Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Love At First Sight - Sehemu ya 62. - Naomi Simulizi

Love At First Sight - Sehemu ya 62.

Na kweli hisia za Raza zilikuwa sahihi. Alimnunulia cheni nzuri sana ya dhahabu. “Bado mama.” Raza akazidi kucheka. “Ni nzuri sana.” “Umependa?” “Sana. Nzito! Muundo huu sina.” “Sasa ipo full set mpaka ya mguuni! Ushindwe wewe tu.” Raza akazidi kucheka kwa furaha.

“Ila ujue hii ni hongo.” Raza akakunja uso akigeuka vizuri. “Hongo ya nini tena?” “Nakuomba msamaha mke wangu. Najua sikulichukulia vizuri swala la kuzaa na Mina.” Raza hakutegemea! Alilia Raza. Alilia sana kwa uchungu.

Nimekukosea Raza. Nikijifikiria, nahisi kama tokea mwanzo ninge handle hili swala la PJ vizuri, usingefika ulipofika. Na mimi najua nimechangia. Hilo ni la pili, ila kubwa ambalo si sawa, nikuzaa nje ya ndoa. Si sawa, naomba unisamehe.” Hizo ni habari ambazo hakuwa hata na wazo kama atakuja kuzisikia!

Pius anakiri kosa la kuzaa nje! Tena mtoto wa KIUME! Akambembeleza mkewe mpaka akatulia. Huku akimfuta machozi kabisa. “Lakini Naomba uelewe Raza. PJ ni mtoto wangu kama Polla. Hilo siwezi kukwepa tena.” “Naelewa Pius.” “Basi naomba tujipange kwa pamoja. Taratibu, hatua kwa hatua, naamini tutafika tu. Si safari hii unaniombea?” “Sana Pius. Na nimetubu hata swala la mauaji.” Pius akatulia.

“Nisamehe Pius. Na natafuta jinsi ya kumuomba Mina msamaha. Watu wananikimbia Pius!” “Wape muda Raza. Hawa watu umewatisha sana. Tafadhali wape muda. Ila nakuahidi hutakuwa tena peke yako. Tutatembea wote. Mimi na wewe, kuonyesha na sisi tumebadilika. Sisi na watoto wetu. Turudishe heshima tuliyopoteza.” “Wanamkimbia Polla.” Akamsimulia yote jinsi Paulina alivyomtenda binti yao, na yeye akajidai kama ndio anasikia hapo. Akatulia akimsikiliza mkewe akisemelezea ndugu zake. Akalia wee, Pius akimbembeleza.

“Watu wanashindwa kunisamehe Pius!” “Ni muda tu. Tulia kabisa. Waache. Inatosha. Ushaomba msamaha kwa kila mtu uliyeweza kumfikia, wamesikia kama umeomba msamaha. Inatosha. Tulia kabisa.” Hilo likamtuliza, alijawa furaha huyo! Machozi mengi yalichanganyika na ya furaha. Amempata Pius bila MGANGA! Japokuwa ameomba muda mrefu, lakini hatimaye amejibiwa.

Wakatulia kila mtu akiwaza lake. Mwishoe Raza akagutuka. “Kesho ijumaa, siku ya kazi. Acha nikuache na wewe upumzike. Ila ujue nimefurahi sana.” “Huna hata hamu na mimi Raza!?” “Ungejua, ungenihurumia, ila hofu. Sijui kama utanipokea tena baada ya kukuumiza!” “Si na wewe umenisamehe?” Raza akatulia.

Juu ya Ayvin.

“Raza?” “Ndio inakuaje Pius? Una mtoto na Mina. Mtoto WAKIUME!” “Wewe hiyo jinsia isikutishe. Huyo mtoto atafundishwa kukua na kusaka pesa yeye mwenyewe sio akue akichungulia urithi wa dada zake!” Hapo akampata Raza. “Mimi mwenyewe sijarithi mpaka leo na ni mtoto wa kiume wa kwanza kwa mzee Ruhinda. Kama ningekuwa nikisubiria mali za mzee, sisi sote na watoto wetu tusingekuwa na maisha haya. Maana nisingejibidisha, ningebaki tunamsubiria mzee afe ndio turithi. Kwanza mzee mwenyewe hana hata mpango wa kufa! Sasa kuja kupata mali zake si leo, mama.” “Lakini kweli!”

“Wewe unajipa pressure ya bure! Sasahivi tujipange mimi na wewe jinsi ya kulea hao watoto watatu.” “Na mimi Pius?” “Kumbe na nani? Tushaharibu. Tushapoteza heshima huko nje. Tuanze kujipanga upya. Na najua Raza. Najua mke wangu kuwa nimekudhalilisha sana. Lakini si tumekubali kuanza?” “Ikiwa hivyo sawa Pius. Hapo umenituliza. Nilijua unanidharau mimi kwa sababu nimezaa watoto wa kike tupu!”

“Unawezaje kufikiria hivyo Raza!? Napenda binti zangu na najivunia haswa. Sina mtoto wa bahati mbaya kati yao na siwaonei aibu hata kidogo. Ni wanangu! Wewe unafikiri mapenzi ya Poliny yatachukuliwa na PJ?” “Hata sijui Pius! Nilibaki nikidhania tu. Wewe hukuonyesha kama ni kosa mpaka leo! Angalau leo umelizungumzia, umenituliza. Na nakushukuru.”

“Huyo PJ anamajukumu huyo! Ungemuhurumia. Anatakiwa akue huku macho yapo kwa dada zake. Asiwahi kutulia kama Polla wangu yupo matatizoni. Atakuwa akifundishwa mafanikio yake ni pale dada zake wanapofanikiwa wala sio kuwa mrithi wangu! Kwanza kwetu hatuna hata huo utaratibu wa kurishana! Hapa nilipo hata sijui kama nina urithi kutoka kwa baba! Kwanza sitaki. Hata hivyo mzee Ruhinda atanipa nini ambacho mimi sina, tena kwa kiwango cha juu dhidi yake!? Halafu hata mimi nikirithi mali za mzee, yeye mama atakuwa wapi?” Raza akatulia akifikiria.

“Halafu Raza, hakuna anaye kudharau nyumbani kwetu eti sababu umezaa watoto wa kike!” “Unajuaje?” “Kwa sababu mimi mwenyewe sikuwahi kuhisi kudharauliwa eti kwa sababu nina mabinti tu, sina wakiume! Sijawahi poteza heshima kwa wazazi kabla na baada ya Ayan. Alizaliwa wa kwanza wa kiume, tukampokea kama mtoto wetu. Furaha iliongezeka kwa sababu alikuwa mjukuu wa kwanza wa kiume, mtoto ambaye jinsia hiyo hatukuwa nayo, na tukajua jina letu halitapotea hata kama kina Poliny watakuja kuolewa na kuchukua majina la waume zao, basi Ayan atabakia kubeba jina letu, basi. Lakini si kwa kuwa yeye ni bora kuliko wengine!” Akamuona ametulia akiwaza,

“Umeelewa na umenisamehe?” Akamwangalia mumewe maana alishapotea hapo. “Juu ya kuzaa nje ya ndoa.” Pius akaweka sawa. “Kwani mlikuwa na mahusiano ya kimapenzi na Mina?” Angalau siku hiyo akapata ujasiri wa kumuuliza mumewe. “Nakwambia ukweli na naomba uniamini.” Akamsimulia ile siku ilivyokuwa, tena kwa tahadhari sana.

“Kama unakumbuka Mina alikuja pale kwa Paulina siku ile akitapika, hakuwa akijua kama ni mjamzito. Unakumbuka?” “Ndio hapo mimi nilikuja changanyikiwa Pius!” “Kwa hakika yeye hakuwa na hatia kabisa. Hakuwa akijua kabisa kwa kuwa ni kweli nilikuwa naye karibu. Mina hakuwa na mwanaume mwingine. Aliamua kutulia na Andy. Ila mimi nilijua kabisa, ila nilikuwa kwenye mshituko na sikuwa nikijua nitafanya nini ndio maana nilinyamaza na kumuchia yeye abebe lawama zote. Na hilo nilikuja kumuomba msamaha.”

“Kitu ambacho unaweza usiamini Raza, Mina anakuheshimu sana. SANA. Na japokuwa ulikuwa ukimtangaza vibaya kwa watu, lakini yeye alibaki akikutangaza vizuri hata siku anarudi na watoto, mbele ya wazazi. Mina alibaki akikutambua kwa heshima sana. Anavyosema ni kama wewe ndiye mwanzoni kabisa uliyempokea na kumkaribisha kwenye familia, mbali ya Andy. Na anasema aliondoka kwa wazazi na kutoroka kwa heshima yako WEWE, ili isiwe ni kama yeye ndiye amekutoa kwenye familia wakati ulimkaribisha kwa upendo.” Akamsimulia kwa kifupi, akabaki ameinama kwa majuto.

“Mina si mpinzani wako kwangu na kwa wazazi.” “Una uhakika? Maana mwenzangu amekuzalia mtoto wa kiume tuliyekuwa tukimtafuta, ikashindikana.” “Haimaanishi yeye ni bora kuliko wewe ambaye ni mke wangu. Hapa tupo mimi na wewe. Na mimi na wewe ndio katika shida, na raha mpaka kifo. Wewe ni wangu Raza.” Hakika Raza hakuamini, akatulia akitafakari na kutamani hayo Pius angemwambia muda mrefu sana wala hata asingehangaika kwa mateso yote hayo aliyopitia. Kwa hakika alimtuliza nafsi. Akabaki mawazoni. Pius akabaki akimwangalia.

Akamuona anavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu kama ambaye anayejaribu kutulia. Kisha akamwangalia mumewe. “Nimeshindwa kumuomba msamaha kabisa. Nashindwa hata pakuanzia!” “Kwa sababu mimi ndio nahusika.” Raza akamwangalia kama asiyeelewa.

“Mimi nitamuomba Mina msamaha kwa niaba yako. Kwanza. Kama njia ya kutengeneza mazingira mazuri ya kukusikiliza wewe. Mimi ndio nilianza vibaya Raza. Ningeanza vizuri na kukutuliza tokea mwanzo, nina uhakika usingepaniki na kufanya yote hayo. Au si kweli?” “Niliingiwa na roho chafu Pius! Kuna mambo nilikuwa nafanya, nikifikiria sasahivi mpaka najishangaa na naona mama alikuwa sahihi. Alishanionya mno, na kunisihi niache lakini nilikuwa sina jinsi nyingine ninayofikiria isipokuwa ushirikina. Na wala usifikiri vilikuwa vinanipa furaha na amani!”

Pius akabaki akimsikiliza. “Ni vurugu tupu. Havina raha! Mashariti mengi, ya wasiwasi! Unaota mandoto mabaya, kila siku hulali vizuri. Bora sasahivi nikilala, nalala hata sioti mandoto mabaya.” Akajifuta machozi na kujaribu kutulia kisha akaendelea.

Juu ya Familia.

“Nashukuru kunisaidia kwa Mina. Na naomba nikiwa namuomba msamaha, na wewe uwepo Pius. Watu wananiogopa!” “Sawa. Na acha kuwafuata.” Raza akawa hajaelewa.

“Usilie. Inatosha Raza. Nyamaza.” Akamsaidia kumfuta mkewe machozi. “Ila sijaelewa! Kwamba nisiwafuate tena!?” “Wewe si umeshawaomba msamaha?” “Wote, kasoro Mina tu. Mama yangu amenisamehe kabisa. Wala hana neno, tena naona kama ameongeza ukaribu. Angalau anaweza piga hata kuulizia maswala ya watoto na kunikumbusha niwe namwambia maswala ya Polla mapema, ili na yeye awe anahudhuria kama bibi Ruhinda. Ila kwenu! Mmmh! Nimepoteza heshima kabisa.”

“Basi inatosha. Waache kabisa. Watarudi tu wenyewe.” “Kwa namna gani!?” “Wewe tulia kabisa. Na kuanzia sasa acha kulia. Tulia. Angalia ya hapa nyumbani na ya wanao kuzunguka. Basi. Watarudi wenyewe. Mimi nitashugulika nao. Na Polla akikulalamikia juu ya mtoto wa Paulina, tafuta hekima ya kumtuliza. Atakuwa sawa tu.” Hapo akazidi kumtuliza zaidi.

Akamfuta machozi kabisa kitu ambacho kwa wanandoa hao hakikuwa cha kawaida! Kwanza siku hiyo ni kama Pius alitoa muda mwingi sana kwake kitu kilichokuwa kikimshangaza. Alionekana kama hana haraka kabisa na kesho yake ilikuwa ni siku ya kazi! Alimuonyesha yupo kumsikiliza tena bila haraka!

Juu Ya Chezo.

“Nashukuru Pius.” Kisha akacheka. “Nini?” “Umekuwa mwema kuliko nilivyokuwa nikikuloga!” Mpaka Pius akacheka. “Kweli Pius! Sasahivi mpaka nasikia raha kuwa na wewe! Ulikuwa unakuwa mkali kwangu, hunisikilizi kabisa kama mwanao Poliny. Nikawa namwambia Katibu, mbona dawa unazonipa hazisaidii. Pius mkali sana kwangu.” “Usilie sasa. Si umesema sasahivi nakusikiliza?” Akamfuta tena machozi.

“Ila nilikuwa natamani uwe na mimi kama hivi Pius. Ujue hata Chezo si kwamba tulikuwa tukikutana tu kwa mapenzi!” Pius akaanza kubadilika. “Nakwambia ukweli Pius. Si mapenzi. Chezo anauwezo wa kunisikiliza mno. Anaweza akakaa na mimi zaidi ya lisaa, ananisikiliza tu nikilalamika. Ukumbuke nilishakuwa fedheha pale ofisini. Wewe umezaa na Mina, na unampigania mpaka mitandaoni. Watu wakawa wananicheka. Siwezi zungumza na watu ofisini. Mashoga wakawa wananisanifu. Ndugu nao wakawa wananicheka. Nimebadili dini kwa mtu ambaye hanitaki hata kwa tunguli.” Hapo akazidi kulia kwa uchungu. “Pole na samahani Raza.” Akazidi kumbembeleza.

“Ndio nikawa nakaa na Chezo nakuwa nazungumza naye. Ananitia moyo na kuniambia nitulie tu na watoto. Maadamu bado hujanipa talaka, nitulie. Ndio nikamwambia mimi kwetu ni kama hata kaka zangu walinisusa, hawanitafuti kwa la kheri wala la shari sababu nilikana imani ya wazazi. Nikamwambia ukinifukuza leo, sina pakwenda. Ndio akanisaidia kutafuta kiwanja.” Pius hakutegemea.

“Akanibembelezea bei. Nikalipia na kunisaidia mpaka nikaweza pata hati yake. Hivi nilishaanza kujenga, yeye ndio ananisaidia kusimamia na mafundi. Sema mkewe mkali sana. Sasa wakati mwingine akiwa amegombana na mkewe ndio akawa anakwenda kukaa huko site, na ndio ikawa msaada wangu maana anakuwa akiwasimamia mafundi. Ila pesa ni zangu. Mshahara wote nikawa napeleka huko, ananisaidia. Na nimwaminifu kwakweli. Hakuwa akiniibia. Halafu ishi yangu ndio ikawa wewe.”

“Umefikia wapi ujenzi?” “Nakaribia kwenye paa.” “Raza!” “Sasa wewe unafikiri pesa zote ninazolipwa mshahara napeleka wapi?” “Hata sijui! Maana unakazi ya kuomba pesa mchana na usiku.” Raza akacheka sana.

“Najenga mwenzio.” “Hapo nimekusifu. Ila Chezo iwe mwisho Raza. Sitaki.” “Nishamwambia.” “Hata kukusaidia ujenzi, hapana.” “Mimi sina muda Pius. Yeye..” Akasimama kabisa. “Hapana Raza. Hapana.” “Ni kwenye ujenzi tu! Hamna mambo mengine. Kwanza nishamwambia nimebadili maisha yangu. Siku hizi nipo karibu na Mungu. Sitaki tena kumkosea Mungu. Akaelewa kabisa na anaheshimu hilo. Ila kwenye swala la ujenzi ndio atabaki akinisaidia, lasivyo mambo ya hapa nyumbani nitapwaya, Pius! Kazini na kusimamia ujenzi! Hapa sitaonekana.” “Raza, HAPANA.” Hapo akawa ashabadilika.

“Umenisikia Raza?” “Basi nitamwambia asirudi tena kule. Nikuonyeshe hati yangu?” Akamfanyia kusudi atulie. Akabaki amesimama. Raza na yeye akanyanyuka kuelekea upande wa closet ambako kuna nguo zao na viatu. Akaenda upande wake ambako kuna safe yake ndogo kama Pius tu, lakini safe ya Pius ilikuwa kubwa zaidi. Akafungua na kuitoa. Aliporudi, akamkuta amerudi kukaa kitandani. Akampa. Akaisoma.

Juu ya Urithi.

“Hongera sana. Ila ujue hapa ni kwako Raza.” “Ila kama mama yako alivyosema, nilikukuta na mali zako Pius! Hii nyumba ilikuwa inakaribia kuisha.” “Hata kama. Hata kama kuna kurithi, ni mpaka na wewe ufe. Hakuna wa kukutoa hapa. Hata Poliny hapa si kwake. Huyo unayemuhofia, PJ, ndio kabisa. Mungu anipe tu uhai. Urithi wake ni SHULE nitakayomsomesha. Basi. Sio mali. Nilichofanyiwa mimi na wazazi wangu, ndicho na mimi nitamfanyia PJ.” Pius alishindwa kabisa kumuita mtoto wake Ayvin kama wengine.

“Niliye na wasiwasi naye mimi ni Polla. Huyo nahisi ndio mrithi aisee! Amegoma kukua! Michezo mingi! Sio kama dada yake.” Raza alicheka sana. “Usimkatie tamaa!” “Aisee siwezi. Polla! Ukimuhimiza shule, analia! Ukimuhusia mambo ya shule inakua kama unamkera, na ni kama hana mpango kabisaa!” “Anasema wewe mkali kwake.” “Sasa kwa wewe mpole kwake mbona sasa hafaulu?” “Ila hafeli.” Raza akaendelea kutetea.

“Lakini sio kwa kiwango kizuri.” “Tatizo wewe unataka awe kama Poliny, Pius! Awe anapata zote 100. Nilishakwambia hawa watoto hawalingani. Poliny amechukua kichwa chako.” “Siamini kabisa hilo. Huyo mwanao michezo imemzidi aisee! Akili ipo kwenye games zake tu.” “Atakua tu. Tumpe muda.” Wakatulia.

Bado Chezo.

“Ila swala la Chezo naomba tuhitimishe Raza.” “Sawa. Ila ujue na mafundi ni wake.” “Mbona inakua kama hiyo nyumba mnajenga naye!?” “Ni pesa yangu, Pius. Kwanza sio kwamba hata anahela ya kuwekeza hapo. Usiponisaidia wewe  pesa ujue ndio nimekwama.” “Lazima ajue hatutaki tena msaada wake. Na asikutafute TENA. Mimi SITAKI. Tutatafuta mafundi wengine.” “Basi nikitoka kazini kesho nitakwenda tukakabidhiane kabisa.” Hapo tena ikawa shida. Kitu kisicho cha kawaida gafla Pius akawa na wivu na mkewe.

“Mimi hivyo pia sitaki.” “Sasa tutafanyaje Pius!?” “Kwamba yeye ndio anajua kila kitu kinachoendelea huko kama yake?!” “Ndiyo.” Akazidi kumvuruga. “Kwamba nyinyi mlikuwa mpo kama mke na mume kabisa!?” “Umekasirika Pius. Na unaanza kutafuta kujiudhi zaidi. Tafadhali nipe muda nihitimishe vizuri, nisipoteze mahesabu, na pia nijue walipofikia mafundi. Naweza zungumza nao, nikaendelea nao mimi.” “SITAKI. Simtaki yeye wala mafundi wake. SITAKI Raza.” “Sawa.” “Sawa nini, sasa?” “Sichukui hao mafundi wake.” “Na kukabidhiana?” Raza akakwama.

“Raza?” “Hata sijui Pius! Basi nishauri wewe.” “Basi mwambie na mimi nitakuwepo.” “Hawezi kukubali. Chezo anakuogopa sana.” Pius akakunja sura. “Kwa nini? Akamuona anasita. “We Raza?” “Anahisi unaweza msababisha akafukuzwa kazi.” Pius akabaki akimwangalia kama ambaye hajaelewa.

“Kwani wewe umemfahamu Chezo kwa kiasi gani?” Kidogo Pius akatulia akifikiria. Hakutafuta kumfahamu kwa undani huyo Chezo, ila kuishia hivyohivyo tu kama mwizi wa mkewe. Akabaki akijaribu kutafakari. Kuna kina Chezo wangapi anao wafahamu! Kwa ufikiriaji ule, Raza akashukuru Mungu kuwa hamfahamu Chezo kwa undani. Akaona apotezee.

          “Haina maana. Mimi nitamwambia aache kwenda pale.” “Anafanya kazi wapi?” Hilo ndilo alilokuwa akificha sana Raza na kufurahia kuwa hamfahamu kwa undani. Sasa anaanza kuchokonoa tena! Raza hakuwa tayari.

“Naomba hayo tuyaache Pius. Huko tushatoka. Nitamwa..” “Kwa nini sasa unamficha?” Akauliza kwa ukali. “Simfichi, ila naona haina maana.” “Kwangu inamaana. NATAKA kumjua.” Raza akanyamaza.

“Hivi si unajua nikitaka kumfahamu kwa undani, nitamfahamu tu?” “Naomba nisikilize kwanza Pius. Huyu mtu anategemewa sana. Na si na familia yake tu, kwamba mke na watoto! Hapana. Ni mpaka nyumbani kwao, wazazi wanamtegemea YEYE. Kazi aliyonayo inategemewa karibu na ukoo mzima. Hapo alipo anasema ameipata hiyo kazi kama muu..” “Raza?” Akawa ameshakasirika. Akamuita mkewe kwa ukali.

“Anafanya kazi chini ya mzee Ruhinda.” Pius akakunja uso kwa mshangao uliojaa mshituko. “Kwamba na yeye ni miongoni mwa board of directors?!” Raza akanyamaza. “Raza?” “Yupo kwenye maswala ya usafirishaji.” Alishituka Pius akahisi hajamsikia mkewe vizuri .

“Raza, unataka kuniambia huyu mtu ni miongoni mwa MADEREVA wa mzee Ruhinda pale ofisini!?” Raza akashindwa hata kujibu, akabaki kimya. “Yaani wewe ulikuwa na mahusiano na dereva wa baba yangu mzazi!?” Kimya ila wazi alisharudiwa na ile hofu ya zamani aliyoitoa mumewe. “Kweli Raza?!”  Akashindwa kujibu akitetemeka. Mumewe alimtizama kwa muda, na kutoka hapo chumbani kabisa.

Raza naye alipoona hivyo akavua mkufu aliomvalisha. Akaurudisha kwenye mkoba wake akamuwekea pembeni ya mto, akatoka hapo kimyakimya kurudi chumba alichokuwa akilala.

Upepo Wa Usaliti Unaponong’ona Kwa Uchungu

Kamila ndiye aliyeandika kurasa mpya moyoni kwa Pam, tena bila kutegemea. Kamila mnyenyekevu mwenye sauti tulivu alipokuwa akiwapokea alipokuwa na Mill, siye aliyemsikia akimjibu mlinzi wake kikatili juu yake.

Alikuwa kama nyoka aliyejivua magamba na kujionyesha uhalisia wake kwa Pam. Akawa kama chui aliyekuwa amevaa ngozi ya kondooo mbele ya Mill na Mike alipokuwepo Pam. Kamila mnyenyekevu! Aliyejitoa kuwahudumia kuanzia chakula cha asubuhi akitangaza wema wake waziwazi, alimbadilikia Pam na kushindwa hata kumkarimu maji ya kunywa! Aliandika kitu kipya na kigeni kilichoshindwa kutoka moyoni kwa Pam.

Lakini jumapili hiyo akaamua kujikaza na kumfuata Mill huko kwa kina Komba. Walijiandaa kwa ibada, wakatoka hapo wao watatu, Mill, Pam na Shema kwenda kumfuata mama Eric na binti aliyekuja naye mjini kumsaidia kazi.

Alijitahidi kwa mama yake apendeze. Na kweli uzuri ni asili yake mama Eric alikosa tu matunzo. Wakatoka watano hao mpaka kanisani baada ya ibada wakaongozana mpaka kwa kina Komba, mapigo ya moyo ya Pam yakienda visivyo, analazimishia tu safari. Kimya garini, anayezungumza ni Shema, baba yake na bibi yake.

Walifika kwa kina Komba wakakuta wametayarishiwa kwelikweli na wanasubiriwa kwa hamu, maana walienda kupokelewa nje kwenye gari kabisa. Pam kimya akijiangalizia, ila Kamila hakutoka. Akatulia kuangalia kinachoendelea.

Wakakaribishwa ndani ila akagundua kuna kujiwinda kwingi zaidi kwa maneno. Akatulia, wakakaribishwa vinywaji, ilikuwa juisi iliyotengenezwa nyumbani. Nzuri sana. Wakiwa wanaendelea kunywa, akatokea Kamila. Kitu kikaruka moyoni kwa Pam, ila akatulia. Akasalimia kwa kuanza kuwashika mikono. Alipofika kwa mama Eric akakaa kabisa pembeni yake, maana mama Eric mchangamfu. Msambaa asiye hila. Akaanza kumsifia na kutaka kumtambua zaidis. Ikabidi Kamila akae sasa ajitambulishe huku akijaribu kutulia kwa hofu mbele ya Pam akijua Mill anamtizama kwa makini sana.

Mwishoe mama Colins akasaidia. “Huyo naye ni bibi harusi mtarajiwa, mchumba wa Colins. Tukimaliza harusi ya Mill, inakuja ya Colins.” Mama Eric hanaga mengi, moyo wake umejaa amani. Akampongeza hapo akimshika kabisa mkono kwa shangwe huku akimbariki.

Kabla hajamsogelea Pam sasa, baada ya shamrashamra na maneno ya pongezi ya mama yake kwa Kamila, Pam akasimama na kuomba alekezwe chooni. Maana yeye Pam ndiye aliyekuwa akifuata. Ile Mill amesimama ili ampeleke chooni, Shema naye akasimama.

“Subiri hapo na kina bibi, na babu narudi sasahivi, namuonyesha mama yako chooni.” “Mimi naenda na mama yangu.” Shema akamsogelea mama yake karibu kama anayekimbia hapo sebuleni baada ya kuja Kamila. “Sasa utaingia naye chooni bwana Shema!?” “Basi mimi ndio namuonyesha chooni, napafahamu. Wewe ndio ukae hapa. Twende mama.” Pam akaondoka na mwanae Mill akabaki amesimama katikati ya sebule, mama Eric hawaelewi. Akarudi kukaa, Kamila akapoa.

~~~~~~~~~~~~~~~~

“Vipi na wewe?” Kamila akamtizama Mill kinyonge akitafuta pakukaa maana alikuwa akimsogelea Pam na ndio Pam akanyanyuka. “Nifanyaje Mill?” “Huna chakufanya ila kumpa nafasi na hili nilikwambia Kamila. Tafadhali tulia.” Mill akaongea kwa sauti ya chini kama anaye mnong’oneza. “Hata hivyo kufika mpaka hapa, nahesabu ni hatua kubwa sana. Na naona mama anafanya vizuri. Wewe tulia. Mwache kabisa.” Mill akasisitiza kwa sauti ya chini, wengine wote kimya.

~~~~~~~~~~~~~~~~

Pam akarudi na mwanae akionekana ametulia tu, ila sebule nzima ilikuwa kimya. Akarudi kukaa alipokuwa amekaa, na mwanae akamsogelea kukaa naye. “Ona saa yangu amenipa anko.” Akamsogezea mkono mama yake, Pam akacheka akiiangalia. “Umemwambia anko asante sanaaa?”  “Sijasema sanaaaa, ila nimesema asante. Maana hii saa nikitembea inahesabu steps zangu. Nikinywa maji inakuwa inaweka kumbukumbu, na mapigo yangu ya moyo. Inakuwa inatunza rekodi zangu vizuri. Nikikaa muda mrefu itaniambia nisimame nisikae sana niwe active.” “Naona hapo haitakuwa na shida. Maana wewe huwezi kutulia.” Kila mtu akacheka.

“Mbona hapa nimetulia!” “Ishakukumbusha kuwa active?” Mama yake akamuuliza. “Bado.” “Basi haitakaa ikakukumbusha.” Akaanza kucheka mwenyewe kama wengine. “Mimi natulia mama!” “Labda ukiwa unalala.” “Hapo inakuwa inajua natakiwa kulala.” “Basi hicho kipengele hakitakuwa na kazi.” Pam akamjibu mwanae akiitizama saa ya mwanae.

“Ni nzuri sana. Asante Colins.” Pam akashukuru. “Karibu. Na wewe hiyo app unaweza kuwa nayo kwenye simu yako, itasaidia kujua alipo kila wakati.” “Naona nitafanya hivyo. Tunashukuru.”

“Naomba unisikilize na mimi, Pam. Nisamehe nilikuumiza. Ila tafadhali naomba uusikie upande wangu na mimi. Na hapa nia yangu si kutaka kukuumiza zaidi wala kukuudhi japo Mill amenikataza.” “Unataka kufanya nini Kamila?!” Mill akamuuliza kwa kushituka kidogo. “Nataka anisikie Mill. Na baada ya hapa sitamsumbua tena.” Pam kimya akimtizama.

“Kumbuka ulinikuta katikati ya kina Mill.” Pam kimya akimtizama. “Na mimi nilikuwa katikati yao kama mke wa Mike kwa miaka yote. Rafiki zake Mike wote walikuwa wakijua tupo pamoja na Mike tokea shule ya sekondari lakini sijamzalia Mike mtoto hata mmoja useme mtoto alikuja kufa baadaye. Hapana. Leo umekuja wewe, kwa muda mfupi tu, na ujauzito wa kujifungua! Hakika nilipatwa wivu, nikatamani watu wasijue nikaonekana mimi sifai zaidi.” Kamila akaanza kulia.

          “Mwenzio yatima Pam. Yatima nisiyejulikana hata ninakotokea. Hakuna anayejua hata ndugu zangu useme nina kabila fulani! Kina Mike na rafiki zake ndio ilikuwa familia yangu pekee. Mill na rafiki zake wengine waliokuwa wakituzunguka hawakuwa na wanawake, ila mimi kwa Mike. Kila mtu alikuwa akitutizama mimi na Mike kama mfano wa kuigwa na mimi nikawa mwanamke bora katikati yao. Wakinidekeza kama dada yao wa pekee kwa kuwa waliijua historia yangu!”

          “Gafla ukaja wewe. Una kila kitu kizuri. Ile attention yote ikawa imehamishwa kwako. Akili na mawazo pia ya Mike aliyekuwa hajui kugawa upendo wake kwa mwanamke mwingine isipokuwa mimi tu, vikageuka ikawa na wewe! Kila wakati anakuzungumzia wewe na jinsi ya kukusaidia umfikie Mill. Mill naye ikawa hivyohivyo, hakuna mazungumzo kati yao isipokuwa wewe na mipango inayokuhusu wewe tu, mimi tena nikajihisi kama nawekwa pembeni, sina umaana tena.” Pam akakunja uso kwa mshangao.

          “Kamila, ulijihisi tu!” “Kuwa mkweli Mill. Safari zote tulizokuwa tukija kwako na wewe kuwepo hapa nchini baada ya Pam kuingia kwenye picha, hazikuwa tena zikinihusu mimi kama zamani Mike akitaka nipumzike, lengo ilikuwa Pam, na mipango ya kumleta karibu yenu. Tukiwa sisi wote aliyekuwa akizungumziwa ni nani kama si Pam?” Mill akatulia akijaribu kuvuta kumbukumbu ila kama hapati!

“Unakumbuka siku moja mpaka Sandra akawaambia nyinyi wote watatu, kuwa akitokea mtu anatusikiliza pale, anaweza asielewa huyo Pam ni mwanamke wa nani kati yenu. Anaweza fikiria ni mwanamke wenu nyinyi wote watatu maana hakuna tunapokwenda wala hakuna mazungumzo mengine nyinyi mnazungumzia ila Pam tu. Bisha Mill?”

          “Sasa si kwa kuwa yeye hakuwa katikati yetu tulikuwa tunatafuta jinsi ya kumuweka karibu!” “Zaidi ya vile ilivyokuwa! Maana pale tu alikuwa anakosekana Pam mwenyewe, ila uwepo wake ulikuwa umejaa mpaka binafsi nikaona nasahauliwa! Sasa eti anakuja Pam mjamzito! Hakika nilitishika zaidi Pam. Wala sitaongopa.” Kamila akajifuta machozi.

          “Mike ndio sikutaka ajue kabisa, asije akazidi kupagawa na wewe. Kuona mwenzangu umekuja tu na kushika mimba mimi sijaweza hata kubeba mtoto kwa miezi minne! Nikaingiwa wivu na hofu na ndio maana nilitamani uondoke pale kwa haraka ili hata Mike asije kukukuta pale getini au ndani. Ila sio kwamba nakuchukia Pam. Sijawahi kukuchukia. Ni wivu tu.” Akajifuta tena machozi.

          “Najua una haki ya kunichukia lakini jua nia yangu ilikuwa mbaya kwa yeyote ambaye angetokea bora kuliko mimi katikati ya kina Mike. Mwenzio nilikuwa nadekezwa na kila mtu aliyekuwa rafiki yake Mike, na kuonekana wa maana sana.” Mpaka Pam akacheka.

          “Kweli tena, muulize Mill. Hata Sandra aliyekuchukia wewe, ujue mimi mwenzio alikuwa akinipenda.” “Sasa mimi Sandra alinichukia nini?” “Nakwambia wewe ulikuwa tishio kwetu. Umekuja, umetukuta, ukachukua spot light yote! Wanaume wote wanakuimba kama wimbo wa taifa sijui! Mimi na mwenzangu Sandra tukawa hatuna maana tena!” Wakazidi kucheka, Mill akawa akitingisha kichwa kwa masikitiko.

          “Wewe ulikuja ukawa tishio, bwana Pam! Mzuri. Halafu Mill akawa amechanganyikiwa kabisa na wewe, akageuza marafiki wote wakawa wanakutukuza wewe tu! Ulitutisha.” “Sasa mbona na wewe ulikuwa kila kitu lakini Sandra hakukuchukia?” Ikabidi Pam amuulize ila akisikika ametulia.

“Sasa wewe hukuwa umemjulia Sandra. Sandra hapendi kupitwa. Anataka uwe unamsifia. Usimuonyeshe umemzidi. Halafu kitendo cha yeye kuwa na watoto mimi sina, tayari kwake mimi nilikuwa chini yake na kwa kuwa mimi nilishamsoma, nikajua udhaifu wake, basi nikawa siachi kusifia wanae, na kuwaletea zawadi yeye na wanae, kila nikitoka nje ya nchi, ndio maana mwenzio alikuwa akinipenda.” Pam alicheka sana.

          “Kamila!” “Mimi nakwambia kweli Pam. Sasa wewe ukaja kwanza ukawa mkimya. Hajui mambo yako ya ndani ili akulinganishe na yeye ajione amekupita. Ukabakia bora tu! Unaendesha gari jipya na ujauzito juu! Ndio maana mwenzio alikufunga jela, japo mimi hilo sikulijua. Na hata Mike hakujua. Mike asingekubali ukae jela. Kila mtu anamjua Mike.”

“Mbona aliniacha na shida?” Pam akauliza kwa kuumia. “Mimi simsemelezei Mill. Ila jua mwanaume wako huyu, Mill ndio ametuponza kwako.” “Kamila!” “Hakika tena Mill. Acha na mimi nijitetee kwa Pam. Mike hapendi uonevu na angejua kama unashida, kwa hakika angeenda hata kinyume na Mill akakusaidia. Muulize Mill, anamjua.” “Kweli. Mike angejua unashida asingeacha kukusaidia.”

“Basi ndio Mike. Ila huyu Mill alituambia hivi, wewe hapo mzuri sana. Utaulizia kidogo, utaona anakubabaisha, utaachana naye, utaendelea na maisha yako. Tena Mike akamwambia huyu Mike, mbona Pam haachi kukuulizia kwa Jerry! Tena akamwambia unamuulizia sana. Mill huyu, hapo ujue ni wakati huo kesha haribu mipango, Kisha anampeleka kama gari bovu, hawezi tena kukutafuta wala kurudi nchini. Akatuambia tukupe tu muda, utaachana naye, na kumchukia yeye Mill na kuendelea na maisha yako. Si ni kweli Mill?” Sebule nzima wanawasikiliza wao wakiendesha kesi yao.

“Mimi ndivyo nilivyojua. Lakini nishazungumza na mpenzi wangu, mimi amenielewa. Wewe usirudishe dhambi zangu, zilishasamehewa zamani sana. Wewe pambana na hali yako Kamila.” “Sasa wewe wakati ukiomba msamaha wako kwa nini usinitetee na mimi kwamba wewe ndio uliniponza?” “Wewe ulimfanyia ubaya zaidi,  bwana! Ulimnyima hadi maji ya kunywa! Wewe pambana na hali yako Kamila.” Wakaanza kusemeana. Pam akiwatizama tu.

“Sasa na mimi Pam ameshanielewa. Uongo Pam?” “Nyinyi wote mlinifanyia ukatili aisee! Ukatili wa hali ya juu!” “Nisamehe Pam. Ila jua Mungu ashanilipiza kwa ubaya wangu wala huna haja ya kunichukia. Nilipoteza kila mtu na kila kitu, nikawa kama nimechanganyikiwa, mpaka huyu Colins alipo niokoa. Alinikuta na hali mbaya kama kichaa kabisa. Marafiki niliokuwa nikiwalinda wenyewe waliondoka kwenye maisha yangu, nikabaki kama peke yangu. Namangamanga, hata nyumba niliyokukataza usiingie walinipokonya. Isingekuwa Colins ningekuwa nishakufa. Nisamehe Pam.”

“Na usifikiri labda nakuomba msamaha sasahivi sababu ya Mill yupo! Hapana. Sikuwa na huo uwezo kiakili wala mali. Mike alikufa nikajua ndugu zake wamemficha, nikawa na kazi ya kumtafuta mpaka kurukwa na akili.”

“Anapokwambia kurukwa na akili si kidogo! Mimi nilikutana na Kamila aliyekuwa kama kichaa kabisa. Hajitambui alipo wala siku au tarehe. Wazazi wangu na mimi ndio tulio msaidia mpaka kuelewa majira na tarehe, na kuweka mazingira ya kumfanya aamini kama kweli Mike alishaondoka hapa duniani muda mrefu sana. Na anaishi miaka ya mbele sio siku aliyomwacha Mike hospitalini. Kwamba miaka ilishapita tokea siku hiyo. Alipoteza miaka hapo katikati, yeye hana taarifa.”

“Tukafanya taratibu za kuonyesha picha za msiba wa Mike na kumpeleka kaburini na kuona kaburi, ndipo akaamini kama Mike hayupo duniani. Ndipo sasa akaweza kutulia hapa nyumbani maana alikuwa hana hata pakuishi, anamangamanga kama ndege.” Yakawa mageni kwa Pam.

Wakamsimulia mwanzo mpaka mwisho, kidogo Pam akaingiwa na huruma. “Na ukumbuke kipindi hicho hata Mill mwenyewe nilikuwa sijui alipo, maana mara ya mwisho nikiwa na akili zangu, uhai wa Mike, huyu Mill alikuwa amefungwa jela la Kisha. Anakuja kurudi Mill kwenye maisha yangu tena, ndio nimepokelewa hapa, yaani mimi na yeye ndio tunatafuta kutulia, tunaanza upya maisha.”

“Halafu imekuwa kama nina mkosi! Ndoa yangu na Colins nayo wale kituo cha yatima waliokuwa wakinitunza tokea wameniokota, nao walimfungulia mashitaka Colins, wakimtuhumu alinichukua nikiwa chini ya miaka 18, akanifungia kama mke. Asiniendeleze.” Pam akashituka.

“Ilikuwa kesi kwelikweli mpaka Mill alipokuja na kutoa ushahidi kuwa aliyekuwa na mimi si Colins, ila Mike. Baba hapa amekubali kulipa faini kwenye kile kituo cha kulelea yatima na kulipa mahari kabisa, ndio kama tupo kwenye makubaliano, wafute kesi na kutoa vipingamizi kanisani, pengine ndoa ifungwe. Usinichukie Pam. Mill ndio amesababisha yote. Ametuponza mimi na Mike, ila bora mwenzangu Mike hayupo. Ni Mill, usinichukie mimi.” “Kamila!” Mill akashangaa sana hakutegemea umaliziaji ule. Angalau wote wakacheka.

“Ila jua sikuwa na nia ya kuingia katikati yenu na kuchukua nafasi ya hata mmoja wenu.” “Nakwambia sio wewe Pam, Mill huyo! Alifanya ikawa kama tishio! Pam akageuka kuwa gumzo, watu hatunywi maji! Yeye huyu ndiye aliyetuingizia hofu na wivu. Halafu baadaye akaja kututuliza kuwa wewe mzuri sana. Kila mwanamme anakutaka wewe. Hutachukua muda mrefu, utaachana na sisi wote. Na yeye msamehe. Mungu alimpa kiboko yake!” “Kamila unanicheka?” Kamila akafanya wote wacheke maana na yeye mwenyewe alianza kucheka mbavu hana.

“Bwana Kisha alimkomesha Mill, mpaka mwili ukaisha! Kesi kwao haziishi! Mpo katikati ya usingizi, simu kwa Mike. Wamegombana. Nakwambia kwao hata kukitaka kununuliwa chumvi, ni kesi ya kuamuliwa na Mike. Alimnyoosha Mill, halafu kama haitoshi, akamuachia wale wanae.” Pam akashangaa sebule nzima inacheka, Mill anatingisha kichwa.

“Wale watoto!” Kila mtu akazidi kucheka. “Kuja kuletewa Shema, kila mtu akahema.” “Wewe tusamehe tu Pam. Mungu wako ashatulipiza. Alikopita huyo Mill ni kama mimi tu, hatuna tofauti.”

“Hii familia ya kina Kombo, imekuwa kama kituo cha yatima!” Wote wakacheka. “Kweli tena. Wametukuta mimi na Mill tuna tangatanga na dhambi zetu. Wakatupokea kama tulivyo, na kutupa familia.” “Nimeona jinsi walivyo na upendo. Nawashukuru na kumpokea Shema wangu. Ananiambia huwa mnakwenda mpaka shuleni kwao, wakihitajika bibi na babu.” “Mwanao huyo anapendeka. Hana shida. Amejawa shukurani, nakwambia Komba akiambiwa safari za Shema, anaihirisha kila kitu ilimradi awepo tu.” “Mtoto mwenyewe anatia sifa kujulikana unahusika naye! Unafika shuleni unajazwa sifa, sasa kwa nini usiende!” Akajibu mzee Komba kwa mkewe.

“Huyu mtoto umelea vizuri Pam. Wewe na mama yako! Hakika mmeweka msingi mzuri sana.” Wakacheka wakimwangalia huyo Shema. “Basi hilo ni deni la kwenda kucheza mpira baadaye mpaka kuchwe. Utasikia hata bibi amenisifia mimi mtoto mzuri, niache tu nikacheze mpira.” Mama yake akafanya wacheke.

“Mimi mtoto mzuri mama. Na nikicheza mpira siku hizi sichezi kupitiliza.” “Si nilisema mimi? Hilo lishakuwa deni.” Wote wakacheka. “Sisi furaha yetu ni mcheke kama hivi.” Mama Komba akaongeza.

“Sikiliza Pam, mwanangu. Nyinyi mlikutana ni kama kondoo bila mchungaji. Wote mkaishia kufanya mambo vile mnavyoona inafaa. Ndio maana kukosea kukawa kwingi. Huku kukutana tena ni neema ya pekee wanangu. Anzeni upya. Mkishikana nyinyi kama hivi Mill anavyofanya na Colins, hakika mtafurahia. Wanafanya mambo yao kimyakimya lakini mpaka yanashangaza! Wameinuana kiuchumi, kwa muda mfupi sana wapo mbali sana kimaendeleo. Lakini ni kwa sababu wanania mamoja na kubebana. Umoja unanguvu.” Akaendelea taratibu tu.

“Pole Pam mwanangu. Naomba jitahidi kusamehe ili tupate muda wa kumuomba Mungu pamoja pengine mambo ya kila mmoja wenu yatafunguka. Hawa nao waoane, watoke humu ndani.” “Mama unanifukuza!!?” Colins akashangaa sana na kufanya wacheke.

“Umejaa sana humu ndani Colins bwana! Mashariti mengi kwa msichana wangu! Nenda tu kwako. Kwanza ni hapo mlango wa pili tu! Kwa nini hutulii kwako?” “Nipeni Kamila muone kama sitaondoka humu ndani.” “Huyu hatoki hapa bila ndoa takatifu kanisani.” Mzee Komba akadakia. “Basi naona na mimi hapa nipo sana tu.” Angalau mazungumzo yakabadilika. Pam akaona jinsi walivyojawa umoja na upendo.

Kamila akaonekana kama binti wa Komba kabisa. Mill kama kijana wao mkubwa. Wakawaongeza wao kama wanafamilia kabisa. Mipango anayoweka mama Komba anamjumuisha mama Eric kirahisi kabisa akimtaka ushauri. Mpaka wanaondoka hapo wote wapo ukurasa mmoja.

~~~~~~~~~~~~~~~~

Mwanzo mpya umefika – wa amani, wa kujithamini, na wa kupenda tena bila hofu. Ni safari ya kujijenga upya, kama vile mto unaotafuta njia baada ya kuta kuvunjika. Huu ni mwanzo si tu wa maisha mapya, bali ya nafsi iliyozaliwa upya.

Kwa Pius&Raza je?


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment