“Asante kaka yangu kwa kunijali. Na mwambie wifi nashukuru. Anisaidie tu, mimi nitamlipa. Na hiyo ya baba ni kiasi gani?” Akamtajia.
“Basi acha nikurushie hiyo pesa, kaka. Tutaondoa aibu.” “Au tuchangie. Utoe nusu na mimi nusu. Sitaki uanze kuonekana mzigo huko ukweni.” Akamuhurumia mdogo wake. “Hapana kaka, sitakuwa mzigo huko ukweni. Ni ya Pam. Amenipa nishike mpaka nitakapojiweka sawa, usiwe na wasiwasi. Pesa ipo. Sijawahi tumia hata mara moja, yaani leo ndio kwa mara ya kwanza katika hili lamuhimu. Na uzuri inatoka kwa mwanao Pam, hakuna aibu.” Wakacheka wakitaniana kisambaa hapo, mwishoe akamtumia hiyo pesa. Jo akisikiliza tu.
Wema Haujawahi Kuoza. Hata Ukifanya Sirini, Ipo Siku Utavuna Tu.
“Naona kaka na wifi wameshafanikisha mavazi ya wazazi. Hatuna haja ya kwenda tena madukani.” “Twende tu, unaweza na wewe ukapata kitu kizuri hata kwa ajili yako. Kisha twende tukale. Sio mbali nilipoelekezwa, tunakaribia.” Akaendelea kukanyaga mafuta akiwa anaendesha na abiria wake amekaa kiti cha nyuma.
“Joel?” Akawa kama ametoka mawazoni, amekumbuka. Akamwangalia kwa kutumia kioo cha katikati ya gari. “Umesema dada yako ananifahamu?” “Yeye ndiye aliyekuona kwanza. Akaenda kumwambia mumewe kuwa amenipatia mke.” “Jo!?” Akashituka sana.
“Ipo jinsi ulicheka alikusikia, na kumgusa. Aidha ukiwa unamuhudumia au akiwa pembeni ya pale akikusubiria umuhudumie ambapo napo alisema ulimkarimu vizuri sana na kumuombea yeye mwenyewe nguvu na faraja kipindi hicho anachouguza.” Akabaki akijaribu kukumbuka, maana anakutana na watu wengi pale, waume kwa wake, na huwa anazungumza na kila anayefanikiwa kumuhudumia.
“Anavyosema yeye dada, alisikia kicheko kisicho hila. Kinachotoka ndani ya moyo msafi unaweza mpokea mtu wa namna yeyote na kufanyika faraja hata kwa mtu aliyepondeka moyo. Halafu hiyo rangi yako ndiyo iliyomthibitishia eti mimi sitakuwa na ujanja.” “Jo!?” “Hayo ananiambia shemeji! Sasa yule naye muongeza maneno kunogeshakila jambo lake akitaka kulizungumza.”
“Maana pale alikuwa amelazwa na ukuwadi alikuwa akifanya. Nilimpigia simu kumjulia hali, maana alipelekwa hospitalini gafla, nilipopata tu habari nikampigia. Asianze yake ya ugonjwa, akaanza habari alizoambiwa na mkewe. Akaniambia ule ugonjwa Mungu alimpa ili mimi nipate mke. Nikamuuliza kwa nini mpaka augue yeye, ndio mimi nipate mke? Akaniuliza eti mimi daktari nisiyetaka kutibu wagonjwa hospitalini mpaka maporini au vitani, ningeonaje watu wa hospitalini kama si yeye kuwepo pale?” Dorothy akacheka ila bado akisikika na wasiwasi.
“Mimi nikampuuza maana swala la kuoa kwangu hajaanza leo. Ndio akaniambia safari hii si yeye ni dada. Bado nikampuuza. Ndio nikamwambia anielekeze alipolazwa, ndio akanielekeza eti ulipo wewe, wewe ndio unielekeze alipolazwa yeye. Na kama sitaki eti nisiende kumuona. Sharti la kumuona yeye eti ilikuwa ni lazima nipite kwanza kwako, nikikuona ndio niende tukazungumze.”
“Sasa ukamwambia nini?” “Niliwakuta wote wawili wananisubiria maana nilikuwa nao kwenye simu mpaka nashuka garini, hawataki kunielekeza walipo eti wewe ndio unielekeze. Nilipofikishwa na Stella, wakanichangia wote kuwa eti sio yeye.” “Kwani Stella aliingia mpaka ndani!?” “Na kuwasalimia kabisa.” Akashangaa kidogo ila akaamini kweli Stella alichanganywa na Jo.
“Alipoondoka tu mpaka dada akanivamia. Nikawaambia wasipandwe pressure, nilikuona lakini Stella ndiye aliyejitolea kunileta. Swali likawa kwa nini? Nikawaambia yote niliyoambiwa na Stella. Nikadhani yatawarudisha nyuma. Lakini nikashangaa wanaanza mipango ya harusi.” “Ya nani sasa?!” “Yangu na wewe.” “Jo!?” “Wewe hutamuweza shemeji yangu. Mwishoe ndio nikawaambia lakini sijapata jina lako, na wala sijajua kama huna mtu wako. Ndio dada akasema maadamu mbea wangu hajamtaja mume, eti utakuwa huna mume, mimi nikazane tu. Eti nitapona mengi.”
“Nini tena?” “Shemeji akadakia eti kwa jinsi alivyosimuliwa na mkewe, giza la mjini nitalisikia kwao tu wanaosubiria mgao, eti kwangu mimi wakati wote patakuwa pakiwaka kama mchana. Namuuliza mchumba anakuja na jenereta? Anasema eti unawaka kama jua la adhuhuri.” “Jo!” Akashituka huyo Dorothy asiamini, kama huko kwao ndivyo anavyozungumziwa.
“Huwawezi wale kwa maneno na dada anakuwa akisaidiwa kuyapanga na mumewe. Kusudi tu wakijua weupe mimi ndio udhifu wangu. Mpaka naondoka siku ile, hakuna kati yao aliyetaka kuzungumzia maswala ya ugonjwa ila taarifa zako. Mwishoe nikaona nijisomee tu chati yake na kuzungumza na daktari.”
“Wanae wanampigia simu kumjulia hali, anawaambia wanae hali ya mjini ni mjomba wao kapata mke. Waandae nauli za kuja harusini.” “Jo! Watoto wake wako wapi?!” “Nje ya nchi na usifikiri ni watoto wadogo! Watu wazima tu, na hadhi zao. Walioona wadogo wale na kuzaa mapema, ile ya mchana na usiku. Watoto wanapishana mwaka mmoja mmoja, wakwanza mpaka wa mwisho. Walizaa watoto watano. Na wote waliwaacha hukohuko na wao wanafamilia zao.”
“Tumerudi sisi tu. Tuliamua kuja kustaafu huku nyumbani. Kwa hiyo hapa tupo sisi tu watatu. Kaka zangu wawili wanaomfuata dada, wao na ndugu asilimia kubwa ya shemeji, nao pia wapo hukohuko wamekataa kuja kustaafu huku.” “Kwa hiyo wewe ndio wa mwisho kwenu?” “Mimi ndio mdogo wao, na ndio maana nipo sana karibu na dada, ni kama alinilea yeye tokea mama aondoke hapa duniani.”
“Sasa watoto si watakuwa na wasiwasi na baba yao wameshindwa kumjulia hali?!” “Wanamjua baba yao, huwa hapendi kutoa habari mbaya. Hata kama isingekuwa wewe angetafuta habari ingine ya kuzungumzia, ilimradi tu asizungumzie ugonjwa wake. Yaani wewe umekuja wakati muafaka, kutoa ile hali ya wasiwasi ya ugonjwa wake. Umekua kama kinga kwake. Ndio ikabidi sasa baadaye wanipigie mimi kumjulia hali. Sasa mimi kwa sababu ni daktari nikifika huwa nazungumza na madaktari wote waliomuhudumia na kusoma chati yake kama nilivyokwambia, basi mimi ndio huwa nawajulisha watoto wao na ndugu.”
“Maneno mengi. Mipango mingii, hutamuweza. Tokea dada amwambie habari zako, akaanza kuaga pale kwa madaktari anawaambia anatakiwa kutoka pale kwa haraka yeye anamipango mingi sana yakufanya na harusi ya kuandaa.” Dorothy akapoa kama anayewaza kitu.
“Sasa unawaza nini? Nimekutisha?” “Sana! Ila sasa wewe mwenyewe uliwaambiaje?” Akataka kujua zaidi maana alikuwa akizungumzia habari za shemeji yake na dada yake juu yake. “Dorothy, kama mimi mwenyewe sikuvutiwa na wewe, nisingerudi pale mara mbilimbili!” Akamjibu akimwangalia kupitia kioo cha mbele. Akainama.
“Nilirudi kwa sababu safari hii nahisi wamepatia.” Akakunja uso kama ambaye hajamuelewa. “Nitakwambia vizuri wakati tukila. Na kuhusu hawa wawili pia usiogope kabisa. Hivi leo ni kwa sababu nilitaka tu muda na wewe. Lakini wangefurahi sana kama tungeenda kwao. Na ukikutana naye yeye mwenyewe shemeji, ndio hutakuwa hata na nafasi ya kuwaza ila kumsikiliza yeye na hamalizi porojo.”
“Na yeye ndiye aliyenipa huyu fundi aliyenisaidia kutengeneza hiyo sehemu yako ya kukaa hapo nyuma. Yeye ndio kama mwenyeji wangu hapa nchini. Walitangulia kuja, nikawafuata. Anajuana na mpaka machinga. Na huwa hasahau mtu na mpenda watu sana. Kwa hiyo huyo Dorothy unayesaidiana na wenzio kumzika, hazikiki. Uzuri huo haufichiki. Sema asante.” Akamfanya aanze kucheka.
“Hilo cheko ndio lilimvutia dada yangu.” Akazidi kucheka. “Dorothy unaonekana wewe ni mwema sana aisee! Nataka kukufahamu zaidi.” “Mbona nimeshakwambia kila kitu!” “Cha mama Eric, ndiyo. Nataka habari za Dorothy mwenyewe. Acha tushuke, tufanye manunuzi, tukae mahali tule tukizungumza.” Akatafuta pakuegesha gari walikuwa wameshafika.
Akafungua mlango, akamsogezea kabisa wheelchair yake, akahamia hapo kirahisi na kushuka garini bila shida. Alikuwa akifurahi huyo Jo. “Hivyo ndivyo nilitaka kukuona ukiingia na kutoka garini. Sio vile ukijitesa.” “Unanianzishia starehe za muda mfupi hizi!” “Si lazima sikawa za muda mfupi.” “Mwenzio naenda kazini kila siku za kazi na kanisani. Magari ninayotumia ndio kama vile ulivyoona! Na si yangu. Hawawezi kufanya hichi ulichofanya wewe.” “Mimi sina kazi. Nimestaafu. Nitamuomba Mill kazi ya kukuendesha wewe.” Alimfanya akacheka sana.
“Mimi nitakuwa dereva mzuri sana.” “Yaani dereva wewe unapewa kazi na gari ni yako pia?” “Kabisa. Subiri.” Akashangaa anafungua mlango wa nyuma. Akatoka na ubao mwingine akaulaza chini kutengeneza kama daraja kuingia kwenye hilo duka ambalo kweli lilionekana lina nguo za wanawake. Alipoangalia vizuri ni kweli asingeweza kupanda bila hivyo au kama angekuwa Pam angelazimika kumnyanyua kwa shida sana. Huwa kama akishindwa, anamrudisha mama yake garini anaanza kumletea vitu ndani ya gari achague.
“Sasahivi unaweza kupita.” Ilimgusa Dorothy mpaka akapoa usoni. “Twende. Hii itakurahisishia. Utakuwa ukipita hata sehemu zenye ngazi au mfereji, bila shida.” Akamgusa akimpapasa begani kama kumwambia utakuwa sawa usiwe na wasiwasi. Akapita kiurahisi bila shida, akiwa amepoa. Alipopita akakichukua na kukirudisha garini. Akafunga na kumfuata pale alipokuwa akimsubiria.
Wakaingia. “Ni kama hapa nilishawahi kufika na Pam!” “Basi ukiona kitu kizuri hata chako, chukua. Sio lazima uwe kwamba hicho kitu uwe huna! Hata kuongezea. Ona hizi nguo nzuri za kulalia.” “Mimi nilijua ni kwa ajili ya harusi!” “Sikukwambia na sisi tutakuwa tukiponea hapohapo? Yaani wakati tukitatua ya kwao, basi nasisi tunaponea hapohapo. Usijipunje. Wewe niambie rangi unazopenda, nakuwa nikikuonyesha. Kama hii hapa.” Wakaanza manunuzi.
Bwana alimchagulia mapigo ya nguvu ya kulalia! Nguo nzuri sana za kulalia, nywepesi, hata hakuwa kuwa nazo. Halafu very sexy. Akamtia aibu kwa manunuzi ya chupi pia. Nzuri na za thamani. Wakapata tena nguo za mama yake. Kisha akamchagulia nguo nyingine, nzuri haswa, na bei kubwa, tatu za kanisani.
“Umependa?” “Sana ila sikupenda ulivyolipia. Nakutia garama isiyo sababu!” “Kwa hiyo kulipiwa na mtoto ndio sawa?” “Pam…” “Sio jukumu lake.” Akamkatisha. “Pam huyohuyo alipie bibi na babu zake. Halafu na wewe pia! Kweli wakwe watakuchoka. Utakua mzigo.” Akacheka na kunyamaza, Jo akiendelea kuendesha akitafuta njia ya kuwapeleka kula.
Dinner Time. Kujuana Zaidi.
Akamfikisha kwenye mgahawa mzuri, akamsaidia kushuka kama alivyofanya wakati wote. Kirahisi tu. Akaonekana hapo yeye ni mwenyeji. Akamuongoza njia mpaka ndani, muhudumu akawasindikiza pakukaa.
“Sasa nitolee viti vyote nibakishie kimoja tu.” Muhudumu akafanya kama alivyoambiwa na Jo, akamuelekeza Dorothy pakuweka kigari chake. Asikae mbele yake, akaenda kukaa pembeni yake. “Hapa mbali na chakula, huwa nafuata juisi ya embe. Nzuri sana. Ila pia wanajuisi ya nanasi, pia ni nzuri.” “Nitakunywa utakachokunywa.” Jo akacheka kwa kuridhika akaagiza juisi mbili za embe. Muhudumu akaandika na kuondoka.
“Wanavyakula vizuri sana. Angalia kitu unachopenda kula.” “Ni nini kilimpata Betty?” Jo akamwangalia maana macho yalikuwa kwenye menu. “Betty?” Akarudia swali. “Aisee kuna mlevi mmoja, tena kijana mdogo tu ndiye aliyemuondoa Betty hapa duniani kwa ajali ya gari. Tena ilikuwa siku mbili kabla ya siku ya Christmas. Tulikuwa wote nyumbani. Jioni tu. Akatuaga kuna kitu cha mwisho anakwenda kununua kukamilisha zawadi za majirani. Maana tulikuwa busy sana kazini, tukachukua off siku hizo ili kuwa na watoto.”
“Nikamuuliza kama angependa nimsindikize maana tulikuwa tukiangalia mpira na watoto. Akasema mimi niendelee kukaa na watoto, hatachukua muda mrefu, anarudi. Alikuja kumgonga akiwa anarudi, kona ya mwisho kabisa kuingia nyumbani, tena kijana wa hapohapo mtaani. Sitakaa nikausahau ule usiku. Aisee ulibadilisha maisha yetu sisi wote watatu, kabisa.” “Pole Jo.”
“Ilikuwa mbaya sana. Majirani walikuja kutuita, tunafika eneo la ajali na ambulance ndio inamtoa kwenye gari hana fahamu. Watoto wanalia, mimi nimepaniki napigia simu kila mtu atusubiri hospitalini nikiwaambia nakuja na Betty, nahitaji kila mtu awepo kumsaidia. Tunafika hospitalini tukakuta madaktari wamejaa wanatusubiria. Waliitana mpaka madaktari waliokuwepo nyumbani walikuwa wanamiminika hapo kumsaidia Betty. Lakini Betty alifia kwenye meza ya upasuaji. Na uangalizi wote huo. Madaktari wote hao bingwa, lakini Betty hakufanikiwa kutoka chumba cha upasuaji.”
“Ulikuwa ni msiba kwa kila mtu aliyekuwa akimfahamu Betty pale hospitalini. Madaktari kwa manesi. Wafagizi na askari. Maana mimi na yeye tulikuwa madaktari kwenye ER yaani Emergency Room. Tuna deal na Trauma cases tu. Tulifanya kazi pale na watu vizuri sana.”
“Siku nilipo mtoa pale Betty kwa mara ya mwisho, sikuweza kurudi tena pale kwa zaidi ya miaka 5. Nilishindwa kurudi kabisa pale. Yaani kijana wangu mkubwa ndiye aliyekwenda pale na kumalizana nao kisheria, kwa niaba yangu na Betty. Maana yeye ndio tulimwandika kama msimamizi wetu endapo chochote kikitokea kwetu.”
“Mafao ya mama yake na yangu akamalizana nao yeye mwenyewe. Nilikuwa siwezikukaa sehemu ambayo tulikuwa na Betty. Nilikuwa kama narukwa akili, naweza nikajikuta nikimuita nikidhani nimemuona hapo. Nikajua nisipofanya mabadiliko ya haraka, nitafungiwa hospitali ya vichaa. Ndio nikahama mpaka nchi. Kule kuwa kwenye mazingira magumu na kufikiria wengine ndio ikawa dawa yangu.”
“Sasa aliyemgonga alikamatwa?” “Alikuja kutolewa na yeye kwenye gari wala hajitambui kwa kulewa. Aisee nilikuja mfuata jela kabla sijaondoka nchini.”
“Nilimueleza vile alivyotukatili mimi na watoto wangu. Alivyoondoa msaada mkubwa kwa wagonjwa pale kwenye ile hospitali. Maana Betty alikuwa daktari mzuri bwana! Halafu akapewa roho ya kujali! Akiwa kazini wakati mwingine nilikuwa inabidi kumbeba kwa nguvu kumpeleka mahali ale hata kwa dakika tano, vinginevyo alikuwa hajui kukaa chini.”
“Sasa ubaya na pale tulipokuwa tukifanya kazi, wakati wote pako busy, asilimia kubwa ya kila anayekuja pale ni mgonjwa anayehitajika uangalizi wa haraka, basi walimjua Betty. Mpaka wakati mwingine walikuwa wakinitafuta pengine kwenda kumtoa mahali akapumzike! Na yote hayo nilimwambia yule kijana. Basi, ndio Betty huyo. Kunywa hiyo juisi uniambie kama umeipenda au tuagize ya aina nyingine.”
“Mimi si mchaguzi wa vitu. Nakulaga kila kitu labda kiwe kimeharibika.” Akainywa, na kuipenda. “Nzuri. Hiki kiladha cha ndimu kidogo imeongeza ladha ya kipekee.” “Basi ndio nilitaka uipate hiyo ladha. Mimi naipenda sana.” Wakaagiza chakula.
~~~~~~~~~~~~~~
Akamuona anacheka kama anayefikiria. “Huko mawazoni umefurahishwa na nini?” “Nikikwambia usifirie vibaya.” “Nini?” Akacheka tena kidogo akamwangalia. “Sasa unacheka nini, Jo?” “Unakumbuka jana ulivyopanda kwenye gari na mimi nikawepo?” “Nakumbuka.” “Nilikuona, unamiguu mizuri sana. Halafu inaonekana laini kama ya mtoto mchanga, nikawa natamani tu kuishika.” Akamuona kama amebadilika na kujifunika zaidi.
“Hii miguu haina kazi, Jo. Ipo hivyo sababu imegoma kutumika kwa chochote. Haina kazi kama kweli ya mtoto mchanga. Haina maana yoyote.” Akajifunika zaidi na zaidi.
“Kuna vitu vingine tunanunua kwa thamani kubwa, tunaweka ndani kwa ajili ya kupendezesha tu.” Akamwangalia. “Au niambie zile kuta au rembo zinazoongezwa kwenye majumba haya ya thamani, yana kazi gani kama si kuongeza urembo tu kwenye jengo? Lakini hiyo miguu kuwepo hapo ni zaidi ya urembo na kutufurahisha sisi watizamaji. Ikija kukatwa leo, utaona tofauti yake na utagundua kumbe ina kazi yake japo haifanyi kile unachotaka wewe.” Hakujibu na akawa amegeukia mezani.
“Ulisharudi tena hospitalini baada ya matibabu ya mara ya mwisho?” “Hapana Jo. Nilitoka hospitalini baada ya huo upasuaji, nikakaa siku tatu, ya nne nikarudi kijijini nikiwa na baba na mama. Nikauguzwa kidonda mpaka nikapona. Nilipona vizuri tu bila shida na kuweza kurudisha uwezo wa kuzuia choo. Basi.”
“Hapakuwa na uwezo au na hiyo nafasi ya kuendelea na matibabu mengine. Hata hayo matibabu ya kwanza kaka alijitoa sana. Sikuwa na bima ya matibabu. Ilibidi aingie mfukoni na baba akauza shamba, akamsaidia kulipia. Kwa hiyo hakuna aliyekuja zungumzia tena matibabu mengine zaidi ya kushukuru kwa kile kilichopatikanika.”
“Naomba kukugeuza na niiangalie.” Akajua anaionea aibu. “Nataka kuishika. Halafu niambie kama unasikia kitu. Ni sawa?” Alipomuona anatoa lock kwenye kigari chake akajua anataka kugeuka. Akafanikiwa kumgeuza. “Nitaipakata.” Bwana Dorothy alishituka. “Hapahapa!?” Akafanya kuangalia na watu waliopo jirani yao na giza lilishaanza kuingia.
“Ndiyo.” Akamjibu hivyo na kuinyanyua yeye mwenyewe. Na kumtoa viatu, Dorothy akimtizama. “Bwana hii miguu ni mizuri! Mpaka nyayo ni lainiii!” “Haina kinachofanya, haigusi chini. Ipo tu!” Akaanza kumpapasa juu mpaka chini akiiminyaminya.
Alipomuona ni kama anasisimkwa, akajua anasikia jinsi anavyomshika. “Kumbe hisia zote zipo!” “Sio kama mikono au sehemu nyingine ya mwili.” “Na hudhani ni kwa sababu ni sehemu iliyosahaulika kwa muda mrefu ndio maana? Kuna usemi wanasema hivi, na huwa tulikuwa tukiwaambia wagonjwa zaidi waliokuwa na matatizo ya viungo.” “Ulikuwa ukiwaambia nini?” Akamwangalia maana hapo alikuwa akimpapasa kwa hisia zote mpaka akamshangaza vile anavyoonekana kufurahia anachomfanyia huyo Dorothy.
Akaanza kumminya nyayo hapohapo kama anayemfanyia masaji akiwa amejivuta nyuma, miguu yote miwili ameipakata katikati ya mapaja. “Kwa tafasiri nzuri ni kwamba, usipokitumia, unakipoteza kabisa. Kiungo chochote usipokitumia kinazidi kupoteza nguvu. Ulitakiwa kufanyiwa mazoezi baada ya ule upasuaji kama kushitua misuli na kuikumbusha kazi yake. Tatizo ulilopata si geni Dorothy, ila ilihitajika matibabu mazuri na uangalizi wa karibu.” Hayo anaongea macho kwenye miguu.
Akawa akipitisha mkono mpaka chini ya goti halafu anashuka mpaka chini kwenye nyayo, taratibu kisha anavuta kidole kimoja mpaka kingine. Taratibu ila eti yeye mwenyewe akaonekana kama ananogewa na anachofanya. Akapotea kabisa na kumfanya na yeye Dorothy kutulia akisikilizia ile mikono. Akajivuta vizuri akaegemea kijigari chake, akatulia. Pakazuka ukimya hapo, kila mmoja akiwaza lake.
Alimfanyia hivyo kwa muda mpaka chakula kikaletwa. “Acha niivalishe viatu, ili na wewe ule.” “Kama hutajali, naomba iache tu hapahapa. Unamiguu mizuri sana. Inatia raha kushika.” Mpaka muhudumu akaiangalia hiyo miguu ya mlemavu inayosifiwa. “Mnawishe yeye kwanza.” Akamtoa kwenye kushangaa. Akageuka walipogeukia wao, akawanawisha wote mikono na kuondoka.
Jo akawa anakula huku anampapasa miguu. Ilibidi na yeye Dorothy achukue sahani yake kutoka mezani aishikilie mbele kule alipogeuzwa maana huyo Jo hakuonekana kama anatambua tena ustaarabu wa meza. Akashindwa kumuachia.
~~~~~~~~~~~~~~
“Jo?” Akamtoa huko alikokuwa akila huku akimchezea miguu. “Nikikukaribisha kwenye harusi ya Pam, utaweza kuja au utakuwa na mambo mengi?” “Si ndio kazi ya udereva imeanza rasmi leo, au?” Akamfanya acheke sana. “Bwana si kwa sababu ya kuniendesha! Nataka uje kama mgeni wangu.” “Nitafurahi Dorothy. Nitakuja. Na mwambie Mill akitaka msaada wowote ule kufanikisha harusi yao, aniambie. Hata kama si mimi moja kwa moja, ila najua dada anafahamiana na watu. Huwa wanae wakija mchini anafanyaga tafrija nzuri sana.” “Kweli Jo? Sio usumbufu?” “Hata kidogo.”
“Hatuna tunachofanya, Dorothy. Sisi wote, tupo tu. Tulikuwa tukifanya sana kazi huko ugaibuni, acha tupumzike. Tunakazi ya kuzurula tu kila mahali maana hatuna tunachokifanya. Na ndio yalikuwa malengo yangu na Betty. Tufanye kazi kwa bidii, halafu tustaafu mapema. Tupumzike. Tutembelee nchi na miji mbalimbali kabla uzee haujatuweka ndani.”
“Sasa, sasahivi nazunguka na dada na mumewe.” “Nyinyi mnaonekana mpo karibu sana.” “Sana. Siku tatu kabla hajalazwa pale hospitalini tulikuwa nchini Italy. Sisi, halafu watoto wao na wangu wakaja kuungana na sisi. Tulikaa nao kama siku nne, wakaondoka sababu ya kazi. Sisi tukaongeza siku tatu mbele ndio tukarudi nchini. Kwahiyo kujibu swali lako, sisi wazurulaji tu. Au mimi mzurulaji tu.”
“Na nakuibia siri. Naenda nao hao wawili pia kwa ajili ya dada. Wameshakuwa watu wazima sana. Najidai kuwa nao ila pia nia nikuhakikisha wanaungalizi mzuri na wakaribu wa kidaktari.”
“Kuna kipidi dada aliugua sana.” “Nini?” “Utuuzima tu. Vikaanza vitu vidogo vidogo. Akipona hiki kinaanza kile. Ikabidi turudi Marekani kwa matibabu kwa sababu sisi wote tulistaafia kule, kwahiyo tuna uwezo wa kupewa matibabu kule. Tulikaa kule karibia miezi mitatu, alipopona na kufanyiwa mazoezi mazuri, akarudisha uwezo mzuri wa kujitegemea, tukarudi tena. Kwa hiyo nikikwambia tupo, tupo tu.”
“Tukishakaa hivi, kama wote tupo sawa, huwa tunasafiri tena. Wanatuita wazurulaji.” Wakacheka. “Anza kwa kunitambulisha kwa Mill kama vile Pam alivyoniona. Halafu mwambie umenipa kazi ya udereva.” Alicheka Dorothy, alicheka sana. “Akija kukuona dereva mwenyewe, atajua nimemtapeli!” “Tunampa ushahidi wa gari. Kwamba lipo maalumu kikazi. Hatujamtapeli.” “Sawa. Kesho nitazungumza naye ajue na mimi nitakuwa na mgeni wangu.”
Yeye akala chakula chake mpaka akamaliza. “Jo, huli! Ona mpaka chakula kitakuwa kimeshapoa!” Akacheka akikiangalia chakula chake. “Nafurahia muda na wewe Dorothy.” “Kwa nini sasa?!” “Hata sijui! Nahisi dada alikuwa sahihi. Unamoyo mzuri wa kumfanya aliye pembeni yako naye apate faraja. Umeshiba?” “Vizuri tu. Ila nataka kutumia choo.” “Acha nikupeleke.” “Usiwe na wasiwasi nitaweza tu. Wewe omba wakupashie moto chakula, ule. Nitarudi.” Akachukua viatu na kuanza kumvalisha mguu mmoja baada ya mwingine. Akamuweka gauni sawa, Dorothy akimwangalia.
“Twende.” “Tunaenda wote chooni?!” Hakujibu ila akasimama kabisa na kusogeza meza pembeni kidogo ili apate nafasi ya kupita, kisha yeye mwenyewe akaongoza njia kabisa. Dorothy akaanza kumfuata nyuma.
Akaongoza njia mpaka chooni. Akaingia kwanza yeye akimshangaza Dorothy. “Sio pachafu.” “Na pia Pam amepewa na Mill anipe kitu chakupuliza kabla sijakaa. Nitakuwa sawa.” “Hutahitaji msaada wowote?” “Hapana. Nipo sawa.” Akatoka kumpisha. Ndipo akajisaidia, nakutoka akamkuta akimsubiria hapo nje ya choo cha kike.
“Hujala Jo!” “Nitakuwa sawa. Niambie, umeshatosheka chakula au unataka kuongeza kitu kingine, juisi?” “Nipo sawa. Twende ukale kabla hatujaondoka.” Wakarudi mezani.
~~~~~~~~~~~~~~
Akamuita muhudumu. Akaagiza supu mbili. Akamtajia aina ya supu anayotaka atengenezewe, muhudumu akaondoka. “Nilikwambia nimeshiba!” “Nataka uionje tu. Wanaitengeneza vizuri sana. Dada huwa anaipenda kuinywa kabla ya chakula. Nzuri sana. Ametuambukiza sisi wote tunaipenda. Na si nyingi. Wanachanganya mbogamboga na nyama za baharini. Utaona.” Akavuta pumzi kwa nguvu na kuishusha kisha akamgeukia.
“Naomba uanze mazoezi ya viungo, Dorothy. Itakusaidia sana.” “Jo, hivi unajua nimeletwa hapa mjini muda si mrefu na nimeletwa kwenye kazi! Siwezi anzisha mambo mengine wakati nao wana yao hata hawajatulia! Nitaonekana msumbufu nisie na shukurani, nataka kuongeza garama bila sababu, mimi sina Bima!” “Tutajipanga vizuri, usiogope. Nataka utayari wako tu. Basi. Na jua itakusaidia sana, na utaona tofauti. Nimeshika miguu yako, ipo na uhai kabisa, ina senses zote. Utaona tofauti.” Dorothy akavuta pumzi kwa nguvu na kunyamaza.
“Nataka utayari wako tu. Jua utakuwa na mimi ambaye pia ni daktari na najua ninachozungumzia. Unafikiri ni kitu upo tayari kufanya?” “Ningefurahi Jo. Lakini..” “Lakini zoote, Muda wa kufanya hayo mazoezi, ruhusa huko kazini, mahali pakufanyia, pesa na lakini nyingine zote, zitajijibu kwa wakati wake. Nimefurahi kukubali kuanza kuchukua hatua. Naomba nitambulishe kwa Mill, nitapanga naye.” Akamwangalia kama anayemuuliza unauhakika?
Juu Ya Dorothy.
“Dorothy, najua ninachofanya. Usiogope.” “Na kesho hutaamka ukajuta? Maana nahisi ni kama ndicho kilichompata baba yao kina Pam! Jamani yule mwanamme alinigeuka vibaya! Hakika nilikuwa nikijiuliza, yuko wapi yule mwanamme aliyeenda kupiga magoti kwa baba yangu anioe, kwa ahadi kemkem na yule niliyekuwa nikiishi naye!” “Pole Dorothy. Pole sana.”
“Alinigeuka vibaya sana. Kupita nitakavyokwambia! Halafu nilikuwa mdogo Jo! Ni kama alinichagua kuniadhibu bila sababu, halafu sikuwa na hatia! Alinitoa chuoni, na nyumbani kwa wazazi wangu, akaenda kunifungia Ruvuma! Kisha akawa kama aliyelazimishwa kuishi na mimi! Akaishi na mimi kama niliyemkosea! Hapana Jo, kabla hujaweka ahadi yeyote kwangu, naomba ukajitafakari kwanza na ujiulize. Kwa nini mimi Dorothy mlemavu ambaye utawekeza muda wako mwingi kwangu na si kwa mtu mwingine? Tafadhali Jo.” Akamwangalia na kunyamaza kabisa. Wakatulia mpaka akamuogopesha Dorothy.
Supu ikaletwa. “Ni nzuri ukiinywa ikiwa ya moto.” Akamwambia na kuanza kunywa yake. Dorothy akabaki akiiangalia. “Kunywa, utaipenda.” Akabaki ametulia. “Wewe ulitaka nile au?” “Nataka ule.” “Basi ili nile vizuri, na wewe nisindikize. Lasivyo sitaweza kula nitakuwa naona nakupunja.” “Mimi nilishakula vizuri.” “Basi tunywe na hii supu. Hiki ndio chakula changu. Kama ungekuwa umenizoea, tokea mwanzo ningeagiza hii tu supu, basi. Usiku huwa sili sana kama mchana nilikula chakula kingi. Niliagiza kile chakula kukufanya na wewe usijisikie vibaya ukashindwa kula. Ila lengo ni hii supu tu. Naomba kunywa hiyo supu. Ili na mimi nile.” Ndipo akaanza kuinywa hiyo supu.
“Nzuri. Asante.” Akacheka na kuendelea kunywa supu yake na akainywa mpaka akamaliza bila hata ya kuzungumza, na Dorothy akanyamaza akiendelea kula mpaka akamaliza. Akamuita muhudumu akitaka ampe hesabu yake ya mwisho. Akamgeukia, “Kuna kitu chochote unataka akufungie urudi nacho nyumbani kabla hajatupa hesabu ya mwisho.” “Mimi nipo sawa, asante.” Muhudumu akaondoka na kurudi na hesabu akawakabidhi. Akamuona analipia na tip, kisha akamgeukia. “Upo tayari?” “Ndiyo.” Akajibu akitoa lock kwenye kigari chake, akamsogezea tena meza, wakaondoka kimyakimya.
Wasiwasi ukaanza kumuingia Dorothy kwa ule ukimya. Akamsaidia kuingia garini. Akaondoa gari, kimya na yeye akatulia akiangalia nje ya gari mpaka nyumbani kwake. Akafunguliwa geti akavuta mpaka kwenye hicho kinyumba anachoishi.
Pale Mungu Anapofungua Milango, Ni Kuchukua Tu Hatua Kupita Ili Kuweza Kufikia Kile Mungu Alichokuwekea Upande Wa Pili
Katika kila uombacho, kikijibiwa, wakati mwingine unahitajika kufanya jambo ili kupokea majibu yako. Dorothy, alitendwa sana, lakini anahitajika kufungua moyo na imani mpya kuweza kutembea na mtu kama Jo, aliyetoka kwenye mapenzi, na anataka kupenda tena.
Pam na Mill, wamekuwa na mapito magumu. Ahadi zilizokwisha wekwa na kuvunjika kikatili sana. Lakini Mungu ametoa nafasi ya pili, yenye baraka zake, wanachotakiwa ni kuwa tayari kupokea.
Raza, alikosa na kuogopesha watu. Akatengwa. Lakini Mungu alimpa nafasi ya pili, akiwa na uongozi mzuri na maombi, amekubali kutembea mpaka kufikia zile baraka Mungu amemuandalia. Ameweza kuomba msamaha akijishusha na kusamehe wote waliomkosea.
Matendo yake yamemvuta mumewe karibu, mpaka Pius akajikuta anafanya mambo ambayo pengine angeambiwa tu afanye, angekataa. Lakini matendo ya Raza yanamvuta pande ambazo hakuna mwanadamu anaweza amaini.
~~~~~~~~~~~~~~
Siku hiyo ya jumamosi ikawa na hekaheka si kwa kina Mill tu na maandalizi hayo ya harusi, hata upande wa kina Ruhinda. Mina alikuwa akirudi jijini na familia yake. Raza alikuwa na shuguli, utafikiri wanahamia kwake. Aliondoka kwake mapema kwenda kwenye nyumba yao huko Kigamboni, akasaidia usafi akiwa na Polla pamoja na msichana aliyepewa na huyohuyo Mina.
Baadaye Poliny akaungana nao. Yakawa maandalizi mazuri, wakapika na kuweka kila kitu tayari kwa maisha mapya yaanze. Mida ya mchana Pius naye akawepo hapo, akakuta kila kitu kipotayari, wanasubiriwa wenye nyumba.
Mina anafika hapo na wanae wanaolia njaa, akakuta kila kitu kipo sehemu yake. Raza yupo kuwakarimu vilivyo. Baada ya kusaidiana kulisha watoto na kulala, ndipo wao sasa wakakaa mezani kula pamoja.
Simu ya mama Ruhinda ikaingia kwa Pius. “Samahanini. Mama huyu!” “Amenilalamikia umemsusa.” “Mambo yamekuwa tu mengi.” Akamjibu hivyo Andy na kupokea, Raza akimtizama.
Nguvu Ya Mke.
Akamsalimia. “Upo wapi Pius, mwanangu?!” “Nipo mama, mambo tu yamekuwa mengi. Unaendeleaje?” “Upo mjini unashindwa kufika nyumbani?!” “Mama, nimekuuliza unavyoendelea?” “Na kanisani mbona hufiki?” Hapo patamu.
“Raza alipata kanisa walilompokea yeye na Polla, ndio na sisi tumejiunga nao. Siku za jumapili endapo tukiwa mjini, tunakwenda huko.” “Ni RC ya wapi hiyo?” “Sio kanisa la kikatoliki.” Mpaka Andy akaweka kisu na uma chini na kumwangalia kaka yake kwa mshangao kama aliyetangaza amesilimu.
“Vipi lakini afya yako?” “Kwamba umehama dini yetu!?” “Mama, ni dhehebu tu! Mimi bado ni mkristo. Ila naungana na Raza. Siwezi nikatengana na familia yangu siku ya jumapili, eti sababu ya dhehebu. Nimehesabu ni garama ndogo sana ya kulipa kwa familia inayotengwa na kuogopwa kama hii yangu, kulinganisha na garama aliyolipa Raza kuhama dini kabisa.” Wakamuona Pius anaanza kubadilika, akasimama kabisa kuondoka hapo.
“Raza aliacha dini ya wazazi wake, kunifuata mimi huku kwenye ukristo. Halafu huku kwenye dhehebu alilohamia, ndio anakutana na wenyeji wanaomtenga kwa kukosea. Amepata kanisa lililompokea yeye na Polla kwa vile walivyo.” Mina akabaki akimwangalia Raza, ameinamia sahani yake wanasikiliza huko Pius anapoongea akisikika amepandisha tayari.
“Kule Raza anaheshimiwa sana. Amekutana na watu wanaojua alichokifanya, lakini bado wanamshikilia kama ndugu wa karibu. Polla aliyekuwa akiogopewa na watu hata kukataliwa kufika kwenye majumba yao na shuguli za watoto wengine, huko anafanya kukataa mialiko kwenye majumba wanayojua alikotokea na alichofanya. Hawamuogopibinti yangu. Mwanangu amerudisha furaha. Ametengeneza marafiki wengine. Kweli niache kuongozana nao, nibakie huko wanakowahesabia dhambi hata zilizokwisha samehewa na Mungu!?” Pius akaendelea kama aliyepata jukwaa.
“Mimi nitakuwa kiongozi gani wa familia ninayeshindwa kusimama na mwanamke kama Raza? Ni wangapi wanakosa na wameshindwa kujirudi? Raza amekiri dhambi yake hadharani! Tumemuadhibu kwa kumdhalilisha vibaya sana kana kwamba sisi hatukosei! Lakini mke wangu ametusamehe wote, amejirudi kwa vitendo. Leo ameacha shuguli zake zote, ametumia pesa zake, ameshinda akiandaa mazingira mazuri kwa familia ya Andy, ili mtoto niliyemzaa mimi kwa kumfedhehesha yeye ayakute mazingira yaliyo tayari kuishi. Nitapata wapi mwanamke kama Raza, mama?” Mpaka wanae wakashindwa kula wakawa wakisikiliza huko baba yao anakoongea.
“Wengine watashindwa kumpokea, lakini mimi nimechagua kusimama na mke wangu, kama yeye alivyochagua kunisamehe kwa ubaya niliomtendea, na kumdhalilisha kwenye jamii. Kwa hiyo NDIYO. Nimehama dhehebu na si dini kama alivyofanya Raza.”Kimya. Akajua amemshitua sana mama yake.
Pius mtoto wa mama, akahofia asije akampandisha pressure habari ikabadilika, usiku huo akakimbizwa hospitali. Akajirudi kwa haraka. “Ila nilipanga kesho jioni nipite kuwaona baada ya chakula cha mchana atakachoandaa Raza pale nyumbani na familia ya Andy.” Hapo napo akamchanganya. “Kwamba na Mina na watoto watakuwepo hapo!?” “Si ndio familia ya Andy?” “Kwani na yeye Andy amehama romani?!” “Mama, mimi nazungumzia yangu, mke wangu na watoto. Sijui wataabudu wapi, ila baada ya kila mtu kutoka kanisani, Raza ametuandalia au atatuandalia mlo wa pamoja, na baada ya hapo ndipo nitakuja kuwaona.” Mama Ruhinda akajua yeye na Paulina ndio wametengwa.
Wajukuu halisia wa Ruhinda, hivyo vidume ndio vimeshahamia kwa Raza! Ukawa mshituko, juu ya mshituko. Raza kambadili mwanae dhehebu! Halafu isitoshe, ameweza kuwavuta kina Mina pia! Alikuwa akingojea hao wajukuu wakina Ruhinda halisi kwa hamu sana. Akijua wakija atawatawala na safari za kuwafuata Dodoma zimekwisha. Sasa wamekuja, wamefikia mikononi kwa Raza! Mtihani.
~~~~~~~~~~~~~~
Ni nini kitaendelea? Usikose muendelezo.
0 Comments:
Post a Comment