“Hebu Ruhinda niambie ulichoambiwa na Patel?” Wakajua kumbe mzee Ruhinda alichelewa kufika hapo alikwenda kuzungumza na daktari aliyempasua Ayvin. “Ni vilevile alivyotuambia. Nikusubiria mpaka amalize dozi nzima, watamrudisha tena kwa kipimo cha MRI kujua uvimbe ulipofika, kama umeisha ndio watamtoa kwenye coma. Sasa na nyinyi mbona mmeishia hapa nje?” “Baba anauliza.” Paul akaongeza swali kishabiki akimtizama Paulina, dada yake.
“Twende ukamsalimie mama, Ayan.” Mama Ruhinda akamchukua Ayan kutoka kwa babu yake na kuingia ndani bila ya kujibu swali la Paul. Mina aliposikia mwanae anaingia, akasimama kwa haraka. “Mama!” “Umependeza Ayan!” “Dada Judy ameondoka. Bibi ndiye amenivalisha, babu amenifunga tai.” Mina akashituka na kumwangalia mama yake mkwe.
“Kaa naye huyo, usimbebe.” Andy akamuwahi kabla hajamnyanyua. “Kwanza urefu ameshakupita!” Paul akaongeza. Mina akamwangalia Ayan na kucheka kidogo. Akamshika mkono na kwenda kukaa naye pembeni ya mumewe.
Hakuna Msiba Usiokuwa Na Mwenzie.
Likawa jambo juu ya jambo kwa Mina. Mtoto mgonjwa na msichana wa kazi waliyemtegemea kubaki na Ayan nyumbani wakati wakiuguza hospitalini, ameondoka.
“Sikutaka kuwasumbua asubuhi asubuhi, ila tunachohisi jana tulipokwenda kuwachukua, atakuwa alibeba vitu vyake vyote. Ameondokea nyumbani kwangu. Tumeamshwa na mlinzi akisema wamemzuia getini akitaka kutoroka. Walipomuuliza, akawa hana majibu ya kueleweka ndio wakaja kutugongea.”
“Ruhinda akamuuliza ni kwa nini anashindwa hata kuaga? Akasema anawahi basi la kwanza kurudi kwao, amepigiwa simu usiku mwingi kuwa mtoto wake ni mdogo mgonjwa sana. Kitu ambacho nahisi si kweli.” “Nilijua amenidanganya tu.” Mzee Ruhinda akadakia.
“Ila nikamuuliza kama kuna pesa zozote anadai akasema…” “Kwanza ni sisi ndio tunamdai. Judy alikuwa akiomba mshahara wake hata kabla ya mwisho wa mwezi akisema ni matumizi ya watoto wake. Na hata hivyo alikopa pesa zaidi akaomba awe anakatwa kidogokidogo kwenye mshahara wake, na pia ikawa tukifika mwisho wa mwezi hakuna pesa ya kukata, kwa kuwa anakuwa ameshachukua mshahara wote kabla ya muda.” “Basi sivyo alivyoniambia.” Mina akashangaa sana.
Maana alikuwa amenyamaza akimpapasa mwanae wakati mumewe anamjibu baba yake. “Amekwambia nini!?” “Alisema anaona awaache tu kipindi hiki mnauguliwa, na yeye anaenda kuuguza. Mtoto wake akipona, atarudi.” “Nyie Judy ni muongo! Na anasema ameokoka!” “Si ndiyo hayo nasema! Mpaka washirikina na wachawi siku hizi wanajificha kwenye ulokole!” Paulina akadakia kishabiki, wakajua tu anamsema Raza.
Wewe Utanyamaza Kimya, Nami Nitakupigania
“Paulina, wewe ni mkubwa sana kwangu na ninakuheshimu. Nakwambia haya kwa heshima sana. Wokovu upo, na Yesu ni halisi. Anabadilisha. Hakuna dhambi kubwa na ngumu Yesu anashindwa, kwa sababu kazi ya msalaba ni halisi.” Akaendelea Mina, wote kimya.
“Upande huo uliopo Paulina, hama. Hamia kwa Yesu kama Raza.” Mpaka Pius akamwangalia. “Raza unayemtafuta kwenye uchawi, ushirikina na uuwaji, huko hayupo. Mwenzio Yesu alishamtoa huko muda mrefu sana, wewe unahangaika na dhambi za Raza za nyuma.” Wakajua wote waliwasikia.
“Mimi sihangaiki na Raza, ila nimesema ukweli.” “Ukweli gani huo Paulina wifi yangu, unautafuta kwenye majumba ya watu?! Mpaka kupigia simu wafanyakazi wetu kutafuta mambo yaliyotokea ukiwa wewe haupo, halafu unayasambaza kwa uharibifunamna hii!?” Wote hawakutegemea.
“Kwa nini wewe unakuwa upande wa kuongeza tatizo kwenye kila tatizo linapotokea? Kwa nini unapenda ufitini?” “Mimi sio mfitini. Nimesema kile nilichoambiwa. Sina haja ya kufitini mtu wakati Raza uliyemuamini, amekamatwa na macho zaidi ya sita, na watoto wake wameshuhudia!” “Anachojaribu kusema Mina ni hiki, tukiwa katika hali kama hii. Mtoto anahali mbaya hivi, kwa nini usipigie simu madaktari ukauliza hali ya mtoto, unapigia simu wasichana wa kazi kuuliza kilichotokea?!” Andy akatengeneza kauli ya mkewe kwa dada yake.
“Mtoto yupo hospitalini na najua Paul anahangaika naye.” “Mbona hicho hakijamzua baba kwenda kuzungumza na Patel mwenyewe, wakati anajua sisi tupo hapa, na Paul yupo!?” Andy akazidi kumuhoji dada yake.
“Naona mnataka kunimalizia hasira mimi ambaye nipo hapa na nyinyi, mnamuacha Raza aliyemdhuru mtoto na kujificha.” “Ninajua anachokifanya Raza sasahivi.” Wote wakashangaa na kumgeukia Mina kutaka kujua.
“Kwa asilimia 90, najua tokea huyu mtoto anaanguka mpaka sasa, Raza hajaweka kitu mdomoni anaomba kuliko mimi.” Pius hakutegemea. “Na inawezekana yeye ndio anahali mbaya kuliko sisi wote hapa.” “Kweli Mina binti yangu?” “Baba, Raza amebadilika sana. SANA. Kuna kilichotokea tu akiwa na Ayvin, lakini Raza anampendahuyu mtoto si kwa unafiki. Nishamuona akiwa na Ayvin, wao wawili hawakujua kama nipo mahali nawaangalia, tena zaidi ya nitakavyokwambia.”
“Akitokea Raza na huyu Paulina mbele ya Ayvin, huyu Ayvin atamkimbilia Raza na si shangazi yake.” “Lakini kweli!” Mumewe akaafiki kama anayevuta kumbukumbu. “Na mtoto si mnafiki. Ni malaika wanaojua moyo wa mtu.” Mama Ron akaongeza akisikika kuthibitisha.
“Sawasawa mama. Nikimaanisha hivi, yaani huyu Ayvin, anajua kama Raza anampenda. Ingekuwa Raza anajifanyisha sisi tukiwepo akiwa na Ayvin hampendi, Ayvin asingekuwa akimkimbilia au kumkumbatia.”
“Na kwa hakika, najua alimuona Raza ameondoka pale sebuleni, yeye mwenyewe akamfuata.” Wote wakabaki kumsikiliza.
“Kwamba japokuwa akili ilikuwa kwenye michezo, lakini alikuwa akimwangalia na Raza.” “Sawasawa Andy. Na ndivyo alivyo Ayvin. Akija Andy kutoka kazini mpaka huwa anajificha, kwenda kwanza chumbani kuoga, ndipo anatoka kwa sababu akishamuona Andy, atamfuata mpaka chooni. Ndio maana pia na ratiba zake amezibadili. Anaanza mazoezini kwanza, anakuja kuoga ndipo anatafuta watoto. Hatatoa macho yake kwao mpaka wakalale maana atamfuata Andy mpaka anafunga macho atataka kuwa naye au akicheza basi awe karibu ya Andy, yaani macho yake yawe yanamuona. Vinginevyo akigundua tu hayupo pale, ataacha kila kitu na kuanza kumtafuta mpaka ampate.”
“Na kama mmegundua, anaweza mfuata Raza kuliko hata Pius kama mimi na Andy hatupo. Hata Judy mwenyewe japokuwa tunaishi naye, huwa hamfuati kwa sababu ameshajua Judy anakuwa naye kutimiza wajibu. Na Ayvin anapenda mambo ya kupendana sana. Anajua ni nani anampenda na kumpa muda wake, na nani hamfuatilizi.”
“Sasa nyinyi ni watu wazima hapa, ndio mjiulize, kama Raza aliondoka kwa kujiiba pale sebuleni kama alivyosema Poliny, na kumuacha na wengine wote, ilikuaje Ayvin amfuate mpaka juu?”
“Halafu tusema Raza alitaka sana kumuu Ayvin kama unavyosema wewe Paulina, kwa nini amuue kwa wazi na atafute ushahidi wa watu kushuhudia, asimuue akiwa na Ayvin tu peke yake chumbani hata usiku akimlaza? Kwamba amzibe pua mpaka afe?” “Lakini kweli?”
“Maana kuna wakati mwingine Pius anakuwa hayupo hapa Dar, Raza anamfuata Ayvin hata jumamosi jioni anasema amekuwa mpweke, Polla hana muda naye, anamuomba Ayvin, tutakutana nao jumapili kanisani. Anaondoka na watoto wote, ila Judy anasemaga akifika kule anakuwa hana kazi maana Raza anataka kufanya kila kitu yeye mwenyewe.”
“Sasa jamani, kama huyu Raza alikuwa akitafuta kumuua huyu Ayvin kwa kiasi hiki, si angemuwekea mto usoni huo usiku wakiwa watu wote wamelala, na kujidai asubuhi ndio amekutwa amekufa hata na Judy, ili kuondoa ushahidi kwake?” Pius hakuwa akiamini ndio na yeye kujisikia vibaya kushindwa kumfikiria mkewe kama Mina.
“Kwamba wewe Paulina unamuona Raza ni mjinga sana hawezi kufikiria?” “Mimi simuoni kama mjinga naongea kile watu wameshuhudia.” “Kwa nini? Kwa nini sasahivi, kwenye kipindi hiki ambacho mwanangu amelala mahututi pale, wewe ndio unazunguka kusaka ushahidi wa kuharibu na si kuhangaika mtoto apone?” “Si madaktari wanamshugulikia!?” Akajibu kwa jeuri.
“Umeshindwa wewe hata kuomba kweli!? Kweli Paulina unaona muda huu ndio mzuri wa kusaka ubaya wa watu na sio kutafuta jinsi ya kumsaidia mwanangu? Haya, tufanye kweli Raza alimsukuma kwa makusudi. Habari unazohangaika nazo sasahivi, zinasaidia nini? Na kwa nani?” Mina akaendelea kumuuliza ila kwa hasira.
“Swali zuri sana, na baba mwambie ajibu.” Paul akaongeza. “Maana kila mtu yupo kwenye wasiwasi sasahivi, yeye mwenzetu ni kama haoni kinachoendelea, anashugulikia mengine! Ukute umbea wake ndio umemfanya hata msichana wenu aondoke.” “Paul jiangalie wewe?” “Inawezekana kabisa.” Mzee Ruhinda akaongeza kama aliyefunguliwa macho.
“Wewe kwa nini umpigie simu na kuanza kuzungumzia mambo yasiyokuhusuukitafuta habari ya tukio baya kama hili?” Baba yake akamuuliza. “Na namjua Paulina dada yangu, kuna ambayo hapo aliongea na kuzidi mpaka akamtia hofu.” “Wala sijaongea chochote!” “Kwamba wewe ulimpigia simu tu na kuuliza kisha ukaambiwa, na kukata?!” Andy akamuuliza kwa kumsuta. Kimya.
“Halafu ukatoka hapo na kumpigia simu na msichana wa Raza, ukauliza na kukata bila ya kuzungumza chochote?!” Andy akaongeza kwa kumsuta. “Mimi nilitaka kujua.” “Ndio Mina anakuuliza, ILI IWEJE?” Paul akauliza kwa kumsuta zaidi.
Familia hii fujo zao zinaongezeka kwenye matatizo. “Sasa ushajua kama Raza kamsukuma. Ndio wazazi wa mtoto wanakuuliza, unataka nini sasa?” Paul akazidi kumuuliza. “Unafiki tu!” “Sawa, mimi mnafiki. Jibu sasa! Maana wewe kazi yako wakati wote ni kutafuta matatizo Paulina, kana kwamba yako yapo sawa! Wivu tu na roho mbaya.” “Wivu kwa lipi? Sina hata wivu naye huyo Raza.”
“Ni wivu na roho mbaya kuona sasahivi hii familia inaamani, Raza na Mina wanapatana, wewe umewekwa pembeni, roho yako inasumbuka. Sasa mama wa mtoto ameshasema Raza HANA HATIA. Haya pasuka sasa.” “Kwa lipi? Kwa lipi?” Paulina hata hakuonekana kukubali kushindwa!
“Upande huo uliopo Paulina wifi yangu, HAMA. Hama ili Mungu pengine atakuja kukupa Raza wako ambaye kwenye siku ya shida yako kama mimi hii leo, ataweza fichauso wake kwa wanadamu, na kubaki akimlilia Mungu kwa niaba yako. Akimsihi Mungu akutane na shida yako. Ni hilo tu. Jua Mungu yupo na anabadilisha.”
“Anabadilisha wale ambao wameshindikana kwa fahamu na akili za binadamu. Acha kushindana na kazi ya msalaba, hutashinda.” “Mimi sishindani.” “Unashindana na kazi ya msalaba Paulina. Na kila wakati Mungu anakuonyesha kuwa yeye ni Mungu, hachunguziki kwa akili ya kibinadamu, lakini unakataa kukubali.”
“Unakumbuka ulipokuwa ukihangaika kusaka habari zangu?” “Ndugu zako wenyewe ndio waliokuwa wakiniambia.” “Kwa kuwapigia simu wewe mwenyewe.” Mama Ron akadakia.
“Ukakusanya habari zangu zote. Ukazitoa msalabani ambako Mungu alishanisamehe, kwako zikawa mzigo mzito zikikulemea, ukaanza kuhangaika nazo ukidhania ni siri na mdogo wako hanijui nilikuwa nani. Nikakuthibitishia uliyoyatafuta ni kweli na zaidi. Andy akakuthibitishia ananijua na amenioa akiwa ananijua. Nikakwambia vile mama yangu alivyokuwa akiniombea mpaka nikabadilika. Ukahangaika wee kuweka ufitini kila mahali juu yangu. Hapo napo ukakwama maana ulikutana na nguvu za Mungu. Mungu akakuthibitishia kuwa huwa anachukua takataka na kuzitengeneza.”
“Sasa hivi unahangaika na Raza. Unamtafuta aliye hai katikati ya waliokufaPaulina! Huko unakomtafuta Raza, hayupo na hutampata. Sasa ukiendelea hivyo, huko unakomtafuta Raza kwa nguvu hivyo, utakuja kukutana na hasira ya Mungu wake. Shauri yako!” “Mimi simta…” “Paulina unashupasa shingo, na itavunjika. Nakuhakikishia achana na Raza huyu.”
“Huyu Raza wa sasahivi ni mwingine, mimi mwenyewe ananitishaa. Jamani Raza anatembea na nguvu ya Mungu ya ajabu sana, binafsi huwa ananitisha au kunishangaza. Kuna jinsi Mungu anamtumia Raza, hakika nawaambia sio kawaida. Ipo siku mama Briana atakuja kuwapa ushuhuda wake, vile Raza alimuombea kijana wake, alikuwa na tatizo ambalo lilishindikana hospitalini, lakini Raza akamuombea kwa kumuwekea mkono, palepale yule kijana akapona, kaka Nyange anasema mpaka Raza mwenyewe akaogopa nusu akimbie, maana hakujua kama Mungu atafanya palepale. Siongopi, kaka Nyange anaweza kuja kuwashuhudia maana huwa haachi kumcheka Raza juu ya hilo. Na nafikiri ndio maana shetani anahangaika naye.” Mina akaongea kwa uhakika kabisa na kuwashangaza.
“Kuna kitu kilitokea kati yake na Ayvin, wote sisi hatujui kwa hakika. Na mimi sitaki mtu amsumbue kwa kumtoa alipo sasahivi, hata kama yupo kwenye hofu, kwangu ni faida ili aendelee kumlilia Mungu wake.” Paul akacheka kidogo.
“Unamtumia vibaya?” Akamuuliza akicheka kidogo. “Sina jinsi Paul! Raza ananguvu ya maombi ya ajabu sana. Hakika akiomba miujiza inatokea. Naona hiyo hofu yake huko alipo, akihisi anachosema Paulina ndicho wote tumeamini, ni bora, ili aendelee kumuita Mungu wake, mwanangu atoke pale kitandani. Hata kama atakuwa kipofu, ilimradi aamke tu.” Mina akaanza kulia.
“Wewe sasa unaharibu Mina. Ushajua tunaomba. Na unaye Raza anayekuombeahata sasa. Basi tembea kwenye imani.” “Naogopa Ron!” “Najua. Najua inaogopesha. Lakini si umesema ipo miujiza?” Akatingisha kichwa akifuta machozi.
~~~~~~~~~~~
“Basi jua Ayvin ni ushuhuda wako wa kesho. Tembea hapohapo usitoke, usiyumbe au kuyumbishwa. Na sisi tunasimamia hapohapo. Tunaamini uponyaji, ila tunaomba Mungu aje atuthibitishie kwa macho haya ya nyama. Unanielewa?” Kaka yake akamuuliza na kuendelea.
“Yaani sasahivi, sisi wote tunaamini Mungu yupo kazini. Kile wanachofanya madaktari wanao mshugulikia, na kile kinachoendelea kwenye ulimwengu wa Roho, tutakuja kukithibitisha kwa macho. Tuombe.” Bwana Ron aliomba mpaka akawashangaza kina Ruhinda.
Taratibu ila kwa kumaanisha na kwa ufasaha. Aliomba mpaka wakafurahia. Akanyamazisha kelele zote za ibilisi na kukataa sauti zote za ungurumaji. Akimsihi Mungu kuwatuliza ili wanao shugulika na Ayvin waweze kumsikia yeye tu na kuhusika kwenye uponyaji wake. Akaomba amani katikati yao na umoja ili Mungu aamuru Baraka. Mpaka anasema Amen, Mina anatumaini jipya.
~~~~~~~~~~~
Bwana Ron alifunga huo mjadala kwa hekima ya namna yake! Ni kama alimkemeana Paulina. Akikataa maneno maneno. Maombi yanaisha kila mmoja na tumaini jipya ila hukumu kwa Pius.
“Niliwezaje kumkasirikia Raza na sikufikiria kama anavyomfikiria Mina!?”Akajilaumu sana akijua wazi alikwenda kuchukuwa watoto kwa Mina ili tu kumfurahishayeye. Aliporudi nyumbani kutoka hospitalini, hakumkuta Raza chumbani, akajua anajificha chumbani kwa Poliny aliyeamua kurudi zake chuoni bila kurudi tena nyumbani mpaka patulie.
Pius akijua mkewe alipo, asimfuate, badala yake akamshukuru Mungu kwamba hatamuona usiku huo wala kuzungumza naye, akiwa hajui aongee naye vipi maana aliamini kuwa alimsukuma. Alichokuwa hajui ni kumsukuma kwa bahati mbaya au la! Sasa kwa kuwa hakutaka kudanganywa, akajiambia amuache tu huko alipo.
~~~~~~~~~~~
“Asante Ron.” Mina akaongea akimwangalia kaka yake. “Karibu. Na usisahau. Kila hofu ikikujia, jua Mungu wetu yupo kazini. Hasinzii wala halali. Na hata sasa anatuona. Hili jambo halijamshitua. Alilijua, na analishugulikia.” “Asante Ron. Asante kwa kunisaidia hata mimi. Nilishakuwa na hasira aisee! Nilikuwa siwezi jisaidia.” Andy akaongea.
“Ndivyo alivyo shetani na kazi zake. Huwa analeta tatizo na kuanza kukaribisha mafarakano ili wote tuache kumuangalia Mungu, tunaangaliana sisi ambao hatuna uwezo wa kusaidiana. Akijua kwenye umoja ndipo Mungu anaamuru baraka.” Mama Ron alijisikia fahari huyo, kuona kijana wake anazungumza pale na wanamsikiliza. Akamshukuru Mungu moyoni mwake na kubariki mikesha na kufunga alikokuwa akifanya juu ya hao watoto wake wawili.
Pakatulia kabisa. Angalau Pius akaweza hata kusimama na kumshika mkono mwanae kama mama yake alivyokuwa akimfanyia. Wakamuona anampapasa taratibu, akimbusu huo mkono mara kadhaa, kisha kumfunika kama akiweka sawa shuka alilofunikwa vizuri.
~~~~~~~~~~~
“Umemwambia bibi asante kwa kukuchagulia nguo nzuri na kukuvalisha, na babu kukufunga tai?” Mina akawa akimuuliza Ayan. “Mwanao anashukurani huyo! Hasahau kukushukuru kwa kila unachomfanyia. Umemfundisha vizuri, Mina.” Mama Ruhinda akajibu yeye kwa haraka. “Kazi ya Andy hiyo. Tena huwa anamrudisha kwenda kumshukuru Judy, kama amesahau.” “Ndio maana kumbe!” Andy akamwangalia kijana wake.
Ukweli palibadilika hapo, hata hali ya hewa ikawa ya amani na utulivu fulani hivi, sio kama ilivyokuwa mwanzo tokea wanakutana hapo kwa ugonjwa wa huyo mtoto.
Love At First Sight
Huku kwa Tuma yeye ilikuwa ni jumapili iliyoanza na mwanzo mpya wenye tumaini jipya. Si kwa upande wa kurudisha hadhi yake tu kwa upande wa kuthaminiwa kimapenzi, bali hata mabadiliko ya kiuchumi. Mpaka inafika saa nane mchana, Tuma na mdogo wake wakawa wameshahamia Kinondoni, nyumba ya vyumba viwili. Na Tuma akiwa ameshajiridhisha ni kodi anayoweza kulipa mwenyewe hata hapo baadaye.
“Narudisha gari ya watu, nachukua yangu. Oga na ujiandae. Nikirudi nakuja kukuchukua, tunakwenda kwangu. Palepale wanapika chakula japo sijui ubora wake.” “Sawa. Nitakuwa nikikusubiria.” Jerry akaondoka na kumuacha Eli akipanga chumba chake. Hakuwa na kitanda ila wakaingiza kochi moja kubwa hapo chumbani kwake.
Jerry alishamsaidia Tuma kufunga kitanda chumbani kwake. Wala hakujiangaisha na kupanga. Akakimbilia kuoga na kujitengeneza. Akamaliza yote ndipo Jerry akawa anaegesha nje. “Natoka.” Akatoka kwa haraka.
~~~~~~~~~~~
“Umependeza sana Tuma. Sikujua kama umebadili nywele!” “Nilifunga kitambaa ili zisichafuke wakati wa kuhama.” “Hakika Tuma wewe ni mrembo. Kwa nini ulijizira kwa kiasi kile?!” “Nilikwambia Jerry! Nilijisikia kudhalilishwa vibaya sana, nikaona sina thamani tena. Ikawa kama najificha kwa watu.” “Usirudi kule tena. Huko ni kumpa mwanadamu nguvu kubwa sana, tena asiyo stahili.” Akatulia akiendesha mpaka Msasani.
Msasani Kwa Jerry.
Walipofika tu akamkaribisha ndani. “Sio pakubwa sana. Karibu unisubirie nioge.” “Ila ni pazuri! Hewa imechujwa!” Jerry akacheka na kushukuru. “Asante. Unataka chakula tule hapa au kule baharini?” “Wakati mwingine. Leo tutulie hapahapa. Tupate muda wetu kabla ya kusafiri.” Ikamgusa Jerry kuona Tuma anamuhitaji yeye zaidi kuliko kuhadaika hata na mazingira! Maana ni kweli hapo panavutia. Ingekuwa mwingine angechagua kubarizi!
“Na mimi nataka muda na wewe Tuma.” Akacheka na kuinama kwa aibu ya penzi, Jerry akimwangalia kama amfanyie kitu, lakini akashindwa. “Wapigie simu, agiza unachotaka, waambie watuletee huku.” Akamuonyesha simu ya mezani, akaingia chumbani.
~~~~~~~~~~~
Baada ya muda Jerry akatoka akiwa ananukia vizuri, halafu amevaa sweatpantsnyeupe, na juu akavaa kata mikono nyekundu. Na vile alivyomweupe! Bwana alipendezaile ya kuvutia haswa mpaka mate yakamtoka Tuma. “Unanunikia vizuri!” “Asante. Naipenda hii pafyumu na lotion zake, vimetulia. Na hapa sijapulizia pafyumu. Ni sabuni yake yakuogea, lotion na body spry tu. Hawajaleta tu chakula?” “Wamesema itachukua muda kidogo maana ndio wanaanza kupika.” “Basi tuanze na juisi.” Akammiminia juisi kutoka kwenye friji. Ilikuwa ya boksi aina ya apple.
“Sina ingine ndio maana sijakuuliza kama ungependa. Punguza njaa.” “Asante.” Kabla hajaanza kunywa wakasikia hodi. Akamfungulia na kumpisha mlangoni. Akaingiza chakula. “Mbona mapema! Kimeiva kweli?” “Usipopenda unipigie simu.” Wakacheka, akamlipa huyo kijana, akatoka kuwapisha.
Wakakaa mezani. Wakala kimyakimya tu, wote walipenda chakula. Jerry akatoa vyombo kama vilivyo akaweka nje ya mlango kwenye meza. “Hatuoshi?!” “Hapana. Watakuja kuchukua.”
~~~~~~~~~~~
Tuma akabaki amekaa kwenye meza, ametulia, Jerry akamsogelea. “Unawaza nini sasa?” “Hamna.” “Njoo tujilaze hapa kwenye kochi, uniambie kile unafikiria.” Akashangaa amejilaza kabisa, anapigapiga kochi mbele yake. Tuma alifurahi huyo! Analala pembeni ya Jerry!
Akasogea na kujilaza kwenye mkono wake kama mto, lakini akiwa amegeukia mbele amempa mgongo. Akamvuta karibu yake kabisa kisha akambusu shingoni. Mwili mzima ulisisimka! Bado haamini! Akatulia tu lakini huo moto uliokuwa ukitembea katikati yao, kama shoti ya umeme! Na kila mmoja wao alisikia. Siye mguswaji tu, hata amgusaji.
Jerry akaanza kumchezea upande wa juu wa shingo mpaka kwenye nywele pembezoni mwa sikio, taratibu. Tuma akishindwa hata kutikisika akihofia asije akatoa mkono wake hapo anapomchezea na kuleta hisia ambazo hata hakujua zipo ndani yake! Kimya hapo kochini amelalia mkono mmoja wa Jerry akisikilizia pumzi zake na alivyokuwa akinukia vizuri!
Akajisogeza karibu zaidi kana kwamba yupo mbali. Akambusu tena na kumuuliza kwa kujali. “Unawaza nini?” “Ulisema mnarudi lini?” Kama ambaye hataki aondoke na kumuacha. “Nitarudi Tuma.” Akajibu akimbembeleza. “Ila kujibu swali lako, kila kitu kikienda sawa, siku ya jumamosi. Nitakuachia hili gari ikusaidie usafiri.” AlimshituaTuma! Akakata stimu yote mpaka akataka kukaa, akamrudisha.
“Acha kupaniki! Sasahivi unaishi kwenye nyumba nzuri, yenye uzio na walinzi. Mtakuwa salama.” “Nitamwambia nini mama J!? Mumewe? Naomba fikiria mwenyewe Jerry! Naomba usiniache na maswali yatakayonifanya nishindwe kuyajibu.” “Basi nitazungumza nao kabla ya kuondoka.” “Utawaambia nini!?” “Nakuachia wewe gari. Sihitaji kujieleza sana. Na kama kuna maswali nina uhakika wataniuliza mimi. Usiogope.” “Naogopa Jerry!”
Kupenda.
“Nigeukie nikwambie.” Akageuka. “Sitakuficha kwa yeyote, Tuma. Kwa kuwa siibi wala sifanyi kosa. Mungu akipenda, kila kitu kikienda sawa, kesho namalizana kisheria na Sandra. Nipo huru. Na hili nimemwambia hata kaka akiwa na Jeremi. Nina hamu ya kupendwa mimi kama Jerry. Natamani maisha waliyo nayo na wapenzi wao. Natamani kumuweka mwanamke mkononi kama hivi tukatulia bila hofu ya kila wakati kuhusu pesa. Sasa yote hayo nitayapataje nikianza kuficha?” Kimya.
“Mimi sio kijana mdogo! Umri umekwenda. Sina muda wa kupoteza tena. Najua ninachokitaka, ni wewe Tuma.” “Kweli!?” Ndio kwa mara ya kwanza akafunguka kwa uwazi huo, Tuma asiamini akimtizama vile anavyovutia pale alipojilaza.
“Sina sababu ya kukuweka hapa karibu na mimi kama sina nia na wewe Tuma. Mimi sio muhuni na sina udhaifu wa ngono kwamba inanipelekesha inabidi nijitahidi, au kukudanganya ili nikuvue nguo!” Mpaka akamtia aibu Tuma. “Na hili nimekuwa nikilirudia sana kwa Sandra ili kumtuliza lakini nasikitika kwamba mpaka leo ameshindwakuliingiza akilini.”
“Haya, nilitaka kukwambia kesho nikiwa nimeshaachana na Sandra, lakini maadamu tumeanza, acha nikwambie tu. Nakupenda Tuma.” Mwili mzima wa Tuma ukapata vipele vya baridi kwa msisimko.
“Na nimejikuta tu. Isingekuwa hivyo, pengine ningesubiri sana baada ya kuachana na Sandra, lakini kwako nimejikuta nakupenda na siwezi kujizuia wala kusubiri. Na naona kama tunaendana kupita kiasi! Au wewe unaonaje?” “Mimi nilikuwa naona ni mapema sana nilivyokusoma, nikaona nipunguze mwendo.” Jerry akacheka.
“Usicheke bwana Jerry! Umekuja mkamilifu sana mpaka naogopa!” “Usiogope maana na mimi nimeshajaribu kujionya hivyohivyo nikijiambia nipunguze mwendo lakini nimeshindwa! Inakuwa kama unasoma hisia zangu na kuzitekeleza bila ya mimi kukwambia na hunipuuzi Tuma.” “Basi na mimi nimeona hivyohivyo. Halafu unaweza usielewe hili Jerry, lakini unanipumzisha. Kila wakati unaponiambia nitulie, unataka muda na mimi, nasikia kutulia maana nilikuwa nikihakikisha naweka akili kwenye kila kinachonijia nisikae chini nikajifikiria. Nikajisahau kabisa!” “Ulijificha kwenye kazi.”
“Basi wewe umejua. Na vile nilitokea kupatana na mama J, akaniamini hata na funguo za pale, ikanisaidia kufanya hata ambayo sitakiwi kuyafanya, ilimradi tu niwe mbiombio. Kwa hiyo nakushukuru na usichoke kunikumbusha. Nimekuwa hivi kwa muda mrefu!” “Tutakuwa sawa Tuma, usiogope.” “Unafikiri hivyo?” “Nimefanya kazi nikizungukwa na wanawake kwa muda mrefu, nimeshajua jinsi ya kuwasoma. Wewe ni watofauti, ninauhakika hatutashindwana.” Akahema kwa nguvu na kurudi kugeukia kama mwanzo. Wakatulia.
Jerry akampapasa kwa muda kisha akamkumbatia kwa mikono yote miwili akiwa ameikutanisha mbele. Akambusu mara kadhaa shingoni na kumnong’oneza sikioni. “Nakupenda Tuma.” “Na mimi nakupenda Jerry. Na asante kuja kwenye maisha yangu.” Akambusu na kutulia. Wakapitiwa na usingizi baada ya Jerry kuamua kuzitisha hisia zake.
~~~~~~~~~~~
Alikuja kuamshwa na mikono ya Jerry tena ikimpapasa. “Jerry!” “Tumepitiliza usingizi.” Akajinyoosha. “Sasahivi ni saa ngapi?” “Saa mbili.” Akambusu mara mbili kwenye ule mkono aliokuwa amemlalia. Akakaa.
“Naomba nirudi nyumbani.” “Kesho nitakuwa huru Tuma. Nivumilie.” Akawa amemuelewa. “Nikupe pole?” “Kwa sababu nimekupata wewe, inakuwa smooth transition.Nipo sawa. Si utavumilia?” “Na nina kusubiria pia. Usiwe na wasiwasi.” Wakaangaliana kama waongee kitu au wafanye kitu hata kiss, ikashindikana. Tuma akakwepesha macho, akainama kama anayewaza kitu.
Akamvuta mkono akiwa vilevile bado amejilaza, akaubusu kwa muda mrefu akiwa amefunga macho, akamuachia na kusimama. Jogoo alikuwa amesimama wima mpaka Tuma akakwepesha macho, akamuona na kuingiza mikono mfukoni akaondoka hapo.
“Chakula cha usiku?” Akauliza akiwa chumbani. “Bado nimeshiba.” “Unauhakika?” “Nilipika jana. Nikisikia njaa nitakula tena. Na wewe?” “Nipo sawa kwa sasa. Nikisikia njaa nitaagiza.” “Kama hivyo ni sawa.” Akabaki ametulia, amejiinamia akisubiria ila akiwa na furaha ya ajabu moyoni.
Akatoka ameshavaa. “Mbona umenyongea tena?” “Nafikiri usingizi tu, lakini nipo sawa. Twende ili na wewe urudi kupumzika.” Wakatoka kimyakimya kila mmoja na lake moyoni.
Akamshusha kwake, ila nje tu ya geti. “Kesho nitakuja kukupeleka kazini. Baada ya kifungua kinywa nitaondoka.” “Utarudi au ndio moja kwa moja?” “Lazima nirudi kukuchukua japo nina jiandaa na ile safari. Sina chochote cha safari, hata sanduku au begi la kusafiria, sina! Ndio naanza moja kabisa. Inabidi nipate muda wa kutosha kujiandaa.” Akamuelewa.
“Ila tutawasiliana usiwe na wasiwasi.” “Sawa. Nitakuona kesho Jerry.” Akashuka, alipoingia ndani ndipo akaondoka.
~~~~~~~~~~~
Raza akiwa magotini, anakabiliwa na shutuma kali, ambazo angeweza jitetea, lakini akaficha uso wake kwa wanadamu, hatimaye Mungu wake ameshuka kumtetea, Anapigana vita yake.
Usikose talaka yakusikitisha na ya kuumiza ya Jerry.
Nani ataachwa na maumivu?
Usipitwe….
0 Comments:
Post a Comment