“Sasa basi, kwa kuwa honeymoon sio muhimu, muhimu ilikuwa ndoa, si lazima kwenda. Turudi nyumbani tukaendelee na maisha yetu.” Akaendelea.
“Nakwenda kumshukuru mama na Jo, kwa msaada waliokuwa tayari kutupa, nafikiri tuwaache tu huru waendelee na ratiba zao.” Akaanza kuondoka bila ya kusubiri kujibiwa.
“Mbona ni kama ulisema kuanzia sasa tutakuwa tukizungumza?” Mill akageuka. “Si ndio tumezungumza hapa! Au ulitaka nini!?” Akauliza kwa ukali kidogo. “Hapa umetoa maamuzi yako, hujanisikiliza na mimi.” Mill akakunja uso kama ambaye hamuelewi tena.
“Maamuzi ya kwenda honeymoon!” Akawa kama anamkumbusha. “Pam, tafadhali tusiendelee kupoteza muda. Ushanipinga kila kitu nilichokiandaa kwa heshima na juhudi zote tokea majuzi. Umenipinga mbele ya kina Jo, ukionyesha sina uwezo wa kufanya jambo ukalikubali. Naomba turudi nyumbani tukapumzike. Hata hivyo najihisi kuchoka.” Ukweli Mill alishabadilika na kuonekana amechoka mpaka usoni. Ile morari yote iliisha.
“Mimi nataka twende.” “Kilichobadilika ni nini? Mbona unanizungusha bila sababu?! Au sasahivi tunakwenda kwa sababu wewe umesema?” “Hapana. Tokea mwanzo sikuwa nimekataa, ila nilikuwa na wasiwasi na mtoto.” “Kwamba wewe ndio unajihisi unauchungu sana na Shema, mimi simjali. Namtelekeza tu bila mipango?” “Nisamehe Mill. Na naomba nipe muda. Huyu mtoto nimelea kwa kumfikiria mimi mwenyewe kwa muda mrefu. Najisahau.” “Ulitaka nifanye nini ili ujue kama mimi ni baba yake Shema na ninamjali na kumpenda?”
“Tatizo sio wewe. Ni mimi. Nimekosa Mill. Naomba twende.” Pam mkorofi alipiga sharp corner huyo! Akajirudi kwa haraka sana ila ikawa tayari kidonda kishaingia chumvi! Kwa mara ya kwanza maishani, Mill akajishangaa moyo wake imetibuka haswa! Mzuka umekwisha kabisa. Hataki tena.
~~~~~~~~~~~~~~
Ila sasa tena ikawa kama amebanwa kwenye kona, hawezi kujitoa. Ndoa ndio mpyaa! Ashaombwa msamaha, mama mkwe anasubiri akijua wanakwenda kutengeneza, ili waende fungate. Na Jo yupo! Anawaambiaje tena wanarudi nyumbani!
Na isivyo kawaida ya Pam, hapo alijirudi haswa. Akili nayo ilishatoka likizo. Akakumbuka tayari anamimba ya mtoto wa pili, ashaolewa hadharani. Mill kumbadilikia haitakuwa kazi ngumu. Wanaweza kurudi nyumbani na kumuacha afanye vile atakavyo na hao watoto, akiishi naye lakini akiwa hajali tena. Akikumbuka maneno ya muda mfupi ya Jo, halafu Mill ni raia wa Marekani, anaweza akaaga, safari hii akamuachia pesa na hao watoto, halafu asionekane, akakusudia lazima akatengeneza huko fungate.
Asijue moyoni mwa Mill kumebadilika kabisa, akitamani kama mama mkwe na Jo wasingejua safari ya fungate, kwa hakika asingeenda tena. Hamu ilimuisha kabisa ikawa tena si furaha, ila kama adhabu kwake. Anatakiwa kufanya kama kutimiza wajibu, tena wala si kwa mkewe, bali kwa wakwe! Akageuka bila ya kujibu wala kuongeza neno na kuanza kuondoka, Pam akafuata kwa kujaribu kukimbia. Kimya wakirudi kwenye gari.
~~~~~~~~~~~~~~
Wakawafikia. “Sasa hapa kuna mbu. Kama safari yenu nyinyi imekufa, mniambie, mumchukue mtoto wenu, na mimi niendelee na yangu. Vikao vya hapa nje, sitaviweza.” “Tunaondoka mama. Naomba dakika moja na Shema.” “Ya nini tena!? Maana haya mambo yalishapangwa vizuri tu! Tulikuwa tumetulia ndani, tukijua mmeondoka. Umekuja kuanzisha utaratibu mwingine, uondoke, utuachie majonzi! Huyu mtoto alikuwa akicheza ndani na baba zake wadogo, hana wasiwasi. Mwenzio aliweka mpango mzuri, wa amanina utulivu, umeona pasiishe vizuri, utibue.” Mama Eric asijue na yeye anaongeza mafuta ya taa kwenye moto. Pam akainama. Mill kimya.
“Huyu Shema lazima atambue na kuelewa lugha ya baba yake kama yako Pam. Umenisikia Pam?” Kimya. “Wewe umekuwa naye huyu, unalugha aliyokuzoea nayo. Sasa ni lazima, ajifunze lugha ya baba yake na aielewe. Si lazima akaipenda, ila kuelewa na wajibu wake ni KUTII hata kama hakubaliani nayo. Unanisikia Shema?” Yeye na mama yake kimya, Shema akaanza kulia.
“Na usilie unisikilize. Nyinyi wote wawili. Wewe ulizungumza na baba yako, mkakubaliana, anakuja mama yako, unalia. Hapana Shema. Baba yako akikwambia kitu, HUNA pakwenda kuthibitisha, HUNA pakwenda kuuliza kama yupo sahihi ila KUTII. Unanielewa?” Akaendelea kulia akitaka mama yake aingilizie.
“We Shema?” “Mwambie bibi umeelewa na hutarudia tena.” Akazidi kulia kwa kwikwi. “Shema? Unanisikia?” Akakubali kwa kichwa. Jo kimya akisikiliza na kujiangalizia. “Baba yako anakupenda sana, hata mama yako hakupata bahati uliyopata wewe.” “Mama jamani!” Pam akashangaa sana.
“Lazima ajue ukweli na atambue juhudi za baba yake. Kwani watoto wangapi wanatelekezwa tu? Wanaachwa bila msaada! Lakini wewe baba yako anajituma si kwa pesa tu. Mpaka yeye mwenyewe amejigeuza kuwa kama mtumwa wenu na bado mnamuendesha! HAPANA Shema. Iwe mwisho na nione mabadiliko. Wewe ni mtoto mzuri sana. Unauelewa mzuri. Sitaki uharibike. Sawa baba mzazi?” Hapo akajirudi akianza kumbembeleza.
“Haya aganeni hapahapa, sisi tuondoke. Naenda kula.” “Mama wewe, si ulishakula?!” Angalau wakacheka kidogo ila Mill alibaki ametulia sana. “Mwanao mwenyewe huyo alianza kula upyaa. Ni Jo tu ndiye mwenzetu amekuwa na kiasi, anakunywa maji tu. Mavyakula yamejaa mle ndani yanaenda kumwagwa tu.” “Mimi mwenyewe nina njaa.” Pam akalalamika.
“Ulikuwa ukicheza muda wote, hujala!” “Huko tunapokwenda nimeshawapa oda ya chakula chako. Nimewaambia tukifika tu, watuletee chakula chumbani.” Mill akaingilia lakini wazi alionyesha kuishiwa morali, Pam akajisikia kumpenda zaidi mumewe na kujutia kutibua mambo.
“Ona sasa! Unachotaka ni kutuchelewesha tu hapa nje. Nyinyi ondokeni, sisi tukaendelee kusherehekea.” “Nyie mama! Bila maharusi!” “Wewe si umesikia huko nako umeandaliwa? Sasa? Haya, Shema aga hapo twende. Hakuna kikao kingine.”
“Ila kama unataka chakula naweza kwenda kukuchukulia uwe unakula njiani.” “Hapana Mill. Nashukuru. Acha nitunze njaa yangu nikale hicho ulichoniandalia huko. Haya Shema. Uwe mtoto mzuri. Umsikilize bibi na Jo.” Akakubali. Alishaacha kulia.
Mama yake akamkumbati na kumbusu, baba yake akabaki akimwangalia. Akaenda kumpa mkono. “Uwe na safari njema.” Mill akamkumbatia na kumbusu. “Kila kitu kipo nyumbani. Na mkila mkimaliza, mwambie bibi, watanunua vingine. Umesikia?” Akakubali na kuanza kuondoka.
“Muwe na mapumziko mema. Msiwe na wasiwasi na huku. Kila kitu kitakuwa sawa.” Jo akamalizia. “Nashukuru sana Jo. Asante kwa kila kitu. Asante kwa kuja kuhudhuria siku yetu muhimu, na asante kwa kukubali kunibebea majukumu ya familia.” “Usijali kabisa. Mkapumzike.” Wakaagana na kuondoka.
Mill&Pam Fungate.
Garini Mill akawa ametulia kabisa ule mzuka hata wa kiss kama mwanzo hakuwa nao. Akajiegemeza na kunyamaza kabisa. Pam naye akawa anajiwinda. Akatulia. Kimya hapo garini wanapelekwa fungate kama waliopoteza kabisa muelekeo.
Mara kadhaa akamuona anajishika tumbo lake kisha anavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu. Akatamani kumuongelesha, ila akaona amuache tu, aingize mazungumzo yote kichwani na kujipanga kwa upya. Mill akamuacha kabisa. Kimya kila mtu akiangalia dirishani.
~~~~~~~~~~~~~~
Wakafika hotelini. Gari ikaegeshwa mpaka karibu ya mlango. “Tumefika.” Ndio akagutuka. Ilikuwa hoteli kubwa sana hata hakuwahi ingia humo. Akaona kamoyo kanaanza kuhamasika. Akashuka garini. Akashangaa kuna masanduku mawili yanashushwa. Pam hakuwa hata na wazo kwamba akitoa hiyo nguo ya harusi atabadili nini! Akaja mtu wa kuchukua masanduku, wakawa wakifuata nyuma baada ya kuagana na dereva.
Kimyakimya, mpaka mapokezi. Wakachukua kadi na kupanda lifti kutafuta vyumba. “Kumbe humu ndani ndio pazuri hivi!” Pam akajaribu kusifia maana Mill alikuwa ametulia kupita kiasi. “Asante.” Akaongeza shukurani baada ya kutojibiwa, Mill akamgeukia wakiwa ndani ya lifti. “Nimepapenda. Nilikuwa nikipasikia tu, na kupaona kwa nje, lakini sijawahi ingia ndani. Asante.” “Karibu.” Akajibu kwa ufupi tu. Wakaendelea kupanda mpaka juu kabisa.
~~~~~~~~~~~~~~
Muhudumu aliacha masanduku yao hapo na kuondoka. Alipofunga tu mlango akamgeukia Pam. “Sasa simu hiyo ukiwapigia, nakuagiza unachotaka watakuletea. Vinginevyo ukichelewa, wataleta nilichoagiza mimi ambacho kinaweza kisiwe chaguo lako.” Akaendelea.
“Ukitaka kuoga, mataulo yapo bafuni, na nilikutayarishia hilo sanduku, sasa sijui na lenyewe nilipatia! Kama hakuna kitakachofaa, tumia rob ya hoteli kwa usiku huu, kesho unaweza fanya utaratibu utakao penda wewe na kuona utakufaa kwa hizo siku mbili tutakazokuwa hapa.” “Nilifikiri umesema siku tatu!?”
“Ya tatu tunaondoka. Ila pia endapo utaona mazingira hayafai, tunaweza punguza siku. Mimi natoka kwenda kutembea kidogo, kusafisha kifua na kichwa. Nitarudi baadaye.” “Chakula?” “Nipo sawa.” Bila ya kusubiri nyongeza, akaelekea chumbani. Akatoa koti la suti, akavua na tai, akatoka Pam akiwa amesimama na gauni lake la harusi. Ndio fungate ikaanzia hapo.
~~~~~~~~~~~~~~
Kwa sekunde kadhaa alizosimama hapo akimwangalia vile Mill alivyombadilikia, akaingiwa hofu ya ajabu sana. Ndio usiku wao wa kwanza wa ndoa, ndio wapo hivyo! Akajua maji yameshazidi unga.
Akatoa gauni la harusi na kukimbilia bafuni, akitaka kutumia choo ndipo aoge. Mpaka mkojo ukaisha jinsi huko bafuni kulivyokuwa kumeandaliwa vizuri tena kwa ustadi wa hali ya juu! Ila wazi ilikuwa kwa madhari ya kuoga watu wawili wala si peke yake. Akazubaa hapo kwa muda kisha akafanikiwa kuoga na kutoka amejifunga taulo.
Akasogelea sanduku ambalo aliandaliwa asijue humo ndani kumewekwa nini! Alipofungua mpaka akahamaki kwa sauti. Ukweli Mill alimuandalia hilo sanduku vilivyo. Kulikuwa na mpaka chupi kitu kilichomshangaza kwamba yote hayo ameyafanya lini!
Akakaa akijisikia kuumia vile alivyoweka hiyo juhudi na ni kama amemvunja moyo! Akatoa nguo moja hadi nyingine akiweka kitandani. Akatafakari jinsi huo usiku ambavyo ungekuwa mzuri kama si kumtibua! “Mill anaonekana alijiandaa sana! Nimemvunja moyo.” Akaendelea kuwaza.
Akawaza vile anavyo mtetemekeaga. Halafu aje ambadilikie gafla! Hofu ikazidi kumtesa. “Mill sio wakuniacha nijiagizie chakula! Au si wakuniacha chumbani.”Akaendelea kuwaza kwa hofu mpaka akasahau swala la chakula. Alimsubiria Mill zaidi ya masaa mawili, harudi.
~~~~~~~~~~~~~~
Kumbe huku kwa Mill alitoka kwenda kutembea. Alitembea kuzunguka hiyo hoteli nzima zaidi ya mara mbili, gizani. Akachoka na kuamua kurudi ndani upande wa hoteli. Akakaa na kuagiza juisi. Mill hakuwa akinywa pombe. Akabaki akivutana na juisi yake taratibu mawazo yapo mbali. Shetani naye akaanza mahubiri yake kichwani na kuzidi kumtesa.
Baadaye ndio anakuja kugutuka walishamaliza jumatatu siku ya harusi yao, mke ameacha ndani. Akaondoka kurudi chumbani. Ilishatimu saa nane ya usiku.
Moyo Uliobeba Uvumilivu Kwa Muda Mrefu
Alimkuta Pam amekaa upande wa sebule amejikunyata kwenye kochi amejifunika mablangeti aliyokuwa ameshapiga simu mapokezi na kuletewa. Popote anapolala Mill nilazima pawe baridi haswa. Pam huishi na mablangeti wakati wote.
Akasimama kwa haraka na kumsogelea wakati akitoa viatu. “Naomba usibadilike Mill.” “Kwa manufaa ya nani!? Maana kwa jinsi ninavyofanya ni kama najidhalilisha tu! Haina maana.” “Kwangu inamaana.” “Maana ya kunidhalilisha mbele ya mtoto kama Shema, na mpaka wageni kina Jo?!” Akawa mkali mpaka akamtisha na kumuongezea hofu zaidi.
“Haikuwa nia yangu.” “Labda useme nia yako ni ipi Pam! Maana kwa mchezomchezo hivihivi, nikimvumilia Kisha, tena kwa ajili yako WEWE Pam, yule mwanamke alinifunga jela. Hivihivi kama wewe hivihivi! Unaelewa Pam?” “Naele…” “Usiharakishe kujibu, tafadhali Pam. Tafadhali sana.” Akageuka vizuri.
“Tokea narudi hapa nchini, kwako, swala langu lakufungwa na Kisha kwa ajili YAKO, sikulificha. Nililiweka bayana kabisa. Sikuwa na NIA ya kumuoa Kisha mimi isipokuwa kuhangaika kufanikisha WEWE uje kule. Nilipata MATESO kwa ajili yako Pam. Nililipa garama mbaya SANA mpaka ulishuhudia kwa macho, aina ya watoto niliokuwa nimebakiwa nao kama kuendelea kulipwa kwa ubaya ambao hata sijui nilikosea wapi!”
“Nilirudi nchini na watoto waliokuwa wakinitesa ambao ni matokeo ya kuhangaika kwangu. Isingekuwa wewe, Pam, nisingekuwa na Kisha. Isingekuwa wewe Pam,nisingefungwa jela. Isingekuwa wewe Pam, mtoto wangu, Shema, asingezaliwa na kukua kwenye maisha ya taabu vile! Hilo hulioni, unaendelea kujiangalia tu wewe, ukidhani wewe ndio unamstahili Shema kuliko mimi uliyenitenga na mwanangu kwa muda wote huo na unafanya juhudi za makusudi, kila leo, kunitenga naye ukimuonyesha kwa wazi kabisa, mimi si kitu kwake.”
“Tuweke pembeni hilo. Nilirudi kwako, nilikueleza ukweli wote wa kile kilichokuwa kikiendelea kule. Mateso niliyopitia ili tu kukufanikishia uje kule mpaka nikanasa kwenye ile ndoa ya mateso, lakini umeshindwa KUELEWA kabisa, ila jeuri, matusi, kunifukuza, na kuhama na kijana wangu mpaka nyumba niliyokukaribisha kwa upendo!”
“Leo nimekaa nikajifikiria vile nimejigeuza mjinga kwa ajili yako Pam! Mpaka najishangaa na kuona kweli unayo haki ya kunidharau! Eti umelala kitandani kwa mama yako, unaniacha mimi najieleza kwa mama yako kama JINGA! Umelala humohumo ndani, hujali! Nakufuata siku inayofuata, eti unanitusi mbele ya kijana wangu, msichana wa kazi wa mama yako na mama yako! Tena unanitusi kwa kunigomba kabisa!”
“Vile ambavyo hunijali, unamrudisha Kisha kwa kunisimanga naye mbele ya watu, mtoto wangu akisikiliza, huku ukijua kabisa vile yule mwanamke alivyonitendaunyama! Na bado eti na mimi naendelea kunyenyekea kama mjinga kwako! WEWE unatofauti gani na Kisha kwangu?” Pam akawa anatetemeka mpaka tumbo.
“Mpaka najihisi nina tatizo! Maana na Kisha naye alifanya hikihiki unachonifanyia wewe. Nikiwa nahangaika na kazi ya kulea wazee, nikikusanya pesa, nikafanya harusi ya heshima ili kwanza kuaminisha watu na serikali, kwa ajili yako WEWE. Na kumuwekea yeye heshima kwao, eti ule usiku au ile siku iliisha kama hivi tu. Matusi na jeuri! Sasa najiuliza, hata kama mimi ni mbaya mwenye mapungufu makubwa kiasi hicho, kweli hakuna hata anayeweza kuwa mnafiki kwangu na kuficha makucha hata mara mojamoja kama kusema asante!?”
“Ungepungua wapi kwenda na mipango yangu? Kwa siku tatu tu! 3! Na wewe ukajifanya mjinga kama mimi ninavyofanya kwako! Ukaficha makucha hata kwa unafikitu kunionyesha angalau katika hili nimepatia, kuliko kwenda kunianika mbele ya watu na kijana wangu, kumuonyesha sina akili ya kufikiria. Halafu sina uwezo wa kufanya jambo lolote zuri! Siku tatu tu?! Hapana aisee! Ipo shida mahali. Haiwezekani kwa wanawake wawili, niambulie hivi. Hapana Pam. Na mimi ni binadamu. Nina nafsi na hisia.”
“Sio muhuni wala sijawa na wanawake wengi, lakini leo umenifanya nimfikirie Brenda.” Pam alishituka sana. “Alikuwa na nidhamu fulani kwangu, nakwambia kweli Pam, SIJAWAHI pata kutoka kwako wala Kisha. Hata kama alikuwa akinidanganya, lakini ilikuwa bora vile. Brenda hakuwahi nipandishia kama hivyo wewe na Kisha.”
“Yule binti niliairisha naye safari ambayo tulikuwa tukiisubiria kwa hamu, tukiizungumzia kwa shauku huku tukihesabu naye siku! Tulishajiandaa kwa kila kitu mpaka mavazi na vitu ambavyo tungeenda fanya huko pamoja. LAKINI niliahirisha kwa ajili yako WEWE. Namwambia sitaweza kwenda, Brenda wazi aliumia maana alichukua likizo kazini kwa ajili ya hiyo safari, lakini alikubaliana na mimi japokuwa sikumpa sababu ya kueleweka. Hakufanya fujo wala kunitukana. Hakuomba pesa useme alitaka kutoka pale akatumie na wengine. Alirudi nyumbani, nilikuja kumpigia simu mida ya saa mbili usiku, alipokea kwa heshima na unyenyekevu akiwa amerudi kwake kulala. Brenda! Binti mdogo tu, mzuri sana, ambaye kukataa kwangu mimi, ingekuwa faida kwa mwingine. Lakini yule binti ni mtulivu sana.”
“Iliniumiza Pam, lakini sikuwa na jinsi kwa ajili yako, WEWE. Akazungumza na mimi kwa hekima tu nikiwa nimemtoa usingizini pengine usingizi alioupata kwa shida kwa ajili ya maumivu niliyomsababishia moyoni, lakini alimudu kuficha makucha yeyote aliyokuwa nayo, kama nilivyokuomba wewe kwenye gari kabla hatujaondoka pale ukumbini, wewe ulishindwa Pam, yule binti aliweza.”
“Yeye aliweza, tena katika muda ambao nilimkosea, au sikufanya kilicho sahihi, sio kama kwako nakosea kwa kutaka kukufurahisha, hapana, kwake nilimkosea kwa kuweka ahadi ambazo nilishindwa kuzitimiza, nimemvurugia ratiba zake, lakini yule binti alijishusha nikiwa sistahili, alizungumza na mimi kama anazungumza na mwanaume anayejielewa. Kwa kuniheshimu! Na hata nilipomwambia nasitisha mahusiano, pia hapakuwa na vurugu, japokuwa wazi alionyesha kuumia lakini aliweza kuzungumza na mimi maneno yaliyobaki moyoni mwangu mpaka leo uliponifanya nikae chini nijitafakari kwa upya.”
“Ndio najiuliza, kwenu nyinyi wawili nilikosea wapi au nakosea wapi, mpaka muwe majasiri kwa kiasi cha kuweza kunidhalilisha kwa kiasi hiki!? Nini haswa nyinyi wanawake wawili, niliyetoa muda, pesa na utu wangu kwenu, kunitendea ubaya wa namna hii!?” Hapo Mill anauuliza akimtizama kabisa wala hapepesi macho wala asingeweza jibu.
“Hapana Pam. Hapa unapotaka kunipitisha wewe, ameshanipitisha mwenzio, Kisha. Na kunifunga jela. Tena akiwa amenifilisi kabisa. Sipo tayari kupita hapo tena. Sitafanyahivyo. Kwa sababu sina sababu ya kufanya hivyo. Kwanza ni kama si sawa hata kwa Shema kijana niliyemkuta vizuri sana.”
“Wale watoto wa Kisha hawakuzaliwa vile. Ila walikulia kwenye mazingira kama hayahaya unayompitisha Shema sasahivi. Kidogokidogo baada ya muda, aina ya mahusiano kati yangu na mama yao, yakawaingia na kuanza kuwaathiri. Wakageuka kuwa watoto wa ajabu, wakizungumza na mimi vile walivyomuona mama yao akizungumza na mimi. Hilo sitakubali likatokea kwa Shema.”
Maamuzi MAGUMU Kutoka Kwenye Hisia Zilizo Umizwa.
“Sasa kwa kuwa nimeona kazi nzuri uliyofanya kwa Shema. Nilimkuta umemkuza ni mtoto mwadilifu kuliko wale niliokuwa nimekuja nao, na sipo tayari kumbadili awe kama wale, nitakuachia ulee hao watoto vile unavyotaka wewe ila safari hii ukiwa na uwezo mzuri na mazingira mazuri ya kumkuzia na mdogo wake.”
“Naona shida yako ilikuwa ni ile ndoa ambayo ndugu zako walikuwa wakikusema vibaya kuwa unazaa bila ndoa, ndio maana umekuwa ukiipigania kwa garama zote, sasa nimekupa. Hilo umekamilisha. Huyo uliyebeba kama nilivyokwambia, sina jinsi ya kukusaidia, nibebee tu. Ila chochote utakachohitaji, tuzungumze kwa sababu sina uwezo wa kuota au kujua kile unachotaka, nikafanya bila kukukera. TUZUNGUMZE. Niambie kile unachotaka nisaidie, nitafanya. Nikishindwa pia nitakwambia.”
“Nyumba ile ipo. Ukishindwa kuishi pale, bila ugomvi, wala matusi, niambie, tutafute sehemu utakayotaka kuishi wewe na watoto wangu. Nitatafuta nyumba. Tafadhali isiwe uswahilini kwenye yale mazingira niliyokukuta nayo. Watoto wangu wataishi kwa uwezo wangu mimi. Nitakununulia nyumba yako kwengine, ila pale sitahama. Nimeijenga ile nyumba kwa vile ninavyotaka mimi na ndio maana nakuona wewe na Shema mnapata shida kuishi pale kwa ile baridi. Pale sitakupisha, ila nipo radhi kukutafutia sehemu nyingine. Na siku ukiwa unahamia huko na Shema, iwe kwa heshima Pam, sio kauli za ugomvi. Nitakusadia, utahama kwa utulivu kama nilivyofanya wakati mnahamia Kinondoni.”
“Ila, tafadhali sana Pam, iwe mwisho wako kuzungumza na mimi kama mjinga.Nashindwa kusema kama mtoto kwa sababu nimeona ukiongea na Shema kwa heshimakubwa sana, kuliko mimi. Huwezi zungumza na mimi kwa heshima, tuweke utaratibu ambao utakuwa wazi kabisa, ambao hatutaingiliana kwa maneno.”
“Narudia tena, isiwahi tokea unanitukana au kuniongelesha hovyo mbele ya kijana wangu au watoto wangu. Jambo halijakufurahisha, niambie sio kunipandishia. Mimi si mjinga kama unavyodhania, hata ukinieleza kwa kifupi, nakuhakikishia nitaelewa. Na nikishindwa kukuelewa, nakuahidi nitakuuliza. Sitafanya jambo lolote bila ridhaa yako.” Akaweka kituo na kuelekea chumbani.
~~~~~~~~~~~~~~
Pam alihisi miguu imeishiwa nguvu kabisa, akajitahidi kujivuta mpaka kwenye kochi. Akakaa tumbo likinguruma kwelikweli. Alikuwa akitetemeka mpaka akakalia mikono. Alikaa hapo akitetemeka hajui kama ni baridi au hofu. Meno yanagongana kama ametolewa kwenye friza.
Gafla tumbo kama la hedhi likaanza. Akahisi ni baridi kali. Akakusanya mablangeti pembeni na kujifunika akisikia Mill akioga. Kwa muda ule amekaa hapo, maneno yote ya Mill yakawa yakimrudia ila sasa kwa sauti ya Mill ila kwa juu sana. Akajikunyata juu ya kochi akizidi kutetemeka vile Mill anavyozidi kumfokea huko kichwani mwake.
Sauti ya ukali ikamrudia vile alivyomfananisha na Kisha. Kwamba yeye hana tofauti na Kisha. Pam mkorofi, mbabe, kwa mara ya kwanza akawezwa ila ikawa imepitilizasasa. Siku mbaya ambayo hakutegemea na wakati mbaya. Alikuwa na hali mbaya akizidi kujisogeza nyuma ya kochi kwa hofu. Ubaya wote aliowahi mfanyia Mill tokea anarudi nchini, ukawa unamrudia kwa wazi kabisa. Kwamba Mill alikuwa akiumia ila kuvumiliatu muda wote!
Yeye baba yake alipata mke mzuri, akaishia kumtesa na kukimbia. Sasa na yeyejeuri, Mill amerudi na utajiri mkubwa, akijinyenyekeza, na kujinyima, lakini amekuwa akimtenda ubaya! Pam akazidi kuingiwa hofu.
Brenda! Hapo ndio akazidi KUOGOPA. Kwamba sio kama Mill amekwama! Bado kuna wanawake wanamuhitaji huko na ni bora kuliko yeye! Halafu kumbe bado Brenda amebaki moyoni kwa Mill! Na ametoka kumsifia kwa wazi kabisa! Akajiambia ndio ataishia na ndoa jina, watoto na mali za Mill lakini hana Mill mwenyewe. Pam akazidi kuwaza asijue ANAISAIDIA pressure kupanda!
~~~~~~~~~~~~~~
Kwa mimba changa kama ya Pam, ukipata kitu kinaitwa severe emotional shock, kama aliyopata hapo, mshituko mkubwa ulio muingiza hofu ya ajabu kwa kiasi hicho, inaweza sababisha madhara ambayo kama hayajawahiwa, huleta madhara makubwakwa mama mwenyewe na mtoto. Na mbaya zaidi Pam anahistoria ya kuwa na pressuretayari tokea ujauzito wa Shema. Ila ilikuja kushuka baada ya kujifungua. Sasa sababu ya ugumu wa maisha, hakuwahi ifuatilia tena hata kujua iliishia wapi au inaendeleaje!
Bahari Ishatibuka
Aliposikia pametulia, akajua ameshatoka bafuni, ameshapanda kitandani, anataka kulala. Akajikaza mpaka chumbani akiwa amevaa ile rob nyeupe ya pale hotelini. Pam anatetemeka kupita kiasi na kizunguzungu kilishamuanza ila kwa kuwa hakuwa akijifikiria, akasogea mpaka pale kitandani, upande aliokuwa amelala Mill na kujifunika shuka.
Mill akafungua macho alipohisi amemsimamia pale. Akapiga magoti pembeni yake. Pam alikuwa akitetemeka mpaka Mill akashituka kidogo, ila akajikaza kiume. Si hataki kuchezewa tena! Basi akakaza roho. Alikuwa amebadilika usoni, siye Pam jeuri anayemjua yeye, asijue ni hofu imemkamata na hapo pressure ipo juu zaidi ya moyo wake unavyoweza kuhimili.
Akainamia kitanda kwa muda akijaribu kuweka maneno sawa huku amepiga magoti vilevile. Mill akimtizama pale alipoinama. Akajua neno samahani pekee kwa maneno yale yote aliyopewa tokea hawajafika hapo, halitoshi.
“Tabia zangu mbaya zimekuwa zikikuumiza, Mill. Nimeshindwa kuangalia matendo yako mazuri, nimebakia nikikuweka kwenye kundi moja la wanaume kama baba yangu, na kumlinda Shema na kuwa kinyume na wewe, ambapo wala sikuwa nikitakiwa kufanya hivyo. Nimekosa Mill. Nimekuwa nikiendelea kukuumiza bila kutosheka, lakini tatizo sio wewe, ni mimi.”
“Hata kama Mungu angeniletea malaika anioe, sio wewe, nafikiri kama nisingepata mtu wa kuzungumza na mimi na kuwa muwazi kama hivi, nahisi hata huyo malaika pia ningemkosea tu na kumuumiza kama hivi wewe.” Akashikilia kitanda maana alianza kuona giza, ila akajikaza.
“Na nashukuru umezungumza na mimi japo kwa kuchelewa. Na naomba usiache kunikumbusha. Hali kama hii ikinipata, naomba usinikatie tamaa, nikumbushe mpenzi wangu. Nimeathirika tu tokea zamani. Nahisi wababa wote wapo kama baba yangualiyekuwa rahisi kwake kututelekeza au kuendelea na maisha yake angali sisi tupo!”
“Ila kweli wewe huna tatizo Mill. Ni mimi. Umehangaika sana kwa ajili yangu na Shema. Samahani sana. Na sikusudii na wala sikujua ninakuwa kama Kisha. “Nisamehe mume wangu.” Mill akatabasamu kidogo kusikia mume wangu. “Nakuahidi nitazungumza na Shema kumuwekea msisitizo. Hii hali nitabadilisha. Na yeye atajua ukizungumza wewe baba yake ndio inauzito hata kuzidi mimi. Na huyu pia atakua akikuheshimu.”
“Naomba unisamehe, na nakuahidi nitaanza kujifanyia kazi mimi mwenyewe. Nimegundua nina shida Mill, nahitaji kubadilika kibinafsi ili nisiendelee kukuumizawewe na kuathiri wanangu. Nakuahidi nitabadilika, usifikirie tutengane. Hata ikichukua muda, jua kuanzia leo najiangalia kwa karibu sana na najifanyia marekebisho.”
“Naomba tukitoka hapa tukaishi wote. Sitatafuta pakwenda, sitaki nyumba ingine, nakutaka wewe kama Mill, sio ndoa tu kwa ajili ya familia yangu. Nakutaka tuishi pamoja, kile nilichokosa mimi, watoto wangu wakipate. Familia na nakuahidi sitakuumiza kwa namna yeyote ile hata maneno mabaya wala kukuingilia kwa Shema, nitaacha kabisa. Nitakuacha uwe baba yake kwa uhuru wote.” Akahisi kuna kitu kinachuruzika. Hakuwa amevaa chupi.
Akakusanya ile rob nyeupe aliyokuwa ameivaa na kuisokomezea katikati ya mapaja kama kujikinga, asijue zilikuwa damu. Akaweka vizuri na kutoa mkono huko ili ashikilie kitanda maana alishaanza kuona chumba kinazunguka.
Ile anarudi kushikilia kitanda pembeni ya alipokuwa amejilaza Mill, Mill akashangaa vidole vimejaa damu mpaka amepaka kwenye shuka jeupe alilokuwa ameshikilia. Alishituka Mill mpaka akaka kwa haraka.
“Sitarudi tena, naomba…” Hapohapo akamuona ameanguka. Kimya. Mill aliruka pale kitandani kumuwahi pale sakafuni, ndipo akagundua nyuma ya rob ilijaa damu. Kwamba alianza kutokwa damu tokea amekaa kwenye kochi baada ya maneno makali aliyopokea, na mbele aliposokomezea ile rob ilishalowa damu. Amepoteza fahamu, hata hatingishiki!
~~~~~~~~~~~~~~
Kuna maumivu ambayo hukaa kimya moyoni kama kivuli cha jioni. Hayapigi kelele lakini huzidi kuwa mazito kila siku. Kuyaficha ni kama kufunika moto kwa majivu. Kwa nje kuna utulivu lakini ndani kuna mwako unaochoma polepole.
Siku ukifanikiwa kufunua jivu la juu, ndipo utakapoona moto wa ndani.
Ndicho kilichompata Pam usiku huo kwa Mill aliyekuwa amefunika mengi kwa muda mrefu.
Ni nini Kitaendelea fungate!
0 Comments:
Post a Comment