“Ni nini?” “Naomba iwe hapa wanakoishi na mama yake, tafadhali mama yangu. Na najua utapafurahia. Kwanza pako salama. Hewa nzuri. Na nilikuwa nikishauri muhamie hapa kwa sababu wao watahamia nyumba kubwa.” “Unauhakika?” “Kabisa mama. Sasa si patakaa tu bure bila kazi wakati nyinyi mnakaa huko, kwanza tunalipia, halafu padogo. Kesho mnaweza kuja kulala hapa na Shema. Tukirudi kutoka mapumzikoni Pam akishatoa vitu vyao, ndio muhamie rasmi.” Hilo likakaa sawa. Na palivyo pazuri, mama wa watu akaona ni baraka juu ya baraka.
“Na mimi nina ombi baba Shema.” “Karibu.” “Mbali na familia ya kaka, nina mgeni wangu, naruhusiwa kumkaribisha kesho kwenye harusi ya Pam?” “Kabisa mama. Haina shida.” “Kuna nyongeza.” Akamuwahi kabla hajakata.
“Bado nipo.” “Anauliza kama unahitaji msaada wowote kwenye harusi.” Hapo akamfanya aongeze umakini maana aliitika tu hata hakujali huyo mgeni ni nani na wajinsia gani. “Unamaanisha nini?” “Yeye amesema kwa chochote utakachohitaji na ameomba nikuombe nimtambulishe kwako.” Baba Shema akashangaa sana maana yeye alimchukulia poa. Ni mama mlemavu, tena anatokea milimani! Akabaki kimya.
“Huyu mtu ni muhimu sana kwangu, baba Shema. Kwa muda mfupi amenifahamu ameonyesha kujali hata upandaji wangu gari! Amebadili gari yake kabisa ambayo inafanana kama hiyo yako inayonisaidia usafiri, ili iwe rahisi kwangu kupanda na kushuka bila yakujidhuru, na bado anajitolea kuniendesha yeye mwenyewe.” Hapo akamsogeza karibu zaidi.
“Jana nilikwama usafiri kwenda madukani kumtafutia mama nguo za harusi, akajitolea kunizungusha ilimradi tu kufanikisha harusi ya binti yangu, na pia mimi mwenyewe nisipate shida.” “Sawa. Unaweza tu kumpa namba yangu, lakini kwenye swala la kusaidia siku ya harusi ni kama kila kitu kipo sawa.”
“Nitampa, na naomba upokee simu yake.” Akaweka msisitizo. “Inaonekana huyu mtu ni muhimu sana kwako, eeh!?” “Natamani na wewe uumpe nafasi yakumfahamu kama Pam.” Hapo akashangaa. “Kwamba Pam yeye alishakutana naye?” “Ndiyo.” Hakuwahi msikia huyo mama aking’ang’ania jambo. Akaweza msikia Pam kwenye huo msisitizo wake. Akajua ndiko alikorithi uking’ang’anizi.
“Basi nitatenga muda maalumu kwa ajili yake.” Hapo akamsikia amefurahi. “Basi nampa namba yako sasahivi, japo anakuja kunipeleka kuwaona baba na mama.” “Kwamba ndio mpo karibu kwa kiasi hicho!” “Ananijali sana, na amenipokea vile nilivyo.”Akamuelewa.
“Basi naona kuna umuhimu na mimi nimfahamu. Nisaidie namba yake, na wewe mpe ya kwangu. Lakini swala la kuwa na Shema mpaka tutakaporudi hilo si halina tatizo? Maana sitaki akose shule au ratiba yake ibadilike sisi tutakapoondoka.” “Hilo halina shida kabisa.” “Asante.” Wakaagana, Dorothy akiwa ameridhika kuwa ameeleweka uzito wa Joel. Akamtumia kila mmoja namba ya mwenzie. Kisha akaenda kujisafi sasa akijua Jo anakwenda kumchukua na maandalizi ya shule aliyoahidiwa kupewa.
Mill&Joel
Mill alipopata tu namba akawa muungwa. Akamtumia ujumbe. ‘Naitwa Mill, baba yake Shema, mume wa Pam. Nimepata namba yako kutoka kwa mama mkwe wangu. Nashukuru kwa utayari wa kutaka kusaidia.’ ‘Tunaweza kuzungumza?’ Akamrudishia majibu, Mill akapiga.
Baada ya salamu Joel akaenda moja kwa moja. “Asante kwa kunipigia, nilipanga nikutafute ili tufahamiane kwa karibu. Lakini najua sasahivi upo kwenye maandalizi ya harusi. Hongera sana.” “Nashukuru japo itakuwa ni harusi ndogo tu. Ila natamani kiwe kitu kizuri, nimfurahishe Pam.” “Kuna msaada wowote ungehitaji?” “Kwa sasa naona kila kitu kimekaa vizuri. Labda kama kikijitokeza kitu kingine.” Akamsimulia mpango wa mwanzoni juu ya hiyo harusi mpaka hapo walipofikia.
“Na mtoto huyu anayekuja ameshabadili ratiba yote. Inabidi kwa sasa kila kitu nikipeleke harakaharaka, ili kumtoa Pam hapa nchini kabla ujauzito haujawa mkubwa. Akashindwa kusafiri.” “Hongera sana. Unampango wa kwenda kuishi wapi?” Hapo napo katika mazungumzo ndipo Mill akagundua anazungumza na mtu mzito kuliko hata Dorothy na Pam walivyodhania.
~~~~~~~~~~~~~~~
Mtanzania, daktari nchini Marekani! Mill ambaye yupo kwenye hiyo fani yao ya uuguzi, akaongeza adabu na kutamani sasa kumuona huyo Jo mwenyewe. Akajua yupo na nafasi nzuri sana kwenye maisha na anapoulizia msaada, hazungumzii msaada wa kuongeza chupa za soda harusini.
Wakaendelea na kufahamiana huku akikanyaga mafuta kumfuata huyo Dorothy mwenyewe lakini Mill akishangazwa na wawili hao. “Huyu mama amewezaje kumpata mtu kama Jo!?” Akajiuliza akiendelea kuzungumza na Jo.
Ila ni kama hakushangaa sana. Pam alichukua uzuri wa mama yake. Ngumu kumficha hata nyuma ya dirisha. Wakajikuta wakizungumza lugha moja sasa ya hukowalikotoka. Vicheko. Mazungumzo yakawa mepesi hata kuteta mambo fulanifulani.
~~~~~~~~~~~~~~~
“Shema na bibi yake nitawarudisha mimi nyumbani hiyo siku ya jumatatu. Mwache tu dereva ashugulike na wazazi. Au ndugu wa upande wa kina Pam. Hawa wawili niachie mimi. Pengine kuwe na ratiba ya tofauti.” “Ni hapo tu. Kutoka ukumbini kurudi nyumbani. Maana madereva wote wawili watakuwa busy kusaidia usafiri kule kwa mjomba. Ukinisaidia hao, najua hata Pam atakwenda mapumzikoni akiwa ametulia.” “Hilo limekaa sawa, hamna shida kabisa. Ila nisaidie kunielekeza kwa mjomba wake Pam ili nimpeleke Dorothy kuona wazazi.” Mill akagundua jinsi anavyomtambua mama mkwe wake. Akamuheshimu zaidi.
“Nashukuru sana. Dereva ndiye huyo ameenda kuwachukua bibi na babu. Na dereva wa kazini anafanya kazi jumatatu mpaka ijumaa. Kwa hiyo nakushukuru.” “Usijali. Unaweza usiamini, lakini najihisi kwa namna ya tofauti sana, ni kama ni wajibu wangu pia.” “Kweli!?” Mill hakuwa akiamini.
“Kabisa. Tutakuja kuzungumza ukitoka kwenye mapumziko yako na Pam. Lakini juu ya Dorothy, usiwe na wasiwasi kabisa. Nipo naye si kwa kulazimishwa, ila ni kama wajibu wangu ambao niliwaachia watu wengine. Wengine walifanya vibaya mpaka kumuumiza na kumuacha akiwa ameathirika kiakili na mwili wake. Halafu wengine wamejitahidi kwa kadiri ya uwezo wao, ila mimi najihisi ndio nawajibika kukamilisha kuwajibika kwa Dorothy si mtu mwingine.” Kwa hakika alimshangaza Mill ila kumfurahisha kwa namna ya kipekee sana. Wakapanga kukutana weend inayofuata. Akamuelekeza kwa mjomba wake Pam. Wakaagana.
Jo&Dorothy.
Alifika akakuta anasubiriwa kwa tabasabu zito. “Jana umenichanganya, mpaka nimeondoka na vitu vyako na mama.” Akamfanya acheke kwa aibu. “Nilikumbuka wakati nataka kulala, nikaona nikuache. Nachukua vyangu sasahivi, vya mama tutampelekea.” “Umeshajua wamefikia wapi?” “Wameshafika.” Akamuona kama amepoa gafla.
“Ni nini?” “Nilitaka tupate muda wetu kabla ya kwenda huko?” “Sasahivi?” “Na baadaye. Nataka muda na wewe Dorothy. Kwanza umeshapata kifungua kinywa kizuri?” “Nilikula. Na wewe?” “Mimi nipo sawa. Ndio maana nilitaka twende tukaegeshe gari sehemu, tukae hapo kwa muda wetu. Na baadaye kabla ya kurudi kulala, pia tupate muda wetu.” Ongea yenyewe ikawa ya kubembeleza mpaka akamtia hamu huyo Dorothy ya huo muda wa peke yao.
“Wapi? Na mimi ningependa. Mwenzio sijawahi ishi hayo maisha Jo. Natamani.” “Basi twende, nina sehemu nzuri tunayoweza pata muda wetu mtulivu.” Akamuita binti yake, ili kumkabidhi mizigo waliyonunua jana yake, Jo akamuwahi. “Na huu mfuko pia ni wako. Nimekununulia vitu vizuri.” “Ni nini tena?” “Chungulia uone.” Dorothy akafurahi huyo!
Akafungua na kukutana na nguo nzuri sana za kulalia. “Niliziona jana pale dukani, zikanivutia, nikahofia bei. Nzuri sana.” “Ndio maana nilirudi kwenda kuzichukua.” “Kumbe ulikuwa ukiniangalia!” “Muda wote. Na nilijua ulipenda.” “Asante kunijali. Nakushukuru.” Akacheka na kumbusu shavuni. Akafurahi huyo akabaki akichekacheka huku akiendelea kuangalia zile nguo. Kitambaa cha silk kizuri sana kilionekana garama. “Mpe binti yako tuwahi. Utakuja kuangalia vizuri ukirudi.” Msichana akachukua, wao wakaondoka.
Maandalizi Ya Kunywa Tamu Ya Mpenzi
Kwa muda mfupi tu kuwa na Dorothy, vile anavyomjali, na kuonyesha kumuonea wivu akiwa vilevile mlemavu, Dorothy akaanza kuachia moyo kujifunza kusikiliza midundo yake ya ndani, kuacha hofu ipumzike, na kujiandaa kupokea mwanga wa upendo. Kama maua yanavyojifungua asubuhi, ndivyo roho ya Dorothy ilivyoanza hujifunua taratibu, ikijivika subira, matumaini, na shauku. Hapo alipokuwa amekaa garini, alikuwa na furaha, hajui hata atarajie nini mbeleni, siku hiyo, ila vile alivyo Jo, alijua siku yake itaisha vizuri.
“Onja hizi pipi mbili. Utakayoipenda uniambie ili na mimi nile na wewe ndiyo hiyohiyo uile.” Akampa walipokuwa njiani. Dorothy akapokea akicheka na kuanza kuanza kula, Jo akisubiria.
“Hii ya kwanza ni pipi kama ya kifua. Kali kidogo.” “Na ya pili?” “Sijui ladha yake sijawahi kuila ila nimependa, imetulia mdomoni.” “Hiyo uliyopenda ni ladha ya strawberry. Basi acha na mimi nile aina hiyohiyo, ili uje uipate hiyo ladha midomoni kwangu.” Mama wa watu akawa hajaelewa.
Jo akajua na kuanza kucheka. “Mimi sijaelewa bwana!” “Nilikwambia nakuja kukupa SHULE. Hayo ndio maandalizi ya mwanzoni. Hiyo ambayo hujapenda, weka pembeni, halafu hiyo uliyopenda endelea kuila kisha nitakwambia kwa vitendo.” Basi akaanza zoezi la kumumunya pipi huku Jo akiendesha.
Akaendesha mpaka ufukweni sehemu tulivu ya peke yao akahamia kiti cha nyuma, bado gari ikiendelea kuwaka. Madirisha yote yamefungwa na milango. Na vioo vyote kasoro cha mbele vilikuwa na tint nzuri sana na kufanya ile gari ya rangi ya Silva izidi kuwaka vizuri.
~~~~~~~~~~~~~~~
Akakaa pembeni yake na kumfungua mkanda akicheka. “Jambo la kwanza. Hakuna mtu anapenda kula kitu kinachonuka au chenye ladha mbaya. Si ndivyo ilivyo?” Dorothy akaafiki. “Hivyohivyo kwenye romance, mtu anapotaka midomo yako, hategemei kukutana na harufu mbaya ya mdomo au kwa mwanaume uwe unanuka mdomo au ndevu. Moja kwa moja unapunguza ile ladha ya kissing.” Akamtia wasiwasi. “Nilipiga mswaki baada ya kula pia.” Jo akacheka.
“Huko ndio kunaitwa kuwa in tensional. Unakusudia kuwa bora kwenye mapenzi bila kuweka uvivu wala mazoe. Kwa hiyo, sio kila siku tutakuwa tukila pipi kwa ajili ya kissing, ila mimi huwa natembea na spray za kupuliza mdomo wangu mara kwa mara. Inasaidia pia kuweka ladha nzuri mdomoni, ila hiyo ni baada ya usafi kama uliosema wewe. Mswaki.”
“Sasa usije sema mimi nafanya hivyo na watu wengi, hapana. Nafanya hivyo kama mazoea tokea nipo daktari. Ili nisikere wagonjwa wangu kwa harufu mbaya ya mdomo. Na kipindi kile nilipokuwa na Betty. Nilihakikisha kinywa changu kipo fresh wakati wote ili nisimkere ninapoomba kiss.” “Kwani baada ya Betty hukujaribu kutafuta mtu mwingine?” Akaona aulize tu kujua wapo wangapi.
“Nilipoamua kustaafu, nilipanga kuja huku na kina dada kama nilivyokwambia. Sasa huko nilikokuwa nikifanya kazi, nilipata muuguzi mmoja, alikuwa miongoni mwetu au miongoni mwa manesi waliokuwa wakiongozana na sisi. Mzaliwa wa hukohuko. Yeye alikuwa mweupe. Yakaanza mahusiano ya karibu, lakini hatukufika mbali sana. Tulikuja gundua tupo tofauti sana, na hakuwa tayari kustaafu kwa wakati huo. Alitaka kuendelea kufanya kazi. Tukasitisha.”
“Lakini moyoni nilijiambia pengine utofauti ule pia ni kwa sababu niliishi na Betty, aliyezaliwa na wazazi wa huku nyumbani, kwamba alibeba maadili ya huku nyumbani. Nilipofika huku nikajaribu tena.” Akamuona anacheka.
“Ni nini?” “Hakuwa mtu mzima kama mimi, na hakuwa binti mdogo. Ila alikuja na mambo mengi! Hakika nilishindwa. Nilijiambia sitapumzika. Maana ni kama niliacha kazi ya kuhudumia watu wengi, nikawa nimehamia kwake.” “Alifanyaje?” “Mmmh!” Akamuona kama anayefikiria.
“Sijui niweke vipi! Kwanza msumbufu.” Dorothy akaanza kucheka. “Sikutanii. Ni msumbufu ambaye inakuwa ngumu kujua umpe nini ili aridhike. Kwa mfano kama vile jana wewe ulikuwa ukiogopa bei na kung’ang’ania ujilipie, yeye pale ingekuwa tofauti. Kwanza angeomba pesa za manunuzi. Halafu akiwa huko dukani atapiga tena akikwambia hazijatosha. Halafu akitoka hapo, ataomba tena. Halafu ataomba na tena. Kisha ataomba tena. Usifikiri kesho yake itakuwa hana uhitaji! Atakuwa nao ila kwa lugha ingine.”
“Nikajikuta mahusiano yetu, wakati wote tunazungumzia uhitaji wake yeye, hajali wala hajui kinachoendelea kwangu. Wewe siku ya kwanza tunazungumza kwa ujumbe, unakumbuka uliniuliza kama nilikula?” Dorothy akatulia akivuta kumbukumbu, na alimuuliza asijue kama hata ilileta maana kwake.
“Sasa kama ingekuwa ni yeye, vile nilivyomuuliza kama amekula, asingejali upande wangu, hapohapo angepata nafasi ya kuomba pesa akale na shoga zake, au akitaka nimfuate sehemu nikamlipie akiwa na mashoga zake. Halafu mkiwa wawili, hana haiba ya kusikiliza ila kuzungumza. Nikawa najisikia kichwa kinazunguka wakati wote, nahitaji muda wa utulivu wa peke yangu mbali na yeye.”
“Likaja tatizo jingine, anataka nimkaribishe kwangu.” “Wewe hukutaka?” “Ningepumzika wapi Dorothy? Hakika katika hilo nilijiambia HAPANA. Mapumziko nilikuwa nikiyapata mbali na yeye, sasa kama ningemkaribisha nyumbani kwangu, inamaana angejaa mpaka kwangu, na mimi kwangu nimehakikisha ni patulivu kwa makusudi ili nipumzike. Sitaki kelele. Nisingeweza karibisha kelele yake pale.”
“Nilipoona anang’ang’ania afike kwangu, huku akinituhumu pengine namficha kwa kuwa nina familia, yaani mke ndio maana sitaki afike kwangu, ndio ikabidi sasa niwe muwazi kabisa kwake na kusitisha chochote kilichokuwa kikiendelea.” “Sasa ulimwambia nini?” “Ukweli kwamba simuoni kama anaweza kuwa kwenye maisha yangu. Na nikamwambia pesa sio tatizo, ila amenifikisha mahali najisikia ni kama maisha yangu yote yamekuwa ni YEYE tu, nikimtumikia. Kifedha, muda na anafanya akili zangu hazitulii.”
“Akatoa utaratibu mwingiiii ili kurekebisha yote hayo.” “Mfano nini?” “Niwe nikimpa kiasi fulani cha fedha kila juma.” “Joel!?” “Hakika tena sidanganyi. Tena kiasi chenyewe akakitaja kabisa. Kwamba nikiwa nikimuwekea hicho kiasi kutakuwa hakuna kuniomba tena pesa, tutatulia, itakuwa sisi tu. Wazo halikuwa baya, lakini nilishamuona hanijali. Itakuwa nakuwa naye kama mtu ninayemlipa ili awe na mimi! Nikamwambia namshukuru kwa anachotaka kunisaidia, lakini HAPANA.” Acha Dorothy aangue kicheko.
“Kwamba yeye ndio anakusaidia?” “Hakika ndivyo alivyoiweka. Yaani kama mimi ndio mwenye shida vile! Nikaona tuagane. Maana nilijiambia hatakaa akafika kwangu hata iweje. Angenisumbua sana. Sasa kuanzia hapo, nikaona nipumzike tu kwenye swala la mahusiano. Nimejibu swali lako?” “Ndiyo.” “Umeridhika?” “Ndiyo.”
“Haya, na wewe baada ya baba yake Eric alikuja nani?” “Wewe Jo!” “Nini?” “Yule mwanamme alinirudisha kijijini nikiwa sijiwezi, na watoto wawili. Hakurudi tena.” “Haiwezekani Dorothy!” “Huyo Pam na kaka yake nimesaidiwa kulea na baba yangu mimi mzazi. Sijamuona tena yule mwanaume mpaka leo tunavyozungumza hapa. Kaka alirudi kule tulipokuwa tukiishi, akaambiwa alihama, hawajui alipo.” “Pole sana.”
“Asante. Kwa hiyo nilikuwa mlemavu yule mgonjwa. Isingekuwa mama yangu na huyu Pam, ningekuwa ni yule mlemavu wa kunuka. Lakini huyu Pam alikuwa akisoma na kunishugulikia mimi tokea kameanza kupatwa akili. Alikuwa akiona tu nimejichafua, ananisaidia kunisafisha, japo kufua nilikuwa nikifua mwenyewe. Ananiletea maji na kunisaidia kuanika. Tokea kapo kadogo. Na wao ndio walinifanya nisinuke. Lakini nilikuwa mtu wa mavumbini, nikijisaidia bila kujijua. Mwanaume gani angenisogelea huko milimani?”
“Halafu pia yule mwanaume aliniumiza sana. Alinichukua nikiwa bado mdogo, halafu akaanza kunitesa. Jamani mwanaume alinitesa yule! Hapana. Ile kunirudisha nyumbani kwa wengine ilikuwa mbaya, lakini kwangu ilikuwa pumziko.”
“Alikuwa akifanyaje?” “Mnyanyasaji. Mbahili. Mkali. Mkali sana. Halafu ni kwangu na kwa watoto pia. Hakuna amani akiwepo nyumbani. Halafu ana mkono wa kupiga.” “Dorothy!” “Sana. Vibao vya usoni! Kwangu na kwa watoto.” “Kwa kosa gani?” “Atakalochagua yeye atakaporudi hapo nyumbani. Chakula shida.” “Hatoi pesa?” “Alikuwa hatoi na ukitaka umuudhi, ni umuombe hela. Hapo hapatakalika.”
“Alikuwa akifanya manunuzi anayojisikia yeye. Unga wa ugali, maharage, na mkaa. Akimaliza hapo asiombwe pesa hata ya chumvi na ni mpaka atakapoamua yeye kununua tena. Ikabidi nijifunze kupika vitu vya kuuza, ndio ikawa pona yangu na wanangu.”
“Aisee pole sana.” “Asante. Kwa hiyo nilitoka kwake nilikuwa sina hamu, halafu na hali niliyokuwa nayo pia hapakuwa na wakunisogelea. Nilipokuja huku mjini ndio zikaanza salamu pale dirishani, lakini wewe unajua. Pale kila mtu anaona sura tu, hawaoni chini. Kwa hiyo kila salamu iliyoonekana inamuendelezo nilikuwa nikiwafanyia kama nilivyokufanyia wewe. Kuwaonyesha chini. Hakuna aliyetaka kubaki ndio maana wewe umenishangaza au niseme unanishangaza!”
“Hata mimi sijielewi Dorothy! Kuna namna najisikia kwako. Tukiachana natamani tuje tuonane tena. Kuna namna ya kipekee najisikia kwako. Na hii ni tokea mara ya kwanza nakuona.” Akawa kama anayevuta hisia nzuri.
“Nilipokuja mara ya kwanza pale dirishani nikakuona, moyo ukapata hali ambayo sikutegemea. Kama unakumbuka hatukuzungumza sana. Ila ulinikaribisha, ukanipa pole ya kuuguliwa, ukanielekeza na kuniambia unaniombea mgonjwa wangu apone haraka. Unakumbuka?” “Nakumbuka na ukataka nikupeleke kabisa ukijidai hujaelewa njia.” Jo alicheka sana.
“Nia ilikuwa ni nikutoe pale ndani. Nikashangaa Stella yeye ndio akachangamkia!” “Mwenzio yule alikupenda tokea unatuongelesha pale.” “Kwanza Stella si mwenzangu, pili hakunipenda, alinitamani tu kwa sababu zake. Nia yangu ni wewe.” Akamsogelea na kumbusu hapo juu ya mdomo.
“Ninapokukiss ndani ya mdomo, mara nyingine nitataka na ulimi.” Akamshangaza haswa. “Ulimi!?” Jo hana mbavu. “Sasa unanicheka nini?” “Bwana ulivyoshangaa ni kama umeona joka.” “Wewe si mwalimu mzuri! Unanifundishaje huku unanicheka bwana! Sasa hapo kwenye ulimi ndio unafanyaje?” Jo hana mbavu.
“Nyie Jo! Wewe sasa utakuwa mwalimu gani?!” “Acha nifurahi bwana Dorothy!” “Unafurahia nini sasa?” “Acha kushangaa sana. Ni rahisi sana endapo unampenda mtu. Kikubwa ni hisia. Kama mimi nimekutamani nikushike vizuri nipate hiyo midomo yako.” Akamfanya aone aibu.
“Mapenzi hayana kinyaa ila epuka tu kujaza mate mdomoni, itakera, vingine unifuatishe. Nakuahidi ni hisia nzuri sana, pengine uwe hujisikii hiki ninachojisikia mimi kwako. Vinginevyo utafurahia ila relax. Upo na tension Dorothy.” “Naogopa kukosea, na kukukera kama kwa baba yao kina Pam. Alikuwa akinisema vibaya sana kitandani.” “Pole. Lakini nahisi yeye ndio alikuwa na tatizo.”
“Nafikiri ni mimi, Jo. Sikuwa na uzoefu. Kama hivi leo. Hicho unachotaka kufanya sijawahi.” “Ndio maana nakwambia yeye ndio alikuwa na tatizo. Alijipunja bahati yeye mwenyewe. Kwa mfano hivi leo unaniambia hujawahi fanya kissing. Mimi ndio na bahatika kukufundisha, inamaana nitakufundisha kile ninachopenda ufanye na mimi. Faida kwangu zaidi kwa kuwa nitapata kissing ninayopenda mimi, siyo uliyozoea kufanya kabla. Sijui kama unanielewa?” “Nisipoweza?” “Hakuna kuweza na kukosea kama unampenda mtu. Na mapenzi ni sanaa. Kila mmoja anafanya kwa utalaamu wake na uwezo wake. Usiogope. Naomba tulia.”
“Na nakuahidi kwangu upo salama Dorothy. Hutanikera.” “Unajuaje Jo?!” “Kama unaniamsha hisia kwa kukushika tu miguu yako, unategemea nini?” Alicheka Dorothy, alicheka sana akijifunika uso.
“Mimi sio dhaifu bwana! Sasa fikiria miguu tu, hali mbaya. Nikikushika wewe mwenyewe! Na tutatafuta jinsi yetu sisi wawili itakayoturidhisha, sio mitindo ya watu wengine. Kile tutakachoweza sisi ndio tutafanya. Na chochote kigumu kwako, unaniambia tunabuni kitu chetu pamoja, mpaka tutakuwa ukurasa mmoja. Kwa hiyo usiogope.”
“Kama hivyo ujue umenitoa hofu. Na unichukulie taratibu.” “Kama hivi?” Akaanza kumkiss taratibu, mpaka vikakolea na kusahau hata walimaliza kufundishana saa ngapi! Ikawawia rahisi, kila mmoja anamtaka mwenzie.
Vikaendelea hawajali muda, Dorothy hajali tena wazazi kama wamefika au la. Anasikia raha, mwili huo haujawahi shikwa kwa mapenzi ya kiasi hicho. Naye Jo, hiyo romance haikuishia midomoni tu, mpaka masikioni, shingoni, Dorothy masikini hajui kama na masikio yanaletaga raha. Akabaki akitetemeka kama baridi! Kuja shingoni, ndio kabisaa, Jo akammaliza. Hajawahi toa minung’uniko ya mahaba, wala hajawahi sikia, lakini siku hiyo mtoto wa mzee wa kanisa, akajikuta analalama kama anayeonewa! Na hapo bado hajavuliwa nguo!
Jo alikuwa mtundu, akimchukulia taratibu. Shule ya udaktari ikamsaidia kuonyesha umahiri wake hapo, akishika sehemu zinazoibua hisia haswa. Walikaa humo ndani ya gari zaidi ya masaa matatu, ndio wakagutushwa na simu ya kaka yake, kuwa wazazi walishafika, wakala na kulala kidogo, wameamka, wanamuulizia.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Au nikufuate?” “Nashukuru kaka, nitakuja muda si mrefu. Ila nakuja na mgeni wangu.” “Sawa.” Akaitika kirahisi. “Hapana kaka. Huyu mgeni ni muhimu kwangu, nataka mkutane naye. Na nyinyi mumfahamu.” Kaka yake akatulia upande wa pili. “Ni mtu mzuri.” “Dorothy, naomba kuwa makini dada yangu. Huu mji wamejaa matapeli. Sitaki mtu akuchezee.” Hapo akawa ameshasahau dada yake si binti mdogo.
“Ananijali sana, na kuniheshimu sana kaka yangu, si tapeli.” “Ulisema hivyohivyo kwa baba Eric. Akakutoa shule, akakuzalisha na kukurudisha nyumbani ukiwa mgonjwa. Sasa huyu wa sasahivi anatofauti gani? Wakishakuona hivyo umependeza, wanapatwa tamaa, ukishawafungulia moyo, wanakuumiza.” Yaani huyo mama Eric kwao hakui!
“Kaka, huyu ni tofauti.” “Anatofauti gani?” Hapo akakwama. “Eti Dorothy? Huyo anatofati gani na yule TAPELI aliyekwenda mpaka kwa baba, akapiga magoti akitaka akuoe, akiahidi atakuendeleza na shule. Nilikutahadharisha hivihivi, unakumbuka uliniambia maneno kama haya?” “Sasa huyu ananidanganya nini na ulemavu huu!?” “Kwani kutotembea ndio kunabadilisha nini?!” Akauliza kwa kushangaa kabisa.
“Wangapi hawana miguu kabisa na bado wanaolewa na kupata watoto? Nani amekwambia ulemavu ndio unakufanya usiwe mwanamke!? Umeshapendeza, umetulia ndio wanajisogeza tena.”
“Walikuwa wapi siku zote hizo ulipokuwa ukiteseka kijijini? Sasahivi ndio wanajisogeza kwa kukudanganya ili tu kukutumia? Utajifunza lini Dorothy wewe?” “Basi kaka. Nakuja kuona wazazi.” “Tafadhali kuwa makini Dorothy. Usiwe mtu wa kukubali kuumizwa kila wakati.” “Sawa kaka.” Akakubali na kukata simu akiwa amepoa, Jo alikuwa akisikiliza huku ameinama pembeni yake. Wakatulia kimya wakiwa kama wamepoteza dira. Kutoka kwenye hisia kali mpaka kukemewa hivyo, ni kama kupigwa kibao cha uso.
Pam&Mill
Alikuja kufungua macho ni mchana. Akamuona Mill amekaa kwenye kochi yupo kwenye kompyuta. “Mill!” Akasimama kwa haraka. “Sasahivi nasikia njaa. Mmebakisha chakula?” “Nimejaza vyakula humu ndani sikujua ni nini utataka ukiamka.” “Naona nataka kitu kitakachoshika tumbo.” “Ila naona uache kula vile vyakula vyenye malimao mengi kwa sasa. Vimeshatengeneza asidi nyingi ndio maana unatapika.” Akamuona anafikiria.
“Bado unahamu na ugali?” Akamuuliza kwa kujali akibembeleza. “Ugali ndio unakaa tumboni muda mrefu.” Akawa anatoka kitandani. “Nitakuletea. Pumzika.” “Kweli? Maana nasikia kizunguzungu kweli!” “Wewe tulia hapo mimi nipo hapa kwa ajili yako.” Shema akaingia wakati baba yake akitoka. “Ulikuwa ukicheza wapi mbona unamwagika jasho hivyo?” “Anko Colins alikuja. Tukacheza naye, akaniacha nacheza na mlinzi.” Mama yake akacheka.
“Sasa hao walinzi wanalinda saa ngapi?” “Nimecheza naye palepale getini. Anajua mpira huyo! Anasema alikuwa akicheza sana zamani.” “Sasa hapo usikae Shema, pitiliza kuoga.” Akacheka na kurudi chumbani kwake.
~~~~~~~~~~~~~~
Mill akarudi na sinia lenye matunda na ndizi za nyama. “Naomba jaribu na hizi ndizi. Kamila anasema ni nzuri, utapenda. Zipo nyingi. Na kuna matunda pia.” “Havitakaa tumboni Mill!” Akacheka akimuwekea hapo kitandani.
“Usiwe na wasiwasi. Na usisubiri njaa mpaka ikuanze. Kila wakati kula kitu kidogo. Ukimaliza, chakula, matunda, chakula, juisi. Hivyohivyo. Nitakuongezea mayai ya kuchemsha pia.” “Hapo sawa. Ila kula ndizi ndio iwe basi! Havitakalika.”
“Sasa wakati wa Shema ulikuwa ukila hivihivi?” “Ukumbuke wakati ule sikuwa na uwezo. Kwa hiyo nilikuwa nikiamka tu nasonga ugali na chai ya rangi.” “Pam! Mbona unaniumiza!” “Sikuwa na jinsi Mill. Pesa sikuwa nayo, na njaa ilikuwa ukinisumbua mpaka kukaribia kuchanganyikiwa. Hakuna kitu kinakaa tumboni kama si ugali. Haya, mchana ndio naongeza na maharage na mboga za majani. Usiku nikiishiwa maharage basi huo ugali hauwezi kukosekana na mboga za majani. Ugali lazima. Lasivyo silali.”
“Nilimzaa Shema kama mtoto wa miezi miwili tayari mpaka walikuwa wakishangaa kule leba alivyotoka. Mrefu halafu mkubwa. Nilichanika wakati najifungua, sina jinsi nikakwambia maumivu yake. Nilijiuguza kidonda kwa maumivu makali mno zaidi ya mwezi.”
“Pole Pam wangu. Safari hii unakwenda jifungulia kwa wataalamu wakisasa. Wanakuchoma sindano, yale maumivu ya uchungu unayaona kwenye mashine tu wala huyasikii. Unamtoa mtoto huyo bila maumivu.” “Mill! Kweli?” “Mambo yamebadilika mama. Wewe nibebee tu mpaka miezi tisa. Atatoka kwa utulivu japo kuchanika hutaepuka. Lakini napo hicho kidonda hakitakutesa.”
“Huku Tanzania huduma hizo utazipatia wapi?” “Huyo raia wa Kimarekani, Pam. Anaenda kuzaliwa kwao.” “Mill!” “Oooh kabisa. Hizi fujo za kubadilishana uraia zinaishia kwa Shema. Huyo mtoto naona ashabadilisha ratiba yetu. Tutaondoka hapa mapema sana. Uangalizi wake nataka wa uhakika, sitaki habari za kiswahili zile ndefuuu! Mara hospitalini hakuna hiki, mara hakuna kile! Hapana. Twende tukafuate huduma nzuri hukohuko kwao.”
“Hapa umenikuta nilikuwa nikiangalia nyumba ya kununua, lakini mitaa ninayoona itafaa kukuza watoto wangu.” “Mill! Huko Marekani!?” “Kabisa. Ila sitaki tena turudi kule kwenye mji ule nilioishi na Kisha na wanae. Nataka mpate mwanzo mpya.” “Sasa nyumba huko si ni garama sana?” “Sana tu, tena zaidi aina ninayotaka mimi. Ila usiwe na wasiwasi, tutafanikiwa tu. Kuna ambazo nishaanza kuzitenga ili baadaye tuziangalie wote, tuchague, nianze kuifuatilia hiyo tutakayoipenda.” Pam hakuwa akiamini.
“Kila kitu kitakuwa sawa.” “Sasa safari hii watanipa Visa? Si nimesikia Tanzania haturuhusiwi kwenda tena huko?” “Kwa sababu maalumu, kibali maalumu. Halafu safari hii hawana sababu ya kukunyima tena. Pesa ipo, nalipa kodi kule bila kukosa. Wewe mke wangu, mwanao pia raia. Nimekaa kule sina nilipoharibu. Hawana sababu ya kukunyima tena. Yaani naanza mchakato mapema sana ili tusichelewe kuondoka.” Furaha ilimjaa Pam, mpaka Mill akamuona usoni.
~~~~~~~~~~~~~~
Hakumsikia mama yake kabisa siku hiyo asijue nikupatwa kwa Jo. Alikuwa ameng’ang’aniwa anapewa ambayo hajawahi hata dhania anaweza pokea. Halafu kwa mapenzi haswa. Anaitwa Dorothy, sio mama Eric! Alishasahau hata wazazi wake mpaka jioni hiyo ndio anakumbushwa.
Hata ujio wa bibi na babu yake hapo jijini hakuwa na taarifa nao. Heshima aliyomrudishia mama yake, ni hivyo alikuwa hajui tu. Dorothy huyu hata wifi yake aliongea naye kwa heshima haswa.
Mill aliijaza hiyo nyumba vyakula, kuashiria wazi anatambua ugeni ni wake yeye aliyewaalika hapo mjini. Dereva aliwaleta asubuhi ya siku ya jumapili, akakuta Mill alishafanya manunuzi hapo, ili asiwalemee mbali na malazi. Sifa za Mill zilikuwa zikiimbwa hapo kama kamungu kadogo.
~~~~~~~~~~~~~~
Alilala Pam jumapili siku nzima. Jioni Mill akaenda kuoga kwake. Akahakikisha kila kitu kimekaa sawa ndipo akarudi kwa Pam, akamkuta amejilaza tu. “Naomba nije nilale hapa. Nitakusaidia usiku.” Pam akacheka taratibu kimtizama. “Hufukuziki Mill wewe!” Akacheka akipanda kitandani.
“Jana nililala kwa shida! Usiwe unanikimbia bwana!” Pam akavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu, akajifunika vizuri na kugeuka upande wa dirishani akatulia. Mill akajisogeza karibu yake mpaka akamgusa, akavuta mto juu ya kitanda kabisa, akawa anamchungulia kule aliko geukia.
“Nakupenda Pam. Au ushawahi nitilia mashaka juu ya hilo?” Akamuuliza akimsugua begani mpaka kwenye kiwiko. “Eti Pam?” “Hapana Mill. Ila naona tunakuwa na mipangoyetu ambayo haikamiliki wakati nakuona jinsi unavyofanikisha vizuri mipango yako, tena kwa haraka. Lakini ikifika kwenye mipango inayonihusu na mimi ni kama nahisi unapuuzia!”
“Hata kidogo. Na usifikiri swala la ndoa ni wewe tu ndio mwenye shida nalo. Na hili narudia kwako tokea mwanzo. Nahangaika kukufanya uwe wangu kihalali Pam. Na pia si kwa ajili yetu tu! Nafanya pia kwa wale ndugu zangu. Najihisi nina wajibu wakufanya pia kwa kulipa deni kwa baba. Nataka ndugu zangu pia waone ninachofanya ili hata nikiwaambia acheni uhuni, niwe na ujasiri.”
“Sasahivi nakuwa nikiwakemea, ila si kwa ujasiri sana maana mimi mwenyewe nakuwa sina tofauti na wao. Na nimewashirikisha harusi yetu makusudi ili waone japokuwa nilizaa kabla ya ndoa, ni ajali na nahangaika kutengeneza ndio maana unaona nimemuhimiza Colins ajitahidi kuwapenyeza katika kila kamati, wasimamie ila si kushika pesa.” Pam akacheka kidogo.
“Nataka waone na wajifunze kwa vitendo. Nahisi hapo ndio nimepitiliza nikitaka iwe nzuri ili kuweka mfano bora, ila si kwamba sitaki ndoa, Pam. Nimehangaika kwa muda mfupi upande wangu wote wamekamilisha mpaka mavazi.” “Sasa usije wasahau wale wadogo zako. Watakujia na njisi.” “Wanavyopenda kuvaa! Kama baba. Ni bora wasile ila wanunue nguo. Ila pia nilihakikisha na suti zao niliagiza pamoja na zangu. Nikikwambia kwa upande wangu nimekamilisha, nimekamilisha mama. Ilikuwa ni huo ukumbi tu.” Pam akatulia.
“Nakupenda mpenzi wangu. Na nataka kukuoa. Nachelewa kwa ajili yako. Kukutayarishia kitu kizuri sana. Unastahili Pam.” Hakujibu, akanyamaza. “Kama nilimwaga pesa kwa Kisha, huoni wewe ni zaidi?” “Sikuwahi kuwa na ndoto za kuolewa nikiwa mama, Mill! Tena watoto wawili!” “Hata mimi Pam. Tafadhali na wewe kuwa shahidi yangu katika hili. Kumbuka jinsi nilivyokuwa nikiharakisha hata kukuchumbiana kulipa mahari! Mpaka kina Mike walikuwa wakinishauri nipunguze kasi. Lakini Pam, niliamua kuwa na wewe. Na nakuahidi tutafunga ndoa mpenzi.” Akamsikia akivuta punzi tena kwa nguvu na kuzishusha taratibu, bila ya kujibu.
Akambusu shavuni. “Nasinzia kwa madawa.” “Kula hata matunda ndio ulale. Ili usiamke na njaa kali. Au unataka yogurt?” “Ile ya vannila nimependa.” “Basi ngoja nikupe ili usiamke na njaa kali.” Akamtayarishia na kumletea na kujiko. Akakaa na kuanza kula.
~~~~~~~~~~~~~~
Akaenda kukaa miguuni kwake na kuanza kumminya miguu taratibu, starehe yaoyeye na Jo. “Kesho naomba usiende kazini.” Pam akamtizama. “Naamini nitajisikia vizuri. Kichefuchefu kimeisha kabisa.” “Nataka tuanze maandalizi ya safari. Kuna watu nataka nikakutambulishe kwao. Jioni. Usiwahi kuamka labda kama ni njaa. Ila naomba ukiamka ukishakula, nenda katengeneze nywele, na wakutengeneze vizuri sana, ile ya kupania.” Pam akacheka.
“Unanikutanisha na kina nani hao unaotaka nikuwakilishe vizuri?” “Nataka baadaye usije jilaumu ukasema ningejua ningevaa hivi au vile. Na itakuwa jioni. Kwa hiyo vaa kiusiku, tena vizuri. Nitakuja hapa mchana, nikupe dawa ingine ili usitapike. Mimi nitarudi kazini. Lakini tukutane pale kwenye ule ukumbi tuliolipia, tuzungunze nao kwa pamoja, ndipo twende.” “Sawa.” Pam akakubali bila hata kujua kumbe anakwenda kwenye harusi yake mwenyewe.
“Nakupenda Pam.” Akazidi kurudia. “Najua Mill! Najua. Ila sikutegemea kushika mimba ya mtoto wa pili kabla ya ndoa. Sijui nilijisahau vipi!” “Naomba usijute tafadhali. Amini kila kitu kitakuwa sawa.” Ikawa ngumu kuamini. Moyo unasita. Akavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu.
“Najua katika hilo unatilia shaka ndio maana unashindwa hata kujibu. Basi naomba hata kukusikia ukiniambia kama bado unanipenda.” “Wewe unajua kama nakupenda Mill. Ila tu nakuwa na wasiwasi. Ukija niacha na watoto wawili bila ndoa?” “Naenda wapi Pam!? Karibu mali zote sasa hivi zipo kwa jina lako. Kampuni ile pale hospitalini kisheria ni kama yako kabisa. Mikataba yote sasahivi umeandikishana wewe na kina Komba, nimejitoa kabisa kwa sababu wewe ndio raia. Nyumba hii nayo ndio tunashugulikia ili vyote viwe kwa jina lako wewe ambaye ni raia. Sina ninachokuficha.”
“Sasa mimali yako hapa itanisaidia nini ukiniacha hapa na watoto wasio na baba?” “Pam, sasa kama nimekupa kila kitu changu, unafikiri nitaenda wapi na nitaishije?” “Wewe si raia wa hapa Mill. Na kuna kufa pia. Ukifa na kuniacha bila ndoa?”
“Labda kifo. Lakini hakuna ninapo kwenda. Na wanangu niwaachie nani? Watoto wa Mgini nao je? Halafu nikatafute mwanamke mwingine wapi tena?” “Mimi sijui Mill!” “Wewe umeona wale watoto wa Mgini wamegoma kukua, na wanaangamia bila mimi. Ni ahadi nimempa baba, siwezi epuka. Na naona na wewe umesimamia kwako. Mbali yetu sisi wawili, tunajukumu la hao vijana tuliomkubalia mzee Mgini.”
“Sina ninapokwenda bila WEWE Pam. Sina maisha mengine hapa nchini kama sio WEWE na kina Komba wanao nisaidia kuishi hapa kwa kibali cha kazi. Na ndoa yetu ndio itanihalalishia kuishi hapa nchini bila maswali au kufilisiwa. Ndio ujue ulivyo wamuhimu kwangu hata kama ukihisi sina mapenzi ya dhati kwako, basi jua nakuhitaji sana.”
“Nakuhitaji kwa mengi Pam. Sina maisha popote bila wewe. Na unanijua mimi mtu wa familia. Siwezi telekeza watoto wangu.” “Nilikuona na wale watoto wa Kisha. Walikulemea lakini bado ulipambana.” Mill akaanza kucheka. “Bwana watoto walikuwa wakiniendesha wale! Kama gari bovu! Sijui huko walipo watakuwa na hali gani aisee!” Pam akamuona amepotelea mawazoni lakini bado akimpapasa miguu
“Nasikia usingizi.” Akamtoa mawazoni. “Lala. Njaa ikija niamshe nikuletee kitu chakula.” “Asante.” Hapohapo akalala.
~~~~~~~~~~~~~~
Usikose Harusi Ya Surprise Ya Pam.
Jo Naye Ameanza Kwa Kukataliwa Ukweni. Itakuaje Na Mrembo Dorothy, Mlemavu? Atapambana Mpaka Mwisho Au Ataachia Ngazi?
Usiache Kufuatilia.
0 Comments:
Post a Comment