Baada ya miezi mitatu, Jerry akarejea nchini akiwa ametulia kabisa. Akahamia kwenye nyumba yao ikiwa imekamilika. Ila haina vitu ndani. “Naweza kukusaidia kununua thamani za ndani. Jumamosi tutoke, tukamilishe.” “Nitakamilisha na Tuma.” Kukazuka ukimya hapo! Wote wakihofia asije rudia uchizi wa kumsaka tena Tuma.
“Kuna ahadi alinipa Tuma, sio kwa kupaniki, ila najua kwa hakika ipo siku kila kitu kitakuwa sawa tu.” “Ila utahitaji kitanda Jerry. Huwezi kulala chini.” Hakujibu.
Ndipo ikabidi Jeremi kumwambia sasa kama Tuma alishika mimba, na kwamba hata Mbaki alimuacha kwa kugundua kama ni mjamzito. “Atakuwa ni mtoto wangu tu.” Akaongea akisikika mawazoni.
Anayeng’ang’ania Mlango, Siku Moja ….
Tarehe ya kwenda ubalozini ikafika. Pam mzoefu wa kukataliwa Visa zao. Mara nyingi alishakwenda hapo ubalozini na kukataliwa. Hakuwa hata na kujiandaa! Alishapazoea hapo, alishajua anaanzia wapi na kuishia wapi. Alishakuwa na uongo mwingi akiwa na karatasi za kueleweka lakini pia mara zote alishanyimwa.
Hapo alishakuwa mzoefu na taratibu zote. Hakuwa hata na wasiwasi wala paniki yeyote ile, kwani hakuwa na chakupoteza. Mill yupo nchini, na hapo amemsindikiza! Shema yupo naye! Maisha safi! Huwezi mbabaisha Pam na Marekani.
Akajivuta na tumbo lake baada ya kushushwa na Mill nje ya ubalozi wa Marekani, na kutembea kama anayelazimishwa! Taratibuuu.
Akamsalimia mlinzi getini, akafuata utaratibu kama wengine na kuongoza njia mpaka ndani. Akajikalia kihasara akisikiliza wengine wakihojiwa na kunyimwa. Akabaki akijichekea tu. Maana hapo walipo hao, yeye ashapita karibu kila dirisha na jibu likawa moja tu. Denied.
Hati yake ya kusafiria iliyoisha muda wake tayari, yaani ya zamani, ilijaa mihuri iliyokuwa ya kukataliwa tu. Hapo alikuwa na hati mpya. Ila alijua wazi wanazo kumbukumbu zake za zamani walizokuwa wamemkatalia.
Akajituliza hapo akiangalia mpaka aliposikia jina lake. Nchi ya Tanzania bado ilikuwa imefungiwa kuingia nchini Marekani. Kwa hiyo alisimama hapo mbele ya huyo mwanamke akisubiria mgongee muhuri wa denied, kuwa amekataliwa, kisha aondoke zake. Mill hakuwa mbali na hapo akimsubiria.
“Unahitaji mkalumani?” Likawa swali la kwanza. Kwa kuwa alijua hapatakuwa na mazungumzo mengi, akakataa. Anacho kilugha cha kuombea maji, alijua hatashindwa kumjibu maswali machache atakayomuhoji kabla hajamkatalia.
Akashangaa huyo dada anampa tabasamu na kumuuliza juu ya ujauzito wake. Pam akacheka akishika tumbo lake na kulipapasa taratibu. Akamwambia mbali na pressureinayomsumbua mara kwa mara na kumsababishia bed rest, anaona huyo mtoto ni mzima tu. Akaongeza akicheka kwamba anajihisi kubeba huko tumboni kama mtoto wa miaka miwili. Akamwambia anahisi atakuwa mkubwa kama kaka yake aliyechukua umbile la baba yake. Wakacheka kidogo akashangaa anamwamba arudi kesho kuchukua hati yake ya kusafiria. Amepata Visa.
Pam akatulia kidogo na kumuuliza. “Huhitaji kitu kingine chochote?” Maana hapo alibebeshwa maripoti kibao ya daktari ili kumuaminisha, cheti cha ndoa, sijui cheti cha Shema cha kuzaliwa, ilimradi tu Mill alimfungashia kila kitu ili kuwathibitishia, japo taarifa zake nyingi zilishaambatanishwa na barua ambayo yeye mwenyewe Mill alishawaandikia hapo akieleza juu ya hali ya mkewe akitaka wampe Visa.
Akamjibu akicheka kuwa hahitaji chochote kisha kumwambia, “Karibu nchini Marekani.” “Nisaidie maji ya kunywa.” Ndilo aliloweza kusema Pam akirudi kutafuta sehemu ya kukaa. Akamuuliza kama yupo sawa. Akamwambia yupo sawa ila midomo imemkauka gafla. “Sikutegemea kabisa!” Pam alijibu kuku akikaa sehemu waliyokaa wengine akipapasa tumbo lake.
~~~~~~~~~~~
Amakweli kukataliwa kwingi si hukumu ya milele, kesho kunaweza kuwa siku ya kukubaliwa. Hatimaye Pam ilifika siku ambayo mlango uliokuwa umefungwa kwa muda mrefu, umefunguliwa tena kipindi ambacho hata mamilionea wa Tanzania waliokuwa wakiingia nchini humo na kutoka kila siku, walikuwa wakikataliwa.
Bila kutarajia ndoto za muda mrefu siku hiyo zikawa zimetimia. Akabaki akinywa maji taratibu aliyokuwa ameletewa pale, HAAMINI! Huku wakitaka kuhakikisha kama yupo sawa au wamtafutie daktari amuangalie.
Aliposisitiza yupo sawa, alihitaji tu kutulia, “Nahisi nilisimama kwa haraka. Nipo sawa. Asanteni.” Akamalizia hivyo tu, na kuondoka zake.
Alipotoka tu, akampigia simu Mill. “Nimemaliza, naomba urudi kunichukua.” Akawa anaondoka hapo taratibu, bado amepigwa ganzi.
~~~~~~~~~~~
Na kwa kuwa hakumwambia kama amepata au kunyimwa, yeye Mill akajua moja kwa moja amenyimwa. Akarudi akiwa anaanza kujipanga maisha hapo nchini. Jinsi ya kupanua hiyo kliniki yao ya vipimo. Akajiambia inabidi wanunue mashine nyingi na za kisasa zaidi na watafute eneo lao kabisa.
Akaendelea kuwaza huku akirudi maeneo ya ubalozi wa Marekani kumchukua mkewe. Akamuona kwa mbali Pam anatembea taratibu ndipo akaongeza mwendo kumfikia kwa haraka asitembee sana.
~~~~~~~~~~~
Akasimamisha gari pembeni yake, Pam akaingia. “Pole. Wamekuuliza maswali mengi ya kukukera?” Hata hakusubiri ajibiwe, akaendelea. “Nilijua tu, ila sikuta kukukatisha tamaa. Jina langu limeharibika sana. Wasingeweza kukuruhusu uingie ukaishi na mtu kama mimi.” “Basi kwa taarifa yako wamenipa.” Mill akanyamaza kidogo. Pam akaanza kumcheka.
“Acha masihara bwana Pam!” “Nimeambiwa nirudi kesho saa nne, nikachukue hati yangu ya kusafiria, kwamba hapa nilipo nina Visa na nishakaribishwa huko Marekani kwenu ambako mwanao hamalizi kuniringishia.” Ulikuwa muujiza mkubwa sana kwa Mill.
Pam akamsikia akimshukuru Mungu wake na kujisifu eti kuwa, juhudi zake Mungu ameziona.
Jua Linaweza Kufunikwa Na Mawingu,
Lakini Haliachi Lichomoza.
Hivyo hivyo baraka zinaweza kuchelewa, lakini kufika tu. Huyo Pam alikuwa akibarikiwa na mama yake tokea ni katoto kakimsitiri kila alipokuwa akijisaidia. Basi kila anapomtoa mama yake nguo na kumsaidia maji ya kujisafisha kisha kukimbilia mtoni kufua. Akihakikisha mama yake hanuki japo alikuwa akisota mavumbini, mama yake alikuwa akimbariki sana.
Naye babu yake hakuacha kumbariki Pam kwa vile alivyokuwa akimuona anavyomlea mama yake kwa bidii bila kulalamika au kuchoka. Ikawa hivyohivyo na bibi yake pia. Alijawa baraka huyo Pam, usingeamini kule alikokuwa akipita na kuteseka. Ungeweza sema zile baraka zote alizokuwa akibarikiwa ilikuwa bure tu.
Maisha yalishampiga hapo nchini akiwa na huyo mtoto, ungesema analaanaanahitaji kuwekewa mikono au kupakwa mafuta ya upako. Lakini aliendelea kubarikiwa bila ya kuona hizo baraka kwenye maisha yake. Alilea kwa mateso makali huku bado akimtunza na mama yake. Alifika chini kabisa kiuchumi, hakujua kama kuna chini ingine iliyokuwa imebakia chini yake.
Na hapo pia alikuwa na baraka za baba mkwe wake. Mzee Mgini aliyemsaidia Mill hospitalini akiwa naye, mzee ananuka, mtu mwingine asingeweza kuwa karibu. Lakini Pam hakumkimbia Mill, wakamuuguza, mzee akiwabariki sana, mpaka kifo chake.
Napo hapo zikawa kama zile baraka ni hewa tu, kwani ndipo walipotengana hao wawili kwa miaka 10 na Mill kuishia kumuoa Kisha, nakupata majanga yakumtosha.
Akiwa na baraka za baba yake, nyingi tu. Lakini ndio akaishia kufungwa jela na kupoteza kila kitu. Ikawa na yeye ni kama hakuwa amewahi kutamkiwa baraka!
Kumbe Mungu wao alikuwa akizitunza zile baraka na kuwapitisha kwenye shule ngumu huku wakilipa garama ya makosa yao mpaka vichwa vilipokaa sawa na kutulia, ndipo na Mungu alipoliangalia kapu lao, nakuona jinsi lilivyojaa, akaanza kufungua madirisha ya mbinguni.
~~~~~~~~~~~
Wawili hao wakiwa na mtoto mmoja tayari, tena kaka mkubwa tu na ujauzito, hatimaye ndoto zilizogoma kutimia kwa muda mrefu, zikatimia kukiwa hakuna matumaini wala juhudi zao, ila Mungu tu. Waliondoka nchini kwa haraka sana kama wanao kimbizwa!
Pam akatua nchini Marekani akihisi bado yupo ndotoni. Maisha yao yakaanza yakiwa yamejaa mafanikio makubwa sana. Kwani hata kabla ya Pam hajarudi chuo kusomea mambo ya unesi, Jo kwa makusudi akaomba kazi kwenye hospitali ileile aliyokuwa akifanya kazi akijua jinsi alivyoondoka na jina zuri. Walipomjibu kwa haraka, akawapa sharti la kumuombea Visa na mkewe, yaani Dorothy. Jo akawaambia anahitaji barua kutoka kwao, lakini atalipia kila kitu.
Uzuri wa Jo aliacha kazi hapo, lakini hakuacha kutibu. Aliendelea kutibu watu nje na ndani ya hiyo nchi ya Marekani. Na uzuri wa udaktari ni kwamba, muda unavyozidi kwenda, na kuzeekea kazini, inamaana wewe ndio bingwa, na thamani inaongezeka.
Baada ya miezi michache baadaye, naye Dorothy akaondoka nchini akiwa na Jo. Jo akamsaidia Mill, kwa kutumia jina la Pam, wakafungua kampuni kubwa aliyokuwa akitamani Mill.
Alijawa shukurani Mill, maana milango ile iliyokuwa migumu sana akitumia njia nyingi za uongo kufanikisha na pia kushindwa, Mungu alikuwa akifungua kwa urahisi kama mchezo tu, akijidhihirisha kuwa yeye ni Mungu, badala yake hakuna mwingine.
Wasambaa hao wawili, wakajikuta wapo tena pamoja upande wa pili wa dunia.
~~~~~~~~~~~
Pam alizaa watoto wengine watatu, akafikisha wanne akiwepo Shema. Mill aliposhika mtoto wa nne wa kike, hapo akachora mstari.
“Aisee inatosha Pam. Mimi sitaki timu kubwa kama ya mzee Mgini.” “Cha mwisho! Na huyu naye apate mdogo wake wa kucheza naye! Tunaweza bahatisha wakike mwingine.” “Hakika HAPANA. Ulisema unataka wa kukufunika nguo ukiwa mzee. Ushapata. Huyu atacheza na kaka zake, lasivyo hatutakaa tukamaliza.” “Mmoja wa mwisho! Watano ndio namba iliyokamilika.” Mill akatingisha kabisa kichwa akikataa.
“Hivi nakwenda kufanya vasectomy kabisa. Maana nakuona wewe mwenzangu hii kelele na vurugu humu ndani unapenda. Utakuja nishikia mimba nyingine uje uniambie ni bahati mbaya. Hapana. Acha mimi nijiwahi.” Hakutaka mengi, yeye Mill ndio akaenda kufunga uzazi, kuepusha watoto wa bahati mbaya.
~~~~~~~~~~~
Akiwa na jina hilohilo baya nchini humo, Mungu alimrejeshea Mill mali zotealizopoteza na zaidi. Maana safari hii alikuwa na uungwaji mkono wa Pam, ambaye walikuwa wakielewana kitamaduni. Migogoro ya ndoa ilikuwepo kama kawaida, lakini kulikuwa nakuheshimiana na kunia mamoja wakijua wanajenga chao na kwa faida ya watoto wao.
Huo ndio MWISHO wa Pam, Mill, Jo & Dorothy.
~~~~~~~~~~~
Zindiko la moyo ni mtu wako, hata akienda mbali, mtakutana kwenye njia panda.
Miezi 5 ilikuwa imeshapita tokea tukio la birthday yake. Kazi na maisha yakiendelea, ila haachi kumpigia simu Tuma. Kila akitulia anampigia kujaribu. Namba ileile. Anaweza piga hata mara 10 kwa siku ila bila paniki. Pale alipokuwa akiishi na Eli alishahama na hakujua alihamia wapi.
Siku moja jumamosi alikuwa kwake akiangalia movie. Saa saba usiku akajaribu kumpigia tena Tuma. Akashangaa inaita. Alishituka Jerry, akakaa kwa haraka sana. “Tuma!?” Kimya kwa muda. “Mbona upo macho mida hii?!” “Nina vichomi vikali!” “Pole. Ulikwenda hospitalini?” “Nilikwenda kama siku mbili zimepita, wameniangalia, hakuna kitu. Ila nitakwenda kuonana na daktari mwingine pengine kuna vipimo atataka nifanye. Waone kama kuna tatizo.” “Pole.” “Asante.” Kimya kwa muda.
“Sasa kuna mtu anakusaidia?” “Nilikuwa na mama hapa, pamoja na Eli. Wote wameondoka. Eli alibahatika udhamini wa kwenda kusomea udaktari nje ya nchi. Alituma maombi kwa imani tu. Tena hata matokeo yalikuwa hayajatoka. Akaweka matokeo ya nyuma, wakamjibu ameingia kwenye orodha ya wanao mfikiria, akipata ya mwisho awatumie. Matokeo yalipotoka, amepata zote A, akawatumia. Wamempa udhamini kwa asilimia 100 kwa sababu alifanya vizuri sana.” “Wapi?!”
“Nchi moja ipo mashariki mwa bara la ulaya. Belarus.” “Hongera Tuma! Hongera sana.” Tuma akacheka taratibu. “Aisee ulijinyima sana kwa ajili yake.” “Amefurahi huyo! Ameondoka hapa kama anilambe!” Wakacheka.
“Na mama?” “Alikuwepo hapa, tulibakia naye hapa baada ya mwanae kuondoka. Tulikaa naye hapa karibia mwezi, akajirudia zake kwake, ila ameniambia atarudi.” “Kwahiyo umebakia peke yako?” “Nipo tu.” Kimya.
“Tuma?” “Nipo Jerry. Nimekumiss mwenzio!” Jerry akajikuta machozi yakimtoka nakushindwa kujibu. “Nimemmiss Jerry yule tuliyekuwa tukila naye ugali, tembele na maharage.” Akaendelea taratibu.
“Sio Jerry huyu aliyekuwa na mamilion ya pesa na matenda ya mabilio! Hapana. Jerry yule ambaye…” Akawa kama anayefikiria. “Yule ambaye katikati ya kelele za jiji. Kelele za kudhalilishana. Kelele zilizojaa purukushani za mahangaiko yasiyo na utoshelevu, kusaka bila kuridhika. Ushawishi usio koma, lakini katikati ya fujo zote hizo, aliweza kusikia maneno ambayo mdomo ulishindwa kutamka.”
“Jerry yule aliyekuwa na uwezo wa kusikia moyo wangu, katikati ya yote hayo, nakuweza kujibu.” Akatulia tena na kuendelea. “Nimemmiss Jerry yule ambaye hisia zetu zilikuwa zikiweza kuendana na kujibishana kwa upendo.” Kimya akimsikiliza.
“Jerry yule mbaye tulikuwa tukinywa naye chai ikisindikizwa na andazi tu, sio mikate iliyojazwa mengi, masoseji na mayai lakini macho yake hayawezi kuniangalia!”
“Nammiss Jerry yule tuliyekuwa tukikaa na kuweza kuangaliana na kuonana mpaka mtu wa ndani. Jerry anayejali. Ambaye hata ukiwa naye karibu, hujisikii upo mbali. Jerry tuliyeweza kutoana upweke.”
“Jerry asiye bosi wangu, ambaye tukikaa tunazungumzia majukumu yangu tu, na pesa. Asiyeniona mimi kama mfanyakazi tu, ila mimi kama Tuma pia. Asiyenitizama kama baba J anitazamavyo.”
“Nammiss Jerry ambaye alikuwa akiniambia anahitaji muda na mimi zaidi. Aliyekuwa akichukia kukimbizana na pesa tu, ila kuthamini muda wetu wa pamoja. Kila kitu kinasimama, tunakaa sisi wawili tu. Kunaweza kusiwe na la kuzungumza. Ila ukimya na uwepo wa kila mmoja wetu ukatosheleza kila kitu. Tukatoana upweke, sisi wawili tukawa na nguvu kama jeshi kubwa. Huyo ndiye Jerry niliyempoteza.”
“Nimerudi Tuma. Tena nimerudi Jerry bora kuliko huyo uliyekuwa naye, aliyekuwa akitembea ameharibika ndani, ila uwepo wako ulimsaidia kutembea mjini. Sikujua kama nilikuwa bomu, ulilokuwa ukilishikilia, mpaka ulipoondoka. Aisee ilikuwa mbaya Tuma!” Tuma hakuwa ameelewa.
“Mbaya ile ya kurukwa na akili, kuwa mwendawazimu napewa dawa za vichaa!” Tuma alishituka sana. “Jerry!” “Acha Tuma. Ilikuwa mbaya sana. SANA. Nilikuwa kwenye matibabu miezi mitatu, hivi ndio nimerudi nchini na kuendelea kukutafutanikijitahidi iwe mara 10 tu kwa siku, ili nisichanganyikiwe tena.”
“Yale maneno ya mwisho niliyokwambia siku ile ya birthday yangu, yaligeuka risasi inanipiga mimi mwenyewe. Ikaanza kichwani. Yanajirudia vile nilivyokwambia neno kwa neno, yakanitesa na kushindwa kufikiria kabisa, na ofisi nikafunga.” “Haiwezekani Jerry!”
“Oooh ilikuwa mbaya. Mbaya sana, na mbaya maneno hayarudi na hayafutiki. Yakitamkwa yametamkwa.” “Lakini ulikuwa sahihi Jerry! Nilifanya kitu ambacho ulishaniambia hutaki!” Hapo hakuchangia, akaendelea.
“Nilikuwa siwezi kufikiria wala kitandani siwezi kutoka maana nikaanza kusikia na misuli inanibana. Siwezi kula, siwezi kutoka kitandani na kina Jeremi nafikiri waliamua kuniacha tokea siku ile nilipoharibu kwenye birthday yako. Kwa hiyo nikawa nipo peke yangu. Nakupigia kwa kurudiarudia zaidi ya sekunde Mungu alizoweka hapa duniani. Nakutafuta wewe na Eli kama mwehu!”
“Siku moja usiku ndio nikazidiwa, nikahisi nitakufa peke yangu. Nilikuwa siwezi kuhema natapatapa kitandani peke yangu, wewe sikupati. Ndio nikampigia simu bro. akaita gari ya wagonjwa, nikakimbizwa hospitalini. Nimetoka pale baada ya siku mbili, moja kwa moja uwanja wa ndege, nchini Marekani.” “Jerry!”
“Nilikuwa na hali mbaya sana. Sikujua maisha yale niliishi na Sandra na wanae kwa miaka yote ile kumbe yaliniathiri vibaya vile! Maana nilikuwa nikiyabeba, na kuyavumilia kila siku. Ile ya watoto wangu kuniita majina mabaya, tena kwa wazi kabisa, ilikuwa ikiniingia vibaya sana, na sikuwa na jinsi ila kuyabeba tu. Iliniathiri mno.”
“Basi, matibabu ya akili yakaendelea kwa muda. Daktari alipoona kichwa kimeanza kukaa sawa ndipo sasa nikaanzishiwa matibabu ya mwili na nafsi. Therapy ya muda mrefu kuweza kufunguka kwa uhuru kueleza kile kilichokuwa kikiendelea huku kila mtu mpaka wale madaktari nimewapa namba yako ya simu nikiwaambia wawe wanajaribu kukupigia.” Tuma akazidi kushituka.
“Jerry!” “Ilikuwa ni kazi ya kila mtu, mpaka Jemimi akaniomba achukue yeye hiyo kazi ili ninapokuwa na madaktari wawe na kazi ya kunitibu mimi, yeye awe anakutafuta wewe.” “Pole Jerry. Pole sana.” Akavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu.
“Jemimi akashika kazi ya kuwa anaangalia muda wa huku, anakupigia sasa ili niwe nalala. Na nikiamka nataka kuona jinsi alivyokupigia, ndio naridhika. Bro ikabidi aje sasa kule, yaani yeye ndio akawa bora kuliko therapist aliyekuwa akimlipa anisaidie, maana Jemimi alimwambia baba yake, yule therapist amemwambia nikiwa naye nataka awe anakupigia tu wewe. Ndio bro akaja sasa kule.”
“Alizungumza sana na mimi mpaka nikatulia, nakuanza kuzingatia matibabu.” “Alikwambia nini?” Tuma akihofiwa asiwe alimwambia aachane naye. “Aliniambia kwa wakati ule, sipo kwenye nafasi ya kuwa kwenye mahusiano ya aina yeyote ile, na kwa yeyote yule. Aliniambia siwezi nikatoa kitu ambacho sina. Aliniambia lazima nipone. Nijijenge mimi kwanza. Kikombe changu kikijaa ndipo naweza kugawia wengine. Hapo ndipo nikaweza kuweka simu pembeni na kuendelea na matibabu kwa kuzingatia sasa.”
“Akachukua likizo yeye na mkewe. Jeremi naye akaja na familia yake kule. Angalau kukawa na mazingira ya kinyumbani. Tunafanya mambo pamoja. Tukatoka pale tukaenda Jamaica kwa kama siku nne hivi. Nafikiri bro alipoona nimetulia, ndipo tuliporudi Marekani yeye na mkewe wakaondoka kurudi huku, na kuniacha nimalizie matibabu.”
“Ila Jeremi na familia yake tulikaa nao mpaka tukaja kurudi nao huku nikiwa nimepona kabisa na nina mipango yakueleweka ya kuendelea. Na ndipo waliponiambia ulishika mimba.” Kimya kwa muda.
“Hofu ya kuwa usije kuwa ulitoa mtoto wangu, ikaniingia, nikikumbuka alichokifanya Umi alipojigundua ana mimba ya Mbaki na Mbaki hamtaki. Nikakumbuka kuwa tokea mwanzo wewe hutaka mtoto, ila mimi. Ndio kazi ya kukutafuta tena ikaanza.” “Pole Jerry. Pole sana.”
“Pole na samahani wewe Tuma. Nilikulipa ambacho hukustahili.” “Sasa kazi?” “Nilifanikiwa kufungua tena milango ya ile ofisi. Nimemrudisha Juli, na nimeajiri vijana wengine wawili. Mmoja ambaye atakuwa akihusika na manunuzi ya tenda zote, na mwingine wa kutunza kumbukumbu za stoo na kufuatilia mambo madogo madogo. Ila ofisi yako bado ipo vilevile. Au ulishapata kazi kwingine?” Tuma akabaki ametulia akifikiria.
“Tuma? Bado nakuhitaji katika kila eneo la maisha yangu. Naomba nafasi ingine. Utaona tofauti.” “Naomba safari hii iwe tofauti Jerry. Tuchukulie taratibu.” “Ukimaanisha nini?” Jerry akauliza kwa wasiwasi.
~~~~~~~~~~~
Usikose sehemu ya mwisho ya Simulizi hii ya
Love, at first sight.
0 Comments:
Post a Comment