“Tuma unamaneno!” “Sikuongopei! Wengine ajira zetu zimeandikwa kwa penseli. Basi ni kazi ya kukolezea kila siku ili usifutwe. Kapate kifungua kinywa, nimekuja na maandazi mengine?” “Kwamba yalibakia huko yalipotoka?” “Kabisa. Mahesabu makali mjini. Lasivyo unaumbuka. Karibu.” “Sasa sisi si tunakuharibia?!” “Familia za kiswahili mlo hauwi wa mtu mmoja. Nenda tu kale, na ya kesho yatakuwepo mpaka jumamosi. Akipita mama J akisomba yote, tunahamia kwenye mkate. Wewe nenda kale.” Jerry akacheka akielekea jikoni. Kweli njaa ilikuwa imemkamata.
Alikotoka kwenye ndoa yake asubuhi lazima mayai na soseji. Maziwa moto na kitu cha nyongeza kilichonunuliwa na Sandra. Sambusa, au kitumbua, au chapati. Inategemea na Sandra. Na mchana mkewe alikuwa akituma mtu alete chakula chao wote wawili. Hakuwahi kujifikiria chakula. Kwa hilo akakumbuka ya kale.
“Sasa huko unakotoa haya maandazi, wanaobakia wanakula nini?” “Uji na hayohayo maandazi.” Alicheka Jerry, alicheka sana. “Tuma!” “Unaweza sema nadanganya. Yaani watu wengine wanakunywa chai asubuhi, lakini mwingine anaona chai haitoshi. Anaona apike uji kabisa, na maandazi.” Akazidi kucheka. “Nani huyo?” “Mtoto wa mama yangu mzazi.” Akamfanya azidi kucheka. Alicheka Jerry asimalize, na yeye Tuma kimya akiguna huku akisafisha.
“Hivi leo nimekuja na kiporo cha ugali na maharage.” “Kwamba?” “Mama yake akija mjini lazima atubebe unga.” “Ndio zawadi?” Jerry akauliza. “Tumbo la mwanae! Hatuishiwi unga wa ugali. Na uzuri mwanae hana makuu! Akishakuona unalia shida, yeye hata uji wa chumvi anachemsha anakunywa, bora umpe nauli ya kwenda shule, mlipie tution na mnunulie vitabu, hana makuu. Utafikiri maktaba!” Jerry akazidi kucheka.
“Mtoto wa mama yako mzazi huyo?” “Mwingine nani? Nishamwambia nikiishiwa kabisa nakusanya vitabu vyake naenda kuuza!” “Ndio mali pekee uliyonayo?” “Umemaliza. Mshahara mzima anaonilipa mama J, ni vitabu. Sasa unajiuliza, usomaji gani huu au Mungu kaamua kunikomoa!” Jerry hana mbavu.
“Yupo kidato cha ngapi?” “Hata sijui! Nitakuulizia.” “Haiwezekani Tuma!” “Ni ngumu kumuelewa yule mtoto. Kama mtu mzima, halafu kama mtoto!” “Kwamba haeleweki?” “Wewe unafikiri nabeba ugali maharage kazini hivihivi? Anasoma vitabu vya watu waliofeli shule.” “Kwahiyo wewe kazi ni kutoa tu pesa?” “Nilijaribu kuelewa na shule yangu ya VETA, ikashindikana.” Alicheka Jerry, alicheka sana.
“Nikaona nifanye marefu kuwa mafupi, niwe natoa tu pesa. Siku hizi siulizi tena. Ukifika hapo kwetu kuna vitabu, sahani ya chakula unashika mkononi. Anasoma usiku kucha na hataki maneno mengi. Ndio maana najionea bora nikae tu hapa. Nikifika kule nikuoga, najifunga kanga machoni nalala.” “Tuma?” “Sasa nifanyaje? Chumba ni kimoja, mwenzio anasoma hamalizi! Kumkataza huwezi, katumwa mjini kusoma. Mama yake anamfuatilia kutaka maendeleo yake. Sasa mimi ndio nionekane namkwamisha?” “Huwezi.” “Basi ndio maisha hayo. Khanga ikitoka usoni, jua ndio muda wako wakutoka kitandani umefika, siku inaanza.”
“Haendi shule?” “Tena amka yake lazima na wewe utaamka tu. Chumba kimoja na sebule!” “Na mtoto wa mama yako mzazi?” “Huyohuyo sina mwingine. Chumba kimoja na sebule. Tukafanikiwa kupata na bafu letu humohumo ndani. Sasa muda wa bafuni huwa haupendi hata kidogo.” “Unamchelewesha?” “SANA. Na mimi ndio muda wangu wakumlipiza kisasi. Lazima aoge asubuhi na usiku.” Jerry akazidi kucheka.
“Mbona utajua kama anaoga!” “Maji?” “Uswahilini makopo. Halafu kama namuhisi anagongesha kusudi tu, kuniambia naoga. Na oga yake ni alfajiri, maana anatoka nyumbani kama mimi. Mapema, hataki mtu amcheleweshe huko barabarani akienda safari zake.” “Shule?” Jerry akauliza akicheka.
“Huwezi kumuweza yule. Anaweza akaondoka jumamosi anawahi kitabu fulani, maktaba kuu ya hili jiji. Kisa mimi sina hela ya kukinunua hicho kitabu. Sasa utamkataza?” “Huwezi.” “Huthubutu. Maana pesa ya hicho kitabu ndio mboga ya mwezi mzima. Unaona bora akavifuate hukohuko, na pesa ipone.” Mara Umi akaingia.
~~~~~~~~~~
Amependeza mwenyewe! Jerry akaangalia saa. Saa mbili na dakika 55. “Foleni kweli leo!” Akajiongelesha akiweka pochi akijua wapo jikoni watasikia tu. “Kulikuwa na ajali mbaya!” Tuma akaanza kucheka. Akaenda hukohuko jikoni. “Sasa unacheka nini?” “Umesema kulikuwa na ajali?” “Mbaya sana, tokea saa moja asubuhi, magari yalikuwa hayasogei kabisa!” “Mpigie mama J umpe hizo taarifa zako, maana leo kapita mapema sana hapa.” “Acha kunitisha bwana!”
“Ndipo utakapomueleza ajali hiyo imetokea wapi wakati mnatokea njia moja, na wao wamepita hapa saa mbili kasoro.” “Mtumee!” Akaweka mikono kichwani, Jerry akamtizama na kutoa vyombo vyake pale kwenda kuosha.
“Au niwe nimepishana naye tu?” “Kwamba uwe umefika hapa saa ngapi?” Tuma akamuhoji. “Mbili na robo.” “Ajali hamna tena?” Tuma akamuuliza akicheka hana mbavu, Jerry kimya kama siye aliyekuwa akicheka hapo na Tuma.
“Tuma naye! Sasa si ndio ajali hiyo ikanichelewesha!” “Kwamba wewe siku hizi unachelewa dakika 15 tu?!” “Kweli! Acha nimtafutie mmteja hata mmoja, nikimpigia simu iwe ni ya salamu na habari za mteja.” “Hayo ndio maneno.” Akatoka hapo jikoni, Tuma akaendelea kula, Jerry akarudi ofisini kwake na kurudi tena jikoni.
“Nashukuru kwa kifungua kinywa. Njaa ilikuwa ikiniuma!” “Wewe ukaribie muda na wakati wowote bila kuuliza wala kujali. Usiumwe na njaa. Ukisikia njaa tu, pitiliza jikoni, jitengenezee kitu cha kunywa, chukua mandazi utakayo. Hakuna wa kukuuliza, hakuna pakuripoti. Nguvu yako tu. Na mchana ugali, maharage na tembele. Vipo kwenye friji. Bila kuuliza, jipakulie kwenye sahani, pasha moto, kula. Usiteseke na njaa. Hapa kuna neema ya chakula. Uwe tu mchaguzi!” “Nashukuru Tuma.” “Karibu.” Akarudi ofisini na kutulia.
~~~~~~~~~~
Hakukaa sana, akamsikia akiaga tena. “Nishampanga mama J, nafuatilia soko.” “Sasa urudi na habari njema, Umi. Utamtibua mama J, na yeye atakutimua hapa, muanze kumuingiza baba J katikati na kesi zisizoisha.” “Siku hizi mimi na yeye damudamu. Shoga yangu.” “Sawa!” “Naleta na mteja bwana acha kunitisha!” “Mimi sijakubishia, ila nakupa angalizo. Maana wewe mwepesi wa kuomba msamaha wa machozi, ila huachi kumtibua.” “Kesho tunadamka wote.” Akabaki akimtizama.
“Acha kuniangalia hivyo!” “Utaweza kukiacha kitanda wewe?” “Kwa siku hizi tatu nne, lazima. Lasivyo mama J atanitimua kweli.” “Kiukweli unaenda wapi?” Akamsikia akimuuliza, akaanza kucheka.
“Wewe niambie ukweli.” Akamsikia Tuma akimsisitiza. “Sasa sio uanze kunikaripia.” “Wewe sema ukweli.” “Kuosha nywele.” “Haaa!” Mpaka Jerry na yeye huko ofisini akashangaa.
“Acha kelele Tuma! Leo kunakuaga hamna kabisa wateja! Na jumamosi sijaosha nywele sa…” “Nimekusikia ukidanganya kwamba jumamosi tulichelewa sana kutoka wakati wewe uliondoka hapa hata nusu saa haikuzidi!”
“Narudi bwana Tuma! Nimemwambia yule dada wa saluni nimkute ananisubiria. Sichelewi na wateja pia nitawatafuta. Leo jioni mama J lazima afurahi.” “Sawa Umi.” “Nikuletee nini?” “Wewe acha kutaka kunihonga. Nenda na uwahi kurudi.” “Sasa nimuage au?” “Alikwambia nini jana?” Akaanza kucheka.
“Maisha hapa yatakuwa mazuri sana.” “Ila ujue anakuangalia tu.” “Lakini kweli! Bora nikamwambie nafuatilia masoko, nitarudi.” “Ushakatazwa Umi! Muache.” “Na alivyo mzuri!” “Ushamtamani hivyo! Mume wa mtu ujue.” “Na mkewe alivyo kisirani!” Akazidi kucheka.
“Lakini vya watu pia vinaliwa bwana! Chakula cha jirani kitamu kuliko cha nyumbani. Na huyu anaonekana mtamu kwelikweli. Lazima kumuonja.” “Umeanza Umi!” “Kuonja tu na wewe! Umeviona vidole vyake lakini?” Jerry akakunja uso na kujiangalia vidole vyake huko ofisini.
“Umeanza Umi! Kwamba umeshaangalia mpaka vidole vyake!?” “Nimekwambia naonja tu na wewe! Nikimuonja huyu! Haki ya nani nitalala naota. Sinilikwambia tokea wakati ule?” “Ukasema mkewe anambana?” “Ndio ujue Mungu anavyonipenda!Kanisogezea hapahapa karibu.” “Ushindwe mwenyewe?” “Siwezi. Huyu namchukulia taratibuuu. Atakuja ingia tu kwenye 18 zangu.” “Kama Mbaki?” “Unataka tuanze kugombana wakati hata wewe mwenyewe ulishasema Mbaki ni malaya tu. Kama isingekuwa na mimi basi angekusaliti na mwingine. Au umesahau shoga yangu?” Tuma akabaki akimtizama ila wakaibua maswali kwa Jerry.
“Basi shoga yangu. Mbona hayo tulishamaliza kitambo sana!” “Ndio unazidi kuchelewa.” Akamsikia Tuma akimjibu tu hivyo. “Basi akitoka, ikitokea ananiulizia mwambie ndio nimetoka.” “Maana yeye hapo ofisini kwake hana kamera za getini? Kwa nini usiende jioni ukitoka hapa?” “Kuna mahali nakwenda na Chidi, jioni.” “Si ulisema unamuacha!?” “Nampa siku mbili mbele, utamuhurumia anavyonibembeleza kama sio yeye! Lakini mimi namjua, havina muda mrefu. Ataanza tu majanga yake.” Akamsikia akitoka. Hiyo ilikuwa saa nne asubuhi.
~~~~~~~~~~~
Mpaka saa 6 mchana akawa hajarudi. Ila Tuma akaenda kumgongea. “Mbali na ugali tembele, upo wali na maharage. Nyama kwetu mpaka sikukuu.” Jerry akacheka. “Nakushukuru Tuma. Basi nakuja.” “Wewe ukitaka hata nikuletee ulipokaa sina shida.” “Hapana, nashukuru. Maadamu umeleta mpaka hapa kutokea nyumbani, acha nije nifuate mwenyewe hapo jikoni. Asante.” “Karibu.” Baada kama ya dakika 10 hivi akatoka na kufuata chakula. Akakuta alishakipasha.
“Unaweza kukirudisha kwenye microwave kidogo, kitakuwa kimepoa.” “Haya maharage na wali vinanukia kama pilau!” “Kwa mlo wangu mimi, ni lazima kujiongeza ili kudanganya akili kila siku sikukuu.” Jerry akaanza kucheka tena. “Tuma wewe una maneno sana.” “Nakwambia ukweli, bila kujipoza mwenyewe, utaishi na stress kila siku. Pua zikidhania ni pilau, ubongo hauna jinsi ila kuamini tu.” “Macho?” “Macho rahisi sana kuyadanganya. Unayapeleka vile unavyotaka wewe. Na hivi ubongo ushakubaliana na taarifa kuwa ni pilau, macho unayaaminisha kinachoona ni pilau nyama, moyo safiii!” “Sawa Tuma. Ila mimi napenda sana nyama.” Tuma alicheka sana.
“Huna tofauti na Umi. Kama fisi vile! Wewe punguza njaa. Ukitoka hapa ndio ukale nyama.” Akacheka tu, Tuma asijue huyo Jerry jinsi alivyoishiwa. Hana hata shilingi ya kununulia wali nyama kwa mama lishe. Pesa yote aliyopewa na Jeremi mdogo wake ilishaisha muda tu.
“Wazo ulilotoa jana nimelipenda sana. Nalitendea kazi.” “Kweli!?” “Kabisa. Wazo lako linaakili.” “Mungu akufanikishe. Na ukipata sehemu nzuri, utakuwa ukila nyama kila siku.” Alicheka Jerry, alicheka sana.”
“Tuma!” “Nakuhakikishia.” “Sasa usije mpa mwingine hilo wazo.” “Nani wakuniuliza mimi?!” “Huwezi jua!” “Mie najua na najijua. Hakuna wala usijali. Wakija tu hapa, wakishaniangalia, wanajua ni wa VETA, zaidi ya salamu, hakuna wakuniuliza tena.” “Acha hizo bwana!” “Si upo hapa?” “Kwa muda tu.” “Basi nitakuja kukwambia kama nitaulizwa tena.” “Nikiona kimya?” “Ujue sijaulizwa.” Jerry akacheka akitingisha kichwa.
“Na ukiulizwa usiseme. Waache wakafikirie wenyewe.” “Wala usijali.” “Basi acha mimi nikale huku naweka hilo wazo sawa. Asante sana kwa chakula.” “Karibu na nyongeza ipo kama hutashiba.” Akashukuru na kutoka na sahani ya chakula aliyotoa kwenye microwave baada ya kupasha.
Ubaya Husambaa Kwa Haraka
Baada ya muda akasikia Umi amerudi. “Nina ubuyu!” “Ulete.” Akashangaa wote wanaanza kucheka. Ilishakuwa imetimu saa saba. “Nimekuja na chakula changu nile hapahapa ili nisitoke tena.” Akakaa. “Chidi kanipitishia chakula saluni.” “Nasikia harufu ya kuku!” “Kaniambia ni nusu nzima!” “Kuna ulichompa usiku.” Umi alicheka sana.
“Wewe tulia uolewe na Chidi. Hamtakaa mkaachana nyinyi!” “Haaa! Umenikumbusha. Nimepata habari za huyo bwana hapo ndani.” Akawa amepunguza sauti. “Usimuone yupo hapa kwa mdogo wake, unaambiwa mwanamke kamtimua kama mwizi!” Jerry ikabidi avute sikio.
“Haiwezekani Umi!” “Mungu mmoja! Nasikia kamfukuza na kumpokonya kila kitu mpaka nasikia chupi aliyovaa, anamdai. Yote hayo nimesikia saluni. Kayamwaga mdada anayefanya kazi huko kwenye hiyo kampuni ya aliyekuwa mkewe huyu.”
“Kumbe wao haikuwa kama hivi baba J na mkewe. Vitu vyao vyote ni vyao. Unaambiwa huyu alimuoa yule mwanamke akiwa na mali zake zote. Ikawa kama huyu anamfanyia tu kazi. Ndio kumpelekesha kote kule ulikokuwa ukikuona. Kumbe mkewe ndiye aliyekuwa mwenye mali. Alivyojidai kuleta jeuri, unaambiwa mwanamke kamtimua mchana kweupee! Tena mbele ya wafanyakazi wote. Nasikia nusura amtoe nguo alizovaa! Kampokonya kila kitu, kamtoa pale mikono mitupu na onyo la asifike kwake.” Tuma akashangaa sana.
“Kwamba amemfukuza mpaka nyumbani!?” “Kumbe! Nasikia walikuwa wakiishi kwenye bonge la mjengo, pesa ya mwanamke.” “Inamaana yeye huyu muda wote huo wamekuwa pamoja yeye hakutengeneza pesa!?” “Sasa kama wewe uje ufukuzwe kazi hapa, halafu uje ujidai hapa kwako kwa sababu ulianza hapa na mama J, vinakuja kweli?!” “Mimi nilianza hapa kama mfanyakazi, wao walikuwa wanandoa. Havifanani Umi!” “Ndio unaambiwa mwanamke kamtoa kama mbwa au paka mwizi. Hapo alipo nasikia hana kitu. Ila anadaiwa chupi aliyokuwa amevaa siku hiyo anamtimua na nguo.” Akasikia kimya kwa muda.
“Mmmmh! Ila mimi sioni kama ni sawa!” “Ndio hivyo. Hapo nasikia hana kitu yupo kama alivyo.” Tuma akakumbuka kumuona kufika hapo siku ya jumatatu iliyopita akiwa amechoka na ndiye aliyempa funguo za gari alizoambiwa ampe na baba J. Akahisi ni siku hiyo.
“Usicheze na wanawake wa mjini! Hawataki ujinga.” “Yule alikuwa mkewe Umi si hawara! Wala si jambo la kushabikia! Sidhani kama nisawa.” “Sasa kajidai ujuji, akamfukuza. Wewe unasaidiwa, badala, unyenyekee, unajidai kuleta uwanaume! Ndio imekula kwake. Sasa hivi tupo naye fungu moja. Wote heshima kwa mama J, atuweke mjini.”
“Na kuonja tena hutaki?” “Akuuuu! Tujikute wote tunalia shida! Labda kumuonjakwelikweli! Hakuna mazoea. Kimoja, cha hamu, basi. Kikinoga, basi ni mara moja moja tena kwa makubaliano ya starehe tu! Mjini hapa, kuishi kwa akili. Asije kuzoea kubebwakila wakati au kuonjeshwa bure. Akuuu!”
“Tena nasikia mkewe alimjua tokea mwanzo kama amempendea pesa ndio maana alikuwa makini naye sana. Nasikia alikuwa akimfuga kama paka ili asije tumia pesa zake na wanawake wengine. Unaambiwa yule dada hatakagi ujinga. Wakati wote macho yake yalikuwa kwenye pesa yake na huyu bwana. Ndio kakosea stepu tu, akamtimua.” Hakusikia Tuma akijibu tena. Pakatulia. Umi akila.
~~~~~~~~~~
Jerry alishavurugwa, alishindwa kabisa hata kufikiria kile alichokuwa akifanya. Alibaki ameduaa akiangalia sehemu moja sababu ya maneno ya Umi. Hata sahani aliyolia chakula alishindwa kuitoa. Akabaki amekaa tu hapo ofisini.
Kweli Umi akaleta mteja. Ikabidi Tuma atoke kwenda kutoa matairi. Umi alijaa furaha huyo! “Kwa hili shoga nakupongeza.” “Si umeona mimi si maneno matupu?” “Nakuaminia.” Akazidi kucheka akijigamba. “Sasa kesho tena kuna mwingine anakuja. Na wakesho atakuchukua mengi zaidi, maana anataka kujionyesha utajiri ili nimkubali. Sasa mimi namchora tu nijue nguvu yake. Asinipotezee muda.” “Hutaki shida?” “Mimi mwenyewe ninashida Tuma. Halafu niende nikaongeze shida ingine! Nitaweza wapi?” Tuma akacheka tu.
“Halafu na yule baba mwenye gereji wanayonitengenezea gari yangu, naye namwambia aje achukue tena!” “Umi utamfilisi yule mzee wewe!” Akamsikia Umi akicheka sana. “Yeye si anataka dogodogo! Ndio akazane kujionyesha!” “Mpumzishe hata majuma mawili bwana! Katoka kununua juzi tu! Unapata dhambi sasa!” “Haya basi. Namuacha mpaka week ijayo. Utamuhurumia zaidi jinsi anavyohangaika. Hata nikiharibikiwa gari mbali vipi au usiku wa vipi, nikimpigia tu kama akimbie! Anatuma kijana wake haraka kuja kunisaidia.” “Basi muache kidogo.”
“Na nilishaongea na mama J, kakubali kumpunguzia. Anampa kwa bei ya jumla. Kwa hiyo akija tena, tunampa kwa bei ya jumla.” “Hayo ndio maneno. Sio kumnyonya tu!” “Ungejua shuguli yake yule, wala usingemuhurumia. Hamalizigi haraka.” Tuma alicheka, alicheka sana. Jerry akiwasikiliza tu. Akavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu. Pakatulia maana Umi alicha kumzungumzia yeye.
~~~~~~~~~~
Kumi kasoro akamsikia akiaga. “Kumeshakuchwa mwenyewe!” “Kuna mahali naenda na Chidi bwana! Kesho nawahi.” “Nakuombea kusiwe na ajali barabarani.” Umi alicheka, alicheka sana. “Nitawahi bwana!” “Sawa.” “Sasa si nimuage?” “Wewe unashida naye tu, huna lolote.” “Nahivi kaachika! Lazima na mimi nimuonje mwanamme mzuri.” Tuma alicheka kwa sauti.
“Uongo Tuma? Hawa wazuri bwana! Angalia hata watoto wanaozaa kwa wake zao. Baba J kalanda watoto wake wote. Na huyu naye watoto wake si uliwaona? Na hivi hawaongei kiswahili, unaweza sema matoto yamechanganya na damu ya kizungu! Sasa uje umuweka huyu kitandani! Unamvua nguo mchana kweupe. Na kama usiku huzimi taa.” Tuma akazidi kucheka.
“Nakwambia ukweli Tuma. Na dhambi hupati, maana kaachika.” “Wewe ungeenda tu kwa Chidi.” “Ndio anayeniwekea kauzibe huyu Chidi! Halafu kajaa, sina raha! Vitu vizuri kama hivi vinanipita tu kwa ajili yake. Haki namuhesabia siku, aniache nipumue.” Tuma akabaki akicheka.
“Sasa kesho usimpe chakula, nitamletea mimi.” “Kwanza usije tangaza huko nje kama namlisha mimi humu ndani. Umesikia Umi?” “Jamani Tuma!” “Hukawii kwenda kumtangaza huko kwenye masaluni yenu kuwa yupo hapa, analishwa na Tuma. Nisikusikie Umi. Anakunywa chai ya ofisi na maandazi ambayo hata mama J na mumewe wanayala.”
“Na hata mama J akinikuta nakula tembele langu, maharage na ugali, haachi kupitisha mkono akikomba mpaka harage la mwisho. Uongo?” “Sijasema Tuma!” “Na ibakie hivyohivyo, sitaki uzushi. Maana huwa mnajigeuzaga kama miungu kwenye maisha ya watu, mkifanya kana kwamba maisha ya wengine hayaendi bila nyinyi.” “Unanikaripia bure mimi masiki ya mungu! Mimi ninachotaka kesho iwe chakula maalumu kutoka kwangu na ajue si hiki cha jumuiya kama unavyokiita. Ni hivyo tu shoga yangu ili nimvutie.” Huwa Umi hataki ugomvi.
“Kama ni hivyo sawa. Sasa kama kweli unataka ale chakula maalumu kutoka kwako, wahi na kifungua kinywa kizuri, umpe. Ukichelewa jua atakunywa chai na maandazi ya jumuiya, hapo jikoni.” “Mmmh!” “Kuwahi huwezi? Maana na yeye kabla ya saa mbili anakuwa ameshafika hapa” “Huo mtihani. Basi mchana nikienda kununua chakula, namletea na yeye.” “Hayo ndio maneno. Na usichelewe. Ukichelewa atakula ugali wa jumuiya.” “Tuma naye! Si usije na chakula?” “Halafu mie nile nini!?” “Na wewe nitakuletea. Tena nawaletea wote ili asinishitukie.” “Akuuu! Usiniingize kwenye mitegoyako halafu uje uanze kunidai kama wakati ule?”
“Yaliisha na wewe Tuma!” “Wewe kama unamtaka, lipa garama ya kuwahi. Mimi nakuja hapa na chakula kama kawaida na kitakuwa kwenye friji kama kawaida. Ashajua ni chakula cha jumuiya hakina mwenyewe, hakina mashariti, hakuna wakumuuliza wala wakumuomba. Jua akisikia njaa, atakula. Labda sasa, ukiwa unatoka umwambie kabisa asubirie chakula, utamletea.” “Au kesho mapema, naagiza kiletwe hapahapa tule naye.” “Hayo ndio maneno.” Akaondoka. Kiofisi chenyewe kidogo. Hata ukinong’ona unasikika.
Taka Kwa Huyu, Thamani Kwa Mwingine.
Huku kwa Mill akaweza kuzungumza na Simon juu ya lengo la Jo, kwa dada yake. Ukweli hakuamini. “Kwamba kweli anataka kuhalalisha kabisa!” “Sijui kama ni kuhalalisha, ila kwa mujibu wa Jo, anataka kumuoa kabisa kanisani. Lakini kwa heshima ya dada yako, hataki kuruka hatua hata moja. Anaheshimu mila za kwenu, anataka kufuata taratibu zote, ila anaomba mumrahisishie.” Mill akaendelea kuzungumza naye kwa wazi ila kwa heshima. Ni kama mkwe wake.
“Jo, hana wazazi. Walio kama walezi wake ni dada yake na shemeji, na ni watu wazima sana. Sidhani kama safari za milimani kama nilivyofanya mimi itakuwa salama kwao.”
“Kwa jinsi nilivyofurahi! Najua hata wazazi watafurahi sana. Hata bure watampa.” “Hapana. Jo anampenda sana. Na anataka kujisikia amefanya kitu cha thamani kumpata. Kumpa bure ataona mnamdharau Dorothy, kitu ambacho hatakifurahia.” Kaka mtu hakuamini.
“Kweli Mill!?” “Kabisa. Hakuna pesa mtamtajia Jo, atashindwa kumlipia dada yako. Anampenda sana. Na ana uwezo mkubwa sana kiuchumi. Msiwe na wasiwasi.” “Kwamba na yeye apewe mahari kama ya binti kabisa?!” “Na ndivyo amuonavyo dada yako. Anampenda sana. Hakuna mahari mtakayo mtajia akashindwa kulipa. Kuweni huru. Ila ameomba kama atalipa kwa pesa.” “Acha nikifika nyumbani nikazungumze na wazazi. Bado siamini kama yupo radhi kumuoa Dorothy vile alivyo!” “Sivyo amuonavyo. Nakuhakikishia kabisa. Yeye anaona amebahatika kupata mwanamke atakayeishi naye kwa upendo na amani.” “Aisee nashukuru. Tutakujibu kwa haraka tu.” Wakaagana na kukata simu.
~~~~~~~~~~
Je, Umi atabahatika kumuonja Jerry?
Inaendelea….
0 Comments:
Post a Comment