Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Love At First Sight - Sehemu ya 82. - Naomi Simulizi

Love At First Sight - Sehemu ya 82.

 Akiwa amepotelea kwenye kazi, akasikia tena mlango unafunguliwa. “Natoka kwenda kupata chai. Sitachelewa.” Umi huyo. “Naomba uingie ndani kwanza tuzungumze.” Akaingia Umi pisi kali. Akajaza manukato ofisi nzima aliyokuwa amekaa Jerry, na kwa utulivu ule wa harufu hata Jerry mpenda vizuri alijua ni ya gali.

Hapo akamuona vizuri vile alivyojipangilia juu mpaka chini. Hakuhitaji kujua umbile. Hapo alipomsogelea likawa bayana kwa vazi aliloliona wakati anaingia hapo kazini asubuhi. Nguo nzuri ya thamani aliyoweka mwilini mwake ilimchora vizuri sana kwa heshima na kumfanya azidi kuvutia macho. Alikaa kwa kupishanisha miguu, nao ukawa umebeba umbile zuri sana la mguu mpaka magotini.

Rangi ya mwili alionekana wazi aliibadili. Kwani alikuwa na weupe uliopitiliza karibu afanikiwe kuifanya rangi kama ya mzungu. Ila alijaliwa ulaini haswa. Kwa kumtizama tu alionekana na ngozi nyororo. Lipstick yake nyekundu aliipaka na kufanya midomo yake minene ivutie. Akajiweka kitini.

Sasa Jerry alishafanya kazi na warembo wa Sandra, anajua tabia zao. Wakiwa mwezini, wakiwa wamegombana na wapenzi wao, wakiwa wanamtaka kimapenzi, yote. Alishawajulia.

“Na wewe unataka kuniagiza kitu?” Umi akamuuliza asijue Jerry hana hata shilingi. “Hapana. Nilitaka kujua ratiba yako ya hapa, na huku kuagana au kuelezana kuingia kwako hapa na kutoka ni mara ngapi kwa siku! Naona..” “Vishakuchosha?” Umi mwenyewe akamalizia kwa swali akicheka kama mazuri.

“Sitaweza.” “Muda wa kazini hapa ni saa mbili.” “Lakini leo umekuja saa tatu. Na sasahivi ni saa nne, tayari unatoka kwa chai na mbaya zaidi unaniaga. Inamaana na mchana tena,…” “Chakula cha mchana saa sita na nusu. Kutoka saa 10 kamili. Sema leo kama nilivyokwambia, nilikuwa naumwa, halafu jumamosi walituchelewesha sana kutoka.” “Saa ngapi?” “Hiyo jumamosi?” Na yeye akamuuliza Jerry.

“Ndiyo.” “Kwa maana siku za jumamosi saa sita na nusu tunatakiwa kutoka. Ila kukawa busy ndio mama J akatuomba tubaki.” Hilda ndio mama J, mke wa Jeremi. “Uliondoka saa ngapi?” “Mimi?” “Ndiyo.” “Kama kwenye saaa…” Akawa anajaribu kukumbuka ila alijua wazi anatafuta kudanganya.

“Labda nikamuulize Tuma, maana nilimuacha hapa.” “Iwe baadaye. Ila tufanye hivi, kufika kwakokuchelewa kwako, na sababu zozote zile, uwe unampa mama J.” Akamtamka kama yeye mwenyewe Umi. “Kwamba niwe nampigia kama nimechelewa?” “Chochote unachotaka kuniambia mimi juu ya kutoka kwako na kuingia kwako, wewe mtumie ujumbe au hata mbeep, atakupigia, utamueleza yeye. Kwangu iwe maswala ya kazi tu. Itaturahisishia sana. Au unaonaje?” 

“Na kwamba kumtaarifu kama nimechelewa, nilazima kwako?” “Hata kidogo. Kama vile unavyojisikia kuniambia mimi, basi mwambie yeye.” “Kwahiyo kama siku hiyo nimeishiwa bando?” Akamtega.

“Yaani hata usipojisikia kujieleza kwa nini umechelewa, pia ni sawa kwangu. Kwamba hainihusu.” Alifurahi sana. “Na kama nataka kwenda kula?” “Jipange na Tuma.” “Wewe hujamjua Tuma.” Akaanza. “Kwanza halagi nje. Anachopika kwake usiku, ndio anabeba kuja nacho hapa. Hathubutu kwenda kula chakula cha kununua hata kama ni siku tuliyolipwa mshahara.” Jerry akakaa sawa kama aliyekuwa akimwambia amalizie.

“Hata andazi, anapika kwake anakuja nalo hapa. Hathubutu hata kununua mkate. Mwenzio pesa yake ya kuchungulia! Halafu maisha yake ni hapahapa. Mwenyewe anasema anapenda A/C ya bure hapa kazini. Alfajiri anakuwa amefika hapa na ndio wamwisho kuondoka. Kwa hiyo kama unadhani atataka kutoka, niagane naye, hilo wala usijali bosi wangu.” “Sawa. Lakini na yeye awe miongoni mwa unao wataarifu kutoka kwako.” “Mbona kama ni hivyo raha sana! Maana mimi nilijua hapa tutaanza kubananaunoko, na kupelekeshana.” Akawa ametulia kabisa kitini.

“Naona Tuma atanishika uongo! Maana tulikuwa tukikuona ukija na yule mkeo amri moja, wewe hata salamu ulikuwa hutoi na watoto wenu hawajui kuongea kiswahili. Tukawa tunasema pengine hamtuongeleshi sisi kwa sababu ya lugha! Basi vile ulivyokuwa, ndio nikamwambia Tuma kazi tutakuwa nayo! Hata mama J nilimuuliza kama wewe unazungumza kiswahili. Maana siku zote ulizokuwa unakujaga hapa na mkeo mlikuwa mkipitiliza moja kwa moja ofisini humu ndani ofisini mara nyingi baba J akiwepo, halafu hamtoi hata salamu! Ndio nikamwambia Tuma, kama wewe utahamia hapa, maisha yetu yatabadilika sana. Kumbe mwenyewe huwa tu hutakagi mambo mengi!” “Ni hilo tu. Asante.” Ikawa kama anamsaidia kuhitimisha na kumtoa hapo. Umi mwenyewe anaakili, akaelewa na kutoka bila ya kuongeza. Siku ya kazi ikaanza.

Love at First Sight.

Huku kwa Dorothy, alifuatwa mapema tu. Wakiwa njiani kuelekea kazini Jo akaanza. “Mwenzio nataka kuoa.” Dorothy akashituka ila akanyamaza. Jo akamchungulia kupitia kwenye kioo. “Najua umenisikia Dorothy.” Akacheka kidogo tu. “Wivu tu! Hata hongera hamna!” “Hongera Jo. Unaoa lini?” “Hayo ndio maneno. Haraka iwezekanavyo. Tena na umri huu mwenzio naoa ndoa takatifu kabisaa.” Dorothy akashangaa mpaka usoni.

“Naanza mchakato wa kutuma posa kwa wakwe zangu. Nitaomba kurahisishiwamchakato. Nikipewa tarehe ya mahari, nawaambia vijana wangu ili wajipange waje kuhudhuria. Wakishathibitisha tarehe zao kutokana na kazi zao, napanga tarehe ya harusi, namfikisha mpenzi wangu kanisani kwa haraka sana. Maisha yaendelee. Au wewe unasemaje?” Kwa hakika alimmaliza maneno Dorothy.

Na alimfanyia kusudi kujua kama akimuomba kumuoa atakubali au la! Yupo tayari kwa ndoa? Akamchungulia tena kwenye kioo huku akiendelea kuendesha, akamkuta ameduaa. Akamuacha kama kumpa nafasi ya kuyaingiza moyoni.

Alimfikisha mazoezini, akawa akifanyiwa mazoezi ya kunyooshwa kuanzia chini ya kiuno mpaka unyayo kisha kutembea ndio kulikuwa kukifuata. 

~~~~~~~~~~~~~

Akiwa amekaa anamsubiria akamtumia ujumbe Mill. ‘Ukipata nafasi tafadhali nipigie.’ Hapohapo akapiga. “Naamimi sijakusumbua?” “Hata kidogo. Nipo njiani kuelekea kazini. Kwema?” “Nataka kumuoa Dorothy.” Mill akacheka sana. “Hongera sana.” “Hongera hizo zije na msaada, Mill. Nisaidie kuniwakilisha huko kwao. Nisaidie kujua taratibu za kuoa kwao zilivyo.” Mill akamueleza alichofanya yeye na marehemu baba yake kwa Pam.

“Tena kwa kuwa bado wapo hapahapa mjini, hatua ya kwanza ya posa itakuwa rahisi.” “Hawawezi kukubali kupokea mahari hapahapa mjini kunipunguzia mlolongo mrefu? Na kabla hujajibu hilo, hayo majembe na mablangeti hawawezi kubadilisha kwa kupokea pesa?” “Hata mimi niliuliza lakini wanasema hivyo ni vya mila, havibadiliki. Hilo blangeti la bibi anapewa kweli bibi, sasa kwa kuwa hana bibi, sijui ila nitakuulizia. Kuhusu kupokea hapa mahari au nyumbani kwao, nalo hilo nitakuulizia. Maana wapo kwa kaka yake. Ingekuwa rahisi.” Mill akaendelea.

“Ulitaka iwe lini?” “Nikipata wakupeleka posa hata kesho mimi sina neno. Nishamgusia shemeji, amesema leo tutazungumza. Nilitaka kujua availability yako. Ili na wewe uwepo kwenye mazungumzo hata kwa simu tu, si lazima kwa leo tukakutana. Nampenda Dorothy, kwa hakika nataka kumuoa. Si jeuri, mpole sana aisee! Naona yeye ndio ataniwezea.” Alicheka Mill, alicheka sana.

“Sikutanii Mill. Umri umekwenda, sitaki tena kuwa na mtu atakayenivuruga kichwa au kunianzishia maradhi ya moyo kwa kelele na hekaheka badala ya kuyatuliza. Nataka mtu wakumalizia naye kwa utulivu na amani kama hivi dada na shemeji. Mnapanga safari, mnafika na kufurahia sio kelele zinakuwa nyingi hamna maelewano! Hapana aisee! Naona Dorothy tunaendana. Na kwa kuwa naona kwake nimemaliza, nataka tufunge ndoa kabisa, nimalize hicho kipengele.”

“Hongera sana Jo. Na kwa asilimia 100 nakuelewa. Kuishi na mtu mnaye elewana aisee ni muhimu sana, lasivyo hata kama nyumba imebarikiwa kiuchumi, hutafaidi matunda yake. Yanakuwa machungu, hayaliki.” “Naona wewe umenielewa.” Wakajipanga hao wawili mpaka mipango ikakaa sawa. Ikabakia jukumu la Mill kumtafuta Simon, kaka yake Dorothy na kuulizia utaratibu.

~~~~~~~~~~~~~

Mtu wa mazoezi akatoka na kumfuata Jo nje. “Naona leo tuishie hapa.” “Mara hii! Kwa nini?!” Jo akashangaa sana. “Naona leo hayupo vizuri. Na tukiendelea hivi anaweza akajiumiza.” Bado Jo akawa hajaelewa. “Kwa nini?” “Sijui ni nini kinaendelea, ila hayupo sawa. Ile hofu ya mwanzo kabisa tulipokuwa tunaanza, imerudi. Nikategemea pengine kwa hiyo hofu angeahirisha, lakini napo ni kama anafanya zaidi na kupitiliza. Anatetemeka na kutokwa jasho. Nahofia anaweza kuanguka na kujiumiza zaidi.”

“Nimejaribu kumtuliza naona imeshindikana, anataka aendelee tu. Nashauri atulie tuendelee kesho au baadaye kabisa.” “Acha nikazungumze naye.” Akajua amepanikisababu ya kusikia ndoa ya kualika watu tena ya haraka.

Akamkuta anakazana, tena peke yake. Halafu ipo hatari ya kuanguka. Akamsogelea. “Dorothy!” Akamuita taratibu. Nusu aanguke akigeuka, maana alikuwa akitembea kwenye reli ya mazoezi. Akamdaka. “Pumzika kidogo.” “Sijachoka. Nataka kuendelea.” “Najua.” Akamuweka sawa kwenye hizo reli akining’inia, kisha akavuta kigari chake.

“Kaa.” “Mimi nipo sawa. Sema nilitaka kuanguka kwa kugeuka kwa haraka. Umenishitua uliponiita. Nilijua nipo peke yangu. Nilimuomba aniache nifanye mwenyewe. Maana anakuwa akinielekeza kila siku, sifanyii mazoezi anayonifundisha. Nitaendelea hivyo mpaka lini?” Hapo anajieleza, amekuwa mwekundu na jasho linamtoka.

“Naomba ukae, Dorothy.” “Nataka kuendelea kidogo.” “Najua. Lakini naomba ukae kwanza.” Akakaa taratibu kama mtu anayeingiliwa. “Tunaondoka?” “Tunaweza kurudi baadaye. Njaa inaniuma, nisindikize nikapate kitu kidogo. “Pole, nilisahau kukuuliza kama ulikula.” “Hamna neno.” Wakaondoka hapo, akampeleka sehemu wanayouza kweli chakula. 

Wakaenda kukaa kwenye meza yao, peke yao. Jo hakuwa hata na njaa! Kwanza huwa hali kitu mapema hivyo wala usiku pia haweki kitu tumboni. Labda kwenye sherehe au wakiwa mapumzikoni, napo anakuwa na kiasi. Saa 11 jioni mwisho wa kula mpaka tena saa sita mchana ndipo anaweza kula. Kuanzia hapo atakula mpaka hiyo saa 11 ndio mwisho. Anaita mfungo mfupi, kwa afya lakini.

Akaagiza maziwa moto, yeye Dorothy akasema hasikii njaa. “Naomba uagize hata kitu kidogo tu, kunisindikiza.” “Nilishakula Jo! Sasahivi sijisikii kula.” “Basi akuletee hata juisi tu na yai.” Alimjua Dorothy ni mlaji. Akamuagiza muhudumu akaondoka na kurudi bila ya kuchelewa.

“Naamini nikijibidisha nitaweza kutembea.” Akaanza kwa wasiwasi. “Hujawahi kuzembea, Dorothy. Ila jua itachukua muda. Sio jambo la mara moja.” “Hata kama nikikazana sana!” “Kitakachotokea ni kujiumiza zaidi. Tafadhali jipe muda na jiambie itachukua muda sio jambo la haraka. Hujatumia hiyo miguu kwa muda mrefu, unachohitaji ni muda ukiendelea kuikumbusha misuli kila wakati.” Hayo hayakuwa mageni kwake, walishazungumza na hata huko mazoezini wataalamu walishamwambia. Akamuona amekosa raha.

“Wakati nakufuata siku ya kwanza kabisa, kuzungumza na wewe, nilikujua Dorothy. Hakuwa mgeni kwangu, na hata sasa wewe sio mgeni kwangu. Nakupenda hivyo ulivyo, na nitakuoa jinsi ulivyo. Usiogope. Usiwaze watu watakao kuangalia siku ya harusi yetu ila agano utakaloingia na mimi. Sisi wawili tu, ndio wa muhimu.”

“Picha zetu, mimi na wewe tayari vijana wangu wanazo.” Akashituka sana ikawa tena kama anamtisha zaidi. “Wanakufahamu Dorothy. Na unajua nini?” Akabaki akimwangalia. “Hakuna hata mmoja wao aliyemzungumzia huyo Dorothy unayehangaika naye sasahivi na kumfanya aonekane tofauti kwa haraka ila uzuri wako tu. Dada anaimba wema wako kwa kila mtu. Huko kwetu Dorothy anayezungumziwa na kusubiriwa kuja kuwa mmoja wa familia yetu siye uliyenaye kichwani na unayejaribu kumbadilisha.” Akaendelea kuzungumza naye taratibu, akamuona anaanza kutulia.

“Nakupenda Dorothy, tafadhali nisikie ninachokwambia na ikusaidie kuondoa macho yako kwenye upungufu wowote unao jifikiria unao na kuyaweka kwenye mazuri yanayo nivutia kwako. Sawa?” “Nilikuwa natamani siku hiyo na mimi niwe nimesimama.” “Naelewa shauku yako, na sikupingi, ila naomba jiambie hivi, usimame tena, usisimame tena, upo na mtu anayekupenda na kukujali vile ulivyo. Hata ukiweza kutembea leo na miguu yako yote miwili, haitabadilisha chochote wala si kwamba itaongeza kitu! Bado nitakupenda kwa upendo huuhuu.”

“Na ninakuhimiza mazoezi si kwa ajili ya siku ya harusi au ili utembee kwamba itaongeza kitu fulani! Hapana. Mimi ni daktari. Nimeona kuna uwezekano ukarudisha uwezo wako, ndio nikaona ufanye. Ni lini uwezo wako utakurudia kabisa, hakuna anayejua. Kwa hiyo tulia.” Akavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu, akamuona ametulia kabisa.

“Kunywa juisi yako.” “Asante Jo. Asante kunituliza. Nimetoka kwenye maisha ya kukosolewa kosolewa, wakati mwingine najishuku tu.” “Upo sawa Dorothy. Natamani ungejijua ulivyo, na vile wengine wanavyokutizama. Nahisi ingekusaidia sana. Usikubali mtu mmoja akakubadili.” Akaendelea kuzungumza naye mpaka akatulia kabisa, stori na vicheko vikaanza. Dorothy anaolewa! Ndio akili kutulia na kufurahia.

Uimara Wa Nyumba, Msingi Wake

Huku kwa Jerry, njaa ikazidi kumsumbua. Pesa hana. Cha mchana alikula nyumbani kwa Mill, akaondoka kabla hawajapata cha usiku akiwa ameshacheza sana mpira wa miguu. Hapo tumbo lilikuwa tupu mpaka akili haifanyi kazi. Akatoka angalau apate hiyo chai ya bure ya ofisi. Akaelekea upande wa jikoni na ndipo wanapokula. Palikuwa pametulia haswa.

 Upande huo wa ofisi wapo watatu tu. Na ofisi ni kama imegawanya sehemu kuu nne. Chumba alichopewa yeye peke yake, na nje ya hicho chumba ndio meza mbili, wanakaa hao warembo wawili. Choo na hicho chumba cha jiko. Pasafi, kunavutia kwa namna yake.

Akashituka kidogo alipoingia Jerry. Akasimama. “Wewe endelea tu kula. Mimi naangalia chai.” “Nikusaidie?” “Hapana. Wewe endelea tu kula.” “Kuna na maandazi hapo. Kama alivyosema Umi, huwa napika mengi, nakuja nayo kazini yanasaidia kitafunwa. Kwa hiyo kuwa huru.” “Sitakuharibia bajeti?” “Hata kidogo. Wewe jichukulie tu utakavyo. Akipita mama J hapa anakuwa na kazi ya kuyala, mwishoe anabeba kabisa.” 

“Njaa inaniuma, wala sitajivungaNashukuru.” “Usijali. Huwa yanakuwa hapohapo kabatini muda wote. Ila siri yake ni kuyarudishia kama hivyo, yasikauke. Vinginevyo na kesho utayakuta malaini hivyohivyo.” Akarudi kwenye sahani yake akaendelea kula.

Akagundua anakula wali na maharage. Ila vikatoa harufu nzuri sana kama pilau! Jerry akahisi ni njaa ndiyo inayomsumbua. Akajitengenezea kikombe cha Milo, akachukua na mandazi matatu, akakaa hapohapo akaanza kula macho kwenye simu, kimya. Tuma yeye akamalizia chakula chake kwa haraka. Akamuona anasafisha vyombo na kufuta hapo, akatoka.

Mara akasikia mlango unafunguliwa, Umi. “Nimerudi na mishikaki kibao!” Akamsikia akizungumza akiwa anaingia hapo. “Kanawe mikono na wewe ule japo kuonja.” “Nishakula, nimeshiba. Wewe kula tu. Umehongwa na nani?” Akamsikia Tuma akijibu na kuuliza akisikika anacheka. “Chidi anahangaika!” “Tokea jumamosi!?” “Kaniharibia mipango yangu yote. Kaniganda na hana muendelezo.” “Ila anakupenda!” “Hana lolote. Akihangaika huko ndio anajidai kurudi. Na hana muda mrefu, ataanza mapepe yake. Ahadi nyingi, na si mtekelezaji.” Akamsikia Tuma akicheka tu. Akapotelea mawazoni. Kazi zikaendelea.

~~~~~~~~~~~~

Akiwa ofisini akasikia Umi anaaga huku akimfanya Tuma azidi kucheka. Akatega sikio. Akaangalia muda. Kweli ilikuwa saa kumi kamili juu ya alama. “Na gari kaniwekea mafuta, mpaka juu. Anataka leo aje alale kwangu.” Akagundua Tuma anacheka tu. “Nitampiga chenga mpaka ashangae.” Mwishoe akauliza. “Hutaki?” “Wewe habari zangu na Chidi umeanza kuzisikia leo? Vituko haviishi! Namuuliza kunijazia gari mafuta ndio anataka kuhamia kwangu? Ananiambia anaona umri umekwenda tutulie.” “Na kweli!” “Akuu! Aache ujinga wake. Kama umri umekwenda ni wake. Aliponiacha ndipo amenikuta, asitake kujitoa akili.”

“Kwa hiyo?” “Hakika sitaki. Anamashariti mengi sana, Chidi. Wakati wote ni kuninyima raha tu. Hakika sitaki tena. Akija leo, namwambia sitaki mipango yake, aondoke na shilingi mbili zake.” Kisha akasikia hodi mlangoni, taratibu na safari hii akasubiri.

“Wewe si umeambiwa usiwe unampa habari zako za kuingia na kutoka?” Akasikia Tuma akinong’ona, Umi akacheka. “Ndio hata kuagana jamani! Aje aulizwe niliondoka saa ngapi, aseme hajui! Na unamjua mama J.” Akagonga tena ila kiustarabu, Tuma hana mbavu ila kwa sauti ya chini.

“Nilikuwa nakuaga kama Tuma tu!” Umi akajisemesha nje ya mlango, bado hajakaribishwa ndani. Alimfanya Tuma acheke kwa sauti. Mlango ukafunguliwa. Wote wakanyamaza kimya kwa gafla waliposikia mlango unafunguliwa. Jerry akatoka. Tuma akainamia kompyuta kama anayejifanya yupo busy.

“Nasema jioni njema, tutaonana kesho. Na Tuma naye nimemwambia hivyohivyo.” “Sawa.” Jerry akamjibu akimwangalia. Akamgeukia Tuma. “Hutaki lifti?” “Ya kwenda wapi?” Akawa anamuuliza akicheka. “Tuma naye! Kesho basi.” Huyo akaondoka zake. Jerry akapitiliza jikoni. Alikunywa Milo na maandazi, njaa ilishaanza kumsumbua tena. Akatengeneza chai akachukua na maandazi matatu tena, akarudi nayo ofisisini. Ukimya ukatanda hapo.

~~~~~~~~~~~~

Kwenye mida ya saa 11 akamsikia Tuma anasalimia. “Mama J, kanituma maandazi. Ameomba nimpelekee japo mawili.” Sauti ya mdogo wake. “Sawa.” “Na mizigo yako ipo kwenye gari. Shusha kabla sijaondoka nayo tena.” “Mwambie mama J, adumu.” Akagonga na kuingia. 

Kwa asili hao ndugu walifanana mpaka haiba zao. Sauti zao si za kelele. Wakizungumza ni mpaka utulie uwasikilize kwa makini. Wakiwa sehemu wakafunga mlango, huwezi kuwasikia wakizungumza. Halafu wakafanana wote sura mpaka umbile.

Jeremi akazungumza na mdogo wake huko ofisini hakukaa muda mrefu akaondoka. Wakajikuta wamebaki hapo ofisini peke yao. Jerry yeye alikuwa na sababu. Hana pakwenda. Anapoishi joto, na pale kweli hali ya hewa ya ubaridi ni bureee! Akajikuta ametulia hapo ofisini wala hafanyi kazi. Anawaza yake mpaka saa 12:30 ndio akagutuka na kutoka.

~~~~~~~~~~~~

“Bado upo tu?!” Tuma akanyanyua macho kumtizama. “Kwani huwa unatoka saa ngapi?” Akacheka kama anayefikiria. “Inategemea. Lakini huwa nasubiri wenye haraka zao na majumbani kwao wamalize fujo zote humo barabarani ndio na mimi nitoke, nipate sehemu ya kukaa kwenye daladala.” “Sasa si unafika nyumbani usiku sana?” “Kwangu sio mbali sana na hapa. Daladala moja tu nimefika. Ndio maana huwa nawahi kuingia na sina haraka yakutoka.” Jerry akajisogeza.

“Sasa wewe majukumu yako hapa ni nini?” “Inategemea na siku, na pia mama J anavyotoa maagizo. Kwa mfano leo siku za jumatatu tunakuwa hatuna mambo mengi sana, mzigo unaingia ijumaa.” “Matairi?” “Ewaah! Ila na oil. Jumamosi kunakuwa busy sana. Watu wengi ndio wanakuja. Wanao taka kununu magari, basi wanapita kuangalia kwa wingi. Wengine wanakuwa wametokea kule yadi kubwa alipo baba J, wanakuwa wameelekezwa hapa kufuata aina fulani ya gari. Inabidi kuwa nao huko nje kuwaonyesha magari ila sio wengi kama wanao taka kufungiwa matairi mapya kwenye magari yao na kubadilishiwa oil kwenye magari yao.”

“Hapo mama J anatakaga macho na masikio yangu yawe stoo, sababu ya wizi.” “Aliniambia Jeremi. Kuwa makini na vitu vidogo vidogo.” “Ewaah! Vimakopo vya oil vinakwenda sana siku ya jumamosi. Usipoweka hesabu makini, mnajikuta kazi imekuwa kubwa, pesa haijaingia. Kwahiyo kujua zikitoka kopo kiasi fulani basi gari ngapi zipefikiwa. Kwa hiyo nakuwa nawasaidia stoo, kutunza hesabu. Au kwa kifupi mimi ndio natunza kila kitu stoo na hesabu zake."

"Na Umi?" “Umi yeye mzuri sana wa masoko na anafahamiana na watu wengi. Rafiki zake wote wanakuja kubadilisha oil hapa na wananunua matairi hapa. Na pia mzurisana kwa biashara. Anajua kuzungumza na wateja. Kama kweli mtu anashida na gari, akikutana na Umi, hata kama hatanunua hapohapo jua atakuja kurudi tu. Anawasaidia sana pia kuwatangaza. Kama nilivyokwambia, anafahamiana na watu wengi. Na anajua matangazo.” Akawa amepata picha.

“Kwa hiyo hapako busy sanaa, mpaka mwisho wa juma. Napo ni kuwa tu makini na vitu vidogovidogo ambavyo vinaonekana kama havina maana, lakini ndio vyenye faida.” “Nimeelewa. Sasa kama hapo unafanya nini?” Akacheka. 

“Kule kwa mafundi wanafunga saa 10:30. Mpaka wasafishe mtu wa mwisho anaondoka saa 11. Ndio napata muda wangu wakufunga mahesabu kwa siku, ili ikifika alhamisi, mama J apate stock nzima, atume mzigo hapa siku ya ijumaa kutokana na uhitaji. Sipendi kulundika, halafu nifanye siku ya mwisho. Na wakati mwingine akiwa na safari zake, anaweza akataka kutuletea vitu hata vya siku 20, nakuwa najiandaa kwa maswali yake yote, maana ni ngumu kumtabiri.”

“Kwa hiyo kama hapa nimeshapita kule mpaka jikoni. Nishajua nini chakuwaombea.” “Kwamba mpaka kule nao wanapewa chai ya bure!?” “Kama hapa tu. Ndio maana vya hapa ndio ameleta baba J, jioni hii. Nilimtaarifu mkewe tokea jumamosi. Kwao kule nishaandika kila kitu, ikifika jumatano namtumia. Basi. Kwa hiyo muda mwingine nakuwa tu hapa kama Umi tunasubiria wateja. Wakifika getini tunaona kwenye kamera, tunatoka kwenda kuzungumza nao. Basi. Si pagumu, ukipazoe. Na wenyewe hawa ni bora uwe mwaminifu, na ufanye majukumu yako. Hawana shida.”

“Umeshakaa hapa muda gani?” Akacheka. “Nimeanza hapa na mama J. Sema utakuwa hunikumbuki tu. Lakini tokea mwanzo unamsaidia baba J kupaweka hapa sawa, na mimi nilikuwepo. Mimi na mama J ndio tulianza hapa.” “Mambo yalikuwa mengi, kweli sikumbuki.”  “Hata Umi ameshakaa, nafikiri huu ni mwaka wake wa pili sasa. Hapa kama shida yako ni kazi tu, si sehemu mbaya ya kufanyia kazi. Utapafurahia.” Akawa anampa moyo akijua na yeye ile ni ajira kumbe mpitaji.

~~~~~~~~~~~~

Kwa haraka sana akawa ameshamsoma na kuona ametulia na akili inayojielewa. “Nikuulize swali?” “Juu ya nini?” “Wewe umekaa sana hapa. Na unajihusisha karibu sana na hizi biashara zote mbili. Kama ingekuwa wewe, ungefanyaje?” Akacheka taratibu akifikiria. “Sijawahi ulizwa hilo swali.” “Nipo kujifunza biashara yao, ili kama nikiona ni kitu kinafanyika na mimi nikifanye. Na najua wanakutegemea sana hapa. Kwamba unajua mambo mengi. Naomba mchango wako, kujua unachofikiria.” Jerry akajishusha kabisa na kumfanya hata Tuma kutulia.

“Acha nikwambie ukweli. Hawa wameshajijenga muda mrefu sana. Wameanza zamani, kiasi ya kwamba jina lao linawauza, na tayari wanayo pesa. Kwamba hawategemei mauzo ya siku kuendesha biashara zao. Washajijenga sana, najua wewe unajua.” “Kwa mtu anayeanza je, ungemshauri nini?” 

Nisingemshauri afanye biashara ya magari kwa kuyaweka hapa kwa muda mrefu. Hiyo yote hapo nje ni pesa ambayo bado haipo mfukoni.” “Au imeshatoka mfukoni.” “Ewaa! Sasa kwa mwenzangu na mimi unayetegemea gari iuzwe ndipo upate pesa, magari yatakuchelewesha.” Jerry akajiweka sawa akijua anazungumza na mtu aliye na uelewa.

“Biashara ya matairi hata wao ndio utajiri wao. Mtu hawezi kusema naacha kununua tairi kama kweli gari linahitaji tairi. Ila unaweza kugairisha kununua gari. Wanauza matairi hapa kupita utakavyodhania. Na hapa ni padogo kulinganisha na kule anakofanya baba J. Unaambiwa wanavifaa vya kisasa vya kuweka matairi, wote vijana wa hapa ndoto zao ni kuhamishiwa kule alipo baba J.”

“Wanauza sana, na wanafanya kazi sana. Siku za jumamosi hapa, kule kwao ni kila siku. Ndio maana walipoona hapa pamekaa sawa, mama J amehama hapa, wapo kule wakisaidiana, hapa wanapita tu.”

“Ila na eneo la pale pia ni zuri.” “Hicho pia walipatia sana. Pako barabarani wanakopita watu wengi. Halafu ile sehemu ya kusubiria waliyotengeneza pia nzuri sio kama hapa.” “Nilipaona.” “Sawasawa. Watu wanavutiwa na vitu vidogovidogo.” “Kwa hiyo kama ingekuwa wewe ungefungua biashara ya matairi tu?” “Kama unataka pesa yako isikae sana nje, ndiyo. Halafu badala ya kuuza magari ongezea huduma ya kusafisha magari na hiyo ya kubadilisha oil. Yaani mtu anakuja hapo anatoka na gari kama mpyaa. Unachukua pesa ya tairi, kubadili oil na usafi.” Jerry akacheka kwa kuvutiwa.

“Ndio maana mama J anakupenda.” “Sio kwa sababu hiyo bwana! Wale washajijenga muda mrefu sana. Maswala hayo walishayapita muda mrefu. Kwanza hawataki kujipanua zaidi, wanasema watakosa muda wao.” Jerry akacheka akimjua mdogo wake na mkewe. 

“Wanasema wao hawataki kumiliki ulimwengu. Kutwa wapo pamoja.” “Nawafahamu. Ila nashukuru kwa mawazo.” “Ni pesa tu. Ila najua inalipa. Inalipa sana biashara ya matairi na kubadili oil, ni huduma ambayo yeyote mwenye gari hawezi kukwepa, ni jinsi tu ya kuwafikia.” “Ni kweli.” “Acha mimi niondoke. Naona hapa nishamaliza. Usiku mwema.” “Nashukuru kwa maandazi.” Akacheka.

“Si nilikwambia usijivunge? Mama J anatumaga watu wamchukulie kama si kupita mwenyewe na kuyabeba.” “Unayapika vizuri sana.” “Kazi ya jumapili hiyo nikiwa nipo nyumbani tu. Usiku mwema.” Akaondoka na kumuacha Jerry. Akaongeza chai ingine na maandazi, ndipo na yeye akarudi nyumbani akifikiria wazo alilopewa na Tuma.

~~~~~~~~~~~~

Inaendelea…

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment