Pius naye
akapandwa mashetani akaanza kupiga yowe na kujitupa kama Polla. Poliny analia
sana kwa hofu. Nyange akaendelea kukemea, ya Polla tena yakapanda,
yanadai vitu. Nyange akayakatalia na kuwaambia watoke kimyakimya, na yawaache
wote huru. Akiwa peke yake, maana hapo ndio hali ilikuwa mbaya zaidi. Mama
Ruhinda analia akihisi Pius anaweza kufa, kila mtu akazidi kukaa mbali. Bora
Polla alikuwa mtoto na baba yake alijikaza akitoa vitu asijuimize. Safari hii
ni wote wawili. Hakuna aliyetaka kuwa karibu nao ila Nyange ndio alionyesha
ujasiri.
Akayakemea, wala
haikuchukua muda, Pius na binti yake wakaachwa huru. Pius anarudiwa na
akili zake, yupo sakafuni. Haelewi alifikaje pale. Nyange akamsaidia kusimama.
Akamueleza kilichotokea. “Na Polla?” “Yupo huru. Lakini lazima kuzungumza naye
ili akubali kuachilia hivi vitu na tuchome moto.” Ndipo wakakaa sasa.
Pius akaeleza mwanzo
kuanzia pale alipowasilimulia mwanzoni kwenye pochi, mpaka kwa mganga
walipoachana ila kwa sitara ili wanae wasiumie zaidi na hakuzungumzia
juu ya mahusiano ya mkewe ya nje. Poliny ni kama alijua tu mambo ya mama yake.
Hakushituka.
“Sasa, sasahivi mama
yuko wapi?” Poliny akauliza swali lililomfanya Pius asite. “Maana nimemtafuta
kweli huyo Raza mpaka nikaingiwa wasiwasi. Nimekwenda kwanu, nimeambiwa wote
hampo. Mpo hapa na hakuna mtu kuingia ndani. Ndio nikasema nije nijue
kulikoni.” Mama yake akaongeza.
“Raza amepelekwa
jela.” Hapo ndipo wakashituka. “Ameshitakiwa kwa kosa la kukusudia kutaka kuua. Hawezi toka.” Bwana watoto wa Raza walilia. Wote wawili kama msiba.
Polla anamtaka mama yake au apelekwe na yeye huko polisi akakae na mama
yake. Poliny amepiga magoti wamsamehe mama yake. Atolewe. Huyo Polla ya
uchawi alishaelewa. Hataki tena hata begi. Ila anamtaka mama
yake. Watoto walilia hao. Hawasikii la mtu. Hapo ndipo Pius alipoelewa madhara
ya kilichotokea kwa mkewe. Ila afanye nini? Raza ameshitakiwa. Kila mtu
kimya.
Mama Ni Mama Tu.
Wanasema mtoto
wa mwenzio mtamu akiwa amelala. Wakamuona Poliny anapiga simu, lakini bado analia
sana. Hawakujua anampigia nani. Ikawa imepokelewa huko.
Wakamuona
anapiga magoti. “Nimepiga magoti, naomba msamehe mama yangu. Nakuahidi hatarudia
tena.” Mtoto alilia huyo kwenye simu kama amechinjwa
na si Poliny wanao mjua wao.
Huyo mtoto alikuwa
mbishi kwa mama yake kutwa wanabishana kwa hili na lile. Hata Pius hakutegemea alie
hivyo baada ya kusikia yaliyompata mama yake. Kesi zake na mama yake ilikuwa ni
kila leo kwa Pius. Na mara nyingi alizira kurudi nyumbani na kubakia hosteli
sababu ya kugombana na mama yake.
Lakini usiku
huo, ungejua alibebwa na tumbo la Raza miezi 9. Yale mapenzi kwa mama yake
yalikuwa dhahiri hataki baya limpate mama yake. “Tusaidie
mimi na Polla. Msamehe mama, anti Mina.” Pius aliposikia
hivyo akashituka sana. Akataka kumpokonya simu, baba yake akamkataza. “Mwache.”
“Tutazidi kuingia matatizoni baba!” “Yeye ndiye aliyempigia anti yake.
Sio wewe. Mwache.” Poliny akazidi kulia.
“Tumeombewa wote. Tumepona. Na mama
ataombewa, atapona. Msamehe mama yangu. Usimfunge, hatamdhuru tena Ayvin.
Msamehe mama yetu, anti Mina. Polla hataweza kufanya kitu, bila mama. Shule
itamshinda kabisa. Leo ameshindwa kulala na kusoma sababu mama hajarudi
nyumbani, na kesho anamtihani. Msamehe mama.” Mtoto
alilia huyo akisaidiwa na mdogo wake kama msibani. Nyumba yote simanzi.
“Naomba kuzungumza na baba yako
Poliny.” Poliny
akampa simu baba yake. Pius akapokea na kuweka spika wote wasikie. “Mina, nipo na wazazi, Paul, Paulina, Davi na mama yake
Raza pamoja na Nyange aliyekuja kutuombea. Nimeweka spika. Nakuapia na
Mungu wangu ni shahidi na hawa watanitetea, huyu mtoto amekupigia simu, mimi
sijamtuma. Tafadhali mwambie Andy asije kasirika.” “Nipo hapa Pius. Aisee
poleni sana.” Kwa kuchanganyikiwa
na paniki akawa hajaelewa, hiyo ‘pole’
ya Andy ikawashangaza wengine. Hawakutegemea.
“Naahidi hawatasumbua tena. Nitazungumza
nao.” “Hapana Pius. Hao watoto ni wadogo sana. Hutaweza kuwakuza bila mama yao.
Mina hana hofu na hayo mambo ya kichawi. Na tumezungumza kwa kina baada
ya kupewa taarifa za kufungwa kwa Raza.” Pius akaendelea
kusikiliza.
“Hivi tulipanga kumtafuta Sonia
asubuhi nakumwambia tunafuta hiyo kesi. Raza ni mama Ruhinda. Kumfunga
yeye ni kujidhalilisha sisi wote akiwepo mama aliyehangaika kujijenga
sana hapo nchini na anaaminiwa na kuheshimiwa na wanawake wakubwa sana
hapa nchini. Itakuwa tunamdhalilisha mama zaidi na kutesa watoto wake wasio
hatia. Si sawa. Sisi tupo tayari kumaliza hayo mambo kifamilia si mahakamani. Kwanza
Mina mwenyewe anaona hakuna kesi hapo, kwa sababu anasema hata huyo
mganga asingeweza muua Ayvin. Anaona hamna kesi.” Mpaka Pius akalia. Bwana alilia Pius. Mpaka baba yake akachukua simu. Mama
Ruhinda mwenyewe hakuamini.
“Nakushukuru sana Andy. Asante.
Kibinafsi nakushukuruni sana. Mwambie Mina natoa shukurani zangu toka moyoni, asante.”
“Hapana baba, tumefika mbali sana. Nafikiri ni wakati wa kuweka kikomo kwenye
haya mambo. Lasivyo hapatakuwa na mwisho.” “Ni kweli Andy. Kweli kabisa. Ila
nawaahidi mimi mwenyewe nitazungumza na Raza, naahidi hatarudia tena.” Mzee Ruhinda akaendelea.
“Raza anamtoto anayemtegemea sana.
Ndio tumekuja kugundua leo, kumbe maisha ya huyu mtoto yanamtegemea mama yake
kwa asilimia 100! Sidhani kama kweli atakuwa tayari kurudia kosa na kuacha
binti yake alelewe bila yeye. Asanteni sana.” “Hamna shida baba. Nyinyi muwe na
usiku mwema. Kesho tutawasiliana na Sonia. Tumalize hayo mambo. Sasahivi
imeshakuwa usiku, naona tusimsumbue.”
“Sonia si wakulala sasahivi. Hivi
anasubiri nimpe maendeleo ya hapa baada ya maombi. Naweza kumwambia awapigie
sasahivi. Akisikia kutoka kwenu, anaweza mtoa Raza.” Nyange akaingilia mazungumza yao. “Sio mpaka asubuhi!” Mzee Ruhinda
akauliza kwa kushangaa. “Sonia ataweza wasaidia. Au niseme nilazima atatoa
msaada. Huyu mtoto hawezi kulala na kilio hivi.” Polla bado alikuwa akilia.
“Eti Andy?” “Hamna shida baba. Sisi
tulishakubali haya mambo yaishe ila tulidhani hatakuwa na uwezo wa
kufanya chochote usiku huu.” “Huyo Sonia anafahamika pale polisi kama ni moja
ya ofisi yake. Baba yake na bibi pamoja na babu yake waliacha jina zuri sana
hapa nchini.” Nyange
akaendelea.
“Na bibi yake yupo nyuma yake
kwenye kila hatua ya maisha yake. Hakuna sehemu akienda na jina lake hilo la
Tambo, milango isifunguliwe. Hana cha usiku wala mchana. Anaweza fanya mambo
mpaka akawashangaza. Kichwa kizuri cha sheria kama baba yake.” “Na kweli baba
yake alikuwa jaji mzuri sana.” “Basi ndio Sonia. Akili kama baba yake. Mwenyewe
jaji Mkuu huwa anasema ni mwanasheria mmoja tu hapa nchini, anaweza mfunga.” “Sonia?” Mzee Ruhinda akauliza na kufanya angalau wacheke.
Nyange kwa asili
ni mtundu na maneno mengi. “Anasema ni binti yake tu, ndiye anayemshinda
kwa hoja na si mwingine. Kwa hiyo Andy, ni wewe tu.” “Kama nilivyotangulia
kusema, sisi hatuna shida. Akitupigia,
tutazungumza naye.” “Basi acha nikazungumze na Sonia.” Nyange akatoka. Andy akaaga. Nakukata.
~~~~~~~~~~~~~~
Baada ya muda Nyange
akarudi. “Anawapigia kina Mina. Ila ameniambia niwaambie mjue na yule mganga
wake ataachiwa, maana hatakuwa na kesi ya kumshikilia.” Pius akabaki
ameinama. “Na akiachiliwa yule, inamaana yupo huru kuendelea kuharibu
familia nyingine.” Wote kimya.
“Naomba muombe
Sonia amwachie kwa onyo. Kama kumtisha tu, ili Raza arudi kwa watoto
wake. Tafadhali Nyange. Najua ni hatari. Lakini kwa kushikiliwa yeye, na
kuwekwa ndani itakuwa ameingiwa hofu.” Mzee Ruhinda akatoa ombi. “Au yeye
anaweza akamshikilia hata kwa muda kidogo ndipo akamuachia.” Nyange mwenyewe
akatoa wazo na kutoka kwenda kuzungumza tena na Sonia.
Alikaa huko nje
kwa muda wa kutosha tu. Poliny akaenda kumkumbatia mdogo wake akimbembeleza,
yeye mwenyewe akilia taratibu. Akarudi. “Sasa naona kila kitu kimekaa sawa.
Nimemwambia Sonia mimi ndio nitaenda kumchukua Raza, familia yake ikiwa kwenye
gari ya mumewe ili njiani tukiwa tunakwenda kwake nipate muda naye, tuzungumze
kabla hatujafika kwake na kufanya maombi.”
Pius nusu apige
goti akishukuru jinsi Nyange alivyojitoa kwao. Ilibidi Poliny aache gari hapo,
aongozane na baba yake pamoja na Polla, kituo cha polisi kumtoa mama yao. Bado
alikuwa akilia. Nyange aliomba mama yake Raza, awaache kwa usiku huo, wasiongozane.
Wote wakaelewa. Akaondoka na dereva aliyemleta, maana mama huyo hakuwa
akiendesha usiku. Na wao safari ya kuelekea kituo cha polisi, ikaanza.
~~~~~~~~~~~~~~
Walifika kwenye
kituo cha polisi ambako bado Raza alikuwa hapo akisubiria kupambazuke, apelekwe
jela. Alishangaa sana kukutana na Nyange. “Mimi naitwa Nyange. Nimeongozana na
familia yako.” Raza akabaki na mshangao. “Nitakuchukua kukurudisha nyumbani.
Tutakuwa na wewe njiani, ili tunzungumze kabla hujakutana na binti zako.”
Akakubali akiwa amepoa sana ila hailewi kinacho endelea.
Wakaondoka.
“Nimetoka kuomba na familia yako.” Nyange akaanza. “Unajua madhara
ya vitu unavyofunga kwenye begi ya Polla, binti anayekuangalia wewe kama
mfano wa kuigwa?” Nyange akaendelea kuzungumza naye taratibu tu. Kimya. “Una binti
wazuri sana Raza. Lakini njia unazoendea, unawadhuru binti zako wewe
mwenyewe. Kinga au msaada unaotafuta kwa nia nzuri kwa binti zako, matokeo yake
ni ya muda tu, na huishia kuwadhuru wao wenyewe, hata wewe. Shetani hana
zawadi ya bure Raza, mimi ni shahidi wa haya. Mwisho wake ni fedheha.”
Nyange akamsimulia historia yake.
“Dhambi yangu
mimi, iliangamiza familia nzima. Mwanya mdogo niliomfungulia shetani,
alitumia kudhuru familia yangu. Kwa wakati ule sikuona madhara yake,
lakini niliharibu familia vibaya sana. Shemeji niliyekuwa nikiiba naye penzi la
kwa siri, alifika umbali mbaya sana. Kwanza kwa mshituko wa kujua wizi
niliokuwa nikifanya na mdogo wake, mke wangu alipoteza mtoto niliyekuwa
nikimsubiria kwa hamu sana.”
“Haikuishia
hapo, yule shemeji alianza kuloga ili kunimiliki sasa, baada ya kuona dada yake
amenisamehe na tunaendelea. Ukweli alifanikiwa kunipata, ila kwa garama kubwa
sana. Hivi analipa mpaka leo. Ninachotaka kukwambia, ni kwamba, unaweza ukawa
na sababu nzuri sana za kueleweka kufanya unachofanya, na shetani
akakufanikishia kwa muda, lakini mwisho wake ni kama huu.”
“Binti yako
alikuwa amefungwa na nguvu za giza, nisingewahi angeweza hata kufa!
Mumeo mwenyewe ulimfunga, alikuwa amefungwa na nguvu za giza. Jiangalie wewe
mwenyewe ulipokuwa! Ni fedheha Raza. Umesumbua familia yako bure!
Niambie umepata faida gani?” “Wala havina faida ila mateso tu.” Nyange hakutegemea.
“Nimepata muda pale mahabusu,
nikawa nikihesabu faida, ni mateso kaka yangu, wala sitakudanganya. Nihivyo
sijui chakufanya tena.” “Ulipofika si mbali. Mungu aliupenda
ulimwengu hata akamtoa mwanae wa pekee Yesu kristo. Kwa kila amuaminie,
asipotee bali awe na uzima wa milele. Yesu anaita wote wasumbukao na
mizigo, kwa ahadi yakupata pumziko. Ameahidi kusamehe dhambi zetu zote
na ahadi ya kutokukumbuka kabisa.” Nyange alizungumza naye taratibu kwa
upendo huku akielekea nyumbani kwao.
Mpaka wanafika
kwake, yaani Raza mwenyewe ndiye anayetoa mauchawi akimuomba Nyange amsaidie kuyachoma
na amuombee. Pius na watoto wake walibaki na hofu wakiangalia vitu
anavyokusanya Raza na kuviweka hapo sebuleni. Nyange alikuwa ametulia tu
akisubiria amalize.
Alizunguka
kwenye hiyo nyumba, kila kona akitoa mauchawi aliyokuwa ameficha. Jumba hilo
lilikuwa limewekwa hirizi na nyingine amechimbia nje. Pius alikuwa haamini. Mzee
Ruhinda akafika hapo na mkewe wakakuta ndio Raza anakusanya vitu.
“Raza!” Pius
akashangaa sana wakati akimwaga vya nje hapo sebuleni. “Nimekosa Pius.
Na nakubali kudhalilika mbele ya wanangu na wakwe zangu ili uone nimekusudia
kuacha maisha mabaya. Si ningenyamazia tu dawa nyingine?” “Tafadhali muache
amalize kutoa kila kitu. Hiki anachokifanya ni muhimu sana kwenye hatua ya
kukombolewa. Mwache tu.” Raza akakusanya kila kitu, Nyange akachoma moto ndipo
akaanza kumuombea sasa Raza. Ilikuwa shuguli mpaka watoto wake wenyewe
walikimbia. Mpaka Polla aliyekuwa akimtaka mama yake alikimbia.
Akabaki Pius na
wazazi wake wakitetemeka wakati Nyange akiomba. Hayo majini yalidai hiki na
kile ili yaondoke, lakini Nyange aliwakatalia na kuwaamuru yaondoke na kumuacha
Raza huru. Mwishoe karibu panapambazuka, ndipo yakatoka na Raza kuwekwa huru. Akawaita
wote sasa kama familia. Akazungumza nao sana. Kisha akawaombea baraka na kutoka
na Pius kuzungumza naye.
Kwa Pius.
Akamueleza
makosa aliyomfanyia mama Briana, mkewe. “Ninapokwambia naishi nikiwa na deni
mbele za Mungu na mke wangu, jua ni deni ambalo Mungu akiniita popote akitaka
nikatumike kama hivi, nashindwa kukataa. Mungu alinisamehe na kuniponya
nikiwa na hali mbaya mno. Mke wangu alinisamehe kabisa pamoja na
watoto.”
“Baraka
alizokuja kunirejeshea Mungu, ni zaidi ya mwanzo nilizopoteza kwa upumbavu
wangu. Najua ni ngumu. Lakini Pius, Raza ni mke wa ndoa takatifu. Hizi
ndio zile katika shida na raha zenyewe tulizo apiana.
Tafuta jinsi ya kusamehe, ili kuweka hii familia pamoja. Hii nyumba
haina madudu tena. Ila haimaanishi hayawezi kurudi! Yakifunguliwa
mlango kwa namna yeyote ile, yanarudi.”
“Tena bibilia
inasema hali ya mtu yule inakuwa mbaya kuliko mwanzo. Maana yanakwenda kuitana
zaidi. Ishi maisha matakatifu wewe na mkeo. Nyumba yenu muigeuze nyumba
ya sala. Akazungumza na Pius akionekana kabisa upo ugumu mpaka usoni. “Raza
tena!” Akaendelea kujiuliza huku akimsikiliza Nyange. Lakini Nyange
alizungumza naye tu akielewa ugumu anaopambana nao moyoni. Mwishoe akaaga na
kuondoka.
Maisha Yashachukua
Sura Mpya.
Kurudi ndani,
akamkuta Polla amelala mapajani kwa mama yake. “Naweza kumuomba mama nikakae
kwake kwa muda Pius.” Akaongea kwa kunyenyekea kama anayemsihi amsamehe. “Hivi
unajua aliyesaidia kutoka kwako ni huyo mtoto hapo?” “Na kweli Raza! Mwanao
huyo amelia, akikutafuta kuanzia muda aliojua unatakiwa kurudi nyumbani
mpaka sasa. Amekutafuta kwa kila anayejua anakufahamu, kwa kilio na kutapika
usiku kuchwa.” Mama Ruhinda akaongeza na kumfanya alie sana.
“Sasa unapoaga
sasahivi ili akiamka aanze kulia tena?!” Pius akamuuliza kwa ukali kidogo.
“Kilio chake huyo ndio kimemfanya dada yake ampigie simu auntie yake usiku na
kulia kwa machozi akimsihi akusamehe, urudi nyumbani kwa ajili ya mdogo
wake na akikiri atazungumza na wewe USIRUDIE tena. Tafadhali
tulia Raza, ulee binti zako.”
“Hicho
unachohangaikia mbona ni kama umepata! Kwa nini unafundisha watoto njia
mbaya? Umejaliwa na Mungu watoto wenye akili nzuri na uwezo mzuri
sana darasani na wana vipaji vizuri tu. Kweli unafundisha watoto kuwa hawana
uwezo wa kufanya mambo au kufikiria mpaka hirizi!? Kweli Raza binti yangu?” Mzee Ruhinda akamuuliza kwa kuumia.
“Yaani unaondoa
ujasiri kwa binti yako, unataka aishi kwa kutegemea vimikoba vilivyotengenezwa
na mwanadamu ambaye yeye mwenyewe hana hata nusu ya ulicho nacho!” “Mimi
mwenyewe alinitisha eti nikimuacha, nitaharibikiwa! Kwamba
sijafika hapa nilipo kwa akili zangu, ila kwa nguvu zake yeye na huyo mganga wake.” “Haiwezekani!” Mama
Ruhinda akashangaa sana. “Si huyo hapo abishe. Tena kwa kunihakikishia eti
nikimfunga yeye, nitajuta.”
“Wewe Raza
hukumkuta Pius na kazi yake na nyumba hii alishakuwa anakaribia kumaliza?
Sijawahi peleka mtoto wangu kwa mganga wala sisi wenyewe hatuamini kwenye hayo
mambo, mbona wanangu wote wana maisha mazuri tu? Kwa nini unataka kumdanganya
mwenzio?” Mama Ruhinda akawa mkali kabisa.
“Ilikuwa njia ya kumfanya
asinifunge mama, nirudi kwa wanangu. Nimekosa jamani, na naahidi kubadilika.” “Aisee acha kabisa Raza. Unamtia majini mwanangu asie na hatia!
Unamtesa bila sababu wakati wewe ukiendelea na maisha yako huko nje! Muda mfupi
uliopita sisi tulijua tutampoteza kabisa huyu kwa jinsi alivyokuwa
akitupwa na madudu uliyokuwa umemuwekea! Anajipigiza kila mahali, kwa
sababu ya ubinafsi wako tu! Unataka mpaka kuua mtoto wa mwenzio!”
“Tena kwa kutekeleza mauuaji kwa kiumbe kisicho hatia! Kweli Raza?!”
Mzee Ruhinda akaongeza kwa mkewe.
“Huyo Pius kama
mpaka leo angekuwa akisubiria kurithi kutoka kwangu hata wewe mwenyewe
usingekuwa na maisha uliyo nayo! Sikuwajenga vijana wangu wakue wakisubiria
kurithi mali zangu, ila kujitegemea. Si huyo Pius na wenzie wamehangaika
wenyewe kwa akili zao mpaka wamefanikiwa tena kunipita hata mimi baba
yao! Kwa nini wewe unahangaika kufikiria kurithisha binti zako mali za
baba yao ambaye yupo hai, badala ya kuwafundisha kupambana wawe mbali kumzidi
baba yao? Unalinda mali hizi chake tu wakati binti zako wana akili nzuri sana!
Wafundishe, waamini kwamba wanaweza fanya makubwa kuliko wewe na baba yao ili
wasikae wakisubiria mali za baba yao!”
“Acha fikra
potovu Raza. Acha fikra za mauuji kwa kulinda mali ambazo hata hujui
Pius mwenyewe atakufa lini au hata akifa kama bado atakuwa nazo!” “Au na yeye
ulipanga kumuua?” Mama Ruhinda akamuuliza akiwa wazi anaonyesha hasira. “Hapana
wazazi wangu. Nampenda Pius. Nimefanya…” “Acha uongo.
Utaniudhi zaidi Raza. Kama kweli ungekuwa ukinipenda ungenifanyia yote haya?!
Unanilaza kwenye majini na kunifanya niwe dhaifu? Unaniulia
kijana wangu kwa sababu zako binafsi tu! Unamahusiano ya kudumu huko nje na
unarudi kwangu ukiniangalia vile ninavyohangaika bila hata huruma! Tafadhali
kama umekusudia kubadilika, na uongo uache.” “Nisamehe Pius. Nabadilika.”
Raza alizidi kulia.
“Na usisahau
kupiga simu kwa Mina, umuombe radhi kwa kumaanisha. Umenisikia Raza?”
“Nimesikia
baba.” “Muombe radhi. Muahidi kwa kumthibitishia
kwamba hutarudia tena. Kisha umshukuru yeye na mume wake. Walishapanga kufuta
kesi hata kabla ya mwanao kukuombea msamaha. Kisha pata muda wa kuzungumza na
binti zako. Futa kabisa hayo mafundisho machafu uliyopanda kichwani
mwao. Zaidi kwa Polla. Umeharibu kichwa cha binti yako, hajiamini yeye kama
yeye mpaka wewe, na hizo hirizi zako.” “Nitafanya hivyo baba yangu.”
“Aisee hapana Raza.
Hakika badilika. Na isiwahi jirudia tena akilini mwako kumtesa
tena Pius na wajukuu zangu. Iwe MWISHO. Sitakubali na jua nitakuwa
makini sana na wewe. Umesikia Raza?” “Ndio mama. Nakuahidi ninaacha.
Sitarudia tena hayo maisha.” Raza alikuwa
anakaribia kupiga magoti akiwa bado na mwanae.
“Msaidie huyo
akalale. Tutawaambia shule huo mtihani atafanya kesho. Leo hawezi kwenda shule.
Amelia sana na kujipigiza. Inabidi kumuangalia.” “Nashukuru.” Raza hakuamini kama ameruhusiwa kubaki pale.
~~~~~~~~~~~~~~
Akachukua binti
zake akilia. Akamsaidia Polla mpaka juu chumbani. Akamwambia wakati akioga, na
yeye anakwenda kuoga kisha kurudi kukaa naye mpaka alale. Akakubali. Raza
akaenda kuoga chumbani kwao akiwa amemuacha mumewe na wazazi wake hapo
sebuleni.
“Unajisikiaje?”
“Vizuri mama. Najisikia mwepesi kweli!” Hizo zikawa habari zilizomtuliza mama
Ruhinda. “Nawashukuru baba na mama. Niliwahitaji leo.” “Kapumzike Pius.
Tutazungumza baadaye mkiamka.” Wakaondoka.
Pius akabaki
ametulia hapo sebuleni hataki kurudi kulala kwenye kitanda chao. Kumbukumbu
ya vitu walivyochoma na vile yale mapepo yalivyokuwa yakipiga kelele kwa kila
mmoja aliyeshuhudia yakimtoka, na yeye kuambiwa hali yake ilikuwa hivyohivyo,
japokuwa aliambiwa aliombewa na yametoka hata hapo nyumbani
kwake, lakini bado alikuwa na hofu.
Hapohapo akamtumia
ujumbe mmoja wa wafanyakazi wake anayemtuma mara kwa mara na ni mwepesi,
anayajua maisha yao. Akamuagiza maduka yakifunguliwa, aletewe godoro jipya, ukubwa
kama lililopo hapo chumbani kwake, mashuka na mito mipya.
~~~~~~~~~~~~~~
Raza akatoka
kuoga, akaenda kulala chumbani kwa Polla. Na Poliny naye akawafuata. Wakalala
watatu hapo kitandani. Raza amelala chali binti zake wamemlalia kila mmoja
ubavuni akawakumbatia. Pius yeye akapitiwa na usingizi kwenye kochi vilevile na
nguo zake na viatu mpaka msichana wa kazi alipozidisha shuguli jikoni asubuhi
hiyo ndipo akaamka.
Hakumkuta Raza
chumbani, akaenda kumuangalia chumbani kwa Polla, akawakuta wote wamelala na
mama yao. Akaangalia kwa muda, akafunga mlango taratibu akarudi chumbani kwao.
Akaingia kuoga
na kutoka. Raza alikuwa ametoa matandiko yote kitandani. Akamuita kijana wao wa
kazi hapo ndani. Akamwambia atoe matandiko yote kabatini na hayo aliyotoa Raza,
mito na godoro. “Weka jalalani na choma moto.” Akahisi hajamsikia bosi wake
vizuri.
“Si kuna mafuta
ya taa stoo?” “Ndiyo.” “Mwagia. Hakikisha vinateketea isibakie hata kitambaa
kinachozagaa.” Kijana akaelewa. Kazi ya kutoa hapo ikaanza. Aliporidhika hakuna
kilichobakia hata foronya, kimebaki kitanda tu, akatulia akiangalia kile
kitanda. Kilikuwa kizuri sana cha ngozi. Thamani ya juu mno, tena alinunua huyohuyo
Raza.
Akaona haitoshi.
Akamuita tena atoe na hicho kitanda. “Na hiki choma moto.” “Nakiomba mimi bosi
wangu.” “Unanisikia?” “Sawa.” “Tena kaongeze mafuta ya taa, choma mpaka
kiteketee kabisa.” Kazi ya kukitoa ikaanza tena safari hii akimsaidia mpaka
jalalani na kuanza kukibomoa akitupa vipande jalalani. Kisha akamuacha akimwagia
mafuta ya taa. Ndipo akaridhika na kurudi sasa chumbani kwake.
Akajitupa kwenye
kochi la hapohapo chumbani. Alilala Pius, alikuja kuamka mchana wa saa saba,
hata kazini hakwenda. Ila alishatuma ujumbe kwa wenzie kuwataarifu anadharula
ya kifamilia, siku hiyo hatafika ofisini. Pius mwadilifu wa kazi. Hakosi kazini
hovyo, wakamuelewa.
~~~~~~~~~~~~~~
Raza ndiye
aliyemtoa usingizini wakati akiingia. “Sikukusudia kukuamsha.” Akamtizama
akigeuka. “Vipi Polla?” “Anaendelea vizuri. Nilikuwa namsaidia kusoma kwa
mtihani kesho. Ila nataka kwenda naye kumtafutia nguo za kuogelea.
Wanamashindano jumamosi.” “Wakati unamuandaa na mitihani ya shule, hakikisha
unamtoa ujinga uliomuingizia kwamba hawezi fanya kitu bila madudu
yak…” Akajirudi.
“Mfundishe kuwa
anao uwezo wa kufanya vizuri bila manjia ya ajabuajabu kama babu
yake alivyokwambia jana.” “Nimeshazungumza nao. Na nimewaleza njia nilizokuwa
nikitumia si sahihi kwanza wala hazikuwa na uwezo wa kuwasaidia. Ni
imani mbaya tu.” Hakumjibu.
“Poliny amesema
nikuage. Amerudi chuo. Anamtihani jioni.” Hapo akatoka kochini alipokuwa
amelala na kuanza kusaka simu yake. Akaipata ili ampigie simu binti yake. “Sitarudia
tena Pius. Na hata mambo mabaya ya nje naachana nayo kabisa. Hutamsikia
tena Chezo, wala mtu mwingine. Siweki tena namba ya siri kwenye simu yangu.
Muda na wakati wowote chukua angalia. Utathibitisha nimebadilika.” “Kwani
mwanzoni ulikuwa ukiacha jumbe zako na Chezo? Si ulikuwa unaweka dissapiring,
wewe? Hivi unajua ni pesa kiasi gani nimetumia kufufu hizo jumbe?”
“Nimekosa Pius.
Sitarudia tena.” “Unasema hivyo kwa sababu umekamatwa, lakini si kwa
sababu umekusudia kuacha umalaya wako. Acha kunifanya mimi mjinga. Hata
jana mlikuwa na miahadi ya kukutana! Inamaana mida ile kama nisingekuita mimi,
ungekuwa naye hotelini, mkifanya yenu, halafu mimi huku unanifanya hanisi,
joka la kibisa. Mkatili usiye hata na chembe ya huruma.” Akazidi kuwaka
kwa uchungu.
“Ulikuwa na mimi
humu ndani ukinisanifu tu usiku, halafu wewe unaenda kukatwa kiu
zako huko, mchana kutwa. Halafu sasahivi unasema nini?!” Hasira zilikuwa
zimempanda Pius, anamtizama kwa jicho baya, Raza kimya akishindwa hata
kumtizama mumewe.
Akamtizama kwa sekunde kadhaa na kurudisha
macho kwenye simu. Akampigia binti yake na kutoka hapo chumbani kabisa.
~~~~~~~~~~~~~~
“Ulipata muda wa kupumzika kweli
wewe?” Akamsikia akimuuliza binti yake. “Inatosha
dad. Nataka nijisomee tena kidogo kabla ya mtihani.” “Umekula sasa?” “Nitakuwa
sawa, usiwe na wasiwasi.” “Kula lazima. Kula ndio usome.” Akamsikia ametulia kabisa wakatia akizungumza na binti yake. Alimjua
jinsi anavyompenda Poliny. Akaenda kwa Polla.
~~~~~~~~~~~~~~
Akamkuta
ametulia chumbani kwake, anasoma. “Vipi kichwa?” “Mama amenipa dawa. Njoo ukae
hapa na mimi.” Pius akacheka na kwenda kukaa pembeni yake, kitandani. “Niambie
unasoma nini.” “Ila sio uanze kunifundisha au kuniuliza maswali. Wewe na Poliny
wakali.” Pius akaanza kucheka tena.
“Kwanza mama
ashanisaidia.” “Polla kwa wasiwasi!” “Wewe hapo hukawii kuanza kunigombesha.
Unataka niwe kama Poliny, kuelewa kwa harakaharaka.” “Kwa kuwa akili zako muda
wote zipo kwenye game zako hizo ndio maana nataka urudishe akili kwenye
masomo.” “Mbona mama yeye ananichukulia taratibu mpaka naelewa?” “Basi
namuachia mama yako. Ila wakati anaenda kukununulia nguo za kuogelea na mimi
nakuja, ili nipaone.” Alifurahi huyo Polla. Akaanza stori kwa baba yake
akimtajia rangi anazotaka. Wakabaki hapo wakizungumza akafurahia akiona
ametulia. Yeye shida yake mama yake awepo.
~~~~~~~~~~~~~
Je, Maisha Ya
Pius&Raza Yatakuaje Baada Ya Wanandoa Hawa Kufikishana
Umbali
Huo Wa Kuumizana Na Majanga Waliyofanyiana Wote Wawili Huku Wakiwa Na Watoto Wanao
Wategemea Na Kuwaangalia Kwa Karibu, LAKINI WOTE WAMESHAOMBEWA NAKUTOLEWA
MAPEPO?
LAKINI Bado
Mioyo yao imebeba kumbukumbu mbaya na majeraha bado ni mabichi kabisa, japo AHADI YA MUNGU IMESIMAMA PALEPALE. Waebrania 8:12, Yer 31:34b{Mungu
amesamehe kwa ahadi ya kutokukumbuka dhambi zao daima.}
Ni Nini
Kitaendelea Kwa Love At First Time?
Mina&Andy! {Wakiwa na mtoto wa Pius?}
Mill&Pam! {Kwenye Mwanzo Mpya wa Maisha, Mill akiwa na familia mpya yenye
Kamila ambaye Pam bado hajamalizana naye? Na Familia waliyoachiwa
wawili hao na marehemu Mzee Mgini? Maisha Marekani au Tanzania? Safari hii watafanikiwa Ndoa Takatifu?}
Inaendelea….
0 Comments:
Post a Comment