Ilikuwa ni hali ambayo hata Tuma alishindwa kujielewa, eti umia ya Jerry,inamuathiri na yeye! Ikawa kama hisia zao zimeunganika! Moyo wake na yeye ukanyong’onyea kwa kukosa kwake raha, asijue jinsi anavyoweza rudisha kicheko alichomshukuru kukirudisha baada ya muda mrefu kupotea.
Ile hali ya kuwa karibu pekee ikawa faraja kwa kila mmoja wao. Ikawa ni kitu wote wawili wanatamani kisiishe. Kuangaliana kwa karibu wakisaidiana kwa hili na lile taratibu kwa kubembelezana wakijaliana, ikaongeza hisia za mvuto kwa kila mmoja wao.
Akamgeukia baada ya fundi kutoka na matairi. “Njaa imeanza kukuuma?” Akamuuliza kwa kumjali. Jerry akamwangalia. “Nikuletee maji ya kunywa?” Akaangalia saa. “Nitakwenda tu kufuata mwenyewe. Hata hivyo muda umekaribia, tunatoka.” “Inabidi nikaoge kabla ya kuzunguka. Nanuka!” “Sawa.” Akatulia.
~~~~~~~~~~~
Akaingia mama J. “Nimeona kule kumekaa sawa, nikaona nije tu. Nyinyi muwe huru kuondoka. Ila Jerry usizoee bwana! Mimi namtegemea sana Tuma.” “Ole wake mtu yule amtegemeaye mwanadamu!” Jerry akamjibu akinukuhu maneno hayo kutoka kwenye bibilia akiwa anasimama. “Mungu mwenyewe ndiye aliyenipa Tuma!” Tuma akawa anacheka tu. Kisha akamuomba wazungumze. “Wapi tena?” “Nataka tukae kabisa, si kitu kirefu ila muhimu, na ni ombi.” Wakatoka hapo na kurudi ofisini, wakakaa jikoni.
Kuachilia Jana, Kukaribisha Kesho
Moyo wa kale ni kivuli kinachochelewa jioni, hukumbatia mwanga uliopita bila kuurudisha. Ukipenda kumbukumbu kuliko kesho, utafunga mlango wa upepo mpya. Japokuwa ni ngumu, kulishakuwa na historia ya muda mrefu, lakini Tuma aliamua kuachilia, kama mti uachiliavyo majani yake ya zamani, ili chemchemi ipate nafasi ya kuchanua tena.
“Kwema?” Akauliza mama J taratibu baada ya kukaa, na kumuona ni kama Tuma anatafuta pakuanzia. Akacheka kidogo, akaona amueleze tu maana alishajua fika, mapenzi mapya hayakai penye mabaki ya jana. Yanahitaji ardhi safi, na roho iliyo tayari kuanza upya.
“Jumapili kama moja imepita sasa tokea Mbaki aliponitafuta akisema lazima tuonane ana kitu cha msingi chakuzungumza na mimi. Kama unavyomjua. Akang’ang’ania weee, mwishoe nikamkubalia lakini sikutaka kwenda naye sehemu ya starehe, nikamwambia anisubirie kituo cha daladala. Nikapanda kwenye gari yake nikamwambia tuzungumze pale.” Akawa akama anayefikiria tena.
“Ni nini?” “Aliongea maneno mengi, lakini mama J, yule kiumbe amenitoka moyoni kabisa. Nilikuwa nikimsikiliza, moyoni ninaumia. Siwezi msamehe na kusahau dada! Na yeye nilimwambia hakuna jinsi nikarudisha imani kwake. Sitakuja kuwa na furaha nikija kuwa naye. Siwezi kuja muamini tena. Ila kama unavyomjua Mbaki, amekataa. Anasema ananipa muda zaidi, yeye anaamini nitakuja msamehe.”
“Kweli umeshindwa kabisa!?” “Kabisa dada yangu. Sina hasira naye, lakini siwezi rudi kuwa mpenzi wake. Tena ndio nazidi kujishangaa niliweza vipi kuwa na mtu kama Mbaki! Pombe za kila siku kama baba yangu! Siwezi dada!” “Na hilo nilimwambia akasema hilo anaweza kubadilika.” “Sio kweli. Kwao wale ni wanywaji wale wa mapombe yale makali ya kitajiri. Mpaka mama yao alikuwa akinywa. Mbaki hawezi acha pombewala wanawake. Hapana dada. Nimeamua kutoka moyoni, basi.” Mama J akabaki akifikiria.
Akakumbuka. “Sasa unaomba nini?” “Nashukuru. Cha kwanza mimi mwenyewe najiona nahitaji kufanya jambo la ziada ili kumuhakikishia hapatakuwa na kurudiana tena ili awe huru kuendelea. Hivi ninavyoishi na Mbaki si sawa kwake na kwangu.
“Mbaki si mchumba wangu tena, sasa kwa nini nakwenda mpaka kwenye shuguli za kwao?” “Lakini kweli!” “Umeona dada yangu? Si sawa. Leo akiumwa, eti anataka mimi nikamuuguze! Kama nani? Mbaki ameshapoteza hizo privileges.” Bwana mama J alicheka! Alicheka sana.
“Amepoteza privileges za kulelewa na Tuma?” “Kabisa. Na yeye nitamwambia, hana tena hizo privileges. Kitendo cha kumtoa mwanamke hapa, tena kwa siri! Na kwenda kukaa naye huko eti siku tatu! Hakika amepoteza privileges zote. Naamini huo ukweli nikiweka kwenye matendo, itamsadia kuendelea. Atafute wa kufanana naye, aoe, wanawake wengine wapumzike.”
“Kama watapumzika! Mbaki anapesa ya kuhonga, wanawake wanamlilia.” “Basi atajijua mwenyewe, ila na mimi niendelee na maisha yangu bila simu zake za matatizo akitafuta sababu ya kuniona tu. Hapana dada.” “Nimekuelewa. Na mimi akinipigia nita…” “Hapana.” Akamkatiza kabla hajamaliza.
“Mbaki atakusumbua sana. Usipokee simu zake. Hivi hapa nilikuwa nataka kukuomba simu ile anayojua namba yako, nimfungie mimi mwenyewe, kwamba kuanzia leo asiwe anakupata tena.” “Si atakufuata hapa!” “Kabla ya kubadili namba, nitamtumia ujumbe nimueleze ukweli ndipo nabadili namba.” Mama J akavuta pumzi kwa nguvu.
“Niunge mkono tu, mama J, dada yangu. Bila hivyo nitazeeka na Mbaki mgongoni wakati mwenzangu anaendelea na wanawake zake. Hapana.” “Sawa. Hamna shida.” Akamkabidhi simu yake. Tuma akaanza kumblock Mbaki kila mahali mpaka akaridhika na kumrudishia mama J simu yake.
~~~~~~~~~~~
“Ngoja niwahi nisimuweke shemeji yako muda mrefu.” “Kwani mnaenda wapi!?” “Wewe umeambiwa nini jana?” Mama J akaanza kucheka. “Mambo mazuri hayataki haraka. Kukikamilika amesema atawashirikisha. Acha niwahi.” “Sasa usiende naye popote hivyo ulivyo Tuma. Hawa kwao ni wasafi sana wa mwili. Si umemuona kaka yao jinsi alivyo?” “Nyeupe tupu juu mpaka chini!”
“Ewaa! Umeona na sendozi aliyovaa kaka yao?” “Mguu mweupee! Ila hata baba J na Jerry wasafi sana.” “Basi ndivyo walivyo. Wanathamini sana mwili. Sana. Jeremi havai kila kitu. Mchaguzi wa nini aweke mwilini mwake, mpaka chupi. Na Jerry hivyohivyo. Sasa huko kujizira kulikokupata, leo jitahidi mdogo wangu.”
“Pitia nyumbani, oga harakaharaka, piga yale mapigo yako ya zamani, ndio muende huko unakomsindikiza.” “Nishasahau kupendeza dada!” “Jitahidi. Usitoke naye ukawa kama mfanyakazi. Una umbile zuri sana, na nywele nyingi. Kajiweke vizuri.” “Nitajitahidi.” Akatoka na kumkuta Jerry kwenye gari, amepoa haswa.
Hisia Za Kutoka Ndani
Akamuhurumia akihisi anachotesekea. “Nimekuweka sana?” Akamuuliza kwa kumjali akisikika kumbembeleza. “Hamna neno. Lakini njaa imeanza.” Akaondoa gari. “Basi nikaoge harakahara, tukale, halafu kama kutakuwa na nafasi naomba unisindikize nikasajili namba mpya.” Jerry akamwangalia na kumuuliza. “Kwa nini unataka kuwa na namba mbili?” “Niseme nabadili namba.” “Kwa nini?” Tuma akatulia akifikiria.
“Tuma?” “Kwa ajili ya Mbaki. Siku kadhaa zimepita aliniomba mazungumzo.” Akamuelezea kama alivyomueleza mama J. “Kwa jinsi tunavyoishi, naona sio sawa kwake na kwangu pia. Yeye haoi mpaka sasa akiamini tutakuja kurudiana. Na jana ulinifanyanifikirie. Naishi naye kama tupo kwenye mahusiano wakati si kweli! Mimi si mpenzi wake tena, kwa nini nimuuguze?” Akaendelea.
“Ndio naona nitazidi kumchelewesha kwa kumuwekea matumaini ambayo hayapo. Japokuwa amekataa kunisikiliza, anasema yeye bado atanisubiri tu, naona nifanye zaidi. Nitamtumia ujumbe wa mwisho kumpa msimamo wangu na kumshauri aoe tu. Kisha nabadili namba kabisa ili mtindo wakutafutana hata usiku wa manane akiwa anataka kuniona huku akijidai anamatatizo, ufe. Bila matendo hatutatoka hapa.”
“Si akikukosa wewe atamtafuta Hilda?” Akaona aulize asije furahia bure. “Nimezungumza kifasaha na mama J, na amenielewa. Nimechukua simu yake kabisa, nimezifungia simu za Mbaki kote. Sasahivi hata akitaka kumpigia, hatampata. Au wewe unanishauri nini?” “Ni wazo zuri. Na asante.” Hakutegemea kumsikia akisema hivyo, na yeye Jerry akawa kama ameropoka tu.
Tuma akamwangalia na kujirudisha kitini akatulia. Akamsikia akivuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha kama aliyepata aghueni, ndipo akahakiki kubadilika kule na kusema hakulala vizuri ni kwa sababu ya habari za Mbaki, ndizo zilizomnyima raha. “Kwamba anawivu na mimi!? Jerry!” Akabaki akijiuliza hili na lile, kwa kuwa hawakuwa wameambiana chochote, akaona anyamaze tu.
~~~~~~~~~~~
“Utachukua muda gani mpaka kuwa tayari?” “Wewe ukimaliza tu njoo, nitakuwa tayari.” “Sawa. Na nimefurahi tumefanikiwa kutoka.” Tuma akacheka na kutulia. “Tutakuwa sawa Tuma, usiogope. Unanisikia?” Akatingisha kichwa kukubali ila safari hii jinsi alivyoongea, kulikuwa na hisia nyingine zaidi mpaka Tuma mwenyewe akazisikia mpaka moyoni. Ikamtuliza. Maana usiogope hiyo ikawa kama imebeba na ahadi nzitondani yake.
Wakatulia akiendesha mpaka kwake, “Ndani ya lisaa nitakuwa nimesharudi kukuchukua. Sidhani hata kama nitazidisha dakika 45.” “Na mimi utanikuta tayari.” Akamshusha na kuondoka ila hata Tuma alimuona amebadilika sivyo kama alivyokuwa amepoa kazini. Akajua Mbaki ndiye alimchanganya.
~~~~~~~~~~~
Safari hii akaamua kuvunja sanduku. Na hivi anakuja kuchukuliwa na gari! Jerry msafi! Na anajijulia kwenye kuvaa. Ikabidi aanze kusaka. Uzuri Eli alikuwa maktaba akijisomea, alihangaika, mpaka akafanikiwa. Nywele zake hufunga tu nyuma na kubana. Siku hiyo akajiweka Tuma wa enzi kabla hajajizira.
Alishajua ana macho mazuri yakuvutia. Alipataga aina fulani hivi za kope kama za asili, akawa akiongezea kwenye macho yake! Akikuamulia kukuangalia, lazima utasalimu amri. Sasa alikuwa akiziagiza nje ya nchi nyingi, anatunza. Alipojizira, nazo zikawa moja ya vitu alivyofungia na vipodozi vingine. Sasa siku hiyo akaziweka hizo kope.
Na Tuma ni mrembo kwelikweli, amesoma na warembo halafu akachezeaga pesa ya Mbaki mpaka akajua ni nini kinamkaa sawa, nini hakimpendezi. Na anakipaji cha mkono wa kujitengeneza. Bwana alipendeza mpaka akajua, akabakia na kazi ya kuchekacheka kwenye kioo.
~~~~~~~~~~~
Jerry anarudi kumchukua, akabaki ameduaa. “Tuma!” “Nimezidisha?” “Hakika usingesimama hapo nje nisingekutambua! Kumbe unamuonekano mwingine kabisa! Aisee umependeza mno! Sana. Sijawahi kukutana na Tuma huyu!” Tuma akawa akicheka kwa furaha kuona amemvutia. “Nimebadili mawazo, sikupeleki kula kule nilikotaka nikupeleke. Twende kwenye kisu na uma!” Alicheka Tuma, alicheka sana.
“Nashauri tukale harakaharaka kisha tuanze kazi ya kuzunguka. Kesho ndio twende kwenye kisu na uma.” “Ni mara ngapi nikwambie muda na wewe, kwangu ni muhimu?” Akajisikia vizuri huyo!
“Unamuona Jeremi na Hilda? Wao wapo kama bro na mke wake. Familia kwanza. Ni mimi tu ndio sikubahatika. Ilikuwa mali kwanza. Lakini napenda utulivu Tuma! Hizi pesa zikitafutwa bila umakinifu mwisho wake ni uharibifu.” “Nimeelewa.” “Usiku hatutakuwa wote. Naomba tupate muda sasahivi, ndio tuzungukie hayo maeneo. Na si lazima tumalize leo. Si ni sawa?”
“Sawa. Ila na wewe umependeza kama kawaida yako.” “Acha nikwambie ukweli Tuma, mimi ni bora nisile, ila nivae vizuri. Napenda sana kuvaa na nipo makini na kila kitu ninachoweka mwilini mwangu. Nikimaanisha mpaka aina ya kitambaa. Sivai kila kitu hata kama ni kizuri vipi kwa muonekano, lakini lazima niridhike na aina ya kitambaa.” “Ndio maana wakati wote upo nadhifu!” “Katika hilo huwa sizembei.” Akaanza kuamini maneno ya mama J.
Akaendesha mpaka kwenye mgahawa mzuri wa hadhi kweli. Wakaingia na kutafuta kona yao, wakaa hapo. Na muhudumu hakuchelewa akafika kwa haraka. Wakaagiza kwanza vinywaji. Wote wakataka juisi ya embe, Jerry akaomba aletewe na maji. Wakabaki wametulia wamekaa kwa kuangaliana. Jerry akawa anamtizama kwa kutulia na kumfanya aone aibu.
“Umeshajua tutaanzia wapi?” Akacheka maana alimuona ameanzisha mazungumzo kama kumtoa kwake. “Tuma wewe ni mzuri sana. Una vitu vizuri sana mwilini mwako.” Akachukua menu na kujifunika nayo usoni akicheka. “Hata vidole vyako ni vizuri.” “Acha bwana Jerry!” “Mimi nakwambia ukweli. Sema basi asante.” “Asante. Ila najua wewe unajijua kama ni mzuri, tena SANA.” Bwana Jerry alicheka. Alicheka sana.
“Tumaaa! Niangalie basi.” “Sitaki.” Jerry akazidi kucheka. “Hizo sifa za nyuma ya pazia hizo, mimi siamini.” “Bwana niambie tunaanzia wapi!” “Niangalie sasa!” Akamchungulia. Jerry akazidi kucheka.
“Haya, nisikunyime raha. Nishauri wewe tuanzie wapi.” Wakaanza kujipanga. “Na nimefikiria kitu kingine, Jerry?” “Nakusikiliza.” “Tunaweza kwenda kuangalia maeneo ambayo pia yapo karibu na Pub, kwenye mabaa au sehemu wanayouza vyakula kama pale uliponipeleka kula jana. Mtu anapata chakula au kinywaji, gari yake inakuwa inashugulikiwa. Unaonaje?” “Halafu eti Hilda anafikiri nitamuachia wewe!” Tuma alicheka sana.
“Utaniiba?” “Tena mbele ya macho yake. Labda unikatalie.” “Mama J atachanganyikiwa. Anapenda kuwa na mume wake kule, washinde siku nzima pamoja, akijua mimi nitakuwepo huku kwingine.” “Itabidi ajipange tu. Hamna jinsi. NakuhitajiTuma. Nakuhitaji sana. Nilikuwa mpweke nilipotoka kwa Sandra, nikawa nimepoteza dira. Kwanza kumbuka ni kama alikuwa amenifungia kwa muda mrefu. Nafanya kila kitu kwa vile anavyotaka yeye. Sikuwa na mpango wa kuondoka ni kama alinishitukiza tu. Kwa hiyo nilitoka kwake sijui nianzie wapi! Na nafikiri bila wewe, ningekaa sana pale kwa Jeremi.”
“Nikuulize kitu Jerry?” “Uliza tu.” “Najua ni mke wako na mmekaa naye muda mrefu. Kwa jinsi nilivyosikia hayo ni maisha yenu tokea mnaanzana. Kwa nini ulikubali hayo maisha?” “Kwanza sio kweli. Hakuwa hivyo tokea mwanzo. Pesa ilimbadilisha zaidi japo kwa asili ni mkorofi na anapenda yeye ndio awe anaongoza mambo ila mwanzo haikuwa mbaya kwa kiasi hiki.”
“Na mwanzo wetu hapakuwa na kauli za changu, mpaka alipoleta mtaji mkubwa wa pesa, tukafungua ile kampuni na kuanza kuingiza pesa nyingi nafikiri pale ndipo pesa ilipoanza kumbadili na lugha kuanza kubadilika. Ila swala la wivu ni kweli alikuwa nalo tokea zamani.”
“Ana wivu ule wa kurukwa na akili. Anakuwa kama anahehuka. Hawezi niona nazungumza na mtu mwingine kwa muda mrefu yeye asiwepo, hata kama anamfahamu. Mike na Mill walikuwa wakimfahamu. Wakinitaka sehemu kwa muda mrefu, basi yeye awepo. Na alikuwa muwazi kabisa kuwa hataki mtu akae na mimi muda mrefu, na hataki hata wanawake zao wawe na mazoea na mimi.”
“Unafikiri ni kwa sababu ya huo muonekano wako?” “Sidhani! Kwani Jeremi au browanatofauti gani na mimi? Tunafanana kwa kila kitu, kama mapacha tu. Lakini mbona wao wake zao wamebakia kuwapenda na kuwaheshimu?” “Lakini kweli!”
“Ni tabia mbaya tu aliyokuwa nayo na pengine alificha makucha kwa wakati ule ili nimuoe yeye.” “Kwamba kulikuwa na mwanamke mwingine?” “Mpaka nahisi Mungu ananilipa kisasi. Nilimuacha yule msichana wa wakati ule, sasahivi ni mama na familia yake, mpaka nilikuja kujuta Tuma. Alikuwa mtulivu sana. Sana. Sijui Sandra aliniingiavipi, nikaachana na yule mwanamke nikamuoa yeye! Hakika nilikuja kujuta. SANA.”
“Nakwambia familia yangu ndio inatia aibu mbele ya ndugu zangu. Sio mke sio watoto. Mpaka nikaja kuacha kwenda kwenye mikusanyiko ya sisi watatu na familia zetu, nikaanza kuwakwepa! Naomba tuyaache hayo Tuma. Tuendelee na leo.” Tuma akavuta pumzi kwa nguvu na kutulia.
~~~~~~~~~~~
Walipomaliza tu kula, akamkumbusha. “Naomba usisahau kunipitisha kununua namba mpya.” “Kweli.” Wakatoka hapo na kuhakikisha wanapata namba mpya na kuisajili. Waliporudi garini akaanza. “Nimekuja kugundua sina hata namba yako ya zamani!” Tuma akacheka tu na kunyamaza.
“Ni sawa nikiomba namba mpya?” “Itatusaidia mawasiliano Jerry. Mimi nilijua pengine huhitaji!” “Hapana. Nikupitiwa tu. Lakini ningependa tuwe tunawasiliana wakati wote. Chukua simu yangu hapo, niwekee kisha ujipigie.” Akaivuta.
“Imefungwa.” Akamtajia password kwa urahisi sana mpaka akashangaa! Mbaki ilikuwa hataki simu yake ishikwe na ilikuwa na password nyingi mpaka ya facial recognition pia kama mfanyakazi wa FBI, kwamba anaitunza mtu asiibe siri za Marekani. Ilikuwa hata ukiiba simu ya Mbaki, huwezi ifungua.
Akafungua, akajitumia ujumbe mfupi tu wenye jina lake. ‘Jerry.’ Kisha akatunza namba yake kwenye simu ya Jerry kwa kuandika jina lake. ‘Tuma.’ “Nimeandika tu Tumanikitumaini hakuna kina Tuma wengine isije kukuchanganya.” “Hakuna. Ni watu wachache sana wanao hiyo namba mpya.” “Basi kumbe nimepatia.” Akatunza vizuri na kumrudishia simu yake bila kuperuzi kwingine.
~~~~~~~~~~~
Wakaendelea na kutafuta eneo la biashara. Walianzia palepale walipokula wakilifanyia kazi wazo la Tuma. Wakajikuta wanapata wepesi humo barabarani wakazungukia maeneo yote akipiga picha, mwishoe wakaamua kwenda mtaa wa Sinza. Wanaegesha gari mahali, wanagawana kutembea kwa miguu wakipiga picha. Mmoja akipenda hapo zaidi, anamuita mwenzie kuangalia. Wakafanya hivyo mpaka maeneo karibu na Mwenge nyuma ya kituo cha mabasi.
“Hapa ni pazuri Jerry, na pana eneo la wazi kubwa, sema kuna hiyo nyumba hapo. Kungekuwa na uwezo, ungefanya kama alivyofanyaga Mbaki. Alipenda eneo lenye nyumba ya mtu. Alichokifanya akamuomba mwenye nyumba amuhamishe, akampa eneo jingine kubwa zaidi ya pale, na kumlipa pesa nzuri mpaka akakubali. Ndio amejenga yeye.” Jerry akapaangalia tena pale vizuri.
“Kweli hapa ni pazuri. Akazunguka tena na tena, akaafikiana na Tuma.” “Na kama sio hapa, basi pale Sinza pembeni ya ile baa. Kuna eneo kubwa tu pembeni ya ule mgahawa unaonekana unakaribia kufa.” “Kwa hiyo tubakiwe na sehemu mbili tu?” “Ya tatu iwe kule eneo la wazi, Ubungo kwenda Buguruni ambako pengine hutapata shida kupapata ila itabidi kujitangaza na kuweka vivutio vingi sehemu moja. Hata kufungua sehemu ndogo tu ya nyama choma na vinywaji.”
“Hapohapo!?” “Kabisa. Unatafuta kijana mzuri. Unamuwekea kisehemu kizuri cha hadhi, hapohapo pembeni ya biashara kubwa ya kuosha magari na gereji ya matairi, unapaweka vizuri na viti vya kawaida tu. Biashara inaanza. Akichoma nyama vizuri, wanaokuja kula nyama wanaona sehemu ya kuoshea magari yao.” “Tuma! Kwani hicho kichwa chako kimebeba nini?!” “Mwenzio ni uwezo tu sina. Ila nina kuwa mambo mengi sana natamani kufanya humu duniani! Mpaka nahisi nitakuja kufa nayo.”
“Mbona sasa mimi nishapenda hili wazo la mwisho? Si unasema ni kujitangaza tu?” “Na huduma nzuri. Watakuja wenyewe.” “Basi acha nikamshirikishe bro. Ila naomba nikurudishe nyumbani sasahivi, niwahi nikaoge ndipo niende, nisije nikawaweka sana.” “Ila ujue tunaweza kuachana hata hapa. Au nisogeze hapo Sinza kwenye saluni nilikuwa nikienda zamani. Nisafishe nywele, nitarudi nyumbani mwenyewe.” “Una uhakika?” “Kabisa. Utakuwa umenisaidia na nimeua ndege wawili kwa jiwe moja.” Akamrudisha Sinza, yeye akaondoka.
Moyo Unapopata Mwanzo Wa Kweli
Bwana Tuma alijisafi! Kuanzia kichwa mpaka miguu kuhakikisha anamrudishaTuma wa zamani. Akajinunulia vitu baadhi vya kujipendezesha na kurudi kwake. Ilishakuwa saa mbili usiku. Akaanza kupika maana alijua Jerry anapenda kukaba. Hataki mawazo yake yawe kwengine ila kwake yeye tu. Akapika maandazi ya kutosha. Mazuri kama kawaida yake na vyakula aina mbalimbali ila si vingi sana maana Jerry alishasema hapendi kurudia vyakula, ila akahakikisha anapika chakumtosha na mdogo wake.
~~~~~~~~~~~
Huku kwa Jerry yeye alifanikiwa kufika nyumbani kwao. Walikozaliwa wote, ila wakaja kupapangisha. Wakakutana kwa wakati. Jeremi alishamwambia mwenye nyumba watakuwa hapo kupaangalia ili kufanya tathimini ya matengenezo. Kaka yao alikuja na mtu mwingine aliyekuwa akipiga picha na kuandika kila kitu. Wakazunguka hiyo nyumba mpaka wakaridhika.
“Sasa Jeremi ameniambia unapoishi sasa, kuna joto sana.” “Ila sio pabaya. Panatosha kwa sasa. Usiwe na wasiwasi.” “Nimebahatika kupata apartment maeneo ya Msasani. Zipo pembezoni mwa bahari kabisa. Nzuri. Zina kila kitu, unahamia na begi lako tu. Na kuna A/C.” “Usihangaike bro! Mbona mimi nipo sawa tu!” “Nimeshalipia kwa miezi mitatu. Twende tukaangalie, ukalale huko kuanzia usiku wa leo. Huna sababu ya kujibana.” “Nashukuru. Asante.” Akatulia. Kaka yake akagundua ana kitu kingine.
“Ni nini?” “Sioni sababu ya kumaliza mambo yangu na Sandra siku ya jumanne. Nataka kuwa huru. Nataka kupenda na kupendwa kwa dhati.” Wakacheka sana. “Nilijua utakinahi!” Mdogo wake akamtania. “Hata kidogo. Hujui ni kwa kiasi gani nimekuwa mpweke ndani ya ile ndoa. Nataka kuhitimisha kwa haraka sana. Japokuwa watu wanafikiri Sandra amenikomoa, ila mwenzenu naona ni Mungu amenihurumia kunitoa chini ya kifungo cha yule mwanamke. Nisaidie kuhitimisha kwa haraka, bro. Jumatatu iwe mwisho wangu na Sandra.”
“Naona upo sahihi. Hamna sababu ya kuvuta zaidi. Nitazungumza na yule wakili, nimwambie kesho amtafute Sandra. Ampe orodha ya vitu unavyohitaji afike navyo jumatatu mnapomalizana. Na kwa kuwa namfahamu Sandra, nitamsisitiza amwambie nyaraka zako zote muhimu afike nazo bila kukosa, lasivyo atakuwa akinitafuta mimi na hatafurahia kunipata. Vyeti vyako vyote vya shule sio mali yake. Hajakusomesha.” Wadogo zake wakatulia wakijua hiyo kitu imemuumiza sana. Anajikaza tu kwa kuwa amebaki na watoto wa Jerry.
Ila Jerry mwenyewe alifurahia, maana alijua huyo wanamuogopa sana, mambo yatakwenda kwa haraka bila kusumbuana naye. “Lakini bado safari ya Dubai si ipo?” “Tutakwenda. Nina maslahi mapana zaidi, nashukuru kwa kunijumuisha.” Akamuelezea juu ya wazo la Tuma, ila hakumtaja hapo. Kaka yake akaangalia picha. Akaafiki bila kupinga.
“Nitampa hiyo kazi mtu, kuanzia jumatatu aanze kupafuatilia. Na nashauri kupanunua kabisa, isiwe unaanzisha kitu kizuri hivi, halafu baada ya muda wanaanza kukuhamisha.” “Si itakuwa garama sana?” “Aridhi haijawahi kuwa bad investment hata mara moja. Na thamani yake hupanda wakati wote.” Akajua kama akiafiki yeye basi ameshajishindia eneo. Wakaenda huko Msasani.
Dunia Yazidi Kufungua Mikono kwa Jerry
Yaani usiku huohuo akahamia kwa haraka bila kufikiria mara mbili. Kweli kulikuwa kuzuri, hewa safi. Akacheka moyoni akijitupa kochini na kumtafuta Mill. “Upo kaka?” “Nipo. Mzima wewe?” “Mzima. Nashukuru.” “Sijakutupa. Mambo yamekuwa mengi mno. Napambana na muda.” “Usijali kabisa. Nakupigia mida mibaya, lakini nilitaka kujua, pale Kinondoni kwa mama mkwe wako, unampango gani?” Ndipo akamueleza kuwa yeye alishahama, kuna mtu angenufaika na pale, asipaachilie.
“Acha nizungumze na Pam juu ya vitu vilivyopo hapo, lakini kwa hakika hapana matumizi tena. Mama amehama hapo, nataka asije kurudi tena huko. Hapa ni pazuri na kuna kila kitu, lakini panakuwa wazi tu. Akiwa hapa inamsaidia hata Pam kuwa karibu na mama yake. Inamtuliza. Nitakujibu baada ya muda.”
Akamtumia ujumbe Tuma. ‘Umeshalala?’ Alifurahi huyo kupata ujumbe kutoka kwa Jerry. Mpaka akacheka na kukaa. ‘Namalizia usafi hapa, nikaoge.’ ‘Naomba unipigie kabla ya kulala.’ ‘Sawa.’ Kwa hiyo akawa akisubiria simu kutoka kwa Mill na Tuma ila akitamani ya Mill iwe ya kwanza ili akizungumza na Tuma awe na habari njema.
~~~~~~~~~~~
Mill akampigia na kumtaarifu kuwa vitu vimepata mtumiaji. Mjomba wake Pam atakwenda kuvifuata kesho yake mapema sana, siku ya jumapili. Kwa hiyo huyo anayehamia hapo anaweza kuhamia hapo mapema tu, na mwenye nyumba atakuwepo kuingia naye mkataba mpya. Hilo likakaa sawa. Akabakia kumsubiria tuma.
~~~~~~~~~~~
Baada ya lisaa ndipo Tuma akampigia. “Nilijua nimekuchelewa.” “Nisingelala bila kukusikia. Vipi Eli?” “Naona leo amechoka, anakoroma pale kwenye kochi.” Jerry akacheka. “Ulifanikiwa saluni?” “Nilifanikiwa, nilimkuta hana wateja wengi. Akanishugulikia. Nimerudi hapa na kuanza kupika kwa kuwa sikujua ratiba yetu ya kesho. Sikutaka iingiliane.” Jerry akafurahi huyo, akijua ameshaanza kumuelewa.
“Muda wetu ni muhimu Tuma. Ila kama ukiona nakuchosha uniambie.” “Hata kidogo. Ungejua na mimi nilivyokuwa mpweke! Mwenzio nilijizira kabisa Jerry. Mbaki aliniumiza na kunidhalilisha vibaya sana. Na ile watu kusema eti ame upgrage, iliniondolea ujasiri kabisa.” “Ndio maana ulijitupia kwenye kazi tu?”
“Wewe ndio umeelewa. Hata kwenye masaluni niliacha kwenda kabisa, sababu ya aibu. Nikawa najifanyia mambo yangu nyumbani. Maisha yakawa nyumbani, kazini. Angalau leo, baada ya muda mrefu, nimeweza kurudi saluni, nimetengenezwa nikaridhika. Nimerudi hapa, Eli hajaamini.” “Ulivyopendeza?” Akacheka na kurekebisha. “Kubadilika. Kwa hiyo nashukuru kunikumbusha kutulia. Inanisaidia sana kutulia mpaka moyoni.” “Tutakuwa sawa Tuma.” Akagundua hilo neno analirudia rudia.
“Naamini hivyo. Sasa leo utalala vizuri?” “Sana. Na pale nimehama.” “Jerry! Umehamia wapi?!” Akamueleza kila kitu. “Hongera. Na nikweli unastahili. Hawa watu wanatuachaga pabaya! Kurudi chini kabisa sio haki. Bora unakuwa na maumivu ya kuachwa ila kimaisha inakuwa si pabaya.” “Binafsi sina maumivu ya kuachwa. Na nimemwambia bro, jumatatu nataka nihitimishe naye.” “Itawezekana?” “Hana kitu anashindwa yule. Na lile eneo amesema tununue sio kukodisha.” Akamueleza mengi, Tuma akampongeza sana kana kwamba wazo lilikuwa lake kumbe ni yeye mwenyewe alimpa. Akamtia moyo, asijue anazidi kujipandishia CV kwa Jerry.
“Sasa pale pako wazi na kumelipiwa kodi ya miezi 6, imebakia 5. Sio sawa kuishi na kaka yako chumba kimoja. Hitimisha hapo kwa mwenye nyumba, kesho uhamie pale.” “Nashukuru Jerry. Kesho nitamtafuta mwenye nyumba.” Wakatulia.
“Nasafiri Tuma.” Akamsikia hajibu. “Tutaondoka siku ya jumatano, tutarudi jumamosi. Nikuletee nini?” “Wewe. Naomba urudi kwangu salama Jerry. Hayo tu ndio maombi yangu.” Wakatulia, Jerry akijaribu kuyaingiza moyoni.
Akamsikia anavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu. “Kesho nitakuja kukusaidia kuhama, halafu itakuwa sawa tupate muda wetu tena?” “Nitafurahi.” “Sawa. Basi pumzika. Kwenye majira ya saa nne, nitakuwa nimeshafika hapo.” “Na mimi muda huo nitakuwa nimeshapata gari ya kutuhamisha, tunapakia vitu.” “Acha nimuulize Jeremi kama anaweza kutupa gari. Nakurudia sasahivi.” Akashituka sana.
“Subiri kwanza Jerry! Utamwambia nini baba J? Si utamshitua akisikia unatafuta gari kwa ajili yangu?” “Ulitaka kunificha kwao sababu ya Mbaki?” Akauliza swali lililojaa wivu na kumshitua zaidi. “Hapana Jerry! Mbaki nimeshamalizana naye, hata mama J anajua.” “Basi kumbe hapatakuwa na shida.” “Ndiyo. Hamna shida.” Akapoa. “Mimi sina mpango wa kukuficha Tuma. Sina sababu.” “Na mimi sitaki kukuficha Jerry. Sina sababu.” “Basi acha nitafute usafiri.” Akakata na kumuacha Tuma na furaha sana.
~~~~~~~~~~~
“Jerry!” Akajikuta akicheka peke yake asiamini kama ndipo Jerry alipo na yeye! “Wanaume kama Jerry ndio zile ndoto zisizooteka!” Akazidi kufurahi ila akaanza kujifikiria vile mama J atakavyoshituka. Akatulia akisubiria.
Kwa Jeremi.
Akampigia mdogo wake na kuamsha maswali mengi sana. “Umesema ni kwa ajili ya kumuhamisha Tuma?!” “Unazingatia lisilo la muhimu Jeremi! Wewe nani kakufundisha umbea siku hizi? Hukuwa hivyo!” Jeremi alicheka sana. “Gari, Jeremi?” “Lipo kaka. Na jibu la swali langu?” “Waambie vijana wako nitalifuata saa tatu asubuhi. Kwaheri.” Jeremi akazidi kucheka, kaka yake akamkatia simu bila ya kumjibu.
~~~~~~~~~~~
Akamrudia Tuma na kumpa habari njema. “Au ulitaka niwahi zaidi?” “Hapana. Ukifika hapa saa nne utakuwa muda mzuri, ndio utanikuta nimeshafungasha kila kitu. Ukija utatukuta tayari. Kwanza hatuna vitu vingi.” “Basi nitakuona kesho.” “Leo ulale Jerry.” “Nitalala. Leo sina sababu ya kutokulala. Na wewe uzime simu sasahivi, ulale.” “Nitafanya hivyo ili asubuhi niamke na nguvu za kuhama.” “Na baadaye kupata muda wetu.” “Na baadaye kupata muda wetu.” Akacheka na kuagana. Wote wakalala wakiwa na furaha yakupitiliza, kama ambao hawaamini kinachoendelea katikati yao.
0 Comments:
Post a Comment