Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Love At First Sight - Sehemu ya 67. - Naomi Simulizi

Love At First Sight - Sehemu ya 67.

 Akapata wazo, akamfuata nyumba ndogo bila ya kumjibu mwanae, naye Shema akafuata nyuma haelewi baba yake anakwenda wapi! Kufika, Pam hayupo. “Mimi njaa inauma. Kwani mama yuko wapi?” “Shema! Nimekwambia kunywa kwanza maziwa. Mbona yapo kwenye friji ndani! Chakula kinakuja sasahivi.” Akampandishia kidogo mwanae, Shema akapoa.

~~~~~~~~~~~~~

Akatoa simu yake akampigia simu mama yake. Ikaita, haijapokelewa. Akampigia bibi yake hapohapo mbele ya baba yake. “Mama yuko huko?” Mill akamtizama aliposikia hivyo. “Yupo. Amelala kama mfu!” “Mwambie mimi njaa…” “Si nimekwambia nakupa chakula Shema! Mbona inakuwa huna subira?” Mill akamuwahi kama asisemelezee.

“Mimi siwezi kunywa maziwa bila kitu kingine.” “Basi usimsumbue bibi, twende tukale.” “Nini?” “Mbona maswali mengi hivyo?! Wewe shida yako si ni chakula?” “Ila mimi nasikia njaa sana. Hata sioni!” Mama Eric akabaki akimsikiliza mjukuu kwenye simu akijibishana na baba yake. “Basi ndio twende sasahivi. Acha kumsumbua bibi.” Akajua Pam amewafanyia kusudi. Akacheka na kutingisha kichwa.

~~~~~~~~~~~~~

“Naomba kunywa maziwa. Uoge. Twende tukale halafu tumfuate mama yako.” Baada ya kulalamika kwingi, akisema hana hata nguvu yakusimama bafuni na hili na lile, mwishoe akakubali. Ilikuwa siku ya ijumaa. Wote wakaoga na kubadili nguo vizuri na kwenda kula. Mill akaomba afungashiwe ugali tena na mboga kama mchana wake. Akambebea na mkwewe chakula kizuri tu cha hamu, na vinywaji ndipo akaenda kwake.

Kwa Mzaa Chema.

“Pam yuko wapi?” Akauliza baada ya salamu. “Amelala kama mzoga huko chumbani na ametoa amri, asiamshwe.” Pakawa pagumu. Chumbani kwa mkwe anaingiaje? Yeye Shema akatoa viatu akaenda hukohuko chumbani. Kweli akamkuta mama yake amalala. Alichofanya ni kujilaza pembeni yake. Kwa uchovu na shibe, akapotelea usingizini.

Basi wenye nyumba wakala, na kufurahia chakula kilicholetwa na baba Shema. Msichana wa kazi akasafisha, akaoga na kwenda kulala. Pam hajatoka chumbani wala hajaamka.

Wakabaki baba Shema na mkwewe. “Sio kwamba mimi sitaki kumuoa Pam.” Akaanza, mama Eric akamgeukia maana ni luninga ndio ilikuwa ikiendelea hapo kwenye kisebule hicho kidogo, maana wao wawili hawana mengi ya kuzungumza na wazi kulionekana hapako shwari. Kwa hiyo hata mazungumzo yalishakuwa mazito kidogo.

“Mimi ninaweka mipango mizuri. Si hata wewe mama unajua?” “Kabisa. Mmefikia wapi?” “Ile sehemu tuliyochagua kufungia harusi na tafrija ni sehemu inayopendwa sana. Nzuri mno, na ni ya hadhi, japo pesa ni ya juu lakini nikasema inastahili kusubiriwa. Lakini tarehe zakaribuni zote zimejaa. Ndio tukazungumza, tukaona tusubiri. Tumekula ng’ombe mzima, tusibakize mkia.” “Sawa.” Hee! Hii ‘sawa’ ikawa inafanana kama ya mwanae Pam.

Mill akajua napo si sawa ya sawasawa. “Mtu anaweza uliza kwani kwenye jiji kama hili hakuna kumbi nyingine kama hizo?” Bwana Mill alizungumza hapo, mkwewe akisikiliza tu hachangii. Na hakuna mazungumzo magumu kama mkiwa wawili, tena na mkwe, halafu wewe mwenyewe ndio unazungumza bila kuungwa mkono. Aliongea Mill akiweka mipango yake na kamati yake waziwazi. Akajieleza mpaka akachoka maana hapakuwa na uungwaji mkono na joto la hapo si saizi yake. Lilishamlemea tokea anaingia hapo, kunapikwa na ni nyumba ndogo.

Anajieleza huku akijifuta jasho lililokuwa likimwagika kama anamwagiliwa maji! Saa tano mama wa watu akawa amechoka. Hata kama ni chakula cha bure, si kwa garama ya kukesha naye! Akaamua kwenda kuoga na yeye alale. “Shema naye yuko wapi, naona amepotea?” “Ngoja nimwangalie ndipo nioge na mimi nijipumzishe.” Ndipo akagutuka na kuangalia saa.

“Niangalizie na Pam, mwambie nipo hapa.” “Sawa.” Mama wa watu akaenda, akakuta amebakishiwa kaupande kadogo kakulala, Pam na mwanae wamelala hawana habari. Tena Shema alifanya kumuwekea kabisa mama yake mkono. Akacheka nafsini mwake. Akarudi sebuleni alikomuacha mgeni wake ameloa jasho.

~~~~~~~~~~~~~

“Wamelala hawana habari!” Bado jasho lilikuwa likimtiririka. Wazi alionekana kuzidiwa japo mapishi yalishaisha lakini palikuwa na joto, kwa Mill ilikuwa ni zaidi ya adhabu kukaa hapo kwa muda mrefu hivyo.

“Sasa wakijaa kitandani kwako hivi, wewe utalala wapi?” Ikawa kama anamuhurumia mkwewe kumbe ana yake. “Nalalaga nao hawa kwenye kitanda kidogo kuliko hiki. Tutakuwa tu sawa. Wewe nenda kapumzike baba, usiwe na wasiwasi nao.” Mill akakwama.

Pam si mke wa ndoa takatifu na mama mkwe alishamwambia lazima watubu kwanza, ndipo wafunge ndoa takatifu waishi maisha kama wakristo wa kweli. Sasa ndoa anayoandaa yeye ndio inamipango mingiii, haikamiliki. Leo anamdaije hapo kwa mkwewe. Ikabidi aage atoke. Akaondoka hapo mnyonge, bila Pam wala Shema.

~~~~~~~~~~~~~

Alipofika tu kwenye gari akampigia simu Colins. “Hivi hatuwezi tafuta sehemu ingine ya kufungia harusi.” “Tunaweza. Kwani unataka kubadili tena tarehe? Maana kumbuka kila mahali tushatanguliza nusu pesa. Ukumbi, vinywaji, chakula na…” Colins akamtajia walipofikia kana kwamba huyo Mill hajui wakati wanaandaa naye bega kwa bega. Ukweli walikuwa wameshatumia nusu ya bajeti. Napo akakwama. Akarudi kwake akiwa amenyongea.

Nilipofunga Mlango wa Moyo Bila Kuangalia Nyuma

Alipomaliza kuoga akasikia ujumbe umeingia kwenye simu yake. Akashangaa kidogo. Mtu anayewasiliana naye sana tena mpaka mida hiyo ni Pam na huyo mjukuu aliyelala hapo. Wazazi wake hawajui hata kutuma ujumbe zaidi ya simu yao kupokea na kupiga! “Nani huyu usiku huu!”  Akaisogelea kuifuata.

‘Sijui nimekuchelewa sana! Natamani kujua siku unaimalizaje! Ulifanikiwa kumtuliza Pam? Umekula?’ Akashangaa kiroho kinaanza kudunda sivyo, akamjibu. ‘Nashukuru Mungu amelala.’ ‘Na wewe?’ Bado akataka kujua yake yeye kama Dorothy. ‘Ndio najiandaa kulala.’ ‘Ulifanikiwa kula vizuri, ukashiba?’ Akashangaa kidogo aina hiyo ya kujali, ila akamjibu. ‘Ndiyo. Na wewe?’ Akawa muungwana.

‘Nimedoea kwa watu.’ Akacheka aliposoma vile. ‘Umekula kwa nani?’ ‘Nilienda kumuona mgonjwa, na mimi nikaponea hapohapo. Naomba kukusikia Dorothy.’ Akashituka akaanza kujiangalia. Hata nguo hakuwa bado amevaa ila kitenge alichojifunga alipotoka kuoga na kujifunika taulo. Akaanza kujishuku kama anaye muona.

‘Upo?’ ‘Ni usiku sana. Sio usumbufu!?’ ‘Kukusikia wewe si usumbufu, labda kwako.’ ‘Pam na mtoto wake wamelala hapa.’ ‘Ni sawa nikikuomba usogee sehemu ingine tuzungumze? Japo kukusikia tu kwa muda mfupi.’ ‘Saa hizi!?’ Akajikuta akizidi kuuliza kwa kushangaa zaidi. Naye Jo akang’ang’ania tu. ‘Ndiyo.’ Akajibiwa hivyo.

Ikabidi atoke hapo chumbani akijisukuma na kigari chake cha kawaida tu, akaenda sebuleni, akampigia. “Asante kunipigia Dorothy. Nimefurahi.” Hakujibu maana bado hakuwa akielewa anawezeje furahia kuzungumza na mtu kama yeye!

“Vipi lakini, mgonjwa anaendeleaje?” “Maneno mengiiii! Nyumbani kwake hakuishiwi watu! Kumejaa kama bungeni. Kila mtu anamsikiliza yeye. Naona kapona kabisa yule. Ndiye aliyeniweka muda wote huo kwake, hamalizi!” Akacheka kidogo kwa wasiwasi kama ambaye bado anayejituliza kuzungumza na mtu kama Jo.

“Lakini afadhali kama amerejesha furaha.” “Hakuwahi ipoteza. Maneno yake mengi yapo hivyohivyo, siku zote. Alikuwa akichekesha manesi na madaktari mpaka ikabidi wamtoe tu hospitalini.” Akacheka lakini hakuwa akijua aseme nini tena. Akawa ameshamaliza. Na Jo alimgundua anajitahidi tu hayo maongezi.

“Umeshajua tunakutana muda gani?” “Mimi si mtu wa kutegemea, Jo. Nina makorokoro mengi mno, na yote hayajakaa sawa.” “Kama nini?” “Bado mambo ya Pam hayapo sawa. Kama nilivyokwambia, yupo hapa na anakwake. Sijui atakaa hapa kwa muda gani na si mzungumzaji wa mambo yake ni mpaka aamue yeye, na hapo ujue ni kwamba yamemfika shingoni ndio atasema. Na anategemea mtoto wa pili, hana msaada isipokuwa mimi. Kwa hiyo ni kama nimekwama. Sijui ni lini mambo yangu yatakuja kukaa sawa kiasi cha kuja tena kuanza kutoka. Ndio maana nilikushauri ni bora kina S..” “Tafadhali usiendelee kunitafutia wanawake, Dorothy.” Safari hii akasikika akimaanisha.

“Mimi ni mtu mzima na ninaona Dorothy. Tafadhali amini nilimuona vizuri sana Stella. Kama utakumbuka yeye ndiye aliyejitolea siku ya kwanza kabisa kunipeleka mpaka alipolazwa shemeji yangu. Nilikuwa naye na tukazungumza naye. Na Stella ni muongeaji sana. Najua kama unajua hilo. Na yeye ndiye aliyeniambia ni kwa nini wewe uliyenielekeza upande zilipo wodi za wanaume, hukunipeleka wewe, akajitolea yeye.” Tayari akajua Stella alishamwambia kama yeye ni mlemavu. Akapoa.

“Kurudi siku ya pili pale hospitalini, dirishani kwenu, kuwasalimia nikiwashukuru kwa kuniongoza njia mpaka alipo mgonjwa wangu, ilikuwa mara ya tatu si ya pili kama ulivyodhania wewe siku ile. Maana siku ileile ya kwanza aliponipeleka Stella kwa mgonjwa wangu, wakati natoka, nilirudi tena pale. Unajua kama nilikutana tena na Stella akiwa pale peke yake, akaniambia umetoka na binti yako kwa mapumziko yako ya chakula cha mchana? Alikwambia?” “Aliniambia kama ulirudi kumshukuru kwa kumfikisha mpaka kwa mgonjwa wako.”

“Kwa vyovyote alivyoiweka yeye, lakini nilimwambia wazi kabisa, nilirudi kukushukuru wewe kwa kunielekeza.” “Yeye alisema ulimfuata yeye kumshukuru.” “Tuyaache yote hayo, lakini wewe hudhani kwamba na yeye nilimuona vizuri tu?” “Mimi sijui!” “Tafadhali fikiria vizuri Dorothy. Nilimuona na inawezekana hunifahamu vizuri, ila kwa muda mfupi kuniona na kuzungumza na mimi, unafikiri mimi nina tatizo la kuelewa?”

“Sioni kama unatatizo la kuelewa, ila pengine hukuwa umefungua macho vizuri kuona kitu kizuri kilichopo mbele yako.” “Hata kama ni mpofu wakutoona ‘hivyo vizuri’ unavyozungumzia, basi hata nisisikie na kuelewa nia yake kwa mara zote alizoniomba namba yangu ya simu? Kweli!?”  Hapo akamfanya na yeye ajiulize. Maana swala la namba ya simu ya Jo, uhitaji wake Stella aliweka bayana kabisa bila kificho.

Akatulia akifikiria akaona aulize. “Sasa kwa nini hukumpa?!” “Nina akili zangu timamu, ninauelewa na nina maamuzi yangu. Ile mara ya pili tu narudi pale kwenu, ambapo sikukuta, nilikuwa nilishakufahamu kwa asilimia kubwa. Uliyokuwa umeniambia leo mchana ukidhani siyajui, yalikuwa ni marudio, lakini sikuambia jina lako. Ndio maana nilikuwa na shauku na jina, maana niliambiwa unaitwa mama Eric na unabinti mkubwa tu ambaye mumewe ndiye mwenye ile ofisi pale mnakofanya kazi, anaitwa Pam.” Mama Eric akashangaa sana wepesi wa Stella kusema habari zake.

“Lakini nikasema mama Eric sio jina lako. Hiyo ni sifa yako lakini si jina lako kamili. Niliposema hivyo ndipo nikaambiwa wewe ni bibi kabisa na unamjukuu mkubwa tu, mtoto wa Pam na huyo bosi wenu. Nikasema hiyo pia ni sifa yako, lakini bado nikataka kujua jina lako. Ndio maana nilirudi tena pale, leo mchana. Kwa nini nakwambia yote haya?” Kimya.

“Kukuhakikishia namfahamu Stella, kwa kumuona juu mpaka chini na kumsikia yeye mwenyewe, na bahati nzuri kwa muda mfupi nimeweza usoma mpaka moyo wake. Namfahamu Stella na wewe. Ambalo sikuambiwa juu yako, au sikulijua ni kama una wajukuu wengine wawili na kama Pam ni mjamzito. Naona kwa upande huo aliyenitambulisha wewe, kwangu na yeye hakuwa na hizo taarifa.” “Hao wajukuu wengine wawili ni watoto wa Eric. Kwa hiyo hajakosea. Mimi ni bibi.” “Hongera sana.” Akatulia akiwa anafikiria.

“Bado natamani muda na wewe Dorothy. Usio na muingiliano, na isiwe pale dirishani kwenu.” “Acha nikwambie ukweli Jo. Najiona kama sipo tayari kabisa! Hayo maisha ni kama yalishakufa au kuuwawa zamani mno hata kabla sijamzaa Eric. Huo upande na hicho unachotaka kukianzisha, kilishakufa na kuzikwa hata kabla hakijachanua, tena kwa miaka mingi mno. Nikiwa binti mdogo sana. Tumaini lake lilifunikwa nikiangalia na sikuwa na hatia, wala jinsi ya kujisaidia.” “Pole sana.” Akamuhurumia.

“Moyo ulishazoea. Nikaweza funga huo ukurasa kwa amani. Naogopa hata kufikiria kuja kufungua huo ukurasa hata kwa kuangalia tu bila kuusoma. Ni ukurasa, mkubwa, uliojaa fedheha, aibu na machungu, sina jinsi nikaeleza ukaelewa kwa kule nilikopitishwa.”

“Haufai hata kusimulika. Na nilishaweka amani kwenye kuufunika, siwezi kuruhusu mtu ausome na kujua kilichokuwa kikiendelea kwa uhalisia wake. Na nashukuru Mungu hakuna aliyewahi hata kutaka kuujua. Kwa hiyo kwa miaka yote hiyo, nilifanikiwa kuufunga na kuutupilia mbali hata na mawazo yangu. Sipo tayari kurudi huko, Jo. Si mimi. Wala usipoteze muda. Sasahivi nawaza wajukuu na watoto waliopatikana kwenye huo kurasa. Basi.”

“Japokuwa nitataka kuja kujua ni kwa nini ufikie maamuzi hayo, kwa kuwa kwa ukweli wewe bado ni mdogo Dorothy. Mdogo hata kwangu. Unaonekana uliwahi tu kuzaa. Halafu wewe ni mzuri wa kuvutia. SANA. Nitataka kujua ni kwa nini uhitimishe kwa kujipunja kwa kiasi hicho. Lakini nitakwambia kitu huyu shemeji yangu aliniambia kwa kurudiarudia sana baada ya kifo cha Betty.”

Pale Penzi Linapokoma Gafla Na Kikatili

“Ni kama hapo ulipo, na mimi nilikuwepo. Ila kwa sura ya tofauti. Nilikufa ganzi, halafu mwenzio nilipoteza dira kabisaa. Kabisaa. Bora wewe unasema ulifanikiwa kufunga kurasa zake na kuweka mbali. Mimi ni kama nusu yangu ilikufa na Betty, halafu nusu ikaachwa hapa duniani ikiwa kwenye kisiwa cha peke yake, isijue ndio inatakuwa kufanya nini kuanzia hapo.”

“Na ukumbuke hapo Betty aliniachia vijana wake wameshakuwa wakubwa, wanajitegemea. Yaani maisha yangu yalikuwa ni mimi na yeye, halafu yeye akaondoka, tena gafla tu!” “Pole Jo.”

“Asante. Lakini nataka kukwambia yalikuwa ni maisha ya upweke kupita nitakavyokwambia. Na wakati huo hata sikuwa na wajukuu wakusema nijishugulishe nao, nipoteze muda! Hakuna. Maisha ya huko tulipokuwa yakawa ya upweke sana.”

“Huyu shemeji yangu ni mume wa dada yangu wa kwanza, lakini alitusaidia tokea vijana wadogo na yeye ndiye aliyenipeleka kusoma kwenye chuo ambacho kilikuwa kwenye mji aliokuwa akiishi na dada.”

“Kwa kifupi yeye ndiye aliyesaidia ndugu zangu mpaka kufika tulipofika. Kwa hiyo ni shemeji lakini akageuka kama kiongozi wa familia yetu. Sisi wazazi walifariki tukiwa bado hatujasimama vizuri kimaisha. Ndoa ya dada ndio ikawa ukombozi kwa familia yote. Nitakueleza haya baadaye.”

“Lakini aliona mwanzo wangu na Betty. Betty nilimkuta nchini Marekani akiwa na wazazi wa kitanzania, lakini yeye alizaliwa kule. Alikuwa raia wa kule. Wazazi wake walikuwa wakifanya kazi na shemeji ndio chanzo chakufahamiana na Betty. Mwanzoni tulikuwa marafiki tu wakawaida maana sikumfikiria Betty kama mke. Hakuwa na rangi ya mwanamke ambaye nilitaka kuja kuoa. Lakini Dorothy, nikagundua japokuwa rangi haikuwa matakwa yangu, lakini alibeba sifa karibu ZOTE za mwanamke niliyehitaji kuwa naye, na kupitiliza. Kasoro hiyo rangi tu. Kwamba hata yale ambayo sikuwa nikidhani naweza yapata kwa mwanamke, alikuwa nayo Betty.” Akasikia kumuhurumia na yeye kupoteza mtu muhimu hivyo!

“Kufupisha habari, nikamuomba kumuoa. Safari yetu ikaanzia hapo. Unaweza usiamini, lakini Betty alikuwa ni wale watu wanaoweza kukufanya umfuate kila mahali. Tukasoma kitu kinachofanana na tukawa tukifanya kazi hospitali moja. Hebu niambie, kwa mtu ambaye mlikuwa naye hivyo kwa zaidi ya miaka 20, katika magumu na marahisi, kila mahali mpo naye, gafla anakuacha hivihivi tu! Kwa hakika nilipoteza dira na ni kama niliacha kuishi bila mimi kujua.”

“Yaani shemeji ndiye aliyenishitua na kuniambia, maadamu bado nipo duniani, nisiache kuishi. Maana nilishindwa kuendelea kwenye ile kazi niliyokuwa nikifanya naye, nikajiingiza kwenye doctors without borders program. Nchi zote masikini bila kujali rangi wala nywele, kule kwenye uhitaji ndio nilikuwa nikienda mimi. Kulikokuwa na vita, ndiko nilikuwa nikienda na madaktari wenzangu kusaidia bila kujali hatari yake ya kuwepo huko. Ilimradi tu nisiweze kujifikiria mimi wala Betty.”

“Nilijitoa kwa mali na hali. Niliuza vitu vyote ikiwemo nyumba tuliyokuwa tukiishi na Betty, nikarudi kuishi na dada na huyu shemeji yangu, endapo narudi nyumbani. Lakini naweza kukwambia kwa mwaka, pengine mwezi mmoja ndio nilikuwa nikirudi nyumbani, ila muda mwingine wote, nilikuwa nikiishi sehemu pengine nalala kwenye vijihema tu au nje kabisa nikihudumia watu. Ndipo shemeji akaniambia kabisa, nisiache kuishi.”

“Kumbuka hapo watoto alioniachia Betty wakawa hawana tena nyumbani. Nimeuza nyumba ambayo na wao ilikuwa kwao kila wanaporudi kupumzika. Nikauza bila kufikiria, ndipo nikaanza kuzunguka ulimwenguni kitu kilichomuathiri sana mtoto wangu wa mwisho. Nilimtisha vibaya sana. Akaingiwa hofu ya kupenda akiogopa yasije mpata yaliyonipata. Kwa ufupi sikuwa mfano mzuri kwao. Na yeye ndiye alikuwa kipenzi cha Betty, ungeweza sema hakuacha kumnyonyesha.” “Poleni sana.”

“Asante. Kwa hiyo pale kwa dada na huyu shemeji ndio pakawa na kwa watoto wangu pia. Wote watatu tukajikuta kwa dada ndio kimbilio. Hatuna kwetu tena, aliondoka nako Betty.” Akaweza hisi uthamani wa huyo mkewe.

“Kufupisha habari, nataka kukwambia hichi nilichoshauriwa mimi kuwa, maadamu upo duniani, jua wewe kama Dorothy, unawajibu wa kuishi. Usimzike Dorthy kabla Mungu mwenyewe hajaamua kumzika. Upo hapa duniani kwa kusudi. Na umama au ubibi si kusudi pekee linalokubakisha hapa duniani. Umenielewa?” Akamsikia akivuta pumzi kwa nguvu.

“Dorothy?” “Nimekusia Jo.” “Sikupotoshi. Ila nakukumbusha tu. Na jua na mimi nipo na familia. Watoto na wajukuu kama wewe. Na nakuahidi tutasimama pamoja. Sitakutenga na majukumu yako ya umama au wajukuu, lakini maadamu bado upo kwenye hii dunia, tafadhali na wewe kama Dorothy, ISHI. Ulikopitishwa na maisha, isiwe mwisho ila fundisho. Wewe bado unanguvu. Na Dorothy, wewe ni mzuri bwana! Sana.” Hizo ni sifa alizozoea kusikia zamani sanaa. Akamkumbusha mbali na kumfanya ajisikie aibu japo hakuwa akimuona. Akacheka akisikika yupo mawazoni.

“Acha kujipunja. Bado unayo nafasi ya kuishi vizuri kama wewe bila kofia ya umama au wajukuu. Ni sawa?” “Hata sijui pakuanzia tena! Nimetoka huko muda mrefu sana. Nilishapoteza dira kabisa.” “Niruhusu kukushika mkono wakati tukitafuta ramani ya kuendelea mbele sio kurudi nyuma. Nilikwambia sio mambo yote yanafikiwa na miguu. Unakumbuka?” “Mmmh!”  Ikawa ngumu kusadiki. Kama alitendwa akiwa na uwezo wa kutembea, leo mlemavu!

“Ni utayari, imani na kufungua moyo. Tutafika tu. Usiogope na kuwaza mengi sana kwa wakati mmoja. Hatua mojamoja, kila siku. Nakuhakikishia utakuwa sawa. Si ni sawa?” “Tutaona.” Bado alimsikia akiwa na moyo mzito. Akaona amchukulie taratibu.

“Nikuache ukapumzike, kisha tuiangalie kesho inavyokwenda. Hata dakika 10 tu kama hivi. Sisi wawili tu. Hata tukishindwa kuonana ila angalau nikusikie kwenye simu, itatosha.” “Kama hivyo ni afadhali. Maana unajua toka yangu ni mpaka dereva ambaye anakuwa na gari ambayo baba Shema anatoa kubwa kwa ajili ya kubeba kigari changu. Na siku ambazo siendi kazini namtumia dereva huyohuyo wa Shema, anakuwa na mambo mengi.”

“Na pia kama sio huyo dereva basi huwa anakuwa ni Pam. Na nikiwa na Pam nakuwa sina wasiwasi. Na yeye ananijulia kama mama, siwi na hofu na kufika popote, najua watanisaidia tu. Na nikiwa na Pam yeye huwa ananibebea kiusafiri changu cha kawaida. Walker au wheelchair ya hawaida ya kusukuma. Pagumu anakuwa akinisaidia. Siwezi daladala.” “Usijali. Tukiwa tunatoka, mimi mwenyewe nitakuwa nikija kukuchukua. Acha tuone kesho itatupa nafasi gani na ya namna gani.” “Sawa.”

“Nashukuru kwa muda wako. Sasahivi nalala kwa furaha nikijua angalau lipo tumaini.” Akacheka tu. “Usiku mwema Dorothy. Ulale salama. Nitakusikia kesho.” “Na wewe.” Ndipo wakaagana. Ila alijawa na furaha huyo Dorothy, hakutegemea kabisa kama kitu kama hicho kinaweza kuchipua tena moyoni mwake. Hakujua kama ni tumaini au ile hali ya kujaliwa yeye kama yeye!

Wakati anapitiwa na usingizi akimtafakari Joel, mawazo yakaanza kumuingiza hofu. “Iweje asinitafute tena? Alale aamke afikirie amefanya kosa kwa mtu kama mimi mlemavu?” Hilo nalo likafanikiwa kuanza kumpokonya kale kafuraha moyoni.

Mapenzi Ni Karata, Kila Mtu Hucheza Kwa Uzoefu Wake Na Vile Alivyojaliwa

Wakati mama yake akiwa amelala akiitizamia siku ya kesho kuona mwendelezo wa Jo, yeye Pam alilala akitaka apotee kabisa hapo duniani kwa masaa mengi asipate muda wa kujifikiria kabisa. Na Mungu akamsaidia alilala kama mfu. Akaja kuamka asubuhi ya saa moja na nusu. Njaa. “Mama, nasikia njaa sana.” Mama yake akiwa usingizini akamsikia akilalamikia njaa hapo pembeni yake. “Jana usiku uliletewa ugali na baba Shema. Kawasubiri hapa, wewe na mwanao mpaka saa tano usiku, akaondoka.” Ndipo Pam kuangalia vizuri akamuona na Shema naye amelala hapohapo, pembeni yake.

“Hata sikumsikia akija! Ndio maana kusumwa kulikuwa kwingi!” “Naona alikuwa amechoka. Amefika tu na kukufuata na kulala. Umeletewa ugali. Upo. Nenda ukale.” Akamuweka mwanae vizuri hapo kitandani, akatoka kwenda kula.

Alikula ugali wote na mboga zote. Akaoga na kutoka kwenda kutafuta vitafunwa vizuri akijua mwanae yupo hapo akiamka, ataanza kumsumbua bibi yake chakula. Akaenda kufanya manunuzi, mama Eric anaamka na kufika jikoni, akajua huo ugeni si wa usiku mmoja. Maana kulijaa hapo jikoni kama chakula cha mwezi!

“Unga huu ni wa dona, huu ni wa uwele. Wote ni wangu, nimeupata mbali kweli! Wenu huu hapa.” “Kwanza hamna mpenzi wa ugali humu ndani. Wala usihangaike kutenga.” Pam akacheka huku akitoka jikoni.

“Baba Shema alikusubiri hapa mpaka saa tano usiku.” Akamfanyia kusudi akijua hataki kumzungumzia. “Nimekuja na feni jingine. Nimeona Shema anakazi yakulowesha tu kitanda kwa jasho.” Akajua amemsikia sana. Akamjaribu tena. “Sasa vitafunwa vyote hivi ndio mpango wake ukoje?” “Utajua kama ni vichache atakapoamka Shema. Na bado atakulalamikia! Hashibi mjukuu wako.” “Najua alikorithi.” Akamsikia akicheka huku akiingia chumbani.

Alipotoka akiwa anaelekea tena uwani, akamuwahi tena. “Sasa utakunywa chai au ugali tena? Maana tulipika tu wali, maharage na nyama, lakini hatukula, baba Shema alileta vinono.” “Sasa mwambie mrembo wako, mimi nimetoka kula ugali. Akiniandalia hizo chapati nilizoleta mbili, hayo maharage na nyama. Nikanywa na ile chai yako! Hapo mtakuwa mmenitendea vizuri.” Akaingia bafuni, wazi akimwambia mama yake hataki aambiwe habari za baba Shema. Akamuacha akijiambia asije nunua ugomvi, na Pam anamjua.

~~~~~~~~~~~~~

Akatoka uwani akatoa nguo akajifunga kitenge cha mama yake na kwenda kula. Wakati anakula Shema akaamka. “Nikisimama hivi, naona nyumba nzima inazunguka.” Pam akacheka. “Ndio maana bibi yako anasema umerithi kwangu kupenda kula. Sasa wewe njaa hiyo kali unaitoa wapi Shema mwanangu na ndio umetoka tu kitandani! Kweli?” “Mimi siwezi kwenda hata kufuata kikombe.” “Shema!” “Kweli mama. Naona bora nikae tu hapahapa niletewe kila kitu.” Pam akacheka na kupunguza sauti.

“Bibi yako akikusikia!” “Mwambie wewe mama.” “Haya njoo Shema.” Wakamsikia mama Eric jikoni kwamba ameshawasikia wakinong’ona. “Njoo uchukue chache iliyopo hapa jikoni, huku ukisubiria nikimalizia kupika chai ingine. Maana iliyokuwepo mezani mama yako kamaliza chupa nzima!” “Mama naye! Analalamikia chupa ndogo hivi!” “Ndio kiasi inayowatosha wanao ishi humu ndani je! Vitu vyakututoshea sisi tu. Sasa wewe umekaribishwa, huna aibu, unahamia na chupa ya chai nzima sakafuni, umekunywa chai yote!” Pam akaanza kucheka.

“Ulisema chapati mbili tu, naona upo ya nne, na huna mpango wa kunyanyuka hapo. Unakazi ya kuagiza uongezewe maharage tu. Njoo Shema uchukue mwenyewe, dada anakazi zingine.” Ikabidi Shema aende, alimjua bibi yake hataki awe anatumikiwa kama hana mikono. Akapewa chai, vitafunywa mezani. Asikae mezani, akaenda kukaa sakafuni kama mama yake, wanakula huku wanapepewa na feni. Stori zikaanza anamsimulia mama yake mambo ya shule huku anakula.

Mtakuja.

Hodi mlangoni. Wakajua wazi ni baba Shema. Kimya. Shema anamwangalia mama yake, mama yake anaendelea kutafuna kama ndio ameanza kula. “Hivi nyinyi wawili hapo chini, hamsikii hodi?” “Hapa kwako bibi.” Shema akamfanya mama yake acheke. “Mama alisema tusikukaribishie wageni.” “Anakufundisha ujinga.” Pam hana mbavu, hakanushi. Akamtuma msichana wake akafungue.

Bwana Mill alijifungasha kama alijua mwanae anavyokula na mama yake. Mwanae akasimama kumpokea maana msichana wa kazi alilemewa. “Wewe Shema twende wote kwenye gari.” Ilikuwa saa tano asubuhi. Akawa amerudi na mafeni mengine, lakini yake yalionekana yana nguvu zaidi, tena ya kisasa.

“Sasa moja chumbani kwa bibi, haya mawili chomeka pale sebuleni.” Akamsikia akimwambia mwanae hapo nje. Akajua joto la usiku alipokesha hapo lilimkomesha. Alimjua Mill na joto, si marafiki. Kimya hapo sakafuni akiendelea kula.

Wakaingiza vitu mpaka wakamaliza. Akaingia Mill mwenyewe. “Karibu baba Shema. Tungekukaribisha chakula, lakini Pam na mwanae naona wamemaliza chote.” Pam alicheka sana. “Nyie mama! Angalia hapo mezani kama hatujabakisha.” “Alileta vitafunywa hapa! Ameenda kuvifuata asubuhi! Mimi nikadhani ni vya mwezi! Akaniambia vitatutosha sisi sote na Shema mlaji sana. Amekaa na mwanae hapo sakafuni, namsikia anakazi ya kumuagiza mwanae aongeze, hamalizi kula! Hapa namsongea ugali ili tupumzike.”

“Nimeleta vingine mama.” “Ila acha tu na ugali uwepo.” “Nimeleta uliokwisha songwa kabisa. Pumzika mama mama yangu. Na wewe njoo ule. Na kuhusu mimi msihangaike. Nimeshakula. Nipo tu sawa.” ‘Sasa mimi niongezewe chapati ya mwisho, nilale, nikiamka ugali.” “Hapana Pam. Kuwa na kiasi bwana! Na sisi tunataka chapati.” Pam hana mbavu. “Si mle hivyo alivyoleta Mill!” “Na chapati pia tunataka. Nzuri sana.” Pam akavuta mto wa kwenye kochi, akajinyoosha hapohapo mbele ya sahani zake na kikombe. Akalala sakafuni.

“Haya, Shema. Mletee mama yako maji, anawe mikono kabla hajapitiwa na usingizi hapo.” “Mama usilale kwanza. Baba kaleta maandazi mazuri kweli!” “Wewe nisaidie ninawe mikono mwanangu. Na ukiniletea na mto mkubwa pale chumbani ndio utakuwa umenitunza.” Shema akacheka na kuondoka hapo akitafuna.

“Umelalaje na mtoto?” Akajua wazi Mill anamuongelesha yeye, lakini akajidai kama hajamsikia. “Niletee na kitenge cha bibi hapo chumbani, Shema. Uje unifunike kabisa. Kaubaridi hapa kazuri kwelikweli.

“Pam, kabla hujalala, naomba tuzungumze.” “Hapa nilipojilaza, sitanyanyuka. Wewe zungumza tu nakusikiliza.” “Ni jambo muhimu.” “Si ndio nakwambia nakusikiliza!” “Nataka tukiwa wawili tu.” “Wewe Mill ni msumbufu sana aisee! Ushalala kwako, usingizi umekuishia, ndio unakuja sumbua wengine. Mida ya mazungumzo hutaki kuzungum…” “Haya Pam nenda kamalizie hiyo sentensi yako huko nje. Sio hapa kumtia mtoto wasiwasi.”

“Nasikia usingizi mama!” “Ukirudi, utalala. Huo usingizi si wakuisha kwa kulala sasahivi. Haya nyanyuka hapo. Shema niwashie nyimbo zangu za dini.” Pam akajishauri hapo, ila akasimama na kutangulia nje. “Asante mama.” Mill akashukuru akifuata nje kwa haraka.

Mapenzi Yatafuta Bandari Ya Milele

“Wewe ni msumbufu Mill! Ni nini kwenye majumba ya watu asubuhi asubuhi?!” “Naomba tuzungumzie ndani ya gari. Hili joto linanitesa mno.” Hapo alishaanza kutokwa jasho. Akafungua gari na Pam akapanda. Akamgeukia kumsikiliza. Akawasha AC mpaka mwisho, Pam akimtizama tu.

“Naona wazo lile la jana ni zuri, tulifanyie kazi.” Pam akabaki akimtizama. “Nazungumzia lile wazo ulilokuja litoa pale ofisini. Maana maandalizi ya harusi hii nyingine inaendelea na nishalipa nusu ya bajeti nzima. Wote tuliowalipa wanaonekana tarehe za kabla, wanashuguli zingine, hatuwezi badilisha. Kwahiyo tufanye mpango wako.” “Ujue unanitania Mill wewe!” Mill akawa hajaelewa tena.

“Ulipokuwa ukimlipa Kisha pesa umuoe, ulikuwa ukizungumza kwa mafumbo hivihivi? Sasahivi unasema eti mpango wangu! Inamaana wewe huna shida na ndoa, ni mimi nakulazimisha?” “Sio…” “Basi sitaki tena. Na mimi sina shida.” Akafungua mlango na kushuka. Mill naye akaanza kumfuata.

“Pam! Pam!” “Acha kunipotezea muda na kunifanya mimi ndio mwenye shida sana ya ndoa, wewe huna. Umenikuta sijaolewa wala sina mwanamme ndio..” “Nilikukuta na Mgaya.” Akamrekebisha kwa tahadhari.

“Unanitania Mill?!” “Nilikuwa najaribu kuweka sawa taarifa. Sio kutaka kukuudhi zaidi.” “Kwa hiyo kunikuta na mtu kama Mgaya ndio ukadhania mimi nimekwama sana! Unarudi na kunifanya mimi mjinga! Eti ule mpango wangu! Acha kujifanya kama huelewi mambo, wakati wewe ukitaka YAKO, upo hodari sana wa kufanikisha. Usinifanye mimi mjinga.” Akarudi ndani. Wakamkuta Shema amekaa kwenye kochi ashakuwa mwekundu kwa wasiwasi.

Baba yake akaingia. Mama Eric na msichana wake wamekaa mezani wanakula, Shema kwenye kochi. “Hatujamaliza mazungumzo yetu Pam.” “Mimi nimemaliza.” Akarudi ndani, chumbani kwa mama yake, akabadili nguo tena. Akajifunga kitenge. Akarudi kujilaza palepale sakafuni. Joto.

“Shema, dereva anakuja kukuchukua muda si mrefu. Hapa huna jezi zako. Muanzie kuchukua jezi kwanza. Beba maji ya kunywa ya kutosha, na kitu chakula baada ya mazoezi.” “Kule nyumbani hakuna kitu chakula mama!” “Hapa vimeletwa vikorokoro vingi. Muokotee.” Bibi yake akaongeza. Pam akasimama.

“Haya nenda kavae viatu, dereva anakuja sasahivi.” “Utamwambia anirudishe hapa?” Akamuuliza mama yake kwa wasiwasi. “Usiwe na wasiwasi.” “Mama!” Akawa kama ameshaingiwa wasiwasi anataka uhakika. “Nitamwambia akulete. Haya nenda.” Akaanza kumfungashia mwanae.

“Nakupenda Pam. Na ujue unaona ni kama inavuta, lakini ni kwa sababu nakuandalia kitu kizuri. Lakini naona mpango wak…” “Bwana neno hilo linanipandisha hasira! Bora unyamaze tu. Umekazania mpango wako, mpango wako! Ulipokuwa ukimlipa Kisha pesa na kutaka naye ndoa, ulimwambia mpango au uliyasema wazi?” Kabla hajajibu akaendelea.

“Umeniona mimi mjinga, kwa sababu nakuzalia tu watoto, ndio unasema mpango wangu! Wako upo wapi, kama si kutaka kunidhalilisha tu? ‘eti mpango wako!’ Maana..” “Pam, ni aidha utulie, ili huyo mwanao akayafanye hayo mazoezi, au mumuache leo asinde mpaka hasira zikuishe. Mwanao amejificha mlangoni pale chumbani hata viatu sidhani kama amevaa.” “We Shema?”

“Hapana Pam. Nilikwambia mkazungumze nje, ukijua Shema hapendi kusikokuwa na maelewano. Unammaliza nguvu kabisa! Umeona huko nje hapatoshi, mmemfuta humu ndani kumchanganya. Hana anachokwenda kufanya huko. Atafika huko analia, atarudishwa hapa kama mgonjwa na wewe unamjua Shema.” Pam akamfuata.

“Nyamaza mtoto mzuri.” Wakamsikia akimbembeleza mwanae kwamba alishaanza kulia. “Sasa leo ni mashindano au mazoezi tu?” Akawa akimlaghai kwa swali ili atulie. “Nataka kurudi hapa.” Wakamsikia Shema akilia kwa wasiwasi. “Usiwe na wasiwasi. Kwanza mimi naona nikupeleke mpirani, mimi mwenyewe.” “Hulali tena?” Wakamsikia akimuuliza mama yake huku akilia. “Nitalala tukitoka mpirani.” “Bora!” Pam akamsikia mama yake akidakia nje.

Akacheka. “Mama hapendi wageni!” “Wavunja amani, hapana.” “Eti Shema mtoto mzuri? Sasa leo ni mazoezi tu au mashindano? Nijibu huku unavaa.” “Leo mazoezi, halafu ijumaa tunakwenda kushindana.” Wakamsikia Shema ameshabadilika, amechangamka kwelikweli, anavaa huku akimsimulia mama yake habari ya timu pinzani. Mama Eric akabaki akitingisha kichwa.

Wakatoka chumbani yeye na mwanae wapo tayari. “Nimemwambia dereva asije, mimi nitawapeleka.” Mill akamdaka mara walipotoka. Pam akamtizama kwa sekunde kadhaa, akaingia jikoni kumchukulia mwanae kitu chakula baada ya mazoezi. Nakutoka akiwa amefungasha chakula chakumtosha mwanae. “Twende Shema mtoto mzuri.” Wakatoka wote watatu, wakaacha kukiwa kumetulia.

~~~~~~~~~~~~~~

Wawili hao wakamsindikiza Shema kwa utulivu kabisa mpaka akafanya mazoezi akamaliza. Mill kimya akijihami hajui mwisho wa hapo ni nini. Wakati wanatoka Mill akatoa wazo. “Twendeni tukale sehemu nzuri.” “Mimi nishaagiza chakula changu kule kwa mama. Naenda kwanza kule kwako, ndipo nirudi Kinondoni, kwa mama. Naona safari yangu na wewe inaishia hapa.” “Na mimi naenda na mama.” Shema akawahi. Mill akajiweka sawa.

“Nina wazo.” Pam akabaki akimtizama. “Tule ndipo tupate muda wa mazungumzo.” “Wewe umekusudia kunikera bila sababu.” “Sio nia yangu. Nataka…” “Nisikilize Mill. Na ujue sitajirudia.” “Kumbuka kuna mtoto hapa, Pam.” “Basi twende Shema.” “Pandeni niwapeleke mnakotaka kwenda.” “Panda Shema na utupekeke kwako si kwingineko.” “Sema kwetu, Pam! Pale hapana raha bila nyinyi. Maisha…” “Naomba nyamaza Mill. Shema, kula upunguze njaa.” Akampa mwanae chakula, na juisi. Akaanza kula, Mill anaendesha kuelekea kwake hajui wanaenda huko kufanya nini.

Pam akatulia garini kimya akaanza kusinzia. Mill alipomwambia wamefika akamwambia Shema asubirie kwenye gari hatakawia. Mill akaona afuate nyuma. Kimyakimya mpaka chumbani kwake ambako ndipo wanalala na huyo Pam. Akasimama kuangalia anachotaka kufanya.

Gafla akamuona anaanza kufungasha. “Acha hizo Pam! Umeshindwa tu kunielewa. Nakuandalia kitu kizuri.” “Kitakapo kamilika, utanitafuta.” Akaendelea kukusanya vitu vyake baadhi. “Na hivi vingine vitabaki kwa muda. Nikiona hiyo tarehe yangu imefika na kupita hata siku moja, na bado unamipango yako isiyoisha, nakuja kukusanya vitu vyangu vyote na mwanangu, tunaondoka.” Akampita hapo na kuhamia chumbani kwa Shema.

“Sasa kuliko kwenda kumsumbua mama kule, na nyumba ndogo hiyo hapo nilikupa, na nikakwambia ni pako hakuna maswali. Kwa nini sasa usirudi pale kuliko kwenda Kinondoni?” Pam akasimama akifikiria.

“Hilo wazo zuri sana mpenzi wangu. Pale kwako. Usiende jitesa na kujibana kule kwa mama. Rudi hapo kwako kwa muda. Jioni tukizungumza…” “Usinitanie Mill.” “Basi naomba usimpeleke mwanangu kule, mwache hapa kwao.” Akaona wazo sio baya. Akaanza kuhamisha mizigo. “Nikusaidie nini?” “Sitaki.” Akaendelea kupambana na vitu vyake.

“Sasa mbona ni kama ulisema vingine unaacha hapa mpaka ile tarehe?!” “Nimebadili mawazo, na pale nisikuone Mill. Ukija tu, ujue naondoka kabisa.” “Basi wakati ukihamia kwako, acha nikawaletee chakula.” Pam hakumjibu akaendelea kukusanya.

“Ushafikiria picha unayoiweka kwa mtoto lakini?” “Wala haitaji picha ya mimi kumuonyesha. Anaona kila kitu. Na leo atajifunza ni mwiko kumchezea mtoto wa kike. Kama anamtaka huyo mwanamke amuoe, sio kuonea mtu sababu ya umasikini wake au unyonge wake, ndio anakazi ya kumchezea tu kama doli. Ajifunze kwa vitendo. Maana bila hivyo historia ya kwenu inamuhusu Shema.”

“Haya maisha umekua ukiyaona Mill, ndio maana huna shida ya kuishi na mimi, bila ndoa.” “Sio kweli Pam!” “Wewe nenda kaniletee ugali wangu kwa mama pamoja na pochi yangu ipo simu ndani, na umpe Shema. Kule nisikuone Mill. Acha kunifanya mimi mjinga.” Mill akatoka, baada ya muda mfupi Shema akaingia.

“Baba ameniambia nije kukusaidia.” Yeye na mwanae wakaanza kazi ya kuhama tena, wanarudi nyumba ndogo. Mwanae yupo kimya hajauliza swali, yeye bora awe na mama yake.

~~~~~~~~~~~~~~

Usitingishe kiberiti kama hakijajaa. Pam alishajihakikishia nafasi yake kwenye moyo wa Mill. Ipo thamani aliyojihakikishia ameweka kwa Mill, akijua si rahisi kwa Mill kumwacha aende. Wana historia ndefu. Kuna misingi walishawekeana wao wawili kama Andy& Mina, ndio maana historia haiachi kuwarudisha Pamoja.

Hakuna Mavuno Kusipopandwa.

Jo naye anaonekana kumng’ang’ania Dorothy, mama Eric akimjua fika yeye ni nani. Historia ya Pam inajirudia kwa mama yake. Kung’ang’aniwa na mwanaume ALIYEKWISHA WAHIWA na Mrembo mwingine.

Ni Nini Kitaendelea Kwa Love At First Sight Hawa?

 


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment