Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Love At First Sight - Sehemu ya 65. - Naomi Simulizi

Love At First Sight - Sehemu ya 65.

Chezo alimuacha Pius haamini. Alijuta hata kwa nini alimtafuta. Akabaki amevurugikiwa hajui hata awaze kipi! Ujumbe wa Raza nao ukaingia na kumtoa kwenye mawazo ya Chezo. ‘Kama majukumu yamekubana, usiwe nawasiwasi, naweza tu agiza matunda, nitakula vizuri nyumbani, nikitoka.’ “Mimi ndio nionekane sijali!” A kajiwazisha Pius na kurudisha ujumbe. ‘Nakuja sasahivi.’ Ndipo akatoka. Nakumfuata tena mpaka ofisini kwake na kumchukua.

Raza alimuona wazi amebadilika tokea anaingia ofisini kwake. Kikamnyima raha. Akahisi anaanza kulemewa kutoka naye kwa chakula cha mchana kila siku. “Si unajua mimi nitakuwa sawa tu hata ukishindwa kuja kula na mimi mchana? Usilazimishe kuja kama umebanwa na majukumu kazini. Huna sababu ya kufanya hivyo.” Ikabidi amwambie kabla hajaondoa gari. Kimya. Huku akijiambia mbona Chezo yeye alikuwa akikutana na mkewe kila siku mchana! “Wasinichezee akili. Hata mimi naweza.” Akajiambia lakini ukweli wawili hawa si sawa. Pius anamajukumu mazito sana ya kiofisi. Hapo amevurugwa tu, hawezi kufikiria sawasawa.

“Mimi naweza kurudi tu ofisini nikaagiza waniletee matunda ofisini.” Raza akaweka msisitizo. “Nataka twende ukanionyeshe hiyo nyumba mnayojenga, maana jioni ya leo tunamiahadi na huyo contractor.” Raza akatulia baada ya kusikia, ‘mnayojenga’, halafu na sura ambayo kama imejaa hasira! Akatulia na kumpa maelekezo ya awali. Akatoa gari, Raza kimya ametulia kitini.

“Najiuliza, hivi ikitokea nafukuzwa kazi sasahivi. Biashara zote zinakufa, bado utabaki na mimi?” Raza akashangaa sana hayo yanatoka wapi ila akajikaza na kumjibu. “Nilifikiri tumekubaliana kuanza upya! Na kwamba sasahivi tumebaki mimi na wewe kama ulivyosema! Kwani kuna nini tena?!” “Kwamba tunabaki wote kwa sababu tumejikuta tu pamoja, kosa la ndoa lilishatokea, inatubidi kubaki tu, au kwa sababu kuna mapenzi?” Akamuona anaanza kupandisha hasira.

“Maana unaweza kuta hata hii ndoa inageuka kuwa mzigo! Mwanaume siye uliyekuwa ukimtaka. Nikimaanisha si mwanaume wa ndoto zako. Umekwama kwenye ndoa, ishatoa matokeo ya watoto, na pengine kuna maslahi mengine yanayo kubakisha.” “Ukimaanisha nabakizwa kwako na pesa zako?!” Raza akamuuliza kwa kumshangaa sana, asijue mwenzie anajifananisha na Chezo vile alivyo, na maneno machungu aliyompa.

~~~~~~~~~~~~~~

Pius japokuwa anapesa na alikuwa kwenye ofisi nzuri wakati akikutana na Chezo lakini Chezo alimtisha. Alikuwa na umbile la kiume japo urefu hawakupishana. Amejazia hata kwenye shati alilokuwa amevaa alionyesha amejenga misuli. Safi utafikiri ni mkurugenzi aliyekuwa ameacha koti la suti kwenye gari na kwenda kukutana na Pius. Halafu akajibeba vizuri kwelikweli! Bila paniki wala hofu na kuweza kumuachia maneno yaliyobaki yakimsumbua Pius.

Mwizi akamtisha mwenye mali mwenyewe, Pius akajiona kipanzi. Kwamba Raza kurudi kwake ni kama anamuhurumia tu. Akamuona Chezo ni bora kuliko yeye! Japokuwa mwishoni alitumia ubabe lakini wazi kwa hoja alimshinda.

~~~~~~~~~~~~~~

“Ni nini tena, Pius?! Mbona mwanzo uliosema ni kama tena unaanza na manyanyaso?” Kidogo akashituka na kujua amepitiliza. “Si kwamba nakunyanyasa, ni kutaka kujua kwa ajili yako wewe mwenyewe. Sitaki uje uache maisha yako huko, unakuja kujipunja kwangu.” “Maisha niliyoishi hayakuwa sahihi mbele za Mungu, Pius! Nimebadilika kwa kupenda kwangu nikitaka kuishi maisha matakatifu nikimtegemea Mungu. Ya kale yamepita, Mungu ameniahidia mapya. Tafadhali naomba na wewe unisaidie sio kunirudisha kwenye maisha ya nyuma.”

“Chochote nilichokuwa nikifanya zamani, nimekusudia kubadilika! Nimeacha ushirikina na mengine yote.” Asijue wala tatizo sio uchawi ni Chezo aliyekwenda kumtafuta yeye mwenyewe.

“Sasahivi nina amani na utulivu nafsi kwangu.” “Huna majuto?” Raza akashangaa sana. “Najutia nini!?” Pius akababaika haswa ila akionekana ameshapoa kama aliyejishitukia kwamba amempandishia hasira mtu ambaye hata hakuwa na wazo!

“Sitaki uishi na mimi kwa kunivumilia tu.” “Kuna tatizo gani nikikuvumilia wewe mume wangu!?” Akamuuliza vizuri tu na kumfunga mdomo. “Maana ni kama ulisema sasahivi tumebaki mimi na wewe! Sasa kama tumebaki wawili, si ndio tunabebana katika kila hali!”

“Na tafadhali swala la nyumba yangu lisikunyime raha Pius. Nimejitahidi kwa juhudi zangu nimefika hapo nilipofika.” “Sema juhudi zenu!” Raza akatulia. Pakatulia kwa muda akiendelea kuendesha. Kimya.

“Hapa niende wapi?” “Naomba nirudishe tu kazini, Pius. Hili jambo nafikiri litatukosanisha.” “Kwa hiyo hutaki niingilie kumbukumbu yenu? Unaona kama mimi nitakuwa mvurugaji tu?” Raza hakujibu kwenye hilo, akamuelekeza mpaka wakafika.

~~~~~~~~~~~~~~

Wakashuka garini, akaanza kuzunguka akishika kila mahali. Kimyakimya Raza akifuata nyuma. Akazunguka mpaka akamaliza. Wakarudi garini.

~~~~~~~~~~~~~~

“Kwanza nakupongeza. Umejitahidi sana.” Raza kimya. Akamuita. “Raza, nimekupongeza!” “Asante.” “Lakini nimeshika ukuta, wazi unaonekana mchanga ni mwingi kuliko cement.” Akaanza kukosoa. Raza kimya huku wakirudi ofisini, maana muda ulishaisha hawakuweza kupita kula.

Akalalamikia ujenzi wa hiyo nyumba kuanzia msingi mpaka ilipofikia, utafikiri anayo shahada ya fundi nyumba! Raza kimya ila akihisi tatizo ni Chezo tu kuhusika kwenye hiyo nyumba. Kimya hakumjibu mpaka anamshusha ofisini. Ule moto wa kuanza upya ukawa umeshamwagikiwa na tui la nazi jikoni, na kuzimisha. Wakapoa tena kama waliopoteza dira.

~~~~~~~~~~~~~~

Alirudi nyumbani usiku akamkuta Raza jikoni akimalizia kusafisha. Kwa asili Raza alikuwa msafi sana. Huacha jiko safi ndio anakwenda kulala. “Nimemchelewa Polla?” “Muda si mrefu. Pole na kazi.” “Na wewe. Vipi hapa?” Akauliza huku akitafutia samaki nafasi kwenye friji.

“Ni nini hicho?” “Samaki, alileta Chezo ofisini kwangu.” Alishituka Raza karibu aangushe sahani, ila akaidaka ikimponyoka mara kadhaa mikononi mwake. Tumbo likaanza kuvuruga. Pius akajua kabisa ameshituka, akatoka hapo kwenda mezani alijua chakula kinamsubiria. “Nashukuru kwa chakula.” Akamsikia akishukuru huko mezani. Lakini alishindwa hata kujibu! Akaweka sawa hapo jikoni, akapitiliza juu chumbani kwenda kuoga.

Akiwa bafuni ndio kama akili ikaanza kumjia kuwa mumewe amekutana na Chezo, ndio maana alitibuka mchana. Wasiwasi walichozungumza ukamuingia, ila hana wakumuuliza. Chezo asingethubutu, na mumewe hivyohivyo.

Nyumba ile ikaanza kuwa tatizo. Akajua itabaki kuwa tatizo kwa sababu imebeba kumbukumbu za Chezo. Akabaki akiwaza hajui chakufanya. Ni jasho lake na kweli alitaka angalau awe na kitu chake kinachotokana na jasho lake. Lakini napo akakumbuka jinsi mumewe alivyokuwa akiikosoa! Ikakosa raha kabisa.

~~~~~~~~~~~~~~

Wakati akijipaka mafuta Pius naye akaingia kuoga. Raza hakumsemesha hapo kwenye chumba cha bafu. Akavaa na kutoka akajiwahi kitandani. Pius naye hakukawia kama aliyekuwa akimuwahi. Alipojiweka tu kitandani, Raza akamgeukia.

“Naona tu niuze kile kiwanja na ile nyumba ilipofikia, nikaanze kujenga upya kwingine. Hata hivyo kama ulivyosema, mchanga ni mwingi kuliko simenti.” “Nilikuwa na contactor huko jioni hii ndio maana nimechelewa. Hata yeye ameona jinsi ilivyojengwa vibaya. Hata msingi wenyewe unaonekana haupo imara.” Akaanza kukosoa tena. Raza kimya akisubiri hitimisho.

“Kwahiyo kesho wanaanza kuibomoa.” Raza akashituka akahisi roho inataka kutoka. Akakaa kwa mshituko bila kutarajia. “Yote!?” Akauliza kwa mshangao wa wazi kabisa. “Mpaka msingi. Kwanza pale ilipo tumeona sio sehemu nzuri. Ataisogeza kabisa wajenge sehemu nzuri ili kuwepo na bustani nzuri na ya kueleweka. Nafikiria mpaka kupata uwanja mzuri kuja kuweka bwawa. Hata yeye ameona ni wazo zuri, ipo karibu na bahari, uchimbaji wa pool hautakuwa shida. Tutapata maji kwa rahisi.” Raza kimya mapigo ya moyo yakiendelea kwenda sivyo.

“Wanaanza kazi mara moja, wameniahidi ndani ya miezi 6 itakuwa tayari hata kuhamia. Au kuna kumbukumbu unatunza pale?” “Ni jasho langu ndio maana nimeshituka Pius! Lakini nashukuru kwa kunihangaikia.” Akarudi kujilaza akiwa amenyongea moyoni. Hakutaka hata kuzungumza jingine akaona alale tu.

“Hela nzima ya ujenzi nitaihamishia kwenye akaunti yako, tutakuwa tukimlipa kwa awamu. Nitakuonyesha mkataba wake na hiyo ramani mpya. Na hii sio ya kwenda kusimamia kila siku. Ndio uzuri wa contractor.” Hapo kidogo akatulia. Kuna leo na kesho. Akianguka na kufa Pius gafla na nyumba kambomolea! Hapo kidogo akaona bora pesa itakuwepo, tena kwenye akaunti yake. Mapigo ya moyo yakaanza kutulia. “Nashukuru. Asante.” Akajua wazi amepoa.

~~~~~~~~~~~~~~

“Nimezungumza na Andy, ijumaa hii tukitoka kazini, tunaelekea Dodoma, nyumbani kwao. Tulimalize hili kabla hawajarudi hapa Dar. Au unampango mwingine?” “Hamna. Nashukuru kunisindikiza.” “Pia itatupa mapumziko mengine. Nilipata wakati mzuri na wewe tulipokuwa Mauritius. Natamani tuwe tunajitengenezea mazingira kama yale mara kwa mara. Ikawa sasa kama anayempuliza baada ya kumng’ata.

Raza akatulia akiwa na mengi yanayoendelea kichwani mwake akijaribu kurudisha mudi. Kubomolewa nyumba aliyohangaikia kwa kiasi kile! Bado alikuwa akijaribu kuingiza akilini, huku akijilaumu kumwambia kama na Chezo alikuwa akisimamia.

“Au unataka  twende na kugeuza?” “Ningependa wakati mwingine mzuri. Tunakwenda na watoto?” “Inabidi na wao wakamuone kaka yao. Si ni sawa?” “Hamna shida. Nashukuru.”

Wakapanga tena mipango wa hiyo safari ya Dodoma. Siku ya kwanza ilikuwa ni ya kwenda kuomba msamaha kwanza, wawaache watoto hotelini. Ndipo siku ya jumamosi waende na watoto wao hapo kwa kina Andy. Hilo likakaa sawa.

Lakini kulikuwa na uzito usiku huo, hakuna hata aliyekuwa na hamu ya mapenzi. Walilala kila mtu akiwaza lake. Kale kahali kafungate, upepo ukakapitia, wakarudi kulala kama wanandoa wa kongwe, kavukavu bila hata kugusana.

~~~~~~~~~~~~~~

Asubuhi ndipo akasikia chuchu zinashikwa taratibu. Akiwa usingizini hakujua kama ni mumewe, akageuka upande wa pili akidhania ni ndoto. “Usinichukie Raza, na kunikataa. Nia yangu ni kujenga chetu, tena kizuri chenye hadhi.” Ndio Raza kutoka usingizini sasa baada ya hayo malalamiko. “Pole, nilikuwa nimelala nikadhania ni ndoto.” Akageuka vizuri.

“Na sijakuchukia.” “Unauhakika?” “Sema nikushituka tu. Ile nyumba nimehangaikia Pius! Nishaiona ikiwa imeshaisha kabisa. Kusikia inabomolewa si kitu kidogo!”

“Sasa tutakuaje na kitu chetu, au mwanzo wetu na Chezo katikati yetu?” Hapo la moyoni likawa bayana. “Umeichukulia vibaya tu. Chezo alifanya kama mfanyakazi tu. Kusimamia. Hajaweka pale hata shilingi yake!” “Kuna kujenga kwa kujitolea kwa hali na mali. Yeye amejitoa kwa hali, wewe mali. Sasa mimi hapo nipo wapi?”

“Na ndio maana wewe unajeuri hata na hii nyumba Raza. Umenikuta nikijenga. Tulikuwa tukija wote hapa kipindi ikijengwa. Maua yote kwenye hii nyumba na ukoka ni wewe ndiye uliyekuwa ukileta hapa hata kabla ya ndoa yetu. Unahaki na jeuri ya kusema hapa ni kwako pia hata kama hukuwekeza pesa ya ujenzi wa hii nyumba kama jengo, lakini unamchango wako hapa. Lakini Kule itabakia ni wewe na Chezo daima! Ila kama itakuumiza, basi, nipo tayari niache nisikuingilie.” Asubuhi hiyo alionekana mnyenyekevu kama si yeye!

Lakini Raza alijua wazi, akitaka amani humo ndani na mengine yaendelee vizuri, hiyo nyumba kubomolewa ndio itakuwa garama ya kulipa. Akamua anyamaze.

~~~~~~~~~~~~~~

Muda wake ulikuwa umeshaisha, alamu iliita ikabidi kukurupuka na kwenda kusamdia Polla, awahi shule na kuandaa kifungua kinywa cha mumewe. Pius akaachwa bilabila hapo kitandani. Huyo Raza akawa hagawanyiki na hesabu ikakaa sawa. Kazini anahitajika kwa asilimia zote, nyumbani mambo yote yanamtizama yeye, na kitandani! Hapo ikabidi Pius awe mpole. Akajituliza kwa kujipoteza mawazo kwenye hili na lile akisubiria na yeye alamu yake, atoke kitandani, siku ianze.

Kila ‘Samahani’, Hubeba Gharama.

Kuomba msamaha si maneno matupu. Ni sadaka ya moyo inayotolewa kwa unyenyekevu. Ni safari ya kuvuka daraja la kiburi, ukiachilia mizigo ya hasira ili kubeba uzito wa ukweli. Walifika Dodoma jioni mapema tu kabla giza halijafukuza mwanga, maana waliwahi kutoka ofisini. Wakaelekea hotelini kuacha watoto wao ndipo wakaenda kwa Andy.

Wakakuta wameandaliwa vilivyo. “Sisi tulijua mnakuja na watoto kama Pius alivyosema! Mpaka pakulala tumewaandalia nyinyi na watoto.” “Tumekuja nao ila tumewaacha hotelini. Tuliona tuje sisi kwanza, tuzungumze.” “Karibuni.” Wakaingia ndani maana Andy ndiye aliyekwenda kuwafungulia mlango baada ya kusikia geti linafunguliwa akiwa amembeba Ayvin. Walituma dereva wao kwenda kuwapokea.

“Nipe huyo nimsalimie.” Ayvin akamkataa kabisa baba yake akabaki amejificha begani kwa Andy akimng’ang’ania. “Hapo ndio ujanja wote humuisha. Ila kwa kuwa hajiwezi kwa utundu, mkikaa kidogo ataanza kuwachungulia mwishoe atashuka tu hapa yeye mwenyewe aanze kuzunguka. Mpeni muda. Karibuni ndani.” Wakaelekea mpaka sebuleni alipokuwa amekaa Mina na Ayan.

Mina alikuwa ametulia kimya walipoingia, akasimama na kuwapa mkono akiwakaribisha. “Meza imejaa vyakula tukijua mnakuja na watoto!” “Tumekuja nao ila tumewaacha hotelini, ili sisi kwanza tuzungumze.” Andy akakaa na Ayvin begani ametulia kama sio yeye.

“Mbona huyo kwenye video anaonekana mtundu sana?” Pius akauliza akionyesha wazi anatamani kumshika mwanae. “Ujanja wake unaisha akishasikia hodi. Anatulia kama si yeye mpaka mgeni aondoke. Eti Ayvin?” Andy akamchungulia pale alipojificha. Akazidi kumng’ang’ania. Mina kimya kama Raza.

“Basi wewe Ayan njoo uchukue zawadi yako. Dady amesema unapenda vitabu, si ndio?” Akakubali akitingisha kichwa. “Basi Poliny amekutafutia vitabu vizuri sana, utapenda. Njoo.” Akawa anasita huku akimtizama mama yake kwa hofu. “Huyo, hapo hawezi sogea. Anamuogopa sana Raza.” Mina akaongea maana walishangaa Ayan ameshindwa kabisa kusogea japo alionekana amependa zawadi.

“Raza alikuwa akimpiga sana Ayan ndio maana anamuogopa.” Mina akaongea kwa jazba. “Sio sana!” “Unabisha nini wakati hata Polla aliniambia na kumwambia babu yake kuwa ulikuwa ukimchapa na kumnyima maziwa? Labda useme kama Polla ni muongo ila na Mamu naye pia alishasema unamchukia mwanangu na unampiga SANA japo mtoto mwenyewe ni mkimya.” Mina akaongeza kwa hasira.

“Ndio maana nimekuja kuomba msamaha.” “Wakutaka kumuua, sawa. Lakini jua ashajua humpendi, anakuogopa.” Kidogo pakatibuka kama maziwa yaliyokuwa yakichemka taratibu gafla kumwagika na kutibua jivu. “Itachukua zaidi ya vitabu kuwaamini nyinyi wote wawili maana wakati mwingine na wewe Pius ulikuwepo wakati mkeo akimpiga mwanangu.” “Hajawahi mpiga mbele yangu.” “Basi jua Ayan anajua kama na wewe ulikuwa ukijua kama mkeo alikuwa akimtesa na hukumtetea. Ndio maana kama umegundua alikuwa akikupenda sana zamani. Akaja kukubadilikia. Siku hizi akikuona mahali anakukwepa kwa hofu, hakukimbilii kama zamani alipodhania ulikuwa kimbilio lake.” Mina akawa ameshapandisha.

“Ayan nenda kasome vitabu vyako ndani.” Baba yake akamtoa hapo. Hakuchukua hata sekunde, mtoto akakimbilia ndani kama mshale. Gafla pakapoa hapo, wakawa kama wamepoteza dira. Kimya. Andy akajisogeza nyuma na mtoto begani, akajiegemeza kwenye kochi, akatulia. Kimya kwa muda.

Ukifunika Kosa Leo, Kesho Litakuja Kama Dhoruba Kali

Ni kweli siri ya makosa ni kama tu. Mwishoe hutoka hata ukiziba kila ufa. Muda mfupi uliopita, kabla na hata walipokaribishwa ndani ni kama kulionekana maisha yaliweza kuendelea. Lakini kumbe ndani bado kulikuwa na madonda mabichi yaliyokuwa yamefunikwa na ngozi kavu kama kovu.

Pakatibuka kwa machungu ya dhambi ya nyuma ambayo ilionekana ndogo na kushindwa kutubiwa. Walikuja na la uuwaji, kumbe kuna mengine alifanyiwa mnyonge Ayan sirini, Mungu akaona na hilo liwekwe mwangani.

 Pius alikusudia watoke hapo wakiwa wameyamaliza. Akaangalia ile hali, akaona yeye ndio aanze maana ni kama Raza alinyong’onyea, akashindwa jinsi ya kuendelea kuanzia hapo.

“Kuna makosa mengi yametokea, naomba nianze na kubwa na la kwanza, swala la mtoto. Ukiangalia kwa makini na kufikiria tokea mwanzo, mimi ndiye niliyekosea tokea mwanzo.” Akaanza Pius. “Mimi ndiye niliyekosea kuanzia kutungwa mimba yake mpaka anarudishwa baada ya kuzaliwa. Kosa moja ni lakuficha ukweli wa mambo, ilimgarimu Mina na Andy.” “Umeruka Pius. Tafadhali kama umekusudia kuomba msamaha, omba ueleweke.” Akaingilia Andy.

“Ushikwaji wa mimba ulitokea wapi?” Akamuuliza na yeye kaka yake kwa ukali. “Ni kweli.” Pius akakubali kwa kujishusha. “Tokea mwanzo kumpa Mina pombe.” “Na kuingia kwenye chumba changu na kulala kwenye kitanda changu cha ndoa, tena takatifu! Uliwezaje Pius?!” Hapo na Raza naye akamgeukia mumewe vizuri. Makosa yasiyoelezwa hukua kama kivuli kinachokuandama hata jua likiwaka. Pius alishindwa kuepuka huo ukweli.

Nimekosa Andy na naomba tu niwe muwazi. Tulijenga ukaribu na Mina nafikiri hapo ndipo nilipopitiliza. Nimekosa Andy, naomba msamaha.” Ungemuona Pius huyu mpaka akawashangaza na wao.

“Na katika hili hata Raza narudia kukuomba msamaha. Nimekosa mke wangu, naomba na wewe unisamehe. Kuanzia kabla na baada ya mimba, jamani, sikufanya vizuri. Ningefanya vizuri hata baada ya kujulikana kama mtoto ni wangu, nina uhakika wote nyinyi, mpaka wazazi, Raza zaidi, asingefika alipofika.”

“Mimi ndiye niliyemtia hofu Raza. Nikampuuza mpaka akatishika na kufanya aliyoyafanya.” “Sema kutaka kuua watoto wangu. Kama kweli mmekuja kuomba msamaha, ombeni mueleweke msiweke kificho na hapo ndipo kupona kwa kila mtu. Msiweke lugha ya mafumbo wakati kila mtu anajua Raza alikusudia KUUA wanangu lakini akakutana na Mungu aliye HAI. Na kama isingekuwa nguvu za Mungu, inamaana pengine sasahivi nisingekuwa na mtoto hata mmoja!” Bwana wenye nyumba hao walikuwa wakali!

Raza akapiga magoti kwa haraka. “Nimekosa Mina. Nimekosa sana. Niliingiliwa na roho chafu na nakiri niliiruhusu mimi mwenyewe sababu ya wivu tokea mwanzo. Mtoto wa kiume nimemtafuta jamani, karibu kuchanganyikiwa. Na hapo ndipo lilipokuwa anguko langu. Nilifungulia milango mingi na shetani akajua udhaifu wangu, akanitumia.”

Nisamehe Mina. Nimekosa na nimetubu. Nimempa maisha yangu Yesu, sasahivi naishi kwa kuongozwa na yeye.” “Hapo sasa ndio itakuwa pona yako. Maana hivihivi utajikuta kila mwaka mnarudi hapa kuomba msamaha. Shetani hanaga mpango wa kukamatwa na kumuachia mtu. Jua atakujaribu tena na tena maana naona na Mungu naye ameamua humu ndani kuzaliwe madume matupu. Sasa utashindana na Mungu mpaka lini?”

“Nimeacha kabisa Mina. Hata mambo ya waganga nimeacha kabisa. Na japokuwa bado watu hawajanisamehe, lakini moyoni nipo kama nimetua mzigo mzito. Kwanza mimi mwenyewe nilikuwa nikiteseka! Havina raha na wala havikuwahi nisaidia. Nimekosa Mina. Nimekosa hata kumchapa Ayan.”

“Sasa hilo ndio kosa lililokuwa likiniuma sana, Raza. Kumchapa mwanangu asiye na hatia kabisa! Ulimuonea mwanangu bila sababu! Ukatumia upweke na unyonge wake kumuadhibu mwanangu. Mtoto aliyekuwa ametelekezwa na wazazi wake! Mnyonge asiyeweza kujitetea wala kukushitaki kwa mtu, ukamchagua kumtesa yeye, sababu tu, eti amezaliwa wakiume!”

“Halafu kwa utajiri wote mliojaliwa nyinyi wawili, kweli kumpa mwanangu maziwa ukawa unaona shida! Mnamnyima mwanangu chakula kilichojaa ndani kwenu mpaka kuharibika na kutupwa! Roho mbaya gani hiyo Raza wewe!? Chakula tu!?” Mina akawa ameshakuwa juu haswa. Hasira.

“Hakika hapo ndipo uliponiumiza na kunikosea Raza. Lakini huko kumuua mimi sikujali kwa kuwa nilijua HUTAWEZA, hata uende kwa shetani mwenyewe, huwawezi wanangu.” Mina akakaa sawa akiwa bado na hasira, Raza kapiga magoti mbele yake.

“Hakuna mchawi atagusa mwanangu, akafanikiwa. Ndio maana waliposema wanakufunga kwa uchawi wakutaka kuua wanangu, nikasema hapo wala sioni kosa. Ila kuchukia wanangu, ukiwaonea na kuwanyanyasa, halafu na kusambaza maneno mpaka kumchanganya mama yangu ukimuabisha! Hapo HAPANA Raza. Bora ukaloge utakavyo ila usimuuwe mama yangu kwa fedheha.”

“Wala na hilo usiwe na wasiwasi nalo. Watu wananikimbia sasahivi. Huyo Mamu ndio utafikiri ametumwa kunitesa! Ananitangaza ubaya kwa kila mtu! Mwenzio nimegeuka kichekesho kwa watu, mpaka ndugu! Ananitangaza ubaya mpaka kwa wafanyakazi wangu, kwamba mimi nawaloga ndio maana wanakaa pale muda mrefu. Eti nimewafanya kama msukule. Msichana wa kazi aliyekaa na mimi zaidi ya miaka 10, ameondoka sababu ya Mamu! Watu wananikimbia Mina! Mimi mbaya.” Raza akazidi kutokwa na machozi.

“Sasa na wewe usikubali kujisemea mabaya. Wewe si umempa Yesu maisha?” Akakubali akitingisha kichwa mumewe akamsaidia kumfuta machozi. “Wewe ni mbarikiwa sio mbaya. Yakale yote yamepita, wewe sasahivi umekua mpya.” “Kwahiyo sasa umenisamehe?” Mpaka Mina akacheka.

“Si umesema mwenyewe yakale yamepita, nimesamehewa? Basi na wewe nisamehe Mina! Tulee wote watoto.” “Na uache kuwapiga wanangu.” “Hata wakikosa?” Raza akauliza akikaa na kujifuta machozi. “Basi hawaji huko kwenu.” “Nakutania bwana! Siwachapi tena. Wakija nitakuwa nawapa maziwa na nitakuwa mama mzuri kwao. Hakika nimebadilika Mina. Nilikuwa nimebeba chuki, sijui kwa nini!”

“Si hata Poliny mwenyewe alikuwa hawezi kuishi na mimi? Unakumbuka hata kwako alikuwa akikulalamikia?” “Nakumbuka.” “Sasahivi mpaka yeye anasema eti anakuwa na hamu na mimi!” Wakacheka. “Kila siku ananitafuta mwanangu na kunijulia hali kitu ambacho hakikuwepo kwake! Mpaka ananiomba mimi ushauri na kutaka niwe namuombea!”

“Nisamehe tu Mina. Nilijichanganya tokea nilipoanza kwenda kwa waganga. Huko ndipo nilipokwenda kubeba maroho mengine ya ajabu yakawa yakinipelekesha mpaka kudhuru watu.” “Yameisha. Na kama una shida na msichana wa kazi wewe niambie. Kuna mtu anatafuta kazi. Alikuwa akitusaidia hapa kabla sijatoroka na wanangu, sasa nimerudi na huyu, amezoea wanangu na naona wenyewe tunaelewana kwa kusukumana hivyohivyo, sitaki kumbadilisha.”

“Sasa yule wa kwanza amerudi na anashida sana. Ni mdada mzuri, anamcha Mungu na ndiye aliyenisaidia kunihimiza kuzungumza na Andy kipindi kabla sijajua mumeo ndio baba mtoto.” Akamtizama Pius kwa hasira.

“Nilikosea Mina, ila ujue nilipanga nije kukwambia.” “Wewe ni mbaya Pius. Uliniacha nadhalilika, ukabaki kimya!” “Na hilo natubia. Tafadhalini naomba mnisamehe. Andy, tafadhali nisamehe. Kwa yote. Kuanzia Mina mwenyewe mpaka kuzaa naye. Si sawa. Nimekosa.” “Hilo ndilo nilitaka kukusikia.” “Nimekosa. Na nilikosea tokea mwanzo. Tafadhali naomba unisamehe.” “Naona na kosa lenyewe limekuja kuwa baraka kwangu.” Akamchungulia Ayvin pale alipojilaza begani kwake. Alishalala.

Pale Mungu Anapobadilisha Ubaya Kuwa Wema.

“Ayvin ni mtoto mzuri sana. Hata wewe Raza, ukimfungulia moyo kwa ukweli, utagundua Mungu ameleta faraja kwetu SISI WOTE. Amekuwa mpaka dawa kwa mzee Ruhinda bwana! Yaani mzee Ruhinda anafanya mambo ambayo hata mama anasema hakuwa akiyafanya kwetu! Na ili usipatwe wivu, jua ni Ayvin tu wala si watoto wa kiume maana Ayan mwenyewe hamchangamshi babu yake kama huyu.”

“Ayvin ni faraja na kicheko mpaka kwa Ayan mwenyewe. Kwa hiyo mpe nafasi bila kujali jinsia yake, kwa hakika utamfurahia. Na hata hili nilimwambia Mina. Kama tutamkuza hivihivi kwa upendo, kusiwekwe hofu kama mlivyofanya kwa Ayan. Mkimnyanyasa bila hatia, mkamuingizia hofu kijana wangu. Mkiepuka hilo kwa Ayvin. Akapewa uhuru wa kuwa vile Mungu alivyomuumba, basi mjue familia ya Ruhinda kila mmoja atamfurahia. Ni mtoto mzuri sana. Na si mchoyo hata kidogo.”

“Kwa udogo wake huyu, ukimpa kitu kizuri, akakipenda. Hata ukimuwekea mdomoni, atatoa na kumpa Ayan.” “Aisee kweli! Kumbe na wewe umemuona?” Mina akaingilia hakuwa amejua kama mumewe amegundua. “Kabisa. Mpaka mimi ananishangaza! Huna kitu ukampa yeye, kaka yake na yeye asipate. Sasa hebu niambie afundishwe hivyo kuwa dada zake woote, aambiwe nao ni ndugu zake. Halafu akafanikiwa kwenye maisha. Baada ya miaka 50 kuanzia sasa sisi tukiwa hatupo hapa, si tutakuwa tunauhakika tumeacha watoto wote kwenye uangalizi mzuri?” Mpaka Pius akashangaa na kujikuta akitokwa na machozi. Akayafuta kwa haraka sana.

“Nakushuru Andy. Aisee asante sana. Nashukuru.” Pius akajikuta akisema hivyo. “Haiba yake si yakuficha huyu. Ngoja awazoee, halafu akue kidogo muone jinsi tutakavyokuwa tukinyang’anyana. Ila tu isitokee wakumuharibu akili. Na haya mambo ya MALI hili hata Mina nimemwambia. Na wewe Raza nakuomba. Acha kufundisha vijana wangu maswala ya mali zetu. Waache wakue, wajue mali ni za baba na mama, wao watafute ZAO!” “Nashukuru Andy.” Pius akaongeza.

“Hakika tutawadumaza. Utakuja kuta tunakua na vijana wasio pambana kwenye maisha, wanasubiria mali ambazo kwanza si zao na wanaweza hata wasije kurithi mpaka wanakuwa watu wazima, wanasubiria tu! Tuangalie sisi vijana wa Ruhinda. Hakuna aliyerithishwa, lakini wote tunapambana. Na tulipofika hapa, hebu niambie mzee Ruhinda atatupa nini ambacho sisi hatuna?”

“Hata Pius ameniambia hivyohivyo! Ni uelewa mbaya shemeji yangu. Nimekoma, naomba na wewe unisamehe!” “Aisee kwa huyu nitakuwa mkali hata kwa baba yake. Naomba tusije mchanganya. Ni mtoto mzuri sana. Hajijui jinsia yake ila anajua watu wanao mzunguka na kuwapenda sana. Hakika sitaruhusu mtu amchanganye.” Hata Mina ilimgusa. Hakutegemea kwa umbali huo aliokuwa akiusema. Andy alionekana kumaanisha kutoka ndani.

“Tafadhali naomba nimshike akiwa hivyohivyo amelala!” Andy akaenda kumpa. “Nimepitwa na mengi sana.” Pius akaongea kwa kulalamika akimwangalia kijana wake. “Sio sana. Kuanzia wanarudi mpaka sasa, nimechukua kumbukumbu zake nyingi sana ili asije bisha baadaye. Ayvin ni mtundu sana aisee.” Wakacheka vile Andy alivyoongea ila kwa kuvutiwa sio kwa ubaya.

“Mpaka siku ya kwanza anaanza kutambaa kabisa. Nilikuwa naye, na nilifanikiwa kumpata vizuri sana kwenye video.” Andy akaongeza. “Tafadhali nitumie kila kitu.” Pius alikuwa akimtizama huyo mtoto kama asiyeamini, kama ameokota alumasi!

 “Aisee amekua! Halafu anamwili!” “Mlaji mzuri. Hasumbui kula labda akimuona mama yake, napo namuona kama ameanza kubadilika sio kama zamani akimuona mama yake, hataki kula kabisa anataka kunyonya tu.” “Itakua kukua.” Pius akaongeza. “Na michezo mingi. Wakati mwingine anakuwa amezidiwa michezo hata hajui kama nipo mahali. Na Andy akiwepo ndio kabisa! Akili zinakuwa kwa Andy tu. Anajua yeye ndio anampatiliza.” Mina akaongeza. Pius akamuweka kifuani vizuri akaanza kumpapasa.

~~~~~~~~~~~~~~~

Alikuwa msafi, ananukia vizuri, utajua yupo na matunzo mazuri. Kwa asili Mina alipenda kuvalisha wanae mpaka walikuwa wakimsema hana akili ya matumizi ya pesa. Anamaliza pesa kwa kununulia mtoto nguo. Watoto wake wakati wote ni wasafi haswa, kama Andy baba yao. Wakabaki wakimwangalia.

~~~~~~~~~~~~~~~

“Akiamka hatalia?” “Anaweza asilie. Tutaona. Sio mida yake ya kulala sasahivi. Msingekuwa nyinyi kuwepo, angekuwa kila mahali hapa amezagaa na jina lake likitajwa kila kona na kila mtu, akikatazwa asifanye hiki au asishike kile. Hapo ni hofu tu inamlaza. Ataamka tu.” Raza akavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu akimtizama huyo mtoto.

“Amebeba damu nyingi ya Mina mpaka rangi si ya kina Ruhinda!” Raza akasifia na kufanya wote wamwangalie tena pale alipokuwa amewekwa kifuani na Pius. Wakatulia kwa muda.

“Msamaha Ni Upepo Unaofuta Vumbi, Ukiacha Njia Mpya Iangaze.”

“Jamani si mmetusamehe kabisa?” “Yameisha Raza. Kuwa na amani.” “Nashukuru Mina, lakini acha tuombe. Tumshukuru Mungu kwa kutusamehe mimi na familia yangu, na kuomba mwanzo mpya wenye msingi imara wa Yesu.” Wakaona si wazo baya. Wakataka yeye mwenyewe Raza ndio aombe. Bwana Raza aliomba mpaka akawashangaza!

Alianza kwa kutubu akimtubia kila mmoja wao hapo kama wazazi. Alitubu Raza mpaka kwa machozi akimsihi Mungu awasamehe pale walipokosea na kuzembea kwenye ndoa zao na malezi ya watoto wao.

Kisha akaja kutamka baraka kwa Mina na watoto wake mpaka Mina akafungua macho kumtizama asiamini kama ni yeye Raza. Akamuombea Ayan uponyaji wa nafsi na fikra akimsihi Mungu awasaidie, kumsaidia na yeye kuwa kile Mungu alichomkusudia. Akamuombea Andy na Pius. Akaomba hekima ya Mungu juu yao wao kama wazazi awasaidie kulea hao watoto wawe baraka kwao na kwenye jamii.

Aliomba Raza! Ungemsikia ungejua ipo nguvu ya msalaba na Mungu ni mwingi wa rehema, na hana upendeleo. Mpaka wanasema ‘Amen’, kila mmoja anajisikia vizuri. Na kujiona ni wazazi wenye jukumu moja.

~~~~~~~~~~~~~~~~

“Sasa watoto si mkawalete ili tule pamoja?” Andy akatoa wazo. “Na mnaweza kuwaacha hapa walale nyinyi mkaenda kupata muda wenu huko hotelini. Polla aje afanye fujo zake hapa, aungane na Ayvin kwa siku hizi mbili. Watuchangamshe ndio muondoke nao.” Mina akaongezea kwa mumewe. Pius na mkewe wakaona si wazo baya. Japo yeye Raza ndio alifurahi zaidi kuona Polla wake na yeye hapo anakaribishwa kwa upendo na si kama kwa shangazi yake alipofungiwa milango.

Wala hakufikiria mara mbili, Raza mwenyewe akarudi hotelini kwa binti zake. Pius alikuwa hataki hata kumuachia mwanae. Alibaki amemkumbatia, amejituliza kwenye kochi hataki hata kujitingisha akihofia asije muamsha, akaondoka hapo mikononi mwake.

~~~~~~~~~~~~~~~~

Lakini baada ya muda mfupu akaamka na kufungua macho akiwa amesimamisha kichwa. Pius akamtizama kwa upendo. Mina akamfanyia ishara Andy anyamaze kabisa kisha Mina akajifunika na mto hapohapo kwenye kochi. Akabaki akimtizama Pius kisha akageuka. Alipomuona Andy amekaa kochi la mbali kidogo akaanza kukunja kamdomo akionekana anataka kulia. Kisha akanyoosha mikono akitaka Andy amchukue. Pius aliumia sana mpaka alionyesha.

~~~~~~~~~~~~~~~~

Inaendelea….


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment