Tuma akaanza kusikia mabadiliko kwenye mwili wake. Kwa msaada wa JJ, wakapata kampuni nyingine mbili wanazofanya nao kazi, kuwapelekea bidhaa, kukawa busykwelikweli. Wakihakikisha hawazembei ili kuweka jina zuri na waendelee kupata tenda nyingine kwenye makampuni hayo mapya.
Hali ya uzito kati yao ilikuwa ikiendelea. Tuma akakumbuka wakati mzuri waliokuwa nao kabla. Ile hali ya kusomana mioyo na kuhangaika kumfurahisha mwenzio hata kama inagarimu. Kalikuwa kakipindi kafupi, lakini kila mmoja akajua kwa hakika Mungu amejibu maombi yao na amekusudia kuwatoa upweke kwa kupitia kila mmoja wao.
Lakini gafla shilingi ikapinduka, uhalisia ukajiweka dhahiri. Jerry alishakuwa mume wa Sandra king’ang’anizi, akajua udhaifu wake na ndio aliokuwa akiutumia miaka yote hiyo mpaka kumuweka kwenye ndoa. Mbali na hapo, wana watoto wawili.
Tayari yale aliyokuwa akiyakimbia hata kwa Mbaki, yakawa yamemrudia, ndoa ya mitala. Tena safari hii ikawa ameruka majivu, na kukanyaga moto. Mbaki alikuwa malaya wa siri mpaka kufumaniwa, Jerry ana wanamke anayemsaka kwa udi na uvumba.
Mbaki mtamu wa maneno. Hata atoke kufanya dhambi zake, maneno kwa Tuma ni matamu kwelikweli, akimtanguliza yeye kila mahali. Jerry alikuwa na hasira, anashindwa hata kufungua mdomo kama si lazima.
Basi upweke wa Tuma ukarudi vilevile ila na zaidi. Maana Jerry alikuwa yupo, lakini hata kwa kumwangalia usoni, huthubutu kusema lako ila lile analosema yeye. Kugombana na wakili wake aliyewasimamia talaka, kwenye simu ikawa jambo la kawaida, akirudisha maneno machungu kwa Sandra, Tuma akijiangalizia tu.
~~~~~~~~~~~
Siku hiyo akiwa hajisikii vizuri akabaki ametulia tu ofisini kwake akiwaza. Kama ni ujauzito, analeaje mtoto kwenye hayo mazingira ya tension hivyo! Anamwambia nini Jerry aliye kwenye hali kama hiyo!
Akaanza kujilaumu siku ile ya kwanza wakifanya mapenzi na kumkubalia Jerry kukojolea ndani wakati zilikuwa siku zake za kushika mimba. Akakumbuka vile alivyomwambia anataka mtoto naye, atakuwa wao. Akajicheka asiamini aliweza vipi kwa Mbaki na kushindwa vipi kwa Jerry.
Juli akaingia kumuulizia chakula, akajifikiria, hakujisikia kula kabisa, hata mida ya asubuhi wakiwa wanakula na Jerry, hakula kitu zaidi ya chai ya rangi. Jerry hata hakujua kwa sababu alikuwa kimya kwenye simu yake. Yeye akanywa chai tu na kumaliza kila mtu akarudi ofisini kwake. Jerry wa zamani angejua kama Tuma hajala.
Tuma akakumbuka siku ile alipomwambia tumbo limejaa gesi, akahangaika mpaka kwenda kumtafutia heating pad na kumtengenezea chai ya moto, na ndipo akamkataa Umi, Tuma akapokea uponyaji wake hapohapo. Lakini hiyo ilikuwa siku ya tatu, Jerry hajui hata kama Tuma hali! Maana na cha jana yake kililetwa, Tuma akagusagusa na kuishia kukimwaga, akaosha sahani yake na kurudi ofisini, hata Jerry hakuwa na habari. “Kweli wanaume wana mwanzo, mwisho hawana!” Akajiwazia Tuma.
Chakula kilipoletwa akamsikia akimwambia Juli ampelekee ofisini kwake na uma pamoja na kisu. Kimya, akamuacha Tuma akiwaza.
~~~~~~~~~~~
Kazi wakawa wakifanya vizuri sana. Tuma wakujituma na akili anazo. Mipango inakwenda na kutelekeza bila kugomeana. Kabla Jerry hajamtuma, ameshafanya. Na yeye akawa akimpa Tuma pesa nzuri tu.
Birthday ya Jerry ikawa imefika. Tuma akaona amfanyie kitu kama kumfurahisha na pengine kuwarudisha kwenye ile hali yao ya mwanzo, maana alimwambia huwa hapendi kabisa siku zake za birthday. Haziishagi vizuri kila wakati kuna jambo baya linatokea. Wanaweza kuishia kugombana na Sandra ambaye huwa anamwandalia za mapesa mengi, akialika mashoga zake, lakini mwishoni, wao huishia kugombana vibaya sana.
Tuma alipomuuliza huwa wanagombana nini siku kama hiyo, anamwambia kwa sababu tofautitofauti tena wakati mwingine anaweza kufokwa kwa jambo lolote analochagua Sandra, zaidi akisema alimuabisha kwa hili na lile mbele ya wageni wao. Na kila mwaka wanapomaliza huwa anamwambia asimfanyia nyingine, lakini Sandra alikuwa akimwandalia.
Basi ndio Tuma safari hii akaamua kufanya mabadiliko. Kubadili historia, ili kumfurahisha.
~~~~~~~~~~~
Akamtafuta mama J kwa simu. “Nisaidie dada yangu.” Tuma akaanza. “Wewe tena! Hata ukitaka nikubebe mgongoni, nitakubeba.” Tuma alicheka sana. “Tumekuwa na wakati wa hekaheka dada yangu, hakuna kupumua.” “Mwanzo kote kugumu, mkija kuweka mambo sawa na utaratibu wa kueleweka, mtatulia.” “Naamini hivyo dada yangu.”Akaendelea.
“Birthday ya Jerry inakuja, ni jumamosi hii. Nataka kumfanyia surprise. Ila kwa maneno yake huwa hapendi kwa sababu huwa ilikuwa haiishii vizuri.” Akamsimulia alichoambiwa.
“Usicheze na Sandra, wewe! Yeye mjuaji masaa 24, na huwezi jua ni wakati gani atakubadilikia.” “Sasa nataka kubadilisha hilo dada yangu. Angalau ajue ni siku yake na afurahie. Nimechoka dada na sijisikii vizuri, lakini naona nimfanyie tu, au unasemaje? Angalau aone kuna mwanzo mpya, na huko ameshatoka.” “Nakuunga mkono kwa asilimia 100. Unataka mimi nikusaidiaje?” Hapo akamfurahisha Tuma.
“Nakushukuru. Kwanza ifanyikie pale tulipokuwa tukifanya naye kazi. Niombee kwa Jeremi kwenye mida ya saa 11 amuite kule upande wa stoo, tukiwa sisi tumejificha kule kwenye yale makabati kwa nyuma, amwambie afike kwa mazungumzo atakayochagua yeye. Halafu kule stoo tupapambe vizuri ila sio vikubwa, ila vitu vichache, ikiwemo baloons.” Wakaweka mipango hapo wakipeana vichwa, kucheka kwingi. Naye Mama J akaweka mawazo yake, ikafana kweli! Kitu kizuri, cha muda mfupi.
~~~~~~~~~~~
Ilikuwa siku ya ijumaa. Nayo ikawa kama siku nyingine. Alifika kumchukua Tuma asubuhi, baada ya salamu wakahamia kwenye mipango ya siku hiyo ya kazini. Wakiwa njiani wakaendelea kujipanga. Hawakujizungumzia wao wenyewe na hata Tuma hakumwambia hali ya kuumwa anayojisikia. Viungo vyote vilikuwa vikimuuma. Halafu anasikia baridi, hakumbuki mara ya mwisho kula mlo mzuri, uliokamilika. Ni kama alikuwa na shibe wakati wote.
Hakumtakia hata happy birthday, akajifanya kama hakumbuki akabaki kusikiliza na kuchangia mipango ya siku hiyo.
“Halafu nimeamua kwenda tu kumalizana ana kwa ana na Sandra, niweke kikomo. Ananinyima usingizi bila sababu! Siwezi kufikiria mchana wala usiku akituma jumbe zake kupitia wakili bila kupumzika. Naona sitakuwa na amani mpaka nimfikishie ujumbe mimi mwenyewe, aelewe sio kwamba namkimbia, ila ninamaanisha. Tumefika mwisho na sitarudi nyuma. Si kwa mazungumzo tu, kwa chochote kile.” Tuma akaona wazo si baya.
“Sandra hanidai, si mdai kitu.” Akaanza kupandisha hasira sasa. “Nimemuachia kila kitu, hata watoto pia sitaki tena. Yaani hata akiwarudisha sasahivi kama chambo, haitasaidia. Hatanipata tena. Kwanza watoto wenyewe ni wanangu jina tu, kwamba mbegu yangu ndio iliwatengeneza.” Tuma akashituka na kumwangalia.
“Amewakuza vile atakavyo yeye. Watoto wenyewe wananitukana kama vile mama yao! Wanafaida gani na mimi? Wa nini mimi kama sio kwamba anataka kuwarudisha kwenye maisha yangu sasahivi kuniongezea pressure tu. Sina shida na watoto mimi.” Hapo akagongelea msumari moyoni kwa Tuma, akaanza kuhesabu siku zake mara ya mwisho kuzipata ni lini!
Yaani hapo Jerry alikuwa akigomba juu ya Sandra, yeye anahesabu siku zake. Ni lini mara ya mwisho kuona damu ya hedhi. Akahesabu vidole vya mkono vikaisha. Akaanza kukopa na vya mguu. Anafanya kukandamiza kabisa kila kidole cha mguu anachokihesabu huku gari ikienda, hesabu haiji.
“Kama Mungu akinisaidia nikiwa sijashika mimba mimi, hakika nakwenda kufunga kizazi kabisa!” Hayo anayasema Tuma baada ya hesabu kuzidi kuchenga.
Akili ikamrudia akiwa ndio gari inaegeshwa, wamefika eneo la ofisi. Hata akawa hajasikia Jerry alikuwa akiendelea kulalamika nini, ila hofu na ya kwake. Akavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu. Alipoona kimya, akajua alimaliza kuzungumza, akashuka na pochi yake na kuelekea ofisini kwake, siku ya kazi ikaanza. Hata hakuna aliyetoka kwenda kula muda wa chai ulipofika.
~~~~~~~~~~~
Kwenye mida ya saa 7 kwenda nane mchana akamgongea Tuma. “Mimi ndio nakwenda kukutana na Sandra kwa yule wakili. Na leo ndio nitaweka kikomo hata kwa yule wakili kupokea jumbe za Sandra na kunifikishia mimi. Akipokea jumbe zake, ajue chakufanya nazo, asinivuruge akili.” “Na kwa kuwa na mimi hapa naona pako vizuri, nitatoka nikatengeneze nywele. Nikikutana na foleni, nikachelewa kumaliza, nitapitiliza tu nyumbani." "Basi tutawasiliana. Usafiri? Au nikuachie gari?" “Nitakuwa sawa tu. Wewe nenda nalo, nitaita usafiri uje unichukue.” “Sawa. Lakini ukikwama, usisumbuke, niambie nirudi kwa haraka.” “Sawa. Asante.” Akatoka.
Kuliko Ungua Shoka, Kukabaki Mpini
Huku kwa Tuma hapohapo na yeye hakuchelewa. Akatoka kufuata keki sehemu aliyokuwa ametoa oda na baadhi ya vitu vingine vya kula. Mama J alimwambia atatafuta hayo mapambo. Atawahi kutoka, na kwenda kuanza kutengeneza huko stoo.
Akiwa njiani akampigia simu mama J kumwambia ameshatoka. “Nafuata vitu, naelekea huko.” “Mwenzio nimezua jambo! Nimemsimulia Jeremi na kumpanga, si na yeye ameenda kumwambia kaka yao! Hivi JJ anakuja.” “Mama J?!” “Nakwambia hutamuweza JJ kwa wadogo zake. Ameniambia Jeremi amefurahi sana, eti umeweza mfikiria mdogo wake, eti na yeye kila kitu kitasimama ili aje kukuunga mkono.” “Kweli!”Asiamini.
“Nakwambia wewe umemgusa JJ pabaya! Ukikohoa tu, atasikia. Sasa ili tusifanye vituko, mbele yake, nimeamua kufanya jambo la kueleweka. Hapa nimetafuta mpaka wapambaji wa harakaharaka. Nimemuomba mke wa JJ aniombee kwa mtu wake anayemfanyia catering, aniletee vitafu…” “Nyie mama J jamani! Mpaka mkewe tena?!”
“Anapenda shuguli huyo! Angenilaumu kuona mumewe amealikwa, yeye kaachwa. Siri yakubakia kupendwa mwenzio ni kujikomba kwa yule mwanamke na kujifanya namtegemea kwenye mambo fulanifulani kama hilo kujidai kwamba ni gumu, mimi siliwezi. Basi mwenzio ndio anaona sifa. Atalifanikisha kwa nguvu zote, na kuzidi.” “Mmmh!” Akaguna.
“Nakwambia jambo limekuwa kubwa, na litanoga. Umemfurahisha mpaka mke wa JJ. Mimemwambia umeona umfurahishe. Na kumuwekea mwanzo mpya. Akaniambia eti hata JJ anakusifia sana.” Tuma akashangaa sana.
“Mama J!” “We nakwambia mbona ushakuwa mwana familia! Hao wawili wakikupenda, nakwambia watakulinda kwa kila hali.” Tuma akahema kwa nguvu.
“Sasa huyo Jerry aitwe saa ngapi?” “Hapa alipo anakutana na Sandra.” Mama J akashituka sana.
“Sandra tena?” “Imekuwa shuguli dada yangu, Sandra amerudi kwa gia zote. Penzi lote limeisha. Jerry amekuwa mtu wa hasira, nina jambo langu nilidhani lingekuwa jema la kumwambia Jerry, lakini dada yangu, nimeshindwa. Amekuwa mtu wa hasira kupita kiasi. Simu na huyo wakili ni kila wakati! Hata hatuzungumzi tena. Hapa naumwa dada, siwezi mwambia.” “Pole Tuma.” Akajikuta akicheka na machozi.
“Nimekaa leo na maumivu mpaka nikamkumbuka Mbaki.” “Alivyokuwa akijua kukubembeleza!” “Acha dada! Mambo yamebadilika kwelikweli, hata sikutegemea! Ndio maana nimeona pengine nikifanya hiki, atafurahia, ataona kuna tumaini huku kwingine. Vinginevyo, hakuna tena penzi dada, nipo kama mfanyakazi wake tu.”
“Pole Tuma mdogo wangu. Na Sandra ana nguvu ya ajabu sana kwa Jerry. Sijui huwa anafanyaje bwana! Hakuna umbali kati yao asimfikie akili yake na kumvuruga.” “Basi amemvuruga kwelikweli! Jerry yule tuliyekuwa naye hapo, si huyu. Bora pale mwanzo tulipokuwa tukifanya naye kazi hapo kwenu akiwa ndio ametoka kuachana naye. Sasahivi imekuwa mbaya kwelikweli! Uhalisia umejifungua wazii.” Wakaendelea kuzungumza wawili hao naye Tuma akashindwa kuficha kabisa. Akasema kama anayetua mzigo kwa mama J.
Wanakogombana Tembo, Wanaacha Manyasi Kuumia
Huku kwa Jerry alifika na kukuta anasubiriwa. Kwamba Sandra alishafika hapo mapema hata kabla ya muda. “Unataka nini kwangu Sandra?” Akamuuliza hata kabla hajakaa. “Sasa si ukae!” “Linaweza kuwa ni jibu fupi nikakujibu tukaondoka bila ya kupotezeana muda.” Wakaanza kubishana hapo, Sandra anang’ang’ania hawezi kuzungumza mpaka akae.
Kama kawaida yake huwa anashinda. Baada ya ubishani wa muda wakutosha, Jerry akakaa. “Unataka nini?” “Unakumbuka ile pesa tuliyokopa kwa JJ?” Akamfungulia kijalida kabisa. “Nime print kila kitu ili uone mwenyewe.” Jerry akakunja uso na kuvuta kijalida. “Hii pesa ulinituma nikukopee kwa JJ ili kuongeza mtaji wa kampuni yako.” Jerry akamjibu na kumsukumia hicho kijalida.
“Lakini kipindi hicho na wewe ulikuwa ukifanya kazi pale kama msaidizi wangu. Si ndio?” “Acha kunipotezea muda na jambo tunalojua majibu yake. Swali ni lilelile unaloshindwa kunijibu. Unataka nini kwangu?” “Sasa, sasahivi JJ anadai pesa yake eti kwa sababu tumeachana.” Jerry akabaki akimwangalia, akimsikiliza kama anayesubiri aongee pointi inayomuhusu.
“Ndio hivyo.” “Umechanganyikiwa Sandra?” “Kwa nini sasa na wakati kaka yako ananifanyia kusudi?” “Kwa nini hunijibu swali langu? UNATAKA NINI KWANGU? Maana usiponijibu ndani ya sekunde tano, ninaondoka. Na safari hii nikiondoka hapa, jua hata huyu wakili naye nafunga naye mkataba. Atakuwa kama wewe tu. Hatanipata tena kwa simu. Maana hii michezo uliyoamua kucheza naye na kuniingiza mimi katikati yenu nyinyi wawili, sitaivumilia.”
“Nilipewa maagiza na kaka yako kuwa chochote anachotaka Sandra kwako, iwe kupitia mimi.” “Basi ndio nakwambia, kuanzia baada ya hiki kikao, funga mkataba na mimi. Kazi yako ilikuwa talaka. Ulishatukamilishia. Ulimsikia Sandra siku ile. Hana ninachomdai, na mimi sina ninachomdai. Huduma zako, sihitaji tena.”
“Na watoto je?” Sandra akadakia. “Maana hata kama ugomvi ulitokea ni kati yako na mimi sio watoto wetu.” “Hilo umegundua lini?” Yaani yeye Jerry, alikuwa hajui kinachoendelea, JJ alikuwa akifanya yake kimyakimya.
Asijue hali ya Sandra aliyeachana naye, si huyu kabisa. “Iwe nimegundua kwa kuchelewa au la! Ile ni damu yenu, na JJ umkumbushe. Akidhania ananikomoa mimi, ajue anakomoa watoto wako.” “Tokea umekuwa na mimi, ushawahi kuniona nikiingia leba mimi?” Mpaka yule wakili akamgeukia kwa mshangao.
Sandra akaanza kubwabwanya. Aliyoongea kwa kiburi siku ya talaka, sasa hivi yanamrudi, hayamezeki hata kwa asali. Aliongea Sandra, hamalizi. “Hayo yote uliyozungumza hayanihusu, kwa kuwa sio matatizo yangu. Wewe unaakili sana tu kama ulivyokuwa ukisema na siku ya talaka uliwathibitishia hapa.”
“Najua utajua kitu chakufanya juu ya shule yao. Ukishindwa kuwalipia ada hapa wanakosoma sasahivi, peleka wanakosoma wenye uwezo unaolingana na pesa yako! Mbona rahisi sana hata mimi fala, bwege, kama unavyoniita wewe na watoto wako, nalijua hilo! Ugumu upo wapi?” Sandra hakuamini. Mpaka huyo wakili akahisi pengine hajasikia vizuri.
“Kwamba unatelekeza watoto?!” “Sina mtoto natelekeza, kwa sababu sijawahi kuwa na mtoto hapa duniani.” “Na kina…” “Ulishawahi wasikia wale watoto wakiniita mimi baba kwa heshima isipokuwa wanashida, vinginevyo wananiita na kunitambua kwa majina uliyowafundisha wewe waniite? Sasa ni kipi leo kinachokupelekea ufikiri mimi ni baba yao?” Sandra alibaki haamini.
“Siku ya talaka ulipoulizwa juu yao, ulijibu nini hapa?” “Siku ile…” “Hakuna kitakachobadilika Sandra. Eti kwa sababu wewe ndio umebadili mawazo, unafikiri wote tutayumba!? Hata kidogo. Nimekuja leo kumalizana na wewe rasmi kwa kile ulichokianzisha WEWE mwenyewe. Sina shida na watoto. Kwanza siwataki.” “Huwezi kataa damu yako!”
“Nenda kanishitaki. Kashitaki popote unapotaka wewe. Ila usiwahi warudisha wale watoto kwenye maisha yangu, maana itakuwa ni kama kurudishiwa wewe mwiba, kwenye maisha yangu. Ukitaka watunze, ukiwashindwa, maana najua watakuja kukushinda tu, maana ni mabomu uliyokuwa ukiyakumbatia, sasa ukishindwa, wagawe. Vinginevyo jelaitakusaidia kuwatunza. Kama huna jingine, naondoka.”
“Na iwe MWISHO kunitafuta. Narudia tena, hunidai, wala sikudai.” “Watoto…” “SITAJIRUDIA. Nimeshakwambia siwataki. Andika popote, nitaweka saini na wenyewe kawaambie yule jinga, fala, bwege, HAWATAKI. Mimi si fala? Bwege, kama wewe na wanao mnavyoniita? Sina kitu chakuwafundisha? Sasa waambia bwege, amewakataa. Wala sitawatafuta kwa uzima wala maradhi.” “Akifa mmoja wao?” “Zika! Wewe vipi Sandra?” Mpaka yule wakili alikuwa haamini.
Sandra akaanza kujikanyaga kwa hili na lile. Akaongea mengi mno mengine akijirudi na kulalamika. “Kaka yako amefukuza kazi ndugu zangu wote eti kunilipiza mimi kisasi! Baba pia akamfuta kwenye biashara zake.” Ndio Jerry anasikia hapo, hakutegemea. “Mambo yako na mimi yanahusianaje na ndugu zangu?” Akaongeza Sandra, hapo mpaka machozi.
“Ananikomoa mimi wakati ile ni damu yenu wenyewe? Akininyang’anya kila kitu naishije na wale watoto?” Jerry akasimama. “Naona hayo ni matatizo yako binafsi Sandra, hayanihusu kabisa. Kwanza kama ulivyokuwa ukisema, unatoka kwenye ukoo wenye akili sana. Kweli mnashindwa kukaa nyinyi wenye akili watupu, kuzungumzia mambo yenu mpaka kunitafuta tena mtu kama mimi, niliyekuwa nikikuchelewesha kwenye mambo yako?” “Ni kwa sababu…” “Sina muda wa kukusikiliza Sandra. Huo muda ulishauhitimisha. Acha kunipotezea muda wangu.”
“Na wewe, leo iwe mwisho kunipigia simu kunipa jumbe za Sandra. Kazi uliyoajiriwa kwa ajili yangu umeshaikamilisha ramsi, huna ulilobakiza. Na mwajiri wako atakupigia simu leo kukuthibitishia hili. Kuendelea kunitafuta utakuwa ukikiuka sheria, ndipo na mimi nitakufungulia mashitaka na kukuwekea restrain order kama ambayo nakwenda kumuwekea Sandra. Muwe na jioni njema.”
“Na ile pesa tuliyomkopa JJ?” Sandra akamuwahi kabla hajatoka. “Imefanya nini mbona unazidi kunipotezea muda?” “Tulikopa wote Jerry, na wewe unatakiwa kulipa?” “Umechanganyikiwa wewe?! Hukukopa ile pesa kama kampuni mpaka ukataka kwenda kuifuata wewe mwenyewe, ukisema unaongeza kwenye mtaji wa kampuni ambayo kampuni ulikuja kunifukuza kama mbwa, ukisema ni yako?!” Jerry hapo ni mwekundu kwelikweli. Na yeye anaongea kwa kufoka, sauti ya juu usingejua ni yule Jerry mkimya.
Yaani hata Sandra hakuwahi kukutana na Jerry wa namna hii. Mkali haswa, anaunguruma na sauti yake kama simba. “Lazima tugawane ile pesa. Hata JJ namlipa nusu, namwambia nusu akudai wewe.” “Kama nilivyokwambia, HAYANIHUSU. Na nafikiri hata JJ si mjinga. Anadai alikokopesha. Na unamjua yule huwa hacheki na kima. Sasa wewe mzungushe, utamjua vizuri.”
Alishafungua mlango akatoka, ila akarudi kama aliyekumbuka kitu. “Restrain orderyako na wanyumbani kwako na kwenu, itakufikia hivi punde. Usiwahi kunitafuta tena Sandra. Leo iwe mwisho kuniitisha kikao cha aina yeyote kile. Hunidai, sikudai. Fanya chochote unachoona kinafaa kama zamani na wale watoto. SIWATAKI TENA.” Ndipo akaondoka sasa.
Maji Yaendelea Kumwagika
Alikuwa akichemka hasira, anashindwa kutulia. Akatoka hapo kweli akaenda moja kwa moja kituo cha polisi kumshitaki Sandra. Akaandika maelezo kuwa anamfanyia fujo za kimtandao ili kumfikia, na akasema anahisi familia yake ipo hatarini kutoka kwenye familia ya kina Salamba. Akataja majina ya familia yake wote mpaka Tuma, akasema hao watu wake anahofia wanaweza kudhuriwa na kina Salamba. Akaomba restrain order. Akapewa. Asijue na JJ alishawawekea kama hiyo mpaka watu wa ofisini kwake kasoro tu Tuma hakuwa ameingia kwenye picha.
Hapo anachemka kwelikweli. Akarudi tena kwa yule wakili na kumkabidhi. “Kwa kuwa ulikubali kutumiwa na Sandra, hakikisha hii inamfikia.” Akairusha mezani kwake na kuondoka.
Moyo Ulishajaa Nyongo, Hasali Haitamani
Alipofika garini akijaribu kutulia akampigia Tuma. “Uko wapi?” “Nipo kwa mama J, kule nilikokuwa nikifanya kazi.” “Basi nakuja kukufuata. Naona na Jeremi naye ananitafuta.” “Sawa.” Tuma akawatangazia wote kuwa yupo njiani, anakuja. Wote wakaanza kuhamia stoo wakihamisha magari kabisa sehemu ya mbele ambayo wanajua ataingilia yeye. Mama J akawaambia wafanyakazi wake wote kuwa kuna ulaji, wasiondoke.
JJ alikuwa hapo na mkewe. Na mkewe alifanya vizuri sana. Kitu cha haraka ila kikawa cha hadhi, kizuri mno. Wakasaidiana na wapambaji, hapo stoo pakatengenezwa vizuri.
Wakati Jerry anakaribia kufika na Mbaki naye akawa amefika. Tuma akashangaa sana. “Unataka nini Mbaki wewe jamani?!” “Nina shida sana na wewe Tuma. Lazimatuzungumze.” “Haiwezi kuwa sasahivi.” “Nitasubiri lakini siwezi kuondoka bila ya kuzungumza na wewe.” “Mbaki akikazania jambo! Sasa huu muda mbaya, utaharibu kila kitu. Njoo huku.” Mama J akaingilia na kumvuta Mbaki sehemu ambayo wote wanaelekea wakichungulia getini.
Walipoambiwa ameingia getini, wote wakaenda nyuma ya makabati, kujificha ili akifika hapo wamshitukize kwa kusema ‘surprise!’. Basi wakatulia kimya ila simu ya Tuma ikaita. Alikuwa Jerry. “Upo upande gani?” Akaweka swali. “Njoo huku upande wa stoo namsubiria mama J. Njoo na wewe huku, nitakusubiria hapa nje.” “Nakuja.” Ndipo yeye akatoka, wengine wote wakabaki wamejificha, kimya kama hakuna mtu.
~~~~~~~~~~~
Jerry akaenda huko stoo na kumkuta Tuma nje. “Vipi mambo yako ya nywele hukufanikiwa kwenda?” Wakawa wanaingia, kabla hao watu hawajafanyiwa ishara na Tuma ili waseme wote kwa pamoja ‘Surpriseee..!’ na kutoka wote, yeye mwenyewe akaona yale mapambo na jina lake lililoandikwa kwa kwa urembo juu, vimeninginizwa.
Akagundua kwa haraka sana. “Umefanya nini Tuma?” Akauliza kwa ukali. “Nilikwambia nini juu ya mambo ya birthday?” Akazidi kuuliza kwa hasira. “Nilitaka kukufurahisha Jerry na ku..” Tuma akaona havina maana, kwani alichokitegemea sicho.
“Kwa nini unafanya kama Sandra? Unatofauti gani sasa na alichokuwa akinifanyia Sandra ya kufanya kile unachokitaka hata nikisema hapana? Unakuwa unataka…” “Basi Jerry. Samahani. Natoa kila kitu na kutupa. Naomba fanya kama sijafanya, ili hiki kitu kiishe. Samahani sikukusudia kukuudhi. Hata keki natupa.” “Mimi bado nataka kipande changu. Usitupe.” Alikuwa JJ akitokea nyuma.
Jerry ALISHITUKA SANA. “Hata mimi nataka keki. Na ilivyo nzuri, wala usitupe.” Alikuwa mama J. “Ikibaki vijana wangu watanywea chai kesho.” Mama J akaongeza “Na hivyo vyakula pia sio vyakutupa Tuma. Tunza mama. Umehangaika sana. Acha sisi tutakao weza kula tule, watakao taka kubeba wabebe. Tusiwe tumeingia hasara ya bure.” Alikuwa mke wa JJ. Wote wakajitokeza hapo mbele.
Jerry hakutegemea kama watu wote walikuwa hapo. “Tuma mama, si naruhusiwa kukata yangu? Au muongozo ukoje?” Alikuwa JJ, wakajua anafanya kusudi kama kutuliza ile hali. Jerry alikuwa amepigwa butwaa.
“Karibu. Kata tu. Karibuni wote. Kama italiwa ni afadhali kuliko kutupwa.” Akamgeukia tena Jerry. “Samahani sana.” Akaomba tena msamaha na kutoka hapo walipokuwa wamesimama na kwenda kumsogezea JJ vifaa ili akate. Alikuwa akitetemeka kwa hasira na aibu. Ilikuwa ni kama amevuliwa nguo hapo mbele ya watu.
Alikuwa na hali mbaya, hawezi kuangalia mtu machoni. Aibu! Hali ile ya ugonjwa ikamrudia kwa kasi. Akasikia mtu akimshika bega. “Umefanya vizuri Tuma. Umeandaa kitu kizuri. Mimi nimependa.” Alikuwa Mbaki akimwambia kwa upendo, mpaka akamtoa machozi Tuma, akajifuta machozi kwa haraka na kucheka kwa masikitiko.
“Twende. Ukanimbie ulichokuwa ukinitafutia.” “Kwa nini unanifungia simu zangu Tuma?” “Acha kuanza kulalamika! Twende.” “Lakini unajisikiaje? Nimekuona umenyongea tokea mwanzo. Upo kama umekaukiwa! Nikataka kukuuliza lakini mama J akanivuta. Umenyongea Tuma, unakula vizuri kweli?” “Subiri kwanza.” Akamsogelea mama J maana alikuwa akipakulia vijana wake chakula.
“Naomba nirudi kesho kusafisha, tafadhali dada yangu. Nilikwambia sijisikii vizuri, acha nikapumzike.” “Pole.” Akacheka na kuondoka hapo. Walikuwa wakizungumza kwa sauti ya chini tu wao wawili.
Akamsogelea mke wa JJ. “Nakushukuru kwa muda wako na msaada mzima. Ni kweli hapa pamependeza sana. Asante, Mungu akubariki.” Akacheka. “Kama alivyosema mwenzio, umefanya kitu kizuri sana. Na hizo ndio akili tunazozitaka. Zakufikiria kwa haraka na kutenda. Nategemea kukuona nyumbani jumapili, Tuma. Usiache kuja.” Alikuwa amekinahiwa mpaka rohoni! Yaani mpaka mwaliko kama huo, wa kutoka kwa mtu kama mke wa JJ haukuleta maana tena. Hakutaka kusema jingine, ila akatumia akili ya haraka akamjibu tu, “Asante.”
“Hii keki ni nzuri Tuma. Nzuri sana.” Alikuwa JJ hata hajamgeukia mdogo wake, ila Jeremi akabaki na yeye ameduaa kama Jerry. Ila Jeremi yeye akawa akimwangalia Jerry na mambo yanavyokwenda hapo. “Asante kwa kuacha shuguli zako na kuja kujumuika na sisi. Mungu akubariki.” “Nisingeweza kukosa jambo zuri kama hili.” “Asante.” Akashukuru mpaka goti na kuondoka hapo.
Akamsogelea Jerry. “Uwe na usiku mwema na samahani sana. Sikukusudia kukuudhi.” Hakusubiria jibu, akamgeukia Mbaki. “Twende Mbaki.” “Aisee keki ni tamu!” “Acha ulafi Mbaki! Twende.” Wakaondoka Mbaki akicheka. Yaani shuguli aliyoiandaa Tuma, wakaishi kusherehekea wengine hata mlengwa mwenyewe hakuhusika. Alimuacha Jerry amesimama kama sanamu. Hajasogea wala kuongeza neno. Ni ameingia aibu zaidi ya Tuma? Hakuna ajuaye.
~~~~~~~~~~~
Wakapanda kwenye gari ya Mbaki. “Naomba unisindikize kwa wale madaktari wako uliokuwa ukiwalipa wanidanganye unaumwa.” Mbaki alicheka sana kwa sauti. “Muone!” Akaondoa gari hapo. Angalau Tuma akawa ameondoa sura yake hapo na aibu aliyokuwa ameingia.
~~~~~~~~~~~
Inaendelea...
0 Comments:
Post a Comment