Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Love At First Sight - Sehemu ya 76. - Naomi Simulizi

Love At First Sight - Sehemu ya 76.

 

Mill akiwa na nguo za kulalia akapiga simu mapokozi akiomba gari ya wagonjwa. Alipoona wana maswali mengi akampigia simu Colins kwamba apigie gari ya wagonjwa hospitalini kwao na kuwafuata hapo kwa haraka, Pam amepoteza fahamu na kunahatari ya kupoteza mtoto.

Alichofanya kwa kuwa alimuona jinsi alivyoanguka, akajua hajavunja kiungo chochote, alishuka taratibu tu akijaribu kupambana kushikilia mashuka ya kitanda. Akajua haitamdhuru kumwanyanyua. Akamuweka ubavu upande wa kushotoakamnyanyua miguu kwa kumuweke mito ili kusaidia damu kufika kwenye ubongo. Kwa kuwa alikuwa amevaa rob, akamfungua mkanda wa katikati ili usimbane huku akimuita jina lake. Mill ni nesi alijitahidi asipaniki ili kumsaidia japo alishaingiwa hofu. Akaendelea kumpa huduma ya kwanza.

Wakati meneja wa hoteli na wahudumu wengine wanagonga, simu ya mzee Komba ikawa inaingia. “Hakuna gari ya wagonjwa lakini kuna usafiri wa kumpeleka hospitalini kama utakuwa tayari kufanya hivyo, vinginevyo nimeshaita gari ya wagonjwa, lakini inaweza chukua muda.” 

Simu ikaendelea kuita, akampokea mzee Komba. Moja kwa moja akaanza kumpa maelekezo. “Hakikisha damu yakutosha inakwenda kwenye ubongo. Na usimlaze chali.” “Nimeshamuweka ubavu na kumnyanyua miguu juu.” “Pressure ipo ngapi?” Mill akamgeukia yule meneja.  “Unayo mashine ya kupuma pressure?” Mmoja akamkabidhi kisanduku cha huduma ya kwanza. Mill akafungua kwa haraka. “Hamna mashine hapa!” “Itabidi umpime kwa mkono.” Mzee Komba akatoa wazo.

“Kuna dalili nyingine?” Akaunganisha swali. “Ameanza kutokwa damu.” “Nahisi pressure itakuwa imepanda sana. Mpime uniambie. Gari imeshatumwa, wanakuja hapo, lazima awekewe oxygen. Mtanikuta hospitalini na daktari wa wakina mama. Ila nijulishe pressure yake na hakikisha unaendelea kumuita akuitike.” Akakata. Mill akampima mapigo ya moyo kwa kuweka vidole vyake viwili kwenye mkono wa Pam karibu na viganja/palm wrist, akiangalia saa huku akihesabu.

Akashituka sana. “Hii pressure ipo juu sana! Mtu asimguse. Ipo gari ya wagonjwa inakuja. Lazima apate oxygen sasahivi. Kumsafirisha hivyo bila oxygen itakuwa hatari kwake. Na naomba mpungue hapa chumbani apate hewa.” Anaongea hivyo huku anabadili nguo hapohapo mbele yao. 

“Tokeni humu ndani tafadhali, hamna mnachoweza msaidia ila kumaliza hewa tu. Na naomba mkapokee watu wa ambulance, mmoja wenu awalete huku juu.” Wote wakatoka ila meneja akabaki hapo ndani. “Nisaidie nini?” “Ongeza mto mwingine miguuni, kusaidia damu kwenda kichwani.” Mill akaendelea kumuita akimpa huduma ya kwanza mpaka akaja kuchukuliwa na kupelekwa hospitalini.

~~~~~~~~~~~~~~

Alikutwa akisubiriwa huko hospitalini na madaktari wa kila namna. Kwa haraka sana akarudiwa ufahamu. “Nipo wapi?” Hapo alikuwa na dripu ya maji tayari. “Hospitalini. Usitoe hiyo oxygen puani. Wote nyinyi wawili mnaihitaji hiyo.” Daktari aliyekuwa akimuhudumia akamjibu na kuendelea akirudishia oxygen puani. “Pressure ilipanda sana, ulipoteza fahamu.” Akashituka sana. “Huyo huko chini anafanya nini!?” Akauliza kwa wasiwasi. Anakuwekea catheter ili upumzike na kukuhifadhi ili usichafuke kwa damu. Hapo ndio akashituka zaidi, akijua kwa hakika mimba imetoka.

“Mungu wangu mtoto wangu!” Akaanza kulia, Pam hatulii hataki tena kumsikiliza yeyote hapo ndani, ikabidi Mill aitwe. Wote wa nje wakaingia tena ndani kwa paniki. “Naomba wengine wasubirie nje. Bado anavalishwa.” Colins na baba yake wakatoka wakiwa na Kamila pamoja na mama Komba. 

“Pam, Pam! Naomba utulie, na unisikilize.” “Nimeua mwanangu!” Akaendelea kulia. “Mtoto hajafa. Yupo salama kabisa. Wametoka kusikiliza mapigo yake ya moyo. Hao wanakuvalisha ili uwekewe mashine ya kum monitor mtoto. Tulia ili pressure nayo ishuke, mtoto abaki salama.” Ndio akatulia.

“Tulia kabisa.” Wakamvalisha, mzee Komba akaingia na familia yake, nashauri apewe dawa ya usingizi alale kabisa kwa usiku huu.” Wakaona si wazo baya, wakamuwekea dawa ya usingizi huku macho yapo kwenye mashine inayoonyesha mapigo ya mtoto. Yalikuwa sawa. Akabaki akiangalia hapo mpaka akapotea usingizini kabisa.

Fungate, Hospitalini

Alilala, ikiwa imeshakuwa siku inayofuata baada ya harusi, yaani siku ya jumanne. Akaamka mchana akiwa anabadilishwa. Akamuona Mill amesinzia pembeni ya kitanda, shuguli za hapa na pale za huyo muuguzi wote wawili wakaamka. “Vipi mtoto?” Pam akauliza taratibu akiangalia mashine. “Mwanao mcheza mpira. Si unamsikia hapo.” Akavuta pumzi kwa nguvu, Mill akakaa sawa. Muuguzi akamaliza yake na kutoka.

“Unajisikiaje?” Akauliza kwa kujali. “Usingizi. Nasikia tu kulala.” “Pumzika kabisa. Inamsaidia mtoto na wewe kushusha pressure.” Akarudisha macho kwenye mashine inayoonyesha mapigo ya mtoto. Akatulia kwa muda.

“Mama?” “Alikuwa hapa muda wote, ilinibidi kurudi hotelini na kutoa mizigo yetu, na kurudisha nyumbani.” Pam alilia sana akishindwa kunyamaza. “Nimeharibu mapumziko mazuri mimi mwenyewe!” “Nisikilize Pam. Nimetoa kile chumba kwa sababu tupo hapa. Na hawawezi kukutoa hapa mpaka wafanikiwe kushusha kabisa hiyo pressure. Kwa hiyo sijakitoa kile chumba kwa kukasirika ila ni kwa sababu kwa sasa, hatutaweza kukitumia. Ni garama itabidi tulipe sababu ya mtoto. Afya yako ikikaa sawa, tutajipanga tena.” Kidogo akaanza kutulia.

Nitabadilika Mill. Nakuahidi nitabadilika. Usinikatie tamaa. Tafadhali nipe muda. Ndio nimeelewa kwa uwazi maafa ninayo…” “Pam! Pam!” Akamuita akitaka atulie asije mpandisha tena pressure na kuzua taharuki nyingine tena hapo hospitalini. Akamsogelea kabisa pale kitandani. “Msamaha wa jana unatosha.” “Lakini nimekuwa nikikuumizaMill, kama baba yangu alivyokuwa akimfanyia mama yangu! Mimi sio mtu mzuri.” 

“Nisikilize Pam, najua nimekuogopesha sana jana, ni kwa vile umekuwa mtu wa mwisho kugongelea msumari wa mwisho kwenye maumivu yaliyosababishwa na wengi kwenye maisha yangu. Yaani wewe ndiye uliyekuwa karibu, na wa mwisho kama nilivyokwambia, uligongelea msumari wa mwisho, nikiwa na mambo mengi kichwanikuchoka, ndipo nikakumalizia wewe hasira zote.” “Lakini nimekuwa nikikuumiza! Naomba nisamehe.” “Yameisha Pam. Yameisha kabisa. Naomba utulie. Wamekupa dawa upumzike.” Akaendelea kwa tahadhari akitaka atulie kabisa. 

~~~~~~~~~~~~~~

Maana hata ukweli wa kilichotokea na kutibuana kwa kiasi hicho, hakuna aliyeweza sema. Wawili hao wakanyamazia ukweli kabisa. Watu wakajua ni kuchoka tu kwa Pam na sherehe ya harusini imempandisha pressure wasijue walikuwa kwenye kutibuana karibu juma zima. Siku ya harusi ni kama walifikishana juu kabisa, ndipo mwili wa Pam ukasalimu amri.

~~~~~~~~~~~~~~

“Unakumbuka nilikuomba unibebee huyo mtoto?” Akatingisha kichwa akikubali ila machozi yakimtoka. “Basi hata sasa, naomba nibebee tu. Hatima yake inategemeana na wewe bila hivyo, tutampoteza. Jaribu kutulia. Unasikia njaa?” Akakataa kwa kutingisha kichwa, na kupotelea usingizini akiwa amejifunika mpaka kichwani.  Akalala na hiyo siku nzima.

Siku Ya Jumatano Hospitalini

Dorothy&JO

Siku inayofuata, yaani siku ya jumatano, wakaacha kumpa madawa ya usingizi ila kuhakikisha anapumzika. Maana siku ya jumanne siku nzima ilikuwa kulala tu. Kwenye majira ya saa sita na nusu akaona mama yake anaingia. “Sizuruli bosi. Huu ni muda wangu wa chakula cha mchana.” Mill akacheka. “Karibu mama.” “Sasa na wewe zamu yako. Toka kidogo unyooshe miguu.” “Unauhakika? Maana nina kitu nataka nikafanye pale ofisini.” “Wala usijali. Stella alishaniruhusu nije hapa muda tu, lakini nikamuhurumia. Nilitaka akale kwanza kwa uhuru ndipo nije. Wewe nenda tu nitakuwepo.” Mill akatoka akionekana na haraka.

Pam akamwangalia na kucheka. “Mbea wewe! Sasa kinachokuchekesha nini?” “Umebadilika mama wewe! Unaonekana unafuraha!” “Ninavyodekezwa!” Pam alicheka mpaka machozi.

“Mama!” “Hakika na uzee huu mimi sikujua kama naweza pata mtu kama Jo! Bwana mwanaume ananipenda!” “Mama!” “Hakika sijisifii tu. Kwanza kwa vile baba yenu alivyonitenda ubaya wakati nikiishi naye! Ile hali ya kutoridhika kwa chochote ninachomfanyia! Akinikosoa kwa kila juhudi ninayofanya! Hakuwahi nisifia hata kwa chakula nilichokuwa nikimlisha kwa jasho langu! Hakuna kitu nilifanya kwake akafurahia.” Pam akajisikia vibaya, akajifananisha naye.

“Sasa nafikiri aliniathiri akili zangu kabisa. Sikujua kama mimi kama Dorothy ninaweza nikapata mtu akanipenda kwa kiasi cha Jo. Pam?” Pam akarudisha mawazo pale. “Yule mwanaume ananipenda aisee, mpaka najiuliza anachanganywa na nini!” “Mama wewe ni mzuri sana. Halafu unamoyo mzuri ambao haufichiki. Mimi mwenyewe na jeuri yangu nikiwa na matatizo nataka uwe karibu yangu.” Mama yake alicheka sana.

“Kweli mama. Ukiwa karibu na mtu yeyote mwenye magumu, unamfanya ajisikie kutulia.” “Kweli Pam? Maana eti na Jo naye anasema hivyohivyo! Eti ananiambia akiwa na mimi anajisikia haihitaji tena kitu.” Pam alicheka sana.

“Na mimi nilicheka hivyohivyo, nikajua ni kunipamba tu. Eti anasema anajisikia si muhitaji tena. Anajisikia kafika kabisa. Anapumzika.” “Basi ujue ndivyo ulivyo mama. Kwanza si mlalamishi hata! Upo hivyo tokea nakua. Hata nikilalamika shida, unakuwa na neno la kunituliza. Nimemlea Shema kwenye ugumu lakini ukiniongoza ukiniambia nitaweza tu, mpaka amekua! Ndivyo ulivyo mama. Halafu pia, imani yako kwa Mungu ukute ndio inakulipa mama yangu. Umekua ukimuamini Mungu hata palipokuwa hakuna tumaini!” “Labda Pam! Lakini najua Mungu ana mambo yake kwa hakika! Jo! Ananipenda yule mwanaume! Ananipenda sana na kunitakia mema.”

“Hongera mama.” “Namshukuru Mungu. Nimetoka pabaya Pam wewe! Pabaya sana. Baba yako aliishi na mimi akiniumiza nafsi, akili na mwili wangu kila siku! Kunirudisha kwetu ilikuwa nafuu kuliko vile nilivyokuwa nikiishi kwake mzima.” “Kweli mama?!”

“Acha Pam. Ni bora mara 100. Na sikudanganyi. Ilikuwa bora kurudi kwetumlemavu, nikisota mavumbini, kuliko alivyoishi vile na mimi.” Pam akazidi kuumia sana akimfikiria kule alikokuwa na yeye akimpitisha Mill. “Lakini Mungu amenifuta machozi kwa nguvu! Mpaka siamini! Amenitumia Jo, ni kama Mungu kazini. Eti siku ile ya harusi yako uliponipa wewe mkufu wako na kunipuliza pafyumu, ananiambia eti amejisikia yeye vibaya!” “Kwa nini tena?” “Anasema yeye ndiye aliyetakiwa kuyagundua hayo na kuyatimiza. Sio kusaidiwa. Anasema yeye sio kipofu na anapenda sana pafyumu. Anasema alitakiwa kufanya yeye sio wewe.” “Jamani!” Akamgusa zaidi Pam.

“Ona shingoni na mkononi!” Akamsogelea, Pam shabiki mpaka akajinyanyua kuangalia. “Mama! Hii dhahabu nzuri sana! Itakuwa imemgarimu sana, kupita kiasi!” “Bado kuna ya kanisani. Ameniletea jana alipokuja nichukua. Anasema hizo za kanisani dada yake alienda kumsaidia kununua.” “Mama! Mpaka wifi!” “Bwana mwanaume anahangaika huyo! Hivi alitaka siku ya alhamisi akinitoa hapa, twende kwake. Mwenyewe anasema anataka akanipikie, na kunipa romantic dinner nyumbani kwake! Lakini leo nimemwambia sitaweza. Wewe mgonjwa.” Pam alishituka mpaka akakaa.

“Sasa hapa nitafukuzwa! Kwani huwezi kuongea kwa mdomo tu bwana Pam!” Ikabidi acheke. “Rudi kulala, rudishia mashine ya mtoto vizuri, acha umbea.” “Usithubutu kuacha kwenda kwa ajili hii mama! Tulivyoteseka peke yetu muda wote huo!” “Na wewe?” “Sasa mimi ulitaka kunifanyaje!?” Mpaka mama yake akacheka.

“Kwa nilivyosikia na alivyo Mill, hapa kitandani nimefika.” “Bwana Mill na huyo mtoto! Utafikiri kaambiwa mayai yameisha hiyo ndio mbegu ya mwisho!” “Basi utamuhurumia. Kila saa anauliza kama damu imetoka. Saa ingine nimelala, nasikia ananiangalia.” “Kaingiwa hofu na mwanae.” “Basi nakoma mama. Hataki hata nigeuke! Utafikiri nina jibu hataki litoneshwe!” “Kule ofisini ameshasema upo hapa kupumzika, watu wakuache upumzike. Sio tena kupishana hapa, kutoa pole.” Wakazidi kucheka.

“Nenda mama yangu wala usijipunje. Nenda kapendwe.” Alicheka, alicheka hana mbavu. “Kweli mama! Unastahili. Wewe mtu mzuri sana mama yangu. Roho yako nzuri. Nenda ukafurahie maisha. Kwanza kesho nitakuwa nimesharuhusiwa kama hii pressureitatulia kama hivi leo.” “Sasa nikirudi si mtakuwa mmeshalala! Ntagongaje kukujulia hali?” “Mama naye! Si hata kesho yake, ijumaa!” “Na ijumaa pia naenda tena.” “Huko kwake!?” “Kumbe!” “Makubwa!” “Kasema anataka iwe hivyo, jumamosi ndio alitaka wote mfike, mpafahamu kwake, mpaka baba na mama.” “Mama wewe! Ndio vimekua hivyo!”

“Nakwambia kakazana kwelikweli! Mpaka wifi naye kaomba na yeye aongozane na kina baba. Alishamwambia baba Shema mkitoka huko mapumziko na nyinyi jumamosi muungane nasi. Akakubali. Sasa na haya mabadiliko sijui vinakuaje?” “Nitamuuliza daktari mbele ya Mill, tujue masharti. Lasivyo Mill atanilaza kitandani muda wote, na huyu mtoto nitashindwa kuja kumsukuma. Lakini usiache mama. Nenda.” “Unauhakika?” “Kabisa. Tena wala usizembee. Sasa matayarisho yakoje?” Mama yake akaanza kucheka kwa aibu.

“Usinde kutia aibu mama! Usafi wa kina.” Wakaendelea kuongea lakini alimuacha mwanae na hukumu kubwa sana akijifananisha na baba yake. Ila akijitahidi kumuelekeza mama yake vizuri, nini chakuvaa na usafi kweli mpaka wa ndani.

~~~~~~~~~~~~~~

Kwenye majira ya saa 12 jioni, ya siku hiyohiyo aliposhinda na mama yake, wakiwa wamekaa tu hapo, Pam ameamka baada ya usingizi wa jioni Jerry akapiga tena. “Naona Jerry anataka kweli tuonane! Sijui ni kwa sababu hawakuja kwenye harusi!” “Kwani uliwakaribisha!?” “Niliwakaribisha yeye na Sandra. Ila hawakutokea, na ikawa kimya mpaka leo. Alitaka kuja mchana, nikamwambia umelala.” “Kumbe anajua kama nimelazwa!” “Nilimwambia umepuzishwa. Tunategemea mtoto wa pili. Hajaamini! Amefurahi huyo mpaka amenikumbusha Mike. Aisee namkumbuka yule kiumbe mpaka roho inaniuma! Vipindi kama hivi vigumu maishani, ndio namkumbuka zaidi Mike.” 

Pam akabaki akijiuliza kipindi hicho kigumu anachozungumzia, je yeye ndio amechangia au wasiwasi wa hatari ya kumpoteza mtoto! Akajiuliza na kushindwa kumuuliza. Ila akaona ampunguzie mawazo. “Mkaribishe tu. Nimelala muda wote huo! Ni sawa hata akija upate mtu wa kukumbushia enzi.” “Na uzuri Jerry hanaga sauti ya juu. Anaongeaga kama ananong’ona. Hatasumbua.” Akajua kumbe alishataka kumkaribisha. Akajituliza. Akamuona anampigia maana simu ilishakata.

Moyo Unapochoka Kuyapigania Mapenzi

Baada ya kama nusu saa akawa anaingia. “Pole sana Pam na hongera.” Akaanzia kwa Pam moja kwa moja, kisha kwenda kukaa pembeni na Mill. “Hivi nilikuwa nimekaa tu hotelini siku nzima ndio maana nilitaka nije tukae wote.” Mill akashangaa. “Hukwenda kazini?” Ikawa kama amefunguliwa mic, akapewa jukwaa.

“Unajuaga ule upuuzi wa kuona tabia ya mtu, unaifumbia macho unakuja sema atakuja badilika, unamuoa?” Japokuwa hakuwa amemjibu lakini kwa sehemu Mill akawa ameshamuelewa. Alimfahamu Sandra hata kabla hajamuoa. Na tabia zake hakuwa akificha.

 “HAWABADILIKI kaka. Mtu na tabia yake, ni yake jana, leo mpaka kesho. Hata ufanye nini. Yaani jumatatu siku ya harusi yako ndio kama kwa mara ya kwanza baada ya miaka 15, ya usingizi mzito, nikivumilia mengi, ndio kama nikaamka kutoka usingizini. Na mbaya nimeamka na kujikuta kama mwanzo.” “Unamaanisha nini?” “Sina kitu kaka. Sina watoto, sina mali, sina hata simu kwa jina langu, kumbe hata hizi nguo nimevaa ni mali ya Sandra, ndio amenikumbusha siku ile ya jumatatu.” Jerry akaendelea. Huwa anaongea taratibu kwa utulivu.

“Ila si kwamba alishawahi kuwa mnafiki kwangu! Hapana. Ni nikama nili nili…” Akabaki akifikiria na kushindwa kueleza. “Aisee sijui nikwambiaje Mill! Eti kwa mara yakwanza, nikiwa nimetoka kwake, baada ya miaka mingi, nikiwa sina kitu, eti ndio nimelala garini usingizi ambao sikujua kama mtu unaweza ukalala usingizi sehemu ‘kama ile’ na ukapafurahia! Sijui kama unanielewa?”

“Japokuwa hujaniambia kwa undani upande wako, ila hapo na mimi nilipita. Ile ndoa mlikuwa mkinilaumu sikuwakaribisha, ilianza kama hivyo wewe na Sandra. Nikidhanianaweza kuja kutulia, lakini sikufanikiwa Jerry. Nilimpa maisha ambayo yalikuwayakinigarimu kila eneo la maisha yangu. Yaani nilikuwa nikiishi kama mtumwa wake lakini hakuwahi ridhika!”

“Hakuna pesa unayofikiria ungeniomba, nisimpe. Lakini hapakuwahi kuwa na utulivu.” “Mimi nilijua kwa sababu amenikuta sina kitu!” “Hapana. Kama ulivyotangulia kusema, ni tabia tu. Ni tabia ya mtu ambayo hata umfanyie nini, roho yake hairidhiki au niseme nafsi yake haitulii. Ipo kutafuta machafuko na uharibifu. Ili urudi pale ulipokuwa nikakuuingilia. Nakwambia hivi, nakuelewa unaposema unaweza ukalala sehemu ya ajabu, lakini ukapata usingizi kuliko kwenye kitanda unachopulizwa na A/c.”

“Siku yule mwanamke amenikamatisha kwa polisi..” “Subiri kwanza Mill! Ndio mlifika hapo!?” “Ninapokwambia nakuelewa unachosema japo hujamaliza, jua nakuelewa. Bwana nililala jela! Nililala sana. Sikuwa nimelala hivyo kwa miaka mingi sana. Maana ilianza kazi ya kufanya kazi mchana na usiku kukusanya pesa nimlipe yeye na nimlete Pam huko. Kaka, niliwajibika kama mtumwa! Ikaja kazi ya harusi hiyo ya kitapeli kuaminisha serikali ya kule kama ni ndoa ya kweli, ili nipate uraia mimi, nimuache yeye, nimuoe Pam aweze kuja kule kirahisi. Napo ni pesa.”

“Ikaja kazi ya kutafuta pesa kumtunza yeye na watoto wa uongo alionibambikizia wa mwanamme wake.” “Acha Mill! Kumbe ndio ilikuwa hivyo!” Mill akamuelezea kwa kifupi ilivyokuwa ile ndoa, Pam akisikiliza na kuzidi kuhukumiwa. Ikawa kama anasutwa yeye!

“Jerry, si nimepokonywa mali, nipo jela!” “Ehe?” “Nilikuwa kama kwa mara ya kwanza nimetuliwa mzigo. Nilikuwa nikilala kule jela mpaka yule mwenzangu alikuwa akinishangaa. Nilikuwa na uchovu wa mpaka nafsi, akili na moyo. Usiombe kuishi na mwanamke mwenye kelele, gubu, halafu ALISHAKUDHARAU! Kaka! Usiombe. Huna utachofanya akaridhika, kila kitu ni KOSA.” Pam alitamani afunge hicho kikao lakini Jerry akapokea.

“Naona huyo hana tofauti na Sandra. Ila bora wewe Mill ulikuwa na pesa. Sasa mimi nilikuwa nikikumbushwa kila siku kuwa kampuni ni YAKE. Sasa siku ya jumatatu mimi nikajua tunakuja kwenye harusi yako. Kumbe yeye nafikiri akawa bado na wivu na Pam na ile aibu ya kumfunga jela. Mimi nimemaliza kazi zangu zote eti namwambia nawahi nyumbani nijiandae, ananikataza!”

“Sasa nikamuuliza ni kwa nini anikataze kwa mwaliko tuliokuwa tukikulaumuhutushirikishi kwenye mambo yako, leo umetushirikisha, pia tukatae! Akaanza sasa kupayuka eti kwamba ule si ukaribisho wa kweli ni kama unakwenda kutusuta!” Mpaka Mill akashangaa.

“Namuuliza anatusuta kwa lipi, akaanza kueleza dhambi zake zote alizomfanyia Pam, nikamwambia mimi namfahamu Mill kwa kukua naye tokea shuleni, haupo hivyo. Hilo ni moja, na nikamwambia kama nikusutwa, basi tulitakiwa tuwe tumeshasutika maana Mill alisharudiana na Pam muda mrefu tu. Haelewi, ndipo nikamkumbusha yote anayozungumzia ni yeye ndiye aliyemfanyia Pam, mimi sihusiki. Kwa hiyo kama yeye anaona aibu kuhudhuria harusi, asihudhurie, ila nikamwambia mimi nitahudhuria.”

“Kama kawaida yake akaanza ubabe. Kwamba siwezi kwenda ni kama nitakuwa nikiwasaliti ofisi nzima! Hapo anaongea kwa sauti kila mtu asikie, sio heshima tena. Yaani kama anayetaka uungwaji mkono wa wale wasichana pale. Sasa mimi nikamshangaa sana! Maana hapo akawa amekusanya sasa wale wasichana pale wakitaka kumsaidia wanikumbushe vile Pam alivyowasaliti kwa kuvunja kanuni ya pale kutochukua mwanaume aliyekwisha wahiwa. Yaani mpaka kumkubusha Lona akimwambia Pam alikuiba kwake.” “Mpaka leo!”

“Kusudi tu kunidhalilisha. Lakini pia ndio njia aliyotumia pia kuwageuza wale wasichana wakawa kinyume na Pam. Hiyo ndio njia yake ya kupata ushindi. Akawa anaongea pale kwamba hiyo harusi ilitakiwa iwe ya Lona na Mill, lakini Pam amepora,mimi sioni, naunga mkono, nakuwa msaliti.” “Haiwezekani Jerry!” Bado Mill hakuwa akimini. “Hakika tena. Lakini yeye hakuwa akijua kuwa ndio alikuwa akigongeleamsumari wa mwisho.” Roho ya Pam ikalipuka paa, akikumbuka neno kama hilo kutoka kwa Mill.

“Gafla nikawa kama nimefunguliwa macho yote kwa wazi kabisa. Nikasikia kwa mara ya kwanza, sina sababu ya kuendelea. Nikapatwa na uchovu ambao sijui nikwambie nini! Mpaka nikajishangaa! Kumbuka ni kama ndoa yenyewe ilikuwa ikishikiliwa na Mike kwa miaka mingi sana. Baada ya Mike kuondoka mambo mengi nikawa nikivumilia bila kuleta maana zile alizokuwa akinipa Mike.”

“Nakwambia kama vile Adamu alivyokula lile tunda na kufunguliwa macho na kujiona uchi! Hakika siku ile nilimuelewa ni kwa nini alijificha mpaka kumwambia Mungu anaogopa yupo uchi! Ndipo na mimi nilipita hapo. Nilifunguliwa macho kwa wazi kabisa nikaweza muona Sandra kwa vile alivyo na kile anachonifanyia kwenye maisha yangu, kwa uwazi kabisa! Nikajiambia sitakaa nikaendelea kumsikiliza tena maneno yake machafu, dhihaka na kashifa kwangu.”

“Nikamwambia mimi nilazima nitakwenda, Mill ni miongoni mwa rafiki zangu wachache sana waliobakia kwenye maisha yangu. Na yeye siwezi mpoteza. Kwanza ni kama sina rafiki tena kwa sababu yake. Ki ukweli ni kama umebaki wewe tu. Anyways,nikamwambia nitakwenda harusini lakini sitachelewa kurudi nyumbani baada ya harusi. Si akamalizia kusema mbele ya wafanyakazi wake eti amenikatazahaniruhusu kwenda!” Mill akatingisha kichwa kwa masikitiko.

“Si neno geni, lakini aisee siku ile ilikuwa tofauti kabisa. Lilisikika kwa wazi kama alivyotamka. Nikarudi tena, nikamwambia simuombi ruhusa ila namtaarifu kuwa nakwenda nyumbani kujiandaa, niwahi harusini.” Wakamuona anacheka kwa masikitiko.

“Nini?” “Eti akaniambia huko ninakokuita nyumbani, ni kwake maana kumejengwa na pesa yake.” “Haiwezekani Jerry!” “Subiri. Mbona pananoga zaidi. Maana nikamuuliza, anamaanisha nini? Akanikumbusha ile ni kampuni aliyoanzisha kwa jacho lake yeye, sisi wote pale ametuajiri tu na anatulipa, kwa hiyo pesa yeyote inayotokana na pale kufanya chochote ni YAKE. Kwamba ile nyumba tulijenga kwa pesa iliyotokana na kampuni YAKE. Na akanikumbusha, hata gari ninayoendesha inatokana na pesa yakeNguo ninazovaa eti huwa anaagizaga yeye kutoka nje ya nchi. Simu ninayotumia pia ni ya kampuni yake yeye.” “Haiwezekani Jerry!” Mill akazidi kuumia.

“Bwana Sandra alinichambua, mpaka anaweka kituo, sina changu mpaka boksa niliyovaa ni yake. Kwa hiyo sina jeuri yeyote mbele yake.” “Aisee pole sana Jerry. Sasa ukafanyaje?” “Ndio kwa mara ya kwanza akanisaidia kujua hangaika yangu yote kwa miaka yote 15 ilikuwa bureHavijawahi na havitakaa kuwa vyangu daima.”

“Nikamwambia namshukuru kwa kazi niliyomtumikia kwa miaka yote hiyo. Siku ileile nikamwambia ninaacha kazi. Na yeye akaniambia bila aibu, eti kwa sababu sijatoa notice ya mwezi, sipati mshahara wa ule mwezi.” “Jerry haiwezekani!” “Usicheze na Sandra. Na usidhani amenibadilikia! Ni tabia yake tokea zamani sema ndio alinifikisha kikomo. Nikamwambia sawa na kumuongezea kuwa, sababu gari yangu imetokana na pesa ya kampuni, namuachia. Akanijibu na simu. Nikatoa line yangu nikamkabidhi simu.”

“Nikamwambia chochote alichoninunulia pale kwenye ile nyumba yake, achome kama hana mwingine wa kumpa. Akigundua kuna changu ambacho nastahili, aniachie kwenye kibanda cha mlinzi, nitafuata. Hapo akashituka sasa, kwamba naondoka nyumbani!” “Na Sandra hawezi ishi bila kujua ulipo.” “Ewaaa! Kumbuka na simu keshachukua.” 

“Sasa akafanyaje?” “Akanitisha eti sitakaa kuona watoto. Nikamwambia maadamu wanabaki na yeye mwenye pesa, mama yao na uzuri wamechukua tabia zake, sina wasiwasi. Watakaporudi kunitambua mimi kama baba yao, na kama ni wangu kweli, basi siku moja watakuja kunitafuta. Nikamuongozea, nikamwambia sitaenda kuwadai popote, nampa zawadi, naenda kuanza upya sehemu ingine ambako nitapata watoto wangu na mke wangu, kwenye familia YETU.” “Subiri kwanza Jerry, kwani wale watoto…” “Wapo kama Sandra mama yao.” Akawahi kwa jibu.

“Vile walivyokuwa wakimuona mama yao akinifanyia ndio na wao hivyohivyo. Ukiwaambia kitu, wanakwambia mama hajasema hivyoHawafanyi na wala huwatishi.Na wanaweza kunisemea kwa mama yao, ili waone mama yao akinisema hovyo mbele yao.” Pam alitamani kuingia ndani ya shuka, au huyo Jerry awe anazungumza na mtu mwingine sio Mill. Inakuwa kama anaongeza petrol kwenye moto! Ikawa kweli ni bad timing.

Wasiwasi sasa na aibu mbele ya wafanyakazi wengine. Eti ananitisha nisije nikaenda anzisha biashara kama ile, atanishitaki.” “Kwani biashara ya kukopesha pesa ni moja!?” “Hofu yake ni nisije muibia wateja maana asilimia kubwa ya wateja nazungumza nao mimi na mimi naifahamu ile biashara kwa asilimia 100. Nikamwambia wanasema, adui muombee njaa, nikamwambia kwanza yeye si adui yangu, pili simuombei njaa. Namuombea mafanikio makubwa zaidi ya yale. Awe na pesa nyingi sana zaidi za zile, ili wanangu waishi maisha hayo anayotaka kuwapa ya kitajiri yasiyo na ubinadamu ili dunia ije iwafunze wote watatu.”

“Nikamuhakikishia na kumwambia hata akitaka kuandaa karatasi, siku tukiandikishana talaka nitazisaini kumuhakikishia sitaanzisha biashara kama ile. Nikamwambia simdai hata watoto, wala sitataka hata shilingi yake, na yeye hanidai ila nguo nilizovaa, boksa na talaka ambayo nilimuahidi hivi karibuni itaandaliwa na kufikishiwa ili tuhitimishe kwa heshima, na nguo nitamrudishia nikivua. Niliondoka pale haamini!” 

“Sasa ulilala kwenye gari gani, kama ulimuachia mpaka gari?” “Jeremi! Sikumwambia kwa undani, ila kwa ufupi tu kuwa nimekwama, naomba msaada wa usafiri na pesa. Hapo ukumbuke hata simu sikuwa nayo nimeazima pale posta.” “Hivi si bado anafanya biashara ya magari mpaka leo?” Mill akajaribu kukumbuka.

“Mpaka leo. Na kuuza matairi ya magari. Bwana yule alioga mwanamke! Wengine tulikuwa tukicheza tu. Walianzana na dogo hata kabla ya kifo cha wazazi. Sisi tukajua anaweza muacha Jeremi baada ya wazazi kuondoka, hamna tena pesa za kuchezea, lakini aisee wameshikana mpaka leo. Ukiwa nao sehemu mpaka aibu na ile familia yangu!” “Mimi nakuelewa sana tu. Nilirudi na aina hiyo ya watoto, sina jinsi nikakueleza ukaelewa.” “Wala huhitaji maneno mengi. Sasa bora wawe watoto wadogo sana, wale wangu ni ma teenager Mill! Na mama yao ni hivyohivyo! Inamaana hawakunjiki tena.”

Anyways, baada ya muda Jeremi akaniambia ameacha maagizo kwenye yard yao, niende pale. Ndio nikafika pale nikakuta ametoa maagizo nipewe hii gari ninayoendesha sasahivi, akaniachia moja ya simu yake. Si mpya ila ipo na hali nzuri tu kama unavyoiona na pesa. Hiyo ilikuwa jioni, sijui pakwenda maana nilishafungiwa kwenye aina ile ya ndoa kwa miaka 15. Nikaishia kulala kwenye gari.”

“Leo asubuhi ndio Jeremi akanitafuta sasa kuniuliza kulikoni, akanifuata nilipokuwa nimeegesha. Akataka kunikaribisha kwake, aisee nimekataa Mill.” “Kwa nini?” “Aibu! Dogo amepiga maendeleo wakati tumekua naye nyumba moja! Hapana. Acha nianze peke yangu. Kwanza nishaingiwa woga kujiegemeza kwenye vilivyokwisha ng’aa. Naona nianze tu. Ila alinielewa. Akanisaidia kutafuta hoteli, nikaenda kuoga na kulala mpaka mchana nilipoanza kukutafuta.” 

“Sasa utafanyaje?” “Nitatafuta pakuishi. Naanza aisee. Naanza upya kabisa, ila sijui kwa nini, nina amani ambayo sikuwa nayo kwa muda mrefu Mill. Moyo umepoa, nikijiambia nitaweza tu. Hata kama nimechelewa, lakini…” “Hujachelewa Jerry. Ukiweka nidhamu kwenye chochote utakachoanza, utaweza.” “Dogo ameniambia naweza nikashikilia kwenye matairi ya gari. Nikiona ni kitu napenda, niingie naye ubia, nifungue kwingine ila kwa jina lake ili nisianzie chini.” “Mimi naona sio wazo baya Jerry.”

“Nimemuomba kama siku 3, nitulie kabisa, ndipo nimjibu. Nitafute pakuishi. Akili itulie, nafikiri nitafuata ushauri wake. Aisee Jeremi na mkewe wamefanikiwa! Sana. Halafu wametulia, huwezi jua. Hamna kelele. Mkewe naye mtulivu hana hekaheka. Mnyenyekevu hajawahi mbadilikia Jeremi na anamuheshimu.” Mill akabaki kimya amepotelea mawazoni. Kimya chumba kizima kwa muda. Pam alikuwa na hali mbaya, kama alikuwa akisemwa yeye! Ikawa tena kama Jerry amekuja kuwarudisha tena mwanzo. Akajisikia kama tena kumetibuliwa.

~~~~~~~~~~~~~~~

Kuna wakati moyo huchoka kupigania mapenzi kama askari na ngao, ukipambana na baridi ya ukimya na maumivu ya ahadi zilizovunjika. Huamua kunyamaza si kwa sababu haukujua kupenda, bali kwa sababu ulijifunza kuwa si kila upendo hujibu kwa upendo. Na hivyo hujisitiri ndani ya kifua, ukijifunga bandeji za subira, ukingoja siku ambayo jua la thamani litachomoza tena bila MAFANIKIO.

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment