Alipoona sasa wameshika adabu, wametulia kwa hofu, akajua huo ndio wakati muafaka wakuwapanga sasa. Hata hivyo alishamuhurumia mpenzi wake. Akaenda kupiga magoti mbele yake. “Nisikilize na usiogope. Tutakuwa sawa. Nikimaanisha mimi na wewe. Twende tukapime. Kama mimi nitakutwa nimeathirika, nitaondoka wala sitakutafuta tena.” “Nikikutwa mimi ndio nimeathirika?” “Nitahakikisha unaishi kwa furaha na wala hutaona mabadiliko. Nakuahidi Dorothy. Mimi ni daktari, najua ninachozungumzia. Hutaona tofauti na hutaona upungufu.” Akazidi kujibebea utukufu hapo mbele ya wakweze.
“Hapa nishaona upungufu tayari. Ndio tutaishije?! Maisha yananipunja kila wakati na bila kosa!” “Sio safari hii, tena ukiwa na mimi. Nakuahidi Dorothy. Twende, usiogope. Na nitakupenda kwa upendo uleule.” “Unauhakika?” “Chukua hatua ya kwanza kama kaka yako alivyoshauri. Twende tukapime, ndipo utaona kuanzia hapo.” Pakatulia hapo sebuleni! Ujasiri wote wa ukwe ukawaisha, ikawa tena kama msibani.
~~~~~~~~~~~~~~
“Umeanzisha jambo, ona sasa! Sikukwambia mimi usubiri mpaka harusi ya mama Shema iishe?” Mama mtu akaanza kulalamika. Lugha ikabadilika, kikaanza Kisambaa. Mama anaongea kisambaa kwa sauti inayosikika si jambo la kheri, mwanae, yaani Simon ameinama kimya hazungumzi kama wengine hapo sebuleni.
Aliongea huyo mama, mumewe ametulia. Kisha akamalizia kwa lugha ya kiswahili. “Unataka kuniua, Simon. Unipeleke kaburini niache mwanangu.” “Sio nia yangu mama. Dorothy hajaathirika.” Wakamuona ananyanyuka
“Haya tupeleke sasa huko kwenye kupima.” “Mama umekasirika sana.” “Si umetaka vipimo viwe leo wewe? Ndio twende. Na iwe sasahivi ili watu wajue moja. Naenda kufuata viatu, twende.” Akaingia ndani na baba mtu naye akasimama. “Naona na mimi niongozane na nyinyi tu.” Akaingia ndani.
“Kama mtahitaji lifti, twendeni. Gari yangu itakuwa na nafasi ya watu wawili zaidi.” “Naomba uongozane na wazazi. Nitafuata nyuma.” Simon akaomba kwa unyenyekevukama sio yeye! “Hamna shida. Ulikuwa na hospitali ambayo ungependelea?” Jo akauliza kiuungwana tu, lakini wazi ujasiri ulishaongezeka, Simon aliyekuwa mbabe wake amepoa haswa.
“Nia yangu ilikuwa nzuri tu.” Jo kimya akimtizama na kumsikiliza. Alipoona Jo hajibu tena, akarudisha akili kwenye swali. “Ile hospitali anayofanyia kazi Pam na mama yake ni garama sana. Lakini ingefaa. Inavifaa vya kisasa.” “Kama hiyo ndio ungependelea, mimi nitalipia. Acha tutangulie kwenye gari.” Akamgeukia Dorothy. “Ungetaka kutumia choo kabla hutujaondoka?” Akamuuliza Dorothy kwa sauti ya chini akionyesha kujali. Akakubali. Akaenda chooni, Jo akatoka nje.
~~~~~~~~~~~~~~
Akasikia tena wanazozana ndani, yeye akatulia kimya huko nje akiwa amewasha gari lianze kupata ubaridi. Mwishoe akaona wanatoka. Dorothy, wazazi wake, kaka mtu na mkewe. Watoto wao wakisindikiza kwa nyuma. Akataka kumbeba dada yake, Jo akawahi kuweka kidaraja ili ashuke kiurahisi, kisha akaweka tena vizuri garini, akapanda wakishangaa vile anavyomjali. Akamfunga kabisa mkanda. “Unataka maji?” “Hapana. Nipo sawa. Asante.” “Ukisikia kiu, uniambie. Bado tunayo maji.” Mama yao akaguna kwa masikitiko. Wote walisikia.
“Mzee wangu wewe unaweza kukaa mbele, mama akakaa na Dorothy hapa nyuma.” Ikabidi wafuate, kaka mtu na mkewe wakapanda gari yao, safari ya hospitalini ikaanza. Kimya garini.
Wakiwa kwenye mataa akamgeukia. “Nikupe maji?” “Nitasumbuka huko hospitalini.” “Ni kweli. Njaa haijaanza kukusumbua?” Wazazi wakabaki kusikiliza.
“Sasahivi hata akili haifanyi kazi.” “Usiogope. Hakuna matokeo ya leo yatabadilisha chochote. Tukapime, halafu twende ukale. Nitakupeleka sehemu nyingine. Huwa wanapika chakula kizuri sana.” “Zaidi ya pale?” “Ila sio pahadhi ile. Huko nitakapokupeleka hata ukila kwa mkono, hawatajali.” Angalau Dorothy akacheka.
“Au ulipapenda palepale?” “Nilipenda juisi yao. Nzuri kama unakula embe la kwetu! Ila kama ni garama, sio lazima.” “Sio mbaya. Twende wote, pengine na wazazi watafurahia.” “Tusikuingize garama zaidi. Sisi tunaweza kurudi kula pale kwa kaka yake huyu.” “Mimi naomba ukapate juisi ya embe kwanza, ndipo utaamini maneno ya Dorothy. Wanatengeneza juisi nzuri sana.” Angalau akafanya waanze kuzungumza jambo jingine mbali na la hivyo vipimo. Maana aliweza kuwageuzia kibao, yaani binti yao ndio akawa matatizoni kuliko yeye waliyetaka kumbambikizia maradhi.
Hospitalini, Kujua Mbivu Na Mbichi
Baadhi ya wauguzi waliowakuta pale walishamfahamu mama Eric, haikuchukua muda kuandikiwa vipimo na kwenda maabara. Wakajikuta wamekaa hapo wote watano wanasubiria maana walichukua ile ya Rapid HIV Test, waliambiwa itachukua nusu saa. Lakini wakiwa kwa daktari alishamuomba amfanyie Dorothy annual checkup akisema wanataka kujua ni nini kimepungua kwenye huo mwili wake. Kwa hiyo yeye Dorothy akachukuliwa damu nyingi wakati yeye Jo, kwa rapid test ya HIV tu alichukuliwa ya kidoleni.
~~~~~~~~~~~~~~
“Unawaza nini?” Wakamsikia akimuuliza kwa sauti ya chini na kumvuta mkono. “Nina wasiwasi Jo! Nina wasiwasi sana. Yule mwanaume alikuwa mchafu sana. Malaya asiye na adabu wala aibu.” “Nilikuahidi nini?” Akavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu.
“Majibu yote nitapewa leo?” “Mengine yatachukua muda, sio leo. Ila hatua ya kwanza ya vijidudu vya UKIMWI ni leo. Vingine na kipimo kingine kikubwa cha UKIMWI haitakuwa leo. Ushafikiria utakavyo pendeza kesho?” Angalau wakamuona mama Eric akianza kucheka.
“Hujaniambia ratiba. Kazini, saluni na harusini au kazi kesho hamna?” “Mimi mama wa bibi harusi, lazima nipendeze.” “Dereva wako anataarifa lakini kama kuna safari ya saluni?” Akazidi kucheka mpaka kwa sauti.
“Maana mipango hiyo ni mizito, lazima uhakika wa usafiri. Vingenevyo utakwama.” “Nina uhakika na dereva wangu. Usiwe na wasiwasi.” Jo alicheka sana. “Dorothy!” “Sasa wewe unataka kunitishia mambo madogo hayo! Mimi sio mwenzio.” “Usiniambie!” “Naingizwa mpaka garini!” “Eeh!” “Nafungwa mkanda!” Jo alicheka asiamini, mpaka watu wakawageukia wao.
“Usinitishe na mambo madogo madogo kama hayo.” “Sawa Dorothy. Nisamehe mimi.” “Dereva wangu si wa mchezo. Kwanza msafi, ananukia vizuri, anajali na…” Akaangalia wanao mzunguka, akamfanyia ishara msogelee ampe sikio. Jo akafanya kwa haraka akicheka. “Na dereva wangu ananiminyaminya miguu, na kunikiss.” Alicheka. Alicheka sana. “Hakika siamini!” “Ndio uanze kuamini.” Akawa akicheka huku akimwangalia haamini.
~~~~~~~~~~~~~~
Kisha akawageukia wazazi na shemejie pale walipokuwa wamekaa kinyonge. “Nimeambiwa kesho lazima tucheze mdumange.” Akawafanya wacheke kwa jinsi alivyomudu kuitamka vizuri. “Ni ngoma ya kwetu hiyo, baba.” “Na mimi nimealikwa na Mill harusini, lazima nitacheza.” Akafanya kusudi kuwaonyesha mpaka Mill anamfahamu.
“Kumbe unafahamiana na Mill?!” Simon akauliza kwa kushangazwa haswa. “Na Pam pia. Mji aliokuwa akisoma Mill ndio nilikuwa nikiishi huko na familia yangu kabla ya mke wangu kufariki. Na kama mambo yatakwenda kama anavyopanga, huko atakapokwenda kuishi na Pam, ni karibu sana na mji nilioacha Condo yangu na kwa shemeji. Nilikuwa nikimtania jana na kumshawishi atafute nyumba karibu na kwangu, naona nimeanza kufanikiwa kwa asilimia fulani.” Simon akapoa kabisa.
~~~~~~~~~~~~~~
Jo, si mgeni kama alivyodhania yeye. Alidhani yeye ndio alikuwa wa kwanza kumfahamu, kumbe na Mill, kamungu mtu kao, anamfahamu mpaka kukubali ushauri wake! Na Jo aliwafanyia kusudu ili kuwatuliza zaidi. Mazungumzo yakabadilika kabisa na heshima ikaongezeka. Kwanza jinsi anavyomchukulia Dorothy na hiyo hadhi yake. Wakanywea kabisaa.
~~~~~~~~~~~~~~
Wakaitwa kupewa majibu. Akasimama na kumgeukia Dorothy. “Twende, na usiogope. Wataanza kutupa risala ndefuuu. Haimaanishi ndio umeathirika.” Wakaondoka hapo wakisikia wanazungumza. Walibaki wanyonge hapo kama wapo msibani. Simon akijutia angalau angesubiria kwanza amfahamu vizuri, akajua anazungumza na nani, ndipo apenyeze swala la upimaji kwa heshima. Akajutia kutosikiliza ushauri wa mama yake wa kusubiri. Wakabaki hapo wakishindwa hata kuendeleza mazungumzo.
~~~~~~~~~~~~~~
Baada ya muda wakaona wanatoka. “Vipi?” “Naona ulikuwa sahihi.” Wote wakashituka alivyomjibu hivyo Simon. “Ni mimi ndio nimeathirika.” Pakazuka kimya hicho, na wao wakawafanyia kusudi wakabaki wakiwatizama kuona watasema nini. Tayari walishaanza kumpenda Jo. Alionekana kumjali Dorothy. Watafanyaje? Wakapoa kabisa.
Wakaona Dorothy anacheka. “Anawatisha tu. Hakuna aliyeathirika kati yetu.” Angalau wakaanza kucheka tena na utani. “Mimi nahisi kama nimeanza kukubalika sio kama mwanzo! Ni kama mliingiwa na kijihuruma fulani hivi!” Utani ukaendelea mpaka sehemu ya kulia chakula.
Jo&Wakweze
Kila mtu akaagiza walichokuwa wakishawishiwa na Jo, wakiendelea kucheka na utani mwingi tu. Wakaona vile kila wakati akitaka kujua Dorothy anavyoendelea na kumfanya kama kabinti kadogo! Alikuwa na raha huyo Dorothy! Ungemuona ungejua anapendwa. Wakapata muda mzuri wa pamoja, akiwakarimu kwa garama zake, mpaka mke wa Simon akaona awe muungwana.
“Naona ulikuja kwetu tukashindwa kukukarimu hata maji ya kunywa!” “Hata kigoda cha kukalia sikupewa japo Dorothy alijaribisha, naona shemeji yangu akakataa kabisa!” Akaongea akicheka. “Tunaomba radhi. Watu wamekuwa wakimuonea sana Dorothy. Ile picha alivyorudishwa nyumbani na watoto akiwa mgonjwa, inashindwa kunitoka kabisa. Utanisamehe Jo. Sikutaka aje apite hapo tena. Hata kama ingekuwa dada yako na wewe, ungekuwa na sehemu ya kujilaumu na kutamani isije tokea tena.” “Naelewa kabisa.” Jo akawa muungwana na yeye.
“Sehemu kama hizi hatujawahi fika sisi. Niseme mimi na mke wangu. Sijui Simon. Tunashukuru kutuleta hapa, asante kwa kila kitu. Najua ni garama sana. Chakula kizuri na tumesafisha macho.” Baba mkwe na yeye akaona ashukuru kwa kuwa mkweli. Wakacheka wakitaniana hili na lile lakini wakakubaliana waaganie hapohapo, wazazi warudi na Simon pamoja na mkewe, yeye amrudishe Dorothy nyumbani akapumzike.
~~~~~~~~~~~~~~
“Kabla hamjarudi kijijini, naomba niwakaribishe na kwangu.” Dorothy hakutegemea. Alisema mwanamke aliyeachana naye hakutaka hata kumkaribisha kwake! “Mje muoneninakoishi, na mkutane na dada yangu pamoja na mumewe. Ni watu wangu wa muhimu sana. Ni kama wazazi wangu. Naweza hata kuwafuata kama Simon atakuwa na shuguli nyingi.” “Hata mimi ningependa kuja. Au ukaribisho huo ni kwa wazazi tu?” Wifi mtu akauliza kwa utani akichangamkia.
“Karibuni wote kama mtakuwa na nafasi. Hivi nilitaka kuzungumza na Mill kwamba hata yeye na Pam ningependa siku hiyo ndio wakaribie. Waliniambia watakuwa na mapumziko mafupi baada ya harusi yao. Kwa maana nyingine jumamosi ijayo watakuwa wamesharudi nyumbani, ndio siku hiyo nilipanga niwakaribishe wote.” “Basi na sisi utuhesabu.” Mke wa Simon hakujivunga kabisa. Akaweka huo ukaribisho wa wazi kwa wote akiomba idadi ya watakao fika ili afanye maandalizi mazuri, na kuagana.
Dorothy&Jo
Dorothy akawa ametulia garini. “Unawaza nini tena?” “Uliniambia mwanamke wa mwisho ulimkatalia asifike kwako, Jo. Sitaki tuje tukosane mimi na wewe. Mwenzio haya maisha ya amani na kujaliwa hivi sijawahi ishi.” “Sikumkaribisha kwangu kwa kuwa sikuwa nikiona muendelezo wetu. Wewe naiona kesho yangu na wewe.” “Kweli Jo?!” “Kabisa! Hivi wewe unafikiri ningewekeza muda wangu kwako kwa kiasi hiki!? Si ningekutafutia dereva na kumpa gari awe anakusindikiza sehemu unazotaka!”
“Natoa muda wangu kwako kwa sababu nakujali Dorothy. Na hili nimekwambia kwa kurudiarudia sana. Tafadhali amini sifanyi hivi kwa kila mtu. Nina pesa ya kumpa yeyote, lakini si muda wangu. Nipo hapa na wewe, nazunguka na wewe kila mahali! Si kawaida yangu, Dorothy! Muda wangu ni garama kuliko pesa ambayo naweza mpa mtu akakuzungusha na wala nisijisikie kama nimepoteza pesa, kwa sababu isingenigarimu sana.”
“Natoa muda wangu kwako, jua ndio kipimo changu cha juu sana cha mapenziyangu kwako. Inathamani kuliko pesa yeyote ninayoweza kukupa. Dada atakwambia. Mimi sipendi kufanya manunuzi au kwenda madukani. Hata Betty alikuwa akijua na kunisaidia kwa asilimia kubwa sana. Usifikiri Betty alikufa akiwa peke yake kwa bahati mbaya! Sisi tulikuwa tukiongozana kila mahali isipokuwa kufanya manunuzi tu. Mara nyingi alikuwa akinihurumia na kuniacha. Ni kitu sifurahii.”
“Vaa yangu nafanya mtandaoni, vitu vinifuate nilipo. Vije mpaka mlangoni kwangu. Ndio ujue ni kwa kiasi gani nachukia kwenda madukani. Lakini kwako nimefanya.”
“Na kingine, mimi napanga mambo yangu Dorothy. Kama isingekuwa wewe, leo kaka yako asingenipeleka hospitali.” Akapoa. “Eti yeye ndio anipangie chakufanya kwa wakati wake! Hata kidogo. Lakini nimeona hiyo ni garama ndogo sana yakulipa ili kukufanya wewe uwe na furaha.”
“Najijua mimi sina UKIMWI. Ni Betty tu ndiye niliyekuwa nikilala naye bila kinga. Wengine wote hata kama tunapima, siamini bila kinga. Kwanza kwa umri wangu huu, sikutaka mtoto na mtu mwingine, na pia sikutaka maambukizi ya aina yeyote yale. Ni mimi ni mgumu sana kuamini mtu.”
“Mpaka mimi mwenyewe nimejishangaa jinsi ambavyo pale kwa kaka yako, yale mazungumzo jinsi ambavyo hayakunikera na kunifanya niage. Kwanza ni kuondokawala si kuaga maana hata kiti hawakunipa.” “Kwamba ungeondoka?!” “Bila ya kufikiria mara mbili na wala nisingegeuka nyuma.” Ikawa kama haamini.
“Kweli?!” “Wewe hujanijua vizuri nisipotaka jambo!” Akamfanya afikirie vizuri. “Ni kama nilikuona kwa Stella alipokuwa akikuomba namba ya simu!” “Na ujue ustaarabu ule ilikuwa nikijikaza kwa sababu yako wewe. Sikutaka uje unikatae sababu yakuniona mkorofi.” “Kwamba ungefanyaje?” Akamuona anacheka.
“We Jo?” “Ningempa jibu la wazi kumuhakikishia anaelewa kuwa sitaki, na asirudie kuomba tena.” “Palepale?!” “Kabisa.” Dorothy akajikuta akicheka kwa sauti ila akimfikiria vizuri huyo Jo.
~~~~~~~~~~~~~~
Walifika kwa Dorothy, wakabaki garini wakiromance bila ya kutosheka, na kupitiliza. “Wakirudi kina Pam, na kuweza kuwa na Shema, kabla wao hawajafika nyumbani kwangu, naomba ukaribie kabla yao.” Dorothy akajivuta pembeni na kujiweka sawa kwa mshangao.
“Lini?!” “Siku nikikuchukua kutoka kazini, badala ya kukurudisha nyumbani moja kwa moja tunaenda kwangu. Tunaweza fanya alhamisi na ijumaa.” “Siku mbili!?” “Wewe fikiria wakati kama huu tuupate kwa kujinafasi, sio kujibana hapa garini!” Acha Dorothy aanze kucheka akimwangalia.
“Utafurahia zaidi. Lakini kabla ya ijumaa, nitakuwa nishazungumza na Mill na kujipanga naye zaidi juu yako. Zaidi ratiba yako pale kazini. Lazima kuanza mazoezi.” Akamuona ametulia kama anayefikiria kitu. “Unanisikiliza lakini?” “Nakusikiliza, ila nimepata tumaini!” “Juu ya nini?” “Ujue ni kama niliikatia tamaa miguu yangu? Ilikuwa hata nikiosha, naosha kwa kuichukia tena hata naweza nisiiangalie. Pam alipokuwa akija kijijini ndio mara nyingi alikuwa akinipaka rangi za kucha, tena hata siiangalii. Kama niliyekuwa nimeisusa.”
“Lakini mbona ni misafi sana? Namaanisha ipo nadhifu.” “Sijui ni Pam kunihurumia au la, kuna sehemu ananipeleka. Wanaiosha na kuipaka rangi kama hivyo, na yeye mwenyewe ndio ananitafutia aina hii ya viatu. Anasema amerithi miguu mizuri kutoka kwangu. Basi yeye ndiye anayehangaika na hii miguu, mimi niliizira kabisa. Yaani hata kuiangalia kwa kuitizama sikuwa nikifanya hivyo.”
“Walipokuwa wakiiosha, huwa naangalia pembeni kabisa. Lakini tokea uanze kuishika kwa kuithamini, eti naanza kuihisi ina uhai!” “Kwa sababu inayo uhai. Na wewe ukianza kuipokea, ukaifikiria, na kuiamuru ifanye kazi yake, utashangaa hata mazoezi yake yanajibu kwa haraka tu. Usiikasirikie. Na yenyewe ni mihanga.” Akaendelea kuipapasa kwa upendo. Wakatulia kabisa hapo garini.
“Nasikia faraja ya ajabu sana ukifanya hivyo!” Akamwangalia maana alikuwa amepotelea kwenye hiyo miguu anasikia raha yeye mwenyewe. Akamsogelea midomoni na kuanza kunyonya kwa fujo kama amvue nguo, naye Dorothy hatosheki! Kuja kuangalia saa, wanakaribia kuanza siku ingine, wakaachiana.
Jumatatu.
Alikuja kuamka mida ya saa nne asubuhi Mill alipokuwa akiingia. “Unaendeleaje?” “Kwani sasahivi ni saa ngapi?” “Saa nne kwenda tano asubuhi. Vipi?” Akakaa kwa haraka. “Nimepitiliza.” “Nilikuacha kusudi ili upumzike. Na sikukupa dawa makusudi ili usilale siku nzima. Vipi?” “Sijisikii kutapika, ila njaa!” “Niliandaa kila kitu kabla ya kuondoka.” Pam akawa hajaelewa.
“Ilibidi niende kwanza kazini, nilipoona kimya, ndio maana nimerudi kukuangalia.” “Nashukuru nimelala mpaka najisikia vizuri.” “Umeamuaje sasa juu ya saluni?” “Nitakwenda mara baada ya kula. Muda si uleule tunakutana saa 11 jioni?” “Bila ya kuchelewa.” Akajibu akikaa na kufungua laptop yake, alipomuona amezama huko, yeye akaenda kuoga.
Akatoka nusu uchi na Mill akamuona, akashangaa hata hajahamasika, anaendelea na yake. Pam akashangaa sana. Akatoa taulo kabisa na kuendelea kujipaka mafuta mbele yake, Mill kimya kama yupo na Shema hapo chumbani! Kidogo kikamsumbua Pam. Mill mpenda mwili wake, asiombe hata kugusa! Akaona bora tu avae. Akayafanya yote hapo chumbani mpaka kutoka kwenda kula, Mill busy tu.
~~~~~~~~~~~~~~
“Haya ndio madhara ya kuzaa na kuishi na mwanaume kabla ya ndoa. Keshakinahiwa.” Akawaza akila. “Mill alikuwa si mtu wa kutonishika siku mbili na wala asishituke nikiwa uchi!” Akaendelea kusononeka rohoni, hapo Mill yupo chumbani kama alivyomuacha, macho kwenye anachokifanya.
~~~~~~~~~~~~~~
“Naona Jo amekazana na mama!” Akamtoa kwenye mawazo akiwa anakula. Pam akawa hajaelewa. “Mbona Jo ameniambia mmeshakutana?” “Oooh! Joel? Yupo?” “Sana.Naona na kazi ya udereva ameomba apewe yeye, amuendeshe mama.” “Mill!” “Hakika tena. Nimekutana naye asubuhi hii akiwa anamshusha. Aisee utashangaa Pam. Ametengeneza ile gari yake, mpaka amenitia hukumu kwamba sisi hatukuwa tukimjalimama ipasanyo.” Akamsimulia Pam vile anavyofanya kumtoa mama yake garini na kumpandisha, Pam akashangaa sana.
“Ila ameongea jambo lililonifanya nifikirie.” “Nini?” “Ujue mama alipofanyiwa yale matibabu ya upasuliwaji, hakufanyiwa mazoezi kabisa?” Pam akabaki haelewi. “Alitakiwa mazoezi, Pam. Alitakiwa baada ya pale viungo vifanyiwe mazoezi ili kuvikumbusha kazi yake.” “Hakuna aliyekuwa akijua wala kujali, Mill. Ile kumsaidia kurudisha uwezo wa choo ulikuwa msaada ambao tulijua ndio mwisho. Wewe mwenyewe umemkuta akisota.” “Naelewa mazingira hayakuwa yakiruhusu, lakini naona Jo yupo sahihi. Anatakiwa afanyiwe zaidi.”
“Hapa tunapozungumza, palepale hospitalini ameshamuanzishia kliniki ya mazoezi ya viungo. Anafanyiwa sasahivi.” “Mill!!” Pam hakuwa akiamini. “Sio hivyo tu, kesho amempatia appointment ya kuonana na daktari kwa upya. Anataka wajue alipatwa madhara kwa kiasi gani wakati akijifungua. Anataka aanzishiwe vipimo kwa upya.”
“Nimemwambia kila kipimo kitakachohitajika, iwe juu yetu sisi. Iwe pale au sehemu ingine, sisi ndio tugharamie. Anasema atatujulisha. Ila anaonekana kumjali sana mama.” “Mmmmh!” Pam akabaki mawazoni. Maana mwanzo wao aliuona, hakujua kama Jo angekuwa serious kwa kiasi hicho.
“Nitakuona baadaye.” “Sawa. Sitachelewa.” Akashangaa anatoka bila hata kiss ya shavuni! Akazidi kutaabika nafsini mwake. Akaona ampigie simu mama yake.
~~~~~~~~~~~~~~
“Pam, mama yako ameomba nimpokelee simu, anafanyiwa mazoezi.” Pam akacheka. “Jo?” “Ni mimi. Vipi hali yako? Mill ameniambia ulikuwa ukitapika.” “Naona nimepona, hapa nakula, sishibi!” Jo akacheka. “Ndio vizuri mtoto akue vizuri.” “Unamuonaje mama na mazoezi? Ni kitu kitamsaidia?” “Mapema kusema. Acha tufanye vipimo vyote. Ila kwa jinsi nilivyogundua, miguu yake bado nerves zake zipo hai na zinafanya kazi kwa asilimia kubwa. Mazoezi ni msaada mkubwa sana. Ndio ameanza, tumpe muda.”
“Nikwambie ukweli Jo?” “Karibu.” “Hivi unavyoniona mimi na mama yangu ni Mungu kazini.” “Unamaanisha nini?” Pam akajikuta machozi yakimtoka. “Mungu yupoJo, na anafanya kwa ajabu sana. Mimi na mama yangu tulikuwa mwisho kabisa wa dunia, tunaishi kama watoto wa ndege. Kile anachopewa bibi na babu, ndio na sisi tulikuwa tukiponea hapohapo.” Jo akajisikia kuumia.
“Mama huyo alijisahau kabisa kama anaishi. Kila aliyeonyesha anauwezo na anaweza kumsogelea, ilikuwa akitutanguliza mimi na Eric, tusaidiwe kwanza. Sasa kwa kuwa sisi tulisaidiwa kwa namna yao hao wenye kutusaidia walivyoweza, yeye alikuwa mtu wa mwisho kabisa kusaidiwa.” Pam akaendelea kwa uchungu.
“Ameishi maisha ya kifukara huyo mama, akitambaa sakafuni kama nyoka! Ila hakuwahi kuacha kuomba. Nimuombaji sana huyo na anampenda sana Mungu, mwenyewe anasema tokea binti mdogo, Mungu amekuwa ndio nguzo yake. Japokuwa tulikuwa kwenye magumu yasiyo tamkika, eti yeye hakuwahi mtilia mashaka Mungu mpaka mimi nilikuwa nikimshangaa! Anayo imani kubwa sana kwa Mungu na anampenda Mungu bila kuona mkono wa Mungu juu yake au Mungu akimtendea jambo, lakini eti yeye anampendaga tu Mungu.” Akajifuta machozi.
“Nimegundua hilo. Na anamoyo mzuri sana. Ila Pam, wewe ni fahari ya mama yako. Umemtunza sana mama yako, mpaka anakosaga jinsi ya kukueleza kifasaha akahisi nitamuelewa vile ulivyokuwa umejitoa kwake!” “Sikuwa na uwezo. Tulikuwa tukigawana kidogo nilichokuwa nikipata. Sikuwa nikifanya sana kwake kama ilivyotakikana. Yaani Mill ndio anayehangaika na sisi wawili tokea mwanzo. Mill amekuwa kama ndio majibu ya maombi ya mama yangu.” “Na yeye anakiri hivyo.” Wakatulia kwa muda.
“Nakushukuru sana Jo. Asante kwa kutusaidia.” “Mama yako anastahili zaidi ya hivi Pam. Anamoyo mzuri sana. Ni kama maisha yalimuonea tu. Halafu mzuri.” Alimfanya Pam acheke sana.
“Jo!” “Sasa wewe unafikiri ningeng’ang’ania bure?” Akazidi kucheka. “Kwa hiyo unang’ang’ania?” “Sana.” Pam akazidi kucheka. “Nilitaka ucheke hivyo. Sasahivi unaishi kwa ajili yako na mtoto pia. Sitaki uwe mnyonge.” “Umenikumbusha mbali sana. Hakuna aliyetujali kwa umbali huo Jo. Alikuwa Mill, mpaka nilikuwa nikimuhurumia, sasahivi na wewe. Umenigusa. Asante.” “Karibu. Kazana kula, na uanze kliniki mapema.”
“Nitafanya hivyo, asante kujali. Msalimie mama, mwambia akiwa peke yake anipigie.” “Ili mnitete.” Pam akacheka sana. “Jo!” “Wewe sema ukweli.” “Kidogo tu!” “Sawa Pam. Uwe na siku njema.” “Na wewe Jo.” Wakaagana na kumuacha Pam akiendelea kucheka.
~~~~~~~~~~~~~~
Inaendelea…
0 Comments:
Post a Comment