Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Love At First Sight - Sehemu ya 106. - Naomi Simulizi

Love At First Sight - Sehemu ya 106.

“Unataka uje unikimbie Tuma!” Ikawa kama aliyemgundua hila yake. “Mimi sijasema hivyo, ila sikutaka tuharakishe.” “Kuna tofauti gani ya jumamosi ijayo na sasahivi? Kama si sababu ya kujitoa ukiona nakujia na matatizo?” Tuma akatulia kwa muda akifikiria. Kimya kwa muda ameinama.

“Tuma?” Jerry akamuita kwa kuumia. “Mimi nataka ndoa na wewe Jerry, na nakuahidi sitakukimbia. Wewe nakupenda.” “Sasa kwa nini hutaki kufunga ndoa?” “Nataka. Lakini mwenzio nilikuwa na ndoto za kuingia kanisani na nivae gauni la harusi kabisa kama bibi harusi! Hivi vya haraka hata tukija kurudia haitakuwa sawa.” “Usilie mama. Niambie kile unachotaka.” JJ akaingilia akimtuliza.

Jerry akamsogelea karibu akianza kutulia. “Niambie unataka nini. Mimi nitafanya.” “Sio lazima sherehe, ila nivae shela.” Acha Hilda aanze kucheka. “Tumaaa! Unalilia shela!” “Ndoa za kikristo ni mara moja tu. Na mimi natamani!” “Hilo si tatizo kabisa. Usilie mama. Yaani wewe ukisema tu ndiyo, nakuletea watu wakukupamba hapa, na gauni lako naagiza liletwe. Maana hautakuwa na mabadiliko makubwa tokea ijumaa tulivyoenda kujaribisha. Utaingia kanisani umependeza sana.” “Mimi nataka kuolewa na Jerry, ila nikiwa nimevaa shela kabisa.” “Hilo limekamilika. Niambie kitu kingine unachotaka.” 

“Hamna. Mimi hata sherehe zile za ukumbini sio lazima, kwanza ni kama Mungu ameshatupa sherehe nzuri jana, japo hatukuwa pamoja na Jerry, lakini ilikuwa nzuri na ni kama alishatupa fungate. Lakini kanisani nikiwa na shela ndio napenda.” “Unauhakika mama?” JJ akaendelea kuuliza kwa kubembeleza.

“Kabisa. Hilo tu. Nampenda Jerry na sina shida kuolewa naye. Na wala hana matatizo ya kumkimbia! Anioe au asinioe leo, sitamkimbia. Ila nilitaka tutulie, ili tupate kitu kizuri. Nataka aniamini, asiharakishe, tukajipunja kitu kizuri kwa wasiwasi eti kuwa umaana wake ni kuwepo siku mtoto anazaliwa, wakati huyu mtoto atakuwepo maisha yetu yote!” 

“Na ninawaahidi sitakimbia jamani! Siwezi kumkimbia Jerry kipindi yupo matatizoni. Niende wapi?” “Basi tusaidieni tufunge ndoa leo. Bado ni mapema.” Jerry akasimamia palepale. Yeye anachotaka ni ndoa na huyo Tuma.

“Baba yake hayupo Jerry!” Jeremi akamkumbusha. Jerry akasimama kwa hasira kabisa. “Kila ninavyojaribu jambo kunakuwa na vipingamizi! Sijui nina mkosi gani mimi!  Yaani nakuwa kila nikisogelea kitu kizuri, jambo linatokea!” JJ akazidi kuumia akimlaani Sandra. Huwa anajitahidi kuwapa wadogo zake kila kitu wanachokitaka. Hapo anafanyaje? Ukimya ukatanda Jerry akiendelea kunung’unika.

“Mimi naona tufunge tu hiyo ndoa, leo. Mama yangu yupo, atamuwakilisha. Baba anaweza akakosa kabisa, sina shida.” “Unauhakika mama?” “Kwa asilimia 100. Ilimradi mama yangu yupo, twendeni huko kanisani, tukafunge hiyo ndoa niachwe nikiwa mke halali, pengine itamsaidia Jerry kutulia. Nakufikiria watoto.” Ikawa kama anaye sacrificesfuraha yake.

“Unauhakika Tuma? Usije juta baadaye.” Jeremi akawa kama amemuhurumia. “Si bora hivi kuliko vile vya Mbaki, baba J?” Akatabasamu kwa upole kama anaye muhurumia. “Bora hivi vya Jerry wangu kuliko ile fedheha. Acha tulimalize hili. Nayo ni bahati, inaweza isinirudie tena. Nishaahirisha ndoa, hii ni ya pili. Si wakati wote nitapata ninachotaka. Tufanyeni tu. Ilimradi nivae shela na niingizwe kanisani!” “Usijali mama. Tutafanya kitu kizuri cha muda mfupi. Kinaweza kisifikie tulichopanga jumamosi, lakini akirudi tunaweza fanya kubwa zaidi.” “Na utapambwa vizuri. Utavaa gauni lako, utapendeza. Usiwe na wasiwasi.” Akaanza kucheka.

Angalau hali ikabadilika mipango ikaanza sasa, JJ akampigia simu mchungaji kumuomba awafungishe ndoa siku hiyo badala ya jumamosi ijayo akimueleza dharula waliyoipata. Uzuri JJ anajitoa sana kanisani, na sadaka zake ni zile za KUGUSA haswa. Yeye na familia yake wakitoa mchango hapo kanisani, jua jambo litakamilika. Wanaheshimika sana maana pia mkewe naye yupo mstari wa mbele hapo kanisani. Hawakupata shida. Wakaweka mambo sawa kwa muda mfupi.

~~~~~~~~~~~

Wakataka kunyanyuka ili waanze kujindaa. “Jamani tuombeni. Hatutapoteza muda mrefu. Tunaweza kupunguza safari ndefu kwa muda mfupi tutakaochukua kwenye maombi. Alinifundisha mama Junior.” Akimaanisha mke wa JJ. Akamfurahisha sana huyo mama.

“Tutulie, tuwaombee watoto na mama yao. Kule ambako macho yetu hayaoni na mkono wa Jerry na mama yao hauwafikii, basi Mungu awakumbatie na kuwaficha na uharibifu wote mpaka mtakapowafikia. Na tuombee safari yenu hiyo ya kesho.” “Na ndoa yetu leo.” Jerry akaongeza, wakajikuta wote wanapiga magoti hapo sebuleni, mama JJ akaanza kuongoza maombi. 

Aisee waliomba hapo! Na kijana wa JJ mkubwa alikuwa muombaji sana. Siku hiyo aliomba, mpaka mama yake akanyamaza. Alivunja na kuharibu roho ya uharibifu kwa hao watoto na familia nzima.

Alikemea kila silaha inayonyanyuka juu ya familia yao. Akang’oa kila pando la uharibifu lililomea kwa siri kwenye hiyo familia yao. Akafunga kila mwanya na madirisha ya uovu walilofungua wao wenyewe kwa kuzembea au kwa bahati mbaya, akitubu kwa machozi. Aisee waliomba hapo mpaka wakaridhika.

~~~~~~~~~~~

Kabla hawajatawinyika, Jerry akawahi. “Najua mnajipanga kutufanyia kitu na Tuma baada ya kanisani. Nina ombi. Sijapata muda naye kwa juma zima, akiwa hapa na ninamuacha kwa matatizo, tena akiwa anakaribia kujifungua. Niwashukuru, lakini nitahitaji muda naye wakutosha. Najua hichi alichokubali kufanya sasahivi ni kinyume kabisa na ndoto zake. Sisi watatu tunamjua Tuma. Jeremi na Hilda najua wanajua ninachozungumzia.”

“Kwahiyo siwezi kupoteza muda, baada tu ya kufunga ndoa, lazima tuwekane sawa, ndipo niondoke, nikijua nimemuacha tukiwa ukurasa mmoja.” Tuma alibaki ameinama tu.

“Kama nimekuelewa, ni kwamba hutaki mambo marefu baada ya ndoa.” “Tafadhalini sana. Iwe chakula, sisi tuondoke akiwa hajachoka, ili tuweze kuweka msingi wetu. Sherehe zote hizo hazitakuwa na maana kama baada ya yote, naondoka nikimuacha kama ilivyo.” 

“Tulijiandaa sana, au niseme tulikuwa na mipango naye mikubwa sana siku ya harusi, na baada ya siku hiyo huko mapumzikoni. Lakini na mimi sikuchagua hili. Nasikitika na yeye analipa garama ya maisha yangu ya nyuma. Na pengine anaweza asipate harusi ya ndoto zake, ila nataka na hili lituache salama.” “Sawa kabisa. Eti mama?” Akimuuliza mkewe.

“Tukitoka tu kanisani, chakula pale nyumbani, mnakwenda kupumzika. Hakuna atakayewasumbua mpaka kesho muda wa kuondoka Jerry.” “Asanteni sana na samahaninikwa kwa mambo yangu yasiyoisha.” “Acha kusema hivyo. Kutakaa tu sawa.” Kaka yake akaongea akimtuliza ndipo wakatawanyika

Mizizi Ya Jana, Majuto Ya Kesho

         JJ na wadogo zake hao wawili waliondoka nchini Tanzania kuelekea nchini Marekani hawajui kitakachowakabili ila maombi ya wake zao kwamba wafanikiwe. Jerry alikuwa ametulia, na pete yake kidoleni. “Macho na masikio yako kwa Tuma. Tafadhali sana Hilda. Usizembee wala asijisikie yupo peke yake.” “Usijali. Na tutakuwa tukiwasiliana kila siku.” Huo ndio msisitizo mpaka uwanja wa ndege wakiagana.

Nchini Marekani.

         Walitua nchini moja kwa moja nyumbani alipo Jemimi. Hawakumkuta, alikuwa na kazi siku hiyo. Wakaingia kuoga, wakachukua moja ya gari na kuelekea hospitalini. Walimkuta Sandra amelala na mashine za kupumulia. Ikabidi kumtafuta nesi aliyewapa taarifa.

         Akawapa namba ya simu ya polisi anayefuatilia watoto, usiku huohuo wakampigia na kuomba wakutane naye. Wakakutana kituoni. Akawaeleza walipofikia, nakuwaambia kwa habari njema, mpaka siku hiyo hapakuwa na mwili wa mtoto yeyote wa umri wao uliokotwa popote inamaana wapo mahali, wapi na baridi hiyo! Ndio wasiwasi waliokuwa nao hata hao polisi.

         “Ni sawa na sisi tukiwa tunatoka na kuzunguka pale mtaani walikokuwa wakiishi ili kuulizia hata kwenye vituo vya mafuta, kuona kama kuna aliyewaona?” “Tunaweza kuongozana kesho mapema tu, kwa usalama hata wenu.” Kazi ya kuzunguka mtaani wakiwa na picha zao ikaanza kitu kilichosaidia pale Jerry alipoweza kutoa picha zao, wakatengeneza mpaka matangazo wakawa na kazi ya kubandika mpaka kwenye miti.

Ubaya ulikuwa msimu wa baridi kali, kwamba hata wasio na makazi, kipindi hicho hulazimika kukimbia mitaa, na kutafuta hifadhi za jumuiya. Kwa hiyo hapakuwa na watu wengi wanaotembea tu barabarani. Ikaongeza ugumu.

~~~~~~~~~~~

Hali ya Sandra ikaimarika na kutolewa mashine za kupumulia. JJ na Jeremi wakiwa wameenda kupumzika baada ya siku ndefu ya kuzunguka na baridi, yeye Jerry alirudi hospitalini kukaa kidogo na Sandra. Alimkuta hana mashine ila amelala. Akabaki kitini amejiinamia.

“Jerry!?” Sauti ya chini ikamtoa Jerry mawazoni. Alishatoka kuzungumza na Tuma, wakaagana anakwenda kulala. Tayari nchini Tanzania ilishakuwa usiku. Akasimama na kusogelea kitanda. “Vipi? Unajisikiaje?” Akakohoa kidogo, akiwa bado anakukereketwa na mikwaruzo iliyoachwa na mipira ya upumuaji aliyokuwa ameingiziwa kooni. Akamsogezea kikombe cha maji kilichokuwa pembeni yake na mrija. Akavuta kidogo na kuacha.

“Watoto?” “Bado hatujawapata!” Akaanza kulia. Alilia Sandra, Jerry akarudi kukaa, kimya. Akalia mpaka akanyamaza mwenyewe, na kupitiwa na usingizi tena. Jerry akabaki amekaa hapo mpaka kaka yake na Jeremi wakarudi hapo hospitalini wakiwa wamemletea chakula.

Sandra alipoamka tena na kukutana na sura ya JJ, alitamani angepoteza fahamu. Akabaki wakiangaliana mwishoe JJ akamtupia swali bila ya salamu. “Ulipokuwa na watoto hapa, kuna sehemu zozote ulikuwa ukienda nao?” “Nilikuwa nikijitahidi nisiwaache peke yao nyumbani.” “Kwa maana nyingine walishakuwa wenyeji kwamba wanajua jinsi ya kutoka na kurudi nyumbani?” “Hapana.” Akajibu akitetemeka mpaka midomo.

“Unafikiri hata address ya pale mlipofikia watakuwa wakiijua?” Jeremi akaongeza swali jingine. “Sidhani.” Pakatulia. “Msione kwamba sikujipanga. Nilijipanga ila nilipofika tu hapa, nikaibiwa pesa zote na vitambulisho vyote.” “Hati zao za kusafiria?” Jerry akamkatiza kwa swali maana hao watoto walikuwa wakimiliki hati za kusafiria za Kimarekani, kama raia. “Nilikuwa nazo sema niliugua gafla wakaja kunichukua kwa gari ya wagonjwa, mizigo niliacha kwa yule dada niliyeshukia kwake, naamini bado atakuwa na mizigo yetu.”

“Unajua kama yupo ameshikiliwa na polisi akiwa na shutuma nyingi tu. Angesharudishwa nyumbani ila anamashitaka ya kujibu ikiwepo kutumia vitambulisho visivyo vyake. Kwa maana nyingine pale alipokuwa akiishi kumefungwa na polisi.” Hapo tena akaanza kulia wee, kina kaka hao kimya hapo ndani, mwishoe wakaondoka.

~~~~~~~~~~~

Kulishakuwa usiku, lakini Jerry akaomba warudi tena kwenye ule mtaa waliokuwa wakiishi, wakaulizie kituo cha zima moto kilichopo karibu. “Kwa nini?” “Wao ndio wanahusika na dharula zozote pale mtaani kwao. Pengine watakuwa waliwaona.” Hilo ni wazo alilipata Jerry akiwa amebaki peke yake pale hospitalini akiwaza kwa muda mrefu.

Wakafika hapo kituoni na kupokelewa vizuri tu. Wakaeleza na tarahe waliyopotea. Mkuu wa hapo akawa mtu mzuri. Akaangalia ni nani aliyekuwa kwenye zamu siku hiyo, akawaita wakawa hawana taarifa zao. Ila wakasema siku hiyo sababu ya baridi kali sana, palikuwa na magari mengine mawili ya watoa huduma ya kwanza, walijitolea kuzunguka mtaani kuangalia kama kutakuwa na raia mwenye uhitaji, lakini siku hiyo hawakuwepo kazini.

JJ akawasihi kama wanaweza kuwapigia huko majumbani kwao na kuwauliza kama waliwaona hao watoto. Wakawapa na picha. Wakazipiga picha na kuwatumia wenzao ambao hawakuwa kazini siku hiyo. Mmoja wao, alikuwa mdada, akasema anakumbuka kukutana na vijana wa kiume, wanaweza kuwa umri wa hao anaowaona pichani, waliwakuta mtaani wakitembea kwenye barafu kali, wakawachukua na kuwapeleka kwenye shelter ya kanisa.

Zikawa habari mpya ila zenye tumaini. Wakapewa address na kuelekea huko. Walifika hapo ilishakuwa saa nne na nusu, mlango umefungwa, wakaambiwa warudi kesho yake, hawawezi kufunguliwa na hata hivyo uongozi wa hapo walishaondoka.

Jerry alitamani kulia akihisi vijana wake wapo nyuma ya huo mlango, lakini ikabidi kuheshimu na kuondoka.

~~~~~~~~~~~

Njiani Hilda akampigia. “Mkeo amenipigia simu yupo hospitalini. Anasema alianza kusikia dalili za uchungu, akapuuza, akidhani ni maumivu ya kawaida. Ila vilivyomzidia, ameelekea hospitalini akiwa na mama yake, wamemwambia ni uchungu. Hapo naongea naye vilishaanza kuchanganya, na ameniambia hakupati.” Jerry akashituka sana.

Kuangalia simu vizuri, amekuta missed calls kama 7 kwenye WhatsApp yake, kutoka kwa Tuma, hakuwa na taarifa. “Si ndio unakwenda huko?” “Naona na bimkubwa anakimbilia huko.” “Nawashukuru Hilda, acha nimpigie.” Akakata kwa haraka, simu ya JJ nayo ikaanza kuita, na ya Jeremi pia. Kila mmoja anampigia mumewe, Jerry akarudisha simu kwa Tuma, tena kwa video.

Iliita mpaka akachoka. “Naomba muulize Hilda kama amefika hospitalini.” “Hapa ndio alikuwa akinielezea kuwa wamefika kwa kuchelewa, Tuma ameshaingizwa leba ila yupo na mama yake, hata wao hawajamkuta.” Alivurugikiwa Jerry, alitamani apae arudi Tanzania.

Tuma amepiga mara zote hizo, hajaona! Kumbe alipomalizana naye, wakaomba pamoja na kumuaga anakwenda kulala, yeye Jerry akatoa sauti ili akiwasiliana na polisi au ndugu zake hapo alipolazwa Sandra, asimsumbue. Simu ikabakia mfukoni, akisaka watoto wa huku, huku wa kule anazaliwa.

Akamsikia JJ akiuliza kama daktari waliyemlipa awepo wakati wa kujifungua kwake alikuwepo. “Nimempigia, yupo njiani anakuja.” “Sasa kwa nini mpaka sasa hayupo hapo na mimi nilimuaga kabisa kuwa hatutakuwepo hapo, namuachia Tuma? Kwamba macho na masikio yake viwe kwake muda wote!” Akasikia kaka yake akigomba, akabaki hajui chakufanya, kwamba hata msaada mzuri wa kidaktari hamna! Jerry akajihisi anakosa bara na pwani.

~~~~~~~~~~~

Wakarudi walipofikia, kwa Jemimi, wakiwa garaji ndio wanaegesha gari mlango wa garaji unateremka, mke wa JJ akapiga kwa video. “Angalia video JJ, umuone mama yako mzazi.” Wote wakamsogelea kaka yao hapo mbele sehemu ya dereva.

Jamani walifurahi hao wanaume. Kelele. “Tuma yuko wapi?” “Anashonwa. Hivi daktari wake amekuja, nikamwambia mnahali mbaya, wakati mama yake akimaliziwa kuhudumiwa, anipe huyo mkwe, niwaonyeshe. Ila anasema Tuma anaendelea vizuri. Amejifungua salama. Nikuchanika tu.” “Amefanana na Jerry huyo!” “Amefanana na nyinyi wote. Halafu yupo kama Jemimi. Muangalie vizuri JJ.” “Kweli bwana!” JJ akaafiki akicheka, Jerry yeye ndio anafuta machozi.

~~~~~~~~~~~

Simu yake yeye ikaanza kuita tena alikuwa Tuma. Akapokea kwa haraka. “Tuma?” “Ni mimi baba, ameniambia nikupigie kukutoa wasiwasi. Yeye yupo salama, mtoto amechukuliwa na mama yake mkubwa!” Alikuwa mama Tuma. Hakutegemea kupoozwa na silawama kama kwenye ndoa aliyotoka. Kila kitu ilikuwa ni kosa na kukosolewa.“Nashukuru mama yangu. Nimemuona. Naomba muwekee simu Tuma sikioni. Angalau nimsikie.” “Acha nikupe kabisa.” Pakatulia kwa muda akasikia akimuita taratibu.

“Jerry?” Akashuka kabisa garini. Maana alimsikia kama analia. “Samahani Tuma. Samahani sana. Simu ilikuwa kwenye mfuko haina sauti. Sikuona mpenzi wangu. Tafadhali nisamehe.” “Usijali. Mimi nipo salama kabisa. Nilipuuza uchungu, nikajua ni vichomi tu vya kawaida. Kumbe njia ilishafunguka. Nimefika hapa hata sijakaa sana, nimejifungua. Wote tupo wazima. Vipi huko, umepata watoto?” “Lipo tumaini. Nitakuwa na jibu zuri kesho.”

“Umenisamehe?” “Usiwe na wasiwasi na sisi. Umemuona mama yako lakini? Amezaliwa yupo tayari kwa saluni. Manywele kila mtu alikuwa akiyasema humu ndani na kucha za kupaka rangi tayari.” Angalau Jerry akaanza kucheka.

“Nimemuona. Mrembo kama mama mwenyewe. Nimefurahi Tuma, nimefurahi sana. Angalau umenipa kicheko. Lakini vipi wewe? Nasikia umechanika?” “Bichwa la mwanao kama lako.” Jerry alicheka sana. Angalau usiku huo ukaisha vizuri.

~~~~~~~~~~~

Kesho yake alfajiri na mapema, wakampigia simu yule polisi aliyekuwa akifuatilia kesi ya watoto wakamwambia kituo ambacho wanaweza kuwepo, wakakubaliana wakutane hapo.

Baada ya muda akafika hapo na kuwakuta JJ na wadogo zake ndani ya gari wakimsubiria yeye. JJ hakutaka binti yake ajihusishe na hiyo hekaheka kabisa ili wasimvuruge akili na kumuingilia mipango yake. Na wote walijua yupo hapo akiwa ameacha shuguli zake zote, kuhakikisha Jemimi haingiliwi na mtu. Alikuwa akizungumza naye kwa kifupi sana akimuepusha na wasiwasi.

Alipowagongea kioo cha dirisha, ndipo wakashuka wote garini. Baridi mno. Hapo walikuwa ndani ya gari wamewasha heater. Hawakutaka kuingia ndani bila huyo polisi wasije kukataliwa tena. 

Akiwa na picha ya hao vijana, akaenda mpaka mapokezi, kina JJ wanafuata kwa nyuma. Akajitambulisha yeye na kina Jerry ndipo akaonyesha hiyo picha. Wakaambiwa wasubirie.

Wakatoka watoto wa Jerry kama sio wao! Mmoja ameshikilia mkono kama unaomuuma sana. Bwana watoto walilia hao kwa baba yao, kama sio wao! Walilia wamemshikilia baba yao, wanamuomba awachukue. Hakuhitajika tena kitambulisho cha kuonyesha kama ni baba yao. Jerry akaondoka nao.

~~~~~~~~~~~

“Naomba sisi mtushushe hotelini, ili waoge wale wakati mkienda kuwatafutia nguo za baridi.” Jerry akijua kabisa hao watoto na mama yao hawakaribishwi kwa Jemimi, akawa muungwana. Wakatafuta hoteli nzuri tu. Wakawashusha nje, wao wakaelekea madukani. Maana ungewatizama hao watoto ungejua kweli wamesaidiwa. Walikuwa wamevaa mavazi ungejua si ya umri wao, wamepewa nguo za mtu mwingine. 

Walikuwa wamechoka sana. Nywele zilishakuwa ndefu. Wamedhoofu. Akachukua chumba chenye queen beds mbili. Wakaelekea chumbani na kuwawashia heater, kufanya chumba kiwe na joto.

Wakati huyo mkubwa akitoa nguo, akamuona ni kama anaalama za mikanda mgongoni. Akashituka sana. “Nani alikuwa akiwapiga?” Akajifunika taulo kwa haraka na kuelekea bafuni bila ya kumjibu baba yake kama anayeficha.

Walibadilika hao watoto. Walipoa. Kwa hakika Jerry akajua wamekutana na mwalimu dunia. Akawahurumia akihisi wamefundishwa kupitiliza. “Umeweza kumuona mama?” Huyo mziwanda wa Sandra akauliza. “Bado yupo hospitalini, ila anaendelea vizuri. Watamruhusu tu. Mkono umefanyaje?” Akamuona anasita kusema.

“Unauma?” “Sana.” Akaanza kulia. “Toa hilo sweta niangalie.” Ukawa mpaka umevilia damu, upo mweusi kabisa. Jerry alishituka. “Umefanyaje?!” “Yule dada alikuwa akitupiga bila sababu. Aliporudi na kukuta mama amepelekwa hospitalini, tumebaki pale akaanza kutupiga anatuambia kwa nini hatukwenda na mama. Ndio tukatoroka. Njiani wakatukuta watu wa gari ya wagonjwa, ndio tukadanganya tumepoetea, hatujui pakwenda. Ndio wakatupeleka pale shelter.”

“Alikuwa akianza kunipiga mpaka Bright anakuja kunikingia apigwe yeye.” “Pole.” “Ila sasahivi sisi tumebadilika dad. Sio kama zamani. Ukituambia kitu, tunafanya.” Akawa analia kwelikweli akimsihi baba yao. “Nenda ukaoge twende hospitalini ukaangaliwe huo mkono.” “Usiturudishe kule kwenye shelter. Tutakusikiliza. Hatuwi wabishi tena.” Jerry akabaki ametulia anafikiria.

Kaka yake akatoka kuoga. “Bright, si sisi siku hizi tunasikiliza sio wabishi?” Akawa akimuuliza kaka yake kwa hofu analia. “Nenda kaoge baridi isikuingie.” Kaka yake akamfunika vizuri mpaka akamshangaza Jerry vile alivyokuwa akimjali mdogo wake. “Nenda, usilie kichwa kitauma. Njaa inakuuma sana?” “Nasikia maumivu, Bright.” “Kaoge nitakuombea dawa. Usilie.” Jerry akabaki akiwasikiliza hao watoto, asiamini kama ni wao.

Chakula kikaletwa mdogo akiwa anaoga. “Kula.” “Namsubiria Brian. Achague anachopenda kwanza. Hakushiba hata jana usiku, amelala na njaa.” “Kwani pale mlikuwa hampewi chakula chakutosha?” “Ni kidogo sana. Na wenyewe pale wanasubiria vyakula vya msaada. Wakati mwingine kunakuwa hamna chakula.” Akavuta shuka na kujifunika, akamuona ametulia kwenye kochi, kimya. Jerry naye akamuacha. Hicho kichwa ni copy ya Sandra. Dakika nyingi zilishakuaga mbele.

Ila hapo akawa ametulia sana. “Sijui mama anaendeleaje? Tokea walipokuja kumchukua, hatujamuona tena na hatujui alipo.” Akawa kama anawaza kwa sauti. “Anaendelea vizuri.” Lile jibu likawa kama limemshangaza. Nakumshitua kidogo.

“Kwani umemuona?” “Ndiyo.” Wakabaki wanaangaliana. Maama hao wawili ilikuwa ni shida sana kuzungumza. Jerry huwa hamalizi sentensi kwa huyo mtoto. Jeuri na alimdharau sana baba yake.

Akatoa simu yake mfukoni na kumpigia simu Jeremi. “Naomba mnijie na dawa za maumivu.” “Nini tena?” “Inaonekana Brian aliumiza mkono, inabidi mkirudi niwarudishe mkapumzike, nimpeleke hospitalini wakamwangalie.” “Sawa.” Akaagana na mdogo wake na kusimama kabisa hapo akisogelea dirishani, mbali na huyo mtoto.

“Ulikuja kufanya nini huku?” Hilo swali likamfanya Jerry amgeukie kijana wake. Akamtizama tu, kisha akarudisha macho nje ya dirisha. Walikuwa gorofa ya juu kabisa. Kimya mikono mfukoni.

“Ulijuaje kama tupo pale?” Jinsi alivyouliza hilo swali, sio asili yake kabisa. Alishamwambiaga baba yake hana uwezo wa kufikiria. Kitendo cha kutambua yeye ndiye aiyejua walipo, akajua kweli ameshikishwa adabu. Kimya, Jerry hajui amjibu nini. Ajieleze alikuwa hapo nchini muda wote huo akikosa kuzaliwa kwa binti yake akiwatafuta wao ambao hawakuwahi hata kutambua uwepo wake! Akajikuta hana chakujibu.

“Nilitaka kusema asante kwa kuja kutuchukua pale. Mara nyingi tulikuwa tunalala na njaa. Hamna chakula chakutosha, na kulikuwa na baridi sana.” “Pole. Poleni sana.” “Asante. Na nilipoondoka kwa Getu, niliondoka na hati zetu za kusafiria.” Akaongea kama anayembembeleza baba yake. Na alimuelewa sana tu, anachokitaka. Akamwangalia na kunyamaza akirudisha macho dirishani.

“Tokea tuje hapa, hatuenda shule.” Akaendelea kujibembelezesha kwa baba yake. Jerry akabaki akisikiliza hata hamwangalii. Mawazo yapo mbali akitafakari maisha ya hao watoto. 

Brian akatoka. “Njaa inauma, Bright. Na nasikia maumivu.” “Utaletewa dawa. Toa hilo taulo, nakufunika shuka. Tule. Tumeletewa chakula kingi. Utashiba.” Jerry kimya. Akamuona anamfunika mdogo wake. Akachukua taulo dogo na kumning’niza mkono kwa kumfunga shingoni.

“Nikiweka hivi sisikii maumivu sana.” “Pole.” “Asante. Nasikia njaa Bright!” Akamsogezea mdogo wake sahani. Akamsikia anacheka. “Kuna soseji!” “Muone. Usijimwagie sasa. Angalia hiyo juisi. Au unataka maziwa.” “Nataka vyote.” Akamsikia kaka yake anamcheka.

“Kaa tule wote. Vitamu!” “Kula kwanza ushibe.” “Hicho chakula ni kingi sana. Kisipotosha nitawaagizia kingine. Kula.” Baba yao akaingilia. “Wewe huli?” Jerry alimtizama huyo mtoto asiamini kama amemsikia sawasawa. Ila akamjibu hatakula. Waendelee tu.

Ungesema ni watoto wanaotokea nchi za vita. Walikula hao watoto mpaka punje ya mwisho. “Utaturudisha kule ulikotutoa?” Brian akamuuliza baba yake kwa wasiwasi. “Kule hamtarudi tena. Mkishaletewa nguo, tutaenda ukaangaliwe huo mkono halafu nitawapeleka kwa mama yenu.” “Wewe utaondoka?” Jerry akamtizama huyo mtoto mfuata mkumbo! Aliiga kila kitu kaka yake na mama yake wanafanya akionekana huwa haelewi kitu. 

“Pumzikeni mpaka mtakapoletewa nguo.” “Nimeshiba, asante.” Mpaka Jerry akashangaa kwa macho kabisa. “Nani amewafundisha kushukuru?!” Wasijue ndio moja ya sababu Getu alikuwa akiwapiga nayo.

Walikuwa ni watoto wanaojua kupokea bila kikomo, na wanaojua wanastahili kupewa au kutumikiwa. Alipoona wamepoa hawawezi kujibu, wakajua ni mwalimu duniatu. Na huwa anajua jinsi dunia ambavyo hufundisha kwa maumivu. Akawaacha tu akimlaani Sandra kufikisha hao watoto hapo walipo. Wakapanda kitandani, hapohapo wakalala.

~~~~~~~~~~~

Akatoka kuzungumza na Tuma, akimpa habari za kupatikana hao watoto. “Pole Jerry. Pole sana.” “Aisee wanahali mbaya, Tuma! Mbaya sana.” “Pole.” “Naomba endelea kunivumilia. Au unanihitaji sana nirudi na kina Jeremi.” “Kwamba wao wanakuacha?!” 

“Huu ni msalaba wangu Tuma! Bro anamajukumu mazito, na kama unavyojua bado Junior yupo Tanzania. Huwa anajitahidi akiwepo nyumbani, hasafiri. Ili awepo naye na mama yake. Kuja kwake huku ni vile ananijali sana. Jeremi hivyohivyo majuku yake na familia yake inamuhitaji nyumbani. Siwezi kuendelea kuwashikilia wakati tumeshapata watoto. Lazima niwaache waondoke. Vinginevyo useme umefika mwisho, huwezi subiria tena.”

“Hapana Jerry. Sisi tupo salama kabisa. Nakumiss. Lakini usile ng’ombe mzima ukabakisha mkia. Umebakisha nini tena? Au unataka kurudi nao?” “Huko sitajihusisha nako. Wapi wanaishi kuanzia hapa, bado ni juu ya mama yao. Lakini ni lazima kama wanabaki huku, niwaache kwenye mazingira yakueleweka. Kama nilivyokuwa nikikwambia, walipokelewa na mtu aliyekuwa akisoma na kaka yake Sandra.”Akamsimulia jinsi walivyoishi na Getu, Tuma akaumia sana.

“Lakini ulisema Jerry!” “Mimi nilijua tu, Marekani aliyokuwa nayo kichwani Sandra, ni Marekani ya Jemimi. Akajua Marekani yote ipo hivyo. Ameijua vizuri sana. Lakini pia nitamuachia mwenyewe. Akiamua kubaki hapa, tafadhali nivumilie Tuma. Nikishamtoa tu hospitalini na kumkutanisha na wane, basi. Mengine atapambana nayo mwenyewe.” “Kwamba hutabaki mpaka apate pakuishi?” “Hapana Tuma. Mimi si mumewe. Haya ni maisha alichagua kwa kunidhalilisha sana. Atapambana yeye mwenyewe mpaka asimame. Hainihusu.” Tuma hakuchangia.

“Hapa alipo hana vitambulisho vyovyote vyakuonyesha anastahili kuwepo kwenye hii nchi. Viliibiwa. Hana sifa ya kupangisa popote wala kununua chochote kwa sababu hana kipato. Anafanyaje akitoka hospitalini, hakika hayanihusu.”

“Lakini akiamua kurudi nyumbani, pia sitachangia. Ila huyu mdogo.” “Brian?” “Huyohuyo, anaonekana alipigwa na kuumizwa mkono vibaya sana. Yupo kwenye maumivu, inabidi akatibiwe kabla ya yote. Tafadhali nivumilie Tuma.” “Wewe usiwe na wasiwasi na sisi.” Jerry akavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu.

“Jemma anaendeleaje?” “Anakazi ya kula na kulala tu mwanao. Wakija anti zake hapa wanamshugulisha aamke, lakini wapi! Anapenda kupendwa huyo mwanao! Akimuweka mkononi unamuona anajikunja vizuri, kama kajitoto kakangaroo.” Jerry alicheka sana.

“Bibi yake anasema eti anajua akiwa mikononi. Tunamcheka hapa!” “Muweke nimuone.” Tuma akaweka video. “Muone alivyojikunja! Basi hapo atalala hutamsikia kama amejisaidia ila njaa ikianza utamsikia akianza kugeuka.” “Anazidi kuwa mrembo!” “Mama yake mkubwa alikuwa hapa ndiye kamvalisha hivyo vyote mpaka vya kichwani. Kaleta mtu wa kumpiga picha, walikuwa na kazi ya kumpiga picha mpaka kwenye vikapu hata nisivyovijua!” Jerry akazidi kucheka akijua ndio utamaduni wao.

“Alikuwa na JJ kwenye video muda wote. Akataka aamshwe wasalimiane. Nimemsikia JJ akiongea hapa, hamalizi.” “Yaani mimi nimewatuma nguo na dawa, naona hawarudi, kumbe wapo na Jemma huko.” Tuma akacheka sana.

“Na ujue si vyamuda mfupi. Junior naye kafanya fujo zake zote hapa akiwa na Jemimi kwenye simu, naona mpaka wakaridhika. Wameondoka muda sio mrefu.” “Najua watatuma hizo picha na video kwenye kundi. Acha mpiga picha aziweke sawa, nizione vizuri. Niamshie na mimi.” “Bwana Jerry! Ndio amelala tu! Walikuwa wakimsumbua muda wote ili wampige picha! Subiri apumzike kidogo!”

“Wewe umesema halii. Sasa si uniamshie na mimi nimsalimie kisha atarudi kulala? Natamani kumuweka kifuani huyo mpaka huwa nasikia kuumwa.” “Pole. Basi acha nikupunguzie hamu.” Jerry na mwanae wakaanza tena hapo mpaka kina Jeremi wakarudi hapo na masanduku.

~~~~~~~~~~~

“Sikujua kama mmeenda kufanya manunuzi ya msimu mzima!” “Wameingiwa baridi, wanahitaji makoti na viatu vya kueleweka. Wanaendeleaje?” “Sasahivi wamepumzika ila Brian yupo na maumivu. Niwashukuru kwa yote, ila nashauri nyinyi mrudi nyumbani.” Kaka yake akabaki kimya kwa muda.

“Utakaa huku mpaka lini Jerry? Unamke nyumbani na mtoto ambaye hujamuona. Tafadhali usijisahau?” “Nimetoka kuzungumza na Tuma, nimemueleza uhalisia ulivyo.” “Atachoka Jerry! Atachoka. Kama alivyosema bro, usijisahau, ukajikuta unarudi kwenye kufungwa na maisha ya Sandra.” Jerry akabaki akitafakari chakufanya akiwa ameshanaswa katikati ya wanawake wawili wenye watoto wake.

“Lakini siwezi muacha hivi ilivyo jamani! Hana vitambulisho. Hana pakuishi wala usafiri. Kama kweli nataka nirudi nikatulie na Tuma, nilazima kama anabaki huku, basi angalau kumuacha sehemu fulani.” Hapo akamtibua JJ. “Watoto wa Salamba ni wajinga sana. Wanajidai wajuaji, lakini hamna kitu kichwani.” JJ akaanza kugomba akijua kwa sehemu Jerry yupo sahihi. Hawezi telekeza wanae. 

“Wanasimamia na kujivuna kwenye juhudi za watu, wakijionyesha wanaakili. Wakiachwa wao wenyewe wafikirie, matokeo yao ni kama haya. Kutafuta mtu mwingine kusafisha makosa yao, kuwasaidia kuwasogeza tena na tena. Narudia tena Jerry, kuwa makini sana. Sandra ni mzuri sana wa maneno, lakini hana akili na uwezo wa kuendesha mambo.”

“Utajikuta upo na Tuma, bado yeye anakutegemea kwa kila kitu, mwisho ndoa itakushinda. Sasahivi utamtafutia pakuishi, atakuja kukutafuta tena amekwama hili na lile kwa sababu sisi wote tunamjua Sandra. Anapenda kukuweka karibu ili umsaidie kuendesha mambo huku akijisifu.” Aisee JJ aliongea, na hapo ndipo wakajua hasira yake kwa Sandra. Aligomba bila kuchoka akimkumbusha hili na lile, Jerry ametulia tu.

“Kuwa makini Jerry. Kuwa makini sana. Binafsi swala la kuturuhusu kuondoka nalipoea kwa haraka sana. Hivi naangalia tiketi hata leo usiku nirudi nyumbani.” “Kwamba uondoke leo!?” “Siwezi muacha Hilda na watoto kwa kipindi chote hichi! Kwanza sina sababu ya kuwepo huku mimi isipokuwa wewe Jerry. Na kama ulivyosema. Maadamu umepata watoto, hakuna kilichobakia. Acha na mimi nirudi kwa watoto wangu.”

“Na utanisamehe Jerry, mimi hata hospitalini kwa Sandra sitarudi. Nampigia simu Jemimi aje anifuate hapahapa, nijipange.” “Naelewa Jeremi. Na asante sana kuwa na mimi huku.” Akamgeukia kaka yake kutaka kujua msimamo wake.

“Unahitaji kitu chochote?” “Nipo sawa kabisa. Ila mwambie Jemimi chakula cha usiku nitakuja tule naye kama nyinyi mnaondoka.” “Alisogeza likizo kwa ajili ya mabadiliko yako ya harusi. Alikuwa akinisubiria mimi tu, turudi naye nyumbani akamuone Jemma na mama yake.” “Kwamba mnaondoka naye?” “Ila sisi itakuwa kesho. Tutazungumza vizuri ukirudi usiku nyumbani. Ila hii gari tunakuacha nayo, sisi tutafuatwa na Jemimi. Wewe endelea tu.” “Asante. Na sitachelewa kurudi.” “Na hata ukichelewa, asubuhi tutapata muda kabla sijarudi nyumbani.” Wakamsaidia kuingiza masanduku yote chumbani.

~~~~~~~~~~~

Watoto wakaamka. “Nasikia maumivu, dad.” Brian akaanza kulia. “Toka hapo kitandani, uvae, twende hospitali. Pole sana.” JJ akajiangalizia, akamwambia Jeremi wao waondoke, wakamsubirie Jemimi sehemu ya mgahawa. Hao watoto hawakuwa hata wakiwatambua upande wa baba yao, kabisa. Ila wajomba zao tu. Hao ndio walikuwa wakiwaheshimu. Wakatoka na kumuacha Jerry na vijana wake. 

Baada ya sekunde chache JJ akarudi. “Nimesahau kukuachia funguo za gari.” “Asanteni kwa kuja kututafuta.” Bright akamuwahi JJ kabla hajatoka.

JJ alibaki amepigwa na butwaa, kama ambaye haamini alichokisikia. “Asante.” Akarudia tena mpaka Jeremi akarudi na yeye kuangalia na kusikiliza. “Najua mlikuja kututafuta. Asante.” Akaongea mpaka machozi yakamtoka huyo mtoto kopi ya Sandra. “Karibu. Ila mjue baba yenu ndiye amehangaika kujua mlipo. Polisi wote hawa walishindwa kufikiria na kujua mlipo mpaka baba yaenu alipopata wazo na kulitendea kazi.” JJ akaanza.

“Kwa hiyo wakati mkimuita baba yenu mjinga, hana akili za kufikiria, mjue akili hiyohiyo mnayoidharau nyinyi na mama yenu, ndio imewatoa kwenye baridi na kuwapa joto. Ndio imeweza kuweka chakula kwenye matumbo yenu.” “Sasahivi naelewa anko. Najua. Nimepata muda wa kufikiria na kuona mambo yalivyo, sasahivi naelewa. Na samahanini sana.” “Huo msamaha unatakiwa uanze na baba yako uliyekuwa ukimtusi bila adabu. Sio mimi. Umeelewa Bright?” JJ akampandishia kabisa huyo mtoto, Jerry kimya akimsaidia kumvalisha mdogo.

“Umebeba laana ya baba yako, Bright. Na hapo ulipo hutatoka mpaka utambue nafasi ya baba yako. Hata kama anayo madhaifu, hauruhusiwi wewe hata kuyatamka. Ni laana, na Mungu ameahidi adhabu kwa watu wa aina yako, kama alivyoahidi baraka na maisha marefu kwa wanao heshimu wazazi. Haupo kwenye nafasi ya kumnyooshea kidole baba yako. Nikujilaani.” Bwana JJ alimmalizia huyo mtoto uchovu wote.

“Unanielewa Bright? Sasahivi mmekwama huku, unawaona wajomba zako wameacha shuguli zao na kuja kuwasaidia?” “Hapana.” “Acheni dharau na kiburi ambacho hakiwasaidii ila kuwatenga na watu. Msifuatishe nyayo mbaya mkidharau watu wakati mnaishi na watu. Hamuwezi kuepuka watu. Popote mtakapokuwa. Haijalishi nchi, wawe weupe au wakijani, mtaishi na watu. Thaminini watu ndipo mtakapoweza ishi vizuri. Hamuwezi mkadharau viumbe vilivyoumbwa na Mungu, halafu Mungu akawaachahivihivi! Hata kidogo. Atawapatiliza tu.” “Sasahivi nimeelewa anko. Samahanini na dad samahani.” Akatoka kabisa kitandani akisihi msamaha.

Mpaka JJ akajirudi. “Juhudi unazoweka shuleni, ziweke na kwenye mazingira ya nje. Itakusaidia Bright. Kila la kheri.” “Msalimie Jemimi.” Wote wakamgeukia huyo mtoto kwa sekunde kadhaa kwa mshituko. Ni kama useme nisalimie moyo wako huku umeshika kisu kikali umekielekezea kwenye huo moyo, haijulikani kama nia ni kuchoma au kukiweka chini. Chumba kikapoa kwa muda, JJ akageuza na kutoka bila yakumjibu.

Mahusiano Si Ya Kurishana

“Nisikilize Bright. Mahusiano hujengwa. Ulishaharibu sana.” “Sasahivi najua dad. Na naomba msamaha.” “Hapana Bright. Kwa maisha yenu yale mlivyokuwa mkiishi na familia yangu na watu wengine wanao wazunguka, wakiwasaidia hata majukumu yenu pale nyumbani, neno samahani halitakaa kubadili kitu. Sijui kama unanielewa?” “Najua.”

“Hapana Bright, hujui kwa sababu hujawahi ishi maisha mengine useme ulibadilika. Nyinyi mmekuwa watoto wenye kiburi, wabaya kwa tabia, maneno machafu na makalisana kwa watu. Hamna uhusiano mzuri na yeyote isipokuwa familia za wajomba zenu tu. Neno samahani halitakaa likaeleweka kwa yeyote isipokuwa matendo na muda.” Akapoa huyo mtoto, kimya.

~~~~~~~~~~~

Mkono wa Brian ulikuwa umevunjika. Akafungwa POP na kurudi kwa Sandra akiwa na simu. Alilia Sandra, asiamini. Japokuwa walikuwa wamedhoofu, ila akaona ni wasafi, kwa mara ya kwanza akamshukuru sana Jerry. Jerry alishindwa hata kuitika.

“Hapa unaruhusiwa Sandra, mpango ukoje?” “Nilipanga kuishi huku, lakini naona sitaweza Jerry. Sina uwezo wa kuendesha maisha huku. Nimekwama.” Akawa muwazi na kujikuta akikiri mbele ya wanae.

“Kwa nini ulikuja huku na kwa nini unagairi na kutaka kuondoka?” Sandra akajieleza mengi lakini alisikika yupo muwazi. “Nyumbani ile biashara ilinishinda kabisa, na unajua siwezi kuajirika kule.” Akikumbuka wizi alioufanya na watu kujua ila kuachiwa ili benki isiingie skendo. Waliacha jina hao yeye na wenzie, wengine wakiwasifu walifanya wizi wa akili, lakini waajiri wakiwakwepa.

“Nikajiambia pengine huku naweza kuanza kitu, hata biashara fulani, ikatusaidia sisi na watoto.” “Sasa unapotaka kurudi nyumbani, unafikiri utaishije kule? Maana ulichokimbia bado kipo.” “Nisaidie mawazo Jerry.” Alishangaa Jerry, hakuamini.

“Mimi!?” Akamuuliza kabisa akijishika na macho ameyatoa akishika kifua kabisa na ndipo wakaona pete ya ndoa. Aliumia sana Sandra, lakini akaamua kuendelea. “Najua nimekuwa mtu wa maneno mabaya. Nikikudharau. Lakini najua ulikuwa ukinisaidia Jerry. Ni jeuri tu, lakini najua wewe ndio ulikuwa ukiendesha mambo pale kazini hata nyumbani.” Bwana Sandra alijishusha, kama sio yeye! Alibaki akimtizama, na kutoka kabisa hapo akamuacha na wanae kwa muda.

~~~~~~~~~~~

Aliporuhusiwa, akawatoa hapo na kuwarudisha hotelini alipokuwa amechukua chumba, yeye akarudi kwa Jemimi. Ilikuwa usiku, hakuwakuta, walikuwa wamempeleka Jeremi uwanja wa ndege, alipata ndege ya kumrudisha nyumbani.

Kesho yake ikawa tena JJ na Jemimi wanarudi nyumbani. Jerry akaachiwa hilo jumba na gari. Akarudi alipoacha familia yake.

~~~~~~~~~~~

“Nisaidie nauli, nirudi tu nyumbani kwetu kwa wazazi Jerry. Watoto hawajasoma muda wote huo! Nitawaharibia maisha.” “Nisikilize Sandra. Mwanzo kwa yeyote sio mrahisi. Nyinyi kwenu hamjui hili kwa sababu mmezoea kutumia watu vibaya. Utakapoondoka hapa sasahivi itakuwa ni kukimbia, na kile ulichokuwa ukikikwepawatoto wako wasijifunze kwangu sasa ujue watajifunza kwako na wajomba zao. Unanisikia Sandra?” Akawa muwazi kabisa mbele ya watoto wake.

“Umeona sisi kwetu? Wote tunaanzisha jambo, tunasubiria mpaka linakuwa. Uliponifukuza kwako ukinitusi wewe na hawa watoto wako ukiwa umenipokonya kila kitu, NILIANZA Sandra.” “Ndio umeoa?” Akauliza kinyonge, kwa wivu.

“Kabisa. Tena safari hii Mungu amenipa mke mzuri SANA. Ananiheshimu mimi na ndugu zangu. Tunajenga CHETU, na Mungu ametubariki binti mzuri sana.” Bwana walishituka hao watu, wote hawakutegemea.

“Maisha ni lazima yaendelee kwa garama yeyote ile. Ulikubali kuja huku kuanza, anza na vijana wako wajifunze kwa vitendo, sio kukimbia huku na kwenda kuishi kulikokwisha jengwa kwa mzee Salamba. Anza CHAKO ambacho safari hii utakuwa na kiburi chakusema ni chako kweli sio kujisifia kwenye juhudi za wengine. Umesikia Bright?” “Nimeelewa.”

“Sio kweli kwamba hukuwa shule kwa muda wote huo. Mungu alishawaona nyinyi mnayo elimu nzuri ya darasani, na kwa kuwa anawapenda, ila mnakiburi, mmekataakufundishika kwa upendo, akaamua kutumia njia hii kuwafundisha upande mwingine wa maisha. Kipindi chote tokea mnatua hii nchi na mama yenu, MLIKUWA SHULENI.”

“Sasa, ni lazima kumuonyesha Mungu kuwa mmeelewa, na mpotayari kuishi kama binadamu aliowakusudia muwe. Vinginevyo, hapa nilipowakuta, patajirudia tena na tena mpaka Mungu ahakikishe mnaelewa kwa sababu anakusudi na nyinyi.” Wakaanza kulia.

Maana ndio kwa mara ya kwanza wanampa baba yao nafasi ya kumsikiliza na kuona anaongea mambo ya msingi kiasi hicho! “Saidianeni na mama yenu, katika kila hali, hapa mlipo mtoke kwa vitendo sio kukimbia kwenda kutaka wafanyakazi wa bibi yenu wakawatumikie tena. Nyinyi ni watoto wa kiume, fanyeni kazi. Jifunzeni kufikiria na kufanya mambo. Hii nchi ni nchi yenye nafasi nyingi sana, mnaweza kuwa mtakacho, endapo mkijituma.”

“Acheni kiburi na dharau. Na kama ulivyoambiwa asubuhi, huu ulimwengu umejaa watu wa kila namna, sio ndugu wa mama zenu tu, jifunzeni heshima, muishi na watu kwa nidhamu. Ndipo mtaweza kuishi vizuri na watu, na watu kuwaheshimu.” Wote wakaomba msamaha kwa kutaja mabaya waliomfanyia baba yao ikiwepo majina mabaya waliyokuwa wakimtambua nayo, Jerry alikuwa akihisi anaangalia filamu. 

Maana walikuwa wakikumbushana moja hadi jingine. “Na kutokukusikiliza hata ulipokuwa ukisema tunaweza toa vyombo vyetu wenyewe, tusiwasumbue kina dada wanakazi nyingine.” “Na kutowashukuru pia kina dada.” “Na kushindwa kutandika vitanda vyetu wenyewe.” “Au kukataa kuokota hata nguo zetu wenyewe.” Bwana watoto walitubu hao, mpaka Jerry akaanza kucheka. 

“Mmejifunza wapi hayo yote?” “Getu. Alikuwa ukisahau kushukuru, anakupiga.” Wakawa wanamsimulia angalau wakawa wanacheka wakisumulia sasa kama stori, Sandra ametulia akiangalia wanae na baba yao. Akiumia vile alivyowanyima wanae mahusianomazuri na baba yao. Lakini maji yalisha mwagika, hayazoleki tena. Akaangalia pete ya Jerry kidoleni na vile alivyokuwa akicheka na vijana wake, akabaki amejituliza, amejifunika, ila amekaa kitandani.

Brian alikuwa akimsimulia baba yake kila kitu, kaka yake akiongeza ila kwa kucheka sio kilio tena. “Alitukomesha.” “Hapana. Hamkustahili kujifunza kwa uchungu hivyo. Ni makosa yetu mimi na mama yenu. Hayo yote mlitakiwa muwe mnayajua tokea zamani. Poleni sana.” Akawatuliza.

~~~~~~~~~~~

“Mtoto mpya anaitwa nani?” Brian akauliza. “Tumempa jina la mama yangu, anaitwa Jemma.” Wakamuona mpaka sura inabadilika na kujawa furaha kabisa. Sandra akaona aibuvile alivyokataa yeye peke yake katika wake wote, watoto wake wasiige mambo ya majina ya kwao hayo yanayo anzia na ‘Je’. Akajua kwa hakika safari hii Jerry ameoa mke wa ndoto zake na kuunganisha familia yao. Akajua ameshakosa bara na pwani. Hawezi toka tena. Akubali matokeo.

“Naomba kumuona.” Brian asiye na makuu ila fuata mkumbo akajisogeza. Jerry akatoa simu yake na kumuonyesha video. Ungejua Jerry anapenda anachokiangalia. 

“Ni mtulivu sana kama mama yake.” Akasifia kwa makusudi. “Mzuri huyo mtoto wako! Mzuri sana.” Brian akasifia nakumfanya baba yake acheke akiafiki. “Yeah, she is so beautiful. Just like my mom.” Kijana wake mkubwa naye akaomba kumuona. Sandra macho chini.

Kesho Ya Mtu Ni Fumbo Kubwa Sana

“Sasa ni hivi, nina siku mbili tu na nyinyi ikiwepo leo, baada ya hapo narudi kwa familia yangu.” Jerry akafanya watulie. “Mimi na mke wangu kuna kiasi cha pesa ambacho tumekubaliana kuwasaidia ili kuanza maisha yenu.” Kimya, Sandra akisikiliza kwa makini.

“Nitampa mama yenu hiyo pesa. Sasa basi, swali kwako Sandra, mbali na pesa, ulitaka niwasaidie nini kabla sijaondoka? Maana baada ya kesho, hamtaniona. Narudi nyumbani kwa mke wangu na binti yangu.” Akiwa amempokonya mpaka chupi, leo kibao kinageuka. Wanae wakamgeukia mama yao.

“Nashukuru Jerry, lakini sina vitambulisho kabisa na sina usafiri wa kunizungusha hapa. Ila nimekusudia kutulia kwenye huu mji. Nitasogea kwenye mtaa mzuri kidogo wenye shule nzuri na eneo salama.” “Sawa.” Akaafiki bila shida.

~~~~~~~~~~~

Jerry akatoka hapo na Sandra pamoja na hao watoto mpaka kituo cha polisi. Wakashauriwa kutafuta sehemu ya kuishi ili kuwa na anuani yakueleweka. Mpaka inafika usiku, Sandra na wanae wakawa wamepata apartment yao ya chumba kimoja. “Vifaa vya humu ndani!” Akawa akijiwazisha kwa sauti, Jerry hata hakuchangia.

Hiyo apartment ilikuja na vitu muhimu tu, mpaka mashine za kufulia hapohapo ndani, friji, majiko na microwave. Ikabakia thamani zao kama vitanda na makochi.

~~~~~~~~~~~

Kesho yake aliporudi, akamkuta Sandra ameandika orodha za sehemu za kusindikizwa kwa makini na mpangilio, akajua ameelewa soma. Maana hiyo ilikuwa siku yake ya mwisho, na alimuhakikishia asingerudi tena hapo. Anarudi kwa mkewe na binti yake.

Sandra mtoto wa mjini, akatumia akili usiku kuchwa akijipanga. Alishajua Jerry maisha yamemkalia njema. Akajua asingeacha wanae walale chini. Kwahiyo manunuzi yote ya thamani za ndani akafanya na Jerry siku hiyo mpaka wakapata sehemu wanayouzia magari yaliyotumika.

Sandra akanunua gari ya chini, mpaka akamshangaza Jerry na kuamini kweli elimu dunia amehitimisha shule. Somo limeeleweka. Sandra wa makuu, amekutana na uhalisia wa maisha.

Usiku akiagana nao, kwa asilimia 85 maisha ya Sandra na wanae yalishaanza kuchukua sura fulani, ila uchungu kuagana naye.

Mtu waliyekuwa akiishi naye nyumba moja, wakimdharau, leo amekuwa watofauti! Jerry alikuwa amebeba uthamani ambao wao walishindwa kuutumia. Waliposema tu cha nini, ulimwengu haukuchelewa. Ukampokea Jerry na kumpa mke na watoto. Usiku huo wanamuaga Jerry, hawaamini jinsi walivyopoteza nafasi waliyokuwa wakichezea. Watoto wake walilia sana. Lakini Jerry si baba yao peke yao tena, anaye binti mwingine na mama yao alishamfukuza. Hapo walikuwa wakila matokeo ya janga, alilochuma mama yao.

Mwisho

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment