~~~~~~~~~~~~~~~~~
Zikapita kama siku mbili hivi, mida ya mchana
akamfuata tena Jelini. “Kwani wewe unakaa maeneo haya!” Ikabidi amuulize. “Sio
mbali na hapa. Ni kama tu njiani nikiwa nakwenda kwangu. Nimetoka kukutana na
mtu sehemu. Tukapata chakula cha pamoja, nikaona nikuchukulie na wewe.” Jelini
akakunja uso. “Mimi huwa sipokei vitu vya watu hovyo, Ezra! Sipendi kuhongwa.”
Kama kawaida yake, akaongea bila kuchuja fikra zake.
Ezra akacheka
taratibu akimtizama. “Ni chakula tu, Jelini! Hakuna hongo hapa. Kama bado
hujala basi nimekupunguzia haso yakutafuta mlo wa leo. Ila kama umeshakula,
unaweza mpa yeyote hata wafanyakazi wako.” Jelini akajishauri, akamtizama
akifikiria, kisha akakataa kabisa.
Na hapo Ezra akawa
muungwana. “Tafadhali usinielewe vibaya.” “Hata kidogo. Uwe na amani kabisa.
Nilileta nikidhani ni kitu kidogo tu, sikufikiria inaweza kubeba sura ya hongo!”
Jelini akafikiria kama ajitetee akaona haina maana. “Uwe na mchana mwema.”
Akamuaga na kuondoka zake. Hakumuona tena Ezra ila akaanza kumfikiria. Ezra
hakuwa mweusi ila maji ya kunde. Mrefu wa kiasi. Kijana anayevutia tu. Ila
hakufanana na Colins kabisa.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Hawakuacha kwenda
kanisani, ila wakagundua hata Jelini anamkwepa. Akiona anawasogelea kwa salamu,
basi atajifanya anasimu inayompasa kwenda kuzungumza pembeni ya hapo. Naye Ezra
hata katika hilo akawa muugwana, alipoona anafanya hivyo mara tatu akaacha kabisa
hata kuwasogelea kwa salamu. Jema hakupenda.
“Ezra ni kijana
mzuri.” Akaanzisha mazungumzo wakiwa wote wanakula. Jumapili hiyo walipanga
kwenda kula pamoja. “Nimejaribu kufuatilia habari zake, anaonekana ametulia.”
Mpaka James akapaliwa na juisi aliyokuwa akinywa. “Hapo unakaribia kuharibu
Jema!” “Ni kwa uzuri!” “Hapana. Utaniua kwa pressure bure, nikuache na JJ.
Kwamba unamfuatilia zaidi ya kukutana naye pale kanisani!?” Mama Jema
hana mbavu.
“Ni kwa wema tu!
Namuona kama ni kijana aliyetulia. Mstaarabu na…” Alipomuona mumewe anaweka
kila kitu mezani, kisu na uma, anamkodolea macho akaona afupishe. “Kwamba ni
mtumishi wa Mungu.” Mpaka Jelini akacheka. “Sifa zote hizo zake yeye tu Ezra!?”
“James naye!” “Hapo hapana aisee! Hivyo mimi ishaanza kunisumbua. Na
sipendi.” “Basi yaishe.” Wakaona kama hajaridhika.
“Kwamba umemchunguza
ukapata sifa zote hizo!” Mama Jema na Jelini wakazidi kucheka. “Leo ukuwadi
utakutokea puani.” “Mara ya pili! Mpaka najuta mama yangu. Niliongelea kwa
uzuri tu!” “Sasa hapo ndipo panaponitia wasiwasi. Huo uzuri wake umepitiliza!”
“Lakini hawezi kukufikia wewe mume wangu. Wewe viwango vingine kabisa!” James
akamtizama kwa kumsuta, Jelini anacheka mpaka machozi.
“Kweli James. Au wewe
mama unasemaje?” “We! Ishia hapohapo. Ujichanganye mwenyewe, unataka
unikosanishe na baba JJ, mimi! Wewe endelea tu.” Mama Jema akajitoa. “Mama
naye! Jelini mwaya nisaidie. Wewe unamuonaje Ezra?” “Binafsi sijapata muda wa
kumchunguza. Kwa hiyo simjui.” “Ewaaa! Sasa eti jamani, mke wangu mimi,
eti ameshapata mpaka muda wa kumchunguza huyo Ezra! Ni sawa kweli?
Au ndio kuporwa tonge mdomoni mchana kweupe hivihivi!” “Huibiwi bwana James!
Mimi ni kama dada yake tu!” “Hakika huo undugu uishie hapohapo,
tafadhali Jema mke wangu.” “Sawa.” James akabaki akimwangalia. Jelini na mama
yake wakicheka huku wanamwangalia Jema alivyopoa.
“Unataka nikuongezee
kinywaji mpenzi wangu?” Wakazidi kumcheka. “Eti baba JJ wangu?” “Hamu ya kunywa
imeisha.” “James naye!” Akampooza hapo akimpamba kwa mengi mpaka akapoa.
Wakaendelea na mengine, wakaachana na habari za Ezra.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Kila walipokuwa
wakienda siku ya jumapili hawakuwa wakimuona tena Ezra, kama na yeye akawa
akiwakwepa. Jema naye akaacha kabisa kumtaja.
Colins.
Huku kwa Colins
alianza maisha na Love akifanya kila anachoagizwa bila shida. Furaha ya Love
ikatimilika. Anaishi kwenye jumba la ndoto yake ambalo hata hakutolea jasho,
kisha akampata na Colins tena akiwa amemshinda Jelini akisaidiwa na mpambe
Kemi. Mtumishi alikuwa akiendelea
kwenda kumshugulikia Colins. Akajawa furaha ndani ya jumba hilo la
kifahari akitumikiwa na wafanyakazi kwa kupitia nafasi ya Colins aliyopewa huko
kwenye makapuni ya wazazi wao. Pesa yote anayolipwa Colins ikawa yake
akiipangia majukumu na kuitumia apendavyo. Colins hana shida anafanya na
kufuata kila anachomwambia.
Miezi mitatu ikawa
mizuri. Mambo swafi. Mwezi wa nne, akaanza kusuasua. Akaanza kuonyesha uzubaifu. Love akamwambia huyo mtumishi wa Kemi. Akaenda
nyumbani kwao. “Mbona anakuwa kama anazubaa zaidi!?” Akalalamika kwa mtumishi. “Nikuzidi kuomba tu.” Na hapo akapata muda na Colins huko
chumbani, akamuacha amelala.
Mpaka mwezi wa nne
unaisha, Colins akawa hana afanyalo. Akikaa mahali, amepoa kama hayupo! Love
akajaribu kumlazimisha kwenda kazini. Akiwa anakwenda kazini na yeye,
anamlazimisha kwenda. Akamtafutia dereva, ilimradi tu kumtoa hapo ndani. Wakawa
wanatoka wote asubuhi.
Juma la kwanza la
mwezi wa tano likawezekana. Juma la pili wakati Love amefika kazini, dereva
akampigia kumwambia tokea amefika hapo nyumbani, alikuwa akimbembeleza Colins
aingie garini, lakini ameshindwa. “Mwache tu, usiwe na
wasiwasi. Nikuchoka. Jana alikuwa na siku ndefu. Hata kesho usiwe na wasiwasi,
nitampeleka kazini mimi mwenyewe.” Huo ukawa mwisho wa kwenda kazini kwa
Colins. Hilo likamkera sana Love na kumpandisha hasira kali sana dhidi yake.
Akawa kama anampa adhabu ya kutokwenda kazini, nakutomjali kabisa ili ajirudi,
lakini wapi.
Ikawa yeye ndio
muenda kazini. Akamuombea likizo kuwa wanasafiri kwenda mapumzikoni kwa majuma
matatu, ilimradi tu kupunguza maswali ya kutoonekana kwake kazini. Akakusudia
ndani ya muda huo, basi amtafutie suluhu. Akamtafuta tena yule mtumishi, akawa hapatikaniki tena.
Tamu
Yageuka Shubiri.
Akaamua sasa
kumtafuta Kemi. Akamueleza yote juu ya Colins, tofauti na alivyotarajia, Kemi
akamjia juu. “Ndoa zina mambo yake. Lazima ujifunze
kuvumilia. Uling’ang’ania mwenyewe, nimekufanikishia kukuingizia mwanaume
ndani, kazi kwako. Huu mtindo tena wakupigiana simu na kuelezana ya undani, tutachoshana.
Maana na mimi nina yangu, mengi tu. Lakini hunioni nikikupigia simu na
kulalamikia yangu.” Simu ikakatwa na kumuacha Love haamini!
Nani Kama Mama!
Akaamua kumtafuta
mama yake. Wakakutana muda wa chakula cha mchana wote wakiwa kazini. Wakatafuta
hoteli nzuri ya hadhi yao, wakakaa hapo. Akazungumza naye kwa marefu na mapana
juu ya Colins. “Hebu niambie mama yangu, nafanyaje? Na pale mimi nishafika,
sitaki kutoka kwenye lile jumba. Kila mtu anajua naishi pale. Nishakaribisha
rafiki zangu karibia wote na watu wa kazini kwa tafrija nzuri sana, imebaki gumnzo
na nimejipatia heshima kwa watu. Kweli gafla nitoke tu na nishatangaza utajiri
kwa kiasi kile!” “Sasa hapo ndio shuguli! Bora mngekuwa mmeona. Akitoka yeye,
na wewe ujue utatoka tu pale. Maana ile nyumba ni nusu kwa nusu. Ukisema tu
wewe umeshindwa, ujue unaondoka. Bora uburuzane naye hivyohivyo mpaka
uone mwisho wake.” Ushauri wa mama Simba kwa mwanae ukaendelea.
“Mshahara wake si
bado unaweza kuufikia?” “Hilo nimehakikisha namdhibiti tokea mwanzo.” “Bora.
Sasa hapo wewe ndio akili kichwani. Jiweke sawa, na mimi nitaenda kuzungumza na
baba yako. Ila maisha yako yasikwame Love. Una ndoto kubwa sana, usikubali akakukwamisha.
Maana hata mama yake anakajiasili cha uvivu. Si unakumbuka wakati ule
namuhimiza turudi wote shule, yeye akakataa akijificha kwenye kulea watoto?”
“Nakumbuka.”
“Kile kilikuwa
kisingizio tu! Ni uvivu tu na roho ya kukataa kuthubutu makubwa. Kaambukiza
kijana wake, kapewa majukumu makubwa, ndio anajidai utahira, sasa wewe
usikwame nao. Japokuwa mama yake alikuwa rafiki yangu sana, lakini lilipofika
swala la maendeleo, nilipomuona anataka nikwame naye, mimi nikarudi shule.
Mpaka leo yeye nesi vilevile, ona mimi nilipo! Sasa wewe asikuzubaishe.”
“Hathubutu.” Wakajipanga na mama yake. Wakawekana sawa.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Baba yake alibanwa
sana na mambo ya kitengo kipya alichokabidhiwa cha mambo ya moyo huko kwenye
hospitali kuu ya taifa ya Muhimbili. Ikawa safari pia nje ya nchi zimeongezeka.
Mara nyingi hakuwepo nchini kwa hiyo mambo ya kliniki zao akawa amemuachia mzee
Simba na kijana wake Colins. Kazi yake ikawa ni kuulizia kwa mzee Simba tu.
Kila akiulizia, anapewa sifa njema za Colins, mzee anaendelea na yake.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Siku moja ya jumamosi
mama Colins akajifungasha mpaka Kigamboni kumuona kijana wake na Love. Kilicho
cha ajabu, hakupokelewa kama alivyozoea. Alimtuma msichana wa kazi akawaite
huko chumbani. Msichana wa kazi aliporudisha majibu kuwa wanakuja, alikaa hapo
sebuleni zaidi ya lisaa ndipo akatoka Love na uso wa kusumbuliwa. “Kumbe bado
mlikuwa mmelala?” “Ndiyo. Yaani hapa hata Colins bado hajaamka. Jana kachelewa
na kazi, tumelala usiku sana.” Mama Colins alivyoona huo upokelewaji, tena hapo
Love anazungumza akiwa amesimama hata hajakaa, akaaga na kuondoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Juma jingine likapita
kimya hata Colins asipige simu kumwambia mama yake alipata habari kuwa alifika
nyumbani kwao! Mama Colins akaanza kupatwa wasiwasi. Mama huyu hana majukumu
mazito tokea zamani ila wanae. Ajue walipo na wanachofanya, ndio na hiyo
kazi yake ya uuguzi. Basi. Sasa ule ukimya ukamfanya amfuate kazini. Hapo
kazini akaambiwa hayupo. Lakini jinsi alivyojibiwa, hakupenda. Ni kama
waliokuwa wamepewa maagizo kuwa akiuliziwa Colins, apigiwe Love. Mama Colins
hakufanya hivyo.
Akaamua kumfuata tena
kwake. Akamkuta msichana wa kazi. Akamwambia Colins ametoka. “Amekwenda wapi!?”
Ikabidi aulize. “Dada amesema umpigie yeye.” Mama Colins akaingiwa na wasiwasi.
Akabaki akifikiria, tena mlangoni. “Mida gani mizuri naweza kumkuta?” Akaogopa
kumwambia. “Mimi nataka kumsalimia tu.” “Ila usimwambie dada?” “Usiwe na
wasiwasi. Mimi siwezi kukuchongea.” “Shem huwa anaondokaga hapa asubuhi. Wakati
mwingine anarudishwa na Issa usiku. Issa anasema anakuwa anamkuta mbali kabisa
ya hapa. Anakuwa kama kuna kitu anatafuta, halafu hajui jinsi ya kurudi
nyumbani.” Mama Colins akawa hajaelewa kabisa.
Ila huyo binti
akapata simu. Wazi alionekana anaongea na mtu mwenye mamlaka kwake. Ila baada
ya hiyo simu, akamjibu kwa kifupi mama Colins kuwa, mpigie simu dada mwenyewe
ndio anamaelezo yote.” Kisha akaingia ndani, akafunga mlango kwa ndani na
kumuacha mama Colins amesimama nje ya mlango.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Kesho yake akafika
hapo kama kwenye mida ya saa tatu asubuhi. Aligonga getini, mpaka akachoka.
Akataka kukata tamaa, lakini roho ikazidi kumtuma asichoke. Akaanza tena
kugonga. Mwishoe akatoka mlinzi. “Wote hawapo mama yangu.” “Na msichana wa
kazi?” “Naye pia hayupo.” “Nilimkuta hapa jana tu!” “Kaondolewa leo asubuhi.
Hapa nyumba haina mtu, nipo mimi tu.” Mama Colins akabaki haelewi. Mlinzi
akafunga geti. Akaachwa tena nje ya geti, amesimama.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Akampigia simu
mumewe. “Kuna kitu kinaendelea, na hakipo sawa.”
Akamuelezea kwa jinsi ilivyokuwa kuanzia siku alipoenda na Love kumuonyesha
kana kwamba anawasumbua. “Hayo ananiambia akiwa amesimama,
na nilimsubiria zaidi ya lisaa, sikumuona Colins.” Akamueleza pia alikwenda
ofisini kwake hakumkuta kijana wao, na jinsi alivyojibiwa, kisha kurudi tena
hapo mpaka safari hiyo kukutana na mlinzi
“Kwani wewe
mara ya mwisho kuzungumza na Colins ilikuwa lini?” “Mara ya mwisho kumpigia, niliporudi
tu juma lililopita, nikampigia, alipokea Love, akasema Colins ametoka, amesahau
simu. Lakini wapo sawa kabisa. Akazungumzia swala la kazi ya Colins na vile
anavyofurahia na kushukuru kwa hiyo nafasi, basi.” “Mmmh!” Bado huyo mama akawa
na wasiwasi.
“Acha
wasiwasi bwana! Kama mpaka sasa Simba hajalalamika, ujue kila kitu kipo sawa.”
“Hapana baba CJ. Hawa watu wanamsikiliza sana Love. Inawezekana wanajibu na
kuongozwa na kile wanachotumwa na Love. Huyu binti anayo nguvu na mamlaka ya
ajabu sana. Na ni kama amenibadilikia kabisa. Tafadhali nenda kwao, na
hakikisha unakutana na Colins.” “Basi bora niweke mazingira yakutoka mapema,
nimtafute. Nitaanzia kazini.” “Kazini hayupo. Nimekwambia
nimetoka huko. Tafadhali nenda kwao na wasiliana na Love. Na ujue nasubiria
majibu. Mimi sili wala kulala mpaka nipate taarifa za mwanangu.” “Acha kulia sasa. Mbona nakwenda na nitamwambia Colins
akupigie mzungumze? Tulia bwana mama CJ!” “Siwezi
kutulia. Roho yangu haina amani. Wewe kanitafutie mwanangu.” Mzee akajua
mama hataki utani. Lazima achangamke.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Colins yupo wapi? Usipitwe.
0 Comments:
Post a Comment