Sonia
alimfikisha Raza na Katibu polisi. Akawashitaki ramsi. Wakawekwa ndani
ndipo akatoka sasa kumpigia simu Mina. “Unanafasi tuzungumze?” “Nalisha
timu yangu hapa. Nimeloa uji mwili mzima, Ayvin anakazi ya kutema tu hamezi, na
kilio juu!” Sonia akacheka. “Mpaka
nahisi tutarudishana kwenye kunyonya tu. Sioni dalili hapa.” “Basi atanyonya
huyo mpaka kwa mkewe.” Mina alicheka sana.
“Unafikiri nakutania! Wewe
muendekeze tu. Na ujue anakusoma na kukupima. Anataka kujua utaishia wapi.
Ukimrudisha tu kwenye nyonyo, jua mchezo ni huohuo.” “Acha kunitisha bwana!”
“Utakuja niambia. Watoto wanaakili kutuzidi sisi. Atatema hapo na kulia, utamuhurumia,
kumbe mwenzio anakupima tu. Ukiyumba tu, basi ujue amekuweza. Wewe nenda
naye taratibu bila ya kukata tamaa. Kidogo kidogo mpaka ajue hiyo nayo ni njia anayotakiwa
kuishi kuanzia sasa. Usiache. Endelea hapohapo. Maana itakuja na kumuachisha
diaper.”
“Mchezo utakuwa huohuo. Hataki poti
anataka diaper tu. Sasa shule ataendaje na diaper?” “Na kweli! Acha nipambane
naye hivyohivyo. Kwema?” “Wewe maliza kulisha wanao, tuzungumze kwa utulivu.
Kwako kuna fujo bwana.” Mina akacheka. “Na
usifikiri fujo hii ni ya wengi. Mtoto mmoja tu kama jeshi!” Sonia hana mbavu. “Nitakupigia dada yangu acha mimi nipambane
naye.” Wakaagana.
~~~~~~~~~~~~~~
Baada ya kama
masaa mawili, akampigia. “Nipo na Andy. Nimekuweka kwenye spika.” Mina akamuwahi. “Au hutaki?” “Ni wewe tu. Kama umeridhia ni sawa. Ila nina
ujumbe kutoka kwa Pius.” Mina akamuangalia mumewe.
“Ni ujumbe gani?” Andy akauliza. “Kwanza yeye ndiye aliyenifuata. Amekuja ofisini kwangu na
ushahidi, kile anachokifanya Raza kwake, wewe Mina na mtoto. Akaniomba yeye
ndio achukue hatua, sio kumtisha Raza, maana nikwambie tu ukweli Mina, Raza
amefika mbali.” “Unamaanisha nini?” Ndipo sasa
Sonia akamueleza Mina kuanzia mwanzo mpaka mwisho.
Andy alishituka
sana ila si Mina. “Mimi siogopi dada. Hata aende kwa shetani mwenyewe, hakuna wakugusa
wanangu. Nina uhakika na Yesu ninaye muomba. Hajawahi kuniangusha. Mimi uchawi
wake siogopi kabisa.” Mina akazungumza kwa kujiamini.
“Nimefurahi kukusikia hivyo Mina,
lakini yeye Pius ameingiwa hofu SANA. Kupita nitakavyokueleza. Ameomba
nikwambie kwa sasa hata yeye hajiamini na Ayvin. Anagopa majitu
aliyotupiwa yasije mdhuru mtoto wake. Amenituma nikwambie, anampenda sana mtoto
wake, lakini hataonekana huko kwa muda mpaka aombewe na kuwekwa huru.” “Hapo
atakuwa amefanya jambo la maana. Bila Mungu, ajue atatwanga maji kwenye kinu.” Andy kimya kwenye mshituko.
“Hata mimi kwa hilo nampongeza. Ila
kwa hakika ameingiwa hofu na anajutia sana. Anajiuliza bila jibu, hajui
amepatwa na nini kiasi cha kufanya aliyokuwa akiyafanya kama mwehu. Ameomba
yeye ndio ashugulike na Raza. Yeye ndio amshitaki, wewe ukae pembeni. Ila
ametoa ombi kwako.” “Ombi gani?”
“Huko kwa mganga inavyoonekana walikushindwa.
Sasa anaomba hicho ulicho nacho umuombee na mwanae akipate ili wasije mdhuru.”
“Dada, nakuhakikishia. Na hata yeye mwambie atakayeua hawa wanangu ni Mungu
aliyewaumba wala si vinginevyo. Kama isingekuwa hivyo pengine huyo Raza
angemuua mwanangu tokea yupo tumboni. Hawana uwezo wa kuua wanangu.
Mwambie yeye ahangaike na huko kwake. Ila Ayvin anaulinzi wa kimungu.
Hakuna silaha itainuka kinyume naye ikafanikiwa.” “Mina!” Sonia akashangazwa na imani yake.
“Hakika dada. Mimi namjua Mungu wa
mama yangu. Ni hivyo tu ujana ulikuwa mwingi. Namjua kwa kumuona kwa mama. Na
nikwambie wazi kabisa, nilipopata habari za Raza tu, za ushirikina,
tokea nina Ayan, au alipojua nimezaa mtoto wa kiume wa kwanza mjuu kwa kina
Ruhinda, nikaambiwa nijiandae na Raza, haraka sana nilijua Yesu ndio
atakuwa msaada wangu. Ni ubinadamu tu, kwenye kuyumba. Lakini najua kwa
hakika tumaini langu lisiloyumba na haliongopi ni
YESU.”
“Mimi mwenyewe nilikuwa na madudu
hayohayo, mama yangu alihangaika na mimi mpaka nikapona na kuwekwa huru. Najua
nguvu ya msalaba. Najua ulinzi wa Kimungu. Kwa hiyo mwambie Pius, kwa hawa
watoto wangu, aondoe wasiwasi. Ayvin ataishi na atayashuhudia makuu ya Mungu.”
“Amina.” Sonia akaitika akicheka.
“Na swala lake la kutokuja
umeelewa?” “Nimeelewa dada. Hamna shida. Yeye atakapokuwa tayari, mwambie siku
zake ni zilezile na masharti ni yaleyale.” “Sawa. Kwa hiyo kuanzia leo, jua na
yeye ni mteja wangu, nitafanya naye kazi mpaka mwisho.” “Sawa. Na ninakushukuru
dada yangu. Wewe kweli ni wakuaminiwa.” Sonia akacheka
na kuwaaga.
Historia Ya Raza.
Raza alizaliwa
kwenye familia iliyokuwa imeshika dini sana. Yeye alikuwa mtoto wa nne kati ya
familia ya watoto watano. Ilikuwa ni familia ya swala zote bila kuzembea tokea
anaakili zake. Amekuzwa kwenye maadili ya dini. Watoto wakike walikuwa wawili
tu. Ila yeye tokea mdogo hata baba yake alishamuona alikuwa mtoto mdadisi
na mtaka zaidi.
Ndugu zake wote
hawakusoma kama Raza. Tena si kwa wazazi kukosa uwezo, ni wenyewe hawakupenda kuendelea
na shule. Kaka zake walioa mapema tu, wakajitupia kwenye biashara za baba yao hapo
jijini. Maana mzee wao alifanikiwa sana kibiashara. Alikuwa na maduka matatu.
Jumla na rejareja. Kariakoo na Msimbazi karibu na kwao. Kwa hiyo walipomaliza
tu shule zile za awali, kidato cha nne ambaye ni kaka mkubwa, wadogo zake hata
hawakumaliza kidato cha nne, wote wakajiunga na baba yao na wakawa wakifanya tu
vizuri.
Mdogo wake Raza ambaye anamfuata, wakike, na
yeye alishika dini si kama Raza. Alipomaliza tu kidato cha nne, aliolewa na
kuanzisha familia, akatulia kwenye ndoa yake. Ukiwatizama ndugu wa Raza na Raza
mwenyewe, usingesema wanatoka nyumba moja na kulelewa na wazazi aina moja.
Usingemkuta Raza
na hijabu nje na nyumbani kwao tokea zamani hata kabla hajabadili dini. Alificha
kwenye mkoba na kuivaa akiwa anakaribia nyumbani kwao. Alifaulu shule nzuri,
hakutaka kwenda kusoma shule za dini. Na baba yake alikuwa akimuunga mkono
kwenye kila hatua ya elimu anayofikia. Na ndugu zake wengine walisema baba yao
alikuwa mkali sana ila linapofika swala la Raza, analegeza kamba kabisa. Akawa kama
mtoto wa baba haswa.
Kwa asili Raza likuwa mpambanaji kwenye maisha
kupita ndugu zake wote. Kitu kilichomtofautisha na wenzie. Wakati wote alitaka zaidi
na kitu cha tofauti na anachojua wenzie wamefikia. Ilimsaidia kufanya vizuri
kwenye kila kitu kwa sababu alijifunza kupambana.
Mambo yaliharibika
siku alipokwenda kusema nyumbani kwao kuwa anaolewa na Pius Ruhinda, ndoa ya
kanisani! Hakuna ndugu hata mmoja aliyetaka kumsikia tena. Hata mama yake mzazi
hakufika kwenye harusi yake, na baba yake alimfukuza kabisa nyumbani kwao. Raza
hakujali. Akabadili dini na kuolewa na Pius.
Hata baba yake
alipofariki, kaka zake hawakumpokea tena. Mdogo wake alikuwa mtulivu
mno. Mtu wa familia. Yeye aliolewa na mtu ambaye mshika dini kama kaka zake au
baba yake. Naye ametulia kama yeye. Wakajaliwa watoto wao, kimya. Akabaki akijiangalizia
maisha ya dada yake na kumuacha tu. Raza ni mtu ambaye akiamua jambo lake ni
ngumu kumbadilisha.
Mama yake
alikuja kurudi pichani miaka ya baadaye sana, hata Polla alikuwa ameshazaliwa. Ndio
yakawa mahusiano napo si ya karibu sana, kwa sababu ya misimamo ya Raza. Mama yake
akawa mtu wa kumwangalia tu na kunyamaza. Kwa hiyo Raza ndio akabakiwa na
familia hiyo ya Ruhinda tu, na wanae. Na ndugu zake upande wa mama kidogo tena
walimsogelea kwa kumuomba pesa wala si mahusiano ya undugu. Raza msomi, anakazi
nzuri na mume asiyeuliza mshahara. Kwa hiyo alikuwa na pesa wakati wote.
~~~~~~~~~~~~~~
Polla hakurudi
kusoma kama alivyomwambia baba yake. Akampigia tena simu mama yake, akamkosa na
kuamua kumpigia simu bibi yake, yaani mama yake Raza, kumuulizia kama amemsikia
mama yake.
“Mama yako sijamsikia leo, pengine
ametingwa.” “Ametingwa na nini?” Polla akamfanya
bibi yake atulie na kufiria maana alikuwa akimjibu tu. “We kwani
mara ya mwisho kuzungumza naye ilikuwa saa ngapi?” “Asubuhi wakati naenda
shule. Na aliniahidi leo atawahi kuja kusisaidia kujiandaa na mtihani asubuhi
halafu nina mashindano kesho kutwa.”
“Na mimi aliniambia kama naweza
nije. Ila jumamosi nina shuguli. Kuna mjukuu wa shoga yangu anachezwa,
na nimeshalipia. Sare pia ninayo tayari. Nimemwambia hivyo naona akanikasirikia,
sijamsikia tena.” “Labda kwa sababu kila siku unatoa sababu, bibi.” “Wala si
sababu. Yeye ananiambia mambo yake kwa kunishitukiza wakati na mimi ninakuwa
nishaweka mipango, nimeahidi watu. Siwezi kuwa kigeugeu.” Polla akanyamaza.
“Kwani baba yako amesemaje?”
“Ameniambia amesafiri wakati mama hasafiri.” “Mama yako si mtu wa safari.”
“Umeona bibi! Mimi ninazidi kuingiwa na wasiwasi. Nampigia auntie kumuulizia.” Huyo mtoto akakata simu kwa bibi yake akaendelea KUMSAKA mama yake. Uzazi
mzuri.
~~~~~~~~~~~~~~
Aliwaza mpaka
akashindwa ikabidi kuwapigia tena simu wazazi wake. Aliwaeleza kila kitu bila kificho,
kwa hakika waliingiwa na hofu. “Utafanyaje Pius?” “Ili asije dhuru mtu
mwingine, wao wawili hivi tunavyozungumza wameshapelekwa polisi. Lakini sijui
nifanyaje na Polla! Hivi ndio nimegundua maisha ya yule mtoto ni mama yake
kwenye kila kitu. Hapa tunapozungumza hajalala, na amekataa kuja hapo,
anamsubiria mama yake. Anamtihani kesho asubuhi, na ana mashindano jumamosi.”
“Na kweli Raza alituambia. Hivi tuliahidi kuhudhuria. Si unamjua Raza na hayo
mashindano!” Mzee Ruhinda akazungumza kama aliye mawazoni.
“Subiri kwanza Pius. Swala la Ayvin
ambalo wamesha tuma hayo majeshi?” Bibi mtu
akauliza kwa wasiwasi. “Hata sijui mama! Nimevurugikiwa! Sonia, yule mwanasheria wa
Mina ndiye na mimi namtumia. Nimeomba awasiliane na Mina, kwanza ajue hali ya
mtoto, na pili amwambie Mina ukweli kwa kile kilichotokea ili Mina amuombee
mtoto bila ya kuzembea. Inavyosemekana Mina anayo nguvu ya kimungu
ambayo eti hata walivyokuwa wakimuita huku kwa mganga wake wanashindwa.
Sasa mimi sijui hayo mambo mama. Ila kama wao wamemshindwa Mina, basi pengine
anacho kitu cha tofauti.”
“Nataka hicho alichonacho
Mina, kimsaidie na mwanangu mama. Nimeingiwa hofu kupita kiasi.” Wazazi wakabaki hawajui chakusema kwa hofu. “Ila kwa hakika
mimi na wanangu tunatakiwa kufanyiwa kitu ili kutoa yote ambayo Raza
ametuwekea.” “Kwa njia gani? Na wewe uende kwa mganga!?” “Huyo dada amenieleza
kisa kinachofanana na hiki changu. Ila anasema wao hao waligeuzwa mpaka vichaa
kabisa na wakasahauliana. Wakaja kuombewa. Sasa anasema atanipeleka kwao
wakaniombee na mimi. Amenionya nisiende kwa mganga.” Wazazi hao wa RC damu, wakabaki kimya, ila hofu.
“Nakuja mama.” “Sasa unakimbia
kwako?” Baba yake akamuwahi kabla hajakata simu. “Nataka
kutoa kila kitu kwenye ile nyumba mpaka wafanyakazi wake Raza nawafukuza.
Kusafishwe kabisa. Sitaki hata kijiko alichonunua Raza. Naanza upya.” Wazazi kimya.
“Maana kwa vitu tu vilivyotoka
kwenye pochi yake, najiuliza ni vingapi vimeachwa huko nyumbani? Naogopa hata
wazo la kufikiria kurudi pale.” “Pole sana Pius. Pole sana. Acha mimi nitoke
nikamnunulie vitu Polla. Utanikuta ukija.”
Poliny Kwa
Baba Yake.
Mara simu ya Poliny
ikawa inaingia. “Poliny ananipigia. Acha nimpokee nimwambie na yeye
aje ili nizungumze nao wote kwa pamoja.” Pius akawaaga
wazazi wake na kupokea simu ya binti yake. “Mama yuko wapi? Maana Polla
amenipigia simu analia mpaka ametapika baba. Anasema hampati mama kwa simu na
kila anayempigia simu, anamjibu hajamsikia mama leo. Analia sana. Hivi
nimemwambia dada amsaidie kuoga. Amejichafua, na bado analia. Wewe umezungumza
na mama leo?” Mara simu ya mama yake Raza nayo ikawa
inaingia kwenye simu yake. Ya Paul nayo ikawa inaingia, kisha Paulina. Akajua
huyo mtoto alipigia kila mtu anayemjua mama yake.
“Inabidi kuzungumza Poliny. Nenda
kamchukue Polla, uje naye kwa bibi, nitawaambia kila kitu. Lakini mama yenu
yupo mzima kabisa.” “Wapi?” Kimya. “Dad? mama
yuko wapi?” “Sio kwamba nimekwambia ukamchukue Polla nyumbani uje kwa bibi yako
nitazungumza na nyinyi?” Akamuuliza kwa ukali kidogo. Poliny alimjua baba yake. Yeye akakubali na kukata
simu.
~~~~~~~~~~~~~~
Bado alikuwa
mbali na nyumbani kwa wazazi wake. Akaendelea kukanyaga mafuta bila ya kujibu
simu yeyote ila ikitaka azungumze na binti zake kwanza kabla ya maneno kuzagaa
na kuwafikia.
Ilipoingia simu
ya Sonia, akapokea. “Nimezungumza na Nyange, amekubali kuja usiku huu. Ni mtu mzuri
sana. Anaelewa mnakopita. Jambo kama hilo huwa halazii damu. Amekubali. Nimempa
namba yako, nikikata tu, atakupigia.” “Nakushukuru sana Sonia.” Alipokata tu, Nyange naye akampigia. Akamueleza kwa kifupi, Nyange
akamwambia anatoka kwake kwenda kukutana nao huko nyumbani kwa wazazi wake.
Akamshukuru na kuendelea kukanyaga mafuta kuwahi.
Usiku Wa Hekaheka.
Ikawa kama
ameingia tu na binti zake. Anafika sebuleni na wenyewe ndio wanaingia hapo,
Poliny anamsalimia babu yake, Polla ametulia kama aliyekuwa akilia. “Mama bado
hajarudi?” Pius akamuuliza baba yake. “Nafikiri atakuwa anakaribia.” Pius
akakaa. “Njoo Polla mtoto mzuri.” Akamsogelea baba yake. “Usilie mtoto mzuri.”
Akamsaidia kufuta machozi. “Nilikwambia uache kila kitu nyumbani, mbona una huo
mkoba tena?” “Begi langu la shule, lina madaftari yangu.” “Nitakununulia
jingine. Hilo toa vitu ulitupe.” Polla akashangaa sana.
“Amenipa mama!”
“Ndio nakwambia tutanunua jingine.” “Mimi nataka hilihili dad! Kwa nini
ubadilishe? Kwanza lina ulinzi wangu.” Pius akawa hajaelewa.
“Ulinzi gani?” “Ameniwekea mama.” Hapo akashituka akikumbuka madudu yaliyotoka
kwenye pochi ya Raza.
“Ulinzi wa
nini?” Mzee Ruhinda akashituka. “Sijui lakini mama ameniambia nikiwa na hili
begi, na ulinzi wake, hakuna baya litanipata. Nitakuwa naelewa sana darasani na
hata kwenye mazoezi nitakuwa nafanya vizuri. Nitakuwa nawashinda wote.” “Sio
kweli Polla.” “Ni kweli. Na ndio maana nafanya vizuri. Mama yuko wapi?” Akalibeba begi lake vizuri na kusogea mbali kidogo na baba yake, Pius
naye akamwangalia baba yake na Poliny aliyekuwa akijaribu kumpigia tena simu
mama yake akiwa amesimama mbali kidogo na hapo.
“Ushawahi ona
huo ulinzi wenyewe?” Babu yake akamuuliza. “Amenifungia kwenye zipu ya ndani,
ile ndogo. Hamna haja ya kuitoa kila wakati. Naficha hata rafiki zangu
hawaoni.” Akazungumza akiweka sawa hilo begi lake la
shule huku akifuta machozi. “Umempata mama, Poliny?” “Sasa hivi hata simu yake haiiti.” Polla akaanza kulia tena. Poliny
akarudi kupiga tena.
“Naomba hilo begi.” Akasita kumpa baba yake.
“Kwani alikwambia hata mimi nisishike?” “Mama aliniambia nisimuonyeshe mtu,
lasivyo itakuwa haifanyi kazi.” “Sio kweli Polla.” “Ni kweli.
Mbona nilikuwa sifikishi ule muda niliokuwa nikitakiwa kumaliza kila siku
mazoezini. Kila siku nilikuwa nikijitahidi sifikii muda, nachelewa nakuwa
namaliza kuogelea muda sio ule niliotaka. Ndio mama akaniambia atanisaidia.
Akanisaidia, kuanzia wakati huo nikawa nakuwa wakwanza na hakuna mtu anaufikia
muda wangu. Naogelea kwa haraka na muda mfupi kwa round zote.” Pius akaumia sana.
“Basi nipe
nione.” Akakataa kabisa mpaka akahama kochi. “Ni nini tena? Mbona analia tena?”
Poliny akasogea pale. Kabla hawajamjibu dada yake, bibi yao naye akaingia.
Katika vitu alivyomnunulia ni pamoja na begi la shule.
“Haya, umeletewa
begi jipya, hamishia hapa madaftari yako.” “Nalitunza mpaka mama
anibadilishie. Mama yuko wapi?” “Mimi naweza kukuhamishia.”
Akamkatalia baba yake kabisa.
Hasira
zikampanda Pius, akampokonya kwa nguvu. Mtoto alilia huyo mpaka
akatapika tena. Anataka begi lake. Pius akalichukua kama lilivyo akaenda tupa
nje kabisa jalalani. Poliny akashangaa sana akiumia. “Kwa nini unafanya hivyo
dad, na yeye amekwambia ni begi alilopewa na mama!?” “Hilo begi limebeba madudu
matupu.” “Kuna madaftari yangu pia. Nataka begi langu.” Polla akazidi kulia kwa sauti na hasira ya ajabu.
“Mimi naenda
kumchukulia ili atulie mpaka mama atakapokuja.” “Usithubutu Poliny. Nakuonya.”
Hasira kwa mkewe na habari za hofu alizokuwa amebeba Pius, ilikuwa kama makaa
ya moto ndani ya kifuu cha nazi. Alikuwa akilipuka na kushindwa kujizuia kwa
binti wasio hatia. Yeye amewaka, Polla analia kwa uchungu. Anamuita mama yake.
Poliny akabaki akimtizama baba yake kwa kuumia. Kisha akamsogelea mdogo
wake akitaka kumtuliza, gafla akajirusha sakafuni.
Anatapatapa
akigaragara. Nyumba ilikuwa ndogo. Mtoto anatambaa sakafuni kama joka.
Ametoa macho kama anakata roho. Kina Ruhinda ni wakristo wasio na ugomvi na
Mungu wala shetani. Mambo ya kiroho kwa undani hawayajui.
Nyumba ikataharuki
hawajui chakufanya, ikabidi ampigie simu Nyange. “Kuna nini mbona kelele?”
“Tafadhali tusaidie.” Hapo Pius anakimbilia jalalani kuokota begi
amrudishie.
Poliny analia
haswa kila anavyomuona mdogo wake vile. Mzee Ruhinda alishampigia simu Paul
daktari wa familia, afike hapo kwa haraka kusaidia. Nyumba ikachangamka
kwelikweli! Msichana wa kazi alishakimbia kujifungia chumbani kwake. Pius akawa
anampa begi lakini ni kama Polla hana ufahamu tena.
~~~~~~~~~~~~~~
Hawakuwa na chakufanya mpaka Paul mwenyewe
alifika hapo akawa anaogopa kumshika! Wakabaki wote wanamkwepa maana
anahangaika sakafuni, Pius kilio huku akisaidia kusogeza meza na viti ili binti
yake asijiumize zaidi. Mara Paulina naye na mumewe wakafika hapo kwa haraka.
Hawajakaa sawa,
mama yake Raza naye akawasili hapo na dereva akiwa na wasiwasi. Maana Raza
hampati kwenye simu, na alipokwenda nyumbani kwao mlinzi alimkatalia
kuingia ndani akisema nyumba imefungwa, haruhusiwi mtu kuingi na hakuna
mtu ndani. Ndipo mama yake Raza akaamua kuwafuata kina mzee Ruhinda kuuliza
kulikoni maana na Pius naye hakuwa akipokea simu zake! Ndio akakutana na hiyo
hali ya mjukuu wake akijirusha sakafuni.
Ukweli aliogopesha.
Hakuna aliyeweza msaidia huyo mtoto mpaka Nyange alipoingia hapo. Aliikuta ile
hali pale mpaka akawahurumia.
Akamsogelea Polla.
Akakemea kwa dakika chache tu, mara Polla akatulia kimya sakafuni na
kuacha kugaragara akijipigiza sakafuni. Wote wakatulia wakimwangalia alipolala
pale sakafuni. “Ndio amepona?” “Bado.” Nyange akajibu akimtizama. “Labda tumpe
begi lake.” Nyange akawa hajaelewa. Ndipo Pius akamsimulia chanzo cha hilo begi
na mkasa wa pochi ya mama yake huyo Polla.
“Anasema ni
ulinzi wake.” “Ndio mambo nilikuwa nikigombana na mama hayo. Anataka kunipa mavitu
ya ajabu, eti yanisaidie chuo, nikamwambia mimi nina akili zangu.
Nitajitegemea. Nikishindwa nitaongeza juhudi kwenye kusoma lakini si mavitu
ya ajabu.” Poliny akaongeza akilia sana.
Nyange akaomba
apewe yeye hilo begi. Akalifungua na kumwaga vitu vyote chini, hakukuta kitu
zaidi ya vitu vyake vya shule. “Amesema vipo zipu ya ndani mama yake anamfungia
huko.” Mzee Ruhinda akasaidia. Ndipo Nyange akafungua zipu ya ndani. Akakuta
kama hirizi imefungwa vizuri na kushiliwa na pini. Si rahisi kudondoka au
kuonekana kwa urahisi. Akaitoa na kuogopesha wote.
“Naomba dada
yake au bibi yake amuangalie mwilini kama kuna kitu amevaa.” Mama Ruhinda
ameingiwa woga, hataki hata kusogea. Mama yake Raza yeye ndio ilikuwa mbaya
zaidi, kama ameona mzimu! Hataki hata kusogea alipo Polla. Pius akaanza
kumpapasa, ndipo Poliny naye akaanza kukagua sehemu zote alizokuwa akielekeza Nyange,
hapakuwa na kitu.
“Sasa aina hizi
za vitu vyote ni vya kuchoma. Na Sonia ameniambia kuna vingine vimewekwa
kwenye mto unao lalia?” Akamuuliza Pius. Akiwa amejawa hofu, anachohitaji ni
msaada wa haraka Pius ikabidi asimulie tena YOTE. Poliny akazidi kuogopa.
“Nilimuonya mimi
Raza, na mambo yake ya kukimbilia kwa waganga. Nikamwambia, mume
ushapata, mganga tena wa nini?! Kutwa yupo kwenye kuzindika kusikoisha.
Haki nilimuonya mimi Raza. Na ndio maana mimi ananiona mbaya.
Nilimwambia kwa kumpa mfano wangu wa waziwazi. Nimezaa mimi watoto
watano, tena uswahili katikati ya watu, na mlango wa mganga siujui! Mbona
wote wamekuwa hakuna mwenye shida! Basi mimi ndio kuniona mbaya! Simtakii mema!
Yako wapi sasa? Ona jinsi anavyotesa watoto wasio hatia! Faida yake ipo wapi
sasa?” Mama yake akaongeza akiwa na masikitiko. Wote wakamgeukia mama yake Raza
aliyekuwa akizungumza pembeni kidogo na pale walipokuwa wamemzunguka Polla. Yeye
hataki hata kusogea kwa hofu.
Pale Unapokula Mbivu
Baada Ya Uvumilivu
Mapenzi ya kweli
ni kuvumilia ukimya, pale ambapo
sauti zimekoma. Na wakati mwingine penzi la kweli huwa kama taa
ya mwanga hafifu, pale moyo wa mwenzako anapokuwa gizani. Ndicho kilichowatokea
wawili hao. Walipita mengi, lakini hatimaye wakajikuta wamesimama pamoja. Walishinda
hapo kitandani. Kila mmoja akiwa na furaha ya aina yake. “Kwa hiyo huna shida
ya kuishi Marekani?” “Nikiwa mkeo hata ukiniambia twende tukaishi Mlalo,
milimani, sina shida.” Mill alifurahi sana. Ukweli hakuwa amepanga kuishi hapo
nchini. Kwanza alikuwa akiishi kwa vibali tu, kama mgeni.
“Na hii kwa
ajili ya kumuhangaikia Shema. Nimefurahi! Nimefurahi sana Mill. Sikutegemea
kama ulikuwa ukifanya kitu kikubwa hivi!” Hapo tena akapongezwa kwa
penzi la haja. Akapambwa sifa huyo Mill, akatamani atoe tarehe ya ndoa hapohapo
kitandani ila akaona afanye taratibu, apange kitu cha kumfurahisha.
~~~~~~~~~~~~~~~
Alipohangaika na
huo mwili wa Pam mpaka akatulia ndipo akatoka kwenda kuchukua maji. Akarudi na
maji ya Pam. “Njaa inauma Mill!” Akarudi kwenda kupasha chakula walichobeba kutoka
hotelini.
“Nimefikiria.” Pam akakaa maana alirudi na
sahani mbili. “Nianze kwa kukuuliza swali.” “Juu ya nini?” “Ni juu ya nani, sio
nini.” Mill akakaa hapohapo kitandani na sahani yake, baada ya kupokelewa moja.
“Ulisema mama
alirudi nyumbani kijijini sababu ya ugonjwa?” “Sio alirudi Mill. Alirudishwa
na mumewe, sababu ya ugonjwa. Na alivyo mkatili yule mwanaume, akamrudisha na
watoto wawili ambao hakuwahi kuhangaika matunzo.”
Pam
akaanza kupandisha hasira. “Sasa Eric akaona baba yake amefaidi, akaona amuige.
Ni mshenzi sana. Na aisee jana ilikuwa mbaya! Ilikuwa mbaya
sana.” “Jana uliponiambia ulikwenda kukutana naye kwa chakula cha mchana?”
“Chakula chote kiliishia mwilini mwake na nikamuogesha na ile soda,
kisha kummwagia maji juu.” Mill hakutegemea! Akashituka sana.
“Pam!” “Nilishaanza
kumrushia ngumi, ndio wakanishika. Nilijaza watu pale!
Nilimtukana Eric mpaka nikajisikia vizuri.” “Pam!” “Aisee ilikuwa mbaya.
MBAYA mno. Hujawahi ona.”
“Basi mimi
nilijua ulipata wakati mzuri!” “SANA, ambao sikujua kama ningekuja kuupata na
yule mwanaume. Hivi unajua aliniacha jela nikiwa mjamzito, namlilia
shida!” “Pole Pam.” “Mimi sawa, lakini Eric amemtupa mama kabisa! Mama aliyemuombea
nafasi ya kuja mjini! Kwa kumsikia akiomba kwa kunyenyekea! Tena kwa shangazi!”
“Mwanzoni ni
kama alimkatalia. Nikiwa nasikiliza mazungumzo yao, nikamsikia mama akimsihi
shangazi au wifi yake, akamwambia kabisa, ‘ni hivi sina uwezo wa kupiga
magoti, wifi, nisaidie japo Eric tu. Nitolee huku kijijini, asogee mjini,
asome’. Akamuomba akimsihi kwa unyenyekevu. Akimwambia vile Eric
alivyo na juhudi ya shule lakini kule kijijini hatafika mbali.” “Naomba usilie Pam. Tulia.”
“Hakika naumia Mill. Eric anakuja
mjini, anaolewa, anamsahau mama! Anasema anajijenga yeye na mkewe, hawawezi
msaidia mtu, huku anajua mama ni mlemavu hana msaada! Anasahau
alivyotoka kwa kusaidiwa na yeye na watu! Anakua kama baba tu!”
“Kwani ilikuaje
mpaka mkakutana tena jana? Naomba tulia unielezee.” Akajifuta machozi kabisa na
kuendelea. “Yeye mwenyewe alinikuta natoka benki. Sikujua kama amehamia kwenye
ile benki. Sikumuongelesha. Yeye mwenyewe akanianza kunisalimia tena kwa
kunifuata. Nikaitika salamu na kuamua kumuacha. Maana aliniacha jela akiniambia
hatanitoa, nijifunze. Nimetoka jela nikawa nahangaika na mwanangu
huku nikimsaidia mama bila ya kumtafuta, huku nikijua anao uwezo
ila hatanisaidia maana nasikia alikwenda kunawa eti mikono kwa mama kwamba hataki
kunisikia tena mimi na mama eti kwa kuwa ananiendekeza, basi na yeye anaachana
naye! Kweli Mill?”
“Haikuwa sawa
Pam. Lakini jua mimi ndiye niliyemponza mama. Isingekuwa mama kuja kukusaidia
Shema, asingeingia matatizoni.” “Nilikwambia hata mama mwenyewe anajua
ni kisingizio tu. Eric si mtoaji tokea mwanzo. Aisee jana nilimsema!
Nilitamani nipigane naye, nimg’ate mpaka nimtoe ngozi! Sema walinishika.” Mill
akaanza kucheka.
“Angekupiga?”
“Si na mimi ningekuwa nimempiga! Nilipanga nimwachie alama abaki nayo ya kudumu
kila akiingalia awe anakumbuka alipotoka. Maana jana nilimkumbusha hatua
kwa hatua. Mpaka nikamwambia nilikuwa natamani kuiona sura ya baba lakini kwa
kuwa nishamuona yeye, inatosha. Hawana tofauti.” Mill akavuta pumzi kwa
nguvu na kuzishusha. Wakaendelea kula.
Uzazi Mzuri.
Hakuna anayetoa
kumzidi Mungu. Haijalishi nafasi na kile ulichonacho, msaada ni mbegu. Huota
kwa kadiri ya Mungu anavyojalia malipo yake. “Naona tumrudishe mama mjini
kwenye maisha yake.” Pam akahisi kama hajamsikia vizuri. Akabaki amekodoa
macho.
“Mama si anajua
kusoma na kuandika?” “Anajua Mill! Ila sidhani kama…” “Kazi ya kupokea pale
pesa na kuingiza kwenye kompyuta haiitaji shahada ya uhasibu. Mgonjwa anapoenda
kulipia, akimtajia kiasi cha pesa cha kipimo chake, anamlipa, anaingiza kwenye system,
risiti inajitoa yenyewe, anamkabidhi, kazi imeishia hapo.”
“Kwamba ndio
mama afanye?!” “Unadhani itakuwa ngumu sana?” “Hapana Mill! Ataweza. Na
nakuhidi nitamfundisha atakapokuwa anakwama au muda wangu wa chakula cha
mchana nitakuwa nikiutumia naye.” “Sitamtoa nyumbani na kwenda kumuweka pale!
Hapana Pam. Atapata muda wa kutosha tu pale wa kujifunza mpaka nitakapoona yupo
tayari, ndipo watakapokuwa wakipokezana na yule msichana pale. Anabanwa,
anakosa hata muda wa kula!” “Nimemuona. Ila si mlalamishi kabisa!”
“Ni rafiki wa
karibu sana wa Fatma. Huwa nawafurahia utendaji kazi wao. Hutawasikia
wakilalamika hata mara moja. Ndio maana mara nyingine huwa nawapa posho kama
shukurani tu. Tulianza wachache sana, na wamejitoa bila kumlalamikia yeyote,
hata Mbise anawasifia. Hutamkuta Fatma amekasirika hata mara moja.” Pam akaona haitoshi.
Akatoka kabisa
kitandani na kupiga magoti chini ya kitanda, pembeni yake. “Nakushukuru
Mill. Asante sana. Hujui unachofanya.” Na machozi juu!
“Acha bwana Pam! Wewe unataka kunigombanisha na Mungu, aone namchukulia utukufu.”
Ikabidi Pam acheke tu. “Kuna kipindi nilitaka arudi mjini moja kwa moja, ila
akaniambia tuwe tu wakweli. Hali yangu mbaya, akija ndio itakuwa mbaya zaidi.
Bora abakie kijijini hatashinda njaa. Maembe na matunda mengine yapo, halafu
mjomba haachi wazazi wake na njaa. Watakachokula wazazi wake, na yeye atakula.
Akaniambia ni bora nikipata cha ziada niwe na mtumia kuliko aje na yeye awe
mzigo huku mjini.” “Haya simama hapo tujipange zaidi.” Akasimama.
“Unafikiri
atahitaji msichana wa kazi?” Pam akabaki akifikiria maana kijijini hapakuwa na
msichana wa kazi ila yupo jirani aliyekuwa akiwasaidia mambo muhimu. “Itabidi
kumuuliza. Tutamuweka wapi sasa?” “Ninaposema aje huku, natamani arudie maisha
yake. Yaani awe na kwake na mamlaka yake. Asijisikie anakula kwa shikamoo!
Awe huru.” Pam akacheka akifikiria.
“Nafikiria
akaishi kule ulikokuwa unataka kukimbilia.” Pam akacheka kama mazuri. “Usicheke
bwana Pam!” “Mwenzio nataka unioe.” Mill akamtizama kwa kumsuta. “Sasa
huko tusirudi tena bwana harusi wangu. Tuendelee na mipango.
Huwezi jua naweza kukupa asante nyingine!” “Au unishukuru kabisa
ndio…” “Hapana bwana, tulia! Wewe huchoki! Tokea asubuhi unashukuriwa
tu, na hujamaliza jambo unataka kushukuriwa!” Mill alicheka hana mbavu. “Pam!”
“Wewe endelea kutoa pointi za maana ili uzidi kunipandisha mzuka.”
“Maana pale
nishalipia ya miezi 6. Na kuna kila kitu bado vichache sana. Halafu…” Pam
mwenyewe akaanza kuhamasika. “Mama yangu anarudi mjini na ajira juu! Hakika
Mungu ana mambo yake. Kuna kipindi, zamani lakini, alikuwa akizungumza na mimi
tukiwa tumelala, hata kabla sijamzaa Shema. Akaniambia alikwenda mjini akiwa amejaa,
akarudishwa mtupu na watoto. Aliiongea kwa uchungu.
Akasema amepoteza nusu ya uhai wake akiwa mjini, na kurudishwa nusu. Nilimuhurumia
na hapo ndipo niliposema nitakuja kumrudisha mjini nije niishi naye.” Akatulia akifikiria
akawa kama kitu kimepita kichwani.
“Ulikuwa
umepanga aje lini?” “Wewe zungumza naye umsikilize. Akikubali ijumaa wakati
dereva akimshusha Shema hapa jioni, anakwenda kumfuata. Jumamosi mchana
wanarudi.” Pam alifurahi huyo, hakuwa akiamini. “Asante Mill! Asante sana. Na
mahari nimekusamehe!” “Acha uhuni Pam. Unataka kunitapeli wakati
nimeambiwa sidaiwi!” Pam alicheka sana.
“Nilijua
hujaelewa vizuri!” “Wewe nishukuru ili niendelee kufikiria vizuri.”
“Naona kweli ukishukuriwa akili inatulia, na kutoa mambo mazuri.”
“Sasa hii ni siku ya kwanza tu. Zikikamilika zile siku mbili nilizokuomba, nikushike
bila muingiliano.” “Naona tutanunua dunia.” Mill alicheka sana na kutoka hapo
kitandani akiwa amemaliza kula anarudisha sahani jikoni.
“Nimeshiba Pam.”
“Urudi nikubembeleze ulale.” Akamsikia akicheka huko. “Ninavyopendwa Mill
mimi!” “Na hapo bado hujatangaza ndoa! Ukitangaza je?” “Mama wewe utaolewa
kanisani! Mbona ujumbe wangu nilishaupata! Na kufukuzwa juu!” “Sasa hivi unapendwa
sana.”
“Twende basi
kule ndani kwangu kuna sehemu nataka tukafanyie mapenzi.” “Mill!” “Utafurahia. Nakuhakikishia.
Pazuri sana. Kwanza kule kuzuri Pam. Twende ukapaone. Patakuwa kwako pia.
Twende.” “Mbona umeng’ang’ania hivyo?” “Kule kuna nafasi Pam. Nafanya mapenzi
na wewe huku mazingira yananiunga mkono.” “Mbona hapa pazuri tu kama kule kwa
Mike?” “Hilo daraja Mungu alishanivusha Pam.” Alicheka Pam, alicheka sana.
“Mill!” “Nakuwa
mkweli. Mazingira haya ni wakati mwanafunzi. Sasa Mungu ashanibariki,
kwa nini niishi kwa kujibana? Nimeinuliwa mwenzio!” Pam akamtizama. “Si
kwa kujivuna tu, twende ukapaone na wewe, ili ujue ninachozungumzia?”
“Kwa hiyo mimi ndio ngazi hii?” “Kwa kuchagua kwako Pam. Mimi
nilikuwa nikihangaika ili tufaidi wote. Na haya nilikwambia tokea siku
ya kwanza kabisa kuzungumza na wewe kwenye simu. Bisha.” “Kweli.” Pam
akakumbuka kipindi hicho alikuwa akifanya kazi kwa Sandra.
“Sasa? Mwenzio
nilijiona nipo juu na wewe. Ila naona mwenzangu unang’ang’ania
vya chini. Mara uswahilini walipo mashoga zako. Haya, mara kwenye
vijumba visivyo hata na madirisha! Tumehangaishana weee, umekuja
kuishia kwenye kinyumba cha pembeni, hutaki kuingia ndani! Tena
unakasirika kabisa kama si kuchagua maisha ya shida ni nini?” “Mbona hapa
pazuri sana! Tokea nazaliwa mimi sijawahi ishi kama hapa.” “Ndio nakwambia,
makubwa zaidi yapo hapo mlango wa pili tu, twende ukajionee jinsi unavyojipunja
na kumtesa mmarekani wangu.” Pam alicheka, alicheka sana.
“Shema huyo!”
“Kumbe! Si mtanzania tena. Sasa wewe unataka kutupunja bila sababu!” Pam
alikuwa haamini akicheka. “Kuishi na watanzania kazi!” “Mmeanza
kuninyanyasa Mill!” “Bwana wewe mbishi sana Pam! Jambo dogo unalifanya…”
“Kuolewa mimi si jambo dogo.” “Nishakwambia nakuoa. Nipe huo
mwili na kesho. Nikitoka hapa naandaa harusi. Tatizo ni nini mama? Kwa nini
tuishi kama wakati ule mwanafunzi? Maana mimi siwezi kulala kule wakati wewe
umelala hapa na mwanangu. Najiona kama mbinafsi!” “Basi Mill.” Pam akaona aende
akajionee.
~~~~~~~~~~~~~~
Raza Alipanda Mbegu
Ya Dhambi Kimykimya, Ikaota Mizizi Chini Ya Udongo Wa Siri; Mavuno Yake
Ndio Hayo, Yanamtumbua Usiku Usio Na Mwanga.
Mwisho Wake Ni
Upi?
Ya Pam
Yanakwenda Zaidi Ya Alivyotarajia. Nao Mwisho Wao Ni Upi?
Love At First Sight.
0 Comments:
Post a Comment