Hakujua
kama ni laana au mkosi unaomwandama katika maisha yake. Kila akijiangalia
hakuona tofauti kubwa aliyonayo na wasichana wengi wanao tamkwa ni warembo! “Sasa
kasoro yangu mimi ni nini?” Ni swali lililokuwa likimuumiza sana
Nanaa, binti aliyekulia kwenye nyumba ya dada wa mama yake, mama yake mkubwa,
tokea anazaliwa mpaka anakua.
Kwa hakika wakiitwa wasichana wazuri, na yeye
akakisimama, hawezi akaambiwa akae. Hata umbile halikuwa na tofauti sana na
maumbile ya wasichana wengine wanaofanya wanaume washindwe kujizuia
kuwasindikiza kwa macho. Hata ngozi yake ya mwili, si wanaume tu walioisifia
kuwa ana rangi nzuri, tena moja mwili mzima, bali hata wasichana wenzake
walitaka kujua ni nini anatumia kinachomfanya kuwa na rangi nzuri kiasi hicho!
~~~~~~~~~~~~~~
Mama
yake Nanaa, Wini, alishika mimba akiwa mwanafunzi wa sekondari ya shule ya
wasichana Weru Weru. Akiwa binti mdogo wa kidato cha tatu tu, ndipo alipotimiza
kusudi zima la kuletwa Nanaa duniani. Ugumu ulikuja kwa Wini, asijue tumbo hilo
analipeleka wapi kwa kuwa alikuwa akilelewa na mama ambaye alishawapa msimamo
wake tokea wanakuwa. Alishajiwekea misingi na kanuni ambazo aliwahakikishia
hazitawahi kuvunjika. Mojawapo ni kutoleta nyumbani kwake mtoto nje ya ndoa,
zaidi mtoto huyo akiwa hana majibu yakutosheleza. Kama baba yake.
Hayakuwa maneno ya bure ya vitisho tu kwa binti
zake, alimaanisha mama huyo. Kwani mama yake Wini na Maria ambaye ndio dada
mkubwa, alishakuwa gumzo pale kijijini. Hakutaka watoto hao watimize kile watu
wanachosema juu ya uzazi wake. Baada ya kashfa nyingi akichekwa hapo kijijini,
Kirua Vunjo, hapo hapo Moshi. Ilimbidi mama huyo kuangukia kanisani. Alishika
dini bila kupenda. Kanisani ikawa ndio kimbilio pekee. Masista na mapadri,
wakageuka kuwa rafiki zake hapo kijijini baada ya kuachwa na mumewe.
Nyumbani kwa Ulimali, yaani baba yake Wini na
Maria, na mkewe huyo mkubwa, ilikuwa huzuni kila mwaka. Kama sio mimba ya mama
huyo kuharibika, basi mtoto aliyebahatika kuzaliwa, atakaa siku chache tu,
kabla ya kutimiza hata mwezi, tena mara zote wanakuwa watoto wakike, hufariki
bila hata ugonjwa. Mtoto wa kwanza ambaye ni Maria, alizaliwa bila shida. Mara
tu baada ya mama huyo kuolewa, akampata Maria. Mzee Ulimali akajipa moyo akijua
mtoto atakayefuata, atakuwa wa kiume kama alivyotarajia. Miaka ikazidi kwenda, vifo
vya watoto wa kike vikaongozana, mpaka mzee Ulimali akakata tamaa.
Alitafuta mke mwingine. Hakutaka kwenda mbali
sana. Alioa hapo hapo kwenye kijiji cha Kirua Vunjo. Lakini safari hii alipata
mke upande wa kaskazini, na kumuacha mkewe mkubwa upande wa kusini. Alibahatika
kuoa binti mdogo tu. Mkewe huyo wa pili akaanza kwa kuzaa watoto wa kiume
mapacha, jambo lililomfurahisha huyo mzee, nakuamua kuachana kabisa na mkewe wa
kwanza, ambaye alikuwa na uzazi wa shida, tena wa watoto wakike watupu ambao mzee
Ulimali hakuwataka. Aliwaita hasara.
Wakati mzee Ulimali anaondoka rasmi kwa mkewe,
alimuacha akiwa mjamzito. Mkewe hakutaka kumwambia kwa kuhofia historia
kujirudia. Asije akamwambia ni mjamzito, baada ya siku chache mimba
ikaharibika, au akaja kuzaa mtoto mwingine wa kike, tena asikae muda mrefu,
akafa. Akaamua anyamze na ujauzito wake. Akaachwa na mtoto mmoja tu wa kike,
Maria. Ndipo baada ya miezi tisa kutimia, hatimaye ndipo akazaliwa mama Nanaa,
yaani Wini, ambaye naye alibahatika na kifo cha utotoni. Wini mwenyewe
alipatikanika au alizaliwa wakati baba yake alishakimbia nyumba hiyo, aliyosema
ina mkosi.
Akasaidiwa kulea watoto wake hao wawili wa kike
na kanisa katoliki la Uchira, yeye kama mwajiriwa wa kanisani hapo. Kanisani
kukawa ndio kimbilio pekee kwa mama huyo. Kusali na kwenda kwenye misa, kwao
haikuwa ni swali. Ratiba za kanisani zilijulikana nyumbani humo kama wanavyojua
majina yao. Kuanzia jumatatu mpaka jumatatu. Asubuhi mpaka jioni. Kipindi cha
kwa resma, kufunga halikuwa ni jambo la mjadala. Kulipikwa chakula cha usiku tu
wakati wakufungua.
Dini na maadili yake ndio ulikuwa wimbo ndani ya
ile nyumba. Mama yao aliwasisitiza kufuatwa bila kukwepa au kukosea. Watoto
wake wote walishapitia mafunzo ya komunyo ya kwanza na kipaimara na wakafuzu.
Waliijua katekisimu ukurasa kwa kurasa. Walijua Sala za kuombea mambo mbali
mbali na mtakatifu nani anasaidia nini ili wamuombe, halafu huyo mtakatifu
awaombee kwa Mungu. Kama ni safari, basi walijua wazi, mtakatifu Christopher
ndiye mtakatifu sahihi wa kuwa naye safarini. Ikija kwenye kusali rozari, hapo
hawakuhitaji hata kufikiria. Walijua wapo kifungu gani, wamtaje nani au watamke
nini, bila shida yeyote na bila kukosea. Kwa kuwa sala ilikuwa sehemu ya maisha
yao.
Akitaka kusisitizia jamii kuwa yeye hatetereki
kwa kuachwa na mumewe sababu ya kuzaa watoto wakike watupu, ambao ni Maria, na
Mama yake Nanaa, ambaye ndio Wini, mama huyo wakichaga, alipapambana kufa na
kupona kulea binti zake kimaadili na kusomesha. Alimpa mtoto huyo jina la Wini
baada ya kufanikiwa kushinda kifo, na kuzaa akiwa na umri wa utuuzima. Sista
aliyekuwa akimsaidia kipindi alipojifungua mtoto huyo, ambaye walikuwa
marafiki, alimshauri ampe jina hilo la Wini. Kwani alishakaa muda mrefu sana
bila kushika mimba baada ya kuzika watoto wengi, wakati Maria mtoto wake wa
kwanza akiwa ameshakuwa binti mkubwa tu.
Kumpata mama yake Nanaa, aliyefanikiwa mpaka
kutoka naye hospitalini akiwa hai, ulikuwa ushindi mkubwa sana kwake. Hata aibu
ya kuwa ni mtoto wa kike, iliisha. Baada ya kutoka naye hospitalini, akarudi
naye nyumbani, mwezi ukapita mtoto huyo akiwa bado hai, ukawa ushindi wa namna
yake. Na ndipo alipombatiza jina la Wini. Lakini akiwa hana mume tena,
na anajulikana ana mkosi.
Watu walisubiri kifo cha Wini, lakini wakashangaa
akikuwa mpaka akafaulu vizuri sana kwenda shule ya wasichana Weru Weru
sekondari. Mtoto huyo alijulikana pale kijijini kama ana akili sana.
Aliwaendesha wakaka aliokuwa nao darasani, kitu kilichofuta machozi ya mama yao.
Mama yao alifanya kila aliwezalo kutunza binti zake
waliokuwa na tofauti kubwa sana ki umri. Hakuwa masikini wala tajiri.
Alifanikiwa kuwapa wanae maisha ya kawaida tu. Dada mkubwa alibahatika kupata
mume akiwa binti mdogo baada ya kuhitimu chuo chake cha ualimu, akaolewa kwa
heshima kubwa sana pale kijijini, wakati bado mama yake Nanaa, Wini yupo
shuleni.
~~~~~~~~~~~~~~
Mara baada ya Wini kushika mimba, hapakuwa na
mjadala. Kuepusha aibu, mama yake alimfukuza nyumbani kimya kimya. Hatimae yale
yaliyokuwa yamezungumzwa na baba yao na watu wengine yakatimia. ‘watoto
wa kike ni bure kabisa. Wanaishia kuzaa nyumbani tu!’ Ndio usemi huo
aliokuwa akiusema baba yao mpaka kuondoka kwake. Akiwa anaficha aibu hiyo, mama
yake alimtoa yule binti bila kutaka kujua atakapo kwenda na huku akimuonya
asije wahi kurudi tena pale kijijini bila ya ndoa au na huyo aliyempa mimba.
“Ukirudi hapa uwe na baba wa huyo mtoto, tena akiwa anakuja kulipa mahari.
Akuoe.” Ndivyo alivyoagwa Wini nyumbani kwao.
Baada ya kufukuzwa kwao, Wini alitoka kijijini
kwao na kuhamia mjini akiwa bado binti mdogo, asiyejua maisha. Akajitupa jijini
Moshi akijaribu kupambana na maisha bila mafanikio. Alitoka kwao akidhania
angeweza kuishi peke yake, lakini akagundua maisha si rahisi kama alivyodhani.
Aliona vile mama yake akihangaika na kazi za shamba na hapo kanisani ambako
aliajiriwa, akajua ingekuwa rahisi kwake.
Wakati anakua, alimuona wakati mwingine mama yake
akibeba parachichi na ndizi kwenda kuuza kwenye uzio wa kanisani na mashuleni.
Kwa pesa chache alizokuwa ametoka nazo nyumbani, na yeye akaiga. Hakuhitaji
mtaji mkubwa kununua sinia na parachichi. Akaanza huku akijiwekea mikakati kama
alivyomuona mama yake akifanya wakati anamlea yeye na dada yake kabla ya
kuolewa. Ndivyo alivyojua na yeye atapambana mpaka mtoto wake akue.
Mambo hayakuwa marahisi hivyo. Alianza kutanga
tanga jijini Moshi, akitafuta pakuishi bila mafanikio. Kufunga na kufungua
akajikuta ni omba omba mkamilifu, asijue chakufanya mtaani. Jua, baridi, mvua,
vyote vilikuwa vyake. Hakuna aliyekuwa akimuona yeye kama yeye. Cha kwanza
walilitambua tumbo. Binti mdogo, mjamzito. Tayari ikawa sababu tosha kwa jamii
kumnyooshea kidole.
Kwake siku hazikuwa zikikimbia kama alivyokuwa
akisikia kwa watu wengine wakilalamika. Aliweza kuhesabu sekunde, dakika, saa,
siku, juma, mwezi, akiwa hana tumaini. Maisha yale duni aliyokuwa akiona
wanaishi nyumbani kwao na kutamani maisha ya wengine, gafla akageuka kuyatamani
sana. Alikuwa akilia nakutamani arudishe siku nyuma ili awepo nyumbani kwao.
Hata nyumba ya mama yao akaanza kuona ilikuwa ni Jumba la kifahari, akatamani
arudi, lakini alikumbuka jinsi alivyotolewa kwa siri pale kijijini.
~~~~~~~~~~~~~~
Ilikuwa ni alfajiri sana. Mama yake alimpandisha
kwenye gari ya kwanza iliyokuwa ikipita pale kijijini kwao, ili hata mtu
asimuone baada ya usiku uliopita kupata uhakika Wini ni mjamzito. Hakutaka
kujua aliyempa mimba wala hakutaka mjadala. Baada ya kuona mabadiliko kwa
mwanae huyo aliyekuwa yupo likizo, wakati anakaribia kurudi shuleni, ilibidi
kumuuliza. Kwa kuwa alikuwa mkali sana, ilimbidi Wini akiri kuwa kweli ni
mjamzito. Mama yake hakutaka kesi. Alimwambia aende kulala. Wini akijua
yamekwisha, alishangaa anaamshwa kukiwa hata hapajapambazuka. Akaambiwa akaoge,
ndipo alipopewa maneno yake ya mwisho, na kuagwa rasmi hapo nyumbani asiamini
kama kweli yamemkuta.
~~~~~~~~~~~~~~
Kitanda cha kawaida sana alichokuwa
akilalia nyumbani kwao, akaanza kukiona kilikuwa cha thamani kubwa sana kila
inapofika usiku na kutafuta pakujilaza. Hofu ya kubakwa kila siku usiku
anapolala huko mtaani, ikamfanya aanze kutanga tanga kila siku usiku akibadili
sehemu za kulala ili wahuni wasijue usiku huo alipo. Alihangaika kila sehemu
mpaka dada yake mkubwa alipomchukua na kumuhifadhi nyumbani kwake.
Tena alimuhifadhi kwa kuwa watu walikuwa
wakimsema na kumtaka msaidie mdogo wake aliyekuwa akitangatanga mtaani na tumbo
kubwa. Hakujulikana anaishi wapi, lakini alionekana akizunguka mchana akitafuta
kazi au msaada kwa ndugu jamaa na marafiki.
Ndipo habari zikamfikia dada yake, yaani Maria.
Alipotolewa nyumbani, mama yake alitangazia kila mtu kuwa Wini alikwenda kwa
dada yake huko mjini. Akitoka huko atarudi shuleni moja kwa moja, hatarudi tena
pale kijijini. “Dada yake amemuita huko mjini, kabla hajarudi
shuleni.” Huo ndio ukawa usemi wa mama yao kwa kila aliyemuulizia Wini
pale kijijini. Kwa hiyo kwa pale kijijini ikawa mama huyo ametoa balaa hilo, la
aibu kwa muda. Hakuna aliyejua kama Wini alikuwa mjamzito.
Isipokuwa majiraji wa chache wa dada yake
palepale mjini. Walikuwa wakimuona Wini akimfuata dada yake kazini kuomba
msaada hata wa pesa ya kwenda kula. Mwanzoni Maria alidanganya walimu wenzake
kuwa hamfahamu ni nani. Lakini ikawa ngumu. Rangi zao za mwili zilifanana sana.
Wakachukua umbile linalofanana na mama yao. Kuanzia urefu na muonekano mzima wa
nje. Maria na Wini walifanana kwa asilimia kubwa, japo Wini alikuwa mdogo sana
kwa Maria.
Wini alikuwa akihangaika. Akiona amekwama kabisa,
njaa imemlemea, ndipo alikuwa akikimbilia kazini kwa dada yake aliyekuwa
akimsema sana ndipo anamsaidia vijisenti kidogo. Dada yake alipoacha kazi,
akahamia kuomba msaada pale nyumbani kwake. Wakati mwingine alikuwa akifika
hapo nyumbani kwa dada yake kwa kujiiba. Anajificha mpaka ahakikishe shemeji
yake hayupo ndipo anamfuata msichana wa kazi, ataomba hata kiporo. Akishakula,
anaondoka kwa haraka sana ili shemeji yake asimkute nyumbani kwake kwani
alishampiga marufuku yeye na dada yake. Akikataa kabisa Wini kukimbilia pale.
Alimtaka Wini arudi nyumbani kwao, akaombe msamaha, atulie kijijini baada ya
kushindwa shule kuliko vile anavyotangatanga mjini. Na hapo ndipo majirani na
wafanyakazi wenzake Maria, ndipo walipomuona Wini na kujua kama ni ndugu na
Maria.
~~~~~~~~~~~~~~
Lakini huo haukuwa wakati wa dada yake, Maria,
kumkaribisha mtu yeyote aende kuishi nyumbani kwake. Kwanza ndio na yeye
alikuwa kwenye bed rest ya mimba aliyokuwa ameitafuta kwa takribani miaka 10,
tena kwa shida sana. Alishakuwa kwenye ndoa ya muda mrefu, alijaliwa mtoto wa
kwanza wa kiume. Wakamuita James. James alibaki mtoto wa pekee kwa muda mrefu
sana huku wazazi wakihangaika kutafuta watoto wengine lakini baba yake, au
mumewe Maria akiwa hana pressure sana, kwani tayari analo dume lake, James.
Shuguli ilikuwa kwa Maria akitaka watoto wengine. Alikumbuka shida alizokuwa
akimuona mama yake akipata wakati akitafuta watoto, akazidi kujiogopesha kitu
kilicholeta kuchanganyikiwa zaidi. Hakutaka apitie alikopita mama yake. Lakini
angalau yeye alitanguliza mtoto wa kiume. Ikawa nafuu kwenye ndoa.
James alipatikanika mwaka wa kwanza tu
baada ya wazazi wake kufunga ndoa. Ilikuwa faraja kubwa sana. Baada tu ya
kujifungua James, Mama yao na Wini akiwa bado mdogo tu, walifika hapo mjini
kumsaidia kumlea Maria akiwa kwenye uzazi. Baada ya siku chache alimchukua
Maria na mwane huyo mchanga James, na kurudi naye kumlea kipindi hicho cha
uzazi pale kijijini. Wakaomba James abatizwe pale pale kijijini kwa bibi yake.
Angalau tu kusuta watu na kuwaonyesha watu kuwa hakuwa na uzazi mbaya. Mume wa
Maria alikuwa na kazi nzuri. Alijijenga mjini maeneo ya Majengo. Kwa hiyo muda
Maria yupo pale kijijini analelewa uzazi, ndio Wini naye yupo binti mdogo tu.
Baba yake James akaweka heshima pale kijijini. Kulikuwa kukiletwa vyakula hapo
nyumbani kwao kila kukicha. Na siku ya ubatizo wa James, kukachinjwa na
ng’ombe, watu wakaalikwa. Wakala na kunywa mbege mpaka wakachoka. Bia
zakueleweka zilikuwepo.
Ukweli Maria alimpa heshima mama yake. Maria
ukawa ndio mfano anaoimbiwa Wini tokea anakuwa mpaka anafukuzwa kwao. Ni kweli
Maria alifanana zaidi na mama yao, hasa tabia. Wote walikuwa wazungumzaji sana.
Na walipendana na mama yake kama marafiki. Ukimkuta Maria anazungumza na mama
yake, utafurahi. Ungejua ni marafiki walio shibana. Kwa mshahara wake wa
ualimu, hakuacha kumsaidia mama yake kumtunza Wini. Tena alipoolewa na mume
mwenye uwezo, ndio kila mtu alijua. Maisha ya mama yao yakaleta aghueni kubwa
sana.
~~~~~~~~~~~~~~
Lakini baada ya kumzaa James. Kipenzi cha bibi
yake. Maria alikaa miaka 10, akihangaika kila mahali kutafuta watoto. Huku
akikumbuka kashfa na adha ya mama yake aliyomuona akipitia mpaka baba yao
kuwakimbia, wakati anakuwa. Hofu ya kuolewa mke wa pili au kukimbiwa, ikaanza
kumtesa. Mama yao alizunguka kila mahali na Maria, kuhakikisha anashika mimba
ya pili. Hakutaka kile alichopitia yeye, ndio Maria apitie. Alimsaidia bila
kuchoka. James akageuka kuwa mtoto wa bibi kipindi hicho mama yake akihangaika
na uzazi.
~~~~~~~~~~~~~~
Mwaka huo mama yake Nanaa anafukuzwa nyumbani,
ndio na dada yake naye alikuwa ameshika mimba. Akawa radhi kuacha kazi na
kuchukua bed rest ya ujauzito wa mtoto aliyemtafuta kwa shida sana.
Wakati Wini anahamia kwa dada yake akiwa na mimba ya miezi 6 anaelekea 7, dada
yake ndio alikuwa amebakisha siku chache ajifungue.
Wakati mtoto wake wakiume James alishatimiza
miaka 10 anatafuta 11, ndipo akajifungua mtoto mwingine wa kike. Wakampa jina
la Viola. Na ndipo baada ya miezi mitatu baadaye, binti huyo mdogo, yaani mama
yake mdogo James na Viola, Wini, akiwa hajulikani mwenye mimba hiyo ni nani,
akapatwa uchungu mida ya saa tatu usiku.
Alihangaika mwenyewe chumbani akitaka asisumbue
wenye nyumba wake. Hasa shemeji yake aliyetamka wazi wazi na yeye hamtaki mle ndani.
Lakini muda wa mtoto kutoka au kuzaliwa ukifika, umefika tu. Hauchagui
mazingira wala ulipo. Haujali hali ya mama aliyonayo kwa wakati ule. Akitakiwa kutoka duniani,
lazima atoke. Alihangaika mpaka usiku sana chupa ikapusuka akiwa peke yake
chumbani. Aliingiwa na hofu pale alipoona damu zinatoka, ndipo akaenda
kumgongea dada yake. Akakimbizwa hospitalini. Akaingizwa chumba cha
kujifungulia, lakini binti huyo mdogo, yaani mama yake Nanaa hakufanikiwa
kutoka humo kwenye chumba cha kujifungulia, akiwa hai. Hata hakubahatika
kumnyonyesha Nanaa. Alipata matatizo ya uzazi, akafariki wakati daktari wa zamu
alipokuwa akimsaidia kumtoa mtoto. Damu chache aliyokuwa nayo Wini, iliendelea
kumwagika mpaka mauti ilipomfika.
~~~~~~~~~~~~~~
Ndipo ilipobidi Maria, dada yake Wini arudi na
huyo mtoto, nyumbani bila kutarajia. Jina hilo la Nanaa, Wini alimuachia James,
mtoto wa dada yake. James alikuwa akijisogeza sana karibu na Wini wakati yupo
nyumbani kwao. Siku moja alimfuata mama yake mdogo, akamuuliza mtoto akizaliwa
ataitwa nani, akamwambia Nanaa. Baada ya mtoto kurudishwa nyumbani, Maria akiwa
amechanganyikiwa. Hajui chakufanya na huyo mtoto asiye na mama wala baba, ndipo
James akawaambia wasimuite tu mtoto, anaitwa Nanaa. Kila mtu alimshangaa James.
Lakini alionekana anauhakika na huyo mtoto. Ndipo kuanzia hapo akaanza kuitwa
Nanaa.
Alilelewa kwa shida sana kwani alikuwa ameingilia
penzi la mtoto aliyetafutwa kwa shida yaani Viola, na mume wa Maria alikuwa
akimuhesabia Wini siku ili atoke nyumbani kwake. Alimruhusu Wini kujifungua tu,
kisha akamwambia mkewe baada ya hapo anataka Wini aondoke na mtoto wake. Wakati
Viola mtoto wao anatimiza miezi mitatu ndio Nanaa alizaliwa na kuachwa akiwa
hajulikani baba, ila mama aliyefariki. Kwa hiyo ikabidi siku za mwanzoni na
yeye kunyonyeshwa kama Viola na mama huyo ambaye aliona mtoto wake anapunjwa.
Huku mumewe akimlaumu mkewe kumpokea Wini, mama yake Nanaa tokea mwanzoni. Kila
Nanaa alipokuwa akilia wakati mdogo, mumewe alitoka nje kabisa akisema hataki
kusikia sauti ya huyo mtoto. Alimlaumu mkewe kuleta matatizo ndani ya nyumba
yao.
Nanaa alikataliwa hata kwa bibi yake. Alikataa
kabisa Nanaa asirudishwe pale kijijini. Kwanza alikataa hata kumtambua kama ni
mjukuu wake. Baba yake James, ambaye ni mume wa Maria, alikuwa akimsimanga
mkewe, mchana na usiku. “Kama hata mama yake mzazi alimfukuza, kwa nini
wewe ulimpokea? Huyo binti ni tatizo mke wangu. Unajitafutia balaa.” Hayo
ndiyo maneno aliyokuwa akiyapata kutoka kwa mumewe wakati wa uhai wa Wini. Tena
mbele yake. Mbaya zaidi ni pale mdogo wake alipofariki.
Ni kweli balaa likatokea. Akaachiwa mtoto ambaye
hawakujua pakumpeleka. Mumewe alisema sana. Kwani hata mazishi ya Wini ni kama
yalifanywa na rafiki za dada yake. Mumewe alikataza kabisa maswala ya msiba
nyumbani kwake. Maiti ya Wini iliagwa katika hospitali ya taifa KCMC na
kupelekwa makaburini. Alizikwa kimya kimya, bila ibada wala mama yake kuwepo.
Ni kama alitupwa tu, habari ikaisha.
Baada ya kuzunguka na huyo mtoto akitaka amtoe
pale ndani na kushindwa, ndipo ikabidi amlee Nanaa mlemle ndani. Lakini kwa
shida sana. Mumewe alikataa kumsaidia kabisa. Hakutaka hata shilingi yake
kumtunza huyo mtoto aliyejua ni balaa ambalo mkewe amelileta ndani ya hiyo
nyumba. Watu walisema mama yake Nanaa alikufa sababu ya kulaaniwa na mama yake.
Kwa hiyo hata Nanaa, amebeba mkosi.
~~~~~~~~~~~~~~
Kwa shida, dhiki na mateso, Nanaa akakua. Alikula
chakula kama watu wote mle ndani. Alinunuliwa nguo pale inapolazimu, hasa sare
za shule. Lakini mara nyingi alivaa nguo za watoto wa mama yake mkubwa pale
zinapokuwa ndogo kwao au mama huyo anapotaka kubadilisha nguo za mwanae Viola,
ndipo alipopewa Nanaa. Kwa Nanaa hakuona shida, kwani alikuwa akikua akiona
hivyo. Na tangia anapata uelewa wake, akiwa mtoto mdogo sana, mama huyo
alihakikisha anamuelewesha Nanaa na kuelewa kuwa pale alipo anasaidiwa tu. Kwa
hiyo Nanaa alikuwa akijua anasaidiwa tu. Na alisimuliwa vile alivyokuwa
ikimlazimu mama huyo kukesha kumlea yeye, badala ya kupumzika na mumewe. Kwa
hiyo kila alichokuwa akipewa Nanaa, alishukuru sana na kufurahia.
Alishajua hastahili chochote mle ndani. Yeye
anasaidiwa tu. Tena aliaminishwa pale alipo ni sehemu ya thamani sana kwake,
kwani alikataliwa kila mahali. Hata bibi yake alimkataa. Alimuona hata akifika
pale hataki kumgusa wala hata kuzungumza naye. Alikaa naye mbali kabisa huku
akimkaripia kila akimsogelea. Alimuona bibi yake vile anavyompenda Viola,
mjukuu wake aliyemuhangaikia sana mpaka kushikwa mimba yake. James ndio alikuwa
kipenzi kabisa cha bibi huyo. Na hata Nanaa alijua. Yale mazingira yote
yakamfanya kuelwa na kujua ni kweli pale alipo ni sehemu sahihi, na yale ni
maisha anayopaswa kuyatumikia vizuri.
Usingemkuta akilalamika kama anateswa. Hakujua
maisha mengine zaidi ya yale aliyokuwa akiishi pale kwa mama yake mkubwa. Kwa
hiyo akajua inamlazimu kuishi vile. Tena alitakiwa kushukuru sana. Ila kadiri
alivyozidi kukua na kuona mapenzi anayopewa Viola na wazazi wake, kitu kipya
kikaanza kujengeka ndani yake. Ikaanza kuibua shauku ya kutaka kupendwa na
kuthaminiwa na yeye kama Viola. Lakini hakuacha kukumbushwa bahati aliyoipata
baada ya mama yake kumuacha na mama yake mkubwa kumpokea. Kwa upande mwingine,
ikabidi awe mpole.
~~~~~~~~~~~~~~
Walipofikisha miaka miwili tu, Viola akiwa
amemtangulia kwa miezi 3, mama mkubwa akapata mimba ambayo hakutegemea. Akazaa
mtoto wa kike mwingine ambaye alimuita Vai. Hapo ndipo Nanaa alipokuwa mtu
mzima gafla. Akaanza kutumwa hiki na kile kumsaidia mama mkubwa kulea mtoto
huyo mchanga. Baada ya muda mfupi mtoto huyo mdogo, aliyekuwa akilingana kabisa
na watoto wake akageuka kuwa mtumwa, akiwatumikia wanae wote mle ndani. Nanaa
akageuka kuwa mkubwa kuliko hata James. Alibeba majukumu makubwa kuliko wenzake,
na akalinganishwa na msichana wa kazi.
Yeye alisoma shule za kawaida za serikali, lakini
wenzake walisoma shule za kulipia. Walikuwa wakifuatwa na basi la shule pale
nyumbani, yeye ilimlazimu kuamka mapema kama anavyoamka msichana wa kazi pale
nyumbani, ambaye alikuwa akilala naye chumba kimoja. Anaandaa kifungua kinywa
na kusaidia usafi, baada ya kula ndipo awahi shuleni akitembea kwa miguu. Na
jioni anapotoka shule, ilimlazimu kusaidia kazi za pale ndani. Ikiwemo kupika,
kunyoosha nguo za wazazi wa mle ndani, na ndugu zake kama alizilifua siku hiyo
asubuhi, na kuwawekea vyumbani kwao, na kusaidia kazi nyingine za mle
ndani.
Kama ungelimuuliza Nanaa kuwa anateswa,
asingesema anateswa. Aliambiwa anawajibika kufanya yote hayo ili baba yake
mkubwa asije kutafuta msichana mwingine wa kazi, akachukua nafasi ya kuishi
yeye mle ndani. Kwa hiyo alipambana kwa kadiri ya uwezo wake kuonyesha hamna
kazi ya kuhitajika msichana wa kazi wa pili mle ndani. Yeye na msichana wa
kazi, wanatosha kabisa, kumudu kazi zote za mle ndani. Mwanzoni majukumu ya
kuwahudimia wenzake yalimlemea sababu ya umri mdogo na kazi nyingi. Lakini
kadiri siku zilivyozidi kwenda na umri uliposogea, akaweza kumudu majukumu yake
vizuri, hakuona shida tena. Alijipendekeza kwa kadiri ya uwezo wake ili
kuwafurahisha walezi hao ambao baba mwenye nyumba hakuwa hata na muda naye.
~~~~~~~~~~~~~~
Mida ya jioni walikuwa na utaratibu wa kula
pamoja, na kila mwenye habari zake huo ndio muda wakuziongea na kucheka kabla
ya kwenda kulala. Kina Viola walikuwa wao ndio wenye habari za kuvutia kwani
walisoma shule za kisasa na walikutana na watoto wa matajiri, lakini sio Nanaa.
Kwanza anakuwa amechoka, na pili alikuwa akiomba Mungu wamalize mazungumzo hayo
mapema ili wakamalizie kazi za siku hiyo na wao wapumzike. Yeye Nanaa na dada
wa kazi ndio walikuwa wa mwisho kulala ili kuhakikisha sinki la jikoni halilali
na vyombo vichafu na jikoni panaachwa pasafi kila siku.
Muda wa kuangalia tamthilia ukifika, watu wote
walikusanyika sebuleni wanaangalia tamthilia pamoja. Mama yake mkubwa alikuwa
mcheshi sana, maneno mengi hayakuwa yakimwisha. Basi huo nao ukawa muda wake wa
kuchekesha kila mtu mle ndani. Baada ya watoto wake kukua, alijitupia kwenye
biashara. Hakuweza kurudi tena kwenye kazi yake ya mwanzoni, ya ualimu.
Alikuwa na maduka ya nguo na vipodozi anayomiliki
hapo mjini. Kwa hiyo alikutana na watu wengi tofauti tofauti na vituko vingi
alivyokuwa akisimulia arudipo nyumbani kila siku. Mumewe alikuwa meneja wa
kampuni ya kahawa mjini Moshi. Aliweza kuongeza kipato hapo nyumbani, nakufanya
maisha ya familia yake kuwa mazuri. Lakini alihakikisha pesa yake au jasho lake
linakwenda kwa wanae aliowazaa yeye tu, na si vinginevyo.
Alijulikana kama mwanaume mbahili, lakini si kwa
watoto wake. Tokea Nanaa anazaliwa na kuletwa pale nyumbani, alishawekeana
makubaliano na mkewe, huyo mtoto wa nyongeza sio jasho lake na yeye hatahusika
kwa lolote. Kwa hiyo Nanaa aliishi pale, lakini akihudumiwa na mama yake mkubwa
huku akikumbushwa mara kwa mara tokea mtoto anasaidiwa tu. Na kila pesa
iliyotumika kwake kibinafsi, aliambiwa ni kiasi gani na ni jinsi gani
ilivyomgarimu mama yake mkubwa. Iwe ni ada au michango midogo midogo
aliyotakiwa kupeleka shuleni. Tena shule yenyewe ilikuwa ya bure ya serikali. Lakini
ilikuwa lazima awekwe chini na kuelezwa ugumu wa pesa alionao huyo mama.
Majukumu mazito yanayomkabili yeye kama mama mwenye watoto watatu wenye
mahitaji kama yake Nanaa, lakini anawanyima wanae, au anajinyima yeye, au
anashindwa kumsaidia mama yake mzazi kule kijijini, inabidi apewe pesa hiyo
yeye ambaye baba yake hakujulikana na mama yake alishafariki. Kwa hiyo Nanaa
alikuwa akikuwa akijijua yeye ni mzigo kwa mama yake mkubwa, na inamgarimu sana
kuwepo pale na kumsaidia.
~~~~~~~~~~~~~~
Japokuwa hapakuwa na mateso ya moja kwa
moja ambayo mtu anaweza kulalamika kuwa anateswa, lakini yale maisha
yaliendelea kuibua shauku mbali mbali ndani ya Nanaa. Akitamani kuwa na chake
au mtu anayemuhitaji, asiyemuona mzigo wala kumlalamikia kwa kila kitu. Ni
kweli hakuwa akiteswa kwani alitakiwa kufanya kazi kama watoto wengi
wanavyokuzwa, japo wenzake hawakuwa wakifanya kazi pale nyumbani. Alitakiwa
kuamka asubuhi na mapema, kama mtoto mwingine yeyote anayepewa malezi mazuri ya
kufundishwa maisha, japo ilimlazimu yeye kuamka kuwaandalia mazingira mazuri
wenzake kina Viola na Vai, wenye umri unaokaribiana sana na yeye, ili waende
shule wakiwa hawajachoka.
Alikwenda shule kwa kutembea tofauti na wenzake,
lakini hilo pia aliambiwa ni baba yao ndio anawalipia usafiri wa kuwaleta na
kuwarudisha shule, yeye Mama Mkubwa hana pesa ya kumsomesha huko wanakosoma
wenzake, kwa kuwa inabidi kununua chakula cha kutosha na yeye ale vizuri na
alale pazuri. Nanaa hakuwahi kulalamika. Akaelewa ni kweli anatakiwa kuwa mtu
wa shukurani. Tena wakati mwingine alifanya kwa ziada ili kumfurahisha mama
yake mkubwa. Alijitahidi sana kufanya kazi pale ndani ili kumfanya Mama Mkubwa
akitoka kazini apate muda wa kupumzika tu. Kila alipokuwa akirudi nyumbani,
Nanaa alimuwahi na kikombe cha chai, au maji na ikitokea kuna juisi, basi
alimpa Mama Mkubwa hiyo juisi na tabasamu kubwa usoni lililojaa unyenyekevu
huku akitoa pole na kupokea mkoba.
Alijitahidi sana asiwe tatizo mle ndani ya
nyumba. Kila wakati alikumbushwa yaliyompata mama yake. Akajitahidi kutulia
kabisa. Hasa katika mapenzi. Japo Mama Mkubwa alisharuhusu kama kuna mmoja wao
amepata mwanaume, basi ahakikishe huyo mwanaume anafahamika hapo nyumbani.
Alitoa ruhusa ya kuletwa pale nyumbani afahamike. Aliwaambia binti zake kuwa
hiyo itasaidia kuongeza heshima kwa huyo mwanaume. Kwa hiyo hata kama alikuwa
na wazo la kumchezea tu, kama mama yake Nanaa alivyochezewa, basi huyo mwanaume
ataogopa.
~~~~~~~~~~~~~~
Japokuwa ni kama walilingana na Viola lakini
mwenzake alimpita mbali sana kimakuzi. Alizungumza lugha ya kingereza kwa ufasaha.
Alikuwa binti mwenye kujiamini. Alisoma shule nzuri. Alijua kuzungumza mbele za
watu bila shida na alishaleta wanaume pale kwao kama marafiki, tena vijana
wazuri tu na wanaonekana wasomi kama yeye mwenyewe Viola na Vai. Na Nanaa
alihusika katika matayarisho ya pale ndani ikitokea Viola na mdogo wake
wanataja siku ya wanaume zao kufika hapo nyumbani.
Nanaa alikuwa akiwatamania wenzake waliofanikiwa
kupata wazazi wanaowapenda na kuwajali, na pia isitoshe, walibahatika kupata
wanaume wazuri. “Na mimi nikija kumpata mwanaume wangu kama huyo kaka,
nitampenda sana. Nitahakikisha tunaoana naye ili tukizaa watoto wetu tuwalee
wenyewe wasihangaike au kusumbua watu kama mimi. Tutaishi kwenye nyumba yetu
nzuri na watoto wetu wazuri, tuta..” Ni mikakati aliyokuwa akijiwekea
Nanaa kila siku alipokuwa akikaribisha wanaume wa Viola na Vai.
Alikuwa akimshangaa Viola vile anavyochezea
bahati. Alipata bahati ya wanaume waliompenda lakini hakuwahi kuridhika.
Hawakukosa kasoro. Akaishia kuwabadilisha mchana na usiku huku akieleza vituko
vyao na kuwafanya hata mama yake acheke, kama jambo la kawaida tu.
~~~~~~~~~~~~~~
Mpaka Nanaa anamaliza kidato cha nne, katika
shule za kutwa hakuwa akimjua mwanaume kimapenzi. Alipata vishawishi vingi.
Zikiwemo lifti za kurudishwa nyumbani. Walimu na wanafunzi wa shuleni hapo Old
Moshi sekondari. Wakimpa ahadi nyingi zakuvutia, lakini Nanaa akafunga moyo.
Akakana nafsi yake, akamaliza kidato cha 4. Alifaulu kwenda kidato cha 5.
Akachaguliwa katika shule ya wasichana Ashira.
Mwanzo Mpya.
I |
likuwa
furaha kubwa moyoni mwa Nanaa. Angalau anakwenda kuanza maisha sehemu nyingine,
mbali na nyumbani hapo kwa mama yake mkubwa. Shule zilipofungua, akaondoka
rasmi nyumbani akiwa na matarajio ya pumziko huko shuleni. Akaanza kuonja ladha
ya maisha mapya. Akafurahia utulivu aliokuwa akipata mbali na kelele za pale
ndani kwa kina Viola ambazo alikuja kujua upo uwezekano wa kuishi mahali
pengine na ukafurahia maisha mengine mbali na maisha aliyoaminishwa ndio maisha
pekee hapa duniani. Shule akawa mkombozi wa kwanza wa Nanaa. Ikampa ladha
ambayo hakutarajia. Moyo wake ukapenda na kuthamini zaidi elimu. Akajiambia
shule ndio mkombozi wake.
Akaanza kupendeza na kuvutia. Shule hiyo
iliyokuwepo juu kabisa ya kimlima kikali cha Marangu, kwake ilikuwa ni mbingu
ndogo. Hakuwa akitamani shule zifungwe. Hakuwa akielewa wanafunzi wengine
waliokuwa wakilalamikia maisha ya pale shuleni. Alituliza akili zake zote
shuleni. Baada ya muda mfupi tu, akapata na rafiki ambaye ndio aliongeza ladha
nzuri zaidi ya maisha hapo shuleni. Aliitwa Anni. Wakaanza kuongozana kila
mahali na Anni.
Alex.
Siku moja Anni alitembelewa na kaka yake Alex.
Akamtambulisha Nanaa kwa kaka yake. Alex akampenda sana Nanaa. Akaanza kutafuta
sababu za kuwepo shuleni hapo kwa kisingizio anakwenda kwa dada yake. Kila
wazazi walipotaka kumtumia kitu Anni shuleni, Alex akawa mtu mzuri sana
wakujitolea kwenda Ashira kupeleka mahitaji ya dada yake. Hakujali mlima huo wa
Marangu kufika shuleni hapo, nia ni kumuona tu Nanaa. Ukaanza urafiki kati ya
Nanaa na Alex pia.
Safari za Alex kumtembelea Anni dada yake Ashira
zikawa nyingi. Nyumbani kwa kina Alex na Anni ilikuwa Arusha. Kwa hiyo Alex
akapata sababu nzuri sana ya kila siku za jumamosi kuwepo kwenye shule hiyo ya
wasichana Ashira, tena akigaramiwa na wazazi wao, wakijua anakwenda kumtembelea
Anni, binti yao mdogo.
Hisia za
kimapenzi zikaanza. Nanaa akavutiwa na ujio wa mara kwa mara wa Alex kwenda
kuwatembelea. Lakini Alex alisisitiza huwa anakwenda pale maalumu kwa ajili
yake yeye. Nanaa akaona ni upendo ulioje! Arusha mpaka Marangu! Tena kupandisha
kilima kikali kile ili kumfikia yeye tu. Alex akafanikiwa kuuteka moyo na
mawazo ya Nanaa.
Kumbuka, shauku kubwa ya Nanaa, ilikuwa kupata
mtu atakayeonyesha anamuhitaji YEYE. Hakujali sura wala umbile. Yeyote yule
atakayemuhitaji, basi alijiapia kujitoa kwake. Sasa kumpata Alex aliyeonyesha
utayari wa kuvunja ratiba zake zote, ili awe naye! Ilimgusa sana. Akajua yeye
ndio atakuwa mwanaume wakumtoa pale nyumbani kwa mama yake mkubwa. Amuoe, kisha
wakaishi naye popote kule Mungu atakapowajalia. Ampunguzie mzigo mama yake
mkubwa na kuepuka chuki ya baba yake mkubwa ambayo wala hakuhitaji kuificha.
Alimuonyesha kila mtu waziwazi, kuwa hataki kujihusisha na huyo mtoto.
Mahusiano ya mapenzi yakaanza. Nanaa akamwaga
moyo wake wote kwa Alex, akionyesha wazi yupo tayari kufanya lolote kwa kijana
huyo. Kama ulishaona wanawake desparate hapa duniani, basi Nanaa
aliwashikia bendera. Akawa kama aliyechanganyikiwa na Alex. Naye Alex
akaonyesha kumuhitaji vilivyo. Kwa mara ya kwanza, Nanaa akapata mtu baki,
mbali na kaka yake James, anayempenda na kumjali. Akapata faraja ya ajabu
moyoni. Akapata mwanaume wa kwanza, mbali na James, anayeweza kukaa naye na
kumsikiliza.
Anni alipokuja kugundua, akaamua awe anawapa
nafasi. Alex anapokuja shuleni, anafikia Ashira B, atajificha sehemu ambayo
alikuwa akikutana na Anni na Nanaa. Anni atamsalimia kaka yake na
kuchukua mizigo yake, na kuwapisha. Yakaanza mabusu yakuagana. Akifika tu
shuleni hapo, wa kwanza kuitwa ni Nanaa, ndipo ataitwa mdogo wake. Yakaja na
mabusu ya kukaribishana. Moto wa mapenzi ukawaka ndani yao. Wakaona hawatosheki
kwa mabusu. Tena mbaya zaidi mabusu yenyewe hayakuwa ya muda mrefu sababu ya
mazingira. Wote waliona hamna sababu yakusubiri tena, wakakubaliana kipindi cha
likizo fupi, kabla Nanaa hajarudi nyumbani, watafute chumba mahali, watumie
siku hiyo kuridhishana, kisha jioni ndipo aende nyumbani akijidai ndio ametoka
shuleni.
Na ikawa hivyo. Nanaa akiwa hamjui kabisa
mwanaume kwa umri huo akiwa kidato cha 5, akaamua kugawa bikra yake kwa Alex.
Haikumsumbua wala dhamira haikumuuma kwani walikubaliana kuona mara Alex
atakapo maliza chuo. Alex alikuwa chuo cha uhasibu Arusha. Ndio alikuwa mwaka
wa 1, wakati Nanaa yupo kidato cha 5. Kwa hiyo Nanaa alikuwa amejitoa kwa moyo
mweupe kwa mwanaume atakayekuwa mumewe pindi atakapo maliza chuo hicho. “Hata
hivyo sifanyi kosa kama mama. Mimi nafahamika na Anni dada yake. Halafu Alex
sio muhuni kama mwanaume aliyemrubuni mama. Mimi nitakuwa mwangalifu, sio kama
mama. Siwezi shika mimba.” Hayo ndio maneno aliyokuwa akijifariji nayo
Nanaa anapokwenda kujifungia nyumba za wageni na Alex.
Kwa kuwa hakukamatwa mara ya kwanza, basi
wakajenga mazoea ya kukutana mahali, nakutumia siku nzima kufanya mapenzi,
ndipo Nanaa anarudi nyumbani. Mwaka wao wa kwanza wa mapenzi ukaisha vizuri.
Nanaa anapokuwa likizo, basi mawasiliano hayakukauka. Alex akiwa jijini Arusha,
Nanaa nyumbani kwao Majengo, mjini Moshi. Wakati mwingine akiwa likizo, Alex
alikuja Moshi kumtembelea Nanaa.
Siku za kufungua shule zinapofika, Alex
alimsubiria Nanaa mjini, akiwa ameshachukua chumba mahali. Nanaa anakwenda
hapo. Wanatumia siku hiyo wakiwa wawili, kisha jioni Nanaa anakwenda shuleni,
au analala mpaka kesho yake ndipo anakwenda shuleni. Na siku za kufunga shule
hivyo hivyo. Alex alimfuata mpaka shuleni. Anamchukua asubuhi hiyo, wanakwenda
Moshi mjini. Wanachukua chumba kwenye nyumba za kulala wageni. Mpaka jioni
ndipo Nanaa anarudi nyumbani na kuendelea kwenda kumtembelea Alex hapo
hotelini. Atamtumikia mwanaume huyo bila kuchoka, mpaka anapoondoka kurudi kwao
Arusha.
Penzi likakolea. Alex akawa anapata anachokitaka
kwa Nanaa, japo kwa upande wa Nanaa, yeye mapenzi hayakuwa muhimu. Hakujali
kama anafurahia yale mapenzi. Ilimradi alipata mtu atakayemtoa kwenye yale
maisha. Ni kweli hapakuwa na shaka kama watakuja kuona pindi watakapomaliza
shule. Alex alishamuhakikishia maisha mazuri mara baada ya kuona. Basi Nanaa
alitoa mwili wake kwa Alex kama mumewe huku akiwa mwangalifu asishike mimba,
asije zaa kabla ya kufunga ndoa. Wakachagua majina ya watoto wao. Wakapanga
idadi na jinsia ya watoto watakao zaa. Penzi likaendelea mpaka Nanaa alipomaliza
kidato cha 6. Akaona ndio muda muafaka na yeye kupeleka mwanaume nyumbani kwao.
~~~~~~~~~~~~~~
Wakati Nanaa anapanga kumpeleka Alex nyumbani,
alikuwa ndio anajiandaa kwenda kumaliza mwaka wa mwisho chuoni. Nanaa na Viola
ndio walikuwa wamemaliza kidato cha sita, wapo nyumbani wanasubiria matokeo
yao. Baada ya kumaliza tu shule yake ya kidato cha sita, Viola akaenda jijini
Dar kumtembelea James, kaka yake. Alikaa kwa muda kidogo tu, ndipo Vai naye
baada ya kufunga shule akamfuata Viola dada yake. Wote waliondoka huku
wakimringishia Nanaa kuwa wanaenda jijini Dar, kwenye starehe. Yeye anatakiwa
abaki asaidie kazi za mle ndani.
Nanaa alitamani sana na yeye aongozane nao,
angalau akapaone tu Dar, au atoke nje ya mkoa wa Kilimanjaro, lakini mama mkubwa
alimkatalia. Kwanza alimwambia hana pesa ya kumpa ya nauli halafu anamajukumu
pale nyumbani. Hawezi kumruhusu asafiri. Nanaa akaridhika. Akabaki mle ndani
akifanya kazi. Siku Alex alizoweza kwenda kumtembelea, basi Nanaa ilimlazimu
kutoroka nyumbani mida ya mchana ambayo mama yake mkubwa yuko kwenye majukumu
yake ya kila siku, anakwenda kumuhudumia Alex huko hotelini kisha kurudi kwa
wakati.
~~~~~~~~~~~~~~
Maisha yakaendelea. Nanaa akitafuta wakati
mtulivu wakumtambulisha Alex kwa mama mkubwa. Kila mama mkubwa aliporudi
nyumbani, hakuacha kueleza starehe wanazopata wanae huko jijini Dar kwa kaka
yao James na vile kaka yao anavyowafurahia. Ikawa hamna nafasi ya mtu mwingine
kuzungumzwa pale ndani, wala kusikilizwa. Ni matambo ya mama mkubwa tu, kwa wanae
huko jijini Dar.
Siku wasiyotarajia, kabla hata shule ya Vai
haijafungua, akaona Viola na Vai wanarudishwa pale nyumbani na kaka yao James.
Alimuona James akizungumza na mama mkubwa, lakini hakujua kulikoni. Lakini
akamuona kaka James akiondoka bila mmoja wao!
Lakini yeye akafurahi kuona wamerudi, akajiambia
ule ndio wakati wa kumtambulisha kwao Alex, ili wasiendelee kumdharau. Ilikuwa
ndio kwa mara ya kwanza na yeye Nanaa ana habari njema kama wenzake ya kupeleka
mwanaume anayempenda nyumbani kwao. Kwa muonekano Alex hakuwa mbaya. Aliweza
kutambulishwa kokote bila shida. Swala la kuwa ana lafudhi ya kiarusha ikawa ni
mojawapo ya kivutio kwa Nanaa. Wala hakujali. Na ukichanganya pesa ya wazazi
wake, basi Nanaa alijua lazima ataweka heshima hapo nyumbani.
Tofauti na matarajio yake, alijua angesifiwa
baada ya kutoa habari hizo. Lakini walimcheka sana. Wakijua kwa ushamba alio nao
kwa wanaume, ataleta kituko mle ndani. Wasijue Alex ni mtoto wa mjini na Nanaa
sio mshamba kama wanavyodhani. Alishakuwa na huyo mwanaume kwa takribani miaka
miwili. Na Nanaa hakuwa bikra kama walivyodhani. Alex alikuwa akifaidi penzi
lake kwa siri kwa muda mrefu tu.
~~~~~~~~~~~~~~
Huo Ulikuwa
Utambulisho Tu, Kuweka Msingi Wa Mengi Mazito Ya Mbeleni.
Usipitwe na Mikasa ya Mapenzi Kwenye Saafari ya Nanaa.
Kipi kiliendelea kati yake na Alex?
Je, alienzi penzi la Nanaa?
Usikose Muendelezo.
0 Comments:
Post a Comment