Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Love At First Sight - Sehemu ya 93. - Naomi Simulizi

Love At First Sight - Sehemu ya 93.

Pius alitoka hospitalini akiwa na hukumu moyoni, njia nzima mawazo kwa mkewe. Kwanza akimuhurumia. Akaendesha mpaka nyumbani kwake, akakuta nyumba imetulia kuashiria kila mtu amekwenda kulala, ila chakula chake kipo mezani. Kwa jinsi kilivyopangwa, akajua ni Raza tu.

Akaingia chumbani, hakumkuta. Akaamua kuoga kabisa. Ilishakuwa ikienda saa nne usiku. Kwani wote waliondoka hospitalini na kumuacha Mina na mama yake. Ilimbidi Andy aondoke na Ayan kwa ajili ya shule kesho yake. Na Mina alimtia moyo mumewe akapumzike kwa ajili ya kazi kesho. 

~~~~~~~~~~~

“Huna utakachofanya hapa. Nenda tu, tusiharibikiwe kotekote. Tugawane. Wewe kazini, mimi hapa na Ayvin.” Mina alimwambia mumewe akiwa ametoka naye nje wanazungumza, wengine wapo ndani. “Na huyu kaka mkubwa anahitaji kulala. Nenda tu, nitabaki na mama.” Akafikiria na kuona ni kweli. Mina asingeweza ondoka hapo na kumuacha mwanae, na yeye anahitajika kazini.

Akatumia akili. Akaingia ndani na kuomba wote wafunge siku kwa maombi, na kuwaambia Mina anatakiwa kupumzika. Wakajua ndio anataka waondoke hapo. Walipoomba kwa pamoja, ndio wakaondoka wote. Hapo ndipo na yeye Andy akaondoka na Ayan aliyekuwa amelala. Ron alishamrudisha mama yake nyumbani, akaoga na kuchukua nguo baadhi ndipo akarudi hospitalini kuwa na Mina.

~~~~~~~~~~~

Pius akala ndipo akaamua kumsaka mkewe aliyejua atakuwa chumbani kwa Poliny. Aliingia bila hata ya kugonga. Alishituka Raza! Alikuwa amepiga magoti, akasimama kama akimbie pale Pius alipofungua mlango na kumuona ameingia. Akasogea mpaka mwisho kwenye kona akijifuta machozi aliyokuwa akimlilia Mungu wake. Pius akamuhurumia sana, akizidi kuhukumiwa.

“Pole.” Raza hakuamini, akaangua kilio hicho, kama aliyefiwa. Akamsogelea pale alipokuwa ameegemea ukuta akilia. Akamgeuza na kumkumbatia mkewe. “Pole.” Bado hakuwa akiamini kama anapewa pole, maana alijua safari hii, kwenye hili, hatakuja iona tena sura ya Pius.

Anavyompenda huyo mtoto! Zaidi ya nafsi yake, kama Poliny! Hutoa muda wake wote kwa hao wawili. Alijua hakuna lugha atakuja kuzungumza naye, akaelewa. Akambembeleza kwa muda wakiwa wote wamesimama hapo mpaka akatulia.

~~~~~~~~~~~

 “Twende tukazungumzie chumbani kwetu.” Akamshika kabisa mkono na kutoka naye hapo ila akiwa na wasiwasi hajui ni nini kinaendelea.

“Asante kwa chakula.” Akaanza mara walipokaa. “Karibu. Vipi hali ya Ayvin?” “Hali sio nzuri, Raza.” Akaanza kulia tena. “Kwani ilikuaje?” Ndipo akamuuliza. “Hata nikikueleza huwezi niamini Pius, lakini mimi siwezi mdhuru Ayvin. Na mimi kwangu amefanyika faraja, mpaka nashangaa! Siwezi mdhuru.” “Hata Mina anaamini hivyo. Anachotulaumu nacho Andy ni kuona ni kama tulizembea. Kwanza kutoweka kile kigeti alichotushauri tuweke, na kumuacha bila ya uangalizi.” Ikawa kama hajasikia kwa hofu ila ikabidi ajieleze.

“Nilimuacha na kina Judy nikiwa nafuata simu chumbani, nikiamini hajaniona. Ilikuwa nije kwa haraka, nichukue ili hata ukinipigia, usinikose. Sikujua kama alikuwa akinitafuta maana nilimuacha katikati ya michezo mingi.”

“Nikiwa najua nipo peke yangu huku juu, kila mtu nimemuacha chini, akili imezama kwenye simu, nikahisi kitu kimenigusa. Nilishituka Pius. Na ndipo nilipomsukumampaka kujigonga. Ile nataka kumdaka, akaniponyoka mkononi na ikawa ndio kama nimezidi kumsukuma.”

“Ila Mungu wangu nishahidi Pius, si katika ulimwengu huu ambao wewe upo au haupo, siwezi mdhuru Ayvin. Kwanza ananipenda na ananipa faraja ya ajabu hata mimi sielewi imekuaje!” “Hata mama yake amesema.” Raza akabaki akimtizama mumewe na machozi yakimtoka.

“Mina anajua kwa hakika hujamdhuru Ayvin.” “Kweli Pius!?” “Kabisa. Anakutetea kwa kila mtu.” “Nimemsikia msichana wake akinisema kuwa wameniona  nikimsukuma mtoto!” “Ndicho walichoshuhudia kwa upande wao, na ndicho walichosema. Ila kwa namna ya ajabu sana, ambayo hata mimi sikutegemea, japokuwa walisema wamekuona ukimsukuma Ayvin, Mina ameshindwa kuamini kama unaweza mdhuru Ayvin.” Raza alilia sana, ASIAMINI.

“Naomba tuombe wote Raza, mwenzio sijui kuomba! Najiona sina msaada wowote ule, na hali sio nzuri. Ukweli ambao hata Mina hajui ni kuwa Ayvin anaishi kwa mashine tu. Yaani endapo ile mashine ikitolewa hata sasahivi, yule mtoto ndio basi tena.” Akazidi kushituka.

“Andy ameomba asiambiwe kwa undani huo kwa hali yake ilivyo. Anahofia mimba isije toka, akapoteza na huyu mtoto mwingine. Lakini hali sio nzuri Raza. Sio nzuri kabisana sijui chakufanya.” “Nisamehe Pius, nisamehe mume wangu. Ayvin ni kiumbe wa mwisho naweza mdhuru.” “Najua Raza. Naelewa.” Wakatulia Raza akijifuta machozi.

“Basi tuombe wote. Omba na mimi, mwambie Mungu wako afanye muujiza, amponye Ayvin.” Akasikika Pius kufika mwisho kabisa. Hata pesa yake haina kazi tena. Raza akamuhurumia mumewe. Alijishusha, hajawahi kumuona Pius mwenye hofu ya kiasi hicho, maana akawahi kupiga magoti kabisa.

“Na nakuomba kesho ukamuone Mina.” “Naogopa Pius! Naogopa hata kuionyesha sura yangu kule.” “Sio kwa Mina. Kuna jinsi anakuchukulia!” Akawa kama asiyejua jinsi ya kuieleza.

“Lakini naamini ukienda, ukawa naye, na kuomba naye, utamtia nguvu. Nyinyi wote mnaamini kwenye kuomba. Msitengane.” “Unauhakika Pius? Nisije nikaenda nikaharibu zaidi.” “Si kwa Mina. Nina uhakika mkiwa pamoja itasaidia. Mina anakupenda na kukuamini sana, Raza. Sivyo hata mmoja wetu alivyodhania! Hana hukumu na wewe, na yeye ndiye ametuambia sasahivi upo kwenye maombi yakumuombea mtoto.” Raza hakuamini, ila akashindwa jinsi ya kuuliza.

“Tuombe, upumzike, kesho tuwahi hospitalini.” Raza alitiwa nguvu kwa ajabu sana. Hofu ikaisha, ikaongeza ujasiri baada ya kujua Mungu wake anapigana vita yake na anamtetea. Akapiga magoti pembeni ya mumewe wakaanza kuomba, Pius akimsikiliza kwa makini vile anavyoomba. 

~~~~~~~~~~~

Alipomaliza tu, Pius akaenda kumletea chakula akimsihi ale japo kidogo, na kuendelea na maombi kesho yake. Raza akamshangaa Mungu vile anavyo bembelezwa! Kutoka kwenye kujiona yupo hatiani, gafla anageuka kuwa wamuhimu! Mumewe akimbembeleza, mpaka akahisi anataka penzi usiku huo. Lakini akalala bila hata ya kumgusa kimapenzi, ndipo akajua kweli hali ya mtoto imemkamata. Akamuhurumia akishindwa jinsi ya kumsaidia.

~~~~~~~~~~~

Aliamka akidhania ni wa kwanza kama kawaida, lakini akamkuta Pius amejilaza tu hapo kitandani. “Pole Pius, pole sana.” Akavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu. Akamgeukia. “Nawaza vile Mungu alivyo! Ni kama alinionjesha tu mapenzi ya huyu mtoto halafu…” “Usikate tamaa Pius. Tafadhali naomba tutamke uzima.”

“Najua inaogopesha, lakini sisi tuamini Mungu hajampitisha tu huyu mtoto kwenye maisha yetu ila alitupa kwa upendo. Nimetubu kwa kuzembea. Naamini Munguamenisamehe.” “Ni wote Raza!” “Basi Mungu ametusamehe pale tulipokosea. Atapona. Na wao watanisamehe na kuja kutuamini naye tena, atakuja kurudi tu hapa. Tuombe.” Raza akaomba kwa kifupi ili awahi.

~~~~~~~~~~~

“Na mimi nafunga kama wewe, Raza. Usinitayarishie kifungua kinywa. Msaidie Polla, halafu uje tujiandae, twende.” “Basi nimtengenezee kitu na Mina. Sitakawia.” Akatoka hapo chumbani kwa haraka. Kwa asili huwa Raza analimudu jiko. Hakuchukua muda mrefu hapo jikoni akawa amesharekebisha mpaka cha kupeleka hospitalini.

Akarudi chumbani kujiandaa wakatoka hapo bado alfajiri tu.

~~~~~~~~~~~

Japokuwa aliambiwa Mina hamuhukumu, lakini bado mtoto alianguka akiwa naye. Hofu haikumuacha, hajui akifika atamuanza vipi Mina! Akabaki kimya njiani. Na kwa kuwa na Pius alikuwa na yake kichwani, hata hakumuongelesha. Kimya kimya ila mwishoe mkewe akaanza kuomba akimsihi Mungu asimuache huko katikati ya macho ya watu, zaidi Mina na Andy.

~~~~~~~~~~~

Walifika alfajiri hiyo wakamkuta mama yake amelala kwenye kochi hana habari, Mina amepiga magoti pembeni ya kitanda cha mwanae. Wakamuhurumia sana, na kujua wao ndio wakwanza kupita hapo.

Pius na Raza wakabaki wamesimama kwa muda hawajui wasalimie au la! Mina alikuwa ameinamisha uso, mpaka wakahisi pengine amepitiwa na usingizi. Pius akamtizama Raza kama yeye ndio anaelewa zaidi, afanye kitu.

Akamgusa. Mumewe amebakiwa na kikapu cha chakula mkononi. “Pole Mina.” Akanyanyua kichwa kumtizama. Walipoona uso umejaa machozi, wakajua hakuwa amelala. “Njoo tuombe wote Raza. Wewe Mungu anakusikia.” Raza akajisikia vibaya zaidi.

“Hata wewe anakusikia, Mina. Pole.” “Njoo nisaidie kumsihi Mungu, anitolee mwanangu hapa kitandani.” Raza akapiga magoti pembeni yake. Pius alivyoona vile na yeye akaweka kikapu pembeni, ndipo mama Ron akaamka. Nakuona Mina na Raza wamepiga magoti. Akajisikia vibaya kukutwa amelala hana hata habari ya mgonjwa na huyo Mina mwenyewe.

Akamsalimia kwa sauti ya chini kama asisumbue wanao omba, kisha akaenda kupiga magoti pembeni ya mkewe. 

Na yeye akaenda kuosha uso, na yeye akaenda kupiga magoti pembeni ya mwanae, wakaendelea kuomba, Raza akiongoza hayo maombi, akimsihi Mungu atende muujiza.

Mwisho Wa Ahadi Za Milele

Ilikuwa ni saa 12:30 asubuhi wakati Jerry akiegesha gari nje. Tuma akatoka. “Leo ulilala?” “Kwa shida sana. Ila nilipopitiwa na usingizi, nililala mpaka asubuhi alamu iliponiamsha.” “Kwanini hukulala tena?!” “Nilikuwa natamani kuendelea kukuwekamkononi tu.” Tuma akacheka na kujifunika uso akiwa ameelewa. 

“Na wewe ulilala?” “Sasa mwenzio nimelala nikiwa na furaha, hata sijageuka mpaka alamu. Ningekuazima usingizi wangu.” Akacheka akiendelea kuendesha mpaka kazini.

Walifika hapo kama kawaida yao wakwanza. Akaanza kusafisha wakati Jerry yupo ofisini akimsubiria wapate kifungua kinywa ndipo atoke. Akamaliza na kwenda kumuita. Akatoka bila ya kuchelewa, wakakaa na kuanza kupata kifungua kinywa pakiwa pametulia, wao tu wawili. 

Kabla hata hawajaanza kuteta yao, akaingia mama J na mumewe. “Tuma?” “Njoo huku jikoni tupate kifungua kinywa.” “Sisi, tulishakula.” Akaingia hapo jikoni na mumewe. “Kwani kikao chenu ni saa ngapi!?” Jeremi akamuuliza kaka yake akihisi ni kama ametulia sana, kana kwamba hakuna kinachomtokea siku hiyo!

“Tatu na nusu.” “Huofii kuchelewa!?” “Natoka muda si mrefu. Vipi nyinyi?” Akamuuliza akiendelea kula. “Safi tu. Nimekuja kukuona kabla ya kikao.” “Mimi nipo sawa.” Akajibu akimalizia kikombe cha kahawa.

Akasimama. “Bro alitaka nikusindikize.” Tuma akamsikia akimwambia kaka yake. “Nipo sawa. Wewe endelea na kazi. Kukiwa na lolote nitawajulisha. Halafu nitakapoondoka jumatano gari nitamuachia Tuma imsaidie usafiri.” Akasikia kimya, mama J akamwangalia Tuma. Akacheka na kujifunika uso. 

“Wewe vipi?!” Akamsikia Jeremi anaanza kucheka baada ya kuulizwa na kaka yake. 

“Hukuwa hivyo Jeremi! Ni nini?!” Akacheka kwa sauti zaidi. “Nitawaona baadaye. Na mtu asimuulize Tuma swali lolote.” Mama J akaanza kucheka na yeye kama mumewe, kishabiki. 

“Zaidi wewe Hilda. Mwacheni kabisa. Maswali yote msubiri mje kuniuliza mimi. Naomba nisindikize Tuma.” “Jerry unaupendeleo! Mimi nimejitolea kukusindikiza umenikatalia, lakini Tuma unafanya kumuomba kabisa!” Tuma akakimbilia nje, Jerry akamfuata akicheka kama Hilda.

~~~~~~~~~~~

Akamsindikiza mpaka kwenye gari. “Naamini mambo yatakwenda haraka, mchana nitakuwa nimerudi.” Akabaki ameinama dirishani, Jerry amekaa. “Nitarudi Tuma. Niamini nitarudi.” Akatingisha kichwa bila ya kumwangalia na kuondoka hapo garini, akaelekea stoo. “Hawa ni wanandoa wa kanisani. Wanahistoria. Akifika huko na kuombana msamaha vikafana!” Ndio ulikuwa wasiwasi wa Tuma. Ila Jerry akajua maneno pekee hayatamuaminisha ila matendo. Akaona awahi tu akija mtafuta amwambie yupo single.

~~~~~~~~~~~

Hakuna popote kunakovunjwa agano la Mungu kukawa rahisi, kusijulikane lipo jambo baya limetokea. Huko kwenye kikao cha kuhitimisha agano la ndoa, walikutana kwenye ofisi ya huyo mwanasheria. Alikuja Sandra amependeza kama kawaida yake, ila mikono mitupu. Jerry kimya akiwa amelitegemea hilo lakini hakujua kwa umbali alioenda safari hii huyo Sandra.

Baada ya salamu kwa Sandra aliyechelewa dakika kama 10 hivi na yeye akawa amekuja na wakili wake, akaenda moja kwa moja kwenye lililowakutanisha. “Naona talaka yenu haina mambo mengi, Jerry ameamua kukuachia kila kitu.” “Kwa sababu ni VYANGU.” Yule wakili akamwangalia na kuendelea. 

“Pitia nyaraka zote kisha uweke saini.” “Ni mpaka wakili wangu naye asome ajiridhishe.” “Sawa.” Jerry kimya.

Huyo wakili alikuwa kijana mtanashati haswa. Safi juu kichwani mpaka kiatu alichovaa. Akasoma na kuridhika. “Ameweka wazi kuwa kila kitu anakuachia.” “Hiyo mbona ndivyo ilivyo! Mali zote zilikuwa ZANGU! Sikutegemea vinginevyo.” “Acha nikwambie Sandra, sijui wapi unakotolea taarifa zako, lakini chochote mlichochuma ndani ya ndoa ni chenu. Kwamba mlitakiwa…” “Acha tu. Acha.” Jerry Akamkatisha.

“Mwenyewe huyo anajua ndio maana hathubutu kudai hata shilingi.” “Kama mmekubaliana na kilichoandikwa huko, naomba uweke saini yako tumalize kipengele cha ndoa.” “Haina shida.” Sandra akasaini kwa jazba tu. Akamkabidhi na Jerry akasaini. 

Akazipitia yeye kama wakili akaridhika. “Kwa hiyo kwa mujibu wa sheria, nyinyi siwanandoa tena.” “Afadhali!” Sandra akadakia ila si kwa sauti ya juu, kejeli na tabasamu kama aliyetuliwa mzigo.

Jerry kimya. “Ila kuna swala la watoto.” “Watoto gani?!” Hapo Sandra akahamakihaswa. “Nyinyi mmezaa watoto wawili, ambao…” “Sema mimi nimezaa watoto wawili! Sikumuona akinisaidia kusukuma hata mmoja kule leba. Abishe hapa atuonyeshe tumbolililobeba mtoto.” Jerry kimya.

“Hilo hakuna atakayekubishia. Ila kumbuka nyinyi ndio mmetengana, lakini bado Jerry wale ni watoto wake na watabaki kuwa ni damu yake.” “Hilo ameligundua lini?! Muulize tokea ameondoka nyumbani amejisumbua hata kuwaulizia hali?! Anajua wana hali gani na wanakula nini?” Akamgeuzia kibao kwa haraka sana akifoka kama kawaida yake huwa hakosi makosa ya Jerry.

“Yeye ametelekeza familia, hata simu ya salamu ilimshinda kupiga kujulia hali watoto anaojidai kuwaulizia sasahivi! Huo si unafiki tu mbele za watu kuonyesha anajali watoto ambao hata nyumbani hakuwa na mahusiano nao mazuri! Kutwa kulalamikiawanangu! Sasa mwambie huyo unayemwakilisha, siku alipoamua kuondoka nyumbani, ndio ameondoka kwenye maisha ya watoto wangu. Kama hamna jingine nataka kuwahimajukumu yangu.” “Sandra,.…” “Sawa. Ni sawa tu. Acha.” Jerry akamuwahi akitaka asimbishie.

“Lakini unawanyima watoto wako wewe mwenyewe haki ya kuwa na baba, Sandra! Unawapokonya…” “Kwa baba yupi!? Ni nini wanatakiwa wajifunze kwake huyu! Hata wao wanamjua. Hajigusi kwa matunzo yeyote kwa wale watoto anaotaka kukudanganya hapa anawataka! Hata wao wakija hapa hawana hata soksi iliyotoka kwa baba yao. Baba jina!? Acheni ujinga.” Hapo Sandra anawaka kwelikweli, mpaka wakili anamtukana!

“Mnataka kuharibu vijana wangu wawe wazubavuWajinga hawajui kuchapa kazi! Mwanamme ukimwambia kazi, anakimbilia weekendUlalamishi hauishi, kazi ni za kumsimamia na kumpa muda wa kumaliza! Kweli mnataka watoto wangu waendelee kukua na kuzungukwa na mfano mbovu huu! Acheni kunichezea akili. Kama kuna aliyenisaidia kusukuma hata mmoja leba, ndio nimsikie akizungumza hapa. Vinginevyo msinipotezee muda wangu.” Akasimama.

“Jambo la mwisho.” “Naona wewe unachokifanya sasahivi ni kunitibua. Jerry si mume wangu tena. Unachoniweka naye hapa ni nini!?” “Nilikutumia orodha ya vitu vyake binafsi alivyoomba umletee. Viko wapi?” “Kama kuna chochote alikiacha kwangu kwa muda wote huo ambao alishindwa kuvifuata wala kuwasiliana kusema anavihitaji mpaka jana, basi nilijua hahitaji, NIMECHOMA moto.” Jerry alishituka hakutegemea.

“Kwamba na vyeti vyangu vya shule pamoja na hati yangu ya kusafiriaumechoma!?” “Kwangu siweki takataka na wewe unajua Jerry. Kila kitu kinakaa sehemu yake, vingenevyo ni UCHAFU. Ulipoacha vitu vyako kwangu kimyakimya kwa muda wote huo bila kusema kitu, nilijua huvihitaji! Tumekusanya mpaka mswaki uliokuwa ukitumia, tumetupa jalalani na kuchoma moto.”

“Kama huamini nina video za kuchoma vitu vyako nikiwa nimemaliza na wewe ramsi. Kama ulivyosema, hunidaisikudai. Muwe na siku njema.” Kama utani, Sandra akatoka. 

JJ WA ACTION.

Hakika Jerry alitokwa na machozi. Hakusema kitu akaondoka hapo mpaka kwenye gari na kushindwa kuondoa gari akabaki ameduaa. Wakili akampigia simu JJ kaka yao mkubwa. Akamueleza mambo yalivyokwenda bila kumficha, na maneno yote ya Sandra.“Nimekutumia nilivyomrikodi kwa siri. Najua ni kinyume cha sheria, lakini nilitaka umsikie mwenyewe.” “Nashukuru, nitakuwa nayo makini isisambae. Jerry yuko wapi?” “Ametoka.” “Basi nakushukuru sana kukamilisha hilo. Asante.” Simu ikakatwa.

~~~~~~~~~~~

Shida za maisha zilimfundisha JJ kufikiria kwa haraka na kuchukua hatua bila ya kuchelewa. Kila anapopata changamoto, kabla halijamvuruga na kushindwa kufikiria, anatabia ya kutafutia suluhu kwa haraka ndipo anaweza kuanza kulitafakari na kuumiakama mwanadamu.

Walimjua jinsi alivyo mwepesi wa kutafakari na kutoa suluhu. Baada kama ya dakika 20 akampigia Jerry. “Wahi Uhamiaji, kuna mtu anakusubiri achukue taarifa zako, akutengenezee hati ya kusafiria, ili jioni waifuate washugulikie Visa. Halafu tutakaporudi tutashugulikia vyeti vyako vingine vya shule. Vinaweza kuchapishwa na ukapewa. Nijulishe mambo yatakavyokwenda huko. Nakutumia jina la mtu anayekusubiria na namba yake ya simu.” “Asante.” Simu ikakatwa. Angalau hilo likamfariji ila alikuwa ametibuka, hajui hata akifungua mdomo atazungumza nini.

Alichokifanya ni kwenda kuacha taarifa zake ili kusaidia kutengeneza hati yake ya kusafiria, akarudi kwake.  

~~~~~~~~~~~

Akamtumia Tuma ujumbe. ‘Mambo hayakwenda kama nilivyotarajia akili imevurugika kwa sasa nashindwa kufikiria vizuri, ila nashukuru Mungu kwa upande wa talaka tumemalizana. Naomba nivumilie, Tuma. Nahitaji kutulia. Nina hasira zakupitiliza. Leo sitarudi hapo kazini. Nitakuja kukuchukua jioni. 12:30 nitakuwa hapo. Pole na samahani.’ Tuma akasoma na kutulia kwa muda akitafakari. Mwishoe akamjibu. ‘Pole.’ ‘Asante.’ Hiyo siku ikaendelea. 

~~~~~~~~~~~

Saa sita mchana akaingia hapo Umi. “Shoga nimerudi.” Tuma akacheka akiwa na yake kichwani. “Ila mama J yupo hapo nje anamalizia kuongea na simu, anakuja sasahivi.” “Mmekubaliana nini?” “Siku akiamka huko anakolala kama mfu, akajikuta amechelewa, ASIRUDI hapa.” Akajibu mama J akiwa anaingia. Tuma akaanza kucheka akimwangalia Umi.

“Lakini si siku hizi nawahi?” “Na ibakie hivyohivyo Umi! Usije hapa kwa kuchelewa. Siku unayochelewa kuamka jua na kazi huna. Na mama yako ameniunga mkono.” “Basi unakumbuka siku ile nampigia mama simu naomba anisaidie kuzungumza na mama J?” “Ulipotaka akusaidie kudanganya?” Tuma akamuuliza akicheka.

“Jinga kweli hili!” “Badala yake eti mama akampigia kunisemelea.” “Umi!” Tuma hakutegemea. “Muulize mama J! Mwanzo mpaka mwisho. Kwamba mimi nataka kumtia dhambini na kumuua. Mara nimsingizie kifo, mara maradhi. Mimi nataka kumuuayeye. Na yeye simfaji! Eti mama J amuombee yeye wala si mimi.” Tuma alicheka, alicheka sana. 

“Halafu eti anamshauri mama J, anifukuze tu kazi, nikaishi na shangazi zangu. Ndio nitajifunza adabu.” Tuma hana mbavu. “Sasa nikuone Umi.” “Si nimebadilika! Mama J naye! Wewe usimsikilize mama.” Akamtizama na kurudisha macho kwenye simu kama anayesoma ujumbe, akaguna.

Pale Unapotukana Mamba, Wakati Hujavuka Mto

“Hakika ni vile Sandra hashauriki!” Akawa anaongea huku anaangalia simu. “Hajui anaingia kwenye vita vikali sana na JJ, na hatashinda.” “Kwa nini?” “Kwanza Sandra si ni yule mke wa Jerry?” Umi akaongeza kwenye swali la Tuma.

“Huyohuyo! Hakika namuhurumia! Angekuwa mtu mwingine kwa haraka sana ningemkumbusha, vita anayofanya si na Jerry, ila JJ.” “Unamaanisha nini?” Tuma akaendelea kudadisi akitaka kujua zaidi. 

“Mkewe anasemaga JJ ni mkimya na mwema sana, unaweza hata muweka kidole cha jicho akakuomba wewe msamaha, ila usiguse wadogo zake! Anacharuka kama Farualiyejeruhiwa, au Simba. Na hajifanyi.”

“Walipofariki wazazi wao, yeye alikuwa nje ya nchi akisoma shahada ya uhandisi. Unaambiwa ana ile akili ya kutosahau halafu anakipaji kikubwa sana kwenye uchoraji. Anaweza akakuchorea jengo, mpaka ukashangaa. Basi, walipofariki wazazi si wakafilisiwa vibaya sana! Jerry na Jeremi wakawa hawana pakuishi, wanamangamanga wakaishia kuchukuliwa na mapadri, parokia waliyokuwa wakisali na wazazi wao, baba yao alipokuwa akimwaga mapesa. Hiyo nayo ni stori ingine. Maana na mimi niliteseka!” “Kwamba ulikuwa ukiwafahamu hawa tokea zamani!?”

“Acha Tuma. Tulianzana na Jeremi tukiwa wadogo. Eti wazazi wao wanafariki sina pakumpata Jeremi! Nilikuwa kama mgonjwa, nalia bila yakunyamaza. Namtaka Jeremi.” Akaanza kujicheka. 

“Ikawaje?” “Ilibidi baba na mama kunisaidia. Walipokuja kuanza kuishi kwa mapadri, kaka yangu mkubwa akajua, ndio wakawa wananipeleka. Naenda nikitoka shule, nakuja kuchukuliwa jioni mpaka kaka yao akaja kuwachukua! Ilikuwa mbaya siku hiyo uwanja wa ndege! Mimi nalia, Jeremi analia hatujui kama tutakuja kuonana tena.”

“Tulipotezana bila mawasiliano kwa muda mrefu sana, lakini tuliapiana kusubiriana. Jeremi aliniahidi hatakuja oa mwanamke mwingine, hata iweje! Akaniambia atatafuta njia atanirudia tu. Hapo nalia, kaka zangu wote wapo uwanja wa ndege wamenisindikiza kumuaga Jeremi! Sitaki aondoke naona kama sitakuja muona tena.” 

“Jamani! Kumbe mmetoka mbali?!” “Sana. Na Jeremi! Mno. Tokea tupo sekondari wakati huo wazazi wao wanapesa sana. Ila Jerry alikujaga kufauli shule ya bweni, ya serikali, akataka kwenda kuonja maisha mbali ya wazazi. Nikabakia na Jeremi wangu. Mziwanda kwao. Alikuwa roho ya mama yake! Alikuwa akipendwa Jeremi na mama yake! Kama yai lisipasuke! Halafu leo ananisema na mwanangu! Tena namwambia nisimsikie.” Angalau wakacheka.

“Lakini maisha yaliwabadilikia vibaya sana. Sana. Usingeweza amini kama walikuwa wao. Halafu gafla tu. Shule tuliyokuwa tukisoma ilikuwa ya mapesa mengi, akashindwakuendelea. Yakawa majanga, juu ya majanga, halafu sasa hawakuwa na msaada!” “Hawana ndugu?” “Wewe unajua maswala ya ndugu. Kwanza unavyoona wana damu kali hivyo, baba yao alioa mtoto wa shangazi yake.” “Haiwezekani!” “Tumbo moja na baba yake. Dada wa kunyonyo ziwa moja na baba yake, akaoa binti yake. Hilo likawa kosa kubwa sana kwenye ukoo. Akamtorosha yule binti ambaye ni kama dada yake, akaenda kumuoa huko nje ya nchi, akarudi anamimba ya JJ. Nafikiri kukawa na kesi kifamilia na wao wanapendana. Wakajenga kujihami na kujitenga na familia. Wakina Jeremi wakawa ukoo wao ni baba na mama tu. Wametengwa. Ukiona picha za wazazi wao, utadhani kaka na dada waliotoka tumbo moja. Au mapacha.”

“Basi, JJ aliposikia wadogo zake wanahangaika kama ndege, akarudi nchini. Akawashugulikia Visa, akaondoka nao wote wawili kurudi shule.” “Mama J!” “Acha Tuma. Wenyewe wanasema kaka yao alikuwa akilala kwenye gari. Anaunganisha shule na kazi ili waweze kuishi huko ugaibuni. Chumba kimoja wakawa wanaishi wote watatu. Wao wanakwenda shule kama kaka yao, ila yeye anafanya shule na kazi alikuwa nazo kama tatu. Hapumziki.”

“Alipelekwa na serikali kusoma shahada ya pili. Alimaliza kwa kufauli sana, akataka kuendelea, hukohuko wakampa udhamini na kazi. Kwa hiyo akawa anasoma shahada ya tatu na chuo kinamlipa huku akifanya kazi. Lakini ukumbuke hapo ni serikali ya Tanzania ndio ilikuwa imempeleka, hawezi kubadilisha. Walimpa ile Visa ya JV. Akaongeza shule zaidi ili wadogo zake wafaidike elimu huku akijiweka sawa. Akafanya mpaka akamaliza hiyo shahada ya tatu, akachukua na kiji kozi kingine chakuvutia muda, ndio serikali ya huku ikamdai, akarudi sasa na wadogo zake, ila hapo sasa jua alishakusanya pesa huko na hapa akawa na ajira.”

“Ndio historia yao ikabadilika kuanzia hapo maana kaka yao akaingia kwenye ujenzi wa barabara, mihela ikaanza kuingia. Na JJ akikufahamu, lazima atakusaidia. Ndivyo alivyo.”

“Alipopata tu mwanamke akamwambia ‘nataka kukuoa, lakini nakuja na wadogo zangu wawili, hao ni sehemu ya maisha yangu.” “Akamwambia huyo mwanamke?” “Mapema sana kabla hajamuoa. Sasa mkewe anasema yeye hakuchukulia kwa uzito mpaka ndani ya ndoa. Anasema utamfanya chochote JJ, ila usiguse wadogo zake walausiwazungumzie asivyopenda yeye, ni KOSA ambalo hawezi kunyamaza na atahakikisha umeelewa umevuka mpaka asio ruhusu uvuke.”

“Anasema mwanzoni ilimsumbua karibia aachane na JJ, lakini ndio mama yake akamwambia ni ujinga, hatapata mwanaume kama JJ, kwanza pesa anayo. Halafu yupo kama wadogo zake, JJ hajui kulala na mwanamke mwingine isipokuwa mkewe. Hawa kwao si malaya hata wakuonja nje. Na utafikiri wanaambiana! Tuache hilo, mkewe akawa ananiambia alipohesabu hasara na faida za kuachana na JJ, akaona yeye atapata hasara na baba yake pia alimwambia. JJ ameinua sana familia yao.” “Ya mkewe JJ?” Tuma akauliza.

“Na wala sio wao tu. Nitakwambia. Ila kwa wakati huo ndugu zake mke wa JJ karibia wote akawa amewatafutia kazi masehemu ya juu sana. Sasa ndio wazazi wake wakamuuliza, bora lipi, kupokea hao wadogo wa JJ ambao nao hawana shida, au kuwakataa na aachane na JJ, wakose kote?” 

“Kwamba JJ angemuacha!?” “Kwa haraka sana na alikuwa tayari kumuandikia talaka bila masharti. Alimwambia tokea mwanzo alimwambia anakuja na jukumu la wadogo zake, na halikuwa na mjadala, na akakubali. Kubadilika kwake yeye, hakutambadili yeye mawazo. Ndio mkewe kutulia sasa na kulielewa kifasaha.”

“JJ akikufahamu, ukaingia kwenye maisha ya wadogo zake, wewe ni ndugu. Na ukitaka umfurahishe JJ, wadogo zake. Ndio maana mimi ananipenda sana.” Wote wakacheka na mama J mwenyewe akacheka.

“Mkewe mwenyewe kuniambia! Haachi kuniulizia na kutaka mkewe awe ananijualia hali kila mara, ndio mkewe akaniambia ni kwa jinsi ninavyoishi na Jeremi. Sasa anachokifanya Sandra sasahivi, anacheza na jicho la JJ, mkewe anasema JJ ametibuka, hata chakula hakipiti kooni, na halali.” “Kafanya nini tena!?” Tuma akauliza.

“Nasikia kamtimua kama mbwa!” Umi akawahi kujibu kishabiki, ikabidi mama J amsikilize. Umi akamsimulia aliyosikia saluni. “Basi na mimi nimesimuliwa na mke wa JJ, na yeye kasikia saluni kama Umi. Nasikia Jerry alitaka kumficha kaka yao. Hakusema kilichotokea, lakini JJ akaja kuambiwa na mkewe. Si ndio JJ kumsaka mdogo wake nakujua alilala kwenye gari sijui! Unaambiwa JJ machozi yalimtoka. Lakini nasikia eti Jerry akamsisitiza kaka yao kuwa Sandra anabaki na wanae. Ndio ikawa kama kumtuliza.”

“Lakini nasikia alichokifanya leo kwenye talaka, ndio nasikia ni kibaya SANA. JJ anawaka kama moto wa tanuru! Mpaka mkewe anasema anamuhurumia Sandra.” “Kafanyaje tena?!” Tuma akazidi kudodosa.

“Unaambiwa huko kwenye talaka amekwenda na wakili, acha amtukane Jerry mbele yao! Akamtukana haswa. Jerry kimya. Sasa JJ akasema hataki hizo mali, aachiwe kama anavyodai zote ni zake, ila anataka vyeti vya mdogo wake.” “Ambavyo ni mali yake yeye, Sandra hausiki navyo!” “Bwana Tuma wewe unaakili! Kama ulikuwepo kwenye mdomo wa JJ. Anasema vyeti vya Jerry ni jasho la marehemu wazazi wao, na anamwambia mkewe, yeye alikuwa halali ili wadogo zake wasome. Vyeti vya wadogo zake, pia ni jasho lake yeye, hakuna mwenye mamlaka navyo isipokuwa wadogo zake tu.” “Sasa kwa nini huyo Sandra naye asimpe mambo yakaisha?!” Umi akauliza akishangaa.

“Mkewe kanitumia video ndio nilikuwa nikiangalia hapo nje na kuzungumza naye kwa simu.” “Video?!” Tuma akahamaki. “Asubuhi Sandra aliposema mali zote zake na matusi mengine, yule wakili wa upande wa Jerry, aliyetumwa na JJ, akaona hilo aliache maana hata Jerry mwenyewe hakutaka kitu, ila akamkumbusha Sandra vitu alivyomtumia aje navyo siku hiyo ya talaka. Hati ya kusafiria, na vyeti vyote vya shule vya Jerry, maana si amemkataza Jerry asiende nyumbani. Sandra si akamjibu amechoma moto vitu vyote vya Jerry!” “Mungu wangu!” Mpaka Umi akashangaa.

“Unaambiwa ni mbaya kuliko hivyo mlivyoshangaa nyinyi. Hapa tunavyozungumza ameshamtafutia mdogo wake hati nyingine ya kusafiria.” “Leoleo!” “Hapa tunavyozungumza inachapishwa ingine, ipelekwe ikawekwe VISa ya Dubai, wanaondoka naye. Vyeti vya shule vya hapa, anashugulikia na vya huko nje ya nchi pia nasikia anashugulikia ili mdogo wake apewe vingine. Itakuwa rahisi maana wote sisi tuna Green card, kasoro watoto wetu tu ndio raia wa huo.” “Subiri kwanza mama J. unamaanisha nini?” Tuma akawa hajaelewa.

~~~~~~~~~~~~~~~

“Mkewe JJ huyo ndio alitutia shuguli, mimi na Sandra tukaiga. JJ alinunu bonge la jumba huko Marekani alipo binti yake sasahivi. Basi kila mimba ikifika miezi 8, tulikuwa tunaenda huko kukaa mpaka kujifungua, ili watoto wapate uraia. Mtoto mkubwa wa JJ alipofikisha umri wa miaka 18, akampa baba yake Green Card, mkewe pia.”

“JJ alipopata tu, akawaingiza wadogo zake wote. Sasa kwa kupitia wadogo zake, ndio na sisi kama wake, tukapata hiyo Green Card. Ila watoto wetu wotewanauraia wa kuzaliwa Marekani kasoro mtoto wa kiume wa JJ yeye anauraia pacha, wa Marekani na Uingereza, maana anaishi Uingereza.” “Mama J?!” Tuma akashangaa sana.

“Sisi wakati wote tunaingia nakutoka Marekani bila kuomba VISA. Ni hivyo tu Tanzania haikubali raia pacha, ndio maana tumebaki na Green Card. Lakini tuliwahi mapema sana kupata Green Card, na kule tunayo sehemu ya kuishi kabisa. JJ huyo! Binti yake anasoma na kuishi hukohuko. Tuyaache hayo.”

~~~~~~~~~~~~~~~

“Turudi kwa la leo. Unaambiwa JJ amesema Sandra amemkosea vibaya sana. Hana tofauti na waliowatupa wadogo zake nje, wakiwa yatima. Mkewe anasema leo tena mumewe alikuwa kwenye simu anarudia kumuelezea, kama hajawahi elezea vile alivyokuwa akiwa na njaa, halali, anapata lisaa la kusinzia kwenye gari ili afanye kazi kusudi wadogo zake waende shule na waishi vizuri. Anasema leo Sandra anachoma moto vyeti! Anasema ni kosa ambalo atahakikisha anajua amekosea, na atamfundishaasiwahi kurudia hivyo tena.” “Sasa atamfanyaje na keshamfukuza mdogo wake?” Umi akauliza.

~~~~~~~~~~~~~~~

AKIWA amemsihi kaka yake akumbuke Sandra anabaki na watoto wake, lakini JJ amekusudia kumfundisha somo Sandra, ili ajue amevuka msitari ambao HARUHUSIWI

Ni nini atafanya?

Usikose na video ya kusikitisha aliyochukua Sandra akichoma vitu vya Jerry.

Ayvin bado ni mahututi

Wanamsihi Mungu asiyepoteza, atende muujiza ili Ayvin aamkie upande wao, hapa ulimwenguni vile alivyo. Kipofu au tahira, ilimradi awe hai.

Ni nini kitaendelea? 

 


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment