Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com More than Saying - Zaidi Ya Kutamka - PART 3 - Naomi Simulizi

More than Saying - Zaidi Ya Kutamka - PART 3

Sam alipoteza kumbukumbu kabisa ya kitu alichokuwa akiongea, akabaki amesimama akimwangalia Sonia kupitia mtu aliyesimama mbele yake. Kila mtu alishindwa kuelewa kinachoendelea. Ndipo Afisa mwajiri wao, {HR} naye huku amejawa kigugumizi kikubwa aliamua kusaidia. 

“Kwa hiyo kama alivyosema Mheshimiwa Samweli hapa, kwamb.., yaani watu wote mjiandae kwa mabadiliko makubwa. Ni makubwa kwa kweli. Makubwa sana, yenye kuleta mafanikio makubwa sana, tena sana kwa benki yetu….. yanakuja na kwa kuwa tutakuwa hapa kwa siku mbili tatu, tutaendelea kuelekezana.” Na yeye akanyamaza.

Kwa mshangao mkubwa ilibidi meneja wa tawi awatawanyishe wafanyakazi wote na kuwatakia siku njema ya kazi, huku wakikatisha mazungumzo yao katikati. Sam alikuwa akiongea mambo ya muhimu sana, na tena alifika sehemu ambayo wafanyakazi wote walitaka kuuliza maswali, lakini ujio wa Sonia katikati wa kikao hicho, uliharibumtiririko mzima wa maongezi na kufanya kikao kufungwa mapema hata kabla ya muda. 

Taratibu Sonia aliondoka na kwenda ofisini kwao. Wakati anaanza tu kumuhudumia mteja wake wa kwanza aliyekuwa amekaa mbele ya meza yake, alishangaa kumuona Sam naye amemsimamia mbele ya meza yake. “Samahani Mzee, naomba uhamie kwa yule dada pale, atakuhudumia. Nataka kuanza kumkagua huyo dada. Tuko kwenye marekebisho ya ‘system’ zetu ili kuboresha huduma zetu. Si unaelewa Mzee, mambo ya teknoloji yanavyobadilika kila siku?” Sam alimfukuza mteja wa Sonia. 

“Ni kweli Baba.” Mteja alijibu huku akinyanyuka kuelekea kwenye meza ya mfanyakazi mwingine. “Hapana Sam, huyo ni mteja wangu nimeanza naye tokea jana! Lazima mimi ndio nimuhudumie.” Yule Mzee akarudi kukaa kwenye meza ya Sonia. 

“Nipe mafaili yake atahudumiwa na mtu mwingine sio lazima uwe wewe.” Sam akakusanya mafaili yote yaliyokuwepo mezani kwa Sonia na kuyarusha kwenye meza ya jirani yake Sonia. Yule Mzee naye alimfuata nyuma nakukaa kwenye meza ya huyo jirani yake Sonia. 

“Hayo mafaili sio ya huyo mteja, Sam jamani! Mimi nitamuhudumia tu.”  Mzee akarudi tena kwenye meza ya Sonia. “Nipe mafaili ya huyo Mzee basi.” Ofisi nzima na wateja wote walibaki wakiwaangalia Sonia na Sam. 

“Kwa nini wewe usiende kumkagua mtu mwingine Sam? Ukaacha mimi nimalizane na huyu mteja halafu ndio ukaja kwangu! Huyu Mzee amesumbuka siku nyingi kuomba mkopo ni mteja mpya, afisa mkopo aliyetakiwa amuhudumie ameugua gafla ndio meneja ameniambia nihakikishe leo anapata mkopo.” 

“Kwa hiyo unanipangia kazi, Sonia?” “Hapana, Sam!” “Mimi nimetoka makao makuu, nimekuja mpaka hapa! Nayajua majukumu yangu. Najua naanzia wapi na kumalizia wapi. Naomba usinipangie kazi. Nimesema naanza na wewe.” “Sawa.” Sonia akajibu, na kuinamia droo zake kuendelea kutafuta faili ya huyo Mzee. 

Alipolipata alitaka kunyanyuka nalo kumpelekea mwenzake, lakini Sam akalichukua kutoka mkononi mwa Sonia nakuanza kulisoma akiwa bado amesimama na kila mtu akiwashangaa. 

Sam alitoa kitabu chake cha hundi kutoka mfukoni na kuandika ile hela yote huyo mzee aliyokuwa akitaka kukopa na kumpa. “Sasa Mzee, hii si ndio hela uliyokuwa ukitaka?” “Ndio baba.” “Basi, ukienda kule dirishani wanapogawa pesa, watakupa hii pesa. Ukafanye biashara mzee, sawa? Usiende kuoa mke mwingine.” “Kwa hiyo umenipa bure mwanangu?” Kila mtu alianza kucheka, kasoro Sonia alirudi kukaa nakubaki akiangalia kompyuta yake. 

“Changamka Mzee, nenda kabla hajabadili mawazo.” Mfanyakazi mwenzie Sonia alidakia huku akicheka. “Asante sana baba. Na wewe Mungu akujalie, zikazidi kujaa mwanangu, wakutunze wanao…” “Amina Mzee.” Sam alimkatisha na kumgeukia Sonia. 

“Nakaa wapi?” “Kwani unataka kufanya nini Sam jamani?!” “Kuangalia utendaji kazi wako, jinsi unavyoingiza kumbukumbu zako kwenye kompyuta na mambo mengine mengi. Au unataka nikwambie kila kitu?” Akachukua pochi yake, akampisha kiti. 

“Unaenda wapi sasa?” “Natakiwa kwenda kutembelea wateja, Sam! Nimekuachia kompyuta, na kila kitu kipo hapo, unaweza kuendelea.” “Hivi mbona kama nimejieleza vizuri sana Sonia!? Nina kukagua. Au hujui maana ya kukaguliwa? Lazima wewe uwepo. Kama hutaki, unaona mimi sifai kukukagua, nenda kaongee na afisa mwajiri wetu. Labda mimi nifukuzwe kazi atafutwe mtu mwenye vigezo vya kukukagua wewe.” Watu wote walikuwa wakiwasikiliza, na kumshangaa Sonia anawezaje kumjibu mtu mkubwa kama Sam. Sonia aliweka pochi yake chini na kukaa kwenye kiti kama mteja. Sam akakaa kwenye kiti cha Sonia. 

Muda ulizidi kwenda Sam akiendelea kufanya kazi zake kwenye kompyuta ya Sonia bila hata kumuuliza swali lolote wala kuangalia kazi za Sonia. Aliendelea kupokea simu zake kama kawaida kutoka kwa mameneja wa matawi tofauti tofauti, na kuendelea kuwaelekeza kitu chakufanya palepale kwenye kiti cha Sonia, tena kwa kutumia kompyuta ya Sonia.

Akaingia huyo Afisa mwajiri mkuu wa benki nzima nchini, Mr.Mwansasu, kila mtu akasimama kumsalimia. Moja kwa moja na yeye akasogea kwenye meza ya Sonia. 

“Vipi Mkuu?” Sam alimuwahi Mr. Mwansasu. “Njaa inauma Sam, twende tukapate kifungua kinywa.” Akamgeukia Sonia aliyekuwa kimya kabisa ameinamia simu yake. “Hujambo Sonia?” “Shikamoo.” “Unapaonaje Dodoma?” “Pazuri sana na nimeshapazoea.” “Safi sana. Kwa hiyo nikikwambia tuondoke leo turudi Dar?” Sonia alitingisha kichwa kuashiria kukataa. 

“Tulikuudhi nini watu wa jiji la maraha?” Sonia akatabasamu kinyonge na kujibu. “Naona huku kuna utulivu kuliko Dar. Hakuna foleni, watu wana upendo na ubinadamukuliko Dar.” “Watu wa Dar hatuna ubinadamu?” Mr.Mwansasu aliendelea kuuliza huku akicheka. “Mhh! Hapana kwa kweli. Watu wa Dar pesa kwanza, halafu mengine hayanamaana kabisa.” Sam alikuwa ametulia kimya kabisa akiwasikiliza huku ameinamia kopyuta ya Sonia. Mr.Mwansasu alizidi kucheka. 

“Utakuwa umeondoka muda mrefu sana Sonia. Mambo jijini yamebadilika sana. Wewe rudi ukajionee mwenyewe.” “Siwezi tena. Mume wangu anafanya kazi hukuhuku na tuna mtoto mdogo ambaye siwezi kumtenganisha na baba yake. Hata hivyo tumesha jijenga sana huku, na nina ona mwenzangu ana papenda sana Dodoma kuliko Dar.” Palizuka ukimya wa ghafla. 

Sam alimgeukia Sonia na kumwangalia kwa muda, kisha akageukia tena kompyuta bila kusema kitu. Muda wote Sonia alikuwa akiongea huku akichezea simu yake. 

“Sonia wewe mbaya bwana! Unafanya harusi hutualiki ndugu zako?” Mr. Mwansasu aliongeza kuvunja ukimya. “Ilikuwa harusi ya haraka haraka, hatukualika watu wengi.” “Daah! Hongera sana.” “Asante.” Sam alibaki amekodolea macho kompyuta ya Sonia bila kufanya chochote. Mr Mwansasu alijua. “Sasa Sam, twende basi.” Sam akanyanyuka bila ya kuaga wala kusema kitu. 

 *********************

Hakurudi tena pale kazini mpaka kesho yake asubuhi kwenye kikao.  Sonia aliweza kumuona Sam alivyoumia usoni. Lakini aliweza kuongea mambo yake yakitaalamu na kujibu maswali yote kiufasaha mpaka kikao kilipoisha. 

Hakusogea kabisa kwenye ofisi ya mikopo, ambako anafanyia kazi Sonia. Alishinda kwenye meza ya pembeni ya mapokezi akiwa kama mgonjwa. Hakutoka kwenda kula kitu chochote. Alibaki amekaa hapo kwenye meza tu, akitumia “Laptop” aliyokuwa amekuja nayo. 

Kila mtu alijua kuna tatizo kubwa limempata Sam. Kwani sura aliyokuwa amekuja nayo siku iliyopita ya uongozi ilibadilika ikawa kama kondoo aliyemwagiwa maji ya baridi sana. 

Sonia alitoka na kwenda kutembelea wateja wake, akarudi mchana na kumkuta bado Sam amekaa palepale kama mgonjwa. Alipouliza kama alitoka kwenda kula, akaambiwa hajanyanyuka kwenye hicho kiti tokea alipokaa na hata wenzake aliokuja nao walipomwambia watoke wakale, hakutoka. 

Akamuhurumia, akamwandikia ujumbe mfupi kwenye kikaratasi, akakitupia kwa nyuma yake, kwenye meza aliyokuwa ameinamia. Sam akakifungua hicho kikaratasi bila ya kugeuka kuangalia aliyekiweka. ‘Nilidanganya jana. Bado sijaolewa na wala sina mtoto mwingine.’  Sam alivuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha huku akitabasamu. Akasimama.

“Kiongozi?” Sam akamuita Mwansasu huku amechangamka kama sio yeye. “Vipi?” “Tukapate chakula cha mchana.” “Mbona tulisha kula Mkuu!” “Daah! Njaa inauma kweli!” “Nilikwambia tukale, ukakataa.” “Tumbo lilikuwa limejaa gesi kweli!” “Tokea jana asubuhi tumbo lilikuwa limejaa gesi?” Mwansasu alimtania Sam. “Ushapata dawa nini? Maana naona na Uzima umerudi usoni.” Sam alicheka na kurudi kukaa kwenye meza yake.  

Mara akashitukia mtu amemsimamia pembeni yake. “Vipi?” Sam akageuka vizuri. “Kuna chakula chako jikoni.” Bila kupoteza muda, Sam akaelekea jikoni, alikuta chakula kimeandaliwa mezani, akabaki akitabasamu. Japokuwa hakumkuta Sonia pale jikoni, lakini alijua yeye ndiye muhusika.Alikaa na kuanza kula huku amejawa furaha sana moyoni. Alipomaliza tu kula, akarudi moja kwa moja mezani kwa Sonia. 

*********************

“Nimerudi kumalizia kazi yangu ya jana.” Sonia alitabasamu huku akiangalia kompyuta yake. Akavuta simu ya Sonia hapo mezani, nakujipigia. Kisha akasogeza kiti chake pembeni ya Sonia bila kusogelea kompyuta yake, akamtumia ujumbe Sonia. 

Alipoona ujumbe umeingia kwenye simu yake, Sonia akausoma. ‘Asante kwa chakula, nimeshiba. Lakini sio kitamu kama unachopika wewe.’  Aliposoma alitabasamu kwanza, kisha akaanza kuandika ujumbe kama kurudisha majibu kwa Sam, lakini akasita katikati, nakubaki akiingalia simu yake kwa muda. 

Kama aliyekuwa amekumbuka kitu, taratibu Sonia akarudisha simu yake mezani huku akijitahidi kuzuia machozi yake lakini alishindwa. Sam aliweza kuona machozi yakimtoka. Aliinama kama anayevaa viatu vyake ili watu wasimuone na kuendelea kulia. 

Sam hakujali wateja wala wafanyakazi wengine, aliweka mkono wake mgongoni kwa Sonia na kuanza kumbembeleza taratibu. “Pole Sonia.” Sam na yeye aliinama, huku akimuongelesha taratibu na kuendelea kumpapasa mgongo wake kama kumbembelezakwa muda, mpaka Sonia alipotulia na kufuta machozi. 

Alitulia kwa muda, kisha akamgeukia Sam wakiwa vilevile wote wameinama. “Tutaonana kesho.” “Mbona mapema, Sonia?” Sonia akafuta machozi. “Napitia kwa mama Briana kwanza.” “Mama Briana, Dodoma!?” Sam alikunja uso kwa mshangao. “Ndiyo.” Sonia akakaa vizuri. 

“Tena nilitokea huko asubuhi, nimemuacha ana homa. Nataka kujua anaendeleaje?”Sonia alijibu huku akiendelea kukausha machozi usoni mwake. “Sielewi Sonia!” “Naomba nikusimulie kesho Sam, acha sasa hivi niwahi.” “Twende wote, utanisimulia njiani.” Sam na Sonia wakaondoka pamoja. 

 

Kika Pando, Lina Mavuno Yake

Njia nzima Sonia alikuwa akimsimulia Sam huku akilia. Sam alikuwa kwenye mshituko mkubwa sana, asiamini anachosimuliwa. “Mungu wangu!” Sam alizidi kusikitika huku akimuita Mungu. “Haiwezekani!” Walifika mpaka hospitali ya Mirembe, walimkuta mama Briana. 

Sam alitokwa na machozi. “Mbona amekonda hivi?!” Sonia alimshika kichwa. “Afadhali homa imeshuka kidogo. Asubuhi ilikuwa juu sana.” Sam aliomba wakae kidogo.

“Mama Bree! Vipi?” Sam alimuita. Mama Briana alimuangalia Sam kwa muda mrefu na kuinama. “Unajisikiaje?” Mama Briana alinyamaza tu. Sam alibaki akimwangalia huku machozi yakimtoka. “Mungu wangu saidia!” Mama Briana alikuwa amebadilika kama sio yeye!

Kwa kuwa alikuwa mweupe, majeraha na makovu yaliweza kuonekana sawia mwilini mwake. Alikonda na kuwa kama mtoto wa shule ya msingi. Japokuwa walimkata nywele zote, lakini uzuri wake ulikuwa upo vilevile.

Sam alianza kuzunguka hicho chumba na kushindwa kuongea kitu kingine huku ameweka mikono kichwani mpaka muuguzi alipowaomba wamwache apumzike. “Nitakuja kukuona kesho Shem. Sawa?” Mama Briana alitingisha kichwa. Sonia hakuamini. “Ameanza kuelewa!” Sonia alifurahi sana.  

Sam azidi kushtushwa na Maisha mapya ya watoto wa Nyange.

Walitoka hapo na kuelekea nyumbani kwa Sonia lakini njia nzima Sam alikuwa kimya kabisa, akionekana mwingi wa mawazo na mshituko mkubwa. Sam alizidi kuchanganyikiwa kukuta watoto wa Nyange kwenye mazingira yale. “Mungu wangu! Nahisi naota. Huyu ni Briana wa Nyange!?” Sam aliuliza kimyakimya. 

Ilikuwa ngumu kuingia akili kwa Sam kila akijiuliza wale watoto wa Nyange waliwezaje kuishi kwenye mazingira kama yale! Kana alimkimbilia Sam nakumkumbatia. Briana alikuwa ametulia sana huku akichezea vidole vyake. 

“Vipi Briana?” “Amekataa kula leo, tokea asubuhi shuleni hajala kitu.” Kana akajibu. “Njoo mpenzi wangu.” Sonia alimkumbatia Briana. “Vipi?” “Nataka kumuona Mama Briana.” Briana alianza kulia. Kila mtu alianza kulia mpaka Sam. “Mungu wangu! Ni nini hiki?” Sam alikuwa haelewi kabisa.

“Nikuombe kitu Briana?” Briana akatingisha kichwa. “Uvumilie twende tukamuone jumamosi nikitoka kazini. Ili tupate naye muda mrefu wa pamoja. Sawa?” “Tutakuwa wote Briana. Usiwe na wasiwasi.” Kana aliongeza. Briana akatingisha kichwa kukubali. Mama yake Sonia, Sonia, Asifiwe na Mchungaji bado walikuwa kwenye maombi makali sana ya kufunga na kumuombea Nyange na mkewe. 

*********************

“Ukapumzike Sam. Tutaonana kesho kazini.” “Usingizi umepaa Sonia! Daah! Nahisi nipo ndotoni, au naangalia filamu! Siamini haya yaliyo tupata!” Sam alikuwa kwenye mshituko mkubwa sana. 

“Kana! Unataka twende tukalale wote?” Sam akauliza. “Tutaenda na Briana?” Kana naye akauliza na kumwacha Sam na kigugumizi kwa kuwa kitanda kilikuwa kimoja na Briana alishakuwa binti mkubwa, sio mtoto kama Sam alivyomuacha. 

“Siwezi kuondoka na kumuacha Briana.” Kana aliongeza kwa wazi kabisa. “Basi nitakuja kuwachukua kesho, ngoja nikatafute chumba kikubwa. Leo nitaenda na Brayan tu. Nitamrudisha asubuhi wakati nakuja kumchukua Sonia ili twende kazini.” “Tunakushukuru sana kwa kuja kututembelea, Sam.” Mama Sonia alimshika mkono Sam. Brayan alifurahi sana kwenda na gari ya anko Sam. 

 *********************

Kana na Briana waliingia chumbani kwao, Sonia aliwasikia wakiongea. “Nilikwambia Briana, usikate tamaa. Unaona sasa hivi Mungu amemleta anko Sam, na Sonia ameahidi kutupeleka kwenda kumuona mama Briana siku ya jumamosi. Kila kitu kitakuwa sawa tu, wala usiogope.” “Nimefurahi tumebaki wote Kana. Pale nilikuwa nimeshaanza kuogopa, nilijua utaniacha.” Kana alianza kucheka. 

“Na ningeondoka nikuache mwenyewe!” “Nisingeweza kulala, Kana.” “Najua. Siwezi kukuacha Briana. Usiwe na wasiwasi. Unataka nikuletee hata maziwa? Hujala tokea asubuhi, hutalala vizuri ukiwa na njaa.” “Njaa inaniuma.” Briana akajibu. “Nisubiri basi, nikaangalie kama kuna chakula jikoni.” Sonia alikuwa amesimama nje ya mlango wao akiwasikiliza, alikimbia haraka kurudi sebuleni, mara aliposikia Kana anafungua mlango. 

“Na watakuja kukukamata siku moja unawasikiliza, shauri yako.” Mama yake Sonia alimwambia Sonia alipomuona anakimbia na kujitupa kwenye kochi. Sonia alianza kucheka. 

“Vipi Kana?” “Naangalia chakula. Briana anaumwa na njaa.” Sonia akawahurumia sana Kana na Briana, alisimama kwenda kumpashia Briana chakula. “Usikifanye cha moto sana, ataungua.” Kana aliyekuwa amemsimamia Sonia akisubiria chakula cha Briana, ilimbidi kumshitua Sonia kwani alikuwa amekiacha chakula kikizidi kupata moto na yeye amepotelea kwenye mawazo yake.

“Daah! Nimejisahau kabisa! Kuwa mwangalifu, ni chamoto kweli.” “Asante.” Kana aliaga nakurudi chumbani kwao. 

Alimkuta Briana mlangoni. “Unaenda wapi?” Kana akamuuliza. “Nilikuwa nakufuata.” “Pole, nimechelewa. Sonia alikuwa anakipasha moto.” “Tutakula wote?” “Mwenzio nimeshiba.” “Kula hata kidogo Kana.” Sonia alianza kucheka kwani walikuwa wameacha mlango wazi kwa hiyo Sonia na mama yake walikuwa wakiwasikia kila kitu walichokuwa wakiongea chumbani. 

“Sipendi kula peke yangu, naomba tule wote.” “Kidogo tu. Kingine unakula wewe na uwe mwangalifu, kina moto sana.” Kana alikaa pembeni ya Briana akimsubiri amalize kula. 

“Umeshiba?” “Nimeshiba. Asante.” Kana alirudisha sahani jikoni. “Asante Sonia, Briana ameshiba.” “Mlale sasa, kesho shule.” Aliwasikia wakicheka taratibu huku wakiongea mpaka walipopitiwa na usingizi. 

*********************

Sonia akaingia kuwachungulia, walikuwa wamejifunika shuka na wamegeukiana. “Utakuja kusutwa Sonia wewe! Mimi nakuangalia tu.” Mama Sonia alikuwa amelala kwenye kochi ametulia kimya anamwangalia Sonia anavyohangaika na mwanae. Sonia alianza kucheka taratibu. 

“Hivi mama, hawa watoto mwisho wao nini? Akija kupona mama Briana nakumchukua Briana na Brayan, itakuwaje?” “Wala usiumize kichwa. Hakuna wakuwatenganisha hao watoto. Nyange mwenyewe kanawa mikono hapo. Jeuri yake yote hapo amegonga mwamba. Tuwaombee Nyange na mkewe uzima tu.” 

 *********************

Asubuhi na mapema Sam alirudi na Brayan. “Usiku Brayan si kanibadilikia. Anamtaka mama yake. Ikabidi nimzungushe mle hotelini mpaka akapitiwa na usingizi. Kwani hawajawahi kumuona mama yao tokea augue?” “Hapana Sam. Hali ya mama Briana ilikuwa mbaya sana. Nisingeweza kuwapeleka wakamuone mama yao akiwa na hali ile.”

“Hata hivyo BB anaposema mama, anamaanisha Mama Sonia, sio Mama Briana.” “Kweli?!” “Anamuita mama. Amemzoea sana mama tokea wanaishi na wazazi wao. Ndiye alikuwa akishinda naye pale nyumbani. Na mama naye naona kama amemdekeza sana BB. Unajua anambeba mgongoni mpaka leo? Halali mpaka mnyweshe maziwa, au akae amempakata mpaka apitiwe na usingizi, ndio anamlaza.”

“Ndio maana jana alivyokubali kwenda na wewe, nilijua tu atakubadilikia mkifika huko. Hawezi kulala bila mama.” “Maskini! Ningejua hivyo ningempa maziwa, labda angetulia.” Sam alikuwa akiongea na Sonia taratibu wakati akisubiria watoto wawe tayari awapeleke shule. 

*********************

“Leo muujiza. Watoto wanaenda na gari shule!?” “Kwani walikuwa wakiendaje shule?” “Wanatembea na miguu, Sam jamani! Ningepata wapi gari yakuwapeleka shule?” “Daah kweli! Lakini Sonia, nawapongeza SANA wewe na mama yako. Mlichofanya sio kidogo. Kuwaokoa hawa watoto! Kwa chochote mlichoweza kuwapa, asanteni sana.”

“Ingekuwa rahisi kuwatelekeza tu mkaondoka, kwanza walikuwa kwao, kwa hiyo mlikuwa na sababu zote zakueleweka kama mngewatelekeza. Kitendo mlichofanya, binafsi kinanishangaza.” Sonia alikuwa akifuta machozi. 

“Siamini Sam!” “Hata mimi Sonia. Hawaja wasumbua?” “Hata kidogo Sam! Zaidi ya Briana kumtaka mama yake, hata kusema nyumba ina joto, mtoto huyu aliyezoea kulala kwenye AC au hata kulalamika kutembea kwa miguu, au kwamba shule ni mbaya, hajalalamika hata mara moja.”

“Brayan yeye ilimradi amuone mama, basi. Hajawahi hata kuulizia wazazi wao. Ila ukiwaangalia kama ulikuwa ukiwafahamu wote wawili tokea zamani, utagundua kuna kitu hakipo sawa maishani mwao. Lakini sio kulalamika.” Sonia alifuta machozi. “Kweli hawa watoto ni wa Penninah! Afadhali.” Sam alibaki anakuna kichwa. “Daah!” Na kuendelea kulalamika. 

 *********************

Alianza kumshusha Brayan kwanza shuleni kwao, ndipo wakaenda shuleni kwa kina Kana na Briana. Sam alikuwa kwenye mshituko mkubwa sana, alijawa na simanzi moyoni baada ya kuiona ile shule. “Daah!” Sam alikuwa bado haamini. 

“Nitamtuma dereva aje awafuate mkitoka shule. Mkitoka tu, mtamkuta dereva na gari ya benki akiwasubiri hapahapa. Sawa?” “Asante sana anko.” Kana akamshika Briana mkono na kuondoka. Sam alibaki ameduwaa. “Mungu wangu! Uwii! Nahisi nipo usingizini! Natamani kuamka mwenzenu.” Sonia na mama yake walibaki kimya tu ndani ya hiyo gari.

“Nyange akija kuona hii shule anayosoma Briana! Ataumia sana.” Sam aliendelea kuumia. “Lakini Mama Sonia, asante sana, mama yangu. Asante sana. Najua mmejitoasana kwa hawa watoto. Asanteni sana. Ungeweza kuondoka nakuwa….” Sam alishindwa kuongea, aliinama. “Daah!” Walikaa palepale shuleni kwa kina Briana kwa muda kila mtu akiwaza lake.

Mwishowe Sonia akamshitua. “Twende Sam. Tutachelewa kazini.” “Daah!” Sam alimpeleka mama Sonia kazini kwakwe na kumuaga. “Kazi njema mama.” “Asante na nyinyi pia.”  

Sam na Sonia Tena!

Wakiwa njiani wakielekea kazini, Sam akamgeukia. “Kwa nini uliondoka Sonia?” Sonia alibaki kimya. “Eti Sonia? Kwa nini ulinikimbia?” “Nilichoka Sam. Nilivumilia mpaka nilifika mwisho.” “Nilikuwa nahangaika kwa ajili yetu, Sonia!” “Hivi unajua ni wanaume wangapi wenye pesa zao walikuwa wakinitaka Sam? Lakini niliamua kutuliana wewe, kwa kuwa ulikuwa ukinijali sana.”

“Lakini ulikuja kunibadilikia vibaya kweli! Ukawa hunijali mimi mwenyewe, unakazana kunipa pesa tu. Nilichoka Sam. Nilikuwa mpweke, wakati wewe ulikuwepo. Ulimthamini G na kazi yako kuliko mimi. Nakutumia ujumbe hujibu, Sam! Hata tukionana unashindwa kuongelea chochote juu ya ujumbe niliokuwa nakutumia!”

“Nakwambia naumwa hata hukujali?” Sonia alianza kulia. “Nimelazwa hospitalini, ulishindwa hata kuja kuniona! Kweli Sam, leo unaniuliza kwa nini niliondoka? Ulitaka nikae pale nifanye nini?”

“Sikuwa nikitaka pesa zako, nilikuwa nakutaka wewe Sam. Hata baba yake Kana aliniahidi pesa nyingi sana kama ningemkubali kimapenzi. Aliniahidi maisha mazuri sana, mimi na mama yangu, lakini nilikubali kuteseka kuliko kuwa na yule baba.”

“Ulipokuja wewe, nilianza kuhisi kitu cha tofauti kwako ndio maana nikakukubali. Lakini umegeuka kuwa kama wanaume wengine Sam, pesa umeziweka mbele ukasahau mahusiano yetu kabisa. Ulishindwa kunipa hata dakika tano tu, kwa siku! Muda wote ulikuwa busy, kama sio kazini basi kwenye simu.” Sam alibaki kimya, Sonia aliendelea kulia. 

Akaamua kuegesha gari pembeni ya barabara. Akajiweka sawa, na kumgeukia Sonia “Unajua Sonia, ninategemewa sana nyumbani kwetu. Kama unavyojua mimi ni mtoto wa kwanza. Tokea napata akili zangu timamu na kuwaona wazazi wangu wanavyoishi na mimi nilianza kuhangaika kivyangu nikitafuta pesa mchana na usiku, ili kusaidia nyumbani.

Haya, unakumbuka maisha niliyokuwa nikiishi na Leah? Matusi, masimango na dharau ya waziwazi mbele za watu juu ya umasikini wangu. Ukweli vyote hivyo viliniathiri SANA. Leah aliniacha akisema ananipenda lakini alichoshwa na umaskini wangu. Nilikuwa nikiumia sana Sonia, lakini sikuwa na jinsi ya kujisaidia.”

“Ghafla mambo yote mazuri yakatokea kwa wakati mmoja. Nikakupata wewe, biashara ikachanganya na kuanza kupandishwa cheo kazini. Vyote vilinijia nikiwa sijajiandaa na sikujua jinsi ya kuishi nikiwa na majukumu yote hayo mbele yangu.”

“Nilipoona hujawahi kulalamika, nilifurahi sana. Nikajua unanielewa, nikawa najiambia nikusanye pesa nyingi, nimalize nyumba ili ukimaliza tu shule, tukisha oana, tuhamie kwetu na wewe ukipata kazi ndipo niache kitu kimoja, kazi au biashara, ili tupate muda wa pamoja.”

“Kumbe nilikosea mahesabu. Mwenzangu ulikuwa ukiumia sana, huniambii! Ukaondoka wakati ndio mambo yanakuwa mazuri Sonia! Sikuwahi kushika pesa nyingi maishani mwangu Sonia, wala sikuwahi kupendwa na kujaliwa kama ulivyokuwa ukinijali wewe.”

“Sikujua jinsi ya kukutunza vizuri wewe na pesa. Nikalemea upande mmoja. Naomba niamini Sonia, nilikuwa nahangaika ili nisije kuwatoa pale kwa Nyange wewe na Kana halafu niwaweke tena sehemu mbaya. Nakiri nimekosa sana. Ni ulimbukeni ndio ulinisumbua Sonia, si vinginevyo. Kama kukudharau au kutokukuthamini. Hapana. Tafadhali nielewe na unisamehe.” 

“Umemaliza sasa ujenzi?” “Nashukuru Mungu nilimaliza, naishi na wale wadogo zangu wawili, wamwishoni, yule anayenifuata ameanza kujitegemea.” “Hongera!” Sam hakujibu hiyo pongezi. 

“Nakuahidi Sonia, ukinisamehe, nitabadilisha maisha yangu kabisa. Hata ukitaka hii kazi nitaacha nihamie kwenye biashara ili tupate muda wapamoja. Nakuthamini sana Sonia kuliko pesa. Ulipoondoka nilijaribu kujisogeza kwa kina dada wengine…” “Sam wewe jamani!” Sonia akamkatisha na kulalamika. 

“Kumbe ulikuwa na wanawake wengine?!” “Nisikilize basi Sonia, sijafanya nao chochote Mungu shahidi, nilitaka kukwambia nilishindwa hata kufikiria swala la mapenzi. Kile kitu nilikuwa najisikia {connection}, nikiwa na wewe hata kabla sijakuchumbia, sijawahi kukipata tena kwa msichana mwengine yeyote.” Sonia akatulia akitafakari. 

“Nakupenda Sonia.” “Lakini ulibadilika sana Sam, uliacha hata kunibusu!” Sam akamvuta taratibu nakuanza kumbusu Sonia💏. Kwa muda mrefu sana walishindwa kuachiana💏. Sonia alikuwa akifurahia sana kushikwa na Sam. Hata Bob alipomshika hakusikia ile hali inayompata anaposhikwa na Sam {msisimko}. 

 *********************

Baada ya kissing ya muda mrefu kuendelea wakiwa kwenye gari, Sam alimuachia. “Funga mkanda, tunarudi kwa mama.” “Kuna nini tena? Tumesha chelewa kazini, Sam!” “Twende tu, usiwe na wasiwasi na kazini.” Sam akarudi tena pale alipo mshusha mama Sonia. 

Akamfungulia mlango Sonia na kumshika mkono. “Kuna nini Sam?” “Twende ndani kwa mama.” Wakaingia ndani wakamkuta mama Sonia na baadhi ya wateja wake wakiongea na Asifiwe. 

“Mama!” Sam alimuita mama Sonia akiwa amemshika Sonia mkono. Mama Sonia alishituka sana kumuona Sonia na Sam mida ile pale. Alijua kuna jambo baya limetokea kwa Mama Briana. 

“Vipi?”  “Uliniomba nimsubiri Sonia mpaka amalize shule. Nimevumilia mama yangu mpaka amemaliza. Naomba Baraka zako.” Sonia hakuwa akielewa kitu Sam anachoongea na mama yake. Mama yake Sonia alivuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha huku akifikiria na kutabasamu. 

“Tafadhali sana mama yangu. Nampenda sana Sonia. Na nina ahidi mbele zako, nitamlinda na kumtunza yeye na Kana, nitakuwa mwaminifu kwa Sonia mpaka kifo changu.” Machozi ya furaha na sintoamini yalikuwa yakimtoka Sonia. 

“Nawaombea kila la kheri, Mungu awasaidie.” Mama Sonia akajibu. Harakaharaka Sam akatoa waleti yake na kufungua zipu ya pembeni ilipokuwepo ile pete aliyokuwa amerudishiwa na Sonia, akamvalisha Sonia. “Nakupenda sana Sonia.” Sonia alimkumbatia Sam. “Na mimi nakupenda sana Sam.” Watu wote waliokuwepo pale walibaki na mshangao. 

Mbele ya mama yake, Sam akamkumbatia vizuri na kumbusu kidogo tu na kumshika mkono. “Asante sana mama.” Sam akashukuru na kuondoka na Sonia. 

 Hatimaye..

Sam aliendesha mpaka hotelini kwake. Akamtoa garini na kumshika mkono mpaka chumbani kwake. Akaanza kissing mpya tena safari hii za uchu. “Nilikuwa na hamu na wewe Sam!” “Nakupenda sana Sonia. Hakuna pesa inayoweza kulinganishwa na thamani yako kwangu. Naahidi kubadilika mpenzi. Naomba unisamehe. Najua nilikuumiza sana.” 

“Nimefurahi kukuona Sam. Nakupenda.” “Nimefurahi sasa hivi umekuwa wangu kihalali Sonia.” Sonia alitabasamu huku akiangalia pete yake. Sam alianza kumbusu tena na tena huku amemkumbatia kwa mkono mmoja na mwingine ukimpapasa kila mahali. 

Taratibu Sam alimuweka Sonia kitandani huku akiendelea kumbusu na kumfuta machozi. Alianza kukiss shingo yake, taratibu mpaka kifuani, alisita kidogo lakini akaamua kujitosa. ‘Sasa hivi Sonia ni mke wangu kihalali.’ Sam alijitia moyo. 

Alimpapasa kifua chake juu ya nguo zake za kazini, alipoona Sonia anamng’ang’ania na yeye, ndipo alipopata ujasiri wakumvua nguo zake zote. Bila kuchelewa Sam tayari alikuwa mtupu akifaidi mwili wa Sonia, ambao haukuwa mgeni kwake, kwani alishamuogesha lakini hakupata nafasi yakuuchezeaa atakavyo. 

Haikuwa mara ya kwanza kwa Sonia kulala na mwanaume maishani mwake, lakini ilikuwa ni mara yake ya kwanza kupata mwanaume aliyeweza kuutendea haki mwili wake. Hapakuwa na jinsi Sonia angekubali Sam amuache siku ile bila kumalizia jambo alilolianzisha.

Kwa tahadhari kubwa sana, akikumbuka maumivu Sonia aliyomsimulia aliyapata kutoka kwa baba yake Kana, Sam alitumia ustaarabu wote kufanya mapenzi na Sonia siku ile. 

Simu ya Sam ilikuwa ikiita kila baada ya dakika moja, lakini Sam alikuwa kama hasikii. Wakati Sonia anapumzika. 

Akamtumia ujumbe Mwansasu, ‘HR manager’ aliyekuwa amekuja naye. ‘Samahani sana Kiongozi, nipo na Sonia.’ Baada ya muda kidogo ujumbe uliingia. ‘Mimi sio mtoto.’ Sam akacheka, akazima simu kabisa na kuitupa simu sakafuni, akarudi tena mwili kwa Sonia aliyekuwa akiiangalia pete yake kama asiyeamini kama imerudi tena kidoleni mwake. 

 *********************

“Utanioa Sam?” Sonia aliuliza wakiwa bafuni wanaoga. Sam alimvuta karibu kabisa. Nakuanza mapenzi tena palepale bafuni. “Kwa mara ya pili? Hapa tunayo ndoa halali na baraka za mama juu yetu.” Sonia alitabasamu. Walishinda kitandani hapo, Sonia akishangaa kutokupokea simu yeyote kutoka kwa bosi wake. 

“Leo ni maajabu! Bosi hajanipigia simu mpaka sasa hivi!” Sam akacheka. “Nilishakuombea ruhusa.” “Sam?!” “Kweli. Nilitaka leo nilipe deni langu.” Sonia alianza kucheka kwa aibu. 

“Sijui bado nadaiwa?” Sam akauliza huku akimpapasa. Sonia akatingisha kichwa kukubali. “Kweli Sonia?” “Hata nusu yamalipo bado.” Akajua  amemfurahia. “Utakuja usiku tulale wote?” “Unataka unizoeshe tabia ya kulala na wewe halafu uondoke uniache nateseka?” “Nani amekwambia nakuacha?” “Tutafanyaje Sam?” “Hivi unafikiri nitaacha mke wangu Dododma? Nitachanganyikiwa bure!” Sonia alicheka sana. 

Alikumbuka wivu wa Sam. “Kwanza siwezi kukuacha wewe na watoto kwenye hali hiyo Sonia.” “Sijui Sam, naona unategemewa sana kazini!” “Hilo ni jambo ambalo nalo itabidi tulizungumze baadaye. Kwanza tuanze mambo ya msingi. Nimekuahidi hakuna kitakacho kuja kati yetu. Wewe kwanza, mengine baadaye. Nimejifunza Sonia, nimeteseka sana ulipoondoka. Siwezi kurudia kosa.” Sonia alibaki akiwaza. 

“Lakini tutafanyaje Sam? Mimi nafanya kazi Dodoma na wewe upo Dar. Itakuaje?” “Huku sio kwako Sonia. Naweza kupaita ni mafichoni. Lazima urudi kwako. Umesahau tulivyokuwa tukishinda wote juani, tena wakati mwingine na njaa, wakati tunajenga ile nyumba? Huwezi kulala sebuleni wakati nyumba unayo Sonia. Tunarudi wote Dar, nyumbani kwako.” Machozi yalianza kumtoka Sonia. 

“Asante Sam. Lakini kazi yangu nitafanyaje?” “Tutashugulikia uhamisho, usiwe na wasiwasi.” Sonia alifurahi sana, alijivuta mpaka kifuani kwa Sam, Sam akamkumbatia. “Asante sana Sam.” “Nakupenda sana Sonia. Tena sana.” “Na mimi nakupenda Sam.” Walibaki hapo kitadani wamekumbatiana, kila mmoja akiwaza lake.

“Inabidi twende kwa mama Briana kwanza. Nataka nikaongee naye. Nataka tuondoke wote. Siachi mtu hata mmoja hapa Dodoma. Mama Briana sio kichaa. Lazima arudi kulea watoto wake mwenyewe. Nimekataa Sonia, mama Briana sio kichaa. Nilazima atoke pale.” Sam aliongea kwa uhakika sana. Walivaa na kuelekea hospitali ya Mirembe.  

*********************

Walipofika tu, walimkuta Asifiwe na Mchungaji nao wakimsubiria mama Briana atoke wamuombee. Ilikuwa ndio mara ya kwanza kwa Mchungaji kufika hospitalini hapo kumuona mama Briana. Siku zote walikuwa wakiomba hukohuko kanisani. Sonia alimtambulisha Sam kwa Mchungaji kama mume wake. 

Mchungaji alibaki akimshangaa Sonia kwani alimfahamu Sonia ambaye hakuwa hata na mchumba! “Umeolewa lini Sonia?!” Sonia akababaika kidogo, alijisahau. “Sam alikuwa mchumba wangu tuliyekuwa tukiishi naye Dar, amekuja jana na leo asubuhi….” Akaishiwa maneno na kuinama.

“Nilienda kuomba baraka za mama. Amekubali na kutubariki. Kwa hiyo nimemchukua Sonia kama mke wangu. Tuna ‘Ndoa Halali’.” Sam alimalizia na kumshika mkono Sonia. Asifiwe alikumbuka yaliyotokea pale saluni kwa mama Sonia asubuhi ya siku ile, lakini Mchungaji alibaki akiwaangalia, ghafla mlango ukafunguliwa na mama Briana akaingia akiwa na manesi wawili. 

“Itabidi tuongee vizuri na nyinyi wote wawili.” Mchungaji alisimama kumsalimia mama Briana huku akimwangalia Sam na Sonia. “Umesikia Sonia? Lazima tuongee kwa pamoja swala la ndoa kwa jumla.” Mchungaji alirudia. “Ndiyo, nimesikia.”  

 Kwa Mungu Wa Yasiyowezekana Kwa Wanadamu

Mchungaji alinyosha mkono, akamshika mama Briana mkono wake wakulia kama kumsalimia. Ghafla ilitokea hali yakutisha sana, mpaka manesi wote wakakimbia. Sonia alijificha nyuma ya Sam huku akitetemeka. Mama Briana alianza kurushwa kama mpira, na mapepo yalianza kulipuka. 

Ile hali ya mwanzo ya kujipigiza ilirudi tena ikawa mbaya zaidi. Sonia alianza kulia alijua mama Briana anataka kufa. Mchungaji akiwa amejawa nguvu za Mungu, alikemea hayo mapepo kwa jina la Yesu, baada ya muda mfupi mama Briana akatulia kimya.“Nilijua atakufa tu! Nitamwambia nini Briana?!” Sonia alizidi kulia. 

Sam akamsogelea mama Briana na kuinama. “Shem? Shem! Mama Briana? Mama Briana?” Akaanza na kumtingisha. “Abee!” Mama Briana alishituka kama aliyekuwa kwenye usingizi mzito sana. 

“Sam?” “Vipi Shem?” Mama Briana akatulia kidogo. Sam akamshika mkono na kumnyanyua kutoka chini sakafuni. Akamkumbatia kwa muda mrefu sana huku akilia. “Mama Briana!!” “Kuna nini Sam!? Nipo wapi?” Mama Briana aliendelea kuangaza macho huku Sam akishindwa kumuachia.

“Nyange na wanangu wako wapi?” Kulikuwa na hali ya kushangaza na ya maajabu, hakuna aliyeweza kumjibu. Naye Sam alibaki amemkumbatia mama Briana huku akilia. 

Mwishoe, akamuachia. “Una homa kali sana Shem. Twende kwanza wakakuangalie hospitalini ndipo tutaongea.” Ndipo naye Sonia akiwa na mshangao akaweza kumsogelea. “Dada?!” “Sonia?” Sonia naya ndipo akamkumbatia. 

“Brayan wangu yuko wapi na dada yake?” Mama Briana aliendelea kuhoji akiwa anaonekana ana akili zake zote timamu. “Wapo salama kabisa dada, usiwe na wasiwasi.” Akapumua. “Kichwa kinaniuma sana.” Taratibu manesi walianza kutoka. “Anahoma kali sana. Anapewa dawa?” Sam akauliza. “Tokea asubuhi joto halishuki!” Mmoja wao akajibu. Sam aliomba aondoke naye ampeleke hospitali nyingine akaangaliwe zaidi. 

“Kwani niko wapi?” Mama Briana alizidi kuuliza huku akiangaza kila mahali. “Sonia?” Mama Briana alimwita tena Sonia. “Naomba uwe mvumilivu dada, mama Sonia atakwambia kila kitu.” Mama Briana akatulia huku akionekana mwenye maswali mengi. Sam aliongea na daktari aliyekuwa zamu, mama Briana akaruhusiwa baada ya kupimwa na daktari, na daktari kujiridhisha ni mzima kabisa. 

 *********************

Wakiwa njiani Sam na Sonia wakimpeleka mama Briana hospitali nyingine kwa vipimo vya kujua chanzo cha homa, mama Briana akamgeukia tena Sam aliyekuwa akiendesha. “Sam? Nyange yuko wapi?” “Yupo Dar!?” “Dar? Kwani hapa wapi?” “Dodoma, Shem.” “Dodoma!?” Mama Briana alizidi kuchanganyikiwa! Alibaki akiwaza kwa muda mrefu kama anayejaribu kuvuta kumbukumbu lakini alishindwa. 

“Watoto wangu wako wapi?” “Wapo Shem. Naomba ushuke kwenye gari kwanza, utibiwe, ndipo tutaongea vizuri.” Akashuka akiwa bado ana wasiwasi. 

Sam alimpeleka kwenye hospitali ya kulipia ili wapate huduma nzuri na kwa haraka. Waliingia kuonana na daktari, Sam aliomba alazwe chumba chake, akatolewa damu kwa vipimo zaidi. Wakati wakisubiri vipimo kujua kinacho msababishia homa mama Bree, Sam akamwambia Sonia anatoka nje, kwenda kuongea na simu atarudi. 

Baada ya muda kweli Sam akarudi. “Lazima tuondoke kesho asubuhi Sonia. Mama Briana ataenda kutibiwa Dar, sio hapa.” Sam aliongea na Sonia kwa sauti ya chini sana, ili wasimsumbue mama Briana. 

“Na mimi kazi?” “Nimetoka kuongea na Mr.Mwansasu, nimemweleza kwa kifupi. Ameshauri uandike barua yakuomba likizo, wakati tunashugulikia uhamisho. Amemtuma dereva, aje akuchukue urudi ofisini, ukakabidhi kila kitu nakuandika barua, ndipo uondoke.” 

“Nitakuonaje sasa?” Sonia alianza kuonyesha wasiwasi usoni. “Mimi nipo hapa na mgonjwa, ukimaliza tutawasiliana.” Akabaki kimya kama ambaye hajaridhika. “Siwezi kumuacha mama Briana peke yake Sonia!” “Basi tumuite mama aje akae naye wakati sisi tunaenda ofisini. Siwezi kurudi ofisini peke yangu.” “Mama akija hapa, watoto watabaki na nani, Sonia? Maana dereva alinitumia ujumbe, alishaenda kuwachukua shuleni na kuwapeleka pale kwa mama.” 

“Yupo msichana pale saluni, mama anaweza kuwaacha nao.” “Kama ni hivyo ni sawa.” Akampigia dereva simu, kumuomba abadili safari. Badala ya kwenda pale hospitalini moja kwa moja, akamfuate mama yake Sonia kwanza, na kumleta pale hospitalini. Sonia naye alimpigia simu mama yake kumueleza kwa kifupi kinachoendelea. 

 *********************

Baada ya muda mfupi mama Sonia alifika pale na kuingia kwenye chumba alicholazwa mama Briana. Bila kusema kitu akamsogelea pale kitandani, akamkumbatia kwa muda mrefu sana huku akilia. “Watoto wangu wako wapi, mama Sonia?” “Nipo nao mama Bree usiwe na wasiwasi, tena ndio wametoka shule sasa hivi, nimewaacha wanacheza.” 

“Shule?! Mpaka Brayan wangu anasoma? Kwani leo ni tarehe ngapi na kwa nini tupo huku Dodoma, halafu Nyange yuko Dar?” “Uliugua mama Briana, ndio maana ukaletwa huku Dodoma.” “Unazidi kunichanganya mama Sonia.” Mara mlango ukafunguliwa, daktari aliingia na mafaili ya mama Briana. 

Alimbidi kuongea na mama Sonia juu ya mgonjwa wao kwani Sam na Sonia walishaondoka. Manesi waliingia na kumuwekea dripu ambayo waliambiwa itawekewa dawa, zitakazo msaidia. Walimuomba mama Briana alale, ili apumzike kabisa. 

 *********************

Sam na Sonia walirudi ofisini. Bosi wake Sonia alisikitika sana kuondoka kwa Sonia. “Hongera sana Samweli, umepata mwanamke mtulivu sana. Wote tulikuwa tukijiuliza juu ya Sonia, hakuna aliyekuwa anapata jibu! Nilikuwa napokea pesa hapa kutoka kwa wale wateja wakubwa sana, wote wakitaka nimfikishie Sonia. Lakini Sonia alikuwa akikataa kabisa, kila nilipokuwa nikijaribu kumsoma nakujua tatizo liko wapi!”

“Kwa nini hataki wanaume hata waliosema wapo tayari kumuoa, wakati ni binti mzuri, mwenye sifa zote za kuwa mke wa mtu, nilishindwa kupata jibu. Walikuwa wakipishana hapa wakubwa kwa wadogo, bila mafanikio. Kumbe Mzee ndio umeshika mpini!” Sam na Mwansasu walikuwa wakiongea na Bosi wake Sonia ofisini kwake wakati Sonia akiendelea kukusanya vitu vyake kwenye ofisi yao. 

Sam alifurahi sana kusikia hivyo, wote walikuwa wakicheka. “Asante sana Mkuu. Inatia sana moyo kusikia ripoti nzuri kama hizo, hasa kutoka kwa watu kama nyinyi.” “Lakini umenichukulia mtu muhimu sana hapa tawini kwangu, naombeni mfanye haraka kuniongezea mtu mwingine. Najua ni ngumu kuja kuziba pengo la Sonia, lakini tafadhali sana Mkuu, niletee mtu anayeendana kidogo. Maana ukweli Sonia ni mchapa kazi na mwaminifu sana. Sikuwahi kupata naye matatizo hata siku moja tokea aanze kazi hapa.” 

“Nitajitahidi kufanya hivyo. Kabla ya mwisho wa mwenzi huu, nitakuletea mtu mwingine.” Mr. Mwansasu ambaye ndiye afisa mwajiri wake alimpa ahadi ya kumtuliza. 

Sonia alimaliza kukabidhi kila kitu, Sam akachukua gari mojawapo ya kazini, kati ya yale waliyokuwa wamekuja nayo kutoka Dar, nakurudi hospitalini. 

 *********************

Walimkuta mama Briana amelala, mama Sonia aliwaeleza ripoti ya daktari. “Amesema, hana tatizo kubwa. Mkojo tu ndio mchafu {UTI}. Amewekewa dawa hapo. Amesema hata kesho wanaweza kumruhusu na kupewa dawa nyingine atakazo tumia nyumbani.” “Afadhali.” Sam aliitikia, nakuongeza. 

“Nataka kesho tuondoke mama.” “Wapi tena?!” “Nashugulikia uhamisho wa Sonia kikazi, ili Sonia arudi kwake mama. Amekimbia nyumbani kwake anakuja kulala huku kwenye makochi! Najua tunakuzungusha kweli mama yangu. Lakini naomba utuvumilie, hii ndio safari ya mwisho. Tunarudi nyumbani kwetu.” Mama Sonia alifurahi sana kusikia hivyo, alicheka kidogo. 

“Hapana Sam, sio usumbufu hata kidogo. Si tunaondoka na mama Briana?” “Wote tunaondoka. Niliongea na daktari, apumzike leo wamuangalie hali yake, kesho asubuhi tutakuja kumchukua, turudi Dar.” Mama Sonia alifurahi sana. 

“Asante sana Sam. Mungu akubariki.” “Wewe zaidi mama. Maana tunakuhangaisha kweli! Najiona ni kama tumekutoa Mwanza na kukuingiza kwenye matatizo.” “Ukisema hivyo unakufuru Sam! Umesahau ulipotutoa mimi, Sonia na Kana? Haya ni mapito tu ya maisha, naamini yatakwisha tu.”

“Lakini lazima ujue Sam sisi ndio tumenufaika sana na nyinyi kuliko haya tuliyofanya sisi. Bila wewe, si Sonia wala mimi tungekuwa na uwezo wakusaidia. Asante kwa kila kitu. Kila kitu. Kuanzia Mwanza, kumsaidia Sonia, mpaka hii leo bado upo na sisi! Mungu akubariki sana.” “Nashukuru mama.” Walijaribu kumuamsha mama Briana ili wamuage lakini alionekana amechoka sana, wakaamua kuondoka. 

 *********************

Waliwafuata watoto saluni kwa mama Sonia, wakarudi nyumbani kwa Sonia. Sam aliwaita watoto wote na kuanza kuongea nao. “Kesho tunarudi Dar.” “Na mama Briana?” Briana aliuliza kwa wasiwasi sana. “Ndiyo, tunaondoka naye.” Briana alifurahi sana kusikia wanaondoka na mama yao. Alisimama na kumkumbatia Sam. 

“Asante sana anko.” “Unajua Briana wewe ni mtoto mzuri sana?” Briana alicheka. “Nimefurahi umekuwa mvumilivu kipindi chote hiki kigumu hujamsumbua Sonia wala Mama Sonia! Pole sana.” “Asante anko. Nimefurahi umekuja kutufuata.” Sam alizidi kuumia kila alipomuangalia Briana. 

Alikuwa akimfikiria Nyange akija kujua maishi waliyoishi wanae, alijua itamuumiza sana. “Inabidi muwahi kulala, kesho tunasafari ndefu. Tutaondoka asubuhi sana kabla hapajapambazuka vizuri.” 

Sonia alibaki anababaika, Sam akajua. Akamuita kwa mkono, Sonia akasogea pembeni yake. “Vipi?” “Ulisema na leo tutalala wote?” Sonia alimnong’oneza sikio. Sam akacheka. “Sio leo tu Sonia. Mpaka kifo kitakapo tutenganisha.” Sonia akafurahi sana. 

“Sasa hapa nibebe nini niache nini?” Akauliza akiangalia nyumba yake. “Naomba mchukue nguo tu. Hatuta hitaji kitu hata kimoja hapa.” Sonia akamuita Asifiwe na kumkabidhi kila kitu chake. 

“Tunakushukuru sana kwa kutusaidia kuomba.” “Hatutakusahau Asifiwe.” Mama Sonia aliongeza kwa binti yake. “Zaidi msimsahau Mungu. Msiache kuwa karibu na Mungu, shetani halali wala hachoki kujaribu watu. Ila mkidumu katika uwepo wa Mungu, hamuwezi kuangamia tena.” Baada ya mazungumzo mafupi Asifiwe akaondoka nakuahidi kurudi kesho yake kuchukua vitu vyote mara baada ya wao kuondoka. Sam alihakikisha kila kitu kinachohitajika kipo kwenye mabegi ndipo alipotulia. 

 *********************

Sam aliomba kuongea na Mama yake Sonia. Wakatoka nje, Sam alikuwa na wasiwasi kidogo, lakini akajikaza kiume. “Samahani mama kwa usumbufu.” “Bila shida.” “Naomba niondoke na Sonia, tutarudi asubuhi kuja kuwachukua.” Mama Sonia alifikiri kidogo. “Sawa. Lakini kabla ya yote, kuna jambo nataka nikushukuru kwa kipekee Sam.” Kidogo Sam alibabaika kwani, Mama Sonia alishatoa shukurani zake zaidi ya mara moja. 

Mama Sonia alitulia kidogo kama anayefikiria. “Sonia alipopata huyu mtoto, sio yeye tu alikuwa na wasiwasi wakuja kupata mwanaume atakaye mpenda na kumuheshimu kwa dhati kama wewe, hata mimi nilikuwa na wasiwasi sana.”

“Kitendo cha kumpokea Kana na kumtunza tokea tuko Mwanza, tena kama mtoto wako! Ona mpaka leo hii jinsi unavyo mthamini Sonia na mwanae, na kuamua kuwapokea na kukubali kutuweka pamoja! Sio kitu kidogo kwangu mimi kama mzazi wao wa pekee.”

“Huwezi jua ni kiasi gani binafsi nilivyokuwa nikitamani na kuhangaika kuja kuwaweka hawa wawili pamoja tena wakiwa na furaha, lakini nilishindwa kabisa mpaka ulipokuja wewe kunisaidia.”

“Ni kweli tumeishi hapa Dodoma pamoja, siwezi sema kwa shida sana, lakini Sonia hakuwa na furaha kabisa kwa ajili ya wewe kukosekana kwenye maisha yake. Alikuwa akisononeka sana kukukosa.”

“Haya, angalia haya mazingira tunayoishi na watoto wa watu! Tumeishi kwa kujibana sana, tukiwa hatujui mwisho wake ni nini! Tulishindwa kuhamia kwenye nyumba kubwa sababu ya kubana pesa ili angalau hawa watoto waweze kula chakula angalau kinachofanana na kwao.”

“Sasa leo wewe kuja na kututoa hapa, ukisema tunarudi nyumbani! Kwangu sio kitu kidogo Sam, kama ulivyotuokoa Mwanza tukiwa kwenye hali mbaya sana ndio hivyohivyo unafanya sasa. Asante sana Sam. Angalau Sonia anacheka toka moyoni, Kana ana uhakika wakupata malezi ya baba na wote unatupa makazi ya kudumu maishani. Nakushukuru sana Sam. Asante.” Sam alikuwa akisisimkwa mwili mzima. 

Hakutegemea kusikia yote yale kutoka kwa Mama Sonia. “Asante sana mama. Ni kweli nampenda na kumthamini sana Sonia. Hata mimi sikuwa na furaha kabisa alipoondoka. Ndio maana nilishindwa kuoa. Namshukuru Mungu nimempata akiwa bado ananipenda na hajapata mwanaume mwingine.” Mama Sonia akacheka. Walipeana mikono na kuingia ndani. 

Walikuta Sonia alishawalaza watoto wote wakiwa nafuraha yakurudi Dar kesho yake. “Twende ukapumzike na wewe Sonia.” Sam alimgeukia Sonia na Sonia akamgeukia mama yake kutaka kujua kama anaruhusiwa. “Unaniangalia nini sasa?” Mama Sonia akamuuliza kwa kumsuta.

Sonia akaanza kucheka kwa aibu huku akimsogelea mama yake na kumnong’oneza. “Naomba niondoke na Sam.” Lakini mama yake akajibu. “Hapana.” “Mama jamani!” Sam alibaki akiwaangalia huku akicheka. “Nakutania bwana. Nyinyi nendeni tu.” “Asante mama.” Sonia alifurahi sana kuruhusiwa na mama yake mpaka akampa hagi. 

“Muone alivyofurahi! Alikuwa amepooza hapa kama mgonjwa! Sasa hivi meno yote nje.” “Mama jamani! Si nilikuwa na mawazo na mama Briana!” “Na kilichokuwa kikikuliza wakati una tutoroka Dar, ni nini kama sio Sam?” “Wala sio Sam!” Sam aliendelea kucheka. “Pole Sonia.”  “Usimsikilize mama bwana! Wala nilikuwa sijapooza. Ni uchovu wa kazi tu na wakati ule naondoka Dar wala sikulia.” Wote walikuwa wakicheka. “Twende Sam, kabla hajabadili mawazo.” Wawili hao wakaondoka.

*********************

Usiku ule kwa Sam na Sonia, ulikuwa usiku wa aina yake. Ulikuwa usiku uliojaa furaha na mapenzi mazito kati yao. “Sonia wewe ni mzuri sana mpenzi wangu, huchoshi!” Sonia alifurahi sana kusikia Sam anamsifia yeye, na kumwambia anamfurahia kimapenzihasa baada ya mrembo Leah kupita kwenye maisha ya Sam kama mpenzi. 

“Inabidi ulale sasa Sam. Kumbuka kesho wewe ndio dereva.” “Kweli bwana! Nimenogewa.” “Nimefurahi umekuja kutuokoa, Sam. Asante.” “Mimi zaidi Sonia. Kukupata tena, kwangu sio jambo dogo. Picha ile ukiwa uchi ilikuwa ikinitesa sana.” “Sam wewe! Kumbe siku ile ulipokuwa ukiniogesha ulikuwa ukinichungulia!? Halafu ukajidai kama hujaona kitu.” Sam alicheka sana. 

“Nilikuona siku ile ulivyokuwa unahangaika kwa aibu! Mimi mwenyewe nilijikaza kweli, nilijua bila kufanya vile usingeoga siku ile. Wakati ulikuwa umejitupatupa sana jana yake na ulishaanza kunuka.” Sonia alicheka sana kwa aibu. 

“Tabia yako mbaya Sam.” “Nilijua nitakuoa Sonia, ndio maana sikuona shida kukuogesha.” Walisahau kama waliambiana kuwahi kulala. Sam alijikuta anaanza upya kumpapasa huku akimbusu Sonia na kuamsha hisia zao wote. 

Ukweli Wa Kilichokuwa Kikiendelea Bila Kuambizana Kwa Wapenzi Hao Mpaka Kusababisha Kutengana. 

Mawasiliano Ni Msingi Muhimu Sana Kwenye Mahusiano.

“Unajua kwa nini niliacha kukukiss, Sonia?” “Si ulikuwa umenichoka!” “Hapana bwana! Nikuchoke wakati nilikuwa wala sijaanza.” Akamfanya Sonia acheke. “Unajua Sonia, kila nilivyokuwa nikikubusu, ndivyo picha yako yakuwa uchi ilivyokuwa ikinitesa mawazoni. Kwa upande mwingine nilijutia kukuona ukiwa uchi. Niliteseka sana.”

“Nilitamani sana kufanya mapenzi na wewe wakati uleule, lakini unajua mama yako aliniomba, nihakikishe unamaliza kwanza shule kabla sijakugusa.” “Haiwezekani Sam!” “Kweli. Mwanzoni nilikuwa sijamuelewa alikuwa anamaanisha nini, ndio Nyange akanielewesha.” 

“Nyange?!” “Tulimfuata mama yako mimi na Nyange kuulizia taratibu za kulipa mahari. Sasa baada yakuongea na mama yako akakataa mahari ila akatoa maombi yake au tuseme masharti ambayo sikuwa nimeelewa mwanzoni anamaanisha nini, mpaka Nyange aliponielewesha.” Sonia bado alikuwa na mshangao hakujua hata kama alitaka kulipiwa mahari!

“Alikwambia nini!?” “Alisema ‘naomba Sonia amalize shule, bila miingilianomingine.’ Akasema kwa wakati ule akili yako ilikuwa ikiwaza shule tu, lakini kukitokea chochote kile itakusumbua tena kufikiria masomo yako. Nikaitikia haraka sana bila hata kufikiria, 'sawa kabisa mama.' Ndio baadaye Nyange akaniita tena nakuniambia, ‘Ujue mama Sonia ndio amekuomba kiutuuzima hivyo. Anataka usimguse binti yake mpaka amalize shule? Hataki Sonia apate mimba katikati ya masomo.’ Niliogopa sana.”

“Maana na mimi ndio nilikuwa nimekata tiketi mbili za ndege, twende wote Mwanza kipindi kile cha birthday yako.” “Sam wewe? Kwa nini sasa hukuniambia mambo yote hayo?! Maana nilikuomba tutoke wote kwenye birthday yangu ukaniambia una kazi nyingi!” 

“Pale nilikuwa nakuandalia surprise Sonia! Simu nyingi nilizokuwa nikizungumza na G, zaidi unaposhuka wewe kwenye gari na kuniacha nikizungumza naye, ilikuwa ni anisaidie mipango ya hiyo surprise. Sikutaka ujue kabisa ili uje ufurahie tukifika huko. Nilimuomba G atutafutie hoteli nzuri sana ya sisi kwenda kupumzika pamoja.” Sonia alizidi kushangaa.

“Nilipompa hiyo kazi ndio akaanza kufuatilia. Akaja kuniambia kuna sehemu nzuri sana ameipata, itatufaa. Nikawa nimefurahi sana, nikaomba na ruhusa kazini, nikakubaliwa. Sasa siku hiyo nikiwa nimejawa furaha ya hiyo safari, nikawa naongea na G chumbani kwa Josh na Josh alikuwepo, nikawa nimejisahahu kabisa tunataniana na G huku tunacheka.”

“Nikawa namwambia G kila kitu jinsi nilivyokuwa nikikumezea mate kwa muda mrefu sana ndio maana nilitaka tusafiri wote twende tukajifungie Mwanza siku tatu bila kutoka huku G akiendelea kutania na Josh alikuwa akitusikiliza.”

“Sasa kutokana na vile mama alivyoniambia nilipokwenda na Nyange kuomba taratibu za mahari, akasema yeye hataki mahari yoyote anataka nisikuguse mpaka umalize shule, nilipaniki Sonia. Nilijua Josh alimwambia kila kitu mama ndio maana mama akatoa lile sharti.”

“Ikabidi kuanza kukukwepa kumuhakikishia mama na Nyange nimetunza ahadi ya kukusubiri. Kumbe naharibu kwako. Lakini sikuwa na nia mbaya Sonia, hali yangu ilikuwa mbaya mwenzio. Nilizidiwa, nisingeweza kuendelea na ule mtindo wa kukiss tu, halafu basi. Niliona ni kama kujitesa tu.” Sonia alibaki kama amemwagiwa maji ya baridi. 

“Ungeniambia tu Sam, mbona ningeelewa tu!” “Usingeelewa Sonia. Hata wewe mwenyewe ulikuwa umelemewa sana. Nilikuona ulivyokuwa tayari kwa mapenzi.” Sonia alificha uso wake kwa mto huku akicheka na kujitetea. “Hapana bwana! Mimi nilikuwa sina hata wazo la mapenzi.” Sam alicheka sana. 

“Wewe Sonia au mwingine? Ni leo tu hapa, ulikuwa unalia niliacha kukukiss na kukushika!” “We acha tu Sam. Ulivyokuwa unanikumbatia vile na kunibusu, nilikuwa natamani umalize kila kitu.” Sam alicheka sana. “Nilikuwa nakuona, na ndio ulikuwa ukizidi kunitesa mwenzio. Lakini sasa hivi shule imeisha, mama ametupa Baraka zake. Sasa hivi tuna ‘Ndoa Halali’, kwa hiyo RUKSA.” Sonia aliendelea kucheka kwa furaha. 

 *********************

            “Nafurahia kuwa na wewe Sam.” “Bob je?” Sonia alishituka sana ila akajitahidi kujibaraguza. Alishamuona vile alivyoshituka, akaingiwa na wasiwasi. Sam alimjulia Sonia kuliko Sonia alivyodhani. Kwa Sam, Sonia alikuwa kama gazeti lililo wazi. Aliweza kumsoma kwa kumuangalia tu na kujua kuna kitu kingine mbali na anachoongea. 

“Nataka kwenda chooni.” Sonia akanyanyuka, akavuta shuka na kujifunga vizuri, akaelekea chooni. Aliamua kukaa chooni kwa muda ili angalau anaporudi, amkute Sam amelala, lakini alimkuta amekaa vizuri palepale kitandani akimsubiria. 

Akaanza kubabaika tena, alijua uangaliaji ule wa Sam ni wakutaka kuambiwa kila kitu. Kwa kukaa kwa karibu sana na Sam kwa muda mrefu, na yeye alishamjua Sam vizuri sana. Wivu wakupindukia. Alimjua ana wivu naye wa kupitiliza na kipindi kile alimtajia Bob kusudi kama kumrusha tu roho kumuonyesha japokuwa yeye anakosa naye muda, lakini yupo Bob anayemfuata na kwenda naye kula. Alikuwa akimwambia kusudi tu na kuingia chumbani kulala, akimuacha kusudi akiteseka. Sasa siku imefika yakujieleza, ndio anahangaika.

Alikaa pembeni yake, huku akiwaza aanzie wapi. Sam naye alibaki kimya akimtizama.  “Sikufanya naye mapenzi, Sam.” Sonia aliongea kinyonge kama aliyebanwa kwenye kona, lakini bado Sam alikuwa amenyamaza kimya akimsikiliza. Akajua bado Sam anataka maelezo zaidi juu ya Bob. 

Aliogopa kumwambia kama walikuwa wakitoka naye mara kwa mara na kama alishafika mpaka nyumbani kwake. “Sijafanya naye mapenzi.” Sonia alijikuta akirudia maneno yaleyale. “Nimekusikia Sonia.” “Tulikuwa tukiwasiliana naye, na…” Akasita na kubaki kimya. 

“Kesho mimi ndio dereva, Sonia. Nataka kulala.” “Ndio tulikuwa tukiwasiliana tu, wakati mwingine alinifuata kwenda kula.” Sonia alimwangalia Sam machoni kuona ana hali gani. Akakuta amebadilika usoni mpaka akamuogopesha. 

“Ndio baada ya mitihani kwisha alinialika nyumbani kwake, nikaenda. 

Tulipokaa muda kidogo, ndio aliponi…Yaani ali..” Sonia alianza kuhangaika, alisogea mbele kidogo, akarudi kujiegemeza kwenye kitanda kama alivyokaa Sam, mwishowe akarudi kukaa kama alivyokuwa amekaa mwanzoni. Lakini Sam alikuwa ametulia vilevile. 

“Hakuna kitu kibaya alichofanya mwanzoni. Ndio nikamwambia anirudishe chuoni. Nikabadili kabisa namba ya simu, hata kabla yakuja huku. Sijawasiliana naye tena mpaka sasa. Tokea nikimbie nyumbani kwake. Mungu ni shahidi.” Kwa muonekano wa Sam tu, Sonia alijua anatwanga maji kwenye kinu. 

Maelezo yake mwenyewe yalikuwa yakijichanganya sana, hata yeye mwenyewe hakuwa akijua anachoeleza. Alianza kusikia joto. Kile kitendo tu chakutoka na kwenda kula na Bob alijua Sam hakuwa akikifurahia hata kidogo, sasa leo ajue alimkumbatia na kumbusu! Sonia alishaanza kujipepe.

 Tayari hali ya hewa ya pale chumbani, ilishambadilikia kupita kaisi. Aliendelea kuhangaika wakati Sam ametulia kimya akimsubiri atulie aongee yote. 

Akaona hatulii na muda unazidi kwenda. “Sonia?” “Abee!” “Mlifanya nini na Bob ulipokuwa nyumbani kwake? Alikurudisha chuoni au ulitoroka. Na kwa nini? Nini kilitokea ulipokuwa nyumbani kwake?” Ukweli jasho lilishaanza kumtoka Sonia. Alianza kujipepea na shuka alilokuwa amejifunga. 

“Kwanza alinipikia chakula, tukala mezani, halafu tukahamia kukaa kwenye makochi. Ila mwanzoni tulikaa mbalimbali, akasema kuna kitu anataka kuniambia, ndio akahamia kwenye kochi langu. Halafu akani….,” Sonia alisita, kisha akaendelea. 

“Akanikumbatia. Sio kwa nguvu sana kama kunibaka, hapana. Lakini alinikumbatia. Ndio akanibusu hapa.” Sonia alinyanyua mkono wake kuonyesha mdomo wake, Sam aliweza kuona vidole vya Sonia vinavyotetemeka kama amepigwa na shoti ya umeme. 

“Haikuwa muda mrefu Sam na ilikuwa nje ya mdomo tu, lakini nikamsukuma kwa nguvu sana kwa kuwa alikuwa ameshanilalia kwenye kochi.” Sonia alianza kutokwa na machozi. Hofu ilishamkamata tayari. Alikumbuka vile Bob alivyokuwa amemkandamiza, nusura abakwe tena. Akajilaumu kujipeleka kwenye mazingira hatarishi yeye mwenyewe. Ndipo ilipombidi Sonia afunguke ili kujiponya hata kwenye hayo mahusiano na Sam. Alihofia isijekuwa huo ukawa mwisho wa kuo mwanzo ulioanza masaa machache yaliyopita 

“Nilipomsukuma akaanguka pembeni ya kochi, nikasimama kwa haraka. Nilipomuona ananifuata nikakimbia upande wa pili wa kochi, aliruka kwenye lile kochi akiwa amebadilika kama simba. Niliogopa sana, Sam. Na hapakuwepo na mtu yeyote pale ila sisi tu.” Sonia aliendelea kulia. 

Sam akamsogeza karibu na kumkumbatia baada yakumuona hali yake inazidi kuwa mbaya. Alikumbuka ile hali aliyoipata alipokumbuka alipobakwa na baba yake Kana na kuchanganyikiwa mpaka kulazwa, kidogo hofu ikamuingia Sam akihofia asije tibua yaliyolala. 

“Alininyakua na kunibeba mpaka chumbani kwake. Alichana gauni langu lote na kunitupia kitandani kwake, alipokuwa anavua nguo zake, nilikimbia upande wa pili wa kitanda, nikatoka nje, nikakimbia.” Sam alivuta pumzi kwa nguvu sana, nakuzishusha. 

Sonia bado alikuwa akitetemekana. “Pole Sonia. Pole sana.” Sonia hakutegemea kusikia pole kutoka kwa Sam tena huku amemkumbatia! Alijua mwisho wao hapoulikuwa umeshakaribia. Kidogo ikamtuliza. 

“Samahani Sam.” “Hapana Sonia, kosa lilikuwa langu. Najua mimi ndio nilikusukumia kwenye mazingira hatarishi. Nisamehe mpenzi wangu. Nakuahidi kuanzia sasa, nitabadilika. Nitapunguza mambo mengi tutakuwa wote. Hakuna mtu atakaye kusogelea tena.” 

Sam alitamani amkamate Bob nakumpa ngumi kadhaa. ‘Ipo siku tu.’ Sam aliwaza. Aliendelea kubembeleza Sonia, na kwa hofu aliyokuwa nayo Sonia, Sam alijua haitaji tena kumpa onyo. Alijiambia atakuwa amejifunza. “Asante Sam.” “Nakupenda sana Sonia.” Bila kujijua Sam na Sonia walijikuta wakiendelea kufanya mapenzi usiku huo, bila kuchoka. 

Sam alijisikia vizuri sana kuona yeye ndio ameaminiwa na kupewa mapenzi na Sonia. Na ni kweli Sonia alikuwa akitamanisha. Alijaliwa mvuto wa aina yake. Sam aliendelea kumfaidi binti huyo mpaka alipoona Sonia amechoka sana. 

*********************

Waliamka asubuhi Sonia akiwa amechoka sana. Walienda kuwachukua watoto na mama yake Sonia, lakini Sonia libaki amelala kwenye kiti cha mbele cha gari, pembeni ya dereva na mama yake alipoingia kwenye gari hakutaka hata kuuliza kulikoni, alibaki kimya kama hamuoni mwanae. 

Walipo wachukua watoto na mama Sonia, walielekea moja kwa moja hospitalini, Sonia akiwa bado amelala kwenye kiti cha mbele bila hata habari. Briana alibaki amekunja mikono akimsubiria mama yake kwa hamu sana. Sam na mama Sonia walishuka. Ilibidi Sam amwamshe Sonia, ili abaki na watoto kwenye gari. 

“Vipi Briana? Mbona unatetemeka tena?” Kana alianza kumuongelesha Briana kwa sauti ndogo, lakini Sonia alikuwa akiwasikia. “Naogopa.” Briana alinong’ona. “Usiogope. Mimi nipo.” Sonia alicheka kimya kimya. 

Briana akamgusa Brayan aliyekuwa amepakatwa na mama Sonia na kuachwa kwenye kiti akisinzia. “Njoo nikupakate, BB.” “Namtaka Mama.” “Anakuja sasa hivi na Mama. Umesikia BB? Na Mama Briana anakuja.” Brayan alinyamaza kimya. 

Ikabidi Sonia ashuke, akaenda kiti cha nyuma yake, akamchukua Brayan na kumpakata. “Namtaka mama.” Brayan akarudia kumwambia Sonia wakati amempakata. “Mama Sonia atarudi sasa hivi. Umesikia Brayan?” Akatingisha kichwa kukubali na kujiegemeza vizuri kwa Sonia. 

 Ubaya Unao Mwisho

Baada ya muda, walirudi na mama Briana akiwa ameshikwa na mama Sonia, ili asianguke. Alionekana amedhoofu sana. Briana aliinama nakuanza kulia sana. Walimsaidi kupanda kwenye gari, akajigemeza kwenye mto. Mama Sonia akamchukua Brayan kutoka kwa Sonia na kurudi kukaa naye karibu na mama yake. 

“Njoo baba.” Mama Briana alimuita Brayan kipenzi chake. Brayan alimuangalia kwa muda nakujificha kwa mama Sonia. Ukweli mama Briana alibadilika sana. “Naomba unikumbatie Briana.” Briana bado alikuwa akilia huku ameinama. Kana akamgusa na kumnong’oneza kitu, Briana akahama kutoka kiti cha nyuma kabisa alipokuwa amekaa na Kana na kuhamia viti vya katikati alipokuwa amekaa mama yake, Mama Sonia na Brayan. Akamsogelea mama yake nakumlalia kifuani huku amemkumbatia. Kila mtu alikuwa akilia kimyakimya kwenye hilo gari. “Mama!” Briana aliendelea kulia huku akimuita mama yake mpaka alipopitiwa na usingizi kifuani kwa mama yake. 

 Jijini Dar Tena

Walifika Dar mapema sana. Sam aliwapeleka moja kwa moja nyumbani kwake. Mama Briana alikuwa ameandikiwa dawa zakutumia, kwa hiyo hawakuwa na haja yakwenda hospitalini tena. Nyumba ya Sam ilikuwa kubwa, lakini haikuwa kama Jumba la Nyange. Ilikuwa na vyumba vitatu tu ndani na kimoja nje. 

Aliwaita wadogo zake sebuleni ili kuwatambulisha. Alimsogelea Sonia. “Huyu ndio Sonia.” Wote walishituka sana. Mdogo wake wa kiume, Daudi alisimama na kumsogelea Sonia na kumpa mkono. “Karibu sana shemeji.” Sonia na Mama yake walibaki wamepigwa na butwaa. “Asante sana.” 

Mdogo wake wa kike Sam naye alisimama. “Mimi naomba nikukumbatie wifi.” Sonia alikuwa haamini. “Heri umekuja mwenyewe, maana nilikuwa nakaribia kuaga. Kila chakula ninachopika humu ndani hakifanani na ‘cha Sonia’.”

“Kunyoosha nguo zake ndio ameamua hiyo kazi ampe Dobi kabisaa, maana alikuwa anagomba hapa kila siku asubuhi wakati anaenda kazini, anasema kama Sonia alikuwa anaweza, kwa nini mimi nashindwa kunyoosha nguo zake vizuri? Kila siku nguo zake nilizomfulia na kumpigia pasi zina kasoro! Kama hiyo siku sijakosea suruali, basi vyote viwili. Sijawahi patia hata mara moja.” Wakacheka kidogo. 

“Sam wewe!” Sonia alimgeukia Sam huku akifuta machozi ya sintoamini, furaha kuona anatambulika mpaka kwa ndugu zake, wengine wakiendelea kucheka. “Anakuza bwana, usimsikilize.” Sonia akasimama na kumkumbatia mdogo wake Sam, Ruth. 

Wote walionekana wana muheshimu sana Sam. Sonia bado alikuwa haamini mapokezi aliyoyapata nyumbani kwa Sam. Sam alimalizia utambulisho kwa wote waliobaki. Wadogo zake waliwakaribisha vizuri tu kwa heshima na upendo.

“Sasa kwa kuwa mwenye nyumba upo, utatupanga jinsi ya kulala basi. Maana nyumba yenyewe ina vyumba vichache kweli, lakini najua tutatoshea tu.” Sam alimgeukia Sonia. Kidogo Sonia alianza kubabaika. Hakuwahi kupata majukumu mazito na ya heshima ya kiasi hicho na hakuwa amejiandaa kabisa. 

Wote walimgeukia Sonia, kumsikiliza. “Labda kwanza nikaangalie vyumba vyenyewe.” “Twende nikuzungushe wifi.” Sonia alianza kujisikia vizuri moyoni. Kutoka kwenye chumba cha kupanga uswahilini mpaka kukabidhiwa nyumba na Sam! Tena mbele za watu! Kwake hakikuwa kitu kidogo. Alipoviona vyumba, alirudi kwa Sam. “Inabidi kesho kununua vitanda vingine Sam. Vitanda havitoshi.” Alimsogelea Sam nakuongea kwa sauti ya chini. Sam alibaki akiwaza kidogo. 

“Ila mama Briana angeenda kupumzika wakati tunaandaa chakula.” Sonia alitoa wazo, Ruth wifi yake Sonia akaanza kucheka. “Mbona unacheka, Ruth?” Sam akauliza. “Afadhali leo tule chakula chako wifi.” Wote walicheka mpaka Daudi. 

“Hakuna mgeni siku ya kwanza jamani!?” “Hapana wifi, utatusamehe kwenye kupika. Maana kwenye mapishi ndio shida kabisaa. Kila siku kaka analalamikia mapishi yetu mabaya. Mpaka Daudi amejaribu kupika humu ndani, akashindwa. Tena heri mimi chakula changu huwa kinaliwa mara moja moja, cha Daudi akiweka kijiko kimoja tu mdomoni, kaka harudii tena. Analalaga na njaa mwenzako huyo. Chai ndio hanywagi kabisa humu ndani, anasema haiivi.” Wote walikuwa wakicheka sana. 

“Hamna bwana, wakati mwingine mlikuwa mnajitahidi.” Waliendelea kutaniana kidogo, wakati akili za Sonia zikiendelea kufikiria watakavyo lala. 

Mwishowe Sonia alitoa mapendekezo yake. “Eti ni sawa Kana akienda kulala na Daudi? Ili Briana alale na Ruth, halafu Mama, mama Briana na Brayan walale chumba kile chenye kitanda kikubwa, mpaka kesho tutakaponunua vitanda vingine?” 

“Wazo zuri sana. Umeona mambo yanavyokwenda vizuri? Nilijua tutatosha tu.” Sam alimpongeza Sonia. Kidogo walianza kumuona Briana akitokwa na machozi. “Vipi Bree?” Sonia aliuliza kwa upole na kumbembeleza. Kama aliyetonesha kidonda Briana alianza kulia zaidi, nakushindwa kuongea. Mama yake alibaki akimwangalia kwa kumuhurumia.

“Njoo kipenzi changu.” Sonia alimuita Briana lakini Kana alishamsogelea karibu kabisa. “Usilie.” Kana alianza kumbembeleza kanakwamba alishajua kinachomliza Briana. 

“Eti Kana? Analia nini?” Sonia aliuliza huku wengine wote wakibaki namshangao. “Atakuwa anaogopa jinsi ya kulala usiku.” Ndio wote wakakumbuka hilo tatizo. Mama Briana akatabasamu nakuinama. Mama Sonia akamgeukia mama Briana nakumnong’oneza. “Tatizo letu lipo vilevile, halijawahi kuisha.” Mama Briana akatingisha kichwa kwa masikitiko. 

“Usingempanga kulala na mtu mwingine.” Kana alimgeukia Sonia na kuongea kwa sauti ya kulaumu na ukali kidogo. “Nilisahau.” “Unasahauje, Sonia?! Ona sasa analia!” Sonia hakujua afanyaje tena. “Kwani vipi wifi?” Ruth akauliza. “Huwa Briana hawezi kulala bila Kana.” Ruth alishangaa kidogo na kuwaangalia tena Kana na Briana. 

Kisha akauliza. “Unamaanisha kitanda kimoja au chumba kimoja?” “Vyote.” Sonia akajibu. “Basi hamna shida, mimi nitawapisha chumbani kwangu nitalala hapo kwenye makochi.” “Kweli Ruth?” “Wala usijali wifi yangu. Mimi mpaka kwenye mkeka naweza kulala.” “Asante sana. Kesho Sam ataenda kuongeza vitanda vingine, utarudi kulala nao tu hapo chumbani kwako.” “Wala usijali wifi.”

Kisha akawageukia Kana na Briana. “Twendeni nikawaonyeshe chumba chenyewe.” “Asante sana.” Kana akashukuru kwa haraka nakufanya kila mtu abaki kimya na kuzidi kumshangaa jinsi alivyokuwa mstari wa mbele kuhakikisha Briana anapata kila anachotaka. 

“Nyamaza Briana, usilie. Tumepata kitanda?” Kana aliinama na kumuongelesha Briana kwa sauti ya chini na ya upendo. Taratibu Briana alianza kufuta machozi. “Twende ukakione kitanda chenyewe.” Kana alisimama huku amemshika mkono Briana, na kuelekea chumbani na kuacha kila mtu akiwashangaa lakini wao hawakuwa hata na wazo la pili. 

 *********************

Ruth alirudi na kumsindikiza Sonia jikoni kupika, harakaharaka alishaivisha chakula nakukiweka mezani. Kwa kuwa mama Briana alikuwa ameinama muda wote, Sonia aliamua amuwekee chakula palepale alipokuwa amekaa kwenye kochi. “Kula dada, chakula kitapoa.” Walimuona machozi yakitoka. 

“Nini dada!?” “Nini kinaendelea? Mbona simuoni Nyange? Kwa nini tupo hapa na sio nyumbani kwetu? Mama Sonia aliniambia niliugua tu nikapelekwa Mirembe, na akasema Nyange yupo Dar.” Ukimya ulitanda wa gafla. 

“Mama Sonia? Nyange yuko wapi?” “Kwa nini usile kwanza, halafu ukapumzika, kesho ndio tukaongea vizuri?” “Siwezi kula kama sijui Nyange alipo! Au amekufa, mnaogopa kuniambia?” “Hapana Mama Briana, hajafa yuko hai!” “Sasa ni nini kinachoendelea? Mbona hamnipeleki nyumbani kwangu?” Kila mtu alinyamaza kimya. 

Ndipo Sam alipoomba aambiwe tu ukweli, kwani ni kweli mama Briana aligomakufanya kila kitu. Ilimbidi mama Sonia awaeleze wote kuanzia mama Eliah na Leah walipofika pale nyumbani kwa mama Briana, mpaka Sonia alipokuja kuwachukua. Na maombi ya uponyaji aliyoyapata mama Briana. 

Mama Briana alijawa na nguvu za ajabu, akasimama na kumgeukia Sam. “Unaweza kunipeleka nyumbani kwangu?” Kila mtu alianza kuogopa. 

“Ungepumzika leo kwanza dada, bado hujapata nguvu.” Sonia aliamua kumshauri. 

“Napumzikaje, wakati umesikia yaliyotokea? Sijui hali ya Nyange ikoje! Sijui kama mzima au la! Sijui kama analishwa au na yeye amekuwa kichaa! Leah HAMPENDI Nyange hata kidogo, anachotaka ni HELA zake tu. Sasa kama ameshapata pesa za Nyange, nataka akanipe mume wangu.” Kila mtu alibaki na mshangao. 

“Sasa dada, kama wamezaa na Nyange na hakukumbuki tena kama wewe ni mke wake?” “Nyinyi si mliniombea nikapona? Kitakacho shindikana kwa Nyange ni nini? Nyange ni mume wangu jamani, hata kama amezaa na Leah ni mume wangu mimi. Niacheni niende mimi mwenyewe nikajionee hukohuko.”

“Kama huyo Nyange atanikataa, ndipo nitajua baada ya hapo, lakini siwezi kukaa hapa, wakati sijui Nyange yuko na hali gani. Wote hamjui kama mimi ndio nimemuingizamume wangu matatizoni, tokea mwanzo kabisa.” Mama Briana akaanza kulia tena. 

“Nyange sio muhuni hata kidogo, mimi mwenyewe ndio nilimsukumia kwa Leah, halafu eti leo nimuache anateseka!? Hapana. Nakuomba unipeleke Sam tafadhali. Kama hutaweza, acheni mimi mwenyewe niende.” “Hapana shem, usiende peke yako. Tutakwenda wote.” Tayari mama Briana alishafika mlangoni. 

“Basi naomba tuombeni kwanza kabla hatujaenda.” Mama Sonia ilimbidi aingilie baada yakuona mama Briana amekusudia kwenda. Mama Briana aliendelea kulia. “Basi shem usilie. Ngoja tuombe kwanza halafu ndio twende.” Walishikana mikono wote, mama Sonia akiwa muombaji mkuu. 

 *********************

Kabla ya kuondoka waliona vema kumpigia simu Mchungaji aliyemuombea Mama Briana. Wakamueleza nia yao yakumfuata Nyange. Aliwatia moyo kwenda kwani aliwaambia Mama Briana ndiye aliyeunganishwa na Nyange, ana haki ya kwenda kumdai mumewe, na hakuna haja yakuogopa tena, kwa kuwa sasa hivi hata mama Briana mwenyewe alishapatanishwa na Mungu, anao ulinzi mkubwa na yeye anawaombea. 

Mama Briana alifurahi sana, ujasiri ndani yake ukaongezeka. Yule Mchungaji akampigia simu Mchungaji mwingine ambaye alikuweko hapohapo jijini Dar, na kuwaunganisha nao. Aliahidi kuja kuwatembelea kesho yake. 

*********************

“Na mimi nataka kwenda Sam.” Sonia alimnong’oneza Sam. “Hatuwezi kuondoka wote hapa, wewe baki uangalie mambo ya hapa nyumbani. Hakikisha watoto wamekula na kulala.” Sonia aliona ni wazo zuri. “Sitalala, nitakuwa nakusubiria Sam.” Sonia alimnong'oneza tena Sam kwa sauti iliyoweza kusikika na kila mtu. 

Sam alijisahau mbele za watu, akamvuta Sonia karibu na kuanza kupata denda/kissing. Kila mtu aliinama na wadogo zake Sam walianza kuondoka mmoja baada ya mwingine, baada yakuona kaka yao amemkumbatia Sonia huku anambusu. Walipomaliza, walikuta kila mtu ameinama na wadogo zake hawapo. Sam alitoka nje kimyakimya Sonia alirudi mezani kuwaangalia watoto wakila bila ya kuongeza neno. 

 Kila Shetani, Na Mbuyu Wake

Walipofika nyumbani   kwa   Nyange, mlinzi waliyemkuta aliwaambia mama mwenye nyumba amekataza mtu yeyote asiingie ndani ya geti. Hakuna aliyeamini jinsi mama Briana alivyoshuka kwenye gari kama simba na kuelekea getini. “Wewe si una risasi? Nipige nayo sasa. Hii ni nyumba yangu HAKUNA wakunizuia nisiingie humu ndani.” Mama Briana aliingia ndani na kumuacha yule mlinzi akishangaa kwa kuwa alikuwa mgeni, tena alionekana ni mlinzi wakawaida tu, sio wakutokea kwenye shirika la ulinzi walilokuwa wakilitumia wao, hakuwa akimfahamu mama Briana. 

Ilimbidi Sam aweke gari pembeni, na kushuka na mama Sonia, kumfuata mama Briana. 

Mama Briana alifika kwenye mlango mkubwa wakuingilia ndani, akagonga kengele. Leah alitoka baada ya muda kidogo. Nusura aanguke baada yakumuona mama Briana. 

Bila salamu, Leah alianza kuropoka. “Hii nyumba ni yangu na hati pia ninayo kwa jina langu.” “Hicho sio kilichonileta leo. Kilichonileta ni Nyange, lakini ujiandae kutafuta pakuishi, maana hata iweje hutakaa kwenye hii nyumba, kwanza ni ya Briana na ndipo alipozikwa Junior. Kwa hiyo ujiandae, nikija kurudi hapa siku nyingine nisikukute.” Leah alitulia kidogo.

“Umenisikia wewe?” Mama Briana alikuwa akihema kwa hasira. “Nyange yuko wapi?” “Naomba muondoke nyumbani kwangu lasivyo nawaitia polisi.” Leah aliongea kwa jeuri sana kama kawaida yake, akiwa bado amesimama mlangoni. 

Mama Briana alimsukumia ndani mpaka akaanguka chini, ili ampishe mlangoni. Alianza kumuita mumewe kwa nguvu sana. Huku akimtafuta Nyange kila mahali. Alipandisha ngazi akikimbia kama anawahi kuokoa kitu.

“Shem?” Sam aliamua kumsimamisha mama Briana aliyekuwa akikimbia kuzunguka kila chumba. “Labda hayupo. Twende tu.” “Hapana Sam, siwezi kuondoka hapa bila Nyange. Nilipokuwa kwenye gari nimelala wakati tunarudi huku Dar leo, nilimuota Nyange ananiita. Yupo kwenye shida sana.” Mama Briana alianza kutokwa na machozi.

Akamsogelea Leah na kumrukia tena kama simba, wote walianguka sakafuni, huku mama Briana akiwa amemkalia Leah. Hakuna aliyeamini kama ni mama Briana. Alimkaba Leah kwa muda mrefu, kisha akamwachia. “Nyange yuko wapi?” Leah aliogopa sana. Hakuwahi kumuona dada yake akiwa vile. 

Mama Briana alimkandamiza tena sakafuni. “Nitakuua Leah, usiponiambia Nyange alipo.” Mama Sonia aliyekuwa amepigwa na butwaa ilibidi ajaribu kuingilia kwani Leah alishaanza kutapatapa. Nguvu alizokuwa nazo mama Briana alishindwa kumtoa. 

“Unajua mama Briana, ukimuua huyu, tutashindwa kujua Nyange alipo.” Kama kitu kilipita akilini kwa mama Briana, akapata wazo. “Yupo chumbani kwa Josh. Twendeni.” Mama Briana alinyanyuka haraka sana na kumuacha Leah sakafuni akitapatapa, akakimbilia mlango wa nyuma kuelekea nyumba ndogo ya nje aliyokuwa akiishi Josh.  

 *********************

Ilibidi mama Sonia na Sam wafuate nyuma, walitokea mlango wa jikoni kukifuata chumba hicho. Walipofungua mlango wa chumba hicho, Sam alirudi nyuma. Kulikuwa na harafu kali sana kama kitu kilichooza. Bila kusita mama Briana aliingia, akawasha taa. 

Walimuona Nyange amelala kitandani akiwa hoi, anaita kwa sauti ya chini sana, “Penninah! Penninah!” Alikuwa ni kama mtu anayekata roho. Nyange alikuwa amedhoofu sana, alibaki mifupa mitupu. Alijawa kinyesi na mikojo vilivyo msababishia kuungua vibaya sana. Alijawa madonda mengi hasa kwenye makalio na upande aliokuwa amelalia. 

Chini ya kitanda alichokuwa amelalia walikuta sahani nyingi zilizokuwa zimejaa vyakula, na vyenyewe pia vilionekana ni vya muda mrefu na vimeoza, na pia vilionekana Nyange hakuvigusa hata kidogo. 

“Leah ana roho mbaya huyu msichana jamani! Yaani alikuwa akimtupia chakula hapa kama mbwa?” Mama Sonia alikuwa akiongea kwa sauti ya chini huku akikusanya zile sahani ili wapate sehemu ya kupita kumfikia Nyange hapo kitantani. 

Bila kupoteza muda, mama Briana alipanda kwenye hicho kitanda na kumgeuza mumewe bila yakusema kitu. Alianza kumtoa nguo harakaharaka. Sam alipoona vile, aliamua kusogea na yeye. “Unataka kufanya nini shem?” “Nimsafishe, tumpeleke hospitali.” “Basi nikusaidie tumpeleke bafuni.” Mama Sonia na Sam walimbeba Nyange mpaka bafuni. 

Mama Briana alikimbia ndani mpaka chumbani kwake na Nyange, akachukua nguo baadhi za Nyange na kurudi haraka sana na taulo safi mkononi. 

Kwa kuwa alikuwa na madonda karibu mwili mzima, mama Briana alianza kumkausha maji taratibu sana kila mahali. Ni kweli Nyange alionekana alikuwa kwenye mateso makali sana.  

“Nikusaidie shem?” “Asante Sam. Naomba tumvalishe nguo harakaharaka, lakini kwa makini. Madonda hayo yanaonekana yana muuma sana, halafu tumfunike shuka. Anatetemeka sana, itakuwa anahisi baridi. Naona wa moto sana. Homa itakuwa ipo juu.” 

“Pole Shem. Ngoja nikusaidie.” Bila ya kusema kitu mama Briana alitoka tena akiwa ana kimbia bila kuaga, wakati Sam akimvalisha Nyange. Alitoka nje kabisa, akafungua geti yeye mwenyewe bila hata kuongea na mlinzi kitu chochote, akaingiza gari ndani, karibu kabisa na nyumba ndogo alipokuwepo Nyange. 

“Nimesogeza gari. Naomba tuwahi hospitalini.” Kila mtu alikuwa akishangaa nguvu na ujasiri wa Mama Briana aliyekuwa amezoea kulia kwa kila jambo. Alikuwa jasiri kama sio yeye. 

Hakuna aliyekuwa na hamu ya kurudi tena nyumba kubwa alipokuwepo Leah. Mama Briana alikaa nyuma akiwa amemshikilia Nyange. “Pole sana D. Utapona mume wangu. Pole.” Mama Briana alisikika akimwambia mumewe kwa sauti ya chini iliyotulia wala si paniki. Mama Sonia alikaa mbele na Sam akiwa dereva. 

Nyange aliendelea kuita Penninah kwa sauti ya chini sana bila kunyamaza, huku akitetemeka sana baridi. Kwa kuwa mama Briana hakutaka kumtia gharama zaidi Sam, alimwambia Sam wampeleke mumewe hospitali ya serikali tu, huku roho ikimuuma sana. Walifika mapokezi, Nyange akapelekwa wodini. Walipoona sehemu aliyolazwa ndipo waliporudi nyumbani na ilishakuwa usiku sana. 

 *********************

Walifika nyumbani kwa Sam, ama Briana akiwa amekaa kwenye gari ameinama chini, nyuma ya kiti cha dereva. Sam alizima gari na kumgeukia mama Briana. “Pole sana shem.” “Asante, lakini najua Nyange atapona. Unafikiri Sam? Nyange atapona tu.” “Atapona shem.” “Ninauhakika Sam. Nyange atapona.” Mama Briana alikuwa akirudia mara kwa mara. 

“Najua Nyange atapona. Mungu yupo.” Kweli hali ya Nyange ilikuwa ikikatisha sana tamaa, lakini sio kwa mama Briana. “Tushuke ukapumzike Shem, ili kesho tuwahi hospitalini.” Mama Sonia ambaye alikuwa na yeye amekaa kimya kabisa kiti cha mbele alishuka na kumfungulia mlango mama Briana na kumshika mkono. “Twende ndani.” 

Walimkuta Sonia kwenye makochi akiwasubiria. Walimueleza kila kitu, Sonia alibaki akilia. “Huna haja yakulia Sonia. Nyange atapona tu. Inaweza kuchukua muda mrefu, lakini najua mume wangu atapona.” Sam alikuwa akinuka sana, aliingia chumbani kwake moja kwa moja, kwenda kuoga. 

Sonia aliingia na mama Briana na mama yake chumbani kwao. “Inabidi dada na wewe uoge, ule, ili unywe dawa. Watoto na baba Briana wote wanakuhitaji sana sasa hivi, huwezi kurudi kudhoofu tena.” Sonia ilimbidi kuzungumza baye kwani alikuwa amekaa chini kabisa pembeni yakitanda ameshika shavu. 

“Ni kweli Sonia.” Alinyanyuka na kuingia bafuni, alipooga akala vizuri sana, akanywa dawa zake na kurudi kukaa kitandani akiwa na mawazo. “Inabidi ulale sasa. Unahitaji kupumzika.” Sonia aliongeza.

*********************

“Sasa wewe mwenzetu, unalala wapi? Maana pale sikukusikia ukisema unapolala!” Mama Sonia alimgeukia binti yake. Sonia alianza kubabaika. Mara alisikia mlango ukigongwa. “Sonia?” Sam aliita. “Nitarudi mama.” “Naurudi kweli! Umesikia Sonia?” Sonia alianza kucheka. “Mama jamani, nini?” “Nini gani?” “Nakuomba mama yangu.” Sonia alianza kumbembeleza mama yake kwa sauti iliyojaa aibu na tabasamu. “Usinichekee Sonia.” “Unajua Sam ananiita? Halafu hajala. Kwanza wewe mwenyewe ulishatubariki mimi na Sam.” Kisha akafungua mlango nakukimbia. 

“Njaa inauma kweli!” Sam alikuwa amekaa kwenye kochi. “Pole. Njoo basi ule.” Sonia alikaa na Sam, lakini alimuona Sam jinsi alivyojawa na mawazo. “Pole Sam.” “Daah! Siamini Sonia. Hivi mwanadamu anawezaje kuwa mkatili kwa kiasi hicho?!”

“Tumemkuta Nyange katika hali mbaya sana. Hata mnyama hawezi kufanyiwa hivyo! Sidhani kama Nyange ataishi na hata akiishi sidhani kama atarudi kuwa mtu wa kawaida. Ana hali mbaya sana.” “Atapona tu. Unakumbuka hali tuliyomkuta nayo Mama Bree?” “Huwezi kumlinganisha na Nyange hata kidogo! Nyange ameoza Sonia! Upande mmoja wa kulia umelika kabisa, mpaka unaona ndani karibu na mifupa!”

“Hana ufahamu kabisaa. Homa ni kali. Amebakia akimuita mkewe kwa sauti ya chini sana, mpaka anatia huruma! Sijui Leah alimfungia mle ndani kwa muda gani! Matako yote yameungua kwa kinyesi na mkojo! Mwili wake ni madonda matupu. Hafai!” 

“Kula basi na wewe.” “Chakula hakiendi kabisa, twende tu tukalale.” “Namuogopamama mwenzio! Wewe nenda tu kalale. Tutaonana kesho.” “Wee! Haiwezekani hata kidogo. Nilikwambia mpaka kifo kitutenganishe Sonia. Twende tukalale wote. Atakufuata hukohuko chumbani kwetu. Wewe ni mke wangu Sonia, na tuna ‘ndoa halali’. Acha kuogopa.” Sonia alianza kucheka kwa sauti ya chinichini. 

“Basi tuondoke kimyakimya asije niita.” Sonia alikimbilia chumbani kwa Sam, na Sam akamfuata nyuma. 

 *********************

Gafla akaona Sam amechangamka. “Wewe si umesema una mawazo?” Alimvuta Sonia huku akicheka. “Nimefurahi umerudi nyumbani Sonia. Karibu sana.” “Asante Sam. Nimejisikia vizuri sana kwa kuniheshimu mbele za wadogo zako.” “Sio wao tu. Mpaka nyumbani wanakujua. Hivi nasubiri pakitulia tu, nikupeleke kijijini kwetu ukawaone wazazi.” Sonia akafikiria kidogo. 

 Akamwangalia na kumuuliza. “Sasa ungenikuta nimeolewa?” “Sijui ningefanyaje Sonia! Lakini nilikuwa naomba Mungu kila siku nikupate ukiwa hujapata mwanaume mwingine.” “Nakupenda sana Sam siwezi kuwa na mwanaume mwingine.” “Asante Sonia.” Sam alimkumbatia vizuri.

 “Nikuombe kitu Sonia?” “Unataka nini Sam?” “Naomba umuige mama Briana. Kuanzia upendo, ukarimu wake, yaani kila kitu.  Najua umekaa naye unamfahamu vizuri. Ukiwa kama yule mwanamke, maisha yetu yatakuwa mazuri sana.” Sam alifikiria kidogo. 

“Daah! Nimemnyanyulia mikono mama Briana! Ungemuona anavyomuhudumia mumewe!” “Mungu atatusaidia Sam, tusipitie walipopita wao. Kweli inatisha.” Sam na Sonia walilala wakiwa wamekumbatiana. 

Pale Wema Unapooza Kwa Wanadamu Wengine

Mama Briana aliamka asubuhi nakuomba apelekwe hospitalini. Sam alimpeleka na Sonia akatoka kwenda kutafuta shule za watoto. Mama Briana alisikitika sana kukuta mumewe bado hajahudumiwa. Walikuta homa ipo juu vilevile, na hakuwa amepewa dawa yoyote tokea walivyomuacha hospitalini hapo, wakidai kumsubiria daktari amuone kwanza. 

Alitoka hapo na Sam akiomba apelekwe sehemu bila ya kumwambia Sam waendako. Mama Briana aliamua kwenda kwanza kwa rafiki yao wa karibu sana, Mr Chao kuomba msaada wa fedha ili ampeleke mumewe hospitali ya kulipia, lakini alimnyima kabisa. 

Aliamua kuzunguka kwa baadhi ya marafiki zao wengine hasa wale aliojua walikuwa wakidaiwa na mumewe, lakini WOTE WALIMKATALIA kabisa.  

 *********************

Mwishowe alirudi kwenye gari alipokuwa amemuacha Sam, akaanza kulia kwa uchungu sana. “Kwani ni nini kinaendelea shem? Mbona unazunguka kwenye maofisi mwenyewe hutaki twende wote?” Mama Briana alikuwa akimuomba Sam amsubiri kwenye gari, hakutaka kabisa Sam ajue kwamba anazunguka kukopa pesa.  

“Eti Shem?” “Hawa watu wote nilioenda kwao, nilitaka msaada wa pesa. Na wote wamenikatalia wakati wote hawa ndio walikuwa hawakauki nyumbani kwetu na ofisini kwa Nyange kukopa hela. Mmoja ananiambia niachane na Nyange, kwa kuwa yeye alinisaliti na kuishi na mdogo wangu. Sikutaka hata kupoteza muda nikaondoka.”

“Huwezi amini Sam, Mr.Chao alifilisika kabisa, mpaka benki ilitaka kumpokonya ile nyumba wanayoishi sasa. Nyange akaniomba tuwakopeshe pesa yeye na mkewe. Tukawasaidia kukomboa ile nyumba na kuwapa pesa ya kufufua biashara yao. Leo namuomba pesa ya kumpeleka 

Nyange hospitalini, ananinyima bila hata aibu!” Mama Briana aliendelea kulia kwa uchungu sana. 

“Pole sana Shem.” “Sifurahii pale alipo Nyange. Hawamuhudumii vizuri na hali yake kama unavyoiona. Nyange anahitajika matibabu ya karibu na ya haraka.” “Sasa kwa nini hukuniambia shem?” “Utatusaidia mangapi Sam? Watoto wangu wote wako kwako, tunakutegemea kwa kila kitu! Sikutaka tukuongezee mzigo.” Sam aliumia sana. Alijua moyo wa mama Briana na mumewe wakusaidia watu. 

Palepale bila yakumsemesha kitu kingine mama Briana aligeuza gari mpaka alipolazwa Nyange, aliongea na wauguzi kuomba kumuhamisha Nyange. Akampeleka hospitali ya kulipia, ndipo Nyange alipoanzishiwa vipimo na matibabu ya haraka. 

 *********************

 Nyange alikaa hospitalini hapo na mkewe mchana na usiku kwa majuma mawili mfululizo akimuita mkewe tu bila ufahamu wowote kumjia. Hakuna muda mama Briana aliacha kumuombea mumewe, na hakuwahi kuondoka pembeni ya kitanda chake akimuhudumia mchana na usiku kwenye chumba hicho alichokuwa amelazwa peke yake. 

Sam alikuwa akilipia pesa nyingi sana kwa matibabu ya Nyange na kweli alipata matibabu mazuri. Baada ya majuma matatu homa ilikwisha kabisa na madonda yalikauka. 

Japokuwa uzima ulirudi usoni kwa Nyange lakini hakuwa akimtambua mtu yeyote,wala akiongea chochote zaidi ya kuita jina la mama Briana kila wakati. 

*********************

Siku anarudishwa nyumbani, Briana alilia sana. Moja kwa moja alimuuliza Kana huku akilia, “Kwani anti Leah amemfanya nini dady wangu?” Briana alionyesha kuumia sana. Kana alimshika. “Usilie Briana. Dady atapona.” “Unamuona alivyochoka? Hawezi hata kutembea mpaka anko Sam amshike! Halafu hanitambui tena, wala haniiti mimi!” “Kwa kuwa anaumwa. Akipona atakutambua.” 

Kila mtu alikuwa kimya kabisa akimshangaa Nyange. Mama Sonia alimpigia simu Mchungaji aliyekuwa ametambulishwa wa hapohapo jijini nakumuomba afike wasaidiane kumuombea Nyange. Aliahidi kufika siku inayofuata nyumbani kwa Sam. 

Kwa Mungu Wa Yasiyowezekana Kwa Watu

Kweli siku inayofuata Mchungaji alifika nyumbani hapo na timu nzima ya waombaji na kuanza kumuombea Nyange. Wakati wakimuombea Nyange, na yeye alianza kulipukamapepo. Alikuwa amefungwa sana na nguvu za giza. 

Baada ya muda mrefu wa maombi, hatimaye Nyange alifunguliwa na kuacha nyumba nzima ikishangaa. Sam alihisi ni mazingaombwe. 

“Mama Briana?” Ndio kitu cha kwanza alichokitamka Nyange baada ya kuzinduka pale sakafuni. Mama Briana alikuwa akilia sana. “Njoo basi.” Nyange alijaribu kusimama ili amsogelee mkewe lakini alishindwa. Bado alikuwa amedhoofu sana. 

Sam alimsogelea na kumnyanyua hapo sakafuni nakumuweka kwenye kochi. “Pole sana kaka?” “Kuna nini Sam!?” Nyange alianza kushangaa watu waliokuwa wamemzunguka na mazingira mageni machoni kwake. 

“Nipo wapi hapa?” Naye ilibidi aelezewe kila kitu kilichokuwa kimempata. Nyange alilia sana kama mtoto, mwishowe aliomba aelezewe kila kitu juu ya Mungu. Akaomba na yeye aongozwe sala ya toba. Kwa mara ya kwanza Nyange akaokoka. 

Nyange alibaki ameshika kichwa. “Kipenzi changu kipo wapi jamani? Briana!” Nyange alianza kuangaza macho tena kumtafuta Briana. Briana alifurahi sana kusikia jina lake likitajwa na baba yake. Alienda kumkumbatia kwa muda mrefu sana huku akilia. “Dady!” Briana alizidi kulia. Nyange naye alianza kulia tena kama mtoto. 

“Nawashukuru sana kwa kunitunzia watoto wangu jamani! Asanteni sana.” Nyange aliendelea kulia. “Daah! Sam! Mama Sonia, Sonia…. Asanteni jamani!” “Wala usijali kaka. Unakumbuka ulisema sisi ni ndugu? Akiumia mmoja, wote tunaumia? Tuko pamoja kaka.” “Daah! Siku nasema hayo maneno, sikujua kama mimi naweza kuwa kwenye upande wa kuumizwa kabisa! Nilijua nitabaki upande wa pili wakusaidia tu.” 

Nyange aliomba mama Sonia amsogelee ampe mkono. “Nakushukuru sana, tena sana. Sonia! Asante mama, asante sana. Kweli nyinyi watu mnaupendo wa kweli na Mungu aliwaleta kwenye maisha yetu kwa makusudi. Asanteni sana jamani.”

“Sam mdogo wangu! Asante kwa kunitunzia familia. Asante sana. Nakushukuru Mungu wangu kunirudishia Penninah wangu jamani! Asante Mungu wangu. Sijui itakuwaje, lakini ninachojua sasa hivi, Mungu atatusaidia tu.” Wale watu wakanisani wakapiga makofi. “Sasa hapo muheshimiwa, umeongea kabisa. Mungu akiwa upande wenu, hakuna litakalo washinda.” 

 *********************

Hakuna siku iliyopita bila Nyange kuomba watu wote waombe kwa pamoja ndipo walale. Alimkumbuka Mungu wa baba yake Mzee Nyange na kuanza kufuatilia mambo ya Mungu kwa karibu sana. Sio kwamba Nyange hakuwa akijua mambo ya Mungu, ila ni mtoto aliyekuwa muasi. Baba yake alipojikuta ndiye mtoto wa kiume pekee, alijitahidi sana kumkuza katika maadili ya Mungu. 

Tokea ni mtoto alikuwa akipelekwa kanisani, na baba yake alijitahidi sana kumsisitiza kusoma sana ili aje kuwa mkombozi wao. Japokuwa baba yake alikuwa fukara sana pale kijijini kwao, baba Briana alimuona jinsi alivyojitoa kwa Mungu na kumsomesha kwa shida sana. 

Lakini alipofika kidato cha pili Nyange akiwa amefaulu shule ya bweni ya wanaume, alijiingiza kwenye makundi mabaya sana, yaliyobadili moyo wake kabisa na kuwa mtoto asiyesikia la mtu yeyote na ndipo alipofeli kidato cha nne. 

Hata hivyo baba yake hakumkatia tamaa, alimpeleka chuoni kusomea mambo ya Stoo mwaka mmoja, na ndipo alipojitupia jijini Dar na kusahau kabisa kama ana wazazi mpaka alipompata mama Briana, ndiye aliyerudisha mahusiano ya Nyange na wazazi wake. 

Nyange hakuwahi kuona umuhimu wa Mungu anayemtaja baba yake hata siku moja, zaidi yakumuita Mkoloni, kwani alimuona jinsi alivyokuwa akifuata kwa makini na kwa uaminifu mambo aliyosema ni sheria za Mungu huku akimuona vile alivyofukara. 

Alishamuuliza kama huyo Mungu yupo kwa nini hamsaidii yeye mwenyewe, amemuacha kuwa fukara kuliko mtu yeyote pale kijijini kwao? Wadogo zake wote Mzee Nyange walioa wake wawili wawili kasoro Mzee Nyange alibakia na mke mmoja tu na kuwa mwaminifu kwa mkewe daima, achilia mbali ibada alizokuwa akimuona baba yake akifanya bila yeye kuona matokeo yake kwa macho. 

Alipokuja mama Briana kwenye familia ya Mzee Nyange, alisema Mungu amemjibu kwa kumletea Mama Briana. Wakati wote alisema Penninah anayo mbegukutoka kwa Mungu. Kwamba Penninah anapanda mbegu sehemu yenye rutuba, ndio maana kila anapokanyaga mama Briana, pana barikiwa sababu ya maombi aliyokuwa akiomba yeye mwenyewe Mzee Nyange. 

Wakati wote wa ufukara wake alikuwa akiwaambia watu kuwa Mungu alishajibuwasubirie waje kuona kwa macho yao, baraka Mungu alizozimimina juu yake na familia yake, kitu alichoshindwa kuelewa baba Briana kabisa na kushindwa kumuamini Mungu na kumuona baba yake amechanganyikiwa tu, kwani ni kweli walibaki kuwa maskini mpaka alipokuja mama Briana na kubadilisha hali ya nyumbani kwao. 

Mzee Nyange akageuka kuwa gumzo pale kijijini kwao. Kwani walihamia kuishi kwenye nyumba nzuri sana kuliko watu wote kijijini kwao na siku zake za mwisho, ndio baba Briana aliwapelekea gari iliyokuwa ikiwazungusha waendako. 

Na ndio maana Mzee Nyange wakati wote alikuwa akimuombea sana mama Briana na uzao wake wote kila kukicha, kwani alikiri yeye ndiye aliyetumwa na Mungu kuinua ukoo wake, lakini pia baba Briana na mkewe hawakuwa hata wakienda kanisani. 

Walibakia wakifurahia mafanikio yao makubwa bila kujua mafanikio hayo ni maombi ya baba mzee Nyange. Na ndio maana hata Leah alishindwa kuwaloga tokea mwanzoni sababu ya ulinzi mkubwa alikua nao baba Briana na nyumba yake. 

 *********************

Kwa kuwa Sam alimjua Nyange haamini mtu yeyote na mtoto wake, alichukua jukumu la yeye mwenyewe kuwa dereva wa Briana. Sam alikuwa akiondoka nao asubuhi sana akiwa anaenda kazini na kuwashusha shuleni na kuwafuata jioni. 

“Asante sana Sam na Sonia kwa kuendelea kumwangalia Briana wangu.” “Nyange wewe! Kwani ni Briana tu?!” Nyange alianza kucheka. “Wewe huoni hiyo kazi ya ziadawaliyonayo Sam na Sonia? Ona mwanangu anavyopendeza, halafu angalia foleni za mjini hapa, lakini Sam anajitahidi asubuhi kuniwahishia mwanangu shuleni ili na yeye awahi kazini? Najua sio kazi ndogo na wala haikuwa lazima. Si wangempandisha tu kwenye basi la shule kuliko kumpeleka?” 

“Nilijua utakufa ukisikia anapanda kwenye basi.” “Afadhali mdogo wangu unanifikiria. Hawa makonda hawaaminiki kabisa bwana. Wanaweza wakaanza kumchezea mwanangu bure. We si unamuona Briana mwenyewe alivyo?” “Mbona Junior anafuatwa na basi husemi?” Mama Briana aliingilia tena. 

“Mtoto wakiume huyo, lazima apambane.” Kila mtu alikuwa akicheka. “Upendeleo huo Nyange!” “Naye akue atafute magari yake bwana! Sio kutwa anataka abebwe. Wakina Nyange hatupo hivyo kabisa Brayan. Sisi ni wapambanaji. Umesikia Brayan? Changamka bwana, acha kudekadeka na kulialia. Wewe mtoto wa kiume, unatafuta, hakuna wakukutafutia.” 

Mapenzi ya Brayan yalisha rudi kwa mama yake. Aliacha kuendelea kumfuata mama Sonia kila mahali, nakuanza kumganda mama yake. Alisha acha kabisa kulala na mama Sonia akaanza kulilia kulala na mama yake

Asubuhi alipokuwa akienda kuchukuliwa chumbani na Sonia ili atayarishwe kwenda shule alikuwa akilia sana, nakutaka kubaki na mama yake. Mwishowe mama Briana aliomba aachwe naye kwa muda mpaka angalau hamu imuishe. 

 *********************

“Hawa nao bado wanafuatana tu hivyohivyo?” Nyange alianza kuwateta Kana na Briana, akiwa na mkewe. “Yaani naona vinazidi, huyo Briana hana anachoelewa hapo bila Kana. Ile kazi yako yakuitwa shuleni imempata Sam na Sonia. Kutwa yupo nyuma ya Kana, akitoka tu darasani kwao nasikia moja kwa moja mpaka mlangoni kwenye darasa la kina Kana kama zamani.”

“Huyo Kana mtoto wa watu nasikia hana hata marafiki, kutwa na huyo mwanao. Uongozi huko shule pia nasikia unamshinda huyo Kana sababu ya huyo mwanao.” “Ushaiona shule yenyewe lakini? Ina hadhi gani?” “Sijaenda D! Mawazo yangu yote yalikuwa kwako. Hata hivyo tushukuru kwa hivyo wanavyosomeshwa D. Sam na Sonia wanajitahidi sana. Kwa majukumu yote haya na bado kutusomeshea watoto kwenye shule za kulipia! Sio jambo dogo.” 

“Ni kweli kabisa! Ngoja nikipata nguvu nitaenda mwenyewe huko shuleni kwao. Angalau nikafahamiane na hao walimu wake Briana, niwaweke sawa. Sitaki wamsumbue mwanangu.” “Hivi Nyange, umenisikia lakini nilichokuwa nikisema? Anayesumbuka sasa hapo ni huyo Briana au Sam na Sonia? Nakwambia kutwa wanaitwa shuleni kwao, wewe unasema anayesumbuka Briana!” Nyange alikuwa akicheka tu. 

“Lakini Penninah, namshukuru sana Mungu.” “Kwa nini?” “Moyo wako huo, ndio Amempa na Briana wangu. Kwa mabaya aliyonisimulia Briana niliyokuwa nikimtendea, na bado kinaniambia ‘nakupenda sana dady wangu.’ Yaani mpaka machozi yalikuwa yakinitoka. Nimetesa sana watoto wangu, bila kujijua Penninah! Namshukuru sana Kana.”

“Briana ananiambia kuna kipindi alinichukia sana, lakini Kana alikuwa anamkumbusha jinsi ninavyompenda na alimwambia, mimi ni mgonjwa. Waendelee kuniombea tu nitapona.” Mama Briana alikuwa akilia. 

“Asante Penninah kwa mapenzi ya kweli. Ingekuwa rahisi kuniacha usinifuate pale uliposikia ninaishi na mpaka nimezaa na Leah.” “Nitamuachia kila kitu, lakini sio wewe D. Nisingekukuta pale siku ile! Nahisi ningemuua.” “Asante sana Penninah, ungechelewa, labda ningekufa.”  Mama Briana alibaki kama anafikiria kitu huku anafuta machozi. 

“Nini?” “Unajua tulipofika pale kukutafuta, nilizunguka nyumba nzima lakini sikumuona mama wala huyo mtoto!” Nyange alikaa kimya. “Vipi D?” “Katika adhabuMungu atakuwa amenipa hapa duniani ni kuwa na mtoto na Leah. Sijui nitafanyaje Penninah! Naogopa hata kuja kumuona tena yule msichana.” “Mungu atatusaidia D, wala huna haja yakufikiria zaidi. Kuna mambo mengine duniani hayana majibu, yanajijibu yenyewe kadiri siku zinavyozidi kwenda.” “Ni kweli.” Walitulia kidogo kila mtu akiwaza lake.

*********************

“Lakini Nyange, hapa tumebanana sana, kwa nini tusimuombe kaka Eliah tuhamie kwake kwa muda, wakati tunajipanga? Tunamlemea sana Sam, wakati ndio na wao wameanza maisha, wala hawaja furahia nyumba yao wenyewe na sisi tumejazana humu!” “Ni kweli, wazo zuri. Lakini inabidi, tusubirie Briana afunge shule.” Nyange alifikiria kidogo. 

“Hivi huyu Sam amemuoa mtoto wa watu? Au anaishi naye tu?” “Wenyewe wanasema wana ‘Ndoa halali’.” “Ndio nini?” “Sijui D. Mimi akili yangu yote ilikuwa kwako. Naona hata hukukosea kumkabidhi Briana kwa Sonia. Watoto pia walinishindatokea nitoke hospitalini sijui chochote juu ya hao watoto. Mama Sonia ndio anahangaika na Brayan na Sonia ndio namuona anahangaika na kila kitu cha Briana. Kuanzia shule mpaka mavani. Kila kitu Sonia ndio anafuatilia.” 

“Daah! Asante kwa kunijali Penninah. Hawa watu ni kweli Mungu alijua yatakayotupata ndio maana akawaleta kwenye maisha yetu. Lakini lazima niongee na Sam. Hawezi kuishi na Sonia bila ndoa takatifu. Hiyo ndoa yao wanayosema, mimi siielewi na wala siikubali hata kidogo.” “Anasema mama yao aliwabariki.” 

“HAPANA. Sam asilete uhuni. Lazima aoe kanisani. Ndoa takatifu ina baraka zake. Watuone sisi jinsi Mungu alivyotutetea kwenye ndoa yetu.” Mama Briana alianza kucheka. 

“Nini sasa?” “Nakuona siku hizi ulivyoshika dini! Unataka kuwa Mchungaji nini?” Baba Briana alicheka. “Nikuasi tu. Mimi nilikuwa nikimjua Mungu tokea zamani. Hekaheka za maisha ndizo zilinifanya nikamsahau Mungu.” 

 Mahusiano Yaliyokwisha Ota Mizizi, Ngumu Kung’oa

Baada ya Briana na Kana kufunga shule mama Briana alimtafuta kaka yake akaja pale nyumbani kwa Sam. Kaka yake alibaki akilia sana baada yakufika nakusimuliwa kila kitu. “Kwani mama yuko wapi, kaka? Sikumkuta pale nyumbani kwetu nilipoenda kumchukua D.” Mama Briana alimuuliza kaka yake. 

“Sijui dada, na wala sitaki kujua. Unajua dada, ulipofiwa na wazazi wa baba Briana nilimpigia simu mama, tena alikuwa na Leah nyumbani. Nikamuomba sana mama asiachekwenda kwenye msiba. Tena nikamwambia ni msiba mkubwa sana kwako kwa kuwa wale ni kama wazazi wako kabisa.”

“Nikamuelezea jinsi nilivyomsindikiza baba mpaka kwa Mzee Nyange na kukukabidhisha kwake rasmi sio kama mkwe bali mtoto kabisa. Nikamrudia tena, ‘Penninah amepoteza watu wa muhimu sana kwenye maisha yake’, nikamuomba asiache kuja. Sitaki kukwambia alichonijibu dada. Nilikata simu na sikuwatafuta tena.” Mama Briana alibaki kimya. 

Nyange aliwaita watu wote pale sebuleni siku hiyo ya jumamosi na kuwashukuru, huku akiwaaga akiwaambia yeye na familia yake wanaenda kuishi na kaka yake mama Briana mpaka watakapo pata nguvu yakuanza kufanya kazi. Ilikuwa ni huzuni sana kati yao. 

Mambo yalianza kubadilika pale mama Briana alipomwambia Briana achukue vitu vyake wanaondoka. “Tufanye haraka Kana, twende.” Watu wote walibaki wamezubaa. “Hapana Briana. Kana anabaki.” Briana hakuwa anaelewa kabisa. “Mnaniacha tena? Mtarudi lini sasa?” “Hapana Briana, tunaenda wote Kana ndiye anayebaki.” 

“Yaani tunaondoka bila Kana?!” “Ndiyo. Kana inabidi abaki.” “Kwa nini hatuwezi kwenda na Kana?” “Kana anabaki na mama yake.” “Siwezi kwenda bila Kana.” Akarudi kukaa pembeni ya Kana. “Sasa wewe Nyange mbona hunisaidii jamani?!” Mkewe huyo. 

Wakati wakipanga mipango yao, walisahau ‘Kana na Briana’. “We Nyange!?” “Mimi naona wewe endelea tu kuongea naye. Wewe anakuelewa zaidi.” “Unavyomuona mwanao pale, amenielewa? Hebu ongea naye bwana Nyange, ni nini!?” Briana alishaanza kulia. 

“Sasa unaongeaje na mtu anayelia mama Briana jamani? Hebu wewe Sonia ongea naye basi.” Baada ya mjomba mtu, Eliah kuona kila mtu amebaki kimya wanashindwakuongea na Briana, alikasirika sana na kubaki akishangaa. Alibadilika na kuwa mkali sana kwa Briana kitu kilichomuumiza kila mtu.  

Alimshika mkono Briana na kumpandisha kwenye gari kwa nguvu huku Briana akilia sana. Kana naye aliondoka akilia wasijue anaenda wapi. Kila mtu aliwahurumiawasijue chakufanya. Nyange alibaki akiumia sana na kumlaumu Leah. 

Katika vitu ambavyo hakuwahi kutarajia Nyange, ni kumuona Briana ana shida maishani, akashindwa kumsaidia. Lakini maisha yaliwageukia, hawakuwa hata na shilingi wanayo miliki wao wenyewe. 

Alibaki akimwangalia kipenzi chake akinyanyaswa na shemeji yake ilimradi tu wapate pakuishi. 'Ni heri vile nilivyokuwa sina ufahamu wangu sikuona wanangu wanavyoteseka, kuliko kuwa hivi nina akili zangu halafu nashindwa kusaidia wanangu.' Nyange aliendelea kuumia moyoni. 

'Mungu wangu nisaidie.' Nyange alianza kuomba kimya kimya. 'Afadhali kufa kuliko macho yangu kushuhudia familia yangu ikiteseka hivi na mimi sina uwezo wa kuwasaidia.' Kilio cha Briana pekee, bila kukosa pesa, kwa Nyange yalikuwa mateso yakupitiliza.

Kaka yake mama Briana na familia yake walikuwa wakiishi Moshi. Waliondoka mida ya mchana na kuacha nyumba nzima kama wagonjwa. Hakuna aliyeamini kama ndio maisha yanawatenganisha hivyo! Kutoka kumiliki mali nyingi na Jumba la kifahari, Nyange na mkewe wamegeuka kuwa fukara kuliko hata ndege wa porini, wasijue watakula nini wala wataishi wapi na kugeuka kuwa ombaomba! 

*********************

Nyumbani kwa Sam na Sonia walibaki kama msibani. “Sasa mama mbona unapika chakula kingi tena wakati Nyange na familia yake wameondoka?” “Amekwambia nani? Unamjua Nyange na mwanae au unamsikia? Umemsahau mama Briana na wanae? Watarudi tu.” 

“Hawawezi kurudi mama. Maisha yamesha tutenganisha. Tulikuwa familia kubwa, lakini ona tulivyogawanywa! Tumeachwa wakiwa kweli! Sam ndio kapooza huko chumbani kama mgonjwa. Kwanza Kana yuko wapi?” “Sijui.” Kidogo Sonia aliingiwa na wasiwasi. 

Alizunguka nyumba yote, ndani na nje bila ya kumuona Kana. Alianza kupaniki na kukimbilia chumbani kwao. “Sam!? Sam!?” Sam alikuwa ameshapitiwa na usingizi. “Kana amepotea.” “Acha kulia bwana Sonia, hawezi kupotea. Ngoja nikamwangalie kule madukani.” 

“Giza limeanza kuingia, wakimuiba?” “Nisubiri nikamwangalie. Usilie sasa.” Sam akatoka na Sonia alimfuata nyuma. “Si nimekwambia usubiri, Sonia?” “Siwezi. Naomba tukamtafute wote.” 

Walimkuta Kana amekaa pembeni ya duka la ‘Mangi’ peke yake anachora chini. Sonia alimsogelea baada ya kufuta machozi. “Niliingiwa na wasiwasi sana Kana. Kwa nini umekaa huku peke yako? Twende nyumbani.” Kana alisimama bila yakuongea na mtu akaanza kuongoza njia kurudi nyumbani. 

“Ungeoga kwanza ndio ule.” Sonia aliongea kwa sauti ya upole, akimuhurumia mwanae. Japokuwa hakuwa na pesa nyingi na Kana hakuwa akijua kama ni mama yake, lakini Sonia alijitahidi sana, kumfanya mwanae aishi vizuri na kwa furaha. 

Kana alikuwa na haiba za kiutu uzima sana. Tangia yupo mtoto alikuwa mtu wa kujitegemea na hakuwa na mambo mengi ya utundu wa kitoto kama watoto wengine. Wakati wote alikuwa mtoto mtulivu, na aliongea mambo ya kueleweka. Kila mwalimu aliyebahatika kumfundisha Kana, alikiri kuwa ana uelewa wa hali ya juu. 

*********************

Wakati wamekaa mezani wanaanza kula Nyange na familia yake nao waliingia. Sonia aliruka alipokuwa amekaa, na kumkimbilia mama Briana na kumkumbatia. “Dada!” Mama Sonia alianza kucheka. “Si nilikwambia watarudi?” 

Bila ya kusema kitu wala kuingia ndani tena, Eliah aliwashusha yeye akageuza gari na kuondoka. “Mbona dereva wenu kama kakasirika?” Mama Sonia aliuliza huku akicheka kana kwamba anajua kinachoendelea, huku Sam na wadogo zake wamebaki wameduwaa. 

Briana alishamkimbilia Kana na kukumbatia huku akiendelea kulia. “Karibuni dada. Si ndio mmerudi moja kwa moja? Au mnaondoka tena?” Sonia aliuliza huku akimwangalia Nyange. “Tuna pakwenda? Bwana mama Briana huyu! Muoneni hivyohivyo. Kanigombanisha kabisa na shemeji yangu! Hivi hapa tumepigwa marufuku tusimtafute tena.” Mama Briana alianza kucheka. 

“Unacheka nini bwana?” “Ukae sasa, utaanguka D.” Mama Briana akamsaidia Nyange kukaa. “Kwani imekuaje?” Sonia ndio alikuwa haamini. “Mama Briana mwenyewe aliniambia hapa tumebanana na tunamlemea Sam na Sonia, kwa hiyo tumuombe kaka yake aje atuchukue tuhamie kwao kwa muda.”

“Sikuwa na shida, nikamkubalia. Kampigia simu, tena yeye mwenyewe, tena Jamaa wa watu alikuwa na shuguli zake, kaacha akaja kutuchukua. Tumetoka hapa mida ile ya mchana, Briana akiwa analia, gafla naona mwenzangu na yeye anaanza kulia. Sijakaa sawa, Brayan naye kaona mama yake na dada yake wote wanalia na yeye akaanza kulia.”

“Namwambia mwenzangu, mbona tena hivyo? Anasema ‘hatuwezi kumuacha mtoto aendelee kuteseka, heri turudi tu’.” Nyange alitulia kidogo, akaanza kucheka mwenyewe. 

“Acha kaka yake amjie juu, akidhani atanyamaza. Kumbe hamjui dada yake, akitaka jambo lake lazima alipate kama mwanae Briana. Kaniharibia mtoto huyu!” Mama Briana alikuwa akicheka mpaka machozi. 

“Natabia yake ni hiihii, akishapata jambo lake kama sio yeye aliyekuwa akilia, heri mwenzie angalau anaendelea kulia.” Briana bado alikuwa akilia. 

“Basi, mjomba mtu anagomba, na wenzangu hawa wote wanazidi kulia. Tena kwa sauti ya juu kama tupo msibani! Mwishowe nikamwambia shemeji yangu, hii safari ni uchuro mtupu, na hivi mimi mgonjwa, najisikia kama nasindikizwa mimi maiti, naenda kuzikwa na familia yangu.”

“Bwana niligeuziwa kibao! ‘Unawaendekeza sana hawa, kuwa mwanaume bwana.’ Shida hazina adabu! Leo nimetukanwa kama mtoto mdogo! Naambiwa namlea Briana kama jipu. Nilivyoona ananikosea adabu na mimi hasira si zikanipanda. Nikamwambia nisikilize shemeji.” Nyange akakaa vizuri kabisa. Watu wote walianza kucheka. 

“Tena hapo aligusa pabaya kweli baba Briana. Kwa Briana tena!?” “Ulijuaje mama Sonia?” Kila mtu alikuwa akicheka sana. “Nikawa mwanaume sasa kama alivyosema niwe. Nahivi alisha nigombeshea mwanangu, halafu akamvuta kwa nguvu mbele ya macho yangu, hasira zilikuwa zinawaka ndani yangu, nilikuwa naungua huko moyoni kama nimetupwa kwenye tanuru ya moto!”

“Nilimbadilikia jamaa wa watu utafikiri sio sisi wenye shida! Nikamwambia ‘mke ni wangu, watoto ni wangu, acha niwaendekeze nitakavyo na kama huyo Briana ni jipu, acha linipasukie mwenyewe mkononi. Nataka uturudishe sasa hivi nyumbani kwa Sam. Na usirudie tena kunigombeshea mke wangu na MWIKO kumgusa mwanangu tena katika maisha yako yote hapa duniani.”

“Hata ukisikia nimekufa leo, usithubutu kumshika kwa namna yeyote ile Briana kwa nguvu, mwache kama alivyo mwanangu. Ana akili zake timamu na lazima kuheshimu hisia zake. Huwezi kuendelea kumvuta na kumsukuma wakati unaona analia. Nimekwambia turudishe sasa hivi na kama huwezi kuturudisha, tushushe hapahapa Sam atatufuata’. Hapo nimekuwa mkali kwelikweli!”

“Bwana gari liligeuzwa kwa hasira, hata hapa kufika ni bahati tu. Hiyo spidi yake! Roho zilikuwa mkononi. Tena tumeambiwa tusije wahi kumtafuta tena, maishani mwetu. Kwa hiyo hapa Sam na Sonia, tumefika. Milango yote imefungwa.” Kila mtu alikuwa akicheka sana. 

“Unajua mama alisema mtarudi, nikawa siamini! Kumbe kweli bwana!” “Mimi niliona dalili tokea hamjaondoka, kwanza kwa mama Briana mwenyewe. Nilimuona jinsi sura yake ilivyobadilika wakati mwanae anavutwa hapa, halafu nikajua hawezi kuvumilia aendelee kumuona Briana analia, na nilijua Briana hatakaa anyamaze hata wamchape, ambapo nilijua huyo ambaye angemchapa Briana ingebidi amuanze Nyange kwanza ndipo amchape Briana, halafu na Nyange naye nilishamuona anavyosugua meno hapa wakati mjomba mtu ana mgombesha Briana.”

“Nikataka kumwambia huyo mjomba mtu, huyo mtoto hagombeshwi wala haguswi kwa nguvu hata kidogo. Akiguswa huyo ni kukumbatiwa, basi. Lakini kwa kuwa nilitaka mrudi, basi nikaona ninyamaze tu, nikajua na mama Briana naye akiongeza nguvu yakulia na hivi Nyange naye akimuona mkewe analia akili haifanyi kazi, nilijua mtarudishwa tu hapahapa. Haya njooni mezani mle.” Kila mtu alikuwa akicheka sana. 

“Karibuni sana jamani. Najua nyumba yetu ni ndogo, lakini hatutashindwa kuishi humu ndani.” Sam alimalizia. 

 *********************

Kesho yake siku ya jumapili wakati wameshatoka kanisani, wakiwa wamepumzika walishangaa kumuona Eliah anarudi. Kila mtu alibaki akimwangalia. Mama Briana akasimama. “Samahani kaka yangu kwa yote niliyofanya jana. Najua nilikosea. Lakini naomba uelewe kaka, hawa watoto tuliwaacha kwa muda wote wakiteseka bila sisi. Najisikia vibaya kuona ndio tunarudi, halafu na kuanza nao mahusiano vibaya. Naona tutazidi kuwaadhibu. Samahani sana kaka yangu.” 

“Hapana. Mimi mwenyewe nilikosea. Sikupaswa hufanya vile. Nimekuja kuomba radhi kwa shemeji yangu. Nilimkosea heshima. Nafikiri ni matatizo ninayopitia ndio yamenifanya nimeshindwa kuwafikiria. Najua nyinyi wote mnapitia kwenye hali ngumu na mnahitajiana sana. Samahani shemeji.” Eliah alienda kumpa mkono Nyange. 

“Hamna shida bwana. Tunashukuru umerudi.” Eliah alikaa chini akionekana na mawazo. “Kuna nini kaka?” “Nimetokea nyumbani kwenu. Nimekutana na Leah.” Mama Briana alikaa chini. 

Kila mtu akasogea karibu kusikiliza. Eliah aliomba watoto waondoke. “Nilienda kumuomba angalau awapishe kwenye ile nyumba na awarudishie gari moja. Lakini nimeamini yule mtoto ni SHETANI. Amenitolea hati za nyumba zenu zote, ambazo Nyange amesainishana naye mpaka kwa wanasheria kwamba amemkabidhi yeye mali zote, mpaka magari yote yapo kwa jina lake.”

“Magari ameuza yote amebakiwa na gari moja tu ambalo lilikuwa na jina la Briana, Nyange alilibadilisha kuwa la kwake Leah.” “Daah!” Nyange alishika kichwa huku akisikitika. “Yaani sijui mtafanyaje dada! Ni kweli vitu vyote ni vyake kihalali. Anaushahidi sio tu wa makaratasi, mpaka amemrikodi Nyange akiongea na mwanasheria, akimuapia kuwa anafanya hayo yote kwa akili zake timamu.”

“‘Rikodi’ zinasema yeye mwenyewe Daudi Nyange ameamua kumkabidhi Leah mali zake zote bila shindikizo lolote. Nikamwambia kisheria ni kweli mali ni zake, lakini sisi ni ndugu, na nikamwambia Peninnah anahitaji mahali pakuishi na familia yake, nikamuomba basi awape angalau ile nyumba moja anayoishi sasa hivi angalau mpate pakuishi, lakini amekataa katakata.”

“Ameniambia undugu na sisi ulishaisha tokea zamani. Alianza kunikumbusha mambo ya kitoto ya zamani tuliyofanyiana tokea tupo pale nyumbani kwa wazazi na kusema sisi wawili tulikuwa tukimdharau sana yeye, na kumuona hana akili.”

“Anasema wakati wote tumekuwa tukimkandamiza yeye, na mimi na baba tumekuwa tukikutetea sana wewe wakati wote. Amekusudia kutuonyesha jinsi yeye alivyo na akili kuliko sisi wote.”  Kila mtu alibaki na mshangao. Kwani wote walijua jinsi mama Briana alivyokuwa akimpenda na kujitolea kwa Leah.  

“Lakini kaka, ile nyumba atarudisha tu. Ile nyumba ni ya Briana na ndipo alipo Junior, hawezi akaichukua.” “Utafanyaje dada? Nimekwambia kila kitu anacho kihalali.” “Nimekusikia sana. Ngoja mume wangu apate nguvu, nitapigania ile nyumba mpaka nitairudisha mikononi mwetu.”

“Labda safari hii aniue, lasivyo nitaipata tu ile nyumba. Na labda isiwe jasho letu. Lakini kama tulihangaika mimi na Nyange, tukajenga, na kama nilimbemba mimi Junior miezi tisa, akamuua mwanangu na leo anataka kuchukua na kumbukumbu yake, ile nyumba itarudi tu. Wala sina wasiwasi.” Kila mtu alikuwa kimya. 

“Nisamehe Mama Briana.” Nyange alikuwa akitokwa na machozi. “Wala huna haja yakulia D. Tutapata mali zetu zote usiwe na wasiwasi. Nakuombea Mungu tu upone, kila kitu kitakuwa sawa mpenzi wangu wala usijilaumu. Wote alituharibu akili.” “Daah! Afadhali wewe ulikwenda Mirembe mke wangu, kuliko mimi aliyekuwa akinitoa kafara kila siku na kunifanya zezeta namfanyia chochote anachotaka yeye!” Nyange aliendelea kusononeka. “Daah!” wakatulia kwa muda.

Roho Ya Uharibifu Haina Mipaka

 “Sasa naomba mimi niwaache, mtoto wangu yule wa kwanza mgonjwa sana, hata mkisikia amekufa leo, msishangae.” “Nini tena kaka?” “Alianza kupooza tu mwili. Hana anachofanya, kila kitu ni hapohapo kitandani.” “Jamani kaka!” Mama Briana alianza kulia. 

“Mlimpeleka hospitali, shemeji?” “Hawaoni tatizo, ni zaidi ya mwaka sasa. Ndio maana hata mlipougua sikuwa na taarifa. Muda wote huo nilikuwa nahangaika naye. Yupo tu nyumbani mama yake ndio ana muhudumia, hata kazi ameacha sababu ya kumuhudumia.” 

“Kaka! Nashauri huyo mtoto akaombewe. Najua huamini katika maombi, lakini sisi tumefunguliwa na maombi. Kama mama ameweza kutufanyia hivi sisi, hashindwikukufikia na wewe. Tena na hivi wewe wakati wote umekuwa mkipingana naye, huwezi kujua amemfanya nini mtoto. Huna utakachopoteza akiombewa. Jaribu tu kaka yangu.” Eliah alifikiria sana nakuanza kulia. 

“Nini?” “Nimekumbuka kitu.” “Nini kaka?” Eliah alisimama nakuanza kuzunguka huku akilia. “Yaani mama!” “Nini kaka? Naomba utulie tuzungumze.” Eliah alirudi kukaa. Walimletea maji, akanywa akatulia kidogo. 

“Unajua, kuna likizo moja Junior mtoto wangu aliniambia anataka kwenda kwa bibi yake akamsalimie. Mimi na mama yake tukamkatalia kabisa. Alipotaka kujua sababu ya kutokwenda kwa bibi yake huku akisema mbona wao wanaenda upande wa mama yao tu kwetu hawaendi tokea babu yao afariki, ndipo mama yao akaniambia ni heri tumruhusu aende asije akaelewa vibaya.” 

“Nilimuomba dereva ampeleke na baada ya siku tatu wakarudi akiwa anafuraha sana na kusema bibi yake alimtunza vizuri. Na ndio baada ya muda kidogo tukagombana tena na mama sababu ya maneno aliyonijibu baada yakumsihi sana aende kwenye msiba wa wakina Nyange. Tuligombana sana kwenye simu, nikamkatia simu kwa sababu alianza kunitishia na kunipa laana.”

“Baada ya muda Junior akiwa mpirani akaanguka, na kupooza. Nilijua inawezekana alivunja uti wa mgongo, lakini nilimpeleka mpaka India kwa uchunguzi, lakini wakaniambia mwanangu ni mzima kabisaa, hana alipovunjika lakini amepooza.” Mama Briana alilia sana. 

“Hivi mama ameingiwa na nini jamani!? Naomba mpigie simu wifi atafute watu wakwenda kumuombea mtoto. Atakuwa amemchezea mtoto kama alivyotuchezea sisi.”“Akimuua mtoto wangu, nakuapia Penninah, na mimi nitamuua, tena kwa mikono yangu mwenyewe. Ni hivyo sijui alipo. Ningempigia simu.” 

“Mimi naona wakumpigia simu ni wifi kwanza atafute watu wa Mungu, wamuombee mtoto na sisi hapa pia tuombe, lakini sio kumpigia simu mama. Utamwambia nini?” “Mama Briana ameongea kweli, shemeji. Kikubwa mtoto apone kwanza.” Nyange naye akaongeza. 

*********************

Eliah alimpigia simu mfanyakazi mwenzake aliyekuwa ameokoka nakumuelezea kila kitu juu ya mtoto na kumuomba wakamuombee mtoto wake. “Hivi na mimi nipo njiani narudi nyumbani.” Wakati Eliah anaondoka aliomba kuongea na Nyange na dada yake. 

“Sina pesa nyingi kwa sasa, naomba mchukue hizi kiasi, mpate pakuanzia halafu mambo yakikaa sawa, nitatuma nyingine. Nataka niwahi nyumbani.” “Hizi zinatosha kabisa shemeji, angalau tupate zakumpa Sam aongezee mafuta ya gari, yakumpeleka Briana shule.” Wote walicheka na kuagana.   

*********************

Siku zilizidi kwenda, mama Sonia akiendelea kuwauguza Nyange na mkewe, kwa upendo, huku akizingatia milo yote. Mama Briana alionekana amepona kabisa, lakini Nyange alionekana kupona taratibu. Ukweli madhara aliyokuwa amepata Nyange yalikuwa makubwa, alikuwa ameisha na kubaki mifupa iliyoshikiliwa na ngozi tu. 

Alipata nguvu za kutembea lakini kwa kukutumia bakora. Japokuwa alionekana mdhaifu lakini alijitahidi kusaidia kufanya kazi ndogo ndogo za pale nyumbani ili kumpunguzia Sam gharama za kuajiri vibarua. Mara kwa mara alitoka kusafisha uwanja. 

“Sasa kaka hapo unazidisha bwana!” Sam alimkuta Nyange na Brayan wakiwa nje, Nyange akifweka majani uwanjani na kutengeneza maua. “Hamna shida kabisa Sam. Mbona hata kwangu ndio kazi nilikuwa nikifanya na Josh? Halafu imebidi kumtoa huyu dogo nje bwana!” 

“Kwa nini?” “Wananiharibia kabisa huyu mtoto!” “Kwani vipi?” “Bwana wanamnywesha uji mpaka leo! Eti anapakatwa ndio alale na maziwa mdomoni!? Yaani maziwa yanawekwa kwenye zile chupa za kunyonya watoto! Balaa gani hili!” Sam alianza kucheka. 

“Nimechukia kabisa! Eti na yeye ametulia kabisa mtoto wa kiume analishwa! Umeona ripoti zake za shule?” Sam alikuwa akicheka sana. “Zina nini kaka?” “Eti wanaandika ni mtoto mtulivu sana. Wameshaniharibia mtoto! Watakuwa wakimpiga sana wenzake huko shule. Mtoto gani wa kiume kazubaa hivi?”

“Halafu eti akitoka shule wanamuogesha halafu wanambembeleza alale! Nimechukia kabisa! Nimesema hamna tena huo ujinga. Akitoka shule akute ugali na aanze kufanya kazi sio kupakatwa.” “Lakini bado mdogo sana huyo, kaka?” “Ana udogo gani? Wakati mimi nikiwa na umri kama huo nilikuwa naenda kuchunga ng’ombe! Aache habari zake kabisa. Tena huyu umasaini ana mke tayari.” Sam alikuwa akicheka sana kila akimwangalia Brayan mwenyewe na baba yake. 

“Ona chupa ya maziwa ile pale mama yake kamletea! Nimemwambia hamna kunywa yale maziwa, mpaka amalize kuzoa hizo taka, tuchome ndio tukae, tule wote.” Sam alizidi kucheka. 

“Lakini kaka, Briana pia anakunywa maziwa na uji mpaka sasa.” “Sasa na wewe Sam mfano gani huo wakulinganisha bwana? Briana yule habari nyingine kabisa! Kwani wewe hukusoma ‘biology’? Watoto wakike wanatakiwa kula virutubisho vingi sana, sababu ya maumbile yao.” Sam alijua Nyange hawezi kukosa sababu kwa Briana. Alizidi kucheka. 

“Changamka Brayan, sawa eeh?” Brayan aliendelea kuokota nyasi kidogo kidogo na kuzikusanya alipoambiwa na baba yake. “Huyu hawezi kuleta ripoti ya kupigana hata siku moja!” “Ulitaka apigane?” “Sio apigane. Niitwe basi baba mtu, niambiwe mwanao amempiga mtoto fulani. Wakiume lakini, sio watoto wa kike. Kupiga watoto wa kike mwiko. Umesikia Brayan?” Brayan alitingisha kichwa kukubali. 

“Maskini mwanangu! Hebu muone Sam. Hata kusema ndiyo hawezi! Wameniharibia mtoto kweli! Maneno hayatoki kabisa mdomoni! Lakini atachangamkatu, na hivi nimepona mwenyewe, nitamchangamsha tu.” Sam alikuwa akicheka, mbavu hana.  

“Pole na kazi Sam.” “Na nyinyi. Maana naona nyumba mpaka imebadilika! Mnatengeneza bustani za maua?” “Nimeona tuongeze maua, sijui ni sawa? Maana tumeanza hii kazi bila kuuliza!” “Hamna shida kabisa, tena ndio vizuri nyumba izidi kupendeza. Nimependa huu mpangilio, kaka.”

“Basi usiwe na wasiwasi, siku si nyingi utapafurahia hapa. Na hivi ninaye mwenzangu hapa, bustani utaipenda hii.” “Lakini kaka tulikuwa tukiongea na Sonia, tunaomba utusaidie kusimamia ile biashara ya dagaa, ili mimi nitulie na kazi hii yakuajiriwa. Naona nalemewa, nakosa muda na Sonia kabisa.” Nyange alikaa kimya kwa muda. 

“Nataka kuongea na nyinyi kwanza baada ya chakula cha usiku wa leo.” Sam alishituka kidogo. “Kwema lakini?” “Kwema kabisa, ni mazungumzo tu.” “Sawa nitamwambia na Sonia.” 

 *********************

Baada ya kila mtu kwenda kulala na mama Briana kumlaza Brayan, Nyange alimgeukia Sam. “Ulimtoa wapi Sonia?” “Alikimbilia Dodoma bwana!” Wote wakacheka. “Sonia!” Nyange alimgeukia Sonia. “Wewe umekaa na mama Briana dada yako, si umeona tunavyoishi?” “Ndiyo.” 

“Usirudie kutoroka tena. Kukiwa na tatizo, lazima kuzungumza. Hata kama ni kubwa kiasi gani, lazima uzungumze na mwenzako usikae unaumia peke yako. Naweza kusema Mungu aliwakusudia muwe pamoja, maana kwa kipindi hicho cha wewe kuondoka, Sam angeweza kupata msichana mwingine akaoa, leo usingekuwa hapa wala sisi tusingekuwa hapa. Umesikia Sonia?” “Nimeelewa shemeji.” 

“Usimkimbie mwenzako. Tunawategemea sana kwa ushauri wa kujenga hizi familia. Usimuone dada yako mkimya hivyo, lakini mambo yangu karibu yote yeye ndiye anayaongoza kwa kunishauri. Wakati wote nasema isingekuwa yeye, tusingefika kule tulipokuwa. Sio kwamba nilikuwa nikimsifia tu, ni kwa kuwa ni kweli ndio mshauri wangu mkuu.”

“Mwenzangu ndiye aliyetangulia kushika pesa nyingi na ndiye aliyesomea mambo ya biashara na mahesabu. Kwa hiyo ndio mshauri wangu mkubwa. Bila yeye, nisingekuwa na uwezo wa kufanya mambo yote yale. Usimuache mwenzako peke yako na usijidharauhata siku moja. Unapoona unawazo lakumsaidia mwenzio, mwambie tu halafu ndio mjadiliane. Umesikia Sonia?” “Nimeelewa shemeji.”

Nyange alitulia kidogo, kisha akaendelea. “Naomba nikushukuru tena Sonia, kwa kuokoa familia yangu. Briana amenisimulia kila kitu, tokea ulipoenda kumtoa Brayan hospitalini na kuwachukua kuishi nao Dodoma mpaka leo unawatunza vizuri sana. Briana wangu anazidi kupendeza. Asante sana.” Nyange alipiga magoti nakutaka kumshika mkono Sonia. Sonia aliogopa sana. Mama Briana alikuwa akitokwa na machozi. 

“Hapana shemeji naomba usipige magoti. Mbona ulishashukuru?” “Kwangu sio kitu kidogo Sonia! Kwani si ungemchukua mtoto wako tu na mama yako mkaondoka? Lakini ulikubali kubeba mzigo wote ule bila kujua lini ungeutua, tena uliishi nao kwa upendosana.”

“Sam aliniambia ada uliyokuwa ukimlipia Brayan katika shule aliyokuwa akisoma Dodoma, tena ya hela nyingi wakati na wewe ndio ulikuwa ukianza maisha na mshahara wako mdogo, huku ukihangaika na dada yako hospitalini Mirembe, mpaka Sam alipokuja kuwachukua. Asante sana.” Sonia alikuwa akilia. 

“Asante Sonia. Sina jinsi nyingine yakuonyesha shukurani zangu kwako, lakini ujue nina kushukuru sana. Asante.” Nyange alirudia. “Asante kushukuru shemeji.” Nyange alirudi kukaa wote wakiwa wanafuta machozi.

*********************

Baada ya kutulia akamgeukia Sam. “Vipi Sam?” “Nipo kaka?” “Mbona umeniangusha mdogo wangu?” “Nini tena?” “Unakaaje na binti wa watu bila ndoabwana?” Sam alishtuka. 

“Mama yake ameniruhusu kaka na ametupa baraka zote. Hapa tulipo tuna ‘Ndoa halali’.” “Hapana Sam. Mipango yetu tokea mwanzo ni ‘Ndoa takatifu’. Najua kulikuwa na mambo mengi hapa katikati lakini naomba mfikishe huyu binti KANISANI. Mama yake hawezi kuwa anafurahia kuona unaishi hivyo na binti yake, ni hivyo hawezi kusema.”

 “Lakini LAZIMA mfunge ndoa takatifu. Ndoa yenye baraka za Mungu, ina faida zake, wadogo zangu. Alicho kiunganisha Mungu, mwanadamu hawezi kukitenganisha. Si mmeona mimi na Penninah? Wamehangaika kweli kututenganisha, lakini mlipo mliliaMungu kwa ajili yetu, Mungu alikumbuka agano letu na baraka alizokuwa ametubariki siku ile.”

“Ndoa takatifu aliyoiunganisha Mungu mwenyewe, haitetewi na mwanadamu, Mungu mwenyewe anaitetea na kuwalinda. Umenielewa Sam?” “Nimesikia kaka.” “Tafadhali sana. Tufanye taratibu mapema kabla hamjaanza kuwa na watoto.” Sonia aliinama. Nyange akashituka kidogo. 

“Vipi Sonia? Au mambo tayari?” Nyange aliuliza lakini Sonia alinyamaza akiwa bado anaangalia chini. “Eti Sonia?” Sam akamsogelea karibu. “Ndio maana huna rahatokea majuzi?” Sam alimuuliza kwa taratibu. Sonia alianza kulia. Alificha, hakutaka mtu yeyote ajue. 

Sam alimkumbatia. “Usilie bwana! Kwa nini hukuniambia sasa?” “Niliogopa!” “Hapana bwana, mwenzio nataka sana watoto.” “Kweli Sam?” “Sana tu!”  Sam aliitikia kwa haraka. “Mbona ulikuwa hata huongelei swala la watoto?” Sonia aliuliza huku akilia kwa sauti ya chini. 

“Umesahau mpenzi wangu? Nilikwambia tokea Kana yupo Mwanza. Nilikwambia ninapenda sana watoto. Sema sikutaka kurudia rudia, nilihofia usije ukadhani nakaa na wewe kwa ajili yakunizalia watoto.” Sam alimkumbatia Sonia na kuanza kumbusu palepale mbele ya Nyange na mkewe bila aibu. 

“Nimefurahi sana!” Nyange alianza kucheka. “Nyange! Usianze kabisa.” Mama Briana alimkatiza. “Waache wafurahie mtoto wao wa kwanza.” “Kwani mimi nimekataa? Ila ninachoona Sam anafurahishwa na mengi sio mtoto tu.” “Na yapi mengine? Halafu sio mtoto wetu wa kwanza, ni wa pili bwana!” “Hongereni sana.” Mama Briana aliwapongeza lakini Nyange alizidi kucheka. 

“Kwa taarifa yako wala sijali tena.” Sam alijibu. “Utajali vipi na ushatimiza kusudi lako? Sasa hivi hata Sonia akitaka kuondoka hawezi tena, maana hakuna wakumpokea tena na tumbo hilo! Ndio kashafika hapa kwa Sam.” Sam alikuwa akicheka sana.

“Nyange wewe!?” “Wewe mama Briana humuoni Sam alivyofurahia? Kashatimiza lengo lake, roho imemtulia.” “Daah! Siamini! Asante Sonia.” “Endelea kushukuru, lakini kabla huyo mtoto hajazaliwa Sam, uwe ushamuoa Sonia. Umesikia?” “Nimekuelewa kabisa kaka.” Sam bado alikuwa haamini. 

“Nitafurahi tukifunga ndoa Sam.” Sonia aliongeza. “Umeona? Hata Sonia mwenyewe anataka ndoa.” “Mbona hukuniambia sasa? Mimi nilijua umeridhika na ile ‘Ndoa halali’. Maana hujawahi hata kugusia.” Bado Sam alikuwa amemkumbatia Sonia. 

“Hilo eneo nalo nila kushugulikia Sonia. Lazima ujifunze kuzungumza na mwenzio. Sio kuweka mambo moyoni. Umeelewa Sonia?” “Nimeelewa dada. Utanisimamia kwenye harusi yangu?” Nyange alianza kucheka. “Unababaika nini sasa? Wewe si umemwambia ajifunze kuongea kilichopo moyoni? Ndio bubu kaanza kusema, jasho linakutoka!” “Nyange bwana! Ona haya makovu mwili mzima kama kenge! Siwezi kupendeza! Nitawaharibia picha zenu za harusi.” “Mimi nakutaka wewe dada.” Mama Briana alibaki kimya. 

“Mimi sitajali unavyoonekana dada, ilimradi tuwe wote pale kanisani.” “Usimkataliemke wangu bwana!” Sam aliongeza. “Eti Shem?” Mama Briana alifikiria kwa muda na kumgeukia mumewe. “Eti D? Tutawasimamia?” Nyange alianza kucheka. “Nini sasa? Nyinyi ndio mtatufaa bwana. Maana mmeanza na sisi tokea zamani.” “Mimi sina neno, lakini hivi nilivyoisha? Sijui suti inakaaje hapa! Labda tufunge msuli.” “Nyinyi msijali. Ilimradi harusi ifanyike.” 

“Sawa, kama nyinyi wenyewe ndio mnaona hivyo.” Sonia alienda kumkumbatia Mama Briana. “Asante dada.” “Karibu na hongera sana Sonia.” “Ila naomba usimwambie mama kama nimepata ujauzito tena.” “Mbona anajua?” Sonia alishituka mpaka akakaa chini. 

“Dada wewe!?” “Kweli tena. Mimi alishaniambia muda tu naona hata wewe mwenyewe ulikuwa bado hujajijua kama umepata mimba tayari. Mama yako anakuangalia kwa karibu sana Sonia, na anakujua vizuri sana kuliko hata unavyojijua mwenyewe. Wakati wote lazima ujue wewe ndio kila kitu kwa mama yako.”

“Kwa hiyo kila unachotaka kukifanya uwe unamfikiria na yeye pia.” Sonia aliingiwa na hofu, akaanza kulia. “Amekasirika?” Sonia aliuliza huku akilia. “Wewe tafuta muda uongee naye.” “Naogopa hata kumuangalia usoni.” “Na yeye anajua kama unamkwepa.” “Dada!?” “Kweli Sonia.” Sonia aliinamisha uso wake viganjani kwake na kuendelea kulia, Sam alimvuta tena karibu na kuweka mikono yake mabegani mwake. 

“Usiogope Sonia, tupo pamoja.” Sonia aliendelea kulia. “Usilie. Tena ukiwa kwenye hali hiyo ujitahidi sana kuweka mbali hisia za majonzi. Inamuathiri mtoto. Tufanye hivi.” Nyange alikaa sawa ili andelee kuongea. 

“Asubuhi kabla ya kwenda kanisani lazima tumwambie kwanza swala la kufunga ndoa. Halafu ndio mseme sasa swala la ujauzito. Umesikia Sam?” “Kweli kaka. Tuanze kutangaza ndoa kwanza ndio wewe Sonia uongee naye.” Sonia aliinama huku akilia.

“Usilie bwana!” “Namuogopa sana mama, Sam. Huyu ni mtoto wa pili nazaa bila ndoa. Naogopa hata kumsogelea.” Sonia aliongea kwa sauti ya chini iliyojaa hofu. 

“Huyu ni tofauti Sonia. Mimi nipo na nimekubali kukuoa. Basi kesho tutakuwa wote wakati unaongea na mama juu ya huyu mtoto, usiogope.” “Wazo zuri sana Sam. Sam akiwepo itaongeza uzito.” Nyange alidakia. 

 *********************

“Kingine naomba niwashukuru kwa kazi hiyo mnayotaka kunipa.” “Hatukupi kazi kaka! Ni unafanya biashara ya dagaa.” “Ndio hayohayo. Tunashukuru sana, maana naona wadeni wangu na marafiki wote wamenikimbia.”

“Nimezunguka humo maofisini kukopa nianzishe biashara nimeishia kutukanwa tu, hata shilingi sijapewa! Hivi hapa mimi na mke wangu tulikuwa kwenye maombi makali sana, tukimsihi Mungu atukumbuke na sisi. Tunashukuru sana, mnavyotupa pakuanzia. Najua nikiwa huko nje akili itafanya kazi, kuliko kukaa tu humu ndani, mkinilisha mimi na familia yangu.” 

“Sam na Sonia, binafsi sina neno lakuwaambia, lakini mjue nawashukuru sana. Asanteni.” Mama Briana alitulia kidogo na kuendelea. “Nyange anaposema tumekwama, mjue ni kweli tumekwama kila mahali. Tuna jina baya sana kwa watu tuliokuwa tukiwaita marafiki. Milango yote imefungwa. Tumeishia kukejeliwa na kutukanwa.”

“Mimi ndio nimeamua kuacha kuzunguka kukopa kabisa, maana naona nadhalilishwa tu. Marafiki walewale wa Nyange tuliokuwa tukiwasaidia, leo wananitaka kimapenzi ili wanisaidie!” Mama Briana aliinama nakuanza kulia. “Pole dada. Pole sana.” 

“Tumeona hapa tunawabana, tukaenda kuonana na mwanasheria juu ya mali zetu. Tulimuuliza kama tunaweza hata kukomboa ile nyumba moja, lakini ametukatisha tamaa kweli! Sijui kama tutapata mali zetu tena.”

“Usikate tamaa shem, ninaye rafiki yangu ni mwanasheria. Nitamuomba aje muongee naye muone mtakapofikia. Lakini kaka, naomba kabisa msijione mzigo hapa kwetu. Hamuwezi amini huzuni mliyotuachia siku mlipotaka kuhamia Moshi. Hapa kwetu, palikuwa kama msibani! Kila mtu alikuwa akisononeka kuondoka kwenu.”

“Mpaka wadogo zangu ambao walikuwa hawawafahamu tokea mwanzoni, nao pia waliumia. Hivi kesho jioni yule mdogo wangu anayenifuata, atakuja kuwachukua akaishi nao, angalau mpate nafasi yakuwatosha.” “Msifanye hivyo Sam! Ni kama unawafukuza wadogo zako kwa ajili yetu! Hatuwezi kuwatenganisha.” 

“Usiwe na wasiwasi kaka. Hilo ni wazo walilolitoa wao wenyewe. Na Sonia alipatwa na wasiwasi huohuo, akajaribu kuzungumza nao. Lakini wanaonekana wameridhia kwa moyo mmoja. Kwa hiyo msiwe na wasiwasi kabisa. Muwe na amani.” “Daah! Asanteni sana.” 

*********************

         Mama Sonia hakuamini aliposikia Sam anataka kumfikisha Sonia kanisani. “Kweli Sam? Siamini! Maana nilipojua ni mjamzito tu, nilikata tamaa kabisa yakuja kumuona mwanangu anaolewa!” Mama Sonia alijibu mbele za watu wote, nakufanya Sonia ainame. 

Sonia hakutaka watu wengine wajue kama ni mjamzito mpaka baada ya harusi. Alipanga kumvuta mama yake pembeni baada ya kuambiwa swala la harusi, ndipo yeye na Sam wamalizie swala la ujauzito wakiwa wao watatu tu. Lakini mama yake ni kama alikuwa ametoa siri yake na kufanya kila mtu amgeukie yeye mpaka shemeji yake. Sonia alibaki ameinama. 

“Samahani sana mama. Lakini nakuahidi nitamuoa Sonia kabla hata mtoto hajazaliwa. Nampenda sana Sonia, mama yangu. Naahidi nitamtunza yeye na watoto wote.” “Asante Sam.” Sonia alimsogelea mama yake na kuongea kwa sauti ya chini huku ameinama na machozi yakimtoka. “Samahani mama.” Sam naye akamsogelea Sonia. 

“Unalia nini sasa badala ufurahi?” “Niliogopa mama!” “Unaogopa nini?” “Najua nimekuudhi mama yangu. Huu haukua mpango tuliokuwa tumepanga mimi na wewe.”“Kumbe bado unakumbuka tuliyoongea na ahadi yako kwangu?” “Lakini Sam amekubali kunioa kabla mtoto hajazaliwa, mama.” Sonia alijibu kwa hujitetea huku akilia kwa kujutia. Sam aliumia sana.

“Samahani sana mama. Najua mimi ndio nimemfanya Sonia avunje ahadi yake kwako, lakini nilijua vile ulivyotubariki kule Dodoma, inatosha.” Sam aliingilia mazungumzo. “Sasa hapo wewe ndio unaharibu kabisa Sam. Hiyo sentensi ya mwisho ungeacha tu.” “Nimeelewa kaka. Unisamehe mimi, mama yangu. Naona mimi ndio nimemuingiza Sonia kwenye matatizo.” “Huo ndio uanaume Sam.” Mama Sonia alicheka kidogo.

“Ni kweli baraka zangu zote bado mnazo, sasa nataka mpate na za Mungu.” “Tumeelewa mama. Usilie sasa Sonia, njoo mama watoto wangu.” Nyange alianza kucheka na kuamsha vicheko kwa kila mtu, zaidi Sam. 

“Bwana mtoto kafurahiwa huyoo! Naona Sam ana kazi yakucheka tu.” “Sikutegemea kabisa kaka! Daah! Nimefurahi sana.” Sam alimkumbatia tena Sonia huku akicheka. Mama Briana na mama Sonia waliangaliana nakucheka. “Hongera Mama Sonia.” “Asante. Lakini naona kama mama mtoto mwenyewe hajafurahia kama baba mtu!” Mama Sonia aliongea na yeye kwa utani kumfanya Sonia atulie maana bado alionyesha hofu. 

“Kama umenisamehe ndio nitafurahi. Nilikuwa naogopa kweli tangia nilivyojua ni mjamzito!” Sonia alianza kucheka huku anafuta machozi. “Sonia bwana! Ungeniambia tu!” “Niliingiwa na hofu sana Sam. Kwanza nilikuwa namkwepa sana mama. Kila nilikuwa nikikumbuka vile nilivyo muapia na kumpa ahadi ya mpaka niolewe, ndio nilikuwa naogapa hata kumsogelea”

“Nilikuwa nakuangalia tu unavyohangaika, mpaka nikamwambia na mama Briana” “Mama jamani! Si ungeniuliza tu yakaisha!” “Ulitaka yaishe vipi wakati umevunja ahadi yako kwangu!?” “Lakini si yameisha? Eti mama yangu?” Sonia aliongea kwa sauti iliyo jaa aibu huku akifuta machozi, akimwangalia mama yake na tabasamu. 

“Muone anavyocheka sasa hivi! Ulikuwa unahangaika humu ndani, hata kuniangalia usoni ulikuwa unashindwa kwa aibu. Hongera.” Sonia alifurahi sana kupata hongera kutoka kwa mama yake. “Asante mama. Sasa hivi ndio nitaanza kumfurahia mwanangu. Na hivi Sam na yeye anataka mtoto, moyo wangu umejaa furaha sasa. Asante sana mama.” Sam bado alikuwa akicheka. 

“Saana Sonia. Nimefurahi kupita kiasi! Hapa nahisi ni ndoto. Na mimi nitaanza kuitwa baba! Maana Nyange amezidi kuturingia na wanae.” Bado Nyange alikuwa akicheka. “Sawa Sam mdogo wangu. Lakini sikio halizidi kichwa. Aliyetangulia, katangulia tu.” “Na mimi nakuja taratibu kaka.” Wote walikuwa wakicheka. 

“Hongera shem.” “Hongera wifi.” Wadogo zake Sam nao walimsogelea Sonia na kumpa mkono. Wote walionekana ni watoto wenye maadili mazuri. “Asanteni sana.” “Sasa tunaenda kusherehekea wapi?” Nyange alimchokoza Sam. “Daah! Nimechanganyikiwa kaka. Hata sielewi tena. Chagueni nyinyi popote pale.” Kila mtu alikuwa akicheka. Mama Sonia ndiye aliyekuwa na furaha kupita wote. 

 *********************

“Naomba niwashukuru nyinyi wote. Nyange na mkewe, na Sam, kwa kutimiza ndoto zangu. Mnakumbuka niliwaambia Paul alivyoniomba nifanye juu chini Sonia asome? Nilikuwa nikiishi na deni la ombi la Paul. Lakini sasa hivi najihisi nimetua mzigomkubwa sana. Sina deni na mtu yeyote. Mmemsomesha mwanangu na sasa hivi anaolewa! Siamini! Tena mbele ya macho yangu ndoto hizo zinatimia! Ninafuraha yakupita kiasi. Asanteni sana.” Mama Sonia alikuwa akiongea huku akicheka na kufuta machozi. 

“Hongera sana Mama Sonia.” Mama Briana alirudia. “Asante. Nimekuachia wewe kijiti mama Briana.” “Mbona mimi nilishakutangulia mama Sonia? Mwenzio nasubiri kutangaza tarehe ya harusi tu hapa. Mkwe nilishapata.” Mama Briana aliongea kwa mafumbo ili Briana na Kana wasielewe. Kila mtu alicheka. 

“Na inabidi niwe karibu naye kweli huyo mkwe mtu. Naona kabanwa hana pakuhemea!” Nyange alidakia akimaanisha Kana. Kila mtu alikuwa akicheka sana. “Mke atakuwa kapata, lakini na yeye cha moto atakiona! Mpaka namuonea huruma bwana huyu mtoto. Anafuatwa mpaka chooni! Hana rafiki wa kiume wala wakike, ni huyo peke yake! Kutwa kamshikilia mkono.” Nyange aliendelea kuwatania Briana na Kana, na kufanya kila mtu aendelee kucheka kasoro wao wenyewe waliendelea na mazungumzo yao kimya kimya bila kujua linalo endelea. 

 Pale Vitendo Vinapoongea Zaidi Ya Maneno

Siku inayofuata ya jumatatu jioni, Sam alirudi nyumbani na baadhi ya marafiki zake, akiwemo Mr. Mwansasu. Sonia alishituka sana. “Nimefukuzwa kazi nini?” Sonia alijikuta akiropoka baada ya kutoka chumbani alipokuwa amelala, baada ya kuitwa na Sam sebuleni na kukutana na Mr. Mwansasu na wafanyakazi wengine aliojua ni viongozi wa kubwa pale kwenye benki. 

“Kuna nini Sam?” “Usiogope. Njoo usalimie.” Alikuwepo Nyange, mama Briana na mama yake. “Nilitaka kuwatambulisha Sonia mwenyewe na mama yake kabla hatujaanza kikao chetu cha kwanza.” Sonia alipumua kidogo na kucheka. Mr. Mwansasu alisimama na kumpa mkono Sonia. 

“Hongera sana. Nasikia na mjomba anakuja.” “Sam wewe!” Sonia alimgeukia Sam kwa aibu. “Ulitaka iwe siri shem?” Rafiki yake mwingine Sam naye aliyekuwa amesimama ili amsalimie Sonia alidakia kwa kuuliza swali. “Mbona kila mtu anajua! Maana tumetangaziwa na Kiongozi hapa, leo asubuhi kwenye kikao cha viongozi wote. Mpaka CEO anajua ujio wa mjomba. Sio siri tena.” “Sam wewe jamani!” Vicheko vilitawala pale sebuleni huku wakiendelea kusalimiana. 

“Kabla hatujaanza chochote, naomba nimshukuru Sonia kwa kuwa mvumilivukwangu katika kipindi chote hiki cha mahusiano yetu na kukubali mimi ndiye niwe mume wake.” Watu wote walitulia ili wamsikilize Sam. 

“Sonia alinikubali wakati wengine wakinitukana. Wakati ule Sam huyu anaitwa fala, lofa huku nikiambiwa sina hadhi ya kuwa na mwanamke kama Sonia. Lakini nyinyi wote hapa ni mashahidi, mliona vile Sonia alivyonipenda na kuniheshimu hata pale wakati natunzwa nyumbani kwa Nyange, nikiwa sina kitu, nimelemewa na majukumu na kushindwa kumudu hata kulipia kodi ya chumba nilichokuwa nikiishi, wakati tunajenga hii nyumba.”

“Nakumbuka wakati ule anasoma na tuna gari bovu, lililokuwa likituharibikia mara kwa mara na Sonia tukiwa njiani. Wakati mwingine mvua ilitunyeshea, jua lilituchoma baada ya gari kutuharibikia njiani na kutulazimu kutembea umbali mrefu sana, kutafuta usafiri mwingine au kurudi nyumbani kwa miguu, tukitembea.” Sam alicheka kidogo. 

“Kuna nyakati nyingine nakumbuka nakuwa na Sonia hapa siku nzima, wakati ule tunaijenga hii nyumba. Nakuwa nimeshinda naye juani siku nzima, bila kula wala kunywa kuanzia asubuhi mpaka jioni, tunatoka hapa nakuwa nimeishiwa hela hata yakumnunulia Sonia maji ya kunywa njiani, nakuwa sina, tunaishia kukimbilia ugali wa mama Briana, nyumbani kwake.”

“Lakini Sonia hakuwahi kulalamika hata mara moja zaidi ya kunitia moyo. Alikuwa akinihudumia kama vile ninamiliki majumba yote hapa jijini! Alijua navaa nini, nakula nini, na vyote hivyo alikuwa akifanya yeye mwenyewe kwa mikono yake hata alipokuwa amebanwa na majuku ya shule, lakini Sonia aliniweka mimi mbele.”

“Najua hakuna kitu nitakachompa kitakacholingana na mapenzi yake kwangu ila kuwa mwaminifu kwake daima. Lakini pia sio vibaya kwa mara ya kwanza maishani mwake, mimi ndiye nikawa wa kwanza kumzawadia gari mpenzi wangu.” Sonia aliyekuwa amekaa pembeni ya Sam, akiwa ameinamisha kichwa chini huku akifuta machozi, alishituka sana. “Gari!?” Sonia aliuliza huku akimwangalia Sam kwa mshangao. 

Sam alitoa funguo na kumkabidhi Sonia huku akicheka. “Sijawahi hata kushika usukani wa gari, Sam jamani! Nitaendeshaje hilo gari? Mi naona uache tu.” Sonia aliongea huku akitetemeka na machozi yakimtoka. “Usiogope Sonia. Mimi nitakufundisha.” Mama Briana aliyekuwa kimya muda wote akisikiliza kwa makini, aliingilia. 

“Sam anajeuri mbaya! Hebu kwanza twende Sonia tukaone gari yenyewe. Isije kuwa imechokachoka.” Nyange alitania nakuinua vicheko tena. “Wewe unamuona Sam kwa wasiwasi nini? Leo siku nzima hajafanya kazi, alikuwa anazunguka kutafuta gari ya kumfaa Sonia. Tumemwambia aagize Japani, kasema litachelewa.” “Namjua Sam kwa Sonia. Hajiwezi kwa lolote mdogo wangu huyu!” Nyange alimalizia na kuzidisha vicheko. 

“Twende basi ukaone gari yenyewe.” Mama Briana alisimama na kumshika mkono Sonia wakatoka nje. Macho yaliwatoka baada yakutoka nje na kukutana na SUV ya nguvu. “Lote hilo, Sam wewe!?” Sonia aliropoka na kumkumbatia Sam. “Asante sana, mpenzi wangu.” “Umelipenda lakini?” “Sanaa. Sikuwahi hata kuwa na ndoto yakuja kuwa na gari langu.” Watu wote walicheka. 

“Naona mtoto kaja na baraka ya gari! Wapili nyumba. Ujiandae Sonia.” “Waache bwana Nyange!” Mama Sonia alikuwa kama amepigwa na butwaa. Alisimama pale nje akiwa anashangaa. “Nimepewa gari, mwenzio!” Sonia alimsogelea mama yake nakumwambia kwa sauti ya chini kama kumnong’oneza. 

“Naona! Hongera Sonia mwanangu. Unaona kutulia kunavyolipa? Hongera sana mama.” “Asante mama yangu, siamini!” Sonia aliendelea kunong’ona na mama yake pembeni wakati Nyange akitaniana na rafiki zake Sam huku wakimpongeza Sam. 

“Sasa sijui ile biashara bado ipo, au ndio tumefunga kabisa sababu ya kumnunulia Sonia gari?” “Ipo kaka, usiwe na wasiwasi kabisa.” Waliendelea kucheka. Mwishowe walirudi sebuleni kwa ufunguzi wa Kikao cha kwanza cha harusi ya Sam na Sonia. 

 *********************

Siku inayofuata Nyange na mkewe waliwasindikiza Sonia na Sam kanisani kuandikisha ndoa yao. Walitoka kanisani siku hiyo lakini mama Briana alionekana na mawazo sana, kila mtu alijua. Sam aliwaomba wakae mahali wale chakula cha mchana kabla yakurudi nyumbani.

“Sonia ameomba tuwape ile gari kwa matumizi yenu na kama mama Briana akipata muda amfundishe kuendesha.” Sam alivunja ukimya mara baada ya muhudumu kuwawekea vinywaji. Nyange na Mama Briana walishituka sana. “Eti nini?!” Nyange akauliza akiwa kama amepaniki, Sam akacheka tu. 

“Hapana Sonia! Hutuwezi kuendesha hiyo gari. Hapana kabisa. Mnayotusaidia yanatosha jamani! Hapana. Hata mama yako hatafurahia. Badala hata umpe mama yako, unatupa sisi! Sio sawa Sonia. Usifanye hivyo.” Mama Briana alijibu huku akitingisha kichwa, kukataa kabisa. 

“Mama mwenyewe amesema ni wazo zuri. Kwanza hata yeye mwenyewe hajui kuendeshea na sehemu aliyopata pakuanzisha saluni yake ni palepale karibu na nyumbani, atatembea tu. Kwa hiyo unaona dada? Litakuwa likikaa tu pale nyumbani? Sam amesema nisianze kazi mpaka nitakapo jifungua, halafu kama wewe unavyonijua dada yangu, mimi huwa sina pakwenda. Najisikia vibaya mnapotaka kutoka, wewe au shemeji inabidi mkasubirie daladala wakati shemeji bado hajapata nguvu vizuri!”

“Juzi nimewasikia mlivyokuwa mnaongea wenyewe pale sebuleni jinsi mlivyokuwa mmesimama kwenye daladala na kubanwa njia nzima. Nakuomba dada, mtumie tu hilo gari tafadhali. Siwezi kujisikia vizuri, eti mnaacha gari pale nyumbani halafu mnaenda kupanda daladala!” Mama Briana alikuwa akitokwa na machozi. 

“Kwanza huoni mtakuwa mnanisaidia na mimi kuwapeleka watoto shule? Na wao pia watapata muda wakupumzika zaidi, maana inabidi waamshwe mapema sana ili niwawahishe shuleni kwao na mimi niwahi kazini kwangu.” Sam aliongeza. 

“Daah! Nyinyi watu, mnauhakika lakini?” “Kabisa kaka. Wala msiwaze mara mbili, chukueni tu hilo gari, mtumie kwa muda huu mnapo jipanga upya. Huyu akiwa na shida yakutoka atawaambia mapema, ikitokea ana dharula halafu mkawa mbali, mimi nitamfuata tu.” “Daah! Sijui tuseme nini jamani!” “Hamna hata haja yakusema kitu chochote, nyinyi muwe huru tu.” “Asanteni sana.” Mama Briana alimalizia kwa unyonge sana. 

“Kingine.” Sam alitaka kuongea tena. “Mnataka kutupa na ile nyumba nini? Maana nyinyi watu mmepitiliza.” “Hapana kaka.” Walicheka kidogo. “Nimeonge na yule rafiki yangu mwanasheria, ameomba kesho muonane. Anaonekana anaweza kuwasaidia kesi yenu.” “Tunashukuru Sam, lakini sidhani kama tutaweza tena. Hivi kuzunguka kote huku, ilikuwa ni kutafuta wanasheria. Lakini wote wametutajia pesa nyingi sana, hatuna huo uwezo kwa sasa na wametukatisha sana tamaa.” 

“Usijali kaka. Huyo mwanasheria, nimeshamuelezea hali yetu, ameelewa. Amesema mkifanikiwa ndio mtamlipa.” “Kweli Sam?!” Mama Briana aliuliza kwa sauti ya kukata tama. “Kweli kabisa. Nyinyi kesho muende mkamuone, mzungumze halafu ndipo tutajua pakuanzia kuanzia hapo.” “Na hivi sasa hivi tuna gari, tutaenda kumuona hiyo kesho.” Nyange aliongea kwa utani na kufanya wacheke kidogo. 

“Siwatanii tu wadogo zangu, mmenifuta machozi. Hivi mnafikiri nilikuwa najisikiaje, kumpandisha mke wangu kwenye daladala? Nilikuwa nalia sana moyoni. Siongopi, nawaambia ukweli. Hakuna siku inapita nisitamani kurudisha nyuma ile siku ya kwanza nilipolala na Leah.”

“Najuta na kuitubia hiyo dhambi mpaka naona Mungu amechoka kunisikiliza. Kila nikimuangalia mke wangu na watoto wanavyoteseka sasa hivi, kwa maamuzi mabaya niliyoyafanya mimi, naumia kupita kiasi. Namuomba Mungu asinichukue kabla sijarudisha familia yangu kwenye yale maisha yetu ya zamani. Na ninaamini Mungu atanisaidia tu. Nitaweza.”

“Hata kama nimepoteza kila kitu, na nitashindwa kesi mahakamani, lakini bado nina imani yakupata mali nyingine, tena kwa jasho langu mimi mwenyewe bila ya kudhulumu mtu. Naomba Mungu anijalie nguvu, niweze kutembea vizuri. Hakika wanangu na mke wangu watakuja kuishi maisha ya kifahari sana hapa duniani. Mungu yupo.” Mama Briana alikuwa akitokwa tu na machozi bila ya kuchangia hilo. “Tunawaombea kaka, na tupo pamoja.” 

 *********************

Kwa mara ya kwanza tangie wapatwe na matatizo, mama Briana na mume wake wanaanza kuona mwanga maishani. Waliamka asubuhi ya siku inayofuata, wakiwa na shukurani mbele za Mungu kwa kuwapunguzia adha ya kugombania daladala. Waliamka na kushikana mikono palepale kitandani, Nyange akiwa muombaji mkuu. 

Mama Briana alitoka kitandani akiwa na uso uliojaa tabasamu, na kuwaandaa wanae yeye mwenyewe. “Usiwe unaamka tena alfajiri kwa ajili ya kuandaa watoto, Sonia. Nitakuwa nafanya tu mimi mwenyewe. Rudi ukapumzike.” Mama Briana alimrudisha Sonia mlangoni, alipokuja kuwagongea kama kawaida yake, kumchukua Brayan amwandae kwa ajili ya kwenda shule. “Una uhakika dada?” “Kabisa. Nimeshapona, ngoja na mimi nikupokee ili upate muda wa kupumzika.”

Aliandaa kifungua kinywa kwa wote, alipohakikisha watoto wake wameshiba ndipo walipoondoka. Walipokuwa njiani aliwaambia kuanzia siku hiyo yeye ndio atakuwa akiwapeleka shule. Briana alifurahi sana. “Utashuka uwasalimie walimu wangu, dady?” Briana aliuliza wakiwa wanakaribia shuleni kwao. 

“Sio leo mama. Ngoja nipate nguvu kidogo. Watakucheka wenzako wakiniona hivi nilivyo.” “Sitajali dady! Twende ukaangalie darasa letu, sio mbali sana na darasani kwa kina Kana.” Nyange alifikiria kidogo, akamgeukia mkewe aliyekuwa akiendesha huku machozi yakitaka kumtoka. “Mbona upo sawa tu D. Twende tu tukapaone.” 

Briana hakuwa akifanana na baba yake hata kidogo. Kwa uzuri na rangi ya Briana na ukimlinganisha na vile baba yake alivyokuwa sasa, ilikuwa rahisi kwa mtu yeyote kusema Nyange ni mfanyakazi wa kina Briana. 

Bado Nyange alitembea kwa shida kidogo, japokuwa alikuwa na nafuu kubwa sana tokea atoke kwenye mikono ya Leah, lakini bado alionyesha mdhaifu. Rangi yake ya weusi, ilikolea mara mbili yake. 

“Tutaenda wote dady?” Briana alirudia baada yakumuona baba yake amebaki kimya akiwaza. “Nitafurahi sana tukienda wote dady. Naomba twende wote.” “Tutaenda wote Briana. Lakini itabidi unishike mkono nisianguke.” Nyange alimgeukia Briana akimfanyia utani ili acheke. Briana alicheka kidogo. “Nitakushika dady, hutaanguka.” 

Kila mtu siku hiyo alijua Briana amefurahi. Alitembea huku amemshika baba yake mkono na sio Kana kama walivyozea wanafunzi wengine na walimu kumuona akizunguka akiwa ameshikwa mkono na Kana. Alikuwa akicheka wakati wote huku akimuonyesha baba yake maeneo mbali mbali ya pale shuleni kwao. Mama Briana na Kana walikuwa wakitembea nyuma yao. Waliouliza aliwatambulisha wazazi wake kwa furaha yote bila hata kufikiria mara mbili. 

*********************

Nyange alitoka pale akiwa hana furaha hata kidogo. “Vipi D?” “Daah! Mungu wangu anisaidie jamani!” Nyange alianza kusononeka. “Najua Sam analipia hii shule pesa nyingi, lakini haina hadhi kabisa ya Briana kusoma hapo. Naumia kupita kiasi. Siamaini kama mwanangu ndio ameishia kwenye shule kama hii! Maisha yangu yote nimetamani wanangu wapate elimu bora sana, kwa pesa yoyote ile. Ndio maana nilikuwa sijali mapesa niliyokuwa nikimwaga kwenye ile shule. Daah! Kweli Nyange nimeishiwa jamani. Nikumbuke Mungu wangu, usinipite. Nisamehe Mungu, nibariki tena!” Machozi yalikuwa yakimtoka Nyange. Alibaki ameweka mikono kichwani. 

“Pole D. Nilijua tu utaumia. Pole mume wangu. Kila kitu kitakuwa sawa. Twende tukamsikilize na huyo mwanasheria mwingine, tuone na yeye atatuambia nini. Sitachoka D, nitapambana na Leah mpaka aturudishie kila kitu hasa ile nyumba tuliyokuwa tukiishi.”

“Na pia nilikuwa nafikiria ukipata nguvu vizuri, nirudi kuomba kazi kule nilikokuwa nikifanya kazi zamani. Labda wataniajiri tena. Najua nikipata kazi na mshahara wakueleweka, hatutashindwa kupanga hata vyumba viwili. Tuanze maisha yetu D. Hatuwezi kuendelea kuwa mzigo kwa hawa watoto wadogo. Lazima maisha yetu yaendelee.” Nyange alibaki kimya, akizidi kuumia. 

 *********************

Walifika ofisini kwa Mwanasheria huyo ambaye ni rafiki wa Sam, wakiwa hawana tumaini hata kidogo. Walimueleza kila kitu bila kuficha, kuanzia mwanzo mpaka mwisho kwa kadiri walivyokumbuka na vile walivyosimuliwa na mama Sonia. 

Lakini kwa mara ya kwanza walikutana na mtu aliyewatia moyo na kuwaambia inawezekana. “Japokuwa nchi ya Tanzania haiamini uchawi, lakini ipo sheria yakichawi, {Whitch craft art}. Ambayo imekuwa ngumu sana kuendeshea kesi zake.” Mwanasheria huyo aliwatia moyo na kuendelea kuwaeleza. 

“Kesi zote za ‘kichawi’ zinahitaji ushahidi wakutosha kukamilisha kesi hizo. Kwa hiyo na sisi nilazima kujiandaa na kutafuta vithibitisho vitakavyomridhisha hakimu kama kweli Mheshimiwa Nyange hakuwa na akili zake timamu wakati huo alipokuwa akiingia mikataba hiyo, ya kumkabidhi mali zenu Leah.” 

Walikubaliana kumshitaki Leah kwa kosa la kutumia ushirikina kuharibu akili ya Nyange na kuingia naye mikataba wakati hakuwa na akili zake timamu. 

Cha Mtu Mavi!

Kwa kuwa Leah alikuwa na pesa, aliposhitakiwa tu, akarudi tena kwenye kampuni ileile ya wanasheria aliyokuwa akiandikishiana mikataba na Nyange na kuwalipa pesa nyingi akitaka wasimamie kesi hiyo. 

Kesi ilianza kuwalemea wakina Nyange. Kwani kutokana na mahusianowaliyokwisha kuwa nayo Nyange na Leah zamani na mama Briana kuthibitisha hilo mahakamani hapo, huku akimtetea mumewe kwamba walishaachana, lakini Leah alikataa katakata kuwa wao hawakuwahi kuachana tokea walipoanza mapenzi na Nyange. 

Leah alisema baada ya mama Briana kujua mahusiano yao ya kimapenzi na kuondoka nyumbani na mtoto, ilimbidi Nyange kumdanganya mkewe kwamba mahusiano yao {Leah na Nyange} yaliisha ili kumfanya mama Briana arudishe mtoto nyumbani. Leah aliendelea kusema kwamba Nyange hakushituka hata kidogo mkewe alipoondoka nyumbani baada ya kugundua mahusiano yao, lakini alipomtaka mtoto wake, Briana, dada yake alikataa kabisa. 

“Ndipo ilipombidi Nyange kumdanganya ili kumfanya mama Briana arudi. Sio kwa sababu alimtaka mama Briana, shida yake ilikuwa ni mtoto tu. Japokuwa dada alirudi nyumbani, lakini ukweli wa mambo sisi tuliendelea na mahusiano yetu kama kawaida.”

“Alipokuja kugundua tena dada yangu, ndipo Nyange aliponiomba niwe mke wake kihalali.” Leah aliendelea kusema kwa ujasiri kabisa, akiwa ametulia hapo kizimbani. 

“Haikuwa siri, Nyange alitoka kazini, na kunikuta nikiwa na mama yangu mzazi na watu wote tuliokuwa tukiishi nao pale ndani, akaniomba niwe mke wake. Sikukataa kwa kuwa wakati ule dada yangu alikuwa mgonjwa na walisema asinge pona, na HATA hivyo Nyange alikuwa mpenzi wangu wakutokea zamani ila dada yangu Penninah ndiye aliyemdanganya Nyange tokea mwanzoni na kumlazimishia ndoa ya kanisani.” Leah alianza kulia kwa uchungu. 

“Niliumia sana. Lakini niliamua kusamehe kwa kuwa wakati huo dada ndiye alikuwa na pesa, kwa hiyo alikuwa akimuhonga pesa nyingi sana mpenzi wangu Nyange, mpaka akafaulu kumchukua. Walipofunga ndoa, ndipo Nyange alipogundua madhaifu mengi ya dada yangu na kurudi kwangu kuniomba msamaha.”

“Mwanzoni nilikataa kurudiana na Nyange, kwa kuwa tayari walikuwa na mtoto mmoja. Lakini Nyange alinisihi sana na kunibembeleza turudiane kuwa wapenzi, kwa kuwa na mimi nilikuwa nikimpenda, nilimsamehe, tukaendelea na mahusiano yetu akiwa bado kwenye ndoa.”

“Alitaka kumuacha mkewe kabisa, lakini nikagundua dada tayari alikuwa mjamzito na alikuwa pia akisumbuliwa sana na pressure. Nikamshauri Nyange asimuache wakati ule kwa kuwa isingekuwa vizuri kumuacha akiwa mjamzito tena mgonjwa.”

“Sasa safari hii mama Briana alipougua na ikasemekena hatapona tena, ndipo Nyange mwenyewe akasema huo ndio wakati wakutimiza ndoto yetu. 

Ndipo akaniomba tufunge ndoa mahakamani.” Mama Briana na Nyange walishituka sana pale Leah alipotoa cheti chao cha ndoa. 

“Kwa hiyo, na mimi Nyange ni mume wangu kihalali na cheti chetu cha ndoa anacho hapo mwanasheria wangu.” Ni kweli, ikathibitika kuwa Leah na yeye ni mke halali wa Daudi Nyange. 

Milio ya picha tu ndio iliyokuwa ikisikika mahakamani hapo wakati cheti cha ndoa cha Leah na Nyange kikipitishwa kwa Hakimu pamoja na waamuzi wa kesi hiyo. Nyange aliinama.

Mahakama ilikuwa ikufurika watu, siku za kusikilizwa kesi hiyo. Magazeti yaliandika kisa hicho cha kusisimua na kila mtu aliongelea mkasa wa Leah na dada yake. Leah alisha jiandaa kuliko walivyodhani. 

Na kweli alitafuta mwanasheria mzoefu aliyekuwa akijua anachokifanya. Mwanasheria huyo alitoa ushahidi wakutosha na wakueleweka akimtetea Leah. 

Walitoa uthibitisho wote, kuanzia wa sauti ya Nyange waliyokuwa wame mrikodi akiongea na mwanasheria, mikataba aliyosaini Nyange mwenyewe na picha zao za harusi ambayo haikuwa na watu wengi isipokuwa marafiki wachache wa Leah pamoja na mama yao, mama Eliah.

Mwanasheria anayesimamia kesi ya Leah alihakikisha anasambaza picha hizo za harusi mahakamani hapo, akahakikisha zinamfikia Nyange na mkewe sehemu waliyokaa mahakamani hapo. Kwa uthibitisho ule aliokuwa umetolewa, hata mtu asiye kuwa mwanasheria haikuhitaji ushahidi mwingine kuonyesha kwamba ni kweli Nyange alikuwa au yupo kwenye mapenzi ya kweli na Leah ILA Mama Briana ndiye kipingamizi.

 Harusi ya Leah+Nyange

Siku hiyo ya harusi yao ambayo walifungia mahakamani, Nyange na Leah walionekana wamependeza sana kwenye hizo picha. Japokuwa Leah hakuwa amevaa shela lakini alivaa nadhifu sana na uzuri wa umbile na sura aliyokuwa amejaliwa na Mungu, ni kweli Leah alikuwa amependeza pichani. Nyange naye alivalia suti nzuri ambayo hata mama Briana alishindwa kuitambua pichani. 

Ukumbi wa shere ya harusi hiyo ulikuwa mdogo, lakini ulikuwa umepambwa kwa hali ya juu. Ulijazwa maua ya rose kila mahali, vyakula na watu waliokuwa wakihudumia hapo, pichani, ilionekana iliwagarimu pesa nyingi kufanikisha harusi yao. 

Walionekana wakicheza mziki pamoja, na kulishana keki, tena Nyange akionekana pichani, anafurahi afanyalo. 

*********************

Ushahidi wote aliotoa Leah ulionyesha Nyange hakuwa na tatizo lolote la akili au hakuwa kwenye msukumo wowote mbaya uliompelekea kumuoa Leah na kumkabidhi mali zake zote isipokuwa mapenzi tu. 

“Kama kweli Nyange alikuwa amechanganyikiwa, aliwezaje kutafuta ofisi za wanasheria na kujieleza vizuri kwa kiasi hicho mlichomsikia kwenye rikodi zake, huku akitaja mali zake zote? Mmemsikia mwanasheria mwenzangu aliyefuatwa na Nyange tena amethibitisha Nyange alifika ofisini hapo akiwa peke yake bila Leah tena zaidi ya mara mbili kubadilisha mikataba hiyo.”

“Mara nyingine alifika kwenye ofisi zetu na mwanasheria wa kampuni aliyokuwa ameingia nao mkataba wa nyumba yake nyingine aliyokodisha kwa biashara. Mmemsikia hapa Nyange mwenyewe akiamuru kuanzia hati mpaka malipo yote yahamishiwe kwa Leah kutoka kwa mwanamke aliyekuwa mke wake {Penninah}, ambaye alikuwa hospitalini Mirembe, akisumbuliwa na tatizo la akili.”

“Bwana Nyange alisema na kutoa hii barua ya hospitali kuwa mkewe Penninah hawezi kulea watoto, wala hana uwezo wa kusimamia tena mali hizo kwa kuwa amekuwa kichaa kabisa, kwa hiyo ameonelea mkewe Leah, mdogo wa mke wake ndiye atakuwa sahihi kusimamia mali hizo, kwani yeye ndiye mtu waliyeanza naye maisha tokea mwanzo.”

“Naomba kwa mara nyingine tena, tusikilize sehemu fupi tu ya mazungumzo ya bwana Nyange na mwanasheria mwenzangu akiwa ofisini kwetu. Hatuta rudia mazungumzo yote, naomba turudie kwa kifupi tu, kuweka msisitizo.” Hakimu alikubali na ile rikodi ikawashwa tena. Nyange alisikika akiongea vizuri na kiuhakika. 

‘Leah ndiye anayenifahamu vizuri tokea mwanzo kabla ya aliyekuwa mke wangu, Peninnah. Na amedumu na mimi miaka yote. Anajua jinsi nilivyohangaika, kutafuta hizi mali zote. Na yeye ndiye alikuwa akiwalea watoto wangu hata pale mke wangu aliposhindwa kumudu kuendesha familia yetu sababu ya kazi zake nyingi.”

“Mke wangu alikuwa ni mtu wakusafiri sana akitafuta pesa. Hakuwa akinijali mimi wala watoto. Aliweka pesa mbele kuliko familia. Lakini Leah alikuwa radhi kuacha kazi na kuja kukaa na mimi na watoto wangu.”

“Leah alijua nina kula nini, na nina vaa nini. Anahangaika sana hata na watoto wa dada yake kama ndiye yeye aliye wazaa, tangia dada yake yupo anahangaika na kutafuta pesa.’ Nyange aliendelea kusema.

‘Najua hata Leah akibaki na mali zote, atatunza tu watoto wangu kwani yeye ndiye aliyekuwa akiwalea tokea wapo wadogo sana, walipokuwa wakiachwa na mama yao.’’

*********************

Mahakama nzima ilibaki kimya ikimwangalia Nyange na mkewe Penninah. Wote walikuwa wameinamisha vichwa chini, Nyange akishikilia cha kwake kana kwamba kisiangunge. 

Mwanasheria wa Leah aliendelea. “Hayo yote alikuwa akiongea bwana Nyange na ushahidi wote mnao. Mmemsikiliza wenyewe bwana Nyange akijieleza kwa ufasaha kabisa. Je hapo mlipo msikiliza, anasikika kama mtu aliyechanganyikiwa? Na je, picha mlizoona za harusi yake na Leah, mmemuona ni mtu ambaye hakuwa na furaha na amelazimishwa ndoa?” Kimya ila minong’ono ilizidi pale mahamani kwa washuhudiaji.

Hakuna kesi iliyokuwa NGUMU kuisimamia kama kesi ya Nyange. Mwanasheria wa kina Nyange alibaki kimya kabisa akisubiria maamuzi ya mahakama, akijua wazi mwishowa kesi hiyo ni nini.

Mara aliona anapewa kikaratasi kutoka kwa mama Briana. ‘Naomba uombe mahakama ituruhusu mtu mmoja aje atoe ushahidi.’ Akiwa hana uhakika sana, yule mwanasheria alisimama kwa haraka kabla Hakimu hajatoa maamuzi akiomba na wao walete shahidi wao. 

Kwa kuwa ilikuwa ni haki yao kisheria na wao kutoa ushahidi, Hakimu aliahirisha kesi na kutoa tarehe nyingine ya kusikilizwa kesi hiyo. 

 *********************

Watu walianza kutoka mahakamani hapo lakini Nyange na mkewe walibaki wamekaa. Mwishowe Nyange alitoka pale mbele alipokuwa amekaa na mwanasheria anayesimamia kesi yao na kumsogelea mama Briana. 

*********************

Sam naye alikuwa amekaa kiti cha mwisho kabisa, kwa kuwa alikuja kwa kuchelewa. Walimkataza Sonia kuhudhuria mahakamani tena. Kwani siku zote alizokuwa akihudhuria mahakamani hapo, Sonia alikuwa akilia sana, kitu kilichokuwa kikimuogopesha Sam, na kuhofia kinaweza kuibua pressure kwa Sonia, na kupoteza mtoto wao. 

Kwani kila siku walipokuwa wakifika mahakamani hapo, Leah alikuwa akitoa ushahidi uliowafunga mdomo kabisa upande wa kina Nyange. Sam alisha muomba mama Briana na Nyange kutokumwambia Sonia ukweli wote kila wanapotoka mahakamani. Kwa hiyo mara zote kila walipotoka mahakamani walimwambia Sonia mambo yanaenda vizuri. 

*********************

Sam akawasogelea Nyange na mkewe, alimuona Nyange ameinama akiwa analia. Mama Briana alibaki kama amemwagiwa maji. “Pole sana kaka.” Mwanasheria wao akawasogelea akiwa na sura ya hasira sana. “Umeharibu kabisa bwana Nyange! Mlipofika ofisini kwangu siku ya kwanza kabisa, niliwaomba mnieleze kila kitu bila kuficha. Kwa nini hukuniambia kama mlifunga ndoa na Leah?”

“Na mjue hapa sio mnaharibu kesi yenu tu kwa kuficha ukweli, bali mnaniharibia kazi yangu pia. Mnachafua jina langu. Sipendi kufanya kesi ambazo nashindwa kuzitetea hata kidogo. Kila tunapofika hapa, tunakutana na jambo jipya kabisa ambalo hamkuwahi hata kunigusia!”

“Mungu wangu nishahidi, na mimi ndio nasikia leo kama nilimuoa. Maneno yote mliyoyasikia nyinyi leo nikiongea na kuapa, na mimi ndio kwa mara ya kwanza, nayasikia hapa leo! Kama nisingeitambua sauti yangu, ningekana kama sikusema. Sina sababu ya kuongopa Mkuu.” Uso wa Nyange ulijaa machozi, aliogopa hata kumwangalia mama Briana. Hofu ilikuwa imemkamata Nyange, asijue maisha yake ya ndoa yatakuaje baada ya kutoka mahakamani hapo. 

 *********************

Kwa mara nyingine tena, siku hiyo Leah alitoa ushahidi wauhakika ambo hata kama mama Briana anampenda vipi Nyange, kila mtu alijua mambo hayatakuwa kama yalivyokuwa zamani kati yao. ‘Mama Briana atajua nilihusika kumfanya kichaa ili niwe na Leah! Atajua labda Leah baadaye alinigeuka.’ Nyange aliwaza huku akiendelea kutokwa na machozi. 

Na kwa kuwa kesi yao ilikuwa ya mwisho kusikilizwa siku ile, walijikuta wamebaki wao wenyewe mahakamani hapo. ‘Mungu wangu nisaidie. Siwezi kupoteza mali na Penninah.’Nyange alijikuta akiomba kwa sauti ya chini sana, huku ameinamisha kichwa chake chini, akilia. 

 *********************

“Nishahidi gani mwingine mlisema mnaye?” Mwanasheria wao alivunja ukimya. “Yupo mtu alikuwa akiishi na sisi tokea zamani. Ameshuhudia mambo mengi sana yaliyokuwa yakiendelea nyumbani kwetu, labda anaweza kutusaidia.” Mama Briana alijibu kinyonge sana, wazi alionekana ameshakata tamaa. 

Mwanasheria wao alinyamaza kwa muda wazi akionekana kusita. “Unamaanisha ni ushahidi wa mdomo tu au ana…” Aliulitupia swali jingine, lakini akasita kama ambaye alishapata jibu lake, akaamua aache tu kuendelea kuuliza. Wote walinyamaza. Mwishowe walitoka nje ya mahakama. 

*********************

“Hebu tuambie tu ukweli, Mkuu. Unaonaje?” Sam alijaribu kudadisi. “Ukweli hii kesi ni ngumu sana, kwa kuwa Leah anaonekana anaushahidi wa uhakika. Anaonekana alishajipanga tokea siku ya kwanza anaingia kwenye maisha yenu, na mbaya zaidi, mmeona jinsi anavyotoa ushahidi mpya na wa uhakika kila siku.”

“Kwetu inakuwa ngumu kujipanga kwa kuwa muhusika au Nyange mwenyewe hana kumbukmbu yeyote ya mambo ya nyuma! Ndio maana kila tukija hapa, kila kitu kinakuwa kigeni tunashindwa kujitetea kabisa.”

“Lakini hakuna cha kupoteza kama tukitupia hiyo karata yetu ya mwisho. Kwa kuwa tumepewa muda mrefu, mjiandae pale mtakapo weza, mumlete huyo shahidi naye tuone atatufikisha wapi.” Wazi kulionyesha hakuna tumaini, lakini Sam aliwatia wote moyo. 

“Nashauri tuendelee tu msikate tamaa. Naelewa jinsi ilivyokuwa ngumu kwako Mkuu, lakini naomba utuvumilie tu. Huwezi jua.” “Sawa Sam.” Waliagana, Sam alirudi kazini na Nyange na mkewe walipanda kwenye gari ya Sonia kurudi nyumbani. Njiani mama Briana alikuwa akiendesha akiwa kimya na alionekana mwenye mawazo, kitu kilichomuogopesha zaidi Nyange. 

 *********************

Mama Briana alibadilika kabisa. Ujasiri ulimwishia, alibaki na hukumu tu moyoni. Picha ya Leah na Nyange wakifunga ndoa ilimtesa sana, kana kwamba ndio mara ya kwanza kujua Nyange alikuwa na mahusiano na Leah. 

Haikuhitaji mtu kuambiwa kinachoendelea moyoni mwake, uso wake ulionyesha kushindwa kabisa. Alijilaumu sana kutokumsikiliza Nyange kipindi kile alipokuwa akimbembeleza aache kazi na kukaa nyumbani kwa muda ili alee watoto. 

Alikumbuka vile alivyokuwa akimwacha Briana kwenye mikono ya wasichana wa kazi wabaya, waliokuwa hawamjali kabisa Briana na kumpelekea Briana kuwa kama ana kwashakoo huku yeye akikimbizana na kazi za ofisini kwao. 

Maneno ya Nyange akimbembeleza na kumuomba angalau basi achukue likizo ya mwaka mmoja bila malipo ili angalau atulie nyumbani, amlee Briana mpaka watakapo pata msichana mzuri wakumlea mtoto au angalau Briana akue kidogo, yaliendelea kujirudia akilini mwake mara kwa mara. 

‘Nikweli nilimkaribisha Leah kwenye ndoa yangu mimi mwenyewe! Sasa hivi si mdogo wangu tu, ni mke mwenzangu pia! Tena kihalali! Sina thamani tena kwa Nyange kama niliyokuwa nayo zamani. Nyange alivumilia mpaka akachoka. Makosa ni yangu.’

Mama Briana aliendelea kuteseka na mawazo huku akiogopa hata kutoka kutafuta kazi tena. Alibaki akifanya kazi za mle ndani kama punda, huku akisaidiana na Sonia, kwani mama Sonia alishaanza kazi kwenye saluni yake kusaidia kuongeza kipato hapo ndani. 

Mama Briana ndiye alipeleka watoto shule na kuwachukua. Alifanya kazi zote za hapo ndani huku akimsisitizia Sonia kupumzika. Na kweli ilipokuwa ikifika usiku mama Briana alikuwa akichoka sana. Akijitupa kitandani, hageuki mpaka asubuhi. 

Kula yake ikaanza kuwa ya shida kwa mawazo na kazi nyingi. Na hapo ndipo taarifa za kuwa wamefilisika ndipo zilipokuwa zikimuingia vizuri akilini. Hakuwa na msaidizi yeyote, kwa hiyo alifua nguo zote yeye mwenyewe kwa mkono yake, maisha aliyokuwa ameachana nayo muda mrefu sana. 

Yeye ndiye aliyekuwa akideki nyumba nzima, kazi aliyokuwa akifanyiwa na Josh na kupika chakula cha watu wote mle ndani. Lakini hayo siyo yaliyokuwa yakimtesa moyoni hata kidogo. Mama Briana hakuwa mvivu. Kilichokuwa kikimuumiza ni kuwepo kwa mwanamke mwingine kwenye maisha ya Nyange, tena kihalali kama yeye. 

 *********************

         Nyange   naye hakuweza hata kumtizama mkewe. Alimkwepa kwa kadiri ya uwezo wake. Aliingia chumbani kulala baada ya kuhakikisha mkewe amepitiwa na usingizi kabisa.

               Asubuhi aliamka mapema kufanya mazoezi na Sam. Alijitahidi kufanya mazoezi sana ili arudishe afya yake kwa haraka aanze kufanya biashara, angalau atoke pale ndani. Alianza kukimbia na kunyanyua vyuma kama Sam. 

               “Kaka naona kama unazidisha!” “Najitahidi Sam. Lazima nipate nguvu haraka nitoke humu ndani na mimi nikatafute pesa.” Walipokuwa wakiachwa wenyewe hapo ndani ya nyumba, Nyange alishinda nje akitengeneza mazingira kumkwepa mama Briana ndani.

               ‘Sio kosa la Peninnah kutonisamehe. Nimemuumiza sana mke wangu.’Nyange aliendelea kuwaza. ‘Mungu nisaidie nisimpoteze mke wangu.’  Alianza kumuhurumia mkewe kwa kazi nyingi alizokuwa akifanya mle ndani, peke yake bila msaidizi. 

               Nyange alianza kumsaidia mkewe kufua nguo chafu. Kila mkewe alipotoka kuwapeleka watoto shule, Nyange alikusanya nguo zao zote chafu na kuzifua. Waliendelea kukwepana bila kupata muda wa pamoja wamazungumzo. 

 *********************

Shahidi wa Nyange alikuwa ni mama Sonia peke yake. Siku zilizidi kwenda huku Nyange akijishauri kama aendelee na hiyo kesi au aache tu na kutafuta mali kwa njia nyingine. Lakini kadiri siku zilivyozidi kwenda ndivyo mahusiano yake na mkewe yalivyozidi kuwa mabaya, ndipo Nyange akaamua kurudi tu mahakamani kwa msaada wa mama Sonia, pengine wangefanikiwa kurudisha mali zao, na kumfurahisha mkewe. 

Japokuwa kwake yeye ilikuwa nikujidhalilisha sana kuwepo mahakamani, lakini alikubali kuendelea kudhalilishwa na Leah mahakamani ilimradi aponye ndoa yake. ‘Nikimpoteza Penninah ndio nimepoteza watoto wangu wote. Briana hawezi kukaa mbali na mama yake hata kidogo.’ Nyange alizidi kuwaza. 

‘Mungu wangu nisaidie. Siwezi kupoteza wazazi na familia yangu pia.’ Ilimbidi Nyange aombe kuongea na Mama Sonia. 

*********************

Mama Sonia alirudi kutoka kazini kwake akiwa amechoka sana, lakini alikubali kukaa kuongea na Nyange. “Naomba unisaidie kuwa shaidi yangu mahakamani. Mambo yamebana sana mama Sonia. Nisadie, hali ni mbaya.” “Ulitaka nifanye nini?” “Ukaelezee vile ilivyokuwa, kuanzia mwanzo mpaka mwisho. Tafadhali sana mama Sonia, nisaidie.”

“Mimi nimeshindwa kuongea chochote, kwa kuwa sina kumbukumbu na chochote kile. Kila siku nakutana na mambo mapya mageni tena ya aibu tupu. Nisaidie tafadhali. Nampoteza mama Briana.” “Huwezi kumpoteza Peninnah hata iweje.” “Safari hii ni mbaya Mama Sonia. Leah ameleta ushahidi kuwa mimi ni mume wake.” “Mume!?” Mama Sonia alishituka sana. 

“Kabisa. Tena kihalali. Kumbe tulifunga na ndoa bwana! Sina habari! Kaleta cheti cha ndoa, picha za harusi tuliyofunga, na anasema na video pia anayo ya siku hiyo ya harusi! Mama Briana anashindwa hata kunisemesha kabisa! Tangia siku ile naona amebadilika sana. Nisaidie mama Sonia, labda nitaokoa mali zangu, na pengine mke wangu hatanikimbia.” Mama Sonia alikaa vizuri. 

“Wewe umekaa na mkeo muda wote Nyange, unamjua tabia yake vizuri. Shida ya Penninah ni wewe, wala sio mali hata kidogo. Mama Briana analia wivu sio mali. Anakupenda sana mkeo. Kitu cha kwanza kuuliza alipopata akili zake ni wewe. Tumemtoa Mirembe tumefika hapa, alikataa kabisa kula, wala kulala mpaka akuone.”

“Ilibidi kumleta kule kwenu, ulipokuwa ukiishi na Leah usiku usiku. Mama Briana hakujali ulivyokuwa ukionekana, alichokuwa akitaka upone, muwe wote.”

“Wote tulikukatia tamaa isipokuwa yeye. Alikuwa akishinda pembeni ya kitanda chako hospitalini, mchana na usiku akikuuguza.” Nyange aliumia sana. Machozi yalianza kumtoka huku akikumbuka ile rikodi ya maneno yake, waliyoisikiliza mahakamani. 

“Penninah anakupenda sana. Mali haziwezi kumfanya akakukimbia hata kidogo.” “Sio hiyo ndoa peke yake inayomchanganya mke wangu. Kuna mengine mengi yametokea huko mahakamani.” Mama Sonia alikunja uso. 

Nakuamua kuuliza. “Nini tena?!” “Kuna maneno niliyasema, Leah ameyarikodi.” Nyange akasita. “Maneno gani?” “Daah! Mungu nisaidie jamani!” “Ulisema nini Nyange?” “Ni maneno mabaya sana. Penninah hawezi kunisamehe tena. Na Mungu wangu ni shahidi mama Sonia, wala sikumbuki kuyasema hayo maneno. Lakini sauti ni yangu kabisa.”

“Nimemchafua mke wangu mbele za watu. Najua Penninah atajua nimipango nilifanya na Leah, kumchanganya yeye akili, ili aondoke pale ndani ili mimi nimuoe Leah, na labda atafikiri baadaye Leah alinigeuka. Lakini sio kweli. Nampenda sana mke wangu. Ni kweli nilifanya kosa kulala na Leah, lakini nampenda mke wangu. Akinikimbia Penninah, nahisi nitachanganyikiwa kabisa safari hii. Nisaidie Mama Sonia.” Mama Sonia alimuhurumia sana Nyange. Walikuwa wamekaa nje kwenye baraza ili mtu yeyote asiwasikie. 

Japokuwa mama Sonia alikuwa akiogopa sana kusogelea mahakama, sababu ya swala lake la uraia. Ilimbidi akubali tu, kwani Nyange alikuwa akihuzunisha sana. Alibaki akilia na kuvuta kamasi kama mtoto mdogo.  

“Nisaidie Mungu wangu, Penninah asinikimbie.” Nyange aliendelea kuomboleza. “Umepata muda wakuongea naye lakini?” “Naanzia wapi mama Sonia? Nasemaje? Nisaidie. Maana harusi ni kweli nimefunga na maneno ya kumchafua ni kweli nimesema. Sauti ni yangu kabisa, haina ubishi. Namuogopa, nashindwa hata kumuangalia mke wangu.”

“Sasa hapo ndipo unapoharibu kabisa Nyange. Unamkwepa tena wakati mwenzio yupo kwenye maumivu? Atajuaje kama hukumaanisha uliyoyasema? Au atajuaje kama yeye ndio mke wako halali na Leah ni mwizi tu?”

“Unataka kumfungulia Leah mlango mpaka kwenye moyo wa mkeo!? Umoja na mapenzi ya dhati mliyokuwa nayo na mkeo, ndio kitu pekee kilichokuwa kikimuumizaLeah na ndiyo nguvu kubwa mliyonayo na kubakiwa nayo. Mkipoteza hiyo, nakwambia ukweli Nyange, dunia utaiona chungu mara mbili ya hivi.”

“Pata muda ongea na mama Briana kabla hajafika mbali. Namjua mkeo roho yake ilivyo ndogo, ni kama Briana tu. Ni heri akose kila kitu maishani lakini sio wewe. Anaweza hata kujiua.” Kama aliyefunguliwa akili. Nyange akapata nguvu mpya. “Asante sana mama Sonia. Asante!” Nyange alikausha machozi, akanyanyuka haraka kuingia ndani kumtafuta mkewe. 

 Ndoa Takatifu!

Alianzia kumtafuta jikoni, akakuta jiko safi, alishasafisha vyombo vyote na kupiga deki, yeye hayupo. Alijua atakuwa chumbani kwao. Nyange alitoka haraka kama anayewahi kitu, moja kwa moja mpaka chumbani kwao. Akamsikia akilia bafuni. Akaumia sana. 

Aliingia bafuni na kumfunga taulo mkewe na kutoka naye nje. Tangia watoke mahakamani, Nyange ndio alipata nafasi yakumwangalia mkewe. Alikonda sana, na alionekana amechoka. “Pole Penninah. Pole sana.” Mama Briana alivuta chuka vizuri nakujifunika. 

“Nisamehe D. Naomba usiniache mume wangu. Nitakufa. Heri nipoteze kila kitu lakini sio wewe. Najua Leah ni mke wako pia, lakini niamini nakupenda, D. Nakiri nililemea kwenye kazi kuliko wewe na Briana, lakini nilikuwa kwenye wakati mgumu sana ofisini. Nakuahidi nitabadilika, D. Hata kazi sitatafuta tena, nitakaa tu nifanye kazi za nyumbani. Nisamehe.” Mama Briana alikuwa akilia sana, kitu kilichomuumiza Nyange. 

“Nikuache niende wapi Penninah? Wewe unajua Leah anavyonichukia! Yote hayo ametufanyia makusudi ili achukue mali zetu, hakuna wala hapajakuwepo na mapenzikati yangu na Leah hata siku moja. Amechukua mali zetu zote, na sasa hivi anafanikiwa kututenganisha. Najua yale maneno yamekuingia mke wangu. Lakini naomba uniamini, sikuwa hata nikielewa nilichokuwa nikiongea.”

“Sijui amefanyaje yule msichana! Sijawahi hata kukulaumu kwamba umetutelekeza mimi na Briana, eti kwa sababu ya kazi! Mbona pesa zote ulizokuwa ukipata ulikuwa ukileta nyumbani? Nakupenda Penninah na wala sikudanganyi?” “Mbona sasa hujanigusa hata mara moja tokea upone? Tumetoka mahakamani hata hukukanusha jambo hata moja?”

“Nilikuwa sina nguvu kabisa. Sikuwa na uwezo wa kufanya mapenzi, Peninnah! Mpaka niliogopa nilijua Leah ameniharibu! Tulipotoka mahakamani nilikuwa nakuogopa. Niliingiwa na hofu! Hata kukuangalia nilikuwa nashindwa.” Mama Briana alikunja uso kama asiyeelewa. 

“Kwa nini?” “Nilijua utakuwa umekasirika kwa ile rikodi ya pale mahakamani na vile ulivyojua nilimuoa Leah!” Mama Briana alifikiria kidogo. “Nikuulize kitu D?” “Nini?” “Kati yangu mimi na Leah, unampenda nani? Naomba uwe mkweli tu, usinifiche.”Mama Briana aliuliza huku akilia sana. 

“Unawezaje kujilinganisha na Leah? Nasikitika sana ameweza kufikia moyo wako Penninah, na hilo ndilo lilikuwa lengo lake. Tafadhali mke wangu urudi. Umefika mbali sana, na umeniacha nyuma. Mapenzi yetu ndio ilikuwa nguvu yetu. Kama kweli leo umefikia kiasi cha kujilinganisha na Leah, basi ujue atakuwa amefanikiwa kwa kiwango kikubwa sana.”

“Ule uhakika uliokuwa nao zamani, kuwa nakupenda wewe kuliko mtu mwingine yeyote, nakuomba urudi Penninah. Tafadhali mke wangu. Leah ametuchezea mchezo mchafu sana, tusiruhusu akaingilia na mapenzi yetu. Nakupenda sana Penninah mke wangu. Naomba usiamini vinginevyo.” Mama Briana alifurahi sana, alianza kufuta machozi huku akitabasamu. 

“Umekuwa na kifua kama cha Sam?” Nyange alicheka. “Ninafanya naye mazoezi.” “Kwa hiyo umepona kabisa?” Mama Briana aliuliza kwa aibu. “Sijui. Labda umpeleke Brayan akalale na mama Sonia leo, ndio tujue kama nimepona au bado.” Nyange alijibu huku akicheka. Alimnyanyua mkewe kitandani nakuanza kumbusu.

“Umekonda kweli Penninah! Huli?” “Chakula hakiendi D. Nilikuwa naona unavyonikwepa, nikajua hunitaki tena.” Mama Briana alianza kulia. “Daah! Kumbe heri tungezungumza tu siku ileile. Mwenzio nilikuwa nakuogopa! Nilijua hutaki hata nikuguse! Huoni nilikuwa nalala mwisho kabisa.” Mama Briana alicheka huku machozi yakimtoka. 

“Nakupenda sana D.” “Nakupenda Penninah. Nimekosa mke wangu. Nilikosa haswaa. Nisamehe. Nakuahidi kila kitu kitakuwa sawa. Nitafanya kazi kwa bidii, tutarudia maisha yetu yale ya zamani, na sio kwamba sitaki ufanye kazi, nilikushauri wakati ule kwa kuwa mtoto alikuwa mdogo na hatukuwa na msaidizi.” 

“Nakuombea mume wangu. Najua tutafanikiwa tu.” “Basi mtoe huyu mtoto, tuone kama nimepona!” Mama Briana alianza kucheka. “Umeanza D.” “Sasa utajuaje kama nimepona?” “Si useme tu!” “Bila vitendo!? Ukidanganywa?” Angalau Mama Briana alianza kucheka. 

Alimbeba Brayan mpaka chumbani kwa mama Sonia. “Nilijua tu nitaletewa mwanangu leo. Hapa nilikuwa nahesabu dakika. Nilikuwa nahamu naye kweli!” Mama Briana alianza kucheka. “Nyange huyo!” “We nipe mwanangu nilale naye. Asubuhi nitawaamsha niwaandae kwenda shule. Wala usihangaike kuamka mapema. Pumzika. Nitamwambia Sonia awapeleke shule.” 

“Mwanafunzi wangu unataka kumwingiza barabarani akiwa peke yake?” “Si ameshapata leseni? Sasa ataanza kuendesha lini akiwa yeye peke yake? Ndio mazoezi yenyewe hayo.” “Sam hataona namsumbua mkewe?” “Wewe usijali. Akiona usumbufu atawapeleka yeye mwenyewe huyo Sam.” Mama Briana alicheka na kurudi chumbani kwao kwa haraka. Alimkuta Nyange akimsubiri kwa hamu. 

*********************

“Mbona umechelewa kurudi!?” “Nyange wewe! Dakika moja tu hapo, nimechelewa?” “Hivi unajua ni miaka mingapi sijafanya mapenzi?” “Si ulikuwa na Leah?” Nyange alinywea mwili mzima, mama Briana alijua na kujilaumu sana. 

“Daah!” “Samahani D.” “Nikuombe kitu Penninah?” Mama Briana alizidi kujilaumu kumtaja Leah katikati ya wakati mzuri wa mapenzi waliyokuwa wakiyatizamia kwa hamu. “Samahani D.” “Nakuomba sana mke wangu, usinitajie tena Leah, hasa tukiwa kwenye wakati kama huu. Utaniadhibu kuliko unavyofikiria.” “Samahani D. Samahani sana.” 

“Na nikwambie ukweli?” Mama Briana alipooza sana. “Unakumbuka mara ya mwisho tulikuwa bafuni tukioga mimi na wewe, tulifanya mapenzi sana siku ile tulianzia chumbani tukahamia na bafuni? Tena mama yako na Leah walikuwepo? Baada ya hapo tukashuka chini kwenda kunywa chai ndio ukaanza kuumwa?” Mama Briana aliishiwa nguvu alishindwa hata kujibu, kwani alimuona jinsi Nyange alivyoishiwa nguvu na kunywea kabisa. 

Ile sura ya furaha ya Nyange aliyokuwa nayo muda mchache uliopita, ilipotea kabisa, akapoteza ujasiri wote na kubaki akijitetea kama mtoto mdogo. “Mungu wangu ni shahidi Penninah, sikumbuki kufanya tena mapenzi. Wewe ndio kumbukumbu yangu ya mwisho.”

“Sikumbuki hata kulala kitanda kimoja na Leah! Na samahani kusema hivi, namuomba Mungu mchana na usiku hizo kumbukumbu zisiwahi kutokea akilini mwangu kabisa. Kitendo tu cha kuwa niliishi na Leah nyumba moja hasa baada ya kifo cha Junior, na kuwatesa wanangu, kinanimaliza nguvu zote. Sitaki hata kufikiria kama nilikuja kufanya naye tena mapenzi.”

“Najua nilikosea Penninah, nikamkaribisha Leah kitandani kwetu, lakini naomba tusimkaribishe tena kwenye mapenzi yetu.” “Nimeelewa D. Samahani sana.” Nyange alimvuta karibu mke wake, akamfunika shuka vizuri, wakalala usiku huo bila yakufanya mapenzi tena.  Mama Briana alibaki akijilaumu sana. 

 *********************

         Mama Briana aliibua hofu mpyaa ndani ya Nyange. Siku zilizidi kwenda Nyange akishindwa kabisa kufanya mapenzi na mkewe. Alianza kushituka usiku akidhani amelala na Leah. Aliishia kulala sebuleni akiangalia tv kwa hofu. 

Kila mama Briana alipomgusa, aliruka kana kwamba anataka kubakwa na kupoteza usingizi kabisa. Nyange alikesha akijiwinda, nakujikumbusha yule ni Penninah sio Leah, bila mafanikio. ‘Nimepona bwana! Hizi ni akili zangu kabisa na haya ndiyo maisha ya kweli. Leah hayupo humu ndani.’ Nyange aliendelea kujikumbusha kila wakati, lakini bado alihisi bado amefungwa akili zake, ile sura ya Penninah, ni Leah mwenyewe anamchezea akili zake. 

Alianza kuwa kama anachanganyikiwa, ikitokea analala usiku na mama Briana, hushituka usiku na kumwangalia mkewe kwa muda mrefu sana na kufikicha macho akitaka kuhakikisha anachoona ni kweli au bado ni mazingaombwe ya Leah. 

Aliishia kutokulala kitandani na kukimbilia kwenye makochi kila siku huku akijiwinda sana, asiguswe suruali yake. ‘Asije kuwa ni Leah anafanya mapenzi na mimi.’ Nyange aliendelea kuteseka na kushindwa hata kumgusa mkewe kimapenzi. 

 *********************

Kwenye hiyo nyumba ya Sam mengi yalikuwa yakiendelea. Mama Sonia naye kadiri ukweli ulivyokuwa ukimuingia kuwa atasimama mahakamani, alishindwa kula wala kunywa kwa HOFU. Hakutaka kabisa kujihusisha na mambo ya kiusalama kwa ajili ya uraia wake. 

Alijua Leah anajua fika kama yeye sio raia wa Tanzania, na yupo hapa nchini isivyo halali, alijua lazima Leah atatafuta kila mbinu yakumfanya siku hiyo mahakamani ashindwe kuongea. Sonia alimuona mama yake hana raha, akaamua kumuuliza. 

“Kuna nini mama? Mbona kama huna raha?” “Hamna kitu Sonia. Usiwe na wasiwasi. Wewe jiangalie tu afya yako.” “Naomba usiwe kama Sam, mama bwana! Kwani mimba ugonjwa? Ananificha kila kitu!” Sam alishaongea na mama Sonia, akamuomba asimwambie Sonia kama atakwenda kutoa ushahidi mahakamani. 

“Niambie mama. Kuna nini?” “Kwanza niambie kliniki wamewaambia nini?” “Sam anaharaka kweli! Sijui amekutana na nani amemshauri nianze kliniki mapema. Amekuja kunichukua hapa, tumefika hospitalini, wamenipima kila kitu kipo sawa! Damu ninayo yakutosha na wanasema mtoto anaendelea vizuri.” Sonia alianza kucheka. 

“Nini?” “Tumeonyeshwa leo mtoto wetu. Sam kafurahi kweli! Anazunguka na picha yake kila mahali.” Mama Sonia alicheka. “Mmeshajua ni mtoto gani?” “Nimekataa. Sitaki kujua mpaka siku anazaliwa.” “Mwenzio amesemaje?” Mama Sonia alizidi kudodosa taratibu. 

“Wewe si unamuona Sam alivyo changanyikiwa na huyu mtoto? Hajali kabisa jinsia. Anasema mtoto ni mtoto.” “Hongera.” “Asante mama. Mwenyewe nimefurahi kweli kuona nabeba mimba ya mtoto anayekuja kwenye mazingira mazuri, sio kama Kana mwanangu. Tulimlea kwenye mazingira magumu kweli! Nashukuru mama kwa kunisaidia wakati ule. Nilikuwa sielewi chochote, nilikuwa naogopa sana.” Sonia alianza kulia. 

“Usianze kulia sasa, mumeo atakuja sasa hivi!” Walianza kucheka. “Asante mama.” “Japokuwa nilikuwa nimekasirika sana, lakini nilimshukuru Mungu kutupa Kana.” Waliendelea kukumbushana maisha yao wakiwa wamekaa peke yao, huku wakicheka na kulia. 

Sonia alifanana sana na mama yake. Na kwa kuwa mama yake hakuwa na mwili mkubwa, wengi walisema ni mtu na dada yake. Walijaliwa wote urefu, rangi zinazofanana, na maumbile mazuri. Ukiwa na haraka unaweza kusema ni mapacha. 

“Lakini hujaniambia ni nini kinakusumbua mama!” “Nyange ameniomba kwenda kutoa ushahidi mahakamani.” Sonia alitulia kidogo akijaribu kuelewa tatizo lilipo.

“Lakini naogopa sana Sonia. Nahofia Leah asije kuibua mambo yangu ya uraia.” “Kweli mama! Au niongee na Sam usiende?” “Nimeshaongea na Sam, anasema hali ni mbaya sana. Leah anatoa uthibitisho unao aminika.” “Kama nini? Maana Sam hataki kabisa tuongelee mambo ya mahakamani. Sijui ni kwa nini? Kila nikimuuliza, ananiambia mambo yanaenda vizuri. Nahisi pia ameongea na mama Briana. Maana majibu yao yanafanana. Watakuwa wananificha.” 

“Sam anahofia sana afya yako.” “Afya gani jamani! Mbona mimi mzima tu!” “Alituomba tusikwambie kitu chochote. Alisema usije ukaanza mambo ya pressure ya mimba kama alivyosumbuka mama Briana wakati mjamzito.” “Jamani Sam! Mbona mimi ni mzima tu! Wewe niambie mama.”

“Halafu uanze kulia hapa, Sam aje tugombane?” Sonia alianza kucheka. “Silii mama bwana! Wewe niambie.” “Hapana Sonia mimi nakujua wewe. Ila ujue tu nilazima niende nikawasaidie hawa watu.” “Naogopa mama!” “Hata mimi naogopa kweli! Lakini hawana mtu mwingine wakuwatetea Sonia. Nisipo enda mimi, nani atawatetea?” Sonia na mama yake walibaki wakiwaza usiku huo wakuamkia siku ya kwenda mahakama. 

“Ngoja niende tu Sonia liwalo na liwe. Hawa watu ndio wametufikisha hapa tulipo. Wametulipia gharama kubwa sana. Pengine bila Sam sasa hivi tusingekuwa na Kana, na mimi ningekuwa nimeshakufa.”

“Unakumbuka nilivyokwambia niliugua sana, nikawa nipo tu nyumbani mpaka Sam alipokuja kunipeleka hospitali? Haya usisahau Sam alivyookoa maisha ya Kana!” “Siwezi kusahahu mama. Ndio maana nipo hapa leo na Sam. Kila nikifikiria aliyonifanyia huyu kaka, nashindwa hata kumfikiria mwanaume mwengine.”

“Walikuwa wakinifuata wanaume wengi kweli wakati nilipoondoka wakati ule, lakini ile picha ya siku ile Sam amenikuta sokoni nauza chakula, tena nikiwa nimechoka na kukata tamaa, akayajua maisha yetu yalivyo duni, halafu akaja kujua tena historia yangu ya kubakwa na kumpata Kana lakini bado akanipenda na kunithamini!”

“Haya akaniweka kwenye maisha ya mama Briana. Ona huyu dada alivyonitunza mama! Alikuwa akinifanyia mambo ambayo ni ngumu kwa mwanadamu yeyote kuingia akilini. Dada ananipenda sana, wewe ni shahidi mpaka shule wao ndio walikuwa wakinilipia ada na huku wanamsomesha Kana kwenye shule ya gharama vile na bado wakawa wakikulipa wewe mshahara!”

“Haya nikamtoroka Sam na bado alibaki na pete yangu kwenye waleti yake mama, akisubiri kuja kuirudisha tena kidoleni mwangu! Wakati alikuwa ameshafanikiwa sana kimaisha na wanawake wakimsumbua mpaka leo, lakini bado Sam ananipenda na kubaki kuwa mwaminifu kwangu!”

“Ona Nyange na mkewe wanavyo tufuatilia mimi na Sam. Siwezi kuwasahahu hawa watu, mama. Ni kweli ulivyosema kutoa huo ushahidi ndio itakuwa njia pekee yakuwalipa.” Sonia na mama yake wote walikuwa wakitokwa na machozi. 

“Nisiporudi Sonia uni….” Mama Sonia alianza kutoa wosia huku akitokwa na machozi. “Utarudi mama. Usiwe na wasiwasi.” “Naweza nisirudi Sonia!” “Siwezi kukuacha mama. Hata wakikurudisha Rwanda, nitakufuata. Kwani Rwanda ni kuzimu? Siwezi kuishi bila wewe mama yangu. Nitafanya kila niwezalo tuwe wote.” 

“Huwezi Sonia, wewe ni mke wa mtu sasa, na ninamuona jinsi Sam anavyokupenda na kumfurahia huyo mtoto. Hawezi kuruhusu uhamie Rwanda na mtoto wake.” “Usiwe na wasiwasi mama. Hakuna wakunitenganisha, mimi na wewe. Tutatafuta njia tuwe wote pamoja. Usiogope mama yangu.” Mama Sonia alinyamza kwani alijua kutokea kwake mahakamani ni kama kwenda kujikabidhisha yeye mwenyewe kwenye vyombo vya usalama, lakini hakuwa na jinsi nyingine yakufanya. 

 Siku Ya Mahakamani.

Siku ya mahakama ilifika. Mama Briana aliamka asubuhi, akapeleka watoto wote shule na kurudi nyumbani. Aliingia moja kwa moja jikoni kuandaa kifungua kinywa cha watu wote kabla ya kwenda mahakamani. Baada ya muda mfupi Sam naye alirudi toka kazini. 

“Mbona umerudi mapema?” Nyange alimuwahi Sam wakati anaingia ndani. “Nimeona nirudi niwe na Sonia leo mahakani.” “Kwani na Sonia anaenda?!” “Lazima aende. Anawasiwasi sana na mama yake kufika mahakamani. Na hali yake hiyo ya ujauzito, sitaki kumuacha peke yake.” Nyange hakuwa ameelewa. 

“Sijaelewa Sam. Tatizo liko wapi?” “Si mambo yale ya uraia wa mama yake. Anaogopa wasije yakatibuka huko halafu mama yake akaingia matatizoni.” “Daah! Nilisahau kabisa! Nimemuingiza mama wa watu kwenye matatizo!” Nyange alipooza gafla. 

“Naona tuache tu. Huyu mama asiende. Nishaharibu maisha ya watu wengi sana akiwemo Penninah, siwezi kuendelea kuharibu maisha ya watu wengine. Sonia na mama yake wamejitoa sana kwetu. Halafu ndio kwa mara ya kwanza maishani, maisha yamewanyookea! Wapo pamoja tena nyumbani kwao! Siwezi kuwapokonya hiyo furahayao hata kidogo.” Kumbe mama Briana alikuwa akiwasikiliza. 

“D! Naomba uniamini mpenzi wangu, sikulaumu kabisa. Na wala hujaniharibiamaisha.” “Unanitia tu moyo Penninah. Lakini ukweli upo palepale. Nimefilisi familia.” “Nakwambia ukweli D, usiwe na wasiwasi kabisa na mimi. Shida yangu ilikuwa nikupate wewe na ile nyumba BASI. Nakumbuka tulipotoka mimi na wewe. Mali zinatafutwa na tulichonacho mimi na wewe ni ngumu sana mtu yeyote kukipata.”

“Nilikuwa nikimwangalia Leah pale mahakamani na mali zetu zote alizo nazo, lakini haonekani na furaha hata kidogo. Amejawa na wasiwasi usoni, wakati angetakiwa afurahie maisha kwa pesa nyingi zinazoingia kwake. Nyumba zetu zote zinamwingizia pesa, ana uwezo wakuishi bila kufanya kazi yeye na huyo mtoto wen..” Mama Briana akakumbuka alivyoharibu mara ya mwisho, akanyamaza. 

“Sikukusudia kuzaa naye, mke wangu! Niamini nikikwambia sikuwa hata na habari wakati na lala na Leah, kipindi ulipougua. Mungu nishahidi.” “Ngoja kwanza D. Umegundua kitu?” “Nini?” “Mbona hamzungumzii huyo mtoto kabisa? Kama angekuwa na huyo mtoto ndio angemtumia sana pale mahakamani. Mtoto yuko wapi!?” 

“Sijui Penninah! Natamani hata tusimkumbushie mambo ya huyo mtoto, asije akaanza habari nyingine. Ingekuwa ni amri yangu, hiyo kesi ningefuta kabisa ili nisiwahi hata kuwa na yule msichana chumba kimoja maishani. Naogopa hata kumtizama!”

“Halafu leo aje aseme tuna mtoto naye! Unafikiri maisha yangu yatakuaje? Inamaana itabidi niwe naye kwenye maisha yangu yote. Mungu aniepushie hiyo adhabu. Adhabu yangu yakutoka nje ya ndoa, naona nimeilipia kupita kiasi na kupita mtu yeyote hapa duniani! Naomba Mungu anipunguzie hiyo adhabu jamani! Ni kubwa, na ni kali sana.”

“Hakuna siku inapita bila kuitubia hiyo dhambi. Kulala tena na Leah baada ya mke wangu kuugua, kumeathiri kichwa changu kabisa.” Mama Briana aliumia sana. “Kila nikimgusa mke wangu nahisi bado Leah ananichezea akili sio mke wangu ni yeye Leah.” “Pole D. Mungu yupo na sisi. Kila kitu kitakuwa sawa.” Sam alibaki akiwasikiliza na kuwahurumia sana. 

“Nina wazo D.” “Wazo gani?” “Badala ya kuingia tena mahakamani, naona mimi niongee na Leah tumalizane nje ya mahakama. Kwa ajili ya mambo mawili, kwanza kumuepusha mama Sonia kuingia mahakamani. Nitaumia sana chochote kikimpata mama Sonia. Ni mtu ambaye sitaki kuja kumpoteza maishani. Brayan anajua ni mama yake pia.”

“Halafu pili na wewe kukuepushia ile kero na aibu ya pale mahakamani. Nitamuomba Leah achukue kila kitu atupe ile nyumba tu, tulipomuweka Junior, siwezi kuacha kumbukumbu za Junior zipote hivi hivi.” “Akikataa?” Nyange akauliza akitaka uhakika. 

“Basi D. Tutamuamini Mungu kwa njia nyingine sio mahakamani tena. Kwanza kesi yenyewe ni kuendelea kujidhalilisha tu, hatuwezi kushinda. Leah alijipanga muda mrefu sana, ndio maana kila kitu alishokufanya ufanye alikuchukua video na kukurikodi kwa ushahidi. Mwenzetu aliziona hizi siku za mahakamani tokea hajatugeuza vichaa.”

“Leo ndio mwisho wa hiyo kesi D, tutawaambia tumesamehe kila kitu. Kwanza inatupotezea muda wa kuhangaikia mambo mengine. Tumeshindwa hata kuanza kufanya biashara waliyotupa kina Sam sababu ya kuwaza hiyo kesi! Tuachane nayo tu.” Walitulia kidogo. 

“Daah! Naogopa kabisa kusogea kwenye hiyo biashara ya Sam sababu ya mawazo yasiyoisha. Kila ninapokumbuka natakiwa kurudi tena mahakamani kudhalilika mbele za watu tena kwa ajili ya jasho langu, akili inavurugika kabisa. Nashindwa hata kufikiri chochote. Nikiwaangalia hivi nahisi kama nyinyi sio watu wa kweli, labda bado Leah ananichezea akili zangu, bado naishi naye.”

“Natamani kuachana na yule msichana moja kwa moja maishani labda akili yangu itakuja kupona.” Sam alimuhurumia sana Nyange. “Pole sana kaka.” “Daah! Nimeshikwa pabaya kweli mdogo wangu! Siwezi kulala, nahisi mama Briana ni yeye ananifanyia mazingaombwe tena.”

“Nashindwa kula, nahisi chakula kina dawa zake. Siwezi kuwaza jema wala baya! Naogopa kusogelea hata biashara yako Sam, najiambia nisije nikagawa tena. Nahisi bado nimefungwa akili zangu. Nipo kwenye mateso makali kupita ninavyoonekana!”

“Natamani mimi ndio angenigeuza kichaa na kunipeleka Mirembe, kuliko hivi ninavyoonekana nje nimepona kumbe ndio mgonjwa kupita mwanzo.” “Pole sana kaka. Lakini maisha lazima yaendelee. Lazima ukubali umepona na usonge mbele. Familia inakutizama wewe.” “Daah!” Nyange alibaki anawaza.

“Nikuombe kitu D?” “Sema tu.” “Leah ameshanipokonya vitu vingi sana maishani. Naomba asifanikiwe kututenganisha tena. Nitakufa. Siwezi kuendelea kuishi kama hivi tunavyoishi D. Huwezi hata kunikumbatia au kunibusu! Nikikushika unashituka, nikikubusu unatetemeka. Nitachanganyikiwa tena tukiendelea kuishi hivi. Sitaweza.”Mama Briana alianza kulia mbele ya Nyange na Sam. 

*********************

Kwa mara ya kwanza Nyange akapata ujasiri wa ajabu akamsogelea mkewe na kumkumbatia kwa nguvu sana huku akimbusu. Mwishowe waliamua kuhamia chumbani. “Kaka! Kaka!” Sam aliita, lakini Nyange alifika kwenye ‘Point of no return.’ Hofu tu ndiyo ilikuwa imemtawala sana, lakini alikuwa na hamu sana na Penninah. 

“Kaka! Tumebakiza muda mfupi sana tunatakiwa mahakamani.” “Kila kitu kitasubiri Sam. Nahitaji muda na mke wangu.” Nyange alijibu na kumbeba mkewe mpaka chumbani. Nyange alijifungia chumbani na mkewe kwa muda mrefu. Kila mmoja alikuwa na hamu na mwenzake. 

“Tutaendelea baadaye D. Twende tuwahi tukamalizane na hayo mambo ya mahakamani.” “Daah! Asante sana Penninah, hali ilikuwa mbaya!” Mama Briana alianza kucheka. 

“Nimefurahi sana. Nilikuwa na sononeka moyoni kupita kiasi.” “Pole mpenzi wangu. Usiamini vinginevyo wala usiwahi kujifananisha na mtu yeyote, Penninah. Nakupenda wewe.” “Asante D.” “Tukitulia, nitatafuta mwanasheria, anishauri jinsi yakufanya kuifuta hiyo ndoa ya Leah na tuibariki ndoa yetu tena, tutoe huu mkosi.” Mama Briana alifurahi sana. 

“Nitafurahi sana D, tubaki sisi wenyewe. Sio na Leah katikati yetu.” “Hajawahi wala hatawahi kuwa katikati yetu.” Mama Briana alijawa furaha kubwa sana. 

 Nguvu Ya Mapenzi

Walitoka wakiwa na sura za tofauti kabisa kama sio wao! Nyange yule wazamani akiwa tajiri, alirudi usoni. Ujasiri uliongezeka, na hofu ilimuisha kabisa. Waliamua kwenda wao wawili tu mahakamani, kumalizana na Leah bila kumuhusisha mtu yeyote. 

Wakati wanatoka, mama Sonia, Sam na Sonia walishangaa wanaondoka peke yao. “Mbona mnatuacha?” “Tumebadili mawazo, mama Sonia. Hatutaki kukuingiza matatizoni. Tunaenda kuongea na Leah nje ya mahakama, akikataa basi, tunafuta kesi.” Mama Briana alijibu. 

“Hapana. Nyinyi mnamjua Leah, hawezi kukubali kabisa. Naombeni nikajaribu bahati yangu. Acha nikaeleze kila kitu tuone kama hao wanasheria hawatanisikiliza. Tukishindwa safari hii ndio iwe basi. Lakini lazima na mimi nikajaribu, nitoe ushahidi wangu. Leah hawezi kuondoka na mali zenu zote.” Kila mtu alikaa kimya kwa muda wakiangaliana. 

Kisha Nyange akauliza. “Unauhakika Mama Sonia?” “Rwanda sio kuzimu. Nisehemu kama hapa. Wakimrudisha tutatafuta njia nyingine. Hakuna wakututenganishasisi wala watoto wetu.” Sonia alidakia akiwa na uhakika kabisa. “Asanteni sana. Naomba tuombeni kwanza.” Nyange aliongoza maombi kisha wakatoka wote watano wakiwa wamechelewa sana. 

Hakuna Aliyewahi Kutoa, Kumzidi Mungu

         Walifika mahakamani na kukuta watu wote walishaingia, wakisubiriwa wao tu. Hakimu alishaingia, lakini wao hawakuwepo. Wakati wanaelekea mlangoni wakiwa na haraka sana walisikia mtu akiita “Ishimwe!? Ishimwe?!” Kwa kuwa Sam, Nyange na mkewe hawakumjua Ishimwe ni nani, wao waliendelea kutembea kwa haraka kuelekea mlango wa mahakama, kasoro Sonia ambaye hakulisikia hilo jina kwa muda mrefu sana, isipokuwa kwa mama yake tu, alisimama kwa mshangao na mama Sonia naye aligeuka akitafuta anayemwita. 

“Paul?” Ilibidi kila mtu asimame na kumgeukia huyo Paul aliyekuwa amezungukwa na ‘Bodygurd’, Maaskari na watu wengine walionekana ni wa maana sana. Paul akitoka katikati ya hilo kundi, alizidi kumsogelea mama Sonia akiwa ametoa macho haamini anachokiona mbele yake.

“Haiwezekani kama ni wewe Ishimwe!” Mama Sonia alifunga macho huku amefunika uso wake, nakuanza kulia sana. Paul alisogea kwa haraka na kumkumbatia mama Sonia, nakuacha watu wote, kuanzia watu waliokuwa nao yeye mwenyewe Paul ambao wasingethubutu kutaja jina la Paul kama Paul na kina Nyange pia walibaki wamepigwa na butwaa. 

Bodygurd alisogea na kusimama nyuma ya Paul, ndipo wakina Nyange walipojua ni mlinzi wa Paul. 

Wakiwa wamechelewa sana lakini mshangao uliwafanya wazidi kusogea karibu kumshangaa vizuri Paul. Walibaki wamezubaa bila yakusema kitu, wakimshangaa Paul waliyekuwa wamesimuliwa wakidhani ni kijana wakawaida sana, kumbe ni mtu mkubwasana katika nchi ya Tanzania.

 Sam, Nyange na mama Briana walishamtambua Paul na hakuwa mtu mgeni kwao, walishamuona mara nyingi tu kwenye luninga, na kumsikia kwenye vyombo vya habari mara kadhaa, isipokuwa hawakujua kama ni Paul wa Mama Sonia. 

Katika nchi ya Tanzania alijulikana kama Mheshimiwa Paul Tambo. Paul na mama Sonia walibaki wamekumbatiana kwa muda mrefu sana, Mama Sonia alikuwa akilia sana, na Paul akifuta machozi huku akiita “Ishimwe!” Sonia alimsogelea Sam karibu na kuinama. 

 Malipo ya Mungu…

Paul akaendelea. “Nimetoka kwenye kaburi lako hata mwezi haujaisha, Ishimwe! Mama aliniambia ulikufa siku ile nilipo kuacha naye Mwanza!” Mama Sonia alikuwa akilia tu. “Nimekuwa nikienda kutembelea kaburi lako mara kwa mara.” Paul aliendelea kuongea huku amemkumbatia mama Sonia huku akimbembeleza na yeye kujikausha machozi. 

Aliwasogelea msichana aliyekuwa kwenye kundi la Paul. “Mheshimiwa! Wamepiga tena simu. Unasubiriwa wewe tu, kikao kianze.” Yule dada alimwambia Paul. Paul akamgeukia ‘Bodygurd’ wake, “Naomba mtupishe kidogo, nataka tuongee.” Kweli maskari wote walio kuwepo pale na watu wengine waliokuwa upande wa Paul, walisogea kuwapa nafasi. 

Aliporidhika wapo peke yao, akamuuliza Ishimwe aliyekuwa bado amemkumbatia kama asiyetaka aondoke tena. “Unafanya nini hapa? Umepatwa na matatizo?” Paul aliuliza. Kwa kuwa mama Sonia alikuwa bado akilia, ilimbidi Nyange ajibu. 

“Hapana. Hana matatizo. Yeye amekuja kutoa ushahidi na tumechelewa sana. Sijui kama tutasikilizwa tena.” “Basi tangulieni ndani tunakuja.” Paul aliongeza. Nyange, mkewe, Sam na Sonia waliingia ndani, na kumuacha Paul bado amemshikilia mama Sonia, walimkuta Hakimu anaahirisha kesi yao. 

Kabla hawajakaa sawa, tayari ule ukimbi ulijaa maaskari wakikagua na kumfanya kila mtu ashangae mpaka Hakimu mwendesha kesi! “Kuna nini?!” Hakimu aliwauliza wale maaskari. “Mbona mnanivamia?” “Judge Mkuu anataka kuingia humu ndani.” Askari mmoja aliyeonekana ni kiongozi wao alijibu. Sonia alishituka sana. 

Wakiwa bado kwenye mshituko na ukumbi mzima ukiwa kimya kabisa na mapaparazi wakiendelea kupiga picha, Hakimu mwendesha kesi alibaki akijiuliza, ‘Judge Mkuu wa Tanzania!’ anafanya nini kwenye chumba kile!

Wakiwa katika maswali mengi Paul na mama Sonia waliingia wakisindikizwa na ‘Bodygurd’ wa Paul. 

“Jamani samahanini sana kwa usumbufu. Nimeingia humu ndani kama raia wakawaida tu, namsindikiza mama watoto, anatoa ushahidi wake leo. Kwa hiyo naomba nyinyi muendelee kama kawaida tu. Na niombe radhi kwa kuwachelewesha upande wa washitaki.” Paul aliongeza akiwa amesimama.

Alipoona watu wote bado wapo kimya kama wamepigwa na butwaa, aliangalia ilipokuwa imekaa familia ya Nyange, mlinzi wake aliwasogeza watu waliokuwa wamekaa sehemu aliyoiangalia Paul, Paul na mama Sonia wakakaa hapo. Tayari mandhari ya pale mahakamani ilikuwa imeshabadilika, ulinzi ulikuwa mkali sana, waendesha kesi wote walikuwa kimya. Milio ya kamera pekee ndiyo iliyokuwa ikisikika mahakani hapo na wote walionekana kumpiga picha mama Sonia na Paul. 

“Usiwe na wasiwasi Ishimwe, kila kitu kitakuwa sawa.” Kina Nyange waliokuwa wamekaa kiti cha mbele ya Paul na mama Sonia, walimsikia Paul akimnong’oneza mama Sonia. “Naogopa kesi isije kunibadilikia Paul!” Mama Sonia aliongea kwa sauti ya chini sana iliyojaa mtetemeko akiashiria bado analia. 

“Ndio maana nipo hapa Ishimwe. Sitaondoka mpaka nihakikishe unatoka hapa salama. Nakuahidi kila kitu kitakuwa sawa. Usiogope. Naomba utulie tu, ujiandae kutoa ushahidi wako.” Mama Sonia alivuta pumzi kwa nguvu. 

“Amekula vizuri lakini?” Paul aliendelea kumnong’oneza mama Sonia kwa sauti ya chini. Sonia alikuwa kimya kabisa akiwasikiliza huku ameinama. “Nimekula.” “Mbona midomo imekauka?” “Labda wasiwasi tu, lakini nimekunywa chai.” Mama Sonia aliendelea kufuta machozi. “Unataka maji ya kunywa?” “Siwezi kunywa kitu sasa hivi Paul, mpaka tumalize.” “Maji yatakusaidia kutulia Ishi. Utajisikia vizuri.” “Sasa hapa maji tutapata wapi Paul? Acha tu nitakuwa sawa.” Paul aligeuka kumtizama ‘Bodyguard’ wake. Akasogea.

Alimnong’oneza kitu, yule Bodyguard naye alimgeukia yule dada aliyekuwa amemuongelesha Paul wakiwa nje, akimwambia Paul wamepigiwa simu, anasubiriwa. Yule dada alitoka nje kwa haraka. Baada ya muda mfupi sana alirudi na shupa ya maji ya baridi. Akamkabidhi Paul, na Paul naye akayafungua na kumkabidhi mama Sonia. “Asante.” 

“Kunywa japo kidogo, kabla hujaitwa.” Mama Sonia alicheka kidogo huku akifuta machozi. “Hujabadilika Paul!” “Nini sasa?” Mama Sonia aliendelea kunywa hayo maji taratibu huku Hakimu mwendesha kesi akiendelea na kesi yao. 

Zamu ya Mama Sonia ilifika, akatakiwa asimame, aende mbele. Wakati anasimama, Paul alimvuta mkono. “Usiogope, kila kitu kitakuwa sawa. Mimi nipo hapa. Sawa?” “Asante Paul.” Mama Sonia alikwenda mbele, akaapishwa akiwa ametulia kabisa. Usoni hakuonyesha woga tena.

Kabla yakujibu swali alilokuwa ameulizwa na wakili wa upande wa Nyange, akitaka kujua mahusiano yake yeye na Nyange, mama Sonia alimwangalia kwanza Paul, akavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu ndipo alipomgeukia Wakili aliyekuwa akimuuliza maswali kisha akaanza kueleza. 

Mama Sonia alieleza kuanzia mwanzo Sonia alipoenda Dar kufanya kazi za ndani, na yeye kuitwa pale kusaidia kazi. Aliendelea kueleza vile Nyange na mkewe walivyo waheshimu na kuwatunza kama ndugu na sio wafanyakazi. 

“Nyange na mkewe ni wanandoa wanaopendana na kuheshimiana sana. Na walijenga familia ambayo sikuwahi kuona tangia nizaliwe! Walifungua milango nyumbani kwao kwa kila muhitaji. Japokuwa tulikuwa wafanyakazi watatu mle ndani, lakini Nyange hakuwa akila chakula cha mtu yeyote mle ndani isipokuwa kilichopikwa na mkewe. Na alijua ladha ya chakula kilichopikwa na mkewe.”

“Mama Briana alimuhudumia mumewe kwa kadiri ya uwezo wake, hata pale alipokuwa mgonjwa, alihakikisha yeye ndiye anampikia mumewe labda kipindi alichokuwa amelazwa hospitalini na siku ambazo mama yake na mdogo wake Leah walipofika pale nyumbani.” Mama Sonia alitulia kidogo kama anayefikiria. 

“Kwa mara ya kwanza tokea nifike nyumbani kwao, ndipo nilipo ona mtu mwingine mbali na mama Briana akipika chakula cha Nyange, wakati mama Briana akiwepo pale nyumbani. Mama Eliah ambaye ni mama yake Leah na Mama Briana, alifika nyumbani kwa Nyange akiwa na Leah, wakidai wamefika kutoa pole ya msiba wa wazazi wake Nyange.”

“Siku moja waliamka asubuhi sana, nakuniambia niwaachie jiko wanataka wao ndio waandae kifungua kinywa cha mama Briana na mumewe. Wakiwa wanaandaa supu hiyo jikoni, nilimsikia Leah na mama yake wakiongea kitu. Mama yao alimuuliza kitu Leah ambacho sikuwa nimeelewa mpaka mambo yote haya yalipotokea.” “Ulisikia nini?” Mama Sonia aliulizwa. 

“Nilimsikia Mama yao akimuuliza Leah kama ameshaweka? Na kama hajachanganya? Leah alimjibu mama yake. ‘Niko makini mama. Leo lazima kieleweke’. Ndipo mama Eliah ambaye ndiye mama yake mke wa Nyange, akazitoa zile supu jikoni na kuziweka mezani.”

“Akamkabidhi mama Briana ya kwake kwenye bakuli ambalo Leah alishamwambia mama yake, ‘humu ndimo ilipo ya Penninah, na hili bakuli jingine ni la Nyange. Usije kuchanganya mama wakati ukiwapa’. Na kweli yule mama alifanya kama alivyo elekezwa na Leah.”

“Mambo yalibadilika mara baada ya Nyange na mkewe kunywa ile supu. Mama Briana alianza kuwashwa sana huku akilia kichwa kinamuuma, wakati mumewe anataka kumpeleka hospitalini, tukashangaa mama Briana, Penninah anaanza kuvua nguo, akawa amechanganyikiwa kabisa.”

“Na baada ya muda Nyange naye aligeuka kuwa kama mjinga kabisa. Hakuwa akielewa chochote kinachoendelea mle ndani. Mwanzoni nilijua nikuchanganyikiwa kwa sababu ya kuugua gafla kwa mkewe, lakini haikuwa hivyo. Maana hata safari za kwenda kumuona mkewe hospitalini, Dodoma ziliisha kabisa.”

“Nyange alipoteza kumbukumbu zote, hakuwa akimtambua mtu yeyote isipokuwa Leah tu. Hakujua kama ana mke anaitwa Penninah au watoto wawili aliokuwa akiwapenda sana.” Mama Sonia alitulia kidogo kama kuzuia machozi. 

“Mambo yaliendelea kuwa mabaya pale ndani, hali ya Nyange ilizidi kuwa mbaya nakuanza kumtia wasiwasi hata Leah mwenyewe. Nilijua kuna kitu wamemfanyia Nyange na mkewe, lakini sikuwa na uhakika, ndio siku moja, mimi nikiwa jikoni, wao, yaani mama Eliah na mwanae Leah wakiwa sebuleni nilimsikia Leah akimlalamikia mama yake, kwamba anahisi amemzidishia Nyange dawa.”

“Kwani Nyange hakuwa akitaka kwenda kazini kabisa, alitaka akae na Leah tu, pale nyumbani. Nimeshakaa na watu makatili duniani, lakini sijawahi ona kama Leah jamani!” Hakuna mwanasheria aliyenyanyua mdomo kumkatiza Mama Sonia. Mama Sonia alikuwa akiongea kwa kujinafasi. Kila mtu {Hakimu mwendesha kesi, mawakili na waamuzi} wote waliongeza heshima mbele ya kiongozi wao Paul, kwa hiyo walianza kutizama upande wa kina Nyange uliokuwa umezoea kuzidiwa nguvu na Leah na wakili wake kila wanapofika mahakamani hapo, kwa mtazamo wa tofauti sasa. 

*********************

Paul akijua kabisa anakiuka maadili ya kazi yake, kuwepo mahakamani hapo yeye kama kiongozi wa ngazi ya juu na akijitambulisha yupo kwenye upande wa kina Nyange, alishindwa kujizua. 

Wazi alijua kuwepo kwake tu mahali pale ni kuwafanya waamuzi hao kushindwa kuamua kesi hiyo vizuri, na ni wazi wangependelea, lakini Paul aliahirisha ratiba zake zote za asubuhi ile, ili awepo pale na Ishimwe. 

Paul alikuwepo Mahakamani hapo asubuhi sana ya siku hiyo wakiwa kwenye moja ya ukumbi walizozoea kutumia wanasheria hao kwenye vikoa vyao vya kila mwezi, mahakamani hapo. Paul akiwa kama Judge Mkuu wa Tanzania, alikuwa akikutana na Mahakimu wote angalau mara moja kwa mwezi kuzungumzia mambo ya mahakama nchini. 

Siku hiyo alifanya kikao hicho asubuhi na mapema, akiwa na kikao kingine cha muhimu sana, Ikulu. Lakini mambo yalibadilika baada ya kumuona Ishimwe na kusahau kabisa maadili ya kazi yake. 

Kuwepo Paul kama kiongozi mkubwa sana mahakamani hapo ni kusababisha Hakimu muendesha mashitaka kushindwa kufanya kazi yake kwa ufasaha na kulazimika kupendelea upande aliokuwepo ‘Bosi’ wake. Hayo yote Paul aliyatupilia mbali na kumuomba ‘Secretary’ wake kuomba radhi kwa Mheshimiwa raisi (aliyekuwepo madarakani muhula huo) kuwa asingeweza kuhudhuria kikao kwa wakati uliopangwa kwa kuwa yeye amepata dharula. 

Alikubali kupoteza kila kitu siku ile, isipokuwa Ishimwe. ‘Sitampoteza Ishimwe kwa mara nyingine tena.’ Paul aliendelea kuwaza kila alipokuwa akihesabu garama ya kuwepo kwake mahakamani hapo kwa muda ule. Alikumbuka maamuzi aliyoyafanya siku wanaachana na Ishimwe mbele ya mama yake, na kumpoteza Ishimwe kwa miaka yote hiyo. ‘Hapana, kila kitu kitasuburi leo, lakini sio Ishimwe.’ Paul alindelea kujipa moyo kila alipokuwa amekaa mahakamani hapo na kukumbuka majukumu ya muhimu yanayomkabili kwa wakati ule. 

 *********************

Mama Sonia aliendelea. “Leah alianza kutesa watoto wa dada yake kwa kuwapiga kama wezi, alizuia chakula kisiliwe na mtu yeyote mle ndani isipokuwa yeye, mama yao na Nyange tu. Hata watoto wa dada yake alikuwa akiwanyima chakula, mpaka Sonia, binti yangu, alipokuwa akituma pesa za matumizi ya mle ndani.”

“Aliwafukuza kukaa mle ndani ya nyumba yao, walifunguliwa asubuhi kama kuku na kuruhusiwa kuingia usiku tu, wakati wanaingia chumbani kulala. Kwa kuwa alijua ninawalinda sana wale watoto, alianza mtindo wa kuwaita ndani na KUWAPIGA SANA, huku akiwaonya kwa kuwatishia wasiniambie, lasivyo atawaua.”

“Briana, mtoto mkubwa wa Nyange ilimbidi kumsisitiza sana mdogo wake asithubutu kuja kuniambia juu ya unyama wanaofanyiwa na Leah pindi anapowaita ndani, lasivyo Leah atawaua.”

“Wasiwasi ulianza kuniingia baada yakumuona mtoto yule mdogo anaanza kunyongea. Alianza kulia sana kila ninapomshika, hasa kipindi cha kumuogesha. Nilihisi anamaumivu makali sana, lakini alishindwa kabisa kuniambia anachofanyiwa na Leah. Kwa kuwa nilikuwa nikishinda na yule mtoto muda mwingi, sikujua kabisa kama kipindi Leah anapomuita ndani akijidai anataka kumtuma, kumbe nia yake ilikuwa nikunitenganisha nae ili amsulubishe wakiwa wao peke yao.”

“Alizidi kuwa mdhoofu kitu kilichoniogopesha sana, na kurudia kumfunga Brayan mgongoni kama mtoto mchanga.” Mama Sonia aliinama nakuanza kulia. 

“Siku moja aliamka akiwa na maumivu makali sana, kwa kuwa sikuwa na hela yakumpeleka hospitalini na Sonia mtoto wangu alibanwa kazini, aliniahidi angetuma pesa jioni yake akitoka kazini ili tumpeleke mtoto hospitali akachunguzwe, kwa kuwa Leah aliacha kuwahudumia watoto kabisa.”

“Kwa hiyo nilishinda nimembeba mgongoni siku nzima mpaka dada yake aliporudi kutoka shule, Brayan alitaka kushuka amsalimie dada yake. Dada yake alitaka kumkumbatia, lakini Brayan alikataa kabisa, kitu kisichokuwa cha kawaida kwa watoto wale waliozoea kusalimiana wakati wote kwa kukumbatiana.”

“Ndipo Briana alimvuta pembeni ili amuulize kwa siri. Bila kujua kuwa nawasikiliza, Briana alinong’ona huku akimuuliza, ‘na leo amekupiga tena?’ Brayan akamjibu hapana, kwa kuwa nilikuwa nimembeba siku nzima. Kumbe jana yake ndiyo alimpiga tena zaidi.”

“Wakati nawasikiliza huku nikiendelea kufua palepale nje, kwa kuwa Leah alinikataza kabisa nisitumie mashine ya kufulia kwa hiyo nilikuwa nikifua kwa mikono, nilisikia Leah akimuita Brayan. Niliwaona wale watoto jinsi walivyoingiwa hofu gafla baada yakumsikia Leah anaita. Briana akamwambia mdogo wake, ‘Kimbia asije kukuumiza zaidi.’ Br..” Mama Sonia alianza kulia kwa kwikwi na kushindwa kuongea. 

“Pole sana Ishimwe.” Paul alijikuta akiropoka mahakamani hapo.  Kisha akaendelea kuongea huku akilia. “Briana alianza kunyata kuingia ndani, kumfuatilia mdogo wake, kama kawaida yao. Kumbe ilikuwa Brayan akipigwa na Leah, Briana alikuwa akimchukua na kuzunguka naye upande mwingine wa nyumba ambapo alijua sitawaona, na kumbembeleza mdogo wake mpaka anapotulia ndipo walikuwa wakirudi kwangu huku wakificha maumivu yao.”

“Lakini siku ile ilikuwa tofauti. Briana alipokuwa akichungulia wakati mdogo wake anasulubiwa, alishindwa kuvumilia nilimsikia akiniita kwa sauti ya juu sana, huku akilia, akinisihi niwahi kumuokoa mdogo wake, anakufa.” Mama Briana alilia kwa sauti, kwa kwikwi na kumfanya hata mama Sonia mwenyewe kushindwa kuongea kabisa na kubaki akilia. 

“Nilikufanya nini Leah wewe, kiasi cha kuadhibu watoto wangu hivyo?” Mama Briana aliuliza kwa uchungu sana huku akilia. Sonia naye alikuwa akilia sana, lakini Sam alikuwa amepitisha mkono wake mmoja juu ya mabega ya Sonia na kumshika mikono yake huku akimfuta machozi, akimsihi atulie. 

Paul aliomba Ishimwe apewe maji. Alipokunywa maji ndipo Mama Sonia alipoweza kuendelea. 

“Jamani Leah ana roho mbaya huyu msichana nyinyi! Hapana! Hamjawahi kuona hapa duniani! Sijui hata anawezaje kulala usiku!” “Tunaomba uendelee Mama Sonia.” Wakili wa upande wa Nyange aliingilia.

“Nilikimbia haraka sana kuingia ndani, nilimkuta Leah amemkanyaga kichwa Brayan mtoto mdogo wa Nyange akimpiga mwili mzima na mwiko kama anaua nyoka, bila hata huruma! Alikuwa akimpiga yule mtoto akiwa hana fahamu, amekakamaa pale chini sakafuni na anatokwa na mapovu mengi mdomoni.”

“Nilimchukua yule mtoto na kumkimbiza hospitalini, nikiwa na watoto wengine. Mungu alikuwa upande wetu, tuliwakuta madaktari wengi sana pale mapokezi wakiongea tu baada ya muda wao wa kazi kuisha. Kwa kuwa mtoto alikuwa na hali mbaya, ilibidi nieleze kisa chao na wazazi wao kwa ufupi. Waliwahurumia sana wale watoto, Brayan alipokelewa hospitalini pale na akaanzishiwa matibabu ya haraka.”

“Brayan alikuwa amevunjika mkono wa kulia sehemu tatu, na mbavu zake tatu Leah alizivunja kwa kumpiga.” Hakuna aliyeacha kulia mahakamani hapo, mpaka aliyekuwa akisimamia kesi ya Leah aliinama. Lakini Leah alibaki kimya kama sio yeye anayetajwa pale ndani. 

“Ilibidi tulazwe, nikawaacha wale watoto wawili wengine tuliokuwa tukiishi nao pale kwenye nyumba ya Nyange, na kaka mwengine aliyekuwa akifanya kazi nyumbani kwa Nyange nje ya wodi, huku nikiwa nimewaachia maagizo warudi nyumbani, lakini Briana alianza kulia akikataa katakata, kurudi tena nyumbani kwao mpaka Sonia alipokuja kutoka Dodoma akawachukua na kuwapeleka hotelini.”

“Wale madaktari walianza kupokezana kutuletea vyakula pale wodini, na walipojua Sonia anakaa na watoto hotelini, kwa kuwa Briana hataki kurudi nyumbani kwao, ndipo wakawatoa hotelini na mmoja wao akawachukua kwenda kuishi nao nyumbani kwao mpaka Brayan alipopata nafuu na kuruhusiwa, ndipo Sonia alipotuchukua tukaishi naye Dodoma.” Kila mtu alikuwa akifuta machozi. 

“Kwa nini Briana alikataa kurudi nyumbani?” Mama Sonia aliulizwa tena. “Briana ni kipenzi cha baba yake. Hakuna anayemfahamu Nyange, asifahamu mapenzi aliyonayo kwa mwanae Briana. Sio nyumbani, wala shuleni kwa kina Briana, Nyange alifahamika kwa kumpenda na kumjali huyo mtoto.”

“Lakini hata Briana mwenyewe alikuja kugundua baba yake anatatizo la akili.Aliona jinsi baba yake alivyobadilika. Nyange alibadilika jamani, akawa kama sio yeye! Alikuwa kama zezeta, mjinga, au kama mtu aliyeshushwa kwenye ulimwengu mwingine, asiyejua lugha yao wala sura zao.”

“Hakuwa akiongea wala kuona mwanadamu yeyote mle ndani isipokuwa Leah tu. Hakuna jinsi Nyange angemuona mtoto wake ana shida asimsaidie. Anampenda mtoto wake huyo wa kike kuliko nafsi yake. Kabla Briana hajalia shida, baba yake anakuwa ameshaitatua.”

“Huyo mtoto alikuwa na dereva wake na alikuwa akiendeshwa kwenye gari la kifahari sana, kuliko hata magari ya wazazi wake. Chumba cha Briana chenyewe, sijawahi ona hata kwenye luninga. Hata wazazi wake wenyewe hawakuwa na chumba kizuri kama hicho cha Briana.”

“Na wakati wote Nyange alikitunza hicho chumba kwa ajili ya Briana, na kahuruhusiwa mtu yeyote mle ndani kulala kwenye chumba hicho isipokuwa yeye mwenyewe Briana na Kana basi.” “Kanamugire!?” Paul alishituka na kutamka kwa sauti ya kuhamaki, ya juu, nakumfanya kila mtu amgeukie. 

“Ndiyo, Kanamugire. Lakini sio wangu Paul.” Hakuna aliyewaelewa Mama Sonia na Paul, lakini aliyekuwa akimuhoji maswali alitaka aendelee. “Ndio nilikuwa nikisema, hata Briana mwenyewe aliona mabadiliko kwa baba yake kwani aliona vile ambavyo, baba yake alinyamaza wakati akipokonywa chumba chake na Leah. Maana Leah alihamia kulala chumbani kwa Briana na wakati nilionyeshwa chumba ambacho alikuwa akikitumia Leah kabla hajaondoka kwenye hiyo nyumba.”

“Leah alichukua gari ya Briana mbele ya macho ya Nyange na kumuacha Briana akitembea kwa miguu kwenda shuleni, kitu ambacho Nyange na akili zake timamu, ASINGEWEZA KURUHUSU hata iweje.”

“Japokuwa sasa hivi hana hela, Nyange alipopata nguvu kidogo tu, baada ya kuugua sana, alianza kufanya vibarua kwa watu vya kukata majani si kwa ajili ya kumnunulia mkewe nguo, hapana, anafanya vibarua ili kupata pesa za kusaidia kuongeza mafuta kwenye gari la Sonia linalo mpeleka Briana shule, mpaka Sam, mume wa Sonia alipomkatalia.”

“Leah alimtoa Briana kwenye shule nzuri sana, aliyokuwa akisomeshwa na baba yake, akidai ni ya gharama sana, nakumuhamishia mtoto huyo kwenye shule ya Kata, mbele ya macho ya Nyange, kitu ambacho kwa akili ya Nyange ASINGERUHUSU kitokee hata iweje.” Mama Sonia alikunywa tena maji kidogo. 

“Kitu kingine ni pale Briana alipougua sana, nikamuomba pesa Leah, kwa kuwa yeye ndiye alikuwa akiachiwa pesa zote na Nyange, lakini alikataa kabisa kunipa pesa za kumpeleka Briana hospitalini. Akiwa amezidiwa yule mtoto usiku nilienda kuwagongea kwenye chumba walichokuwa wakilala.”

“Leah alitoka, nikamweleza hali ya mtoto. Leah alinitukana huyu msichana jamani, kana kwamba namuomba pesa za kwenda kutengeneza nywele zangu saluni. Wakati Leah anaendelea kunitukana, Nyange alitoka akiwa amezubaa, akionyesha wazi kabisa HAMFAHAMU Briana ni nani na haelewi kwa nini nimuombe Leah pesa.”

“Nilimpeleka Briana hospitali, akalazwa siku tatu. Nikiwa hospitalini nikimuuguza Briana, nilimtuma Josh kijana aliyekuwa akifanya kazi pale kwenye Jumba la Nyange, akamwambie Nyange, Briana anaumwa sana na amelazwa. Josh anasema Nyange hakuwa anaelewa kabisa, anahusikanaje na ugonjwa wa huyo Briana! Kwa siku tatu tulizokuwa tumelazwa na Briana, sio Nyange, wala Leah na mama yake waliokuja kumuona mtoto.” Mama Sonia aliunganisha. 

“Tulipomtoa mama Briana katika hospitali ya Mirembe na Sam alipokuja kutuchukua kuturudisha kuishi naye tena hapa Dar, mama Briana alikataa kulala usiku ule pale nyumbani kwa Sam, mpaka akamuangalie mumewe. Tulifika nyumbani kwakwe, pale kwenye nyumba yao, lakini Leah alitukatalia katakata kutuonyesha alipo Nyange. Mpaka mama Briana aliposema tukamwangalie chumbani kwa Josh. Hiko chumba kipo kwenye nyumba ndogo ya nje ya hilo Jumba la Nyange.” Mama Sonia alitulia nakuanza kulia. 

“Jamani, nimeamini kuna watu wanaroho mbaya kuliko wanyama!” Mama Sonia aliendelea. “Tulimkuta Nyange amefungiwa humo ndani kama mnyama! Mgonjwa, hajitambui, ameoza sehemu za matakoni kote mpaka chini mapajani, ananuka, amejisaidia hapohapo kitandani haja zote, na tukakuta sahani zilizoonekana aliwekewa chakula muda mrefu sana bila yeye kula, zote zilikuwa hapo sakafuni.”

“Nyange alikuwa na homa kali sana. Tulimsaidia mama Briana kumsafisha mumewe, na kumkimbiza hospitalini. Wamekaa hospitalini kwa muda wa majuma matatu, bado Nyange akiwa hajitambui kabisa mpaka alipoletwa nyumbani, tukaita watumishi wa Mungu kumuombea Nyange akatolewa mapepo na kurudishiwa ufahamu wake ndipo Nyange alipoweza kumtambua mkewe na mtu wa kwanza kumulizia pindi alipopata ufahamu wake alikuwa Briana kipenzi chake.”

“Na muda wote huo akiwa hospitalini, mkewe ambaye naye alikuwa mgonjwa, akiwa ndio ametoka tu hospitali ya Mirembe, ndiye aliyekuwa akimuuguza mumewe, mchana na usiku, bila kutoka pale hospitalini, wala kujali kuwa mumewe hamtambui na Nyange naye akiwa hana ufahamu wowote, neno moja tu ndilo alilokuwa akiweza kulisema ni Penninah.”

“Hawa watu walipoteza kila kitu maishani, LAKINI sio wao wawili, na hapo ndipo kila aliyewaona baada ya matatizo yao, ndipo walipogundua hawa watu wanamapenzi ya kweli sio kujisingizia kama Leah anavyosema hapa anapendana na Nyange, wakati alimtesa kuliko hata mnyama wa porini.”

“Huyu msichana ni muongo na muuaji kabisa, msimsadiki hata kidogo. Hana neno la kweli linaloweza kutoka kinywani mwake, labda Mungu amuumbe tena.” Mama Sonia alimaliza kuongea kwa uchungu, huku akifuta machozi. Kulikuwa na ukimya mkubwa sana, kila mtu akikausha machozi yake. Paul naye alikuwa akitokwa na machozi.  

Mama Sonia aliambiwa ashuke kizimbani, na kurudi kukaa. Akarudi kukaa pembeni kwa Paul. “Pole sana Ishimwe. Pole sana kwa matatizo.” Kesi iliahirishwa tena. Paul alikuwa wa kwanza kutoka na Mama Sonia.

*********************

 “Ninatakiwa kuonana na Mheshimiwa baada ya muda mfupi sana kuanzia sasa. Kuna kikao nimeahirisha asubuhi nikawaomba wenzangu tukizogeze, sababu ya kuwa hapa. Naomba nije kukuona baadaye.” “Kweli utarudi?” Mama Sonia aliuliza huku akilia. 

“Sitakupoteza tena Ishimwe. Nina kitu cha muhimu sana natakiwa kuongea na Raisi. Baada ya hapo nitakupigia simu, nataka nije nyumbani.” Kina Nyange walikuwa wemetoka na wao wamesimama nyuma ya Mama Sonia, wakiwa wameduwaa. 

Bado Sonia alikuwa amesimama pembeni ya Sam ameinama. Kumbukumbu za kumuona baba yake akimwapisha raisi aliyekuwepo madarakani zilimjia, lakini hakuwa akijua kama ni baba yake! “Natangulia kwenye gari.” Sonia aliaga kwa sauti ya chini akimwangalia Sam, nakuanza kuondoka, nakuacha kila mtu akimwangalia. “Nisubiri Sonia twende wote.” Sam alimkimbilia. 

Paul alibaki akimwangalia Sonia. “Umefanana naye sana. Hajachukua kitu hata kimoja kwangu!” Paul aliongea bila ya kuuliza kama ni wake. “Amechukua akili zako na tabia zake kama wewe. Kila alivyokuwa akikua ndivyo nilikuwa nikihisi naishi na wewe. Utakuja kuona. Ana akili sana.” Mama Sonia alijibu huku na yeye akimwangalia Sonia. 

“Hapa hatuwezi kuongea vizuri, si unaona wanavyotupiga picha tu. Kesho utaonyeshwa kwenye kila gazeti.” Paul aliongea kwa utani, akimtania mama Sonia. “Nitakuona baadaye Ishimwe.” Paul akifutana na Mlinzi wake walimsindikiza mama Sonia mpaka kwenye gari, akachukua namba ya simu ya mama Sonia, alipohakikisha wakina Nyange wameondoka ndipo na yeye akaondoka pale mahakamani. 

 *********************

Walirudi nyumbani kimya kimya. Sonia hakuongea na mtu kitu chochote, aliingia chumbani kwao moja kwa moja. “Asante sana Mama Sonia. Asante kwa kila kitu.” Nyange alimsogelea Mama Sonia aliyekuwa amesimama akiwa bado kwenye mshituko na kumpa mkono. “Nimemuona Paul jamani!” Ndilo lilikuwa jibu la mama Sonia na kuanza kulia. “Nimemuona Paul! Sikujua kama bado atanikumbuka tena!” Bado Mama Sonia alikuwa amesimama. 

“Walimwambia nimekufa!” “Kaa basi mama Sonia.” Mama Briana alimshika mkono. “Siamini kama nimemuona Paul mwenzenu!” Mama Briana alianza kucheka. “Naona mwenzangu ushakuwa maarufu!” Mama Briana alimtania. 

“Bwana mimi niliingiwa na hofu, nikajua ndio umekamatwa na polisi. Gafla naona unakumbatiwa pale na mabusu uso mzima!” Kidogo watu walianza kucheka. “Mwenzetu ukaingia mahakamani na ulinzi bwana!” Nyange aliendelea. 

“Lakini kaka, ushahidi wa leo naona kama umewachoma wengi. Mpaka yule Wakili anaye muwakilisha Leah, aliishiwa nguvu! Nilimuona na yeye ameinama.” “Pale yalikuwa mengi yanaendelea Sam. Bosi wao alikuwepo, halafu bosi akajitambulisha kwamba mtoa ushahidi ni mama watoto! Unafanya mchezo nini?” Kila mtu alianza kucheka. 

“Nahisi ile kesi itachukua sura mpya.” “Kabisa Sam. Hivi shemeji yetu Judge Mkuu! Acha mchezo.” Kila mtu alikuwa akicheka. “Jamani, ngoja nikamwangalie mke wangu.” Sam alisimama. 

“Daah! Sammmm.” Nyange alianza kucheka. “Nini sasa?” “Umeukata mdogo wangu! Kama utani, unaoa mtoto wa Judge Mkuu wa Tanzania bwana! Hongera mdogo wangu.” Wote walianza kucheka mpaka mama Sonia. “Mimi namuoa Sonia bwana!” “Haya bwana Sam. Hongera.” Sam alicheka na kuingia chumbani. 

Nyange naye akamgeukia mama Briana. “Ulisema tutaendelea baadaye.” “Nyange wewe jamani! Mbele ya mama Sonia!?” Mama Briana alinong’ona akiwa ameshituka sana na kumfanya Mama Sonia acheke na kuinama. 

“Samahani mama Sonia. Nakumbushia ahadi yangu. Naona watoto watatoka shule halafu nizidi kupigwa tarehe. Maana akishakuja yule mwanae wakiume akili yake haifanyi kazi kabisa. Nitaachwa hapa kama hanijui! Heri nidai vyangu mapemaa.” “D wewe!?” Mama Briana alimfinya kidogo Nyange, akaruka. “Ngoja mimi nikaandae chakula jamani.” Mama Sonia alisimama na kuingia jikoni huku akicheka.

“Usingesema hivyo mbele ya mama Sonia bwana, D!” “Hakuwa ameelewa bwana mpaka wewe ulivyomwambia. Twende basi.” Nyange na mkewe nao wali potelea chumbani kwao huku wamejawa matumaini mapya. 

 *********************

Sam alimkuta Sonia akilia sana kitandani. Alipanda na yeye kitandani na kumkumbatia. “Usilie Sonia.” Sam aliendelea kumbembeleza. “Ujue kila hali uliyonayo wewe, iwe ya furaha au huzuni inamuathiri mtoto tumboni? Unakumbuka pressurealiyosumbuka nayo mama Bree kipindi mjamzito? Sitaki upitie kule bwana. Sitaki tumpoteze mtoto wetu. Umesikia mpenzi wangu?” Akambusu na kumuuliza swali. 

“Hivi ulisema tutamuita nani tena?” Sonia alianza kutabasamu huku akifuta machozi. “Usilie bwana!” “Si ulisema tusimuite Junior kwa sababu ya Kana? Sijapata jina jingine.”Sonia alijibu huku akitabasamu na kupapasa tumbo lake. 

“Itabidi tutafute la wakike na wakiume tupige kura na Kana kaka yake akiwepo.” Kidogo Sonia alitulia na kuanza kucheka. “Unataka kula nini?” Sam akamuuliza kwa kujali. “Nitakuletea hukukuhu chumbani.” “Huendi kazini?” “Ukitulia nitaenda mara moja kuchungulia halafu nitarudi.” Sam alikuwa akimdekeza Sonia kupita kiasi. Alimuhudumia kwa kila jambo na wakati wote alihakikisha Sonia anafuraha.

“Unataka kuondoka hivihivi?” Sonia alimuuliza Sam huku akimbusu. “Si ulikuwa ukilia wewe?” Sonia alianza kucheka. “Nakupenda sana Sonia.” “Asante Sam.” Sam alimvuta tena karibu yake huku akimwangalia kwa utulivu na tabasamu na kuanza kumbusu. 

“Unazidi kuvutia Sonia. Huyu atakuwa mtoto wa kike.” “Utafurahi au utasikitika?” “Nisikitishwe na nini? Mtoto ni mtoto Sonia. Atakaye tuchagulia Mungu, ujue ndiye atakayetufaa.” “Ndio maana nakupenda Sam wangu.” Sam alicheka na kuinama kuendelea kumbusu. 

Baada ya wapenzi hao kutosheka Sam alinyanyuka nakuanza kuvaa. “Kwa mwendo huu nitafukuzwa kazi.” Sonia alicheka huku akivuta shuka vizuri, akijifunika. “Hawawezi bwana. Wanakuhitaji sana kazini.” Sam alitoka kwenda kumletea Sonia chakula. 

Alipohakikisha mpenzi wake amekula na kushiba, alimfunika vizuri bila hata kutaka kuongelea chochote juu ya baba yake, kama Sonia alivyokwisha kumuomba tokea zamani. Akambusu tena. “Nitakuona baadaye kidogo.” “Usisahau bajia.” Sam alicheka. “Nilishatoa oda tayari, hapa zinanisubiri ofisini kwangu.” “Asante Sam.” “Nakupenda sana Sonia.” “Asante. Na mimi nakupenda Sam.” Ndipo akatoka. 

*********************

Alimkuta Nyange na mkewe wanakula sebuleni. “Nakuomba kaka, leo ukachukue watoto shule. Nataka Sonia apumzike kidogo. Alikuwa akilia sana. Nataka alale kidogo atulie na mimi sitakawia, nitarudi baada ya muda mfupi tu. Nataka nikachungulie kidogo hapo ofisini na kumchukulia bajia zake halafu narudi sasa hivi.” “Hamna shida kabisa, mimi nitakwenda. Najua Briana atafurahi sana kuniona.” Nyange alijibu, Sam akaondoka. 

 *********************

Mama Sonia alibaki ameinama, kisha akasimama. “Ngoja nikaoshe vyombo jamani.” Mama Briana akamfuata jikoni. “Vipi?” “Sonia anauchungu sana moyoni. Najua anatulaumu sana, mimi na Paul.” “Kwa nini?” Mama Sonia alinyamaza nakushindwa kujibu. 

Nyange alitoka kwenda kufuata watoto wote shule na kurudi nao nyumbani. Ilipofika jioni Sam naye aliingia. 

“Sonia ameamka?” Sam aliuliza. “Hajatoka humo chumbani tokea alipoingia.” Mama Briana alijibu. “Ngoja nimuamshe aje kula.” Sam alimkuta Sonia amekaa kitandani. “Vipi?” “Pole na kazi.” “Asante. Twende tukale.” Ndipo wakatoka pamoja. 

Akamchukulia chakula mezani, na kumletea palepale sebuleni alipokuwa amekaa Sonia. “Asante Sam, lakini nakiona kingi! Nataka nifaidi bajia zangu.” “Sasa hivi kula chakula, halafu bajia ziwe za baadaye ukisia njaa.” Sam alikaa pembeni yake. 

Mahusiano, Huchukua Muda Kujengwa.

Wakiwa wote wanakula walisikia mlango unagongwa. Sam alisimama kwenda kufungua mlango, alimkuta Paul na ‘Bodygurd’ wake wamesimama nje ya mlango. “Karibuni ndani.” Paul na mlinzi wake waliingia, Sam alirudi kukaa pembeni ya Sonia. 

Paul alianza kupita kwa kila mmoja akisalimia kwa kuwashika mkono kasoro Sonia. Hakunyanyua hata uso kumwangalia baba yake, alibaki ameinama pembeni ya Sam. Paul alibaki amesimama huku amenyoosha mkono wake mbele ya Sonia. Kila mtu alikuwa kimya kabisa. Mwishowe Paul alimuomba mlinzi wake asubiri nje. 

“Poleni na matatizo.” Paul alimgekia Nyange. “Asante Mkuu.” “Naomba niwashukuru kwa dhati kuwapokea Ishimwe na Sonia, na kuishi nao kama ndugu.” “Sio sisi tu Paul!” Mama Sonia alimkatiza. “Na Kanamugire. Wamewasomesha Kana na Sonia.” 

Paul akamsogelea mama Sonia. “Kwani uliolewa tena?!” “Hapana Paul jamani! Kana ni mtoto wa Sonia.” “Nini?!” Kana aliyekuwa amekaa na Briana wakiwa kimya kabisa muda wote wakila alishituka sana. Na mama Sonia naye akashituka zaidi kwani na yeye aliropoka. 

Kana akasimama nakurudia swali. “Mama?!” Akamsogelea mama Sonia ambaye alikuwa ni kama amepatwa na ububu wa gafla. Mwishowe Kana akamsogelea Sonia na kumuuliza. “Kwa nini hukuniambia?” “Hukuuliza Kana!” “Kweli!?” Kana alimkazia macho mama yake.

“Ulipokuwa ukikua ulipoona mimi namuita Mama na wewe ukawa ukimuita mama. Lakini sio kwamba nilikuwa nakuficha Kana. Na nilikuwa mdogo sana wakati nakuzaa, sikujua jinsi ya kukulea, ndio maana mama alikuwa akikaa na wewe muda mwingi, halafu mimi nilikuwa nikitafuta pesa. Kila mtu huwa namwambia kama wewe ni mtoto wangu Kana. Sijawahi kukuficha au kukukana kwa watu.” 

“Kasoro mimi mwenyewe ndio ulishindwa kuniambia?” Kana aliongeza na kumfanya Sonia kuishiwa na nguvu, akarudisha macho kwenye sahani yake. Kana alisimama pale kwa muda akimwangalia Sonia kama anayejaribu kuunganisha mambo fulani, kisha akaondoka kuingia chumbani kwake. 

“Na mimi naenda na Kana, dady.” Briana akasimama kumfuata Kana. “Ungemaliza chakula kwanza, Briana!” Nyange alimuwahi Briana kabla hajaingia na yeye chumbani. “Siwezi kula bila Kana, dady!” Briana aliondoka nakuingia chumbani kwao. 

“Daah! Briana bwana!” Nyange alisimama na kufuata sahani ya Kana na Briana na kuwapelekea chumbani kwao. Kila mtu alibaki kimya, Paul alibaki amesimama akijilaumu. 

 *********************

Kana alishakuwa kaka mkubwa wa miaka kumi na nne, ndio alikuwa akimalizia darasa la saba. Kila Sonia alipokuwa akimwangalia Kana, ndivyo alikuwa akimuona baba yake. Kuanzia sura mpaka maumbile. Hata ukali wa Kana, wakati wote Sonia aliufananisha na ukali wa baba yake Fau. 

Vile alivyokuwa akimfungia Fau na kumuwekea sheria kali kila siku. Fau rafiki yake Sonia, ni kweli alikuwa mtoto wa geti kali. Baba yake hakuona shida kumchapa Fau hata mbele ya Sonia. Ni mzee aliyekuwa akiogopewa sana hata na mke wake. 

 *********************

 “Samahanini sana jamani. Sikukusudia kuharibu.” Paul alijikuta akijutia, na kuona aombe tu radhi. “Umeshaharibu sasa! Mimi na Sam tulipanga kumuita Kana na kumwambia kama mimi ni mama yake. Ona umekuja tu leo na kuniharibia mahusiano yangu na mtoto wangu.” Na yeye Sonia akasimama na kuingia chumbani kwao. Sam naye akafuata nyuma. 

Mama Sonia alianza kulia. Paul alibaki amesimama asijue aseme nini. “Samahani sana Ishi, sikukusudia kuharibu. Nilijua uliolewa tena!” “Sikuolewa tena.” “Unafikiri tunaweza kutoka hapa tukaenda kuongea sehemu? Nitakurudisha kesho.” 

“Siwezi kuondoka nakuwaacha hivi walivyo Paul. Mimi ndio mtu wa pekee kwenye maisha yao. Lazima niongee nao, watulie.” Paul alibaki hajui chakusema. “Daah!” Aliendelea kulalamika. “Sam ndio baba wa Kana?” Paul aliuliza tena. “Hapana. Nayo hiyo ni habari nyingine?” 

“Nini tena?!” Mama Sonia alimnong’oneza kitu Paul masikioni. “Mungu wangu!”Paul alipiga yowe. Kisha akaanza kutokwa na machozi. “Mungu wangu mtoto wangu!”Paul alirudia tena na kutafuta sehemu akakaa. Mama Sonia alikuwa akilia na Paul alikuwa akilia huku akimwita Mungu wake. “Mungu wangu!” Paul aliendelea kusononeka. 

“Mungu ni shahidi Ishimwe, nilijua umekufa. Wamenionyesha mpaka kaburi walipokuzika, nimelijengea. Nakwenda huko mara kwa mara. Sijawahi kukusahau mpenzi wangu. Nisingeacha unateseka kama ningejua upo hai! Nisamehe.” Nyange na Mama Briana ndio walikuwa wamebaki sebuleni hapo wakiwa kimya hawajui chakusema. 

“Atalipa unyama wote aliomfanyia mtoto wangu. Nakuapia Ishimwe, huyo baba atalipa.” Paul aliendelea kuugulia maumivu. “Naomba tutoke Ishimwe, kidogo tu, nitakurudisha.” “Sonia ni mjamzito Paul. Siwezi kumuacha analia. Amelia siku nzima ya leo, sio vizuri aendelee kulia.” “Ni mjamzito!?” Paul aliuliza tena kwa mshangao. 

“Mama Sonia? Kwa nini wewe usiende mimi na Sam tutawatuliza? Najua nyinyi mna mambo mengi sana yakuongea. Nenda tu kila kitu kitakuwa sawa.” Mama Briana aliingilia maongezi. “Siwezi kuondoka. Sonia ndio ataumia zaidi, nikimuacha kwenye hali hiyo.” “Wewe unamjua Sonia. Anayeweza kumtuliza ni Sam peke yake, huna utakachokifanya sasa hivi, wewe nenda tu, atakuwa sawa. Sam yuko naye.” Nyange naye aliongeza. 

“Mna uhakika? Sitaki ujio wa Paul uwatie nyinyi kwenye hekaheka.” “Wala usijali. Unahitaji sana huu usiku wa leo, mama Sonia. Wewe nenda ukapumzike. Ukirudi kesho naamini kila kitu kitakuwa sawa.” Mama Sonia alikubali kwa shingo upande, akiwa na wasiwasi sana na Sonia. Wakatoka na Paul. 

 Ishimwe & Paul

Wakiwa njiani, Mama Sonia alivunja ukimya. “Hongera Paul, naona umekuwa mtu mkubwa kweli.” “Lakini sikuwahi kufurahia kicho cheo hata mara moja Ishimwe. Maisha yangu yamejaa simanzi kweli.” “Kwa nini tena, wakati mambo yamekunyookea?” Paul alimpeleka mama Sonia kwenye hoteli nzuri sana ya kifahari. 

Walipoingia humo ndani, mama Sonia alianza kubabaika. “Ishi! Unakumbuka tulivyokuwa tukilala chini? Wakati ule sikuwa na hela.” Machozi yalianza kumtoka mama Sonia. 

“Ulioa, Paul?” “Ndiyo. Nilimuoa yule msichana mama aliyenitafutia. Nimezaa naye watoto wawili wakiume.” Mama Sonia aliinama na kuanza kulia kwa uchungu sana. “Ilinibidi kuoa Ishimwe.” “Hongera!” Mama Sonia alijibu huku akilia. 

Paul alibaki kimya kwa muda akimwangalia mama Sonia akilia. Wote walikuwa wamekaa kwenye kochi kubwa hapohapo chumbani. “Pole sana Ishimwe. Pole mpenzi wangu.” Paul alitaka kumkumbatia lakini mama Sonia alisogea akimkwepa. 

“Sikujua kama upo hai Ishimwe, ilinibidi kuoa. Kuna vyeo vingine vinakuja na majukumu. Lakini sikuoa kwa mapenzi na ndio maana ilinibidi kumuoa yuleyule msichana aliyemtaka mama. Maana nilijiambia kama sio wewe basi ni mtu yeyote. Sikutaka tena kuanza kutafuta wanawake wengine. Sijui umenielewa?” “Nimekuelewa Paul. Ndio maana sikulaumu, ni muda mrefu sana umeshapita, ni haki yako kuoa.” “Lakini bado nakupenda Ishimwe. Nakupenda sana.” Paul alimsogelea, akitaka kumkumbatia tena mama Sonia, lakini Mama Sonia alimkwepa tena, akasimama. 

“Siwezi Paul. Wewe ni mume wa mtu sasa.” Mama Sonia alihamia kitandani huku akiendelea kulia, mwishoe aliamua kuingia bafuni kuoga ili atulie.  

Maisha ya Ishimwe baada ya kuachwa na Paul.

Wakati mama Sonia yupo bafuni Paul aliagiza chakula. Mama Sonia alitoka bafuni na kurudi kukaa kwenye kochi lakini mbali kidogo na Paul. Paul alibaki akimwangalia. “Umekuwa mkubwa Ishimwe!” Mama Sonia alitabasamu kinyonge na kujibu. “Miaka emekwenda Paul. Nakaribia wajukuu wawili sasa.” 

“Uliteseka sana?” “Mimi nilishazoea shida, lakini Sonia ndio ameteseka kupita kiasi. Kwanza nilimzalia nyumbani, kwenye chumba changu nikiwa peke yangu. Sikuwa na pesa kabisa. Zile pesa ulizokuwa umeniachia, ziliisha mapema sana, hata kabla mimba haijafikisha miezi mitano.”

“Uliponiacha na mama yako, ni kweli alinipeleka hospitalini, nikafanyiwa vipimo. Nilipogundulika ni mjamzito, mama yako alichanganyikiwa sana. Ilinibidi kutoroka pale hospitalini nikiwa bado mgonjwa baada ya kumsikia mama yako anapanga na daktari wanitoe mimba. Nikaenda kupangisha chumba. Nikatafuta kazi nikakosa, nikaanza vibiashara, ndio vikawa vinanisukuma.” “Mungu wangu mama! Alitaka kumuua mwanangu? Pole na asante Ishimwe. Pole sana kwa mateso.” Mama Sonia alinza kutokwa na machozi. 

“Tumeteseka sana Paul. Kuna siku zilikuwa zikipita bila kula. Tulikuwa tukilala njaa hata siku tatu au nne. Maisha yetu yalikuwa duni sana, hakuna jinsi nikakueleza ukaelewa Paul. Afya yangu ilikuja kuwa mbaya baada ya Sonia kurudishwa nyumbani akiwa mjamzito. Niliumia sana. Nilijua mimi ndiye nilimsababisha kuanza uhuni wakati yeye alikuwa mtoto mtiifu sana na alikuwa anaongoza darasani kila siku tangia aanze shule.”

“Kwa nini ulijilaumu Ishimwe?!”  “Sababu ya umaskini wangu, Paul! Kuna vitu alikuwa akiniomba lakini nilikuwa nashindwa kumtimizia. Kuna kipindi alirudi nyumbani akaniomba nimlipie afundishwe masomo ya ziada ‘tuition’ kwa kipindi hicho cha likizo, kwa kuwa hawakuwa na mwalimu mzuri, lakini nilishindwa kabisa kupata pesa ya ziada, nilikuwa nikihangaika kukusanya ada yake.” 

“Baadaye akaniambia anarafiki yake Shinyanga huwa anamfundisha wakiwa shuleni, wazazi wake wamekubali Sonia aende akasome naye, kwa kuwa yule mtoto analetewa walimu mpaka nyumbani kwao. Nikakubali kwa kuwa nilimuona jinsi alivyo sononekabaada ya kushindwa kumlipia hiyo ‘tuition’.”

“Ndipo safari za Shinyanga zikawa hazimuishi. Shule zikifungwa wazazi wa yule binti walikuwa wakija kuwachukua wote wawili mpaka huko kwao, akikaa huko kidogo anaomba aletwe huku aje anione. Kwa hiyo akawa akiletwa na huyo dereva, akikaa na mimi siku mbili tatu, anaomba kurudi kule tena ili aendelee na kusoma, haya dereva anatumwa tena anakuja kumfuata.”

“Yakawa maisha ya kuhangaika kweli kwake. Masomo anataka, kuishi mbali na mimi, hawezi. Si ndio baadaye akaja kupata mimba, nikajua zile safari za Shinyanga ndizo zilizomponza mwanangu. Nilijilaumu kupita kiasi. Nilichukia hali yangu ya umaskini, hofu ya kesho ilinitinga nikiwa na watoto wawili sijui nawalisha nini au tutaishije.”

“Kumbe yule baba wa rafiki yake alimbaka mwanangu huku akimtishia akija kuniambia atanifunga jela na kunirudisha Rwanda.” Mama Sonia aliinama nakuzidi kulia kwa uchungu. “Pole sana Ishimwe. Daah!” Paul alisimama huku ameweka mikono kichwani. 

“Nilianza kuugua sana, nahisi nilikuwa na pressure lakini sikuwa nikijua, mawazo yalikuwa hayaishi Paul. Nilijua kabisa nilikuwa mgonjwa lakini nilishindwa kabisa hata kufikiria kwenda hospitali au hata kumwambia Sonia kinachoendelea kwenye mwili wangu kwa kuwa sikuwa na pesa kabisa na kazi ngumu nilikuwa siwezi kufanya, yeye ndio alikuwa akihangaika. Sonia aliteseka sana.”

“Alikuwa akihangaika yule mtoto kufanya kazi mchana na usiku. Nilikuwa nikimuona jinsi anavyoumia akitoka kwenye kuhangaika lakini sikuwa na jinsi ya kumsaidia. Mimi nilikuwa mgonjwa sana, na nilimuona alivyoingiwa na hofu baada ya kumpata yule mtoto. Hakuwa akijua lolote juu ya yule mtoto. Ilinibidi kuingilia kati na mimi kuwa mama wa Kana angalau kumpunguzia matatizo, lakini haikusaidia sana.”

“Kana naye akaanza kuumwa karibu ya kufa. Nakumbuka siku moja nikiwa nimempaka yule mtoto kwenye kile chumba, anachemka joto, huku nikizuia machozi yangu nisimshitue Sonia aliyekuwa akilia na yeye, kwa kukata tamaa. Nilijua kabisa yule mtoto asingefika asubuhi yake.” Mama Sonia na Paul wote walikuwa wakilia. 

“Sonia anamsimamo kama wako Paul. Akiamua jambo lake, hakuna chakumbadilisha. Nikijua hatuna hela hata shilingi pale ndani ya kumpeleka yule mtoto hospitali au hata yakumnunulia yule mtoto dawa ya kushusha homa, kumbe mwenzangu ana begi lina mamilioni ya pesa, aliliokota siku alipotoka kwenda kukopa pesa ya kumpeleka mtoto hospitali lakini alipanga kumrudishia mwenyewe ambaye ni Sam. Hakuniambia kabisa.”

“Tumekaa pale ndani, tukisubiria kifo cha Kana, huku mimi mwenyewe naumwa sana mgongo, ndipo Sam na rafiki yake wakaingia kuchukua begi lao. Kuanzia hapo maisha yetu yalibadilika sana. Sam ndio akawa kama binadamu aliyetumwa na Mungu kutuokoa.” “Mgongo ulifanyaje?” Paul akauliza akikausha machozi yake. 

“Kuna siku nahisi ‘pressure’ ilikuwa juu sana, nikaanguka nikiwa bafuni, tokea siku ile nikaanza matatizo ya mgongo.” “Daah! Pole sana Ishimwe.” “Niliugua sana Paul. Sana. Hata Sam alipomtafutia Sonia kazi huku Dar, akaondoka na kuniacha na mtoto wake aliniacha nikiwa mgonjwa sana lakini sikutaka ajue. Nilikuja kuzidiwa hata kitandani nilikuwa siwezi kutoka.”

“Lakini Sam alinihudumia mpaka nikapona. Yeye ndio alikuwa akija kumchuka mtoto kukaa naye au alikuwa akimtuma rafiki yake aje amchukue mtoto akae naye kipindi hicho natibiwa. Nilimuomba asije kumwambia Sonia kabisa, nilijua Sonia akijua ninaumwa, angerudi akae na mimi, halafu maisha yarudi kuwa magumu vilevile. Anaupendo sana Sonia, kama wewe Paul.” Paul alitabasamu huku akifuta machozi. 

“Sam ndiye aliyemtoa Kana mtaani na kumuanzisha shule. Tena ilikuwa shule nzuri kweli ya kufuatwa na basi palepale nyumbani na ndiye aliyemrudisha Sonia shule. Nilishakata tamaa mwenzio ya Sonia kusoma, lakini Sam alihangaika naye kweli. Ndiye alikuwa akimpeleka na kumrudisha shule kila siku na kumfundisha mpaka pale alipo Sonia ana ‘Advan…Diplo...’ Bwana sijui mnaitaje wenyewe. Lakini upande wa mambo yenu hayo ya mahesabu.” “Advance Diploma in Accounting?” Paul alimsaidia kumalizia kwa kuuliza. 

“Eheee, hivyo hivyo ulivyosema.” Wote walicheka. “Daah! Sam alibeba mzigo mzito kweli!” “Sana. Kumbuka Sonia alikuwa ameishia kidato cha pili. Alihangaika naye mpaka alipo anza chuo ndio kina Nyange wakamsaidia. Huku anahangaika na Sonia, na bado alikuwa akipiga simu kuwasiliana na walimu wa Kana wakati mimi na Kana bado tupo Mwanza, kufuatilia maendeleo ya Kana shuleni.”

“Wakati mwingine alikuwa akija kutuona kule Mwanza na kutuachia pesa, tena hapo ni baada ya kutununulia kila kitu ambacho aliona tunakihitaji.” Mama Sonia alieleza kila kitu na kumuacha Paul analia kama mtoto. 

“Ndio maana Sonia ananichukia sana. Hata mimi ningechukia. Mwanangu alifanya kazi za kwenye majumba ya watu, kama kijakazi!?” Paul alikuwa haamini. “Mungu wangu! Sijui nitamtizamaje mama yangu tena? Amenikosea kupita kiasi.” Walikesha usiku huo wakiongea. Paul naye alimueleza kila kitu kuanzia siku walipoachana mpaka walipokutana. 

“Paul baada ya kuachana na Ishimwe.”

         “Si unakumbuka nilimaliza hapo chuo cha Mlimani nikiwa nasomea sheria?” “Wakati ule nilikuwa hata sielewi kitu.” Paul akacheka. “Basi wakati ule tulikuwa tunalala chini, mwenzio nilikuwa na shahada ya sheria.” Wote walizidi kucheka. 

“Haya, nilivyotoka pale baada ya kuagana na wewe, nilikuta mizigo yangu yote kwenye gari. Sikurudishwa nyumbani, nililetwa mpaka hapa Dar. Kesho yake nikaambiwa na mama niende ubalozi kwenda kuomba Visa, yeye alikuwa ameshaandaa karatasi zote nilizokuwa natakiwa na kumbe nilikuwa nimeshachelewa chuo. Mama alikuwa amenitafutia chuo cha kusomea mambo ya uongozi nje ya nchi.”

“Kwa kuwa nilikuwa nimechelewa chuo na si unajua Mama alikuwa kiongozi mkubwa sana wakati ule, kwa hiyo niligongewa Visa siku ileile na mama akasema niondoke kesho yake. Nikamwambia siwezi kuondoka mpaka niagane na wewe, akaniambia nikiwa uwanja wa ndege nimpigie tuongee kwa kuwa ilishakuwa usiku na yeye alishatoka hospitalini.”

“Kesho yake wakati nipo uwanja wa ndege nilimpigia simu zaidi ya mara tano akawa hapokei. Nikaamua kumpigia simu baba, nikamwambia amwambie mama, asiponipa Ishimwe niongee naye, sitaondoka. Hata dakika haikupita akanipigia, kuniambia walikuta tatizo kubwa sana tumboni, ikabidi upangiwe kufanyiwa upasuaji huku akinilaumu mimi kwa nini sikukupeleka hospitali mapema.”

“Nikamuuliza kwa nini sasa hakutaka kupokea simu yangu ili anipe hizo taarifa mapema? Akasema hakutaka kunitia wasiwasi, mpaka utakapotolewa chumba cha upasuaji na kuhakikisha hali yako inaendelea vizuri ndipo angenipigia.”

“Akaendelea kuniambia ulicheleweshwa kuingizwa chumba cha upasuaji kwa hiyo bado upo ndani. Aliniambia nisiwe na wasiwasi baada ya kutolewa na ukiamka, atanipigia ili tuongee. Nilisubiri Ishimwe mpaka ndege ilitaka kuniacha.”

“Nikampigia tena mama, akasema bado hujatoka chumba cha upasuaji. Ikanibidi kuondoka. Nilipofika tu, nikampigia simu kukuulizia hali yako. Ndipo akaniambia ulikufawakati wa upasuaji. Nilichanganyikiwa Ishimwe. Nililia na kujilaumu kupita kiasi.”

“Nilimpigia simu baba nikamsihi sana, wakuzike sehemu nzuri. Maskini baba najua mama kama kawaida yake alimtishia ili anidanganye. Baada ya siku nne, walinitumia picha za kaburi lako. Sikutaka kurudi kabisa Tanzania kwa muda.”

“Nilikaa hukohuko chuoni miaka yote bila kutaka kurudi nyumbani siku za likizo huku nikifanya kazi kama punda kwa hasira. Nilikuwa nikijilaumu nikijiambia kama sioumaskini wangu usingekufa, labda ningekuwahisha hospitali wakati ule ungepona. Nilichukia ile hali ya umaskini, nikawa nikifanya kazi usiku na mchana kutafuta pesa, mpaka nilipomaliza chuo, nikawa nina mwaka mwingine mmoja wakukaa hukohuko kufanyia mazoezi ya nilichosomea, nao huo mwaka nikautumia vizuri sana kwa kufanya kazi kwa bidii.”

“Baada ya miaka minne tangia kuondoka hapa nchini nilirudi nyumbani nikiwa nina cheti kizuri sana na pesa yakutosha. Sikutaka kurudi tena kuishi nyumbani na mama. Lakini nilimuomba anipeleke kwenye kaburi lako. Akakubali, akanipeleka kwenye kaburi alilosema ni lako, nikajengea, nakurudi zangu Dar.” “Pole sana Paul.” Paul alitulia kidogo. 

“Baada ya muda mfupi mama akanipigia tena simu kuniambia amenitafutia kazi, niende nikaonane na waziri wa sheria. Huyo Waziri akanipa kazi nzuri sana, nikaanza kuingiza pesa, lakini kila nilipokuwa nikikumbuka shida tulizopata wote na hela nilizokuwa nikiingiza wakati ule ndivyo chuki na mama ilivyozidi, siku hadi siku.”

“Sikuwa nikienda nyumbani wala kuwapigia simu kuwajulia hali mpaka baba alipougua sana, akatuma mtu aje aniite. Nilimkuta yule msichana pale nyumbani akiwahudumia mama na baba. Wote walikuwa wagonjwa sana, na yule dada alikubali kuacha kazi yake ya ualimu huko Mororgoro na kukaa nyumbani kwetu, akiwahudumia wazazi wetu.”

“Nilikaa naye pale tukiwauguza wazazi wangu mpaka muda wangu wakurudi tena kazini ulipofika. Yeye ndiye akawa mtu tunayewasiliana naye pale nyumbani kuwajulia hali wazazi. Dada zangu wote na kaka zangu wote wakawa wakiwasiliana na yule msichana pale nyumbani. Yeye ndio akawa kila kitu pale nyumbani mpaka baba alipofariki.” “Pole Paul. Kumbe baba alifariki?” 

“Aliugua sana kisukari. Alianza kuoza akiwa hai, lakini huwezi amini Ishimwe, yule dada alikuwa akimuuguza bila kinyaa! Kabla ya kufariki baba, alituita watoto wote pale nyumbani nakutuambia yule msichana ni moja ya watoto wake pia. Hata atakapokufa tusimsahau. Baada ya siku chache baba alifariki, lakini mama akaja kupona kabisa.” Paul alianza kutafuta maneno. 

“Unakumbuka yule msichana nilikwambia alikuwa akifanya kazi Morogoro?” “Nakumbuka ulisema alikuwa mwalimu.” Ishimwe alijibu. “Sasa kwa kuwa mimi ndiye nilikuwa hapa Dar… Si unakumbuka dada zangu wote wawili na kaka yangu yule mkubwa wote hawaishi hapa nchini?” Ishimwe aliona Paul anaanza kubadilika. Kubabaika kukawa kwingi. Alimtizama kwa muda. 

Akaamua kufupisha. “Unajua pale kwenu mimi nakufahamu wewe zaidi kuliko ndugu zako wote? Na sikuwahi kukutana na hao dada zako wala kaka yako.” “Kweli kabisa Ishimwe.” Paul alikaa vizuri kama anayetafuta aanzie wapi. 

“We Paul! Kwani kuna nini?” “Sasa. Kama nilivyokuwa nimekwambia, vile baba alivyosema yule msichana ni kama ndugu sasa. Kwa hiyo kila alipokuwa akija Dar, alikuwa akishukia nyumbani kwangu. Unakumbuka nilikwambia wakati nipo masomoni nilifanya sana kazi?” “Nakumbuka.” 

“Na kumbuka bado mama alikuwa akinisomesha na kunitumia pesa za matumizi nikiwa kule, kwa hiyo nilikuwa na pesa yakutosha. Nimejenga nyumba nzuri sana, Ishimwe. Nitakupeleka uione.” “Hongera.” Paul alifikiria kidogo. 

“Yule msichana akawa akija pale kwangu wakati mwingine wa likizo zake. Kama nilivyo kwambia ndugu zangu hawapo hapa, mimi tu ndio nikawa ndugu yake niliyebaki hapa mjini. Kwa hiyo akawa anakaa pale hata ‘week’ moja au mbili.” Ishimwe alimuona vile Paul alivyoanza kubabaika tena na kurudia mambo aliyokwisha kumsimulia. 

“Unajua baada ya kifo chako, niliamua nisioe tena?” Ishimwe alibaki akimwangalia, Paul anavyojitetea. “Sikutaka kuoa tena, sababu ya hofu ya makosa niliyofanya kwako, nikiogopa yasije kujirudia, lakini baadaye yule msichana akanipigia simu akiwa Moro, kuwa ule ujauzito unamsumbua sana, na hospitalini wamemshauri apumzike kabisa, apate ‘bedrest’ lasivyo atapoteza watoto.” Mama Sonia akakunja uso, akawa hajaelewa. 

“Mbona sijaelewa Paul! Ujauzito tena?” “Ndiyo. Alipata mimba.” “Mimba ilikuwa ya nani?” Paul alitulia kidogo. “Yak…” Paul alikohoa kidogo kama kusafisha koo huku Ishimwe akimtazama kwa makini. “Ya nani?” “Aliniambia ni ya kwangu Ishimwe.” 

“Sikuelewi Paul. Kwani mlikuwa na mahusiano?! Si ulisema hukutaka kuoa tena!?” “Siwezi kuyaita mahusiano! Lakini siku moja tulitoka naye kwenye harusi ya rafiki yangu, tukarudi nyumbani ilikuwa usiku, halafu unajua kwenye harusi pombe kido..” “Hebu subiri kwanza Paul. Umeanza kunywa pombe lini?!” “Sio mimi Ishimwe, ni yeye!” Ishimwe alibaki akimwangalia Paul kwa macho ya kumsuta.

“Yeye ndio alikuwa amelewa, aka…” “Paul jamani, mbona unapata shida wakati mimi nakuelewa tu. Ulijua kama nimekufa, na ulikuwa karibu na yule binti. Inaeleweka kabisa. Sikulaumu!” Paul alibaki ameinama kama mtoto aliyebambwa na sukari mdomoni. 

“Lakini tulitengana na yule mwanamke, Ishimwe.” Ni kama Paul alijaribu kujiteteakwa Ishimwe “Kwa nini tena?!” “Tulikuwa na ndoa ya ajabu sana, huwezi amini.” Paul alimtizama Ishimwe kwa kujikaza sana.

“Kumbe baada ya hapo mlifunga na ndoa kabisa!? Hongera sana Paul.” “Acha basi Ishimwe!” Mama Sonia alianza kucheka. “Sasa nini Paul? Kumbe mwenzangu una ndoa halali!” “Si baada ya kushika hiyo mimba, ikabidi kumuoa tu. Mama alisema anaheshimiana sana na wazazi wa yule binti kwa hiyo lazima kumuoa. Ndio tukafunga ndoa ya harakaharaka, kabla watoto hawajazaliwa. Walikuwa ni mapacha.”

“Baada ya kujifungua tu akaanza vituko kama sio yeye! Alibadilika sana. Aliyatoa makucha yake yote. Alizidisha pombe kupita kiasi. Alikuwa akirudi nyumbani mara zote amelewa. Kazi hataki kufanya, hata baada yakujifungua alikataa kufanya kazi tena. Hakuna siku iliyokuwa ikiisha kwa amani hata siku moja.”

“Siku moja nilikuwa nimetoka safari nawakuta wanatukanana na rafiki yake pale ndani, tena mbele ya watoto.” “Rafiki yake?” Ishimwe akauliza akiwa hajaelewa. 

“Si mama. Mama si ndiye alikuwa akitaka nimuoe. Walianza kufichuliana siri zao mbele yangu. Mipango waliyokuwa wakipanga ili nimuoe. Kumbe mama ndiye alimwambia aache kazi ahamie pale nyumbani kumuuguza baba, ili nimuone anavyojali familia yetu kama wewe ulivyokuwa unawajali wao.”

“Alimwambia eti mimi nawapenda sana wazazi wangu, ndio maana nilikataa kuishi nchi za nje kama wenzangu ili nikae karibu nao, na kilichonivutia kwako ni vile ulivyokuwa ukiwatunza pale nyumbani kipindi kile. Kwa hiyo nilivyoona vile, ndio maana nikakupenda.”

“Haya, akaendelea kusema hata kuja mara kwa mara pale nyumbani kwangu akitokea Morogoro, ulikuwa ni mpango wa mama, kumfanya awe karibu na mimi, na kunishawishi kimapenzi mpaka nimuoe na akaniambia nisipokubali kumuoa ajishikishe mimba.” “Paul!” Ishimwe hakuamini. 

“Kweli tena! Nakwambia nilikuwa ndio nimefika kutoka safari, nilitafuta mahali pazuri pakukaa ili niwasikilize vizuri. Walikuwa wakitukanana kama mtu na mke mwenzake. Yule dada anasema waziwazi yeye hakuwa akinipenda, ila mama na wazazi wake ndio waliokuwa wakimshawishi wakimwambia mimi ni mtu mzuri sana.”

“Alikuwa akilalamika nakusema wamemuaribia maisha yake. Yeye alikuwa na mpenzi wake huko Morogoro walianzana tokea wapo sekondari, wakamwambia amuache mpenzi wake kwa kuwa hajasoma na hana pesa, kwangu atapata maisha mazuri yenye furaha na pesa nyingi. Akaendelea kulalamika hiyo furaha aliyokuwa ametarajia kuipata kutoka kwangu hajaipata zaidi ya mateso.” 

“Alisema nina roho mbaya, wala sina mapenzi ya kweli. Hapo na yeye ndio alikuwa amerudi nyumbani, siku tatu aliondoka akaacha watoto na msichana wa kazi. Sasa mama alikuwa amekuja Dar, akaamua kuja kusalimia pale nyumbani akaambiwa wote tumesafiri, ndio akaamua kukaa na watoto.”

“Alinipigia simu akiniuliza tunawezaje kusafiri wote na kuacha watoto na msichana wakazi peke yake, nikamwambia mama yao yupo. Ndio akaniambia ni siku ya pili hayupo hapo nyumbani. Na aliambiwa na msichana wa kazi kila ninaposafiri na yeye alikuwa akiondoka mpaka siku za kukaribia kurudi kwangu ndio na yeye alikuwa akirudi.” “Haiwezekanikani!” Ishimwe alihisi ni stori tu. 

“Sikutanii Ishimwe, nilikuwa na ndoa mbaya hujawahi ona. Nilikuwa kwenye mateso ambayo siwezi nikakusimulia ukaelewa. Unatoka safari umechoka au kazini hujala siku nzima, ukifika nyumbani, ni ugomvi, hakuna chakula, mke amelewa. Msichana amelemewa na watoto wakiume wawili. Na wale watoto walikuwa watundu, kupita maelezo.”

“Nashukuru Mungu nilipata dada aliyekuwa mvumilivu. Alikuwa akijitahidi kweli na mambo ya watoto. Lakini hakuweza kufanya jambo jingine mbali na wale watoto. Kwa hiyo ndio nilikuwa nikitoka kazini nianze kumsaidia kazi nyingine, kama kupika. Ukitafuta msichana wa pili, hawakai sababu ya mama mwenye nyumba kelele na matusi.” 

“Jamani Paul, pole sana. Ikawaje sasa?” “Mama aliponipigia tu simu nakuniambia watoto wameachwa na msichana wa kazi peke yao, ikabidi kesho yake nirudi nyumbani haraka sana, ndio nikawakuta wanatukanana na yeye anasema anataka kuondoka amechoshwa na mimi.” “Watoto?” 

“Uzuri hakuwa akinitaka mimi wala watoto. Kwa hiyo alitaka tugawane mali tu aondoke zake.” “Paul! Si ulisema hakuwa akifanya kazi? Sasa mnagawana vipi mali?” “Lakini alikuwa mke wangu Ishimwe! Na kwa kuwa sikuwa nataka tupelekane mahakamani, nilimwambia achukue kila kitu kasoro ile nyumba niliyokuwa nimeijenga kwa jasho langu kabla hajaja kwenye maisha yangu, aondoke. Sikutaka aniharibie jina kabisa. Nilijua siku moja nitafika hapa nilipo, nilianza kutengeneza njia yangu mapema sana. Sikutaka aje aniharibie ndoto zangu.”

“Hata mama mwenyewe alikuwa ameshachoka naye. Kumbe na yeye alikuwa akiambiwa mambo yanayoendelea pale ndani na msichana wa kazi lakini hakuwa akitaka tuongelee, sababu ya aibu. Alikuwa akisutwa moyoni kwa aliyonitendea na kuniona ninavyohangaika na yule mwanamke bila hata kulalamika, Ishimwe.”

“Nilimkubali kuwa ni mke wangu, vilevile alivyo. Isingekuwa kutaka kuondoka yeye mwenyewe, wala nisingemfukuza. Nilikubali kuishi naye hivyohivyo. Lakini aliondoka nakuniachia watoto wangu. Alipoondoka tu, sikutaka kurudia tena yale maisha Ishimwe, nilikwenda kwa mwanasheria kukamilisha maswala ya talaka. Nikahakikisha ameyapata hayo makaratasi ya talaka na ameyasaini.”

“Tumeachana kwa amani, na sikia mwenzangu alirudi kwa yule mwanamme wake wanaishi naye tena. Lakini maisha yangu yamekuwa ya upweke kweli Ishimwe. Sana. Japokuwa kwa nje ninaonekana nina maendeleo, lakini ndani ni kama mgonjwa mahututi. Najiona natembea kama mfu!” “Pole sana Paul.” Mama Sonia, alimuhurumia sana Paul, akamsogelea karibu, akamuegemea huku akimwangalia na kumshika viganja vyake taratibu. 

“Sasa watoto wanaendeleaje na shule?” “Daah! Hao nao ni shida nyingine Ishimwe. Sijui nikukosa malezi mazuri ya mama au vipi? Sijui! Najiuliza nimekosea wapi kuwalea wale watoto, sipati jibu.”

“Watoto wananiendesha kama gari bovu. Utakuja kuwaona. Ndio maana ukiniambia Sonia anapenda sana shule, nafarijika kweli, naona sijaambulia patupu. Mmoja hataki shule kabisa, hasikii chochote kama hana masikio, angalau huyo mwenzake anakinafuu kidogo. Anaenda shule lakini hakuna matokeo mazuri anayoyaleta hapo nyumbani hata siku moja. Lakini angalau yeye anaelekea sio huyo kaka mtu. Ni shida Ishimwe.”

“Walitakiwa wawe kidato cha tano mwaka huu, lakini huyo mmoja aliacha kwenda shule kidato cha pili na mwenzie Walimu walishauri arudie, ndio yupo kidato cha tatu. Sina raha hata kidogo! Kila nikifikiria mwisho wa wale watoto, nashindwa kujua utakuwa nini!”

“Kazi yao ni kubadili simu kila ikitoka simu mpya na wao wanataka, na kununua nguo na viatu vya gharama basi, hawawazi kitu chochote kile kichwani mwao.” Paul alipotelea mawazoni. 

Mama Sonia alimrudisha kimawazo kwa kuzungusha mkono wake kwenye viganja vyake. Paul akamtazama. “Pole.” Ishimwe aliongea kwa sauti ya upole na upendo sana, akimuhurumia Paul. “Asante Ishimwe. Na wewe? Ulipata mwanaume?” “Mwenzio sikutaka kuolewa tena. Kuna kipindi nilipata mwanaume lakini, mmmh! Nilikuja kuachana naye wala hatukufika mbali.” “Alikufikisha kitandani?” “Paul wewe jamani!? Swali gani hilo?”

 “Nataka kujua Ishimwe.” “Mbona wewe ulioa?” “Mwenzako nilioa baada ya kuambiwa umekufa! Sasa wewe uliwezaje kulala na mwanaume mwingine ukijua nipo hai?” “Sikulala naye bwana! Ndio kilicho tugombanisha.”

“Alitaka mapenzi wakati hata hatukuwa tukifahamiana vizuri, halafu sikujua atampokea vipi Sonia, nikaona anaharaka ya mapenzi hataki hata kuzungumzia swala la maisha yetu ya baadaye. Nilipo achana naye sikutaka kuwa na mahusiano mengine ya kimapenzi, mbali na wewe. Naheshimu ahadi yangu kwako Paul!” “Asante Ishimwe na pole sana.” Walibaki wakiangaliana wasijue waanzie wapi. 

Lakini Paul alimuona Ishimwe na mawazo fulani. “Vipi Ishi?” “Nikuulize swali Paul?” “Uliza tu.” “Naomba ufikiri kabla hujanijibu na ninakuomba usinielewe vibaya.” Paul akamtizama Ishimwe kwa makini na kukubali. 

“Sawa.” “Ulisema yule msichana alikuwa akiishi Morogoro, na alikuwa na mpenzi wake tokea zamani?” “Ndiyo.” “Sasa ulijuaje kama mimba ilikuwa yako? Au kama watoto ni wako?” Paul alishituka sana kama mtu aliyeshituliwa kutoka usingizini.

 “Aaaaa…., aliponia…” Paul alisimama baada yakujikuta hana chakujibu, akaweka mikono mfukoni huku anazunguka zunguka chumba. 

 *********************

Paul aliendelea kuzunguka ndani ya hicho chumba, akiwaza hili na kuunganisha lile. Mwishowe ilimbidi Ishimwe amshitue. “Nataka nilale Paul. Kesho niwahi kurudi kwa watoto.” Mama Sonia alihamia kitadani, akajilaza. Paul alikaa pembeni yake akimwangalia. 

“Pole Paul.” Paul alitabasamu huku akimwangalia, wazi alionekana ana mawazo. “Unafikiri Sonia atanipokea kama baba yake?” “Wewe ukimtaka Sonia, uwe karibu na Sam. Anampenda sana Sam.” “Wameoana?” “Ndio wapo kwenye maandalizi ya harusi yao.” “Daah!” Paul alizidi kuumia.

“Tumepitia pagumu sana Paul. Maisha yetu yalikuwa hayatabiriki, ndio maana tumeangukia kwenye mikono ya Sam. Hata mimi sifurahii hivyo wanavyoishi. Lakini ndio kwa mara ya kwanza katika maisha yetu tunapata nyumba ya kuishi na Sam kumtambua Sonia kama mama mwenye nyumba.”

“Anampenda sana Sonia. Alipogundua tu kama Sonia ni mjamzito, alimpa zawadi ya gari. Japokuwa hana pesa nyingi, lakini anamjali sana Sonia. Anajitahidi sana kumtimizia mahitaji yake.”

“Sasa hivi Sam na Nyange wapo kwenye maandalizi ya kwenda kumtambulisha Sonia kwao, kabla ya harusi.” “Nitaenda naye mwanangu. Ndiye binti yangu wa pekee. Lazima niwe naye karibu sana. Naamini atanielewa na kunisamehe.” 

“Mbishi huyo, kama wewe Paul. Aking’ang’ania jambo lake! We utamuona tu.” Paul alicheka. “Naamini atanielewa bwana. Kwanza nimkamate huyo aliyembaka. Hatakaa akasahau maishani. Atajuta siku aliyolala na mwanangu. Atalaani kuzaliwa mwanaume. Hivi hapa nishatuma watu wapo njiani wameenda kumfuata.” “Paul wewe!” 

“Unafikiri nakutania? Kesho asubuhi nimewaambia wawe wamemleta hapa. Nataka kumuona uso wake.” Mama Sonia alibaki ametoa macho. “Sikubadilisha uraia mwenzio.” “Uliniambia pale mahakamani. Usiwe na wasiwasi. Nitafuatilia, kila kitu kitakuwa sawa Ishimwe, usiogope.” Mama Sonia alifikiria kidogo. 

“Unafikiria nini?” Paul akamuuliza tena. “Unafikiri Nyange na mkewe watarudishiwa mali zao?” “Hiyo ndio itakuwa shukurani yangu kwao, kwa kuwapokea nyinyi, nakumsomesha Sonia na Kana. Nitahakikisha wanarudishiwa kila kitu chao, hata ada waliyowalipia Sonia na Kana nitawarudishia.”

“Kesho nitampa mtu hiyo kazi ya kufuatilia ada waliyokuwa wakiwalipia, nikipata jumla yake, niwalipe. Tena mapema sana.” Mama Sonia alitoa machozi ya furaha. “Asante sana Paul. Asante mpenzi wangu!” “Wewe si umenikataa?” Mama Sonia alicheka huku anafuta machozi. 

“Uliniambia umeoa bwana Paul! Niliheshimu ndoa yako.” Paul alicheka. “Nakupenda sana Ishimwe. Unakumbuka tulivyokuwa tuna..” Mama Sonia alikaa na kumbusu Paul. “Nilikuwa na hamu na wewe mtoto wa Kinyarwanda, mpaka nilikuwa nahisi kuchanganyikiwa.” Mama Sonia alicheka. 

“Mimi mwenyewe nilikuwa na hamu na wewe Paul!” Mama Sonia aliendelea kumbusu Paul mfululizo bila kumuachia huku machozi yakimtoka. “Asante Ishimwe.” Paul alimuweka kitandani vizuri huku akimtazama kwa uchu. Usiku huo ulikuwa mfupi sana kwa mama Sonia na Paul. Walikumbushana mambo mengi sana. Vilijaa vilio na vicheko kati yao. 

 *********************

Simu ya Paul ndiyo iliyowatoa usingizini. “Nakuja sasa hivi.” Paul alikata simu mara baada ya kujibu kifupi. “Saa ngapi?” Ishimwe akauliza. “Imeshakuwa saa sita. Mpaka nimepigiwa kwenye hii simu yangu ya mkononi, ujue nimetafutwa sana.” “Wanao wako wapi?” “Nyumbani. Lakini wakubwa, hawana shida. Nimewaaga jana.” “Umewaambiaje sasa!?” Paul alicheka. 

“Naomba nikurudishe nyumbani, halafu nitakufuata tena baadaye. Nataka nikajitambulishe kwa huyo Mzee aliyembaka mwanangu.” “Wameshamleta?!” “Nilikwambia, niliwapa amri, asubuhi nimkute hapa Dar, kituoni akinisubiri.” Mama Sonia alibaki na mshangao. 

 Nyumbani Kwa Sam Tena

Waliporudi nyumbani kwa Sam na Sonia, walikuta kila mtu sebuleni kasoro Kana na Briana walikuwa nyuma ya nyumba wakicheza na Brayan. Paul alisalimia tena kwa kushika mkono kila mtu mpaka alipomsogelea Sonia. Sonia aliinama tu bila kumwangalia wala kumpa mkono. 

“Sikuwa nimemkimbia mama yako Sonia! Niliambiwa amekufa! Na kaburi hili hapa nimelijengea.” Paul alitoa simu yake ili kumuonyesha Sonia picha lakini Sonia hakutaka hata kuangalia. Alibaki ameinama pembeni ya Sam akichezea vidole vyake. 

“Na nina kuahidi kumshugulikia yule mzee aliyekutendea wewe ukatili. Nimetuma watu jana usiku Shinyanga akamatwe, wameshamleta. Ndio naenda kuonana naye sasa hivi. Nitahakikisha analipa mabaya yote aliyokutendea.” 

Sonia alimwangalia kwa mshituko mkubwa sana. “Unamaanisha baba yake Kana?!” Paul alitulia kidogo. “Mama?!” Sonia alimgeukia mama yake. “Ndiyo, Sonia.” Mama yake alijibu kwa upole akiwa ameishiwa nguvu. “Kwa hiyo unataka mwanangu akue kama nilivyokuwa mimi?”

“Umeshafikiria juu ya Kana lakini? Au bado unajiangalia nafsi yako tu?” Sonia alikuwa akitetemeka kwa hasira huku akimwangalia Paul, baba yake. “Hata hivyo sikushangai, hujui umuhimu wowote wa baba katika maisha ya mtoto. Unataka yule baba afungwe kifungo cha maisha, halafu mtoto wangu akose baba maishani, kama mimi? Halafu aje ajue kuwa baba yake alinibaka akae akimchukia baba yake daima.”

“Kama wewe ulishindwa kuwa baba kwangu, nakuomba sana Paul, uniache mimi na maisha yangu na mtoto wangu. Unafikiri mimi ni mjinga, kushindwa kumshitaki mpaka leo? Hata hivyo napoteza muda wangu kukuuliza maswali ambayo hutakaa unijibu, wewe uliyezaliwa kwenye familia ya kitajiri, ulikuwa unalishwa milo yote, unasomeshwa nchi za nje! Ndio maana ulipojua mama yangu ni mjamzito ulimkimbia na kwenda kuoa mwanamke mwengine.”

“Unamdanganya ulipiga simu waje kukusaidia kumpeleka hospitali wakati mjamzito, kumbe nimipango uliyokuwa umefanya na mama yako, ili kumtelekeza mama yangu.” “Sio kweli Sonia. Ishimwe ni shahidi.” “Kwa kuwa unamuona anashida ndio maana unamchezea akili zake. Kila unaporudi kwenye maisha yake anamkuta ana shida ndio maana kila unalomdanganya anakubali tu. Lakini sio mimi, Paul.” 

“Waliniambia watamrudisha Rwanda.” Paul alijitetea kwa shida sana, kwani alikuwa amepatwa na mshituko mkubwa sana. Hakutegemea Sonia kumjia juu kwa kiasi kile. 

“Kwani Rwanda ni kuzimu mpaka ushindwe kuwa na mwanamke unayempenda? Ulimuacha mjamzito tena mgonjwa! Leo unarudi na picha za makaburi, ili uzidi kumdanganya zaidi. Kweli sheria kwako wewe sio kazi tu bali ipo damuni, ndio maana unauwezo wa kuitumia kila mahali kufunika madhambi yako.”

“Umeshasoma magazeti ya leo lakini? Magazeti yote yameonyesha “Judge Mkuu” akiwa amemkumbatia mwanamke huku anambusu. Umemtambulisha pale mahakamani, mbele ya waandishi wa habari kama mama watoto wako. Wakati unafanya hayo yote ulikuwa ukifikiria lakini au ulikuwa unafanya tu?”

“Umeshafikiria itakuaje kwa huyo mama yako ‘mungu mtu’ akijua kama mama yangu yupo hapa nchini? Umeshafikiria umeshamuweka mama yangu kwenye mazingira hatarishi kwa kiasi gani? Kwanza wewe kama Judge Mkuu na mume halali wa mtu? Umeshafikiria maisha yangu yanakuaje wakishamuweka mama yangu chini ya ulinzi?” “Sitaruhusu hayo yote yatokee, Sonia.” 

“Kama uliruhusu wakati ule yatokee na kuamini maneno ya mama yako uliyejua wazi, anamchukia mama yangu kupita kiasi, sasa hivi litakalokuwa limebadilika ni nini? Wewe una ndugu wanao kuzunguka, tena wote wana uwezo, mimi sina. Mama yangu ndiye ndugu pekee niliyenaye hapa duniani. Ndiye baba yangu, mama yangu na ukoo mzima nilio nao hapa duniani. Ni yeye peke yake na….” “Na mimi nipo Sonia. Sitawaacha tena.”

 “Sasa hivi ndio upo? Ulikuwa wapi wakati nalala njaa? Nilikuwa nazunguka miguu peku, bila viatu huku ninachomwa na jua kutafuta kazi. Unajua tulikuwa tunauza chakula Sokoni mimi na mama ili tuishi?”

“Unajua ni mara ngapi mwili wangu ulikuwa ukishikwa na wateja niliokuwa nikiwauzia chakula, bila ridhaa yangu? Lakini ilinibidi kuvumilia bila kumwambia mtu yeyote ili angalau haohao wateja wanao nidhalilisha mimi, kesho yake warudi kutuungisha, angalau tupate pesa ya kuishi na mwanangu Kana.” Sonia alianza kulia. 

“Unajua jinsi nilivyokuwa nikijipendekeza kwa kina Fau lakini? Nilikuwa namuonea wivu rafiki yangu kuwa na wazazi wote wawili wanaompenda na kumjali binti yao. Nilikuwa nikijipendekeza ili na mimi angalau tukifunga shule nilipiwe “tution” kama Fau, ili kupata elimu ya bure au na mimi nipate simu, au vitabu vya kusoma, au nguo mpya. Wakati wewe uko Ulaya unasoma na kuoa na kuzaa. Unajua matokeo yake lakini?”

“Nilibakwa Paul! Sababu yakutaka elimu na vitu vya bure kutoka kwa mababa za watu, NILIBAKWA. Tena sio mara moja. Alinilevya yule baba, na kuendelea kutumia mwili wangu siku mbili mfululizo, usiku na mchana anatumia mwili wangu bila huruma. Aliporidhika na kuchoka, alinitukana sana huku akinionya nisiwahi hata siku moja kumuita yeye baba, kwa kuwa sina hadhi ya kuwa na baba kama yeye na kunifukuza kama mbwa huku akinitishia nisiseme.” Sonia aliendelea huku akilia sana. 

“Unajua aibu niliyoingia wakati nafukuzwa shule na kurudishwa nyumbani sababu yakuwa na mimba, tena bado nikiwa mtoto na jamii ikinitukana kama msichana malaya? Unajua ni kiasi gani nilikuwa natamani na mimi kuwepo shuleni? Lakini walinifukuza, nikiwa na mimba nisiyoweza kusema ni ya nani. Huku mtaani wakinishauri nitoe hiyo mimba, nimuue mtoto wangu kuepusha aibu. Lakini nilikataa, Paul.”

“Sikutaka kuwa kama wewe unayekimbia majukumu yako. Nilikubali kumbeba mtoto wangu kwa miezi tisa iliyokuwa migumu kuliko nitakavyo kueleza ukaelewa, japo kwa sehemu. Njaa, aibu na upweke viliniandama. Mtu wa pekee niliyekuwa naye maishani aliacha kuongea na mimi kabisa, akijua ni matokeo ya kutokumsikiliza na kukimbilia wanaume.”  

“Niliteseka nikiwa mtoto niliyejawa hofu, aibu na lawama. Upweke ulikuwa ndio ukinilaza macho, lakini nilikuwa najipa moyo, kwamba katika ile hali kipo kitu kizuri kinakuja maishani mwangu, ambaye ni Kana. Wakati wengine wakimwita mtoto wa bahati mbaya, mimi nilikuwa najifariji kuwa angalau katika yale mateso ya kubakwa siku mbili mfululizo, Mungu aliniona akanihurumia kwa kunifuta machozi kwa kunipa Kana.”

“Japokuwa sikuwa nikijua atakula nini na kuvaa nini, lakini nilijua ndio zawadi yangu pekee na Pole kutoka kwa Mungu wangu. Ndio maana waliponishauri nimuue mwanangu wakati yupo tumboni, nilijua hawajui wanachokiongea, na wala hawajui nilimpataje Kana.” Sonia alikuwa akiongea, huku analia sana. 

“Hivi unajua ni mara ngapi nilikuwa nikikulilia nikijua umekufa? Hakuna siku maishani iliyopita nikiwa kwenye mateso makali nisikulilie Paul. Nilikuwa nikikuliliamchana na usiku nikimlaumu Mungu kukuchukua. Nilikuwa nikijiambia kama baba yangu angekuwepo, asingeruhusu haya yote yanipate. Kumbe wewe unastarehe na wanawake wengine na watoto wako wengine unao wajali na kuwapenda.” Sonia alikuwa akitokwa na machozi kama mvua. 

“Unaweza kumfikiria mtoto anaye lilia mapenzi ya baba yake, gafla anageuka kuwa mama, anayeliliwa na mtoto mwenzake amnyonyeshe mchana na usiku? Tena nikiwa na njaa! Hebu pata picha kidogo, Paul. Lakini nilijitahidi kwa kadiri ya uwezo wangu kufanya nilichoweza kumfikisha Kana hapo alipo.”

“Nilikuwa sili wala kunywa ili Kana mwanangu ale yeye, aishi. Kwa kuwa sikuwa najua kumlea, na mama alikuwa mgonjwa, ilibidi mama ndiye abaki akimlea na mimi kugeuka kuwa mtafutaji wao. Mchana na usiku, mvua na jua nasaka pesa yakufanya mwanangu na mama yangu waishi, tena bila lawama, nikiomba Mungu anipe uwezo wakumsaidia mwanangu.”

“Sikuwahi hata kupata wazo la kumkimbia mwanangu, hata siku moja. Wakati wote niliwaweka wao mbele, lakini wewe ulishindwa Paul. Ulichagua maisha mazuri, ukatutelekeza. Tena mama akiwa mgonjwa na ukijua amebeba mtoto wako!? Uliwezaje kumuacha akiwa na hali ile, tena kwenye mikono ya mtu unayejua hampendi, mama yako!?” Sonia alimliza kila mtu aliyekuwepo pale sebuleni, mpaka Paul mwenyewe alikuwa akitokwa na machozi. 

“Sijui ulimwambia nini mama yangu au sijui ulimwapisha nini! Maana na yeye alikuwa akikataa kila mwanaume, hata wale walioahidi kututoa kwenye dhiki aliwakataa, wakati wewe unakula starehe na wanawake wengine. Muulize Sam chumba alichotukuta tukiishi mimi, mama na Kana.”

“Hata mbwa hawezi kukaa humo ndani. Ilibidi kukaa kwenye stoo ya hiyo nyumba ya kupanga, tena uswahilini kwa kuwa hatukuwa na pesa yakulipia chumba kingine angalu chenye madirisha kama wanadamu wengine wanavyoishi.”

“Tumekaa humo kama mbwa, mpaka Sam alipotutoa pale. Kwa hiyo kabla hujasema unataka kuwa baba, mtafute Sam kwa muda wako akufundishe kina baba wanatakiwa waweje, ndio upate nguvu ya kumkamata baba yake Kana.”

“Kaa mbali kabisa na mimi, na mtoto wangu tafadhali, Paul. Usiwahi kuingiliamaisha yangu hata mara moja. Ulishindwa kuwa baba kwangu wakati huo nikikuhitaji, sasa usitake mwanangu apite nilipopita mimi. Ni ngumu kuliko nitakavyo kwambia.”

“Amebahati yeye Kana, mwenzangu ameangukia mikononi mwa Sam akiwa bado mdogo, anamtunza kama mtoto wake. Lakini nataka niwaambie nyinyi wote wawili, yaliyotokea ni kati yangu mimi na baba yake Kana. Hayamuhusu mtu yeyote kati yenu. Naomba umuache baba yake Kana kabisa.” Sonia alitaka kuondoka lakini ni kama aliyekumbuka kitu. 

“Paul? Naomba wala asiguswe huyo Mzee. Na kama amepigwa, hakikisha anatibiwa na apone. Hujui ulilolifanya hata kidogo. Sikutaka kumpeleka Kana kwa baba yake hivi karibuni. Nilitaka kutengeneza familia yangu ya baba mmoja ambaye ni Sam tu.”

“Lakini sasahivi, kwa hili ulilofanya, najua yule baba hawezi kutulia tena mpaka amuone Kana, kwa kuwa alikuwa akitafuta sana mtoto wa kiume. Fau aliniambia jinsi wazazi wake walivyohangaika kutafuta mtoto wa kiume, lakini walishindwa. Leo umeshamwambia nina mtoto wake wa kiume, unafikiri itakuaje?”

“Halafu ukumbuke ni jana tu ulimwambia mimi ndio mama yake, kwa hiyo atataka kujua baba yake. Maisha yetu yote tumekuwa tukijua hatuna baba, na wote tuliridhika. Hapakuwa na maswali wala wazo la baba. Umekuja tu na kutibua kila kitu. Sasa unajua swali lake linalofuata kwangu? Atataka kumfahamu baba yake. Unafikiri nitafanyaje kama utakuwa umemfunga huyo Mzee au umemuharibu sura? Au unafikiri na mimi nimwambie mwanangu, ‘Mama ya baba yake, yaani bibi yake Kana, alimwambia baba yake akasome Ulaya?’ Au mama na wewe unanishauri nimwambie mwanangu ‘baba yake amekufa?’ Sitamdanganya mwanangu kama wewe na mama mlivyo nidanganya mimi, hata siku moja.”

“Na wala hatakaa ajue kama baba yake alinibaka. Nataka mwanangu aje awe na mahusiano mazuri na baba yake mzazi. Na ukumbuke Paul, katika maisha yangu yote, sikuwahi kuwa na shida na Judge Mkuu mimi hata siku moja, nilikuwa na shida na baba. Kitu ulichoshindwa kunipa kwa kisingizio cha mama yako. Kwa hiyo naomba usitumie cheo chako katika maisha yangu hata siku moja.” Sonia aliondoka kwa hasira nakuacha kila mtu akifuta machozi. Paul alikaa chini akiwa amelemewa, asijue aseme nini. 

Watu wote walikuwa kimya kasoro mama Sonia alisikika akilia sana. Paul alisimama na kumsogelea mama Sonia. “Pole sana Ishimwe. Naomba unisamehe.” Mama Sonia alikuwa akilia sana, alishindwa hata kuongea. “Nitarudi baadaye.” Paul alimbusu kichwani, nakutoka. 

Sam naye alikuwa ni kama amepigiliwa misumari hapo alipokuwa amekaa. Alishindwa hata kusimama. Hakuwahi kumuona Sonia akiongea vile. Mama Briana alisimama na kumsogelea mama Sonia. “Pole sana. Pole mama Sonia. Twende ukapumzike ndani.” Akamsaidia kumnyanyua kisha akageuka. “Sam? Naomba usiongee chochote na Sonia. Wewe umfanye atulie tu. Halafu baadaye mimi ndio nitazungumzanaye.” “Sawa Shem. Ngoja nikamwangalie kama ametulia.” 

Mama Briana alimwingiza mama Sonia chumbani, akamuacha kitandani, yeye akaingia jikoni kupika. Aliivisha chakula na kukiweka mezani. Aliita kila mtu aende kula. Lakini Sam na Sonia hawakutoka. Alikwenda kugonga mlangoni kwao. Alimsikia Sonia akilia sana. Sam akatoka. “Ameshindwa kutulia kabisa.” “Wewe nenda ukale, ngoja mimi nitaongea naye.” Mama Briana aliingia na kufunga mlango. 

*********************

Akamsogelea Sonia na kumkumbatia. “Pole mdogo wangu. Pole sana.” “Haiwezekani dada. Miaka yote hiyo tumekuwa tukiteseka eti leo ndio anakuja nakujidai eti ni baba yangu!? Haiwezekani.” “Pole Sonia. Pole sana. Naomba ukanawe uso uje tuongee.” Ndipo alipoingia bafuni kwake na baada ya muda mfupi akatoka na kukaa pembeni ya mama Briana. 

 Pale Wema Unapovunwa Kwa Wakati Wa Uhitaji

 “Pole Sonia kwa yote uliyopitia. Pole mdogo wangu.” “Asante dada.” “Lakini Sonia, umeshajiuliza kwa nini Paul anawataka sasa hivi, wewe na mama yako? Tena akiwa mtu mkubwa sana hapa nchini, akiwa na uwezo wakumpata mwanamke yeyote anayemtaka, tena ana watoto tayari? Hana shida na wewe wala mama yako. Kwa nini unafikiri bado anawang’ang’ania?” Sonia alipooza gafla. 

“Eti Sonia?” “Sijui dada!” Sonia alijibu kwa upole huku akifuta machozi, kama sio yeye. “Unakumbuka unyama alionifanyia mama yangu wakunizaa?” Sonia alinyamaza. “Sonia?” “Abee dada!” “Unakumbuka ubaya mtu anaoweza kumtendea mwanae wakumzaa? Unakumbuka jinsi mama yangu alivyonigeuza mimi na Nyange, kuwa vichaa, tena mbele ya macho yenu? Ulishawahi kufikiria, kama mama anaweza kumfanyia hivyo mwanae wa kumzaa?” Sonia alikuwa ametulia sana kama aliyepigwa na bumbuwazi. 

“Umeshajiuliza ni mateso ya kiasi gani mama yako alipitia baada ya kuachwa na mwanaume aliyekuwa akimpenda, tena akiwa binti mdogo sana, halafu mjamzito?”

“Unaweza kufikiria ni mara ngapi mama yako amekuwa akijitoa kwako, Sonia? Alikwambia lakini kwa nini alikuja kuishi pale kwetu? Anasema hakuwa na shida na kazi hata kidogo, Sam alishamtengenezea maisha akiwa Mwanza, lakini alikubali kuacha kila kitu na kuja kufanya kazi, tena kazi za ndani. Ilimradi tu awe karibu na wewe.”

“Unakumbuka saluni yake ya Dodoma? Anasema aliifunga ikiwa inamuingizia pesa nyingi tu ambazo hata mngemuacha wewe na Sam, kule Dodoma, anasema angeishi kwa furaha kabisa. Lakini alikubali kurudi tena huku Dar kwa ajili yako Sonia. Mama yako hajawahi kuishi maisha yake hata mara moja tokea anakuzaa wewe, tena na yeye alikuwa mtoto mdogo sana, amekuwa akiishi kwa ajili yako wakati wote. Unajua unachowafanyia wazazi wako, sasa hivi?” Sonia alibaki kimya.   

“Ni kama vile Briana aje kutuchukia na kutuadhibu mimi na baba yake kwa yale tuliyopitia hapa majuzi. Tena atuadhibu baada ya bibi yake, yaani mama yangu kututenda kama alivyotutenda vile, na kujaribu kututenganisha mimi na baba yake.” “Hapana dada!” Akashituka kabisa akikataa mpaka na mabega.

“Ni hivyo Sonia. Hawa wazazi wako wameadhibiwa na mama yake Paul tokea hujazaliwa. Sasa sasa hivi Mungu amewatoa huko wakiwa bado hawajapona madonda ambayo wamesababishiwa na ‘Mama Paul’ wanakuja kukutana na wewe mtu wa muhimu sana katika maisha yao, halafu na wewe unawawekea kipingamizi tena!”

“Unawaadhibu sana wazazi wako Sonia. Mama yako alikuwa akikataa kutoka jana na Paul mwanaume aliyekuwa akimsubiri kwa miaka yake yote, kwa ajili yako. Mpaka mimi na Nyange tulipomlazimisha atoke.”

“Mapenzi ya kweli ndio yanamrudisha baba yako Sonia. Anaonekana ana mapenzi ya kweli kwenu. Sema amerudi hajui afanye nini, aanzie wapi na asaidie nini, kwa kuwa amekutana na nyinyi bila ya kutegemea, tena watu alio ambiwa wamekufa!”

“Na yeye yupo kwenye mshituko mkubwa sana Sonia. Hebu fikiria Sonia, Paul anakutana na mwanamke aliyekuwa akimpenda sana, aliyeambiwa amekufa, gafla anakutana naye akiwa hai, tena mahakamani, akiwa na watoto ambao hakuwaacha nao, anauliza anaambiwa mmoja ni mtoto wako, tena ulibakwa. Huoni Paul atakuwa kwenye mshituko na anajilaumu kuliko utakavyo mlaumu wewe?” Sonia alianza kulia tena. 

“Umeona mapenzi ya Nyange kwa Briana? Umeona anavyohangaika kumlinda mwanae? Yote hayo anafanya asije Briana akapatwa kama yaliyokupata wewe Sonia. Tokea Nyange ajue yaliyokupata wewe, ameingiwa woga kweli. Kila wazo linalopita akilini mwake ni jinsi ya kumlinda Briana. Wewe unamuona jinsi anavyohangaika. Sasa hebu fikiria eti Nyange vile alivyokuwa mgonjwa, apone aambiwe Briana alibakwa, unafikiri angefanyaje?” “Nisamehe dada, kweli nimekosa sana.” Sonia alikuwa akilia. 

“Nikuombe kitu Sonia?” Sonia aliitika kwa kichwa. “Najua una maumivu makali sana, hakuna kati yetu anayeweza kuyaeleza, lakini nakuomba kwa mara ya kwanza katika maisha yako, ishi na wewe kwa ajili ya mama yako.”

“Paul ni mtu ambaye mama yako ana muhitaji sana maishani. Lakini hawezi kuwa naye kama wewe utamkataa Paul. Wewe umenitunzia wanangu, hata walipomuona baba yao akiwakosea, mliwapa sababu za kuzidi kuwasogeza karibu na sisi, sio kuwaweka mbali na sisi. Unafikiri kama sio nyinyi kuwa karibu nao mkiwafariji na kuwaambia mambo mazuri juu yetu, unafikiri mahusiano ya Briana na baba yake sasa hivi yangekuwaje?”

“Wakati alimuona akilala na mwanamke mwingine mbele yao. Briana alikuwa na sababu zote za kumchukia Nyange aliyekuwa amechanganyikiwa kwa yote aliyoyafanya, lakini walipata watu sahihi wakuwaeleza vitu sahihi mpaka leo anampendababa yake. Bahati mbaya sana kwako Sonia, huna mtu mwingine aliyeshuhudiayaliyowapata wazazi wako, akakusimulia magumu na machungu waliyopitia.”

“Paul anakuhitaji sana Sonia. Wote wanakuhitaji wewe. Naomba usiendelee kuwaadhibu. Mama yake Paul ameshawaadhibu vyakutosha, naomba na wewe usiendelee kuwaadhibu. Mambo mengine hayana majibu yake, kubali yaishe mdogo wangu, ili kuleta amani. Umesikia Sonia?” “Nimekuelewa dada. Naomba uniombee msamaha kwa shemeji. Nilikuwa na hasira sana. Nimewakosea heshima wote. Naomba mnisamehe.” “Pole Sonia. Usiwe na wasiwasi na Nyange. Nitaongea nae.” Mama Briana akatoka. 

 *********************

Baada ya muda Sonia na yeye alitoka moja kwa moja mpaka chumbani kwa mama yake. Alimkuta mama yake amelala. Akapanda kitandani na kulala pembeni yake. “Mama?” Mama Sonia akafungua macho. “Nisamehe mama yangu.” Mama Sonia hakuwa akiamini alibaki akimwangalia mwanae. 

“Nilikosea jinsi nilivyompokea Paul, mwanaume uliyekuwa ukimpenda na kumsubiri miaka yote. Nyinyi hamna tofauti na yaliyowapata mama Briana na mume wake. Nimejisikia vibaya mama, nimeona nimekuwa mbinafsi, nimejiangalia mwenyewe bila kuwafikiria na nyinyi. Nisamehe mama yangu.” Machozi yalikuwa yakimtoka mama Sonia, hata Sonia mwenyewe alikuwa akilia sana. 

“Paul anatupenda sana Sonia. Sana. Hana sababu yakutung’ang’ania isipokuwa mapenzi ya kweli. Mama yake nimkorofi na mkatili kupita kiasi. Mbali yakumuonyesha kaburi letu, lazima kuna vitisho vingine alimpa, ila Paul hawezi kusema.”

“Naomba unisamehe kwa kukudanganya Sonia. Niliona shida tulizokuwa nazo, nilijua nikikwambia kama baba yako yupo hai, nilijua siku moja ungekuja kushawishikakwenda kumtafuta, halafu uangukie mikononi mwa yule mama. Niliogopa anaweza kufanikiwa kukuuwa safari hiyo. Sina ndugu mwenzio Sonia. Wewe, Kana na Paul ndio ndugu zangu mlio baki hapa duniani. Nilijua siwezi kuwa na Paul, nisingeweza kukupoteza na wewe mwanangu. Nisamehe Sonia, lakini nilikuwa na kulinda mwanangu.”Sonia alikuwa akilia sana. 

“Nisamehe mama.” Sonia na mama yake walibaki kitandani hapo wakilia mpaka mama Briana alipoingia kuwaambia Paul amerudi. Lakini alitoka bila mama Sonia wala Sonia mwenyewe kujibu kitu kwani bado walikuwa wakilia. 

 *********************

“Naona wewe uingie tu humohumo ndani, uongee nao.” Mama Briana alimwambia Paul. Paul aliingia na kukaa pembeni ya kitanda, akionekana bado ana mawazo. “Nisamehe Sonia, kwa kuwaacha mnateseka. Naomba unisamehe. Nina majutomakubwa sana moyoni mwangu.”

“Natamani nirudishe nyuma ile siku nikiwa nimemuacha mama yako pale sakafuni akiwa anaumwa, ili nifanye maamuzi mengine sio kumuacha anateseka peke yake, lakini siwezi Sonia. Sijui nilipaniki au vipi!? Lakini nafikiria kama ingekuwa ninapewa nafasi nyingine, naapa ningefanya tofauti.”

“Nampenda mama yako, nampenda sana. Na sijawahi kumsahu, Mungu wangu ni shahidi. Mama alitukatili sana.” “Nilikuwa nakulilia kila siku. Mchana na usiku nilikuwa nikikulilia baba. Nilikuwa namuomba Mungu angalau anioteshe hata sura yako tu nikuone.” Paul alikuwa akilia sana. 

Sonia alimsogelea baba yake na kupiga magoti palepale kitandani. “Naomba unisamehe baba. Nimekukosea heshima. Nilikuwa na uchungu mwingi sana moyoni.” Paul alimkumbatia binti yake kwa mara ya kwanza, wote wakiwa wanalia. 

Baada ya muda, walitulia. Paul akambusu Sonia. “Naomba uniangalie Sonia.” Sonia alikausha uso wake vizuri na kumwangalia baba yake. “Umefanana sana na mama yako, kama mapacha!” Sonia alicheka kwa unyonge huku machozi yakiendelea kutoka. “Naomba unisamehe Sonia. Nisamehe mwanangu kwa kuwatelekeza. Nikweli nilikosea. Samahani sana.” Sonia alianza kulia tena. Paul alibaki akimbembeleza. 

“Najua hakuna kitu kitakacho ondoa machungu ya mateso uliyopitia Sonia, lakini nataka ujue, wewe hukuwa mtoto wa bahati mbaya kwangu, hata kidogo. Nilishakuwekea mipango mingi sana tokea upo tumboni, na mama yako ni shahidi. Hatukuwa na mali zozote, lakini natamani ungeona furaha niliyokuwa nayo siku nilipojua Ishimwe ni mjamzito.”

“Tulijiwekea na Ishimwe mipango mingi sana juu yako, na hata mama alipotutenganisha, bado sikukata tamaa. Nilijua jinsi mama yako alivyo mjasiri na mvumilivu, nikajua katika shida zote, atabeba huo mzigo kwa muda mfupi wakati mimi najipanga vizuri. Nilijua nikishajiweka sawa huko chuoni, ningerudi mwenyewe kuja kuwachukua.”

“Mungu ni shahidi yangu Sonia, nisingesubiri hata uzaliwe, ningekuja kuwachukua na nilipanga tuondoke na tusije kurudi tena hapa nchini, tukae mbali kabisa na Mama Tambo. Lakini walipo niambia Ishimwe amefariki na kunitumia picha ya mpaka kaburi lenu, niliamini. Na ndio maana nilishindwa kabisa kurudi tena Tanzania kwa muda wa miaka minne kwa hasira na hofu ya kurudi kuishi huku bila mama yako na nilikuwa nikijilaumu sana kwa kifo chake.”

“Mahusiano yangu na mama hayajawahi kupona mpaka leo. Wakati kila mtu alijua mimi ndiye kipenzi cha mama. Lakini tangia aliponikatili, urafiki wetu haujawahi kurudi tena na haikuwahi kupita siku nikamsahau mama yako kwa muda wote huo tokea tulipoachana.” 

“Japokuwa mama yako ni mdogo sana kwangu, lakini ndiye mwanamke pekee niliyewahi kuishi naye, tukaelewana. Si elimu niliyonayo wala pesa zangu, zilizowahi kuziba pengo la mama yako. Ninasema ukweli Sonia, sikupanga kuwatoroka. Nakuomba uniamini mwanangu.” Sonia alikuwa bado akilia. 

“Sonia?” Paul alimuita tena kwa upendo. “Nimekuelewa baba.” Paul alimsaidia kukausha machozi. “Pole sana kwa matatizo na asante kwa kunibebea majukumu yangu.” “Asante baba.” Paul alibaki akimwangalia kwa muda. 

“Niombe tena radhi juu ya swala la baba yake Kana. Nakiri nimekosa. Nimefanya bila kufikiria.” Sonia aliinama na kuona aibu. “Samahani baba, pale nilikuwa na hasira sana na wivu.” “Wivu wa nini sasa?” “Niliogopa ulivyomchukua mama mkaenda naye usiku kucha mpaka mchana! Halafu mama hajawahi kuniacha nikiwa nalia vile. Nikaona sasa hivi hanijali tena mimi, kwa kuwa wewe umekuja. Hofu yakumpoteza ilishaniingia wakati sasa hivi ndio namuhitaji sana, ndio maana nilikuwa nimekukasirikia. Naomba unisamehe, niliwakosea adabu.” “Umeona Paul? Mimi niliwaambia jana, nisiende mpaka utulie. Lakini Nyange na mkewe wakasema, Sam atakutuliza. Nisamehe Sonia. Sikukusudia kukupuuza mwanangu.” Ishimwe naye aliingilia. 

“Yameisha mama yangu. Naomba unisamehe na mimi.” “Pole Sonia. Lakini nataka uamini sitaruhusu kitu chochote kiwatenganishe wewe na mama yako, hata mimi mwenyewe sitathubutu kufanya hivyo. Nitahakikisha mnakuwa naye karibu tena kihalali. Nipe tu muda kila kitu kitakuwa sawa na ninakuahidi kuwa na wewe wakati wote. Sitawaacha tena.” “Asante.” Sonia alifikiria kidogo na kutabasamu kwa aibu huku akimwangalia baba yake, akajikausha machozi vizuri. 

“Upo kama mama yako. Rahisi sana kuwasoma nyinyi. Nini sasa?” Paul alishajua Sonia anawaza kitu anachoona haya kusema. “Nilikuwa najiuliza baba yake Kana sasa hivi atakuwa wapi? Kwani Ulishamwachia?” “Wewe si uliniambia nisimguse hata kidogo?” “Sasa pale si nilikuwa na hasira? Usingenisikiliza!” Wote walicheka. 

“Sikutaka hata kumuona sura yake, nisije nikamuua bure, ukashindwa kunisamehe.” “Kwa hiyo umemruhusu!?” “Si ndivyo ulivyotaka? Au?” Sonia alifikiria kidogo. 

“Nilitaka nije kwenda na wewe nikamuone, nimwambie alikuwa sahihi, sina hadhiya kuwa na baba kama yeye. Hadhi yangu ni ya juu sana. Mimi ni mtoto wa Judge Mkuu wa Tanzania.” Paul alicheka sana, tena kwa sauti. 

“Kweli baba, angalau na mimi nimringishie. Alinitesa sana yule Mzee. Ashukuru matokeo yake nilimpata Kana, lasivyo angejuta hata kunigusa.” “Hilo halina shida kabisa. Utakapokuwa tayari wewe uniambie twende wote. Si tutaenda na Mnyarwanda wetu?” Paul alimgeukia mama Sonia.

“Akimshitaki mama yangu!?” “Sasa wakati huo atakuwa mke halali wa Judge Mkuu wa Tanzania, hatathubutu kumgusa.” Sonia na Mama yake walishituka kidogo. 

“Nimesoma magazetini kuwa umeoa na una watoto wawili wakiume.” Sonia alimwambia baba yake. “Ni kweli nilioa na kaka zako wapo. Lakini tuliachana na yule mwanamke, sasa hivi natafuta mchumba nioe tena.” Wote walicheka. 

“Nimefurahi kukuona baba.” Paul alimbusu tena Sonia, na kumvuta karibu zaidi. “Muulize mama yako nilivyokuwa nikikuongelesha ukiwa tumboni. Halafu Ishimwe nakudai.” “Hahahaha.” Mama Sonia alicheka. “Mwenzio nilikuwa najikausha, nilijua umesahau!” “Nini?” Sonia aliuliza huku akimwangalia baba yake.  

“Hapana Ishmwe, hii kichwa haisahau kitu. Safari hii lazima unilipe Ishimwe.” “Nini?” Sonia alirudia kuuliza huku akicheka. “Nilikuwa nikimwambia mama yako wakati upo tumboni, huyo ni Sonia, yeye amekazana ni Kanamugire. Mpaka tukapinga na akaahidi kunilipa. Sasa nadai haki yangu.” Wote walikuwa wakicheka. Paul alikuwa mcheshi sana na alionekana kumpenda sana mama Sonia. Mama Sonia alikuwa kama mtoto mbele ya Paul. 

 *********************

 “Sonia! Nilikuwa nikiongea na mama yako, nafikiria kumlipa Nyange na mke wake pesa walizo kusomesha wewe na Kana. Kwanza kama shukrani yangu kwao kuwapokeanyinyi wote, najua ni ngumu kuwalipa kwa wema wote walio watendea, lakini pili ni kuwasaidia kwa kipindi hichi kigumu walicho nacho.” “Kweli baba!?” Sonia alishituka sana. 

“Kabisa. Walibeba jukumu langu, acha nilipe fadhila. Kama utaona sawa lakini.” Sonia alianza kulia. “Unajua itakuwa kama na mimi nilisomeshwa na baba yangu? Asante sana baba.” Paul alijisikia vibaya sana. “Daah! Natamani wale wadogo zako wangependa shule kama wewe Sonia. 

Wananisumbua kweli.” 

“Pole Paul.” Mama Sonia alikaa vizuri na kumwegamia Paul begani huku amepitisha mkono wake kiunoni mwake. “Pole mpenzi wangu.” Sonia alibaki akiwaangalia kwa aibu. Hakuwahi kumuona mama yake akiwa kwenye mapenzi. Walijikuta wakijisahau mbele ya Sonia. Paul alimgeukia Mama Sonia na kumbusu. 

“Asante Ishimwe. Lakini nahisi mama yao ndiye anaye waharibu akili. Wakitoka huko kwa mama yao wanakuwa kama wamechanganyikiwa! Fujo mtindo mmoja. Hawasikii lolote ninalo waambia, kama hawana masikio!” Paul alibaki na mawazo. 

“Pole baba.” “Asante Sonia.” Paul alijibu kinyonge, kisha akatabasamu. “Nimefurahi sana kukupata tena Ishimwe. Labda kwa mara nyingine tena maisha yangu yataleta tena maana.” “Nakupenda Paul.” Bado mama Sonia alikuwa amejiegemeza kwenye bega la Paul akimtazama kwa upendo sana huku akimuhurumia, na bado Paul alikuwa amemkumbatia Sonia. 

“Asante Ishimwe. Unakumbuka tulivyokuwa tukicheka usiku kucha?” “Ulikuwa huishiwi vituko, Paul!” Wote walicheka. “Tokea tuachane, hazijawahi kujirudia tena hizo nyakati, Ishimwe. Sijawahi kulala usingizi ulio nafuraha labda usiku wa kuamkia leo, ndio kwa mara ya kwanza nililala vizuri.” “Ndio maana ulikuwa unakoroma?” 

“Umeanza kusingizia Ishimwe. Mama yako siku zote yeye ndio mkoromaji, halafu anasema mimi!” Wote walikuwa wakicheka. “Muulize Sonia kama mimi na koroma.” Mama Sonia alitaka utetezi kutoka kwa Sonia. “Ukichoka sana huwa unakoroma mama.” Paul alicheka sana. “Asante Mungu kuniletea mtetezi wangu.” Paul aliendelea kucheka.  

“Sonia wewe!?” “Kweli mama.” “Unamtetea tu huyo.” “Basi ndio kazi yake ya kuruka mambo. Muone hivyohivyo. Hata asipochoka anakoroma tu. Mimi nishamzoea. Mida ya kukoroma ikifika najiambia mziki umeanza, nalala vizuri bila shida. Hapo Sonia kajibu kistaarabu. Ulikuwa ukimtesa kweli mwanangu, usiku mkilala.” 

“Hamna bwana! Eti Sonia?” “Nilishazoea.” Paul alicheka kwa sauti ya juu. “Daah! Maskini mwanangu. Umeteseka na mengi! Pole mama. Mpaka ikabidi uzoee!” “Paul wewe! We jidai mjanja sasa hivi.” “Hukoromi bwana! Hivi wewe Sonia kwa nini unamkosea mama yako adabu?” 

“Ni Sonia au wewe? We jidai hivyohivyo.” “Njoo mpenzi wangu.” “Sitaki Paul. Mi sinakoroma?” “Hukoromi bwana! Sonia huyo!” Sonia alibaki akicheka huku akiwafikiria. ‘Kweli hawa watu wanapendana sana.’ Sonia aliwaza. 

“Poleni.” Sonia aliwakatisha. “Pole ya nini?” Paul akauliza. “Sijawahi kumuona mama akiwa na furaha hivyo. Ndio maana alikuwa hataki kuolewa tena!” Mama Sonia alitulia kidogo kama anafikiria. “Asante Sonia. Ni kweli nilipoteza furaha. Sasa sijui kwa kuwa niliishi na Paul nikiwa mtoto mdogo sana, halafu akanionyesha mambo ambayo sikuyapata kwa wanaume wengine? Au Sijui!”

“Kila nilipotaka kuwa na mwanaume karibu, niliona tofauti kubwa sana waliyokuwa nayo na Paul. Japokuwa nilijua Paul lazima angeoa mwanamke mwingine, lakini nilikuwa nashindwa kukubali mwanaume mwingine.” Mama Sonia alianza kutokwa na machozi. 

“Pole sana Ishimwe. Lakini tushukuru Mungu tumekutana tena na Mungu ametupa nafasi ya kuwa pamoja.” Walibaki wote kimya kwa muda. 

 *********************

 “Eti Sonia?  Kwa hiyo niwalipe kina Nyange hiyo pesa?” Paul alivunja ukimya. “Ningefurahi sana baba.” “Basi nina cheki hapa, nilishaambiwa ni kiasi gani walikuwa wakimlipia Kana kwenye ile shule aliyokuwa akisoma, na chuoni kwako. Nimewaandikia pesa yote. Nitawapa.”

“Lakini wanaweza wasikubali kupokea, Paul.” Mama Sonia alikumbuka tabia ya Nyange na mkewe. “Nitaongea nao tu, najua watakubali.” “Hawawezi Paul. Mimi nawajua.” Mama Sonia alirudia. “Umeanza ubishi Ishimwe. Nakwambia watapokea. Au na hili nalo unataka tupinge tena?” “Kabisa tupinge Paul. Nakwambia HAWAPOKEA.” Sonia alikuwa akiwaangalia na kucheka. 

“Umemuona na kumsikia mama yako Sonia? Halafu hakomi. Kila siku kazi ni hiihii yakupinga na wakati wote anashindwa lakini, hakomi!” “Unamdanganya mtoto Paul. Ni mara moja tu ndio nimeshindwa kwenye swala la jinsia ya mtoto, lakini mara zote mimi huwa nakuwa sahihi.” Walianza kubishana kama watoto wakikumbushana mambo yao ya zamani, ya kitoto kuliko Sonia alivyotarajia. Sonia alikuwa akicheka sana. 

“Wewe Sonia naomba uwe shahidi yangu mwanangu. Tukitoka hapa, nyinyi nyamazane kimya muone kama hawatapokea.” “Sawa.” Sonia alibaki akiwatizama. 

“Nimefurahi kweli baba! Sikutegemea eti na mimi siku moja nitakuja kuwa na baba! Nilishakata tamaa.” Sonia alirudia. “Pole sana, na mimi pia nimefurahi sana Sonia. Sikutegemea kuja kuwaona tena.” Paul alijibu.  Walikaa pale kwa muda wakiwa wote wamemuegemea Paul. 

“Sijui naanzia wapi kumshukuru Sam!? Huyu kijana amebeba majukumu yangu yote kwa muda mrefu sana.” “Ni kweli Paul. Bila yeye tusingekuwa hapa.” “Amesema atanioa, baba.” “Ameniambia mama yako. Sasa unaolewa kwa kuwa unampenda au unalipa fadhila kwa aliyowafanyia au kwa kuwa umejikuta una mimba yake?” Sonia alishituka kidogo na kuanza kufikiria. 

“Eti Sonia? Sitaki uje uishi kwenye ndoa kama nilivyoishi mimi. Niliteseka SANA. Nitaumia kama utakuwepo kwenye ndoa kwa sababu imebidi tu. Lazima ujiulize ni kwa nini unataka kuolewa na Sam. Na naomba iwe mapenzi tu mwanangu, sio vinginevyo.” Sonia alitoka kwenye mikono ya baba yake na kukaa vizuri huku akifikiria. Paul alimvuta karibu kumrudisha kwenye mikono yake tena huku akimwangalia. 

“Sasa hivi nipo na wewe, sitakuacha. Katika kila maamuzi utakayoamua, nipo kukuunga mkono kwa asilimia zote. Watoto wote ulio nao, au utakao kuwa nao, usije ukafikiri ni jukumu lako peke yako au lako na mama yako peke yenu. Kuanzia sasa hivi, ujue ni mimi na mama yako tutakuwepo wakati wote kukusaidia kuwalea, bila shida.” Sonia alianza kulia taratibu. 

“Nakupenda sana Sonia. Sana mwanangu.” Paul alimkumbatia tena vizuri na kumbusu kwenye kipanda uso. “Asante.” Mama Sonia alibaki akiwaangalia akitamani kusikia jibu kutoka kwa Sonia. Kwani hakuwahi kumuuliza binti yake juu ya ndoa anayotarajia. Wakati wote alitaka binti yake aolewe haraka kufunika aibu ya kuzaa mtoto wa pili bila ndoa. Walibaki wamekumbatiana na Ishimwe amemuegemea Paul, huku Sonia akiwaza. 

Mwishowe Paul alivunja ukimya. “Sasa Sonia twende ukashuhudie ushindi wangu.” Wote walicheka. “Na Paul ukishindwa wewe, sijui utaweka wapi huo uso wako!” “Usiniogopeshe Ishimwe, wewe unanijua vizuri, sijawahi shindwa hata siku moja.” “Haya twendeni.” Mama Sonia akasimama. 

“Na ndio mnyamaze kabisa, hamna hata kucheka Sonia. Mtu mzima nifanye mambo yangu.” Walisimama ili watoke. “Lakini baba!” Sonia alisita kidogo. “Vipi?” Paul akamsogelea. “Nampenda sana Sam. Naona ndiye mtu ninayeweza kuishi naye kwa furaha.” Sonia aliongea kwa sauti ya chini na upole. 

“Ana upendo, na ananijali sana, mimi na Kana.” Paul alifurahi sana. “Hongera Sonia.” “Amesema ataenda kunitambulisha kwao kabla ya harusi.” “Tutaenda wote.” “Kweli baba?” “Kabisa. Siwezi kukuacha ukaenda peke yako. Lazima huko ukweni wakujue una wazazi wanao kupenda na kukujali.” Sonia alifurahi sana. Alimkumbatia baba yake huku machozi yakimtoka. “Asante sana.” Paul alibaki amemkumbatia Sonia kwa muda. Kisha wakatoka. 

*********************

Walitoka wote wakionyesha nyuso za furaha. “Tuwapishe mkae hapa, mama Sonia?” Tayari mama Briana alisimama. “Hapana, hata hapa panatosha tu, naweza hata kumpakata huyu.” Paul alijibu huku akimvuta mama Sonia karibu yake kumtaka wakae karibu. 

“Nimemlea mwenyewe huyu Ishimwe. Msimuone hivi! Kalikuwa kadogoo. Kamekuwa mikononi mwangu, hakaaa! Nimemfundisha kila kitu, mimi mwenyewe. Halafu msimzeeshe mpenzi wangu, haitwi Mama Sonia anaitwa Ishimwe.” Kina Nyange bado walikuwa na hofu na Paul, hata cheka yao ilikuwa ya kujihami. 

“Nyange amepata mwenzake. Paul ni mchokozi huyu, Nyange haoni ndani. Pale tulipokuwa tukiishi, ilikuwa ikifika jioni wapangaji wote wanakusanyika kumsikiliza porojo zake. Alikuwa anawachekesha wee, mpaka tunaenda kulala.” Mama Sonia aliongeza. 

“Waongo wale, mimi nilishawashtukia Ishimwe. Walikuwa wakifuata chakula chetu. Si unajua nyumba za uswaz? Wapangaji wote kupika na kula, ni nje. Sasa si mnajua Ishimwe kwa kukaangiza? Hana dogo, hata maharage kwake ni shida!”

“Bwana salamu zilikuwa haziishi mtaani. Nilikuwa maarufu mimi sababu ya mke wangu. Utasikia ‘Shikamoo ka Paul!’ Mpaka watu wazima, walikuwa wananisalimia, kumbe shida yao niwakaribishe wakale chakula cha mke wangu. Kutwa vitoto viko mlangoni kwetu, utasikia ‘Tunapenda kweli pazia lenu la maua ua.’ Kumbe waongo wanataka chakula alichopika Ishimwe.” Kila mtu alikuwa akicheka. 

“Sasa Ishimwe akanihurumia, akaona nitakuwa nalala njaa kila siku. Maana mimi nilikuwa sijazoea kula huku watu wananisindikiza matonge yangu. Nikawa nawakaribisha tu, nawaachia chote. Ishimwe alivyoona hivyo, akawa akipika ananifichia kingine ndani, halafu kinachobaki tunaenda kula nje na wapangaji wengine.”

“Utawasikia, ‘Kwani Ishimwe hayo maharage, maharage ganii!? Mbona yananukia hivyo?’ Kumbe wanataka tu kuonja. Halafu onja yao sasa! Ishimwe unamkumbuka yuleMama mwenye nyumba lakini?” Ishimwe alikuwa akicheka jinsi Paul alivyokuwa akiongea kwa kuwaigiliza sauti zao, kuanzia sauti ya watoto mpaka wakubwa, alitingisha kichwa kukubali. 

“Bwana mama analeta na kibakuli kabisa, bwana! Utamsikia ‘hebu nipunguzie kidogo!’ Basi tena hapo ni mwenye nyumba, huwezi kumpa kidogo, unamjazia kabisa bakuli, ili ukipitisha siku ya kulipa kodi, akumbuke maharage yenu.” Walikuwa wakicheka sana. Kila wakimwangalia Paul vile alivyo sasa na maisha wanayosimulia waliishi na Ishimwe, ilikuwa kama utani tu. 

“Yaani tulikuwa tukicheka na Paul, usiku kucha. Haishiwi maneno na vituko huyu Paul!” Mama Sonia aliongeza na ndiye aliye kuwa huru na Paul, lakini wengine walijihami kidogo, kwani Paul waliyemfahamu wao, ni Jugde Mkuu wa Tanzania, lakini mama Sonia kwake Paul alikuwa kijana waliyeanza naye maisha, wakiwa wanalala chini baada ya kutoroka kwao. Kila alipomtizama Paul alikuwa kimuona mwanaume aliyempenda, na wala sio Judge Mkuu wa Tanzania. 

 Hakuna Anayetoa, Kumzidi Mungu

         “Jamani naomba nitoe shukurani zangu za dhati, kwenu nyinyi wote watatu kwa kupokea familia yangu na kuwatunza kama ndugu zenu. Asanteni sana.” “Bila shaka Mheshimiwa. Wao ndio wamekuwa msaada mkubwa sana kwetu kuliko sisi tulivyokuwa msaada kwao.” Nyange alijibu kwa haraka. 

“Pili niwashukuru kwa mzigo mliokuwa mmeubeba kwa niaba yangu, kwa kuwasomesha Kana na Sonia. Asanteni sana. Sasa, kwa kuwa ni JUKUMU langu mimikama baba yake Sonia kumsomesha, naomba ibakie kuwa mimi ndiye mwenye jukumu hilo.” Paul alisimama akatoa cheki akiwa amebadilika sura kabisa. Alivaa sura ya kazi, sio utani tena. 

“Najua sitaweza kulipa kila kitu lakini naomba MIMI ndiye niwe nilimsomesha mwanangu. Hii ni pesa yenu yote kuanzia vitabu mpaka ada mliyomlipia Sonia na Kana. Nisingependa mtoto wangu awe amesomeshwa na mtu mwingine ila MIMI tu.” Paul alikuwa akiongea huku akimwangalia Nyange na mkewe bila kupepesa macho. 

“Naomba mpokee hii pesa yenu.” Hofu iliwaingia Nyange na mkewe, wakasimama. “Lakini hatukutaka utulipe, Mkuu!” Nyange alijibu kwa unyenyekevu sana. “Naelewa kabisa. Lakini ningependa kubeba majukumu yangu mwenyewe. Nisingependa na sitaruhusu mtu yeyote yule anipokonye HAKI yangu ya kuwa baba kwa Sonia. Sijui nimeeleweka?” Akauliza kwa ukali kidogo.

 “Umeeleweka Mkuu!” “Basi hii ndiyo pesa yenu.” Paul alinyoosha mkono kuwakabidhi hundi. Nyange alibaki ametoa macho. “Zote hizi? Hatukulipa pesa yote hii Mkuu.” “Nimeambiwa wewe ni mfanyabiashara. Hiyo pesa ungewekeza kwenye biashara zako, wakati ule, leo ungekuwa umepata faida kubwa kuliko hiyo.” Nyange alimpa hiyo hundi mkewe ili aone. Mama Briana alibaki akitokwa na machozi. “Asante sana.”

 *********************

Paul aligeuka na kuanza kucheka huku akimwangalia mama Sonia. “Jamani Paul wewe! Kwa nini hukui? Umewaogopesha bwana!” “Nipe ‘kumi na tano’ zangu Sonia.” Sonia alianza kucheka. Paul alienda kugonga na Sonia mara tatu. Juu, katikati na chini. 

“Wala hujashinda, kwa taarifa yako. Umetumia mabavu kushinda.” “Kwani mimi nakushangaa Ishimwe? Unazidi kumthibitishia Sonia jinsi ulivyo mzulumishi? Pale ndani tulikubaliana njia za kushinda au tulipinga ushindi?” Sonia alikuwa akicheka sana. 

“Nisaidie Sonia.” “Mlipinga ushindi.” Sonia alijibu huku akicheka sana. “Wewe mtete tu huyo! Hatabiriki hata kidogo! Kesho atakugeuka tu, utaona. Ujanja wake hauishi. Yeye ndio mzulumishi namba moja, huyo Paul. Na NAKATAA hujashinda kwa kuwa umetumia mabavu.”

“Lakini mama sio sawa. Kubali tu kushindwa.” “Afadhali Sonia mwanangu unitetee. Na kama ulikuwa humjui, basi jua tabia yake ndio hiyooo mama yako. Akishindwa, haishiwi visingizio.” Kina Nyange walibaki wakicheka wasijue kinachoendelea. 

“Eti mama Briana, hapo mmepokea hiyo pesa kwa hiyari yenu au Paul amewaogopesha ndio mkapokea?” Mama Briana aliinama huku akicheka. “Kwa kweli mimi niliingiwa na hofu.” Nyange akajibu yeye. “Mmeona wewe Paul na Sonia? Paul umeshinda kwa kutumia mabavu.”

“Sikatai Ishimwe. Lakini kwani tulikubaliana nini?” “Hapana Paul, wakati wote tunapopinga unanitega mahali ili ushinde. Ujanja ujanja mwingi sana, wewe Paul, siwezi kukubali.” “Kosa ni lako Ishimwe, ulitakiwa usiingie kwenye mkataba bila kufikiria.” “Hata useme nini, sikulipi Paul.”

“Nishakuzoea uzulumishi Ishimwe. Sishangai.” Ilibidi Sonia awasimulie ubishani unaoendelea kati ya wazazi wake. Kila mtu alikuwa akicheka sana “Daah! Kweli niliogopa. Mkuu alivaa sura ya kazi kabisa, akidai haki yake ya ubaba.” Nyange aliongeza. “Samahani sana bwana Nyange, ilibidi kuweka sura ya kazi kidogo, nilishaambiwa hamtapokea hiyo hela.” “Kweli umetuweza Mkuu.” Walianza kucheka tena. 

 *********************

 “Sasa niombe ruhusa kwa Sonia. Naomba niondoke na mama yako, nitamrudisha.” Sonia alicheka kwa aibu akikumbuka alivyomwambia baba yake alimkasirikia kwa kuondoka na mama yake. “Anarudi lini?” “Kweli wewe mwanangu na sheria ipo kwenye damu. Maswali hayaishi!?” Wote walikuwa wakicheka. “Nitamrudisha, lakini sio kesho.” Mama Sonia alianza kucheka. “Mama wewe! Hata huulizi?” Mama Sonia alizidi kucheka. 

“Nyange na mama Briana kwa mara nyingine tena nawashukuru sana, kwa kuwapokea hawa watu. Sina jinsi yakuwalipa. Lakini shukrani yangu inakuja.” “Tena Mkuu?” “Kwani nishawashukuru? Hapo nilikuwa nadai haki yangu ya ubaba kwanza. Sijashukuru.” “Daah! Tulilala masikini tumeamka matajiri. Asante Mungu wetu.” Wakacheka vile Nyange mpaka alivyonyanyua mikono juu akimshukuru Mungu.

Paul akamgeukia Sam. “Sasa wewe Mheshimiwa, ndio nilipewa amri nikutafute kwa wakati wangu. Tukirudi kutoka safari na Ishimwe tutaongea zaidi. Mbali ya kudaiMAHARI ya Sonia, nina mengi ya kuzungumza na wewe Sam.” “Lakini nimeambiwa Sonia halipiwi Mahari.” Sam alijitetea akicheka. 

“Amekwambia nani?! We Ishimwe?” Paul alimgeukia Ishimwe. “Mimi niliona hamna haja Paul!” “Wewewewe… Huyu mtoto sio Mnyarwanda. Tafadhali sana Ishimwe! Kabinti kangu kapekee haka, unataka nikaringie wapi?”

“Tena nataka mniambie tarehe mapema, niwaambie wazee wenzangu waje nyumbani tupokee mahari ya Sonia. Umesikia Sam na Nyange? Anzeni kujipanga, nataka mahari yangu.” “Daah! Mahari ya kumlipa Judge Mkuu wa Tanzania!? Mbele ya wazee wenzake! Si watajaa maraisi humo ndani na mawaziri watupi?” Nyange aliwaza kwa sauti na kufanya watu wote wacheke mpaka Paul mwenyewe.  

“Mahari ya kawaida kabisa Nyange, usiwe na wasiwasi. Tena hamtaruka hatua hata moja. Mkija kutoa posa, nitawapa orodha ya vitu vya kuleta siku ya mahari yake. Sitaongeza hata kidogo, nitawapa ya mila ya kwetu. Tena wakisema panga, mniletee panga. Kasoro ng’ombe tu sina pakuwaweka hao ng’ombe.” Wote walicheka.

“Au utaanza kufuga Ishimwe? Maana mimi si mfugaji.” “Hapana bwana Paul, ng’ombe wa nini?” “Basi mjipange. Huyu anaitwa Sonia Tambo. Na kina Tambo, tunapokea mahari.” “Nimeelewa. Nipo tayari.” Sam alijibu kwa haraka na kufanya wote wacheke. 

“Kweli umekusudia kumuoa binti yangu. Nikirudi tutaongea vizuri.” Paul aliongeza. “Lakini kuna mambo mawili hayawezi kusubiri, kwanza lazima ujue unakaa na mboni ya jicho langu. Nilimpenda Sonia kabla hata sijaiona sura yake, na nilikuwa na mipangonaye huyo, ni hivyo walinikatili tu.”

“Kwa hiyo lazima niwe karibu sana na wewe kuliko yale majoho ya U Judge na pili naomba upokee shukrani zangu za dhati kwa kuokoa maisha ya mpenzi wangu, Ishimwe, akiwa Mwanza. Asante sana Sam.” Paul alimsogelea Sam na kumpa mkono. 

“Nakushukuru sana. Asante.” Sam alitabasamu kwa hofu kidogo. “Karibu sana Mkuu.” “Sasa wewe unataka nifukuzwe tena humu ndani na Sonia. Amesema yeye hataki Judge, shida yake ni baba. Nikiwa nyumbani mimi ni baba, sio Mkuu. Sawa?” “Nimeelewa.” Sonia alikuwa kicheka huku ameinama pembeni ya Sam. 

Paul alimsogelea na kuchuchumaa mbele yake, akambusu tena na kumkumbatia. “Nitakaporudi tena, ujiandae kwenda kukutana na kaka zako.” Paul alimnong’oneza. “Naogopa.” Sonia aliongea kwa sauti ya chini. “Nini?” “Wakinikataa. Wasipo nipenda, je?” Paul alicheka kidogo kama anayefikiria. 

“Najua watashituka sana, maana wote niliwaambia ulikufa wewe na mama yako. Na nilisha wapeleka mpaka kwenye kaburi lenu.” “Kweli!?” “Kabisa. Tena mmoja wao, yule niliyekwambia ana nafuu, alisema anatamani Mungu angekurudisha ili na wao wapate dada.” Sonia alifurahi sana. 

“Basi nipeleke, sasa hivi.” “Daah! Kweli mama yako hajakosea! Upo kama baba yako! Ukitaka jambo nilazima upate saa hiyohiyo! Nimekwambia nikirudi Sonia! Ngoja kwanza nikamfute machozi mpenzi wangu, hao kaka zako utakuja kuonana nao tukirudi.” Kila mtu alikuwa akicheka, Paul akambusu tena Sonia na kuondoka huku amemshika mkono mama Sonia. “Sijachukua hata nguo Paul!” “Utavaa za kwangu, usijali.” Wote walicheka nakutoka. 

 Huamuri Mashariki, Na Magaribi Kutoa Kwa Ajili Ya Wakati Wa Mavuno Yako. Unapanda Nini Maishani?

Bila kupoteza muda, mara baada ya Ishimwe na Paul kutoka, Nyange aliazima simu ya Sam na kutoka nayo nje. Baada ya muda alirudi na sura ya furaha sana. “Mungu mkubwa Penninah! Akiamua kukubariki, milango yote inafunguliwa kwa ajili yako.” Nyange alikaa huku akitokwa na machozi ya furaha. 

“Mungu amenisamehe Penninah!” “Nini Nyange?” Nyange alitulia kwanza. “Umeona Mungu alichofanya? Ametuletea pesa. Wazo likanijia gafla niwatafute wale jamaa waliokuwa wakiniuzia mbao, kama bado wanaweza kuniuzia. Wamesema mzigo wanao upo tayari, ni mimi kwenda kuufuata tu.”

“Haya nikajiambia mzigo ninao, Soko je? Nikaamua kuwapigia simu wateja wangu wa zamani, wote wanataka niwapelekee mbao, tena hata kesho.” Mama Briana alibaki ametoa macho akimshangaa mumewe kwa uharaka aliofanya. 

“Si walisema Chao ndio amechukua masoko yetu yote?” “Ndio nakwambia Mungu akiamua kukubariki, anakubariki Penninah! Hata milango ya adui zako inafungwa kwa ajili yako. Mungu amenirudishia wateja wangu wote. Imekuaje sijui! Ninachojua kesho asubuhi naondoka na kwenda Iringa kufuata mzigo.” Mama Briana alianza kulia. 

Nyange alimsogelea na kumkumbatia. “Wewe baki na watoto. Ngoja mimi nihangaike Penninah, baada ya muda mfupi mambo yetu yatakuwa mazuri tu.” Sam na Sonia walibaki wakiwaangalia kwa furaha. 

“Hongera kaka.” “Daah! Siamini Sam! Nikirudi safari, tutaongea vizuri juu ya ile biashara yenu ya dagaa. Nimepata wazo jingine litakalo waingizia pesa zaidi. Naombeni muendelee kutuvumilia, naamini mambo tayakuwa mazuri hivi karibuni, tutakuwa na uwezo wakupangisha hata vyumba viwili, tuondoke humu ndani.” Sonia alishituka sana.

“Mnaondoka dada?” Tayari machozi yalianza kumtoka Sonia. “Hatuwezi kuendelea kubanana humu ndani Sonia. Lazima tuwapishe. Sio mnatoka kwenye harusi, unarudi nyumbani kwako unakuta nyumba imejaa tena. Au mtoto anakuja huna pakumuweka.” “Jamani dada msiondoke, mbona tupo sawa tu. Mtoto tutalala naye.”

“Hapana Sonia. Lazima uanze kujiandaa. Wote tutaondoka. Na ujue hata mama yako akirudi mambo hayatakuwa kama zamani.” “Kwa nini tena?!” Sam alishaanza kumuonea huruma Sonia. “Unafikiri ataondoka na yeye? Mama hawezi kuniacha.” Sonia alishapaniki.

“Siwezi kuishi bila mama yangu jamani! Nitachanganyikiwa. Paul hawezi kumchukua mama yangu moja kwa moja. Wameenda tu kupumzika, atamrudisha.” Sonia alizidi kuchanganyikiwa. 

“Ndio kukua huko Sonia. Ukishindwa kufanya hivyo inamaana haupo tayari kwa ndoa. Inamaana umuache hapa Sam ukakae na wazazi wako. Lazima ukubali, Paul na mama yako hawawezi kutengana tena, hata iweje. Sasa ni wewe uamue kubaki hapa na Sam au uondoke na mama yako.” Nyange aliongeza na kumfanya Sam abaki akimwangalia Sonia. 

Sonia alitulia kidogo na kuinama kama anayefikiria. “Na useme haraka, kama unaondoka na wazazi wako tusimamishe vikao vya harusi.” Nyange aliongeza. Kidogo wasiwasi ulimwingia Sam. ‘Daah! Sonia ataniacha tena. Na hivi ashapata baba mwenye uwezo na anae mjali! Anaweza kweli kuondoka.’ Sam alianza kuwaza huku akimwangalia Sonia aliyekuwa ameinama muda wote. 

“Eti Sonia? Harusi ipo au unataka ukafikirie kwanza nyumbani kwenu ndipo utoe uwamuzi?” Mama Briana aliongeza swali lililozidi kumchanganya Sam. ‘Ataondoka na mtoto wangu?’ Sam alizidi kufikiria wakati Sonia akiendelea kufuta machozi. 

“Sikuwa nimefikiria hivyo dada. Nampenda sana Sam, siwezi kuondoka na kumuacha peke yake.” Sam alivuta pumzi na kumshika Sonia. “Daaah! Nilisha changanyikiwa. Nilijua ndio naachwa hivyo!” “Nilikuona Sam.” Nyange alianza kucheka. 

“Nakupenda Sam, siwezi kukuacha.” Sonia alimgeukia Sam na kumwambia kwa sauti ya upole na unyonge. “Asante Sonia.” “Sasa hapo ndio umeshakuwa mtu mzima. Upo tayari kuolewa sasa. Huwezi kukaa na wazazi wako wakati wote Sonia. Hata hivyo ukumbuke wote tutakuwa hapahapa Dar, sio mbali. Wewe mwenyewe umesema hakuna kutengana. Ni kweli. Hatuta tengana tena. Najua dada yako atakuwa na wewe wakati wote utakao muhitaji na mama yako vilevile. Huna haja ya kuogopa.” “Eti dada?” Mama Briana alianza kucheka. 

“Usiogope bwana Sonia! Kwanza unatakiwa usiwaze swala la kuwa peke yako, waza jinsi utakavyofurahia ndoa yako. Vitu mtakavyo fanya ukiwa na Sam peke yenu humu ndani. Kuna mambo mengi sana, hujafanya na Sam sababu ya watu kuwa wengi kwenye nyumba yenu.” Sonia alicheka na kuinama. 

“Tutakufundisha vizuri kabla ya ndoa. Utafurahia sana utulivu utakao upata mkiwa wewe na Sam tu humu ndani.” “Na Kana?” Kama aliyeshituka kutoka usingizini, Sonia alimkumbuka mwanae. Nyange na Mama Briana waliangaliana. 

“Nataka kukaa na mwanangu dada. Maisha yake yote amekuwa akilelewa na mama. Naogopa atazidi kunifikiria namsukumia mbali, wakati nilikuwa silali sababu ya kumfikiria yeye. Hataweza kuamini maneno tu kama sitafanya na vitendo. Kwa kuwa Sam amekubali kumpokea kama mtoto wake, nataka tuishi naye. Hata mama akiondoka nitamuomba asimchukue tena, aniachie mwanangu.” Mama Briana alipooza gafla na Sonia alijua. 

“Kwani nitakuwa nimekosea?” Sonia hakuwa ameelewa. “Hapana Sonia. Ni uamuzi mzuri sana. Lakini tulitaka kuwaomba mtupe Kana kwa muda tukakae naye, mpaka tutakapo muweka sawa Briana. Kwa kuwa mimi nitakuwepo nae muda mwingi nitamfundisha mambo mengi, najua ataelewa tu. Naamini atazoea tu maisha bila Kana.” Sonia alibaki kimya. 

“Tafadhali Sonia, lasivyo unamjua Briana, hatakubali kuondoka hapa bila Kana. Na ameshakuwa mkubwa sasa, hawezi kuendelea kuishi hivyo. Itamtesa yeye mwenyewe na Kana pia.” 

“Basi itabidi kabla ya kuondoka, siku moja tutoke mimi na yeye tu, tukaongee. Nataka tuwekane sawa, asije akafikiria simtaki kwenye maisha yangu. Wakati nampendasana mwanangu.” “Hilo ni wazo zuri.” Sonia alipotelea kwenye mawazo, taratibu waliona machozi yakimtoka. Sam alipitisha mkono wake juu ya mabega ya Sonia kama kawaida yake, kumfanya ajisikie vizuri. “Usilie Sonia.” Sam alimbembeleza. 

 Utayari Wa Kuingia Kwenye Milango Iliyofunguliwa Na Mungu

Nyange aliamka asubuhi na mapema kuwahi mabasi ya kwenda Iringa. Mama Briana ndiye aliyemsindikiza kituo cha mabasi Ubungo. “Nakuombea D. Usafiri salama na ufanikiwe.” Nyange alimbusu mkewe akiwa na tumaini kubwa, zaidi safari hii wakiwa upande wa Mungu.

“Asante. Sitakaa huko muda mrefu. Nikifanikiwa tu, kesho kutwa nageuza.” “Nakusubiri.” Nyange alimwangalia mkewe kwa muda kisha akaondoka. Mama Briana alibaki amesimama hapo nje ya basi huku akifuta machozi, akimwangalia mumewe anavyopanda kwenye basi. 

Alikaa hapo mpaka alipoona basi limeondoka ndipo na yeye akaondoka kituoni hapo. Njia nzima Nyange alikuwa akimshukuru Mungu, na kumuombea mkewe. 

 *********************

Kwa kuwa mama Briana alimsindikiza mumewe kituo cha mabasi, ilimbidi Sam ndiye awapeleke watoto shule ili Sonia apumzike. Na yeye aliamka asubuhi na mapema ili kuwaamsha watoto wajiandae watoke mapema, kuwahi foleni. Alimkuta Kana alishavaa yupo jikoni. 

Kidogo alishituka. “Unafanya nini huku?” Sam alimuuliza Kana. “Nilikuwa namwandalia Sonia kifungua kinywa.” Kidogo Sam akatulia huku akimtizama. “Niliwasikia jana wakati mnaongea, wote mlisema mtaondoka asubuhi asubuhi. Nikajua atabaki peke yake bila chakula.” Sam alibaki akiwaza, ni mangapi Kana aliyosikia kutoka kwenye mazungumzo yao waliyokuwa wakiongea kwa uhuru, wakidhani Kana hayupo, au hasikii.

“Atakuwa ameamka?” Kana alimtoa Sam mawazoni. “Unafikiri nimpelekee chumbani au niache tu hapa mezani?” Kana aliongeza swali jingine wakati bado hajajibia swali la kwanza. Mwishowe alibaki na yeye akimwangalia Sam. “Nimemuacha macho, kitandani. Labda ukamuulize mwenyewe.” Kana alienda kugonga taratibu chumbani kwa Sonia. 

“Nani?” Sonia akauliza. “Ni mimi Kana.” Sonia alishituka sana kumsikia Kana mlangoni kwao. Hakuwahi hata kumuona amesimama karibu na mlango wa chumbani kwao! Akajiweka sawa na kumkaribisha. “Ingia tu.”

Kana akaingia. “Vipi?” “Nilitaka kujua umeamkaje?” Sonia alibaki ametoa macho na kushindwa kujibu. Japokuwa walikuwa wakiishi nyumba moja, lakini hawakuwa karibu hata kidogo. Wakati wote waliongeleshana vitu vya muhimu tu, tena Sonia ndiye aliyekuwa akianzisha mazungumzo. Kama kumuulizia habari za shule na kumuita kwenda kula basi. 

Mara zote Sam na Ishimwe ndio walikuwa karibu naye, zaidi Ishimwe. Kila alipokuwa na shida alimwambia Ishimwe, kwa upande wa Sam ni mpaka Sam mwenyewe amuulize. Muda mwingi Briana ndiye aliyekuwa amejaa kwenye maisha ya Kana, tokea watoto. Hakuwa na muda na mtu mwingine isipokuwa Briana aliyekuwa akimfuata kila mahali. 

Baada ya kuona Sonia amenyamaza. Kana akaongeza. “Nimekutengenezea kifungua kinywa, unataka kula sasa hivi, nikuletee humu ndani?” “Nitashukuru sana.” Akatoka na kumuacha Sonia akijiuliza alichotengenezewa na Kana ni nini? Kwani hakuwahi kumuona hata siku moja jikoni. 

Mara baada ya muda Kana akarudi na stuli, akaweka pembeni ya kitanda chao, kisha akatoka tena na kurudi akiwa amebeba sinia yenye bakuli. Sonia alishatoka ndani ya chandarua, akakifunga vizuri, na kukaa akisubiria hicho kifungua kinywa. 

Kana aliweka sinia juu ya ile stuli. Sonia alibaki ametoa macho baada ya kuona uji wa ulezi kwenye bakuli kubwa. “Nilipika mwingi kidogo, mwingine nimekuwekea kwenye chupa, utakunywa baadaye ukisikia njaa.” Machozi yalikuwa yakimtoka Sonia, alishindwa hata kumshukuru, alibaki akifuta machozi. Kana akatoka.

Sam alirudi akamkuta Sonia bado analia. Alikaa pembeni yake akiwa bado amepigwa na yeye, na butwaa. “Ngoja mimi nionje huo uji wa Kana.” Sam alivunja ukimya. Alivuta bakuli na kuanza kunywa. “Wewe Sam ndio kuonja gani huko bwana? Umekuwa kama wale wapangaji wa kina mama, tuliosimuliwa jana!” Sam alicheka. 

“Bwana uji mtamu huo! Haiwezekani kama huyu mtoto anajua kupika kuliko mimi!!” “Bwana Sam, utamaliza uji wangu. Ni nini lakini?” Sonia alianza kufuta machozi na kumpokonya Sam bakuli la uji. “Siamini Sam!” “Mimi naona niende kwanza kazini, nikisha shika ile kompyuta yangu, ndio naona nitaelewa vizuri. Bado nipo kwenye mshituko.” 

“Unakaribia kuchelewa Sam. Wahi kuoga.” Sam alibaki amekaa hapo kitandani akimuwaza Kana. Aliogopa kumwambia Sonia kama Kana alikuwa akiwasikiliza. “Kweli bwana.” Akasimama na kuingia kuoga. ‘Itakuaje kama amesikia kila kitu mpaka maongezi ya Sonia akiwa anaongea kwa hasira jana na baba yake?’ Sam aliendelea kuwaza siku nzima. 

 *********************

Mama Briana alirudi na kumkuta Sonia sebuleni. “Pole nimechelewa sababu ya foleni. Najua hapo njaa itakuwa inakuuma umeshindwa kulala. Ngoja niwahi huko jikoni.” “Dada hebu njoo kwanza.” “Nini?” “Si unakumbuka juzi Kana alijua kama mimi ni mama yake, akakasirika kwa nini sikumwambia tokea zamani?” “Eehe!” 

“Sasa jana usiku nikawa namwambia Sam, najua Kana amenikasirikia sana, nataka tutoke naye weekend hii tukaongee. Sam akasema wazo zuri. Sasa maajabu, ameamka asubuhi, amenipikia uji na kuniletea chumbani kwangu.” “Kana!?” “Ndiyo Kana. Aliingia pale chumbani kwangu akaniulizia nimeamkaje, nilishindwa hata kujibu dada, kwa mshituko.” Mama Briana alianza kucheka. “Kweli dada! Hata asante sikumbuki kama nilitoa!” “Makubwa. Labda ameamua kusamehe.” “Labda!” 

 *********************

Jioni ilipofika mama Briana aliingia na watoto kutoka shule. Kana akamfuata Sonia kwenye kochi. “Hujambo Kana?” “Sijambo. Nimekuletea huu ubuyu, Briana anaupenda sana, sijui na wewe utapenda?” “Asante sana. Nashukuru Kana.” Alitabasamu na kutaka kuondoka, lakini Sonia akamuwahi. “Kana, asante na kwa uji wa asubuhi. Japo Sam na mama Briana wamenimalizia.” Kana akacheka. 

“Basi kesho nitapika mwingi.” “Sonia mimba hiyo inakuja na uchoyo!” Mama Briana aliingilia na kumfanya Sonia na Kana wacheke. “Nimekunywa bakuli moja tu, unanishitakia!” “Haukuwa mwingi Mama Bree, ndio maana ulimaliza.” Kana alimtetea Sonia. “Kana wewe!?” Mama Briana alimgeukia Kana. “Lakini hamna shida, kesho nitapika mwingi.” “Hayo ndio maneno, na wengine tuponee hapohapo.” Mama Briana aliongeza. 

 *********************

Kana alibadilika sana, kila mtu alikuwa akimshangaa. Alimjali sana Sonia. Hata alipokuwepo nyumbani, alitaka kuwa karibu na Sonia na kutaka kujua hali yake. Kila alipomuona mama yake yupo sebuleni alijisogeza kwa mbali kidogo na kubaki akimwangalia kwa makini sana, mpaka Sam alijua na kumwambia Sonia. 

“Hivi unajua Kana anajiiba kukuangalia? Anakaaga kule mezani, anakuangalia wewe kwa muda mrefu sana.” “Na naona na mapenzi yamezidi! Kila siku asubuhi lazima aje anigongee anisalimie na akirudi kutoka shule lazima aniletee zawadi.” Sonia na Sam waliendelea kumteta. 

 *********************

Ni kweli Mungu alikuwa upande wa Nyange, baada ya siku tatu akarudi na mzigo akasambaza wote siku inayofuata. Ilikuwa kama funga na kufumbua, mambo yaliwabadilikia Nyange na mkewe. Pesa walizolipwa na Paul, zilizaa mara mbili yake, wakabaki wakiwaza kama wakapange nyumba, au wasubirie hiyo zawadi ya Paul. 

“Tusubirie kidogo mke wangu. We unafikiri zawadi ya kutoka kwa Judge Mkuu wa Tanzania itakuwa nini kama sio kurudishiwa mali zetu? Pesa kashatupa, nini tena kingine kimebaki kama sio hicho? Tusije peleka pesa yote kwenye kodi ya nyumba, halafu tukarudishiwa nyumba zetu tukakosa pesa ya kukarabati.” “Kweli D. Tusubiri.” Nyange na Mkewe wakakubaliana kusubiri. 

 Penzi Lisilokufa

Baada ya siku tano Paul akamrudisha mama Sonia akiwa amebadilika kama sio yeye! “Umevalishwa na pete ya uchumba mama!?” Sonia aliuliza kwa mshangao huku akiangalia vidole vya mama yake. Mama Sonia alikuwa akicheka kila wakati. 

Na kwa kuwa alijua mambo ya urembo alijitengeneza vizuri na kubadilika kabisa. Alirudi na mavazi ya thamani sana. “Umependeza mama, kama sio wewe!” Paul alikuwa akicheka. “Sasa mjiandae jumamosi ijayo harusi yetu.” Kila mtu akashituka sana. “Kweli mama!?” Sonia aliuliza kwa mshangao mkubwa. 

“Haiwezekani uolewe wewe kabla ya mama yako.” “Mama!” “Hongera mama Sonia.” Mama Briana alinyanyuka kumpa mkono. “Nilishawaomba jamani msimuite Mama Sonia. Jina lake ni Ishimwe.” Kila mtu alikuwa akicheka kwa furaha, walisimama wote na kumpa mkono wa pongezi. 

“Sasa na sisi ndio tumerudi kutoka safari. Hata nyumbani hatujafika. Tumeona tuje kuwachukua kwanza, Sonia akaonane na kaka zake. Ndio na sisi tupumzike moja kwa moja.” “Kwani mama ndio anaondoka leo, moja kwa moja!?” “Ulitaka na mimi nihamie hapahapa?!” Paul akamuuliza Sonia.

“Hapana. Lakini…” Sonia alianza kulia. “Itakuaje sasa mama jamani?!” Mama Sonia alipooza gafla nakubaki kimya. “Na huyu mtoto nitamleaje sasa? Halafu…” Sonia alishindwa kuongea aliendelea kulia.  

Japokuwa huyo alikuwa mtoto wa pili kwake, lakini mbali ya mama yake kumfundisha jinsi ya kumshika mtoto wakati wa kumnyonyesha, hakujua hata kuogesha mtoto mchanga. Mama yake ndiye aliyemlea Kana kuanzia siku anazaliwa mpaka wakati huo. 

“Nilifikiri tutakaa wote mama, mpaka nijifungue!” Nyange na mkewe walikuwa wamekaa kimya wakisikiliza. “Mama yako yupo Sonia, na mimi nipo. Ukitutaka hata kama ni saa nane za usiku, wewe piga tu simu, tutakuja. Umesikia? Nilikwambia kila mtoto utakaye mzaa, mimi na mama yako tutakusaidia kulea. Sio mama yako peke yake atakusaidia kulea na mimi nitakuwepo.”

“Na usinidharau, nina ujuzi mzuri sana wa kulea watoto. Nimewalea wale kaka zako kwa karibu sana. Nafahamu kila kitu juu ya watoto.” Sonia alitabasamu huku akilia. Sam akamsogelea Sonia. “Usilie bwana, kila kitu kitakuwa sawa. Mbona na mimi nipo? Ukijifungua zile siku za mwanzoni nitachukua likizo, tukae wote nyumbani Sonia. Usiogope bwana, hutakuwa peke yako.” “Njoo Sonia.” Paul alimuita. Sonia akasogea karibu na baba yake. 

Paul akamsogeza karibu zaidi na kumkumbatia. “Tunahitaji baraka zako sana katika hili, Sonia. Siwezi tena kukaa mbali na mama yako. Maisha yangu yote yamekuwa ya simanzi. Mara litokee hili au lile. Kila mtu akiniangalia mimi, anamuona Judge Mkuu wa Tanzania, lakini hakuna mtu anayeweza kunitazama mimi kama Paul isipokuwa mama yako tu.”

“Hata nyinyi pia, nimekuwa nikiwaangalia tokea nilipofika hapa, mmeshindwa kabisa kunipokea mimi kama Paul, wote mnaniita Mheshimiwa. Mungu amemrudisha Ishimwe kwenye maisha yangu sasa hivi akijua ni kiasi gani nina muhitaji mama yako.”

“Nakuahidi Sonia, sikutenganishi na mama yako. Ataendelea kuwepo daima kwenye maisha yako. Muda na wakati wowote utakapomuhitaji atakuwepo kukusikiliza. Au unataka twende tukaishi wote kwa muda?” Wote walimgeukia Sonia. 

“Hapana baba, siwezi kumuacha Sam.”  “Basi nakuomba Sonia, umruhusu mama yako niende naye. Hawezi kuwa na furaha kama akikuacha hivyo. Namwitaji sana mama yako.” “Kwa hiyo mama utakuja kunisaidia?” Sonia alimgeukia mama yake huku akiendelea kukausha machozi. 

“Hata ukitaka kila siku asubuhi wakati naenda kazini niwe na mshusha hapa halafu usiku nikitoka kazini niwe namfuata pia, hamna shida.” Sonia alicheka na kumuuliza baba yake kwa aibu kidogo. “Nani atakuwa akikupikia sasa?” “Kumbe unajua! Asante Sonia. Lakini ujue mimi na mama yako tupo na wewe Sonia. Hatuta kutelekeza. Labda kwa miezi hii michache ya mwazo ndio tutakuwa hatuonekani.” “Sasa hapo Paul ndio unaharibu tena kabisaa! Unataka aanze kulia tena? Tutakuwepo mwaya Sonia wala usiwe na wasiwasi. Huyo mtoto tutamlea, hata ukitaka unipe niondoke naye kabisaa. Hamna shida.” Wote walicheka. 

“Sasa wakati mama yako anafungasha vitu vyake, naomba umwambie na Kana mjiandae twende wote mkapaone nyumbani kwenu.” “Si tunaenda na Sam?” Sonia aliuliza nakumfanya Paul acheke. “Sawa.” Sonia alifurahi sana. “Asante baba. Sam naye akapaone kwetu.” Sonia alitulia kidogo. 

“Nini?” Paul akamuuliza. “Unajua sikuwahi kufikiria maishani kama na mimi nitakuja kuwa na kwetu. Yaani nyumbani kwa wazazi wangu! Asante Paul.” Sonia alimsogelea Paul na kumpa mkono. 

“Huruhusiwi kuniita mimi Paul. Umesikia Sam na Sonia? Wala msiniite Mheshimiwa. Mimi ni baba. Mmeelewa?” Sonia alianza kucheka. “Kweli kabisa. Wewe ndio binti yangu wa pekee bwana, usinipokonye haki yangu.” “Sawa baba.” “Hayo ndiyo maneno. Haya mjiandae twendeni. Mama yenu amechoka na safari.” “Kwani mlienda wapi?” “Umeanza Sonia?!” Wote walicheka. 

“Nataka kujua jamani!” “Tulikuwa hapo Nairobi tu wala sio mbali. Mama yako bado hana hati ya kusafiria. Ndio na shugulikia. Hatuwezi kwenda mbali.” “Hongereni.” Sam na Sonia waliingia chumbani kwao kujiandaa. 

 *********************

 “Nimeambiwa harusi haifungwi bila nyinyi kuisimamia.” Paul alimgeukia Nyange na mkewe. “Sisi?!” Mama Briana alishituka sana nakumfanya Paul acheke. Mama Sonia alitoka na kumuita Kana. “Jiandae tunaondoka wote.” “Tunaenda wapi?” Kidogo mama Sonia alisita alikumbuka Kana hafahamu chochote. 

“Huyu ni baba yake Sonia, kwa hiyo ni babu yako. Tunaenda nyumbani kwake.” Kana akatulia kidogo kama akijaribu kuelewa ila akauliza. “Sijaelewa! Tunahama tena?” “Hapana Kana. Tunaenda kupaona tu, halafu wewe utarudi na kina Sonia.” “Na wewe?” Mama Sonia alipooza gafla. Alikumbuka maisha ya Kana yote hajawahi kuishi na mtu yeyote yule ila yeye tu, huku akimuhesabu kama mama yake mzazi. 

Sonia alitoka chumbani na kubaki mlangoni akitokwa na machozi. Ulikuwa ni utengano ambao hakuna hata mmoja kati yao aliyewahi kufikiria maishani. Walishajua maisha yao ni wao watatu, na wengine wataongezeka juu yao, lakini sio kutenganishwa. Paul amekuja kama zawadi, lakini na garama kubwa sana ya kulipa. 

“Mama?” Kana alimuita tena mama Sonia. Mama Sonia naye alianza kulia. Paul akajisikia vibaya sana. Alikumbuka Ishimwe alishamwambia kuwa yeye ndiye alikuwa akimlea Kana maisha yake yote. “Tunaweza kuishi naye Ishimwe, haina shida.” “Kweli Paul?” “Haina shida kabisa. Ile nyumba ni kubwa sana. Kuna vyumba hata havijawahi kutumika.” “Asante sana Paul.” 

Kisha mama Sonia akamgeukia Kana. “Tutaenda kuishi wote.” “Bila Sonia? Siwezi kumuacha tena Sonia. Na unajua siwezi kwenda popote bila Briana.” Sonia hakuamini, alizidi kulia. Mambo yalizidi kuwa magumu. Mama Briana na Nyange walizidi kumuonea huruma mama Sonia. 

“Mimi naona nibaki tu Paul. Naona mambo yanazidi kuwa magumu.” “Na mimi je, Ishimwe!?” Paul naye alijikuta akiropoka kwa kuhamaki na kwa sauti ya juu. Akasimama kumsogelea mama Sonia. Mama Sonia alibaki hajui chakufanya. 

“Kwa hiyo ulitaka kuniacha!?” Kana naye akamuuliza kwa mshangao mkubwa sana, kama asiyeamini alichokuwa akitaka kukifanya mtu aliyekuwa akijua ni mama yake kwa karibia maisha yake yote. 

“Hapana Kana!” Mama Sonia alijibu kwa kujitetea, wazi alionyesha amezidiwa. “Sijakuelewa mama! Uliwezaje kufikiria kuondoka bila mimi?!” Mama Sonia alirudi kukaa kwenye kiti huku ameinama. Kana naye alimsogelea karibu. “Eti mama?!” Ilibidi Sonia asogee na yeye. 

“Kana! Mama hatuachi, ila anaenda kuishi na baba. Hapa ni padogo, hatuwezi kutosha wote na baba. Ndio maana imebidi tugawane, wao wakakae kule na sisi hapa. Lakini baba amesema kule pia milango ipo wazi. Unaweza kuwa mnaenda na Briana siku nyingine kutembea, au ukitaka mnaweza kulala. Ndio maana leo tunaenda kupaona, nyumbani kwetu. Ili wakati wowote utakao taka kwenda kumuona mama, tutakupeleka.”

“Leo Sam amekununulia simu atakupa baadaye, kwa hiyo itakuwa rahisi kuwasiliana na mama wakati wowote utakao taka. Natamani tuishi wote Kana, usihamie huko kwa babu na bibi yako. Lakini upo huru kuchangua pakuishi popote unapotaka milango ipo wazi.” Kana alibaki akimwangalia mama Sonia. 

“Naomba tubaki wote Kana. Usiwe na wasiwasi, kila kitu kitakuwa sawa tu.” Sam aliingilia kumsaidia Sonia. “Naona nibaki tu na nyinyi. Asante sana anko Sam.” Sam alijisikia vizuri sana. “Karibu Kana. Basi nenda ukajiandae tuondoke.” “Naweza kwenda na Briana? Siwezi kumuacha peke yake.” Kana alimuuliza Sam. Naye Sam akamgeukia Paul. “Eti tunaweza kwenda na Briana?” “Bila shaka. Tunaenda wote na baba yake na mama yake pia.” Paul alijibu. 

*********************

Japokuwa haukuwa mpango wake kuwachukua watu wengine, ilimbidi Paul akubali tu. Alitamani hiyo siku ya kwanza iwe ni siku ya familia tu. Lakini aligundua amekutana na watu ambao hawezi kuwatenganisha kwa urahisi. Kuanzia watoto mpaka wakubwa. 

*********************

“Na sisi Mkuu!?” Nyange aliuliza kwa mshangao kidogo kama ambaye haamini. “Si nimewaambia bibi harusi wangu, amesema hamna harusi mpaka nyinyi msimamie? Ndio inabidi kufahamiana zaidi.” Nyange na mke wake walibaki wanababaika. Mara simu ya Paul ikaanza kuita. “Naomba nikaongee na hii simu.” Paul alimtoa Ishimwe huko mawazoni kwa kumshika bega. “Hamna shida.” 

Paul akatoka nje kuongea na simu. Alitumia muda mrefu sana huko nje kisha akaingia ndani akakuta watu wote wameshajiandaa wanamsubiria sebuleni na mabegi ya Ishimwe mlangoni. 

*********************

Alipoingia tu watu wote walibaki wakimwangalia kasoro mama Sonia akasimama na kumsogelea. Alimshika mkono. Wengine walibaki wakishangaa wasijue kinachoendelea lakini ni kama mama Sonia alijua tu baada ya kuona sura ya Paul. 

“Njoo ukae kidogo.” Mama Sonia alimvuta mkono mpaka kwenye kochi jingine. Alikaa pembeni yake, Paul akainama. “Pole mpenzi wangu. Pole sana.” “Daah! Siamini?” Alisikika Paul akilalamika wengine wasielewe. “Ni kwambie kitu Paul?” Mama Sonia alikuwa amemuegemea kwenye bega la upande wa kulia huku akimchungulia usoni. Paul akanyanyua kichwa na kumwangalia. 

Ishimwe alipitisha vidole vyake taratibu kwenye shavu la Paul huku akimwangalia. “Wewe nenda nyumbani, ukaweke mambo sawa, halafu utakapotulia, ndio uje utufuate. Hamna haraka.” Paul aliinama tena nakufikiria kidogo. “Na sisi je?” Paul alimuuliza Ishimwe. “Mimi nipo Paul. Sina ninapo kwenda. Nitakusubiri tu hata kama utahitaji mwaka mzima wa kuweka mambo yako sawa. Nitakusubiri mpenzi.” “Kweli!?” “Kabisa Paul. Wewe nenda tu. Wote tutakuwa sawa.” Ishimwe aliendelea kumfariji.

“Daaah! Moto umeniwakia pabaya kweli!” Paul aliendelea kulalamika na kuibua wasiwasi na maswali kwa watu wote waliokuwepo pale. “Na Sonia?” Paul alimgeukia tena Ishimwe, nakuuliza tena. “Unataka kumwambia sasa hivi?” “Kuliko asikie magazetini, heri mimi ndio niwe wa kwanza kumwambia.” “Kuna nini?” Sonia aliuliza kwa sauti iliyojaa hofu kubwa. “Eti baba?” 

 *********************

Usikose Part 4, na ya MWISHO, Ujue Hatima Ya Yote.

 

 

 

 

 

 

 

 

AUTHOR 

 

https://4.bp.blogspot.com/-CDRegWnsyq4/V0igX2GDbfI/AAAAAAAAvWM/z3ZMlD_-sZ4w5wJRKYznd44nnTmmh_NkwCKgB/s320/share%2B%25287%2529.jpg 

Naomi Mwakanyamale Ng’imba 

 

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment