Kilitanda kimya cha muda kama ambao hawajui waendelee vipi kuanzia hapo, lakini mwishoe Jo akamvalisha viatu alivyokuwa amemtoa akimpapasa nyayo na miguu hapo garini. Akamuweka sawa sehemu za nguo alipovuruga akimapapasa kipindi amepandwa mzuka akinyonya ndimi zake, na kumfunga mkanda huyo Dorothy. Kisha akarudi kukaa mbele na kuondoa gari kuelekea nyumbani kwa Simon, kaka yake Dorothy, kimyakimya. Kwa kuwa alishaelekezwa na Mill, haikumuwia ngumu sana kufika.
Simon alikuwa na maisha tu ya kawaida na nyumba ya kawaida sana tu. Hapakuwa na geti useme ni ngumu kuona gari likiegeshwa mbele ya nyumba. Na madirisha sio kwamba yalikuwa juu sana na rembo nyingi kwamba usione nje. Kwa hiyo wakati wanaegesha gari wa ndani waliwaona.
Akatoka kwenda kumpokea akijua anashushwa, atahitaji msaada wa kupanda ngazi. Akatoka na kukuta Jo anamsaidia kushuka garini kirahisi tu, kisha akaweka kidaraja chake akapandisha mpaka juu. Jo akafunga gari na kuwasogelea maana walikuwa wakisalimiana.
“Naona umebahatika kupata kiwanja sehemu nzuri! Hapapotezi kabisa.” Akaanza Jo kirafiki akitafuta jinsi ya kumuingia shemejie. “Tulinunua viwanja enzi hizo unajipimia tu.” “Nyinyi ndio mlibahatika aisee! Siku hizi unanunua kiwanja bei ya kujenga nyumbakabisa! Na si sehemu nzuri kama hizi zenu. Hongereni sana.” “Tunashukuru. Na uzuri si mbali hata na kituo cha daladala. Karibuni ndani.” Dorothy yeye akatangulia akiingia ndani. “Asante. Hongera kwa ugeni mzito wa wazazi.” Jo akaendelea wakifuata nyuma.
“Tunashukuru wamefika salama. Karibu.” Kwa jinsi alivyoingia na kukuta anavyosubiriwa na wote wapo kimya hapo sebuleni, akajua kaka yake aligomba mpaka watu wote hapo ndani walisikia ndio alikuwa akisubiriwa yeye.
Akaenda moja kwa moja alikokua amekaa baba yake. “Umependeza mama, umependeza sana, lakini huna furaha! Ni nini tena?” “Mimi sio mtoto mdogo baba.” “Mimi sijasema hivyo.” Kaka yake akadakia akiwa anafuata nyuma. Akaingia sasa mwenyewe huyo Jo. Msafi haswa, wazi akafanya hata wenyeji wake wajiweke sawa.
“Ninachotaka ni kukusaidia ili usirudie kosa.” Kaka yake akaongeza. “Sio nilikwambia mimi haya mazungumzo uyaache ili kuwe na amani? Huyu anaozesha binti yake, jambo ni la amani, unataka kumnyima raha bure kusipo sababu!” “Mama, sio naondoa amani, najibu kutokana na anavyomlalamikia hapo baba. Nia yangu ni nzuri na ninamlinda.” “Kwa hiyo unaona nilazima iwe leo?” Baba mtu akadakia na yeye.
“Baba na mama, narudia tena, nia yangu ilikuwa nzuri. Sitaki Dorothy aje arudie kosa.” “Ndio kwa kumkumbusha mambo ya zamani?” “Katika hili, sitapuuza kama mwanzo wazazi wangu. Mwanzoni huyu alichukuliwa akiwa mzima tu. Wakaenda kumuharibu na kumrudisha nyumbani wala asikumbukwe tena. Alikuwa amesahaulika, hakuna anayemsogelea. Iweje iwe sasa? Kosa langu ni mimi kutaka kitu bora kwake?” Akaendelea kaka mtu.
“Dorothy ana moyo mzuri sana. Na ni mwema. Ni rahisi mtu kumdhulumu na akavumilia akiteseka. Hapana jamani! Lazima kukumbushana na safari hii wote tuwe walinzi wake.” “Sitafanya hivyo kwa Dorothy.” Wote wakamwangalia Jo.
“Nimekuja naye mpaka hapa, kwa kuwa namjali.” “Kwani baba Eric alisema nini?” Kaka mtu akauliza kwa ukali kabisa.
“Alikwenda mpaka kwa baba akapiga magoti akimtaka huyu. Tukamuamini. Tukampa Dorothy aliyemzima, binti mdogo, akaenda kumchakaza dada yangu, akamrudisha Dorothy mgonjwa na watoto wawili!”
“Baba huyu ndio akaishia kulea wale watoto tukihangaika kusaidia pale tulipoweza. Mama ndio akaacha kila kitu ili awe na Dorothy. Aliyekuja kumuomba kwa magotihatujamsikia mpaka hivi tunavyozungumza.” “Nisingekuja naye leo kama nia yangu ni kumchezea tu Dorothy.”
“Kungekuwa na umuhimu gani wa kuja mpaka hapa kwenu kama sina nia naye nzuri? Si ningemtafutia tu taksii au dereva mwingine akamleta hapa na ningeendelea kuonana naye kwa vificho bila nyinyi kujua?” Pakatulia.
“Nimeacha shuguli zangu zote, nipo naye hapa, kwa sababu namjali sana. Sihitaji mtoto kwake. Sihitaji chochote kwake isipokuwa yeye kama Dorothy.” Akamgeukia kaka yake.
“Kama ulivyosema. Dada yako ni mwema sana, lakini si mjinga. Anaakili zake na nafikiri mapito aliyopita nyuma, imekuwa fundisho kubwa sana kwake. NakuhakikishiaDorothy yupo makini.”
“Kama usingekuwa umakini wake, pengine sasahivi mimi nisingekuwa peke yangukwake, maana kuna msiruru wa wenzangu wanao mvizia pale anakofanya kazi, lakini Dorothy ana hekima ya kuchanganua mambo. Sivyo kama mnavyofikiria.” Kidogo wakatulia.
“Na mimi nipo hapa na yeye si kwa kubahatisha. Tumekubaliana kuanza safari yetu kwa vile Mungu atakavyojalia na maisha ya nyuma kuwa ni kama fundisho. Narudia tena, nisingekuwa hapa na yeye sasahivi kama si mapenzi ya dhati kwake. Nampenda Dorothy na nimekusudia kuwa naye.” “Kwa nini Dorothy na sio mtu mwingine wakati wewe unaonekana unao uwezo wa kupata mwanamke mwingine yeyote?” Simon akauliza na kumshangaza Jo kwa wazi kabisa.
“Labda nikuulize kwa heshima kabisa. Ni kwa nini awe mwanamke ‘mwingine yeyote’ na asiwe Dorothy?” Hapo akakwama kujibu, na kufanya wote wamgeukie sasa yeye kaka mtu kumsikiliza, na Jo naye akafanya kusudi kunyamaza amsikilize jibu lake.
Akaongea mengi akiruka hili na kurudia lile, lakini hapakuwa na jibu la kueleweka. Na Jo naye kimya akimpa nafasi. Bwana kaka alizungumza huyo! Mpaka akaanza historia ya dada yake tokea anazaliwa. Jo kimya, ila akasikia mtu akimvuta, akageuka. Alikuwa Dorothy. “Kaa!” Akamwambia kwa sauti ya upendo.
Kumbe hata mgeni mwenyewe alikuwa hata hajakaribishwa! “Karibu ukae baba. Na akimaliza tu kaka yake huyu, nataka mkanionyeshe hivyo ulivyotengeneza gari kwa ajili yake huyu.” Mama mtu akadakia na kufanya wamgeukie na yeye tena. “Sio kitu kikubwa sana mama yangu. Ni kumrahisishia tu upandaji wake garini na kwenye ngazi.” “Hakuna mtu aliyejitoa hivyo kwake huyu. Unapomsikia kaka yake anakuwa mkali, si kwa sababu ingine yeyote lakini ni kule kuona vile watu wakimtumia vibaya huyu. Anamoyo kama wa baba yake. Mwema, anaye amini kila mtu ni mwema.” Mama huyo alikuwa na yeye mwalimu wa enzi hizooo.
“Aliponiambia umeharibu gari yako ya maana kwa jili yake, na vile unavyomchukulia, nilitaka nikija huku nikushukuru.” Jo akacheka kwa heshima akijaribu kutulia maana shemeji alishamtibua, ila sasa ni kama mama mkwe alionyesha ashamkubali.
“ASANTE sana.” “Karibu mama. Lakini kama nilivyosema, si kitu kikubwa sana. Hii gari inakuwepo tu. Na nipo peke yangu. Kutoa kiti cha katikati kwa ajili ya Dorothy si garama kabisa, kulinganisha kwa jinsi nilivyoona anavyopanda kwenye gari kila siku. Isingechukua muda mrefu kumuathiri upande wa juu. Kama mabega, ubavuni na mikono.”
“Unaposema upo peke yako unamaanisha nini?” Simon akadakia. “Tafadhali mkaribishe kwanza akae!” Baba yao akamwambia kaka mtu. “Karibu, karibu sana.” Mkewe ndio akamkaribisha huyo Jo. “Samahani. Mmeingia na mengi tumesahau kukukaribisha. Karibu sana. Mimi ndio mama mwenye nyumba, wifi yake mama Pam. Mke wa huyo kaka mtu hapo.” “Naona kweli kabla ya kujibu maswali tusalimiane kwanza.” Jo akampa mkono huyo wifi mtu na wengine wote wakasalimiana, ila kushindwa kukaa maana mwenye nyumba wake, Simon, alikuwa bado amesimama ameegemea ukuta wa hapo sebuleni na uso wa kutaka majibu ya kueleweka.
Akamgeukia yeye tena. “Kujibu swali. Nipo peke yangu nikimaanisha naishi pekeyangu. Vijana wangu wawili hawapo hapa nchini, na kama wakija ni mara moja moja sana tena ni kama hawajarudi huku kwa muda mrefu sana. Walipo nchini Marekani kwao, ndio nyumbani. Walizaliwa huko na mama yao alizikwa hukohuko. Upande wa mama yao, bibi na babu yao pamoja na ndugu wa marehemu mama yao wapo hukohuko tokea wanazaliwa. Mimi huku nyumbani niliondoka nikiwa kijana mdogo, wazazi walishafariki zamani sana, hata watoto wangu hawawajui wazazi wangu.”
“Dada yangu mkubwa ambaye ndiye alifanyika kama bibi yao, naye tulikuwa tukiishi nao hukohuko na ndugu wengine. Kwa kifupi tulihama hapa nchini miaka ya tokea 80, dada ndio tokea miaka ya 70. Ila mimi, dada na shemeji ndio tuliamua kuja kustaafia hapa chini, napo naona sababu ya uzee, hawa wawili wanahitaji uangalizi mzuri wa madaktari, itawalazimu warudi huko.” Dorothy akamtizama kwa mshituko, akijua na yeye ndio anaondoka.
Jo akaelewa. “Kabla sijakutana na Dorothy, ilikuwa rahisi sana. Ningesema ningerudi nao huko, lakini Dorothy anaanza kubadili ratiba ya maisha yangu. Nipo kama mtoto wa dada na shemeji. Walipo ndipo nilipo. Lakini sasahivi ameongezeka Dorothy, sio rahisi kusema kesho yangu mpaka nijipange naye tena kwa upya.” Ikawagusa hapo karibu wote na kuwashangaza, na kuanza kumtizama huyo Jo vizuri. Yaani hata Dorothy mwenyewe hakujua kama anauzito huo kwa huyo Jo. Ni juzi tu!
“Mkeo alikufa kwa ugonjwa gani? Na je, upo tayari kupima kabla hujaendelea na Dorothy? Maana ni LAZIMA kupima. Tena naona nilazima mimi mwenyewe nihudhurie. Yaani niwep…” “Kaka!?” Dorothy akashituka sana. “Kabisa na katika hili sitazembeamama Eric. LAZIMA. Kama hataki basi.” Wazazi kimya.
“Na mimi naona si wazo baya kabisa.” Jo akaongea akisikika kutulia wala hana pamiki. “Kwa hiyo upo tayari kupima UKIMWI.” “Baba, unamuona…” “Sasa kwani kuna tatizo gani?! Maana amesema mkewe alikufa. Wewe unajuaje kama si kwa haya maradhi! Kwanini hutaki kujifunza Dorothy?! Unataka na safari hii uachwe na maradhi mengine ya kudumu?”
“Uliachwa mlemavu. Na safari hii unataka uachwe tena na maradhi ambayo yatakufanya uishi kwa madawa tu mpaka kifo?! Kama kweli anakupenda kama alivyosema, haitakuwa tatizo kupima. Na katika hili ni LAZIMA, Dorothy. Kama hataki, mlango upo wazi. Ni bora aondoke akuache salama na maisha aliyokukuta nayo. Hata kama kwake ni duni, lakini ni bora hivyo kuliko akutengenezee magari halafu akuache nusu mfu. HAPANA.” Yaani mpaka hapo sebule ikarudi kuwa moto na kupitiliza. Kimya kaka mtu akiwaka.
“Na mimi naungana na hilo wazo. Kwa asilimia 100, naona upo sahihi kabisa. Jamani, kutenda kosa si kosa, ila kurudia kosa. Sitaki Dorothy awe anaachwa muhanga kila siku. Na ili kufanya kila mtu awe na imani na mimi, nashauri mchague hospitali mnayo amini, twende sasahivi.” “Samahani Jo.” Dorothy akawa amepoa kabisa.
“Huna haja yakuomba msamaha. Binafsi nimefurahi sana. Natamani nguvu hiihii ingetumika tokea upo binti mdogo, hujaolewa ndio ingetumika, pengine ungekuwa salama Dorothy. Imeniongezea heshima kwako na familia yako. Unapendwa na kujaliwa sana.” Hapo akaanza kuwatuliza, ila wasijue jinsi alivyotibuka nafsini kwake.
“Fikiria kama kweli mimi ningekuwa tapeli tu, na kweli nimeathirika! Kama kusingekuwa na mtu wa kukukumbusha kufanya hichi alichoshauri kaka yako, ni kweli ungeachwa na maradhi. Maana mapenzi yanauwezo mkubwa sana wa kukufanya mpofu. Kitu kama hiki na mimi sikukifikiria kabisa. Nimeanza na wewe kwa mapenzi mazito tu, na ningeendelea na wewe pengine mpaka ndoa, bila kufikiria kupima bila kujali au kujua aliyekuwa mume wako alikuachaje!” Hapo wakashituka. Na akawafanyia kusudi.
“Mimi ninauhakika wa afya yangu kwa sababu ya vipimo ninavyofanyiwa kila mwaka ninapokwenda kuangalia afya yangu kwa ujumla. Annual checkup. Lazimawanipime kila kitu bila kuzembea. Najijua afya yangu, lakini sijui wewe mara ya mwisho walikupima afya yako lini, na kwa umbali gani.” Pakapoa. Dorothy akaanza kukumbuka umalaya wa mumewe.
“Kwa hiyo hili alilolizungumza kaka yako ni kwa faida yetu sisi wote wawili.” “Mmmh! Baba Eric alivyokuwa malaya yule! Tena wakuleta wanawake mpaka ndani, mbele ya macho yangu! Sidhani kama nitakuwa mzima mimi?” Wote wakashituka.
“Kwamba alikuwa akiwaleta wanawake ndani?!” Kaka mtu akahamaki. “Mpaka kitandani akiniambia niwapishe, nyumba ni yake, nikalale na wanangu. Mimi sijui kitu. Majirani wote walikuwa wakijua kama anaingiza wanawake ndani wala haikuwa siri. Alikuwa anasema hawezi akagaramia nyumba za kulala wageni wakati nyumba anayo. Jiendee tu Jo, acha mimi niendelee na maisha yangu.” “Si kirahisi hivi, Dorothy. Huwa sikubali kushindwa kijinga hivyo.” Sebule nzima sasa kimya, kitu alichokuwa akitaka Jo. Alitumia saikolojia tu, akawa ameshawasoma, ndipo akawatuliza, zaidi kaka mtu.
“Tunakwenda kupima mimi na wewe, sasahivi na kaka yako akitusindikiza.” “Sasa kutakuwa na faida gani nikikutwa nimeathirika?” “Unaanza kutumia dawa, na tutafundishwa jinsi ya kuishi na huo ugonjwa na nakuhakikishia utakuwa sawa Dorothy.” Wote wakashangazwa.
“Unajuaje? Jiachie tu Jo. Wewe kaendelee na maisha yako.” “Dorothy, ulizaliwa ukiwa unatembea na miguu yako yote miwili. Ikapoteza nguvu. Je, wakati upo pale hospitalini unaambiwa hutatembea tena, ukiwa na ndoa ya ajabu vile, ulijua utaishije?” Wakamuona anaanza kulia.
“Mbona leo upo hapa, mzuri wa kuvutia na wakupendeza! Acha hofu. Nakuahidi utakuwa sawa, twende.” Shamrashamra ikageuka kuwa hofu sasa. “Kwanza upo salamamama Eric, usiogope.” “Wewe unajuaje?” Jo akamuuliza shemejiye.
“Alishaachana na baba Eric miaka mingi sana. Kama angekuwa ameathirika si angeshakufa?” “Hilo ni sahihi kabisa, lakini kama aliathirika kwa wakati ule, akala vizuri bila kujamiiana kwa muda wote huo na asiugue au akaugua na kupewa matibabu sahihi kwa haraka, anaweza akaishi vizuri tu. Dorothy alikuwa kijijini akila vitu halisi ambavyo vinaweza kumuongezea kinga mwilini, akaishi na vijidudu bila kuugua.” Huwezi shindanana dokta akikuamulia kwenye fani yake.
“Na pili, kujamiiana si njia pekee ya kuathirika. Mimi ni daktari niliyetibu watu kwenye nchi za ulimwengu wa kwanza. Matajiri sana wenye kila nyenzo na madawa. Na pia baada ya kufiwa na mke wangu niliathirika kwa msongo wa mawazo nikakimbia nchi nikaenda kutibu watu wenye shida, nchi masikini na zenye vita pia.”
“Kujibu swali la mke wangu alikufa kwa ajili ya nini kabla sijaendelea, aliuwawa kwenye ajali ya gari. Alikuwa akirudi nyumbani, kijana mmoja akiwa amelewa akasababisha ajali. Mke wangu alikuwa daktari kama mimi hukohuko nchini Marekani. Na hatukuwa tumeathirika.”
“Ila najua mtu anaweza kuathirika mbali na kujaamiiana. Huduma mbovu mtu anayoweza kupewa hospitalini kwa sindano, akiwa anafanyiwa upasuliwaji, pia anaweza kuambukizwa vijidudu vya UKIMWI, na asiugue mpaka kinga ya mwili itakaposhuka. Kama nilivyotangulia kusema, kazi yangu imenionyesha mengi, sana. Imenikutanisha na mengi. Sio wote walioambukizwa vijidudu vya UKIMWI, walikuwa ni waasherati na wanzinzi.”
~~~~~~~~~~~~~~
Kilizuka kimya kikubwa hapo! Kwamba Jo alikuwa daktari Marekani! Amezunguka ulimwengu! Dorothy ndiye anaweza kuwa muathirika na si yeye! Kimya kuwapa muda kuingiza taarifa kichwani. Na aliwafanyia kusudi kama anayewaambia mkome kudandia treni kwa mbele!
Hakuna Anayetoa Kumzidi Mungu
Mwisho wa ubaya wakati wote huwa ni aibu. Huwezi shindana na Mungu anapoamua kuaibisha wenye hekima. Huinua wonyonge kutoka mavumbini. Na huwezi kushindana na aliyenyanyuliwa na Mungu. Ndio Raza. Kufumba na kufumbua Raza aliyekuwa mkosaji, akawa kiungo muhimu sana cha kuunganisha kile akili za wanadamu hawakujua watafanyaje! Kwa kutubu na kutii, Mungu akaweka uthamani mubwa sana kwake.
Mama Ruhinda akamuona vile mume wake alivyobadilika baada ya Mina na Andy kuondoka akajua wazi maji yameshazidi unga. Akabaki akijifikiria, akajua ndio ametolewa kwenye picha. Akajiambia endapo wakifanikiwa kukutana katika hilo kubwa la kiasi hicho, kwa Raza, hawatakaa wakarudi kwake.
Haraka sana akaomba simu ya mumewe akampigia Raza mwenyewe. Naye akapokea kwa haraka akijua ni mzee Ruhinda. “Baba?” “Ni mimi Raza, mwanangu. Najua upo na haraka za kuwahi kanisani, lakini na sisi tunaomba tukaribie kumkaribisha huyo mume wangu hapo nyumbani.” Kwa sekunde kadhaa Raza akapatwa na kigugumizi, haamini kama yanamtokea.
“Najua kuna mambo yalitokea, tukapoteza utaratibu mzuri tuliokuwa nao. Lakini naamini wewe ukiamua, unaweza kuturudisha, tukaweza kuwa pamoja tena.” “Karibuni, lakini mjue ninapika au nitapika mimi mwenyewe.” “Hamna shida. Ulitaka tulete nini?”Mara Pius akapokonya simu.
“Hili jambo ni la kheri mama, sitaki mje, muanze kumtibua Raza.” “Na sisi tutakuja kwa amani, kabisa.” “Unaposema sisi, unamaanisha na nani!?” Akahoji kwa ukali kabisa. “Mimi, baba yako, Paul...” “Paul najua.” “Kwamba yeye alishaalikwa!?” Akashangaa sana na kumgeukia Paul.
“Kwamba wewe mwenzetu unamualiko, unatusanifu tu hapa!” Mama Ruhinda akamjia juu kiziwanda wake. “Mimi sina shida na Raza. Na nishatoka naye tukala pamoja zaidi ya mara moja na mara ingine tulikuwa na mumewe. Nyinyi ndio mnashida naye.” “Naomba nikuage mama. Lakini Paulina na familia yake naomba wasubiri kwanza.” Pius akaweka msimamo wake wazi bila kumumunya maneno.
“Ulishasema ni jambo la kheri, sasa kwa nini usilifanye la kuleta amani na kuturudisha pamoja? Makosa yalishatokea Pius, mwanangu. Hili jambo wewe hutaki liishe?”
“Sitaki maneno maneno na kuzidi kumtibua Raza. Umemuona jinsi alivyomuongelesha mke wangu muda mfupi hapo, akimtupia yeye lawama kana kwamba mimi sina akili zangu, naburuzwa tu!” “Hayatatokea baba. Mimi nakuahidi.” Pius akafikiria, moyo ukasita.
“Hapana mama. Kama wewe na baba mnataka kuja na hamna tatizo na Raza, sawa. Lakini familia ya Paulina isubiri kwanza, mpaka atakapobadilika. Kwa heri.” Paul akaanza kucheka.
~~~~~~~~~~~~~~
“Acha kucheka Paul.” Baba yake akamkemea. “Mdomo huo wa mwanao umeanza kuvuna matunda yake. Watu wamekuwa wakali na wake zao! Hawataki uchonganishi kwenye familia zao. Sasa wewe mtakatifu nenda kapike ule na wanao peke yenu, ndio utamjua mchawi ni nani.” “Mambo ya uchawi yalishaisha.” Paulina akajibu kwa utulivu.
“Yaliishaje na yaliisha lini!?” Paul akamuuliza kwa kumsuta. Kimya. “Asubuhi hii unamvaa kwa kumdhalilisha mbele ya watu! Hukujua kama Mina na Andy wapo upande wa Raza, mkadhani mtakusanya nguvu muwe kinyume chake. Sasa nikwambie kabisa Paulina, mumewe sasahivi yupo makini sana na mkewe, na kama unavyomjua Pius, hatakagi ujinga. Akisimamia jambo lake, hakuna wakumyumbisha. Umemuona hata mama amemkatalia.” “Nitamuomba msamaha huyo Raza.” Mpaka wakashangaa.
“Sasa unashangaa nini?” “Na iwe kweli Paulina ili ulete amani kwenye hii familia. Ushatusumbua sana kwa maneno maneno. Ukisikia Raza amebadilika, mimi nimekaa naye kwa chakula, jamani Raza yule mpenda maneno ya kuhamishahamisha na ushari si huyu. Tumeshakuwa wawili tu zaidi ya mara mbili. Mwanzo mpaka mwisho, Raza hakuongea la mtu. Hata kusemelea kama mnamtenga, hakusema. Tukala, akazungumza ya mwanae, na mpaka hili la leo alinisimulia. Nikampongeza kwa kubadilika yeye na kumjenga mwanae. Sema mimi nilimwambia sina uhakika wa kuhudhuria maana nitakuwa on call. Sikusema sababu amehama dhehebu.” “Kwamba na wewe ulijua kama Pius amehama?!”
“Kabisa mama. Na kwa jinsi ninavyomjua Pius na yule binti yake mwenye akili kama za baba yake, nilijua ni jambo zito linaloendelea, na Pius AMEKUSUDIA. Sikuonyesha kwamba ni jambo la ajabu, ila tu nilimwambia naweza nisiende kanisani ila nyumbani niliwaambia ni lazima niende. Sasa nilipopata simu kama hujisikii vizuri, nishamuomba mtu anisaidie zamu yangu, na mimi leo si mkatoliki, nafuata nyuki. Sitaki makundi mimi.” “Kwamba unaenda mpaka kanisani?!” Mama yake alishituka sana.
“Mama Ruhinda, kama bado hujaelewa, hii treni ishaondoka. Ni hivyo Andy hakusema tu hapa. Na yeye anakwenda hukohuko.” “Andy!?” Wote wakahamaki. Maana Andy ni kama Padri asiyevaa joho kwa vile ukatoliki ulivyo kwenye damu.
Paul naye akawashangaa kama ambaye hawaelewi! “Nyinyi mlitegemea nini?! Raza kampokea mtoto wa Mina. Mina na Raza wameungana. Anayepokelewa leo ni Ayvin, LAKINI kwa nilivyosikia kutoka kwa Pius wanawafanyia surprise Mina na wanae, ila walishamuomba ruhusa Andy. Wamewaandalia wale watoto wakiume chumba chao.” “Hapo kwa Pius?” “Na Raza mama. Naomba badilika. Ni kwa Pius na Raza.” Paul akaweka msisitizo.
“Anasema Pius, mkewe alitafuta mtu wakukipaka rangi na kukichora kabisa hicho chumba. Wamekifanya kizuri kama chumba walichokiona wakikitumia kule kwao Dodoma. Pius anasema mkewe amekitengeneza vizuri na kwa hali ya juu sana, na yeye pamoja na wanae wamesaidia kukimalizia kukiandaa. Yaani leo ndio wale watoto na mama yao wanaenda kukabidhiwa rasmi hicho chumba pale kwao.”
“Turudi kwa Andy, mkumbuke Mina sio mkatoliki, madhehebu yanafanana kama huko anakokwenda Raza sasahivi. Mina kaungana na Raza, leo ni siku ya kina Raza kuwa na yule mtoto, inamaana ni lazima Mina naye aende huko aliko mwanae. Na jicho la Andy sasahivi lipo kwa Mina masaa yote. Aliapa kutorudia kosa. Hata kama wamepatana na Pius, lakini abiria chunga mzigo wako. Inamaana alipo Mina ndipo atakapokuwa Andy, labda Mina abakie nyumbani. Sijui kama mnanifuata mpaka hapo?!”
“Kwa maana nyingine ni hivi, bila kujali alipo, au mlango atakao ingia siku ya jumapili, alipo Mina ndipo Andy atakapokuwepo. Inamaana hizi familia mbili zitabaki kuwa pamoja wakati wote.” “Naona baba wewe umeelewa zaidi.” Akamgeukia dada yake.
“Umebaki peke yako Paulina. BADILIKA. Kwa hivyo ulivyo, hakuna atakayekukubali tena. Watu washakujua. Na safari hii washajua umefanikiwa kumuingiza mumeo kwenye hila zako, wote nyinyi mnakimbiwa.” Alipoa Paulina, alipoa kama si yeye.
“Na umeona jinsi waume zao walivyobadilika na kuwa wakali zaidi.” “Kumbe baba umewasoma!” “Sana. Pius na Andy si wakuhama katoliki. Nawajua kwa kuwalea mwenyewe. Mmewasukumia huko. Na hata Raza, asingehama kama angesaidiwa tokea alipokosea. Sisi wote tulijisahau tukabweteka.” Mzee Ruhinda akaendelea.
“Kama mama yenu akiendelea vizuri lazima nitakwenda kuungana nao. Fahariyangu sasahivi ni hawa wajukuu. Sina kitu kingine isipokuwa wao. Nyinyi nishamalizana na nyinyi. Siwezi pitwa na ya wajukuu zangu.” Mzee Ruhinda akaweka msimamo wake wazi.
“Tuombee baba.” Wote wakamgeukia Paulina. “Ili ukavuruge huko, baba alaumiwe?” “Si nimesema nabadilika? Wewe vipi Paul! Upo kama unafurahia kutengwakwangu!” “Tunataka AMANI Paulina. Umesikia?” Mzee Ruhinda akawa mkali kabisa. “Hizi vurugu zisizoisha, kila mtu amechoka nazo. Tushajidhalilisha sana. Inatosha.” “Nitabadilika baba.” Akamtizama binti yake kwa sekunde kadhaa. “Nakuahidi baba. Safari hii nanyamaza.” Akachukua simu.
~~~~~~~~~~~~~~
Akatoka, akampigia Pius. “Mama, sisi..” “Ni mimi.” Wakamsikia mzee Ruhinda akizungumza. “Hii familia imeshatengana kwa muda mrefu na machafuko haya hayataisha isipokuwa WEWE kuweka juhudi za makusudi kurudisha hii familia pamoja.” “Baba, Paulina ana…” Akawa kama amekumbushwa kitu. Akanyamaza na kuacha kujilalamisha kama toto.
“Umeelewa Pius?” “Ndiyo baba.” Akasikika kama aliyerudiwa akili zake. “Wewendio unalo hilo jukumu. Kwanza kama kaka yao, pili ukijua umuhimu wa familia kuwa pamoja. Umenielewa?” “Sawa baba.” Akajishusha kabisa. “Basi tutakuja hapo nyumbani kwa chakula cha mchana. Na sisi utuhesabu. Kama kutahitajika msaada wowote, mwambie Raza amjulishe mama yake, bado ni mapema, tutajiandaa vizuri, kina Polla waje wacheze na wenzie.” Akajua ndio anaambiwa na familia ya Pualina itakuwepo. Akakubali na kukata simu.
~~~~~~~~~~~~~~
Raza alifurahia kuona japokuwa asubuhi hiyo ilianza na makwazo, akamuomba Mungu akimsihi alichoandaa kisivurugike. Japokuwa alikuwa pale hospitalini, lakini moyoni alikuwa akimsihi Mungu asimamie mipango yake kwa siku hiyo. Raza huyu alikuwa muombaji hata kama hajafunga macho. Alijua kuzungumza na Mungu wake bila hata kupiga magoti, akiwa anafanya kazi, basi akipata jambo au akitaka kuzungumza na Mungu wake, basi hataacha anachokifanya, ataendelea kuzungumza na Mungu.
Akiwa hospitalini aliendelea kumsihi Mungu tu. Hata walipofika nyumbani akiwa anaandaa familia yake kwa hiyo ibada ambayo Polla alikuwa akisimama mbele ya kanisa yeye na watoto wengine wa Sunday school, aliendelea kumsihi Mungu asimamie siku hiyo. Huwezi shindana na mwanamke muombaji, asiye hila, anayelilia amani na umoja. Hapo ndipo Mungu anapoamuru baraka.
~~~~~~~~~~~~~~
Ilipofika majira ya saa nne na robo walikuwa wameshawasili kanisani wakabaki nje wakiwasubiria wageni wao. Bila ya kuchelewa Mina naye na familia yake wakawa wamewasili. Wakashangaa na Paul naye anampigia simu Pius. “Aisee hapa ndio inakuaje?”Pius akamuelekeza walipokuwa wamesimama. Akaegesha gari na kuwafikia.
“Naona mzee naye na mama wanakuja.” Raza alishituka kama Pius na Andy, wakaangaliana. “Nafikiri wanataka kushuhudia tukio la Polla tu.” Akaona aweke wazi kuwa sio kwamba wanahama dhehebu.
“Basi acha mimi niingie kuwahi viti, sehemu tutakayokaa wote kwa pamoja.” Mina akaongozana naye. Wakina Ruhinda huwa hawajui kuchelewa mahali. Ibada inaanza, wote wakawa wameshafika mpaka kwenye viti walivyowahiwa na kina Raza.
Polla alifanya vizuri. Akaongea mistari yake ya bibilia kiufasaha, akichukuliwa video na picha nyingi tu kama kumbukumbu. Ikawa nzuri yakuvutia mpaka sasa watoto wa Paulina wakatamani. Gafla na Polla yule aliyekuwa akiogopewa kwa kutembea na nguvu za giza, akaonekana mwenye heri haswa. Alionekana ametengeneza marafiki wa kweli hapo kanisani, na kweli wanafundishwa Mungu aliye hai. Kwamba ni kweli anahudhuria kanisani, si bora liende. Wakampa maua waliyokuwa wamemletea, na zawadi, wakarudi nyumbani kwa Raza.
Kama kawaida wote wakaingia jikoni kupika. Kile kilichokuwa kikifanyika nyumbani kwa mama Ruhinda, ndio wakakifanya hapo kwa Raza. Wakapika na kukaa mezani kama familia, kukiwa kumejawa utulivu ila kujiwinda kwa maneno wakijua Pius na Andy wameungana, na hawataki tena fujo. Paulina alitulia kama aliyekuwa na vidonda vya mdomo. Hakuongea hata kwa kuropoka. Kimya kama mumewe wakiangalia mambo yanavyokwenda.
Mazungumzo yakawa ya kawaida. Baada ya kula ndipo wakamkaribisha ramsi Ayan na Ayvin hapo nyumbani, wakaonyeshwa na chumba chao. Kwamba wakati mwingine, wakienda hapo, isiwe kushinda tu, mpaka kulala wakiwa na msichana wao wa kazi. Ukweli Raza alijitoa kwa mumewe, akijitahidi kwa kadiri ya uwezo wake.
“Asante Raza. Nakushukuru.” Mina hakuwa akiamini. “Huyo mtoto tulimtafuta Mina! Aisee tulimtafuta sana. Ila naona Mungu aliamua kumpitishia kwako.” Hilo nalo likawa fumbo kwa hata Mina mwenyewe.
“Siku zetu za kuwa naye, naomba awe anakuja na kaka yake, walale kabisa hapa. Tuwe tunapata muda naye.” Wakaendelea kuzungumza wao wawili peke yao, wakati waume zao wakiendelea kunywa sebuleni na familia yao. Wao walibakia hapo chumbani tayari Ayvin akichezea toys zake hapo chumbani.
“Huyu mgeni mtamchoka. Hata siku haijaisha, ona chumba kimekuwa kama kimepigwa bomu!” Raza akacheka tu, lakini kwa asili alikuwa msafi sana. Nyumba yake ilikuwa safi, kila mahali, kila wakati kumepangiliwa. Yaani hata yeye mwenyewe ukimkuta nyumbani kwake ni msafi haswa.
~~~~~~~~~~~~~~
Raza amejitoa kwa mumewe, akimkarimu mtoto aliyezua gumza kwenye jamii, akifanya makubwa na magumu, mpaka kugeuza mioyo ya watu na kumuangalia YEYE kama kiungo maalumu kwenye familia. Kutoka kwenye dhambi yake iliyokuwa ikinuka, fedheha mbaya mpaka hatari ya kufungwa jela, leo matendo yake yamemfanya kuwa mwenye heri, wakukimbiliwa, kutetewa na Kulindwa. Sasahivi vita yake inapiganwa na wengine, yeye anachukua ushindi.
Upo usemi unasema, ‘Keep Your Friends Close and Your Enemies Closer’
Je ndicho ameamua kufanya Raza kwa Mina ili KUSIRUDIWE KOSA?
Akili kumkichwa.
Andy amejifunza kutokana na makosa. Amejua palipo amani, ndipo muovu/shetanianapenyeza uharibifu kwa kuwa watu hubweteka.
Abiria, Chunga Mzigo Wako. Alipo Mina, ndipo atakusanyika Andy bila kuzembea.
Kwa sababu upumbavu wa Mungu una HEKIMA zaidi ya wanadamu, na udhaifu wa Mungu, una nguvu zaidi ya wanadamu. (1Kor1:25)
Dorothy&Joel? Pam&Mill?
Inaendelea…
0 Comments:
Post a Comment