Kwenye saa 12:15 jioni akatoka. Akamkuta Tuma ametulia kimya kwenye simu yake. “Naona leo mmeuza vizuri kweli!” “Umi huyo! Akibahatika, anabahatika kweli. Na kesho naona amepata tenda nzuri. Kwa hiyo kesho patapendeza zaidi. Mzuri sana kwa masoko na anafahamiana na watu wengi.”
“Nilikuwa nikiangalia mashine za kusafishia magari.” Tuma akakaa sawa. “Kumbe kweli umeanza kufanyia kazi!” “Kwa haraka sana.” Mara baba J akaingia, mdogo wake. “Vipi?” “Nimeleta mzigo kwa imani tu nikijua Tuma atakuwepo. Twende ukanifungulie stoo niweke matairi. Mama J, amenituma nishushe hapa.” “Sasa si vijana wote wameondoka?” “Muda mbaya, sikutaka kusumbua mtu. Nitashusha mwenyewe na mlinzi. Sio mengi.” Tuma akachukua funguo na kutoka. Jerry naye akafuata.
~~~~~~~~~~
“Nimezungumza na yule mpangaji. Nimemwambia nampa pesa ya miezi mitano iliyobakia. Nampa mwezi awe anahama pale.” “Nilikwambia usiharakishe Jeremi!” “Ile nyumba ni yetu sisi. Hata bro ameona sio sawa ukaishi kwa kujibana wakati nyumba ipo! Itakuwa hamna maana ya kuwepo ile nyumba kama haitusaidii sisi wenyewe. Mpangaji mwenyewe analipa kwa shida. Halafu mama J alipita pale, anasema ameharibu. Sio kama ilivyokuwa. Wanapika na mkaa, tena mpaka ndani! Hapana bwana!” Tuma akawa anasikiliza huku wakienda upande wa pili ilipo gereji yao na stoo.
“Akitoka tu yeye na familia yake, inabidi ukarabati mwingine wanguvu kuirudisha kama ilivyokuwa. Hakuna tena kuipangisha. Inatosha.” Akagundua Jerry hajajibu tena. “Kwa hiyo jipe kama miezi miwili tu.” “Acha kuwa nawasiwasi wewe! Hata bro, nimemwambia. Ninapoishi sasahivi sio pabaya.” Kisha akawa kama amekumbuka. “Ila joto!” “Si ndiyo hayo sasa! Kwa nini ukajibane kama mtu unayeanza maisha bwana! Tushatoka huko Jerry! Kurudia hayo maisha ni kukufuru!” Hakujibu.
Wakasaidiana kuingiza hayo matairi. Jerry alimkataza Tuma kubeba, akasema watasaidiana na mdogo wake. Wakawa wanaingiza na kupanga mpaka wakamaliza.
~~~~~~~~~~
“Kuna mtu unafahamiana naye China?” “Wengi sana.” “Kwamba nikiamua kwenda naweza pata wenyeweji?” “Kabisa. Jipange tu kisha unijulishe. Watakupokea na kukutafutia sehemu ya kukaa kwa muda wote utakao kuwa huko.” “Sawa.” Jeremi akaaga na kuondoka kwa haraka, kama anayewahi mahali. Alikuwa na gari kubwa ya ofisi yao wanayobebea mizigo.
~~~~~~~~~~
“Unakwenda China?” Tuma akamuuliza wakiwa wanarudi ofisini. “Nafikiria nikija kutaka kununua mashine za kusafishia magari, niende mwenyewe. Nahisi naweza pata vitu vizuri kwa bei nzuri. Kuliko kuagiza. Ila eneo ndio bado. Kama ulivyosema, kunatakiwa eneo la wazi. Acha nijipange zaidi. Ila nahisi sitachelewa kuanza.” “Utafanikiwa tu.” Akaongea kama kitu cha kawaida, asijue ndio maneno nafsi yake iliyojeruhia inahitaji kusikia kwa wakati huo.
Walipoingia ndani hakukaa tena, akachukua pochi yake ili atoke. “Tuma!” Akageuka. “Nakushukuru.” Akakunja uso na kuuliza. “Kwa nini?” “Chakula. Kinanisaidia sana. Hata ningekuwa na chakula, sijui kupika hata uji!” Tuma akacheka, Jerry akajua hajui undaniwa hizo shukurani na ukweli halisi wa alipo kimaisha. “Nakuwa mkweli Tuma! Jana usiku nililala njaa hivihivi!” “Nitakuletea mtoto wa mama mzazi akufundishe. Bingwa wa uji huyo!” Jerry akaanza kucheka akijua ameelewa kwa sehemu tu. Kumbe Tuma anamsitirikwa kuweka utani, asijisikie duni.
“Dakika tano nyingi, keshaivisha, anakunywa na shule hachelewi.” “Na maandazi?” “Umemaliza. Na uji wake hauna mambo mengi. Maji na chumvi basi. Unga analetewa na mama yake.” “Kutoka kijijini!?” “Usifanye mchezo. Hataki mwanae aumwe njaa. Ndio maana nakwambia usijivunge chakula cha hapa. Kipo kingi. Akija mjini ujue tumeongezewa unga wa ugali. Maharage mabichi na makavu. Chumvi. Ushindwe wewe tu. Na ikitokea wanachinja mbuzi huko kwao. Ujue kuna vipande vitakaushwa, vitaletwa mjini na tembele lililokaushwa.” “Kweli hulali njaa.” “Uwe mchaguzi tu.” Jerry akacheka akifikiria.
“Kwa hiyo wala usijali. Na mimi naponea kwa mtoto wa mama mzazi.” “Najisikia vibaya, nahisi kama nakuharibia bajeti!” “Nikikwambia usijali, usijali kweli. Sijui ni neema! Mwenzio huwa siishiwi chakula, na sikudanganyi. Mama J mpenda maandazi alivyonogewa, akaanza kuniletea unga wa ngano na mafuta. Hivi jana ulipomsikia mumewe ameniletea mizigo, hivyo pia vilikuwepo. Nikikwambia nina chakula kutoka kijijini, jua hata mwezi haujapita tokea mama atuletee. Sili nyama kwa kuwa najibana tu, ili mwanae akitaka jambo nisikwame na kuna mahali najenga kibanda changu.” Jerry akashangaa sana.
“Alifaulu tena shule ya palepale kijijini. Sasa kwa kuwa anapenda sana shule, nikamuhurumia maana ndio ilikuwa shule mpya, haina hata walimu wa kutosha, nikamuhamishia huku mjini. Sikupata uhamisho. Anasoma shule ya kulipia.” “Wewe ndio mlipa ada?!” “Kwa silimia 100. Na nikikwambia anasoma vitabu, hakika anasoma. Sasa naona bora huyu msomaji kuliko angekuwa mvuta bangi.” “Unafanya vizuri Tuma! Mpaka kujenga!”
“Kidogokidogo. Naona kama hii kodi ninayomwaga kwenye majumba ya watu ni nyingi sana. Bora niwe na kwangu tu. Maana hapo tunapoishi, mama anapokuja kutuona ni mtihani! Chumba kimoja na sebule! Padogo kwelikweli, lakini hiyo pesa ninayowalipa! Mpaka inauma roho.” “Hongera!” Akacheka.
“Acha nikapumzike. Ila kuhusu chakula, wewe jilie tu wala usifikirie mara mbili. Kipo. Na hivi nimeshajua hupendi ugali, nikifika nyumbani, wakati naoga, nakuwekea wali, mpaka nalala, vitakuwa vimeiva.” “Usisumbuke!” “Wala si kusumbuka. Mama J mpenda kula na mimi. Akifika hapa akinikuta nakula jua hatapakua chake wala hatauliza. Anaosha mkono anaendelea hapohapo aliponikuta nikila. Na usifikiri ni tonge mbili!” Jerry akacheka.
“Umi huwa anamwambia mpaka akomboleze sahani ndio ananyanyuka. Sasa alinipa mashine ya kupikia wali. Natumbukiza hapo mchele, maji mafuta na vikorombozwevingine, unajipika wenyewe mpaka mwisho. Ndio maana nakwambia chakula hapa wala si chakufikiria, au kujivunga, ushindwe tu wewe. Na usifikiri ni wewe peke yako ndio unayekula chakula cha jumuiya. Sisi wote tunaponea hapahapa. Hakuna wakukuuliza mbona umekula sana au kidogo, nguvu yako tu. Na ni cha wote. Kikiisha leo, jua kesho kitaongezwa. Na sisumbuki kupika maana ugali ninaye mpishi.” “Mtoto wa mama mzazi?” Akauliza akicheka.
“Hapa nikifika nakuta alishasonga upo kwenye poti. Acha nitoke. Usiku mwema.” “Na wewe Tuma.” Alihakikisha amemtaja kabisa kama kumtambua yeye kama yeye. Tuma akacheka na kutoka. Akagundua anaakili iliyokomaa sio kama Umi. Anamambo mengi makubwa ndani yake, na moyo mkuu. Akala tena wali na maharage. Akabeba na maandazi ndipo akatoka na yeye kwenda kupumzika.
Jumatano
Kama kawaida akamkuta Tuma alishafika. “Kweli wewe hutaki kusumbua matajiri.” “Hata kidogo. Mapema sana, nadamka kupita humo mabarabarani, ili kuwapisha wenye nazo.” Mara mama J akaingia. “Mbona leo mapema sana?!” “Tuna safari mchana. Nataka nikamilishe mambo mapemaa. Niambie. Mzigo alioleta jana baba J, utatosha au nitakuharibia mahesabu ya mpaka jumamosi?” “Ijumaa mama J!” “Sawa ijumaa. Nishachanganya.” “Iwe kweli ijumaa, lasivyo jumamosi nitakwama.” “Kwanza nitakuwa nimerudi. Sitakaa sana.” “Sawa.”
“Jana nimekuta msichana wangu amepika nyama nzuri hiyo, nikasema lazima uje uonje.” Jerry akashangaa sana haya mahusiano yao. “Mbona udumu!” “Sio nyingi na wewe, usianze kufurahia.” “Hata finyango! Nashukuru.” “Nakuwekea jikoni. Ni nyama ya foili. Na shemeji yangu leo nimedamka nikampikia vinono, ajilambe.” Jerry akacheka.
“Nimekutengenezea Branch ya nguvu!” “Nakushukuru. Asante sana. Ila usinge hangaika!” “Wewe unamjua Jeremi kwa kupenda kula. Bila hivyo siku ya kazi inakuwa ngumu sana kwangu. Anakulalamikia njaa, mpaka huwezi kufanya kazi. Sasa kwa kuwa nilijua naanzia hapa, ndio maana nimeona nikutengenezee na wewe. Na usijali, hunisumbui.” “Nashukuru.”
“Mle mshibe.” “Nitambakishia na Umi.” Tuma akaongeza kusudi tu kumchokoza. “Ale hapa ili akose sababu ya kutoka?” Tuma akaanza kucheka. Jerry akajua kumbe anamfahamu. “Ameniambia siku hizi nyinyi damudamu.” Akaguna. “Wewe utamuweza Umi? Jana ananipigia simu za mteja, namuuliza kwani alifika kazini saa ngapi? Maana ndio zake.” Tuma alicheka sana.
“Kumbe unamjua?” “Halafu akili yake ilivyo ndogo, yeye hajui kama mimi namfahamu sana tu. Akanizungusha kwa maneno mengi weeee. Namsikiliza tu.” “Ila kaleta kweli mteja.” “Najua. Kwa hilo tu, namshukuru. Na hana kiburi. Mwepesi sana wakuomba msamaha.” Wakaanza kucheka.
“Siku ile Jeremi aliniambia hivi, mambo yangu na Umi niwe namalizana naye mwenyewe lasivyo atakuja mvua suruali mbele za watu.” Walicheka, walicheka sana. “Umi!” “Halafu akianza kulia na kupiga magoti utafikiri sio yeye!” “Mnyonge wake Jeremi. Atajiliza wee huku akimpa maneno ya uchungu.” “Huku amemshika suruali! Basi utamuhurumia baba J. Yupo kama hajui tena afanye nini! Umi analia kapiga magoti, mkewe kasimamia pakali, Umi aondoke.” “Halafu lilivyo jinga lile toto, hapohapo unamsamehe, anaanza stori na wewe aliyekuudhi mpaka mwisho, yeye keshasahau kabisa!” “Umi! Huwezi mkasirikia. Na ujue mteja wa jana kamtafuta sababu nilimwambia umepita, umemkosa.” “Nilihisi tu kuna jambo.” Jerry akawa anasikiliza tu.
“Sasa jana kaja na sababu gani?” “Ajali mbaya sana barabarani.” Jerry akadakia nakufanya Tuma acheke. “Kumbe unamsikiaga?” “Sana tu.” “Na Umi kwa kutunga sababu! Ajali hiyo mbona sisi hatukuiona?” “Si ndio kwa kumkamata uongo nikamwambia mmeshapita na hamjasema kama kulikuwa na ajali. Ndio kubabaika na kuleta wateja! Amesema leo atawahi.” “Usimwambie kama nasafiri. Ujue na yeye ndio ataenda likizo.”
“Sithubutu. Amesema hili juma lote atakuwa anawahi.” “Hata leo hatawahi. Na kumtia tumbo joto, akifika tu hapa, mwambie nimemwambia akifika tu, anipigie.” “Atamuua mama J!” “Bila hivyo hatafanya kazi. Ukijisahau tu kwa Umi, jua ndio unampoteza. Mwambie anipigie. Asinitanie.” “Ataanza kumpigia simu baba J, ampange.” “Sasa mwambie simu ya huyo baba J, nitakuwa nayo mimi.” Wakaanza kucheka, akatoka.
~~~~~~~~~~
“Kumbe wote wanamjua Umi?” “Anasomeka kama kitabu. Na huwezi kumkasirikia. Wanatibuana hapa na mama J, mkombozi wake baba J. Akianza kulia hapa, mpaka baba J anakuwa mwekundu.” “Analia nini sasa?” “Anakuwa amefukuzwa kazi na mama J, anamtaka atoke muda huohuo. Na yeye hapa anapapenda sana.” “Sasa kwa nini? Au ndipo anapokutaniana na watu wake?” Ikawa kama ameshamsoma Umi akamuelewa. “Na pia anasema wote aliowaacha shule wakihangaika na elimu, eti anawaringishia kuwa walikazana kusoma, lakini yeye anakazi nzuri sana, ya ofisini.” Jerry akacheka akitingisha kichwa.
“Sasa akiwa amefukuzwa na mama J, anataka aondoke, anamgeukia mumuwe anamwambia yeye hajasoma. Wazazi wake walifariki tokea mtoto. Hapo analia kwelikweli!” “Na nikweli hana wazazi?” “Muongo tu. Anaye mama. Basi hapo amemshika baba J suruali anamng’ang’ania kuwa hana pakwenda. Yeye yatima. Kwao anategemewa.” “Na ni kweli?” “Muongo! Hana hata anayemtegemea ila mwili wake tu na starehe.”
“Basi eti yeye hajasoma sababu hajabarikiwa wazazi kama mimi. Hakuchagua yeye kuwa yatima! Angetamani kuwa kama kina J, yaani wanae baba J, lakini Mungu amemnyima. Kusudi tu kumtia hukumu baba J, anajua mpole. Atalia hapo wee! Huku anamwambia eti kumfukuza yeye ni kumfukuza yatima.” Jerry akazidi kucheka.
“Mama J, anamwmabia hana uyatima wowote, ashapitisha muda wa kuwa yatima, aondoke. Basi analia hapo akisihi wee, mpaka baba J anamuhurumia na kumbembelezea. Akisamehewa, dakika hiyohiyo keshachangamka, anamtaka mama J urafiki.” “Sasa hapo anakuwa amefanya nini?”
“Hutamuweza Umi. Cha kwanza usimpe kazi nzito inayohitaji utekelezaji wa haraka, au kumfanya akae chini afikirie sana. Kwanza akipewa kazi jua atasahauhapohapo, hafanyi. Na si kwamba hafanyi kwa sababu mjeuri! Si jeuri hata kidogo na hataki kumuudhi mtu. Ila kichwa kina mambo mengi, hakumbuki.” Akamuona anaanza kucheka.
“Nini?” “Siku hiyo alipolia hapa, alitumwa kule stoo amwambie kijana wa stoo kuwa asubiri mzigo utaletwa. Mama J na mume wake wakamsisitiza, wakaondoka. Sasa kule gereji wanamjua. Akitokea tu wanaitana wote, wanaacha kazi kabisa wanaanza kumchokoza. Na yeye anapenda kuongea. Akafika kule asiseme alichotumwa, akaanza kujibishana nao, akitukanana nao. Zikaanza stori. Akaongea wee mpaka akamaliza, kasahau alichotumwa. Muda wake ulipofika kabeba pochi yake, kaondoka.”
“Kama kawaida yangu yakutoka kwa kuchelewa. Nimekaa hapa mlinzi ananigongea, mzigo umefika. Nikamwambia awafungulie, kuna mtu anawasubiria kule waende. Baada ya muda akarudi tena hapa, ananiambia kule hakuna mtu hata mmoja. Sasa yule kijana aliyekuwa akifanya stoo, anakoishi mbali. Nikampigia simu akasema yeye hawezi kurudi. Hata hivyo alikuwa jeuri sana, hapatani na vijana wenzie kule, alikuwa akiwadharau. Akanikatalia na kunikatia simu. Sasa nifanyaje kama si mama J?” “Haiwezekani!” “Sikuwa na jinsi! Ilikuwa washushe mzigo au waondoke nao.”
“Nikampigia na kumuomba arudi. Bwana mama J alikasirika, halafu yule mwanae mdogo anayemdekeza alikuwa mgonjwa. Weee!” “Kumbe mnajua?” “Mama J hajiwezi kwa yule mtoto. Kama yai lisipasuke! Turudi kwa Umi. Sasa kesho yake watu wote wamekusanyika hapa, mpaka baba J siku ile alikuwa hapa, kasoro Umi tu ndio alikuwa hajaingia. Akasubiriwa mpaka saa tatu ndio anawasili. Akakuta wamejaa hapa, wanamsubira yeye.”
“Hilo nalo ni kosa jingine.” “Sawasawa. Na ujue hapo sio mara ya kwanza. Mchelewaji aliyekwisha pewa onyo zaidi ya nitakavyokumbuka. Kesi ikaanza sasa. Iweje mtu wa stoo aondoke, wakati Umi alimwambia abaki!”
“Umi anaulizwa, hakumbuki. Kwanza ukumbuke hapo alishapaniki kuchelewa na kumkuta baba J na mkewe hapa, na kijana wa stoo wanamsubiria yeye. Utachoka.” Tuma akaanza kucheka mwenyewe. “Nini?” “Eti anamuuliza mama J, mbele ya mumewe na mimi niliyekuwepo jana yake nikisikia akitumwa, eti kama kweli alimtuma. Bwana alimcharua mama J, akamwambia hapohapo aondoke. Kilio kama amefiwa. Eti anamwambia baba J, yeye alipokuwa mdogo aliugua sana, tena ugonjwa mbaya, ndio maana kichwa chake hakikumbuki mambo.” Wakazidi kucheka.
“Na ni kweli?” “Muongo. Muongo kwelikweli. Na mbaya zaidi siku moja mama yake alikuja hapa, baba J hakuamini.” “Acha!”
“Hivyo unavyomuona Umi, mama yake mtupu. Ila ni wale wanawake wa mjini. Maneno mengi kama Umi. Sasa mama J akamuuliza mama yako kafufuka? Hana mbavu. Ikabidi amsimulie mama yake.” “Mama yake akasemaje?” “Akaanza kumtukana hapahapa kwamba anamuua, mwishoe atakuja kufa kweli. Umi analaana kama za shangazi zake. Anataka kumuua. Sisi tumekaa hapa, wanagomba pale. Umi kasimama, amempisha kiti amekaa. Akasema siku nyingine akisema amekufa, apigiwe simu. Yeye si mfaji. Baba J, hoi. Hapo anacheka Umi, hana mbavu. Ila kweli baba yake alifariki.”
“Ndio maana hakusoma?” “Mama yake alisema siku ileile kuwa Umi hakusoma si kwa sababu ya uwezo, alikataa shule kidato cha pili.” Jerry alicheka sana. “Hapohapo?” “Hapohapo mbele ya Umi mwenyewe. Umi hana mbavu.”
“Alivyo Umi sasa, siku hiyo alipokuwa akilia wakati anafukuzwa, akajirudi kwa mama J, kamlamba mpaka akamsamehe, yule wa stoo akaishia kufukuzwa yeye kazi, ndio nikaachiwa mimi funguo. Hakuajiri tena mtu wa stoo, amebakia na Umi wake wakisumbuana. Twende tukapate kifungua kinywa siku ianze.
~~~~~~~~~~
Wakapata wakati mzuri hapo jikoni. Angalau siku hiyo Jerry akapata kifungua kinywa chakueleweka. Na kweli alimuandalia vinono na kumpangia vizuri.
Mkasa Wa Umi Na Kuchelewa.
Saa tatu na nusu ndio akawa anaingia. “Gari iliniharibikia katikati ya barabara, ndio…” “Yaani wewe usijieleze kwangu. Hayo maelezo mama J anayasubiri huko upande wa pili wa simu.” Akatulia kwanza, eti kisha akauliza. “Mama J yupi?” “Kwamba gafla wewe humjui mama J? Alipita hapa mapema sana.” “Tuma ujue utaniua wewe!” “Kama nakudanganya, kaangalie nyama jikoni, ameleta asubuhi, nimekubakishia.” Akakimbilia jikoni.
“Huyu mwanamke leo atanifukuza moja kwa moja wala hapatakuwa na kusikilizwa.” “Hivyo unazidi kuchelewa maana amesema muda utakaofika tu hapa, umpigie.” “Namuanza baba J.” “Na alijua. Amesema atakuwa na simu ya mumewe!” “Mungu wangu!” Akamuona anatoa simu.
“Nisaidie mama yangu mzazi!” Tuma kimya anamsikiliza. “Mpigie simu mama J, mwambie unaumwa, na mimi usiku kuchwa nilikuwa kwako nakuuguza.” Yakaanza matusi. “Acha kunitukana mama, nilikuwa naumwa, usiku kuchwa sijalala, nimekuja kulala asubuhi na alamu haijaniamsha.” Matusi mengine kwa muda, akamsikia akijitetea tena.
“Sio mimi mama yangu!” Akanyamaza akisikiliza. “Mimi sijalaaniwa. Labda ni vile nilivyologwa. Nisaidie mama yangu mzazi. Nitafukuzwa kazi.” Tuma akabaki akimsikiliza akijua maneno anayopata kutoka kwa mama yake.
Kisha akaongeza. “Ile hela uliyoniomba nitakupa, tena leoleo.” Tuma akaguna asiamini. “Ukinirekebishia kwa mama J, nakupa ile hela na ukimwambia jioni unaomba niwahi kutoka nikakununulie dawa, ndio sikudai kabisa.” “Haaa!” “Sasa nini na wewe Tuma? Kwa hiyo unataka nifukuzwe kazi?” Tuma akabaki akitingisha kichwa kumuonyesha anakataa.
“Umi, nakuonya. Usimuingize mama yako dhambini maana mama J, anakujua. Utamtibua zaidi. Wewe piga simu msikilize kisha omba msamaha.” “Tuma!” “Haki tena nakuhakikishia. Safari hii acha uongo. Jaribu kwa ukweli, anaweza hata kukata simu asiamini kama umesema kweli. Vinginevyo atakufukuza na utamvunjia mama heshima.” “Basi mwaya mama.” Akakata.
“Lakini sikuchelewa kwa makusudi. Nilipitiwa na usingizi alamu haijanimsha.” “Hizo ni sababu nyingi sana na unazidi kuchelewa. Jaribu ukweli safari hii.” “Ndio ukweliwenyewe huo na Chidi ndio anayeniponza. Nimemwambia akisababisha nifukuzwe kazi namuacha kabisa na...” “We Umi, unazidi kuchelewa kwa kujieleza kwangu.” “Nisaidie Tuma.” “Mie huyu!?” “Kesho nawahi. Nakuhakikishia kesho nawahi na leo sitoki.” Akaanza kulia.
“Nitaenda wapi mimi nikifukuzwa? Mimi sijasoma, hakuna mtu ataniajiri bila cheti. Kule kwa mama amesema nikifukuzwa hapa, kwake nisirudi tena. Nisaidie. Wewe mama J anakusikiliza. Anza kumpigia wewe halafu nipe.” Akamsikia kweli analia. Ikabidi atoke. “Kuna nini!?” “Nishaumbuka mjini mimi! Na kosa ni alamu. Haijaniamsha kaka yangu. Lakini Mungu wangu nishahidi nilipanga niwahi.” Jerry akashangaa analia kabisa, anambembeleza Tuma ndio apige simu. Hakuamini.
“Naomba mpigie mama J. Tafadhali Tuma.” Yaani Jerry mwenyewe akaingiwa huruma. Ikabidi Tuma apige tu na kuweka kwenye spika.
“Umi kakutuma unipigie?” Moja kwa moja akaenda kwenye swali. “Nimechelewa mama J, nimekosa mimi. Simu ili,…” “Unaanza kudanganya Umi.” “Pale mwanzo sijadanganya. Kwanza leo nitachelewa kutoka. Yule mteja wangu alisema atachelewa kuja. Ndio nikaona nibakie tu mwenyewe mpaka mwisho atakapokuja. Na ameongeza oda. Nilikuwa nikizungumza naye barabarani. Mimi siwezi kukuangusha mama J.” Kama si yeye.
“Unakumbuka mara ya mwisho kuzungumza na wewe, nilikwambia kuchelewa kwako ni kujifukuzisha kazi?” Akazidi kulia. “Mimi wananiloga ndio maana kila nikitaka kuamka nakua siamki, napitiliza usingizi kusudi tu nifukuzwe kazi. Nina usingizi wa kushakiziwa.” Mpaka Jerry akaanza kucheka akimwangalia.
“Umi! Umi wewe mtoto!” “Ni shetani mama J. Na mpaka mama alikuomba uniombee.” “Sasa nisikilize Umi. Wewe huna shetani na wala huna anayekuloga.” “Uchawi upo mama J! Na mimi wananifanyia kusudi kabisa kuniharibia.” “Sasa nisikilize Umi, nina mambo mengi unazidi kunipotezea muda.” “Nanyamaza.”
“Nina nafasi yako ya mwisho, ambayo ipo huku.” “Mungu wangu mimi jamani!” “Nimekwambia nini?” “Nanyamaza.” “Sasa hapa kuna barua zako mbili. Moja ninayo mimi, yakuanza kazi huku kwa makubaliano mapya. Kila siku saa mbili kamili asubuhi uwe ulishafika kwenye meza yako umekaa. Na katika kazi hii mpya unanafasi mbili tu zakuchelewa. Ukichelewa mara ya tatu, nisikuone hapa.” “Masikini mimi!” Yaani akawa anajihurumia mwenyewe.
“Sasa basi, ili uipate hii ajira, uwe umefika hapa muda niliopo mimi ili uipate hii barua. Usiponikuta mimi, ujue utakutana na barua ingine ambayo niyakufukukuzishakazi.” “Nakuja mama J. Mimi nataka barua yako, sitaki hiyo nyingine.” “Ni juu yako. Ukichelewa jua safari hii sitakusikiliza sababu yeyote ile utakayochagua kunidanganyanayo.” “Sichelewi, ila nina wazo.” Wote wakatulia kumsikiliza wazo lake.
“Kwani nafasi ya hapa umeshaijaza?” “Umi unachelewa wewe!” “Ni wazo zuri mama J, ungenisikiliza tu!” “Unataka nini?” “Labda nije nichukue hiyo barua, halafu mtu unayetaka aje hapa, tubadilishane naye. Mimi nibaki hapa, yeye …” Simu ikakatwa. “Mama J? Mama J!” Akaanza kuita, kimya.
~~~~~~~~~~
“Amekata! Mimi kule mbali sana, hakika saa mbili kamili ni kujaribiwa kabisa. Atanifukuza tu kazi.” Akawa anatilisha huruma. “Sasa Umi, jua mama J na mumewe wanasafiri leo. Ukiendelea kujilalamisha hapa bila kuondoka, utamkosa kweli!” “Au mwambie wewe kuwa unataka kufanya kazi na mimi, tunaelewana.” “Umi! Utamkosa mama J, wewe!” Akanyanyuka haraka.
“Ni hivyo mama J, haniamini. Ila uchawi upo, na mama alimwambia kabisa. Mimi walinilogaga! Yaani unategesha alamu, lakini haiiti!” Akawa analalamika huku akikusanya vitu vyake. “Watu wananionea wivu mimi. Kusudi tu niharibikiwe. Sasa mama J naye mtu wa Mungu badala anipiganie kunitoa kwa shetani, ndio ananisukumiahukohuko.” “Umi!” Tuma akamshitua. “Naondoka! Na njiani namnunulia zawadi.” “Umi!” “Sichelewi! Kwani si namnunulia hata pipi tu kwenye mataa! Hamna wakunihurumiamimi! Nakua natupiwa mimi lawama wakati nimelogwa.” Akatoka akilalamika.
~~~~~~~~~~
Jerry akabaki akitingisha kichwa. “Kwani huyu Umi, anamiaka mingapi?” Tuma akaanza kucheka. “Ni mwili tu huo. Lakini sidhani hata kama amefikisha miaka 21. Ila amewahi sana maisha. Aliondoka kwa mama yake anavyosema akiwa hata hajatimiza miaka 18. Sasa acha akamchangamshe kidogo.” “Kwamba atamrudisha!?” “Haraka sana. Huko atawakera mpaka basi. Sema wewe ulimuwahi mapema sana! Lasivyo asingekauka ofisini kwako na kila aina ya sababu. Iwe anatoka au anaingia, ana jambo lakujieleza.” “Na haishiwi safari.” “Ewaa! Hawezi tulia sehemu moja. Tukiwa na mama J au mumewe hapa, anaanza kuomba kutumwa.” Alicheka sana Jerry.
“Wapi?” “Popote tu, ilimradi atoke, asikae hapa siku nzima. Yupo radhi atumwe hata sokoni, ili tu asikae sehemu moja kwa muda mrefu. Na huwezi kumkasirikia muda mrefu Umi. Si umeona wewe mpaka umemuhurumia? Sasa anamuwezaga baba J. Nakwambia mdogo wako anakuwa mwekundu, mpaka unamuonea yeye huruma, unataka ugomvi wao uishe, kuwe na amani, na yeye atulie.”
“Sasa kwa nini habadiliki?” “Anavyosema yeye anakuaga na usingizi mzito sana.” “Hapa kasema shetani.” Acha waanze kucheka. Walicheka sana. “Umi! Hutamuweza kwa sababu. Mama yake alikuja hapa akawa anasema eti hapa kuna Mungu ndio maana amekaa. Umi amelogwa, hawezi uza hata nyanya akafanikiwa. Kila mahali anafukuzwa.”
“Mimi nahisi nipo kama mama J, hana shetani ni nidhamu tu hana.” “Basi ndio maana anamkazania hivyo.” “Kwamba hatamfukuza?” “Anamuhurumia. Ujue kweli hana hata cheti cha sekondari! Anaona akimfukuza ndio ataharibikiwa zaidi. Anamchachafyahivyohivyo. Utakuja kumrudisha tu. Utamuona. Kwenye siku 10 hivi anakuwa mtoto mzuri. Atawahi na kutulia. Ngoja sasa asahau! Anaanza tena. Na hapo mpaka mama J anaondoka leo, watakuwa washapatana. Huwezi mkasirikia Umi.”
“Unafikiri kweli atamnunulia hiyo pipi?” “Akili yake inavyomtuma ndivyo atakavyofanya. Atakuja kutusimulia mama J. Ila atakwenda kumpooza huko, mpaka watapatana tu. Na hivi baba J yupo hukohuko, atawatuliza wote.” Jerry akarudi ofisini akicheka.
~~~~~~~~~~~
Pakawa na utulivu wa aina yake. Wawili tu hapo ofisini. Hamna kelele. Kwa kuwa walishapata kifungua kinywa kila mtu akatulia mezani kwake. Kimya. Tuma alitoka mara kadhaa kwa kazi za stoo. Kwenye majira ya saa sita akawa amerudi mezani kwake.
Atafutaye Asiyechoka
Saa saba akaingia mtu na chakula akaulizia Jerry. Ikabidi kwenda kumgongea. “Kuna mtu ametumwa kwako. Nimwambie aingie?” Jerry akakunja uso na kusimama. Tuma akatoka akiwa ameelewa anamfuata nyuma.
“Karibu.” Tuma akawa anajiangalizia tu. Alionekana ameleta chakula kinanukia ofisi nzima. “Nimetumwa chakula kwako. Nikiweke wapi?” Jerry akakunja uso akimsogelea. “Subiri kwanza. Nani amekutuma?” “Umi.” Tuma alishituka, kwa hakika hakutegemeakama Umi angefanya kweli!
~~~~~~~~~~~
Inaendelea…
0 Comments:
Post a Comment