaanza kuangaza macho.
Akakutana na mapicha
makubwa sana ya watoto. “Kwani Naya nyinyi mna watoto!?” Yaani mpaka Naya
mwenyewe akashangaa. Kwamba Joshua hajawaambia! Wakawa wameingia Joshua
na Bale.
“Tulijaliwa mapacha.”
Vai akamtizama Bale kwa mshangao. “Wakubwa tu sasa. Hizo picha zao za miezi
mitatu. Hivi za miezi sita ndio tunasubiri ziletwe. Tulitengeneza kama hizo.”
“Hongereni sana. Ila hapo wanaonekana wamefanana sana, huwezi kuwatofautisha, halafu
ni kama kopi ya baba yao!” Wakamsikia Joshua anaanza kucheka.
“Wala sio kila kitu! Kuna
vitu wamefanana na mimi.” Joshua akazidi kucheka na kupiga makofi kabisa. “Ni
hivyo Vai amewatizama kwenye picha, tena kwa haraka. Mtu akitulia na
kuwaangalia vizuri, utagundua kabisa wamefanana na mimi.” Wote wakacheka. “Wala
hujashinda.” Joshua akazidi kucheka.
“Kumbe bora Vai umekuja! Hao watoto ni kopi
yangu, kuanzia utosi mpaka ukucha wa mguu. Kama si Naya au mimi mwenyewe,
wakikuzunguka mara moja tu, unaweza usijue yupi ni yupi. Sasa ukisema
wamefanana na mimi, humu ndani hapatanyweka maji! Wataanza kuchambuliwa,
ilimradi itafutwe hata nywele moja inayofanana na mama yao. Mimi huwa nasema,
Mungu ndio muumbaji. Na humpa amtakaye. Ajiachie tu, pengine wajao,
watafanana naye. Hilo limeshindikana! Karibuni sana.”
“Asante.” Wakaitika
kwa pamoja wakicheka kutokana na maelezo yake. “Hongera Naya, kuwa mama.” “Na
watoto wenu wazuri.” Vai akaongezea kwa Bale. “Asanteni.” Kabla hapajazuka
ukimya wa tofauti, Joshua akawahi. “Sasa karibuni hapa ndani kidogo, tumwambie
Mungu neno la shukurani.” Akaongoza njia mpaka kwenye kinanda chake, mkewe
akafuata na wao wakafuata. Akakaa kwenye kinanda moja kwa moja.
“Nyinyi kaeni tu
hapo.” Aina tu ya makochi yaliyozunguka hiyo aina tu ya kinanda, ungejitizama
mara mbilimbili kama unafaa kuwepo hapo au unahitaji ukajiandae zaidi. Nyumba
safi, na kila kitu humo ndani kipo sehemu yake.
“Tutambue uwezo
wa Mungu. Tuseme tupo hapa, sasahivi, wakati huu, kwa
ajili yake. Bila yeye, siku ya leo pengine wote tusingekuwa hapa.” Naya akawa
ameshajua aina ya wimbo anaotaka kuimba mumewe. Akaanza kupiga kinanda.
Kisha akaanza kuimba.
“Yeesu, tupo hapa. Yeesuu, tupo hapa. Yeesuuu, tupo
hapa, tupo hapa, kwa ajili yako.” Vai akasikia mkewe akipokea kwa sauti nzuri
yakuvutia. “Sio maneno magumu. Ni hivyo tu, mnaweza kurudia na nyinyi.” Akaongea
Joshua akiendelea kupiga kinanda, mkewe akiimba. Bale akaanza kulia tena,
lakini Joshua hakuacha. Alipiga huo wimbo, na kuongeza mwingine wa kuabudu. Ile
hali pale, ndio Vai akaelewa ni ule utulivu pale unatokana na aina hiyo ya
ibada. Wawili hao waliimba, mpaka Vai mwenyewe ustaarabu ukamuisha, akajikuta
akiabudu kwa machozi. Walipata muda mzuri, tena mrefu ambao hawakuutarajia
uweponi kwa Mungu.
Joshua akamshukuru Mungu
wake kwa kufungua milango ambayo hakuna mwanadamu awezaye kufungua ila Yeye.
Akashukuru kwa reunion hiyo, akatubu kwa niaba ya wote, kisha akaomba
Mungu awe msingi wa chochote kitakachozaliwa kuanzia hapo. Wakamaliza.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Bale akapiga magoti
kumuomba Naya msamaha akilia sana. “Umenipokonya baba, Bale. Umebadili maisha
yangu. Watoto wangu wanakua bila kukutana na baba Naya! Hilo tu ndilo linaniuma
sana. Ila nimesamehe. Yaishe tu. Kama alivyosema Joshua, Mungu atusaidie tujue
jinsi ya kuenenda kuanzia hapa. Hatuwezi kuishi kama tunavyoishi sasa. Itakuwa
ni kupuuza juhudi za baba.” Naya akaendelea taratibu tu.
“Baba alikutafuta
Bale! Mpaka alikuwa akitia huruma. Muulize Joshua. Alikwenda kutafutwa huko
alikokuwa amekwenda kukutafuta wewe, akiwa ametekwa na kupigwa sana. Kina
Joshua na Geb wamemrudisha hapa Dar akiwa amejeruhiwa vibaya sana. Siku anatua
pale uwanja wa ndege na kina Joshua, na kuanza kuanguka kama anakifafa, sababu
ya kupigwa na hao majambazi huko. Lakini baba hakukata tamaa. Isingekuwa
kulazwa sababu ya huko kujeruhiwa, na siku yangu ya harusi kumkutia hapa ni
mgonjwa, muulize Joshua na kina Magesa. Alikuwa tayari kuacha harusi yangu, na
aliachia kila mtu maagizo, harusi iendelee bila yeye, kwa kuwa alikuwa arudi tena
kukutafuta wewe. Hakuogopa hata kuuwawa kwa ajili yako, Bale.” Bale
alilia sana.
“Malon
alinidanganya Naya. Alituma mtu kunitoa jela. Akanisikilizisha mazungumzo
aliyowarikodi alipowafuata hapa na kuwaambia anajua habari zangu, atazungumza
na nyinyi endapo Joshua akiondoka pale. Mkakataa. Ikasikika sauti ya baba
akizungumza kama hajali.”
“Si kweli Bale. Baba ali..” “Na mimi nilikuja
kukuta mazungumzo ya kweli. Yale alinitengenezea mimi tu ili niwe kwenye
mipango yake.”
“Hata
hivyo Naya. Mungu wangu nishahidi. Sikukusudia kuuwa familia yangu. Japokuwa
nilikuwa na uchungu wa ajabu wa kutengwa au kukutaliwa nyumbani
kama Malon alivyoniaminisha, lakini nia yangu nilitaka kuharibu ile mali yote
ya baba, nikijua Joshua ndio amempa na kumfanya anitupe mimi. Kisha nirudi
kwake. Kwa sababu wakati ule nilikuwa na pesa nyingi sana. Mimi mwenyewe kama
mtoto wa kiume, na mkubwa pale nyumbani, nijenge kwetu.” “Baba asingekubali.
Na wewe alikwambia Bale. Tena mbele ya Joshua, pengine nyinyi muwe mlisahau.”
Akamtizama Joshua.
Hapo Joshua alikuwa
kimya, akiwa ndugu msikilizaji tu. Na yeye akamtizama Bale kama anayemkumbusha.
“Nilisahau Naya. Ndio Joshua alikuja kunikumbusha
baadaye sana nilipolilipa deni la baba kwa kina Magesa, na kutaka kujenga pale.
Ilishindikana kabisa. Ndio Joshua akanikumbusha kuwa baba alinimbia hata nikija
kufanikiwa huko, nisije kujenga kwake, nijenge kwangu. Nimeacha kabisa, na hata
hati ya nyumba nilirudisha kwa Joshua. Sijasogea huko, na Mungu wangu
nishahidi.” “Basi sisi tumejenga Kiluvya.” Akaanza Naya sauti yake ya
ubishani kwa Bale kama kawaida yao. Ila Bale hakuamini, mpaka machozi
yakakauka.
“Haiwezekani Naya!” “Muulize
Joshua. Alitafuta mafundi. Tumemjengea Mungu kanisa hilo, ukiliona utajua Mungu
yu hai. Kwa kumbukumbu ya baba Naya. Bado hapajakamilika, lakini hakika ni
pazuri sana.” “Na kina Magesa wanachangia pia.” Joshua akapenyeza neno hapo.
“Na mimi naweza kuchangia?” “Sitaki.” Naya akakataa kwa haraka. Joshua
alishawazoea hao wawili kwa kubishana. Akanyamaza kimya kujua watafikia wapi.
“Sasa si ni kanisa!
Kanisa si yeyote yule anajenga!” “Lakini sio wewe. Pale sitaki.” “Basi
Naya. Ila ingekuwa mtu kama Joshua, angesema acha nifikirie au nimuombe
Mungu kwanza.” Joshua akacheka akitingisha kichwa taratibu. Vai yeye
alishaingiwa hofu. Kumbe wawili hao jinsi yao ya kuzungumza ndio ubishani.
“Sasa mimi ndio
Joshua?” “Wewe unaishi na mtu kama huyo, si vitu vingine uige tu!” “Sitaki.
Hatutaki mchango wako. Kajenge kwako, acha kukaa kwenye nyumba za kupanga. Huko
baba alishatutoa zamani sana. Nashangaa kwa nini unakazania kukaa kwenye nyumba
za watu!” “Nitajenga mama. Taratibu.” “Sasa unataka kuoa halafu umpeleke mkeo
akaishi kwenye nyumba za wanaume wengine?” “Naya, ndio nimepata kazi mama. Nipe
muda.” “Basi peleka pesa zako sehemu sahihi, sio kudandia miradi ya watu. Pale
tunajenga sisi, yaani kina Kumu, na kina Magesa tu. Hatutaki kuingiliwa.”
“Nimeelewa. Ila hivyo
ulivyo sasahivi umekua kama mama kabisa.” “Achana na mimi. Twende mwaya Vai,
tukale. Hapa kwetu tunampishi mzuri sana. Akikupikia, lazima utafurahia chakula.
Twende Joshua wangu.” “Na mimi Naya?” Akamchokoza Naya. “Wewe nitakufikiria.
Sijui ukoje Bale! Mtu hata hujasamehewa vizuri, umeshaanza uchokozi!” Akajibu
hivyo na kuondoka. Angalau ile hali pale ya tension ikapungua.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Kufika sehemu ya
kulia chakula napo Vai akakwama tena. Bale akaanza kumcheka. “Sawa Bale. Kwani
Naya, ni mgeni mimi tu ndio napashangaa hivi hapa kwenu?” Wote wakacheka.
“Kumbe Vai ni mtundu hivi!” Joshua akaingilia. “Na hawezi kuweka
anachokifikiria moyoni, na ndio maana hawezi kununa. Kila kitu kinachopita
kichwani kwake, ujue utajua tu.” Akaongeza Bale. Wakacheka.
“Halafu kumepangiliwa
bwana! Hakuna kitu kilichopo sehemu hovyohovyo tu. Halafu ni yale mavitu
ya thamani tupu! Mazuri yote!” “Basi, Vai. Mengine tutazungumza tukiwa
peke yetu.” Wakazidi kucheka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Wakaanza kula pamoja,
stori zikaanza. “Nasikia James kakutimua kwake.” Walicheka mpaka machozi.
“Bora. Na ukome.” “Bwana ilikuwa mbaya Naya! Ilikuwa mbaya sana. Nimekua
mchoma moto watu.” Wakazidi kucheka. Huyo Bale akiwa na Joshua, wala Vai si
mzungumzaji hivyo. Naya akazidi kucheka. “Yaani James ananifukuza huku
ananisihi nisirudishe moto kwake.” Hapo wakazidi kucheka.
“Mimi mwenyewe
amenituma, nikiwa naye huyu nimsihi asije akatuma moto kwake, kwenye nyumba
yake, ya mama, na kwa baba.” Bale akawa anatingisha kichwa kwa masikitiko. “Ukome
Bale.” “Kidogo? Na kwambia nimekoma Naya mimi, hata leo ukiniambia nisubirie
jambo kwa miaka 10, sina neno. Nitasubiri tu. Haraka zote zimeisha.”
“Pole Bale.” “Aisee pole wewe. Tafadhali nipe nafasi, najitahidi sana kuwa vile
Mungu anatamani niwe. Siwezi sema nipo sahihi, lakini najifunza aisee. Nipe
muda. Naamini nitakuwa hata kile baba alitamani kuona kwangu.” “Mungu atazidi
kukusaidia.” Akajibu hivyo wakatulia.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Joshua kimya
akisikiliza ndugu hao wakirudisha mahusiano. Moyoni akazidi kumtukuza Mungu
wake. Kila mara alijikuta akisema, ‘Wewe ni Mungu, badala yako hakuna mwingine’. Ila hata yeye
aligundua damu nzito kuliko maji.
Naya huyu, si Naya angeweza kumfanya akawa hivyo hata iweje. Hakumuona wa aina
hiyo tokea wakiishi nyumbani kwao Kiluvya. Usiku huo kuna jinsi alifunguka
upande mwingine, ambao hakuna angeweza kufunguka kwake hivyo, isipokuwa kwa
huyo Bale tu. Na uzuri, haikuchukua siku nyingi tokea amfungulie mlango Bale.
Ikawa kama switch ya kuwasha taa. Ikawashwa na kubadilika papohapo.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Wakapata wakati mzuri
na kuondoka ila wakashangaa kutosikia hata sauti ya watoto! Bale naye akawa
mvumilivu. Hakutaarifiwa kuwa wapo, na yeye hakutaka kuuliza. Alijua wazazi
hao, Joshua na Naya, wanajua wanachokifanya. Akajua wakiwa tayari kumtambulisha
kwa hao watoto, watamtambulisha tu. Lakini alifurahi sana kufunguliwa milango
kwa dada yake. Wakaondoka wakiwa wamejawa furaha.
Kwa Jema.
Sasa huku kwa Jema
kikabaki kikimsumbua. Kutoka walipokutana na kina Bale hospitalini akipata
mguu, Joshua hakuzungumza naye juu ya Bale kabisa, na Naya naye ikawa
hivyohivyo. Wanapigiana simu wanazungumza kila kitu, lakini hajawahi kugusia
kabisa juu ya kufukuzwa kwa kaka yake nyumbani kwake. Na Jema hakuwa
amemwambia mumewe kabisa kama alikutana nao tena hospitalini.
Sasa jumamosi hiyo Jema alimpigia simu Naya wakutane jioni
hata kwa muda mfupi tu kama kawaida yao wakiwa na watoto, wazungumze
mambo ya watoto huku watoto wakicheza. Naya akamwambia kiurahisi tu, “tupange jumamosi ingine, jumamosi hii nimemualika Bale na
Vai kwa chakula cha usiku.” Jema akaitika na kuagana, ila akabaki na
butwaa. Maana Naya alizungumza kiurahisi tu bila maelezo mengi, na kuonyesha
hilo ni la msingi kwake kuliko umuhimu wao au utaratibu wao na watoto!
Linapokuja swala la watoto kwao wanafanya tukio.
Huenda mahali kukaa huko wakicheza. Mara nyingine Nanaa na wanae huwafuata.
Mwishoe wanajikuta wanakusanya na waume zao hapo bila kupanga. Basi familia
hizo tatu watakaa hapo wakizungumza na kucheka mpaka usiku, kila mmoja anarudi
kwao. Lakini safari hiyo, jumamosi hiyo, Naya akatoa kipaumbele kwa Bale na
Vai. Kikabaki kikimsumbua Jema.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
James anarudi mida yake ya jioni, anakutana na Jema aliyepoa
haswa. Jumamosi huwa hachelewi kumalizi majukumu yake. Mapema sana huwa anakuwa
ameshaungana na mkewe pamoja na mtoto. Inategemeana na Jema atakapokuwa. Ndio
kama anakuwepo na Naya, basi atawafuata huko kama Joshua tu. Basi na wao wapate
muda wakucheza na watoto. Maana siku za jumamosi waajiriwa hao wote hufanya
kazi nusu siku. Siku ya Joshua huisha kutokana na mipango ya Jema. Ila mara nyingi
saa sita huitimisha kazi. James yeye wakati mwingine mpaka saa tano anakuwa
amemaliza, anahamia kwenye biashara zake mpaka kwenye mida ya saa kumi jioni
ndio anamtafuta Jema.
Sasa siku hiyo akajua Jema yupo tu nyumbani. Alivyoona ule
ukimya James akaanza kujishuku. Akajaribu kufikiria alipo kosa. “Au
nimekosea kukumbuka siku yake ya kuzaliwa?” Akajiuliza James huku akijitahidi
kuwa mwema kupita kiasi. Maana majibu ya Jema yalikuwa mafupi, halafu kama
mnyonge. James akagundua sio siku yake ya kuzaliwa wala si annivesary
yao. “Sasa nimefanya nini mimi!?” Hapo anajiuliza huku anajituma
kwelikweli hapo ndani karibu adeki nyumba nzima kwa wasiwasi.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Hivi huwa mnawasiliana na kina Vai au Viola?” Akaulizwa. James
akaendelea kumbadili mtoto diaper iliyokuwa kavu kabisa. Aliamua kumbadili tu
ili kuonekana anasaidia hapo ndani. Ni katika kujishuku. “Ndiyo. Huwa
tunawasiliana. Kwani vipi?” “Kwamba huwa unawatafuta kuwajulia hali kama
ulivyokuwa ukifanya kwa Nanaa?” Hapo akajua ANATEGWA. Kuna jambo. “Sasa sijui wamekosana na Nanaa tena?”
Akajiuliza James huku akifikiria jinsi ya kujibu asije akaharibu.
“Si unakumbuka
historia ya kwetu Jema? Nanaa alikuwa kama mtoto niliyelea mwenyewe. Kwake
nilikuwa kama mama na baba. Wakati mwingine nilibaki peke yangu kwenye maisha
yake. Na tulikuwa tukiishi nyumba moja. Kwa hiyo hata mahusiano yetu yakawa
tofauti na kina Viola. Kwani vipi?” “Hamna tatizo. Maana nilimsikia akimwambia
Joshua, kuwa ni kama yupo tu peke yake. Hakuna anayejua kuugua kwake au uzima
wake. Mama yenu yupo busy sana na majukumu yake, baba yenu yupo mbali, na wewe
hamna mazoea ya kutafutana kujuliana hali isipokuwa jambo la msingi.” James
akashangaa sana. Keshachanganywa. Kavurugwa.
“Kwa nini anamwambia
hivyo Joshua!? Inamuhusu nini?! Na wewe umejuaje?” “Wewe unajua kama Joshua
ndio amegeuka kuwa kama mzazi wa Bale?” Akauliza na kumfanya James
atulie. “Mimi mwenyewe sikujua uzito wa Bale kwa Joshua kwa kiasi hicho. Ila kama
juma moja lililopita, Joshua aliniambi siku hiyo ya jumatato ambayo ilikuwa
busy sana, nilazima nimwachie dakika 30 zisizo na muingiliano.
Nikaangalia ratiba. Sikuwa na hizo nusu saa kwa muda huo wa asubuhi.
Nilipomwambia, akaomba kuona ratiba. Hivi unajua alihamisha kikao na mtu wa
muhimu sana muda huo, ili kutengeneza nafasi?” James kimya akisikiliza.
“Nikashangaa sana. Sasa
siku ilipofika, baada ya kikao cha kwanza cha asubuhi kilikuwa maeneo ya Posta
mpya, akamwambia dereva atupitishie hospitali ya Muhimbili, kitengo cha MOI,
sasa kwa kuwa kuna kitu na mimi nilikuwa nikimsomea, nikashuka naye garini.”
“Kufupisha habari,
nikaja kugundua kumbe yupo pale kwa ajili ya Bale! Alikuwa akiwekewa mguu wa
bandia, inavyoonekana ni wa pesa nyingi sana, tena mnunuaji ni huyohuyo Joshua.
Na hapo napo ndipo nikakutana na Vai pia akiwa amesindikiza Bale. Sasa baada ya
hapo wakati tunataka kuondoka, hapo Bale alishashituka sana pale Joshua
alipomtambulisha kuwa mimi ni mke wako.” Jema akamsimulia alivyopaliwa mpaka
akamletea na maji na aliyomwambia baada ya kunywa maji. “Mimi sikumjibu kitu
Bale, ila kurudi kwenye gari.” Akaendelea kumsimulia.
Vile Vai
alivyomkimbiza Joshua ili kuzungumza naye. “Ikawa kama anajitetea kwa Joshua!
Ikabidi kuongeza umakini. Kumbe hawa wawili wanaishi kwa kusaidiana haswa
katika kila khali. Ila nafikiri ni kama Vai alishaondoka kwa Bale, ikawa kama
akaishia hotelini na mwanaume mwingine.” Ikabidi hapo napo amsimulie tena,
maana hasira zilishampanda kaka mtu kusikia alikuwa hotelini na mwanaume.
“Maana Joshua
alimuuliza kwa ukali kidogo. Kama anayemlinda Bale. Akamwambia Vai, inawezekana
amesikia mambo mabaya sana juu ya Bale kiasi ya kwamba akaanza kumchukulia Bale
poa au kubweteka, maneno kama nayayofanana na hayo. Hapo joshua
ni mkali James, mpaka Vai alikuwa akitetemeka mpaka machozi. Akamuuliza ni kwa
nini aliondoka kwa Bale na kwa nini alirudi.”
“Ndio akajieleza
sababu ya kuondoka.” Akamsimulia yote mpaka kuwa Vai hana uwezo wa kuzaa. James
alibaki hoi mpaka ikabidi akae akiwa amebeba mwanae. “Kwa hiyo ndio akaondoka.
Akamsimulia kisa cha kuishia hotelini na mwanaume mwingine akiwa hayupo kwa
Bale. Hapo anajieleza kama vile Joshua anataarifa zote. Ndio nikazidi kuamini
Bale yupo karibu sana na Joshua, inamaana anamwambia kila kitu. Ndio Vai akajieleza
kuwa ni kama alilewa alipokaribishwa chakula huko hotelini na rafiki
yake, akaamka akiwa amelala na huyo mwanaume. Akajieleza kwa muda mrefu haswa.”
Jema akamueleza mumewe bila kumficha.
“Sasa kilichoniuma na
kuona Joshua atakuwa anatushangaa ni pale alipojieleza sababu ya kurudi kwa
Bale. Kuwa aliugua. Na hakuwa na pakwenda au mtu wa kumuuguza. Akamwambia Bale
ndio huwa akimuuguza muda wote. Yaani ikawa ni kama binti anayeishi
katikati ya watu, au ndugu, halafu hana mtu. Ndio akasema akakwama chakufanya
akampigia simu Bale, akaenda kumchukua, na kumuuguza. Akamwambia Bale ndio
amemfanya atulie chuo. Anamsaidia kwa kila hali. Akamwambia yeye hajajaliwa
akili nyingi sana za darasani, lakini Bale ndiye anamuhimiza shule. Anasoma
naye na..” Akamueleza mambo mengi. James hoi.
“Cha mwisho ni kama
akawa anaomba baraka za Joshua, kuwa na Bale. Akamwapia amebadilika. Hatarudia
alipokosea na hatamuumiza Bale, anaomba Joshua na yeye amsamehe na kumuamini
kama Bale. Na kuomba ni kama aseme kitu kwa Bale juu yake. Akasema ni kama
itamsaidia Bale kitu kama hicho au baraka zake juu yao. Kitu kinafanana na
hicho. Nikafikiria inamaana nafikiri kule kuondoka kwake na kujifungia na
mwanaume mwingine hotelini nafikiri ni kama Bale alimwambia Joshua halafu hakufurahia,
nafikiri au sijui kinachoendelea. Ila yeye alizungumza na Joshua kama anayejua
kinachoendelea katikati yamahusiano yake na Bale. Ikawa kama anamsihi amsamehe
na Bale ajue.” “Sasa huyo Joshua akamjibu nini?” James akauliza.
“Wewe unamjua Joshua.
Neno lake moja linamaanisha mambo mengi. Ila akamjibu kwa kifupi tu, anawaombea.
Akaondoka. Sasa hapo hilo linaweza likawa na maana nyingi.” “Na kama
hakuendelea kumuhoji Vai, inamaana alimuamini maneno yake.” James akazungumza akiwaza. “Na mimi
nilifikiria hivyo hivyo. Hili ndio kubwa
zaidi.” “Nini tena?” James akataka kujua.
“Nilijua wazi kuwa
mahusiano hayo ni ya Joshua tu. Naya hausiki. Maana mara ya mwisho kuzungumza
na Naya juu ya kaka yake, aliniambia hawana mawasiliano kabisa na wala hataki
hata afike kwake.” “Hilo hata Joshua aliliweka wazi ndio maana nashangaa!” “Sasa
sikiliza. Leo ilikuwa tupeleke watoto wakacheze, kama kawaida. Juzi nikampigia
simu kumuuliza kama bado mpango leo upo, akaniambia leo amewakaribisha nyumbani
kwake Vai na Bale kwa chakula cha usiku.” “Haiwezekani!” James akahamaki haswa.
“Kabisa. Na unawajua
wale ni watu wa maneno yao. Inamaana hivi tunavyozungumza, kina Bale walikuwa
nyumbani kwao pamoja na Vai. Kwa maneno mengine, huyu Vai amepokelewa kwa kina
Kumu. Na kama Joshua amempokea, na kubariki hili, ujue na Geb yupo nyuma
yake.” “Hakuna analofanya Joshua lakifamilia bila Geb.” “Ewaaah! Inamaana
mahusiano ya Bale na Joshua, yalikuwa yakiendelea bila Naya, ila Geb akiwa
nyuma yake. Inawezekana bila Nanaa, sababu uliwapiga marufuku asimsogeze Bale
kwa Nanaa. Ila nafikiri sasa, Naya alipojua kaka yake amefukuzwa hapa kwetu,
yeye kama ndugu, maana damu nzito kuliko maji,
akaingiwa huruma, akaona na yeye asiwe kama sisi. Akamfungulia milango ya
kwao.” James hoi.
“Inamaana Joshua
anajua kama nilimfukuza Bale hapa?” Akawaza kwa sauti. “Kabisa James. Maana
siku ile pale hospitalini nilimsikia akimuuliza Vai, atafanyaje na Bale, wakati
wewe humtaki?” “Haiwezekani Jema. Joshua!?” “Kwa kumsikia mwenyewe.
Anajua kabisa. Ila nimeshangazwa sana. Naya nishazungumza naye mara kadhaa
baada ya kuwafukuza hapa, hata hakulizungumzia na mimi!” “Na mimi
nishakutana na hao wote wawili. Joshua na Geb, hawakulizungumzia kabisa, kana
kwamba hawajui kinachoendelea! SIJAPENDA.” “Sasa hapo lazima kuwa makini
James.” “Nini? Kwa nini wanakuwa na mimi kama wananichora tu?” Kikamuuma na kawivu
kidogo.
“Kumbuka wewe ni kaka
ya Vai na Nanaa. Inamaana mambo yafuatayo. Joshua na Geb wanajua, kwa
Nanaa hukutaka kabisa Bale amsogelee. Ila kwa Vai ulimfukuza naye, na kuwaambia
waondoke pamoja. Na akiwa naye amkumbushe asitume moto. Hayo ni mambo mawili
tofauti. Kwa Nanaa ulimkataa kabisa Bale, ila kwa Vai hukutaka afike kwako. Ni
mambo mawili tofauti.” Jema akamfanya James apoe kabisa.
“Kwa kuwa tatizo hapa
ilikuwa ni humtaki kwako, ndio wao wamemfungulia milango ya kwao.
Inamaana watakuja kuungana na kina Magesa. Sisi tutabaki peke yetu tusioweza
kusamehe kwa mambo yasiyo tuhusu.” Hapo akambadilikia mumewe.
James akamtizama.
“Maana aliyekosewa mwenyewe amemsamehe na kumpokea Bale na Vai vile alivyo.
Tena akiwa sio mtakatifu. Ametoka kukosa, na bado wamemsamehe Vai na
kumkaribisha kwao. Na wewe unajua kwa Joshua ni jambo kubwa sana. Hakaribishi
kila mtu kwenye maisha yake, ndio maana mmebaki wewe tu na Geb kuwa watu wake
wa karibu kwenye maisha yake. Sasa mimi hili sitaki liniharibie
mahusiano yangu na Joshua kazini, na Naya.” Mama JJ akaendelea kuweka
msisitizo.
“Sina mpango wa
kutafuta kazi kwengine. Nataka kubaki nikifanya kazi kwa Joshua anayeniamini
kikazi. Aliniamini wakati hakuna mtu mwingine anaona uwezo wangu pale kazini.
Amenitengenezea nidhamu ya kazi na kunifanya mjuzi kwenye hichi ninachokifanya.
Anapigania masilahi yangu, akiwaambia watu wote mpaka wenye kampuni, kazi zake
haziendi bila mimi, ndio maana unaona nalipwa mshahara mkubwa sana, wakati sina
shule ya maana kichwani, na pale kazini ninaheshimika karibu sana na kama
Joshua.” Jema akaendelea kubadili gia angani.
“Na huku mtaani mimi
sina rafiki ninayeendana naye kama Naya. Maana huyo Nanaa unayempenda
wewe, alinifukuza kwake.” “Nilifikiri yaliisha!” James akauliza kwa upole. “Sasa
umeona nipo naye karibu kama Naya?” James akaona ili usiku huo asikose
yote, hapo asijibu.
“Naya ndio rafiki
yangu. Tunaendana na tunalea watoto wetu pamoja. Tunayo mengi yanayo endana
kuliko yeyote yule. Na sijawahi kuwa narafiki mzuri kama Naya. Tunaomba pamoja.
Na tuna siku maalumu ya kuombea watoto wetu pamoja na familia kwa ujumla.
Napata wapi mimi rafiki kama huyo?” Kimya. “Na usisahau Joshua ni god father
wa JJ. Inawezekana kwako isiwe na muhimu, lakini nataka JJ amjue Mungu na
kulelewa kwenye misingi ya kumjua Mungu kama Joshua.” “Naona umuhimu wake,
mama. Mbona tulishakubaliana yeye ndio atakua msimamizi wa JJ?”
“Sasa tengeneza.”
“Jema?!” “Hakika James. Sitakuwa tayari kumpoteza Naya, sababu ya dhambi za
Bale ambazo hata Mungu mwenyewe hazikumbuki. Kama humtaki hapa kwako,
basi. Lakini ijulikane ni hutaki tu aje kwako lakini huna neno jingine. Mimi
nataka mahusiano na kina Kumu. Yananisaidia kikazi na mtaani, pamoja na JJ.
Isingekuwa wewe, leo ningekuwa kwenye ukurasa mmoja na Naya. Lakini
amenitenga na si kawaida yake. Tunazungumza kila kitu na kupanga mipango yetu
pamoja. Lakini katika hili kumeshaanza kutengana, na najua moja litaanzisha
jingine, nitarudi kuwa peke yangu.” “Mbona ni kama unanilaumu tena?”
“Sasa wewe hujisikii
vibaya, mdogo wako wa kuzaliwa tumbo moja anakarimiwa na watu baki, wakati
kwako ulimfukuza?” Kimya. “Kila mtu atakuwa akituona sisi wa ajabu, zaidi
Joshua. Atajua wazi hujali dada zako.” “Sasa hilo si nila kurekebisha tu.
Nitaanza kuwa makini kwao pia.” “Wakati unarekebisha hilo, tafadhali rekebisha
na kwa Kumu.” James hoi.
“Tafadhali James.
Mimi nilifukuzwa na Nanaa, unakumbuka nilivyoumia?” “Na mimi niliumia Jema!”
“Basi tengeneza ukiwa unaelewa na Joshua ameumia, pamoja na Naya.
Na usisahau muhanga mkubwa hapa ni Vai, mdogo wako aliyeona
ukimuhangaikia Nanaa mpaka akaolewa, yeye umemfukuza na Bale.”
“Sasa si kwakuwa
nilikuwa nikimjua vizuri Geb!” “Yeye Vai anayajuaje hayo? Mtu haupo naye hata
karibu! Hujui anaishije! Nani anamtunza! Nani anajua uzima wake! Nani amempokea
kama alivyo! Na wewe ukaenda kufanya kama kile alichonifanyia Nanaa, mdogo
wako, au sijui mwanao! Unajua wewe mwenyewe mahusiano yenu na Nanaa. Lakini na
wewe umefanya kama alichonifanyia yeye huyo Nanaa, mwanao sijui, ukijua
madhara yake kabisa. Sasa rekebisha James. Mimi nataka mahusiano na kina
Kumu.”
“Nimeelewa Jema!”
“Huonekani kunielewa James. NATAKA MAHUSIANO NA KINA KUMU. Rekebisha kabla siku
ya kubarikiwa JJ kufika. Sitaki tension kwenye siku ya kubarikiwa
mwanangu.” Kisha Jema akaondoka. Kwa mara ya kwanza tokea amfahamu Jema, siku
hiyo akaona upande huo wa Jema.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Kibao Kimegeuka. Mungu Anayetenda Kwa Wakati, Yeye
Mwenyewe Ameanza Kutingisha Kuta, Milango Inafunguka Yenyewe.
James Atatengeneza Vipi?
Colins?
Yajayo Yanafurahisha Zaidi.
Usipitwe.
0 Comments:
Post a Comment