Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com More than Saying - Zaidi Ya Kutamka - PART 2 - Naomi Simulizi

More than Saying - Zaidi Ya Kutamka - PART 2

Historia Yataka Kujirudia

Kilikuwa ni kitendo cha sekunde chache lakini kilicho muogopesha sana Sonia na kumfanya aishiwe na nguvu kabisa. Alianza kulia. “Naomba uniachie.” Tayari midomo yake iliyokuwa akitoa harufu kali ya pombe ilishafika kwenye shingo ndefu ya Sonia. 

Aliaanza kumbusu na kumnyonya kwa fujo huku akimpandisha gauni lake kwa haraka. Muda wote huo alikuwa bado amemminya Sonia kwa nguvu sana mwilini mwake, kama kumkumbatia. “Usiogope. Nitakupa chochote utakachotaka.” “Hapana. Mimi sitaki kitu. Naomba niachie.” Sonia alishalemewa kabisa, alibaki akilia sana kwa kwikwi na hofu illishamlemea na kwa kuwa mziki ulikuwa mkubwa, alijua wazi hakuna atakaye msikia. 

Kumbukumbu za alivyobakwa huku akishindwa kujitetea kabisa ziliendelea kumdhoofisha. Alishafanikiwa kumlaza juu ya mifuko, waliyokuwa wameikuta kwenye stoo hiyo na tayari alishampandisha gauni mpaka juu ya kiuno nakumuacha na chupi tu huku akiendelea kumpapasa kwa fujo bila kumuhurumia Sonia aliyekuwa akilia sana kwa kwikwi.   

Sonia akiwa amelazwa chali, na jamaa yupo juu yake amemminyia chini kwa nguvu zote, hana ujanja tena, hofu ya yaliyomtokea zamani imemmeza na kufanikiwa kumnyong’onyeza, tena akiwa nusu uchi ndipo alipokumbuka siku ile anao msaada, hayuko peke yake tena. “Saaam! Saam!” Japokuwa kulikuwa na kelele kubwa sana, Sonia alijitahidi kupaza sauti huku akilia sana na bado yule bosi alikuwa amemng’angania sana akiendelea kumnyonya kila alipoweza. 

Alisha fanikiwa kumfungua nywele zake zilizokuwa zimebanwa vizuri saluni, zilizokuwa zimempendeza sana na kufanya sura yake kuonekana bayana na macho yake makubwa, meupe yalishakuwa mekundu kwa kulia. Zilikuwa ni dakika chache sana, lakini alimvuruga Sonia vya kutosha na kuibua kumbukumbu kali sana moyoni mwa Sonia. 

 **********************

Wasiwasi ulimpata Sam baada yakuona Sonia harudi pale mezani. Akaamua kumfuata chooni. Alipomuuliza msichana aliyekuwa akitokea choo cha kike kama amemwacha mtu mwingine mle ndani nakuambiwa hapana, Sam aliingia chooni mwenyewe, alipomkosa choo cha kike akaingia  na cha kiume, huku akiwapigia simu rafiki zake pale mezani kuwataarifu kupotea kwa Sonia, na kuwaomba kama akirudi pale mezani wampigie, kumtaarifu. 

Na wao bila kupoteza muda walisimama na kugawana kumsaidia kumtafuta na wengine walimfuata Sam, baada yakuambiana meza mbili tatu. Kelele za Sam akiwa amepaniki akimuita Sonia ziliweza kusikika kila mahali, baada ya muda mfupi tayari ukumbi mzima ulijua Sonia anatafutwa. 

Akiwa amechanganyikiwa, Sam aliweza kusikia sauti ya Sonia kwa mbali ikimwita. Alianza kuifuata huku amejawa na wasiwasi kwani Sonia alisikika kwa mbali sana kama mtu aliyekuwa anakata roho!

Sam aliweza kusikia kukuru kakara ndani ya kile chumba kwa mbali. Baadhi ya rafiki zake na watu wengine waliokuwa wakimfuatilia Sam kwa nyuma walisimama baada ya Sam naye kusimama, kwani ile sauti Sam aliyokuwa akiisikia ya Sonia na kuwaambia wenzake amemsikia Sonia maeneo yale ni kama ilipotea na kile chumba kilichokuwa pale kilikuwa ni giza na hapakuwa na dalili yakuwepo mtu ndani. Lakini Sam alizidi kukisogelea kile chumba. 

“Sonia? Sonia?” Kimya. Akajaribu kusukuma mlango lakini ulikuwa umefungwa, na palikuwa kimya kabisa kuashiria hakuna mtu ndani. Rafiki zake walijaribu kumtuliza Sam na kumwambia asiwe na wasiwasi labda Sonia ametoka tu nje ya hoteli, wakajaribu kumwangalia nje na ile haikuwa sauti ya Sonia ni mawazo tu. 

“Hapana. Namfahamu Sonia. Hawezi kwenda mahali bila kuniambia na ninaijua sauti ya Sonia hata kama nipo usingizini.” “Sasa Mzee, wewe mwenyewe umeona hayupo hapa, si twende tu chini tukaulize pale mapokezi kama wamemuona akipita?” Rafiki yake Sam akasisitiza. 

Bila kujibu kitu, Sam akaanza kurukia ule mlango. Rafiki zake walibaki wakimshangaa. “Ungesubiri basi tuwaite wahusika Sam. Utaharibu mlango wa watu, Mzee!” Kwa nguvu sana, Sam alipiga teke na mlango ulifunguka huku ukizuiwa na mifuko iliyokuwa imepangwa nyuma ya ule mlango. Watu wote walisogea karibu na mlango.  

Macho yaliwatoka baada yakumwona Mr Mponza amemlalia Sonia, akiwa ameshusha suruali mpaka magotini na amemkandamiza Sonia chini huku amemziba mdomo kwa nguvu sana mwisho kabisa ya kile chumba. 

Kama mshale, Sam aliruka na kumnyakua Bosi wake na kumtupa nje kama paka. Sonia alishindwa hata kujisogeza. Alikuwa akitetemeka sana huku amejawa jasho jingi na machozi. Bado alikuwa akimwita Sam kwa sauti ya chini sana, “Sam! Sam!” Ukweli alikuwa kwenye hali mbaya. 

Sam alirudi kumwangalia, lakini alipata matumaini baada yakumkuta bado amevaa chupi yake. Alimnyanyua na kuanza kumshusha gauni lake, lakini Sonia hakuacha kulia huku akimuuita Sam. 

Kwa hasira zisizo za kawaida Sam alipohakikisha amemsitiri Sonia vizuri, alimfuata bosi wake tena ambaye alikuwa ndio amenyanyuka kutoka sakafuni alikomtupa, akifunga suruali yake huku watu wakishangaa kama waliopigwa na butwaa, kwa kuwa Mr Mponza alikuwa kiongozi wa kuheshimiwa sana pale kazini kwao, hakuna aliyemudu hata kusema jambo zaidi ya kusogea pembeni kama kumpisha.  

Sam alimsogelea na kumpiga ngumi tatu za nguvu tena mfululizo bosi wake. “Mbwa tu wewe Sam. Huna lolote. Mimi ndio nimekufikisha hapo ulipo. Kazi yenyewe nimekufundisha mimi, upo hapa leo kwa kuwa mimi ndio nimekuchagua. Fala tu wewe, huwezi kumtunza msichana kama Sonia hapa mjini. Utaishia kumchafua tu, na kushindwa kumpa hata sabuni yakuogea.” Bosi wao aliongea huku akiweka koti la suti yake vizuri na kuondoka pale kuingia ukumbini.  

Sam alimfuata kwa nyuma na kumpiga ngumi moja ya mgongoni iliyomuingiza ukumbini na kufanya ukumbi mzima kutulia gafla. Sam alimkandamiza pale sakafuni alipokuwa ameanguka nakumpiga ngumi za usoni mfululizo kama aliyepagawa. 

Ukumbi mzima waliwazunguka Sam na Bosi wake akiwa sakafuni akitokwa damu nyingi sana usoni. Sam hakujali aliendelea kumkaba kwa mkono mmoja huku mkono mwingine ukimshindilia ngumi kama bondia ulingoni, akisaka kombe la dunia. 

Walikuja wanaume wawili na kumvuta Sam juu, kumtoa kwenye mwili wa bosi wake aliyekuwa akicheka kilevi sana. “Wewe fala tu Sam!” Alirudia huku akivuja damu nyingi sana usoni mwake, akasimama. Sam alitaka kumrudia lakini walimshika kwa nguvu kama kumzuia, kwani ni kweli hali ya bosi wake ilikuwa mbaya japo alikuwa akicheka kilevi, kitu kilichozidi kumkera Sam nakutamani arudie kumpiga tena. 

Akarudi tena kwa Sonia na kuendelea kumtengeneza gauni lake vizuri huku akijaribu kuweka nywele zake sawa. Sonia alikuwa akitetemeka sana, na alisimama kama sanamu bila hata kujigusa. Sam akaamua kumkumbatia kama kumtuliza ndipo na yeye akamshikika kwa nguvu sana kana kwamba anaogopa asiondoke tena. “Pole Sonia, pole sana.” Sam alichukia unyama aliofanyiwa Sonia na yeye kushindwa kumsaidia. Kila mtu alibaki ameduwaa huku wakimwangalia Sonia kwa kumuhurumia sana.  

Mkewe yule bosi alivua kiatu kimoja nakuanza kumpiga nacho mumewe mfululizo huku akimtukana sana. Tayari sherehe yote ilishabadilika na kuwa huzuni, mziki ulisha zimwa. Mpaka DJ alisogea kushuhudia kinachoendelea. 

Bado Sonia alikuwa akilia sana huku akitetemeka kwa hofu. Sam aliamua kuondoka. Akamtoa nje na kumbembeleza lakini Sonia bado alikuwa akilia kwa kwikwi sana. Alijaribu kumuweka kwenye gari lakini Sonia bado alikuwa amemng’angania shati lake. 

“Siondoki tena Sonia. Nataka turudi nyumbani.” Lakini hakuna jinsi Sonia alikubali kumuachia. Bado alimng’angania Sam kwa nguvu sana. Ndipo rafiki yake mmoja Sam aliyewasindikiza nje ilimbidi amshauri Sam akae naye nyuma, halafu yeye ndio awaendeshe kuwarudisha nyumbani.       Waliingia nyuma ya gari ya Sam kwa shida sana, kwani Sonia alikuwa amebana miguu yake kwa nguvu sana na alikuwa amekakamaa mwili mzima. Walikaa kwa shida mpaka nyumbani kwa Nyange, kwani Sonia hakutaka hata kusogea na bado alikuwa amemng’ang’ania Sam huku ameficha uso wake kifuani kwa Sam.  

 **********************

Mlinzi alifungua geti, rafiki ya Sam akasogeza gari mpaka karibu kabisa ya mlango wakuingilia kwenye jumba hilo la Nyange, lakini Sonia alikataa kusogea wala kuinua macho yake. “Sonia! Sonia!” Sam alimuita taratibu, lakini aliendelea kulia. Yule rafiki yake akajaribu kumsaidia Sam kumtoa pale, haikuwezekana. Sonia alikuwa bado amekakamaa na alirusha mateke kila alipoguswa na mtu mwingine bila kunyanyua uso. Huku akisema. “Nisaidie, nisaidie!”

Ndipo wazo la kwenda kuitwa mama yake likamjia Sam. Yule rafiki ya Sam alienda kubonyeza kengele ya mlangoni, Nyange akatoka. Aliambiwa Sam anamuita ndani ya gari. 

Akaenda na sintofahamu usoni. “Naomba nisaidie kumtoa Sonia hapa ndani akapumzike.” Akiwa kwenye mshituko sana, Nyange naye akajaribu lakini akashindwa. 

Ndipo alipoenda kuitwa mama yake. Mama Sonia alishituka sana. Akapanda ndani ya gari kwenye kiti cha mbele, na kuanza kuongea na Sonia kwa sauti ya chini sana kwa lugha ya kwao, ambayo hakuna aliyeelewa anachosema. Lakini ikaonekana Sonia alitambua na kumtoa kwenye mshituko mkali aliokuwa ameupata. “Mama?”

Taratibu Sonia alianza kutulia na kuanza kutafuta sauti ya mama yake huku amemshikilia Sam. Mama yake alitoka nje ya gari upande aliokuwa amekaa Sonia, na kuendelea kumuongelesha kwa kilugha kumuashiria kushuka kwenye gari. 

Wakaona anamuangalia mama yake kwa muda, harakaharaka kama kumbukumbu zilimrudia, akachomoka pale kwa Sam na kumkimbilia mama yake na kumkumbatia. Kila mtu alibaki kimya. 

Sam aliumia sana. Hakujua atamueleza nini Nyange, mkewe na mama yake Sonia. Alichukia sana kushindwa kumuokoa Sonia kwa wakati, mpaka kudhalilishwa kwa kiasi kile.  

 **********************

Mama Briana akatoka chumbani. “Kuna nini? Mbona Sonia analia?” Mama Sonia hakujibu kitu, akamchukua binti yake mpaka chumbani na kumsaidia kumpandisha kitandani. Aliweza kuhisi mwanaye anavyotetemeka. Akamfunika huku akimuongelesha kikwao, mpaka Sonia alipotulia na kupitiwa na usingizi. Ndipo akatoka kurudi sebuleni.

Shati la Sam na kizibao vyote vilijaa damu. Alikaa chini huku ameshikilia kichwa kana kwamba kisianguke. “Kuna nini Sam?” Mama Briana alishuka ngazi nakuendelea kuuliza. Nyange na Mama Sonia walio kuwa wamemuona Sonia tokea kwenye gari, wao walibaki kama sanamu. 

“Samahani sana Mama.” Sam alimgeukia mama Sonia kwa sauti iliyojaa uchungu na hofu sana. “Yaani ni jambo lililotokea mama yangu ndani ya muda mfupi sana.” Sam alianza kujitetea kwa mama yake Sonia. 

“Yaani mama, hata dakika tano ni nyingi yote hayo yalivyotokea! Sonia aliniaga anaenda chooni, aliniacha kwenye meza. Nilipoona harudi, tena wala sikukaa sana mama yangu, nikaamua kumfuata, hata rafiki zangu waliniambia nisiwe na wasiwasi kwa kuwa hata dakika tano zilikuwa hazijaisha, lakini mimi nilikuwa nimeshaingiwa na wasiwasi, yaani kama Mungu tu. Ndio nikamkuta bosi wangu…” Sam alisimama huku akizunguka na kukuna kichwa. 

“Daah!” Sam aliendelea kulalamika. “Akifanyaje Sam?” Mama Briana aliendelea kuhoji. Taratibu machozi yalianza kumtoka mama Sonia na kushindwa kujizuia. “Yaani shem. Hata dakika tano zilikuwa nyingi tulipoachana na Sonia. Mungu wangu ni shahidi. Mimi nilijua yupo chooni. Angechelewa kidogo tu, mbona ningemfuata? Si unanijua shemeji yangu mimi ninavyo mjali So…” “Sam? We Sam?” Mama Briana alimstua Sam, tayari alionekana amepaniki na majuto usoni mwake. 

Nyange alibaki kimya kabisa kama aliyepoteza ufahamu, maneno yote yalimwisha. “Naomba uniamini mama yangu, nisingemuacha Sonia ateseke. Ni muda mfupi sana.” Mama Briana akamsogelea Sam na kumvuta shati. “We Sam? Hebu niangalie mimi.” Sam akatulia kidogo. 

“Bosi wako alimfanya nini Sonia? Amembaka?” “Hapana! Alitaka kumbaka lakini nilimuwahi. Alikuwa ndio anamshika na kuanza…. Daah!” Kila mtu alipumua kwa nguvu na kukaa kasoro Sam aliendelea kuzunguka huku akielezea bila kunyamaza. 

“Sam? Sam?” Mama Sonia alimuita. “Naam!” “Nakushukuru kwa kumuokoa.” Sam alishituka sana, hakutegemea kusikia hivyo kutoka kwa mama yake Sonia. Alijua kila mtu atakuwa amemkasirikia na kumlaumu yeye. 

“Na ninavyoona umechafuka damu hivyo, lazima utakuwa umemfundisha adabu.” Nyange akadakia. “Nashauri, ukaoge ubadili hizo nguo ukapumzike Sam. Uzuri ulikuwepo karibu na ukaweza kumsaidia. Usijilaumu kabisa.” “Lakini nilichelewa kidogo tu kaka! Yaani ilinibidi kuvunja mlango, alimvutia kwenye kijichumba cha stoo, halafu akafunga mlango kwa ndani.”

“Nimeingia mle ndani nimemkuta amemkandamiza chini na kumziba mdomo. Nimechelewa kaka, nimemkuta ameshampandisha nguo tayari. Daah!” “Sam?” Mama Briana akasimama nakumshika tena begani. “Umefanya ulichoweza. Usingeweza kumsindikiza chooni. Hukujua kama bosi wako angefanya hivyo. Lazima ushukuruuliweza kufika pale kwa wakati. Kama ungewasikiliza rafiki zako, huoni kama sasa hivi tungekuwa tunazungumza mengine? Huoni kama umemsaidia Sonia? Unatakiwa ushukuru sio kujilaumu tena.” “Kweli shem!?” “Kabisa. Sasa naomba, ukaoge halafu upumzike.” Sam akaondoka. 

“Asante sana Mama Sonia kwa kumfariji Sam.” Mama Bri alimgeukia. “Sam ameingiwa na hofu sana. Sijawahi kumuona Sam kwenye hali hiyo. Nakushukuru umemtuliza.” Mama Briana akaongeza kama kuleta amani zaidi.

“Ni kweli sio kosa lake. Amefanya alichoweza.” Mama Sonia alijibu huku akikausha machozi. “Niliogopa sana, nilijua wamembaka tena. Namshukuru sana Sam.” Wote walibaki kimya kwa muda. “Jamani Sonia wangu!” Mama Briana alijikuta akiwaza kwa sauti iliyoweza kusikika. “Naona tukalale sasa.” Nyange akasimama baada ya ukimya mwengine kupita. 

 **********************

Nyumba nzima, usiku huo walishtuliwa na kilio cha Sonia. Alikuwa akilia sana usingizini huku akiomba msaada. Alikimbia kutoka kitandani mpaka kwenye kona ya jikoni huku ameweka mikono yake yote sehemu za siri kama kujifisha kuhu akipiga sana kelele kuomba msaada. 

Watu wote walisimama mlangoni wakishangaa. Sonia alikuwa akilia sana, huku jasho likimtoka. Alikuwa amekaa chini kabisa huku amebana miguu yake kwa nguvu sana. “Mama? Mama yangu nisaidie!” Sonia aliendelea kulia. 

Hakuwa akimsikiliza mtu yeyote na kila aliyemshika alirusha mateke. Alijawa nguvu za ajabu sana. Mtoto wake alianza kulia na Briana naye akaanza kulia. Mama Briana aliwabeba na kuwarudisha chumbani kwa Briana. 

“Wewe Nyange? Unashangaa nini badala ya kumuwahisha mtoto hospitali?” “Anapiga mateke, mama Briana!” Nyange alijitetea kama mtoto mdogo kwa mkewe. “Yaani nyinyi wanaume watatu mnashindwa na huyo Sonia? Mmebaki mmesimama tu mnamshangaa kama mpo mbuga za wanyama! Wewe Sam na Josh, hebu msaidieni mwenzenu. Lazima apelekwe hospitalini. Umesikia Nyange? Acha uoga bwana, wewe vipi?” Ndipo Nyange, Sam na Josh walipomkamata na kumuingiza kwenye gari mpaka hospitalini.  

Sonia alikuwa akitokwa na jasho jingi sana. Alibana miguu yake, hapakuwa na jinsi mtu yoyote angeweza kumshika miguuni akakubali. Walimshika mikono yake na kumvuta mpaka mapokezi. 

Daktari aliyekuwepo zamu alipomuona vile, haraka akamchoma sindano iliyomfanya Sonia kulegea na kupotelea usingizini muda uleule. Aliwekwa kitandani. 

“Ni nini hiki?!” Nyange akauliza. “Amepatwa kichaa?” Daktari alikaa nao chini, Sam alielezea historia ya Sonia ya kubakwa na tukio lililotokea usiku ule, nakuacha Nyange, Josh na daktari wakimuhurumia sana Sonia. 

“Tukio la leo limetibua mambo yote ya nyuma. Msiogope, akipumzika leo, kesho atakuwa sawa tu.” Sam alirudi kwenye kitanda alichokuwa amelala Sonia, alimwangalia kwa huruma sana. Simu ya Nyange ilianza kuita.

“Naomba uje mchukue mama yake. Ana hali mbaya sana. Atachanganyikiwa asipo muona mtoto wake.” “Daah! Kweli. Nakuja. Lakini mwambie asiwe na wasiwasi, ametulia.” “Wewe njoo tu mchukue, aje ajionee mwenyewe. Hawezi kuamini kwa maneno matupu tu.” “Nakuja.” Mama Briana alikata simu na kubaki akimwangalia mama Sonia, asijue cha kusema. Nyange alikwenda kumchukua na kuwaacha hospitalini na Sam. 

**********************

“Saaam?” Siku inayofuata wakamsikia anaita akiwa bado amelala. “Nipo hapa Sonia.” Akafungua macho na kumuangalia Sam kwa muda kidogo. “Naogopa sana.” “Usiogope, mimi nipo hapa na mama, hatuondoki. Pumzika tu.” “Usiondoke. Sawa?” “Sitaondoka.” Sam akamfuta machozi, akapotelea usingizini tena. 

Alichomwa sindani nyingine, alikuja kuamka imeshakuwa jioni, siku ya pili. “Pole Sonia.” “Asante mama. Nasikia kichwa kizito, shingo ina… Sam yuko wapi?” “Mimi hapa Sonia.” Sam naye akamsogelea pale kitandani. Akamgeukia na kumwangalia kidogo, akafunga macho. “Pole Sonia.” “Asante. Najisikia kuchoka!” Aliongea huku amefunga macho. 

“Pumzika.” “Kwani utaondoka Sam?” “Sitaondoka.” Sonia alilala tena. “Mama, mimi naona ukapumzike tu nyumbani. Umekaa macho tokea jana usiku. Mimi nitakuwa naye, usiwe na wasiwasi. Chochote kikitokea nitakupigia simu.” “Wazo zuri sana Sam. Hata hivyo, Sonia mwenyewe anaonekana anamuhitaji zaidi Sam.” Nyange akadakia kishabiki. 

“Nyange wewe! Hivi wewe ukoje lakini!?” “Jamani mama Briana, si nasema kweli tu. Kuliko kumuacha hapa Mama anateseka, si heri akapumzike tu nyumbani. Wote tuko hapa, hata salamu, hatujapewa! Naona anauliziwa Sam tu. Au wewe mama Sonia unasemaje?” Kidogo watu walianza kucheka. 

“Ni kweli.” Kweli mama Sonia alikuwa amechoka na aliona ni kweli mwanae hamuhitaji kwa wakati ule. Aliyekuwa akiitwa na kuombwa asiondoke pale ni Sam peke yake. 

Mama Briana na Nyange na wao walifika hospitalini pale kumuona Sonia. Josh aliachiwa watoto wote watatu. Chakula walichokuwa wamekileta pale, alikila Sam wakaondoka na vyombo na mama Sonia. Walimuacha Sam na Sonia kwenye chumba ambacho Nyange aliomba Sonia awekwe peke yake. Kwamba anamlipia private.

**********************

Sonia alilala mpaka katikati ya usiku. Alishituka na kukaa kitandani, akaita tena. “Sam?” “Nipo Sonia.” Akapumua kwa nguvu sana, Sam alisimama na kumsogelea. Alimshika taratibu kama kujaribisha kama ametulia. Alipoona hafanyi fujo, akamsogelea karibu zaidi na kumshika kwenye nywele zake kama kuziweka sawa. 

“Unajisikiaje?” Akamuuliza kwa upendo. Akatoa tabasamu la kinyonge na kurudi kujilaza. Hatimaye aliweza kuona uzima na furaha kwenye macho maangavu ya Sonia. Alijua amefurahia alipomshika. 

Akakaa pembeni yake nakurudisha mkono wake kichwani kwa Sonia huku akimwangalia kwa karibu zaidi. “Pole sana.” “Nini kilitokea? Kwa nini nimeletwa hapa na sio nyumbani?” Kumbukumbu za Sonia ziliishia pale ukumbini. Gafla uso wake ulibadilika na machozi yalianza kumtoka tena baada ya kukumbuka kuanza kumjia taratibu. 

“Alinibaka?” “Hapana Sonia! Hakukubaka.” Alishaanza kutetemeka huku akifunga tena miguu. “Hakukubaka. Pole sana.” Akawahi kumfuta machozi akimtuliza. “Samahani sana Sonia. Nilichelewa kuja kukusadia.” “Hapana. Uliwahi. Ungechelewa, angenibaka, alishanizidi nguvu. Asante sana.” “Uliniita muda mrefu sana?” “Hapana. Nilikuwa nimepaniki, nilijaribu kujitetea kwanza, niliposhindwa, ndipo nilipo kumbuka sipo peke yangu tena. Nipo na wewe.” Machozi yaliendelea kumtoka taratibu. 

“Ni kweli Sonia. Haupo peke yako tena maishani, upo na mimi. Naahidi kuwa na wewe daima.” Sonia alifurahi sana kusikia hivyo, alikaa na kumkumbatia Sam. “Asante sana.” Akashukuru huku bado ameficha uso wake kwenye shingo ya Sam. Sam alijisikia vizuri huyo! Kama amekumbatia alumasi! Walikumbatiana kwa muda mrefu mpaka Sam akahisi amepitiwa na usingizi, baada ya muda Sonia akarudi kujilaza. 

Akiwa amejilaza, Sonia akakunja uso. “Nini?” “Nasikia joto, nanuka halafu mdomo mchungu sana. Natamani kupiga mswaki halafu nioge.” “Mama Briana alikuletea vitu vyako. Ngoja nikuangalizie.” “Mama Briana alikuja?” Sam akatabasamu tu. 

“Nilikuwa nimechoka kweli!” “Na mama pia alikuwepo hapa usiku kucha, ilibidi kumshauri kwenda kulala. Alionekana amechoka sana.” “Jamani mama yangu! Kwani ilikuwaje nikaja hapa?” Akamuelezea kwa kifupi ilivyokuwa.

 “Poleni kwa kuwatia wasiwasi. Sijui nilipatwa na nini!” “Kila mtu alikuwa na wasiwasi na wewe Sonia. Lakini daktari alitutoa wasiwasi, alisema utakuwa sawa tu. Nyange mwenyewe uchokozi wote ulimuishia. Natamani ningemchukua video niwe namuonyesha. Kumbe muoga vile!” Sonia akaanza kucheka. 

“Haujamuishia hata kidogo. Wewe subiri turudi nyumbani utamsikia.” Sam naye akacheka. “Atatuigilizia kila kitu, mpaka tutakoma. Hata hivyo alipoona umeamka unaniita tu mimi, alianza uchokozi wake kama kawaida.” Wote walicheka. 

“Yaani baba Briana! Haishiwi maneno! Anatusikiliza kwanza vizuri kwa makini utafikiri mtu ambaye yupo na wewe, halafu baadaye ndio anaanza uchokozi wake. Ukimuona anacheka tu, ujue ana lake moyoni.” Wote walibaki kucheka. 

Sonia alisimama lakini akajisikia kizunguzungu, akarudi kukaa. “Vipi?” “Nahisi hali ya kizunguzungu, kichwa kizitoo na shingo inauma sana.” “Pole. Ulikuwa ukijipigiza kichwa sana jana usiku, halafu yule jamaa naye alikukandamiza sana. Ameniudhi kweli, sijui na yeye atakuwa na hali gani?” “Kwani ulimpiga?” Sonia alishituka. 

“Naona hatakaa akasahahu maishani. Twende nikakusaidie kuoga, utajisikia vizuri.” Sonia alishituka sana na kuinamisha kichwa chini. “Utajisikia vizuri. Twende utakaa kwenye choo wakati wakupiga mswaki halafu nitakusaidia kuoga. Nimepata mswaki, dawa na nguo za ndani za kubadilisha.” Sam alimsaidia kusimama, akapiga mswaki alipomaliza, Sonia akaanza kujishauri. 

Alikuwa amevalishwa nguo ya hospitalini. “Nikusaidie kuvua?” “Ngoja nijaribu tu mwenyewe.” Sam alifungua maji kwenye sehemu ya kuogea ili kuruhusu kutoka ya moto. Haraka haraka wakati Sam anaangalia maji, akatoa hilo gauni, akavuta taulo nakujifunika. 

“Unasikia baridi sana? Ngoja kidogo, maji yakipata moto ndipo uingie.” Sonia alimshangaa sana Sam, hakuonekana kuwa hata na wazo la pili lakumuona akiwa uchi. ‘Ataniogeshaje sasa? Atafunga macho au ataniogesha nikiwa nimejifunika hili taulo?’ Sonia alibaki kimya huku anawaza. 

“Naona yana moto mzuri sasa.” Sam alikuwa akiyashika hayo maji yaliyokuwa yakitiririka kutoka kwenye bomba la juu. Sonia aliwaza kuoga na nguo ya ndani, lakini akasita.

“Nikusaidie kusimama?” Kabla yakujibu, Sam akamsogelea na kumnyanyua taratibu.  “Ukioga utajisikia vizuri.” Alisisitiza wakati Sonia akiweka taulo lake pembeni. Taratibu hofu ya Sonia ilianza kupungua baada ya kumuona Sam ni kama haoni anacho kitizama. 

Alimsaidia kugeuka kulia na kushoto wakati Sonia anajipaka sabuni na kujisuuza povu. “Naona mapovu yameisha yote.” Alifunga maji na kumfunika taulo. “Asante sana.” “Unajisikia vizuri?” “Afadhali.” “Twende ukapumzike kitandani, nitarudi kufua hiyo nguo.” Sonia alijiuliza. ‘Anataka na kunifulia nguo yangu ya ndani tena? Sidhani kama ni sawa!’ Aliwaza. 

“Au ngoja niifue tu mwenyewe.” Akajibaraguza. “Wala usijali. Wakati umepanda kitandani kabisa, nitarudi kuja kuifua. Twende ukapumzike, usiingiwe na baridi.” Alimuacha Sonia amekaa kitandani, akaenda kumtafutia nguo nyingine ya hospitali ya kubadilisha kwa nesi aliyekuwepo usiku huo. Baada ya muda mfupi akarudi na taulo jingine na gauni. 

Akainama na kumkausha miguu vizuri. “Hakuna mafuta.” Sam aliongea huku akitabasamu. “Hamna neno. Nakushukuru sana.” “Toa hilo taulo, ili uvae hii gauni, utaingia baridi. Limelowa sana.” Akatoa taulo Sam akimsaidia kulinyanyua na kumsaidia kumvalisha kwenye mikono, kisha akamfunga vimikanda vidogo vilivyokuwa vikining’inia pembeni ya gauni hilo. 

Akarudi kwenye mfuko uliokuwa na vitu vyake. Akamtolea nguo yake ya ndani na kumkabidhi. Nikusaidie kusimama. “Nipo sawa.” Sonia akavaa na kurudi kitandani. “Jinyooshe kitandani upumzike.” Akamfunika vizuri na kurudi chooni. Alimuacha Sonia akiwa amepigwa na butwaa. Lakini Sam hakuonyesha kama kuna jambo lolote baya au la tofauti lililokuwa likiendelea. Kwa hofu kubwa iliyokuwa imemkamata, Sonia alipitiwa na usingizi mpaka asubuhi. 

**********************

Aliamshwa na sauti ya madaktari waliokuwa wanapita kuangalia wagonjwa. “Unajisikiaje?” Mmoja wao akamuuliza Sonia. “Vizuri.” “Kichwa?” “Sasa hivi kimetulia.” Walijadiliana kwa muda na kumgeukia tena. “Tutakuruhusu. Lakini hakikisha unapata muda wakutosha kupumzika.” “Sawa.” Akakaa nakuanza kuzungusha macho kwenye kile chumba kama anatafuta kitu. 

“Nipo hapa Sonia.” Sam alikuwa amesimama upande wa juu ya kichwa cha Sonia kuwapisha madaktari. “Vipi?” Sonia akahema kwa nguvu. “Nilijua umeondoka!” “Siwezi kuondoka Sonia.” Taratibu akarudi kujiegemeza kwenye mto. Wale madaktari walibaki wakiwaangalia bila kusema kitu. 

Walitoka na Sam akarudi kukaa kwenye kitanda. Aliweza kuona uso wa Sonia ulivyofunguka na kujawa tabasamu. “Unajisikiaje?” Akamuuliza huku akijaribu kumshika tena kwa upendo, huku akimpapasa taratibu juu ya mabega. “Sasa hivi najisikia vizuri kabisa. Natamani kula kitu.” “Nitamuomba huyo nesi akuletee chakula.” “Wewe umekula?” “Nilikula. Walipitisha chakula wakati umelala.” Sam akabaki akimwangalia. 

“Asante sana Sam kwa kuwa na mimi hapa hospitalini.” “Wala usijali. Nimefurahi unaendelea vizuri.” “Sema nimepona bwana!” “Haya, nimefurahi umepona.” Wote wakacheka taratibu wakiangaliana kwa upendo. 

 **********************

Walishitukia mlango unafunguliwa bila yakubishwa hodi. “Basi hapo kuna mtu anatamani Sonia asipone, awe naye tu hapa hospitalini.” Nyange alianza kumtania Sam mara tu alipoingia. “Sasa kwa taarifa yako Sam, tumeshaambiwa Sonia amepona, tunarudi naye nyumbani.” Kila mtu alikuwa anacheka mpaka mama yake Sonia. 

“Unajisikiaje?” “Najisikia vizuri mama.” “Mimi nilijua tu utapona, na hivi Sam yuko hapa! Nilijua lazima upone. Lakini mimi nina swali.” “Hatutaki Nyange” “Basi ngoja nimuulize mama Sonia, mwenzangu tuliyefukuzwa wote jana.” “Hamkufukuzwa, bwana Nyange nini?” Wote walikuwa wakicheka. 

“Basi bwana kama hata swali siruhusiwi kuuliza, ngoja nikalipie turudi nyumbani. Maana hapa nishapigiwa simu na dada yako zaidi ya mara kumi. Mara niulizwe afya yako, au kama nimekuona, haya mara niulizwe unaonekanaje, maswali yote hayo yangu, wakati ndio nimeachana naye sasa hivi wakati tunakuja hapa. Heri tutoke tu, akakuone mwenyewe.” Nyange akatoka.

Baada ya muda mfupi akarudi na simu mkononi. “Hebu ongea na mama Briana. Ana wasiwasi kweli dada yako. Kila nikimwambia Sonia mzima haamini. Yeye hakulala usiku kucha anakuombolezea, wakati mwenzie unabembelezwa na Sam huku hospitalini!” Sonia alicheka na kujifunika uso kwa aibu.

“Mama Briana? Mama Briana?” “Nini Nyange? Nipe bwana Sonia.” “Ungewaona walivyokaa hapa. Ungeshangaa kama wako bustanini au hospitalini! Sam kafanya kukaa pembeni ya kitanda cha Sonia, ubavuni, anamchezea nywele mgonjwa.” “Nyange wewe jamani! Ujue mama yake yupo?”

“Wewe ndio unawasiwasi na mama yake, lakini huyo Sonia mwenyewe hata kuamka kumsalimia mama yake, hajaamka! Katulia tuli, amejiegemeza kwenye mto wanaangaliana na Sam! Wanavyotufanyia hapa, yaani kama sisi hatumo humu ndani! Hata kuangalia mama yake kavaa nguo gani, hajajisumbua hata kidogo kugeuza shingo yake. Kweli uzazi kazi!” Kila mtu alikuwa akicheka, Sonia akajifunika shuka kabisa mpaka kichwani, Sam akatoka nje, Mama Sonia yeye alikuwa akifuta machozi kwa kucheka. Nyange akampa simu Sonia ili aongee na mama Briana, akatoka nje. 

 **********************

Walirudi wote nyumbani Sonia akijisikia vizuri kabisa, lakini kwa namna fulani mahusiano yake na Sam yalianza kubadilika. Taratibu ‘Kaka Sam’ ilianza kupungua, ikabaki Sam. 

Baada ya siku tatu tokea Sonia atoke hospitalini, Nyange na familia yake wote wakiwa sebuleni wakiongea huku wakiangalia tv kama kawaida yao mida ya jioni baada ya kazi hukutanika hapo. Mlinzi kutoka getini alipiga simu kumwambia Nyange kuna wageni. “Kina nani tena!?” Nyange alimuuliza mlinzi. “Amesema Bosi wake Sam.” Nyange akamgeukia Sam. 

“Umeona Sam! Uuguzaji gani huo hauishi bwana? Mbona Sonia mwenyewe mzima kabisa huyo. Umeacha kwenda kazini wameamua kukufuata hapahapa.” Walianza kucheka lakini Sam alibaki na maswali. “Atakuwa nani huyo?” Sam akauliza, Nyange akarudi kwenye simu. “Waambie waingie.” 

Walishangaa kumuona Mr. Mponza yule bosi aliyekuwa ametaka kumbaka Sonia na mkewe wanaingia baada ya Josh kuwafungulia mlango. 

         Ukimya wa gafla ukazuka. Mr. Mponza bado alikuwa amevimba sana uso na jicho moja lilionekana jekundu sana kwa ndani na pembeni limevilia damu nakuwa jeusi. Baada ya kujitambulisha, Nyange akaanza kucheka sana. 

“We Nyange!” Mama Briana alishituka sana, asiamini na kumfinya mumewe. “Jamani kwani hapa msibani mama Briana? Mbona unanionea?” “Unacheka nini sasa!?” Akazidi kucheka huku akimwangalia Mponza na kupiga makofi. “Bwana Nyange nini lakini?!” Mama Briana akarudia kwa mshangao mkubwa.

“Kweli hujafa, hujaumbika!” Nyange aliendelea kucheka. “Bwana Sam kiboko! Yaani mkuu, japokuwa sikufahamu, lakini Sam amebadilisha kabisa muonekano wako wote wa sura.” “Nyange wewe!” Nyange alizidi kucheka mpaka machozi. 

“Kwani humuoni anavyotisha, mama Briana?” “Samahani sana dada yangu. Huyu ndivyo alivyo.” Ilimbidi mama Briana aombe radhi kwa mke wa yule bosi aliyekuwa amempigia magoti Sonia akiomba msamaha. Nyange aliendelea kucheka. 

“Josh? Josh?” Nyange aliita. “Naam baba.”  “Naomba funga huo mlango mkubwa nipe funguo zake, nikae nazo hapa.” Kila mtu akabaki anashangaa ni nini Nyange anataka kufanya tena. Josh akafanya kama alivyoagizwa.

“Briana mama?” Nyange akaita tena. “Simu ya dady iko wapi?” Briana akaileta simu waliyo kuwa wakichezea na Kana. Nyange alipiga namba fulani nakusubiri kwa muda kidogo. “Haloo?” “Haloo. Nyange hapa anaongea. Huwezi amini mambo ya Mungu.” Waliweza kusikia sauti upande wapili, lakini hawakusikia maneno. “Si yule jamaa! Amejileta mwenyewe hapa nyumbani kwangu.” Kila mtu hakuwa anaelewa. “Baada ya muda gani?” Nyange akauliza. “Asante sana.” Akashukuru na kukata simu, akumrudishia simu Briana achezee, kisha akarudi kukaa kimya kana kwamba hakuna alichofanya. 

“Wewe Nyange? Nini kinaendelea?” Mama Briana akauliza. “Huhusu nini?” “Kuhusu hawa wageni wamekuja kuomba msamaha. Mbona huwafuatilizi?” “Oooh! Huyo? Ataenda kuomba msamaha mahakamani sio hapa kwangu.” Nyange alishabadilika sura.

“Wewe mama, na wewe ni mpumbavu kabisa. Ingekuwa mtoto wako amefanyiwa kitendo cha kikatili kama hiki, ungekubali kusamehe tu? Hakuna mtu anayegusa mtu wa humu ndani akawa salama. Ulifikiri Sonia ni mtoto pori? Sasa alichokufanya Sam, ni kidogo. Mimi ndio kaka yao. Nakwambia kabisa umecheza na Nyange. Nitakuonyesha mjini wanaume wanaishije.” Mponza akionekana bado anamaumivu makali, akapiga magoti mbele ya Nyange. 

“Ni pombe ndugu yangu, naomba nisamehe.” “Najua ni pombe. Nataka kukufundisha mjini walevi wanaishije na ujue jinsi yakuweka mikono yako mbali ya mali za watu. Ulimuona Sam amekuja na msichana wake, pombe zako zikakufanya uweke dharau kwa Sam nakujiona wewe ndio unafaa kwa Sonia.”

“Sasa utaenda jela, wanaume wenzako wakakufaidi. Ndio utajifunza adabu wewe na wenzako wote wenye tabia kama zako. Nilikuwa nakusubiri sana utoke hospitalini.” Kila mtu akashangaa.

Yule mama na mumewe wote walianza kulia kama watoto wadogo. “Mama? Unaogopesha watoto wangu. Naomba ufunge mdomo kabla sijakuchapa na wewe makofi. Unawezaje kumleta mumeo mwenye sura mbaya hivyo kwenye nyumba iliyo na watoto wadogo? Wakishindwa kulala usiku?” Kila mtu alikuwa amepigwa na butwaa. Hawakuwahi kumuona Nyange amekasirika kiasi hicho. 

“Nisamehe bwana.” “Walikwambia unatafutwa eeh? Nilikuachia ujumbe pale hospitalini wakati umelala, usithubutu kutoroka nitakukamata tu, popote utakapo kimbilia nitakukamata, tena kwa garama yeyote ile. Utakuwa ulipata ujumbe wangu ndio maana umeleta sura yako hapa.” “Nisamehe.” 

“Nilishalipa pesa nyingi sana ukamatwe. Sitakuacha. Nilitamani sana wakuchukue palepale hospitalini wakati umelazwa lakini walisema ulikuwa umepasuka sana na wamekushona sehemu kubwa, huwezi kuruhusiwa. Sasa kaa na mkeo mpange mipango yenu ya mwisho maana unaenda kufia jela. Unajua madhara uliyoyasababisha kwa Sonia lakini?” “Nisamehe Sonia.”

 “Hata kama yeye atakusamehe, lakini unakwenda jela kwa kosa la ubakaji na nilishaandikisha kesi.” Hakuna aliyekuwa akimuelewa Nyange kwenye familia yake, kwani hakuwahi kuzungumzia chochote juu ya Mbakaji wa Sonia. 

Baada ya muda mfupi mlinzi akapiga tena simu kwa Nyange. “Kuna gari ipo hapa nje na watu wamevaa nguo za kiraia, lakini wamejitambulisha kama askari, wamesema wanataka kuingia.” “Wafungulie kabisa geti. Kuna mzigo wanakuja kuchukua.” Yule mama akazidi kulia. 

“Msamehe tafadhali. Nina watoto wadogo nasomesha. Nitafanya nini? Na mimi sina kazi.” “Hayo mlitakiwa muwe mmekwisha yazungumza na mumeo nilipowapa muda wakuagana. Hainihusu tena.” Gari ya polisi iliingia, maaskari kanzu watano walishuka na kubonyeza kengele ya mlango mkubwa. Nyange mwenyewe akasisimama kwenda kufungua. 

“Vipi Chaz? Mmekula lakini?” Nyange akaanza kupiga stori na wale maaskari huku wakicheka sana, kana kwamba hakuna lililotokea. “Karibuni jamani. Kwanza muingie ndani mumsalimie mwenye nyumba.” Nyange akawakaribisha wageni wake bila wasiwasi. 

“Sasa huyo ndio mwenyewe, anayetuweka mjini.” Nyange alimnyooshea mkewe kidole. “Mama Briana, na yule ndiye Briana kipenzi cha Daudi Nyange, ukiniona mjini nahangaika na kutokwa jasho, ujue ni sababu yake yule. Na yule dogo pale nampigia mahesabu makali sana, anaitwa Kana, ndiye mpinzani wangu mkubwa sana hapa duniani. Ujanja wangu wote, pale nimefika mwisho.”

“Msimuone mdogo vile, mchana kweupe amenipokonya binti, na alivyo na jeuri, hata mahari hajalipa.” Wale askari wote na Nyange walikuwa wakicheka kasoro wenyeji bado walikuwa kama wamepigwa bumbuwazi! Wao wakaendeleza utani. Kisha akamgeukia Sam.

“Huyu ndio yule mdogo wangu niliyekwambia, anaitwa Sam, hiki ndicho kifaa chenyewe, Sonia.” “Kweli sio utani!” Chaz akamkata Nyange. “Sasa hapo Chaz, kuwa makini ndugu yangu. Mimi simo kabisa hapo, Sam hana mchezo. Si umeona alivyobadili muonekana wa jamaa?” “Sam anaonekana ana huruma sana. Huyo bado hajabadilika sura. Uje kesho kituoni umuone atakavyokuwa amependeza.” “Mungu wangu wee!” Mke wa Mponza alipiga yowe.

“Tafadhali nyamaza, usiendelee kuniharibia usiku wangu.” Nyange akamkaripia na kumgeukia Chaz kwa uso wa tabasamu. “Sasa huyu ndio mzaa chema, Mama Sonia.” “Mbona mama mwenyewe kama binti tu?” Nyange aliendelea kucheka. 

“Sasa lazima kutafuta gari ya safari Chaz. Mahari ni Rwandaaa. Vitu hivi havipatikaniki mjini hapa.” “Kweli! Hata mimi mwenyewe nimeona. Lakini na mimi si unakumbuka sijaoa, Nyange?” Nyange alianza kucheka mpaka alikaa kwenye kochi. 

“Na mama yake pia?” Nyange akauliza. “Wewe mwenyewe umesema vitu hivi mjini hadimu. Heri na mimi nimalize kabisa.” “Sasa hapo itabidi uongee na mama Briana. Nisije fukuzwa chumbani.” Wote waliendelea kucheka, mama Briana alibaki ameangalia chini. 

“Yule pale ni Josh, mpinzani wa Sam. Kazubaa zubaa hapa mpaka Sam kamzidi nguvu. Huoni alivyonywea? Kapokonywa mtoto wa Kinyarwanda, mchana kweupee. Tatizo la humu ndani Chaz, huwa sisikilizwi Mkuu. Nilishamwambia Josh, changamka. Kabakia kung’ata kucha kama mtoto wa kike, Sonia kaondoka kiulaini.” Wote waliendelea kucheka. 

“Sasa lipo dume lenyewe lipo juu limelala. Huyo ndio mlinzi mwenzangu, tunamlinda Briana. Yeye analala mida hii, mimi nikienda kulala yeye mwenzangu anaamka kuhakikisha mtu hakatishi anga za Briana. Anaitwa Brayan. Tunahakikisha ulinzi kwa Briana ni masaa 24.” 

“Ndiye yule ulisema aliamua kujia hapahapa nyumbani?” “Ewaaaa! Kumbe unakumbuka? Sasa amelala. Kwa hiyo hii ndio familia yangu jamani. Karibuni sana.”  

“Ila Nyange hapo kwa Briana! Jasho litakutoka.” “Huoni ninavyokonda na kutokwa mvi? Mvi hizi sio uzee jamani, mawazo. Kila akikuwa huyu mtoto, mimi sina raha.” Nyange aliendelea kutaniana na wageni wake bila kumjali mtu. 

         “Sasa nyumba hii hakuna pombe. Mwenye nyumba amepiga marufuku pombe ya aina yoyote kuingizwa humu ndani. Hata chupa zake marufuku. Sijui mtakunywa nini?” Nyange aliongeza. “Ndio maana hunywi nini?” “Yaani ile harufu tu, kitandani hupandi. Ndio maana mimi sipiti kabisa karibu ya viwanda vya pombe.” Wote waliendelea kucheka. 

“Eti Josh, kuna nini ndani?” Kabla ya Josh kujibu Chaz akdakia. “Usisumbuke kabisa Nyange. Hapa nyumbani. Tutarudi tu. Wewe turuhusu tuondoke na mgeni wetu, halafu tutawasiliana.” “Bila shaka. Ruksa. Ila sijui mama naye anataka kuongozana na mumewe?” Tayari Nyange alishabadilika sura. 

“Eti mama?” “Naomba mumsamehe jamani!” “Usipoteze pumzi yako mama, utaihitaji sana mahakamani mbele ya hakimu.” Tayari wale maaskari walishabadili sura na kuvaa sura za kazi. Walimfunga Mr. Mponza pingu, wawili wao walimnyanyua kwa nguvu pale alipokuwa amepiga magoti na kumtoa nje. 

“Mama? Unamsindikiza mumeo?” Chaz akamuuliza kwa ukali. “Nanii, funga pingu na huyu mama ingiza kwenye gari.” “Akuu. Wakati namwambia aache pombe hanisikii, leo anataka kufa na mimi? Wala sihusiki baba yangu.” Tayari yule mama alishabadilika. 

“Na wewe unakesi ya kujibu. Kwa kosa alilofanya mumeo, halafu unakuja kuomba naye msamaha hapa, badala yakumpeleka kwenye vyombo vya sheria! Ulitaka tabia hii aendelee nayo mpaka kwa watoto wako wakike ndipo umfikishe kwenye vyombo vya usalama? Hebu funga pingu huyu.” Chaz alishabadilika kabisa. “Nilimwambia twende polisi akasema nimlete kwanza hapa. Mbona mimi ningempeleka tu polisi. Unafikiri baba?” Wote walibaki namshangao. 

“Wewe Nyange?” “Vipi mama Briana?” “Usisimame tu hapo bwana, ongea na hao marafiki zako, wamwachie mama wa watu. Wewe hujasikia amesema ana watoto wadogo?” Mama Briana alishaingiwa na hofu baada ya wale polisi kuvaa sura za kazi. 

“Kumbe una watoto?” Nyange akaanza kucheka tena. “Nyange!?” Mama Briana akamvuta suruali. “Ninao baba. Tena wadogo kweli.” “Eti unasemaje Chaz? Mimi naona mama akalee.” Walimfungua pingu nakuondoka bila kuaga. 

“Sasa mama, una dakika moja ya kupotea humu ndani mwangu. Nikikuona bado unashangaa, utaondoka kwa style aliyoondoka nayo mumeo. Potea na nisiwahi kukuona hapa kwetu tena.” Yule mama alianza kukimbilia mlangoni. 

“Mama nanii? Ponza, sijui Pozi?” Nyange alianza kumwita huku akicheka sana. Tayari yule mama alishafika mlangoni, akasimama huku anatetemeka. “Umesahau pochi na funguo za gari.” Alitaka kurudi. “Aaaaa! Ahahahh! Hapo hapo ulipo vitakufuata. Nimekwambia usiwahi kurudi hapa ndani. Au huelewi?” “Naelewa baba.” Nyange akamrushia vitu vyake. Yule mama aliokota na kuondoka kwa kasi sana. Gafla pakawa kimya kabisa.  

 **********************

“Sijui taarifa ya habari imeisha jamani? Briana mama! Mpe dady remote.” Nyange aliwasha tv na kutulia kimya kana kwamba hakuna alichofanya. “Nyange wewe jamani!” “Unataka tukalale mama Briana? Subiri basi nisikilize taarifa ya habari.” “Hebu zima kwanza hiyo tv.” “Basi ukishasikia amri inatoka kwa mama Bree, ujue upo matatizoni. Si usubiri basi nimalize taarifa ya habari mpenzi wangu?” 

“Zima bwana Nyange nini?” “Haya mama.” Nyange akazima tv nakumgeukia mkewe. “Hivi wewe ukoje Nyange jamani!? Huna huruma? Si tungeyamaliza haya mambo hapahapa nyumbani?” “Angekuwa Briana kafanyiwa hivyo, tungeyamaliza hapahapa nyumbani? Yaani kwa yeye kuja tu hapa na kupiga magoti na kutoa maneno mazuriyaliyojaa huruma, iwe ndio basi!?” Mama Briana akanyamaza kidogo kama anayefikiria, na kumwangalia Briana. 

“Basi niruhusu mke wangu niangalie taarifa ya habari, wakati unatafuta jibu.” Mama Briana alikaa kimya kwa muda, akaamua kuondoka. “Sasa vipi mama Bree? Naruhusiwa kuja chumbani?” “Mi naona wewe leo ulale hapohapo unapoangalia taarifa ya habari.” Mama Briana akajibu huku akipandisha ngazi kuelekea chumbani kwao. 

“Mama Bree? Mama Bree? Penninah, mpenzi!” Nyange aliendelea kumchokoza. “Nini Nyange?” “Lakini leo mke wangu nimekusifu!” “Bwana Nyange!” “Kweli tena mpenzi wangu. Leo hujalia kabisa!” “Naomba uniache Nyange. Unafikiri ulivyofanya ni vizuri?” “Nataka kumfundisha adabu bwana mama Bree, usinichukie. Siku mbili au tatu watamtoa.” “Kweli Nyange?” Mama Briana akarudi kukaa huku anacheka. 

“Muone alivyofurahi. Anahuruma huyu!” “Ndio maana nakupenda mume wangu!” “Kwani kweli ndio ulikuwa umenifukuza chumbani?” “Bwana tuongee mambo ya maana.” “Aliniumiza sana yule jamaa. Niliumia sana kumuona Sonia kwenye ile hali. Asubuhi ile wakati Sonia yupo hospitalini, nikampigia simu Chaz nikamuelezea. Akaniambia nisiwe na wasiwasi, jioni yake akaniambia ameshapata taarifa zote za yule jamaa, lakini ana hali mbaya sana hospitalini hawezi kutolewa.”

“Nikaamua kwenda kuhakikisha mwenyewe, nikamkuta amelala, mimi mwenyewe nilitoka na kumwambia Chaz basi. Na nilishaambiwa ni kweli ana watoto wadogo na mkewe hana kazi. Nikaona nitawaadhibu watoto wake kama nitamuweka baba yao jela, lakini Chaz akasema japokuwa ameshapata kipondo lakini lazima tumpe onyo jingine ambalo hatakaa asahau.” 

“Wewe Chaz umemfahamia wapi?” “Tulisoma naye chuo, halafu mtu wa kwetu.” Nyange akajibu. “Lakini atakuwa amejifunza. Sidhani hata kama atarudia tena pombe.” Mama Briana alikuwa akiongea huku akicheka. “Sasa hivi ndio unajidai kucheka!” “Uliniogopesha kweli mwenzio! Unajua wewe Nyange ni mkorofi sana?” “Ulimuona mkewe lakini?” Kila mtu alianza kucheka. “Bwana mwanamke hamtaki tena mumewe! Fanya mchezo na jela wewe?” Nyange aliendelea kutania. 

 **********************

Sam alivuta mkono wa Sonia na kuushika. Nyange akaanza kucheka tena. “Unajua nini Sam?” “Sitaki Nyange.” “Mngekuwa basi mnanisikiliza hata siku moja moja jamani, khaa!” Nyange alizidi kucheka. “Mimi nikikifilisika, nafungua biashara ya ndondi nchini. Wewe ndio utakuwa mwajiriwa wa kwanza na utakuwa ndio msimamizi wa hicho kituo. Hakika tutatengeneza sana pesa.” Sam alianza kucheka na kila mtu alicheka. 

“Mimi sio mwana ndondi bwana! Namlinda Sonia tu.” Nyange alicheka sana. “Si mlikuwa mnanibishia humu ndani kama Sonia halindwi kama raisi? Sasa mmemsikia Sam mwenyewe! Halafu mama Sonia, usimuone mwanao alikuwa akisomea hapa ndani. Hakuanzia kusomea hapa ndani huyo.” “Nyange wewe!?” Mkewe akashituka, hakutegemea kama mumewe atatoa siri.

“Jamani! Mi nataka kumwambia kisa cha Sonia kusoma humu ndani, asije dhani tulishindwa ada yakumpeleka mtoto shule. Hata kidogo mama Sonia. Tena tulishalipa ada yote, ila mwalimu wa Sonia naye pia alipata kipondo tena yeye kwa kosa la kupiga simuna kutaka kumsaidia Sonia bila baraka za Sam.” 

“Nyange hana siri!” “Hukiniambia nisiseme bwana mama Briana! Mbona unapenda kunilaumu bure?” Kila mtu alikuwa akicheka sana. 

“Nitakupa Brayan umfundishe kulinda. Sitaki watu wamsogelee Briana wangu.” “Haolewi huyo Briana?” “Weee. Huyo mume wa Briana ajipange vizuri.” “Kana tu hapa kakutoa jasho. Ukimwita Briana siku hizi mpaka Kana akubali kuja naye.” “Yaani huyu Kana huyu, namwangalia sana. Dawa yake ipo jikoni. Nitamsemea kwa Sam mimi!” Kila mtu alizidi kucheka. 

 **********************

“Lakini baba Briana, naomba nikushukuru sana. Hatukuwahi kutetewa na mtu maishani kwetu. Yaani nyinyi watu, ndio wa kwanza. Tumekuwa watu wakudharauliwana kunyanyaswa kila tuendapo, kasoro hapa kwenu.” Mama Sonia alianza kutokwa na machozi. 

“Maisha yetu yamekuwa ya kugandamizwa kweli! Na hivi mimi hii sio nchi yangu! Sina sauti na sina pakushitaki.” “Sisi ni ndugu sasa, mama Sonia. Mtu akikuumiza wewe, sisi sote tunaumia.”

“Ubinadamu mliotuonyesha wewe na Sonia, hatukuwahi kuona maishani mwetu.” Nyange aliongea kwa kumaanisha. “Ni kweli.” Mama Briana aliitikia na Sam naye alidakia. “Kweli kabisa.” Huku bado ameshikilia mkono wa Sonia. 

“Fikiria juzi tu hapa, umemzalisha mke wangu salama kabisa. Nimetaka kukupa ile pesa tuliyokuwa tumetenga ya kulipia garama zote za kujifungua mama Briana hospitalini, ukakataa katakata.”

“Haya, unavyomuona Briana hivyo, hakuwa hivyo hata kidogo, mama Sonia. Ilikuwa mpaka aibu kutoka naye huyu mtoto humu ndani. Mtoto alikuwa na kwashakoo. Na wakati vyakula vipo ndani na wasichana wakazi walikuwepo, tena tulikuwa tukiwalipa mshahara sawa na tunao mlipa Sonia. Wakubwa kwa wadogo wamepita humu ndani. Lakini Sonia amembadilisha huyo mtoto mpaka akawa hivyo unavyomuona.”

“Sam ndio akiongea kuhusu Sonia hatakaa amalize. Alimuuguza Sam akiwa peke yake ndani ya nyumba isiyo na kitu! Achilia swala la pesa alizokuwa ameziokota na kuzirudisha.”

“Josh ndio naye wakati wote anawasifia. Tena yeye ndio mtu wakaribu na nyinyi sana kuliko sisi, kwa kuwa mnafanya naye kazi ndio anawafahamu kwa karibu zaidi.”

“Kwetu nyinyi ni ndugu tena ndugu tunao wathamini na kuwajali sana. Nihivyo hatuna jinsi ya kuwalipa maana wote wewe na mwanao hamtaki kupokea pesa zetu. Hamlipiki.” “Nikweli kabisa. Tunawashukuru na mjue tunawapenda sana. Sisi ni ndugu sasa. Hatuwahesabu kama wafanyakazi.” Mama Briana akaongezea. 

“Tena mama Sonia nataka tuanze kufuatilia mambo ya uraia wako tuone kama utafanikiwa kupata uraia wa hapa nchini. Sio uishi kwa mateso hivyo.” Mama Sonia alianza kutokwa na machozi. 

“Nini tena mama? Badala ufurahie! Unalia tena?” Sonia akamsogelea mama yake. Mama Sonia alikuwa ametoneshwa kidonda. “Nawashukuru sana jamani! Sina chakusema. Nimeshanyanyaswa hii nchi, sitakaa nisahahu!” “Nini kilitokea?” Nyange akauliza na kufanya kila mtu kumgeukia mama Sonia kutaka kujua kilichompata. Mama Sonia alifikiria kidogo na kuanza kuelezea historia ambayo alikuwa ameificha na kumtesa sana moyoni mwake. Hata Sonia hakuwa amemwambia.  

**********************

Mama Sonia alianza historia yake tokea anafika nchini. “Nilipokuwa pale kwenye kambi ya wakimbizi,          Shinyanga, nilifuatwa nikaambiwa kuna kiongozi mkubwa sana wa hii nchi anatafuta msichana wa kazi za ndani. Kwa hiyo mimi niende nikasaidie. Nikatoka pale nikahamia nyumbani kwao.”

“Maisha yalikuwa mazuri na nikaweza kumudu kazi zangu. Siku moja yule mama mwenye nyumba akaniambia kuna mtoto wao amemaliza shahada yake ya sheria hapo chuo kikuu cha Mlimani kwa hiyo anarudi nyumbani siku ya ijumaa, nitayarishe chakula kizuri sana siku hiyo.”

“Basi ile siku ikafika, yule kijana akaja pale ndani tukatambulishwa jina lake anaitwa Paul. Paul alisifia sana chakula nilichopika. Baada ya siku mbili kupita yule mama akasema kuna wageni wengine watakuja pale nyumbani niandae chakula cha jioni kizuri sana.”

“Kumbe     walikuwa    wamemtafutia   kijana        wao mchumba. Alipoletwa yule binti, Paul, yaani kijana wa pale ndani hakumpenda kabisa yule binti. Ikawa ugomvi mkubwa sana baada ya hapo. Yule mama alikuwa mkorofi sana, alitaka mwanae amuoe yule binti lakini Paul alikataa katakata.”

“Baba yake Paul alikuwa mtu mzuri sana na muelewa, wakati wote alikuwa akimwambia mkewe, ‘Paul ndio muoji na ndiye atakaye kuwa akiishi na huyu mwanamke. Kama yeye hamtaki, kwa nini usiheshimu maamuzi yake?’ Lakini bado yule mama aling’ang’ania, akisema hata kaa ampokee mwanamke yeyote kama mkwewe asipokuwa yule msichana aliyemtafuta yeye.” Mama Sonia alitulia kidogo. 

“Wakati huo mimi nina miaka 14. Taratibu Paul akaanza kujenga mazoea na mimi. Akitumwa mahali, ananiomba twende naye, nikipika jikoni, atakuja kusaidia kama nikuosha vyombo, au nikipewa nguo za kufua lazima atanisaidia tu. Ikawa hivyo ilimradi tu tuwe wote.

“Akaacha kutoka mle ndani kabisa, hata kwa marafiki zake aliacha kwenda na akitokea anatumwa mahali, lazima anisaidie kazi niliyokuwa nayo wakati huo, ili twende naye.” Nyange akaanza kucheka. “Nyange bwana!” Mama Sonia akainama. 

“Jamani mama Briana! Si hata unilize basi nacheka nini!” “Sitaki. Mama Sonia endelea mwaya!” “Sawa bwana! Lakini ni kitu kizuri.” “Hapana Nyange.” “Basi nanyamaza.” Lakini Nyange aliendelea kucheka taratibu nakufanya kila mtu aanze kucheka. 

“Si umruhusu tu aseme shem? Hawezi kunyamaza huyo, mpaka aseme kinachomkera rohoni. Na atakuwa anatucheka mimi na Sonia tu, hana jipya mumeo.” Sam aliingilia. 

“Eti Nyange, unamcheka Sonia na Sam?” Mama Briana akamuuliza. “Kweli embe halidondoki kwenye mchungwa. Kumbe sumu hiyo Sonia kaitoa kwa mama yake! Sam amemganda Sonia, hasikii haambiwi kutwa yupo nyuma ya mgongo wa Sonia. Wewe ushaona mtoto wa kiume anachuja tui la nazi?” “Si nilikwambia ni uchokozi tu? Hana lolote mumeo.” Sam alidakia, kila mtu alianguka kicheko. 

“Mpaka Josh mwenyewe alikuwa hamuelewi Sam, amebaki katoa macho kwa mshangao. Mtu anafanya kazi za kompyuta, tena bank, lakini anakimbilia kuchuja tui la nazi nyumbani, tena na tai yake shingoni! Yaani kule kuingia ndani tu na kwenda kubadili nguo pia anaona anamchelewa Sonia!”

“Kweli mama Sonia kiboko, kamrithisha mwanae kila kitu! Mi nilijua ni uzuri tu. Sam amekuwa kama kalogwa, mdogo wangu!” Sonia naye alikuwa akicheka huku ameinama, mama yeke ndio alikuwa akifuta machozi kwa kucheka. 

“Unaona unamfanya mama Sonia anashindwa kuongea? Nyamaza Nyange bwana, lasivyo tunakufukuza.” “Jamani mama Briana muonezi! Mimi ndio nimeuliza, nasimuliwa mimi, gafla nyinyi ndio mmegeuka wakereketwa wa hii habari, wakati siku zote mlikuwa naye hapa mama Sonia, mbona hamkumuuliza? Mimi ndio muulizaji halafu mnataka tena kunifukuza! Nitaondoka na mama Sonia akanisimulie baa mimi!” Wote walikuwa wakicheka sana. 

“Endelea mwaya mama Sonia. Usimsikilize Nyange hata kidogo.” “Taratibu tukajikuta kwenye mapenzi na Paul. Lakini nilikuwa mdogo sana, hata bado nilikuwa sijakuwa. Mama yake alipokuja kuhisi, alitamani kuchanganyikiwa. Paul alikuwa hasikii la mtu yeyote, alisema yeye ananipenda anataka kunioa.”

“Alipoona mama yake anazidi kuninyanyasa. Tulitoroka na Paul kutoka kwao Shinyanga mpaka Mwanza. Tulikaa na Paul karibia mwaka mzima amenifungia tu ndani na ndio kipindi hichohicho wakati nipo naye nikakua na yeye ndio alinifundisha kila kitu.”

“Maisha yetu yalikuwa yamejaa amani na furaha, tena wenyewe tulikodi chumba kimoja tu wala hatukuwa na vitu vingi lakini sikuwahi kufurahia maisha kama kipindi hicho. Paul alikuwa akinijali kupita nitakavyoeleza. Anajua kupenda, sijawahi ona hapa duniani.” “Kuliko hata Sam?” Nyange alidakia. 

“Nyange!?” “Mimi nauliza tu jamani! Ona Sam wawatu anavyohangaika, sasa unaambiwa hajamfikia Paul!” “Bwana unaharibu stori nzima kwa uchokozi wako kwa Sam. Mbona hujilinganishi na wewe?” Mama Sonia aliendelea kucheka kwa aibu. 

“Eti Mama Sonia, mimi je?” “Usimjibu mwaya, endelea.” Sam alicheka sana. “Ndio maana nakupenda mama Bree. Muone mumeo alivyopooza. Umemshika pabaya kweli!” Mama Bree alianza kumcheka vile alivyopooza. 

“Ananipenda sana mume wangu. Eti Nyange?” “Mimi nakuangalia sana, mama Briana. Maana mwisho wa siku tunabaki mimi na wewe tu.” “Nakutania bwana na wewe! Wenyewe tunapenda na D wangu. Lakini unyamaze mpaka stori iishe. Endelea Mama Sonia.” 

“Matatizo yalianza nilipoanza kuugua. Paul alichanganyikiwa sana, kwani nilikuwa natapika asubuhi mpaka asubuhi. Nikaishiwa nguvu kabisa nikawa siwezi hata kusimama. Paul akiwa amechanganyikiwa, akilia kama mtoto, alimpigia baba yake simu, usiku usiku akiomba msaada.”

“Baada ya masaa machache nikashitukia yule mama amesimama mlangoni kwetu. Kabla ya salamu wala kuniangalia ninaendeleaje, akaanza kumpa Paul sharti.” “Sharti gani tena?” Sonia aliuliza kwa mshangao.

“Alimwambia kama ananipenda mimi na anataka nisaidiwe nipone, lazima arudi chuoni akasome shahada yake ya pili, tena nje ya nchi, akimaliza ndio atanioa, lasivyo aliambiwa hatakaa anione tena, watanirudisha Rwanda nikiwa vilevile mgonjwa. Tena hapo alikuja na vijana wawili aliosema ni askari kanzu.” Mama Sonia alianza kutokwa na machozi.

“Nakumbuka jinsi Paul alivyokuwa akilia huku amempigia magoti mama yake akimsihi amuache asomee hapahapa nchini, lakini yule mama alikataa katakata. Alichomwambia achague, yeye ndio anaondoka na wale askari kurudishwa nyumbani kwao, halafu yeye mwenyewe yule mama, ndio anipeleke hospitalini nikipona alimwambia nitarudishwa kwao nimsubiri amalize shule tuoane, au mimi ndio niondoke na wale askari nirudishwe Rwanda muda ule ule, tena vilevile nikiwa mgonjwa. Paul alikuwa akilia sana akimbembeleza mama yake, angalau basi hata aniuguze kwanza mpaka nitakapo pona ndio ataenda chuoni, lakini yule mama alimpa dakika 5 tu za sisi kuagana, yeye akatoka nje na kumwambia atakaporudi ndani lazima mmoja wetu ataondoka na wale askari.”

“Tulishindwa kuongea kwa muda mrefu mimi na Paul tukilia sana. Mwishoe aliniomba kitu, kwa kuwa mama aliyekuwa ametupangisha hicho chumba alikuwa akitupenda sana mimi na Paul alituambia ninaweza kuwa ni mjamzito. Paul aliingiwa na hofu sana kwani ndio nilikuwa nina miaka 15. Lakini yule mama alimwambia Paul asiogope naweza kujifungua vizuri tu sababu ya umbile langu la urefu.”

“Ndio wakati tunaagana Paul aliniomba sana nisikubali kwa namna yoyote kumpoteza mtoto wetu, aliniomba sana kumtunza kwa namna yoyote ile. Kabla ya hapo tulikuwa tumeshapanga idadi ya watoto tutakao wazaa, na kila siku Paul alikuwa anakuja na majina mapya.”

“Ndipo nilipomuomba kwa kumbukumbu ya wazazi wangu kama atakuja wa kike tumpe jina la mama yangu, Sonia na kama ni wakiume nikamuomba tumwite Kanamugire jina la baba yangu. Paul alikubali. Lakini yeye alisema anauhakika yule atakuwa ni Sonia. Kwa hiyo wakati tunaagana aliniomba sana, ‘Naomba hakikisha Sonia anasoma’. Huo ndio ulikuwa wosia wake wa mwisho, akaniwekea pesa zote tulizokuwa nazo kwenye nguo yangu ya ndani, wale vijana waliingia nakumfunga pingu Paul, wakaondoka naye.”

Sonia alikuwa akilia sana. Sam alimsogeza karibu nakumkumbatia. Asijue aseme nini. Mama yake Sonia naye alikuwa akisimulia huku machozi yakimtoka, mwishowe akanyamaza nakushindwa kuendelea kwa kulia. 

**********************

“Samahani mama Sonia. Naomba utumalizie tafadhali. Ikawaje kwa upande wako?” Nyange akavunja ukimya kwani hata mkewe mwenyewe alikuwa akitokwa na machozi. 

“Nilitolewa pale nikiwa sijiwezi kabisa na kupelekwa hospitalini, nikawekewa chupa za maji usiku huohuo, asubuhi nikachukuliwa vipimo, majibu yaliletwa nikiwa na yule mama. Tuliambia sina ugonjwa wowote ule, ila ni hali inayotokana na ujauzito wangu.”

“Yule mama alikaribia kuchanganyikiwa. Alianza kuropoka palepale kwamba hawezi kuruhusu huyo mtoto azaliwe, akasogea na yule daktari pembeni nikamsikia akimuomba amtafutie daktari mwingine atakaye nitoa hiyo mimba kwa garama zozote zile. Nilijifanya kama sijasikia, alipoondoka tu na mimi ndipo nikapata mwanya wakutoroka kwa kuwa sikujua walikubaliana nini na yule daktari. Ndio nikatoroka mpaka leo.” Sonia akajitoa mikononi kwa Sam na kumgeukia mama yake huku amekunja uso. 

“Kwa hiyo huyo Paul hajafa?!” Mama Sonia akaanza kubabaika alikumbuka alivyo mdanganya Sonia kama baba yake alisha kufa. “Mama!?” Sonia aliita tena kwa mshangao. “Sijui.” “Sasa kwa nini ulisema kama amekufa!?” Mama yake alikuwa ni kama amepatwa na baridi kali alibaki akibabaika. “Nili..” Sonia akasimama nakuingia chumbani kwake na kuacha kila mtu kimya wasijue chakusema. 

**********************

Upendo na umoja ulizidi kwenye nyumba ya Nyange. Waliheshimiana na kutegemeana kwa kila jambo, kasoro Sonia na mama yake. Kila mama yake alipotaka kuongelea zaidi swala la baba yake, Sonia alikuwa mkali kabisa nakuomba wasiwahi kuzungumzia tena juu ya Paul. 

“Wewe ndio unamjua Paul, lakini mimi tangia mdogo namjua baba yangu aliyekufa. Naomba ibaki tu hivyo mama, tafadhali sana.” Ilimbidi mama Sonia akubali kwa kuwa Sonia alionekana anamaanisha anachoongea. Hata mama Sonia alipomuomba Sam aongee naye, Sonia alimuomba Sam wasiwahi kuja kumuongelea baba yake kabisa. 

“Hainisaidii, wala haitanisaidia chochote tena Sam, zaidi yakunifanya nifikirie mambo yatakayo zidi kuniumiza zaidi. Yataibua maswali mengi yatakayonipelekea kwenye chuki kwa wazazi wangu wanao onekana wao walipendana sana na ninajua hata nikimuuliza hayo maswali mama, hatakaa ayajibu ila Paul mwenyewe.”

“Kwa hiyo naomba nibaki na habari za kifo cha baba yangu tu, itanisaidia kuendelea kusonga mbele na kupambana na haya maisha.” Sam alikubali na maisha yaliendelea kama kawaida.   

**********************

Matokeo ya Sonia yalipotoka alikuwa amefaulu vizuri sana, kwa daraja la kwanza. Mama yake Sonia alikuwa akiimba nyimbo za kwao kila wakati. “Hongera bwana Sam.” “Kwani mimi ndio nilifanya mtihani, baba Briana? Mbona hivyo?” “Mwalimu ulikuwa wewe, dereva wewe, na siku ya mtihani ukachukua na likizo kabisaa. Sasa hustahili hongera?” “Hapana bwana! Mimi nilifanya kwa ajili ya Sonia.” Nyange alianza kucheka. 

“Wala sitakusikiliza.” “Najua hutanisikiliza, kwa hiyo heri niendelee tu kucheka. Sasa tunaenda kusherekea wapi?” “Tumuulize mama Bree. Yeye ndio hajatoka humu ndani shemeji yangu, tangia ajifungue.” “Sema mke wangu na sisi tuponee humohumo.” Mama Briana akaanza kucheka. 

“Sasa na wewe sio uanze kuchagua sehemu za kuchezea watoto! Taja maeneo ya nguvu. Sam anatutoa.” “Unakumbuka kule tulipoenda Kigamboni?” “Umemuona mambo yake huyu? Yaani mke wangu huyu, mambo yake rahisi rahisi. Sasa ndio wapi kule? Taja maeneo bwana, watu tukale na kunywa, halafu tulale kabisa hukohuko hata siku mbili ndio turudi.” 

“Jamani Nyange! Sam anajenga!” “Wewe humjui Sam nini? Atafanya chochote kumfurahisha Sonia. Uongo Sam?” Sonia akainama kwa aibu. Mama yake alikuwa akicheka tu. 

“Bwana waache. Sitaki kumtia garama Sam wangu.” “Mbona mwenyewe hajakataa? Briana mama, njoo kipenzi changu. Mpe dady simu yake.” Nyange alipiga simu kwenye hoteli moja Bagamoyo na kuwekeza vyumba vyakuwatosha watu wote, mpaka Josh. 

“Sasa mjiandae weekend hii tunaenda Bagamoyo, kumpongeza Sonia. Au unasemaje Sam?” “Kabisa kaka. Anastahili pongezi.” “Daah! Afadhali bwana! Kwa mara ya kwanza tumekubaliana na mdogo wangu, ni kweli Sonia anastahili pongezi, maana amejikaza kweli kweli si mchezo.” Kidogo watu walitulia wakidhani kwa mara ya kwanza Nyange na Sam wanaongea mawazo yanayo fanana. 

Lakini Nyange akaendelea. “Yaani mama Sonia, huyu mwanao anatakiwa pongezi, tena pongezi kubwa sana. Maana anaonekana akikusudia jambo anahakikisha linafanyika, ingekuwa msichana mwengine asingeweza.”

“Ilikuwa shuguli hapa kipindi anasoma, sio mchezo! Heri hukuwepo. Maana ungekuwepo tokea mwanzoni, ungemuhurumia mwanao. Heri umekuja hekaheka ndio zina malizika. Maana ilikuwa mara walimu wake wapigwe! Mara akataliwe kwenda kujisomea na wenzake! Mara shule inahamishiwa hapa ndani! Leo na mwalimu huyu, kesho mwalimu anafukuzwa analetewa mwingine!”

“Mara shule inahamishiwa maktaba, mara shule inahamishiwa site huko kunako jengwa nyumba! Mara week hii anapewa simu, mara week nyingine ananyang’anywa na akirudishiwa namba si ile ya zamani, inakuwa ishabadilishwa! Lakini mtoto wa watu akakubali yote. Mungu naye amemuangazia, amefaulu bwana! Hongera mama. Hongera sana.” Nyange akasimama kabisa kumpa mkono Sonia. 

“Usimpe mkono, Sonia. Anakuchokoza tu.” Wote walikuwa wakicheka sana. Nyange akarudi kukaa. “Mimi sio mbishi Sam. Usije kunipiga bure. Simpi mkono.” “Bwana Nyange nini?” “Nakwambia mimi mke wangu! Ukitaka kuona ubaya wa Sam, msogelee Sonia au hata mpigie simu. Utajuta kuzaliwa.” Sam akanyanyuka nakuondoka huku akicheka. 

“Sam, safari ijumaa jioni.” “Nimesikia kaka.” “Sasa mbona umemuacha Sonia? Josh atamtorosha, we jidai kuondoka.” Sam alitingisha kichwa nakutokea mlango wa nyuma. 

 Mapumziko Ya Bagamoyo.

Kila mtu aliisubiri siku ya ijumaa kwa hamu sana. Waliondoka jioni karibia usiku kwa kuwa ilibidi kumsubiria Nyange na Sam watoke kazini. Sam alimuendesha Sonia, mama yake Sonia na Josh kuelekea Bagamoyo. Nyange alimuendesha mkewe na watoto wote. 

Kwenye chumba cha kina Sonia alilala, yeye na mama yake kitanda kimoja, Kana na Briana kitanda chao kama kawaida yao kutokuachana asubuhi hadi asubuhi. Briana alimfuata Kana kila mahali na usiku Briana ilikuwa lazima alale na Kana ndipo pakuche kwa amani. 

Nyange na mkewe walibeba kitanda kidogo cha Brayan, na kukiweka kwenye chumba chao, Sam na Josh walilala chumba chao. Wote walienda kulala baada ya kula chakula cha usiku pamoja, kasoro Sam na Sonia walikaa nje wakiongea. 

“Zawadi ya Sonia kwa Sam.”

“Nimekununulia zawadi Sam.” “Zawadi ya nini?” “Kukushukuru kwa kunisaidia, katika kila kitu. Sio shule peke yake. Kila kitu.” Machozi yalianza kumtoka Sonia. “Sina jinsi yakueleza shukurani zangu kwako. Lakini ujue nakushukuru sana. Umekuwa kama baba kwangu na kwa Kana pia. Umetufanya mimi na Kana tusione pengo la baba maishani mwetu. Asante sana.” Akafungua mkono wake ulikuwa na kijimfuko kidogo cha Sonara. 

Akatoa cheni ndogo ya dhahabu ya kiume. Sam alibaki ameduwaa. Sonia alivuta mkono wa Sam nakuiweka kiganjani kwake. “Asante Sonia.” Sam akabaki akiiangalia. “Umeipenda? Sikuwa na hela nyingi, ningeifanya kubwa kidogo na nzito lakini hela haikutoshea.” Taratibu Sam alipitisha mkono wake kwenye shingo ya Sonia, nyuma ya kichwa chake, nakumuangalia kwa muda. 

“Hii inatosha Sonia. Asante sana.” Akamsogeza karibu na kuanza kumbusu midomoni mwake. Ilikuwa ni kwa mara ya kwanza Sonia kupata busu kutoka kwa Sam, alifurahi sana. Machozi ya furaha yaliendelea kumtoka wakati bado Sam akimbusu. 

“Nakupenda Sonia.” Sonia aliinama na kuficha uso wake kwenye miguu ya Sam. Sam alianza kuchezea nywele za Sonia taratibu sana. “Nakupenda sana Sonia.” Akarudia. Sonia alinyanyua uso wake huku machozi yakiwa yamejaa usoni mwake. “Utanioa Sam?” Sonia aliuliza kwa unyonge sana. Sam alitabasamu na kumvuta tena Sonia na kuanza kumbusu tena. Kisha akamwachia na kumwambia. “Nakupenda sana Sonia. Ukinikubali. Nitakuoa.” Sonia akatabasamu huku akifuta machozi. 

Sam aliweza kuyaona macho ya Sonia maangavu yalivyo jaa furaha pale gizani walipokuwa wamekaa karibu kabisa, ya sehemu ya kuogelea. Huku mwanga wa mbalamwezi ukiwamulika na kuwawezesha kuonana vizuri. “Nitafurahi ukinioa mimi, Sam.” “Nitakuoa Sonia.” Sonia alianza kucheka huku akirusha miguu yake kwenye maji. 

“Nimefurahi sana. Nilikuwa nikimwambia mama, nakupenda.” “Sasa kwa nini hukuniambia mimi mwenyewe?” Sonia alitulia kidogo huku akiendelea kuchezea maji kwa miguu. “Nilikuwa naogopa, sikujua kama utanipokea kama mpenzi wako.” Sam akakunja uso kama ambaye hajaelewa. 

Akaona amuulize. “Kwa nini ulifikiri hivyo!?” “Sababu ya Kana. Nilijua kwa sababu nimeshazaa, au niseme kwa kuwa nina mtoto ndio kipingamizi changu kikubwa kitakachonifanya nisipendwe au nisiolewe.” Sam alicheka na kufikiria kidogo. “Kana hawezi kuzuia chochote. Nakupenda wewe na nina kuahidi kumtunza Kana kama mtoto wangu.” Sonia hakuamini. 

“Asante sana.” “Lakini nataka usome kwanza Sonia. Nimeulizia chuo cha mambo ya biashara, kwa kuwa unapenda mahesabu najua utakimudu. Nataka usiende kidato cha tano na sita badala yake usome diploma miaka miwili halafu baada ya hapo, ujiunge na advance diploma mwaka mmoja. Ndio ufanye post graduate huku unafanya mitihani ya bodi. Unafikiri utaweza?” 

“Kwa kuwa tutakuwa wote. Najua nitaweza. Lakini nina wasiwasi na ada!” “Nimeshauliza, sio kubwa sana. Naona tutamudu.” “Asante sana Sam. Nakushukuru kwa kunisaidia kutimiza ndoto zangu. Asante.” Usiku huo hapakuwa na maongezi mengi zaidi ya kupeana mabusu mfululizo bila kuchoka. Hakuna aliyetamani kwenda kulala. Kila mmoja alimfurahia mwenzake. 

 **********************

              “Kwani nyinyi,   jana mlilala saa ngapi?” “Umeanza Nyange. Waache bwana!” “Sawa. Lakini mimi nauliza kwa uzuri tu.” “Huna uzuri wowote ule unaoulizia.” “Sawa Sam. Maana naona chai pia imemshinda Sonia. Leo nilitaka tukachezee maji, lakini simuoni mwendaji hapo.” “Mbona sisi tuko sawa tu.” “Muone mwenzio anavyosinzia.” “Hayo ndio macho yake bwana!” Sam alijibu, nakumfanya Nyange acheke sana. Alicheka na kucheka mpaka kila mtu akaanza kucheka.

                    “Bwana Sam mimi sikuwezi! Kumbe Sonia ana macho ya kurembua!? Hebu niangalie vizuri Sonia.” “Usimwangalie Sonia.” Sam akadakia, Sonia akabaki ameinama akicheka kwa aibu. “Mwache mtoto bwana Nyange, ni nini?” Mama Briana alidakia. “Basi bwana! Ngoja ninyamaze.” Nyange alitulia kidogo akaanza tena. 

                    “Soniaaa!” “Wewe si umesema unanyamaza? Unachoimba jina la mtoto wa watu nini?” “Bwana huyu mtoto sijui kalishwa nini na Sam bwana! Anavyomtii! Ujue hapo hataniangalia mpaka Sam amwambie aniangalie! Kweli kila mtu na mtuye. Basi bwana! Ngoja na mimi nirudi kwa Briana kipenzi changu.”

                     “Lakini Sonia ujue nimekukabidhi mwanangu huyo, akiharibikiwa nina wewe. Nataka atulie kama wewe hivyohivyo.” “Sio kama mimi mama yake?” “Mmh! Akiwa kama wewe nitachanganyikiwa bure, itabidi waje waishi palepale ndani na mumewe ili niwe napambana na mumewe mimi mwenyewe. Maana wewe umezidi mama Briana. Moyo wako huo! Kaa nao tu mwenyewe, usimwambukize mwanangu.”

                    “Kwanza Sonia mwenyewe ni hivyo tu sina jinsi naona kama mnafanana fanana vile! Ushamuambukiza mtoto wa watu, maana na yeye kutwa mgongoni kwako.” “Niache na Sonia wangu.” “Mimi tena? Sisemi lakini umesikia Sonia? Briana huyo!” “Nimesikia shemeji, nitaendelea kumwangalia.” Kila mtu alikuwa na wakati mzuri. 

“Zawadi ya Sonia kutoka kwa familia ya Nyange.”

Vilikuwa vimetawala vicheko kati yao wakati wote walipokuwa Bagamoyo, kweli walikuwa na wakati mzuri sana wapamoja. Siku inayofuata jioni wakati wamekusanyika tena kwa ajili ya chakula cha jioni, Nyange alimuomba mkewe aseme kitu. 

“Tunakupongeza Sonia kwa kufaulu. Sam amesema umekubali kwenda chuoni. Sasa na sisi kama familia kwa kutaka kukuonyesha tunatambua juhudi zako tumekuandalia pesa hii, itakusaidia katika mambo yako ya chuoni. Yaani ada, vitabu na mambo mengine mengi.” Mama Sonia, Sam na Sonia walishangaa sana baada ya mama Briana kutoa hundi iliyonona.

Zilikuwa pesa nyingi sana kwao. Sonia na Mama yake walibaki wakitokwa na machozi ya furaha na sintoamini. Mama Sonia alipiga magoti kabisa. “Asanteni sana. Mungu awazidishie.” “Usifanye hivyo mama Sonia bwana! Sisi ni ndugu. Naomba usimame.” “Dada na Baba Briana asanteni sana. Sijui niseme nini. Nawashukuru sana.”“Daah! Mimi mwenyewe sikutegemea!” Sam aliongeza. “Asante kaka.” Sam akasimama kabisa kumshika mkono Nyange. “Asante sana shem.”  Sam akamshukuru na mama Briana pia, kwa kumshika mkono. 

“Sam Amua Kulinda Penzi Lake Kwa Sonia.”

Wote wakiwa kwenye hali ya furaha iliyo changanyikana na kutotegemea kwa pesa kubwa vile, Sam akaanza. “Nimekaa, nikafikiria kumtoa Sonia pale ndani kumpeleka chuoni hivihivi, nikaona nitachanganyikiwa bure.” Nyange alianza kucheka kwa sauti ya juu mpaka watu wengine waliwageukia. 

“Sammmm! Sema mdogo wangu. Na hapo umeshikwa pabaya! Maana huwezi tena kumfungia na kumfundisha mwenyewe, lazima akaonane na wanaume wengine. Na huko nje, sio utani. Sikuogopeshi Sonia, lakini watu ni waongo sana. Wanahonga mpaka magari, ilimradi tu wakuweke kitandani. Shauri yako, kuwa makini.” “Nitatulia.” Sonia akajibu.

“Kweli mdogo wangu, jikaze tu. Na uzuri huo, watakung’ang’ania kweli! Akili zako zote ziweke kwenye masomo.” “Na mimi bwana! Mbona hivyo shemeji?” Mama Briana alianza kucheka. “Ataziweka kwako kwa mdomo tu? Changamka.” Mama Bree, akaongeza. “Wewe unamuona Sam kwa wasiwasi nini? Subiri uone jeuri yake. Unafikiri tumekuja huku bure? Kuna jambo.” Mama Briana, Josh na Sonia walibaki hawaelewi lakini mama Sonia alibaki kucheka. “Kuna nini?” Mama Briana aliuliza.

Sam akatoa kimkoba nakukifungua. “Nataka nikuchumbie Sonia. Nataka kukuvalisha hii pete. Kila anayeiona ajue wewe ni wangu.” Sonia hakutegemea kabisa. Yaani kama ni surprise, Sam alipatia. Mrembo alificha uso wake huku akitokwa na machozi. 

“Nakupenda sana, najua utakuwa mwanamke utakayenifaa maishani. Utakapo maliza tu chuo, tutafunga ndoa.” Mpaka mama Briana mwenye hisia za karibu, alitokwa na machozi.

Sam alisogea pembeni ya kiti cha Sonia na kuutoa mkono wake wa kushoto usoni na kumvalisha pete. Ilikuwa nzuri sana. Sonia bado alikuwa akilia. “Mama Briana bwana! Kwani hujamfundisha Sonia kukumbatia? Maana hapo tena alitakiwa asimame amkumbatie Sam halafu…, sema mama yupo. Lakini hata kukumbatia tu jamani!” “Mwache bwana mtoto bado yupo kwenye mshtuko.” “Basi Sam chukua pete yako mpaka mshituko wake utakapo muisha.” Sonia akarudisha mikono yake nyuma kama kuficha ile pete. Wote walianza kucheka. 

“Kumbe mume umempenda! Hongereni sana wadogo zangu. Mungu awasaidie mtu asiwatenganishe. Sonia umepata mwanaume mzuri sana, usiwahi kurubuniwa na mtu yeyote. Utulie.”

“Naweza kusemea upande wa Sam kwa kuwa nimekaa naye muda mrefu namfahamu. Ujitunze sana. Umesikia Sonia?” Nyange alizungumza kwa kumaanisha si utani tena. “Nimesikia shemeji. Nitatulia. Nampenda Sam.” Kila mtu alicheka tena. “Na mimi nakupenda Sonia.” “Mnachosha kuangalia nyinyi! Kumbatianeni basi hata kidogo!” “Waache Nyange bwana!” Sonia alibaki ameinama. 

 Kuna Ndoto Huchelewa, Lakini Wema Na Mkono Wa Mungu Hufuatiliza Mpaka Kutimiza Kusudi

Sonia alianza chuo, madarasa ya asubuhi kama kawaida. Alitoka na Sam anapokuwa akienda kazini na wakati mwingine wa mchana walikula pamoja. Mapenzi yao yalikuwa na kumea sana. Hakuna aliyemjua Sonia asimfahamu Sam. Kila aliyemsogelea Sonia, alitambulishwa Sam. Sonia hakuwahi kuona mwanaume kama Sam. Akili na mawazo yake yote yalikuwa kwa mchumba wake. 

Sam na Nyange walijaribu kumtega Sonia katika mambo mengi lakini walishindwa. Kwani Sonia alikuwa na msimamo uliokuwa ukimshangaza kila mtu. Hakurubuniwa na vitu wala mtu. Mawazo yake yalikuwa kwa Sam na shule yake tu. Alizidi kupendeza kwa mavazi mazuri na ya thamani aliyokuwa akinunuliwa na Sam. 

 **********************

Mzee Nyange aliomba Brayan apelekwe kijijini kuna jambo la muhimu sana anataka kufanya. Kama kawaida yao yakuongozana kila mahali, Nyange akachukua familia yake yote mpaka kijijini. Walikuta kuna shamrashamra. Ilibidi baba Briana aulize kulikoni, ndipo mzee Nyange alipomwambia siku inayofuata, siku ya jumapili ndipo anapomuweka wakfu mrithi wake. 

Mzee Nyange alikuwa Mzee aliyeshika dini sana, tofauti na aba Briana mwanae, na familia yake, waliokuwa hata hawaendi kanisani. Alichinja ng’ombe na kuita ndugu zake kutoka sehemu mbali mbali. 

Siku ya jumapili ndugu wote waliombwa na mzee Nyange wamsindikize kanisani, kwanza akatoe  sadaka ya shukurani kwa Mungu kwa kuona kizazi chake cha pili na kumkabithi mrithi wake wa ukoo mbele za Mungu. Alisimama mbele ya kanisa akiwa amembeba Brayan yeye mwenyewe, na Mchungaji alimuombea Brayan baada ya mzee Nyange kutoa sadaka yake ya shukurani madhabahuni akisindikizwa na mkewe na watoto wake wote na wenza wao. 

“Mzee mkorofi huyu! Sasa kinachomshinda kunirithisha mimi mtoto wake wa pekee wakiume ni nini, mpaka afanye fujo zote hizi kwa mtoto asiye ongea?” Nyange alimnong’oneza mkewe wakiwa kanisani. “Acha wivu D. Na uache kuongea kanisani. Akikuona, atakufukuza humu ndani.” Baba Briana akaanza kucheka. “Wala hujakosea. Atanikimbiza na bakora yake mgongoni.” 

Baada ya maombezi kwa Brayan, mzee Nyange alitoa neno. “Sasa hivi hata Mungu akiniita sina shida ya kwenda, najua nimeacha mji wangu kwenye mikono salama. Kwa heshima na upendo aliotuonyesha Peninah mwanangu, nimekuwa nikimuombea sana. Zaidi nilikuwa nikimuomba Mungu anipe mrithi kutoka kwake kwa kuwa najua atakuwa amebeba moyo wa mama yake na hata kama akianza kupotea mama yake atamrudisha kwenye mstari sahihi.” “Na sio baba yake?!” Nyange akashangaa sana. 

Akaendelea kulalamika. “Hivi umemuona huyu Mzee anavyonitukana mbele za watu!?” “Nyamaza D, jamani! Atakusikia alafu uniponze mwenzio.” “Anavyokupenda huyo! Makosa yote yatakuwa yangu.” “Bwana nyamaza.” Mama Sonia alikuwa haelewi heshima alizokuwa akipewa mama Briana ukweni kwao! Ilikuwa nzito na ya kushangaza. 

 **********************

Diploma yake ya miaka miwili iliisha vizuri. Sonia akiwa amefaulu vizuri. Sam alimtaka aunganishe Advance diploma ndipo waowane. “Kote huko Sam jamani? Bado utanisubiri tu? Sitaki kukuchosha, halafu ukabadili mawazo ukaoa mwanamke mwingine bwana. Tuone tu, nakuahidi nitaendelea kusoma.” Sam akacheka. 

“Nitakusubiri Sonia. Ni mwaka mmoja tu mpenzi wangu. Tuvumilie. Nataka umalize shule utulie nyumbani, sio hizi pilikapilika za shule, asubuhi mpaka jioni. Hata hivyo ndio nyumba yetu itakuwa imeisha. Tukiona tunahamia kwetu.” Bila kupinga Sonia akarudi shule bila kupumzika. 

Mama yake Sonia alifurahi sana. Alimshukuru sana Sam kumtia moyo Sonia. “Asante Sam kwa kutimiza ndoto zangu na Sonia. Nilishahangaika na huyu mtoto asome, karibu ya kuchanganikiwa. Sikujua kama anaweza kuja kurudi shuleni tena!” “Sonia mwenyewe anatia moyo mama. Anajitahidi sana shuleni, halafu ametulia.” Mama Briana na Nyange waliendelea kusaidia kulipia ada ya Sonia, kwa hiyo Sam hakuwa na mzigo mkubwa sana kifedha ila muda. 

Nguvu na akili zake zilihamia kwenye ujenzi. Hakutaka kumtoa Sonia na Kana kwenye Jumba la Nyange na kuwahamishia kwenye nyumba ya ajabu. Alianza kuhangaika sana kuzisaka pesa kwa kadiri ya uwezo wake. Hakuwahi hata kufikiria mwanamke mwingine, isipokuwa Sonia. 

 Uhalisia Wa Maisha

Ratiba ya Sonia haikubadilia sana, ilikuwa kama ile ya zamani alipokuwa akisoma Diploma, akimaliza madarasa yake mapema, alikuwa akienda maktaba kubwa ya mkoa na kujisomea wakati akimsubiria Sam atoke kazini.  Ratiba ya Sam ilinza kubana. 

Alipandishwa cheo kazini na kuchukua nafasi ya Mr Mponza. Lakini yeye ilikuwa tofauti, Sam alikuwa kiongozi na mtendaji. Hakutaka jambo lolote liharibike mikononi mwake. Alijulikana na kila kiongozi pale kwenye hiyo benki na matawini. 

Muda mwingi aliutumia ofisini akiwasiliana na matawini kuhakikisha mifumo yote ya kwenye kompyuta inaenda sawa na ikitokea kuna tatizo na watu wa chini yake wameshindwa kutengeneza kwa wakati, Sam alikuwa akienda yeye mwenyewe kuhakikisha mambo yanaenda sawa tena bila kuchelewesha. 

Vikao vya hapa na pale vya asubuhi na jioni vilizidi kumchukulia Sam muda mwingi sana na kumfanya Sonia kukaa muda mrefu akimsubiri atoke ili warudi wote nyumbani. 

Taratibu mambo yalianza kubadilika kati yao. Sam alikuwa akichoka sana na karibu muda wote anapokua kazini alikuwa na mambo mengi ya kufanya na yote alitakiwa akamilishe kabla siku inayofuata. 

Zile jumbe za mapenzi zilianza kupungua kwa Sonia, na yale maisha ya kula chakula cha mchana pamoja yaliisha kabisa. Sam alizidi kuwa busy kupita kawaida. 

Anapotoka tu kazini ilimbidi kuanza kupiga simu huku na kule kufuatilia biashara zake. Alianza kuingiza pesa kila upande lakini alikuwa akichoka sana. 

Wakati mwingine anapokuwa anamfuata Sonia maktaba ili warudi nyumbani anakuwa anaongea na simu mpaka nyumbani, na wakifika nyumbani alikuwa akibaki kwenye gari kwa muda kumalizia maongezi na watu wanaomfanyia biashara, kuhakikisha haibiwi na pesa zake zote za mauzo zinaingizwa benki kila siku bila kukosa, lakini alijitahidi kula na Sonia chakula cha usiku. 

Taratibu walianza kukosa muda wa pamoja. Hata ule muda ambao Sonia aliokuwa akiupenda wa usiku kukaa kwenye ngazi na Sam, ulianza kuisha taratibu, kwani Sam alikuwa akichoka sana. 

Wakati mwingine alishindwa hata kula alikuwa akifika tu nyumbani, basi anakimbilia kulala. Na kwa kuwa alijua huo ndio mwaka wa mwisho wa shule ya Sonia, alikazana kujenga nyumba yao harakaharaka. 

Kwa hiyo hata siku za weekend zote alizitumia site kwenye nyumba wanayojenga na ikimlazimu sana alienda kazini au alifanya yote kwa pamoja. Alikwenda kazini kidogo halafu anahamia kwenye nyumba yao kuhakikisha ujenzi hausimami na hakuna kinachokosewa kwenye hiyo nyumba yao. 

Safari za Mwanza nazo ziliingilia kati. Wakati mwingine ilimlazimu Sam kwenda Mwanza kufuatilia mzigo wa dagaa. Wakati Nyange, mama Briana na mama yake Sonia wakiwapongeza kwa mafanikio makubwa waliyokuwa nayo, Sonia alikuwa na upweke mkubwa sana moyoni.

 Alijitahidi kuvumilia, na kuto kumuonyesha mtu yeyote yanayoendelea kati yao, kwani bado walitoka pamoja asubuhi nakurudi jioni pamoja kama zamani, lakini hapakuwa na aina yeyote ya mahusiano kati yao. 

Yale mapenzi aliyokuwa akiyapata kutoka kwa Sam yaligeuka yakawa pesa. Sam alikuwa akimpa pesa nyingi sana Sonia, lakini sio muda wake. Huku akikumbuka matusi na kejeli za Leah na Mr. Mponza wakimwita maskini, hana hela yakumtunza Sonia mjini, Sam alizidi kuhangaika kutafuta pesa kila alipoweza kumridhisha Sonia. 

 **********************

‘Ninahamu na wewe Sam!’ Sonia alituma ujumbe, ule muda wa mchana alipokuwa amekaa mwenyewe mezani akila baada yakutoka darasani. Alisubiria majibu kutoka kwa Sam mpaka muda wakuingia kwenye kipindi kingine ulipofika. 

Kwa kuwa ratiba yake ilikuwa ni ileile, akitoka chuoni anaelekea maktaba kusoma, wakati anamsubiri Sam.  Alipotoka darasani alianza kutembea taratibu kuelekea maktaba huku ameshika simu yake mkononi akisubiria majibu kutoka kwa Sam. 

Siku hiyo hakusoma kitu chochote, alikaa akiwaza maisha yalivyowabadilikiampaka muda wakufunga maktaba ulipofika. Alitoka nje kumsubiria Sam mpaka giza lilipoingia. 

Alimsogelea mtu mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Bob. “Nimekuona umekaa hapa muda mrefu sana. Unamsubiri mtu?” “Namsubiri Sam, ni mchumba wangu.” Sonia aliongea kwa ujasiri huku akiangalia pete yake. 

“Oooh! Safi sana. Lakini hapo ulipokaa sio salama sana hasa giza likishaingia. Ungesogea upande ule mwengine. Au hata uingie hapo mgahawani upate juisi wakati unasubiri. Maana naona na mvua inataka kunyesha” “Atakuwa yupo kwenye kikao ndio maana amechelewa, lakini atakuja muda sio mrefu. Nitakuwa sawa tu kaka yangu. Asante.”  Bob akatoa tabasamu na kumjibu, “Karibu.”   Kisha akaondoka. 

Baada ya muda manyunyu yalianza, ndipo wazo lakukimbilia kwenye mgahawani lilipomjia Sonia. Alipoingia tu akakutana na Bob. “Pole, naona manyunyu yamekupata.” Sonia alitabasamu huku akijifuta. Kila mtu alikuwa akimwangalia. Kidogo alibabaika pakukaa. 

“Karibu kiti.” Bob alisimama huku akimuonyeshea kiti cha upande wa pili ya meza aliyokuwa amekaa yeye. “Asante.” Alipokaa tu muhudumu alisogea. “Utakunywa nini?” “Asante. Sitakunya kitu chochote.” Bob akatabasamu. 

“Sasa unacheka nini?” Sonia akamuuliza. “Unaonekana jamaa anakufungia kweli! Umenikalia kiwoga woga!” “Hapana bwana. Sam hayuko hivyo.” “Natamani ujione ulivyokalia hicho kitu. Kama kina moto vile!” Sonia alivuta pumzi nakujivuta vizuri kwenye kiti, ni kweli alikuwa amekalia nusu kiti. 

 **********************

Sonia aliangaza macho kwenye huo mgahawa. Palikuwa pazuri sana, pakubwa na palionekana ni pagarama. Bob alikuwa ametulia tu akiendelea kumwangalia huku akinywa juisi yake taratibu. Sonia alitoa simu yake nakuendelea kuangalia kama Sam atampigia simu au alirudisha majibu ya ujumbe wake. 

Alikaa hapo zaidi ya saa moja, bila kumsemesha chochote Bob na Bob naye alikuwa kimya kabisa akimtizama tu. Haikuhitaji kuambiwa Sonia yupo kwenye hali gani, wazi alionekana mwingi wa mawazo na mnyonge. Hakuwa hata na habari na alipo au nani yupo mbele yake, mawazo yake yalizama kwenye simu yake tu. 

Baada ya muda wakutosha kupita, hatimaye Sam akapiga. “Pole na kazi, Sam.” “Uko wapi? Samahani sana, Nilikuwa kwenye vikao tokea asubuhi, na vimemevuta kweli hivi ndio tunatoka na simu niliiacha ofisini ipate chaji. Pole sana.” “Usijali nipo sawa tu.” “Uko wapi na mvua hii?” “Nipo hapa kwenye huu mgahawa karibu na maktaba. Ukifika hapo maktaba unipigie nitatoka.” “Basi ninakuja.” Uso wa Sonia ulifunguka kabisa kwa furaha baada ya kusikia sauti ya Sam. 

“Anakuja, yupo njiani.” Sonia alimwambia Bob ambaye hakuwa hata amemuongelesha kwa zaidi ya lisaa, Bob akatabasamu tu, kama kawaida yake. 

**********************

Sam alipiga simu kumtaarifu Sonia kuwa amefika. Kwa furaha Sonia hakujali mvua. Alijitosa kwenye maji mpaka alipofika kwenye gari. “Pole sana Sonia wangu. Nachukia kukutesa hivi!” “Labda niwe nachukua tu daladala kurudi nyumbani.” “Hapana Sonia. Nitajitahidi kuwahi. Nitawaomba wenzangu tubadilishe muda wa vikao.” “Ulipata ujumbe wangu?” Kabla Sam kujibu simu yake ilianza kuita. “G huyoo.” Na kupokea hapohapo.

“Haloo?” Sam aliongea na G kwa muda mrefu sana mpaka Sonia alipopitiwa na usingizi kwenye gari tena akiwa amelowa sana. Walifika nyumbani, Sonia alishuka lakini Sam bado alikuwa akicheka na G ndani ya gari. 

**********************

Sonia alipita moja kwa moja chumbani, akaoga na kujitupa kitandani. ‘Sam amebadilika sana. Anaona ni heri kuongea na G kuliko mimi!? Siku hizi anapuuza kila ujumbe ninao mtumia na wala haonyeshi kujali tena.’ Sonia aliendelea kuwaza huku akitokwa na machozi. “We Sonia? Mbona unalala bila kula?” “Nimechoka mama. Nitakula kesho.” “Masomo hayo na tumbo tupu! Utaweza mwanangu?” “Nimenyeshewa sana na mvua mama. Najisikia baridi sana. Nataka nisitoke hapa kwenye haya mashuka angalau nipate joto. Usiwe na wasiwasi nitakuwa sawa tu.” 

**********************

Ratiba za Sam hazikuweza kubadilika hata kidogo. Bado Sonia alikuwa akikaa akimsubiri kwa muda mrefu sana na bado alikuwa na uchungu wa kutokujibiwa ujumbe wake. Siku zilikwenda bila Sam kupata muda na Sonia kabisa. 

Siku hiyo Sonia alitoka chuoni na kuelekea maktaba akiwa anaumwa sana na tumbo. Alimtumia ujumbe Sam, kumuomba awahi amrudishe nyumbani, kwani tumbo linamuuma sana. Sam alijibu ‘Pole mpenzi wangu. Umekunywa dawa?’ ‘Nipo maktaba Sam. Dawa napata wapi?’ Ule ujumbe haukujibiwa. 

Sonia alikaa akisubiri ajibiwe mpaka ulipofika muda wa kufunga maktaba. Ilimbidi atoke nje kusubiri mpaka giza lilipoingia bila Sam kutokea wala kupiga simu. 

Ndipo alipoamua kuingia tena kwenye ule mgahawa, kwani tumbo lilikuwa likimkata sana na alihitaji kutumia choo. Alitembea kwa shida mpaka ndani, akaulizia choo na kuingia moja kwa moja chooni. Alikuwa kwenye siku zake kwa hiyo alikuwa amechafuka. Akajisafisha na kutoka.

Alirudi nakukaa kwenye meza mojawapo huku ameegemeza kichwa chake mezani. 

“Vipi?” Sonia alinyanyua kichwa kuangalia anayemsemesha. “Habari Bob?” “Nzuri, lakini unaonekana mgonjwa!” “Tumbo linaniuma sana tokea mchana.” “Ungependa nikurudishe nyumbani?” “Nitashukuru, Bob.” Walipotoka tu nje ya mlango, Sonia alianza kutapika sana. 

Bob alimsaidia kumpandisha kwenye gari akiwa amechafuka sana, akamrudisha nyumbani. Akiwa vilevile amechafuka huku akilia, Bob alimshika na kumsaidia kuingia ndani. 

**********************

“Vipi?” Kila mtu alisimama wakati Sonia anaingizwa na Bob. Alikuwa akiugulia maumivu makali sana ya tumbo. “Anaumwa. Alikuwa anatapika sana. Ndio nimemleta.” “Sam yuko wapi?” Mama Briana akauliza. “Sijui dada yangu. Naomba mimi nitoke, naamini Sonia atapona.” “Asante.” Mama Briana akamsaidia Sonia mpaka chumbani. Alikuwa akilia sana.

Akamsaidia kuoga, alipoona ametulia kitandani, mama Bree alizima taa na kutoka chumbani. 

Alipiga simu ya Sam bila majibu. Mama Briana alichukia sana. Baada ya muda mrefu kupita Sam alimpigia simu mama Briana. “Sonia yupo nyumbani? Simpati kwa simu yake.” “Yupo.” Mama Briana alikata simu. Sam aliingia akiwa amechoka sana. 

“Naomba uje ukae hapa Sam.” Sam na Nyange hawakuwahi kumuona mama Briana akiwa amekasirika hivyo. “Wewe ulijua kama Sonia anaumwa?” “Aliniambia mchana.” “Ulimpigia simu kumjulia hali yake?” “Nilikuwa nimebanwa na kazi, shem. Na simu ikaishiwa chaji kabisa.” Mama Briana akanyanyuka nakuondoka. 

“Inakuaje Sam?!” Nyange akauliza akionyesha amekasirika usoni. “Kweli mtu anakwambia anaumwa, halafu unashindwa kupiga simu ndugu yangu?! Ameletwa na jamaa hapa yuko hoi! Huyo jamaa anasema amemkuta analia sana, tumbo linamuuma, tena anatapika. Ameletwa amechafuka hatizamiki.” “Daah!” Sam akanyongea.

“Vipi Sam?!” “Kaka mambo yamekuwa mengi kweli.” “Kuna mambo yakuchezea mdogo wangu lakini sio haya. Pesa hiyo unayokimbizana nayo, itakubadilikia itakuwa chungu kuliko shubiri. Si unamuona huyu binti kama sio wa muhimu? Atakuja kushikiliwa na mwanaume anayejua kujali, hutakaa upone hayo maumivu yake.”

“Mungu amekutoa kwenye mikono ya Leah, amekupa Sonia kukufariji, badala uenzi ulichonacho mkononi, unaanza kuhangaikia usiyoyajua! Utakuja kulizwa mjini hapa na hela zako, wewe endelea hivyohivyo.” Nyange naye akanyanyuka nakuondoka. 

 **********************

Sam alikuwa amebanwa kazini akishugulikia tatizo la tawi la Kibaha siku nzima kwenye simu bila mafanikio. Aliambiwa na uongozi wote ni lazima asubuhi yake aanzie kazi tawini huko, kwani kazi zilikuwa zimesimama siku mbili na ndio ulikuwa msimu wakulipa mishahara ya wafanyakazi wa serikali, kwa hiyo tawi lilikuwa limefurika wafanyakazi wakisubiria pesa zao.”

“Simu za malalamiko kutoka tawini hapo kwa uongozi wa benki hiyo hazikuisha. Kwa hiyo ilimlazimu Sam ndio aende siku inayofuata kwani wafanyakazi walio kuwepo chini yake walishindwa. Sam ndio alikuwa akiaminiwa sana kwenye benki hiyo. Hakuna kazi aliyoshika yeye isikamilike.”

Kwa hiyo macho na masikio yote ya uongozi wa benki hiyo, yalikuwa kwa Sam kwenda kuokoa jahazi. Kwani wateja wao wengi walitishia kuhamisha akaunti zao kwenye benki nyingine. Uongozi usingeruhusu hilo litokee kwani mishahara iliyokuwa ikipitia kwenye tawi hilo ndio iliyokuwa ikiingizia tawi faida kubwa. 

 **********************

Alikaa pale akiwaza jinsi ya kufanya bila jibu. Alienda kugonga chumbani kwa Sonia, lakini mama yake alimwambia Sonia amelala. Alikwenda kulala akiwa na mawazo na hofu yakumpoteza Sonia. ‘Nitachanganyikiwa Sonia akiniacha.’ Sam aliendelea kuwaza usiku huo. 

**********************

Aliamka asubuhi na mapema, akarudi tena kumgongea Sonia. Lakini alitoka mama yake akamwambia Sonia ndio anapitiwa na usingizi, kwani alikesha akitapika. “Daah! Poleni sana mama. Nakimbilia mara moja kazini, kuna kazi natakiwa kuifanya. Lakini kwenye saa nne, nitakuwa nimesharudi. Najua Sonia atakuwa hajaamka.” “Sawa, kazi njema.” Akaondoka.

Lakini hali ya Sonia ilizidi kuwa mbaya, aliendelea kutapika, huku akilia tumbo linamuuma sana. Mama Briana akaamua kumpeleka hospitali. Alichomwa sindano ya kuzuia kutapika na kuwekewa maji kwa kuwa alikuwa amekosa nguvu. Alilala pale hospitalini mpaka jioni, ndipo aliporuhusiwa kurudi nyumbani. Hakuna aliyesikia simu wala ujumbe kutoka kwa Sam. Sonia aliingia kuoga baada ya kula, akalala. 

**********************

Sam alirudi nyumbani akiwa amechoka sana. Mama Briana na Nyange walishaenda kulala. Sam aligonga tena chumbani kwa kina Sonia, mama yake akatoka. 

“Shikamoo mama.” “Marahaba. Pole na kazi.” “Asante. Naweza kuongea na Sonia?” “Ndio amerudishwa kutoka hospitali, amelala.” “Hospitali?!” “Si nilikwambia usiku hakulala? Sasa hali ilizidi kuwa mbaya, mama Briana alibidi amkimbize hospitalini. Alikuwa ameishiwa nguvu kabisa, wamemuwekea maji na kumchoma sindano za kuzuia kutapika, naona hizo ndizo zinazomfanya kama mlevi. Amelala.” Sam alitamani kukaa chini. 

“Daah! Poleni sana mama. Niliondoka na simu ilikuwa imeishiwa chaji kabisa, nilisahau kuchaji jana usiku wakati naenda kulala. Nimefika tu kazini nataka kupiga imezima, na chaji yake nikawa nimeiacha hapa nyumbani. Mitambo yenyewe nilijua ingefaa mapema, ndio imekubali usiku huu na simu za pale hazitoki simu za mkononi.” “Pole.” Sam aliondoka akijilaumu sana. 

‘Mama Briana na mumewe hawatanielewa kabisa!’ Sam alizidi kuwaza. ‘Najua Sonia ananielewa, lakini mama yake je?’ Sam alikesha akiandaa ripoti aliyotakiwa kuisoma asubuhi yake kwenye kikao cha viongozi wote kabla yakuanza kazi. Alilala saa saba akiwa amechoka sana. 

Aliamka saa moja na nusu asubuhi na alitakiwa kwenye kikao saa mbili kamili kuwakilisha ripoti hiyo. Simu za kuuliziwa alipofikia na ripoti yake, zilianza asubuhi hiyo. “Si unajua na CEO atakuwepo? Kwa hiyo usituangushe tafadhali.” Sam alivaa harakaharaka akakimbilia kazini. Mara baada ya kikao kuisha alirudi nyumbani haraka sana. 

**********************

Alimkuta Sonia na ama Briana wakinywa chai. “Vipi Sonia?” “Safi tu.” Sonia alijibu huku akiangalia chini. “Unajisikiaje sasa hivi?” “Tumbo limetulia kabisa, na sijatapika tena.” “Daah! Afadhali.” Kulitokea ukimya kidogo. 

“Dada? Asante kwa chai, mi naomba nikapumzike kidogo.” “Haya.” Sonia akaondoka. Simu ya Sam ikaanza kuita mfululizo. Mama Briana naye akanyanyuka nakuondoka. Sam alikuwa akitafutwa kazini. 

Ni kweli Sam alipandishwa cheo na alikuwa akilipwa pesa nyingi sana, lakini alihitajika sana kazini. Alijikuta hata yeye mwenyewe anakosa furaha. Ilimbidi tu kuondoka na kurudi kazini. 

Sonia naye alilala mpaka mchana, akaogo na kuamua kurudi chuoni. “Si ungepumzika tu leo, halafu ukaenda huko chuoni kesho?” Mama Briana alimuwahi Sonia kabla yakutoka. “Nimebakiza week chache zakumalizia hii shule dada. Acha nijikaze niende tu.” “Haya. Usiache kupiga simu lolote likitokea.” “Asante dada.”

**********************

Kwa mara ya kwanza Sonia alichukua daladala mpaka chuoni. Japokuwa alikosa vipindi vya asubuhi, lakini alijitahidi kuomba madaftari kwa waliokuwepo. Alipotoka alienda maktaba kujisomea kama kawaida yake. Alipoona muda wakufungwa maktaba umefika, aliamua kwenda kumtafuta Bob. 

Alimkuta Bob amekaa palepale mgahawani tena peke yake. “Vipi Sonia?” “Safi tu.” “Nimeona tabasamu. Bila shaka umepona.” “Najisikia vizuri.” Sonia alivuta kiti kwenye meza aliyokuwa amekaa Bob, na kukaa upande wa pili wakitizamana. 

“Vipi?” “Sitakaa sana leo, nimekuja kukushukuru. Asante kwa msaada wako.” Bob akatabasamu akimwangalia. “Karibu.” “Basi uwe na usiku mzuri.” “Mbona leo mapema? Jamaa yupo nje nini?” Uso wa Sonia ukabadilika gafla. 

“Hapana, leo sitamsubiri. Nitachukua tu daladala au taksii hapo nje.” Bob akamwangalia Sonia kwa muda bila ya kusema kitu. Sonia alibaki ameinamisha kichwa kwa muda kama anayetafakari kitu, kisha akanyanyuka nakutoka nje. 

“Naomba kabla hujaondoka ule kitu kidogo, Sonia.” Bob alimkimbilia nje. Sonia akageuka, lakini uso wake ulikuwa umejaa machozi mengi sana. “Na mimi natoka hapa muda sio mrefu. Naomba tule kwanza halafu nitakusogeza mpaka nyumbani kwenu.” Sonia alifuta machozi na kukaa kimya kidogo kama anayefikiria tena, kisha akakubali. 

**********************

Walirudi kula chakula pamoja, bila mazungumzo yeyote kisha wakatoka. Bob alimfungulia mlango wa kiti cha mbele, Sonia alipokaa, Bob akamfungia mlango. Aliendesha bila maswali yeyote. Wote walikuwa kimya kabisa, mwishowe Sonia akaamua kuvunja ukimya. 

“Kila siku unakuwepo pale mgahawani?” “Huwa najitahidi nisikose.” Sonia alibaki na mshangao. “Ule ni mgahawa wangu.” Akaongeza. “Kwa hiyo nikitoka kazini, napitia pale, nakakaa mpaka nikiona wanakaribia kufunga ndipo na mimi naondoka.” “Oooh! Hapo nimekuelewa.” Bob akatoa tabasamu lake. 

“Nilitaka kukupigia simu kukujulia hali Sonia, lakini sikuwa na namba yako.” “Siku ile nilikuwa na maumivu makali sana. Nilisahau hata kukuuliza namba yako ili nije kukushukuru baadaye. Hivi leo nilikuja kubahatisha tu, sikujua kama ningekukuta pale tena.” “Unaweza kuchukua namba yangu leo.” “Nimeacha simu nyumbani. Nitakuja kuchukua wakati mwingine.” Bob alimgeukia na kutabasamu. 

“Kweli Bob, nimeicha simu nyumbani.” “Basi nipe ya kwako.” “Si unaendesha? Utaandikaje sasa?” “Wewe itaje tu.” Sonia akaitaja. “Au nirudie?” “Hamna haja.” Sonia alibaki akishangaa. Alimshusha nje ya geti lao, Bob akaondoka.  

 **********************

Alipoingia ndani alikuta gari ya Sam, alijua yupo ndani. Nyange na mkewe walikuwa sebuleni, Sam na mama yake walikaa sehemu yakulia chakula. “Vipi tumbo Sonia?” Nyange aliuliza mara Sonia alipoingia ndani. “Naendelea vizuri kabisa. Asante shemeji.” “Umerudije nyumbani? Si utakuwa umepata shida ya usafiri jioni hii?” Mama Briana akaongeza swali. 

“Hapana dada. Nilipoenda kumshukuru yule kijana aliyenileta hapa wakati naumwa, Bob, akaamua kunileta.” Sam alikaribia kuchanganyikiwa. “Afadhali. Usiku huu kwenye madaladala sio vizuri. Ukikwama usafiri, uwe unaniambia Sonia, nitakufuata.” “Asante dada, lakini naona Bob atanisaidia. Muda wake wakutoka kazini, unafanana na wangu wakutoka kusoma na anakuwa pale karibu na maktaba. Amesema tutakuwa tukiongozana wakati wakurudi nyumbani. Kwa hiyo nitakuwa sawa tu.” Kimya cha gafla kilitanda, Sonia akataka kuingia chumbani. 

“Si ule kwanza?” Mama yake alimuwahi Sonia kabla yakufungua mlango wa chumbani. “Tulisha kula mama. Asante. Ngoja nikapumzike.” Sonia aliingia ndani moja kwa moja bafuni. Alipotoka alimkuta mama yake chumbani. 

“Sam anakuita.” Sonia hakujibu. Alivaa nguo zakulalia na kupanda kitandani bila yakusema kitu, akalala. Mama yake hakurudia kwa sababu alijua alimsikia. Akamuacha.

**********************

Aliamka asubuhi na mapema, akanywa chai nakuondoka bila yakuonana na mtu yeyote. “Sonia yuko wapi, mama?” Sam akauliza. “Nimemsikia asubuhi asubuhi kweli anajiandaa kuondoka, atakuwa ameshaondoka. Nilikuwa namsikia akimwambia mama Briana wanakaribia mitihani ya mwisho. Naona hiyo ndio inamuweka macho.” Sam akabaki kimya.  

**********************

Kwa muda wa siku tatu mfululizo Sam alikuwa akipishana na Sonia bila kuonana. Na Sonia aliacha kutembea na simu yake kabisa. Aliizima na kuiweka juu ya meza. 

Siku ya jumamosi Sonia aliamka saa nne asubuhi akaoga na kuvaa kabisa ndipo alipotoka na begi lake la shule. Alipokuwa akinywa chai jikoni Sam naye akaingia. 

“Vipi Sonia?” “Safi tu.” “Mbona sikupati kwa simu?” “Niliizima, ipo hapo chumbani.” Sam akatulia kidogo. “Kwa nini?” Sonia akiwa bado anakula huku macho yake yameangalia chini bila kumtazama Sam, alikunja uso. “Eti Sonia? Kwa nini hutembei tena na simu?” “Najikuta sina matumizi nayo.” Sam akanyamaza. 

Sonia alirudisha vyombo kwenye sinki, akanyanyua begi lake, wakati anataka kutoka Sam akamuita. “Sonia?” “Abee.” Sonia akasimama huku akiangalia chini. “Pesa yako ya matumizi hii hapa.” Sam alichomoa bahasha. “Nashukuru sana. Lakini bado nina pesa zile ulizonipa mwezi uliopita. Kwa sasa sihitaji pesa yeyote. Nikihitaji nitakwambia.” Sam akabaki ameshikilia bahasha yake huku Sonia akiangalia chini.

“Nawahi shule.” “Leo jumamosi Sonia!” “Kuna kundi la kujisomea nimejiunga nalo kwa ajili ya maandalizi ya mtihani. Tunakutana leo saa tano asubuhi.” “Nisubiri nikabadili nguo basi, nikupeleke.” “Haina haja. Wewe endelea tu na shuguli zako.” Bila kusubiri jibu, Sonia akaondoka. Sam alijua Sonia amekasirika sana. 

**********************

Sonia alijitahidi kumkwepa Sam kwa kadiri ya uwezo wake. Alitoka kila siku asubuhi na mapema, nakurudi usiku. “Mbona unachelewa kurudi Sonia? Na ni kama unanikwepa!” “Nawahi daladala za kwanza za asubuhi ili nisipate shida ya kugombania na jioni tunakuwa na wenzangu tunajisomea.” 

“Kwa nini hutaki nikupeleke?” “Sitaki kuingilia ratiba zako. Najua una kazi nyingi, na mimi nimebakisha week chache sana nianze mitihani. Sitaki kujichanganya na mambo mengi.” Sonia aliingia chumbani bila kutaka kuendeleza maongezi.

Kwa kuwa walikuwa hawaonani kabisa, siku hiyo usiku Sam aliamua kumsubiria Sonia mpaka aliporudi nyumbani. “Mbona usiku sana Sonia? Sio salama kwako peke yako, na ukija nasikia hauli. Utashindwa kusoma vizuri.” “Nakuwa siko peke yangu.” Sam akatulia kidogo na kuuliza. 

“Unakuwa na nani?” Sonia akasimama kimya kwa muda. “Sonia? Maana siku hizi hata maktaba kwenyewe nikienda kukufuata sikukuti.” “Nakuwa nasoma na wenzangu palepale chuoni, halafu Bob anakuja kunichukua tunaenda kula, ndipo ananirudisha mpaka hapo getini. Kwa hiyo nipo salama kabisa. Sipo peke yangu.” Sam alipatwa na ububu wa gafla. 

Maneno ya Nyange yalianza kumsumbua masikioni, Sonia aliendelea kusimama kwa muda huku akiangalia chini, na Sam alibaki akimtizama. 

“Naomba nikapumzike. Nataka kuwahi kuamka.” “Naomba kesho unisubiri twende wote.” Sonia hakujibu kitu. Akasimama kwa muda akiwaza. 

Mwisho akaaga. “Usiku mwema.” Sam akamsogelea karibu kutaka kumgusa lakini Sonia akamkwepa. 

Ilikuwa ni zaidi ya miezi sio Sam kumbusu tu, bali hata kumgusa. Machozi yalianza kumtoka Sonia kama mvua, akajifuta nakuingia chumbani kwao. Sam aliumia sana. 

 **********************

Sonia alishapata mtu wakulala naye chuoni kwa kipindi hicho cha maandalizi ya mitihani na week zote mbili za mitihani yake. Alishamuaga Nyange, mkewe na mama yake. Aliamka asubuhi kama kawaida yake, alitoa begi ambalo aliweka nguo zake na vitu vyake ambavyo angevihitaji. “Mbona begi kubwa hivyo?” Mama yake alitoka kitandani. 

“Nitakaa huko kwa muda mrefu kidogo, mama.” “Kwani hurudi kuja kuniona?” Sonia akanyamaza kwa muda. “Sonia?” “Nitarudi mama. Lakini nahitaji muda wakutulia mama yangu. Acha nikakae huko kwa kipindi hiki, ili nitulize mawazo ni malize hii shule vizuri.” Sonia akaanza kutokwa na machozi. 

“Wewe unajua maisha yetu yanategemea hii shule. Acha nikazane mama, ili juhudi zangu zisipotee tena bure.” “Ni kweli mama. Kazana Sonia. 

Nakuombea ufanikiwe.” “Asante mama.” Mama Sonia alijua kabisa mwanaye hayupo sawa. Alijua Sam amemuumiza sana, lakini aliamua kutokuingilia kabisa, akanyamaza tu.

“Naomba nikuachie hizi barua mama. Usizigawe mpaka nitakapo kwambia.” “Sawa.” Sonia alitaka kutoka. “Mbona unaacha simu?” “Sitaihitaji. Ni ya Sam, naomba uumpe simu yake.” Mama Sonia akabaki akiwaza. 

Sonia alikuwa ameshatafuta taksi yakuja kumfuata asubuhi hiyo ya saa kumi na moja. Aliondoka pale na karibia kila kitu chake. Sam naye aliamka mapema sana ili asimchelewe Sonia, alipojitayarisha alimfuta chumbani kwao. Alitoka mama Sonia akiwa na usingizi, kwani alirudi kulala mara baada ya Sonia kuondoka. 

“Alishaondoka.” “Saa ngapi!? Mbona nilimwambia anisubiri?” “Alisha ondoka.” Sam alijaribu kupiga simu ya Sonia, bila majibu. “Ooh! Sam?” Mama Sonia alitoka tena nakumkuta bado Sam amesimama palepale nje ya mlango wa chumbani kwao, akiendelea kupiga simu ya Sonia. “Sonia amenipa hii simu nikurudishie.” “Kwa nini?!” Mama Sonia alibaki akimwangalia. Alipoona wamebaki wakitizamana, Sam aliondoka na ile simu kimya kimya. 

 **********************

 Alipofika tu kazini aliamua kuiwasha simu ya Sonia. Gafla jumbe zilianza kuingia kwenye simu ya Sonia, na zote zilionekana hazijawahi kusomwa. Sam aliamua kufungua. ‘Hii ndio namba yangu Sonia. Bob.’ Huo ulikuwa ujumbe wa kwanza. 

‘Nimefurahi kukuona tena Sonia, lakini naumia kukuona unalia. Kama unataka mtu wakuongea naye, nipo kukusikiliza. Hata kama nina mambo mengi, nitatafuta muda kwa ajili yako ili kurudisha tabasamu nililo liona mara ya kwanza tulipo kutana.’ Ujumbe mwingine. 

‘Naomba uwe huru kunitafuta wakati wowote, iwe mchana au usiku nipo kwa ajili yako, Sonia.’ Na jumbe nyingine nyingi zakumfariji Sonia. Sam alianza kutetemeka.  

Moja kwa moja akafungua sehemu za ‘outbox’ kuangalia kama Sonia alishawasiliana naye kabla na amejibu nini. Alikutana na jumbe za kimapenzi alizokuwa Sonia akimtumia yeye mwenyewe Sam. Na ya mwisho ni ile aliyomwambia anahamu naye. ‘Imekuaje huu ujumbe sikuuona?’ Sam alianza kuwaza kwa sauti. 

Alivuta simu yake kuangalia ‘Inbox’ yake kujua kama ule ujumbe ulifika. Alikuta kwenye simu yake jumbe nyingi sana kutoka kwa Sonia na zote zilionyesha hakuwahi kuzifungua. Sam alizidi kuvurugukiwa. “Mungu wangu nisaidie!” Siku hiyo kazi hazikufanyika kabisa. 

Sam alirudi nyumbani mapema sana. Hakuna aliyemuongelesha kabisa, lakini hakushangaa alijua kabisa kila mtu amemkasirikia. Aliendelea kuzunguka mle ndani bila hata kukaa chini akijiandaa kumpokea Sonia na maneno mazuri ya msamaha. 

**********************

Nyange alirudi nyumbani kwake alimkuta Sam bado anahangaika. “Vipi Mheshimiwa? Kazi zimepungua nini? Naona leo mapema!” Nyange alimuuliza kwa kumkejeli. “Sonia ameondoka tokea asubuhi, ameacha na simu yake hii hapa, halafu naona anachelewa kurudi.”  Nyange akamwangalia vizuri, huku akimpa tabasamu la kejeli. 

“Ni muda kweli kukuona una wasiwasi na Sonia.” “Nilibanwa na kazi kaka.” “Ooooh!” Nyange alijibu nakugeukia tv, Sam akakaa. “Kweli kaka nilibanwa.” “Mbona hilo halina ubishi kabisa Sam? Kila mtu amekuona humu ndani jinsi ulivyokuwa umebanwa.” Sam alibaki akibabaika.  

Mwishoe alibakia amekaa hapo kimya kwa muda, kisha akasimama akatoka nje, akarudi tena ndani na kukaa. Kila mlango ulipofunguliwa alisimama akijua ni Sonia. Aliendelea kuhangaika pale sebuleni kila mtu akimtizama bila yeye kujali. 

Alichofikiria ni usiku huo kuweka mambo sawa na Sonia. Wivu ulikuwa ukimtesa na hofu ya kunyang’anywa Sonia ulishamuingia. Mikakati ya kubadili maisha yake ili apate muda wakutosha na Sonia iliendelea kichwani kwake huku akimsubiria. ‘Nitachanganyikiwa wakinipora Sonia. Mungu wangu nisaidie!’ Sam aliendelea kuwaza wakati watu wakiendelea kuaga kwenda kulala. 

“Kamba Yamkatikia Pabaya Sam.”

Mwishowe Nyange alimuonea huruma. “We Sam? Sonia alituaga, hatarudi mpaka amalize mitihani.” “Daah! Kote huko!” “Mbona sikuelewi Sam? Kama unamtaka yule mtoto, halafu kama unampuuza! Vipi?” “Nampenda sana Sonia, kaka. Lakini mambo mengi yalinifunga. Nilikuwa nahangaika kutafuta pesa, ili nimalizie ile nyumba. Nilitaka akimaliza tu shule yake tuone halafu tuhamie kwetu.” “Hiyo mipango yako ulimwambiaSonia?” Sam aliwaza kidogo. 

Kisha akajibu. “Lakini atakuwa anajua kaka, nimebanwa kweli na kazi na biashara.” “Kweli ulibanwa mdogo wangu, ukamsahau kabisa Sonia! Kwa jinsi alivyonieleza mama Briana, kweli unaonekana ulibanwa.” “Mama Briana?” Sam aliuliza kwa mshangao. 

“Wewe hukuondoka hapa nyumbani kwenda kazini baada ya kuambiwa na mama yake kuwa Sonia hakulala usiku sababu ya kuumwa? Achilia mbali jana yake umemuacha yule binti mgonjwa siku nzima, bila hata kumpigia simu! Basi wewe umebanwa kazini, ulishindwa hata kupiga simu kutujulisha!?”

“Ameokotwa wapi sijui huko ameletwa hapa amejaa matapishi na damu mwili mzima. Ukaona haitoshi ukamuacha hapa ukaenda kazini ukarudi usiku, bila hofu unamwambia mama yake mzazi simu iliishiwa chaji! Huogopi?”

“Yaani wewe ulishindwa hata kuomba simu ya mtu kumjulia hali mwanamke unayesema unampenda? Hayo ndiyo niliyoyaona. Mengine aliyomsimulia mama Briana ndio yananishangaza Sam. Mama Briana alikuwa anaongea huku akilia. Umepatwa na nini wewe?” Sam alibaki kimya kabisa. 

“Mara ngapi umemuacha yule binti nje ya maktaba akikusubiri au tuseme mtaani akikusubiri uende kumchukua? Tena unamuacha mpaka usiku!? Huofii hata usalama wake, hata kusema jamani nimelemewa naomba mkamchukue Sonia, umeshindwa na nyumba imejaa magari na watu tupo!”

“Anasema uliacha kabisa kujibu kila ujumbe wa mapenzi aliokuwa akikutumia, na ulipokuwa naye kwenye gari, unakuwa wewe na simu tu mpaka mnaachana!”

“Anasema siku yake ya kuzaliwa alikuomba mtoke, ukasema unakazi nyingi. Akakuomba tena angalau mpate muda wa pamoja hata kama hamtatoka lakini angalau mkae tu mzungumze hapahapa nyumbani, lakini ukasafiri! Ulikuwa unawaza nini Sam?” Sam alibaki na majuto. 

Ni kweli hakujua kama alikuwa akimuumiza Sonia kwa kiasi kile. Alijua Sonia anaelewa kila kitu. Nia na kusudi la Sam nikuhangaika kutafuta pesa nyingi ili kumfanya Sonia aishi vizuri. 

“Daah!” Sam aliendelea kuhamaki kadiri yalivyokuwa yakimuingia moyoni. “Sijui bwana! Lakini katika mabinti waliokuwa watulivu, yule binti alikuwa mmoja wao. Umemsukumia mwenyewe kwa wanaume.” Nyange akatabasamu. 

“Sikuwa nimemwambia mtu yeyote. Lakini nilishamtega Sonia kwa wanaume wawili.” Sam akashituka sana. “Mmoja mwanafunzi wa palepale, na mwengine ni jamaa wa mtaani tu. Niliwapa pesa, wamshawishi Sonia mpaka akubali, ili tu nimjue tabia zake. Lakini wote wawili waliniambia walishindwa.”

“Yule mtoto alikuwa akikutaja kwa kila mtu, Sam. Uzuri ule wa Sonia, na yote uliyokuwa ukimfanyia, lakini aliamua kutulia na wewe tu. Naona mwenzangu ukadharau.” “Sikudharau kaka. Sijui nilipitiwa na nini? Ila nilijua ni maisha ya muda mfupi tu, biashara ingechanya ndipo ningeacha kazi, nikabaki na Sonia na biashara tu.” “Haya bwana!” Nyange akasimama ili na yeye aondoke. 

“Nitafanyaje kaka?” “Nahisi kama hilo swali umechelewa Sam. Ungeniuliza mwezi mmoja kabla, ningekuwa na jibu zuri sana. Lakini sasa hivi sina jibu, kwa kuwa naona kama ameshaongezeka mtu mwingine katikati yenu. Na ninaona mwenzako amekazanakweli! Anajua kupangilia kazi zake na anapata muda na Sonia.” “Mungu wangu kaka! Ni huyo Bob?” Nyange alicheka nakuondoka. 

“Maisha mapya ya Sonia na Bob.”

Bob na Sonia walianza kutoka. Bob alikuwa mcheshi sana. Sonia alikuwa akicheka kila wakati kwa utani wa Bob. Kila alipomaliza kujisomea, nakuhitaji kupumzisha akili zake, alimtafuta Bob. 

Kama sio kuonana, waliongea kwa simu mambo mengi ambayo hayakuwa na maana yeyote lakini walikuwa kwenye simu muda mrefu sana wakiongea na kucheka. Walipeana habari na vituko walivyokutana navyo siku nzima, na asubuhi Bob alikuwa akimtumia Sonia ujumbe mzuri wakumtakia awe na siku njema, kitu kilichokuwa kikimfurahisha sana. Tabasamu lake ni kweli lilirudi usoni, na akatuliza kweli akili kwenye masomo. 

**********************

Mwezi mmoja ulishakuwa umepita tokea Sonia alipoona tangazo la nafasi za kazi benki. Alituma maombi yake kwa kutumia cheti chake cha diploma. Wakati yuko kwenye mitihani, alipigiwa simu ya kwenda kwenye usahili/interview. 

Hakuchelewa, alienda kufanya hiyo interview, alifaulu vizuri. Lakini aliambiwa nafasi ya kazi ipo jijini Dodoma. Hakukataa, alifurahi sana. Lakini aliomba amalizie mitihani ndipo aende. Walimruhusu. Kwa hiyo alikuwa akifanya mtihani huku akiwa mwajiriwa kamili wa benki.  

 **********************

Alijitahidi sana kutulia ili amalizie mitihani yake. Hakuruhusu mawazo yoyote yaingilie malengo yake. Japokuwa alisha nunua simu nyingine lakini hakutaka hata kumpigia simu mama yake. Bob tu ndiye aliyekuwa akifahamu hiyo namba. 

Alitulia mpaka mitihani ilipoisha, ndipo alipo mpigia simu mama yake, siku hiyo usiku nakumpa habari njema. “Hongera Sonia mwanangu. Ona Mungu alivyotukumbuka! Sasa kazi yenyewe ni wapi?” “Nitakupigia simu nitakapo tulia mama. Lakini naomba uendelee kunitunzia mwanangu. Nikitulia, nitawaita mje tuishi wote.”

“Naomba univumilie tu mama yangu, najua nakuachia mzigo wa mtoto wangu kila mara. Lakini naamini hii ndio mara ya mwisho, nitatulia ili nimlee mwenyewe.” Sonia alikuwa akilia. 

“Wala hilo lisikutie wasiwasi, Kana sio mzigo kabisa. Kwanza nafurahia kuwa naye baba yangu.” Mama Sonia aliongea kwa utani kumfariji mwanae. “Kweli mama?” “Kwanza hata ungemtaka nisingekupa.” “Asante sana mama.” Sonia alicheka kwa unyonge, wakati wote alichukia sana kutengana na mama yake na mtoto wake. 

“Bado unazo zile barua nilizokupa?” “Ninazo.” “Basi naomba umpe kila mmoja ya kwake.” Sonia alimwandikia kila mmoja wao barua pale ndani mpaka Brayan ambaye tayari alikuwa ana miaka mitatu. 

**********************

Mama Sonia alisubiri kila mtu alipomaliza kula na wamekaa sebuleni ndipo alipowapa barua zao. Sam alikuwa akiingoja siku ya kurudi Sonia kwa hamu sana. Alishajiandaa jinsi yakuomba msamaha. Na kwa kuwa alijua Sonia anampenda sana, alijua atamsamehe tu. 

Bila kupoteza muda Sam alifungua ya kwake harakaharaka. Kitu kilianguka chini kutoka kwenye bahasha yake. Kila mtu akamgekia. “Mwenzetu umewekewa na hela nini?” Nyange akauliza. Sam aliinama kutafuta kitu kilichokuwa kimeanguka chini ya kochi. Akili yake iligoma kuamini pale macho yake yalipokutana na pete ya uchumbaaliyokuwa amemvalisha Sonia. Machozi yalianza kumtoka taratibu. Alifungua barua yake. 

“Sam!

Neno asante halitoshi kufikisha shukurani zangu kwako. Nakushukuru kwa kila kitu. Nikianza kutaja kimoja kimoja, hakuna karatasi linaloweza kutoshea yale uliyonifanyia. Asante kwa kunitoa mavumbini na kunifikisha hapa nilipo. Bila wewe ni kweli mimi na familia yangu tusingekuwa hapa tulipo. Asante sana. 

Nasikitika mahusiano yetu ya mapenzi hayakufanikiwa, Sam. Nilijua wazi ingekuwa ngumu kunipenda na kunithamini mtu kama mimi. Sikulaumu kabisa, ninajua jinsi ilivyo ngumu kuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi na mtu mwenye historia ya maisha kama yangu, wakati sasa hivi una pesa nyingi sana na umezungukwa na wasichana wengine wadogo na wazuri, tena wenye historia za maisha zinazo eleweka, sio kama mimi. 

Lakini pia nakushukuru kwa nafasi ya mapenzi ya muda mfupi uliyonipa. Imenisaidia kufungua moyo wangu. Sasa hivi najua naweza kupenda tena, kama nikipata mtu atakayekubali kunipokea jinsi nilivyo. Nakutakia kila la kheri.   Sonia!”  

“Haiwezekani!” Sam alisimama huku machozi yakimtoka. “Sonia hajanitendea haki kabisa mama. Hakunipa nafasi yakujieleza hata kidogo! Sio sawa mama yangu, naomba namba yake ya simu.” “Amenipigia simu, lakini namba yake haionyeshi. Angalia simu hii hapa.” Akamkabidhi simu.

Mama Briana na baba Briana!

Nawashukuru sana kunipokea mimi na familia yangu. Asante kwa kunitunza vizuri na kwa upendo mkuu. Tumekuwa tukihangaika kwa muda mrefu sana mimi na mama yangu bila kupata watu wanaotupenda na kutujali. Lakini nyinyi mmekuwa zaidi ya ndugu. 

Asante kwa kunisomesha pia. Nimeamua kuondoka kwenda kutafuta maisha sehemu nyingine. Ninawaahidi, nitakapotulia nitarudi nyumbani kuwasalimia. 

Lakini kwa sasa naomba muendelee kumtunza mama yangu na mtoto wangu mpaka nitakapopata sehemu ya kuwaweka. Naomba Mungu isichukue muda mrefu. Ningetamani kuendelea kukaa na nyinyi muda mrefu, lakini naona haitakuwa sawa, si kwangu tu, hata kwa Kana. Nataka akue akijijua yeye ni nani, atambue uhalisia wa maisha yake ili asibweteke. Sio hapo kwenu kwenye kila kitu na yeye kujihesabu kama Brayan. Nina wapenda sana. Sonia!

Mama Briana ndiye aliyekuwa akilia kuliko wote. Aliondoka kwenda chumbani kwake akilia. Josh alisoma barua yake kimya kimya. Mama Sonia aliziweka barua zake na Kana pamoja bila hata kufungua. 

Gafla nyumba ile ilijaa huzuni. Sam aliendelea kujilaumu sana. “Sikuwa nikimpuuza Sonia mama yangu, nilikuwa natafuta pesa ili tuje tuishi vizuri. Nampenda sana Sonia. Nilijisahau tu, lakini nia ilikuwa nzuri. Nilijua tupo pamoja naye katika kila kitu. Hakuwahi kunilalamikia hata siku moja! Wakati wote alinionyesha anaelewa.” Sam alimsogelea mama yake Sonia na kuendelea kujieleza.

“Naomba uniamini mama, simdharau Sonia hata kidogo. Nampenda sana Sonia na Kana. Hangaika yangu yote ni yeye Sonia. Amefanya haraka kuondoka. Naomba uniambie alipo, ili nikaongee naye.” “Hajaniambia bado. Amesema mpaka atakapojiweka sawa, ndipo atakuja kutuchukua.” 

“Mungu wangu! Siamini kama ndio nimempoteza Sonia!” Sam alisimama huku ameweka mikono kichwani. “Lakini sitakata tamaa. Nitamtafuta Sonia. Naomba Mungu nimpate kabla hajaolewa na mwanaume mwingine. Sonia ni wangu mama.” Sam aliendelea kuongea huku akizunguka sebuleni na sehemu yakulia chakula. 

“Unakumbuka nilikwambia Sam? Hizo pesa unazozitafuta ipo siku zitakugeuka, ziwe chungu kama shubiri. Umeamini sasa? Lazima ukubali Sam, wewe ulijisahau sana. Hukujua nguvu uliyokuwa nayo yakutafuta pesa na kufanikiwa ulikuwa ukipata wapi. Achilia mbali furaha yako, vyote hivyo hukujua vinatokana na nini.”

“Hukuwa hivyo Sam. Sonia alikubadilisha sana na kukufanya uonekane unafaa mbele za watu. Yule mtoto alikuwa akikupenda na kukujali sana. Akili zake zote zilikuwa kwako, wewe ukahamishia akili zako zote kwenye husaka pesa.”

“Ona sasa. Pesa unazo, nyumba yako ya kifahari ni kama imeisha, lakini vyote vimepoteza maana. Utakuja kuoa mwanamke mwingine atakayekufanya hata ile nyumba uliyoihangaikia, ushindwe kuikaa na pesa zako mwenyewe kuziona chungu.” Nyange aliendelea kumlaumu sana Sam. 

“Najuta kaka! Lakini nia yangu ilikuwa nzuri. Sikutaka nimtoe Sonia hapa halafu nimpeleke kwenye mazingira ya ajabu.” Mama Sonia alikuwa kimya kabisa bila kusema kitu. 

**********************

Taratibu nyumba ya Nyange iliyokuwa imezoea vicheko ilianza kubadilika. Sam naye alimaliza nyumba yake aliyokuwa akiijenga yeye na Sonia akahamia, akiwa haamini kama ndio amempoteza Sonia. 

Ndoto na mipango yote aliyokuwa amepanga kwenye maisha na Sonia, vilitoweka mbele ya macho yake na yeye akiwa amechangia kwa asilimia zote. ‘Siamini kama ndio nimemuozesha Sonia kwa mwanaume mwingine, tena mimi mwenyewe kwa akili zangu timamu! Mungu wangu nisaidie.’ Sam aliendelea kuwaza na kujilaumu sana. 

Huku Kwa Sonia.

Alipomaliza mtihani wake wa mwisho, alirudi kwenye chumba alichokuwa wakiishi na rafiki zake na kujitupa kitandani. Mara simu ya Bob iliingia. “Pole na hongera Sonia.” “Umejuaje kama nimeshamaliza mitihani?!” Sonia alishangaa kidogo. “Nilikuwa na ratiba ya mitihani yako yote.” “Bob wewe!?” Bob alianza kucheka. 

“Unampango gani sasa hivi?” “Nimechoka sana, usiku sikulala vizuri. Hapa nipo kitandani nataka kulala.” “Basi pumzika, lakini naomba nikukaribishe rasmi kesho, nyumbani kwangu.” “Rasmi!?” “Nataka uje upaone nyumbani kwangu Sonia. Sipendi tunavyoishia mtaani tu. Angalau ufahamu ninapoishi.” Sonia alicheka. 

“Naamini utafurahia. Unakumbuka nilikwambia najua kupika sana?” “Kila siku.” Wote walicheka. “Unanisingizia bwana! Sikwambii kila siku.” “Tatizo lako unasahau Bob, ndio maana unarudia rudia.” “Sawa bwana, umeshinda. Sasa nataka kesho ukija nikupikie chakula kizuri, kama kukupongeza kwa kumaliza mitihani.”

“Asante Bob. Utakuja kunichukua saa ngapi?” “Mapema tu. Nataka tuanzie sokoni. Tukanunue vitu vya kupika kwanza, ndipo twende nyumbani.” Sonia alifurahi sana “Asante Bob. Nitakuwa nakusubiria.”

 **********************

Siku hiyo ya jumamosi Sonia aliamka akiwa amejawa na furaha sana. Uchovu wa mitihani ulishaisha kwani tokea alipojitupia kitandani pale jioni iliyopita hakuamka mpaka asubuhi hiyo. Aliingia kuoga, akatoka bafuni akiwa amejawa tabasamu usoni. 

Akajitengeneza vizuri na kuvaa kigauni chake kilichokuwa kimemkaa vizuri sana. Na kilionekana kinafaa kuvaliwa popote. 

Bob alibaki akimwangalia Sonia, pale alipofika kwenye gari yake baada ya kumpigia simu nakumwambia atoke anamsubiri nje ya hosteli yao. 

“Nini bwana Bob?” “Nimebaki na kigugumizi.” “Kwa nini sasa?” “Umebadilika sana?” “Nimechukiza nilivyoachia hizi nywele? Nimeona na zenyewe zipumzike leo. Nimekuwa nikizibana karibu mwaka mzima. Leo na zenyewe zipo mapumzikoni. Zina sherehekea kumaliza chuo.” Sonia alijibu huku akitabasamu. 

“Hapana! Umependeza sana. Umezidi kuvutia Sonia.” Sonia alianza kucheka kwa sauti. “Tatizo lako unafikiri kila wakati nakutania. Lakini safari hii sikutanii, ni kweli umependeza sana. Huchoshi kuangalia Sonia.” “Asante Bob.” Sonia alijibu kwa aibu kidogo. 

Waliponunua kila kitu alichokuwa akikihitaji Bob kwa mapishi ya siku hiyo, walirudi nyumbani kwa Bob. Ukweli Bob alikuwa amejijenga sio kama Sam. Sonia alibaki akiangaza macho. “Una nyumba nzuri sana Bob.” “Asante.” Alimkaribisha kinywaji.

“Unataka tukae wote jikoni wakati ninapika?” “Ndio vizuri nikusaidie.” “Hapana Sonia. Nimekwambia mimi ndio mpishi leo. Nataka wewe ukae tu hapo kwenye meza tuongee wakati napika.” Sonia alikuwa haamini. Hakuwahi kuhudumiwa hivyo haswa kupikiwa. Alishazoea kumtumikia Sam, kuanzia kumpikia, kufua na mambo mengine mengi ya nyumbani. Alibaki akimtazama Bob huku akitabasamu. 

“Nini sasa? Unafikiri sijui kupika?” “Hapana, sitajali chakula kitakuwa na ladha gani, mimi nafurahia mapumziko yangu ya leo. Sikumbuki kufanyiwa hivi hata siku moja.” Bob alicheka, wakaendelea na mazungumzo yao kama kawaida. Sonia akicheka kwa vituko vya Bob, alikuwa akipika na kucheza miziki ya rumba aliyokuwa ameweka. 

Alipoivisha kila kitu, walikaa mezani nakuanza kula. “Sitathubutu kukupikia hata mara moja Bob.” Bob alicheka sana. “Kwa nini Sonia?” “Sasa hivi naelewa kwa nini ulitaka kupika mwenyewe.” “Hamna bwana! Mgeni siku ya kwanza. Siku nyingine utapika wewe Sonia.” “Ili unicheke?” Waliendelea kula na kunywa mwishowe wakahamia kwenye makochi na vinywaji vyao mara baada ya kumaliza chakula. 

Lakini kila muda ulivyozidi kwenda ndivyo jinsi hali ya Bob ilivyozidi kuwa mbaya. Alishaenda chooni mara kadhaa, alisimama na kukaa lakini Sonia hakuwa ameelewa kitu chochote. Aliendeleza story bila hata kuelewa hali ya Bob. 

Sonia alishangaa kuona Bob anahamia kwenye kochi lake. “Naomba nikwambie kitu Sonia.” Sonia alipoona uso wa Bob umebadilika sio wautani tena, akamgeukia vizuri. “Mbona unaniogopesha, wewe Bob!?” Kabla hajakaa sawa tayari Bob alishamvamiapale kwenye kochi na kuanza kumbusu. 

Alimng’ang’ania Sonia huku akitetemeka sana. Sonia alipoona mambo mabaya alimsukuma Bob na kukimbia upande wa pili. “Bob!? Unafanya nini wewe?” “Nakupenda Sonia. Nakupenda sana.” Sonia alibaki akitetemeka huku anamshangaa. 

“Mapenzi gani ya hivyo!?” “Kweli nakupenda Sonia.” “Naomba nirudishe chuoni tafadhali, Bob.” “Bado unamfikiria Sam? Mwanaume asiyekujali? Mimi nakupenda, na ninakujali Sonia. Nakuahidi sitobadilika kama Sam.” 

“Usiwahi kujifananisha na Sam hata siku moja. Sam hawezi kufanya unachotaka kunifanyia wewe sasa hivi. Nimekaa naye muda wote hajawahi kunilazimishia mapenzi hata mara moja.” “Kwa kuwa hakupendi Sonia. Inawezekana lengo lake lilikuwa nikukusaidia na kukufikisha hapo ulipo tu. Sio mapenzi.”

“Mimi nina mapenzi ya dhati na wewe. Nakupenda Sonia, nataka uwe wangu. Mwanaume yeyote mkamilifu na anayekupenda kwa dhati bila kukudharau hawezi kukuacha tu msichana mzuri kama wewe bila kukugusa. Nakupenda Sonia, na nina kuhitaji.” Yale maneno yalimchoma sana Sonia na kumdhoofisha sana. 

 **********************

 ‘Lakini kweli!’ Sonia alianza kuwaza. ‘Sam atakuwa alikuwa na nia yakunisaidia tu. Maana hata mabusu yenyewe aliyowahi kunipa yana hesabika, na alikuja kuacha kabisa hata kunigusa. Bob yupo sahihi. Kama angekuwa akinipenda kwa dhati angeniweka mimi mbele, asingeshindwa hata kuja kuniona hospitalini. Ndio maana alikuwa akishindwa hata kujibu jumbe zangu za mapenzi.”

“Sam alichoka kujificha nyuma ya pazia la mapenzi. Ni mimi tu nilishindwa kumsoma na kumuelewa kwa muda mrefu. Sam ni mstaarabu sana, asingeweza kuendelea kuishi maisha ya kinafiki ya kuigiza, kuwa sisi ni wapenzi.’ Machozi yalianza kumtoka Sonia kadiri alipoendelea kuwaza.  

 **********************

Akarudi kukaa kwenye kochi. Bob alirudi kukaa pembeni yake. “Lakini nampenda sana Sam.” Sonia aliropoka wakati akiendelea kuwaza. “Pole Sonia. Najua inavyouma kupenda usipopendwa.” Sonia aliendelea kulia. “Mtu yeyote anayekupenda Sonia anakujali. Wakati wote mapenzi yanaenda na kujali. Ona mimi ninavyokujali. Natafuta pesa na bado wewe nakuweka mbele.” Bob alimsogelea Sonia zaidi na kumkumbatia. 

“Nakupenda Sonia.” Sonia alibaki kimya huku bado akilia. Bob alianza kumpapasa taratibu. “Acha Bob, sasa hivi nahisi nimechanganyikiwa. Nahitaji muda wa kufikiria.” “Mpaka lini, Sonia?” “Sijui. Lakini nahitaji muda wakufikiria. Sikuwahi kukufikiria wewe kama mpenzi Bob. Wakati wote nilikuchukulia kama rafiki. Kwanza hata sikufahamu kwa undani. Hatuwezi tu kurukia kwenye kufanya mapenzi. Tafadhali naomba uniache.” Sonia alijaribu kujitoa mikononi kwa Bob lakini Bob alishindwa kumuachia. 

Mwili wake mzima ulikuwa ukitetemeka kwa tamaa. “Nakupenda Sonia, naomba usiniache hivi.” “Wewe Bob vipi jamani? Naomba uniachie.” Baada ya purukushani zakutisha ndani ya ile nyumba ya Bob, Sonia alifanikiwa kutoroka akiwa nusu uchi. 

Kisicho Riziki

Alifika chuoni akiwa hoi! Alitoa ile namba ya simu iliyokuwa kwenye simu yake na kuitupia chooni, kesho yake alinunua namba ya simu nyingine na kuiweka kwenye simu yake. Huo ukawa mwisho wake na Bob. 

Aliondoka jijini Dar kuelekea Dodoma kuanza kazi bila kuaga wala kumwambia mtu yeyote anapoenda. Alipangiwa kwenye benki ambayo tawi lake lilikuwa Mazengo, Dodoma, kama mtunza fedha, {Bank taller}, kwa kupitia cheti chake cha diploma.

Alichapa kazi bila maneno wala ubishi. Hakuwahi kuomba ruhusa yeyote kazini. Kiongozi wa tawi lake alimpenda sana Sonia. Hata walipopata wateja wengi sana, hakuwa na wasiwasi. Alijua maadamu Sonia yupo kwenye kibanda mambo yataenda haraka na vizuri. Hakuwahi kupata hasara hata mara moja wala kulalamikiwa na wateja. 

Matokeo yake ya Advance diploma yalipotoka alifaulu vizuri sana. Sonia aliomba nafasi ya kazi katika benki hiyohiyo tawi hilohilo ya Meneja mikopo. Ndani ya mwaka mmoja Sonia alishapanda daraja. Kwa kuwa walikuwa wakivaa sare kazini, na alikuwa na nguo baadhi alizokuwa akinunuliwa na Sam, alibana matumizi kwa kiwango cha juu sana. 

Alikusanya pesa zake ili aweze kukodisha nyumba kubwa yakuja kuishi na mama yake na mtoto wake mkoani hapo. Sonia alipendwa na kila mtu, lakini hakutaka kujiingiza kwenye maswala ya mapenzi hata kidogo. 

Kwa kuwa yeye ndiye alikuwa akikopesha wafanyabiashara wakubwa, alipokwenda kutembelea biashara zao ili kuidhinisha mikopo yao, wengi walimpa ahadi nyingi na kubwa ili awakubali kimapenzi, lakini Sonia alibaki na msimamo wake uleule. Alibaki akiwa peke yake, bila rafiki wa kike wala wakiume kitu kilichowashangaza wengi na hakuna aliyejua anapoishi. 

Kila atokapo kazini wakati wote alizima simu yake. Hakuonekana baa, wala kanisani isipokuwa kazini na saluni siku anapokwenda kutengeneza nywele zake, basi. 

 **********************

Sam naye alijitupia kazini moja kwa moja. Aliingia kazini asubuhi na mapema na kurudi nyumbani usiku sana. Biashara zake zilizidi kuchanganya, pesa zilikuwa zikiingia kuliko alivyotarajia. Kila alipopata muda wa ziada alikimbilia gym kufanya mazoezi na kujiepusha kabisa na starehe. 

Kwa uzuri wa kiume aliokuwa nao Sam, na jinsi alivyokuwa akizunguka kikazi matawini, alisumbuliwa sana na kina dada. Hata alipokuwa mazoezini wadada wengi walijaribu kumfuata kumuomba awaelekeze hiki au kile ilimradi tu kumvutia Sam, lakini aliamua kuweka pembeni kabisa swala la mapenzi na starehe. 

Maneno ya Nyange hayakuwahi kumtoka kichwani. ‘Hawajui shida nilizopitia hata kidogo. Matusi na dhihaka nilizovumilia mpaka kufikia hapa nilipo. Wananipenda sasa hivi sababu ya pesa. Wanachopenda kwangu ni pesa tu hakuna mwenye mapenzi ya kweli kwangu hata mmoja wao. Sam ni yule yule sikuwahi kubadilika, lakini kila mmoja wao leo ndio anachanganyikiwa na mimi na kuniapia kunipenda kwa dhati. Wanachotaka ni ndoa ili waje wafaidi jasho langu na Sonia, kisha waanze kunitesa moyo wangu.’ Sam alizidi kuwakwepa mchana na usiku. 

Simu na jumbe za mapenzi kutoka kwa kinadada mbalimbali zilikuwa haziishi kwa Sam. Kuanzia wanawake wakubwa mpaka visichana vidogo walimuwinda Sam. Lakini Sam alibaki na msimamo wake. 

Ukweli Sam alishindwa kabisa kumtoa Sonia kwenye maisha yake. Japokuwa alihisi atakuwa na mwanaume mwingine, lakini aliogopa kabisa kukaribisha mwanamke mwingine kwenye maisha yake. Kila msichana aliyejaribu kuwa naye karibu aliona utofauti mkubwa sana kati yake na Sonia. 

‘Sonia ndiye aliyenipenda kwa dhati. Alikuwepo nikidhalilishwa na Leah, lakini bado aliniheshimu na kunipenda hata wakati nikiwa chini sana kimaisha, nikiwa naishi kwenye chumba kimoja bila hata kochi au meza, wakati ule gari lenyewe nililokuwa nalo lilikuwa lakawaida sana, lakini bado Sonia aliniheshimu sana.’ 

Alikumbuka siku walizokuwa wakiharibikiwa na gari usiku njiani, huku mvua ikiwanyeshea na kuishia kutembea umbali mrefu sana, kutafuta taksii au daladala bila ya Sonia kulalamika bali kumtia moyo na kumwambia kila kitu kitakuwa sawa tu. 

Kulikuwa na kitu cha pekee sana kati yao ambacho Sam alikiri kuto kikisikia hiko kitu kwa msichana mwingine yeyote ila Sonia. “Uwii! Mungu wangu nisaidie. Naomba nirudishie Sonia wangu.” Wakati wote Sam alikuwa akijisemea kila alipokuwa akimkumbuka Sonia. 

 **********************

Aliwachukua wadogo zake waliobaki, aliokuwa akiwasomesha kutoka kijijini na kuishi nao mjini. Mdogo wake wa pekee wa kike ndiye aliyekuwa akimsaidia sana Sam mambo ya nyumbani lakini bado aliona tofauti kati yake na Sonia. ‘Hawezi kufikia mapishi ya Sonia hata afanyaje. Ona ufuaji wake wa nguo, na unyoshaji wake suruali! Sio kama Sonia.’ Wakati wote Sam alikuwa akilalamika. 

Sonia alishamzoeza Sam vibaya wakati wakiishi naye kwa Nyange. Japokuwa kulikuwa na mashine ya kufulia nguo nyumbani kwa Nyange, lakini Sonia ndiye alikuwa akizifua nguo za Sam na kuzipiga pasi. 

Hata Josh alipokuwa akikusanya nguo za watu wote kufua, Sonia alihakikisha yeye ndiye anayemuhudumia Sam, kuanzia chakula, mpaka mavazi tokea akiwa hana kitu. ‘Hakuna msichana anayeweza kumfikia Sonia bwana!’  Wakati wote Sam alikuwa akisema, tena wakati mwingine mbele za watu. 

Hata wasichana wengine walipomsogelea aliendelea kutoa sifa za Sonia. Sonia alijulikana kila mahali anapojulikana Sam, kasoro sura yake tu. Wasiwasi na hofu vilikuwa vikimpata Sam kila alipofikiria uzuri wa Sonia na uhuru alio nao kwa wakati ule, alijua wazi anaweza kuwa ameshapata mwanaume mwingine. 

 **********************

Hata mwezi mmoja ulikuwa haujapita tokea baba Briana na mkewe walipotoka kuwazika wazazi wa baba Briana. Kifo cha wazazi wake baba Briana kilimuumiza sana mama Briana kuliko hata baba Briana mwenyewe. Alikuwa akilia mchana na usiku kila akikumbuka. 

Kaka yake Eliah tu ndiye aliyehudhuria mazishi hayo kutoka upande wa mama Briana. Si mama yake wala Leah walioonekana kwenye msiba huo. Mzee Nyange na mkewe walipata ajali mbaya sana ya gari na kufa papo hapo, pamoja na dereva aliyekuwa akiwaendesha kuwapeleka mjini nyumbani kwa Nyange kwenye sherehe ya kutimiza miaka hamsini ya ndoa yao na miaka mitano ya Brayan. Nyange na mkewe walikuwa wameandaa sherehe hiyo maalumu na walitaka wazazi wao waje wakae mjini kidogo kama kupumzika pia. 

**********************

“Mimi naona kama hii sherehe tuiache tu bwana Nyange.” “Kwa nini?” “Naona kama imeshaingia mkosi! Kwanza walengwa wenyewe hawapo, tunafanya kwa ajili ya nini au nani?” “Na mwanangu je? Hatusherehekei birthday ya Brayan tena?!” 

“Hata mwezi haujaisha tangu tuzike, D. Halafu unataka kutumia mapesa yote hayo kwa ajili ya mtoto tu jamani!? Angalau hata wazazi wangekuwepo ndio ingeleta maana zaidi, kwamba tunasherekea na miaka yao hamsini ya ndoa. Sasa Brayan tu!? Tuache bwana, atakata tu keki hapahapa nyumbani.” 

“Nishaalika watu mama Briana, na nishalipa baadhi ya pesa. Hutuwezi kuacha pesa yetu ipotee bure. Kwanza Mzee Nyange mwenyewe angekuwepo angefurahi kuona maisha yetu yanaendelea sio kuendelea kuomboleza kama hivyo unavyo fanya wewe. Kwanza umesahau anavyompenda Brayan? Unakumbuka sherehe aliyomfanyia wakati anamrithisha? Dume la ukoo hilo! Lazima tumuenzi Mzee Nyange kuendeleza alichokuwa akimfanyia Mrithi wake.” 

“Lakini naona unatumia pesa nyingi sana kwa mtoto wa miaka mitano tu, D jamani!” “Ukiniahidi utanizalia mwingine, nafuta hii sherehe.” “Mmh! Minaona sherehe iendelee tu.” Nyange alianza kucheka. “Najua pakukubania. Mwanangu wa mwisho bwana, acha afaidi. Hata hivyo umejifungia sana humu ndani, kutwa unalia. Unatakiwa utoke kidogo, ukutane na watu tofauti tofauti, akili itachangamka.” 

“Unajua baba ndio alikuwa nguzo yetu D. Wazazi wako walikuwa wakinipenda sana, sitakaa kupata upendo wa namna ile tena. Mwenzio nimepoteza watu wa muhimu sana maishani mwangu.” “Pole mpenzi wangu. Lakini ndio maisha. Wote tunapita hapa duniani. Ila heri Mungu angenibakizia hata mama jamani!” 

“Kwa kuwa ndio alikuwa anakuendekeza D.” Mama Briana aliongea huku akifuta machozi. “Sikuwahi kukua kwa yule mwanamke.” Nyange alicheka kidogo. “Ungekuwepo wakati akinitetea kwa baba, mpaka ungekuwa unamuonea huruma. Wakati wote alikuwa upande wangu hata nilipokuwa nikikosa, halafu baadaye ndio ananifuata nikiwa peke yangu na kuongea na mimi kwa upolee na heshima zote. Mama yangu alikuwa akinipenda na kuniheshimu sana.” 

“Pole D. Tuanze kuwaenzi kwa kwenda kanisani, mpenzi wangu. Unajua sisi tupo mbali sana na mambo ya Mungu D?” “Usijali tutaenda bwana. Ngoja tutulie kidogo.” 

 **********************

Mama Briana alishamuomba kwa kumbembeleza mama Sonia angalau akae nao mpaka Brayan atakapoanza shule. Mama Sonia hakukataa kwani hata Kana alisomeshwa kwenye shule ya gharama sana kama Briana. Hata lugha yake ilishaanza kubadilika. Lugha waliyokuwa wakiongea na Briana mara nyingi ni ya kingereza na Kana alikuwa akifanya vizuri sana darasani, na alichaguliwa kuwa kiongozi kwenye shule hiyo ya kimataifa jijini hapo. 

Mama Sonia alimwambia Sonia asiwe na wasiwasi, wao wapo salama tu, yeye aendelee kujipanga taratibu. Hata hivyo Brayan mwenyewe alimzoea sana mama Sonia ambaye ndiye alikuwa kama mama yake wa pili kwani ndiye alikuwa akishinda naye nyumbani muda mwingi wakati Nyange na mkewe wanapokwenda kazini na Kana na Briana wanapokwenda shule.  

 **********************

“Usiwe na wasiwasi kabisa Sonia. Mwanao anaongoza huko kwenye hiyo shule. Kaniambia amechaguliwa kuwa kiongozi mkuu hapo shuleni. Kutwa Nyange anamsifia. Naona haitakuwa vizuri tumtoe kwenye shule nzuri kama hiyo halafu tumpeleke kwenye shule za kawaida. Naona tutumie hii nafasi ya yeye kusomeshwa na Nyange vizuri. Hatuna uwezo wa kumtoa hapo na kumpeleka kumsomesha kwenye shule nyingine ambayo angalau inafanana kama hiyo.”

“Nimeelewa mama. Lakini nina hamu na nyinyi.” “Vumulia tu mwanangu. Ipo siku tutakuwa wote. Namuomba sana Mungu aje atuunganishe siku moja. Hata mimi sifurahii haya maisha, ni hivyo basi, sina uwezo.” Maisha yakaendelea.

 **********************

Briana na Kana walikuwa wakisomeshwa kwenye shule nzuri sana jijini hapo, na kuendeshwa kwenye gari ya kifahari kupelekwa shule. Gari hilo Nyange alilinunua kwa pesa nyingi sana kuliko hata gari anayoendesha yeye mwenyewe na mkewe. 

Nyange alifanya maisha ya Briana kuwa ya anasa sana kuliko hata anayoishi yeye na mkewe. Kila kitu cha Briana kilikuwa cha thamani. Chumba chake alichokuwa akilala na Kana kilikuwa na kila kitu cha thamani. Nyange alimpenda Briana kuliko kitu chochote na kila mtu alikuwa akijua hata Briana alikuwa akisema, ‘Dady yangu ananipenda sana.’

Alimwaga mapesa mengi sana kwa binti yake. Ugomvi mkubwa wa Nyange na mkewe ni ubadilishwaji wa madereva wa Briana. Nyange aliwabadilisha mchana na usiku. Akikuona tu unamwangalia binti yake asivyofurahia yeye, kazi huna. 

Kila dereva aliyemwajiri kumwendesha Briana, Nyange alihakikisha anamfahamu mpaka kwa wazazi wake na kuandikishiana naye mpaka polisi, ili kuhakikisha chochote hakitokei akiwa anamwendesha binti yake, lakini bado aliwafukuza kazi. 

 **********************

“We Nyange, huyo babu hapo nje ni nani?” Mama Briana alirudi nyumbani kwake siku hiyo ya jumamosi akitokea saluni kusuka kwa mara ya kwanza tokea apatwe na msiba wa wakwe zake na kukutana na babu nje ya nyumba yao akiwa kama mgonjwa. Nyange alikuwa amebaki na watoto nyumbani hakwenda kazini. 

“D?” “Si ndio dereva mpya.” “Hapana Nyange, uliniahidi hutabadili tena dereva. Tulikubaliana Isaya ndio ataendelea kuwepo kazini. Kwanza kwa nini umemfukuza tena Isa, kijana mzuri, mtulivu, ukaenda kumleta huyu babu?”

“Kwanza hivi umemwangalia vizuri huyo babu yako? Kusimama tu kwenyewe kunisalimia ni shida! Sijui hata kama anaona.” “Mzima bwana, mama Bree.” “Hebu nenda kamwangalie hapo nje sasa hivi ndio uje useme kama anaweza kuendeshea gari huyo!” “Wazee ndio wazuri mama Briana, hawana tamaa.” 

“Hapana Nyange. Kwani imekuaje tena na Isa?” “Nimemfukuza.” “Unahangaika sana na hao madereva! Ni nini lakini? Unakuwa kama huna kazi bwana! Mwishowe utaajiri mpaka majambazi! Naomba umpigie simu Isaya, mwambie jumatatu arudi kazini” 

“Wewe umemuona Isa anavyomwangalia Briana lakini?” “Hapana Nyange. Wewe kila dereva anakasoro kwa mwanao. Lazima Isa arudi.” “Nimembamba juzi anamsindikiza mwanangu kwa macho! Ndio anaanza kumtamani hivyo.” “Hapana Nyange, wewe umezidi bwana! Yule kijana ndiye peke yake amekuvumilia.”

“Kutwa ulikuwa unamtishia hapa kuhusu huyo Briana, lakini kijana wa watu hakuwa na shida. Sheria mpya kila siku lakini amekuwa akikuvumilia tu. Huwezi kupata dereva mzuri kama Isaya. Naomba mpigie simu arudi kazini.” “Mama Briana bwana! Akitaka jambo lake, mpaka liwe.” 

“Ndiyo Nyange. Wewe mpigie simu. Yule kijana anamatatizo kweli, amekwambia mkewe mgonjwa. Halafu unamfukuza kazi sasa hivi, wakati wa matatizo! Unafikiri ataishije?” “Umeanza mama Briana na huruma zako, badala yakuangalia usalama wa mtoto?” “Bwana huyo atakayemgusa huyo Briana nani bwana Nyange? Wakati unawatishia hapa kila siku na kuwapeleka polisi kuwaapisha!”

“Haya, akitoka kumchukua mtoto roho haikutuli, kutwa uko kwenye simu na huyo dereva mpaka amshushe Briana nyumbani au shuleni. Sasa atamgusa huyo Briana saa ngapi bwana na Kana yupo? Bwana piga simu.” 

“Sasa hivi?” “Ndiyo sasa hivi. Kwani ulimfanya nini mpaka hutaki kumpigia simu?” “Ni mambo ya kawaida tu.” “Jamani Nyange wewe!? Usiniambie kama ulimpiga kama yule mwengine.” Nyange         alianza kucheka.

“Usicheke bwana Nyange. Umemfanyaje?” “Nikwambie unikasirikie?” “Basi piga simu sasa hivi, nikusikie unavyoomba msamaha, nakumuomba arudi kazini.” “Daah! Penninah jamani! Yaani nimpigie simu dereva ninayemlipa mimi, halafu nimuombe msamaha? Ujue namlipa pesa nyingi sana.” “Si anafanya kazi? Au unataka nikupeleke mpaka kwakwe, ili ukamuombe msamaha vizuri?” “Naona nipige tu simu.” Mama Briana akakaa vizuri huku akimwangalia mumewe. 

“Sasa siuende tu. Nitaongea naye kwa muda wangu.” “Hapana Nyange. Sasa hivi wakati mimi nipo hapahapa. Kwani mimi sikujui wewe?” Nyange alianza kucheka. “Sawa bwana, kama hutaki kuwa upande wangu.” “Katika hilo, wala Nyange. Nakujua sana wewe ikifika maswala ya Briana, hutaki kufikiria kabisa. Kila siku upo shuleni kwa huyo mtoto. Unachohangaika ni nini lakini?” “Sio kila siku bwana! Mara chache tu.” 

 **********************

Nyange hakuacha kupita shuleni kwa kina Briana mara kwa mara kusalimia walimu wa shuleni hapo na kuwachekesha kidogo. Aliweza kuwapamba kwa kadiri ya ucheshi wake kuwa wao ndio wazazi wakubwa sana wa Briana, kwani binti yake hutumia muda mwingi shuleni kuliko nyumbani. 

Na karibia walimu wote walimpenda Nyange. Kila alipotokezea shuleni hapo, walijua ni siku ya Neema. Aliwapa offer mbalimbali, kama ni kipindi cha mchana, alitoa chakula kwa walimu wote atakao wakuta ofisini huku akiwaambia anatambua mchango wao mkubwa kwenye malezi ya watoto wake, yaani Kana na Briana. 

Kila siku asubuhi Nyange alihakikisha anaagana na Briana akiwa anaenda shule ndipo na yeye aende kazini au kama yupo safarini nilazima kumpigia simu kabla ya Briana kwenda shule na usiku kumtakia usiku mwema kabla hajalala. 

Kila dereva anapomshusha shuleni au nyumbani ni lazima aongee na Briana kwanza kidogo ndipo dereva anaruhusiwa kuondoka. Gari hiyo inapokuwa imembeba Briana, haikuruhusiwa kusimama popote isipokuwa kwenye mataa tu wanapokuwa barabarani. 

Nyange alimpenda na kumlinda binti yake pasipo kuchoka. Wakati wote alikumbuka unyama aliofanyiwa Sonia, nakuzidi kuogopa.

  **********************

“Unavyohangaika na huyo mtoto Nyange jamani! Hata mimi mama yake hunijali hivyo.” “Acha wivu Penninah. Si hata wewe unamuona mtoto mwenyewe alivyo? Bwana kila akikua huyu mtoto anazidi kunichanganya! Naogopa kweli wasije mrubuni mwanangu akaishia pabaya au wakambaka.”

 “Wakumbaka huyo Briana nani? Mikakati yote hiyo bado huamini kama atakuwa salama? Utachanganyikiwa na huyo mtoto, D. Naomba utulie kidogo angalau uwe unafikiria. Kila mtu mbaya kwa Briana. Mtoto hana hata marafiki?” 

“Swala la marafiki sio kosa langu kabisa. Yeye mwenyewe mwanao kutwa yupo mgongoni mwa Kana. Huko shuleni kwenyewe nasikia haongei na mtu yeyote isipokuwa Kana. Akipewa hata dakika tano za mapumziko au za kwenda kujisaidia nasikia yeye anaenda moja kwa moja darasani kwa Kana hata kama mwenzake ana mwalimu darasani.” 

“Nyange jamani! Umeongea naye sasa?” “Kwani mimi mwalimu wake mama Briana? Mbona unataka niingilie majukumu ya watu!” “Hapo tu, ndipo unaponishangazana kunichosha. Huwezi kabisa kuongea na Briana, Nyange jamani! Unachomuogopanini?” “Simuogopi bwana! Wewe si unamuona jinsi alivyo mkimya? Ongea yake yenyewe ya shida, halafu sina muda kabisa na mwanangu. Wewe unataka muda huohuo mfupi tulio nao, tena ndio tuutumie kugombana? Nishakuona hunitakii mema na mwanangu wewe.” 

“Haya kwa nini hao walimu wao basi hawamwambii asimsumbue mwenzie darasani?” “Kwani wewe humjui Briana kama ana tabia kama za mama yake? Huna utakalo mwambia akaelewa akitaka jambo lake.” Mama Briana alianza kucheka. 

“Wewe cheka tu. Umeniharibia mwanangu kweli! Nasikia wakimuongelesha hajibu lolote anakaa kimya tu, wakimkazania anaanza kulia. Maswali yenyewe darasani hajibu wala haulizi swali lolote. Nasikia yupo kimya kila wakati. Nashukuru tu Mungu anajiweza darasani, lasivyo nahisi ningechanganyikiwa zaidi ya hivi?” 

“Si kwa kuwa Kana anamfundisha humu ndani kila wakirudi. Kana ana kazi yakupitia madaftari yake kila siku na kumuuliza maswali.” “Wewe unafikiri namsomesha Kana bure?” Mama Briana alianza kucheka. 

“Na jasho litakutoka.” “Na nimebanwa pabaya mimi! Sina jinsi. Mtoto haendi shule yeyote bila Kana!” Mama Briana alizidi kucheka. “Lakini piga simu sasa hivi. Na umwambie Isa kesho tunaenda kumtembelea mkewe.” “Na mimi?” “Ndiyo. Wewe na wanao wote tutaenda kumuona huyo mgonjwa, mke wa Isa. Lazima tumuonyeshe ubinadamu kwamba tunamjali kama yeye anavyowajali watoto wetu.” 

“Mama Briana bwana! Maongezi yote hayo bado hujasahau tu? Kwanza sio kwamba anawajali wanangu, ni kwa sababu namlipa, tena namlipa pesa nyingi sana, hatakaa alipwe hivyo popote atakapoenda.” “Piga bwana Nyange. Acha kunizungusha.”

“Lakini naona uzito kuongea naye, kwa niliyomfanyia juzi.” “Nilijua tu, ndio maana unanizungusha. Sasa hivyo ndio vizuri hutarudia tena. Wewe piga simu, uanze na salamu uone itakavyokuwa rahisi.” “Ukimpigia wewe mama Briana nakuahidi sitarudia tena mke wangu.”

“Wewe piga umpe pole ya mgonjwa, mwambie kesho tutaenda kumuona mgonjwa halafu muombe jumatatu arudi kazini. Nakuomba mpenzi wangu.” “Ujue Nyange utaishia kumwendesha huyo mtoto mwenyewe! Wewe endeleza ukorofi wako tu.” “Ndio maana nakupenda mke wangu.” “Una kazi yakuharibu halafu unataka nikusafishie kila siku.” “Kwanza umejiona ulivyopendeza, mke wangu?” “Sitaki.” Nyange alinza kucheka. 

Japokuwa baba yake alikuwa akihangaika naye sana, kwa uzuri wa binti yake ambao sio wa sura tu, hata umbile lilikuwa kama mama yake. Tokea mtoto mdogo, tayari umbile lake lilishajigawa vizuri sana na kadiri alivyoendelea kukua ndivyo alivyozidi kugawanyika vizuri na kung’aa kitu kilichokuwa kikimuweka macho Nyange akimlinda, lakini Briana alikuwa binti mtulivu sana, mpole na mwenye upendo kwa kila mtu. Hakupenda makuu kabisa kama mama yake tu. 

 Roho Ya Uharibifu Haitulii Mpaka Itimize Kusudi

Wakiwa kwenye maandalizi ya sherehe hiyo ndipo alipotokea Leah na mama yake, siku hiyo jioni wakiwa wamechoka sana. Mama Briana alifurahi sana kuwaona, kwani ilikuwa ni miaka mitano sasa hakuwa amewasiliana nao kabisa kwani mama yake alishampiga marufuku yeye na kaka yake wasikanyage       kabisa nyumbani kwao. 

Aliwatayarishia chakula na chumba chakulala. Hakuwahi kumuona mama yake akiwa mkarimu kiasi kile. Kila alipotaka wazungumzie swala lile la ugonjwa wa Leah, mama yake alisema yameisha kwani hata yeye alikuwa na makosa. 

“Nimekuja kukupa pole kwa msiba, mwanangu. Eliah alinipigia simu, kunitaka nihudhurie mazishi, lakini nilikuwa mgonjwa. Unisamehe mwanangu, najua kwako huu msiba ni mkubwa sana, kwani mzee Nyange alikuwa karibu sana na wewe kuliko mtu yeyote” “Hamna neno mama yangu. Nimefurahi sana umekuja mama. Karibu sana. Nilikuwa na hamu na wewe.” 

Kwa namna ya ajabu ila ya upendo sana, kwa mara ya kwanza mama yao akawa karibu sana na mama Briana. Leah naye alionyesha mabadiliko makubwa sana, aliwapenda watoto wote bila ubaguzi. Alibadilika sana mpaka mama Briana alianza kuingiwa na wasi wasi. 

“Kazi vipi Leah!?” “Nilipata matatizo kidogo kazini, nimesimamishwa kwa muda. Lakini najua kila kitu kitaenda sawa.” “Tangia kipindi kile hawajakurudisha kazini?” “Sikurudi tena pale, nilitafuta kwengine.” Mama Briana aliamua kunyamaza asiendelee kudadisi. 

Kila siku usiku mama yao aliomba wakusanyike pamoja waombe kama familia! “Namjua mzee Nyange alivyokuwa mcha Mungu. Hii pekee ndio jinsi ya kumuenzi baba yenu.” Hayo ni maneno ya mama Eliah kila walipokuwa wakikutana kuomba usiku. Ni kweli mama Briana na Nyange waliona mabadiliko makubwa kwa mama Eliah na Leah na kubaki wakishangaa. 

 Sio vyote ving’aavyo, ni dhahabu!

Siku hiyo ya sherehe ya mtoto wao, mama Briana aliamshwa na harufu nzuri sana ya supu. Mama Eliah ndiye aliyekuwa ameandaa kifungua kinywa hicho. Mama Briana na Leah walichukua ujuzi wakupika kutoka kwa mama yao. Ilikuwa mama yao akiwa jikoni nilazima utakula tu, hata kama huna njaa. 

Nyange naye alishuka na kukaa mezani na mkewe na kuanza kula. “Mama Sonia njoo tule bwana. Punguza shuguli.” Mama Briana aliongea huku akiendelea kufaidi supu yake na chapati. “Nilishakunywa chai. Inatosha.” Nyange na mkewe walifurahia sana kile kifungua kinywa. 

“Mbona nyinyi hamli?” Nyange alimuliza mkwewe na Leah. “Tushakula wakati nyinyi mmelala.” “Na kweli leo tumechelewa kuamka sababu ya stori za mama Briana usiku. Hanyamazi!” “Nyange wewe!? Ni mimi au wewe ndio ulikuwa ukiongea?” “Mkubwa jalala bwana, mimi nakubali yote.” Wote walicheka kwani walijua Nyange ndio alikuwa muongeaji sana kuliko mkewe. 

Kama kawaida ya Nyange uchekeshaji, kila mtu alikuwa akicheka wakati wao wakila. 

 **********************

Kadiri muda ulivyozidi kwenda Nyange alianza kupooza na Mama Briana alianza kulalamikia kichwa na taratibu alianza kuwashwa mwili mzima! “Au ukaoge halafu upumzike kidogo kabla ya kwenda kwenye sherehe?” “Si tumeoga wote Nyange jamani! Unataka nikaoge tena?” “Sikumbuki kukuona ukipaka sabuni.” “Nyange! Heshima yangu.” Nyange alicheka lakini mama Briana alizidi kujikuna mwili mzima. 

Hali ilizidi kuwa mbaya, kila mtu alimsaidia kumkuna. Alianza kulia kichwa kinamuuma. Wakati Nyange anafikiria kumpeleka hospitalini, mama Briana alianza kuvua nguo palepale sebuleni. “Vipi tena?!” Mama Sonia alikimbia ndani kwake kuleta kitenge ili amfunike. Lakini akiwa anatoka chumbani na kitenge mkononi, mama Briana naye alianza kukimbilia nje akiwa uchi. 

“Nini kinaendelea jamani?!” Nyange alimkimbilia mkewe, lakini tayari alishatoka getini. Josh alitoka na yeye ili kumkimbiza, bila kupoteza muda Mama Sonia naye akiwa na kitenge chake mkononi alifuata nyuma. Mlinzi aliyekuwa akilinda hapo mchana, alikuwa na mafunzo ya kiaskari. 

Nyumba ya Nyange ilikuwa ikilindwa mchana na usiku na kampuni ya ulinzi. Na yeye alitoka na mbio kumkamata mama Briana. Alishafika mbali sana, na kila mtu alikuwa akimshangaa kwa kuwa alikuwa uchi kabisa.

Nyange aliwaomba wamshike ili yeye arudi kuchukua gari. Mama Sonia alijaribu kumfunga kitenge angalau chini tu, kwani alifanya fujo sana. 

Walimkimbiza hospitalini. Lakini alikuwa amechanganyikiwa kabisa. “Mungu wangu ni nini kimempata mpenzi wangu?!” Kila mtu alikuwa kwenye hali ya mshituko na huzuni sana. Mama yao ndio alikuwa akilia kupita kiasi. 

Baada ya majuma mawili kupita mama Briana akiwa hospitalini bila nafuu, ilimbidi ahamishiwe hospitali ya vichaa Mirembe, Dodoma. Kwani daktari aliwaambia kwa hali aliyonayo nilazima akahudumiwe hospitali ya vichaa kabisa. 

**********************

Nyange alikuwa kwenye mshituko mkubwa sana. Maisha yalimbadilikia gafla tena mbele ya macho yake. Ule uchungu wakufiwa na wazazi wake ndipo ulipoongezeka. Alitamani kama baba yake angekuwepo labda angemuombea mkewe akapona. Kwa mara ya kwanza maishani mwake ndipo alipoona umuhimu wa baba yake, maishani mwake. 

Wakati wa uhai wa maisha ya baba yake mara nyingi walikuwa kwenye mikwaruzano na mama mtu akimkingia mwanae kifua. Mzee Nyange alitamani sana baba Briana afuate mambo ya Mungu kwa karibu, kitu kilichomshinda kabisa baba Briana, hata kuombea tu chakula ilikuwa ni shida. 

Nyange aligeuka kuwa kama mgonjwa kwa mawazo. “Mungu wangu? Naishije humu ndani bila mama Briana?” Hilo ni swali lililokuwa likimuumiza sana Nyange, hakuacha kujiuliza mchana na usiku. Marafiki zao wengi waliosikia ule mkasa walifika nyumbani kwao kumfariji. “Pole sana Nyange. Lakini wewe ndio umebaki, lazima uwe jasiri sababu ya familia, tena ushukuru Mungu, mdogo wake na mama yake wapo. Watakusaidia sana.” Rafiki mkubwa wa Nyange, Mr Chao, alikuwa akimfariji siku hiyo alipokuja na yeye kumpa pole. 

“Hakuna anayeweza kuishi na mimi vizuri kama Penninah. Hakuna.” Nyange alijibu huku ameinamisha kichwa na kukishikilia kana kwamba kisianguke, mbele ya mama mkwe wake, Leah na kila mtu aliyekuwepo pale. Tena wote walisikia ila walinyamaza tu. 

 **********************

Briana alishakuwa binti wa miaka tisa lakini bado hakuwa akiweza kulala bila Kana. Hakujua maisha mengine mbali na Kana. Waliendelea kufanya kila kitu pamoja, na Kana ndio alikuwa msiri wake mkubwa. Wakati wote walipotaka kujua kitu kutoka kwa Briana, aliulizwa Kana. 

Kwani wakati wote wanapotaka kumfurahisha Briana na kujaribu kumdadisi ni kitu gani angependa anunuliwe, wakati wote hujibu ‘kitu chochote tu, nitapenda.’ Hakuwa mpenda makuu, lakini Kana alijua jinsi ya kuongea naye na alimjulia sana Briana. 

Kipindi chote hicho Briana alijua wazi kila kitu kinachoendelea. Alikuwa akilia sana. Mama Sonia na Kana ndio walikuwa faraja yake kubwa, kwani baba yake mwenyewe alionekana anahitaji faraja zaidi. 

Kwa kuwa alikuwa akilala na Kana, alimuomba wahamie chumbani kwa mama Sonia ili angalau walale naye chumba kimoja. Mama Sonia aliwapenda sana kina Briana kama mama yao mzazi. Kwa hiyo chumba kimoja kulikuwa na vitanda viwili cha Kana na Briana, halafu mama Briana alilala peke yake kwani Brayan tokea mtoto alikuwa akilala chumbani kwake, peke yake. 

 **********************

“Ninahamu na mama Briana.” Briana aliamka usiku huo akiwa analia sana. Baba yake alikuja kumchukua. Akambeba mpaka chumbani kwake. “Mama atarudi Briana. Huna haja yakulia. Naomba uwe mvumilivu. Sawa Bree?” Briana alikuwa copy ya mama yake, ni kama Penninah alijizaa mwenyewe. Si uzuri tu wa Briana uliomfanya Nyange amlinde kuliko pesa yake, bali hata tabia zilikuwa kama za mama yake, kitu kilichokuwa kikimuogopesha pia Nyange. 

Aliona ni rahisi sana binti yake kuonewa. Kwa hiyo wakati wote yeye Nyange ndiye aliyekuwa akimkingia mwanaye kifua. Kila mahali, alipokuwa Briana, Nyange naye alihakikisha na yeye yupo ili mwanae asionewe. 

Ndio maana alijulikana shuleni kwa mwanae kama Kaka Mkuu wa hiyo shule. Wanafunzi wote na walimu walimjua Nyange na mwanae. Mara zote, kwa muda tofauti tofauti alipita shuleni kwao kuangalia usalama wa mtoto wake. Kila wakati mama Briana alikuwa akimuuliza mumewe, “Hivi huyu Briana ataolewa kweli?”  

Kila Nyange alipokuwa akimwangalia Briana usiku ule wakati amelala naye alimkumbuka mkewe. Nyange alikesha akilia kwa uchungu na hofu. Hakujua jinsi ya kufanya kumsaidia mkewe. 

Hakuwa mtu anayemjua Mungu hata kidogo na kila alipoenda kumtazamahospitalini hapakuwa na dalili yeyote yakupona mama Briana. 

Kanisani kwenyewe hawakuwa wakienda kabisa. Kwa kuwa alikuwa na kazi nyingi sana kuanzia jumatatu mpaka ijumaa, tena akirudi inakuwa usiku na anakuwa amechoka sana. Hata wakati mwingine ilimlazimu kwenda kazini hata siku za jumamosi. Kwa hiyo siku za jumapili alizitumia na mkewe tu. 

Walijifungia chumbani na mkewe kutwa nzima, jioni ndipo utakapo muona Nyange anatoka nakuanza kuongea na watu wengine na kucheza na watoto. 

Nyange alishatangaza kuwa siku ya jumapili ni ya mama Briana. Waliangalia tv hukohuko chumbani kwao na kuletewa chakula hukohuko. Inapotokea haendi kazini siku za jumamosi, Nyange alishinda sebuleni na watoto akicheza na kumtania kila mtu pale ndani na kutumia siku hiyo ya jumamosi pia kumsaidia Josh usafi wa nje na mambo mengine mengi lakini sio siku ya jumapili ya mama Briana. 

 Mtumwa anapoongoza..

Kwa kuwa safari za Dodoma, Mirembe hospitali zilikuwa nyingi sana kwa Nyange, taratibu Leah akaanza kushika usukani pale ndani. Yeye ndiye aliachiwa pesa za matumizi. Kwa hiyo aliamua kupikwe nini na chakula kiliwe saa ngapi. Taratibu fujo zikaanza. 

“Ndio maana dada yangu alichanganyikiwa. Mmejaa sana humu ndani! Hakuna hata pakukanyaga jamani! Watoto wengine hata hawajulikani wanani na wenyewe wapohumuhumu ndani! Kwanza inabidi nianze kukata matumizi. Naona pesa haikai kabisa!”

“Siwezi kununua umeme kwa pesa yote hii! Eti mpaka vijakazi nao pia, nguo zao zinafuliwa na mashine? Kwa nini? Hamna mikono? Kuanzia leo, nguo zinazofuliwa kwa mashine ni zetu, Nyange na watoto walio zaliwa na dada yangu tu, sio kila mtu analeta minguo yake humu ndani. Ndio mwanzo wakuambukizana magonjwa.”

“Na chakula kuanzia leo, mimi ndio nitakuwa nasimamia. Sio kila mtu anajiamulia kupikwe nini na kwa wakati wake, halafu anapika. Nyumba gani eti mpaka wafanyakazi wanakula milo mitatu!? Nalo hilo pia nilakutizama.”

“Halafu eti mimi nile kuku na mfagizi pia anakula kuku!? Ndio maana hatuheshimiani humu ndani.” Hakuna aliyemjibu Leah hata kidogo wote walibaki kimya wakimsikiliza siku hiyo ya jumamosi asubuhi, pale Nyange alipoondoka tu, kuelekea Dodoma kumuona mkewe. 

 **********************

Leah alitayarisha chakula cha mchana, akaweka mezani. Alimwita Briana na Brayan tu kwenda kula. Briana alikaa pale mezani akiwa ameinamia sahani yake bila kula. “Kula sasa na wewe, au umeshiba?” Leah aliongea kwa ukali. “Siwezi kula bila Kana.” Briana alijibu kwa hofu sana huku machozi yakimtoka. 

“Naona umeshiba wewe. Haya nyanyuka, kwenda jikoni huko!” Leah akamfukuza Briana pale mezani bila ya chakula, Briana alitoka pale na kwenda kwa Kana aliyekuwa amekaa jikoni na Mama Sonia. 

“Ungekula tu Briana. Utakaaje na njaa?” Kana alimuongelesha kwa sauti ya upole sana. “Usilie sasa, twende tukacheze kule alipo Josh.” Kana akamshika mkono, wakati wanatoka tu pale jikoni Leah akaingia akiwa amejawa na hasira sana. 

“Tena kuanzia leo, wewe Kanu sijui Kanini, hakuna kulala humu ndani. Umenielewa wewe mtoto? Kuanzia leo utakuwa unalala na Josh.” “Siwezi kulala bila Kana, auntie.” Briana alijibu kwa unyonge sana huku akiendelea kulia. “Naomba   usimtoe      Kana          humu         ndani.” 

“Nitakupiga Briana wewe. Unajibizana na mimi? Wamekulea vibaya sana wewe mtoto. Huna adabu hata kidogo! Nanitakufundisha adabu. Mkubwa anaongea na wewe unaongea! Nikikufuata hapo!” Mama Sonia akacheka. Na kumwambia. “Huna utakalomfanya Leah. Nenda Briana.” 

“Utanifanya nini?” Leah akamsogelea mama Sonia   kwa   jeuri sana akimuuliza. “Nakwambia hivi, huna utakalomfanya Briana, acha kumtishia mtoto na kumnyima raha bure.” Mama Sonia alitoka na yeye nje na kumuacha Leah amesimama palepale jikoni. 

 **********************

Uchungu wakuuguliwa na mama yake, na baba yake kutokuwepo kwenye maisha yake kumtetea, uliongezeka mara dufu kwa Briana. Tangia Kana afike nyumbani kwao wakiwa wadogo sana, hakuwahi kulala na mtu mwingine yeyote isipokuwa Kana. Hata kule kuamka tena usiku akilia, kuliacha kabisa tokea Kana aanze kulala naye. 

Kitendo cha kufukuzwa Kana mle ndani na kuhamishiwa chumbani kwa Josh, ilikuwa ni adhabu ambayo Briana asingeiweza kuihimili hata kidogo. Alikuwa akilia usiku kucha akimtaka Kana. Hakuweza kulala bila Kana. 

Chakula cha mchana kwa Josh, Kana na mama Sonia kilifutwa kabisa, waliruhusiwa kunywa chai asubuhi, akiwepo Nyange na chakula cha usiku anaporudi Nyange. Hakuna aliyeruhusiwa tena kukanyaga stoo ya vyakula mle ndani mpaka kwa ruhusa ya Leah. Kwanza alifunga mlango huo na kutembea na funguo zake. 

**********************

Chuki ilimtawala sana Leah, alikuwa akiwinda kupiga watoto wa dada yake bila sababu ya msingi. Kila alipoona mama Sonia hayupo karibu nao aliwaita ndani na kuwatafutia sababu ya kuwachapa, ilimradi tu kuwanyanyasa hao watoto. Aliwapiga kwa makosa hata yasiyo ya msingi! 

Siku moja mama Sonia akiwa nje alisikia glasi imeanguka, akakimbilia ndani akihofia Brayan asije kuwa karibu, akajikata. Alipoingia tu akakuta Leah anampiga Brayan kofi kubwa sana. Mama Sonia alibaki ametoa macho akitetemeka. “Una wazimu wewe Leah? Unawezaje kumpiga mtoto mdogo kiasi hicho? Tena kwa kosa la kitoto hivyo!? Hapo unanitafuta kabisa Leah. Fanya mambo yote lakini sio kuwapiga hawa watoto. Brayan ni mdogo sana kuanza kumpiga. Siwezi kukubali.” Mama Sonia alienda kumchukua Brayan akiwa analia. 

“Wewe unaongea kama nani?” Bibi mtu akauliza. “Utanijua mimi ni nani, pale mwanao atakapo mshika tena mtoto hata mmoja na kumpiga.” Mama Sonia alimchukua Brayan na kuondoka naye na kuwaacha wote kimya. Mama Eliah alikuwa akimuungamkono Leah mwanae kwa kila analofanya. 

 **********************

Nyange naye alibadilika sana. Ilikuwa ngumu kujua kama ni mawazo ya mkewe au kuna laziada! Hakuwa akiongea, kabisa. Hata shuleni kwa Briana aliacha kutokea. Hakujua wala kujali mambo ya watoto wake hata kidogo. Hakujishugulisha na kula yao, soma yao wala furaha yao. 

Mahusiano ya Nyange na kila mtu yalikatika kabisaa. Leah alishakataza wageni mle ndani akidai wanamsumbua shemeji yake ambaye yupo kwenye matatizo. Kila mgeni aliyewatembelea, Leah ndiye aliyetoka nje kuongea nao na kuwaomba waondoke hata ndani wasiingie. Alipiga marufuku wageni kukaribishwa ndani, wote waliishia nje. 

Nyange hakuwa akiongea na yoyote zaidi ya Leah aliyekuwa akimsubiria kwenye makochi arudi ili ampe mashitaka ya mle ndani. Kila Nyange alipoingia ndani ya nyumba yake, alipokelewa na malalamiko ya uongo kutoka kwa Leah na kama haitoshi alimiliki mpaka simu ya Nyange.

Nyange alianza kuamini kila kitu anachoambiwa na Leah. Maisha yalizidi kuwa magumu sana kwa kila mtu pale ndani kwenye Jumba la Nyange. 

Leah na Mama yake walijaa kwenye hiyo nyumba hapakuwa napakukanyaga wala pakukaa. Masimango, kelele na matusi ya waziwazi yaliendelea ndani ya hiyo nyumba. Mama Sonia alivumilia sababu ya wale watoto waliokuwa wakinyanyaswa mchana na usiku na mama yao mdogo. 

**********************

“Daah! Natamani kuondoka mama!” Josh alikuwa akiongea na mama Sonia. “Unaenda wapi? Na hawa watoto tunamwachia nani? Lazima kuvumilia Josh. Mimi mwenyewe natamani kuondoka lakini kila nikikumbuka wema wa Nyange na mkewe, siwezi kuwaacha hawa watoto wanateseka.” “Lakini Nyange amebadilika sana. Unajua amenipiga sana jana pale nje.” Machozi yalikuwa yakimtoka Josh. “Kwa nini?!” “Leah amemwambia alinituma, nikakataa. Wakati sio kweli mama!” Mama Sonia aliumia sana.

“Miaka yote nimeishi nao hapa, Nyange hakuwahi hata kunikaripia! Tulikuwa tukiheshimiana sana na Nyange.” “Naomba umsamehe tafadhali Josh. Naomba usiondoke. Akili zile sio za Nyange.” “Unamaanisha nini?” “Siwezi kukwambia zaidi, ila naomba uvumilie tu.” “Mpaka lini mama? Huu ni mwezi wa tatu silipwi mshahara. Nitafanyaje mama yangu? Na mimi nina maisha yangu. Nategemewa kijijini. Haya, chakula chenyewe hatupewi, nafanyaje kazi na njaa mama?”

“Hata mimi silipwi Josh. Ningekuwa nalipwa ningekupa zangu ili tu ubaki usiondoke. Tutawatesa sana hawa watoto tutakapo ondoka. Naomba uvumilie. Kumbuka wema wa mama Briana tafadhali. Angalau Briana yupo na Kana, lakini Brayan amekuzoea sana wewe. Ataumia sana ukiondoka.” Josh alikubaliana na mama Sonia wakaamua kukaa hivyohivyo kwa mateso. Kila walipo kuwa wakikumbuka wema wa Mama Briana, waliona unazidi mabaya ya Leah na Mama yake. 

 **********************

Leah ndiye aliyemuhudumia baba Briana kwa kila kitu. Kuanzia kumpikia chakula, kumpangia nguo za kazini kama alivyomuona dada yake akifanya na pia alimsubiri Nyange atoke kazini jioni wale naye. 

Safari za Mirembe, Dodoma ziliisha kabisa kwa Nyange. Hakuwa hata akikumbuka kwenda kumuona mkewe. Leah alikuwa akimbembeleza Nyange kama mtoto mdogo. Mara amvue viatu na soksi, amkate kucha, na Nyange naye hakuwa akibisha kabisa. Alitulia kama yote hayo alikuwa akifanyiwa na mama Briana!

Muda mwingi alipokuwa nyumbani, Leah alimbana sana. Alisha waambia watoto, baba yao anaporudi nyumbani waache kumsumbua kabisa, wakae naye mbali kwani anakuwa amechoka sana, anahitaji muda wa mapumziko. 

Kwa hiyo kila Nyange anaporudi nyumbani alikuwa na Leah tu. Alimpokea mizigo yake na kutangulia mpaka chumbani kwa shemeji yake na dada yake. Na huo muda anapokuwa na Nyange huko chumbani, aliutumia kuongea mambo mengi ya uchonganishi na ndipo Nyange anapotoka huko anakuwa kama simba kwa kila mtu isipokuwa Leah tu. 

Mapenzi ya Nyange yaliahamia kwa Leah, hakuwa akisikia lolote lile ila Leah. Aliyetaka kumuona pale ndani ni Leah tu sio mtu mwingine yeyote. Simu za kumjulia hali Briana ziliahamia kwa Leah. Inapotokea ametingwa na kazi nyingi ofisini, alimpigia Leah simu kumuomba asilale mapema amsubirie mpaka amuone. 

Briana alikuwa na hamu sana na daddy yake. Siku moja akaamua amsubirie angalau amsalimie tu, kwani ilikuwa ni shida sana kumuona Nyange. Lakini siku hiyo Nyange alichelewa kidogo. “Kwa nini tusiende kulala Briana, halafu kwa kuwa kesho kutwa ni jumamosi huendi shule, kesho unaweza kumsubiria tu daddy mpaka atakaporudi. Utasinzia kesho darasani.” 

“Siwezi. Ninahamu sana na daddy. Naomba tumsubiri tena kidogo.” Mama Sonia alibaki kwenye meza ya chakula akiwa amempaka Brayan, aliyekuwa akisinzia, huku akimsubiria Briana aonane na baba yake, wakalale. Leah alikuwa amekaa kwenye makochi na mama yake. Josh na Kana nao walikuwa wamekaa upande mwingine kabisa wa sebule. 

Mara mlango ukafunguliwa, wote walijua ni Nyange, Briana aliyekuwa amekaa pembeni ya mama Sonia alisimama kwa haraka sana. “Daddy!” Kwa sauti ya unyonge lakini iliyojaa furaha, Briana alisimama akimuelekea baba yake. Kama mshale, Leah naye akasimama na kumkimbilia Nyange. 

“Vipi Nyange?” “Pole sana Leah, nachukia kukutesa, unakaa macho ukinisubiria! Kwa nini usihamie tu chumbani kwangu ili hata kama nikichelewa kurudi angalau usiku niwe nakuona?” “Wazo zuri Nyange.” Bila kuzungusha Leah alikubali palepale mbele za watu wote. 

Wote walishituka sana kasoro mama Eliah alicheka huku akitingisha kichwa kama akiafiki. “Hongera sana Leah.” Mama Eliah alisema kwa sauti ya chini kidogo lakini kila mtu alisikia. “Asante sana mama. Asante.” Leah alimgeukia mama yake nakumshukuru kwa kumaanisha kabisa. 

Kwa mshituko mkubwa sana mama Sonia huku akiwaangalia Leah na mama yake wakipongezana, akachukua watoto wote na kuwaambia wakalale. Taratibu Briana aligeuka huku machozi yakimtoka na kuingia chumbani kwa mama Sonia, kwani Nyange alikuwa ni kama hakuona mtu yeyote pale sebuleni ila Leah. 

Alimkumbatia Leah. “Umekula sasa?” Nyange akamuuliza kwa kujali. “Siwezi kula bila wewe Nyange, nilikuwa nakusubiri.” “Asante Leah kwa kunijali.” Siku zilizidi kwenda bila ya Nyange kuulizia hata hali za watoto wake au hata kuonyesha dalili ya kuwa ana watoto maishani. Briana alishakata tamaa na baba yake akabakia kumuwaza mama yake tu. 

 **********************

 “Mbona kama namsikia Bree wangu analia jamani?” Sonia alibahatisha kumkuta mama yake na watoto siku hiyo usiku alipopiga simu kuwasalimia. “Yupo sawa tu.” Mama Sonia alijibu kwa woga. Wakati wote alihakikisha Sonia haongei na watoto kabisa ili asijue kinacho endelea. 

Kila alipokuwa akipiga simu baada ya mama Briana kuugua alikimbilia sehemu ambayo watoto hawapo ili wasijue kama anaongea na Sonia. Na kila Sonia alipoomba kuongea nao, mama Sonia alitafuta sababu ya uongo ili wasiongee na Sonia. 

“Nipe niongee naye.” “Wanataka kulala Sonia. Kwa nini usipige wakati mwingine?” “Lakini mbona namsikia kama analia?! Atalalaje huku akilia? Kwa nini Kana hambembelezi au Nyange mwenyewe yuko wapi?” Sonia alijua watu wanaoweza kumtuliza Briana ni Kana na Nyange mwenyewe. 

Mama Sonia akanyamaza. “Mama?” “Briana ametulia.” “Kwa nini hutaki niongee naye?!” “Sio kwamba sitaki kukupa uongee naye, ni usiku sana sasa hivi wanatakiwa kulala mapema, kesho shule.” “Tokea lini Briana analala na wewe chumbani kwako na sio chumbani kwake na Kana?” Mama Sonia akatulia. 

“Mama? Unanisikia!?” “Ngoja nikupe Briana umsalimie. Lakini usimuweke sana, ili alale.” Huku akiwa na wasiwasi mama Sonia akamsogelea Briana. “Sonia anataka kukusalimia.” Briana alifurahi sana. “Vipi Briana? Mbona unalia?” “Namtaka Kana, halafu nina hamu na mama Briana.” “Mama Briana?! Kwani yuko wapi?” “Anaumwa, auntie.”“Hebu nipe mama Sonia.” Briana alirudisha simu kwa Mama Sonia akiwa bado analia. “Mbona sijamuelewa Bree.” Mama yake alibaki kimya. 

“Mama?” “Sikutaka kukwambia Sonia.” “Kuna nini?” Kwa mara ya kwanza Mama Sonia alianza kulia kwa uchungu sana kama aliyekuwa amebanwa        na     kitu   na     kukosa       pakukitolea. 

“Mama?” “Mama Bree, amechanganyikiwa kabisa, yuko Dodoma hospitali ya vichaa. Leah ndio mama mwenye nyumba. Watoto wananyanyaswa sana.” “Nyange yuko wapi?” “Kawa kama mjinga! Hela zote anampa Leah. Hana analosikia wala kuelewa.”

“Hivi analala naye hukohuko chumbani kwao, na mama yao yupo humuhumu ndani. Kelele kuanzia asubuhi mpaka tunaachana. Kana amefukuzwa shule sababu ya ada. Leah alipewa pesa ya kwenda kulipia ada ya Kana na Briana. Kalipa ya Briana tu.” “Kwa hiyo mwanangu haendi shule?”

“Ni mwezi sasa?” “Kwa nini hukuniambia mama jamani!?” Sonia alianza kulia. “Niliogopa Sonia, nilijua nikikwambia utasema tuondoke, halafu Briana na Brayan watabaki na nani? Wana nyanyasika sana hawa watoto. Hivi dereva wa Briana alishafukuzwa kazi, gari yake anatumia Leah.”

 “Sasa Bree anaendaje shule?” “Anafuatwa na basi la shule. Yaani Sonia ungemuona huyu mtoto akienda shule ungemuhurumia. Analia sana, kuanzia anaenda shule mpaka anarudishwa hapa.”

“Amepewa barua awaletee wazazi wake, imebidi niifungue tu nisome. Walimu wanasema hasomi kabisa akiwa shule. Analia siku nzima, anamtaka Kana. Wanasema Nyange hapokei simu, kama kuna namba nyingine ya simu wapewe, ili waweze kuwasiliana na wazazi wake. Amekonda kama mgonjwa! Ana kazi ya kulia mpaka anaporudi hapa ndani na kukutana na Kana ndio ananyamaza.” Mama Sonia akajikuta anashindwa kujizuia. Machozi yaliendelea kumwagika. 

“Mungu wangu mama! Huyo mtoto anapanda basi?! Nyange anajua?” “Nakwambia hana analoelewa. Nyange huyu sio unayemjua wewe. Hata kujua sura za wanae siku hizi zinafananaje, hazijui kabisa. Kwanza sijui hata kama anajua kama ana mke anaitwa Penninah na kama alizaa naye watoto. Haelewi chochote.”

“Hivi tumepigwa marufuku na Leah kukaa sebuleni kabisaa. Kwa hiyo ni ngumu hata kumuona huyo Nyange mwenyewe. Alikuwa akienda kumuangalia mkewe huko Dodoma, siku hizi hata hamtaji jina lake tena.” Sonia alianza kulia tena.

“Kwa hiyo mwanangu haendi shule tena?” “Josh amemtafutia shule ya kata, amepata. Ataanza jumatatu.” “Shule ya Kata, mama jamani!?” Sonia aliendelea kulia kama amekatwa kidole. 

 **********************

Asubuhi hiyo ya jumamosi aliwahi kazini na kwa kuwa ilikuwa nusu siku, alipotoka alikimbilia moja kwa moja kwenye hospitali ya Mirembe. Hakuamini baada yakuonyeshwa alipofungwa mama Briana. 

Ni kweli alikuwa amechanganyikiwa na walimfunga ili asijipigize. Sonia alipatwa na mshituko mkubwa sana, alibaki akilia bila kujua cha kufanya. Alitamani mama yake na mwanae waondoke pale, lakini mama yake alishamkatalia kabisa kuwaacha watoto wa mama Briana peke yao. 

Kila wakati na yeye alikumbuka jinsi Nyange alivyomkabidhi binti yake siku ile alipokuwa akivalishwa pete ya uchumba na Sam. Alijua anajukumu kubwa la kufanya kwa hao watoto. Alibaki akijiuliza cha kufanya mchana huo baada ya kutoka hospitali bila jibu.  

 **********************

Siku hiyo Briana alirudi kutoka shuleni akiwa na homa kali sana. Moja kwa moja alienda chumbani kwa Josh kumtafuta Kana. Aliingia na kukaa pembeni yake akilia. “Naumwa sana kichwa, Kana.” “Sababu ya kulia Briana. Usilie bwana. Kila kitu kitakuwa sawa. Mama ameniambia na mimi nitaanza shule muda sio mrefu, wote tutakuwa tukienda shule.” Kana alijaribu kumfariji. 

“Twende ndani tukamwambie mama ili akupe dawa. Usilie. Sawa?” Briana alitingisha kichwa kukubali na Kana alimshika mkono mpaka kwa mama yake. Mama Sonia alimshika, homa ilikuwa kali sana na hakuwa na nguvu. 

Akamfuata Leah sebuleni akiwa anaangalia tv na mama yake. “Briana anaumwa sana. Homa ipo juu.” “Si anajiliza hovyo. Ataachaje kupatwa homa?” “Naomba pesa nimpeleke hospitali, angalau wamwangalie, tujue tatizo ni nini?” “Si nimeshakwambia tatizo ni nini? Au unachotaka ni pesa ili uzitumie wewe?” “Basi mpeleke wewe huko hospitali ili akatibiwe. Mimi shida yangu apone tu huyu mtoto.” “Nina mambo mengi yakufanya, naomba usinipangie majukumu mengine yasiyonihusu.” Leah alijibu kwa jeuri akasimama kama anayetaka kuondoka. 

“Basi naomba hata pesa kidogo Leah, nikamnunulie dawa yakushusha homa.” Leah alifyonza nakuondoka. Mama Sonia alirudi chumbani alipokuwa amewaacha watoto wote, na kuamua kumuogesha Briana, kisha akamuomba Kana akae naye kitandani kwa muda angalau alale kidogo. Kwa kuwa Kana alikuwepo karibu, Briana alipitiwa na usingizi muda uleule. Mama Sonia alibaki akiwaza cha kufanya bila jibu. 

Aliogopa sana kumwambia Sonia kama hawalipwi mshahara na hata chakula chenyewe pale ni cha shida. Alijua kitakachofuata ni Sonia kuja kumchukua mwanae na Briana kuendelea kuteseka zaidi. Aliendelea kumkanda na maji lakini homa ilikuwa juu sana, na Briana alionekana ni mdhaifu. 

Hofu ilimuingia mama Sonia, akaamua kwenda kuongea na Nyange. Alitoka chumbani na kukuta kila mtu alishakwenda kulala. Akaamua kwenda kumgongea Nyange lakini akatoka Leah. “Homa imepanda sana.” “Kwa hiyo nifanyaje?” “Naomba kuongea na Nyange ampeleke mtoto wake hospitali, kama wewe huwezi, Leah.” 

“Amelala. Na nina kuomba uondoke, usitusumbue.” “Kwani shida yako nini Leah jamani? Kama hutaki kwenda wewe au Nyange, nipe mimi basi hiyo pesa nichukue taksi, nimpeleke mtoto akapate matibabu!” “Huna lolote wewe mwanamke, shida yako naijua ni Nyange tu.”

“Na nina kwambia hata uking’ang’ania vipi kukaa hapa ndani, kwa kigezo unawalea hawa watoto, hutampata Nyange hata kidogo. Nyange ni wangu sasa hivi. Hatakaa akupende hata ukijipendekeza vipi.” Wakati Leah anaendelea kugomba na kutukana, Nyange naye akaamka. 

“Kuna nini?” “Si huyu Ajuza anataka kulala na wewe. Kinaona nafaidi sana.” Mama Sonia aliondoka huku akitokwa na machozi. “Twende tukalale mpenzi wangu.” Nyange alimvuta kiuno Leah na kumtupia kitandani. “Leah wewe ni mzuri sana.” Leah alicheka kimahaba huku akimbusu Nyange. “Mimi ni mzuri kuliko mama Briana?” Nyange alishituka sana baada yakusikia jina la mama Briana. Alibaki kama anawaza bila ya kupata jibu huko kichwani mwake, taratibu akamfunika Leah vizuri na kurudi kulala.  

 **********************

Leah aliona haitoshi kunyang’anganya gari ya Briana, akaamua kumuhamisha na shule pia. “Mtoto mdogo anasoma shule ya msingi na kulipiwa ada inayoweza kununua kiwanja na kuweka msingi!? Kwa kipi mno? Anachosoma huko ni nini? Mbona watoto wengine wanasoma shule za Kata na wanafaulu tu? Tena waende na miguu kwanza hapo nikaribu tu.” 

Hakuna kitu kilichomfurahisha Briana kama hicho. Leah akidhani ana mkomoa Briana, lakini Briana alikuwa akifurahia kutembea kwa miguu kwenda shule akiwa na Kana. Wala hakujali mazingira aliyokutana nayo pale kabisa. 

Ilikuwa ni ngumu kuamini kama ni Briana yuleyule wa Nyange aliyekuwa akisoma shule ya kimataifa pale jijini ndiye yuleyule aliyekuwa akisoma shule ya Kata tena anaenda na fagio shuleni na kidumu cha maji cha kumwagilizia maua tena akitokea katika Jumba la kifahari sana. 

Kwa muda mfupi aliojiunga na shule ile, tayari alisha jifunza kufagia kiwanja chake na Kana akimsaidia kubeba maji na kumwagilizia maua yake, kwani hata pale Kana alishachaguliwa kiongozi. 

Kwa hiyo muda wa asubuhi Kana anapotakiwa kusimamia usafi, muda huo aliutumia pia kumsaidia Briana kufanya usafi katika eneo lake na wakati wote Briana alimaliza haraka na kusogea mstarini kusubiria kengele. 

Kwa muda mfupi aliofika kwenye shule hiyo ya msingi tayari walishajulikana kila mahali, si kwa walimu tu, mpaka kwa wanafunzi, wote waliwafahamu Kana na Briana. 

Na kwa kuwa wote walikuwa na akili nzuri sana darasani na nidhamu kwa kila mtu, walianza kuwa mfano wakuigwa.  Kila mwalimu aliwatolea wao mfano. Angalau tabasamu lilirudi usoni mwa Briana, na muda mwingi Kana aliutumia kuhakikisha Briana hana mawazo, ila anasoma vizuri, na anafaulu darasani kwao katika kila somo. 

Mama Sonia na Kana walikuwa wakiongea sana na Briana juu ya mabadiliko ya baba yake. Angalau Briana alianza kumuelewa baba yake nakuacha kuumia. Alibaki akimuhurumia baba yake. 

“Unafikiri dady atakuja kupona, halafu akanikumbuka tena mimi na Brayan?” Briana alianza kumuuliza maswali Kana wakati wanatoka shule wanarudi nyumbani. “Akipona, atawakumbuka.” Briana akatulia.

 Mti Wa Uovu Huzaa Tunda La Usaliti

Taratibu Leah alianza ukali mpaka kwa mama yake mzazi. Alikuwa akimfokea na yeye kwa kila jambo na kumtuma hiki au kile wakati yeye amekaa tu sebuleni au akitoka kwenda kuzurula na gari ya Briana. Alimuachia maagizo kibao mama yake na kila aliporudi alianza kumuuliza maswali kama mtoto mdogo huku akimgombeza. 

Mama Sonia aliishi nao kama hawaoni kabisa. Hakuchangia chochote zaidi ya kuangalia mambo ya watoto. Alinyanyua mdomo wake pale tu walipowasogelea watoto wa mama Briana, hapo ndipo aligeuka mama Sonia kuwa kama Mbogo aliyejeruhiwa na wenyewe walijua na kujitahidi kukaa na wale watoto mbali, mpaka mama Sonia anapokuwa hayupo ndipo walikuwa wakiwachapa au kuwagombesha, kitu kilichomfanya Mama Sonia kurudia kumfunga Brayan, kaka mkubwa mgongoni kila aendapo. Alihakikisha yuko na Brayan kila mahali. 

**********************

“Sijui ni hiyo hali yake ndio inamfanya hivyo!?” Baada ya kumtukana sana mama yake, mama Eliah alitoka nje nakuanza kujiongelesha kwa mama Sonia akiwa anafua. Mama Sonia hakujibu kitu chochote aliendelea kufua nguo za watoto ambazo nazo pia alishapigwa marufuku zisifuliwe kwenye mashine. 

Mama Eliah alizidi kujiongelesha hapo nje. “Si unajua kila ujauzito unakuja na vyake? Naona huu wa safari hii umemjia vibaya kweli!” Mama Eliah aliongeza. Mama Sonia alishituka sana kusikia safari hii Leah amefanikiwa kushika mimba ya shemejiyake. Lakini hakutaka kumuonyesha chochote mama Eliah, alinyamaza kimya nakuendelea kufua.

**********************

Leah alianza kutapika mchana na usiku. Nyange alijawa na furaha sana. “Asante Leah kuamua kunizalia mtoto. Nilikuwa natamani watoto kwenye maisha yangu.” Maneno ya Nyange kana kwamba hajawahi pata watoto maishani. Leah alikuwa akideka kupita kiasi. Nyange alikuwa kama amechanganyikiwa na huo ujauzito. 

Sheria za hiyo nyumba zilibadilishwa mchana na usiku. Kwa kuwa alisema anasikia kichefuchefu sana, hakuruhusu mtu yeyote hata kupita mle ndani isipokuwa Nyange tu au mpaka akuite yeye. 

Watoto hawakuruhusiwa tena kukaa ndani, sebuleni wala kula chakula ndani isipokuwa usiku wanapoingia tu kwenda kulala. “Mnachafua nyumba, halafu mkiingia humu ndani mnachafua hali ya hewa. Nyumba zima inanuka majasho yenu.” 

Mbali na usafi Josh aliokuwa akifanya ndani ya hiyo nyumba, hakuruhusiwa hata kukanyaga kabisa mle ndani jikoni. Watu wote walipoamka asubuhi hawakuruhusiwa kukaa humo ndani mpaka usiku muda wa kwenda kulala, hadi mama yake mzazi alisema anaharufu kali sana.

Kidogo Leah alikuwa na hofu na mama Sonia, kitu kilichokuwa kikimshangaza Josh. “Naona mwenzangu hufokewi sana. Afadhali yako.” Josh alimchokoza mama Sonia, wakiwa nje wanakula. “Hakuna nafuu Josh. Anajua pakunipatia ni kwa hawa watoto. Sheria zote unazosikia wanapewa watoto ni zangu, sema ananiogopa, hawezi kuniambia waziwazi. Anajua kabisa siwezi kukaa ndani kama watoto wako nje.” “Sasa haya maisha mama, yatakuwa hivi mpaka lini?” “Sina jibu lake Josh. Sijui mwisho ni nini. Lakini hata iweje sitakaa niwaache hawa watoto.” 

 **********************

Hasira juu ya watoto wa dada yake ilizidi. Shauku yake ya kuzaa na shemeji yakeilitimia, kwa hiyo alijawa na furaha kupita kiasi lakini wakati wote alitamani kama yeye tu ndio angekuwa amezaa na Nyange sio vinginevyo. 

Alitamani kama hao watoto wangekuwa wamekufa ili watoto atakao zaa yeye na Nyange ndio wawe watoto wa pekee Nyange alionao duniani. Alianza kuwatuma watoto wa dada yake hapo ndani kama vijakazi. Akiwa yeye amekaa sebuleni au amejilaza chumbani. 

Anaweza kumuita mmoja wao kwa sauti ya kawaida sana, huku akitegemea kwa sauti hiyo kwa Jumba hilo wasikie kutoka nje na kukimbilia ndani alipo yeye. Anayechelewa kufika ni lazima ampige sana na kuwatishia wasimwambie mama Sonia lasivyo atawachinja. 

Alizidi kuwachapa watoto hao, huku akiwaonya wasitoe hata chozi. Na kweli si Briana wala Brayan waliothubutu kusema kama wanapata kibano wanapoingia ndani. Kwa kuwa Briana alishajua kinachompata yeye kila akiitwa ndani, alihisi ndicho kinachompata mdogo wake kila anapoitwa ndani na yeye. 

Akawa akimuwinda. Kila Brayan anapoitwa na yeye anamfuata nyuma kwa kujificha ili Leah asimuone. Kwa hiyo aliona unyama wote aliokuwa akifanyiwa mdogo wake. Kupigwa ngumi za nguvu mgongoni au mabegani huku akimfinya sana sehemu ambazo alijua mama Sonia hawezi ona kwa urahisi. 

Wakati wote Briana alipoona mdogo wake anaruhusiwa baada ya kipigo kikali, alimchukua na kuzunguka naye upande mwingine wa nyumba na kumbembeleza. Kwa unyama ule Briana alimsihi sana Brayan asimwambie mtu. 

“Umesikia BB? Usiseme eeh, atakuumiza zaidi. Jitahidi akikuita tu, unakimbia usichelewe, sawa?” Brayan alitingisha kichwa huku akifuta machozi. Lakini Briana hakujua mateso aliyokuwa akiyapata mdogo wake anapokuwa anamuacha yeye akiwa anaenda shule. 

Wakati mwingine mama Sonia alijua Brayan anacheza na Josh, kumbe alishaitwa ndani anakula kipondo kimya kimya. Brayan alizidi kudhoofu sana, kula yake ikawa ya shida kitu kilichomchanganya mama Sonia. 

 **********************

“Mbona huna raha Mama?” Kama kawaida ya Sonia kupigia simu kwa mama yake kuwajulia hali. “Afya ya Brayan inazidi kuwa mbaya! Wakati mwingine nikimshika analia, nahisi anamaumivu hawezi kusema.” “Au alianguka?” “Sijui!” “Jaribu kuongea na Josh na Kana, waambie wawe waangaifu wakati wanacheza naye. Ukiona hali inaendelea kuwa mbaya umpeleke hospitali.”

“Naona nimpeleke tu hospitalini wakamwangalie. Huyu mtoto hayupo sawa Sonia. Akimuogesha analia kweli, na sio kawaida yake. Siku hizi chakula hali vizuri, amedhoofu sana.” “Basi nitatuma pesa ili umpeleke hospitali wakamwangalie.” Siku inayofuata Brayan aliamka kama mgonjwa kabisa, hakuwa na homa lakini alikuwa amepooza sana. 

Mama Sonia alibaki amemfunga mgongoni mwake. Kila Leah alipomwita mama Sonia alimjibu amelala, kwa hiyo afanye mwenyewe kazi zake au amtume mtu mwingine. Brayan alikaa mgongoni kwa mama Sonia mpaka mchana wakati Briana ameingia na Kana, ndipo Brayan alipoomba ashushwe. 

Akashuka na kumkimbilia Briana. “BB!” Briana akamkumbatia mdogo wake lakini alihisi anamaumivu makali kwani Brayan aligugumia. Alizoea kumwita BB kama mama Briana alivyokuwa akimwita ‘Baby Brayan’ kwa kumdekeza. Au ‘BB.’ Mpaka watu wote wakazoea kumwita BB. 

Briana akamnong’oneza ili mama Sonia na Kana wasisikie. “Amekuchapa leo?” Brayan akatingisha kichwa kukataa. “Niambie tu, usiogope sitamwambia mtu.” “Hapana. Mama alikuwa amenibeba.” Mama Sonia alihisi kuna kinachoendelea, akasogea karibu, kwa kujiiba ili awasikilize vizuri. 

“Unaumwa?” Briana aliendelea kumuhoji mdogo wake kwakumnong’oneza. BB akatingisha kichwa kukubali. “Umemwambia mama Sonia?” BB alitingisha kichwa kukataa. “Niambie mimi, sitamwambia mtu. Nini kinauma?” BB alionyesha bega la kulia mpaka kwenye kiwiko. Briana alimvuta pembeni kidogo mbali na mama Sonia na kujisahau kunong’ona. 

“Alikuumiza hapa?” Briana alimshika kwenye mkono, BB akatingisha kichwa kukubali. Mama Sonia aliwasogelea. Briana alishituka sana. “Kuna nini Briana?” Mama Sonia akauliza. “Hakuna kitu.” Briana akajibu huku amesimama mbele ya mdogo wake kama kumkinga.

Gafla wakasikia Brayan anaitwa. Mama Sonia aliona uso wa Briana na Brayan ulivyobadilika gafla kwa hofu alijua kuna kinachoendelea. Briana alimgeukia mdogo wake kwa haraka sana. “Kimbia haraka.” Kwa shida sana Brayan alikimbilia ndani. Mama Sonia alimuona Briana anamfuata kwa nyuma huku akinyata. 

Akiwa anajaribu kuunganisha yale mazungumzo ya Briana na mdogo wake, huku asira zikizidi kumpanda na machozi yakimtoka, akijua Leah anawachapa anapowaita ndani, alimsikia Briana anaita kwa nguvu huku akilia sana. “Mama Sonia! Mama Sonia! Njoo haraka anamuuwa Brayan. Msaidie.”

Mama Sonia alikimbia ndani akiwa anatetemeka kwa hasira. Alimkuta Leah amemkanyaga Brayan chini sakafuni akiendelea kumpiga kama anaua nyoka. Brayan alikuwa akitetemeka sana, huku amekakamaa hapo sakafuni na povu likimtoka mdomoni. Bibi yao alibaki ameweka mikono kichwani, bila ya kusema kitu huku ametoa macho.  

Kama Swala, mama Sonia aliruka na kumsukuma Leah mpaka sakafuni na kuanza kumpiga mfululizo kama aliyepagawa. Alimpiga Leah vibao, ngumi kila mahali bila kujali kama ni mjamzito. Aliendelea kumrarua kwa hasira huku akichana nguo zake na kumvuta nywele zake, kama anayemaliza hasira zote mwilini mwa Leah. 

Aliendelea kumkwangua na makucha kuanzia usoni mpaka mwilini kama chui huku mama Sonia akilia kwa uchungu sana. Alimpiga mfululizo bila kupumzika, ngumi, vibao, huku akiendelea kumfinya Leah. 

Briana naye aliendelea kumwita mdogo wake kwa sauti iliyojaa kilio cha uchungu. “BB? BB? Amka.” Briana aliendelea kuita kwa nguvu huku akimsukuma sukuma mdogo wake. Kelele zilizidi, ikabidi Josh na Kana nao waingie kuangalia kulikoni. Walibaki na mshangao kumkuta mama Sonia akimpiga Leah kikatili sana kama aliyepagawa, na Leah alikuwa hoi pale sakafuni akitokwa damu, akishindwa hujitetea kabisa. 

“Mama? Msaidie BB.” Kana aliita. Kama aliyeshituka kutoka usingizini, mama Sonia aliruka pale alipokuwa amepiga magoti akimpiga Leah na kumnyanyua Brayan kutoka sakafuni. “Josh! Josh!” Mama Sonia alikuwa akikimbilia nje huku akimwita Josh. 

“Nenda kaniletee taksi. Briana wewe kanichukulie mkoba wangu ndani.” Briana alikimbia ndani na mara moja akatoka. Mama Sonia aliona anachelewesha, akiwa bado amembeba Brayan aliyekuwa hana fahamu kabisa, alikimbilia kutoka getini, huku Kana na Briana wakimfuta nyuma. Alikutana na Josh akiwa anarudi na taksi njiani, wote waliingia nakumuomba mwenye taksii awawahishe hospitalini. 

Walifika hospitalini lakini Brayan bado hakuwa na fahamu. Taksii iliwasogeza karibu kabisa na mapokezi, mama Sonia alishuka kwenye taksii na Brayan mikononi mwake, akikimbilia mapokezi huku akipiga sana kelele kuomba msaada wa haraka, kila mtu alimpisha. 

Brayan alipokelewa kwa haraka na kuanza kuhudumiwa huku mama Sonia, Josh, Kana na Briana wakiwa nje wamejawa na wasiwasi na wote walikuwa wakilia. Baada ya kupata huduma ya kwanza palepale mapokezi, Brayan alizinduka wakamwita mama Sonia. Mama Sonia alibaki akilia huku amemshikilia Brayan. “Asanteni sana jamani. Asanteni.” Mama Sonia alisikika kwa sauti iliyojaa kilio cha furaha.

Alihamishiwa wodini kuendelea na matibabu.  Josh alishampigia simu Sonia, naye bila kupoteza muda, aliomba ruhusa kazini, akawahi basi la mwisho lililokuwa likielekea Dar. Alipotuwa tu jijini, moja kwa moja akaenda mpaka hospitalini. 

Alifika ilishakuwa usiku sana, alimkuta Kana na Briana wamemuegemea Josh, wakiwa wamelala na wote wakiwa na nguo za shule bila hata viatu. Sonia alilia kwa uchungu. Wote walionekana wamechoka na wamekonda sana. 

Kila Sonia alipokuwa akiwaangalia vile jinsi walivyo sasa, na akikumbuka alivyo kuwa amewaacha wale watoto mikononi mwa mama Briana wakiwa na furaha na afya nzuri, na kwa kweli walikuwa watoto wa hali ya juu, alibaki akilia. 

Josh naye alibaki akitokwa na machozi. “Nimefurahi umekuja Sonia.” “Mbona mmekaa hapa nje kwenye mbu hivi?” Sonia akauliza. “Mama yupo wodini na mtoto, sisi tumefukuzwa. Haturuhusiwi kukaa huko ndani wote, mpaka tena kesho asubuhi. Na Briana amekataa kabisa kurudi kwao bila mama Sonia.” “Poleni sana.”

Taratibu Sonia aliwaamsha hao watoto, walipoamka na kukutana na Sonia, walifurahi sana. Briana alimkumbatia kwa muda mrefu Sonia huku akilia kwa uchungu mkubwa. “Pole Bree. Pole sana.” “BB anaumwa, auntie. Kila mtu mgonjwa. Mama Briana mgonjwa, wamempeleka hospitali siku nyingi, lakini hajapona. Daddy naye hanikumbuki tena.” Sonia aliumia sana. 

Aliendelea kulia wakiwa hapohapo nje ya wodi. “Pole sana Bree. Watapona tu na kila kitu kitakuwa sawa.” Briana alibaki kimya kama anawaza. “Twendeni tukatafute chakula, halafu tukalale.” “Unaturudisha nyumbani? Nakuomba usiturudishe nyumbani auntie. Auntie Leah huwa anatuchapa sana. Amesema hatupendi kabisa, anatamani tufe. Lakini anamuogopa sana mama Sonia. Ukienda kutuacha sisi wenyewe ata…” Briana alizidi kulia kwa uchungu. 

“Usinirudishe nyumbani auntie.” “Siwezi kuwaacha tena Briana. Nimekuja kukaa na nyinyi. Kwanza haturudi nyumbani sasa hivi. Tunaenda kutafuta hoteli.” Briana alimkumbatia tena Sonia kwa furaha. “Asante auntie.”

Wema Wa Penninah, Wanaendelea Kuvuna Wanae

 Wakiwa njiani wakielekea hotelini, Sonia aliomba mwenye taksi asimame dukani. Akanunua chupa mbili za chai na kwenda hotelini. Walifika wote wakiwa wamechoka sana. Alihakikisha watoto wameshiba ndipo alipowaambia walale na kurudi mapokezi. 

“Jiko linafunguliwa saa ngapi?” “Kuanzia saa mbili asubuhi.” “Naweza kupata uji na mtori mapema kidogo? Nina mgonjwa hospitali.” “Hakuna shida dada.” Sonia aliwaachia hizo chupa na kurudi kulala. Aliamka asubuhi na mapema, baada yakuwaletea chakula chumbani Josh, Briana na Kana, yeye akarudi tena hospitalini kumuona mama yake na mtoto. 

 **********************

Brayan alifurahi kumuona Sonia. “Pole BB.” “Wamenichoma sindano ya mkono.” Brayan akamuonyesha Sonia sindano aliyowekewa yakupitishia maji. “Pole sana. Utapona.” “Asante auntie.” Brayan naye alikuwa amechanganya sura ya mama yake na Nyange kidogo. Alikuwa mtoto mzuri sana na mtulivu kama dada yake. Hakuwa mtoto mtundu hata kidogo. 

Wakati wote Nyange alilalamika. “Mtoto gani wakiume amezubaa hivi jamani? Eti Brayan? Changamka bwana! Mwanaume anatakiwa kunguruma.” Wakati wote Nyange alikuwa akimnyanyua Brayan na kumtingisha tingisha kama kumchangamsha, kila anapomkuta amekaa ametulia. 

Sonia alimgeukia mama yake. “Poleni sana mama. Naona wote mmekonda kweli!” “Asante. Nashukuru niliwahi Sonia, Leah angemuua huyu mtoto.” Sonia alianza kulia tena. “Siamini mama kama ni hawa watoto wa Nyange jamani! Jinsi wanavyoteseka hivi, tena bila wazazi wao waliokuwa wakiwapenda vile! Nahisi kama naota!” “Ndio hivyo Sonia. Lakini na mimi nilichomfanya Leah, hatakaa anisahahu. Kama bado atakuwa mjamzito, nitamsifu.” “Mama wewe!? Umemfanyaje?” 

“Ambacho sijamfanya nikuto kumuua. Roho inaniuma Sonia, kupita nitakavyoeleza. Kumbe alikuwa akipiga watoto, halafu anawaambia wasilie wala wasiniambie, atawauwa! Wewe ongea na Briana. Nimeumia sana Sonia. Sana. Kumbe watoto walikuwa wakiteseka, mimi sijui!?”

“ Wamempima huyu mtoto jana wanasema anaweza kuwa ametenguka bega na kuvunjika mkono na sehemu za mbavu. Hivi leo inabidi akafanyiwe tena x-ray. Kila mahali wakimshika mtoto, wanahisi amevunjika!” “Mama wewe!?” “Ungemuona alivyokuwa anampiga jana, wala usingeshangaa kuambiwa amevunjika! Wangenipeleka polisi ile jana nilipokuja naye hapa, ni hivi nashukuru nilikuja nimembeba huku napiga mayowe, nikiomba msaada. Lasivyo wangenifunga Sonia, wakijua mimi ndiye nilikuwa nikimtesa huyu mtoto.”

“Nimewaelezea kwa kifupi madaktari nilio wakuta pale mapokezi, historia ya hawa watoto na wazazi wao, wamesikitika sana. Wengine mpaka wamelia. Hivi hapa tunatibiwa buree, wanakuja kila wakati kumwangalia.”

“Angalia vyakula walivyotuletea hapa usiku, na mmoja amepitisha chupa za uji na maziwa asubuhi hii kabla hata hatujaamka. Kila mtu amewahurumia sana hawa watoto.” Sonia alikuwa akilia sana.

“Siamini mama kama maisha yanaweza kubadilika kwa kiasi hiki! Ukiambiwa hawa ndio watoto wa Nyange! Huwezi amini. Briana amekonda, nimemkuta hana hata viatu, amevaa nguo za shule! Ukimuona mama yao alivyobadilika! Mama, utalia. Wamemnyoa nywele mama Bree, amekonda sana, halafu ana vidonda kila mahali, yaani…” Sonia aliendelea kulia.  

“Tutafanyaje mama?” “Siwarudishi hawa watoto pale, Sonia. Nitahangaika nao mpaka watakuwa tu. Kama niliweza kuwalea wewe na Kana mpaka mkakua, Mungu atanisaidia nitawalea hawa watoto mimi mwenyewe. Watakuwa tu. Siwezi kuwarudisha tena pale kwenye ile nyumba.”

“Kwanza baba yao hajui hata kama ana watoto. Hawahudumii pale kwa lolote. Si chakula wala mavazi. Pesa unazotuma wewe ndizo zimekuwa zikitusaidia wakati wote. Nyange hana ufahamu kabisa, si kwake tu, hata wanae.” “Mama!” 

“Kweli Sonia! Hana akili kabisaa. Hata kazini kwenyewe nilimsikia Leah akimwambia mama yake inabidi amuhimize atoke mle ndani na anamsisitiza akae huko huko kazini. Wakati wote eti anataka kurudi hapo ndani kumuona Leah.” “Mama wewe jamani! Kwani wapepatwa na nini?” 

“Tutaongea vizuri huyu mtoto akipona. Acha sasa hivi niweke akili zangu kwa huyu mtoto kwanza, Sonia. Wamekuwa wakiteseka mbele ya macho yangu bila mimi kujua! Naomba ukakae na kina Kana ili umruhusu Josh aondoke arudi kwao.” “Mama wewe!? Josh anaondoka?” 

“Hawezi kukubali kurudi tena pale wakati mimi sipo. Na hata BB akipona, nimekwambia sirudi tena pale na hawa watoto Sonia. Mwache Josh aende tu, hata hivyo alikuwa akikaa pale kwa ajili yangu. Halipwi mshahara na Nyange alishaanza kumpiga. Mwache tu aende akatafute riziki sehemu nyingine, ila mwambie kabla yakuondoka akanichukulie mizigo yangu na watoto pale nyumbani.” “Leah akikataa.” Sonia aliendelea kufuta machozi.  

“Hathubutu. Mwambie, amwambie mama Sonia amenituma, atampa tu. Kwanza atafurahi kuto kuiona hii sura yangu tena. Sonia, yule msichana alikuwa anawapiga hawa watoto sio kuwaadhibu, niya yake ilikuwa nikuwaua kabisa. Briana anasema alikuwa akimpiga sana Brayan huku anasema akifa roho yake ndio itatulia. Hawataki kuwaona hawa watoto kabisa pale ndani.”

“Atafurahi sana kusikia tunaondoka pale ili abaki yeye na Nyange tu. Mpe hela akodishe taksii ya kubebea mizigo yetu. Mwambie asiache kitu hata kimoja.” Sonia alitoka kurudi hotelini na kumpa Josh maagizo aliyopewa na mama yake. 

 **********************

Alipofika alimkuta Leah na mama yake nao ndio wanaingia kutoka hospitalini. Leah alionekana mwenye maumivu makali sana. Bila salamu kwa Josh alimgeukia mama yake. “Fanya haraka basi kuandaa hiyo supu.” Mama yake alipitiliza jikoni, Leah aliingia na kujilaza kwenye kochi. Akiwa amejawa hofu sana, Josh alifuata kwa nyuma yao huku ameacha taksii nje kabisa ya geti. 

“Nimetumwa na mama Sonia vitu vyake vyote na vya watoto. Amesema nisiache kitu hata kimoja.”  Josh aliongea huku amesimama mlangoni kama anayesikilizia jibu la Leah. “Afadhali. Chukua mavitu yao yote humu ndani, usibakize hata kitu kimoja. Tena mwambie asiwahi kukanyaga tena hapa, yeye na hao watoto.” Leah alitaka kusimama, lakini akarudi kukaa. 

“Mama? Mama?” Mama yake alikuja akitokea jikoni huku anakausha mikono yake. “Hiyo supu bado tu jamani? Njaa inauma kweli!” “Ndio naandaa Leah!” “Hebu msaidie Josh kukusanya vitu vyao vyote, wanaondoka wote humu ndani.” Mama Eliah alibaki amesimama kama anawaza kitu. 

“We mama? Changamka bwana, fanya haraka, msaidiane na Josh. Sitaki Nyange aje hapa apishane na mabegi mlangoni.” Leah alimuamrisha mama yake. Josh na Mama Eliah walikusanya vitu vyao vyote wakaweka kwenye taksii, Josh akaondoka. 

 **********************

 Sonia alibaki namshangao alipomuona Josh amerudi na mizigo yote kama alivyoagizwa, tena ndani ya muda mfupi. “Mimi nilijua atakukatalia!” “Alivyofurahiakuondoka kwetu! Wala hakutaka nichelewe. Hata hivyo ana muogopa sana mama yako.” Josh aliomba kabla yakuondoka waende wote hospitalini akamuage mama Sonia na Brayan. 

Waliongozana wote mpaka hospitalini. Briana alifurahi sana kumuona mdogo wake. “BB!” Alitamani kumkumbatia lakini tayari alishakuwa amefungwa POP mkono mzima mpaka begani. “Pole Baby Brayan. Utapona eeh!” Briana aliongea kwa sauti ya chini na ya upendo huku akitokwa na machozi. Kwa Brayan salama yake nikuwa na mama Sonia karibu. Alijawa tabasamu usoni kama sio yeye. 

“Naona maumivu yamemwisha. Mgonjwa huyu ana kazi ya kula tu, tokea asubuhi ulivyotuacha hapa.” Mama Sonia alikuwa akiongea huku akimtekenya Brayan. Angalau kila mtu alikuwa akicheka. 

“Mmekula?” Mama Sonia aliuliza huku akiwaangalia watoto. “Wamekula mama.” Sonia alijibu kwa haraka. “Asante Sonia mwanangu. Najua nakutia kwenye shuguli, zisizo kuhusu.” “Zinanihusu sana mama. Hawa watu ndio ndugu wa kwanza Mungu alio nipa hapa duniani. Nasikitika yamewakuta yaliyo wakuta, lakini hawa ni ndugu zetu sasa.” Muda wote Sonia alikuwa akiongea na mama yake lakini Josh alionekana ana mawazo kidogo. 

“Nini Josh?” Mama Sonia akamuuliza. “Mmh! Nilivyokuwa nikimuangalia yule mama yao, shuguli itakuwa imempata. Leah ana mgombeza sana mama yake kama mtoto! Na anaonekana yule mama kama ana majuto fulani hivi! Hakufurahia kabisa kuondoka kwa hawa watoto! Alijaribu kuulizia hali ya BB wakati tunapandisha mizigo kwenye taksii kwa sauti iliyojaa majonzi kweli, lakini sikumjibu.”  

“Afadhali hukumjibu. Achana nao kabisa hao watu, Josh. Yeye alikuwa palepale wakati wajukuu zake wanateswa! Kwa nini wakati wote huo asiseme kitu? Sasa hivi mambo yamemgeukia ndio anajidai kuulizia. Jana nilimkuta kaweka mikono kichwani wakati Brayan anasulubishwa pale, kilichomshinda kumtetea mtoto ni nini?” 

“Lakini Sonia, kuna kitu wamemfanyia mama Bree na mumewe sio bure.” Josh aliongea kwa uchungu sana. “Umeanza kuamini, Josh?” Mama Sonia alidakia. “Lipo jambo tu mama. Sio bure. Nikimwangalia Nyange ni kama amepoteza ufahamu kabisa! Sio yeye Nyange!” Josh aliongeza. 

“Kwanza najiuliza sipati jibu, labda unisaidie wewe Sonia uliyekuwa ukiishi nao karibu tokea mwanzo. Ni jambo gani baya mama Briana amemtendea mama yake, kiasi cha kumuadhibu mwanae wa kumzaa kiasi hichi? Nini alifanya mama Briana?!” “Wewe si umemuona mama Briana jinsi alivyo? Ndivyo vilevile alivyo yule dada. Labda wanamuadhibu kwa roho yake nzuri, ya kupita kiasi.”

“Huwezi amini mama, alimchukua Leah toka kijijini baada ya kufeli, akamleta mjini. Nasikia mama Briana ndiye aliyemsomesha na kumtafutia kazi. Alimtendea mabaya mengi dada yake, ikiwemo kutembea na Nyange, lakini yule dada alisamehe.” “Haiwezekani! Yule msichana alisha tembea na Nyange zamani?” 

“Ndiyo mama, tena akasababisha mpaka kifo cha Junior, yule Mama Briana aliyekuonyesha kaburi lake pale kwao, lakini yule dada alisamehe kila kitu na kumuomba tena Nyange wamsaidie Leah kwa mara nyingine.”

“Maana Nyange anasema baada ya kulala na Leah mwanzoni wakati mkewe amesafiri, Leah akamlazimisha Nyange waendeleze mahusiano hata pale mkewe aliporudi. Nyange alipokataa akamtishia atamwambia dada yake kama walishakuwa na mahusiano kama hawataendelea kuwa wapenzi.”

“Kwa hiyo Nyange alikuwa akiendelea kulala naye Leah kwa lazima, huku akiwa na hasira naye sana. Baada ya mambo yote kujulikana na mkewe kumsamehe, Leah akarudi tena na uongo mwingine.” “Nini tena?” Akauliza. 

“Alirudi mjamzito, akidai ile mimba aliyokuwa nayo ni ya shemeji yake.”  “Yule msichana ana tatizo la akili jamani! Shida yake nini?” “Sam anasema Leah ni mkorofi sana, hapendi kupitwa na dada yake hata kidogo. Anataka wakati wote yeye ndio awe anaonekana amemzidi dada yake na anapenda sana pesa.”

“Kwa hiyo wakati wote amekuwa akitaka kuzaa na Nyange ili angalau apate mali za Nyange na kumuonyesha mama Briana yeye ni zaidi yake. Sam anasema Leah anaumia sana vile Nyange anavyosema mali zote ni za mama Briana.”

“Na kitu kilichomtibua zaidi Leah, ni nyumba ile aliyokuwa akiijenga yeye na Samkwa pesa Leah aliyokuwa akikopa kwa Nyange akidhani Nyange atamsamehe kwa kuwa alikuwa akilala naye, kumbe mwenzake Nyange alikuwa akimuandikisha na kutunza kumbukumbu ya kila senti aliyokuwa akimkopesha kuanzia nusu ya pesa waliyokuwa wamenunulia kile kiwanja mpaka ujenzi.”

“Sasa Sam na Leah waliposhindwa kummalizia mwenye kiwanja nusu ya ile pesa, mwenye kiwanja akataka kukiuza ili apate pesa yake ya kiwanja, inayobaki awalipe Sam na Leah. Ikawa rahisi sana kwa Nyange. Nyange akakinunua yeye na kumalizia kuijenga ile nyumba, kwa ramani nzuri zaidi ya ile ya Leah na Sam, kisha akaiandika jina la Mama Briana.”

“Halafu mbaya zaidi, siku ya ‘birthday’ ya mama Bree kumbe Nyange baada yakumaliza kuijenga ile nyumba, wakati huo mama Briana hana hata habari anahangaika na ujauzito wa Brayan, Nyange akaalika watu kwenye ile nyumba pale, halafu akamtuma Sam aje atufuate sisi wote pale nyumbani.”

“Tena ndio kilikuwa kipindi hicho hicho mama Bree hayupo kwenye maelewano mazuri na mama yake na Leah. Nyange akamwambia Sam atupeleke kwenye ile nyumba bila kumwambia mama Briana tunapoenda. Tulipofika, tukakuta marafiki zake Nyange kibao pale wanamsubiri mama Briana, Nyange akamkabidhi ile nyumba mkewe siku ile, tena mbele za watu. Ikafuatiwa na sherehe kubwa kweli. Josh unakumbuka ile siku?”  “Nakumbuka sana. Namkumbuka mwenyewe mama Briana alishindwa kuongea kabisa. Alibaki akicheka huku analia tu mpaka mwisho.” Mama 

Sonia alianza kutokwa na machozi. “Nyange anampenda sana mkewe jamani!”Mama Sonia aliongea kwa uchungu sana. “Anampenda sana. Si unamuona mama Briana alivyo mpole vile? Lakini Nyange wakati wote anasema yeye hakusoma, lakini Mungu amempa mke msomi na wakati wote yeye ndiye anayemshauri. Nyange anamsikiliza sana mkewe.” “Nimewaona. Sasa ikawaje? Leah alikuwepo, hiyo siku ya makabidhiano?” Mama Sonia alifuta machozi.

“Hakuwepo, lakini si unamjua Nyange mpenda makuu. Alifanya fujo pale, zisizo za kawaida. Lazima habari zilimfikia tu Leah. Maana alialika pia mashoga zake Leah waliokuwa wakifanya kazi na Leah na Nyange zamani. Sam alikuwa akiniambia, Nyange alifanya makusudi kuwaalika wale wafanyakazi wenzake wa zamani.”

“Lengo lake lilikuwa ni kama kuwasuta, kwa kuwa nasikia walikuwa wakimdharausana Nyange pale ofisini kwao, wakiongozwa na Leah na pia alitaka habari zimfikie Leahhuko aliko. Lakini Sam hakuwa na furaha hata kidogo, alikuwa akisema Nyange amekosea sana kumfikishia ujumbe Leah.”

“Sam alisema, Leah hatakaa akubali hata iweje ile nyumba apewe mama Briana. Kwa kuwa Sam alikuwa anasema ile nyumba Leah aliihangaikia sana mwanzoni, kabla ya Nyange kuipokonya. Hata huko kulala na Nyange, alikuwa anasema kwa Leah alikuwa anajikaza sana, ili tu apate pesa kutoka kwa Nyange amalize ile nyumba, lakini si kwamba anampenda Nyange hata kidogo.”

“Alisema ataumia sana, kuona juhudi zake zimeishia kuwa tunzo kwa mama Briana ambaye ni mshindani wake mkubwa sana. Sasa nikamuuliza Leah atafanyaje na wakati ile nyumba ishakabidhiwa kihalali kwa mama Bree. Sam akaniambia, ‘wewe humjui Leah hata kidogo.’ Sasa sikuwa najua atafanyaje.” 

“Kwani ni nyumba gani?” “Bonge ya Jumba mama. Ukiiona, utaongeza heshimakwa Nyange na mkewe.” “Ile yenyewe tu pale tulipokuwa tukiishi, si mchezo! Sasa anakaa nani huko?” “Baada ya Nyange kumkabidhi mkewe, wakaamua kuikodisha kwa kampuni moja ya kigeni. Sam alikuwa anasema inawaingizia pesa nyingi sana. Usiwaone vile wale, Nyange akituchokoza mchana na usiku na mama Briana akicheka pale ndani, wanahela sana wale.” 

“Najua. Ndio maana Leah anahangaika.” “Na ana hangaika kweli! Unajua ile mimba niliyokwambia alirudi nayo, kumbe alipoachana na baba Briana tu, Leah akaenda kumlipa mwanaume ampe mimba ili aje amdanganye Nyange mtoto ni wa kwake ili Nyange ampe tena ile nyumba, lakini kumbe Nyange alikuwa ameshajua mipango yote ya Leah. Leah alipokuja na mimba yake pale ndani, tena mbele za watu na dada yake akiwemo, akijigamba mimba ni ya Nyange na mtoto ni wa kiume, ungemuonea huruma Nyange alichomfanya.” 

“Alimfanyaje?” “Si unajua Nyange na mkewe wanavyopenda watu pale kwao? Sasa siku hiyo jioni, walikuwa wamealika watu kibao pale kwao kuja kuangalia mpira na Leah naye ndio hiyo siku alipokuwa amekuja akiwa mjamzito wakujifungua.”

“Si unamjua Nyange alivyo mkorofi? Alitaka kumpiga palepale mbele za watu, ndio mama Briana akaanza kumsihi Nyange amsamehe.” “Jamani mama Briana! Anahurumayule mwanamke!” “Huwezi amini mama. Kila mtu alikuwa akimshangaa mama Briana, alikuwa amempigia magoti Nyange amsamehe mdogo wake, tena huku akilia yule dada jinsi alivyokuwa na upendo.”

“Mama Briana anampenda sana Leah, na kila wakati amekuwa akimsamehe. Ndio siku hiyo Leah mwenyewe alikiri kuhangaika sana kwa waganga kuwaloga Nyange na dada yake lakini alishindwa. Sasa huwezi jua ameenda kusema uongo gani kwa mama yake, wakakubaliana kuunganisha nguvu kuwaloga tena Nyange na mkewe. Maana nilisikia yule mama anampenda sana Leah kuliko watoto wake wote.”

“Nahisi safari hii kwa kuunganisha nguvu, wamefanikiwa.” “Na kweli wamefanikiwa, na wameweza kumuadhibu yule dada. Mbele ya macho yetu, yule dada alichanganyikiwa ile ya kuwa kichaa kabisa! Wakajidai wanalia siku za kwanza, lakini walikuja kugeuka vibaya wakawa kama chui aliyekuwa amevaa ngozi ya kondoo.” “Daah!” Josh aliendelea kunung’unika. 

“Mama Briana best yangu jamani! Mwenzenu siamini! Kila nikikaa nakumbuka cheka yake mwenyewe! Kutwa nzima tulikuwa tunacheka. Nilikuwa nikimtania yule dada, kama sio bosi wangu! Pesa na elimu aliyokuwa nayo yule dada, havikuwahi kumbadilisha utu wake! Mpole na upendo kwa kila mtu. Alikuwa akiniambia nikimpelekea mchumba atanifanyia harusi kubwa sana. Daah!” Josh aliendelea kuumia. 

“Mimi alini….” Sonia na mama yake, wao walishindwa hata kuendeleza kueleza upendo wa Mama Briana juu yao. Ukimya wa muda kila mtu akijaribu kuingiza taarifa kichwani na moyoni huku wakilizwa na mengi ulitanda.

“Naona mimi niwahi kuondoka kabla giza halijaingia.” Mwishowe Josh aliamua kuaga. “Asante sana Josh kwa uvumilivu. Mungu akusaidie huko uendako.” Mama Sonia aliongeza, huku akifuta machozi. Wote walianza kulia palepale wodini kama msiba. 

Josh alimpenda sana mama Briana, hata wakati mwingine mama Briana alipokuwa kazini, Josh alipiga simu kumsalimia tu, au kumchokoza. Josh aliwaaga na kuondoka.

**********************

Umoja na furaha waliyokuwa nayo ilitoweka mbele ya macho yao. Hakuna aliyetegemea kuachana kwa majonzi kwa kiasi kile. Mama Briana ndiye aliyekuwa nguzo iliyokuwa ikiwashikilia wote. Lakini Leah aliivunja na kufanikiwa kuwasambaratisha wote bila huruma. 

 **********************

Daktari mmoja aliamua kuwatoa Sonia na watoto hotelini na kuwahifadhi nyumbani kwake, kwa muda ambao bado Brayan alikuwa akipata matibabu. Waliishi bure, na kupewa mahitaji yao ya muhimu, mpaka Brayan alipopata nafuu. 

Hakuna Aliyewahi Kutoa, Kumzidi Mungu

Wakati Nyange na mkewe hawajitambui, watoto wao walikuwa wakivuna matunda ya mbegu walizopanda. Baada ya siku nne, waliruhusiwa, Brayan akionekana na nafuu kubwa tu. Sonia aliwachukua wote mpaka Dodoma anapoishi yeye. 

Alikuwa amepangisha upande mdogo wa nyumba yenye chumba kimoja kikubwa, sebule, choo na jiko. Kila kitu kilikuwa kikijitegemea. Hakuingiliana na wapangaji wengine. 

“Mvumilie hapa kwa muda, mpaka tutakapopata nyumba kubwa.” Sonia aliongea kwa kujitetea, mbele ya watoto wa Nyange waliozaliwa na kukulia kwenye hekalu. 

“Kwako pazuri, auntie.” Briana alisifia nyumbani kwa Sonia nakumshangaza kila mtu mpaka Sonia mwenyewe. Kwani ukichanganya vitu vyote alivyokuwa akimiliki Sonia havikufika hata nusu ya thamani ya chumba chake huyo Briana. Lakini Sonia alikumbuka Briana hana tofauti na mama yake hata kidogo. Wote sio wapenda makuu ila Nyange ndiye aliyekuwa akipenda kukuza mambo. Kabla Briana hajalia shida, Nyange alishamtimizia.

Alihakikisha anaweka thamani kubwa sana kwa Briana, kila aliyemuona alijua ni mtoto wa milionea. Si kwa mavazi, gari, wala chumba chake mwenyewe. Kila kitu alichokuwa nacho Briana, Nyange alihakikisha nicha thamani sana. Briana alikuwa gumzo kwa kila familia iliyokuwa karibu na familia hiyo ya Nyange. 

**********************

Tatizo kubwa walilokuwa nalo kati ya wapenzi hao wawili {Nyange na Briana} ni Kana tu. Kila Nyange alipokuwa akimshauri Briana kuanza kufikiria kulala peke yake sio kulala na Kana, Briana alikuwa akilia sana. “Ongea naye wewe basi, mama Briana, mpenzi wangu! Labda wewe mwenzangu atakuelewa.” “Ukishafika kwenye swala lakuongea na Briana unaniita majina yote mazuri unayoyajua wewe? Kinachokushinda wewe kuzungumza naye ni nini Nyange jamani?” 

“Wewe si unatusikilizaga kila siku maongezi yetu? Hatufiki popote. Kabla hata sijamaliza kujieleza, anaangua kilio.” Nyange alikuwa akitamani sana mtoto wake aache kulala na Kana na kujaribu kujifunza kulala peke yake lakini alishindwa. 

“Eti mpenzi wangu? Nimwite mzungumze naye?” Nyange aliendelea kubembeleza mkewe. “Wewe unavyomuona huyo mwanao, nimuelewaji? Huna utakalomwambia akakuelewa juu ya Kana. Unajitafutia matatizo bure na huyo mtoto, usiku huu. Ataanza kulia hapa usiku kucha, tuharibu usiku wa leo. Mwenzio nimechoka nataka kuwahi kulala, kesho nina kazi nyingi ofisini. Kama wewe unataka kukesha, nenda mkaendelee kubembelezana huko huko chumbani kwake, sio hapa kitandani kwangu. Kwanza wewe mwenyewe unavyoongea naye huyo Briana! Kama unambembelezea pumzi!”

“Ashanijua udhaifu wangu, ndio maana ananichezea akili. We ngoja nimbadilikie.” “Hujiwezi kwa lolote kwa Briana. Kila siku unaniambia kauli hiyohiyo, akikuonyesha tu ile sura yake ya upole unaishia kumbembeleza badala ya kumkazia sauti.” “Umemuona anavyonililia lakini?” Mama Briana alianza kucheka. 

“Wewe waache bwana.” “Ujue anazidi kuwa mkubwa huyu, atalala na Kana mpaka lini?” “Wewe ndio unamuona mkubwa. Lakini mwenzio hana analo elewa kichwani mwake hata kidogo. Ndio maana kila siku anakuuliza kwa nini asilale na Kana, unabaki unababaika huna hata sababu ya kumpa.” 

“Bwana huyu mtoto ataniua na presha bwana! Umemuona wakiwa wanacheza?” Mama Briana alizidi kucheka. “Usicheke bwana! Mtoto anacheza na chupi tu. Anakuwa lini sasa? Ukimwambia vaa nguo, anakwambia anasikia joto. Nafanyaje mama Briana, hebu amka bwana tushauriane.” Mama Briana alikuwa akicheka mpaka machozi. 

“Na kweli utakufa na presha. Nakuona unavyomfuatilia. Hana analojua mwenzio huyo. Wewe muache tu. Akikua utamuona atakavyobadilika. Hutamwambia jambo, atafanya mwenyewe.” Juhudi za Nyange zilikuwa zikigonga mwamba kila siku. 

 **********************

“Kweli auntie, hata redio yako nzuri.” “Asante Bree. Lakini nyumba yenyewe ndogo kweli!” “Mbona hapa panatosha Sonia. Umejitahidi sana mwanangu. Hongera.” Mama yake alidakia kwa haraka kama kumtia moyo mwanae kwa maendeleo aliyoyapata. 

Sonia alianza kumuona Briana anaanza kukosa raha kadiri muda ulivyozidi kwenda. Akaamua kumuita azungumzw nayw. “Vipi Briana?” Briana alianza kutokwa na machozi. “Niambie tu. Usiogope” “Naomba kulala na Kana.” “Kwani si ndio mlikuwa mkilala hivyo kila siku nyumbani?” Briana alitingisha kichwa kukataa. 

“Eti mama?” “Kana alifukuzwa kulala mle ndani, kwa hiyo tulikuwa tukiibia wakati mwingine Leah akilala ndipo tulikuwa tukimuungiza Kana ndani. Briana alikuwa akilia usiku kucha akimtaka Kana.” Sonia aliumia sana. Alikumbuka tokea akiishi nao, wazazi wao walishajaribu kumtenganisha Kana na Briana lakini walishindwa. 

Ile tabia ya Briana kuamka usiku na kulia wakati yupo mtoto, ilirudi upya asipolala na Kana. Kila siku alipokuwa Nyange anamwambia alale peke yake chumbani kwake, kwanza ilimbidi Nyange amsubirie mpaka apitiwe na usingizi ndipo Nyange aondoke na bado Briana alikuwa akiamka usiku na kwenda chumbani kwa wazazi wake kuwalilia anamtaka Kana. 

Waliishia kulala naye mpaka asubuhi, mwishowe mama Briana alimwambia Nyange, Kana arudi tu huko chumbani kwa Briana yeye hawezi kuendelea kukesha akibembelezana na Briana kila siku usiku. Briana aliishi na Kana kama pacha wake, hakuwa hata na wazo la pili. 

“Basi usilie Briana. Nyinyi mtalala hapo kitandani, mimi na Mama Sonia tutalala kwenye makochi.” Briana alifurahi sana. Akamkumbatia Sonia. “Asante sana auntie.”

 **********************

Watoto walipolala Sonia akamsogelea mama yake. “We mama! Huyu Briana hajabadilika tu?” Sonia alinong’ona. “Unajua kameshakuwa kakubwa sasa!” Mama Sonia alianza kucheka. “Mimi mwenyewe na mama yake tulikuwa tunashangaa hivyohivyo. Utamkuta chumbani kwao na chupi tu anacheza na Kana.” “Mama wewe?! Na kilivyo na matako makubwa kama mama yake!” Wote walikuwa wanacheka taratibu. 

“Kweli tena. Hapo alipo hana hata wazo kwamba yeye ni mtoto wakike na mwenzie ni wakiume. Akitoka kuoga, anavaa hapohapo mbele ya Kana alipo, hata hajifichi. Nyange alikuwa anakaribia kuchanganyikiwa.” Sonia alizidi kucheka.  

“Sasa mama Bree alikuwa anasemaje?” “We si unamjua mama Briana? Anabaki kumcheka Nyange anavyohangaika nao. Kutwa yupo nyuma yao kuwaangalia kinachoendelea kati yao. Nasikia usiku Nyange alikuwa halali anawatembelea chumbani kwao kuwaangalia.” Sonia alizidi kucheka. 

“Kajaribu kila njia kuwatenganisha, lakini kashindwa. Huyo Briana asipomuona Kana hata dakika moja tu ni shida. Anaanza kuitwa huyo Kana na machozi juu. Nyumba nzima mtakosa raha Kana asipoonekana. Mpaka Nyange mwenyewe atasimama kumtafuta huyo Kana, mpaka ampate.”

“Tena mnyonge wake baba yake. Asipomuona tu Kana, anaenda kumlilia baba yake, akamtafute Kana. Basi utamsikia Nyange ananyanyuka kimya kimya huku anasema, ‘Uzazi kazi jamani!’ Leah alipowatenganisha usiku, ungemuonea huruma.” “Basi kazi ipo!” 

“Utawaona tu. Wewe subiri. Na hutamsikia huyo mtoto akikuongelesha au akakulalamikia kitu zaidi ya salamu basi. Anaongea na Kana peke yake. Hata aumwe vipi, wa kwanza kuambiwa ni Kana. Nyange mwenyewe akitaka kujua mambo yake anamuuliza Kana.” Sonia alikuwa akicheka sana. 

“Ujanja wote umemuisha Nyange!” “Kwa huyo mtoto, kweli jasho linamtoka. Na anavyompenda, roho yake. Anahangaika naye kupita kiasi. Ilimbidi ampende tu Kana, na shule amsomeshe hukohuko anakosoma Briana.” “Mwenyewe nilishangaa. Ada yote ile!” 

“Hapakuwa na jinsi. Briana alikuwa haondoki pale kwao kwenda shule bila Kana. Na kurudi ni hivyohivyo. Kana akichelewa kutoka darasani kwao anaenda kumngojea mlangoni, darasani kwa kina Kana. Mwenzake si kiongozi? Sasa akiwa kwenye vikao labda na walimu, halafu wakachelewa kumaliza hicho kikao, Briana anaenda kusubiria mlangoni.”

“Nyange kashaitwa huko shuleni mpaka wamewazoea. Kutwa yupo mlangoni kwenye darasa la kina Kana. Nasikia Kana naye akimuona tu anatoka kwenda kumfuata, anamshika mkono anaingia naye ndani anamvutia kiti, anakaa naye hapo pembeni ya dawati lake mpaka mwalimu amalize au Kikao kiishe.” “Mama wewe?” 

“Mama Briana ndio alikuwa anamcheka Nyange hana mbavu. Wazazi wake wakiitwa tu shuleni, mama Briana anamwambia Nyange yeye ndio aende. Lakini si unamjua Nyange maneno mengi? Akafanikiwa kuwaweka sawa walimu wote, kwa hiyo pakawa hamna shida.”

“Shule hii nyingine waliyohamia mambo yakawa hivyohivyo, kutwa wameshikana mikono. Kana kiongozi, si anatakiwa kusimamia usafi, sasa nasikia kazi yake ya kwanza, kumsaidia kwanza Briana. Wakimaliza kwenye eneo la Briana, anampeleka mstarini kusubiria kengele ili asije chelewa akachapwa ndio yeye anarudi kusimamia usafi.”

“Lakini huko waliwapenda sana sababu wote walikuwa wakiongoza darasani halafu nidhamu kwa kila mtu.” “Kweli Nyange atakufa na presha na huyu mtoto.” “Anavyompenda! Ndio maana nakwambia sio akili za Nyange zile! Nyange sio mtu ashindwe kufuatilia mambo ya wanae!”

“Alikuwa hajali tena wanae, wala hakuwa akijua kama Briana alikuwa akitembea kwa miguu kwenda shule.” “Na akija kurudiwa na akili zake, huyo Leah akae mbali. Nyange alivyo mkorofi yule, atamuua.” Sonia na mama yake waliendelea kunong’ona usiku huo uliokuwa umechanganyikana majonzi na furaha ndani yake. 

“Nilikuwa naitamani hii siku mama!” “Siku gani?” “Hii yakuja kuishi wote tena.” “Hata mimi Sonia. Nimefurahi sana. Kwanza najivunia mwanangu, umejitahidi sana, Sonia. Hongera.” “Kidogo tu mama.” “Sio kidogo Sonia. Umesahau tulipotoka mwanangu?” “Nakumbuka sana. Siwezi kusahau mama yangu.” Kimya kilitanda. 

Mama Sonia alimuona vile mwanae alivyopotelea mawazoni. “Kwani huku Dodoma hakuna wachumba?” “Umeanza mama?” Mama Sonia alicheka kidogo. “Kwani hutaki kuolewa tena mwanangu?” Sonia alinyamaza kwa muda. 

Kisha akasema. “Nilikuwa natamani sana Sam ndio angekuwa mume wangu, mama. Lakini ilishindikana. Naona shida kweli kuanza mahusiano mengine. Wanaume wengi waongo mama. Wengi wakiniona tu, wanachofikiria nikuniweka kitandani lakini sio kutaka mahusiano na mimi ya muda mrefu. Wanataka tu kunichezea.” Sonia alianza kutokwa na machozi. 

“Najiuliza mama sipati jibu.” “Nini?” “Nilikosea wapi kwa Sam? Nimeishia kujiambia labda ningefanya hiki au kile angenipenda kwa dhati. Nimeingiwa na hofu, mama. Najiambia kama nilishindwa kwa Sam, hata nikienda kwa mwanaume mwingine sitaweza.” Sonia aliendelea kulia taratibu. 

“Wala usilie. Mambo ya Mungu ni mengi, ni ngumu kuelewa. Lakini sitaki uje uishie kama mimi mwanangu. Kuishia umemuweka mwanaume mmoja tu moyoni, nakushindwa kuendelea na maisha mengine! Hapana Sonia. Jaribu kufungua moyo ili uje uolewe uwe na kwako. Najua unaweza kupata mwanaume mwingine mzuri tu, akakupenda na kukujali. Inawezekana Sam hakuwa andiko lako. Usikae hapo muda mrefu unasononeka, lazima maisha yaendelee, Sonia. Umenielewa?” 

“Naeelewa mama. Lakini simpati huyo mwanaume mwingine wakunipenda na kunijali.” “Utamuonaje wakati wewe bado unawaza ulipokosea kwa Sam? Sidhani hata kama unatoka humu ndani, mbali na kazini.” “Naenda wapi, sasa mama jamani?”

“Umeona? Sasa huyo mwanaume mwingine utampataje Sonia, kama umejifungia humu ndani?” Sonia aliendelea kuongea na mama yake usiku huo, mpaka walipopitiwa na usingizi. 

 **********************

Maisha yalianza, Mungu akiwa upande wao. Kana na Briana walitafutiwa shule. Na baada ya muda Brayan kupona kabisa na kurudisha afya yake naye alitafutiwa shule akiwa mwingi wa furaha huku akimwita mama Sonia, mama. 

Kwa kuwa mama Sonia alikuwa na ujuzi wa kusuka, baada ya Brayan kupona na kuanza shule, Sonia alimfungulia sehemu yakusuka. Watu wengi walimpenda mama Sonia kwa kusuka, baada ya muda mfupi alianza kufahamika na watu wengi na yeye akaanza kuingiza pesa yakutosha. 

Mteja wake mmoja alikuwa dada mmoja aliyejulikana kwa jina la Asifiwe, kwa kupenda kutoa salamu ya ‘Bwana Yesu asifiwe’ kwa kila mtu. Alimpenda sana mama Sonia. Hata kama hakuwa na haja ya kusuka, lakini alipita saluni kwa mama Sonia kumsalimia. 

Taratibu maisha yao kifedha yalianza kubadilika. Wakakodisha sehemu kubwa ya biashara, wakatengeneza chumba kidogo hapo hapo Saluni, kwa ajili ya kupumzikia watoto wanapotoka shule. Kwani Sonia na mama yake wote walikuwa wakichelewa kutoka kazini. Sonia alikuwa akitoka asubuhi na mapema kwenda kazini kwake kila siku kasoro siku za jumapili, na mama Sonia alikuwa akimpeleka Brayan shuleni asubuhi na kuelekea kazini kwake. Brayan peke yake ndio alisoma shule yakulipia na Sonia ndiye alikuwa mlipa ada hiyo. 

Kana alikuwa akiongozana na Briana kila siku shuleni. Tabia yao yakuongozana kila mahali na Kana kumkingia kifua Briana kwa kila mtu mpaka walimu ilifahamika haraka sana pale shuleni kwao. Kwa muda mfupi waliofika hapo shuleni walishafahamika na kila mtu. 

Kutokana na kufaulu kwao kwa asilimia za juu sana, kila mwalimu alivutiwa nao, wakaamua kuwapa uongozi. Wakiwa mstarini siku hiyo asubuhi, walisikia majina yao yakitajwa kuwa wamechaguliwa kuwa viongozi. 

Haraka sana Kana alimgeukia Briana kumwangalia hali yake baada ya jina lake na yeye kutajwa kuwa amechaguliwa kuwa kiongozi, akamuona ameinama. Kana alijua wazi Briana hawezi kuongea na watu, aliamua kumfuata mwalimu mkuu huku amemshika Briana mkono.  

“Briana hawezi kuwa kiongozi, naomba msimpe uongozi wowote.” Mwalimu Mkuu alishitukia Kana na Briana wamemsimamia mbele ya meza yake, ofisini kwake asubuhi hiyo mara baada ya wanafunzi wote kutawanyishwa mstarini, nakuambiwa waingie madarasani. 

Alibaki akiwaangalia wote wawili kwa muda. “Eti Briana?” Alimgeukia Briana. “Kwa nini huwezi kuwa kiongozi?” Tayari machozi yalikuwa yameshaanza kumtoka Briana na kumshangaza yule mwalimu. 

“Basi hamna shida Briana. Lakini wewe Kana utaweza?” “Mimi nitaweza, lakini naomba mumuache Briana.” Kana aliendelea na uongozi, Briana alitolewa kwenye uongozi lakini hakupewa kazi yoyote pale shuleni. 

Kwa hiyo kila wanapokwenda shuleni Briana alienda kusaidia watoto wadogo usafi wakisaidiana na Kana aliyekuwa kiongozi wao wa usafi kwa darasa la kwanza mpaka la tatu. 

Walijawa na furaha kila wakati, na kila wanapokuwa wakitoka shuleni, moja kwa moja walienda kwenye saluni ya mama yake Sonia. Kana ndiye alikuwa mwalimu mwingine wa Briana. Kila walipotoka shuleni walimkuta Brayan alishatoka shuleni. 

Kabla ya Kana hajajisomea kidogo, alipitia alichofundishwa Briana siku hiyo, na kumuuliza maswali kuhakikisha ameelewa, nakuendelea kujisomea mpaka muda wakula. Wakisha kula chakula wanachokuwa wameandaliwa na mama Sonia, Kana anatoka nao {Briana na Brayan} kwenda kucheza mpaka usiku wanaporudi na mama Sonia au kama amebanwa na kazi siku hiyo, Sonia alipita kuwachukua watoto na kurudi nao nyumbani na hayo ndiyo yalikuwa maisha yao ya kila siku.  

 **********************

Taratibu walianza kuzoea lakini wakati wote Briana alipokuwa na Kana hakuacha kumlilia mama yake. Kana alikuwa akimbembeleza Briana kila siku usiku wanapokuwa wakilala. Briana alilala katikati, halafu Kana na Brayan walilala pembeni yake.

Briana alimpenda sana kaka yake. Kila alipotoka shule hakuacha kumuuliza Brayan habari za shule kama mama yao alivyokuwa akimfanyia yeye. Watoto hao walikuwa wakipendana sana. Hapakuwahi kuwa na ugomvi katikati yao hata siku moja. 

 **********************

“Nikuulize kitu Kana?” Briana alimuuliza Kana walipokuwa wakitoka shule wakielekea saluni kwa mama Sonia. “Nini?” “Unafikiri nitakuja kumuona mama Briana tena?” “Kwa nini humuulizii dady tena?” “Dady hanipendi siku hizi. Alinikuta nachapwana Leah wala hakunitetea, aliniacha palepale yeye akaenda ndani.”

“Unakumbuka nilipolazwa wakati naumwa? Dady hakuja kuniona.” Kana alinyamaza kwa muda. “Unajua nini Briana?” Briana alishaanza kulia. “Usilie Briana. Nimesikia mama Briana yupo hospitalini hapahapa Dodoma. Nitamuomba Sonia atupeleke.” Kana bado hakuwa akijua kama Sonia ndiye mama yake. 

Kwani wakati wote alilelewa na bibi yake. Kwa hiyo bibi yake alimuita mama kama alivyomuona Sonia akimuita mama. Wazo la Sonia kama ni mama yake halikuwahi hata kupita akilini mwake. 

 **********************

“Mbona hujaenda kulala Kana?” Sonia alitoka kazini na kumkuta Kana akimsubiri. “Nilikuwa nakusubiria wewe.” Sonia akakaa. “Nataka nikuombe kitu.” “Unataka nini?” “Briana huwa anamlilia sana mama yake. Naomba kama tutaweza, tumpeleke akamwone.” Sonia alijisikia vibaya sana. Hakujua kama Briana huwa analia. 

Alibaki akifikiria kidogo. “Jumamosi nilipoenda kumuona mama Briana, bado hali yake haikuwa nzuri. Nisingependa Briana amuone mama yake katika hali ile. Kama unaweza kumwambia asubiri kidogo mpaka atakapopata nafuu itakuwa vizuri. Nitawapeleka wote tukamuone.” “Kumbe mwenzetu huwa unaenda?” Mama Sonia aliyekuwa ameshajilaza kwenye kochi akaingilia maongezi yao. 

“Ndiyo. Kila jumamosi huwa naenda kumtembelea. Lakini mama, hali ya mama Briana ni mbaya sana.” Wote walibaki kimya. 

 **********************

Ilimbidi Sonia apunguze shuguli nakuanza kutafuta muda wa kuwa karibu na Briana. Alikumbuka jinsi Nyange alivyomkabidhi Briana na kumuomba amwangalie binti yake tokea akiwa mtoto mdogo. Alipoongea na Briana, aligundua Briana anamalalamikomengi sana juu ya baba yake. Sonia aliumia sana, kwani alijua ni kiasi gani Nyange na Briana walivyokuwa marafiki. 

Nyange alimpenda sana Briana kuliko kitu chochote kile maishani mwake. Alikuwa kila akitoka kazini, akiingia tu ndani kabla hajasalimiana na mtu yeyote, Nyange huanza kuimba, ‘Nimepoteza kipenzi changu mjini Dar es salaam.’ Briana alipokuwa akisikia hivyo tu hata kama yuko mbali kiasi gani, alijua baba yake amerudi nyumbani na anamtafuta yeye.”

“Alikuwa akimkimbilia daddy wake, atamrukia na Nyange atambeba na kuanza kumuongelesha maneno mawili matatu ndipo aendelee na mambo mengine. 

Wakati wote Nyange alitaka kujua Briana alipo na anafanya nini. Kila mtu alimjua Briana kama ni kipenzi cha Nyange. Hata alipokuwa na rafiki zake, Nyange alimwaga sifa za Briana tu. 

Sonia alijaribu kumfariji Briana kwa kadiri ya uwezo wake. Alimueleza baba yake ni mgonjwa, lakini bado anampenda sana. Kwa Briana ilikuwa ngumu kuelewa kwani kwa nje alimuona vile baba yake alivyoonekana mzima, lakini kwa kuwa alimuamini Sonia aliona akubali tu. 

 **********************

“Mama? Briana amenieleza mambo yakusikitisha sana juu ya baba yake. Ninavyomjua Nyange, hiyo kweli siyo akili yake hata kidogo! Unakumbuka nilikusimulia jinsi Leah alivyosema alikuwa akijaribu kuwaloga? Ukute safari hii amefanikiwa mama.” 

“Nilikwambia Sonia. Leah na Mama yake kuna walicho fanya. Nyange amebadilika sana, hujawahi ona. Yaani namwambia Nyange, Briana anaumwa, amelazwa, wala hashituki? Sio Nyange ninayemjua mimi.” “Sasa tutafanyaje, mama?” 

“Yupo msichana huwa anapenda sana kuja pale saluni nakuongea mambo ya Mungu. Anasema alishakuwa mgonjwa karibia ya kufa, lakini aliombewa, akapona. Labda niongee naye, atupeleke na sisi hukohuko alipoombewa yeye na sisi tukawaombee Nyange na mkewe, labda watapona.” “Wazo zuri mama.” 

Huku nyuma, Maisha ya Leah

Leah alianza kumtesa sana mama yake. Na yeye alianza kumuhesabia chakula. Alitaka amtumikie mchana na usiku. Kwa kuwa Josh hakuwepo, alimuamsha asubuhi sana, kufagia nje na kufanya kazi za ndani. 

Pia aligundua kila anapolitaja jina la mama Briana, Nyange anabadilika kidogo. Aliamua kumuongezea dawa ili amsahau mkewe kabisa, kitu kilichosababisha kuharibu zaidi akili ya Nyange. Alibadilika akawa kama zuzu. Kazi zilimshinda kabisaa. 

Kazini akawa haendi tena, akabaki na kazi yakumganda Leah kila aendapo mle ndani mpaka chooni. Leah alianza kuchukia kufuatwa kila mahali. Alianza kumkaripia sana Nyange na kumpiga mara kwa mara. Na wakati wote Nyange ndio alimuomba msamaha Leah. “Naomba uniamini Leah. Nakupenda. Siwezi kuishi bila wewe mpenzi.” Leah alimfanya Nyange vile atakavyo. 

“Kama unanipenda mimi, nipe ile nyumba ya mama Briana.” Nyange hakukataakabisa. Leah alitafuta mwanasheria, akamchukua Nyange wakaenda kuandikishana, tena Nyange akiapa kumkabidhi Leah, yeye mwenyewe kwa akili zake timamu mbele ya mwanasheria. 

Kisha yeye mwenyewe Nyange alifuatilia ubadilishwaji wa jina wa ile hati ya ile nyumba waliyokuwa wakijenga Leah na Sam na kuandika jina kamili la Leah. 

Kwa kuwa Nyange aliikodisha hiyo nyumba kwenye kampuni ya kigeni, iliyokuwa ikiwaingizia pesa nyingi sana, Leah alimwambia ampeleke kwenye hiyo kampumi na kubadilisha mkataba. Alimtaka Nyange kuidhinisha malipo yote yaingie kwenye akaunti yake yeye Leah. 

Bila kubisha huku amejawa furaha Nyange alifanya kama Leah alivyotaka na kuandikishiana mkataba mpya na hiyo kampuni, Leah akiwa mmiliki halali. “Kweli nimeamini unanipenda Nyange.” Nyange alianza kucheka 

“Unakumbuka nilikwambia mimi mjamzito?” Nyange alimkumbatia Leah lakini Leah alimsukuma. “Hebu acha ujinga bwana, tuongee mambo ya maana. Ujue anakuja mtoto wetu wa kiume? Utampa nini sasa?” “Chochote utakacho mpenzi wangu. Wewe chagua tu.” “Unasemaje juu ya hii nyumba?” Nyange alianza kucheka. “Unachekacheka nini sasa? Ndio uchangamke dume linakuja.” 

Hiyo nyumba nayo ilikuwa na jina la Briana na ndipo alipokuwa amezikwa Junior. Hapakuwa na jinsi mama Briana angekubali hiyo nyumba ichukuliwe na mtu yeyote. Leah akifahamu hilo, lakini alihakikisha anamshawishi Nyange mpaka anampa yeye hiyo nyumba, tena kihalali kabisa. 

Taratibu Leah alihakikisha MALI ZOTE za Nyange na mkewe, zipo kwa jina lake yeye, tena kihalali kwa maandishi chini ya usimamizi wa mwanasheria wake. Alipohakikisha mali zote zimekuwa kwa jina lake ndipo alipotulia na kuendelea kumnyanyasa Nyange apendavyo. 

Pesa zilikuwa zikiingia kwa jina lake yeye tena kwenye akaunti yake Leah, kwa hiyo kazi yake kubwa ilikuwa kula, kulala na kutoka kwenda pasipojulikana akitumia gari la Briana kama lake, lakini wazi alionekana hana furaha. 

Nyange alianza kupigwa makofi kama mtoto. Hata alipokuwa akililia mapenzi kwa Leah, sio tu alikuwa akimpiga makofi tu, bali alimfukuza kabisa mle ndani akamuhamishia alipokuwa akiishi Josh akimuona ni kero mle ndani. Maisha ya Nyange nayo yalianza kuwa ya mateso makali sana, hata kula yake ilianza kuwa ya shida. Aliugua bila yakupata msaada wowote. 

Kwa Mungu Wa Wasiyowezekana

Asifiwe alipita saluni kwa mama Sonia kusalimia, na kama kawaida yake na kuongea mambo ya Mungu kama afanyavyo kwa wengine. Mama Sonia alimuomba wazungumze. Alikaa akamueleza mwanzo mpaka mwisho wa familia ya Nyange. Asifiwe alisema yeye anajua shetani ndio muovu, na wakati wote anaangalia roho ya mtu iliyo tayari kutumika, ndio anamtumia huyo mtu kufanya uovu wake kuumiza watu wengine lakini wala sio binadamu na chakufanya nikuingia kwenye maombi. 

“Mungu tu ndiye mwenye uwezo wakumshinda shetani, si vinginevyo.” Asifiwe aliongeza. “Kwa hiyo utatupeleka kwa mchungaji wako akawaombee.” Asifiwe akacheka kidogo. “Unajua hata mimi na wewe tunaweza kuomba?” Mama Sonia alisita. 

“Unajua sisi hata kanisani hatuendi! Sasa leo uniambie kuombea kichaa! Nitaweza wapi?” “Usiogope kila kitu ni hatua.” Asifiwe aliongea sana na mama Sonia kimapana juu ya Mungu mpaka mama Sonia alipoelewa vizuri na kumkaribisha kanisani kwao. 

**********************

Siku ya jumapili kwa mara ya kwanza mama Sonia na watoto wote walienda kanisani. Baada ya ibada Asifiwe aliwatambulisha kwa Mchungaji na kupata muda mrefu wa pamoja. Mchungaji alisema kuanzia kesho yake, yaani jumatatu waingie kwenye maombi ya kufunga na kumuombea mama Briana na Nyange. 

“Naomba na mimi nifunge.” Briana alikatiza mazungumzo na kumfanya kila mtu abaki akimwangalia. “Na mimi nitafunga, ili nimuombee mama Briana.” Briana alirudia. “Si tutafunga wote Kana?” Kama kawaida yake tokea wako watoto, Briana hakufanya kitu bila Kana. “Tutafunga wote Briana.” Kana alijibu na kumshika mkono. 

Wote waliingia kwenye maombi kasoro Brayan ambaye hakuwa akielewa. Asifiwe aliwafuata kila siku usiku kuomba nao nyumbani kwao na siku ya jumatano walienda kanisani kwenye kipindi cha maombi kuomba na watu wengine. 

Walipotoa ushuhuda wao siku hiyo ya maombi walipokuwa kanisani, wote waliokuwepo pale kwenye maombi siku hiyo walitaka kuwaunga mkono kwenye maombi na Mchungaji aliwashauri ijumaa waende kanisani kwa mkesha. 

 **********************

Kama kawaida yake, baada yakutoka kazini siku ya jumamosi alimpitia mama Briana. “Anaendeleaje leo?” “Tunaona mabadiliko makubwa sana. Ile hali yakufanya fujo imeisha. Ametulia kweli.” Sonia alishituka sana. Kwani siku zote alikuwa akimchungulia dirishani na wakati wote alimkuta amechomwa sindano amelala apumzike baada ya fujo nyingi sana au alimkuta akiwa anajitupatupa sana. 

“Unaweza kuingia tu ukamuona.” Sonia alianza kulia sana baada yakumuona mama Briana uso kwa uso. “Dada? Dada?” Sonia aliita. Mama Briana alikuwa kimya tu. “Mama Briana?” Alinyanyua kichwa nakumwangalia Sonia. “Briana na Brayan wanakusalimia. Briana anakulilia sana kila siku usiku anakutaka wewe. Lazima upone dada, utoke hapa ukalee watoto wako. Umesikia dada?” Mama Briana alikuwa akisikiliza tu. 

Sonia aliendelea kulia mwishowe alipoona mama Briana hajibu kitu akaamua kuondoka nakurudi nyumbani. Alimuelezea Mama yake kila kitu. “Mimi naendelea na maombi Sonia. Mama Briana anaweza kupona!” Mama Sonia aliamua kuendelea kuomba. 

 **********************

Siku ya jumatatu Sonia alimuomba bosi wake apitie kwenda kumuona mama Briana kwanza ndipo aende kazini. “Lakini usichelewe Sonia. Kuna wageni kutoka makao makuu wanakuja kukagua. Afisa mwajiri mkuu wa Bank {HR Manager} pia atakuwepo na viongozi wengine. Najua watataka maelezo mengi kwenye kitengo chenu cha mikopo na nina kutegemea wewe.” “Sitachelewa Bosi wangu. Nitajitahidi kuwahi.” 

Kutokana na maombi ya nguvu waliyokuwa wamefanya siku ya jumapili, Sonia aliamka asubuhi na mapema kuelekea tena hospitalini Mirembe, huku akiwa amejawa na tumaini la kupona kwa mama Briana. 

Alifika pale, akaambiwa hali ya mama Briana inaendelea vizuri, hata amepunguziwa dawa alizokuwa akipewa. Sonia aliendelea kumkumbusha juu ya watoto wake, huku akimtaja sana Baby Brayan. “Amekuwa mkubwa kweli! Ukimuona utafurahi sana dada. Mpole kama wewe, lakini mrefu kama Nyange. Wanashindana urefu na Kana.” Sonia aliendelea kujiongelesha, mwishowe akaamua kuondoka kuwahi kazini kama alivyoombwa na bosi wake asichelewe. 

Hatimaye…

Sonia alipoingia tawini alikuta magari mageni(V8) za nguvu hapo nje kwenye tawi lao, akajua wazi wageni alio ambiwa watafika kutoka makao makuu, Dar, wameshafika. Alikuta tayari wafanyakazi wenzake wote wamekusanyika sehemu wanayo kutania kwa ajili ya vikao vya asubuhi. 

Alitembea kwa kunyata mpaka sehemu walipokuwepo wafanyakazi wote. Alipofika karibu, nusura aanguke. “Sonia!?” Sam ambaye ndio alikuwa mzungumzaji kwenye kikao hicho, naye alishituka sana kumuona Sonia pale, nakufanya kila mtu amgeukie Sonia. 

“Sonia?!” Afisa mwajiri naye alishituka kumuona Sonia Dodoma. Kwani na yeye alimfahamu Sonia tokea siku ile alipotaka kubakwa kwenye sherehe za kufunga mwaka za ofisini kwao. Kwa hiyo hakuacha kufuatilia habari za Sonia kupitia Sam.  

Kulizuka ukimya mkubwa, wafanyakazi wote walibaki wakiwashangaa mabosi hao, waliokuwa na nafasi za juu sana katika benki hiyo, waliofika siku hiyo asubuhi, wakimshangaa Sonia, msichana mrembo wa kuvutia, aliye kuwa mkimya sana pale tawini, na wala hakuwa na rafiki hata mmoja. Aliyeacha wateja wakipigana vikumbo pale tawini bila mafanikio yeyote kwa Sonia. Wakati wote Sonia alibaki fumbo, lililoshindwa kufumbuliwa si na wafanyakazi wenzake tu, hata wateja wao. 

Hakuonekana popote pale isipokuwa pale kazini tu. Hakuongelea chochote na wafanyakazi wenzake juu ya maisha yake binafsi isipokuwa maswala ya kazi yake tu. 

**********************

“Samahani nimechelewa, nilipitia hospitalini kwanza.” Sonia aliamua kuvunja ukimya na hali ya mshangao iliyokuwa imetawala pale. “Hujachelewa sana. Ndio mheshimiwa Samweli alikuwa akituelekeza juu yamabadiliko ya “System” nzima za benki.”

“Ambayo tutahamia miezi michache kuanzia sasa.” Kiongozi wa tawi, Bosi wake Sonia alijibu nakumgeukia Sam kumtaka aendelee. Lakini Sam alibaki akimwangalia Sonia bila hata kupepesa macho na kufanya kila mtu abaki akishangaa. Taratibu Sonia alijivuta nyuma ya mtu aliyekuwa amesimama pembeni yake na kuinama kama kujificha nyuma yake. 

 **********************

Machungu yasiyoweza kutamkika yanaendelea kwenye familia ya Nyange. Leah ameshika usukani wa mali zote na maisha ya familia ya dada yake, tena safari hii kihalali . 

* Je Nini kitaendelea kwenye familia hiyo iliyo sambaratika, na Nyange aliyefungiwa chumba cha nje?

Sam ndani ya nyumba. Uso kwa uso na mrembo Sonia. 

Majeshi Yamehamia Dom.  

*Je nini kitaendelea, ndani ya jiji kuu la Tanzania?   

Usikose Part 3 yenye mengi ya kusisimua.

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment