Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Love At First Sight - Sehemu ya 86. - Naomi Simulizi

Love At First Sight - Sehemu ya 86.

Tukumbushie sehemu ya 62 ambapo kulitokea upatanishi kati ya Kamila, Pam na Mill. Baada ya machafuko ya muda mrefu. Pam akiwa ameumizwa na marafiki hao watatu, Mill, marehemu Mike na mpenzi wake Kamila. Lakini siku hiyo Kamila akiwa amekatazwa na Mill asitibue mambo, kinyume chake akapata ujasiri wa kuomba msamaha kwa Pam. Akidhania anazidi kulaaniwa kwa alichomtendea Pam akiwa mjamzito. Alisema hivi…..

“Halafu imekuwa kama nina mkosi! Ndoa yangu na Colins nayo wale kituo cha yatima waliokuwa wakinitunza tokea wameniokota, nao walimfungulia mashitaka Colins, wakimtuhumu alinichukua nikiwa chini ya miaka 18, akanifungia kama mke. Asiniendeleze.” Pam akashituka.

“Ilikuwa kesi kwelikweli mpaka Mill alipokuja na kutoa ushahidi kuwa aliyekuwa na mimi si Colins, ila Mike. Baba hapa amekubali kulipa faini kwenye kile kituo cha kulelea yatima na kulipa mahari kabisa, ndio kama tupo kwenye makubaliano, wafute kesi na kutoa vipingamizi kanisani, pengine ndoa ifungwe. Usinichukie Pam. Mill ndio amesababishayote. Ametuponza mimi na Mike, ila bora mwenzangu Mike hayupo. Ni Mill, usinichukie mimi.” “Kamila!” Mill akashangaa sana hakutegemea umaliziaji ule. Angalau wote wakacheka.

 Baada ya ya usuluhishi na mpaka kina Komba kuingilia kati wakimueleza Pam upande mwingine wa kusikitisha alikopita Kamila baada ya kifo cha Mike, hatimaye, baada ya muda mrefu wa machungu siku hiyo Pam alisamehe, na kuweza kupatana. Kama utakumbuka mama Komba alifanya maombi mazuri sana kuita amani na kusihi umoja katikati yao. Ndipo walipoweza kuishi kwa umoja mpaka sasa, wakitegemeanakama ndugu. 

Lakini siku ile kwenye sehemu ya 62, mwishoni mama Komba alimalizia hivi, “Umejaa sana humu ndani Colins bwana! Mashariti mengi kwa msichana wangu! Nenda tu kwako. Kwanza ni hapo mlango wa pili tu! Kwa nini hutulii kwako?” “Nipeni Kamila muone kama sitaondoka humu ndani.” “Huyu hatoki hapa bila ndoa takatifu kanisani.” Mzee Komba akadakia. “Basi naona na mimi hapa nipo sana tu.” Angalau mazungumzo yakabadilika. Pam akaona jinsi walivyojawa umoja na upendo.

Kamila akaonekana kama binti wa Komba kabisa. Mill kama kijana wao mkubwa. Wakawaongeza wao kama wanafamilia kabisa. Mipango anayoweka mama Komba anamjumuisha mama Eric kirahisi kabisa akimtaka ushauri. Mpaka wanaondoka hapo wote wapo ukurasa mmoja. Mwisho wa sehemu ya 62.

~~~~~~~~~~~

Wanasema kwenye amani Mungu huamuru baraka. Kamila akaanza kufunguliwa asijue mama mkwe wake anafunga na kuomba kwa ajili yake. Mambo magumuyaliyomfunga kwa muda mrefu akishindwa kuyafungua hata alipokuwa na Mike, yakawa yakifunguka kimyakimya. 

Tokea walivyompokea kama binti yao, akambeba Kamila kama Connie binti yake. Alimuhisi amefungwa mahali, japokuwa yupo katikati ya wao ambao mambo yao yanafunguka kirahisi, lakini yeye yupo kama amekwama!

Bado palikuwa na vipingamizi, wakashindwa kuoana na Colins kijana wake wa kwanza. Akahisi lipo jambo, lakini hakuwa na jinsi ya kufanya, walishaingilia uchumba wa Colins na Jelini, wakaharibu mpaka Colins kuharibika akili kabisa. Yakatokea mengi na familia hiyo kugawanyika mpaka alipokuja Kamila kwenye maisha yake akidhani anamsaidia kumbe akafanyika msaada si kwa Colins tu, na kwa familia nzima. Kamila akafanyika kiungo muhimu sana kwenye familia yao, hatimae wakarudi kuwa pamoja na kuzidi.

Wazazi hao wakapata somo. Wakajionya kutoingilia, na kuheshimu maamuzi ya kijana wao. Ndio mama akazama kwenye maombi. Kila anapoona lakurekebisha, basi anang’ang’ana na Mungu wake magotini.

Akatenga siku za jumatano akawa anafunga kavu bila kuweka kitu mdomoni, kimya kimya bila kumwambia mtu, kwa ajili ya Kamila tu. Ikawa siri yake hata Kamila mwenyewe hakuwa akijua kama mama Komba anamuombea

Bado alikuwa akiishi kwa mama Komba kama binti yake, lakini wakijiiba kwa penzi. Wazazi hao wakisafiri, basi Colins ndio anahama naye kabisa huyo Kamila na kwenda kujifungia naye sehemu kama fungate mpaka akijua mzee Komba anarudi, basi anamrudisha huyo Kamila.

Basi mapenzi ya Colins na Kamila yakawa matamu wakati wote kwa sababu ni ya uwizi, kama wanao onja kila wakati, wakingojea siku kituo walichomlelea Kamila wafungue kipingamizi kanisani, wafunge ndoa takatifu kama matakwa ya mzee Komba.

Kumtegemea Mungu Kuna Faida

Hakuna aliyewahi kumtegemea Mungu, akaabika. Hata kama huchukua muda mrefu, lakini siku Mungu anaporudisha majibu majibu ya maombi yako! Akakukuta ulipokuwa ukimsubiria! Haubaki kama ulivyokuwa. Siku moja ya jumatano jioni alipokuwa nyumbani, amewahi kutoka. Maana yeye hutoka saa nane mchana. Hupata muda mzuri wa kuomba bila mwingiliano. Lakini akajisikia kuendelea na maombi. Siku hiyo hakufungua akaendelea kufunga mpaka kesho yake siku ya alhamisi. Akawa anazidi kusikia mzigo juu ya Kamila, hajui aombe nini ila kulia tu mbele za Mungu. 

Jioni yake walipokuwepo wote nyumbani baada ya kazi, akaitisha maombi. Huwa hawana siku maalumu ya kuomba kama familia ni mpaka mama Colins awaambie basi wanakutana wote na kufanya maombi ya pamoja ndipo wanakwenda kulala. Akawasomea neno, wote wakisikiliza kisha akaomba. Kawaida tu ila Kamila akaangushwa na mapepo.

Colins akashituka na kuingiwa hofu ya ajabu, kama baba yake tu. Alisumbuka sakafuni, mapepo hayatoki. Ndipo Colins akatoka nje kumtafuta Kumu aliyemsaidia yeye kumuombea mpaka akawekwa huru“Najua muda umekwenda Kumu. Kwa hakika nisingekusumbua. Anahali mbaya, anaweza jiumiza zaidi.” Ikishafika swala la Mungu, Kumu anakuwa hana ubishi hata kama hataki, atafanya tu. 

Akamuaga Naya, nakutoka kwa haraka kuwahi kwa kina Komba. Alimkuta mama Colins akiendelea kuomba na Kamila bado sakafuni. Akaungana na mama Colins kukemea mpaka Kamila akawekwa huru kabisa. Hiyo siku ikaisha kwa amani.

~~~~~~~~~~~

Muda ulishapita hata kusahau tokea tukio la kufunguliwa kwake. Kamila akiwa kazini akamtafuta mama Komba. “Leo nakuja tule wote chakula cha mchana.” “Mmmh! Ushakimbiwa nini?” Kamila akaanza kucheka. “Nakujua wewe! Vikishindikana huko, ndio unanikumbuka mimi.” “Sasa nikwambie? Leo namtosa Colins kwa ajili yako.” “Mmmmh!” “Kweli tena mama! Nakujia na chakula kizuri, tunakaa zetu kwenye gari, tunakula. Wawili tu.” “Tutakuona kama hujanijia na Colins.” “Nakwambia leo ni mimi na wewe tu. Hata baba akitaka kukutoa, mwambie nishakuwahi.” Wakakubaliana na kuagana akijua lazima anajambo tu. Kamila si wakumuacha Colins mchana.

~~~~~~~~~~~

Alipofika tu hospitali ya Muhimbili, akampigia, mama Colins akatoka na kumfuata garini. Akaingia kiti cha mbele na kukaa vizuri. Akamgeukia. “Haya, kuna nini?” “Chakula.” “Najua sicho kilichokuleta. Tuongee tu. Hiki chakula naweza kula hata ukiondoka.” Akacheka akijua amemkamata.

“Ila ujue nakupenda. Sio kwamba eti unakuja baada ya Colins!” Akajishuku akicheka. “Huna lolote! Wewe ongea.” Akacheka na kujaribu kutulia. “Unakumbuka siku ile mliponiombea nikatokwa na mapepo ambayo hata hamkujua kama ninayo?” “Kwamba wewe ulikuwa ukijua kama unamapepo!?” Akamuona anasita. “Kamila!?” “Kwa asilimia fulani, lakini sikuwa na uhakika  kamili, mama yangu. Nataka kukwambia kitu nilikificha muda mrefu, sijawahi mwambia mtu ila Kumu.” Akashangaa kidogo.

“Kama unakumbuka siku ile mlipomaliza kuniombea, akaaga, nikamuombakuzungumza naye kidogo.” “Mkatoka nje?” “Sawasawa. Kuna kitu nilimwambia, nikamwambia asije mwambia mtu, ni siri nilikuwa naficha, naogopa watu wasije jua, wakanichukulia vibaya.” Mama Komba akakunja uso na kukaa sawa.

“Naomba usishituke mama yangu.” “Ni nini?!” Kamila akavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu, akamwangalia usoni vizuri. “Si na mimi unanipenda kama Connie?” “Wewe unajua Kamila. Au ushawahi tilia shaka?” “Hapana. Ila naogopa hiki nitakachokwambia kisije badilisha mahusiano yetu, ukanitizama tofauti.” “Usiogope. Kama upo tayari kukizungumza, kizungumze tu. Utabaki salama.” Akamtizama na kuridhia. Mama mwenyewe mtulivu mpaka usoni. Akaona aseme tu.

“Kuna ndoto nilikuwa nikiziota tokea nipo na Mike. Mwanzoni nikawa nikiogopa, lakini nikaja kuzoea, nikawa naona kama kawaida.” “Ndoto gani?” “Mtu ananijia usiku nikilala, anafanya mapenzi na mimi.” Akamtizama mama Komba, ambaye ni mkwe kuona kama amepaniki au kushituka, ila akamuona bado amebeba sura ya kimama.

“Pole.” “Inapokuja sehemu mbaya ni vile nilivyozoea mama yangu! Ikawa ni kama kitu nilichokubaliana nacho. Hata Mike alipokuwa akiishiwa nguvu za kiume, sikuwa na wasiwasi kabisa. Au sikuona tatizo. Nikawa nikimfariji tu. Lakini nikijua kuna kitu hakipo sawa. Ila nikakinyamazia, maana nilikuwa kama nimeshazoea! Mimba zinaharibika bila sababu za kidaktari. Wakiniangalia mimi na Mike, wote tulikuwa hatuna tatizo ila mimba hazikomai!”

“Sasa siku ile mliponiombea, kwa mara ya kwanza nikaenda kuzungumza na Kumu kule nje, nikamueleza ukweli wote juu ya yule mtu anayenijia usiku na kufanya mapenzi na mimi.” “Kwamba alikuwa akiendelea kuja hata ulipokuwa na Colins?” “Kwa asilimia 90 aliacha. Na hapo nilipozungumza naye nilimwambia Kumu, hajaja kwa muda mrefu lakini nikamwambia Kumu nina wasiwasi anaweza rudi. Maana baada ya kifo cha Mike ni kama alipotea, huko kuja kwake sikuwa na uhakika kama ni kweli ni yeye au mawazo tu kwa sababu ya kuficha kwa muda mrefu.”

“Nikamwambia Kumu ilikuwa ni kama mahusiano mengine ya siri. Nikamwambia naogopa asije kuwa anarudi kweli au akaja kurudi tena. Nakumbuka baada ya kuzungumza na mimi kidogo, akaniombea tena. Kisha akaniambia anaweza akawa anarudi kuangalia hali yangu ya kiroho, kama anaweza kukaa au la! Akaniambia lazima nijiweke msafi na kumruhusu Roho mtakatifu aishi ndani yangu. Kuomba bila kukoma ila si kwa hofu ila kama mshindi.”

“Basi nikaanza kujiombea mwenyewe kama alivyonifundisha na kujitahidi maisha matakaifu ila sasa Colins anakuwa ananiangusha dhambini!” Yeye mwenyewe yakawa yanamchekesha. Mama Komba akabaki akimtizama kwa kumsuta.

“Hakika ni Colins, mama!” “Wewe endelea.” “Basi, kiukweli tokea wakati ule wa maombi yangu na Kumu juu ya hilo, maana pia aliniahidi atakuwa akiniombea, hajaruditena na hofu juu yake ikawa imeisha kabisa. Nikilala, nalala vizuri, sipati ndoto mbaya. Maana nakua nikiomba kila usiku na kwa kumaanisha. Na wakati mwingine nakuwa nafunga mimi mwenyewe nikijiombea.” “Unafanya vizurisana.” “Etimama eeh!” “Kabisa. Lazima wewe mwenyewe uwe mlinzi wa nafsi yako. Haya, niambie. Maana najua hayo sio uliyoniitia.” Akacheka kidogo na kuendelea.

“Miezi mitatu iliyopita, baada ya muda mrefu sana, nikajigundua ni mjamzito.” Akashituka sana mama Komba.

“Nikajipima kuhakikisha. Nikagundua ni kweli, nikaliweka moyoni.” “Kwa nini hukusema!? Usingebakia peke yako kwenye kipindi kigumu. Colins anakupenda sana Kamila. Uwe na mtoto usiwe naye, na sisi tutakupenda kwa upendo uleule. Usihuzunike peke yako. Mungu ndiye…” “Mama! Mama! Mpaka sasa mimba haijatoka.” Ikabidi amuwahi. Mama Komba akapigwa butwaa.

“Nilikuwa naogopa kusema asije mtoto akatoka wakati kila mtu alikuwa akimsubiria kama Mike! Nikasema nisubirie kwanza nione. Hapa nilipo ni mjamzito unakwenda mwezi wanne!” Hakuamini.

“Kamila!” “Kweli mama. Nimeona kwa mara ya kwanza mimba inakua kubwa, sina shida yeyote, lakini nikajiambia sio sawa kwa mtoto mwenywe na Colins. Mtoto anahitajika kliniki na Colins kujua.” Mama Komba akajikuta machozi yakimtoka.

“Kuna usiku nilikuota unanyonyesha, nikamwambia Komba. Akasema ni mawazo tu.” “Kweli mama!?” “Kabisa. Atakuja kukwambia baba yako. Hongera Kamila. Ila acha tumshukuru Mungu, halafu nikuombee wewe na mtoto.” Akatulia kidogo.

“Natetemeka mwili mzima!” Akawa anaongea akicheka kwa furaha na machozi. “Siamini!” “Hata mimi mama, ila naogopaNaogopa sana. Akija toka? Au tusimwambie mtu kwanza ibakie siri yetu sisi tu wawili? Nitafutie kliniki hapa. Nifanye kwa siri. Maana kule Colins atajua tu. Nishaharibu mimba nyingi sana mama yangu! Naishia kuvunja moyowatu!”

“Hapana. Usiogope tena. Wewe umeshakuwa kiumbe kipya. Na ya kale yote yamepita. Huyo mjukuu wangu atazaliwaataishi wala hatakufa. Uhai wake huyo umefichwa ndani ya Kristo Yesu.” Akaanza kumtamkia baraka akimuombea, mpaka hofu kwa Kamila ikaisha na kujiona si jukumu lake kulinda uhai wa huyo mtoto. Ipo nguvu kubwa zaidi inayohusika na huyo mtoto. 

Machozi ya furaha yalikuwa yakiwatoka wote wawili wakati wakipokezana kuomba hapo garini. Wakamshukuru Mungu pamoja kisha wakamaliza wakabaki wakiangaliana.

“Umewezaje kuficha lakini?!” “Uzoefu mama. Ilinibidi kujifunza tokea nipo na Mike. Nilichoka kumuumiza na kumkatisha tamaa. Sijawahi fikisha mimba ya miezi mitatu hata mara moja.” “Kweli Kamila!?” “Mungu nishahidi. Kabla haijatimia miezi 3, napoteza mtoto. Nashangaa huyu bado yupo!” “Hongera sana.” 

~~~~~~~~~~~

“Sasa namwambiaje baba?” Mama Komba akaanza kucheka. Alicheka mpaka machozi. “Ni Colins huyo!” “Basi na yeye umwambie hivyohivyo.” “Mmmh! Alivyonihusia vyote vile nisikubali kuchezewa. Anayenipenda atanisubiri! Leo namjia na ujazito! Nisaidie mama yangu.” “Sasa hivi ndio unataka msaada wangu?” “Ni Colins! Hakika ni yeye mama. Anavyotiaga huruma! Mpaka anakuwa mwekundu na mnyonge. Nakuwa sina jinsi yakufanya. Nisaidie tu.” Mama Komba akabaki akicheka akimtizama.

“Au niseme ni ya Roho mtakatifu?” Alicheka mama Komba mpaka machozi tena. “Unataka kumdanganya daktari?” Hapo ndipo akakumbuka, hadanganyiki. “Hakika namwambia Colins mwenyewe akamkalishe baba na kumwambia. Ameniponza.” “Hayo ndio maneno.” “Nyie mama! Kweli unajitoa? Nisaidie mama yangu.”

“Tulia wewe! Kwanza ujue hizo ni habari njema kwa kila mtu.” “Kweli mama?!” “Hakika tena. Huyo Colins anautoto gani asiye na mtoto? Wewe sasahivi rudi kazini, ukazungumze naye uone atakavyofurahia. Baba yako mwenyewe atasahau masharitiyote, akili zitahamia kwa mjukuu. Usiogope. Sasahivi furahia mimba yako uliyoteseka nayo peke yako kwa muda wote huo! Pole na hongera.” “Ukisema hivyo sasahivi ndio naanza kufurahia, mama yangu. Ila usiache kumuombea, huyu kweli ninyonyeshe mama. Nina hamu!” “Huyo utanyonyesha wala usiogope.” Akamuacha anafuraha, na chakula alichomletea, akarudi ofisini hata yeye mwenyewe hakuwa amekula.

~~~~~~~~~~~

Akapitia duka la madawa, akanunua kipimo. Alipofika tu ofisini. “Unatafutwa.” Hizo ndio zikawa salamu za mapokezi. Akacheka na kupitiliza mpaka juu zilipo ofisi zao. “Nimeambiwa ukifika tu, nimjulishe.” “Usimwambie, muache kwanza.” “Anavyokuulizia!” “Subiri, usimwambie.” Akapitiliza chooni. Akakiweka kipimo kwenye mkojo, akabaki akisubiria. 

“Bado hajarudi tu!?” Akasikia sauti ya Colins akimuuliza sekretari wake. “Ameingia chooni, amesema..." Akasikia mlango ukigongwa. “Kamila? Nifungulie.” Akamfungulia na kuingia. “Yaani ndio muda wote huo ulikuwa kwa mama tu!?” “Subiri nikuonyeshe kitu.” Akawa bado amekificha nyuma, anasubiria muda utimie, majibu yaingie kwenye kipimo.

“Mimi sijala. Njaa inaniuma.” Akaanza kulalamika. “Nilikwambia ule Colins! Mimi nilienda kula na mama.” Abaki akimwangalia. “Basi nikishamaliza kukuonyesha kitu, nitaenda kukuletea chakula.” “Mimi huo utaratibu unaotaka kuuanzisha sasahivi, siutaki. Maana mchana ni muda wetu sisi, sio tena…” Akamkabidhi kipimo.

“Angalia.” Kwa sekunde kadhaa kile kijiti chenye alama ya msalaba kikawa kama hajakielewa, halafu kama amekielewa ila anaogopa kuuliza. Akakiangalia kwa muda kisha akamwangalia Kamila, akamkuta na yeye anamsubiria. 

“Ndio nini?!” Akauliza ila akisikika na wasiwasi maana sauti yenyewe ilijawa kutoamini hata swali lake mwenyewe.

“Mwenzio ni mjamzito.” Colins akabaki ameduaa kwa sekunde za kutosha tu. “Nakwenda miezi minne sasa!” Kamila akaongeza, Colins akamshika mkono na kumtoa hapo chooni bila ya kusema kitu mpaka akamtia hofu.

Akamuongoza njia asijue anapokwenda. Alipoona wanakwenda upande wa Ultrasound, ndio akaelewa anachotaka kufanya. Ni kuthibitisha. Akatulia kumuacha tu. Akafika kwa mtu wa Ultrasound, akakuta mtu mmoja nje, anasubiria. Akamuomba radhi na kuingia akiwa bado amemshika Kamila mkono.

Akamkuta mfanya vipimo anaandaa chumba kwa ajili ya mtu anayesubiria nje. Na yeye akamuomba radhi kwa kumuingilia. “Lakini siwezi kusubiri hata dakika moja mbele. Tafadhali tusaidie.” Ikabidi atoke, ili Kamila atoe nguo. Hakukawia akawa tayari yupo kitandani, Colins akatoka kwenda kumuita.

Akashangaa machozi yanamtoka baba mtu baada yakuona mtoto. “Huyu mtoto amekomaa kabisa Kamila! Kwa nini umenificha!?” “Usinilaumu Colins. Sikuwa na uhakika kama atafika hapa alipo. Mwenzio naharibu mimba! Haijawahi tokea nikabeba mtoto mkubwa hivi. Niliogopa Colins. Sikutaka kukwambia lipo jambo halafu baada ya muda mfupi hakuna.” Bwana Colins alijawa kilio, haamini. Yeye analia, Kamila naye analia akijieleza. Ikabidi wapishwe ili wamalizane kesi na furaha.

“Samahani Kamila. Naomba usilie. Nahisi nimepaniki. Sikutegemea kabisa. Yaani hata wazo halikuwepo! Naomba usilie.” Akaanza kumfuta machozi. “Nimefurahi! Aisee siamini!” Akaanza kujifuta machozi na kumfuta na yeye akitaka atulie.

“Daaah! Unasikia mapigo yake ya moyo lakini?” Akawa anauliza akicheka na kuongeza swali jingine. “Sasa hapo amelala?” “Sijui Colins!” “Aje amuamshe nione.” “Pengine bado. Tuache kwanza. Naogopa Colins. Naogopa sana.” “Kwa nini unaogopa na wakati unasikia mapigo hayo ya moyo?” “Sasa kwanini hata hazunguki!” Akaona anamtia hofu. “Vaa twende kwa daktari.” Ikaanza kliniki muda huohuo na ushauri kwa wazazi hao wapya. Maswali mengi, hawamalizi.

~~~~~~~~~~~

Baada ya muda mfupi, mpaka mzee Komba akawa amefika hapo na Connie akiwa na mchumba wake, wakitaka kumuona huyo mtoto kwenye Ultrasound. Mama Komba alikuwa na kazi ya kucheka muda wote. Wakarudi chumba cha Ultrasound vipimo vikaanza upya, na hapo wakamuona anazunguka. Kamila alifurahi mpaka kilio kabisa.

“Mnataka kujua jinsia?” Anayewafanyia vipimo akauliza. “Kwamba huyu mtoto ndio anaukubwa huo!?” “Kabisa.” Akawahakikishia. “Eti Kamila?” Wote wakamuangalia yeye. “Au unataka kusubiri?” “Ni wewe tu Colins. Sasahivi ni juu yako.” Akamfanya ajisikie vizuri huyo Colins katikati ya watu! Mpaka akampa kiss ya kutosha tu, tena mbele ya baba yake. 

“Na mama yako alikuota ukinyonyesha.” Mzee Komba akarushia hilo, macho kwenye ultrasound“Mama aliniambia! Jamani msiache kuniombea na mimi nije kunyonyesha kweli.” “Amini Kamila. Safari hii na wewe utanyonyesha.” Huyo alikuwa Pam. Chumba kilijaa hapo! Hata Mill aliacha kazi na kwenda kushuhudia. Maana Colins alikuwa na furaha hawezi kunyamaza. Ndani ya muda mfupi sana watu wake wote wakaribu aliwaambia. Na jinsi anavyokwambia, lazima uache shuguli zako ukashuhudie. Chumba kilijaa hapakuwa hata na pakukanyaga.

~~~~~~~~~~~

 Huku kwa Jerry akajikuta peke yake ofisini, mpaka mida ya mchana Tuma hayupo. Alishatoka kumuangalia zaidi ya mara tatu! Ilipofika mida ya saba njaa ikazidi kumsumbua, akatoka sasa kumsaka. Kwa kuwa alijua ofisi za stoo na kwa kawaida hawakuwa wakiitumia hiyo ofisi. Mara chache sana siku za jumamosi wanapokuwa busy. Akajua atakuwa amejificha huko, akamfuata na kumkuta ametulia kupita kawaida. Amenyongea.

“Tuma?” Akashituka na kugeuka. “Vipi?” “Safi tu, kuna mambo nilikuwa nikiweka sawa huku.” Akabaki akimtizama kama anayejaribu kumsoma zaidi, Tuma akarudisha macho kwenye kijalida kilichokuwa mbele yake. “Njaa inaniuma.” “Kila kitu kipo jikoni.” “Najua Tuma! Kuna nini?! Na usiniambie unafanya kazi huku maana sio kweli. Oda zote ulishakamilisha, nimeona. Na najua leo sio siku busy. Kwa nini umeamua kuhamia huku?” “Na huku pia huwa nakaa. Ni moja ya majukumu yangu.”

“Umi amekwambia nini?” Akamuona ameshituka kidogo. “Tuma?” “Hamna kitu! Twende tukale.” Ikawa kama anayekwepa kujibu hilo swali. Akasimama kwa haraka na kuongoza njia kurudi ofisini, moja kwa moja jikoni bila ya kuongeleshana. 

“Nikwambie tu kweli?” Jerry akageuka haraka kusikiliza, kwa matumaini ya kujua kinachoendelea. “Sijisikii kabisa kula. Tumbo haliko sawa. Lipo kama linavuruga. Siwezi kuweka kitu.” “Ni kama gesi?” “Nafikiri. Ila nitakuwa sawa. Wewe kula tu, mimi naweza kunywa hata chai.” “Basi narudi sasahivi, acha nikakuletee dawa.” Akamshangaza sana, hakutegemea! 

“Hapana! Usihangaike, ninazo nyumbani. Nikifika nitatumia. Kaa ule.” “Jaribu kutumia choo, nitarudi baada ya muda mfupi.” Akatoka na kumuacha Tuma amepigwa butwaa. “Kwamba anakwenda kunitafutia dawa!?” Hakika hakutegemea.

~~~~~~~~~~~

Akabaki hapo jikoni mpaka karudi na hot bottle, akamjazia humo maji ya moto kiasi. “Umejaribu kutumia choo?” Akaona aibu. “Umefanikiwa?” “Ndiyo.” Akajibu kwa aibu. “Weka tumboni. Shikilia na kitambaa, itatuliza misuli ya tumbo. Halafu tafuna na hizi dawa, utajisikia vizuri zaidi.” Akamsaidia kuweka tumboni kabisa, Tuma akishangazwa

“Ni moto sana?” “Hapana. Ina joto zuri. Asante.” “Unaweza kuinamia kwenye meza kama kushikilia kwa tumbo lenyewe.” Akafanya kama alivyomuelekeza, akaegemeza kichwa kwenye meza, akatulia akimwangalia anavyojitengenezea sahani yake. 

Akaweka sahani yake kwenye microwave na kuanza kutengeneza chai ya rangi akidhani anajitengenezea mwenyewe, akashangaa anampa yeye. “Kunywa ikiwa bado ya moto.” Kwa hakika alimchanganya jinsi anavyo muhudumia! “Asante.” “Karibu.” Akakaa mbele yake. Kimya. Jerry akainamia simu yake huku akila, angalau akaweza kuinywa hiyo chai kwa utulivu. Ilishakuwa 10 na robo jioni lakini ndio wakafanikiwa kukaa kula cha machana.

~~~~~~~~~~~

Mara wakasikia mlango unafunguliwa. Tuma akamwangalia, Jerry akasimama kwa haraka na kutoka. Alikuwa mrembo Umi. “Nimetoka kazini, nikaona nije kuwasalimia. Na kukukaribisha dinner.” Tuma akabaki kimya akisikiliza, tumbo likaanza upya kuvuruga asijue ni hofuwasiwasi au la. Hakusikia Jerry kujibu, ila Umi akaendelea. “Si muda wa kazi umeisha? Tunaweza kwenda na gari yangu, halafu nitakurudisha. Ni sehemu nzuri sana, utapenda.” Tuma akabaki kujisikilizia akijua kwa mara ingine tena, historia inajirudi.

~~~~~~~~~~~

Ujanja ni kuwahi au kupata?

Nani atapata, Umi akiwa amewahi?

Je, Jerry amerudi sokoni, yupo tayari kwa mapenzi akiwa hata hajakamilisha talaka?

Inaendelea… 

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment