Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Love At First Sight - Sehemu ya 91. - Naomi Simulizi

Love At First Sight - Sehemu ya 91.

Wakati jumamosi ya kina Jerry inaisha kwa tumaini la huba, mwanzo mpya uliojaa ahadi za penzi la kulipiza walikotoka kuumizwa, lakini zilizoshindwa kutamkika kwa wazi, kama walioambiana acha matendo yetu yazungumze. Lakini huku kwa Mina usiku ulimkuta pembeni ya kitanda alicholazwa mwanae akiwa hana fahamu, amepiga magoti.

Mumewe alimuhurumia, ikabidi amuwekee mto chini. Akabaki amepiga magoti upande ule ambao hakuwa mtoto wake amewekewa dripu. Akabaki ameshikilia mkono wa mwanae, amepiga magoti, kichwa amekiweka kitandani. 

Ilikuwa hali ya wasiwasi, hakuna aliyejua chakufanya, na kama ni kuomba, wao walishamaliza, wakarudia, kisha wakamaliza, halafu wakarudia tena. Waroma hao, tena wasomi, wakawa hawana jinsi nyingine tena ya kuzungumza na Mungu walio amini si kiziwi. Kwamba alishasikia. Ila sasa, mama mwenye mtoto hakuwa akizungumza, ila maombi tu. Na alishakataa kula. Ikabidi ndugu nao wakae mkao wa kama wapo ibadani. 

Waliambiwa kwa umri wake Ayvin, daktari amekataa kumpasua kichwa. Akihofia madhara zaidi kuliko kumsaidia. Uvimbe uliopo kwa ndani karibu ya ubongo anajaribukuumaliza kwa dawa. Na walimu induce coma. Kwamba kwa muda huo wa hayo matibabu, huyo mtoto watamuweka kwenye nusu kaputi mpaka uvimbe uishe. Na ndipo watajaribu kumuamsha tena. Na endapo ataamka, ndipo watajua madhara yake. Kulikuwa na hatari ya kama atazinduka basi anaweza asiwe na akili timamu. Kwamba akawa tahira au kupoteza kuona kabisa. Akawa kipofu.

Ila upasuaji wa mbavuni walifanikiwa. Wakaweza kusogeza kwa kuitoa ile mbavu iliyokuwa imevunjika, ikabonyeza mapafu nakumfanya ashindwe kupumua na kupasua moja ya mrija wa damu, na maji yalishaanza kujaa. Hiyo dokta Patel aliwaambia atakuwa sawa. Nikusubiri kujua endapo atazinduka, atakuwa ni mtoto wa aina gani, na ndipo wafundishe jinsi ya kuishi naye kuanzia hapo. 

~~~~~~~~~~~

Mina alilia sana. Alilia kwa kusononeka, akalia kwa uchungu sana wakati dokta Patel alipotoka chumba cha upasuaji na kuwapa hizo taarifa. Alilia mpaka akakaa chini,akikataa kubembelezwa na mtu. Kila alipofikiria ni jana yake tu alikuwa akizungumza na Ayvin mzima, akichekesha kila mtu, leo hana uhakika wa kuamka kwake! Na hata akiamka hatarudi kuwa kama zamani! Mina akazidi kulia.

~~~~~~~~~~~

Ilikuwa hali ya kuhuzunisha kwa mtoto aliyekuwa amezaliwa mzima, aliyekuwa amejawa uzima. Upendo na alijaza furaha kwenye kila familia, kuja kugeuka tahira au mpofu! Au kuondoka duniani kwa staili hiyo! Gafla tu! Tena akiwa mdogo hivyo! Ilimuhuzunisha kila mtu.

Kwenye mida ya saa 12 jioni Andy alirudi nyumbani kumuona Ayan na kuoga. Akafanya yake na kumchukulia nguo mkewe, pamoja na chakula, akarudi hospitalini akamkuta mkewe bado ameegemea kitanda.

~~~~~~~~~~~

“Kwa sasa sidhani kama kuna kitu cha ziada chakufanya. Naomba mkapumzike mpaka kesho na Mina naye apumzike.” Wakaelewa kwa wepesi. Mzee Ruhinda akasema waombe tena sala ya kumwombea mgonjwa wakimuhusisha mtakatifu Yuda Tadei ambaye ni mlinzi wa mambo yasiyowezekana na wagonjwa mahututi. Wakaomba na sala ya salamu maria fungu moja kisha wakamalizia na sala ya Baba yetu, wote hapo chumbani wakaomba tena wakapiga magoti kama Mina. Wakamaliza na kumuaga Andy kwani Mina alisikika akilia taratibu wakati wakimalizia kuomba.

~~~~~~~~~~~

“Nijulishe chochote kitakachoendelea Andy. Simu itakuwa wazi.” Akanyamaza kwa muda na kusema. “Umezembea Pius! Mmezembea kwa jambo nililowasisitiza nalo sana! Kwanza nimezungumza na Judy, ameniambia mpaka leo bado hamjajengea kile kigeti cha kwenye ngazi. Na nilikwambia umuhimu wake!” “Mama alimuita kaka Muhidini, akamuahidi jumamosi ijayo.” Poliny akaingilia akijaribu kumtetea baba yake na kuharibu zaidi.

“Sio mimi nilikwambia Pius ni kazi rahisi sana hata cha nyumbani kwangu nilijenga mwenyewe, nije kuwasaidia kujenga, mkanikatalia kwa ahadi mtafanya wenyewe? Iweje leo nisikie kuwa ni kazi mlimpa Muhidini, sijui!” Pius alinyamaza kimya, akashindwa hata kujibu. Alikuwa na hali mbaya huyo Pius, ilikuwa bora Mina anayeweza kulia. Andy akashindwa kuendelea na lawama maana Pius mgovi alinyamaza kama aliyekubali makosa yote.

~~~~~~~~~~~

“Ni sawa nikienda kuwachukua Judy na kaka mkubwa? Ili leo tuwe nao. Wasibaki kule kwenu peke yao.” Mama Ruhinda akauliza kwa tahadhari. “Sijui mama! Maana hata Judy ameniumiza sana. Mimi mwenyewe huwa nafanya majukumu anayotakiwa awe anayafanya yeye ilimradi tu kumpunguzia kazi anapobaki na Ayvin nyumbani. Ili akili na mawazo yake viwe kwa Ayvin ambaye anahitaji uangalizi wa karibu sana! Leo mtoto anamtoka akiwa amekaa tu, akiangalia tv!? Hana habari!” Andy akajibu akisikika kuumia.

Pakatulia kidogo, mzee Ruhinda akaongeza. “Nafikiri sio wazo baya tukiwachukua. Ili kesho twende naye kanisani. Tukitoka kanisani naweza kuwapitisha hapa, akakaa na mama yake kidogo, amnuse, mpaka atulie kabisa, ndipo wakarudi nyumbani kwa matayarisho ya shule jumatatu.” Angalau akaweka utani kidogo kupunguza ile hali ya wasiwasi pale, ila pia kama kumkumbusha Mina, analo jukumu la mtoto mwingine. Na kweli ikasaidia kumgutusha“Nitashukuru wazazi wangu. Asante.” Mina akajibu akijifuta kamasi na machozi.

“Pole mama. Pole sana.” Mina akaweka mikono kichwani na kuzidi kulia. “Mungu wangu nisikie jamani! Msaidie mwanangu mimi jamani! Mungu usimuache mwanangu!”Akaendelea kulia taratibu, kwa kusononeka, macho kwa mwanae pale kitandani. Kila alipofikiria aje aamke tahira au haoni tena! Mina akazidi kulia zaidi alipojiwa na wazo la kwamba anaweza pia asiamke tena!

Andy akaenda kumnyanyua pale. “Twende ukaoge.” Akafanikiwa kusimama na tumbo lake, akaingia naye hapo bafuni. Wengine wakaondoka. 

~~~~~~~~~~~

Alipomaliza tu kuoga, akarudi kupiga magoti pembeni ya kitanda cha mwanae. Andy akatumia akili kwa haraka. Akaenda kupiga magoti pembeni yake, akaongoza yeye maombi. Kisha akawaombea na watoto wake wengine kwa kuwataja kabisa majina mpaka wa tumboni. Akamuombea Mina na afya yake, kisha akamalizia kwa kumuombea usingizi mzuri, akasema kabisa ‘Amen’. Kumuonyesha wanafunga kwa usiku huo. Mina alipoitika tu, akamgeukia.

“Naomba ulale kidogo tu. Ukiamka hata mimi nitataka kuomba tena na wewe. Tafadhali Mina. Kumbuka unamtoto mwingine anayekutegemea kula yako na furaha yako, na hujala, hujapumzika hata kidogo. Pumzika ili na Ayvan asidhurike.” Hapo ndio kumbukumbu ya kuwa ni mjamzito ikamrudia na kuamua kutulia. Mumewe akajiweka sawa na kumuweka kifuani. Akapanga tumbo lake akapotelea usingizini bila ya kula.

Penzi Halina Umri

Ikawa ndio na siku hiyohiyo Jo naye amejibiwa majibu yake ya posa kwa Dorothy. “Naona ombi lako la sehemu kubwa ya mahari iwe pesa, limepokelewa.” Mill mrudisha majibu akawa akimwambia Jo, baada ya kumtumia. “Aisee nakushukuru SANA. Naona na dada naye amenihakikishia wepesi wa kupata vitu vilivyobaki. Amesema haitachukua muda mrefu kuvipata.” “Kwa hiyo?” Mill akauliza akitaka muongozo.

“Waambie jumamosi tutakuwa tayari kulipa mahari ya Dorothy.” “Jo!?” Mill hakuamini huo uharaka. “Hakika namuoa. Tena kwa haraka sana. Sina sababu ya kusubiri. Na hivi wamenikubalia kuipokelea mjini! Sitachelewa. Umri umekwenda na sitarudi kuwa kijana.” Mill akacheka akimuelewa. 

Lakini akamuuliza. “Utafanyaje na immigration wamefunga mchakato mzima wa hii nchi, na nyinyi mnataka kuondoka mapema?!” Jo akatulia akifikiria. Maana kweli uhamiaji wa nchini Marekani wameacha kabisa kufanyia kazi Visa ya aina yeyote ya kutoka nchini Tanzania, isipokuwa kuna sababu maalumu. 

“Sina majibu yote kwa sasa, ila ninachojua cha kwanza lazima nimuoe Dorothy. Halafu uzuri, hata kina dada wakiniacha, kule wana uangalizi mzuri. Kijana wangu yule mdogo anafanya kazi kwenye hospitali ambayo daktari wao yupo. Watakuwa sawa.” “Kwamba upo tayari kubakia hapa kwa kipindi chote ambacho jamaa yupo madarakani?!” “Bila kufikiria mara mbili.” Mill akashangaa sana.

“Kweli Jo?!” Bado hakuwa akiamini. “Hundred percent.” Akamuhakikishia kwa haraka bila ya kusita. Nimehangaika sana Mill. Nimezunguka huu ulimwengu baada ya kifo cha mke wangu, nikitangatanga, nikijaribu kujaza pengo nililokuwa nikilisikia moyoni. Si kwenye nchi nilizoenda hata kwa starehe au kwenye kuhudumia watu kama tulivyokuwa tukifanya au kupanga na Betty kulikonipa utulivu na kuridhika, mpaka nilipomfikia Dorothy.”

“Kwa hakika anaziba pengo ambalo nahisi nilikuwa nalo muda mrefu mpaka nilipatwa hukumu! Dorothy ametulia Mill! Hana tamaa! Si msumbufu. Hajali namiliki nini! Kwanza hata hajisumbui na nilichonacho ila mimi kama Joel. Natulia nikiwa naye, sihitaji kujiuza kwa lolote. Wanao nifahamu kule nilipokuwa, walikuwa wakinisogelea wakiangalia ninachomiliki, au jinsi jina langu litakavyo wasaidia kwenye fani yetu. Na unajua wanawake wakule walivyo. Unaweza chelewa kutoa taka ndani kwenye nyumba aliyokukuta nayo, ukaombwa talaka, wanataka mgawane mali.” “Sasa mimi nilipoteza mali zote kwa mwanamke wa kule.” 

“Basi kumbe unaelewa ninachozungumzia. Ile nchi unaweza iona chungu kwa maamuzi madogo tu! Nitakuwa popote na Dorothy kwa sababu nishajua si sehemuitakayokuja niletea utoshelevu ila yeye.” “Nakuelewa. Basi nitarudisha majibu, kuwaandaa kwa kupokea mahari siku ya jumamosi.”

“Lakini Dorothy mwenyewe anajua?” Mill akaongeza swali. “Niliharibu siku ya kwanza nilipomkaribisha hapa kwangu. Jana nilimuomba aje tena, akashindwa kabisa. Kila nilivyojaribu kumueleza safari hii itakuwa tofauti, alikuwa na uzito. Alikuwa tayari na sehemu zote kasoro hapa. Sasa nataka kufanya hili kwa ukubwa na haraka, ili kumuhakikishia nipo serious naye, pengine itamfanya arudishe imani kwangu. Nahisi nilimtisha sana.” Katika hilo Mill hakuchangia. Kwanza akijifanya hajui kumbe Pam alimuelezea kila kitu pili alijiambia kama angetaka kumshirikisha, angeongea kiundani zaidi. Akaonelea awe muungwana. Kwanza alimuheshimu sana Jo. Hakutaka kuvuka mipaka. 

“Kwa hiyo kwa kujibu swali lako, nilimgusia utayari wa kutaka kumuoa kwa haraka na kwamba nasubiria majibu kutoka kwa wazazi wake. Nisaidie nini siku hiyo?” “Sisi upande wa bibi harusi tumejipanga.” Jo alicheka sana, hakutegemea.

“Unanitosa Mill!” “Kuanzia hapa, hatujuani. Sasa hivi nipo upande wa bibi harusi, tunaandaa kupokea mahari. Sasa usiniangushe.” “Sithubutu. Ila naomba kiwe kitu kizuri sana Mill. Nataka kuweka kumbukumbu nzuri kwa Dorothy. Pesa isiwe tatizo.” Wakaendelea kujiapanga mpaka na muda. Ndipo wakaagana.

Hospitalini.

Siku ya jumapili aliamshwa na Pius akiwa amerudi hapo. Akaingia kuoga tena, na kutoka, akarudi kupiga magoti. Andy akawa mwaminifu wa naneno yake, akaenda na yeye kupiga magoti pembeni yake, wakaanza kuomba. Pius naye akaenda kupiga magoti, akabaki ameinama hata hajui aombe nini. Wakabaki wakimsikiliza Mina anavyomsihi Mungu wake mpaka Andy akasema ‘Amen’. Maana alikuwa akirudia rudia tu.

Wakarudi kukaa. Kimya hapo chumbani Mina amejiinamia. Hazikuzidi dakika 10, akarudi kupiga magoti pembeni ya kitanda cha mwanae akabaki amejilaza kichwa hapo kitandani, amevuta mkono wa mwanae na kuuweka usoni kwake. Kimya. 

Manesi na madaktari wakiingia kufanya hiki na kile, wakatoa ripoti ya mtoto kwa Andy na Pius, Mina akisikiliza tu akiwa bado amepiga magoti. Wakatoka na yeye akaendelea na maombi. Paul naye alifika hapo mapema tu. Akaangalia ile hali ya Mina kupiga magoti tu, baba watoto wamekaa kama wapo msibani, akaaga na kusema anaenda kuzungumza na daktari wa watoto, atarudi. Akatoka.

~~~~~~~~~~~

Mama yake Mina na Ron, wakaingia hapo. “Kwani ilikuaje?!” Pius akashindwa kabisa kujibu akihofia asije sikika tofauti. Andy akaeleza bila ya kutupia lawama. “Ameanguka kutoka juu ya ngazi mpaka chini, tena baada ya kujigonga kichwani.” Andy akajibu na kuelezea vipimo na aina ya matibabu anayopewa.

“Nilimwambia Judy, tena kwa kumsisitiza sana, awe makini naye sana huyu, kwenye majumba yenu hayo ya gorofa!” Mama Ron akaongea kwa kuumia. “Upo kama mimi mama yangu. Kwa hakika ameniumiza sana. Mtoto anaanguka akiwa anaangalia tv! Hapana aisee! Na akiwa anakwenda nao huko, kazi yake ni moja tu, jicho lake kwa watoto tu. Raza huwa hampi kazi kabisa. Najiuliza alizembeaje!” Ron akabaki akiangalia.

Akamsogelea dada yake pale alipopiga magoti. “Poleni.” Kisha akamgusa Mina begani. “Mina! Pole. Pole sana.” Akaanza kulia. “Mimi na Ron tumemuombea sana. Mungu atasikia Mina, mama. Jipe moyo.” Mama yake akamsogelea.

“Haya, Ron msaidie kusimama hapo, ale kidogo.” “Sisikii kula mama.” “Basi jua unamdhuru huyo mdogo wake huko tumboni. Yaani hapo unachofanya mwishoe utakuwa na watoto wawili wote wanamatatizo.” “Usiseme hivyo mama bwana!” “Kweli Mina. Sasahivi kula kwa ajili ya mtoto. Nipo mkono.” “Naogopa Ron.” “Najua. Lakini wewe una imani Mina, huu ndio wakati wa kusimama wala si kukubali hofu. Njoo mama tuombe naye tena kidogo, ndipo ale.” Na kina Andy nao wakasogea hapo kitandani, wote wakapiga kabisa magoti na kuanza kuomba.

Ron akaomba vizuri tu, akamaliza na kumsaidia dada yake kusimama. Mama yake akamuwekea chai, chapati na supu. “Na wewe ule kidogo?” “Nashukuru mama. Maadamu wewe umekuja, acha nikimbie nyumbani, nioge, nile, ndipo nirudi. Hiko chakula muachie Mina.” Andy mla mezani, hawezi shikilia bakuli kama si lazima. Na Pius naye alipokaribishwa, akakataa na kubaki ameinama tu.

“Huyo kaka huko tumboni anasemaje?” Mama yake akamuuliza kusudi akiwa ameelezwa mengi na Andy, zaidi hali ya binti yake. Kwa hiyo alimuomba akifika hapo, amtoe mawazo ya ugonjwa wa Ayvin, na kumkumbusha ni mjamzito. Hapo alishalia usiku kuchwa. Akimsihi Mungu amsaidie mjukuu wake, ndipo akaja hapo.

Ikawa kama mama yake amemkumbusha akashika tumbo. “Naogopa mama! Naogopa sana.” “Pole. Naamini atapona. Kuwa na imani. Tunakataa habari zote mbaya, tunaamini habari njema tu.” Mina akatulia akiendelea kula na kujifuta machozi.

“Sasa usilie. Au huamini alichokwambia mama? Maana hofu haitokani na Mungu.” Ron akawa anazungumza na dada yake taratibu, wakiwapa nafasi wazungumze naye wao wakijua watamuwezea. Ni wa nyumbani kwao. Akatulia na kuendelea kula mpaka akamaliza. Akarudi kupiga magoti hapo kwa mwanae. Mama yake akamwangalia Andy. Andy akamtumia ujumbe kuwa ampe muda kidogo tu, kisha kwenda kumnyanyua. Maana yeye ndio alionekana mgonjwa kuliko.

~~~~~~~~~~~

  Walipotoka tu kanisani, wakina Ruhinda nao wote, wakaelekea hospitalini. Ibada yao ileile ya kwanza ya lugha ya kingereza.

Ubaya Una Mabawa, Wema Hutembea Kwa Miguu

Mina akiwa amemshika mwanae mkono, amejilaza kichwa pembeni yake. Wala hakuwa akiomba! Andy na Pius kimya hapo chumbani kama Ron na mama yake hata hawaongeleshani, wakasikia Paulina nje ya chumba anasema kwa kunong’ona. “Ndio ujue ni kweli mama.” “Mmmh!” Wakasikia mama Ruhinda akiguna tu. “Lakini si nilikwambia mimi mama?” “Naomba tuyaache tu. Mungu mwenyewe anajua. Kama amefanya kusudiau la, Mungu anajua.” 

“Ni kusudi, kila mtu amemuona ndio maana anashindwa hata kuleta sura yake hapa! Hakujua kama watu wangekuja kwa haraka na kumuona anachokifanya kwa mtoto.” “Paulina wewe mtoto!” “Maneno ya mwanae mwenyewe! Na hata msichana wake mwenyewe Raza, mbali na Judy, pia amenithibitishia. Unaambiwa Poliny alivyomuuliza kwa nini amemsukuma mtoto vibaya vile, alishindwa hata kujibu, akawa kama ameshituka kukamatwa! Ndio tukawa tunasema na Devi, ukute ile kelele ya kwanza aliifanya kusudi, ili akimsukuma aje ajitetee baadaye kuwa hata yeye alishituka. Lakini Mungu amemuweka mwangani. Amekamatwa.” Akaendelea.

“Umejitahidi kiunafiki cha muda ili kujidai amebadilika, anampenda mtoto aliyetaka kumuua, mpaka watu wamesahau hila yake ya kutaka kumuua Ayvin. Akajidai kama etiamempokeaUongo gani huo kama si unafiki tu!? Yaani mtoto yuleyule aliyetaka kumuua, eti gafla ajidai eti ameokokaanampenda kiasi cha kukaa naye! Kweli mama? Fikiria tu uone kama inaingia akilini.” Wakasikia kimya kutoka kwa mama Ruhinda, hajajibu.

“Hata wewe mwenyewe fikiria mama, uone kama inaingia akilini! Yaani utake kumuua mtu, halafu gafla ujidai unamapenzi naye ya kupindukia! Kweli mama, kama si unafiki huo wa kupindukia ni nini?” Akaendelea kuweka msisitizo kama anayetaka kumuaminisha mama yake au kuvuta watu wengi upande wake.

Kampumbaza mwenzie kwa kujidai eti anampokea na kumsamehe yeye aliyezaana mumewe na mtoto wake! Raza alivyo na wivu na mumewe! Kweli!? Kwamba ile kuzaa na mumewe gafla tu iwe sawa! Hata na wewe fikiria mama! Kamfanyia ile baby shower ya kumwaga mapesa kama mwenda wazimu, tena kwa mtoto wa tatu kama sio uongo ule ni nini!? Mtoto wa tatu unamfanyia mtu baby shower ya kwenye boti! Watu wote eti kula na kunywa vile! Kwa kipi mno kama si unafiki kumvuta karibu huku akimuangamiza mwenzie anayezaa madume tupu!” Paulina akaendelea.

“Mimi nilikuwa nikiwaangalia sana tu, kuwaona mwisho wao. Halafu eti mimi ndio wakawa wananitenga kama mbaya wao! Wanakuwa wakunipa taarifa tu! Yako wapi? Yako wapi sasa?” Kimya. 

Alinitenga nao kusudi akijua mimi si mjinga, hawezi nichezea michezo yake ya kijinga, nitamgundua, ndio maana akawa hanitaki kwenye mambo yao, jumapili hawataki kuja kukutania kwangu, kutwa kwa Raza, wakijidai eti ndio bi mkubwa! Kusudi tu kumpumbaza mwenzie ili ampate Mina na mwanae peke yao, afanye yake. Sasahivi ametulia kwake kimya, anamuacha mwenzie anauguza peke yake kama si keshatimiza lengo ni nini?”

~~~~~~~~~~~

Ukweli Raza alimfanyia Mina baby shower ya nguvu kama ndio mtoto wa kwanza! Ilikuwa gumzo. Alikodisha boti, akaalika watu kiasi tu. Halafu wote wakavaa nyeupe, juu mpaka chini. Wakaenda kuifanyia baharini. Bwana ilipendeza! Picha zao zilikuwa hazichoshi kuangalia. Mama Ruhinda na mama Ron pia walikuwepo. Na ni Raza mwenyewe ndiye aliyeandaa.

Asante peke yake ilikuwa haitoshi kwa alichoandaa Raza kwa Mina. Ilikuwa nzuri sana. Kulijaa maombi, kwani hata mama Briana na Sonia pia walikuwepo. Kikawa kitu kidogo, kizuri, cha hadhi ya juu mno wakimuombea Mina na watoto wake.

~~~~~~~~~~~

Pius alibaki ameinama anasugua mikono, nakushindwa hata kupepesa macho. Na si kwamba Mina hakuwa akisikia! Alikuwa akisikia kila kitu hapo alipokuwa amepiga magoti ameshikilia mkono wa mwanae. Mama Ron alibaki kimya akisikiliza kama Ron na Andy tu. Na ndio mama Ron na Ron wakajua kilichotokea kwa huyo mtoto kutoka kwa huyo wifi mtu.

~~~~~~~~~~~

Hauhitaji mwaka kwenye kubomoa, unaweza pata hata wasaidizi, lakini kujenga!

Ni nini kitaendelea kwa 

Jo & Dorothy?

Pam na mchakato wa kuondoka nchini? 

Tuma na Jerry ambaye bado ni mume wa Sandra waliyezaa watoto wawili?

Talaka yao itakuaje? 

Mina na Familia ya Ruhinda?

Inaendelea…. 

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment