Paul alijiweka sawa akifikiria aanzie wapi kumuelezea Sonia na watu wengine wanao msikiliza. “Njoo kwanza hapa karibu yangu.” Sonia akasogea karibu na baba yake akakaa upande wa kushoto. Paul akamvuta karibu yake zaidi. “Ewaaah! Sasa unisikilize kwa makini.” Sonia akatabasamu.
“Niliporudi kutoka masomoni, nikajenga hiyo nyumba tutakayoenda kuishi na mama yako. Babu na bibi yako waliugua sana, na sisi hatukuwepo kuwauguza ila huyo mwanamke niliyekuja kumuoa baadaye, ndiye aliyekuwa akiwahudumia na ndiye msichana niliyetakiwa kumuoa tokea zamani lakini nilimkataa na kutoroka na mama yako.”
“Sisi ndio kina nani, ambao mlitakiwa kuwauguza wazazi wako?” Paul alicheka kidogo na kumgeukia Ishimwe. “Hiki kichwa kweli changu, sihitaji kupima.” Ishimwe alicheka lakini wazi alionekana kumuhurumia Paul.
“Una shangazi zako wawili na anko wako mmoja. Lakini wote wamechuka uraia wa nchi za nje, hawaishi hapa. Kwa hiyo tulizaliwa wanne, mimi nikiwa mtoto wa tatu, katikati ya dada zangu. Umeelewa?” “Kwa hiyo wa kwanza ni kaka yako, akafuatwa na dada yako, halafu wewe, na wa mwisho ni dada yako.” “Ewaaaa! Safi sana.”
“Sasa wakati wazazi wakiugua wote hatukuwepo nyumbani kasoro huyo mchumba mtu, aliyekuwa ametafutwa na mama kwa ajili yangu, ndiye aliacha kazi zake Morogoro na kwenda kuwauguza wazazi wetu Shinyanga. Baba alipofariki na mama alipopona yule ‘mchumba’ akarudi kwake Moro. Akawa anakuja Dar kwangu kutembea. Baada ya muda akanipigia simu kuniambia ni mjamzito.” Sonia alishituka kidogo na Paul akamuona.
“Usiulize tena swali jingine Sonia. Wewe sikiliza tu.” Sonia alicheka. “Ulijuaje?!” “Kwa kuwa tabia zako hazitofautiani na za baba yako. Kwa hiyo kuanzia sasa, maswali yamezuiliwa.” Wote walicheka.
“Ndio tukaoana, akajifungua hao watoto mapacha. Baada ya muda akaamua kuondoka, akisema alikuwa na mchumba wake tokea zamani pale kwangu hana furaha, anataka kurudi kwa mpenzi wake. Basi akaondoka na kuniachia hao watoto wakiume mapacha, tena wakiwa wadogo sana.”
“Sasa sijui nilifungwa vipi macho na kushindwa kuelewa bwana, mpaka mama yako aliponifungua macho hapa majuzi. Ndio maana nakwambia namuitaji sana mama yako maishani. Kabla hatujasafiri nilimuomba Ishimwe anisindikize hospitalini kufanyiwa vipimo na kuagiza dereva awalete wale watoto pale, ili na wao wapimwe, nijue kama kweli ni watoto wangu au nilikuwa na hangaika na watoto wa watu.” Kila mtu alikuwa makini kusikiliza.
“Sasa ndio nimepigiwa simu sasa hivi kupewa majibu.” “Pole baba.” Sonia alishajua majibu kutokana na unyonge wa gafla wa Paul. “Na kweli nahitaji pole mwanangu. Nimewalea wale watoto kwa shida sana, na miaka yote nikijua ni wangu! Tangia wanazaliwa mpaka sasa, nalea mwenyewe, tena kwa mateso makali, bila msaada wa mama yao.” “Pole sana. Sasa utafanyaje?” Sonia alirusha swali jingine, lakini Paul alitulia kwa muda, akifikiria.
“Pole sana Mkuu.” “Pole sana Paul.” Kila mtu alimpa pole. “Daah! Asanteni.” Paul aliendelea kuwaza. “Naona wazo la Ishimwe ni zuri. Leo sidhani kama ni siku nzuri ya kwenda wote huko nyumbani, ngoja nikaweke mambo yangu sawa, ndipo nije niwachukue.”
“Sitaki niharakishe kumtambulisha Sonia au Ishimwe na Kana kwa wale watoto. Wanatabia mbaya sana. Sijui nafanyaje!?” Kila mtu alibaki akijiuliza hao watoto ni watoto wa namna gani.
“Hamna shida kabisa. Wewe nenda ukatulie, upate muda wakufikiria, ili ujue cha kufanya.” Sonia aliongeza, kukubaliana na wazo la mama yake. “Mnivumiliejamani. Naamini kila kitu kitakuwa sawa.” “Wala usijali Paul. Sisi tupo sawa kabisa. Tunakuombea hekima ya Mungu kwenye maamuzi yako.” Ishimwe alizidi kumfariji mpenzi wake.
“Asante, lakini namshukuru Mungu kuniletea Sonia. Sijui ningeumia kwa kiasi gani kujikuta na uzee huu sina mtoto hata mmoja! Nashukuru Mungu hata kwa kunihurumia na kukumbuka mateso niliyoyapata na wale watoto, akanirudishia mwanangu. Nahisi ningechanganyikiwa zaidi. Angalau sasa hivi nina mmoja.”
“Usiseme hivyo baba, naweza kupata mdogo wangu mwingine.” Sonia alimchokoza mama yake. “Sonia wewe!?” Ishimwe alishituka sana. “Kweli bwana Sonia. Huwezi jua. Ishimwe anaweza kunihurumia akaniongezea mwingine wa mwisho.” “Paul! Na uzee huu?!” “Kwani shida ipo wapi? Sonia atamlea. Au unasemaje Sonia?” “Tena nitafurahi kweli! Sam anapenda sana watoto, tutamlea mdogo wetu. Nyinyi ongezeni mwingine.” “We Paul acha kumsikiliza Sonia, sisi tumeshazeeka.” “Hapana bwana! Mimi ndio nimezeeka, wewe mwenzangu ndio kwanzaa unaanza miaka arobaini, unaogopa nini?” Ishimwe alibaki akifikiria.
“Usije kunikimbia bure, nakutania bwana.” “Siwezi kukukimbia Paul. Wewe nenda ukatatue hili kwanza, mengine yatajileta yenyewe.” “Ndio maana nakupenda Ishimwe wangu.” Paul alimgeukia Ishimwe na kumbusu bila aibu. “Naomba nisindikize Ishimwe.” Paul na Ishimwe wakatoka nje. Wakati wote mlinzi 'bodyguard' wa Paul alisubiri nje.
********************
“Naomba uchukue hizi pesa za matumizi ya hapo nyumbani, angalau kumsaidia Sam.” “Usiwe na wasiwasi Paul. Sisi tupo sawa.” “Kwa hiyo unataka Sam aendelee kunilishia mke wangu, na watoto?! Huoni aibu mke wa Judge Mkuu mzima, unakula na kulala kwa watu bure?” Mama Sonia alicheka. “Asante Paul.” Akapokea.
“Lakini sitakawia Ishimwe, nitakuja kukuchukua.” “Usiwe na wasiwasi kuhusu mimi Paul, nitakusubiri tu.” Akamvuta Ishimwe karibu yake zaidi, mbele ya mlinzi wake na kuanza kumbusu kwa muda mrefu kisha akamwangalia.
“Hivi nilishakwambia nakupenda?” “Mhh! Sikumbuki Paul.” Wote walicheka. “Basi nakupenda sanaaa.” “Asante. Hata mimi nakupenda Paul.” “Sasa ngoja mimi niwahi. Lakini muda si mrefu, tutakuwa wote tena Ishimwe.” “Naamini hivyo Paul. Kila la kheri.” “Asante.” Waliagana tena kwa busu, kisha Paul akaondoka.
*********************
Asubuhi ya siku inayofuata, ilikuwa siku ya jumamosi, wote walichelewa kuamka. Walisikia mlango ukigongwa. Sam aliamka kwenda kufungua. “Karibu.” “Nimetumwa na Mkuu nilete mizigo, ipo kwenye gari.” Sam alishangaa kidogo. “Unaweza kunionyesha pakuweka?” Dereva aliuliza.
“Bila shaka. Karibu.” Sam alimsaidia kushusha, hayo magunia ya vyakula kwenye gari na kuingiza ndani. Sababu ya kukuru kakara nyingi, kila mtu aliamka na kutoka kushuhudia kinachoendelea. Walibaki wakishangaa.
“Nani ameleta!?” Nyange akauliza. “Baba yake Sonia.” Vilikuwa vyakula vingi sana, vilivyowatoa macho watu wote. Mama Sonia aliingia ndani na kuchukua simu yake, akatoka kurudi jikoni alipokuwa Sonia na mama Briana wakisaidia kupanga hivyo vitu vilivyoletwa, akatuma ujumbe wa kushukuru kwa Paul.
“Si ungempigia kushukuru, kuliko kutuma ujumbe? Hivi vitu ni vingi sana mama, sijui hata tutaweka wapi! Friji imejaa.” “Sitaki kumsumbua, najua yupo kwenye wakati mgumu sana sasa hivi, anahitaji muda mtulivu wakufikiria. Nikipiga simu sasa hivi, nitakuwa nikimwingilia.” Sonia alifikiria kidogo.
“Nimekuelewa mama. Na mimi nimejifunza kitu.” Wote wakacheka. “Kweli tena mama, ingekuwa mimi hapo ningeshampigia simu zaidi ya mara kumi tokea tulipoachana.” “Sonia wewe! Sasa huo muda wakufikiria ataupata saa ngapi?” “Mbona nitajirekebisha! Maana Sam mpaka wakati mwingine namuonea huruma! Kila saa nampigia simu.” Walizidi kucheka wote watatu wakiwa jikoni.
“Kazi zitamshinda huyo Sam.” Mama Briana aliongeza. “Ndio maana nimesema nitajirekebisha jamani! Kuanzia jumatatu akienda kazini simpigii simu hata moja mpaka arudi hapa.” “Wewe huyo Sonia au mwingine?” “Utaniona dada.” Wote walicheka.
“Anawadanganya mwenzenu.” Sam alikuwa akiwasikiliza kwa nje ya jiko akiwa stoo na Nyange wakipanga magunia yaliyoletwa. “Sam wewe!” Sonia hakujua kama Sam anawasikiliza. “Yaani mama Sonia, nikitoka hapa nasema naenda kazini, ujue ni kama naenda kufanya kazi ya u ‘operator’. Kutwa nina kazi ya kupokea simu zake huyo, mpaka kila mtu anajua huko ofisini.”
“Simu yangu ikiita tu, utasikia kila mtu anasema ‘Soniaaa!!’.” Kila mtu alianza kucheka mpaka mama yake Sonia. “Sam wewe! Kweli?” “Nakwambia kweli tena Sonia. Unajua mpaka Mr. Mwansasu yule afisa mwajiri, rafiki yangu, imenipa zawadi ya ‘Bluetooth’ ya kuvaa tu sikioni, ili ukipiga tu simu hata kama nipo kwenye kikao, niwe na bonyeza tu uwe unasikia na kujua nilipo bila hata yakuse ‘Haloo’.” Kila mtu alikuwa akicheka.
“Na alivyo Sonia, hata akipiga akinisikia labda nipo kwenye kikao au nalumbana na mameneja matawini, unafikiri atakata? Anaweza kubaki anakusikiliza hapo kwenye simu hata nusu saa.” “Sonia wewe! Ukoje?! Basi sisi tunajua yupo chumbani kalala.” “Basi mkiona hayupo hapo sebuleni, mjue yupo chumbani kwenye simu.” “Kwa hiyo Sam unanisemea kwa mama na mama Briana?” “Hamna bwana mimi nafurahia.” Wote walicheka.
“Mapenzi yana wenyewe bwana!” Nyange aliyekuwa kimya muda wote alitupia neno. “Basi nitajirekebisha.” “Sio ndio ujirekebishe usipige simu kabisa!” “Afadhali unitetee shemeji yangu.” “Upige, lakini na wewe sio ndio unataka ubembelezwe kwenye simu siku nzima! Kazi zitamshinda mwenzio. Asubuhi mkiagana hapa, muache mwenzio afanye kazi mpaka mchana kujua kama amekula, basi.” “Hee!” Sonia alishituka sana.
“Mara moja tu jamani!?” Wote walicheka. “Si niliwaambia, hawezi huyo!” “Hapana na wewe Sam, sio ndio uwe unapigiwa tu wewe kila wakati! Unapopata nafasi kidogo, na wewe mpigie kumjulia hali.” “Afadhali shemeji umwambie Sam. Akitoka hapa, hanikumbuki tena!” “Kweli kazi hapo unayo mama Briana!” Mama Sonia alimgeukia mama Briana aliyekuwa akicheka muda wote huku akisikiliza. “Nitaongea naye biharusi wangu, ataelewa tu.” Wote walikuwa wakicheka.
Mtu na Mtuye.
Ilipofika jioni walishangaa Paul anaingia akiwa amechoka sana. “Umekula?” Mama Sonia alimuwahi mara tu alipokaa. “Nina usingizi Ishimwe! Naomba twende tukalale kidogo. Halafu tutarudi baadaye.” Mama Sonia alibaki haelewi. “Tunaenda wapi Paul?!” “Si kwetu?” “Wale watoto?” “Nishawarudisha kwa wazazi wao Morogoro.” “Paul!” Kila mtu alibaki akishangaa.
“Sijalala mwenzio tokea jana usiku, nazunguka humo mabarabarani. Yaani mida hii tumetoka Morogoro, tukamshusha mama uwanja wa ndege, nikamwambia dereva tupitie hapa nije kukuchukua, ndio twende nyumbani.” “Ulikuwa na Mama Tambo!?” Ishimwe alishituka sana.
“Shuguli haikuwa ndogo! Naomba twende nikapumzike, nikiamka ndio nitakuelezea kila kitu. Nimechoka sana na kichwa kimevurugika kweli, lakini siwezi kulala bila wewe kuwepo pale. Naomba twende.” “Pole sana Paul. Basi ngoja nijiandae, ili twende.”
“Pole.” “Asante Sonia. Naomba tupe muda, mama yako akishaandaa hapo nyumbani, atawaita ili na nyinyi mje kupaona. Pamevurugika kweli, hapafai! Hamna hata pakukanyaga.” “Hamna neno. Wakati wowote ule sisi tutakuja kuwatembelea.”
Paul alibaki ameegemeza kichwa chake kwenye kochi huku amefunga macho, akimsubiria Ishimwe, wazi alionekana amechoka. Baada ya ukimya wa muda kidogo Sonia akamsogelea baba yake. “Asante kwa vyakula, tumeletewa leo asubuhi.” “Afadhali kama vimefika. Maana nilikuwa natoa maagizo huku nimechanganyikiwa sikujua hata kama alielewa yule Mzee wa watu.”
“Pole.” Sonia alirudia. Paul alitabasamu huku akimwangalia Sonia. “Asante Sonia.” Sam naye alisimama kumpa mkono. “Asante sana. Naona hatutanunua vyakula humu ndani mpaka mwakani.” Paul alicheka kichovu. “Nyinyi mpo wengi hapa mna….” Paul alibaki na kigugumizi baada ya kumuona Ishimwe. Alibaki amemkodolea macho. Alitoka akiwa amependeza sana.
*********************
Kwa asili Ishimwe alikuwa na kipaji cha upambaji. Kuanzia nyumba mpaka mavazi. Hata kama nyumba ina vitu vichache kiasi gani, au vingi visivyo na mpangilio, akiingia yeye kwenye hiyo nyumba, anaweza kukupangia nyumba vizuri ikapendeza, kadhalika na urembo wa mwili pia.
Watu wengi walipenda saluni yake kwa kutoa ushauri, kabla hajakutengeneza. Kila mteja aliyefika kwenye saluni yake, alimpa ushauri unaoendana na sura na aina ya nywele zake. Alihakikisha kila mtu anayetoka saluni kwake, amependeza na ameridhika. Kutokana na hekaheka za maisha, hakuna aliyewahi kumuona Ishimwe asilia.
Ishimwe wa safari hii, alifanyiwa ‘shopping’ ya nguvu na Paul. Alimpeleka madukani, akamwambia anunue kila kitu anachohitaji kuanzia asubuhi anapoamka, mpaka usiku anapolala. Chochote kile anachohitaji, awe anatakiwa kutoka kwenda kwenye safari za maana au za kawaida, Paul alimwambia achague, yeye atanunua kwa garama yeyote ile, asijali wala kuogopa pesa.
Na kweli siku hiyo Ishimwe alinunua kila kitu, akisaidiwa kuchagua na Paul, huku Paul akimsisitiza, kutojali garama. Kwa hiyo alikuwa na kila kitu kilichohitajika mwilini mwake. Tena vitu vyote alivyonunuliwaa vilikuwa vizuri na vya thamani.
Alijiapia kutorudia kuvaa nguo hata moja ya zamani. Alijibadili akawa watofauti sana. Kila mtu alimuona jinsi alivyobadilika. Kila alichokiweka mwilini mwake, kilivutia. Ishimwe alirudi kuwa mrembo kuliko hata mwanae Sonia.
Siku hiyo alivaa kigauni chenye rangi moja tu, kijani kibichi. Kutokana na rangi yake ya mwili, rangi za gauni hilo zilimfanya azidi kuvutia. Lilimkaa vizuri sana kwenye umbile lake kama alilomrithisha mwanae. Nywele alizokuwa ametengenezwa huko alipokuwa amekwenda mapumzikoni na Paul kwa siku tano, nazo zilizidi kumfanya apendeze. Aliziachia nyuma, mbele akazibana kutokana na sura yake.
Alivaa na sandals ya juu kidogo, wazi mbele, iliyofanya kucha zake zilizokuwa zimetengenezwa saluni akiwa na Paul, kuvutia zaidi. Ukweli Ishimwe alizidi kupendeza na kuonekana mdogo zaidi. Utajiri ulionekana kuanzia alipotokezea, harufu yake ilibadilishwa na Paul, akanukia vizuri sana. Sebule nzima ilinukia manukato aliyojipulizia.
*********************
“Usingizi umeisha mwenzenu!” Paul alimtania Ishimwe. Wote walicheka. “Ndiomaana niliona nije tu kukuchukua, nisije nikaibiwa bure! Kupendeza gani huko? Au unanifanyia kusudi?” Ishimwe alicheka sana. “Twende bwana Paul ukalale. Ona ulivyochoka!” “Kwa mwende huo uchovu unakuwa haupo!”
“Hivi nyinyi wenzangu mlimsikia lakini Ishimwe pale jana wakati akinifukuza hapa? Eti ‘wewe nenda tu, hata mpaka mwakani’! Basi mimi kule nilipokuwa, akili zilikuwa hazifanyi kazi kabisa mwenzenu! Kila nikijaribu kufikiria matatizo yangu, nakumbuka nilivyoambiwa niondoke mpaka mwakani, nikajua kuna mchezo Mtu Mzima nataka nichezewe. Na hivi mwenzangu ndio kuna kuchwa, nikahisi nitachanganyikiwa bure! Nikaona ni heri nije nimchukue tu, roho yangu initulie.” Wote walizidi kucheka mpaka Ishimwe mwenyewe.
“Nilikuwa sikufukuzi bwana Paul! Nilitaka utulie, ufanye maamuzi mazuri.” “Kwa utulivu gani unaomaanisha wewe? Heri tu twende wote. Ukishaingia kwenye ile nyumba, ndio nitatulia.” Ishimwe alizidi kucheka.
“Umependeza sana mpenzi wangu!” “Asante.” “Umependeza mama, na nguo zako nzuri!” “Amenichagulia Paul huyo!” “Umependeza sana Ishimwe.” Mama Briana alidakia. “Ewaaah! Ni Ishimwe sio Mama Sonia. Twende zetu mpenzi wa Paul.” Walicheka na kuondoka.
Andiko La Mungu…
Njia nzima Paul alikuwa amelala. Hakuongea kitu, lakini dereva alijua wazi wanapoelekea. Ishimwe alibaki ameshikilia mkono wa Paul akiwaza maisha mapya anayoenda kuanza tena na mwanaume anayempenda. ‘Naamini safari hii ndio mpaka kifo. Mungu ameamua kunipumzisha. Nimetangatanga vyakutosha.’ Ishimwe alijiambia huku akimwangalia Paul.
‘Enzi zinarudi jamani! Tunaanza maisha mapya tukiwa wawili tu, kama mwanzoni! Mimi na Paul wangu.’ Ishimwe alicheka kidogo na kuendelea kufikiria. Alikumbuka wakati wanatoroka mara ya kwanza nyumbani kwa kina Paul, kwenda kuanza maisha yao, bila ya kujua waendapo, wakiwa hawana kitu chochote isipokuwa mapenzi tu.
Lakini sasa mambo yamewabadilikia. Wanaenda kuanza maisha mapya wakiwa na kila kitu wanachokihitaji maishani. Mawazo kadhaa yaliendelea kupita kichwani kwa Ishimwe, akiwa kwenye gari hilo. Si dereva, wala Mlinzi wa Paul aliyemuongelesha mwenzake. Wote walikuwa kimya kasoro wao wawili tu ndio walikuwa wakiongea wakiwa njiani, kabla ya Paul kupotelea usingizini.
‘Nimerudi kuwa Ishimwe, lakini sio Ishimwe wa zamani, karibuni sana nitajulikana kama Ishimwe Tambo. Itakuaje? Mke wa Judge Mkuu wa Tanzania!’Ishimwe alitabasamu, huku gari ikiendelea kushika kasi asijue waendapo.
Gafla hofu ikamuingia. Taratibu hali ya kupaniki ilimnyemelea. ‘Marafiki wa Paul wote tokea zamani ni wasomi na watu wakubwa sana hapa nchini. Kama sio mawaziri basi ni Maraisi. Maongezi yake yote ni ‘rafiki yangu yule waziri wa… au tulienda kwa chakula cha usiku Ikulu.. na tukaenda nchi...’ Itakuaje? Sijasoma wala sijui kuongea kingereza. Nitamtia aibu Paul! Hivi ameshalifikiria hilo? Au tumekurupuka tu.’ Hakujua walipo wala wanapoelekea, muda wake wote aliutumia kuwaza huku akimwangalia Paul aliyelala na kweli alionyesha amechoka.
Mara aliona geti likifunguliwa bila honi wala kiashirio chochote. Kulikuwa na maaskari kadhaa mlangoni. ‘Hawa wote ni walinzi au kuna tatizo.’ Macho ya Ishimwe yalipokelewa na madhari nzuri sana ndani ya lile geti. Alibaki ametoa macho jinsi nyumba ya Paul ilivyokuwa kubwa na nzuri. ‘Ni kubwa kuliko ya Nyange!’ Ishimwe aliendelea kuwaza huku dereva akisogeza gari karibu kabisa ya mlango mkubwa, wazi alijua ndio mlango wakuingilia ndani ya nyumba hiyo.
*********************
Nyumba yenyewe ilikuwa karibu kabisa na baharini. Gari lilisimama. Ishimwe alibaki kutoa macho nje ya dirisha la upande wake. Baada ya muda kidogo kama aliyeambiwa amefika, Paul akafungua macho na kuangalia dirishani. “Tumefika Ishimwe. Karibu nyumbani.” Mlinzi wa Paul alimfungulia Paul mlango wa gari. Baada ya Paul kushuka, akazunguka upande alipokuwa amekaa Ishimwe, kisha akamfungulia na yeye mlango. ‘Mmh!’ Ishimwe akaguna mawazoni.
Aliwasogelea askari aliyekuwa amevaa sare za kipolisi. “Pole na safari Mkuu!” “Nashukuru sana. Na niombe radhi kwa usumbufu.” Paul alijibu akiwa amemshika mkono Ishimwe. “Bila shaka. Kila kitu kipo sawa kabisa. Nitaacha tena askari wawili wa ziada, kwa hizi siku mbili mpaka tujiridhishe kabisa kama pako salama.” Yule askari aliendelea kuongea na Paul, na kuibua hofu kwa Ishimwe.
‘Mbona kama Paul anaonekana anaishi kwenye mazingira hatarishi!? Ninikilitokea?’ Ishimwe aliendelea kuwaza. “Asante sana. Basi na mimi naomba nikapumzike, tutapeana taarifa baadaye.” “Asante sana.” Yule askari akaondoka.
*********************
Aliwaacha Paul na Ishimwe wakiwa bado wamesimama. “Nimechoka sana, nataka nikalale.” Paul alimgeukia Ishimwe aliyekuwa amemshika mkono wakati wote, lakini Ishimwe alionekana kuwa mbali sana na lile eneo. Akili zake ndio zilikuwa zimevurugika zaidi ya Paul. Kila kitu cha mahali pale kilizidi kumchanganya Ishimwe.
‘Ndio nitaanza kujulikana kama mama mwenye nyumba hii?! Mbona siendani kabisa na haya mazingira?’ Taratibu alimgeukia Paul kutaka kujifananisha naye. ‘Kweli tumekuwa watu wazima. Paul ameanza na kuzeeka!’ Uchovu wa Paul ulionekana mpaka usoni. ‘Hapana, huu ni uchovu tu. Hatujapishana sana ki umri na Paul. Kwani kulitokea nini tokea tuachane? Mbona Paul wangu amezeeka gafla!?’ Ishimwe aliendelea kuwaza.
*********************
“We Ishimwe vipi bwana!? Mbona naongea peke yangu?” Ishimwe alicheka kidogo. “Nilijua bado unaongea na yule polisi.” “Polisi gani? Mbona alishaondoka muda mrefu? Unawaza nini?” Ilibidi Ishimwe azungushe macho kuangalia ile nyumba tena huku akimtafutia jibu Paul. Macho yake yalitua kwenye baharini iliyokuwa mbele ya nyumba hiyo.
“Nashangaa nyumba yako Paul!” “Unashangaa nini sasa?” “Ilivyo kubwa na nzuri. Kwani hapa wapi?” “Ipo mpakani mwa Mikocheni na Kawe. Halafu usiseme kitu kwanza, mpaka uingie ndani ukajionee mwenyewe, ndio umwage hizo sifa zote.” Kwa nje kulikuwa kukivutia sana.
“Twende tuingie ndani, mwenzako nimechoka sana, nataka kulala. Tukiamka ndio tutatoka nje uzunguke ili upaone vizuri.” “Naona mwenzangu unaishi baharini kama meli!” Paul alicheka. “Hili eneo alinipa mama. Si unajua hawa wazee wa zamani waliwahi viwanja vikubwa enzi hizo? Wote tulizaliwa na kukulia hapa kabla ya baba kustaafu na kuamua kurudi kuishi kwao Shinyanga. Sasa niliporudi tu kutoka masomoni, nikiwa bado nimemkasirikia sana mama na nikakataa kabisa kurudi kuishi nao kule Shinyanga, nikaenda kukodisha nyumba Sinza.”
“Ndio mama akaniambia nije kuishi hapa. Akaniambia hata nikitaka nibadili hati ya hili eneo, niweke kwa jina langu. Kama nilivyokwambia palikuwa na nyumba ya kawaida tu ya familia, sikutaka kuitoa kwa ajili ya kumbukumbu yetu sisi watoto, ipo kule kwa nyuma. Ndio nikaamua kuhamia kwenye hiyo nyumba ndogo huku nikijenga hii taratibu bila hata haraka.”
“Maana nilikuwa nikiishi huko nyuma peke yangu, kwenye hiyo nyumba ya familia. Usiione hii nyumba kubwa hivi, nimeijenga kwa muda mrefu sana, zaidi ya miaka sita, nikahamia nilipooa.” Paul alimtazama Ishimwe. “Nini sasa? Nilijua lazima uoe Paul jamani, wala sikulaumu. Hongera.” Paul alicheka na kufungua mlango wa nyumba hiyo.
Mwanzo wa aina yake…
Harufu nzito na mbaya ilimfanya Ishimwe arudi nyuma. Paul alicheka. “Njoo bwana, sio pabaya hivyo.” “Nini kinanuka hivyo? Kama harufu za pombe na….” “Njoo basi.” Ishimwe aliingia na kukaribishwa na shupa za pombe mbalimbali na zote zilionekana za pesa nyingi. Kulikuwa kama kumepigwa bomu!
Ishimwe alibaki ametoa macho. Aliweza kutambua kama ni sebuleni kwa kuwa aliona makochi. Kulijaa vitu vingi ilikuwa ngumu kujua kama pale ni sebuleni, au ni baa, au chumba cha mtu ambaye ameacha kabati la nguo wazi, nguo zote zikamwagika kila mahali, au ni jikoni, au ni droo ya nguo za ndani, limefunguliwa na kumwagwa kila kitu hapo chini. Ulikuwa ni mchanganyiko wa vitu visivyoeleweka.
“Kwani huna mfanyakazi?” Ishimwe alimuuliza Paul akiwa bado amesimama ametoa macho. “Nachanganywa na mengi mwenzio wala si moja. Hakuna msichana wakazi anayeiweza hii nyumba na wale watoto wakiwepo humu. Ilikuwa ni FUJO Ishimwe wewe, hakuna mfano.” Paul alianza kutoa nguo na chupa zilizokuwa kwenye kochi mojawapo na kutupia sakafuni ili wapate pakukaa.
“Hiyo si chupi ya kike!?” Ishimwe alishituka sana. “Unashangaa chupi tu? Mpaka kondom zipo hapa.” “Paul wewe!?” “Heri nijiachie, watu wakusafisha watakuja kesho, watashugulikia. Nimechoka.” Paul aliamua aache baada ya kila alivyojitahidi kukusanya vitu pale ndivyo alivyokumbana na vitu vya ajabu zaidi.
“Twende tukakae chumbani kwangu kuna nafuu kidogo. Huko huwa hawafiki, najitahidi kupafunga kila nikitoka.” Walielekea chumbani kwa Paul huku wakipishana na chupa za pombe, sahani, viatu na nguo kila mahali.
*********************
Kweli chumbani kwa Paul kulionekana kuna nafuu kubwa. Japokuwa kitanda hakikuwa kimetandikwa, lakini angalau palieleweka. Vitu vyake vilikuwa vimepangiliwa vizuri sana chumbani humo. Kulikuwa na chumba kingine ndani ya chumba hicho, ambacho kiliwekwa nguo na viatu vya Paul tu. Vilipangiliwa vizuri sana, tena kwa usafi wa hali ya juu.
Ishimwe aliendelea kusogea kwenye chumba hicho taratibu huku akishangaa. ‘Viatu vingi sana, kama dukani! Paul hajabadilika. Bado anajipenda kama zamani.’ Ishimwe aliendelea kuwaza. Suti zilining’inizwa upande wake, kwa mpangilio wa rangi tofauti tofauti. ‘Suti zote hizi!’ Suruali na mashati na vyenyewe vilipangiliwa kwa rangi, pamoja na tai zake.
Palikuwa na sehemu alipokuwa akiweka nguo chafu. “Chumba chako kizuri!” Ishimwe alimgeukia Paul lakini tayari Paul alishapotelea usingizini akiwa vile vile amevaa nguo zake na viatu vyake mguuni.
‘Maskini Paul wangu! Kwani nini kiliendelea tulivyoachana? Hakuwa amechoka hivi!’ Ishimwe alimsogelea karibu. Akamvua viatu na soksi. Akamfunika vizuri na kubaki akimwangalia huku akicheka taratibu. ‘Atakuwa alipata kiboko yake. Ujanja wote umemuisha Paul!’ Ishimwe alibaki akiwaza cha kufanya. Hakuwa akiifahamu hiyo nyumba kabisa. ‘Sidhani kama amekula huyu!’ Aliendelea kuwaza huku akipingana na wazo la kutoka pale chumbani na kwenda kupika.
‘Sithubutu hutoka humu ndani. Naweza kukutana na nyoka bure hapo nje ya huu mlango.’ Alikaa hapo akiwaza, mpaka alipoona giza linaanza kuingia na bado mwenyeji wake amelala. ‘Akiamka hapo, atakuwa anasikia njaa. Heri nitoke tu nikatafute jiko lilipo, nipike.’
Hapakuwa na Mgeni siku ya kwanza…
Ishimwe alitoka kurudi mpaka sebuleni. ‘Jiko haliwezi likawa mbali na sehemu ya kulia chakula.’ Wazo lilimjia na kuanza kuangalia sehemu ambayo angeweza kuona meza ya kulia chakula na viti vyake. Alipotambua, aliendelea kusogea mpaka alipoona jiko. Macho yalimtoka baada ya kukumbana na jiko kubwa na la kisasa. Kulikuwa pia na meza nyingine ambayo haikuwa kubwa sana kama aliyokutana nayo nje ya pale jikoni, nayo ilikuwa ya kulia chakula. Ilikuwa imezungukwa na viti vyake vizuri sana humohumo jikoni. ‘Ndio maana alijenga hii nyumba kwa muda mrefu. Ni pazuri sana, panaonekana pamekosa tu matunzo.’
Kila kitu hapo ndani kilionekana cha thamani kubwa. Ishimwe alianza kusafisha kwanza jikoni kwa kukusanya vitu vyote ambavyo havikutakiwa pale jikoni na kurundika kwenye chumba kingine kidogo kilichokuwa hapo karibu ya jiko. Kilifanana na stoo. Kulijaa kila aina ya vitu hapo jikoni.
Sinki ilijaa vyombo vichafu ambavyo vialianza kutoa harufu mbaya. Mifuko ya kuku na chips ndiyo ilizagaa jiko zima, huku ikitoa harufu ya kachumbari iliyochacha. Alikusanya matakataka yote mpaka nguo alizozikuta huko jikoni, akakusanya na kutupia kwenye stoo hiyo, huku akiweka pamoja mifuko michafu ya vyakula.
Vyombo vilivyofaa kuosha, aliosha harakaharaka na kusafisha ‘counters’ za hapo jikoni na meza. Kisha akapiga deki na moja ya taulo alilokuwa ameokota hapo hapo jikoni. Baada ya muda jiko liligeuka kuwa zuri sana, hata harufu ilibadilika. Ishimwe akacheka. ‘Afadhali panapendeza. Angalau Paul wangu akimka apate pakukaa.’ Aliendelea kuwaza huku akifurahia na kujipongeza kwa kazi nzuri aliyoifanya.
‘Ngoja sasa nipike.’ Alijisemea huku akisogelea mlango wa friji kuangalia vitu vilivyomo ndani. Alibahatika kupata baadhi ya vitu alivyohitaji. Akaanza kupika huku akisafisha friji hiyo nakutupa vyakula vingi vilivyokuwa vimeoza. Baada ya muda mfupi tayari jiko lilishajaa harufu nzuri.
*********************
“Matumaini ya kuishi yamerudi mwenzio. Heri tumerudi wote Ishimwe.” Ishimwe alishitukia Paul amesimama mlangoni. Akamsogelea karibu, akambusu tena kwa muda mrefu huku amemkumbatia. “Ndio ukaribishaji gani huo Paul jamani!? Unamleta mgeni halafu wewe unapotelea usingizini!” Paul alianza kucheka. Wazi alionekana amepunguza uchovu.
“Niliona nakuongelesha mwenzangu umekazana kushangaa! Kila nikijaribu kukuita naona kama hunisikii kabisaa. Nikaona nikuache ushangae kwanza mpaka uridhike, wakati mimi nalala. Pole naona umependezesha jiko.” “Hivi nyinyi mlikuwa mkiishije humu ndani?” “Sijui Ishimwe. Siwezi kueleza ukaelewa. Lakini ndio hivyo tulikuwa tukiishi.”
“Lakini sio siku zote panakuwa pachafu hivi. Kuna kampuni moja ya usafi huwa nawatumia, wanakuja kusafisha nyumba nzima angalau mara moja kwa mwezi.” Ishimwe alibaki akimtizama Paul. “Nini sasa?” “Siamini Paul. Na usafi wote ule, unawezaje kuishi hivi?” “Maisha Ishimwe! Wewe acha tu. Unajikuta upo kwenye hali ambayo huwezi kujinasua.” “Pole.”
“Naona na meza imesafishwa! Naomba nikae nile Ishimwe. Njaa inauma kweli.” “Pole. Kama nilijua nikapika.” “Harufu hiyo ya chakula, ndio imeniamsha.” Wote walicheka na kukaa hapohapo kwenye meza ya jikoni na kula.
*********************
“Karibu sana na pole kukutana na mazingira ya ajabu. Nilitamani kusubiri mpaka kesho wakishakuja kupasafisha ndio nije kukuchukua, lakini niliona sina cha kujificha kwako na nisingeweza kuendelea kusubiri. Niliona tumeshasubiri vya kutosha. Uchafunao hauwezi kutuzuia kuwa pamoja.” “Hamna neno Paul, asante. Naona hata sura yako inamatumaini, ulikuwa umechoka!”
“Sikulala mwenzio tangia tulale wote ile juzi.” “Kwa nini tena!?” Paul alimalizia juisi iliyokuwa imebaki kwenye glasi yake na kumsaidia Ishimwe kutoa vyombo mezani huku akisifia chakula alichopika.
“Hujapoteza ujuzi wako wa kupika!” Ishimwe alicheka. “Naona na Sonia amerithi, Sam anasifia kweli chakula anachokipika.” Paul alicheka, akamalizia kusafisha meza na kurudi kukaa kutaka kumsimulia Ishimwe yaliyokuwa yamejiri.
Yaliyomsibu Paul Na Watoto Wa Kubambikiziwa.
Paul alianza. “Unakumbuka tulipoachana jana ukaniambia nije niweke mambo sawa?” Ishimwe akaitika. “Basi nikarudi hapa, wale watoto wakijua bado nipo safarini. Sikuwaambia lini nitarudi. Nimekuta nyumba imejaa watu mpaka getini. Mzikiumefunguliwa mpaka mwisho. Mdogo mtu amelewa mpaka hajitambui, amelala sakafuni. Kaka mtu naye kumbe ameanza kuvuta bangi. Nimemkuta amezivuta, mpaka akawa kama amechanganyikiwa, anapigana na kijana mwingine, huku msichana ambaye nilikuja kuambiwa ni wake, yupo sakafu anavuja damu, hana fahamu.” “Paul! Kwa nini?”
“Wanasema Junior, huyo mvuta bangi, amemfumania huyo msichana wake chumbani kwake akifanya mapenzi na huyo rafiki yake aliyekuwa akipigana naye. Junior akampiga sana huyo msichana, mwishowe akamchoma na chupa ya Whiskey aliyokuwa ameivunja huyo Junior.” “Mungu wangu Paul wewe!”
“Ilikuwa inatisha Ishimwe, usiwahi kuona. Nilichanganyikiwa. Fikiria msichana anakuja kukutwa amekufa nyumbani kwangu, mimi kama Judge Mkuu ambaye najulikana sina mke, unafikiri ingekuaje?” “Uwiii!”
“Ikabidi kuita polisi waje washuhudie kwanza, na wawatoe watu wote humu ndani, huku gari ya hospitali imeitwa ije imchukue yule binti na huyo mdogo mtu aliyekuwa yupo sakafuni hajitambui. Hapo nawaza nitawaambia nini wazazi wa yule binti.” “Na wao ni wazazi wa namna gani wanaoweza kuruhusu watoto watoke usiku huo kwenda kwenye majumba ya watu?”
“Huwezi jua Ishimwe, labda na wenyewe wanamaisha kama yangu, hawapo nyumbani. Lakini niliwaambia wale polisi wafuatilie kujua wazazi wa yule binti. Nikiwa hospitalini walinipigia simu kuwa wengi wa wale wasichana waliokuwepo pale ni machangudoa.”
“Wakasema hao watoto wangu walikuwa wakienda kuwakusanya kwenye baa moja huko Sinza na kuwaambia kunasherehe kwa Judge Mkuu. Wanakodi magari wanawapandisha humo na kuja kuwamwaga hapa kwangu.” “Mungu wangu Paul! Hao watoto watakufa kwa UKIMWI.” “Sijui tena Ishimwe.” “Lakini walikuwa wakiingiaje humu ndani na polisi wote wale?” “Sio kwamba siku zote tunalindwa hivyo Ishimwe. Ilinibidi kuwaita jana sababu ya ile hekaheka. Tunao askari wanao pokezana kulinda hapa mchana na usiku, lakini ukumbuke wale ni watoto wangu sio wezi. Hawawezi kuwakatalia wakitaka kuingiza wageni wao, nyumbani kwao. Na wala hizo fujo za jana sio mpya.” “Paul wewe!?” Paul alicheka.
“Acha tu Ishimwe. Watoto ni walevi wale na ‘Party’ humu ndani zilikuwa haziishi. Ukiwaaga tu na kuwaambia unasafiri, jioni yake nyumba imejaa watu. Patanywewa pombe humu ndani kama baa, kutavutwa bangi na madawa ya kulevya mpaka siku nitakayokuwa nakaribia kurudi. Kondomu ndio utakutana nazo mpaka getini.” Ishimwe alikuwa akishangaa sana, na kushindwa kuelewa.
“Na zote hizo ni pesa zangu. Ukiwaambia mnahatarisha maisha yangu msifanyie haya mambo humu ndani, au walinzi wakiwakatalia kuingiza watu wengi humu ndani, au ukiwakaripia, wanaondoka bila kuaga. Siku hata tatu hujui walipo. Nakuwa nabakia na kazi yakuwatafuta wao tu. Mara usikie wapo hoteli hii, mara wako na mke wa huyu, huku wakitumia jina langu kama kigezo cha kufanya madudu yao. Nimeteseka na wale watoto, wewe acha tu.” “Pole sana Paul.” Paul alibaki akiwaza.
“Sasa huyo msichana anaendeleaje?” “Ilibidi ashonwe. Amekaa chumba cha upasuaji sijui masaa mangapi! Huku nipo na yule mtoto wangu mdogo naye anafanyiwa matibabu, kutolewa hiyo sumu mwilini. Sijui alichanganya nini huko mwilini mwake, vikageuka kuwa sumu. Naye ningechelewa kidogo tu, angekufa.” “Jamani Paul!”
“Wewe acha Ishimwe. Nilichanganyikiwa. Wakati nipo hospitalini ikabidi kumpigia simu mama, nikamuomba aje. Amefika tu na ndege ya asubuhi, moja kwa moja hospitalini. Nimemsimulia kila kitu. Akashauri tuwarudishe kwa mama yao, wasije wakaja kunifia mikononi kwangu, wazazi wao wakanigeuka.”
“Mama alikuwa amekasirika mpaka anatetemeka. Akamuomba dereva amlete hapa nyumbani. Anasema alimkuta yule kaka mtu bado amelala hana hata wazo. Akamwamsha na kumtoa humu ndani vilevile alivyotoka usingizini.” “Hakukataa?” Paul alicheka.
“Umemsahau mama? Na uzee wake ule, lakini mkorofi vilevile. Alisema alimwamsha na amemshikia risasi.” Ishimwe alianza kucheka. “Jamani Mama Tambo ni mkorofi! Sasa risasi aliipata wapi?” “Si nyumba ilikuwa imejaa maaskari, akachukua ya mmoja wao, huku akimwambia yule mtoto, ‘Najua hawa polisi hawatawapiga kwa kuwa wanamuogopa Paul ambaye mnafikiri ni baba yenu, lakini mimi nitakuua, na sitafanywa chochote na mtu yeyote.’ Alimleta hospitalini hata viatu hajavaa.” Ishimwe alikuwa anacheka sana.
“Mama Tambo kiboko. Lakini ujue mama yako anakupenda sana Paul?” “Najua sana. Katika watoto wake wote mimi ndio kipenzi chake. Lakini bwana mapenzi yake yule mwanamke, hayaeleweki. Sasa subiri usikie kisa chote.” “Ehee!” Paul alicheka.
“Si nilikwambia aliniacha hospitalini?” “Ndiyo.” “Sasa baada ya muda kupita, naona anaingia na askari kanzu wawili. Moja kwa moja mpaka kwenye kitanda cha yule mtoto, kachomoa dripu za maji, na kumtoa yule mtoto kitandani. Akaniambia tunaondoka saa hiyohiyo kwenda Morogoro kuwarudisha wale watoto.” “Paul wewe!”
“Namwambia si tungesubiri ile dripu ya maji iishe? Akawageukia wale askari kanzu, na kuwaambia wampeleke yule mtoto kwenye gari, vilevile bila hata viatu, na waahakikishe asiwatoroke hapo njiani mpaka sisi tutakapofika kwenye gari.” Ishimwe alikuwa akicheka, mpaka anatokwa na machozi. Kila alipokuwa akikumbuka vituko vya Mama Tambo alizidi kucheka.
“Lakini unafikiri Ishimwe, mama aliongea jambo la kweli kabisa. Alisema wale watoto wanaweza wakaniingiza kwenye matatizo makubwa sana, kwa kunidhuru mimi mwenyewe au hata wao wenyewe. Walifika pabaya sana.” “Lakini kweli!”
“Tukaingia kwenye gari, hapo tulishaambiwa anayetaka kwenda chooni aende kabisa, hiyo gari haitasimama popote mpaka Moro.” Ishimwe aliangua kicheko tena. “Bado ana mwili mdogo mdogo vilevile?” “Hajabadilika chochote. Mazoezi yake ya kukimbia ni yaleyale mpaka leo. Akiamua kuja kulala hapa, utamuona saa kumi na moja ya asubuhi yupo kule baharini anakimbia. Uso tu ndio utajua amezeeka lakini kamwili kake, kapo vilevile. Na ameacha kula nyama siku hizi. Anakula mboga za majani tu, wakati mwingine ndio anakula samaki.” Ishimwe alizidi kucheka.
“Haya, tukaondoka hapo na gari nyingine ya polisi ikitusindikiza nyuma.” “Paul wewe?” “Kweli tena. Sijui alipata wapi hao askari kanzu, tulikuwa tunasindikizwa kama majambazi sugu yanapelekwa jela. Namuuliza sasa hao maaskari wote wa nini?” “Akasema ‘unapotaka kutupa paka wa nyumbani kwako, hata umpeleke mbali vipi, mara nyingi huwa wanarudi nyumbani, labda umuue. Sasa nataka kwenda kuuwa undugu na hawa watoto na mama yao kabisaa. Na kwa kuwa mama yao mkorofi kama hawa watoto wake, nataka ushahidi wakutosha kwa lolote litakalo tokea.’ Mama alikuwa amekasirika Ishimwe, hujawahi ona.”
“Alikuwa akitetemeka, mpaka mwenyewe niliingiwa na hofu. Aliwasema wale watoto njia nzima bila kupumzika. Alikuwa akiwatukana kama amechanganyikiwa, mpaka nikamuhurumia mama yangu.” “Sasa wewe ulikuwa unasemaje?” “Mimi tena? Nilikuwa kimyaa kabisa. Nimejiegemeza kwenye kiti nimefunga macho yangu kama siwaoni wala kuwasikia.” Ishimwe alicheka tena.
“Sasa mlipofika kwa mama yao alisemaje?” Paul alicheka tena kidogo. “Hiyo fujomama aliyofanya huko Moro, mimi mwenyewe nilibaki nimetoa macho. Kwanza wakati tupo njiani alishapiga simu kuomba ulinzi kwa askari wa Morogoro. Tumeingia tu Moro, tukakuta tunasubiriwa na magari mawili ya polisi tena wote wamevaa sare. Akashuka kuongea nao, alipomaliza akarudi kwenye gari tukaongozana na hao maaskari mpaka nyumbani kwa mama yao.” “Paul wewe?”
“Yaani ilikuwa fujo, mimi mwenyewe nilikuwa sielewi mama anataka kufanya nini. Tulikuwa tumezungukwa na maaskari kama kuna tishio la ugaidi! Tulipofika tu akawaambia wale maaskari wakague ile nyumba, na kuwafunga pingu wale watoto.” “Paul! Hukumkataza?” “Huyo Mama Tambo?” “Ndiyo!” “Si umesema hujamsahau wewe? Nimekwambia ukorofi wake, upo vilevile, kasoro sura tu. Nilikuwa kimya kabisa wala sikutaka kujisumbua.”
“Akasema yule mama atolewe mle ndani, aone watoto wake. Kwanza hakuaminikuniona mimi na mama pale kwake, pili wale wanae na pingu mkono.” Paul akacheka. “Acha atetemeke bwana! Ukorofi wake wote ulimwisha. Nakwambia tulifunga mtaa kwaulinzi. Mama kamjia na ripoti za polisi. Kwanza kumbe kabla hajaja kumchukua yule mtoto hapa nyumbani, alipitia kituo cha polisi. Akawafungulia wale watoto mashitaka. Mmoja kwa kujihusisha na madawa ya kulevya na mwingine majaribio ya kutaka kuua.” “Jamani Paul!?”
“Shuguli ya Mama Tambo ilikuwa sio ndogo. Sikiliza sasa.” “Ehe!” “Akamtolea na yule mwanamke ripoti ya kwake aliyokuwa amemshitaki na yeye, kwa kumtukana akiwa amelewa alipokuja siku ile nyumbani kwetu. Sasa na yeye alimwambia siku ile alionekana pia ametumia madawa ya kulevya.” Ishimwe alianza kucheka tena. “Huyo ndio Mama Tambo bwana! Hacheki na kima.”
“Na ukumbuke, hapo kumejaa polisi, yule dada alikuwa anatetemeka, alishindwa hata kuongea. ‘Ulifikiria mimi ni mjinga nilipokukaribisha kwenye familia yangu?’ Mama alianza kumuuliza maswali yule msichana. ‘Sasa tumeshajua kama hawa watoto sio damu yetu, na vipimo hivi hapa.’ Mama akamtupia chini zile karatasi za majibu ya hospitalini, akamuamuru aokote asome.”
“Akaendelea. ‘Sasa, kuanzia leo, sio wewe wala watoto wako, mnaruhusiwa kutumia jina la Tambo, au kukanyaga nyumbani kwa Paul. Taarifa zenu zote za ujambazi zipo polisi. Mkionekana tu karibu na maeneo aliyopo Paul, hamtakaa mkatoka jela. Na muombe Mungu lolote lisimpate Paul. Akiumwa tu hata kichwa, kama nilivyokuja hapa leo, ndivyo nitakavyo rudi tena hapa na askari mara elfu ya hawa, na hamtakaa mkanisahau maishani mwenu. Mmenielewa?’ Mama akawauliza kwa hasira.”
“Yule mama akaitikia. ‘Nina msaada mmoja wa mwisho nataka kukusaidia, kwa heshima ya wazazi wako.’ Nikajiweka sawa nisikie huo msaada mama anao taka kutoa. Bwana msaada wenyewe huyo mama mtu aliopewa ndio nilichoka zaidi.” Ishimwe alianza kucheka.
“Nini?” “Alimwambia hivi, ‘Kwa kuwa hawa watoto wako wamekuwa majambazi sugu, yanaenda kukaa jela siku tano. Yakajifunze adabu na kufikiria maisha yao yatakuaje baada ya kutoka jela, tena bila jina la Tambo maishani mwao. Baada ya hizo siku tano kuisha, ndipo wewe mwenyewe utaruhusiwa kuwatoa jela, kwa dhamana watakayo kupangia wao polisi.’ Akaendelea.”
‘Endapo hiyo pesa hautakuwa nayo kamilifu, watakaa huko jela mpaka utakapopata pesa yote, ndipo wataachiliwa. Ukifa leo, ujue na wanao watafia jela. Huyu aliyetaka kuuwa msichana wa watu, yeye bila ubishi atahukumiwa kifungo cha maisha, na huyu unayeuza naye madawa ya kulevya, kama atabahatika kutoka huko akiwa hai atakuwa ameshakuwa mzee sana. Kwa hiyo changamka kutafuta pesa.’ Acha yule mama aanze kulia kama vile Mama Tambo anababaishwa na machozi.” “Paul!”
“Nakwambia tena. Halafu akaendelea ‘Nakufundisha na wewe adabu. Ulinitukana na kunidhalilisha mbele ya mtoto wangu.’ Basi yule mama akaanza kuomboleza. ‘Sina hela Mama Tambo. Naomba usiwapeleke jela.’ Jamani mama alilia huyo mpaka akampigia magoti mama, lakini ilikuwa kazi bure mbele ya Mama Tambo.” “Maskini mama wa watu! Paul usicheke bwana! Halafu unawaigiza mpaka sauti, sio vizuri bwana!” Paul alikuwa akicheka huku akisimulia na kuigiza sauti ya kila mmoja wao, mpaka mama yake.
“Msikie sasa Mama Tambo shoga yako. ‘Wakati ukiwafundisha wanao ujambazihukuwa umefikiria hii siku ya leo? Au ulifikiri utatudanganya kuwa hawa watoto ni damu yetu mpaka lini? Wenzako wenye akili wanatumia nafasi kama hizo vizuri sana, kuhimiza watoto wasome na kufanya mambo ya maendeleo. Wewe ulikuwa unawachekea wanapokuja hapa wakiwa wamelewa, huku ukiwafundisha kumuibia pesa Paul halafu wakuletee.’
‘Nasikia na kazi umeacha, unakula jasho la mwanangu tu, kwa kupitia haya majambazi yako. Hata kusaidia nyumbani kwenu, umeshindwa. Wazazi wako wanashida kupita kiasi. Nashindwa kuelewa ulikuwa ukipeleka wapi hizo pesa walizokuwa wakikuletea wanao. Nyumba yako yenyewe mbaya, wewe na huyo mwanaume wako wote mpo kama wagonjwa.’ Mama alikuwa akiwaangalia kama awameze.”
“‘Huyu ndio baba yao?’ Mama aliuliza, huku akimwangalia yule mwanaume. Akaitikia kwa kichwa kukubali. Mama aliomba tuondoke kabla hajawaweka wote ndani.” “Paul wewe! Kwani hao watoto walikuwa wakikuibia?” “Sanaa. Mpaka viatu vyangu walikuwa wanaiba. Dereva wao alikuwa akiniambia, jinsi walivyokuwa wakiniibia hapa, na kumpelekea mama yao. Sasa sijui alikuwa akiuza au vipi, mimi sijui!”
“Saa za mkononi ndio usiseme. Kila wakitaka kwenda kwa mama yao, ilikuwa lazima waingie chumbani kwangu, wakusanye wanachotaka ndio waende. Si ndio maana nikaanza kufunga mlango wa chumbani kwangu?” “Kwa hiyo wakaenda jela?”
“Fanya mchezo na Mama Tambo. Alihakikisha wanaingizwa kwenye gari ya polisi na kuondoka kabla yetu.” “Ulifanyaje sasa?” “Nilikuwa na usingizi Ishimwe, usiku kucha nilikuwa macho hospitalini na sikupata muda wakulala njiani sababu ya kugomba kwa mama. Na nilijua hakuna nitakachomwambia nikabadili maamuzi yake.”
“Nilirudi kukaa kwenye gari wakati yeye anaendelea na kesi zake. Tumefika karibu ya Ubungo akasema yeye anarudi kwake, nyumba yangu chafu sana hawezi hata kurudisha mguu wake hapa. Tukamrudisha uwanja wa ndege, nikasubiri alipoondoka na mimi nikaja kwako.” Ishimwe alipooza gafla.
*********************
“Nini sasa?” “Ulimwambia kama nimerudi?” Paul akamcheka. “Bado unamuogopanini?” “Sio kwamba namuogopa tu, lakini pia namuona yupo sahihi Paul. Jiangalie hivyo ulivyo halafu jilinganishe na mimi. Ni vitu viwili tofouti.” Paul akakunja uso. “Sikuelewi Ishimwe!” “Naomba tuwe wakweli Paul. Najua familia yako, najua aina ya marafiki au watu wanao kuzunguka, halafu mimi..…” Ishimwe akanyamaza.
“Unaongea nini Ishimwe!?” “Hebu iangalie hii nyumba na mimi jinsi nilivyo Paul. Vitu viwili tofauti! Ukialika marafiki zako, itakuaje? Hata kuongea kingereza siwezi. Sijasoma.” Paul alibaki akimwangalia Ishimwe kwa mshangao.
“Umeingiwa na nini Ishi!?” “Sioni maisha kati yetu Paul!” “Kwa nini? Maana umenipoteza kabisa Ishimwe, sikuelewi! Tatizo ni kwamba hujasoma, au hujui kuongea kingereza?” Hakujibu. “Hivi unajua wakati nakutorosha nyumbani kwetu, nilikuwa najua hujasoma, na mimi nilikuwa na shahada ya kwanza ya sheria tayari?”
“Sitegemei tofauti yoyote kwako ya kielimu sasa hivi kwa kuwa sikukuacha shuleni, nilikuacha ukiwa kwenye matatizo. Kwa hiyo nina shida na WEWE Ishimwe, kama mke wangu sio msomi. Naajiri wasomi kila siku, kwa kadiri ya uhitaji wa kazi zangu ofisini. Wageni wote watakao kuwa wakija hapa kwetu, wanakuja kututembelea tu, hawaji kikazi. Watataka kupokelewa kwa upendo na kukarimiwa basi.”
“Sijawahi kukuona umeingiwa na hofu hivi Ishimwe. Vipi? Au ni hii nyumba?” Ishimwe alishindwa kujibu. “Nilifurahi sana ulivyonipokea tokea mwanzoni, japokuwa ulijua nimekuwa Judge Mkuu, lakini bado ulibaki kuniangalia mimi kama Paul, kitu ambacho sijakipata kwa mtu yeyote isipokuwa kwako. Naomba ibaki hivyo. Sawa?”
“Mali na elimu visiwahi kuingilia mahusiano yetu. Tafadhali sana Ishimwe.” Ishimwe alibaki kimya kwa muda akiwaza.
“Au umeona nimezeeka, hunitaki tena?” “Hapana Paul jamani! Bado nakupendasana tu. Kwanza acha kujizeesha, bado unadai kabisa.” Paul akacheka kidogo na kuuliza. “Sasa tatizo ni nini?” “Bado namuhofia Mama Tambo, Paul. Na sijakusikia hata kama ulimwambia kama mimi nimerudi!”
“Kweli Ishimwe? Wewe unamjua jinsi mama alivyo. Alikuwa kwenye Usalama wa Taifa hapa nchini. Tena ndio alikuwa kiongozi mkuu. Unafikiri nahitaji kumwambia kitu gani asichojua? Masikio na macho yake, vyote vipo kila mahali. Sihitaji kumwambia kitu. Ananifuatilia kupita kiasi! Kwanza amenipa bahasha nikuletee. Sijui ina nini ndani. Ngoja nikailete, niliiacha kwenye gari.” “Bahasha yangu mimi!?” Ishimwe alishituka sana, lakini Paul hakujibu, akasimama na kutoka nje kwenda kufuata hiyo bahasha, huku akimwacha Ishimwe kwenye mshangao uliochanganyikana na hofu.
Zawadi ya Mama Tambo kwa Ishimwe
Baada ya muda alirudi na bahasha kubwa ya njano, ameshika mkononi. Jinsi alivyoandika nje, ilimtoa machozi Ishimwe. “Sasa maana yake nini?!” Paul alicheka kidogo. “Fungua basi tuone kilichopo ndani.” “Ndio unafikiri amenikubali?” “Ndio maana yake. Jinsi anavyolilinda hilo jina, halafu leo akuandikie ‘Ishimwe Tambo!’ Tena kwa mkono wake! Ujue ndio ameomba na msamaha hapo. Ni hivyo tu ni mkorofi na hajui neno samahani maishani mwake.” Ishimwe alibaki akitetemeka huku akilia.
“Naogopa kufungua ndani Paul. Kwani wewe ulimwambiaje?” “Alianza yeye mwenyewe. Akasema ‘Naomba umlete Sonia na Sam nyumbani kabla ya harusi yao.’Nilikuwa nimefunga macho nimeegemea kwenye kiti. Halafu akasema tena. ‘Naomba usimrudishe tena Sonia mahakamani, sio salama kwa afya yake.’ Nilishituka Ishimwe lakini sikutaka kumuonyesha. Nilibaki nimefunga macho bila kumjibu kitu.”
“Paul wewe!” “Ndio maana yake. Hapo alikuwa anataka kuniambia anajua kila kitu kinachoendelea na kwa namna nyingine alikuwa anatoa maagizo, hataki tena tujihusishena hiyo kesi. Iwe mwisho sisi kutokea mahakamani, niimalize mimi mwenyewe hiyo kesi, kabla yeye hajaingilia.” Ishimwe alibaki ametoa macho.
“Nishamzoea mimi, hanipi shida. Ana masikio kila mahali! Hapo ujue ameshamchunguza kila mmoja wenu, ndani na nje. Kwa kusema Sonia aende nyumbani na Sam, inamaana ameridhishwa na Sam. Sitashangaa kama hata jinsia ya mtoto aliyobeba Sonia anaijua. Hana asichofuatilia yule, hasa kitu chochote kinachojihusisha na Tambo.”
“Na tetemeka Paul!” “Naomba uache kulia na ufungue hiyo bahasha, tuone ina nini ndani. Maana yule, haishiwi vituko.” Ishimwe akafungua. Macho yaliwatoka baada ya kukutana na Hati ya Ishimwe ya uraia wa Tanzania, na hati yake ya kusafiria/passport. Vyote viliandikwa Ishimwe Tambo.
“Paul wewe?! Hii picha yangu kwenye hati ya uraia ni ya zamani sana! Naonekana mtoto mdogo! Ameipata wapi hii picha na hii saini yangu na alama za vidole vyangu?” Paul alifikiria kidogo. “Wakati unaanza kazi pale nyumbani, hamkuandikishiana mahali?” Ishimwe alifikiria na yeye kidogo kama kuvuta kumbukumbu.
“Nakumbuka aliniita kule ofisini kwake palepale nyumbani kwenu, akawa ananihoji maswali huku anaandika mahali, kisha akanisogezea wino akaniambia niweke wino kwenye vidole vyangu vyote vya mikono kicha niweke kwenye moja ya hizo karatasi alizokuwa akiandika. Kisha aliletwa mpiga picha palepale kwenu akanipiga picha. Sikuuliza picha ni za nini na wala sikupewa mimi hizo picha.”
“Angalia hii picha! Ni kama ya siku ile waliyonipiga picha! Ni ya zamani sana!” “Ulikuwa mdogo kweli! Lakini mzuri sana.” Ishimwe alicheka. “Sasa na hii sahihi je? Maana siku ile sikuweka sahihi popote.” Paul alicheka. “Nini?”
“Yaani mama ananifuatilia jamani! Atakuwa amepata kwenye hii safari tuliyosafiri juzi.” “Kweli bwana! Maana hata hii picha ya kwenye hati ya kusafiria, {passport}, ni ya juzi! Lakini amevipataje?” “Unakumbuka kabla ya kwenda Nairobi, nilikuacha hotelini mara moja, nikaenda ofisini, halafu baada ya muda nikakupigia simu kukwambia dereva yupo chini amekuja kukufuata akupeleke kwa mwanasheria, ukatengeneze hati ya kusafiria ya muda?”
“Paul wewe!? Nakumbuka kweli nilisaini siku ile! Sasa amepataje yeye?” “Wewe bado hujamjua mama kumbe. Nakwambia masikio na macho yake vipo kila mahali. Hapo ametengeneza haraka sana, ili pakija kuibuka chochote juu yako, isiniharibie mimi. Itakuwa ameshasikia watu wamejua kama wewe sio raia. Akajua itaniharibia mimi kazi na hilo jina analolitunza la Tambo.”
“Wewe angalia hiyo hati yako ya uraia. Ina tarehe ya tangia unaishi nyumbani kwake, kuthibitishia watu, kwamba ulishakuwa raia wa Tanzania kabla ya mimi na wewe kukutana.” “Huyu mwanamke nimemnyanyulia mikono. Nilikuwa sijaona hii tarehe.” Paul alibaki kucheka tu.
“Lakini nimefurahi amenikubali Paul!” “Hata mimi. Hapo ujue ndio ametuambia ametupa baraka zake. Halafu wakati anaingia kupanda ndege, ujue aliniulizaje?” “Nini tena?” Paul akacheka kidogo kwa masikitiko kila akimtafakari mama yake nakushindwa kupata jibu. “Eti aliniuliza, ‘Nakaribishwa kwenye harusi?’ Nika..” “Paul wewe?” Ishimwe alimkatisha Paul maongezi.
“Harusi yetu!? Ameshajua!?” Paul alibaki akitingisha kichwa. “Ulimjibuje sasa?” “Nilibaki nikimwangalia tu. Nikaondoka zangu. Hapo najua, ataibebea bango kama yake.” “Atafanyaje!?” “Si nilikwambia nataka iwe ndogo tu?” “Ndiyo.” “Basi ukimsikia hivyo, hamna dogo tena. Hapo atakuwa amewapigia simu wanae wote waje.” “Hao waliopo nje?” Paul alicheka. “Hana watoto wengine Ishimwe, ni haohao tu.”
“Sasa si ni jumamosi ijayo tu? Muda wenyewe mfupi! Kama wanakazi?” “Unavyomuona anajali yule? Haombi waje, anatoa amri waje. Utawaona watakavyokuja wamenuna.” Mara simu ya Paul ilianza kuita.
*********************
“Mama ana maisha marefu! Tunamsema na yeye anapiga simu.” Ishimwe alishituka sana mpaka akajikuta amesimama. “Mimi naondoka Paul!” Paul alianza kumcheka. “Hii ni simu Ishimwe hakuoni, hebu tulia acha kupaniki. Rudi ukae.” Paul aliendelea kucheka. “Bwana usicheke Paul, pokea hiyo simu.” “Nitaongeaje Ishimwe, wakati unataka kunikimbia?” Taratibu Ishimwe akarudi kukaa.
“Ewaaah! Umetulia sasa?” “Bwana Paul acha kuniuliza hivyo bwana! Natuliaje sasa? Hebu pokea hiyo simu. Unamjua mama yako asivyopenda kusubiri.” Kila Paul alivyokuwa akimwangalia Ishimwe, alivyopaniki alizidi kucheka. “We Paul! Acha kucheka bwana, ongea naye.”
Akabadili sura kama sio yeye na kupokea simu yake iliyokuwa ikiendelea kuita. “Shikamoo mama.” “Huna aibu kumleta Ishimwe kwenye nyumba chafu kama hiyo?” “Ndicho ulichonipigia simu?” “Nilitaka kukwambia siku ya alhamisi ndio itakuwa siku nzuri kwa Sonia na Sam kuwepo hapa nyumbani, kwa sababu baba yake mkubwa atakuwepo na shangazi zake wote wawili watakuwepo.”
“Mama jamani! Kulikuwa na umuhimu gani wakuwasumbua wakati wapo kazini? Angalau ungewakaribisha kwenye harusi ya Sonia, sio sisi watu wazima!” “Aliyekwambia hawatakuwepo na kwenye harusi ya Sonia ni nani? Naomba kuongea na Ishimwe.” Paul alibaki akiingalia ile simu kwa muda kama aitupe.
“Wewe Paul? Najua yupo hapo pembeni yako. Mpe hiyo simu niongea naye.” Paul alivuta pumzi. “Anataka kuongea na wewe.” “Mungu wangu Paul wewe!” Ishimwe alinong’ona, lakini Mama Tambo alisikia kwani Paul alishakuwa amenyoosha mkono kumkabidhi simu hiyo. Ishimwe alikuwa akitetemeka kama aliyetolewa kwenye friji.
Wakati anapokea simu kwanza aliiangusha kwa kutetemeka, huku akifikiria anaongea nini na mwajiri wake wa zamani, aliyemtoa kwenye kambi ya wakimbizi, na kumsaliti kwa kutokumtii hata alipompa vitisho aachane na mwanae.
*********************
Mara kadhaa Mama Tambo alishamuita Ishimwe kumuonya kuachana na Paul na kumtuma Ishimwe amshawishi Paul amkubali mwanamke aliyemtafutia yeye, lakini kila Ishimwe alivyojitahidi kupata muda wa kuzungumza na Paul ili kumshawishi kumkubali mwanamke aliyetafutiwa na mama yake, ndivyo walivyojikuta wakizama kwenye mapenzi wao wawili, na kuishia kuongea mambo yao na kupanga mikakati ya kumkwepa Mama Tambo.
Mpaka Paul alipoona mateso kutoka kwa mama yake kwa Ishimwe yanazidi, ndipo alipoamua kumtorosha. Paul aligeuka kuwa kama mfanyakazi wa ndani wa nyumbani kwao. Kila aliposikia Ishimwe anagongewa alfajiri na mapema na mama yake, tena kwa kelele, Paul alikimbilia na yeye chumbani kwa Ishimwe, kama kumzuia mama yake asije kumpiga Ishimwe.
Kila aliponyoosha mkono kutaka kumpiga Ishimwe, Paul alimkinga na kuishia kupigwa yeye na mama yake badala ya Ishimwe. Kila kazi aliyopewa Ishimwe, na Paul naye aliifanya.
Paul aliacha urafiki na kila mtu, na kubaki kuwa na Ishimwe hapo nyumbani kwao. Alifua nguo za mama yake kwa mikono yake, tena alijitahidi kuzifua vizuri ili Ishimwe asije kuingia matatizoni, alideki mbele ya wazazi wake, na kumsaidia Ishimwe mambo ya jikoni.
Mama Tambo alipoona mtoto aliyekuwa ana malengo naye makubwa SANA hapa nchini, anageuka kuwa mfanyakazi wake wa ndani, ilimbidi kumpunguzia kazi Ishimwe, ili kumfanya Paul angalau atulie na kufikiria maisha yake ya baadaye. Alijaribu kuongea na Paul bila kuchoka, huku akimpa hasara atakazopata kuwa na mahusiano na mtoto mdogo kama Ishimwe, tena asiye Mtanzania. Lakini Paul alikuwa kama amekatwa masikio! Katika hilo hakusikia lolote na wala hakumuogopa mama yake tena, alikuwa tayari kwa lolote.
Alimwambia mama yake, anawajibu wa kusoma, na yeye hajakataa kusoma, alimwapia mama yake, atakuwa na Ishimwe na bado atasoma, lakini mama yake alikataa na kusema Ishimwe ataharibu ndoto zake zote, lazima amuache.
Kila mtoto aliyemzaa Mama Tambo, alishaona mwisho wake tokea mwanzo. Aliwalea watoto wake tokea wadogo, akiwaambia watakuwa kina nani kutokana na kipaji alichoona ndani mwao. Alijitahidi kuwalea watoto wake kwa karibu na makini sana. Yeye ndiye alikuwa mstari wa mbele katika kutengeneza njia za wanae.
Hakuna mtoto wake aliyehangaika kutafuta chuo wala kazi, Mama Tambo ndiye aliyekuwa akifanya kila kitu, ila tu ilikuwa lazima usome. Kusoma ilikuwa sio hiyari kwenye familia ya Mama Tambo, ilikuwa ni lazima. Na alishawaambia watoto wake, hakuna mtoto atakayemkubalia aanze kazi au kuoa au kuolewa bila shahada mbili, tena yeye mwenyewe akiwa mlipa ada.
Na kweli hakuna mtoto wa Mama Tambo aliyewahi kuwa na shida ya pesa maishani, na wala kumsumbua. Walimuogopa mama yao kuliko mtu yeyote duniani. Walimpa majina ya watu wote walio wajua ni makatili hapa duniani. Baba yao tu ndio alikuwa rafiki yao, lakini sio Mama Tambo.
Kila anapoongea jambo lake, cha kwanza hakuwahi kurudia, na lazima litekelezwena hao watoto wanne, aidha wanapenda au hawapendi. Sheria zote za nyumbani kwake yeye ndiye aliziweka, na hakuna kuvunja. Watoto wake walimjua kama mama asiye na huruma, inapofika katika sheria na mipaka aliyoweka yeye, hapakuwa na msamaha. Hakutishiwa na machozi ya wanae, wala hakuruhusu mtoto yeyote abishane naye.
Kila sheria aliyoiweka yeye ina adhabu yake kali, ikitokea unavunja. Na ilikuwa lazima atekeleze adhabu aliyopanga bila kupepesa macho endapo mtoto yeyote atavunja moja ya sheria alizopanga yeye.
Watoto wote walimlalamikia baba yao wakisema, Paul tu ndiye anayependelewamle ndani, kwani mara nyingi mama yao alitafuta sababu, ya kukwepesha adhabu za Paul. Ndio maana kaka yake na dada zake, waliamua kuwa mbali kabisa na mama yao mara baada yakumaliza shahada zao za kwanza katika Chuo Kikuu cha Mlimani. Waliita ‘Maisha ya kifungoni’. Waliita hivyo, kwa kuwa hakuna mtoto yeyote aliyeruhusiwakukaa bweni/hosteli au mbali na nyumbani kwao hata walipofika ngazi ya chuo kikuu.
Ilikuwa lazima wote wakae nyumbani angalau mpaka shahada ya kwanza, ndipo unapoweza kuruhusiwa kuchagua mahali pengine pakusomea shahada ya pili ndipo uanze kazi na si vinginevyo. Wote walitoka asubuhi na kurudi nyumbani kwao usiku. Wakati huo wakiishi hapohapo Dar.
Alijua ratiba ya kila mtoto wake. Kila rafiki wa mtoto wake, alihakikisha anamfahamu mpaka wazazi wake. Swala la pombe na sigara kwa watoto wake, halikuwahi kuwa na mjadala, hawakuruhusiwa hata kuonja. Alishasema adhabu yake haitofautiani na adhabu ya kukataa shule, ambayo kaka mkubwa alijaribu kuvunja hiyo sheria, yeye ndiye alitolewa kafara na Mama Tambo kama kuonyesha mfano.
*********************
Haraka haraka wote wawili Ishimwe na Paul waliinama chini ya meza kutafuta hiyo simu. Ishimwe aliiwahi kuiokota na kuikimbiza sikioni. “Shi..ka..moo mama.” “Marahaba Ishimwe, habari za siku nyingi?” Ishimwe alikuwa na hali mbaya sana lakini jinsi Mama Tambo alivyojibu salamu yake, kidogo akatulia. “Nzuri. Asante kwa bahasha. Nimepokea. Nashukuru sana.” “Umeshajua unavaa nini siku ya harusi yako?” Machozi yalianza kumtoka Ishimwe.
“Sijajua mama.” “Wifi yako yule mdogo atawahi kuja. Kama utaona sawa, naweza kuja naye hapo kwako siku ya jumanne, kesho kutwa, tukakuchukua tukusindikize kutafuta nguo na vitu vyako vingine utakavyohitaji kwenye harusi yako.” Ishimwe alibaki anababaika. “Nitamwambia Paul. Asante mama.” Simu ikakatwa. Ishimwe alivuta pumzi kubwa na kuzishusha huku machozi yakimtoka.
*********************
“Siamini Paul! Mama Tambo amenikubali!” Paul alibaki kama amepigwa na bumbuwazi kwa muda. Alibaki ametoa macho. “We Paul!” “Si nilikwambia wanae wote watakuja? Hapo nasubiria simu za lawama. Kaka ndio atakuwa anatamani apasuke, na wanavyojua kukwaruzana na mama! Sipati picha.”
Ishimwe alianza kucheka. “Sasa utampeleka huyo Sonia na Sam?” “Unauliza jibu? Ndio maana yake. Hapo kashaita kila mtu ili amtambulishe Sonia. Lazima tujipange kuongea kwanza na Sonia mwenyewe, halaf…” “Wewe Paul si unamjua mwanao alivyo? Akikataa kwenda?” “Nitaongea naye, najua atakubali. Ngoja nimalize hiyo kesi ya Nyange kwanza, ili nikionana naye mama, asinikere kwa maswali mengi.” “Utafanyaje?” Paul alifikiria kidogo.
“Nitahakikisha inamalizika nje ya mahakama. Hatutarudi tena mahakamani kama mama alivyosema.” “Wewe humjui Leah!” “Kwa kuwa na yeye hanijui mimi. Utaona tu.” Ishimwe akabaki akimfikiria Leah na kutaka kubisha tena. “Na nina kushauri usipingeIshimwe, maana nitashinda tu.” Ishimwe alicheka.
“Kwanza umemsikia Mama Tambo?” Paul alianza kucheka na yeye. “Nilikuona unavyotetemeka!” “Kwanza ameniambia wifi yangu yule mdogo. Upo hapo Paul?” Paul aliendelea kucheka. “Halafu amesema wanakuja kunichukua hapa nyumbani kwangu, kunisaidia kutafuta gauni la harusi yangu na Paul Tambo. Umeelewa lakini?” “Umefurahi mwenyewe!” “Saaanaa. Kufuatwa na Mama Tambo, eti anipeleke kutafuta gauni la harusi yangu na Paul, mwanae kipenzi! Si mchezo!” Paul alicheka kwa sauti.
“Hongera.” “Na ninaomba ukumbuke Paul, hapa nilipo, mimi ni raia kamili wa Tanzania, na nina hati ya kusafiria popote nitakapo, zaidi ya hapo nishakuwa Ishimwe Tambo, shida iko wapi? Eti Paul?” “Huna shida Ishimwe. Ushafikiria juu ya kuongea kingereza lakini?” Akamchokoza makusudi. “Hicho hakinibabaishi tena, wewe ndio utakuwa mkalimani wangu.” Paul alicheka sana.
“Ujue kwenye harusi yetu, atakuwepo Mheshimiwa raisi wa Tanzani, mawaziri, na watu wakubwa wenye vyeo vyao, utafanyaje?” “Na mimi nitawapa Judge Mkuu wa Tanzania wahangaike naye. Usinione hivi, nimejipanga eti!” Paul alikuwa akifa kucheka. “Kweli hujabadilika Ishimwe. Vituko vyako viko vile vile.” Wote waliendelea kucheka.
Paul ndiye aliyepata muda mzuri sana usiku huo. Nyumba iliyokuwa imejaa vurugu, matusi, na upweke, wakati alikuwa akiishi na watu zaidi ya mmoja, ILIBADILIKA. Ishimwe aliweza kubadili ile hali ya upweke kwenye hiyo nyumba ya Paul kwa muda mfupi tu aliokanyaga hapo ndani, na kumfanya Paul mwenye furaha na tumaini jipya.
*********************
‘Kweli pesa sio kila kitu. Ni kweli Ishimwe anakamilisha maisha yangu.’ Paul aliendelea kufikiria huku akimwangalia Ishimwe aliyekuwa amemkumbatia kitandani kwake. Ishimwe alikuwa amelala kama aliyekufa kwa kuchoka na kazi ya kusafisha sehemu chache tu za Jumba hilo la Paul.
Paul alimbusu tena kichwani, akamuweka kwenye mto taratibu ili asimuamshe na kumfunika vizuri. Alivuta simu yake na kuamua kumtumia mama yake ujumbe. ‘Asante sana mama.’ Alipomaliza kutuma ujumbe huo mfupi, akarudisha simu kwenye meza ndogo ya pembeni ya kitanda hicho, akijua wazi mama yake hawezi kujibu kwani walishapoteza mawasiliano ya kawaida kwa muda mrefu sana. Akabaki akifikiria.
*********************
Ilikuwa ni zaidi ya miaka ishirini sasa tokea amtumie mama yake ujumbe wa kawaida kama huo. Ni kweli Paul alikuwa mtoto wa mama. Katika watoto wote wanne aliozaa Mama Tambo, Paul peke yake ndiye aliyekuwa akimjali sana mama yao. Watoto wote walikuwa upande wa baba yao, kila walipowasiliana na mama yao, ilikuwa ni kuomba pesa, au mama yao ndiye aliyekuwa akiwatafuta. Lakini Paul alimpenda sana mama yake.
Ndiye aliyekuwa akimtafuta mara kwa mara kumjulia hali tokea utoto wake. Mwanzoni ndugu zake walimcheka wakisema anajipendekeza, lakini Paul alimpenda sana mama yake. Hakuwahi kulala kama mama yake amechelewa kurudi kutoka kazini.
Hata Mama Tambo alipokuwa na hasira kwa kiasi gani, Paul peke yake ndiye aliyejua kumwingia na wote walimtumia Paul kumuingia mama yao, endapo wanahitaji kitu kwake. Barua za kawaida, barua pepe, simu za Paul kwa mama yake hata akiwa mbali naye ni salamu na kumwambia anampenda, au kumpa pole na majukumu sio vinginevyo au tofauti na ndugu zake, waliokuwa wakimtafuta wakati wakiwa na shida tu.
Japokuwa Mama Tambo alikuwa mkorofi sana, hakuwahi kuonyesha au kukubali udhaifu wake mbele za watu hata siku moja, lakini ilikuwa ngumu inapofika kwa Paul. Walikuwa marafiki sana. Kuna kipindi Paul alikuwepo na ndugu zake wawili chuoni, lakini wakati mwingine Mama Tambo alikuwa akienda chuoni hapo muda ambao Paul anakula chakula cha mchana na kula naye, bila ndugu zake.
Hakuna mtoto hata mmoja aliyewahi kutamani bahati hiyo kwa kuwa walikuwa wakimkwepa sana mama yao. Ndio maana muda wao waliokuwa wakiambiana wakifungoni ulipoisha, kila mmoja aliomba kusomeshwa nje ya nchi ili wakae mbali na mama yao. Na mama yao alijua lakini hakujali, yeye aliangalia maisha ya baadaye ya watoto wake tu, na alijua hata wakiondoka wote, Paul atabaki tu.
Lakini urafiki wao ulikoma kabisa na Paul kukata mawasiliano na mama yake pale mama yake alipovuka mipaka. Ishimwe pekee ndiye mpaka ambao Paul hakutaka mama yake auvuke, lakini kama kawaida ya Mama Tambo hakuwahi kutoa sababu yeyote kwa mtu yeyote kila anapofikia maamuzi yake, kwa hiyo aliamua kwa makusudi kuvuka mpaka huo na kuvunja kabisa urafiki na Paul.
Lakini kwa mapenzi makubwa Paul aliyokuwa nayo kwa mama yake, kila alipofikiria kuondoka kuishi mbali na mama yake kama wenzake, alimuhurumiamama yake, akaamua arudi kuishi tu Tanzania. Japokuwa hawakuwa karibu kama zamani, lakini angalau aliweza kumuona kila mama yake alipokuwa akija Dar kwa mambo yake binafsi au Paul alitafuta sababu yeyote ya kumfanya awepo Shinyanga, japo kwa masaa machache tu, akijisingizia yupo kikazi, lakini nia ilikuwa amuone mama yake.
Japokuwa hakuwa akiongea naye, lakini hakuacha kurudi nyumbani kwao mara mojamoja kwenda kumuona mama yake, kwa visingizio mbalimbali lakini mama yake alijua wazi, kinachomrudisha nyumbani ni kumuona yeye, sio sababu alizokuwa akitoa.
*********************
Wakati bado anawaza, alisikia ujumbe umeingia kwenye simu yake, alijua tu ni mama yake. Alifurahi sana. Akakwapua simu kwa haraka kujua nini mama yake amejibu. ‘Asante kushukuru Paul, ni katika machache ninayoweza kukufanyia.’ Paul alibaki ametoa macho kwa furaha. Haraka alijibu kabla mama yake hajapitiwa na usingizi. ‘Pamoja na kunisaidia kufika hapa nilipo, lakini hili pekee ndilo lilikuwa limebaki kunikamilisha mama yangu. Na pia nikushukuru kwa kumpokea Sonia na Sam. Asante. Nitafurahi kukuona kwenye harusi yangu.’ ‘Nitakuona jumanne.’ ‘Usiku mwema mama.’ ‘Asante na wewe Paul.’
*********************
Sio Paul peke yake aliyelala usingizi mzuri nyumbani kwake kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi, tena pembeni ya Ishimwe mwanamke aliyempenda na kumthamini sana, hata Mama Tambo pia alilala usingizi mzuri baada yakuona urafiki wake na Paul umerudi tena. Kwani Mama Tambo ndiye aliyekuwa akihangaika kuwapitisha wanae katika kila hatua ya maisha yao, lakini Paul ndiye mtoto pekee aliyekuwa nashukurani.
Hakuna kitu ambacho mama yake alifanya Paul asikisifie, lakini sio ndugu zake. Kila kitu waliona wanastahili. Lakini hayo yote kwa Paul yalikoma tokea mama yake alipomlazimisha kwenda kusoma na kumuacha Ishimwe mjamzito. Hata alipokuwa akitumiwa tena pesa za matumizi akiwa chuoni, hakuwahi hata kusema asante tena kwa mama yake.
Mama Tambo ndiye aliyehangaika kumfikisha mpaka kwenye ngazi hiyo ya Judge Mkuu, kwa elimu na kumuunganisha na watu wakubwa nchini, lakini Paul hakuwahi kumshukuru tena, kwa hasira na chuki aliyokuwa amebeba moyoni mwake.
*********************
Akiwa anawaelekeza wafanyakazi walioletwa kusafisha na kupanga upya nyumba ya Paul vile alivyotaka yeye Ishimwe, Paul alimpigia simu na kumwambia ajiandae dereva anakuja kumchukua. “Wananipeleka wapi?” “Nataka kukuonyesha upande mwingine wa Paul ule uliokuwa ukibisha jana usiku.” Ishimwe alianza kucheka. “Bwana nina kazi Paul, nimechoka kubishana na wewe. Halafu kumbuka Mama Tambo na dada yako wanakuja nyumbani kesho, angalau wakute nyumba safi.”
“Wewe mwachie maagizo huyo kiongozi wao. Watafanya tu. Kama hutafurahia upangwaji, tukirudi jioni nitakusaidia kupanga.” “Na usiponisaidia Paul wewe! Kesho huendi kazini.” Paul alicheka. “Jiandae dereva yupo njiani.” “Nivaaje sasa? Kiofisi, au kawaida tu?” “Pendeza kama kawaida yako.” Ishimwe alicheka na kukimbilia chumbani kwao kwenda kujiandaa.
*********************
Baada ya muda mfupi kweli dereva alifika, akamchukua na kumpeleka ofisini kwa Paul. Alianza kubabaika. “Nini sasa?” “Ndio una ofisi nzuri hivi!?” Paul alianza kumcheka. “Halafu mbona hao masekretari wako wazuri hivyo?” “Kwako wewe ndio unawaona wazuri, kwangu mimi mzuri ni Ishimwe peke yake.” Ishimwe aliguna huku akitabasamu. “Unavyojua kunipamba!” “Kuna sehemu nataka twende mara moja.”
Walitoka hapo mpaka kwenye ofisi moja ambayo Ishimwe aliweza kujua ni mahakamani lakini safari hii, hawakuingia wanapoendeshea kesi. Mlinzi wa Paul ndiye aliyewafungulia mlango wa kuingia kwenye chumba hicho. Macho yalimtoka Ishimwe na kumgeukia Paul, mara walipoingia kwenye chumba hicho. Paul hakuonyesha hata chembe ya tabasamu.
Watu wote waliokuwepo kwenye chumba hicho walisimama mara baada ya Paul kuingia, akiongozana na Ishimwe na mlinzi wake. Ishimwe alizungusha macho yake taratibu kuzunguka chumba hicho, akiangalia kila mtu aliyekuwepo ndani ya chumba kile na wao walibaki wamemkodolea macho Ishimwe, wakimshangaa jinsi alivyobadilika na kuonekana mwanamke wa thamani sana.
*********************
Ukimya ulitanda kwa muda, kama wote wakitaka kusikia kutoka kwa Paul. “Nimemleta Ishimwe, mkishamaliza nitarudi kumchukua. Naomba niwapishe.” Paul aliongea kwa kifupi kuvunja ukimya. “Bila shaka.” Alijibu hakimu aliyekuwa akiendesha kesi yao. “Nitakuona baadaye basi.” Paul alimstua Ishimwe kwa kumshika bega, lakini bado Ishimwe alikuwa kwenye bumbuwazi na bado walikuwa wamesimama mbele ya watu wote waliowakuta mle ndani ya kile chumba.
Wote walikuwa wamezunguka meza kubwa, wazi kilionekana ni chumba cha mkutano. Paul alisogea kutafuta kiti ambacho hakikuwa na mtu, akakivuta nyuma taratibu, kisha akamwangalia Ishimwe kama kumwashiria akae. Ishimwe akakaa taratibu huku akiendelea kuwangalia watu alio wakuta ndani ya chumba hicho.
Aliendelea kuzungusha macho yake akimuangalia mmoja baada ya mwingine. “Ishimwe!” Paul alimuita tena taratibu. “Naondoka, nitarudi baadaye kukuchukua.” “Unaondoka tena!? Itakuaje sasa?” Ishimwe akauliza kwa kunong’ona, lakini kila mtu alikuwa akiwasikiliza, japo hakuna aliyeweza kuwaangalia kwa uhuru. “Usiwe na wasiwasi, kila kitu kitakwenda sawa.” Paul akatoka na mlinzi wake.
Ubaya Unamwisho
Macho ya Ishimwe yalitua kwa muda kwa Mama Eliah aliyeonekana mgonjwa, kisha akamtazama Leah aliyeonekana na wasiwasi mwingi usoni. Alitamani kumsalimia kwa kumkumbatia mama Briana aliyekuwa amekaa pembeni ya mumewe akiwa kimya kabisa huku ameinama chini, lakini aliona sura za kazi walizokuwa wamevaa hakimu aliyekuwa akiendesha kesi hiyo tokea mwanzo na mawakili wa pande zote mbili.
Ishimwe akajivuta taratibu nyuma ya kiti alichokuwa amekalia na kujiegemeza vizuri. Kabla hakimu hajasema chochote, mlango ulifunguliwa tena, aliingia mlinzi wa Paul na chupa ya maji mkononi, moja kwa moja akayaweka mezani, mbele ya Ishimwe. “Asante.” Ishimwe alishukuru na kubaki akiyaangalia hayo maji kwa muda, huku kila mmoja ndani ya kile chumba akiwa kimya kabisa akiwaza lake.
Mwishowe Hakimu akaomba mama Eliah ambaye hakuwahi kutoa ushahidiwake, yeye ndio aongee. Mama Briana alibaki ameinama muda wote, alishindwa hata kumwangalia mama yake usoni. Mama Eliah alikuwa amechoka sana, alionekana amedhoofu. Aliombwa kujitambulisha kwa majina yake yote. Kwa shida sana aliweza kuongea, huku akirekodiwa.
Alitoa maeleze mengi sana, yaliyojaa majuto, na lawama ndani yake. “Penninah aliponipigia simu kuwa Leah ni mgonjwa amelazwa hospitalini, nilishituka sana. Sikupoteza muda nikapanda basi mpaka hapa Dar. Sikumkuta Nyange wala mkewe pale kituo cha mabasi, ila dereva wao tu. Nilichukia sana, lakini nikajua labda Penninah yupo hospitalini na mdogo wake kwa kuwa na simu yake ilikuwa haipatikaniki. Wazi ilionyesha ameifunga.”
“Dereva alinichukua pale kituoni mpaka hospitalini. Nililipofika hospitalini nilimkuta Leah akiwa na hali mbaya sana kiafya, na yupo peke yake. Aliniambia alipata matatizo ya kazi, akapoteza nyumba na kila kitu chake. Anasema alimfuata dada yake akiwa mgonjwa sana, akimuomba hifadhi, lakini dada yake alimkataliakatakata sababu ya wivu.”
“Alisema Penninah alianza vituko na hata kuanza kumtesa mumewe, pale alipoona Nyange anampenda sana Leah kuliko yeye. Alisema Penninah alimwendea mumewe kwa mganga ili kumfunga, kwa hiyo hata maamuzi anayofanya Nyange na kumkubalia kila kitu mkewe sio akili zake.”
“Nilimuuguza Leah nikiwa peke yangu pale hospitalini mpaka alipopona, nikarudi naye nyumbani, akiwa hana raha kabisa. Alisema yeye na Nyange wanapendana sana, lakini tokea mwanzo Penninah alitumia pesa kumshawishiNyange amuoe, kwa kuwa yeye Penninah hakuwa na bahati yakupata wanaume.”
“Leah alikubali yaishe akijua Nyange amemchagua dada yake. Lakini alisema baada ya Nyange kumuoa Penninah, Nyange alimfuata tena yeye Leahakimlalamikia sana juu ya tabia za dada yake, akimwambia amechoshwa naye na yeye bado anampenda sana Leah. Leah alisema, huruma ikamwingia baada ya kumuona kweli Nyange hana raha pale nyumbani kwake, mkewe anasafiri atakavyo, huku akimuacha mtoto wao mdogo bila uangalizi wowote na hata Nyange alipomshauri atulie alikataa kabisa.”
“Leah anasema akamshauri Nyange aondoke lakini Nyange alishindwa, wazi alionekana amelogwa na mkewe. Leah akaniambia ikabidi yeye mwenyewe aende kwa mganga ili kumsaidia Nyange na mtoto wa dada yake, waliokuwa wakiteseka.”
“Lakini anasema alipofika huko kwa mganga, alikutana na mambo ya kusikitisha zaidi. Aliambiwa mbali ya dada yake kumloga Nyange, lakini pia amemuharibu kabisa yeye Leah. Amechukua Nyota yake, anaitumia yeye, na ndio maana dada yake anafanikiwa sana, halafu yeye Leah mambo yake, yanaharibika.”
“Anasema alipotaka kujitengeneza huko kwa mganga, mganga alimwambiwa dada yake anaenda kwa waganga wakali sana, yeye huyo mganga hatamuweza. Nilimbishia sana Leah kwamba dada yake sio mshirikina kabisa, huyo mganga anamdanganya. Lakini Leah alisema anamwamini sana mganga wake, kwani yote aliyotabiriwa juu yake anayofanyiwa na dada yake ni ya kweli.”
“Alisema yeye anamwamini kwani ni kweli kila mara alipomtambulisha mwanaume wake kwa dada yake, alishangaa mahusiano hayo yanakufa. Hata mwanaume huyo aliyekuwa amebeba mimba yake alikubaliana naye wafunge ndoa waanzishe familia yao pamoja, lakini mara baada ya dada yake kujua, gafla yule mwanaume akabadilika sana, na kila kazi aliyokuwa akitafuta, akifanya kazi muda mfupi tu anafukuzwa, na yule mganga alimtabiria hayo yote na kumwambia dada yake ndiye anayemfanyia hayo yote, kwa kuwa alichukua nyota yake.” Mama Briana aliguna na kutingisha kichwa kwa masikitiko bila ya kumtizama mtu yeyote.
“Kwa kweli niliumia sana. Kila nilipokuwa nikimwangalia Leah ambaye na yeye amesoma, mzuri wa sura na umbile, halafu nikimlinganisha na maisha ya dada yake yalivyokuwa yakizidi kushamiri tu wakati ya Leah yanaharibika, nilizidi kuchanganyikiwa mimi kama mama. Kwa macho yangu nilikuwa nikimuona Leah akituma maombi ya kazi kwenye maofisi mbali mbali bila mafanikio yeyote.”
“Baada ya kuhangaika sana kutafuta kazi, ndipo Leah akaniomba nimsaidiekama kuna mganga yeyote yule nina mfahamu nimpeleke ili akarudishe Nyota yake, na kumsaidia Nyange pia. Nikampeleka kwa mganga lakini Leah aliniomba kuingia ndani peke yake, mimi nimsubirie nje.”
“Baada ya muda akatoka, akaniambia hata huyo mganga amemthibitishiakwamba ni kweli Penninah amemloga, lakini yeye anaweza kumsaidia. Kuna vitu huyo mganga alivitaka tumpelekee kabla ya kufanya chochote. Kwa kweli vilikuwa vitu vya pesa nyingi kidogo, na hatukuwa na hiyo pesa kwa wakati huo.”
“Nikampigia simu Eliah mara nyingi sana ili kumuomba msaada wa pesa akawa hapokei simu zetu, mpaka tulipomtumia ujumbe kumwambia tunashida sana. Ukimywa wa Eliah haukunishangaza kwani tulikwaruzana naye kidogo baada ya msiba wa wazazi wa Nyange, kwa hiyo nilijua bado anahasira na mimi. Hakujibu ule ujumbe, lakini baada ya kama juma moja kupita, akamtuma dereva amlete mtoto wake anisalimie.”
“Ukweli yule mtoto alikuja na vyakula vingi sana, lakini bila pesa. Leah akaanza kulalamika sana, kwamba kwa nini kaka yake hajatuma pesa badala yake ameleta mtoto tu? Nikamwambia kwa sababu ameleta vyakula vingi sana, labda ameishiwa. Lakini Leah alisema kwamba kaka yake anadharau kama Penninah. Akanieleza mambo mengi sana ya kuniumiza juu ya kaka yake pia. Huku akisema kuliko kutuma dereva kumleta huyo mtoto, si heri hiyo hela ya mafuta ya gari angenitumia mimi tu? Tena nikiwa nimeshamlalamikia nina shida!” Kila mtu aliyekuwepo pale alikunja uso kwa mshangao, huku wakiwaza juu ya malalamko ya Leah.
“Leah akashauri tuuze vile vyakula alivyoleta kaka yake, ili tupate pesa ya kununulia hivyo vitu tulivyoagizwa na huyo mganga huku akiniambia nisiwe na wasiwasi kwa kuwa yeye akifanikiwa atanichukua tukaishi naye huko mjini. Basi nikakubaliana naye, yule mtoto wa Eliah alipoondoka tu, tukauza vile vitu vyote, tukapata pesa, tukanunua vile vitu mganga alivyohitaji na kumpelekea yule mganga.”
“Tulipofika kwa yule mganga kwa mara ya pili, Leah aliingia tena peke yake na vile vitu, na kuniacha mimi nje. Baada ya muda mrefu sana Leah akatoka nakuniambia mganga ananiita ndani.” Mama Eliah alipumzika kidogo.
“Nilikuwa bado nina wasiwasi sana na Penninah, nikaamua kumuuliza yule mganga kama kweli Penninah anamloga mdogo wake? Lakini yule mganga akaniambia mambo ya kushitua zaidi. Alisema kweli ameona jinsi Penninah anavyomloga mdogo wake, lakini pia anamuona jinsi Eliah anavyohangaika kuniloga mimi ili nife, achukue mali zote alizoacha baba yake.”
“Akaniuliza kama Eliah alituma mtu yeyote pale nyumbani? Nikajibu hapana ila mtoto wake alikuja kunisalima. Akasema yule mtoto ndiye aliyetumwa kuja kuchukua mchanga wa pale nyumbani kwangu ili Eliah aupeleke kwa mganga wake, aniue. Nililia sana. Sikuamini. Lakini akasema, yule mtoto bado hajamkabidhi baba yake, tunaweza kumuwahi tumuue.”
“Nilikataa katakata. Nikamwambia yule mganga siwezi kuua mjukuu wangu, tutafute njia nyingine. Ndio akasema anaweza kumpoteza kabisa akili yule mtoto asiweze kuongea na kumpa baba yake ule mchanga. Nilikubali kwa haraka sana, huku nikimuuliza atataka nimuongezee kiasi gani cha pesa? Lakini akasema anachotaka kwangu ni ruhusa tu, yeye atamalizana na Leah.”
“Basi akafanya mambo yake kwa yule mtoto, akasema ameshamaliza sasa ni zamu ya dawa ya Nyange na mkewe.” Penninah alishituka sana. “Mama wewe jamani!? Uliwezaje kuruhusu mtoto asiye na hatia kuangamizwa? Roho mbaya ya namna gani hiyo?!” “Naomba mnisikilize mpaka mwisho.” Mama Eliah aliongea kwa shida kidogo.
“Nikamuuliza sasa hizo dawa za Penninah na Nyange ni zakuwafanya nini? Akasema atatupa dawa ya kuwawekea kwenye chakula, ya Penninah ni ya kumpumbaza tu, ili amsahau kabisa Nyange na kumfanya aache kumfuatilia kabisa Leah na kurudisha Nyota ya Leah.”
“Na alisema kwa kuwa Penninah ametumia Nyota ya Leah kuchuma mali, basi atamrudishia Leah mali zote. Na dawa ya Nyange itakuwa yakumsaidia kurudisha ufahamu wake, Penninah aliokuwa ameuchukua. Naomba mnisaidie maji ya kunywa.”
*********************
Mama Eliah alionekana kweli anauhitaji wa maji ya kunywa. Kwani mbali ya kukaukwa midomo yake, lakini hata sura yake na mwili vilionyesha amedhoofu. Ilikuwa ngumu kujua kama ni njaa ya muda mrefu au alikuwa na ugonjwa ambao haujatibiwa, badala yake unammaliza taratibu!
*********************
Ishimwe akamsogezea ile chupa ya maji, aliyokuwa ameletewa na mlinzi wa Paul. Alipokunywa ndipo alipoweza kuendelea.
“Tulipotoka tu pale, Leah akaniomba nimsindikize kwa dada yake. Kwa kuwa alisema akienda peke yake hawatampokea. Nikamkubalia, ndipo tukaenda nyumbani kwao, na kuwapa hizo dawa. Mara ya kwanza hata mimi nilishituka nilipoona Penninah amechanganyikiwa kabisa. Nikamuuliza Leah kulikoni!? Mwanzoni aliniambia nisiwe na wasiwasi, ataongea na yule mganga ili arekebishe.”
“Baada ya mwezi nikaona Penninah haponi, nikamuuliza tena Leah mbona haponi? Akasema mganga amemwambia inaweza kuchukua muda, lakini atapona nisiwe na wasiwasi. Nikaamini kwa kuwa nilimuona vile Nyange anavyompendaLeah kwa dhati nikajua ni kweli dawa zimefanya kazi. Leah aliniambia ndivyo Nyange alivyo tokea zamani, anampenda sana, na yule mganga ni mzuri ameweza kumrudishia Nyange akili zake, ndio maana Nyange ameweza kurudisha mapenzi yake kwake.”
“Sasa matatizo yakaanza baada ya Leah kushika mimba ya shemeji yake. Ukali ukazidi kwa kila mtu. Mwanzoni nikajua ni mimba.” Mama Eliah alitulia kidogo.
“Alianza kuchapa sana watoto wa dada yake, na vituko vingine vingi vilivyompelekea kupigwa na mama Sonia, akaharibu tena mimba yake. Baada ya mateso mengi pale ndani mama Sonia aliondoka na wale watoto wa Nyange na mimi nilitamani kuondoka lakini nilimuonea huruma kwa kuwa ndio alikuwa amepoteza mtoto wake na hana msaidizi wa kumsaidia kipindi hicho mgonjwa.”
“Nilimuuguza huyu mtoto kwa shida jamani, tena akinifanya kama punda au mbwa. Watoto walipoondoka tu, akamwambia Nyange wafunge ndoa. Nyange akasita kidogo. Hakuwa akikataa moja kwa moja, lakini alikuwa akichekacheka tu. Kile kitu kilimshitua sana Leah. Akaanza kumnyanyasa sana Nyange ili amkubalie kufunga naye ndoa.”
“Alipoona japokuwa anamnyanyasa Nyange lakini bado hakubali swala la ndoa na mimba nyingine pia akawa hapati kwa kuwa Nyange alianza kupata tatizo la…” Mama Eliah akasita kidogo.
“Ndipo akaamua kuanza mkakati mwingine wa kutaka kuhamisha mali zoteza kina Nyange kwa jina lake. Leah alijua wazi kuzaa na Nyange ndiko kutakako muhakikishia kumiliki mali zote za Nyange kihalali. Nia yake ni kuzaa watoto watatu ili kumzidi dada yake aliyekuwa amezaa na Nyange watoto wawili tu.”
“Alipoona Nyange hana uwezo huo tena, ndipo alipomuomba sasa Nyange aandike mali zote kwa jina lake yeye Leah. Katika hilo Nyange hakubisha hata kidogo, alikubali. Lakini tatizo Nyange alikuwa ni kama amezidi kupumbaa zaidi, akili yake ilianza kupoteza kumbukumbu kabisa, kwani kila Leah alipokuwa akimfundisha maneno ya kwenda kusema huko kwa mwanasheria, akitaka akaape kuwa ameamua yeye mwenyewe Nyange kumpa Leah mali zake zote, au vitu vinavyofanana na hivyo, Nyange alikuwa akishindwa au baada ya muda anasahaukila kitu.”
“Leah alizidi kumpiga Nyange mchana na usiku, wakati mwingine akimnyima chakula, akimwambia mpaka aweze kukariri vizuri maneno aliyokuwa akimwandikia ndipo atampa chakula au kumruhusu kulala, lakini Nyange alishindwa kabisa.”
“Siku moja Leah aliamka asubuhi na mapema akiwa na kabegi kadogo kama mtu aliyekuwa anasafiri. Aliondoka bila kuniaga, kwa kuwa tuliacha kuongeleshana kabisa kwa mateso aliyokuwa akimpa Nyange. Alikaa huko kwa muda wa siku tatu ndipo akarudi, tena aliondoka na gari ya Briana. Aliporudi, nikamuuliza alipokuwa amekwenda, akanijibu kwa kifupi ‘kutengeneza akili za Nyange.’ Na kweli, baada ya muda Nyange akakubali kufunga ndoa, na akafanikiwa kumpa Leah mali zake zote tena akaenda mpaka kwa wanasheria kuapa na kuongea kila kitu alichofundishwa na Leah.”
“Sasa baada ya kama mwezi hivi Leah akaanza kutapika tena. Nikajua ni mjamzito. Nikamuacha mpaka mimba ilipoanza kuwa kubwa ndipo nikamuuliza, hiyo mimba ni ya nani? Akanijibu ni ya Nyange. Nilimkatalia kabisa, na kumwambia aniambie ukweli kwani nilikuwa najua bado Nyange hajapona, kwa hiyo asingeweza kumpa Leah ujauzito.”
“Nikamkumbusha siku waliyokuwa wametoka kwenye fungate, baada ya harusi yao, hakuwa na raha kabisa. Nilipomuuliza akasema, itabidi atafute njia nyingine ya kumtibu Nyange kurudisha nguvu za kiume, kwa kuwa bado hajapona, hata huko walipokwenda baada ya harusi yao, walishindwa kufanya tendo la ndoa kabisa.” Nyange alipumua kwa nguvu kama aliyepata ahueni kisha akasema, “Asante Mungu wangu”🙏. Kila mtu akamgeukia.
“Nikamkumbusha hayo yote, nikamwambia lazima aniambie hiyo mimba ni ya nani. Kama mnavyojua jeuri ya Leah, alinitukana na kuniambia hayanihusu. Akaanza kuhangaika kumtibu Nyange kwa dawa za hospitalini bila mafanikio yeyote, ndipo hapo chuki ikazidi kwa Nyange.”
“Jamani mtoto ni mkatili huyu, kama shetani. Alikuwa akimpiga Nyange na kumtumikisha mle ndani, kama punda. Kila alipokuwa akimtuma Nyange afanye kitu, halafu Nyange asifanye vile anavyotaka yeye Leah, alikuwa akimuadhibu vibaya sana. Mpaka mimi niliposhindwa, nikaamua kuondoka.”
Hakuna Ubaya Unaodumu.
“Lakini niliamua kurudi kwa yule mganga aniambie ni nini kinachoendelea, kwa Penninah ambaye haponi na Nyange ambaye amechanganyikiwa kabisa. Ndipo mganga aliponiambia ukweli wote.”
“Kumbe Leah alinidanganya tokea siku ya kwanza tulipoenda kwa yule mganga.” “Kwa taarifa yako, wala sio hilo tu alilokudanganya. Yote aliyokwambia mwanao, unayempenda na kumwamini kuliko mtu yeyote hapa duniani, niya UONGO. Kila kitu alichokwambia kuanzia siku unamkuta hospitalini amelazwa, akisema alikuwa peke yake, mpaka leo, ni UONGO MTUPU.”
“Nasidhani hata kama alishawahi kusema ukweli huyo, tangia unamzaa. Amejawa chuki na wivu moyoni mwake, ndio maana hawezi kupenda wala kumthamini mtu yeyote maishani mwake. Ona alichokufanyia wewe mwenyewe. Amekutenganisha na kila mtu hapa duniani, na mwishowe amekuacha peke yako ukiteseka.” Penninah alimkatisha mama yake, na kuongea kwa jazba sana. Hakuna aliye mnyamazisha, kwani wote walikuwa wamepigwa na butwaa. Mama yake alianza kulia.
“Tunaomba uendelee mama.” Alikuwa ni wakili wa upande wa Nyange aliyemtaka aendelee, baada yakumuona analia tu, bila kumalizia. “Huyo mganga wenu, alikwambia nini juu ya Leah?” Mama Eliah alifuta machozi na kunywa tena maji kidogo, kisha akaendelea.
“Tulipoenda kwa mganga kwa mara ya kwanza kabisa, halafu Leah akaniambia mimi nimsubirie nje, kumbe mwenzangu alienda kuongea mambo mengi ya uongo na mganga, kisha wakakubaliana kunidanganya mimi na aina ya dawa watakazo mpa Nyange na mkewe. Na kumbe maskini mtoto wa Eliah wala hakuwa ametumwa kuja kuchukua mchanga! Maskini mjukuu wangu ni kweli alikuja kunisalimia na wala Eliah hana shida na mali za baba yake.”
“Kumbe Leah alimuahidi yule mganga mapenzi endapo atafanikiwa kupata mali zote za Nyange. Kumbe tokea mwanzo huyu Leah hakuwa hata na shida na Nyange, shida yake ni hizo mali za wenzake. Sasa siku ile mganga akamwambia yeye atamfanyia lakini lazima wafanye mapenzi. Leah akamwambia yule mganga, hatalala naye mpaka afanikiwe. Akisha fanikisha mipango yake yote, ndipo atarudi kwa yule mganga tena kutimiza ahadi yake ya mapenzi.”
“Mganga anasema alipoona mambo yamekamilika huku kwa kina Nyange, na dawa zake zimefanya kazi kama Leah alivyotaka, akaanza kumpigia simu Leah kutaka kukumbushia ahadi yake, lakini Leah akawa hapokei simu zake. Yule mganga anasema akaamua kumfunga zaidi Nyange, ili Leah asifanikiwe, na anasema alijua lazima Leah angerudi tu kwake.”
“Zile siku tatu nilizowaambia Leah aliondoka bila kuaga, kumbe alirudi kwa yule mganga. Lakini yule mganga alisema alimwambia hawezi kumsaidia dawa nyingine tena, mpaka atimize ahadi aliyoweka mbele ya mizimu, la sivyo mambo yatamrudia yeye mwenyewe. Ndipo ilipomlazimu Leah kukubali, tena kwa masharti mapya ya mganga.”
“Mganga anasema alimwambia Leah lazima wakae naye siku tatu kama mkewe huku akimuagua kwa kuwa ameshakasirisha mizimu. Baada ya hizo siku tatu ndipo akamruhusu na dawa zilizomfanya Nyange akubali kumuoa na ZAWADI ya mimba ya huyo mganga alipewa huyo Leah.”
“Sasa jana walipokuja wale askari kanzu nyumbani kwangu kunichukua kwa ajili ya kutoa ushahidi, niliwaomba tumfuate na yule mganga kwanza ili tuje naye huku anisaidie kuwa shahidi yangu, maana wale askari WALINITISHA SANA na kuniambia safari hii nililoga mke wa Judge Mkuu wa Tanzania. Hakuna jinsi nitapona, nitafia jela. Nilijaribu kujitetea kwa wale askari kuwa sio mimi ni Leah, lakini hawakunielewa kabisa. Waliniambia nilazima tuondoke, usiku uleule, ili asubuhi tuwe tumefika hapa.”
“Niliwaambia ushahidi wangu hautakamilika mpaka huyo mganga, kwa hiyo ni lazima tuondoke na yule mganga. Wakaniambia nisubiri wapige simu kwanza kama wataruhusiwa kumchukua na huyo mganga, baada ya muda wakaniambia wameambiwa wamlete na huyo mganga, lakini lazima tuwe tumefika hapa Dar leo asubuhi.”
“Tulipofika nyumbani kwake, tulimkuta na yeye yule mganga ni mgonjwa sana, lakini wale askari wakamwambiwa wamepewa amri, wamchukue hivyo hivyo. Yeye akawaahidi kitu na kusema, tumwambie Leah akiri kila kitu, AKIKATAA tumpigie simu kumjulisha, na tumwambie zilezile dawa walizomtengenezea dada yake, atamtengeneza na yeye pia.” Leah alishituka sana.
Mama yake alimgeukia Leah. “Yule mganga aliniambia alikufunga kwa makusudi kwamba asimtoe mtoto wake, ndio maana kila ulipokuwa ukijaribu kutoa ile mimba, ilishindikana.” Leah alibaki kimya.
“Aliposhindwa kutoa ile mimba ndio akaamua aje asingizie mtoto ni wa Nyange. Alipoona nimejua, akajua nitatoa siri yake. Akabaki hajui chakufanya. Mganga alituambia na wale maaskari, kuwa Leah alijifungua salama, mtoto wa kikelakini alikuwa mlemavu kabisa. Yule mganga anasema Leah alipoona amezaa mtoto wa vile akampigia simu aje amchukue yule mtoto wake huku mjini, yeye hawezi kumpeleka kule kijijini kwetu, hataki kuniona.”
“Yule mganga akamwambia, mama yako mgonjwa sana, lakini Leah hakutakakabisa kuniongelea na wala hakujali, akamjibu anampa siku tatu, kama hatafika kumchukua yule mtoto, yeye atamuua. Yule baba ana wake wawili, alisema wake zake wasingekubali kulea mtoto asiye wao. Sasa swali ni je, Leah ulimpeleka wapi huyo mtoto wenu na mganga wako?” “Hayakuhusu.” Leah alijibu kwa jeuri kama kawaida yake.
“Ni kweli hayanihusu.” Mama Eliah alijibu na kuongeza swali jingine. “Haya, je unakubali kukiri uliyomfanyia ushirikina Nyange na dada yako na mtoto wa kaka yako?” Leah alianza kubabaika.
“Jamani naomba niongee.” Mama Briana aliingilia. “Karibu.” Hakimu alimkubalia. “Sisi hatutaki kumsikiliza tena Leah, nafikiri wote mmesikiliza vya kutosha. Sisi tunachotaka ni mali zetu, basi. Hatutaki maneno mengi.” Mama Briana alibadilika na kuwa jasiri, kama sio yeye, ‘chaulizi’. “Na mimi naona yaishe.” Leah akajibu harakaharaka.
“Hapana jamani! Msifanye mambo kienyeji. Kwanza tunataka kujua mtoto huyo aliyezaliwa yuko wapi na tunataka kusikia kutoka kwa Leah mwenyewe, anakiri hilo kosa la kichawi?” Hakimu aliuliza huku akimwangalia Leah. Leah alibaki kimya. “Naombeni simu jamani, nimpigie yule babu.” Mama Eliah aliongeza. “Mama na wewe nini kimbelembele? Hayakuhusu.”
“Huyu mtoto ni wangu jamani! Namjua kuliko mnavyomjua nyinyi. Atawazungusha sana hapa, hatutakaa tutoke humu ndani na mimi mgonjwa. Leah hawezi kukubali kosa, tutakesha hapa. Nipeni mimi simu nimpigie yule babu, mganga wake, atayasema yote. Na yule mganga anamtaka mtoto wake.” Leah alianza kuhaha.
“Kwani nani kakwambia nimekataa?” Leah alijibu kwa sauti ya chini lakini uso wake ulijaa kiburi kama kawaida yake. “Na mtoto?” Mama Eliah akahoji. “Si mwenyewe ulisema alizaliwa mlemavu, kwani walemavu wanaishi?” “Amekwambia nani walemavu hawaishi, hawana roho? Mganga anamtaka mtoto wake na anataka useme ukweli, lasivyo amekwambia utamfuta huyo mtoto alipo. Ulimuua mtoto wake?” Leah alinyamaza.
“Yaani wewe Leah una roho mbaya, jamani! Utafikiria shetani! Unaua mpaka mtoto wako wa kumzaa mwenyewe, sababu ya ulemavu!? Hakika Mungu atakulipa Leah.” Ishimwe alikuwa akiongea huku akilia.
“Mtoto yuko wapi Leah?” Hakimu aliuliza na yeye. “Alikufa.” Leah akajibu kwa kifupi. “Alikufa au ulimuua?” “Niliamka asubuhi nikamkuta amekufa.” “Ulitoa ripoti kokote?” “Sasa natoa wapi ripoti? Mtoto wangu, halafu ulitaka nitoe ripoti kwa nani?” Leah akamjibu Hakimu bila hofu.
“Kwa hiyo unakiri kosa la kupokonya mali za Bwana Nyange na mkewe kwa kutumia ushirikina?” Hakimu akauliza, lakini Leah alibaki kimya. “Leah?” “Ndiyo.” Hakimu akaamuru kuanzia wakati huo Leah arudishe kila kitu cha Nyange na mkewe, na Leah aliwekwa chini ya ulinzi.
*********************
Kama mchezo, Nyange na Mama Briana walirudishiwa mali zao zote siku hiyo. “Asante Mungu wangu.” Nyange alisikika akisema. “Asante sana Ishimwe. Asante.” Mama Briana alimsogelea Ishimwe na kumkumbatia. “Siamini mwenzako!”Ishimwe alinong’ona. Vilijaa vicheko na vilio kati yao, Nyange, mama Briana na Ishimwe wakiwa bado kwenye hichohicho chumba.
Leah alifungwa pingu na kutolewa mle ndani, lakini hata mama Briana hakutaka kumwangalia na wala yeye mwenyewe hakuonekana kujutia.
Mama Briana, Nyange na Ishimwe walitoka kwenye hicho chumba bila hata kumsemesha mama Eliah. Walimkuta Paul nje ya hicho chumba akiwasubiria. Ishimwe aliongeza mwenda mpaka karibu ya Paul akataka kumpa mkono wa shukurani lakini Paul alimvuta karibu na kumkumbatia.
“Asante Paul.” “Mbona sasa unalia badala ya kufurahi?” “Huyu msichana ana roho mbaya sana Paul. Kumbe alizaa na mganga wake, alipoona mtoto ni mlemavu, akamuua!” Paul alibaki ametoa macho.
Alisogea mama Briana akiwa analia, pamoja na mumewe. “Sijui tuseme nini Mkuu!” Paul alibaki akiwaangalia huku amemkumbatia Ishimwe. “Asante sana Baba Sonia, sijui niseme Paul? Asante sana.” Mama Briana aliongeza. “We Paul? Wanakusemesha bwana!” Ishimwe akamsukuma kidogo kwa kujitingisha.
“Daah! Nimeshituka sana kifo cha huyo mtoto mdogo ambaye hakuwa na hatia! Hakuchagua kuzaliwa mlemavu jamani! Amemuadhibu huyo mtoto bila kosa!” Shukurani zote alizokuwa akipewa Paul, hazikuleta tena maana. Alibaki na huzuni, kila alivyofikiria jinsi alivyokuwa akitamani watoto, halafu wengine wanaua wa kwao! Alibaki akisononeka moyoni. Alitamani hata Mungu angempa yeye huyo mtoto mlemavu.
“Ningejua nisingekusimulia juu ya huyo mtoto! Hapo ndio nishampoteza tena Paul. Anapenda watoto huyu! Wakati ule tunaishi naye Mwanza, alikuwa anakusanya watoto wote wa pale mtaani kwetu, anakaa nao nakuanza kuzungumza nao kama watu wazima, na wao walikuwa wasipomuona siku hiyo wanamfuata mpaka kwetu, na chumba chenyewe kilikuwa kimoja. Basi watoto walikuwa wanajazana humo ndani eti anaongea nao, mpaka unakasirika. Anapenda sana watoto Paul.” “Daah! Lakini hongereni jamani. Mnastahili, ni haki yenu.” Paul akajibu.
*********************
“Naumwa sana Penninah!” Sauti ya mama Eliah iliwakatiza mazungumzo yao. Wote wakageuka kasoro mama Briana alibaki kimya ameinama. Hakuna aliyeweza kujibu. Wazi mama Eliah alionekana mgonjwa. “Sina pesa, na sina pakwenda hapa mjini.” Mama Eliah aliongeza huku machozi yakimtoka. “Na sisi wenyewe tunahifadhiwa nyumbani kwa Sonia. Sina pakukuweka.” Akajibu bila ya kumwangalia mama yake. Walisimama hapo kwa muda wote wakiwa kimya, mwishowe Paul akamwambia Ishimwe watangulie kwenye gari kama kuwapa nafasi.
“Unafikiri ni sawa tukimsaidia huyo mama?” Paul aliuliza mara walipoingia kwenye gari. “Sijui Paul! Nafikiri tumuulize Penninah mwenyewe.” Nyange na mkewe wakatoka. Paul alimtuma Mlinzi wake awaite kabla yakupanda kwenye gari.
Wakawafuata garini. “Eti Penninah, kama ungekuwa na uwezo wa kumsaidia mama yako, ungemsaidia?” Paul aliuliza lakini mama Briana alishindwa hata kuongea, alibaki akilia tu.
“Naomba niongee kitu kimoja jamani, kama mtaniruhusu lakini. Eti Nyange?” Paul aliuliza kwa heshima. “Hamna shida Mkuu.” “Na hapa naongea kama Paul, sio vinginevyo. Najua mnachopitia sasa hivi, ni ngumu sana hakuna maelezo yake, mimi nafahamu. Naweza kusema hivyo kwa kuwa na mimi au mimi na Ishimwe tumepita mlipopita nyinyi.”
“Hakuna lugha rahisi yakueleza maumivu yake, mtu mwingine akaelewa zaidi unapokuwa umetendwa na mama yako mzazi. Lakini kwa bahati mbaya sana hatuna mamlaka ya kuhukumu wazazi wetu hata kidogo. Amri tuliyopewa na Mungu ni KUWAHESHIMU tu.”
“Sisemi kama ni lazima mumpokee na kurudi kuishi naye tena, lakini sidhani kama ni sawa kumuacha vile akiwa mgonjwa.” “Nitafanyaje sasa?” Mama Briana akauliza huku akilia. “Mumsaidie kutokana na uhitaji wake, basi. Kama sasa hivi ni mgonjwa. Basi mpelekeni hospitalini. Akipona mumrudishe kwake, basi.”
Nyange akamgeukia mkewe. “Eti Penninah?” Mama Briana aliendelea kulia. “Na sio lazima ukafuata ushauri wangu Penninah. Upo huru kufanya kile unachojisikia moyoni na wala hatutakuhukumu kwa hilo.” Mama Briana akatulia na kujibu. “Mimi nataka kumsaidia mama yangu. Sasa sijui Nyange!” “Hamna shida kabisa.” Nyange naye akaridhia.
“Basi naomba nikuombe Nyange, kwa kuwa sasa hivi tuna magari mawili, hili la Briana tulilorudishiwa na mahakama, na la Sonia, naomba mimi nichukue gari moja nimpeleke mama hospitalini, halafu wewe ukachukue watoto shule.” “Nitakusindikiza mama Briana.” Ishimwe alidakia, akakwapua pochi yake na kushika mlango wa gari akijiandaa kutaka kushuka kwenye gari.
“Wewe Ishimwe vipi bwana?! Mbona hata hatujaongea!? Hujajua nina ratiba gani na wewe, mwenzangu unataka kuondoka tu na kuniacha barabarani!?” Paul aliongea kwa ukali kidogo na kumfanya Ishimwe kupooza gafla na kurudi kukaa pembeni yake.
Alishazoea maisha ya uhuru aliyokuwa nayo. “Samahani Paul. Nilijisahahu.” Paul alibaki akimwangalia. “Nitakupigia simu baadaye kujua hali ya mama inaendeleaje, mama Briana.” “Hamna neno kabisa. Mmeshatusaidia vyakutosha. Nyinyi nendeni tu.” Waliwaacha pale Nyange na mkewe wao wakaondoka.
*********************
“Samahani Paul. Nilishajisahau.” Ishimwe alirudia tena. “Unakumbuka nilikwambia nataka kuongea na Sonia? Halafu tunatakiwa kuwepo Shinyanga alhamisi ya kesho kutwa. Na bado mama na wifi yako wanakuja kesho? Na usisahau harusi yetu ni jumamosi hii.” Ishimwe akanyamaza.
“Vyote hivyo vinakuhitaji wewe Ishi. Wewe ndio kiungo cha kila kitu. Bila wewe kuwepo na akili zako zote kuziweka sehemu moja, siwezi kufanikisha kitu hata kimojawapo hapo. Nakuhitaji sana Ishimwe.” “Nimeelewa Paul. Naamini kila kitu kitaenda sawa. Sikutaka kumuacha Mama Briana peke yake.”
“Naelewa Ishimwe. Na mtaendelea kuwa marafiki, lakini naomba sasa hivi mgawane majukumu. Yeye ashugulikie mambo yake na wewe ushugulikie yetu. Tutakapotulia, mtaendelea kufuatana mtakavyo.” Ishimwe alinyamaza. Waliendelea kwenda Ishimwe akiwa bado kimya, akionekana ana mawazo.
“Nimekuudhi Ishimwe?” “Hapana.” “Mbona upo kimya sasa?” “Nafikiria tu.” “Unafikiria nini?” Hakujibu. “Eti Ishimwe?” “Naona maisha yamenibadilikia!” “Yamebadilika yamekuwa mabaya au mazuri?” Hakumjibu. “Unataka nimwambie dereva akurudishe hospitalini ukamsaidie Penninah?” Na yeye akajirudi.
“Eti? Naweza kumwambia akurudishe.” “Hapana Paul. Naona upo sahihi. Nafikiri ni wakati mwafaka na mimi kujenga kwangu. Sasa hivi ndio tunaweka msingi wa familia yetu na sisi, sitaki kupitwa. Nataka niwe na wewe kwenye kila hatua, tukisaidiana.” Paul alimwangalia huku akitabasamu, moyoni akijisikia vibaya jinsi alivyomjia juu mbele ya Nyange na mkewe.
“Asante Ishimwe na samahani, najua niliongea kwa ukali kidogo.” Ishimwe alitabasamu, akainama na kubaki kimya. Paul akamsogeza karibu na kumbusu. “Samahani Ishimwe, nahisi nimepaniki. Naona mambo yamekuwa mengi na yote yanatakiwa yakamilike ndani ya juma hili.”
“Usichanganyikiwe bwana Paul! Mbona mambo yote yanaenda vizuri tu? Usichukulie kama ni wajibu unaotakiwa kutimiza, itakuchosha na kukunyima raha. Chukulia kama Mungu ametufungulia milango ya baraka week hii. Mambo yote mazuri tuliyokuwa tukiyatamani maishani mwetu yanatokea ndani ya hili juma.”
“Tutafunga ndoa yetu, kingine mama Tambo amenikubali mimi na mtoto wetu. Halafu tumepata hati zangu zote tulizokuwa tukizihitaji. Kwa hiyo ni baraka mpenzi wangu, sio majukumu.” “Umeona sasa? Maneno hayo machache tu uliyo sema, yameshanibadilisha mtazamo wangu, nakuanza kujisikia vizuri. Ndio maana nataka uwe unakuwa karibu yangu kila wakati Ishimwe, unajua kunituliza.” Alitabasamu na kumbusu Paul kama kumwambia yameisha.
“Kila kitu kitakuwa sawa mpenzi wangu, na nitakuwa na wewe kila wakati. Ila uwe unanikumbusha, najisahau mwenzio. Nimeishi maisha ya peke yangu kwa miaka karibu 28 sasa, najisahu naendelea kujifikiria mwenyewe.”
Mahusiano Hujengwa..
Dereva alisimamisha gari mbele ya nyumba ya kina Sonia. “Hii nyumba nayo niyakuzungushia ukuta na kuwekwa geti. Sipendi hivi palivyo waziwazi.” “Sijui kama wana hela sasa hivi ya kujenga tena. Akili zao zote zipo kwa mtoto.” Ishimwe alimjibu Paul. “Nitaongea na Sam.” Waliingia ndani, na kumkuta Sonia amelala kwenye kochi, hana habari.
Paul akamsogelea na kumshika kichwa chake. Sonia alishituka. “Unaumwa?” “Hapana nimepumzika tu. Nimejikuta nipo peke yangu humu ndani, nikaamua kulala. Karibuni.” Akakaa. “Mama anazidi kupendeza!” Ishimwe alicheka. “Mmekula?” Akawauliza wazazi wake. “Hatutakaa sana Sonia. Nilitaka tuongee.” Sonia alikaa vizuri nakubaki akiwaangalia mama yake na baba yake jinsi wanavyoangaliana.
“Kuna nini tena? Au na mimi sio mtoto wako?” Sonia alimuuliza swali Paul. “Sonia wewe?!” Ishimwe alishituka sana. Paul alianza kucheka. “Bwana usicheke Paul! We Sonia sasa unafikiri baba yako nani?” Sonia naye alikuwa akicheka. “Mimi ndio baba yako bwana! Ila tulitaka kukwambia kuwa bibi yako anataka mkamuone kabla ya harusi.” Uso wa Sonia ulibadilika gafla. Alibaki akiwaangalia wote wawili.
“Mnanitania au kweli?!” “Ni kweli Sonia, bibi yako anataka kukuona.” Ishimwe alijibu, Sonia akakunja uso. “Kwa nini?!” Akamuuliza baba yake, lakini Paul alibaki kimya.
“Yaani mtu aliyetaka kuniua, leo anataka kuniona! Ili iweje?” Sonia aliuliza tena. “Au niulize tena. Nyinyi mlimjibuje?” “Sikujibu kitu. Lakini anataka kukuona wewe na Sam. Anataka kuwatambulisha kwa ndugu wengine.” “Na Sam?!” Sonia alishituka sana. “Ndiyo Sonia.” Alibaki akiwaangalia wote wawili kama haelewi.
“Jamani nashukuru sana Paul, kwa nia yakutaka kunitambulisha kwa hao ndugu zako, lakini HAPANA. Sioni umuhimu hata kidogo.” Ishimwe alimgeukia Paul kumuangalia hali yake. Majibu ya Sonia hayakumshitua Ishimwe hata kidogo, aliyatarajia kwa kuwa anajua vizuri tabia ya Sonia, lakini alimuhurumia Paul.
“Naomba nikaandae chakula jamani. Sam ataingia hapa muda sio mrefu.” Sonia alisimama. “Naomba unisikilize Sonia.” “Kama ni kuhusu utambulisho, HA PA NA. Nakwenda kuongea nini na mtu aliyetaka kuniua jamani? Tunaenda kuambiana nini? Hebu wewe mwenyewe fikiria.”
“Sitaki kulea watoto wangu kwenye familia za namna hiyo hata kidogo au maisha kama hayo. Nataka kujenga familia itakayoongozwa na mama na babammoja, ambae ni mimi na Sam tu. Tena kwa kuheshimiana. Nataka nyumba yenye amani na utulivu.”
“Sio tena maisha yetu yaje kuwa kama yenu! Hamna maamuzi yenu binafsi mpaka mama yako aamue! HAPANA. Nimeamua hivyo na ninaomba na nyinyi mniunge mkono katika hilo. Sijawahi kukaa kwenye familia hata siku moja. Wakati wote nimekuwa na picha ya familia ambayo nilikuwa natamani mimi ndio ningekuwepo humo.” Sonia alianza kulia.
“Kila nikitaka kutulia, jambo linatokea! Sijui kama mama amekwambia? Hatujamaliza hata mwaka hapa. Ndio tulikuwa tumeanza kutulia, na maisha yalianza kuleta maana. Kwa mara ya kwanza na mimi nikapata mtu anayenipenda na kunijali kwa dhati. Amenikaribisha mimi, mama na mwanangu kwenye nyumba yake. Anatujali sana, na kwa mara nyingine ninatarajia mtoto ambaye wa safari hii anasubiriwa kwa hamu sio mtoto wa aibu.”
“Kila kitu kikaonekana kinaeleweka maishani, gafla mama akaondoka. Halafu maisha ambavyo hayanihurumii, eti tena mnataka kunirudisha kwa mtu aliyekuwa anatafuta kutoa uhai wangu! Halafu mnataka tena mimi ndiye nimfuate! Jamani nawaombeni kama nyinyi kweli ni wazazi wangu, mnifikirie na mimi, angalau mara moja tu maishani mwenu.”
“Wala siwaombi mali au hata hilo jina la Tambo mimi silitaki, ninachotamani nikuwatengenezea wanangu aina hiyo ya familia, ambayo mimi sikubahatika. Na kwa kuwa nimempata Sam, naombeni mnielewe, na mniache na mimi nitulie. Nijenge familia yangu na nyinyi muendelee na maisha yenu.”
“Samahani sana kama nitakuwa nimewaumiza. Lakini sipo tayari na wala sioni kama kuna umuhimu wa kukutana na mama yako kwa sasa.” “Nimekuelewa Sonia.” Paul akajibu. Ishimwe alikuwa amebaki kimya muda wote akimwangalia Paul kwa kumuhurumia. Paul aliaga akiwa kama amenyeshewa mvua. Wakaondoka.
*********************
Njia nzima Paul alikuwa kimya kabisa bila kusema kitu, mpaka walipofika nyumbani kwao. “Pole Paul.” Paul alitabasamu kinyonge nakujitupa kitandani. “Tutafanyaje sasa?” Ishimwe alijisogeza karibu na yake, akavuta mto akalala pembeni yake. “Sijui Ishimwe! Lakini namuelewa kabisa Sonia, wala simlaumu. Hata hivyo nashukuru Mungu kwa kunipokea mimi.”
“Unafikiri mama yako atafanyaje?” “Kwa mara ya kwanza maishani mwangu, nitakuwa mkali sana kwake. Nitaweka msimamo wa waziwazi, nitamuomba akae mbali kabisa na Sonia, tena asithubutu hata kumfuata, mpaka Sonia atakapokuwa tayari yeye mwenyewe. Sitakubali aniharibie mahusiano yangu na mwanangu. Nataka tumuache Sonia aamue vile anavyotaka yeye. Mtoto mwenyewe ni huyohuyo mmoja niliye naye, sitaki apotelee kwa Sam, halafu mimi niambulie patupu.”
“Pole sana Paul. Naomba umpe muda mpenzi wangu. Unajua mambo mengi makubwa na yakumchanganya akili yanamtokea, kwa muda mfupi mfupi, bado hajatulia na kuyaingiza vizuri moyoni. Anahitaji muda.” “Daah! Najuta Ishimwe wewe, acha tu. Natamani nirudishe siku nyuma, lakini siwezi.” “Mpe muda. Na usimuone jeuri vile, ndani yupo mdhaifu sana Sonia. Anakuhitaji kuliko atakavyokuonyesha. Wewe si ulimuona siku ile jinsi alivyolia sababu ya kuondoka bila kumbembeleza?”
“Ni kwako Ishimwe! Alikuona jinsi ulivyokuwa ukihangaika naye, ameona shida ulizozipata naye bila kumkimbia au kuchoka. Mimi kwake ni hivyo kwa kuwa wewe umenikubali na ni baba yake, lakini Sonia hana mapenzi na mimi hata kidogo! Kila nilipojitahidi kumuonyesha na mimi nataka niwepo kwenye maisha yake, wakati wote amenifungia moyo wake. Ananionyesha wazi anakutaka wewe na Sam tu.”
“Nimemsikiliza maongezi yake yote, namuona wazi bado anahasira na mimi. Na nimeharibu zaidi, kukuchukua kuja kuishi hapa na mimi. Sonia anaonyesha wazi anakuhitaji wewe Ishimwe sio mimi.” “Paul jamani! Mbona unakata tamaa mapema? Sonia hakufahamu mpenzi wangu. Na yule mtoto anatabia kama zako Paul! Hana rafiki wa kudumu, wala hajui kutengeneza marafiki zaidi ya wale watu pale anao ishi nao.”
“Maisha yake yote anajifungia ndani kama vile tulivyomkuta leo, tokea mtoto yuko hivyo Sonia. Swala la mimi kumuacha pale, najua litamuumiza kwa muda, kwa kuwa Sonia ameishi na mimi tu, maisha yake yote, hajui maisha mengine. Hata kipindi cha nyuma tulipokuwa tukitengana, tulikuwa tukiambiana ni kwa muda tu na alikuwa akilia sana kila anapoondoka na kuniacha sehemu.”
“Hata alipopata nafasi ya kwenda kuishi kwa huyo rafiki yake Fau, ambaye baba yake ndiye alimbaka, japokuwa alikuwa akipewa kila kitu huko, na alikuwa anasema walikuwa na nyumba nzuri, lakini alikuwa hawezi kuishi mbali na mimi. Alikuwa radhi aache starehe huko, aje tuishi wote kwenye kile chumba kilichokuwa kama tanuru la moto!”
“Na nina jua pale alipo anahofu kubwa sana na huyo mtoto atakayemzaa. Vile unavyomuona ana mtoto mkubwa vile, lakini hajui kabisa mambo ya watoto. Hata kushika mtoto mchanga mkononi au kumuweka mgongoni, hawezi. Ungemuona Kana wakati anazaliwa ungemuhurumia Sonia.” Ishimwe alianza kulia.
“Nilikuwa naingia chooni, nalia mwenyewe. Hakuwa akijua kabisa kitu cha kufanya na yule mtoto. Ilibidi mimi ndiye niwe mama yake Kana. Kunyonyeshakwenyewe ilibidi kumfundisha alale chini, ndipo amnyonyeshe mwanae. Alikuwa mdogo sana, halafu alijawa hofu kupita kiasi. Mtoto alikuwa akilia na yeye alikuwa analia kupita mtoto mwenyewe.”
“Kwa hiyo tumpe muda Paul. Bado ile hofu ya mtoto wa kwanza haijamwisha na ule mshituko wa kwamba kila mmoja wetu anaanza maisha yake, pia bado haujamwisha. Mpe muda tafadhali.”
“Na nilazima kumuonyesha kwa vitendo, kwamba hatujatengana, ila ndivyo maisha yanavyotakiwa yawe. Na mimi nitajitahidi, angalau kwa hizi siku za mwanzoni nikishamaliza kazi zangu hapa, niwe naenda kukaa naye kidogo. Atazoea tu na utamuona baada ya muda yeye mwenyewe ataanza kukutafuta hata kwa ujumbe. Na huo sasa ndio utakuwa wakati mzuri wa kumtambulisha kwa Mama Tambo pia.”
“Hata jana nilitaka kukushauri hivyohivyo, kabla hujamtambulisha kwa Mama Tambo, jitahidi kujenga naye wewe kwanza mahusiano, ukisha muweka karibu, ndipo umtambulishe kwa mama yako au ndugu zako. Nafikiri sababu ya uchovu, nikasahau kukwambia usubiri kwanza.”
“Ana upendo sana Sonia, wewe utakuja kuona. Lakini pia anachukua muda mrefu sana kuamini watu. Na akikupenda na kukuamini, unaweza kumshauri kitu chochote, na akafanya. Ilimradi tu ajue kama wewe utakifurahia, atafanya. Hata kama kitamgarimu yeye kwa kiasi gani, atakubali kufanya, ilimradi tu akufurahishe, asikuudhi.”
“Nimeelewa Ishimwe. Nahisi nimefanya haraka sana. Ni kweli ningemuacha kwanza. Nimefanya haraka, sikumfikiria. Imekuwa ni kama nimekutoa wewemaishani mwake, halafu nataka kumpa mama, mtu anayejua hampendi. Nitamwambia mama amuache kwanza. Nataka hii harusi yetu iishe kwa amani, ili tumsaidie na yeye afunge ndoa yake akiwa ametulia.” “Wazo zuri.” Paul akatulia kidogo.
*********************
“Naomba nikuombe kitu Ishimwe.” “Hamna shida.” “Najua mama yangu ametukosea sana, hakuna jinsi ya kumtetea, au akajitetea kuhalalisha alichokifanya. Lakini naomba tumsamehe. Najua haitakuja kukaa ikatokea, yeye mwenyewe akatuomba msamaha, lakini najua anajutia alichofanya. Nakuomba sana, tumsamehe mama. Ni mama yangu, na ninampenda sana. Sana.”
“Hata nilipoondoka hapa kwenda masomoni nikiwa nimemkasirikia sana, nikatamani nisuridi tena hapa Tanzania, lakini nilishindwa. Miaka yote minne niliyokuwa mbali naye, nikiwa masomoni niliona najitesa mimi mwenyewe. Nilijiambia nimekupoteza wewe, siwezi kumpoteza na yeye. Hata niliporudi, akanitafutia kazi, nikaja kuishi hapa, nakuamua kutomtafuta tena, maana hapo nilishakuwa nimepata kazi nzuri ya ndoto zangu, na nilijua nikiongeza juhudi kazini na hivi nilikuwa najulikana kama mtoto wa Tambo, nilijua siku moja nitafika hapa nilipo, bila mama.”
“Kwa hiyo nikaamua niendelee kumnunia kabisa, nisimtafute. Lakini nilikuwa nahangaika, ungeniona, ungenihurumia. Nilikuwa natunga safari za uongo kwenda Shinyanga, ilimradi tu nikamuone, hata kama sitaongea naye kitu chochote zaidi ya salamu na kuiona sura yake ilikuwa ikinifariji sana.”
“Japokuwa ana mambo yake yanayokera na kuudhi sana, lakini ni mama yangu Ishimwe. Sitakuja kupata mama mwingine, hata nifanyaje. Na amekuwa akihangaika na sisi kweli. Tokea tupo wadogo mpaka leo, mama hapumziki. Japokuwa hutamuomba msaada, lakini anatufuatilia watoto wake kwa karibu sana, na kutusaidia kwa kadiri ya uwezo wake.”
“Mpaka najiuliza ni lini atakuja kuishi maisha yake yeye mwenyewe! Na hivi tena amekuja na Sonia, najua hatakaa apumzike mpaka amuone na yeye Sonia anamaisha yatakayo mridhisha. Kwa hiyo ombi langu kwako Ishimwe, nakuomba na wewe umsamehe mama, na kumpokea kama mama yako.”
“Kama hivyo anavyojaribu kujisogeza karibu yako, naomba umpokee, mpe nafasi, labda unaweza na wewe kuona upande wake mwingine, ukampenda.” “Wala usijali Paul. Mimi sina neno kabisa. Hapa naona kama nimepewa ulimwengu mzima! Mama Tambo kunitafuta!? Wala huhitaji kuniomba nimfungulie mlango. Mbona milango yote ipo wazi.” Paul alianza kucheka.
“Kweli tena nakwambia! Hata akitaka nimbebe mgongoni, mbona nitambeba tu. Nimefurahi kweli.” “Acha utani bwana Ishimwe. Mwenzio namaanisha.” “Unafikiri mimi nakutania Paul? Hata kidogo. Mwenzio sina ndugu kama wewe na Sonia mnavyoringiana. Mwenzako kila anayenisogelea karibu na mimi na mng’ang’ania, namfanya ndugu.”
“Mimi ndiyo baba yako Ishimwe, nilishakwambia. Au umesahau?” Ishimwe alibaki kimya. Taratibu Paul aliona machozi yakimdondoka Ishimwe. “Na wewe uliondoka Paul, ukaniacha. Nikarudia yale maisha ya ukiwa tena.” Paul alimvuta karibu na kumkumbatia. “Nimerudi Ishimwe, sasa hivi nipo mpaka kifo changu, nakuahidi nitakuwa na wewe. Sikuachi tena. Nimerudi kuchukua nafasi yangu kwako ya ubaba, mume na rafiki.”
“Niliteseka sana ulipoondoka. Siku za mwanzo uliponiacha nilikuwa nalia usiku kucha. Ule uchungu wa kufiwa na ndugu zangu ulirudi upyaa. Zile ndoto za siku niliporudi kijijini kwetu na kukuta kijiji kizima kimechomwa moto, zilianza kunirudia upyaa. Nilikuwa na kulilia Paul mchana na usiku.” Ishimwe alizidi kulia kwa uchungu sana. Paul alibaki akiumia roho.
*********************
Aliondoka, akijua wazi ni kiasi gani Ishimwe ana muhitaji. Alimuacha akiwa mtoto mdogo, tena mjamzito. Alipoingia kwenye maisha ya Ishimwe, alimuona jinsi Ishimwe alivyobadilika. Alijawa na furaha, na akagundua vitu vingi vizuri, vilivyokuwa vimefichwa ndani ya Ishimwe sababu ya huzuni. Ahadi ya kuwa baba, rafiki na mume kwake, alishaiweka kwa Ishimwe tokea zamani.
Paul alimpenda Ishimwe kuliko kitu chochote maishani mwake. Kwa asili Paul alikuwa mtu mwenye upendo sana, na kujali. Hakupenda kumuona mtu yeyote anapata shida. Hata kama umemuudhi kwa kiasi kikubwa sana, alijua jinsi ya kukubali yaishe. Alikuwa mcheshi sana na mwaminifu. Hata watu waliokuwa wakifanya kazi chini yake, walimsifia sana.
*********************
“Ishimwe!” Paul alimnyanyua uso wake, aliokuwa ameuficha wakati akilia. “Naomba uwe mkweli kwangu. Ni kweli unaniamini kwamba sikuwa nimekukimbia?” “Nakuamini Paul.” “Kweli Ishimwe au umekubali yaishe?” “Nakuamini mpenzi wangu, lakini uliondoka kipindi nilichokuwa nikikuhitaji sana.” “Samahani Ishimwe, najuta kuliko nitakavyo kueleza. Lakini nafikiri wakati ule na utoto ulikuwa ukichangia. Maamuzi mengi niliyokuwa nimefanya hayakuwa sahihi.”
“Nilichanganyikiwa ulipoanza kuumwa. Hofu ya kukupoteza iliniingia, ndio maana nilimpigia simu baba kutaka msaada na nilimuomba asimwambie mama, lakini nikashangaa mama ametusimamia mlangoni. Sijui mama alijuaje, lakini nilimlaumu sana baba. Mpaka anakufa nilikuwa nikimlaumu kwamba alinisalitiwakati mimi nilimwamini yeye.”
“Nakumbuka mara ya mwisho nimeenda kumuangalia wakati mgonjwa sana, pia nilimwambia, usaliti wake umenifanya nipoteze mwanamke ninayempenda na mtoto. Hakutaka kuniambia nini kilitokea, lakini akanipa tu pole na kuniomba niendelee na maisha mengine na nijifunze kuachilia mambo moyoni. Lakini alinihakikishia kuwa mama yangu ananipenda sana kuliko kitu chochote au mtu yeyote hapa duniani na hakuwa na nia yakuniumiza hata kidogo.”
“Aliniambia kama mama angeziona siku zangu zile za upweke na simanzi tokea mwanzo, baba alinihakikishia, mama angefanya tofauti. Nashukuru na yeye tulipata muda wakusameheana, lakini kama unavyomjua baba, hakuwa muongeaji sana, kwa hiyo hakuniambia ni nini kilitokea.” Paul alimvuta vizuri Ishimwe mpaka kifuani kwake, akabaki amemkumbatia huku akimbembeleza. “Naomba unisamehe Ishimwe.”
Huku kwa Sonia.
Huku nyuma alianza kuteseka na kuhukumiwa moyoni. Kila alipokumbuka sura ya majonzi aliyoondoka nayo baba yake, alizidi kuumia lakini asijue cha kumsaidia tena. ‘Siwezi kuwa mnafiki. Siwezi kukubali undugu na mtu aliyetaka kuniua. Naamini nipo sahihi kabisa. Undugu kati yangu mimi na Paul unatosha. Sio lazima kuwa ndugu na ukoo mzima.’ Sonia aliendelea kuwaza na kujipa moyo katika maamuzi yake.
*********************
“Mbona mapokezi ya leo sijayaelewa?” Sonia aligutuka na kugeuka. “Samahani Sam, sikukusikia wakati unaingia, nilikuwa nje napika, ndio nimefunikia wali sasa hivi, na kuingia humu ndani ili nimalizie kuandaa mboga nipike. Pole na kazi.” Sam alibaki ameshikilia mlango wa kuingilia jikoni huku akimwangalia Sonia.
“Kweli sikukusikia Sam mpenzi wangu. Nisingeacha kuja kukupokea.” “Kwema lakini?” “Kwema. Namalizia kupika mboga sasa hivi nakuja tuoge wote.” “Mbona huonekani kama kwema? Hiyo sio sura niliyokuacha nayo asubuhi.” “Kila kitu kipo sawa, labda kwa kuwa nimetoka usingizini.” “Unalia usingizini siku hizi?” Sonia alinyamaza.
“Njoo kwanza.” “Nataka kumaliza kupika kwanza Sam, nitakuja.” “Hapana, nataka tuongee kwanza. Hicho chakula hakina haraka. Walaji si ni sisi wenyewe?” Sonia alibaki amesimama akifikiria. Sam akamsogelea.
“Kuna nini? Na naomba usiniambie hakuna kitu, kwa kuwa mimi nakujua vizuri sana Sonia. Najua kuna kitu kimetokea hapa katikati. Nimekupigia simu zaidi ya mara tano hujapokea.” “Simu nimeacha sebuleni.” “Tokea lini unaacha simu sebuleni wakati unajua tunawasiliana kila wakati? Umenitia wasiwasi mpaka nimempigia simu mama Bree, akaniambia hayupo hapa nyumbani na wewe, akasema Nyange ameenda kufuata watoto shule. Nimeendesha kama nimechanganyikiwa nikijua kuna kitu kibaya kimekupata na uko peke yako.”
“Pole, lakini nilijua mama atanipigia, sikutaka kuongea naye kwa sasa.” “Kwa nini?” Hilo silo jibu Sonia alitaka kutoa kwa wakati ule, alijikuta ameropoka mbele ya Sam.
“Eti Sonia? Kwa nini hukutaka kuongea na mama?” Sonia alibaki kimya. “Kuna nini?!” “Walikuja hapa yeye na Paul, wakaniambia mama yake Paul, anataka kutuona.” “Kutuona?!” “Ndiyo. Mimi na wewe, Sam.” Sam alifikiria kidogo.
Kisha akaona aulize. “Kwa hiyo?” “Wewe umesahahu kuwa mama yake Paul ndiye aliyetaka kuniua? Sasa ananitakia nini sasa hivi? Sitaki undugu na ukoo wa Paul kabisa, Sam. Nataka tuanzishe familia yetu kwa amani na utulivu.” Sam alibaki akifikiria kisha akamwangalia.
“Kwanza naomba usilie Sonia, halafu twende tukaongelee chumbani.” Akakausha machozi, akaongozana na Sam mpaka chumbani kwao. Wakakaa kitandani kwao.
“Wananitakia nini mimi? Paul nilishamkubali, sasa kwa nini anataka nikutane na mama yake?” Sonia alianza tena kuongea mara tu alipokaa kitandani pembeni ya Sam. “Nikwambie kitu Sonia?” Sonia akakunja uso, kuachiria hataki kabisa kuingiliwa katika maamuzi yake.
“Najua uliniomba tusiongelee swala lako na baba yako, lakini naona sio sawa. Wewe unataka tuanzishe familia pamoja, lazima nijihusishe na maisha yako kwa asilimia zote, hivyohivyo na wewe. Kama tukiwekeana mipaka katika mambo fulani fulani, muda sio mrefu, hiyo familia yenye amani na utulivu, tutaisikia kwa watu wengine tu. Sijui umenielewa?” Sonia alinyamaza.
“Kwanza nikuulize Sonia, kwa nini imekuwa ngumu sana kwako kumpokea Paul kama baba yako?” “Mbona nimempokea Sam jamani!? Au nilitakiwa kufanya nini?” “Umeshindwa kabisa kumuita baba, japo ameshakuomba mara kadhaa, usimuite Paul!” “Mbona namuita baba?” “Kweli Sonia?” “Mara nyingine huwa namuita baba.”
“Naona bado kuna kitu moyoni mwako Sonia. Kama kweli ungekuwa umesamehe kabisa, ungeanza kumpenda na kumthamini. Unashindwa kabisa kumtambua kama baba yako.” Sonia aliinama na kuzidi kulia.
“Kuna nini Sonia?” Sonia aliendelea kulia. “Naomba uniambie ukweli, unamfikiriaje Paul.” “Paul amebadili kabisa maisha yangu. Tokea nazaliwa mpaka sasa.” “Ki vipi?” “Aliniacha na mama, tukiwa tunamuhitaji sana, sasa hivi anarudi kwenye maisha yetu, tukiwa ndio angalau maisha yanaanza kueleweka, tupo pamoja, tumepata nyumba, halafu yeye amemchukua mama, bila kutufikiria mimi na Kana.”
“Paul anajiangalia yeye wakati wote. Yupo kama mama yake. Ni ukoo unaojiangalia wao tu, hawajali watu wengine. Yule mama alikuwa hamtaki mama yangu kwa kuwa aliona mama yangu hamfai mtoto wake. Leo mtoto wake, ameshazunguka huko, vya familia vimemuharibikia huko, ndio anarudi anasema anamuhitaji sana mama yangu. Ni kama watu wanao taka kutumia watu tu, hawana mapenzi ya kweli hata kidogo.” Sonia aliendelea kulia.
“Siwataki hao watu Sam. Acha tu mama awe karibu nao. Lakini mimi na watoto wangu, nataka tukae nao mbali kabisa. Wanafikiri pesa na mali zao, ndio kila kitu. Hapana Sam.” Akaona amshike ili kumtuliza.
“Lakini Sonia, wewe si ndio unataka kuanzisha familia yenye amani na utulivu?” “Ndiyo.” “Umeshajiuliza familia ni nini?” “Si mimi na wewe na watoto wetu!?” Sam alitabasamu. “Usicheke bwana Sam! Mwenzio nimekasirika sana. Paul anazidi kunichanganya akili kabisa.” “Amekuomba usimuite Paul, Sonia.” “Hata nikimuita baba, inabadili nini?”
“Kwanza unatakiwa ujue, hakuna familia ya namna hiyo, unayosema wewe. Ya baba, mama na watoto. Labda kama mwenzangu wewe sio Mwafrika. Hatuchagui familia Sonia, tunachagua marafiki tu. Kila mtu Mungu anamuweka kwenye familia au ukoo anaoutaka yeye Mungu.” “Sasa kwa nini mimi niwekwe kwenye ukoo wa ajabu? Mbona wewe mwenzangu ukoo wenu umetulia haupo kama wetu?”“Umejuaje? Au kwa kuwa sikwambii kila kitu kinachoendelea kwetu?” Sonia alibaki kimya.
“Hatuwezi kuanzisha familia ya namna hiyo Sonia, kama ukishindwa kupokea ndugu zako waliojirudi na wanakutafuta sasa hivi, itakuaje kwa wazazi wangu?” Sonia alishituka sana.
“Usinielewe vibaya Sam, wazazi wako nitawapenda sana tu. Mbona niliishi na wadogo zako vizuri?” “Sijui Sonia! Sijui mpenzi wangu! Kila nikikuangalia na kuwakumbuka wale wazazi wangu, sidhani kama mtawezana hata kidogo.” “Jamani Sam!” Sonia alisikitika sana. Lakini Sam alijua analoongea.
“Nakwambia kweli Sonia. Kama umeshindwa kumpokea Paul, nakuhakikishia wale wazazi wangu watakusumbua sana akili. Nakufahamu Sonia na hivyo ninavyokuona, ungejua hata nusu ya mambo ya wazazi wangu, najua ungeshangaa hata kwa nini bado naendelea kuwatunza wazazi wangu na kuwasomesha ndugu zangu.” Sonia alijisikia vibaya zaidi.
“Naomba usinikatie tamaa Sam!” “Hapana Sonia, sikwambii kwa nia mbaya. Nakwambia hali halisi ilivyo.” Sam alifikiria kidogo.
*********************
“Hivi Sonia, umeshawahi kujiuliza ni kwa nini mimi nimekuwa kama baba wa familia yetu wakati wazazi wangu wote wako hai na ni wazima hawana tatizo lolote? Umeshajiuliza ni kwa nini nilikuwa nikiishi na ndugu zangu hapa wakati wana wazazi wao wote wawili?” Kimya.
“Labda hujaelewa Sonia. Nawatunza wazazi wangu kwa kila kitu, tena pamoja na watoto wao wananitegemea mimi, wakati wao wapo, na hawana tatizo lolote linalowafanya washindwe kubeba majukumu yao. Ushawahi kujiuliza ni kwa nini?” Kama aliyefunguliwa macho hilo swali lilianza kumuumiza kichwa Sonia.
Aligundua kwa muda wote aliokuwa akiishi na Sam akidhani anamfahamu, kumbe kuna mambo mengi hajawahi hata kudadisi kwa upande wa Sam. Alibaki akiwaza wakati Sam akiendelea kuongea.
“Wakati wote unaniambia ulitaka usome sana, au ungekuwa mbali kama baba yako angekuwepo kukusaidia. Mwenzio nipo hapa nilipo, hata kujiendeleza na shule nilishindwa nimeishia na shahada moja tu, sababu sina uwezo. Majukumu niliyonayo ni mazito kweli Sonia, na wazazi wote wawili ninao!”
“Wewe baba yako amerudi, anakutaka kwa hali na mali, anataka kukuonyesha familia inayokuhitaji, unakataa!? Mungu amekupa hiyo nafasi yakutimiza ndoto zako, za kujenga familia yenye amani na utulivu, usiiachie. Itumie vizuri. Tengeneza hiyo familia mpenzi wangu.”
“Hakuna familia eti ya kwangu mimi na wewe tu! Hapana Sonia. Ndugu wote wanao tuzunguka, ni familia yetu. Ndio maana mimi nakazana sana na ndugu zangu, ili kuwakomboa kwenye ukoo wetu.”
“Wewe umepata neema kubwa sana. Kazi yako ni ndogo sana, kusamehe tu na kuwapokea ndugu zako, basi. Mimi nahangaika mchana na usiku, JASHO LANGU ndio njia pekee ya kuwaweka familia yangu pamoja.”
“Wewe umesema wao ni wabinafsi, basi wewe usiwe mbinafsi. Mshukuru Mungu amekupa mimi, Nyange na mkewe na Kana anayekupenda sana siku hizi, na wote tuko na wewe Sonia. Basi kubali na Paul naye awe na mama yako. Usitake Paul awe peke yake, wakati unajua kabisa historia ya Paul, baba yako. Unajua yuko peke yake, hana mtu sasa hivi.”
“Amekwambia mahusiano yake na mama yake yameharibika kabisa, kutokana na kumtenganisha na nyinyi. Hana mke. Wakati wote, tumemsikia akimtambua mama yako kama ndiye mkewe wakutokea zamani, haya ni juzi tu amegundua hata watoto aliokuwa akiwahangaikia pia sio wake. Huoni kuwa baba yako anawahitaji sana?”
“Au huoni kuwa huu ndio wakati wako na wewe wa kutengeneza hiyo familia uliyoitamani Sonia? Hakuna maisha ya kuishi na mama milele, hata Nyange na mama Briana walikwambia, Sonia. Wewe umemuona hata mama Briana, hakuwa akiishi na mama yake. Wazazi wanakuja kusalimia na kuondoka.”
“Najua kwako wewe ni tofauti kwa kuwa umekuwa ukiishi na mama yako wakati wote, lakini Mungu amekupa kitu ulichokuwa ukikitamani. Uwe kama familia za watu wengine. Tumia hiyo nafasi vizuri. Waweke ndugu zako pamoja kwa amani. Samehe Sonia, mpokee Paul kama baba yako, ndipo utakapo weza kumuita mama yake, bibi.”
“Mambo mengine yanatokea hapa duniani hatuna majibu yake. Amri aliyotupa Mungu ni nzito kweli, lakini hatuna budi kuitii, ‘Waheshimu baba na mama yako, ili upate miaka mingi na heri duniani.’ Basi. Hatupo kwenye nafasi ya kuwahukumu hata kidogo. Muachie Mungu Sonia, maisha yaendelee.”
“Sikulaumu hata kidogo ila nataka ufikirie zaidi. Hata mimi mwenyewe kuna kipindi nilitamani sana kuondoka nyumbani moja kwa moja, nisiangalie nyuma ili kutimiza ndoto zangu bila majukumu yeyote ya kifamilia kunifuata nyuma, lakini nilishindwa.”
“Najua sasa hivi pengine ningekuwa nimeshaoa. Pengine ningekuwa labda nina watoto wakubwa tu kama rafiki zangu, au pengine ningekuwa na elimu kubwa zaidi ya hapa, au labda na mimi ningekuwa na Jumba la kifahari, lakini najua lipo kusudi la mimi kuwekwa kwenye familia kama ile.”
“Lakini hii nyumba mbona nzuri tu Sam, inatutosha?” “Unafikiri nafurahia hivi tunakaa kwenye nyumba ambayo haina uzio? Au unafikiri nafurahia kukuona unapikia nje, tena na mkaa kama upo kijijini, wakati umetoka kwa Nyange, ulikokuwa ukipikia gesi wakati wote? Ni kwa kuwa sina uwezo Sonia. Mambo mengi. Nina majukumu kweli mwenzio.”
“Kila nikisema hili litaisha, linakuja jingine. Lakini sikati tamaa, najua ipo siku, tutatulia tu mimi na wewe, mambo yatakuwa mazuri. Lakini katika yote, changamotoninazopitia siachi kuwasaidia na kuwakusanya ndugu zangu kwa kadiri niwezavyo.”
“Watu wote tunakosa mpenzi wangu, hatuwezi kusema wao wamekosa sana na sisi huwa tunakosea kidogo, kwa kuwa sisi hatuna kipimo cha maumivutunayowaachia watu tulio waumiza. Wao ndio wanaweza kutoa ushahidi juu yetu, kama tumewakosea kidogo au sana, kama wewe unavyoona juu ya baba yako na bibi yako, ukute wapo watu na wao wanakuhesabia hivyohivyo makosa.”
“Hunabudi kusamehe Sonia. Itakusaidia sana wewe mwenyewe, na familia yetu pia. Utawaumiza sana wazazi wako kama utaendelea hivyo, zaidi mama yako. Mkubali Paul kama baba yako.” Sonia alizidi kujisikia vibaya. Alijiona vile na yeye alivyo mbinafsi, alibaki akijilaumu.
“Pole Sam. Naomba unisamehe mpenzi wangu kwa…..” Akasita hata kuendelea. Kila alipofikiria mambo aliyomfanyia Paul tokea wanakutana kwa mara ya kwanza mpaka sasa, tena Paul akijitahidi sana kumueleza huku akimuapia hakuwa na nia yakuwatoroka, alijiona vile alivyo mpumbavu na mbinafsi zaidi.
Aliinama na kufunga macho huku akisutwa moyoni. ‘Sikufikiria kama namuumiza na Sam, na kumfanya ashindwe kuniamini na ndugu zake. Kweli sikufikiria.’ Sonia aliendelea kuwaza.
“Nakuahidi kubadilika Sam. Nitajirekebisha. Nilibeba CHUKI moyoni kwa muda mrefu sana, halafu nikaruhusu chuki ndio initawale fikra zangu. Naomba unisamehe na usinielewe vibaya.” Sonia alibaki akifuta machozi. Sam aliweka mikono yake tena kwenye mabega ya Sonia kama kawaida yake.
Ukiona Kwako Kunaungua, Kwa Mwenzio Kunateketea
“Samahani Sonia najua nimekuwa mkali kidogo. Kuna mambo yanaendelea kichwani mwangu, nahisi ndiyo yananichanganya. Lakini sina jinsi nyingine ya kukueleza ukweli juu ya maisha jinsi yalivyo isipokuwa kuwa mkweli kwako.” “Hapana Sam, upo sahihi. Nilihitaji kusikia hayo.” Wote wakatulia kwa muda.
“Sam! Naomba nikuulize.” “Uliza tu?” “Nini kinakusumbua mpenzi wangu? Namaanisha hicho ulichosema kinakuchanganya. Halafu umenifanya nifikirie na kujiuliza, juu ya familia yako. Natamani na mimi nifahamu upande wa familia yako. Kwa nini wewe ndio umekuwa kama baba kwa wadogo zako?” Sam alibaki kimya akifikiria.
“Eti Sam?” “Nafikiria, sijui nikwambie kipi na kuacha kipi.” “Natamani uniambie kila kitu. Usinifiche.” “Usije nikimbia lakini!” “Nikukimbie sababu ya wazazi wako? Au kitu gani kingine kinaendelea?” “Haohao wazazi wangu.” “Hapana bwana! Nakupenda Sam, hakuna kitu cha kututenganisha. Niambie tu ili nijue ni nini kinakusumbua.”
*********************
1Yohana4:2 IMEANDIKWA, “Mtu akisema, Nampenda Mungu, naye anamchukia ndugu yake, ni MwONGO. Kwa maana asiyempenda ndugu yake ambaye amemwona, hawezi kumpenda Mungu ambaye hakumwona.”
*********************
Sam alifikiria tena kidogo, nakuamua kuwa tu muwazi. “Umeshawahi kuona watu wanaoelewana katika mambo yao, hata kama jamii nzima haiwaelewi?” Sonia alibaki akiwaza. “Basi kama hujawahi ona, utakuja kukutana na wazazi wangu, kama Mungu akitupa uhai.” “Hongera Sam.” Sam alicheka kidogo. “Sijawahi ona watu wanaoelewana katika maamuzi yao kama wazazi wangu, Sonia.”
“Samahani kusema hivi, ni kama kipofu amuongozaye kipofu mwenzake na wote wanatumbukia shimoni, lakini hata watu wenye kuona wanapo jaribu kuwasaidia na kuwaambia, mnaelekea shimoni, hiyo siyo njia sahihi, ni kama tena hawana masikio.” “Unanichanganya Sam.” Sam alijua tu Sonia hatamuelewa mwanzoni.
“Si unajua kuna zile familia, wazazi wanahangaika kutafuta pesa ili watoto wao waishi vizuri, au tuseme wasome?” “Si ndivyo wazazi wote wanavyofanya?” “Sio wazazi wangu Sonia. Wao wanachojua ni pombe tu. Nikikwambia kwetu ni mafukara sio kwa sababu wazazi wangu wamejaribu kuhangaika kutafuta pesa wakashindwa, hapana.”
“Ni kwa kuwa wameamua kutofanya kazi. Na wakifanya kazi, wakilipwa hata kidogo tu, hiyo inakuwa ni pesa yao wao wawili tu. Siku hiyo wakiwa na hela watashinda kilabuni. Watakula na kunywa hukohuko, wao wawili tu, wakirudi wamelewa, hawajali mtoto yeyote yule au hata kurudi na unga wa ugali mkononi kwa ajili ya watoto wao, hapana, hawafanyi hivyo. Sisi tumekuwa watoto wa kila mtu pale kijijini kwetu.” Sonia alibaki ametoa macho.
“Unamuona huyu mdogo wetu wa kike wa mwisho, Ruth? Tumemlea tangia anatolewa hospitalini mpaka leo hii, au tuseme nimewalea hao watoto tokea wadogo. Mama alikuwa akiwaacha tokea wachanga, hamna matunzo yeyote.”
“Wakati nasoma pale kijijini nikiwa shule ya msingi, ilikuwa ikinibidi kuamka asubuhi sana, ili niwapikie uji hawa wadogo zangu wawili wakiume wanao nifuata, ndipo niende shule, na nikirudi niwapikie tena, kama nitakuwa na hela, maana siku za jumamosi na jumapili ndizo siku nilikuwa nikizitumia kutafuta vibarua kwenye mashamba ya watu. Nikibahatika kupata kazi na nikilipwa, naficha hiyo hela kwa ajili ya chakula cha wadogo zangu, maana baba au mama walikuwa wakiniona na pesa, wanazichukua na kwenda kuzinywea pombe.”
“Bahati nzuri pale jirani kulikuwa na bibi, alishafariki lakini, yeye ndiye alitusaidia sana. Nilikuwa nikimuachia hawa wadogo zangu wa kiume wawili, wakati naenda shule, au nikipata kazi kubwa ambayo najua nitakaa huko siku nzima, nilikuwa namwomba huyo bibi akae na Daudi wakati huo yeye ndio alikuwa mdogo sana, halafu naenda na huyu mdogo wangu wa kiume anayenifuata, Jose.”
“Tutashinda huko tukifanya kazi kwenye mashamba ya watu mpaka jioni, ndio tunarudi nyumbani. Hapo tunakuwa hatujala kitu chochote zaidi ya uji wa asubuhi. Haya, hapo inabidi kurudi nyumbani huku mnakimbia kuwahi kumchukua Daudi kabla giza halijaingia ili naye yule bibi apumzike.”
“Ukimchukua mtoto, anakuwa hatizamiki kwa uchaafu. Vumbi jekundu mpaka kwenye kope. Inabidi hapo kuwabeba wote mpaka tena mtoni kuwaogesha. Angalau Jose aliwahi kujitegemea japo na yeye alikuwa mdogo sana lakini kazi ya ulezi ilikuwa kubwa kwa Daudi. Ukitoka tena hapo mtoni unarudi kupika ili watoto wale halafu walale. Hapo hujui hata mama na baba watarudi nyumbani saa ngapi. Sikuwahi kupata muda wakujisomea hata mara moja. Kama sikuelewa darasani ndio basi tena.” Sonia alikuwa akilia.
“Kwa nini sasa wazazi wako walichagua maisha kama hayo?” “Sijui Sonia! Lakini yule bibi alikuwa akiniambia wakati waliponizaa mimi haikuwa mbaya kwa kiasi hicho. Alisema angalau mimi walikuwa wakinibeba, naenda nao mpaka kilabuni. Lakini anasema ndio nitashinda nao huko bila chakula wala matunzo yeyote. Anasema walizidisha pombe mara baada ya kumzaa huyu mdogo wangu anayenifuata, Jose.”
“Sasa nilichanganyikiwa alipozaliwa huyu mdogo wetu wakike, Ruth. Maana mimi nilijua Daudi ndio angekuwa mtoto wao wa mwisho. Wakati huo Daudi alikuwa darasa la tano, mimi nilikuwa nimefaulu nikachaguliwa shule ya bweni ya Ilboru sekondari, nilikuwa kidato cha tatu nakaribia cha nne, Jose huyu anayenifuata, na yeye alichaguliwa kwenda kidato cha kwanza katika shule ya bweni ya Mzumbe sekondari na yeye ndio alikuwa ameanza kidato cha kwanza.”
“Mbaya zaidi yule bibi aliyekuwa akinisaidia kukaa nao wakati wadogo ndio na yeye alikuwa ameanza kuumwa, hawezi kumsaidia tena Daudi na mtoto mchanga ambaye ndio alikuwa Ruth. Ikitokea Daudi anamuacha anakwenda shule, akidhani labda mama atakaa naye mpaka arudi, Daudi atamkuta mtoto anakaukia kitandani kwa kulia, mama na baba hawapo.”
“Mimi ndio nilikuwa siwezi kurudi kukaa na Ruth kwa kuwa ndiye mtu pekee waliyekuwa wakinitegemea kwa kila kitu. Shule zikifungwa nilikuwa naenda kukaa kwa kina G, yule rafiki yangu wa Mwanza, nafundisha wanafunzi ‘tuition’ ili nipate pesa. Nikipata pesa nawahi kurudi nyumbani kabla shule hazijafungua, ili nimpe Jose, ada ya kwenda kulipa shuleni kwao na matumizi kidogo ili asichelewe au asifukuzweshule, halafu nyingine ndio nampa na Daudi za matumizi yake ya shule na pale nyumbani.”
“Sasa alipozaliwa Ruth, mambo yakazidi kuwa magumu. Swali la nani anabaki nyumbani kumlea Ruth ndilo lilikuwa likitutesa sana. Ikabidi tumuombe Daudi yeye ndiye aache shule, abaki nyumbani amlee kwa muda, angalau miaka miwili hata akimuacha kwa majirani anacheza wakati yeye yupo shule, ni afadhali. Uzuri, huwa tunaelewana sana na wadogo zangu, Daudi akakubali.”
“Lakini Sonia, ungemuonea huruma Daudi siku ile nimerudi nyumbani na kumuomba aache shule, abaki nyumbani amlee Ruth. Alikubali bila shida, lakini alilia siku nzima bila ya kula. Alilia sana, lakini ilikuwa hamna jinsi, Ruth alikuwa ndio kamezaliwa na hana matunzo yeyote, tungemuacha vile, angekufa yule mtoto.”
“Na Jose ambaye alitamani sana kumlea Ruth, asingeweza kuacha shule halafu abaki nyumbani, sababu ndio na yeye alikuwa amechaguliwa kidato cha kwanza, angeacha kwenda shule ndio ingekuwa basi tena. Wangemfukuza. Na mimi ndio kabisaa. Ningebaki pale nyumbani kumlea Ruth, hakuna hata mmoja wetu angesoma, maana wote walikuwa wakitegemea pesa kutoka kwangu. Basi ikabidi Daudi ndiye aache shule na kubaki nyumbani na mtoto.” “Pole sana Sam. Pole mpenzi wangu.” Sam alitabasamu huku akifikiria.
“Kuna kipindi mama aliugua sana, sikuwa na hela, nilikuwa ndio nimetoka kuwalipia ada wadogo zangu wote na mama naye ndio alikuwa mgonjwa karibu ya kufa. Nilichanganyikiwa Sonia, nilikuwa sijui nifanye nini, na ndio kipindi kile Leah alikuwa amehamia pale kwenye kile chumba changu. Nilipomwambia Leah, akanisaidia pesa za kumpeleka hospitalini, lakini nilikuja kujuta na huo msaada wa Leah. Alinisimanga nao jamani, kila mtu alijua. Na kila wakati alikuwa akinikumbushia.”
“Lakini alisaidia, maana mama alitibiwa, akashauriwa aache pombe kwa kuwa alikutwa na tatizo kwenye figo. Nikashukuru Mungu nikajua atakuwa ameelewa, lakini ni kama hakusikia alichokuwa ameambiwa na madaktari. Alirudia pombe kama zamani. Nikikwambia ni walevi, uelewe ni walevi kwelikweli.”
“Kijijini kwetu pale, ni watu wakudharaulika sana. Nakwambia sisi tumekulia katika nyumba ya MATOPE Sonia, huku tukizungukwa na nyumba za kawaida. Sio nyumba za kisasa, lakini ujue ni zile nyumba zakawaida zenye nafuu, za kijijini. Lakini kwetu ndio palikuwa hovyo. Nyumba ya matope na ilikuwa imeezekwa na nyasi.” “Pole Sam.” “Asante.” Sonia alihisi anasikiliza hadithi sio kweli. ‘Mzazi gani anaweza kufanya hivyo jamani!? Ukatili na ubinafsi wa kiasi gani huo?’ Sonia aliendelea kuwaza huku akifuta machozi.
“Ninacho mshukuru Mungu, alitujalia sisi sote akili za darasani. Hata wadogo zangu wote, wanaakili sana, hakuna anayemsukuma mwenzake kusoma. Hakuna kati yetu aliyewahi kushika nafasi ya pili darasani. Wakati wote tumekuwa tukiongoza na ukiangalia alama zao, sio kuongoza kwa alama za chini, alama za juu sana.”
“Jose alipata bahati kama yangu. Na yeye alipomaliza tu pale chuo kikuu siku ya mahafali, kwa kuwa alikuwa amefaulu sana, palepale alipata makampuni kama matatu yaliyokuwa yanamtaka aanze kazi kwao. Nashukuru Mungu sasa hivi ana kazi nzuri sana na mwenzangu alijitahidi, kufanya kazi na kusoma madarasa ya jioni, amemaliza shahada yake ya pili.” Sam alitulia kidogo.
“Sasa turudi katika kitu kinachonichanganya.” Sam alicheka na kumgeukia Sonia kumuangalia hali yake. “Kama unalia sikwambii.” Sonia alitabasamu na machozi mengi usoni. “Pole Sam. Kumbe na wewe umepitia pagumu kuliko hata mimi.” Sam alicheka. “Hapana bwana. Kila mmoja wetu alipita kwenye mapito yake, na kuumizwa na maisha. Pole na wewe Sonia.”
“Asante. Lakini ningependa kujua kinacho kuchanganya sasa hivi. Kama bado mzigo mzito, nashauri uongee na Mr. Mwansasu anirudishe kazini. Najua na mimi nikirudi kazini itatuongezea kipato, Sam.” “Sio hicho kinacho nichanganya, Sonia. Wewe hujawa mzigo kwangu. Na angalau sasa hivi Jose ananisaidia mambo ya Daudi na Ruth, majukumu sio kama zamani.” “Sasa tatizo ni nini?” Sam alifikiria tena.
“Jose alipopata kazi, tukaamua kujenga kwetu, angalau wazazi wetu wakae pazuri na Ruth na Daudi wakiwa wanarudi nyumbani kutoka mashuleni kwao, wawe na pakuishi. Nilianza mimi kujenga, Jose akaniongezea pesa kidogo, tukamalizia hiyo nyuma. Haikuwa hata ya kisasa, lakini ya matofali na bati. Nikawawekea umeme, maji hayasumbui ni yakuchota mtoni tu, na sio mbali na nyumbani kwetu.”
“Wakakaa hapo kama miaka miwili. Mwaka jana Daudi anatoka chuoni anarudi nyumbani, anakuta nyumba ilishauzwa.” Sonia alishituka sana. “Sam wewe? Na nani?” “Si baba na mama? Daudi alikasirika nusu ya kumpiga baba.” “Sasa wanaishi wapi?”
“Uzuri hawakuuza eneo zima. Kuna shule ya sekondari imejengwa pale kijijini kwetu, sasa wamemuuzia huyo Mwalimu Mkuu hiyo nyumba na eneo kidogo linalozunguka hiyo nyumba, halafu wao wakajenga nyumba nyingine tena yamatope, ndogo kama chumba kimoja na jiko la nje. Wakajitengenezea choo chao cha shimo, wanaishi hapo bila shida.”
“Sasa Daudi alinihurumia, hakutaka kuniambia kwa haraka ili yeye ahangaike akusanye pesa, amlipe yule waliyemuuzia ile nyumba, akomboe hiyo nyumba. Huwezi amini Sonia, kipindi hicho cha likizo, wale watoto walikuwa wakiishi hapo kwenye hicho chumba kimoja na wazazi wao.” “Jamani!” Sonia alishindwa kuamini na kuelewa.
“Sasa ikawa kama Mungu tu, tena wakati huo ndio nilikuwa nimehamia tu hapa, hata mwaka sijamaliza. Nikajua wao wapo likizo nyumbani, siku hiyo nikatoka zangu kazini nikasema ngoja niendeshe taratibu mpaka nyumbani, nikawaone kabla hawajarudi mashuleni kwao.”
“Nimefika usiku kweli, naenda kugonga kwenye ile nyumba, anatoka mtu nisiyemfahamu. Namuuliza wewe nani? Na yeye ananiuliza wewe nani unayegonga nyumbani kwangu usiku usiku! Nikajitambulisha, si ndio akanieleza kila kitu na kunionyesha kibanda walichojenga baba na mama! Nililia Sonia, kama mtoto wa kike.”
“Nilimkuta Ruth amelala chini, nikikwambia chini ni chini kwenye mkekaaliokuwa amenunua Daudi, na mbu wanawang’ata. Kila kitu waliuza. Kama kawaida yao, sikuwakuta wote wawili, baba na mama. Sikutaka hata kuwafuta huko kilabuni, kuongea nao. Niliwachukua wadogo zangu usiku uleule na kurudi nao hapa.” Sonia alibaki anafuta machozi.
“Ni ngumu Sonia, we acha tu. We unafikiri kwa nini nashindwa kukupeleka nyumbani mpaka leo? Sijui nakupeleka wapi, sijui kama siku tutakayoenda kama tutawakuta hapo nyumbani kwao, au la. Sijui kama watakuwa wamelewa au vipi?”
“Sasa mama yako anasemaje?” “Cha ajabu, katika ulevi wao wote, sijawahi kuwaona hata siku moja wakipishana maneno. Kutwa wameongozana wao wawili. Mchana na usiku ni wao tu. Huwezi kumsema baba kwa mama, wala mama kwa baba. Hakuna alipokuwepo baba, mama asiwepo. Hata wakifanya vibarua kwa watu ili kupata pesa ya pombe, wanakuwa wao wawili, hawaachani popote.”
“Ungemuonea huruma baba wakati mama amelazwa hospitalini. Kuanzia asubuhi mpaka usiku yupo naye. Akifukuzwa ndani wodini, anakwenda kusubiria nje ya wodi aliyolazwa mama, usiku kucha, mpaka mama aliporuhusiwa kurudi nyumbani.” “Pole Sam.”
“Asante, lakini ndio hivyo Sonia. Na ndio maana naichukia pombe kupita kiasi, hata harufu yake sitaki kuisikia. Inanikumbusha makuzi yangu.” “Sasa tutafanyaje?” “Kuhusu nini?” “Bado utanipeleka kunitambulisha?” Sam alicheka sana.
“Bado unataka kwenda kuwaona?!” “Ni wazazi wako Sam! Ningependa na mimi kuwafahamu. Lakini pia nakusikiliza wewe. Vyovyote utakavyo amua, mimi nipo tayari.” “Nimechanganyikiwa Sonia, na hivi ameongezeka na baba yako, tena anataka twende wote huko kwetu! Sijui nafanyaje? Nyange ndio amechanganyikiwakabisaa.”
“Kwani Nyange na yeye anajua historia ya nyumbani kwenu?” “Unajua Nyange ni kama kaka yangu kabisa? Tumetoka naye mbali, anajua kila kitu kuhusu mimi na familia yangu. Sasa swala la kuongezeka ‘Judge Mkuu’ kwenye picha, ndio kitu kinatuumiza kichwa Sonia. Afadhali ingekuwa ni wewe na mama yako tu, lakini na baba yako!? Halafu sasa hivi tena anataka kuongezeka na bibi yako!”
“Kwani huyo bibi ana nini?” “Kumbe wewe humfahamu huyo mama!” “Hapana.” “Alikuwa ni miongoni mwa wanawake waliokuwa wamevuma sana kipindi cha nyuma. Ni kati ya wanawake wa somi sana wazamani, alikuwa kwenye ngazi ya juu sana katika usalama wa hii nchi. Ni mama anayejielewa, sio mama wakawaida tu. Hata hilo jina la Tambo linajulikana sana hapa nchini. Mumewe, yaani baba yake Paul, au babu yako, alishakuwa Waziri kipindi cha Nyerere. Na alistaafu na jina zuri sana.” Sonia alibaki kimya kwa muda akifikiria.
“Lakini acha kufikiria hayo yote Sam bwana! Kwani unaoa ukoo mzima au mimi tu?” “Hata kama Sonia, nawapeleka wapi? Nakwambia nyumba waliiuza. Na sasa hivi tumekubaliana, kila atakayepata pesa ampe Ruth ili ajiandae na mambo yake ya Chuo. Anatamani sana kwenda kusomea mambo ya udaktari nje ya nchi. Na kwa kuwa anaakili sana, tumeamua kumsaidia atimize ndoto zake. Hakuna anayefikiria kujenga tena kule kijijini kwa sasa.”
“Nina wazo Sam.” “Wazo gani?” “Kwa nini tusiwalete wazazi wako hapa?” Sam alishituka sana. Kana kwamba ametajiwa kifo. “HAPANA.” Akasimama kabisa. “Nisikilize kwanza Sam.” “Hapana Sonia, wale watu niwalevi, hawawezi kuishi bila kunywa pombe, na mimi siwezi kuruhusu pombe ndani ya hii nyumba hata kidogo.”
“Hata ukisema waende kunywa baa ndio waje hapa kulala tu, pia HAPANA. Halafu na ulevi ule waje kuishi hapa, baba yako awe anakuja kila siku awakute humu ndani tena wamelewa, na wewe ndio umejifungua, unafikiri atanielewaje? Hapana Sonia.” “Ngoja kwanza Sam mpenzi wangu. Kaa kwanza chini.” Sam akarudi kukaa, lakini wazi alionyesha kutotaka Sonia kumuingilia katika maamuzi yake.
“Wewe umetoka kuniambia nini juu ya swala la familia? Mbona sasa wewe mwenyewe unawakimbia wazazi wako, eti sababu ya baba yangu!?” Hapo akatulia. “Naomba tukawachukue kijijini, tuje nao hapa. Watakutana na Paul na kila mtu atakayetaka kuonana nao hapa nyumbani kwetu, huku ukitafuta ushauri wa madaktari kujua jinsi ya kuwatoa kwenye hiyo hali ya ulevi ‘addiction’.”
“Huwezi kuwaacha wakafa kijijini. Lazima kuwasaidia na wao. Kazi yako haikuwa ni wadogo zako tu Sam, acha kukimbia majukumu yako.” Sonia alicheka na kumpiga Sam mgongoni. “Yaani nakuelewa kabisa unachosema Sonia. Lakini…” Sam alisita kabisa.
“Nini sasa?” “Hebu naomba tupate muda wa kufikiria hili jambo kwa makini kwanza. Sitaki wao wakawa ndio mwanzo wa matatizo kati yetu. Sijawahi kutulia hivi maishani. Angalau sasa hivi nakuwa nipo kazini najiambia narudi nyumbani kwa mke wangu. Nakuta nyumba imetulia na kuna amani. Sitaki kupoteza hiyo kitu kabisa, kwa sababu yao Sonia.”
“Najua wakija kuishi hapa mambo mengi yatabadilika, amani na utulivu unaoupata sasa hivi wakati unaishi na mama Briana sio kama utakayoipata pindi wazazi wangu watakapo hamia hapa. Naomba tufikirie kwanza Sonia. Ila nashukuru sana kwa moyo wako wakutaka kusaidia.” Sam alianza kumbusu Sonia.
“Acha bwana Sam, sijamaliza kupika.” “Si kidogo tu.” “Hapana bwana! Twende tukamalizie kupika kwanza. Watoto watarudi kutoka shule, wakiwa wana njaa, halafu wasikute chakula humu ndani. Kwanza moto utakuwa umeshazima!” “Sonia naye wakati mwingine! Kwani si kidogo tu?” “Hapana Sam, mimi nakujua vizuri sana. Hatutakaa tukatoka humu ndani. Twende ukanisaidie kupika ili tumalize mapema, ndio tuongee mambo mengine.” “Sawa bwana kama ‘unanibania’.” Sonia alianza kucheka.
“Basi naomba utangulie, nakuja sasa hivi nataka kuongea na baba.” Sam alicheka. “Kweli somo limekuingia. Mpaka unamuita na baba!” Sonia alicheka na yeye. “Nenda bwana, nisaidie kuongeza mkaa jikoni halafu upepee ili moto ushike haraka, mimi nakuja sasa hivi.” Sam alibadili nguo za kazini na kutoka.
Mwenye Kutenda Kosa Na Kujirudi, Ndiye Mwenye Hekima
Alichukua simu yake na kumpigia mama yake. Ishimwe na Paul bado walikuwa kitandani wakibembelezana. “Nani huyo?” Paul akauliza. “Sonia. Sijui ana nini?” “Hebu ongea naye. Kama anamatatizo twende sasa hivi.” Akapokea simu. “Vipi? Kwema?” “Kwema mama. Nimekusumbua?” “Hakuna usumbufu wowote mwanangu. Wakati wowote na muda wowote tunaweza kuongea.” “Asante mama. Naweza kuongea na baba?” Ishimwe alishituka sana baada yakumsikia Sonia akimwita Paul, baba! Kwani hata yeye alishamgundua inamsumbua sana kumwita Paul, baba.
“Kwema?” Alirudia tena. “Jamani mama! Kwani mtu haruhusiwi kuongea na baba yake?” Ishimwe alicheka. Paul aliyekuwa akiwasikiliza mazungumzo yao muda wote, alimpokonya simu Ishimwe. “Hata mimi nashangaa Sonia, kwani lazima uwe na sababu ya kunipigia?” Paul aliongeza na kumfanya Sonia acheke.
“Si unajua hata mimi nina simu?” “Sina namba yako baba, ningekupigia moja kwa moja.” Kitendo cha kuitwa baba na Sonia, kilifungua moyo wa Paul, na kumfanya ajisikie vizuri sana. “Nitakupa mwangu ili wakati wowote na muda wowote uwe unanipigia mimi mwenyewe moja kwa moja, sio kupitia kwa watu wenginewanaokuhoji maswali mengi, halafu ndio wanipe simu. Huhitaji kuwa na sababu yakunipigia Sonia.” “Paul wewe jamani!?” Ishimwe alilalamika na kuwafanya Sonia na baba yake wacheke, kisha Sonia akaendelea.
“Nitafurahi kupata namba yako. Lakini nili…” Akasita. Alishindwa kuendelea, hakujua aanzie wapi kujieleza kwa baba yake, hasa baada ya kumfukuza, muda mfupi uliopita. Na Paul alishajua kama Sonia anashindwa kuongea alichotaka kumwambia. Akaamua kuvunja ukimya. “Ushaivisha, nije kula? Au chakula ni cha Sam tu? Maana huku kwetu naona hapaliwi leo.” “Paul wewe jamani! Naenda kupika sasa hivi bwana, kwanza wewe mwenyewe ndio ulikuwa una….” Paul akamziba mdomo Ishimwe, kisha wote wakacheka.
“Nitafurahi mkija tule wote, nimepika chakula kingi, kitatutosha wote.” “Basi tunakuja sasa hivi.” “Asante baba.” Walikata simu. Paul alikuwa na furaha yakupita kiasi. “Muone alivyofurahi.” “Twende bwana Ishimwe, acha kunichelewesha.”
*********************
Sonia naye alitoka kwa haraka kurudi jikoni, alikuta Sam hajafanya chochote alichomuagiza, moto ulikuwa umezimika kabisa wala Sam hakuwa na habari, alikuwa akiongea na simu palepale jikoni. Sonia alimfinya mgongoni. “Awuuu! Nimefanyaje?” Sam aliruka. “Nilikwambia uwashe moto.” Sonia alinong’ona na yeye kama Sam ili aliyekuwa upande wa pili wa simu asisikie.
“Nawasha bwana! Ngoja nimalizane na huyu meneja wa tawi la Mbezi.” “Utanichelewesha bure. Naomba nipishe.” “Naweka bwana Sonia, nini?” “Nimewakaribisha mama na baba wanakuja kula chakula cha jioni.” Haraka sana Sam alikata simu.
“Wewe Sonia ukoje bwana?! Mbona hujaniambia?” “Si ndio nimekwambia?” “Sonia bwana! Wewe unamkaribisha Judge Mkuu kula chakula hapa bila maandalizi yeyote? Unataka kunitia tu aibu!” “Na wewe alishakwambia akiwa nyumbani usimwite hivyo, muite baba.” “Unazidi kunichanganya Sonia!” “Na hivyo unavyo changanyikiwa sasa hivi, haisaidii Sam. Tunazidi kuchelewa, hivi wapo njiani wanakuja.”
“Nikusaidie nini sasa? Halafu tutawapa chakula gani? Sio zile habari za ‘wali nyama’. Mwenzio yule kaishi nchi za nje, na kakulia nyumbani kwa Waziri. Hajui chakula cha mboga moja.” “Bwana Sam acha kuchanganyikiwa, atakula kilichopo, we nenda kalete soda, wakati mimi namalizia kupika mboga.”
“Ujue ushaniingiza matatizoni, Sonia wewe! Sikupanga kabisa mwanzo wangu na baba yako uwe hivi! Nilitaka tuanze vizuri, na kwa heshima. Sio kwa kushitukizana hivi!” “Bwana we nenda Sam, acha kuniingizia hofu kama wewe. Nitashindwa kupika bure, ni baki nimepaniki kama wewe.” “Daah! Ndio uongeze mboga ziwe nyingi.” Sonia alianza kucheka.
“Ujanja wote umekuisha.” “Wewe unafanya mchezo na Judge?” “Ni BABA.” “Haisaidii kabisa. Baba yako wewe, mkwe wangu mimi!” “Ujue nitaacha kupika Sam wewe, tubaki tumepaniki wote halafu waje hapa, wasikute chakula!” “Nakwenda bwana! Umesema nikalete soda gani?” “Wewe kalete zozote.” “Zozote?! We Sonia vipi bwana?” “Basi ngoja nikupe namba yake ya simu ili umpigie yeye mwenyewe, umuulize anakunywa soda gani?” “Mimi naona nikalete tu soda.” Sonia alizidi kumcheka. Sam akatoka na kumuacha Sonia anaweka mkaa kwenye jiko.
*********************
Wakati anapika nje, alisikia mlango wa jikoni unafunguliwa. “Ziweke kwenye friji kabisa, zisipoe.” Sonia aliongea huku akiendelea kupika. “Nataka na mimi kusaidia kupika.” Sonia alishitukia baba yake na mama yake wapo jikoni. Alifurahi sana, akasimama kuwasalimia.
“Huyu baba yako hajui kupika hata chai ya rangi, ukimpa jiko huyo, leo tutalala na njaa.” Wote walicheka. “Nimefurahi mmekuja. Ningewapa mkono lakini ni mibichi, ina maji.” “Basi nikumbatie.” Paul akasogea kwa moyo mweupe, usingedhania ni yeye aliyefukuzwa muda mfupi uliopita hapo. Sonia alicheka na kumsogelea baba yake, akamkumbatia. “Ewaaah! Hapo safi.”
“Nilijua ni Sam amerudi kutoka dukani, kumbe ni nyinyi!” “Sam amesharudi kutoka kazini?” Ishimwe akamuuliza. “Amewahi kidogo leo, nimemtuma akawaletee soda.” Ishimwe alijua wazi, Sam ndiye amebadili mawazo ya Sonia na kumfanya ampigie tena baba yake simu. Akamcheka moyoni. “Baba yako huwa hanywi soda.” “Kwa nini?!” Sonia aliuliza kwa mshangao.
“Wanachanganya vitu vingi sana humo ndani, sipendi. Ila napenda juisi anazotengeneza mama yako.” “Hatuna juisi!” Sonia alijibu kinyonge kidogo. “Lakini naweza kuwatengenezea haraka haraka. Ngoja Sam arudi nimtume matunda.” “Atakunywa maji huyo. Anapenda maji kama nini sijui!” “Wala usihangaike. Mimi maji yananitosha.” Paul aliongeza. “Kweli baba? Tunaweza kukutengenezea juisi. Haitachukua muda mrefu.” Sonia alionekana na wasiwasi kidogo.
“Wewe usiwaze juu ya kula yangu au vinywaji, hiyo ni kazi ya mama yako. Mimi nafurahia tu kuwepo hapa. Niambie nikusaidie nini?” “Utachafuka na masinzi baba, nyinyi nisubirini sebuleni.” “Nataka kukaa hapahapa nje na wewe, mpaka umalize kupika.” “Kweli!?” Sonia alimuuliza baba yake akiwa haamini. Paul alikaa kwenye ngazi za hapo nje, jikoni kisha akamgeukia Sonia.
“Mama yako hajaongopa, sijui kupika hata kidogo. Lakini alishanifundisha, kukatakata kitunguu, karoti, nyanya, hoho. Na nimpenzi kweli wa kitunguu swaumu, kwa hiyo hata hicho pia naweza kukusaidia kumenya na kutwanga.” Wote walicheka.
“Asante lakini nilishaandaa kila kitu, namalizia tu kupika mboga.” “Basi mimi nikusaidie kuosha vyombo.” Ishimwe alitoa beseni la vyombo vichafu akaanza kuosha nje karibu na bomba huku wanataniana na Paul. Vicheko vilijaa pale nje, wakati Sonia akiendelea kupika, Paul ndiye alikuwa mpiga stori mkubwa, huku akiigiza sauti ya kila mtu.
Baada ya muda Sam aliingia na mfuko wa soda, alipomuona Paul jikoni kwake, tena amekaa chini kabisa kwenye ngazi, huku akimwangalia mwanae akipika kama yupo kijijini na mkewe akiosha vyombo kwenye beseni, tena nje! Alipaniki. Bado hawakuwa wamevuta maji ndani ya nyumba. Maji yalikuwa yakitoka kwenye bomba moja tu, tena hilo la nje. Wakati anababaika pale mbele yao, walishangaa kuona chupa za soda zikianguka zote kutoka kwenye tundu la mfuko aliokuwa ameubeba Sam, na kuangukia kwenye kona ya karo alilokuwa akiosha vyombo Ishimwe. Ishimwe alijua, akaanza kucheka.
“Daaah! Na hii kiu niliyonayo, ukiambiwa sipati kitu!” Paul alimchokoza Sam. “Samahani sana. Unajua wakati nipo njiani narudi, mfuko ulitoboka, sasa nikawa nimeushikilia juu na chini kwenye hilo tundu. Sijui nimejisahau vipi bwana! Nimeachia tundu la chini, chupa zote zimevunjika! Ngoja nirudi tena dukani, nikakuchukulie soda zingine.”
“Wala usihangaike Sam, anakuchokoza huyo! Huwa hanywi soda. Wewe mpe maji tu.” Ishimwe aliongeza. “Hujaumia Sam?” Sonia alisimama na kumsogelea. “Hapana. Mfuko ndio ulikuwa umetoboka.” Sam aliendelea kujitetea, lakini wote walijua ameshituka kumuona Paul jikoni kwake. Sam aliendelea kubabaika pale mbele ya Paul, asijue afanye nini tena. ‘Daah! Huyu jamaa atajua sina uwezo wa kuishi na mwanae. Na hivi mtoto mwenyewe ni huyuhuyu mmoja tu! Ataniona sifai.’ Sam aliendelea kuwaza.
“Pole Sam, ungemuomba Mangi akuwekee kwenye mifuko miwili.” “Nilikuwa nimeishiwa hela yakuongezea mfuko wa pili.” Sam aliropoka na kujilaumu hapohapo. ‘Daah! Najidhalilisha zaidi. Naona ninyamaze tu, nazidi kuharibu. Hata mfuko wa plastiki umenishinda!’ Sam aliwaza tena.
“Si unajua sitembei na pesa?” Sam alijaribu ‘kuua So’. Akajitetea tena mbele ya mkwewe akishindwa kunyamaza. “Tatizo sio kwamba sina pesa kabisaa, ni kwamba sikuwa nazo pale dukani.” Wote walibaki wakimwangalia. Aliona ndio anazidi kuharibu akaamua kukubaliana na wazo lake la mwanzoni la kunyamaza. Akanyamaza huku bado ameshikilia mfuko wake mtupu wenye tundu kubwa chini na mkono mwingine anakuna kichwa.
Sonia alibaki akimwangalia akitamani kucheka. “Pole Sam.” Sonia alirudia tena. “Asante.” Sam alirudi kuwa mnyonge kama mtoto wa kike wa darasa la pili. Aliona ni kama amewekwa katikati ya uwanja wa mpira, uliojaa mamilioni ya watu wakimshuhudia alivyoshindwa kufunga goli kirahisi wakati mchezaji alikuwa yeye peke yake uwanja mzima.
Alibaki amesimama mbele ya Sonia akimwangali kwa huruma kama anayeomba aokolewe katika ile hali. “Pole Sam.” Sonia alirudia tena, asijue kingine chakusema. “Sonia unaunguza huku, mwanangu. Naona humalizi kutoa pole huko!” Paul aliamua kuingilia. “Wewe huwezi hata kukoroga Paul jamani!” “Unanitafutia matatizo tu Ishimwe! Nikimwaga je?” “Bwana we koroga tui lisimwagike.” Sonia alicheka na kurudi alipokuwa akipika, karibu ya alipokuwa amekaa baba yake.
“Usihangaike baba. Nitamalizia tu kupika.” “Afadhali mwanangu, maana wengine na moto, vitu viwili tofauti! Au wewe mwenzangu Sam unajua kupika?” Sam alijisogeza karibu huku akichekacheka. “Huwa najitahidi.” Sam alijibu. “Basi itabidi nitafute siku na mahali ambapo tutakuwa wawili tu, sio na watu wengi kama kina Ishimwe, halafu unifundishe kupika. Tutaanza na somo la jinsi yakupika chai ya rangi kwanza.” Angalau wote walianza kucheka.
Viliendelea vicheko pale jikoni mpaka Sonia alipomaliza kupika kila kitu na mama yake alishaandaa meza tayari, kwa hiyo walibaki wakiongea tu palepale jikoni.
*********************
“Baba!” Sonia aliita kwa heshima mpaka Paul akaisikia rohoni. Wote wakamwangalia. “Mimi na Sam tupo tayari kwenda kumuona bibi.” Paul alitulia kwa muda. “Unauhakika Sonia? Maana hakuna haraka. Wakati wowote ule naweza kukupeleka.” “Nipo tayari kwenda, baba yangu. Na mimi nataka nikamuone bibi yangu, labda nitakuwa nafanana naye hata kidogo.” Paul alicheka kidogo na kuongeza.
“Labda akili za darasani.” “Na TABIA.” Ishimwe naye akaongeza na kumfanya Paul acheke sana. “Jamani! Kwani nivibaya? Eti baba?” “Hapana bwana! Lakini inawezekana, na inawezekana labda ndio sababu nawapenda wote. Ukweli nampenda sana mama yangu. Sidanganyi. Kwa yote mabaya aliyonifanyia, lakini bado anachukua nafasi kubwa sana moyoni mwangu. Najua kwako inaweza kuchukua muda mrefu kumsamehe, lakini naomba nikuombe kitu Sonia.” “Ndiyo.” Paul alisimama kabisa.
“Kwanza njoo hapa karibu yangu.” Paul alimkumbatia binti yake. Sonia alijisikia vizuri sana. Kutoka kwenye maisha ya upweke na dhiki aliyokuwa akiishi mpaka kufika mikononi mwa baba yake, anayeonekana mwenye kujali na upendo mkubwa, alijua ndio sababu pekee iliyomfanya mama yake ashindwe kuolewa tena. Huwezi kushikwa vile na kusahau.
“Kwanza nakushukuru sana kwa kukubali kuonana naye. Nimefurahi sana. Na pili, naomba nikushauri kitu, naomba mpe nafasi. Amekuwa mtu mzima na hana mtu ambaye yupo karibu naye, naamini amegundua ubaya aliotutendea mimi na Ishimwe, ameamua kujirudi. Naomba mpokee. Najua anatabia ngumu sana kuishi naye, lakini ana upendo sana.”
“Nimeshasamehe baba, na mimi naomba unisamehe tena. Niliishi maisha ya mimi na mama tu, sijui maisha mengine yeye akiwa mbali na hasa nikijua hatutakaa tukaishi naye tena na sijui kuishi na watu wengine kama yeye hayupo! Bado nilikuwa kwenye mshituko, na bado naogopa baba. Nimekubali kama inambidi kuondoka lakini bado nimebaki na hofu kweli!” Sonia alianza kulia tena, Paul alimuhurumia.
“Lakini Sam ananisaidia kunielimisha. Naamini nitakuwa sawa.” “Pole Sonia. Lakini huhitaji kuogopa hata kidogo. Sisi tupo na wewe wakati wote. Ni hivyo Sam ameniwahi tu, lakini ningefurahi sana kama tungeishi wote angalau hata mwaka mmoja tu, ndipo uolewe.” Sonia alicheka huku akilia.
“Kweli Sonia! Natamani na mimi kama ningebahatika kupata nafasi kama aliyoipata mama yako ya kukulea hata kama ni mwezi mmoja tu lakini basi, hata hivi nashukuru Mungu.” Paul alimsaidia kumfuta machozi.
“Asante.” “Nikuulize swali Sonia?” Sonia alitingisha kichwa kuashiria kukubali. “Imechukua muda gani tokea tulipoongea kwenye simu na tukakwambia tunakuja mpaka tulipofika hapa?” “Muda mfupi.” “Umeona sasa? Ndivyo ilivyo kati ya umbali wako na mama yako.”
“Na ukijifungua, nitamuomba Sam akuruhusu uje tuishi wote nyumbani tukusaidie mpaka utakapo pona kabisa na mtoto atakapo changamka.” Sonia alifurahi sana.“Asante sana baba.” “Siwezi kukuacha unateseka tena Sonia. Najua umemzoea sana mama yako, lakini naomba na mimi unipe nafasi maishani mwako! Japo niwe babu kama nafasi ya ubaba nimeikosa.” Sonia alicheka kidogo.
“Unanicheka? Mimi nitakuwa babu mzuri mpaka utashangaa. Kwanza najua kulea watoto wa kila umri. Ngoja huyo mtoto akizaliwa, utaona. Najua kuogesha watoto wachanga, hata vile vilivyotoka kuzaliwa naweza kuvisafisha na kuvivalisha, usinione hivi! Kupika tu ndio sipendi, sababu yakuogopa moto.” Wote walicheka.
“Asante sana baba yangu. Angalau hofu imeisha. Maana nilikuwa naogopa juu ya huyu mtoto baada ya kuzaliwa! Mama ndiye aliyenisaidia wakati nimejifungua Kana.” “Huna haja yakuogopa kabisa. Tena huyu wa safari hii atazaliwa kwenye neema, bibi na babu wote tunamsubiri kwa hamu.” Moyo wa Sonia ulijaa furaha.
*********************
Paul alimgeukia Sam. “Sam! Nakushukuru sana kwa kila kitu. Naamini kweli wewe ndio unamfaa Sonia. Naona jinsi unavyomuongoza vizuri na pia nikushukuru kwa kuendelea kubeba majukumu yangu na kuwa kama baba kwa Sonia na Kana. Naelewa jinsi maisha yalivyo magumu. Lakini umekubali kubeba majukumu yote, wewe mwenyewe ili tu Sonia apumzike na kumlea huyo mtoto aliye naye sasa hivi.”
“Naomba uendelee kunivumilia kwa haya majuma mawili, nimalize mambo yangu ya harusi, tukitoka kwenye fungate, ‘Honeymoon’ yetu, tutaongea vizuri. Najua sitaweza kukulipa kama nitakavyofanya au nilivyo fanya kwa wengine, kwa kuwa uliyoyafanya wewe kwa familia yangu HAYALIPIKI kwa pesa hata kidogo, lakini angalau nikupokee majukumu.”
“Lakini naomba upokee shukurani zangu za dhati. Asante sana.” “Asante.” Sam alifurahi sana, kuona baba mkwe wake anatambua juhudi zake. Yale aliyodhani yangemletea sifa kwa mkwewe kumbe hayakuwa na maana kwa Paul hata kidogo. Paul aliangalia picha kubwa ya maisha kwa jumla.
“Sasa sijui utapata ruhusa kazini siku ya alhamisi?” Paul aliendelea kuongea na Sam. “Maana bibi yenu ameomba hiyo siku ndiyo tuwepo nyumbani kwake. Nilitaka tuondoke na ndege ya asubuhi, ili tupate muda naye hiyo siku nzima, halafu usiku ndio tugeuze, ili Ishimwe apate muda wa kupumzika ijumaa na kujiandaa kwa harusi yetu jumamosi.”
“Hamna shida kabisa. Nafikiri tunaweza kwenda tu. Si tunaenda na Kana?” Sam aliuliza kwa kujali. “Kabisa. Najua mama atataka kumuona pia.” “Basi itabidi nikamuombee ruhusa shuleni, kwa hiyo siku.” “Asante sana Sam.” Paul alirudia.
*********************
Walirudi sebuleni wote wakiwa na furaha sana, Paul akimshukuru Mungu kwa familia kubwa aliyompa, Sam kuona anakubalika na mkwewe, Sonia yeye alifurahia kuwepo katikati ya wazazi wake wote wawili wanaonekana wanapendana sana na Ishimwe yeye alikuwa na furaha kumuona Paul anafuraha.
*********************
“Tunashukuru sana kwa msaada wa kurudisha mali za kina Nyange. Kaka amefurahi sana. Ameniambia yupo njiani, ameniomba nimsindikize akaingalie nyumba yao, kama ipo kwenye hali nzuri wahamie ndani ya juma hili, na kama kuna matatizo, ajue mapema ili atafute mafundi wakukarabati mapema, wahamie.” Sam alimwambia Paul. Mara simu ya Ishimwe iliita wakati Paul anataka kujibu. “Nani tena?” Paul akauliza kama asiyetaka kumshiriki Ishimwe na mtu!
“Mama Briana. Nilimtumia ujumbe kutaka kujua hali ya mama yake.” Ishimwe alijibu kwa kujitetea kidogo. “Pokea basi.” Paul alijibu. Angalau Ishimwe alifurahia baada ya kuona Paul hana shida, maana hata ujumbe wenyewe aliokuwa amemtumia mama Briana, alituma kwa kujificha.
“Vipi mama Bree?” “Tupo tu. Tulipofika tu hapa alianguka akapoteza fahamu, anaonekana sukari ipo chini sana, hana nguvu kabisa! Sijui alikuwa hali! Wamemuwekea maji, dripu ya kwanza ilipoisha, akazinduka, sasa hivi wamemuongezea nyingine, ndio nipo hapa nasuburi.” “Pole sana. Usiache basi kunijulisha mambo yatakavyo kwenda.”
“Bila shaka. Umewasiliana na Sonia?” “Nipo naye hapa, mzima biharusi wako.” Wote walicheka. “Maana Sam alinipigia simu akiwa na wasiwasi hampati mkewe kwenye simu.” “Nipo nao wote hapa.” “Haya basi baadaye. Ngoja niendelee kumsikilizia mama.” “Pole sana.” Ishimwe alikata simu na kubaki na mawazo.
*********************
“Kuna nini mama?” “Mama Eliah mgonjwa.” Ishimwe alijibu. “Unamaanisha mama yake mama Briana?!” Sonia alishituka sana. Ikabidi Ishimwe amuelezee kila kitu. Sonia aliumia sana huku akishangaa, Mama Briana anawezaje kujitoa tena kwa mama yake.
“Sam, naomba mimi niende nikakae na dada. Hatuwezi kumuacha dada akakaa peke yake huko hospitali.” “Ngoja nikuwekee chakula kwanza, ule ndio uende. Usije na wewe ukaanguka kwa njaa bure!” Sam alisimama kuelekea mezani. “Niwekee kidogo tu Sam, nasikia tumbo limejaa. Sijui kwa nini!” Sonia naye alimfuata nyuma.
“Tungeenda wote Sonia, lakini Nyange anaonekana anataka kuhamia huko kwao haraka sana. Ikiwezekana hata kesho. Kwa hiyo lazima tukapaangalie leo.” Sam aliendelea kuongea kwa sauti ya chini wakiwa wamekaa mezani na Sonia, lakini Paul alikuwa akiwasikiliza.
“Hamna shida. Nitakuwa sawa tu. Wewe nenda naye mkaangalie nyumba, halafu mimi niende nikakae na dada. Tutawasiliana, kama kukiwa na tatizo lolote nitakujulisha.” Sam na Sonia walibaki wakiongeleshana palepale mezani bila kukumbuka kama wana wageni. Paul alikuwa kimya kabisa akifiria ushirika walio nao hao watu.
“Kwa kuwa na mimi ningependa kwenda kuiona hiyo nyumba ya Nyange, kwa nini Sonia usiende na mama yako huko hospitalini, halafu sisi tukimaliza kila kitu huko nyumbani kwa Nyange, ndio nitamfuata mama yako?” Ishimwe alishangaa kidogo na kuuliza.
“Unataka kwenda na kina Sam na Nyange?!” “Ndiyo. Au?” Ishimwe alitabasamu na kuongea kwa sauti ya chini. “Asante Paul.” Alijua wazi Paul anafanya hayo yote kwa ajili yake. Paul alitabasamu huku akimwangalia Ishimwe. Sonia alirudi tena sebuleni. “Karibuni mezani.” “Mimi nilijua ndio tushasahauliwa hivyoo!” Paul alitania wakati anasimama. Sonia alicheka. Walijisahau yeye na Sam wakaelekea mezani bila wageni wao. “Samahanini, tulijisahahu, karibuni.” Sonia alirudia.
*********************
Wakati wanakula, Nyange aliingia na watoto akionekana ana mawazo. “Pole kaka na foleni!” “Daah! Namfikiria mama Bree! Yuko peke yake huko na mgonjwa halafu..” “Usiwe na wasiwasi shemeji, mimi na mama tunaenda sasa hivi kukaa naye.” Sonia alimkatisha.
“Kweli?! Na hali yako hiyo, ukakae hospitali!” “Sam amesha kuambukiza na wewe shemeji! Mnanifanya kama mgonjwa? Mimi nipo sawa tu.” Nyange aliongea vile kwa kujipendekeza tu kwa Paul. “Nahofia mbu bwana! Malaria na ujauzito sio vizuri.” “Halafu kweli, bwana!” Sam alishituka sana. “Basi hapo tena safari ndio ishakufa! Usingesema hivyo baba Briana! Hapo ushamchanganya Sam.”
“Naona heri niende tu mimi mwenyewe nikakae naye huyo mama Briana. Sitaki tuanze kuuguzana malaria, Sonia.” “Sam bwana nini?! Nitabeba khanga yakujifunika! Wewe nenda na wenzio mkaangalie nyumba. Labda utapata muda wakumfundisha baba kupika chai ya rangi.” Wote walicheka.
“Lakini kweli Sonia! Kwa hali yako hiyo jitahidi usijiweke kwenye mazingira ya mbu, ukaugua. Matibabu ya malaria kwa mama mjamzito ni magumu sana, utahatarisha maisha ya mtoto.” Paul aliongeza. “Usiwe na wasiwasi baba. Mimi nitakuwa salama. Nitavaa nguo zitakazo nisitiri vizuri. Mbu hawawezi kuning’ata” Nyange alibaki kama ameduwaa kidogo.
“Vipi kaka?” Sam aliuliza. “Na Mkuu naye yupo njia moja na sisi?” Nyange naye aliuliza kwa mshangao. “Nafahamiana na watu wawili watatu wanaoweza kusaidia ukarabati wa nyumba kwa haraka. Nilitaka tuongozane ili nione kama wataweza kuwasaidia. Kama naruhusiwa lakini.” Paul alijibu. “Bila shaka Mkuu. Ndio vizuri na wewe ukaone tulichokuwa tukikipigia kelele huko mahakamani.” Waliendelea kuongea mambo mawili matatu wakati wakila.
*********************
Kabla ya kuondoka Paul alimuita Sonia na mama yake pembeni. “Naombeni mnitambulishe kwa Kana jamani! Ndio mjuu wangu wa kwanza! Sipendi hivi tunavyosalimiana kwa mbali.” Sonia alifurahi sana. “Asante sana baba.” Alianza kutokwa na machozi. “Nimefurahi na wewe umemtambua mwanangu.” “Nikwambie kitu Sonia?” Sonia alitingisha kichwa.
“Siri kubwa ya ukoo wa Tambo, ni FAMILIA. Tuna umoja sana. Hakuna anayeachwa nyuma. Na hiyo ni kazi ya bibi yako. Sio kwamba hatuna matatizo yetu ya kifamilia, hapana. Tunayo, lakini nguvu yetu sisi ni umoja tu. Utakuja kuwaona hao shangazi zako na baba yako mkubwa. Bibi yako ndio mpaka nakuhurumia. Hatatulia mpaka aone umefika sehemu nzuri.”
“Na sio wewe tu, kila mtoto anayetokana na yeye, anamjali. Anahuruma na upendo sana. Hata mimi atanishangaa kama mpaka sasa hivi sijajenga urafiki na Kana.” “Asante baba.” Baada ya kutambulishwa kwa Kana. Paul alipata naye muda kidogo, na kumuahidi kesho yake jioni angerudi amchukue kuna kitu angependa kumuonyesha. Kana hakuonekana na shida yeyote kumpokea Paul, zaidi alionekana kufurahia sana, kupata familia kama watu wengine. Alijua jinsi familia zilivyo, lakini hakuwahi hata kuuliza ukoo wao. Aliridhika na mama Sonia na Sonia basi.
Misingi iliyojengwa kwa upendo, uvumilivu na kuvumiliana
Kana aliachiwa nyumba na majukumu ya kumwangalia Briana na Brayan, Nyange na Sam waliendesha gari ya Sam kuelekea nyumbani kwa Nyange, Paul aliondoka na mlinzi wake akiwafuata nyuma, mara baada ya kuongea kidogo na Ishimwe nje. “Tafadhali Ishimwe, kama ukiona mazingira sio mazuri kwa mtoto, mrudi bwana. Asije anza kuugua sasa hivi wakati ni mjamzito.” “Usiwe na wasiwasi. Nitakuwa makini.”
“Kukiwa na tatizo lolote lile unipigie tafadhali.” “Sawa.” Paul alimbusu na kuingia kwenye gari yake, wakaondoka. Sonia naye bila kupoteza muda, akaingia kwenye gari yake aliyokuwa akiendesha Nyange moja kwa moja yeye na mama yake, mpaka hospitalini alipokuwepo mama Briana. Walimkuta amejiinamia peke yake.
“Pole dada.” Sonia alimsogelea. Mama Briana alifurahi sana kuwaona. “Njaa inauma kweli!” “Kama mama alijua! Tumekuletea chakula.” “Afadhali.” Walikaa hapo nje wakiongea huku mama Briana akila. Tayari walikuwa ni ndugu ambao huwezi kuwatenganisha. Tatizo la mmoja wao, linakuwa kama la watu wote. Walikuwa na upendo na umoja wa aina yao. Kila mmoja alimjali mwenzake.
*********************
Huku kwenye jumba la Nyange nako, Paul, Nyange na Sam, walianza kuzunguka kila chumba wakitathimini cha kufanya. Mwishowe waligundua ni marekebisho machache sana na Paul alishauri nyumba ile ipigwe rangi kwa upya. “Hiyo itakuwa taratibu mkuu. Unajua rangi nilizokuwa nimepaka hapa tokea mwanzo ni zile za ghali kweli! Nikisema nianze hiyo kazi ya rangi tutashindwa kuishi kabisa.” Nyange alijitetea kwa Paul.
“Unakumbuka nilikwambia nitakushukuru kwa kunitunzia binti yangu na mke wangu?” Paul aliuliza. “Ulishatusaidia Mkuu! Si ndio tumerudishiwa mali zetu?! Inatosha kabisa.” “Hii ilikuwa haki yenu bwana! Nilichofanya mimi, nikufupisha tu kesi. Lakini sasa naomba mimi ndio nisaidie kuwarudishia nyumba yenu katika hali iliyokuwepo tokea mwanzo.” “Asante sana Mkuu.” Nyange alimpa mkono.
“Basi nitaongea na hao wahusika, nitawapa na namba yako ya simu ili iwe rahisi kuwasiliana. Nafikiri watahitaji kuja kupaona kesho na kuanza kazi mara moja.” “Asante sana.” Bado Nyange alikuwa haamini.
“Basi naomba mimi nikamfuate Ishimwe, ili awahi kupumzika. Kesho ana ugeni pale nyumbani.” Paul aliaga. Hata lisaa lilikuwa halijaisha tokea aachane na mkewe, lakini alishaona inatosha. Paul alikuwa na maisha kama ya Sonia. Hakuwa na marafiki wengi sana, na alikuwa mtu wa ofisini, nyumbani basi. Sio kuzunguka mtaani hasa baada ya kazi zake za kutwa nzima.
“Bila shaka Mkuu. Na sisi tunataka kumalizia kufunga hapa, ili tuelekee huko huko.” Paul aliondoka na kuwaacha Sam na Nyange wakimalizia kufunga nyumba.
Watu Sahihi Kwenye Maisha
Wakati mwingine tunakwepa watu sahihi Mungu anaowaweka kwenye maisha yetu kwa jinsi walivyo kwa wakati huo, bila kujua wamebeba hatima zetu za baadaye. Wakati Sam akimpokea Sonia, na kumsaidia pamoja na familia yake, hakuwa kitu kabisa. Na wakati mama Briana akimuajiri Sonia na mama yake, akiwaheshimu na kuwakarimu akiwasogeza karibu kama ndugu, hakujua kama wangemfaa siku ya uhitaji wake.
“Siamini Sam!” “Mungu mkubwa kaka. Kama utani!” “Kumbe ulikuwa umetuletea bahati kwenye maisha yetu bwana! Huyu Sonia na mama yake wamekuwa msaada zaidi ya tulivyotegemea!” “Wakati ule namleta kwenu kama mfanyakazi wenu, mimi mwenyewe nilikuwa hata simjui vizuri. Nilitaka kulipa tu fadhila, halafu niachane naye.” “Sasa ikawaje?” Sam alianza kucheka.
“Twende bwana kaka, na mimi nikamuwahi mke wangu. Kakae na mkeo wewe mwenyewe bwana!” “Kwani mimi nakataa! Lakini turudi kwenye swala la Sonia. Maana gafla nikaona unaanza kummiliki mtoto wa watu! Au ulishanusa harufu ya pesa kwake nini?” Sam aliingia kwenye gari huku akicheka sana.
“Acha hizo bwana kaka!” “Ni nini sasa? Au umbo lile kama la mama yake?” “Hamna bwana kaka, kwani anatofauti gani na Leah?” “Kweli bwana! Sasa ikawaje?” “Sonia anapendeka sio utani. Halafu kumbuka pale ndio nilikuwa nimetoka kwenye ‘janga’ Leah, halafu kama utani Mungu akanisogezea Sonia.”
“Yaani nilikuwa ni kama nimetolewa jehanamu halafu nikahamishiwa mbinguni, tena karibu na Mungu kabisa.” Nyange alicheka sana. “Kweli kaka! Sasa unafikiri ningefanyaje kaka yangu kama sio kung’ang’ania? Pale nilikuwa sina pesa, majukumu kibao, lakini nilijiambia potelea mbali, nitahangaika naye Sonia, hivyohivyo mpaka mwisho.”
“Nilikuwa nakuona mdogo wangu! Uliamua kufa na tai shingoni.” “Kabisa. Niliamua kujitosa kaka. Tena huku nina hofu ya kuporwa mjini, lakini kumbe mtoto mwenyewe hana hata wazo la wanaume wengine.” “Lakini utafia pazuri, Sam, mdogo wangu. Naona baba mkwe mambo yake sio mchezo! Unaoa mtoto wa watu wenye uwezo na jina kubwa sana nchini.”
“Mimi namuoa Sonia bwana!” “Hata hivyo, wewe si umeona jeuri ya kina Tambo? Hata mwezi haujaisha, tayari mama Sonia, kabadilika. Kwanza amebadilishwa jina, tumeambiwa anaitwa Ishimwe, ona mavazi yake. Pesa tupu. Heri imekuzukia mdogo wangu. Usinitupe tu kaka yako. Nikumbuke katika ufalmewako. Mjini tupo wachache kweli!” Sam alikuwa akicheka sana.
“Usifikiri nakutania. Ukiitwa huko kwenye ufalme wa kina Tambo, uwaambie una kaka yako.” “Acha hizo bwana!” “We unafikiri maisha yako yatakuwa hivyo tena? Unaishi na mtoto wao! Lazima wakupige na wewe msasa. Ndio ujipange sawasawa, maana unaweza kuulizwa swali la harakaharaka, ‘Tukusaidie nini?’ Hapo tena unatakiwa uwe unamajibu yakueleweka sio kung’ata kucha kama mtoto wa kike.”
“Acha kunitisha bwana! Unajua alhamisi tunatakiwa kwenda kumuona bibi yake Sonia?” Nyange alishituka sana. “Acha masihara? Mama Tambo mwenyewe?!” “Sio yeye tu, nasikia na ndugu zake Baba Sonia, wameitwa hapa nchini kutambulishwaSonia.” “Daah! Si umeniamini sasa? Umeuchinja mdogo wangu! Unaenda kutambulishwa kwa watu wakubwa sana. Unatakiwa ujipange vizuri, na majibu yanayoeleweka.”
“Sio wanakuuliza yale maswali yao ya kisomi kama, ‘Unatarajia nini baada ya miaka mitano kuanzia sasa?’ Hapo mdogo wangu sio unaanza kusema 'watoto'. Anza kutafuta majibu mapemaa.” “Daah!” Sam alipotelea kwenye mawazo. Wakajikuta vicheko vimeisha ndani ya gari, wanaendesha kimya kimya, kila mmoja akiwaza.
“Kichwa kinanizunguka kaka, juu ya hao ndugu za Sonia!” Sam alivunja ukimya, nakuendelea. “Naona wanakuja kwa kasi kweli! Nafikiria jinsi ya kuwatambulisha kwa wazazi wangu. Nafanyaje kaka?” “Basi tulikuwa tunawaza jambo moja. Mimi mwenyewe nawaza hivyohivyo. Sina jibu mdogo wangu. Ukisikia mtihani wa maisha, basi ndio huo.”
*********************
Paul alifika pale hospitalini, akaomba ruhusa ya kuingia ndani kumuona mgonjwa. Akaruhusiwa kuingia, baada ya muda Paul akiwa ndani Nyange na Sam nao walifika. Wote walionekana wana mawazo. “Vipi D? Mbona hamna raha? Mmekuta nyumba ipo vibaya sana?” Mama Briana alisimama na kumsogelea mumewe.
“Hapana, ni vitu vichache tu vya kurekebisha na tumepewa ‘offer’ na Baba Sonia, yeye ndiye atalipia gharama nzima ya matengenezo yote na upigwaji rangi. Amesema ndio shukurani yake kwetu kwa kuishi na familia yake. Kesho asubuhi ataleta mafundi ili waanze kazi mara moja.” “Jamani huyu baba amejitoa kupita kiasi! Asante sana mama Sonia.” “Ishimwe bwana, sio mama Sonia!” Hawakuwa wamemuona Paul aliyekuwa anawasogelea kutoka ndani wodini, alipokuwa amepumzishwa mama Eliah. Wote walicheka.
“Asante sana. Mungu akubariki.” Mama Briana alimpa mkono Paul. Ishimwe naye alisimama na kumsogelea Paul. “Asante mpenzi wangu.” “Karibu.” Paul alijibu kwa kutabasamu.
“Asante baba. Kweli nimefurahia, na nimeamini unatujali.” Sonia alisimama na yeye akamsogelea baba yake huku machozi yakitaka kumtoka. “Najiuliza kama ungekuwepo tangia zamani, sijui ningekuwa wapi sasa hivi!?” “Ungekuwa shuleSonia. Wala huyo Sam usingekutana naye.” Paul alijibu na kufanya kila mtu acheke.
“Sheria mojawapo ya Tambo, ni hakuna kuolewa wala kufanya kazi mpaka uwe na shahada mbili. Kwa hiyo upande mwingine ushukuru Mungu sikuwepo, maana huyo Sam wala usingekuwa naye.” Sonia aliendelea kucheka. “Basi afadhali umechelewa chelewa kuja.” Paul alimkumbatia binti yake.
“Vipi hali ya mgonjwa? Maana sisi tumekataliwa kuingia huko ndani, kumuona.” Nyange aliuliza. “Naona mama anaendelea vizuri. Wamemfanyia vipimo kadhaa, wanasema ni sukari tu ilikuwa chini, anaonyesha hakuwa akila. Akimaliza hayo maji anaweza kuruhusiwa.” Mama Briana alishituka sana. “Sasa wakimruhusu leo, nitamuweka wapi usiku huu?” Wote walibaki kimya wakimwangalia. “Si pale tunapoishi dada jamani!” Sonia alijibu na kumfanya Paul akaribie kuchanganyikiwa.
“Itabidi kurudi tu kwetu, usiku huu huu. Hatuwezi kuendelea kubanana pale. Hayo marekebisho ya nyumba, tutafanya tukiwa humohumo ndani.” Nyange alijibu na kumfanya Paul apumue kwa nguvu. Ishimwe alimwangalia na kutabasamu. Alijua kinachoendelea kichwani mwa Paul.
“Kwa hiyo mnaondoka dada?” “Itabidi Sonia. Siwezi kuruhusu mama kuishi pale na wewe. Sijajua kama amebadilika au la. Na hata kama amebadilika, sijajua ni kwa kiwango gani. Kama bado anamadudu yake, heri yakatupate sisi wenyewe.” “Hakuna baya litakalo wapata tena, Mungu yuko upande wenu mama Briana. Usiogope.” “Asante Ishimwe.” Mama Briana alijibu.
Sam alimuona jinsi Sonia alivyobadilika. “Nini tena?” Akamuuliza taratibu akiwa bado ameshikiliwa na baba yake. “Naona kila mtu anaondoka! Tutabaki mimi na wewe tu! Tutapooza sana.” Sonia alijibu. “Ni usiku tu ndio tunatengana Sonia. Lakini mchana tutakuwa wote mdogo wangu, wala usiwe na wasiwasi. Nikitoka kuwapeleka watoto shule, nitakuwa nakuja kukuangalia na kukusaidia kazi. Umesikia?” Sonia alitingisha kichwa kukubali. “Basi naomba sisi tutangulie tukaanze kufungasha.” Nyange aliaga, nakuondoka na Sam.
*********************
Sonia alibaki ameinama. “Utakuwa sawa Sonia, usiwe na wasiwasi. Umesikia?” Paul alijaribu kumuongelesha. Alinyanyua kichwa kumwangalia baba yake na kutabasamu huku machozi yakimtoka. “Nataka nikuombe ushauri baba, sijui itakuwa sawa?” Paul alitamani kurukaruka kwa furaha. “Bila shaka. Karibu.” “Tunaweza kusogea pembeni?” Sonia aliuliza huku akifuta machozi.
“Twende tukaongelee kwenye gari yangu. Hapa kuna mbu sana.” “Kwani hamtaki mimi nisikie?” Ishimwe aliuliza nakumfanya Paul aanze kucheka. “Sasa unanicheka nini, we Paul? Siri hizo zitawaua niwaambie mapemaa. Jambo gani msiloweza kuongea mimi nikiwepo?” “Ishimwe hapendi kupitwa!” Paul aliongea akizidi kucheka.
“Sasa na wewe badala yakunicheka, si ungemwambia huyo Sonia niwepo kwenye hayo mazungumzo? Mazungumzo gani mnayoongea bila mimi?” Mama Briana na Sonia walikuwa wakicheka sana jinsi Ishimwe alivyokuwa aking’ang’aniaawepo kwenye hayo mazungumzo ya Paul na Sonia.
“Ishimwe, mi naona wewe ukae tu hapa na mimi. Waache wakaongee.” Mama Briana aliingilia. “Lakini huo sio ustaarabu bwana!” “Mama jamani!” Kila akimwangalia Ishimwe, Paul alikuwa akicheka sana. “Wewe nicheke tu.” “Ishimweeee.” Paul aliendelea kumchokoza Ishimwe.
“Basi unaona umenipita! Wala sina shida ya kujua mnachotaka kuongea.” “Mmh! Mbona hukai sasa?” “Ujue Paul nakuangalia wewe! We endelea tu.” Paul aliendelea kucheka. “Bwana Ishimwe kwa kupenda kunitishia! Sasa mimi kosa langu hapa ni lipi? Wote tumemsikia Sonia anataka kuongea na baba yake. Au mimi nimesikia tofauti? Eti jamani?” “Ni kweli baba. Naomba sasa hivi niongee na baba tu, halafu tutakushirikisha baadaye, mama.” Ishimwe akaguna.
“Twende mwanangu. Mimi namjua huyo vizuri sana! Hapo roho inamdunda. Hapendi kusimuliwa, anataka kushuhudia kila kitu, yeye mwenyewe, hasa mimi nikiwepo.” “Wala sio uongo. Nataka kujua sana.” Wote walicheka tena. Mama Briana ndio alikuwa akicheka mpaka machozi.
“Mambo mengine uwe unayaacha yakupite Ishimwe mpenzi wangu!” “Nyinyi nendeni, lakini lazima mje mniambie kila kitu mlichoongea.” Paul na Sonia waliondoka huku wakicheka. Walikwenda mpaka lilipokuwa limeegeshwa gari la Paul.
*********************
“Tukae humu ndani, nje kuna mbu sana.” Akamfungulia mlango, akaingia ndani. Paul aliomba dereva wake na mlinzi wamsubirie nje ya gari, wakabaki yeye na Sonia tu ndani ya gari. Walikaa kwenye kiti kikubwa cha nyuma, akawasha taa akabaki akimwangalia binti yake.
Ujauzito wa Sonia ulishakuwa bayana. Hata usoni alionyesha ni mjamzito. Sonia alianza kubabaika. “Si unajua unaweza kuniambia kitu chochote, Sonia?” Paul alijaribu kumtuliza. Sonia alijaribu kucheka, lakini Paul aliona jinsi alivyojawa hofu, hata cheko yake ilitawaliwa na hofu kubwa.
Akamvuta mkono wake na kumshika huku akimwangalia na tabasamu kubwa la kibaba usoni mwake, ili kumfanya atulie. Sonia alivuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu. Baada ya kuvuta pumzi mara tatu, alianza kuonyesha utulivu usoni. Paul aliendelea kumwangalia taratibu huku akifikiria jinsi ya kubadili maisha ya binti yake. Angalau sasa hivi ugeni wa nyumbani kwake unapungua. Kidogo hilo alianza kufurahia nafasi atakayoipa Sonia akiwa nyumbani kwake, sio kama alivyokuwa akiishi na familia ya Nyange.
Kila alipokuwa akienda kumtembelea pale nyumbani kwake, alizidi kugundua marekebisho makubwa yanayotakiwa kufanyika ndani na nje ya hiyo nyumba ya Sam, angalau kuendana na maisha aliyokuwa amemkusudia mwanae. Baada ya kuona kila kitu hakifai kwenye hiyo nyumba ya Sam, Paul alibaki kujiambia, ‘Hii sio nyumba anayostahili kuishi mwanangu’. Ukweli Sam alijitahidi kujenga, lakini alijenga nyumba ya kawaida, ila eneo zuri.
Kingine, Paul alipenda kuvaa sana, na alijua nguo nzuri. Lakini kila alipokuwa akimwangalia binti yake na mavazi aliyokuwa akimuona nayo, aliendelea kuumia. Lakini alishindwa hata kumwambia Ishimwe kwani wote wawili walikuwa wakijisifia ndio wameingia kwenye maisha mazuri, hapo nyumbani kwa Sam. Wakati wote tangia arudi kwenye maisha yao, Paul amekuwa akifikiria jinsi ya kubadilisha maisha ya binti yake bila kuonekana anadharau juhudi za Sam.
*********************
“Kila kitu kitakuwa sawa Sonia, nimerudi baba yako. Nitahakikisha unaishi maisha niliyokuwa nikiyafikiria tokea uko tumboni kwa mama yako. Najihisi nimechelewa lakini naamini tutakuwa pamoja na tutarekebisha kila kitu hatua kwa hatua.” Paul alijikuta akiongea mawazo yake waziwazi, nakumfanya Sonia aanze kulia. Alimsogeza karibu na kumkumbatia.
“Nitafanya kwa kadiri ya uwezo wangu kukusaidia Sonia. Haupo tena peke yako.” “Asante baba.” “Nini kinakusumbua?” “Sam anatatizo. Naumia sana kwa kuwa sijui jinsi yakumsaidia na yeye amekuwa msaada wangu tokea zamani.” “Pole.” Alianza kumbembeleza kama mtoto mdogo, ili atulie, waweze kuzungumza.
*********************
“Niambie Mama Judge. Maandalizi ya harusi yakoje?” Mama Briana alimchokoza Ishimwe mara baada ya kukaa. “Afadhali umenikumbusha! Sijui nimechanganyikiwa!” “Nini tena?” “Mama Tambo na mdogo wake Paul wanakuja kesho kunichukua ili tukatafute nguo za harusi.” “Sasa kinacho kuchanganya nini, badala ya kufurahi?” “We mama Briana? Namwangaliaje tena yule mwanamke machoni baada yakumsaliti?” “Umemsaliti!? Mbona sikuelewi?” Mama Briana alimgeukia Ishimwe vizuri.
Ishimwe akaanza kucheka. “Kwani vipi?” “Unajua nilipofika nyumbani kwa kina Paul, mama yake alikuwa akinipenda na kuniamini sana, sababu ya usafi wa nyumba yake, kupika chakula kizuri na uaminifu. Ilikuwa kila mgeni aliyekuwa akifika pale akila chakula changu, anasifia sana.”
“Basi yule mama akawa ananikubali sana kwa mambo ya jikoni na walikuwa hata wakisahahu kiasi gani cha pesa mezani au kwenye nguo zao, nikiingia kusafisha au nikiwa nawafulia nguo zao, nawawekea pesa zao kama zilivyokuwa. Japokuwa ni mkorofi huyo mama…” Mama Briana alianza kucheka.
“Unafikiri nakutania? Bwana mwanamke ni mkorofi huyo! Hata wanae wanashindwa kuishi nae, kasoro Paul ndio kipenzi chake. Sasa Paul alipomkataa yule msichana aliyekuwa amemletea, wote tulikuwa hatujui sababu ni nini. Akawa akinituma niongee na Paul kumdadisi kwa nini hamtaki yule msichana kwa kuwa Paul alikuwa karibu sana na mimi, kwa hiyo mama yake akajua, mimi ndiye naweza kujua sababu yake. Kumbe mimi ndio nilikuwa sababu.” Mama Briana alizidi kucheka.
“Sikudanganyi mama Bree, mimi nilikuwa sina hata wazo! Nilikuwa nikimfuata Paul nafanya kila kitu alichokuwa akinituma mama yake kumfanya amkubali yule msichana, kumbe Paul anasema ndio alikuwa anazidi kuvutiwa na mimi.” “Ishimweeee! Ulimchanganya kijana wa watu!” Ishimwe alianza kucheka.
“Sasa hebu niambie namtizamaje yule mama kesho wakati mimi ndio nilikuwa mjumbe, nikaishia kutoroka na mwanae?” Mama Briana alizidi kucheka. “Tena ujiandae kesho tutakufuata tukatafute wote hizo nguo za harusi.” “Mimi sina shida Ishimwe, ukiwa tayari tu unipigie.” “Natamani uje pale nyumbani tuwe wote wakati mama Tambo anakuja. Naogopa kweli!” “Paul yupo bwana, usiwe na wasiwasi.” Mama Briana alijaribu kumliwaza, Ishimwe.
*********************
“Sam anatatizo gani?” Paul aliuliza taratibu. Sonia alimuelezea kila kitu kuhusu familia ya Sam, na jinsi Sam alivyohangaika kuwatunza ndugu zake, na hofualiyonayo sasa hivi, yakumpeleka Paul na familia yake nyumbani kwao. Kilicho mshangaza Sonia, ni utulivu aliokuwa nao baba yake. Hakuonyesha kushangaa hata kidogo. Sonia alizidi kupata moyo wa kuwa muwazi zaidi.
“Nimemshauri kuwaleta wazazi wake hapa mjini tuishi nao, lakini Sam amekataa.” “Unafikiri kwa nini amekataa?” Sonia alitulia kidogo. “Eti Sonia?” “Anakuogopa wewe baba!” Sonia alimwangalia vizuri baba yake machoni kutaka kujua anafikiria nini juu ya hilo.
“Unafikiri ni sawa, kama kesho nikipata muda wa kuongea na Sam mwenyewe? Ili nimsikilize vizuri na tushauriane chakufanya?” “Nitashukuru sana baba yangu. Itampunguzia hofu.” “Basi usiwe na wasiwasi juu ya hilo, limeshaisha. Una kitu kingine ulitaka kunishirikisha?” “Ni hicho tu baba. Sipendi Sam akiwa kwenye msongamano wa mawazo. Anakuwa hana raha kabisa.” “Naamini tutayamaliza kesho.” Sonia alifurahi sana hata baba yake alimuona usoni. “Asante sana baba yangu. Nakushukuru.” Paul alicheka na kumkumbatia tena.
Mungu Anapoamua Kulimpa Aliyekubali Kutumika Kwa Kutoa
Huwa Mungu hachelewi, wala hawahi. Kwa wakati wake, kujidhihirisha. Ndivyo ilivyokuwa kwa familia ya Nyange. Siku hiyo wanaamkia nyumbani kwa Sam na Sonia, hawakujua kama Mungu alishaiona siku hiyo, akaibariki na kuamua yale yote yaliyokuwa yamekusudiwa kuwa ubaya kwao, kuwaangamiza, anayageuza kuwa mema. Walishaanza kuvuna wema wao. Na usiku huo alikusudia kuwarudisha kwenye mjengo wao.
Usiku huo ulikuwa wa hekaheka sana kwa familia ya Sam na Nyange. Paul na Ishimwe walishajitoa mapema. Paul aliomba Ishimwe akapumzike sababu ya ugeni wa kesho yake. Sonia alirudi nyumbani kwake akiwa peke yake na kumuacha mama Briana akijiandaa kuondoka hapo hospitalini na mama yake kurudi nyumbani kwao. Mama Briana hakutaka kabisa mama yake hata akanyage nyumbani kwa Sonia na Sam.
Sonia alimkuta Kana, Brayan na Briana wamekaa sebuleni wakisubiri kuondoka wakati Nyange na Sam wakimalizia kuingiza mizigo yao kwenye gari. Sonia hakupenda kabisa maisha yakutengana, zaidi na mtoto wake. Alihisi Kana ataona hamtaki. “Poleni.” Sonia aliongea kinyonge wakati akiingia ndani. “Asante. Vipi?” Sam alijibu. “Safi tu. Nimemuacha mama Briana anakaribia kuondoka kuelekea kwake.” “Na sisi tunamalizia vitu safari ya mwisho ili nimpeleke Nyange na watoto nyumbani.”
“Naomba kuongea na Kana kabla yakuondoka.” “Hamna shida, japo nahofia kweli muda wa kulala. Usiku umeenda sana na kesho wanatakiwa kwenda shule.” Sam alijibu na kuendelea na shuguli zake, huku akijua wazi ni ugumu gani Sonia anapambana nao kuagana na mtoto wake.
Alimuomba Kana waingie chumbani kwake kwa ajili ya mazungumzo mafupi. Brayan alikuwa amemuegemea Kana huku akisinzia, akamuweka vizuri kwenye kochi na kumfuata Sonia. Wakakaa kitandani. Kana alikuwa ametulia sana pale alipokuwa amekaa kitandani kwa mama yake, akisubiria hayo maongezi.
Sonia alitaka kuongea lakini alishindwa kutoa neno hata moja, aliinama nakuanza kulia kwa muda mrefu sana mpaka Sam alipoingia. Alimkuta bado akilia. Alikaa pembeni yake.
“Nilishaongea na Kana, nimemwambia wazazi wa Briana ndio walio omba aende kuishi nao kwa muda, mpaka Briana atakapozoea kulala peke yake.” Sonia alianza kukausha machozi. “Nakupenda Kana mwanangu. Namuomba Mungu aje atusaidie siku moja tuje tuishi wote pamoja.” Sonia aliongea huku akilia. Kana alikuwa amenyamza kimya kabisa ameinamisha kichwa chini.
“Sijawahi kukukimbia au kukuficha kwa mtu yeyote, ila maisha ndiyo yamekuwa yakitutenganisha. Lakini naamini siku sio nyingi tutaweza kuishi wote.” “Kama alivyosema mama yako, tunakuhitaji sana Kana, sisi ni familia. Na ninaamini hata kabla ya mdogo wako hajazaliwa utakuwa umerudi hapa nyumbani, ili umpikie ule uji kama unao mpikia mama yako.” Sam alimpiga Kana mgongoni, nakumfanya acheke kidogo.
“Tutakuwa tukionana?” Kana aliuliza. “Kabisa.” Sonia aliitikia haraka haraka na kuongeza. “Hata kama wasipokuwa wanakuleta hapa, mimi nitakuwa nakufuata ili angalau tuonane kila siku.” “Tutakuwa tunaonana Kana na kwa kuwa unayo simu, basi tutawasiliana mara kwa mara.” Sam aliongeza. “Asanteni sana. Asante anko Sam.” Kana alisimama kumpa mkono Sam. Sam naye akasimama.
“Ukiwa na shida yeyote, wakati wowote, wewe tupigie tu simu.” “Nitafanya hivyo.” Kana alibaki akijifikiria, kama anayetaka kumwambia kitu Sonia, lakini alishindwa. Alibaki amesimama mbele yake huku ameinamisha kichwa chake, wakati bado Sonia amekaa kitandani na yeye ameinama. Hawakuwa na mazoea ya karibu hata kidogo. Kana hakujua kama aenze kumuita Sonia, mama au aendelee kumuita vilevile Sonia! Upande wa Sam ndio kabisaa. Tokea mtoto mdogo alishazoea kumuita Sam, anko. Ilikuwa ngumu kurudi tena kumuita baba.
*********************
Nyange aligonga na kuwaambia wapo tayari, anaomba Sam awapeleke. Walitoka kimya kimya, Kana aliaga tena na kupanda kwenye gari. Sonia alibaki amesimama peke yake pale nje. Sam alimuhurumia, akashuka kwenye gari. “Mimi naona kaka, wewe utangulie na watoto tu. Mimi nitakuja huko kwenu na Sonia kufuata gari yangu.” “Hamna shida, nawashukuru sana.” Nyange alijibu na kuondoka na watoto wote.
Waliwaacha Sonia na Sam wamesimama hapo nje. Akamgeukia Sonia, “Twende tukaoge, ulipe deni lako, ndio tukafuate gari.” Sonia alicheka. “Husahau tu?” “Ahadi ni deni Sonia. Uliniambia ukishapika.” Sonia alifurahi sana. Sam alimkumbatia na kuanza kumbusu hapohapo nje walipokuwa wamesimama, huku akiongoza njia mpaka ndani chumbani kwao.
Milima Pekee Ndiyo Haikutani, Lakini Si Wanadamu
Kesho yake Ishimwe aliamka alfajiri na mapema, kuandaa kifungua kinywa kizuri cha Mama Tambo na wifi yake. Akiwa amejawa hofu, alirudi chumbani kujiandaa. “Nisaidie kuchagua nguo Paul.” “Wewe vaa vyovyote tu utapendeza. Usiogope. Sitaondoka mpaka waje, tunywe wote chai, wakati mnaondoka na mimi ndio nitaondoka.”
“Afadhali. Maana nilikuwa nawaza, kama watanikuta humu ndani peke yangu!” “Siwezi kukufanyia hivyo Ishimwe. Lazima niwepo hizi siku za mwanzoni, mpaka nitakapo kuona umewazoea ndipo naweza kukuacha nao.” “Asante Paul kwa kunifikiria.” Walijiandaa na kutoka sebuleni kuwasubiria.
Baada ya muda kengele ya mlangoni iligongwa. Paul alianza kucheka. “Unacheka nini bwana Paul?” “Unavyohangaika! Ngoja nikwambie kitu Ishimwe. Hawa ni wageni wetu. Tena wanakuja kwetu, huna haja yakuogopa. Umenisikia?” “Haya, kafungue basi mlango.” Paul aliendelea kucheka. “Nenda bwana Paul, nini? Si unamjua mama yako asivyopenda kusubiri?” “Tulia basi.” “Natuliaje sasa, kwa mazingira kama haya? We nenda tu bwana.” Ishimwe aliendelea kunong’ona.
“Ujanja wote umekuisha!” “Nenda Paul, tafadhali mpenzi wangu, nenda. Halafu urudi kukaa hapahapa pembeni yangu.” Paul alisimama huku akicheka kuelekea mlangoni kabla mama yake hajabonyeza kengele kwa mara ya pili, kwani ni kweli Mama Tambo hakujaliwa subira hata kidogo. Mambo yake yote yalienda kwa mpangilio. Na wote walimfahamu hivyo.
*********************
Paul alifungua mlango “Karibu mama! Mbona simuoni Matilda?” “Anaongea na simu kwenye gari.” Mama Tambo alijibu na kuongeza. “Afadhali sasa hivi tunakaribishwa na harufu nzuri kwenye hii nyumba, sio kama zamani!” Paul alitingisha tu kichwa bila ya kujibu kitu akiwa bado amesimama mlangoni na mama yake akiwa bado nje ya mlango.
“Nipishe sasa mlangoni, wewe vipi Paul?!” Ndipo alipompisha mama yake mlangoni. Alipomuona tu Mama Tambo, Ishimwe alisimama kama askari na kubakia kama sanamu asijue aseme nini. “Umekuwa mkubwa sana Ishimwe na umependeza.” Kidogo alipumua na kujibu, “Asante mama, shikamoo.” “Marahaba.”
Matilda mdogo wake Paul aliingia, alifanana sana na Mama Tambo. Alimkumbatia Paul. “Nimefurahi kukuona Paul.” “Asante. Hata mimi nimefurahi kukuona Mat. Karibu sana.” Paul alijibu huku akitoa tabasamu kubwa usoni, kuashiria furaha ya kumuona mdogo wake. Walibaki wamekumbatiana kwa muda.
Mwishowe Paul alimwachia na kumsogeza mbele kidogo huku akimwangalia. “Mbona unazidi kuwa mdogo? Huli nini?” Alimuuliza mdogo wake. “Nakimbia uzee mwenzio.” Waliendelea kuongea wawili hao, huku Ishimwe na Mama Tambo wakiwaangalia.
“Umemuona mke wangu lakini?” Paul aliuliza, Matilda akacheka. “Nimemuona na nina mizigo yake kibao kwenye gari. Mama Tambo alinitumia picha zake, nijaribu kumuangalizia gauni la harusi. Nimekuja nayo mawili, sijui atayapenda?” Ishimwe alishituka sana, lakini si Paul. Alishazoea vituko vya mama yake.
Matilda alisogea na kumpa mkono Ishimwe. “Afadhali tumepata Mama Tambo mwingine, maana kina Mama Tambo wa familia hii, hawaeleweki vizuri. Huyo mwingine ndio kabisaa, hatuelewani misemo.” Ishimwe alicheka kwa hofu akionyesha kutokuelewa na Paul alifahamu hilo.
“Kaka yangu yule mkubwa ameoa, mmarekani mweupe. Ndiye huyo anayemsema Matilda na mwingine ni mama.” “Aahaa!” Ishimwe aliitikia, kuashiria kuelewa. “Ujue Matilda nakusikia wewe!” Mama Tambo aliingilia mazungumzo yao na kuwafanya wacheke kidogo.
“Hongera Paul, mkeo mzuri kweli!” Ishimwe alitamani aanguke. “Hilo nalijua vizuri sana.” Paul alijibu kwa kujivunia. Matilda akacheka. “Mbona hatukai sasa? Kwanza njaa inauma. Kunaliwa humu ndani?” Mama Tambo aliuliza. “Niliwaandalia kifungua kinywa mama. Ngoja nikaweke mezani.” Kama aliyepata ruhusa, Ishimwe aliondoka haraka sana.
Matilda alianza kucheka. “Umeanza Mat. Nini sasa?” “Naona safari hii umeamua kutafuta dawa ya kutibu maradhi yako. Nishajua ulichompendea huyu mtoto wa watu.” “Mama umemuona Matilda, ameanza?” “Kwani mama wewe hujui ugonjwa wa mwanao?” “Sijui na sitaki kujua.” Matilda aliendelea kucheka.
“Nampenda mke wangu kwa kila kitu.” Matilda alizidi kucheka kwa sauti na kuongeza. “Ndivyo unavyomdanganya mtoto wa watu?” Matilda aliuliza. “Simdanganyi bwana! Nampendea tab…” “Huna lolote we Paul. Umbile lake tu, ndilo linakuchanganya. Kwani mimi sikujui wewe? Na ndio ugonjwa wako Paul, tokea tupo shule.” Paul alicheka kidogo huku akitingisha kichwa, akasimama na kuondoka kwa aibu, mbele ya mama yake.
“Sasa unaenda wapi Paul best yangu?” “Nimechoka kukusikiliza, naenda kumsaidia mke wangu kuandaa chakula.” Matilda alikuwa akicheka sana. “Unajua Matilda nitakufukuza humu ndani wewe! Maongezi gani hayo unaongea na kaka yako, mimi nikiwepo?” Mama Tambo alimgeukia Matilda mara baada ya Paul kuondoka kabisa pale walipokuwa wamekaa wote.
“Basi mama yaishe. Ndio nimefika tu, sitaki tuanze kugombana. Nilikuwa na hamu na wewe kweli, mama yangu.” “Huna lolote. Mbona hukuja mwenyewe mpaka nilipokuita?” “Mama kwa kuhesabu! Ona mimi ndio nimefika hapa wa kwanza, wala sijakubishia. Ulivyosema tu nije, nilikubishia?” “Mimi mwenyewe mpaka nikaogopa! Nikahisi nimekosea namba, naongea na mtu mwingine.” Mama Tambo alijibu na Matilda kuzidi kucheka.
“Ndio ujue nilikuwa nina hamu na wewe. Na nimeleta magauni mazuri kweli ya mkweo, najua utayapenda.” “Umeleta na nguo za mtoto wa Sonia?” “Si ulisema nilete rangi nyeupe?” “Kumbe wewe umeleta rangi zipi?” “Nyeupe, mama! Mbona unawasiwasi?” “Kwa kuwa sitaki uniharibie utaratibu wangu.” “Mimi na wewe mama yangu?” “Hebu acha kunidanganya.” “Watu hamjui kupendwa jamani!” Matilda alikuwa sebuleni na mama yake wakiendelea kuongea na Ishimwe alikuwa akiwasikiliza akiwa jikoni na kubaki akimwangalia Paul kama asiyeelewa.
“Nguo za mtoto wa Sonia?!” Ishimwe alimnong’oneza Paul. “We utamuweza mama? Hapo kila mmoja kaagizwa vitu vya kuleta.” Paul naye aliongea kwa sauti ya chini. “Nenda kawaambie chakula tayari.” “Si uende mwenyewe, Ishimwe!” “Nakuomba mpenzi wangu uende.” Ishimwe aliendelea kubembeleza kwa sauti ya chini ili wageni wao wasisikie.
“Unachoogopa nini, Ishi? Ndio nafasi yenyewe hii ya kuwazoea.” “Kweli?” “Kweli tena. Hapa ni kwako Ishimwe, lazima uwe kama mama mwenye nyumba, sio kubaki unajifichaficha kila wageni wanapotutembelea.” Ishimwe alivuta pumzi na kutoka.
“Karibuni huku jikoni, chakula tayari.” Mama Tambo ndiye aliyesimama wa kwanza na kuelekea jikoni. “Yaani Ishimwe ni msafi huyu mtoto! Nyumba hii ilikuwa imeoza! Hongera mwaya.” Mama Tambo alisifia na kumfanya Ishimwe alijisikie vizuri. “Asante mama.” Paul alikuwa akitabasamu huku anatingisha kichwa.
“Kwani uongo?” Mama Tambo akamuuliza Paul. “Haikuwa chafu wakati wote, bwana mama!” “Basi sikumbuki kuja hapa, na kuikuta safi hivi. Tokea unaishi na yule mwendawazimu.” Mama Tambo alijibu na kuvuta kiti, akakaa. Wote walikaa na kuanza kupata kifungua kinywa.
Walipomaliza tu kula, Matilda akamgeukia Paul, “Naomba utupishe Paul. Tunataka muda na bibi harusi wetu. Naona kila saa unamwangalia!” Paul alicheka. “Matilda mkorofi wewe. Sema umenikuta leo sina haja yakugombana na wewe. Mimi naondoka zangu muda si mrefu, wala sikai hapa na wewe.” Paul alisimama, nakuanza kutoa vyombo mezani.
“Acha tu Paul nitamalizia, ili uwahi kazini.” “Nisindikize basi mpaka hapo nje.” Matilda alianza kucheka tena. “Nimekwambia nitakutoa humu ndani Mat wewe! Wewe endelea tu.” “Kwani nimefanyaje mama jamani? Eti Paul?” “Najua unataka tuanze kubishana hapa mpaka jioni, nimekwambia leo sina huo muda. Nawahi kazini.”
“Afadhali Paul uende. Maana hawa wakianza kubishana hapa, hawamalizi. Tunaendaga kulala tunawaacha bado wanabishana, tena vitu vya kijinga. Na hivi wote wanasheria, hawatii hamu kuwasikiliza. Wataanza kubishana huku wakikosoana juu sheria za Tanzania na Marekani mpaka wanaenda kulala hawana jingine wanaloongea. Heri uondoke Paul ili msiniharibie siku yangu ya leo.” Mama Tambo aliingilia.
“Nishakuwa mtu mzima siku hizi, nimestaafu kubishana na watoto wadogo.” “Jajiiiii…” Matilda aliendelea kumchokoza kaka yake. “Nini Mat?” “Nilikuwa na hamu na wewe kweli Paul, kaka yangu.” “Achana na mimi.” Paul alijibu na kutoka, akiwa amemshika mkono Ishimwe.
*********************
Siku hiyo ilikuwa nzuri sana kwa Ishimwe zaidi ya alivyotarajia. Ni kweli kipingamizi alikuwa ni Mama Tambo peke yake, katika mapenzi yake na Paul. Baada ya kukubaliwa na Mama Tambo, kila mtu katika nyumba yake alishamwambia jinsi ya kuishi na Ishimwe. Matilda alikuwa na haiba ya ucheshi sana, kitu kilicho mrahisishia Ishimwe, na kujisikia kuwa huru kutoa maoni yake katika kila zawadi alizokuwa ameletewa.
Magauni yote mawili yalimkaa vizuri sana, akabakiwa na kazi ya kuchagua tu. “Umemchanganya vibaya Paul, wewe?” Matilda alimchokoza Ishimwe, mbele ya mama Briana wakati wanajaribisha nguo chumbani. “Akili ya Paul haifanyi kazi kabisa! Kama siye yeye!” Matilda aliendelea. Vilijaa vicheko kati yao kwani Matilda alikuwa akimtania kila mtu aliyekuwepo pale mpaka mama Briana aliyekuwa mgeni kabisa kwao.
Hakuacha kumtania na mama yake kila alipomuona amekuwa kimya sana alimtupia maneno mawili matatu.Walizunguka madukani kutafuta nguo za mama Briana pamoja na vitu vingine ambavyo wangehitaji kwa ajili ya harusi. Baadaye walipata Saluni ambayo Matilda aliridhika nayo, na kuona itamfaa wifi yake.
*********************
Walikuwa wameshazunguka sana na wote walikuwa wamechoka, walihitaji kitu baridi, kuburudisha koo. Waliamua kuingia kwenye mgahawa mzuri sana na ulionekana wa hali ya juu. Mama Tambo ndiye aliye papendekeza hapo na kusema ni mojawapo ya Mgahawa anayoiamini.
Hakuwa akila hovyohovyo, kila mahali. Alikuwa na sehemu zake maalumu ambazo alizikubali kukaa na kunywa, lakini mara nyingi alipenda kula chakula kilichopikwa nyumbani kwake. Wote waliingia na kukaa kwenye meza moja.
“Nataka ukitokea kanisani, Paul azidi kuchanganyikiwa. Tena tukitoka tu Shinyanga kwa mama, hakuna kurudi pale kwenu. Tunaenda zetu kukaa hotelini mpaka siku ya kubariki ndoa yenu.” Matilda aliongeza. “Kwa nini mkae hotelini? Karibuni kwangu kwa hizo siku mbili. Kuna vyumba vyakutosha.” Mama Briana aliingilia.
“Kweli?!” Matilda akauliza. “Hamna shida.” “Sitaki tukusumbue.” “Hamna usumbufu. Ndio nitafurahi kukaa na bibi harusi wangu.” Ishimwe alikuwa kimya muda wote, mama Tambo alishajua kinachoendelea kichwani mwa Ishimwe. Cheko yote, ilimuisha.
“Katika hiyo mipango yenu yote ya kumchukua Ishimwe kwa siku hizo mbili kabla ya harusi yao, mmemshirikisha Ishimwe mwenyewe? Maana nawasikia mkipanga tu bila hata kumuuliza mwenyewe.” Mama Tambo aliuliza mara baada ya kuagiza kinywaji alichotaka, na kumfanya Matilda na mama Briana waliokuwa wakiendelea na mipango ya harusi, kumgeukia Ishimwe.
“Eti wifi wa mimi, kwema? Mbona umepooza gafla?” “Na Paul naye?” Ishimwe alijibu kwa kuuliza swali na yeye, mama Tambo akatabasamu na kugeukia pembeni. Matilda alikuwa hajaelewa. “Paul hatakuwa na neno. Mimi nitaongea naye?” “Huyu naye mzito kuelewa!” Mama Tambo aliongeza na kumfanya Matilda ashindwe kuelewa zaidi.
“Kwani nini?” Matilda alimwangalia mama yake. “Unaniangalia nini mimi? Muulize mwenyewe?” “Kwani vipi wifi.” Mama Briana alianza kucheka, nakusema, “Kweli Ishimwe kamwambukiza mwanae kila kitu. Tabia zao sawasawa!” “Sio hivyo. Nikiondoka nani atampikia, halaf…” Ishimwe alisita nakumfanya Matilda aanze kucheka sana.
“Bwana Paul safari hii kapatwa! Ndio maana kabadilika kabisa kaka yangu! Kwa hiyo wewe unafikiri huyo Paul kwa hizo siku mbili tu, atakufa au?” Mama Briana alizidi kucheka na kuongeza. “Na mwanae yupo hivyohivyo.” “Nina hamu kweli ya kumuona Sonia.” “Acha kimbelembele Matilda. Nishakwambia alhamisi anakuja nyumbani. Wewe fanya yako niliyokuitia hapa, basi.” Mama Tambo alijibu.
“Kazi uliyonipa mama yangu mbona naifanya vizuri tu. Nitakuletea mkweo pale kanisani, utamshangaa kwa kupendeza. Lakini mimi shida yangu mwanangu Sonia.” “Nimekwambia Sonia atakuja nyumbani.” “Si anakuja nyumbani kwako wewe mama Tambo? Kwani mimi nikienda kumuona leo kuna shida gani?” “Unataka kuwepo kwenye harusi ya Paul au unataka kuondoka na ndege ya usiku huu kurudi kwako?” Matilda alianza kucheka sana.
Kisha akaongeza. “Na msifikire Mama Tambo ananitania hivyoo?” Matilda alimuuliza Ishimwe na mama Briana. Ishimwe alianza kucheka huku ameinama. “Oooh! Namjua huyu, dakika tano nyingi. Sasa hivi utaona ninafuatwa na watu hapa nasindikizwa uwanja wa ndege kama utani.” Mama Tambo alikuwa kimya kama hamsikii.
“Huyo ndio Mama Tambo mwenyewe! Si mmetuona tunavyofanana?” “Huwezi kufanana na mimi hata kidogo.” Matilda alizidi kucheka. “Bwana Mama Tambo ana watu wake. Halafu itabidi nije kuongea na Paul vizuri. Sijui kampa nini Mama Tambo bwana! Anapendwa yeye, mpaka wajukuu zake!”
“Hapa nimemletea nguo ya kuvaa kwenye harusi kwa lazima. Kila nilipokuwa namuuliza nikuletee nguo gani ya kwenye harusi, akawa ananijibu eti yeye anachotaka nguo za watoto wa Sonia tu. Lakini usifikiri wajukuu ndio hao tu, anawajukuu zake kibao, mpaka wengine wakizungu, lakini hutamsikia akikuagiza nguo au zawadi za hao wajukuu zake wengine hata mara moja.” “Sasa niliwasomesha nyinyi kwa nini, kama mnashindwa kuleana? Sonia hajawahi kula hela ya Tambotokea anazaliwa yule mtoto.” Matilda alianza kucheka tena.
“Basi mama, tushamjua mrithi wako. Maana watu wote tulikuwa tunaulizana mrithi wa Mama Tambo nani? Hakuna mwenye jibu. Lakini leo nimeshamjua, na nitawaambia kina kaka waache kujipendekeza kwa Mama Tambo, hawatapata kitu. Mwenye mali kaja.” “Kumbe nyinyi mlifikiri mtarithi mali zangu?” “Kumbe! Sisi si ndio wanao, au?” “Hata kijiko, hampati.” Mama Tambo alijibu tena.
“Na hatanii hivyoo! Muoneni hivyohivyo Mama Tambo. Tabia yake, harudiikuongea jambo lolote, kwanza haropoki. Kila neno analolitoa mdomoni mwake ujue kalifikiria. Tangia tumezaliwa sisi wote wanne, ndio safari hii kwa mara ya kwanza, amejirudi kwa jambo alilosema HAPANA. Ndio maana kila mtu anakuja kushuhudia aliyemudu kuweka mapinduzi kwa mara ya kwanza katika historia ya familia ya Tambo. Haijawahi kutokea. Ishimwe ndio mwanadamu wa kwanza.”
“Na wala haitakaa ikatokea tena.” Mama Tambo alimalizia na kumfanya Matilda aanze kucheka tena, lakini Mama Tambo hakuwa hata na tabasamu usoni. “Si mmemsikia mwenyewe? Mi nakwambia wewe wifi yangu unabahati ya pekee. Mama Tambo akishasema hapana. Ujue ni HAPANA. Wanae wale wawili wakubwa, watakusimulia habari za Mama Tambo vizuri. Afadhali mimi kidogo nilipona kidogoo na kasheshe za Mama Tambo. Paul ndio hamjui kabisa huyu. Kwa Mama Tambo, Paul ni kama malaika.” “Sababu sio mkorofi je?” “Mmmmh!!!” Matilda aliguna.
“Hamkosei sababu! Badala angenipenda mimi mziwanda wake, basi watu wote wanajua Paul ndio mziwanda wa Mama Tambo. Tulikuwa tunasema tangia watoto kuwa Paul peke yake ndio mtoto wa Mama Tambo, wengine alituokota.” Mama Briana mpenda kucheka yeye ndiye alikuwa akicheka sana, Ishimwe alikuwa akimwangalia Mama Tambo kwa kwa kujiiba, lakini alikuwa akicheka taratibu kila wakati huku ameinama.
“Maneno mengii, utanifanya nichelewe ndege yangu. Nataka kurudi kwangu leoleo.” “Leo ndio tunaondoka mama? Si tungelala?” “Wapi?” “Si hata hapa kwa Paul? Eti wifi?” “Ningefurahi sana, kama tungerudi wote nyumbani.” “Usimsikilize huyo! Mimi nina mipango yangu mingine. Nataka leo niwe kwangu. Na wewe tunaondoka wote, hakuna kubaki huku. Umesikia Mat?”
“Mimi tena? Mbona nimekusikia vizuri tu. Mipango inayofuatwa si ni yako tu, siku zote?” Mama Tambo alimwangalia Matilda. “Si kwa kuwa mipango yako mizuri mama na wewe!” “Hebu mpigie simu Paul aje amchukue Ishimwe sisi twende uwanja wa ndege.” “Hatuli?” Matilda alimchokoza tena mama yake.
“Sili vyakula vya mitaani. Nitakwenda kula kwangu.” “Mwenyewe Mama Tambo huyo! Ndio maana mwenyewe afya yako nzuri. Huzeeki!” “Bwana hebu mpigie Paul simu.” Mama Tambo alikaza sauti. “Yes Ma'am!” Matilda alijibu na yeye akiwa amekaza sauti. Mama Tambo akaguna.
Pale Unapoketishwa Na Wakuu.
Huku kwa Paul. Alipofika tu ofisini kwake, kabla ya kuingia ndani ya ofisi yake, aliomba mmoja wa secretary wake apige simu kwenye benki anayofanya kazi Sam, aulizie jina hilo kwenye kitengo cha IT kisha amuunganishe na simu yake ya mezani, ofisini kwake.
Asubuhi hiyo Sam na yeye alikuwa kwenye mkutano na viongozi wa benki hiyo wakati secretary wao, alipoingia mkutanoni, kumwambia Judge Mkuu yupo kwenye simu anamsubiria, anataka kuzungumza naye. Viongozi wote walimgeukia Sam kwa mshituko, CEO akauliza, “Kuna nini Sam!?” Sam akiwa amepaniki kupigiwa simu na mkwewe asubuhi hiyo alisimama kwa haraka.
“We Sam vipi?” Mr. Mwansasu alimuwahi kabla ya kufungua mlango. “Ni baba yake Sonia?” Sam alijibu kwa kifupi. “Sonia, Sonia?” “Ndiyo, Sonia wangu. Tutaongea baadaye.” Sam alijibu na kutoka kwa haraka. Ukimya mkubwa ulitanda kwenye chumba kile cha mkutano kila mtu akijiuliza maswali.
Baada ya muda kidogo Sam akarudi. Kila mtu alibaki akimwangalia Sam kama kutaka kujua au kuthibitisha habari zilizokuwa zimevuma, kwani wote walimfahamu Sonia na Sam. Lakini hawakujua kama ndiye mtoto mpya ambaye magazeti yalikuwa yameandika.
*********************
Baada ya Paul kumtambulisha Ishimwe mahakamani kama mama watoto wake, na kuonekana wakipeana mabusu nje ya mahakama hiyo, magazeti mengi yalipambwa na kashfa ya vichwa vya habari tofauti tofauti, ‘Judge Mkuu alizwa kwenye mapenzi.’ Magazeti mengine yaliandika, ‘Judge Mkuu alea watoto wawili mapacha wasio wake.’
Na magazeti mengine, ‘DNA yamtoa chozi Jaji Mkuu wa Tanzania.’ Na mengine yalishaandika. ‘Judge Mkuu azidiwa mahesabu na mkewe.’ Mengine yaliandika. ‘Hakuna ujanja kwenye mapenzi. Hata Judge Mkuu alizwa na mwanamke.’ Zilikuwa kashfa nyingi za kuumiza, lakini zilimudu kwa siku mbili tu, kwani bila kutarajia, zilizimika gafla bila jibu lolote.
Hakuna magazeti yaliyoandika tena habari za Paul. Lakini Paul alijua ni kazi ya mama yake, ndiye aliyezima zile kelele. Na ni magazeti machache sana, ambayo yalionyesha habari ya Ishimwe akiwa amekumbatiwa na Paul. Yenyewe yalitoa ujumbe mzuri kidogo. ‘Mke halali wa Jaji Mkuu arudi kumfuta machozi mumewe.’ ‘Baada ya kupotea kwa muda mrefu sana, mke halali wa Jaji Mkuu arejea.’ Na mengine yalitoa maelezo, ‘Baada ya ndoa ya Jaji Mkuu kugonga mwamba na kuambulia patupu katika swala la watoto, hatimaye mkewe wa zamani arejea na mtoto wa halali wa Muheshimiwa.’
Hata sura ya Ishimwe haikuonekana vizuri pichani, katika magazeti hayo, na wala Sonia mwenyewe hakuwahi kutokea kwenye magazeti hayo hata mara moja. Kwa hiyo lilibaki fumbo kubwa sana kwa wa Tanzania, wakitaka kumjua mtoto huyo wa Jaji Mkuu wa Tanzania. Nayo hiyo pia, ilikuwa kazi ya Mama Tambo.
*********************
“Samahanini sana kwa usumbufu wakubwa, ilikuwa simu kutoka kwa baba yake Sonia. Lakini sasa hivi tunaweza kuendelea” “Hebu subiri kwanza Sam, acha kuongoza kikao.” Mr. Mwansasu aliingilia na kufanya kila mtu acheke.
“Kumbe Sonia ndiye huyo mtoto wa Jaji Mkuu?” Sam alicheka kidogo bila kujibu ndio au hapana. “Ndio maana!!” Mwingine aliitikia. “Nini sasa?” Sam aliuliza. “Sam! Lazima tuongeze ukaribu Mkuu.” Kila mtu alimtania Sam, kikao kikabadilika, ukawa utani mtupu, hata heshima kwa Sam ikaongezeka.
*********************
Sam na Paul walikubaliana wakutane ofisini kwa Paul kwa mazungumzo, muda wa saa tano kamili asubuhi hiyo. Bila kuchelewa Sam alisimama mbele ya masecretary hao wawili wa Paul, saa tano kasoro tano, akitaka kuonana na Judge Mkuu. Paul alipopigiwa simu, alitoka yeye mwenyewe kwenda kukutana na Sam ili amkaribishe ndani.
Wote walishangaa, kwani kwa kawaida, mgeni yeyote wa kawaida alipokuwa akifika ofisini kwake, na alipokuwa akipigiwa simu kuwa ana mgeni anayetaka kumuona, kama Paul alikuwa na nafasi, alisema aambiwe huyo mgeni aingie ndani, sio yeye atoke nje!
Isipokuwa kwa wageni wake wa heshima sana, akiwepo mama yake, Mama Tambo, ndipo Paul aliposimama na kutoka yeye mwenyewe kwenda kuwakaribisha. Na sasa ameongezeka Sam, aliyepata mapokezi ya heshima.
Akiwa amejawa hofu kama mtoto wa darasa la tatu aliyefanya koso na kuitwa kwenye ofisi ya mwalimu mkuu, Sam alibaki amesimama nje ya ofisi ya Paul, akitetemeka mpaka Paul alipotoka. Paul alimpa mkono na kumtambulisha kwa kila mtu pale ofisini kwakwe.
Alimzungusha ndani ya ofisi chache ndani ya jengo hilohilo akimtambulisha kwa wafanyakazi wenzake. Sam alijisikia vizuri sana, kuona Paul anamtambulishakwa furaha na heshima kubwa. Mfanyakazi mwingine aliyeonekana Mzee kidogo, alionekana kumzoea Paul alijaribu kuuliza kwa utani na Paul akajibu, “Ndiyo bwana! Huyu ndio mwenyewe anaeoa binti yangu.” Paul alimpigapiga Sam mgongoni, kisha wakarudi ofisini kwa Paul.
Paul alitoa tena shukurani zake za dhati kwa yote aliyomfanyia kwa familia yake hasa katika kipindi hicho ambacho yeye hakuwepo. Baada ya hayo yote alimtupia swali la moja kwa moja lililomtoa Sam jasho ndani ya ofisi hiyo iliyokuwa na kiyoyonzi {AC}. “Wazazi wako wapo wapi na wanafanya nini?” Paul hakutaka kumwambia mazungumzo aliyokuwa nayo na Sonia usiku uliopita.
Lakini alitaka kujua Sam yupo mkweli kwa kiwango gani. Baada ya kujikanyaga kanyaga sana mbele ya mkwe wake, hatimaye Sam alijikuta akimwambia ukweli wote Paul, kitu kilichomfurahisha sana Paul.
“Unafikiri utawasaidiaje wazazi wako?” “Sijui kabisa. Nimechanganyikiwa.” Sam alijibu kwa unyonge sana. Paul alimtazama kwa muda na kumuahidi kusaidia kumtafutia wataalamu watakao wasaidia kuwatoa katika hali ile ya ulevi. “Asante sana.” “Lakini si unajua, ni lazima wao wenyewe waamue kuacha ulevi kwanza?Unaelewa kuwa unaweza kumpeleka punda kisimani lakini huwezi kumfanya anywe maji?” Sam alibaki kimya kwa muda.
“Hapo ndipo pagumu sana. Sijui nitafanya nini?” “Lazima nyinyi watoto wote, mkae na wazazi wenu, mzungumze nao kwa mapana, huku mkiwaambia madhara mnayopitia nyinyi kama watoto bila wao kujihusisha na maisha yenu. Na lazima kuwaonyesha umuhimu wa wao kama wazazi kuwepo sasa hivi kwenye maisha yenu hata kama walishindwa kuwalea zamani, lakini bado mnawahitaji. Sijui umeelewa?” Paul aliuliza na kumfanya Sam afikirie zaidi.
“Sikuwahi kuwa na mahusiano kabisa na wazazi wangu.” “Lazima uanze sasa, kwa ajili yako wewe mwenyewe na watoto wako pia.” Sam alivuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha. “Na ndio baada ya hapo, uwaambie yapo matibabu ya kuwasaidia kurudia hali ya kawaida. Tutawatafutia mahali pakuishi, iwe hapa mjini au kuwarudisha kijijini, lakini baada ya kuridhishwa na afya zao.” “Asante sana kwa ushauri. Nitaufanyia kazi juma hilihili.” Paul alimwangalia kidogo kama anayetaka kumkumbusha kitu lakini hofu iliyokuwa ikimzunguka Sam alishindwa kukumbuka kabisa, wakabaki wakitizamana.
“Unakumbuka alhamisi kesho kutwa, tunatakiwa kusafiri kwenda kumuona bibi yenu? Na jumamosi ni harusi yetu, ningependa uwepo.” “Samahani, nilisahau kidogo. Nitashugulikia juma lijalo.” “Harusi yenu mmeipanga iwe lini?” Paul alimrushia swali jingine lililombambaisha tena Sam akishindwa kutoa jibu la moja kwa moja.
“Au hunampanga wa kufunga ndoa na binti yangu? Unataka kuendelea kuishi naye tu bila baraka za Mungu?” Sam alishituka sana. “Hapana. Hapana kabisa. Nataka sana kufunga naye ndoa, lakini bado tupo kwenye kukusanya michango. Michango ndio inasumbua sana. Wengine wanakuahidi mchango leo, ukiwapigia simu hawapokei tena. Yaani ni shida sana. Lakini nampenda sana Sonia. Ningekuwa amri yangu hata kesho ningemuoa. Lakin….” Sam alisha paniki alikuwa akiongea bila kituo huku akionyesha hofu usoni.
Paul alimrushia swali jingine. “Bajeti ya harusi yenu ni kiasi gani?” Sam alisha changanyikiwa, na kusahau kila kitu. Hata Paul angemuuliza jina lake mwenyewe ni nani kwa wakati ule, asingeweza kukumbuka. Paul alibaki akimwangalia kwa muda.
Kisha akamuuliza tena kwa kutomuelewa. “Hufahamu bajeti yako ya harusi?!” “Nafahamu. Nafahamu kabisa. Niliandika. Ni kama… Niii….. Lakini Nyange ndio anatunza mahesabu yote. Yeye ndio mwenyekiti wa kamati ya harusi. Naweza kumpigia simu na kumuliza sasa hivi.” Paul alikuwa ametulia akimtizama, Sam alivuta simu yake huku akiwa anatetemeka. Akafuta jasho kwa viganja vyake huku akipangusa kwenye suruali yake.
“Mambo yamekuwa mengi tu hapa katikati nimepoteza hesabu, lakini nilikuwa nafahamu kila kitu. Kuanzia waliochanga mpaka waliotoa ahadi, wote nawafahamu.” Sam aliendelea kujitetea huku akitafuta namba ya Nyange kwenye simu yake bila mafanikio.
Baada kama ya dakika mbili kupita bila kupata namba ya Nyange kwenye simu yake, Sam aliomba kwenda msalani kwanza. “Naomba kwenda kukojoa.” Paul alishituka kidogo, lakini hakutaka kumuonyesha. Alijua amepaniki sana. Akamuonyesha sehemu kilipo choo, humohumo ndani ya ofisi yake.
“Nilikuwa nayo kabisa, namba ya Nyange. Sijui nani kafuta bwana!?” Sam aliendelea kujitetea kama mtoto mdogo huku akisimama kuelekea chooni. Alijikwaa kwenye kiti kingine kilichokuwa mbele yake, nusura adondoke mpaka chini. Akasimama akiwa anahema hovyo, akajiweka sawa, kisha akaingia chooni, bila Paul kuongeza neno.
Alipoona hali yake inazidi kuwa mbaya, Paul akaamua atoe soda ya kopo kwenye friji ndogo hapohapo ofisini mwake, na kuiweka mezani, ili akirudi amkaribishe, anywe soda baridi, labda atatulia.
Sam alitoka msalani huku akikausha mikono yake kwenye suruali yake ya kaki, ambayo ilionyesha wazi kulowa kwa maji. Paul alimuhurumia. Yaani hata taulo la kukaushia mikono huko chooni, pembeni ya sinki alilotumia, alishindwa kuona, akaamua kujikausha kwenye suruali yake! Hata Paul alijiuliza kwa kumshangaa vile alivyoingia hapo ndani msafi, na kuishia kulowa maji na jasho hapo ofisini kwake.
Akaamua abadili mazungumzo kabisa, wazungumzie kitu cha kawaida alichokizoea Sam, ili atulie. “Unaonaje kazi yako?” Paul alimrushia Sam swali ambalo alijua ni la kawaida sana, mara baada ya kukaa chini, lakini nalo pia lilikuwa swali gumu sana kwa Sam.
Alimzungusha sana Paul, kwa kumtajia kuanzia mwaka alioanza kazi, matawi anayozungukia nchini, idadi ya wafanyakazi waliopo chini yake, mpaka Paul alibaki akiangalia saa yake, kumuashiria muda unazidi kwenda. Kama aliyekuja kuelewa baadaye sana, mwishowe Sam akanyamaza.
Sasa kwa kuwa Paul alikuwa na mambo mengi sana siku hiyo na Sam alionyesha wazi hawezi kutuliza mawazo na kuzungumza naye hata kidogo, Paul aliamua amalizie alichotaka kumwambia Sam, ili waagane na yeye aendelee na shuguli zake.
“Nathamini sana juhudi ulizofanya kwenye maisha yako. Nyumba yako ni nzuri sana, lakini naomba niimalizie kuijenga ili angalau iwe na kila kitu cha muhimu.” “Sawa kabisa.” Sam alijibu kwa haraka sana bila hata kufikiria. Paul alitulia kidogo, Sam akasogelea meza, akanyanyua lile kopo la soda, akafungua na kuanza kunywa mfululizo bila kupumzika wala kukaribishwa, mpaka alipomaliza soda yote ndipo alipo pumzika na kuanza kuchezea hilo kopo kwa kuliminyaminya, huku likitoa milio iliyokuwa ikimkera Paul, lakini Sam hakuwa na habari kabisa na anacho kifanya.
“Nikuongezee soda nyingine?” Paul aliuliza kiustarabu sana, huku akizidi kumuhurumia Sam jinsi alivyo paniki. “Hapana, nimeshiba.” Sam alijibu kama mtoto mdogo. Paul alikunja uso kidogo kushangaa kushibishwa na soda! Lakini akaamua kuendelea ili kufikia angala lengo lake yeye kama la Sam limeshindikana.
“Kwa hiyo kama nilivyokuwa nimekwambia hapo awali, kabla ya Sonia kujifungua, ningependa nyumba iwe imekamilika, na kama unavyoelewa hatuwezi kuitengeneza mkiwa mnaishi mle ndani. Lazima muhame kwa muda ili kupisha ujenzi.” “Bila shaka.” Sam alijibu tena bila kufikiria na Paul alishajua anamjibu tu bila kufikiria.
Akaamua safari kii amfanye afikirie. “Umeshajua sasa mtahamia wapi na Sonia?” Paul alirusha tena swali jingine lililomfanya safari hii Sam kufikiria. “Umesema inabidi tuondoke pale?” Hatimaye akauliza. “Ndiyo. Au ulifikirije?” Sam alirudi nyuma ya kochi akakaa vizuri akafikiria.
“Mshahara wangu wa mwezi huu, nina makato mengi sana. Naomba ujenzi uanze mwishoni mwa mwezi ujao, nitakuwa nimepata pesa ya kutafuta angalau chumba kimoja cha kuishi na Sonia kwa kipindi hicho tunachopisha ujenzi.” Sam alijibu, na kumfanya Paul atabasamu. Alimuona jinsi alivyotulia sasa na kuweza kufikiria na kutoa majibu yakueleweka.
“Naona sasa hivi akili imetulia, tunaweza kuzungumza.” Paul alijibu na kujiweka sawa kwenye kiti.
“Sasa ni hivi, ipo nyumba ndogo pale pembeni ya nyumba tunayoishi sasa hivi mimi na Ishimwe. Watoto wote wa Tambo ndio tumezaliwa na kukulia hapo. Kwa sasa hakuna mtu yeyote anayeishi humo. Mnaweza kuishi hapo kwa muda wakati tunafanya ujenzi kwenye nyumba yako.” “Sonia anafahamu juu ya haya tunayozungumza?” Sam aliuliza akiwa ametulia.
“Wewe ndio wa kwanza kukwambia, kwa kuwa ni nyumba yako, nisingependa kukubaliana na Sonia au Ishimwe halafu uje kukataa.” “Sina shida kabisa juu ya hilo. Nashukuru sana, angalau mtoto wetu, atakuja kwenye mazingira mazuri.” Sam alitulia kidogo kama anayefikiria jambo lililopita kichwani mwake.
Akakosa jibu, akaamua amuulize. “Sasa nimwambie nini Sonia?” “Vyovyote vile utakavyo. Lakini tu, hakikisha anakubali kuja kuishi pale na sisi. Hilo ndilo ombi langu kubwa sana kwako. Nataka tuwe naye karibu sana, ili kujenga mahusiano ya karibu na Sonia, na nina fikiri wewe ndiye utakuwa msaada mkubwa sana, wa kuniunganisha na binti yangu.” “Bila shaka.” Sam alijibu tena harakaharaka na kubaki akimwangalia Paul. “Kazi njema.” Paul aliamua kumuaga ili aendelee na kazi zake.
*********************
Alipofika tu kwenye gari akatoa simu yake na kumpigia Nyange. Wakati Nyange amepokea, Sam akabaki anashangaa. “Sam! Vipi?” “Daah! Nimeharibu kaka.” “Nini tena?” “Yaani ndio natoka ofisini kwa baba yake Sonia, sijui niliingiwa na nini bwana, yaani mpaka namba yako ya simu nilisahau, ndio nimetoka sasa hivi ofisini kwake nipo hapa kwenye gari, nakumbuka namba yako ya simu.” Nyange alianza kucheka.
“Sikutanii kaka. Kama dakika mbili Paul anasubiri nipate namba yako ya simu nikupigie, ili unitajie bajeti ya harusi yetu ni kiasi gani, lakini nimetafuta namba yako kuanzia mwanzo mpaka mwisho kwenye orodha ya majina yaliyopo kwenye simu yangu, kwani nimekuona?”
“Acha masihara Sam! Wewe hujui bajeti ya harusi yako?” “Nilisahau kabisa kaka, ndio nakumbuka kila kitu sasa hivi! Mpaka kiasi cha pesa watu walichoahidi na waliochanga pia, eti sasa hivi ndio nakumbuka! Nakwambia nilichanganyikiwakaka, mpaka nikaomba ruhusa kwenda chooni, kama mtoto mdogo!”
“Nimekuta ameweka soda mezani, hata sikumbuki kama alinikaribisha, nikainywa yote bila kupumzika! Kama nilikuwa na njaa bwana, wakati nimetoka kunywa chai! Nimeharibu sana kaka yangu, sijui atakuwa amenielewaje?” Kama aliyekuwa amerudishiwa ufahamu wake, Sam alianza kukumbuka tukia moja hadi jingine na kubaki akijidharau sana. Nyange ndio alikuwa akicheka kama ametekenywa.
*********************
Kabla Matilda hajapiga simu, Paul naye akampigia simu Ishimwe. “Vipi?” “Safi tu, pole na kazi.” Ishimwe alijaribu kuongea kwa sauti ya chini kwa kuwa wote pale mezani walikuwa wakimsikiliza. “Asante, pole na wewe na kuzunguka.” “Asante, tumekuwa na wakati mzuri sana.” “Safi sana. Mmeshamaliza?” Paul akauliza.
“Ndiyo. Lakini mama anataka warudi nyumbani, Shinyanga leo, njoo unichukue.” “Mpe simu Mat, nataka kuongea naye.” Ishimwe alimpa simu wifi yake, wakaongea kidogo na Paul, akamrudishia simu Ishimwe. “Nitakuona baada ya muda mfupi.” “Sawa.” Ishimwe alikata simu na kubaki akiiangalia simu yake. Mama Briana aliaga, akaondoka na vitu vyake walivyomnunulia kwa ajili ya harusi.
*********************
Baada ya muda mfupi Paul alifika hapo, akambusu Ishimwe na kumsalimia tena mama yake. “Nyinyi ndio mnaofanya mawifi wawachukie wake zenu. Sasa kilichokushinda kunibusu na mimi ni nini?” Paul alianza kucheka. Akasimama na kumbusu Matilda. “Hakuna hata mmoja wenu wakumchukia Ishimwe.” Mama Tambo aliongeza. “Mbona tushakuelewa mama jamani!” Matilda alilalamika na kuongeza.
“We Paul, msubiri kaka yako usikie habari na mkwara wa Mama Tambo aliotupa juu ya Ishimwe. Kila mmoja wetu ameambiwa aje na adabu zake zote hapa kwenye harusi yako.” Paul alicheka taratibu akiwa anajua wazi anachoongelea mdogo wake. Ishimwe alibaki ameinama akifikiria.
Paul alimgusa. “Vipi umepata kila kitu ulichokuwa unahitaji.” “Na zaidi, maana vingine nilikuwa hata sivifikirii, lakini Matilda amenionyesha na mama amelipia kila kitu.” “Safi sana.” Paul alijibu na kumgeukia mama yake aliyekuwa kimya kabisa kana kwamba hayupo pale. “Asante sana mama.” Mama Tambo alitabasamu.
“Umeniamini sasa Ishimwe?” Matilda aliingilia. “Tangia asubuhi wakati tupo na mama, ulimuona akicheka au hata kutoa tabasamu? Amekuja tu Paul hapa, kampa tu asante, muone alivyotabasamu! Yaani Mama Tambo bwana! Mimi nimehangaikanaye tokea asubuhi kukupendezesha mkwewe, hata asante hajanipa.” “Acha kulalamika Mat. Mama amechoka!” “Ona wanavyoteteana. Ndio kazi yake Paul. Huwezi kumsema mama akiwepo. Ndio maana tulikuwa tunamtenga huyu! Mama anamuona Paul kama malaika.” Mama Tambo akasimama. “Nitawaona hiyo siku ya alhamisi.” Alivuta pochi yake nakutoka nje.
“Bwana Mat. Mwache mama bwana! Mkifika nyumbani mfanye apumzike! Umri umekwenda, msaidie apate muda wa kupumzika.” “Ushawahi kumuona mama yako akipumzika? Hapo anamipango kibao huko nyumbani kwake, ndio maana hataki kulala hapa Dar. Tumeacha nyumba imejaa watu kibao, anaandaa nyumba yake sababu ya huo ugeni wa alhamisi.” Ishimwe alisimama na kumkimbilia Mama Tambo. Alimuacha Paul na Matilda wakishangaa. Mama Tambo alishapanda kwenye gari.
“Vipi Ishimwe?” Mama Tambo aliuliza. “Nilitaka kukushukuru mama.” Machozi yalianza kumtoka Ishimwe. “Asante kwa kunipokea, na….” Ishimwe alishindwa kuendelea alibaki amesimama huku ameinamisha kichwa chake chini akilia.
Alishtukia Paul amemshika bega. “Tunakushukuru sana mama. Asante kwa kila kitu.” Paul aliamua kumalizia maana Ishimwe alishindwa kabisa kuongea. Matilda naye alipanda ndani ya gari na kubaki kimya. “Karibu sana Ishimwe kwenye familia yetu. Tutaongea mengi mtakapokuja nyumbani.” Ishimwe alitingisha kichwa kukubali huku akifuta machozi. Dereva aliondoa gani na kuwaacha bado wamesimama.
Hatimaye..
Siku ya alhamis, Paul alimka akiwa na furaha sana. Walitoka asubuhi sana mpaka nyumbani kwa Sonia. Waliwakuta wote wapo tayari kwa safari. Magari mawili yaliongozana mpaka uwanja wa ndege wa Dar es salaam. Moja alikuwepo Ishimwe, Paul na Kana, pamoja na mlinzi wa Paul kama kawaida ya Paul kuzunguka na mlinzi wake kila mahali, na gari jingine alikuwepo Sam na Sonia, wakiendesha na dereva aliyekuja na hilo gari akiwa na Paul na Ishimwe. Sam alimfuata Kana nyumbani kwa Nyange asubuhi sana na kurudi naye pale nyumbani kwake wakiwasubiria Paul na Ishimwe waje ili waende uwanja wa ndege.
Waliondoka uwanjani hapo majira ya asubuhi ya saa mbili na ndege ya serikali. Hapakuwa na abiria yeyote isipokuwa, Paul, Ishimwe, Sam, Sonia na Kana, pamoja na mlinzi wa Paul. Bado ilikuwa ni mapema tu wakati ndege hiyo ndogo ilipokuwa ikituwa katika viwanja vya mjini Shinyanga.
Sonia alijawa na hofu na maswali mengi. Paul akamuita kabla hawajashuka kwenye ndege. “Usiogope, watu wote wako hapa wakitaka kujenga undugu na wewe, mama yako na Kana. Kwa hiyo usiwe na wasiwasi, kila kitu kitakuwa sawa.” Tumbo la Sonia lilishakuwa kubwa kabisa, liliweza kuonekana. Paul alimtengeneza vizuri gauni alilokuwa amevaa, kama mtoto mdogo, akamshika mkono na kushuka naye.
“Sam, karibu sana nyumbani kwetu.” “Asante sana.” Sam alishukuru kwa heshima zote. Ishimwe naye hakuwa mbali na Paul, lakini karibu sana na Kana na Sam. Walikuta watu wa wachache ambao yeye Paul aliweza kuwatambua wote, lakini sio alioongozana nao.
Paul alimwachia mkono Sonia, akamsogelea mama yake, akamkumbatia na kumsalimia. Dada yake mkubwa Paul alimsogelea Paul wakakumbatiana na hivyohivyo kwa upande wa kaka yake. Sonia alijisogeza pembeni kama kumpa nafasi baba yake kusalimiana na ndugu zake, lakini hakuwa naye mbali sana, alibaki amesimama pembeni ya baba yake huku ameangalia chini, na wengine wote walikuwa kimya kabisa wakisubiri utambulisho. Walianza kutaniana mambo mawili matatu huku wakicheka sana.
“Sikujua kama na wewe utakuwepo leo? Nilijua ni familia tu.” Paul aliuliza huku akimwangalia mama yake, na tabasamu la mshangao usoni. “Si Junior huyo! Ametua tu jana usiku, akamtuma mtu lazima leo tuonane. Ndio nikaamkia kwa Mama Tambo asubuhi asubuhi. Hata chai nimekunywa kwa Mama Tambo. Sikujua kama na wewe utakuwepo. Hongera kwa familia dogo.” Yule mtu alimpa tena mkono Paul.
“Asante kaka. Sasa hivi nasubiri mjukuu wa pili bwana! Mkubwa huyu hapa.” Paul alimvuta Kana karibu yake na kumtambulisha yeye wa kwanza. Lakini ile sauti ya yule mtu aliyekuwa akiongea na Paul, akisema ameitwa na Junior, kaka yake Paul, ilimfanya Sonia anyanyue macho na kumtizama, kwani haikuwa ngeni kwa Sonia hata kidogo. Taratibu mapigo ya moyo ya Sonia yalianza kubadilika, jasho lilianza kumtoka, akaanza kujipepea.
“Maamaa!” Sonia aliita kwa sauti ya chini sana kama aliyekuwa amebanwa pumzi akijaribu kuhema kwa shida. Sababu ya kelele na vicheko vilivyokuwa vikiendelea kati ya Paul na ndugu zake hakuna aliyekuwa anamsikia Sonia. “Saam!”Sonia aliita tena kwa sauti ya juu, gafla alipatwa na kizunguzungu.
“Paul mdake Sonia anaanguka.” Mama Tambo alipiga kelele kwa sauti sana, akakimbia yeye mwenyewe mama Tambo na kumdaka Sonia kabla hajafika chini. Kwa haraka sana Paul naye aligeuka na kumpokea Sonia mikononi mwa mama yake, akiwa amepoteza fahamu kabisa palepale uwanjani.
“Nisaidie Martha!” Paul alisikika akipiga kelele huku amembeba Sonia akiomba msaada kwa dada yake ambaye ni daktari. “Tulia Paul. Muweke chini kwanza, halafu lazima apate hewa.” “Siwezi kumuweka chini mwanangu.” Paul alijibu huku akiondoka akiwa amembeba Sonia. “Mama, hembu ongea na Paul, mwambie aache kupaniki bwana! Unaenda wapi sasa Paul?” Dada yake alimuuliza, Ishimwe alianza kulia akiwa anamfuata Paul kwa nyuma.
“Namrudisha kwenye ndege, tuwahi hospitalini.” Paul alijibu. “Hapana bwana Paul! Kumbuka ‘first aid’.” Martha aliendelea kumsisitiza Paul aliyeonekana kama hana anachoelewa tena. “Mama, ongea na Paul, amepaniki.” Kwa mara ya kwanza watu kumuona Mama Tambo kwenye mshituko, alikuwa kimya kabisa nakushindwa kuongea.
Kaka yake Paul alimkimbilia Paul na kusimama mbele yake. “Namuomba huyo mtoto, Paul.” “Hapana Junior, namuwahisha hospitali.” Tayari machozi yalishaanza kumtoka Paul. “Hebu niangalie kwanza Paul.” Paul aliendelea kuongeza mwendo. “Mwambie rubani awashe ndege, tunarudi Dar, sasa hivi, kimbia. Nimesema sasa hivi.” Paul alikuwa akipiga kelele huku akimuamuru mlinzi wake, alimzunguka kaka yake akaendelea na safari yakurudi kwenye ndege.
Kaka yake alisogea tena kwa haraka na kumshika bega kwa nguvu. “Hey Paul! STOP!” Junior kaka yake Paul alisimama mbele ya Paul tena. “Come’on man! Look at me. Do you wanna kill your Babygirl? She needs help, RIGHT NOW, HERE, FIRST, then we all gonna take her to the hospital. Come’on now!” Taratibu Paul alimkabidhi Sonia kwa kaka yake. “Come ‘on Babygirl, I gotch you, gotch you sweetheart. You gonna be fine, veeery fine. I gotch you baby.” Junior aliendelea kumpokea kwa upendo sana Sonia, huku akisema maneno mazuri, taratibu, kwa upendo, kumfanya kila mtu atulie.
Kilikuwa kitendo cha muda mfupi kilichobadilisha madhari nzima ya eneo lile. Vicheko vyote viliisha, ikabaki hali ya kuchanganyikiwa kwa kila mtu.
Kwa mara ya kwanza, Kana alisikika akimwita Sonia, “Mama! Mama!” Akiwa analia sana. Dada yake mkubwa Paul Martha, ambaye alikuwa ni daktari, aliomba Sonia alazwe chini kabisa, chali apepewe. Paul alikuwa kwenye mshituko mkubwa sana.
“Nini kimempata mwanangu?!” Paul aliendelea kulalamika. Mama yake akamsogelea karibu na kumshika mkono. “Nisaidie mama yangu, sitaki kumpoteza mwanangu!” Paul alimsihi mama yake aliyezoea kumuona akifanya mambo mengi asijue katika swala ya uhai, hakuna mwanadamu anayeweza kuhusika, isipokuwa Mungu pekee.
*********************
Walianza kumpepea Sonia, huku Martha akipima pressure yake kwa kushika kiungo cha kiganja chake na mkono. “Mlimpima pressure kabla ya kuanza safari?” Martha alimuuliza Paul mdogo wake. “Hapana.” “How could you do that, Paul?!” Martha aliuliza kwa ukali. “Mnawezaje kusafiri na mtoto akiwa mjamzito bila kumpima?” Martha aliendelea kuuliza kwa kulaumu na ukali.
“Alikuwa mzima kabisa!” Ikawa kama anayejitetea kwa dada yake. “Come ‘on Paul, your smart than that! Unawezaje kumwangalia tu nakusema ni mzima? Unasafirije naye, huna hata mashine ya kupimia pressure! Ndege yenyewe haina hata boksi la huduma ya kwanza, ‘first aid’. How could you do that?” Aliendelea kumgombesha mdogo wake. Paul hakuwa hata na uwezo wakujitetea, alijiona kweli alikosea.
“Hey! Hey Martha! Kugomba hakuta saidia sasa hivi. We need your help, right NOW. Stay focus, please!” Kaka yao aliingilia. “Pressure yake ipo juu sana. Lazima tumuwahishe hospitalini sasa hivi, ili waishushe.” Martha aliendelea kuongea huku akimwangalia Sonia.
“Mwambie rubani awashe ndege.” Paul alimwambia mlinzi wake. “Ipo tayari.” Alijibu. Paul alimnyanyua mtoto wake na kuelekea naye kwenye ndege. Kila mtu alifuata nyuma. “Piga simu hospitali, nataka nikute gari ya hospitali ikitusubiri uwanja wa ndege wa Mwanza, tena wakiwa na vitu vyote vya huduma ya kwanza, mwambie ni mjamzito na pressure ipo juu sana. Baada ya dakika chache tutakuwa hapo. Piga sasa hivi.” Paul aliendelea kutoa maagizo. Wote waliingia ndani ya ndege.
“Humu ndani kuna hewa nzuri. Mlaze tena chini.” Martha alimwambia Paul. Mama Tambo ndio alikuwa mtu wa mwisho kuingia kwenye ndege, alikuwa akiongea na simu. Aliingia ndani ya ndege, moja kwa moja, akamsogelea Paul. “Nimeongea na daktari wa wawakina mama, yupo njiani kuelekea uwanja wa ndege, tutakuta anatusubiri.” Kisha akamgeukia mlinzi wa Paul, “Mwambie rubani aondoe ndege sasa hivi.” Mama Tambo alikaa na kufunga mkanda.
Taratibu baada ya ubaridi kumpiga vizuri, Sonia alifumbua macho. Aliwaangalia kwa muda akamgundua baba yake, na kuanza kulia. “Pole sana Sonia.” “Naogopa sana baba.” “Usiogope Sonia. Kila kitu kitakuwa sawa.” Paul alianza kumshikashika kichwa kama kumbembeleza lakini alikuwa akitetemeka sana kwa hofu.
Kila mtu alisimama kumsogelea. “Hapana jamani! Hamuezi kumzunguka, anahitaji hewa. Naomba mrudi kwenye viti vyenu, mfunge mkanda. Paul wewe endelea kukaa hapo hapo chini akuegemezee kichwa.” Martha aliendelea kutoa maelezo. “Mbona anatetemeka sana!? Au baridi?” Paul alilalamika.
Sonia alizidi kulia, huku akitetemeka zaidi na kukakamaa mwili mzima. Paul aliogopa sana. “Man up, Paul! You can’t cry Infront of your baby!” Kaka yake alijaribu kumsemesha Paul aliyeanza kutokwa na machozi.
“Mama! Mama!” Sonia alianza kuita tena huku amefunga macho, akilia sana. “Paul! Hembu mpishe Ishimwe, yeye ndio ampakate. Labda atatulia. Lazima atulie, lasivyo hiyo pressure itazidi kupanda.” Martha aliyekuwa amemshika mkono Sonia alitoa wazo.
“Sasa nyinyi wote mnalia jamani! Nani atamtuliza huyo mtoto? Hebu wifi jikaze bwana! Paul simama mpishe Ishimwe.” Matilda aliyekuwa kimya muda wote aliamua kuingilia. Taratibu Martha alimpokea Sonia kutoka kwa baba yake, Ishimwe akakaa na yeye chini kabisa katikati ya viti vya ndege akampakata Sonia.
Kama kawaida yake, alinza kuzungumza naye kilugha, taratibu. Hakuna aliyeelewa hata kidogo, lakini Ishimwe aliendelea kuongea naye maneno yaliyomfanya Sonia kuanza kutulia. Baada ya muda Sonia alifungua macho lakini ndege ikiwa inatua jijini Mwanza.
Kama alivyosema Mama Tambo, walikuta gari ya hospitali ikiwasubiri uwanjani hapo. Kilisogezwa kitanda chenye magurudumu tayari kumbemba Sonia. Waliingia vijana wawili wenye nguo za hospitali, wakataka kumbemba Sonia, Paul akakataa akitaka ambembe mwenyewe.
“Hapana Paul, huwezi kumbeba vizuri. Hawa wana uzoefu wa kubeba wagonjwa. Sonia anahitajika ungalifu sana, maji ya uzazi/uchungu yanatoka. Anahitajika utaalamu katika kumnyanyua.” Martha alimshitua kila mtu mle ndani. Sam alisimama kama mchale. “Mungu wangu!” Paul alisimama na yeye na mikono kichwani. “Sikutaka kuwaambia tokea mwanzoni, lakini nilijua tu hili litatokea kama tusipowahi kushusha hiyo pressure. Ipo juu sana.” Matha aliongeza.
“Nilisema mje na huduma ya kwanza. Iko wapi?! Na huyo daktari yuko wapi?” Mama Tambo aliuliza. “Kwenye gari, mama.” Mmoja wao alijibu. “Alaa! Kwenye gari wakati mgonjwa yuko hapa!?” Mama Tambo aligomba. Wale vijana walishuka, baada ya muda mfupi daktari akaingia.
“Shikamoo Mama Tambo.” “Huyo ni mjukuu wangu. HAKIKISHA hatupotezi huyo mtoto.” Mama Tambo alijibu kwa kutoa maagizo. Watu wote walisogea kumpisha huyo daktari, kasoro Paul na Ishimwe aliyekuwa amempakata.
Daktari alianza kumpima na mashine aliyokuwa amekuja nayo. “Naomba mnipishe.” Yule daktari aliongea mara baada ya kumpima Sonia, lakini Paul alibaki amesimama bila ya kujibu kitu wala kuondoka kama wengine walioanza kushuka kwenye ndege ili kupisha.
“Ni kweli hawezi kufanya kazi wakati watu wote mmemsimamia hivyo. Shukeni chini.” Martha aliongeza. “Paul!” “Siwezi kushuka na kumuacha mtoto wangu hapa. Kama hawezi kufanya kazi mimi nikiwepo, aondoke nitafute mtu mwingine.” Paul alimjibu dada yake kwa ukali sana, na kumgeukia daktari. “Unaweza kumsaidia mwanangu au HUWEZI?” Paul aliuliza kwa ukali zaidi. “Naweza Mheshimiwa.” “Basi anza kazi yako, sasa hivi.”
Sonia aliwekewa dripu ya maji akiwa amelala palepale chini kwenye ndege, mama yake akiwa amempakata kichwa huku akiendelea kumuongelesha. “Naogopasana mama.” “Usiogope Sonia. Mimi na mama yako wote tupo, kila mtu yupo hapa kwa ajili yako. Lazima utulie ili pressure ishuke, lasivyo tutapoteza mtoto. Unanisikia Sonia?” Paul aliingilia maongezi yao na kumjibu kwa upendo sana.
Sonia alishituka kidogo na kujishika tumbo. “Mtoto wangu!” Sonia alilia. “Unamuona huyo hapo pembeni yako?” Sonia aliangalia huku akilia. “Ni nani huyo baba?” “Ni daktari, anajaribu kukusaidia wewe na mtoto. Usiogope kila kitu kitakuwa sawa. Umesikia Sonia?” Japokuwa alijaribu kutulia kama baba yake alivyomshauri, lakini bado Sonia alionekana na wasiwasi usoni.
*********************
Mama yake alifananisha ile hali ya Sonia ya sasa na ule usiku aliochanganyikiwa mpaka kulazwa, baada ya tishio la kutaka kubakwa na bosi wake Sam. Wasiwasi ulimwingia Ishimwe akaamua amuulize taratibu.
*********************
“Unaogopa nini Sonia?” Ishimwe aliuliza kwa kiluga. “Baba yake Fau.” Ishimwe alishituka sana. “Nini?” Paul naye aliuliza. “Unamwambia nini!?” “Kaka yako ana mtoto anaitwa Fau?” Ishimwe alijibu kwa kumuuliza swali. “Hapana! Hana watoto wa kike, ana watoto wa kiume tu. Kwani vipi?” “Basi ni yule baba mliokuwa mkizungumza naye pale uwanja wa ndege wa Shinyanga.” “Nini Ishimwe?” Ishimwe alianza kulia.
“Nini Ishi?” “Naomba muulize mama kama anamfahamu yule baba.” “Wote tunamfahamu, ni kama kaka yetu! Rafiki yake sana Junior. Kwani vipi?” Ishimwe aliendelea kulia kwa kwikwi, Paul alitulia kidogo kama akifikiria, ikawa kama aliyepata jibu.
*********************
Gafla alitoka pale kwenye ndege kama Faru aliyejeruhiwa. “Kato ana watoto wangapi?” Paul alimuuliza mama yake akiwa anatetemeka kwa hasira. “Watatu wa kike. Kwa nini unauliza?” “Nilikwambia nini juu ya kuwaalika watu wengine mbali na ndugu?” Paul alikuwa na hasira sana. Hakuna aliyemuona Paul akimuongelesha mama yake akiwa na hasira kiasi hicho.
Mama Tambo alibaki akimwangalia Paul. “Sonia akipoteza mtoto wake, sitakaa nijisamehe maishani mama, kwa kuwa mimi ndio nitakuwa nimemsababisha hayo. Isingekuwa kumleta hapa, yote haya yasingetokea. Nimeshamuharibia maisha mwanangu kwa kuwakimbia yeye na mama yeke kabla hajazaliwa.”
“Unajua shida walizopata, halafu ona sasa hivi kinachompata mwanangu! Na wewe ukiwepo mama! Kwa nini unaendelea kuruhusu mabaya yanipate mimi na familia yangu? Lini na mimi nitatulia mama?” Paul alikuwa akitetemeka kwa hasira.
“Nini Paul?!” “Usinishike Mat. Please.” “Niambie kuna nini Paul.” Matilda alisisitiza, lakini Paul alimgeukia mama yake.
“Wewe mwenyewe ulitaka kuonana na Sonia. Nikakwambia asiwepo mtu yeyote leo, isipokuwa watoto wako tu. Sonia yupo katika kipindi kigumu sana cha maisha, nataka atulie angalau nijenge naye mahusiano. Nimekosa kuwepo katika maisha yake yote mama. ‘You took away all her 24 yrs from me. I have never seen my baby’s first steps, or seen her teething, or read her bedtime story! NEVER. I have never been there to teach her a lot of stuff. I have never put my baby to sleep or put her on my shoulder and tell her is gonna be fine when she cries or scares. You took that mama.”
“You did that to me. And now you know for sure, she is the only precious thing I have and still, you don’t care, mama’! Mungu amenipa nafasi nyingine tena, nimempata mwanangu, unashindwa kunisaidia kumuweka karibu na mimi! Nilikwambia kwa kipindi hiki sitaki aanze kufuatiliwa na watu au kuanza kutoka magazetini. Kwa nini umeruhusu Kato kuwepo uwanjani?” Paul aliendelea kumuhoji mama yake kwa ukali huku machozi yakimtoka.
“Nisikilize Paul tafadhali. Mimi ndio nilikuwa na maongezi na Kato, nikamuita nyumbani. Amefika asubuhi hii ya leo, tukawa na mazungumzo marefu. Kabla hatujafikia kwenye makubaliano, mama akaniambia lazima tukuwahi uwanja wa ndege.”
“Nikamuomba Kato aje na sisi tumalizie mazungumzo yetu pale uwanjani wakati tunakusubiri. Come’on Paul! You know Kato! He is my friend and like a brother to you'all! He will NEVER do anything to hurt you.” “Well then, he did. Your friend RAPE my Babygirl and that kid, Kana, is Kato’s son.” Paul alikuwa akitetemeka na alionyesha wazi pale alipokuwa akimnyooshea kidole Kana.
“What?” “Yes, you heard me. Tena sio mara moja. Alimlevya mwanangu na kuendelea kumbaka for two days, continuously. Na ndio maana alikimbia pale uwanjani. Ulimuona amemuaga hata mmoja wenu?” Paul alikuwa akiongea kwa hasira sana, Kana alikuwa kwa pembeni kidogo, amesimama na Sam, lakini aliweza kusikia mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea.
“Ameweka jeraha la kudumu kwenye maisha ya mwanangu.” Kila mtu alibaki ametoa macho. Matilda na dada yake walianza kutokwa na machozi. Junior alitaka kumgusa Paul. “Don’t touch me Junior. Please don’t. Not now.” Paul alimsukuma kaka yake.
“Baada ya mazungumzo yote yale mama, na kukusisitiza, over and over,nikikuomba mtu yeyote wa nje asiwepo siku ya leo ila watoto wako tu, lakini bado umenipuuza mama.” Paul aliendelea kumlaumu mama yake. “How could you let that happened under your watch, mama? How could you?” Paul aliendelea kumuuliza mama yake huku akilia.
*********************
Sam alishituka sana, alishindwa kuchangia chochote kati ya ndugu hao, waliokuwa wakiongea lugha ya kingereza wakati wote, wakiwa wao wanne na mama yao. Hakutaka kujidhalilisha zaidi, aliamua kukaa pembeni, akiwaza juu ya hatima ya mtoto wake, ambaye hakujua hata jinsia yake hata hivyo aliona Paul na ndugu zake, wanahangaika kwa kadiri ya uwezo wao kujaribu kuokoa maisha yao.
Kwa mara ya kwanza Sam alikumbuka muujiza Mungu aliomfanyia Nyange na mama Briana, akabaki akimsihi Mungu wake kimya kimya, huku akimkumbusha uwezo wake, na mambo makubwa aliyosikia Mungu amefanya.
‘Msaidie mtoto wangu, eeh Mungu wangu. Msaidie na Sonia. Najua kwa sasa, hakuna pesa wala ujuzi wa daktari utakao msaidia mwanangu na Sonia ila wewe. Nakuomba uingilie kati Mungu wangu. Okoa maisha ya mtoto wangu.’ Sam aliendelea kuomba kimya kimya.
*********************
Mama Tambo aliyekuwa kimya kabisa muda wote, alimsogelea Paul na kumshika mkono taratibu. Ilikuwa faraja kubwa sana ambayo Paul alijisikia moyoni. Ni kweli ipo nguvu ya ajabu ya mama kwa mtoto. Akanyamaza, maneno yote yaukali yakaisha. “Samahani sana Paul. Sikuj..… Samahani. Sikukusudia kukuumiza zaidi.” “Naogopa sana mama. Sijawahi kuogopa hivi. Sitaki kumpoteza huyo mtoto.”Paul alianza kulia kama mtoto mdogo, akamwegemea mama yake.
“Samahani mama.” Mama Tambo alibaki kimya kabisa akiwaza bila yakusema kitu. Alimshika Paul kwa muda, kisha akarudi kwenye ndege. “Anaendelea vizuri. Naona ametulia kabisa. Nimemchoma sindano ya usingizi alale, itasaidia.” Daktari alimuwahi Mama Tambo mara tu alipoingia kwenye ndege. “Na mtoto?” “Kwa kuwa sasa hivi ametulia, inabidi tumuwahishe hospitalini kwa vipimo zaidi. Nimeshindwa kusikia vizuri mapigo ya mtoto.”
“Sio hapa Mwanza, naomba tuongozane wote mpaka Dar, watakapo mpokea na kumuanzishia matibabu huko, ndipo unaweza kurudi huku Mwanza. Tunaondoka sasa hivi, daktari mwingine atakupokea tukitua uwanja wa ndege wa Dar. Ni sawa?” “Bila shaka mama.”
*********************
Watu wote walirudi kwenye ndege tena, na safari ya Dar ikaanza. Paul alijisogeza karibu na pale alipokuwa amekaa Ishimwe na Sonia ambaye bado alikuwa na dripu ya maji mkononi. Alikaa kwenye kiti cha pembeni yao, kwa kuwa wao walikuwa bado wamekaa chini kabisa.
Paul alimshika mkono Sonia kwa upendo sana. Sonia alikuwa usingizini. “Pole Ishimwe.” “Asante, lakini usiwe na wasiwasi, nimemuombea, naamini kila kitu kitakuwa salama. Usiogope” Paul alitabasamu, lakini alionyesha bado anahofu.
*********************
Ndege hiyo ndogo ilitua katika uwanja wa ndege wa Mwalimu Nyerere, Dar, na kukuta gari la wagonjwa la ‘Usalama wa Taifa’ likiwasubiria ndani ya uwanja huo. Walilisogeza karibu sana na ndege hiyo. Alishuka daktari mwingine kumpokea Sonia, wakapeana maelekezo machache na yule daktari wa kutokea Mwanza. Mama Tambo akampa maelezo mengine yule daktari wa Mwanza, wakaagana naye palepale uwanjani.
Wakati wanamshusha kwenye ndege Sonia alitoka usingizini. Alianza kuangalia watu waliokuwa wamemzunguka, akasikia sauti ya baba yake. “Pole sana Sonia.” “Wananipeleka wapi? Msiniache naye peke yetu, nimkatili sana, ataniumiza vibaya sana. Unajua alinipiga pia?” Sonia alianza kulia, Paul alimshika tena mkono wake huku akimshika kichwani taratibu.
“Naogopa sana baba. Msije mkaniacha peke yangu.” “Siwezi kukuacha Sonia, nipo na wewe. Tunawahi hospitalini, naamini watatusaidia.” “Kwa hiyo hutaondoka?” Sonia aliuliza tena huku akiwa amejawa na wasiwasi sana. Machozi yalikuwa yakichirizika pembeni ya macho yake, Paul aliendelea kumfuta taratibu.
“Aliniacha kwenye chumba chenye baridi siku mbili mfululizo bila kunifunika, nikiwa uchi. Nikawa nateteme…” Sonia alifunga macho nakuanza kutetemeka tena, huku analia. Paul aliomba kitanda kiwekwe chini kwanza.
“Naomba mkiweke kitanda chini, halafu mtupishe kidogo, nitawaita baadaye.” Paul aliwaambia wale wauguzi. “Nafikiri anatakiwa kuwahishwa hospitalini. Hali yake inazidi kuwa mbaya.” Nesi alijaribu kushauri. “Nimesema weka kitanda chini na muondoke mpaka nitakapo waita tena. Umesikia?” Paul aliongea kwa ukali na sauti ya juu. Ilibidi waweke hicho kitanda chini katikati ya uwanja, na kuwapisha familia hiyo ya Tambo, lakini Sonia akiendelea kutetemeka sana huku akilia.
“Hey Sonia! Sonia! Sonia!” Paul aliita. “Fungua macho uniangalie. Niangalie mwanangu.” Kwa hofu kubwa Sonia akiwa kwenye hali ile alifungua macho huku akitetemeka. “Unaniona?” Sonia alitulia kidogo kama anayefikiria. Paul alitaka amtoe mtoto wake katika ile hofu kabisa kabla ya kwenda hospitalini.
“Unajua unaongea na nani?” Sonia alifikiria kidogo kama anayejaribu kurudisha kumbukumbu. “Baba!” Paul akiwa na sura iliyotulia, alitabasamu kumfanya Sonia atulie.
“Unajua nakupenda sana mwanangu, na sasa hivi nipo, siwezi kuruhusu mtu yeyote akakuumiza tena. Nimekufunika shuka vizuri, hakuna baridi itakayo kupiga tena. Na ukisikia baridi zaidi, nitakuongeza shuka jingine. Nakuahidi nitakuwa na wewe, naomba ulale kabisa, ukijua upo salama, chini ya uangalizi wa watu tunaokupenda na kukujali.”
“Ujue na baba yako nipo, siwezi kuruhusu kitu au mtu mbaya akusogelee tena. Naomba ulale kabisa ukijua muda utakao amka hii ndiyo sura utakayoonana nayo sio vinginevyo.” Sonia alitabasamu, Paul akambusu. Sam na Ishimwe walibaki wakishangaa jinsi Paul alivyoweza kumtuliza kwa muda mfupi.
*********************
Walijua kule kutetemeka kwa Sonia, zilikuwa ni kumbukumbu za baridi ya siku akiwa anabakwa na sasa maneno ya baba yake, yamemuhakikishia ulinzi, uliomfanya kwa mara ya kwanza ile baridi kupotea.
*********************
Wakamuona anafunga macho wakati baba yake anambusu na kufungua tena taratibu akiwa na tabasamu. “Asante baba.” Sonia alijibu kwa sauti ya chini sana, lakini kila mtu alikuwa akisikiliza mazungumzo yao. “Sasa naomba ufunge macho kabisa, ulale ili kupumzisha akili na mawazo yako. Lazima hiyo pressure ishuke ili mtoto naye awe salama.” Sonia alivuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu kama kusafisha kifua chake na kufunga macho yake kama anayesinzia.
“Sam yuko wapi?” Aliuliza tena akiwa amefunga macho. “Nipo hapa Sonia. Usiogope lala. Sisi wote tuko hapa.” Sam alikuwa nyuma ya kitanda alichokuwa amebebwa Sonia kutoka kwenye ndege kuelekea kwenye gari ya wagonjwa, ‘ambulence.’ “Asanteni.” Sonia alisema na kumwangalia mama yake kwa muda, kisha akapotelea usingizini.
*********************
Tatizo likaja pale Paul na yeye alipopanda kwenye gari ya wagonjwa na Sonia na kugoma kushuka. Mlinzi wake hakuwa na nafasi kwenye gari hiyo, kwani tayari gari lilishajaa hata wauguzi wengine waliokuwa wamekuja na gari hiyo walikosa nafasi.
Ilikuwa lazima daktari akae nyuma na Sonia, haya Ishimwe naye akapanda mara baada ya kitanda alicholalia Sonia kuingizwa ndani ya gari, Paul naye akafuata nyuma na kumuacha Mlinzi wake amesimama haelewi chakufanya. Sam na Kana nao waliingia na kukaa kiti cha mbele cha gari hilo. Ndugu zake Paul wakabaki wamesimama na mama yao wakiwaangalia.
“Naona gari imejaa, sina nafasi humo ndani.” Mlinzi aliongea kwa heshima kidogo kama kutaka Paul amsikilize. “Kwa hiyo?” Paul alimgeukia. “Nashauri turudi kwenye gari yako, tuwafuate kwa nyuma. Kwa ajili ya usalama wako.” Paul alimtazama kwa macho ya ukali sana. “Kwa ajili ya usalama wangu au usalama wa kazi yako?” Yule mlinzi alitulia kidogo, akaamua kuongeza.
“Sitapata nafasi humo ndani. Sitaweza kukulinda vizuri. Natakiwa kuwa mita...” Yule mlinzi aliendelea kuongea kwa heshima zaidi, lakini Paul alimkata. “Ulitaka mimi nikufundishe kazi yako? Naomba usizidi kupoteza muda.” Paul alikuwa mkorofi sana siku hiyo, tofauti na siku zote alizowahi kuwa na huyo mlinzi. Ndugu zake wote walibaki wakimwangalia. Siku hiyo alikuwa haambiliki na mtu yeyote.
“Na kwa nini hatuondoki?” Paul alimgeukia mama yake. “Lazima uondoke na mlinzi wako Paul. Huwezi kwenda bila ulinzi.” Mama Tambo alijibu kwa upole kidogo. “Basi fikiria jinsi ya kufanya mama. Na ninaomba iwe haraka, lakini mimi sitashuka humu ndani, nakaa na mtoto wangu.” Paul alijibu na kumgeukia Sonia aliyekuwa amelala, huku akimuachia mama yake majukumu yake.
Mama Tambo alifikiria kidogo, mwishowe akaenda kuongea na Sam ili washuke waingie kwenye gari nyingine, ili Mlinzi wa Paul apate nafasi kwenye gari hiyo ya hospitali.
Baada ya kuhakikisha kila mtu amepanda kwenye gari, Mama Tambo alirudi kwa Paul. “Tupo nyuma yenu, tutakutana hospitalini.” Paul hakutaka hata kumgeukia mama yake, alibaki kimya. “Asante sana mama.” Ilimbidi Ishimwe ndio ajibu.
*********************
Kwa kuwa Sonia alichomwa sindano ya usingizi, alifika hospitalini akiwa bado amelala. Alipokelewa na wauguzi wa hospitali hiyo ya Usalama wa Taifa, akaingizwa kwenye chumba fulani na kuanzishiwa matibabu. Paul na Ishimwe walibaki nje, ya chumba hicho wakisubiria. Mama Tambo na watoto wake, wakiwa na Kana na Sam nao wakaingia. Mama Tambo alikaa pembeni ya Paul bila hata kumsemesha kitu.
“Vipi mtoto?” Paul alisimama na kuuliza mara baada ya daktari kutoka katika chumba alichokuwa ameingizwa Sonia. “Tumemuwekea machine ya kusikiliza mapigo ya mtoto tumboni kwa mama yake, mtoto anaonekana anaendelea vizurikabisa, na tutaiacha hiyo mashine kwa muda ili kuendelea kufuatilia mapigo ya moyo ya mtoto.” Paul alipumua kwa nguvu.
“Na Sonia mwenyewe?” Mama Tambo aliongeza swali. “Pressure imeshuka, ipo sawa kwa sasa. Lakini amepoteza maji mengi ya nyumba ya uzazi, nilazima apate mapumziko kwa muda mrefu sana ili kuhakikisha huyo mtoto anakaa humohumo ndani mpaka siku zake zitimie. Kwa ..…” “Kwani ni ujauzito wa muda gani?” Mama Tambo aliuliza tena swali na kumkata usemi yule daktari.
“Ndio mwezi wa saba sasa. Ndio maana ni lazima kuhakikisha huyo mtoto anatunzwa humo ndani mpaka atakapo komaa vizuri.” “Fanya kile unachoweza, ilimradi wote wawe salama.” Mama Tambo alimaliza na kutaka kuingia ndani ya chumba alichokuwemo Sonia.
Paul akamuwahi. “Asante sana mama, na samahani sana nilikuwa nimepaniki.” “Ishimwe! Nyinyi mnaweza kuingia tu kumuona Sonia. Na sisi tutakuja sasa hivi, nataka tuongee hapa nje kidogo.” Mama Tambo alisema, akimaanisha kutaka muda kidogo na watoto wake tu.
Kabla ya kuingia Sam akaona na yeye atoe shukurani zake. “Asanteni sana kwa kila kitu. Kumsaidia Sonia na mtoto wangu. Nashukuru sana.” Sam alijikaza kiume mbele ya wasomi hao kina Tambo, walionekana wenye UWEZO wa kufanya chochote kwa wakati wowote. Heshima na hofu iliongezeka zaidi kwa Sam. Aliona yale mambo aliyodhani hayafanyiki au hayawezekani kwa nchi ya Tanzania, yaliwezekanika kwa familia hiyo ya Tambo kwa kupiga tu simu, kila kitu kiliwafuata walipo. Ukweli wangepoteza mtoto kama sio juhudi za familia hiyo.
“Sina jinsi nyingine ya kuwashukuru jamani. Asanteni sana.” Sam alirudia kinyenyekevu sana mbele yao wote, wakimtazama huku amemshika Kana. “Sonia ni jukumu letu sote Sam. Sasa hivi tupo pamoja. Asante na wewe kwa kubeba majukumu yote peke yako kwa muda mrefu. Asante sana.” Paul akamshika bega, Sam alijisikia vizuri sana kwa Paul kuendelea kumtambua hata mbele ya ndugu zake.
“Asante sana Sam.” Mama Tambo na yeye alinyoosha mkono kushukuru. “As..asan-ente.” Sam aliitikia kwa shida sana, kwani alikuwa akitetemeka mbele ya kina Tambo, lakini alijikaza kiume tu. Baada ya kusafisha koo mara kadhaa aliweza kuitikia. Akamshika vizuri Kana, wakaingia ndani na Ishimwe.
Wakati wanaingia Sonia alifungua macho kidogo. Kana alisogea karibu kidogo ya kitanda. “Pole mama.” Sonia alifurahi sana, machozi yalianza kumtoka taratibu kama Kana. “Asante Kana. Sogea karibu na mimi.” Kana alisogea, Sonia alimshika mkono. Kana aliendelea kulia kwa muda, Ishimwe alimvuta karibu na kurudi kukaa naye kwenye kochi akimbembeleza.
“Mama yako atakuwa salama, usiwe na wasiwasi Kana.” Sam naye alimsogelea Sonia akambusu na kuanza kumfuta machozi. “Pole Sonia wangu.” Sonia alitabasamu. “Unajisikiaje?” “Vizuri, lakini nina usingizi sana.” “Walikuchoma sindano ya usingizi ili upumzike. Unatakiwa kulala ili upumzishe mwili wako na mawazo, ili hiyo ‘pressure’ ikae sawa. Lala usiwe na wasiwasi, sisi tupo hapahapa hatuondoki.” Sonia alizungusha macho kwenye kile chumba, Sam alimuona amebadilika gafla.
“Vipi?” Sam akauliza. “Baba aliniahidi hataondoka!” “Yupo hapo nje wanaongea na ndugu zake.” Sonia alinyamaza kimya na kugeuza kichwa upande mwingine bila ya kujibu kitu. Taratibu machozi yalianza kumtoka tena. Ishimwe alijua mawazo ya Sonia, akaamua kutoka kwenda kumuita Paul.
“Samahani mama, Sonia ameamka anamuulizia Paul.” Ishimwe aliongea kwa sauti ya chini kidogo kwa kuwa Mama Tambo ndio alikuwa katikati ya mazungumzo. Kama mshale Paul alisima kuelekea chumba alicholazwa Sonia. Alisogea karibu kabisa ya kitanda. Sam alimpisha. Paul alinza kumshikashika kichwa tena taratibu ili kumfanya ageuke. Sonia aligeuka, akafungua macho huku machozi yakimtoka.
“Nilijua umeondoka.” “Siwezi kuondoka Sonia. Nilikuwa hapo nje naongea na mama. Unaonekana una usingizi sana. Funga macho ulale, mimi nipo hapahapa, mpaka utakapo amka. Umesikia?” “Kweli?” Paul alitabasamu, akainama na kumbusu Sonia kwenye kipanda uso na kumshika kiganja chake, cha mkono uliokuwa hauna dripu. “Huu mkono wangu, utakuwa hapahapa mpaka utakapo amka.” Sonia alitabasamu na kupitiwa na usingizi muda uleule bila kuongeza neno.
*********************
Baada ya masaa kadhaa, Sonia aliamka. Akatabasamu baada ya kumuona baba yake amekaa pembeni yake akimwangalia, huku bado amemshika mkono. “Naona hata sura imebadilika, imekuwa ya furaha.” Sonia alicheka kidogo. “Nimelala usingizi mzuri nikijua upo hapa pembeni yangu, hakuna baya litanipata tena.” Sonia alijibu kwa sauti ya chini sana huku akitoa tabasamu na machozi kidogo. Paul alisimama na kumfuta tena machozi.
“Nitakuwa na wewe Sonia. Sitaruhusu mtu yeyote akuumize tena.” Paul alimnyanyua juu kidogo kutoka kwenye mto aliokuwa amelalia na kumkumbatia kwa muda. “Asante baba.” Sonia alijibu akiwa bado amekumbatiwa na baba yake.
“Nakupenda sana Sonia, mwanangu.” “Na mimi nakupenda baba.” Kila mtu aliyekuwepo kwenye chumba hicho aliwahurumia Paul na Sonia. Taratibu alimuweka chini, na kumfunika vizuri binti yake.
“Unajisikiaje Sonia?” Mama Tambo aliuliza mara baada ya kusogea karibu naye. “Najisikia vizuri. Asanteni kwa kuwa hapa na samahanini kwa usumbufu. Najua nimewaharibia mipango...” Akaanza kulia. “Usijali kabisa Sonia. Nimefurahi tumeweza kuwa na wewe kwenye kipindi hiki kigumu, na kumsaidia mama yako pia. Pole sana Ishimwe kwa kulea peke yako. Na pole sana Sonia kwa matatizo.”
“Na ukumbuke sisi ni ndugu Sonia, akiumia mmoja wetu, wote tunakuwa kwenye maumivu. Hujatusumbua hata kidogo. Na kuanzia leo, lazima ujue wewe ni jukumu letu wote, sio mama yako peke yake. Ukiwa na shida yeyote, sisi wote hapa tutakuwa na wewe, umbali wetu na wewe ni simu tu. Muda na wakati wowote ukitupigia simu, tutakuwepo kukusikiliza. Umesikia Sonia?” Mama Tambo aliongea huku akimwangalia Sonia.
Sonia alijisikia vizuri sana. “Asante sana bibi.” “Pole sana Sonia mjukuu wangu.” “Asante.” Ndugu zake Paul wote walisimama na wao kumsogelea Sonia. “Pole sana.” “Pole sana Sonia.” “Can I have a hug too?” Kaka yake Paul aliyekuwa nyuma ya mama yake aliuliza, Sonia alitabasamu. Walimpisha akasogea mpaka karibu kabisa na alipokuwa amelala Sonia, akamnyanyua kama Paul baba yake alivyofanya mwanzo na kumkumbatia.
“We love you so much, baby girl. Don’t you ever forget that. Okay?” Sonia alitingisha kichwa akiwa bado amekumbatiwa na baba yake mkubwa. Alimuweka chini taratibu na baba yake akamfunika tena. “Asanteni sana.” Sonia alijibu huku akijaribu kuzuia machozi yake ya furaha lakini alishindwa. Paul aliendelea kumfuta taratibu huku akimbusu.
*********************
Baada ya kutulia, Paul aliamua kuvunja ukimya. “Sasa utambulisho unaweza kuanza.” Paul alitoa utambulisho kwa ndugu zake wote akiwa ametulia kabisa. “Nimefurahi kuwafahamu.” Sonia alijibu huku akiwaangalia mmoja baada ya mwingine, mpaka aliporudisha macho yake kwa bibi yake, akatabasamu na kunyoosha mkono kumgusa, kwa kuwa na yeye alikuwa karibu sana na kitanda chake.
“Nimefurahi kukuona bibi yangu. Nilikuwa natamani kweli kuwa na ndugu! Tumekuwa tukiishi mimi na mama tu, mpaka Mungu alipotupa Kana na baadaye akaja Sam kutuokoa kwenye dhiki kali sana. Halafu Sam akatutambulisha kwenye familia ya Nyange, nilipokuwa nimeenda kufanya kazi za ndani, kisha wakaja kumuajiri na mama. Kusaidia kazi za ndani. Waliruhusu na Kana aje aishi na sisi. Kwa hiyo mimi na mama tukawa tukiwafanyia kazi hapo nyumbani kwao, lakini tulikuja kugeuka kuwa kama ndugu kwao. Hatukuwahi kuwa na ndugu wala rafiki waliowahi kututhamini kabla ya hapo. Asanteni sana.” Sonia na mama yake waliendelea za kulia taratibu.
Mama Tambo alizidi kuumia moyoni na kujilaumu sana. Aliupokea mkono wa Sonia na kuuminya minya kwa upendo sana. “Hata mimi nimefurahi kukuona Sonia. Pole sana kwa matatizo. Pole sana.” Mama Tambo alirudia na kutulia tena kidogo kama anayefikiria cha kuongea.
Ukubwa Wa Mtu Hujulikana Anapokubali Kosa
“Wakati umepoteza fahamu, niliogopa sana nilifikiri hatutapa tena muda kama huu. Nilikuwa nikimuomba sana Mungu anipe nafasi hata ya dakika moja tu, ili niongee na nyinyi wote, na wewe Sonia ukiwepo.” Mama Tambo aliongea na kumgeukia Ishimwe pia.
“Na kwa kuwa Mungu amesikia maombi yangu, amekurudisha kwenye ufahamu wako, na mtoto anaendelea vizuri, naomba nisipoteze huu muda, naomba niongee nilichokuwa nikitaka kukisema.” Mama Tambo alitulia kidogo, kila mtu alikuwa akimsikiliza kwa makini sana.
“Paul na Ishimwe, naomba mnisamehe sana. Niliwakosea na kuwasababishia majeraha makubwa sana kwenye maisha yenu, ambayo hakuna jinsi yanaweza kufutika. Natamani ningetoa sababu zangu zilizonipelekea kuwafanyia nilichowafanyia lakini naona haitasaidia.” “Itasaidia sana mama. Ningependa sana kujua ni kwa nini…” Paul alimkatiza mama yake na kukwama.
Mama Tambo alinyamaza. “Tafadhali mama.” Paul alibaki akimtizama mama yake. “Nilijua ni mapenzi ya utoto Paul. Nilijua uzuri wa Ishimwe ndio ulikuchanganya na kukufanya usahau au utupilie mbali ndoto zako. Nilitaka kukuokoa. Nilimuona jinsi Ishimwe alivyokuwa mtoto mdogo, nilijua siku moja akishakuwa mkubwa, akakutana na mtu mwingine, akagundua anampenda kwa dhati kuliko wewe, nilijua angekukimbia, halafu ukabaki unateseka mwanangu.”
“Nakujua moyo wako jinsi ulivyo Paul. Najua jinsi ulivyojawa na mapenzi ya dhati, sikutaka Ishimwe aje akuumize baadaye na kukusababishia madhara kama aliyokuletea yule mwanamke niliyekutafutia mimi, halafu akakuharibia kazi yako. Nakiri udhaifu wa kufikia maisha yenu nyinyi wote kwa maendeleo ya nje, bila kuwafikiria kwa ndani.” Quiet
“Najua madhara mengi niliyowasababishia mpaka sasa, nyinyi watoto wangu wote, zaidi kwa Sonia na Ishimwe ambao niliwatenganisha na Paul. Sikujua kama Ishimwe alikuwa na mapenzi ya kweli tokea zamani. Kitendo cha kutoendelea na maisha na wanaume wengine, na kuendelea kuhangaika kumlea Sonia akiwa peke yake, tena bado akiwa binti mdogo, mrembo, huku akipambana na shida nyingi sana hapa nchini, akilea damu ya Tambo, nitakithamini daima. Asante Ishimwe na samahani sana mwanangu. Ni kweli nilikukosea, naomba msamaha.” Mama Tambo alimgeukia Ishimwe na kumtizama.
Chumba kizima kilikuwa kimya sana, wakimsikiliza na kumshangaa Mama Tambo, zaidi wanae, ndio waliohisi wapo ndotoni. Hawakuwahi kumuona mama yao kwenye hali ya unyenyekevu vile.
Akamgeukia Sonia. “Sonia mjukuu wangu. Naomba nikupe pole kwa matatizo yote niliyo kusababishia. Namjua baba yako jinsi alivyo na upendo.” Watoto wake wote walianza kukohoa na kusugua makoo kama wamebanwa kohozi, Paul alicheka. “Mnawivu nyinyi!” Paul aliwageukia ndugu zake. “Mtoto wa Mama Tambo huyo! Sifa zake haziishi!” Kaka yake Paul alitania. Wakacheka kidogo na kunyamaza.
“Najua kama ungekuwa na baba yako tokea unazaliwa, usingepitia ulipopitia. Unisamehe Sonia.” Sonia alianza kulia. Paul alimsogelea karibu zaidi na kuanza kumbembeleza tena.
“Paul! Najua nilikupokonya maisha ya Sonia wakati anakua. Najua hakuna jinsi ya kulipa hiyo, lakini naomba unisamehe sana mwanangu.” Ishimwe alisimama, na kumsogelea Mama Tambo. “Asante sana mama kwa kutupokea. Nashukuru.” Kwa mara ya kwanza Mama Tambo alimkumbatia Ishimwe. Ulikuwa ni wakati uliochanganyikana furaha na uchungu katikati yake.
Mwishowe wote walitulia wakaanza kutaniana mle ndani kila mtu alikuwa akicheka kasoro Kana alikuwa kimya kabisa. Sonia alijua.
*********************
“Naomba niwaombe kitu kimoja.” Sonia aliwakatiza kidogo. “Najua kitendo alichonifanyia baba yake Kana ni cha kikatili sana. Hakuna jinsi anaweza kujitetea kikawa sawa. Lakini naomba tumsamehe. Binafsi bado nina muogopa sana, lakini katika mabaya yote aliyonifanyia, namshukuru Mungu nimempata Kana. Japokuwa kitendo kilikuwa kibaya, lakini Kana kwangu sio mtoto wa bahati mbaya.”
“Nampenda mtoto wangu, na sikutaka ajue kabisa yaliyotokea kati yangu mimi na baba yake, lakini kwa bahati mbaya amefahamu. Naomba Kana umsamehe baba yako, na atakapojirudi umpokee. Nilijiapia kutokwambia kabisa, ukatili alionifanyia baba yako, ili usije wahi kumchukia baba yako.”
“Sitaki uje kukua kama mimi, bila mapenzi ya baba. Ni ngumu sana Kana, usithubutu kumchukia baba yako hata iweje. Naomba umsamehe.” Kana alianza kulia kwa uchungu sana. “Na wengine pia hivyohivyo, naombeni mumsamehe tu. Najua Sam anamlea Kana kama mtoto wake, lakini hatuwezi kuepuka ukweli, yule ni baba yake Kana, hata iweje.”
“Tafadhali baba, naomba yaishe. Naomba tumsamehe tu. Hata kama hatakaa akaomba msamaha, lakini kwa ajili ya Kana, naomba tumsamehe, ili Kana naye awe na mahusiano mazuri na baba yake.” Sonia na Kana wote walikuwa wakilia. Paul alimsogelea Kana na kumkumbatia.
“Pole sana Kana. Unajua ilikuwa nilazima uzaliwe? Tulikuwa tumepanga mimi na bibi yako, akishazaliwa Sonia, tulimuomba Mungu atupe Kana. Haijalishi umezaliwa na Sonia au Ishimwe, kwangu naona Mungu ametujibu maombi yetumimi na Ishimwe. Tutakupenda kwa upendo uleule kama vile ungezaliwa na mimi na Ishimwe.” Aliendelea kumbembeleza.
“Umesikia Kana? Wewe sio mtoto wa bahati mbaya hata kidogo. Tunakuhitaji sana katika familia yetu. Kwa hiyo usijisikie vibaya hata kidogo. TunakupendaSANA.” “Asante.” Kana alijibu kwa kifupi huku akijaribu kufuta machozi yake.
“Daah! Kweli hao wanao Paul.” Kaka yake alisema. “Mimi nishampigia simu Kato na kumwambia naomba barua yake yakuacha kazi, na sitaki kumuona tena, lasivyo nitamuua. Nilitaka nimfilisi mpaka nyumba aliyojenga kwa pesa yangu.”
Historia Ya Kato Kwenye Hiyo Familia Ya Tambo
Kaka yake Paul alijulikana kama Tambo Jr. Alisomea mambo ya madini. Kwa hiyo alikuwa Muhandisi {Engineer} wa mambo ya madini huko nchini Marekani. Alikuwa akiingiza pesa nyingi sana. Alifungua kampuni ya madini nchini na kumuweka Kato kama msimamizi wa kampuni hiyo.
Kato na Junior walikutana katika chuo kikuu cha Mlimani wakati Junior, akisoma shahada yake ya kwanza, hapa nchini, na baada ya kumaliza shahada hiyo, Junior alihamia nchini Marekani kwa masomo zaidi, na huko huko ndipo alipoajiriwa.
Matokeo yao ya mwaka wa mwisho katika chuo hicho cha Mlimani, jijini Dar, yalipotoka, Kato alikuwa amefeli kabisa. Wengi walisema alifanyiwa kusudi na walimu wa chuoni hapo, kwa kumfelisha, sababu ya kutembea na mke wa mwalimu mmoja wa chuoni hapo na kuvunja ndoa yake.
Kato alichanganyikiwa mara baada ya matokeo yake ya mwisho kutoka na kujua amefeli kabisa. Ndoto zake zote na jitihada zake zote alizokuwa ameweka chuoni hapo zilikuwa bure kabisa. Alianza kuzunguka mtaani bila ajira yoyote, kwani hakuwa na cheti chochote kilichoonyesha kuwa yeye ni muhitimu au ana shahada ya Uhandisi.
Aliteseka mtaani mpaka rafiki yake Junior alipomsaidia. Alipomaliza shule yake nchini Marekani na kufanikiwa sana, pamoja na msaada wa wazazi wake, Junior aliamua kufungua kampuni ya madini nchini na kumuweka rafiki yake huyo, Kato, kuwa msimamizi wa kampuni hiyo. Kwa kuwa walifahamiana na Junior, na ni kweli Kato alikuwa na akili sana darasani, mara nyingi Kato na Junior ndio walikuwa msaada mkubwa darasani kwao, wakiwafundisha wenzao, Junior hakumdai cheti chochote cha shule, akaanza kazi.
Kato alikuwa mchapa kazi na mwaminifu sana kwa Junior, kitu kilichowafanya wazidi kuwa karibu na kugeuka kuwa kama ndugu. Kato hakuwa na mzazi hata mmoja, kwa hiyo Mama Tambo akageuka kuwa kama mama yake. Hakuhitaji kualikwa nyumbani kwa Tambo, aliingia na kutoka atakavyo.
Hata binti zake kina Fau walimuita Mama Tambo bibi na Junior ndiye aliyewasaidia watoto wakubwa wa Kato au tuseme dada zake Fau kwenda kusoma nchini Marekani. Na huko nako nchini Marekani watoto wa Kato waliishi na Junior kama baba yao. Kwa hiyo walikuwa na mahusiano ya karibu sana, hata Mama Tambo hakujua ni adhabu gani itakayo mstahili Kato. Aliamua kunyamaza tu.
*********************
“Naomba umsamehe tafadhali.” Sonia alimwangalia baba yake mkubwa huku akimsihi. “Yameisha sweetheart. Na nina kupongeza kwa moyo huo mzuri. Mungu akusaidie upone, ulee watoto wako vizuri.” Junior alimsogelea karibu na akambusu. “Karibu sana kwenye familia Sonia. Baba yako ana mawasiliano yangu yote. Muda wowote na wakati wowote uwe unapiga, hata kusalimia tu. Na wapo kaka zako, najua siku moja mtakutana, ili mfahamiane zaidi.”
“Kaka J, umemwambia Sonia kama wanao ni wazungu lakini?” Matilda alitania na wote wakacheka. “Bwana Mat anavyonisonga na wanangu na mama yao! Sina raha! Haya, Sonia, ushawahi kusikia kina Tambo wakizungu?” Sonia alitingisha kichwa kukataa.
“Basi wapo kina Tambo wakizungu, nitakuletea wakuone dada yao.” “Asante sana.” “Sema asante sana anko.” Sonia alicheka. “Unajua mimi ndio Tambo mwenyewe? Yaani nikisimama hapa nina kofia mbili. Ya kwanza namuwakilisha Mzee Tambo mwenyewe, yaani babu yako na pili mimi mwenyewe, kaka mkubwa wa ukoo. Hapa nasubiri mahari kutoka kwa Sam. Au dogo ushakula kimya kimya?” Alimgeukia Paul.
“Sijala kaka.” “Basi Sam, ukiwa tayari, wewe unipigie tu simu, nitakuja kupokea mahari ya Sonia. Bila mimi harusi haichezwi. Umesikia Sam?” Sam alitoa tabasamu la wasiwasi kidogo na kuitikia. “Umeona Sonia? Kwa hiyo lazima uwe unanitambua vizuri.” Junior alikuwa mcheshi sana kama Matilda. “Asante sana Anko.” “Ewaaa!” Junior alijibu huku akicheka.
“Dogo, hongera kwa familia nzuri.” “Asante kaka.” Vilijaa vicheko tena na utani. Tayari ilishakuwa familia moja. Sonia aliamini usemi wa baba yake, kwamba kweli nguvu yao wote ni kushikamana.
*********************
Paul alimuomba Ishimwe watoke nje. Baada ya muda wakarudi. “Jamani ninawashukuru sana kwa kuja kukutana na familia yangu na kushuhudia na mimi nikifikisha mwanamke ninayempenda kanisani, lakini naona harusi tutaiahirisha.” “Kwa nini!?” Sonia alishituka sana.
“Daktari amesema, umepoteza maji mengi sana Sonia, hawawezi kukutoa hapo mpaka utakapojifungua. Ukitoka tu hapo, utahatarisha maisha ya mtoto. Na sisi tungependa kufunga ndoa yetu na wewe ukiwepo.” “Wazo zuri Paul. Hata hivyo hamna haraka. Heri kuangalia afya ya mtoto wenu.” Matilda aliingilia.
Sonia alifikiria kidogo. “Eti baba, kwani kama sio kuwa na matatizo kati yenu, si mngekuwa mlishafunga ndoa?” Paul alicheka. “Kuna kitu tulikuwa hatujawahi kumwambia mtu. Tulipotoroka nyumbani, moja kwa moja tulienda kufunga ndoaserekalini, Ishimwe alidanganya miaka. Kwa hiyo Ishimwe alishakuwa mke wangu tokea hujazaliwa Sonia, au kabla hata sijamgusa mama yako, nilihakikisha nimemuoa kwanza. Nataka tu kupata baraka za Mungu. Kwa hiyo hatuna tutakachopoteza tukiendelea kusubiri.”
“Mimi naomba muendelee baba. Msiache kubariki ndoa yenu tafadhali. Mimi nitaangalia picha na video.” “Kwani huku hakuna ile njia ya kumuwekea video Sonia akawa anaona kila kitu kinachoendelea akiwa hapahapa? {Live.}” Junior akauliza.
“Hata kama ni pesa nyingi tutalipia ili asikose.” Martha aliyekuwa kimya kabisa muda wote aliongeza. “Na mimi naweza kubaki na Sonia.” Mama Tambo aliongeza. “Ningependa sana mama uwepo. Siwezi kumkosa baba na wewe kwenye harusi yangu.” Paul naye aliongeza.
“Mimi nitabaki na mama yangu. Msiwe na wasiwasi, kukiwa na tatizo lolote nitampigia anko Sam simu.” Sonia alitabasamu. “Wewe tena Kana!? Ndio huwezi kukosa kabisaaa, lazima uwepo. Bila wewe ni heri hiyo harusi isubiri. Wewe ndio baba yake Ishimwe. Sasa ataolewaje bila wewe kuwepo!” Paul alishamsogelea Kana karibu na kumshika mabegani huku akiongea naye.
Baada ya aibu kubwa na kujisikia ni kama mtoto aliyekuja kwa aibu, huku akimlaumu sana baba yake kwa ukatili aliomfanyia mama yake, Kana alianza kujisikia umuhumu kwenye familia hiyo. Alicheka kidogo lakini wazi alionyesha ana uchungu moyoni. “Wewe ndio Mkwe wangu bwana Kana, au hujui?” Kana alibaki kucheka.
“Mahari umelipa lakini Paul?” Junior alitania. “Ishimwe alikataa mahari.” “Acha hizo Paul! Lazima uongee na Kana vizuri. Ishimwe sio anayepanga mahari, Kana ndiye mpangaji.” Kila mtu alicheka. “Eti Kana? Utanidai kiasi gani?” Paul alimuuliza Kana. “Ngoja kwanza wazee wa upande wa Ishimwe tukae kwanza chini tuzungumze. Nimpange kwanza Kana, wakati unaleta barua ya posa, tutamjibu mshenga wako.” Junior aliongeza.
“Mmmh! Kama wewe utakuwa upande wa kupanga mahari, mke sipewi tena. Unaweza kunifilisi mali zangu zote!” Waliendelea kutaniana na kujisahau kabisa kama wapo hospitalini.
*********************
“Wewe Kana ukitaka upendwe na bi mkubwa, Mama Tambo, uwe kama babu yako, Paul. Hapo mtaelewana vizuri. Anachotaka Mama Tambo ni mtu asome sana, asiwe muongo, maana hapendi mtu muongo hata kidogo na ufuate maelekezo yake, hapo mbona utakula mema ya nchi! Hutakaa ukapata shida maishani.” Junior aliongeza huku akimwangalia Kana.
“Kaka! Kaka J! Mpe Kana mkasa wako na Mama Tambo.” Matilda alichokoza, na kufanya kila mtu acheke, mpaka Mama Tambo mwenyewe alitabasamu kidogo. “Mmbeya huyu!” Mama Tambo aliongeza. “Si kidogo tu mama jamani!” “Mbona yako huyasemi?” Mama Tambo aliuliza huku akikaa chini.
“Mama, umesahau mimi nilivyokuwa mtoto mzuri?” Wote walicheka. “Muogahuyo! Muoneni hivyohivyo na maneno mengi.” Mama Tambo aliongeza, wote wakacheka tena.
“Yaani Matilda nimuoga wa kupitiliza. Alikuwa akifanya kosa tu, hata kama amekosea akiwa shuleni, yaani yeye mwenyewe akirudi nyumbani atajisalimishakwa mama, na kama mama hayupo atampigia simu yeye mwenyewe ajielezee kosalake, kabla Mama T, hajamkamata.” Wote walicheka tena.
“Halafu Mat ndio alikuwa wa kwanza kwenye gari, si asubuhi mkienda shule, au mkirudi.” “Na wa kwanza kuamka ili asigongewe na mama.” Kila mtu alianza kumsema Matilda. “Halafu anaenda kulala kwenye gari wakati anatusubiria. Dereva alikuwa akimpenda kweli Mat! Wakati huo kalikuwa kadogo.” Matilda alikuwa akicheka sana.
“Nilikuwa namwona Kaka J na dada Martha, wanavyoingia matatizo kila siku, nikawa najiambia sitaki kupitia huko. Kwanza mimi mwoga sana wa fimbo.” “Wewe mwoga wakila kitu Matilda.” Dada yake aliingilia. Kila mtu alikuwa akicheka.
“Paul peke yake ndio alikuwa kwenye mstari.” Mama Tambo aliongeza na kufanya kila mtu akohoe. “Hata mkikohoa. Kwani uongo? Tangia anaanza shule ya msingi mpaka chuo kikuu, sijawahi kusikia amekosea popote. Sijawahi kuitwa shule hata mara moja. Muulizeni mwenyewe. Tokea anaanza shule alikuwa anachaguliwa kiongozi, mpaka vyuoni alikuwa kiongozi. Kila chuo alichosoma Paul alimaliza akiwa alishashika nyadhifa ya uraisi wa chuo.” Mama Tambo aliendelea kutetea.
“Haya bwana mama! Paul tena? Hamna ubishi. Lakini na sisi tunakupendasana.” “Mmmh!” Mama Tambo akaguna. “Tatizo lako huamini mama.” Junior aliongeza huku akiwakonyeza wenzake. “Mimi mwenyewe nampenda kweli Mama Tambo.” Martha aliongeza. “Hamnishindi mimi.” Mati naye alidakia. “Hamna lolote, mnanidanganya tu.”
“Wote mlinikimbia hapa, kasoro Paul, akaamua kubaki na mimi. Hata nilipomuudhi bado alibaki na mimi. Japokuwa tulipoteza mawasiliano lakini bado alikuwa anahakikisha ananiona kila week angalau mara moja. Alikuwa anakuja nyumbani kunitembelea kila ‘Week’ mpaka nilikuwa namuhurumia, nikaanza kuwa nakuja mimi mwenyewe huku Dar angalau apumzike na majukumu mengi aliyokuwa nayo.”
“Lakini nyinyi, nisipowapigia simu hata mwezi mnaweza kumaliza.” “Jamani mama! Mbona na mimi huwa nakupigia sana? Hata mara mbili kwa siku.” Matilda alijitetea. “Wewe simu zako za matatizo tu.” Kila mtu alicheka.
“Kweli bwana, Mat akikupigia simu, ujue anashida. Kama sio watoto wakewagonjwa basi ni shida zake nyingine. Na mwanae akiumwa, atataka wote muende mkamwangalie huyo mtoto. Hajali kazi ya mtu wala nini, atakulilia kwenye simu hata kama ni usiku uende kwake.” Martha aliongeza, kila mtu alikuwa akicheka.
“Huyo, hata mwanae akijigonga kwenye mlango atakupigia simu hata kama upo usingizini au kwenye kikao cha muhimu, anataka lazima kwa muda wake yeye, upokee simu yake. Na hana salamu, ukipokea tu moja kwa moja anaenda kwenye shida yake. Utasikia, ‘Sasa mama mimi nifanyaje, mwanangu analia sana.’ Ukiona tu simu yake unaanza kujiliza sijui limezuka lipi huko kwake, lakini si salamu.” Kila mtu alikuwa anacheka sana.
“Lakini Paul anamwigiza Kaka yake katika swala la upendo kwa mama.” Junior alimchokoza Mama Tambo. “Tena wewe ndio nyamaza kabisa. Ukitoa hapa kichwa chako, simu itakayofuata ni maagizo ya biashara zako tu. Hata salamu huna. Unanituma kama mtoto mdogo. Hamisha pesa hapa, peleka kule. Mpigie huyu simu, mwambie huyu hili, basi. Simu ya salamu utakayopata ni kutoka kwa wanae sio huyu baba mtu.” “Si nakuwa nawatuma?” “Huna lolote.” Kila mtu alikuwa akicheka.
“Lakini si unajua nakupenda mama yangu. Au sijakwambia vyakutosha?” Junior alimsogelea Mama Tambo nakumbusu. “Huna lolote! Ukiwepo hapa utanidanganya danganya kwa kunibusu na kunikumbatia kila wakati. Utanibeba hapa, utanibembeleza hili, ukiondoka hapa ndio sikusikii tena.” “Basi kuanzia leo, nitakuwa napiga kila siku kukutakia usiku mwema. Umesikia kipenzi changu?” “Wala huyawezi hayo. Mwachie tu Paul.” Kila mtu alikuwa akicheka sana. “Mimi na wewe Mama T? Ujue Paul alitukuta huyo?” “Mmmh!” Mama Tambo aliguna na kunyamaza.
“Bwana Kaka Junior, acha kumdanganya mama, wote tunajua hutapiga simu. Wewe tusimulie mkasa wako na Mama Tambo, basi.” Junior alicheka sana na kufanya kila mtu aanze kucheka upya. “Mat anapenda kunigombanisha na mama jamani! Nimesema nitabadilika, ile kazi inayonifanya niwe busy, nitaiiacha kabisa nibaki na mapenzi na mama yangu basi. Au unasemaje Mama T?” “Unavyopenda pesa wewe?” “Kweli tena kwa ajili yako naacha. Narudi kuishi na wewe.”
“Bwana hebu tusimulie Kaka J. Kila mtu anajua unamwibia mama.” Matilda aliendelea kusisitiza. Kila mtu alikuwa akicheka. “Basi ndio mnyamaze niwasimulie. Maana hii hata Paul mwenyewe haijui vizuri.” Junior naye alikuwa muongeaji kama Matilda. Ule utani uliokuwa ukiendelea kati yao, ulimfanya hata Sam kidogo kutulia. Ilikuwa ngumu sana kwa Sam kukaa chumba kimoja na watoto wa Tambo. Kwanza walionekana wasomi sana, sura zao tu zilinukia pesa tupu. Kwa utani ule, hata Sam kidogo alitulia na kuungana nao kucheka.
Mkasa Wa Junior Kwenye Mikono Ya Mama Tambo
“Si mnakumbuka ile sheria ya Mama Tambo yakutokukaa bweni au hosteli hata mkiwa chuoni? Au tuseme kabla kujamaliza shahada ya kwanza lazima wote mkae nyumbani kwa Mama T.” Junior aliuliza na ndugu zake wakaitikia.
“Sasa ujue ukiishi kwa Mama Tambo, hakuna kuvuta sigara wala kuonja pombe ya aina yoyote ile, upende, usipende. Nimesema ile kuonja tu hairuhusiwi, sio kunywa.” Kila mtu alicheka.
“Halafu marafiki zetu wote lazima awajue yeye, na kuwakubali, lasivyo hakuna urafiki hapo. Kingine cha kushangaza kwa Mama T, alikuwa anajua ratiba ya shule ya kila mtoto wake, kutoka asubuhi mpaka jioni mnaporudishwa na dereva hapa nyumbani. Kila kipindi kinachoendelea shuleni, yeye anajua. Na usafiri ni mmoja tu wakutuzungusha hapa mjini, gari yake Mama T na dereva wake.”
“Hata kama vipindi chuoni vinaisha saa nne za usiku, utakuta dereva anakusubiri nje. Hakuna kulala nje ya nyumba ya Mama T, hata iweje. Hata kama ni mgonjwa, utalazwa chumbani kwako, daktari atakuhudumia nyumbani, sio ukalale hospitalini. Labda siku mkienda kutembea nje nchi au sehemu fulani mbali na nyumbani, tena yeye akiwepo ndio mtalala hotelini. Si mnakumbuka jamani?” Junior aliuliza, kila mmoja aliitikia huku wakikumbushiana vituko kadhaa vya enzi hizo wanaishi nyumbani kwao.
“Endelea anko.” Sonia alitaka stori iendelee maana waliendelea kukumbushana huku wakicheka mpaka machozi. “Basi bwana. Nikawa nawatamania sana wenzangu jinsi wanavyo acha kuingia kwenye baadhi ya vipindi na kwenda kufanya starehe. Tukirudi chuoni siku za jumatatu walikuwa wakielezea starehe walizokuwa wakifanya jumamosi na jumapili. Basi mimi ndio nilikuwa naonekana mshamba kweli.”
“Kwani bibi alikuwa hawaruhusu kutoka siku za weekend?” Sonia aliuliza. “Subutu! Unaenda wapi?” Junior alijibu. “Si kutembea kwa marafiki zenu.” “Wewe acha mchezo kabisa. Siku hizo ndio za kufanya shuguli za nyumbani. Kwanza ukisema unaenda kwa rafiki yako, anakuuliza kwa nini huyo rafiki yako asije yeye hapa nyumbani? Kutoka ilikuwa siku ya jumapili, tena kanisani, mkishatoka hapo ndio baba alikuwa anatupeleka mahali kula, halafu mnarudishwa nyumbani, kuanza kujiandaa na shule kesho.”
“Siku za likizo, Mama T alikuwa anatutafutia kazi, wote mpaka Matilda alikuwa anatafutiwa kazi. Mnaondoka asubuhi na kurudi jioni. Hacheki na mtu huyo.” Wote walicheka.
“Mimi nilianzia kazi ya umesenja, mama alinitafutia kwenye ofisi ya mtu wakati huo nipo sekondari. Natengenezea watu chai na kusaidia usafi. Mwishowe nikaanza kufanya kazi za ofisini.” “Sio wewe tu Mat. Wote tulianzia hukohuko. Cheo kinapanda kutokana na elimu.” Paul aliongeza. Kila mtu alianza kucheka na kukumbushiana ajira zao za kwanza kabisa wakati wakiishi kwa mama yao.
“Anko endelea.” Sonia alimshitua baba yake mkubwa. “Sasa nikaanza kuchekwa chuoni, sina mwanamke, sijui starehe yeyote ile, kila wimbo unaoingia mjini, mimi siufahamu. Nikaamua kubadili maisha yangu kimyakimya bila kumwambia mtu. Nikaamua nianze mkakati wa kutoroka na wale wenzangu.”
“Nikapanga kuwa, tukiwa tunashushwa na dereva asubuhi pale chuoni, nakaa kidogo, wenzangu wakiingia mtaani niwe naenda nao, mpaka mida ya jioni ya kipindi cha mwisho na mimi narudi kwenye gari kama kina Martha na Paul wakati huo Paul sijui alikuwa ndio mwaka wa kwanza, au sekondari na Mat. Sikumbuki vizuri. Maana dereva alikuwa anaanza kuwapitia wadogo shuleni kwanza, ndipo anakuja kutuchukua na sisi chuoni.”
“Basi bwana, siku hiyo wale rafiki zangu nikawasikia wanapanga kutorokavipindi vya asubuhi ya siku inayofuata waende Bagamoyo, walisema kuna beach mpya imefunguliwa wanataka wakaione. Basi na mimi nikawaomba niongozane nao hiyo kesho yake, wakakubali.”
“Asubuhi ya siku inayofuata dereva alitushusha chuoni kama kawaida. Nakumbuka ilikuwa siku ya jumatano, tuliingia kwenye kipindi cha kwanza cha asubuhia, kisha tukaondoka mjini kuelekea Bagamoyo kwa kutumia gari ya mwenzetu tuliyekuwa tukisoma naye.”
“Tena jamaa mwenyewe alikuwa anafahamika sana pale chuoni. Alikuwa na gari na pesa za kumwaga. Sasa si unajua enzi hizo mwanafunzi akiwa na gari, ndio kila mtu anamjua pale chuoni? Basi jamaa alikuwa anajulikana chuo kizima.”
“Tukaondoka naye bwana! Hapo kwenye begi langu nilikuwa nimebeba nguo za kubadilisha, na vitu vya beach. Asubuhi yake tuliagana na Mama T, akatupa na hela ya kula kila kitu, akatukumbusha majukumu ya kufanya siku hiyo kila mmoja wetu atakaporudi nyumbani, yeye akaondoka zake kwenda kazini, sisi tukaondoka na dereva wetu kuelekea shuleni.”
“Asubuhi ilikuwa lazima wote muondoke pamoja, saa moja. Hata kama vipindi vyako vinaanza saa nne asubuhi, ilimradi mmoja wenu anakipindi cha mapema sana, Mama T alikuwa anasema mnaondoka wote, mkajisomee.” Wadogo zake Junior walianza kucheka kila walipokuwa wakikumbuka sheria za Mama Tambo.
“Basi bwana, hapo nikawa nishamdanganya Mama T, anipe pesa za ziada. Akanipa bwana, kumbe mwenzangu anajua kila kitu kinachoendelea mimi sina habari. Njiani wakati tunaelekea Bagamoyo, nakwambia mimi ndio nilikuwa kinara, nimechangamka kweli kweli. Nawapigisha jamaa stori, tunacheka mpaka huko Bwagamoyo, kwenye maraha.”
“Tukaingia zetu kwenye hiyo hoteli mpya, tukaagiza vinywaji, wenzangu wakachukua pombe, mimi nikaagiza soda yangu tukaelekea baharini. Kwanza wenzangu wote walianza kunicheka kwa nini nakunywa soda na sio pombe, lakini nikawaambia ni heri waendelee kunicheka kuliko yule mwanamke aje kugundua nimeweka pombe mdomoni kwangu, nitanyongwa.” Wote walicheka. Sonia alikuwa akicheka pia. “Usicheke Sonia, mbona utamu bado.” “Eehe!” Sonia alitaka aendelee.
“Ile nataka kuingia tu ndani ya maji, nashangaa jamaa watatu wamesimamapembeni yangu. Nasikia ‘Tambo Junior.’ Nilitamani kufa. Nilijikaza kiume mbele ya wenzangu, lakini nilijua wazi kifo changu kimewadia. Nikajifanya sio mimi. Wakarudia tena. ‘Tambo Junior.’ Nilijua kabisa huyo ni Mama T ndio anayeniita, maana shule najulikana kama Junior Tambo. Lakini ukishasikia ‘Tambo Junior’, ujue huyo ndio mwenyewe Mama T na ujue wapo pale kumuwakilisha Mama T.”
“Nikawajibu, hapa hakuna mtu mwenye jina hilo. Mmoja wetu akataka kufanya fujo. Walimchapa makofi, halafu mimi nikaambiwa nichukue vitu vyangu, tunaondoka. Jasho lilishaanza kunitoka. Kumbe wale walikuwa askari kanzu bwana. Nikaingizwa kwenye gari, nikajua napelekwa ofisini kwa Mama T.”
“Njia nzima nikawa napanga cha kujitetea nikifikishwa huko alipo Mama T. Eee bwana wee, nashangaa napelekwa Ostabay polisi. Sikuamini! Nikajua labda mama yuko pale. Nimefikishwa pale, nikapokelewa begi langu la shule, si wakaniingiza rumande. Acha niogope nakuanza kupiga kelele. Eti nawaambia, mnajua mimi ni nani? Mimi ni Junior Tambo mtoto wa waziri Tambo. Kwani kuna aliyekuwa ananisikiliza?” Martha ndio alikuwa anacheka mpaka machozi. Kila mtu alikuwa akicheka kasoro Sonia.
“Sasa watakuwa walikosea!? Mtoto wa Mama Tambo tena wanakupeleka jela!?” Sonia aliuliza. “Wewe kumbe hujaelewa Sonia? Wale askari walikuwa wametumwana Mama T, mwenyewe. Wewe unamchezea Mama T? Hapo walipewa maagizo wanikamate, halafu waniweke jela.” Hapo ndio kila mtu alianza kucheka, kasoroMama Tambo mwenyewe alibaki kimya anaangalia simu yake.
“Njaa ilianza kuuma, mbu, halafu chumba chenyewe kilikuwa giza, wakati ilikuwa bado asubuhi. Ilikuwa kama saa tano nilipoingizwa mle ndani. Nilikaa humo mpaka usiku, natetemeka kama nimetupiwa kwenye chumba cha baridi kali sana, kumbe hofu bwana.”
“Nawasikia tu wale maaskari wanavyonisema, ‘Humo yumo mtoto wa Mheshimiwa Tambo’. ‘Unamaanisha mtoto wa Mama?’ ‘Ndiyo.’ ‘Mkuu wa kituo anafahamu kama mtoto wa wenyewe yupo rumande?’ ‘Nasikia Mama mwenyewe ndio amesema awekwe humo, na amesema mtu yeyote asiongee naye.’ Halafu wakaacha kuniongelea mimi wakaendelea na kazi zao kama kawaida.”
“Sikupewa chakula wala maji ya kunywa, siku nzima. Baadaye sana, yaani yalishapita hata masaa saba labda, nikasikia wanaambizana tena, ‘Anakuja, anakuja. Mkuu amesema tukae tayari yupo njiani anakuja. Na yeye anakuja sasa hivi ili kumpokea.’ ‘Kwani mkuu hajaondoka mpaka sasa hivi?’ Wale polisi wa zamu wakawa wanaulizana hapo mapokezi, mimi nasikiliza tu.
‘Anaondoka vipi wakati mtoto wa wenyewe yupo humu ndani? Lazima asuburi maelezo ya ziada.’ Basi hapo nikajua tu huyo anayesemwa anakuja ni Mama T. Gafla nikasikia huyo Mkuu wa kituo cha hapo Ostabay ametoka, akawapanga polisi wengine, huku akiwaambia watu wa usalama watafika hapo muda sio mrefu kukagua hapo kabla Mama mwenyewe hajaja. Nilianza kusikia mkojo unauma, halafu hakuna choo ni ndoo.” Kila mtu alikuwa akicheka sana.
“Baada ya muda nikaanza kusikia salamu za heshima zinatolewa, nikajua mwenyewe amefika. Nikasimama kama mshale huku najipanga maneno yakumwambia. Nikashangaa Mama T kasimama mlangoni pale nilipokuwa nimefungiwa.”
“Kabla sijasalimia, akanitupia swali. ‘Unataka kuendelea kuwa jambazi, au unataka shule?’ Hapo natetemeka kama nimepigwa na radi au umeme. Mpaka meno yalikuwa yanagongana. Nikajibu shule. Basi bwana mimi si nikajua mambo yameisha, naondoka naye.”
“Akawageukia wale polisi, ‘Kesho saa moja kamili asubuhi dereva atakuja kumchukua kumpeleka chuoni kwao, saa mbili kamili ana mtihani. Nimeomba majibu ya huo mtihani kesho hiyohiyo kabla ya saa kumi jioni. Akifanya vizuri kwenye mtihani wake, jioni baada ya vipindi vyote atarudi nyumbani, akifeli tu, hata kwa kupata alama ya B kwenye huo mtihani, nitajua amechagua kuwa jambazi, atarudishwa hapahapa, ndipo atakapohukumiwa kama majambazi wengine.” “Haaaa!” Sonia akashangaa sana, wengine wanakaukia kucheka.
“Subiri Sonia. Mbona bado!” Anko wake akaendelea kumuigiza mama yake. “Akawageukia askari wake. Akawaambia. ‘Asubuhi ya leo amenidanganya, nikampa pesa. Hilo ni kosa la wizi. Na mimi pale nyumbani nina watoto wengine watatu, siwezi nikawaweka nyumba moja na jambazi. Nitakuwa nahatarisha maisha ya watoto wangu, hata hivyo pale sio jela yakutunza majambazi.” Walizidi kucheka mpaka Paul alikuwa akikaukia, mama Tambo mwenyewe kimya kama hasikii.
Na Junior alikuwa akimuigiza mama yake mpaka sauti. ‘Na tukimuachia akakaa mtaani bila kumdhibiti mapema, muda sio mrefu ataanza kuvunja majumba ya watu na mabenki ili aibe. Sasa maadamu yupo chini ya ulinzi wetu, lazima kumdhibiti mapema sana, kabla hajafika mbali.’ Miguu ilianza kuishiwa nguvu, nikahisi naota. Nikakaa chini. Bila kuaga wala kuongeza neno, nikamuona anaondoka, ananiacha palepale.” Kila mtu alikuwa akicheka mpaka machozi.
“Kwa hiyo ulilala jela!?” Sonia aliuliza kwa mshangao. “Unafanya mchezo na Mama T, wewe? Kwanza ujue mama huwa haropoki, na wala harudii kuongea. Machozi ndio hayambambaishi hata kidogo. Basi bwana, nikakaa pale kama baada ya dakika moja nikamsikia anarudi, akaniambia, ‘Eti nina msaada mmoja kwako.’Nikasimama haraka haraka, nikajua, natolewa mle ndani nikapewe chakula au nihamishwe mle ndani.” “Kumbe!?” Sonia aliuliza tena kwa mshangao.
“Subutu yangu! Sikiliza sasa msaada wa bibi yako. Eti, ‘Utakapo kuwa tayari kujiandaa na mtihani wako wa kesho, utawaomba hao polisi hapo mapokezi, wakupe madaftari yako uliyokuwa umeyaacha kitandani kwako leo asubuhi, nimekuletea na kurunzi. Ili…” “Kurunzi!?” Sonia aliuliza. “Kurunzi, ni yale matochi makubwa, ili nisome sasa, lakini humohumo jela, kwa ajili ya kujiandaa na mtihani.” Sonia alicheka sana.
“Kama utani bwana, nililala pale pale polisi. Nakwambia usiku kucha nilikuwa nasoma, tena bila kula.” “Ulifaulu sasa?” Sonia aliuliza huku akicheka. “Ningekuwa Enginer sasa? Au ningekuwa hapa leo? Nakwambia nilisoma usiku kuchwa. Asubuhi nikaja kufuatwa na dereva huku nasindikizwa na askari kanzu mwingine, mpaka chuo. Nikakimbilia mgahawani kwanza kupata supu, maana nilikuwa na njaa balaa.”
“Niliingia kwenye mtihani kila swali lililoulizwa siku ile kwenye ule mtihani, nilikuwa nina jibu lake. Ndio kwa mara ya kwanza siku hiyo nilimuomba Mungu kwa kutulia na kumaanisha, ili anitendee muujiza, nifaulu sana, ili nisirudi jela. Hapo nipo na yule askari kanzu ananifuatilia kila ninapoenda, ili kama nimefeli, anirudishe rumande.”
“Hapo nilikuwa nina hasira na Mama T na yule askari kanzu, aliyekuwa akinifuata mpaka chooni! Ilipofika mida ya mchana nikaona amepigiwa simu kisha akaondoka, tena bila kuaga, nikajua nimefaulu. Ndio kuanzia siku ile, hata wale marafiki sikuwataka tena. Nikaamua nitulie kabisa na kujitenga nao.”
“Halafu Mama T jinsi alivyo, kama baada ya miezi miwili akatupeleka kwenye ileile beach sisi wote hapa. Tulikaa huko siku nzima. Nilifurahi kweli.” “Sasa baba yenu alikuwa anasemaje.” Sonia aliendelea kuhoji. “Unamuona baba yako jinsi alivyo hivyo? Basi ndio baba yetu alivyokuwa. Hivyohivyo. Lakini baba alizidi ukimya. Ilikuwa ukimsikia anaongea baba, ujue anamfariji mtu, au kukutia moyo au kukufundisha kitu, na ucheshi, tena kidogo sana. Hajui kugombana na mtu yeyote. Mambo ya shule yote, nidhamu, na mambo mengine ya kesi zetu ilikuwa ni kazi ya Mama T, yeye kimya.” Wote walikuwa wakicheka sana.
“We Junior! Mbona hujamaliza kuwasimulia mpaka mwisho?” “Nini tena mama?” “Wale rafiki zako uliokuwa umewaacha Bagamoyo.” “Eeeh bwana wee! Kweli mama! Unajua wale rafiki zangu tuliokuwa tumeenda nao Bagamoyo, nikawaacha wana kunywa na kuogelea walipata ajali mbaya sana!”
“Kama baada ya siku mbili tukaja kusikia walipata ajali sababu walikuwa wanaendesha huku wamelewa. Mmoja alifariki papo hapo, wengine waliumia vibaya sana na chuo walifukuzwa kabisa kwa kosa la kutoroka katikati ya vipindi na kwenda kufanya starehe.”
“Nilishituka sana, nikajua na mimi ningekuwa mmoja wao. Nilimwandikia mama barua ya kumshukuru sana.” “Kumbe afadhali bibi alikuokoa, anko?” Sonia aliongeza. “Bwana Mama T anakuaga sahihi, lakini adhabu zake bwana! Yani mpaka wazo likikujia la kurudia kosa, unajichapa makofi mwenyewe.” Wote walicheka.
Mkasa Wa Binti Wa Pili, Wa Tambo, Martha, Mikononi Kwa Mama Tambo
“Martha msimulie Sonia na wewe mkasa wako.” Walikuwa wakicheka na kukumbushana mambo yao ya utotoni. Wote walikuwa wakicheka sana, lakini Mama Tambo alikuwa kimya kabisa. “Eeh bwana Martha! Tusimulie na wewe.” Junior aliongeza. “Sonia asije akafikiria mimi ndio nilikuwa mtoto mtukutu peke yangu.” Junior alimalizia.
Martha alicheka kidogo. “Haya, sheria ya Mama T, nyingine ilikuwa lazima mpaka shahada ya kwanza usomee ukiwa nyumbani kwake, lakini shahada ya pili ndio chaguo lako, unaweza kusomea popote. Halafu kingine ilikuwa lazima kila mtoto asome shahada mbili ndipo unaruhusiwa uendelee na maisha yako.”
“Kama unataka kufanya kazi au unataka ndoa hapo ndio ruksa, sio vinginevyo. Nilipomaliza shahada yangu ya kwanza, nikamwambia mama nataka nikasome nje ya nchi. Basi, Mama T akanitafutia chuo South Africa. Nikatoka zangu hapa mpaka South Africa, tena wakati huo ndio kulikuwa na ubaguzi balaa, lakini watoto wote wa viongozi wa nchi mbalimbali tuliheshimiwa sana.”
“Hapo nilikuwa nafuraha zangu zote, nipo huru mbali na Mama Tambo, kanilipia ada, halafu akanipa na pesa za kujikimu nyingi zaidi ya nilivyofikiria. Nikafika zangu huko chuo, sasa mwaka wa pili nikakutana na mwanaume, tukapendana, tukaamua kuhamia mtaani, tutafute chumba, tuishi pamoja.”
“Mimi ndio nilikuwa tajiri sana wakati huo. Mama T, kwa kutoa hela hana neno. Wewe mtajie tu hela yoyote na maelezo mazuri, anakupa hela bila ubishi. Halafu pia alitufundisha kuweka pesa tokea tuko shule. Si unakumbuka Junior alisimulia kipindi cha likizo wote tulikuwa tukifanya kazi?” “Nakumbuka.” Sonia alijibu.
“Basi ule mshahara kila mmoja alikuwa anatunza benki. Sasa turudi kwa mikakati yangu na mupenzi wa kule South.” Wote walicheka. “Hapo nimechanganyikiwa kweli kweli kwa mapenzi. Ndio mwanaume wangu wa kwanza, nipo huru, hamna Mama Tambo wala sheria inayonifunga, halafu pesa ninayo ya kumwaga.”
“Tukatafuta chumba, tukapata sehemu ya kuishi mtaani. Nikahama hosteli na huyo mwanaume kwenye hicho chumba. Tulikuwa tuna raha wenyewe, nakwambia mapenzi mazito.” “Shule?” Sonia akauliza. “Shule tena! ‘Who cares?’” Martha aliuliza huku anacheka. “Kwani Mama Tambo anaona? Shule nilikuwa naenda nikipenda au nikijisikia. Siku nyingine nikawa siendi, nakaa nyumbani na MUPENZI.”
“Naona hata mwezi hatukumaliza, siku hiyo jioni nashangaa mlango unagongwa. Nikafungua mlango nikaona wanaume wawili wamenisimamia mlangoni, tena wa kitanzania. ‘Martha Tambo?’ Nikawaambia ndio mimi. ‘Twende’. Yule mwanaume au mpenzi si akataka kufanya fujo, akachapwa na yeye makofi akawekwa kitandani, wakachukua hati yangu ya kusafiria tu, tukaongozana mpaka uwanja wa ndege na tiketi yangu walishakata.”
“Ndege imetua tu uwanja wa ndege wa hapa Dar, nikamkuta Mama T akinisubiria. Nilikuwa natetemeka kwa hofu, lakini kwa kuwa na mimi jeurisikutaka kumuonyesha mama.” Wote walianza kucheka tena.
“Bila salamu, akaanza, ‘Unataka kusoma, au unataka kuendelea na biashara ya ukahaba?’ Hapo akili ikachemka haraka sana. Nikajiambia, nikijitetea chochote, nitazidi kujiweka matatizoni, nikaamua kusema shule.”
“Akanijibu ‘Nimekutafutia chuo cha kusomea udaktari, nchini India, utaenda kuanza upya mwaka wa kwanza, kwa kuwa umepoteza muda mwingi huko South Africa kwenye biashara yako ya ukahaba, utasoma mpaka umalize bila kukatisha hata mwaka mmoja. Umenielewa?’ Nilitamani kurukwa na akili.”
“Nikamuuliza kwa ukali, ‘Umesema mwaka wa kwanzwa!?’ Akanyamaza kimya akiniangalia, kama kawaida yake harudii jambo. ‘Kwa nini nisihamishie masomo yangu niliyokuwa nikisomea huko South Africa?’ Nikauliza tena, hakujibu lakini akanitizama kwa jicho hilo, nikajua ndio adhabu anayonipa.”
“Yaani amenihesabia kama nilikuwa sisomi huko South Africa, nilikuwa nafanya uhuni tu. Nikakasirika na mimi, nikaamua kujitutumua nikamwambia, ‘Kama ni hivyo shule sitaki. Sisomi tena.’ Akanijibu kwa kifupi tu, ‘Sawa.’ Kisha akageuza kichwa nyuma, nikawa najiuliza, anaangalia nini? Sijakaa sawa, nasikia ‘Martha Tambo upo chini ya ulinzi, kwa kujihusisha na biashara ya ukahaba nchini South Africa.’ Unajua Mama Tambo aliniangalia, akatabasamu, akageuka na kuondoka zake! Aliniacha palepale uwanja wa ndege na wale polisi?” Kila mtu alianza kucheka tena.
“Haiwezekani anti!” Sonia alishangaa sana. “Unacheza na Mama Tambo wewe? Nikabebwa mpaka Ostabay polisi. Wakati nipo humo ndani, selo, ilikuwa siku ya ijumaa, nikaona wanaingizwa kina dada wengine, walionekana kabisa ni machangu. Wakaanza kupiga story zao bila wasiwasi. Nikaanza kuwauliza maswali mawili matatu.” “Ulikuwa huogopi anti?” Sonia aliuliza. “Mimi nahisi nina roho kama ya mama. Mpaka unione nimeingiwa na hofu, ujue ni kitu kibaya sana.” Alijibu Martha.
“Na mimi kwa kuwa namjua jeuri yake, ndio maana nilimjia na polisi kabisa tena walikuwa wamevaa sare za kipolisi na nilisha waandaa kabisa, nikawaambia huyo ni jeuri kweli kweli. Nilijua angenibishia tu. Kwa hiyo nikaona nimpe tu nafasi moja ya kumjaribu kama angekubali kwenda India kusoma.”
“Nikawaambia wale polisi wanisubirie niongee naye kwanza, ili asije laumubaadaye kuwa sikumpa nafasi ya kurekebisha makosa yake. Nikawaambia akikataa ndio wamchukue.” Mama Tambo alijibu bila wasiwasi. Wote walikuwa wakicheka sana.
“Sasa bibi ulikuwa huwaonei huruma?!” “Ndio huruma yenyewe hiyo! We unafikiri bila hivyo wangekuwa hivyo walivyo sasa hivi? Ilibidi kuwa nao makini sana, lasivyo wangeharibikiwa wote hawa. Walizaliwa kwenye mafanikio sana. Walikuta baba yao amejijenga, halafu anajina zuri nchini. Mama ndio hivyo, ingekuwa rahisi sana kubweteka na kuwa watu wa ajabu.” Wote walikuwa wakicheka sana.
“Sasa ikawaje anti Martha?” Sonia aliendelea kuhoji. “Nikaanza kuwauliza maswali wale machangu, wakati huo ilikuwa mwiko biashara ya machangu.” “Hata sasa ni mwiko.” Mama Tambo aliingilia. “Basi, walikuwa wamekamatwa na polisi waliokuwa doria, ndio wakaletwa pale.”
“Nikaanza kuwaauliza maswali. Kila mmoja akaanza kunielezea historia ya maisha yake, niliumia sana. Wote walikuwa kwenye mazingira yaliyowalazimisha kufanya hizo biashara ya ukahaba. Nakumbuka tulikuwa tukiongea usiku kucha. Waliponiuliza kisa changu mimi, walinishangaa na kunisema sana. Huku wakiniambia nachezea bahati.”
“Basi, palipo pambazuka, nikaomba wale polisi waliokuwa zamu, wampigie simu BABA aje niongee naye. Baada ya muda, nikasikia sauti ya Mama T akisalimiana na mapolisi pale kituoni. Nikajua kazi imeanza.”
“Akaja pale kwenye mlango akaniambia baba amesafiri kikazi, lakini amemtuma yeye aje pale nizungumze naye. Kwa kuwa nilikuwa nimemkasirikiasana, nikamwambia ampigie simu baba, nataka kuzungumza na baba sio yeye. Akaniambia huko alipo baba hawezi kuzungumza na mimi. Nikamwambia na mimi sitaki kuongea na yeye.” Marta akaanza kucheka.
“Nini?” Sonia akauliza. “Unajua mama akageuka na kuondoka mpaka pale mapokezi bila hata yakunijibu kitu. Nikasikia akimwambia yule mkuu wa kituo. ‘Tambo yupo safarini kikazi, baada ya siku kumi ndipo atarudi. Wakati mnawapeleka wafungwa wengine jela, naomba mumpeleke na yeye huko huko jela, kama baba yake atachelewa kurudi na kesi yake ya ukahaba itatakiwa kusikilizwa mahakamani, tafadhali, apelekwe na ahukumiwe kama wafungwa wengine wakawaida, kama baba yake atarudi na kuamua kumtafutia wakili wa kumtetea basi hiyo itakuwa juu yao.’ Hofu ikaanza kuniingia. Kisha Nikamsikia anaagana nao.”
“Acha nipige kelele namuita. Kwani alirudi?” “Hakurudi!?” Sonia alishangaa sana. “Wewe humjui Mama Tambo. Nikaanza kulia kwa sauti sana, nikamsikia afande mmoja anamwambia. ‘Huyo ni mtoto wako mama, anakuita’. Mama akajibu, lakini nikajua wazi ananijibu mimi. Eti yeye alikuwa na dakika tano tu pale kituoni na zimeshamwishia, anawahi ofisini kwake. Lakini atarudi tena pale kituoni kesho yakeatakapotoka kanisani, kama bado nitakuwa sijapelekwa jela, basi tunaweza kupata muda wa maongezi lakini kama nitakuwa nimepelekwa jela, eti huyo polisi aniambie baba atakuja kunifuata huko jela, yeye hawezi kufika jela.”
“Nilitamani kuchanganyikiwa, nikifikiria kulala tena pale! Nilikuwa sina hamu.” “Aliondoka?” “Mimi naona Sonia hujaelewa tunachokwambia.” Junior aliingilia. “Nakwambia Mama T haropoki, na harudii neno. Akiongea neno lake mara moja, ujue ndio AMEMALIZA.” Kila mtu alikuwa akicheka.
“Aliondoka na kuniacha pale mpaka kesho yake, tena jioni ndio akarudi kama saa kumi hivi. Hapo nilikuwa nina hasira natamani kupasuka. Halafu alivyo mkorofi mama jamani! Eti akafika pale mlangoni, ananiambia ana dakika moja tu yakuongea na mimi, ikiisha hiyo dakika moja, akiondoka, hatakaa arudi tena pale.” Waliendelea kucheka sana huku wakimwangalia Mama T aliyekuwa ameinamia simu yake.
“Eehe?” “Sikutaka kupoteza muda, nikamwambia nataka kwenda shule. Akanijibu, kila kitu changu kipo tayari, naondoka na ndege ya saa nne na nusu usiku kuelekea nchini India, kuanza masomo ya udaktari na polisi ndio watanisindikizauwanja wa ndege.” “Bibi wewe?!” Sonia alishituka sana.
“Usimuone hivyo huyo anakusimulia kwa upole hapo. Mkorofi kwelikweli na roho yake ni zaidi ya simba. Bila hivyo huyo angekuwa jambazi sugu la hapa nchini akisaidiana na kaka yake huyo. Nikaona hiyo roho yake inafaa akapasue wagonjwa huko hospitalini.” Mama Tambo alijibu, kila mtu alianza kucheka upya.
“Na kweli dada Martha ana roho ngumu ya kupitiliza jamani! Sisi wenyewe tulikuwa tuna muogopa.” Matilda aliongeza. “Sasa ikawaje?” Sonia alihoji tena. “Unauliza jibu Sonia? Kashaniambia ana dakika moja pale kituoni, unafikiri anakutania? Alipomaliza kuongea hivyo tu, akaondoka bila swali, wala jibu.”
“Ilipofika saa tatu usiku, nikaja kutolewa mle ndani, nikakuta kila kitu changu kinanisubiria pale mapokezi, nikaingizwa kwenye gari ya polisi kama mwizi, mpaka uwanja wa ndege. Nikaanza chuo changu cha udaktari bila ubishi.”
“Baada ya kama mwezi hivi, baba akaja kunitembelea. Jamani siku ile nililiakama nimefiwa. Tulikaa na baba siku nzima, bila kuongea kitu chochote mpaka akaniaga, nilikuwa nikilia tu. Sijawahi kulia hivyo tena.”
“Unamuona hivyo Paul, baba yako anavyo kubembeleza? Ndivyo alivyokuwa baba yetu. Alibaki akinibembeleza siku nzima, bila kula wala kunywa, tulikuwa tumekaa hotelini kwenye chumba alichokuwa amefikia, nalia tu. Wakati tunaagana uwanja wa ndege, baba akaniachia barua kutoka kwa mama, ilikuwa barua nzuri sana.”
“Aliomba msamaha?” Sonia aliuliza. “Msamaha!? Mama Tambo aombe msamaha? Yaani leo ndio kwa mara ya kwanza sisi kumuona mama anaomba msamaha.” Martha alijibu. “Kwa kuwa sikuwahi kukosa je!” Mama Tambo akajibu, watoto wote walianza kukohoa, kasoro Paul alibaki kucheka kimya kimya.
“Sasa ilikuwa barua ya nini?” Sonia alihoji tena. “Aliniambia maneno mengi mazuri, kama mama kwa mtoto, lakini kikubwa alikuwa akinituliza na kuniambia ni kiasi gani ananipenda na anataka nifanikiwe sana katika maisha yangu, na anaamini ipo siku nitapata mwanaume anayenipenda na atakayeniongoza vizuri.Nilifurahi sana, ile barua ninayo mpaka leo.”
“Basi tulikaa na baba, nikalia mpaka nikajisikia vizuri, akaondoka usiku, akasema anawahi kwenye mkutano sijui nchi gani hata sikuwa nasikiliza kwa uchungu. Nakumbuka nilimsindikiza mpaka uwanja wa ndege nikabaki nimemkumbatia baba huku nalia, mpaka aliponiambia nilazima aondoke lasivyo ataachwa na ndege, ndio akanipa na hiyo barua ya mama, akaondoka.”
“Hakukugombeza kwa maisha uliyokuwa ukiishi South Africa?” “Baba alikuwa mpole sana, na alijua mkewe anatumudu sisi wote. Kwa hiyo yeye alikubali kuwa ndio kimbilio letu.” “Daah! Mzee Tambo tutamkumbuka daima jamani.” Junior aliongeza.
“Natamani angekuwepo ukutane naye Sonia. Sijawahi kukutana na mtu mzuri kama baba yetu, jamani! Alikuwa mwema sana.” Paul naye aliongeza. “Yaani mimi na jeuri yangu yote, pale ilikuwa mwisho. Kila wakati alikuwa akiniona nafanya ukorofi, utamuona ananiita na kuanza kuniambi kwa upole, ‘Unajua Martha wewe ni mtoto mzuri sana?’ Hata nifanye nini au nifanye ukorofi wa namna gani, yeye neno lake kwangu lilikuwa ni hilo tu.” Wote walipooza gafla vicheko vilikoma kwa muda kama wanao tafakari. Walimuona Mama Tambo akifuta machozi na kutoka nje. Paul akamfuata.
“Poleni jamani.” Ishimwe alijaribu kuwafariji. “Daah!” Junior aliendelea kulalamika. “Mimi ndio alinilea kama kiziwanda kweli kweli. Sikuwahi kukua kwa baba jamani! Nilikuwa namsumbua kipindi kile mjamzito kama ndio mume wangu! Hata usiku nikitapika nilikuwa nampigia yeye simu. Nitalia na kulalamika kwenye simu, basi baba atanibembeleza mpaka nalala.”
“Hakuwa na maneno na mtu yeyote kama Paul. Mtu akimchukia Paul, ujue yeye ndio mwenye tatizo. Paul anaweza kuishi na kila mtu, na mahali popote kama baba.” “Mmmh! Mat wewe ulizidi kudeka kwa baba bwana! Ulikuwa ukimzungusha yule Mzee kwenye ndege kukufuata kama rubani! Akiona simu inatoka kwa baba, ujue Mat anatatizo. Utasikia nenda kamuone mtoto. Hata kama umelala, utasikia, “nenda tu Martha mwanangu, halafu ukifika huko nipigie simu niongee naye”. Basi ilimradi tu awe na uhakika Matilda hayupo peke yake.”
“Mpaka nikaamua huyu Matilda ahamie karibu na ninapoishi kupunguza usumbufu kwangu na baba. Maana safari za nyumbani kwake zilikuwa haziishi.” Walitulia kidogo. “Na baba naye alikuwa karibu na babu?” Sonia aliuliza. “Paul yeye wakila mtu, lakini zaidi Mama Tambo. Huwezi jua anamwingiaje mama! Mnaweza mkamkasirikia mama watu wote lakini sio Paul. Anampeda sana mama, na hawezi kweli kuishi mbali naye kitu kilichokuwa kikimshangaza kila mtu.”
“Paul na baba ndio watu pekee waliokuwa wakimuweza mama. Ndio watu pekee wanao mjulia Mama Tambo.” “Jamani mama alilia siku ya mazishi ya baba.” “Sio kulia tu, alishindwa hata kuzika. Alizimia, akakimbizwa hospitalini. Sijawahi kuona mama akiwa ameumia hivyo!” Waliendelea kumkumbuka baba yao, kwa muda. Paul alirudi akiwa amemkumbatia Mama Tambo.
*********************
“Tumeongea na daktari, nimeomba Sonia ahamishiwe nyumbani, watakuwa wanakuja kumtibu palepale nyumbani. Sipendi haya maisha ya hospitalini hata kidogo.” Mama Tambo aliwataarifu mara baada ya kuingia mle ndani. “Afadhali. Asante bibi. Maana nilikuwa nafikiria kukaa hapa hospitalini mpaka kujifungua! Ningechoka sana. Asante.”
“Karibu. Lakini si tunaenda wote nyumbani kwa baba yako?” Mama Tambo alimuuliza Sonia. “Tulianza kuongea na Sam juu ya hilo. Naomba tupate muda wakuzungumza kwanza, halafu nitakujibu bibi.” “Basi tutoke, mzungumze. Maana tumepata muuguzi ambaye amekubali kwenda na sisi. Nataka ukalale nyumbani leo.” “Kumbe ni leo!?” Sonia aliuliza kwa mshangao.
“Ndiyo, leo. Nataka nihakikishe umetulia kwanza na kila kitu kipo sawa ndipo naweza kurudi kwangu. Siwezi kukuacha hapa hospitalini. Hata hivyo ni kwa kuwa sikuacha mambo vizuri nyumbani kwangu, tungelala wote. Nataka niende nikarekebishe, halafu kesho asubuhi nitarudi tukae wote, ili mama yako apate muda wakujiandaa na harusi.” Sonia alifurahi sana.
“Asante bibi.” “Mimi nitabaki nyumbani na Sonia hiyo siku ya harusi.” Sam aliingilia. “Basi kazi imeisha. Si mmeona mambo yalivyokwenda vizuri? Sam atakuwepo na Sonia nyumbani, harusi ikiisha tu, Mama T atarudi kukaa na Sonia wakati nyinyi mpo kwenye fungate/honeymoon yenu. Kwa hiyo msiwe na wasiwasi.” Junior aliingilia.
“Asante sana mama.” Paul alimgeukia mama yake, aliyekuwa bado amemkumbatia, akashukuru na kumbusu kichwani. Paul alikuwa mrefu kwa mama yake. “Mbona namuona Ishimwe hana raha?” Mama Tambo aliuliza. “Naona kama tunakuachia majukumu mazito mama! Unahitaji na wewe kupumzika, sio kukaa na mgonjwa tena.” “Wala usijali Ishimwe. Acha na sisi tukupokee huu mzigo wa Sonia.”
“Kwanza ndio nafurahia. Sasa hivi sina kitu chakufanya. Angalau najiona ni kama nitakuwa na kitu cha muhimu cha kufanya kuliko kukaa tu nyumbani. Wewe si ulikuwa unamtaka Paul?” Ishimwe alianza kucheka huku ameinama.
“Eti Ishimwe?” “Ndiyo mama.” “Sasa umempata. Umekaa miaka yote hiyo ukimsubiri, Mungu amekurudishia mumeo, sasa inabidi ufurahie. Huyu Sonia utamkuta tu. Na ukirudi tu, tutamfanyia babyshower akiwa hapo hapo kitandani.” Watu walianza kucheka kidogo.
“Na mimi nilileta zawadi za mtoto, Sonia. Nitampa mama akuwekee mpaka hiyo siku ya baby shower.” Matilda aliongeza. “Mimi nitakuja nazo za kwangu ukijifungua.” Martha naye aliongeza. “Makubwa! Utarudi Martha?” Mama Tambo alishangaa sana. Wote wakacheka. “Nitarudi mama jamani! Nishakuwa mtu mzima. Lazima nije kuona mjukuu.” Wote walicheka. “Asante Martha. Na karibu sana, milango yetu iko wazi, muda na wakati wowote.” Paul alishukuru.
“Kwa kuwa mimi nimepewa kazi ya ujenzi wa nyumba, naona nihakikishe hiyo nyumba inakuwa tayari kabla Sonia hajajifungua.” Paul alishituka sana na kumgeukia kaka yake. “Nyumba gani?” Paul aliuliza. “Si hiyo ya Sonia na mumewe? Kwani mama hajakwambia?” Paul alimgeukia mama yake.
“Mwache yeye ndio arekebishe hiyo nyumba, Paul. Una mambo mengi sana. Ndio umepata familia sasa hivi. Najua utakuwa na majukumu mengi sana, mpaka uje kuweka sawa mambo yote, utahitaji pesa nyingi. Acha wenzako wakusaidie.” Mama Tambo alijibu.
“Wala usiwe na wasiwasi Paul, tumepiga mahesabu na Kat..” Junior alikumbuka. “Daah! Mnisamehe sana jamani, maana Kato ndio kama mtu wangu hapa nchini, namtumia kwa kila kitu. Ndio maana nilimuita nikitaka tuzungumzie huo ujenzi, sikujua kama ni mtu mbaya hivyo.” Paul alibaki kimya kama anayefikiria kwa undani.
“Lakini hamna shida Paul, sitaki nikuvurugie familia yako. Kato aliniambia anaye rafiki yake mwenye kampuni ya ujenzi, tulishaongea nao na kukubaliana bei, lakini tutatafuta kampuni nyingine ya ujenzi ambao watatusaidia kujenga hiyo nyumba vizuri na kwa haraka. Usiwe na wasiwasi Sonia. Sawa sweetheart? Siwezi kumrudisha tena kwenye maisha yako.”
“Hapana anko, hata nifanyeje huyo Kato atakuwepo tu kwenye maisha yangu, ni baba yake Kana.” Paul alikuwa kimya kabisa akifikiria. Mama Tambo alimshika mkono wake uliokuwa begani mwake.
“Unafikiria nini Paul?” “Nafikiri sasa hivi tumuache kwanza Kato mpaka Sonia atakapokuwa tayari kukutana naye. Naomba asijihusishe na kitu chochote kinachonihusu mimi, mpaka nitakapo weka mambo sawa. Najua Sonia inamlazimu kumkubali sababu ya Kana, lakini hatuwezi kuepuka ukweli kwamba alimuumiza, na Sonia anahitaji muda wa kuingiza hilo swala akilini mwake, hatua kwa hatua, lasivyo litaendelea kumuumiza sana kama tutafanya haraka.”
“Naomba kwa sasa tumuache afikirie afya yake na mtoto aliyenaye tumboni. Tutafute mtu mwingine wakuijenga hiyo nyumba.” “Sawa baba. Asante kunifikiria, ni kweli naumia sana, lakini sina namna nyingine ya kufanya.” Sonia alianza kulia. Paul alimsogelea.
“Usiwe na wasiwasi Sonia, tutakuwa wote katika hii hali, mpaka akili na moyo wako vitakapo kubaliana naye. Kana yupo na sisi, na baadaye tutamtambulisha kwa baba yake. Haina haraka. Si eti Kana.” “Naombeni msinitambulishe kabisa mama, mimi nimeridhika na anko Sam. Ananitosha. Amenilea tokea mtoto nikiwa mgonjwa nakaribia kufa mpaka sasa. Naomba nibaki tu na Anko Sam.” Kana alianza kulia, Sam alimsogela na kumshika kwa karibu.
“Kweli, naona Paul yupo sahihi. Nyinyi wote wawili mnahitaji muda wakupona. Sonia na Kana tupo pamoja na nyinyi wakati wote. Tutatafuta mtu mwingine wakujenga hiyo nyumba. Na nitaongea na Kato, asitutafute mpaka tutakapo mtafuta.” “Asante bibi.” Mama Tambo alitabasamu. “Pole sana Sonia.” “Asante.”
*********************
Kila mtu alikuwa amechoka kwa kukaa siku nzima hospitalini hapo mpaka jioni. Wakati Sonia anatolewa hospitalini hapo kupelekwa nyumbani, wakiwa wanasindikiza kitanda kilichombeba Sonia kukiingiza kwenye gari hiyo ya hospitali kwenda nyumbani kwa baba yake, walishangaa kumuona Kato amesimama nje ya mlango.
Kila mtu alibaki amepigwa na butwaa! Sonia alikuwa ameshikwa mkono na baba yake akiwa amelala kitandani hapo, aliuminya kwa nguvu, lakini safari hii hakutetemeka wala kulia wakati akimtizama Kato.
*********************
Kato alipiga magoti mbele ya Mama Tambo na wanae. “Naomba nisamehe mama yangu. Tafadhali Mama Tambo, naomba nisamehe.” Kila mtu alikuwa kimya akimtizama Kato. Paul ndio alikuwa na hasira kupita kiasi. “Kwa nini umekuja hapa bila taarifa?” Mama Tambo.
“Nilijua utaniua mama yangu, nimekuja kujisalimisha mimi mwenyewe kabla hujanitumia mtu aje kunikamata, na nilitaka ujue najutia kitendo cha ukatili nilichokifanya mama. Najuta, nimekosa, naomba unisamehe.” Kato alikuwa akitetemeka na kulia kama mtoto mdogo.
Alipiga magoti akitubu kama anayesubiri rehema za Mama Tambo ambaye ni kitendo cha kutamka tu, na maisha yake yangekuwa yamefikia mwisho. “Nimekosa mama.” Kato aliendelea kumbembeleza Mama Tambo huku amepiga magoti na kuinamisha uso wake chini mpaka aridhini kama anayesujudu.
Hasira Ya Ubaba
Paul alienda kumuinua Kato pale chini kwa nguvu na kumpiga ngumi moja ya pua nakuanza kuvuja damu. “You ruined my baby’s life. Unamuona amelala pale?”Paul alimnyanyua uso kwa nguvu kumuelekezea alipolala Sonia. “Unamuona?” Kato alikuwa akivuja damu nyingi sana.
“Bado analipa garama ya unyama uliomfanyia.” Hakuna aliyemzuia Paul, aliyeonekana na hasira za kupita kiasi. “Nilikosa Paul mdogo wangu, naomba unisamehe.” “Ulitakiwa umuombe Sonia msamaha sio mtu mwingine yeyote.” Paul alimsukuma kwa nguvu, akaanguka chini.
Sonia alianza kulia lakini sio kama zamani, Paul alirudi kumkumbatia binti yake. “Pole sana Sonia.” Paul alinza kumbembeleza. “Naomba mnisamehe ndugu zangu, nimekosa.” Sonia aliendelea kulia wakati bado amekumbatiwa na baba yake.
*********************
“Sonia! Naomba nisamehe. Nilikosa. Naomba nisamehe.” Kato alisimama na kusogea karibu na Sonia. Sonia alikausha machozi “Nimesamehe.” Sonia aliongea kwa sauti ya chini na iliyoonekana kutulia. “Lakini nilipata mtoto. Huyu hapa anaitwa Kana.” Sonia alijaribu kukaa vizuri akijitoa kwenye mikono ya baba yake, ili kumtambulisha Kana kwa baba yake. Kana alikuwa kama kopi ya baba yake. Kila kitu alifanana na Kato.
Kato aliinama na kulia sana. Hakuna ambaye hakutaka kumsulubisha Kato kati yao, lakini waliheshimu ombi la Sonia, kasoro Paul ndiye alishindwa kujizuia na kumpiga ngumi.
“Nisamehe Kana.” Kato alitaka kumsogelea mtoto wake, lakini Kana alirudi nyuma kabisa nakuendelea kulia kwa uchungu huku akimwangalia. “Naomba unisamehe mwanangu.” Kato alirudia na kupiga magoti. “Usithubutu kuniita hivyo hata siku moja.” Kana aliongea kwa hasira na kumshitua kila mmoja kati yao.
“Hata siku moja, usiniite hivyo na wala usinitafute tena.” Kana alikuwa akiongea kwa hasira sana huku akilia. “Ninaye baba yangu sio wewe. Anko Sam alinitunza tokea mtoto na ananipenda na anajiheshimu. Sio wewe.” “Sikujua kama umezaliwa Kana, nisingeacha…...” Kato alitaka kuendelea kujitetea lakini Mama Tambo aliingilia.
“Naomba uondoke sasa hivi Kato, usiwahi kurudi tena kwa Sonia, mpaka Kana atakapokutafuta yeye mwenyewe. Huna mahusiano na yeyote kati yetu isipokuwa Kana. Kwa hiyo ondoka.” Kato alinyanyuka kwa haraka sana.
“Kato!” Mama Tambo aliita tena kabla hajaondoka. “Ndiyo Mama.” “Hakikisha hatuonani sura zetu tena, mpaka Kana atakapokutafuta. Wewe na familia yako hamkaribishwi tena nyumbani kwangu, wala usikosee kupiga simu yangu tena. Na mkeo hivyohivyo.” Mama Tambo alimaliza.
“Na usiwahi kumtafuta Kana, hata mara moja, Kato. Kama mama alivyokwambia, Kana ndiye atakayekutafuta wewe, akipenda na akiwa tayari. Nisiwahi kukusikia umesogelea eneo lolote alilokuwepo Kana. Nikisikia kama ulifika eneo alilopo Kana, mjukuu wangu, hata bila wewe mwenyewe kujua kama Kana yupo eneo hilo, ujue upo MATATIZONI.” Paul aliongeza.
“Tena MATATIZO MAKUBWA SANA. Ondoka na nisikuone tena, mpaka Kana atakapo kutafuta.” Mama Tambo alimaliza. “Asante mama. Asanteni sana.” Kato alikuwa akiongea huku akirudi kinyumenyume na huku ameweka mikono yake mbele akishukuru. “Asante sana Sonia kwa kunisamehe, asante sana.” Wakati anaendelea kushukuru huku akirudi kinyumenyume, Kato alijikwaa akaangukia kwenye maua.
Hakuna aliyempa pole, wote walibaki wakimwangalia kasoro Matilda alianza kucheka sana. Kato alinyanyuka akiwa amelowa sana, kwani walikuwa wakinyweshea maua jioni hiyo. Matilda alizidi kucheka kwa sauti. “Mat wewe!!!”“Jamani da Martha! Kwa nini nisicheke? Tena kaka Kato umshukuru Sonia, ndio amekuombea msamaha. Ungefia jela wewe.” Matilda aliendelea kuongea huku akicheka sana. “Asante sana Sonia.” Kato aliendelea kushukuru huku akitetemeka sana. Ukweli alionekana ameingiwa na hofu.
Uchungu wa Mwana…
Wakati anataka kuondoka moja kwa moja, Ishimwe alimkimbilia na kuanza kumpiga mfululizo bila kupumzika huku akilia sana. “Huwezi kuondoka hivi hivi. Umemtesa sana mwanangu wewe. Umemwaibisha, ulinisabishia maradhi baada ya kujua amepata mimba na hawezi kusema kama ulimbaka sababu ulimtishia mwanangu.”
“Umenitesa sana wewe baba. Unajua shida nilizopata na hawa watoto baada ya kumbaka Sonia?” Ishimwe aliendelea kumpiga mbele ya Mama Tambo na watoto wake na kushangaza kila mtu. Alichana shati la Kato na kuendelea kumkwangua na kucha.
“Naushukuru Mungu, sina uwezo kwenye hii nchi. Ningekufunga hata kama Sonia amesema usamehewe. Nisingejali kama wewe ni baba yake Kana wala nini.Ningekufunga na kuhakikisha unafia jela. Nimemlea mwenyewe Kana, na anaweza kuishi vizuri tu bila wewe. Nimeteseka sana.”
“Juhudi zangu zote zakumsomesha Sonia, zilikuwa bure baada ya wewekumbaka mwanangu. Alifukuzwa shule sababu yako. Pesa yangu yote niliyokuwa naitafuta kwa shida, ilipotea sababu ya ukatili wako.” Ishimwe alivua kiatu chake na kuendelea kumpiga nacho Kato kila mahali huku akilia mpaka Paul alipoamua kwenda kumtoa pale.
“Amemtesa sana mwanangu huyu. Sijui kwa nini mnamsamehe!” Ishimwe alizidi kulia kwa sauti kama amefiwa. “Usimsikilize Sonia, we Paul. Naomba afungwe huyu baba. Haki itendeke. Usimsamehe. Nimuuaji.” Paul aliendelea kumshika Ishimwe kwa nguvu ili asirudie kumpiga tena Kato.
“Wewe Paul, ungemuacha kwanza wifi. Mimi naona yupo sahihi kabisa.” “Hivi wewe Matilda ukoje jamani!? Hebu nyamaza bwana!” “Haya nanyamaza dada yangu. Lakini nilikuwa nataka kusema huyu Kato…” “Wewe si umesema unanyamaza?” Mama Tambo alimgeukia Matilda. “Nilitaka kuongeza kidogo tu mama. Kuwa….” “Hapana Mat, nyamaza.” “Sawa mama yangu.” Matilda aliendelea kucheka taratibu. Ishimwe aliendelea kulia huku ameshikiliwa Paul.
Kana Naye Kwa Baba Yake
“Usilie Mama.” Kana alisogea na kumkaribia bibi yake aliyezoea kumuita mama. “Nitakutafuta Kato.” Kana alimgeukia baba yake. “Nakuapia kwa Mungu, nitakutafuta na utalipa ulichokifanya kwa mama yangu. Nakuahidi nitakulipisha. Utalipa kila chozi, uchungu na aibu uliyomsababishia mama yangu. Hutakaa ukasahau maishani mwako.”
“Dunia itasimulia malipo nitakayo kulipisha. Mungu alikubali nizaliwe ili nikuweke wewe mfano na fundisho kwa watu wote wenye tabia kama zako. Nitahakikisha ulimwengu unaona malipo nitakayo kulipisha Kato. Vyombo vya habari vitatangaza, mitandao itaonyesha unyama nitakao kufanyia.” Kana alikuwa akiongea akiwa ametulia na kumshitua kila mtu aliyekuwa pale.
“Nakuapia kwa Mungu, nitakutafuta na kukulipisha. Na baada ya hapo, hutakuwa na sehemu ya kuficha uso wako isipokuwa kaburini. Utajuta msamaha huu wa leo wanaokupa hawa ndugu zako kina Tambo. UTAJUTA na kulaani msamahauliopewa na mama yangu. Utawalaani kwa majina yao, huku ukikumbuka sura ya kila mmoja aliyesimama hapa leo, wakijua wazi ubaya uliomtendea mama yangu na kukuachia huru.”
“Utatamani wangekuweka jela leo, kuniepuka mimi. Mkono huo huo wa wakina Tambo uliokutangazi uhuru wako leo, utaulaani milele. Nakuahidi utaikumbuka siku ya leo na kuilaani, na kutamani badala ya kuja hapa kumuomba msamaha Mama Tambo tena sio mama yangu, maana tangia unafika hapa unajali msamaha kwa Mama Tambo sio wa mama yangu, utatamani hii siku irudi ili uwe ulikimbilia polisi, kukiri makosa yako wakufunge, kuepuka mkono wangu mimi na sio hapa.”
“Nitakuja kama malaika wagiza, nitakuharibu hakuna mwanadamu atataka kukuangalia tena, na hutakuwa na uwezo wakumwangalia mwanadamu yeyote, isipokuwa kaburi ndio itakuwa kimbilio lako.” Kana aliogopesha kila mtu, Kato alibaki ametoa macho.
“Nitakuja, nitakuja kukutafuta Kato. Uombe kifo chako kikujie kabla sijakufikia, lakini nina uhakika hutakufa mpaka ulipe uovu wako. Mungu alitangaza hukumu yako siku aliporuhusu mimba yangu itungwe. Akijua wazi nguvu na mamlaka inayokuzunguka, alijua wazi watakuachia huru, aliruhusu nizaliwe ili kukulipiza uovu uliotenda.”
“Utasamehewa lakini hutaacha kulipa garama ya ukatili uliomtendea mama yangu. Na kwa kuwa ilikuwa ni lazima ushitakiwe mahakamani kihalali kwa unyama uliofanya, lakini hawa watu wote hapa, wamekuhukumu nje ya mahakama na kukutangazia uhuru wako, mimi nitahukumiwa kwa niaba yako kwa kile nitakacho kufanyia.”
“Nitachukua nafasi yako mahakamani siku nitakapo malizana na wewe, hakuna hakimu atakayeridhika na adhabu yeyote itakayonistahili kwa kile nitakacho kutenda, isipokuwa kifo. Nitakutafuta Kato, nakuahidi nitakutafuta, tena sio siku nyingi kuanzia sasa, lakini uwe na uhakika NITAKUTAFUTA.”
“Hakuna pesa wala ulinzi utakao kuficha nisikufikie. Wala jina la Tambo halitakuokoa na mimi. Nakuahidi nitakutafuta, nanitatimiza azma yangu.” Kila mtu alikuwa akitetemeka, kwani Kana hakuonekana kama amekurupuka, alionekana anajua anachoongea na alionekana anamipango tayari.
“Nibahati mbaya Kana. Nilikosa naomba unisamehe mwanangu.” Kana alimsogelea karibu zaidi. “Haikuwa bahati mbaya. Usidanganye. Siku mbili mfululizo!? ULIKUSUDIA. Tena ni mpango uliokuwa umeupanga kwa muda mrefu kumuangamiza mtoto mdogo uliyemuona ana DHIKI na SHIDA, ukijua hana utetezi.”
“Hivi unajua wakati unamtendea ule unyama alikuwa na umri kama huu wangu au mdogo kidogo kwangu? Ulipaswa kumuona kama mtoto mwenye shidana umsaidie, lakini ulitumia shida zake kumuangamiza. Sijui ulipanga uovu wako kwa muda gani mpaka ulipotimiza azma yako? Lakini ujue na mimi napanga mipango yangu, tena kwa makini sana mpaka nikufikie.”
“Si umesema mimi ni mtoto wako? Basi ujue roho ileile mbaya uliyonayo wewe, ndiyo iliyokuwepo ndani yangu mimi. Usiku na mchana hukulala ukipanga kumfanyia mtoto mdogo uovu, tena aliyekuwa akilingana na mtoto wako! Ndivyo hivyohivyo na mimi ninavyofanya. Hakuna siku inayopita, tangia nijue ubaya uliomfanyia mama yangu, nisiwaze na kupanga ubaya nitakao kufanyia.”
“Nitakuhukumu mbele ya ulimwengu wote ukikutazama, na ubaya wako utasimuliwa kwa kila taifa ili wenye tabia kama zako, kila watakapo kuwa wakikusudia kufanya kama ulichofanya wewe, wakikumbuka nitakachokufanyia wewe, hakika watagairi.”
“Nakuahidi utaikumbuka siku ya leo, nakujutia shukurani unazowapa kina Tambo kwa kukusamehe, utatamani wangekukamata, ukahukumiwa mahakamanimbele ya macho ya watu wachache, kuliko mimi nitakavyo kuhukumu mbele ya ulimwengu. Lakini najua ni mipango ya Mungu, ili wewe uje kuwa fundisho kwa wote. NI TA KU TA FU TA. Hakika nitakutafuta, na itakuwa ni zaidi ya hivi ninavyokutamkia leo.” Kana alimaliza, akabaki kimya akimwangalia baba yake machoni bila kupepesa macho. Mwishowe Kato aligeuka akaingia kwenye gari yake, akaondoka.
*********************
Ulipita ukimya mrefu kila mtu akiwa amesimama kama sanamu, Sonia alibaki ametoa macho akiwa amekaa kitandani anamwangalia mtoto wake. Hakuna aliyeweza kuongea, mpaka Mama Tambo mwenyewe alibaki ametoa macho. Madaktari na manesi waliokuwa wanamsindikiza Sonia, nao pia walibaki wametoa macho.
Mwishowe Sam akamsogelea Kana aliyekuwa amesimama kimya kabisa huku akiangalia upande wa gari ya baba yake lilipoelekea, Sam akamshika mabegani. “Twende nyumbani.” Alimuongelesha kwa sauti ya chini iliyotulia. Kana akamgeukia na kuanza kulia kwa uchungu sana.
“Twende ukapumzike.” Alimuongoza Kana mpaka kwenye gari akiwa bado analia. “Inabidi umuage mama yako Kana, nakurudisha kwa Nyange, kesho unatakiwa kwenda shule.” Sam alijaribu kumuongelesha mara baada ya kupanda kwenye gari. Lakini alitingisha kichwa kuashiria kukataa. “Basi hamna shida. Utampigia simu baadaye kujua anaendeleaje. Sawa?” Hapo akatingisha kichwa kukubali.
*********************
Alipohakikisha amemuacha sawa ndipo akarudi alipowaacha kina Paul. “Inabidi nimrudishe Kana nyumbani kwa Nyange, naona usiku umeingia, anatakiwa kuwahi kulala, kesho shule.” “Kwa nini anaishi nyumbani kwa Nyange!?” Paul aliuliza kwa kushangaa sana.
“Walituomba akakae nao kwa muda.” “Hapana Sam. Humuwezi kufanya hivyo hata kidogo.” Paul alimgeukia Ishimwe. “Unanisikia Ishimwe. Hamuwezi kumlea Kana kwa namna hiyo hata kidogo. Leo anarudi nyumbani. Hatuwezi tukawa tunaishi huku halafu yeye anatelekezwa kule. Siyo maisha ninayotaka ayaishi hayo. Mungu ametupa nafasi yakuwa pamoja, naomba tuitumie vizuri. Wote tunaenda kuishi nyumbani kwangu, sio vinginevyo.”
“Leo Kana amekuwa na wakati mgumu sana. Siku nzima amemuona jinsi mama yake alivyoteseka, halafu mnamtoa kwa mama yake mwenye uchungu naye, akaishi na familia nyingine!? Hata kidogo. Kana anahitaji mapenzi yetu sisi wote, tena ya karibu sana. Lazima ajue kwa vitendo, kwamba tunamuhitaji kwenye hii familia na yeye sio mtoto wa bahati mbaya.”
“Hatuwezi kumsukumia kwa watu wengine. Mwenye shida naye Kana, atamfuata kwetu, sio vinginevyo. Unanisikia Sam?” “Ndiyo.” “Kabisa, tafadhali. Huyu mtoto anakutambua wewe kama baba yake, halafu na wewe unaruhusu watu wengine wamlee! Hapana Sam.”
“Kana anarudi nyumbani na sisi, LEO, sasa hivi. Mpigie simu Nyange na mkewe, uwataarifu hivyo. Huyu sio mtoto wa jamii nzima, ni mtoto WETU. Hawezi kuendelea kuzurula kwenye majumba ya watu.” “Sawa.” Sam aliitikia. Sonia alifurahi sana.
“Asante sana baba yangu. Hata mimi nilikuwa sifurahii. Nilijua ataona simpendi, ni kama namsukumia mbali.” “Mungu ametupa nafasi yakuwa pamoja Sonia, lazima tuitumie vizuri.” Paul alijibu huku akimwangalia Ishimwe aliyeonekena bado anahasira kali. Alimsogeza karibu na kumuwekea mikono mabegani kwake.
*********************
“Mama!” Paul aliita na kumsogelea mama yake akiwa bado amemshika Ishimwe. “Tunawashuru sana kwa kuwa na sisi hapa hospitalini, na poleni kwa uchovu. Nashauri mrudi tu nyumbani mkapumzike mpaka kesho kutwa siku ya harusi.” “Nataka nihakikishe Sonia amefikishwa nyumbani salama na yupo kwenye mazingira mazuri. Usiwe na wasiwasi Paul, mimi nitapumzika tu. Twendeni tuongozane, tutarudi Shinyanga hata usiku.”
“Usiku ndio huu mama! Nenda kapumzike bwana. Sonia atakuwa sawa tu. Sisi tupo naye.” “Hapana Paul. Nafsi yangu haitatulia bila kumuona amefikishwa nyumbani na yupo salama.” Paul alimbusu mama yake. “Asante nashukuru. Basi ndio tuondoke sasa hivi.”
*********************
Waliongozana mpaka nyumbani kwa Paul. Alitaka wote waishi kwenye nyumba yake sio kwenye nyumba hiyo ya familia yao kama alivyoongea na Sam. Walipoonyesha chumba atakachokuwa akilala Kana, Sam alimsindikiza humo, alipohakikisha ametulia ndipo alipotoka kurudi kuwashukuru kina Tambo.
Watoto wengine wa mama Tambo wazi walikuwa wamshafika mwisho wa hiyo siku, wako tayari kabisa waimalize. Walibaki wamekaa sebuleni kimya tu, wakimsubiria mama yao amalizane na nesi aliyekuwa akimuhudumia Sonia kwa usiku huo, ili warudi naye Shinyanga.
Paul aliwaita wote kwenye chumba alichokuwepo amelazwa Sonia, akiwa amerudishiwa mashine ya kusikiliza mapigo ya moyo ya mtoto wake aliyepo tumboni na yeye mwenyewe mashine za kuangalia pressure yake. Paul aliongea maneno machache, akielezea furaha yake ya kuwaweka pamoja na kuwaambia umuhimu wa kila mmoja wao kwenye maisha yake.
Hakutaka kuzungumzia kabisa juu ya Kana na baba yake. Lakini alijitahidi kumwambia Kana ni jinsi gani anavyompenda na kumuhitaji katika familia hiyo.
Sonia kwa Kijana wake.
“Namimi nitakuwa nikimsaidia mama. Kwa hiyo muwe mnanipa majuku yeyote nitaweza kufanya.” Kana aliongea kwa kifupi tu na kumfanya Sonia aanze kulia. “Wakati unafanya mipango yako yakulipiza kisasi kwa baba yako, umeshanifikiria na mimi?” Sonia alimgeukia mtoto wake.
“Unataka mateso na aibu yangu vipotee bure? Unataka awe amechukua usichana wangu na wewe pia?” Sonia alianza kuongea kwa ukali kidogo. “Kwa nini unataka kujiingiza kwenye matatizo yatakayo tutenganisha mimi na wewe? Yaani upo tayari ukafie jela kuliko kusamehe na kuishi na mimi?”Sonia aliuliza. Wote walibaki kimya kama ambao hawakutegemea kama Sonia angelipuka tena.
Japokuwa walikuwa sehemu nzuri, madhari nzuri ambayo hawajawahi ishi maishani, lakini kuna jambo bado halikuwa limekaa sawa. Kwa kuwatizama tu, ungejua WOTE, japokuwa wamepewa ukaribisho mzuri, lakini hawako sawa.
“Shida zote zile tulizopata, sasa hivi Mungu ametupumzisha, unataka kuanza matatizo mengine! Umeshafikiria maisha yangu na mimi, bila wewe?” “Anaroho mbaya sana yule, mama. Umeona ameshindwa hata kukuomba msamaha? Anawaomba watu wengine msamaha sio wewe! Anatudharau sisi kwa kuwa anajua hatuna uwezo.” Kana na yeye akaanza kulia. Na kumfanya mama Tambo aliyekuwa akikaribia kuondoka, ashindwe tena. Akarudi kukaa sebuleni na wanae wengine wakisikiliza.
“Nilikwambia tokea mwanzo Kana, mimi nilisamehe, kabla hata ya yeye kuomba msamaha. Na nimekwambia namshukuru Mungu kwa yaliyotokea, kwa kuwa nilikupata wewe! Bila ukatili alionifanyia baba yako, nisingekupata wewe. Leo unageuza baraka zangu kuwa laana!?”
“Sio kweli kwamba uliletwa hapa duniani kulipiza kisasi, Kana. Mungu amekuleta hapa duniani kuwa faraja yangu. Umesikia Kana? Roho hiyo iliyokuingia siyo sahihi na ujue kwa chochote kibaya unachofikiria kukifanya, utakuwa umeshirikiana na baba yako kuniadhibu wala sio kulipa kisasi.”Sonia alizidi kulia.
“Umenisikia wewe Kana? Siku utakapoondoka nakumfanyia baba yako ubaya, ujue ndiyo siku unayoniua na mimi.” Hapo Kana akazidi kulia kwa sauti ya juu iliyojaa hasira. “Nenda chumbani kwako ukafikirie kama unataka kuniuana mimi, au unataka kugeuka nakuwa faraja yangu.”
“Na ukumbuke wewe ni baraka na sio laana na huna roho mbaya hata kidogo. Nimekaa na wewe muda wote, umekuwa mtoto mzuri na mfano wa kuigwa kila mahali waliobahatika kuwa na wewe. Na kila shule uliyowahi kwenda, si walimu sio wanafunzi wanao acha kukusifia.”
“Usikubali kosa la baba yako likakuangamiza Kana. Nenda ukafikirie huko chumbani kwako, halafu kesho ukitoka shule utanipa jibu. Umesikia Kana?” Kana alitoka hapo kurudi chumbani kwake huku akilia sana.
Yameshindwa Kuzungumzika
“Samahani sana baba na mama.” Sonia akaendelea. “Na Sam. Naomba mumsamehe Kana. Najua bado ana uchungu. Lakini kama alivyosema baba, tumpe muda, atatulia.” “Kwa hiyo Sonia, ni kweli hutaki yule baba ashitakiwe?” Ishimwe akauliza kama ambaye na yeye bado hajaridhika.
“Itasaidia nini mama? Yameshatokea mama yangu, naomba na wewe usamehe yaishe, kuwe na amani.” Ishimwe alianza kulia. Paul na Sam walikuwa kimya kama walio wekwa katikati hawajui tena chakufanya.
“Unajuaje kama kuna amani na hafanyii hivyo binti wengine?!” Hilo likawashitua wote mpaka mama Tambo na wanae huko sebuleni waliokuwa wamekaa kimya hata hawaongeleshani.
“Wewe ulibahatika Sam. Je hao binti wengine ambao ni wapweke, waliofanyiwa au anaoendelea kuwafanyia unyama kama wewe kwa sababu ya pesa yake? Unajua hali zao huko walipo?” Kimya na hicho kikamuingia hata Sonia. “Ona madhara aliyokuachia. Mpaka ulikaribia kupoteza mtoto leo. Ushafikiria wenzio wanaopitia kwenye hali kama yako na hili jitu likiendelea kuzunguka tu mtaani?” Kimya, kikiwa kimemuingia hata Sonia mwenyewe.
“Wewe unababa yako sasahivi. Wapo binti wanafukuzwa kwenye familia kabisa kwa kushika mimba za namna hii na hawawezi kujitetea. Wapo wanaobakiwa na majeraha ya ubakwaji moyoni kama wewe. Hawana pakulilia, hawana wakuwasaidia. Wanabakiwa na kicho kilema daima. Ushawafikiria hao?” Ishimwe aliendelea kugomba akilia. “Hapo sijafikiria mama.” Sonia naye akaanza kulia.
“Unang’ang’ania uhuru wa shetani huyu ili aendelee kuangamiza mabinti wengine, halafu unataka eti siku moja aje kuwa baba wa Kana! Kweli wewe Sonia? Atakuwa baba wa namna gani huyu! Kwa shida gani tuliyonayo kwenda kumtoa Kana kwa mwanaume kama Sam, aliyemuona akiishi kwa mfano mzuri, kwenda kumtambulisha kwa shetani yule?”
“Kahika usubiri ukishanizika ndipo umrudishe Kana kwa shetani yule, lakini nisiwe hai. Nikiwa mimi hai, Sam ndio atabakia baba yake Kana, na si vinginevyo. Na naomba msije kuniacha naye huyo baba, kwenye chumba kimoja. Nitamuua.” Ishimwe aliongea huku akilia sana.
“Na asijenge nyumba watakayoishi wanangu.” Ishimwe aliongea kwa uchungu sana. “Umesikia Paul? Hata asiguse hata tofali moja.” “Sawa Ishimwe.” “Na asithubutu hata kutoa shilingi yake akawapa wanangu. Nipo radhi nirudi kutafuta pesa mimi mwenyewe nimtunze Kana na Sonia, kuliko wanangu watumie pesa za yule shetani.” “Sawa Ishimwe.” Paul akaitika lakini ikawa kama Ishimwe hajaridhika. Yeye analia, na wanae wote wanalia kwa uchungu sana.
Lazima Kulipa Garama…
Mama Tambo alipoona hiyo hali. Akarudi chumbani kwa Sonia, wanae wakimfuata nyuma. Bado Ishimwe alikuwa akilia, na Sonia analia. “Unatakiwa kutulia kabisa Sonia, ili huyo mtoto akomae.” Akaendelea mama Tambo. “Nataka ufikirie na unipe mimi maaumizi yako, lakini nataka unyamaze kabisa kwa sababu nitakuuliza swali moja tu.” Mama Tambo akaendelea.
“Naomba utulie. Nyamaza.” Akamsaidia kabisa kumfuta machozi. “Mama yako ameongea jambo lililonifanya kufikiria japo sipo kwenye kukubadili mawazo kwenye maamuzi yako. Hatujui huyu Kato hii tabia yake kama ni kwako tu, au alianza zamani, na kama bado anaendelea! Hakuna mwenye hilo jibu.”
“Swali langu kwako ni, bora yupi akae ndani. Kana au Kato?” “Sitaki kumpoteza mwanangu. Na samahani mama, sikuwa nimefikiria wengine.” Bila ya kuongeza neno, wakamuona Mama Tambo anatoa simu yake.
*********************
“Kato!” Wote kimya. “Elekea kituo cha polisi cha Ostabay, moja kwa moja, kuchukua nafasi yako. Kana ni baraka kwetu, hutabadilisha hilo kwa Kana kulipa garama ya makosa yako. Umenielewa Kato?” Akaendelea wote wakisikiliza.
“Hakikisha unaulizia mkuu wa kituo. Utaandikisha kosa lako, kwake yeye mwenyewe. Utakiri kila kitu bila kuruka ulichofanya, kwa kuwa Sonia hatarudia ulichomtendea. Mkuu wa kituo ataporidhika na maelezo yako, mwambie anipigie simu mimi mwenyewe.” Kimya kwa muda.
“Na Kato, hakikisha unaeleza KILA KITU, kwa kweli na uwazi bila kuficha kitu. Isijetokea nikagundua polisi hawana taarifa sahihi na kamilifu, ya uhalifu wako. Na pia hakikisha unaacha maelezo ya kweli na ya kutosha kwa mkeo na binti zako.”Wakajua hiyo ni adhabu nyingine anapewa. Kujishitaki kwa familia yake yeye mwenyewe.
“Utatulia gerezani mpaka Kana atakapokuja kukutafuta yeye mwenyewe, vinginevyo nisisikie unatafuta mwanasheria wakukutetea kwa namna yeyote ile ambaye itamlazimu Sonia kusimama mahamani na kujidhalilisha zaidi.” Mama Tambo akaendeleza hukumu ya nje.
“Kutafuta wakili yeyote utakayetaka aanzishe kesi na kumrudisha Sonia na Kana mahakamani, utakuwa umenikosea mimi kibinafsi, ZAIDI ya hivi sasa.”
“Na, kutafutwa kwa Tambo yeyote yule, na mkeo au binti zako, kwa simu au ujumbe, utakuwa umekiuka mashariti na ujue utaingiza familia yako matatizoni.”
“Kuelekea sehemu nyingine yeyote ile na sio kituo cha polisi kama nilivyokuelekeza, SASAHIVI, ni kutaka mimi mwenyewe nikutafute.” Simu ikakatwa.
Yale aliyoyafanya Kato sirini, akiwa amemtoa mkewe na binti yake nyumbani ili amtende unyama Sonia, akidhania hatawajibishwa maana Sonia wa wakati ule alijawa dhiki, lakini Mungu aliyaona yote, akayaandika na kuyatunza. Kato akidhani amepona, lakini baada ya miaka zaidi ya kumi kupita, Mungu anamtolea hati yake ya mashitaka. Nakumtaka awajibike.
*********************
Ishimwe alipiga magoti mbele ya mama Tambo na wanae akilia. “Nakushukuru mama. Asante. Na samahanini. Huyu baba ananiuma kama kidonda! Jamani nilihangaika ili mwanangu asome! Nilihangaika sana na mwenyewe alikuwa akipenda sana shule. Nina uhakika Sonia angekuwa mbali sana kama si huyu baba. Alimkatili mwanangu vibaya sana. Siwezi ruhusu akaendelea kuharibu binti wengine. Na kwa hakika, HAWEZI kuwa baba wa Kana. Sio leo wala kesho.”
“Pole sana Ishimwe. Sonia bado mdogo. Atasoma mpaka afikie ngazi ya kina Tambo. Tumuombee tu uzima.” Paul akamnyanyua Ishimwe pale alipopiga magoti. “Sasa hivi nenda kapumzike, mama. Twende hata mimi nitakusindikiza kwa amani.” Angalau Ishimwe akafanya wacheke kidogo. “Kweli jamani! Na naona leo nitalala vizuri. Asante sana.” Ishimwe aliongeza. Angalau mama Tambo akaondoka akaacha kukiwa na amani.
*********************
Ishimwe akaenda kuzungumza na Kana. Kumueleza juu ya Kato. Akazungumza naye sana mpaka akatulia, ndipo na Sam naye akaenda huko chumbani kwake. Wakajikuta watatu wakizungumza mpaka Kana akatulia kabisa.
Msamaha Sio Sababu Ya Kutenda Kosa
“Lakini siwezi kulala na kumuacha Briana, mama. SITAWEZA kabisa. Atateseka sana.” Akawa akimwambia Ishimwe, bibi yake. “Utafanyaje Kana? Babu yako hayataki hayo maisha yakutengana!” “Hata mimi siyataki, lakini siwezi lala nikijua Briana atakuwa akinisubiri.” “Nishawaambia wazazi wake.” Sam akaingilia.
“Namjua Briana. Hawezi kukubali kulala mpaka niende. Atakuwa akinisubiria kwa sababu nilimuahidi nitarudi. Na sitaki nimuache akitesekaleo, halafu nije kumuomba msamaha kesho! Sitaki kufanya hivyo anko. Naomba Mungu anisaidie nisimfanyie hivyo Briana, eti kwa sababu nitakuja kumuomba msamaha baadaye.”
“Sonia amepita hapo, na mama pia umepita hapo. Watu kuwatendea ubaya kwa makusudi, wakiwapuuza tu, wakijua kesho watawaomba msamaha, yataisha. Sitaki kumfanyia hivyo Briana. Na wewe naomba nisaidie anko.” Walipoa hao wawili hapo, na kushangazwa na huyo mtoto.
Hakuwa akizungumza nao lakini alikuwa akijua kila kitu kinachoendelea. Sam akahisi na yeye amesemwa hapo maana alimkosea Sonia, ikajulikana alikuwa akimpuuza, mpaka akaondoka lakini Sam alirudi na kuomba msamaha, yameisha. Ishimwe naye aliachwa na Paul, akateseka sana na hao watoto, hatimaye amerudi na kuomba msamaha, amesamehewa, wanaendelea.
“Sitaki kujenga mahusiano ya namna hiyo. Kufanya jambo kwa makusudi, kama hivi, nalala nikijua kabisa Bree analia, halafu eti kesho nakutana naye, namuomba msamaha tu! Hapana. Yupo pale alipo au amepita yeye na mdogo wake kwenye ugumu kwa sababu kama hizihizi. Mahusiano ya kukoseana, kwa makusudi tu, na kuombana msamaha. Ameteseka sana Bree kwa kipindi chote cha matatizo ya wazazi wake. Sitaki kuendelea na mimi kumtesa.” Walipoa hapo chumbani, hakuna aliyemtizama mwenzie. Kasoro Kana alikuwa akiwatizama kwa zamu, wao wameinamisha vichwa chini kila mmoja akiwaza lake.
“Naomba nikazungumze na babu na mama, nimuombe niende. Niwe naye kwa muda nikimsaidia. Anakuaga na ndoto mbaya sana. Wakati mwingine inabidi kumuamsha kutoka usingizini, anakuwa analia sana na anatokwa jasho jingi. Anakuwa akitetemeka kabisa. Inabidi nikae naye mpaka arudi kulala.”
“Sikujua! Alimwambia mama yake?” “Anasema alishamwambia zamani.” “Wakati ule hawakuwa wakimjua Mungu. Sasahivi lazima tumuombee. Yule anti yake alikuwa na mambo ya ajabu sana. Asijekuwa amemtupia madudu. Twende tukazungumze na babu yako.” Wakatoka.
Walimkuta Paul amekaa chumbani kwa Sonia. Wazi alionekana amechoka, ila alikaa pembeni ya kitanda cha binti yake akitaka atulie na alale.
“Naombeni mniruhusu nirudi kwa Briana.” Wote wakamwangalia Kana. “Siwezi kulala nikijua ananisubiri na atapata shida usiku.” Kana akaendelea kwa heshima. “Nilimuahidi nitarudi, najua kwa hakika hatalala, atakuwa akinisubiria. Na kama wamemwambia sitakwenda, najua sasahivi analia. Na mimi siwezi nikamuacha akiteseka. Nitakuwa nikimfanyia ukatili.”
“Lakini tutaishije hivyo, Kana? Na mimi nataka tuishi wote.” “Ni kwa muda tu mama, wakati nikimsaidia. Atazoea tu.” “Halafu kumbe anakuaga na ndoto mbaya. Anaamka usiku au inabidi Kana kumuamsha usiku katikati ya ndoto mbaya sana.” “Hata mimi nilipoanza kazi nyumbani kwao alikuwa hivyohivyo.” “Kumbe ni tokea mtoto?” Mama yake akauliza.
“Tokea mtoto, yaani ilikuwa kila siku usiku kama mama yake hayupo, mimi ndio nilikuwa nikienda kumtoa kitandani kwake, nakaa naye mpaka alale au wakati mwingine nilikuwa nikilala naye.” “Basi lazima aombewe. Nitamwambia Nyange na mkewe, tumuombee.”
“Naombeni mniruhusu, niende.” Kana akasisitiza maana aliona wanaendelea na mazungumzo yao, wamesahau kilichompeleka pale. “Mkishamuombea, na nikajua ameacha ndoto mbaya usiku, nitaanza kumfundisha jinsi yakulala peke yake. Naweza kuwa naye kwenye simu mpaka alale na kumwambia anipigie akiwa anaamka, au nitakuwa nikiwaomba wazazi wake siku nyingine awe anakuja hapa, kama anakaribishwa.”
“Hapa ni nyumbani Kana. Marafiki zako ambao mama yako na bibi yako watakuruhusu kuwakaribisha, uwe huru kabisa. Ujisikie upo nyumbani kama vile ulivyokuwa ukiishi na bibi yako. Na hapa kutakuwa na dereva wa kukusindikiza popote utakaporuhusiwa pamoja na shule. Sema usiku huu hayupo. Ila kuanzia kesho tutaweka mipango mizuri.” “Asante.” Kana akashukuru.
“Asante baba.” “Naomba ulale Sonia. Unahitaji kupumzisha sana akili zako. Yule nesi yupo chumba kile kingine, atakuwa akija kukuangalia usiku, kwa hiyo msije kushituka.” Akamgeukia Sam. Lolote litakalo tokea usiache kuja kutugongea.” “Asante sana. Nashukuru kwa kila kitu.” Sam akashukuru kwa unyenyekevu wote. Paul akatabasamu. “Na wewe nenda kalale mama. Kapumzikeni.” Sam akamrudisha Kana kwa Nyange.
*********************
Walimkuta Briana analia kama amefiwa na baba yake mzazi. “Aisee Kana alikuwa sahihi!” Sam akanong’ona. Maana Nyange na mkewe walibaki naye hapo sebuleni akisema yeye anamsubiria Kana, Kana alimuahidi atarudi. Asilazimishwe kwenda kulala.
Kana akakaa pembeni yake na kumuongelesha kwa upole karibu na sikioni, maana alishindwa hata kusogea, aliinama Kana alipoingia. “Pole Bree nimechelewa.” Akaendelea kulia. “Umenisubiri sana?” Akatingisha kichwa kukubali akilia huku ameinamia magoti. “Pole. Twende ukaoge tulale, kesho shule. Na usiendelee kulia, kichwa kitauma.” “Sasahivi kinauma.” “Basi usiendelee kulia. Nyamaza, nakutafutia dawa. Tangulia ukaoge, ukimaliza kuoga na kuvaa, nitakuja na dawa, sawa?” Akabaki amekaa amejiinamia, akivuta kamasi.
“Twende nikusindikize.” Hapo ndipo akanyanyuka. “Acha mimi nikatafute hizo dawa. Wewe msindikize chumbani kwake.” Nyange akasimama kwa haraka sana. Mama Briana akabaki ameshika shavu.
“Usilie. Sitaondoka tena. Tutapanga kila kitu pamoja. Umesikia?” Wakamsikia wakimwambia Briana wakati wakipandisha ngazi. “Halafu tutaenda wote harusini.” “Harusi ya nani?” “Usilie sasa, nitakusimulia kila kitu.” “Waliniambia hurudi tena, umekwenda kwenu.” “Nilikuahidi nitarudi Bree. Nisingeacha kurudi. Nyamaza.”
*********************
“Hivi tutafanyaje Sam?” “Hivi unavyomuona Kana, anayo mipango juu ya Briana. Na ametugomea kabisa wote, amesema hawezi kulala akimuacha Briana akiteseka. Nikamwambia nishazungumza na nyinyi. Akaniambia ndio itakuwa mbaya zaidi, atakuwa akilia.” “Kama aliyejua! Hapa tumebembeleza mpaka tumechoka. Amekataa kwenda kulala, anasema anamsubiria Kana, alimuahidi atarudi. Kila tulichomwambia, alikataa. Sikutegemea kuwaona!”
“Ametuambia yeye hatamfanyia Bree kama sisi tulichowafanyia nyinyi.” Mama Briana akawa hajaelewa. Ndipo Sam akamuelewesha na kumuacha mama Bree ametoa macho.
“Sam!” “Hakika tena. Wewe unafikiri kwa nini nimemleta? Nimejisikia vibaya sana. Na ameniomba maalumu, nimsaidie asiishi na Bree, kwa kumfanyia jambo analojua ni kumkosea, halafu aje amuombe msamaha. Amesema hatakiaje ampitishe Bree kule tulikowapitisha wewe, Sonia na bibi yake.” “Haiwezekani Sam! Amesema hivyo!?” “Kwa wazi kabisa bila kumumunya maneno. Ametuambia hawezi kulala akijua Bree anateseka huku.”
“Wewe unajua kama anakuaga na ndoto mbaya?” Mama Briana akakunja uso akijaribu kuvuta kumbukumbu. “Najua zamani alikuwa akilia usiku. Tukawa tunaenda kumchua chumbani kwake tunalala naye.” “Basi kumbe hajaacha. Kazi hiyo kaipokea Kana. Hivi bibi yake amesema atakuja kuzungumza na nyinyi, mumuombee. Kwa alivyotueleza Kana, anaonekana anateseka sana usiku, wakati mwingine anasema inamlazimu kumuamsha kwa sababu anakuwa akitesema ndotoni mpaka wakati mwingine anakuwa akilia usingizini.” Wakamuona Kana anatoka chumbani kwa Briana, anashuka chini.
“Vipi?” “Ametulia, anaoga. Pole anko kwa usumbufu na asante.” “Wala usijali. Acha mimi nirudi kwa mama yako. Usiku mwema, nitawaoa kesho.” “Asante.” “Nakushukuru Sam. Waambie huko, tunawashukuru SANA na samahani sana kwa usumbufu. Kesho nitakuja kumuona Sonia, tutazungumza zaidi. Naamini na hili litakaa sawa tu.” “Sawa. Watasikia. Niagie Nyange.” Sam akaondoka.
Kesho Yake
Bila kutegemea, asubuhi na mapema walishangaa kumuona mama Tambo amerudi na wanae wote, tena na mizigo yao. “Naona tuje tu, tukae wote kwa kipindi hiki. Hawa ndugu zako, wataondokea hapa hapa kwako kurudi makwao.” “Asante sana mama. Umelala lakini?” “Utalala vipi na cha maneno yupo?” “Mama wewe!? Mbona mimi sijaongea sana!” Matilda alijitetea na kufanya kila mtu acheke.
“Kafurahia harusi huyo, utafikiri anaolewa yeye! Njia nzima wakati tunarudi nyumbani na usiku wote, anapanga mipango ya harusi! Nikaona nimlete tu hapa kwa Ishimwe wapange vizuri juu ya hiyo harusi.” Wote waliendelea kucheka.
“Karibu wifi yangu.” Ishimwe alimgeukia Mat. “Mbona nimeshafika. Na nimekuletea makeups/vipodozi vya kupaka siku ya harusi. Nilikununulia wakati nakununulia nguo za harusi, nilivisahau kwenye begi langu. Nataka nikupeleke mimi mwenyewe huko saluni tukiwa na vitu vyetu.” Wote walicheka. “Kweli inaelekea hukulala mama.” Paul alimalizia. “Umeamini sasa? Anamipango mingi huyo, Ishimwe atachoka mwenyewe.”
*********************
Baada ya kupata kifungua kinywa kwa pamoja, Paul na Sam waliondoka kwenda kazini, Martha na kaka yake walirudi kulala, walisema wamechoka sana. Matilda na yeye aliomba aondoke na Ishimwe akaanze kufanyiwa matayarisho ya harusi huko saluni.
“Unahitajika kufanyiwa massage ya nguvu na kuwekwa kwenye Sauna. Akili na mwili wako vitulie wifi yangu. Kesho ukitokea pale kanisani, wake za maraisi, mawaziri na mabalozi wababaike.” Matilda alikuwa akiongea na wifi yake wakati wanamsubiria mama Briana waondoke. “Ukimsikiliza huyo, atakuzungusha kichwa mpaka uchanganyikiwe. Anamipango mingi kweli. Wala hutaiweza.” Mama Tambo aliingilia.
“Hamna neno mama. Ndio nafurahia. Maana nilikuwa hata sijui cha kufanya.” Ishimwe alijibu huku akicheka. “Umesikia mama? Nimetumwa na Mungu.” “Mmmmh!” Mama Tambo akaguna na kuangalia pembeni.
Sonia na Bibi Yake.
Nyange na mkewe waliingia, baada ya salamu, Matilda aliondoka na Ishimwe na mama Briana. Akabakia Nyange, mama Tambo na Sonia wakiongea kwenye chumba alicholazwa Sonia. “Pole bibi, naona mwanzo wetu umekuja na hekaheka! Tunakusumbua tokea jana hujapumzika!” “Wala usiwe na wasiwasi na mimi. Wewe ndio nakuhurumia zaidi. Najua umeingia kidonda ndugukilichofunikwa na ngozi inayoonekana kama kovu, linalodanganya umepona, lakini nirahisi kutoneshwa.” Sonia akafikiria kidogo.
“Lakini wakati mwingine najifariji najiambia pengine na hilo nalo pia ni mpango wa Mungu. Isingekuwa hivyo, ningempataje Kana?” Walimuona Mama Tambo amepoa. Gafla akapoteza sura ya furaha kabisa usoni. Kisha akaguna kwa sauti.
“Ni nini bibi?” “Mmmh! Nafikiria hiyo mipango ya Mungu.” “Kwa nini?” Sonia aliendelea kumuhoji bibi yake. Huku Nyange akiwasikiliza tu, kimya. “Hiyo mipango yake huyo Mungu, ni migumu jamani! Migumu sana.”
“Nakumbuka kipindi Tambo anaumwa, tulizunguka humo makanisani tukiombewa bila mafanikio, mpaka tukaokoka kabisa lakini wapi? Wachungaji wakawa wanakuja mpaka nyumbani kumuombea, lakini huyo Mungu hakusikiakabisa wala hakujali, huku akijua kabisa Tambo ndiye rafiki wa karibu na wa pekee niliyewahi kuwa naye hapa duniani.”
“Ndiye mwanadamu peke yake aliyekuwa akinijulia mimi, lakini alimchukua mume wangu na kuniacha mpweke kuliko kitu chochote hapa duniani! Najiuliza, nasema labda sikuwa nimeomba vizuri! Lakini hapana. Hakuna kipindi maishani niliomba kama hicho jamani! Niliomba huku nikimsihi Mungu tena bila kuchoka!”
“Nilimlilia huyo Mungu, anibakishie mume wangu, lakini Tambo alikuwa anaoza kila kukicha, mpaka siku anakata roho alikuwa hafai!” “Pole sana bibi.” Mama Tambo aliongea kwa uchungu sana.
Kwa Mungu Asiyechunguzika Kwa Akili Za Kibinadamu
Kama kitu kilichemka ndani ya Nyange, hofu ya nafasi yake kimaisha ya hapa duniani kumlinganisha na mama Tambo ikamuisha na kuona fulsayakuzungumza na mwanadamu anayeishi na uchungu mwingi sana moyoni. Akaanza taratibu na kwa heshima. “Pole sana mama Tambo!” “Asante.” Alijibu huku akitabasamu, lakini wazi alionekana ana uchungu mwingi moyoni.
“Lakini unajua mama, katika hilo baya lililokupata, ukitulia na kufikiria kwa makini utagundua lipo kusudi, na Mungu hajawahi kukuacha wewe na Mzee hata mara moja. Namaanisha tokea siku ya kwanza mlipomtanguliza yeye na kumuita kuwa msaada wenu, alishawasaidia.” Mama Tambo alimwangalia Nyange kama aliye changanyikiwa.
“Kitu chakwanza alihakikisha amewapatanisha nyinyi na YEYE. Wokovu mliokuwa mmepokea siku ile haukuwa bure. Tuangalie upande wa baba. Alimpa neema ya kujiandaa kurudi nyumbani. Najua unajua kuwa wote tutakufa, mama yangu.”
“Swali la msingi sio lini, swali la msingi ni baada ya kifo, unakwenda wapi? Hilo ndilo kila mmoja anatakiwa ajiulize kwa kuwa jibu lake linaweza kupatikana kwa rahisi tu, sio utakufa lini. Swali la utakufa lini, halina jibu lake. Na hakuna anayejua siku wala saa. Lakini hatima yako baada ya kifo, unaweza kuiandaa wewe mwenyewe.”
“Nimefurahi sana kusikia kama baba alirekebisha mahusiano yake na Mungu kabla hajafa. Kwamba alikubali Yesu ampatanishe na Mungu. Mzee hajafa mama, amepita mauti na kwenda uzimani. Swala linabaki kwako wewe mama yangu, je upo tayari kwenda kukutana na rafiki yako siku moja?”
“Bahati au neema ileile aliyokuwa amepewa Mzee Tambo, na wewe ulipewa mama. Sasa nijukumu lako kutengeneza njia yako kufika alipo. Umepewa maishani kitu cha thamani sana, Mama Tambo. Tena umepewa mara moja tu. WOKOVU. Ni wewe sasa kuamua je, utatupa hiyo bahati na kuendelea kuumia kwa kifo cha Mzee Tambo, na kumkosa milele, au utatumia huo wokovu, kukupa Amani, sasa na umilele na Mzee Tambo?”
“Amani hiyo naipata wapi mwanangu wakati Tambo ameniacha?” “Lazima ukubali mama, kifo ndio njia pekee ya kumrudia Mungu wetu. Halafu mahusiano ulioyorudishiwa na Mungu wetu kwa njia ya wokovu, ukiyatumia yenyewe tu, bibilia inaahidi ipo amani ipitayo fahamu zetu, Amani isiyotokana na Mafanikio yeyote au utajiri, itakaa ndani yako. Ipo Amani ya ajabu Mama Tambo ndani ya Mungu.”
“Kwani hujawahi ona mtu anayeonekana fukara kabisa kwa macho ya kibinadamu, hana mali wala kitu chochote, lakini anafuraha na Amaniinayomuwezesha kulala usiku? Halafu utakuta tajiri mwenye kila kitu, anashindwa hata kupata usingizi! Analala kwa kutumia madawa.” “Naona unanisema mimi.” Nyange alicheka.
“Kweli mwanangu. Sipati usingizi.” “Basi ipo siri mama yangu. Kule kuokoka kwako siku ile, haikuwa kwa bahati mbaya. Ugonjwa wa Mzee, ulikuwa fulsa pia ya kwako kukutana na Mungu wako hapa duniani kama yeye alivyokutana na Mungu wake huko mbinguni, ili ubaki salama.”
“Mzee hakukuacha peke yako. Amekuacha kwenye mikono salama yaMungu, ule wokovu ilikuwa ni hatua ya kwanza na ya pekee ya kukuandaa ukiwa hapa duniani. Kazi ni kwako wewe baada ya kupokea wokovu ule, unaufanyia nini? Je unaendeleza mahusiano yako na Mungu au unautupilia mbali? Ni swali la mtu binafsi na kila mmoja anatakiwa ajijibu kwa kadiri anavyoishi.” Sonia alikuwa akiwasikiliza kwa makini sana. Nyange aliendelea kuwafafanulia na kujaribu kujibu maswali yao yote mpaka waliporidhika.
“Na hapa sio kwamba napuuzia maumivu ya kupoteza mume wako! Au sisemi maumivu ya kubinadamu yataisha! Hapana. Kama mwanadamu ni kweli umeondokewa na mwenzio. Hakuna jinsi ya kuziba hilo pengo, lakini ninachosema au ninajaribu kukufungua macho, ni kwamba, ipo faraja. Pale unaposikia uchungu wa kupitiliza, tunaye MFARIJI mama.”
“Ile hali yako ya uchungu ulio nayo wewe mwana wa Mungu, inakuwa tofauti kabisa na mtu asiye na Roho wa Mungu. Tena huyu Mungu anaweza kuitumia hiyo hali yako unayojisikia, ya upweke na kuumia na kubadili kwa namna ambayo ukashangaa sana mama yangu. Akajaza hilo pengo kwa namna yake, ukabeba hiyo hali si kwa uzito mkubwa kama wana wa dunia hii walio mkataa yeye. Muachie yeye hicho unachojisikia uone jinsi atakavyo kubeba.”
“Si yeye mwenyewe amesema njooni kwangu nyinyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo?” “Amesema na kuahidi kuwapa raha nafsi mwao au tafasiri nyingine inasema nani nitawapumzisha.” Mama Tambo akamalizia hilo andiko kutoka {Mathayo 11:28}. “Sawasawa. Basi jua huo wito ni wako pia, na hilo nalo ni mzigo ulionao. Mwambie kwa wazi kabisa, umenichukulia Tambo, nina maumivu, siponi, naomba NISAIDIE. Uone jinsi atakavyofanya.”
“Na kingine kabla sijasema chamwisho, jua pia lipo tumaini la kuja kumuona tena mwenzio kama utaendelea kuishika imani. Utakuja kumuona tena.” Akaendelea.
“Na naomba nimalizie kwa kusema hivi mama, kabla hatujaomba pamoja, naomba nisisitize kitu hapa. Wokovu uliopewa wewe ni wako binafsi sio wakanisa zima au kiongozi fulani wa dini au rafiki. Kumbuka ni kati yako wewe peke yako na Mungu.”
“Unatembea nao wewe, ukijilinganisha na kujipima na Mungu kwa kupitia NENO lake ambalo lipo kwenye bibilia, sio mwanadamu. Kila wakati, ujipime wewe kibinafsi na Mungu wako kwa kupitia hilo neno lake, na sio vinginevyo, lasivyo utachanganyikiwa sana kwenye hii safari yako ya kwenda aliko Mzee Tambo ambako ni mbinguni kwa Mungu.” Mama Tambo alijiweka sawa.
“Naongea hivi nikiwa na maana hii, ipo hatari kubwa sana, mtakapo fananisha wokovu mliopewa nyinyi na watu wengine. Wapo watu mtakao wakuta makanisani ambao na wao watasema wamepokea wokovu kama nyinyi, nakuamua kuishi njia zinazoonekana wazi hazimpendezi Mungu, ukajifananisha nao na kukata tamaa.”
“Kama nilivyosema, haya ni maisha ya mtu binafsi na Mungu wake. Anaishije, anaendelea au anatembea vipi katika njia hiyo ni UAMUZI wa mtu binafsi. Kila mtu ana uamuzi baada ya kupokea bahati hiyo yakupatanishwa na Mungu, kuendelea kushika ulichonacho kwa kusoma maagizo ya Mungu na kutembea katika njia zake, au kubaki na jina tu la wokovu, lakini moyoni ukijua wazi ulishatenganishwa tena na Mungu.” Nyange alitumia siku hiyo kuzungumza nao juu ya mambo ya ufalme wa Mungu bila kuchoka, mpaka mama Tambo alipoelewa kabisa na kuomba Nyange amuombee tena.
“Unajua na mimi shemeji sikuwa nimeelewa hivyo! Wakati ule nyinyi mkiwa wagonjwa nilikuwa nikiomba tu na kina mama, lakini nikajua wokovu ni kama dini. Lakini leo nimeelewa vizuri, kwamba ni mahusiano yangu binafsi na Mungu. Na kumruhusu afanye na kutenda ndani yangu.” “Kabisa Sonia. Unakusudia kuacha yale yasiyompendeza, na kumuomba akuongoze na kukuwezesha kutenda yanayompendeza YEYE. Utashangaa amani utakayokuwa nayo na jinsi njia ilivyo nyepesi. Hujipiganii tena!”
“Basi na mimi nataka uniombee. Nataka kuwa na mahusiano mazuri na Mungu wangu. Ni kweli mtu haujui siku wala saa, unaweza kuondoka wakati wowote ule, ukaishia kupotea tu.” Sonia aliongeza. Nyange alifanyika msaada mkubwa sana kwa familia hiyo ya Tambo.
Alijitahidi kuongea nao, wasomi hao kina Tambo, yeye akiwa hajasoma sana, akitumia lugha nyepesi kwa kadiri Mungu alivyowasaidia mpaka wote walipopokea Neema hiyo ya wokovu. Walirudi majumbani kwao wakiwa wamebadilishwa sana kimtazamo na mahusiano yao na Mungu.
*********************
Pia Nyange alijitahidi kupata muda mwingi na Kana. Aliweza kuongea naye mara kwa mara huku akimuombea, mpaka Kana alipoweza kuachilia uchungumkubwa aliokuwa amebeba juu ya baba yake.
Na kwa kuwa alijua yeye ndio yupo karibu na binti yake, Briana, alihakikisha anamsogeza sana karibu ya Mungu. Alikuwa akimfundisha mambo mengi mpaka akafanikiwa kumuombea, akajazwa nguvu za Mungu.
Kila aliyemuona Kana, alijua kuna tofauti na watoto au vijana wa rika lake. Mungu alimtumia Kana kufikia watoto na vijana wa umri wake, huku akiwa na Briana kila mahali.
Alikuja kumtafuta baba yake akiwa gerezani, amekwisha kabisa. Kato huyu, sio Kato aliyekuwa na jeuri ya pesa. Dhambi yake ilimla vibaya sana. Akamtangazia msamaha, lakini akamwambia kwa wazi kabisa, Sam ndiye atabakia kuwa baba yake. Na hapo ndipo Kato alipotolewa jela akiwa amepoteza mahusiano na si familia ya kina Tambo tu, bali familia yake pia. Kwani binti zake walipoona baba yao yupo kifungoni kwa kashfa mbaya na mama yao anazidi kudhalilika kwenye jamii akiwa amefilisika kabisa, walijibana huko walipokuwa ugaibuni, bila msaada wa aliyekuwa anko wao Junior Tambo, wakamchukua mama yao na Fau. Kato anatoka gerezani, hana familia tena, hana kina Tambo. Maisha yalimbadilikia Kato, akabaki na sifa mbaya ya ubakaji. Kutoka juu, akashushwa chini kabisa.
Mahusiano yake na Kana hayakuwahi kurudi kuwa ya kibaba. Mtoto wa pekee wa kiume aliyekuwa akimtafuta akitaka kuja amrithishe mali zake na jina, alikuja kubadili jina lake kabisa na kutumia jina la Sam la ukoo. Akamuomba Sam rasmi, amuite baba badala ya anko, kitu kilichomfurahisha sana Sam na kuongeza sifa kwa kina Tambo.
*********************
Nyange alirudi kuongea na Ishimwe pia, na kumkumbusha agano alilokuwa ameweka na Mungu wake akiwa Dodoma. “Matatizo yetu yalikusaidia pia kukukutanisha wewe na Mungu, Ishimwe. Usije kurudi nyuma. Ile roho ya kuomba sio bure. Ni huduma Mungu amekupa wewe kama mama, kwa ajili yako, familia yako na ufalme wa Mungu. Usije ukaacha na kurudi nyuma. Songa mbele.”
Nyange alimkumbusha Ishimwe na kumfanya Ishimwe arudie mahusiano yake na Mungu. Akawa mama muombaji sana. Hakuna siku iliyopita kwa Ishimwe asikusanye familia yake wakaomba pamoja, akafanikiwa kumfundisha na Paul taratibu mpaka alipoelewa na kuombewa akawa mfuasi kwelikweli wa Mungu. Ishimwe alifurahi na kila wakati alimwambia Paul anafurahia kwa kuwa Taifa la Tanzania sasa limepata muamuzi au ‘Judge’ mzuri, mwenye hofu ya Mungu.
*********************
Mama Tambo ndiye aliyekuwa akimlea Sonia kwa karibu sana. Walianza safari yao na mahusiano yao na Mungu pamoja. Hawakuacha kusoma bibilia pamoja na kuomba. Hilo likawafanya Sonia na bibi yake kuwa karibu zaidi ya walivyotarajia. Walijikuta wakikua pamoja katika kumjua Mungu na kuwa na mengi ya kuzungumza pamoja. Maana Mama Tambo hakuwa na mtu mwingine wa karibu isipokuwa Sonia aliyekuwa akiachwa naye muda mwingi. Tokea Paul na Ishimwe wafunge ndoa na kwenda fungate kwa muda mwingi wakutosha, na hata waliporudi Paul akawa anakuwa busy na Ishimwe. Ndoa changa.
Kwa hiyo Sonia na bibi yake wakajikuta wanakuwa pamoja kwa muda mrefu. Mama Tambo alihamia nyumbani kwa Paul kabisa mpaka Sonia alipojifungua mtoto mwingine wa kiume.
*********************
Sam na familia yake walikaa nyumbani kwa Paul mpaka ujenzi wa nyumba yao ilipokamilika. Junior ni kama aliijenga hiyo nyumba ya Sam kwa upya. Alitafuta kampuni nzuri sana aliyoikabidhi kazi ya kuijenga. Nyumba ya Sam ikageuka ikawa moja ya nyumba za kisasa sana hapo jijini.
Maisha ya Sam yalibadilishwa, yakapigwa msasa na kina Tambo, akawa mtu mwenye uwezo sana. Sam yule wa zamani hakuwa Sam wa sasa hivi aliyekutana na familia ya Tambo, Sonia, Kana na Ishimwe. Akidhani alikuwa akiwasaidia kina Sonia, kumbe alikuwa akipanda wema wake kwenye udogo wenye rutuba.
Alithaminiwa na kuheshimiwa sana kwenye familia hiyo ya Tambo. Walimfungulia biashara zilizokuwa zikimuingizia pesa za kutosha. Ni kweli huruma na fadhila za Sam kwa wazazi wake, ndugu zake, Ishimwe na watoto wake, zililipa tofauti na alivyotarajia.
*********************
Sonia na Sam walifunga ndoa yao kanisani, wakarudi kuishi nyumbani kwao, kwa furaha na amani wakiwa familia ya watu wanne. Sam, Sonia, Kana na mtoto aliyejifungua Sonia. Lakini safari hii walianza maisha mapya wakiwa na kila kitu kipya. Kuanzia familia, uchumi, mahusiano, zaidi wote walirudi kuwa na mahusiano mazuri na Mungu wao.
Sam naye alibadilika sana kiimani. Alikubali Mungu kuwa kiongozi wao wote. Makampuni yote aliyofungua Sam, aliyapa jina la SAMS, yaani Sam&Sonia. Hapakuwa na kitu cha Sam na Sonia tofauti tofauti, walichuma mali pamoja na vyote waliviita vya kwao.
Umoja, upendo na mshikamano kati yao vilidumu, huku familia ya Tambo ikiwa imeongezeka kwenye picha lakini sasa hivi, wote waliishi kwenye hofu ya Mungu. Mahusiano yao na Mungu, yalikuwa ni “Zaidi ya Kutamka tu.” Wote walihimizana kuishi kwa kumcha Mungu.
**********Mwisho**********
0 Comments:
Post a Comment