Akabaki akisononeka moyoni kwani alishampenda Jerry na kupitiliza. Alikuja kwake akawa zaidi ya ndoto zake. Akajikumbusha jinsi alivyojionya kwake. ‘He is too good to be true.’ Alijionya Tuma kila alipokuwa na Jerry na kusaka mapungufu yake, nakuyakosa. Alikuja mkamilifu kupita kiasi!
Akakumbuka jinsi alivyomuweka mikononi. Alivyokuwa akimpapasa na kumnong’oneza kuwa anampenda! Kochi lilikuwa jembamba, lakini bado alihisi wapo mbalimbali. Akaendelea kujisogeza kwa Jerry, naye akampapasa mpaka kupitiwa na usingizi huku akifurahia harufu nzuri kutoka kwake. “Labda aliona hapatakuwa na muendelezo ndio maana na kwangu alihakikisha hanivulii nguo kama alivyomwambia Umi!” Akaendelea kusononeka kana kwamba mwaka ulishapita!
~~~~~~~~~~~
Wakati amebaki akimuota Jerry, huku kwa Sandra nako ndio macho yakawa yamefunguka, nakuona madhara ya kumtoa Jerry kwenye maisha yake. Ikawa ni kama kitambaa kinafunguliwa siku hadi siku na kuona uhalisia wenyewe.
Mzee wake bado alikuwa hospitalini, amepatwa stoke, iliyomsababisha kupooza upande wa kulia wote. Huo wote ni mshituko wa kuondokewa na mkono wa JJ kwenye biashara yake. Umri umekwenda, hawezi anza tena. Pesa aliyokuwa akiingiza kutoka kwenye kampuni ya JJ ni pengo ambalo halizibiki. Ukawa mshituko mkali sana.
Rodrick, kaka yake ndio huyo akawa amefukuzwa kazi tena kwa kufunguliwa jalida kabisa kuwa alifukuzwa kazi kwa makosa ambayo hakuna kampuni ambayo ingeweza muajiri endapo watampigia simu mwajiri wake wa zamani. Wangejua sababu ya kufukuzwa kwake kazi, kwamba hana nidhamu ya kazi. Hawezi kufanya kazi na wenzie. Haheshimu mamlaka. Mchelewaji kazini na anaondoka kazini atakavyo, tena bila ya kuaga.
Nani atamuajiri! Na pesa aliyokuwa akilipwa kwenye kampuni ya JJ ni pengo hata kwake, hakuna kampuni ingemlipa hivyo. Na yeye akawa kama mgonjwa wa akili. Ni kufunga na kufungua, maisha naye yakawa yamembadilikia. Watoto anasomesha kwenye mashule ya mamilioni ya pesa. Maisha anayoishi yeye tu, kabla ya mkewe ni ya kitajiri sana. Anafanyaje!
Kaka mkubwa huko alikokuwa ametafutiwa kazi na JJ na yeye tumbo joto, hajui kinachofuata. Maana ukimchunguza bata, huwezi mla. Ndio kiongozi kwenye familia hiyo iliyojaa kiburi na dharau. Hata yeye alijua, endapo watataka kumfukuza, hawata kosa sababu. Familia nzima tumbo joto.
Walijua kile Sandra alichomfanyia Jerry, kumfukuza kama mwizi, mbele za watu, mwanzoni hawakujali. Wakaona kwa vile Sandra alivyokuwa akimlalamikia mumewe, na wao wote kujiona bora kuliko yeyote, waliona bora amemfukuza, wasijue wamejipalia makaa kwenye maisha yao.
Hata shemeji zake walikuwa wakimdharau Jerry, huku wakiona dada yao anateseka na mzigo huo wa ndoa, bila kujua upande wa pili wa historia ya ndoa hiyo. Jerry anayelalamikiwa, ndiye aliyekuwa akiendesha hiyo kampuni kwa asilimia kubwa tu na kufanya maisha ya Sandra kuwa marahisi asijue Jerry ndiye anayehangaika, na kaka yake akisaidia chini ya pazia.
Jerry akijua wazi Sandra anadharau mchango wowote unaoleta yeye kwenye hiyo kampuni, lakini hakujali ila kupapamba na kumtaka atulie, asiwe nawasiwasi kila kitu kitakwenda sawa kauli iliyokuwa ikimfanya aonekane eti ni dhaifu, hataki kufikiria au kujishugulisha, kumbe yeye Jerry alijua anachozungumzia. Alijua misingi ya biashara hiyo na bado kaka yake hakuacha kumshauri huku akimsaidia kwa kila namna ndio maana yeye hakuwa akiona sababu ya kupaniki kila changamoto ilipokuwa ikitokea kwenye hiyo kampuni. Alijua hawawezi haribikiwa.
Akiwa anahangaika nyuma ya pazia kila kitu kiende sawa, mbele ya watu Sandra akijizolea sifa akijigamba yeye mpiga kelele ndiye anayefanya mambo yaende. Jerry hakujali, alikuwa akinyamaza tu.
Sasa mdogo wake alipotoka kwenye picha, JJ alikusudia kuwafungua macho kwelikweli bila kuwabakisha. Huo ulikuwa mwanzo tu, Sandra hajui mizizi ya Jerry kwenye hiyo kampuni aliyokuwa akitamba ni yake.
~~~~~~~~~~~
Katika yote, mbaya zaidi JJ alihakikisha familia nzima ya Salamba, hakuna atakayeweza mfikia tena. Si kwa simu tu, hata walinzi wake, sehemu zote, aliwaamuru, wasifunguliwe geti popote bila ridhaa yake yeye. Ikawa hakuna mtu kwenye familia hiyo ya Sandra, ambaye angeweza mfikia JJ TENA. Kwa hakika akawa amefuta mahusiano na kina Salamba kabisa.
Habari za kufukuzwa Jerry na Sandra kinyama vile, JJ alijua wazi, kama ziliweza mfikia mkewe, inamaana hata ndugu wa upande wa Sandra, walijua lakini walinyamazia. Inamanaa walikubaliana na hilo. Sasa eti leo na yeye JJ anapigia mstarihayohayo mahusiano waliyobariki yavunjike, wanajirudije kinyumenyume! Wanarudi kwa nani na kwa sababu ipi! Akaweka kikomo kwa vitendo.
Na Jerry mwenyewe hakuwa anapatikana kwa simu kitu kilichokuwa kikimhehushaSandra, aliyekwisha zoea kumchunga kama kuku wa kizungu. Akajifanya amesahau kabisa kama alimpokonya simu nakubaki akimsaka kama mwehu. Hata kabla ya siku ya talaka, alimtafuta sana kwa visingizio tofauti tofauti na kumkosa kitu kilichompandisha hasira na kuishia kuchoma vitu vyake moto. Yote hiyo ilikuwa hasira ya kumkosa Jerry kwa simu na kuona anakosa mamlaka naye, kitu ambacho hajazoea.
~~~~~~~~~~~
Sasa ili kupunguza makali yanayo wapata kama familia, akampa Rodrick kazi kwenye kampuni yake. Kwamba achukue nafasi ya Jerry kwa muda wakati akijipanga huku akijua wazi itamchukua muda mrefu kuja kuajiriwa tena kutokana na jinsi alivyoondoka kwa JJ ambaye tayari alishamuwahi mpaka kwenye vyombo vya usalama.
Baba yao akiwa hospitalini, Rodrick ndio ameanza kazi hapo kwa Sandra na amerithi ofisi ya Jerry, wakionyesha wengine kila kitu kinakwenda sawa, hawajayumba, maisha yao yanakwenda kama kawaida. Kazi zikaendelea Sandra akisifiwa ni simba jike, hataki ujinga, hayumbishwi na yeyote.
~~~~~~~~~~~
Ijumaa ikiwa ndio imeanza tu, akapokea barua kwenye bahasha. Kwamba mtu ameileta na kutaka aliyepokea asaini kuwa amepokea. Akasaini na kumpelekea Sandra. Ilikuwa ikitokea kwa mmiliki wa hilo jengo, akimtaarifu kuwa tokea anunue hilo eneo, miaka 6 iliyopita, hakufanyia ukarabati wa kina japo kulionyesha kuna mambo kadhaa ya kurekebisha. Hivyo basi angemtuma mtu/ inspector, kukagua siku inayofuata. Akiwa na mambo mengi kichwani, akaweka hiyo barua pembeni akaendelea na yake wala asitilie maanani.
~~~~~~~~~~~
Wahenga husema, akifa nyani, miti yote huteleza. Kwenye majira ya saa nne asubuhi, siku hiyohiyo, mwanasheria wa JJ akampigia. Akapokea asijue anazungumza na nani. Akataka kujua anazungumza na nani na kama ni Sandra mmiliki wa kampuni. Sandra akakubali.
“Natumaini umepokea barua pepe yangu.” Sandra akakunja uso na kufungua kompyuta yake upande wa emails. “Inakuhusu nini?!” “Madai yote, na jinsi ya kuyalipa.” Akamjibu kwa ufupi na kumshangaza sana Sandra. “Mimi sidaiwi!” Kimya upande wa pili.
“Hallow?!” Akaita kwa ukali. “Wewe ni nani, unayesema unanidai!?” “Kama ungefanikiwa kuisoma barua pepe niliyokutumia, ungekutana na jina langu. Lakini kwa sababu tunazungumza, sio mbaya kurudia.” Akajitambulisha jina lake kwa heshima, kisha akaongeza. “Ni muwakilishi wa JJ.” Moyo wa Sandra ulipasuka kama kumeangushwa chuma sakafuni, kwenye chumba kitupu halafu kulikuwa kimya.
“Kama utafanikiwa kufungua hiyo barua pepe, utakutana na nakala za mkopo na sahihi zako ulizowekeana na muhasibu wakati akikukabidhi hiyo pesa. Lakini tokea wakati ule ambao ni miaka zaidi ya 8 sasa, mpaka leo, hujafanikiwa kulipa.” Kimya, maana ni kama JJ hakuonyesha kabisa kama anahitaji kurudishiwa hiyo pesa!
Sandra alitoa macho karibu kumwagika. “Kama kutakuwa na swali lolote, tafadhali usisite kuwasiliana nami. Ninapatikana kwa simu na barua pepe, na vyote vinapatikana kwenye hiyo barua pepe. Ila kuanzia mwezi ujao hiyo pesa itaanza kutengeneza interestyaani riba. Unatakiwa kuilipa kwa wakati ili kupunguza usumbufu na ongezeko la riba. Siku njema.” Simu ikakatwa.
Kijasho chembamba kikaanza kumtoka Sandra. Japokuwa hakuwahi kudaiwa hiyo pesa, lakini ni kweli walipewa na kuongeza kwenye mtaji wa hiyo kampuni. Akatulia akitafakari jinsi ya kukabiliana na hiyo hali.
~~~~~~~~~~~
Akapiga mahesabu ya haraka haraka na kibabe akajiambia hana sababu ya kubeba huo mzigo peke yake, lazima Jerry na yeye ahusike. Akiwa ameshasahau kuwa alisema ni kampuni yake, na si ya Jerry, akaanza kazi ya kumpigia tena simu Jerry kama mwendawazimu, akisahau hiyo namba alishakuwa akimpigia tokea siku anamfukuza, na hakumpata.
Akajaribu kuvuta kumbukumbu kama siku ya talaka alimuona na simu, akashindwa kukumbuka maana siku ile alifika pale kumkomoa wala si kumalizana pekee. “Lakini hawezi ishi mjini bila simu!” Akawaza na kuendelea kumpigia.
“Mwanaume mshenzi huyu! Sasa hapatikaniki kwa simu wakati ana watoto! Wanae wakiugua!” Tayari akawa ameshasahau alisema hakuna aliyemsaidia kusukuma leba mtoto hata mmoja! Huwa linapofika swala la pesa, Sandra anakuwa kama mwehu! Anaipenda pesa kuliko nafsi yake. Zoezi la kumsaka Jerry kwa simu likaendelea ili ambebeshe yeye mzigo.
~~~~~~~~~~~
Kwa hakika Sandra aliruka, bila ya kuagana na nyonga. Na kwa kuwa ndugu zake Jerry walimjua ni mshupaza shingo, JJ alikusudia kuhakikisha inavunjika na walimwengu wasimulie habari zake kama walivyosimulia habari za mdogo wake.
~~~~~~~~~~~
Jerry akageuka mali hadimu. Wanawake wawili wanamuhitaji kama alumasi, huku mmoja akimsaka kwa udi na uvumba japo kwa malengo tofauti tofauti. Ila kwa hakika uthamani wake ukaongezeka kwao wote wawili. Kwa Tuma, mapenzi aliyokuwa akimpa, vile alivyomjali na alivyojibeba mwenyewe huyo Jerry, kwa Tuma ulikuwa muujiza ambao hata hakuwa amewahi kuuomba kwa ukubwa huo akijiambia, nisimjaribu Bwana Mungu wangu!
Ni ndoto ambazo hakuwahi ota, ila zikatimia, kisha kupotea gafla! Alikuwa akiteseka moyoni, hana wakumuulizia, hana wakumwambia. Kwa Jeremi ndio kabisa! Aanzie wapi kumuulizia kaka yake na wakati ni kama alishamuonyesha hausiki na mambo yao! Mama J naye? Angeanzisha chochote naye juu ya Jerry, asingeepuka maswali ambayo alijua wazi hana majibu yake, akaendelea kufa nalo rohoni, akisononeka kumkosa Jerry.
Kwa upande wa kina Salamba, kuondoka kwa Jerry kwenye maisha ya Sandra lilikuwa piga baya sana. Kila mtu aliguswa na kujua wamempoteza Jerry waliyekuwa wakimdharau kutokana na maneno ya kashfa ya Sandra yasiyoisha na kumlalamikia tena wakati mwingine kwa wazi kabisa, mbele ya ndugu zake, hata baba yake, akimkashifuhuyo Jerry, na mara nyingi Jerry mwenyewe anakuwepo akisikiliza jinsi mkewe anavyomuongelea vibaya kwa nduguze na watoto wake wakisikiliza.
Kwa hiyo wote wakamchukulia kama ni mzigo tu kwenye maisha ya Sandra, asiye na maana, tena hata kumshauri angeachana naye asiendelee kumchelewesha kimaendeleo, wasijue nyuma ya pazia jinsi Jerry anavyochapa kazi kwenye hiyo kampuni, ni Sandra tu ndiye aliyekosa shukurani na jicho la utoshelevu japo akaunti benki zilikuwa zikisoma vizuri SANA. Wote wakabaki kusubiria kupatikana kwa Jerry.
Ijumaa hiyo ikawa ngumu kwa wanawake hao wawili, kila mmoja kivyake. Jerry amepotea.
Kuliko Pokelewa Penzi Lililopuuzwa.
Tuma akiwa anajiambia anamkosi, ameandikiwa kufa peke yake, akiwa anakaribia kutoka, simu yake ikaanza kuita. Kuangalia alikuwa Jerry. Alishituka na mapigo ya moyo yakabadilika, akabaki akiiangalia mpaka ikakatika. Akaona ujumbe unaingia. ‘Ni mimi Tuma, naomba pokea simu yangu tafadhali. Jerry.’ Alipoona amesoma, akampigia tena. Ikaita karibu na kukatika, akapokea.
“Tuma?” “Abee!” Akaitika kinyonge. “Nilijua ungekuwa kazini, nikakuwahi kabla hujatoka kwenda kupumzika.” Kimya. “Nimekumiss Tuma!” Akajikuta machozi yakimtoka, Jerry akahisi akilia kwa mlio wa kusafisha pua.
“Upo mzima?” Kimya akiendelea kulia taratibu. Ikawa kama aliyemsoma, akajua kinachoendelea. “Samahani niliondoka bila ya kukuaga. Nilikuwa na hali mbaya Tuma, nilikuwa siwezi kutoa neno mdomoni.” Kimya akimsikia akiendelea kulia. “Pole na samahani kwa kukuumiza. Naomba usilie, unaniumiza zaidi. Tafadhali nisamehe.”“Unaendeleaje sasahivi?” Akamuuliza akisikika akijitahidi kutulia.
“Vizuri, nahisi bila bro, ningechanganyikiwa. Amechukua muda mrefu sana kunifungua macho kwenye maeneo fulanifulani tokea mwanzo wa mahusiano yangu na Sandra, mpaka kweli ikanisaidia kutulia. Angalau nipo sawa. Nina habari njema. Lakini kwanza niambie na wewe unaendeleaje?” “Mimi sikujaliwa kaka wala dada kwamba nikipatwa na matatizo niwakimbilie.” Akaanza Tuma taratibu akijaribu kutulia.
“Mama yangu alikuwa kila akishika mimba au akizaa, watoto wanakufa. Na kule kwetu ndoa ni sifa kwa mwanaume si kwa mwanamke. Huwa wanaoa zaidi ya mke mmoja. Mama akawa mke wa pili katika ndoa ya wanawake watatu. Na kila mama anawajibika na kulea watoto wake kwenye nyumba yake, sio jukumu la mume.” Jerry kimya akisikiliza Tuma akizungumza kwa unyonge.
“Sasa wenzie mama walikuwa wakizaa, ila mama yeye kazi yake ilikuwa kuzika tu mpaka alipojua maswala ya dini, akaamua kuwa muombaji ndio akanipata mimi. Akakaa muda kidogo bila kushika mimba, lakini baadaye akaja kumpata Eli. Ila nafikiri kwa ile hofu ya kuzika watoto, huwezi mwambia mama hata kama kichwa kinakuuma!”
“Yeye ndio anakuwa mgonjwa mara mbili yako, na hali. Naishia kuwa na matatizo yangu sina mtu wa kumwambia maana hata ndugu zangu upande wa baba kwetu sisi tuligeuka nyumba yenye mkosi ni kama wanakwepa boma ya mama. Na hata baba naye ni kama anapuuza watoto wa mama kwa kuwa ni kama hatuna uhakika wa kuwepo kesho.” “Pole Tuma.”
“Mimi sina kimbilio kama wewe Jerry! Kwamba nikipatwa tatizo nina sehemu ya kwenda nikatulizwe kwanza ndipo nirudi kukutafuta, tuendelee! Sina bahati hiyo.” Hapo ndipo Jerry akamuelewa ni kwa nini amesema hayo yote, akajisikia vibaya na kumuhurumia.
“Naomba niwe muwazi kwako Tuma. Kwenye mahusiano niliyotoka, kulalamikakwa jambo lolote lile, kusema hata unaumwa ilionekana ni uzembe na udhaifu kwa mtoto wa kiume. Kwamba mtoto wa kiume hatakiwi kusema kinachomsumbua, anapambana nacho kiume. Ikanijengea hali fulani ya kufa na tai shingoni. Unang’ang’ana na jambo mpaka mwisho. Kwangu kukujia vile nilivyokuwa ilikuwa ngumu na sikujua nakwambia nini! Sikutaka mwanzo wetu uwe wa kidhaifu au unione ninakuja na matatizo yangu!”
“Nilishindwa kabisa kuzungumza hata na Jeremi! Bro mwenyewe alizungumza na mimi kutokana na alichojua kilichokuwa kikiendelea wala si kwa sababu nilifunguka kwake.” “Mimi sikujua kinachoendelea Jerry! Ulishindwa kunitafuta na kunieleza! Uliniambia huwezi fananisha wanawake wote na Sandra, na wanaume wote sio Mbaki! Lakini ni kama umeniweka kundi moja naye!”
“Unaniachia gari ambalo mimi sikuwa nashida nalo Jerry, ila wewe! Ni bora ungenipa matatizo yako ukaniacha nayo kuliko kuniachia gari, wewe haupo!” “Najua nimekuumiza Tuma, ila hujui ni kwa kiasi gani nilivyokuwa nikitamani kusikia mtu akiniambia hivyo. Inakuwa kama dawa kwenye moyo wangu, hujui ni kiasi gani unaniponya. Tafadhali nipokee na haya mapungufu yangu na endelea kunivumilia,ukinisaidia kuzungumza kama hivi.”
“Na nakuhakikishia Tuma, mimi ni kimbilio lako katika kila hatua ya maisha yako. Hutamuhitaji mama wala mtu mwingine yeyote unapokuwa kwenye shida, kwa kuwa mimi nitakuwepo.” “Na mimi nitajiona nakuwa mzigo kwako!” “Nakuahidi nitabadilika. Kwa sababu umeshaniambia huna neno na matatizo yangu!” “Kila hali Jerry. Sio unakuwa upo kwenye matatizo nakuwa nasikia tu kwa watu! Inakuwa kama vile alivyoondoka Mbaki na Umi, wakaenda huko kufanya anachojua ndipo na yeye akarudi. Hivyo vinanitisha Jerry!”
“Lakini Mbaki aliondoka na mwanamke mwingine wakati mimi nimeondoka na kaka yangu! Tena kikazi! Sio sawa Tuma.” “Anayeachwa ni nani kama sio mimi?” “Basi Tuma, haitarudia tena. Umenisamehe?” “Nimekumiss Jerry!” Eti ikamuingia Jerry mpaka rohoni. “Ulianzisha kautaratibu fulani kwenye maisha yetu, halafu ukapotea gafla! Nakuwa mpweke.” Hayo masikio ya Jerry yalishasau kusikia hayo maneno.
~~~~~~~~~~~
Kwamba eti mtu analia hayupo! Anamuhitaji! Kwamba anafurahia wanachokifanya pamoja! Moyo wake ukazidi kumpenda Tuma maana ni kama alikuja kwa wakati muafaka. Akakabidhiwa mtu aliyehitaji upendo tu na nafasi ya kufikiria.
Jerry hakuwa mjinga wala slow kama alivyokuwa akilalamika Sandra. Alihitaji tukutambuliwa anachokifanya na kupewa nafasi yakufanya tena na tena hata kama anaweza akawa hajafikia kiwango cha huyo mtu.
~~~~~~~~~~~
“Narudi mpenzi wangu. Narudi tuwe wote, kila mahali, kila wakati mpaka uchoke.” “Mimi sichoki.” Alicheka Jerry, alicheka sana jinsi alivyomjibu kwa deko. “Usiwe unanitenga na kunikimbia Jerry! Naingiwa hofu, nadhania ndio basi au umebadili mawazo! Unaniona sifai tena.” “Haitakaa ikatokea tena. Na hivi nishajua unanitaka nilivyo!” “Hivyohivyo na uwe unaniambia na mimi vile unavyojisikia. Hata kama sitakuwa na uwezo wa kukusaidia kama watu wako wa karibu, lakini nakuahidi hutajisikia mpweke au peke yako.”
“Nakupenda Tuma.” “Nakupenda Jerry.” Wakaendelea kuzungumza mpaka Tuma anafika nyumbani bado yupo kwenye simu na Jerry anacheka kwelikweli! Roho ishasuuzwa, wakati Sandra anatapatapa.
Wapo Watu Wengine Wanakuja Kwenye Ndoa
Na Baraka Zao.
Kuwa makini sana usijivune unapofanikiwa ndani ya ndoa hata kama wewe ndio unayeleta kipato ndani ya ndoa, haimaanishi baraka hizo zinatokana na juhudi zako. Unaweza kuta mkono wa Mungu upo juu yako kwa sababu hata ya yule anayebaki tu nyumbani akionekana hana mchango mkubwa kiuchumi kwenye familia. Huwezi jua agano la Mungu juu ya mwenza wako.
Baraka za Mungu na agano lake kwa mtu fulana, vinaambata na huyo mtu bila kujalisha wakati wa mwanadamu, mazingira yake na vile aonekanavyo. Na ndipo wengine wa karibu hunufaika kupitia yeye. Huwa mara nyingi ukimtoa huyo mtu kwenye maisha, huondoka na huo mkono wa Mungu hata yale manyunyu ya baraka huondoka nayo na kubariki wengine watakao fanikiwa kuwa naye upande wa pili wa maisha yao. Kuwa makini. Mafanikio si kile unachoweza tengeneza, ila ni jinsi unavyoweza kumudu kuishi navyo. Usipandishe kiburi.
~~~~~~~~~~~
Wakiwa ndio wameanza hiyo nusu siku ya kazi, wakaja vijana watano, wamevaa sare na mashine nyingi tu mpaka wakamshangaza Sandra. “Mnataka nini hapa?!” “Tuliambiwa ulishatumiwa barua ya uwepo wetu hapa!” Wakajibu wakimshangaa Sandra na kumuonyesha kuwachelewesha.
Ndipo akakumbuka kupewa barua aliyoipuuza jana yake na kutingwa na mengi huku akichanganywa na deni kubwa la JJ alilodaiwa kwa kushitukizwa. Ikabidi kurudi tena kuisaka hiyo barua na kuisoma kwa upya. “Sisi tulitegemea tukute ofisi tupu!” Kiongozi wao akazidi kuweka msisitizo. “Leo ni siku ya kazi kama kawaida! Itabidi kujitahidi kufanya pamoja.” Ikabidi Sandra kusalimu amri. Hapakuwa na namna.
Ilikuwa fujo hapo ndani, wasingeweza fanya kazi kwa utulivu. Walikuwa na kuingia toka kwingi! Wakipima hiki na kile mpaka darini. Juu kwenye paa huku wakiitana kwa hili na lile, na huku wafanyakazi wa Sandra nao wakiendelea na majukumu yao.
Pisha hapa, sogeza meza hii, toa hiki na kile vikaendelea kwa muda mrefu tu mpaka mchana wakaonekana kumaliza kazi yao, na muda wa kufunga hapo nao ukawa umefika.
“Mmepaonaje? Maana sisi tunaofanya hapa hatujaona tatizo lolote.” “Kwanza nashangaa mnawezaje kuwepo hapa!” Kiongozi wa wale vijana akajibu. “Kwa nini? Mbona sisi tupo sawa tu!” “Kwa jinsi kulivyo, ndani ya hili jengo kulitakiwa kusiwepo kiumbe chochote kile. Lakini acha nitengeneze ripoti, nimpelekee mwenyewe. Mtawasiliana. Nisizungumze yasiyo nihusu.” Akaondoka na kumuacha Sandra amechanganyikiwa zaidi.
~~~~~~~~~~~
Hilo eneo si kwamba wanategemea tu hilo jengo la ofisi! Hilo jengo linazungukwa na eneo kubwa, zuri sana kwa usalama. Nje pana yadi ambayo anawekea magari ya wanaoshindwa kulipa. Akiwapokonya ndipo anapoyahifadhi hapo nje.
Alishakuwepo hapo muda mrefu, panafahamika, haitaji tena kujitangaza kuvutia wateja. Watu wanaambiana tu na kuja hapo kuomba mkopo. Leo anaambiwa hapo hapafai! Anahamia wapi ambako ni kama ataenda kuanza upya! Nani atampangisha sehemu kubwa inayofanana na hiyo! Wakazidi kumvuruga Sandra.
~~~~~~~~~~~
Huku kwa Tuma yeye jumamosi yake ilikuwa tofauti. Busy, nakushindwa hata kufikiria jingine ila kazi tu. Kwanza alishazungumza na Jerry usiku uliopita. Akahakikishiwa bado penzi lipo. Akili ikabakia kazini tu. Na hiyo siku kwake ilikuwa busy kupita kawaida yao kwani ilikuwa mwisho wa mwezi. Kila aliyekuwa akifumbia macho matengenezo ya gari yake, siku hiyo akataka ahudumiwe. Basi akawa busy tokea anaingia, na Umi naye akafika mbili kamili bila kuchelewa, mida ya saa 5:15 asubuhi Umi yeye alifanikiwa kutoka na kupata chakula cha mchana ila Tuma hakufanikiwa.
6:30 juu ya alama, bila kuchelewa, Umi akabeba pochi yake na kuondoka kukiwa kuna foleni watu wanasubiria zamu zao. Ikabidi tu abaki akijua na siku hiyo atatoka tu jioni. Alishinda hapo peke yake mpaka saa 10 jioni, wakaacha kupokea magari ili kumalizia yaliyokuwa yakisubiria.
12:45 jioni hiyo ndio walikuwa wakimalizia gari ya mwisho. Baadhi ya mafundi nao walishaondoka wakawa wamebakia wawili tu waliokuwa wakimalizia, na Tuma akiwasubiria. Saa moja usiku akajikuta peke yake na walinzi akipambana kumalizia kufunga mahesabu hapo stoo akilinganisha na oda alizokuwa akiletewa na mafundi.
Upweke Unapokutana Na Faraja
Mama J akaingia hapo. “Pole Tuma. Pole mama.” Tuma akacheka. “Nimekuletea sambusa na soda upunguze njaa.” “Mbona udumu!” Akaanza kula bila hata kunawa mikono! “Sasa leo si utakuwa umeishiwa kabisa!” Alikuwa Jeremi, akageuka na kumjibu kwa msisitizo. “Kabisaaaa! Yaani mwambie dereva, kesho alete au jumatatu kabla ya saa mbili, awe amefika.” “Nishatoa maagizo.” Mama J akajibu yeye.
“Mambo mengine utamalizia jumatatu Tuma, nenda na wewe ukapumzike!” “Hata hivyo nishamaliza. Sambusa tamu!” “Njaa tu hiyo wala hazina uzuri wa hivyo!” Akamuona mumewe anacheka taratibu asielewe, mkewe akamuona. “Jeremi naye!” “Hivi kitu kisipokuwa kizuri, kweli mtu unaweza kukila na kupitiliza? Maana alikuwa akizilalamikiahizo sambusa ila haishiwi kuweka mdomoni.” “Si njaa! Sasa mimi ningefanyaje!” Tuma akaanza kucheka. Alimjua mama J kwa msosi. Na hachagui. Ilimradi kiwe chakula, atakula tu.
~~~~~~~~~~~
Wakawa watatu hapo stoo, mara Jerry akaingia Tuma alikuwa ameupa mgongo mlango. Akasikia sauti ya utulivu, nzito ya kiume ikimuita. “Tuma!” Alishituka na kugeuka kwa haraka, akashindwa kujizuia akamkimbilia, Jerry akamkumbatia kwa nguvu zote na kusaka midomo huko alikokuwa ameficha uso mpaka akaipata na kuanza kuinyonya taratibu. Tuma akajisahau . Na alivyokuwa na hamu naye! Akajituliza, mabosi wake wakabaki wamekodoa macho wasiamini wanachokiona.
“Niliambiwa kituo cha kwanza ni kwa Tuma. Nikasema nisigeuzie getini, niingie mpaka ndani na mimi nimuone huyo Tuma.” Alikuwa kaka yao, mpaka mama J akasimama kama ambaye hakutegemea. “Shikamoo.” Mama J akasalimia kwa heshima zote akimsogelea na cheko. Na Jeremi naye akamsalimia. Tuma akajitoa kwenye mikono ndipo aibu sasa. Akasalimia mpaka kwa kushika mkono na goti.
“Kumbe wewe ndio Tuma, niliyesikia habari zako!” Tuma akazidi kucheka kwa aibu akimwangalia Jerry. “Naamini sio habari mbaya.” Tuma akajibu akicheka kwa aibu iliyojaa heshima. “Nisingekuja kukusalimia.” JJ akajibu. Mama J akajua tayari!
“Poleni kwa safari.” “Ilikuwa nzuri tu. Kwa hiyo hili jina Tuma mbona nahisi ni kama limefupishwa?” Wakajua bado anataka kumfahamu.
“Naitwa Tumainieli.” “Waw! Na najua limebeba maana. Si ndivyo?” Wote wakacheka maana kwa Tuma alionekana hana haraka na kweli anataka kumfahamu. “Mama alikuwa na matatizo, kila akizaa mtoto anakufa.” “Ooooh! Poleni sana.” Ndio wote sasa wakaweka umakini.
“Ehe!?” “Alizika watoto watano. Akaja kumjua Mungu, akaanza kuomba sasa. Aliposhika mimba yangu ndio akasema kwa imani tu kuwa, Tumaini langu ni kwa Mungu. Ndio jina la Tumainieli.” “Kumbe ni bora nimeuliza! Wewe ni mtu wa maana na wakipekee! Kwa hiyo mama alifanikiwa mtoto mmoja tu?” “Alipata mwingine. Lakini tokea akiwa mjamzito, kwa imani tu, akaamini Mungu amempa mtoto mwingine wa kiume, akasema jina lake ataitwa Elihuruma, yaani Mungu amenihurumia.” “Waw!” Wote wakashangaa wasijue Tuma ndio amebeba historia nzito hivyo! Yaani hata na Jerry ndio kwa mara ingine akasikia kwa undani huo.
Akacheka akimwangalia Jerry kwa aibu. “Kwa hiyo nyinyi ni watoto mliopatikana kwa rehema za Mungu tu. Si ndivyo?” “Hilo jina la mama.” Alivyojibu hivyo akawashangaza na kufanya wacheke sana. “Tuma!” “Kweli mama J. Ndio jina la mama yetu, baada ya kumjua Mungu na kubatizwa. Akabadili jina akisema yale mabaya yote, adhabu zote alizostahili kupata yeye, Mungu amemrehemu yeye.”
“Safi sana Tumainieli. Sasa mimi huko nyumbani nasubiriwa mezani kabisa. Nishaambiwa chakula kitapoa, lazima niwahi. Ila nimefurahi sana kukufahamu. Tutaweka mazingira mazuri haya mazungumzo yasindikizwe na vyakula pamoja na vinywaji. Au unasemaje?” “Nitashukuru.”
“Kama ndio hivyo, mipango inaanza kwa haraka. Muwe na usiku mwema.” Kabla hajageuka na kuondoka, Tuma akamuwahi. “Asante kuwa na Jerry, naona amerudi na furaha. Mungu akubariki.” Wote hawakutegemea! Tuma ni mdogo kwao, lakini akaongeza ujasiri na kuonyesha kwa wazi kabisa kumjali Jerry, kitu kilichomgusa sana JJ.
Jerry akambusu shavuni. “Atakuwa sawa. Usiwe na wasiwasi. Sasa Jeremi?” “Nipo. Pafyumu umeleta lakini?” Akamuuliza kaka yake aliyekuwa akiondoka huku akimfuata. “Ninavyo vitu vyako vyote.” Akajibu Jerry na yeye akiwafuata kwa haraka.
Akawa kama amekumbuka kitu. “Naona safari ya Jeison imekaribia. Jemimi ameniambia.” “Anataka kuniua tu na pressure shemeji yangu wala hakuna jingine.” Wakacheka wote. “Hutaki aende?” “Yupo kwenye maombi hivyo anamsihi Mungu ambadili mwanae mawazo.” “Mungu amegoma kujibu?” JJ akamuuliza akicheka.
“Mungu wangu hajawahi niangusha. Ni muda tu.” Ikawa kama wanamcheka. “Ila ujue Jemimi ameshaanza kuandaa mazingira yake.” “Na ujue Jemimi ndiye anayempa kichwa! Nimezungumza naye sana Jemimi, ila naona hanisikii, anang’ang’ania aende eti kuna madarasa anatakiwa ayafanye sasahivi ili kumuandaa! Namwambia aniambie hayo madarasa ayasomee huku mpaka amalize high school, ananizungusha tu. Mara asema elimu ya huku haitamuandaa vizuri kuja kujiunga kwenye chuo chao. Najua ananitapeli tu!”
“Lakini ujue yupo sahihi. Anasema yeye alihangaika sana alipoanza kile chuo, sababu ya mama yake kumkatalia kwenda kusoma kule high school. Alisumbuka sana, ndio maana hataki wadogo zake wapitie huko.” “Hata sijui shemeji yangu! Naona bado mdogo jamani! Wangenipa hata miaka mingine miwili mbele, nimsogeze sogeze kidogo!” “Watakuwa sawa tu. Na hivi Jemimi yupo kule ameshatengeneza njia! Watakuwa sawa. Usiogope. Usiku mwema.” Akaondoka na wadogo zake.
~~~~~~~~~~~
“Jua JJ keshakupenda.” Mama J akamgeukia Tuma. Tuma akacheka akijifunika uso. “Nimefurahi Jerry amerudi.” Alicheka Hilda, alicheka sana. “Tuma!” “Sijui dada yangu, lakini tumetoka kuelewana sana na Jerry. Najua nimapema sana kusema, lakini yupo kama anajua kusoma mawazo yangu! Hanipuuzi.”
“Basi hicho na yeye anachojisikia kwako, jua ndicho amemwambia kaka yake, ndio maana umemuona JJ, mwingi wa shuguli, amekupa muda akitaka kukufahamu zaidi na kukukaribisha mfahamiane zaidi. Huwa haropoki na hatoi ahadi za uongo. Jua atahakikisha unafika kwake kukupa nafasi zaidi.” “Kweli?”
“Kabisa. Jicho lake lipo kwa wadogo zake sana. Na anawapenda hao wawili kuliko nafsi yake, na hawajawahi kukua kwake.” “Anaoenakana.” “Hongera Tuma. Jerry ni mtu mzuri sana. Sana. Ni vile hakubahatika tu mwanamke mwenye mapenzi naye. Halafu kwao hawa wametulia mno. Hawana hekaheka na ujue utabakia wewe tu kwa Jerry. Sio kama kwa Mbaki.”
“Eti dada? Hatabadili mawazo hapo baadaye?” “Sio kawaida yao. Kwa sababu pia sio malaya, hawakurupuki kwa wanawake. Usifikiri atakuja kuanza kuangaza macho huko nje tena! Jua ndio amemaliza, ushindwe wewe tu.” “Nimefurahi mama J, dada yangu! Nimefurahi sana. Nilikuwa na hamu naye!” “Tuma! Si aliondoka juzi tu?” “Hata kama! Kuna jinsi ananijali, huwezi tosheka naye. Na leo kanikiss.” Mama J alicheka, alicheka sana.
“Kwamba alikuwa hajawahi!?” “Mwenyewe alisema bado hajaachana rasmi na Sandra.” “Sikukwambia mimi? Hawa sio malaya kabisa.” “Hilo nimeamini. Kuna siku tuli…” Wakaingia bila kutarajia. “Hilda acha umbea. Twende Tuma ukapumzike.” “Ila ujue namtegemea sana Tuma!” Mama J akaongea kwa kulalamika. Mumewe akaanza kumcheka.
“Hakika anza kutafuta mtu, Hilda.” “Nyie Jerry!” “Nakuhakikishia, na iwe haraka SANA.” Akaenda kumshika Tuma mkono kabisa. “Twende kama umeshamaliza hapa.” “Kila kitu kipo vizuri. Ungechelewa kidogo tu, na kama sio mama J, msingenikuta hapa. Nimefurahi umerudi!” Hapo akanong’ona, Jerry akacheka na kumpa kiss ya mdomo, akanogewa na kutulia kabisa, wakaona.
“Mweeee! Niandike tu maumivu!” Mama J akamalizia akichukua pochi yake. Tuma alicheka mpaka akaondoka hapo akikimbia kwa aibu maana alikuwa akinyonywa midomo. Ndugu hao wakazidi kucheka, Jerry akamfuata nyuma.
~~~~~~~~~~~
Alikuta masanduku nje ya gari. “Baadhi ni yetu, hilo la kijivu ni la Hilda, kubwa jeusi nitamuomba amtume dereva kumpelekea Sandra, vitu vya watoto.” Akasogea na kuyatenga, mengine akachukua na kumsaidia Tuma kuingiza ndani ya gari, na Tuma hakuchangia.
Jeremi na mkewe wakasogea. “Ukiweza kumtuma dereva apeleke hili sanduku kwa Sandra, ni vitu vya watoto, ningeshukuru sana.” “Hiyo kazi ya kesho. Au unataka iwe leo?” “Hapana. Havina haraka. Siku yeyote ile. Nawashukuru, acha sisi tuondoke.” Wawili hao wakaondoka, Jerry akiwa dereva.
Jerry&Tuma
“Naomba tukalale kwangu.” Tuma alisikia raha huyo! “Au itakuwa shida kumuacha Eli?” “Ilimradi awe na chakula, hana shida. Ila naomba tupitie nikazungumze naye kwanza.” “Hamna tatizo. Na nina tisheti zake hapo, nilimnunulia.” Tuma akashangaa mpaka akamgeukia. “Jerry!” “Ni tatu tu, wala sio nyingi, na soksi nilipata zipo pamoja, 5. Basi.” “Nakushukuru sana. Sana.” “Usijali.”
“Nimekuja na habari njema SANA.” Tuma akacheka. “Uliniambia. Ni nini?” Jerry akafikiria jinsi ya kumueleza jinsi alivyobadili mawazo, kutofuata ushauri wake na kuamua kubuni biashara ingine, bila ya kumuumiza Tuma aliyekuwa amejitoa na kuzunguka naye siku ya jumamosi.
~~~~~~~~~~~
Sandra ndiye aliyemfikisha hapo. Ikawa ni kama aliyemfungua macho kwa wazi kabisa. Japokuwa kilikuwa ni kidonge cha aibu, ngumu kukimeza mbele za watu, lakini jinsi alivyomtukana mbele za wanaume wenzie wawili waliofanikiwa kwenye taluma zao, siku ile ya talaka yao, ndio ikamfikisha kujifikiria kwa upya.
Alijiona ni kweli alifanya kazi kwa bidii sana kwenye kampuni aliyodhani ni yao, lakini ni kweli lilikuwa ni wazo la Sandra! Akaona anarudia tena kosa. Amepata nafasi nyingine maishani kama alivyoambiwa na Tuma, lakini anarudia kosa lilelile. Kuanza kitu kipya kwa wazo la Tuma! “Inawezekana nina tatizo.” Akiwa na hasira akajifikiria.
“Kwani nina tatizo gani la kujifikiria na mimi nikabuni kitu changu?” Akiwa na hasira na uchungu mwingi, akaendelea kujifikiria zaidi. Sky was a limit. Kaka wa kutembea juu ya moto ili kumfanikishia jambo lolote atakalo anaye. Kwa nini awaze kidogo! Ndipo katika ukimya huo wa hasira, akapata wazo zuri, kubwa na la thamani sana.
~~~~~~~~~~~
Inaendelea….
0 Comments:
Post a Comment