Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Love At First Sight - Sehemu ya 87. - Naomi Simulizi

Love At First Sight - Sehemu ya 87.

Tuma akabaki ameshikilia tumbo lake, masikio kwa Umi na Jerry! “Naomba niwe muwazi kwako ili kutupunguzia usumbufu.” Akaanza Jerry. “Hutalala na mimi, Umi.” Alishituka Tuma, hakutegemea. 

Sifikirii na sitaki. Sio sasa, wala baadaye.” “Kama Tuma amekwambia maneno, jua ni uongo. Mimi sina nia mbaya na wewe.” “Ulimtuma nini Tuma kwangu?” “Sijamtuma kitu, ndio ujue amekudanganya.” “Amenidanganya nini?” “Kwamba mimi nakutaka kwa maslahi yangu!” Akaanza kujisemea yeye mwenyewe. Akaongea mengi, asijue Jerry alikuwa anataka kujua kilichomsibu Tuma. Umi akaongea mengi akijishitakia na kumlaumu Tuma.

“Najua ananilipiza kisasi kwa sababu ya Mbaki. Lakini hata yeye mwenyewe alishasema hata kama isingekuwa mimi, angekuwa mwanamke mwingine. Kwanza mimi hata sikujua kama huyo Mbaki ni mwanaume wake wa kukaribia ndoa mpaka tulipofika kule. Mimi wala nisingemchukua. Kwa hiyo kama ananinilipiza kisasi, ajue kosa lilikuwa la mwanaume wake wala si mimi.”

“Sasa hayo yote kama ulimshirikisha Tuma, alishindwa kabisa kuniambia. Nashukuru kuniambia alichoshindwa kuniambia Tuma. Lakini wewe hutanionja. Na kabla hujaanza kusema ni Tuma ameniambia, nilikusikia mimi mwenyewe ukizungumza. Kwanza ni kama ulisema umeshajua kama mimi sina kitu, hutaki shida. Sasa jana nikawa najiuliza, ni kwa nini umebadili tena mawazo, unanitaka mimi nisiye na kitu!? Ndio leo umenijibu wewe mwenyewe.”

Sina uwezo wa kukutunzia ajira yako kwa sababu mimi ni mpitaji hapa. Hivi karibuni nitaondoka. Bosi zako hawajaniajiri mimi kama wewe. Hivyo basi, kinachoendelea hapa na huko ulikohamishiwa, havinihusu kabisa. Nikiwa na maanisha hivi, siwezi kuingilia nani anaajiriwa, nani anafukuzwa kazi. Hatima hiyo unayo wewe.” Jerry akaendelea taratibu.

“Wewe ni binti mdogo, na hii nayo ni nafasi nyingine Mungu amekupa ukiwa hustahili Umi. Wewe ulikataa shule, wakati wapo waliohangaika darasani, wanavyo vyeti lakini hawana kazi kama hii ambayo unaichezea. Huna nidhamu ya kazi. Unaingia na kutoka utakavyo. Huna shukurani hata mbele za Mungu aliyekupa kitu ambacho hustahili kabisa. Huwezi kulipa fadhila kwa waajiri wako kuwaonyesha kwa vitendo, unatambua wanachokufanyia. Unacheza na kazi ambayo wapo watu wanaomba na kukesha, hawapati.”

Unatumia watu vibaya kama matoi! Ulianza na mimi ukitaka kunionja, sasahivi unaniambia unanitaka ili kukusaidia kutunza ajira ambayo unayo, hujapoteza, ila hutakikuweka nidhamu. Upo tayari kutoa mwili wako ilimradi tu kuendelea na tabia ambayo ipo siku hata baba J, kama unavyomuita atachoka. Na ninakuhakikishia Umi, mimi ningekuwa nikifanya kazi hapa kama ulivyodhania, WEWE, ungekuwa kosa la kwanza kulirekebisha.” Tuma akashangaa sana.

“Nisingekupa nafasi unazopewa na kuzichezea kwa kiasi hicho. Kwanza kwa nini iwe wewe! Kwa hakika ningekufukuza haraka sana. Unanisikia Umi?” “Nimebadilika, siku hizi nawahi kazini.” “Na iwe kweli, acha sababu za kitoto ukisumbua watu na majukumu yao. Chagua moja. Unataka ajira ya kuajiriwa au ujiajiri mwenyewe uwe unaingia kazini utakavyo. Na kama ukiamua kuajiriwa, heshimu kazi za watu.”

“Cha mwisho, acha mtindo wa kutumia watu kwa maslahi yako. Ni tabia mbaya sana na hautaishia pazuri. Umenielewa?” “Ndiyo. Na samahani sio kwamba nilikuwa nataka kukutumia vibaya. Nia..” “Sina huo muda. Sitapoteza muda wangu kukusikiliza ukinidanganya maana umesema mwenyewe ukidhani Tuma alikusemea. Ni maneno yako wewe mwenyewe. Hutakaa ukaniona bila nguo. Na sitalala na wewe, Umi. Nishaweka kikomo cha kutumiwa vibaya na wanawake. Na nakuonya, isiwahi kurudia tena. Haya, jioni njema.” Kwa hakika Tuma hakutegemea.

Ulikuwa mshituko kwa Umi, haijawahi mtokea hata mara moja tokea anazaliwa! Yaani mwanaume kuzungumza naye vile au kumkataa! Maana Umi ni bantu shepuTAMANIO la wanaume wengi weusi. Kiuno na tumbo utafikiri hali! Laini wakuteleza kwa kumwangalia tu, kama ushike! Mzuri kuanzia utosi mpaka unyayo. Sauti nzuri, laini. Alimtizama Jerry kisha akaondoka maana ni kama alimfukuza.

~~~~~~~~~~~

Pakatulia kwa muda, kisha akarudi jikoni. Hakumsemesha Tuma, kama aliyekuwa akijaribu kutulia. Akarudisha chakula alichobakisha kwenye microwave na kwenda chooni. Tuma akavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha, akasikia kutoa gesi. Akatoa kwa mdomo na kushangaa tumbo linatulia kabisa. Akamalizia chai yake. Na njaa ikaanza kumuuma.

Akatoa chakula kwenye friji, wakati anajipakulia Jerry akatoka. “Nimekutolea chakula, kitakuwa kimepata moto.” “Asante.” Akachukua na kurudi kukaa kimya macho kwenye simu.

Akajipashia na yeye chakula chake, akarudi kukaa na kuanza kula taratibu, kimyakimya na yeye akiwa ameingiwa hofu na huyo Jerry. Kimya. Akapotelea mawazoni. Jerry akamwangalia, akakuta amepotea kabisa hapo, ameshikilia hot bottle tumboni. Akabaki akimwangalia akiwa amejiegemeza kichwa ukutani, sahani yake karibu.

“Hicho chakula kitapoa, Tuma.” Akamwangalia. “Vipi tumbo?” “Naona kweli ilikuwa gesi. Limetulia. Asante kwa dawa na hii chupa.” “Karibu. Ila nashauri tupunguze maharage.” Tuma akajikuta akicheka kwa jinsi akivyosema. 

“Umechoka maharage?” “Hata tumbo lako limesalimu amri!” Akazidi kucheka. “Angalau tubadili mara moja moja Tuma! Kila siku!” “Sasa unataka nini?” “Chochote ila sio maharage. Angalau kwa muda tu. Kwa mfano kesho kuna wali, na naona nyama zitabaki. Kuwe na mchuzi hata wa njegere.” Tuma akatoa macho.

“Hupendi njegere?” “Hata sijui huwa wanaziuza wapi!” Jerry akaanza kucheka. “Zilivyo hadimu?” “Na ni msamiati kwangu! Kwanza huwa wanapikaje!” “Acha hizo Tuma!” “Mboga za matajiri hizo!” “Hapana bwana! Basi tutoke, tupitie mahali, mimi najua wanapoziuza. Halafu tutamuuliza yule mama jinsi wanavyopika. Nina uhakika sio ngumu.” “Najua bwana jinsi ya kupika, ila nilikuwa nakuvunja moyo.” “Sio garama hivyo. Twende tukitoka hapa.” “Itakuwa usiku sana!” “Tutoke saa 12 kamili sio na nusu.” Akafurahia huyo Tuma, wakakubaliana.

“Basi acha nikaweke sawa kule stoo, halafu nitarudi.” “Sio sasa upotelee huko.” Akacheka na kutoka hapo bila ya kujibu, Jerry akimwangalia. Ila alishamgundua, anatishwa sana na Umi. Na akajua aliogopa Umi atawaingilia. Akamcheka moyoni akijua na yeye anamfurahia. Akarudi ofisini.

 ~~~~~~~~~~~

Saa 12:30 wakawa wameshakaa garini wanaondoka. “Saa ngapi unatakiwa uwe umeshafika nyumbani?” “Acha bwana kuniuliza kama mtoto mdogo anayeishi kwa wazazi.” Jerry alicheka sana. “Mimi ‘sitakiwi’ bwana!” “Nimekukuta na utaratibu wako usiobadilika. Sitaki niharibu siku ya kwanza, halafu kesho nikikuomba tutoke ukanikatalia.” Akamwangalia na kukunja uso kidogo kama ambaye hajamuelewa vizuri, lakini akanyamaza bila ya kumjibu.

“Sasa huko tunakokwenda ni karibu na kunakouzwa nyama. Nimepazoea kwa sababu ni bucha inayouza nyama aina nyingi. Nilikuwa nikienda kununua, basi nafanya manunuzi ya muda mrefu. Swali, unafriji kubwa yenye nafasi nyumbani?” “Kiasi. Lakini usijimalize. Hamna sababu ya kufanya yote kwa wakati mmoja. Nimeshajua nini unapenda, nitaongezea wakati mwingine.” 

“Usiwe na wasiwasi. Ilimradi kuwe na nafasi. Maisha ya kununua vitu kila siku, ni kama utaratibu mzuri ila unachukua muda. Napenda nikinunua kitu, nanunua halafu sirudi tena huko mara kwa mara. Labda kama uniambie unapenda nyama fresh kila siku.” “Hapana. Nafikiri ni swala la bajeti tu. Sitaki ujimalize!” “Wewe unamuamini sana Umi, eeh?” Akashituka na kuuliza.

“Kwa nini?” “Kwa sababu alikwambia nimefukuzwa kwa Sandra mikono mitupu, kwa hiyo umeamini kabisa kwamba sina pesa?” “Ndivyo alivyoniambia! Kwani sio kweli?” “Ni kweli.” “Basi usiwe na wasiwasi! Kwa mfano leo mimi nina pesa. Sio kwamba nimeishiwa kabisa, ila huwa naishi kwa bajeti. Ila kwa sababu umeongezeka na wewe, tununue mboga kwa kiasi, nitakupikia nyama, upumzike maharage, mwisho wa mwezi tutafanya hayo manunuzi makubwa.”

~~~~~~~~~~~

“Nakushukuru Tuma, na nimefurahi kukusikia ukisema hivyo. Nimeujua moyo wako. Japo ni kama naendelea kuthibitisha tu. Ila nimependa moyo wako, na jua umenisaidiasana. SANA, zaidi nitakavyokwambia. Ila jua sasahivi nina pesa.” Tuma akamwangalia kama ambaye hamuelewi. Ni alhamisi, amefukuzwa ijumaa, hata juma halijaisha, anapata wapi pesa! Akajiuliza na Jerry akamuelewa.

“Kweli nimeondoka kwa Sandra au kufukuzwa kama ilivyo, hajanipa kitu na sitaki kitu kutoka kwake. Nimekubali hivyo na hata kwenye talaka yetu nitaweka kwa maandishi. Sandra ni mnyanyasaji sana lakini pia ni mama wa watoto wangu wawili. Chochote kilicho haki yangu ambacho najua kama ningedai mahakamani, tungegawana nusu kwa nusu, kama ulivyomwambia Umi, ningepewa. Maana alikuwa mke wangu na nimefanya naye kazi bega kwa bega kufikia nilipomuacha.” Tuma akajua huwa anasikia kila kitu. Akajisikia vibaya.

“Wazazi walituachia mali nyingi lakini tulifilisiwa kila kitu. Lakini baada ya kujiweka sawa, bro alifanikiwa kurudisha nyumba iliyokuwa imebeba kumbukumbu yetu. Sisi wote tulizaliwa pale, hakutaka tupoteze kila kitu. Akaona angalau aokoe nyumba. Alikuja kuinunua kwa mtu.” 

“Najua mpo watatu. Si ndivyo?” “Sawa sawa. Kaka yetu mkubwa, mimi halafu Jeremi ndio wa mwisho. Hawa wawili wao walijiajiri lakini mimi niliamua kufanya kazi na Sandra, nikijua naendeleza chetu. Mwanzoni kabisa hata bro alitaka nikafanye naye kazi kwenye kampuni yake ya ujenzi, lakini niliona niendelee na Sandra tu. Kwa hiyo nilikuwa nikifanya naye si kwa sababu nilikwama, ila nilijua tunajenga kwetu.”

“Wazazi walipofariki kweli tulipitia pagumu sana mpaka bro alipoanza kutoka kimaisha ndipo akainunua ile nyumba ya wazazi, lakini mpaka anakuja kufanikiwa kuirudisha kwetu ikawa haina tena matumizi, tukaamua kuikodisha, pesa yake ikawa inawekwa kwenye akaunti ya ndugu.” “Nyinyi watatu?” “Ndiyo. Kaka aliamua tuifungue hiyo akisema ni mbali ya hata familia zetu. Tunaiita Safe Heaven.”

“Alisema ni kwa ajili ya sisi watatu kutokurudi kule tulipoachwa na wazazi. Kwamba ikitokea mmoja wetu anao uhitaji, basi tusije anza chini, kuwepo na hiyo pesa. Kwa hiyo kodi zote, na kila mara kwa kila anayeweza anatumbukiza pesa humo. Ni yetu sisi watatu tu, kama nilivyokwambia, hata wake zetu hawahusiki huko.”

“Hayo aliyokwambia Umi, aliyasikia mke wa bro pia, akaenda kumwambia bro.Aliumia SANA. Yeye na Jeremi sikutaka kuwaambia kwa umbali huo. Ila tu kuwaambia nilitoka kwa Sandra. Kufupisha habari ndefu, ndio bro, akasema kwa sababu bado wao wananguvu, akaunti isiguswe, bado hiyo sio dharula. Akaniambia nifikirie kitu chakufanya, pesa ipo. Sasa ukumbuke mimi akili ilikuwa kwenye akaunti yetu.”

“Na Tuma, nakwambia haya kwa sababu nakuamini sana. Sitegemei kusikia haya kwingine.” “Sithubutu Jerry. Kwanza nitamwambia nani? Siwezi kukuanika. Nimepita hapo ulipo, mama J ndio akafanyika kimbilio langu. Kwa hiyo nakuelewa.” “Nashukuru. Sasa nikiwa sijajua pakuanzia ila tumaini nikijua pesa ipo, pengine weekend hii tutakaa tuzungumze ni kiasi gani wataidhinisha nichukue, ndio juzi, jumanne bro akanitaarifu kuwa kuna hundi imewekwa kwenye akaunti yangu, niipe muda ita clear. Nikajua pesa ya mboga.” Akamuona anacheka.

“Nyingi?” “Aisee nimeangalia jana mpaka nikashindwa kupepesa macho. Sijaamini! Kuja kumpigia simu baada ya kuangalia akaunti yetu sisi watatu, pesa ipo vilevile. Ndio nikamuuliza kulikoni, ndio akanijibu nilipo sasahivi bado sio dharula yakutumia ile akaunti. Bado yeye anayo nguvu. Anataka niendelee na maisha, sio nianzeSikuamini!” 

“Afadhali Jerry. Pole na hongera. Hustahili kuanza.” “Kwakweli sistahili Tuma. Namshukuru Mungu amenilipa kupitia bro. Nilijitoa sana nikiwa na Sandra nikijua tunajenga kwetu. Na imekuwa kama Mungu alikuwa na sisi, japo mwanzo haukuwa wakihalali. Ila tokea tuanze mpaka sasa, kwa hakika tumetengeneza pesa.”

“Nimefurahi nitamuacha pazuri, watoto wangu hawatapata shida, na yeye ataniacha kwa furaha akijua amenikomoa kama wanavyonitangaza. Kwa hiyo Tuma, hatuanzi chini. Maharage iwe kwa hamu.” Tuma alicheka sana.

“Sio mboga ya kila siku?” “Japokuwa nayapenda, lakini isiwe kila siku tafadhali. Tubadili. Na nakwambia tubadili, nikimaanisha na wewe. Ulinipokea ukijua sina kitu. Ukanilisha siku ile ya jumatatu maana nilikuwa kweli sina pesa. Niliondoka kwa Sandra nikimaanisha ofisini kwake, nikiwa na wallet isiyo na pesa kabisa, na line ya simu, basi.” “Na nguo zake ulizokuwa umevaa?” Tuma akauliza kwa kumuhurumia.

“Ambazo nilijua ni zangu. Lakini ndio akanikumbusha, kuwa hata chupi niliyokuwa nimevaa ni yeye alinunua.” “Ambayo ni kweli?” “Kwa asilimia kubwa alikuwa sahihi. Kama utakuwa umemuangalia Sandra na mimi, au familia yetu, tunapenda sana kuvaa, tena kwa thamani ya juu sana, kitu nilichomfundisha mimi tokea tunaanzana. Na sisi kwetu mpaka bro, tulikuzwa hivyo. Kuthamini mwili wako hata kwa kitu unachokivaa. Ikatuingia akilini, tukawa hatujui jinsi ingine ya kuvaa ila ubora wa mavazi.”

“Hata baada ya wazazi kuondoka, maisha yalikuja kuwa magumu sana, hatukuwa na pesa, lakini ilikuwa bora bro atununulie nguo moja moja yenye ubora mzuri, kuliko kwenda kuokota nguo nyingi sizizo na ubora. Sasa nilipoanzana na Sandra, akanielewa kwa haraka sana na kuiga. Ikawa akishagundua sehemu ina quality ya juu ya nguo fulani, basi huko ndiko atafanya manunuzi ya hizo nguo. Tena za familia nzima. Kama ni soksi na chupi, atadumu kwenye hilo duka. Na akajiwekea utaratibu wa muda ambao anabadili nguo za ndani na soksi kwa familia nzima. Kwa hiyo unakuta umebadilishiwa soksi zote, chupi na katamikono ya ndani. Akanilemaza, maana hata mavazi mengine mara nyingi akawa kama hataagiza nje ya nchi, basi sisi wenyewe tukiwa nje ya nchi kwa mapumziko, maana bro ananyumba kubwa tu huko anaishi binti yake anaye soma.”

“Sasa mara kwa mara tunapokwenda na ndio wakati wa yeye kununua nguo, na yeye anapenda sana shopping. Ni kitu anakipenda kukifanya kwa furaha na hatalalamika. Anajua kila msimu na nguo wanazokuwa wanazitoa sokoni, basi ananunua kwa bei ya chini, ila nguo zenye ubora mkubwa. Hata Hilda anafanya hivyohivyo. Msimu wa joto kule ukiisha, wakiwa wanaingia wa baridi, nguo za joto zinakuwa zikitolewa madukani ili kupisha za baridi. Kwa hiyo unakuta bei chini, na ndio nguo zinatufaa sisi huku nchini.”

“Kwa hiyo kwenye maswala ya mavazi ikawa ni yeye, kwa silimia zote. Hata chakula pia. Japokuwa sio kwamba yeye ndiye aliyekuwa akipika, lakini alihakikisha wakati wote, kuna chakula mezani. Japo nyama mara nyingi huko tunapokwenda leo ndiko nilikokuwa nikitoa nyama ya familia. Au hata tunapokuwepo kazini, basi mtu wa usafi alikuwa akijua muda wa kwenda kutununulia chakula na Sandra ndiye aliyekuwa akijua tunakula nini, mimi naletewa mpaka mezani.”

“Kwa hiyo kwa upande wa chakula na mavazi, hakika ninaanza. Isingekuwa wewe kunipa chakula, ningepata sana shida. Nilitoka kwa wazazi tulikuwa tukipikiwa. Nimesoma shule za bweni, tulikuwa tukipikiwa. Tukaoana mapema, tukawa na mpishi japo najua wapi pakupatia mchele mzuri na nyama. Kazi zangu zilikuwa ofisini tu, nyumbani sifanyi chochote. Na alipenda utendaji wangu kazi sababu ya kichwa cha hesabu, na bajeti za ofisi. Nini kifanyike kwa haraka ili kukwepa hasara. Au mwezi huo tuongeze nini kutengeneza faida zaidi, ilikuwa mimi. Lakini nani afanye nini, ilikuwa ni yeye na kusimamia zaidi wafanyakazi. Alijua nani ampange wapi ili kazi ziende.”

“Umeelewa?” “Sasa hivi nimeelewa.” “Hofu ya pesa imeisha?” “Bado, mpaka uanze hiyo biashara. Sasa kama mtaji wote utaishia kwenye nyama!” Jerry akazidi kucheka. “Tutakuwa tunakula nyama tu!” “Hela ya mtaji pembeni, haiguswi. Kwa hiyo usiwe na wasiwasi. Tule tu nyama, na maharage yetu tusiache. Ila mara moja moja kwa hamu.” Tuma akacheka sana.

 “Jerry muoga wa maharage!” “Sio kila siku bwana! Mwenzio nimesoma shule ya bweni, Tuma. Nimekula sana maharage, naona inatosha kwa dozi ya kila siku.” “Haya twende tukanunue nyama.” “Tumeshafika.” Ilikuwa ni bucha iliyopo Mwenge.

Sehemu wanayofanyia kazi kwenye biashara ya Jeremi na mkewe ilikuwa Mikocheni B. Hapo ndipo alikuwa na yadi kubwa ya magari na upande mwingine ndio biashara ya matairi. 

“Sasa tuwahi kwenye njegere kabla hawajafunga. Buchani huwa anachelewa mpaka saa nne ndio anafunga.” Wakaingia sokoni. “Unachohitaji chukua.” “Kitunguu swaumu, tangawizi na…” “Tutachukua hapohapo. Huyo mama anavitu vingi. Twende ukaangalie.” Wakaenda. Kweli alikuwa na asilimia kubwa ya vitu alivyohitaji. Wakanunua mpaka akaridhika ndipo wakaenda kuchukua nyama. Napo akanunua samaki, kuku, nyama ya ngombe, maini na nyama ya kusaga. 

“Leo kama sikukuu!” Jerry alicheka sana. “Acha kucheka bwana! Manunuzi haya ni mpaka Yesu akiwa anazaliwa.” “Mwezi wa 12?” “Basi. Sikukuu za Idd kushiba harufu kwa mama mwenye nyumba wangu.” Jerry alikuwa akicheka huyo! Kama sio yeye aliyefukuzwa na mke. 

“Kisa, dada anajenga?” “Kabisa. Mahesabu makali sana. Na hivi Eli si mlalamishi, anakulaga chochote. Hata ukichemsha tu maharage ukayaweka chumvi, hatauliza. Ila usidhani hajui kitu kizuri!” “Anajua?” 

“Sana na anapenda. Huwa mara mojamoja namnunulia chips kuku! Utachoka stori zake. Hapo jua kafurahi. Anakula huku anakusimulia mambo mpaka ya walimu wake!” “Hapo kafurahia chakula?” “Umemaliza. Hutalala. Sasa kwa kuwa namjua, namnunulia siku za jumamosi, ili hata akinifanyisha mkesha, kesho yake kanisani ni mpaka saa nne, tunachelewa kuamka.” Wakacheka.

“Nikuombe kitu kabla ya kurudi nyumbani? Au utachelewa sana?” “Unataka kwenda wapi tena wakati mwenzio nimepata moyo wa kwenda kupika! Leo nina nyama.” “Usiku huu! Acha bwana utapika kesho ukitoka kazini.” “Sasa kesho mchana utakula nini na wewe maharage hutaki?” “Acha kuishi kesho wakati leo hatujamaliza.” “Unataka kwenda wapi tena?” “Kupata juisi pale Mlimani city.” Tuma akacheka na kutingisha kichwa kwa masikitiko.

“Tukanywe kwanza ndio utaniambia kama nilikuwa sahihi au la. Aisee ni nzuri mno! Twende, hatutakaa sana.” Wakakubaliana kwenda.

~~~~~~~~~~~~~~

Ukweli walipata wakati mzuri, mtulivu. Wakicheka mambo hata madogo madogo yasiyo maana. Wakawa na wakati mzuri. Ila akamwambia waagize na chakula. Tuma akala nusu, nusu akambakishia mdogo wake. Jerry akashangaa na kuliweka moyoni jinsi anavyomjali mdogo wake.

“Acha na yeye akakionje hiki chakula.” “Si ndio hatalala sasa?” “Ili animenyee kitunguu swaumu, na tangawizi. Avitwange wakati akiongea, ananisaidia kazi, hajui.” Alicheka Jerry, alicheka sana. “Tuma!” “Hujamjua Eli na kitabu. Na akiwa na jambo lake anataka kulisoma, hata umchokoze vipi, hadanganyiki. Majibu yake mafupi mafupi! Sasa wakati mwingine nakuwa nataka tuongee, hana muda na mimi.” “Ndio unamrubuni kwa chakula?” “Wakati mwingine naona nimuache tu. Maana na tv yenyewe huwezi washa, anasoma. Najibakia kwenye simu na mama yake au naangalia ujinga mtandaoni.”

“Ni sawa nikikurudisha nyumbani? Naweza nisiingie ndani.” “Kwa nini?!” “Huwezi jua!” “Kwetu kwa jumuiya. Padogo, lakini kila mtu anakaribishwa. Wakija na wakijijini, mpaka kwenye mkeka tunalala. Kwetu hapajai. Wakati wote kuna nafasi ya mtu. Kwa hiyo karibu.” “Asante.” Wakaondoka hapo.

~~~~~~~~~~~~~~

“Tunaelekea wapi?” “Magomeni. Nyuma ya kituo, unaingia ndani kidogo, ila gari inafika na barabara sio mbaya. Twende nitakuelekeza.” “Unajua na mimi naishi Kinondoni makaburini?” “Ulipanga hapo?” “Nimeachiwa.” Akamuelezea juu ya Mill.

“Kumbe nivizuri kuwa na marafiki?” “Ila wamenivumilia sana aisee! Sandra hakuwa akitaka kabisa niwe karibu na yeyote. Hata wao ambao ni marafiki wa tokea shule ya sekondari, ilikuwa karaha tupu! Ilikuwa anaridhia mara chache sana, tena wakati mwingine alitaka na yeye mwenyewe awepo.” “Kwa nini!?” “Aaaah! Tuyaache hayo.”

“Ila nilitaka kukwambia ni pakubwa, japo kuna joto. Unataka kulinganisha kodi yake ili nikihama nikuachie hapo angalau Eli na yeye apate chumba chake? Pako patulivu, ndani ya uzio wa mwenye nyumba. Pako salama. Sio mbali na barabarani. Ni joto tu.” “Hata hapo tunapoishi ni joto sana. Niulizie nije kulinganisha bei.”

“Basi nitakuulizia ili ujue. Kuna dalili naweza kuhama hapo mapema. Naona broamesisitiza nihame pale, nirudi kuishi kwenye nyumba ya wazazi. Kesho amesema anakwenda kuzungumza na yule jamaa tuliyemkodisha pale. Anamlipa na kumuomba aondoke, ili nirudi pale.” “Nyinyi mnaonekana mnajaliana sana!” “Kama wewe unavyomjali Eli.” Wakacheka huku wakielekea kwa Tuma.

~~~~~~~~~~~

Walifika hapo wazi Jerry alionekana kutoridhika nako ila Tuma akamuelewa. Jerry mtoto wa uzunguni. “Sio pabaya hivyo bwana Jerry!” “lla pia sio pazuri. Padogo. Pako uswahilini. Pako…” “Jerry wewe jamani! Yaani unakaribishwa kwa watu unaanza kupakosoa!” Alicheka sana, lakini akaendelea. 

“Sasa hapa si mtu anaweza hata ingiza mkono hapo ndani na kuvuta kitu?” “Ujue hutakaribishwa ndani wewe!” “Basi nanyamaza.” Wakaingia na kumkuta Eli anasoma.

Akasimama kusalimia na kupokea mizigo. “Ulivyokuwa ukisema Eli, nikajua mtoto! Kumbe mpaka urefu amekupita!” Wakaanza kucheka. “Kachukua ufupi wa mama.”  Eli akaongeza nakufanya Jerry kucheka sana akimwangalia Tuma. “Ujue kwenye koo nyingine mimi ni ngongoti wao!” “Hapo sibishi.”  Jerry akaafiki ila Eli akaongeza. “Lakini ni koo chache sana.” Akafanya Jerry azidi kucheka, dada yake hakujibu akaendelea kupanga vitu. 

Akawa kama amekumbuka, akaona atoe utambulisho. “Huyu anaitwa Jerry.” “Anafanana na baba J!” “Kumbe anawajua!?” “Asiwajue wakati anakujaga kudai pesa pale kama alinikopeshaga, sijamlipa!” “Tatizo Tuma anakua anakuahidi jambo, halafu hapokei tena simu.” Jerry alicheka mpaka akakaa. 

“Kwa hiyo unamfuata?” “Nitafanyaje na mimi nakuwa kwenye shida!” “Hana lolote. Kwani vitabu vinakimbia?” “Na hela ya tuition je?” “Wewe unapendaga kunisumbua tu, huna lolote. Haya, huyu ni kaka yake baba J.” “Ndio maana! Mmefanana sana. Karibu kwetu.” “Nashukuru Eli. Nimekaribia japo kweli nipadogo sana, mpaka ndani!” “Nyie Jerry wewe ujue ni mgeni wa ajabu sana!” Wakazidi kucheka. 

Akampa mdogo wake chakula alichombakishia. Bwana alifurahi huyo! “Sasa uwe unatafuna huku unanimenyea vitunguu swaumu na tangawizi. Na utwange.” “Hilo tu, usijali.” Jerry akawa anawaangalia huku akicheka. Hakukaa sana akaaga. Tuma akamsindikiza.

~~~~~~~~~~~

“Nikwambie ukweli Tuma?” “Juu ya kwangu kwamba ni padogo sana na…” “Hilo umenikataza, naacha japo kweli hapafai.” “Jerry wewe!” “Basi nanyamaza.” Wakacheka kidogo, akaegemea kwenye gari.

“Nakushukuru umenipa kicheko nilichopoteza kwa muda mrefu sana.” Tuma akatulia. “Tumekuwa wote kwa muda mfupi sana, lakini nimekuwa na wakati mzuri. Sijacheka hivi kwa miaka mingi sana. Asante.” Tuma akacheka taratibu tu, Jerry akaendelea.

“Na asante kunisitiri hata ulipodhania sijui.” Akakunja uso kama anayemuuliza lini! “Umi alikufikishia habari zangu mbaya, ungeweza kuwa kama wao. Ukanisema vibaya na kuanza kunidharau. Lakini badala yake ukaendelea kunikarimu, ukijua sina kitu, huku ukiniuza kwa Umi. Nikaonjwe.” Tuma alicheka. Alicheka mpaka akainama mbele yake akiona aibu na hakujibu akijua ametupa lawama japo kwa kejeli. 

“Asante. Kwa hakika nakushukuru Tuma.” “Karibu. Na mimi napata wakati mzuri.” Akamwangalia nakumfanya aone tena aibu.

“Asubuhi ungependa nikupitie?” “Hapana. Hizo starehe za muda mfupi mimi hapana. Acha tu, nitakuwa sawa.” “Kwa nini unasema ni za muda mfupi?!” Tuma akashindwa aielezee vipi, akanyamaza na kuhama hapo alipokuwa amesimama mbele yake na kuegemea gari kama yeye, pembeni yake.

 “Kwanza utakuwa na mchuzi. Utapanda nao kwenye daladala?” “Nitakuwa sawa Jerry. Usije kunichukua.” “Kwa nini unanikatalia?! Mimi naishi hapo Kinondoni makaburini! Muda ninaotoka kunakuwa hakuna foleni. Kwa nini nisiwe nakuja hapa kukuchukua?!” “Na ukihamia huko kwako?” “Kwa nini unawasiwasi wa kesho wakati hata hatujaishi leo?!” Akasimama kabisa mbele yake akimshangaa kabisa.

“Naomba usije Jerry. Nakushukuru. Lakini hapana.” Akabaki akimwangalia. Akaona amuage. “Usiku mwema. Nenda na wewe ukapumzike, acha mimi nimalizie hapo ndani, na mimi nilale.” “Saa moja kasoro uwe tayari. Nitakuwa nimefika hapa.” “Mimi sioni sababu.” “Naomba sisi tusiwe tunabishana Tuma. Tafadhali sana.” Akamwangalia na kuinama mbele yake. Maana ni kama alikuwa akimfikishia ujumbe.

“Vitu vidogo kama hivi, havina sababu ya kubishana na kuweka hofu za baadaye. Sio mbaya tukiishi sasahivi. Hatuna sababu ya kujipunja leo kwa hofu ya kesho. Ya kesho hatuna control nayo. Ila leo, sasahivi, tunaweza kujipanga na kufanya.” Akaendelea taratibu na sauti yake ya kiume tulivu.

“Alhamisi iliyopita kama leo, sikujua kama nitakuwa sina ndoa, nipo huku uswahili, nimesimama. Lakini ona nilipo! Habari zangu, tena mbaya zipo mpaka kwenye masaluni ya kike! Na sio kwa kupenda kwangu.” “Lakini kweli!” “Ndio maana naomba sisi tusiwe tunabishana kwa vitu vidogovidogo, ni maisha nimeishi kwa muda mrefu, nimechoka.” “Basi Jerry. Lakini sikutaka usumbuke bila sababu. Daladala hazipo mbali na hapa. Na kwa muda ninaotoka, kuelekea kazini nakwenda kinyume na foleni, hamna shida.”

“Najua. Na ninajua huna shida na usafiri wangu. Lakini na mimi nataka kukufanyia kitu Tuma. Na sio kwamba nalipiza! Najisikia kufanya hivyo. Naomba usinipinge.” “Samahani kama imesikika nakupinga. Sikuku..” Akasita. “Nitakusubiri na michuzi yangu.” Angalau wakacheka kidogo. 

“Ingia ndani kabisa. Ukishafunga mlango ndio niondoke.” “Ujue hapa kwetu nisalama we Jerry! Usipadharau.” “Sawa. Lakini wewe ingia tu. Nikishakuona umefunga na mlango upo ndani ndio nitaridhika.” Tuma akacheka na kutingisha kichwa, akaondoka. Alipofunga mlango ndipo na yeye akaingia ndani ya gari yake na kuondoka.

~~~~~~~~~~~

Inaendelea…

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment