Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Love At First Sight - Sehemu ya 85. - Naomi Simulizi

Love At First Sight - Sehemu ya 85.

Akamwangalia Jerry akaonekana kubadilika kabisa usoni.  “Naomba ukirudisheulipokitoa. Mwambie asante, lakini HAPANA.” Kisha akarudi ofisini na kumuacha Tuma na mshangao zaidi akishindwa hata kupepesa macho.

“Inamaana niondoke na chakula chote hiki!? Ujue ni nyama mbuzi?” “Si umemsikia mwenyewe?” “Ujue kimeshalipiwa! Au nikiache tu hapa?” “Utamuachia nani hapa?” Jerry akamsikia Tuma akimuuliza. “Hata wewe! Sasa si hii ni hasara tu?! Maana alitoa oda tokea jana kuwa leo mchana tukilete hapa bila ya kuchelewa.” “Sasa uniachie mimi kwani umetumwa kwangu?! Wewe rudisha ulikokitoa na fikisha ujumbe uliopewa. Mimi sina shida na vya bure.” Ikabidi aondoke na chakula chake na kubakisha harufu tu. Pakatulia.

Mwishoe Tuma akaona aende akale chakula alicholeta kutoka nyumbani. Wali maharage. Na hivi kulikuwa na nyama alizoletewa na mama J, akajipashia na kuanza kula. Akasikia mlango unafunguliwa, akajua Jerry anatoka ofisini kwake anakuja hapo jikoni, akajiweka sawa.

Akanyanyua macho kumuangalia wakati akiingia hapo. “Njaa imeanza kuniuma!” “Kuna kidogo kilichobaki asubuhi. Lakini kuna wali, maharage na nyama alizoleta mama J.” “Afadhali. Si naweza kuchanganya vyote?” “Mimi nimeshachukua chakunitosha, hata ukimaliza ni sawa.” “Nashukuru.” Akaanza kujipakulia ila akimshangaza! Anakataa vinono anajibana naye kwenye wali maharage! Akatulia kimya hata hamwangalii anachokifanya.

Akapasha na kukaa mbele yake. “Nashukuru kwa chakula.” Tuma akamwangalia akiwa na uso wa maswali, ila akajibu “Karibu.” Wakatulia kwa muda.  “Naomba ushauri wako.” Tuma akamwangalia. “Katika kupita kwako kwenye hili jiji. Sio lazima ikawa sasahivi, ila naomba upate muda unisaidie maeneo ambayo unadhani yanaweza faa kwenye ile biashara.” Tuma akatulia akifikiria.

“Hamna haraka. Kula tu. Lakini ukikumbuka hata usiku unaweza nitumia.” Tuma akacheka. “Kuna maeneo baadhi niliona. Nikayafikiria. Nitakuandikia nikupe.” “Nitashukuru.” “Unataka kuanza lini?” “Haraka iwezekanavyo.” Tuma akatulia akifikiria. Alisikia ameachikahana kitu. Pesa ya kuanzisha biashara kubwa hivyo atapata wapi! Akabaki akijiuliza, kimya kwa muda mwishoe akaona aulize.

“Kwa maana nyingine hapa unapita tu, hutakaa sana?” “Ndio maombi yangu hayo. Nisikiae sana. Nijifunze kwa haraka, nianze changu japo kwa kuchelewa.” “Unamaanisha nini kwa kuchelewa?” “Ndio kama naanza maisha! Kwa umri huu kuanza! Huoni kama nimechelewa sana?” Hakusubiri jibu akaendelea kwa kulalamika kidogo. 

“Nimepozeza muda wangu mwingi kujenga kwenye mchanga, mvua imenyesha, nyumba imebomoka na kuniacha mwangani na fedheha.” “Pole.” Akacheka na kunyamaza.

“Nikwambie kitu?” Jerry akamwangalia. “Inaweza isilete maana. Lakini jiambie hivi, safari hii unaanza ukiwa unauelewa mkubwa sio kama mwanzo. Kwamaana nyingine, utakwenda mbali kwa haraka sana na unaweza kupita hata waliotangulia kwa sababu ya uzoefu.” Jerry akatulia kabisa akimsikiliza.

Unashule kubwa sana ya maisha. Ulishajua wapi ulikosea, na sasahivi ni wapi upite usiharibu tena. Umekaa kwenye biashara kubwa, ukiwa unaona na kushiriki utendaji kazi wake na ukaona makosa yote. Sasahivi upo hapa kuangalia kwa wazi kabisa kinachoendelea. Huoni kama ni kama Mungu amekupa nafasi ingine nzuri maishanikuanza upya tena akiwa amekupa na nyenzo kabisa?” Akazungumza naye taratibu tu akijua anakopita maishani.

“Ukiiweka hivyo angalau. Nilikuwa nimeumia Tuma! Niliumia sana. Acha niwe mkweli kwa sababu umenifungua kwa upande mwingine, na unaonekana una utu na muelewa. Nilikuwa na maumivu ambayo sikuwa nalala vizuri.” “Pole. Kwa hiyo sasahivi utalala?”

“Nikianza kujiangalia kwa hivyo ulivyoniambia, labda.” “Ndivyo ilivyo. Najua kama binadamu kuna kuumia, lakini wakati mwingine huwa nahisi eti Mungu naye anahusika.” “Kwa nini?” Akacheka akifikiria.

Wakati Mwingine Nafasi Za Pili Anazotoa Mungu Zinakuja Na Maumivu

“Wewe niambie tu.” “Ushasikia usemi wa kisicho riziki, hakiliki?” “Si ni yaleyale kama ninavyojilaumu mimi kuwa mali isiyo yako hata ukiikimbiza vipi haishikiki?” “Ewaah! Lakini wewe ulikuwa ukijenga kwenu, mlishahalalishwa na Mungu. Kilichotokea, ni matokea ambayo hukutegemea!” “Kitu ambacho sitakuja kumlaumu nacho Sandra, hakuwaga mnafiki na si kwamba alinibadilikia. Mapema sana, alipopata ile pesa na kusema tuanze naye ile biashara alihakikisha anaweka wazi kuwa ni yake, sema mimi ndiye nilijifanya mjinga na kuendelea kuwekeza muda wangu na mambo mengine, nikijifanya imekuwa yetu. Sasa ukiniuliza ni kwa nini, sijui! Endelea na ulichotaka kuniambia.” 

“Mbaki nilikutana naye katika kuhangaikia mkopo wa chuo. Wenzangu wote walipata mkopo, wangu ukasumbua, ikabidi nije Dar, mpaka bodi ya mikopo kuangalia kulikoni! Ndipo nikakutana na Mbaki na kuyabadili maisha yangu kabisa. Ilikuwa ni kama nimeokota alumasi kwenye pochi. Kirahisi sana. Halafu sio mbishi, mwepesi wa kuomba msamaha! Na wala si mchoyo. Kasoro ndogondogo kama binadamu mwingine yeyote.”

“Tukaendelea naye mpaka nikamaliza chuo, yupo na mimi bega kwa bega akinisaidia kwa asilimia zote. Kuanzia ada mpaka matumizi. Nikamaliza chuo yeye ndiye aliyenishauri nije kutafuta kazi huku Dar. Sikuwa na pressure ya kupata kazi maana pesa si nilikuwa nayo! Lakini Mungu akanisaidia nikapata hapa tena mama J akiwa amenianzia mshahara wa chini tu. Sikujali maana sikuwa na shida na pesa ila sababu ya kunitoa ndani kila siku.”

“Ila sasa, nikaja hapa ikatokea tunaelewana sana na mama J. Tunapanga mambo pamoja na yanafanyika. Ikaongeza furaha ya kuja kazini. Huku naendelea na Mbaki.”

“Alipokuja Umi hapa, alinikuta ndio tunakaribia ndoa na Mbaki. Nikikwambia tunakaribia ndoa, ni kwamba mpaka mahari alishakuwa amelipa. Tena kwa wazazi wake na ndugu kwenda mpaka nyumbani! Wakalipa kabisa kila walichotakiwa kulipa, vikao vya harusi vinakaliwa, na sisi tupo kwenye mafundisho ya ndoa. Sisi wawili na mchungaji.”

“Kwa kina Mbaki nafahamika na kuchukuliwa kama mke wa Mbaki kabisa. Na kwao walikuwa wanauwezo sana. Ila wakatokea kunikubali. Mpaka mama yake alikuwa akinipenda.”

“Umi akaanza kazi hapa akiwa bado mgeni, Mbaki akawa amepita hapa sijui kuleta nini, akakutana na Umi. Unamjua jinsi Umi anavyovutia.” Jerry hakuafiki akabaki akimtizama. “Namaanisha vile alivyo mzuri wa sura na umbile.” “Inategemea mtu anaangalia nini, ehe?” Akamtaka aendelee maana ni kama Tuma alikuwa akitafuta uungwaji mkono wa kuwa Umi ni mzuri sana.

“Basi, Mbaki akachanganywa na Umi. Sijui akafanyaje huko kazini, ila siku ambazo alikuwa akizitunza kwa ajili ya harusi, akachukua tatu, na Umi naye akadanganya hapa amefiwa, eti anakwenda kuzika kijijini kwao, wakaenda Zanzibar na Mbaki.” “Haiwezekani Tuma!” “Acha. Ilikuwa mbaya mno. Mimi sijui, sina taarifa.”

“Wamekaa huko siku tatu, ndio wakarudi. Tukijua Umi alikuwa msibani, Mbaki amesafiri kikazi. Nafikiri sijui huko walipo walitibuana, nafikiri Mbaki akaamua kusitishakabisa mahusiano na Umi, Umi akawa amenogewa na pesa ya Mbaki, sasa wamerudi, Mbaki amemfungia simu, Umi anamtafuta hampati. Na nahisi kabisa alimwambia asije niambia kama walikuwa naye.”

“Umi akakaa mwezi wa kwanza akajigundua ni mjamzito.” “Tuma! Mimba ya Mbaki?” “Subiri sasa. Unamjua Umi, kapaniki, hampati Mbaki na hajui anapofanya kazi, na mimi hawezi niuliza, maana alipita tu mara moja hapa, sijui wakabadilishana vipi namba, na kukimbilia Zanzibar, nafikiri huko ndiko kujua mimi na Mbaki ni wachumba wakukaribia ndoa, wakagombana. Sasa si ndio kurudi, kujigundua ana mimba! Anasema ni ya Mbaki asiyemtaka tena.” “Tuma!”

“Acha! Mimi sina taarifa. Sasa kutapika kukaanza, kuficha tena hawezi. Ndio ikabidi sasa amwambie mama J. Ilikuwa kesi hapa, Mbaki hataki mtoto, anasema anamsingizia, Umi hajatulia, ana mabwana wengi, kwa nini abambikiziwe yeye hiyo mimba! Na Umi naye akawa anasema kwa kipindi kile hakuwa na mtu mwingine ndio Mbaki.” “Huku vikao vya harusi vinaendelea?” “Kama kawaida. Nakwambia mimi sina habari wala kuhisi!”

“Ndio mama J akamwambia hatathubutu kunificha, lazima aniambie. Niliumia, sijawahi umia maishani kama vile. Aibu. Na kama unavyomjua Umi sasa, maadamunimejua, akaona sio siri tena, ikawa amepata jukwaa sasa, anamlalamikia kila mtu na kila mahali kuwa mchumba wa Tuma ni tapeliamemdanganya, amempa yeye mimba halafu anakimbia. Vikao vyangu vya harusi vikageuka kesi sasa. Mbaki hataki mimba, anasema Umi anamshakizia, Umi anasema mimba ni ya Mbaki. Kesi ilipokuwa kubwa, mama J akanihurumia akaniambia nichukue likizo, nikapumzike mpaka nikae sawa.”

“Pole Tuma.” “Asante. Nikaondoka kabisa kwenye hili jiji maana hongera ziligeuka pole. Kila nikipita naona watu wananiangalia mimi! Wengine wanasema ni haki ya Mbaki, ali upgrade.” “Jamani!” “Acha! Ilikuwa fedheha ya hali ya juu. Ukimlinganisha Umi na mimi, watu wanasema hata mimi natakiwa kuwa muelewa. Nikaona nitachanganyikiwa, kila mtu ananiona mimi mjinga, mbona ni jambo la kawaida tu!” “Wala si kawaida!” Jerry akakanusha kwa haraka sana.

“Nashukuru Jerry, maana wengi eti waliniona mjinga. Nachanganyikiwa jambo la kawaida. Eti kuonja nje sio jambo la ajabu! Na hapo wanaongea wakubwa kwa wadogo, wake kwa waume. Nikawa naonekana eti mimi nakuza tu jambo. Na eti nakufuru, kuacha ndoa na mwanaume kama Mbaki! Napiga teke bahati! Siwezi kupata mwanaume kama yeye!” “Jamani!” “Kweli tena! Gafla mimi ndio nikageuka kituko. Si Mbaki wala Umi, MIMI.”

“Basi, ndio nikaenda nyumbani kabisa. Nilikaa huko nikiwa sina hata mpango wa kurudi tena kwenye hili jiji. Hapo nikawa nimeishiwa, sina kazi sina kitu. Nimerudia maisha ya shida yale ya zamani. Maana niliondoka hapa jijini na nilichokuwa nacho. Nikarudi kwa mama tukatumia vipesa vyote nilivyokuwa navyo, na mimi nikaanza kutunzwa tena na mama akiwa amefedheheshwa na yeye vilivyo.” 

“Kwamba na watu wa huko kijijini walijua kama unaolewa?” “Mbaki na watu wake walifanya fujo kwelikweli wakati wa kulipa mahari. Ilikuwa shuguli kubwa, ikawa gumzo kuwa hatimae kwa mama yangu nako kuna shuguli au jambo jema linatokea. Naolewa.” Akaibua maswali hapo napo, lakini ikabidi awe mvumilivu kusikiliza.

“Mbaki alikuja na mashabiki zake wote kutoka mjini. Ndugu kibao. Na ikawa kama kila familia imekuja na gari yake! Kulijaa magari pale kijijini, haijawahi tokea. Hiyo ilikuwa mahari tu. Ikavuta macho na masikio ya wengi sana pale kwetu. Habari ikaenea kwa umbali mkubwa jinsi walivyofanya hekaheka. Kila mtu alikuja kumsindikiza Mbaki, mlevi mwenzao.” Jerry akacheka.

“Hakuna utapita mahali na yule kiumbe asiwe anafahamiana na watu au mtu! Mcheshi na maneno mengiii! Kwa hiyo watu walikuwa wakisubiria harusi, halafu kimya, hakuna kitu. Lakini pia ilibidi baba aambiwe kuwa ile ndoa haitakuwepo tena.” “Aisee pole sana Tuma.” “Asante. Lakini ilikuwa bora kuishi na mama kimasikini na maneno ya watu wanaotuzunguka kule ambao tulishawazoea kutusema vibaya. Kwanza walisema walitegemea.” “Jamani! Kwa nini?” 

“Hiyo nayo ni habari ingine. Lakini niliona bora kwa mama kuliko kurudi huku kwa watu waliokuwa wakiniona mjinga. Nalia wivu kijinga. Na kuniambia mimi sio muelewa. Nikatulia kwa mama kimya.”

“Basi, ndio mama J alipoona kimya kwa muda mrefu, ikabidi anitafute na kunisihi sana nirudi. Alizungumza sana na mimi akinitia moyo. Ndipo nikarudi huku mjini sasa, sitaki hata kumuona Mbaki. Nilipokuwa nikiishi nilipafunga tu. Walinzi wananilindia nje.” Kidogo Jerry akashangaa hayo maisha aliyokuwa akiishi, ila akaliweka moyoni akikumbuka kusikia Mbaki anayo pesa, ila si kwa mshahara anaolipwa hapo.

“Niliishi kwa mama J karibia mwezi.” “Nyumbani kwake?!” “Ni hivyo tu hunikumbuki. Lakini nilishakuona hata pale kwao. Mlipita na familia yako, ilikuwa jioni, na mimi siku hiyo nikawepo.” “Hayo macho yako nisingesahau Tuma!” Tuma alicheka. Alicheka mpaka kujifunika.

“Sikumbuki kabisa kukuona. Pengine ulikuwepo lakini hata sikukuangalia.” “Upo sahihi. Hatukusalimiana kwa karibu.” “Useme hivyo. Ila nisingekusahau.” “Ila na hapa ulishanikuta zaidi ya mara moja.” “Mimi ni mbaya wa kukumbuka majina, lakini sura si rahisi. Tena kwa hayo macho yako! Hakika nisingekusahau.” Tuma akaona aibu ila akajikaza kwa kujibaraguza, maana alijua hata Mbaki cha kwanza alivutiwa na macho yake.

“Kwa hiyo Umi alizaa na Mbaki?” “Thubutu! Unamjua Umi wewe! Mwenyewe anasema yeye bado mdogo, hawezi kulea mtoto asiye na baba. Alitoa ile mimba.” Jerry alishituka mpaka akapaliwa. “Kunywa maji.” Akasimama kumletea maji. “Pole.” Akanywa akatulia.

“Aisee sikutegemea mwisho huo!” “Ndio ujue ni Mungu huyo. Fikiria sasahivi mimi ningekuwa na ndoa ya namna gani! Pengine nisingekuwa na shida ya pesa, lakini pengine nimeathirika. Inamaana huo ndio ulikuwa mchezo wa Mbaki na hatumii kinga. Na huyo ni Umi ambaye nilimfahamu, na nisio wafahamu?” “Aisee pole sana.”

“Nashukuru. Lakini ndio nakuja kwako. Ukiwa unapita hapo, inauma sana. Ila hujui Mungu amekuokoa na mangapi! Na kwa sasa unapoanza upya, hutaanza kama mwanzo. Unaanza ukiwa na uelewa mkubwa zaidi, huwezi rudia kosa.” “Kwa hiyo safari hii hujarudia kosa?” Akacheka akiwa amemuelewa.

“Sijui jiliingiwa hofuSikutaka kurudia tena. Nikajifungia hapa, kimya.” “Sasa mbona hapa ndio pazuri kabisa. Wanakuja wenye hela.” Tuma akacheka sana. “Hao wenye hela wakianza na mimi kisha wakaja kukutana na Umi habari inabadilika kabisa. Kila mtu anataka ku upgrade.” “Sio kila mtu. Sema hao mnao kutana nao nyinyi. Na pengine vigezo vyao, Umi anavyo.” “Sasa kuna mwanaume asiyetaka vigezo alivyonavyo Umi kweli?!” “Wewe Tuma unakutana na wanaume wa namna gani wewe!?” “Hata sijui!” “Sio wanaume wote ni kama Mbaki. Na sio wanawake wote ni kama Sandra aliyekuwa mke wangu.” Tuma hakutegemea.

“Unamuona Jeremi na Hilda au mama J kama mnavyomuita nyinyi?” “Nawaona.” “Wote hao walitokea kwenye familia za kitajiri sana na Hilda ni mzuri hivyohivyo tokea msichana mdogo. Wazazi walipofariki sisi wote tulijua Hilda atamkimbia Jeremi maana tulifilisiwa kabisa, lakini si huyo Hilda yupo na Jeremi mpaka leo na ujue wamesafiri sio kikazi.” “Kumbe?!” “Wanamtindo wa kuchukua siku chache wanakwenda mahali kujifungia kwa siku chache ndio wanarudi. Na wapo hivyo tokea zamani. Sasa nawezaje sema wanawake wote wapo kama Sandra au kama Umi?” “Huwezi.”

“Haya, si Jeremi huyo amefanya kazi na Umi muda wote. Ushawahi muhisi hata mara moja akimtizama Umi kwa kumtamani kimapenzi? Kuwa tu mkweli maana sitakwenda kusema.” “Lakini kweli! Hata mara moja!” “Si umeona sasa? Acha kuingiwa hofu kwa kosa la mtu mmoja au watu wachache. Upo usemi unasema we are equal, but not same.”

“Si wanaume wote ni wadhaifu kwa ngono, Tuma.” “Hapo na wewe umenisaidia. Sikuwa nimefikiria kwa umbali huo! Ila kwa baba J naye nilijua ni kwa kuwa ni mume wa mama J, na mkewe ni mzuri sana, ndio maana.” “Sio kweli. Wapo wanaume, unakuta wanawake wazuri tu waliopendezwa na vigezo vyao mpaka kuwaoa, au unaweza kuta wakawa wanafanana kabisa na huyohuyo Umi na bado wakamtaka mwanamke mwingine kama Umi au hata asiyefanana na Umi. Ni tabia mbaya tu ya mtu.”

“Na kama mimi mwenyewe nakwambia, alichofanya Mbaki si kitu cha kawaida. Si sawa. Na ninajua wapo wanaume wenye msimamo kama wangu. Hakuna ruhusa kuonja nje. Unaweza kutulia na mwanamke mmoja bila kujalisha alivyo.”

“Japokuwa nilikuwa nikizungukwa na wanawake, lakini sijawahi msaliti Sandraaliyekuwa mke wangu. Jeremi pia, hajawahi kuonja nje. Ni mkewe tu. Na kwa asilimia 100, nina uhakika na bro naye ni hivyohivyo. Kwa hiyo si wanaume wote ni wabaya. Acha woga.” Akacheka na kutulia wakaendelea kula kwa muda mrefu tu, ila kwa utulivu mpaka wakamaliza, wakasafisha hapo ndio kila mmoja akarudi sehemu yake ya kazi.

~~~~~~~~~~~~~~

Baada ya muda Jerry akasikia hodi taratibu, akajua tu ni yeye. “Ingia Tuma.” “Sitaki kukusumbua ila nimekuandikia maeneo ambayo unaweza kuyazungukia kujiridhisha.” “Nashukuru sanaaaa.” Akaanza kuyasoma kwa sauti, Tuma naye akimuelekeza yalipo. “Mmmh! Naona kwingine itabidi twende wote Tuma. Au unakuwa busy hata weekend?” “Nisipokuwa hapa, ujue nimekaa tu nyumbani.” 

“Basi naomba unisindikize. Au nitakuwa nimezidisha?” “Hapana. Naweza kukusindikiza.” “Nitashukuru. Lini sasa?” “Ukiniambia mapema nitajipanga.” “Tugawe. Baadhi siku ya jumamosi na mengine siku ya jumapili.” “Wazo zuri.” Akabaki akimwangalia, mpaka akamfanya Tuma aanze kujishuku na kuingiwa aibu, kisha akarudisha macho kwenye hayo maeneo.

Akaona aage, atoke hapo. Maana kuna jinsi alimwangalia, akashindwa kuvumilia. Akatoka na kwenda kukaa mezani kwake akishindwa hata kuwaza ila kuduaa akijaribu kutafakari. “Amekataa chakula cha Umi, anakula changu cha kimasikini!” Akajaribu kujiuliza hapo bila kupata jibu.

“Kweli Umi ni mzuri, lakini baba J hajawahi hata kumtongoza! Ukute kweli sio wanaume wote ni kina Mbaki!” Baada ya muda mrefu wa machungu na kinyongo akiwa amesusia mapenzi, akaanza kujisikia kufunguka. Akiwa amepotelea kabisa mawazoni, akasikia mlango unafunguliwa. 

“Inabidi nitoke. Naweza nikarudi lakini kwa kuchelewa.” “Sawa. Si unafunguo za hapa?” “Ninazo. Na kutoka kwako si mida ileile?” “Ndiyo. Pengine kuwe na maagizo ya tofauti ndio naweza nikachelewa, vinginevyo 12:30 nitakuwa nikitoka.” “Nikikuomba unisubiri endapo nitachelewa kabla ya hapo ni sawa?” Sasa uliza yenyewe ikawa tena sio ya kibosi.

Akababaika kidogo. “Ila kama utakuwa umechoka. Nisikutese. Unaweza kuondoka tu.” “Sina haraka, naweza kusubiria.” Ila akawa hajaelewa. Amesema funguo anazo, sasa kwa nini asubirie! “Na usile kitu kingine, nikukute na njaa.” Tuma akacheka sana. “Hata ugali tembele?” “Hapana bwana! Umekula huo tokea jumatatu! Subiria, sitachelewa sana.” “Sawa.” Ilikuwa saa 9 mchana. Akajishangaa kiroho kinafurahia kumsubiria.

Hakuna Aliyewahi Kutoa Kumzidi Mungu

Saa 12 na robo akawa amerudi. “Si nimewahi?” Tuma akacheka. “Mbona kama ulikuwa ukikimbia?” “Nilikuwa napambana na muda. Njoo tule.” “Naipata harufu ya nyama choma.” “Nimenunua nyingi. Unaweza beba ya kupeleka nyumbani, na ingine ikabakia kwenye friji tukawa tunakula na chakula cha mchana. Kuna mahali huwa wanachoma vizuri sana. Nikiwapa oda huwa wananitengenezea vizuri na kunitunzia.” Tuma akacheka na kumfuata jikoni, na kukaa alipokuwa amekaa mchana.

“Kumbe ulienda kuchukua nyama?” “Na kurudisha chupi kwa Sandra.” Akamjibu bila ya kumtizama, akamfanya Tuma kuganda hajui aseme nini! “Umi alipokwambia amenipokonya kila kitu, hakukudanganya. Ilikuwa KILA KITU kweli, kasoro chupi na nguo nilizokuwa nimevaa kwa wakati huo. Ndio nilikuwa sijamrudishia. Sasa nilishafua lakini sikuwa nimepata ujasiri wakurudisha, nikabaki nikizunguka nazo kwenye gari tu.”

“Sasa leo kwa sababu fahamu zangu zimefunguka na kuweza kuliangalia hili jambo kwa jicho ulilozungumza na mimi kuwa sio kwamba nimeshushwa chini ila Mungu amenipa nafasi ingine, ndio nimeweza kumrudishia.” Tuma akabaki ametulia hapo jikoni ameinama anashindwa hata kuchangia! Ila kujisikia vizuri kuona  maneno yake yameweza kumjenga.

“Nimekuwa nikikimbiakimbia tu. Angalia kama ameweka ndizi za kutosha na viazi vya kukaanga. Acha nimtaarifu Sandra kama nimemuachia vitu getini.” Akaandika kisha akamuona anasita. “Hapana. Atajua namba yangu mpya, na kuanza kusumbua. Naamini mlinzi atampa tu.” “Kwamba umeviacha getini hata ndani hujaingia?!” Akamuona anacheka kwa masikitiko.

“Alipokwambia Umi nimefukuzwa, jua ALINIFUKUZA kweli.” “Pole. Mimi sikujua kama unatusikia wakati tukizungumza! Sikutaka kukuumiza.” “Sio zaidi ya siku ile alipokuwa akinifukuza huku akinivua nguo mbele ya watu. Wewe ulisema ulipata fedheha, lakini ni ya kuhisi Tuma. Mimi ni kwa kuona maana alikuwa akinishambuliayeye na wafanyakazi wake, kama kwake nilikuwa takataka na si mume wa ndoa! Kwa wazi bila hofu wala sitara!” “Pole.” “Nahisi moyo umeshaanza kupoa. Na nimefurahi zaidi kuwa hanidai tena kitu. Nimeondoka kwake nikiwa sina chake.” Tuma akabaki na maswali mengi hajui anaulizaje.

“Tule ukapumzike.” Wakaanza kula kimyakimya. “Nikuulize kitu?” Tuma akavunja ukimya. Akamwangalia. “Tulipoachana na Mbaki, sisi ilikuwa rahisi. Hatukuwa na watoto. Wewe utafanyaje swala la watoto? Nyinyi ni wazazi!” “Kuna ndoa hizo! Sijui nikuelezaje! Heshima ileile aliyokuwa akinipa ndivyo alivyowafundisha vijana wake jinsi ya kuniheshimu.”

“Wale watoto ni wangu kwa nje, lakini nawahurumia kwa kupunjwa. Walivyo vile, hata hawajui baba anatakiwa awe vipi na wao wanatakiwa kuwa vipi kwa baba yao.” “Ndio ilikuwa mbaya hivyo!” “Kupita nitakavyokwambia. Sidhani hata kama wataona kama wamepungukiwa na mtu. Ila najua watashukuru kuondoka kwangu maana ilikuwa kama nawaghasi tu. Hawataki kurekebishwa kama mama yao.” “Pole.”

Najilaumu, naona nimechelewa kufanya haya maamuzi, nimeathiri watoto wangu, sijui kama wanamfano mzuri wa ndoa, au hata familia yenye baba! Nawasikitikia, japo kwa sasa wao hawaoni umuhimu wangu. Kwa hiyo kwa upande wao, ilimradi wanaye mama yao. Watakuwa sawa tu.” Akashindwa kuchangia kwenye hilo. Wakala hapo kama ambao wapo kwao. Hamna mwenye haraka.

“Nikuulize tena?” Jerry akamwangalia. “Kwa nini umeleta chakula tule wote?” Akakunja uso kama ambaye hajaelewa swali. “Maana usije kuwa umenunua na kutaka kula na mimi kama kulipiza! Hapa sitaki ujisikie kama unafanyiwa wema, utakuja kusimangwabaadaye au utaanikwa baadaye au pengine utatakiwa kulipa fadhila. Mimi sipo hivyo na sitakufanyia hivyo. Kwa hiyo usiishi kama vile inabidi kulipiza.” Akaendelea taratibu.

“Sasa hivi wewe upo kwenye kujijenga upya. Unaanza. Tuliza mawazo kwenye hilo, usiwe na wasiwasi na mambo madogo madogo. Na ninakuhakikishia hiki chakula kwangu si tatizo kabisa. Na nikikwama, utaona hakuna chakula. Na hutasikia ikizungumzwa popote kwa sababu mimi mwenyewe nakiita chakula cha jumuiya. Mama J mwenyewe anachangia. Na leo umeona. Sitathubutu kumsimangia mtu chakula au hata kitu. Usiwe na wasiwasi.”

“Ningekuwa nina wasiwasi nisingekula na wewe. Au niseme nipo nimekaa na wewe hapa kwa sababu sina wasiwasi kabisa. Najua hutanisimanga Tuma.” “Kweli?” “Labda iwe nimekusoma vibaya na kwa haraka.” “Nakuahidi sitakusimanga. Kwanza hamna hata chakusimangia hapa! Kwa haya maandazi na ugali tembele!? Hamna.” “Ipo siku nitakuja kukwambia ulichonifanyia. Kwa sasa unaweza usinielewe au isilete maana kwako, ila ipo siku utaelewa. Kula ukapumzike. Ila jua nilitaka tule wote kwa kampani tu. Nilitaka kampani yako.” Akatulia kidogo akimwangalia, Tuma akaona aendelee kula.

“Au nimekosea?” “Hapana. Nashukuru. Nimefurahia chakula.” “Hata mimi nimefurahia. Umesema unapoishi ni daladala moja tu?” “Ndiyo.” “Sasa sasahivi sio umechelewa tayari?” Akaangalia saa. Saa mbili usiku. Akashituka sana.

“Sikujua kama muda ndio umekwenda hivyo! Acha niwahi.” “Nitakusindikiza kituoni, na nitakusubiri mpaka upate daladala. Ukikosa nitakupeleka. Usiwe na wasiwasi. Malizia chakula, halafu chukua kitakachowatosha nyumbani, ndio twende.” Ndipo akatulia na kula. Ila safari hii pakawa kimya mpaka wakamaliza. Akamchukulia mdogo wake kidogo. 

“Asante. Najua mtoto wa mama mzazi atafurahi huyo!” “Si utamkuta ameshalala?” “Saa hizi! Mapema sanaaa. Mpaka saa nne na nusu ndio analala. Asante, Jerry.” “Karibu.” Wakamalizia hapo ndipo wakatoka.

Wanafika tu kituoni na daladala ya mwisho inapita. Akamuaga na kuondoka kwa haraka. Na Jerry naye alipohakikisha ameondoka ndipo akarudi kwenye gari yake na yeye akarudi nyumbani tayari kwa kulala.

~~~~~~~~~~~~

Alimuacha Tuma na furaha ila hamuelewi! Maswali mengi bila ya majibu! Alimuonyesha kumjali fulani hivi! Ikamgusa moyo. Na yeye Jerry ni kama alifurahia fulani hivi kuwa na Tuma. Alimuona anamoyo unaoweza kumsitiri, akabaki salama.

Alhamisi.

Alifika kazini kama kawaida akafanya usafi mpaka akamliza bado hakuna aliyekuwa ameingia. Saa mbili na dakika kumi ndio Jerry akawa anaingia. “Leo na mimi nimekuwa Umi.” Wakaanza kucheka. “Na mimi ni kosa la alamu. Imeniamsha, sijasikia.” Tuma akacheka tu. “Nimelala vizuri, nashukuru kwa maneno ya jana ya faraja.” “Kidogo vile!?” “Kwako, ila kwangu nimefunguliwa kwa sehemu kubwa sana. Nilikuwa nimevurugikiwahuko kichwani, lakini sasahivi najiambia Mungu amenipa nafasi ingine, lazima kuitumia vizuri. Nimepata morari wa kuanza.” Tuma akacheka.

“Mbona umekaa hapo, umeshakula?” “Bado, ila leo hapakuwa pachafu. Nimemaliza kusafisha mapema, nimekaa tu.” “Tuma unajua kujituma! Basi mimi siku ile ya kwanza nikajua mesenja!” Alicheka sana. “Kweli tena!” “Kajiofisi kenyewe kadogo haka! Halafu tuongezewe na mtu wakuja kutufagilia tu! Kweli!?”

“Mwingine angetaka, na Jeremi angekutafutia tu.” “Niliona hakuna sababu. Kama unavyopaona hapa, nipadogo na sio kwamba eti tupo busy wakati wote. Muda mwingi tunakaa tu. Kuna chai nzuri. Karibu.” “Wewe bado hujapata njaa? Tungekula pamoja.” “Sawa.” Wakahamia jikoni.

~~~~~~~~~~~

Wakajiwekea vitu vya kula. Nyama walizokuwa wamebakiza jana yake na maandazi, wakaa kuanza kula. “Umi alipiga simu kulalamikia, kukataa chakula chake jana. Anasema alikuagiza tokea juzi.” Hakumjibu akaendelea kula na macho kwenye simu yake. Kwa kuwa alijua amemsikia, akaona aachane na hayo. Akaendelea kula. Kimya kwa muda.

“Hujaniambia.” Tuma akamwangalia. “Ulifika salama na ukalala kwa wakati au ndio na wewe ukaanza kusoma?” Angalau wakacheka baada ya kumpitisha Umi. “Na vile nilivyokuwa nimeshiba, nilimkuta Eli anasoma, nikamwambia nimemletea nyama. Acha afurahi na vitabu akaweka pembeni. Nimetoka kuoga stori nyingiii!” “Nyama choma hiyo?” “Usifanye mchezo. Nikamwambia apunguze uchangamfu tulale.” Jerry alicheka sana.

“Kumbe anaitwa Eli?” “Elihuruma, ila tunamfupisha. Tunashukuru.” “Mpaka leo bado shukurani za nyama zinaendelea?!” Tuma alicheka sana. “Eli huyo, sio mimi!” “Mmmh! Inatosha bwana. Utanifanya nijisikie vibaya.” “Basi, sishukuru kwa nyama tena.” Wakaendelea kula simu ya Tuma ikaanza kuita. “Umi huyo! Kuwahi kazini imekuwa shida! Acha nimpokee.” Jerry kimya. 

Mjini Kuishi Kwa Akili

“We Tuma? Sasa amesemaje?” Akaona atoke hapo jikoni. “Nimemwambia lakini hajajibu kitu.” “Au hajakusikia?” “Tulikuwa naye jikoni, kwa hakika amesikia.” Jerry alisikia akinong’ona wakati akitoka nje kabisa ya hiyo ofisi.

“Au nimpigie, nimwambie jumamosi tutoke?” Tuma akashangaa sana. “Ni huko kumuonja tu?!” “Nahisi nitakuwa na maslahi naye zaidi. Na mimi nataka niwe mama J mkubwa, itanisaidia kunitunzia ajira.” Kwa hakika Tuma hakutegemea. “Umi!”Akashangaa sana. 

“Sasa kwani burebure na wewe? Si na yeye nampa! Sasa unafikiri mdogo wake akijua kama natoka na kaka yake, si hata mama J ataniangalia kwa heshima! Wewe vipi Tuma?!” Hapo Umi akawa mkali kabisa. Akionyesha si jambo alilokurupuka nalo, ashalifikiria na ndio anachukua hatua.

“Ila kuwa muangalifu Umi, usije haribu. Maana alikataa kile chakula kwa wazi kabisa.” “Nitampa chakula kitamu zaidi ya hicho alichokataa jana, nimnase. Wewe subiri. Nikishamuweka kitandani mara moja tu huyo! Jeuri yote kwisha. Nitampa ya kuweweseka, yeye mwenyewe atabaki akiniota.”

Nitamkoleza huyo mpaka anifuate nyuma kama paka, Chidi haoni ndani. Akishakaa sawa, yeye mwenyewe atanilindia ajira yangu. Mwenzio sijasoma Tuma, mjini lazima kuishi kwa akili. Hawa wanaume wanakuja na kuondoka, lakini kazi kama hii ni ya uhakika. Lazima nijilinde.” Tuma alipoa mpaka akahisi kuishiwa nguvu kabisa. Kile kifuraha chote kilichoibuka jana yake walipokuwa wawili wakila na kuangaliana kwa karibu, na kusifiwa macho mazuri, kikapotea kabisa.

~~~~~~~~~~~

Umi alikata, lakini akamuacha amesimama hapo nje amepigwa butwaa. Akajishangaa anaumia kutoka rohoni, asijue anaumizwa na nini! Nafsi ikawa kama aliyepokonywa tonge mdomoni! Kwa hakika Umi alimtisha. Umi ndoto za wanaume wa jijini. Alifanikiwa kuvunja uchumba wake kwa Mbaki, tena kwa wepesi sana. Leo amempania Jerry! Akajikuta anaumia, akizidi kukumbushwa mbali. 

Akabaki hapo nje kwa muda wa kutosha, mwishoe akajiona ni mjinga na si sawa hata kwa Umi. Jerry yupo huruHana mke. Umi amemuwahi, na kumng’ang’ania. Mbaya zaidi mwenzie nyenzo anazo. Akaamua kujiweka pembeni. Asije jichanganya buree. Akaamua kuendelea na maisha yake kama zamani, kujituliza na kuachana na wanaume. Hata hivyo, akajimbia kwenye ulimwengu wowote aliokuwepo yeye na Umi, hana nafasi ya kushinda kwa mwanaume yeyote.  

~~~~~~~~~~~

 Akaamua kurudi ndani, aendelee na maisha ya kazi yasiyo na maswali na anako aminiwa, na kupewa heshima. Ya mapenzi awaachie kina Umi wanaopenda kwa kichwa wala si moyo. Njaa ilishamuisha kabisa.

Akarudi jikoni alikokuwa ameacha kikombe cha Milo na sahani ikiwa bado na nyama pamoja na andazi. Hakutaka kukaa tena, akawa anakusanya vyombo vyake asafishe. Jerry alimuona vile alivyoingia na amebadilika. “Kwema?” “Kwema. Inabidi niende stoo, kuna mambo yakuweka sawa.” “Sawa.” Akatoa vyombo vyake na kutoka akiwa amemuacha hapo jikoni tena bila ya kumtizama au kumuaga. Akajua kuna jambo halijakaa sawa. Aseme nini hata na yeye hajui kipi kimemsibu!Akahamisha makazi stoo. Akaenda kukaa huko akishindwa kurudi kabisa ofisini. 

~~~~~~~~~~~

Umi wa Chidialiyekwisha fanikiwa hata kumpata Mbaki, akimtoa Tuma tonge mdomoni, sasahivi amehamishia nguvu kwa Jerry. 

Hajawahi shindwa kuweka mwanaume aliyempania kitandani. 

Anauzika bila kelele nyingi. Kila aliyewahi kufika hapo na kuhudumiwa na Tuma, huchanganywa naye mpaka atokee Umi. Basi Tuma huwekwa pembeni na Umi kuibuka mmiliki.

Baada ya muda mrefu wa kufungia moyo mapenzi, ni jana yake tu, tena usiku, hata masaa 24 hayajamalizika tokea Jerry kufanikiwa kumtoa hofu, na kuanzisha kijihisiafulani moyoni mwake, Umi kama mwewe kwa kifarangaanapita tena kunyakua.

Itakuaje?

Dorothy & Jo?

Usikose muendelezo wa Mahusiano ya Mina&Raza kwenye malezi ya mtoto wa Pius. Kila uhusiano hupimwa. Kipi kipimo chao?

Je, safari hii familia ya Ruhinda  itaweza kusimama tena?

Inaendelea…

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment