“Mimi mwenyewe ndio nasikia hapa sasahivi.
Sijajua hata kama amekufungashia wewe chakula. Nilijua ni chake huyu.” “Amesema
ataleta asubuhi ili aje amsalimie na bibi.” Shema akaongeza na kuzidi
kumshangaza Mill. Maana ni kama aliwaomba wamuache Pam kabisa!
“Nisikilize Pam. Huyu mama ananipenda sana
na ananijali. Ila kama unaona hutaki kuingiliwa, naweza wakataza.”
“Hapana. Ila naona ni usumbufu usio na maana!” “Kwa jinsi ninavyomjua huyu mama
kwake si usumbufu kabisa. Aisee wamejawa upendo hawa watu, kupita
nitakavyokwambia. Ila siamini.” “Nini?” Pam akauliza.
“Nimetoka kuwaonya kabisa wakuache,
na Shema huyu ni shahidi.” “Ila bibi alikutuma, dad. Amesema umwambie mama
anamuhesabu kama binti yake. Umesahau?” “Sijasahahu ila nilitaka atulie kwanza.
Tusimpe mambo mengi kwa wakati mmoja.” Pam akabaki akifikiria kwa muda kisha
akamwambia Mill.
“Naomba mpigie simu nimshukuru.” Mill hakuamini.
“Au unasemaje? Naona anajitoa kupita kiasi!” Hakutaka kuweka neno ila akampigia
simu mama Colins. “Pam anataka kuzungumza na wewe.”
Kisha akamkabidhi simu.
Upendo husitiri wingi wa dhambi. “Mama shikamoo.” “Hujambo Pam mwanangu?” “Sijambo. Nataka
kushukuru kwa chakula. Asante.” “Karibu.
Nimekupakulia cha kwako tu maana mjukuu ameniambia yeye ameshiba sanaaa!” “Huyu
hana utani na chakula. Akikwambia ameshiba, jua ameshiba kweli. Asante.
Ila naomba usihangaike kesho. Pumzika bwana! Mama mwenyewe Mungu akipenda
ataingia hapa usiku usiku. Itabidi akute chakula, kwa hiyo atalala, kuja kuamka
ni mchana. Usisumbuke.”
“Basi wewe pika cha usiku huu, cha
mchana niachie mimi. Nitakileta na kuja kumsalimia na zawadi zake.” Pam akacheka asiamini. “Kweli?!” “Kabisa. Nimefurahi kweli, nataka na sisi tuwe
miongoni mwa watu wa kwanza kumkaribisha mjini. Nimuonyeshe saluni zinazotutoa
uzee.” Pam akaanza kucheka. “Hutaki uzee
mama yangu?” “Hakuna mzee mjini. Nikishampeleka saluni, nikamuonyesha maduka
yetu ya kututoa uzee. Apate vitu viwili vitatu ndio roho yangu itatulia. Sio
aje huku akumbuke nyumbani kwa upweke kama wenyeji hatupo bwana!” Pam
alifurahi sana.
“Yaani wewe ukiwepo kazini, yeye
anakwama kama vile ndugu ni mmoja tu mjini! Shema amenionyesha picha zake,
nishajua wapi pakumzungusha. Miili yetu inaendana kabisa. Wewe niruhusu
kesho na mimi nije. Tufahamiane. Uniachie mimi.” “Nimefurahi mama, nimefurahi
sana. Asante kumfikiria mama yangu. Najua na yeye atafurahi. Asante mama. Basi
karibuni hiyo kesho. Nitakuelekeza wala hutapotea.” Mill aliposikia hivyo,
akahema kwa nguvu.
~~~~~~~~~~~~~~
Katika mavumbi ya maanguko,
chipukizi huota. Kutoka kwenye kilio, sauti ya matumaini huzaliwa.
“Mama naona ujio wake wa mjini unaanza kwa baraka! Anaanza na wenyeji.”
Akaongea akimrudishia Mill simu yake asijue jinsi alivyofurahi huyo Mill. “Nimesikia.
Na utamfurahia huyo mama. Mtulivu sana kama binti yake Connie.” “Nimemsikia
hata zungumza yake. Tulivu.” Akamuona anafikiria.
“Ni nini tena?” “Nina wazo. Tulaleni hap…”
“Hapana Pam bwana! Si tumekubaliana tutarudi akifika? Wewe unataka nilalie
kitanda cha mama mkwe!” Pam alicheka sana. “Kwanza hapa pako tayari.
Twende tukapumzike. Wakiwa wanakaribia watatupigia simu, tutarudi na chakula.
Mkishasalimiana ndio tunaondoka.” “Au mimi nibaki nitakuja baadaye au mtakuja
huku na Shema mchana?” Mill akabaki akimtizama.
“Basi twende. Naona unataka kuanza kukasirika.”
“Naona unanigeuka gafla wakati tuliweka mipango vizuri tu.” “Basi twende.” Wakatoka
hapo kurudi kwao wakiacha hapo mazingira mazuri. Ila Mill hakutaka kabisa
kumzungumzia Kamila. Akaona aache yatakuja jitengeneza yenyewe.
Hatimaye Mwangaza
Mwishoni Mwa Giza Nene.
Njia ya mama Eric imekuwa ndefu, moyo ulishachoka,
lakini hatimaye mbele kumeanza kutoa mwangaza. Mwangaza wa matumaini, wa neema,
wa kufufuka kwa ndoto zilizozimia. Pam, Mill na Shema walirudi tena
mchana baada ya kumuacha apumzike yeye na msichana aliyekuwa amekuja naye.
Akahakikisha mama yake ameoga vizuri na kuvaa
mavazi mazuri kabla ya mama Colins kufika hapo na chakula. Ungejua Pam anayo
furaha. Mill alikuwa akimwangalia tu anavyohangaika na mama yake. Mwishoe
akaona aende akachungulie ofisini. Akawaacha.
Mida ya saa saba mama Colins na Connie wakawa
wameingia hapo na vyakula kibao! “Nakushukuru mama. Asante sana. Naviweka
mezani tuanzeni kula sasahivi.” Nyumba ikazidi kuchangamka. “Ila umepika
vingi!” “Kamila huyo. Alikuwa akipika tokea asubuhi.” “Na Kamila anapika!
Nilikuwa nikila vyakula alivyokuwa akimpikia Mill, alipokuwa akienda kwake!
Aisee amejaliwa kupika. Nawashukuru sana.” Wakagundua amejitoa kwenye
ukaribisho aliokuwa akifika kwa kina Mike hapo zamani. Kwamba alikuwepo kwa
kina Mike kwa mgongo wa Mill sio yeye aliyekuwa akikarimiwa. Wakalibeba na
kulinyamalizia. Zikaanza stori, mama Colins akizungumza na mama Eric na
vicheko.
“Kesho kanisani. Nimekuletea nguo ya kanisani na
viatu vyake. Mkoba na hereni. Connie nenda kalete. Naamini utapenda tu na nina
uhakika vitakuenea. Shema alinionyesha picha zako, kama nimekosea basi kidogo
sana.” Mama Eric akajisogeza kwenye kochi walilokuwa wamekaa na kumpa mkono
kabisa akishukuru.
Bwana mama Colins alijifungasha! Vingine mpaka
Shema ikabidi atoke. “Hizi nguo za ndani nilijua tu zitakufaa. Ila sidiria ndio
sikujua size yako. Ila magauni ya kulalia haya ndio mazuri na joto la huku
kwetu Dar. Na mafuta mazuri. Haya yatakufanya unukie wakati wote.” Akaendelea
kumpa. Ikawa ni zaidi ya kuomba msamaha kwa Pam. Akabaki akingalia jinsi
walivyowakarimu.
~~~~~~~~~~~~~
Baada ya muda Mill akarudi. Akawakuta bado Connie
na mama yake wapo lakini ndio wanakaribia kuondoka. “Kesho jumapili mje
nyumbani kwa chakula cha jioni.” Pam akamtizama Mill, Mill naye akabaki
akimtizama. “Mje na mama. Apaone nyumbani kwa kina Mill, tujipange mambo ya
harusi. Tujue tunavaa nini. Sisi wamama wa maharusi tunatakiwa tukitoka pale, tumependeza
na tuvae kitu kinachofanana. Au unasemaje?” Yaani mama Colins alikuja hapo
akiwa amejindaa kumfanya Pam ajisikie ni mmoja wa familia.
Mama Eric yeye hana moja, furaha tele. Akakubali
kwa haraka na shukurani kubwa kuona amepokelewa vizuri. “Na mimi
nilitaka nimuombe baba anilete kwa anko, kuna saa amesema alininunulia, ila
aliicha ofisini. Amesema niwe navaa wakati wote, na app yake ataniwekea kwenye
simu. Itakuwa rahisi kujua nilipo kila wakati hata kama nikiacha simu
mahali, atajua nilipo. Na itakuwa ikimwambia afya yangu. Si na wewe
alikwambia?” Akamuuliza baba yake.
“Aliniambia.” Akamjibu na kumtizama Pam. “Wewe
kesho ukiamka ni kujiandaa, uje umchukue mama. Kanisani, mje kule nyumbani.” Pam
akacheka kama anayesita bado akimwangalia Mill. “Eti Pam?” “Nashukuru mama.
Asante kwa upendo wako.” Kisha akarudisha macho kwa Mill.
“Naomba tuzungumze na Pam hapo nje kwanza.” Mill
akatoka, Pam akamfuata. “Nisikilize Pam, uamuzi ni wako. Kama hutaki
kwenda, naweza kuzungumza nao na wakaelewa tu.” “Najiona sipo tayari!” “Jua
haitakaa ukasikia upo tayari, ni mpaka uchukue hatua, Pam. Moyo wako umeumizwa
na Kamila. Lakini Pam, hawa watu wana upendo sana. Nimekutanishwa nao na
Kamila, lakini naona jinsi wanavyonichukulia, utafikiri na mimi ni mtoto wao.
Wamenipokea na kunifungulia mikono yote. Wananifanya ni kama mimi ni kijana wao
mkubwa na Kamila ambaye ni yatima wamefanya kama mtoto wao kabisa.”
“Hawa watu wanajua jinsi tulivyo kuumiza.
Mimi nikiwa kiongozi wa wote. Kisha Mike, Kamila mwenyewe na rafiki zangu wote.
Walinituma kibinafsi nikwambie wao kama wao wanaomba nafasi kwako. Na
nakuhakikishia hutajuta. Wana upendo kama vile wamezidiwa nao, na hawana
pakuupeleka wanatafuta pakuupeleka huo upendo wakati wana watoto wawili wazuri
sana. Colins na Connie. Kisha huyo Kamila waliyemkumbatia, kama binti yao.”
“Colins huwa ananilalamikia kuwa baba yake anamlinda
sana Kamila mpaka kwake yeye ambaye alimpeleka pale. Anasema bila yeye wala
wasinge mfahamu Kamila, lakini mzee amekuwa mkali naye, hataki hata
Colins amsogelee hovyohovyo. Ninachotaka kukwambia ni watu wazuri sana.” “Kamila
ni mnafiki Mill. Na mimi siwezi watu wanafiki. Inaniwia vigumu
sana hata kuwa naye sehemu moja nikamsikia anachozungumza maana najua atanidanganya
tu ili wewe umuone mzuri. Kamila ni mnafiki kwangu Mill. Nyoka anayeweza
kukuua hivihivi na..” “Unaanza kupandisha hasira Pam. Tafadhali tulia.”
“Nimeshazungumza na Kamila, nimemuomba akuache
kabisa.” “Lakini sasa ndio nitakuwa nikimfuata kwao!” “Wewe pima na uamue
ukijua nipo nyuma yako. Lakini jiulize tu, kipi bora kukaa mbali na
Kamila na kukosa watu wazuri kama hawa, ambao pia wamempokea mama yako vizuri,
au kuendelea kufanya kama alichokufanyia Kamila, halafu ukose upendo wa
kina Komba, mama yako akose mtu mzuri kama mama Komba na Shema akose anko kama
Colins.” “Mill!”
“Mimi nakwambia ukweli Pam. Hutakuwa na
tofauti na Kamila. Yeye alikufungia milango ya kwake, na wewe umeshindwa
kumfungulia milango yako. Halafu mbaya zaidi wewe umebeba hatima yetu
sisi wote watatu. Mama yako, Shema na mimi. Na nikwambie ukweli tu, hata Shema anamkwepa
Kamila.” “Haiwezekani Mill! Mbona huwa unakwenda naye?”
“Mwanao anakusikiliza na kukuangalia sana Pam.
Tokea siku ile alivyogundua Kamila alikutenda ubaya, akiwa nao kina
Komba, zaidi Kamila akiwepo, hata nikimwambia anisubirie nakwenda chooni, jua
atanifuata na kunisubiria nje ya mlango.” “Haiwezekani!” “Nakwambia kweli. Anamkwepa
Kamila mpaka Colins amejua ndio maana unamuona anahangaika na kumnunulia zawadi
ili tu kumfanya awe karibu. Akishamsalimia Kamila, akimuongelesha tena,
unamuona anakosa raha kabisa anazidi kunisogelea karibu kama ambaye anamuogopa.
Huwezi muacha na Kamila sehemu moja akatulia. Anajawa wasiwasi, anabadilika
mpaka anakuwa mwekundu.”
“Nafikiri Kamila alivyogundua, akawa anamuacha.
Akimsalimia hatamuuliza kitu tena anaweza ondoka kabisa hapo kama mimi sipo ili
kumfanya atulie. Haya, na ujue hawa watu siwezi wakaribisha nyumbani
kwetu nikijua wewe upo na umeshindwa kuwapokea. Siwezi. Inamaana
itaishia ni mimi kuwa nikienda tu kwao na si vinginevyo. Kwa hiyo jua umebeba hatima
yetu sisi wote watatu.” Pam akabaki akifikiria.
“Lazima wewe uwe zaidi ya Kamila ili kulimaliza
hili. Lakini si kwa kufanya kilekile alichokifanya yeye. Pengine atajifunza
kutoka kwako. Kwamba utamsaidia abadilike.” Akatulia akionekana anauzito
bado. “Chukua hatua ya mwanzoni. Taratibu ruhusu kuipokea kila siku
itakavyokujia. Usifikirie mambo mengi kwa wakati mmoja. Utajichosha na hutakuwa
na majibu yote.” “Sawa. Na samahani Mill. Kamila aliniumiza sana.”
“Natambua na usifikiri sijazungumza naye. Nimezungumza naye tena kwa ukali
kabisa. Hakufanya vizuri.” Wakatulia kidogo, akamuona anarudi ndani, Mill
akamfuata.
“Mama Colins, ulitaka tuje nyumbani saa ngapi?” Alifurahi
Mill, akamtizama mama Colins kwa shukurani maana alifanya jambo kubwa sana
hakutegemea.
“Mkitoka tu kanisani, nyinyi mje. Sisi huwa
tunakwendaga ile ibada ya kwanza kabisa. Kwa hiyo tunawahi kutoka. Tutakuwepo
tu nyumbani.” Huyo mama akatoka hapo akiwa amejenga daraja ambalo
pengine ingechukua muda mrefu sana kujengeka na neno samahani
wala lisingefaa.
Wakati wanaagana, Mill akamkumbatia kwa nguvu
zote mpaka mama Colins akacheka. Kisha akamnong’oneza sikioni kwa sauti ya
chini. “Asante.” Mama Colins alicheka tu bila ya kujibu. Wakaondoka.
Baada Ya
Dhoruba Za Ndoa Zilizosheheni Majonzi Na Majaribu.
Pius alifika
kwake akiwa amechelewa. Maana simu ya Nyange ilimkuta amekaa mgahawani akila
huku akisoma magazeti na kuangalia taarifa ya habari. Ule mgahawa ulikuwa
tulivu, ulimfanya atulie na kupoteza mtiririko wa masaa.
Alifika kwake nyumba
ilikuwa kimya mno, kuashiria kila mtu alishakwenda kulala. Akapandisha ngazi
taratibu akijua wazi Raza hatakuwepo chumbani kwake. Akaingia chumbani kwa
Polla kwa kunyata. Akamkuta amelala na toi lake. Akamuhurumia sana binti
yake. Akakaa pale kwa muda akijua Raza amelala chumbani kwa Poliny.
Akatoka kwenda
kuoga na kwenda chumbani kwa Poliny. Akamkuta Raza amepiga magoti sakafuni
lakini ameegemeza kichwa kitandani, amelala hana habari, na bibilia
imefunguliwa na kuachwa wazi hapo pembeni. Akavuta pumzi kwa nguvu na
kumsogelea pale alipopiga magoti. Akatoa mashuka kitandani, akawa anamnyanyua.
Akashituka sana.
“Nakusaidia
kupanda kitandani.” “Nimepitiwa na usingizi.” “Panda ulale vizuri.” Hata
hakuongeza neno. Akapanda. Akamsaidia kumfunika vizuri. “Asante akashukuru
akijiweka sawa asiamini akihisi ni ndoto. “Pius!” Akabaki akijiuliza.
“Unataka chandarua?” “Hamna mbu. Juzi alipita mtu wa famigation.
Nitakuwa sawa. Nenda na wewe ukapumzike.” Pius akahema kwa nguvu na kuamua
kutoka.
Akamuwahi
alipofika mlangoni. “Pius?” Akageuka. “Nimeacha kuweka vitu vibaya
kwenye chakula. Usiogope kula nyumbani ukajitesa kula nje. Chakula kipo salama.
Unachokula wewe ndicho anachokula Polla, na mimi nakula hichohicho.
Nimebadilika mume wangu.” Pius akabaki amesimama.
“Na kama hujala,
nimekubakishia. Kipo mezani.” “Labda kesho asubuhi kabla sijaenda kazini.
Sasahivi nimeshiba.” “Kwa hiyo asubuhi nikuandalie?” Pius akabaki kimya kwa
sekunde kadhaa kama ambaye anashindana na nafsi lakini akasema, “Nitashukuru.”
“Asante Pius. Asante sana.” Pius akatoka.
Raza alilala na
kilio cha furaha. Akatamani kumwambia mtu, ila akatulia. Akakumbuka kumshukuru
Mungu na kulala.
~~~~~~~~~~~~~~
Asubuhi akawahi
kuamka mapema akiwa amejawa morali kwelikweli. Machozi yaliyomwagika yameotesha
maua ya matumaini, na maumivu ya jana yamekuwa mbolea ya kesho yenye
furaha. Raza mfanyakazi wa kuajiriwa, na yeye anatakiwa kazini kama Pius tu.
Ila alijaliwa mkono mwepesi na mzuri sana jikoni. Alijua mumewe hukipenda
chakula chake. Akamtayarishia kifungua kinywa cha nguvu na kurudi chumbani
kujiandaa.
Akamkumta
anamalizia kuvaa. “Kila kitu kipo mezani, tayari.” “Sasa wewe mwenyewe
umekula?” “Nilikuwa nakula huku nikitayarisha. Sitaki kuchelewa.” “Polla?” “Na
yeye anamalizia. Isa ameshafika kumchukua. Nilimsikia akimuhimiza akazane
watoke.” Pius akaendelea kuvaa.
Raza akawahi
bafuni, akashitukia Pius anafungua mlango. “Mchana una ratiba gani?” “Nakuwepo
tu ofisini. Vipi?” “Nitakupitia twende tukale.” Raza alibaki amepigwa ganzi
katikati ya shower, na sabuni mwilini, maji yakiendelea kutoka
ameshikilia dodoki lenye sabuni. Baada ya kilio cha Raza kisichosikika, na
maumivu ya moyo yaliyotafuna usiku, leo moyo wake unainuka polepole kama jua la
mapema. Pius akatoka bila ya kujibiwa. Akala na kuondoka akiwahi foleni.
Ndoa Na
Iheshimiwe Na Watu Wote
Akiwa ofisini
kwake mida ya mchana akamsikia Pius akitaniana na sekretari wao hapo nje.
Akajua amefika lakini akawa kama bado haamini! Pius! Tena amemfuata
mpaka ndani ofisini na si kumuita atoke! ‘Kama ni usingizi saidia nisiamke
Mungu wangu.’ Kweli baada ya dhiki, imekuja faraja kwa Raza. Na baada ya
giza nene, jua limeanza kuangaza kwa nguvu za aina yake. Akachukua pochi yake
na kutoka.
Bwana Raza
alipendeza mno. “Umependeza.” Akamsifia mkewe wakiwa wanasubiria lifti.
“Asante.” Ndilo aliloweza sema Raza, kwa hofu akijiwinda maneno.
“Unahamu ya kula
nini?” Mumewe akamuuliza. “Chochote.” “Unauhakika?” “Kabisa. Nashukuru kuja
kuni…” Akasita. Pius akamtizama. Akamuona amepoa. “Karibu.” Wakaondoka na gari
ya Pius.
Raza akashangaa wanarudi
kwenye mgahawa uleule aliomtoa mahirizi kwenye pochi. “Hapa siwezi
kuingia Pius. Nasikia aibu! Hakika siwezi.” “Sasa utakimbia mpaka lini? Si bora
unarudi na mimi niliyekuabisha siku ile?” Raza akashangaa kidogo
na kumtizama. Maana alikuwa kama anayejilaumu tena
“Mimi
ndio natakiwa kuona aibu sio wewe. Nilikudhalilisha Raza. Haikuwa
sawa kwako.” Bwana Raza alilia, hakuamini.
“Nilikuwa na
hasira, nikashindwa kukusitiri. Yale yote nilitakwa kuyafanya sehemu ya
ndani. Haikuwa sawa, na mimi nilikosea. Samahani.” Aisee hakuwa
akiamini. Akamuacha akilia na yeye kama ambaye hakutegemea alichofanya, akabaki
ametulia kwa muda mkewe akijaribu kutulia.
“Ila kama bado unaona
haupo tayari, twende sehemu ingine. Hapa nimeshafanya mazoea. Nina sehemu
maalumu nakaa wakati nakula. Na wahudumu wake wameanza kunijulia kama wewe.”
Raza akacheka akijifuta machozi.
“Masharti mpaka mahotelini!” Pius akacheka tu. “Kwa hiyo hapa ndio wapinzani wangu?” “Hawafiki hata robo yako. Na wala si nakupamba! Kifungua kinywa cha leo
ulichonitengenezea ni bora mara elfu kuliko walichokuwa wakinipa hapa
kila siku. Twende ukale chakula chao ndio utaamini.” Raza akaanza kujisikia
vizuri. “Au unataka twende kwingine?” “Naomba tutafute kwingine Pius. Najisikia
aibu sana. Bado sijapata ujasiri.” Pius akaondoa gari hapo bila nyongeza.
Akamfikisha
kwenye mgahawa mzuri sana. “Nashukuru kunielewa.” Akacheka tu na kwenda
kumfungulia mlango. “Asante.” Wakaongozana mpaka ndani, wakatafuta mahali
wakakaa. Kila mtu akaagiza kinywaji na chakula, wakatulia hawajui wazungumze
nini.
“Hivi ujue mimi
sijui kusoma bibilia?” Pius akaanzisha hilo na kumfanya Raza acheke. “Naona
mwenzangu umekazana!” “Mimi mwenyewe ndio najifunza. Mambo mengine magumu
nilikuwa hata sijui! Huwa namsubumbua kweli kaka Nyange.” Pius akacheka.
“Kama nini?”
“Mambo ya Roho mtakatifu.” Raza akaanza kumuelezea mumewe angalau wakapata
mazungumzo ya kuongea. Pius akabaki akimwangalia, akimsikiliza, kweli akagundua
ni Raza wa tofauti. Akamuona taratibu anaanza kutulia, mpaka akatulia kabisa hata
mikono na midomo vikaacha kutetemeka. Akamuhurumia na kuamini maneno ya Nyange
kwamba kweli anamuogopa sana. Na yeye akawa anafanya kusudi kumuuliza
maswali kumuonyesha hajui na anaamini anachokisema. Akaongeza ujasiri kumuelezea
akiwa ametulia. Wakazungumza mpaka muda wao ulipoisha na kumrudisha ofisini
kwake.
~~~~~~~~~~~~~~
Mida ya jioni Raza
huwahi kutoka na kufika nyumbani kabla ya mumewe ambaye mara nyingi hutoka na
kupitia biashara zake. Siku hiyo nayo akajitahidi kuwahi kupika vizuri. Na hivi
ashasifiwa anapika kuliko ile hoteli, basi ndio akazidisha.
Ila akashangaa
siku hiyo Pius hajachelewa kurudi. “Polla yuko wapi? Au nishamchelewa?”
“Nilikuwa namlazimisha atulie hapa, asaidie kupika, ndio akacheze game
zake. Kamaliza kunisaidia mboga, kanikimbia. Atakuwa chumbani kwake anacheza game
zake!” Pius akacheka.
“Acha nikacheze
naye kidogo.” “Ujue atakushinda.” “Kwani mimi huwa nambishia? Poliny ndio
mbishi. Mimi nilishasema sijui. Na nikamwambia asishindane na mimi, yeye
anashinda kwenye game muda wote, siwezi mfikia.” Raza akacheka tu.
“Nitarudi, acha nikakae naye kidogo. Ndio nije tule.” “Yeye ameshakula na kuoga
huyo. Amebakisha kupiga mswaki, nije tuombe naye, awahi kulala. Kesho shule.
Asije akakulaghai ukajisahau na wewe.” Pius akacheka akitoka. Maana walimjua
Polla kwa game kama mtoto wa kiume! Na ukimchekea hapo, halali. Atakesha
akicheza kama siku za ijumaa kuamkia jumamosi.
Akamsalimia baba
yake wakati akiingia macho kwenye game. “Polla bwana! Hata huniangalii!”
“Wataniua dad! Njoo ukae kiti cha pembeni.” Pius akavuta kiti na kukaa pembeni
yake, Polla yupo busy anashindana na mwenzie mtandaoni, tena wa kiume
huko upande wa pili. Pius akawa anamsikiliza. Mikono yote imeshikilia rimoti, busy
akicheza hata hajali uwepo wa baba yake. Pius alipoona hivyo akaona bora
aondoke tu, maana kila akiomba kucheza anaambiwa asubiri kidogo, hapewi.
“Sasa hapo
usijisahau Polla. Mama yako amesema umebakiza mswaki na kusali.” “Sijisahau.”
Anamjibu lakini macho yapo kwenye monitor. Screen ndogo tu
iliyopo hapohapo chumbani kwake kwenye meza ya pembeni ya games zake.
Akatoka na kumuacha. Huna utakachomwambia Polla na games. Na ukitaka
kumfurahisha hata kwenye birthday zake, zawadi ziwe games. Hapo
mtapatana.
~~~~~~~~~~~~~~
Akarudi chumbani
kwake kuoga. Wakati anatoka bafuni akamkuta Raza hapo chumbani akimsubiria.
“Ungependa tuombe pamoja na Polla? Nimemwambia azime michezo yote, apige mswaki
nitarudi niombe naye.” “Basi acha na mimi nije niwaunge mkono. Kwani mliacha
kuomba na hawa vijana hapa?” “Naona tunavutana vutana. Nimebakiwa na Polla tu.
Wao nafanya nao kila ijumaa. Hiyo nimewaambia nilazima.”
“Usichoke bwana
Raza! Ulivyokuwa ukifanya ni vizuri sana.” “Kweli?!” “Kabisa. Jua una kondoo
unaotakiwa utuhimize. Leo umenipata mimi. Kesho waambie wote hata
Poliny, mwambie kuna ibada ya familia nyumbani, aje hata kwa masaa machache.
Usichoke.” Raza alifurahi huyo!
“Au Poliny
umwambie wewe?” “Hapana. Asikie kutoka kwako wewe mwenyewe.” “Mimi atanikatalia
Pius. Unamjua Poliny kwangu. Lazima atanibishia tu na kunipa sababu akisema ana
mitihani.” “Wewe mwambie kwa kumuhimiza. Atakaponipigia simu akilalamika,
nitamwambia ni muhimu. Wewe mchungaji gani wa familia unashindwa na
kondoo wachache hivi?” Raza alicheka sana. “Mchungaji mwenyewe sijui mambo
mengi!” “Bora wewe unayejua machache. Nina uhakika Poliny yupo kama mimi tu.
Wewe tupe kile kidogo unachokuwa unakielewa, tuwe tunakua pamoja.” Alimfanya
Raza ajisikie vizuri sana.
Wakatoka hapo na
kwenda chumbani kwa Polla. Akasoma naye neno lakini akitetemeka mbele ya
Pius. Ila akajikaza. Kufafanua kwenyewe akawa anababaika, ila Pius akawa
akimsikiliza kwa makini kitu kilichomtia moyo. Mwisho akampa nafasi Polla ya
kuomba. Pius akashangaa mwanae anajua kuomba vizuri tu. Akaamini kweli huyo
mtoto ni wa mama. Aliomba kwa uzoefu tena vizuri tu bila hata katekisimu.
Akimuombea baba yake, Poliny, mama yake na ndugu wengine. Akamaliza ndipo
wakamuacha amelala.
~~~~~~~~~~~~~~
Pius akapitiliza
kwenda kula, Raza akarudi jikoni. “Kwani wewe ulishakula?” “Nilikuwa nikila na
Polla hapa, ili atulie. Tulikula chakula nilichokubakizia jana. Hicho
nimekupikia niliporudi.” “Asante.” Akamshukuru, Raza akacheka na kurudi jikoni
maana alitoka alipokuwa akimjibu. Alishamuwashia taarifa ya habari akijua Pius
anapenda sana habari. Akawa akila huku anaangalia BBC, Raza yupo jikoni
akisafisha.
“Mbona shuguli
haziishi huko jikoni Raza na wewe upumzike? Kwa nini usimuachie dada amalizie?!”
“Aliondoka.” Pius akashituka sana, hakuwa hata na taarifa. “Lini tena?!”
“Muda kidogo. Walimpa maneno ya vitisho juu yangu, akakimbia. Polla
alirudi nyumbani hakumkuta. Akanipigia, ikabidi nirudi nyumbani, usiku wake
nikamuuliza yule kijana akasema ameondoka kwa hofu. Kina Mamu na watoto wa
shangazi walikuja hapa na kumpa maneno, akakimbia.” Pius akazidi
kumuhurumia.
“Daaah! Sikuwa nikijua kabisa! Sasa unafanyaje?”
“Hivyohivyo. Nishazungumza na Polla. Akiwa anarudi nyumbani, anakuwa anaendelea
na ratiba yake ileile na kumwambia asubiri asiogope. Na mimi najitahidi
sichelewi kurudi ili asikae peke yake muda mrefu maana sitaki kijana awe naye
ndani peke yao. Nakuwa nikimpigia mara kwa mara kuhakikisha yupo salama mpaka
nikirudi mwenyewe.” Pius akabaki akifikiria na kuzidi kushangazwa.
~~~~~~~~~~~~~~
Kwa hakika yake
hayakubadilika kabisa hapo ndani kiasi cha kuonyesha utofauti. Bado alikuta nguo
zake safi na zimepangwa vilevile kila wakati. Chakula ni yeye tu alikuwa akikataa
kula, ila hakuwahi kukosa chakula sehemu yake ambayo hupenda kukaa. Hakujua hata
kama hakuna msichana wa kazi, kumbe Raza ndiye anayepambana kufanya yote hayo
na yeye akiwa na majukumu ya kiofisi! Akabaki akitafakari.
~~~~~~~~~~~~~~
Alipomaliza ya
jikoni akawahi kuoga chumbani kwao ili ampishe Pius alale. Akaingia kuoga, Pius
naye akarudi kusafisha meno. Wakati anatoka na taulo, akamkuta mumewe kwenye
sinki hapo nje ya bafu hukohuko chumbani akisafisha meno. Bafu la chumbani kwao
lilikuwa kubwa. Lina chumba cha choo, bafu na hilo sinki kubwa lililo na pande
mbili. Wake na wa Raza ambako kuna mafuta yake baadhi na pafyume zake kama
upande wa Pius tu. Mbele yake, yaani ukutani kulikuwa kuna kioo kikubwa.
Akasogea
kusafisha na yeye meno Pius akimtizama kupitia kioo akiwa amesimama upande wake
akiendelea kusugua meno. Kimya kila mtu akifanya lake. Pius akamaliza na
kujikausha, akarudi chumbani. Raza naye akamaliza akajipaka mafuta yake ya
usiku, akavaa nguo zake upande wa nguo, chumba cha pili ilipo closet,
hukohuko chumbani kwao. Akatoka.
“Usiku mwema
Pius.” Akawa akimuaga ili atoke. “Njoo kwanza. Nina zawadi yako.” Raza akacheka
akisogea. “Asante.” “Sasa unashukuru hata hujajua ni nini!” “Kile kitendo tu
cha kunifikiria. Nashukuru.” “Sasa ukiona zawadi yenyewe ndio utapiga goti
kabisa. Kaa.” Raza alicheka sana. “Pius!” “Sasa wewe hujaona zawadi yenyewe unashukuru.
Ukiona je?” “Haya tuone.” “Kaa, halafu nipe mgongo.” Tayari akajua ni nini
amemnunulia. Akafurahi.
~~~~~~~~~~~~~~
Roho
iliyovunjika sasa inapumua tena, ikiamini kuwa kila giza lina mwisho. Hatimaye,
{Mama Eric, Kina Komba, Mill, Pam, Mina, Andy, Pius hata Raza,} wanatembea
kwenye njia mpya wakiwa na tumaini mkononi, na imani moyoni, kuwa hata baada ya
dhoruba, huchanua tena, na maisha huanza upya kwa mwangaza mpya.
Ni nini
kitaendelea mbeleni?
Usipitwe.
0 Comments:
Post a Comment