Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Love At First Sight - Sehemu ya 98. - Naomi Simulizi

Love At First Sight - Sehemu ya 98.

Akiwa anajiwinda na huko alikotafutiwa kazi na JJ, yeye peke yake, mtoto wa kwanza wa mzee Salamba, Cory, akiwa bado hajafikiwa na mkono wa JJ, akahisi pengine ni kwa sababu sio kampuni yake, hana atakachoweza kumfanya, ila wasiwasihaukumuacha. 

Bado baba yao alikuwa hospitalini, Sandra na Rodrick wadogo zake wanapumulia mashine, hali tete kiuchumi, mambo ya kampuni hayaendi sawa, habari zao alishazipata jana yake siku ya jumatatu kuwa wanasaka pakuhamisha ofisi, JJ amewafukuza pale kiakili.

Akazidi kujiwinda. Siku hiyo akaingia ofisini mapema hata kabla ya bosi wake hajafika. Akaanza kufanya hata ambayo hayamuhusu. Kikao cha asubuhi kilipoisha hajaitwa ofisini kwa bosi wake, akahema kuwa na siku hiyo yupo salama.

Kwenye majira ya saa nne asubuhi, ndipo wasiwasi wake ukathibitishwa. Bosi wake akamfuata ofisini kwake. “Aisee nilisahau barua yako Salamba.” Akairushia mezani. Moyo wa Cory ukapasuka, paaa! 

“Barua tena! Nafukuzwa kazi nini!” “Inaweza kuwa ni habari njema. Fungua usome. Maana imetoka juu.” Akatoka hapo ofisini mwenzie akimwangalia. Ilikuwa ni ofisi ya watu wawili.

Barua ilikuwa ya uhamisho, kuelekea Ngudu, kufungua tawi jingine la hiyo kampuni yao ya TPDC, Shirika la Maendeleo ya Petroli TanzaniaAlishangaa Cory, hakuamini. 

Ngudu ni wapi?!” Akamuuliza mwenzie ambaye wapo ofisi moja. “Ipo wilaya ya Kwambi. Vipi?” Yaani akazidi kumchanganya Cory mtoto wa mjini ambaye tokea shule ya chekechea mpaka shahada yake ya kwanza alisomea Dar. Halafu shahada yake ya pili ya mambo ya Environmental Science alisomea chuo kikuu cha Rutgers, kilichopo mjini New Jersey, nchini Marekani. 

~~~~~~~~~~~

Kwa kuwa nyumbani kwao mambo yalikuwa safi, na akashindwa kubadili statuskutoka ya uwanafunzi ili kuweza kuajiriwa, Cory hakutaka kuwa mkimbizi, au mtumwa, nchi ya ugenini wakati kwao wanaishi kama wafalme. Alipomaliza chuo akapata mwaka mmoja wa Internship huku akihangaikia kubadili uraia. Alipoona mambo mengi, havieleweki, kusumbuana kwingi na Uhamiaji, kabla hajaaribu nchini Marekani, akaondoka kwa heshima.

Alirudi nchini, JJ ndio akamsaidia kupata kazi hapo TPDC kirahisi mno, akaanza kula mapesa ya kufa mtu. Alikuwa mchapakazi, ila kiburi cha pesa kilikuwepo. Sasa leo umwambie NGUDU!

~~~~~~~~~~~

“Umesema ni Kwimbi! Ndio wapi huko!!??” “Ipo Mwanza. Kwani vipi?” “HAIWEZEKANI!” Bado akawa haamini. “Hakika haiwezekani.” “Ni nini?” Akatoka na barua yake mkononi mpaka kwa kiongozi wake wa hicho kitengo aliyemkabidhi barua muda mfupi uliopita. 

“Mnataka kunituma Ngudu sijui Ngwidi, ambako mimi hata sipafahamu! Halafu Ngudu na petroli, wapi na wapi?!” “Yaani wewe ndio unaniambia kilichoandikwa humo ndani. Ilitoka kwa mkurugenzi tokea jana, ikachanganywa na mafaili yangu, ndio asubuhi hii nachambua, nakuikuta. Kwa hiyo kama kuna jambo halijakaa sawa, peleka juu. Ila Ngudu!” “Kukoje?” “Sijui! Nisikuchanganye, labda kuna makosa. Nenda juu.” Cory akatoka hapo kama faru.

Sekretari wa Mkurugenzi wa Idara ya Mipango na Uwekezaji akamwambia yupo kwenye simu, akimaliza atamruhusu aingie. Akakaa hapo nje akisubiria, mapigo ya moyo yakienda ndivyo sivyo! “Ngudu! Hakika hapana!” Akaendelea kuwaza kila akifikiria jinsi ya kuacha maisha yake aliyojijenga kwa thamani kubwa sana hapo jiji!

“Haiwezekani!” Akapinga kabisa. Ataachia mamilioni ya pesa yaliyokuwa yakiingia kama mshahara na posho nyingine, na wakati yapo tayari kwenye bajeti ya kila siku ya familia! Akazidi kuvurugikiwa hapo nje! 

“Hii kampuni si ya JJ tusema inaendeshwa atakavyo yeye na watu wake! Hapana.” Akapinga kabisa akisahau aliyemtafutia kazi hapo ni JJ na sio kwamba yeye peke yake ndiye aliyekuwa na uhitaji wa hiyo kazi, na kwamba hakuna mwingine aliyekuwa na vigezo vya kufanya kazi hapo! Walikuwa wengi, lakini hakushangaa kirahisi sana akapata yeye hiyo kazi! Akajisahau.

Sikio Halizidi Kichwa

Baada ya kama dakika 17 hivi akiwa amepotelea mawazoni ndio akaambiwa aingie. Akasalimia kwa heshima na kukaa.

“Nimepata barua ya uhamisho, kwenda kufungua tawi Ngudu! Natakiwa kuripoti huko siku ya ijumaa. Yaani juma hilihili!” Kimya akimtizama kama ambaye anamsikiliza. “Kwanza Ngudu kwenyewe sikufahamu. Pili, kwa nini iwe mimi?!” “Na kwa nini usiwe wewe?” Akamuuliza taratibu tu na kuendelea.

“Kuna mpango wakupanua shirika. Wewe ndio unaonekana unautaalamu, au niseme elimu ya kutosha juu ya hili. Tumekuwa tukifanya shuguli zetu vijijini na pembezoni mwa miji kupitia miradi ya usambazaji wa gesi asilia. Vituo vipo mbali na hapa Dar, ambako makao makuu yapo Dodoma. Kama unavyojua vituo vya usambazaji vipo mikoa ya Kusini tu. Mtwara na Lindi. Ndio tumeshauriana na makao makuu tukaona ni lazima kujipanua na Kaskazini.”

“Nani mwenye taaluma nzuri na uzoefu! Ndio umechaguliwa wewe. Kuna tatizo gani?” Cory hakuwa akiamini. Akijua kabisa hata iweje Cory hatakwenda, akaongea kwa hekima kabisa. “Yaani umepewa nafasi ya kwenda kuanza kitu chako, sehemu yako, wewe mwenyewe ndio unaongoza mambo, na utawezeshwa kwa kadiri ya uhitaji. Tatizo lipo wapi?” Mkurugenzi wake akamtupia swali jingine, nakushindwa kujibu.

“Kama hakuna laziada, nina simu nyingine ya muhimu natakiwa kujibu.” “Na nikishindwa kwenda?” “Ni rahisi sana. Andika barua ya kupinga uhamisho, itakayoeleza kushindwa kufanya majukumu yako. Lakini ukumbuke, kwa sasa hapa hauna nafasi yako tena. Nafasi yako ipo huko ulikotumwa.”

“Nikimaanisha hivi, mshahara wako, kuanzia sasa, na marupurupu yako yote, yanatokana na utendaji kazi wako kwenye ofisi yako mpya.” Akahitimisha na kunyanyua simu. “Nipo tayari kwa simu ya Makao makuu.” Akajua anamwambia sekretari wake apige na kumuunganisha na makao makuu, kwamba hapo mjadala umeisha.

“Kuna kitu hakipo sawa, na wewe unajua.” “Sijawahi kukusikia ukilalamika unapotumwa nje ya nchi kikazi, Salamba! Kiongozi wako anapokuwa akikupa barua za kusafiri kikazi, sijawahi kukuona ukija hapa kulalamikia safari hata moja na kuuliza kwa nini iwe wewe! Unakusanya posho zako kimyakimya na kwenda nchi tofautitofauti bila hata kuniaga! Kwa nini katika hili inakuwa kelele?” Hapo Cory akatulia.

“Kama huna la ziada, tafadhali nipishe.” “Mimi siwezi kuhamia Ngudu wakati nina familia yangu hapa jijini! Hawezekani! Kwamba nyinyi mnatenganisha familia!” “Halijawahi kuwa tatizo kwako mpaka sasa. Ulitumwa nje ya nchi kwa miezi 6. Kampuni ilikulipia garama zote. Sikukusikia ukilalamika kutaka kurudi kwa familia yako, ila kutumia miezi yako yote 6, kwa mafunzo mafupi huko nje ya nchi.”

“Na haikuwa mara moja. Sasa ili usinipotezee muda na mimi, unauamuzi mwingine, andika barua ya kuacha kazi, uondoke hapa kwa heshima. Ila vinginevyo, nitataka kukusikia umeripoti kituoni kwako siku ya ijumaa. Uwe na siku njema.” Cory akasimama na kutoka, maana mzee alishambadilikia.

Mwanzo Mpya, Umeanza

Wakati kwa kina Salamba kuna teketea, huku kwa Jerry ndio kulikuwa kuna nuru mpya ya tumaini. Walishajipanga wapi pakuanzia, nini chakuanza. Pesa si ipo! Nafasi ipo! Ilikuwa mipango tu. Mali bila daftari! Hawakutaka kupoteza chochote, wakawa walishaandika kila kitu, yaani hiyo ofisi ya Jerry ilishaanza siku ya jumatatu, wakichanganya mapenzi na kazi hapo kwenye apartment ya Jerry.

Siku hiyo ya jumanne utekelezaji ukaanza. Baada ya kifungua kinywa kizuri na penzizito la asubuhi, majira ya saa nne asubuhi hiyo ndipo wakafanikiwa kutoka hapo na kuelekea kwenye eneo ambalo wataweka ofisi yao. 

Palikuwa pakubwa, halafu pazuri. Uzuri hapakuwa katikati ya jiji, hakuna kupambana na foleni. Vyumba vilikuwa vikubwa, vimegawanywa. Vitatu vilijitegemea kama ofisi kuu, na kukawa na chumba kingine kikubwa sana ambacho wangeweza weka meza hata nne endapo wataamua kuajiri watu wengine zaidi.

“Hapa ni lazima kutafuta mtu wa kusafisha.” Tuma akacheka. “Kwamba unanipokonya kazi ya usafi?” “Kabisa Tuma. Ule mchezo wa chai inasubiria mpaka umalize usafi, halafu unakwenda kuwahudumia wanaume wengine kwanza!” Tuma alicheka sana.

“Jerry! Kule kwa wale mafundi sio kuwahudumia! Nilikuwa nikienda kuongeza sukari na majani ya..” “Iishie kulekule sio hapa. Hapa tunatafuta mtu wa kutusaidia wote. Nataka hicho kichwa kinisaidie kwenye mipango ya humu ndani tu. Tuna…” Simu yake ikaanza kuita. Akamuona anakunja uso.

~~~~~~~~~~~

Akapokea. Akaona Jerry ameshangaa sana. “Kikao cha nini tena!?” Akamsikia akiuliza kwa mshangao, na kuongeza swali jingine, “Na Mimi!?” Mpaka kajishika kifua. “Kwa hakika utakuwa hujamsikia vizuri. Mimi ni mtu wa mwisho kabisa kutaka kunisikia! Wewe mwenyewe si ulimsikia siku ile ya talaka!?” Akaongeza swali kisha kimya akisikiliza. 

Kisha akamuona amebadilika kabisa sura na kuondoka hapo akiendelea kusikiliza, ila baadaye akamsikia anajibu na sauti imebadilika kabisa. “Sina cha kuzungumza naye. Kama analolote, akwambie wewe. Tulishamalizana naye. Hanidai, simdai.” Kimya kwa muda. “Basi akwambie wewe, halafu wewe ndio utanifikishia ujumbe.”

~~~~~~~~~~~

Tuma alijua wazi anayezungumziwa hapo ni Sandra. Akaona atoke kabisa hapo ndani. Hayamuhusu. “Tuma! Tuma!” Hata hajafika popote akasikia akimuita ila si kwa sauti yake tulivu. Tuma akasimama. “Tuma!” Akatoka kabisa. Akamuona amebadilika ni mwekundu haswa.

“Mbona unaondoka na kuniacha?!” “Narudi.” “Kwa nini huniagi sasa?” Tuma akatulia akimwangalia kama anayemwambia tulia. Akaanza kujirudi. “Unakwenda wapi?” “Naangalia na huku nje. Narudi Jerry.” Akamsogelea. “Naomba tuwe tunazungumza Tuma. Sio kuachana tu bila taarifa.” “Ulikuwa kwenye simu. Na nisingechelewa kurudi. Twende nisindikize hapo nyuma. Nimeona kuna mlango kule wa kutokea huko nyuma, umefungwa, nataka kuangalia na huko nyuma kuna nini. Twende.” Wakazunguka kuendelea kuangalia.

“Funguo zote ninazo. Amenipa mlinzi.” Akafungua huo mlango wa nyuma kuingilia ndani. “Ni pakubwa. Na magari tunaweza kuwa tukiegesha huku nyuma.” Akamuona anajaribu kutulia ila bado. Tuma akaendelea kujizungumzisha, mlinzi akawafuata.

“Nina ombi.” Jerry akamgeukia kama Tuma. “Najua ndio mnaanza hapa. Kama mtahitaji msaada, nina kijana wangu anaweza akawasaidia shuguli zote za usafi na mkawa mnamtuma. Nimuaminifu sana. Hana mkono wa birika. Si mjeuri. Ni hivyo tu hakuwahi kubahatika kazi.” Tuma akamwangalia Jerry.

“Ana umri gani?” “Kijana mdogo tu.” Jerry akabaki akimtizama akisubiria ataje umri, lakini akaendelea. “Hata ukimuita sasahivi anaweza kuja, labda akwame tu nauli.” Alikuwa mzee wa makamu, si babu. Na alijua wazi JJ ndiye aliyempa kazi. Anapenda kuwapa kazi watu wa kawaida mpaka imlazimu sana kuipa kazi kampuni kubwa kama kwenye kampuni yake maana ni kubwa. Ila ofisi kama hiyo, ndogo tu, anampa mtu binafsi.

“Unasemaje?” Akamuuliza Tuma. “Kama ulivyosema, tutahitaji msaada. Naweza nikamtumia pesa ya nauli. Akaja leo tukazungumza naye.” “Ila nataka tutoke tukatafute vifaa vya ofisi.” “Anaweza hata saidia kuwabebea.” Akadakia huyo mlinzi.

“Mwambie awepo hapa saa nane kamili.” Jerry akahitimisha na kuingia ndani. Tuma akamgeukia huyo mlinzi. “Asante kwa msaada wa kijana wako. Anaitwa nani?” “Juliasi. Sisi tunamuita Juli. Nikijana mzuri sana mama. Atawafaa.” “Sawa. Naweza mrushia pesa ukamwambia ni nauli.” Akawekana sawa na huyo mzee akamfuata Jerry ndani.

“Naona mwanzo umekuwa wa baraka. Tumepata na msaada bila ya kuhangaika. Unataka tufanye nini sasahivi?” “Tutoke tukaangalie vifaa vya humu ndani, ila tusisahau kuna kukutana na…” Wakaweka mipango hapo siku ikaanza, Jerry akionekana hayupo sawa. Tuma akajiangalizia bila ya kuuliza, siku ikaendelea na hekaheka zake.

~~~~~~~~~~~

Vitu vilishushwa hapo kama kwenye saa 10 jioni. Huyo Juli akawa akijituma kwelikweli. Ila ananuka jasho haswa. Ofisi nzima ilijaa harufu yake. Mpaka inafika saa moja usiku, kukawa angalau vyumba vitatu vinasura ya ofisi.

“Sasa uchukue pesa, ukanunue deodorant. Kesho uje ukiwa umeoga vizuri na umepaka deodorant kwenye makwapa. Si unajua ni nini nazungumzia?” “Ndiyo.” “Na hizo nguo ubadili. Uje msafi ukiwa umeoga vizuri. Na vaa viatu sio hayo makobazi.” Tuma alijua tu kwa Jerry hilo asingeweza livumilia.

“Namaanisha ukitoka hapa, ukafanye manunuzi ya nguo nzuri za kuvaa hapa, viatu na deodorant. Oga asubuhi kabla hujaja hapa. Uwe msafi. Unielewa?” “Leo nimekuja kwa kukimbia. Baba aliniambia nisichelewe. Ila kesho nitakuja msafi. Asante.” Ukweli alionekana ni kijana mtiifu sana ila kama ambaye yupo kwenye dhiki! Akampa pesa, Juli akaondoka. Akawaacha hapo.

~~~~~~~~~~~

“Naomba na mimi nikuage niende nikalale kwangu leo.” “Kwa nini?!” Tuma akashangaa sana. “Tulilizungumza hili Jerry. Siwezi hamia kwako.” “Unanikimbia Tuma!” “Kwa nini unafikiria hivyo! Nilikwambia mwanzo kabisa. Siwezi kuishi kwako. Halafu kumbuka nina dhamana ya Eli. Siwezi nikapotea  pale wakati mama yake anajua mimi nipo naye! Kwanza haileti picha nzuri hata kwa Eli mwenyewe. Na mimi hayo maisha siyawezi Jerry. Nilishakwambia.” Huwa Tuma anamsimamo wake kwenye vitu vyake anavyovisimamia.

Huo usiku ukawa umeshaharibika kwa Jerry. Kashikwashikwa weekend nzima, akasahau yote. Amerudi Sandra, na Tuma naye anaondoka! Hapakuwa na jinsi ya kumkataza japo hakupenda kabisa watengane. Lakini Tuma si mkewe wala hajamlipia mahari! Mbaki mwenyewe aliyekuwa wanakaribia ndoa pia alimwambia hawakuwa wakiishi unyumba. Leo yeye analazimishaje?” ikabidi kwenda kumshusha kwake lakini kimyakimya.

~~~~~~~~~~~

Maisha yao ya kazi yakaendelea, ila Sandra akawa akisumbua haswa. Anamtafuta wakili wa Jerry ili azungumze na Jerry, Jerry naye hataki. Hilo likatengeneza tension hata katikati yao, Jerry na Tuma maana wakati wote Jerry anakuwa kwenye hasira ya Sandra.

Ikawa kama anayekumbushwa mabaya yake ya nyuma, kwenye maisha mapya. Akasimamia msimamo wake kama kumthibitishia Sandra, hayupo chini yake tena, hawezikumtawala kama zamani. Na Sandra naye hajui jibu la hapana. Akizungumza hili na wakili, akirudishiwa jibu, anamtuma jingine. Ikawa ni mazungumzo ya kwenda rudi, kwenda rudi. Kila mmoja ameshikilia pakali, Jerry hajui anazidi kuharibu kwake. Tuma kimya akijiangalizia tu akikumbushwa ndoa ya wazazi wake.

Maisha ya kazi yakawa yakienda vizuri tu. Wote wanajituma kazini, lakini wao wawili pakawa na tension. Tenda ya kwanza tu kupeleka kwenye kampuni ya JJ, kweli walivuna pesa, mpaka Tuma akashangaa kama kuna watu wanamapesa yote hayo hapo jijini. Bado walikuwa wakifanya kazi watatu tu. Wao wawili walikuwa wakimudu kazi kama kawaida na Juli akawa msaada kwelikweli.

Penzi La Kweli Hujaribiwa Kwa Gharama

Kadiri siku yao yakuondoka ilipokuwa ikikaribia, ndio uhalisia ulipokuwa ukiwajia wote wawili. Kutengana tena! Si kwa Pam tu peke yake, hata Mill mwenyewe alishaona ugumu wa kuondoka na kumuacha Pam. Maisha ya unyumba, familia iliyotulia, alishayazoea. Akayapenda, sio kama vile alivyoishi na Kisha. Leo anarudi nchini Marekani, bila Pam! Na yeye akanyong’onyea, kama hofu iliyokuwa ikimsumbua Pam ila kwa kuwa yeye alikuwa muendesha shoo nzima, ilibidi kupambana kiume, asionyeshe ila kuonyesha upo mwanga mbeleni. 

Maana walikuwa wakirudia njia ileile kama mwanzo, ila safari hii wakitegemea matokeo ya tofauti! Kwa hakika picha ya makubaliano ya mwanzo kati yao, ilikuwa ikimjia Pam kana kwamba yalitokea siku chache zilizopita, kumbe ni miaka zaidi ya 10, hawana mtoto hata mmoja, sasa wanategemea wa pili.

Mill aliondoka kwa ahadi nzuri sana akimpa matumaini makubwa kama hivyo tu! Lakini ikashindikana. Leo anarudi na maneno yaleyale, tena anaondoka na mtoto aliyelea kwa shida vile! “Akikwama tena huko! Ndio atanirudishia mwanangu ana mke.”Akabaki akiwaza Pam. Asijue Mill ndio zaidi akiogopa na safari hii kutofanikisha. 

~~~~~~~~~~~

Kamila alikuwa na mimba kubwa kuliko Pam aliyegundulika ujauzito mapema. Siku hiyo wanafanya tafrija ya kuwaaga Mill na Shema, alikuwa mstari wa mbele kuandaa hapo nyumbani kwao. Pam alikuwa amepoa mwanzo mwisho, wote walimuona. Ilikuwa ngumu kusema kinachoendelea kwa muonekano wake.

Wawili hao walikuwa wakiondoka siku inayofuata na ndege ya KLM ya saa sita na nusu usiku. Wakakusanyika nyumbani kwa Mill anakomuacha Pam. Walikula na kunywa ila pakawa na utulivu wa aina yake sababu ya alivyokuwa huyo Pam akiangalia wanavyoingia nakutoka hapo akikumbuka wema wa huyo Kamila na Mike kwake wakati akiwa na Mill. Alipoondoka tu Mill, na mahusiano yakafa vibaya sana. Hata simu ya salamu kutoka kwa Mike au hata kukosea kumpigia, hapakutokea tena ndio kuja kusikia kumbe alishafariki.

Hata kujaa huko na hekaheka zote alizokuwa akiona kina Komba wakifanya hapo alijua wazi wanafanya kwa ajili ya Mill tu. Akiondoka hapo, kugeukwa alikutegemea sana tu. Akabaki amepoa akijiangalizia tu, historia ya nyuma ikimtesa.

Wakafanya maombi ya pamoja, kuagana wakiwatakia kila la kheri kwenye safari yao, na Shema ambaye ni mgeni nchini huko. Wakafanya yao na kutawanyika Pam akiwa kama amepigwa butwaa muda wote.

~~~~~~~~~~~

Ulikuwa usiku wa simanzi, wakiagana. Ila zaidi Pam. “Usije ukapotea Mill! Na mambo yakiwa magumu huko, vikashindikana kurudi, naomba nirudishie mwanangu. Usije ukapotea naye huko miaka 10 mingine ndio ukarudi!” “Umejaribu kufikiria sababu yeyote inayoweza nikwamisha huko?” Kimya.

“Niambie tu, ili tuizungumzie. Safari ya kwanza ilikuwa inabidi nioe ili nipate uraia, nije kukuchukua. Safari hii sina sababu. Mpaka nyumba ipo kwa majina yetu sisi wawili. Hata nikifika huko nikataka kuiuza hiyo nyumba huko nchini Marekani, jua nilazimawewe uidhinishe.” “Kumbe!” Hata hakuwa akijua.

“Siwezi uza ile nyumba au hata kupangisha, bila saini yako, Pam mke wangu. Nimejifunga kwako.” Akamuona ametulia. “Niambie wasiwasi wako mwingine.” “Hata havijulikani!” “Mimi nakuhakikishia vinajulikana Pam. Sijaja huku kwa ajili ya Shema. Kwamba nimekaa na wewe muda wote huo, mpaka eti ndoa ili niweze kuondoka na Shema hapa nchini! Hapana Pam! Wewe ni mke wangu, na nakupenda Pam. Wewe nakupenda. Na safari hii hakuna kitakachotokea. Nitarudi mapema sana.”

“Kwanza kwa jinsi nilivyoangalia mambo, sidhani kama nitachukua muda mrefu.” “Kweli Mill!” “Hakika tena. Si tutakuwa tukiwasiliana na utakuwa ukinishauri! Na pia nilipata wazo jingine. Acha nimalize hili kwanza nisikuchanganye.” “Niambie tu labda itanituliza.”

“Nilikuwa nikizungumza na Jo, akanifanya na mimi nifikirie na kutamani kumuiga. Amesema baada ya ndoa, atasafiri na mama nchi mbalimbali ili hati yake ya kusafiria iwe na visa nyingi, ijulikane sio matapeli. Naona na sisi tuige. Na hivi tumeshahakikishiwa hauna matatizo! Nikirudi tufanye safari hata mbili, nje ya hapa, pamoja kama familia. Ilimradi tu kuonyesha tupo kama familia.” Hapo akampata Pam.

Angalau akaona kuna mipango ya kuwa pamoja na sio hivyo vyakuachana kwa muda mrefu. Hofu ya kutengana tena ndio ilikuwa ikimsumbua. Angalau usiku huo wakaagana kwa penzi la kina.

~~~~~~~~~~~

Mill alishaaga kazini rasmi. Akawataarifu Pam ndiye atakaye kuwepo badala yake. Alishamuomba na Colins kumpa ushirikiano mkubwa. Kwahiyo siku hiyo hakuwa akienda kazini. Akabakia tu hapo nyumbani Pam akisaidia kufungasha mpaka mama yake akamshangaa! Jana yake alikuwa watofauti, lakini siku ya safari yenyewe akaamka na kukutana na Pam wa tofauti, kumbe kama mwanamke mwingine yeyote, alitaka kuhakikishiwa kuna kesho ya pamoja na ipo mipango yakueleweka.

Usiku Mill na Shema wakaondoka nchini kurudi nchini kwao na kumuacha Pam na mama yake wakiwa wamesindikizwa na Jo. Mill alipata naye muda hapo uwanja wa ndege, tena kwa kujitenga kabisa akiendelea kumuhakikishia mapenzi yake kwake na kurudi kwa haraka.

Kwa maana, upumbavu wa Mungu una hekima zaidi 

ya hekima ya wanadamu(1Wakorintho1:25)

Ayvin alimaliza dawa. “Kuanzia sasa, tunaanza kumtoa kwenye koma ili kumrudishia uwezo wake mwenyewe wa kutumia kichwa chake kufanya mambo. Kama kuhema na mengineyo ili aamke. Kwa hiyo muda wowote kuanzia kesho, madawa yakianza kuisha nguvu mwilini, ataweza kuamka.” Hayo alikuwa akizungumza daktari aliyekuwa akimuhumia huyo mtoto.

Siku nne zikawa zimepita hajaamka. Hata waliojitahidi kuacha kwenda kazini ili wawepo hapo kushuhudia kuamka kwake wakashindwa sababu ya ajira. Walisubiria siku mbili mfululizo, asubuhi mpaka usiku mwingi, mtoto haamki. Ya tatu wakaanza kuagammoja baada ya mwingine kwa kumwambia Mina, kukiwa na mabadiliko yeyote yale, basi wapigiwe.

Mina akajikuta anabakia tena na mama yake tu. Ugonjwa umevuta! Familia hiyo ya kisomi wanamajukumu mazito. Hata Raza mwenyewe ni mwajiriwa, lazima aende kazini. Kwa hiyo kuja yake ilikuwa alfajiri akiwa anakwenda kazini, na jioni akitoka kazini. Anakaa kidogo anawahi kurudi nyumbani kumuwahi Polla. Msichana wake naye alishakimbia sababu ya maneno ya Paulina. Kwahiyo Raza na Mina wakajikuta wote hawana msichana wa kazi.

Mina hakuacha kumuombea mwanae ila safari hii hofu ikaongezeka maana haamki! Kinachomlaza hivyo ni nini na yeye hatumii madawa makali! Akazidi kuwa nawasiwasi akipiga magoti hapo pembeni ya kitanda cha mwanae bila kupumzika. Andy alishamtafunia mto mzuri wa kupigia magoti ili asijiumize.

~~~~~~~~~~~

Siku hiyo mchana yupo na mama yake. Amekaa kwenye kochi maana walishaomba hata huo mchana, yeye akabaki amepiga magoti. Kimya hapo chumbani. Mara chupa ya uchungu ikapasuka. Sasa sio kwamba Mina hakuwa anauchungu! Ulishaanza tokea asubuhi yake ila akanyamazia akificha mtu asijue zaidi mama yake, ili asije tolewa hapo kwa mwanae na kumlazimu kuhamia upande wa wakina mama, akiandaliwa kwenda leba. Akawa anagugumia maumivu ya uzazi wa mtoto watatu, kimyakimya.

Mama yake akashangaa maji sakafuni, pembeni yake. “We Mina?” Akajua ameshakamatwa, maana alikuwa akifikiria jinsi ya kuyafuta kabla mama yake hajayaona. Akili ilikuwa haifanyi kazi hata kufikiria hawezi kuzalia hapo.

“Chupa imepasuka.” “Lakini mimi nipo sawa kabisa. Na uchungu wangu unaweza hata kuchukua masaa 12, kwa hiyo usiwe na wasiwasi.” Akanyanyuka hapo kwenda kujisafisha, akabadili nguo hata hakuoga, akarudi akamkuta mama yake amefuta hapo chini, akarudi kupiga magoti.

“Ni lazima ukaangaliwe.” Kimya, ameinamia kitanda cha mwanae. “Mina?” “Mimi mjamzito nimeshasema sina uchungu. Unataka nitoke hapa, wakaniweke huko nikisubiria uchungu siku nzima pengine mpaka hata kesho, halafu nimuache mwanangu peke yake!” Akaanza kulia.

“Siwezi mimi nikamuacha mwanangu! Itakuwa nikumtelekeza kama asiye na thamani, kwa sababu napata mtoto mpya! Sio sawa kwake. Hata kama ataamka ni kipofu au tahira, bado ni mtoto wangu. Na anathamani kama ndugu zake. Nampenda mwanangu.”Akaendelea kulia, mama yake akajua hapo hatatoka na atakuja zalia sakafuni. Akasubiri amalize maneno yake na kurudi kumuombea mwanae.

~~~~~~~~~~~

Alipogeuka tu, akamtumia ujumbe Andy. ‘Mkeo atazalia sakafuni. Chupa ya uchungu ilishavunjika, hataki kwenda upande ule wa wakina mama. Na nahisi hata uchungu ulimuanza mapema sana leo asubuhi. Kuna jinsi nilimuona akihangaika, nikajua ni hali ya maombi, ila nina uhakika ni uchungu tu. Hana muda mrefu, atazaa.’ Andy alipopata huo ujumbe alishituka sana. ‘Nashukuru. Nakuja sasahivi.’

 Hapohapo akatoka kurudi hospitalini njiani akampigia simu Paul kumueleza. Akamwambia anamtafuta daktari wake. “Ila siku bado, Andy!” Paul akashangaa. “Nilihisi tu sababu ya hofu yakuona Ayvin haamki japo ameacha kupewa madawa. Hofu ndio imesababisha yote hayo na sitashangaa kuona na pressure yake ipo juu. Naomba na hilo umtaarifu daktari, ili wajiandae naye kwa lolote. Tafadhali Paul.” “Sawa, na mimi nakuja huko. Leo sikuwa na kazi huko. Acha niombe msaada wa haraka.” Akakata akiendelea kukanyaga mafuta. 

~~~~~~~~~~~

Andy akafika hapo kama ambaye alikuwa akikimbia. Akamkuta ameinamia kitanda. “Vipi?” Mumewe akamsogelea na kumshika, akaanza kulia. “Mina?” “Nahisi mtoto anatoka Andy!” “Si nilikwambia mimi!” Mama yake akahamaki ila sauti ya wasiwasi na hofu juu. 

“Endelea kuhema.” Akamnyanyua kutoka hapo sakafuni akamlaza kwenye kochi linalogeuka kitanda hapohapo. “Usiache kupumua na jilaze, usiogope. Kila kitu kitakuwa sawa. Naenda kuita msaada.” Akili ikamjia kubonyeza kengele kuita muuguzi huku Mama yake akaamua kumchungulia. Akaona kichwa cha mtoto. 

Alishituka hakutegemea. “Huyu mtoto anatoka, baba!” Andy kuangalia, kweli kichwa cha mtoto. “Huyu hafiki leba. Mtaua mtoto.” Nesi akaingia kwa haraka. Maana hapo si waitaji wa manesi kwamba wanasumbua. Kwa hiyo wakiita, wanasikilizwa.

Kufika kukutana na hiyo hali, na yeye akaafikiana na mama Ron. “Hawezi kufika upande ule ilipo leba. Acha niite msaada wa haraka.” Mina analia kwelikweli. Hofu sasa.

“Mimi sijazembea, Andy!” “Najua Mina. Naomba utulie. Wanakuja kukusaidia. Ila naomba endelea kuhema ili mtoto apate hewa. Ni kweli yupo mlangoni kabisa.” Hapo Andy mwenyewe anakaribia kuanguka kwa mshituko kuona kichwa cha mtoto! Hajawahi ona hayo tokea anazaliwa. Ila akajikaza.

         Baada ya muda wakawa wamefika daktari aliyepigiwa simu na Paul, na manesi wakijua mtoto ameshaanza kutoka. Akataka apimwe kwanza pressure. “Ipo juu!” Daktari akaongeza wasiwasi. Wakamuona anafikiria, kisha akamwangalia Mina.

         “Nafasi ya kuzaliwa huyo mtoto kwa njia nyingine mlango wake umeshafungwa, na yupo karibu sana. Jaribu kutulia, nitakuongoza taratibu, utakuwa sawa tu.” “Mama usiondoke.” Akasikika Mina akilia kwa wasiwasi. “Siondoki nipo mama yangu mzazi. usilie. Utaweza tu. Fuatisha kila kitu, utafanikiwa tu. Usiogope. Sawa?” Alimjua Mina mpenda kupendwa. Hapo akaanza kumbembeleza huku manesi wakiweka mazingira ya kujifungua.

         “Mbona hufanyi kitu! Mtoto atakufa!” Andy akagomba. “Hatakufa. Sasa nisikilize Mina. Nikikwambia sukuma, nataka usukume kwa nguvu zako zote, shika hata…” “Mimi.” Andy akapiga magoti kwa haraka. 

         “Basi minya huo mkono kwa nguvu zote, mtoto wako yupo tayari kutoka. Sawa?” “Sawa. sasahivi?” “Hapana, baada ya ….” Kabla hajamalizia uchungu ukawa umefika akamwambia, “Sasahivi sukuma.” Alipambana Mina jasho likimtoka na kelele humo chumbani, amemng’ang’ania mumewe kama atakayemvunja mkono. Lakinihakufanikiwa, akazidi kulia kwa hofu.

         “Sasa hivi nipe ya mwisho kwa nguvu zaidi.” Akazidi kulia. “Nimefanya kwa nguvu zote jamani! Sijaweza. Mimi nimezembea jamani! Nitaua mwanangu.” “Mina! Mina! Niangalie. Mtoto yupo karibu mno. Jaribu tena ya mwisho, kama ulivyofanya mwanzo, atatoka tu. Usilie na kupandisha pressure zaidi. Umenisikia?” Hapo mpaka kamasi zinamtoka.

         Akamfuta. “Sasahivi Mina. SUKUMA.” Daktari akamuhimiza. Alipiga yowe huyo akisukuma mpaka akajikuta anakaa kwa nguvu, ndio mtoto akatoka na kuanza kulia. Ndipo akarudi kujilaza akihema. 

         Kilio cha mtoto ndani, wakasikia nje wakishangilia. Kina Ruhinda. “Huyu mtoto si wakiume!” Akahamaki mama Ron. “Jike la nguvu.” Mina alifurahi, akakaa akilia haamini. “Ayana!” Hakutegemea. “Waliniambia sio yeye, ni kaka yake ndio yupo tumboni!”Alisikika Mina huku akitaka apewe mtoto wake. Akatayarishwa na kukatwa kitomvu, ndipo akapewa mtoto wake, haamini kama Andy. 

         “Tulionyweshwa kabisa ni wa kiume!” Andy akazidi kushangaa. “Makosa huwa yanatokea na ndio maana huwa hawakwambii ni kwa asilimia 100. Na pengine alijikunja kitomvi chake kikatokea kwa nyuma!” Bado hao wawili walikuwa hawaamini.

         “Kumbe Mungu alikuwa ameshanijibu!” Mina akawa anaongea akimwangalia Ayana. “Na huyu kakufanana Mina! Andy shuguli atakuwa nayo.” Andy akacheka kwa furaha, akijivuna, na kujisogeza karibu zaidi kama kujaribu kushibisha macho yake

Akajikuta akicheka zaidi kwa furaha. “Na amekimbia rangi yangu kabisa Ayana!” “Shangazi zake Mina mtupu huyo! Mpaka unyayo huo. Nakwambia hapo ujiandae baba.” Andy akazidi kucheka kwa furaha akimuangalia mrembo wake. 

“Eti Ayana! Dad aongeze urefu wa ukuta?” Mpaka manesi wakacheka. “Eti, upo kama kaka Ayvin? Maana naye kadiri anavyokuwa, anazidi kukolea rangi ya mama yake!” Hapo Andy akajikuta anageuka kumwangalia Ayvin pale kitandani alipokuwa amelala muda wote, na ndipo kukutana na muujiza mwingine!

Akakuta Ayvin ametulia tuli, amefungua macho, kimya kitandani anaangalia juu.

“Ayvin!” Akashituka sana. Kumbe kelele za mama yake akijifungua mdogo wake ndio, zilimzindua. Andy akamkimbilia nusura aanguke maana alijikwaa na vitu hapo sakafuni vilivyokuwa vikimsaidia Mina kujifungua.

         Naye Mina akataka kukaa kwa mshituko, haamini kama Ayvin amemka. “Bado tunakusafisha Mina. Tulia kidogo.” “Mlete Andy.” Sasa Andy akawa amepatwa na wasiwasi vile alivyokuwa ametulia pale kitandani anaangalia sehemu moja, akajua amekuwa kipofu.

         “Ayvin?” Akamuita taratibu akimshika. Aliponyanyua vimikono vyake ambembe, Andy akajikuta akicheka na kilio. “Kumbe unaniona!” “Jamani tuingie?” Sauti ya mama Ruhinda. “Wewe tu ndio unaweza kuingia, uje ushike jike la nguvu! Na kaka yake ameamka kutusaidia kulea.” Alikuwa mama Ron. Mama Ruhinda akaingia kwa furaha kwelikweli.

         Yaani hiyo kwao ikawa double blessing kwa kina Ruhinda. Kwa Mina akathibitisha ukuu na uwezo wa Mungu kama ilivyoandikwa katika kitabu cha Daniel 4:17&32 ‘Aliye juu anatawala katika ufalme wa wanadamu, naye humpa amtakaye, tena humtawaza juu yake aliye mnyonge.’ 

Na mstari wa 32 kitabu hichohicho, unamalizia kwa kusema, naye humpa amtakaye, awaye yote.’

Alitokea chini, akikuzwa na mshahara wa mwalimu aliyeachika na kutelekezwa. Asiye na kitu, ila kung’ang’ana magotini na Mungu wake, akimuita Yesu wake mchana na usiku, akipambana kulea wanae hao wawili.

Mungu wake amemjibu ni kama kwa kuchelewa, ila kupitia Mina, mtoto aliyemsumbuamchafu ananuka kwa dhambi, ndio Mungu akawaaibisha wenye hekima, kwa kumnyanyua huyo yeye. 

Ameonyesha uwezo wa kutoa kwake, kwa kumpa Mina watoto watatu huku akiwajibu wasomi kina Ruhinda kuwa, akili zake yeye Mungu hazichunguziki hata kwa vyombo vya kitekinolijia, na ni mtenda muujiza. Zaidi anajibu kwa wakati.

Mahusiano yake na Raza yakawa imara kuliko mwanzo. Mina akapata dada na rafiki ambaye hakuwahi kufikiria kama angeweza mpata. Ile imani yake kwa Raza, iliwaadabisha wote waliosikia. Huyo Mina akafanyika mama hata kwa watoto wa Raza, zaidi Poliny ambaye alishangazwa na imani ya anti yake kwa mama yake ambaye yeye mwenyewe aliishia kumuhukumu huyo mama yake akiamini alimsukuma Ayvin.

Paulina ilibidi kupunguza sana, japo ni tabia aliyogoma kubadilika. Ila kwa wawili hao, alinyanyua mikono. Hata yeye Paulina alishindwa kupenya katikati yao kwa msingi wao walioweza kujenga kuanzia chini kwenye fedheha.

Ni kama Mungu naye alimjibu Raza kupitia uzazi wa huyo Mina. Akampa Ayvin. Ikawa ni kama anaishi nyumba mbili, na Raza kama mama yake kabisa. 

Akizidisha fujo kwao, basi anafungashiwa mizigo yake, anapelekwa kwa Raza ili Mina atulie na Ayana wake. Akazidisha utundu, ila uchekaji vilevile. Ikawa kama ni mtoto wa Raza, maana naye akafanyika ushuhuda wake. Kwamba ni kama alikufa, Mungu akamfufua na kumrejesha.

Huo ndio mwisho wa wakina Ruhinda.

~~~~~~~~~~~

Sandra amerudi kwenye maisha ya Jerry na safari hii amemkuta tena kwenye mahusiano na Tuma. Amefanikiwa kuweka tension kwao hata penzi zito lililokuwepo limekuwa tatizo

Je, na safari hii atafanikiwa kumtoa Jerry kwa Mina kama alivyofanikiwa kwa msichana wa kwanza wa Jerry aliyekuwa amepanga kumuoa?

Ikiwa Tanzania ni moja ya chini zimefungiwa kuingia nchini Marekani, Mill bado ana imani ya kumvusha Pam. Safari hii ameondoka na Shema kwa ahadi ya kurudi. Watafanikiwa?

Inaendelea…

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment