Pam akabaki akiwaza. Akajua mambo hayakwenda kama walivyopanga. Akajikuta akimuhurumia yeye. Huo usiku kwake ukawa unaishia, anataka kulala, hajamsikia. Akamtumia ujumbe. ‘Pole na majukumu Mill, mume wangu. Sisi tunalala.’ Akaona amesoma. Halafu anaandika, anaacha. Anaandika tena, anaacha. Pam akasubiri mpaka akachoka.
Akampigia. Akapokea. “Vipi?” “Nimekuwa na siku mbaya Pam, hata sijui nikwambie nini! Nahisi nimekuangusha mpenzi wangu. Garama yote uliyolipa imekuwa bure. Sina kitu. Sikujua kama yule mwanamke amenimaliza vibaya kwa kiasi hiki.” “Pole. Ni nini?” A` kamuelezea lakini Pam aliweza sikia sauti iliyajaa uchungu mkali, majuto na fedheha.
“Nisikilize Mill. Tanzania ni nyumbani. Hatujafukuzwa. Na hii kliniki hapa inaendelea vizuri sana. Sina nia ya kukatisha tamaa, lakini nataka kukwambia, hatuna chakupoteza. Hata ukiweka tena hayo maombi yangu huko ubalozini, hakuna jibu la kutushangaza. Iwe ni huko, au huku, ilimradi tupo sisi pamoja na watoto wetu. Basi. Tutaendelea tu, na ninaamini Mungu atatubariki. Hatuna chakupoteza isipokuwa sisi wenyewe.”
“Kwamba wewe hujaona nimekuangusha na umelipa garama ya bure?” “Umehangaika kadiri ya uwezo wako, mume wangu. Mungu ndiye anayepanga. Huwezi badilisha. Inawezekana andiko letu ni huku! Huwezi jua mpaka ufanye kwa upande wako, tuhakikishe Mungu ameamua kutuweka huku.” “Kwa hiyo bado unataka nikuombee uje huku?”
“Bora tuwe wote. Iwe huko au huku, mimi sijali.” “Mimi ni raia wa huku Pam. Narudije nyumbani? Siwezi ishi kwa kuombewa vibali!” “Nisikilize Mill. Najua ndoto zako zipo huko. Weka tena maombi juu yangu. Wakininyima, unaapa tena kuukana uraia wa huko, unarudi nyumbani, maisha yetu yanaendelea kama kawaida. Nakuahidi tutafanikiwa.”
“Na endapo ukifanikiwa kupata je?! Mimi huku siwezi ajiriwa tena Pam. Nina rikodi mbaya sana. Leo ndio wamenitumia majibu ramsi kuwa siwezi kuja kufungua ile kampuni ya kulea wazee.” “Basi kile ulichokuwa ukitaka ukifanye wewe, mimi nitakifanya.” Mill akatulia kidogo.
Kisha akamuuliza. “Kwamba uje huku uwe nesi!?” “Kile unachotaka kukifanya wewe kisheria, na ukashindwa, mimi nitakuwa. Kama ni kurudi shule, najua utanisaidia kuweza kusoma, nitakuwa nesi. Na hiyo kampuni tutafungua kwa jina langu kama tulivyofanya huku.” Mill akakaa kwa haraka.
“Kweli Pam?!” “Kabisa. Wewe utanielekeza. Tutafanikiwa popote tulipo. Usikate tamaa, na usiogope.” Mill alifurahi sana. “Yaani hapohapo subiri.” Akavuta laptop yake akiwa na tumaini jipya.
“Mungu alikuleta kwenye maisha yangu akijua nitaharibu Pam. Asante mpenzi wangu. Nilikuwa nimechanganyikiwa! Nilijua nilikuangusha vibaya sana.” “Muone sasa unafanya nini?” “Nakutumia maombi sasahivi, tuchague kabisa tarehe ya wewe kwenda ubalozini. Ukipata au kukosa, tunaendelea. Si ndivyo tulivyokubaliana?” “Kabisa.” Hapo Mill akawa amehamasika, akapata tarehe ambayo Pam akamwambia hakuna tatizo, atakwenda, basi akamuwekea appointment.
Ndipo angalau akatulia nafsi. “Asante Pam. Nilikuwa na hali mbaya!” Pam akaanza kumcheka na stori kuendelea akimpa ya nyumbani na mtoto aliyebeba. Akabadili hali ya mumewe kabisa.
~~~~~~~~~~~
Juma lilishapita hajasikia lolote kutoka kwa Tuma wala mdogo wake. Akatoka hapo mpaka alipo mama J. “Naomba nifungulie simu yako.” “Kwa nini?” “Simpati Tuma.” Mama J akabaki akifikiria. “Hilda!” “Ngoja nikwambie Jerry, Tuma akiamua usimpate, hutakaa ukampata. Niamini mimi.” “Wewe nipe simu.” Jeremi kimya akimwangalia kaka yake. Maana alimfuata Hilda ofisini kwake, akaambiwa yupo ofisni kwa mumewe, akaenda kuingia bila hodi.
Akampigia Tuma tena na tena, hapatikaniki. Akamrudishia simu yake akamgeukia Jeremi. “Naomba simu yako.” “Anachokwambia Hilda ni kweli Jerry. Tuma akiamua usimpate, hutampata, sisi tunahistoria yake. Hapo ulipo, alipita Mbaki. Alimtafuta karibia kuchanganyikiwa.” “Wewe nipe simu yako.” Jeremi akampa.
Akapiga zaidi ya mara tano, ni kama Tuma hakuwa hewani kabisa! “Tuma anamsimamo ule wa kutisha, na hayumbi. Hicho alichoamua kichwani kwake, hakitabadilika hata iweje. Nakushauri ujipange Jerry.” Mama J akamalizia na kutoka hapo akimuacha na mdogo wake.
“Nilimuona akiondoka na Mbaki! Unayo namba ya Mbaki?” “Unataka kumwambia nini Mbaki, Jerry? Tafadhali tulia kwanza na utafakari ni nini unataka.” Akabaki akipiga simu.
“Ulipopita wewe na Tuma, ni pabaya kuliko alikopita na Mbaki, na hakumsamehe.” Hapo akakunja uso na kumwangalia mdogo wake. “Unazungumza nini wewe?!” “Alichokifanya Tuma siku ya birthday yako, ilikuwa ni kama suluhu ya mwisho kwenu. Alizungumza na Hilda na kumueleza mnakopitia na mlipo. Haijakaa sawa Jerry!”
“Yule binti kwa mara ya kwanza amemkumbuka Mbaki mwanaume aliyekiri mapenzi yaliisha! Lakini alimwambia, amemkumbuka Mbaki. Na mapungufu yake yote aliyokuwa nayo Mbaki, alikuwa akimuenzi Tuma na kuishi naye kwa kumjali SANA.” Jeremi akaendelea taratibu.
“Jana yenyewe tu, katikati ya yote, kama ulikuwa makini utagundua jinsi Mbaki alivyo makini na Tuma.” Kimya akisikiliza.
“Yule binti ni mgonjwa Jerry, sijui kama unajua?” Kimya, Jeremi akapata jibu la swali lake. “Inamaana hujapata naye muda kabisa na kumwangalia!” Kimya, akaendelea. “Katika mazungumzo yao, wakiwa wanachagua ni nini chakula kwenye birthday yako, alimwambia Hilda ana muda mrefu, hajaweka kitu tumboni. Hajisikii kula kabisa. Imekuaje wewe hujui kinachoendelea kwake halafu Mbaki amemgundua kwa muda mfupi sana aliomuona, nakujua hayupo sawa?” Jerry akabaki kimya akivuta kumbukumbu.
“Mbona huwa tunakula wote kila mlo na…” Akatulia kujaribu kuvuta kumbukumbu nakushindwa kujua kama alikuwa akila au la!
“Nampenda Tuma, ila sema Sandra amenipitisha kipindi fulani hivi, akanichanganya kabisa. Nakwambia kweli Jeremi, nilikuwa siwezi hata kulala.” “Hapo ulipokaa wewe, na Mbaki alishakaa zaidi ya mara tatu, na pale ofisini kwa Hilda ilikuwa ndio kituo chake. Simu zake zilikuwa haziishi kwa Hilda mpaka nilipompiga marufuku.”
“Tatizo la Tuma nalihisi linakuwa hili. Anamtindo wakujifanya mtumwa popote anapokuwa, rahisi kumpuuza mpaka anapoondoka kwenye maisha…” “Sijampuuza Tuma.” “Sawa Jerry. Lakini kwa jinsi yeyote ulivyokuwa naye huyo Tuma na kumchukulia, huwa akiondoka, pengo lake ni gumu sana kuziba. Muulize Mbaki na sisi.”
“Pale alipokuwa akitufanyia kazi ukamtoa, mpaka leo, muda huu, tunahangaikakuziba pengo lake, muulize Hilda. Na wafanyakazi watatu tulioajiri, mpaka masaa machache yaliyopita, bado tuna matatizo kule, simu haziishi, hivi Hilda inabidi aende akakae pale, wakati alipokuwa Tuma, pale, hapakuwahi kuwa natatizo.”
“Ila sasahivi tumeajiri mtu wa stoo, wakusafisha na kumsaidia Umi, watu watatu, lakini ni fujo, hujawahi ona. Kazi ya Tuma, wamepewa watu watatu, na bado hakuna anayeimudu. Na alipokuwa pale, alikuwa kimyaa. Unaweza ukafika pale usijue kama yupo, ukadhania muendesha ile ofisi ni mtu mwingine kabisa. Lakini Hilda aliligundua hilo mapema sana. Alikuwa akimtunza kama mboni ya jicho, akihakikisha anamlipa mshahara ambao hakuna mtu anaweza mrubuni. Mwanzoni nikamshangaa.”
“Ndipo Hilda akanipa hiyo siri. Anafanya kazi za watu wanne, kwa mshahara wa mtu mmoja na halalamiki, hazembei na hutamkumbusha majukumu ya pale. Kuna jinsi alipawezea pale, ungesema ni Hilda mwenyewe ndio yupo pale, na wale vijana wakajua ni Hilda wa pili pale. Lakini kimya kimya tu. Wewe mweyewe ulimkuta pale ukadhani ni mfagizi kumbe ndio kichwa cha pale.”
“Sasa ndivyo alivyo Tuma. Anajua kujipenyeza kwenye sehemu uliyomfungulia mlango. Anaweka mizizi kimyakimya. Unashangaa huku juu matawi ni kijani kwelikweli! Unasahau kunakotokea rutuba, akiondoka, shida sana kubaki salama.”
“Mbaki anakwenda huko, na pesa yake yote, anarudi kwa Tuma. Warembo wamejaa hapa mjini kibao. Anaweza pata yeyote. Lakini anajikuta mke wa kuweka ndani, nakutuliani Tuma. Ukimuuliza kilichokufanya usitulie, ni vile Tuma anavyoweza kukufanya ukajisahau.”
“Na jua kweli anamsimamo. Anamsimamo kwelikweli. Kile alichoamua kichwani mwake, hutambadili kwa sababu pia anamfano mbaya sana wa ndoa ya wazazi wake. Alishamuapia Hilda, ni bora asiolewe, kuliko kukaa kwenye mahusiano waliyonayo wazazi wake. Ambayo nikiangalia ni kama mlipo sasahivi.” Jerry akashangaa sana.
“Si kweli! Mimi nimeshaachana na Sandra! Huwezi nifananisha na baba yake! Kwangu Tuma hajawahi kuwa mke wa pili na hatakaa kuwa mke wa pili.” “Kimwili, lakini Jerry, akili na nafsi yako havijawahi kumuacha Sandra na ndio maana anakuchezea akili na kukuweka macho. Mtu usiyemjali na mmeachana, halafu ukawa na mahusino yako mazuri, unarudije kwake?” “Nilienda kumsikiliza tu!”
“Jana ndio ulikwenda kumsikiliza. Lakini mlikuwa naye muda wote kipindi cha zaidi mwezi! Akaingia katikati yako na Tuma, na akafanikiwa kukutoa kwa Tuma kama alivyofanikiwa kukutoa kwa Lisa.” Alishituka Jerry. Akashituka sana.
“Pata muda wa kufikiria, utagundua hapa ulipo na Tuma, ndipo ulipopita na Lisa, na yeye mlimpitisha hapohapo. Sasa kwa sababu na yeye Lisa alikuwa mpole sana, Sandra akatumia huo udhaifu wake, akafanikiwa kabisa kukutoa kwa Lisa aliyekuwa akikupendana kukunyenyekea kama hivi Tuma, ukamuacha yeye ukaenda kumuoa Sandra kwa haraka sana. Naye Jimmy alipoona tu umemuacha mwanamke mzuri vile, ikawa kama ameokota lulu! Asikwambie rafiki yangu unafanya kosa, akafuta urafiki na wewe kabisa, haraka sana akamuwahi Lisa. Ona ndoa yao na yako. Jimmy ametulia kabisa na Lisa. Wana ndoa tulivu na watoto wakueleweka.”
“Sasa, sasahivi unarudia kilekile, halafu unategemea matokeo ya tofauti! Haiwezekani.” Akamuona anapiga tena simu kama mara tatu kwa kutumia simu yake, kisha akamrudishia na kuondoka.
Jumapili.
Shuguli ilikuwa inaanza baada ya ibada. Kanisani hawakumuona Jerry wala Tuma. Kaka mtu akaona, akanyamaza tu, hata Jeremi hakumuuliza. Wakarudi nyumbani kwa JJ ambako iliandaliwa hiyo shuguli. Mke wa JJ hakuwa akijua kujipunja kwenye mambo yao. Nyumba yao yenyewe ni bora kuliko ukumbini. Huwa anaandaa kutokana na idadi ya watu alioalika. Ungependa kuwepo. Ikafana kwelikweli, watu wakila na kunywa.
Ilipofika saa 10 jioni, JJ uzalendo ukamshinda, akamsogelea mdogo wake. “Umewasiliana na Jerry?” “Hapana.” JJ akaangalia saa na kuendelea na wageni wao. Ila hata mkewe alimuona hayupo sawa.
Kwenye majira ya saa 12 jioni, akaingia Jerry wazi alionekana kuna linalomtatiza. Mtoto wa JJ wakiume kutoka Uingereza akawa wa kwanza kumuona, akaanza naye stori. Alikaa hapo kama lisaa tu, kaka yake akamuona anaondoka. Akamuacha wala hakumuongelesha, shuguli ikaendelea.
~~~~~~~~~~~
Mambo ya Jo na Dorothy yalikwenda vizuri, na watoto wa Jo wote wakaahidi kufika kwenye harusi ya baba yao pamoja na watoto wa dada yake. Ikawa imepata uungwaji mkono mzuri.
Dada yake Jo, yaani Josephine akaamua kufanya shuguli ingine tena, kabla ya siku ya harusi, ndugu kufahamiana. Ikawa furaha juu ya furaha. Dorothy mwenyewe alikuwa na watu wanaomsaidia kufanya manunuzi ya kila namna. Hapo alikuwa na nguo za thamamani na vito vya thamani vya kila namna na bado Josephine alituma binti yake alete vitu vingine, ilimradi tu kumpendezesha wifie.
Swala la kwamba siku hiyo atakuwa kwenye kigari cha walemavu na si kutembea kwenye siku yake ya harusi kama mara ya kwanza, lilishapotea kichwani kwa furaha aliyokuwa ameweka Jo, moyoni mwake na wakwe zake. Hawakuonyesha ulemavu wake ni kitu cha ajabu, Josephine alimchukulia kawaida na popote walipokuwa wakienda au kumkaribisha, Jo mwenyewe aliweka mazingira rahisi sana kwake kupafikia mpaka akasahau kama ana ulemavu, au kujiona tofauti.
~~~~~~~~~~~
Siku tatu kabla ya harusi, Mill na Shema wakarejea nchini, Pam alijawa furaha huyo! Hakuwa akiamini kama wamerudi. Ila Mill akagundua kuna nafasi tena zimefunguka kwenye ubalozi wa Marekani. Akasogeza jina la mkewe tena kwamba aende mapema. Nia ni kutafuta kujua hatima yao ya maisha ipo nchi gani.
Yeye Pam alikuwa akiomba Mungu, kule mkono wake Mungu utakapoendelea kuwa nao, ndipo wawepo. Hakujali eneo tena. Japokuwa alitamani na yeye kwenda nchini Marekani, lakini moyo wake ulishakuwa na amani na popote. Alishaona maisha mazuri waliyonayo hapo nchini, hapakuwa na chakupoteza kwa yeye aliyetokea chini. Lakini kwa Mill aliyekuwa alishafika juu, kwa hakika hakutaka kurudi chini.
Kila Anayevumilia Dhiki, Huonja Utamu Wa Mafanikio.
Uvumilivu si udhaifu, ni daraja linalokuvusha kutoka kwenye majaribu hadi kwenye ushindi. Ndivyo ilivyokuwa kwa Dorothy. Mungu alimjibu zaidi ya hata alivyoomba na kumtunukia furaha ya kupitiliza. Safari nzima ya maandalizi ya kabla ya harusi, siku yenyewe na baada ya hiyo harusi alikuwa akizungumza na Jo hatua kwa hatua. Na Jo naye alikuwa akimwambia kwa kumuhamasisha kwelikweli.
Kila tukio alilikuza ilimradi tu kumfurahisha. Basi na hivyo alikuwa akipenda kucheka, Msambaa huyo asiye hila, ungejua amejibiwa na Mungu wake. Na dhiki zote alizopitia, Mungu ameshuka kumfuta machozi.
Baada ya harusi ndio kwa mara ya kwanza atapanda ndege kuelekea kisiwa cha Santorini, Greece. Yaani kwake hayo ni mambo makubwa mawili. Kupanda ndege na kutoka hapo nchini. Yaani ilikuwa ni kutoka mavumbini mpaka enzini!
Hapo napo Jo alimwaga mapesa kwa uchu aliokuwa nao kwa huyo Dorothy. Alishakubaliana naye kusubiri mpaka ndoa. Mwanzoni ilimsumbua, ila baadaye akajiambia aache tu na yeye apate kitu cha kutizamia baadaye. Nafasi ya aliyoona ni ya kipekee ya kumvua nguo huyo Dorothy. Kwa hiyo hapo hata yeye japokuwa alishakuwa kwenye manchi ya ajabu na ya kifahari, safari hii ikaongeza shauku ya kwenda sababu ya penzi la Dorothy.
Kadiri siku zilivyokuwa zikisogea ndio uchu wake uliongezeka ndipo sasa akamwaga hayo mahela kwenda kumfaidi mbali na kila mtu, wawe peke yao, bila kuitwa bibi wala mama. Ndipo akaamua ampeleke kwenye hivyo visiwa, akamfaidi kwa nafasi. Akate kiu ya muda mrefu. Na hivi rangi ya Dorothy humuamsha hisia hata kabla ya romance, Jo alisubiria kwa hamu asijali garama.
Na hivi pesa ilikuwepo, Jo mtu wa utalii. Alijua kwa hakika huko ndiko kutamfaa Dorothy. Maji yaliyozunguka kisiwa hicho maarufu kwa fungate yalikuwa masafi sana, tena ya rangi ya bluu ile iliyokolea haswa. Majengo yalitengenezwa kwa mawe, juu ya mlima, pazuri sana. Aligaramia nauli zao na hiyo hoteli ambayo alichagua kabisa iwe karibu na ufukweni, chumba alitaka kiwe kinaangalia baharini kusudi kelele watakayokuwa wakilala nayo na kuamka nayo iwe ya mawimbi ya bahari tu na wao wenyewe.
Mizigo ya Dorothy ya kwenda huko aliyeandaa alikuwa Josephine, wifi yake aliyezoea aina hizo za safari tokea wapo vijana na mumewe. Ilikuwa kila anniversary yao, wawili hao nilazima watoke nje ya nchi, japo siku tatu tu. Basi akamuandalia Dorothy sanduku la vitu alivyojua angehitaji huko. Na mama Komba naye akamtayarishia vya fungate. Basi kila mtu alitaka afanikiwe kwa namna yake.
Ndugu wa Jo kutoka kijijini nao walifika mjini kuhudhuria harusi hiyo. Siku mbili kabla ndipo sasa watoto na wajukuu kutokea nchini Marekani wakawasili. Ilikuwa shamrashamra ya namna yake, ungejua akiba ya maombi ya Dorothy tokea msichana, na imani yake kwa Mungu bila kuyumba, imejibu.
Kwenye hiyo rehearsal dinner, siku moja kabla ya harusi, ilikuwa ni ndugu wakaribu ili kufahamiana, kama alivyotaka Josephine. Na kwakuwa hapakuwa na shuguli ingine isipokuwa harusi tu, basi nayo hiyo ikafana.
Ilifanyika nyumbani kwa Josephine, nje tu kwenye bustani yake. Kuliandaliwa vizuri sana na vyakula alihakikisha ni vya hadhi ya aina ya watu wake. Kina Komba pia walikuwepo.
Ndipo Jo akapata nafasi ya kumtambulisha Dorothy kwa vijana wake. Hata yeye Jo alishangaa vile ambavyo hawakuona kuna utofauti wa ulemavu wa Dorothy. Walikuwa vijana watulivu, lugha ndio ilikuwa ikisumbua. Hawakuwa wakizungumza kiswahili kabisa, japo baadhi ya maneno walijaribu.
Naye Mill alikuwa mstari wa mbele kuhakikisha anakuwa katikati ya Pam na mama yake pamoja na hao wageni. Kikawa kitu kizuri mno. Kulijaa vicheko wakati wote. Ila waligundua watoto wa Jo na wa dada yake ni wale waliostaarabika haswa. Na wakaonekana hata huko walikotokea, wamefanikiwa.
~~~~~~~~~~~
Harusi yao walifunga kanisani kabisa, hawakutaka mengi ya kisasa. Baba yake ndiye aliyetembea naye mpaka kumkabidhisha kwa Jo, mbele ya mchungaji. Ilikuwa nzuri mno. Kulimwagwa maua, ungesema ni binti mdogo anayeolewa. Shemeji yake Jo huwa anawatu wengi wanaomfahamu hata hapo jijini, basi na wenyewe wakawepo.
Mzee alikuwa haamini kama anamuoza mwanae kwa hali ya juu ya kiasi hicho kwanza akiwa mlemavu halafu alishakuwa bibi! Heshima waliyopewa, hawakujisikia ni watu wa hali ya chini kutoka huko milimani. Shemeji yake Jo alikuwa mcheshi sana na alijaliwa karama ya kuendana na watu. Hata kama uwe hujui kusoma, hutashindwana naye. Atashuka chini ulipo, mtajikuta mnalakuwachekesha tu.
Na kwa kuwa alisoma sana na alikuwa na maisha ya hali ya juu tokea ujana wake mpaka kuja kumuoa Josephine, ukimkuta katikati ya wasomi, japokuwa alishastaafu, lakini pia aliweza kukaa katikati yao na kufanya utani wa kisomi na asiboe.
Wakajikuta wanajisikia vizuri katikati ya matajiri hao waliosoma. Japo Josephine yeye alikuwa mkimya kidogo, na akiwepo mumewe ndio anamfunika kabisa kwa porojo.
Harusi iliisha, wawili hao wakaondoka ukumbini kwenda kuanza fungate ambayo Jo aliaga akisema watakuwa Greece kwa siku 10. Wakawasindikiza, nakuondoka.
Asiyethamini Cha Mkononi, Akipoteza Ndipo Hujuta.
Mara nyingi moyo hutambua thamani ya mpenzi baada ya kuondoka, pale ambapo majuto hayawezi kumrudisha. Jerry hakusikika kwa ndugu kwa muda wa kutosha, nao wakaamua kumuacha kabisa. Wasijue amejipa kazi ya kupiga simu tu.
Hakuna anachofanya, wakati wote anahakikisha simu zake zina chaji. Alikuwa akimpigia simu Tuma, mpaka akasahau kula na kushindwa kulala. Hakuwa akijua mchana ni upi wala usiku. Na akianza kupiga simu kwa Tuma, unaweza dhania ndio anaanza mpaka anapagawa au kupitiwa na usingizi ameshikilia simu zake kwenye mikono.
Akajisahau yeye mwenyewe, akitaka kurekebisha makosa aliyoyafanya kwa Lisa, yasije rudia tena. Kumbukumbu ya Mbaki kuondoka naye ilikuwa ikimtesa kila akikumbuka maneno aliyokuwa akiyasema mbele ya Tuma.
Alikuwa akizidi kupiga kama mwehu akitamani angalau apokee, ajielezee kwa hili na lile hata maswala ya watoto. “Nilikuwa nikimaanisha wale watoto wa Sandra, sio na Tuma.” Anajiambia na kuanza kupiga tena na tena mpaka anapitiwa usingizi.
“Mimi Tuma nampenda na sina shida ya kuzaa naye.” Anajitetea kwa sauti kabisa kama mwehu huku akiendelea kupiga. “Kweli historia ya Lisa inajirudia hivihivi, Mbaki atafanikiwa kumuoa Tuma.” Hapo napo atapiga bila kula wala kunywa. Gafla akawa kama kizee. Hata saluni haendi tena.
~~~~~~~~~~~
Usiku mmoja kwenye majira ya saa nane, JJ akiwa amelala nyumbani kwake na mkewe katikati ya usingizi mzito simu yake ya familia ikaanza kuita, akaangalia alikuwa Jerry. Akapokea kwa haraka. Akamsikia akilia. “Siwezi kuhema kabisa. Kifua kinabana.”Akaruka kitandani kama mshale. “Uko wapi?” Hapo mkewe akamuona anakimbilia chumba cha nguo.
Akamsikia akimwambia, “Natuma gari la hospitali na mimi nipo njiani nakuja. Jaribu kutulia.” “Kuna nini?” Mkewe akauliza, akamuona anatoka na viatu mkononi akikimbia. “Ni Jerry. Nitakujulisha. Rudi kulala.” Ndani ya dakika 6, JJ alishapotea hapo chumbani, akamsikia akishuka ngazi akikimbia kwelikweli! “Sasa taratibu JJ, usivunje mgongo bwana!” Hakusikia jibu ila milango chini ikifunguliwa.
~~~~~~~~~~~
Jerry alikuwa na hali mbaya, jasho linamtoka anagaragara hawajui ni nini. Pressurehaikuwa mbaya, oxygen ipo nzuri mwilini. Kaka yake alikuwa mwekundu kama nyanya kwa wasiwasi. Jerry alikuwa kama kibabu, ndevu zimejaa, hazijakatwa, kama sio yeye!
“Ni nini?!” Akamuuliza daktari aliyekuwa akimuhudumia. “Labda tumfanyie vipimo zaidi. Ila mpaka sasa, kila kitu kipo sawa. Ila…” Akajaribu kumtizama tena na tena. Jerry anagaragara kwenye kitanda, ameshika kichwa. Jeremi alipigiwa simu na mke wa JJ, akafika hapo bila ya kuchelewa.
“Ni nini?” “Hakuna anayejua!” Hapohapo akampigia simu binti yake. Akamueleza kwa haraka na kwa kifupi. Na yeye akamuuliza maswali machache tu, na vile anajua ni wapi anko wake anapita, akaomba kuzungumza na daktari anayemuhudumia.
Na yeye akamueleza huyo daktari kwa kifupi, akashauriana naye. Sasa binti wa JJ alivyo mnyenyekevu, unaweza fanya anachokutuma bila kujua wala kubisha. Akamshauri dawa yakumchoma, huyo daktari hakubisha. Alipochomwa tu, akatulia kabisa na kupotelea usingizini.
~~~~~~~~~~~
Baba yake akampigia tena Jemimi. “Ni nini uliwaambia wampe?” “Anko amekuwa na tension ya muda mrefu. Na kutokana na mama alivyoniambia, yupo na stress ya muda mrefu. Hapo alipo anamsongo wa mawazo, ila kilichompata ni panic attack. Amesumbua misuli, alikuwa kwenye maumivu makali. Hiyo sindano imemsaidia kutuliza misuli na mishipa ya fahamu. Atakuwa sawa kwa sasa, lakini dad!” Akaendelea Jemimi.
“Anko anahitaji therapy, ili kumrudisha kwenye hali ya kawaida. Hakutakiwa kuendelea kwa haraka na mahusiano mengine baada ya ile ndoa ngumu ya kwanza. Lilikuwa ni bomu ambalo lazima lingelipuka tu. Ilikuwa ni swala la lini. Nina watu wanao weza kumsaidia. Na nina nafasi. Mwache aje huku. Nakuahidi nitampa wakati mzuri, atakuwa sawa, dad. Usiwe na wasiwasi.” JJ akavuta pumzi kwa nguvu, ila kuzishusha ikawa kazi. Kifua kimebana kwa wasiwasi wa mdogo wake.
“And no. You don’t need to be here.” Akimjua baba yake na hao wadogo zake, akamkatalia kwa haraka, asiende naye. “Kwa nini!?” JJ akashangaa sana maana hapo alishaanza kujipanga kichwani jinsi ya kubadili ratiba yake, ili aende naye huko. “Naomba uniamini dad. Anko anahitaji mwanzo usio na anko Jeremi, na zaidi wewe.” “Ndio nauliza tena, ni kwa nini? Maana mimi ndio nikiwa naye huko naweza kumsaidia kama nilivyomsaidia Dubai.”
“Niamini mimi, dad. Kwa sasa anko Jerry hawahitaji nyinyi. Zaidi wewe.” “Wewe niambie ni kwa nini?” Jemimi akasita ila akaamua kumwambia baba yake. “Kwa nilivyosikia, anko anahisi amekuangusha.” “Kwa nini!?” “Wewe unajua kama ofisi mpya aliyofungua, amefunga?” JJ akashituka sana. “Hapana! Mbona ana…” Akasita na kunyamaza.
“Mom ameniambia kwa jinsi alivyosikia, aliacha kupokea simu za anko Jeremi kabisa. Ndio siku moja akaamua kupita ofisini kwake, mlinzi akamwambia hawajaonekana hapo zaidi ya siku 10. Ofisi imefungwa. Anasema kuna msichana alikuwa akifanya naye kazi hapo, na kijana ambaye alikuwa akiwasaidia mambo ya huko ofisini kwao. Akaanza kuacha kuja huyo msichana.” “Atakuwa ni Tuma tu!” JJ akaingilia akisikiliza kwa makini sana huku akijilaumu kumtupa mdogo wake.
“Inawezekana. Lakini huyo mlinzi alimwambia anko Jeremi, alipoacha kufika huyo Tuma, anko Jerry aliendelea kwenda kama kwa juma moja, na yeye akaacha kwenda. Huyo kijana aliyebakia amekwama, hajui chakufanya maana ni kama anko Jerry hapokei simu, na huyo msichana hapatikaniki kwa simu pia.”
“Sasa nahisi anakopita anko kwa sasa, anahisi kukuangusha maana biashara aliyokwambia angeweza kufanya, ameshindwa kabisa kuifanya.” JJ akavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu akifikiria. “Lakini nisingejali kama ameshindwa!” “Mimi najua dad, lakini anko anahitaji kufika hapo. Ninachohisi, yeye anajihisi kati yenu nyinyi watatu, yeye ndio ameharibikiwa kwenye kila kitu. Uchumi na kifamilia. Ndio maana nakwambia, mpe muda, atakuwa sawa.”
“Mwache aje huku. Apate matibabu, nakuahidi atarudi akiwa sawa.” “Lini?” “Akitoka tu hapo, mwache aje, mimi nitampokea. Na nakuahidi dad, atakuwa sawa. usiwe na wasiwasi.” “Nakuamini sweetheart. Lakini najihisi nimeshindwa vibaya sana.” Akaanza kujilaumu.
“Nilitakiwa nimfuatilie sio kumuacha peke yake tena baada ya…” Akasita akikumbuka jinsi alivyoachana naye siku alivyoharibu kwenye birthday yake, aliyoandaliwa na Tuma. Na alipofika kwake siku ya shuguli aliyoandaa mkewe, baada ya ibada maalumu ya shukurani kwa Mungu wao, ambayo huwa mkewe anafanya kila mwaka. Anatoa sadaka kubwa sana kanisani kama kumshukuru Mungu kwa yote anayowatendea kwenye familia yao, kisha kukaribisha watu kusherehekea pamoja, kula na kunywa nyumbani kwake, sasa hata siku hiyo, ni kama hakumpa muda wake kabisa.
“Atakuwa sawa dad. Na mtapata muda mzuri wa kuzungumza. Nakupenda dad.” “Najua Jemimi. Ila natamani niwe naye kipindi hiki!” “Kama ni kuja, nitakwambia lini uje, ila sio sasahivi.” Akazungumza na baba yake mpaka akakubali. Maana walijua likifika swala la wadogo zake, inabidi kumchukulia taratibu sana.
~~~~~~~~~~~
Jerry aliondoka nchini kuelekea nchini Marekani akiwa peke yake na kaka yake akijaribu kumtuliza na kumwambia kila kitu kitakwenda sawa, akiwa amejawa hukumu akihisi na yeye amechangia kumchangaya. Alikuwa mkali kwake na hakumtafuta tena.
"Majuto Ni Kivuli Kinachofuata Baada Ya Jua La Mapenzi Kuzama."
Na kutotulia kwenye mapenzi ni kama kuchoma daraja unalohitaji kulivuka kesho. Ndio akawa Mbaki. Siku hiyo mchana mama J akashitukia Mbaki amemsimamia mbele yake. “Unataka nini Mbaki?” “Simpati Tuma. Naomba namba yake.” “Sina.” “Unaninyima bure mama J! Mimi nina nia nzuri na Tuma. Na nikwambie kabisa, nipo tayari kumpokea jinsi alivyo.” Mama J akakunja sura na kukaa sawa.
“Nitamtunza mtoto aliyenaye kana kwamba ni wangu kabisa.” Mama J ndio kujua kama Tuma ni mjamzito. “Na kabla hujasema nilimwambia sitaki kumsikia tena, wakati na mimi nilitoroka na Umi. Jua na mimi ni binadamu mama J, ule ni mshituko tu. Sikutarajia kama Tuma anaweza shika mimba ya mtu mwingine.”
“Tuma alinikatalia kabisa mtoto kipindi kile mama yangu mgonjwa. Nilimuomba angalau tupate mtoto, mama asife kabla hajaona mwanangu hata mmoja, lakini Tuma alinikatalia, akasema mpaka ndoa. Leo anabeba mtoto wa mtu baki tu! Kweli? Hata ingekuwa wewe unge…” Akawa amemuacha mbali sana mama J.
Akaongea mengi hapo, mama J akimtizama ila akili ipo mbali. Anawaza hili nakufuta lile akiunganisha mazungumzo yake ya mwisho na Tuma. “Kwa hiyo?” “Tokea utoke na Tuma siku ile pale, sijamsikia wala kumuona. Na mimi simpati.” “Basi akikupigia mpe ujumbe wangu. Tumetoka mbali sana na Tuma, mambo ya katikati hayawezi kututenganisha.”
“Anisamehe katika lile la Umi, na mimi namsamehe katika hili.” “Tena acha huo ujinga Mbaki. Wewe ulimsaliti mkiwa kwenye mahusiano. Tuma aliendelea na maisha yake, hamkuwa pamoja. Usijifananishe kabisa. Tena ondoka zako. Unataka kunichanganya kabisa hapa.” “Sasa kosa langu ni nini hapa? Nishasema ninamsamehe.” “Unamsamehe kwa kosa gani!? Wewe unamtoa pale mgonjwa, halafu unakwenda kumtelekezeahospitalini akiwa hana kosa! Ni akili hiyo?” Jeremi akaingia ofisini kwa mkewe.
Akamkuta anawaka na hasira zote anamalizia kwa Mbaki. Mwishoe akamwambia Mbaki aondoke. Mbaki wawatu akaondoka akiwa ameloa lawama kwelikweli! Yaani yeye ndio akawa amemsababisha Tuma aondoke wala si Jerry. “Na nisikuone tena hapa.” Ndio yakawa maneno yake ya mwisho akifukuzwa.
~~~~~~~~~~~
“Kwani kuna nini tena?” “Kumbe siku ile Tuma alipoondoka pale kwenye ile shuguli aliyokuwa amemwandalia Jerry, aliniambia anajisikia kuumwa. Sasa akaondoka na Mbaki akimsindikiza hospitalini, akagundulika ni mjamzito.” Jeremi akatoa macho.
“Sasa Mbaki naye anataka kunichanganya.” Akamsimulia malalamiko ya Mbaki yote. “Subiri kwanza Hilda, si ni ya Jerry?” “Sasa unafikiria ni ya nani na wewe?” Mkewe akamjia juu. “Haya, samahani najua ni swali la kijinga, ni mshituko tu. Na najua hata Jerry naye hajui. Si ndio?” “Kwamba wewe ulikuwa hunisikilizi tokea mwanzo?” Jeremi akatulia kidogo.
“Unajua anaendeleaje huko?” “Jemimi amemwambia bro anaendelea na matibabu. Ila anaonekana kweli kichwa kilikuwa kimevurugika.” “Usicheze na Sandra. Yule anaweza kukupa tatizo la kudumu la akili. Sasa?” “Ndio anaendelea na matibabu. Ila bro anajilaumu kwelikweli!” Wakabaki kimya wakifikiria.
“Utamwambia?” “Siwezi. Nitamuacha mpaka amalize matibabu, asije acha matibabu na kurudi. Ni kweli anatakiwa apone kabisa ndio aje akabiliane na changamoto zake, ila aisee namuhurumia Sandra.” “Kwa nini?” Jeremi akacheka kwa masikitiko na kutulia.
“Ni nini?” “Sasa usianze kunilaumu kwamba sikukwambia, ndio na mimi nimejua.” “Nini?” “Bro amewatenda vibaya sana. Yaani sijui Sandra ataishije hapa mjini.” Akamsimulia mkewe kila kitu.
“Jeremi!” “Unaambiwa bro amemnyang’aya mpaka senti ya mwisho aliyomkopesha na kumtoa kwenye kila kitu alichokuwa ameshika kwa jina lake. Unaambiwa ameenda kumuongezea restrain order, asiwahi fika kwake wala kwangu. Iwe nyumbani au ofisini, asiwahi kumuona. Nasikia amemwambia siku akijisahau na kumtafuta Jerry hata kwa ujumbe, akasikia, atauona mji mchungu. Amemwapia kumuhamisha jiji, ampishe Jerry.” “Jeremi!”
“Nasikia ilikuwa mbaya mno. Na hayo nasikia alihakikisha anamwambia Sandra mwenyewe, uso kwa uso, kituo cha polisi ili asije msingizia. Nasikia alihakikisha Sandra anafikishwa polisi alipo, akaenda kumkabidhi hiyo hati. Alipoulizia watoto, unaambiwa JJ alimjibu kuwa wale watoto hawakuwahi kuwa wa Jerry, hawamtambui Jerry kama baba yao, ila kama mwanaume aliyeshindwa kwenye maisha.”
“Akamuonyesha ile video waliyokuwa wakimcheka baba yao nakumuita majina mabaya wakati wakishangilia wanavyo choma vitu vyake. Akamsikilizisha tena maneno yake yeye mwenyewe Sandra ya siku ile ya talaka juu ya hao watoto kwa Jerry. Kisha akamuuliza, watarudi kwa Jerry kama nani yao?” “Na ile ilikuwa mbaya sana.”
“Sasa unaambiwa JJ amemwambia Sandra, asiwahi kumsikia. Akamwambia kama anataka wale watoto wabakiwe na mama, basi akae mbali na Jerry, eti lasivyo atahakikisha anafufua mambo yake ya nyuma, mpaka ajira yake ya mwisho kabla ya kufungua ile kampuni.”
“Mungu wangu Jeremi! Ambayo ndiko alikoiba na kupata ule mtaji wa ile biashara?” “Sawasawa. Unaambiwa JJ amemwambia asiwahi msikia tena labda amsikie kutoka kwenye kinywa cha Jerry mwenyewe na si vinginevyo.”
“Amemuhakikishia. Ikitokea hata amepita alikomkataza, atamuadhibu vibaya sana. Akamwambia amemvumilia sana kwa kipindi chote alichokosa adabu hata mbele ya watoto wake, ila akamwambia safari hii hatamuacha. Kwa hiyo nasikia Sandra na familia yake, JJ amewamaliza kabisaaa.” “Nilisema mimi! Sandra alidhania anaingia kwenye ugomvi na Jerry, kumbe na JJ.” Wakabaki kimya kila mmoja akiwaza lake.
~~~~~~~~~~~
Inaendelea….
0 Comments:
Post a Comment