Hadithi hii ni kazi ya utunzi tu. Majina, sehemu na matukio yote yaliyotumika kwenye hadithi hii ni mawazo ya mtunzi wa hadithi hii. Tutangulie kuomba radhi kwa jina au mahali husika, litakalokugusa moja kwa moja.
Ilianza kuandikwa kuanzia 11/24/2015 - 5/27/2016.
Hakimiliki © 2016 Naomi Mwakanyamale Ng’imba.
E-mail: naomisimulizi@gmail.com
Blog: naomisimulizi.com
Haki zote zimehifadhiwa, hakuna sehemu ya kitabu hiki au machapisho haya inayoweza kuchapishwa kwa mara ya pili au kuhamishwa au kusambazwa katika namna tofauti bila idhini ya mchapishaji ambaye ni Naomi Mwakanyamale Ng’imba.
More than Saying – Zaidi ya Kutamka
DEDICATION
To my beautiful children: - Trinity, Trinas and Trisun. You Got full of life a head of you. Just plant yourselves in the word of God, y’all be safe.
To my husband Suleman, the Love of my life: - Thanks for going far beyond my expectation in life to make me happy.
To all my Fans: - thanks for your support.
PART 1
Sonia alibaki kituoni hapo kwa muda mrefu sana, akiendelea kukiangalia kile kikaratasi alichokuwa ameandikiwa na daktari, cha dawa za mtoto wake. Pesa alizokuwa nazo hazikutosha kununu dawa hizo alizokuwa ameandikiwa kwa ajili ya kutibu ugonjwa wa mwanae, ambaye bado alikuwa akipandisha joto kali sana.
Kila mtu alikuwa akikimbia kutafuta sehemu ya kujificha na mvua iliyokuwa ikitaka kunyesha, lakini Sonia bado alibaki palepale kituoni akipigia mahesabu hela chache alizonazo, kama bado azitumie kupandia daladala au atembee tu kurudi nyumbani ili kuzibania pesa hizo, pengine atabahatisha nyingine aongezee, aweze kununua dawa hizo.
Kundi la wanafunzi waliokuwa wamekimbilia kituoni hapo ili kujificha na mvua iliyokuwa imeanza kunyesha, huku wakicheka sana, lilihamisha mawazo ya Sonia kabisa, nakumtoa pale alipo na kumrudisha enzi zake alipokuwa na yeye mwanafunzi. Sonia alicheka, kisha akainama.
**********************
Sonia wa wakati ule alikuwa Sonia kweli kweli, sio mtaani tu, hata shuleni kila mtu alimfahamu. Hakuna mwalimu aliyeacha kumsifia na kumtolea mfano Sonia alipokuwa shuleni. Usafi wake binafsi, utulivu aliokuwa nao, nidhamu kwa kila mtu, na juhudi alizoonyesha shuleni, zilimvutia kila mtu aliyebahatika kumfahamu.
Hata alipogundulika ni mjamzito akiwa shuleni, sio nesi tu ambaye alishtuka sana bali shule nzima ilikuwa ni gumzo. Mwalimu wa nidhamu wa shuleni hapo ambaye alikuwa rafiki mkubwa sana wa Sonia, alishindwa hata kumtizama Sonia machoni.
**********************
Sonia alishtuka nakujikuta amebaki kituoni pale, peke yake na giza lilishaanza kuingia. Alitoa simu yake ili kuangalia muda. Tayari ilishakuwa ni saa 12:30 jioni na mvua ilikuwa ikinyesha sana katika jiji hilo la Mwanza.
Mara alimuona mtu anakimbilia kituoni hapo akiwa na vifurushi vingi mkononi kama msafiri. Alianza kujikung’uta baada yakuweka vitu vyake vyote chini.
“Samahani dada, naomba uniazime simu yako, ili nimpigie Jamaa yangu nimuelekeze hapa nilipo.” Bado Sonia alikuwa akimtizama bila yakusema kitu chochote.
“Simu yangu imeishiwa chaji wakati namuelekeza nilipo. Atakuwa anahangaika njiani hajui atanifikiaje. Taksii niliyokuwa nimepanda imeharibika katikati ya barabara” Aliendelea kujieleza baada ya kumuona Sonia bado ameduwaa na simu yake mkononi. “Simu yenyewe haina hela yakutosha, labda umtumie ujumbe.”
Sonia alijibu huku akimkabidhi simu yake. “Asante. Ngoja ni 'mbipu', apige.” Na kweli baada ya muda simu ya Sonia iliita, wakaanza kuongea. Lakini Sonia aligundua anavyomuelekeza alipo, itamsumbua sana kwa rafiki yake kufika hapo kituoni na simu yake ilishaanza kutoa mlio wakuishiwa chaji.
Baada ya mazungumzo hayo ya muda mrefu, ilimbidi Sonia amsaidie kumuelekeza yule mtu kwenye simu. Baada ya dakika chache tu, kweli ilisimama gari nzuri sana kituoni hapo, lakini mvua ilikuwa ikinyesha sana.
“Rafiki yangu amefika, nashukuru sana kwa msaada wako. Unataka tukusogeze?”Gari yenyewe ilikuwa nyeusi, giza lilishaingia, mtu mwenyewe hakuwa akimfahamu. Hofu ilimuingia Sonia. “Hapana. Mimi nitakuwa sawa tu.” Honi ya gari iliendelea kusikika tena na tena, kuashiria kuitwa na rafiki yake aliyekuwa bado yupo ndani ya gari.
“Giza limeshaingia na sidhani kama ni sawa kuendelea kukaa hapa kituoni peke yako!” “Daladala zitakuja muda sio mrefu. Asante sana.” Alitoka rafiki yake kwenye gari. “Ni mimi Mzee. Vipi? Twende.” Kwa shingo upande, yule aliyeazima simu ya Sonia aliondoka kwa haraka, huku akimuhofia Sonia kubaki pale kituoni peke yake.
Hata dakika tano hazikuisha, daladala ilifika pale kituoni. Wakati anataka kukimbia kuingia ndani ya daladala aligundua yule aliyemuazima simu ameacha begi dogo. Sonia alilibeba na kukimbilia nalo kwenye daladala.
Alibahatisha kiti akakaa chini akiendelea kuwaza, akichukia kurudi nyumbani mikono mitupu, bila dawa za mwanae wala pesa. Alikumbuka hali aliyomuacha nayo mtoto wake, alichukia umaskini alionao.
Japokuwa hakuwa amejiandaa kuzaa kwa wakati huo, lakini alimpenda sana mtoto wake. Alichukia kuwa mama anayeshindwa kumsaidia mtoto wake hasa kipindi hicho ambapo ni mgonjwa sana.
Aliingia chumbani kwao, nakukuta mtoto wake amelala. “Vipi umefanikiwa?” “Hapana mama. Tina amesema hana hela ya kunikopesha.” Mama Sonia alinyamaza, nakutoka chumbani kwao. Hapakuwa na kitu chochote kilichokuwa kimepikwa, wazi alijua na mvua ile mama yake alishindwa kutoka na kufanya biashara jioni hiyo.
Sonia alitupa vitu vyake vyote pembeni nakuanza kujikausha taratibu huku akimwangalia mtoto wake alivyolala pale kitandani. Wazi alionekana ni mdhaifu. Alipobadili nguo, alikumbuka kibegi alichokiokota pale kituoni. Alisogea karibu na chemli huku akijaribu kukifungua ili aone kilichopo ndani.
Pale Unapokuwa Kwenye Shida Na Milango Mingi Kufunguka Kukupa Suluhu Bila Kujua Upi Ni Sahihi.
Macho yalimtoka Sonia baada yakukutana na noti mpya za pesa za kitanzania, zilizokuwa zimefungwa na rababendi kwa mafungu ya noti kubwakubwa. Mapigo ya moyo yalianza kwenda kasi.
Haraka haraka akiwa amejawa hofu, alikifunga robo tatu ya kibegi hicho huku upande mwingine ukigoma kufunga, mwishowe akaamua kukitupia chini ya kitanda vilevile.
Wazo la kwanza lililomjia, nikuchukua baadhi ya hizo pesa na kumpeleka mtoto wake hospitalini haraka sana. ‘Akipona mwanangu, tutahama hapa, nitanunua nyumba, nitaanzisha biashara kubwa, itakayoweza kunisomesha mimi na mwanangu. Itabidi mama ndio awe msimamizi wahiyo biashara.’ Sonia alizidi kupanga mipango mingi sana ya zile pesa alizoziokota.
Tabasamu lilimjaa usoni. Alianza kuona heshima aliyokuwa ameipoteza kwenye jamii ikirudi. ‘Wataanza kumuheshimu na mama yangu.’ Sonia aliendelea kuwaza huku akitabasamu. “
“Kuna maandazi hapo kabatini, kunywa na chai ipo kwenye chupa.” Mama yake Sonia aliongea kwa kifupi tu baada yakuingia na kumkuta mwanae amekaa kwenye kiti akiwaza. “Naona tubakize kwa ajili ya asubuhi.” Sonia alijibu. “Acha na mimi nijilaze. Nasikia mgongo unaniuma kweli! Usikawie kuzima hiyo chemli, tusije ishiwa mafuta ya kesho.” “Pole mama.” Sonia alisema kwa unyonge sana. “Asante.”Mama yake Sonia alijilaza pembeni ya mtoto wa Sonia na kumuachia Sonia nafasi yakulala upande mwingine wa kitanda hicho.
“Vipi joto lake?” “Nilimpa dawa ya kushusha homa kabla hajalala. Naona limeshuka kidogo.” Sonia alizima chemli ili asimalize mafuta, nakubaki gizani peke yake akiwaza juu ya yale mapesa aliyoyaokota.
Taratibu ukweli ulianza kumsuta moyoni. ‘Hapana, hili ni jasho la mtu. Siwezi kutumia.’ Taratibu alivuta mkoba wake kutafuta simu ili kumpigia rafiki ya yule mwenye mkoba, aliyempigia pale kituoni lakini alikuta simu yake imezimika.
‘Atakuwa na wasiwasi sana.’ Sonia alianza kuwaza kama amwambie mama yake au la. Lakini alihofia sana, kwa shida walizonazo mama yake anaweza kuingiwa na tamaa na kumshawishi wazifiche hizo pesa. Aliamua kujilaza kitandani kwenye sehemu aliyobakishiwa, akaendelea kuwaza mpaka alipopitiwa na usingizi.
**********************
Aliamshwa asubuhi na kilio cha mtoto wake akiwa na homa kali sana. Mama yake ndiye aliyekuwa akimbembeleza na kila alichopewa na bibi yake alikataa. Bibi yake alimpa dawa ya kushusha tena homa, nakumbeba mgongoni ili atulie.
Mama Sonia alimpenda sana mjukuu wake. Japokuwa alikasirika sana kitendo cha Sonia kupata ujauzito akiwa shuleni, lakini alimpenda sana mjukuu wake. Alimpa jina la baba yake, yaani babu yake Sonia. Kanamugire, lakini walizoea kumwita Kana.
Japokuwa hakuwa akiongea sana na Sonia tokea apate ujauzito lakini hakuacha kumuhudumia mjukuu wake. Alimpenda sana Kana, hata Kana mwenyewe alijua bibi yake ndiye mama yake na Sonia ni dada yake tu. Hakuwahi kumwita mama hata siku moja, alimuita Sonia kama alivyozoea kumsikia bibi yake akimuita Sonia.
Sonia alibaki ameshika shavu akimwangalia mwanae jinsi anavyohangaika. Baada ya homa kushuka kidogo na mtoto kutulia, Sonia alitoka kwenda kibandani kwa rafiki yake, kuchaji simu yake. Alirudi nyumbani na kutoka na sinia ya maandazi aliyoshindwa kuuzamama yake siku iliyopita, wakati yeye akihangaika mtaani kutafuta kukopa pesa za kununulia dawa za mtoto wake.
Alijikuta kadiri siku zinavyo zidi kwenda, ndivyo shida zilivyokuwa zikiwaandama. Alikuwa akiuza vitu vyake kimoja baada ya kingine ili kuweza kukabiliana na changamoto za maisha zilizokuwa zikiwakabili mpaka alipomaliza kuuza kila kitu chake na kubakia mtupu kabisa.
Alikwenda kujipanga karibu na barabara ili kuuza kama wenzake. ‘Yule kaka atakuwa na wasiwasi sana. Inabidi nikaangalie simu kama imepata chaji hata kidogo, ili nimpigie kumtoa wasiwasi.’ Sonia aliwaza.
Aliamua kurudi kwenye kibanda cha simu kuangalia simu yake kama imepata chaji hata kidogo, ili apige atoe taarifa kwa muhusika kuwa anazo pesa zake. Akarudi tena pale kibandani. “Vipi Salma, umeniwekea simu yangu kwenye umeme?” “Pole shoga yangu, nimeingiwa na tamaa ya pesa, nimepata wateja wengi wakulipia. Lakini usihofu, ya kwako ipo kwenye foleni. Zikijaa hizi tu, nakuwekea ya kwako.” “Asante. Basi nipo pale barabarani nauzauza, ikijaa mtume hata Abuu aniletee.” “Usijali besti.”
Sonia alirudi kwenye sinia lake la maandazi. Bado yalikuwa mengi. ‘Hivi sisi tunalaana? Mbona kila kitu hakiendi?’ Sonia aliendelea kuwaza huku akiangalia wenzake waliomkuta akiuza. Walipofika tu, walimaliza kuuza na kumuacha Sonia akihangaishana na kufukuza nzi kwenye sinia lake. Mara afunike upande huu mara afungue, ilimradi kuvutia wateja wanunue maandazi yake, lakini waliyapita kana kwamba hawayaoni na kwenda kununua kwenye masinia yaliyokuwa wazi kabisa tena yaking’ong’wa na inzi.
**********************
“Umeuza?” Mama yake Sonia alimdaka Sonia mara tu alipoingia na kuweka sinia chini. “Nimeuza kidogo.” “Inabidi tuyale, yakizidi kukaa yataharibika.” “Vipi Kana? Homa imeshuka?” “Naona safari hii imekataa kabisa kushuka. Labda tumuogeshe. Maana nimemkanda na kitambaa lakini maji yanaishia kuwa ya moto tu.” “Ngoja nikachote maji basi.”
Akiwa bado na njaa, Sonia alichukua ndoo kwenda kununua maji. Wakati yupo njiani kwenda kuchota maji, akiwa na mawazo mengi alimsikia Abuu, mtoto wa Salma akimuita. Akasimama. “Mama amesema nikupe simu yako.” “Asante mwanangu. Mwambie mama nitamuona baadaye.” Sonia aliiwasha simu yake akiwa bombani akisubiria zamu yake yakuchota maji ifike.
**********************
Moja kwa moja alianza kutafuta namba ya mwisho aliyokuwa amepiga pale kituoni siku iliyopita. Kwa kuwa hakuwa na hela alianza 'kubip'. Hata dakika moja haikuisha, simu ya Sonia ilianza kuita. “Habari yako?” Sonia alisalimia. “Uliona begi dogo nililiacha pale kituoni jana? Nimekutafuta tangia jana ulikuwa hupatikaniki, nilirudi mpaka pale kituoni sikukuona.” Alisikika kwa kupaniki.
“Pole. Nilijua utaingiwa na wasiwasi. Simu iliishiwa chaji.” “Unacho kibegi changu? Niambie chochote unachotaka nikupe, unirudishie kibegi changu.” “Ndio maana nimekupigia simu kaka yangu, nilijua rafiki yako ataniunganisha na wewe.” “Naweza kukifuata sasa hivi?” Sonia alimsikia mtu wa upande wa pili akimnong’oneza yule aliyekuwa akiongea naye kwenye simu.
“Mwambie tutampeleka polisi.” “Hamna haja ya kumwambia hivyo George. Huoni amepiga simu yeye mwenyewe?” Sonia aliendelea kuwasikiliza wakibishana. “Tatizo lako wewe unapenda kuamini sana watu Sam, kijizi hicho kidada, mbona kilizima simu?” “Acha hizo G bwana!”
“Halooo?” Sonia aliita tena baada yakuchoka kusikiliza anavyotukanwa kwenye simu. “Samahani dada. Uko wapi tufuate mzigo wetu?” Sonia alishakasirika sana. Alinyamaza kwa muda, akifikiria kama akate simu na kutupia mbali ile line ya simu na kuweka zile pesa au amuelekeze alipo.
‘Hawana shukurani kabisa hawa! Anawezaje kuniita mwizi?’ Sonia aliendelea kuwaza. “Haloo? Halooo?” “Nipo kaka yangu. Nafikiria njia rahisi yakukuelekeza ili muweze kufika kwa urahisi hapa ninapoishi.” “Kwani unaishi wapi?” Sam alihoji. “Tunaishi Mabatini, lakini nyumba tunayoishi sisi imejificha kidogo, na ninaona wewe ni mgeni hapa mjini. Naomba kuongea na huyo rafiki yako anayeniita mimi mwizi, nimuelekeze nyumbani kwetu.” Kimya kikubwa kilitanda kwa muda.
Kisha akasikia. “Samahani sana.” Sonia alinyamaza kimya. “Unajua amekusikia, wewe G? Anataka kukuelekeza kwake. Naomba ukiongea naye uwe mstaarabu, G. Maisha yangu yote yapo kwenye lile begi.” “Acha woga Sam.” Sonia alibaki akiwasikiliza nakuzidi kukereka. Akakata simu.
Mara simu yake ilianza kuita kama mara tatu mfululizo, Sonia alibaki akiingalia simu yake kwa hasira. Alichukia nafsi yake ya ubinadamu. Alitamani angeachana kabisa na wazo la kurudisha hizo pesa, lakini alijua asipozirudisha, atashindwa hata kulala. Aliamua kupokea tu simu ili amalizane nao, aendelee na maisha yake.
Akiwa na njaa, hasira ya maisha, alianza kuongea kwa ukali kidogo huku akimpa maelekezo huyo aliyemsikia anaitwa G. “Natunakuja sasa hivi. Ukizima tena simu nakutafutia polisi.” “Acha kunitisha, mimi ndio nimeamua kuwatafuta.” Akamjibu hivyo na kumkatia simu.
Baada ya muda kidogo simu yake iliita tena, akapokea. “Samahani sana dada yangu.” “Unaomba msamaha wa nini wewe Sam?!” “Naomba unyamaze G.”Walianza kubishana tena, huku Sonia akiwasikiliza.
“Haloo?” Sonia alinyamaza tu. “Naitwa Sam, na wewe unaitwa nani?” Sonia alianza kulia taratibu. Alishangaa kitu kikimng’ang’ania kooni bila kumuachia. Aliendelea kulia kwa muda huku Sam akimsikiliza, wazi alijua analia kwa jinsi alivyojitahidi kusafisha pua zake. “Samahani sana.” Sam aliendelea kurudia neno lilelile, tena na tena.
Baada kutulia ndipo alipoweza kuongea. “Naitwa Sonia. Ukifika tu pale nyuma ya msikiti nilipomwambia mwenzako, atakuta magenge, mkiuliza tu Sonia, mtaletwa mpaka nyumbani.” “Asante sana Sonia.” Sonia hakutaka kujibu kitu chochote, alikata simu. Akachukua ndoo yake ya maji akaanza kurudi nyumbani kwao kwa haraka.
Alikuta joto la mtoto wake bado lipo juu sana, akaamua kumuogesha kama alivyo shaurina na mama yake tokea mwanzoni.
“Naogopa mama. Mwili wake ni wa moto sana.” Taratibu machozi yalikuwa yakimtoka Sonia wakati anamkausha maji mtoto wake. “Mlete nimpakate.” Mama Sonia alimchukua mjukuu wake. Wote walibaki kimya hapo chumbani kwao, wakiwa wamekaa kwenye mkeka, wakiwaza jinsi ya kumuokoa Kana, kwani ni kweli hawakuwa na pesa kabisa.
**********************
“Chumba hicho hapo, ndio kwa kina Sonia.” “Asante sana.” Walisikia watu wakiongea nje ya mlango wao. “Hodii.” Mama yake Sonia alishangaa kusikia sauti asizozijua. “Karibu. Mlango uko wazi, sukuma tu.” Mama Sonia ndiye aliye jibu, mar waliingia vijana wawili waliomtoa macho Mama Sonia.
“Karibuni!” “Habari za hapa?” Mmoja aliinama kumfikia Mama Sonia aliyekuwa amekaa kwenye mkeka, na kumpa mkono. “Nzuri tu.” Macho ya yule aliyesalimia yalitua moja kwa moja kwa Sonia aliyekuwa ametulia kimya kabisa pembeni ya mama yake. “Naona kiti chenyewe kimoja na stuli. Sijui mtakaaje! Lakini karibuni.” “Hamna shida mama. Naitwa Sam.” “Wamezoea kuniita Mama Sonia. Karibuni sana.” Sonia alisimama bila ya kusema kitu nakuelekea moja kwa moja chini ya uvungu wa kitanda chao.
“Mmmh!” Mama Sonia aliguna. “Vipi mama?” Sonia aliuliza huku akivuta ule mkoba. “Joto lake linazidi kuwa kali.” “Mtoto anaumwa?” Sam aliuliza. “Mgonjwa tokea majuzi. Naona leo homa inazidi kuwa juu na haitaki kushuka kabisa.” Mama Sonia alikuwa akiongea na Sam huku akishikashika mwili wa mjukuu wake.
“Begi lako hili hapa. Naomba ulifunge vizuri, nililifungua jana, nimeshindwa kulifunga vizuri.” “Asante sana.” Sam alilipokea hilo begi akiwa haamini. “Unafungaje bila kuhesabu, we Sam?” “Nilikuomba unyamaze G.” “Utanikumbuka Sam! Huwezi kuondoka hapa bila kuhakikisha kama vitu vyako vyote viko sawa.” Kama kawaida yao walianza kubishana mbele ya Sonia na Mama yake.
“Kwani nini kinaendelea? Mbona siwaelewi?!” Mama Sonia akauliza. “Naomba muondoke. Sijagusa kitu chochote humo ndani. Nilipofungua, nikakutana na pesa, nikajaribu kufunga nikashindwa. Wala sijagusa au kuchukua kitu chochote ndani ya hilo begi.” “Asante sana Sonia.” Sam alirudia tena.
“We Sonia? Nini kinaendelea?” Sonia alinyamaza kimya. “Samahani sana Sonia na nina kushukuru sana.” Sonia alinyamaza kimya huku akifuta machozi. Sam alibaki akimwangalia Sonia kama akisubiria jibu la msamaha aliomba na shukurani aliyotoa. Alipoona kimya akamgeukia mama yake.
“Ulisema mtoto anasumbuliwa na nini?” “Mkojo mchafu.” Mama Sonia alijibu kwa kifupi tu. Sam alijua ni ugonjwa wa UTI. “Anatumia dawa zozote?” “Mmmh! Dawa zenyewe gali kweli! Tumeshindwa kununua.” “Aliandikiwa dawa gani?” Sam aliendelea kumuhoji Mama Sonia na yeye alimgeukia Sonia. “Eti Sonia?” “Kile kikaratasi cha dawa, kitakuwa kilianguka jana pale kituoni, nimekitafuta leo asubuhi sikukiona tena.” Sonia alijibu kwa unyonge sana.
“Usianze kabisa Sam! Tena naomba tuondoke. Ushapata kilichotuleta, twende. Nakujua wewe.” Wote walimgeukia G, aliyekuwa karibu kabisa na mlango kama anayetaka kukimbia. Chumba chenyewe kilijawa giza walionana kwa shida kidogo, tena kwa msaada wa mwanga ulikuwa ukipitia kwenye kidirisha kidogo kilichojengewa juu ya chumba hicho kilichokuwa uwani na tena kulionekana kuna nyumba nyingine iliyokuwa imepakana na dirisha lao. Kwa hiyo hata hewa ilikuwa nzito sana hapo chumbani kwao.
“Naomba twende hapo nje tukaongee G.” Walitoka nakumuacha Sonia na mama yake. “Hao ni kina nani Sonia?” “Hata siwajui!” Sonia alijibu kwa kifupi tu, na kumuacha mama yake akimwangalia. Sonia hakutaka kuendeleza yale maongezi kabisa. Akili yake ilishaanza kuzunguka sababu ya njaa iliyokuwa ikimuuma na joto la mtoto wake lililokataa kushuka.
Hakuna Anayetoa Kumzidi Mungu
Baada ya muda mfupi Sam alirudi peke yake bila hata kile kibegi mkononi. “Kwa nini tusimrudishe mtoto hospitalini? Akionana na daktari tena atamuandikia dawa.” Sam alishauri. “Kumuona daktari tena? Na hiyo pesa tunatoa wapi? Dawa zenyewe tulizoandikiwa kumnunulia, zimetushinda!” Mama Sonia aliuliza kwa mshangao mkubwa.
“Tutakuwa pamoja.” Mama Sonia alimgeukia Sonia kwa mshangao. “Wewe! Umesikia? Ndio uchangamke twende kabla hajabadili mawazo.” Sonia alibaki kimya kwa muda. Kisha akajibu. “Huna haja yakufanya yote haya kwa sababu ya kukuokotea kibegi chako, kaka yangu. Huyu mtoto atakuwa sawa tu.”
“Pamoja na hayo. Lakini mtoto hawezi kuendelea kuteseka na uwezekano wakutibiwa upo. Nashauri tumuwahishe hospitalini.” Mama Sonia alisimama kwa haraka bila hata kutaka kumsikiliza mwanae, akamfunga mjukuu wake mgongoni. “Twende Sam kama unataka kutusaidia. Mimi nipo tayari.” Walitoka bila Sonia. Baada ya muda Sonia alifunga mlango na kuwafuata kwa nyuma.
**********************
Walifika barabarani, Sam alikodisha taksi mpaka hospitalini. Mtoto alipimwa na kuandikiwa dawa. “Naomba mnisubiri hapa nikanunue dawa.” “Asante sana.” Mama Sonia alishukuru na Sam akaondoka kuelekea kwenye duka la madawa. Sonia aliamua kumfuata nyuma.
“Sam!” Sam akageuka kumuangalia Sonia. “Asante.” “Karibu. Asante na wewe.” Sonia alitabasamu kwa mara ya kwanza na kuinama. “Samahani nilikuwa nimekasirika sana. Rafiki yako aliniudhi tokea mwanzo kuniita mwizi, halafu na hali ya mtoto ilizidi kunichanganya.” “Pole sana na samahani. Achana na G. Lakini na yeye ni mtu mzuri tu, sema ameshatapeliwa sana, ndio maana haamini watu. Hatujawahi kukutana na mtu kama wewe, Sonia. Ndio maana hata yeye ilimuia vigumu kuamini kama kweli unaweza kuturudishia zile pesa.” “Hamna shida. Nashukuru kwa msaada wako na wewe.” Sam aliwarudisha nyumbani na kuondoka.
**********************
Wakati wanalala, simu ya Sonia ilianza kuita. “Nani huyo?” Mama Sonia aliuliza. “Sijui!” “Pokea sasa!” Sonia aliendelea kuitazama simu yake, nakuamua kuizima sauti.
Baada ya muda ujumbe ukaingia. ‘Nilitaka kujua hali ya mtoto. Sam.’ Sonia alishtuka sana. Akaamua kubipu ili ampigie tena. Hapohapo Sam akampigia. “Samahani kaka, sikuwa najua kama ni wewe na simu haina hela.” “Hamna shida. Mtoto anaendeleaje?” “Anaendelea vizuri.” “Akipata dozi mbili tatu atakuwa sawa. Poleni sana.” “Asante.” “Usiku mwema.” “Asante na wewe.” “G anakusalimia.” Sonia alicheka kidogo. “Msalimie na yeye.” “Amefurahi.” Sam alijibu na kukata simu.
**********************
Sonia aliamka asubuhi na kuamua kujaribu kuwahi kutafuta pesa. “Mama! Wakati wewe unamlisha mtoto, naona mimi nitangulie sokoni nikaanze kuuza chai. Tusije poteza wateja wote.” “Wazo zuri.”
Siku za kazi, Sonia na mama yake walikuwa wakiuza chakula kwenye soko la Kireluu. Kuanzia asubuhi kifungua kinywa, mpaka chakula cha mchana, ndipo walikuwa wakifunga biashara yao. Aliondoka na kumuacha mama yake na Kana.
Alipofika tu, alipika harakahara na kupanga meza tayari kusubiria wateja wao. Alisikia simu yake ikiita kwenye kipochi chake. Sonia aliikimbilia. Alijua itakuwa ni Sam tu.
“Haloo!” “Vipi Sonia? Mliamka salama?” “Ndiyo kaka. Mtoto ameamka na nafuu.” “Afadhali. Basi nitawaona baadaye.” Sonia alifikiria kidogo. “Sonia?” “Nipo kaka.” “Au hamtakuwepo nyumbani?” “Tunakuwa kazini mpaka jioni ndio tunarudi nyumbani.” “Hata mimi nitakuwa na kazi nyingi mpaka jioni, kwa hiyo nikitoka kwenye shuguli zangu nitapita kuwasalimia.” “Sawa. Asante kaka.” Walikata simu.
Aliendelea na kuuza kifungua kinywa na baada ya muda mama yake alikuja na vitu vyakupika kwa ajili ya chakula cha mchana na mtoto mgongoni. “Nafikiri sasa hivi inabidi utafute kazi Sonia. Hii biashara haitatupeleka popote.” Sonia alibaki kimya kwani haikuwa mara ya kwanza mama yake kutoa hilo wazo na alishatafuta sana kazi bila mafanikio.
Akaendelea kupika chakula cha biashara akiwa kimya kabisa. Walikuwa na wateja wachache lakini wote walisifia sana chakula anachopika Sonia. Ilipofika saa kumi jioni, Sonia alianza kuosha vyombo tayari kwa kufunga biashara kwa siku ile kwa kuwa mida ile ilikuwa ngumu kuuza tena.
“Mama! Labda nyinyi mngetangulia tu nyumbani ili mtoto akapumzike. Nitawafuata baada yakumaliza usafi.” Mama Sonia aliondoka na mtoto mgongoni na kumuacha Sonia akimalizia kuuza chakula kilichobaki, huku akiosha vyombo vingine.
**********************
Simu ya Sonia ikaita tena. “Haloo!” “Sonia?” “Ndiyo kaka, ni mimi Sonia.” “Mbona sauti imebadilika?” Sonia akatulia kidogo na kujibu. “Ni mimi kaka.” “Nimemaliza mambo yangu mapema kidogo, nimepata ndege ya kurudi Dar kesho asubuhi sana. Nisawa kuja kukuaga?” “Bado nipo kazini.” “Wapi?” “Nafanya biashara katika soko la Kireluu.” Sonia alijaribu kumuelekeza.
Baada ya muda mfupi Sam alifika kazini kwa Sonia. Alishangazwa sana na maisha ya Sonia. Walipangisha chumba kimoja uswahilini, kitanda kimoja tena kidogo, kiti kidogo na stuli. Nyumba yao haikuwa na maji wala umeme. Biashara anayoifaya wazi ilionekana haiwaingizii kipato kikubwa, yeye na mama yake wote walionekana watu duni sana, lakini bado aliweza kumrudishia pesa zote bila kuchukua hata shilingi!
Alimkuta amekaa kwenye benchi na chakula chake kwenye masufuria. Eneo lake lilikuwa safi sana kuliko kwengine na wauzaji wengine walishamaliza chakula chao nakuondoka.
“Karibu Kaka.” Sonia alisimama. Sam alitaka kumpa mkono lakini Sonia alisita. “Mikono bado mibichi. Nilikuwa naosha vyombo.” “Hamna shida.” Walipeana mikono. “Naona hata shida kukwambia ukae hapa. Utachafua nguo zako.” “Hamna shida.” Sam akakaa kwenye benchi, pembeni ya Sonia.
“Mambo yanaendaje?” “Vizuri tu.” Sonia alijibu kinyonge. “Nilijua utakuwa na mama!” “Ameondoka muda sio mrefu na mtoto. Niliona wakapumzike wakati namalizia.” “Mdogo wako anaendeleaje?” “Mdogo wangu?” Sonia hakuwa ameelewa. “Yule tulimpeleka hospitalini jana.” Sonia alinywea gafla.
**********************
Ilikuwa ni ngumu kumjua Sonia kama ana mtoto wa miaka mitatu. Alikuwa mrefu, mwembamba sana, sababu ya shuruba za maisha. Alivaa kandambili ambazo zilionyesha kushonwa mara kadhaa. Kwa muonekano alionyesha ni msafi lakini mavazi yake yalikuwa duni sana na miguuni alionyesha kujawa na vumbi sababu ya kutembea. Wakati wote alisuka minyoosho au twende kilioni.
**********************
Sam aliweza kuona uso wa Sonia ulivyobadilika baada ya kumuuliza swali. “Yule sio mdogo wangu. Ni mtoto wangu. Anaitwa Kanamugire, ana miaka mitatu sasa. Ila tunamwita Kana.” Sonia aliongea huku anaangalia chini, akichezea vidole vyake. “Hongera sana. Kumbe una kijana mkubwa hivyo!” Sonia alinyamaza kimya bila yakujibu kitu.
“Kesho nitaondoka asubuhi kurudi Dar.” “Ndiko unako ishi?” “Ndiyo. Huku Mwanza huwa nakuja kwa G. Yeye anafanya biashara za kuuza dagaa. Anasambaza mikoani. Niliamua kufanya naye hiyo biashara, awe ananiletea na mimi Dar.”
“Oooh! Umefanikiwa sasa?” “Naona mwanzo sio mbaya. Amenizungusha kwa watu au tuseme maeneo anayokusanya hao dagaa. Nimejiridhisha, inabidi na mimi niondoke nirudi kibaruani. Wasije nifukuza kazi!” Sam aliongea kwa utani kidogo akimtaka Sonia angalau atabasamu na yeye lakini hakufanikiwa. “Jambo la kushukuru Mungu.” Sonia alijibu kwa kifupi na ukimya kidogo ukatanda.
“Naomba upokee hii bahasha kama shukurani yangu kwako, Sonia.” Sonia akakunja uso. “Shukurani ya nini tena!?” “Ile pesa uliyonirudishia, nilikopa kazini kwangu na mchumba wangu aliniongezea kidogo ili kufanikisha hii biashara. Najiuliza bila kupata jibu, kama usingenirudishia, ningefanyaje? Maana ofisini nimeshaanza kukatwa kwenye mshahara wangu, na mchumba wangu anasubiria hii biashara kwa hamu sana. Kwa hiyo nashukuru sana kwa moyo wako wa kimungu.” Sonia alitulia kidogo.
“Lakini kaka, huna haja ya kunilipa. Mimi nimefanya kwa sehemu yangu. Wote tunatakiwa kumshukuru Mungu, kwa kuwa hizo pesa hazikuangukia kwenye mikono mibaya.” “Naomba upokee Sonia, zitakusaidia.” “Hapana kaka. Kama unataka kunilipa, ujue ulishanilipa uwe na amani tu.”
“Siku ile tulipokutana, nilikuwa nimetoka kumuomba rafiki yangu anikopeshe pesa ili nikanunue dawa za Kana. Lakini alinikatalia katakata. Pale uliponikuta kituoni, nilikuwa nimechanganyikiwa, sijui chakufanya. Lakini umeokoa maisha ya mwanangu. Siungefuata ushauri wa G tu, ukaondoka nakutuacha? Lakini na wewe umefanya ukarimu wa hali ya juu. Nashukuru. Sina chakukulipa, lakini pokea shukurani yangu toka moyoni.” Sam alitamani sana Sonia achukue zile pesa. Lakini alikataa kabisa kitu kilichozidi kumshangaza!
**********************
Ukweli Sonia na mama yake, walionekana ni mafukara sana. Sio kwa mtaa wanaoishi katika jiji hilo la Mwanza ambapo palionekana ni uswahilini sana bali hata sura zao pia zilionyesha ndani ya mioyo yao wamebeba jambo linalowaumiza sana.
**********************
Sam alibaki na Sonia pale sokoni mpaka giza lilipoanza kuingia. “Unafanyaje sasa ukibakiza chakula kingi hivyo? Unamwaga?” “Hapana. Narudi nacho nyumbani, na kwenda kujaribu kuuza tena palepale mtaani kwetu.” “Unaonekana biashara unaiweza sana Sonia!” “Wakati mwingine inakulazimu, kaka.” Sonia alijibu kinyonge sana.
“Nikusindikize mpaka nyumbani?” “Hapana kaka yangu. Nisikusumbue. Ungeenda tu kujiandaa na safari. Nakushukuru sana kwa kila kitu.” Bado Sonia alimchanganya sana Sam, lakini aliamua kumuacha tu. Alihakikisha anapata usafiri wakurudi nyumbani kwao, ndipo Sam na yeye alipoondoka.
**********************
Sonia alitamani sana kujua kama Sam alifika salama Dar, lakini aliogopa hata kutuma ujumbe. Alikumbuka Sam aliongelea juu ya mchumba wake. Aliogopa kuzua ugomvi kati yao.
Maisha yaliendelea kuwa magumu kila kukicha. Kila biashara waliyoona wenzao wanafanikiwa, walipojaribu wao, walishindwa. Wakati wote walienda na mtoto kazini. Na mtoto wa Sonia alimzoea bibi yake kuliko hata mama yake. Muda mwingi Sonia alimuacha na bibi yake wakati yeye akizunguka kutafuta vibarua.
**********************
Baada ya juma moja kupita, Sonia alikuta ujumbe kwenye simu yake asubuhi alipoamka. 'Naona mwenyeji wangu, umenisusa. Hutaki hata kujua kama nilifika salama!' Sonia alijisikia vibaya sana. Alikumbuka ukarimu wa Sam, nakujutia kupuuzia lile wazo lakuulizia kama alifika salama. Kwa kuwa simu yake haikuwa na pesa kama kawaida, aliamua kubip.
“Haloo?” “Mnaendeleaje huko?” “Nashukuru Mungu mtoto alipona kabisa, anaendelea vizuri.” “Safi sana. Na wewe?” “Naendelea vizuri. Samahani kwa kushindwa kukujulia hali kaka yangu, nilijua utakuwa na mambo mengi. Sikutaka kukusumbua.” “Hamna shida. Salamu sio usumbufu.” Baada ya maongezi mafupi waliagana.
Sam hakuacha kumpigia simu Sonia ili kumjulia hali. Na hapakuwa na maongezi zaidi ya salamu tu.
**********************
“Mbona mpaka sasa hivi una sauti ya usingizi? Huendi kazini leo?” Simu ya Sam ndio iliyomuamsha Sonia usingizini. “Tulishafunga ile biashara ya sokoni.” Sonia alimjibu Sam, nakujiweka sawa. Alijaribu kuangaza macho pale chumbani, lakini mama yake na mtoto wake hawakuwepo.
“Umepata biashara nyingine?” “Bado kaka. Lakini pale tulishindwa kabisa biashara. Tulikuwa tunaingia hasara tu.” “Utafanya nini sasa?” “Ndio nipo kwenye kuhangaika kutafuta kazi.” “Unataka kazi gani?” “Yoyote tu. Hata za kwenye majumba ya watu, sichagui. Nimezunguka sana bila mafanikio.” “Kwani una elimu gani, Sonia?” Sonia alikwama, hakujua aanzie wapi swala la elimu yake.
“Sonia?” “Nilikwamia kidato cha pili, muhula wa pili.” “Oooh! Ukipata kazi huku Dar, unaweza kuja kuishi huku?” “Tumekwama kabisa kaka, popote pale nitakwenda. Ilimradi niingize pesa hata yakula tu.” “Na mtoto wako?” Sonia alitulia kidogo. Alianza kuwaza maisha bila mtoto wake. Lakini hakuwa na jinsi. Nilazima atafute pesa, popote pale.
“Nitamuacha na mama kwa muda mpaka nitakapojiweka sawa, ndipo nitarudi kumchukua.” “Ni wazo zuri.” “Basi unipe muda. Nitakuulizia. Nikisikia nafasi ya kazi popote, nitakujulisha.” “Asante sana kaka yangu.” Japokuwa hakuwa amepewa kazi, lakini Sonia alifurahi sana. Angalau aliongezeka mtu mwingine maishani mbali na mama yake, aliyeonyesha kujali.
**********************
Siku zilizidi kwenda bila kusikia chochote kutoka kwa Sam, na maisha ya nyumbani kwao yalizidi kuwa magumu sana. Hata kula yao ilianza kusumbua. Sonia alizunguka kila mahali kutafuta kibarua lakini alikosa.
Sam naye alipotea, aliacha kupiga simu kabisa. ‘Atakuwa ameniona nina matatizo mengi sana ndio maana amenikimbia.’ Sonia aliendelea kuwaza huku amekata tamaa, siku hiyo aliyokuwa amezunguka karibu siku nzima bila mafanikio na kuishia kuchomwa na jua kwa kutembea kwa kuwa hakuwa na hela yeyote ya kupanda daladala. Hakuwa amekula wala kunywa maji karibia siku tatu.
Alirudi nyumbani akiwa ameshikilia kandambili yake moja iliyokuwa imekatika, akajitupa kitandani. Njaa, kiu na uchungu mkubwa moyoni vilikuwa vimemlemea Sonia. Hapakuwa na tumaini lolote katika maisha yao. Hawakuwa na ndugu wala rafiki wakumtegemea.
Mama yake alinyanyua macho kumuangalia wakati akiingia, alipomuona machozi yanamtoka, alijua mwanaye hakufanikiwa. Alimuhurumia na kushindwa jinsi ya kumsaidia. Kwani alikuwa akitoka asubuhi sana kwenda kutafuta kazi bila hata ya kula kitu chochote. Na alijua kabisa mpaka mida hiyo atakuwa hajaweka kitu chochote mdomoni. Alirudisha macho yake chini nakuendelea kubembeleza mjukuu wake aliyekuwa akisinzia palepale chini kwenye mkeka.
**********************
Sonia na mama yake walikuwa ni marafiki sana kabla ya Sonia kupata ujauzito. Mama Sonia alipata ujauzito wa Sonia akiwa ndio anaingiza miaka 14 tu, alijiapia kuto kukubaliana na wazo lakutoa hiyo mimba japokuwa alilazimishwa kuitoa, lakini alikataa katakata na kuamua kutoroka asijue pakwenda.
Aliapa kumtunza mtoto wake yeye mwenyewe. Akiwa binti mdogo sana, alifanya kazi kwa bidii sana huku akijinyima, ili Sonia aishi vizuri. Aliacha na kusahau kabisa maswala yote yaliyomuhusu yeye binafsi nakuelekeza nguvu zake zote kwenye kutafuta pesa ili kumtunza Sonia.
Sonia alikuwa na juhudi sana shuleni tokea shule ya msingi. Alifaulu kwenda shule ya bweni ya Ngaza. Ilikuwa furaha na heshima kubwa sana kwa mama yake, kwani katika mtaa waliokuwa wakiishi, ni Sonia peke yake ndiye aliyeonekana ni binti mwenye tabia nzuri na ndiye aliyekuwa akisoma. Kwa hiyo wazazi wengi walimtolea mfano Sonia.
Lakini furaha hiyo haikudumu kwa muda mrefu, kwani mara baada tu yakurudi shuleni baada ya likizo yake ya mwezi wa sita kuisha, akiwa kidato cha pili, Sonia alirudishwa nyumbani akiwa mjamzito.
Ulikuwa mshituko mkubwa sana kwa mama yake. Alipatwa na ububu wa gafla na kushindwa kuongea lolote hata kwa mwalimu mlezi wa shule ya Ngaza aliyekuwa amemrudisha Sonia nyumbani.
Kwani ilikuwa ni majuma mawili tu yaliyokwisha kupita, Mama Sonia alipojikwangua kabisa, kwa kutoa pesa zote alizokuwa nazo, akamnunulia mwanae vitu vyote vilivyokuwa vikihitajika shuleni. Na ili mwanae asisumbuliwe akiwa shuleni, alishalipa ada na michango yote kwa mwaka mzima.
Lakini kama ilivyo desturi ya shule nyingi za wasichana za bweni, kila shule inapofunguliwa ni lazima kupimwa mimba. Baada ya kupimwa kwa muda mrefu sana, Sonia alishangaa alipoombwa na nesi wa shule abaki pembeni wakati anamalizia kupima wanafunzi wengine.
Alibaki akishangaa kuona wenzake wote wanaruhusiwa isipokuwa yeye. Nesi alimuita mwalimu wa zamu na mwalimu wanidhamu, akarudia kumpima tena Sonia mbele yao.
Aliishiwa nguvu ilipothibitika ni mjamzito. Ndoto zote za Sonia zilifutika gafla siku hiyo na kubaki amechanganyikiwa asijue chakufanya.
Mama yake alinyamaza kimya kabisa, hakuwahi kumuuliza Sonia chochote juu ya huo ujauzito, wala kutaka kujua baba wa mtoto. Urafiki kati yao uliisha kabisa.
Hakuna adhabu mbaya aliyompa mwanae kama kutokuongelea kabisa swala la ujauzito wake. Siku zilizidi kwenda, tumbo lilizidi kuwa kubwa, maneno mtaani yalienea ya kumcheka mama yake na yeye mwenyewe, lakini hawakuwahi kuzungumzia na mama yake juu ya ujauzito huo, hata mara moja.
Mtoto alipozaliwa, ndipo Sonia alipoona mapenzi ya mama yake yalivyohamia kwa mjukuu wake. Alimlea mjukuu wake kama mtoto wake! Sonia hakupata shida kabisa ya malezi. Iwe usiku au mchana, mama yake alikuwa na mjukuu wake.
Alipozaliwa tu, alimuomba Sonia kama ni sawa kumpa mtoto jina la babu yake Sonia, Kanamugire. Bila kubisha, kwani Sonia mwenyewe hakuwa na jina lolote alilokuwa ameandaa kwa ajili ya mtoto wake ambaye hakuwa hata amemjua jinsia yake akiwa tumboni.
Usiku Mrefu, Alfajiri Yafika
Sonia alishtuliwa tena na simu yake iliyokuwa ikiita. “Mzima Sonia?” “Mzima kaka. Mbona ulipotea?” “Mambo yalikuwa mengi sana.” “Pole na majukumu.” “Asante. Nipo hapa mjini, unafikiri tunaweza kuonana?” “Ndiyo.” “Unaweza kuja hapa kwa G?” Alipotajiwa sehemu anayoishi G. Sonia alipooza.
“Vipi?” “Sina nauli kaka. Na huko ni mbali na hapa tunapoishi, ningeweza hata kutembea kama kungekuwa karibu.” “Pole. Hapa sina usafiri, G ametoka na gari yake, ningeweza kuja mimi mwenyewe. Unaweza kuchukua taksii nitalipia ukifika?” “Itakuwa pesa nyingi, kaka yangu.” “Usiwe na wasiwasi. Chukua tu, nitalipia.” Sonia alijiandaa haraka haraka, akatoka.
Alisimama barabarani hapo nakushindwa kuondoka. Kila taksii aliyoisimamamisha, alitajiwa pesa nyingi sana, iliyomfanya kuzidi kuwaza. ‘Pesa yote hiyo! Si ningeanzisha biashara nyingine!’ Masaa yalizidi kwenda Sonia bado alibakia barabarani akiwaza.
“Umefikia wapi?” Sam aliamua kumpigia tena simu baada ya kuona kimya kwa muda mrefu. “Bado sijapata usafiri kaka. Wananitajia pesa nyingi sana.” “Acha woga Sonia!” “Ni pesa nyingi sana kaka.” “Basi subiri niongee na G, nione yupo wapi ili akupitie uje naye.” “Asante.”
Baada ya muda aliona gari ya G imesimama mbele yake kidogo. Alionekana yupo na mazungumzo ya muhimu sana kwenye simu yake. Alipofika tu alimuashiria Sonia aingie ndani ya gari, bila ya salamu, G aliondoa gari.
Wasiwasi ulianza kumpata Sonia. Japokuwa alitajiwa mtaa anoishi G, lakini hakujua nyumba yake ilipo na hakuwa amemuaga mama yake. Kwani alipoamka hakuwakuta pale chumbani kwao.
Aliamua kumtumia mama yake ujumbe. 'Nimetoka, ninaenda kuonana na kaka Sam, ameniita.' Kwa kuwa hakutegemea jibu lolote kutoka kwa mama yake kama kawaida yake, alirudisha simu yake kwenye kimkoba chake bila hata kuangalia kama amejibiwa au la.
G alikuwa akiishi kwenye mtaa mzuri sana, Kapripoint. Sonia alijua jeuri ya G inatokana na pesa alizonazo.
Walimkuta Sam akiwasubiri. “Pole G, na samahani kwa usumbufu.” Hiyo ndio ilikuwa salamu ya Sam mara tu walipoingia ndani. G aliweka simu mfukoni. “Utafanyaje kama Mungu ameamua kukuadhibu hapa duniani?” G alijibu huku akitaka kuingia chumbani.
“Kwa nini G?” Sam aliuliza huku anacheka. “Wewe mwenyewe hebu fikiria Sam. Watu wote hawa waliojaa hapa duniani, eti Mungu ameamua kunipa rafiki Padri. Si adhabu hiyo au wewe unafikiri ni nini?” Sam alizidi kucheka sana na G akaingia ndani chumbani kwake.
**********************
“Karibu sana Sonia.” Sonia alikaa kwa kujivizia vizia. Nyumba ilikuwa ndogo tu, lakini ilijazwa vitu vya thamani sana, na palionekana pasafi. Alijitahidi kunawa na kupaka mafuta miguu yake, kabla ya kuondoka nyumbani kwao, lakini vumbi lilishajaa miguuni kwake, sababu ya kusimama barabarani kwa muda mrefu.
Alijitahidi kuficha miguu yake na gauni refu alilokuwa amevaa, ili kandambili alizokuwa amevaa tofauti tofauti zisionekane. Kandambili moja ilikatika mchana wake wakati akitafuta kazi, aliamua kuchukua nyingine iliyokuwa ya zamani ambayo pia mwenzake alishakatika. Moja ilikuwa nyekundu, nyingine ya bluu. Lakini Sam alishakuwa amemuona sababu yakuhangaika.
“Hapa ndipo nyumbani kwa G. Hana wageni labda mimi kama nikija Mwanza ndio nakuwa hapa, lakini anaishi peke yake ndio maana nyumba yake unaiona safi hivi. Kwa hiyo karibu sana.” Sonia alitabasamu kwa woga.
“Asante.” “Unataka kunywa nini?” Sam alianza kumtajia vinywaji mbalimbali vilivyopo kwenye friji, lakini Sonia alibaki anababaika mpaka Sam alipoamua kumletea soda, na glasi ya maji pembeni.
**********************
“Sasa yupo mtu anatafuta msichana wa kazi kwa ajili ya watoto tu. Kwa sasa ana mtoto mdogo wakike, na ni mjamzito. Unafikiri utaweza kwenda kuishi nao?” Kabla Sonia hajajibu G alitoka chumbani. “Au uje uishi na mimi? Uwe unanifanyia kazi za ndani.” “Acha kumzingua Sonia bwana!” “Jamani! Kwani mimi nina nini? Si nitamlipa! Eti Sonia?” Sonia aliinama chini bila ya kumjibu.
Alishamuogopa sana G. Hakuonekana kama ni mkarimu hata kidogo! Alikosa cha kujibu kabisa. Na kwa kuwa aliambiwa anaishi peke yake, aliogopa sana kuja kuishi naye, tena wakiwa wao wawili tu!
“Eti Sonia?” G alizidi kuuliza. “Bwana G, wewe vipi? Mwache bwana afikirie nilichomwambia mimi kwanza.” “Daah! Kweli urafiki wako unamashaka Sam. Unamtoa kijakazi Mwanza, unampeleka Dar, wakati mimi mtu wako nipo, tena nateseka peke yangu!?”
“Acha hizo G bwana! Kwanza wala huhitaji mfanyakazi. Chakula chenyewe hutaki kupikiwa na mtu. Mtu wa kukufulia unaye. Sasa Sonia wa nini?” Sonia alizidi kumchukia G, alimuona hana busara kabisa. ‘Huyu ni mnyanyasaji. Kama ameshaanza kuniita kijakazi, atanitesa sana nikiishi naye.’ Sonia aliendelea kuwaza.
“Kama unaona haupo tayari, hamna neno Sonia. Tutaendelea kutafuta kwengine.” “Nipo tayari kaka. Nitaenda kumfanyia kazi huyo mama.” Sonia alidakia harakaharaka. “Sonia unanitosa?” G aliendelea kumchokoza Sonia.
“Naomba muache bwana! Wewe vipi, G?” G alianza kucheka. “Lakini Sam, umemuangalia vizuri Sonia mwenyewe?” “Ana nini?” G alizidi kucheka. “Sonia sio mchezo! Wewe mwangalie tu vizuri.” “Hebu nenda G. Niache nimalizane na Sonia.” “Haya Padri, mimi nipo ndani.” “Ndani tena? Sio jikoni? Hatuli leo?” “Sawa kaka. Ngoja nikapike.” G aliendelea kucheka akielekea jikoni kupika na kumuacha Sam na Sonia wakiendelea kuzungumza.
“George ni mpishi mzuri sana. Huwa napenda chakula chake. Kila nikija Mwanza huwa sili chakula kingine, isipokuwa anachopika yeye tu.” Sam alijaribu kuvunja ukimya kwani Sonia bado alikuwa akiangalia chini baada ya G kuanza kumwambia Sam amwangalie vizuri.
“Sasa huyo mama, ametoa na nauli yako kabisa. Upo tayari kuondoka lini?” “Siku yeyote kaka.” “Basi ujiandae, halafu kesho kutwa uondoke.” “Nakushukuru sana kaka yangu.” Kwa mara ya kwanza tokea Sam amfahamu Sonia, aliweza kuona uso wake umeonyesha furaha.
Akamsogelea karibu nakupiga magoti. “Asante sana kaka.” Sonia aliendelea kushukuru. “Usipige magoti bwana! Simama tu.” Machozi ya furaha yalikuwa yakimtoka Sonia. Hakutegemea kupata kazi, kwani alishakuwa amekata tamaa kabisa.
Sam alijisikia vibaya sana. “Nakushukuru sana, kaka Sam. Asante.” “Karibu.” Sam alijibu na kuwasha tv, angalau iwasaidie kubadili ile hali ya hewa ya mahali pale, kwani Sonia bado alikuwa akitokwa na machozi.
**********************
George aliivisha chakula nakuweka mezani. Sonia alikuwa na njaa sana. “Sasa kiti hiki changu, pembeni yangu Sonia, wewe Sam unaweza kuchukua chakula chako na kwenda kula sebuleni.” Sonia alivyosikia hivyo tu, tumbo lilijaa gafla. Alibaki ameduwaa na maji yakimchuruzika mikononi baada yakunawa ili ale.
Akamgeukia Sam. “Naona nimeshiba, naomba mimi niondoke, niwahi nyumbani.” G alicheka kwa sauti ya juu sana, mpaka akakaa chini. “Daah! Kweli Sonia hanitaki hapa duniani. Basi bwana, acha mimi ndio nikale sebuleni, Sam wewe chukua nafasi yangu. Lakini ujue Sonia, unapiga teke bahati. Ningekulisha mimi!” Sonia alibaki akiangalia chini huku anakausha mikono yake kwenye gauni lake.
“Naomba uondoke G, tafadhali sana.” “Sawa kaka. Kwani nina neno mimi?” G aliondoka nakuwaacha Sam na Sonia mezani. Sam alimwona Sonia alivyokuwa akila. Alijua ni kweli alikuwa na njaa sana.
**********************
Wakiwa njiani Sam akimrudisha Sonia nyumbani kwa gari ya G, alimuhusia sana Sonia kutulia katika jiji la Dar. “Vishawishi ni vingi sana kwenye lile jiji Sonia. Wapo watu na pesa zao wanatafuta mabinti wadogo na warembo kama wewe, ili tu kuwarubuni. Naomba uwe mwangalifu, utulie.” Kama aliyetoneshwa kidonda, Sonia alibadilika sura kabisa. Aliinama na kunyamaza kimya bila kujibu kitu na Sam alijua akaamua kunyamaza.
Sonia aligeuzia uso wake dirishani na kupotelea mawazoni. “Baba wa mtoto wako yuko wapi?” Sam aliuliza swali ambalo Sonia hakuwahi kuulizwa na mtu yeyote. Aliinama kwa muda mrefu sana bila yakujibu kitu, mpaka Sam alipomwambia wamefika.
“Tutaenda wote Dar?” Sonia akamuuliza Sam. Sam alibaki akimtazama, alimuona jinsi alivyobadilika na macho yake yalishakuwa mekundu, kuashiria anataka kulia.
“Safari hii, nitakaa hapa kwa muda kidogo. Nipo kikazi na kibiashara pia. Wewe utangulie tu. Nitakuja kukuona nitakapo fika Dar.” “Sijawahi kufika Dar. Naogopa nitapotea.” “Nitaongea nao, waje kukupokea kituo cha mabasi. Usiogope, kwa kuwa wewe una simu, hutapata shida. Utulie tu ndani ya basi mpaka atakayekuja kukupokea aingie ndani ya basi kukuchukua.” “Asante sana kaka.” Akashuka garini.
“Sonia?” Sam akamuwahi kabla hajafunga mlango. “Abee!” Na yeye Sam akatoka na kuzunguka upande aliokuwepo Sonia. “Nimekuudhi?” Sonia akajibu kinyonge. “Hapana kaka.” Taratibu Sam aliona machozi mashavuni mwa Sonia. Alijua kuna kitu kinachomuumiza sana.
Alibaki akimwangalia kwa muda, huku Sonia akiendelea kuchora chini kwa kutumia mguu wake ulikuwa na kandambili nyekundu iliyochakaa sana.
“Pole sana Sonia.” “Asante.” Sam alijiona ni mgeni sana kwenye maisha ya Sonia, kuanza kumuhoji mambo mengi. Na giza lilishaanza kuingia. “Nitakapopata tiketi, nitakujulisha.” “Sawa.” “Unisalimie mama na mtoto. Naomba leo nisiingie ndani, nitakuja wakati mwingine kuwasalimia.” “Hamna neno.” Waliagana na Sonia akaingia ndani.
**********************
“Shikamoo mama.” Sonia alisalimia mara baada yakuingia ndani kwao. “Marahaba.” Mama Sonia alijibu kwa kifupi tu, nakumgeukia mjukuu wake. “Kaka Sam amenitafutia kazi.” Mama Sonia hakujibu chochote. “Ni kazi za ndani.” Kimya kiliendelea. “Lakini hiyo kazi ipo Dar.” Sonia hakupewa jibu lolote. “Naomba ubaki na Kana, mpaka nitakapoweka mambo sawa, nitakuja kuwachukua.” Sonia akaanza kulia.
“Nakupenda mama yangu.” Sonia aliweza kuona machozi ya mama yake kupitia mwanga mdogo wa chemli iliyokuwa anakaribia kuzima. Alimuona mama yake akiharakisha kumvua nguo Kana ili amuogeshe na arudi kumvalisha kabla ya chemli kuzimika.
Naye aliamua kuanza kukusanya vitu vyake. Alivuta begi lake alilokuwa amenunuliwa na mama yake alipofaulu kwenda kidato cha kwanza. Alimnunulia vitu vingi sana alipofauli, lakini aliishia kuuza kimoja baada ya kingine kadiri dhikizilivyowaandama mara baada yakujifungua, nakubakisha nguo chache sana na hilo begi alilokuwa analipenda sana. Alilitunza kama kumbukumbu yake.
**********************
Kesho yake Sam alimpigia tena simu kumtaarifu amepata ticketi ya kuondoka kesho yake na basi la Isamilo, linaloondoka mjini Mwanza saa 12 asubuhi ya siku inayofuata, kwa hiyo ajiandae atakuja kumfuata. Sonia alifurahi sana kuondoka katika jiji la Mwanza. Aliapa kutokurudi tena kuishi Mwanza.
Usiku wakati wanalala, alijaribu kumuaga mama yake tena. “Kaka Sam amepata ticketi ya kesho asubuhi sana. Atakuja kunifuata kunipeleka kituo cha mabasi. Nataka kukuaga kabisa sasa hivi, naweza kuondoka ukiwa bado mmelala.” “Safari njema.” Sonia alifurahi sana kujibiwa na mama yake. Alilala usingizi mzuri sana, baada yakupata baraka za mama yake.
**********************
Sam alimpigia simu saa 11:00 asubuhi na kumtaka atoke nje. Kwa kuwa Sonia alikuwa ameshajiandaa, alitoka na begi lake kabisa, tayari kwa safari. “Nyuma ya gari, kuna mizigo ya mama. Naomba tuingize kabla hatujaondoka. Nitakusaidia mpaka mlangoni kwenu, sitaki kuingia nisije kuwaamsha.” Sonia alitoa macho asiamini baada yakuona vyakula alivyonunua Sam.
Walisaidiana mpaka mlangoni kwao, ilimbidi Sonia amuamshe mama yake wasaidiane kuingiza ndani ile mizigo. Aliwaletea safleti ya mchele, galoni kubwa ya mafuta ya kupikia, sukari, unga wa ugali, maharage na aliacha bahasha juu ya ile mizigo bila kumwambia chochote Sonia. Kwani alijua akimwambia kuna bahasha yenye pesa, angekataa.
Mama Sonia alibaki ametoa macho. Usingizi wote uliisha. Alitoka nakupiga magoti kwa Sam. “Asante sana. Asante. Mungu akubariki.” “Usipige magoti mama, tafadhali.” Sonia alishindwa aseme nini, machozi yaliendelea kumtoka. “Tutawasiliana mama, ngoja nimuwahishe Sonia, asije akaachwa na basi.” “Kwa heri mama.” Sonia alimuaga mama yake tena, huku akilia sana. Alisogea na kumkumbatia. “Safari njema.” Mama yake alijibu.
**********************
Sam alihakikisha Sonia amekaa kwenye kiti chake, akampa pesa ya kula njiani na kumuongezea salio kwenye simu ili waweze kuwasiliana akiwa safarini, ndipo akaondoka. Sonia bado alikuwa kwenye hali ya kutokuamini.
Ni kama kwa mara ya kwanza tangia afukuzwe shule, ndio mambo angalau yameanza kufunguka. Aliendelea kutokwa na machozi ya furaha kadiri walivyokuwa wakiliacha jiji la Mwanza.
Mbali ya kwenda Shinyanga nyumbani kwa rafiki yake kipenzi Fau waliyekuwa wakisoma naye Ngaza, hakuwahi kwenda mkoa mwingine wowote.
Alisikia sifa za jiji la Dar, na alitamani sana kwenda kuishi huko lakini haikuwahi kutokea.
Alizaliwa hapohapo Mwanza, alisomea shule za kutwa, na alipofaulu alipangiwa shule ya bweni ya wasichana, Ngaza, hapo hapo jijini Mwanza. Japokuwa mama yake hakuwa na uwezo, lakini alihakikisha Sonia anapata kila anachohitaji ili asiingizwe kwenye vishawishi.
**********************
Baada ya kutulia, aliamua kumtumia ujumbe Sam. 'Kaka Sam, ninashukuru sana kwa kila kitu. Umetutoa katika shida nzito sana. Hatukuwa hata na chakula, chakula pale nyumbani. Angalau naondoka nikiwa sina wasiwasi kabisa wa chakula cha mama na mtoto wangu. Asante. Pia nashukuru kwa ushauri. Naahidi kutulia kaka, na nitafanya kazi yangu vizuri.' Baada ya muda kidogo Sam akajibu ‘Karibu. Nitakuona baada ya siku chache.’ ‘Asante kaka. Kazi njema.’ ‘Asante. Safari njema.’ Baada ya majibizano hayo mafupi, akalala.
Alifurahia sana safari yake. Akiwa njiani alijiwekea mikakati mbalimbali ya maisha. Tumaini la kuja kutimiza ndoto zake zote zilizokuwa zimezimika gafla lilianza kurejea upya moyoni.
Sonia Apokelewa Kwa Namna Yake Jijini Dar
Kama alivyokuwa ameambiwa na Sam, asishuke kwenye basi mpaka anayekuja kumpokea atakapoingia kwenye basi hilo na kumpigia simu ndipo aendoke naye, ndivyo kweli Sonia alivyofanya. Alipofika kituo cha mabasi, jijini Dar hakushuka mpaka alipoingia mwanaume, aliyeonekana kuwa mkubwa kidogo kwa umri, ukimlinganisha na Sam. Akalijitambulisha kwa jina moja tu, Nyange.
Alimchukua Sonia mpaka kwenye gari yake. Ndani ya gari hilo alikutana na msichana aliyekuwa akiwasuburia, akiwa amekaa kwenye kiti cha mbele. “Shikamoo.” Sonia akasalimia. “Habari za safari?” Huyo mrembo akamgeukia na kutupia hilo swali bila ya kujibu salamu yake. Sonia akajibu kwa heshima, “Nzuri.” “Karibu kwenye jiji la maraha.”
Akashangaa anamwambia yeye lakini akimgeukia Nyange nakuanza kucheka. Waliendelea uongea mambo yao bila kumjali Sonia kabisa.
**********************
Maswali yalianza kupita kichwani kwa Sonia. ‘Niliambiwa anatakayekuja kunichukua ni baba mwenye nyumba, na mkewe ni mjamzito. Mbona huyu sio mjamzito na wanaonekana ni kama wapenzi?!’ Maswali yaliendelea kupita kichwani kwa Sonia taratibu bila ya kupata jibu.
**********************
“Sasa! Siutaingia kidogo?” Mrembo akamuuliza Nyange wakati Nyange amesimamisha gari yake mbele ya nyumba, ambayo Sonia hakujua ni kwa nani. Nyange alisita kidogo. “Usianze kiswahili kirefu Nyange, mchana umenikwepa na sasa hivi unataka kunikwepa? Haiwezekani. Shuka japo kidogo.” Nyange alimwambia Sonia asubirie kwenye gari na atarudi baada ya muda mfupi.
Sonia alikaa ndani ya hilo gari mpaka alipoanza kusinzia. Baada ya kama saa moja hivi, Nyange alirudi ndani ya gari. Bila kumsemesha kitu aliwasha gari na kuondoka pale mpaka walipofika kwenye nyumba nyingine iliyokuwa imezungushiwa ukuta mkubwa sana. Mlinzi alifungua geti, wakaingia ndani.
Jumba lilikuwa kubwa na kuliegeshwa magari mengine mawili ya kifahari yaliyozidi kumtoa macho Sonia.
“Tumetoka kituo cha mabasi, moja kwa moja hapa nyumbani. Umesikia binti?” Nyange alimgeukia Sonia aliyekuwa akishangaa nje na kumpa onyo lililomchanganyakidogo Sonia. “Umeelewa?” Sonia alibaki ametoa macho. “Umeelewa binti? Hakuna tulikopitia, tumetoka kituo cha mabasi, tukaja hapa. Usianze kueleza habari nyingine zisizo kuhusu.” Sonia alipatwa na wasiwasi sana.
Mlango ulifunguliwa na mwanamke mjamzito alitoka nje. Sonia alijua huyo ndio atakuwa mama mwenye nyumba wake. Alikuwa ni mama aliyeonekana mwenye upendo sana na busara. Hakuwa na haraka ya kuongea. Sonia alihisi labda ni kwa sababu ya hali yake ya ujauzito. Alikuwa mzuri sana wa sura na mbile ambalo lilikuwa limebeba tumbo kubwa sana.
Japokuwa alikuwa nyumbani, lakini alikuwa msafi na amevaa nadhifu. Sonia aliendelea kumwangalia. “Pole na kazi, Baba Briana.” Akapokea mkoba wa Nyange. “Asante. Nimechoka kweli! Foleni ilikuwa kali sana. Tumekaa njiani zaidi ya lisaa. Nataka kula tu nilale.” “Pole, ndio maana mmechelewa! Nilishaanza kuingiwa na wasiwasi.” “Vipi Bree, ameshalala?” “Ameshalala. Karibu dada, nikupokee mzigo.” “Asante. Lakini nitabeba tu mwenyewe, sio mzito.”
**********************
Sonia alikaribishwa kwenye chumba kizuri sana, tena chenye bafu humohumo ndani. Ni kama ndoto zake zimetimia, lakini mambo aliyokutana nayo njiani yalianza kumuogopesha. Onyo alilopewa na baba mwenye nyumba wake lilizidi kumtia wasiwasi. ‘Nitaishije kwa kudanganya?’ Sonia alizidi kuwaza.
**********************
Gafla mlango ukagongwa. “Kama umeshaoga, twende ukale. Usilale bila kula. Najua umechoka na safari, lakini jikaze tu.” Sonia alishangazwa na upendo wa huyo mama. Alitoka na kwenda kula. Kila kitu mle ndani kilimshangaza!
“Naomba ujisikie upo nyumbani na mimi kama dada yako. Ukiwa na tatizo lolote, usiogope kuniambia. Umeelewa?” “Nimeelewa dada. Asante.” “Familia yetu sio kubwa sana. Tuna mtoto wa kike mmoja, anaitwa Briana, lakini wakati mwingine tunamwita Bree. Ameshalala. Yupo kijana wetu mwingine tunaishi naye hapa anaitwa Josh na kama unavyoniona, tunatarajia mtoto mwingine.”
“Kazi yako wewe ni watoto tu. Kazi nyingine zote Josh ndiye anayefanya, utamuona kesho. Huwa anawahi sana kulala. Na mara nyingi napenda kupika mwenyewe. Mambo mengine mengi tutaelekezana taratibu tu, usiwe na wasiwasi.” “Asante dada.” Sonia alifurahi sana kukutana na mama mwenye nyumba wa namna hiyo. Alionekana ni mtaratibu sana.
“Natakiwa kuamka saa ngapi?” Sonia aliuliza wakati wakuagana. “Kesho pumzika mpaka uchovu wa safari uishe, na kwa kuwa mwenyewe nitakuwepo, usiwe na wasiwasi.” Waliagana na Sonia alirudi chumbani kwake.
**********************
Kabla ya kulala akaona amtaarifu Sam. ‘Kaka, nimefika salama. Nashukuru sana.’ Sam akampigia. “Umeona safari ilivyokuwa ndefu?” “Sio sana, nimefurahi nimeona sehemu nyingi wakati tukiwa njiani.” “Basi pumzika, tutaongea wakati mwingine.” “Kaka Sam?” Sonia aliita kabla yakukata simu.
“Nipo.” “Naomba nikushukuru kwa msaada wa vyakula ulivyopeleka nyumbani kwetu. Asante sana.” Sam alicheka. “Ulishashukuru Sonia! Inatosha. Usiku mwema.” “Asante na wewe.” Alifurahia sana chakula alichokipeleka Sam nyumbani kwao. ‘Angalau watapata chakula, cha kula siku chache kabla sijalipwa mshahara wangu, ili niwatumie na wao pesa kidogo.’ Sonia aliwaza huku akiitazama simu yake baada ya kumaliza kuongea na Sam.
Akaamua kumpigia simu na mama yake ili kumjulisha kuwa alifika samala. “Shikamoo mama. Nimefika salama.” “Pole na safari.” “Asante.” Kimya kiliendelea kama kawaida yao, walishapoteza mtiririko mzima wa maongezi yao ya urafiki. “Muwe na usiku mwema, mama.” “Asante na wewe.”
Sonia alitamani, hata mama yake angemchapa baada ya kurudishwa nyumbani kwa ujauzito aliokuwa amepata, ili yaishe warudi kuwa marafiki, lakini mama yake hakunyanyua mdomo hata kumuuliza ilikuwaje.
Alibaki akiwaza mambo mengi juu ya maisha yake bila ya kupata majibu yaliyo wazi. Alitamani kumtoa mama yake na mwanae kwenye shida inayowakabili ya kiuchumi, lakini hakuwa na jinsi. Kila alichojaribu kufanya kujiongezea kipato, alikwama. ‘Labda hii kazi ndio itafungua milango mingine! Nitajitahidi kadiri ya uwezo wangu, nione mwisho wake.’ Sonia alizidi kuwaza.
**********************
Haikuwa mara ya kwanza maishani mwa Sonia kulala katika mazingira mazuri hivyo. Nyumba yenye AC, iliyokuwa inapuliza wakati wote, choo na bafu la kifahari, sakafu ya marumaru ya hali ya juu. ‘Hapa hata wakinipa kazi ya kudeki kila siku, sitaona shida.’ Sonia aliwaza huku akitabasamu.
Alipafananisha pale na yumbani kwa rafiki yake Fau aliyekuwa akiishi na wazazi wake mkoani Shinyanga. Sonia alikuwa akienda likizo nyumbani kwa kina Fau. Kwa hiyo hakuwa akishangaa sana pale kwa Nyange, japokuwa pale kwenye jumba la Nyange lilikuwa kubwa sana, na kulijazwa vitu vya kifahari zaidi na vitu vingi walitumia mashine. Sonia alilala kwa furaha akijua hata mtoto wake atakuwa amekula na kushiba.
**********************
Alishtushwa na mtu aliyekuwa akimgusa taratibu. Sonia aliruka kitandani na kukaa. “Shikamoo.” Kitoto kidogo, kizuri sana cha kike kilikuwa kimesimama mbele yake. “Marahabaa mtoto mzuri. Unaitwa nani?” “Briana.” “Unajina zuri sana kama wewe mwenyewe.” Briana alianza kucheka huku akishikashika nywele zake.
“Nywele zako nzuri!” Sonia alimsifia. “Kasukwa jana tu huyo, ndio maana amekuamsha akuonyeshe. Anapenda urembo kweli mwanangu!” Sonia alishtukia Mama Bree alishaingia na yeye na kuingilia mazungumzo yao.
“Shikamoo dada.” “Marahaba. Pole na uchovu.” “Nimeshapoa. Nimelala vizuri kweli!” Sonia aliongea huku akitabasamu nakujaribu kumbeba Bree. “Na anavyopenda kupendwa huyo! Hapo mtapatana.” Wote walicheka. “Uje kunywa chai.” Mama Bree alitoka na kumuacha Sonia akishangazwa na ukarimu wa Mama huyo. ‘Au mgeni siku ya kwanza?’ Sonia akajiuliza.
**********************
Baada ya kama siku tatu, Mama Briana alimwambia Sonia yeye ni mtu wa kusafiri safiri sana, sababu ya kazi yake ya ukaguzi wa mahesabu serikalini. Na ndio sababu anatafuta dada mzuri wakukaa na Briana. “Wasichana wengi wanaokuja hapa sio watulivu. Wanakuwa wahuni sana sababu mimi nakuwa sipo na Baba Briana hashindi nyumbani kama unavyoona. Akitoka asubuhi mpaka usiku.”
“Wanakuwa hawana muda na Briana kabisa. Wanamuona mzigo mwanangu. Wanamchapa kweli na hawamkumbuki chakula hata kidogo. Nakuomba mdogo wangu utulie, kama anatatizo lolote usimchape, naomba uniambie tu mwenyewe.” Sonia akamgeukia Briana.
“Mbona Bree mwenyewe anaonekana hana neno!? Mtaratibu kama wewe dada.” Mama Briana akacheka. “Ndio kinachoniumiza mdogo wangu. Briana wangu mpole kweli! Lakini nikiondoka tu, wanaanza kumtesa.” “Eti Briana!” Sonia akambeba.
Mshahara aliotajiwa kulipwa, ulimtoa macho Sonia. “Kweli dada?” Sonia aliropoka nakumfanya Mama Briana aanze kucheka tena. “Unauona mkubwa?” Sonia akatabasamu. “Asante sana dada yangu.” “Usijali kabisa. Ukiwa na tatizo lolote lile nibip tu nitakupigia. Kama ulivyomuona Josh, nikijana mzuri sana, atakusaidia kila kitu.”
“Baba Briana anakuwepo nyumbani siku za jumapili, na wakati mwingine siku za jumamosi anakwenda kazini lakini huwa anawahi kutoka, kwa hiyo ukiwa na shida yeyote ile hata yeye umwambie tu. Pia nina mdogo wangu huwa anakuja kukaa hapa kama nikiwa safirini, anaitwa Leah, atakusaidia utakapokwama. Usiwe na wasiwasi hata kidogo.” “Sawa dada.”
**********************
Josh nikijana aliyekuwa akiishi hapo kama mfanyakazi, alikuwa akilala nyumba ndogo ya nje ambayo na yenyewe ilikuwa nzuri sana na ina kila kitu ndani. Mchapakazi sana na mcheshi. Hakuna kazi angeiona Josh, aache kuifanya, hata kama hakuambiwa afanye. Nyange alimpenda sana Josh. Kila mtu hapo kwenye hiyo nyumba alionekana mkarimu sana.
**********************
“Nani anapika sasa, ukiwa haupo?” Sonia aliendelea kumuuliza Mama Briana jioni hiyo wakiwa jikoni. “Baba Bree mchaguzi kweli wa vyakula, ana watu na watu anaokula chakula chao. Nilikwambia kuhusu mdogo wangu Leah, huwa anakuja nikisafiri. Nimpishi mzuri sana, Baba Bree huwa anapenda chakula chake pia. Kwa hiyo atakusaidia kukuelekeza na Josh pia anajaribu jaribu kupika.” Sonia alitulia kidogo kama anayetafakari kitu.
“Usiwe na wasiwasi, mume wangu sio msumbufu kabisa. Hata ukipika kama hajapenda huwezi sikia akilalamika, ila hatakula.” Mama Bree aliongea kwa kutabasamu, kumfanya Sonia asiogope.
“Naona ujauzito ukifikisha miezi nane, labda nitaacha kusafiri safari za mbali nitakuwa nazunguka humuhumu mjini kwa hiyo tutakuwa wote muda mwingi.” “Hamna shida dada, usiwe na wasiwasi. Siwezi kumtesa mtoto. Nitajitahidi kadiri ya uwezo wangu. Kukiwa na tatizo nitakwambia.” “Asante Sonia.”
**********************
Ukweli Mama Briana, alijaliwa upendo usio wa unafiki. Alipewa uzuri wa kila kitu. Sonia alikuwa akijiiba kila wakati kumwangalia. Japokuwa alikuwa mjamzito lakini alikuwa msafi wakati wote na alijua kuvalisha mwili wake.
Briana naye hakuwa na tofauti na mama yake hata kidogo. Alikuwa mtoto mtulivu sana. Mcheshi, mtiifu na mwenye upendo. Lakini afya ya Briana ilikuwa ikitisha sana. Alikuwa na nguo nyingi sana na zote zilionekana ni nzuri na gharama, lakini zote hazikumpendeza. Alikuwa kama kijiti. Hata ngozi yake haikuwa nzuri. Alionyesha kabisa hana uangalizi mzuri.
**********************
“Lakini dada, kabla hujaondoka naomba ninunulie mafuta ya mtoto. Naona kama haya anayotumia sio mazuri kwa ngozi yake. Labda ndio maana ngozi yake ipo hivyo.” Mama Briana alifurahi sana. “Na kitu gani kingine?” “Sijui itakuwa garama?” “Niambie tu mdogo wangu. Kwa Briana! Hakuna ugarama wowote.”
“Unajua na mimi nina mtoto?” “Hongera. Ndio maana una upendo na watoto!” Sonia akatabasamu. “Kabla mambo yetu ya kifedha hayajakuwa mabaya sana, nilimuona mama kuna vyakula alikuwa akimtengenezea mtoto wangu kwa kuwa nilishindwa kunyonyesha. Alikuwa na afya nzuri sana.”
Akamtajia vitu vyote ambavyo angehitaji vya mtoto, kuanzia uji mpaka chakula cha usiku. “Asante sana Sonia. Naenda kuvinunua hii leo, ili tumuanzishie, labda mwanangu atabadilika.” “Usijali dada. Atabadilika Briana huyu, mpaka utashangaa.” Ikawa amegusa moyo wa mama Bree vilivyo.
**********************
Sonia akamwanzishia Briana uji wa Lishe kila anapoamka asubuhi na saa kumi jioni. Kwa kuwa kazi nyingi za pale nyumbani alikuwa akifanya Josh na Mama Briana, Sonia alibakia na Briana tu. Aliacha kumlisha vyakula vya watu wazima, wakati wote alimpikia Briana chakula chake pembeni na kumlisha. Alimfanya kuwa msafi wakati wote na alimwanzishia kulala mchana.
Kwa muda mfupi sana afya ya Briana ilianza kubadilika. Akili na mawazo ya Sonia yote yalikuwa kwa Briana. Na yeye akaanza kumzoea Sonia kuliko hata mama yake. Mama Briana alifurahi sana, alijua hata akiondoka, atamuacha Briana kwenye mikono mizuri.
Ili kumfurahisha Sonia, Mama Briana alijitahidi sana kumnunulia Sonia nguo nzuri ili angalau na yeye afananie na nyumba yake. Ukaribu kati ya Sonia na Mama Briana ulikuwa mkubwa sana. Kwa muda mfupi walioishi pamoja, walishajenga upendo mkubwa sana kati yao.
**********************
Muda wa kusafiri kikazi wa Mama Briana ukafika, ikambidi aondoke. Lakini safari hii aliondoka akiwa na furaha kwa kuwa alimuacha Briana kwenye mikono ya Sonia, kwa hiyo alijua hakuna litakaloharibika.
Wakati anaondoka alisema Leah atakuja hapo nyumbani. Lakini kwa kuwa na yeye nimfanyakazi huwa anaondoka asubuhi kama Baba Briana nakurudi nyumbani jioni.
**********************
“Sasa kwa nini wasichana wa kazi wa hii nyumba, hawakai humu ndani!? Wakati panaonekana pazuri sana!” Sonia alianza kumdodosa Josh baada ya Mama Briana kuondoka. “Kuna mambo hapa! Wewe subiri uone.” “Mbona unanitisha sasa?” “Nakwambia ujiandae.”
“Ni nini? Mbona mama mwenyewe anaonekana hana shida, na Baba Briana hashindi humu ndani! Shida iko wapi?” “Huyo uliyeambiwa anakuja kukaa na sisi wakati mama amesafiri, ndio jasho litakutoka. Dada ana roho mbaya huyo! Uombe akupende. Lakini tangia niishi hapa, sijawahi kumuona anampenda msichana yeyote wa kazi.”
“Kila msichana anayeletwa hapa, anamchongea kwa Mama Briana, aondolewe. Na mambo mengine utajionea mwenyewe. Siwezi kukwambia. Huwa najinyamazia kimyaaa ili niingize pesa yangu.” Sonia akabaki haelewi.
“Kwani huyo Leah hajaolewa?” “Ana mwanaume wake. Sijawahi ona mwanadamu kama huyo kaka. Mstaarabu sana na mkarimu, hujawahi ona. Amejaliwa uzuri wa moyo, sura halafu ni mtu wa mazoezi sana, amejenga mwili vizuri, mpaka huwa najiuliza kwa nini huyu Leah hatulii na huyo kaka!” Josh aliendelea kumwaga sifa za mwanaume wa Leah.
“Hawajaoana?” “Huyo Leah, ni shuguli! Utamuona tu. Fujo kutwa nzima. Anaongea kama ana mashine ya mdomo. Anampelekesha huyo kaka utamuonea huruma. Hana adabu hata kidogo. Lakini Leah mwenyewe mzuri kweli kama Mama Bree. Halafu anasema ana kazi nzuri sana. Labda ndio maana jamaa katulia.” “Ngoja tumsubirie tuone.” “Kama hatakuja leo, basi kesho. Wala hutauliza kama ni ndio yeye, ukimuona tu, utamjua kama ndio Leah.” Sonia akacheka.
**********************
Siku hiyo ya kwanza baada ya Mama Briana kuondoka kulikuwa na amani sana. Sonia alishinda na Briana vizuri, hakumsumbua hata kidogo. Siku inayofuata jioni Sonia aliamua kuongea na Mama Briana. Akampigia simu. “Dada?” “Vipi Sonia! Kwema?” “Kwema kabisa. Nimeona jioni imeingia hakujapikwa chakula. Sasa Baba Bree akija akikuta hakuna chakula, itakuaje? Naomba nijaribu kupika.” Mama Briana alianza kucheka. “Asante Sonia. Wewe pika tu wala usiwe na wasiwasi.” Walizungumza kidogo, wakaagana.
Paka Ametoka, Panya Kutoa Makucha
Sonia akiwa na Briana, waliingia jikoni na kuanza kujiandaa kwa mapishi. Akampa vitunguu swaumu Briana amenye, kama kuchezea tu wakati yeye akiendelea kupika. Kama kawaida yao, Sonia anapokuwa jikoni akipika huwa anakuwa na Briana. Na wakati wote Briana alikuwa akipenda kumwimbia Sonia nyimbo mbalimbali, kwa kuwa Sonia alikuwa akicheka na kumsifia sana kuwa anasauti nzuri. Kwa hiyo hata jioni hiyo alikuwa akiimba, huku wanacheka na Sonia.
Gafla akasikia mlango unafunguliwa kwa nguvu. “Wewe? Umechanganyikiwa nini? Unawezaje kumwacha mtoto anacheza na kisu?” Sonia akageuka. Alijua huyo ndio atakuwa Leah. Lakini sura ilifanana kabisa na msichana aliyekuja na Nyange kumpokea kituo cha mabasi cha Ubungo.
“Ndio maana nilimpa kisu cha mkate, ili acheze kujipikilisha.” Sonia akamjibu kwa upole. “Kwani hujaona michezo yake? Ana michezo kibao huyo mtoto yakuchezea. Mpaka yakujipikilisha anayo. Akiumia?” “Samahani dada.” Sonia aliomba msamaha kwa unyenyekevu na kumfanya Leah aliyeingia kwa jazba, atulie. “Unapika nini?” Sonia akamtajia. Leah akakunja uso kidogo, nakutoka.
Alipomaliza tu kupika na baba Briana naye akaingia kutoka kazini, moja kwa moja akaelekea jikoni. “Mbona kunanukia hivyo? Unapika nini?” Nyange akauliza. “Daddy!” Briana aliyekuwa amekataliwa kuendelea kumenya vitunguu na auntie yake, nakubaki kimya baada ya auntie kugomba sana, alifurahi sana kumuona baba yake. Baba yake akambeba. “Shikamoo daddy!” “Marahaba, kipenzi changu.” Walitoka na Briana kwenda kukaa sebleni.
Sonia akandaa chakula na kumkaribisha baba Briana mezani. Walikaa mezani na Briana, akaanza kula. “Mmmh! Unaonekana mpishi mzuri sana Sonia.” “Asante.” “Naona na Briana wangu anazidi kuwa mrembo kama mama yake! Unaonekana umemuwezeakweli! Mwanangu amebadilika sana. Alikuwa anatia aibu hata kutoka naye kwenda kwa marafiki. Lakini sasa hivi, aaah! Unazurula naye bila aibu. Asante sana.” Wakati Nyange anamwaga sifa za Sonia, Leah akatokea akiwa amekunja uso.
“Sikujua kama upo Leah!” Baba Briana akajaribu kumuongelesha Leah baada yakumuona amesimama huku amekunja uso. “Kwani umenitafuta wapi, ukanikosa?” “Leo nilikuwa nimebanwa kweli! Vikao tokea asubuhi hata chakula sijala! Ndio maana nimeshindwa kukupigia.” Akavuta kiti nakukaa pembeni ya Nyange.
Alikitizama chakula kwa muda mrefu bila kupakuwa. “Kitamu kweli! Pakuwa ukijaribishe na wewe.” Baba Briana akajaribu kumtupia tena neno huyo Leah. “Mbona hakionekani kama kizuri!” Leah akaongea kwa dharau. “Wakati mwingine macho yanadanganya.” Nyange akajibu. Sonia akaamua kuondoka na Briana, kwenda kumlishia jikoni.
**********************
“Naona umeanza kusifia chakula chake!” Sonia aliweza kumsikia Leah akiongea kwa sauti ya wivu na baba Briana. “Acha wivu Leah! Ni kweli chakula kitamu. Si ujaribu kuonja, uone.” “Naona sifa zake haziishi! Tokea nipo chumbani nakusikia ukimsifia.” Nyange akaanza kucheka. Sonia alishituka kidogo.
Alipomaliza kumlisha Briana akaamua kwenda kumuogesha kabisa kabla ya kulala. Briana alikuwa na kitanda kidogo chumbani kwa wazazi wake. Aliambiwa huwa anashitukashituka sana usiku ndio maana alihamishiwa chumbani kwa wazazi wake.
Alishituka sana alipotoka kumlaza mtoto nakukuta Leah akimpapasa baba Briana sebuleni. “Acha bwana Leah!” “Unaogopa nini sasa?” Baba Briana akahama kochi.
Taratibu Sonia akarudi jikoni ili ale chakula na yeye. “Ushaanza kuona sinema ya bure nini? Naona jicho lilivyokutoka!” Josh alianza kucheka baada ya kuona Sonia ameingia akitetemeka. “Na bado, sinilikwambia jasho litakutoka. Huo ndio mwanzo, utaona mengi kweli.” “Mungu wangu!” Sonia akanong’ona.
“Huyu baba anachotaka nini? Wakati ana mke mzuri vile! Huyo Leah ulisema mzuri kama dada yake, lakini wala hajafika hata nusu ya Mama Bree.” Josh akazidi kucheka.
“Sasa yeye si anahangaikia pesa? Mwenzie anamtunzia mumewe. Na hana chochote anachokifanya humu ndani zaidi ya kumuhudumia shemeji yake. Hata mtoto hamjali.” “Kwani huyo mwanaume wake Leah yuko wapi, wakati Leah anafanya huu uchafu?”
“Utamuona mwanaume mwenyewe. Nakwambia mzuri kwelikweli hata Nyange mwenyewe haingii kwake. Nilisikia anafanya kazi na ameanza biashara anaonekana muda mwingi hayupo nyumbani. Anasafiri sana. Lakini hata hivyo Leah mwenyewe kamuweza huyo kaka, haongei chochote. Leah ndio anaamua kila kitu, hamuheshimu wala hamjali huyo kaka hata kidogo.”
“Sasa dada yake hajui?!” “Si umemuona Mama Bree mwenyewe alivyo? Huwa hana neno na mtu yeyote. Ongea yake mwenyewe ya shida. Mpaka umchokoze chokoze ndio utamsikia akicheka tu.” Josh na Sonia waliendelea kunong’ona.
Mara mlango ukafunguliwa. “Kama hukuambiwa, ndio nataka nikufahamishe, chakula huwa napika mimi. Acha kimbelembele. Umesikia wewe?” Sonia alitabasamu. “Unaleta dharau kwa kuwa umeanza kusifiwa?” Sonia hakujibu kitu. Akageuka na kuelekea kwenye sinki kuosha vyombo.
“Jamani usiku mwema. Nakwenda kulala.” Josh alipoona Sonia amefanya jeuri mbele ya Leah, hakutaka shida, akaamua kuaga, Leah naye akaondoka. Sonia lishamchukia sana Leah. Aliona hamtendei haki dada yake, alimalizia kuosha vyombo nakuingia chumbani kwake huku akiumia sana roho.
**********************
Mara ujumbe ukaingia kwenye simu yake. ‘Mama Briana anakusifia kweli! Usibadilike. Jitahidi hivyohivyo. Ni dada mzuri sana, ukitulia atakusaidia sana.’ Ulikuwa ujumbe kutoka kwa Sam. ‘Nitajitahidi kaka.’ Sonia alijibu kwa kifupi, Sam akapiga.
“Vipi lakini unapaonaje?” “Nimepafurahia. Huyu mama ni mtu mzuri sana.” “Hana shida kabisa Mama Bree. Utazidi kumfurahia.” “Ni kweli. Uwe na usiku mwema kaka.” “Asante na wewe.” Sonia akajibu wakakata simu, nakubaki akiwaza. Mawazo yakamrudisha kwa Leah. ‘Anawezaje kumfanyia hivyo dada yake?’ Sonia akazidi kuwaza mpaka alipopitiwa na usingizi.
**********************
Alishituliwa katikati ya usiku na sauti ya Briana akilia sana, chumbani kwa wazazi wake. Akajaribu kusubiri akijua baba yake atamtuliza lakini bado akamsikia akizidi kulia. akajua pengine baba yake amepitiwa na usingizi mzito. Akaamua kutoka na kwenda chumbani kwao ili agonge.
Akaendelea kugonga kwa muda bila yakujibiwa, ndipo alipoamua kuingia kwa kuwa Briana bado alizidi kulia. Akashangaa kukuta kitanda cha baba Briana kitupu, mwenyewe hakuwepo kitandani kwake wala bafuni na Briana alikuwa amesimama kwenye kitanda chake akiangalia kitanda cha wazazi wake huku analia.
Sonia akambeba. Kwa kuwa aliogopa kukaa mle ndani, akaamua kutoka na mtoto aende naye chumbani kwake, ndipo alipomuona baba Briana akitokea chumbani kwa Leah, huku akifunga shati lake vizuri. Wote walisimama kwa muda wakiangaliana bila yakusemeshana kitu.
Mwishoe Sonia akaamua kushuka ngazi kwenda chumbani kwake na mtoto, baba Briana akaingia chumbani kwao. Sonia alianza kulia na yeye kwa uchungu sana mara baada ya kumlaza mtoto. ‘Sidhani kama nitapaweza hapa.’ Sonia alizidi kulia mpaka alipopitiwa na usingizi.
Asubuhi baba Briana alishuka kunywa chai, mara baada ya muda akamsikia Leah naye anatoka chumbani kwake anamfuata baba Briana mezani. “Ulilala salama?” Akamsikia Leah anauliza. “Ndiyo.” Nyange akajibu kwa kifupi tu. Sonia alikuwa jikoni akiwasikiliza.
Chumba cha Leah, na wazazi wa Briana vyote vilikuwa juu, lakini Sonia alikaribishwa chumba cha chini. Hakikuwa mbali na jikoni. Lilikuwa jumba kubwa sana, na la kifahari. Nyange na mkewe walionekana ni watu wenye pesa sana.
“Utawahi kutoka leo?” Leah akaendelea kudodosa taratibu, baada yakumuona Nyange hamtilii maanani. “Sijui, inategemea na kazi zitakuwaje. Kwani vipi?” “Nataka tuwahi ili tupate muda mzuri wa pamoja.” Hakumsikia Nyange akijibu. Sonia akaona anajiumiza moyo, kwa kuendelea kukaa pale jikoni kuwasikiliza Nyange na Leah. Akaamua kutoka arudi chumbani kwake.
“Nikupitie baadaye kazini?” Nyange akabaki ameinamia kikombe chake cha chai. “Eti Nyange?” Leah akajisogeza mpaka kwenye kiti cha nyange nakumzungushia mkono mabegani kama kumkumbatia. Sonia alikuwa akitoka jikoni kwa kunyata ili wasimuone akipita.
Akakuta Leah akimbusu Shemeji yake shavuni, alitaka kuinama lakini Nyange alishamuona. Walibaki wameangaliana na Nyange. Sonia alishindwa kujizuia aliinama nakuanza kulia akiwa amebaki kama sanamu palepale mbele yao, mwishowe akaamua kurudi jikoni. Nyange naye akasimama na kutoka. “Baadaye basi.” Leah akamuaga Shemeji yake wakati anatoka mlangoni.
Sonia Amtolea Uvivu Leah!
“Ulichokuwa unanyata nini?” Leah akamfuata Sonia jikoni. Sonia alibaki kimya. “Acha umbea wewe msichana! Hayakuhusu, yaache kama ulivyoyakuta. Acha unafiki wakujiliza.” Leah alitoka nakumuacha Sonia akitokwa na machozi.
Fujo za Leah ziliendelea na Sonia aliamua kulala na Briana, hakutaka tena kujua kinachoendelea usiku. Ule uchafu ulikuwa ukimkera sana Sonia. Alimuonea huruma Mama Briana. Alianza kumdharau Leah waziwazi hata wakati mwingine hakuwa akimjibu kabisa hata alipomuongelesha.
“Unaonekana unakiburi sana wewe. Na nitakukomesha.” Leah akamwambia Sonia. “Nimefanya nini?” “Ninakuona tu. Na nina kuahidi nitakukomesha. Utaondoka hapa mchana kweupe.” Sonia alipandwa na hasira sana, nakuanza kutetemeka.
“Nisikilize vizuri Leah. Mimi sio mtu wakutishwa hata siku moja. Usithubutukunitishia maisha yangu. Wewe unaletwa humu ndani na shida zako na mimi naletwa na zangu. Unatimiziwa haja zako na baba Briana acha kelele. Acha kunisumbua kabisa. Leo iwe mwisho kunipigia kelele, wewe sio Mama mwenye hii nyumba na hutakaa uwe. Umenisikia Leah?”
“Kama umezoea kelele sio kwangu. Fanya uchafu wako kimya kimya acha kutunyima raha.” Kwa mara ya kwanza Leah kupata mtu jasiri aliyeweza kummudu. Alibaki amenywea kwa muda. “Utapaona pachungu hapa.” “Utanifanya nini Leah? Huna lolote, kelele tu. Kwanza ondoka huku jikoni, unamfanya mtoto anakosa raha. Kelele kutwa nzima! Huchoki?!”
“Zamu yako yakumpikia baba Briana sio sasa hivi. Naomba utoke huku jikoni.” “Unanifukuza mimi!?” Leah aliuliza kwa mshangao mkubwa sana, kwa hakika hakutegemea.
“Ndiyo. Kama unashida na mimi ongea na mama Briana sio mimi. Sikujui, hunijui. Acha kunipa amri kwa lolote.” Sonia akambeba Briana na kutoka hapo jikoni.
Leah alibaki hapo jikoni kwa muda asiamini kinachomtokea. Hakuwahi kuwezwa na mtu yeyote kwa maneno. Alikuwa na uwezo mkubwa sana wakubishana na hakuwahi kukubali kushindwa hata mara moja. Akianza kuongea nyumbani kwa dada yake, unaweza kusema ni kwake. Jeuri na dharau aliviweka mbele kama mmiliki wa nyumba hiyo.
**********************
Jioni aliporudi, hakumuongelesha chochote Sonia na wala hakwenda jikoni, angalau nyumba ikatulia. Hata Briana alipata muda wakucheza na baba yake. Leah alikaa chumbani muda mwingi akifungasha vitu vyake. Kwa kuwa Sonia alipigwa marufuku na Leah asipike, alipika chakula chake, Josh na pembeni cha Briana kama kawaida yake.
Akaenda kumchukua Briana ili amlishe. “Mbona chakula chenu cha upendeleo jamani? Mimi mbona sikaribishwi chakula?” Nyange akauliza kwa utani huku akitabasamu lakini Sonia alishindwa hata kumwangalia usoni. Akambeba Briana nakutaka kuondoka. “Eti Sonia?” “Leah alisema nisithubutu kukupikia au hata kukutengea juisi.” Sonia akamjibu kwa kifupi huku akimwangalia Briana, nakuondoka naye.
**********************
Wasiwasi ulianza kumpata Nyange. Alijua kama Sonia akimwambia mama Briana mengi yatafichuka. Alikaa pale kwa muda na kuamua kumfuata Leah chumbani kwake.
“Wewe Leah vipi? Umemwambia nini Sonia tena?” “Kwani yeye kakwambia nini?” “Wewe unajua kabisa jinsi mama Briana anavyompenda huyu binti.” “Kwani ni yeye tu anayempenda? Kutwa huishi kumsifia.”
“Ngoja kwanza Leah, acha kunigeuzia mazungumzo. Sitakubali chochote kitokee sasa hivi.” “Unamaanisha nini!?” “Wewe unaona hali ya mama Briana. Haya mambo yakifunguka sasa hivi, itamletea shida sana. Nimekwambia anarudishwa sababu yakuumwa. Pressure ipo juu sana. Huyu msichana akija kumuongezea habari nyingine tena, unafikiri itakuwaje?”
“Lazima uwe mwangalifu Leah. Sitaki chochote kitokee kwa mke wangu au ujauzito wake. Umenielewa Leah?” Sonia aliweza kuwasikia, kwa kuwa Nyange aliongea kwa ukali kidogo. “Leah?” Nyange akarudia kwa ukali zaidi. “Nimeelewa.” Nyange akatoka chumbani kwa Leah.
Usiku huo Nyange hakula. Wakati Sonia ameenda kuchukua nguo za Briana za kuvaa wakati wakulala, alimkuta Nyange chumbani kwake amelala. ‘Masikini mama Briana. Kumbe ana pressure?’ Sonia alibaki akiwaza. ‘Kumbe huyu baba anamjali mkewe! Kwa nini lakini alijiingiza kwa Leah?’ Sonia alizidi kuwaza huku akiumia sana moyoni.
**********************
Nyange aliamka asubuhi na mapema na kuondoka bila hata kuaga au kunywa chai. Leah naye alitoka na mizigo yake kimyakimya bila ya kuaga. “Leo mbona sielewi?” Josh akamuuliza Sonia baada yakuona nyumba iko kimya na kila mtu anaondoka kivyake. “Na wewe usichoelewa ni nini haswa?” “Mbona na wewe leo una hasira hivyo?” Sonia aliondoka na kuingia chumbani kwake na kuanza kulia tena.
**********************
Ilipofika jioni Mama Briana alirudi. Ilikuwa ni furaha kubwa alipoingia mama Briana. Haikuwa kwa Briana pekee, hata Sonia mwenyewe alifurahi sana. Wakati Briana anamkimbilia
mama yake ambembe, Sonia naye akamkimbilia na kumkumbatia huku akitokwa na machozi, kitu kilichomshangaza kidogo mama Briana na kumuogopesha sana Nyange.
Lakini Mama Briana akajua Sonia atakuwa alichoshwa na kelele za Leah. “Pole na safari dada.” Furaha ya Sonia ilimfanya kushindwa hata kusogea mbali naye. Alibaki pale pale pembeni yake. “Asante. Pole na wewe na majukumu niliyo kuachia.” “Asante. Nimefurahi sana kukuona dada yangu. Tulikuwa wapweke.” Mama Briana akaanza kucheka.
“Naona wamenionea huruma sababu ya pressure. Ilipanda kidogo. Wamenipunguzia kazi, wamenipa siku za kupumzika. Wamesema watanipangia kazi za hapahapa Dar, nikisogea sana labda hapo Bagamoyo. Na nikienda Bagamoyo, tutakuwa tukienda wote.” “Mimi na Briana!?” Sonia akauliza kwa furaha sana. “Ndiyo.” Hilo likamfurahisha Sonia na kumgeukia Briana. “Umeona Briana? Tutakuwa tunaenda na mama. Hatuachi tena.” Briana alikuwa akicheka tu.
**********************
Sonia na Mama Briana walizidi kuwa karibu, lakini Nyange alianza kumuogopasana Sonia. Na alibadilika sana. Wakati wote aliwahi kurudi nyumbani, na siku za jumamosi na jumapili alibaki nyumbani hakutoka kabisa. Alijaribu kumkwepa Sonia kwa kadiri ya uwezo wake.
Mwishowe akaamua kumuita Sonia aongee naye. Nyange akiwa anasafisha bustani ya nyumbani kwake, alimtuma Josh akamwite Sonia. Alikaa nao wote wawili nje wakati mama Briana akipika ndani. “Kwanza nataka mjue mama Briana ni mgonjwa. Anasumbuliwa sana na pressure. Lazima wote tumsaidie hali yake iwe nzuri. Maneno mnayojua yatamuumiza na kuhatarisha afya yake na mtoto aliyekuwepo tumboni kwake, msithubutu kumwambia. Sawa?” “Sawa baba.” Josh yeye akaitika kwa haraka, lakini Sonia alibaki ametulia akijaribu kuzuia machozi yake lakini akashindwa. Alibaki akipangusa machozi.
“Umeelewa Sonia? Najua unampenda sana mama Briana, sasa kama unamjali, naomba umwache kabisa. Mimi nimeshajirekebisha kabisa. Hakuna jambo baya tena nitakalofanya. Sawa?” Sonia akatingisha kichwa na kuondoka. Alizunguka kwa upande mwingine wa nyumba akiwa analia sana. Alipotulia ndipo akarudi ndani.
**********************
Briana naye akamng’ang’ania sana Sonia mpaka alihamia kulala chumbani kwake. Taratibu Sonia akaanza kubadilika. Ule wembamba kama fimbo, ulianza kuchukua sura mpya. Alitengeneza umbile zuri sana, na kwa kuwa alijaliwa urefu wa kiasi, hakuchosha kumtazama.
Rangi yake ya maji ya kunde iling’aa vizuri sababu ya kula vizuri, na kupata mapumziko yakutosha sio kuzunguka juani kila siku. Hata mawazo yalipungua kwani aliweza kutuma pesa kwao, kiasi na nyingine alijiwekea akiba. Kwani mama Briana ndiye aliyekuwa akimnunulia nguo na vitu vingine alivyoona Sonia atahitaji, ilimradi tu kumfurahisha Sonia ili aendelee kutulia hapo ndani na kumjali mtoto wake.
**********************
“Wewe Sonia, kutwa na minyoosho kichwani! Lazima uende saluni ukatengeneze nywele.” “Saluni dada? Sitaki kutoka bwana! Kwanza sipajui, nitapotea bure.” Mama Briana akacheka na kuongeza. “Basi nitamwambia msusi wa Briana aje hapa hapa akusuke na wewe." Hilo likamfurahisha Sonia.
“Atanisuka nini sasa?” Sonia na mama Briana waliendelea na mazungumzo yao wakiwa jikoni wanaandaa chakula cha jioni wakati Briana anacheza na baba yake.
“Wewe unataka kusuka nini?” “Rasta kama zako dada.” Mama Briana alizidi kucheka kama kawaida yake. “Utaweza kukaa chini sasa? Mwenzio nimesuka hivi ili nikae nazo muda mrefu.” “Lakini nimezipenda kweli dada.” “Basi nitamwambia awahi, maana zinachukua muda mrefu sana.” “Asante sana dada yangu.”
**********************
Kwa kuwa Briana alikuwa akilala na Sonia na muda mwingi alikuwa akicheza naye, Nyange na mkewe walipata muda mwingi wa pamoja. Alimtoa mkewe sehemu tofauti tofauti za starehe ili kumfurahisha nakumfanya atulie ili pressure ishuke.
Walitoka mara nyingi mida ya jioni na kurudi kipindi Briana ameshalala na wakati mwingine waliondoka ijumaa jioni baada ya Nyange kutoka kazini na kurudi jumapili usiku. Walikuwa na wakati mzuri sana wa pamoja, Nyange akatulia, mapenzi mazito kwa mkewe, utafikiri sio yule aliyekuwa akila mdogo wa mkewe. Kidogo Mama Briana alianza kutulia na afya yake ikaanza kurudi kuwa ya kawaida.
**********************
Sonia hakuacha kuwasiliana na Sam kwa simu. Kila siku usiku wakati analala, hakuacha kumtumia Sam ujumbe mfupi wa kumpa pole ya kazi, na kumtakia usiku mwema. Na Sam naye alijenga tabia ya kusubiria ujumbe wa Sonia kila siku usiku ndipo alale, wakati mwingine alimpigia simu baada ya kupokea ujumbe huo na kuongea naye kidogo, na wakati mwingine alijibu tu ‘Asante’.
Sonia hakujua kama Sam alikuwa akifurahia sana kila apatapo ujumbe kutoka kwake. Baada ya uchovu wa siku nzima na kelele nyingi anaporudi nyumbani, ule ujumbe mfupi tu wa Sonia ulimfanya Sam apate usingizi. Alijiambia yupo mtu mmoja sehemu fulani, anayemjali na kumthamini.
**********************
“Mbona leo kimya?” Sam aliamua kumpigia simu Sonia baada yakuona masaa yanazidi kwenda bila kupokea ujumbe wowote. “Vipi?” “Naumwa kidogo kaka.” “Nini tena?” “Tumbo linaniuma sana. Lakini dada amenipa dawa, ameniambia nipumzike. Nilikuwa natapika sana, ndio maana nimeshindwa kuwasiliana.” “Pole sana. Mbona hukusema sasa?” Sonia alinyamaza.
“Nitakuja kukuona kesho.” “Ulisharudi Dar?” “Muda mrefu tu.” “Sikuwa najua!” “Nilibanwa sana kazini. Angalau sasa hivi nina nafasi.” “Pole kaka na majukumu.” “Asante.” “Ukiwa unaumwa usikae kimya bwana, uwe unaniambia.” “Sikutaka kukutia wasiwasi.” “Hapana. Ningependa kujua. Usikae unaumia peke yako. Sawa Sonia? Naomba uwe unaniambia.” Sonia alijisikia vizuri sana, kupata mtu mwingine anayemjali.
“Nitafanya hivyo kaka.” “Basi wewe pumzika, nitakuja kukuona kesho asubuhi.” “Huendi kazini?” Sonia akaanza kusikia sauti ya mwanamke kwa mbali akigomba. “Samahani Sonia. Nisubiri kidogo. Usikate simu.” Sam akabonyeza ‘mute’ kwenye simu yake ili Sonia asisikie mazungumzo ya upande wa pili.
Baada ya kimya cha muda kidogo, Sam akarudi. “Sonia?” “Nipo kaka.” “Mara nyingine huwa siendi kazini siku za jumamosi. Kwa hiyo kama kesho nitakuwepo tu nyumbani. Nitakuja kukuona.” “Nitafurahi kukuona kaka.” “Umekula lakini?” “Nilikuwa natapika kila nikiweka kitu mdomoni.” “Daah! Pole sana. Unataka nikuletee kitu chochote wakati nakuja kesho?” “Hapana kaka. Nashukuru.” “Basi pumzika, nitakuona kesho.” “Asante.” Sonia alijawa na furaha kujua atamuona Sam kesho yake. Na vile alivyozungumza naye kwa kumjali, akalala kama mtoto mchanga.
**********************
Palipo pambazuka, mama Briana alimtengenezea uji Sonia na kumpelekea chumbani kwake, lakini baada ya muda akautapika tena. “Pole sana Sonia.” “Usiwe na wasiwasi dada. Nitakuwa sawa tu.” “Unauhakika hutaki twende hospitali?” “Hakuna haja. Ni hali inanitokea wakati mwingine ninapoingia kwenye siku zangu. Nitakuwa sawa tu, usiwe na wasiwasi. Briana wangu hajambo?”
“Bado amelala. Usiku kucha alikuwa anakulilia, mpaka baba yake akamgombeza.” “Jamani! Mngemleta tu.” “Niliona upumzike bwana.” “Asante sana dada.” “Basi wewe pumzika.” “Hutaki nikusaidie kitu chochote?” “Niko na Josh jikoni. Hana anachofanya cha maana, ana kazi yakunichekesha tu.” Sonia akacheka. “Basi pumzika.” Sonia akarudi kulala.
**********************
“Sonia! Sonia!” Ni sauti Sam ndio iliyomtoa usingizini. “Kaka Sam!” Akataka kusimama ili kumshika mkono, lakini akamzuia. “Pumzika tu. Nimekuja kukuona.” “Nimefurahi kukuona kaka. Nilijua umenisusa, hutaki kuniona tena.” Sam akatoa tabasamu la kiume.
“Nilitaka uzoee mazingira kwanza ukiwa peke yako. Ningekuwa nakuja mara kwa mara, usingezoea mapema.” Sonia akaona ni kweli. Ikaawa kama Sam haamini kama ni Sonia yuleyule wa Mwanza!
Akabaki akimtizama na tabasamu kubwa usoni huku akijaribu kumtafakari mpaka akamtia aibu Sonia, na kuangalia chini. Kwa muda walioachana tokea Mwanza mpaka hapo, kwa hakika Sonia alibadilika sana. Sonia aliyekuwa amejawa dhikina shida, aliyekuwa akivaa kandambili tofauti tofauti miguuni, tena zilizochakaa, minyoosho kichwani ambayo haijulikani idadi kwa kufumuka au kuchakaa, akiuza chakula sokoni, alisafishwa na kusafishika vizuri sana. Alipendeza na kunawili vizuri.
Uzalendo ukamshinda. “Umependeza sana Sonia. Kama sio wewe! Nywele umetengeneza wapi?” Midomo ikatoa sifa. “Asante kaka. Mama Briana aliniletea msusi humuhumu ndani.” “Ameniambia hutaki hata kutoka nje.” Sonia akacheka na kujibu kwa soni kidogo maana bado Sam alikuwa akimtizama kwa kina.
“Muda mwingi nakuwa na mtoto. Halafu Josh anakuwa ananunua kila kitu. Najikuta sina sababu yakutoka.” “Lakini hivyo ni vizuri. Kama huna sababu yakutoka nje, ni heri tulie tu ndani.” Macho yake yalishindwa kutosheka kumuangalia, akajikuta bado anamtizama na kumfanya Sonia aliyekuwa amekaa aanze kuchezea vidole kwa aibu huku akichezesha miguu yake ilimradi tu kujituliza akijibaraguza kwa hili na lile.
Ukweli Sonia alikuwa akivutia. Mama Briana alimbadilisha sana Sonia, kila kitu mwilini mwake kilikuwa cha kuvutia. Alimnunulia losheni nzuri iliyomfanya anukie yeye na chumba chake. Alionekana nadhifu utafikiri ni mtoto aliyekuwa amezaliwa palepale ndani.
Na kwa kuwa hakuwa akitoka kabisa, zaidi ya kucheza na Briana nje, bustanini tena ndani ya geti, Sonia alinawili kwa haraka sana, kwa kukaa kivulini sio kutangatanga kwenye jua kama alivyokuwa akitaabika jijini Mwanza.
“Kuna kitu kizuri nimekuletea. Unataka kuona?” “Ni nini?” Sam akatoa simu yake na kukaa pembeni ya Sonia. Akaanza kumuonyesha picha za mtoto wake. Sonia alianza kutokwa na machozi asiamini.
Kana, mwanae alikuwa amependeza sana na afya yake pia ilibadilika. Alinyolewa nywele vizuri na alivalishwa nguo ambazo Sonia hakuwa akizifahamu. Aliendelea kuangalia picha alizokuwa amepiga akicheza na George na Sam ziwani.
“Mlikuwa wapi hapo?” “Siku hiyo wanaume tuliamua kwenda kupumzika, peke yetu. Kana ni mtoto mzuri sana, hakusumbua hata kidogo.” Sonia bado alikuwa akitokwa na machozi ya furaha na mshituko. Hakutegemea kuona mtu baki anamjali Kana.
“Hivi jana tu niliongea naye. Tuna salamu yetu wenyewe!” Sonia akaanza kucheka huku akipangusa machozi. “Salamu gani?” “Nikwambie ili uige?” Sonia alizidi kucheka. “G, amesema ataenda kumchukua weekend hii akamfundishe biashara ya samaki.” “Si atamsumbua sana?” “Hapa tunashindana na G. Nani atapendwa na Kana. Lakini naona mwenzangu atanishinda, na hivi wapo karibu! Nikirudi huko Kana atakuwa hanikumbuki tena!”
“Tumekutana mimi na G wote tunapenda sana watoto. Hata nguo yeye ndio anamnunulia. Kila akiona nguo nzuri anamchukulia.” “Asanteni sana. Tena sana kaka Sam.” “Asante tena wakati wenzako tuko kwenye mashindano?” Sonia alizidi kucheka.
“Lakini nikwambie kitu Sonia, Mungu analipa kwa njia nyingi sana. Unapotenda mema na Mungu analipa. Ona unavyomlea Briana vizuri. Mama yake akianza kukuongelea mpaka machozi yanamtoka. Si unakumbuka afya ya Briana uliyomkuta nayo?” “Mimi nilijua mgonjwa!” Sonia alinong’ona, nakumfanya Sam acheke.
“Kweli kaka! Hali yake ilikuwa mbaya kweli!” “Lakini si unamuona sasa hivi? Mpaka kinavutia. Yote hayo ni juhudi ulizoweka kwake. Briana hakuwa na ungalizi mzuri tokea mwanzo. Wazazi wake wote wana kazi nyingi sana na mama yake anasafiri sana. Hawana muda na mtoto kabisa.” “Kamekuwa kazuri kama mama yake.” Wote wakacheka na kuendelea kuongea.
Nafsi Isiyoridhika Na Chochote
Sonia alianza kusikia sauti ya Leah. Mara mlango ukafunguliwa. “Unafanya nini na wewe huku ndani muda wote? Mbona hutoki!?” Leah alianza kumuongelesha Sam bila hata yakumsalimia Sonia. “Sonia, huyu ndiye mchumba wangu. Najua mlishaonana, anaitwa Leah.” Akatoa utambulisho uliomuacha Sonia ametoa macho, kama haamini alichosikia, na kutamani kulia.
Alibaki akimwangalia Leah kwa kuumia sana. “Twende bwana Sam, si ushamuona?” Bado Sam na yeye alikuwa akishangaa jinsi Sonia alivyokuwa ameshituka na kubaki kama bubu.
“We Sam?” Akarudia tena kwa ukali. “Nitarudi jioni Sonia, kuna mahali tunakwenda.” “Asante kaka.” Sam akafunga mlango na kutoka. ‘Mungu wangu!’ Sonia akaanza kulia asiamini. ‘Haiwezekani! Huyu kaka alivyo mstaarabu! Haendani na huyu chakaramu hata kidogo! Wamekutana wapi na mwehu huyu!?’ Akaendelea kuwaza akimsikitikia Sam.
‘Inamaana zile kelele zote za jana usiku wakati tunaongea na kaka kwenye simu, atakuwa alikuwa ni yeye tu. Mungu wangu!’ Sonia alizidi kuwaza huku akifuta machozi, gafla akakumbuka maneno ya Josh kuhusu mwanaume wa Leah. Kidogo akatabasamu.
‘Lakini kweli, kaka Sam ni mzuri sana. Ana umbo la kiume. Hata sura yake inavutia. Hachoshi kumtizama, mpole, ana upendo.’ Akaanza kumfikiria Sam kwa namna nyingine ambayo hakuwa akimfikiria kabla. ‘Sasa anachotaka huyu Leah ni nini? Kwa nini anahangaika na shemeji yake!?’ Akazidi kuwaza bila yakupata jibu.
**********************
Baada ya mawazo mawili matatu akijiuliza hili na lile bila ya kupata jibu, akapitiwa na usingizi, na kulala mpaka jioni. Aliamka akiwa anajisikia vizuri. Briana akaingia chumbani kwake nakuanza kumuimbia Sonia. Sonia alikuwa akicheka sana. “Una sauti nzuri Briana, kama ya Mama Briana.” Briana alikuwa akicheka kila alivyokuwa akisifiwa.
Na ni kweli huyo Briana alikuwa ni kopi ya mama yake. “Naona anazidi kukuchekesha tu huyo. Muda wote alikuwa anacheza hapo nje ya mlango wako, namkataza kuingia. Hapo amenitoroka, nataka akaoge.” Mama Briana aliingia na kukaa pembeni ya kitanda.
“Dada tumbo linazidi kuwa kubwa!” Mama Briana akajitizama na kucheka huku akipapasa tumbo lake. “Nimebakiza siku chache tu na mimi napata kipenzi changu. Maana Nyange amenipokonya mtoto kabisa. Hasikii wala haambiwi kwa Briana. Ngoja Junior wangu aje. Watatukoma.” Wote walikuwa wakicheka.
“Eti Briana? Kaka anakuja?” Briana akatingisha kichwa kukubali. “Anavyohubiriwa mwanangu kuhusu huyo Junior, naona mpaka amechoka kusubiri. Kila habari anayopewa na baba yake nikuhusu Junior.” Wote walikuwa wakicheka.
“Sasa nimealika marafiki zetu kwa ajili ya chakula cha jioni. Sitaki wageni waje wamkute mchafu huyu. Ngoja nikamuogeshe.” “Nitamuogesha dada. Najisikia vizuri kabisa.” “Una uhakika?” “Kabisa dada. Nimelala siku nzima, mpaka nimechoka tena.” Mama Briana akacheka kama kawaida yake.
“Haya basi. Na wewe uvae vizuri, upendeze. Wanakuja na marafiki wa Sam na Nyange. Unaweza pata mchumba.” “Dada wewe!” Mama Briana alizidi kucheka. “Kweli! Kwani hutaki kuolewa mdogo wangu?” “Akuuu! Nataka kukaa na Briana wangu tu. Wanaume wamenichosha, sitaki hata kusikia.” “Ujiandae na kaka yake anakuja.” “Sisi tuko tayari. Sieti Bree?” Briana alitingisha kichwa huku akiruka ruka kitandani kwa Sonia.
**********************
Alimwandaa mtoto, akaoga na yeye, nakumfuata mama Briana jikoni. “Basi na wewe ukaoge dada. Nitamalizia kupika nakuandaa meza.” “Mbona nashukuru. Kwanza nishachoka.” Alishangazwa alipomgeukia Sonia aliyekuwa akizungumza naye amempa mgongo. “Hee! Ndio umependeza hivyo!” Akaanza kucheka kwa aibu.
“Kidogo tu dada jamani!” “Nakwambia leo, lazima tupate shemeji.” “Jamani dada wewe!” “Naoa mwenyewe.” Josh akaingilia maongezi na kumfanya mama Briana azidi kucheka. “Utamuoa nani?” “Si wewe! Eti mama Bree? Kwani mimi sifai kuwa mume wa Sonia? Naona unamtafutia wachumba wengine wakati mwenyewe nipo hapahapa!” Mama Briana alizidi kucheka. “Endelea kuota hivyohivyo.” Sonia alijibu.
Josh na Sonia walibaki jikoni wakisaidiana kuandaa chakula. Mama Briana alipomaliza kujitayarisha, akarudi jikoni kuangalia chakula. “Umependeza dada yangu kama kawaida yako.” Akamsifia. “Naona tumbo tu hapo. Mtoto mmoja kama wako kumi tumboni!” Leah aliingia jikoni na kuingilia mazungumzo ya Mama Briana na Sonia. Sonia aligeuka pembeni ili asimuangalie Leah.
“Umeandaa vizuri sana. Asante Sonia. Na baba Bree anasifia kweli chakula chako.” Leah akaguna baada ya dada yake kumsifia Sonia. “Jamani mnatuumiza pua!” Baba Briana na Sam waliingia jikoni. Sam akabaki anamshangaa Sonia jinsi alivyopendeza. “Kama mke wangu yuko huku na Sonia, leo lazima wageni watajing’ata ulimi.” Baba Briana akatania.
“Kwani mimi sio mtu?” “Kwani umepika Leah? Si ndio umefika tu!” “Naona kutwa unamsifia Sonia!” Leah aliongea kwa sauti iliyojaa wivu na hasira. “Kama mtu ana sifa zake kwa nini asisifiwe jamani? Eti Mama Bree?” Baba Briana akamsogelea mkewe na kumkumbatia kwa nyuma, mikono ikatua juu ya tumbo. “Kweli Sonia ametulia jamani! Anampenda mtoto, msafi wa mwili wake, mpish…” Wakati mama Briana anaendelea kumwaga sifa za Sonia, Leah akatoka nakubamiza mlango wa jikoni kwa nguvu sana, nakuacha kila mtu anashangaa.
“Vipi mwenzio, mzima?” Mama Briana akamuuliza Sam. “Labda kuchoka, tulikuwa site kwenye nyumba, tokea asubuhi tulipotoka hapa. Na mafundi wenyewe hawakufanya kama alivyotaka. Kwa hiyo alikuwa na mambo mengi ya kurekebisha huko.” Sam akajibu.
“Vipi lakini, wamefikia wapi?” Mama Briana akaendelea kumuuliza Sam huku mumewe akiendelea kuchezea tumbo lake. “Sio pabaya. Lakini pesa yote tunatumbukiza humo, nimeishiwa kweli.” “Hongereni na pole. Ujenzi ni kazi kweli! Na nyumba yenyewe Leah ameamua kuifanya kubwa kweli! Lazima itawagarimu sana.”
“Hongera ya nini? Kuhangaika nihangaike mimi, halafu hongera umpe yeye!” Leah akadakia kwa sauti ya juu, akiwa nje ya jikoni, sehemu wanapokula chakula. “Huyo Sam anajiliza bure hapo. Hela aliyoweka hapo inahesabika! Kila ukimwambia atoe hela, kiswahili kirefu tu. Hana lolote. Eti hela yote inaingia kwenye ujenzi, halafu nyumba yenyewe bado hata haijaisha! Huoni aibu mwanaume mzima kusema hivyo?” Leah aliendelea kutokwa na maneno nakufanya kila mtu atulie kabisa na kuanza kutoka pale mmoja baada ya mwingine. Akabaki Sonia na Josh.
Sonia alishangazwa sana na Leah, alizidi kumchukia kwa tabia zake chafu. “Unauhakika kweli kama hawa ni ndugu? Mbona ni kama usiku na giza?” Sonia akamuuliza Josh huku wakinong'ona. “Huoni jinsi walivyo fanana?” “Tena na wewe usinichanganye hata kidogo. Huyo mwendawazimu hafikii hata nusu ya uzuri wa mama Briana.” Josh na Sonia waliendelea kusengenya kwa sauti ya chini, wakiwa jikoni.
**********************
Baada ya muda mfupi, kweli wageni wengi walifika. “Sonia! Njoo usalimie wageni.” Mama Briana akamfuata Sonia jikoni. “Naogopa dada. Nyinyi endeleeni tu bwana!” “Wewe vipi? Njoo bwana.” Akakausha mikono nakutoka na mama Briana. “Usiniache sasa!” Sonia akamvuta mama Briana gauni huku akimnong’oneza. Mama Briana hana mbavu kama kawaida yake.
Alikuta watu wengi hapo sebuleni na kuzuidi kumuogopesha. “Jamani, mdogo wangu mwingine huyu. Anaitwa Sonia.” Kila mtu akanyamaza nakumgeukia Sonia. Kimya kilitanda kidogo na kumzubaisha Sonia hajui chakufanya tena.
“Mama Nyange! Inabidi tuongee pembeni.” “Hapana, mimi ndio nina mazungumzo na mama Nyange.” “Basi mimi naona niongee na Sonia mwenyewe.” Vicheko viliibuka kila mtu akisema lake. Sam alikuwa akitabasamu tu, huku akimtizama Sonia.
“Shikamooni.” “Daah! Mimi naona leo nalala hapahapa. Au unasemaje Sam?” Mama Briana ndio alikuwa akicheka sana. “Wewe ongea vizuri, John. Unaweza kuibuka mshindi.” Sam alijibu huku akimwangalia Sonia kwa utulivu wa namna yake.
“Huyu binti sio mchezo!” Sifa za Sonia zilianza kutolewa, huku Sonia akitamani kuondoka lakini mama Briana alikuwa amemshikilia mkono kwa nguvu, kumzuia asiondoke. Sonia alibaki ameinama chini akichora chini kwa mguu wake, nyuma kidogo ya mama Briana.
Nafsi Isiyoweza Kutulia.
“Hana cha ubinti wowote! Kijitukizima hicho! Na ana mtoto. Wala hamna haja ya kushindana, anaweza kuwamudu nyinyi wote hapa.” Leah aliyekuwa kimya muda wote akichezea simu yake aliingilia furaha ile na kufanya kila mtu anyamaze kimya.
“Kwani uongo? Muulizeni kama sio mama huyo? Shule yenyewe ilimshinda sababu ya umalaya.” Mama Briana alishituka sana. “Kwani vipi Leah!?” “Poa tu. Kwani vipi?” Leah akajibu kwa kiburi sana. “Kwa nini unafanya hivyo?!” Dada yake akaendelea kumuhoji akishangaa sana.
“Vipi? Kwani wewe hujui kama Sonia mtu mzima mwenzako? Anawajua wanaume vizuri sana, tena kakushinda hata wewe. Asikudanganye na sura ya upole hiyo, kumbe simba mwenda pole.” “Usifanye hivyo Leah! Sio vizuri bwana.” “Nakuona sana unavyomtetea. Kila nikikwambia anamtesa mtoto, huamini.”
“Nilimkuta amempa mtoto ammenyee vitunguu ili apike, tena na kisu kikali. Amemuanzishia mtoto kulala mchana ili apate muda wa kwenda kwa mabwana zake. Mtaa mzima wanamjua huyo Sonia kuwa ni 'cha wote'.”
“Hakuna mwanaume aliyembakiza hapa mtaani. Nakuona wewe na mumeo wote mmemkazania. Eti na Sam naye leo ananiambia hawezi kwenda site kabla hajaja kumuona Sonia. Kwa kipi mno?” Leah akaendelea kuongea kwa jazba. Kila mtu alikuwa kimya akimtazama yeye, kasoro Sonia alibaki ameinamisha kichwa chini, alijivuta nyuma kabisa ya Mama Briana.
“Sio kweli Leah! Sonia hawezi kumtesa Briana hata kidogo, anampenda sana kuliko wasichana wote waliowahi kupita humu ndani, na kila mtu ni shahidi. Angekuwa anamtesa Briana, Briana angekuwa hivyo alivyo? Huyu binti amekuja humu ndani na kumbadilisha Briana kupita hata nilivyotarajia.”
“Na ujue uliponiambia tu kuwa anatoka kwenda kwa wanaume, ilibidi nimuulize Josh. Huyu msichana hajawahi hata kutoa mguu wake hapo nje ya geti. Kwa nini unamchukia Sonia?” “Josh anakudanganya kwa kuwa na yeye analala naye. Na kama hajawahi kutoka, hizo nywele kasukia wapi?”
“Anaitwa mama huruma huyo! Hana mwanaume mmoja, hata baba wa mtoto wake hamjui! Kumbuka Sam alivyotuambia, alimuuliza baba wa mtoto wake, akashindwa hata kumjibu.” Sonia alinyanyua uso na kumgeukia Sam. Taratibu machozi yalianza kumtoka Sonia huku amejawa uso wa kuumia sana, kama aliyemwambia Sam, SIKUTEGEMEA.
“Kumbe wakati wote umekuwa ukinidanganya juu ya wasichana wangu wa kazi, Leah! Huyu binti amesukwa hizo nywele humuhumu ndani! Tena kwenye hilo kochi ulilokaa wewe! Hakutoka humu ndani, mimi ndio nilimletea msusi kwa kuwa alikataa kwenda saluni. Unanitia wasiwasi Leah na unanifanya nijiulize mara mbilimbili kwa nini unawachukia wasichana wangu wa ndani?!”
“Kila anayekuja lazima umtafutie sababu, na kwa kuwa nilikuamini na mimi nilikuwa hata siulizi, nawafukuza tu. Kwa nini Leah?” Sonia alishindwa kuvumilia, alizidi kulia kwa uchungu akaamua kuondoka hapo.
Hofu ilimlemea Nyange. Akashindwa kuvumilia, akasimama kwa haraka kabla mdogo wake hajaropoka jingine. “Mama Bree? Mpenzi wangu?” Aliweka rimoti zote chini, akamsogelea mkewe. “Tulia bwana, ona hali yako.” “Nashangaa, kwa nini ananivurugia nyumba yangu? Anajua ninavyopata shida na wafanyakazi! Sonia akiondoka nitafanyaje Nyange? Nataka kujua shida yake nini kwenye nyumba yangu?” “Wema wangu umeniponza! Yaani wewe hii ndio shukurani yako kwangu?!” Leah akaanza tena.
“Naomba utulie mke wangu. Daktari amekwambia hiyo pressure itakusumbua sana kama hutatulia. Huhitaji kupigizana kelele. Tutaongea na Sonia, atatulia tu. Sonia anakupenda sana. Hawezi kuondoka akakuacha katika hali hiyo.” “Yaani wewe Nyange unasema mimi napiga kelele? Kwani mimi chizi? Kwanza wote mnatakiwa mnishukuru mimi, bila mimi msingekuwa mmeoana!” Leah aliendelea kubwatuka.
Nyange akamshika mkewe mkono. “Twende ukapumzike.” Mama Briana alishaanza kulia. “Unasemaje Leah?” Mama Briana akauliza. “Usichoelewa nini? Na utuuzima wako huo ulikuwa umechina bila mwanaume mpaka nilipo kuunganisha na Nyange. Unataka kubisha nini? Nilikuhurumia, nikamkataa Nyange ili dada yangu uolewe. Na bado huna shukurani.”
“Ungekuta sasa hivi mimi ndio nakaa hapa, na wewe bado umechina mtaani.” Sam akanyanyuka kwenda chumbani kwa Sonia. “Sonia? Sonia? Naomba fungua mlango tafadhali.” Sam aliendelea kugonga, lakini Sonia hakufungua mlango wala kujibu kitu, alisikika akiendelea kulia. Wageni wote walikuwa kimya kabisa.
Mama Briana akaanza kujisikia vibaya. “Najisikia vibaya sana Nyange. Nasikia moyo unaenda mbio. Naomba nikapumzike.” “Na mtajibeba mwaka huu!” Leah akaongea kwa kejeli na kuongeza. “Wizi mtupu! Unajidai kumbembeleza sasa hivi! Umechelewa Nyange.” Kila mtu alikuwa hamuelewi Leah. Maana alijawa hasira alizoshindwa zuia mdomo wake.
Chanzo Cha Hasira Ya Leah
Leah alikuwa amebeba hasira sana moyoni mwake. Baada yakuondoka siku ile kwa dada yake akiwa safarini, bila maelewano na shemeji yake, aliamua kutafuta hoteli nzuri sana Bagamoyo ili akapumzike na Nyange, ikiwezekana wamalize tofauti zao warudi kuwa wapenzi. Lakini kabla ya kumwambia shemeji yake mipango aliyokwisha panga juu ya mapumziko yao, Nyange alimpigia simu ya kumuomba wakutane mahali walipozoea kukutana kwa mazungumzo kidogo.
Akiwa amejawa furaha na kujutia kuwa kwenye hedhi siku ile, Leah alijua shemeji yake amemuwahi kumuomba msamaha. Alitoka kazini, wakakutana mahali walipoweza kuficha magari yao, kisha akahamia kwenye gari ya shemeji yake kama kawaida yao, wakati mwingine giza lilipoingia walimalizana kwenye gari.
Kabla ya kuanza vituko vyake alivyozoea kumfanyia shemeji yake wakiwa ndani ya gari, Nyange alimwambia walitoka hospitalini na afya ya mkewe sio nzuri. Pressureinamsumbua sana, waliambiwa kama haitashuka wanaweza kupoteza mtoto au Mama Briana mwenyewe.
Nyange alimsubiria huyo mtoto wa kiume kwa hamu sana. Chumba cha huyo mtoto kilisha tayarishwa. Kila kitu kilikuwa tayari kikimsubiria huyo mtoto.
“Namjua mama Bree sio muongeaji, lazima kuna kitu kinamsumbua ndani ya moyo wake, lakini hawezi kusema. Naomba kusitisha haya mahusiano kabisa Leah. Nataka kutulia na mke wangu.” “Wewe tu muoga Nyange mpenzi wangu. Sababu haiwezi kuwa sisi. Namjua dada yangu alivyo, wala hatuhisi kwa lolote. Ni mambo yake tu ya ujauzito. Wakati mwingine ujauzito unaleta pressure. Tuendelee kuwa makini bwana! Lakini sio kuachana.” Leah alibembeleza.
Historia Ya Nyange Na Ndugu Hao Wawili
Ukweli Leah ndiye aliyemuunganisha Nyange na dada yake. Walishawahi kufanya ofisi moja na Nyange. Nyange alipomwona Leah alimwambia amevutiwa naye sana anataka kumuoa. Leah alicheka sana, kwa kuwa Nyange hakuwa amefikia hata nusu ya vigezo vya mwanaume anayemtaka maishani. Tena angalau Sam alifikisha kwa asilimia kubwa kasoro pesa tu. Lakini Nyange hakumpenda hata kidogo.
Alimuona masikini, mshamba sana, mwembamba kupita kiasi, hajui kuvaa, nywele kama kichaka, hata weusi wake aliukejeli sana. Hakuacha kumcheka waziwazi yeye na mashoga zake pale ofisini.
Kwa kuwa alimdharau sana dada yake, akaamua kumsukumizia Nyange kwa dada yake ili ampunguzie kero maishani. Nyange alipomuona tu mama Briana kwenye picha alizokuwa akionyeshwa na Leah, hakuamini kama kweli mama Briana atamkubali, kwani alimuona ni bora zaidi ya Leah.
Mbali na uzuri wake wa nje ambao hata rafiki zake Nyange walikiri kuwa mama Briana alimpita mbali sana Leah, mama Briana alionekana na pesa nyingi. Wenzake wote walimshauri Nyange asijaribu hata kumsogelea mama Briana, nikujidhalilisha. Lakini Nyange alipiga moyo konde na kumuomba Leah amtambulishe tu, yeye mwenyewe atamaliza mambo yote.
Mambo yalikuwa tofauti kabisa pale Nyange alipokaribishwa nyumbani kwa mama Briana. Ni kama mama Briana hakuwa amemtazama kabisa Nyange kwa nje. Hakujali jinsi alivyokuwa akionekana wala mavazi yake kwa wakati huo. Alimkarimu na kutoa heshima zote kwa Nyange kana kwamba alikuwa amemwalika raisi nyumbani kwake.
Kadiri walivyoendelea kuwa karibu, ndivyo mama Briana alivyoendelea kumjali na kumuheshimu Nyange, kitu kilichozidi kumchanganya Nyange. Nyange alimwambia Leah, dada yake anasifa zaidi alizokuwa akizitafuta kwa mwanamke atakayekuwa mkewe. Leah alimkejeli Nyange na kumwambia kweli wamekutana, Nyange na mama Briana. Akimaanisha wote walikuwa washamba, hawajui vitu vizuri.
Sasa WIVU ulimuanza Leah baada ya kuona mambo ya dada yake na Nyange yanaenda vizuri. Kwa muda mfupi baada ya harusi yao, Nyange alibadilika sana. Afya yake ilianza kubadilika kwa kulishwa vizuri, kile kichaka kilianza kupelekwa kwa kinyozi. Weusi aliokuwa akiukejeli Leah, ulianza kumvutia Leah mwenyewe.
Na kwa kuwa kazi ya mama Briana ilikuwa ikimuingizia pesa nyingi sana, alimshauri mumewe aache kazi ya kuajiriwa, ajitupie kwenye biashara. Kama wengine wanavyosema wapo watu wenye mkono wa biashara, basi Nyange alikuwa mmoja wao. Biashara zilichanganya, gafla Nyange akawa gumzo mjini, lakini wakati wote alikuwa akimtanguliza mama Briana mbele. Kila mahali alikiri mafanikio yake yanatokana na mkewe ambaye hakuacha kuwa pembeni yake akimtia moyo.
Leah alianza kumsumbua shemeji yake bila mafanikio. Baada ya mitego yake yote ya kimapenzi kukwama, siku moja alipokuja kukaa na Briana wakati mdogo sana na dada yake alikuwa amesafiri kama kawaida yake ndipo alipomnasa Nyange.
Mama Briana alitumwa na ofisi yao kwenda nje kwa masomo kwa muda wa miezi sita, kama kuongeza ujuzi. Alimuomba Leah ahamie nyumbani kwake kwa muda huo ili kumsaidia msichana wakazi kumlea Briana na kuangalia mambo mengine ya nyumbani kwake yasiaharibike kipindi akiwa hayupo.
Leah alifurahi sana. Akahamia hapo kwa dada yake akiwa amejiandaa vizuri kumnasa shemejie. Alisubiria mwezi wa kwanza na wapili alipoona shemeji yake anamkumbuka sana mkewe, huku akimbembeleza kwenye simu arudi hata kwa siku chache tu, halafu yeye ndio atagaramia nauli, Leah alijua tayari shemeji yake amelemewa.
Siku hiyo, alisubiri kila mtu amekwenda kulala, akaingia chumbani kwa shemeji yake nakupanda kitandani kwake akiwa mtupu. Nyange alifanikiwa kumfukuza mara ya kwanza na ya pili, lakini Leah alijitahidi kumshawishi mpaka shemeji yake alijikuta akifanya naye mapenzi.
Aliamka akiwa na majuto makubwa sana moyoni, yakumsaliti mkewe tena kwenye kitanda chao! Alijipa moyo, kwa kuwa ameshapunguza haja zake, hatakaa amguse tena Leah, huo ndio mwisho wake atasubiri mpaka mkewe atakapo rudi.
Lakini ilikuwa imebaki miezi minne, ambayo ilikuwa kama miaka kumi migumu sana kwa Nyange, kwani aliishi na kishawishi palepale ndani kwake.
Kazi ya Leah pale ndani kwa dada yake ilibaki kumuhudumia Nyange tu wala si mtoto. Ili asithubutu kujutia alichokifanya, Leah alikuwa akimtumia shemeji yake picha zake akiwa uchi nakumkaribisha kufanya mapenzi hata kipindi wakiwa wote kazini au usiku Leah anapokuwa chumbani kwake.
Alijipiga picha za uchi nakumwambia anamsubiria chumbani kwake aende. Nyange alijikaza mwezi mwingine mmoja bila yakumgusa Leah huku akimwambia waziwazi kitendo walichokuwa wamekifanya sio sawa na hawapaswi kurudia tena. Lakini hizo zilikuwa ni kelele za chura tu, hazikuwahi kumzuia tembo kunywa maji.
Hakuacha kumshawishi shemejie mpaka alipolainika na kuingia chumbani kwa Leah siku hiyo usiku huku akimwapia Leah hiyo ni mara yao ya mwisho. Baada ya hapo asije kurudia tena hata kumtumia picha za uchi. Leah alikubali na kufunga mlango.
Lakini huo ndio ukawa mwanzo wa penzi la kuonja la wizi. Mambo yaliwanogea, Nyange hakuona tena shida ya kuwa mbali na mkewe. Kila mkewe alipopiga simu, alimtakia shule njema, nakumwambia atamvumilia tu mpaka atakaporudi, kitu kilichomfurahisha sana mama Briana nakumfanya atulie kwenye masomo.
Sam hakuwahi kuwa kipingamizi kwa mahusiano yao hata kidogo kwani Leah alimuhakikishia Nyange kuwa amemdhibiti Sam vyakutosha. Japokuwa walikuwa wakiishi wote, lakini Leah ndiye aliyekuwa na sauti katika mahusiano yao. Aliweza kusafiri bila kuaga au hata kumwambia Sam alipo.
Alitoka atakavyo na kurudi muda anaotaka yeye bila kutoa maelezo yoyote kwa Sam. Pesa nyingi alizokuwa akimuomba shemeji yake ndizo ziliwasaidia kujenga nyumba yao, yeye na Sam. Alijitahidi kujenga nyumba kama ya dada yake na alijitahidi sana kushindana na dada yake kwa kila kitu.
**********************
Leah aliendelea kumbembeleza shemeji yake wakiwa bado wapo kwenye gari. “Hapana Leah. Hata hivyo nimefikiria nimeona, ninavyomfanyia mama Briana sio vizuri. Mke wangu ni mpole sana. Na ananipenda na kuniheshimu sana. Najisikia vibaya sana, kwa kitendo tunachomfanyia. Nataka kutulia na mke wangu.”
“Ndio unakumbuka leo kama umeoa? Acha hizo Nyange bwana! Mimi na wewe ndio tulikusudiwa na Mungu tuwe pamoja.” Leah alianyoosha mkono moja kwa moja kwenye zipu ya suruali ya shemejie hapohapo kwenye gari. Kwa hasira sana Nyange aliutoa ule mkono kwa nguvu, kana kwamba walikuwa wakigombana.
“Acha kabisa Leah. Naomba usirudie tena kunigusa.” Leah alishituka sana. “Miaka yote hiyo tupo wote Nyange, leo ndio unanikataa!?” “Nimesema basi. Naomba shuka kwenye gari yangu niwahi nyumbani kwa mke wangu. Narudia tena, leo ndio iwe mwisho. Tuheshimiane kama mashemeji. Umenielewa?” Leah hakuamini kabisa. Alishuka kwenye gari ya shemeji yake akiwa amejawa na aibu sana.
**********************
Haikuwa mara yao ya kwanza kufanya mapenzi kwenye gari. Leah alikuwa na vituko vingi kwa shemeji yake ilimradi tu kumuonyesha yeye ni bora kuliko dada yake. Alishamfuata mara kadhaa ofisini kwake kwa kumshitukiza na kujilalamisha, kushindwa kuvumilia mpaka jioni anahamu naye sana, nakuishia kufanya mapenzi ofisini kwa Nyange.
Hasira na wivu vilimuumiza sana Leah. Alijua huo ndio mwisho wa kuhongwa pesa nyingi sana na shemeji yake. Na bado malengo yake makubwa sana, yalikuwa hayajatimia, Nyange alimkatili vibaya sana. Ukweli, kamba ilimkatikia pabaya sana, kwani safari hiyo aliyokuwa ameipanga kwenda kupumzika naye huko Bagamoyo, ndio ilikuwa safari yakutimiza LENGO lake kuu mbali na ujenzi uliokuwa akiendelea nao. Alirudi nyumbani kwake na hasira sana. Hata Sam alipomuuliza kulikoni. Alimjibu, ‘hayakuhusu'.
Roho Ya Uharibifu Haitulii Mpaka Itimize Lengo
Nyange alimsaidia kumpandisha ngazi mkewe huku amemshika mkono. Alimuweka kitandani vizuri, kisha akambusu. “Pole sana mpenzi wangu. Tulia kidogo. Nakuja sasa hivi. Ngoja nikaagane na wageni.” Nyange akatoka chumbani kwake kama simba.
Alishuka ngazi na kumsogelea Leah, akamnyanyua na mkono mmoja kutoka kwenye kochi mpaka ukutani. “Uwii! Unaniua Nyange?” Leah akapiga kelele. “Usithubutu hata siku moja, kuongea na mke wangu kama ulivyoongea naye leo. Umesikia Leah? Hata kama ni dada yako. Hapa ni nyumbani kwake. Lazima uwe na adabu.” Nyange aliongea na Leah huku amemkunja gauni lake kifuani na kumkandamiza ukutani kwa nguvu sana.
“Wakati unanivua nguo hapa ndani, hukujua kama ni dada yangu?” Kila mtu akashtuka sana, kwani Leah alikuwa akiongea kwa sauti ya juu sana kana kwamba alitaka watu wote wajue.
Sam aliyekuwa mlangoni kwa Sonia akiendelea kugonga, akasogea karibu. Taratibu Nyange akamuweka Leah chini. Leah akaanza kucheka kicheko cha kejeli.
“Ulisahau eeh? Mbona huendelei na hasira zako? Eti sasa hivi ndio unataka kuniua unasema niwe na heshima hapa ni nyumbani kwake! Wakati ushalala na mimi mpaka kwenye kitanda hichohicho unacholala naye, huyo Mama Briana? Sasa tofauti yetu ni nini? Labda yeye kwakuwa umemfikisha kanisani na mimi unanifikisha kwenye mahoteliya maana, ambayo hujawahi kumfikisha yeye.”
“Mimi naweza kukuridhisha popote pale utakapo, kwenye gari yako, mpaka ofisini kwako naweza kukuridhisha, yeye hawezi. Sasa kati yangu mimi na yeye nani bora?” Nyange alikuwa kama amemwagiwa maji ya baridi.
Kumbe mama Briana naye baada ya kusikia kelele aliamua kutoka, akabaki amesimama pembeni ya ngazi za kushukia chini huku akitetemeka.
Wakati habari hizo zikipenya kwa shida sana moyoni na akilini mwake, mama Briana akaanza kupatwa na kizunguzungu wakati jasho jingi likimtoka.
Akaanza kuona nyumba nzima inazunguka akiwa bado amesimama juu kabisa gorofani. Alianza kupapasa akitafuta sehemu ya kushika ili asianguke, gafla giza nene lilitanda machoni mwake, wala asiweze kuona kitu tena. “Naombeni mnisaidie.” Mama Briana aliweza kusikika.
Watu wote waligeuka kumuangalia pale juu alipokuwa amesimama akihangaika. Aliendelea kupapasa ili angalau akae chini, ndipo alipojikwaa na kuanguka kama gunia. Aligonga kwenye marembo ya chuma, yaliyopamba ngazi, alirushwa chini ya ngazi na kuanza kubiringita kama mpira.
Kufumba na kufungua watu wote walishangaa kumuona alishafika chini ya ngazi na damu zikimtoka puani na mdomoni. Kilikuwa ni kitendo cha sekunde chacke sana, tokea aombe msaada mpaka kufika pale chini akiwa hajitambui.
**********************
Nyange alianza kupiga mayowe kama mtoto mdogo. Bila kupoteza muda, vijana watatu akiwemo Sam walimbeba Mama Briana, wakamwingiza ndani ya gari na kumkimbiza hospitalini bila ya kumjali Nyange aliyekuwa akilia na kutetemeka sana. “Mungu wangu! Nimemuua mke wangu!” Nyange aliendelea kulia huku ameweka mikono kichwani.
Hofu ilikuwa imemkamata alishindwa kusimama wala kusogea kabisa. Picha ya Mama Briana akiwa amelala pale sakafuni akitokwa na damu nyingi sana iliendelea kumtesa Nyange.
Leah aliondoka kimya kimya bila ya kuaga. Rafiki mpenzi wa Nyange Mr. Chau alimnyanyua Nyange kutoka sakafuni na kumwingiza kwenye gari bila ya viatu. Kikao kile cha nyumbani kwa Nyange kilihamia hospitalini. Sonia ilimbidi abaki na Briana.
**********************
Bila kupoteza muda mama Briana aliingizwa chumba cha upasuaji. Wasiwasi ulizidi kumuingia Nyange kadiri masaa yalivyozidi kwenda bila mtu yeyote kutoka chumba cha upasuaji na kusema chochote. Hofu ya kumpoteza mama Briana ilizidi kumtesa, alikaa chini kabisa sakafuni akiwa amejikunyata kama kifaranga kilicho nyeshewa na mvua.
Hakuna mtu yeyote aliyeweza kumtizama wala kumsemesha Nyange. Rafiki zake wote walibaki kimya kabisa bila hata kumpa pole. Aibu na hofu vilimkamata. Hakuna aliyeweza kumuelewa Nyange kabisa. Kwa uzuri, utulivu na upendo aliokuwa nao mama Briana, na bado Nyange aliweza kulala na mdogo wake! Tena sio mara moja ni mahusiano ya muda mrefu! Ilikuwa ngumu kuingia akilini kabisa, kila mtu alibaki na maswali ambayo ni Nyange pekee ndiye alikuwa na majibu yake.
Walitamani kujua ni kipi Nyange alichokuwa akikikosa kwa mama Briana aliyemtoa chini kabisa akiwa hana hata shilingi wala hajulikani mjini na kukipata kwa Leah msichana ambaye sio tu ni ndugu wa mkewe, bali ni msichana ambaye hana maadili hata kidogo!
**********************
Baada ya muda mrefu kupita, daktari alitoka na kuwaambia wamefanikiwa kushusha pressure ya Mama Briana ambayo ilikuwa juu sana, na wamefanikiwa kumtoa mtoto lakini alikufa muda mfupi tu baada yakuzaliwa. Nyange alianza kulia tena kama mtoto mdogo. “Mungu wangu!” Nyange alisikika akiomboleza.
Mama Briana alitolewa chumba cha upasuaji akiwa na maruerue ya madawa ya usingizi aliyokuwa amechomwa chumba cha upasuaji na kupelekwa wodini. Iliwabidi watu wote waondoke baada ya daktari kuwaambia mama Briana anahitajika muda mwingi wakupumzika, kasoro Nyange aliomba abaki naye.
Kwa kuwa alilazwa kwenye chumba chake mwenyewe, kwenye hospitali hiyo ya kulipia, Nyange aliruhusiwa kubaki na mkewe. Alikaa pembeni ya kitanda cha mkewe huku akijuta sana. Mama Briana alirudi kulala baada ya kuchomwa sindano nyingine.
**********************
Sam aliomba arudishwe nyumbani kwa Nyange yeye na Josh ili angalau aongee na Sonia. Walimkuta Sonia akiwasubiria sebuleni huku akilia sana. “Josh? Vipi dada?”Sonia alisimama mara walipoingia tu na kumuwahi Josh. Hakutaka kumuangalia Sam hata kidogo.
“Anaendelea vizuri. Lakini tumepoteza mtoto.” Sonia akaingia chumbani kwake huku akizidi kulia. Sam aliamua kwenda kulala na Josh, ili angalau atumie usiku huo kutafakari kidogo kabla ya kukumbana tena na kelele za Leah, usiku huo.
Sonia alikuwa akilizwa na mengi. Alimchukia sana Sam kwa kutoa mambo yake Mwanza na kuyaleta Dar, na pia alimuhurumia sana mama Briana aliyekuwa akimngojea mtoto wake wakiume kwa hamu kubwa. Na alikuwa amebakiza siku chache tu ajifungue. Aliendelea kulia mpaka alipopitiwa na usingizi.
**********************
Aliamka asubuhi sana kuandaa chakula cha kupeleka hospitalini. Alipomaliza alikwenda kumgongea Josh. Alishituka sana alipofunguliwa mlango na Sam. Haraka haraka aliinamisha kichwa chini. “Samahani kwa usumbufu. Nilitaka kumuamsha Josh ili ampelekee dada chakula hospitalini, jana aliondoka bila ya kula.” Bado Sonia alikuwa ameangalia chini.
Sam alishangaa akili za utu alizonazo Sonia. “Umefanya vizuri sana. Ngoja nijitayarishe nikipeleke.” Sonia akaondoka bila ya kuongeza neno, na baada ya muda mfupi, Sam aliingia jikoni kuchukua kikapu cha chakula, alichokuwa amekiandaa Sonia. Alitaka kuongea na Sonia lakini tayari Sonia alishageuka na kurudi chumbani kwake. Sam alisimama pale kwa muda, mwishowe akaamua kwenda tu hospitalini bila ya kuongea naye.
**********************
Alipoingia tu kwenye chumba hicho alicholazwa mama Briana akiwa na kapu lake mkononi, mama Briana naye alishituka kutoka usingizini. “Pole shem.” Mama Briana hakujibu kitu, akaanza kujipapasa tumbo lake taratibu huku akiugulia maumivu. “Junior yuko wapi?” Mama Briana aliuliza kwa sauti ya chini sana iliyojaa maumivu na sononeko.
“Au bado sijajifungua? Lakini nahisi kama tumbo langu lipo tupu ni kama Junior hayupo humu ndani!” Mama Briana aliendelea kuongeza nguvu ya kuminya tumbo lake huku akikunja uso kwa maumivu.
Nyange alibaki akifuta machozi kimya kimya asijue chakujibu. Sam ndio alibaki kama sanamu. Mama Briana alitaka kusimama, lakini maumivu makali yalimrudisha kitandani na bado alikuwa na drip ya maji mkononi na mpira wa kutolea mkojo {catheter}.
“Nasikia maumivu makali sana, mwili mzima una maumivu.” Mama Briana alianza kulia. “Wapi shem?” “Kila mahali. Kichwa, shingo, mba…. Nasikia maumivu jamani! Mtoto wangu yuko wapi Sam?” Mama Briana akazidi kulia. Waliingia manesi, wakamchoma sindano, taratibu akarudi kulala.
Nyange alizidi kulia kama mtoto mdogo hakujua ni lugha gani atatumia kumwambia mkewe kuwa mtoto waliyekuwa wakimsubiria kwa hamu amefariki.
Kila siku usiku kabla ya kulala na mkewe, ilikuwa lazima wazungumze na huyo Junior ndipo walale. Walikuwa wakizungumza na huyo mtoto akiwa tumboni na kupewa majukumu ya kumlinda Briana maishani kana kwamba alishazaliwa, na ni mtu mzima.
Waliombwa wamwache apumzike baada ya kuchomwa sindano ya usingizi. Sam hakutaka hata kumuangalia Nyange usoni, alimuacha hapohapo nje ya wodi nakurudi zake nyumbani kwake.
Huku Kulikoungua Mpini, Kukabaki Shoka
Alimkuta Leah ameshafungasha vitu vyake vyote, anavipanga kwenye gari yake. Sam hakumsemesha chochote, aliingia moja kwa moja ndani nakujiweka kitandani. “Nitarudi baadaye kuchukua vitu vyangu vingine.” Sam alibaki kimya kabisa akiangalia dari.
“Umenisikia wewe Sam? Nitakuja kuchukua vitu vyangu vyote humu ndani. Kuanzia friji, jiko la umeme na gesi, maana nilikukuta na jiko la mkaa, makochi, makabati ya jikoni na chumbani vyote ni vyangu, nilikukuta unaweka nguo zako kwenye begi.” Leah aliendelea kumtajia vitu vyake vyote alivyokuwa amemnunulia Sam kama zawadi, lakini Sam hakunyanyua hata mdomo kusema kitu chochote na wala hakumtizama.
Na kweli jioni Leah alirudi na gari kubwa, alimkuta Sam amekaa kwenye kochi anaangalia luninga. Bila ya salamu alichomoa hiyo tv kwenye umeme, nakuanza kubeba kila kitu kilichomo mle ndani akisaidiana na vijana wawili alikuwa amekuja nao. “Naomba usimame Sam, nataka kuchukua na makochi yangu.” Sam akasimama. Leah akachukua kila kitu na kumuachia Sam kompyuta yake na nguo zake zote alizitoa kabatini na kuzitupia sakafuni.
Historia Ya Sam Na Leah.
Sam alipomaliza tu chuo kikuu, alibahatika kupata kazi ya IT bank. Alijitafutia kinyumba kidogo cha uwani chenye chumba kimoja, sebule, choo humohumo ndani na jiko. Pesa zote alizokuwa akipata Sam, alizituma kusaidia nyumbani kwao.
Alipokuja Leah kuishi naye ndipo alipoanza kubadili kitu kimoja hadi kingine ndani ya kijumba hicho kidogo cha Sam, mpaka aliporidhika. Sam alikuwa akilala kwenye kitanda kidogo tu, tena cha kawaida sana, na jiko lake la mkaa, ambalo wala hakuwa akipika sana, mara nyingi alikula hukohuko kazini akirudi nyumbani ilikuwa ni kulala tu. Leah alitupa kila kitu alichokikuta kwenye nyumba hiyo nakuanza upyaa. Ni kweli alinunua vitu vichache lakini vyote vilikuwa vya thamani sana.
Sam alikutana na Leah, akiwa yupo na marafiki zake kwenye nyama choma. Hakuwa hata na wazo la mwanamke katika maisha yake. Kwani alijiona ana majukumu mazito sana ya nyumbani kwao, kwa hiyo kuongeza mtu mwingine maishani, alijua nikujiongeza matatizo.
Alikuwa akisomesha wadogo zake watatu na bado alikuwa akitegemewa sana na wazazi wake katika kila kitu. Marafiki zake walikuwa wakioa lakini Sam hakutaka hata kufikiri na wala hakujihusisha kabisa na wanawake sababu yakuogopa kuhonga. Alijinyima sana, ili kusaidia nyumbani kwao.
Leah alikuja siku hiyo kwenye nyama choma na mchumba wa rafiki yake Sam. Alipomuona tu Sam alivutiwa naye sana. Japokuwa walikuwepo vijana wengine wengi pale mezani, tena waliokuwa wameonyesha kuchanganywa na Leah, lakini yeye alionyesha wazi kuvutiwa na Sam.
Alishindwa kabisa kuficha hisia zake. Sam alikuwa na vigezo vyote, Leah alivyovitaka kwa mwanaume wake. Bila kulaza damu, alimuomba amtembelee nyumbani kwake. Sam alikataa kwa aibu. Kwani alimuona vile Leah alivyoonekana ni msichana wa viwango vya juu, alijua kumkaribisha sehemu anayoishi ni kujidhalilisha tu.
Lakini Leah alimganda sana mpaka Sam alipomkaribisha. Siku ya kwanza tu alipofika kwa Sam, alikaribishwa kwenye vistuli. Kesho yake Leah alimletea Sam makochi kama zawadi. Taratibu Leah alianza kupika na kusaidia usafi nyumbani kwa Sam mpaka Sam alipoingia laini nakuanza naye mahusiano.
**********************
“Umenisikia wewe Sam?” Sam alinyamaza kimya. “Nimekwambia sitaki kukuona tena kule site kwangu. Maana mimi ndio nimeweka pesa nyingi kwenye ile nyumba tunayojenga kuliko wewe. Na kama unataka nikulipe vijipesa vyako ulivyokuwa ukiwekeza kwenye ile nyumba, nilipe kwanza pesa yangu yote niliyolipia kodi ya hapa ya mwaka huu, usisahau ile niliyokupa utume kwenu wakati ule mama yako mgonjwa, na unakumbuka ada ya mdogo wako yule wakike ya mwaka jana? Nililipa mimi.”
“Haya usisahau jinsi nilivyokusaidia kukarabati kwenu na…..” Leah alizidi kumuhesabia Sam misaada aliyowahi kumsaidia, mpaka waliokuwa wakipandisha mizigo walipomwambia wamemaliza. “Nikikuona site, kwenye ile nyumba tuliyokuwa tukijenga, nakushitaki polisi. Umenisikia Sam?” “Sawa.” Alipoitika, ndipo Leah akaondoka, nakufunga mlango kwa nguvu sana.
**********************
Baada ya Leah kuondoka, Sam alirudi hospitalini kumwangalia mama Briana. Alikuta manesi wamejaa kwenye chumba cha mama Briana, Nyange akilia kama mtoto. Mapigo ya moyo yakazidi kwenda kasi, baada ya kutupia macho kitandani na kumkosa mama Briana.
Alibaki ameshika kichwa akiwa bado amesimama mlangoni. “Mungu wangu, mama Briana!” Sam alisema kwa nguvu na kufanya watu wote wamgeukie. Nyange akamsogelea Sam kwa haraka akapiga magoti huku akitokwa na machozi. “Naomba uongee na mama Briana. Amejifungia chooni, huku akitokwa na damu nyingi sana. Wewe anakupenda, atakusikiliza.” Sam alivuta pumzi kwa nguvu sana na kushusha
taratibu. Alijua amekufa.
“Na yupo mlangoni, hatuwezi kuvunja mlango.” Sam aliomba wale manesi watoke baada yakusafisha sakafu iliyokuwa imejaa damu na mikojo, kwani mama Briana alipoamka tena na kugundua hana mtoto tumboni, halafu Nyange hakuwa akimweleza kitu chochote cha maana juu ya mtoto wake, alichomoa kila kitu mwilini mwake ikiwemo catheter iliyokuwa na mkojo, ndipu za maji nakutupa kila kitu sakafuni.
Alitaka kutoka akamtafute mtoto wake, lakini Nyange alimzuia mlangoni, ndipo nesi alipoingia kuongea naye juu ya kifo cha mtoto wao. Mama Briana alianza kulia sana na kuamua kujifungia chooni, baada yakuomba aletewe mtoto wake hivyohivyo na kukataliwa.
**********************
Baada ya watu wote kutoka Sam akasogea kwenye mlango wa chooni. Aliweza kumsikia mama Briana akilia kwa sauti ya chini sana lakini iliyojaa uchungu. “Pole sana, mama Briana.” Kidogo palitulia. “Sam?” “Ni mimi shem. Tunaweza kuongea?” Mama Briana akatulia kidogo.
“Unataka nikujie na nini huko ndani?” “Nimechafuka sana.” “Basi subiri nikachukue nguo za kubadilisha. Nakuja sasa hivi.” Sam akatoka haraka aliwakuta wote wapo nje ya chumba alicholazwa mama Briana wakimsubiria.
“Amefungua?” Nyange alimdaka Sam kwa swali. Lakini Sam alimgeukia nesi bila ya kumjibu. “Naomba nguo zake zakubadili na vitu vyake vingine atakavyohitaji baada ya kuoga.”
Vitu vya kuvaa mama Briana vilipoletwa, Sam akarudi tena kwenye mlango wa chooni. “Nina kila kitu unachohitaji kuvaa, unataka niingie nikusaidie kubadili?” “Hapana. Nitavaa tu mwenyewe.” Mama Briana alifungua mlango kidogo, Sam akapitisha nguo.
Baada ya muda alitoka akiwa msafi kabisa. “Vipi maumivu?” “Namtaka mtoto wangu Sam. Nimeteseka naye karibia miezi 9, halafu eti leo wananiambia amekufa halafu basi!” Mama Briana alikuwa akiongea kwa sauti yake ya chini sana, huku akilia. “Namtaka Junior wangu, Sam. Unajua alikuwa mzima kabisa? Hata usiku ule wakati napika nilimsikia akicheza. Wameniambia walivyomtoa, hakukaa sana akafa. Sitaki wamtupe Junior wangu. Namtaka mtoto wangu, Sam.” Sam akamsogelea na kumkumbatia.
“Pole sana, mama Briana. Nitaongea nao, ili tufanye taratibu za mazishi. Lakini naomba ukubali matibabu.” “Wananichoma sindano za usingizi tu. Nitalala hapa mpaka lini? Briana ananisubiri nyumbani, na ninataka nikamzike Junior.” “Briana yupo na Sonia, hana shida yoyote. Hakuna atakayemzika Junior bila wewe.” “Kweli Sam?” “Nakuahidi shem, nitaongea na daktari tuone watakuruhusu lini, ndipo mambo mengine yafuate. Lakini sasa hivi kubali matibabu kwanza. Umetoka kwenye operation jana tu! Unahitajika matibabu.” Mama Briana akatulia.
“Pandisha miguu vizuri kitandani, nikufunike halafu nikamwite nesi. Sawa?” Mama Briana akatingisha kichwa huku akikausha machozi.
**********************
Baada ya siku tatu, Sam akiwa ndio muuguzaji mkubwa, mama Briana aliruhusiwa. “Twende nyumbani shem.” Akarudi kukaa kitandani baada ya kubadili nguo za hospitalini nakuvaa za nyumbani. “Tunaondokaje bila Junior?” Sam akamgeukia Nyange aliyekuwa amesimama na mizigo mlangoni. “Siwezi kuondoka hapa bila ya mtoto wangu. Mkaniletee nguo zake kabatini, nitamuogesha mwanangu, na atazikwa palepale nyumbani. Sitaki akawekwe mbali.” Tayari machozi yalikuwa yamejaa usoni kwa mama Briana.
Sam na Nyange wakatoka. Baada ya muda Nyange akarudi ndani, alipoona mama Briana ameinama haraka hataki kumwangalia, akatoka na baada ya muda Sam akaingia.
“Nyange anaenda kushugulikia taratibu za mazishi.” Mama Briana akaanza kulia kwa kwikwi. “Usinielewe vibaya Sam. Ukaona mimi ni msumbufu tu. Junior ni mwanangu niliyeishi naye karibia miezi tisa sasa, nilikuwa nikiongea naye kila mara, alishakuwa rafiki yangu sana. Hata nilipokuwa nikisikia maumivu nilijikaza kwa kuwa nilijua yeye yupo ndani, na ipo siku atatoka na yote yataisha. Siwezi kukubali akatupwa tu. Sio uchafu, ni mwanangu kama vile alivyo Briana.” Sam akashindwa kujizuia. Akasimama na kutoka nje huku akitokwa na machozi.
Kila Mchuma Janga, Hula Na Wakwao
Nyange alirudi na nguo nzuri sana za Junior na jeneza dogo lililoonekana la garama sana. Mama Briana kwa ujasiri, kama siye aliyekuwa mgonjwa, akaongozana na Sam na Nyange, akaomba amsafishe mtoto wake yeye mwenyewe. Alimvalisha vizuri hizo nguo alizokuwa ameletewa na baba yake.
Akabaki akimwangalia kwa muda mrefu kama ambaye bado haamini. “Nimefurahi nimemuona mwanangu.” Alimgeukia Sam huku akifuta machozi. Nyange alikuwa akilia tu. “Nisawa tukipata picha ya ukumbusho?” Sam akauliza.“Siwezi kumsahau Junior maishani.” Mama Briana alijibu huku akimwangalia mtoto wake kwa makini na upendo mkubwa. Sam akamsaidia kumuweka kwenye jeneza vizuri wakatoka nje.
Walikuta umati mkubwa wa ndugu, jamaa na marafiki, ukiwasubiria nje ya chumba cha maiti. Magari yaliongozana mpaka nyumbani kwa Nyange, napo walikuta watu wengine wakiwemo majirani, wakiwasubiria.
Wengine walifika kushuhudia tukio lililotokea. Kumuona Nyange na mkewe na hilo jumba lao, kwani habari zilishakuwa zimeenea kila mahali. Na wengine ni kweli walikuja kuomboleza na mama Briana. Wakina mama walishapika. Mama Briana alikaa pembeni ya jeneza la mtoto wake akitazama bila kukwepesha macho. Watu walikuwa wakila na kunywa lakini sio yeye.
Sam akamfuata. “Lazima ule ili unywe dawa.” “Naomba tumalize hili kwanza.” Mama Briana akajibu kwa upole, kama kawaida yake. “Sawa.” Sam akaona akubaliane na wazo lake.
Ilifanyika ibada fupi nyuma ya jumba hilo la Nyange ambapo palishaandaliwa kaburi la Junior. Baada ya mazishi, Sam ndiye aliyetoa neno la shukurani kwa kuwa Nyange alishindwa kuongea kabisa.
Kwa ustarabu sana, Sam aliomba watu waondoke ili kumpa mama Briana nafasi yakupumzika. Alikuwa kama mtu aliyepigwa na bumbuazi, alibaki amekodolea macho kaburi la mwanae kama ambaye bado haamini kama kaburi ndio limempokea mwanae!
**********************
Watu wote waliondoka, wakabaki familia tu. “Tuingie ndani shem.” Mama Briana akacheka kinyonge huku akifuta machozi. “Siamini Sam! Nahisi labda ni ndoto tu. Inakuwa ngumu kuamini kama kweli safari ya Junior ndio imeishia hapa. Kama utani tu!” “Pole sana. Pole sana mama Briana.”
Sam alihakikisha mama Briana amekula na kunywa dawa ndipo akaondoka. Moja kwa moja akaingia chumbani kwa marehemu mtoto wake Junior, na kujifungia mlango.
**********************
Bado Sonia alikuwa na hasira sana na Sam. Kila Sam alipompigia simu, hakupokea. Na hakutaka hata kusoma ujumbe wowote kutoka kwakwe. Kila ujumbe ulipoingia kutoka kwa Sam aliufuta bila yakusoma. Kwa kuwa Sam alimchukia sana Nyange, alishindwa kurudi tena nyumbani kwao.
Waliamsha uchungu mkubwa sana uliokuwa umejificha moyoni mwa Sonia. Ujauzito aliokuwa ameupata Sonia, hata yeye mwenyewe hakutarajia. Alikatishwa tonge mdomoni. Alikuwa na malengo makubwa sana katika maisha yake, lakini kufumba na kufumbua malengo yake yote yaligeuka kuwa ndoto za alinacha, nakubaki akichekwa na kutaabika mtaani.
**********************
Sonia ndiye aligeuka kuwa kama mama wa Briana. Alimlea kwa upendo sana kwani mama Briana alikuwa akishinda chumbani kwa Junior tu, hata usiku alilala hukohuko. Sonia ndiye aliyekuwa akimpa dawa na kumbembeleza ale chakula. Hakuacha kumlilia mwanae, mchana na usiku. Nyange aliogopa hata kumkaribia.
Usiku wa manane alipokuwa akisikia kimya chumbani kwa Junior, Nyange alinyata kwenda kumwangalia mkewe, mara nyingi alimkuta amelala sakafuni akiwa amekumbatia nguo za Junior. Nyange na yeye alikuwa akikaa pembeni yake hapo, mpaka asubuhi anapoenda kazini.
Kwa kuwa Sonia ndiye aliyebakiwa na majukumu mengi hapo ndani, Nyange aliamua kumuongezea mshahara ili asifikirie kuondoka na atulie. Kama kawaida yake, kila alipolipwa, alimtumia mama yake pesa baadhi na nyingine alizitunza. Maisha ya mama yake na mtoto wake yalibadilika sana. Hakuacha kupiga simu mara kwa mara kuongea na mtoto wake.
**********************
“Ametoka hata kidogo leo?” Nyange alimuuliza Sonia mara tu alipoingia nyumbani kwake, akitokea kazini. “Hapana.” “Tafadhali sana Sonia, naomba uongee naye.” Sonia akabaki kimya akishindwa kumjibu maana hata yeye alimchukia sana.
Mwezi ulishapita, lakini bado mama Briana alikuwa kwenye maombolezo. Baada yakumlaza Briana, Sonia akaenda chumbani kwa Junior akakaa pembeni ya mama Briana aliyekuwa amejilaza sakafuni.
“Mbona hujala dada?” “Sijisikii njaa kabisa! Kwanza nilikuwa nikijilazimisha tu kula sababu ya dawa, sasa nimeshamaliza hizo dawa, acha nipumzike.” “Unajua dada, Briana anahangaika kweli, anakutafuta. Tokea utoke hospitalini, hujamgusa kabisa wala kuongea naye. Kila wakati ananiletea simu, anajua upo safarini anataka muongee. Amepooza kweli.” Kama aliyeshituliwa kutoka usingizini.
Mama Briana akakaa. “Jamani mwanangu! Nimejisahau kama nina Briana. Ameshalala?” “Amelala.” Mama Briana alitulia kidogo. “Unisamehe Sonia. Nimekuachia majukumu yote!” “Wala usijali dada. Tumekununulia zawadi.” Mama Briana akatabasamu kwa mbali.
“Kweli tena dada. Mimi na Briana, Josh alitaka kujiingiza kwenye zawadi yetu, tumemfukuza.” Mama Briana akatabasamu na kuuliza. “Zawadi gani?” “Sasa simpaka mwenzangu aamke ili tukupe wote pamoja!” Kidogo mama Briana uso ukabadilika.
“Najua utaipenda tu.” “Asante sana Sonia. Ngoja nikaoge nilale, ili kesho nipate muda mzuri na Briana.” “Nikuletee nguo?” “Hapana. Leo nitaenda kuoga hukohuko chumbani kwetu.” Walizungumza kidogo, Sonia akamuacha anaingia chumbani kwao, na yeye akashuka kurudi chumbani kwake.
**********************
Nyange alibaki akitetemeka alipoona mama Briana ameingia chumbani kwao kuoga. Alipomaliza kuoga, akavaa na kurudi kitandani kwao, hiyo ikawa kwa mara ya kwanza tangia usiku ule alipokimbizwa hospitalini.
Alibaki akitetemeka, asijue aseme nini. ‘Sijui nimkumbatie? Hapana. Nianze kuomba msamaha kwanza. Hapana, lazima kuomba msamaha kiume, sio kiholela hivyo. Lazima nijipange, kesho kitaeleweka. Nimfunike?’ Nyange aliendelea kuwaza huku akishindwa hata kusogea hapo kitandani, pembeni ya mkewe.
Kisa Cha Mama Briana Na Leah.
Mama Briana alikuwa ni dada mkimya na mvumilivu sana. Wakati wote alipenda kusaidia hata kwa mtu asiyemfahamu. Walizaliwa watatu, kaka yake Eliah, yeye na Leah ambaye walimuita mtoto wa Uzeeni.
Leah na Mama Briana walipishana sana kwa umri, na Leah alipofeli kidato cha nne, alikuwa tu nyumbani na wazazi wake. Ndipo mama Briana alipomleta mjini kuishi naye. Alijinyima sana ili Leah apate elimu nzuri. Japokuwa Leah alikuwa na tabia ngumu sana kuishi naye, lakini mama Briana hakuwahi kulalamika hata mara moja.
Leah alilelewa nyumbani kwao, yaani kwa wazazi, kama yai. Mama yao hakutaka aonywe wala achapwe na yeyote yule hata baba yake mzazi hakuruhusiwa kumgusa Leah.
Alipofika mjini Leah aliacha kabisa mambo yake ya wanaume, akatulia shuleni na alisoma mpaka alipopata shahada yake ya kwanza ndipo dada yake alipomtafutia kazi. Aliishi na mama Briana tokea hajaolewa mpaka walipofunga ndoa na Nyange.
Roho ya wivu ilimwingia Leah pale Nyange alipowafuata kwenye nyumba ndogo waliyokuwa wakiishi wote watatu siku hiyo usiku na kuwaomba watoke, kuna mahali alitaka kuwapeleka. Wote wawili wakiwa na maswali mengi sana, walijiandaa harakaharaka na kuondoka na Nyange mpaka kwenye hilo Jumba.
Walikuta marafiki wengi wa Nyange wakimsubiria mama Briana ndio awe mzinduzi wa nyumba hiyo. Baada ya mama Briana kufungua mlango huo na kuingia ndani, ndipo sherehe ilipoanza.
Usiku huo Nyange aliutumia kumwaga sifa za mkewe, huku akimshukuru Mungu kwa kumpa mama Briana maishani. Kila mtu alikuwa akimpongeza mama Briana kitu kilichomuumiza sana Leah. Hakuwahi kutaka apitwe na mtu yeyote duniani.
Walihama kutoka kwenye nyumba ndogo waliyokuwa wakiishi baada ya kufunga ndoa, na kwenda kwenye Jumba hilo, huku wivu ukimtesa sana Leah ambaye alikuwa akiishi na dada yake kutokea zamani.
Alipompata tu Sam, akamng’angania mpaka Sam alipokubali kulala naye, ndipo alipopata ujasiri wakuanza kuhamisha nguo moja hadi nyingine kutoka hapo kwa dada yake, mpaka nyumbani kwa Sam. Alimleta Sam nyumbani kwa dada yake, sio kwa ajili ya kumtambulisha tu, bali alitaka kumringishia dada yake kuwa na yeye amepata mwanaume mzuri kwa muonekano kuliko Nyange mumewe.
Kwa kuwa alikuwa haambiliki alianza kuishi kotekote. Wakati mwingine alirudi kukaa kwa dada yake siku mbili au tatu na kurudi kwa Sam au hata hotelini. Ilikuwa ngumu sana kuelezea maisha ya Leah na mama Briana alikuwa akimwangalia tu bila yakusema kitu chochote.
Kaka yao Eliah alijitenga nao kabisa baada ya kifo cha baba yao. Mama Briana na Eliah hawakuwa na tofauti ya tabia ya ukimya kama baba yao. Walimlaumu sana mama yao kwa kifo cha baba yao. Kwani alikufa bila msaada wowote, huku mama yao akionyesha alikuwa na majukumu mengi sana yaliyomfanya ashindwe kumtunza mumewe wakati mgonjwa.
Wengine walisema mama yao ni mshirikina sana, wengine walisema ana roho mbaya yakumpita shetani. Lakini ukweli ni kwamba pale kijijini kwao, Mama yao, Mama Eliah, hakuwa na sifa nzuri hata kidogo.
Wakati wapo kwenye msiba wa baba yao, majirani walikejeli na kusema waziwazi, ‘Wanamwaga vyakula msibani wakati baba yao kafa kwa njaa'. Eliah aliumia sana kwani na yeye alikuwa akituma vyakula vingi sana na pesa ya kusaidia nyumbani kwao. Baada ya msiba, Leah na mama yake walianza fujo waking’ang’ania mali zote.
Mama Briana na Eliah walibaki wakiwashangaa sana, kwani hakuna mtu hata mmoja aliyekuwa akitaka mali hizo. Baba yao alikuwa mwajiriwa mstaafu wa enzi hizo. Kwa hiyo alijijenga sana pale kijijini kwao. Baada ya kustaafu, Eliah aliamua kumsaidia baba yao, akikumbuka jinsi alivyojitolea kumsomesha yeye na Peninah, yaani mama Briana, kwa ngazi ya shahada ya kwanza, ambapo baadaye walijiendeleza wao wenyewe.
Baba yao aliishiwa nguvu ya pesa kwa Leah aliyeishia kidato cha nne, tena alimaliza kwa shida sana, katika shule ya kulipia kwani hata darasa la saba, pia alifeli. Hakuwa akisikilizi ushauri wa mtu yeyote na mama yake ndiye alikuwa kinga yake kubwa.
Mama Eliah aliwafukuza na kupiga marufuku ndugu wote wa mume wake, huku akisema, “Maana kilichokuwa kikituunganisha ni huyu ndugu yenu, sasa kafa, mtakuwa mnakuja hapa kufanya nini?” Mama Eliah alizidi kuchachamaa jioni ya siku iliyofuata baada ya mazishi.
Ndugu wote walikuwa wamekusanyika wakiwemo wazee wa ukoo. “Nataka wote mjue, hapa hakuna cha mtoto wa kwanza wala nini! Mali zote ni zangu. Nisione mtu akijisogeza. Na mila zenu za kurithi wake za marehemu, hapa mnikome kabisa. Kwanza sijaona kati yenu hapo mwanaume wakunioa mimi.” Leah alianza kucheka na kuongeza. “Kweli kabisa mama, heri umewawahi. Hawakawii hawa. Kwanza ndio muanze kujifungasha, msiba ushaisha, ndugu yenu ameshafariki, aliyebaki hapa hawahusu.”
“Kwa hiyo naunga mkono wazo la mama. Kila mtu akatulizane kwake. Mumuachie mama apumzike na mali alizozichuma na mumewe. Sio tena kuanza kumfuta nyuma.” “Haswaa. Tena mkiondoka hapa leo, ndio iwe mwisho. Hakuna cha matanga wala arobaini. Tulieni makwenu.” Waliongeza bila hofu wala aibu mbele ya watu hao wazima waliokuwa kimya kabisa wakiwasikiliza jinsi wanavyopokezana maneno.
Kaka yao, Eliah na dada yake Peninah {mama Briana} walibaki na mshangao wasielewe yote yale yalikuwa yakiletwa na nini! Walianzisha ugomvi usio na maana na hakuna hata mtu aliyekuwa tayari kugombana nao.
Eliah alipoona kelele zinazidi, hakuongeza chochote. Alimchukua mkewe na watoto wake, jioni hiyohiyo na kuamua kuondoka. “Unaenda wapi kaka jamani na giza limeshaanza kuingia?” Mama Briana ambaye alikuwa rafiki mkubwa wa kaka yake aliwakimbilia kwenye gari.
“Ungesubiri basi mpaka kesho tuondoke wote.” “Kweli dada!? Wewe huoni aibu kukaa kwenye kikao kama kile na mumeo? Kwani kulikuwa na ulazima gani wa kelele zote zile? Au walifikiri mimi nimekuja kurithi mali? Siwezi kukaa pale na mke wangu aendelee kusikiliza jinsi ninavyodhalilishwa! Nilikuja kumzika baba yangu, nishazika, acha niondoke.” Mama Briana alianza kulia. “Tutawasiliana dada, wala usilie. Wewe unajua siwezi kukutupa dada yangu.” “Naomba mnijulishe mtakapofika nyumbani.”Aliagana na wifi yake na watoto, kaka yao akaondoa gari. Hakurudi tena kijijini kwao.
**********************
Haikuwa mara ya kwanza kwa mama Briana kusalitiwa. Alishakuwa na mwanaume aliyempenda sana. Tena msomi, mwenye pesa, na hata familia yake ilikuwa na uwezo mkubwa sana, lakini naye alikuwa mlevi na muhuni sana. Alipoletewa Nyange ambaye hapendi kabisa pombe, na kumuona mpaka umri ule hana mwanamke, tena anasaidiwa kutafutiwa mwanamke na Leah, alikubali kufungia macho muonekano wa Nyange na kumpokea jinsi alivyo.
Alimpenda na kumthamini sana Nyange, akijua atakuwa peke yake kwenye penzi la Nyange. Amani moyoni mwa mama Briana ilianza kupotea pale alipomkuta mumewe amekumbatiwa na mwanamke mwingine ndani ya ofisi yake.
Kwa hofu kubwa, akijua matatizo aliyokuwa nayo kwa mwanaume wa kwanza ndiyo anakutana nayo tena kwa Nyange, mwanaume aliyemtoa chini sana, aliogopa hata kuzungumzia kile kitu na Nyange. Alibaki amesimama ofisini hapo akiwashangaa kwa muda bila yakusema kitu chochote, kisha akaondoka.
Alikuwa amepita maeneo ya karibia na ofisi ya mumewe, akaamua aingie kumsalimia, lakini alipokutana na hayo mazingira, alitoka na kufunga mlango taratibu sana na kurudi nyumbani kwao.
Nyange alirudi kwa mkewe, alitaka amuelezee juu ya yule mwanamke pale ofisini, lakini mama Briana alimuuliza maswali mawili tu.
“Bado unanipenda na unaona nafaa kuwa mkeo?” Nyange alipojibu ndiyo, mama Briana alimuomba walale na wasizungumzie tena kile kitu. Lakini ndio ukawa mwanzo wa ugonjwa wa pressure kwa mama Briana na kuzidi kuwa mbaya zaidi aliposhika mimba ya Junior.
Tangia wakati ule, kila aliposafiri kikazi alikuwa na wakati mgumu sana, na kila mumewe alipochelewa kutoka kazini au anapoaga anasafiri, japokuwa hakuwa akimuuliza kitu, lakini alikuwa akiteseka sana moyoni, alijua anakwenda kwa mwanamke mwingine.
**********************
Mama Briana alizidi kuwaza usiku huo wakati amelala kitandani kwake huku akiumia sana. ‘Au ndio maana Leah alikuwa akifukuza wasichana wangu humu ndani sababu ya wivu? Au hakutaka mtu yeyote awepo humu ndani ili awe huru na Nyange? Nimekuwa nikikosea wapi, jamani? Nimejitahidi kwa kadiri ya uwezo wangu, lakini bado wanaume wote niliokuwa nao wameweza kuwa na wanawake wengine.”
“Inawezekana nina tatizo kubwa, wanaloshindwa kuniambia. Siwezi kuwaridhisha kwa lolote ndio maana wanahangaika na wanawake wengine.” Kama walivyo wanawake wengi, akajitwika yeye makosa.
“Siwezi kuendelea kuishi humu ndani, nitampoteza na Briana. Ilikuwa kidogo nimpoteze Briana kwa afya mbaya nikifikiri Nyange na yeye yupo busy na kazi kumbe ana kazi ya kumlea Leah tu humu ndani hamjali mtoto wangu. Sasa sasa hivi nimempoteza Junior. Nitang’ang’ania nisipopendwa mpaka lini? Heri niondoke tu.’ Mama Briana alizidi kuwaza.
‘Sitaki tena mwanaume maishani mwangu. Nyange ndio wa mwisho. Hata hivyo sasa hivi hanihitaji tena, ana mali nyingi sana, anaweza kuoa mtu yeyote anayemtaka na kupata watoto wengine sio mimi ninayeteseka kushika mimba. Hata kama wataendeleza mapenzi na Leah, sitajali tena. Ni heri nikae pembeni.’ Swali la wamekuwa kwenye mahusiano kwa muda gani, mama Briana hakutaka hata kuwaza kabisa, alijua litamuumiza zaidi.
**********************
Leah alipoanza mahusiano na shemeji yake, alihakikisha hakuna mwanamke anayemsogelea Nyange. Hakuona shida kupigana na msichana yeyote atakayemkuta na Nyange. Hata wasichana wa kazi nyumbani na ofisini kwa Nyange hawakuruhusiwa kuwa karibu naye. Ilikuwa endapo Leah atahisi tu kama msichana wa kazi anaukaribu wowote na Nyange, nilazima atamshawishi dada yake amfukuze kazi na kama ni ofisini basi Leah atahakikisha Nyange mwenyewe anamfukuza kazi.
Ndio maana alikuwa akipika yeye au dada yake tu. Hakutaka hata msichana wakazi amtengee Nyange maji ya kunywa. Mapenzi kwa shemeji yake yalimkolea, hakuweza kuona mwanaume mwingine kama Nyange.
Na kwa kuwa alimpata Nyange atakavyo, hakuona shida kumchangia na dada yake, aliyekuwa haulizi lolote kwa mumewe. Hata akiaga ana safari ya gafla, yeye atamtakia safari njema tu bila maswali.
Leah na Nyange, walizunguka kwenye nyumba za kulala wageni hata mchana. Ikitokea kama Nyange akikaa kwake siku za weekend bila kutoka, Leah alihakikisha jumatatu au jumanne yake ni lazima atamng’ang’ania Nyange watoke hata kwa lisaa tu au wamalizane hata ofisini kwa Nyange usiku wakati wafanyakazi wote wameondoka.
Alihakikisha anambana Nyange kwa kadiri awezavyo. Wakati mwingine Leah alipokuwa akipata likizo kazini, alitafuta hoteli nje ya mji wa Dar na kwenda kupumzika na Nyange. Alifurahia mapenzi ya Nyange na ndiye mtu pekee aliyekuwa angalau akimsikiliza. Na Nyange naye alikuwa akimpa pesa nyingi sana. Zaidi ya nusu ya nyumba ya Leah na Sam, ilijengwa na Nyange.
Maamuzi Magumu
Palipo pambazuka na kuona mumewe ametoka, Mama Briana alitoka kitandani, akaanza kukusanya vitu vyake na mtoto wake tu, akaviweka kwenye masanduku, michezo ya mwanae akafunga kwenye maboksi. Alimuomba Sonia na yeye achukue vitu vyake vyote. Bila maswali, Sonia naye akakusanya vitu vyake vyote akaweka kwenye begi. Josh aliwasaidia kuingiza kwenye gari ya Mama Briana, wakaondoka na kuhamia hotelini wakati akitafuta nyumba yakuwatosha wao watatu tu.
**********************
Nyange aliporudi kutoka kazini alimkuta Josh akisafisha bustani. Akamwambia mama Briana ameondoka na mtoto pamoja na Sonia. Nyange akakimbilia ndani na kukuta kila kitu kipo kama kilivyo isipokuwa nguo na vitu vya mkewe Penninah, Briana na Sonia.
Akamfuata tena Josh akakaa chini kabisa. “Mungu wangu!” Hakutegemea kama mama Briana angeondoka hasa baada ya kurudi chumbani usiku uliopita. Nyange alijua kama kawaida ya mkewe, amekubali yaishe, na yeye amebakiza kazi ndogo tu.
Alishajiandaa siku nzima na utetezi wake kwa mkewe na maneno mazuri ya kuomba msamaha. ‘Au atakuwa amesafiri kidogo? Ananipenda sana Penninah, hawezi kuniacha.’ Nyange aliendelea kuwaza kwa sauti huku Josh akimtazama kwa kujiiba asijue kama amechanganyikiwa au la.
Kwani ni kweli Nyange alibadilika sana, tokea wapatwe na matatizo. Alikuwa mnyonge sana kama mgonjwa. Utani wote na maneno mengi ya Nyange yaliyomtengenezea marafiki wengi vilimuisha. Hakuna aliyemtafuta kwa simu wala kuwatembelea pale kwenye nyumba yao tena.
“Amekwambia anarudi lini tena?” “Kwa jinsi nilivyowaona, sidhani kama ni watu wakurudi tena.” “Mungu wangu Penninah!” Nyange alianza kupiga simu ya mkewe bila mafanikio. Aliogopa sana kuulizia nyumbani kwao. Kwani alijua tabia ya mama yao.
Maswali na matusi atakayo poromoshewa, alijua hakutakuwa na mwisho, na alijua yule mama atafika nyumbani kwake na kujaza watu kwa fujo. Kwa kaka yake Eliah ndio alitaka afute kabisa namba yake na azuie kabisa simu zake zisiingie kwenye simu yake tena, kwani alijua ukaribu wa mama Briana na kaka yake. Alijua ni kuzua matatizo makubwa zaidi. ‘Eliah ataniua mchana kweupee.’ Alizidi kuwaza kwa sauti.
Sam ndio aliacha kupokea simu za Nyange kabisaa. Alibaki amechanganyikiwa, kwani mkewe hakuwa na marafiki wakaribu. Maisha ya mkewe ilikuwa kazini na nyumbani. Ndoto za mama Briana tangia utoto ni kuolewa na kupata watoto. Alipompata Nyange, alimshukuru sana Mungu, aliachana na marafiki wote, akabaki yeye na mumewe tu. Na kwa kuwa alikaa muda mrefu kidogo bila kupata mtoto, mapenzi yake yote alihamisha kwa mumewe.
Wakawa marafiki wakupindukia. Nyange aliziba mapengo yote kwenye maisha ya Mama Briana na kumfanya asione uhitaji wa mtu yeyote maishani. Na ndipo hapo Nyange aligeuka kuwa Nyange kwelikweli na kumchanganya hata Leah mwenyewe kwa matunzo mazuri ya Penninah. Alijitahidi kwa kadiri awezavyo kumfurahisha Nyange mumewe. Utani mwingi wa Nyange ulikuwa ukimfanya mama Briana kuwa na furaha wakati wote.
**********************
Maisha yao wote yalibadilika sana usiku ule. Kufumba na kufumbua kutoka kuzungukwa na marafiki wengi tena wamaana, familia inayoeleweka, kujaliwa na kutetemekewa na mkewe kama mfalme, Nyange anajikuta ameachiwa jumba na mali zote, lakini bila amani, wala furaha yoyote.
Alijawa aibu na majuto na kila mtu aliyewafahamu alimsema vibaya sana. Alijua hata Sonia na Josh, wanamlaumu sana yeye kwani walishuhudia uchafu aliokuwa akiufanya na Leah, tena palepale ndani anapoishi na mkewe!
**********************
Mbali ya kumpoteza Junior ambaye alikuwa akimsubiria kwa hamu sana, mama Briana alimpoteza Nyange. Rafiki yake kipenzi na faraja ya pekee ambayo alishawahi kuwa nayo duniani. Msiba wa Junior usingekuwa mzito hivyo kwake kama angekuwa na Nyange. Nyange alishamjulia mkewe na alijua jinsi ya kucheza na mawazo yake vizuri sana na kumfanya mkewe awe na furaha wakati wote.
Yale aliyokuwa akiyahisi moyoni, huku akijaribu kuyapuuzia, yalithibitishwausiku ule na Leah, nakumfanya ajichukie sana na kujidharau kupita kiasi. Muda mwingi mama Briana alitumia kulala.
Kile kicheko kiliisha kabisa, likabaki tabasamu tena kwa nadra sana. Alishindwa kumlea kabisa Briana, nakumwachia Sonia majukumu yote ndani ya kanyumba hako kadogo walichokuwa wamepangisha. Sonia ndiye aligeuka kuwa mwenye nyumba. Alijua kutapikwa nini, Briana atavaa nini, kununuliwe nini na yeye ndiye alikuwa akipangia matumizi pesa zote alizokuwa akipewa na mama Briana.
**********************
Sam naye alipoteza faraja ya pekee iliyokuwa imekuja maishani bila kutarajia, Sonia. Tena kwa maneno ya uzushi tu, kutoka kwa Leah. Kila Sonia alipopiga simu nyumbani kwao kumsalimia mtoto wake, siku za weekend aliambiwa, Kana ametoka na George.
George alikuwa akienda kumchukua kila siku jumamosi asubuhi na kumrudisha usiku na Kana alisha anzishwa shule kitu kilichozidi kumchanganya zaidi, kwani sio Sam wala George mwenyewe aliyejaribu hata kuwasiliana naye.
Sonia akashindwa kuelewa kwani Sam aliacha kumtafuta kabisa, kitu kilichoibua maswali mengi sana kwake.
Kuna Wenza Wengine Huja Na Baraka Zao Kwenye Ndoa
Siku hiyo ya jumamosi Nyange akiwa katika hali ya kuchanganyikiwa baada ya juhudi zakumsaka mkewe kugonga mwamba, wazazi wake wakaingia kutoka kijijini. Tokea mkewe aondoke, hakuwahi kupokea simu za wazazi wake akijua wazi wanayemtafuta ni mama Briana na kujua habari za mtoto waliyekuwa na wao wakimsubiria kwa hamu.
Nyange ndiye alikuwa mtoto wa wakiume wa pekee nyumbani kwao, na kaka wa ukoo. Alikuwa na dada wa kubwa wawili na wadogo wawili. Wenzake hawakusoma kama yeye, aliyeishia kidato cha nne, na kusomea mambo ya stores, mwaka mmoja.
Kwa kipindi chote ambacho Nyange aliokuwepo mjini, hakuwahi kuwa msaadamkubwa kwa wazazi wake mpaka alipomuoa mama Briana. Baba yake, yaani mzee Nyange hakuwahi kuacha kulalamika juu ya mwanae. Wakati wote alimjua ni mbahili. Kwani kila alipoombwa hela jibu lake lilikuwa moja tu, 'sina pesa'.
Mambo yalikuja kubadilika sana nyumbani kwa kina Nyange baada ya kuolewa Penninah. Kama kawaida yake ya moyo wa huruma, aliumia sana alipofika nyumbani kwa mumewe na kukuta wazazi wake wanaishi kwenye nyumba ya tembe na kuona maisha duni waliyokuwa wakiishi pale kijijini kwao.
Alimbembeleza sana mumewe wajenge nyumba nyumbani kwao, angalau nyumba ya kawaida tu, “Najua mambo ni mengi Nyange, lakini naomba wazazi wasiendelee kuishi kwenye nyumba ile bwana!” Baba Briana alipoona mkewe amekusuduia kweli, alisimamisha ujenzi wa nyumba yao na kuwajengea wazazi wake nyumba nzuri sana na mama Briana mwenyewe wakati mwingine alikuwa akienda kusimamia kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri na kwa haraka, akijua mumewe akimuona anahangaika vile, ataongeza juhudi.
Kwa hiyo wazi walijua ni juhudi za mama Briana. Na ilipo kamilika alihakikisha mafundi wanajenga na fremu za biashara mbele kwani nyumba yao huko kijijini ilikuwa sehemu nzuri ya biashara.
Aliwafungulia duka la chakula na vitenge hapohapo kwenye hiyo nyumba mpya. Taratibu maisha yao pale kijijini yalianza kubadilika na ndipo heshima ya mzee Nyange ilipoanza kuonekana pale kijijini. Wadogo zake baba Briana walirudishwa shule na mama Briana, na dada zake baba Briana aliwasaidia pesa kidogo kidogo, zakuanzisha biashara.
Japokuwa baba Briana ndiye aliyekuwa akifanya mengi, zaidi akitoa pesa kwao moja kwa moja, au kama kusaidia ndugu zake, lakini mzee Nyange alijua wazi msaada huo WOTE unatoka kwa mama Briana, kwani baba Briana alijulikana kwao kama kijana asiye na msaada wowote na ni mbahili.
Kwa hiyo mama Briana alikuwa akipendwa na kuheshimiwa sana nyumbani kwa kina Nyange, hata Junior alikuwa akisubiriwa na babu yake kwa hamu kubwa, wakijua ndio muendeleza ukoo.
**********************
Mzee Nyange aliweka vitu vyake chini nakuanza kuangaza macho. Baba Bree alijua anamaanisha nini, alinyanyuka na kwenda kuwaletea vinywaji baada ya salamu. “Karibuni.” Nyange aliwakaribisha wazazi wake akionekana na wasiwasi usoni.
“Yupo wapi mwenye nyumba?” Akauliza mzee Nyange mwenyewe. Nyange alibabaika kidogo kisha akajibu. “Amesafiri.” “Amesafiri na watoto wote?!” Mama yake akadakia kwa swali la haraka akishangaa kidogo. “Ndiyo.” Kidogo mama yake akakunja uso.
“Mmh! Mmesahau?” Mzee Nyange akauliza. “Nini tena baba?” “Tuliwaomba akisha kujifungua mama Briana, aletwe kijijini, yeye na huyo Mzee mwenzangu nikamkabithi mji wake. Lakini kila tukipiga simu naona hazipokelewi ndio maana tukaamua kuja wenyewe. Au ameamua kwenda kujifungulia kwao?” Nyange akazidi kubabaika asijue cha kujibu.
“Mngekula kwanza, mpumzike, uchovu ukiisha tutaongea vizuri.” Mzee Nyange akakunja uso. “Wewe unatukaribisha humu ndani kama nani?” Mzee Nyange akamkazia macho baba Briana.
Mzee huyo alijulikana kama mkoloni, alijawa na sheria na wakati wote alifuatiliakanuni alizokuwa amejiwekea mwenyewe. Alimpenda sana Penninah. Wakati wote alipokuwa akifika nyumbani hapo, ilikuwa lazima ziwe ni siku ambazo mama Briana anakuwepo nyumbani.
Alimpenda na kumuheshimu sana mama Briana na wakati wote alimtamka na kuwaambia watu, yeye ndiye Mama Nyange, kwani mkewe ameshakuwa mtu mzima, sasa hivi mama Briana ndiye ana majukumu yote ya ukoo wa Nyange.
“Kuna mazungumzo yakuongea kidogo baba. Ndio maana nimeonelea mpumzike kwanza ndipo tuzungumze.” “Tunapumzika hapa, wakati mwenye nyumba hayupo!?” “Mama Briana ameondoka baba.” “Ulishatuambia amesafiri, mpigie simu tuongee naye tupate ukaribisho kutoka kwake kwanza, ndipo mambo mengine yaendelee.” Baba Briana akajisogeza tena vizuri huku akijaribu kusafisha koo.
“Wala usiwe na wasiwasi baba, kama huna hela kwenye simu yako, mimi nitampigia tu. Naomba hiyo namba yake mpya. Maana ile ya zamani siiipati, tokea nipo kijijini.” Mama yake alitoa simu nakubaki akimwangalia baba Briana baada yakumuona anahangaika, haongei kitu cha maana.
“Kulitokea matatizo hapa ndani, mwenzangu akaondoka bila kuaga” Mzee Nyange akajivuta mbele ya kochi kidogo huku amemkazia macho baba Briana. “Matatizo hayo ni makubwa zaidi ya umasikini aliotukuta nao? Au ni zaidi ya aibualiyotutoa baada ya kukubali kuolewa na wewe, baada ya sisi wote hapa, na wazee wenzangu tulipokuja huku mjini kukulipia mahari nyumbani kwa yule binti uliyetaka kumuoa, kisha baba yake akakukataa mbele ya wazee wenzangu huku akinitukana, kwa kuwa hukuwa na mbele wala nyuma?” Baba Briana alibaki kimya.
“Daudi?” Mama yake akamuita, lakini bado alibaki kimya. “Twende mke wangu.” Mzee Nyange akasimama na kuchukua mkoba wake. “Naomba usiondoke baba!” “Tangia umekuja mjini, hukuwahi kutukaribisha hata mara moja, mpaka alipokuja Penninah kwenye maisha yetu, ndio alikuja kutuchukua kijijini na kutuleta mjini. Wewe jeuri yakutuambia tusiondoke unaipata wapi?”
“Mambo yangu hayakuwa sawa baba! Lakini ningewakaribisha tu.” Baba yake alicheka kwa dharau. “Sikuwahi kukuona mambo yako yamekuwa mazuri, kila siku wewe shida zako zilikuwa haziishi.”
“Sasa umetolewa kwenye shida, umepata vijisenti, umemfukuza mtoto wa watu ili uanze kuhangaika mjini hapa.” “Nimemtafuta sana, sijamuoana baba. Yaani hapa na mimi ndio naingia baba yangu. Siku nzima nilikuwa namtafuta Penninah.”
“Basi utakapo mpata tu, umlete nyumbani. Nisikuone kule bila mama Briana. Hata ukisikia nimekufa sasa hivi, usije kunizika. Wewe uendelee kukaa hapahapa kwenye gorofa lako hili, huku ukipulizwa na huu upepo wa baridi.”
“Mama Briana amefanya haraka yakuondoka baba yangu. Hakunipa hata nafasi, mzee wangu.” “Mama Nyange? Hivi hapa tumekosea nyumba au ndipo penyewe?” Mzee Nyange alimgeukia mkewe.
“Na hivi huyu mama Briana tunayemzungumzia hapa, ndio Penninah? Au mwenzetu ulioa mke mwingine?” Akamgeukia tena mwanae.
“Kweli nguruwe ni nguruwe tu. Hata umuogeshe, umuweke gorofani bado ni nguruwe tu. Unajisikia raha kukaa gorofani hapa, mke wako hayupo. Unataka kuoa tena?” “Hapana mama! Namtafuta mchana na usiku, lakini sijafanikiwa.”
“Nakuapia Daudi mwanangu, hutakaa ukapumzika kwenye hii nyumba bila Penninah. Hizo shilingi mbili ulizozipata, zinakupeleka mbio na kusahau tulipotoka, zitakutokea puani. Twende Nyange.” “Mbona unanilaani mama yangu? Mimi namtafuta mke wangu, wala sifurahii chochote hapa.” “Wala sikulaani mwanangu. Nakwambia ukweli tu, kama wewe mwenzetu umejisahau.” Mama yake na yeye akasimama.
“Hivi wewe Daudi, unakumbuka tulipotoka lakini? Sisi tulikuwa tunakaa kwenye nyumba ya tembe! Sina haja yakukumbusha hali yako. Tulifukuzwa na mbwa kwa wale wakwe zako wa kwanza, sababu ya umaskini wetu. Huyu msichana wa watu, katutoa chini kwenye tembe, kijijini sasa hivi tunaheshimika sababu ya mama Briana!”
“Ananitunza kuliko hata dada zako. Hali yako ilikuwa mbaya, hata sukari ilikuwa ikikushinda kutuma nyumbani. Amekuja na baraka zake yule mtoto, na nina kuapia tena Daudi, ataondoka nazo. Utaharibikiwa mpaka upitilize pale alipokukuta mwanzoni. Mimi ni mama yako, utakuja sema mama alisema.”
“Namjua mama Briana alivyo, sio mtu wakukukimbia wewe. Kama alikupokea ukiwa takataka, kweli aje kukukimbia leo angalau unatizamika? Utanikumbuka Daudi.” “Namtafuta mama.” Mzee Nyange akatoka na mizigo yake. “Wakati laana ya Mungu inatembea humu ndani, isitukute na sisi.” Wakatoka hapo.
“Mngelala basi baba, angalau mpaka kesho.” Baba Briana akamkimbilia baba yake akiwa anatoka getini, lakini mzee Nyange hakugeuka. “Nawaombeni wazazi wangu, tafadhali.” Waliondoka jioni ileile bila ya kunywa wala kula.
**********************
Sonia naye alizidi kuchanganywa, alitamani kujua kinachoendelea nyumbani kwao, Mwanza, lakini kwa kuwa hawakuwa na mahusiano mazuri na mama yake alishindwa kumdadisi kabisa. Kwani mbali ya salamu hakuwa akiongea naye chochote.
Alitamani kuongea na G, lakini hakuwa na namba yake ya simu na alishindwa kumuomba mama yake. Alibaki na maswali yasiyo na majibu. ‘Ningejua nisingeacha kupokea simu za Kaka Sam'. Sonia alizidi kuwaza na kujilaumu sana. Alibaki kumuomba Mungu, Sam amtafute tena, ila ikawa kimya.
**********************
Baada ya siku kadhaa kupita Sonia akapata ujumbe kutoka kwa Sam. Haraka haraka akafungua. ‘Naumwa Sonia, nipo hospitalini.’ Sonia akashituka sana. Moja kwa moja akamuonyesha mama Briana. “Nashauri umpigie.” “Unajua dada, niliacha kabisa kuongea na kaka Sam? Aliniumiza sana.” “Sam!?” “Ndiyo dada. Umesahau maneno aliyosema Leah?” “Kuhusu nini?” “Alivyokuwa ametangaza mimi ni malaya na hata sijui baba wa mtoto wangu!”
“Na yote alisema ameyatoa kwa kaka Sam!” “Kweli Sonia unamsikiliza Leah wewe!? Hakuna mtu muongo kama yule msichana! Ameunganisha vimaneno na kusema vile iliakuharibie wewe na Sam.” “Sielewi dada!” Mama Briana akatulia kidogo kama anayejaribu kufikiria jinsi ya kumueleza akaelewa.
**********************
“Siku moja, tulitoka mimi na Nyange, nilikuwa na hamu ya nyama choma. Nikamwambia Nyange hii nyama hainogi kwa kuwa Sam hayupo. Nyange akampigia Sam simu, nakumuomba atufuate. Lakini Sam alikuwa na Leah nyumbani, Leah akasema na yeye anataka kuja. Ndipo wote wakaja. Wakati tunakula na kunywa, Sam alianza kukuongelea wewe huku akikusifia sana.”
“Alianza kunishukuru mimi kwa kukutunza vizuri. Kama unavyomjua Nyange akaanza kumchokoza Sam juu ya uzuri wako na kujisifia jinsi alivyopata bahati yakuoa mke mzuri, mkarimu na mwenye upendo. Kile kitu kilimuuma sana Leah.”
“Wakati ule sikujua ni kwa nini, lakini sasa hivi ninaelewa. Kwa kuwa wale wote walikuwa ni wapenzi wake na wote walikuwa wakitoa sifa za wanawake wengine sio yeye.”
“Leah ana wivu sana. Nakumbuka Nyange alimtania Sam, ‘angalia Sam usije ukaamua kuoa kabisa’. Samakacheka bila ya kukanusha. Kitu kilichozidi kumuumiza Leah.” Sonia alibaki akiwaza kidogo.
“Nyange aliendelea kumdadisi Sam juu yako na familia yako. Ndipo Sam akasema hamfahamu baba yako ila anamfahamu mama yako na mtoto wako. Leah akadakia kuanza kuuliza kama wewe ulishamtambulisha kwa baba wa mtoto wako. Sam alisema hamkufahamiana muda mrefu, na hata alipokuuliza juu ya baba wa mtoto wako, hukujibu kitu.”
“Leah akaanza kuleta fujo sana pale. Akaanza kukusema sana vibaya, lakini kila mtu alikuwa akikutetea, akashauri nikufukuze kazi kwa kuwa utakuwa ni muhuni sana, unaweza kuleta wanaume ndani, tukaibiwa. Sikumjibu kitu, na hata wiki haikuisha ndipo akaja kuropoka mbele za wageni.”
“Leah hapendi mtu yeyote yule asifiwe mbele yake. Kilimuuma sana kitendo cha wale marafiki zetu kukusifia wewe, sio yeye. Kwa hiyo kama sababu ya kutowasiliana na Sam ni Leah, tafadhali Sonia mdogo wangu, usijipe hiyo adhabu.”
“Sam ni kijana mzuri sana, amemvumilia Leah vyakutosha. Yaani mpaka mimi mwenyewe nilikuwa nikimuonea huruma Sam. Nakuomba na wewe usiendelee kumuadhibu kwa kosa ambalo hakufanya.”
“Mpigie simu na kama amelazwa naomba ukamwangalie. Najua atakuwa yuko peke yake huko hospitalini bila msaada. Leah hamjali kabisa yule kijana.” Sonia akajilaumu sana kutomsikiliza na kumuhukumu moja kwa moja. “Asante sana dada.”
**********************
Sonia akachukua simu na kumpigia Sam. “Pole kaka Sam.” “Asante.” “Uko wapi?” “Bado nipo hospitalini, nasubiria vipimo.” “Ni wapi?” “Tumaini.” “Natamani kuja kukuona lakini sipafahamu.” “Hakuna shida. Nimefurahi umenipigia.” Mama Briana akamgusa Sonia. “Nipe simu niongee naye.” Sonia akampa mama Briana simu.
“Vipi Sam?” “Naumwa shem, tokea juzi!” “Uko na nani?” “Nipo peke yangu.” “Basi tunakuja.” “Asante sana, Shem.” Mama Briana akamwambia Sonia ajiandae wakamuone Sam.
**********************
Alimuogesha Briana harakaharaka wakaenda wote mpaka hospitalini. Walimkuta Sam amechoka sana. “Pole.” “Asante. Natapika sana, tokea juzi! Nasikia baridi kweli! Nahisi nina malaria.” “Pole sana.” Sonia akakaa pembeni yake.
“Nimefurahi kukuona Sonia.” Sonia akatabasamu na kuinama, mama Briana naye akacheka kidogo. “Nini sasa mama Bree?” “Mimi tena Sam? Mimi nacheka na yangu.” “Haya bwana!”
Majibu yalipotoka Sam alikutwa na malaria kali sana. AliandikiwA dawa na kuruhusiwa kurudi nyumbani.
“Leah yuko nyumbani?” Mama Briana akauliza. “Leah!?” Sam akauliza kwa mshangao. “Nilitaka kujua kama una msaada wowote nyumbani. Nakuona umedhoofu sana, Sam. Unahitaji msaada.” “Mbona alishaondoka muda mrefu sana.” Mama Briana alinyamaza kwa muda.
“Basi nitamleta Sonia akusaidie kipindi hiki mgonjwa. Usikae peke yako. Eti Sonia?” “Na wewe dada?” “Mimi nitakuwa sawa tu, tena ndio itakuwa vizuri nirudishe mapenzi kwa mwanangu, naona siku hizi anakutaka wewe tu!” “Asije kunikataa nikirudi!” “Hawezi na anavyokupenda huyu! Itakuwa kazi kweli kumlaza usiku bila wewe.” Sonia akambeba Briana.
“Basi nitamleta Sonia baadaye kidogo, ngoja akachukue vitu vyake baadhi.” “Asante sana shem kwa kujali, lakini nimekuja na taksii, nimeshindwa kuendesha kabisa.” “Pole sana. Basi tuongozane mpaka kwetu, Sonia akishachukua nguo nitawapeleka kwako.” “Wazo zuri shem.” Wote wakaingia kwenye gari ya mama Briana, wakaondoka hapo hospitalini.
**********************
Sam alianza kushangaa kuona wanaelekea sehemu nyingine. “Vipi shem, huku wapi tena!?” “Kumbe sikukwambia? Tulihama.” “Mmejenga hekalu jingine? Maana wewe na Nyange! Siwawezi.” “Hapana Sam, niliondoka kwa Nyange.” “Unanitania mama Briana?!” “Kweli tena. Naishi na Sonia na Briana tu.” Sam alinyamaza mpaka walipofika.
“Kwa nini umeondoka kwako, Shem?” Sam alianza kumuuliza mama Briana mara alipokaribishwa sebuleni wakati wakimsubiria Sonia. “Kinachonibakisha pale ni nini Sam?” Sam akakunja uso kama ambaye hajaelewa.
“Sikuelewi mama Briana.” “Umesahau yaliyonipata?” “Naomba uwe muwazi Shem.” “Nimeshindwa na tabia za Baba Briana. Unajua Leah sio msichana wa kwanza kuwa naye wakati tumeshaoana? Nilimfumania na mwanamke mwingine ofisini kwake, wakiwa wamekumbatiana. Sikutaka hata kumuuliza na alipotaka kunieleza nilimwambia nimemsamehe, yaishe.”
“Kumbe mwenzangu alihamisha mapenzi kwa Leah, tena mdogo wangu! InaniumaSam! Ndani ya nyumba yangu, kitandani kwangu! Alichokikosa kwangu ni nini? Nimejiuliza hata nikibaki pale sina nilichobakiza cha kumpa Nyange akatulia. Nimetoa maisha yangu yote kwa yule mwanaume. Kama bado hanithamini, hata nikirudi au hata ningekaa pale, bado angerudia tena tabia yake kwa mwanamke mwingine, kwa kuwa anachokitaka ameshindwa kukipata kwangu.” Sam akamwangalia kwa kumuhurumia sana mama Briana.
“Unajua siku ile ya ugomvi ndio nilielewa kitu.” Sam alikaa vizuri. “Kitu gani Sam?” “Sonia anaweza kunipikia uji? Nataka niweke kitu tumboni wakati tunaongea, kabla yakunywa dawa.” Mama Briana akaenda kuongea na Sonia, baada ya muda mfupi akarudi.
“Atauleta sasa hivi.” “Asante.” Sam akashukuru, mama Briana akakaa vizuri na kuuliza. “Ulielewa nini Sam?” “Si unajua Leah huwa haniheshimu kabisa?” Mama Briana akaumia sana. “Pole Sam.” Sam akatabasamu.
“Siku chache kabla ya lile tukio pale kwako, nilimsikia anaongea na yule rafiki yake, Ashura. Alikuwa akimwambia kwa mafumbo kwamba, huyo mwanaume amemkataa sasa hivi, amesema hataki mahusiano tena, kwa kuwa mkewe ni mjamzito na pressureinamsumbua sana. Alisema ameamua kutulia na kubaki na mkewe tu, ili asije kusababisha madhara.”
“Nafikiri Ashura alikuwa akimwambia asikubali. Lakini Leah akawa anamwambia na yeye alimshawishi sana na kumwambia pressure ni kitu cha kawaida kwa wajawazito asiwe na wasiwasi, lakini huyo mwanaume alikataa katakata na alimwambia hata hivyo mkewe ni mtu mzuri sana kwake, anajisikia vibaya kwa unyama anaomtendea. Yeye anataka kutulia na mkewe tu. Anampenda sana mkewe. Ashura alimwambia kitu kingine. Leah akawa anamuuliza, ‘unafikiri sikufanya Ashura. Nilitaka kumvua suruali, akanipiga mkono'. Na…” Sam akanyamaza baada yakumuona mama Briana ameanza kulia.
“Usilie bwana shem!” “Naomba uendelee Sam.” “Baada ya hapo nilimuona Leah anakosa raha sana, hata safari aliyokuwa asafiri hakusafiri tena. Na akawa na hasira wakati wote. Na safari hii nilimuonyesha kutokumjali kabisa. Japokuwa nilimuhisi ana mwanamme mwengine, lakini niliona amenidharau kupita kiasi, kuongea habari za mwanaume wake mbale yangu. Nikawa simjali tena, hata nimkute analia nilikuwa simuulizi chochote.”
“Nilianza kumkwepa kabisa swala la mapenzi. Kwa kuwa tulikuwa tukikaa mle ndani hata miezi hataki hata nimguse. Naona alipoona ameshindwa huko nje, akaamua kurudi kwangu. Alianza kama kunishawishi kimapenzi, lakini hhem, nilishakinahiwa na Leah. Naomba niwe muwazi tu. Nilipatwa kinyaa, sikuwa nikitaka hata aniguse tena.” Mama Briana aliinama kama anawaza kitu.
“Sasa siku mmoja kabla ya ile siku ya ugomvi alitaka sana tufanye mapenzi, akawa ananiita chumbani lakini nilibaki sebuleni. Nikamwambia naongea na simu. Kila alipokuwa akinitaka niende chumbani, nilimwambia bado naongea na mtu kwenye simu. Alikuja kwa hasira na kupokonya simu yangu, ndipo alipoona naongea na Sonia. Alichukia sana, nakuanza kufanya fujo.”
“Nilimwambia Sonia anaumwa ndio maana ilikuwa muhimu kuongea naye, lakini alisema namdharau yeye namthamini mtu kama Sonia. Kule kumkashifu Sonia mbele ya watu ni hasira aliyokuwa ameibeba moyoni tangia jana yake.”
“Aliona amenipoteza mimi na Nyange, tena kwa wakati mmoja. Na kwa kuwa aliona yeye amepoteza alikusudia wote tukose. Usifanye huo ujinga kabisa, mama Briana. Usiondoke kwenye nyumba yako sababu ya Leah. Labda uwe unasababu nyingine.” “Na yule mwanamke niliyemkuta naye ofisini kwake, je?” “Kwa nini usimuulize?” Mama Briana akanyamaza. Muda wote Sonia alikuwa akiwasikiliza akiwa jikoni.
**********************
Alileta uji na kuweka mezani. “Karibu kaka.” Sam alikunywa uji wote, hata hakukaa muda mrefu, akautapika wote. “Pole kaka.” Sonia akamfuata chooni. “Asante. Naona nirudi tu nyumbani nianze kunywa dawa za kuzuia kutapika kwanza ndio nijaribu kula kitu kingine.” “Nikuletee maji, unywe sasa hivi?” Sonia aliendelea kuuliza kwa upendo.
“Wamesema zitanifanya nilale sana. Nataka ninywe nikifika tu nyumbani ili nipumzike moja kwa moja.” Sam alitoka chooni nakurudi sebleni. “Pole Sam.” “Daah! Naomba nirudishe tu nyumbani nikapumzike.” Waliondoka mpaka nyumbani kwa Sam.
**********************
Sam aliwakaribisha ndani. Mama Briana alibaki ametoa macho baada ya kuingia na kukuta nyumba ipo tupu. “Mbona nyumba tupu!?” Sam akaanza kucheka. “Mwenye vitu vyake alikuja kuvichukua vyote.” “Haiwezekani Sam!” “Unafanya mchezo na Leah wewe? Nakwambia alinikuta naangalia tv, nikaona tv inachomolewa, ikabebwa na meza yake. Sijakaa sawa, nasikia ‘simama nataka kuchukua na makochi yangu.’ Palikuwa patamu shem!” “Jamani!”
“Nilibakiziwa suruali na mashati yangu tu, tena vilitupwa sakafuni. Nilikuwa sina hata kitu chakutandika chini nilale. Hivi hapa nimeanza upyaa.” “Pole Sam. Mungu atakulipa kwa njia nyingine.” Akawa kama aliyekumbuka kitu.
“Sasa mtalala wapi?” “Unaniona kwa wasiwasi mama Briana, eeh?” Mama Bree akacheka. “Hivi nimeambiwa hata site nisiende tena.” “Haiwezekani Sam!” “Unamchezea Leah wewe? Yaani amesema akiniona tu pale, polisi.” “Jamani Leah! Na hela ulizowekeza na wewe?” “Hizo tena usiulize. Nimetajiwa ninazodaiwa hapa, nakuambiwa zinazidi nilizoweka kwenye ule ujenzi. Mpaka za matibabu ya mama yangu mzazi, aliyomlipia, ninadaiwa.”
“Jamani Leah!” “Kweli. Lakini nimeanzia chumbani. Ukiingia chumbani kwangu, hata kwa Nyange hapaoni ndani.” Sam alianza kumtania mama Bree. “Unavyojisifia?” “Nenda kaone. Nimenunua vitu kwa hasira. Na nimenunua bonge la kiwanja, tena sio uswahilini, hapana. Nimenunua uzunguni karibuna wenye pesa zao, kina Nyange. Sitaki mchezo.” Mama Briana alikuwa akicheka lakini wazi alionekana hana furaha. Sonia alikuwa kimya tu, hakutaka kuchangia chochote.
“Hongera sana Shemeji yangu. Ngoja nikapate fahari ya macho.”Mama Briana akaingia chumbani kwa Sam. “Ni kweli hata Nyange haoni ndani.” Sam akaanza kucheka. “Sasa wewe endelea kumtesa Briana. Unamtoa mtoto gorofani, uzunguni, unampeleka kuishi uswahilini, kwenye nyumba ya kupanga, wakati mwenzio Leah sasahivi anafaidi na wanaume wengine.”
“Mwenzio sikupoteza hata muda. Nilianza kuchangamkia maisha pale tu alipoondoka. Huo ukurasa nishafunga nasonga mbele.” “Heri yako wewe Sam una pakuanzia. Mimi nimefika mwisho.” Mama Briana, aliongea kwa unyonge sana.
“Kwa kuwa umeamua kufika mwisho. Wewe ndio dereva wa gari yako. Ukiona imeisha mafuta, unaweza kwenda kituo cha mafuta ukaongeza mafuta ukaendelea na safari au ukaamua kuliacha gari barabarani bila kuongeza mafuta. Uamuzi ni wako shemeji yangu.” Mama Briana akabaki ameduaa kama anayewaza kitu kwa muda, kisha akaaga
“Naomba mimi niondoke niwahi nyumbani, Sam. Ukazane kula bwana. Umekonda sana. Ukipona tu, nakuja kumchukuan Sonia wangu. Usimzoee.” Sam alicheka tu na kuongeza. “Nakushukuru shem kwa upendo wako.” Mama Briana akaondoka na kuwaacha Sam na Sonia.
**********************
“Karibu Sonia. Hapa ndio kwangu. Sina makochi, ila tv ipo chumbani. Kitanda ndio makochi na ndio meza ya chakula. Usiogope. Najua ushazoea jumba la Nyange, na hapa utazoea tu.” “Hamna shida, kaka.” Chumba kilikuwa kimoja tu. Na hapakuwa hata na mkeka!
Sonia akaanza kujiuliza atalala wapi! Alimpa maji Sam, akanywa dawa, akajitupa kitandani nakupitiwa na usingizi. Sonia alibaki akiwaza chakula cha kumpa atakapoamka.
Alitoka taratibu chumbani, kulitafuta jiko. Alikuta sufuria mbili tu, tena ndogo, sahani tatu, kijiko kimoja na jiko dogo la gesi. Hapakuwa na chakula chochote cha kupika. Akachukua hela kutoka kwenye mkoba wake na kutoka kutafuta sehemu anayoweza kupata chakula. Alitembea sana, mpaka alipokutana na magenge.
Alinunua vitu alivyoona vitawatosha na kurudi kupika. Alitengeneza tena uji, na supu. Akabaki akifikiria cha kufanya. Hapakuwa na pakukaa isipokuwa chumbani kwa Sam. Alipomaliza kufanya usafi, aliingia kuoga na kurudi kukaa chumbani akimwangalia Sam.
Alipoona amelala muda mrefu sana bila kuamka alipatwa na wasiwasi. Taratibu sana alianza kumshika kipanda uso kuona kama ana homa. Akagundua ana homa kali sana. Alikumbuka jinsi mama yake alivyokuwa akitumia kitambaa cha maji na kumuwekea kichwani anapokuwa na homa.
Na yeye akachukua kitaulo chake alichokuwa amepewa na mama Briana chakujisugulia wakati wa kuoga. Akaweka maji ya vuguvugu kiasi, kwenye beseni dogo akarudi nayo chumbani.
Akafungua mfuko wa dawa alizokuwa ameandikiwa Sam, alikuta dawa ya kupunguza maumivu, akaenda kuchukua maji. Alianza kuwaza jinsi ya kumuamsha. ‘Au nimtingishe? Au nimuwekee kitambaa ataaamka? Aunimwite?’ Sonia aliendelea kuwaza.
Dawa alizokuwa amekwisha kunywa zilikuwa ni za kuzuia kutapika tu. Alijisogeza pembeni ya Sam, nakuanza kumuita. “Kaka Sam? Kaka Sam?” Sam akashituka kutoka kwenye usingizi mzito. “Homa ipo juu sana. Kunywa dawa halafu nitakuwekea kitambaa cha maji kichwani, itasakusaidia kushusha homa.” Sam akamwangalia kwa muda kama anayejaribu kutoka usingizini na kuelewa.
Kisha akajiweka sawa. Sonia akampa dawa na maji ya kunywa. “Asante.” “Pole.” Sam akanywa dawa na kujilaza chali huku ameegemeza kichwa chake kwenye mto. Taratibu sana Sonia akaanza kumkanda kichwani na hicho kitaulo huku akikirudisha kwenye maji kila alipoona kimepata moto.
Alifanya hivyo kwa muda, mwishowe alikumbuka anaweza kumkanda shingoni na kwenye makwapa na kifuani. Aliamfungua vifungo vya shati taratibu kuanzia juu mpaka chini, ndipo alipotenganisha upande wa kulia na kushoto wa shati alilokuwa amevaa Sam. Alibaki ametoa macho huku akitetemeka baada ya macho yake kutua juu ya kifua hicho cha kiume. Alianza kusikia sauti ya Josh ikiendelea kusifia kifua cha Sam. ‘Tena kaka mwenyewe mtu wa mazoezi kweli, kifua chake sio mchezo!’ Sonia akabakaki akiwaza na kujutia wazo la kumfungua vifungo.
Taratibu wazo la kumuwekea kitambaa kifuani na chini ya makwapa akalitupilia mbali, akaanza kumfunga tena vifungo. “Vipi?” Sam akafungua macho na kumuuliza. Sonia akaanza kubabaika. “Naona kama vile ni usumbufu, labda nikukande kichwani na shingoni tu.”
“Usijali. Kama unadhani itasaidia kushusha homa sio mbaya.” Akakaa kabisa na kuvua shati lote na kuweka pembeni, akabaki kifua wazi. Sonia alibaki ameinamisha kichwa chini kama ambaye tena hataki kumuona akiwa nusu uchi.
Sam akarudi kulala chali. Taratibu Sonia akamua kurudia kumkanda kichwani, alirudia shingoni mara kadhaa huku akikusanya nguvu za kurudi kifuani. Alipitisha kitaulo hicho chini ya makwapa mara kadhaa ndipo alipoenda kifuani kwa tahadhari sana. Alirudia tena na tena huku akimgusa kipanda uso kutaka kujua kama anachofanya kinasaidia au la.
Alipoona joto limepungua, alichukua taulo jingine aliloona limening’inizwa kwenye mlango wa bafuni na kumkausha vizuri kila alipokuwa amepitisha kitaulo hicho kibichi. Sam naye alikuwa ametulia kabisa huku amefunga macho.
“Unajisikiaje?” Akamuuliza kwa sauti ya chini sana kama asiyetaka tena kumsumbua. “Kungekuwa na kitu cha kula, ningekula kabisa, ninywe dawa ndio nirudi kulala. Nasikia kuchoka sana.” “Nilipika uji.” Akatoka nakwenda kumletea uji.
Alikunywa uji wote aliowekewa, akameza dawa zake, nakurudi kujilaza kitandani. “Asante sana Sonia.” “Pole kaka. Mungu atakusaidia utapona.” “Unaweza kuangalia tv, hutanisumbua.” Kisha akalala. Lakini Sonia akaogopa kuwasha tv, alipomaliza kuosha vyombo akarudi kujilaza pembeni kabisa ya kitanda.
Usiku alimsikia Sam akiwasha taa ya bafuni. Aliogopa kufungua macho, akabaki amejikunja pembeni ya kitanda. Sam alioga, akafungua kabati akatoa shuka, akalifungua nakumfunika Sonia taratibu kisha akarudi kitandani kulala.
Sonia alipoona kimya, akamgeukia. Kulikuwa giza kabisa. “Unajisikiaje sasa hivi?” “Nimekuamsha nini? Samahani.” “Hamna shida. Vipi kichwa?” “Kimetulia. Nilikuwa najisikia joto sana, ndio maana nikaamua kuoga.” “Afadhali.”
“Mbona umelala mwisho hivyo?! Utaanguka ukipitiwa na usingizi?” “Hapana, nipo tu sawa.” “Sogea bwana! Acha woga. Itabidi uvumilie hivyo hivyo. Ndio kama naanza maisha.” “Hamna shida. Hongera, naona mwanzo mzuri.” “Hivyo hivyo. Sogea basi Sonia! Mbona hivyo?” Sonia akajivuta kidogo, Sam akacheka.
“Sogea vizuri, Sonia!” “Naona kama nitakubana na wewe mgonjwa!” “Hapana bwana, wewe sogea.” Ndipo akajivuta karibu sana naye, akamsikia ameridhika. “Afadhali.” Kisha akamfunika tena vizuri, wakalala.
Japokuwa alikuwa na hofu ya kulala na Sam kitanda kimoja, lakini alifurahia kuwa karibu naye. Ulishapita muda mrefu tokea wawasiliane na kuonana. Alishakuwa na hamu naye. Kwani wakati wote Sam alikuwa mtu mzuri sana kwake.
**********************
Sonia alimuuguza Sam kwa upendo mpaka akapopona. “Umenifanya nichukie kupona, Sonia.” Sonia akatabasamu kwa aibu na kuuliza. “Kwa nini?” “Ulikuwa ukinihudumia vizuri sana. Asante.” “Nimefurahi umepona. Inabidi kesho nirudi nikamsaidie kazi dada. Namuhurumia kumuacha peke yake.” Sam alitulia kwa muda.
Walikuwa wamekaa kitandani wakiangalia tv, siku hiyo jioni. “Daah! Nitabaki mpweke! Na hivi uliacha kupokea simu zangu! Najua ukiondoka hapa ndio basi tena. Sitakusikia tena.” Akakosa chakujibu, akabaki kimya.
“Najua nilikuumiza sana Sonia. Naomba unisamehe.” Sonia akaanyamaza kwa muda, Sam akaanza kuona machozi yakichirizika mashavuni kwa Sonia. “Nisamehe Sonia. Leah alikuza yale maneno. Sikuongea kwa ubaya hata kidogo. Alitaka kujua familia yako. Ndipo nilipomwambia sikufahamu sana, ila namfahamu mama yako na mtoto wako.”
“Akauliza kama umeolewa. Ndipo nilipomwambia sifahamu. Aliendelea kuniulizia kama nilikuuliza juu ya baba wa mtoto wako. Nilimwambia nilikuuliza lakini hukuniambia, kwa kuwa hukuwa hata ukinifahamu vizuri. Isingekuwa rahisi kuwa wazi kwa mtu usiyemfahamu hata kidogo. Naomba unisamehe Sonia. Sikukusudi kukuudhi au kukudhalilisha.” Sonia akafuta machozi. Nakutulia kidogo.
“Sonia Atua Mzigo Mzito, Aliokuwa Ameficha Moyoni.”
“Sio kwamba simfahamu baba wa mtoto wangu. Namfahamu. Lakini siku ile nilishituka sana uliponiuliza. Katika vitu nilivyotamani mama yangu aniulize ni hilo swaliulilokuwa umeniuliza wewe. Lakini tangia niliporudishwa nyumbani kutoka shuleni baada ya kugundulika ni mjanzito, mama hakutaka kuzungumzia hilo swala hata kidogo.”
“Haongei na mimi kabisa, zaidi ya salamu, basi. Nilitamani hata anichape, lakini hajawahi hata kunigusa. Anampenda sana mtoto wangu, lakini urafiki kati yetu umeisha kabisa.” “Baba yako yuko wapi?” “Baba yangu alifariki.” “Pole sana.” Sonia akatulia kidogo.
“Unajua kaka, hata baba yangu mwenyewe simfahamu! Mama aliniambia tu alifariki wakati yupo mjamzito, basi.” “Wazazi wa mama yako wako wapi?” “Mama ni mtu wa Rwanda.” “Ndio maana ni mzuri hivyo!” Sonia akatabasamu nakuinama kwa aibu.
“Kweli Sonia! Una uzuri wa namna yako.” Sonia alianza kufikiria uzuri wa Leah aliyekuwa akiishi naye hapo, alihisi Sam anamdanganya. “Asante.” Sam alibaki akimtizama.
Alipoona anazidi kumtia aibu, akarusha swali jingine. “Unafikiri kwa nini mama hakutaka mzungumzie swala la kupata mimba ukiwa shuleni?” Sonia alibaki kimya kidogo kama anayevuta kumbukumbu.
“Mama alikuwa akijinyima sana ili nisome. Na wakati wote alikuwa akinihusia, hutulia nijiepushe na mambo ya mapenzi mpaka nitakapomaliza shule. Lakini kaka Sam, sikupanga kukatisha masoma, napenda sana shule. Na mimi niliumia sana kukutwa mjamzito.” “Nini kilitokea Sonia?” Sonia akajiweka vizuri na kuamua kumuelezea.
“Nilipofaulu kwenda kidato cha kwanza katika shule hiyo ya bweni ya Ngaza, niliweza kuyamudu vizuri masomo yangu ya shule ya sekondari. Watu wengi walikuwa wakinitegemea shuleni. Alinifuata msichana mmoja aliyekuwa akifahamika sana pale shuleni kwa kuwa kwao walikuwa na uwezo mkubwa wa kifedha. Wanaishi Shinyanga na baba yake anafanya kazi kwenye machimbo ya madini. Aliniomba niwe namfundisha, tukaanza urafiki.”
“Kwa kweli ni msichana mzuri, mwenye maadili mazuri. Tulipenda na kuelewana sana. Wakati wazazi wake walipokuwa wakija kumtembelea shuleni, ilikuwa lazima na mimi nitaitwa. Likizo nyingine, walikuwa wakija kutuchukua tunaenda nao kwao mpaka shule zinapofungua. Walikuwa wakitununulia vitu sawasawa, na kutupa pesa za matumizi sawasawa.”
“Tuliendeleahivyo mpaka kidato cha pili. Ilibidi wazazi wafahamiane tu kwa ukaribu tulio kuwa nao. Yule rafiki yangu alikuwa mtoto wa mwisho kwao na dada zake wote wawili walikuwa nje ya nchi. Kwa hiyo walikuwa wakiishi watatu tu kwenye nyumba yao. Yeye na wazazi wake. Na kila tulipokuwa likizo, tulitafutiwa mwalimu wakutufundisha pale pale nyumbani kwao. Baba yake Fau ni mkali sana. Fau alikuwa haruhusiwi hata kutoka nje ya geti.” Sonia akatulia kidogo.
“Siku moja tukiwa likizo nyumbani kwao, mama yake Fau alipigiwa simu kuna msiba kijijini kwao. Ilimbidi kuondoka na Fau, kwa kuwa baba yake alinyimwa ruhusa kazini, wakisema aliyekuwa amefariki ni ndugu wa mbali kidogo na familia yao.”
“Mama yake Fau aliniuliza kama ningependa kwenda nao, lakini niliwaambia nataka kwenda kumuona mama kidogo, halafu nitarudi. Yule mama aliniambia baba yake Fau atanipa pesa ya matumizi na nauli kwa kuwa walikuwa wanaondoka na gari la pale nyumbani na dereva ambaye wakati wote ndiye aliyekuwa akinirudisha au kuja kunichukua Mwanza, kwa mama.”
“Walipoondoka, nikakaa siku ya kwanza na ya pili bila kupewa pesa. Nikamfuata baba yake Fau siku moja akiwa ametoka kazini yupo sebuleni baada ya kula, nikamwambia nataka kuondoka kesho yake. Tulikuwa tumebaki mimi na yeye tu, yule mama aliyekuwa akisaidia kazi za pale ndali alikuwa ameshaondoka. Alikuwa akija asubuhi na kuondoka jioni. Jumatatu mpaka ijumaa. Jumamosi na jumapili mama yake Fau alisema ni siku anazotaka kuwa na familia yake tu. Kwa hiyo yule mama alikuwa haji kazini.” Sonia akatulia tena kidogo kama anayefikiria kitu.
Kisha akaendelea. “Nilipomwambia yule baba nataka kuondoka kesho yake, alituliakidogo kisha akasema nikachukue mfuko wake wakazini ndani.
Niliuleta, akanipa pesa nyingi sana mpaka nikaogopa. Akaniambia nikaziweke ndani halafu nirudi kuna juisi nzuri amenunua, nikajaribu kuinywa kama nitaipenda.”
“Niliziweka zile pesa, nikatoka, nikakuta ameniwekea ile juisi kwenye glasi. Nikainywa. Haikuwa mbaya sana, lakini sikuwahi kuinywa kabla. Nikarudi kwenye chumba tulichokuwa tunalala mimi na Fau. Wakati nakusanya vitu vyangu naweka kwenye begi, nikaanza kusikia kizunguzungu na hali ya usingizi. Nikaamua kujilaza kitandani. Nilipotelea usingizini bila kujua.” Machozi yalianza kumtoka Sonia.
“Kwa mbali sana kama ndotoni, nilihisi mtu akinivua nguo na kuanza kunipapasa. Nilidhani ni ndoto. Aliendelea kunichezea. Kila nilipojaribu kugeuka mwili ulikuwa mzito sana. Nilipotea usingizini, sijui nililala kwa muda gani. Lakini baadaye usingizi ulipoanza kuisha, nilianza kusikia maumivu makali sana sehemu za siri.”
“Kila nilipojitahidi kugeuka nilishindwa. Hata kufungua macho nilikuwa siwezi, ilinibidi kutulia tu. Baada ya muda tena kidogo nilihisi mtu ananisafisha tena sehemu za siri, na kila nilipojaribu kufungua macho nilishindwa. Nilipitiwa na usingizi tena, bila kujua nililala kwa muda gani. Kwa mbali tena, nilimsikia yule baba akiniambie niamke ninywe dawa ya maumivu.”
“Kwa shida sana, nilijaribu kukaa lakini nilishindwa. Alinikalisha na kuninywesha dawa na juisi kama ile ile aliyonipa kabla. Nilimwambia nasikia baridi sana huku nimefunga macho. Nilipojishika sikuwa na nguo yoyote. Alinijibu nimpe muda kidogo atakuja kunipa joto. Kabla sijaongea kitu kingine nilipotelea usingizini kabisa.”
“Nilikuja kuamka nikiwa nafahamu zangu zote siku ya jumapili tena yeye akiwa amelala pembeni yangu, yupo uchi kabisa. Kwa hiyo tulikuwa mimi na yeye tu. Nilijikuta bado nipo uchi vile vile, huku nikiwa na maumivu makali sana.” “Pole sana Sonia.” Sonia akajifuta achozi.
“Alishituka baada ya mimi kuendelea kulia. Akaniambia ameniwekea dawa ya maumivu pale pembeni ya kitanda. Ninywe nitajisikia vizuri. Lakini niliogopa kunywa tena nisije nikalewa. Nikamkatalia, nikanyanyuka kwa shida huku nikiwa na maumivu makali sana na kwenda kuoga. Yeye bado alikuwa amelala kitandani bila hata wasiwasi.”
“Nikamuuliza kwa nini amefanya hivyo? Alianza kucheka, nakuniambia kwanza natakiwa kumshukuru yeye, kwa kuwa nimepata bahati ambayo watu wengi wanaililia. Yeye alisema huwa halali na kila mwanamke. Kwa hiyo uamuzi ni wangu, kuendelea naye na atanipa kila kitu ninachotaka hata nyumba atatujengea mimi na mama yangu, tuache kuishi maisha duni, au niendelee kuchezea bahati. Nilimwambia yeye ni kama baba yangu siwezi kumfanya mpenzi wangu.”
“Alinibembeleza sana na kuniambia nachezea bahati. Yeye anapesa nyingi sana, atanipa maisha mazuri mimi na mama yangu. Alipoona nimemkatalia kabisa, alibadilika sura nakuanza kunitukana. Alisema niache
kabisa kusema yeye ni kama baba yangu, kwani mimi siwezi kuwa na baba mwenye pesa kama yeye, na aliniambia ule ndio mwisho wakukanyaga ule mkoa wa Shinyanga na wala nisimtafute mtoto wake tena.”
“Aliniambia endapo nitasema chochote juu ya lile tukio sitakaa nimuone tena mama yangu. Atampeleka mama polisi kwa kosa la kuishi hapa Tanzania pasipo halali, kwa kuwa mama ni mtu wa Rwanda. Yeye ana pesa nyingi, anaweza kutufanya chochote na tukapotea katika hii dunia kabisa tusiwahi kuonekana tena.”
“Alitaka kunishika tena kwa nguvu, nilikimbia nje. Alipotoka chumbani, nilirudi nikachukua vitu vyangu, nikachomoa pesa baadhi ambazo nilijua zingetosha nauli yangu tu, nikamuachia pesa zote alizokuwa amenipa, nikaondoka. Hiyo ilikuwa likizo ya katikati ya mwaka.” “Pole sana Sonia. Pole.” Sonia akatulia.
“Nilirudi nyumbani, sikutaka kumwambia mama kabisa. Niliendelea na maisha kama kawaida huku nikiwa nakunywa dawa za maumivu kama kawaida. Maumivu yaliisha, na shule zilipofungua, nilirudi shuleni kama kawaida. Fau hakurudi tena shuleni na wala hatukuwasiliana tena. Nilisikia amehamishwa shule.”
“Hatukukaa muda mrefu, kama kawaida ya shuleni, kila mnapofungua shule mnapimwa mimba. Wala sikujua kama nilishika mimba siku ile, japokuwa nilishaanza kusikia mabadiliko kwenye mwili wangu, lakini sikuwa hata na wazo la ujauzito! Nilishtuka sana nesi aliponiambia nina mimba.”
“Basi, niliambiwa nikusanye vitu vyangu vyote, nikarudishwa nyumbani. Mama alipoambiwa na yule mwalimu aliyenirudisha nyumbani, alishituka sana. Alishindwa kusema chochote hata kwa yule mwalimu mpaka alipoaga nakutuacha mimi na mama peke yetu. Nilitegemea labda angeniuliza, lakini hakuniuliza. Na mimi nilikuwa nimechanganyikiwa sana sikujua chakufanya.”
“Siku hiyo nilipoteza shule, na mama yangu ambaye alikuwa ndio rafiki yangu mkubwa na msiri wangu. Najua aliona nimemsaliti au nimekuwa nikimdanganya wakati wote, kuna mambo nilikuwa nafanya kwa siri bila yeye kujua. Lakini kaka, hata angeuliza, nisingethubutu kumtaja yule baba. Sikutaka kumuingiza mama yangu kwenye matatizo.”
“Niliogopa wakimfunga jela na mimi sina ndugu yeyote isipokuwa mama yangu! Nilikubali kubeba ile aibu na uchungu moyoni, ilimradi tu niishi na mama yangu. Hatukuwa na uwezo sana, lakini mama alihakikisha ninaishi maisha mazuri.”
“Pale mtaani nilikuwa msichana wa kutolewa mfano katika kila kitu. Alijitahidi sana kunipa kila ninachotaka, kwa kadiri ya uwezo wake. Tulikuwa tukilala wote, yaani kitanda kimoja. Tulikuwa tukiongea na kucheka karibu usiku kucha. Lakini yote hayo yameisha kabisa. Zaidi ya salamu na kunijibu kwa kifupi sana nikimuuliza kitu, tena akiamua kujibu ndipo atajibu, vinginevyo huwezi kumuona anakaa na mimi tena anaongea hata kidogo.”
“Anampenda mtoto wangu, huwezi kujua kama ni wangu. Mimi na mwanangu wote tunamwita mama. Hata mwanangu hajui kama mimi ni mama yake. Na huo ndio ukawa mwisho wa shule yangu na mahusiano na mama yangu na sijawahi kumwambia mtu yeyote, wewe ndio mtu wa kwanza.” Sam aliumia sana. “Pole sana Sonia.” Sonia akabaki akijifuta machozi yaliyokuwa yakitoka kila alipokuwa akisimulia kisa chake.
“Nilirudi mtaani maisha yakaanza kuwa mabaya sana, kwani mama ambaye alikuwa ndio mtafutaji, alianza kuugua ugua. Biashara zake zikafa, tukaishia na ile biashara ya Mama Lishe. Ambayo wenzetu wote walikuwa wakiuza isipokuwa sisi. Tulikuwa kama tumeingiwa mkosi! Kila siku tunamwaga vyakula wakati wenzetu walikuwa mpaka wanabakisha wateja.”
“Daah! Pole sana Sonia. Pole.” “Asante kaka. Kwa hiyo sio kwamba nilikuwa na wanaume wengi kaka yangu. Naomba usinielewe vibaya. Sikuwahi hata kuwa na mahusiano ya kimapenzi na mwanaume yeyote yule. Nilikuwa na malengo makubwa sana, lakini yote yamezimika mbele ya macho yangu.” Sonia akazidi kulia kwa uchungu sana.
“Sikuwahi kukufikiria vibaya Sonia. Na wala usikate tamaa, wewe bado mdogo sana. Bado una muda wakutimiza ndoto zako.” “Sidhani kaka.” “Kweli Sonia. Usikate tamaa.” Sam akamvuta mkono, nakumsogeza karibu yake baada yakuona anazidi kulia. Alizungusha mkono wake juu ya mabega yake na kubaki akimwangalia huku akimpangusa machozi. “Pole sana Sonia. Pole.” Walikaa hivyo kwa muda wakibembelezana.
**********************
“Hivi unajua Sonia, hujafika hata nusu ya maisha yako? Huna sababu yakukata tamaa. Kila kitu kitakuwa sawa.” “Ningumu sana sasa hivi kujifikiria tena mwenyewe wakati tayari nina jukumu la mtoto. Kwa uwezo mdogo nilio nao natamani sana kumpa mtoto wangu yale yote niliyokosa mimi.” “Yote yataenda pamoja, wala usiwe na wasiwasi. Kwanza Kana ameshaanza shule.” Sonia alishituka sana.
“Umejuaje?” Sam akacheka kidogo. “Nilipoenda kuwasalimia kule Mwanza yeye na mama, nilipata muda kidogo wakukaa pale nyumbani kwenu, nikatoka kucheza na Kana. Sikupenda watoto wanao mzunguka. Kana ni mtoto mzuri sana, niliona akiendelea kukaa tu pale mtaani wataharibu tabia yake. Nikajaribu kukupigia simu ili nikuulize kama ni sawa aanze shule, lakini hukupokea simu zangu kabisa.” Aibu!
“Samahani kaka.” “Nilielewa Sonia. G akanisaidia kutafuta shule nzuri, tukamuanzisha shule na anafuatwa na kurudishwa na basi la shule nyumbani.
Huwa nawasiliana na mwalimu wake, anamsifia sana Kana. Anasema ni mtoto mtulivu sana, na ana uwezo mkubwa sana wa masomo. Kwa muda mfupi tu aliojiunga na shule, tayari amejua mambo mengi sana.” Sonia alikuwa akitokwa na machozi ya furaha haamini.
Hakuwa akiamini kinachotokea. Aliinama nakuendelea kulia sana. “Usilie bwana Sonia. Kila kitu kitakuwa sawa.” Baada ya muda alimgeukia tena Sam. “Asante sana Kaka.Sijui niseme nini! Nakushukuru.” Sam akatabasamu. “Si unaona kila kitu kinavyoenda? Nimekwambia yote yataenda kwa pamoja.” “Najua maisha yangu yameshafika mwisho, lakini maadamu mtoto wangu anasoma, basi inatosha. Nimefurahi sana kaka. Asante sana”
“Kwa nini unasema hivyo Sonia, wakati bado wewe ni mdogo sana?” Sonia alibaki akiwaza na kuona ugumu unao mkabili katika maisha yake. Kurudi tena shule, inamaana aache kazi kwa mama Briana, kwa hiyo atapoteza ajira na watu aliowapata wa kwanza katika maisha yake, wanao onekana kumjali na kumpenda sana. Akakwama.
“Najua una maswali mengi sana, ya itakuwaje? Lakini usijali. Kila kitu kitakuwa sawa.” Sonia alinyanyua uso nakumuangalia Sam jinsi anavyoongea kwa uhakika. Sam naye alimtazama huku anatabasamu. “Najua huamini, lakini ujue kila kitu kitakuwa sawa.” Sonia akarudisha uso wake chini. Kila mmoja alibaki akiwaza lake.
“Kaka Sam?” Sonia alimtoa Sam kutoka kwenye mawazo. “Naam!” “Kesho utanirudisha kwa dada saa ngapi?” “Naomba uondoke kesho kutwa. Nataka leo nimpigie simu Nyange akafuate familia yake. Ukiwepo pale watashindwa kuongea. Heri wapate muda wa kutosha wakiwa wenyewe, ili wazungumze mpaka watakapofikia muafaka.”
“Mama Briana ni mtu mzuri sana, hawezi kuishia kwenye nyumba kama ile. Na ninamjua Nyange, anampenda sana mkewe, sijui alikosea wapi!”
“Halafu pia mama Briana anategemewa sana, si na mumewe tu, hata upande wa mumewe wanamtegemea sana. Baba mkwe wake anampenda na kumthamini sana. Hakuna kinachoendelea kwenye ule ukoo bila mama Briana. Huwa anamwita mwenye Boma. Nyange ndio mtoto wa kiume mkubwa nafikiri na wa pekee kwenye ukoo wao, ni kama watoto wa kike ndio wengi sana pale, kwa hiyo yule Mzee anasemaga mama Bree ndio muendeleza ukoo.”
“Yule Junior alikuwa akisubiriwa na ukoo mzima. Yule Mzee akija kujua aliyoyafanya baba Bree, hapatakalika hata kidogo. Yule Mzee hali wala kunywa kitu chochote akifika pale kwao, kama mama Briana hajaandaa yeye au hayupo.”
“Ni mkorofi sana, hata baba Bree mwenyewe anamuogopa, lakini ukimuona anavyoongea na mama Bree, utashangaa. Tulisha kwenda kijijini kwa kina Nyange, mimi mwenyewe nilishindwa kuelewa.”
“Kiliitishwa kikao, jioni ileile na kuambiwa Mwenye mji amefika, yaani mama Bree, heshima alizokuwa akipewa yule dada, hujawahi ona.” “Jamani! Lakini hata hivyo dada ni mtu mzuri sana, anapendeka. Umefikiria vizuri kumwambia baba Briana.” Sam akatabasamu.
“Halafu kesho nataka nikuzungushe mjini, ili na wewe ulione jiji la Dar. Huwezi jua Sonia, unaweza pata mchumba.” Sonia aliinama kwa aibu. “Mmmh! Nani atamkubali mtu mwenye mtoto kama mimi?” “Ndio unavyojidanganya hivyo?” Sonia akabaki kimya.
“Mtoto hawezi kuzuia mapenzi ya kweli, Sonia. Mtu akikupenda wewe, atampenda na Kana.” Sonia hakutaka kujibu kitu. Kwani alishajua maisha yake yameshakwisha. Alijiaminisha kuwa hakuna mwanaume atakayemfuata yeye na kuacha wasichana wadogo tena wazuri.
Zaidi Ya Kutamka.
“Nyange?” Simu ya Nyange iliita mara moja tu, akapokea. “Vipi Sam?” “Ulishajua mama Briana alipo?” “Daah! Nimemtafuta karibia nachanganyikiwa ndugu yangu. Wewe unajua alipo?” “Ndiyo.” “Naomba niambie Sam, tafadhali.” “Nitakwambia, lakini safari hii ukija kumuumiza tena mama Briana, nakuahidi Nyange utapambana na mimi.” “Samahani sana Sam, najua nimekuumiza sana.”
“Hukuniumiza mimi sababu ya kuwa na mahusiano na Leah hata kidogo. Umenipunguzia matatizo makubwa sana hapa duniani. Lakini nakushangaa sana Nyange!Umekosa nini kwa mama Bree, wewe? Shida yako nini?” “Leah alinishawishi.”
“Nakushauri usiende na hiyo sababu ya kitoto kwa mkeo.” “Samahani Sam. Nilikosa sana.” “Huo ndio uwanaume sasa. Acha kukimbia majukumu yako Nyange.” Baada ya Sam kumsema sana alimuelekeza alipo mama Briana.
“Asante sana Sam.” “Sifanyi kwa ajili yako hata kidogo Nyange. Ni kwa ajili yaBriana na mama yake.” “Hata hivyo nakushukuru.” Sam akakata simu.
**********************
Nyange hakutaka kusubiri mpaka kesho yake. Usiku huohuo akatoka mpaka kwa mama Briana. Aliumia sana kuona kajumba alichochukuwa akiishi mkewe. Aligonga kwa muda ndipo alipoona taa ya ndani ikiwashwa.
Mlango ukafunguliwa, mama Briana akabaki mlangoni amesimama baada yakumuona Nyange. “Samahani kwa kukuamsha.” Mama Briana akabaki kimya. “Naweza kuingia ndani?” Nyange akauliza kinyenyekevu, bila yakusema kitu mama Briana akampisha mlangoni. Alimuona jinsi Nyange alivyokaukwa mdomo na kuchoka, huruma ikamuingia gafla.
“Kuna chakula kidogo, tumebakisha. Nikupashie moto ule?” Mama Briana akauliza kwa kujali. “Nitashukuru. Njaa inauma kweli!” Akamuandalia chakula nakuvuta stuli pembeni yake. “Karibu.” “Asante.” Nyange alikula chakula chote, ukweli alionekana na njaa. Akaondoa vyomba na kurudi kukaa kochi la pembeni ya mumewe kwa unyonge sana.
**********************
“Unakumbuka siku ile ulinikuta pale ofisini na yule msichana?”Mama Briana hakumjibu. “Yule dada alikuwa mchumba wangu wazamani, tulikubaliana kuona lakini kwao walitufukuza na wazazi siku tulipoenda kulipa mahari.” Mama Briana akakunja uso.
“Tulipotezana kwa muda mrefu sana, mpaka siku ile alipokuja pale ofisini kibiashara. Sekretari alimleta ofisini kwangu, ndipo tulipoonana kwa mara nyingine tena, baada ya miaka mingi sana. Alishituka sana kuniona pale kama mmiliki na sio mwajiriwa, kwani tuliachana nikiwa duni sana kama vile ulivyonikuta wewe.” Mama Briana akainama kinyonge.
“Ukweli tulikuwa tukielewana sana na yule dada, lakini kwao ndio walinikataa mimi sababu ya uwezo. Alifurahi sana kuniona akaniambia bado hajaolewa anaomba turudiane, na tuoane. Nilimwambia nimeoa na ninampenda sana mke wangu. Alianza kunikumbusha mambo mengi sana tuliyokuwa tukifanya zamani, lakini nilimwambia nilishafunga huo ukurasa, na sina hisia zozote za kimapenzi juu yake tena.”
“Alianza kunibishia na kuniambia kuna mambo alikuwa akinifanyia hata kama nimechoka sana, nilikuwa nahamasika. Nikamwambia ilikuwa wakati huo, sio sasa. Nilimwambia nimepata mwanamke ninayempenda sana na siwezi kurudi nyuma. Hakuamini, alisimama nakuanza kunibusu na kunishikashika, alipoona nimesimama tu nikimwangalia hakuamini. Nikamwambia niliyokuwa nimemwambia ni kweli, sina hisia zozote za kimapenzi kwake ila kwa mke wangu tu.”
“Pale ulipotukuta alitaka kurudia tena kufanya vile na alitaka hata kushika suruali yangu. Ndio tukaanza kusukumana. Sikumgusa kabisa yule dada, zaidi yakumsukuma, na Mungu wangu ni shahidi, Penninah. Naomba uniamini katika hili. Nakiri kosa nililolifanya, nikumruhusu anishike mara ya kwanza.” Mama Briana alibaki kimya tu.
“Na kuhusu Leah. Unakumbuka kipindi kile ulienda Canada kwa miezi sita?” Mama Briana hakujibu kitu. “Tukiwa tunakula siku moja na Leah, niliropoka, nikamwambia nina hamu sana na mke wangu. Akirudi nitamchukua niende naye tukajifungie mahali hata mwezi. Alicheka, halafu akasema mimi naweza kukusaidia. Sikutilia maanani nilijua ni mambo ya Leah.”
“Wakati nimelala usiku nikasikia mtu ananipapasa. Kushituka nikamuona ni Leah, tena yupo uchi kabisa. Nilishindwa kujizuia mama Briana, hali yangu ilikuwa mbaya sana. Naomba unisamehe na ndio ilikuwa mara hiyo tu tulipofanyia pale chumbani.” “Kwa nini uliendelea niliporudi?” Mama Briana akauliza huku machozi yakimtoka, Nyange akashindwa kujitetea.
“Unajua Nyange, kila nikifikiria hata nikisema leo tunarudiana, sina kitu nilichobakiza kukupa wewe. Nimekupa kila kitu kwenye maisha yangu. Na bado hukuridhika na mimi, ukanizunguka. Tena kwa mdogo wangu! Najiuliza kwa nini mlinifuata mimi mwanzoni, wakati bado mnapendana, sipati jibu! Mnaniadhibu bila kosaNyange!”
“Wewe umekuwa sababu ya mimi kudharauliwa na kutukanwa na Leah kila mahali! Wewe mwenyewe ulinifuata, nikakuuliza maswali mengi kabla yakufunga ndoa, ukasemaumeridhika na mimi. Kwa nini leo unanifanyia unyama wa kiasi hiki?”
“Niamini nikikwambia nakupenda mke wangu. Nakupenda Penninah. Hata Leah anajua hilo. Na nilishakatiza mahusiano naye kabisa, kwanza yalikuwa ni mateso tu, huwezi amini. Nilimwambia nasikia vibaya jinsi tunavyo kufanyia wakati wewe unanipenda kwa dhati. Nilishamkataa Leah kabisa, Mungu nishahidi. Nilisitisha yale mahusiano, niliamua kutulia.” Mama Briana aliendelea kulia taratibu.
“Nisamehe Penninah mke wangu. Nakuhakikishia hizo tabia chafu nimeacha, tena sio kwa kufumaniwa, niliamua mimi mwenyewe mpenzi wangu. Nakuahidi haitakaa itokee tena, mama Briana. Nakupigia magoti mke wangu nimekosa. Naomba unisamehe na urudi nyumbani. Kwanza ile nyumba ni yako Penninah. Isingekuwa wewe nisingekuwa hapa nilipo. Jeuri yangu yote ni wewe mpenzi wangu. Ukiniacha nitaenda wapi?” Wakati baba Briana anaomboleza Briana akaamka.
Alifurahi sana kumuona baba yake. Alimrukia na kumkumbatia palepale alipokuwa amepiga magoti. Kila alipojaribu kumuweka chini Briana ili aendelee kuomba msamaha, Briana alikataa kushuka. Nyange alirudi kukaa huku amembeba mwanaye. Mama Briana bado alikuwa akilia sana.
Mwishoe akamuonea huruma mtoto wake. Alijua nikiasi gani Nyange na Briana walivyo karibu na Briana alimpenda sana baba yake kuliko hata yeye.
“Rudi nyumbani mpenzi wangu. Nakuahidi kila kitu kitakuwa sawa.” Mama Briana aliendelea kuwaza hukuakilia. “Nimempoteza Junior.” Mama Briana aliongea kwa uchungu sana na kuzidi kulia. “Nilikuwa namsubiri kwa hamu sana mwanangu.”Nyange na yeye akaanza kutokwa na machozi. Hakuna aliyeweza kumbembeleza tena mwenzake.
Nyange na yeye alishatangaza ujio wa Junior kila mahali. Kila mtu alikuwa akimwambia, ‘Dume la ukoo linakuja.’ Au ‘Nyange mwenyewe anakuja.’ Chumba cha Junior kilijazwa vitu vya thamani sana. Waliendelea kulia kwa muda, mwishowe mama Briana akasimama na kwenda chumbani akilia.
Nyange alikaa hapo akitokwa na machozi huku akimbembeleza Briana mpaka alipolala. Akamlaza kwenye kochi na kumfuata mkewe chumbani.
“Pole mke wangu. Najua nimechangia kifo cha mtoto wetu. Natubukwako na mbele za Mungu nimekosa. Naomba unisamehe.” Mama Briana akamshika mkono mumewe huku akiendelea kulia. Nyange akamnyanyua na kumkumbatia mkewe. Walibaki wamekumbatiana kwa muda mpaka Mama Briana alipotulia.
**********************
Nyange hakupoteza muda, palepale alianza kumparamia mkewe kwa hamu kubwa sana. Akamng’ang’ania bila kumuachia kwa muda mrefu sana mpaka alipoona wote wameridhika. “Nyange wewe! Mtoto angeingia?” “Nilikuwa na hali mbaya Mama Briana! Uliniogopesha sana ulipoondoka. Sikujua kama nitakuja kukuona tena!”
“Kila wakati kuna sauti ilikuwa ikiniambia hutakaa unisamehe. Hofu ya kukupoteza wewe na Briana iliniingia kweli.” “Pole. Lakini uliniudhi sana Nyange. Umenidhalilishavibaya sana.” “Nisamehe. Najuta sana, lakini basi tena. Nilishafanya. Nakuahidi kutorudia tena. Safari hii hata ukisafiri mwaka mzima. Nitakusubiri mpenzi wangu.” Mama Briana akaanza kuchukia kazi yake. Kama wanawake wengi, akaanza kujilaumu kumwingiza mumewe vishawishini.
Walibaki wamekumbatiana hapo kitanda kwa muda. “Naomba turudi nyumbani.” “Naomba utangulie, sisi tutarudi kesho. Lazima kufungasha.” Nyange akaanza kuzungusha macho. “Mbona sioni cha kubeba hapa? Twende bwana, kesho tutarudi wote nikusaidie kama kuna kitu utakihitaji. Siwezi kuondoka bila wewe. Kile chumba kinatisha ukiwa peke yako.” Mama Briana alianza kucheka.
“Kweli. Nahivi umeondoka na kipenzi changu! Basi ndio kunazidi kupwaya.” “Pole Nyange.” “Tena nahitaji pole kubwa. Unajua Mzee Nyange na mkewe walikuja pale nyumbani?” Mama Briana alivuta shuka nakujifunga vizuri, akakaa.
“Mungu wangu Nyange! Nilisahau swala la wazazi. Ikawaje?” “Hutaki kujua. Si unamjua lakini yule Mzee? Kwanza ulipoondoka tu, kama walijua, walianza kunipigia simu, nikajua tu ni kwa kuwa hawakupati. Nilikuwa nazunguka mjini kama nimechanganyikiwa, maana nilijua ambavyo sipokei simu zao, na wewe hawakupati, angekuja mwenyewe. Kwani hata week iliisha? Nikashitukia wapo sebuleni na mke wake. Ungenionea huruma!”
“Nimelaaniwa, na kupigwa marufuku nisikanyage kijijini bila wewe hata nikisikia kafa, nisiende kumzika kama sijakurudisha nyumbani.” “Haiwezekani Nyange! Kwani uliwaambia kila kitu?” “Sikuthubutu. Angefungua kile kisu chake cha bakora yake anichome nife. Si unamjua anavyo nichukia yule Mzee? Utafikiri mimi sio mwanae, nashukuru Mungu tumefanana mpaka kucha.” Mama Briana alianza kucheka.
“Nakwambia kweli, hakunywa hata maji, akaondoka jioni ileile. Haya nikawatumia ile pesa uliyokuwa ukiwatumia wewe kila mwezi. Nakwambia Mzee alivyokuwa mkorofi yule, alipogundundua mimi ndiye nimetuma, alimtuma mtu azirudishe na maonyo kibao na laana juu.” Mama Briana alizidi kucheka.
“Mi nakwambia pale baba ninaye! Sijui ana matatizo gani na mimi yule! Na akija kujua ukweli, nahisi atanizika nikiwa hai. Naomba tu, turudi nyumbani Penninah, halafu tupange safari ya kijijini akakuone, haya mambo yaishe.” “Pole Nyange. Na mimi nina hamu nao kweli! Mama aliomba uzazi wa Junior yeye ndio atuhudumie. Si unakumbuka alitaka nikajifungulie kijiji?”
“Hapo ndipo tuliposhindwana nao, niliwakatalia kabisa. Mwenyewe nilikuwa nimeshapanga ratiba zangu na mtoto wangu, ni hivyo yametokea yakutokea, basi tena.” Nyange aliongea kwa uchungu sana huku akifikiria. “Pole Nyange, yamepita.” Mama Briana akarudi kulala pembeni ya mumewe wote wakiwa na mawazo.
“Asante Penninah kwa kunisamehe.” “Nilikuwa nakumbuka fujo zako Nyange, nilikuwa siamini kama ndio umefika mwisho wetu! Unajua wewe ndio faraja yangu?” “Yaani, ulikuwa unakumbuka fujo zangu tu?” Nyange akamvuta tena mkewe huku akimfunua taratibu na kumbusu.
“Siwezi kukubali mwisho wa kijinga vile Penninah, nakupenda sana mpenzi wangu.” Kwa mara nyingine tena, Nyange na mkewe waliendeleza mapenzi kwenye kijumba hicho bila yakujali muda.
Furaha ya mama Briana ikarejea usiku uleule bila yakutarajia. Nyange alijua kucheza na akili za mkewe na mwili wake pia. Hakuna jinsi mkewe alikataa penzi la mumewe. Hata alipokuwa amechoka, alipomgusa tu, mkewe alichangamka akijua raha atakayoipata wakati huo, kutoka kwa mumewe. Alipenda na kufurahia penzi la mumewe, na Nyange alijua dawa ya mkewe ni pale anapofanya naye mapenzi. Kwa hiyo ni silaha aliyoitumia kila alipoweza, ili kumuweka sawa na kumtuliza.
Alichokiunganisha Mungu,…
Asubuhi waliongozana mpaka nyumbani kwao. “Tena huyu aondoke kabisa huku chumbani kwetu. Anatunyima uhuru.” “Umeanza kumlalamikia mtoto, baba Briana. Jana umemlaza mtoto kwenye makochi!” “Na leo akacheze na Josh huko nje, atuachie nafasi.” “Nyange!?” “Sasa je? Nataka leo tukae tu humu chumbani, mimi na wewe tu. Kwanza Sonia yuko wapi?” “Nilimpeleka kwa Sam, alikuwa anaumwa sana na yuko peke yake.”
“Unajua Sam ndiye aliyeniambia mlipo?” “Nilijua tu. Maana alikuwa akinilazimisha sana nirudi nyumbani.” “Nimefurahi umerudi Peninnah! Nilichanganyikiwa mwenzako.” “Mimi nilijua ndio utafurahi ili uowe tena!”
“Acha masihara! Nampata wapi mwanamke kama wewe? Nakwambia niliamua kutulia mwenyewe kabla ya ule mkasa. Hujui nikiasi gani nilivyokuwa nikisutwa na dhamira kila nilipokuwa na fanya yale madudu. Kila nikikukumbuka, unavyoniaga kwa upendo na kunipokea vizuri nikiwa narudi, nilikuwa naumia sana.”
“Nilishamwambiaga mara nyingi sana Leah tuachane lakini alikataa. Akaanza kunitishia atakwambia kama nikisitisha mahusiano. Sasa safari hii nilimuweza nikamwambia akikwambia hati niliyonunulia kile kiwanja chao sitampa.” Mama Briana akakunja uso.
“Kile kiwanja umenunua wewe?” Nyange akaanza kutetemeka, hakujua alichosema. Aliropoka tu. “Mwanzoni kabisa mwenye kiwanja aliwakubalia kupokea pesa kidogo kwa masharti ya kumalizia baada ya miezi mitatu. Sasa waliposhindwa kulipa kwa wakati, mwenye kiwanja akakitangaza kukiuza, ndio nikaenda kukinunua mimi. Nikamwambia watakaponilipa pesa yote, ndio nitawapa hati.”
“Hata hivyo mama Briana, acha niwe mkweli tu. Asilimia sabini ya ile nyumba nimejenga mimi.” “Ndio maana nilikuwa najiuliza, Leah anatoa wapi pesa yakujenga jumba lote lile? Kila nikimuuliza ananiambia wanachanga yeye na Sam, mara amechukua mkopo benki, lakini hakusema kitu cha maana. Hongera.” “Na unipe hongera kweli, maana nachukua nyumba yangu.” Mama Briana hakuamini.
“Nyange!” “Kumbe! Aliyonitendea ni madogo? Nilimuomba sana atulie, lakini aliamua kufanya fujo. Na pengine isingekuwa, yeye ningekuwa na Junior sasa hivi. Hapa nawaza kitu cha kumwambia mzee Nyange. Akija kujua ukweli, nahisi atanivulia nguo.” “Kwa kuwa yameisha, naona hamna haja yakumwambia baba kila kitu.”
“Wewe unamjua alivyomkorofi yule, hadanganyiki, na alikuwa akimsubiria Junior kwa hamu kweli! Sijui nafanyaje! Wazee wenzake wote pale kijijini wanamjua Junior. Nimeharibu kweli!” Mama Briana akabaki kimya.
“Itabidi tupange safari nikupeleke kama alivyosema.” “Samahani Nyange, najua nimekutia matatizoni kweli. Lakini nilichanganyikiwa mume wangu. Nikasahau wazazi kabisa.” “Sio kosa lako Penninah, nimeharibu mimi mwenyewe. Najua baba ataumiasana.” “Nashauri tusimwambie kila kitu.” Nyange akabaki kimya.
**********************
Mama Briana akavuta simu yake nakumtumia ujumbe Sam. ‘Nakushukuru shemeji yangu. Sasa hivi nipo kwangu.’ ‘Hayo ndiyo maneno. Nina ombi, moja shemeji yangu.’ ‘Nini tena?’ ‘Naomba niachie Sonia mpaka kesho kutwa, nitamrudisha.’ ‘Nilikwambia usimzoee.’ ‘Nitamleta bwana!’ Mama Briana akacheka nakujibu. ‘Kesho kutwa asubuhi awe hapa Sam.’ ‘Asante.’ Mama Briana akabaki na tabasamu usoni.
**********************
“Nini?” Nyange akauliza. “Naona Sam kanogewa na Sonia hataki kumrudisha.” “Mwache kidogo, kama shukurani yetu kwake. Amenirudishia wewe na Briana! Mwachie tu huyo Sonia, nitazifanya mimi hizo kazi zake.” Mama Briana alianza kucheka.
“Kweli nilikuweza. Ujanja wote umekuisha Nyange. Mpaka umekonda!” “We acha tu. Ujanja huu kwa kuwa wewe upo, mama Briana. Unafikiri nimejisahau hali uliyonikuta nayo? Najikumbuka vizuri sana. Ulinitoa chini kweli, mpaka sasa hivi wananijua mjini, kwa ajili yako. Sina jeuri mwenzio.” Mama Briana akajivuta karibu na alipolala mumewe.
**********************
“Unajua sikuwa nimekwambia habari za Mary.” “Mary?” “Yule uliyenikuta naye siku ile ofisini.” “Nini tena?” “Unajua tulitaka kufunga naye ndoa, nikamwambia nataka nikalipe mahari, nikamuuliza kama kwao watakuwa na kipingamizi, akaniambia hakutakuwa na shida kabisa, niende.”
“Nikaenda kumwambia mzee Nyange, akafurahi kweli. Si unamjua mambo yake ya ukoloni? Kakusanya wazee wenzake wakaja mjini, nikamwambia Mary wazee wamefika, je nyumbani wanataarifa? Akaniambia ndiyo, tena baba yake ameshaalika wazee wenzake pale kwao, ili kuja kupokea mahari.”
“Muda ukafika, nikakodisha kidaladala, mzee Nyange na mahari yake mkononi na wazee wenzake, mpaka nyumbani kwa kina Mary. Wasiwasi uliniingia baada yakufika hapo kwao, bonge la jumba, magari niliyoyakuta hapo nje, jasho lilianza kunitoka.”
“Tukakaribishwa humo ndani, wote jasho lilikuwa linatutoka. Maana hao wazee tuliowakuta humo ndani na wake zao, sio mchezo. Baba akajitambulisha, nakueleza kilichotupeleka. Huwezi amini Penninah.” “Nini?”
“Sijawahi kudhalilika maishani kama siku ile. Yule Mzee alianza kutukana kwa kingereza na kiswahili, huku amechachamaa kweli kweli! Tulifukuzwa kama mbwa.” “Nyange wewe! Alisemaje?” “Alimtukana sana mzee Nyange, akamwambia wakati yeye anahangaika kumsomesha binti yake, yeye mzee Nyange alikuwa akinywa pombe, sasa hivi ndio anataka tuponee kwa mwanae!”
“Aliomba tutoe daladala yetu kwenye nyumba yake, akatupa dakika tano tu, lasivyo litakalo tupata tusimlaumu. Hakutania bwana, aliamuru walinzi kufungulia mbwa, tena mambwa yenyewe yalitoka urefu wa Josh, tulikuwa tunapanda kwenye daladala yetu huku tunatetemeka maana walinzi walikuwa wameshikilia mbwa. Mama alianguka, akaumia. Hivi anaalama mpaka leo.” “Pole sana Nyange. Pole.” Nyange akatabasamu kwa huzuni.
“Haya, nikatulia baada ya muda nikamuona tena Leah. Nilipomtongoza Leah mwanzoni, alinidhalilisha kweli mbele za watu pale ofisini. Jamaa mmoja akamfuata nakumwambia alichofanya sio kitu kizuri. Angenikataa kistaarabu tu. Sio kunibeza na kunichambua mbele za watu.”
“Si unakumbuka kazi yangu ya wakati ule? Leah alitangaza mshahara wangu kwa kila mtu, tena haukuwa na tofauti sana na mesenja wa pale ofisini, basi nikawa kichekeshokwa marafiki zake wote. Baada ya kusemwa sana na yule Jamaa, Leah alinifuata na kuniomba msamaha, ndipo akasema yupo dada yake ataniunganisha naye.”
“Nikamuomba picha yako kwanza kabla hajatukutanisha. Kila mtu pale ofisini alianza kunicheka na kuniambia nisidanganywe na Leah hata kidogo, wewe huwezi kunikubali hata iweje. Yule Jamaa akanifuata tena akaniambia Leah ananidanganya nisikubali hata kukutafuta, kwa kuwa wewe ulikuwa mzuri kuliko Leah mwenyewe. ‘Sasa kama Leah kakukataa na kukudhalilisha hivi! Huyu atakufanyaje?’ Aliendelea kunishawishi.”
“Kidogo hofu iliniingia, huku nikikumbuka mkasa wa Mary. Kwa kuwa Leah alishanipa namba yako baada ya week moja nikaamua kukutafuta kwa kukutumia ujumbe kwanza. Pale mwenzio nilikuwa najaribisha tu. Ulipoomba tukutane nilikaribia kuchanganyikiwa.”
“Yule Jamaa alinicheka sana. Akaniambia nikudanganye nimesafiri ili tuendelee kuwasiliana kwa muda mrefu kwa ujumbe tu, mpaka utakapokolea. Akaniambia nikiharakisha kukuona, unaweza kunikataa kwa jinsi nilivyokuwa nikionekana nimechoka. Lakini ukaniambia unasafiri kwa muda mrefu kidogo, ungependa tuonane kabla hujaondoka. Nilikaribia kuchanganyikiwa.”
“Lakini nikajiambia ni heri nijaribu tu, usije ukapata mwanaume mwingine ukiwa safarini, ukaamua kuolewa, nikajutia zaidi. Nikajitia moyo kuja kukuona nakujiambia sina cha kupoteza, ukinikubali itakuwa bahati yangu, ukinikataa nitakuwa huru kuliko kuendelea kujidanganya na kuishi na wasiwasi.” Nyange alifikiria kidogo na kutabasamu tena.
“Kilichonishangaza ni jinsi ulivyoniona na wala hukuonyesha kunishangaa, wakati mimi nilikaribia kuaga kwa kuwa nilishajua jibu langu. Ulionekana mzuri kuliko kwenye picha. Nyumba yako ilikuwa safi na ulionekana unajielewa zaidi ya Leah. Nilianza kujilaumu sana kwa nini sikumsikiliza yule Jamaa.”
“Lakini ukanikaribisha vizuri sana tena kwa heshima. Kidogo nikatulia. Nakumbuka ulinikaribisha kinywaji nakuniambia ulinitayarishia chakula.” Nyange alicheka kidogo.
“Kidogo ile hali ya uwanaume ikaanza kunirudia. Ujasiri ukaongezeka baada ya kuona unanihudumia kwa heshima kama mwanaume mwenye pesa! Ndipo nikapata nguvu ya kukuuliza maswali taratibu huku nikikusoma. Nilitoka pale nikiwa nimejawa na furaha kupita kiasi, na unakumbuka uliniomba kama tungeonana tena kabla hujasafiri?” Mama Briana akacheka taratibu akivuta kumbukumbu.
“Nilitoka pale kama mwehu! Moja kwa moja nilienda nyumbani kwa yule Jamaa kumuelezea. Wote tulibaki na mshangao.” Nyange aliendeleza maongozi kuku akimpapasa mkewe aliyekuwa amejiegemeza kwenye bega lake kitandani hapo.
“Acha hiyo, kingine kilichonichanganya zaidi na hata mzee Nyange ndio maana anakuheshimu sana, ni baada yakuonana na baba yako. Unakumbuka baba yako alikuwa amekuja kwa matibabu pale kwako, ukaomba nije unitambulishe?” “Nakumbuka.”
“Sasa baada ya kuja kukutana na baba yako tena na yeye alikuwa msomi, tena anajielewa lakini akatuonyesha heshima zote vile, mzee Nyange ilimgusa sana.” “Lakini baba hakuwahi kukutana na mzee Nyange! Si unakumbuka alishindwa kuja kwenye harusi sababu alikuwa mgonjwa?”
“Kumbe hujui?” “Nini?” “Baba yako alikwenda mpaka kijijini kwetu?” Mama Briana akakaa kwa mshituko. “Haiwezekani! Kufanya nini?” “Mzee aliniambia na yeye hakutegemea. Tena baba alisema alionekana mgonjwa kweli! Alikwenda na kaka yako.” “Mbona hukuniambia? Walitaka nini?” “Mzee Nyange alishangaa sana, maana anasema baba yako alikubali kulala pale kwetu. Si unakumbuka ile nyumba ilikuwa ya tembe kabla hatujajenga hii ya sasa hivi? Mzee Nyange anasema hajawahi kumuona mtu mstaarabu kama baba yako.”
“Jamani baba yangu! Nina mkumbuka kweli! Baba alikuwa mpole na mwema sana.” “Kama wewe, Penninah. Umefanana sana na baba yako. Hamna tofauti.” Mama Briana alipooza gafla. Nyange akamvuta tena na kumkumbatia. “Pole sana, lakini sasa hivi unaye mzee Nyange. Anakupenda kuliko hata mimi.” Mama Briana akatabasamu.
“Alikwenda kufanya nini kwa mzee Nyange?” “Alisema alimuomba Eliah ampeleke kwa wazazi wangu ili akukabidhishe rasmi kwa mzee Nyange. Baba alisema waliongea sana, na kuna mambo mengine alisema hawezi kuniambia, lakini kikubwa alimuomba sana, akuangalie. Baba yako alikuwa akikujua jinsi ulivyo mpole.” Mama Briana akaanza kulia.
“Jamani baba! Atakuwa alishajua kama atakufa. Yeye ndio alikuwa msiri wangu.”“Kama mimi na Briana?” Nyange akauliza na kumfanya mama Briana acheke kidogo. “Mmmh! Nyinyi mapenzi yenu yanamashaka.” Wote walicheka.
“Hujui ni kiasi gani ulivyonijengea heshima pale kijijini na kwa mzee Nyange. Sasa ulipoondoka hapa na Briana, ni kama Mungu alianza kuniletea hizi picha zote huku akinikumbusha ile furaha niliyokuwa nayo baada ya kukupata na jinsi ambavyo nimekupoteza.”
“Maneno ya laana ya baba na mama, yalikuwa yakinirudia mchana na usiku. Nilikuwa nikishindwa hata kula, mama Briana. Nilikuwa nikijilaumu sana.”
“Sam aliponipigia simu kuniambia ulipo, nilishindwa kusubiria mpaka pakuche. Nilipanga kama ukikataa kunisamehe nisiondoke kabisa pale.” Mama Briana alicheka sana. “Huo ungekuwa ukorofi Nyange.” Nyange alianza kucheka na yeye. “Kweli nisingeondoka mpaka unisamehe, hata kwenye kochi ningelala tu.” Mama Briana akafikiria kidogo na kujiweka sawa.
**********************
“Yameisha Nyange. Lakini naomba nikuombe kitu kimoja tu Nyange, na ninaomba uwe muwazi. Naomba uniambie ni kitu gani natakiwa kufanya, ili utulie mume wangu. Naahidi kujitahidi kubadilika. Sitaweza tena kuvumilia endapo nitakusikia una mahusiano mengine.” Kidogo Mama Briana akaanza kulia.
“Ni kweli sitaweza. Nishaumizwa sana na wanaume kabla yako. Siwezi kuendelea kuteseka tena maishani. Nilikukubali bila kuangalia mambo mengine kwa kuwa Leah alinihakikishia umetulia. Sasa kuja kukuta na mwanamke mwingine ofisini, nilishtukasana. Ndio maana sikutaka tuzungumzie hilo, niliogopa utanidanganya.”
“Ila kuanzia siku ile nilianza kuwa na wasiwasi sana. Ndio kipindi hicho nilipoanza kuugua pressure, lakini sikutaka kukwambia. Kila nilipokuwa nikitakiwa kusafiri, nilikuwa nikiogopa sana, ndio maana nilikuwa nikimuomba Leah awe anakuja kukaa hapa nikijua nikama atakuwa mlinzi wangu.”
“Ilinibidi kukwambia safari ile kuwa nina pressure kwa kuwa nilianguka kazini na waliniambia mimba inaweza kutoka. Lakini nilikuwa nina uchungu niliokuwa nimeubeba moyoni, tokea siku niliyokukuta na huyo Mary ofisini kwako, na safari zako zilianza kunitia wasiwasi Nyange, lakini niliona nisikuulize ili usinidanganye.”
“Kingine kilichozidi kunitesa ni jinsi Sonia alivyokuwa akikuangalia wewe na Leah, nikahisi kuna jambo linaendelea. Lakini sikujua kama mnamahusiano, nilijua labda alikufumania tena. Lakini niliogopa sana kuuliza. Ndio maana kila nilipoenda kliniki waliniambia lazima nijitahidi kushusha pressure lakini nilishindwa. Nilikuwa nikiumia sana moyoni na hofu ilikuwa ikinisumbua.”
“Niliogopa usije ukaniacha ukaamua kuoa mwanamke mwingine. Nilikuwa nikijiambia usije kuwa umegundua mimi sio mwanamke uliyekuwa ukinihitaji. Kweli niliishi na wewe kwa kujishuku sana. Sasa kuja kusikia Leah ndio alikuwa mpenzi wako! Ndio maana nilichanganyikiwa sana. Sikutegemea.”
“Pole Mama Briana. Naomba uniamini, huna tatizo lolote, hata sijapata mwanamke anayenifaa kama wewe mke wangu. Naomba uamini nilikosa tu. Na ninakuapia mpenzi wangu, haitakaa itokee tena.” “Asante Nyange.” Nyange alimkumbatia mkewe na kuanza kumbusu kwa muda mrefu sana.
Ilikuwa ni siku iliyojaa mapenzi makubwa sana kati ya Nyange na mkewe. Nikama ndio ilikuwa mara yao ya kwanza kulala pamoja. Mama Briana alijisikia huru kwani alishatua mzigo aliokuwa ukimsumbua sana moyoni. Nyange alimfaidi mkewe nakujutia nguvu alizokuwa akipoteza kwa Leah.
Huku Kwa Kina Sam
“Mama Briana amerudi nyumbani.” Sam alimwambia Sonia, akafurahi sana. “Umefanya jambo zuri sana kaka. Nakupongeza.”
**********************
Katika maisha yake, Sam hakuwahi kupata mtu anayesifia chochote anachofanya. Alikaa na Leah aliyekuwa akimtukana na kumdhalilisha hata mbele za watu.
Hakuwa na kumbukumbu za kukaa chini na kuhudumiwa na mtu kwa upendo kama alivyomfanyia Sonia, labda mama yake alipokuwa nyumbani, tena zamani sana alipokuwa mtoto mdogo.
Sam alipomaliza tu darasa la saba alifaulu nakupangiwa shule ya sekondari Ilboru, Arusha. Tokea alipotoka nyumbani kipindi hicho, Sam alikuwa mtu wa shule tu na alisoma shule zote za kulala hukohuko. Alipokuwa likizo aliwafundisha watu ili kuongeza kipato nyumbani kwao. Alijitahidi kusaidia nyumbani kwao kwa kadiri ya uwezo wake. Hata katika kujinyima kote huko ni ili kusomesha wadogo zake na kusaidia wazazi wake.
**********************
“Asante Sonia.” “Itabidi kesho niondoke asubuhi.” “Unakumbuka nilikuomba tukae wote kesho?” “Nilijua ni kwa ajili yakumpa mama Briana na mumewe nafasi yakupatana!” “Hilo ndilo lilikuwa lengo kuu. Lakini nimemuomba mama Briana nikurudishe kesho kutwa, kesho nikuzungushe kidogo mjini. Ni sawa?” “Nitafurahi kupaona Dar. Sijawahi kuzunguka.” “Basi ujiandae kuzurula kesho.” Sonia akatabasamu.
Waliendelea kuangalia tv, huku kila mmoja akiwaza lake. Siku chache walizokaa pamoja, kuliongeza ukaribu fulani hivi. Sam alikuwa na furaha sana kuwa na Sonia. Alitamani asiondoke, aendelee kuishi naye pale kwake. ‘Lakini akae hapa kama nani?’Sam aliwaza. ‘Najisikia vizuri kweli kukaa na kaka Sam! Kweli ni mtu mzuri. Ana upendo na anajali.’ Sonia naye aliwaza kivyake.
**********************
“Unawaza nini Sonia?” Sonia akatabasamu. “Dada Leah yuko wapi?” “Hata sijui! Kwa nini unauliza?” “Nilikuwa nawaza, kwa kuwa mambo yameisha, kwa nini na wewe usimtafute akaja hapa mkaongea na nyinyi mkayamaliza.” Sam alitoa tabasamu la kichovu sana na kubaki kimya. Sonia alibaki na maswali bila ya kujibiwa.
“Ungependa kurudi Shule?” Sam akarusha swali badala yakujibu. “Nina tamani kweli, lakini sijui naanzia wapi! Hivi nipo kwenye kukusanya pesa, ili kama ikija kutokea siku moja napata nafasi ya shule, nije kurudi kusoma.”
“Kila dada akinilipa, namtumia mama kiasi na nyingine naweka akiba. Nilitaka kumuomba dada anipeleke nikafungue akaunti benki ili wakati mwingine awe ananiwekea hukohuko benki asiwe ananipa. Maana najikuta sina matumizi mengi. Ananinunulia kila kitu.”
“Una akili sana Sonia. Hilo ni wazo zuri. Unaweza kuanza kusoma masomo ya jioni, kumalizia kidato cha nne.” “Inawezekana!? Nilifikiria nisomee kompyuta tu.” “Hapana Sonia. Maliza shule. Wewe bado mdogo. Yapo madarasa ya jioni ambayo unaweza kumalizia masomo yako, hata kama utataka kusoma mpaka kidato cha sita. Unaweza kufanya kazi zako mpaka jioni. Mama Briana akitoka kazini, unamwachia mtoto halafu unaenda shuleni.”
“Si itakuwa usiku sana. Naogopa.” “Mimi nitakuwepo, usijali. Kesho twende tukatafute hayo madarasa ujiandikishe. Najua mama Briana hatakataa, ilimradi ufanye kazi zako vizuri.” Sonia alihisi yupo ndotoni. Hakutegemea kuja kurudi shuleni mapema hivyo!
Alikaa kimya akiwaza jinsi mama yake atakavyofurahi akisikia amerudi shuleni. Aliendelea kujiuliza, wenzake waliokuwa nao kidato kimoja watakuwa wapi sasa hivi. Machozi yalianza kumtoka. “Nini tena?” “Yule baba amenikatili sana kaka. Sasa hivi ningekuwa niko mbali sana kielimu. Ameniharibia maisha yangu. Ona watu wanavyonitazama kama msichana muhuni tu, ambaye amecha shule sababu ya kupata mimba!”
“Amevunja mahusiano yangu na mama yangu, ambaye ndiye ndugu pekee maishani mwangu.” Kwa mara ya kwanza Sonia kupata muda na mahali ambapo alitoa uchungu wake baada ya kubakwa. Alikuwa na uchungu mwingi sana moyoni lakini hakuwahi kupata mtu wakumwambia. Aliendelea kumuhesabia Sam, maendeleo ambayo angekuwa nayo kama sio kubakwa.
Sam alimvuta karibu yake na kumkumbatia. “Pole sana Sonia. Lakini nikwambie kitu?” Sonia akakausha machozi. “Tendo lilikuwa baya, lakini umempata Kana. Halafu wewe bado mdogo Sonia, una muda mwingi sana wakurekebisha maisha yako. Umesoma mpaka kidato cha pili, ukikazana, unahitaji mwaka mmoja tu kumalizia kidato cha nne.”
“Kweli kaka?” “Kabisa. Nilisha ulizia, kwa hiyo nina habari za kutosha. Kama kutakuwa na ugumu wowote, nitakusaidia kukutafutia mwalimu wakukusaidia masomo. Usiogope kabisa. Ukiweka juhudi, utasoma mpaka mwenyewe useme basi.” “Sisemi basi. Napenda sana shule.” Sam alianza kucheka.
“Usicheke kaka, kweli mimi napenda shule!” “Basi kesho tutaenda kuulizia jinsi utakavyoanza.” “Asante sana. Nashukuru kwa kila kitu.” Sam alijisahau akabaki amemkumbatia. Sonia naye akatulia kama kifaranga cha kuku chini ya mbawa za mama yake.
**********************
Palipo pambazuka, Sonia aliingia kuoga wakati Sam anaangalia taarifa ya habari ya asubuhi. Alivaa kabisa huko huko bafuni na kujitengeneza. Alitoka akiwa amependeza sana. Sonia hakuwa mweupe wala mweusi. Alijaliwa rangi nzuri sana, na matunzo ya mama Briana alikuwa amenawili vizuri.
Bado alionekana ni binti mdogo, sura ya Kinyarwanda ilikuwa bayana kwake. Alijaliwa macho mazuri na usoni alionekana ni msichana aliyetulia. Sam alitamani kumjua sana Sonia kiundani, hasa tabia yake akiwa amefanikiwa, yaani akiwa hana shida yeyote. Aliwaza na kukataa kumpa sifa zote, kwa kuwa alijua shida inaweza kumfanya mtu yeyote kuwa mwema tu. Alijua, tabia nzuri ya mtu nipale anapokuwa hana shida.
“Kweli walimu wako watapata shida.” Sonia alianza kucheka. “Kwa nini kaka?” “Ukiwa unaenda umependeza hivyo! Watashindwa kukufundisha, Sonia.” Sonia alizidi kucheka kwa aibu. “Hamna bwana kaka! Mbona kawaida tu?” “Haya tutaona.” “Naenda kuandaa chai.” “Leo tunaenda kula nje, hakuna kupika.” Sonia alicheka na kurudi kukaa. “Sawa.”
Naye Sam alioga harakaharaka wakatoka na Sonia kwa kutumia gari yake. Alimpeleka mahali kupata kifungua kinywa, kisha akaamua kumpeleka kazini kwake. “Twende ukaone ninapofanya kazi.” Walienda mpaka ofisini kwa Sam. Kila mtu alibaki amewakodolea macho.
“Heshima yako Sam!” “Leo mpaka shikamoo utatoa, lakini hata namba ya simu hupati.” Wafanyakazi wenzake wote walianza kucheka. “Ulijuaje hiyo ndio shida yangu?” “Najua uhusiano wako na sketi, ukoje.” Kila mtu alicheka.
“Mbona sasa hututambulishi mgeni, Sam?” “Msiwe na haraka. Tutarudi.” Sonia alikuwa na wakati mzuri sana siku hiyo. Alimzungusha sehemu mbalimbali na kutafuta madarasa yatakayo mfaa.
“Nakushukuru sana kaka yangu. Sijui niseme nini?” Sam akaanza kucheka. “Nimekuona ulivyo furahi, nakuanza kumnyeshea maswali yule mwalimu!” “Natamani nianze hata kesho!” “Naona uwape muda mama Briana na mumewe, wakuijenga ndoa yao kwa upya.”
“Unaweza usielewe, lakini kilichotokea kwa mama Briana ni kitu kikubwa sana. Sema yule mwanamke ni jasiri na mvumilivu sana. Wanahitaji sana muda na mumewe kurudisha mahusiano yao. Tukiona wametulia. Ndipo tuwaambie.” “Ni kweli kaka.” Walirudi nyumbani ilishakuwa jioni.
“Sasa ukaoge, tutoke tena.” “Tena!?” “Umechoka?” “Hapana. Ulitaka twende wapi?” “Tukale chakula cha usiku halafu tukaangalie sinema.” Sonia alifurahi sana.
**********************
Walitoka tena jioni hiyo wakiwa wamependeza sana na wote walikuwa na furaha. Usiku huo waliutumia kufahamiana zaidi na zaidi. Walienda kuangalia sinema na kurudi nyumbani wote wakiwa wamechoka.
“Natamani usiondoke Sonia.” Sonia alicheka kinyonge. “Lakini si utakuwa unakuja kwa mama Briana kunisalimia?” “Nitakuja, lakini haitakuwa kama tulivyokuwa tukiishiwote hapa. Umenizoesha vibaya kweli!” Sonia akabaki kimya kitandani hapo wote wakiwa wamelala huku wamegeukiana.
Sonia akabaki amejiegemeza karibu kabisa na Sam, bila ya kugusana. Ni kweli kila mmoja alimfurahia mwenzake. Hata Sonia hakutamani kuondoka. Walipitiwa na usingizi wote wakiwa wamegeukiana mpaka asubuhi.
**********************
Waliamka asubuhi na kubaki wamejilaza kitandani hapo kila mtu akiwaza lake. “Usiache kuja kunitembelea kaka.” Sam akamwangalia Sonia na kumvuta mkono wake taratibu. Akaweka kiganja cha Sonia kwenye kiganja chake. “Nitakuja Sonia.” Wakabaki vile kwa muda Sam akiwa ameshikilia mkono wa Sonia mpaka walipoona muda unazidi kwenda. Hakuna aliyetaka kutoka hapo kitandani, mwishowe Sam akaamua kumrudisha kwa Mama Briana.
Maisha lazima Yaendelee
“Mbona sasa mmerudi kama wote wagonjwa tena?” Mama Briana alianza kuwauliza Sam na Sonia mara walipoingia. “Ni hivyo nakupenda tu shemeji yangu. Lasivyo ningemuiba Sonia moja kwa moja.” Mama Briana alianza kucheka.
“Kweli tena! Badala yakufurahia kupona, nimechukia kupona. Nilivyokuwa na dekana kwa mara ya kwanza maishani nilimpata wakunibembeleza.” Wote walizidi kucheka, Sonia akajificha kwa aibu.
“Nakushukuru sana mama Bree kwa upendo wako.” “Nimefurahi umepona Sam. Lakini Nyange ameniomba nikuombe, utusindikize tena kijijini.” “Kwema?” “Kiasi. Nilipoondoka, mzee Nyange na mkewe walikuja hapa. Nasikia mambo hayakwenda vizuri. Ndio Nyange anataka tukayamalize na wazazi, lakini si unamjua mzee Nyange? Baba Briana anahofu kweli, anasema tukienda wote angalau atakuonea wewe haya.” Sam akabaki kimya.
“Nakuomba Sam na wewe umsamehe baba Briana. Ni kweli amekosea sana, lakini anaonekana anajutia sana kosa lake, naomba umsamehe yaishe, tuanzeni upya kama ulivyonishauri mimi.” Sam akacheka. “Unanigeuzia kibao?” “Nyange anakuhitaji sana katika maisha yake, sisi sote tunakuhitaji, Sam. Ni hivyo tu na yeye ni binadamu.”
“Kweli mama Bree una upendo wa ajabu, shemeji yangu! Umfundishe na Sonia awe kama wewe.” Wote wakacheka. “Yameisha mama Briana. Na hivi na wewe umerudi nyumbani, hamna shida. Mimi shida yangu ni wewe mama Bree wala sio Leah. Naona hata yeye mwenyewe Leah atakuwa ameshukuru kuondoka kwangu. Maana wakati wote aliniona mimi ni mzigo kwake. Kwa hiyo hata mimi mwenyewe sasa hivi napumua. Nakaa kwa amani na utulivu.” Waliongea mambo mawili matatu, Sam akaondoka.
**********************
“Za huko?” Mama Briana akamgeukia Sonia aliyekuwa akicheza na Briana. “Nzuri. Nilikuwa na hamu ya kuwaona!” “Hivi tulikuwa tunakusubiria na baba Briana tukuachie huyo, sisi tunasafiri kidogo, halafu tukirudi twende kijijini.” “Ndio vizuri nibaki na Briana wangu, hatutaki kuingiliwa wenyewe. Eti Bree?” Briana alimpenda sana Sonia, hakuwa na shida yeyote anapokuwa na Sonia. Aliendelea kumchekea Sonia huku akimrukia rukia.
Ndoa Na Iheshimiwe Na Watu Wote
Baada ya siku moja mama Briana na mumewe walisafiri. Hakuna safari aliyofurahia mama Briana kama hiyo. Walikuwa na wakati mzuri sana na mumewe. Nyange alijitahidi kumfurahisha sana mkewe na kumsaulisha kifo cha mtoto wao. “Hata honeymoon yetu hatukufaidi hivi.” Mama Briana alikuwa akiongea na mumewe siku yao ya mwisho hotelini hapo.
“Sasa wakati ule nilikuwa sikufahamu vizuri bwana. Sasa hivi ndio naona uthamaniwako mpenzi wangu. Unanijali sana mama Briana. Asante.” “Nakupenda mume wangu. Nafikiria kuacha kazi.” Nyange alikaa kwa mshituko. Kwani alishamshauri sana mkewe kuacha hiyo kazi, kwani ilikuwa ikimfanya azunguke sana, na muda mwingi hakuwepo nyumbani.
“Kweli?” “Naona inakosa maana. Sipati muda na familia yangu kabisa.” “Hasa mimi.” Mama Briana akacheka. “Asante sana mpenzi wangu. Ni kweli unahitajika nyumbani, Mungu ametusaidia angalau biashara zetu zinaingiza pesa yakututosha.”
“Unajua siwezi kukaa tu nyumbani Nyange. Sio maisha niliyozoea.” “Sasa utafanya nini?” “Nitafungua ofisi yangu ya consultation, palepale mjini. Naamini itaingiza tu pesa na hivi nafahamiana na watu wenye makampuni mbalimbali, najua nitapata wateja.” “Daah! Kweli mke nimepata. Nakushukuru sana. Angalau maisha ya ndoa yataleta maana. Tena kwa kuanzia unaweza kuchukua sehemu pale ofisini kwangu, unajua pale ni pakubwa sana? Angalau na mimi niwe nawaona hao wanaokuja kushauriwa.” Mama Briana alicheka sana.
“Kwa mtindo huo, kazi zitakuwa hazifanyiki.” “Lazima niwe mwangalifu, wengine watakuwa hawana shida za biashara zao, wanataka kuja kukusikiliza tu unavyoongea.” Mama Briana alikuwa akicheka sana. “Naona heri nitafute ofisi yangu kwengine, ofisi moja na wewe, kazi zitakuwa hazifanyiki.” Walikaa hapo kwa juma moja.
Sam hakuacha kupita nyumbani kwa Nyange mara kwa mara, na simu za usiku hazikuwahi kuisha kati yao. Nyange na mkewe waliporudi nyumbani walionyesha wazi kuna kitu cha ziada kimejengeka.
**********************
Baada ya miezi miwili hali ya mama Briana ilibadilika, ndipo alipogundua ni mjamzito tena. Ilikuwa ni furaha kubwa sana kwa familia hiyo. Mama Briana alikuwa na shida sana kushika mimba. Mara nyingi ilimbidi kutumia dawa na msaada wa kitaalamu kupata ujauzito.
Hata Briana mwenyewe ilimchukua karibu miaka mitatu kumpata. Hakutegemea kupata ujauzito mwingine kiurahisi hivyo! Aliamua kutulia kabisa nyumbani asifanye kazi mpaka atakapojifungua.
**********************
Ndipo Sonia naye alipoona ni wakati wakurudi shule. “Kaka Sam?” Sonia alimpigia simu akiwa kazini. “Mbona leo mapema!? Kwema?” “Kuna kitu nataka nikwambie. Au una kazi nyingi?” “Hapana, niambie tu.” “Mama Briana ameacha kazi, atakuwepo tu nyumbani. Unafikiri sasa hivi ni wakati mzuri wa kumwambia mambo ya shule?”
“Kwa nini ameacha kazi!?” “Nafikiri sababu ya ujauzito wake. Lakini sio mgonjwa. Anataka tu kukaa nyumbani.” “Basi jaribu kuongea naye, uone atakwambia nini.” “Sawa. Utanipigia tena baadaye?” Sam akacheka. “Nitakupigia Sonia.” “Asante.” Akakata simu.
**********************
Sonia aliongea na mama Briana akiwa na hofu sana, lakini akashangazwa na vile Mama Briana alivyopokea. “Katika vitu ulivyonifurahisha ni hicho, Sonia. Shule ni muhimu sana mdogo wangu.” Sonia alihisi ni ndoto.
“Tena kama ni madarasa ya jioni, ndio vizuri mchana utapata na muda wakujisomea, na hivi nipo tu nyumbani, utapata muda wa kutosha kusoma.” Sonia alimkumbatia mama Briana kwa furaha. “Asante dada.” Mama Briana alianza kucheka.
“Unataka kuanza lini?” “Hivi kaka Sam aliniambia nisubiri kwanza mpaka utulie. Lakini tulishafuatilia kila kitu wakati ule nilipooenda kumuuguza.” “Kweli Sam ana upendo. Anamfikiria kila mtu! Alijua kipindi kile nilikuwa nakuhitaji sana. Namuhurumia Leah mdogo wangu, amekosa mwanaume mzuri kweli! Sidhani kama atakuja kupata mwanaume kama Sam.” Sonia hakutaka kuongeza chochote.
**********************
Maisha ya furaha na amani kati yao yakarejea. Walirudi kuwa familia moja yenye mshikamano zaidi na kuheshimiana. Sam na Nyange undugu ukarudi, ukawa undugu wenye furaha kuliko hata mwanzoni. Tena wakiongeleshana kwa heshima tofauti na alivyokuwepo Leah, aliyekuwa akiwakosea heshima wote.
Hakuna Aliyewahi Kutoa, Kumzidi Mungu
Sonia akaanza shule, Sam akiwa dereva na mama Briana mlipa ada. Alifanya kazi zake zote asubuhi, ilipofika jioni Sam alikuja kumchukua nakumpeleka shule. Sonia aliweka juhudi sana shuleni na masomo hayakumsumbua kabisa.
Mwalimu aliyekuwa akiwafundisha yeye na rafiki zake, alianza hisia za kimapenzikwa Sonia. Lakini wakati wote Sam alikuwepo pale kwa wakati kumsubiria amalize kusoma na kumrudisha nyumbani, kwa hiyo yule mwalimu alikosa muda wa peke yao na Sonia.
Taratibu yule mwalimu akaanza mazoea na Sonia. Hakuacha kumsifia kwa kila kitu anachofanya darasani. Mwishowe ili apate muda na Sonia, akaamua kumshawishi Sonia kufanya madarasa ya ziada, ili wawe wanaweza kukutana asubuhi wao wawili tu, akamwambia lengo ni kumsaidia kumuandaa vizuri na mitihani ya kidato cha nne. Sonia alifurahi sana.
“Nakushukuru sana. Kwa hiyo itabidi nikuongezee kiasi gani cha pesa?” “Wala usijali Sonia, nataka kukusadia tu.” “Kweli?” Sonia alishangaa na kufurahia moyo wa ukarimu wa huyo mwalimu. “Wala usijali. Nakuona ulivyo najuhudi, naona na mimi nikutie moyo.” Sonia akazidi kufurahi.
**********************
Siku hiyo alipopewa hizo habari baada ya kumaliza muda wa darasa la jioni, Sam hakuchelewa, alishafika akawa nje akimsubiri. Sonia akaingia garini akiwa amejawa furaha. “Pole na kazi kaka.” Alitoa salamu hiyo huku akijiweka sawa kwenye kiti cha gari na kufunga mkanda wa gari kwenye kiti hicho cha mbele.
“Asante. Vipi na wewe shule yako?” “Nina habari njema.” Sam akatabasamu na kuuliza. “Nini?” “Yule mwalimu amesema atanipa madarasa ya ziada mimi mwenyewe muda wa asubuhi.” Sam akatulia kidogo. “Kaka Sam?” “Kwa nini wewe peke yako?” Akamfanya Sonia kutulia kidogo na kutafakari.
“Amesema mimi nimeonyesha juhudi, kwa hiyo ni kama kunipa moyo ili niwe tayari na mitihani ya taifa.” Sam akanyamaza tena. Alishamuhisi huyo mwalimu anammezea mate Sonia. Kwani alikuwa akimuona vile anavyo msindikiza Sonia kwa macho kila alipokuwa akiondoka kwenda kupanda gari, wakati Sam akimsubiria. Hakuacha kumuangalia Sonia kwa nyuma.
Sam alishakasirika. “Mbona sasa husemi kitu?” “Mimi naona uendelee kusoma jioni na wenzako.” “Kwa nini? Kama ni pesa, amesema atanifanyia bure haitaongeza garama. Halafu kama ni swala la usafiri nitakuwa nakwenda mwenyewe na daladala ili nisikusumbue maana najua utakuwa kazini.” Sam alitulia tena kidogo, kitu kilichomtia wasiwasi Sonia.
“Tatizo sio pesa wala usafiri Sonia.” Furaha ya Sonia ilianza kupungua. Alijua Sam angefurahia kama yeye. “Sidhani kama unahitaji masomo ya ziada kukuandaa na mitihani. Hata hivyo umeshafikiria juu ya kazi yako lakini?” Ndipo Sonia alipokumbuka yeye ni msichana wa kazi sio mtoto wa mama Briana. Anajukumu la kufanya kuendelea kuishi pale ndani.
Alipooza sana usoni. “Kila jambo lina wakati wake Sonia. Na kuna mambo fulani yanaweza kuonekana mazuri kwa nje, kumbe yana mtego mkubwa sana ndani yake. Sio vitu vyote vya bure ni vya kukimbilia. Lazima uwe mwangalifu.” Haraka haraka akili ya Sonia ilikumbuka misaada aliyokuwa akipewa na wazazi wa Fau, nakuishia kubakwa.
“Nimeelewa kaka. Kesho nitamwambia hapana.” “Kesho si sikukuu, na ulisema hamtafundishwa?” “Ametukaribisha nyumbani kwake kwa sikukuu.” Sam alikasirikazaidi. “Lakini sio peke yangu kaka, ametukaribisha wote anao tufundisha. Amesema ndio utakuwa wakati mzuri wakufahamiana zaidi, kwa kuwa siku za kusoma muda unakuwa mfupi.”
**********************
Sonia na wenzake walikuwa wakikutana mida ya jioni, jumatatu mpaka ijumaa, wanafundishwa na mwalimu, halafu siku za jumamosi na jumapili wenzake walikutana kwa ajili ya kujisomea wenyewe kama kundi, wakirudia walichofundishwa na kufanya maswali mbalimbali waliyokuwa wakikusanya, ya mitihani ya nyuma, lakini Sonia alikuwa na Sam wakati wote wa weekend, hakuwa akiudhuria.
Siku za jumamosi ambazo Sam hakuwa akienda kazini kuanzia asubuhi mpaka usiku alikuwa nyumbani kwa Nyange na siku za jumapili hivyohivo. Kwenye darasa hilo la kina Sonia, wengine walikuwa ni watu wazima kidogo kwa Sonia. Wote walikuwa wake za watu kasoro Sonia ndiye hakuwa hata na mchumba katika kundi lao.
Alimtambulisha Sam kama kaka yake. Mwalimu ambaye alikuwa akiwafundisha masomo ya English, hesabu na Kiswahili naye alikuwa kijana tu hajaoa, huyo ndiye alimpenda sana Sonia. Hakuacha kumtaja kila walipokuwa darasani na alimtazama Sonia kila alipopita. Lakini Sonia hakuwa hata na wazo.
**********************
“Kwa hiyo utaenda?” Hilo swali likamfanya Sonia afikirie maana yake nini na wakati alishamwambia atazungumza na huyo mwalimu wake siku ya kesho, atakapokwenda nyumbani kwake alipokaribishwa. “Eti Sonia?” “Tumealikwa kaka!” Sonia alijibu akisikika kukosa ujasiri.
“Kwa hiyo na wewe unataka kufahamiana na mwalimu wako zaidi?” Aliegesha gari nje ya nyumba ya Nyange na kumgeukia Sonia. Sonia akainama. “Eti Sonia? Na wewe unataka kwenda kufahamiana na mwalimu wako zaidi?” “Hapana kaka.” “Basi nitakuona kesho.”
“Utakuja?” “Nitakuja kuangalia mpira na Nyange. Kesho kuna kandanda ligi za Uingereza. Alinikaribisha.” “Sawa.” Sonia akajibu kinyonge sana. “Usiku mwema.” “Hauingii ndani?” “Naona mwenyeji wangu hujanikaribisha. Sasa nina ingiaje ndani?” “Twende ukale kwanza ndio ukalale.” Sonia aliongea kwa unyonge.
“Lakini Sonia, kama unataka kwenda kwa huyo mwalimu wako, nenda tu mkafahamiane vizuri. Na kama unataka hayo madarasa ya ziada ya asubuhi, wewe endelea tu.” “Hapana kaka, sitaenda. Naona niridhike na haya madarasa ya watu wote tu.”
**********************
Tokea usiku ule wa mkasa pale nyumbani kwao, hawakuwahi kukutana tena na marafiki zao. Nyange aliamua kuwakaribisha tena wale marafiki zao kuja kuangalia mpira lakini lengo kuu lilikuwa ni kuwaomba radhi kwa yote yaliyotokea kwani ni kama walivunja mahusiano kabisa na Nyange.
**********************
Mama Briana aliamka akiwa na nguvu na kuanza matayarisho ya ugeni wa jioni hiyo, wakisaidia na Sonia na Josh. Nyange na mkewe walikuwa watu wa watu sana. Wote walipenda wageni, na nyumba yao haikukosa watu. Wakati wote walitafuta sababu yakukaribisha watu nyumbani kwao. Utundu na ucheshi wa Nyange uliwafanya wawe na marafiki kila mahali.
“Twende ukaoge upumzike, Josh na Sonia watamalizia.” Nyange alimfuata mkewe jikoni. “Naona kama bado!” “Usijali dada, sisi tutamalizia. Wewe nenda kapumzike. Umesimama tokea asubuhi! Sio vizuri kwa afya yako.” “Sonia yupo sahihi, twende bwana!”
“Halafu wote nataka tuangalie mpira leo. Umesikia Josh? Ukaoge na wewe, uwe msafi uje tuangalie kandanda.” “Sawa baba.” “Na wewe Sonia, usijifungie huku jikoni.” Sonia akacheka. “Namalizia dada sasa hivi na mimi nikaoge.” Nyange akatoka na mkewe kuelekea chumbani.
Haukupita muda mrefu, kila kitu kilikuwa tayari, Sonia akaandaa vinywaji kabisa na chakula, akaweka mezani na kwenda kuoga.
**********************
“Mbona simuoni Sonia?” Sam alianza kumuuliza Nyange na mkewe aliokuwa amewakuta sebuleni. Alishakaa pale zaidi ya dakika ishirini bila Sonia kutoka. “Atakuwa yuko chumbani kwake.” Mama Briana akajibu na kujirudisha pembeni ya mumewe. Nyange alipitisha mkono wake juu ya mkewe nakurudisha macho kwenye tv.
Wageni walianza kufika lakini Sonia bado alikuwa chumbani. Sam alisogea mpaka chumbani kwa Sonia nakuanza kugonga. Sonia akatoka akiwa amependeza sana na simu masikioni. “Nitakupigia baadaye.” Sonia aliongea kwa kifupi na mtu aliyekuwa akizungumza naye kwenye simu, kisha akakata.
Sam alibaki akimwangalia kama kutaka kujua nani alikuwa akiongea naye. “Karibu kaka Sam.” Sonia alijua kabisa anachotaka Sam, lakini hakutaka kusema ni nani aliyekuwa akizungumza naye. Sam alibaki akimtizama.
“Umekuja muda mrefu?” “Sana. Lakini sikukuona.” “Umepata kinywaji chochote?” Sonia akauliza huku akitoka chumbani kwake. “Nani ananipa Sonia?” “Samahani kaka, sikujua kama upo. Naomba unisubiri sebuleni nikakuletee juisi. Nimeitengeneza mimi mwenyewe, ni nzuri sana. Najua utaipenda.” Sam alishaanza kukosa raha. ‘Nani anayeongea naye?’ Alirudi kuangalia tv lakini mawazo yake hayakuwa pale kabisa.
Sonia akamfuata na juisi kwenye glass nzuri na kukaa pembeni yake. “Unapenda mpira?” Sam akamuuliza. “Sielewi chochote.” Sonia akajibu huku akicheka. “Juisi nzuri sana.” “Mama Briana ndiye aliyenifundisha kutengeneza.” “Hongera.” “Asante.” Mpira ulikuwa ukiendelea lakini Sam alionekana na mawazo mengi, akili yake haikuwa pale.
Mti Wa Mapenzi Ukishazama Mizizi,
Dharuba Haziwezi Kung’oa Kirahisi
Wakati mpira uko mapumzikoni, mama Briana alikaribisha wageni wao chakula, na kuwaruhusu kula popote wanapotaka. Sonia akaanza kumlisha Briana. Kila mtu alikuwa kwenye wakati mzuri wakila na kunywa huku stori zikiendelea.
Mara Leah akaingia, akiwa mjamzito wa mimba kubwa tu. Kulizuka ukimya mkubwa sana kati yao, mama Briana alianza kutetemeka. Maswali yalikuwa mengi kwa kila mtu, lakini zaidi kwa mama Briana.
Akiwa bado amesimama bila hofu, huku watu wote wakimwangalia, Leah akamgeukia Nyange, “Nimekuja Nyange na mtoto wako. Tena wa kiume.” Zilikuwa habari mbaya sana kwa mama Briana, kwani alijua ni kiasi gani baba mkwe wake namumewe walivyokuwa wakitamani mtoto wa kiume.
Hofu yakupoteza ndoa yake na uthamani wake kwa wakweze ikamuingia. Japokuwa alikuwa na ujauzito, lakini alikataa kabisa kuangalia jinsia ya mtoto. Yeye na mumewe walikubaliana kusubiri mpaka mtoto atakapo zaliwa.
**********************
Nyange alimwona jinsi mkewe alivyopooza gafla. Akabaki akiangalia sahani yake iliyokuwa bado na chakula kingi bila hata kunyanyua uso wake. Akajisogeza karibu zaidi na mkewe. “Mbona sasa huli?” Nyange akamuuliza mkewe kwa kumjali. “Nasikia tumbo limejaa.” “Ungejikaza bwana, usilale bila kula. Nikuletee juisi?” “Naomba maji.” Nyange akataka kusimama kwenda kufuata maji, Leah akamdaka tena.
“We Nyange?” Nyange akaanza kuangalia kulia na kushoto kama anayemtafuta mtu anayeongeleshwa na Leah. “Naongea na wewe Nyange.” Nyange akasimama huku amekunja uso. “Mbona unatuchanganya Leah? Mara useme Nyange, nikiangalia humu ndani kina Nyange tupo watatu tu, mimi, Penninah na Briana. Au Isa na yeye anaitwa Nyange?” Kidogo Leah akatulia baada yakusikia jina la Isa. Hakuna aliyeelewa.
Nyange alipoona Leah amenywea akaondoka kwenda kumletea mkewe maji ya kunywa.
Aliporudi, Leah akarudia tena, lakini safari hii alionekana ujasiri umepungua kidogo. “Wewe si unataka sana mtoto wakiume? Sasa huyu ni wakiume.” “Namtaka sana, wala si uongo. Ukoo mzima unataka mtoto wa kiume, tena sana tu. Lakini nataka mtoto kutoka kwa Penninah. Na kwa bahati mbaya sana mbeba ukoo wetu, yaani mzee Nyange mwenyewe, ameapa na kufunga mbinguni, duniani mpaka kuzimu uliko toka wewe na wenzako kama wewe, hakuna kiumbe kitakachozaliwa katika familia yake kikaishi, na kuitwa Nyange, kama hakijatoka kwa Penninah. Huyu dada yako unayejitahidi sana kushindana naye, ndio mwendeleza ukoo wa Nyange, lakini sio vinginevyo.”
“Azae wa kiume au wakike watupu, ni yeye tu ndio mwendeleza ukoo wetu. Labda kawatafute kina Nyange wengine wakuzaa nao, lakini sio mimi.”
“Kama huamini ninayokuambia muulize Sam yule pale nyuma, wakati mzee Nyange ananiapia nilikuwa mimi na yeye tu kijijini kwetu, hata mama Briana mwenyewe hajui. Sasa katika hilo, mpango wako huu umeshindwa. Nenda kajipange upya, halafu urudi, tena safari hii tutakupa siku na muda kama huu ambao tutakuwa tumealika wageni wetu tena kama hivi uje kufanya fujo zako, tena vizuri.” Kidogo Mama Briana akapumua, akanywa maji na kurudi kujiegemeza kwenye kochi, Nyange akamvuta tena na kupitisha mkono wake mmoja juu ya bega lake.
“Basi sasa ndio ishatokea, nimepata mimba yako na kwa kuwa humtaki damu yako, wewe nipe ile nyumba niliyokuwa najenga, nikae huko na mtoto wetu, ili nisije kukaa hapa.” Bado Leah alikuwa amesimama. Kimya kilikuwa kimetanda kwa watu wote wakimshangaa Leah.
Sonia ndio alikuwa haelewi kabisa, nguvu hiyo na jeuri, Leah anaipata wapi? Kusimama mbele ya wanaume wote wale na wawili aliokuwa na mahusiano nao, na kuchagua mmoja ndiye baba wa mtoto wake! Tena bila hofu wala aibu! Hata yeye akabaki akimwangalia.
“Sikiliza Leah, naomba usinipotezee muda na maneno mengi yasiyo na maana. Wewe ukubali tu mipango yako safari hii imeshindikana, kajipange upya.
Nilipotaka kukuacha safari ile mke wangu aliporudi toka safari, ulinitishia sana kuja kumwambia madudu yote tuliyokuwa tukifanya mimi na wewe, huku ukisema utakwenda mpaka kijijini kwetu ukawaambie wazazi wangu. Ukanitesa wakati wote ule na kunifanya kama mashine yakufanya mapenzi unapotaka wewe.”
“Umenidhalilisha vyakutosha. Nilikuwa kama mbwa, ulichezea utu wangu vile utakavyo. Mpaka kwenye gari ulitaka nifanye mapenzi na wewe. Nilikusihi sana utulie na kukukubalia kila unachotaka, lakini hukusikia. Umesababisha kifo cha mwanangu, Junior.”
“Lakini Mungu amenihurumia na kunisamehe, mke wangu amenisamehe, tumerudiana na nyumba yangu imekuwa na amani tena. Na kwa taarifa yako nimekwenda mpaka kwa wazazi wangu, nimekiri na nimesamehewa.”
“Nimekaa kwa muda mrefu sana tokea ukininyanyasa na kunitishia utatoa siri yangu ya kulala na wewe, nikawa najiuliza nia yako ni nini kwangu? Kwani ulishanikataa tena kwa kunitukana mbele za watu, ukanipa dada yako nimuoe, ukisema mimi sikufai, Penninah ndio ananifaa, nikamuoa.”
“Nimemuoa tu, baada ya muda tena wala sikumwambia Penninah ukaanza kunisumbua unanitaka tena. Haya, nikajitahidi sana kwa muda mrefu kukukwepampaka ukagundua udhaifu wangu wakati mke wangu hayupo, ukaninasa na kuendelea kuning’ang’ania mchana na usiku.”
“Umekuwa kama mwehu kwangu, wakati nilikutongoza wewe wa kwanza, ukanikataa. Sasa nikawa najiuliza, hivi shida yako wewe haswa ni nini? Lakini sikupata jibu. Madhara uliyoyasababisha siku ile, yalinitia shauku kubwa sana kutaka kujua nia na kusudi lako ni nini kwangu na mke wangu.”
“Nimetumia pesa, siwezi kusema nyingi lakini ujue nilitumia pesa mpaka nimejua kila kitu chako. Nilikuwa na kusubiria sana uje, kwa kuwa nilishapata taarifa zako kuwa unajiandaa kuja kwangu lakini sikujua kama utakuja ukiwa na mtoto au mjamzito. Na pia sikutegemea kama utarudi tena hapa mbele ya uso wa dada yako, ukiwa jasiri hivyohivyo bila hofu, wakati ulimuacha hapo sakafuni nusu maiti.” Kila mtu alikuwa kimya kabisa, wakisikiliza.
Kwa kuwa alikuwa na tumbo kubwa, Leah alishachoka, akataka kukaa. “Usithubutu kushika kitu chochote hapa nyumbani kwetu, hata chini sakafuni usikae. Simama hivyohivyo. Wewe si unajidai mjanja na mkorofi? Sasa leo utayasema yote kwa kinywa chako mwenyewe, watu wote wakujue wewe sio binadamu ni shetani.” Kila mtu alikuwa haelewi kabisa.
Sonia akambemba Briana na kumuingiza chumbani, akamuwashia tv ya chumbani kwake, akafunga mlango, akamuacha humo ndani, yeye akatoka haraka kusikiliza.
“Tunakusikiliza Leah. Wewe si umetaka kuja kuongea hapa mbele za watu? Sasa tunakusikiliza, lasivyo nakuchapa makofi hapahapa mbele za watu mpaka useme.” Nyange alishabadilika uso, akamrudisha mkewe kwenye kochi nakutaka kusimama baada ya kumuona Leah amekaa kimya hataki kusema.
Mama Briana akamvuta shati. “Kuna nini Nyange? Usimpige bwana!” “Muulize mwenyewe, msichana mbaya sana huyu. Unaongea Leah au nisimame?” “Sasa niongee nini jamani?!” “Nimekwambia kila kitu.” Leah akaanza kulia, Nyange akasimama na kutaka kumpiga. Haraka haraka Mama Briana na yeye akasimama. “Naomba usimpige, tafadhali Nyange.” Nyange akasimama kwa muda akimwangalia Leah kwa hasira kama mrarue.
“Tafadhali Nyange.” Mama Briana akarudia huku amemshika mumewe mkono akimvuta, Nyange akarudi akamshika mkewe, wakakaa. “Ungejua aliyoyafanya, wala usinge muhurumia, huyu. Tulikuwa tunaishi na shetani humu ndani.” “Kwani umefanyaje?” Mama Briana akamuuliza Leah. Kimya.
“Nimekwambia ni jeuri huyu. Mpaka nimchape ndio ataongea.” “Labda hajakula.” “Hatakunywa hata maji ya bomba, humu ndani. Na wala asikae.” Mama Briana akaanza kulia. “Nini sasa na wewe mama Briana? Ushaanza!” “Mwone alivyochoka jamani Nyange! Ataanguka.” Ni kweli Leah alikuwa amechoka sana. Ilikuwa ngumu kujua kama ni ujauzito au maisha ndiyo yamemchosha vile.
“Hainihusu kabisa. Yeye si jeuri? Si nilikwambia nitamfundisha adabu? Na bado. Pale alipo hana mbele wala nyuma. Hana kazi wala pakuishi. Ana tangatanga na dunia.” “Haiwezekani Nyange!” “Muulize. Najua habari zake zote.” Mama Briana akazidi kulia akiuliza, “Kwani umemfanya nini?” “Ni mimi tena!? Muulize mwenyewe. Ulifikiri maisha marahisi hivyo? Ulijua ukija tu hapa mjamzito, unataka nyumba ndio basi nakupa nyumba?”
“Wewe ni mjinga kabisa na unafanya mambo yako bila kufikiria. Umesahau kabisa siku niliyokwambia nasitisha mahusiano yetu ulikuwa kwenye siku zako?” Leah akashituka sana. “Umesahau eeh? Ulisahau ulikuwa umejichafua ukataka kuazima koti langu ili ujifunike?” Leah akainama na kuzidi kulia, hakuna aliyekuwa na hamu ya kuangalia mpira tena.
“Nikikwambia wewe mjinga, huamini. Unawezaje kusahau kitu kikubwa kama hicho wakati ukipanga mipango yako miovu? Sasa leo hakuna anayetoka humu ndani, na hutakaa chini mpaka useme kila kitu. Watu wote wakujue uchafu wako.” “Ataanguka Nyange jamani! Labda akae.” “Wala hata kaa huyu. Wewe kama unamuonea huruma mwambie aanze kuongea haraka, akimaliza ndio aondoke.”
“Kwani umefanyaje tena?” Mama Briana akamuuliza mdogo wake kwa upole huku akifuta machozi. “Ashura amenidanganya dada.” “Muone anavyosingizia watu! Na kwambia hatakaa abadilike huyu mchawi. Ni mshirikina huyo, kupita anavyo onekana.” “Mungu wangu Leah! Ulikuwa ukituloga?” “Sio mimi dada, Ashura ndio alinilazimisha.”“Leah wewe! Kwa nini?” Leah akainama chini.
“Mbona leo utashangaa mengi? Subiria umsikie.” “Mimi nilikuwa sina hata wazo dada, Ashura ndiye amenishawishi.” “Na kwa taarifa yako, Ashura huyohuyo mshauri wako ndiye amekuzunguka. Anakushauri wewe, huku ananitaka na mimi. Nimemuhonga na kumdanganya kidogo tu, akayasema yote.” “Na Ashura naye pia alikuwa anakutaka?” Mama Briana akazidi kushangazwa, Leah naye alishituka sana,hakutegemea kama shoga yake kipenzi angemgeuka. Ilimbidi asimulie kwa uchungu sana.
Ipo Siku, Kila La Gizani, Litawekwa Mwangani
“Unakumbuka mimi ndiye nilikutambulisha kwa shemeji?” “Tafadhali Leah. Naomba usimchoshe mke wangu, kwa maswali ya kijinga. Wewe jieleze.” “Labda angekula kwanza Nyange jamani! Naona kama amechoka sana. Ona alivyo kaukwa midomo.” “Sio midomo tu. Kakauka kila mahali. Alipata kiboko yake huko anaitwa Isa. Anampiga kama ngoma!” Mama Briana akazidi kuumia.
“Angekula kwanza.” “Hali huyu mpaka aseme kila kitu.” “Kwani ulifanyaje Leah jamani?!” “Ni Ashura dada. Mlipooana, mimi nikawa nakusifia kwa Ashura kwamba una mtunza vizuri mume wako amebadilika sana. Nikamwambia na siku hizi Nyange ana hela sana. Akasema mimi pia natakiwa kuzifaidi hizo pesa sio kuendelea kuteseka na mwanaume asiye na pesa.” “Unamaanisha Sam?” “Jamani Nyange!? Nyamaza.” Mama Briana akaingilia.
“Ndio aseme kila kitu, asiongee kwa mafumbo. Leo tunataka kujua, tulikuwa wanaume wangapi.” “Wakati huo alikuwa Sam.” “Kwani ulikuwa na wanaume wengine tena!?” Mama Briana aliishtuka sana. “Sio wakati ule jamani, dada!” Mama Briana akapumua. Leah alirudisha heshima zote. “Kumbe huwa unajitoa tu akili, unaweza kuita dada na shemeji, eeh? Endelea sasa?” Nyange naye akaingilia.
“Ndio akaniambia natakiwa kufaidi hizo pesa zako. Sasa kila nilipokuwa nakuomba hela, uliniambia niende kwa mama Briana. Ashura akaniambia jinsi ya kuzipata ni kukushawishi kimapenzi. Tukiwa wapenzi hutaninyima pesa. Ndio nikajaribu sana, ukanikataa. Ndio Ashura akanipa mbinu nyingine tena.” Leah akanyamaza kidogo.
“Lakini nilijaribisha ya kawaida dada, niliposhindwa ndio nikaenda hiyo nyingine.” “Ulifanyaje Leah?” Mama Briana akaendelea kuhoji. “Alinipeleka kwa mganga.” “Mungu wangu!” “Usishangae mama Briana, mbona bado.” “Nini tena?” “Ndio akanipa dawa, akasema wewe ukisafiri, nimshawishi Nyange akishalala na mimi, ndio dawa nitakazoweka kwenye chakula chako na chake zitashika.” Mama Briana alizidi kuogopa.
“Endelea Leah.” Nyange akaingilia. “Si ndio tukawa wapenzi sasa?” “Usinitanie Leah. Nimekwambia useme yote.” “Nimeshasema jamani!” “Nitakupiga Leah, wewe!” Leah akatulia kidogo. “Leah!” Nyange alimwita kwa ukali.
Akashituka sana na kuendelea. “Wakati ule uliposafiri, nilikuwa namsikia shemeji akisema kila siku anahamu sana na wewe, nilipomwambia Ashura, akasema huo ndio wakati mwafaka, nimwingilie chumbani kwake nikiwa uchi halifu nim….” Leah akawa kama amesita kidogo kisha akaendelea.
“Ndio tukawa wapenzi.” “Hujawahi kuwa mpenzi wangu Leah, acha uongo. Wakati wote umekuwa ukinitishia ili nilalale na wewe.” Leah akanyamaza kidogo. “Tuliposhindwa kulipia kile kiwanja, nikamuomba shemeji anisaidie kumalizia kulipia. Akakubali kwa sharti lakuandika jina lako sio langu, akasema nikimlipa pesa yake, ndio atanipa ile hati nibadilishe.”
“Kwa kweli niliumia sana, halafu ikawa kila nikimuomba pesa ana ni sainisha hanipi bure. Nikamwambia Ashura mbona zile dawa hazifanyi kazi? Nyange ananikopeshabadala ya kunipa bure? Ashura akanirudisha kwa yule mganga, yule mganga akasema ni kwa sababu ameshikwa sana na mkewe, tuwatenganishe. Akanipa dawa nyingine, lakini mambo hayakukubali. Tukarudi tena kwa mganga, ndio akasema cha muhimu nikukufunga kizazi usizae. Kama Shemeji akiona huzai atanioa mimi.” “Mungu wangu, Leah wewe!?”Mama Briana akaanza kulia tena asiamini kama mdogo wake anaweza kumfanyia ubaya wa kiasi hicho.
“Endelea.” Nyange akamkaripia tena. “Si ndio kipindi kile ukawa hupati mimba, nikajua ile dawa imeshika. Tukakaa miaka mitatu lakini Nyange akawa hakuachi lakini ile dawa ya Sam, niliona inafanya kazi.” Sam alishituka sana. “Sam tena!?” Mama Briana akauliza kwa mshituko huku akilia.
“Ndiyo dada.” “Leah wewe jamani! Sasa Sam ulikuwa una mlogea nini?!” “Ili na yeye asiniache, yaani kama kumpumbaza.” Sam akatingisha kichwa. “Ndio Ashura akaniambia turudi tena kwa mganga. Yule mganga akaniongezea dawa, lakini baada ya muda wewe ukapata ujauzito, halafu ukajua ni mtoto wa kiume.”
“Sasa Nyange akawa kila tukikutana ana kusifia tu wewe, hana muda na mimi tena. Maongezi yake yote yakawa ‘mama Briana analeta dume la nguvu’. Mimi nikawa nikiumia sana dada, kwa kuwa mimi ndio nilitakiwa kuwa ndiye nimeshika mimba sio wewe. Maana kila siku nilipokuwa nikimtegeshea Nyange anipe mimi ujauzito, nikawa sipati. Ashura akawa ananiambia labda nakosea masaa. Nilijitahidi hata ofisini nilikuwa nikimfuata kama ni siku zakupata mimba, au kama akiwa amebanwa kazini kwenye mkutano nilikuwa namlazimisha hata kwenye gari ili tu nishike mimba na siku ile isipite.”
“Nilipojaribu kwa muda bila mafanikio ya kupata ujauzito, nikaenda hospitalini kutafuta ushauri wa madaktari. Niliambiwa ni kwa sababu nimepaniki tu, lakini sina tatizo lolote la kizazi. Ndio Ashura akaniambia lazima nigaramie huyo mtoto, nitoke na Nyange kabisa tukapumzike mahali hata siku tatu ndipo nitashika mimba.” Leah bado alikuwa amesimama.
“Siku zangu zakushika mimba zilipofika tena, nikambembeleza sana Nyange tusafiri, lakini akawa hataki. Nikaona siku zile za mimi za kupata mimba zinazidi kupita bila mafanikio, ndipo nikamfuata Nyange hapa, kwa kuwa aliacha kupokea simu zangu, nikamwambia nilazima tusafiri kesho yake lasivyo nitakwambia wewe.”
“Mwanzo Nyange alikataa, ndio nikakuita ukiwa naye nikakwambia nina mazungumzo na wewe, Nyange alipoona hivyo ndio ikabidi akuage palepale, akakwambia amepata safari ya dharula lazima asafiri kesho yake. Tulifika kule tukaishia kugombana sana mpaka zile siku za ujauzito zikaisha, hatukufanya mapenzi na sikushika mimba tena.” Mama Briana alizidi kulia.
“Endelea kusikiliza mama Briana, mbona hujafika patamu. Endelea.” “Mengine tena?!” Leah akabaki anababaika. “We Leah?” Kila mtu alikuwa haamini kile anachosimulia Leah. “Si ndio Ashura akasema kuepusha hayo yote ni kumuua tu huyo mtoto. Mganga akatupa dawa nyingine.” “Mungu wangu Leah, wewe!” Mama Briana alishituka mpaka akajikuta amesimama huku ameweka mikono kichwani, akilia sana.
“Naomba unyamaze Leah, tafadhali sana. Nyamaza tu.” Mama Briana alizidi kulia. “Naomba amalize tu.” Nyange akasimama na kumkumbatia mkewe. “Njoo tukae” “Lakini dada wala sikukuwekea ile dawa ya kumuua mtoto, ndio shemeji akanikataa. Akasema hanitaki tena.”
“Nilimbembeleza sana, lakini akasema hataki tena, ameamua kuachana na mimi. Yupo tayari kwa lolote hata kama nitakuja kusema kwako, yeye amefika mwisho. Ndio nikamsimulia Ashura, nikamwambia naona nimepoteza pesa zangu bure dawa zenyewe hazifanyi kazi. Sasa hivi natumia mbinu zangu. Kidogo tuligombana na Ashura, lakini baadaye tukapatana.”
“Siku ile dada alipoonguka hapa, hata mimi niliogopa sana. Nikarudi nyumbani kwa Sam moja kwa moja nikampigia Ashura simu, nilimsimulia kila kitu, nakumwomba ushauri. Akaniambia niondoke pale kwa Sam nikakae naye halafu tutafute mwanaume harakaharaka anipe ujauzito, lakini tutegee siku za mtoto wa kiume kwa kuwa Nyange anataka mtoto wa kiume.”
“Mimba ukishakuwa kubwa na tukishajua mtoto ni wakiume ndio nirudi kwa Nyange nimwambie ni mtoto wake. Kumbe mwenzangu ananizunguka.” Leah alianza kulia sana.
“Mwanaume mwenyewe aliyenitafutia ananitesa kweli dada! Ananipiga. Vitu vyangu vyote kauza. Alikuwa ana kuja kufanya fujo pale kazini karibu kila siku mpaka nikafukuzwa kazi. Ashura alinitafutia huyo Isa, mvuta bangi, halafu kumbe alikuwa mwanaume wake. Anachukua hela kwangu, anampelekea yeye, Ashura.”
“Tumekopa naye kila benki, halafu pesa alikuwa akitumia na Ashura. Nimeugua nikaenda kulazwa hospitalini, hajaja hata kunitazama. Nimetolewa hospitali narudi nyumbani hakuna kitu hata kimoja, mpaka nguo zangu kachukua, hela zangu zote benki amechukua na sijui hata alipo. Najuta dada.” Leah na dada yake wote walikuwa wakilia.
“Nimekosa jamani, nimeamua kutulia, naomba mnisamehe. Naahidi kubadilika.”Leah akamsogelea Sam nakumpigia magoti. “Nisamehe Sam. Nakupenda. Naahidi kubadilika mpenzi wangu. Nitakuwa nakusikiliza kwa kila jambo, naomba nirudi nyumbani.” Sam alicheka kwa dharau na kunyanyuka. Aliondoka bila ya kuaga.
Leah akarudi kwa dada yake. “Nimetoka hospitalini leo asubuhi dada, sina pakwenda. Nihurumie dada yangu.” Mama Briana alikuwa akilia sana. Mke wa Chau, rafiki mpenzi wa Nyange akamsogelea mama Briana. “Pole sana Mama Briana, lakini nashauri huyu Leah akaombewe. Ni pepo huyo mtoto, ukimuacha hivyohivyo atawasumbua sana.” Chau na mkewe wakaondoka, na wageni wengine nao wakaaga na kuwaacha Nyange na familia yake.
“Nisamehe shemeji, naombeni mnisaidie.” Mama Briana alinyanyuka na kutaka kuondoka huku akilia. “Nisubiri Penninah.” Nyange akasimama na kumshika mkewe. Aliogopa asije kuanguka tena kwenye ngazi. “Sasa hapa huwezi kukaa, nenda kakae nje ya geti kwanza, usubiri mke wangu atulie, niongee naye halafu Josh atakuja kukwambia tulichoamua. Lakini hapa usiwahi kukanyaga tena. Umenisikia Leah? Ondoka sasa hivi, nisikuone hapa ndani. Haya, TOKA!” Nyange alihakikisha Leah anatoka ndipo akampeleka mkewe chumbani.
**********************
"Pole mume wangu.” “Nikupe wewe pole. Mimi ndio nimekuingiza kwenye matatizo sababu ya tamaa. Nisingelala naye siku ile ya kwanza, yote haya yasingetupata. Mimi ndio nilimfungulia mlango wala sio dawa zake. Nisamehe mpenzi wangu.” “Najilaumu kukazania ile kazi iliyokuwa ikinifanya niwe mbali na wewe! Mwishowe ukaingia mtegoni.”
“Lakini Mama Briana, wala usijutie ile kazi. Ndiyo iliyotusaidia kupata biashara zote hizi, bila ile kazi yako tusingekuwa hapa. Lakini maadamu tuna hizi biashara sasa hivi, basi inatosha. Pumzika sasa uangalie mambo ya familia.” Mama Briana akaanza kutulia.
“Asante kunisamehe mke wangu. Umenirudishia heshima kwenye jamiii, sijui ningeweka wapi hii sura yangu.” “Nakupenda mume wangu. Nimejisikia vizuri kweli ulivyosema unataka watoto kutoka kwangu tu, na hata kama ni wakike. Nilishaanza kuogopa kama nitazaa mtoto mwingine wakike.”
“Wala usiogope, wote watakuwa wetu na hata kama tutaishia na Briana tu, pia tutamshukuru Mungu.” “Asante D, mme wangu.” Nyange hakupoteza muda, hapo hapo alianza mapenzi na mkewe kumfanya atulie kabisa. Alimbusu na kumpapasa kwa muda mrefu sana. Hakumuachia mkewe mpaka alipoona akili yake imetulia kabisa.
**********************
“Ujue mwenzio ni mjamzito, wewe Nyange!” Nyange akaanza kucheka. “Ndio vizuri.” “Sasa tutamsaidiaje Leah?” “Daah! Mama Briana jamani! Acha basi hata tufurahie kidogo ndoa yetu!” “Namuonea huruma. Umemfukuza bila kula!” “Mjinga sana Leah.”
“Kwani wewe umejuaje yote hayo?” “Yaani kama Mungu tu. Nikiwa katika maswali mengi juu yake, Ashura akanitafuta, akaanza kunitaka kimapenzi. Nikamvutia kwanza kwa kumpa pesa, halafu nikamdanganya kwa kumwambia nataka kurudiana na Leahsiwezi kuwa na yeye. Si ndio akaanza kumsema vibaya shoga yake, huku akinisisitiza nisiwahi kurudiana tena Leah. Nimkubali yeye.” “Mungu wangu hawa watoto!”
“Wajinga kweli, lakini nilimfukuza Ashura na kumpiga marufuku asiwahi hata kukosea kubip namba yangu.” “Lakini lazima tumsaidie Leah. Tafadhali Nyange. Msamehe bwana. Kwanza ona Mungu ametupa mtoto mwingine, tena safari hii wala hatujahangaika.” “Ungejua mzee Nyange anavyo kuombea wewe mama Briana, ungeshangaa. Muulize Sam. Wakati ule nilipokurudisha kijijini kwenda kuomba msamaha, alikuwa anatuambia maneno hayo, mpaka Sam alibaki na mshangao. Anakuombea sana yule Mzee.” “Jamani baba yangu. Namshukuru sana Mungu kwa ajili yake.”
**********************
Haikuwa kawaida ya Sam kulala bila ya kuongea na Sonia. Usiku huo Sonia akasubiria simu ya Sam, mpaka alipoamua kumtafuta kwa kumtumia ujumbe. ‘Uliondoka bila kula. Utarudi?’ Kimya kilipita bila Sam kurudisha ujumbe. ‘Kaka Sam?’ Sonia akatuma ujumbe mwingine. Sam aliondoka pale bila ya kusema chochote mbele ya Leah, na wala hakuaga mtu yeyote.
Baada ya muda Sam akapiga. “Umeniogopesha!” “Kwa nini?” “Nimeona kimya. Halafu uliondoka bila kuaga.” “Sikujua kama unasubiria simu yangu. Nilijua utakuwa ukiongea na yule uliyemwambia utampigia baadaye nilipokuja kukugongea chumbani kwako.” Sonia akanywea.
“Hapana kaka. Yule siwezi kuongea naye usiku.” “Yule, unaongea naye saa ngapi?”Sonia akajua Sam anataka kumjua mtu aliyekuwa akiongea naye, na alijua hakufurahia.
“Ni yule mwalimu, kaka!” Kimya, akajua hajaridhika. “Alikuwa amenipigia tokea asubuhi na mchana nilikuta amenipigia zaidi ya mara tano, lakini nilikuwa na kazi nyingi nikashindwa kuongea naye. Nilipomaliza kazi, ndio nikaona nimtudishie simu zake.” Bado Sam alinyamaza, Sonia alijua tabia ya Sam kutaka kuambiwa kila kitu.
“Kaka Sam?” “Nakusikiliza.” “Asubuhi alikuwa anataka kujua kama nitaenda, alipoona sikwenda akataka kujua kwa nini sikwenda. Na kama nipo tayari kuanza yale madarasa ya ziada jumatatu.” Sonia akatulia kidogo. “Nakusikiliza.” Sonia alijua labda Sam angetaka wazungumzie maswala ya Leah, lakini Sam alionyesha kana kwamba hakuna lililotokea.
Alitulia kabisa, kumuashiria Sonia aelezee yote waliyo zungumza na mwalimu wake. “Ndio nikamwambia, sitaweza kwenda nyumbani kwake, naona inatosha kufahamiana naye palepale darasani na nilimshukuru kwa kutaka kunisaidia kunifundisha peke yangu muda wa asubuhi, nikamwambia sitaweza kwa kuwa ninafanya kazi nyumbani kwa watu. Nilazima nimalize kazi zangu kwanza, ndipo niende shuleni jioni. Ndio akas…” Sonia alitaka kuropoka, akakumbuka anaongea na Sam. Akaamua kukatisha.
“Kwa hiyo ndio hivyo tu kaka.” “Akasema nini?” Sam alikuwa akimsikiliza kwa makini sana, alisikia kila neno alilotamka. “Sonia?” Sam akaita tena. Sonia alinyamaza kwa woga. Alijua akimwambia Sam itakuwa ni tatizo jingine kubwa zaidi.
Sam alikuwa akimchunga Sonia kupita kiasi. Sonia aliogopa kumwambia wazo jingine alilokuwa amepewa na mwalimu wake, alijua kabisa italeta shida.
“Sonia?” “Ndio hivyo kaka Sam. Nilikataa.” “Naona umechoka. Usiku mwema, nitakuona jumatatu jioni.” “Kesho hauji tena?” Sonia akamuuliza huku akijua amemuudhi. “Uliniambia kesho utakuja tukae wote.” Akaongea kama anayembembeleza. “Nitaangalia. Usiku mwema.” “Asante na wewe.” Alijua Sam amekasirika lakini asingethubutukumwambia mazungumzo yote. Alijua kesho yake Sam atakuwa amesahau kila kitu na maisha yataendelea kama kawaida.
**********************
Haikuwa hivyo hata kidogo. Kesho yake asubuhi Sam alimtumia ujumbe Sonia kumtaarifu kuwa hataweza kufika kama alivyoahidi na siku nzima alikuwa kimya kabisa, bila ujumbe wala simu.
Usiku mapema sana, Sam akatuma ujumbe mfupi tu. ‘Usiku mwema.’ Sonia akaiangalia simu yake kwa muda mrefu, akitamani kumpigia lakini akaogopa. ‘Labda amechoka, nimwache kesho atakuwa sawa.’ Alijiliwaza.
**********************
Kama kawaida bila kuchelewa jumatatu jioni Sam akafika nyumbani kwa Nyange kumchukua Sonia kumpeleka shule, akiwa anaonyesha yupo busy na simu za kazini kwake, alimshusha na kumuaga kwa kumpungia mkono huku akiongea kwenye simu, baadaye alirudi kuja kumchukua Sonia ili kumrudisha nyumbani.
“Pole na kazi.” Sonia akajaribu kuanzisha mazungumzo baada ya kumuona Sam yuko kimya sana. “Asante na wewe pole na kazi na shule.” “Asante.” Hapakuwa na mazungumzo yeyote yale. Sonia akajua Sam amekasirika sana.
**********************
“Kaka! Leo ulikuwa na kazi nyingi?” “Sio sana. Vipi?” “Hukunipigia simu mchana.” Sam hakujibu, ikambidi amwambie kila kitu. “Yule mwalimu jana alikuwa amenipa ushauri.” Sam akamgeukia.
“Alisema kama hapo ninapoishi nakuwa na kazi nyingi sana, naweza kwenda nikaishi naye nyumbani kwake kwa muda, ana chumba kingine hapo kwake wala hakitumii, naweza kukitumia mimi, ili nipate muda wakusoma zaidi.” Bila yakuongeza neno, Sam akageuza gari, akarudi mpaka pale wanaposomea kina Sonia.
Alimkuta huyo mwalimu na wanafunzi wengine bado wamesimama nje. “Kaka! Vipi?” “Njoo.” Sam akataka Sonia amfuate. “Samahanini.” Sam akawasogelea wale wanafunzi na mwalimu wao. “Bila samahani.” Mwalimu akajibu.
Sam akamgeukia dada aliyekuwa akisoma na Sonia. Yeye alionekana mtu mzima kidogo. “Wewe ulialikwa jumamosi kwenda kwa huyu mwalimu wenu kwa ajili ya kufahamamiana zaidi?” Yule dada akakunja uso. “Aka!” Akakataa. “Na wewe?” Sam alimgeukia mwanafunzi mwengine wakiume. “Hapana sikualikwa!” “Na wewe?” Wote hawakuwa wamealikwa.
Sonia alibaki na mshangao. “Huyu mwalimu wako alitaka uende nyumbani kwake wewe peke yako.” “Kwa nini sasa?!” Sonia akauliza kwa mshangao. “Muulize mwenyewe?” Mwalimu akabaki na kigugumizi.
“Kwa nini umenidanganya? Ulitaka..” Sonia akakumbuka unyama aliofanyiwa na baba wa mtoto wake. Taratibu machozi yakaanza kumtoka. “Twende Sonia.” Sam akamshika mkono na kutaka kuondoka. Lakini ticha akaharibu kwa kumrushia neno akijikosha. “Una mng’ang’ania, utamuoa wewe?” Aliropoka tu kama kujitutumua mbele ya wanafunzi wake.
Sam alisimama na kugeuka. “Unasema?” “Umenisikia vizuri sana.” Sam akarudi mpaka pale alipokuwa amesimama yule mwalimu akampiga ngumi moja ya pua kwa hasira na kubaki amemshikilia shati. “Amekwambia anataka umuoe wewe? Umeanza kumshawishi ahamie kwako. Unajua alipotoka huyu? Na ni sikusikie unampigia tena simu, leo ndio iwe mwisho hata wakumtumia ujumbe. Umenisikia?”
“Ungemuacha tu kaka!” Sonia alikuwa akitetemeka kwa hofu huku machozi yakimtoka. Hakuwahi kumuona Sam katika hali hiyo. Huyo mwalimu alikuwa akitokwa damu puani. Sam mwenyewe alijishangaa, hakuwahi kufanya hivyo tokea kuzaliwa. Hata alipokuwa mdogo hakuwahi hata kupigana na wenzake.
Walirudi kwenye gari bado Sonia alikuwa akilia. “Samahani sana Sonia. Sijui nilipatwa na nini! Sijawahi kufanya hivyo hata mara moja. Aliniudhi sana.” Sonia akabaki analia huku amekumbatia mkoba wake wa madaftari.
Walifika nyumbani, walimkuta mama Briana akimsubiria mumewe. Sonia akamsalimia na kuingia moja kwa moja chumbani kwake, bila hata kumtizama usoni, akajitupa kitandani kwake. ‘Hasira hizi ni kwa ajili ya yule mwalimu kweli au ni Leah?’ Sonia aliwaza huku akilia.
**********************
“Kwema huko?” Ikabidi mama Briana amuulize Sam aliyeingia na kukaa kwenye kochi na yeye akiwa kimya. “Mbona leo mmerudi tofauti?” “Kwema.” Sam akajibu kwa ufupi tu. “Mbona huonekani kama ni kwema?” Sam alimpenda sana mama Briana. Walikuwa na ukaribu sana tangia yupo na Leah. Walikuwa wakiongea mambo mengi sana, na mara nyingi mama Briana alikuwa akimshauri vizuri.
“Wewe Sam?” “Daah! Leo nimeharibu shem.” “Nini tena?” “Nimempiga mwalimu wa Sonia.” Mama Briana alianza kucheka. Alicheka sana bila ya kumaliza. “Usicheke bwana! Sonia ameogopa kweli! Hapo alikuwa analia njia nzima.” Mama Briana alizidi kucheka mpaka machozi.
“Ujue utaishia kumfundisha huyo Sonia wewe mwenyewe? Wewe fanya mchezo Sam.” “Aliniudhi bwana! Alianza kumpigia simu mara kwa mara, halafu anataka kumfundisha yeye peke yake, tena asubuhi! Sonia alipomwambia yeye anafanya kazi za ndani, eti anamwambia ahamie kwake!” “Haa! Kweli huyo alistahili kuchapwa. Hana adabu kabisa.” “Umeonaa?” Mama Briana alizidi kucheka.
“Ndio maana nakupenda mama Bree. Kaongee na Sonia basi.” Mama Briana akazidi kucheka. Kidogo Sam akatulia. “Naomba ukamwangalie basi, kama amenyamaza.” Mama Briana akamfuata chumbani kwake.
“Mbona umemuacha Sam sebuleni hujampa chakula?” “Kwani hajaondoka?” “Yupo.” “Nakuja.” Mama Briana akatoka bila ya kuzungumzia jingine hata kumuuliza kwa nini analia.
**********************
Sonia akajifuta machozi na kuelekea jikoni moja kwa moja. Harakaharaka Sam naye akamfuata. Sonia akashitukia Sam yupo nyuma yake. “Nakutayarishia chakula.” “Asante. Samahani sana Sonia, yule mwalimu aliniudhi sana.” “Lakini kaka, ungeongea naye tu. Nimebakiza muda mchache tufanye mitihani. Nitafanyaje?”
“Usijali tutatafuta mwalimu mwingine. Sitaki watu wakuchezee Sonia. Nataka utulie na shule. Sikuwa na nia mbaya.” Walikaa huko jikoni nakuanza kula kimya kimya. Walipomaliza kula wakatoka nje ya jiko, wakakaa kwenye ngazi kama kawaida yao ili kupata muda mtulivu wa mazungumzo pamoja.
“Samahani Sonia.” “Basi yameisha kaka.” Sam akatulia. “Nikuulize kitu kaka Sam?” “Uliza tu.” “Au ulikuwa una hasira ya Leah?” “Leah?!” “Namaanisha yale aliyokutendeawakati wewe ulikuwa na mapenzi naye ya dhati.” Sam akabaki kimya. Hakutegemea Sonia angegusia hilo, akavuta pumzi kidogo na kumwangalia. Akakuta ametulia tu.
“Unajua Sonia, siwezi kusema kama kulikuwa na mapenzi ya dhati kati yetu. Hatukuwahi kupata muda mtulivu na Leah kama hivi, eti tukakaa na kuongea kama tunavyoongea na wewe hivi! Hata mara moja. Wakati wote yeye alitoa amri ya kitu gani kifanyike, au tulipokuwa pamoja alikuwa busy na simu yake au alikuwa akisafiri mara kwa mara.”
“Wakati mwingine alikuwa akiondoka hata usiku, na kuniacha kitandani, ananiambia anarudi huku kwa dada yake, ilimradi tu fujo. Na mimi nilikuwa sina sauti kwake hata kidogo. Hakuna kitu ambacho ningeweza kumwambia akanisikiliza.” “Pole kaka.”
“Nafikiri ni msingi mbovu tulioanza naye au haikuwa bahati yangu tu. Wakati mwingine najilaumu nasema labda ningekuwa na uwezo kidogo wakifedha, pengine angetulia. Sijui! Lakini hatuna kitu kinachotushikilia pamoja hata kidogo. Hatuna kumbukumbu zakutufanya kutamani kurudiana zaidi ya kumbukumbu za kuumizana tu.”
“Inawezekana na yeye ana malalamiko yake mengi tu juu yangu, lakini binafsi sina kitu ninachoweza kunifanya nikatamani au hata kufikiria kurudiana naye. Huo ni ukurasa niliokwisha kufunga, na kwa mara ya kwanza tangia kukutana na yule dada, najisikia nipo huru.”
“Sina sababu yakunifanya niwe na hasira kwa ajili yake hata kidogo. Ila nikiri tu nilijisikia vibaya nilipokuja siku ile, nikaa karibu dakika ishirini halafu wewe hukutoka kuja kuniangalia pale sebuleni, halafu nilipokuja kukugongea chumbani na kuta unaongea na simu! Nilihisi kama na wewe unanipuuza! Halafu ulishindwa kuniambia mlichokuwa mnaongea. Nilijiona sina thamani Sonia!” Sonia akajisikia kuumia.
“Hapana kaka! Siwezi kukupuuza hata kidogo. Siku ile sikujua kama upo sebuleni. Nisingeweza kukaa ndani wakati wewe upo nje. Siwezi kufanya hivyo hata kidogo. Halafu niliogopa kukwambia kama alitaka nihamie kwake. Niliingiwa na hofu tu, sio kwamba sikuthamini. Sina mtu mwingine anayenijali kama wewe kaka. Lakini niliogopa tu. Naomba unisamehe.” Sonia alikuwa hachoshi kuongea naye.
Sam alijisikia vizuri mpaka rohoni kuona ana heshimiwa na huyo mrembo. “Tusameheane. Hata mimi nilikosea, ningekwambia tu siku ileile wala nisingebeba chuki siku zote hizo.” “Ndio maana jumapili hukuja?” Sonia akauliza tena kwa kubembeleza. “Tuyaache hayo.” Waliendelea kuongea kwa muda kidogo, Sam akaaga.
Walimkuta Nyange na mkewe sebuleni. “Tutakupa chumba kabisa hapa kwetu, Sam.” Nyange akamtania. “Hamna bwana!” “Naona umeamua kukaba kweli kweli!” Mama Briana akambonyeza mumewe. “Nyange wewe!” “Mimi simtanii. Kuna chumba tena kikubwa tu pale kwa Josh, ahamie kabisa hapahapa, alinde vizuri. Kwani kule si amekodisha? Hapa nampa buree.” “Nyange wewe!” Mama Briana akashangaa. “Msamehe mwaya huyu. Amechoka.” “Fimbo ya mbali haiuwi nyoka Sam. Haya, wewe endelea kuzubaa, atabebwa huyo mchana kweupee.”
“Hawezi bwana! Sonia ametulia sana.” “Sawa Sam. Sisi tupo kukufuta machozi.” Sam akaondoka huku akicheka. “Nyange wewe! Ujue mi naheshimiana sana na Sam? Acha kumtania bwana!” “Unafikiri namtania? Sam ni kijana mzuri sana, ametulia, anajituma na ndio yupo kwenye ujenzi. Hivi unajua aliniomba niende kwenye kiwanja chake?”
“Kwa nini?” “Nikapaone na nimshauri. Amenipa heshima kama kaka! Tulitoka pale tukapata muda mzuri sana wa maongezi. Ukweli amejitahidi sana. Kiwanja kikubwa, kizuri na amenunua sehemu nzuri. Lakini ninacho muhurumia naona ana mzigo mkubwa kweli!”
“Kwa kazi aliyonayo, ajenge, halafu pale alipo analipa kodi, tena analipa ya mwaka, haya anategemewa kwao tena nikikwambia anategemewa, ujue anategemewa kweli kweli. Anasomesha wadogo zake wakiume wawili na wakike mmoja na sasa hivi tena kajiingizakwa Sonia.” Mama Briana akaanza kucheka.
“Sikutanii, hiyo nayo biashara nyingine. Tena anaonekana anampenda kweli huyu mtoto. Ona anavyohangaika naye. Atachanganyikiwa! Anahitaji msaada. Na kwa kuwa ameonyesha kutuheshimu sana tokea zamani, sio mbaya tukamsaidia.” “Jamani Sam! Kweli anahitaji msaada. Nikijana mdogo lakini anajituma kweli! Nitaongea naye vizuri. Lakini akihamia hapa uache kuwatania bwana, D.” Nyange alianza kucheka. “Nitafunga mdomo, nibakie kujiangalizia tu. Patakuwa patamu humu ndani! Ngoja Sam ahamie.
**********************
Mama Briana alishaanza kulemewa, ujauzito ulishakuwa mkubwa, alionekana kuhitaji msaada wa karibu zaidi. Siku hiyo asubuhi Sonia akashangaa kuona dada yake haamki kumtayarishia kifungua kinywa mumewe.
Wakati anapika uji wa Briana aliamua kumtayarishia na Nyange kifungua kinywa kama alivyomuona mama Briana akifanya, akaweka mezani. Nyange alikula na kuondoka kwenda kazini, lakini bado mama Briana alikuwa chumbani kitu kilichomtia wasiwasi Sonia.
Aliendelea na shuguli zake huku akimsubiria aamke. Alipoona kimya akamfuata chumbani. “Dada? Dada?” “Ingia Sonia.” Sonia alikuwa amembeba Briana. “Nimeona huamki. Mzima?” “Najisikia tumbo linaniuma kweli na sio kawaida.” “Unataka twende hospitali?” “Tusubiri kidogo.” Sonia alimletea chai palepale kitandani nakuendelea kuongea naye.
“Vipi shule yako?” “Unajua kaka Sam kampiga mwalimu wangu?” Mama Briana alianza kucheka tena. “Kweli dada! Kaka alibadilika, hujawahi kumuona kaka Sam amekasirika vile! Alimpiga ngumi moja mpaka yule mwalimu alianza kuvuja damu. Hapa nilipo sijui nani atanifundisha!” Mama Briana alizidi kucheka.
“Unacheka!? Yaani mpaka naona aibu kurudi kwenye lile kundi letu tena, kwa fujoalizofanya kaka.” “Usiogope bwana! Yule mwalimu alifanya vibaya. Fikiria mwenyewe Sonia, kama angepata msichana mwengine asiye na akili si ndio angemrubuni, akaondoka hapa na kwenda kuishi naye? Au unafikiri shida yake ni kukufundisha tu?”
“Amekuona mzuri hivyo, akaingiwa na tamaa, basi. Hana lolote la maana.” “Sasa mimi nina uzuri gani jamani dada? Angemuona dada Leah je?” Mama Briana alianza kucheka tena. “Sikatai kama Leah ni mzuri sana, lakini watu wanaangalia mambo mengi kwa msichana, Sonia. Sio nje peke yake. Wewe umetulia mdogo wangu, unanidhamu,upendo, unajituma na pia ni mzuri, usijidharau au kujilinganisha na Leah hata siku moja.”
“Kwa hiyo nirahisi mtu yeyote kuvutiwa na wewe.” “Tena aniache kabisa. Yaliyonipata maishani yanatosha asiniongezee mengine.” Kidogo Sonia akaanza kupooza usoni.
“Nini sasa?” “Hivi dada, unafikiri kuna mwanaume anaweza kunipenda akijua nina mtoto? Tena niliyempata nikiwa shuleni?” Sonia alianza kutokwa na machozi. “Kwani mtoto ndio nini? Mtu akikupenda, amekupenda tu. Kwani wangapi wanaolewa walishakuwa na mahusiano kabla ya waume zao, lakini hawakubahatika kupata watoto?”
“Au wanaishia kutoa tu mimba? Lakini wewe umekubali aibu kwenye jamii, umebeba mimba na ukajaliwa mtoto. Kwani baba yake yuko wapi?” “Ni habari ndefu dada, lakini ujue wala sikuwa na mahusiano ya kimapenzi na huyo baba yake Kana. Alikuwa ni baba wa rafiki yangu.” Mama Briana alishtuka sana. “Ilikuwaje?” Ikambidi Sonia amuelezee na Mama Briana kisa chote.
Mama Briana aliumia sana. “Pole sana Sonia.” “Asante dada. Lakini nashukuru katika hilo nimepata mtoto, sijaambulia patupu.” Mama Briana akamuhurumia sana Sonia huku akimshangaa.
“Pole mdogo wangu. Lakini ona Mungu alivyokusaidia. Umempata Sam, amekurudisha shuleni. Hujapoteza kitu.” “Sio shule tu, kaka Sam ananisaidia mambo mengi sana. Unajua anamsomesha na mtoto wangu?” “Kweli?!” “Kweli dada. Yaani namshukuru sana Mungu kwa ajili yake.”
“Jamani Sam! Nimkarimu sana!” “Namshukuru Mungu kumleta kaka Sam katika maisha yetu, dada. Hatuna ndugu, tulikuwa mimi na mama yangu tu. Mungu akatuongezea Kana, amekuja na kaka Sam, haya sasa hivi na nyinyi. Namshukuru sana Mungu.” Mama Briana alifikiria kidogo.
“Kwani baba yako yuko wapi?” “Mama alisema alifariki, na wala sijui ndugu wa upande wa baba.” “Na ndugu wa mama yako?” “Unajua mama alikimbilia huku Tanzania kipindi kile cha vita nchini kwao Rwanda, akiwa msichana mdogo sana. Anasema siku moja alienda kuchota maji mbali kidogo na kijijini kwao, yeye na marafiki zake. Kurudi hapo kijijini, wakakuta kijiji chote kimechomwa moto.”
“Hapakusalia ndugu yake hata mmoja! Ndio yeye na wenzake wakakimbilia huku. Walishakaa sana Shinyanga pale kwenye kambi za wakimbizi. Lakini yeye alibahatika kazi za ndani kwa mtu mmoja, anasema alikuwa kiongozi serikalini, ndio hata wenzake walipokuwa wanarudishwa Rwanda yeye alibaki, na hakutaka kurudi tena huko alisema ni kama kwenda kujitonesha kidonda cha vifo vya ndugu zake na hakuwa na sababu tena ya kurudi tena Rwanda.” “Jamani Sonia. Pole sana. Una historia zakusikitika kweli!” “Asante dada.” Waliendelea kuongea huku Mama Briana akilalamikia maumivu.
**********************
Alipoenda chooni aliona anatokwa damu. Mama Briana alianza kulia sana. Bila kupoteza muda, Sonia akampigia simu baba Briana. Ndani ya muda mfupi, akafika na kumkimbiza mkewe hospitalini.
“Mtoto wangu!” Mama Briana alizidi kulia. “Usiogope bwana! Kila kitu kitaenda sawa.” Alipopimwa, aliambiwa mtoto yupo salama kabisa ila anatakiwa kupumzika kabisa asifanye kazi.
“Heri umwambie dokta. Mama Briana hatulii!” “Sasa usipoangalia utampoteza huyo mtoto.” “Sasa hivi nitatulia. Sitaki kumpoteza huyu mtoto.” Alipumzishwa wodini kwa muda wa Juma moja akaruhusiwa kurudi nyumbani kwa masharti ya kuendelea kupumzika.
**********************
“Itabidi kutafuta mtu mwingine wa kazi ili amsaidie Sonia. Atalemewa kazi zote peke yake na shule.” “Hilo wazo zuri. Lakini tutapata wapi mtu aliyetulia? Sitaki tuje kuanza kupata pasua kichwa.” “Nitaongea na Sonia, kama huko alipotoka kuna mtu mzuri, tumuombe G amlete.” Kweli mama Briana aliabadilika sana. Hakutaka kumpoteza mtoto wake ambaye bado hakuwa akijua jinsia. Alikuwa na kazi ya kula na kulala tu.
**********************
Shule ya Sonia ilihamia nyumbani, Sam akiwa mwalimu mkuu na alimtafutia walimu wengine wakumfundishia palepale nyumbani. “Dada anatafuta msichana wa kazi. Natamani kumuomba mama ndio aje kumsaidia. Lakini namfikiria Kana, nitamuweka wapi? Naogopa kumtenganisha na mama. Amemzoea sana mama, kama mama yake mzazi. Lakini najua hii kazi ingemfaa sana mama yangu. Ningefurahi kuja kuishi na mama yangu tena. Zamani tulikuwa marafiki sana na mama.” Sonia alianza kuongea na Sam usiku huo kama kawaida yao, nje ya jiko la Mama Briana kwenye ngazi.
“Mama Briana anakupenda sana Sonia. Jaribu kumpa hilo wazo uone atakushauri vipi?” Mara simu ya Sam ilianza kuita. “Nani anakupigia simu usiku huu?” Sonia aliuliza kwa sauti ya wivu kidogo. “Sijui! Hii namba siijui kabisa.” Sam akajibu kwa kujitete kidogo.
Alipoona Sonia ameinama na kunyamaza gafla, akaamua asipokee, akakata nakurudisha simu kwenye mfuko.
Baada ya muda ikaanza kuita tena. Sonia bado alikuwa ameinama, Sam akaitoa simu na kubaki akiiangalia. “Ngoja nizime kabisa isitusumbue.” “Ungepokea tu, huwezi jua labda yupo mtu anashida, anataka msaada wako.” Sam akapokea.
Alimsikia Leah akilia sana. “Leah?” Sonia aliposikia jina la Leah, akataka kuondoka. Sam akamshika mkono. “Usiondoke bwana, si bado tunaongea?” Sonia akarudi kukaa. Sam bado alibaki akimwangalia Sonia. “Usiondoke. Sawa?” Sonia akatingisha kichwa kukubali.
“Leah?” “Naomba nisaidie Sam. Nahisi ni uchungu. Nisaidie unipeleke hospitali. Tumbo linauma sana, na nipo peke yangu.” Sam akatulia kidogo kama anayefikiria, akamgeukia Sonia. “Leah anaumwa, anaomba nimpeleke hospitalini.” “Inabidi uwahi.” Sonia akajibu.
“Kwa nini hukumpigia simu mama Briana?” Sam akamuuliza Leah. “Simu yake imefungwa.” “Nyange?” Akamuuliza tena. “Alinipiga marufuku nisiwahi hata kukosea kubip simu yake. Alisema kama nina shida nimtafute mama Briana.” “Basi nakuja.” Sam akaondoka, na Sonia alikwenda kumwambia mama Briana.
**********************
Leah alikuwa amepewa hela na Nyange yakulipia kodi ya chumba kimoja, na ya matumizi. Na kwa kuwa alikuwa na vyeti vizuri, alijua mara baada ya kujifungua atatafuta kazi nyingine.
**********************
Sam alimkuta amevimba sana uso na jicho la upande mmoja ni jekundu sana. Alilalamika maumivu kila mahali. Ni kama mtu aliyekuwa amepigwa sana. Sam hakutaka kumuuliza kulikoni. Akamsaidia kusimama na kumuingiza kwenye gari yake.
Aliendelea kulia maumivu, njia nzima. Wakati Sam anamshusha kwenye gari wakiwa hospitalini, Leah akaanza kutokwa na damu nyingi sana. Sam aliogopa, akambeba mpaka mapokezi. Aliingizwa chumba cha kujifungulia, Ilimbidi Sam ampigie simu Nyange.
“Hali yake sio nzuri kabisa. Kwanza anaonekana kama amepigwa sana, pili anatokwa damu nyingi sana.” “Daah! Pole sana Sam. Na mimi ndio nimeingia tu hapa ndani toka kazini, hata mama Briana sijamsalimia, nimemkuta anaoga. Sitaki mama Bree ajue kabisa, najua atashituka sana. Huyo mwanamme wake yuko wapi?”
“Sijui! Mimi nimemkuta na dada mmoja, amejitambulisha kama mpangaji mwenzake.” “Basi huyo mwanaume ndio atakuwa amempiga halafu akaondoka. Sasa mimi siwezi kuja, nikitoka tu hapa mama Briana atashituka sana. Lolote litakalotokea naomba unijulishe.” “Sawa.” Nyange akakata simu na kubaki akiwaza sebuleni.
Kidogo akamsikia mama Briana anashuka ngazi. “D! Mimi nipo tayari.” Nyange alishitukia mama Briana alishavaa. “Unaenda wapi!?” “Si hospitalini! Kwani wewe hujasikia Leah mgonjwa sana?” “Wewe umesahau ulivyoambiwa upumzike?” “Napumzikaje na mdogo wangu anaumwa!?”
“Atakuwa sawa tu. Twende ukapumzike.” “Hapana Nyange. Naomba unipeleke.” “Huwezi kwenda mama Briana, twende tukalale, usitafute matatizo mengine. Kwanza yupo na Sam atakuwa sawa tu.” Mama Briana akaanza kulia.
“Tatizo lako wewe mama Briana, mbishi bwana! Basi hapo utalia wee mpaka uende.” Mama Briana akazidi kulia. Sonia akabaki akiwaangaa, asielewe moyo wa mama Briana.
Kwa yote Leah aliyomfanyia na bado leo analilia kwenda kumuona! Alibaki akimshangaa anavyo mlilia Leah asielewe hata kidogo. “Basi bwana, twende. Lakini ukumbuke nilishakuonya hivyo! Nisubiri nikajimwagie maji kidogo.” “Asante.” “Asante gani wakati wewe mbishi bwana. Hushauriki!” Mama Briana akaanza kucheka.
“Wewe cheka tu, nitakurudisha sasa hivi ukalale.” “Twende bwana Nyange, tumuwahi mtoto.” Nyange alijitayarisha haraka haraka, wakaelekea hospitalini.
**********************
Walipofika ndio Leah naye anapelekwa chumba cha upasuaji baada ya kushindwa kujifungua kawaida. “Pole sana Leah mdogo wangu. Mungu atakusaidia utakuwa salama wewe na mtoto.” “Asante dada. Kwani utaondoka?” “Hatuondoki mpaka utoke.” “Asante.” Leah alipoondoka tu kupelekwa chumba cha upasuaji, mama Briana akaanza kulia sana.
“Nani kampiga tena? Ona alivyovimba.” Sam alikuwa kimya kabisa ameshika shavu, alishindwa hata kuongea. Ilikuwa ngumu kumtazama Leah mara mbili jinsi alivyoharibiwa sura. “Itakuwa huyohuyo bwana ake, Isa.” “Kwani alirudi kuishi naye tena? Si ulisema ulimpa pesa za kupangisha chumba?” “Sijui! Uje kumuuliza mwenyewe.” Mama Briana aliendelea kulia. “Sasa nikwambie kitu Penninah, mke wangu? Badala ya kurudi wote nyumbani naona utahamishiwa wodini na wewe. Wewe tulia tu atakuwa sawa.” Mama Briana akakumbuka afya yake, aligopa, akatulia kidogo.
**********************
“Lazima nimjulishe mama nyumbani. Mama atanilaumu sana, akijua Leah anaumwa halafu sijamwambia.” Mama Briana akampigia simu mama yao. “Nakuja kesho.” Mama yao alishakuwa amechanganyikiwa, maana Leah ndio alikuwa kipenzi chake.
**********************
Walikaa hapo, kwa muda mpaka Leah alipotolewa. “Yupo wapi mtoto?” “Nasikitika sana tumemtoa mtoto lakini alikuwa ameshakufa, hata mama mwenyewe amepoteza damu nyingi sana, na anaonekana amevunjika mbavu za upande wa kulia. Yupo kwenye maumivu makali sana.” Dokta aliendelea kueleza lakini Mama Briana alizidi kulia.
Leah alipelekwa wodini. “Mimi naona hakuna kitu cha kufanya twendeni tu nyumbani tutarudi tena kesho.” Nyange alimshika mkewe na kuondoka.
**********************
Sababu ya kuchelewa kulala, Nyange alipoamka asubuhi alizima simu ya mkewe ili watu wasimsumbue na kuacha maelekezo mtu yeyote asimuamshe mkewe, mpaka atakapo amka yeye mwenyewe. Kwa kuwa Sonia alishapika uji wa mgonjwa, Nyange aliubeba huo uji mpaka hospitalini akamuachia Leah, yeye akatoka kwenda ofisini.
Ilipofika mchana Mama Eliah alitua jijini na kumkuta dereva wa ofisini kwa Nyange akimsubiria, alimchukua mpaka hospitalini alipolazwa Leah na kuondoka. Alilia sana alipomuona Leah kipenzi chake yupo katika hali ile tena peke yake.
“Dada yako amekuja hapa tokea asubuhi?” Mama yao akamuuliza Leah. “Sijamuona mama.” Hasira zilimpanda sana. Mbali ya Leah kuwa ni kiziwanda wake, alikuwa kipenzi chake kikubwa. Mbele ya mama yao, Leah alikuwa kama malaika, hakuwahi kukosea hata mara moja.
Hakuna kosa la Leah, mama yake asilitolee sababu. Alikaa pale mpaka jioni bila mama Briana wala Nyange kutokea. Ilipofika jioni Nyange alitoka ofisini, akaenda nyumbani kumchukua mama Briana ili warudi hospitalini.
Roho Ya Uharibifu Haitulii Mpaka Itimize Kusudi
Walipofika hospitalini mama Briana alifurahi sana kumuona mama yake. “Mama!!” Alimsogelea na kumkumbatia kwa furaha sana. “Shikamoo mama.” Alisalimia huku bado amemkumbatia mama yake. “Pole na safari, mama yangu.” Mama Briana alishangaa mama yake yuko kimya na wala hajibu kitu.
Wasiwasi ukamuingia Nyange asijue Leah amesema nini kwa mama yake. Nyange naye akaamua kujaribisha. “Nilimtuma dereva akufuate kituo cha mabasi kwa kuwa nilikuwa na wageni ofisini tokea asubuhi. Hivi hapa wameondoka ndio nikaenda kumfuata mama Briana nyumbani tukaja hapa.” “Sawa.” Josh alishaleta chakula cha mgonjwa.
Nyange alipoona majibu mafupi akaamua atulie kwanza huku akimuhurumia sana mkewe aliyekuwa amepooza baada ya furaha yake yote kuzimwa gafla. Hakutaka mkewe apatwe na tatizo lolote litakalo haribu mimba yake tena.
Mama Briana akamsogelea Leah. “Unajisikiaje sasa hivi?” Kabla ya kujibu, mama yao akadakia. “Kweli umenyima haya! Tokea jana, leo ndio unakuja eti, ‘unaendeleaje Leah?' Sasa hivi ndio unakumbuka kama kuna mgonjwa?” “Mbona sielewi?” “Mtanielewa vipi na nyinyi siku hizi maongezi yenu ni ofisini, pesa, nipo busy?”
“Nyinyi ndio wakumtuma mfanyakazi kumletea chakula Leah! Eti na wewe umelala gorofani kule, mnamtuma dereva aje anipokee bila hofu wala aibu! Eti sasa hivi ndio mnakuja! Ubinadamu umewaisha kabisa, sababu ya pesa tu?”
“Tangia asubuhi hupatikaniki kwa simu na mdogo wako amelazwa hapa mahututi! Eti mchana ndio unanipigia simu! Kweli pesa huleta jeuri. Sasa hivi ndio nawaelewa, ile simu mliyonipigia jana ni kutaka nije kumlea mwanangu mwenyewe. Sasa nimekuja.” Huyo mama alikuwa muongeaji kupita kiasi, hata Leah mwenyewe hamfikii. Akiamua kuongea huwezi kuweka neno katikati mkaelewana.
“Lakini mama Briana na yeye mgonjwa, mama. Na jana alilala muda mbaya sana, kwa kuwa tulikuwa hapa hospitalini tukimsubiria Leah atoke kwenye chumba cha upasuaji.” “Mgonjwa? Alikuwa amelazwa wodi gani?” “Alisha ruhusiwa, amepewa mapumziko ya nyumbani.” “Alaaa! Kwa hiyo hata kupokea simu ni usumbufu, kupiga simu kujua kama nimefika salama au la, pia ni shida?”
“Hata kumjulia hali mdogo wake pia usumbufu?” “Haruhusiwi kuendesha gari, mama.” “Dereva wa kunifuata mimi yupo, lakini wa kumleta yeye hapa hayupo?” “Mimi huwa ndiye namwendesha. Mimi ndiye dereva wake, sipendi mtu mwingine amwendeshe. Yule dereva kuna wakati mwingine hayupo makini, sipendi amwendeshe mama Briana akiwa na hali hiyo.”
“Mimba nayo ugonjwa? Hata simu haruhusiwi na dokta?” Nyange aliyeamua kumtetea mkewe kwa kuwa alijua sio muongeaji sana, alizidiwa nguvu.
“Nilipo amka mchana, nilikupigia simu mama yangu.” “Asubuhi uliambiwa na daktari uzime simu?” Nyange akamsogelea mkewe nakumshika mkono. Tayari machozi yalikuwa yakimtoka mama Briana. Mumewe akamsogeza karibu. “Usilie bwana.” Nyange alimnong’oneza mkewe. “Watu na ndoa zenu! Asiye na mume ndio atakufa mwenyewe hospitalini!” Mama yao aliendelea.
“Samahani mama.” Mama Briana akajaribu kumsemesha mama yake. “Samahani kwa lipi?” “Yote niliyokosea.” “Yapi?” “Kushindwa kukupigia simu na kutokuwepo hapa hospitalini tokea asubuhi.” Mama Eliah akatulia kidogo.
Kisha akaendelea kama aliyekuwa na jambo linamsumbua rohoni, hawezi kutulia. “Kwanza nakushangaa sana wewe mama Briana. Usingizi huo unautoa wapi na kumuacha mdogo wako ana hali hii hospitalini? Wanaume wasikudanganye, wewe! Huyu ni damu yako!”
“Tena ulitakiwa umshukuru sana mdogo wako. Bila yeye hata huyo Nyange usingempata. Mwenzio kakufanyia ubinadamu, kaona asiolewe kabla ya dada yake, kajinyima, kakupa wewe mwanaume, haya ndio malipo unayomlipa?”
“Jeuri imekujaa, unakubali mdogo wako anafukuzwa nyumbani kwako, mnaenda kumpangishia kijichumba? Wewe Penninah ndio wakufanya hivyo wewe?”
“Sasa na mimi nakwambia, kama ulivyomfukuza Leah kwenye hilo gorofa lenu, tena usiku wa manane akiwa anakulilieni shida, mkamtupa nje ya geti na kumsababishia mateso yote haya mwanangu, na mimi na kwambia hutalikaa hilo gorofa. Labda nisiwe nimekubeba tumboni miezi tisa.”
Wakati anaendelea kutukanwa hali ya mama Briana ilianza kubadilika, akamgeukia Nyange. “Naomba nitoe hapo nje, najisikia vibaya sana. Nahisi hali ya kizunguzungu.”“Twende.” Nyange akamshika vizuri kuhofia asije kuanguka tena. “Mama naomba nikapumzike, nitarudi baadaye.” Mama Briana akaaga.
“Nitarudi kukuchukua baadaye, mama.” Nyange naye akajaribu kuongeza baada yakuona kimya. “Unichukue? Unataka kunipeleka wapi?” “Namaanisha hapo muda wa kuona wagonjwa utakapoisha, ndipo nije kukuchukua turudi nyumbani na wewe ukapumzike.”
“Aliyekwambia nimechoka nani? Unafikiri nimekuja kulala gorofani kwa kuwa kwangu sina gorofa? Kilichonileta mimi hapa mgonjwa. Usingizi naupata wapi na mwanangu yupo hoi hospitalini? Hata hivyo nawasifu, na nguvu mnayo.” Yule mama aliendelea kuongea kama dakika nyingine kumi mbele huku mama Briana na mumewe wakisubiri amalize ili watoke pale.
Mama Briana alianza kutokwa jasho jingi sana. Nyange akaamua amtoe pale, waende nje kwenye hewa. Alipoona hali yake inazidi kuwa mbaya, aliamua kuomba msaada palepale hospitalini.
**********************
Walikuja manesi wawili na kumnyanyua Mama Briana aliyekuwa amejilaza chini kabisa huku akitapatapa. Alikimbizwa mapokezi, alipopimwa, pressure ilikuwa juu sana. Ilimbidi apate mapumziko kujaribu
kuishusha.
Nyange aliambiwa kama isiposhuka itabidi wamtoe mtoto ili kumnusuru mama Briana, alishituka sana na kumuhurumia mkewe. Hakuna muda uliopita asijutie mahusiano aliyokuwa nayo na Leah.
Alimchukia sana Leah na mama yake ambaye aliona wanamuadhibu mkewe bila kosa. Alimpigia simu Sam apitie chakula nyumbani amletee mkewe. Alibaki pembeni ya mkewe ambaye alishapewa dawa ya usingizi na kulala pale pale mapokezi.
Kila Mchuma Janga, Hula Na Wakwao
“Vipi tena kaka?!” Sam akauliza mara tu alipoingia. “Pressure bwana! Ndio wanajaribu kuishusha.” Nyange alikuwa amekasirika sana, hakutaka kuongelea kabisa mkasa mzima. “Daah! Itakuwa zile hekaheka za jana usiku. Alilia sana mama Briana.” Nyange akanyamaza tu.
“Usiwe na wasiwasi kaka. Kila kitu kitakuwa sawa.” “Namuombea Mungu amsaidie, mke wangu. Huu ujauzito ukiharibika tena, atachanganyikiwa.” “Afadhali safari hii tumewahi hospitalini, naamini watamsaidia tu.”
“Nakuomba uende nyumbani ukakae nao kwa kipindi hiki ambacho sisi tutakuwa hapa hospitalini. Siwezi kumuacha hapa peke yake. Nasubiri aamke wamuhamishie chumba cha peke yake. Nitakaa naye.” “Hamna shida kaka. Utataka nikuletee nini?” “Naona nipo tu sawa. Ukija asubuhi nitakuacha naye, nikaweke mambo sawa halafu nirudi tena.” “Pole sana.” “Asante bwana.” Sam akaondoka, akamuacha Nyange hapo hapo nje ya mapokezi, akimsubiria mkewe.
**********************
Sam alirudi nyumbani. “Vipi dada?” “Hali yake sio nzuri, wameamua kumpumzisha ili kushusha hiyo pressure. Lasivyo watampoteza mtoto tena. Baba Briana atakuwa naye hospitalini.” “Jamani dada yangu! Mungu amsaidie. Alimuombolezea Junior kwa muda mrefu sana, Mungu asimchukue na huyu tena. Anaweza hata kufa.” Sonia alianza kutokwa na machozi.
“Atakuwa salama tu. Wala usilie.” “Sasa tutabaki na nani hapa nyumbani?” “Baba Briana ameniomba nikae hapa kwa muda.” Sonia alianza kucheka, huzuni yote ya kuuguliwa na dada yake ikaisha. “Unacheka nini sasa?” “Nimefurahia tutakuwa tukiishi pamoja.” Sam akacheka.
“Inabidi nikachukue vitu vyangu kwangu.” “Naomba tukusindikize mimi na Briana.” Sam alibaki akicheka. “Ndio mfanye haraka sasa twende.” Sonia alimvalisha Briana harakahara na kutoka. Walifika nyumbani kwa Sam, Sonia akiwa amejawa furaha sana.
“Sasa hivi kutakuwa hakuna kuagana tena usiku. Tutakuwa tunakaa wote mpaka tuchoke.” “Kumbe unampango wakunichoka!?” “Sio hivyo kaka, namaanisha mpaka tusikie usingizi.” Wote walikuwa kwenye furaha sana.
**********************
Nyange hakutaka kujua Leah anaendeleaje kabisa. Alimuhamisha mkewe hospitali na kumpeleka hospitali ya kulipia kwani walianza kuona hatari ya kupoteza mtoto inazidi. Alipewa mapumziko ya muda mrefu hospitalini.
“Sasa huyu Sonia atafanyaje kazi zote pale nyumbani na shule?” Mama Briana alianza kumuuliza Sam alipofika kumtembelea. “Maana mimi sio wakutoka hapa leo wala kesho. Namuonea huruma, shule na Briana sio kazi ndogo!” “Kuna kipindi alitaka kukuomba kama mama yake angeweza kuja kusaidia. Lakini alikuwa na wasiwasi na mtoto wake.”
“Mtoto wake amefanyaje?” “Hana pakumpeleka.” “Si aje na mama yake!?” “Unamaanisha waje muishi nao pale?” “Ndiyo! Au kuna shida gani?” “Atafurahi sana Sonia. Ngoja nitamwambia.” “Mwambie tu. Kama mama yake akikubali, itakuwa vizuri. Hata yeye akili yake itatulia.” Waliendelea kuzungumza mambo mawili matatu huku wakicheka kama kawaida yao, Mwishowe Sam alimuacha apumzike.
Hakuna Aliyewahi Kutoa, Kumzidi Mungu
Alipomwambia Sonia juu ya kukaribishwa kwa mama yake na mwanae, Sonia alibaki akilia. Kwa mara nyingine tena anaona maisha yanazidi kuleta mwanga. Walikuwa yeye na mama yake tu tokea utoto. Alisikia wengine wana bibi, babu, shangazi na ndugu wengi tu, lakini sio wao. Mama yake alimwambia amebaki yeye mwenyewe, katika ukoo wake wote. Kwani huko kwao Rwanda, waliishi ukoo wote sehemu moja na wote walichomwa moto isipokuwa yeye.
Na hakutaka kuzungumzia lolote juu ya baba yake isipokuwa alisema tu amefariki. Lakini Mungu aliwaletea Kanamugire ambaye amefanyika baraka na faraja kubwa kati yao, japokuwa alikuja kwa njia ya uchungu sana na mateso lakini wakati wote Sonia na mama yake walimshukuru Mungu kwa ajili yakuwapa Kana.
Kama haikutosha Mungu amewaongezea Sam ambaye anaonekana kumjali sana Sonia na familia yake, na sasa anawaweka kwenye maisha ya familia ya Nyange wanao onekana kumpenda na kumthamini sana.
“Namshukuru Mungu kaka.” “Ni kweli ni bahati. Sio rahisi mtu kukupokea wewe na familia yako.” “Siamini kama nakuja kuishi na mtoto wangu tena!” Sam alianza kucheka. “Usilie sasa.” Sam akaanza kumfuta machozi. “Ni ndoto ambazo sikuwahi kujua kama zitakuja kutimia. Nimefurahi sana.”
Ni Bora Ya Kulipwa Na Mungu
Macho ya Sonia yalimtoka wakati mama yake na Kana wakiwa wanashuka kwenye basi. Pesa alizokuwa akimtumia mama yake, hazikuwa zikienda na muonekano wao hata kidogo. Wote walinawili vizuri, walivaa nguo safi.
Alimuacha mama yake akiwa duni sana, mgonjwa na aliyedhoofu. Hata mavazi aliyokuwa akivaa yalikuwa machakavu, alijitahidi kuweka khanga kwa juu kila aendapo kwenye biashara zake na kupaka mafuta ili angalau kuvutia wateja, lakini bado sura yake ilionyesha dhiki na shida.
Kana naye kwa sababu ya ukosefu wa lishe bora, uso wake ulikuwa kama mtu mzima. Mbavu zake zilikuwa karibu sana na ngozi. Sonia alijaribu kumbemba mwanae baada ya kumkabidhi Briana kwa Sam, aliishia kuguna. “Unamlisha nini huyu? Amekuwa mzito!” Sonia aliuliza huku machozi yakimtoka, bado alihisi yupo ndotoni kwa kuunganishwa na familia yake tena.
Mama Sonia bado alikuwa kwenye furaha isiyo na kipimo. Sio tu kufika kwenye jiji la Dar, bali kumuona Sonia. Hakuacha kumuomba Mungu amlinde mtoto wake. Wakati wote alikumbuka mafuvu ya ndugu zake, na kumuomba Mungu ambakishie Sonia.
Sam ndiye aliyekuwa akiwaendesha kutoka kituo cha mabasi Ubungo. Mama Sonia aliendelea kushangaa jiji huku Sonia akiwaunganisha Briana na Kana. Kabla yakufika nyumbani tayari Briana alishapata rafiki. “Watoto hawachelewi. Ona Bree na Kana, utafikiri wamekuwa pamoja!”
Sonia alikuwa akimwambia Sam wakati Kana na Briana wakila mezani, tena kwa mara ya kwanza Briana alikula bila yakulishwa, huku akiigiza kila kitu Kana alichokuwa akifanya.
Bado Mama Sonia alikuwa akishangaa jumba hilo la kifahari mwanaye anapoishi na tena kuonekana kuzoea kila kitu. “Mama amebadilika sana. Sijui anafanya biashara gani siku hizi? Ona walivyopendeza yeye na Kana! Nusura niwasahau!” Sonia aliendelea kuongea na Sam kwa sauti ya chini sana wakati na wao wakila.
“Inabidi leo niwahi kulala Sonia. Kesho nitakuwa na siku ndefu sana.” Sam alishahamia kwenye nyumba ndogo aliyokuwa akiishi Josh, kama alivyokaribishwa na Nyange na mkewe.
**********************
Kila siku Sonia alihakikisha anamlaza Briana mapema baada ya kumlisha na kumuogesha ili apate muda wakuongea na Sam au kusoma. Hawakuwahi kulala mapema, na wao ndio walikuwa wameachiwa nyumba, kwani Nyange ni kama alihamia hospitalini kwa mkewe.
Walifanya kila kitu pamoja. Kuanzia kifungua kinywa mpaka chakula cha usiku walikuwa wakila pamoja. Walifuatana kila mahali kwenye nyumba hiyo. Kama Sonia anapika jikoni na Sam yupo nyumbani, walikuwa wote jikoni, Sam akisaidia kuosha vyombo au kukaa naye tu Sonia, ilimradi wawe pamoja. Anapokuwa kazini, kila mara Sam alimpigia simu Sonia na wakati mwingine alirudi nyumbani kwa chakula cha mchana.
**********************
Sonia alipooza kidogo baada ya Sam kumwambia atawahi kwenda kulala. “Hata hivyo unahitaji muda na wageni Sonia. Huwezi kuwaacha wenyewe chumbani sisi tunaongea hapa nje na ndio wamefika leo!” “Ni kweli. Nitakuona kesho basi.” “Usiku mwema.” Sam akafunga mlango na Sonia akarudi chumbani kuongea na mama yake.
Alikuta Kana alishalala na Briana kwenye kitanda cha Briana, Sonia akaanza kucheka. “Naona ujio wa Kana utambadilisha sana Briana. Kulala mwenyewe hivi! Sio kawaida yake. Mpaka umbembeleze ndio analala.” “Amemuona Kana amepanda kitandani na yeye akapanda.” “Anamwigiliza wakati mwenzake kachoka na safari.” Sonia aliona mabadiliko makubwa sana kwa mama yake.
Alimuona anaongea naye na hata uso wake ulionekana kufunguka. Alikuwa na maswali mengi sana lakini aliona amuanze mama yake taratibu. “Kana amebadilika kweli! Asante mama.” “Umshukuru Sam na rafiki yake. Wanatujali kweli!” “Kaka Sam?” “Ndiyo, Sam. Kijana anajali huyo, hujawahi kuona. Unakumbuka uliniacha na matatizo ya mgongo?” “Nakumbuka.”
“Alimtuma G, akaja kunichukua na kunipeleka hospitali. Kagaramia matibabuyote. Alikuwa akipiga simu mara kwa mara kutujulia hali na kuongea na Kana. Ni marafiki kweli, alikuwa hataki Kana akae mtaani. Akawa akimtuma G awe anakuja kumchukua siku asizoenda shule ili akae naye kwake. Akirudishwa utamuona mtoto ana nguo mpya na amekatwa nywele vizuri.”
“Alikuwa haachi kumtuma G, alete vyakula na hela pale nyumbani. Hivi huyo alikuwa ameanzishiwa maziwa upyaa. Anakunywa maziwa asubuhi akimka na usiku akilala. Tulianza kula milo yote mitatu. Nilipoona anagaramia kila kitu, nikafungua sehemu ya kusuka kwa hela ulizokuwa umenitumia.”
“Hivi nimekubali kuja wala si sababu ya kazi hii uliyoniitia, ni kwa ajili yako tu. Nilitaka tuishi wote Sonia. Sina ndugu mwenzio. Wewe ndiye ndugu yangu. Ulipoondoka kuja huku nilikuwa na hofu sana ya kukupoteza. Sauti ya baba yako akinihusia nikutunze vizuri ilikuwa ikijirudia sana akilini mwangu.”
“Baba yako aliniapisha wakati nina mimba yako, nikutunze mimi mwenyewe kwa kadiri ya uwezo wangu. Kweli nilijilaumu sana ulipoondoka. Nilijuta kukuruhusu, lakini nilikuwa najiliwaza nakujiambia kwa hali ile tuliyokuwa nayo, tungeishia kufa tu pale kama ungebaki.”
“Sasa uliponiambia tuje kuishi wote, sikutaka hata kuangalia nyuma. Niligawa kila kitu, nikajiambia tutakuja kuanza upya mimi na wewe. Lakini ukweli, sikuwa na shida na kazi wala mahali pakuishi hata kidogo. Sam alituhamisha pale tulipokuwa tukiishi wote, akatupeleka kwenye nyumba nzuri na mtaa mzuri. Nakushukuru wewe na Sam kubadilisha maisha yetu.” Sonia akaanza kulia sana.
“Nilijua hunipendi tena mama!” Mama yake akashangaa sana. “Kwa nini?” “Uliacha kuongea na mimi kabisa.” “Niliumia sana Sonia ulipopata ujauzito. Halafu hukuwahi kuniambia kama umeanza mahusiano wakati tulikuwa marafiki sana mwanangu! Hatukuacha kuongea kila tulipokuwa wote. Nilijikasirikia sana. Nilichukia umaskiniwangu, nikajua ulirubunika sababu ya simu tu.” Sonia akawa hajaelewa.
“Unakumbuka uliniomba nikununulie simu, nikakwambia sina pesa, nahangaikia kukusanya ada, hukusema chochote. Uliporudi nyumbani kwenye likizo fupi, nikakuona na simu mpya, tena nzuri sana. Hukuniambia umepata wapi. Sasa kuja kurudishwa nyumbani ukiwa mjamzito, nilijua aliyekupa simu ndiye aliyekupa hiyo mimba.”
“Wala hukukosea mama, aliyenipa simu ndiye baba yake Kana.” Sonia akafuta machozi na kuendelea huku akilia. “Naomba unisamehe mama kwa kushindwa kuwa muwazi kwako. Nilikuwa kwenye wakati mgumu sana. Sikutegemea kumpata Kana kwa wakati ule. Nilishajua nitasoma sana, na nitakuwa mtu mkubwa sana hapa duniani nikutoe kwenye shida mama yangu. Lakini haikuwa hivyo.” Sonia alimuelezea mama yake mkasa wote juu ya baba yake Fau.
Mama yake alikuwa akilia kwa kwikwi sana, mpaka Sonia akashangaa. Ni kama mtu aliyekuwa ametoneshwa kidonda. “Kwa nini hukuniambia Sonia?!” “Niliogopa mama. Alinitishia kukushitaki kuishi hapa nchini bila kibali maalum. Alisema utafungwa na sitakaa nikuone tena. Niliogopa kukupoteza mama yangu.” Mama Sonia alisikitika sana na kumuhurumia mwanae.
“Pole sana Sonia. Huna tofauti kabisa na niliyopitia mimi.” Sonia akashangaa kidogo na kuuliza. “Yapi?” “Nitakwambia wakati mwingine. Leo inatosha, tulale tu.” Walitulia kwa muda, kila mtu akiwaza lake.
**********************
“Nilirudi shule mama.” “Hongera Sonia. Sam ameniambia.” “Yeye ndiye amenitafutia shule, na ndiye alikuwa akinipeleka na kunirudisha kila siku. Ananisaidia sana katika masomo yangu.” “Kwa kweli Sam ni mkarimu sana. Hakuna neno tunaloweza kumwambia likafikisha shukurani zetu kwakwe.” Sonia alilala vizuri sana pembeni ya mama yake akiwa na furaha yakupatana na mama yake.
Malipo ya Mungu
Wakiwa njiani kuelekea hospitalini Sonia na Sam, Sonia aliona ndio wakati muafaka wakutoa shukurani zake tena kwa Sam. “Kaka Sam!” Sam akamgeukia. “Naomba nikushukuru sana, kwa kuwatunza mama na Kana.” Sam alitabasamu kidogo, nakutulia.
“Kwa nini hukuniambia mambo yote uliyokuwa ukiwafanyia?” “Sikujua kama natakiwa kukwambia kila kitu Sonia!” “Sikutegemea. Unajua hakuna mtu aliyewahi kutujali hivyo! Tangia nakuwa na kupata uelewa, nimekuwa nikimuona mama yangu tu akihangaika yeye peke yake! Sijawahi kumuona mtu yeyote akimsaidia kitu chochote.”
“Nakushukuru sana kaka. Asante sana.” “Asante kushukuru Sonia. Unakumbuka zile pesa ulizoziokota?” Sonia alibaki kimya akimsikiliza. “Unakumbuka nilikwambia zilikuwa za biashara? Uliponirudishia, zote nilimkabidhi G, ili anizungushie kwenye biashara zake. Sasa G ana akili sana ya biashara. Kiasi alizitumbukiza kwenye biashara ya dagaa, na nyingine aliniwekea kwenye biashara yake nyingine.”
“Ananipa faida nzuri sana, na soko la hapa Dar la dagaa limekuwa kweli! Napata wateja wengi, na amenifundisha mbinu nyingine ya kusambaza hao dagaa, ambayo ni rahisi na inanilipa vizuri. Kwa hiyo kwa kupitia zile hela ulizonirudishia, nimepata mabadiliko makubwa sana kiuchumi.”
“Sikuwa na njia nyingine ya kukushukuru ila kuwasaidia mama na Kana. Nimeweza kununua kiwanja, na nimeweza kuanza kujenga. Kwa hiyo mimi ndio natakiwa kukushukuru Sonia, kwa kunirudishia zile pesa. Imekuwa ni kama Mungu alizipitisha kwako ili uziwekee baraka. Asante.” Sam alitabasamu lakini Sonia alikuwa kwenye mawazo kidogo.
“Nimesema asante Sonia!” Sonia akatabasamu. “Na mimi namshukuru Mungu, kaka. Hizo pesa zimefungua milango mingi sana kwenye maisha yetu. Tumepata ndugu ambao hata hatukutegemea, yale maisha ya upweke yameondoka, nimerudisha mahusiano na mama yangu, nimerudi shule, na mengine mengi tu.”
“Nafikiria labda nisingezirudisha labda sasa hivi zingekuwa zimeisha na nisingekuwa hapa na wewe.” “Ni kweli kabisa, zimetuunganisha. Nafurahia kuwa na wewe Sonia.” Sonia akainama. “Asante.” “Siku moja nitakupeleka kwenye kiwanja, nilichonunua, na wewe ukakione, labda utaamini na kufurahia mchango wako kwenye maendeleo yangu.” Sonia akatabasamu tu.
**********************
Kwa kuwa mama Sonia alikuwa mchapa kazi, na Briana hakuwa na muda na mtu yeyote isipokuwa Kana, Sonia alijikuta anapata muda mwingi wa kujisomea.
Kila siku alitoka asubuhi na Sam kwenda kumuona mama Briana hospitalini, kwa kuwa alikuwa ameongezewa ‘Bedrest’ hospitalini hapo, kwani alianza kutokwa na maji. Sonia alikuwa akikaa hospitalini hapo na mama Briana huku akijisomea, wakati Nyange anarudi nyumbani kupumzika kidogo na kwenda ofisini kwake mpaka jioni wakati Sam anapokwenda kumchukua, ndipo Nyange anapokuwa akirudi kukaa na mkewe.
**********************
“Nasikia Briana mwanangu amepata mchumba, hata baba yake hamtaki tena?” “Kwani ni baba yake tu? Yaani dada, hata mimi hanitaki tena! Hataki kulishwa, hataki kubebwa. Anaigiza kila kitu anachofanya Kana.” Mama Briana alianza kucheka.
“Amekuwa mwanangu jamani, mwacheni! Eti baba yake anasema sasa hivi anafikiria kama huyu atakuwa wakiume, tutafute mtoto mwingine wa kike, Kipenzi chake kimemkimbia.” Sonia alianza kucheka.
“Mimi mwenyewe nina kuwa na hamu naye kweli Briana wangu. Ukimwita, anaanza kumuangalia kwanza Kana ndio anajifikiria halafu anakuja. Ukimwambia Briana mbusu Sonia, anacheka tu. Amekuwa kama wewe dada, kucheka tu. Hata umbembeleze vipi, siku hizi hambusu mtu yeyote.” Mama Briana alizidi kucheka.
“Mlizoea mabusu ya burebure kutoka kwa mwanangu, acha sasa hivi awaringie.” Walijitahidi kumfanya mama Briana kuwa na furaha wakati wote ili pressure yake itulie, lakini waliambiwa wakati mwingine ni hali ya ujauzito tu.
**********************
Baada ya mwezi aliruhusiwa ndipo alipoenda kukutana na mama Sonia na mtoto wa Sonia. “Kumbe mama mwenyewe msichana hivi! Mimi nilijua mtu mzima!” Mama Briana alianza kumtania mama Sonia. “Na umempa uzuri wote Sonia, mjini hapa wanakanyagana.” Wote walikuwa wakicheka.
“Anavyolindwa huyo Sonia!” Nyange akadakia. “Hata raisi wa nchi halindwi kama Sonia! Ukimsogelea Sonia, uso wako halali ya Sam.” Kila mtu alizidi kucheka. “Nyange wewe!” Mama Briana alimgeukia Nyange kwa kushituka kama asiseme.
“Mimi najaribu kumtoa wasiwasi mama. Asije dhani Sonia anaishi kwenye mazingira hatarishi. Yaani mama Sonia! Si unaniona mimi na utuuzima wangu huu, Briana wangu na mke wangu huyu?” Mama Sonia alikuwa akicheka sana.
“Lakini hatulindwi kama Sonia.” “Kaka acha hizo bwana!” “Uongo Sam?” “Sio kweli bwana!” “Sawa kama mimi naongopa, mwiteni Josh. Sam haendi kulala mpaka ahakikishe milango yote imefungwa, ndio akalale.” “Si ni swala la usalama bwana, Nyange nini?” “Usalama huo umeanza lini Sam bwana? Mbona sisi tunafahamiana muda mrefu sana?”
“Ulikuwa ukiondoka humu ndani hata mlango ulikuwa hurudishii. Yaani mama Sonia, kila siku alipokuwa akitoka Sam humu ndani, ilikuwa inabidi nisimame mwenyewe nirudishie mlango.” Sonia alikuwa ameinama akicheka taratibu.
Mama Briana mpenda kucheka ndio alikuwa akicheka mpaka akitokwa na machozi. “Utawazoea tu hawa. Nyange anapenda sana kumchokoza Sam.” Ilikuwa furaha tupu ndani ya nyumba ya mama Briana. Kila mtu alifurahia kupona na kurudi kwa mama huyo aliyejaa upendo na ukarimu.
Kule Kuliko Ungua Mpini, Kukabaki Shoka
Leah alitolewa hospitalini baada yakupata nafuu, lakini mama yake alisononeka sana kukuta chumba alichokuwa akiishi Leah. “Wamekufukuza kwenye nyumba yao, na kukuweka hapa kama nguruwe!? Nyumba haina kitu kabisa hii! Yaani Penninah ameshindwa hata kukununulia kitanda!?” Leah alinyamaza bila hata yakumwambia mama yake ukweli wa mambo.
**********************
Hata pesa alizokuwa amepewa na Nyange za kujinunulia vitu vyake vya ndani na kukodisha chumba, Leah hakumwambia mama yake. Alipopewa pesa na Nyange, kweli Leah alikodi chumba, akanunua kitanda tu. Aliamua kumtafuta baba wa mtoto wake ili wazungumzie maswala yao, na wasamehene kwa yote kisha aje waishi pamoja na kulea mtoto wao.
Alipokuja Isa, mwanaume aliyekuwa na mahusiano ya muda mrefu na shoga yake kipenzi Ashura, alimwambia amemsamehe na warudi kuishi pale kama mke na mume. Japokuwa Leah hakuona kosa lolote lakuhitaji kusamehewa na Isa, ila yeye ndio alihitaji kusamehewa kwa makosa yote aliyomtendea Leah, Leah alikubali yaishe ili asiendelee kuishi pale peke yake.”
Hazikupita hata siku tatu, Isa alirudia hali yake ileile ya zamani. Kurudi nyumbani amelewa na kumfanyia fujo Leah akiwa amelala. Siku moja alirudi akaanza kufanya fujo huku akinuka sana bangi, alimtaka Leah kimapenzi, lakini Leah alikataa kwa kuwa alikuwa amechoka sana.
Ndipo alipomkamata kwa nguvu, na kufanya naye mapenzi kinyama, na kumpiga sana. Alimuacha Leah akitokwa damu nyingi sana hata hajitambui, akaiba simu, pesa za Leah zote na kutoroka.”
Baada ya siku moja, Leah alizinduka akiwa na maumivu makali sana, na kujivuta mpaka nje. Ndipo mpangaji mwenzake aliyekuwa akitoka asubuhi nakurudi usiku kila siku, alimkuta Leah nje akilia kwa maumivu huku akishindwa hata kutembea. Kwa kuwa wote hawakuwa na gari, alimpa simu yake ili ampigie ndugu yeyote wakaribu, ndipo Leah alipompata Sam kwa simu baada yakumkosa dada yake.
**********************
“Hapa hukai Leah mwanangu. Turudi wote nyumbani, ukishapona kabisa na kurudisha afya yako ndipo nitakwambia kitu kingine chakufanya. Na wala usiogope mwanangu, utapona na utarudia hali yako kama zamani. Na gorofani utakaa kama malkia.”
“Nitahakikisha unatumikiwa na kila mtu.” Leah alirudi kuishi na mama yake. Waliondoka bila hata kumtafuta Mama Briana aliyekuwa amemtumia mama yake ujumbe. ‘Mama, usione kimya. Na mimi nimelazwa, naumwa sana. Siruhusiwi kutoka hapa zaidi ya chooni.’ Alijibiwa kwa kifupi tu ‘Pole.’ Nyange alimshauri mkewe kwa wakati ule aachane na mambo ya Leah na mama yake kabisa mpaka atakapojifungua, ndipo wataenda nyumbani kwao pamoja kuzungumzia hilo swala.
**********************
Sonia na Sam walikuwa kama kumbikumbi! Kila mtu pale nyumbani kwa Nyange aliwajua. Sam hakuwa akila chakula bila Sonia kuwepo au yeye kukiandaa. Mama Sonia na mama Briana wakati wote waliwasema bila wao kujua.
Siku za weekend ambazo Sam hakuwa akienda kazini, walishinda Library wakisoma au walikwenda pamoja site kwenye nyumba ya Sam. Nyange naye hakuacha kumtania Sam na Sonia.
Sonia alijua mambo mengi ya muhimu, juu ya maisha ya Sam. Wakati wote alimpongeza na kumpa ushauri Sam. Kwa Sonia, Sam alikuwa kaka na rafiki wakaribu sana. Hakutaka mtu mwingine yeyote awe karibu na Sam isipokuwa yeye mwenyewe.
**********************
Siku mama Briana anapatwa na uchungu hapakuwa na mtu yeyote nyumbani isipokuwa mama Sonia, ambaye hakujua kuendesha gari. Nyange alipata safari ya gafla.
Sonia na Sam kama kawaida yao walikuwa maktaba, wakijisomea na walizima sauti kabisa ya simu zao. Na wakati wote wanapokuwa wao wawili, walitaka muda wao tu hawakutaka mtu mwingine awaingilie. Hakuna kitu kingine kilichokuwa cha muhimu kati yao isipokuwa wao, wawili.
Josh naye alikuwa amefiwa kijijini kwao, kwa hiyo aliondoka kama siku tatu zilizopita.
Kama kawaida yake ya uvumilivu, mama Briana aliamka akiwa na maumivu na chupa ya uzazi ilivunjika wakati akioga, kwa hiyo hakuwa akijua kama ni uchungu. Kwa kuwa tarahe zake zilikuwa bado kidogo, alikunywa dawa za maumivu, akanywa chai, na karudi kulala. Aliendelea kuugulia maumivu peke yake.
**********************
“Vipi mbona kama unagugumia?” Nyange alimuuliza mkewe wakiwa wanaongea kwenye simu. “Nasikia maumivu.” “Isijekuwa ni uchungu, mama Briana!” “Haiwezekani, siku bado kidogo. Mpaka week ijayo.” “Pole sana mpenzi wangu. Nachukia kuwa mbali, lakini kesho nageuza. Tutaenda hospitalini nikifika.” “Usiwe na wasiwasi, nitakuwa sawa tu.” Waliagana na mumewe, akaendelea kuugulia maumivu peke yake.
Hakuna Aliyewahi Kutoa, Akampita Mungu
Mama Sonia alipoingia kumletea chakula, akamkuta akihangaika. Alipomgusa tumbo, alishituka sana. “Ujue huo ni uchungu, mama Briana?” “Sikuwa najua! Naomba mpigie simu Sam aje anipeleke hospitali.” Mama Sonia alipiga simu mpaka akachoka, Sam hapokei.
“Nisaidie niende chooni.” Aliposaidiwa kusimama, tayari mtoto alikuwa anachungulia. Mama Briana akaanza kulia. “Jamani mwanangu, atakufa!” “Wala usiogope. Nitakusaidia huyu mtoto atatoka salama tu.” “Utanisaidiaje sasa? Daktari alisema lazima nizae kwa operation, siwezi kuzaa kawaida, kwa kuwa nilipasuliwa hata miaka miwili haijapita.”
“Rudi ulale kitandani kwanza.” “Naogopa kweli!” “Usiogope. Kwa hatua uliyofikia hatuwezi kwenda popote, mtoto huyo anatoka. Mimi najua kuzalisha. Kuwa na Imani tu, utazaa salama.” Mama Briana alizidi kuchanganyikiwa.
“Kweli?” “Shida zimenifundisha mengi. Hata Sonia nilimzaa nikiwa peke yangu, nawala sikumpeleka hospitali, na ni mzima mpaka leo.” Mama Briana ilimbidi aamini tu kwani hakuwa na njia nyingine. Akarudi kujilaza kitandani akitetemeka kwa hofu.
**********************
“Fuata kila kitu nitakacho kuelekeza.” Mama Briana bado alikuwa akilia. Hofu ya kumpoteza mtoto wake ilimtawala lakini hakuwa na jinsi ila kupokea msaada wowote atakaopewa. “Sawa.” Mama Briana alijibu kwa woga sana.
Walishalipia hospitali ya garama sana ya kwenda kuzaliwa huyo mtoto. Hawakutaka kosa lolote litokee tena.
Kama mchezo mama Briana kwa kufuata maelekezo ya mama Sonia, aliyemkaribisha kwake na mjukuu, kwa upendo tu akijua anawasaidia, akaishia kuwa msaada mkubwa sana. Ndani ya dakika chache alisukuma na mtoto alitoka vizuri bila madhara yeyote kwake yeye mwenyewe wala mtoto.
Kilichokuwa kimemshangaza mama Briana ni utulivu usoni kwa mama Sonia. Alimzalisha akiwa ametulia bila kuonyesha wasiwasi kabisa. Haraka haraka mtoto alipolia alimzungushia shuka lililokuwepo pembeni, huku mama Briana akiendelea kulia.
“Wala usilie, kidume chako kizima!” Mama Briana alipiga yowe. “Umesema wakiume!” “Tena kidume cha nguvu. Mkubwa kama baba yake.” Mama Briana alifurahi sana. Mtoto alianza kulia na kumfanya Briana na Kana kukimbilia chumbani kwa mama yao. “Njoo umuone kaka yako, Briana.” Briana akabaki ameshangaa.
**********************
Baada ya muda kidogo simu ya Nyange iliingia. “Mama Briana? Nimebahatika ndege ya leo, narudi. Nimeshindwa kuvumilia. Sitaki uteseke peke yako.” Mama Briana akaanza kucheka huku machozi yakimtoka. “Nimejifungua baba Briana.” “Ndio nilikuwa nasema, sitaki tufanye kosa juu ya huyo mtoto. Unaweza sema sio uchungu kumbe ni uchungu.”Mama Briana alijua mumewe amepaniki.
“We Nyange?” “Sitaki tufanye kosa.” Baba Briana aliendelea kusisitiza. “Nyange? We Nyange?” “Naam!” “Naomba usipaniki bwana, wewe vipi?” “Sitaki nifanye kosa jingine Penninah. Umeteseka sana na huo ujauzito. Sitaki uje uambulie patupu. Sitakaa nijisamehe maishani chochote kikija kutokea tena. Hizi pesa zinatafutwa tu, nikikosa leo nitapata hata kesho, lakini…” Mtoto alishaanza kunyonya.
“Jamani baba Briana! Naomba unisikilize basi.” “Huna utakaloniambia nikakusikiliza safari hii. Narudi nyumbani. Ulinilazimisha nisafiri, ona yaliyokupata ukiwa mwenyewe. Sasa hivi sikusikilizi hata kidogo. Narudi nyumbani Penninah.” Nyange akakata simu, mama Briana alibaki akicheka.
**********************
“Mbona hujamwambia?” Mama Sonia akauliza. “Nimeshindwa. Nyange muoga kweli! Asubuhi nilimwambia nina maumivu, sasa amechanganyikiwa hana analoelewa tena. Hivi hapa anarudi. Mwache ataingia hapa muda sio mrefu, yupo tu hapo Arusha. Atakuja kujionea mwenyewe.” Wakacheka.
“Ila hongera na pole mama Briana.” “Asante sana mama Sonia. Sijui ningefayaje kama usingekuwepo! Labda ningempoteza mwanangu.” “Mambo mengine yanatokea kwa sababu. Nimefurahi na mimi nimeweza kukusaidia.” “Umejuaje kuzalisha?” Mama Sonia alikaa baada yakumaliza usafi na kumlaza mtoto. Briana na Kana walishaondoka.
**********************
“Si nilikwambia tulikaa sana kwenye kambi za wakimbizi pale Shinyanga? Hapo ndipo nilijifunza mengi sana. Hata nilipotoka pale nikakimbilia Mwanza nikiwa mjamzito, sikuwa na pesa yeyote ile, nilizaa peke yangu chumbani kwangu, na kwa kuwa sikuwa na pesa ya hospitalini, nilibaki na mtoto wangu tu nyumbani.” “Kweli wewe mwanamke. Hongera.” Mama Sonia alicheka.
“Lakini nikuulize kitu Mama Sonia? Ulitokaje Kambini na kwa nini ulikimbia ukiwa mjamzito? Mumeo yuko wapi?” “Sikuwa nimeolewa.” Mama Sonia alijibu bila ya ujasiri. Kabla ya kuendelea mara simu ya mama Briana ilianza kuita.
**********************
Ikabidi kupokea. “Mwenzangu wewe baba mdogo uliyeachiwa majukumu naona yamekushinda.” “Pole shem. Nilizima sauti tulikuwa maktaba na Sonia, tunasoma. Vipi?” “Safi tu. Nyinyi endeleeni tu na shule, tutaonana baadaye.” “Kila kitu kipo sawa?” “Kila kitu kipo sawa, Nyange yupo njiani anarudi leo.” “Mbona mapema?” “Utamuweza Nyange? Muache tu arudi. Baadaye basi.” Mama Briana alikata simu bila hata kuwaambia Sam kitu chochote.
“Mbona sasa hujawaambia?” “Hao wawili? Hawana wanachoelewa sasa hivi isipokuwa maisha yao tu. Achana nao. Baba Briana akija atatupeleka hospitali.” Mama Sonia alianza kucheka.
“Na kweli Sam amekazana!” “Nakwambia mimi! Hana anachoelewa sasa hivi isipokuwa Sonia. Waache wafurahie. Lakini nampenda sana Sam. Nikijana mzuri sana. Alikuwa mchumba wa mdogo wangu, mimi mwenyewe nilikuwa nikimuhurumia huyo Sam.” Mama Sonia alishituka sana.
“Sonia ndio amevunja huo uchumba?” “Hapana mama Sonia, jamani!” Mama Briana alianza kucheka. “Nimeshituka kweli! Maana na yeye amemkazania kijana wa watu, utafikiri sijui nani! Wakiagana usiku hapo nje, unafikiri huyo Sonia analala? Wanaanza kutumiana ujumbe, usiku kuchwa.” Wote walizidi kucheka.
“Lakini mama Sonia, waache tu. Hata Nyange huwa namwambia. Tuwaache tu tuone mwisho wao.” “Unafikiri mimi nasema kitu? Nimebakia kuangalia tu. Ilimradi asome. Naomba upumzike mama Briana. Ngoja nikakupikie supu, maziwa yatoke. Dume hilo, linanyonya sana. Tutaongea vizuri baadaye.” Mama Briana alicheka na kujilaza vizuri.
**********************
Nyange aliingia nyumbani kwake akiwa amechanganyikiwa kwelikweli. “Pole na Safari.” Mama Sonia alimpokea mizigo. “Simu ya mama Briana haipatikaniki. Mzima?” “Niliizima mimi ili alale, ametoka kula sasa hivi amerudi kulala.” Bila kujibu kitu Nyange alipandisha ngazi huku akikimbia kuelekea chumbani kwao, alipo mkewe.
Macho yalimtoka baada yakukuta katoto kamelala pembeni ya mkewe. “We mama Briana?” “Unachoshangaa nini sasa?” “Huyo mtoto wa nani?” “Si nilikuwa nakwambia naona hunisikilizi.” “Kuniambia nini?” “Mama Sonia kanizalisha.” Nyange alikaa chini.
“Tumepata mtoto wakiume, D.” Nyange alihisi yupo usingizini. “Haiwezekani!” Mama Briana akaanza kucheka. Nyange akamsogelea mtoto. “Kafanana na mimi kweli!” “Umeanza Nyange. Kila mtoto anafanana na wewe.” Taratibu machozi yalianza kumtoka Nyange.
“Nakushukuru Mungu wangu. Pole mpenzi wangu. Umepata shida mwenyewe.”“Huwezi amini D. Huyu mama mtaalamu kweli! Mimi mwenyewe niliogopa sana mtoto alivyoanza kuchungulia wakati nipo chooni, lakini alinituliza. Nimejifungua kirahisi kweli! Ungemuona alivyotushugulikia mimi na mtoto, kama daktari!”
“Daah! Hawa watu wamekuwa msaada kweli kwenye maisha yetu. Lakini twende hospitalini. Sam yuko wapi?” “Wapo wanasoma. Hivi hata hawajui kama nimejifungua, sikutaka kuwasumbua.” “Na wale wakiwa wawili! Hawana wanachoelewa.” Mama Briana akacheka.
“Nimemwambia hivyohivyo mama Sonia.” “Nimefurahi wewe!” “Nakuona. Unavyozunguka chumba, hutaki kukaa!” “Kwanza bado nipo kwenye mshituko. Sikutegemea kukuta mtoto.” “Mshike basi!” “Kweli bwana! Nimechanganyikiwa kwa furaha. Umeniletea dume la nguvu. Tena anafujo huyo! Ameamua kujia nyumbani kwake kabisa.”
“We! Hapa ulisema kwa Briana, usianze Nyange na mwanao.” “Tutajenga kwengine na mwanangu, msitufukuze. Eti Brayan!” “Na jina ushampa?” Nyange alishambeba huku anacheka. “Sasa wewe ndio mwenzangu, Briana kipenzi changu. Kila mtu atamtumikiaBriana. Umesikia Brayan?” Nyange aliendelea kuongea taratibu na mtoto wake mkononi.
“Mimi tena sio mwenzako?” “Acha wivu mama Briana.” “Sijasikia nikitajwa.” “Sasa wewe si ndio mwenyewe. Kwanza Briana amemuona kaka yake?” “Hana hata muda naye. Kamwangalia kidogo tu akaondoka na Kana wake. Mwanangu kachanganywa kweli na Kana.” “Si nilikwambia mimi? Hana anayempenda humu ndani isipokuwa Kana.”
“Nitamtambulisha tena kwa kaka yake, aache habari zake za ajabu. Huyu ndio mlinzi wake mkuu, lazima amjue vizuri. Na kalivyo kazuri kama mama yake, lazima ulinzi uimarishwe.” “Ushaanza kumpa majukumu mwanangu!” “Huyu lazima afanye kazi sana kama mimi.” Ilikuwa furaha kubwa sana kwa Nyange na mkewe. Nyange aliwapeleka hospitali, na kwa kuwa hawakuwa na shida yeyote, waliruhusiwa kurudi nyumbani.
**********************
Sonia na Sam walirudi usiku nyumbani na kumkuta Brayan. Wote walibaki wametoa macho. “Haiwezekani mama Bree. Hata mimi unanifanyia hivyo shemeji yangu!?” Mama Briana alibaki akicheka tu. “Nilipokwambia nakuachia nyumba, nilikuwa namaanisha na mama Briana pia sio Sonia peke yake.” Nyange akadakia.
“Muulize mama Bree kama nilikuwa simjali. Simu kila saa, nilikuwa nampigia.” “Sasa kajifungulia hapahapa nyumbani, wakati baba mdogo alikuwa hapokei simu.” Sam hakuamini. “Kwani ndio kipindi kile mliponikosa?” Sam akauliza. “Bwana wewe achana na Nyange bwana. Cha muhimu mtoto yupo salama.”
Ilikuwa furaha kubwa sana kwa familia hiyo, waliyojikuta wamekuwa ndugu wakupendana na kuheshimiana kwa muda mfupi sana. Mama Sonia alimuhudumia mama Briana vizuri sana. Alimlea kiuzazi kwelikweli.
**********************
Sam alihamisha nguvu na akili zake zote kwenye matayarisho ya mitihani wa Sonia. Ilipofika siku ya mitihani, Sam naye alichukua likizo kazini. Alikuwa akimpeleka Sonia katika shule aliyokuwa akifanyia mitihani yake, nakubaki nje akimsubiri mpaka jioni walipokuwa wakirudi naye nyumbani. Kuanzia mtihani wa kwanza mpaka wa mwisho Sam alikuwa na Sonia. Alihakikisha Sonia hana hofu ya mitihani kabisa.
“Sasa mitihani hiyo anafanya Sonia au wewe?” “Nyange waache bwana!” “Mimi nauliza kwa wema tu jamani!” Sonia na Sam wote walikuwa wakicheka.
Mitihani ilipoisha sababu za kuongozana zilipungua. Ilibidi Sonia abaki nyumbani kusaidia kazi.
**********************
“Sasa unacheka nini baba Briana?” Sam akauliza. “Mimi nimefurahishwa na yangu. Kwani kosa langu nini?” “Ana jambo linalomfanya acheke huyo, na atakuwa anakucheka wewe.” Mama Briana akadakia.
“Sasa ananicheka nini?” “Alikuwa akininong’oneza hapa, eti nikuone unavyo hangaika. Huna tena sababu yakuwa na Sonia karibu.” “Hamna bwana! Mbona Sonia yupo tu.” Sam akajibu. “Mimi nina wazo Sam.” “Wazo lako sitaki kulisikia kabisa, baba Briana. Huna chakunishauri.” Nyange alikuwa akicheka sana. “Mimi mshauri mzuri sana, ukinisikiliza.” “Huna lolote.” “Sawa.”
Zilibaki safari za kwenda site kwa Sam tu. Kwa hiyo kila siku za jumamosi Sam alipokuwa akienda kuangalia ujenzi wa nyumba yake hakuacha kwenda na Sonia, na kumuomba ushauri wa hapa na pale. Kwa hiyo Sam alijenga hiyo nyumba vile alivyoshauri Sonia.
**********************
“Tuna sherehe ofisini kwetu ya kufunga mwaka. Tunaweza kwenda wote?” Sam alimuuliza Sonia jioni hiyo wakiwa pamoja nje ya ngazi za jikoni, kama kawaida yao.
“Mmh!” “Nini sasa?” “Sijawahi kwenda kwenye tafrija kama hizo kaka. Sina nguo, sijui watu wanafanya nini wakiwa huko au wanavaa nini. Naogopa.” “Usiogope bwana. Situtakuwa wote!” “Mi naona kaka, wewe ungeenda tu.” “Unaogopa kuonekana na mimi?” “Hapana!” Sonia alishituka sana.
“Hapana kabisa. Sikutaka kukutia aibu. Lakini kama unaona ni sawa, basi twende wote tu.” “Wewe usiwe na wasiwasi, tutakuwa wote.” Walipoachana tu, Sonia alikimbia moja kwa moja chumbani kwa Mama Briana mshauri wake.
**********************
Alifika mlangoni chumbani kwa Nyange na mkewe akaanza kugonga. “Nini Sonia? Amelala mke wangu. Au nije mimi?” “Hapana, namtaka dada.” “Mimi pia mshauri mzurisana Sonia. Niambie tu mimi.” “Hapana, namtaka dada.” “Mwache mtoto bwana Nyange, Nini? Nakuja Sonia.” “Bwana nyumba hii hawataki ushauri wangu kabisaa!” Mama Briana alicheka na kutoka chumbani.
“Vipi?” “Kaka Sam anataka niende naye kwenye sherehe ofisini kwao. Naogopa.” “Unaogopa nini?” “Sina nguo nzuri. Halafu sijawahi kuwa kwenye tafrija kama hizo dada! Nikikutana na wasichana wengine wamependeza zaidi yangu?”
“Sasa dawa ni moja. Nitakutafutia gauni zuri, na nitakupeleka saluni ukatengenezwe vizuri mpaka kila mtu atakaye kuona abaki anakushangaa wewe, na nitakufundisha kila kitu ili ukifika pale usibabaike.” “Kweli dada? Unafikiri baba Briana atakubali utoke?” Sonia aliongea kwa kunong’ona. “Nasikia hivyo!” Nyange akadakia. “Kwa nini unatusikiliza Nyange lakini? Lala Bwana.”
“Kwa kuwa wewe unanyonyesha, mimi nitampeleka.” Nyange akatoka kabisa chumbani. “Nataka kwenda na wewe dada?” Sonia akamsogelea mama Briana aliyekuwa anamcheka, alimuona vile Sonia alivyopooza gafla na kupoteza furaha yote usoni baada ya Nyange kutoka, na kusema atakwenda naye.
“Anakuchokoza mwenzio, wala usimsikilize. Tutaenda wote.” “Hata hivyo Sam angeniruhusu, jamani? Kama nisinge ambulia ngumi tu, na hivi mwenzangu mnyanyua vyuma! Ngoja nikae pembeni asije niharibu sura bure!” Sonia alianza kucheka huku anaangalia chini.
“Nenda kalale mwaya Sonia, achana na Nyange. Tutaenda wote kutafuta gauni.” Sonia alifurahi sana. “Ndio maana nakupenda dada yangu. Asante.” Sonia alimnongo’oneza mama Briana, lakini Nyange akasikia. “Mimi hunipendi?” Nyange alimtania tena Sonia, nakumfanya abaki ameinama. “Nenda kalale mwaya Sonia achana na Nyange.”
**********************
Siku yenyewe ilipofika, Sonia alienda kutengenezwa nywele vizuri, na mama Briana alishamtafutia gauni zuri sana. Sam alishavaa, akatoka sebuleni kumsubiria Sonia. Sonia alipotoka, Sam na Nyange walibaki wametoa macho kwa muda bila kusema kitu na kumfanya Sonia ababaike.
“Nipo tayari kaka.” Mama Briana alianza kucheka na kuuliza. “Sasa mnachoshangaa nini?” Sam bado alibaki amekodoa macho. “Daah! Kweli wewe Sam mwanaume, mdogo wangu! Unamtoa Sonia hapa ndani, hivyo alivyo na kumpeleka kwa wanaume wengine! Watakuliza mchana kweupe!” “Nyange jamani! Acha kumnyima raha Sam bwana! Waache watoto waende.” Mama Briana akadakia.
“Sawa. Utanikumbuka mimi. Mama Sonia, njoo ujionee mwenyewe.” Kila mtu alikuja kumwangalia Sonia jinsi alivyopendeza. Mama yake alibaki ametoa macho asiamini kama ni kweli ni mwanae.
Kidogo yale maneno ya Nyange yalimuingia Sam, hofu ikamkamata. ‘Wasije wakanizidi mahesabu, na hivi vidoleni hana kitu!’ Sam aliwaza huku bado amesimama. “Asikuogopeshe kabisa huyu, nenda shemeji yangu.” Akawa kama amesoma mawazo yake. “Umeona eeh shem?” “Usimsikilize Nyange. Anakuchokoza tu.” Mama Sonia alikuwa akicheka sana. Kweli Sam alionekana ameingiwa na wasiwasi sana, alishindwa kutoa macho yake kwa Sonia.
“Sawa Sam. Alivyopendeza hivyo! Mimi siendi kulala, nawasubiria hapahapa niwaone sura zenu amtakapokuwa mnarudi, kama tabasamu zitakuwa hazijawaisha.” Nyange aliendelea. “Daah!” Sam alibaki anababaika.
“Nyange nyamaza bwana, wewe vipi? Ujue unamuogopesha Sam! Atagairi kwenda. Niangalie mimi Sam.” Sam akageuka. “Hata kama watamfuata huyo Sonia, wewe mwenyewe si utakuwepo? Usiwe na wasiwasi bwana. Hakuna atakayemuiba?” “Eti Shem eeh?” Sam aliuliza kama kutaka kuhakikishiwa.
“Anakudanganya mwenzio huyo mama Briana, wewe msikilize tu. Wewe ushawahi kwenda kwenye hizo tafrija zenu ukakutana na msichana kapendeza kama hivyo Sonia?” Nyange aliendelea kumtesa Sam.
“Hebu Nyange nenda kaniletee maji ya kunywa, bwana. Ondoka.” Ilimbidi mama Briana amtoe pale Nyange kwani Sam alishakaa chini, akitaka kuahirisha safari.
“Hata kama mnanifukuza, lakini mimi msema kweli. Tena wakimwangalia Sonia mwenyewe vidole vinaita hivyo! Haya Sam!” Nyange alizidi kucheka huku anaondoka. “Nisikilize Sam, achana na Nyange kabisa. Tena usipoenda ndio atakucheka mwaka mzima, kwamba hujiamini. Sonia sio mtu wakupelekwa na matukio, ametulia mdogo wangu.”
“Wewe nenda, hakikisha unatoa utambulisho wakueleweka, na majina yenu hayo ya ‘Kaka Sam’, MUACHE.” Wote walizidi kucheka mpaka Sonia mwenyewe aliyekuwa ameinama chini muda wote alicheka na kunyanyua uso. “Dada wewe!?” “Kweli tena siwatanii. Nyinyi nendeni ila acheni kuitana kaka na dada huko mbele za watu.”
“Mkiendeleza habari zenu za kaka na dada, ndio watamng’ang’ania huyo Sonia, wakidhani dada yako.” Nyange alirudi akicheka mpaka machozi. “Heri yangu mimi mstaarabu, si eti mama Sonia? Ona mambo mama Briana anayowafundisha!”
“Kweli mama Briana kakuamulia leo Sam! Kaenda kumpendezesha Sonia makusudi halafu anataka kwenda kumgawa nje! Heri msiende mbaki tu na mimi tuangalie taarifa ya habari.” Mama Briana akasimama, akachukua funguo za gari mkononi kwa Sam, na kumshika mkono Sonia mpaka nje kwenye gari la Sam. Ilimbidi Sam atoke tu.
Fisi Wa Jijini!
Hakuna aliyeacha kuwaangalia Sam na Sonia wakati wakiingia ukumbini. Na kwa kuwa walichelewa kidogo, kila mtu aliweza kuwaona wakati wanaingia. Sam alitafuta meza ya rafiki zake na kwenda kukaa hapo na Sonia.
Ukweli wote wawili walikuwa wamependeza sana. Sam naye alivaa nusu suti, lakini shati na kizibao chake vyote vilimkaa vizuri sana. Walifanyia sherehe hiyo katika ukumbi uliokuwepo kwenye hoteli nzuri sana ya kifahari hapo hapo mjini. Akili na mawazo ya Sam yote yalikuwa kwa Sonia. ‘Kwanza sijaona mwanaume wakunipora Sonia hapa.’ Sam aliendelea kuwaza huku akijiliwaza wakati wenzake wakifurahia, yeye alibaki kumuwinda Sonia.
Ulipofika wakati wakusalimiana, kila mtu alikuwa akizunguka ukumbini hapo, toka meza moja hadi nyingine wakisalimiana, lakini Sam hakutaka kusogea hata hatua mbili mbali na Sonia.
Kila aliyesogea kumsalimia Sonia, Sam naye alisogea. Ndipo alipowasogelea mkuu wa kitengo chao cha IT, Mr. Mponza, aliyekuwa akiheshimiwa sana kazini kwao.
Baada ya Sonia kumsalimia kwa kumpa mkono, alibaki ameshika mkono wa Sonia akimwangalia kwa utulivu sana. “Karibu sana. Uwe unakuja kututembelea pale ofisini kwetu. Eti Sam? Uwe unamleta Sonia bwana!” Bado alikuwa ameushikilia mkono wa Sonia. Sam hakujibu kitu chochote.
“Ungependa kinywaji gani?” Kabla Sonia hajajibu, Sam akadakia. “Meza yetu hii hapa Mkuu, na tayari tuna vinywaji.” “Oooh! Basi Sonia, ukiwa na shida yeyote nipigie simu na hii ndio kadi yangu ina namba zangu zote za simu. Wakati wowote muda wowote, wewe uwe huru kunipigia.” Akachomoa kadi yake kwenye wallet na kumkabidhi Sonia. Sam alitamani kupasuka.
Aliondoka na kuwaacha Sonia na Sam hawajui kama waendelee kusimama au wakae, na marafiki zake Sam wote bado walikuwa wakiwaangalia. “Naomba uniwekee hii kadi.” Sonia akamgeukia Sam na kumwambia kwa sauti ya taratibu, kwa kuwa alishamjuahakutaka shida, akaamua kumkabidhi tu ile kadi bila hata kuisoma.
Sam aliipokea na kuichana palepale mbele yake na marafiki zake na kuirusha hewani. Sonia hakushangaa hata kidogo, kwani alitarajia kitu kikubwa zaidi ya kile. Walibaki wamesimama kwa muda huku sherehe ikiendelea.
Sam alitaka kuondoka lakini alikuwa ni miongoni mwa wafanyakazi waliokuwa wakisubiri kupokea zawadi ya mfanyakazi bora siku hiyo. Alibaki akijishauri kama waondoke, aachane tu na hiyo zawadi au abaki.
**********************
Sonia alipoona bado wamesimama, tena wao wawili tu, akaamua kuaga ili kubadilisha hali ya hewa ya mahali pale. “Naomba niende chooni.” Akamnong’oneza Sam kwani mziki ulianza kutumbuiza ukumbini hapo, Sam akaamua kurudi kukaa, ndipo Mr Mponza naye alipomuona Sonia akipita karibu kabisa ya meza yao akielekea upande wa choo kilipo.
Macho yake hayakutosheka kumsindikiza Sonia. Alimtazama mbele wakati anapita usawa wa meza yao, alipopita aliendelea kumsindikiza kwa macho, ambayo hayakutosheka na mgongo wa Sonia. Gauni alilokuwa amevaa Sonia lilichora vizuri sana umbile lake. Mbali ya kuonekana ni gauni zuri kwa rangi zilizoendana na rangi ya mwili wa Sonia, pia lilionekana ni la thamani sana.
Lilibana kiuno chake chembamba kilichoshikilia umbile la duara kwa chini, juu lilifanya kifua cha Sonia kuvutia zaidi. Si yule bosi tu aliyebaki amemkodolea macho, bali kila aliyebahatika kumtazama Sonia, alibaki ameduwaa na kushindwa kutoa macho yake kwa mwanadada huyo.
Sonia alikuwa na tumbo dogo sana, huwezi amini kama amezaa. Nywele alizokuwa amesuka, walizitengeneza vizuri kiasi cha kuruhusu sura yake ndefu na macho mazuri maangavu kuonekana vizuri, haikuwa ikichosha kumtazama Sonia. Ukweli alivutia kwa macho. Ilihitaji mwanaume mwenye kiasi tu, kumtazama na kukwepesha macho yake.
Tamaa iliyokuwa ndani ya bosi wake Sam, yaani Mr.Mponza ilishamfikisha chumbani, tena kitandani akiwa ameshamvua Sonia nguo zote na kubaki akimtazama.
Kwenye meza ile waliyokuwa wamekaa VIP, yaani viongozi wa kubwa wa Sam na wake zao, wote walijikuta kwenye mtego uleule wakumsindikiza Sonia wakati wake zao wakinywa na kucheka. Wengi wao walirudisha macho mezani baada ya Sonia kupotelea chooni na kusimama kwenda kucheza baada ya kujigundua wote walikuwa wakimwangalia Sonia, lakini Mr. Mponza aliyekuwa amempendekeza Sam kama mfanyakazi bora wa mwaka, yeye uzalendo ulimshinda.
Alimshitua mkewe ambaye ndiye alikuwa mzungumzaji mkuu kwenye meza ile. “Nakuja sasa hivi, naenda chooni.” Kwa kuwa mkewe alikuwa anaharaka ya kumalizia stori yake aliyokuwa akisimulia na mziki ulikuwa mkubwa, hakumsikia mumewe wakati akiaga na wala hakujali mumewe aliponyanyuka, akaendelea kusimulia huku wanawake hao, wa viongozi hao wakizidi kucheka sana pale mezana.
Historia Yataka Kujirudia
Sonia alishituka sana kumkuta yule Bosi wake Sam akimsubiri pembeni kidogo ya choo. “Sonia!” Akamuita, Sonia akabaki amesita akijishauri kama aende au abaki palepale amsikilize. Lakini kwa kuwa Sam alishamtambulisha kama ni kiongozi wake, akaamua amfuate kwa nyuma kwani alisogea pembeni zaidi kama upande mwengine wa vile vyoo, aliendelea kusogea mpaka kwenye chumba kingine ambacho kilimtia wasiwasi Sonia.
Kilikuwa kama stoo. Mr. Mponza akasimama mlangoni mwa hiyo stoo. “Unaishi wapi, Sonia?” Sonia akabaki na kigugumizi. “Usiogope. Sina nia mbaya. Nikutaka kufahamiana zaidi, nimeona tusogee huku kwa kuwa kule kuna kelele.” Sonia alipeleka macho yake mpaka kwenye mikono ya huyo Bosi. Alishangaa kukutana na pete ya ndoa kidoleni huku yule baba akimungalia kwa uchu sana.
Mara macho yake yakatua kifuani kwa Sonia. Taratibu fikira zake zilizogubikwa na pombe na tamaa hazikuwa zikimuona Sonia na nguo hata moja. Alianza kufurahia kuyaona matiti ya Sonia yakiwa waziwazi.
Kama simba alimvutia Sonia ndani ya kile chumba kwa haraka, na kufunga mlango. Alipitisha mkono wake moja kiunoni mwake na kumvuta karibu sana na yeye kama kumdhibiti asitoke mwilini mwake, huku mkono mwingine ukimpapasa harakaharaka tena kwa nguvu kila mahali juu mpaka chini huku akimminyaminya.
**********************
Mambo ndio kwanzaaaa yameanza.
1.Leah na mama yake wameondoka wakiwa na hasira. Lakini yule mama ametoa ahadi ya Leah kukaa gorofani, nini atafanya?
Makubwa na ya KUSIKITISHA sana yapo mbeleni,
usipitwe.
2.Ipi historia ya mama Sonia? Fuatilia kwa makini, maana yapo mazito mbeleni. Na baba yake Sonia pia yupo. Ni nani? Usikose.
3.Je, Historia Mbaya ya Sonia itafanikiwa kujirudia?
NINI KITAENDELEA KWENYE SIMULIZI HII....
Mengi mnooo.
Usipitwe na Part 2 ya SIMULIZI hii ya KUSISIMUA
iliyojaa VISA na MIKASA kemkem.
0 Comments:
Post a Comment