Jungu Kubwa Lisilokosa Ukoko.
Akaingia na kukaa. “Samahani mama kwa kukusumbua. Nataka kumtuma dereva akawafuate bibi na babu, waje, jumatatu tufunge ndoa kama alivyoshauri Pam.” Mama Eric akawa hajaelewa ndio akamuelezea.
“Naomba niamini kama nampenda sana Pam na si kwamba nampotezea muda. Mimi nilikuwa nikisubiria ndoa ya kanisani mama yangu, na ndio hata na yeye alikuwa akijua hivyo na tukakubaliana kusubiria. Sio kwamba sitaki kumuoa Pam. Nahisi mimi ndio ninashida ya kumuoa yeye kuliko hata yeye kuolewa na mimi. Nipo na hofu kusubiria kuliko mtakavyodhania, nikihofia chochote kisije tokea hapo katikati kabla sijamuoa.”
“Lakini Pam jana alinishitukiza mama yangu. Sikukusudia kumuumiza. Alinifuata ofisini nikiwa nimezama kwenye kazi, akaniambia twende muda uleule mahakamani tukafunge ndoa! Sasa mimi nikashituka halafu nikajua ni kama kule nchini Marekani! Lazima kuweka miahadi kwanza sio kukurupuka tu! Nikamwambia tusubiri, lakini naona anaona ni kama namzungusha kwenye swala la ndoa.”
“Nia yangu ni apate kitu kizuri, mama yangu. Ndoa ya Kisha nilifanya kwa ajili yake yeye mwenyewe Pam. Sasa kama nilimwaga mapesa kwa mwanamke ambaye hata sikuwa nikimpenda, kwa nini kwa Pam nisimfanyie kitu kizuri! Ndio nia yangu na si vinginevyo. Na Pam nilimwambia akaridhia, nashangaa kwa nini amenibadilikia mama!”
“Ndio maana naona nifuate vile anavyotaka yeye ili kumtuliza. Mipango ikikamilika, ndio tufanye nzuri anayostahili si ya kukimbizana. Na nishawaambia kina Komba. Jumatatu tunafunga ndoa na Pam. Wananisaidia kuandaa kitu cha muda mfupi lakini nataka pia kiwe kizuri. Tafadhali naomba niombee radhi kwa bibi na babu kuwa ni kama nawashitukiza, nabadili badili mambo, lakini najua Pam atafurahi kuwaona siku hiyo. Ila naomba usimwambie Pam kama wanakuja ili kuongeza furaha zaidi siku hiyo ya jumatatu.”
“Binafsi najua kama unampenda Pam, na najua hata yeye anajua.” “Nashukuru mama.” “Lakini wewe umejiuliza ni kwa nini amebadilika gafla?” Mill akakunja uso kama anayejaribu kufikiria. “Pam si mjinga, na unajua si mtu wa kukurupuka. Sasa ushajiuliza mtu aliyekuwa akisubiria mipango mizuri ya harusi mpaka na gauni alishatafuta kwa kuhamasika akisubiria tarehe husika, eti leo gafla anabadilika! Ushajiuliza sababu?” Mill akafikiria hakupata jibu.
“Nahisi mambo mengi yanaendelea mama yangu mpaka nashindwa kutuliza mawazo na kufikiria. Maana kama kuna msichana mwingine, hakuna mama. Mimi si muhuni na sijaweka mazoea na mwanamke mwingine yeyote hapa kwenye hii nchi. Yaani sijawah…” Akakwama kama aliyekumbuka kitu. Akawa kama amepaniki tena.
“Kwani wewe amekwambia kuna kitu chochote nimefanya cha kutokuwa mwaminifu? Maana ni kipindi kile aliponikataa ndipo nikaanzisha mahusiano ambayo hata hayakufika mbali mama yangu! Hata Brenda sikulala naye! Kwanza nilishindwa.” Bwana Mill alijitetea mpaka kuapa. Hapo tayari jasho lilikuwa limeshaanza kumtoka mpaka mama Eric akamgeuzia feni.
Anaongea hamalizi, mama mkwe wake kimya hawezi kumkata. Akajitetea wee, mama Eric akamtuliza kwa kumuita msichana wake amletee maji ya kunywa kutoka kwenye friji. Akapewa chupa nzima. Akaanza kuyanywa bila kuweka kwenye glasi.
“Asante.” Akashukuru akijaribu kutulia akiwa ametoa siri ambazo hata mama Eric hakuwa akijua. Pam anakifua. Mpaka aseme jambo lake, ujue limemfika na lipo hadharani. Hakuwa akimwambia mama yake kila kitu. Sasa kwa kupaniki ndio Mill mwenyewe akajikuta anajisemelea.
“Tabia ya Pam kuanza kula ugali kwa wingi, unakumbuka imeanza lini.” Ikawa kama amemleta karibu. Mill ni nesi aliyesomea mambo ya mwili wa mwanadamu. Akawa kama amemfungua macho. Alishituka mpaka akasimama bila kujua. “Mama!” “Jana ndio nimemfanya na yeye akafikiria, ndio kupaniki na kukufuata mfunge ndoa kabla hajaonekana na tumbo la mtoto wa pili asiye na ndoa.” Mama Eric akaendelea taratibu.
“Pam amelelewa kwenye maadili ya ukristo, anajua ndoa takatifu. Babu yake ni mzee wa kanisa anayeheshimika sana kule kijijini. Hofu yake ni babu yake kuja kumuona kanisani na tumbo kubwa na wakati alishazungumza naye alipomzaa Shema na kumwambia alikosea. Alimwambia yeye alifundisha watoto wake. Yaani mimi na kaka. Akamwambia hata mjomba wake hakugusa mkewe mpaka ndoa.”
“Jana amepiga mahesabu, akashituka na kukufuata. Sasa sijui hesabu zake zilimfikisha na ujauzito wa miezi mingapi mpaka kupaniki vile.” “Na inamaana mpaka kuanza kula vile inamaana mwezi ulikuwa tayari, homoni huko mwilini zimebadilika! Pam atakuwa anamimba kubwa tayari!” “Ngumu kuona sababu ya umbile lake lile. Lakini kwa jinsi watoto wake wanavyokuwa wakubwa, na anavyokula, sasahivi atafura, na haitakuwa siri tena, ndio kuchanganyikiwa kote huko.”
“Kumzaa Shema bila ndoa, kulizua maneno mengi sana sababu ya familia inayomzunguka na ndio maana Eric alichukia sana kuona namsaidia wakati anajua maadili ya nyumbani. Hofu hiyo ni kuona watu wataona anarudia kosa na hajali. Ni kweli kimila Pam ni mkeo kwa kuwa ulishamlipia mahari. Ndio maana babu yake alikwambia kwa nyumbani ulishamaliza taratibu zote za ndoa, hudaiwi.”
“Lakini sisi wakristo baba. Waume kwa wake wote wamepita kusubiri mpaka ndoa. Ni Pam tu ndio unamuona anaendelea kuzaa bila ndoa. Kaka yangu naye anabinti wengine wakubwa kuliko Pam, hawajaolewa ila hakuna hata mmoja aliyezaa. Wote wanasubiri na ndio kujigamba kwa wifi yangu kuwa binti zake wameiga tabia nzuri kwa baba yao. Kusubiri. Pam amegeuka kituko kwenye kaukoo kadogo, ni hivyo mimi nimesimama naye na baba ananipenda sana mimi kuliko kaka, ndio imekuwa kinga ya Pam hata kule kijijini na Shema kukumbatiwa na baba kama watoto wengine bila kubaguliwa.”
“Nisamehe mama yangu. Tafadhali nisamehe.” “Sasa wewe usimwambie kwamba nimekwambia. Utamchanganya zaidi na kumuonyesha hujali na humpatilizi, unampuuza. Ni jeuri tu, lakini anapenda sana mtu anayemfuatilisha nyuma kama hivi mimi. Hiki unachotaka kukifanya, nakushukuru, na ninakushauri ukifanye tu hata kama si cha maana kubwa machoni kwa watu, lakini utamtoa aibu ya kubeba tumbo mbele ya ndugu.”
“Pale alipo ana hofu tu. Si kwamba hajui kama unampenda. Wote tunajua kama unampenda Pam. Lakini kumbuka mwanzoni ulilipa mahari, ukawepo kama hivi, ukapoteaakiwa mjamzito kama hivi, kukiwa na mipango ya ndoa ambayo haikukamilika. Sasahivi mtoto wa pili tena. Kuna mipango ambayo haikamiliki! Wewe si mtanzania. Ikikulazimu kuondoka hapa nchini kwa sababu yeyote ile huku mipango haijakamilika kama mwanzoni?” “Safari hii siondoki bila Pam.” “Hiyo ni kauli nzuri sana baba Shema. Ila hakuna ajuaye kesho yako wala yangu. Na kuondoka huku si tu kwenda Marekani. Ukianguka gafla, ukafa? Si utamuacha na watoto wawili waliozaliwa nje ya ndoa?” Hapo Mill akarudi kukaa.
~~~~~~~~~~~~~~
Akabaki ameinama kwa muda akitafakari ukubwa wa jambo na pale Pam anakopita, ndio kama akaanza kumuelewa. “Jinsi gani naweza kumkaribisha mjomba na shangazi? Au unaweza kunisaidia kuwafikia? Eric najua jinsi ya kumpata.” “Sidhani kama Eric atakubali kuja. Alinipigia simu akilalamika Pam amemtukana sana, lazima nizungumze nao wote wawili nimkemee Pam. Nilimjibu kuwa alikuja kunawa mikono mbele ya babu yake kuwa hamtaki tena Pam. Na alimuacha jela akiwa mjamzito. Leo nawakalisha tena chini kumkemea kwa kumvunjia heshima ili iweje? Nikamwambia kama ingekuwa ni kwa sababu ya undugu hapo sawa. Ningezungumza nao kuwapatanisha. Lakini yeye alimtelekeza dada yake kama baba yake alivyotutelekeza sisi.”
“Alilia Eric, akilalamika mimi nampendelea Pam. Simsikilizi yeye. Akaongea mengi akinihesabia jinsi alivyomsaidia Pam huku mjini, mwisho akaishia kunikatia simu. Sijamsikia mpaka leo na sikumwambia kama umenileta mjini. Sidhani hata kama anajua nilipo maana babu yake alisema tumuache kabisa, asije kwama kimaisha, yeye na mkewe wakasema sisi ndio tumemlemea. Hakuna anayemtafuta kwa la kheri wala la shari. Na mimi nimeona nimuache tu. Maana haishiwi malalamiko kila kukicha mpaka huwa najuta kumpigia simu.”
“Hata nikimpigia kumjualia hali, hataanza kwa salamu ila malalamiko vile maisha yake yalivyo magumu. Hatakwambia hali yake na familia yake ila ugumu wa maisha yake na pesa ilivyokuwa ngumu kwake na mkewe. Majukumu ya watoto na shule za wanae zilivyo garama, na mambo mengine chungu mzima. Unamalizana naye kwenye simu, unajikuta hujajua hali yake yeye kama yeye ila matatizo yake na vile itakavyokuwa ngumu kusaidia yeyote japo hajaombwa msaada. Nikaamua kumuacha.”
“Kwa hiyo huyo, ni kumuacha tu. Ila kaka na wifi pamoja na binti zao nitawataarifu, maana Pam alishanipeleka kuwasalimia na kuwaambia nimerudi mjini, ulinipa kazi. Wifi alifurahi sana mpaka kwa machozi. Kwa hiyo hao tupo kwenye maelewano. Rahisi kuwafikia. Ukijua muda na sehemu hiyo siku ya jumatatu, wewe niambie, nitawafikishia kirahisi tu.” “Asante mama. Acha basi niweke mipango vizuri, ifikapo jioni kama si mapema kesho, nitakuwa na kila kitu.”
“Sawa, ila Pam usimwambie kama mimi nimekwambia swala la ujauzito. Ataona hujali. Iwe umegundua mwenyewe, ndio ataona unamfuatiliza, haupo kama baba yake aliyewatelekeza, hawajali. Hilo Pam ameshindwa kusamehe na kuwatenga wanaume wengine na hiyo tabia. Ndio maana ukimkosea kidogo tu, hasira zinampanda zaidi ya kosa lenyewe na hawezi kufikiria vinginevyo, anaona upo kama baba yake. Hujali.”
“Ila nishamwambia wewe si baba yake. Na wapo wanaume wanajali familia zao. Baba yake ni mmoja kwa makumi. Sasa mchukulie taratibu. Acha dada akupe chakula chake na pochi yake naona na simu ipo humohumo, umpelekee.”
“Nakushukuru sana mama yangu. Nakuahidi nitafanya kitu kizuri cha kumficha aibu na kumtoa hofu hiyo siku ya jumatatu. Sitaki anibebee mtoto wangu kama mzigo mzito asiojua jinsi ya kuuficha. Acha nihangaike kuweka mambo mazuri, kwa haraka. Tutawasiliana.” Akachukua alivyoagizwa na kutoka hapo hajui kama ni furaha ya mtoto wa pili au la.
Kwa Colins.
Akampigia simu Colins. “Lazima nimuoe Pam jumatatu. Mvua inyeshe, jua litoke. Namuoa Pam jumatatu, kesho kutwa. Popote. Sijali tena.” “Hivi baba anakwenda kuzungumza na mchungaji. Amekataa wazo la mahakamani. Anasema sisi ni wakristo. Mchungaji ndio atafungisha hiyo ndoa. Anasema mzee Mgini alianza vizuri, lazima na sisi tumalize vizuri. Hatuwezi kukwepa.” Aisee Mill alifurahi sana.
“Na mama anasema kwa sababu ni jumatatu, ule ukumbi upo wazi. Ugumu ni siku za weekend. Ametoka kuzungumza nao sasahivi. Hata mpambaji amesema yeye anakuwa busy siku za weekend. Ila jumatatu anaweza kutupambia bila shida, hayo nayo ni majibu amerudisha Connie muda si mrefu. Hapa nilikuwa nikimsubiria Kamila swala la chakula na ninataka kuwapigia simu watu wa picha na kule studio kama wanaweza kutupa nafasi siku hiyo ili kupata kumbukumbu nzuri.” Mill akazidi kufurahi.
“Sijui niseme nini! Nipo kama nimepaniki!” “Nini tena!?” “Ila ni siri.” Mill akashindwa kujizuia, akawa anacheka kama jinga. “Nini mbona unacheka peke yako?” “Unakumbuka nilivyokuwa nikikulalamikia umri unakwenda nimebakiwa na Shema tu na sikujua jinsi ya kumuuliza Pam swala la mtoto wa pili maana bado ndoa?” “Usiniambie Pam ni mjamzito!” “Acha kaka! Halafu sijui nilifungwa vipi bwana!” Mill akazidi kuhamasika.
“Alianza kubadilika kula, ila mimi sikuwa nikifikiria kama ni ujauzito. Hata yeye hakuwa akijua! Yaani na elimu yangu nzima ya mwili wa mwanadamu, ndio mama mkwe amenifungua macho leo, na ndio aliyemfungua macho na Pam jana kutaka ndoa ya haraka.” “Aaahhaaa!” “Aisee nimefurahi Colins! Nimefurahi sana.” “Hongera kaka. Hongereni sana. Sasa anahali gani?” “Ni njaa tu ndiyo inamsumbua. Ila mzimaa. Hapa nampelekea ugali.” Wakacheka.
“Ila ya jumatatu namfanyia surprise.” Wakaendelea kujipanga Mill amejawa furaha kwelikweli akikanyaga mafuta kutafuta sehemu anunue chakula kingi mpaka cha usiku kwa ajili yake, mwanae na huyo Pam.
~~~~~~~~~~~~~~
Akarudi nyumbani akampigia simu Shema atoke kwenye kijumba chao. Akaanza kazi ya kubeba vyakula kuingiza ndani. “Mpe chakula mama yako.” “Amelala. Alikuwa anatokwa sana jasho huku anahema sana. Nikamwambia alale, chakula kikija nitamuamsha. Ila amesema anaoga na kulala, nisimuamshe mpaka aamke mwenyewe.”
“Basi upunguze kelele huko ndani.” “Najitahidi, ila sasa ni ngumu.” “Shema!” “Wewe niruhusu nicheze mpira huku nje.” “Hapo ndio utamuamsha kabisa.” “Nazunguka kule nyuma. Sitapiga kelele.” “Na jua lote hili! Subiri kidogo hata jioni. Kwanza nakutegemea wewe mle ndani. Mama yako akiamka akitaka kitu, atamtuma nani?” “Kweli.” Hapo akakubali.
“Sasa wewe nenda katulie ndani, hata kama kulala, lala karibu ili akiita usikie, na mwambie kuwa nampenda sanaaa.” Shema akaanza kucheka. “Nimwambie hivyohivyo?” “Hivyohivyo, tena uwe unarudia rudia.” “Wewe amekukasirikia?” Shema anamuuliza baba yake hana mbavu, kama mazuri. “Wewe uwe unarudia rudia.” “Akinikasirikia na mimi?” “Wewe hawezi kukasirikia. Wewe mtoto mzuri.” Shema alicheka sana.
“Wewe usingekuwa unamkasirisha. Halafu unakuwa ukimwambia mwenyewe kama mimi mwenzio. Nakuwa namwambia kila wakati halafu nikimkorofisha anakuwa anakumbuka mimi mtoto mzuri, nampenda.” Mill alicheka sana.
“Wewe unamtapeli mama yako Shema!” “Ndio ujue mwenzio nafanikiwa. Wewe unafukuzwa.” Mill hakuamini. Alikuwa akicheka huku akimwangalia Shema akicheka.
“Haya Shema. Wakati wewe ukijiuza huko, nisaidie na mimi.” Shema akazidi kucheka. “Haya, nenda ukale. Ila akiwa na shida yeyote ile, mimi ndio mtu wa kwanzakuambiwa sio bibi. Usimsumbue bibi. Umeelewa?” “Nitakuwa nakutumia ujumbe kwa siri.” Mill akazidi kucheka.
“Kweli wewe mtoto mzuri.” Wakaagana, Mill akarudi ndani kwake na chakula ila akiwa na furaha, na kazi ya kuwapigia simu watu wachache, kuwakaribisha hiyo siku ya jumatatu. Ikawa tena si ndogo, ikawa ni harusi kabisa.
Kwa Eric.
Akaanza kumpigia simu kaka mtu. “Mimi ni Mill.” “Afadhali umenipigia, maana alichonifanya Pam! Na jinsi alivyonidhalilisha, sikuwa na jinsi ya kukufikia kukutaarifu ukorofi wake. Pam…” “Tafadhali naomba unisikilize kile nilichokupigia Eric. Tafadhali sana. Na acha tabia ya kuanza simu zako na matatizo. Pam ni dada yako wa damu. Hata ufanye nini itabakia hivyo. Huu mtindo wa kumuanika ubaya kwa kila mtu huku ukimsusa, utakusaidia nini wewe?” Mill akawa mkali kabisa.
“Ukibaki kupendwa wewe peke yako. Au kufanikiwa wewe tu kwenye ukoo mzima, inakusaidia nini?” “Sianzi simu zangu kwa matatizo. Una..” “Hakuna siku nimekutana na wewe au kuzungumza na wewe ukawa na habari njema kutoka kwenye kinywa chako! Wewe ni kaka wa familia iliyotelekezwa na baba aliyepaswa kusimama na nyinyi wote. Tafadhali badilika Eric. Kuwa mwanaume unayekubali kuwajibika sio kupiga kelele ukitangaza ubaya tu kila wakati bila kutoa suluhisho!”
“Watu wanajisahau sana. Nani amemleta Pam hapa mjini kama sio mimi?” “Na nani amekuleta WEWE mjini?” Mill akamuuliza kwa ukali kabisa. “Eti Eric? Utahesabumpaka lini wewe!? Unahesabu majukumu yako wewe mtoto wa kwanza wa kiume wa familia!? Badilika bwana Eric. Na wewe ulisaidiwa kufika hapo ulipo. Uhai ulionao ni zawadi kutoka kwa Mungu lakini mama yako amehusika kwa asilimia zote! Tafadhali usijisahau.”
“Na wakati mwingine ukipigiwa simu sio kuombwa pesa!” Akaona amalizane naye kabisa ili hata wakiachana hapo awe amesikia. “Simu nyingine ni kujuliwa tu hali wewe kama jukumu la familia. Nimekuona Eric, wewe huna uwezo wa kusaidia yeyote kiasi cha kuwa na wasiwasi huo.” “Mbona sasa hawakomi kuniomba?” Akawa ameshakasirika na yeye akauliza kwa jeuri.
“Nikuulize tu Eric, na jaribu kufikiria. Mara ya mwisho ni lini wewe kumsaidiamama yako mzazi, sio Pam. Mama yako mzazi?” “Mara nyingi tu hata kumleta Pam huku mjini ni mimi.”
“Nimekuuliza mara ya mwisho ni lini kumsaidia mama yako wa kukuzaa? Maana mara ya mwisho kukuona wewe, uliniambia ulikwenda kunawa mikono sijui au mambo ambayo wewe unayajua mwenyewe ulifanya! Kumsaidia je?” Akaongea mengiiii. “Kwa maneno hayo mengi, inamaana si siku za karibuni hata kumtumia mama yako wa kukuzaa matumizi. Lakini unajua alipo na anavyoendelea sasahivi?” “Yuko hukohuko kwa bibi na Pam ndiye anayemkwamisha.”
“Kwa jibu hilo la sasahivi ni unaonyesha umeshindwa kuwa kiongozi wa familia ila MLALAMISHI tu. Huna unalojua linaloendelea nyumbani kwenu, na inaonekana hata wao, wamekutoa kwenye mambo ya familia.” “Ni…” “Sina muda mwingine wa ziada Eric. Nimekupigia kukukaribisha siku ya jumatatu kwenye harusi yangu mimi na Pam. Tukitambua ni siku ya kazi, tumepanga itakuwa jioni.” Mill akaendelea bila kutaka kumpa nafasi ingine zaidi.
“Kutafanyika ibada na sherehe hapohapo ukumbini. Ni ya watu wachache tu. marafiki na ndugu wa karibu. Ukiwa wewe kama kaka yake Pam, nimeona nikukaribishe. Ukiweza karibu, ukishindwa pia ni sawa. Ila nilitaka ujue kuwa, siku ya jumatatu, kesho kutwa, namuoa Pam, huyo unayemtangaza vibaya. Na namfanyia surprise. Yeye mwenyewe hajui, namtayarishia kitu kizuri sana, kumfurahisha. Usafiri utatolewa kama utahitaji. Au msaada wa mafuta ya gari yako. Wewe na mkeo na familia yako mnakaribishwa.”
“Sina shida ya kuwekewa mafuta kwenye gari yangu na si kwamba nasambaza ubaya wa Pam.” “Uwe na mapumziko mema Eric. Nitakuona siku ya jumatatu kama utafanikiwa kufika. Kwaheri.” Akakata simu kabla hajamaliza kujitetea.
Kule Kulikoungua Mpini.
Akampigia simu Sandra na mumewe Jerry. Wote akawaweka kwenye simu. Wakasalimiana kisha akaenda moja kwa moja kwenye lengo. “Jamani, mara ya kwanza kuoa ili kufanikisha uraia wangu kule nchini Marekani, ilikuwa siri, ambayo sikutaka mtu ajue kwa sababu ilikuwa ndoa feki. Naomba radhi kwa kuto washirikisha sababu ya hofu, nikihofia nisije kamatwa endapo habari ingejulikana.” Mill akaanza kwa tahadhari kwani mahusiano yao yalishakuwa mazito.
“Lakini na sisi kama ungetuona watu wako wa karibu kama kina Mike na Kamila ungetushirikisha tu.” Sandra akatupa lawama. “Sasa, kwa kulitambua hilo, ndio maana leo nawapigia simu kuwataarifu safari hii Mungu amenijalia kufikia lengo. Naoa ndoa ya ukweli na namuoa mwanamke ninayempenda na niliyemtamani awe wangu tokea siku ya kwanza namuona na kuwashirikisha, Pam.” Kimya kikatanda. Hapakuwa hata na hongera. Akaendelea.
“Karibuni kama mtaweza, itakuwa kesho kutwa siku ya jumatatu.” Akawatajia muda na ukumbi. “Naelewa ni taarifa ya muda mfupi na ni siku ya kazi ndio maana nimeweka jioni. Tutafurahi kuwaona siku hiyo kama mkifanikiwa kufika. Ni surprise, hata Pam mwenyewe hajui. Namwandalia kitu kizuri ili kumfurahisha hiyo siku ya jumatatu. Nikimaanisha hivi, nimewatarifu nyinyi, kabla yake.”
“Kama unawasiwasi kwamba sisi tutamwambia, binafsi sina hata mawasiliano naye huyo Pam.” “Basi tutawaona hiyo siku ya jumatatu endapo mtafanikiwa kufika. Niwatakie siku njema.” “Asante na wewe Mill.” Ndio Jerry akajibu na Mill kukata simu.
~~~~~~~~~~~~~~
Siku hiyo ikajaa mipango ya kwenye simu zaidi. Uzuri yeye na Colins walishaagiza suti zao mapema sana zikawa zimeshafika. Colins ndio alikuwa akisimamia na Kamila. Ila yeye Kamila ndio bado hakuwa amekamilisha nguo zake na wasimamizi wengine. Ikabidi kutoka na mama Colins kutafuta nguo nzuri ya kuvaa siku hiyo ya harusi. Gafla siku ikajaa hekaheka na shamrashamra.
Alipowasiliana na mama Eric juu ya ukumbi na muda na yeye akampa majibu kutoka kwa bibi na babu yake Pam. Kuwa wamefurahi sana, na wamekubali kuja mjini, hata kwa basi. Lakini Mill akamwambia anamtuma dereva kuwafuata, wasisumbuke. Nalo hilo likaongeza furaha ya aina yake si kwa wazee hao, hata ndugu waliojua, wakaona Mill anawajali.
Mungu Wa Yasiowezekana Na Binadamu
Ukabaki mtihani kwa mama Eric. Nguo za wazazi wake. Maana yeye na mama Colins zao walishona sare na mama Colins alishampigia simu fundi kumuomba afanye haraka siku ya jumapili kesho yake wakamilishiwe. “Baba Shema hajuagi kitu kidogo. Itakuwa sherehe ya maana. Sitaki wazazi wangu ndio watokee pale, watie aibu.”Akabaki akiwaza mam Eric, hajui chakufanya. Akazidi kukosa raha.
Anafanyaje? Dereva ndio katumwa Milimani kuwachukua wazazi wake. Pam ndio huyo anafanyiwa harusi ya surprise, Mill hataki aambiwe. Sasa atamuombaje amfuate amsindikize kununua nguo za harusi tena! Eric ndio haingiliki. Akabaki amekwama.
Akaaona amshirikishe kaka yake wasiwasi wake. “Tunafanyaje kaka? Tusije ingia aibu sisi, baba na mama wakitokea kituko.” “Naweza kutafuta suti ya baba. Ila mama sitaweza. Na wifi yako ndio naona kaingiwa hekaheka kama yeye ndio anaolewa! Hayupo hapa. Na naona binti zake pia wamechangamkia kweli hiyo shuguli. Kila mtu ametoka hapa akijiandaa na lake.” Akacheka kwa furaha japo upande wa mama yake bado hakujua cha kufanya.
“Nashukuru kwa muitikio wenu. Na wewe ukinisaidia baba, pia nitashukuru.” “Ila pesa ngumu!” “Wewe fanyika tu miguu yangu, kaka yangu. Ukiipata hiyo suti, nijulishe, nakutumia pesa hapohapo.” Akaanza kumtania dada yake. “Nakuona siku hizi mambo yako si mabaya!” “Kuzaa kuzuri kaka. Mungu alinipa Pam akiujua unyonge wangu. Jeuri hii ni pesa yake. Amenipa akaunti zake ili nisiwe naombaomba tena.”
“Sikuwahi kuzitumia kabla kwa kuwa yeye mwenyewe alikuwa akinisaidia manunuzi hata kabla sijamuomba. Lakini naona leo itanifaa. Kwa hiyo wewe niambie tu. Nitamjulisha baada ya sherehe yake.” “Sawa. Nashukuru kunisaidia. Maana na mimi ni jukumu langu.” “Ushasaidia sana kaka. Acha na wewe upokelewe. Tutawasilina basi baadaye, acha nifikirie juu ya mama.” Wakaagana akimuacha na mawazo.
Mwanga Mpya Baada Ugumu Wa Mapenzi
Akiwa mawazoni amekosa dira ujumbe ukaingia. ‘Umeshakula?’ Kwa hakika hakutegemea. Mpaka mapigo ya moyo yakaanza kwenda kasi, wakati akirudia kusoma ujumbe huo mfupi sana. ‘Dorothy?’ Ukaingia mwingine, ndipo akagutuka na kurudisha kwa swali. ‘Cha mchana au usiku?’ ‘Nijibu kile ambacho bado.’ Akajikuta akicheka. Kisha akamjibu. ‘Cha usiku bado.’ ‘Bora twende tukale wote?’ ‘Nikupigie?’ Mara simu yake ikaanza kuita.
“Unafanya nini sasahivi?” “Umenitoa kwenye mawazo. Nilikuwa nimekaa hapa peke yangu. Pam na mwanae wameondoka. Msichana wangu ametoka kwenda kusukwa kiharusi.” “Tuanze na wewe. Unawaza nini, kisha niambie harusi ni ya nani?” “Baba Shema ameamua kumfanyia Pam harusi ya surprise.”
“Hilo ni jipya hata kwangu. Sijawahi ona harusi ya surprise. Hongera sana. Nahisi itavutia sana. Natamani kujua itakuaje! Atamfikishaje kanisani bila ya kumvalisha shela na mengineyo!” “Mimi na mama Komba, ambaye ni kama mama yake Mill tushajipanga. Itakuwa nzuri tu. Ila nina wasiwasi na mama yangu. Leo, baada ya siku nyingi sana, nimejikuta nikitamani kutembea kwa miguu yangu mwenyewe bila kutegemea mtu au kitu. Nimechukia kuwa mlemavu.” Akamuhurumia maana aliliongea hilo kwa kuumia.
“Pole Dorothy? Niambie kwa nini?” “Hawa watu wanauwezo sana, Jo. Sasa hivi kila mtu anajipanga kwa kupendeza. Mama yangu hana nguo nzuri ya maana. Tulijua tuna muda mrefu. Tukajipanga na Pam wakija mjini kabla ya harusi tukamtafutie mama na baba nguo. Lakini baba Shema anataka iwe jumatatu, na hivi tunavyozungumza amemtuma dereva kuwafuata.”
“Na dereva au Pam anayefanyiwa surprise ndio unaowategemea kwenye usafiri?” Jo akawa ameshamuelewa. “Naona umeshaelewa kukwama kwangu.” “Mbona hukunishirikisha mimi huo uhitaji wako?” “Mmmh! Kwanza hata sikujua kama nitakuja kukusikia tena.” Joel akashangaa sana.
“Kwa nini Dorothy na jana usiku tulizungumza?!” “Acha nikwambie ukweli. Nilipoona kimya siku nzima mpaka muda huu, nikajiambia pengine umelala, ukafikiria na kuona unajiingiza matatizoni.” “Unawezaje kufikiria hivyo Dorothy?!” “Mimi ni mlemavuJo. Wewe bado unanguvu na afya njema. Unanafasi ya kuishi vizuri na kufanya kila unalotaka kwa uhuru wote. Ukiniongeza mtu kama mimi hata kwa huo urafiki wa kutoka kwenda kula ni kujishika miguu kusiko na sababu.”
“Ona kama sasahivi! Nimekwama. Sina miguu ya kweli wala ya gari, kunisogeza. Nikajua umejifikiria ukaona ni bora ukae pembeni tu.” “Nikikwambia nimekutengenezeausafiri maalumu kwa ajili yako, utaamini?” Kidogo akatulia akifikiria, akahisi ni kama hajamsikia vizuri.
“Kwamba umetengeneza kwa ajili yangu mimi!?” “Ndiyo. Kwa ajili yako weweDorothy.” Akatulia na kushindwa kuamini. “Mimi ni daktari na nimefanya kazi sehemu zenye vita pia. Nimekuwa na watu ambao wameathirika na vita kwa kukosa baadhi ya viuongo. Nimejifunza jinsi ya kuishi nao na kufanya waishi wakiona hawana upungufu.”
“Gari analotumia dereva wa mume wa Pam, ni zuri sana, na ni ya thamani, lakini Dorothy, ile gari kwa vile ilivyo haikufai wewe. Nimeona jinsi unavyopanda. Si sawa. Baada ya muda utaharibu baadhi ya viungo. Unahitajika gari ya chini au kama ni ya juu basi iwe na kitu kinachoshuka kukuchukua chini mpaka juu kwenye kiti au basi kuwepo na njia ya urahisi ya kufikisha wheelchair yako mpaka karibu kabisa na kiti ili uweze kuhamia kwenye kiti cha gari kirahisi bila kutumia nguvu nyingi sana zaidi ukilemea viungo vya juu. Ukiweka uzito wote kwenye mkono mmoja au upande mmoja wa bega. Sijui kama unanielewa?” “Nakuelewa Jo, lakini yote hayo mimi nayapatia wapi?!”
“Ndio kazi niliamka nayo leo asubuhi. Na ndio maana umeona kimya. Pole. Ningejua basi ningekutumia hata ujumbe wa salamu. Lakini pia mbali na haraka ya kuwahi huko, nilijua ungekuwa na kina Pam, sikutaka kukuingilia.” “Salamu isingekuwa kuniingilia. Ningefurahi.” “Basi kuanzia leo lazima kila tukiamka tuwe tunazungumza japo kwa ufupi. Sawa?” “Nitafurahi.” Joel akacheka akijua ameshaanza kufanikiwa kumsogeza karibu na juhudi zake siku hiyo si bure.
“Pole na kuhangaika siku nzima.” Joel akafurahi huyo, kujaliwa naye! Ndipo akamueleza. “Nilienda kwa fundi nikamueleza kitu ninachokitaka. Amenisindikiza mpaka sehemu ya kununulia bidhaa ya kutengeneza. Nimeshinda naye siku nzima, tumefanikisha. Sio kitu kigumu au niseme cha ajabu sana, lakini utashangaa jinsi itakavyokusaidia.” Bado ikawa ngumu kumuingia akilini.
“Kweli umefanya yote hayo kwa ajili yangu mimi!?” “Kabisa.” “Kwa nini!?” “Kwa sababu nakujali Dorothy. Nakujali, sitaki uendelee kuumia.” Alishindwa hata cha kumjibu.
“Nielekeze ulipo, nakuja kukuchukua nikupeleke kufanya manunuzi kisha tukale.” “Mimi mwenyewe si mwenyeji sana. Acha nitoke niende nyumba kubwa niombe mtu akuelekeze.” “Pole nakusumbua. Ila ni leo tu. Nikishapajua nitakuwa nikija bila usumbufu.” “Mimi ndio naona ni usumbufu kwako, Jo. Nimefurahi mpaka siamini. Nahisi nipo ndotoni. Sitaki kuamka.” “Mimi nipo Dorothy. Usiogope. Hata ukiona kimya, jua upo mawazoni mwangu, nimetingwa tu. Lakini si kukukimbia.” “Nakushukuru.” Akatoka na kubahatika mtu wa kumuelekeza. Akamrudishia simu. “Nitakuwepo hapo kama baada ya dakika 45.” “Na mimi naingia kuoga kutoa jasho. Utanikuta tayari.” “Sawa.”
~~~~~~~~~~~~~~
Kama alivyoelekezwa akafika getini na kufunguliwa geti. Akaelekezwa anapoishi mama Eric, akavuta gari mpaka sehemu ya hicho kinyumba cha uwani. Ukweli palikuwa ndani ya nyumba nzuri sana. Na kanyumba kenyewe si kabaya ila kadogo. Akampigia simu kumwambia amefika. “Huingii ndani?” “Labda tutakaporudi ili tusichelewe madukani.” “Basi natoka.” Alijitahidi kuvaa vizuri ile ya kimama.
Akatoka garini alipomuona anakuja na kigari chake. “Umependeza sana Dorothy, na kuzidi kuvutia.” Akacheka kwa aibu kidogo. “Na wewe ni nadhifu wakati wote Jo. Stella alikuwa haishi kuimba sifa zako.” Alicheka sana. Kisha ni kama akapuuza.
“Sasa acha nikuonyeshe urahisi wa kuingia humu garini.” “Sasa mbona gari yako yenyewe ni kama tu zile ya baba Shema?” “Ila inakitu cha kukurahisishia kuingia garini. Acha nikuonyeshe. Hiyo si ni gari ya umeme?” “Au nichukue ile ya kawaida? Ninayo ingine. Hii naipenda sababu inanisaidia
sisukumi kabisa.” “Hiyohiyo. Subiri uone.” Akaifungua. Akashangaa kiti cha nyuma, cha katikati kimetolewa. Kwamba kuna nafasi mpaka kiti cha mwisho kabisa. Ni gari zile za viti 8.
“Hii ipo na viti vichache. Ile ya baba Shema ina viti 8.” “Na hii ilikuwa hivyohivyo, nimetoa asubuhi ili kukutengenezea uwanja wa kukutoshea wewe.” Alishituka huyo mama! Maana yalikuwa ni yale magari ya thamani sana. “Umeharibu gari kwa kwa…” “Kwa sababu yako. Ndiyo. Na sijaharibu. Nimetengeneza kutufaa sisi wawili. Mimi sina familia ya kuwapandisha humu ndani. Nipo peke yangu. Subiri uone.” Alimgusa huyo mama mpaka akabaki amepigwa butwaa.
Akafungua kama kidaraja kimetoka ndani ya gari kikalala mpaka chini. Akazidi kushangazwa.
“Hii ni chuma nzuri sana. Hutaanguka. Usigope. Jivute mpaka ndani kabisa ya gari utakapokaribia kabisa kiti. Loki gari yako ndio uhamie kwenye kiti cha gari. Na kwakuwa hakuna mwingine anapanda humu, hamna haja ya kutoa gari yako. Itakusubiria hapohapo, ila tutasogeza tu pembeni.” Alifanikiwa kuingia na wheelchair yake mpaka ndani kabisa na kuhamia kwenye kiti cha gari, Jo akimtizama kwa furaha. Hakika ilikuwa rahisi mpaka akashangaa.
“Siamini!” Akacheka alipojiweka sawa kitini. “Wapo watu wanalipwa mamilioni ya pesa ili kukaa chini na kufikiria mambo kama haya tu. Wabuni, na kufanya maisha ya watu yawe rahisi na wasijione wamepungukiwa maishani. Sasa subiri niisogeze gari yako pembeni. Tukija kuwa na kina Shema, tukahitaji nafasi kubwa, ndio nitaweka nyuma.” Alionekana mzoefu wa hizo wheelchair wala hakuhitaji maelekezo jinsi ya kukitoa na kukisogeza upande mwingine na kukifunga ili kisisogee. Akarudi pale alipokaa. Akashangaa anamfunga yeye mwenyewe mkanda na kufunga mlango. Akajisikia kujaliwahuyo!
Alipopanda na yeye garini akamshukuru. “Asante kujali Jo. Mungu akubariki.” “Amina. Nimefurahi tumepata muda.” “Sasa muda wenyewe mbona upo na majukumu?” “Hayaepukiki hayo. Lakini na sisi humohumo ndani tutajichukulia muda wetu. Tukazane tupate vitu vizuri kwa haraka.” Akamgeukia pale alipokaa kiti cha nyuma.
“Upo tayari tuondoke?” “Ujue mimi si mwenyeji kwenye huu mji! Pam ndiye anayenipelekaga kila mahali.” “Usijali. Mimi nitakuwa mwenyeji wako. Na nimemuuliza dada amenipa ramani ya sehemu kadhaa tunazoweza pata mavazi ya wanawake.” Ikamchanganya kidogo.
“Kwani umemwambia dada yako unaenda wapi!?” “Kukusindikiza wewe kununua nguo za mama.” Akakunja uso. “Kwani dada yako ananifahamu!?” “Ulishamuhudumia pale. Nafikiri siku ya kwanza kulipia vipimo vya mumewe kabla hajalazwa. Ni mkimya sana si kama mumewe. Akiwa sehemu kama mumewe hayupo, ni ngumu hata kujua kama yupo. Mumewe ndiye anayemfanya azungumze. Tena kwa kumchokoza tu. Ila vinginevyo, unaweza sema ni bubu. Ila anaakili sana. Wanae wote, mumewe anasema anashukuru Mungu wamerithi akili za mama yao, eti vinginevyo kama wangechukua akili zake, wangekuwa wamesharudi huku nchini muda mrefu sana kuanzisha kilimo.” Mama Eric akacheka ila na wasiwasi ukawa bado.
“Ana maneno hujawahi mpatia mwenzie. Na hamalizi porojo zake. Utajikuta unakazi ya kucheka tu, huangilii muda, mpaka akuage yeye ndio unagutuka kwamba amekuweka muda mrefu.” Akamuona ametulia anawaza.
“Umeenda wapi tena?” Akacheka kwa wasiwasi. “Ni nini?” “Dada yako umemwambia nini juu yangu?” “Hivi unajua mimi si mtoto niliyebalee jana?” Angalau akamfanya aanze kucheka.
“Najua ninachokifanya Dorothy. Acha woga na kujishuku. Wewe ni mwanamke. Tena si tu mwanamke! Ni mwanamke mrembo wa kuvutia si kwa wanaume tu, hata wanawake. Uzuri wako si wa kuficha” “Mmmh!” “Sasa wewe unafikiri mimi mpuuzinachanganywa kirahisi tu?” Alicheka, akacheka asiamini.
“Jo!” “Unanivunjia heshima je! Naona unanisukumia kwa watu kama kina Stella! Yaani kama vile kuniambia mimi sistahili vitu vya hadhi ya juu! Vyangu vya chini!” “Jo wewe! Stella ndio vya chini!?”
“Mbona wewe huangalii picha kubwa unakimbilia watu wengine? Stella amekukaa kichwani mwako unashindwa kujiangalia wewe na kile ninachokwambia! Tafadhali angalia hapa tulipo mimi na wewe. Nakwambia Stella nilimuona, na wewe nilikuona. Lakini leo tokea asubuhi, nimekua nikikuhangaikia wewe. Wewe Dorothy. Sijui kama unanielewa?” “Sikuelewi Jo. Kwa nini?” “Nilikwambia kwa sababu NAKUJALI wewe. Tafadhali jiangalie kwa jicho la kujithamini. Wewe ni bora kuliko ulivyoaminishwa. Natamani ungejiangalia kwa jicho la SISI tunao kutizama.” “Mmmh!” Dorothy akaguna kama aliyekumbushwa mbali.
“Huyo Dorothy unayemzungumzia wewe alishapotea muda mrefu sana.” “Kwa hiyo unakiri kwamba alikuwepo?” “Zamani sana.” “Basi amini nikikwambia kama bado yupo. Dorothy huyo unayehangaika kumzika, amemfanya mpaka dada yangu asiyezungumza azungumze.” Akazidi kumchanganya. “Dada yako tena!?” Mara simu yake ikaanza kuita na kuwatoa katikati ya mazungumzo na swali lililoibuka na kuzidi kumshangaza Dorothy.
~~~~~~~~~~~~~~
Harusi Ya Mill&Pam imekuwa ya Surprise. Itakuje?
Jo&Dorothy!? Usikose Safari Ya Watu Wazima Hawa Ambao Ni Kama Maisha YalishafikaMwisho Lakini Tena ni kama Kuna Mwanga Mpya. Kwa Nini Dorothy Mlemavu Na Si Mrembo Mwingine Kwa Joel Anayeonekana Na Kila Kitu na anauwezo wa kupata yeyote?
Mina&Familia Yake Wanarudi jijini na kuweka tumaini jipya kwa Raza. Itakuaje kwa familia ya Ruhinda.
0 Comments:
Post a Comment