“Una funguo?” Akamuuliza
Pius. Pius akatoa mfukoni. Zichezeshe huku ukimuongelesha. Anapenda michezo kupita
kiasi, sasahivi atakufuata.” “Na Ayan aje hapo. Akimuona Ayan yupo karibu na
Pius na yeye ataanza kujisogeza, kama baba alivyofanya mwanzo kabisa wakabaki
kuwa marafiki.” Mina akaongeza wazo jingine. Wakamuita Ayan.
“Nenda kapokee
zawadi kutoka kwa anko na umwambie asante.” Ndio Ayan akasogea kwa Pius,
akambeba na kumkalisha kwenye mguu wake mmoja. Kisha akampa pole kwa magumu
aliyopitia kipindi cha nyuma. Akamuomba msamaha kabisa. Ikamgusa mpaka Andy.
“Najua una akili
Ayan. Lakini uliletwa kwenye maisha yetu sisi wote tukiwa hatujakuandalia
mazingira mazuri. Tulikukosea. Ila jua tunakupenda sana. Na
kuanzia sasahivi utaona mabadiliko. Hata anti Raza naye ataacha kukuchapa.
Atakuwa anti mzuri kwako. Umenisikia?” Akatingisha kichwa kukubali.
“Umenisamehe na mimi pamoja na anti Raza?” Akakubali bila shida. “Basi
nashukuru na nakuahidi, kuanzia sasahivi, hata dad na mummy wako wasipokuwepo,
wote tutakuangalia kwa upendo. Usiogope tena.” Wakamuona anaanza
kutulia.
Ndipo akaanza kumuuliza
maswali mengine ya shule na kama ametengeneza marafiki. Akataka amtajie majina
yao, mpaka Ayan akatulia kabisa akionyesha hofu imeisha maana Pius
alimuuliza maswali ya shule yaliyoanza kumfanya acheke huku akimsifia kwa hili
na lile. Ayvin akawa anawatizama tu huku amepakatwa na Andy.
Pius
alipotengeneza na Ayan akamwambia amsomee kile kitabu alichomletea. Akaanza
kusoma taratibu mpaka akamshangaza Pius. “Huyu mtoto si mdogo sana kujua kusoma
kwa kiasi hichi!?” Wakacheka.
Akaendelea
kusoma, alipofika katikati Pius akaanza kumuita na Ayvin akimwambia aende
akasikilize hadithi, kaka yake akisoma. “Hapo ndipo uchezeshe hizo funguo. Ndio
atawasogelea na kuanza yeye kutaka kusoma na fujo zote. Hapo anatamani
apewe yeye hicho kitabu cha mwenzie. Anakuogopa tu, lakini angeshamsogelea, akivute,
aanze kusoma huku anamwangalia kaka yake.” “Sasa mwenzie anasomaje?”
“Amejifunza kulala naye hapo sakafuni, wanaweka kitabu chini anasoma na yeye
pia anasoma kwa kelele. Na kwa kuwa hawezi kutulia sehemu moja, mwishoe
anamuachia kitabu chake anaenda kufanya fujo kwingine.” Wakacheka.
Na kweli baada
ya muda akaanza kuchangamka akawasogelea. Mpaka Raza anarudi na watoto wake,
amechangamka, ila alipoa tena walipoingia mpaka Polla cha utundu na yeye
akaanza fujo zake hapo ndio pakachangamka zaidi. Yeye na Polla ndio fujo
wakifanya kila kitu, na Polla akamjualia zaidi anataka acheze naye kama umri
mmoja!
~~~~~~~~~~~~~~~~
Kwa hakika ipo
nguvu ya msamaha. Jambo ambalo lilikuwa gumu wakajikuta wapo wote hapo
kwa furaha zote kama familia moja. Vilijaa vicheko, Raza akamfuata Mina jikoni.
Nikusaidie nini au na wewe unaniogopa nitakuwekea dawa?” “Mimi mwenzio
uchawi siogopi Raza.” “Kweli Mina!?” “Wala si kwa kujisingizia.” Mina
akaendelea.
“Acha nikwambie.
Upande wa baba walikuwa washirikina sana. Na walimtisha sana mama
wakimwambia watamkomesha kwa kuwa ametuchukua kutoka kwao basi hata yeye
ni kama atatukosa. Nafikiri kuna ukweli aliuelewaga juu ya nguvu
ya mwamini na ulinzi wa kiMungu kwa wana wake, hapo mama yangu
hakuwahi kutoka. Hata mimi nilipokuwa nikimsumbua, aling’ang’ana tu
na maombi, basi. Nafikiri na mimi hicho kitu kiliniingia. Siogopi ushirikina
kabisa na wala si kwa kujidai. Ila si mjinga kwamba siamini kama naweza
kujaribiwa! Ila naamini kwenye ushindi wa kiMungu. Wewe karibu fanya
utakacho.”
“Naomba nisaidie
ili kutoa kitu kitakachojaza tumbo la Pius aweze kulala vizuri.” Stori kwa
wawili hao zikaanza. Kuongea na kucheka. Kwa hakika Mina akawa faraja
kwa Raza asijue tu. Jinsi alivyomchukulia! Alivyozungumza naye, hakumuonyesha
kumuhukumu kabisa.
~~~~~~~~~~~~~~
Wakajikuta wamenogewa hapo, wamesahau mabaya
yote wala hawayazungumzii. “Umebadilika Raza! Mpaka neno unajua!”
“Nilipata kaka wa kiroho, na mkewe mtulivu mno. Tena hakika Mungu alibadili mabaya
yangu kwa wema. Sonia aliyekuwa anifunge ndiye aliyenitambulisha kwa
kaka Nyange na mkewe. Aisee, ni watu wazuri! Nilihamia kanisani kwao.
Wanasimama na mimi kwa kila hatua. Pazuri sana.”
“Nakwenda
kanisani mpaka nasikia raha! Polla naye ameanza Sunday school. Poliny
naye na Pius wameniunga mkono.” “Haiwezekani Raza! Pius ameacha kwenda kwa
wakatoliki!?” “Mimi mwenyewe sikuamini. Kina Ruhinda na dhehebu lao, utafikiri walichanjiwa!
Lakini hivyo vichwa viwili vigumu, vimejiunga na mimi. Siamini!”
“Mama Ruhinda atachanganyikiwa.”
“Sidhani Mina. Wananiogopa na kunikimbia kwa wazi kabisa. Watakuwa
wamefurahi nimeondoka kwenye maisha yao. Paulina hamtaki hata Polla
nyumbani kwake!” “Pole Raza. Acha sasa kulia bwana!” “Naumia
Mina, naumia sana. Wanamtenda ubaya malaika wa Mungu huyu hana hatia jamani!”
“Nisikilize
Raza, hawa watu umewatisha sana. Wape muda. Na wewe unamjua Paulina
shoga yako. Ni bendera fuata upepo. Sasa kwa kuwa sasahivi Pius yupo upande
wako, yule mama hajiwezi bila Pius, watarudi tu wenyewe.” “Na
wewe usinitupe Mina. Tukue wote kiroho. Ukija Dar kuwa upande wangu.”
Mina alicheka sana.
“Mimi mwenzio
tokea mwanzo sinaga upande.” “Sio kihivyo na wewe Mina! Tuwe mashoga.
Kwanza familia zetu zenyewe zishajichanganya watoto sijui baba zao wako
huku na kule! Si bora sisi tuwe pamoja halafu nakuwa nakuja kwako na wewe uje
kwangu? Wakikuona wewe wanayekupenda sasahivi upo upande wangu ndio watajirudi
na kuniheshimu kama zamani.”
“Hilo halina
tatizo. Lakini Raza, hata tufanyaje, bado wewe ndio bimkubwa.
Akitoka mama Ruhinda ni wewe.” “Mmmh! Sio kama zamani Mina. Sasahivi wewe unapendwa.
Wewe ndio umeshika ukoo wa Ruhinda.” “Acha mawazo hayo ya kukunyima
raha, Raza. Mwenzio mimi nakuheshimu sana.”
“Hivi
nikikwambia na mimi natamani mtoto wa kike kama wewe utaamini?”
“Mmmh!” “Ndio ujue Mungu naye anayake! Hampi mtu kila kitu. Nimeomba mtoto wa
kike mpaka kwa kufunga na kuomba, lakini naona nimepewa dume jingine. Wala vilio
vyetu havijapishana.” Akamtuliza kwa maneno mengi weee, mpaka Raza
akatulia.
“Wewe
tushikamane. Na tukirudi Dar na mimi nitakuwa nikija kanisani kwenu. Hivi vya wakatoliki
vimenishinda bwana! Anaishiga kwenda Andy na wanae. Nikienda nao, naishia kukaa
mwanzo mwisho na Ayvin anaongeza utundu.” “Sasa huko kanisani kwetu kuna
madarasa ya mpaka umri wa Ayvin.” “Pangetufaa sana tu. Ila kwa Andy kumtoa Roma
yeye na wanae, ni hatua kwa hatua. Kila jumapili anaandaa wanae yeye mwenyewe
na anatoka hapa bila kuchelewa. Itachukua muda sana au inaweza hata isitokee. Ila
jua mimi mshirika wako.” Raza alifurahi huyo!
“Na ule
utaratibu wa kukutana kila jumapili ulikufa Mina. Hawanikaribishi
tena kwao. Wananiogopa.” “Ndio tutakuwa tukikutana kwako, wewe bimkubwa,
mama Ruhinda. Tunapika na kula pamoja. Wakiona kuna amani, watajirudi
tu.” Bwana Raza alifurahi huyo! Huna jinsi yakumtoa kwenye ukweli wa kwamba
Mungu hubadilisha mabaya kuwa mema, akaamini tena.
~~~~~~~~~~~~~~
Kwa hakika
walipata wakati mzuri. Watoto wao walikuwa wakibaki hapo wao wakawa wakienda
hotelini na kurudi hapo wanashinda mpaka
usiku. Hata Poliny mpenda shule akatulia. Akaonekana kufurahia hayo madhari ya
amani. Akamgeuza sasa Andy kuzungumza naye mambo anayoyapenda ya msingi. Uchumi
wa dunia na mengine anayoyafurahia huyo Poliny. Kama si nywele, ungemtizama
ungesema ni Pius kwa muonekano na haiba.
Walikaa hapo
mpaka siku ya jumapili ndipo walipoondoka, wakiwa na Judy, kama msichana wa
kazi. Judy alipanda mbegu moyoni kwa Mina, akashindwa kumsahau. Japokuwa
alirudi kwao, kwa mama yake na watoto wake, lakini bado Mina alikuwa na deni
moyoni mwake huku mjini. Akitaka kumsaidia kama yeye alivyomsaidia mpaka
akapatana na Andy.
Judy ndiye
aliyemtia moyo na kumuombea ili kwenda kuzungumza na Andy akiwa mjamzito, hajui
baba wa mtoto, Andy akimalizwa na hasira za wivu.
Ikawa msaada
haswa kwa Raza aliyekuwa na majukumu ya kazini na nyumbani. Sasa ikawa Raza
amepata mengi kwa wakati mmoja. Dada mtu mzima, mcha Mungu, na yeye anawatoto
kama Polla. Kwa kumwangalia tu Raza alimpenda. Alionekana anauelewa wa mambo si
mshamba wa kuanza kumfundisha kila kitu cha kisasa na ametulia.
Waliondoka kwa
ahadi ya jumamosi inayofuata wao kina Raza kuwa wenyeji wao kwelikweli. Kwamba
Raza na familia yake watatangulia nyumbani kwa kina Mina huko Kigamboni
wakiwasubiria.
Raza alimwambia
Mina wao watatangulia kwenye nyumba yao. Atasaidia usafi na kuandaa chakula
kabisa kwamba wao wakiwa wanafika hiyo siku wanahamia jijini, wanapokelewa
kwenye mazingira mazuri. Yakaanza mahusiano mapya kati yao. Ikawa furaha ya
namna yake angalau Raza akaanza kurejeshewa watu tena, Mina! Moyo ukapoa
kabisa.
~~~~~~~~~~~~~~
Ila kabla ya
kuondoka, akaomba kuzungumza na Mina na Andy. Pius akakunja uso. “Naomba wewe
Pius nisubiri hapa ndani na watoto.” Wakamfuata Raza nje. Andy na Mina
wakamgeukia. “Ni ombi. Na hili hata Pius hajui kama ninalo moyoni. Ila
nilianza kumuomba Mungu kwanza. Na sina nia ya kuwaudhi.” Andy na Mina
wakawa na shauku yakutaka kujua.
“Msikasirike
wala kunisemea kwa Pius.” “Ni nini?” Raza akavuta pumzi kwa nguvu sana
na kuzishusha akionekana na wasiwasi. “Ni nini Raza? Wewe sema tu.” Mina
akamtia moyo. “Jamani, huyu mtoto kwa Pius ni muujiza ambao sina
jinsi nikawaambia mkaelewa. Pius amefurahi SANA. Yaani tukifika hotelini
anakuwa na kazi ya kuangalia video zake unazokuwa ukimtumia wewe Andy, anacheka
sana. Kama mmegundua hizi siku mbili hapa, Pius amebadilika sana. Pius
si wakukaa sakafuni au wakukaa popote bila viatu!” “Nimemuona aisee!” Andy
akaafiki akicheka.
“Mimi kwa mara
ya kwanza ndio namuona Pius anakuwa sehemu mbali ya kitandani bila viatu mguuni kwake, na kukaa sakafuni kabisa!
Hakika sijawahi muona Pius sakafuni na akicheza magari kwa kukimbizana akitambaa.”
Wakacheka.
“Huyu mtoto, amenipa
Pius mwingine kabisa! Hata anaweza kutoa utani kabisa, mkacheka! Pius
amebadilika jamani! Naombeni mumsaidie.” “Nini?” Andy akauliza. “Najua
naomba jambo gumu na ni kama nataka kuwavuruga. Sio nia yangu. Lakini
Paulina aliniambia mlimkatalia Pius asiweke jina lake kwa Ayvin.” Hapo
wote wakapoa.
“Inaweza isiwe
kama vile alivyotaka yeye moja kwa moja. Lakini naombeni angalau aitwe
kama mnavyotaka nyinyi, ila angalau muongeze jina lake Pius, iwe Ayvin Pius Ruhinda. Tuache maswala ya Junior kwa sababu tayari yupo Ayan, ila angalau na
jina lake liwepo tu. Ni hilo tu jamani. Na samahanini kama
nitakuwa nimewaingilia. Na hata mkikataa tena, itaishia hapahapa,
sitatoka na kuanzisha tena habari ambayo ilishazikwa.” Mina alinyamaza
kabisa, hakutaka kumuingilia Andy na kumtibua. Kimya.
“Acheni tuwahi
kuondoka. Tusichelewe.” Raza akawa muungwana kama kuwapa nafasi ya
kufikiria. Akaondoka kabisa hapo na kuwaacha. “Sio lazima Andy. Kama alivyosema
Raza mwenyewe, nafikiri hata Pius ameshakubaliana na hilo. Tuache tu ibakie
kama ilivyo.” “Sawa.” Likawa jibu la jumla. Na Mina naye akaona
aache asije anzisha jingine la kuvunja amani.
Baraka Za Moyo
Ulionyenyekea
Siku ya jumatatu
akiwa ofisini kwake, Andy akampigia simu. “Ulishatengeneza cheti cha kuzaliwa
cha Ayvin?” “Bado. Kwa nini unauliza, au unataka ukitengeneze wewe?” “Hapana.
Ila nimefikiria, nimeona wazo la Raza si baya.” Pius
akawa hajaelewa.
“Ni nini?” “Ayvin ameshalijua jina
lake. Si sawa kuanza kumuita jina jingine. Lakini Raza aliomba angalau tuweke
jina lako katikati. Aitwe Ayvin Pius Ruhinda.” “Nitashukuru Andy.
Nitashukuru sana. Na nakuahidi katika hilo sitafanya fujo kuja kumuita
vinginevyo mpaka atakapokuwa mkubwa akijielewa, ndipo atalitambua hilo jina la
Pius katikati. Na hata hivyo Andy, hakika nakushukuru kuniruhusu niwe kwenye
maisha yake. Unaweza usijue hili, lakini aisee huyo mtoto nilimtafuta, Andy.
Mnoo.”
“Na ukweli, nakwambia na Mungu nishahidi,
sidanganyi, sikutaka huyo mtoto atokee kwa mwanamke mwingine ila Raza
ili kupunguza fujo. Mimi sipendi mabadiliko aina yoyote yale kwenye
maisha yangu, nafikiri ndio maana siwezi mahusiano ya nje. Nilijua hata
nikipata mtoto wa kiume nje, anaweza akaja na fujo zake, akatuharibia
amani pale nyumbani. Ndio maana aliposhindwa Raza, nikarizika na kutulia
kabisa.” Andy aliweza kusikia kweli inayotoka
kwenye moyo wa kaka yake. Akatulia kabisa akimsikiliza.
“Kwa Mina nilifanya kosa,
Andy. Lakini sikuwa na nia yakuzaa naye. Nakwambia hili kwa sababu umempokea
mtoto wangu kiasi ambacho nahisi mimi nilikuja kushindwa kwa Ayan. Ni
kama nilikuja kulegeza kamba baadaye.”
“Lakini wewe Andy, unampenda huyo
mtoto na yeye anakupenda aisee. Nimemuona akiwa mikononi mwako. Sina
budi ila kukushukuru kwa kumwambia ukweli. Sikukusudia kuzaa na Mina. Nilikosa,
na ninajua hata ukinisamehe bado nitabeba hiyo shutuma hata nikiondoka hapa
duniani, vizazi na vizazi watazungumzia hili KOSA langu.”
“Ila kwa sasa nakushukuru kwa jinsi
ulivyolibeba na kumfanya huyo mtoto kuwa baraka kwenye familia nzima ya
Ruhinda. Najua umenisamehe, lakini jua ni deni unanidai mpaka kifo.” Andy akacheka akisikika ametulia.
“Yameisha Pius. Kwa swala la jina?”
“Aisee hilo sitalazia damu. Nahisi mpaka mnakuja jumamosi,
nitakuwa nimeshakamilisha. Nitawaletea na hati yake ya kusafiria endapo
kutakuwa na safari itakayohitajika hati ya kusafiria.” “Ujue hata Ayan hana
hati ya kusafiria?” “Basi acha nitashugulikia zote mbili.” Pius alifurahi, hapakuwa na mfano.
~~~~~~~~~~~~~~
Alipokata tu
simu, hapohapo akampigia simu Raza. “Mbona unafuraha hivyo, katikati ya
siku ya kazi!?” Pius akazidi kucheka na kumuuliza. “Bosi wako
kanuna nini leo?” “Tupo busy sana. Vipi lakini?” “Nashukuru kwa ombi uliloweka
kwa Andy. Amenipigia na kuniambia amekubali.” “Muone anavyocheka!” “Wewe
hujafurahi? Tulimuhangaikia sana huyu mtoto Raza. Mungu amempitisha kwingine na
bado ametusogezea karibu. Tunasababu ya kufurahi.” Alipomjumuisha hivyo hata Raza mwenyewe akajisikia kuridhika.
“Mapenzi Yanayopitia
Dhoruba Kutafuta Utulivu”
Muda wa mama
yake kutoka kazini ufikapo, hurudishwa
na dereva wa hapo ofisini. Inakuwa ni jioni ya saa 10. Hutoka kama
wengine lakini Pam na Mill wao huchelewa kidogo kutoka, wanatoka saa 10:30
jioni. Yaani wanakuwa wamwisho kama wafunga hicho kitengo, japo sio kwamba
wanakuwa wakwanza kufika.
Basi isivyo
kawaida muda wa mama yake ukawa wake siku hiyo. Mama yake akashangaa anaingia
ofisini kwake na pochi yake. “Kwema!?” Kabla Pam hajamjibu mama yake, akafika
hapo dirishani kwa nje ya ofisi waliyopo wao ndani kama mteja. Pam akatulia akijua ni mteja, amekwenda
kulipia japo muda wa kufunga ulikuwa umefika.
Msafi kwa
muonekano. Hakuwa amevaa kiofisi, ila nadhifu haswa. Alionekana ni mtu
mzima ila aliyegoma kuzeeka. Harufu ya marashi ya kiume, tulivu iliweza penya
mpaka ndani walipokuwepo.
“Nimepita kukujulia
hali.” Pam akakunja uso akidhani anamuongelesha yeye na yeye hakuwa akimfahamu.
“Mbona kama nimeambiwa mgonjwa wako ametolewa tokea asubuhi!?” Mama Eric
akamuuliza kwa mshangao akionekana yeye anamfahamu. “Pengine hukuwa
umenisikia.” “Umesema umepita…” Ikawa kama mama Eric hajaelewa tena vizuri, japo
alionekana kukumbuka alichosema, akasita kumalizia.
“Nilisema hivi, nimepita
kukujulia hali.” Akaweka msisitizo na kumchanganya sasa Mama Eric kiasi
chakumgeukia Pam akidhania anazungumza na Pam japo alikuwa akimuangalia yeye
wala si Pam. Pam akapandisha mabega kumkatalia mama yake, kama anayesema si mimi au simfahamu!
Kisha wote wawili wakamgeukia tena. Wakamkuta ametulia na tabasamu.
“Mimi!?” Akauliza
mama Eric kwa mshangao akijishika kabisa. “Ndio wewe mwenyeji wangu hapa.” Jinsi
alivyojibu! Mama Eric akawa kama ameshamuelewa, akaona ampunguzie
shuguli mapemaa! “Ujue mimi ni mama mtu mzima sana? Huyu ni mwanangu wa
mwisho. Ana kaka yake mkubwa kabisa. Naitwa mama Eric.” “Na jina lako kabla
ya Eric?” Aliposikia hivyo, Pam akavuta kiti na kukaa kusikiliza vizuri.
“Wewe! Hivi
unavyoniona mimi, ni BIBI wa wajukuu watatu! Tena wakubwa kabisa.” “Mimi ninao
wawili, sema kijana wangu huyu wa mwisho amegoma kuoa. Ila kaka yake anao watoto
wawili. Jina lako kabla ya Eric walikuwa wakikuita nani?” Akazidi kumchanganya
mama Eric. Pam akajiweka sawa kujua kulikoni. Umbea tu!
“Ujue hapa
ninapokaa, mtu wa hapo nje hanioni kwa huku chini.” Akajivuta nyuma kabisa ili
amuone vizuri na kigari chake cha umeme, cha walemavu, alimpa Mill, kina kiti
kizuri tu. “Hivi unavyoniona mimi, ni mlemavu wa zaidi ya miaka 20.”
Wakashangaa anacheka. “Hapo nimekwambia mambo mawili tu! Kukujulia hali,
na kukuomba kujua jina lako, basi. Lakini ndio unanifukuza
kwa nguvu hivyo! Hivi unajua si mambo yote yanafikiwa kwa miguu?” Bwana
Pam alishangaa mpaka akaachama mdomo.
“Unakumbuka siku
ya pili kupita hapa nilijitambulisha jina langu?” Mama Eric kimya
akabaki amekodoa macho. “Mwenzio aliitika, tena akafungua dirisha kabisa mpaka
akanipa mkono na kujitambulisha kwangu kwa jina la Stella. Lakini sikufanikiwa
kulipata jina lako.” “Sasa wewe kwa nini usiridhike naye binti mdogo
yule na…” Akaanza kucheka akitingisha kichwa.
“Mimi sitakuita
mama Eric.” “Anaitwa Dorothy Shelukindo, na Shelukindo ni jina la babu.” Pam
akadakia yeye. Mama yake akamshangaa sana Pam mpaka kumgeukia. “Mimi naitwa
Pam, kiziwanda wake.” “Basi umechukua uzuri wote wa mama yako.” Pam
akamwangalia mama yake akicheka kama ambaye haamini kinachompata mama
yake. Akawa kama amekumbuka kitu.
Akamgeukia tena.
“Lakini ujue mama atakuwa hakumbuki jina lako!” “Joel kama kwenye
bibilia. Ila marafiki zangu wa karibu wamezoea kuniita Jo. Ila mimi ni kama
nabii Joel kabisa au Yoeli kwa kiswahili.” “Naona umekusudia tusikusahau
kabisa!” Pam akaongeza akicheka.
“Mbea wewe!” Mama
yake akamwambia Pam akimshangaa. “Maana hii sio mara yangu ya kwanza, Pam. Nilishajitambulisha
hapahapa!” “Basi mimi sitakusahau. Nabii Joel.” “Ewaah!” “Mimi
natangulia kwenye gari mama. Tutakusubiri usiwe na wasiwasi.” “Ujue Pam acha ushabiki
wewe!” Pam hana mbavu. Akaondoka na pochi yake kama kuwapa nafasi.
Wakabaki wao
wawili. “Mimi si kama kina Stella, binti wadogo hao ambao maisha hayajawapitisha
kwingi.” Akamuona na tabasamu tu usoni akimwangalia. “Umenisikia?” “Juu ya
Stella?” “Ndiyo. Na ni binti ambaye bado hajaolewa.” Akacheka sana akimtizama.
“Dorothy unajihami!
Mbona mimi sijasema mengi, ila kuja kukusalimia tu?” “Na yeye ndiye
aliyeniambia kama mgonjwa wako aliruhusiwa. Akawa akilalamika
hapa kwamba umeondoka bila ya kumuaga, hamjaachiana mawasiliano. Na wala
hatakuwa amefika mbali. Ameondoka sasahivi na yule binti wa kule ndani ofisini.
Ni marafiki sana na Fatma. Wote ni binti wadogo ambao hawajaolewa.”
Akazidi kucheka akimtizama vile anavyojieleza kwa kujihami.
“Naweza hata
kumpigia kumwambia kama upo hapa, akarudi sasahivi bila ya kuchelewa.” “Kwa
hiyo unataka kuniunganisha na Stella?” “Sio mimi ni yeye mwenyewe!
Unakumbuka ni yeye ndiye aliyekupeleka mpaka alipo mgonjwa wako? Na mara zote ni
yeye ndiye mliyekuwa mkizungumza naye hapa! Naweza kukupa namba yake
ya simu.” “Nipe yako.” “Yangu mimi!?” Mama alishangaa huyo! Kama ameombwa roho.
“Ndiyo.” “Mmmh!” Akaguna kama anayemvuruga kabisa.
“Tutapata muda
uniambie ni kwa nini mpaka leo unatumia jina la mzee.” “Ni…”
“Hapana bwana Dorothy! Si leo, na si hapa.” Akamkatiza kwa haraka na kuongeza. “Hayo
tutayazungumza tukiwa na chakula huku kinywaji kikitusindikiza. Siku gani ni
nzuri kwako?” Akabaki amemkodolea macho.
“Dorothy?” Kimya,
akionekana amevurugikiwa haswa. Hamuelewi. “Nipe basi simu yako
nijipigie.” “Mimi ni mlemavu kabisa, Jo. Kuanzia kiunoni kwenda chini
nimlemavu kabisa. Nilipooza nikiwa najifungua watoto mapacha. Wao
walifariki, mimi nikapooza. Nilikuwa ni wakutokwa haja zote, sijijui
mpaka nikaja kufanyiwa operation.”
“Tena hapo ilikuwa ni baada ya miaka mingi sana baadaye ndipo kaka akaja
kunichukua kijijini na kunileta huku mjini kujaribisha tu kama nitapona.
Sikuweza kurudi kutembea lakini angalau nikarudisha uhisi huku chini.
Ikawa hata mtu akinigusa chini nahisi kama nimeshikwa. Nikarudisha uwezo
wa kujua ni wakati gani natakiwa kwenda chooni. Lakini sikuwahi, kurudi
kuweza kutembea. Mimi ni MLEMAVU kabisa.”
“Pole kwa
kupoteza watoto na matatizo kipindi unajifungua. Pole sana Dorothy.” Ilimgusa
huyo mama, hakutegemea. Ila akajikaza. “Mzazi mwenzie Pam ndiye anayeniwezesha kusogea
sehemu moja kwenda nyingine kiurahisi. Lakini mimi nilikuwa ni mtu wa kusota
aridhini kabisa. Na kama si kifo kuchukua watoto wangu wawili, sasahivi ningekuwa
ni mama wa watoto wanne! Kwa hiyo Jo, mimi si binti mdogo kama
kina Stella!”
“Hilo jina la
Dorothy lenyewe nahisi hata watu walishalisahau! Yaani baada ya miaka
mingi sanaa, ndio leo nalisikia hilo jina mtu akilitamka. Ni kama lilishasahaulika
na Pam amenishangaza hata kulitamka kwa haraka hivyo. Hakuna mtu
ananiita tena hivyo! Mimi ni mama Eric!” Akawa akimuelezea kwa makini
akiweka msisitizo ili aelewe anachozungumza, akihisi Jo hamuelewi kabisa.
“Naelewa maisha
yanaweza kukupa sura fulani hivi! Ukawepo hapo kwa muda mrefu mpaka
ukafanania na vile maisha yalivyokubatiza. Naelewa. Lakini pole sana kwa
kupoteza watoto na kupatwa na matatizo.” “Nimekwisha poa na kuzoea. Asante!” Akaitika
lakini bado akiwa na mshangao usoni, kama ambaye bado hajampata vizuri.
“Mimi na mke
wangu hatukutaka watoto wengi kwa makusudi. Tulitaka wawili tu, tukapata
wakiume wawili tukiwa bado vijana, ikatosha. Wa mwisho nahisi ni mkubwa kwa
Pam. Tulizaa mapema sana. Tulipomaliza tu chuo mwaka wa kwanza, tukaoana,
tukapata mtoto wa kwanza. Shahada zetu za pili, tulisoma tukiwa na watoto wetu wote
wawili. Mark tulimzaa karibu sana na kaka yake Matthew. Mengi tutazungumza tutakapokutana
tena. Niambie ni lini, unanafasi.” Akazidi kumshangaza vile alivyomng’ang’ania!
“Eti Dorothy?” “Sijui
Jo! Yaani leo ndio nimemwambia Pam kama ni mjamzito.” “Hakuwa akijua?” “Hapana!
Na imemshitua sana. Na sidhani hata kama mzazi mwenzie anajua. Hayupo
sawa. Kumuona amenisimamia hapa na pochi yake, mida hii, najua kuna jambo
halijakaa sawa lakini najua hataniambia ila kutaka kuwa karibu na
mimi kama ulivyomuona hapa. Ndivyo alivyo. Sasa sijui hata itakuaje! Siwezi toa
ahadi za uongo.”
“Huoni ukinipa
namba itasaidia mawasiliano?” “Wewe unamke Jo! Mawasiliano na mtu
kama mimi ni ya nini?” “Betty alifariki muda mrefu sana, akaniachia hao
vijana wawili. Mimi si malaya, Dorothy. Namuheshimu sana mke wangu.
Kabla na baada ya kifo chake. Naishi nikimuwakilisha na yeye pia.” “Pole kwa
kumpoteza mwenzio.” “Asante. Kwa hiyo namba yako ya simu?” Ikabidi tu amtajie
maana alionekana ni jambo alilokusudia.
“Nashukuru.
Akaandika vitu kadhaa kisha akamtumia ujumbe wenye jina tu, ‘Jo’. “Nimekutumia ujumbe. Naomba utunze namba yangu. Na niambie rahisi ni
nini? Nisubirie mpaka utakaponitafuta au ni sawa nikikupigia mimi?” “Hata sijui
ndio inakuje Jo! Acha niwe mkweli kwako ili kukupunguzie usumbufu
na uelewe usipoteze muda kwangu.”
“Mimi hayo maisha
sijawahi ishi kabisa. Ndio maana ulimuona Stella yeye alikuchangamkia kwa
vizuri hata akijua ni jambo gani sahihi lakuzungumza na wewe, na nini
akuombe kwa wepesi! Nafikiri ndio maana yeye alishangaa kidogo
ilipotokea kuna uzito wa kumpa namba yako. Alitegemea pengine leo ndio
ungempa.” Jo akacheka tu.
“Tafadhali
naomba unielewe na uniamini. Mimi sio kama hao warembo wadogo kina Stella wenye
uelewa wa mambo hayo yenu ya kisasa.”
“Jeraha la
Moyo kwa Jina la Mapenzi”
Hakuwa
akidanganya. Aliolewaga binti mdogo akiwa hata hajamaliza chuo cha ufugaji
hukohuko mkoani Tanga. Alikutana na baba Eric akiwa chuoni hapo, yeye kama mmoja
wa walimu hapo chuoni. Akamganda binti wa watu akiwa bado mdogo tu. Amemaliza
kidato cha nne miaka hiyo na kujiunga chuoni hapo.
Alipopata yeye nafasi
nyingine ya kikazi mkoani Ruvuma, ndipo akaona asizidiwe mahesabu huku
nyuma. Maana huyo Dorothy alikuwa Dorothy kwelikweli kama Pam anavyo mchanganya
Mill. Akaenda kwa kina Dorothy, akamdai kwa magoti kwa ahadi yakuja kumuendeleza baadaye. Mzee Shelukindo alipoona
huo upendo, akakubali. Akamlipia mahari ndoa ya harakaharaka ikafungwa,
Dorothy akiwa binti wa miaka 19 kwenda 20.
Akaenda
kumfungia huko Ruvuma, kazi ya kuzaa na kulea ikaanza huku akimtumia kwa manyanyaso
makali sana. Hakutaka kukaribisha mazungumzo ya kuja kurudi tena
chuoni. Alikuwa mbabe kwa mkewe, yeye akawa baba mwenye nyumba haswa
anayewaweka mjini. Naye mama Eric bado alikuwa mdogo. Malezi ya kijijini, baba mzee
wa kanisa, na yeye alikuwa binti mwadilifu muimba kwaya kanisani huko kwao milimani,
Lushoto. Maadili mazuri. Binti aliyekuzwa kwenye kusubiri mpaka ndoa. Naye
hakuwa akisumbua nyumbani. Binti mtulivu asiye na makuu kama kaka yake. Hakuwahi
kuwa hata na mwanaume.”
Aliagwa kwao
kwamba, maisha ya ndoa ni kuvumilia. Basi, ndicho alichokwenda kufanya
huko Ruvuma pale huyo mwanaume alipombadilikia. Akatulia akivumilia YOTE
huku akiongeza kipato kwa kufanya vijishuguli vidogovidogo ili angalau kuweza lisha
wanae. Maana baba Eric ugomvi wake ulikuwa ukizidi pale anapoombwa pesa
hata ya chumvi. Hapo atawaka nyumba haitakalika. Basi mama Eric
ndipo alipoanza kupika chapati na kuuza pamoja na maandazi ili kupunguza ukali
kwa mumewe. Lakini haikuwahi saidia. Alikuwa mbahili hata kwa
wanae. Haombeki pesa, na hajui kuzungumza naye kabisa.
Alimbadilikia kama
mchana na usiku. Akimtesa mpaka aliposhika mimba ya hao mapacha na
kupatwa na hayo matatizo. Akarudishwa kijijini na watoto wawili, na ulemavu
juu, bila cheti chochote zaidi ya kile alichotoka nacho kwao, cha kidato
cha nne.
Na hakuwaga romatic
kabisa. Si mwanzo kabla ya ndoa, na ndio ikawa mbaya zaidi alipoingia naye
kwenye ndoa. Hakuwa akijua kubembeleza. Ila aliweza mtongoza na
kuzungumza naye mpaka akakubali ndoa, kwa ahadi ya kumpeka mjini. Ambako ndio
huko Ruvuma alikoenda muonyesha rangi zote.
Mtu wa kuamrisha
wakati wote. Na alikuwa akimshika ujue ni anataka kuingia. Na akimaliza
yeye ujue ndio mchezo mzima umekamilika. Tendo la ndoa ilikuwa ni
anapotaka yeye, na mwisho wake ni pale anaporidhika yeye. Na
hakuwa mlevi wa pombe ila ngono. Alikuwa akimtumia binti wa watu
atakavyo yeye, na kwa muda wake.
Akiwa amejifungua au akiwa kwenye siku zake, ujue wanawake wa nje watamsaidia
kumtuliza huyo baba Eric na haikuwa kwa kificho wala aibu. Anaingia na kutoka
kwake atakavyo huku akimkumbusha Dorothy nyumba ni yake anafanya atakavyo.
Mbaya zaidi, ili
kumdidimiza kihisia na kumfanya mateka wake ili hata asifikirie
kumsaliti. Kama wafanyavyo wanaume wengine, akamtafutia kasoro alizokuwa
akimkumbusha anazo yeye kama mwanamke, tena mara kwa mara mapaka Dorothy
akaamini ni kweli. Kwa sababu kwanza yeye ndio alikuwa mwanamme wake wa kwanza.
Alimuamini kile alichomwambia. Basi Dorothy akapoteza kabisa thamani ya
uzuri wake, akajiona kama anayeishi kwa kusaidiwa na kuvumiliwa
tu na mumewe. Akamuingiza donda la moyo, likajitibu asijue
anatembea na kovu asilojua hata lilipona lini.
Huyo Dorothy
hakuwa akijua hata kama wanawake huwa wanapigaga mabao. Na kwa
maadili ya kwao, mambo ya chumbani, mapenzi, si mambo ya kuzungumza hovyo.
Sasa hayo
anayotaka kuanzisha Jo ni maisha ambayo hata hakuwahi yawaza, kwanza hayajui
maana hata tamthilia hakuwa akiangalia. Huko kijijini kwa wazazi wake
walikuja kuletewa luninga na kaka yake, baadaye sana, wakina Pam washakuwa
wakubwa kabisa wapo mjini. Na ikiwashwa ni taarifa ya habari na mambo ya dini. Leo
Jo anataka kumvuruga tu.
~~~~~~~~~~~~~~
“Basi nitaanza
kwa ujumbe, nikisubiria upate nafasi tutoke. Tafadhali weka mazingira tutoke.
Nakuahidi wakati mzuri.” Kwa hakika alishindwa nini chakujibu ila kuondoka.
“Naomba nikuage. Nimpeleke Pam kupumzika.” “Twende nikusogeze garini.” Napo
hapo alishangaa kwa sekunde kadhaa akiwa amemtolea macho kabisa. Kwamba inawezekanaje!
“Nisaidie nini?”
“Sina chakubeba zaidi ya pochi, nayo naweka hapa kwenye kigari changu.” “Basi
funga twende.” Walishakuwa wamemaliza kazi. Hata kompyuta walishafunga tokea
Stella anaondoka hapo na pesa yote kupeleka kwa Mbise, bosi wake Pam, muhasibu
wa hiyo kampuni.
Akafunga dirisha
mbele ya Jo, akawa haoni tena ndani. Walikuwa wametenganishwa na kioo kikubwa chenye
upenyo wa kuweza kupenyeza pesa na kupokea risiti, mbele ya dirisha. Akachukua
vitu vyake, akawasha kigari chake akageuza kigari chake kuelekea mlangoni.
Alipomsikia
anafungua mlango kwa ndani, akamsaidia kusukuma mlango ili apite na kigari
chake kisha akamsaidia kurudishia mlango. “Lazima nifunge kwa funguo.” “Lete
mimi nifunge.” Akachukua funguo mikononi mwake akaanza kufunga milango mpaka
kigeti cha nje akimuelekeza. “Asante. Lakini ujue huwa nafungaga mwenyewe
wakati wote. Stella huwa anawahi kutoka kupeleka pesa na kumuwahi Fatma rafiki
yake, huwa wanaondoka pamoja. Kwa hiyo naweza kufunga mwenyewe.”
“Nimekusaidia si kwa sababu nilihisi huwezi.” Mama Eric akaanza kuondoka
akawa anamfuata nyuma.
“Lakini nimeona unakitu
hapa. Naweza kukutoa.” Mama Eric akaanza kujipangusa. Jo akamuacha tu. Akajifuta
uso mzima mpaka akaridhika. “Bado hakijatoka.” “Wapi?” “Mikono yangu nimisafi.”
Kisha akamsogelea na kuinama pale alipokuwa amekaa, akaanza kumfuta pembeni ya
mdomo. Mwanzo mama Eric alishituka, ila akaendelea kumpangusa taratibu
kama ambaye hana haraka.
“Naona
kimegandia.” “Pam huyo! Itakuwa mtindi wake huo, umegandia! Acha nikajisafishe
uso tu. Asante.” Akataka kujitoa maana naye huyo Jo alikuwa akimsugua taratibu,
bila haraka na kidole gumba. “Nakaribia kumaliza.” Akaendelea kumfuta
ikabidi atulie maana alikuwa amemuinamia hapo karibu kabisa na uso!
Taratibu mpaka akamaliza yeye na kuridhika.
“Naona sasa uko
sawa.” Ndio akawa anamtoa alikokuwa amepotelea. Alianzisha jambo jipya
kwa huyo mama! Halikuwahi hata kuwepo maishani. Hisia za ajabu za
kujaliwa kwa kipekee kabisa. “Asante.” “Karibu.” Hiyo karibu yenyewe
anavyomjibu! Mpaka akashindwa kumtizama. Akageukia pembeni. Na kuondoa kigari
chake. Wakaongozana mpaka kwenye gari wakitembea kimyakimya akimfuata kwa
pembeni ila kwa nyuma.
“Ile pale ndio
gari yenyewe.” “Nani anapandisha gari yako?” “Dereva hutoka kunisaidia.” “Mpaka
kupanda garini?” “Napanda mwenyewe. Nasogeza gari mpaka karibu kabisa na gari,
napanda, yeye anakuja kutoa hiki kigari na kuweka nyuma.” “Ni sawa nikusubirie
mpaka upande, ndio niondoke?” Na hapo akawa hajui ajibu nini.
“Dorothy, sitaki
kukunyima raha. Ila ningependa kukusubiria mpaka unaondoka. Pam akashuka garini
na kumfungulia mama yake mlango, hawakuwa wamesimama mbali. Bali alishindwa
kujibu. “Twende.” Jo akaongeza mwendo mpaka garini. “Acha nikusaidie mlango
Pam.” Pam akaondoka kabisa hapo na kurudi upande wa pili wa gari. Akaingia na
kujituliza kimya, kiti cha nyuma.
Akasukuma kigari
chake mpaka garini, Jo akiwa ameshikilia mlango. “Nipe pochi yako.” “Huwa
nairushia ndani kisha nadandia.” “Mimi nimesimama hapa, huna haja ya kuirusha.
Nipe.” Pam akabaki kujisikilizia ila hawaangalii. Akampokea, na
kujisogeza pembeni ili kumpisha. Akamuona jinsi anavyopanda garini kama mzoefu
lakini hakupenda. Dereva
akachukua kigari kwa haraka na kwenda kukiweka nyuma.
“Funga mkanda
kabisa, ndipo nikupe pochi yako.” Akajifunga mkanda akiwa amemsimamia hapohapo pembeni
ya mlango, aliporidhika amekaa sawa ndipo akamkabidhi pochi yake. “Mfike
nyumbani salama na uwe na mapumziko mema.” “Asante na wewe.” Mama Eric akaitika
ila kwa utulivu. Pam akamuona jinsi anavyomjali mama yake na kumchukulia
kwa upendo. Akashangazwa sana, asiamini mtu kama Jo anaweza toa
muda wake kwa mtu kama mama yake! Na yeye kikamchanganya.
“Pam, salimia
familia. Na nimefurahi kukufahamu. Naamini kuna siku nitabahatika kumuona na
Eric.” “Na mimi nimefurahi kukufahamu nabii Joel.” Akacheka na kufunga
mlango. Kwa hakika alionekana na ustaarabu usio wa hapo nchini kabisa japo
aliongea kiswahili fasaha sana. Akapunga mkono. Dereva akaondoa gari.
~~~~~~~~~~~~~
Pam akamgeukia
mama yake maana alimuona amebadilika kabisa, amepoa na macho yapo nje ya gari.
Akamuacha maana na yeye alikuwa na yake. Mama yake naye alimuacha
hakumuuliza lolote kwani alimuona hayupo sawa tokea anamfuata na pochi yake
kuashiria anaondoka naye. Huwa anamjua
Pam ni mkorofi. Na huwa anazungumza jambo lake anapotaka
yeye. Kwa hiyo wote wakabaki kiti cha nyuma, kimya. Kila mmoja akiwaza
lake, dereva akiendelea kukanyaga mafuta. Kimya tu hapo garini.
~~~~~~~~~~~~~
Walipokuwa
wakikaribia madukani akamwambia dereva wapitie dukani anunue mtindi. Dereva
akatii bila shida, na hivi mama bosi kasema, akamsogeza mpaka karibu ya duka.
Akanunua na baadhi ya vitu, safari ya kwa mama yake ikaendelea akiwa na chakula
chake.
Kufika akaingia moja
kwa moja chumbani kwa mama yake. Akatoa nguo zote. Akajifunga kitenge. Mama
yake kimya akiendelea na yake na msichana wake anayemsaidia kazi. Akimpa
maagizo nini cha kupika jioni hiyo huku akimwangalia Pam akijua wazi hayupo
sawa.
Akamuona anatoa ugali
wake wa muhogo alionunua mchana alipokwenda kula na Mill. Kuku wa makange.
Pilipili nyingiii na limao lakutosha. Kulikuwa na mboga za majani. Akaomba
atolewe mtindi wake alionunua. Maana dada alishaweka kwenye friji. Akakaa chini
kabisa sakafuni. Ungemuona anavyokula, ungesema ni mbeba magunia kule Kariakoo
sokoni, siku hiyo alifanya kazi siku nzima, hajala. Na ugali wenyewe
haukuwa kidogo. Bwana Pam alikula huku feni ikimpepea.
Alipomaliza
akatangaza. “Nakwenda kulala. Mtu asiniamshe.” Mama yake alimsikia, hakumjibu.
Akarudi kitandani kwa mama yake, akauchapa usingizi. Alilala asijue alipo na
hana habari na yanayoendelea ulimwenguni.
Kwa Mill.
Huku nyuma saa 10:26
Mill akatoka kwa kujiwinda akimfuata warudi nyumbani, hakumkuta ofisini wala
hapakuwa na pochi yake. Akapaniki. Akampigia simu ikawa inaita ila
haipokelewi. Akatoka kumuuliza mlinzi. Akamwambia Pam alisharudishwa nyumbani.
Akapata moyo akatoka hapo kurudi nyumbani.
Shema huwa
akitoka shule anapitishwa mpirani. Wanafanya mazoezi. Mpaka kuja kufika
nyumbani inakuwa karibia muda wa wazazi wake kufika hapo au huwa anawakuta
walishafika. Akajikuta wamefika hapo yeye na mwanae karibia muda mmoja. “Mama
yuko wapi?” Shema akamuuliza wakati akitoa viatu vyake mlangoni. “Yeye
alitangulia kurudi.” Akajibu hivyo na kumuuliza habari za shule ila kama
kutimiza wajibu huku akitaka kukimbilia ndani kumuangalia Pam. Akashukuru Mungu
na jibu la mwanae halikuwa refu ila tu, ‘nzuri.’
Hakuongeza,
akakimbilia ndani akiwa na wasiwasi na hofu akijua kweli ile sawa ya Pam
haikuwa sawasawa. Na ndio maana aliondoka bila ya kumuaga asijue kwamba
wala Pam hayupo hapo.
Shema akaanzia
jikoni akimsikia baba yake akipandisha ngazi kwa kukimbia. “Humu ndani hamna
chakula na mimi njaa inaniuma siwezi hata kusogea!” Akapaza sauti baba
yake asikie, lakini hakupata jibu. Si kwamba baba yake hakusikia, lakini
binafsi alikuwa na yake yakiendelea, hawezi shugulika na njaa ya kijana
wake kabla hajamuona mama mtu.
~~~~~~~~~~~~~
Maswala ya
chakula ni Pam. Alimjua Shema kwa njaa zake. Kila akitoka mazoezini
lazima akute kitu chakula. Sasa Pam hupitia vitu vidogovidogo vya kujitafuta.
Akifika Shema anapata glasi ya maziwa na hivyo vitu kama ni sambusa na bajia au
kababu au eggchop. Kisha ndio ukaja utaratibu mpya wa kusongewa ugali usiku.
Ukawashinda yeye na baba yake, wakawa wakinunua chakula wakati Pam akifaidi
ugali peke yake.
Mill alisahau
kupitia dukani/bekary wanayopitaga na Pam kila siku jioni watokapo
kazini ili kununua vitafunwa hivyo na pia huwasaidia kwa kifungua kinywa
asubuhi. Ni utaratibu wa Pam wala si wake. Na wakati wote hubaki garini
wakati Pam akishuka kununua.
~~~~~~~~~~~~~
Kufika chumbani
kitanda kisafi kama alivyotandika yeye mwenyewe Mill alipokuwa wamwisho kutoka
hapo kitandani. Maana Pam huwahi kutoka kuandaa kifungua kinywa kwa wote. Basi
wakawa wamejiwekea utaratibu anayekuwa wamwisho kutoka kitandani basi ndio
anatandika kitanda. Mara nyingi anakuwa Mill ndio mtandikaji.
“Mama!” Akasikia
sauti ya Shema chini ashapaniki. “Kunywa maziwa.” “Hivihivi!?” Shema akamuuliza
baba yake kwa kushangaa sana. “Mbona mama hanijibu sasa?” “Hayupo.”
“Yuko wapi?” Shema na baba yake wakawa wanajibishana. Shema yupo chini, baba
yake juu akihaha hajui Pam alipo.
~~~~~~~~~~~~~
Mambo
Yanaendelea kusonga.
Usipitwe na
muendelezo.
0 Comments:
Post a Comment