Pius
alibadilisha hicho chumba kikachukua sura yake wala si ya mke wake. Hofu
aliyokuwa nayo Pius akaipata yeye. Akawa anaogopa kuwa na mumewe chumba
kimoja au hata sehemu moja peke yao.
Poliny alipenda
shule na kuizingatia. Kurudi kwake nyumbani ilikuwa ni kama hana mitihani, tena
kwa muda mfupi. Kwa hiyo Raza alikuwa akibakiwa na Polla, na Polla mwenyewe
akiwa nyumbani yupo kwenye monitor yake akicheza game muda wote
mpaka mama yake amlazimishe kula au kusoma au kulala.
Akajikuta mpweke
lakini akifanya kama alivyoambiwa na Nyange. Kila siku jioni anaita wote mpaka
kijana wake wa nje, wanafanya maombi kwa pamoja.
Vikao vya nje
akaacha kabisa. Ikawa kazini, nyumbani. Wakisha kula, anawaambia wasome bibilia
ambayo alikuja pewa na huyohuyo Nyange. Raza hakuwa hata na bibilia. Na Nyange
ndiye alikuwa akimuongoza jinsi ya kuisoma hiyo bibilia. Akiwa na swali, basi
atamtafuta Nyange, atamuuliza mambo ya kiroho na kumsaidia.
Lakini mambo
yake na Pius hayakurudi kuwa sawa. Tabia ya Pius kula nyumbani aliacha
kabisa. Kila Raza alipokuwa akimkaribisha chakula, alimwambia yeye alishakula.
Aliwahi kutoka asubuhi na kwenda kula hotelini. Mchana hivyohivyo na jioni
alipitia kula mahotelini ndipo anarudi nyumbani. Hata maji ya nyumbani hakuwa
akiweka mdomoni. Akijua mama yake yupo nyumbani, anakwenda kula kwao ndipo
anarudi nyumbani.
Raza hakukata
tamaa. Kila aliporudi alimwambia kuna chakula. Jibu lilibaki lilelile, ‘nilishakula’.
Kama atawakuta wakiomba, atakaa hapo sebuleni akimtizama anavyofanya. Wazi
alimuonyesha hamuamini. Akisema fungeni macho tuombe, basi yeye atabaki
akimtizama mpaka amalize kisha kumuaga binti yake, anakwenda chumbani kwake.
Ilikuwa ikimuuma
Raza, ila hana jinsi. Akiingia chumbani atakuta tv ya chumbani ikiendelea na
taarifa za habari yeye akisoma kitabu. Pius alikuwa msomaji wa vitabu kama baba
yake na ndugu zake wote na ndiko Poliny nako alipochukua kupenda vitabu.
Walipenda sana kusoma.
~~~~~~~~~~~~~~
Akiwa anaingia
chumbani endapo atamkuta mumewe basi kimya kama hakuna aliyeingia hapo. Hatatoa
macho kitabuni wala kutingishika kana kwamba hakuna aliyeingia hapo. Raza
ataishia kuoga, kubadilisha nguo za kulalia na kutoka hapo chumbani kwenda
kulala chumba cha Poliny ambaye hayupo hapo nyumbani bila ya kuulizwa la kheri
wala la shari. Wawili hao wakageuka kama wazazi tu, tena wanao lazimika kuwa
sehemu moja.
~~~~~~~~~~~~~~
Hayo maisha hapo
nyumbani kwao yakaendelea. Hakuna kusemeshana isipokuwa ikilazimu. Tena zaidi
yanayowahusu watoto. Pesa ya chakula akawa anatoa kama kawaida, ya ziada
kwa Raza alishamwambia yeye ni mfanyakazi, analipwa mshahara, atumie pesa yake
kwenye mambo yake.
“Sirudii kukupa
pesa yangu kwa ajili ya kuja kuniangamiza mimi mwenyewe na watoto wangu,
halafu ukiitumia kwa starehe zako na wanaume zako. Nakuwa nikihangaika kwa
ajili ya wanaume zako! Hapana Raza. Tumia pesa zako. Matumizi ya humu
ndani, mishahara ya wafanyakazi na magari yote itabaki juu yangu. Mambo yako
binafsi, jigaramie. Na waambie mabwana zako huko nje, unanipumzisha, ni
zamu yao na wao kukutunza.”
“Mimi nilikuwa
nikikutunza, wao wanakufaidi. Sasa waambie maadamu wananufaika na huo
mwili wako, wanawajibika kuutunza pia.” Raza alishindwa kunyanyua mguu.
Ilikuwa kama amegongelewa misumari. “Si Chezo na yeye anakazi?” Kimya. “Nina
uhakika hatashindwa kulipia chumba chenu mnachokuwa mkikutana kila siku mchana,
na kukupa za matumizi yako binafsi kama anavyofanya kwa mke wake.” Akahitimisha
na kurudisha macho kwenye kitabu. Raza akatoka kurudi kulala chumbani kwa
Poliny maana Polla alishalala.
~~~~~~~~~~~~~~
Maisha hayo
yakaendelea, Raza akipambana na maisha mapya ambayo hajawahi ishi kabla. Mapya
halafu machungu. Maisha ya kukutana kwa Paulina na wakwe, wakipika, kupakua
kisha kula pamoja ni kama yalikoma kwa namna fulani, tena kimyakimya.
Kwa wakwe ni kama walisitisha ule mtindo wa kila siku za jumapili kukutana na
kupika pamoja. Shoga yake Paulina aliyekuwa akimpa maneno, ni kama hakutaka
afike tena nyumbani kwake wala asogelee binti zake. Kwa hakika walimkwepa
kwa wazi kabisa.
Raza alikuwa
akiwa peke yake chumbani basi hulia sana. Alikuwa akimlilia Mungu hajui
tena chakufanya. Alishatubu na kubadili njia zake, lakini ikawa ngumu
kupata tena watu. Alikuwa akipiga magoti mwenyewe chumbani kuomba, hawezi
ila kulia tu. Atalia hapo mpaka wakati mwingine huamka asubuhi akiwa amelala
sakafuni. Kufunga ndio halikuwa tatizo kabisa. Tokea binti mdogo kwao walikuwa
wakifunga. Akawa akifunga akimsihi huyo Mungu amsaidie bila ya kuona mabadiliko
yeyote kwa wanao mzunguka. Akawa akikwepa kama mwenye ukoma. Akabaki peke yake
ila hakuacha kujitahidi. Hayo maisha ya upweke yakukwepa yakaendelea.
Machozi Ya Moyo
Uliojirudi.
Akaona ajirudi
kwa vitendo kwa wakwe zake. Muda wa chakula cha mchana, akajitahidi
kutoka kazini na kumfuata Paulina na mama Ruhinda wanao fanya kazi ofisi moja, akiomba
watoke wakale pamoja, wote walikataa kwa kisingizio cha kazi nyingi siku
hiyo. Raza akaondoka.
Alifanya hivyo
zaidi ya mara tatu na mara zote walitoa udhuru. Siku moja alikwenda kula
mchana, akakutana nao wamekaa sehemu wanakula. Akaumia sana. Ila mama
Ruhinda akamwambia avute kitu, ajiunge nao.
Akakaa nao,
akaagiza na yeye chakula. Kwa hakika kilikuwa kipindi kigumu hapo
mezani, haikuhitaji kuuliza. Watatu hao waliokuwa wakipika na kupakua pamoja,
gafla wakajikuta hawana chakuzungumza na kila mmoja anajiwinda kivyake.
Kilichomuumiza Raza ni pale kila mmoja alipovuta sahani yake karibu wakihamisha
vinywaji mbali na yeye. Akaiangalia ile hali pale, mwishoe akaaga nakuamua
kuondoka hata akiwa hajamaliza chakula chake.
~~~~~~~~~~~~~~
Hakukata tamaa,
akajishusha tena. Maana Polla alishakuwa na hamu na binti wa Paulina. Wamekua
pamoja. Marafiki mbali ya undugu. Akawapigia simu kila mmoja kasoro wa Dodoma,
kuwakaribisha kwake kwa chakula cha mchana siku ya jumapili baada ya kutoka
kanisani. Kila mtu alitoa udhuru mpaka mumewe. Raza aliumia sana. Alikuwa
njiani akitoka kazini.
Alilia. Alilia
sana. Njia nzima alikuwa akilia nakushindwa kutulia. Alilia sana hata hakujua
anarudi vipi nyumbani na kukutana na binti yake akiwa na hali ile. Alikuwa na uchungu,
hana wakumwambia ukweli. Kwa mashoga zake, asingethubutu kuwaambia kisha wajue
ya undani! Itakuwa ni kama kujivunguoa mwenyewe hadharani.
~~~~~~~~~~~~~~
Uzuri siku
anaitwa na mumewe na pochi yake kutoa mahirizi, ilikuwa ni
mgahawa wa kitalii, hakuna aliyempiga picha wala kusambaza mambo yake. Siku
anawekwa jela, alitoka kazini akiaga anakwenda kukutana na mumewe kwa chakula
cha mchana. Akaishia kupelekwa kwa mganga wake na kufungwa. Kabla hapaja
pambazuka, kuzaa kukamuokoa, akatolewa jela.
Siku inayofuata
ilikuwa ijumaa. Akapiga simu kuwataarifu ni mgonjwa hatafika kazini. Jumamosi
na jumapili hakwenda kazini. Mpaka jumatatu anarudi kazini, amepoa, hakuna aliyejua
kilichompata. Asingethubutu kushirikisha mashoga zake na kujidhalilisha.
Akajificha nyuma ya tabasamu lenye machungu makali na aibu.
Kwa mama yake
mzazi ndio alisha muonya tokea zamani. Na huo ndio ulikuwa ugomvi wao wa
kuwaweka mbali zaidi, mbali na dini. Raza akimuona mama yake hamtakii mema,
haoni sababu ya kuhangaika kwake. Mama yake akimwambia yeye amekaa katikati ya
jiji. Amemkuza Raza na ndugu zake bila tunguli ya mnganga, mbona
wamekua na kusoma, na mume hajawahi mpa talaka hata mara moja! Hilo likamuweka
mbali na mama yake. Leo anarudije?!
~~~~~~~~~~~~~~
Raza akaendelea
kulia pake yake hajui chakufanya. Ikawa kama bahati, Nyange akampigia akiwa
kwake na mkewe. “Vipi mbona unalia?” “Sijui
chakufanya tena kaka yangu. Nimejaribu kila njia, nimefika mwisho. Njia
hii ni ngumu. Ngumu sana.” “Tulia
niambie kinachoendelea.” Raza akawasimulia Nyange na mama Briana hapo
anapopita, wakamuhurumia sana.
“Hata Polla binti yangu huyu mdogo
wanamuogopa jamani! Shangazi yake amefanya bithday ya binti yake, isivyo
kawaida watoto wengine darasani kwao wamealikwa ila hajamualika Polla! Kweli
jamani!?” “Wanasoma darasa moja?” Nyange akauliza taratibu tu.
“Umri mmoja. Shule moja. Darasa
moja. Yaani tokea wapo tumboni, kliniki tumekuwa tukiwapeleka pamoja. Hawa watoto
hawajawahi kutengana. Leo wanamuadhibu mwanangu kwa makosa yangu! Kweli! Sasa
Polla anahatia gani? Na amejua kama kulifanyika sherehe. Akanieleza na kuniomba
nimpeleke kumnunulia zawadi. Nikafanya hivyo mpaka nikamsaidia kuifunga. Amempelekea
shule, anasema alipokea lakini baadaye akakuta ameitupa kwenye trash bin
ya hapohapo darasani. Niambie kaka, nini nifanye tena. Mbona kama nishatubu
na ukasema huyu Mungu amenisamehe?” Raza alikuwa
akizidi kulia.
“Nisikilize Raza. Ahadi za Mungu ni
kweli na amina. Akisema amekusamehe, yeye kama Mungu amesamehe. Ila
hutakwepa kuwajibika. Sasahivi upo kwenye kuvuna madhara ya ulichopanda.
Wema wako wowote kwa sasa, utaonekana kama ndoto ya usiku. Nakuhakikishia haitakuwa
rahisi hata kidogo.”
“Hawa watu ulikuwa kwenye majumba
yao ukila na kunywa nao. Tena ukiwapikia. Wamejua vitu vibaya ulivyokuwa
ukiweka kwenye vyakula vya kaka yao. Wakaona madhara kwa macho yao, walishuhudia
kaka yao na mtoto uliyemzaa wewe mwenyewe wakijipigiza kwa kupandwa na madudu
uliyopandikiza wewe. Haya, Polla alikuwa ameshikilia hirizi
aliyokuwa akitembea nayo kwenye begi la shule na aliimiliki akiing’ang’ania
kuwa ndio ulinzi wake.” “Lakini
yeye hana hatia kaka Nyange! Mimi ndio nilimpa.”
“Usinione mbaya ila najiweka
pembeni nakupa mtazamo wa kweli wa watu waliokuwa karibu na wewe. Wao
wanachojua ni huyo mtoto anatembea na nguvu isiyo ya kawaida.
Wanamuogopa. Tafadhali wape muda. Unanielewa Raza?” Akazidi kulia.
“Endelea kujionyesha na
kuthibitisha umesamehewa na umekubalika na Mungu.” “Tena bila kuchoka wala
kuzembea. Usitoe mwanya wa kukata tamaa.” Akaongeza mama
Briana. “Unamsikia mama Briana?” “Nimemsikia
kaka.” “Ewaah! Nilikwambia, juhudi ileile
uliyoweka kwenye ushirikina, weka kwa Mungu ukijua huku kwa Mungu utalipwa.
Ni lini, mimi na wewe hatujui. Ila, utavuna kwa wakati, usipozimia moyo. Na
utukufu wa mwisho ni MKUU kuliko wa kwanza.”
“Ila jua kwa hakika sasahivi unapimwa.
Na Mungu pamoja na wanadamu pia.” “Na hata shetani pia anampima.” Akaongeza mama Briana na kuendelea. “Yeye anakupima ili ajue jinsi
atakavyojirudi kwako. Ukizembea tu, jua ndio unamfungulia mlango.” “Umesikia?” “Nasikia.” Akaitika akisikika ameanza
kutulia.
“Ndio jua upo kwenye kipindi muhimu
sana, tena cha thamani. Ndio umezaliwa upya, unajifunza kwa upya. Kila kitu
kama mtoto mchanga. Kilio hicho ni kwa sababu kuna tabia upya zinajengwa ndani
yako, mwili na akili pia havijazoea, kama mtoto mchanga kabisa aliyeletwa hapa
duniani. Sio rahisi mdogo wangu!”
“Kumtegemea Mungu peke yake! Tena
ambaye hakujibu kama amekusikia au
la! Si rahisi. Kwa mganga ilikuwa
rahisi kwa sababu yupo mtu mliyekuwa mkijibizana. Una mpa haja zako, anakuahidi
atafanya. Unaondoka kwa furaha ukijua haja yako umejibiwa. Ila kwa Mungu ni
tofauti. Ni imani tu. Na ndio maana
imeandikwa, bila imani, hauwezi kumpendeza Mungu. Unatembea kwa kuamini yupo mwenye nguvu
zaidi ya wote, amekusikia na atatenda kwa wakati.”
“Wote hao nao wanapitishwa kwenye
wakati mpya kama wewe tu. Kuna kitu kipya kinajengwa katikati yenu. Mahusiano
mapya yanajengwa. Ila uzuri sasahivi mjenzi wako ni Mungu ambaye unamuomba kwa siri
wao hawajui. Sasa akimalizana nao.
Na wewe ukiwa umesimama hapohapo ukimsubiria Mungu! Nakuhakikishia,
safari hii ukiwapata, yaani Mungu akiwarudisha kwako. Hivyo ulivyo ukiwa na
Yesu ndani yako, jua umewapata moja kwa moja na utaitwa heri. Na utakuja
niambia hiyo thamani Mungu atakayokuwekea.”
“Cha msingi ni usiache kutenda wema. Usiache kuwasamehe
huku ukielewa hofu yao kwako. Na ukumbuke, wao walivyo sasahivi, japokuwa
wanakuona wewe ndio mbaya, hawana neema uliyo nayo wewe sasahivi.”
“Ishi nao ukiwatangazia msamaha bila wao kukuomba msamaha. Ishi
nao ukitambua nguvu ya msamaha
uliyopewa wewe. Watakujaribu sana. Lakini wakikuona umesimama, watajirudi tu.
Na usiharakishe. Polepole.” Nyange alizungumza naye mpaka akatulia kabisa.
“Samahani mama Briana na kaka kwa kuwaharibia
muda wenu. Hakika nashukuru kujitoa kwangu.” “Usijali Raza. Hata sisi tunaishi
kwa neema tu. Si watakatifu. Kuna kukosea na Mungu anatusaidia kila iitwapo leo.
Usichoke.” “Nimeelewa, nashukuru.” "Sasa hapa kwangu sina binti wadogo,
lakini Sonia anaye binti nafikiri umri wa Polla. Jumapili hii tunakutana wote
mpaka mama yake na baba yake. Wote watakuja hapa kwangu. Karibu na wewe ubadili
mazingira. Utoke kidogo nyumbani.” “Nashukuru mama Briana. Nitakuja na Polla,
na Poliny kama atakuwa hana mitihani.” “Mkaribishe na Pius.” “Mmmh!” Wakamsikia akiguna.
“Pius ameniambia weekend hii ana mambo yake yakufanya.
Hana muda.” “Basi nyinyi njooni. Na usiache maombi Raza. Omba tu. Omba hata kwa
Roho. Mruhusu yeye Roho wa Mungu akuombee yale ambayo hata hujui utamwambia
nini Mungu. Au umeshapoteza kunena kwa Roho?” “Tokea kaka aniombee, sijaacha
mama Briana. Ila wakati mwingine nakuwa nauchungu nashindwa
kuomba.” Akaanza kulia tena.
“Basi hivyo ndivyo vipindi vyenyewe
vya kuomba kwa Roho, wala usiache. Mruhusu yeye aombe. Itakusaidia sana na hata
huo uchungu utapungua.” Akazungumza naye kwa upendo kama alivyo mama
Briana, mpaka akatulia kabisa na kuagana.
Kwa Pius.
Kwenye mida ya
saa mbili usiku Nyange akampigia simu Pius. “Unaweza kuzungumza?” “Karibu.”
“Samahani kama nakuingilia Pius. Lakini kwa kuwa uliniruhusu,
nitazungumza tu na wewe, au ile ruhusa iliisha?” “Hapana Nyange. Karibu tu.” Akamtania kidogo. Nyange maneno mengi mpaka Pius akajikuta akicheka.
Ndipo akaanza. “Lipo neno
kwenye kitabu cha Mathayo 12:43-45. Nilishakugusia. Sijui kama unakumbuka au unataka
nisome?” “Tafadhali soma tu.” Pius akamruhusu kwa
heshima. Alishakutana na Nyange, amefanikiwa sana kwenye maswala ya
biashara. Halafu akajitoa sana kwake. Heshima ilikuwepo.
“Mstari wa
43 unaanza kwa kusema, ‘Pepo mchafu amtokapo mtu, hutangatanga katika sehemu zisizo na maji,
akitafuta mahali pa kupumzika, lakini hapati.’ Mstari wa
44 unaendelea kusema. ‘Ndipo husema, Nitarudi kwenye nyumba yangu NILIKOTOKA. Naye anaporudi huikuta ile nyumba ikiwa tupu, imefagiliwa na
kupangwa vizuri.’ Mstari wa 45 unaendelea kusema, ‘Kisha huenda na kuwaleta
pepo wachafu wengine saba, WABAYA kuliko yeye mwenyewe, nao
huingia na kukaa humo.’ Hapa ndipo
pabaya maana unamalizia kwa kusema hivi, ‘Nayo hali ya mwisho ya yule mtu huwa ni MBAYA
kuliko ile ya kwanza.’ Sijui umenisikiliza vizuri?” Nyange akauliza. Pius kimya.
“Nazungumza sana na mkeo, Pius.
Sana. Mida ya chakula cha mchana ambayo anatakiwa kula, lakini utakuta anajisomea
bibilia ambayo kwanza HAIJUI. Ukristo ni dini aliyojipa ukubwani kwa sababu yako, WEWE.
Unanisikia Pius?” Kimya.
“Huyu binti aliacha dini aliyokuzwa
nayo. Ambayo kwake nirahisi. Amefuata dini yako, ambayo anaishikilia kwa
ajili yako, WEWE. Haelewi yale mambo ya kawaida kabisa yaliyomo humo
kwenye bibilia au kwenye ukristo kwa ujumla wake, lakini ameyashikilia kwa
ajili yako, WEWE.”
“Raza hakukuzwa kwenye ushirikina.
Anakiri ni mambo ameanza ukubwani tena mtu alimshauri ili akufunge WEWE. Safari
moja, ikaanzisha nyingine mpaka akakosona na mama yake. Mkeo hana ndugu wa
karibu sababu ya kukana dini ya kwao, na kukufuata wewe, na wewe
hili unalijua.”
“Mkeo amefundishwa ushirikina mpaka
ukamkolea. Ni mapepo ndiyo yaliyokuwa yakimuendesha, na wewe ni shahidi
kwa sababu ulikuwepo wakati nikihangaika kuyatoa. Nimekusomea neno. Yale mapepo
kutoka siku ile, haimaanishi hayatarudi tena. Kila wakati yanarudi kuchungulia
kwa mkeo yakitafuta kurudi. Yakifanikiwa kupata mwanya hata kidogo tu,
umenisikia nikisoma. Yatakwenda kutafuta mengine mabaya zaidi ya yale ya
mwanzo. Nakuhakikishia Pius, si hali yake tu yeye Raza itakuwa mbaya, na nyinyi
wote mnaomzunguka hamtabaki salama.”
“Kama mwanzoni alifanya
aliyoyafanya. Sasa fikiria kila moja likaongeze mengine saba, tena mabaya
zaidi, niambie watakaposimama binti zako na kijana wako!” Kimya.
“Ni pabaya kuliko
utakavyofikiria, kwa sababu mama ana nguvu kwa watoto zake mno. Na hujui mwisho
wa yote yatamfanya nini huyo Raza. Kilio cha binti yako siku ile usiku uliweza
kukinyamazisha kwa kumtoa mkeo jela. Niambie yakija kumuua, utaweza
kuishi na kilio cha Polla kwa muda gani?” Kimya.
“Mbali na majini, mkeo ni mzuri
Pius. Mzuri sana kama msichana ambaye hana mtoto hata mmoja. Na kufunga ndio
kumemrudisha kuwa binti mdogo kabisa. Sasa mimi sijui maisha yaliwapitisha wapi
mpaka mkafungua milango ya uaminifu. Lakini mwanamke kama Raza na
wanaume wa hapa mjini, kushinda vishawishi ni kwa neema ya Mungu
kwelikweli, tena hii aliyopokea mkeo sasahivi.” Kimya.
“Ushauri wangu, mimi kama kaka yenu.
Nikiwa natambua kabisa ulipoumizwa na Raza. Na mimi pamoja na wewe
tunajua na wewe upo na sehemu yako ya makosa, pambana kwa kadiri
ya uwezo wako, MSAIDIE mkeo kusimama. Anajitahidi sana. Lakini na yeye
ni mwanadamu, ATACHOKA. Umenisikia Pius?” Kimya.
“Mimi ni kaka yako, nakwambia
ukweli. Ukishindwa wewe kumtuliza Raza, wapo wanaume hawana muda
mwingine zaidi ya wake za watu. Watamtuliza kwa kuanzia kumfariji, maana
sasahivi ni mpweke. Na kwa jinsi ninavyozungumza naye, ametengwa
na kila mtu. Sasa wakifanikiwa kumsikiliza tu, ATAACHA maombi yake
binafsi. Ibada za nyumbani zitakoma. Utamrudisha baa, kule
alikokuwa na marafiki wanao muelewa. Hali yake haitakaa ikawa hata nusu na ya
kwanza.” Kimya.
“Pius?” “Nakusikiliza kaka.” “Rudi
kwa mkeo. Msaidie ASIMAME. Tafuta jinsi ya kumsamehe, na mwambie umemsamehe.
Anakuogopa sana. Sana. Anaogopa hata jinsi unavyomtizama. Mkeo ana hofu
mpaka ukizungumza naye kwenye simu unamsikia akitetemeka. Muulize mama Briana,
juzi ilibidi kwenda kumfuata kazini na kuomba naye ndipo akatulia. Haamini kama
majini yamemtoka. Haamini kama yupo salama, mpaka nikaomba naye tena na
kumuhakikishia yupo salama.”
“Mtetee kwa aliowaumiza.
Msaidie malezi ya Polla aliyemuathiri mpaka kutengwa na ndugu.” “Polla
ametengwa vipi?” “Wewe unajua kama mtoto wa Paulina alikuwa na birthday,
Seacliff hoteli siku ya jumamosi iliyopita na alialika watoto wengi darasani
kwao kasoro Polla?” Pius kimya akiwa ameanza kuumia. Alipenda watoto
wake sana.
“Inamaana umekimbia nyumba Pius!
Yale niliyokwambia uyafanye hujayafanya!” Nyange
akamlaumu. “Binti yako alipojua amemnyima mualiko, alijitahidi zaidi.
Akamuomba mama yake amsindikize akamnunulie zawadi. Lakini alipo mpelekea
zawadi siku ya jumanne maana siku ya jumatatu ndipo alipokutana na hizo taarifa
kwa marafiki, darasani kuwa walikuwa kwenye party ya mtoto wa dada yako,
yule mtoto alitupa zawadi aliyopewa na Polla.” Pius alihisi
mtu anamchoma mkuki moyoni kwa maumivu.
“Polla aliikuta kwenye trash can.
Akaja kumwambia mama yake. Inamaana wewe hayo yote huna taarifa nayo Pius!
Malezi ya karibu kwa binti yako bado unamuachia Raza peke yake!” “Acha
nikwambie ukweli Nyange. Nimeshindwa kabisa kuwa sehemu moja na Raza. Nimeshindwa
kula nyumbani. Hata maji yamenishinda. Nakula mahotelini au kwa mama. Ndio
maana nachelewa kurudi nyumbani, nakuwahi kutoka asubuhi ili nikale mahali
niwahi ofisini. Na hapo ndipo ninapomkosa Polla.”
“Tunaamka wote tukiwa na harakati
za kuwahi, nikirudi nakuta amelala. Ila nimekusikia kaka. Nitabadilika.”
“Msaidie na Raza. Hatua ndogondogo kwa vitu vidogovidogo mpaka utajikuta moyo
unafunguka kabisa. Unaweza kuzungumza naye na ndipo na wewe upate nafasi ya
kumuomba msamaha kuzaa na mke wa mdogo wako.” Nyange akapiga ikulu kabisa, tena makusudi kumkumbusha na yeye
ni mkosaji pia. Pius akapoa.
“Sijui kama umenielewa?” Pius kimya. “Unayo nafasi kubwa sana ya kutengeneza Pius. Usikubali safari
hii ikawa WEWE ndio unatumiwa kuharibu kwako. Ni hilo tu.” Kabla hajakata akamsikia kama mke wake anamuongelesha.
“Pius?” “Nipo kaka.” “Mama Briana
anawakaribisha wewe na familia yako jumamosi hapa nyumbani. Kina Sonia pia
watakuwepo na familia yake.” “Naomba nisitoe ahadi tafadhali. Ila nawashukuru
sana. Asanteni kuwa na sisi na kutuvumilia. Usiku mwema.” Akaaga na kukata simu.
Safari ya
Machungu na Tumaini
Maisha ni safari
isiyo na ramani kamili. Barabara zake hupinda na kupotea,
mara jua linawaka, mara mawingu yanatanda. Kuna siku za njaa,
na siku za shibe. Siku za vicheko, na siku za machozi.
Lakini ndani ya kila giza, kuna mwanga unaojificha. Ndani ya kila huzuni, kuna matumaini yanayoota kama jani jekundu katika jangwa. Huu ndio uhalisia wa maisha. Si rahisi, lakini si
bure. Kwa SUBIRA na moyo thabiti, hata tufani kali hupita, na alfajiri
mpya huangaza tena.
Siku ya pili yake
jioni baada ya mapumziko waliyoyasubiria wawili hao kwa zaidi ya miaka 10, kwa
machungu kila mmoja wao pande ingine ya dunia Mill alitoka na Shema kwenda kwa
kina Komba, baada ya kumshusha Pam, Kinondoni alipokuwa amepanga.
Aliwaomba wote
wawepo. Walifurahi sana kumuona Shema. Hakuwa kama wale watoto wa kwanza wa
Kisha. Basi yeye akifika hapo salamu ya heshima na cheko akiwaita dokta Komba
na mkewe bibi na babu kabisa. Colins na mchumba wa Connie anko. Connie na
Kamila anti. Na Mill pale alishawazoea. Ungejua ni ndugu wa damu.
Ilikuwa ni siku
ya ijumaa ambayo mama Eric ameenda kuchukuliwa Lushoto. Walimshusha Pam hapo Kinondoni kuandaa nyumba maana dereva alitaka
kwenda na kugeuza nao, asilale.
Pam alikuwa
amejawa furaha sana. Akaanza maandalizi ya kutoa vitu vyake na mwanae
ili mama yake akija akute mazingira ya kwake wala si ya Pam na mwanae. Mill
akatuma dereva wa ofisi hapo Kinondoni ili amsaidie kuhamisha vitu vyake na
mwanae. Akawa akifunga na kumpa dereva anaweka kwenye gari, huku akizungumza na
mama yake kwenye simu aliyekuwa akija na msichana wa kazi kutokea hukohuko
kijijini kwao. Furaha kwa wote.
~~~~~~~~~~~~~~
“Hatimae namuoa
Pam jamani!” Kila mtu alicheka hapo mezani kwa jinsi Mill alivyoongea. “Hongera
sana.” Kila mtu alimpongeza. “Lakini wazazi wangu mimi nataka kuoa kabla
ya Colins.” “Haiwezekani Mill!” “Sasa wewe unataka kuoa kabla ya kaka
yako!? Wewe vipi Colins?” “Yangu inakaribia!” “Sasa yangu mimi ishafika.
Na sitaki kikao. Sitaki kuchangisha yeyote. Nataka nyinyi wazazi wangu. Marafiki
zenu wa karibu na ndugu tu. Sio kitu kikubwa, lakini naomba tumuandalie
Pam kitu kizuri.”
“Ndoto zake
anataka kuvaa shela kabisa. Na iwe kanisani. Pesa ipo naomba
msaada wa eneo, chakula, vinywaji na picha.” “Wasimamizi?” Hapo akapoa. “Mwanzo
alikuwa atusimamie Mike na Kamila. Mambo yameharibika. Hata sijui nani atatusimami!
Kwa ubaya wa Sandra aliomfanyia Pam, sidhani kama ni busara kumuomba
Jerry watusimamie.”
“Tuanze taratibu
Mill. Usihamie kwenye majonzi. Najua Mike alikuwa mtu wako wa karibu na
najua hata yeye atafurahia ulichomtendea. Umesimamia haki yake. Umepambana
mpaka umehakikisha aliyemuua amekamatwa.” “Aisee namshukuru Mungu. Nafikiri
hatima ya shemeji yake, nikimaanisha hukumu yake itakuwa mwezi ujao.” Akaendelea
mwanae akimsikiliza na yeye.
“Aisee tenda wema
duniani. Hata ukifa wema wako unakufuata. Ni kama Mike ameendesha kesi
yake mwenyewe! Wamekuja kugeukana wale ndugu! Yule jamaa niliyemuweka
anisaidie upelelezi, anasema walikuwa wakishindana kumtafuta wakishitakiana.
Ila wote walisema mke wa Luca ndiye aliyekuwa anahusika.”
“Walitoa ushahidi
wa kutosha. Na alipoenda kumkamata anasema alimbana kidogo tu, akaishia
kukiri mwenyewe kama aliye changanyikiwa kabisa. Ananiambia eti damu ya
jamaa yangu ni kali.” “Kivipi?” Mama Colins akauliza.
“Anasema ni kama
imemrudi yule mama. Yupo kama amepagawa. Anaomba aadhibiwe yeye ili
wanae wapone. Anasema eti damu ya baba yake Luca na Mike inamlilia na kufuata
mpaka wanae. Wanataka kuwaangamiza.” “Kwamba alimuua mpaka mkwewe?!” Mzee Komba
akashangaa sana.
“Acha baba! Huu
uchu wa kuvuna usikopanda, unafanya watu kufanya mambo ya ajabu sana! Yaani yeye
alimuua yule mzee akidhania akifa atamuachia mumewe mali, akaja kuachiwa Mike
badala ya Luca. Anavyosema akawa anafanya kusudi Mike na Kamila wasizae ili
wasije na wao wakamuachia mtoto wao mali zikazidi kupotea. Mganga aliyemsaidia
kumuu baba yake mkwe ndiye akampa na wazo la kumuua na Mike. Sijui ikawaje, vya
mganga akaona vinachelewa kwa Mike mwenyewe lakini vilikuwa vikifanya kazi kwa
watoto wao au mimba alizokuwa akibeba Kamila, ndio akamuwekea sumu
kwenye kinywaji alichokunywa Mike siku walipoenda kwake kwa chakula. Ndio chanzo
cha kifo chake.”
“Aisee poleni
sana Kamila na Mill. Pole sana.” “Sasa umeishia kumpa nani pesa uliyoahidi zawadi
kwa atakayemtaja muuaji?” Colins akauliza. “Aisee yule mpelelezi amenikataza
kabisa. Amesema itakuwa ni kama nawazawadia kwa uovu wao. Hawa
watu walijua kabisa ubaya aliokuwa akifanya huyu mama tokea
mwanzo Mike mwenyewe akiwa hai. Japo wanakiri hawakujua mauaji ya baba yake
mkwe, lakini mauaji ya watoto wa Mike waliyajua! Kwa nini hawakukomesha tokea
mwanzo?” “Lakini kweli!”
“Na ujue vile
Mungu anavyo waadhibu, aisee hakuna aliye na sawasawa tena. Ni kama wote
waliojua na kushiriki kwa namna moja au nyingine hawajabaki sawa. Mali alizoacha
Mike zote, nikisema zote, ni ZOTE baba. Zimepotea kabisa. Nyumba aliyokuwa
akiishi Kamila na Mike, nikikuonyesha kwenye picha ilivyokuwa zamani na
sasahivi, unaweza sema ni gofu la wapi sijui!”
“Hivi nimemuomba
mazungumzo Luca, ili aniuzie pale. Wote wameshindwa kuishi pale. Wamekimbia.
Na eti wameshindwa kupauza! Sasa mimi nitamwambia napanunua kwa kuendeleza kile
alichotaka Mike mwenyewe. Kamila apate sehemu yake. Alimtoa Kamila kwenye
nyumba za Yatima, hakutaka kumuacha Dar akimangamanga. Nitapanunua kwao. Napajenga
kama Mike mwenyewe, namrudishia Kamila. Yeye na Colins watajua wanachotaka kukifanya
na ile nyumba. Lakini ni nyumba ya Kamila, na ndio yalikuwa matakwa ya Mike
tokea mwanzo.” “Nashukuru Mill.”
“Usijali Kamila.
Kwanza Mike ananidai. Nikimaanisha kunidai, kifedha kabisa. Nakumbuka niliwasimulia.
Kila nilipotaka kumrudishia pesa yake aliniambia nitajua siku
atakapoihitaji.” “Na kweli!” “Basi ndio hivyo. Acha nilipe deni lake.” Wakatulia
wakifikiria.
“Sina nia mbaya
ya kukutoa kwa Mike. Lakini nina swali juu ya Pam. Umejaribu kututambulisha
kwake?” Mill akatulia akifikiria jinsi ya kujibu. Mwanae akamwangalia. “Niseme anawafahamu
na hana neno hata nikija na Shema. Ndio maana mnaona nipo hapa na Shema.” “Niongeze
swali jingine nikiwa na maana yangu.” Mama Colins akaendelea kwa tahadhari.
“Unafikiri
nikimwambia tumfanyie bridal shower atakubali?” Mill akatulia akionekana
ni kama anasita kujibu. “Wewe usisite kujibu Mill. Tuambie ukweli. Nia ni
kuwapa kitu kizuri na kumfurahisha.” “Usihangaike mama yangu. Naomba tumpe muda.
Sijui kama mnanielewa?” “Kabisa.” Mama Colins akajibu.
“Ila jua
nakushukuru sana mama yangu. Asante.” “Kwa hiyo ushauri wa kwamba Kamila aendelee
kuwasimamia na Colins…” Kabla hajamaliza swali lake Mill akaanza kutingisha
kichwa kabisa akikataa huku akicheka. Wote wakacheka.
“Tumeelewa.” “Nawashukuru
kwa kunielewa. Naombeni tumchukulie taratibu. Naamini atafika tu. Nilimuumiza
sana. Na watu nilio waacha nyuma nao wakamtendea ukatili mbaya sana. Kurudi kwa
yeyote yule sasahivi yeye anachukulia wanarudi kwa ajili yangu MIMI,
wala si yeye na mtoto wake.”
“Inavyoonekana
hakubadili namba ya simu mpaka alipojifungua Shema na kuuza simu niliyokuwa
nimemuachia ili kujikimu na maisha. Kina Mike walikuwepo, lakini hakuna
hata mmoja wao aliyejaribu kumtafuta hata kumjulia hali!”
“Sandra ndiye
huyo alimfunga jela akiwa mjamzito. Akamtoa kwa kumpokonya gari. Hakuna aliyeniambia
kama alikuwa mjamzito na wala hakuna aliyemtafuta hata kumjulia hali! Leo wanarudi
kwake kwa sababu ipi kama si mimi tu.” “Pana ukweli, lakini sisi ni
wazazi Mill.” “Wazazi wangu mimi na wa Kamila.” Mill akakaa sawa.
“Kitendo cha
Kamila kushindwa hata kumfungulia mlango na kumpa maji akiwa mjamzito wa
Shema, katika nyumba ileile aliyokuwa akikaribishwa nikiwa naye, na
asiwahi hata kumtafuta hata mara moja, kwake anaamini Kamila alimwambia kwa
vitendo hamtambui yeye isipokuwa mimi. Na hamtaki kwenye maisha
yake. Sasa kwa nini sasahivi! Ndio anarudi kwenye sababu ileile, wote waliopo
upande wangu ni kwa ajili yangu mimi si yeye na watoto wake.” Kimya.
“Tafadhali
naomba tumuache. Hata mimi namchukulia taratibu sana nikijua jinsi tulivyo
muumiza. Haikuwa sawa.” “Haikuwa sawa Mill. Hata kidogo. Ila na sisi tungetaka
mahusiano naye. Tunampenda sana Shema. Sana. Ikija tokea unapata naye muda
mtulivu wa mazungumzo mengine, utuombee nafasi na sisi. Hata kama kama si
undugu wakaribu, basi mwambie na sisi tunamtambua kama binti yetu.” “Lakini
acha nimuoe kwanza.” Walicheka hapo, hakuna aliyeamini.
“Hutaki kitu
kiharibike?” “Aisee hapana. Nimemsubiria Pam, acha nimfikishe kanisani. Nihakikishe
wameshatufunga pingu za maisha, ndio tuanze ujenzi wa nje. Ila mama
Kenny huyo amesema lazima twende kwake. Hasahau jinsi alivyo mkarimu.
Huko nitampeleka na kuona watoto wa Mgini maana na yeye aliachiwa. Hao hajawasahau
japo amesikia habari zao ni mbaya, lakini naona anasisitiza niwakusanye
kwa haraka na kuonana nao. Kwa hiyo natembea kwa tahadhari sana.”
“Nafanya anachotaka.
Jana jioni alitaka twende kwenye kaburi la baba. Alisafisha na kuweka vyungu
vizuri sana vya maua. Na naona alifurahi jinsi nilivyopatengeneza.” “Aisee
umetengeneza vizuri sana Mill. Sana.” “Nashukuru Colins. Yule mzee ndiye
amenipa haya maisha aisee. Bila yeye nisingekuwa hivi. Nataka wajukuu na
vitukuu wapate kumbukumbu yake.” Wakatulia kila mtu akiwaza lake.
“Kwa hiyo
Colins?” “Wewe oa tu, nakupisha.” Wakaanza kucheka na kutaniana. Angalau pakachangamka.
Mzee Komba akalipokea hilo kwa heshima. Mipango ya harusi ya Mill na Pam ikaanza
na kukubaliana siku maalumu ya kufanya kikao kizuri na watu wao.
“Mill,
nikimtafuta Pam nizungumze naye ni sawa?” Kamila akamuuliza kwa unyonge. “Utamwambia
nini, Kamila!?” “Nimuombe msamaha?” “Narudia swali langu, utamwambia nini?
Kumwambia ulikosea, atakuuliza hayo umejua lini? Mpaka niliporudi mimi
nchini na kumtafuta yeye ndio unagundua kosa? Kwa nini usimtafute wakati ule
iwe leo?” Yaani yeye Mill mwenyewe akaanza kupandisha hasira.
“Ulikuwa kwenye
hali nzuri Kamila. Ukijua ni mjamzito, hana kazi, kwa nini hukumtafuta?”
“Mimi sikujua maswala ya kufungwa kwake Mill. Na Mungu wangu ni shahidi. Hilo Jerry
hakusema kabisa.” “Kama ungejua, ungefanyaje?” Kimya.
“Eti Kamila? Ungejua
kama alifungwa, ungefanyaje?” Wote kimya. “Tulikosa Kamila. Tumemkosea sana Pam.
Mbali ya kufungwa kwake ulijua wazi yupo na shida na nilimuacha na mtoto. Hukumtafuta
hata kujua kama alijifungua salama! Ukanyamaza kimya. Sasahivi unarudije?”
“Tafadhali naomba
muache. Kama nilivyokuomba mwanzo, hata pale kazini muache kabisa.
Maana mimi namjua Pam. Akishajua unahusika na ile hospitali kwa Colins na
familia yake kupamiliki pale na wewe upo, inaweza muwia vigumu kuendelea
kufanya kazi pale. Tafadhali naomba tumpe muda. Si mtu mbaya, ila ana vidonda
tulivyo msababishia. Anapona, ila taratibu. Tumpe muda, naamini atafunguka tu
yeye mwenyewe na kukusogelea bila ya wewe kuomba msamaha na kumuumiza
zaidi. Mwache aje aweze yeye mwenyewe kuwa na sisi wote hapa, lakini
isiwe kwa haraka na kumlazimisha.” Shema kimya ila akisikiliza kwa
makini sana.
“Tumekuelewa
kaka. Na nilikuahidi kule kazini tutaweka mazingira matulivu ya yeye kufanya
kazi, itabakia hivyohivyo. Sisi tupange harusi nzuri itakayo mfurahisha
huku tukifikiria wasimamizi.” Angalau Colins akabadilisha ile hali maana Mill
alishambadilikia hata Kamila. Wakapata mlo wa pamoja, na kuondoka kumfuata Pam Kinondoni.
~~~~~~~~~~~~~~
Baada ya
mawimbi makali na upepo wa majaribu, bahari hutulia na angani
huonekana upinde wa mvua.
Maisha,
licha ya machungu yake, hubeba ahadi ya mwanzo mpya.
Upi kwa
Pius&Raza? Pam&Mill? Mina&Andy?
0 Comments:
Post a Comment