Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Love At First Sight - Sehemu ya 81. - Naomi Simulizi

Love At First Sight - Sehemu ya 81.

 

Akaanza kulia kwa hasira. Hapohapo Shema akamtumia ujumbe bibi yake kumuita. Ndio Dorothy kukurupuka. Akatoka, Jo akimfuata. “Bibi wewe unampendelea Eric ndio maana hutaki kunisikiliza mimi.” “Kwani aliyoyafanya Eric ni mageni kwenye hii familia? Kila mtu anamjua kama ni mchoyo, mtoto asiyetaka kusaidia mtu.” “Sio hivyo bibi! Ila uwezo na majukumu.” “Hata kidogo, hiyo ni sababu tu.” Mama yao akaingia na Jo, akakuta bibi yao anaongea.

“Huyu mwenzio Pam, kuna kipindi alikuwa hana kazi, anauza chapati, kidogo alichokuwa akikipata, japokuwa alikuwa na mtoto ambaye anamtegemea, hana msaada mwingine, lakini hakuacha kukumbuka kule kijijini. Muulize babu yako hapo. Mpaka sisi tulikuwa tukimuhurumia jinsi anavyohangaika, kusudi tu mama yenu angalau apate sabuni ya kuogea. Ulishindwa vipi Eric?!” Kimya.

“Hukuacha kulalamikia shida kila wakati. Wakati mwenzio huyu ambaye hakuwa na kitu, alikuwa hazungumzii shida zake hata mara moja! Muulize mama yenu. Hutapokea simu ya Pam ikawa na malalamishi ya shida zake ila salamu. Lakini mama yako alikuwa akiomba pesa ili akupigie wewe angalau kukujulia hali, lakini alikuwa akiishia kusononeka tu! Wakati wote ulihakikisha unatangaza shida zako kama ambaye unatangaza usiombwe msaada! Hujui uzima wa mtu, hujui mambo ya familia yanavyokwenda! Wakati wote ni sababu tu.” Hapo akaanza kumtuliza Pam.

“Ulishindwa vibaya sana Eric. Ulishindwa nafasi yako kama kaka kwenye familia ndogo sana uliyokuwa umepewa dhamana na Mungu. Ukaruhusu baraka hizo zimuendee baba Shema, mtu baki.” Mill akagutuka.

“Kila jukumu Mungu analokupa, linaambatana na baraka zake. Iwe ni umri mrefu, afya njema, kufunguliwa milango migumu isiyoweza kufunguliwa na mwanadamu, basi bila wewe kujijua, unajikuta pale unapomsadia Mungu kufanya hilo jukumu alilokupa, kufikia watu wake, basi na wewe ndio unakirimiwa hivyo. Wewe ulishindwa vibaya sana. Ukamuacha mama yako anasota mavumbini, hujali hata sabuni ya kumsafishia, mpaka alipokuja baba Shema, mtu baki akachukua nafasi yako kwa rahisi sana.”

“Yeye amekuwa akitoa muda na pesa yake bila kulalamika. Na nakuhakikishia Eric, mkono wa Mungu kwa kile ambacho angekupa wewe, kimehamia kwa baba Shema. Hatabakia alivyo hata kama alishabarikiwa. Kuna mambo Mungu aliyotaka kukulipawewe, atamlipa baba Shema na tutajua tu kama Mungu amemlipa.”

“Huyu mtu baki, eti akahangaika kumtoa mama yako mavumbini, na kumkalisha bafuni akioga, kwa kuleta vifaa vya kila namna na wewe upo!” Eric akaanza kulia. “Yaani yeye ndio anahangaika na mama ambaye hata hamjui wala hakuwahi kukutana naye! Anatuma sabuni za kumsafisha mama yako, wewe upo! Anamvalisha mama yako wewe upo! Kweli Eric?!” “Kwani sabauni ni kiasi gani kusema ungefilisika, Eric?” Mjomba wake akaingilia.

“Pam huyo alikuwa akienda kuokota hata mitumba, anampelekea mama yenu! Wewe ulishindwa Eric. Umemuacha mtoto wa kike anapambana kupigania nafasi yako na wewe upo hai na Mungu amekupa nafasi!” “Tena nafasi yenyewe uliombewa na huyohuyo mama yako.” Wote wakamuangalia shangazi yao.

“Nakumbuka mpaka leo. Wifi ndiye aliyeniomba mimi, tumchukue Eric kutoka kijijini ili aendelezwe mjini. Au umesahau Eric?” Kimya akijifuta machozi. “Mama na baba, pamoja na mama Eric mimi niombe radhi hata kwa niaba ya familia yangu. Tulimkosea Pam. Wote tulibeba maneno tuliyosikia, tukafanya kama alichofanya tu Eric.” Shangazi akaendelea.

“Tusamehe Pam. Tusamehe mama. Wote tulikukosea wala sitajitetea. Tulikosa, ila sisi ni ndugu, tunaomba yaishe.” Kimya. Mama yake akamwangalia. Kimya. Sebule nzima inasubiri huyo muombwa msamaha. “We Pam?” Mama yake akamuita kama kutaka amjibu shangazi yake. “Mimi nimewasamehe wote kasoro Eric.” “Sasa hili jambo unataka liishe vipi?” Bibi yake akamuuliza. 

“Niambie nifanye nini ili unisamehe?” “Wewe siwezi kukusamehe maana nakuhisi upo kama baba yako aliyetutelekeza. SITAKI.” “Haya Dorothy, anza kuzungumza naye huyu. Maana unamjua Pam. Na hakuna kuondoka hapa mpaka tuyamalize.” “Mimi nishayamaliza. Eric yupo kama baba yake. Akiona vitu vizuri hatulii mpaka aharibu, ndio anaondoka. Alitoa maneno kwa Sandra akaenda kuyatangaza kila mahali ili kuniharibiakwa watu wakati yeye alikuwa ni kaka yangu! Alitakiwa kunisitiri sio kunitangaza ubaya.”

“Hata kama nilikuwa nimekosea, alitakiwa anibebe hivyohivyo na kunisaidia. Lakini yeye akawa anapita kila mahali na kuninawia mikono ili niangamie kabisa. Sasa sasahivi anataka tupatane ili iweje? Na mimi sitaki kupatana na yeye. Sitaki undugu na yeye kama alivyomwambia mama. Alininawia mikono na kusema nisimtafute tena. Mimi sio ndugu yake. Halafu eti mama anakuja kunisaidia mimi mjini, anamkasirikia na mama!”

“Mimi niliheshimu matakwa yake. Ndio maana nilikuwa nikihangaika na mwanangu peke yangu hapa mjini na yeye nikijua yupo. Jua, mvua, njaa na ugonjwa. Vyote vilikuwa vyangu hapa jijini huku nikijua yeye yupo na ana uwezo. Muulizeni Mill nyumba aliyonikuta nikiishi na Shema!” Kimya.

“Lakini nilitulia kimya na mwanangu na yeye nikijua yupo hapa mjini.” “Na huku akinitunza na mimi.” Mama yao akaongeza. “Sawasawa.” Pam akafurahia kuungwa mkono na mama yake.

“Nimekosa mama. Naomba msamaha.” “Mimi SITAKI.” Pam akadakia. “Jamani, narudi sio kwa sababu na mimi nimeishiwa au kuna kitu nataka kutoka kwenu,..” Hapo akamtibua Pam wala hakusubiri amalize. Akamdaka. “Basi ondoka. Ondoka.” “Hapo ulipokaa usiamke Pam. Unanisikia?” Mama yake akamuwahi maana alishatibuka. 

“Kama hana shida na sisi sasa kwa nini yupo hapa? Ondoka.” “Hajasubiri nimalize! Na naomba mama umuangalie Pam maana anamtindo wakuanza kupigana na pale amebakisha kidogo tu, aanze kurusha ngumi.” “Hatanyanyuka pale. Lasivyo anaenda kulala juu.” “Nimesema leo lazima hili jambo liishe Dorothy. Kafamilia haka kadogo, mnataka kagawanyike mpaka lini!?” 

“Sasa wewe mwenyewe unaona kuna mwisho hapa mama kama sio kukesha tu!” “Zungumza na Pam, atulie.” “Sasa si unaona kaka yake mwenyewe amesema hana shida!” “Mama, Pam ameniingilia, sijamaliza nilichotaka kusema. Nilitaka kusema leo nimekuja hapa sio kwa sababu ingine yeyote, ila mahusiano. Hata mimi sipendi watoto wangu wanavyokuwa wakiulizia bibi yao na shangazi yao halafu…” “Waambie wewe ndio…” “Ukiendelea kumuingilia hivyo, mimi naondoka. Umesikia Pam?” Mama yake akamuwahi, akaanza kulia. 

“Hakuna kumsamehe Eric.” “Niambie nifanye nini ili yaishe Pam. Natamani turudishe mahusiano ya zamani! Kumbuka mimi na wewe tulivyokuwa!” “Kabla hujapata pesa ndio ulikuwa ndugu mzuri.” “Kama nilikuwa mbaya kama baba, mimi ningehangaika kukutafutia kazi?” “Unanihesabia?!” “Na kukumbusha tu na nakuomba ukumbuke Pam. Majukumu ya maisha ndio yaliniingia, na kunichanganyanikajisahau. Lakini si kwamba nina roho mbaya kama baba. Nimekosa, naomba msamaha.”

“Nimejisikia vibaya kuja kukutana na Shema ameshakuwa kijana mkubwa kabisa!” “Uliniacha naye jela.” “Jambo haliishi Pam jamani! Samehe mama kuleta amani.” Bibi yao akaingilia. “Halafu hivi anavyolia si sawa jamani! Naomba tufupishe hiki kikao. Pam ana pressure, atamdhuru mtoto.” Hapo Mill akaingilia.

“Ameshamsiki Eric, mpeni muda afikirie. Kwa sababu kweli Eric umekosa na hili nilikwambia Eric. Ila chakushukuru Mungu kwa hakika umebadilika. Eric niliyekuwa nikizungumza naye siku za mwanzoni, sio Eric ambaye angetulia hapa, akikubali maneno machungu hivi, na kuendelea kujishusha.” “Lakini kweli!” “Eti mama?” “Eric ni mkorofiSANA. Huko kutulia hivyo ni kweli ni muujiza.” Eric akacheka na kutingisha kichwa mama yake alivyoafikiana na Mill.

“Kwani uongo?” “Nakubali mama. Na ninakiri nimekosa. Hapo sitabadilika mama. Nilikutelekeza. Nilikuacha kwenye shida. Najua sasahivi huhitaji kitu kutoka kwangu, na…” “Eric! Wewe ni mwanangu kama Pam! Unafikiri ni kwa nini nilikuwa nikihangaikakukupigia simu, hata kuomba simu ya babu yako iliyokuwa ikiwekwa pesa na mjomba wako?” Kimya.

“Wakati wote ilikuwa si kukuomba pesa! Ile roho ya umama kutaka kujua unavyoendelea na familia yako! Japokuwa ulijitahidi kunitenga nao, lakini walibakia kuwa wajukuu kama Shema, na nilitamani kujua maendeleo ambayo wakati wote ulininyima kwa kuweka vizingiti ili nisikuombe pesa.” Eric akapiga magoti kwa mama yake.

Akafunga mikono kabisa akiomba msamaha. “Nimekosa mama. Naomba msamaha. Na kama ningepata nafasi ya kumalizia nafasi yangu ya kuzungumza, hivi ndivyo nawaambia wewe na Pam. Nimekosa. Na ninarudi sasahivi nikiwa natambua kosa. Sitaki watoto wangu wakue wakiwa hawajui upande wa kwetu. Sihitaji chochote kutoka kwenu ila mahusiano mama yangu. Najua unanipenda ila tu mimi nilikuwa mkaidi. Ndio najirudi mama yangu. Na mimi nataka mahusiano na wewe pamoja na Pam, kama zamani.” “Ulipo…” “Pam!”  Mama yake akamkaripia, akanyamaza.

“Sawa, kama zamani nilipokuwa sina pesa. Nakubali nilibadilika. Nilikosa. Naomba tuanze upya. Jumamosi ijayo na sisi tunawakaribisha kwetu.” “Sitaki.” “Utakuja.” Mama yake akambadilikia Pam. “Sasa kama mimi sitaki je?” Akauliza akicheka kama mazuri. 

“Kwa lazima utakwenda, labda kama baba Shema akatae ila si kwa jeuri yako. Umesikia Pam?” “Huyu Eric…” “Hapana Pam. Inatosha. Kwanza namshukuru Mungu. Hii ni baraka.”

“Kwanza acha niwaambie ukweli nyinyi wawili. Hakuna kati yenu aliyechukua roho ya baba yenu hata mmoja wenu.” “Eric yupo kama yeye.” “Hata kidogo. Eric rudi kukaa.” “Umenisamehe mama?” “Yameisha kabisa. Na umenifurahisha. Na nakuhakikishia Pam, Eric hayupo hata nusu ya baba yenu. Yule kiumbe sijawahi kumsikia akiomba msamaha wala hajui kusema pole.”

“Nyinyi wawili nawahurumia kwa sababu maisha yaliwapitisha pabaya tu hamkujua jinsi ya kuishi mkiwa nazo, zaidi Eric. Hukukua kwenye mfano mzuri wa baba, ukajua mwanaume alitakiwa awe vipi akiwa na majukumu ya familia. Na nyinyi ni wahanga wa yule kiumbe kama mimi tu. Hatuna tofauti.”

“Sasa kwa sababu Mungu ametupa nafasi na roho ya kujirudi, tusimpe shetani nafasi. Na msikubali kumpa nguvu baba yenu juu ya maisha yenu.” Pam akashituka kidogo. “Maana hichi tunachoendelea kuishi sasahivi ni yeye mtupu. Alitutelekeza akijua wazi tunahitajiana sisi kama familia. Akajitoa, akaenda kuanza kwingine au sijui lipi lilimpata. Sasa sisi tusiendelee kama alivyofanya yeye. Mkataa umoja kati yetu huyo…” “Ndio atakuwa baba Eric.” Bibi yao akamalizia na kufanya wacheke.

“Sasa bibi wewe mbona unaniangalia mimi?!” “Hata! Sisi leo ndio tunataka kukutanishwa na baba Eric. Ndio tutajua leo anaishi kupitia nani!” “Kama bibi unafikiri ni mimi, basi jua mimi nimerithi kila kitu kutoka kwa mama.” Walicheka sana. “Dorothy mpole sana.” “Haaa! Anko! Hakika siamini! Sasa hapo unataka kusema nini?” “Mimi nimetoa sifa za dada yangu tu.” Angalau wakacheka, ile tension ikapungua.

“Kwa hiyo jumamosi ijayo si mtakuja na kwetu?” Akiwa anamwangalia dada yake. “Mimi nimepewa bedrest.” “Atakuja. Atakuja kwa lazima. Kama yeye mpumzikaji kweli, mwandalieni kitanda, akija apande kitandani. Lakini sisi tutakuja Eric. Na hongera mwanangu. Sasahivi umekua.” “Sasa mimi naona sisi tuondoke, tukapumzike. Tunashukuru kwa kutukaribisha.” Bibi mtu akatoa shukurani zake zote.

Babu akaomba waombe. Wakashikana mikono hapo. Aliomba huyo mzee, ungejua ni mtumishi wa Mungu. Akatamka baraka kwa baba Shema na familia yake. Akabariki wajukuu zake wote mpaka wa mjomba, akaja na vitukuu ndipo akamliza. Wakaondoka na kuacha Pam naye akiwa amekwenda kupumzika kama Mill alivyoomba.

Mapenzi Si Ukamilifu.

Mapenzi ya kweli huonekana kwa kujali na kusikilizanaKuvumiliana katika nyakati ngumu. Zaidi ni katika kusameheana na kusaidiana kukua kwenye lenu bila ya kubaki kwenye la nyuma lililo watatiza. “Kesho nitakuja kukuchukua asubuhi. Hata kama sio kazini, lakini lazima kuendelea na mazoezi.” Jo naye akawa akimuaga Dorothy. “Nitashukuru.” “Na kwa kuwa na mimi nimesamehewa kama Eric, najua simu yangu itapokelewa.” Akachomekea kwa haraka. Dorothy alicheka sana. “Na jumbe zangu zitajibiwa?” “Usiwe na wasiwasi. Kwanza sikumbuki mimi.” Akainama na kumkiss.

“Nakushukuru. Ila tunahitaji muda wetu Dorothy. Usio na muingiliano. Na isiwe kwako.” “Wapi, maana kwako…” Akasita akikumbuka zile sifa za upendo alizopewa. “Kwangu panafaa. Nimeandaa mazingira. Naomba ijumaa uje kulala.” Alishituka Dorothy.

“Kulala tena?!” “Kabisa. Nakuahidi wakati mzuri sana. Na safari hii nitasimamia. Hakuna kitakachoingilia. Mimi na wewe tu.” “Naomba tusipanie sana Jo. Mara ya mwisho tulipania, ikaishia sivyo.” “Sawa, sitasema zaidi. Ila naomba uweke mazingira ya jumamosi kulala kwangu.” Akamuona anafikiria kama anayesita. “Basi niseme tutajipanga zaidi. Sawa?” “Sawa.” “Si wazazi bado wapo?” “Wapo. Pengine mpaka mwisho wa mwezi.” “Sawa. Nisiseme mambo mengi nisije haribu kama mwanzo.” Akambusu juu ya midomo na kuondoka.

~~~~~~~~~~~

Kama kuthibitisha. Alipofika kwake alivyopanda kitandani akampigia. Safari hii akapokea. “Daaah! Kweli nimesamehewa.” “Kwani ulifanya nini?” Dorothy akamuuliza. “Sikumbuki.” “Hata mimi sikumbuki.” Wakaanzia hapo kuzungumza mpaka walipoagana kulala.

Kesho Ya Mtu Ni Fumba

Wiki mpya ilianza kama upepo mwanana, lakini ndani yake kulibeba kila aina ya hali. Furaha, mashaka, vikwazo na matumaini. Kwa Dorothy usingedhania kama ni mtu yuleyule ambaye leo anaamshwa na ujumbe mzuri hivi kutoka kwenye kulala na kumka kutoka kwenye ndoa iliyojaa machungu na manyanyaso ya mwanaume aliyekuwa akimuonyesha si kitu. Tena wakati mwingine akilala na wanawake wengine chumba cha pili akijua kinachoendelea, lakini leo ametua mikononi mwa Jo ambaye anamuonyesha uthamani wa hali juu.

Kwani wakati walipoagana wanalala, akaweka simu pembeni na kulala kwa furaha, kumbe upande wa Jo alibaki akimuwaza kisha kumtumia ujumbe mzuri sana aliokuta asubuhi hiyo kabla hajatoka kitandani. ‘Lala salama ukijua nakuwaza wewe na nakujali sana. Naamini siku moja Mungu atatujalia wakati wa kulala na kuamka pamoja. Uwe wa kwanza na wa mwisho kukuona. Hiyo siku ndipo furaha yangu itakapo kamilika. Nakupenda Dorothy.’ Akabaki akirudia kuusoma huo ujumbe tena na tena asiamini kama anaandikiwa yeye.

Ila kwa upande wa Jerry yeye alianza hilo juma moyo wake ukiwa umejeruhiwa vibaya sana. Ni jumatatu iliyopita tu alikuwa ndani ya ndoa, familia yenye mke na watoto. Akihudumiwa kwa chakula na mavazi kutayarishiwa. Alilala pazuri msichana wa kazi akihakikisha chumba cha matajiri wake kipo kisafi wakati wote. Lakini jumatatu hii anaamka upande wa pili akiwa na njaa ya ajabu. Ndoa imekwisha kwa kudhalilishwavibaya sana, kilichokuwa kimebaki ilikuwa kukamilisha kisheria wawe wameachana ramsi. 

Ameamka akihesabu muda alipoteza kujenga alichodhani ni chao kumbe alikuwa akijenga kwenye mchanga. Hapo alipo ameamka hana hata shilingi anayomiliki kwa jina lake na anaenda kuanza kama kijana mdogo kwenye kampuni ya mdogo wake. Roho ilikuwa ikimuuma Jerry, hana jinsi.

Ila siku iliyopita, kuwepo katikati ya familia ya Mill, iliyokuwa tulivu. Vicheko vilivyokuwa vimejaa hapo na kisambaa kikizungumza kwa hisia za amani asijue kulivyotibuka baada ya kuondoka kwake. Kisha kumuona Jo vile alivyo kwenye hisia za mapenzi kwa Dorothy. Akauliza kwa Mill historia yao kwa ufupi, kwa hakika ikampa shauku na morari akijiambia hata yeye bado anayo nafasi ingine. Anaweza kuanza na kufanikiwa kupata mapenzi ya kweli. “Na nni!?” Swali lililompotezea muda hapo kitandani na kuamua kukiacha kitanda kwa haraka akikumbuka jinsi alivyoishiwa na alivyojiapia hataanza na yeyote bila kujijenga kwanza kiuchumi ndipo afungue moyo kwenye mapenzi. Na hivi alishajijua si mvivu, alimfanikishia Sandra mpaka kumiliki mamilioni ya pesa, akajiambia juhudi haijawahi mtupa mtu.

~~~~~~~~~~~

Alifika kazini akamkuta Tuma alishafika. Akamkaribisha kwa heshima. Kwake hakuwa mgeni. Alishamuona akija hapo na mkewe, hata watoto wake aliwafahamu vizuri tu, lakini ikawa tofauti kwa Jerry. Hakuwa akimfahamu Tuma akawa ni kama alishamuona ila hakumbuki vizuri. Maana mara hizo chache alizowahi kupita hapo alikuwa anakuwa na Sandra, hata salamu kutoa ilikuwa ni kesi. Kwa hiyo wafanyakazi wa hapo hata kama walishawahi kusalimiana, hakuwahi watilia maanani.

“Ofisi yako ipo tayari na ni safi. Tuliambiwa tokea jumamosi kuwa utafika. Karibu.” Jerry akashukuru kwa jumla na kuingia. Baada ya muda akamfuata tena. Akagonga taratibu kama asimsumbue. “Kuna kahawa na chai. Milo naona inaishia. Ungependa chochote?” “Baadaye kidogo. Asante.” Basi siku ikaanza akiwa anaelekezwa na mdogo wake kwenye simu. Akapotelea kwenye simu na mdogo wake.

Baada ya muda wa kutosha akasikia salamu ya kike ingine. Tena aliingia bila hodi na kumfanya ashituke kidogo na kugeuka. Mrembo wa nguvu! Amejipangilia vizuri halafu mzuri haswa. Alingaa, umbile lilikuwa zuri maana nguo yenyewe aliyoivaa ni kama alifanya juhudi za makusudi kuwakilisha umbile lake. Jerry alisha mscan juu mpaka chini kwa haraka alipogeuka. Harufi tulivu ikajaa hapo ofisini kwake. 

Akaanza bila ya salamu. “Kulikuwa na foleni kweli ndio maana nimechelewa. Usije sema ndio tabia yangu. Mama J akanidhania vibaya. Ni leo tu.” Jerry akabaki amemkodolea macho, hata hamuelewi japo na yeye hakuwa mgeni hapo.

“Halafu nililala naumwa. Hivi nimekuja kwa kujikaza tu. Nimeona nisimuachie Tuma peke yake. Ila hata mama J anajua kama jumamosi hapa tulikuwa busy na tukachelewa kufunga.” “Sawa.” Hivyo tu akajibu  na kurudisha macho kwenye kompyuta na simu. 

~~~~~~~~~~~

“Wewe, kwani umewaambia nini wafanyakazi wako?” Akamuuliza mdogo wake. “Juu ya nini!?” Jeremi naye akawa hajaelewa. “Juu yangu? Maana wanazungumza na mimi kama wanazungumza na bosi wao! Hiyo biashara sitaweza Jeremi. Mimi nataka kujua kinachoendelea hapa, nitimue zangu. Sitakuwa na muda nao.” “Sasa utajua vipi kinachoendelea kama hujajua kila kitengo?” Akaendelea.

“Hapo hakuna sekretari wala mesenj…” “Subiri kwanza. Na huyu msichana aliyeniulizia chai?!” Akamsikia akicheka. “Sio mesenja?! Maana nimemkuta kama akisafisha pia.” “Hapana Jerry! Huyo lazima atakuwa ni Tuma tu. Anashule kubwa tu kichwani ila hajui kuchagua kazi, na hawezi kuona kitu hakijafanywa, akaacha kukifanya tena bila kutumwa. Ni kipenzi cha Hilda, ndiye aliyemuachia hapo kote mpaka gereji. Hakuna kinachoendelea hapo bila Tuma.” Jeremi akaendelea.

“Kwa kifupi, ndiye tunamuamini na kumtegemea sana hapo. Akikaa hapo ni kama amekaa Hilda mwenyewe.” “Kumbe!” “Kabisa. Anajua mambo mengi sana ya hapo. Kwanza amefanya kazi hapo muda mrefu. Au amekuwa na sisi kwa muda mrefu. Halafu hiyo tabia yake ya kuwahi kazini, uwaminifu, na kujituma. Tena huwa wanamwambia hana maisha mengine ila hapo. Atakuwa wakwanza kuingia na wamwisho kutoka na hatalalamika wala kuuliza. Ukitaka jambo lifanyike bila maswali wala kulalamika, mtume Tuma.” Akaendelea.

“Majukumu ya Umi ni machache na hataki kuongezewa ila anamdomo wa biashara sana. Yeye anapenda mteja akija hapo basi akutane naye yeye, azungumze naye mpaka atanunua. Na uzuri anafahamiana na watu wengi mno. Kwa kifupi anatuletea wateja na mteja akija hapo akikutana na Umi, jua atanunua hata matairi japo hakuwa na shida nayo. Ila usimzidishie kazi na muda.”

“Kuwahi kufika hapo kazini kwake ni msamiati wa kichina. Kila siku anayo sababu ya kuchelewa. Na ikifika saa 10 juu ya alama, pochi tayari ipo kwapani, na huna utakachomwambia labda umpe pesa ya ziada. Sasa Tuma huwa analemewa zaidi siku za jumamosi ambazo ni nusu siku, wanatakiwa kutoka saa 6:30 mchana. Lakini kule kwa mafundi wa kufunga matairi, kubadili oil, na kufanyia alignment huwa wanafunga saa 10 jioni. Sasa nani wakuwasaidia wale mafundi muda huo?” “Tuma?” Jerry akajibu kwa swali.

“Naona sasa wewe umenielewa. Ndio maana wakati mwingine inabidi Hilda, awe anakuja kukaa nao hapo, ili akiondoka Umi, abakie na Tuma au awe anamruhusu Tuma na yeye akapumzike. Ila Tuma mwenyewe huwa anabakiaga tu hapo na kumwambia Hilda akapumzike nyumbani na watoto.” Jerry akavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu.

“Ndio maana nimeanza kukuelekeza kwanza kwenye kompyuta upande wa stoo ili kumsaidia Tuma kuagiza endapo sisi tukilemewa na yeye amebanwa na mambo mengine. Hapo ndio pagumu na hatutaki kufundisha watu wengi sababu ya uwaminifu. Anafanya Hilda mwenyewe, na Tuma tu. Kudhibiti wizi. Ilikuwa nilazima Hilda awe anaanzia hapo kila siku asubuhi, akishawekana sawa na Tuma ndipo anakuja huku. Sasa kwa kuwa wewe utakuwa huko, ndio maana umeona leo hajapita huko ili kusijae. Ofisi hiyo ndogo sana.” “Hapo nimeelewa.” Akaendelea kumuelekeza.

~~~~~~~~~~~

Ni kweli Kesho ya Mtu ni Fumbo, na Maisha anapanga Mungu.

Jerry ameanza maisha mapya, dunia imempokea kwa mikono miwili akiwa safari hii na huku nako kwenye kampuni ya mdogo wake anafanya kazi na warembo wawili kama alivyokuwa akizungukwa na warembo kwenye kampuni ya Sandra. 

Nini kitaendelea kwenye mwanzo huo mpya wa Jerry akiwa amejawa fedheha na hana kitu?

Jo amejihakikishia anampenda Dorothy na kumuhitaji. Ni nini kitaendelea na kwao?

Mill&Pam?

Mina na uzazi wa Madume katikati ya wanaozaa majike?

Inaendelea..

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment