“Ni nini Jerry?!” Jeremi akamuuliza kwa sauti ya chini iliyojaa mshangao na lawama wakiwa wanatembea nyuma ya kaka yao. “Mimi huwa sisherehekei birthday, na Tuma nilimueleza kabisa.” Hapo alikuwa amenywea kama aliyenyweshewa na mvua na ameachwa nje kwenye baridi kali.
“Ulikosana wapi na birthday?” JJ akageuka aliporidhika wapo peke yao, upande mwingine kabisa walikokuwa wameficha magari yao, ili Jerry asiyaone na kugutuka. “Nyinyi wote mmesahau! Japokuwa sisi tulipata habari kama baada ya siku tano, lakini siku ya birthday yangu ndio walikufa baba na mama.” Ndio wote wakashituka sasa na kuanza kufikiria.
“Sasa imekuwa inakuwa mbaya, kila mwaka siku hiyo ikifika kwangu haiishi vizuri, kuna jambo lazima linatokea. Ndio maana nilimwambia Tuma. Sitaki tena kusherehekeamambo ya birthday.”
“Nilipokuwa na Sandra alikuwa akilazimishia kwa sababu zake tu. Kupenda shuguli, na mara zote, hata mara moja haikuwahi isha vizuri, kama hivi leo. Nimetoka kugombananaye kwa yule wakili, amenivuruga kichwa kabisa.”
“Hapa nimetoka polisi kumuwekea restrain order. Amekuwa akinisumbua kwa muda mrefu sana. Siwezi kulala na hata kichwa hakifanyi kazi.” Akawaeleza mengi hapo akijitetea kwa hili na lile, ndugu hao kimya wakimwangalia ila kuelewa alikuwa na hasira.
Akajieleza kwa muda mrefu, alipomuona kaka yake anaangalia saa, akajua amemboampaka mwisho, ikabidi anyamaze. Jeremi aliona. “Naona hasira zako zote, umemmaliziaTuma!” “Na hapakuwa na ulazima na wewe kumalizia kitu kizuri kama hiki, kama alivyokuwa akimalizia Sandra. Hilo moja. La pili hapakuwa na sababu yeyote ile, ya wewe mwenyewe kumalizia siku ya kumbukumbu yako ya kuzaliwa leo kama matukioyaliyotokea tokea watoto, ambayo sisi hatukuchagua!” JJ akaongeza kwa Jeremi na kuendelea.
“Hakuna kati yetu aliyechagua kuondokewa na wazazi wetu kwa staili ile na wakati ule! Hakuna kati yetu aliyekuwa tayari. Lakini ona garama tulizolipa ili kubadilisha lile tukio na kuweza kusimama sisi watatu, hapa tulipo leo.” JJ akaendelea kwa ukali kidogo.
“Mazingira ya nje na watu wa nje wanaweza kutufanyia wanachotaka kwetu, lakini sisi tuna hatima na maisha yetu. Kuishi kwetu sasahivi hakutegemei na watu baki ila sisi wenyewe. Usiharibu mbele, kwa makosa ya nyuma, Jerry. Mwishoni mwa yote, wewe ndiye utakayebakia kuwa muhanga wa maisha yako mwenyewe. Usiku mwema.” Akamkabidhi Jeremi sahani aliyokuwa akilia keki na uma, nakuondoka. Amekuwa mwekundu huyo JJ, kama siye yeye aliyekuwa akikata keki ndani. Wote wakajua amekasirika.
Huku kwa Tuma
“Umenifungia simu zangu Tuma!” Tuma alikuwa na mengi yanayoendelea akabaki amejiegemeza kwenye dirisha, kimya. “Kwa nini unanifanyia hivyo kama vile tumegombana, wakati mimi na wewe hatujawahi…” “Ulikuwa unasemaje Mbaki? Maana tuliagana vizuri tu. Sasa ulikuwa ukinitafutia nini?” “Kwani hata tusipooana ndio mahusiano yetu ndio yanakufa kabisa? Sisi tulishakuwa ndugu Tuma. Sio kama hao matapeli wengine tunao kutana nao barabarani.” “Nasikia baridi ya mpaka kwenye mifupa Mbaki. Punguza A/C yako. Inanitesa.” “Sawa Tuma, mimi unanipuuza, wakati…” “Mbaki anapenda kulalamika jamani!” “Sawa.”
“Ulikuwa unataka nini Mbaki?” “Usinifungie simu zangu. Mimi nakuwa kwenye matatizo, sikupati.” “Matatizo gani?” “Niliugua.” Tuma akabaki akimwangalia. “Kwamba wewe hujali tena kama mimi mgonjwa?” “Pole.” “Sasa sasahivi itasaidia nini? UnanitupaTuma, wakati sisi tumetoka mbali sana, sio wakutupana sasahivi.” Tuma hakumjibu tena akabaki akilalamika mpaka wanafika hospitalini.
Walikuta watu wengi, Tuma akabaki ameinama kimya akisubiria kuitwa maana Mbaki alimsaidia kuandikisha kila kitu. Hao wawili washaishi kwa karibu sana. Wanafahamiana kwa undani na mpaka majina ya baba zao. Hamna swali analotakiwa kujibu Tuma kumuhusu yeye akashindwa Mbaki kulijibu.
Akamsukuma kidogo. Tuma akamwangalia. “Nimekusema leo.” “Kwa wema au ubaya?” Tuma akacheka taratibu. “Nilimwambia mama J, nimekukumbuka.” “Mimi mtu mzuri Tuma, ni hivyo tu ni ubinadamu, nakosea. Ila ulitakiwa kunielewa, tuendelee na maisha yetu. Lakini ona unavyopoteza muda!” Tuma akamwangalia tu, na kurudi kuinama.
“Sasa hivi watoto wetu wangekuwa washakuwa wakubwa!” “Na walevi kama wewe?” “Mimi pombe nimeacha Tuma!” Tuma akanyanyua kichwa na kumtizama kwa kumsuta. “Sasa si uninuse!” “Sasa hivi ndio hujanywa.” “Tatizo huniamini Tuma.” “Kilichokufanya uache pombe ni nini?” “Si wewe! Nakuthibitishia naweza badilika.” Akabaki akimtizama kwa kumsuta, mara jina lake likaitwa.
Akamuona na yeye anasimama. “Unaenda wapi?” “Si nakusindikiza ndani!” “Hapana Mbaki. Naomba nikapate faragha na daktari. Subiria hapa.” “Tuma!” “Hakika usinifuateMbaki. Kama ndio hivyo ondoka. Kwanza kuanzia hapa sihitaji kitu kingine, asante, ondoka.” “Mimi siwezi kukuacha hospitalini.” “Basi ndio ukae hapo, usubiri. Usinifuate Mbaki.” Jina lake likaitwa tena. Akabaki akimtizama, Mbaki akarudi kukaa kinyonge kama mtoto mkiwa.
Hapo ukimuona Mbaki mwenyewe, utafikiri anakwenda kazini! Msafi juu mpaka chini. Na yupo hivyo masaa yote kasoro tai. Alivaa shati la rangi ya bahari na suruali nyeusi iliyo kolea, kiatu safiii. Akabaki hapo akisubiria.
~~~~~~~~~~~
Alipomuona Tuma anatoka, akamfuata. Wakaelekea maabara, bado yupo. Akatolewa damu na kupewa kikopo cha mkojo, anamfuata. “Naenda chooni Mbaki, ni kwa nini hutulii?” “Nitakusubiria hapo nje. Twende wote.” Akaamua kumuacha tu amfuate. Akaingia na kutoka, akamkuta amesimama hapo nje kama askari. Wakarudisha mkojo pamoja, ndipo wakarudi kukaa.
~~~~~~~~~~~
“Leo ni ijumaa, kwa nini upo hapa na si baa kwa wenzio? Na usiniambie kama ni kwa sababu umeacha pombe.” “Ukweli nilikuwa nakutafuta Tuma.” “Unanitafutia nini?” “Unataka kujua hapahapa wakati…” “Mbaki?” “Sawa.” Akatulia kidogo na kuendelea.
“Muda wangu wakuoa umefika na kupita.” “Sema ulishafika, ukaona kuyawezi ya kuoa na kutulia, ukaendelea kumangamanga.” “Sawa Tuma. Mbona mimi nilishakubali kosa! Lakini nataka kukwambia siwezi kusubiria tena, lazima nioe. Tena nioe kwa haraka.” Tuma akabaki akimwangalia kama anayesubiria aongee kitu.
“Ndio hivyo Tuma! Mbona sasa umebaki ukiniangalia tu.” “Nakusikiliza Mbaki.” “Ndio hivyo.” “Sawa.” Tuma akarudi kujiinamia. Kimya. “Tuma?” “Ujue mwenzio naumwa Mbaki. Akili yangu imechoka. Nimekuwa na mwezi mgumu, busy na hekeheka, hata siwezi kufikiria vizuri. Kwa hakika kama unajambo unataka kulisema, liseme tu.”
“Sasa tarehe ya harusi lini?” “Ya nani?!” “Si yetu! Maana sasahivi hatuanzii mbali. Tunaendelea tu. Pesa ipo, hatuchangishi mtu. Tunarudi kanisani, tunaandikisha ndoa. Tunaendelea.” Tuma akamtizama na kurudi kuinama.
Kimya mpaka jina lake likaitwa, akasimama kama yeye ndio Tuma, moja kwa moja mpaka chumba cha daktari, Tuma akamfuata, akakuta amekaa kabisa. Hakumuongelesha maana yeye aliwahi kumwambia daktari kuwa yuko naye huyo Tuma.
Dhoruba Katikati Ya Penzi
Akasomewa majibu yake. Tuma hakuwa na tatizo jingine lolote isipokuwa mjamzito. Mbaki aliumia sana. “Kweli Tuma?!” “Nakushukuru dokta. Asante.” “Japokuwa bado ni mimba changa, nashauri utafute daktari wa wakina mama.” “Nitafanya hivyo.” Akanyanyuka na kutoka hapo akimuacha Mbaki akimwangalia kwa uchungu.
Tuma akatoka kwenda kulipia, akaondoka zake hapo ndani. Mbaki akamfuata. “Sijategemea Tuma! Yaani unambembea mtu mwingine mimba wakati mimi ulikuwa ukinikatalia kabisa! Mimi nilivyohangaika na wewe Tuma! Hakika siwezi kukusamehe.”
“Tena wewe ndio unyamaze, sitaki hata kukusikia. Ulivyomtorosha Umi na kumbembesha mimba, ilikuwa sawa kwa sababu mimba hukubeba wewe?” “Umi alinisingizia, mimba haikuwa yangu.” “Kwamba hukulala naye au?” Hapo wanazozana nje ya hospitali, sehemu ya kuegesha magari.
“Unataka kunichanganya zaidi. Achana na mimi Mbaki.” “Lakini jua katika hili mimi siwezi kukusamehe tena. Jua huu ndio mwisho wangu na wewe. Sitakutafuta tena, na wewe usiwahi hata kunitafuta Tuma. Umeniumiza sana.” Kumthibitishia safari hii anamaanisha anachoongea, akapanda gari yake na kuondoka. Akamuacha Tuma amesimama hapohapo.
Usiku Uliobadili Kila Kitu
Alitafuta usafiri wa kumrudisha kwake, ilishakuwa usiku mwingi karibia saa 6. Alimkuta Eli naye anajiandaa kwenda kulala. “Jerry alipiga kukuulizia, anasema hakupati kwa simu.” “Nipe simu yako?” “Unataka nini?” “We nipe.” Akamkabidhi akimwangalia. Akatafuta simu ya Jerry, mama J na kuzi block zisiingie kwa Eli.
“Hawatakutafuta tena.” Akamrudishia simu yake. “Na mama akikutafuta akikwambia hanipati kwa simu mwambie asiwe na wasiwasi, nimesafiri. Nikirudi nitamtafuta.” “Unakwenda wapi?” “Unataka twende wote?” Eli akamuona amemuuliza kishari.
“Hakikisha unamtafuta mama, Tuma. Usipitishe muda mrefu bila kumtafuta, maana unajua jinsi anavyokuwa asipokupata. Na usikawie kuwasiliana.” Akaingia ndani na kukusanya vitu vyake kwa haraka, Eli akashangaa anatoka na sanduku. “Kwamba unaondoka usiku huu?” “Nibebee mpaka nje ya geti. Gari inanisubiria.” “Umekula?” Mdogo wake akamuuliza kwa kujali.
“Umekaukiwa Tuma, mpaka midomo imepasuka! Huko unakokwenda hakikisha unakunywa maji.” Hakumjibu. Wakatoka hapo kimyakimya mpaka nje. Dereva akashuka kupokea sanduku, akampandishia mzigo wake nyuma.
Eli akawahi kufungua mlango aliokuwa amekaa dada yake. “Usisahau mawasiliano Tuma.” “Sasa sio kesho na wewe!” “Sawa, lakini kwa mama isizidi siku tatu.” Akanyamaza. “Tuma?” “Nimesema nitawasiliana. Funga mlango niondoke.” Eli akafunga mlango, dereva taksi akaondoa gari. Akarudi ndani na mlinzi kufunga geti.
~~~~~~~~~~~
Njiani akaanza kufikiria. Akaona sio wazo baya kwenda kupumzika kwa mama yake. Akawaza hili na lile akamtumia ujumbe mama mwenye nyumba wake. ‘Nimesafiri na kumuacha mdogo wangu peke yake. Mtu yeyote yule asiruhusiwe kuingia kwenda kule kwangu kwa sababu yeyote ile. Tafadhali mwambie dada na walinzi usiku. Asante.’Akamtumia ujumbe usiku huohuo.
Akashushwa hotelini, na kuingia kuoga, akajitupa kitandani na kulala kama mzoga. Hapo simu amezima.
Aliamka kesho yake mida ya saa nne asubuhi. Akajisafi na kwenda saluni kujisafi nywele na kucha. Tuma pesa anayo. Amefanya kazi na Jerry, mwisho wa mwezi alishalipwa mapesa ya kutosha na pocho yake. Akaenda kusukwa ndogondogo za kukaa nazo muda mrefu. Kisha akaenda kumnunulia mama yake zawadi.
Na ili wasimfuate nyuma, akaenda kwenye ATM akachukua pesa ya kumtosha yeye na mama yake kwa muda wote atakao kuwa kwake, ndipo akarudi hotelini kupumzika. Ilishakuwa usiku.
Alfajiri na mapema, akaenda kituo cha mabasi na kuliacha jiji la Dar, kurudi kwa mama yake. “Hata hivyo nahitaji mapumziko. Nimefanya kazi mfululizo.” Akajiambia akiwa njiani.
Moyo Uliojeruhiwa Bila Onyo
Aliamka asubuhi na mapema kama kawaida akaenda kwa Tuma akitegemea kumkuta amchukue kwenda naye kazini. Huwa asubuhi haiitaji hata kuingia ndani, anasubiria nje ya geti, anamuita, anatoka wanaondoka.
Akafika na kuegesha mlangoni kabisa akiwa amejipanga chakuzungumza naye. Akampigia zaidi ya mara tatu, simu yake haipatikani. Akamjaribu na Eli. Akashangaa na yeye simu haipatikani! “Huyu Eli si nimezungumza naye usiku, masaa machache sana yamepita!” Akajiuliza na kujaribu tena na tena, hapakuwa na jibu.
Akashuka garini ili kuingia ndani, akakuta mlinzi naye ndio anajiandaa kutoka. “Haparuhusiwi mtu kuingia ndani. Nimeambiwa wapangaji kule wamesafiri.” Huwa ujumbe ukishafika kwa mtu wa pili hubadilishwa. Sivyo alivyokuwa ameambiwa huyo mlinzi. Alichoambiwa ni dada mtu ndiye aliyesafiri. Sasa kwa kuwa amejichokea, amelinda usiku kuchwa, akaona afanye marefu yawe mafupi.
“Mbona nimezungumza na Eli muda si mrefu ni kama masaa..” Akaangalia muda. “Hata sita hayajaisha!” “Na alikwambia yupo ndani?” Hapo akakwama. Maana hakujua anazungumza na Eli akiwa wapi. “Maana mimi nimepewa maagizo na mwenye nyumba alfajiri hii akiwa anatoka hapa kwenda kazini, kuwa wamesafiri. Mtu asiruhusiwe kuingia kule.” Jerry akakwama na kuondoka.
~~~~~~~~~~~
Bwana alimtafuta Tuma, kazi haziendi. Mara ya mwisho ni pale alipomuona Tuma akiondoka na Mbaki. “Inamaana yupo na Mbaki mpaka sasa?!” Akabaki akijiuliza bila yakupata jibu. Akaendelea kupiga sasa na paniki ikaongezeka. Piga nikupige, hakuwa akimpata Tuma wala mdogo wake.
Uamuzi Mbaya Ni Mbegu Ya Majuto Ya Kesho
Maisha yalimfikisha Mill kwenye kuchukua njia fupi ili kubadili uraia wake nchini Marekani, matokeo yake hayakumuacha salama. Na ile hatua moja ya haraka, siku ya kwanza kulala na Kisha alipomtisha, bila ya kufikiria, hatimae imeharibu safari nzima ya maisha yake nchini Marekani.
Ndoto zake zote na hangaika yake yote, ikawa bure japo alipata huo uraia. Alitua nchini Marekani akiwa na Shema. Maswala ya nyumba alifanikisha kwa haraka sana mpaka akampa tumaini Pam la kurudi kwa haraka. Maana hata hakuhitaji kwenda popote. Huduma zote zilimfuata nyumbani.
“Mambo yamerahisishwa sana huku. Yaani umeme, maji, huduma ya taka, cable na internet vyote vimenifuata hapahapa. Sikuwa na haja hata ya kwenda popote! Nimewapigia tu, na kuwapa majina yangu, kila kitu kipo sawa.” Hayo alikuwa akimwambia Pam, mkewe aliyekuwa akimuombea haswa.
Safari hii hakuzembea. Yeye na mama yake walikuwa wakiomba sana ili Mungu wawasaidie wote wawili, waje wajikute tena pamoja, huko ng’ambo ya pili ya dunia. Na Mill naye hakuacha kuzungumza naye akimpa maendeleo ya huko. Kila wakati walikuwa kwenye simu pamoja. Kama si Pam kuomba ushauri jinsi ya kuendesha mambo huku nchini, basi Mill kumpa maendeleo ya huko.
Juma la kwanza tu kuisha, nyumba yao huko nchini Marekani ikawa na kila kitu kasoro tu Pam. Usiku wa Tanzania basi wawili hao watakuwa kwenye simu mpaka Pam anapokwenda kulala, hivyohivyo kwenye usiku wa Mill nchini Marekani, ilimradi tu wajisikie wapo pamoja kwenye kila jambo. Kwa hiyo Pam akawa akijua mengi yanayoendelea nchini Marekani. Yale aliyojua yatamtia mashaka, Mill aliyatunza na kuendelea kupambana nayo akitafuta suluhu.
~~~~~~~~~~~
Tatizo lilianza pale alipoanza hatua ya kufungua hiyo kampuni. Ukweli Mill alijutasana. Maamuzi yake ya pupa yalizaa majuto. Na likatimia kwake kuwa, njia fupi si kila mara hufikisha salama.
Taarifa za kufungwa kwake kwa makosa aliyokuwa amesingiziwa na Kisha, bado zilikuwa kwenye kila kona ya system za Marekani. Japokuwa kesi ilifutwa, lakini Mill alishakaa jela kama mtuhumiwa kwa makosa mabaya sana aliyokuwa amesingiziwa na Kisha ili kuhakikisha hatoki jela.
Yeye alikuwa huru na ni raia mkamilifu wa nchini humo, lakini serikali isingethubutu kumpa kibali cha kufungua nursing homes, ambapo watakuja kuishi wazeewasio jiweza, na yeye tayari alikuwa na hatia ya kumpiga Kisha! Ambalo hilo ni kosa la domestic Assault, kosa baya sana lililomtia Mill doa lisilokuja toka.
Kisha aliita polisi nyumbani kwake baada ya kuwapigia simu akilia sana, polisi wakakimbilia nyumbani kwake na kumkuta na majeraha mabichi aliyosema Mill alimpiga, kisha akakimbia.
Katika mashitaka mengi aliyomsingizia, Mill akapata nala domestic threats/harassment. Kwamba eti Mill huwa anamtisha kila wakati, akalia kabisa kuwa anahofia maisha yake ndipo Mill kwenda kukamatwa akiwa hajui kinachoendelea. Akatiwa pingu, kufikishwa kituo cha polisi ndipo anaambiwa makosa yake na kuona picha za Kisha aliyemuacha nyumbani mzimaa, lakini pichani amejeruhiwa vibaya sana. Hapakuwa na neno angejitetea akaeleweka kwani ni kweli Kisha alikutwa peke yake nyumbani akiwa amejeruhiwa.
Ndipo Mill kusekwa lupango, na Kisha kuhamisha baba watoto wake kwenye jumba la Mill. Baada ya Mill kukubali kumuachia mali zote, na apewe watoto waliokuwa wameshaharibiwa vichwa na pia hawakuwa wake, ndipo Kisha akafuta kesi, lakini rekodi za Mill zikawa zimeshaharibika, vibaya sana.
Mill HAWEZI kuajiriwa tena popote nchini Marekani, na kamwe hakuna mtu angempa kibali cha kuanzisha kampuni ya kutunza wazee wasiojiweza akiwa na hizo felony charges. Aliondoka nchini Marekani akidhania amepona, kumbe Kisha ALIMMALIZA vibaya sana.
Yaani huko kurudi na kutaka tena kufungua kampuni, ndipo MADHARA yote yakafunuliwa mbele yake na macho kufunguka. Alipomtafuta mwanasheria wake, akamthibitishia. “Nilifikiri unajua hilo, Mill!” Yaani yeye mwenyewe akawa akimshangaa Mill ni kwa nini hakuwa akilijua hilo. “Na ndio maana nilidhani uliamua kwenda kutulia Tanzania, na kunishangaza ulipokuwa ukitaka kurudi tena huku, tena ukiwa na familia ingine! Nikajua una mbinu zingine!”
Mill alikuwa na hali mbaya, akiona ndoto zake zikitumbukia kwenye shimo la choo hivihivi!
Mbaya zaidi Mill huyohuyo anayo rikodi ya kumuombea Pam kuingia hapo nchini kama mchumba wanayekwenda kuona. Halafu gafla kumbukumbu zikaonyesha alimuoa Kisha. Halafu Kisha ndiye aliyemshitaki mpaka kumfunga, eti leo anarudi tena na Pam kama mke! Kama sio utapeli huo, ni nini!
Hofu ikazidi kuongezeka walipokuwa wakijadiliana na wakili wake juu ya Pam ambaye alishakamilisha ushahidi wa kihospitali ili kumuombea visa. Lakini wazi walijua Pam hatapewa na yeye Mill kujithibitisha ni tapeli, kuongeza kosa jingine. Kwamba ni ni kweli alimuoa Kisha ili kupata uraia, na alipokamilisha uraia ndio akaanza kumtesa Kisha ili aje arudi kwa Pam! Kwa hakika ilikuwa haijakaa vizuri kabisa.
Hiyo nayo ikawa ndoto ya pili inayokufa kwa maamuzi mabaya yaliyozaa matunda ya huzuni. Usiku mmoja wa zinaa, ukazaa asubuhi ya majuto ya milele. Akiwa na uungwaji mkono mzuri kutoka kwa mtu kama Jo, aliyekuwa bado na kibali cha udaktari nchini Marekani na ahadi ya kumtengenezea japo la watu ili kuweza kufungua biashara ya kuaminika na uhakika wa wateja, lakini dakika ya uzembe ikamgharimu miaka ya taabu. Mill akagonga mwamba kabisa.
~~~~~~~~~~~
Baada ya juma, akapewa majibu ya kukataliwa ramsi kibali cha kufungua biashara hiyo. Mbaya zaidi ,hakuwa tayari kabisa kuishi nchini Tanzania, kama mgeni akiombewa vibali vya kazi. Hakuwa raia. Alishaukana uraia wa kuzaliwa kwake.
Kwa mara nyingine tena, Mill AKAKWAMA. Na mbaya zaidi, kwa nchi hiyo aliyo na uraia, ndio kukwama kabisa. Hakuna kuhonga, hakuna kujuana. Popote kutakapotajwa Mill Mgini, basi makosa yake yote ya nyuma yataambatana naye. Anafanyaje!!
~~~~~~~~~~~
‘Kuna mgeni alikuwa hapa, anazungumza na baba. Wakawa wanasoma barua. Nikamuona baba anatoa machozi kabisa. Ameenda chumbani. Mpaka sasa hajatoka.’ Ulikuwa ujumbe kutoka kwa Shema. Pam akashituka sana. Ndipo akajua kuna mengine yalikuwa yakiendelea, Mill hakuwa akimwambia.
Lakini kwa hakika alikuwa amekwama. Yaani mbali ya kutojua anamwambia nini Pam, yeye mwenyewe alikuwa hajui maisha yake na familia yake yatakwenda vipi kuanzia hapo. Alikuwa na majuto, uchungu, na lawama za kupitiliza.
‘Nitampigia. Usiwe na wasiwasi. Umekula?’ ‘Kuna vyakula vingi huku! Nakula kila saa mama.’ Pam akacheka akimfikiria Shema na anavyopenda kula. ‘Basi muache tu, nitampigia baadaye. Usiwe na wasiwasi.’ Pam akabaki akiwaza.
~~~~~~~~~~~
Inaendelea…
0 Comments:
Post a Comment