Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Love At First Sight - Sehemu ya 88. - Naomi Simulizi

Love At First Sight - Sehemu ya 88.

Alifika kwa wakati, wakaondoka mpaka kazini. Hapakuwa na foleni bado mapema. “Nimeiga kifungua kinywa cha mama J. Nilikuona ulivyofurahia.” Jerry akacheka. “Nakushukuru. Sasa si utakuwa umedamka mapema sana?” “Kawaida, Eli alinitayarishia usiku, asubuhi nimemalizia tu. Ameenda shule amefurahi huyo, maana alikuwa anasoma huku namwandalia na yeye kifungua kinywa. Eti ananiambia nikiwa namfanyia hivyo kila siku atanipenda zaidi.” Jerry alicheka sana.

“Hivi unajua ulipokuwa ukisema Eli, nilijua katoto kadogo!” “Urefu tu, hana lolote. Kaa ule.” Wakakaa na kuanza kula. “Leo natakiwa kupokea mzigo, sababu ya kesho. Kwa kiyo muda mwingi nitakuwa kule stoo nikiweka mambo sawa.” Wakaendelea kuzungumza huku wakipata kifungua kinywa. 

“Nitakuja huko pia nione inavyokuwa. Nafikiri leo nitakuwa gereji kuangalia.” “Siku nzima?!” “Ni muhimu. Siwezi kuwa na biashara ambayo sijui utendaji kazi wake. Nitakuwa nao leo. Nataka kufanya kabisa.” “Umeamua!” “Sina jinsi. Na sitaki kuja kukwama endapo nikijikuta nakuwa kazini halafu pengine mmoja hajafika, wamelemewa, mimi mwenyewe nipo na sijui chakufanya. Nitakuja kwenda hata kule alipo Jeremi nione vifaa vyote.” “Sio wazo baya.” Siku ikaanza kwa utulivu. Wawili tu. 

Ila wakashinda upande wa pili wa ofisi. Ni kama Tuma hakutaka kumuacha huko gereji na mafundi tu. Kuna muda akampelekea maji ya kunywa. Akashukuru akiendelea kuelekezwa.

JJ Mshika Mpini

Ilipofika jioni ya saa 10 karibia wanafunga akaja huyo kaka mkubwa. Utafikiri mapacha! Alijaa neema huyo kaka mkubwa, ungejua pesa ipo. Akamkuta Jerry anabadili tairi. Jasho linamtoka. “Kwema? Mbona umeloa hivyo!?” “Nafundishwa. Subiri kidogo namalizia.” Mara akafika baba J kama ambaye alikuwa akiwahi.

“Vipi, kwema?” “Namsubiria Jerry, naona anabadili matairi!” Ikawa kama anayelalamika. Jeremi akamsogelea Jerry. “Usaidiwe?” “Nitajifunza vipi? Namalizia, nakuja.” “Mambo yamebadilika, vipo vifaa vya kubadili matairi sio lazima kufanya kwa mkono.” Akaongeza kaka mtu wakimwangalia Jerry. Msafi haswa. 

Jerry akamalizia nakutoka akamsogelea kaka yao. “Si unajua zipo mashine sio lazima ukafanya hivyo kwa mkono!” Akaonekana amesumbuka. “Nataka kujua vyote! Kwa mashine na mkono. Kwa kuangalia tu hivihivi sitajua. Vipi safari?”  Akamjibu kaka yao na kumgeukia Jeremi akamtupia hilo swali kama anayetaka wabadili mazungumzo. “Ndio tumerudi. Vipi hapa?” “Kwema kabisa.” Wakaondoka hapo kurudi ofisini wote watatu wakizungumza. Walionekana kumuheshimu sana kaka yao.

Tuma alipomaliza kila kitu akafunga na kurudi ofisini maana hata vijana wa gereji walishaondoka. “Kuanzia saa moja sio mbaya.” Akamsikia baba J akiongea wakati akiingia ndani, walikuwa wapo ndani kwenye chumba cha ofisini ila mlango uko wazi.

“Na nikipata hayo maeneo mapema itakuwa rahisi kuyafuatilia. Kwa hiyo wewe nenda ukazunguke hiyo kesho, chagua utakapopenda. Mimi mwenyewe nitafuatilia kujua utaratibu wa kupapata.” Akamsikia kaka yao akimwambia Jerry.

“Ila vifaa nilitaka nifuate mwenyewe China.” “Sio wazo baya. Nina safari ya kikazi Dubai, week ijayo. Unataka twende wote ukaangalie na huko jinsi wanavyofanya vituo vyao vyakuoshea magari?” Pakatulia kwa muda hakumsikia Jerry akijibu.

“Itakusaidia kubadili mawazo na kupumzika zaidi.” “Nafikiri sio wazo baya, lakini hati yangu ya kusafiria nimeacha kwa Sandra.” “Jumanne yule wakili ameahidi mtakuwa mmemalizana kabisa. Talaka yenu hata yeye amesema ni rahisi sana. Kwenye mali ndio kunakuvutana. Lakini nimemuhakikishia hutabadilika, hutahitaji kitu, umetaka sehemu yako ya mali imsaidie Sandra na watoto. Si ndivyo?” Kaka mtu akauliza kutaka uhakika.

 “Kabisa. Na nashukuru. Nilisahau kukushukuru. Nilizungumza naye jana. Alinitafuta usiku mwingi, akiwa anaandaa hizo nyaraka.” “Basi katika hilo, mpe orodha ya vitu utakavyotaka Sandra akujie navyo wakati mkiwekeana saini. Ikiwepo hiyo hati, ili tujipange kwa safari. Kuna jambo jingine?” Akasikia akiwauliza wadogo zake.

“Hamna. Tukutane hiyo kesho pale nyumbani.” “Dogo unang’aa! Naona nyinyi wenzetu mligoma kumaliza fungate, kabisa!” “Acha hizo bro!” Wakaanza kucheka. Mama J akaingia. “Vipi Tuma?” Akamsalimia. Kabla hajajibu salamu, shemeji yake akamdaka. “Eti Hilda, nyinyi wenzetu fungate imegoma kuisha?” Alicheka mama J, akacheka sana kwa aibu. Akatoka kabisa hapo ofisini kumsogelea mama J. Akaona mama J anamsalimia mpaka kwa goti! Akajua ni zaidi ya ukaka tu! Upo utisho wa kiuchumi

“Vipi bimkubwa?” “Yupo. Anawasalimia. Si amekwambia kama anaandaa shuguli ya sadaka ya shukurani?” “Ameniambia, na namsaidia kuandaa.” “Basi ninyamaze. Kumbe nazungumza na mwanakamati mwenyewe!” Wakawa wanacheka, hapo wakitaniana. Mwishoe akaaga. Wadogo zake wakamsindikiza, mama J akavuta pumzi kwa nguvu.

“Huyu kwa wadogo zake! Hawakui!” Akawa anaongea huku akimchungulia kama ameondoka. “Hapo amekuja kumuangalia Jerry, kutaka kumuona anavyoendelea. Hatakiwadogo zake wapate shida hata kidogo! Alimkuta wapi?” “Anabadili matairi.” Alishituka mama J. “Haiwezekani!” “Lakini mwenyewe amemwambia anajifunza.” “Nakwambia kabisa, hajafurahia. Na atakuja kulalamika tena.” “Ila Jerry amemwambia anataka kujua kwa vitendo, na atakuja kwenda mpaka huko kwa baba J, kujifunza zaidi.” “Labda hivyo. Haya za hapa?” “Nzuri, za safari?” “Nilikuwa natamani kama nisirudi!” Akaanza kumcheka.

“Kupumzika kutamu! Ndio unamuelewa Umi, kupenda kulala hataki kukiachia kitanda.” “Bwana kilichompata Umi!” “Ehe!” Akaanza kucheka, mbavu hana. “Kafanyaje tena? Maana nasikia kule anawahi kwelikweli na ametulia.” “Hapa sidhani kama atarudi, labda Jerry aondoke. Njoo nikusimulie huku jikoni.” Wawili hao wanapendana nahawamalizi

Wakahamia jikoni akaanza kumsimulia mwanzo mpaka mwisho kwa sauti ya chini sana, akamuacha mama J mdomo wazi, ametoa macho. “Haiwezekani Tuma!?” “Kwa ukali kabisa. Lakini mimi nilimuonya Umi, akanipuuza. Alikikataa chakula chake kwa ukali kabisa. Hakutaka kunisikiliza. Ndio likampata lakumpata. Sijamsikia tena.” “Basi atakuwa katia adabu. Nasikia huko amepoa, hana kelele kabisa. Itakuwa Jerry amemshitua sana. Na vile Umi anavyojiamini! Atakuwa amemuumiza sana. Ila alihitaji kusikia, pengine itamsaidia yule mtoto na kutulia.” “Hilda?” Alikuwa mumewe akimuita.

“Nipo jikoni na Tuma.” “Sasa sisi twende. Usianzishe kikao kingine huko.” “Namalizia.” “Uwe unamalizia kweli, Hilda!” Wakacheka na kutoka. 

“Vipi shemeji yangu?” “Nipo.” “Naona mambo yako si mabaya.” Jerry akacheka tu. “Acha sisi tukapumzike baada ya mapumziko mafupi.” “Nina ombi.” Jerry akafanya mdogo wake na mke wake wamgeukie.

Tuma alikuwa amesimama nyuma ya mama J, ila mlango wa jikoni. “Nini?” “Najua kesho kunakuwa busy sana hapa, na mnamtegemea Tuma.” Kimya wakimwangalia kutaka kujua anataka kusema nini. “Ombi la kwanza kabla ya hili la pili ni msiniulize na msimuulize Tuma mpaka nitakapo kamilisha, nitawashirikisha. Ila ombi la pili ni kwamba, naomba kesho Tuma atoke kwa wakati. Kuna mahali nilimuomba anisindikize.” Wote wakamgeukia Tuma kwa mshangao na kurudisha macho kwa Jerry.

“Ndipo linapokuja lile omba la kwanza. Msiulize chochote.” “Subiri kwanza Jerry. Ujue namtegemea SANA Tuma!” “Najua, na ndio maana nimekuomba shemeji yangu.” Akawa anacheka. “Hakika usicheke Jerry! Tuma ndio mimi kwa hapa! Nazurula kwa sababu najua Tuma yupo hapa! Sasa ukianza kumzurulisha, ujue unanifunga mimi miguu!” “Najua. Lakini nakuomba uje umshikie hapa kwa kesho. Tena mchana wala si asubuhi.” Akashangaa mumewe anacheka hana mbavu.

“Sasa unacheka nini?” “Umemshika pabaya huyo! Tuma! Hakika umemshika pabaya. Ona alivyopoa.” Baba J akazidi kumcheka mkewe akimwangalia. “Ni saa sita ndio anatoka! Asubuhi atakuwa hapa kama kawaida.” “Yaani ni kwa vile ni wewe, na ni Tuma. Ila jua umeshaniharibia weekend yangu. Inamaana mimi ndio natakiwa niwepo hapa, lasivyo kesho wale vijana kule watafanya sherehe!” Akaona anambusu shavuni. 

“You’re the best.” Mumewe akazidi kucheka. “Hakika usifanye mazoea bwana Jerry!” “Acha kulalamika Hilda! Ni jambo zuri. Mwenyewe utafurahi.” “Labda…” “Hakuna kuuliza. Wewe saa sita kamili uwe umefika hapa.” Wakamuona anatoka kwa unyonge. “Busu lote lile, halijasaidia!?” “Si kwa Tuma.” Akajibu mumewe akimfuata nyuma akiendelea kucheka.

~~~~~~~~~~~~~~

Wakabaki wawili wakiangaliana. “Tutoke nikaoge, ndipo nile. Siwezi kula hivi nilivyo.” “Kwa hiyo utabeba chakula?” “Hapana Tuma! Kitu kingine juu yangu, sipendi kurudia chakula.” “Nyie Jerry!” Akaanza kucheka vile alivyoshangaa, hana mbavu. “Kula wali mara mbili kama dawa!” “Sasa utakula nini?” “Sasahivi bado mapema. Twende nikaoge. Nibadili nguo, halafu tukale.” Tuma akabaki ametoa macho.

“Acha hizo Tuma! Sasahivi mapema sana. Mpaka kwangu hata dakika 20 haziishi. Naoga chapu, tunakwenda kula, halafu nakurudisha nyumbani. Hatukawii. Utalala kwa wakati.” Tuma akabaki akimwangalia. “Nina hamu na ugali wa muhogo.” “Basi kazi itakuwepo.” “Sio kubwa. Usiogope. Twende.” Wakamalizia hapo na kutoka mpaka kwake.

Tuma Nyumbani Kwa Jerry.

Tuma akaanza kucheka walipokuwa wakiingia. “Ndio maana unadharau!” Jerry alicheka sana. “Pale kwako pako hatarini bwana! Mlango wa kuingilia ndani upo barabarani!” “Sawa bwana! Ila ungeniambia kama wewe mtoto wa geti kali!” Akazidi kucheka wakati akivuta gari yake nyuma kabisa.

“Nishaona hapa sitapaweza.” “Acha woga wewe!” “Ukishaona nyumba zina mageti kama haya na walinzi, jua na kodi yake itakuwa kubwa.” “Na maji ni masaa 24, wanakisima, ushindwe mwenyewe. Twende ndani.” Wakaingia. 

“Ila Jerry wewe sio mtu mzuri! Tumeshinda wote kwenye joto, mwenzangu umekuja kuoga ili ukale vizuri, mimi nanuka jasho!” “Mimi nanuka jasho na nililoa jasho.” “Mmmh!” “Basi tukitoka jumapili, utakuwa na wewe umependeza.” “Jumapili tena!?” “Kesho jioni tunakutana na bro. Anataka tuzungumze sisi watatu. Ila jumapili nitakuwa free. Nitakufuata tukale. Kwa hiyo utakuwa na muda wa kuoga utakavyo.”

“Jumapili mwenzio napika, Jerry! Lasivyo tutaishiwa chakula siku za kazi!” “Sasa unapika siku nzima!?” “Asubuhi kanisani.” “Tuma! Na muda wetu sisi?” Akaanza kutoa shati akielekea chumbani, Tuma akakwepesha macho. “Naoga mara moja tutoke.” Akamsikia akizungumza huko chumbani.

Baada ya muda akamuona anatoka na taulo tu amefunga kiunoni. Tuma alishituka mpaka akafunga macho. Acha Jerry acheke. “Bafu ni moja tu. Na lipo hapo. Pole mgeni wangu.” Tuma akabaki amejifunika macho, Jerry anacheka huku akielekea bafuni. Akamsikia akioga, akabakia kwenye simu huku akimtafakari Jerry. “Huyu si alimwambia Umi hatamuona akiwa uchi! Mbona hapa anajiacha uchi sasa!?” Akawaza macho kwenye simu. Akabaki amepotelea mawazoni.

Akamsikia anatoka. Akainama kabisa. Akapita kimyakimya bila ya kumuongelesha. Akarudi chumbani kwake. Pakatulia. Baada ya muda akamsikia akitoka. “Twende.” Akamwangalia. “Ona ulivyo msafi, halafu ukapendeza, halafu unaongozana na mimi mchafu!” “Jumapili utanilipizia.” Tuma alicheka sana.

“Jumapili pendeza utakavyo!” “Sasa tutakula nini kama tunakuwa tunazurula tu?” “Sio kuzurula! Halafu si tumekubalina tunakwenda kutafuta maeneo yatakayobaki kesho?” “Kama tunaanza saa 6 mpaka jioni tutakuwa tumemaliza.” “Mbona nakuhisi ni kama unanikwepa!” “Sikukwepi Jerry!” “Sasa mbona kama unatafuta sababu za kutokuwa na mimi?” Akakaa kabisa.

“Eti Tuma? Au nimezidisha, unataka nikupe nafasi?” “Hapana! Nilikuwa nikifikiria maswala ya chakula. Nipate muda wa kupika ili tusisumbuke chakula kazini. Week nzima.” “Muda na wewe kwangu ni muhimu kuliko chakula. Chakula tunaweza agiza kikaletwa tulipo, lakini muda wetu ni mfupi na mipango ni mingi. Kweli unataka tuache kila kitu sababu ya kutaka kupika?” “Kupika ingesaidia kubania pesa Jerry! Una malengo makubwa, yanahitaji pesa.” “Nikikwambia pesa sio tatizo tena, utaridhika?” Akatulia.

“Hapa nilipo nasubiriwa niwe na wazo tu, sio pesa. Wazo ni nini nataka nifanye,kianze. Nimempa kaka wazo ulilonipa, amelipokea. Anachosubiria nimpe maeneo ninayoyataka, aanze kufuatilia anisaidie kupata.” “Kweli Jerry?” “Kabisa. Unafikiri pale alipo Jeremi sasahivi na mke wake walipata vipi?” “Sijui!” “Kaka ni mkandarasi mkubwa sana hapa nchini. Anapataga tenda za ujenzi wa barabara, anafahamiana na watu wakubwa sana hapa nchini. Ni rahisi kwake kufikia watu kuliko sisi. Nimemwambia anipe siku ya kesho na kesho kutwa, nitakuwa nimepata jibu, halafu na wewe unanigeuka tena!?” “Siwezi kukugeuka. Basi kweli tufuatilie maeneo kesho. Tunaweza kufanikiwa.” 

“Unachoniambia tukifanikiwa kesho ndio basi?” “Tutajipanga tena Jerry! Umesema tusiishi kesho wakati leo hatujamaliza.” “Lakini nataka uhakika na wewe Tuma! Nataka kujua kama upo upande wangu au unafanya kama kutimiza wajibu tu! Maana nipo na wewe hapa sio kama mwajiriwa wa wakina Hilda.” “Naelewa. Na nipo upande wako.” “Unauhakika?” Akatulia kidogo akijaribu kutafakari kabla hajajibu kwa haraka.

“Au unataka nikupe muda ufikirie?” “Ndio itakuaje huko kunipa muda!?” “Utaniambia wewe vile unavyotaka. Naweza kukuacha kabisa isiwe kama nakughasi.” Akamwangalia na kuinama. “Eti Tuma?” “Haunighasi Jerry! Naomba tuendelee kuanzia hapa. Naamini tutafanikiwa tu. Twende ukale, uje upumzike.” Akabaki amekaa, Tuma akasimama kabisa. “Twende. Umekuwa na siku ndefu, umefanya kazi ngumu, utakuwa umechoka. Twende.” Kwa kubembelezwa huko, akasimama. Na kuondoka hapo. Utulivu njiani kila mmoja akitafakari kile walichoshindwa kuambiana kwa wazi ila kipo.

~~~~~~~~~~~

Akaendesha Tuma akiwa ametulia garini, kimya. Anawaza ambacho hajakielewa vizuri. Na Jerry naye akijiuliza imekuaje kwa Tuma, mbona anashindwa kujizuia! Mbona kama mwendo ni mkali sana! Kasi ya hali ya juu na hazioni breki! Kisha akajiuliza hata kama akizipata breki, yupo tayari kuzishika au aache gari liserereke hivyohivyo! Ndio ukimya huo.

~~~~~~~~~~~

Akaendesha mpaka sehemu wanayouza chakula. Kulikuwa na watu wengi na wengine walishaanza weekend. Wakatafuta meza sehemu yao, wakakaa. “Naomba uagize kitu kizuri ulicho na hamu nacho. Usiogope bei.” “Sijala samaki muda mrefu!” “Basi agiza, ule ushibe. Ukifika nyumbani ni kulala tu.” “Asante.” Jerry akacheka akimwangalia mpaka akamtia aibu.

Muhudumu hakuchelewa akawatajia vyakula walivyonavyo, moja kwa moja Jerry akataka ugali wa muhogo, maziwa mtindi, akabahatika kisamvu na samaki wa mchuzi. Tuma yeye akataka ndizi za kuchoma, kachumbari na samaki wa kuchoma. 

“Wewe hunywi pombe?” “Hapana. Imetokea kwetu hakuna anayekunywa pombe. Hata bro, hanywi kabisa. Na hata wazazi wetu hawakuwa wanywaji. Wewe unakunywa?” Acha Tuma aanze kucheka. “Sasa unacheka nini? Sandra alikuwa akinywa wine.” “Kwa kweli mimi sinywi.” “Kwa hiyo Mbaki alikuwa akinywa?” Hakutegemea, ikawa kama aliyesoma mawazo yake. “Ndiyo. Na anapenda sana pombe.” 

“Alishaoa?” Akarusha swali jingine. “Mmmmh! Nafikiri alipata majukumu makubwa yaliyompa pesa aidha aikiwa mdogo sana, au hakuwa ameandaliwa jinsi ya kuishi na madaraka makubwa akiwa mdogo. Kwenye fani yake amefanikiwa vizuri, na wanamlipa pesa kubwa sanaAnahangaika tu, hata hujui anataka nini! Huwa namuacha tu.” Hapo akamchanganya kidogo.

“Sijaelewa, kwamba bado mpo kwenye mawasiliano!?” “Yupo. Wakati mwingine akili zake eti huwa zinamtuma kumtafuta mama, anaweza kumsalimia tu akitaka kumjulia hali, na wakati mwingine mama huwa ananiambia anamtumia vitu kabisa. Madai yake eti alipolipa mahari eti alitengeneza udugu. Ukimuona hivi, unaweza sema ni mtu kweli! Maneno mazuri, amenyimwa vitendo.” Akawa ameshamvuruga.

Vinywaji vikaanza kuletwa. Alitaka maji, Tuma coke. “Naona watu wameshaanza weekend.” Akavunja ukimya. Jerry akaangalia kulia na kushoto. Akatulia.

“Nitakuja kukupeleka sehemu ingine wanatengeneza ugali mzuri sana na kuku wa makange. Kuna jinsi wanapika yule kuku, Mbaki alikuwa lazima kwa week apate hata mara moja.” Jerry akamwangalia asijue anazidi kumchanganya.

“Ila sio kwamba hapa ni chaguo baya!” Akajishuku. “Namaanisha na kule pia sio pabaya, ni kupajaribisha kuona kama na wewe utapenda.” Kimya. Akimwangalia. “Na simaanishi kutaka kukufananisha eti kwenda kule nikidhani labda na wewe utapapenda! Hapana. Kila mtu anakitu chake anapenda sana, mwingine anaweza ona kawaida.” Kimya akimtizama. 

“Mimi naona niende tu chooni.” Akanyanyuka na kuondoka kabisa hapo akijua ashajichanganya. Ndipo Jerry naye akajua na hapo sio mgeni kama alivyodhania. Alikuja na nani! Moja kwa moja ni Mbaki. Akabaki kimya akimsindikiza kwa macho.

~~~~~~~~~~~

Akakaa huko kwa muda tu ndipo akarudi akakuta na muhudumu amerudi na chakula. Akakaa hata asimwangalie Jerry kwa aibu ya kuropoka. Aliongea mengi mwenzie amenyamaza tu.

Wakanawishwa mkono wakakaribishwa wakaanza kula. Kimyakimya Tuma akiwa amejionya kuwa mchache wa maneno.

“Huwa mnawasiliana na Mbaki?” Alishituka mpaka akaanza kukohoa mfululizo akampa maji yake. Akanywa akimpa pole.

Akatulia akijifanya amesahau swali. Naye Jerry akampa muda kidogo tu na kurudia tena. “Hujanijibu!” “Huwezi kumkwepa Mbaki hata ufanyaje!” “Ukimaanisha nini?” “Nisipopokea simu yake ujue atamtafuta mama J hata kama ni usiku yeye amelewa. Atataka mama J amwambie nilipo na kwa nini sipokei simu zake. Atamsumbua mpaka inabidi sasa mama J anitafute na kuniambia nimsikilize tu.” “Kwa hiyo kujibu swali langu ni kwamba bado mnawasiliana?” “Labda niseme huwa wakati mwingine yeye ndio ananitafuta lakini huwezi sema kwamba tunawasiliana.” Jerry akamtizama kama anayemsuta.

“Basi niseme ndiyo, ila sio mara kwa mara. Pengine akiwa amelewa kama hivyo, akili zake zikimtuma visivyo. Au akiwa anaumwa au kuna msiba kwao. Maana ndugu zake nawafahamu.” “Sasa huyu sio x-wako! Ni kama bado mpo kwenye mahusiano tu!” “Huwezi kumkwepa Mbaki!” “Nafikiri ukiamua, unaweza. Bado hujaamua kwa kumaanisha.” Akaendelea.

“Sandra alikuwa ni kama anaishi na simu yangu. Na akinipa hiyo simu ujue yeye anatoka au mimi natoka, atataka kunipata kila sekunde ndio maana atanipa hiyo simu. Na popote nilipokuwa mbali na yeye lazima awe anapajua, na amepaidhinisha yeye. Na muda aliokuwa amenipangia wa kuwa huko nilipo nisizidishe hata sekunde.” Akashangaa sana mpaka akamuona.

 “Watu wangu wote wakaribu waliokuwa wakitufahamu. Walikuwa wakijua na kushangaa. Lakini ndio alikuwa yeye na jinsi alivyoiendesha ndoa yetu, na nikatii. Ila tokea tumehitimisha mpaka sasa, ninamuonyesha kwa vitendo kuwa, kuna mipaka kwenye maisha yangu. Na haruhusiwi tena kuvuka.”

“Dhamana aliyokuwa nayo kwangu HANA tena. Amepoteza, kadhalika na mimi kwake. Nasubiri kwenda kuhitimisha kisheria, basi. Na hata siku hiyo nitataka kujua mbele ya mwanasheria jinsi ya kuwafikia watoto wangu. Akikataa kwa kuwa watoto wenyewe wapo upande wa mama yao, naweza nikawaacha tu mpaka watakapokuja nitafuta wao wenyewe. Nimemaliza.”

Sitegemei eti kesho anaumwa, anitafute mimi kumuuguza! Kama nani wake?! Hapana. Nafahamu ndugu zake, lakini mahusiano tumeshavunja rasmi. Sitegemei leo eti nakuja kukutana kwa mdogo wake! Hapana. Mdogo wake alikuwa shemeji kwa sababu nilimuoa dada yao! Undugu umekwisha kwa sababu ndoa iliisha. Sio maadui, lakini tunakuwa tumeshamalizana.”

“Na hayo ndio yanayoonyesha kuna mahusiano, au hivyo vitu ndivyo vinavyoshikilia mahusiano. Sasa huwezi niambia mmeachana na mtu wakati bado mpo kwenye shida na raha! Sasa huko kwa wanawake zake anafuata nini kama wewe unampa kila kitu?” Tuma akanyamaza kabisa. Hakujibu. Wakala kimyakimya ila alimuona alivyobadilika.

Alipopiga miayo tu, Jerry akamuita muhudumu. “Ngoja tulipe, ukapumzike. Unakitu unataka kumbembea Eli?” “Hapana. Asante. Nashukuru kwa chakula.” “Umeshiba vizuri?” “Sana. Asante.” Akabaki akimwangalia, Tuma akainama. Muhudumu akafika, akamlipa, wakaondoka.

~~~~~~~~~~~

“Jumamosi huwa mnaingia kazini muda gani?” “Mimi sibadili. Tena kwa kuwa jumamosi panakuwa busy sana, napenda mambo ya pale ofisini nimalize mapema, nahamia stoo.” “Kwa hiyo unakuwa kule siku nzima?” “Kwa asilimia kubwa, labda niwe nakwenda kula, napo wakati mwingine huwa naona ni bora nilie kulekule ili wasisumbuke kuja kuniita mara kwa mara.” “Basi nitakuja kukuchukua muda kama wa leo.”

“Nina wazo.” Akamwangalia akiendesha. “Kwa kuwa jumamosi hakuna foleni, na daladala ni nyingi tena zinakuwa tupu kabisa, watu wengi hawaendi kazini, kwa nini usipate muda wa kupumzika zaidi, mimi nipande tu daladala? Nikimaanisha kesho hata ukifika saa mbili na nusu kazini, ni sawa.” “Si wazo baya, lakini kumbuka nipo kwenye kujifunza. Unachokifanya, ni lazima nijue ili nikianzisha changu, nisiwe mgeni kwenye biashara yangu mwenyewe.”

“Sijui kama na mimi nitajaliwa mtu kama Tuma au la! Sitaki nizembee wakati sasahivi nimepata nafasi ya kujifunza kwa Tuma mwenyewe.” Akacheka kidogo na kuafiki. “Ni kweli.” Wakatulia. 

“Sijali kuja kukufuata Tuma. Sio usumbufu hata kidogo.” “Nashukuru.” Wakatulia tena kama waliopatwa na kipingamizi wanashindwa kukizungumzia kwa wazi, Tuma akajiegemeza na kunyamaza akitafakari juu ya Mbaki. 

Aliendesha mpaka nyumbani kwa Tuma, akaegesha. “Chakula cha mchana si tutakula paleplae kazini?” “Naona na mimi nikaonje chakula cha Mbaki.” Alimfanyia makusudi. “Kwahiyo kesho nitaomba unipeleke huko kwenye vinono.” Tuma alipoa, alipoa haswa. “Au ulikuwa ukifikiria nini?” Akamwangalia. 

“Juu ya chakula.” Ikawa kama anayemkumbusha alichomuuliza. “Kuna chakula hapa nyumbani na mboga, naweza kuleta tukala kazini na kuanza kuzungukia hayo maeneo.” “Ndio tutazidi kuchelewa na kuonekana hatusimamii maneno yetu. Tumeomba saa sita tutoke, basi tutoke. Sio tuonekane tunazagaa pale, kwa kisingizio cha kula.” 

“Sawa. Ila nakuwa nanuka! Kule nje na stoo ni joto sana, natokwa jasho muda wote. Nitaomba nirudi angalau nioge kidogo kama sitakuchelewesha.” “Haina shida. Naweza nikakushusha hapa, wakati ukioga ndipo na mimi nikaoge, twende tukale kisha kuanza kazi.” “Basi nikuache ukapumzike. Kesho.” “Haya, usiku mwema.” Tuma akatulia kidogo kama anayetaka kusema kitu, ila akasita, Jerry akimwangalia. Mwishoe akaaga tena na kushuka, akaondoka. Akasubiria alipoingia na kufunga mlango, ndipo akaondoka. 

Amani iwapo mahali, Uharibifu haukai mbali

Inakuwa ni kama kivuli kinachokua gizani, kikingoja mwanga uzime. Na kunapotokea nafasi,usahaulifu wa mema wote wa nyuma hutokea. Mahusiano kati ya familia hizo mbili, Andy na Pius yakanoga kwa sababu wake zao walikuwa wakielewanaWaromani hao damu hawakuwa hata wakijali mlango wa kanisa wanaloingilia, ilimradi siku za jumapili wanakuwa pamoja na wake zao. 

Na wakitoka ibadani basi wote, mpaka mzee Ruhinda na mkewe pamoja na familia ya kina Paulina, ila wao wakitoka kanisani Roma, basi wanakwenda kwenye nyumba ya Raza, kula na kunywa, mara chache sana kwa Mina kwa sababu watoto wanakuwa wamelala kwa Raza.

Siku za ijumaa Raza alikuwa akitoka kazini kama hiyo weekend ni zamu yao kuwa na Ayvin basi anakwenda kumchukua Ayvin na Ayan, wanakuwa kwake hiyo ijumaa jioni, jumamosi kisha jumapili jioni wanaondoka na wazazi wao, tayari kwa Ayan shule siku ya jumatatu. Napo si kila ijumaa ambayo wanachukuliwa. Weekend zingine wanabaki na wazazi wao, na Andy haendi kazini kabisa, anabaki na familia yake tu akishinda na hao watoto akiwa nao kila mahali, akitoka ujue anatoka nao kwenda kucheza mahali kwenye michezo ya watoto. Lakini hizo weekend wakija kuchukuliwa inakuwa kama Mina amepokonywa roho, mpaka Raza akalalamika

Wakichukuliwa siku ya ijumaa, basi jua chai ya asubuhi Mina anakwenda kuinywea kwa Raza. Mumewe mara ingine siku ya jumamosi hufanya kazi nusu siku. Akitoka tu, jua na Mina naye yupo barabarani kufuata wanae. 

“Kwamba unakuwa huniamini au vipi?” “Raza naye kwa ulalamishi! Kwani hutaki wageni?” “Si waaina yako, tena tulioagana kukutana jumapili! Huniamini na wanao Mina!” “Nakuamini sema nakuwa na hamu nao, halafu najikuta nakuwa kama sina kitu chakufanya!” Akajitetea.

“Peleka tumbo lako hilo likafanyiwe masaji. Kaoshe miguu, tengeneza kucha na nywele. Sio kunijalia hapa, watoto wanakuwa hawana muda na sisi, wanakazi ya kukufauata wewe tu. Sio vizuri.” “Basi mimi najua nakusaidia!” “Unanisaidia vipi wakati inakuwa ni kama mnahama nyumba tu! Mkija hapa wanao wanakutaka wewe tu, sisi tunakuwa hatuna maana! Mnaendelea na maisha yenu humu ndani kwetu kama mpo kwenu, mkitutenga sisi. Sasa hapo zamu yetu ndio inakuje hapo?” “Basi bimkubwa.” Ndio akaacha kwenda nao. Raza anapita kuchukua watoto na dada yao, Mina anabaki peke yake na Andy.

~~~~~~~~~~~

Usiku wanafaidi bila watoto. Wanaweza kutoka au wakibaki hapo ujue ni mchezo mfululizo kulipiza vya juma nzima. Maana watoto wanapokuwepo, hawawezi hata kugusa kwa jinsi kunavyokuwa na hekaheka za Ayvin. Mtundu na yupo kila mahali. Wakilala watoto na wao wapo hoi. Kwa hiyo wakiondoka inakuwa kujinafasi kwa wazazi wao.

 Kesho yake ambayo ni siku ya jumamosi endapo Andy anakwenda kazini, basi Mina atalala hapo kama hakuna kwenda saluni mpaka Andy arudi, wanakumbushia vya ujananikabla ya watoto. Kakageuka kuwa kajiutaratibu kazuri hata kwao. Wakati mwingine wakawa wakisubiria kwa hamu hiyo ijumaa ambayo watoto watachukuliwa.

~~~~~~~~~~~

Pius alikuwa amesafiri kikazi kwa majuma mawili, alikuwa akirudi siku ya ijumaa. Raza akaona kumuongezea furaha, ni aende na watoto wote uwanja wa ndege kumpokea mumewe akijua akimuona Ayvin ndio furaha itazidi. Alishazungumza na Mina kwamba siku hiyo atapita mapema. “Yaani nitakuwa kama ninayemsubiria Ayan tu. Akitoka shule, tunaondoka. Narudi nao nyumbani, kumchukua Polla, tunaenda kumpokea baba yao. Poliny yeye atakuja nyumbani usiku.” Mina akaridhia.

~~~~~~~~~~~

Ndoa ya miaka mingi basi Raza hutafuta kila sababu yakuchangamsha penzi. Kwa hilo, Pius alimpenda zaidi mkewe. Aliwapokea watoto wa Mina, bila shida na hakuwahi kuwalalamikia hata mara moja endapo wako kwake. Amani na utulivu wakati wote. Watoto wawepo kwao au wawepo nyumbani kwa Raza, ni furaha. Watoto walikuwa wakivaa hao, kama wanamitindo! Nguo pande zote, tena nzuri za thamani. Usingekuta watoto wa Mina wachafu. Nadhifu wakati wote kama baba zao.

~~~~~~~~~~~

Pius hakuamini alipofika kupokelewa na familia yake. Kwanza ni mara chache sana, zaidi anapokuwa kwenye safari za kikazi. Dereva ndiye anayekwenda kumpokea, asijue Raza alishampigia dereva na kumwambia asiende, yeye ndio atakuwa dereva.

Cheko lilimjaa alipomuona na Ayvin. Alifurahi Pius, nakushindwa kujizua! Asikae mbele na mkewe, akaenda kukaa nyuma na watoto. Anaongea nao na kucheka kwa kila jambo! Raza akajua amefurahi sana.

Walifika nyumbani na yeye akawa kama Andy, kuwatumikia hao watoto. Akataka kumlisha Ayvin na wakati wa kulala kuwaogesha, kisha kuwasomea kitabu. Ayvin alishaanza kutulia begani kwa Pius kama anavyotulia kwa Andy na kuongeza furaha ya ajabu kwa Pius.

Wakati mwingine Raza humkuta ametulia kochini hapo chumbani, amemuweka mwanae kifuani, anampapasa mgongoni akiwa alishalala. Ukimkuta hapo Pius anakuwa ametulia kimya kochini, mwanae kifuani, hata simu hagusi. Raza akishamkuta hivyo hutoka kimyakimya na kuwaacha. 

Usiku huo Raza alishukuriwa mpaka akajua amefurahia surprise ya huyo Ayvin. Alibaki kurudia vituko vya huyo mtoto hata ambavyo Raza mwenyewe alivishuhudia. Na alikuwa akisimulia kwa hisia huyo, utafikiri anasimulia habari za kipenzi chake Poliny.

Jumamosi

Waliamka, fujo zikaanza. Nikawaida hao watoto wakiwepo hapo, basi kunachangamka maana na Polla naye anakuwa kama wao. Michezo inamzidi kuliko hata Ayan! Kwenye majira ya saa nne, Pius akatoka akimuaga mkewe hatakawia kurudi.

Alitoka kwa kujiiba akiwaacha wote wapo sebuleni wanacheza, kelele, hata wasijue kama anatoka. Alipotoka tu, na Raza naye hakukaa sana hapo chini akapandisha juu chumbani kwake. Kumbe Ayvin alimuona wakati anaondoka, akapandisha ngazi kwa kutambaa mpaka juu kabisa anamtafuta Raza.

Akaingia chumbani kwa Polla. Ikawa kama amemkosa huko Raza, maana alishamzoea na Raza. Alimpenda kwa ukweli huyo mtoto, na mwenyewe akajua kama anampenda. Kwahiyo humfuata kila mahali humo ndani michezo yake yeye ikipungua au Polla na Ayan wakimsahau, dada yao akipotelea na yeye kwenye simu, basi atamtafuta Raza anayeonekena kumpa muda wake kama Pius.

Raza akafika karibu kushuka ngazi, akaona kitu kwenye simu akaona akiperuzi kabla hajarudi kwa watoto chini. Bluetooth kaweka sikioni, watoto wasisikie anachosikiliza. Akabaki amesimama hapo akisikiliza asijue Ayvin amemuona anamfuata kwa kasi kutokea chumba cha Poliny, baada ya kumkosa kwenye chumba cha Polla.

Kufika pale akamshika na kumshitua sana Raza ambaye hakujua kama kuna mtu yeyote huko juu maana wote aliwaacha chini. Ile kushituka akapiga yowe/kelele kwa sauti ya juu akijua kitu cha ajabu kinamshika, bahati yake Ayvin ilivyokuwa mbaya, kule kushituka kwa Raza kulihusisha mpaka mikono yake.

Akajikuta anamsukuma mpaka akagonga rembo la chuma lililopanda kutoka chini mpaka juu pembezoni mwa hizo ngazi. Ile anataka kumdaka akashindwa kumuwahi, wachini nao wakawa wamesogea kufuata ile kelele ya mwanzo kabisa ya kushituka kwa Raza. Lakini wale wa chini walichokishuhudia wakati akitaka kumdaka asianguke kikaonekana ni kama amemsukuma. Kwa hiyo Ayvin kutoka kwenye kujigonga, akabiringita, kutoka ngazi ya juu mpaka kutua chini, KIMYA.

~~~~~~~~~~~

Kilikuwa kitendo cha muda mfupi sana ila waliosogea kujua kulikoni baada ya ile kelele ya kwanza, walifika pale na kushuhudia, kile kilichoonekana ni kama Raza anamsukuma na kumfanya aanguke vibaya vile.

~~~~~~~~~~~

Walishituka wale watoto na dada wa kazi! Swali la kwanza lililotoka kwa binti yake mkubwa. “Mama! Kwa nini umemsukuma Ayvin vibaya hivyo?!” sasa kwa kupaniki, akaanza kumkimbilia mpaka pale chini alipokuwa amelala bila ya kujibu hiyo tuhuma iliyomfanya hata Ayan kumuogopa Raza na kurudi nyuma kwa haraka kama ambaye anamkimbia asije mdhuru na yeye.

“Mungu wangu nisaidie!” Alisikika Raza, Ayvin sakafuni ametulia kimya. Hapohapo akampigia simu Pius. “Pius utaniua bure, sijamuua huyu mtoto kwa kukusudia jamani mimi! Mungu wangu nitetee!” Hapo Raza analia kwa mayoe kupita kiasi. Poliny akamtingisha mdogo wake tena na tena, bila Ayvin kutingishika wala kufungua macho.

~~~~~~~~~~~

Inaendelea…

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment