“Ningefurahi
Pius.” “Najua unahitaji mapumziko. Na Poliny nimemwambia umechoka,
unahitaji kupumzika. Unatutumikia pale ndani bila kuchoka na ni kila
siku! Nikamwambia ni lazima atenge muda asaidie kukupa Off
nyumbani. Ndio amekubali tuongozane. Kwamba atachukua vitabu vyake, twende na
mwanao unayemdekeza. Anasema wakati anacheza game zake, yeye
anasoma. Akianza fujo atatupigia chumbani kwetu, uje umtulize.” Raza alicheka
sana.
“Hivi nyinyi
mjue Polla ni mrahisi sana kuishi naye! Tatizo lenu wewe na Poliny hamjamjulia.”
“Sasa yeye huwa anasoma saa ngapi? Mtoto asiyetaka kusoma hata kitabu cha
hadithi jamani! Ukimwambia, ugomvi!” “Tatizo lenu nyinyi mnamuingilia katikati
ya mambo yake. Polla hataki kuingiliwa. Wewe panga muda unaotaka asome, kisha
ukimkuta katikati ya game yake, mwambia ile game kwa wakati huo
ikifika mwisho, au hata kama haijafika mwisho, wenzie wakimtoa, ameshindwa
hiyo game, afanye jambo unalomtaka afanye. Na unamwambia ukirudi kabla
hajakufuata, unamzimia game nzima hata kama ndio ameanza au yupo
katikati ya hiyo game nyingine. Sasa kwa kuwa hataki kuingiliwa katikati
ya game zake, akifika tu mwisho tu kwenye game uliyomkuta
nayo, anakufuata yeye mwenyewe mmalizane, ili aendelee na game zake.”
“Atafanya kila
kitu tena kwa haraka na makini ili usimuweke. Na huwa ananijua, hawezi
nidanganya maana namuuliza maswali kuhakikisha ameelewa. Basi atazingatia kwa
makini ili kufupisha ule muda wako, awahi yake.”
“Tatizo lako
wewe na mwanao Poliny, mnamuingilia. Halafu mnampa mambo asiyopenda. Wewe
unajua kabisa hapendi kusoma vitabu vyenu hivyo ya historia za ulimwengu,
halafu eti unaanza kumwambia aache game asome historia ya vita ya kwanza
ya dunia! Polla!” Pius alicheka sana.
“Inamuhusu nini
yeye vita ya kwanza ya dunia au uchumi wa ulimwengu?” “Ajue
ulimwengu unavyoelekea!” “Hayo mambo ya mwanao Poliny. Sasa yeye akipewa vitabu
na babu yake. Vikamsisimua yeye, anakuja mlazimisha mwanangu, kwa
muda wake yeye, eti asome, kitabu ni kizuri. Polla akishakitizama na
kile kichwa chake cha habari nzima ya hicho kitabu, anamuuliza kwa nini
yeye asome!” Pius hana mbavu.
“Naye Poliny
anaanza kumuelezea umuhimu wa kile kitabu, Polla hana muda wa
kumsikiliza. Anataka amuache acheze game zake. Poliny anataka lazima
asikilizwe, ndio ugomvi unapoanza, na kumsimanga mwanangu hapendi
kusoma. Polla naye hataki kumsikiliza anamfukuza chumbani kwake.
Ndipo ugomvi unapoanza.”
“Namuuliza
Poliny, dada mkubwa vile kupigana na mtoto mdogo, haoni aibu? Anasema namtetea
Polla kila wakati wakati yeye anamsaidia. Polla naye anasema yeye
hataki msaada wake. Basi eti mwanangu yeye mkorofi!” Pius akazidi
kucheka maana ndio kama anapata picha kamili ya ugomvi wa wanae.
Maana yeye humuamini sana Poliny bila kumsikiliza Polla.
“Ila Polla ni
kweli mkorofi bwana! Akitaka jambo lake anataka libakie hivyohivyo!” “Sasa wewe
jiulize watoto hao wawili wenye aina hiyo ya tabia, wameipata wapi?
Kushikilia jambo, hawataki mabadiliko?” “Raza!” “Taratibu tu. Fikiria
wanao na jinsi wewe ulivyo Pius.” “Lakini bora Poliny bwana!” “Kwa kuwa
misimamo yake inaendana na matakwa yako. Ndio maana unamuona yeye kama malaika.”
“Halafu Pius,
Polla huwa hafeli. Hapati 100, ila mara nyingi anapata A, akifeli
sana mwanangu ni B. Maana anajua akishuka tu hapo, basi namnyima game.”
“Kweli?!” “Muulize mwenyewe. Akileta ripoti mbaya, anapumzika game kwa
muda mrefu tu, ndipo utakapomuona amejaa jikoni na kukufuata wewe mpaka
chumbani akitaka hili na lile, na maswali kwako hayaishi. Basi jua hapo
nimempumzisha game zake. Mpaka arudie ule mtihani, aufaulu tena, ndio
anarudia game.” “Basi mfundishe kusoma vitabu bwana!” “Sasa hapo
unamtaka Mungu maneno.” Pius alicheka sana.
“Sasa kwa hiyo
tunakwenda nao wote?” “Poliny anakwenda ili kunisaidia Polla. Kulala kwa
wakati na kuoga usiku tukiwa chumbani kwetu. Ila muda wa kula tutakuwa nao.
Hivi nimemwambia awahi kurudi nyumbani amsaidie kufungasha vitu vyake ili
tukirudi tu na sisi ni kujiandaa, tunakuja kuchukuliwa saa moja usiku,
tunaondoka.”
“Sasa ili kila
mtu apumzike huko, mwambie Poliny asianze kumfungashia vitabu tu. Atajaa
kwenye kila chumba na ratiba za watu atamiliki yeye, maana hatakuwa na
chakufanya ila kutaka kila mtu amfuatishe anachokitaka yeye.” “Hata kitabu
kimoja jamani!?” “Kama mnataka kweli tukapumzike huko, mwambie amfungashie game
zake na nguo za kuogelea kama tunakokwenda kutakuwa na pool. Kitabu
hatasoma, na ndipo watakapoanza kupigana, tuitwe chumbani kwao.” Pius
akatingisha kichwa kwa masikitiko.
“Na umsisitize
Poliny anayependa kumkazania mtoto.” “Basi nitampigia nimpe hayo maagizo.” “Nashukuru Pius. Nimefurahi SANA.” Furaha
aliyokuwa nayo Raza, hakuna jinsi angeweza eleza mtu akaelewa. Kuna ambayo anajibiwa
hata hakuwa akijua jinsi ya kuomba.
“Tunakwenda
wapi?” “Surprise.” Akazidi kucheka kwa furaha. “Sasa nibebe nini?” “Mama
wewe, surprise. Mbona hivyo! Unataka kunidodosa mpaka niseme! Lakini jua
hati zenu za kusafiria zimehusika.” Akatoa tabasamu akijua wanatoka nje ya nchi,
ila ndani ya Africa kwa kuwa hawajahusika kwenda kuomba Visa popote ila hati
zao kwenda kugongwa tu. Na kwa kuwa ni Pius, akajua ni sehemu ya maana.
“Na ungekuwa
unaweza kuomba ruhusa kazini kwako jumatatu usiende, tungeondoka leo, tukarudi
jumatatu. Poliny yeye amesema hana vipindi siku ya jumatatu.” “Na wewe kazini?”
“Kwangu hili jambo ni la muhimu Raza. Naweza nikachukua Off hiyo siku ya
jumatatu.” “Kweli Pius?!” “Kabisa. Sikumbuki kuwa na muda na wewe mtulivu wa
namna hii ninaotaka upate. Nahisi hata mwanzo wetu haukuwa mzuri.” Raza
akatulia akikumbuka fungate yao.
~~~~~~~~~~~~~~
Ni kweli haikuwa
hata romantic. Kwa Pius ilikuwa ni bora liende. Ikawa kama anatimiza
wajibu tu. Na hawakwenda mbali. Hapohapo jijini. Kitu alichokuwa akifanya huyo
Pius huko fungate ilikuwa ni kusoma vitabu na kusikiliza taarifa za habari za
kila pande ya ulimwengu mpaka mwisho wa fungate.
Hata walipokuwa
wapo mezani wakila wanandoa hao wapya huko fungate, basi atakuwa na kitabu
chake. Anakula huku akisoma bila hata ya kuzungumza na mkewe.
Basi Raza
akajikuta mpweke mbele ya mume huyo wa ndoa mpya. Atakula na kuamua kurudi
chumbani. Ataangalia movie mpaka achoke na kupitiwa na usingizi hapo
kitandani. Baadaye ndipo Pius atafika kitandani. Kama hataomba penzi, basi ujue
asubuhi ni lazima. Atamuamsha huyo Raza kwa kumpapasa. Raza ataamka.
Atajituma hapo kitandani. Akimaliza Pius, anarudi kulala. Raza anaendelea na
yake, kwenye hoteli hiyo nzuri ya kifahari mpaka fungate ilipoisha.
Miaka ikaenda.
Pius anakuja kukubaliana na uhalisia kuwa Irena hatarudi tena kwenye
maisha yake, ameshazaa kabisa na ana watoto zaidi ya wawili, maisha ya ndoa yake
yalishachukua picha kongwe. Raza akawa ameshajitengenezea
marafiki wa nje. Ratiba yake ikawa nyumbani, kazini kisha baa.
Hamjui Pius romantic wala hajawahi kukutana naye. Anaye mjua yeye ni
Pius wa kutumikiwa. Apewe penzi. Chakula kizuri kwa wakati. Nyumba safi
kila wakati na nguo zake ziwe safi kama mpya kila akitaka kuvaa. Na Raza
akayamudu yote hayo akigawa kazi kwa wasaidizi wake nyumbani, maisha yake
yakaendelea bila ndoa ya kufuatana nyuma.
Pius anarudi kutaka
wa kumkumbatia, mkewe hata hajui kama Pius ni kiumbe wa malove
dove. Anajua ni mtu wa kuingia, piga bao, toka. Na
yeye kazi yake ikawa ni kuomba pesa kisha kwenda kufanya yake na wengine.
Na yeye Pius akaanza
upweke mpaka alipompata Mina mpenda mikono, na yupo wakati wote. Basi
ndio akawa anatulia nyumbani kwa mdogo wake.
Raza akirudi
nyumbani anajua Pius hatakuwepo, akifanya yake ya umama, anasambaa baa,
kwa wenzie. Pius naye alishajua mkewe hayupo nyumbani, basi akawa akiwekeza muda
wake zaidi kwenye biashara zake, wazazi, na ndio mpaka akaishia kwa mke wa
mdogo wake.
Wawili hao
walikuwa wakikutana, Raza analojua ni kukata mauno. Mumewe anapiga
bao. Kazi kwisha. Lakini kila mtu alikuwa akienda kuliwazwa kwengine na
watu wengine. Maisha yakaendelea mpaka hayo majanga yakawapata.
Wamejikuta wamerudi kuwa wao wawili. Ndoa kongwe takatifu na binti wawili.
~~~~~~~~~~~~~~
Raza alikuwa
amepotelea kwenye mawazo yaliyomrudisha mbali ila wazi yalionekana ni mawazo yaliyoweza
kumtoa furaha yote na kumpa huzuni. Alibadilika mpaka usoni akanyongea. Ikawa
kama aliyekumbushwa fedheha. Akapoa kabisa mpaka Pius alipomshitua kwa
swali. “Unafikiri wewe na mwanao mnaweza chukua off hiyo siku ya jumatatu?”
Raza akagutuka na kujaribu kurudisha mawazo pale.
“Jumatatu
wanaweza kukupa off ofisini kwako?” Ikabidi mumewe arudie swali na
kuongeza. “Mbona umepotea tena?” “Sijategemea kama unaweza kuja taka
muda na mimi, Pius!” “Naamini sijachelewa. Eti Raza? Si tumekubaliana safari
hii tunaanza upya na vizuri?” “Nitashukuru. Na kuhusu ofisini hakuna tatizo.”
Raza hakuwa na neno, alipokea vile Mungu alivyombariki bila kinyongo.
Katika
Majivu ya Machungu, Upendo Wazaliwa Upya
Dereva alikuja
kuwachukua mapema bila ya kuchelewa. Safari ya uwanja wa ndege ikaanza Raza na
wanae hawajui wanakoelekea. Polla akawa anaimba njia nzima, dada yake anamkosoa.
Wakaanza kubishana. “Umeanza Poliny!” “Sasa huyo mwanao asirekebishwe!?” Baba
mtu naye akadakia. Polla akaanza kulia.
“Kwani nyinyi
kila kitu ni lazima mumkosoe?” “Hata kama maneno anakosea mama jamani!?”
“Kwa hiyo hivyo anavyolia ndio unaona raha?” “Mimi nilikuwa nikimsaidia.” “Niache
mwenyewe, sitaki kusaidiwa na wewe.”
“Nyamaza mwaya
Polla mtoto mzuri. Imba vile unavyotaka. Kwanza sauti yako nzuri.” Acha Pius na
Poliny waangue kicheko, mbavu hawana. Polla akazidi kulia.
“Hivi kwa nini
mnafanya hivyo!?” Dereva kimya, familia hiyo wakizozana. Raza akaanza
kumbembeleza mwanae, Pius na yeye anacheka kimyakimya.
“Na kwenye ndege sikai na wewe,
nakaa na mama!” Hapo Pius akashituka. “Mimi ndio nakaa na
mama yako.” “Mimi nimeshawahi.” “Sasa unawahi
vipi kwenye mipango yangu wewe Polla!? Nishapanga kila mtu anakaa wapi!” “Lakini
hakuna aliyekusikia ukiwahi. Mimi nishawahi na kila mtu amenisikia. Usifanye uonezi
kama Poliny.” Akaanza kubishana sasa Polla na baba yake,
wote wanataka kukaa na Raza, yeye kimya.
Mwishoe Poliny
akamtetea baba yake. “Kwanza hii safari ni ya dad, wewe umekaribishwa tu. Huwezi
jichagulia.” Wawili hao wakaanza kumchangia Polla mpaka akaanza kulia tena.
Baba yake muonezi kama Poliny.
Wakafika uwanja
wa ndege wanabishana kwelikweli, Polla hataki kushindwa. Na anawamudu
wote wawili kwa hoja. Anang’ang’ania yeye amewahi. Mwishoe akasema
warushe moja ya kitufe chake. Kina pande mbili. Yeye akachagua upande wake. Baba
yake akampa upande mwingine. Poliny akamuonya baba yake. “Usikubali dad.
Huna game utamshinda Polla. Hapo anakutega tu,
atakushinda.”
Wakabishana tena
hapo nje ya uwanja wa ndege kila mmoja na mzigo wake mpaka Raza akamwambia
Polla arushe. Ilipotua chini, Polla akashinda. Bwana alifurahi!
Alishangilia hapo kila mtu akawageukia wao. “Raza, zungumza na mwanao. Mimi
nishaweka mipango yangu.” “Kama sikai na mama, mimi siendi. Mwambie
dereva arudi kunichukua, nitakaa mwenyewe nyumbani. Kwanza najua kupika kuliko
Poliny, sina haja naye.” Polla akaweka ngumu hapo wanapita security point
bado wanabishana.
Uzuri wote
walikuwa wakikaa first class viti vinavyofuatana. Polla akaishia kukaa
na mama yake mbele yao, Poliny na baba yake wamepoa. Vicheko vyote vimeisha.
“Nilikwambia game yoyote anayokwambia mshindane Polla, usikubali.”
“Halafu ananiita mimi muonezi wakati yeye anafanya maufilishi!”
Raza hana mbavu amekaa na mwanae.
~~~~~~~~~~~~~~
Safari ya visiwa
vya Mauritius ikaanza wote wamejawa hamasa ya kufika huko, maana ilikuwa mara
yao ya kwanza. Kwa hakika waliandaliwa ipasavyo. Sekretari wa Pius aliandaa
kana kwamba wawili hao wanakwenda fungate mpaka Raza akashangaa. Chumba
chao kilitayarishwa kama wanaingia honeymoon!
“Au wametupa
chumba sicho?” Raza akauliza akijaribu kutafuta pakukanyaga. Maana chumba
kilijaa maua ya roses nyekundu kila
mahali mpaka kitandani!
“Honeymoon yetu ya pili. Ya kwanza haikuwa
imekaa vizuri.” Raza akamwangalia kwa mshangao. “Kumbe unajua! Sasa kwa nini
ulikuwa ukinifanyia vile!?” “Achana nayo.” “Hapana Pius, nataka kujua. Maana
ilikuwa kama umelazimishwa au unanifanyia kusudi! Tena ni kama kikatili
kabisa! Ni kwa nini?!” Akauliza kwa kuumia kabisa.
“Raza,
tumefanikiwa kumlaza Polla, acha tutumie muda huu vizuri. Achana na mambo ya
zamani.” “Wewe umesema tunaanza upya. Mwanzo huu unaweza kuwa bora kuliko wa
mwanzoni. Sasa kwa nini tunaanza kwa kufichana? Niambie tu nijue
kilichokuwa kikiendelea.” Pius akafikiria, akaona amwambie ukweli ila
kwa ufupi.
~~~~~~~~~~~~~~
“Nisikilize
Raza, wewe hukuwa tatizo kabisa, ila ulinikuta nikiwa na mambo mengi, na uchungu,
ndio nahisi nikakumalizia wewe hasira kwa sababu ndiye uliyekuwa karibu yangu.”
Akaanza Pius. Akamsimulia habari za Irena tokea mwanzo mpaka mwisho.
“Yaani wewe
umekuja kwenye maisha yangu umekutana na moyo uliokuwa na maumivu na sijui
chakufanya. Ila kuoa ilikuwa ni lazima na mama naye akawa ananilazimisha.
Siku tunafunga ndoa ndio ilikuwa mbaya zaidi maana kwa mara ya kwanza ndio
Irena alinijibu baada ya muda mrefu. Akaniambia ni kweli aliolewa na alishapata
mtoto wa pili na hana mpango wa kuja kurudi tena Uingereza. Kwa kifupi ndio
alikuwa akiniaga ramsi. Nilikuwa na hali mbaya, na ndio nilikuwa
nikijitayarisha kuja kanisani.”
“Kumbuka
matarajio niliyokuwa nayo ni angalau angemaliza muda wa kutumikia
serikali yake na kuamua tukaishi Uingereza. Nilifika mahali nilikuwa tayari nirudi
nikaishi naye nchini Uingereza. Kufupisha habari, ile harusi ilikuwa natamani ufupishwe,
nitoke mbele ya uso wa watu, nikajifungie mahali. Ila nikawa sina jinsi, wewe upo.
Ndio nikawa nazika hisia zangu kwenye vitabu. Lakini wewe hukuwa
tatizo.”
“Ila
ninachoshukuru, ulinijulia aisee! Ule ukimya na kuniacha, ndio kitu pekee
nilikuwa nikihitaji. Ukawa umenisoma kwa haraka. Ukanijulia.” “Kwa hiyo ndio
msichana unayempenda mpaka leo?” Akauliza kwa wivu.
“Sasa acha
nikwambie ukweli. Akili ilikuja kukubaliana na matokeo tukiwa tumeshapotezana.
Kumbuka baada ya pale ni kama sikuwa nikikaa sana nyumbani. Safari za nje ya
nchi zikawa nyingi. Nakuja kutulia na kujirudi kwako, nikawa nimeshachelewa.”
“Nikakukuta na
wewe ni kama unamaisha yako, na watu wako na utaratibu uliojiwekea. Haupo tena
nyumbani na tukawa tushajiwekea msingi fulani hivi tunao usimamia ikawa ngumu sasa kuanza upya wakati tushakomaa
kwenye maisha fulani. Ndio ikawa tunaishi bora siku zinaenda. Halafu
tukawa hata hatujaweka msingi mzuri wa ndoa. Mahusiano yetu yakawa kama
tuliokubaliana kuishi kwa mtindo fulani hivi! Basi.”
“Swala la mimi kutamani
nje likawa gumu kwa sababu ulikuwa mke sahihi tokea mwanzo. Yaani una VIGEZO vyote,
ndio maana hata mama aliposema nikuoe wewe, nikajiambia kama si Irena, basi
yeyote. Ila sasa ukawa WEWE. Unanijulia kila mahali. Halafu umesoma.
Unauelewa wa mambo. Msafi. Unanijulia chakula. Nyumba
ukawa umeimudu mpaka wafanyakazi wa nje unawajulia. Hilo nikajiambia
swala la mwanamke, nimemaliza.”
“Hata swala la
mtoto wa kiume lilipoanza, nakwambia ukweli kabisa Raza, swala la kuzaa nje
hata halikuwepo. Kwanza nikajihisi usumbufu. Nikajiambia akija
ongezeka mwanamke mwingine hapa katikati yetu, atatuvurugia utaratibu
wetu. Wewe unanijua jinsi nisivyopenda mabadiliko.” Raza
akacheka. Maana alimjua Pius. Hata kochi ndani ya nyumba yake mwenyewe anataka
akalie hilohilo kila siku.
“Natakaga mambo
yangu yasibadilike. Sasa nikasema naweza pata mwanamke akatupa mtoto wa
kiume, lakini akaja na usumbufu na vurugu zake kwenye maisha yetu.
Nikajiambia bora Raza amenipa watoto wawili, inatosha. Hakika sikuwa
nakulaumu wewe hata kidogo. Na swala la kujaribu nje hata kabla wengine
hawajanishauri, mimi nilishapingana nalo. Najijua mimi, siwezi kuanzana
na mwanamke yeyote yule. Kwanza SITAKI.”
“Unaweza
usiamini hili Raza, lakini wewe unanijulia aisee. Naweza nikawa nje ya
nchi, kwenye mahoteli yao hayo wanayo yasifia, hata wanipe nini, nakumbuka
nyumbani. Nahesabu siku nirudi nyumbani nikijua nitakukuta na kila kitu
changu kitakuwa sawa. Kuanzia chakula changu mpaka mavazi yangu. Naweza nikawa
nimefikia kwenye five star hotel, wananifulia nguo zangu, siridhiki
najiambia ningekuwa nyumbani, Raza angehakikisha sitoki hivi.” Raza hakuwa
akiamini kwa furaha.
“Na ndio maana
tokea zamani walipokuwa wakisema unaniloga, sikujali. Kumbuka
nilishajiambia kama si Irena, ni yeyote. Sasa yeyote ukawa ndio wewe, na
wewe unaniwezea. Kwangu ukaonekana hujali vile nilivyo, na maisha
tunayoishi. Ukawa ni kama ulikuwa umejitosheleza.”
“Sikuwa na jinsi
Pius. Kumbuka nilishaondoka nyumbani, nikalaaniwa kwa laana
zote kwa ajili yako. Sina wazazi, sina ndugu kwa
kukimbilia ndoa ya kanisani. Leo narudi wapi! Nasema nini! Ilibidi
nipambane kwa kadiri ya uwezo wangu kuonyesha kila mtu nilichokimbilia sikukosea.
Lakini haikuwa rahisi Pius! Hata kidogo!”
“Lakini kwangu
ulionyesha hujali, bora yako yanakuendea sawa! Na acha nikwambie ukweli
Raza, ulianza kwangu kimaslahi sana. Tuwe wakweli. Mimi nikajua njia
pekee ya kukufurahisha ni pesa ambazo unaomba kila wakati. Ndio maana kama
utagundua linapofika swala la pesa huwa sikuzungushi hata mara moja. Kwa
mara ya kwanza nimekukatalia hivi majuzi. Si kweli?” “Sasa haimaanishi
eti kwamba ndio kitu pekee kilichonifanya niolewe na wewe!” “Raza!” Pius akawa
kama anayemsuta.
“Basi niseme ni
moja ya sababu zilizonivutia.” Akajisalimisha. “Kwa kuwa sina nia ya kurudisha
mambo ya nyuma wala kukuumiza, nipo hapa kujenga na sitaki kukuingiza
dhambini, acha nisikuulize hili swali.” “Swali gani?” “Acha tu Raza. Mimi
nimekubali kwa upande wangu. Nimekubali yote.” “Wewe niulize tu.” “Raza,
binafsi nimekubali yaishe. Tafadhali yaishe.” “Nataka kujua hilo swali.”
Pius akamtizama mwishoe akaamua kumwambia kwa staha tu maana Raza mwenyewe
alionekana kutaka kujua.
“Umesema pesa
peke yake si kilichokuvutia kwangu. Mimi ambaye hata sikukuonyesha
upendo! Usinijibu, lakini kuwa mkweli nafsini kwako na ujijibu,
ni kipi kingine kilikuvuta kwangu mbali na pesa ulizogundua nilikuwa
nazo tokea mwanzo?” Akamuona ametulia.
“Basi mimi
nakuwa mkweli. Mimi nilikusoma, nikajua shida ni pesa, na mimi nikavutiwa
na unayonifanyia, nikasema kwa upande wa mke utanifaa maana hukuonyesha
kuhangaika na mambo ya moyoni. Nikajificha kwenye aina hiyo ya
ndoa, sikujali. Nimekuwa mkweli. Ila wewe usinijibu.” Raza akapoa
kabisa.
Akaamua kwenda
kuoga. “Usinikasirikie, mimi nimekuwa mkweli.” “Mimi sijakasirika, naenda
kuoga.” “Sasa aina hii ya chumba na yote humu ndani ni madhari ya fungate. Hata
huko bafuni wametayarisha kwa muundo wa wawili wapendanao. Si tumekubaliana
kuanza upya?” Ikabidi ajirudi kwa kuanza kutulia maana ni kweli moyoni
alishaanza kusumbuka.
“Tuanze tu.
Najua ni maisha mageni. Lakini naamini hatutakosea. Kwanza umri umekwenda.
Tumebaki sisi wenyewe. Acha tuanze fungate nyingine.” “Sasa unataka tufanyaje?”
“Tuanzie kwenye hilo jaccuz humo ndani. Wewe ushawahi fanya mapenzi kenye jaccuz?”
Raza alicheka sana.
“Kwa uchekaji
huo, ni hujawahi. Sasa twende nikakuonyeshe penzi la majini.” Raza
hakuwa akiamini. “Kumbe mambo unayajua!?” “Nishakwambia nilikuwa nimeumizwa.
Na wewe ndiye uliyekuwa karibu ukamaliziwa hasira. Nikaja kujirudi wewe haupo.
Sasa tulia upend we. Na uache kujivua.” “Navuliwa?” Raza anauliza hana
mbavu kwa cheko.
“Mpaka sidiria.
Na hivyo unavyonijulia mpaka kitandani! Acha ulipwe fadhila. Kaa mkao wa
kupokea tu.” “Sawa Pius.” Kwa hakika walikuwa na wakati mzuri sana. Waliendelea
na huo mwanzo mpya wakiwa wanajuana vilivyo na msingi wa kimungu katikati yao.
Kila Undani
Una Mlango Wa Kushangaza Usiotarajiwa
Yapo mambo yapo
sirini kwa sababu. Mengine ni bora kuacha kuyachambua chambua. Unaweza dharau
ukidhani ni jivu tupu kumbe limefunika makaa yenye moto.
Walirudi
nchini wawili hao ungejua wapo ukurasa mmoja. Hata Poliny aliona tofauti kwa
baba yake jinsi anavyomchukulia mama yao, na yeye heshima ikaongezeka
kwa mama yake.
Ila bado Chezo
alikuwa akimsumbua Pius akili. Kwa hakika alitaka kumuona mwizi wa mkewe.
Akajikuta anampenda Raza, hataki kuja kumchangia tena na mtu. ‘Huyu
Chezo aliyefanikiwa kumtuliza Raza kwa muda wote huo, yukoje na ana nini cha
ziada!’ Maana mkewe mzuri haswa!
Halafu ni mtoto wa mjini! Kweli aje ashie na dereva asiye na hela wakati
alimjua Raza nimpenda pesa kama benki! Yakawa ni maswali yanayomnyima raha
Pius, hawezi tulia nafsi mwake. Kwa Raza alijidai yameisha. Sasa anarudije tena
kumuulizia Chezo na wakati wameshakubaliana wanaanza upya!
~~~~~~~~~~~~~~
Akaona aanzie
kwa bosi wake Chezo. Mzee R uhinda. “Vipi Chezo?” Akauliza swali kimtego baada ya salamu. “Tena naona safari hii
mmewahi vizuri sana! Nimesikia safari hii mkewe ameleta samaki wa ziwani mpema kweli! Hivi nilikuwa
nimtume Chezo awasiliane na Raza, kama atahitaji ili awapelekee nyumbani.” Moyo ukapasuka paa! ‘Mzee anataka kumtuma fisi buchani tena!’
Ila akajikaza na kufikiria kwa haraka.
“Pale nyumbani kwa sasa hatuna
msichana wa kazi. Mida ya jioni Polla anakuwepo nyumbani peke yake, haturuhusu
mtu afike pale mpaka sisi wenyewe tuwepo. Sasa kwa kuwa leo nitawahi kutoka,
mwambie aniletee hapa ofisini kwenye mida ya saa sita, ila awafunge vizuri.” “Nitatoa
hayo maagizo hayo.” Angalau hilo likakaa sawa.
“Pius!” “Bado nipo baba.” “Mbona siku hizi nyumbani
umepotea na jumapili kama mbili tatu sijakuona kanisani.” “Raza amepata
kanisa fulani hivi, naona huko wamempokea vizuri. Polla amepapenda na
ashatengeneza marafiki hapo. Ndio na mimi pamoja na Polliny tukaona tuwe tunaongozana
nao huko!” Mzee Ruhinda kwa hakika si jibu
alilolitegemea hata kidogo! Pius! Mromani damu! Halafu kukawa na jumbe
kwenye hilo jibu lake, akajua amekusudiwa kufikishiwa. ‘Raza
kupokelewa vizuri, na Polla kutengeneza marafiki!’
“Halafu weekend hii mimi na
watoto tulimpeleka Mauritius kwenda kupumzika. Amepitia kipindi kigumu sana, nikaona
akapumzike huko. Ndio tumerudi. Msalimie mama, nikipata nafsi nitapita.” “Uwe
na siku njema.” “Asante baba, na wewe.” Wakaagana lakini
wakaachana kila mmoja na lake.
Kwa Pius
akiwaza. “Kumbe ndivyo jinsi walivyokutana hawa!” Akabaki akiwaza
akimsubiria mwizi wake.
“Mama Pius
atachanganyikiwa akisikia haya!” Mzee Ruhinda
akawa kwenye butwaa. “Pius amehama dhehebu kumfuata Raza!” Akasahau yeye
Raza alihama DINI kumfuata kijana wake. Sasa safari hii kijana wake anahama
DHEHEBU kumfuata Raza! Mzee Ruhinda
hajui mlango wa kanisa lolote isipokuwa la RC.
Polliny ni kopi
ya babu yake na baba yake. Mitazamo yao wote inaendana. Huyo Polliny ni
kipenzi cha mzee Ruhinda. Ukiwakuta wakizungumza utafikiri mzee Ruhinda
anazungumza na mwanauchumi au mwanasiasa wa ulimwengu anayejua sheria. Lugha imenyooka.
Akili safi kama baba yake. Mzee alimpenda sana kati ya wajukuu zake wote. Sasa leo
na yeye haonekaniki kanisani wala nyumbani! Pius kipenzi cha mama ameacha
kupita nyumbani! Mzee akajua shilingi ishapinduka.
Mwana
Kulitafuta…
Kwenye mida ya
saa sita kasoro hivi sekretari wa Pius akamtaarifu anamgeni getini anamzigo
wake, kama aache getini! Pius alikuwa na shauku ya kumuona mwizi wake,
akataka kumchunguza bata! Akasema akaribishwe mpaka ofisini kwake.
Akajiweka sawa
akimsubiria. Baada ya muda sekretari akafungua mlango na kumtaarifu kuwa mgeni
amefika. Akamwambia amkaribishe ndani. Chezo aliyeingia hapo, alimuacha Pius na
mshangao.
Kwanza alikuwa
msafi, amevaa shati jeupe linawaka kama na yeye anapeleka nguo zake dry cleaner.
Halafu mrefu aliyejazia kama mwana ndondi anayefanya juhudi za makusudi kujazia
misuli! Nywele na ndevu vimechongwa
kama mwanamtindo ambaye kazi yake ni kuonyesha uzuri wakiume. Rangi ya maji
ya kunde kwenda mweupe. Mzuri wa sura, wakuvutia. Chezo alikuwa si mchezo!
Aliendana na
Raza haswa. Yaani ukiwasimamisha wao wawili ungesema ni zile couple
zakufunga karne. Muonekano ‘A' mpaka akamvuruga kabisa Pius.
Maana yeye alijua ni Chezo dereva, choka mbaya. Anakuja kukutana na
Chezo aliyemfanya mpaka ajiulize ni kipi Raza kinambakisha kwake!
“Habari?” Chezo
akasalimia kiuungwana akiwa na mzigo mkononi. Akamuita sekretari wake
akamwambia ampokee mzigo na kuuweka kwenye friji. Hapo hata hakuwa amejibu
salamu ya Chezo wala kumkaribisha kiti, alibaki amesimama vilevile kama
alivyoingia.
Sekretari
alipotoka akamwambia akae na wala si kwa kumkaribisha bali kama amri.
“Kaa.” Chezo akaangalia jinsi kulivyopangiliwa pale. Pasafi, kila kiti kimekaa
kwa mpangilio. Halafu na kuna makochi pembeni yamekaa kama sebule ya mtu!
Yamezunguka meza nzuri sana katikati.
Akaangaza macho
akaangalia kile chumba jinsi kilivyo kikubwa! Akababaika kidogo ila akavuta kiti
ambacho kipo mbele ya Pius kwa pembeni kidogo. Akakaa na kubaki akimtizama Pius
kwa utulivu wala hakuonyesha hofu kitu kilichomkera Pius na kumpandisha
hasira.
“Kwahiyo mkeo
akikutuma uuze samaki ndio unaiba na wake za watu?” Chezo akatoa
tabasamu tu, hakumjibu kama aliyemdharau. “Nakuuliza wewe? Unatumia biashara
ya mkeo ya samaki na kuiba au kulaghai wake za watu?” “Sijawahi iba.” Chezo
akamjibu kwa utulivu tu na kusimama.
“Uwe na siku njema.” “Sijakuruhusu uondoke.” “Binafsi naona tumemaliza.”
“Ukiondoka kabla sijakuruhusu, jua umejiingiza matatizoni mwenyewe.” Chezo
akabaki amesimama kama ambaye anajishauri aondoke au la.
Pius naye
akabaki akimtizama kwa jeuri, ila wivu tu. “Kama hakuna jingine
tafadhali naomba mimi niondoke niendelee na majukumu yangu mengine.” “Ambayo yanahusiana
na kuvunja ndoa za watu?” “Huwezi vunja kitu ambacho hakikuwahi
kujengwa.” Pius hakutegemea. Kabla taarifa hazijafika kichwani, Chezo
akaongeza.
“Hukuwahi
mpenda Raza, Pius. Nashangaa ni kwa nini sasahivi ndio unaanzisha fujo zisizo
na sababu!” Hapo akamtibua Pius. “Unasemaje wewe?” “Mimi sitaki matatizo na
wewe. Tafadhali naomba niondoke.” “Kitendo cha kuwa na mahusiano na mke wangu,
ni kwamba tayari ulitafuta matatizo.” “Hayo umegundua lini Pius? Huyu Raza si
alikuwepo miaka yote ukimdharau na kumpuuza tu!”
“Hivi unajua
alipokuwa akiugua ni nani alikuwa akimuuguza? Unajua alipokuwa na matatizo nani
alikuwa naye? Maana kwa hakika si wewe, japo ulikuwepo kwenye nyumba
hiyohiyo ambayo Raza alikuwa akiteseka na maumivu makali sana ya tumbo kabla
hajatolewa zile vimbe zilizokuwa sikimuandama kipindi cha hedhi zake! Leo
unashindwa kujiangalia mwenyewe kwenye kioo na kujilaumu, unatafuta
wakumtupia lawama!” Ya Andy yakamrudia yeye kama ilivyo! Asiamini.
“Na
unachokifanya kwake sasahivi ni ubinafsi tu. Kumtenga na watu wanao
simama naye kwenye upweke wake. Sasahivi unakumbuka shuka, na kumpa
masharti Raza aliyekuwepo kwenye maisha yako karibia miaka 20! Ulikuwa wapi
kipindi akidhalilika kwa kashfa yako ya kuzaa na mke wa mdogo wako?
Sio wewe ulikuwa umejaa mitandaoni ukimpigania mke wa mdogo wako?
Hukuwa umemkumbuka Raza? Hukujua kama na yeye ni binadamu na anayo nafsi
kama binadamu wengine?” Kama alivyomjia juu Andy, ikawa kama
Mungu amembananisha.
Pius alikuwa
kwenye hali ngumu, gafla akakaukwa midomo. “Hivi unajua adha uliyompitisha
lakini au ndio unatokea tu sasahivi na kuamua asitishe mawasiliano na kila mtu,
ili umfungie ndani aendelee kukutumikia kama mtumwa wako, halafu wewe
ukiendelea na maisha yako?” “Chezo…” Hakutaka kumsikiliza, akaendelea.
“Sasa kwa kuwa
mimi simtumii Raza, na ninajali anachojisikia, nitaheshimu matakwa yake.
Nitamuacha kabisa ili nisiendelee kumuumiza. Ila kuwa makini Pius. Takataka
kwako, alumasi kwa wengine. Acheni kuchezea hisia za watu, mkiwafanya
mateka sababu ya nafasi Mungu alizowapa. Uwe na siku njema.” Chezo akatoka
kisha akarudi tena, kama aliyefunga mlango na kuufungua.
“Nina pesa ya
Raza. Niliitumia kununulia baadhi ya vitu. Aliponipa maagizo yako,
yakutowasiliana tena, nimerudisha kwa mwenye duka ambaye ni rafiki yangu. Kwa
hiyo pesa yake ipo kama alivyonikabidhi mara ya mwisho. Naona kwa kuwa sasahivi
wewe ndiye unayetoa muongozo wa nini kifanyike, ndio nauliza, pesa ya
Raza itamfikia vipi?” “Lengo lako ni kumfikia tu mke wangu. Hatuna shida.” “Wewe
ndio huna shida. Hili ni jasho lake. Anajinyima sana Raza kutafuta pesa. Kwa
uzima na ugonjwa, huwa hakosi kazini. Wakati mwingine nilikuwa nikimpelekea
dawa ofisini kwake ili kumsaidia kumaliza siku ya kazi, lakini si kulala
nyumbani. Ni jasho lake, ni lazima limfikie. Acha kupuuza juhudi
za Raza.” “Mpe mzee Ruhinda, atamfikishia.” Chezo akacheka kwa masikitiko na
kutingisha kichwa.
“Wewe si
unathamini sana jasho la mke wangu? Sasa mpe baba yake mkwe amfikishie. Na ole
wako hata ukosee nije nikute simu yako au ujumbe kwenye simu ya Raza, ndipo
utagundua aliyemfikisha Raza kanisani na kula naye kiapo ni mimi
au wewe unayelilia mke wangu. Nitakuita mbele za mabosi zako, na
kuhakikisha mkeo YUPO kwenye hicho kikao akusikie unavyomlilia
mke wangu. Na nitahakikisha baada ya hapo, kila mwajiri hapa nchini anapata taarifa
zako za kutokuwa mwaminifu.” Chezo alimtizama kwa sekunde kadhaa, bila
hata ya kulipwa pesa yake au kuongeza neno jingine, akatoka.
Katikati ya
Kungoja na Kutu.
Mill akashangaa
Pam ametoka kitandani asubuhi na mapema. Akataka kuuliza ila akapitiwa na
usingizi. Kuja kuamka akamkuta jikoni anakula ugali na kiporo cha nyama za jana
yake, mboga za majani. Asubuhi! Akawa hajaelewa. “Leo tunaanzia ugali?!” “Wewe
na mwanao mtakunywa chai. Ila acha nishibe kwanza. Nimeamka na njaa!” Akamuona
anakazana kula, akahisi pengine ni mchezo mrefu wa usiku uliopita wakigeuzana
kana kwamba hawajashikana miaka.
Akaangalia muda.
“Huyu si atachelewa shule? Nisaidie nini?” “Kutengeneza kifungua kinywa chenu.”
Akajibu na kuweka tonge zito tu na alionekana kweli ananjaa. Ikabidi sasa yeye
asaidie mambo hapo, ndipo Shema akafanikiwa kutoka kwa wakati.
Mchana muda wa
kula wakatoka. Akamuona anaagiza ugali wa muhogo, kuku wa makange na mtindi.
Bwana Pam alikula! Akaomba afungiwe tena ugali mwingine na mboga kama vile.
Mill kimya akishangaa nafsini mwake.
~~~~~~~~~~~~~~
Hayo maisha
yakaendelea. Njaa ya Pam inatibiwa kwa ugali. Kila anachopika kikawa ugali
mpaka Shema akaanza kulalamika kwamba amechoka ugali. Ndio Mill naye akaponea
hapohapo lakini hakubadilika. Ugali kwenda mbele na halalamiki kama wao wanajinunulia
kitu chao, basi ujue ndio amepata kifungua kinywa cha asubuhi. Chai, ugali na
mboga walizokataa kula wao usiku, basi Pam atakula kwa furaha zote ndipo waende
kazini.
~~~~~~~~~~~~~~
Mama yake
alishaanza kazi hapo kwenye kitendo cha vipimo. Pam akipita mara kwa mara
kuhakikisha yupo sawa na hakosei kazi ya watu. Siku hiyo akatoka benki akaenda kwa mama yake
na ugali alionunua, nyama choma na mtindi. Akaanza kula kama ametoka shamba na
hajala siku nzima. Mama yake akamwangalia, akajua tayari.
“Njaa hiyo ni ya
tokea lini?” Pam akacheka akiendelea kula kwa shangwe. Akala hapo huku
akizungumza na mama yake. Simu ya Mill ikaingia. “Twende tukale.” “Hapa
nakula. Ila nahisi wamenipunja. Kaugali kadogo!” “Kwamba ulishanunua ugali mapema
hii!?” “Mbona kama swala la upunjwaji wangu huzungumzii?!” “Haya
twende ukale ugali wa mtama, huwa unasema angalau huo unashika tumbo.” Akanyanyuka hapo haraka kama ambaye hakuwa akila.
~~~~~~~~~~~~~~
Aliporudi mama
yake akamuita. “Mara ya mwisho kupata siku zako ilikuwa lini?” Pam akashituka
na kubaki akipiga mahesabu, hayaji. Akatoka hapo bila ya kuaga wala
kutoa jibu mpaka ofisini kwa Mill. Akamuuliza sekretari kama anamgeni,
akaambiwa hana. Akaingia.
~~~~~~~~~~~~~~
Aliingia bila
hodi mpaka Mill akashituka. “Twende.” “Wapi!?” Mill akauliza kwa kushangaa.
“Mahakamani, tukafunge ndoa.” Kwa sekunde kadhaa Mill akawa kama hajaelewa. Pam
akabaki amesimama, anamsubiria aamke kitini. Mill akaona aulize tu.
“Kwamba
tunakwenda kufunga ndoa sasahivi?!” “Halafu ile mipango yako
ambayo haikamiliki, itafuata baada ya sisi kufunga ndoa kisheria. LEO.
Nikimaanisha hivi, hapa ninapozungumza, sasahivi, tunakwenda kufunga ndoa. Halafu
mipango yako na watu wako itakapokamilika, tutaendelea. Lakini tusiendelee
kuishi hivi bila ndoa.” Pam akaweka kituo, akimtizama machoni.
“Hatuwezi
kufanya mambo kwa kukurupuka Pam! Na hatuwezi kwenda sisi wenyewe
bila watu wetu wa karibu!” “Mimi nakutaka wewe uwepo. Basi. Wengine wote
wanaweza kusubiria mipango yako. Huu ni wangu.” “Bado naona
tufanye kwa utaratibu mzuri.” “Sawa.” Akajibu hivyo na kutoka.
Akamuacha Mill
kama hajaelewa vizuri. ‘Sawa’ hii mbona imekubalika kirahisi
hivi! Pam alivyombishi! Kengele ikagonga kichwani akajua hii sawa si
sawasawa. Akasimama kwa haraka na kumfuata.
Alimkuta
amesharudi mezani kwake amekaa. “Pam!” Akamgeukia. “Ila si umenielewa
nilichomaanisha?” Akauliza kwa kujihami sana mbele ya wafanyakazi wengine. Hapo
Mill mpole, mnyenyekevu, akimjua Pam, dakika 5 mbele.
“Ndiyo.” Pam
akamjibu tena kwa ufupi ila kwa ufasaha haswa. Mill akasimama kwa
sekunde kadhaa kama ambaye hajaridhika. Akabaki akimtizama, naye
Pam akimtizama kama anayesubiria la nyongeza. Mill akameza mate kwa wasiwasi
huku wakiangaliana kwa sekunde kadhaa, Pam alipoona hana la nyongeza, akarudisha
macho kwenye kompyuta yake na kuendelea na kazi. Mill akasimama hapo kwa
sekunde kadhaa mbele huku amepewa mgongo, wafanyakazi wengine wakiendelea na
kazi, kimya, akaona aondoke pengine watazungumza vizuri baadaye.
~~~~~~~~~~~~~~
Mtoto wa
pili anakuja, bado hamna ndoa! Akataka hata ya mahakamani, lakini Mill wa mipango. Sasa, safari hii mipango ya
Mill imekutana na Sawa
Ya Pam.
Ni nini kitaendelea?
Pius amechokonoa mpaka amekutana na Penzi la nje la
mkewe Lililokuwa Limekomaa Mpaka Kuota Mizizi. Kumbe
Kuna historia nzito katikati YAO. Ipo thamani kubwa iliyokwisha
jengwa kwa mkewe. Yapo MAISHA ya undani kabisa yaliyokuwa
yakiendelea, yeye hana habari! Hawa wawili walikuwa katika uzima na furaha, zaidi yake yeye na mkewe! Tena si kwa muda
mfupi! Ni miaka!
Gafla yeye
anaonekana muingiliaji na mvurugaji!
Chezo si Mchezo. Alichokitafuta, hatimaye amekipata. Amemchuguza
bata yeye mwenyewe, ataendelea kumla? Chezo amemfanya
ajione kama kipanzi!
Kama vile
Raza si size yake!
Usipitwe.
0 Comments:
Post a Comment