Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Love At First Sight - Sehemu ya 74. - Naomi Simulizi

Love At First Sight - Sehemu ya 74.

Pam akajipatia siku ya kujiswafi asijue kumbe anajiandaa kwa harusi yake mwenyewe, na hiyo siku ilijaa hekaheka vilivyo. Mama yake alitolewa mazoezini na Jo, akampeleka sehemu ya kula. Hao wawili penzi lililokuwa likiendelea kati yao, ungefikiri ni vijana wadogo na wakati wote walitaka kuwa pamoja. Baada ya chakula ikabidi akamuache saluni mbali kabisa anakojua hatakutana na Pam. Akaungana na kina mama Colins, maandalizi yakaendelea.

~~~~~~~~~~~~~~

Mill alichukua vyumba vikubwa viwili aina ya suite, hapohapo kwenye hiyo hoteli. ambayo wangefungia ndoa. Chumba cha wanaume walikitumia zaidi yeye na mwanae kuvaa maana wasingeweza kurudi majumbani mwao. Walikwenda saluni, wakatengenezwa ndipo wakarudi hapo hotelini kuvaa ambapo Colins na ndugu zake Mill walifika hapo kujiandaa pamoja wakisubiria muda mpaka ulipofika ndipo wakahamia kwenye ukumbi mdogo maana walikuwa wachache, hapakuwa na sababu ya kufanyia shuguli yao kwenye ukumbi mkubwa.

Kwa hiyo waliowahi wakawepo hapo wakiendelea kunywa wakisubiria muda, Mill na mwanae wakiwa wamependeza kwelikweli, pamoja na hao wasimamizi wao. Ndugu zake Mill.

Walishafanya mazoezi jinsi ya kusimama mbele ya mchungaji kwenye kijukwaa kizuri kilichotengenezwa hapohapo ukumbini. Walijipanga vizuri sana kulingana na urefu wao, wakajiweka mstari mzuri na bwana harusi, pamoja na Colins. Mill alijitahidi kuvalisha ndugu zake. Na hivi wote walikuwa na miili mikubwa, halafu kuvaa ni jadi yao! Ungependa kuwatizama watoto wa Mgini kwenye hizo suti zao nyeusi.

Yakaendelea mazungumzo na vicheko wakinywa huku wakimsubiria bibi harusi na wageni wengine waliokuwa wakija kidogokidogo.

~~~~~~~~~~~~~~

Jo naye alifika hapo bila ya kuchelewa akiwa amependeza sana, na yeye alivaa suti nyeusi. Kwa kuitizama tu, ungejua pesa ya maana imemtoka. Dorothy alipomwambia amemaliza kuvaa huko kwenye chumba cha wanawake walipokodishiwa, akaenda kumfuata.

Dorothy alipendeza! Ungesema amezaliwa na kukulia kwenye pesa. Alionekana nadhifu, ile ya mama Komba. Yaani kama unadhifu ni hali aliyokulia nayo. Mama Komba alihakikisha anampendezesha asitokee watofauti. Na hivi rangi za mwili walifanana, basi na yeye akatokea kama mama dokta! Safiii.

“Waaaw!” Ndicho kilichotoka mdomoni kwa Jo alipotoka hapo chumbani. “Umependeza sana, Dorothy. Sana. Na wakakutengeneza kichwani vizuri sana. Nimependa mavazi nadhifu uliyovaa. Kwa hakika umependeza.” Akiwa kwenye wheelchair yake akamfanya ajisikie vizuri. “Asante. Na wewe umependeza Jo. Japokuwa ni kawaida yako, lakini hiyo suti imekukaa vizuri sana. Sijawahi kukuona umevaa suti! Unazidi kuvutia.” Akacheka na kushukuru. “Asante. Sasa twende kule kwenye ukumbi. Kumetengenezwa vizuri sana. Na Shema amependeza kama baba yake.” Wakacheka wakiongozana.

Mungu Anapoamuru Baraka

Kufika chini, wakakutana na wazazi wake nao wanaingia na familia ya kaka yake. Wakasalimiana, na Mill naye akasogea akiwa na Shema. Kulijaa furaha hapo na vicheko vya kupita kiasi. “Kwamba mpaka sasa, Pam hajui!?” “Hana hata habari. Nimempigia simu, anaonekana atafika hapa kwa wakati. Anajua nakuja kumtambulisha kwa watu wangu wa maana. Hajui kama tunafunga ndoa leo.” Vikajaa vicheko na mazungumzo.

Mara wakasikia sauti ya Eric kwa nje ya hapo akiulizia walipo. Mill akatoka kuwakaribisha. Maana ni kama walikuwa wameingia ila wapo kwenye ukumbi mkubwa wao walikuwa kwenye ukumbi mdogo.

Akaenda kuwachukua na kurudi nao pale walipokuwa wamesimama. Jo akashangaa familia nzima imenyamaza wakati Eric na familia yake wamewasogelea pale. Vile vicheko vyote vikaisha. Wanawaangalia.

“Shikamooni.” Akasalimia mkewe kama ambaye hajui aanze na nani. Watoto wao nao wakasalimia kwa ujumla. Eric ndio akasalimia na kuanza kushika kila mmoja mkono akionekana kushangaa sana kuwakuta pale.

Jo akagundua Dorothy alipoa kabisa wakati kijana wake akimsalimia. Ikawa kama mgeni kwake wakati yeye ndio alisikia ndio Eric mwenyewe. Alipomalizia kushika wote mkono, kimya kingine.

“Karibu sana, Eric na familia yako. Tunashukuru kwa kuja.” “Asante.” Eric akajibu akimgeukia Mill aliyeonyesha kutambua uwepo wake. “Hapa tunamsubiria Pam aje, ndipo shuguli iianze. Kuna vinywaji na vitu vidogovidogo vya kula upande ule. Mnaweza kuendelea kula wakati tukisubiria, na baadaye kutakuwa na chakula chakueleweka.” “Asante.” Mkewe na watoto wakaondoka hapo maana ni kama walionyeshwa hawajapokelewa na wengine. Na mke wa Eric huwa hajali. Akaondoka bila hata kumpa mama mkwe mkono au kuongea naye cha ziada mbali ya ile salamu ya jumla.

Eric akamgeukia mama yake. “Unaendeleaje?” “Vizuri tu.” Akajibu hivyo kwa ufupi tu na kunyamaza. Akawa kama anataka kuuliza jambo, akasita. “Acha na sisi tukapate vinywaji.” Mjomba mtu akaona aage. 

“Twende nyanya nikakupe soda yako ile unayoipendaa.” “Bora.” Shema akaenda kumshika kabisa mkono bibi yake Pam, au mama yake mama Eric akitaka aondoke naye.

“Sasa hapo Shema taratibu, sio tena uende kuoga soda. Shati hilo jeupe ligeuke rangi za soda.” “Kwani hujanibebea shati jingine lakubadili? Ajali zinaweza tokea bibi.” “Shema!” Mama Eric akashituka sana nakufanya mpaka baba yake, yaani Mill aanze kucheka taratibu. Shema hana mbavu. 

“Umesahau kunibebea shati jingine nini?” “Ujue usifanye mchezo Shema wewe!” “Nakutania bwana bibi! Sijichafui. Nakuwa mwangalifu.” “Na ukumbuke unapotaka kuanza hekaheka zako.” “Bibi anawasiwasi na mimi! Siku hizi nimekuwa mkubwa!” Bibi yake akabaki akimtizama, Jo akicheka akimtizama huyo Shema.

“Basi acha niseme hivi, nikijichafua nageuza shati, mbele nyuma, nyuma mbele hata hutaona.” Bibi yake akamrushia kitu kidogo alichokuwa nacho mkononi akakwepa, hana mbavu. “Hatajichafua mama. Usiwe na wasiwasi alikuwa anakusubiria akuchokoze. Tokea tupo chumbani anavaa alikuwa anakuigilizia utakavyokuwa ukimuwinda asijichafue.” Ndio wote wakaanza kucheka sasa.

“Ujue huna adabu Shema wewe!” Bibi yake akamwambia. “Yaani yeye bibi, raha yake anione msafi kila saa, nisichafuke hata nikienda kucheza nje, anataka nirudi msafi.” Wote wakazidi kucheka. “Yaani upo katikati ya mchezo, anamtuma mama aje aniite nikanywe maji. Ila ujue shida yake ni anione sipo mchafu. Akiona nimechafuka ananiambia nibadili nguo halafu ananichana nywele hata katikati ya mpira, jasho linanitoka.” Wakazidi kucheka kwa sauti, Mill hana mbavu akiwatizama.  

“Muulize nyanya huyu hapa, mpaka anamwambia anisubirie nimalize kucheza mpira kabisa, ndio nioge, nibadili nguo, halafu anichane nywele, bibi hataki.” Wakazidi kucheka. 

“Sasa na mimi nikijua yupo, nikienda mpirani navua shati kabisa. Naweka pembenii! Sitaki mtu aliguse. Ili akiniita narudi msafi kama nilivyotoka nyumbani, inabakia kazi ya kuchanwa nywele tu shati safi, narudi haraka mpirani.” Mill alicheka. Alicheka sana kama Jo. “Maneno mengiii. Na usijichafue Shema.” “Sijichafui bibi bwana! Nabakia hivihivi mpaka mwisho.” “Nitakuona.” Akawa anacheka akiondoka na nyanya yake. 

“Sasa nyanya na wewe huku mjini hawashikani hivi mikono. Unakuwa unanishika kama vile nilivyokuwa mtoto mdogooo!” Wakamsikia akimwambia nyanya yake, akasimama kabisa. “Anapenda kumpanga mama, huyu!” Mama Eric akafanya wacheke wakiangalia anavyomfundisha nyanya yake. Akasimama wima na kukunja mkono. “Haya, ingiza mkono wako hapa ndani ya kwenye kiwiko changu.” Nyanya yake akafanya kwa wepesi. 

“Sawasawa.” Mpaka Jo akajikuta amemkubali Shema kwa jinsi alivyomshika vizuri nyanya yake. “Nimefundishwa na baba.” Akajisifu kwa kujigamba. “Hiyo ndio sahihi. Such a gentle man!” Jo akampongeza Shema kwa wazi. “Umesikia bibi?” “Sasa wewe macho yawe mbele sio tena umuangushe.” Bibi yake akamfanya azidi kucheka. “Ona tulivyopendeza nyanya.” “Mmmh!” Bibi yake akaguna.

         “Babu naona wewe umesahauliwa.” Mill akamwambia babu yake Pam. Shema akasikia. “Yake namletea hapohapo. Nilitaka nimzungushe nyanya kidogo. Nimtoe ushamba.” Mpaka Jo akacheka. Mill akacheka sana akiwatizama. “Muone kichwa chake!” Bibi yake akaongeza, Shema akazidi kucheka. “Mama alishakwambia mimi uzuri wangunimechukua kwa mama yako. Neno baya lolote unaloniambia mimi, ujue unamwambia mama yako. Na anakusikia.” Walicheka, walicheka sana, bibi yake akimtizama. “Twende mwaya nyanya.” Wakaondoka.

~~~~~~~~~~~~~~

         “Kwani mmekuja lini?” Ikabidi Eric aulize. “Kutoka wapi?” Mama yake naye akamuuliza na kumchanganya kidogo Eric na alimfanyia kusudi. “Namaanisha kutoka kijijini.” Jo akawa kama hajaelewa tena. “Mimi na bibi yako tumeingia tokea jana. Baba Shema alitutumia gari kuja kutuchukua.” Akajibiwa na babu yake. Mama yake kimya.

         “Twendeni nikawatembeze na nyinyi kidogo mpaangalie kwa nje. Ni pazuri sanandio maana Shema anasema hivyo. Tulitaka tufanyie nje, lakini sikutaka harufu ya bahari ije imchefue Pam, aanze kutapika. Bado sijajua nini kinamkera.” “Bora umelifikiria hilo, kuliko shuguli nzuri ije igeuke kuwa ni ugonjwa.” Wakaongozana akiwatambulisha kwa ndugu zake kisha wakatoka nje kabisa. 

Eric akifuata kwa nyuma kama mgeni kabisa kwa mama yake mzazi na ndugu zake. Yaani gafla yeye na mkewe ndio wakawa hawafananii tena na uthamani wa mama yake na kina Mill. Wale aliowaacha kwenye shida, gafla wamebadilika na kuonekana borakuliko yeye na mkewe waliokuwa wakificha pesa yao wakiona shida kusaidia.

Mambo yaliendeshwa hapo kitajiri, ungedhania ni mipango ya miaka, kumbe pesa imeongea kwa siku mbili tu, kitu kikatokea. Mama Komba na Kamila walikuwa wakihakikisha wageni wao wanapata kitu chakula na vinywaji wakati wao, kisha kutoka na kuendeleza mazungumzo hapo, wakimsubiria Pam.

Pam.

Ilipofika jioni ya saa 11 kasoro gari ikawa inamshusha Pam nje ya hoteli. Ukweli alikuwa amependeza sana. “Nahisi nimewahi kidogo nilikuwa nikihofia foleni. Wewe umeshafika?” “Safi sana. Ingia, pitiliza moja kwa moja upite kwenye ule ukumbi, utanikuta huku.” “Nakuja.” Mill akatangaza kuwa Pam ameshafika, kila mtu aingie hapo ndani. Waliokuwa nje wakaanza kukimbilia ndani, kumsubiria sasa mlengwa mwenyewe. 

Pam akaanza kujivuta taratibu asijue anavyosubiriwa humo ndani. Ukumbi ulikuwa umepambwa vizuri sana. Kila kitu kilikuwa tayari tokea saa 6 mchana.

~~~~~~~~~~~~~~

Shema siku hiyo alitoka shuleni mapema sana. Asubuhi alifanya tu mtihani na kutoka shuleni. Akamfuata baba yake kutengenezwa kichwa. Na kuhamia hotelini pamoja na kina Colins kwa kujiandaa. Baba Colins siku hiyo na yeye ni kama alifanya kazi mpaka mchana wa saa sita tu na kuungana nao. Kila mtu, mpaka ndugu zake Mill walishakuwa tayari, maana Mill aliwaambia saa 10:30 jioni watu wake wakaribu wawe wamefika. Saa 11 jioni wanafunga ndoa.

~~~~~~~~~~~~~~

Basi Pam alipita mapokezi na kiatu chake cha juu, taratibu akijiweka sawa, ili asimuabishe Mill kwa hao watu wake muhimu na yeye ajiwakilishe ipasavyo.

Watu kadhaa walimsifia alipokuwa akipita na kumuongezea ujasiri, maana alivaa nguo ya usiku wakati bado giza halikuwa limeingia nje. Ujasiri ukaongezeka kadiri watu walipokuwa wakigeuka kumuangalia kisha kupata sifa na minong’ono ya kupendeza kwake.

Akaingia mpaka kwenye ukumbi waliokuwa wamekodi ila wakisubiria tarehe. Palikuwa pasafi tu, lakini hakuna mtu. Kimya kimetanda hakuna hata mziki. Hakushangaa, ilikuwa siku ya kazi. Akaendelea kupita, mlio wa kiatu chake cha juu ndio ulikuwa ukisikika. Asijue huko walipo kina Mill wamenyamazishana wakisikia akija.

Akatembea na kutoka hapo, akaingia kwenye chumba kikubwa tu ila sio kama ukumbi waliotaka kukodi. Ukubwa wa kiasi. Akaona kumependeza sana, kumepambwa kwa unadhifu wa hali ya juu. Pakamvutia macho haswa na kumzubaisha kwa sekunde kadhaa. Akasimama kabisa akiangaza macho vizuri akivutiwa na umaridadi wake. 

Safi halafu kumepoa vizuri kama sehemu inayokaribia kufanyiwa tafrija fulani hivi! Akavutiwa sana asijue anavutiwa kwa sababu ni rangi zake yeye mwenyewe alishachagua apambiwe siku ya harusi yake. Maua ya rose fresh zilizofanya pavutie zaidi na kunukie vizuri. Meza chache zilikuwa zimefunikwa vitambaa vya rangi aliyokuwa amechagua na verses zilezile alizokuwa amechagua kutoka kwa mpambaji wao zimewekwa kwenye hizo meza na rembo zilezile alizochagua! 

Akavutiwa kuona alichochagua kwenye picha jinsi kinavyoonekana kwa uhalisia wake. Akajipongeza rohoni na kujiambia atampigia simu mpambaji wao kumsisitiza asije badilisha. Akahisi mpambaji huyohuyo pengine ndiye aliyekodishwa na hapo kupamba kwa shuguli ndogo ya mtu mwingine. Akasogea na kugusa kabisa moja ya meza iliyokuwa karibu yake. Akatengeneza kitambaa vizuri akiangalia kwa kuvutiwa asijue chumba hicho kina watu wanao mwangalia ila kama wamejificha kidogo.

Mwishoe akagutuka akaona aondoke kumtafuta Mill ili aungane naye.  Wakati anatoka hapo na kuangaza mbele ndipo akamuona Mill amesimama mbele kidogo. “Ona palivyopendeza! Uchaguzi wangu ulikuwa sahihi.” Kabla Mill hajajibu akiendelea kumsogelea akashangaa watu wanaanza kujitokeza wakisogea pale aliposimama Mill. Akakunja uso kadiri alivyokuwa akisogea.

Akamuona na Shema, ila amevaa suti nzuri sana. Miguu ikashindwa kupiga hatua nyingine mbele zaidi alipoona ndugu wa Mill, kina Colins wamevaa suti zinafanana nyeusi. Kisha akaona watu wa ofisini kwao wote wamevalia vizuri. Akasimama kabisa pale alipomuona bibi, babu yake wakiwa na familia ya mjomba wake pia. Moja kwa moja akajua kinachoendelea. Ikawa kama ambaye taarifa kamili zimefika kichwani, wakamuona anaweka mikono yote miwili mdomoni. Akaendelea kuangaza macho, mikono bado mdomoni, ndipo akagundua hata Eric na familia yake walikuwepo. Hapo ndipo akaganda kabisa. Kwa sekunde kadhaa ni kama ulimwengu mzima ukasimama.

“Ujue pale hatasogea tena baba. Ameganda.” Shema akafanya baba yake agutuke na kumkumbuka Pam. Mama Colins akaanza kupiga vigelegele kama kumtoa kwenye ile hali. Wanawake waliokuwepo pale wakapokea kupiga vigelegele. Ikabidi Mill amfuate mpaka pale, wakiendelea kuchukuliwa video, watu nao wakisogea kidogo kushuhudia. Mill alikuwa amependeza sana. 

Akamfikia mpaka pale alipokuwa amesimama. “Umependeza sana Pam wangu. Sana.” Pam alikuwa haamini amebaki ameshika mdomo. Akapiga goti mbele yake. Na Shema akasogea. Akamshika mikono yote miwili akiwa amepiga goti mbele yake.

“Nilikuwa nakuandalia kitu kizuri mpenzi wangu ili kukufurahisha. Ila furaha yangu itakamilika leo, utakapokuwa mke wangu kihalali. Watoto wetu wawe na familia ya kueleweka.” “Leo!?” Pam akawa anauliza haamini. “Sasahivi. Na si serikalini. Tuna mchungaji kabisa, anasubiri ukubali, atufungushe ndoa.” Pam akaanza kurukaruka kwa furaha.

Mill akamvalisha pete ya uchumba, nzuri sana. “Leo tumalizane kabisa.” Pam akawa anacheka hana mbavu. “Mama yuko wapi? Mama!” “Bibi huyu hapa.” Shema akamuwahi mama yake maana alishaanza kupaniki. Akamchungulia alipomuona akamkimbilia akicheka na kumuonyesha pete akawa anacheka akiiangalia. “Mill ananioa, mama.” “Hongera kwa uvumilivu. Umependeza.” “Na wewe mama. Lakini huna mkufu!” “Umeanza Pam! Leo ni siku yako bwana!” “Lakini ungevaa mkufu. Hivyo…” Mama Komba akamshika.

“Pam, hawa watu wote wako hapa kwa ajili yako. Tulikuwa tukikusubiri wewe tu, shuguli ianze. Twende ukabadili nguo mje mfunge ndoa.” Akarukaruka kidogo akicheka mbele ya mama yake. Kisha wakamuona anavua mkufu palepale na kumvalisha mama yake. “Umesahau na pafyumu.” “Pam bwana!” “Hii ni ile unayoipenda mama. Subiri.” Wakamuona anatoa pafyumu kwenye pochi yake, akaanza kumpuliza mama yake kila mahali! 

“Utampulizia bibi mpaka machoni! Nipe mimi nimalizie ukabadili mama.”  Shema akafanya watu wacheke. Pam akaridhika. “Hapo sasahivi umekamilika. Twende mama yangu unisindikize. Naolewa mwenzio.” Jo akabaki akiwaangalia akicheka ila akamuelewa Dorothy. Ukweli Pam ALIMJALI sana mama yake, tena katika kila mazingira, jicho lake halikuacha kumtizama na kumfikiria mama yake! Akashangazwa anawezaje hata katika mazingira kama yale yaliyoonyesha kumchanganya hata yeye mwenyewe Pam, lakini bado aliweza kumuangalia mama yake! Kikabaki moyoni kwa Jo.

Akarudi kwa Mill akionekana ni kama amechanganyikiwa hajui afanye nini tena. Akamshika mikono yote akicheka na kumbusu midomoni kwa juu tu. “Nimefurahi Mill! Nimefurahi sana. Asante.” “Tufunge ndoa basi!” “Mimi mwenyewe nataka.” Watu wakaanza kucheka na vigelegele.

“Gauni lako la harusi limeletwa hapa. Nenda kabadili ili tufunge ndoa LAKINI, tupate picha za ukumbusho ukiwa mchumba kabla ya mke.” Mill alisikika. Yaani yeye Pam hakuwa na shida, hapo akawa anakubali kila kitu. Vigelegele vikaendelea. Wakapata  picha nyingi tu wao wawili tu, nje ya huo ukumbi wakati watu wengine wakiwaangalia. 

Kwa hakika Pam alijawa furaha, kila wakati alikuwa akicheka na kumkiss Mill. Tena wakati mwingine alikuwa akimvuta kabisa ili apate midomo, Mill alikuwa akicheka sana. “Leo mimi napendwa!” “SANA. Na dhambi zako zote zimesamehewa.” Mill alizidi kucheka, na kuzidi kupendezesha picha. 

“Mwenzio nilijua umenikinahi!” Akamnong’oneza wakichukuliwa picha huko nje. Mill akacheka sana. “Nilikuona ulivyokuwa ukihangaika asubuhi! Nilikuwa nakufanyia kusudi, tufaidi baada ya hapa.” Pam akazidi kucheka. “Nimefurahi Mill. Nimefurahi sana.” “Nakuona.” Wakazidi kucheka mpaka wakamaliza hiyo awamu ya kwanza ya uchumba, wakaacha watu kwenye cocktail, Pam akaenda kuvaa sasa kwa harusi.

Ndoa.

Kwa kuwa alishakuwa ametengenezwa vizuri tokea anafika hapo, haikuchukua muda kuwa kibibiharusi. Watu walipoambiwa warudi ndani ya ukumbi tayari kwa biharusi kuingia, Mill alijawa furaha, ungemuona jinsi anavyo sugua mikono akichekacheka,ungejua alilolisubiri kwa miaka yote limetimia. Wimbo wa biharusi kuingia ukaanza, wote wakasimama.

Kwa hakika Pam alipendeza. Alikuwa ameshikwa mkono na mama yake, wanatembea taratibu mama yake akiwa kwenye wheelchair yake ya umeme, akiiongoza taratibuuu! Walipendeza mno. Na vile mama Eric alivyovaa nadhifu na kutengenezwa vizuri akaongeza na cheko, ungependa kumuangalia. 

~~~~~~~~~~~~~~

Eric alikuwa kama anaangalia filamu haamini kinachoendelea. Ndipo akaamini maneno ya Mill aliyomwambia kwenye simu kuwa hajui mengi yanayoendelea kwa familia yake, na wao wameamua kumuachana naye. 

Kulionekana kuna maisha mengine kabisa yaliyokuwa yakiendelea kwenye familia aliyoiona mzigo, na yeye hana taarifa wala hakuwa akishirikishwa tena. Hapo alihudhuria kama mgeni tu, na Pam naye ni kama hakumtambua kabisa, akawa kama wageni wengine. Alimuona akimsalimia bibi yao na babu kwa furaha sana kwamba ndio na yeye anawaona hapo hakuwa na taarifa na ujio wao, lakini si yeye na mkewe waliomuacha jela, akiwa mjamzito wakitaka ajifunze.

Pam alijawa furaha alionekana hata nje ya shela alilokuwa amevaa. Rangi yake nyeupe ya mwili iliwaka mpaka nje ya shela nzuri sana aliyokuwa amefunikwa. Jo naye alibaki akiwaangalia Dorothy na mwanae wanavyotembea wakiwasogelea juu ya kapeti hiyo nzuri iliyokuwa imemwaga maua kama kufuru! ILIVUTIA SANA. Japo mama ni mlemavu yupo kwenye wheelchair, akimsindikiza binti yake kufunga ndoa! Ngeni ilayakuvutia sana. Na Pam alifanya KUSUDI kumtaka mama yake. Alipopewa wazo la kushikwa mkono na mjomba wake alikataa katakata. “Nitakongojana na mama yangu hivyohivyo.” Akang’ang’ania.

~~~~~~~~~~~~~~

Mill alibaki akimwangalia Pam kadiri alivyokuwa akimsogelea. “Umependeza sana.” Pam akaweza soma midomo. “Na wewe umependeza sana. Nimefurahi Mill!” Watu wakamuona Mill anacheka. “Ukumbi?” Akamuuliza, Pam akaangalia tena kulia na kushoto kitembea na mama yake taratibu. “Kila kitu kizuri, na Shema amependeza sana.” Wakaendelea kuongea wakikaribiana. 

Waliposogea akashuka na mchungaji wakawasogelea karibu kabisa na kuuliza, “Ni nani anayemtoa binti huyu leo?” Mama Eric akajibu akijivuna. “Mimi.” Vigelegele, Mill akamshukuru mkwe na kupokea mkono wa Pam mpaka juu walipotengenezewa kufunga hiyo ndoa.

“Nimefurahi, Mill! Sijategemea kabisa.” “Nilikufanyia kusudi. Nilitaka ufurahi kama hivi.” Pam akazidi kucheka asiamini. Mchungaji alifanya ibada fupi isiyozidi dakika ishirini, Mill na Pam wakawa mke na mume kihalali.

Walicheza jioni hiyo, kukaa ilikuwa kidogo sana, muda wote walikuwa wakicheza, ungejua wawili hao wanafuraha. Kulikuwa na utulivu wa namna yake, lakini kila mtu alikuwa nadhifu. Pam akapata muda na bibi na babu yake. Na yeye akawa katikati akicheza mdumange, ngoma ya kwao Sambaani. Mill, Jo na wengine wakawa wakifuatisha vizuri sana wakicheza na kucheka muda wote maana Pam mwenyewe alikuwa akicheka wakati wote, bado haamini. Kwa hakika ilivutia.

Maisha Kuanza Kuchukua Uhalisia.

Hekaheka la Fungate.

Mill na Pam wakatoka ukumbini wakicheza kwelikweli, wanaagwa kwenda mapumzikoni. Pam akajua ni maigizo, wanarudi nyumbani. Akashangaa gari inawashwa dereva anataka kuondoa gari. Akagutuka. “Mwanangu!?” Maana akaona wanaondoka bila mtoto na Mill naye ameinama anataka kupata kiss waanzie fungate garini! “Nimejipanga kwa kila kitu. Mama atahamia pale kwako. Atakuwa naye mpaka tutakaporudi.” “Subiri kwanza Mill. Kwamba sisi tunakwenda wapi bila Shema!?” Ndoa akaanzia hapo.

“Si tunaenda mapumzikoni!” “Kwamba tunaenda sisi wawili tunamuacha?!” “Si ni honeymoon yetu! Sasa ulitaka twende naye?!” “Siwezi ondoka nikaenda popote bila Shema.” “Pam!” “Hakika tena. Sijawahi tengana na yule mtoto kwa usiku hata mmoja, tokea kachanga.” “Kila kitu kitakuwa sawa. Nimejipanga.” “Hakika mimi huko unakotaka kunipeleka sitapumzika akili zangu. Tena utanifanya nichanganyikiwe kabisa. Siwezi.” Hapo bibi harusi keshafunga mikono kifuani, kwamba safari hamna mpaka aitiwe mwanae.

“Unajua kuna kujibaraguza siku ya kwanza ya harusi! Angalau kajiunafiki kuziba makucha. Sasa leoleo unayafungua yote?” “Wewe unajua unayemuoa bwana! Acha kunipoteza malengo. Wewe ukitaka nitulie, niitie mwanangu nizungumze naye, ndio nijue kama namuacha au la.” “Hakika hataenda na sisi.” Maharusi hao wakaanza kubishana hapo ndani ya gari hata nguo za harusi hawajatoa.

“Wakati wewe unalazwa na yale madawa ya kuzuia kutapika, mwenzio nilikuwa naandaa kila kitu.” “Wewe kama kweli unataka nikapumzike huko, niitie Shema hapa nizungumze naye, au niache nirudi ndani nikamtafute mwenyewe. Simu yangu anayo mama.” Ikabidi ampigie Shema. 

“Mama yako anataka kuzungumza na wewe.” “Sio kwenye simu.” Pam akabisha.Mill akamtizama na kurudi kwenye simu. “Toka hapa nje. Mwambie bibi akusindikize.”“Mbona kama nakuhisi unataka kunisemea kwa mama!?” “Sasa wewe ulitaka atoke hapa peke yake?” Wakatulia washakorofishana.

~~~~~~~~~~~~~~

Baada ya muda wakashitukia Shema, bibi yake na Jo wanagonga kioo cha gari. “Mimi nataka kuzungumza na Shema.” “Anachotaka ni twende na Shema honeymoon.”  Jo na bibi mtu wakashangaa sana, lakini Shema akainama, baba yake akashangaa sana. “Wewe Shema, hatujazungumza na tukakubaliana utabaki na bibi! Mbona sasahivi unataka kulia hapa mbele ya mama yako?” “Huyu mtoto sijawahi tengana naye tokea anazaliwa.” “We Pam?” Mama yake akawa kama anayemkumbusha. 

“Ulikaa naye kidogo tu, mama. Kidogo. Yaani yeye mwenyewe hata hakumbuki! Hatuwezi kumuacha peke yake. Itakua kama tunamtelekeza.” “Naomba kuzungumza na Pam.” Jo akaingilia. Wote wakamtizama. 

“Sitachukua muda mrefu.” Kwa kuwa ni mgeni, Pam akakubali kwa shingo upande. Asingembishia yeye kama Mill na mama yake.

“Toa huo mkia wa shela, tukazungumze pembeni.” Akavua nakubakiwa na gauni lililokuwa limemkaa vizuri sana kuendana na umbile lake. Jo akafungua mlango wa gari na kumshika mkono vizuri kiheshima, kumsaidia kushuka garini.

Ndoa Na Iheshimiwe Na Watu Wote, 

Hata Maharusi Wenyewe.

Wakatembea mbele kidogo mpaka akaridhika wapo peke yao ndipo akaanza. “Hongera kwa ndoa.” “Huyu mtoto tunampa mabadiliko makubwa makubwa sana Jo! Ni vile wewe hujui. Kwake inakuwa kama adhabu!” “Unamuamini mama yako akiwa naye?” “Yeye peke yake ndio namuamini naye. Lakini…” Akasita.

“Hiki unachokwenda kufanya na mumeo ni cha muhimu sana Pam. SANA kuliko nitakavyokwambia na kukuelewesha. Na ni hivyo mna mtoto tayari, ndio maana hata Mill amefupisha. Lakini mlihitaji muda wakutosha, nyinyi wawili tu pasipo muingilianomwingine kwa ajili zifuatazo.” Jo akaendelea taratibu na kwa tahadhari kama anayetumbua jipu, asije haribu.

“Leo kwa mara ya kwanza, umepewa Mill kama mume. Na yeye hajawahi ishi na Pam kama mke. Mnahitaji kwenda kuweka msingi wenu nyinyi wawili ndipo wengine, hata watoto waongezeke juu yenu.”

“Huo msingi mnaokwenda kujenga sasahivi, nyinyi wawili, ni muhimu ukajengwa kukiwa hakuna muingiliano wa aina yeyote ile. Kuwe na usikivu na utulivu ambao hata mkiulizana maswali, kuwepo na majibu ya kueleweka, halafu mkitoka huko, maisha yatakapochukua uhalisia wake, kukiwa na kuyumba, basi mnapo pakuangalia na kukumbushana mlichopanga mwanzoni kabisa. Bila hivyo, mkiendelea tu, mtayumbamno. Kwa sababu athari za kuweka msingi mkiwa nyumbani huku mmesongwa na ya nyumbani, mnaweza kuweka msingi wenu kwa mazoea au mkiwa mmevurugwa. Mkaweka mbovu.”

“Ila mkiweka msingi wenu mkiwa mmetulia, huko mapumzikoni, itawasaidia kuweka msingi imara, na mzuri, utakao wasaidia wakati wa gharika za maisha. Mtakuwa mnapo pakuchungulia, palipo sahihi, imara, mnakotamani muwe, na mtajikuta mnaweza endelea. Na isiwe leo tu. Hata baadaye, hiki mnachofanya nilazima mkiendeleze.”

“Muwe mnarudi nyinyi tu wawili, sehemu tulivu, mnajifungia, kwanza mnakumbushana kwa nini nyinyi wawili mliamua muwe pamoja, mlipo, na mnapotaka kuendelea. Nyinyi kama wazazi wa hawa watoto, vinginevyo, msingi wenu utayumba, hata watoto wenu hawatakuwa na sehemu nzuri ya kukulia.”

“Nyinyi wawili kwanza. Kisha watoto na ndugu. Msingi wako na Mill ni muhimu sana. Tena inapofika kwenye kujenga na kuimarisha huo msingi, wewe kama Pam, mama na mke, ndio unatakiwa kudai muda mtulivu ili kumuweka sawa Mill. Hakikisha mudausio na mwingiliano unapatikana, na mnaweza kuweka mazingira ya kujipanga nyinyi wawili bila kuzembea. Vinginevyo, hii furaha niliyokuona nayo leo ukumbini, baada ya muda mfupi sana, itapotea na wote mtajikuta mkifanya mazuri lakini kila mtu akipigana vita peke yake ndani ya nyumba yenu, kwa sababu hamna msingi wenu. Hilo moja na la muhimu sana.”

“Kingine, muda wako na Mill leo, kimwili ni muhimu. Mmekuwa na mipango mingi ya hii ndoa ambayo haikuwahi kutimia. Kabla ya Shema na huyo mdogo wake, nimesimuliwa jinsi mlivyohangaika bila mafanikio, mpaka LEO hii. Mill ameandaa kitu kikubwa sana, na cha garama kwa ajili yako, hatimaye amefanikisha. Huu ni mwanzo, ili kumtia moyo aendelee kuwa mbunifu wa mambo mazuri kama haya, lazima na wewe uende umbali mrefu kama alivyofanya yeye, kumwambia umetambua. Kwa maneno lakini vitendo zaidi.” Mpaka Pam akaona aibu.

“Huko mtakapokwenda, patulivu, ndio muda wakwenda kulipa fadhila. Kimapenzi, kwa uhuru, bila kufikiria kama Shema amekula au la. Ni siku tatu tu. Hata tusipompa chakula, mimi daktari nakwambia, utamkuta hai.” Akacheka taratibu.

“Shema hawezi kukaa na njaa.” “Mumeo amejiandaa SANA. Mill anakupendaPam, na anakufikiria sana. Tokea juzi anahangaika ili kufanya ukatulie huko mapumzikoni. Alishaniomba mimi kuwarudisha nyumbani.” “Kweli?!” “Nakuhakikishia Pam. Mimi ndio nitamrudisha mama yako, Shema na msichana anayemsaidia kazi mama yako, pale ulipokuwa ukiishi. Hapa tunapozungumza, dereva alikuwa akihamishia mizigo ya mama yako pale kwako, ili shuguli ikiisha, mimi nikiwarudisha nyumbani, mama yako akatulie na Shema.” Akamuona amepoa mpaka usoni. Akajua vimefanikiwa kumuingia.

“Hapa nilipo nina ratiba ya Shema kuanzia anaamka mpaka mazoezi ya jioni. Sehemu unayonunua vitu vyake vya kula akitoka mazoezini, tena endapo vitawaishia kabla, maana mumeo amejaza nyumba vyakula. Haya niambie, kuna mumeo alichobakisha?” “Mpaka hapo hakuna.” Pam akajibu akicheka kwa aibu.

“Mill anakupenda Pam, na anafanya kila kitu akikufikiria sana. Alijua bila hivyo hutatulia huko.” “Na mimi nampenda sana, ila sikutaka Shema ajisikie kama mtoto anayesahauliwa na wazazi. Hatumjali.” “Sasa wewe unalo jukumu. Shema anahitaji kukusikia wewe ukimwambia atabaki na sisi, na atakuwa sawa. Safari hii na nyingine mtakazofanya na baba yake, zinazowahusu nyinyi wawili, hataweza kwenda, ila nyingine mtakazopanga kama familia, basi atakuwa na nyinyi. Sawa?” “Sawa.” Akakubali kwa uzito.

 “Mpe siku tatu tu Mill. Tatu tu. Halafu ukirudi utakuja niambia jinsi zilivyowanufaisha.” “Labda kesho jioni nizungumze naye, nijue siku yake imeendaje?” “Nakuhakikishia yeye na mama yako watakuwa sawa. Kuwa mbinafsi kwenye siku hizi tatu, ukapumzike. Najua hujanifahamu vizuri, lakini mimi ni mtu wa maneno yangu. Nitasimamia, atakwenda shule, atakula na utamkuta salama. Hata akiugua, jua kile ambacho ungefanya wewe endapo ungekuwepo, basi jua mimi na bibi yake tutakifanya. Sawa?” “Sawa.” “Unaniahidi utapumzike?” “Ndiyo.” Akabaki akimtizama.

“Kweli. Hata mimi nahitaji muda na Mill. Ni wasiwasi tu kwa sababu sijawahi pata mtu akakubali kuwa na hao wawili kwa uhiari huo. Asante Jo.” “Karibu. Haya, twende ukazungumze na Shema, muondoke.”

Msumari Wa Mwisho

Wakarudi walipowaacha. Mpaka Mill alikuwa ametoka garini amesimama nje. Alionekana amebadilika kabisa usoni. Ile furaha yote ilionekana imeisha.  Pam alimuona, akamuita Shema. “Kabla hujazungumza na Shema, naomba tuzungumze kwanza Pam.” Jinsi alivyozungumza, wote walijua hayupo sawa. Akatangulia kuondoka hapo, Pam akamfuata kwa uso wa wasiwasi.

Wakaenda hukohuko walipokuwa wametokea na Jo. Akasimama baada ya kwenda umbali wa kutosha. Akageuka. Pam akasimama. “Kila kitu, tokea mwanzo wa kufahamiana kwetu, nimekuwa nikifanya kwa juhudi zote ili kukufurahisha WEWE tu.” “Natambu…” “Subiri kwanza. Naomba usiniingilie.” Pam akashituka na kunyamaza.

Umenifanya nijitafakari. Naona nalipa garama kubwa sana ambayo kwako haijawahi leta maana, ila imekuwa kero. Sasa la msingi tumeshalimaliza, sitakuwa na surprise nyingine tena.” Pam akashituka sana.

“Kuanzia sasa nakukaribisha na wewe utoe maoni yako. Ukiona jambo halifai, kuliko kuzua vurugu na kuendelea kunidhalilisha kwa Shema mtoto wang…” “Mill! Umekwenda mbali!” “Hata kidogo. HAKUNA maamuzi nayaaamua mimi kama baba yake, ukayapitisha na kumuonyesha Shema nimepatiaKauli yako kwa Shema ndio MWISHO na yeye amejua hilo. SITAFANYA hivyo tena, kwa ndoa hii. Nilifanya hivyo kwa Kisha na watoto wake, naona historia inajirudia!” Bwana Pam aliishiwa nguvu na kuingiwa hofu, hakujua kama angechukulia kwa umbali huo.

Nilihangaika hivihivi kwa Kisha na watoto wake. Hapakuwahi kuwa na heshimawala kuthaminiwa juhudi zangu ila kuishia jela. Sasa inawezekana nakosea jinsi ninavyofanya. Au najitoa kupita kiasi mpaka na kera.” “Mimi hunikeri.” “Ila ni nini Pam?! Ni nini? Japokuwa huyu mtoto nilikukuta naye, lakini tokea siku ya kwanza, nimesimama kwenye nafasi yangu nikijitoa kwake kwa hali na mali, na huku wewe ukizidi kunionyesha nafasi yangu kwake haitakaa ikabadilika. Wewe ndio unaamua juu yake, na hutataka kupingwa.”

“Na Shema naye amejua kuwa mimi sina maamuzi juu yake. Nikiwa naye ananiheshimu na kunisikiliza. Lakini wewe ukitokea tu, unanipinga vibaya sana, hata mbele ya watu, mpaka Shema mwenyewe anabadilika! Hapana Pam. Mimi ni binadamu na nina hisia zilizokwisha pitishwa hapa unakonipitisha sasahivi, tena nikiwa nikihangaika kama hivi kukufurahisha wewe. Naona INATOSHA.”

~~~~~~~~~~~~~~

Kamba Imekatikia Pabaya.

Kwa bahati yake ilivyo mbaya, siku yao ya harusi, ndio Pam amegongelea msumari wa mwisho kwenye jeneza ambalo lilishafanikiwa kumuweka Mill ndani na wengi waliopita kwenye maisha ya Mill kugongelea misumari watakavyo. 

Alishasukumwa na wengi akavumilia, ila siku aliyoiandaa kwa pesa nyingi na hamasa, kumbe alikuwa ameshafikishwa ukingoni kabisa, alichofanya mke huyo mpya ni kumalizia kumsogeza mwishoni kabisa ya ukuta. 

Ukawa mwisho wake. Akashindwa kabisa kuvumilia na kutoa la mayoni, na BADO.

Mengi na makubwa yapo mbele kwenye siku hiyo iliyokuwa inaonekana imejaa baraka, kumbe na mwovu naye amefanikiwa kupenyeza ajenda yake kufanya uharibifu.

Ni nini kitaendelea? 

Usikose

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment