Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Love At First Sight - Sehemu ya 77. - Naomi Simulizi

Love At First Sight - Sehemu ya 77.

 Siku ya alhamisi madaktari walipoangalia afya yake, waliamua kumruhusu kurudi nyumbani kwa sharti la bedrest, ikiwa ni siku ya tatu kama walivyopanga kuwepo fungate. Mbali na wasiwasi na Mill na maneno aliyomwambia, lakini ujio wa Jerry usiku uliopita ni kama aliongeza chumvi kwenye kidonda. Ilikuwa hata ngumu kumtizama Mill usoni kwa muda mrefu, na hofu ikaongezeka. 

Uzuri alikuwa akishinda hapo mchana wakipokezana na mama yake, ila anakuwa tu ofisini, jioni mama yake akija kuchukuliwa, basi Mill atarudi kuwa hapo kwa muda, kwenye usiku wa saa nne au tano Pam akilala kabisa ndipo anarudi kulala nyumbani kwani ni kama walimfanya awe analala usiku kuchwa mchana walisha mpunguzia madawa. Na ni kweli alikuwa akilala mpaka akiwa anafanyiwa usafi asubuhi ndipo anaamka.

~~~~~~~~~~~~~~

Wakajikuta sasa wawili tu, njiani wakirudi nyumbani. Alikuwa ametulia kimya mpaka Mill akadhania amelala. Alipokohoa ndipo akamuongelesha. “Kunywa maji.” Akanywa, akashukuru na kurudi kukaa kama mwanzo.

“Pale kwako sasahivi anaishi mama. Nilimrudisha Shema nyumba kubwa kwa muda ili ampishe msichana wa mama kwenye kile chumba chake. Kule kwa mama Kinondoni bado pako na vitu vyake, walihamia na baadhi ya nguo.” “Aliniambia.” Akajibu taratibu asijue mwisho wa mazungumzo hayo.

“Sasa basi, upo huru. Kama unataka kurudi kuishi pale, wao waondoke ili Shema naye arudi pale kwenye kile kilichokuwa chumba chake, nitamwambia dereva amsadie kumrudisha yule binti na nguo za mama, na mama akitoka kazini, arudishwe kwake Kinondoni. Uwamuzi ni wako.” Akaishiwa nguvu kabisa.

“Ila kama alivyotushauri dokta,” Akaendelea. “Unahitajika kupumzika mpaka mtoto akomae. Haujatoka kwenye hatari. Nimeshazungumza na bibi kama anaweza tusaidia kutuletea binti wa kukusaidia. Anaonekana kuweza kufanikisha hilo, tumeshatuma nauli, Mungu akipenda jumamosi atakuwa hapa. Ili akusaidie.” “Nilidhani umesema umenisamehe, Mill!” “Kabisa. Lakini kuanzia sasa lazima kuzungumza.” Mill akaendelea.

Sitafanya mipango inayotuhusu bila kukushirikisha na kukusikia unataka nini.” “Hata mambo ya ndoa jamani!?” “Labda uniambie unamaanisha nini. Maana niliyoyafanya siku ya jumatatu yote yalikuwa mambo ya ndoa, lakini sikuwa nimekushirikisha, hayakwenda kama ambavyo nilidhani ungefurahia. Sasa sijui ukisema ‘hata mambo ya ndoa’, unamaanisha nini!? Na tafadhali jua tunazungumza tu, hamna ugomvi na sijakukasirikia.” Kimya.

“Pam?” “Mimi nilijua kwa sababu tumeoana, tunatakiwa tuishi pamoja.” Mill akamtizama kama anayemsuta akiendelea kuendesha. Akakumbuka. “Najua kwenye fungate, niliharibu. Lakini sasahivi nitakuwa makini. Naomba mimi na Shema tuhamie pale kwako, kama hutajali.” “Hata kidogo. Upo huru kabisa.”

 “Ila uwe umeamua kwelikweli Pam. Kusijetokea kumchanganya mtoto au watoto hapo baadaye changamoto zitakapo tokea tena. Unaanza kuhama tena au kutafuta kwa kuhamia, unavuruga watoto. Sasa je, bila haraka, nataka kujua kama unauhakika unataka kuishi pale na mimi, ili ile nyumba ndogo nimpe mama? Na kama pia unahitaji muda wa kujifikiria, sikuharakishi.” Safari hii akasikika ametulia, hana hasira.

“Nina uhakika Mill na asante. Mama anapafurahia pale. Anasema analala kama yupo kwao Lushoto. Baridi.” “Na mimi ameniambia.” Wakatulia ila Mill akagundua Pam amekuwa mnyenyekevu huyo!

“Kingine, sijui kama ulimsikia Jerry jana, lakini anauhitaji wa sehemu ya kuishi. Kama hutakuwa na matumizi na pale Kinondoni, nashauri tumpe yeye, apate pakuanzia.” “Hamna shida.” Kwa kutoendeleza yale mazungumzo, akajua alisikia kila kitu, akaona anyamaze.

~~~~~~~~~~~~~~

Mill akaendelea kukanyaga mafuta, kimya hakuna tena aliyemuongelesha mwenzie. Wanandoa hao wakawa wageni kwa kila mmoja wao, ni kama wakawa wamepotezamtiririko wa mazungumzo yao. Pam alikuwa ametulia. Akiendelea kufikiria. Ni kweli tokea Mill amerudi baada ya kupotea wamekuwa na mkiki mkiki, hapakuwa na utulivu. Ile hali ya furaha na kucheka muda wote waliipoteza hata kabla ya kutungwa mimba ya Shema. Ni kama Mill aliondoka na furaha yote, na aliporudi akitaka waanze tena, kukawa na ukinzani mwingiii.

Alirudi nchini na kwenye maisha ya Pam akiwa na watoto wa Kisha, na kukawa tayari kuna Shema anayewaunganisha. Zikaanza hekaheka za watoto hao, wenyewe hawachangamani, au kuendana hata kidogo. Wa Kisha dakika zilishakwenda mbele, vichwa vina moto wakati wote. 

Akamkuta mtoto wake na Pam shidani. Maisha yakachukua picha yake na mipango ya mvutano huku na kule, kukubali hili na kukataa kile. Amani ya walipokuwa wawili tu wakishinda kitandani siku nzima, haikuwepo tena. Ila akili muda wote kwa watoto na vurugu yao.

Akawepo na Mgaya na mtiti wake. Haya, akapita mrembo Brenda, tuliyemsikia mbali na urembo wake, mdada alikuwa mtulivu na ameacha historia moyoni kwa Mill. Kukapita msuguano hapo, kila mmoja anamuonea wivu mwenzie japo hawapo pamoja, lakini kumbukumbu za penzi lao la zamani zikaendelea kuwasumbua, wakahisi hao wenza ndio tatizo.

 Purukushani za huku na kule wakawaacha Mgaya na Brenda, wakabakia sasa wao wawili napo pia haikusaidia. Kila leo kulikuwa na jambo la hekaheka. Wakadhani wakihalalisha ndoa itasaidia. Lakini ndio siku ya ndoa ikawa mbaya kuliko walivyodhania, karibu kuua mtoto. Kumbe tatizo halikuwa watoto wa Kisha, wala Shema. Si Mgaya wala Brenda. Na wala si kuhalalisha ndoa. Tatizo ni nini!? Kivuli cha umbali juu ya ahadi za zamani

Maana umbali ulianza kama kivuli kidogo tu, lakini kadiri siku zilivyopita, kivuli hicho kikageuka kuwa jua kali lililochoma ahadi zao zote. Maneno matamu ya mapenzi yakapungua, sauti zikawa nadra, na mioyo ikaanza kuzoea ukimya.

Mapenzi hayakufa glafla, yalinyauka taratibu, kama ua lisilopata maji, zikibaki kumbukumbu zenye harufu ya zamani na maumivu yasiyo na sauti. Kuja kurudi kuwa pamoja, walishapoteza mtiririko wao mzima. Wanatapatapa, hawajui wanashika wapi! Kimya hapo garini

~~~~~~~~~~~~~~

Walifika nyumbani kwenye majira ya saa sita mchana wakiwa wamemuacha mama yake kazini, Shema yupo shuleni. “Usije beba kitu chochote kutoa kwenye gari na kupandisha juu. Niagize chochote unachotaka, nitakuletea.” “Nashukuru Mill. Asante. Naweza nisiwe nakushukuru vya kutosha, ila jua nakushukuru. Ni tabia mbaya tu, lakini nakushukuru sana.” “Hujawahi acha nishukuru Pam. Na karibu. Twende ukapumzike. Au unataka kula tena kidogo?” 

“Wala si kula kidogo. Huko tumboni ni kama pale hospitalini sikula! Hii mitori na supu, hakika haishiki tumbo.” Mill akacheka. “Unarudi kwenye ugali?” “Bora kuliko hii adha ya kula kila baada ya dakika mbili. Nitamwambia mrembo wa mama anisongee ugali, ukiiva tu aniletee. Nikipata na tembele na nyama! Hapo nitalala. Ila sasahivi napunguza njaa na hiyo supu aliyoniletea Kamila.” Mill alikuwa akicheka tu. Maana hiyo supu iliwekwa na viazi, na minofu ya kutosha tu. Sasa kusema ndio anapunguza njaa, akajua kweli mwanae anamla huko tumboni.

“Acha nijimwagie maji, nitoe hali ya hospitalini.” “Sasa taratibu Pam. Naona unaanza shuguli nyingiii!” “Ni kuoga tu.” “Na iwe hivyo, lasivyo tutarudi tena hospitalini na ndio wamekwambia hawatakutoa. Sasa bora uwe hapa na wanao wote wawili.” Pam akacheka akielekea bafuni. 

“Naoga tu napanda hapo kitandani. Huyu mwanao wala si mtokaji. Angekuwa wakutoka ni Shema. Nilikuwa nikipandwa na pressure mpaka kutetemeka mikono na kujawa miguu, kama nina ugonjwa wa matende. Lakini sikumuona na dalili yakutoka akabaki kula tu kama mchwa, ametulia ndani kimya. Amezaliwa utafikiri mtoto anayetakiwa aanze kutambaa!” Akaingia bafuni, Mill akaendelea kusombelea vitu ndani.

Akamwandalia kila kitu, anatoka kuoga anakutana na supu inafuka moto. “Hapo umeniwezea.” “Na ugali unasongwa.” “Hapo sasa ndio utaniweka kitandani, nitalala hata kama ukitaka kurudi kazini sitakuwa na neno.” Akawa akiongea akipanda kitandani.

“Kweli Pam? Maana nina mambo yakufanya pale ofisini! Na nakimbizana na muda.” “Huna utakachofanya hapa. Lasivyo huyu mtoto atatuweka hapa tunamwangalia yeye kama yai!” Mill akacheka.

“Unafikiri nakutania! Ukiwa na huo wasiwasi, utakuta tumekwama hapa wote, tunamwangalia yeye tu, mpaka anazaliwa tumefilisika. Wewe nenda kazini, toka muda wako. Huyu cha njaa akija, ata…” “Kuna vyakula humu ndani vimejaa, hatakuwa na kelele.” “Basi wewe nenda. Mimi nikila, nalala.” “Kukiwa na chochote, unipigie.” “Hamna chochote kitakachotokea. Kuwa na imani bwana Mill!” “Sawa ila ukiamka kutoka kwenye usingizi huu, jipime pressure, uniambie. Na pia sasahivi nakupima kabla sijaondoka.” “Na usisahau kula.” “Labda hiyo supu. Inaonekana nzuri.” Akampima tena pressure. Aliporidhika yeye na mtoto wapo sawa, akala na kuondoka.

Jo&Dorothy

Alikuja kumchukua mida ya kawaida hapo kazini. “Umejaribu kukanyaga kidogo?” “Nafanya. Ila nachoka!” “Kwa sababu umekuwa ukitumia wheelchair kwa muda mrefu, mapafu, mabega na sehemu ya juu vimeshasahau kubeba uzito. Lakini hiyo inaweza kuwa kitu kizuri kwa miguu kuanza kusaidia pia. Iamini miguu yako kuwa inaweza saidia. Usiidharau.” “Sasahivi nikiwa kazini natumia walker tu.” “Safi sana. Na nimekuandalia kitu kizuri leo. Utafurahi.” Dorothy akaanza kucheka.

“Ukifika unakwenda kuoga, unavaa nguo nzuri nimekuandalia. Nzuri sana ya usiku. Halafu romantic dinnerNimekupikia chakula kizuri sana.” “Yote hayo kwa ajili yangu tu?” “Peke yako. Na jinsi nilivyopaweka nyumbani sio kwamba pako hivyo kila siku, leo tu kwa sababu ni siku yako maalumu.” Dorothy akazidi kucheka kwa furaha huku Jo akiendelea kuendesha.

Nyumbani kwa Jo.

Jo aliendesha mpaka nyumbani kwake, akaona walinzi wale wa sare kabisa wapo getini na ndio wanao fungua geti. Akakaa sawa kuangalia. “Karibu nyumbani.” Ilikuwa nyumba ndogo tu, ila kulipangiliwa vizuri mno. Kijani iliyozunguka hiyo nyumba, utafikiri mto unapita hapo katikati ya nyumba na kuotesha majani mazuri sana. Palipendezesha sana na maua yake yalipangiliwa kiustadi kiasi cha kumvutia Dorothy zaidi. Palikuwa na gari ingine moja chini ya kama kibanda kinachoweka kivuli kizuri, kilionekana ni maalumu kwa kazi hiyo ya kutunza magari.

“Patulivu!” Akajikuta akiongea kwa sauti na kumfanya Jo acheke. “Unaishi peke yako?” “Huo ukuta hapo nyumba hiyo unayoiona upande wa pili ni kwa dada na shemeji. Tunashirikiana huo ukuta, kageti hako kadogo ni cha kuingilia kwao au wao kuingilia huku.” Kidogo akashituka, Jo akamuona. 

“Leo ni sisi tu. Kwanza huwa hawaji hapa mara kwa mara, mimi ndio nakwendaga kwao. Na leo wanajua kama upo hapa, ndio hawawezi hata kukosea kupiga simu.” Kidogo akatulia ila na aibu kidogo.

“Kwani uliwaambia nitaondoka saa ngapi?” Jo akaanza kucheka. Kisha akacheka sana. “Sasa unacheka nini?” “Wewe unawasiwasi gani Dorothy?!” “Mimi nataka tu kujua, maana wewe na huyo shemeji yako sijui dada yako mnaonekana mnaongea kila kitu bwana!” “Kwa nini?” “Sasa kwani lazima umwambie kila kitu?” “Kwahiyo wewe leo ulitaka usumbufu? Mimi sikutaka hata hodi leo, ni mimi na wewe tu, ndio maana nikawatahadharisha mapema. Na wasianze simu zao.” “Mmmh!” “Twende ndani acha woga.” Akamkaribisha ndani.

Akagundua amemtengenezea mpaka sehemu maalumu ya kupitisha wheelchair yake. “Nashukuru.” Akashukuru wakati akiingia kwa urahisi. Jo akafurahi kutambuliwa juhudizake. Angeweza tu kupita na asiseme kitu. “Karibu.” Akajibu akifungua mlango mkubwa wa mbele.

“Sio nyumba kubwa. Vyumba vingine natunza endapo vijana wangu wakija nitembelea. Lakini wamekuja mara moja tu. Kwa hiyo natumia chumba kimoja tu. Ingia nikutembeze. Palikuwa na vitu vichache, ila vimepangiliwa vizuri na kuvutia. 

Akaona sehemu zote mpaka jikoni. “Pasafi sana. Unapatunza vizuri.” “Asante. Na hiki chumba kingine ndio changu. Nimekuwekea mpaka taulo huko bafuni. Ingia uoge utoe uchovu, nguo utaikuta kitandani. Ukitaka kitu, niite nikusaidie.” “Na nguo nyingine?” Akaanza kucheka vile alivyouliza. Ila akamuelewa. “Dorothy anawasiwasi! Nimekuandalia kila kitu. Wewe ingia kuoga, utakuta kila kitu hapa kitandani. Namaanisha kila kitu, mpaka sidiria. Karibu.” Akacheka na kuendelea kuangaza macho hapo chumbani kwake.

Majivu Yasiyozimika

“Ila unathamani nzuri sana. Sana, zinavutia. Hazichoshi macho!” Dorothy akaendelea kuangaza macho.

“Na huyu ndio mkeo?” Kulikuwa na picha kubwa, yenye fremu nzuri sana. Wazi ilionekana iligarimu pesa nyingi mno. Aliuliza swali la kawaida asijue ukubwa wake na jinsi litakavyobadili kila kitu

Hakujibiwa ila ukimya wa gafla, akamuona anaisogelea hiyo picha na kutulia mbele yake. Akaingalia kwa muda, kisha akamsikia akisema. “Betty!” Na kuigusa picha. Akabaki akiiangalia na kushindwa hata kugeuka akiwa amempa mgongo mgeni wake. Dorothy akawa amepata jibu lake ila akagundua si shwari tena. Wanasema muda ni mchawi. Muda una nguvu ya kubadili mambo kwa njia ya ajabu na isiyotabirika.

Ukimya wa gafla ukatanda. Vicheko vikakoma. Dorothy akasoma mazingira kwa haraka sana. Akajua tayari muda umefichua siri na ukweli halisi. “Nina wazo la tofauti.” Dorothy akavunja ukimya. Ndio ikawa kama amemgutusha mwenyeji wake, akageuka. “Pengine mimi nikaribie tu huko kwenye chakula, nitakwenda kuoga kwangu.” “Kwa nini?” Wazi lilionekana ni swali tu, hakuwa hata na ujasiri nalo. “Naona hiyo ndio itakuwa rahisi.” Akajibu na kuwasha kigari chake, akaanza kutoka. Jo akawa kama amepigwa butwaa, hajui amrudishe au la!

 Alipatwa na hali kama ambaye hakuwa amefikiria vizuri kuleta mwanamke chumbani kwake na mkewe. Akajihisi ni kama anamsaliti mkewe!

Alishakuwa kwenye mahusiano, lakini sio mpaka kuleta mwanamke nyumbani, tena chumbani! Akahisi hakufikiria vizuri. Akajihisi eti ameharakisha! Akasahau Betty alishaondoka duniani muda mrefu sana. Hukumu ya ajabu ikamuingia. Akabaki hapo chumbani pembeni ya picha ya marehemu mkewe. Amepoteza dira. Dorothy yupo sebuleni, Betty pichani, chumbani.

Kwa kuwa alisha mzungusha Dorothy humo ndani kwake, hakupata shida kurudi sebuleni, kama kumpa nafasi. Ikawa mgeni sebuleni, mwenyeji chumbani. Kimya. Hiyo nyumba hata ukiangusha kijiko kitasikika kote. 

~~~~~~~~~~~~~~

Baada ya muda akatoka. “Samahani Dorothy. Samahani sana.” “Usijali hata kidogo. Ila ujue njaa inaniuma mwenzio. Tuonje mapishi yako. Au umeunguza unaona aibu.” Angalau akamfanya atoe tabasamu akijaribu kutulia.

“Mimi ni mpishi mzuri sana.” “Sawa! Tule basi.” Kwa jinsi alivyoonekana Dorothy, ikamsaidia Jo kwenda na ile hali. Akampa kinywaji wakati akiandaa meza ila wazi alionekana mudi imebadilika.

“Nikusaidie nini?” “Wewe andaa tumbo. Vinono vinakuja.” Akamsikia akijibu kutokea jikoni. Kama kawaida yake Dorothy akacheka. Baada ya muda akatoka jikoni.

“Nimeandaa meza ndogo, sio kubwa. Nifuate.” Akafuata na kuona hiyo meza. Ukweli aliandaa vizuri sana. Akacheka. “Haya maandalizi ya meza yanavutia mpaka chakula hata kama ni kibaya vipi kinapita kwa raha.” Angalau Jo akacheka. “Ujue wewe Dorothy huamini kama mimi ni mpishi mzuri sana!” “Wewe acha nile, ndio nikusifie.” Basi wakakaa mezani, akamsogezea vitu karibu, akajipakulia akasubiria na Jo akapakua.

Kabla Jo hajaanza kutafuna, maana aliweka kijiko kimoja mdomoni, Dorothy akamuwahi. “Tumshukuru Mungu kwanza Jo! Njaa gani hiyo?” Akacheka kwa aibu. “Samahani. Huwa siombei chakula.” “Basi tumshukuru Mungu kwa kutupa chakula, nguvu na muda wa wewe kupika. Mwenzio sijawahi pikiwa kwa namna hii!” “Lakini pia hujawahi pata mwanaume mbambaishaji kama mimi.” Akaanza kujishuku.

“Wewe sio mbambaishaji Jo. Katika wababaishaji wewe haupo. Ni mtu wa maneno yako.” “Acha kunisitiri wakati nimetoka ku..ku..” Akasita na Dorothy akatulia tu akamuona mpaka amebadilika sura. “Nilijua ingekuwa rahisi tu. Na…” Akasita tena.

“Nili nili….” Akashindwa tena. “Samahani Dorothy. Niliiandaa hii siku nikitaka iwe nzuri kwetu.” “Mimi mpaka napatwa na wasiwasi na hiki chakula bwana! Mbona kama unanizungusha nisikiweke mdomoni!” Alitoa tu tabasamu akionekana wazi hayupo sawa naye Dorothy hakutaka amuweke kwenye hiyo hali muda mrefu na pia alijiambia hatamsaidia kumuwekea maneno mdomoni au kuzungumzia jambo ambalo hajui kinachoendelea moyoni mwake, mpaka achukue mwenyewe hatua yakufunguka.

Akainamisha kichwa na kufunga macho bila ya kuendelea, akionyesha yupo tayari kwa maombi. Basi Dorothy akamshukuru Mungu kwa huo wakati, nguvu ya kufanya kazi na kumbariki Jo akikumba vijana wake na familia kwa ujumla. Ikawa fupi ila nzuri. “Amina.” “Amen.” Jo naye akaitika.

“Haya sasa, siongei tena ili ufurahie chakula.” “Hayo ndio maneno.” Ndipo wakaanza kula, ila Jo alionyesha kabisa amebadilika kama anayejilazimisha hata kula. Pakawa kimya hapo mezani, hakuna aliyezungumza tena. Naye Dorothy ikawa kama aliyejionya kutomwingilia. Akamuacha akiendelea kula. 

Kimya mpaka wakamaliza. “Mimi naomba nifungashie hiki chakula kidogo, nimpelekee Pam. Maana nikimsimulia, anaweza asiami.” “Kilivyo kibaya?” “Kizuri mnoooo. Kuliko kile unachonipelekaga kula kule unakolipa mapesa mengi.” Jo akacheka kama ambaye haamini tena. “Kweli?” “Kabisa. Nimekuamini kama wewe ni mpishi mzuri, na ili kisiwe kiporo, nirudishe nimuwahi kabla hajalala.” Jo akajua anakuwa tu muungwa, anatumia hekima kumuaga

Ila naye akawa kama amepatwa na hali fulani hivi, hajui jinsi yakuendelea tena. Ilikuwa ngumu hata kulazimishia! Ilishindikana kabisa. Akashukuru hiyo hekima aliyotumia Dorothy, maana alijua anaweza haribu.

Ukweli ilikuwa mapema sana mpaka akajisikia vibaya kumrudisha kwake, lakini hapakuwa na jinsi. Mazingira yalishakuwa si rafiki tena. Ikawa tofauti kabisa na alivyomuahidi Dorothy. Basi akamfungashia chakula, hata hakuosha vyombo. Akamwambia watasafisha wasafishaji kesho yake. Wakaondoka.

~~~~~~~~~~~~~~

 Njiani kimyakimya kila mmoja ametulia. Na yeye alijua akizungumza kitu kabla hajajiandaa, na kujielewa, anaweza akaharibu, na maneno hayarudi. Akaona bora aibu kuliko fedheha. Kimya mpaka kwa Mill ambako alikuwa akipafahamu hakuhitaji kuelekezwa.

“Nashukuru Jo. Asante na uwe na usiku mwema.” Jo akasimama kimya mbele yake kama ambaye hajui aseme nini, amepoa, amebadilika, anashindwa hata kumtizama machoni. Dorothy akacheka kama kumtuliza. “Nenda kapumzike na mimi acha niingie hapo kwa Pam, nipate naye muda kabla ya Mill hajarudi. Urudi nyumbani salama.” Akaondoka kabisa na kigari chake akimuacha Jo amesimama nje ya gari yake.

~~~~~~~~~~~~~~

Wakati anapanda juu kuingia ndani, maana na Mill alikuja tengeneza kama kidaraja kumrahisishia, akaona anarudi garini. Hata hakugeuka ila akampigia simu Shema. “Njoo unifungulie mlango, na umwambie mama yako ashuke chini.” Aliposogea mlangoni akasikia akishuka ngazi akikimbia huku akipiga kelele.

Mlango ukafunguliwa. “Hivi wewe hujaambiwa kama mama yako anatakiwa kupumzika?” “Nimefurahi kukusikia bibi jamani! Umebeba nini?” “Sasa chakula hiki cha mama yako, usimalize Shema. Maana wewe njaa zako haziishi bwana.” Shema hana mbavu. Akampokea bibi yake akaingia ndani na Pam naye akawa anashuka.

“Moja kwa moja jilaze hapo kwenye kochi, Pam.” “Na hicho chakula?” “Hivi wewe na mwanao huwa hamshibi?” Wakazidi kucheka. “Acha nile, ndio nijilaze unipe habari za huko ulikotoka.” Akawa kama amekumbuka kitu. “Lakini mbona mapema hivyo!? Sikukutegemea leo!” Mama yake hakujibu kitu, akamuona hayupo sawa. Akajua mambo hayakwenda vizuri. Akamuacha.

Akaenda kukaa na mwanae akaleta vijiko viwili, wakaanza kula. “Hivi nyinyi! Hata kuweka kwenye sahani jamani!” “Mama naye! Sasa hapa si vinapita mdomoni bila shida.” Wakaendelea kula na mwanae akifurahia, akamuona mama yake amepoa haswa, ameduaa akiangalia kwingine, wazi mawazo hayakuwa pale. Akamuacha. Wakala mpaka wakamaliza bakuli lote.

“Ni vitamu!” “Kapika Jo. Anaonekana mpishi mzuri kweli!” Pam akamtizama akajua hawezi kuongea mbele ya Shema. “Haya, nipishe hapa nijilaze. Nenda kaoshe hili bakuli kisha ukamalizie homework zako ndio uje kuangalia tv.” Akaondoka.

~~~~~~~~~~~~~~

Akamgeukia mama yake. “Kwema?” Akarudisha mawazo kwa binti yake. “Kwema. Vipi wewe?” “Nimelala siku nzima. Nasijapata damu. Naona hatari imepita.” “Afadhali. Ila uendelee kupimzika Pam. Usizembee.” “Najitahidi. Vipi wewe huko kwa Jo?” “Mmmh!” Akawa kama anajaribu kufikiria hapati jinsi ya kueleza.

“Nini?” “Hata sijui!” “Kwani imekuaje?” Akamsimulia kuanzia jinsi alivyokuwa akiisubiria hiyo siku ya alhamisi mpaka alivyomfuata kazini, na maandalizi aliyokuwa amemfanyia. 

“Sasa tulipofika kwake akaniambia ananizungusha nipaone kila mahali. Sio nyumba kubwa kama hii, lakini pasafi sana na vitu vichache vya thamani kwelikweli. Pazuri mno. Ndio akanipeleka chumba cha mwisho, ambapo ndio chumbani kwake, kwamba nioge, na nguo ameshaninunulia kabisa.” “Ana upendo! Halafu anakujali!” 

“Mmmh! Sijui Pam, nafikiri hakuwa amefikiria mbali, mpaka nimemuhurumia!” “Kwa nini?” “Hicho chumba chake kinakitanda hicho, sijawahi ona. Mameza ya thamani mpaka makochi! Mazuri na tv kubwa. Kapeti zuri mno la manyoanyoa. Nikavutiwa. Sikuwa nimewahi ona chumba kizuri vile. Kwanza kitanda chenyewe nicha mviringo, halafu kuna rembo hizo, hakika hujawahi ona, Pam. Kitu kizuri mno.”

“Katika angaza macho ndio nikaona picha kubwa ya mwanamke inaangalia kitanda. Nikamuuliza huyu ndio mkeo? Hilo swali lilimbadilisha kabisa. Kuanzia hapo alishindwa kuzungumza kabisa. Alipoa, kila alivyojitahidi maneno yalikuwa hayamtoki. Sijui hukumu!” “Unahisi ameona ni kama anataka kumsailiti mkewe?” “Nafikiri hivyo.” “Kwani tokea mkewe afariki hajawahi kuwa na mwanamke mwingine?” “Anavyosema keshajaribisha mara mbili, lakini si kufikishana nyumbani. Hilo anasema hajawahi na hakutaka.” Akamsimulia juu ya wanawake wa Jo.

“Mmmh! Mbona sasa imekuwa hivyo!?” “Sijui Pam! Sijui mwanangu, ila mpaka nimemuonea wivu huyo Betty!” “Mzuri eeeh?” Akacheka kwa kuguna. “Kweli Mungu humpa amtakaye na hakuna wakumuuliza kwa nini! Hawaendani na Jo, hata kidogo. Yaani hata!” “Mama!” “Ukiambiwa ndio mwanamke alikuwa daktari tena huko nchi za watu, na alikuwa na maisha mazuri, unaweza usiamini.” “Kwa jinsi alivyo?” Pam akauliza.

“Kwa vile alivyo, au jinsi nilivyomuona. Hata kama ungesema picha ilipigwa vibaya,lakini hataaa! Na ndipo nilipopatwa na wivu na heshima juu. Kwamba mapenzi SI sura wala umbile Pam.” “Na kweli mama. Lasivyo wazuri wote wangekuwa na wanaume.”

“Ewaaah! Kwa vile nilivyomuona yule mwanamke, simsemi vibaya, ila kwa ule muonekano, na kwa jinsi Jo anavyomzungumzia! Na nilivyomuona leo alivyobadilika, hakika natamani ningekutana na huyo mwanamke nijue alikuwa wa namna gani!”

“Maana Jo mwenyewe alisema alikuwa na picha ya mwanamke mwingine kabisa kichwani kwake, lakini Betty akazidi matarajio yake. Anamsifia huyo mwanamke na si kwa kujisingizia. Akimuongelea mpaka atamuhurumia. Sasa na jinsi leo alivyobadilika nilipoingia chumbani kwake ambako yupo bado mkewe, ndipo utagundua kuwa uzuri wa mwanamke si urembo, ni kile alichobeba moyoni.”

“Mama!” “Hakika Pam. Inaonekana yule marehemu mkewe alikuwa zaidi ya muonekano huu wa macho yetu sisi wanadamu. Inamaana alibeba kitu cha thamani sana, maana nasikia hata huko kazini kwao aliacha pengo kubwa sana. Na inaonekana ni pengo ambalo bado lipo moyoni kwa Jo, ameshindwa kuliziba hata kwa alichodhania angeweza.” “Unamaanisha nini?”

“Ndoto za Jo ilikuwa ni kuoa mwanamke mweupe. Nafikiri ndicho kilichomvutia kwangu kwa haraka. Bila ya kufikiria, nafikiri hisia zikampeleka mbiombio, akaanzana na mimi akijua amepata alichokuwa akikitafuta kabla ya Betty. Sasa nafikiri leo ndio amekutana na uhalisia. Kwamba moyo wake hauhitaji mwanamke mweupeulishampataBetty ambaye alikuwa KILA KITU, hamna jinsi akaziba hilo pengo.” “Pole mama.” Alimuhurumia sana mama yake.

“Natamani nikalale usingizi mzito nisiwaze kitu kabisa. Nilale tu.” “Nikupe dawa zangu za usingizi?” “Bora.” Mara simu ya baba Shema ikaingia.

~~~~~~~~~~~~~~

Akapokea na kusalimiana, kisha akaweka ombi lake. “Unaweza kubaki na Pam kesho nyumbani ili mimi niwepo kazini siku nzima?” “Na Stella?” “Atajipanga, usiwe na wasiwasi na ya huku kazini. Nataka Pam atulie kabisa angalau hata hili juma liishe.” “Hamna shida. Na ninashukuru kumjali. Mungu akubariki baba Shema.” Akacheka na kushukuru. Wakaagana.

~~~~~~~~~~~~~~

Akamwambia Pam ombi la baba Shema. “Bora tubaki wote.” “Na mimi nimezidi kumshukuru Mungu. Acha Jo apate muda wamapumziko na yeye. Atakuwa anachoka. Naenda kumtumia ujumbe kesho asubuhi hana haja ya kuja hapa. Nazima simu kabisa, nilale mpaka kesho. Ndio nianze siku nyingine kwa upya nikijua ninapo simamia kuanzia sasa.” “Pole mama yangu. Utakuwa sawa.” “Naamini hivyo!” Akafikiria na kuguna.

“Jo ameanzisha kitu ambacho hata sikujua kama naweza kukipata. Nikakubali kiharaka, nikafungua moyo wangu wote bila kujipa muda. Najuta! Najuta sana kukubali kujiingiza kichwakichwa kama kwa baba yenu! Na yeye alinikuta nimetulia zangu, sina hata mpango wa kuolewa! Kwanza nilikuwa mdogo. Hata akili ya mwanaume haikuwepo. Akanilaghai kwa maneno mazuri, kama hivi tu kwa Jo, nikampa moyo wangu, akaishia kunitesa bila sababu! Najuta sana.” “Pole mama.” Pam aliumia kutoka rohoni.

“Mmmh! Acha nikapumzishe akili na nafsi yangu.” Akamuita Shema, akamtuma dawa. Akampa mama yake, akaondoka hapo akiwa amepoa, Pam akimuhurumia sana. Maana alishabadilika kwa furaha ya Jo, sasa safari hii ndio amerudi chini kabisa. Alinyong’onyea, mpaka akaona kweli ni bora akalale tu. Na yeye akarudi chumbani kwake.

~~~~~~~~~~~~~~

Dorothy akaingia kuoga, akapanda kitandani na kumeza dawa. Wakati anapitiwa usingizi akakumbuka hajamtaarifu Jo. Akatoa simu yake aliyokuwa ameiacha kwenye pochi.

‘Nashukuru kwa kunikaribisha nyumbani. Asante. Kina Pam wamesifia sana chakula chako. Nashukuru kutoa muda wako kupika kwa ajili yangu, Mungu akubariki. Baba Shema ameniomba kesho nibakie nyumbani na Pam, nimsaidie mambo ya hapa nyumbani ili apumzike kabisa. Kwa hiyo sitakwenda kazini. Usije kunichukua, na wewe uanze weekend yako mapema. Pumzika. Usiku mwema. Leo nawahi kulala, sijisikii vizuri.’ Alipotuma huo ujumbe, akazima simu na kupotelea usingizini, asitake hata kujua alipo kwa muda huo maana alikamatwa na hofu ya ajabu. Jo alimuonjesha penzi ambalo hata hakujua kama anaweza kuja pata. Leo ndio iwe mwisho! Aliogopa hata kufikiria, akaona bora alale tu.

~~~~~~~~~~~~~~

Asijue huku kwa Jo hali aliyonayo ni mbaya kuliko yake. Alirudi kwake ikawa kama ameanza upya msiba wa mkewe. Baada ya muda mrefu sana kupita akiendelea na maisha kama kawaida kana kwamba hakuna lililompata, siku hiyo alipatwa hali ambayo hakuwa ameipata kabla. Kitu kilimkaba, akapatwa hali ya uchungu mbaya sana. Akajikuta analia chumbani kwake na kushindwa kujizuia kama ndio Betty amefariki siku hiyo, maiti ipo ndani. 

Alilia Jo hata simu hakujua ilipo, kwamba hata ujumbe wa Dorothy hakuona na wala kitandani hakufanikiwa kupanda.

Na hivi alishasema siku hiyo asisumbuliwe yupo na Dorothy, hapakuwa hata na hodi ya bahati mbaya wala simu ya kujuliwa hali. Alilia peke yake asipate wakumtuliza. Na yeye akawa hajui analizwa na lipi ila uchungu mkali sana.

~~~~~~~~~~~~~~

Kifo ndicho kilimuondoa Betty duniani, ila moshi wa mapenzi yao kumbe badoulikuwa ukimfuata Jo. Msiba wa mkewe haukuwa kaburini, umebaki ndani ya kifua chake akijaribu kusahau na kutaka kuendelea bila kumaliza msiba huo kwanza

Betty alipofariki tu, alikimbia kaziakauza nyumba na kukimbia nchi akijaribu kuepuka kuomboleza.

Akalazimishia kuzika ukweli wa mambo.

Akajaribu mahusiano kwa wanawake wawili ikashindikana akidhania tatizo ni wao, kumbe bado yupo na msiba ALIOSHINDWA kuumaliza.

Leo anakutana na Dorothy asiye na kasoro, akitaka tena kulazimishia mambo, lakini amegonga mwamba.

Hatimaye amekutana na uhalisia. 

Betty alifariki, hakupata muda wa kukaa chini, kupokea ukweli, kufanya mazishi ya kwelikumzika mkewe, kumuombolezea na kisha kukubaliana na uhalisia kuwa alishaondoka dunianihayupo tena kwenye maisha yake.

Mill&Pam Je?

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment