Swali la Umi likamfanya hata Tuma kutaka kujua atakachofanywa Sandra na JJ. “Usitake kujua, mpaka namuhurumia! Sisi wenyewe asilimia kubwa ya biashara yetu mpaka sasa ni msaada wa JJ.” “Mama J!?” “Mwenzio mimi huwa sisahau nilipotoka Tuma, na Mungu amenijalia sina majivuno na mali. Ila si mzembe kama Umi. Nikipewa nafasi, naitumia vizuri.” “Nimebadilika mama J!” Mama J akamwangalia kwa kumsuta na kuendelea.
“Ile yadi ya kule na matairi ya mwanzo, sikudanganyi Tuma. Chetu mimi na Jeremi lilikuwa wazo tu. Ila kuanzia eneo, magari ya mwanzo na matairi, ni JJ.” “Mama J!?” “Mungu wangu shahidi, na katika hilo hazembei na hana mjadala anapotaka kusaidia wadogo zake mpaka wazazi wangu mimi, walishangaa! Magari ya mwanzo na matairi yalijazwa stoo nzima, bure. Akisema ndio zawadi yetu sisi wawili.”
“Maana mimi nilimaliza chuo nikawa nimeajiriwa kama Jeremi, lakini pesa ndogo. Tunatamani kujiajiri ili tuwe wote kila wakati, ila tukawa hatuwezi! Kazi tunafanya mbalimbali! Tukitoka asubuhi ni mpaka usiku! Jumatatu mpaka jumamosi! Vikawa havina raha! Sipati muda na Jeremi wangu!” “Mama J nyie!” Wote wakacheka vile alivyoongea kwa deko akilalamika.
“Sasa ndio maisha gani hayo! Ndio akamshirikisha kaka yake, kama mchezo hivi, biashara ikaanza. Wote tukaacha kazi, tukaanza kufanya biashara yetu. Akawa akituma watu wake wote wakaribu na magari yote ya kampuni yake, makubwa kwa madogo, yakaanza kufanyiwa huduma kwetu. Akitaka magari ya kampuni yake, anaagiza kupitia kwetu, kama hatunayo kwenye yadi yetu. Na marafiki zake ikawa hivyohivyo. Tukajulikana kwa haraka sana. Mungu akaweka mkono wake, tukafungua na hapa.” “Kumbe!” “Kabisa. Ni JJ.”
“Na Sandra amesahau tu. Alianza biashara na Jerry wakiwa wapo vichochoroni huko hamna hata aliyekuwa akiwafahamu. Pale walipo ni sehemu walitafutiwa na JJ, na JJ kuwatafutia wateja wa mwanzo. Baba yake Sandra, ameinuliwa na JJ. Kuna malighafi fulani hivi zina pesa sana, zinatumika kwenye ujenzi wa barabara, unaambiwa hiyo tendandiyo alimpa baba yake Sandra. Ananunua kwake hiyo malighafi, kusudi tu kumnufaisha.” “Kama alivyoinua ndugu wa mkewe?”
“Sasa unaambiwa kwa kina Sandra ni zaidi kwa sababu kwao wengi walisoma na baba yake Sandra alikuwa mfanyabiashara tokea zamani, ila JJ ndio kamnufaisha. Unaambiwa mzee anapesa chafu kuliko maelezo.” “Sababu ya JJ?” “Ewaah! Hicho anachomuuzia JJ, unaambiwa kina pesa mno! Mbali ya hapo kaka zake wawili wanakazi za mahela sababu ya JJ.”
“Mmoja anafanya kazi kabisa kwa JJ. Na yeye ni muhandisi alimaliza hapo chuo kikuu cha Mlimani. Akaajiriwa moja kwa moja kwenye kampuni ya JJ. Ukimtizama yule kaka na maisha yake, huulizi! Sema tu ni malaya na jeuri kupita Sandra. Anamajivunomno. Ila anapesa kama hana akili nzuri.” “JJ huyo!?” Tuma akazidi kushangazwa.
“Nakwambia hivi, ukifahamiana naye JJ, jua shida zako zimeisha. Anatumia kile ulicho nacho kukuendeleza. Mkewe anasema hata asipomuombea mumewe, anajua kuna familia hazilali bila kuomba mkono wa Mungu juu ya JJ. Ni mwema mno. Lakini asisikiewadogo zake wanashida. Mkewe anasema ni kama dunia nzima inasimama! Si unakumbuka siku ile alikuja hapa?” Akamuuliza Tuma.
“Alimfuata Jerry mpaka kule kwenye matairi.” “Bwana unaambiwa hakulala!” “Mama J!” “Kwa kuambiwa na mkewe na mwenyewe kumpigia simu usiku Jeremi. Mkewe anasema alikuwa akilalamika usiku kuchwa kuwa kunagarama analipa ili wadogo zake wasipate shida tena, leo Jerry anatengeneza tairi kwa mkono! Anasema yeye alishayafanya hayo miaka mingi sana kwa garama ya kutolala, ili wadogo zake waishi vizuri.”
“Ndio Jerry mwenyewe akasisitiza alitaka kujifunza kwa ajili yake mwenyewe lakini pia amekataa. Amesema zipo mashine za kusaidia kufanya hiyo kazi sio lazima na yeye ajifunze kuwasha moto kwa mawe.” “Mmmmmh!” “Hakika namuhurumia Sandra! Sijui amejisahau vipi masikini!”
~~~~~~~~~~~~~~~
“Mama J, tuone hiyo video.” Tuma akataka kuonyeshwa ili kupata habari kamili. “Nimesahau!” Akawatolea wakaona vile Sandra alivyokuwa akichukuliwa video na mtoto wake wakati anachoma vitu vya Jerry huku akisema ni takataka, na wanae wakishangilia.
“Mama J wewe! Huyu mama analaani mpaka wanae jamani! Kwa nini kuwaingiza watoto wao kwenye ugomvi wake na baba yao?” “Unaambiwa Jerry anahali mbaya, ameshindwa kutoka kitandani, ameshindwa kuzungumza. Jeremi yupo naye anasema ameshindwa kuweka hata maji mdomoni, amejifunika tu mto usoni. Ila kaka yao amemwambia asimuache peke yake. Ndio yuko huko.”
“Sasa nasikia Sandra si aliondoka kwenye hicho kikao! Wakili akampigia simu JJ kumueleza yote. Baadaye eti JJ akampigia simu akamwambia anaitaka hiyo video ya kuchoma vitu vya Jerry, Sandra aliyosema anayo. Lasivyo yeye atajua bado anavyo vitu vya Jerry, na atamdai mpaka mahakamani. Ila akipata uthibitisho kweli amechoma, basi.”
“Sasa nafikiri alikuwa akimtega ili apate uthibitisho tu, Sandra naye bila kutumia akili eti si akamtumia hiyo video! Unaambiwa ameumia JJ! Si umeona hapo jinsi wanavyo mdhihaki Jerry!” “Halafu mbaya zaidi akiwa na watoto wako jamani! Sio sawa!” “Sio sawa kabisa na hicho kimemuumiza hata mke wa JJ.”
“Anasema matatizo yao, wasingeingiza watoto. Wale ni watoto wa Jerry, hata iweje! Lakini kibaya alichokifanya Sandra, kugeuza watoto wake kumdharau baba yao. Tuma!” “Eeeh!” Tuma akaitika na kumwangalia. Maana alikuwa akirudia video
“Mpaka aibu ukiwa nao wale watoto. Hawajui kujibu mtu vizuri, na wakiwa wanaongea na baba yao, mimi huwa nafukuza wanangu.” “Mama J! Ndio mbaya kiasi hicho?!” “Nakwambia mpaka Jerry akaacha kuja kwenye mikusanyiko ya familia. Alimwambia Jeremi, bora awe anafika peke yake kitu ambacho Sandra alikuwa haruhusu, kuliko kuja na familia yake. Aibu tupu!”
~~~~~~~~~~~
“Sasa watoto wa JJ si unajua wote wawili wapo nje ya nchi wanasoma?” “Umesema.” “Wapole kama baba yao, halafu wakike anaongea kama mama yao. Mtulivu sana na ana akili kama JJ. Anasomea upasuaji wa ubongo, huko Marekani.” “Acha utani mama J?!” Tuma akawa haamini.
“Nakwambia anaakili kama JJ. Kipaji cha uchoraji kama cha baba yake, anakitumia kwenye mwili wa mwanadamu. Unaambiwa ni moto wa kuotea mbali. Wanamnyanyulia mikono huko.” “Mama J!” “Acha mama. Huyo mtoto ni roho ya JJ. Akianza kumsifiahuyo mtoto, hamezi mate! Halafu mzuri kama kamalaika!” “Ila nyinyi watoto wenu wamefanana sana.” “Matoto mazuri kwelikweli!” Umi akaongeza kwa Tuma. “Bibi na babu walikuwa kaka na dada, wataacha kufananana?” Walicheka, walicheka sana.
“Sasa yule binti wa JJ akawa amerudi nchini baada ya kama miaka minne migumu ya shule yake huko. Mama yake mpenda shuguli, akafanya kijipati pale kwao. Na kaka yake kutoka Uingereza akaja. Nikikwambia ni watoto wazuri, ni watoto wazuri sana. Yule wa kiume anampenda sana mama yake. Hapitishi miezi mitatu bila ya kurudi huku nchini kuja kumuona au ujue mama yake atakwenda kumfuata.”
“Basi, tukakusanyika pale, furaha vicheko, ungejua yule binti yupo jinsi JJ alivyokuwa akicheka kwa sauti siku ile. Akaja Sandra na wanae, bwana waliharibu vibaya, mpaka yule binti akawaambia wale watoto mbele za watu, kuwa wanamapungufu kwenye malezi.” “Mama J?!”
“Palepale hakusubiri. Akawaambia kabisa, wanavyozungumza na baba yao siosawa. Wanavyo tumikisha wafanyakazi wa pale sio sawa, kwa sababu wale mabinti pale ni ofisi yao, inapaswa waheshimiwe na wazungumze nao kwa nidhamu. Hapana haja ya kuwaamrisha, kwanza sio wabishi, pili akawaambia wanajua majukumu yao. Na ukisikia msichana wa kazi wa nyumbani kwa JJ, sio kama hawa wetu!” “Wakoje?!” Mama J akacheka.
~~~~~~~~~~~
“Kwanza, kwa uhakika kabisa, kujawahi ona nyumba nzuri kama pale kwa JJ.” “Kweli!?” “Nakwambia hata kwenye tv, nina uhakika hujawahi ona, Tuma. Bwana ni pazuri! Kumepangiliwa mpaka vitasa. Getini mpaka vyumba vya hao wasichana wa kazi. Stoo ya vyakula kila kitu kipo sehemu yake, kwa mpangilio tena kwa herufi. Unawezsa sema umeingia supermarket.”
“Na huwezi pazoea kwa sababu mkewe anabadili rangi ya nyumba na thamani zake, mara kwa mara.” “Haiwezekani!” “Pesa ipo, mama! Kwa nini asifanye? Halafu ni msafi kama mumewe. Wakakutana wanapenda vitu vizuri. Huwezi kulia kijiko cha bati pale kwa JJ. Chuma ile safi, nzito. Wasichana wake wanavaa sare.” “Mama J!” Wote wakazidi kushangazwa.
“Acha mama! Hao wasichana ni safi muda wote. Juu mpaka chini. Wakipika jikoni utafikiri ni hotelini! Kwa mpangilio. Safi. Na yule mama hana kelele, wanae hawana kelele. Nyumba imepoa wakati wote. Kila mfanyakazi anafanya lake kwa wakati. Huwezi kuta hata jani nje, linazagaa. Kijani muda wote. Si kiangazi, si masika. Kwa JJ ni maua, huchoki kuangalia.”
“Sasa si ndio wale watoto wa Sandra wakajaa pale! Jemimi alishindwa kuvumilia. Akaongeza na kuwaambia, kusubiri sio jambo baya endapo wanashindwa kujitumikia, jambo ambalo ni la kawaida. Kwamba hata yeye mwenyewe kuna mambo anajifanyia, hatumi mtu.” “Mama J, kwani walikuwa wakifanyaje?” “Kutukana wale wasichana pale, kuwaita stupid. Hawana akili au hawatumii akili, wakiwatuma bila kikomo. Yaani wanaweza kuwatuma juisi, wakiletewa, wanawarudisha kwa kosa dogodogo na kuwaambia ‘nenda kalete ingine’, bila heshima!” “Mbele ya watu?!”
“Tena kama mbwa! Tupo wote pale mpaka wengine tulishindwa kula tukabaki tukiangalia. Ndio Jemimi yeye ikabidi aongee. Akawaambia kwa wazi kabisa, palepale bila kuficha. Sasa kwa kuwa Sandra anajua roho ya JJ inagongea kwa yule binti yake, alichokifanya ni kuondoka na vijana wake, akamwambia na Jerry naye afuate nyuma. Maana alijua angemjibu tu yule mtoto wa JJ, pale pasingetosha. Wakaondoka.” “Mmmmh!” Ndio na Umi akaweza kumuelewa Jerry. Akajua japokuwa ni wazuri, wanapesa, lakini si wavua suruali hovyo. Heshima ikapanda kwa asilimia 100, akajionyakabisa.
Kisasi.
Upo usemi unaosema, unaporuka, agana na nyonga. Ndilo kosa alilofanya SandraBila kujijua aliposimamia, kukumbuka ni kwa jinsi gani yeye na familia yake WAPO, walipofika, kwa jeuri, akafanya mengi akikataa kujishusha, akaendeleza ubabe bila kutafakari.
Alishazoea kumfanyia mengi mumewe, hakuna anayemfanya kitu, wala ndugu zake hawaingilii. Akaweka mazoea, akidhania ule ukimya hata wa JJ ni wa milele.
Asijue, alibeba hiyo heshima kwa sababu alikuwa mke wa ndugu yao. Hawakutaka kuingilia ndoa yao. Maadamu mwenyewe Jerry aliendelea, na wenyewe wakajiweka pembeni wakisaidia kwa kadiri ya uwezo wao, ili kurahisisha maisha ya Jerry ndani ya hiyo ndoa bila mafanikio mpaka walipo hitimisha wao wenyewe, ndipo JJ sasa akapata nafasi.
~~~~~~~~~~~
Akampigia simu mkubwa wa kitengo cha HR wa kampuni yake. “Mara ya mwisho kufanya assessment ya wafanyakazi ilikuwa ni lini?” Ikamuia ngumu kujibu maana haukuwa utaratibu wa hapo. “Ninaona tuna kundi kubwa sana la wahandisi wanaolipwa bila kuingizia faida kampuni.”
“Waambie ifikapo kesho saa mbili asubuhi uwe umepata taarifa za kila mmoja wao. Waeleze muda wanaoingia na kutoka kazini. Kazi zao kila siku wawapo ofisini, na kile wanachokifanya kinavyonufaisha kampuni. Hiyo ni leo.”
“Kazi ya kesho, kila mmoja atapata nafasi na wewe ya mahojiano. Mbali ya walichoandika wazungumze na wewe, wakitetea kile walichoandika, kisha unipe taarifa zoa vizuri. Nijue nani tunamtoa, nani anabaki.” “Kama nimeelewa sawasawa, ifikapo mwisho, niwe na ripoti aina mbili. Zao na yangu juu yao.” “Kesho tafadhali. Siku njema.”Simu ikakatwa, HR tumbo joto.
Akafanya kama alivyoagizwa, haraka sana taarifa zikaenea kuwa JJ anapunguza wafanyakazi bila kujua anayetafutwa ni mmoja tu! Siku hiyo ikawa imeshakaribika kwa wafanyakazi wote. Kampuni ya JJ wanalipwa mamilioni ya pesa na wanamjua JJ ni mchapakazi, ila mtu mzuri sana. Wasijue shemeji ameshamtibua.
Na Kwenye Mfuko Wa Baba Mkwe
Akampigia simu mtu wa stoo. Akaulizia kiasi cha malighafi anazoleta baba yake mkwe. Ila akaulizia kwa jina la hiyo malighafi, asijue sababu. Ila kwa hofu kubwa maana huwa hazungumzi na yeye moja kwa moja akamwambia bado wanayo na wanategemea ingine baada ya mwezi. “Tunza uliyonayo, usiweke oda ingine.” Simu ikakatwa.
~~~~~~~~~~~
Akampigia mtuma oda. Akamuulizia kama ameshaagiza hiyo malighafi. “Bado. Huwa natuma oda mwishoni mwa mwezi.” “Usitume tena kwenye kampuni ya Salamba. Watakapo kutafuta waambie tumepata sehemu ingine nzuri na kwa bei ya chini zaidi yao. Tumeamua safari hii kwenda na kampuni ingine.” Simu ikakatwa na kumuacha ameduaa.
~~~~~~~~~~~
Kampuni ya Salamba ndio wamekuwa wakifanya nao kazi kwa miaka mingi sana mpaka walishaacha kutangaza hiyo tenda. Maana mwanzoni ilikuwa kila wakitaka, basi wanatangaza tenda. Makampuni mengi wanatuma maombi yao kwa bei mbalimbali, lakini Salamba akawa akishinda kwa sababu ni kampuni ya baba yake Sandra!
Mtuma oda akabaki ameduaa akijua ni kiasi gani ni pigo kwenye ile kampuni maana ni tenda pekee waliyokuwa wakiitegemea na ilimnufaisha sana huyo mzee! Akabaki akijiuliza ni nani mwingine aliyefanikiwa kupora hiyo tenda, asijue anayetafutwa hapo ni baba mkwe.
Sasa kwa sababu na yeye alikuwa akinufaika sana na hiyo tenda, mzee Salamba alikuwa akimpa posho kila anavyomtumia hizo tenda, na posho sio pesa ndogo, alikuwa akimpa mamilioni ya pesa kama kumfurahisha huyo mfanyakazi wa JJ utafikiri kampuni ni yake, kumbe ni ya JJ. Na JJ alijua na yeye ananufaika ila akaacha tu akijua mkwe anaingiza faida kubwa sio mbaya na mfanyakazi wake akanufaika zaidi.
~~~~~~~~~~~
Kwa kuwa alikuwa karibu sana na mzee mwenyewe, akampigia. “Aisee nina habari zisizo njema.” “Ni nini tena!?” “Naona bosi amepata sehemu nyingine yakununua malighafi kwa bei nafuu. Amesema nisiagize tena kwenu.” Mzee alishituka karibu aanguke pressure hapohapo.
Ila akajikaza. “Acha nizugumze naye mwenyewe.” Akakata ili mpigie simu JJ, simu yake ikawa haipatikani tena! Asijue imefungiwa, udugu binti yake ameshauua kwa matusi na dhihaka. Kwamba hata yeye, hawezi mfikia tena JJ, moja kwa moja. Apange foleni kama wengine.
Alipompigia simu sekretari wa JJ, akaambiwa yupo kwenye kikao, apige baada ya lisaa.
~~~~~~~~~~~
Mzee hali ikazidi kuwa mbaya, akampigia simu Sandra na kumueleza. Ndio Sandra akagutuka sasa na kubaki kimya. “Subiri, naona JJ mwenyewe ananipigia kwa simu ya ofisi.” Akakata kwa binti yake akapokea ya JJ kama apige goti kumbe alikuwa sekretari. “Nakuunganisha sasahivi.” Akamwambia kwa sauti ya heshima, JJ akapokea.
“Nilikuwa kwenye kikao mzee wangu. Shikamoo.” Akawa ametulia kabisa. Mzee Salamba akajieleza kwa heshima sana, akamalizia kwa kulalamika kuwa, “Maana kuna ambayo bado ninayo stoo nikitegemea kuwatumia! Nilinunua nyingi ili niwe nayo nisiwe nawacheleweshea.” “Ambayo tayari kampuni yangu ilikutumia oda yake?” Swali la mtego hilo.
“Hapana. Ila kwa sababu tumekuwa tukifanya wote kazi miaka yote na najua kiasi ambacho mnahitaji, nilichukua sehemu kwa bei ya jumla nikatunza.” “Kama nimekuelewa sawasawa kwa sasa huna oda yeyote kutoka kwenye kampuni yangu.” “Ndiyo. Lakini inakuwa kila baada ya miezi…” “Naomba nisikuchukulie muda wako mwingi mzee wangu. Kwa sasa hatutahitaji tena. Asante.” Simu ikakatwa. Mzee akapandisha pressure, ikabidi dereva amrudishe nyumbani.
Huku Kazini.
Jioni Jeremi akaingia hapo na kumkuta Tuma ametulia kwenye meza yake kama kawaida yake, Umi alishaondoka. “Karibu.” “Nimetumwa na Jerry kukupa funguo za gari.” Tuma akabaki amemtolea macho. Jeremi akaelewa.
“Hayupo kwenye hali ya kuja, naomba umvumilie. Hatatumia hii gari. Itakuwa imekaa tu, na yeye anasafiri na bro. Kwa hiyo kuwa nayo mpaka atakaporudi. Imejazwa mafuta. Itakurahisishia usafiri.” Akaweka funguo hapo mezani bila nyongeza juu ya hilo.
“Vipi stoo, tupo vizuri?” “Hapana. Naona jumamosi walitumia kila kitu. Ila nilikuwa na mama J mchana, nimemsisitiza asiniache hivi. Tutashindwa kufanya kazi.” “Kulikuwa busy sana. Nafikiri Hilda aliondoka hapa saa moja usiku. Kama Hilda amesikia, atarekebisha tu. Asante Tuma. Acha niwahi.” Akatoka akijiambia ya ngoswe, amuachie ngoswe mwenyewe. Yake na Jerry, hayamuhusu.
~~~~~~~~~~~
Huku kwa Tuma na Jerry, pakawa kimya, hajamsikia Jerry na yeye akaamua kumuacha baada ya kusikia yaliyompata na hali yake, akaona ajitulize, ila gari yake akajiambia hatajivunga. Ataiendesha akumbushie enzi, mengine atajua mbele ya safari.
Kwa JJ
Siku ya jumanne jioni JJ akiwa ofisini kwake akapokea ripoti kama alivyoagiza. Sasa kwa kuwa walijua mahusiano yake na kaka yake Sandra, na yeye alikuwa jeuri akijua hakuna atakayemfanya kitu, mmiliki ni ndugu, hakuwa akielewana na wengi.
Jeuri na kiburi yule asiyeweza jishusha kwa yeyote. Wengi walimvumilia wakijua ajira yake imeandikwa kwa kalamu, ila alikuwa na kasoro nyingi hata ugomvi na wahandisi wenzie ulishafika kwa HR.
Sasa waliposikia anataka kupunguza watu, HR akamtega JJ kwa kuweka mapungufu yake yeye, shemejie, mbele akijua akishamuona yeye, JJ atashindwa kumfukuza kazi na wengine kuponea hapo asijue anayetafutwa ni yeye tu, wala si mwingine!
~~~~~~~~~~~
JJ akapitia ripoti nzima, akamuita HR ofisini kwake. “Katika haya mapungufu yote ulishakaa na Rodrick kuzungumza naye juu ya hivi ninavyoviona kwenye jalada lake?” “Kwa asilimia kubwa, na ni zaidi ya mara moja. Ila kama unavyomjua Rodrick, inakuwa ngumu hata kumalizana naye kikao.” JJ akakunja uso.
“Sijaelewa!” “Ni ngumu kukaa naye chini na kuzungumza na Rodrick! Kila mtu anamjua! Na anajivuna kwa jina lake hilo la Salamba.” Ikawa kama anazidi kumchanganya JJ.
“Jina la baba yake linahusikaje hapa!?” “Ni ngumu kueleza. Na unajua mimi ni mtu wako JJ, tumeanza wote hapa, nikimaanisha sisi tunafahamiana kwa ngazi ya familia. Na ndio maana kuna mambo nayaelewa na kuamua kuyabeba tu.”
“HAPANA! Hatuwezi kupeleka mambo kindugu huku tukiharibu kazi, iliyebeba hatima ya familia zaidi yetu sisi! Wapo watu hapa, wanaotegemea hii kazi tu, kwa ajili yakuendesha maisha ya familia zao. Hii kampuni ni zaidi ya familia yako na yangu. Kama ameshindwa kukusikiliza mkiwa peke yenu, muite sasahivi uzungumze naye, na umfukuzekazi.” Hicho kipengele cha mwisho kilimshitua, akabaki amekodoa macho.
Hakutegemea kufukuzwa kwake kazi. “Si unasema umeshajaribu kuzungumza naye, ikashindikana?” Kimya. “Sasa nakuwekea mazingira ya kuzungumza naye. Atakusikiliza, na utapata nafasi ya kumfukuza kazi. SITAKI UZEMBE. Lakini kama na wewe unashindwa kufanya kazi yako, nijulishe tutafute atakayeweza kuifanya.” “Hata kidogo! Tena itakuwa vizuri. Itawasaidia wengine kuongeza juhudi na kutozembea.” JJ akabaki akimwangalia. Akajua ndio anaambiwa asiendelee kumpotezea muda.
~~~~~~~~~~~
Akatoa simu na kumpigia Rodrick. “Weka kwenye sauti.” JJ akamuwahi kabla hajapokea. Akaona simu inakatwa zaidi ya mara tatu. Akamuona anapiga simu ya mezani. Sekretari wake akapokea. “Nenda ofisi za wahandisi, sio upige simu, nataka uende mpaka kwenye meza ya Rodrick, niitie.” Simu ikakatwa. Kimya hapo ofisini. HR jasho linamtoka japo ofisi imejaa baridi.
~~~~~~~~~~~
Hodi mlangoni na kuingia. “Wanasema aliwahi kutoka.” “Niitie kiongozi wake.” Akatoka, baada ya muda akarudi kiongozi wao. “Heshima yako mkuu!” “Rodrick hayupo ofisini, nimeambiwa aliwahi kutoka. Saa ngapi, na je, ulimruhusu?” Kwa kuwa walishajua kuna kufukuzwa kazi, akamkana kabisa.
“Na mimi nilisikia hivyohivyo kama ametoka.” “Kwamba hajakuaga!?” “Huwa haagimtu.” JJ akacheka kwa masikitiko huku akitingisha kichwa kama anayekataa, kuwa hiyo haikubaliki.
“Sasa kesho nina safari, ila nitapita hapa kazini. Saa mbili kamili asubuhi, nitakuwa na kikao na mwanasheria wa kampuni, wewe, Rodrick na afisa mwajiri. Tumeelewana?” “Mbili kamili bila ya kukosa.” Kiongozi wa Rodrick akajibu kwa nidhamu.
“Na ili kuhakikisha hilo linakaa sawa, nitamtumia ujumbe wa kiofisi kumtaarifu kikao cha kesho ili asichelewe.” Huyo afisa mwajiri akawa amehitimisha kikao. “Ni hilo tu kwa sasa.” Wote wakatoka bila nyongeza.
~~~~~~~~~~~
Huku kwa Tuma akabakiwa na gari bila Jerry. Hakumsikia hata kwa ujumbe wa kumjulia hali, wala kumuaga, kitu kilichozidi kumchanganya. “Kwamba ndio hata kuniaga jamani!” Tuma akazidi kuwaza macho kwenye simu muda wote, akitegemea hata kaujumbe kafupi! Lakini wapi! Ikawa asubuhi, ikawa jioni! Kimya. Akajihisi si wa maana kabisa kwa Jerry, na kuzidi kunyongea.
“Na mimi ningekuwa wathamani kwake, asingeacha kuwa na mimi kwenye kipindi hiki kigumu!” Hilo nalo likazidi kumuumiza. Alishamzoea Mbaki, hata akiimwa kichwa, atajua na kumtaka ahusike na hilo tatizo.
Bado Kisasi Kwa Familia Ya Salamba
Siku ya jumatano ambayo ndio safari ya Dubai, JJ aliamkia ofisini akiwa kama Mbogo aliyejeruhiwa! Akaweka uso wa kazi, akapitiliza ofisini kwake baada ya salamu na sekretari wake. Ilikuwa saa mbili kasoro 10. Akafanya yake mpaka alipopata simu kuwa wamefika. Akaangalia muda ilishakuwa kasoro tatu. Akawaambia wakaribishwe ndani huku akikataa kahawa aliyokuwa ameandaliwa.
Wakaingia wote wanne. Mwanasheria wake. Safi na kichwani yupo vizuri. JJ alimuheshimu sana. Afisa mwajiri, kiongozi wa wahandisi na Rodrick, shemeji. Wakasalimiana, na kukaa. Walipomuona JJ anaangalia muda wakajua wanatakiwa waanze.
“Jana muda wa kazi tulikutafuta Salamba, lakini haukuwepo na kiongozi wako hakuwa na taarifa zako.” “Kwanza niombe radhi.” Wote wakashangaa sana, mpaka JJ akawaona vile nyuso zao zilivyoonyesha mshangao kama ambao hawakutegemea huyo kijana kuomba radhi, ila akanyamaza.
“Niliondoka jana kwa dharula, mzee alianguka kwa shindikizo la damu/stroke, alikimbizwa hospitalini, akili ikavurugika ikabidi kukimbia. Naomba radhi. Hapo nilikosea.” Akajishusha, usingedhania ni yeye! Wasijue ameshapata habari za baba yake, akajua na hapo kibao kinamgeukia.
“Lakini hii sio mara yako ya kwanza! Unautaratibu wa kutoka bila kuaga!” “Kiongozi wangu huyu hapa, muulize kama huwa simuagi.” Kiongozi wake akabaki akimtizama kama anayemuuliza ulianza lini! JJ kimya macho kwenye kompyuta wapo mbele ya meza yake wakiendesha kikao.
“Tuweke hilo pembeni. Nafikiri unakumbuka kikao chetu cha jana juu ya utendaji kazi wako, napo hatukufikia pazuri.” “Ukimaanisha nini?!” Hapo JJ akaingilia kwa swali. “Ilikuwa kila anayeleta ripoti yake, nikisoma, namuita kwa mahojiano. Nilifanikiwa kwa wote, kasoro Rodrick.” “Ukimaanisha nini? Hapo ndipo sijaelewa!” “Alisema yeye hana muda wa kuzungumzia mambo mara mbilimbili akiwa ameshaniandikia.” JJ akakunja uso na kumtizama Rodrick kisha HR wake.
“Kwamba alikataa?!” “Huyu hapa muulize kama nadanganya. Nimefanya kikao mpaka na kiongozi wake juu ya utendaji kazi wake na kitengo kizima, kasoro yeye peke yake.” “Nilipanga leo nimuombe tufanye kikao.” “Kwamba wewe hapa kwenye hii kampuni ndio unaendesha mambo!?” Kimya maana JJ aliuliza kwa ukali akimshangaa kabisa.
“Mimi mwenyewe siwezi kuitishwa kikao na yeye, nikakataa! Yeye ndiye anayejua nani amuweke wapi, yupi afanye nini ili kuendesha mambo. Sasa basi, nina haraka, na kwa kuwa ulikataa kikao cha kwanza cha hiari hiki cha sasahivi ni kupewa tathimini ya kile walichokiona juu ya utendaji kazi wako na maamuzi. Hapatakuwa na mjadala. Ila utapewa nakala zako kama utahitaji kuzitumia baadaye. Endelea.” Akamtaka afisa mwajiri, huyo HR, aendelee.
“Kutokana na utendaji kazi wako na uhitaji wetu hapa, sitaendelea kukupotezea muda kama unavyosema ‘hutaki tukupotezee muda’. Nakuruhusu utupishe, tutafute mtu atakayeendana na utaratibu wa hapa.” “Kwamba hata onyo sipewi!? Kwamba leo nyinyi wawili mnanigeuka kwa kuja kuniharibia maisha!”
“Hili jalida lina nyaraka ambazo moja wapo ni nakala ya kile ulichoandika wewe mwenyewe baada ya kuomba unitayarishie ripoti ya utendaji kazi wako kwa muda wa miezi mitatu. Ulinipa karatasi moja mengine ukaniambia nimuulize kiongozi wako, nisikupotezee muda.”
Akaendelea. “Nakukabidhi na barua kutoka kwangu na kiongozi wako vile tulivyo kutathimini sisi kama watu tuliofanya kazi na wewe. Ni hiari yako kutunza au kutupa. Na ndani pia kuna malipo yako ya mpaka jana.” Mpaka JJ akashangaa vile alivyojiandaa kwa haraka. Akajua huyo kijana ashawasumbua sana, wamechoka naye.
“Una nusu saa ya kukusanya vitu vyako kwenye meza yako ili kupisha mtu mwingine. Kwangu ni hilo tu.” JJ akanyanyua simu, ‘Niitie mmoja wa askari.’ Wakashituka. “Mimi sijakataa kutoka.” “Najua.” JJ akajibu na kutulia. Baada ya muda mfupi sana askari akawa amefika. Wanalinda hapo.
Akasalimia kwa heshima. JJ akaitika. “Naomba umsindikize bwana Salamba kwenye meza yake, umsubirie akiwa anakusanya vitu vyake, atoke kwa utulivu bila kelele wala matusi. Sitaruhusu fujo na mjadala mwingine wowote tena, maana alishapewa nafasi zaidi ya mara moja, kuzungumza na viongozi wake, yeye mwenyewe alishindwa.”
“Hivyo basi, Rodrick Salamba, si mfanyakazi wa hii kampuni tena. Haruhusiwikuingia pale getini tena. Utaweka picha yake kwenye sehemu ya Ulinzi na Usalama ili kila mlinzi anayeingia zamu hapa, ajue. Na watu wa IT watatoa uwezo wake, kwenye kila system ya hii kampuni wa yeye kuingia humu ndani na kutumia chochote cha hii kampuni. Na Rodrick?” Akamgeukia yeye sasa.
JJ aliweka uso wa kazi, kila mmoja hapo alikaa sawa. “Mimi nitalinda wafanyakazi wangu. Hiki kilichotokea hapa ni cha amani ila taarifa zake zitapelekwa vyombo vya usalama na ndio maana unaona na mwanasheria yupo hapa. Chochote kitakachowapatahawa, jua wewe utahusika moja kwa moja. Ni hilo tu.” Kila mmoja akasimama na kutoka, askari akiwa nyuma ya Rodrick. Angalau JJ akahema kwa nguvu na kutoka hapo akiwahi ndege kwani alimwambia Jerry watakutana uwanja wa ndege.
~~~~~~~~~~~
Inaendelea….
0 Comments:
Post a Comment