“Wanarudi jijini, na Raza ndio mwenyeji wao!” Akajua ameshawakosa vijana wake wawili na wajukuu, damu ya Ruhinda. Akaamua kufanya jambo kwa haraka. Kitu cha kwanza hakumeza tena dawa ya pressure aliyotakiwa kumeza muda huo. Kusudi tu aiache ipande zaidi.
Mzee Ruhinda alikuwepo wakati mazungumzo hayo yakifanyika. Yeye alishajua kuwa Pius amesimama na mkewe katika kila jambo, na dhehebu alishahama, ila hakutaka kumwambia mkewe asije mpandisha pressure.
Akaanza kulalamika, kuwa yeye ndio sasahivi anaonekana mbaya. Akaongea mengi akijipandisha pressure kusudi tu.
Akampigia simu na Paulina. Akaanza kumuelezea huku akilalamika. Akaeleza mengi, mzee Ruhinda kimya akisikiliza, ila alitegemea tu. Pius ni kipenzi cha mkewe. Leo apotelee kwa Raza! Alijua isingekuwa rahisi.
Akamaliza hapo akampigia na mziwanda wake, akaongea mengi. Kwamba yeye sasahivi ndio anaonekana mbaya, wakati yeye alikuwa na nia nzuri. Paul alimjua mama yake mgonjwa wa pressure. Basi akamtuliza hapo, akamkumbusha dawa. Wakaagana. Lakini hakunywa dawa wala hakutaka kupima kusudi tu, jambo liwe zito.
Asijue Pius alishamjua mama yake, alishaiona mpaka hiyo siku anayojipandisha pressure. Lengo lake ilikuwa kuwatia adabu kwa kumuadhibu mpaka binti yake.
Aliumia sana walipotupa zawadi ya binti yake na kuacha kumualika kwenye shuguli zao. Na Raza kulia kwamba wanamkimbia, japo alishawaomba msamaha! Basi Pius akajua pakuwakomesha wote mpaka arudishe heshima ya mkewe na ndio maana alimwambia inatosha, asiendelee kuwaomba tena msamaha. Alijua watarudi tu wenyewe.
Kwa asili naye Pius hafanyi jambo bila ya kufikiria mbele, na madhara yake. Vichwa viwili vikakutana vyote vipo kazini, kimkakati. Mzee Ruhinda kimya, anajiangalizia japo alishajua mwisho wake ni nini. Hao wawili ni uji na mgonjwa.
~~~~~~~~~~~~~~
Alfajiri ya siku ya jumapili, mzee Ruhinda akaamshwa na mkewe kwamba yeye anajisikia vibaya sana, anakaribia kufa. Akamtia hofu mzee Ruhinda, kumpima, ikabidi maandalizi ya haraka ya kumkimbiza hospitalini na si kanisani tena.
Wapo njiani mzee wa watu amepaniki kwelikweli maana kweli pressure ilikuwa juu, na ndio ilikuwa lengo lake. Simu zikasambaa kwa watoto wake kuwa hali ya mama yao sio nzuri, anakimbizwa hospitalini. Basi alilotaka mama Ruhinda likatimia. Watoto wote na wake zao, Paulina na mume wake, ikabidi kukimbilia hapo.
Ibada ya kikatoliki na isiyo ya kikatoliki ikahamia hapo kwenye chumba alichopewa apumzike. Na hapo ni mgonjwa kwelikweli. Hakuna aliyewaza tena kanisani, ila yeye. Usicheze na nguvu ya mama. Yaani yeye ndio sasa akawa center of attention. Tena Pius yupo hapo! Hajaenda kanisani kwa Raza! Kila saa anamuuliza vile anavyojisikia! Mungu ampe nini? Wakati wanae na mumewe wapo hapo kumuuguza, wasiwasi umewajaa, basi yeye akawa anafurahia ushindi. Raza ametulia kimya akijiangalizia. Ila ni kama akamuhisi.
~~~~~~~~~~~~~~
Daktari alipopita na kusema anaendelea vizuri na baadaye angeruhusiwa kwamba kila kitu kimeanza kukaa sawa mwilini mwake, Raza akamgusa Pius. Wakatoka. “Maadamu mama anaendelea vizuri, acha mimi nikamsaidie Polla kujitayarisha twende kanisani. Leo ndio ile siku yao wanasimama mbele ya kanisa na kusema ile mistari ya bibilia waliyopewa kukariri.” “Aisee kweli! Acha tuage, tutoke wote.” “Unauhakika?” “Oooh yeah! Kabisa. Alivyohangaika hivyo kukariri, lazima na mimi niwepo. Poliny mwenyewe alikuwa akimsifia. Acha tuage tutoke.” Raza akafuata kwa nyuma akitaka kuangalia kitakachoendelea.
“Baba, maadamu mama anaendelea vizuri, acha sisi tutoke tujaribu kuwahi kanisani.” “Nasikia umehama dini.” Akaongea Paulina, Pius akamtizama na kurudisha macho kwa baba yake. “Jioni nitapita nyumbani kumuona mama.” Wakashitukia mama Ruhinda anaanza kulia pale kitandani. Raza alishangaa, hakutegemea kama huyo mama angetumia machozi kama silaha.
“Kwa ubaya gani huo mimi nimetenda, mpaka unabadili dini?” “Naomba niwahi. Hayo maswala mengine tutakuja kuzungumza baadaye. Leo Polla anashuguli kanisani na watoto wenzie. Amejituma sana kukariri mistari ya bibilia, wanatakiwa kuisema mbele za watu bila kusoma. Maadamu nyinyi wote mpo hapa, chochote kikibadilika, mtatujulisha, vinginevyo nitapita nyumbani baadaye.” Kisha akamgeukia mama yake.
“Mama, jaribu kupumzika. Nitakuona baadaye.” Kwa hakika hakuna aliyetegemea. Mpaka Raza alishangaa. “Jamani, jumapili njema. Acha nifikishe familia yangu kanisani.” “Utuchukulie video na sisi tumuone mama mkubwa.” Mzee Ruhinda akadakia. “Nitafanya hivyo.” Akamgeukia Raza na kumnyooshea mkono, “Twende.” Wakati wanatoka wamefungua mlango, Paulina akaanza.
“Hivi kweli Raza, huyu angekuwa mama yako mzazi, ungemwambia mwenzio muondoke mumuache hospitalini?” Pius alimtizama, kisha akafungua mlango akiwa amemshika mkewe mkono, wakaondoka bila ya kujibu kitu.
Paul alikuwa kimya muda wote akawaambia hivi, “Mimi sikuwaambia mtafute jinsi ya kuweka mbali tofauti zenu na Raza, kwa sababu Pius amebadilika sana?” Akauliza. “Sikukwambia mama kama Pius wa siku hizi anaweza nipigia simu mchana siku ya kazi ananiuliza mimi ambaye sijaoa, sina mke niliyemzoea, kama nina msichana, ningempelekea zawadi gani?” “Pius?!” Andy akauliza.
“Pius huyu. Anaishi na Raza siku hizi kama eti ndio anamchumbia! Na hili nilimwambia mama. Nikamwambia ni kama kwa mara ya kwanza, Pius amempenda sana Raza. Tena kwa kuniambia yeye mwenyewe kuwa, hakujua kama katika umri huu anaweza kupenda kwa kiasi anachompenda Raza. Nilimwambia mama, na nikamwambia hivi, watafute kwa haraka kuweka sawa mambo yao na Raza, lasivyo watampoteza Pius. Bisha Paulina maana na wewe mshabiki ulikuwepo.” “Pius sio wa kuniacha mimi hospitalini. Kuna kitu amemfanyia mwanangu.” Bwana walishituka! Mpaka Mina akashangaa.
“Na safari hii naona Raza amepatia.” “Paulina wewe acha kuongeza chuki!” Mina akaongea bila kutarajia. “Mungu akusaidie Paulina, hiyo roho unayokubali kuibeba, ukiharibu mahusiano ya watu, kubali ikutoke. Hakika nakwambia.” “Kwani…” “Hapana Paulina. Wewe tumekuachia kwa muda mrefu sana, umekuwa mwiba kwenye hii familia, hatutakuachia tena.” Mina akajikuta anapandisha mpaka mumewe akashangaa.
“Kwa nini wewe kwenye kila ugomvi unakuwa upande wa kuharibu zaidi na si kuleta amani?” Wakwe zake pia wakashangaa. “Wewe upo kwenye kila ugomvi, katikati ukiharibu! Kweli jamani?!” Mina akauliza kwa kumshangaa na kuendelea.
“Jamani wazazi wetu, Raza amebadilika. Amebadilika ile ya kupitiliza na amebeba nguvu ya ajabu sana. Raza mnayemfahamu nyinyi sio huyu wa sasahivi, muulizeni Andy huyu hapa.” Mina akaja juu kabisa.
“Raza yule mchaonganishi na mvurugaji, baba.” Akamgeukia mzee Ruhinda. “Ndiye aliyeweza kuziweka familia zetu sisi na hatimaye kila mmoja ameweza kujua nafasi yake kwa Ayvin. Raza ameweka ramani ambayo pengine ingetuchukua muda sana sisi kuipata.” “Na pengine pia tusingeipata kabisa.” “Asante Andy.”
“Baba, Raza ameweza kutuweka sisi wote. Nikimaanisha mimi, Andy na Pius pamoja, na kukawa na amani kitu kilichotushinda sisi tokea mwanzo. Tena mpaka nikawa nikiwaza, nikasema Raza huyu angekuwepo tokea mwanzo, pengine kule kupigana hadharani na kuchafuana, kusingekuwepo. Raza anaomba jamani, mimi simfikii.” “Na binti yake yule mdogo pia anaomba sana, mpaka nikamwambia Mina.” Andy akaongeza.
“Basi eti huyu Paulina, anamuogopa yule mtoto.” “Acha umbea Paul.” “Wewe ni mbishi Paulina, na sijui utakuja badilika lini. Unakumbuka mimi kuzungumza na wewe pamoja na mumeo juu ya kutomualika Polla kwenye birthday party ya mtoto wenu?” “Haiwezekani?!” Andy akashangaa sana.
“Hawa hapa wawili waulize kama mimi naongopa.” “Ni Paulina jamani!” “Lakini na wewe uliunga mkono. Na niliwaambia siku ileile nilipofika pale na kumkosa Polla, mpakanipa sababu zenu kuwa sijui Polla anatembea na mashetani, hamtaki awape watoto wenu.” Mina aliumia sana.
“Haiwezekani!” Andy akahamaki, Mina aliambiwa na Raza mwenyewe alipokwenda Dodoma kuomba msamaha, ila hakujua kwa ubaya huo. Naye akaumia sana. “Hawa hapa. Nikawaambia, hicho mnachokifanya, ni kumtia Pius kidole jichoni. Nikawaambia, Pius akisikia mnamtenga binti yake, mahusiano yenu hatakakaa yakabaki salama.”
“Devi nilikwambia. Katika vitu Pius anathamini, kimoja wapo ni watoto wake. Adhabu yeyote utakayompa mtoto wake, jua umemuadhibu Pius, na hamtakaa mkabaki salama. Mkanikatalia. Nikampigia simu mama kumwambia, ni bora ile shuguli isifanyike, kuliko ikafanyika bila Polla. Wote mlinipuuza. Mmemuona Pius leo jinsi alivyokuwa hapa?” “Pius si wakuhama dhehebu, kabisa.” “Asante baba. Na wala Pius si wakumuacha mama hospitalini, ila kama mmemgundua, amewabadilikia nyinyi wote. Na niliwaonya.”
“Pius hajalogwa na Raza, ila nyinyi mmempa sababu ya kumsogeza karibu ya Raza zaidi. Yaani sasahivi wale wawili utafikiri ndio wanaanzana mapenzi.” “Na mimi hilo nimeligundua. Wamebadilika sana. Hata kwangu, Pius hawezi acha kumzungumzia Raza. Tena kwa kusema kabisa, amekuja kugundua, asilimia 85 ya maisha yake hapa duniani, yanamtegemea Raza.” “Sawasawa. Na mimi aliniambia na kusema Raza huwa anaenda kazini bila kula, ili kuhakikisha yeye mchaguzi wa vyakula, anaondoka nyumbani ameshiba.” Paul akaongeza kwa Andy.
“Akianza kumzungumzia mkewe, unaweza sema Pius yupo na nyumba ndogo. Na mwenyewe anasema anataka afanye hivyo kusudi ili kumuonyesha Raza na binti zake kuwa alikosa, anajutia kosa, na pia kumuonyesha Raza kuwa anatambua kujitoa kwake, kwake na kwa wanae.”
“Pius anasema yeye anajua kuvaa vizuri, nguo safi, hajui hata zinafuliwa kwa dry cleaner yupi! Na zinapelekwa saa ngapi! Anasema lakini hajawahi toka kuoga, akakosa nguo zilizotayari, hajawahi kukaa mezani kwake, akakosa chakula, tena kizuri kuliko cha kwenye mahoteli, maana anasema alijaribu kuhamia kula mahotelini, lakini hakuwahi acha mkumbuka Raza, mpaka aliporudi kula kwa Raza. Huyo ndio Pius sasahivi, aliposimama na Raza.”
“Na nafikiri ni kama aliniambia alimrudisha fungate! Sina uhakika.” “Hujakosea Andy, alimrudisha Raza fungate, visiwa vya Seychelles.” Wote wakashangaa sana.
“Na alienda na watoto wake wote. Ndipo mjue alipo Pius kwa sasa. Mmemshika mboni ya jicho, na haya ndio matokeo yake. Raza hajamloga.” “Na hata kama anamloga, basi anayenufaika ni Pius.” Akaongeza Andy wakamgeukia.
“Ni kweli. Kama ndivyo anavyomloga vile Pius, basi naona tuwaombee asiache kumloga. Sisi jana tumeingia hapa jijini, tukamkuta Raza amesafisha nyumba yetu, amefanya manunuzi ya vyakula. Friji imejaa na stoo kumejaa.” “Na bado akatupikia.” Akaongeza Mina.
“Na si chakula kimoja, vyakula vyakutosha. Akaweka mazingira sisi tunafika na kusaidiana swala la watoto mpaka kulala. Anamsaidia mumewe kulea yule mtoto aliyekuwa akituvuruga kichwa hatujui itakuaje. Ameweka amani na utulivu katikati yetu na sasahivi anapenda watoto wote. Nafikiri hayo ndiyo yanamfanya Pius kusimama naye. Pius si mjinga. Amevutwa na matendo ya mkewe. Nashauri muongeze umakini. Zile fujo mlizofanya kwenye ndoa yangu, nashauri muweke kikomo.” Andy akaongeza.
“Na sisi naomba tukuache mama upumzike, turudi nyumbani. Bado ni wageni, hatutaki kumuacha yule binti na watoto peke yao. Na mimi nitapita jioni kukuona.” “Ndio mnakwenda kwa Pius?” “Ni ahadi tuliyokwisha toa, jamani. Raza alitaka kumkaribisha rasmi Ayvin nyumbani kwao. Huyo mtoto anasubiriwa na dada zake, na wamemuandalia mpaka keki. Sitabadilisha sasahivi. Itakuwa ni kuwakatili pasipo sababu na itakuwa ni kumpokonya Ayvin nafasi muhimu sana kwake.” Mpaka Mina akamshika mkono mumewe.
“Jambo la kheri hilo, ilitakiwa familia nzima iwepo. Umeanza matabaka yako, ona ulipofikisha familia.” “Kwani mimi ndio nimemwambia Raza afanye shuguli asialike hata wakwe zake?” Paulina akamjia juu Paul. “Nyinyi si mnamtenga Raza, mnaogopa atawawekea uchawi kwenye vyakula vyenu?” Mina akamuuliza kwa kumsuta.
“Sasa angewakaribisha vipi?” Mina akamuuliza Paulina. “Badilika Paulina, ufanyike baraka kwenye hii familia. Acha maneno maneno ya chokochoko. Mungu huyu mnayemng’ang’ania kwenye hayo madhehebu yenu, huwa anasamehe jamani! Na ameahidi hatazikumbuka dhambi zetu kabisa. Kukaa na kukumbuka makosa ya Raza, ni kupingana na kazi ya msalaba, na hamtakaa mkawa salama.” “Na hata sasa hatuko salama Mina binti yangu. Wajukuu hao nilikuwa nikiwasubiria kwa hamu, naona wamekuja na mengii!” Mzee Ruhinda akaongea kwa kulalamika.
“Mama tunaamini utapona tu. Kama mpaka kesho ukishindwa kwenda kazini, nitakubebea wajukuu zako wote waje wakupe pole. Na chafujo akuchangamshe.” Angalau Mina akabadili hali ya hewa. “Anaendeleaje?” “Utundu vilevile, mama yangu! Hajabadilika. Nitakuletea umuone.” “Nashukuru Mina binti yangu.” Mama Ruhinda akaongea kwa kuhuzunika.
“Lakini Mina unayo nafasi ya kuweka sawa haya mambo.” Mina akamgeukia Devi. “Kivipi?!” “Kwa mfano shuguli ya leo si inamuhusu mtoto wako?” “Nikurekebishe. Ayvin sasahivi ashakuwa mtoto wa watu wanne. Si wangu peke yangu, na si kwamba mimi ndio nina usemi juu yake. Pius mwenyewe akitaka kitu kwa yule mtoto anazungumza na Andy.”
“Na kama hujanisikia, nimesema hivi, Raza. Raza ndiye amefanya sisi watatu kuweza kuishi na yule mtoto aliyekuwa akituumiza vichwa sisi wote mpaka wewe. Akiwa kama mama wa kambo wa Ayvin, ameamua kufanya tafrija ya kumkaribisha rasmi nyumbani kwake yeye Raza. Wala si wazo la Pius. Ni la Raza mpaka akatushangaza sisi watatu, muulize Andy. Halafu leo unataka kusema nini?!” Mina akawa mkali kabisa.
“Nimekataa, na ninakataa mbele yenu. Sitachukua upande wa yeyote asiyetakaAMANI. Vinginevyo wanangu mimi Mina, ndio watakuwa wahanga. Mimi na Raza hatuna tofauti. Wote tulikosa, Mungu akatusamehe. Sina shida mimi na Raza. Siogopi uchawi. Nakula chakula chake kwa amani, na sasahivi ndio kama ameshikilia hizi familia mbili tena kwa amani. Sitakubali mtu amtibue Raza, maana narudia tena, wanangu, zaidi Ayvin wangu ndio atakuwa muhanga. Nyinyi ndio mnashida na Raza, sio mimi. Msitake kuniingiza kwenye vita zenu zisizoisha. Twende Andy.”
“Mara moja, Mina. Hili nilimwambia Pius na mkewe. Na ninaomba na nyinyi mlizingatie maana naona mmegoma kubadilika. Sitaruhusu mtu amchanganye Ayvin. Jamani yule mtoto ni mzuri SANA, baba anajua ninachozungumzia. Mlichokifanya kwa kijana wangu, Ayan, sitaruhusu mkifanye kwa Ayvin. Nitakuwa makini sana na nyinyi WOTE. Hamtachanganya vijana wangu kwa wivu na matatizo yenu binafsi yasiyo isha. Muwe na siku njema.” Wakatoka na kubaki hapo kimya.
Kivuli Cha Mapenzi, Yaliyowahi Kuuma
Japokuwa kulikuwa na viashiria vizuri vya tumaini mbeleni, Dorothy alishatendwa, akawa anaogopa kuachia tena moyo wake katika umri huo ambao ni kama hakuna umuhimu tena.
Ilikuwa ni safari ya kurudishwa nyumbani kwake, iliyotanda kimya kizito garini baada ya wakati mzuri wa chakula kilicholiwa kwenye mgahawa wa hadhi ya juu. Jo alikuwa kimya akiendesha hakuwa amemjibu kitu Dorothy, na yeye akabaki kimya Moyo wake umesimama katika mpaka wa hisia, ukiangalia mapenzi kwa macho ya tahadhari. Kila kumbukumbu ya yaliyopita ikimnong’oneza hadithi za maumivu, ikimuacha akitetemeka kabla ya kutoa nafasi kwa upendo mpya. “Nijiingize tena kwenye mapenzi!?” Dorothy aliwaza. Lakini hofu ilizidi kumvuta nyuma, ikimuuliza kama safari hii atapatia au atavunjika zaidi.
Jo alipoegesha mbele ya kajumba hako alikokuwa akiishi Dorothy, hakuzima gari, akafungua mlango wa mbele na kwenda mlango wa nyuma akijua anakwenda kumpa kigari chake, lakini akashangaa anaingia garini nakufunga mlango, na kukalia wheelchair yake. Akajisogeza mpaka mbele yake, Dorothy akimwangalia hajui anataka kufanya nini.
Akamtoa viatu tena na kuipakata miguu yake. Akaanza tena kuiminya kwa taratibu, kuanzia chini ya magoti tena mpaka unyayoni. Taratibu Dorothy akaanza kutulia kwa ile faraja aliyokuwa akipata. Akajivuta mpaka mwisho wa kiti akamsikia akivuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu kama anayetua mzigo moyoni. Mwanga wa taa za nje ulikuwa ukimulika ndani kwa kiasi fulani. Kwahiyo sio kwamba kulikuwa giza hapo walipokaa.
“Sijui kwa nini, Dorothy! Umenigusa moyo wangu kwa namna ya ajabu! Sitaki kukuahidi mambo mengi, naomba tutembee hatua kwa hatua, siku mojamoja, mguu mmoja mbele mwingine ukifuata. Usiogope kwa sababu safari hii nitahakikisha hutatengwa na watu wako wa karibu. Hutakuwa nao mbali. Sitakufungia popote. Nakuhakikishia hutapoteza uhuru wako. Chochote ambacho hutataka, tafadhali uwe huru kusema hapana, hutanikasirisha. Sawa?” “Sawa.” Hapo anapapaswa miguu na kuvutwa vidole vya miguu taratibu, angeongea chochote anachomwambia.
“Basi naomba tuanze kwa kunitambulisha kwa Mill. Nakuahidi sitakuharibia. Ila kuhakikisha tupo nao upande mmoja, na asikuone wewe ni mzigo unao mtegemea yeye peke yake. Ajue na mimi nipo. Sawa?” “Sasa nikutambulishaje?” Akacheka. “Vyovyote itakavyokuwa rahisi kwako.” Akaendelea kumpapasa kidogo kisha akamuachia baada ya kumsoma na kuona ameridhika kabisa.
“Sasahivi hata nikikuacha kwenda kulala, nitakuwa na amani nikijua tupo ukurasa mmoja. Si ni sawa?” “Nashukuru kunijali Jo, asante.” “Karibu.” Akarudi kumpapasa tena. Yaani yeye mwenyewe huyo Jo, akaonekana kufurahia anachokifanya kwenye hiyo miguu, nakushindwa kumuachia, mpaka mizuka ikampanda. “Unamiguu mizuri sana Dorothy. Inatia raha kushika.” Akawa anarudia rudia kumsifia huku akiendelea kumpapasa, na kuiminyaminya.
Wote wakajua wameamshana, ila hawawezi kuachiana, hawawezi kuendelea. Jo akakazana hapo mpaka akasalimu amri. “Acha nikuage kabla sijashindwa kuondoka.” Akaanza kumvalisha viatu, Dorothy kimya ila akimshangaza vile anavyonogewa kwa mtu kama yeye!
Alimuelewa aliposimama. Mpaka akashituka. Alikuwa amesimamisha haswa. Akajidai kama hajamuona lakini wote wawili walijua kinachoendelea. Akamtoa garini alipofunga mlango akainama kumbusu pembeni ila karibu sana na mdomo, tena kwa kugandisha, Dorothy asijue anatakiwa afanyaje. Hakuna aliyewahi mbusu hivyo.
“Usiku mwema Dorothy.” Akamnong’oneza sikioni na kuongeza kiraha cha namna yake. Akacheka akijibu, “Asante na wewe.” “Ukiingia ndani ndio nitaondoka.” Akagonga, mrembo wake akamfungulia. Kalikuwa kabinti kadogo tu. Mlango ulipofunguliwa, akamgeukia, wakaagana kwa kupungiana mkono, akaingia ndani, Jo akaondoka na kumuacha na furaha ya namna yake.
Moyo Uliochoka Kuingoja Ahadi Ya Mapenzi.
Hiyo ndoa aliisubiria Pam, kabla hata ya kutungwa mimba ya Shema. Kila siku ya kusubiri ilimuongezea uzito wa ukimya, hadi hata matumaini kuanza kuchoka. Ikabaki kusubiri si kwa hamu tena, bali kwa pumzi ndefu ya subira iliyochoka na kukata tamaa.
Akamtumia ujumbe Shema. ‘Mama yako amekula?’ ‘Aliamka kuniulizia kama nimekula. Nimemwambia chakula chake na yeye kipo, lakini anasema hajisikii kula mida ile, akarudi kulala. Niende nikalale naye?’ ‘Hapana bwana Shema! Tushazungumzia hilo. Wewe lala chumbani kwako lakini masikio yakiwa kwake.’ ‘Haya.’ Huwa si mbishi, na baba yake anamjua.
Kwenye saa nne usiku siku hiyo ya jumamosi, akamtumia ujumbe baba yake. ‘Mama amekataa chakula. Sema mimi hapa sasahivi nina usingizi. Nataka nilale.’ Mill akacheka na kujiuliza huyu Pam aliyekuwa akila kama mchwa, mbona gafla amebadilika! Akajua ni homoni tu.
‘Msogezee maji ya kunywa chumbani kwake kabla hujakwenda kulala.’ ‘Tayari.’ ‘Kweli wewe mtoto mzuri. Haya. Ulale salama. Kukiwa na chochote hata kidogo usiache kuniambia.’ ‘Nitakwambia wewe sio bibi. Na sijasahau kumwambia kama na wewe unampenda sanaaa.’ Mill akacheka na kumrudishia majibu.
‘Asante Shema, akakujibuje?’ ‘Ameniambia nisiwe na wasiwasi, nikalale tu. Ila sijamwambia kama wewe umenituma. Angekasirika zaidi.’ ‘Kumbe unaakili nyingi hivyo! Usisahau kumkumbusha kumbusha.’ ‘Sitasahau baba. Na wewe ulale vizuri.’ Wakaagana, ndipo Mill naye akalala kipweke maana alishazoea mwili wa Pam hapo pembeni yake. Amshikeshike ndipo apate raha na kulala.
Miguu iliyopandisha jogoo la Joel usiku huo bila kutarajia, ni kama hiyohiyo inayompa starehe Mill mpaka kumpa mabao yasiyo na mpangilio. Akatamani awe analala siku ya jumapili aamkie jumatatu, amuoe, wakajifungie fungate. Amfaidi. Akawaza hili na lile, akapitiwa usingizi.
~~~~~~~~~~~~~~
Kwenye alfajiri ya saa kumi ujumbe kutoka kwa Shema ukaingia. ‘Mama anatapika sana. Halali. Kila saa anatapika, nilimpelekea maji, nikapitiwa na usingizi kitandani kwake. Nimeamka sasahivi namsikia anatapika tena bafuni kwake, nimemkuta amekaa chini pembeni ya choo, analia kimyakimya.’ ‘Asante Shema. Nakuja kumsaidia. Nifungulie mlango, na usimwambie.’ ‘Sawa.’ Mill alitoka kama anayekimbia moto, akiwa bado na nguo za kulalia.
~~~~~~~~~~~~~~
Shema akamfungulia mlango kwa kujiiba. “Asante Shema. Sasahivi nenda kalale. Nitakuwa naye.” Akiwa na usingizi akarudi chumbani kwake bila hata nyongeza.
Alimkuta Pam akilia peke yake, ameegemea choo. Jinsi Mill alivyojenga ni kama vyoo vya nchi aliyotoka. Huwezi kuta choo kina maji sakafuni. Unaweza hata lia chakula kwenye sakafu ya chooni. Pasafi na makapeti mazuri haswa mpaka kuzunguka choo chenyewe.
Pam akashituka sana alipoingia. “Pole.” Akainama akijifuta machozi. “Nipe mkono nikusaidie kurudi kitandani.” “Hapa nimejikojolea kwa kutapika mfululizo mpaka mbavu zinauma!” “Pole. Basi tuanze kuoga kwanza kisha urudi kitandani. Nitaenda kukutafutia dawa ya kuzuia kutapika, utapumzika.” “Kama kuna hiyo dawa, bora ukanichukulie sasahivi, nitaoga mwenyewe.” “Pam! Nipe mkono utoke hapo sakafuni.” Akamsaidia kusimama.
Wakati anatoa nguo akawa ameshafungulia maji ya moto. Akamsaidia hapo bafuni, akampa taulo, akahakikisha amepanda kitandani. “Usinywe tena kitu, hata maji mpaka nirudi na dawa. Yatakupa kichefuchefu tena.” Akaitika na kujiweka sawa kitandani. Mill akatoka kwenda kusaka dawa kwenye maduka ya dawa yaliyopo wazi mida hiyo, tena siku ya jumapili, akiwa na nguo zake vilevile za kulalia.
Alizunguka mpaka Colins akamshauri aende tu hospitalini kwao. Akiwa na nguo za kulalia akatokezea hospitalini akakuta daktari wa zamu ameshamuandalia kila kitu mpaka dripu. Akashukuru na kurudi nyumbani kwa haraka, akamkuta akitapika tena na mwanae anasubiria nje ya mlango. Palisha pambazuka.
“Anatapika sana.” “Pole na wewe Shema. Nimerudi na dawa. Safari hii atatulia. Kula, kisha ukalale.” “Na wewe nikuwekee chakula?” “Hapana. Mpaka mama yako atulie, nikafanye mazoezi, nioge, ndipo nile. Wewe kula kisha jaribu kulala.” Akaondoka ndipo akaingia tena chooni. Akamsaidia kumnyanyua tena. Kuoga na kumrudisha kitandani.
Akamchoma sindano ya kuzuia kutapika. “Sasa hii itakufanya ulale kabisa. Huna njaa kabisa?” “Naogopa hata kuweka kitu mdomoni.” “Pole. Basi pumzika. Hutatapika tena.” Akambusu mara kadhaa kichwani huku akimfunika. Akashangaa hakatai ila kujiweka sawa.
Akaanza kusinzia. “Pam?” “Nasinzia.” “Najua. Ila nilitaka kukwambia najua si wakati wake kukwambia haya. Upo kwenye maumivu, lakini jua nimejawa na furahaSANA. Hongera na asante sana mpenzi wangu.” Pam alishituka mpaka akageuka.
“Nimefurahi Pam, nimefurahi sana.” “Kweli!?” “SANA. Umri umekwenda mwenzio nimebakiwa na katoto kamoja tu! Nilikuwa sijui jinsi ya kukuomba mtoto mwingine kwa kuwa ndoa haikuwa imekamilika. Ila Mungu amenikumbuka Pam! Nimefurahi SANA.” Akavuta Pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu akajirudisha ndani ya shuka vizuri.
“Nakupenda Pam. Nakupenda sana. Nahisi mimi ndio nina shida ya kukuoa kuliko wewe. Nisamehe kama nilionekana nakukatili ile siku ya ijumaa. Ila si kwamba sitakikukuoa. Na mimi sifurahii hivi Shema anavyotuangalia tukiishi bila ndoa. Sipendi na nahangaika kubadilisha hilo. Na kabla hata huyo mtoto hajazaliwa, tutakuwa tumekamilisha. Naomba uniamini.” Akamuona anatingisha kichwa kukubali. Mill akatafuta mdomo ndani ya shuka akambusu tu kwa juu.
“Pumzika, acha mimi nikafanye mazoezi, nioge, nitarudi kukaa hapa na wewe.” “Asante.” “Karibu.” Mill akaondoka akiwa amejawa furaha huyo! Shema yeye alirudi kulala baada ya utulivu hapo ndani. Mama yake akalala kama mfu. Kausingizi kamimba na dawa vilimchukua, alilala Pam asijue alipo.
Kaonja Asali, Anataka Kujenga Mzinga.
‘Sijapata mwaliko rasmi mpaka sasa.’ Ujumbe ukaingia kwenye simu yake. Akacheka. ‘Za asubuhi?’ Akampigia. Akapokea akicheka. “Nimelala nikiota, nikaona nikuchokoze nijue kama uliamka salama.” “Nililala vizuri na nimeamka salama. Na wewe?” “Nimekumiss. Natamani kukuona.” Akacheka kwa furaha.
“Baba na mama wanakaribia kufika. Nimetoka kuzungumza nao. Natamani kwenda kuwaona.” Kimya upande wa pili. “Kaka amejitolea kuja kunichukua.” “Mbona unanitoa umaana bwana?” “Sikutaka kukusumbua.” “Au hutaki nionane na wazazi?” “Hata usingekuwepo, habari zako zimeshafika kwa mama.” Kwa hakika hakutegemea.
“Kweli!” “Sijawahi pata mtu akanijali kwa kiasi chako, Jo. Mill ananisaidia sana, ila najua ni kwa kupitia Pam. Ila mimi kama unavyosema mwenyewe, Dorothy, sijapata na zaidi nikiwa kwenye hali hii! Hakuna Jo. Baba yao kina Eric aliishi na mimi kama mtumwa, akinisaidia tu.”
“Wengi wanao nitongoza pale dirishani wanavutiwaga na juu tu, wakishagundua jinsi nilivyo, wanakimbia. Lakini wewe umebaki! Umetengeneza mpaka gari yako kwa ajili yangu!” “Ushaharibu siku yangu. Kumbe unajijua kama unavutia na unapata wakukutongoza pale!” Hakutegemea Dorothy. Alicheka, alicheka sana.
“Mimi nakwambia mambo ya msingi!” “Hapana bwana Dorothy! Wewe unataka kuniua kwa pressure! Kwangu ulijidai wewe kama si kitu! Eti wewe huvutii, ili kunitoa njiani, kumbe kuna msururu! Ile kazi pale ishaanza kuninyima raha.” Dorothy hana mbavu.
“Mimi sitaki upinzani Dorothy.” “Huna mpinzani bwana!” “Unauhakika?” “Kwa asilimia zote. Nani anataka mtu kama mimi?” “Umetoka kusema nini sasahivi?” “Wale wanaishia mwanzo tu. Wakishajua ni mlemavu wanakimbia. Hakuna mtu anataka kuongozana na shida, ndio maana unanishangaza.” “Kama wewe ndio shida, basi waambie walimwengu waniachie shida yangu.” Alikuwa akicheka mpaka kwa sauti.
“Shida wewe, nakutaka. Tena ubakiwe kuwa wangu tu.” Dorothy anacheka hana mbavu ila kwa hakika akimfurahisha na kumfanya ajisikie wamaana. “Nakutaka ulivyo Dorothy. Umeamsha hisia kali, najua jana uliona.” Hapo alicheka mpaka akajifunika uso. “Unanicheka Dorothy?” Akazidi kucheka. “Na hapo ni kukushika tu miguu! Hakika sitaki mwingine akushike tena.” “Yale mazoezi je?” Akamkumbusha akicheka. “Nitasimamia mwenyewe. Sio tena na wao waponee hapohapo.” Akazidi kucheka.
“Kwa hiyo huna shida nikikutana na wazazi leo pamoja na kaka yako?” “Ningefurahi Jo. Ningefurahi sana. Ingeniongezea furaha zaidi.” “Basi acha nijiandae nije. Na uache kugawa majukumu yangu.” “Ya udereva?” “Ndiyo.” Akazidi kucheka.
“Asante Jo. Ujue nakusubiri kwa hamu.” “Nakuja Dorothy. Tutapata muda wetu, ndio tunakwenda kwa wazazi.” “Kweli?!” Hakuwa akiamini kama anaweza pata mtu akamuhitaji hivyo.
“Nataka nikae na wewe kidogo. Na leo lazima nikukiss.” “Kama jana?” “Hapana bwana Dorothy! Kissing ya kweli.” “Mwenzio sijui!” “Niandalie midomo, nakuja kukupa shule, utafurahia. Ila usijenogewa tu.” Alicheka Dorothy, alicheka sana. “Nakuja na usiache kunitambulisha kwa Mill.” “Nampigia sasahivi.”
~~~~~~~~~~~~~~
Ni nini kitaendelea kwenye kila familia?
Love ta first sight!
0 Comments:
Post a Comment