Pam akimtizama
kupitia kioo. “Unawaza nini? Bado upo na mambo ya Shema tu?” “Bado siamini Pam!
Siamini kama tupo wote.” Pam akacheka na kugeuka. “Nikuulize kitu Mill?” “Kabla
hujanitoa kwenye hii hali, acha nikukumbatie kidogo. Nishaamka kwenye asubuhi
mbaya, bora wewe ulikuwa ukiamka huna pesa, una mtoto anayekupenda. Suluhu
ilikuwa ni kufanya kazi kwa bidii, ukijinyima muda wa kupumzika,
kutengeneza pesa, mnakula na kulala na Shema kwa furaha.” Pam akakunja uso.
“Mimi nilikuwa
na kila kitu. Juhudi zilikuwa zikilipa, ila silali na sina jinsi ya kufanya.
Pesa ipo, mke ndani yupo na watoto wa jinsia zote, lakini hakuna amani.
Aisee usiombe kuishi na mwanamke mwenye kelele Pam! Halafu mlalamishi!
Huwezi kufikiria, huwezi kutulia, halafu yupo na wewe kila mahali. Nyumbani na
ofisini. Huna pakuhemea.” “Pole Mill!”
“Aisee acha
mama. Kila mtu anawasifia, lakini ndani kunawaka moto, na hakuna dalili ya
kuzimika. Hakika nakupenda na nakuhitaji Pam. Ni kama Mungu
alinipitisha kuonja lile fukuto, ili nithamini nilichokiacha huku
nyumbani.”
“Mwanamke
alinitesa yule! Halafu juhudi zangu zote akaishia kutapanya na mwanaume asiye
na mbele wala nyuma! Pesa yangu yote! Mali zangu zote! Kweli?” “Unaanza
kuharibu mudi Mill. Mpaka uso umebadilika wakati muda mfupi tu ulikuwa na
furaha.” Pam akamsogelea. “Huko umeshatoka. Tupo hapa sasahivi. Naomba tulia.”
“Wewe mwenyewe
ulisema tulichonacho hakiwezi kutafutwa, ila mali inatafutwa. Tulia. Fikiria
kwa upya. Anza tena. Tena sio kuanza Mill. Hapa nchini kwenyewe nimeona
unatengeneza pesa nzuri sana.” Mill akakumbuka yeye ndiye muweka pesa benki.
“Unatengeneza
pesa nzuri tu. Na ukiamua kwa jinsi ulivyo na akili nzuri, unaweza fanya kitu
kingine zaidi na ukaingiza pesa ziadi.” “Pesa unayoiona hapa, haifiki hata robo
ya pesa niliyokuwa nikitengeneza kwa siku kule.” “Mill!” “Acha Pam! Acha mama.
Nilitengeneza pesa kule, na ilikuwa ya uhakika. Juhudi zangu zote na pesa
aliyowekeza baba yangu ni kama imepotea bure tu!” Pam akawa hajamuelewa.
“Twende tukale,
kisha unielezee vizuri.” Wakatoka wawili hao kwenda kula sehemu nzuri ya hadhi
ya Mill. Bwana Pam alipendeza, ile ya kupania. Mill alikaa mbele yake.
Wakaendelea kula.
“Acha
kuniangalia hivyo bwana!” Mill alicheka. Akacheka sana. “Mimi nimekuangaliaje?”
“Nimekuona mpaka umepotea! Sasa umefika wapi?” “Kukuvua chupi.” Pam alicheka
mpaka akapaliwa. “Na gauni?” “Hilo nishalirarua zamani sana, lilishanipotezea
muda.” Pam akazidi kucheka asiamini.
“Yaani tumetulia
hapa najua unafurahia chakula!” “Na ndivyo ilivyokuwa mpaka yule muhudumu
alivyokuja na juisi hapa, akapotelea hapo kifuani!” “Ndio maana ukakohoa!” Pam
akacheka sana.
“Maana nilimuona
haondoi macho hapo.” “Alipoondoka?” “Ndio nikajiambia acha niangalie kwa makini
kilichomvutia mwizi yule. Ziwa mama! Nikajikuta nakuvua gauni,
nakutoa sidiria.” “Hapahapa!?” “Kama hakuna mtu vile. Juu ya hiihii meza.”
“Vyakula?” “Nilishavisukuma vyote kwa mkono, ukabakia wewe tu mezani.” Pam
alikuwa akicheka haamini.
“Naomba toa
mawazo huko, tuzungumze bwana Mill!” “Nimekwambia nipe siku mbili.
Nikishakushika hizo siku mbili angalau akili itaanza kufanya kazi. Tena kadiri
nilivyokuwa nikikusimulia hapa, hali ishakuwa mbaya. Tumuite muhudumu,
tuondoke hapa.” Naye Pam hali ilishabadilika, anataka kweli akatolewe hilo
gauni. Wakafungashiwa vyakula na kutoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Kula njiani
wakati nakuendesha.” “Ndio maana nakupenda.” Pam hana mbavu. Mill anakula huku Pam
akiendesha kurudi nyumbani. Akala mpaka akamaliza wakiwa ndio wanaingia getini.
“Naomba ukaribie kwangu.” Pam akashituka na kumgeukia. “Uliniahidi nini
Mill?!” “Acha kukasirika Pam. Ni kwa sasahivi tu! Sio kwamba nakuhamisha. Mbona
mimi nimelala kwako?” “Hapana Mill. Hutaishi na mimi unyumba. Mwishoe
tutajisahau. Tuishie hivihivi, Shema akituangalia, na yeye aje aishi hivihivi kama
wadogo zako. Umeniahidi utaishi maisha ya mfano kwa ajili ya Shema.”
“Pam umepaniki
tu mpenzi wangu.” “Hapan…” “Subiri kwanza Pam. Nilipokwambia nataka kuanza upya
na wewe, na hili likiwemo. Kupafahamu kwangu! Kuna ubaya gani? Au unafikiri na
mimi napenda haya maisha kwamba nataka kumkuza Shema kwenye makuzi ya nyumbani
kwetu?” Akatulia.
“Siwezi. Naanza
kwa heshima na sitaacha kukuoa kanisani. Nilikuahidi na nitatekeleza. Tafadhali
tulia.” Pam akapoa. “Nakupenda Pam.” “Samahani Mill. Samahani.” “Najua kuna
sehemu unajiambia kuhamia hapa ndio umefunga milango yote ya tumaini la ndoa.”
“Na ndio maana jana nilikuwa nikisita Mill. Sisi tunakuwa watu wakuanza,
hatufiki mwisho. Mwenzangu Kisha ulimuoa akawa akijulikana kisheria. Mimi
nimebakia..” Pam akakwama kwa uchungu.
“Kisha sio
mwenzio. Na sikumuoa kwa mapenzi. Nilimuoa kwa ajili yako Pam. Kisha
alikuwa njia ya kumaliza safari niliyoanza mimi na wewe, ila nikakwama kwake.
Sasahivi sina sababu ya kutokukuoa wewe. Wewe hushangai kwa nini sikumfikisha
yeye kanisani?” Pam kimya akiegesha gari.
“Pam?” “Mimi
sijui Mill?” “Kwa sababu kanisani ni sehemu yetu mimi na wewe. Nilijiambia
hakuna mwanamke ataingia kanisani na mimi na kupeana kiapo kama si wewe.
Nitakuoa Pam. Uwe unaishi hapa, au kwingineko, ukikubali tu, nitakuoa.
Ila sikutaka tukurupuke tujikute tu tunakimbilia kanisani!” “Kwa nini?” Pam
akamuuliza na kumshangaza Mill.
“Kwamba wewe
unataka ndoa hata kesho?” “Nataka ndoa ya kanisani na wewe tokea miaka 10
iliyopita Mill. Sijabadilika. Mimi hivyo vyakuanza upya sitaki. Nataka
tuendelee. Utanitoa huko kwenye starehe nikiwa mkeo, sio kama Pam wa
wakati ule. Nishakuwa mama Shema. Nataka tuendelee. Tutaanza mpaka lini?
Maana tusipoangalia, huu mchezo wa kupeana penzi tutauzoea, mtoto
mwingine atakuja, itakuja sababu ingine tena, ndoa ishindikane, nibakiwe na
kazi ya kuzaa tu, wengine ndio wanajulikana ni wake zako. Hivyo mimi sitaki.”
“Na mimi nataka
kukuoa Pam.” “Lini?” Pam akawahi. “Maana safari hii sitaki mambo yakusema unataka…”
“Ndio jambo nilitaka kukwambia Pam. Kule nilifanikiwa sana. Kwa nini tusiondoke
wote watatu. Tukafunge ndoa kule ili…” “Hapana Mill.”
“Nisikilize
Pam.” “Hapana. Huo mchezo sifanyi tena.” Pam akashuka garini kabisa,
akachukua pochi yake na kwenda kwake, kwenye nyumba ndogo.
Mill akashuka na
vyakula akamfuata. Hakutegemea kumkuta anafungasha. “Pam!” “Hakika hapana
Mill. Huu mchezo sifanyi tena. Kama unanipenda kweli na unania ya kunioa,
utakuja nitafuta. Sipotezi tena muda.” “Tafadhali nisikilize.”
“Tulishindwa safari ile, safari hii kitakachowezekana ni kipi? Ubalozi wa
Marekani washaninyima mimi Visa mara tatu! Kweli unataka tuanze upya kabisa! Hapana
Mill.”
“Tafadhali
naomba tuzungumze Pam. Nisikilize acha kufungasha.” Pam akaendelea. “Safari hii
unakwenda ubalozini ukiwa na mimi pamoja na Shema. Mimi nakuombea wewe nikiwa
kama raia wa kule! Hawatakunyima.” “Basi mimi SITAKI.” Mill akabaki amesimama.
“Sitaki. Na hapana
Mill.” “Hutaki kwenda Marekani au hutaki k…” “Hutanianzishia mambo yasiyo na uhakika.
Kwamba hatima yetu inategemeana na tutakayemkuta siku hiyo pale
ubalozini! Huo mchezo sifanyi. Tumkute hana mudi nzuri, aninyime mimi na
mwanangu hiyo Visa kwa sababu zake tu!” “Kwanza ukumbuke Shema yupo chini ya
miaka 18, na yeye ameshakuwa raia kule.” Pam akasimama wima.
“Usikasirike. Na
usipaniki.” “Umefanya nini Mill?” “Nilipowarudisha wale watoto wa Kisha kule,
nikamuanzishia process za uraia. Unakumbuka kuna siku nilikuja kumchukua
nikakwambia kuna sehemu anahitajika?” Pam akabaki akimtizama.
“Huyu mtoto
anakipaji kikubwa Pam. Kuna nchi wanaweza kukitambua na kukikuza kwa kiwango
cha juu sana. Ndio maana umeona nimemuweka kwenye timu kubwa na uangalizi mzu…”
“Umefanyaje Mill?” “Alipata nafasi ubalozini. Wakamchukua alama za vidole,
tukapeleka na picha zake. Nikawaachia. Wameshatuma hata hati yake ya kusafiria
kama raia wa Marekani. Yeye kwake haikuchukua process ndefu. Kwa sababu mimi
baba yake ni raia.” Pam akahisi hajaelewa.
Akakaa
kitandani. “Kwa hiyo mimi na Shema kisheria ni raia wa Marekani.” Mill akamalizia
akicheka kama mazuri. “Unanitania Mill?” “Najua umekasirika. Ila sikutanii.”
Pam akabaki akimtizama. “Labda ungetaka kujua kwa nini sijakwambia?” Pam
akabaki akimtizama. “Eti Pam?” Kimya.
“Ni kwa sababu
kwanza tulikuwa hatupo kwenye maelewano. Halafu nilimuahidi Shema
kumpeleka nilipokuwa nikiishi. Kumuombea Visa, ingekuwa ngumu kuliko kumfanya
awe raia. Halafu Pam, si kitu kibaya. Hata tukiamua mimi na wewe tubakie
hapahapa nchini, wewe unatudhamini.” Pam akabaki akimtizama.
“Niambie
mtanzania wangu?” “Ujue Mill umenikosea wewe?” “Kumfanya Shema kuwa mmarekani
ndio nimekukosea Pam? Hivi unajua faida zake lakini?” Pam akabaki kimya. “Huyu
mtoto anauwezo wa kusoma shule zenye kiwango cha kwanza hapa
ulimwenguni. Hao unaowaona kwenye luninga wakicheza mpira ligi za kimataifa
ndio atakuwa akitazamwa Shema Mgini.” “Shema Shelukindo Mgini. Au
umembadili jina?” “Sithubutu. Acha nikuletee passport zetu.” Mill akatoka kwa
haraka, Pam asiamini.
Kwa upande
fulani hakuamini kwa furaha. Yake yalikuwa magumu sana. Mara tatu,
aliomba uraia akiwa na vithibitisho vyote na kunyimwa. Leo mwanae amekuwa raia!
Akabaki kama amepigwa butwaa.
Mill akarudi na
passport mbili. Zote zinafanana. Akamkabidhi. Pam akazifungua akakutana kweli
na ya mwanae. Shema Shelukindo Mgini. “Hiyo
hati ya rangi hiyo, mama si mchezo.” Akaanza kujisifia. “Huyo
mtoto inamaana anaweza ingia nchi yeyote ulimwenguni hapa bila zile
shida kama zako za kuomba VISA.” “Haiwezekani Mill!” “Wewe kwa nini unafikiri
nilichangamkia kwa haraka? Passport ya Marekani ina nguvu mama. Unaingia
utakapo, wanakuwa wakikugongea tu VISA ukifika uwanja wa ndege wa hiyo nchi,
basi. Mwanangu huyo hatakaa akapata shida kama ile yako ya kuombaomba
VISA. Yaani huyo sasahivi nikimwambia twende zetu, London. Tunakata ticket,
bila swali, mpaka uwanja wa ndege wa Heathrow, hukohuko London, pale ndipo
watatugongea muhuri na kutukaribisha kwa heshima zote.”
“Hakika sikuwahi
hata kufikiria kama unawe..” “Ninapokwambia nakupenda, jua NAKUPENDA na
Shema ni mzaliwa wangu wa kwanza. Nawafikiria kupita unavyofikiria wewe japo
sikuwa nikijua ni jinsi gani nitakupata tena. Ila hivi ndivyo
nilivyokuwa nikitaka kukwambia.” Pam akamtizama maana macho yalirudi kwenye hati
ya kusafiria mwanae.
“Pesa
unayopeleka benki kila siku, sio pesa ile Pam. Kule nina uwezo wa kutengeneza
mara dufu ya hizi. Kile kitu nimeanzisha kwa sababu yako na Shema. Ni nafasi
niliyopewa na kina Komba, nikaikubali nikijua itanisaidia wakati tukiwekana sawa
na wewe na niwe karibu na Shema. Sitaki akue bila baba. Ila ukikubali
kwenda kuishi kule na mimi, au sisi Marekani!” “Mmeshaanza kunibagua?” Mill
akacheka sana.
“Nisikilize
mama. Twende tukatengeneze dola mpenzi wangu. Pesa ya maana isiyo na maswali
wala kubabaishana.” “Kwamba pesa unayotengeneza hapa si kitu?” “Hiyo
unayopeleka benki?” “Mbona nyingi hivi?” “Pam! Hiyo pesa ya kubadilishia mboga,
mama! Wewe unafikiri ni kwa nini Kisha alikuwa akining’ang’ania japo
hanipendi?” “Pesa?” “Pesa haswa. Hapa nilipajenga kama mchezo mpaka Mike
alikuwa akinishangaa. Twende zetu tukatengeneza pesa ya ukweli Pam. Wewe
unanidhamu ya kazi na unajituma. Twende zetu.”
“Ulaya!” Pam
akawa ashahamasika. “Sio Ulaya, Pam! Nilishakwambia.” Akaanza kumcheka. “Wewe
cheka utakavyo. Iwe Ulaya iwe Marekani, japokuwa nataka sana kwenda huko,
lakini hutanitoa hapa bila ndoa ya kanisani. Hakika HAPANA.” “Wenzio
wakisikia Marekani wanarukaruka, hawafikirii mara mbili!” “Hapana Mill. Acha
mengine yaongezeke. Mimi nataka ndoa kwanza.”
“Hudhani kama
wazo langu zuri? Tukifungia kule itakuwa rahisi kupa…” “Hapana Mill.” “Safari
hii hawatakunyima Pam. Itakuwa rahisi. Mwanao mwenyewe ni raia, mimi baba yake
raia, watakunyima vipi?” “Mill, ndoa ya kanisani KWANZA, mengine baadaye. Hutanitoa
hapa mimi na Shema, mimi nikiwa kama hawara. Acha waninyime huo uraia
wao, kwani huku nimefukuzwa?” Mill akatulia akifikiria.
“Nenda kafikirie
kule kwako. Hapa uondoke kabisa.” “Pam! Na ile mipango yetu?” “Unishikeshike
hapa, kumbe mwenzangu una yako? Wewe kama mnywaji sana wa maziwa, nunua
ng’ombe.” Bwana Mill alicheka. “Nilishakununua Pam.” “Miaka yote ile!
Ng’ombe uliyemuacha alishakufa. Unaanza upya.” “Pam!?” “Sasa ulimaliza safari
uliyoanzisha na baba yako? Kama kweli ulimuacha huyo ng’ombe, nani alikuwa
akimlisha?” Kimya.
~~~~~~~~~~~~~~~
“Haya toka humu
ndani, kaendelee kufikiria kwako. Huna lako humu ndani.” Akamuona anatoa simu,
anapiga. “Kapigie simu zako huko kwako, sio hapa.” Akamtizama na kuweka kwenye
spika kabisa. “Baba Shema?” “Shikamoo mama.” Pam
akashituka aliposikia sauti ya mama yake. “Mnaendeleaje huko? Shema na mama
yake?” “Wote wazima mama yangu. Nilikuwa na swali.” Pam akakaa.
“Karibu.” “Najua safari yangu na
Pam tulifika katikati, ndoa ya kanisani nilitaka ikafanyike nilipokuwa nikiishi.
Sasa safari hii nikitaka tumalizie kufunga ndoa ya kanisani, natakiwa kufanya
nini?” Pam hakuamini. “Ni kwenda
kumuona mchungaji. Kwanza inabidi mtubu, mrudishwe kundini. Mlianza maisha
ya ndoa kabla ya ndoa yenyewe. Mmezaa kabla…” Pam
akaanza kucheka kwa sauti ya chini akijua siyo anayotaka kuyasikia Mill. Mama
Eric akaendelea, Mill akiwa ametulia akimwangalia Pam jinsi anavyomcheka
huku akimsikiliza mkwewe.
“Hapo mkweo
anakuita wewe mdhambi.” Pam akamnong’oneza kwa sauti ya chini sana, Mill
akaanza kucheka taratibu huku akisikiliza dhambi zake huko kwenye simu.
Akaweka mute kwenye simu. “Naona mama mkwe anaorodha ya dhambi zangu ZOTE!
Na utaratibu wa kutubu mrefu!” Mill akamwambia Pam na kufanya wacheke
kwa pamoja. Mama Eric bado alikuwa akiendelea.
“Kwa hiyo ndio hivyo baba.” Mill akagutuka na kutoa mute. “Nashukuru sana mama yangu.
Hayo nitayatendea kazi. Na kwa upande wa hapo nyumbani? Natakiwa kuanzia wapi?”
“Ukimaanisha nini?” “Swala la mahari?” Mill akajibu. “Huko
tulishapita Mill mwanangu. Umesahau jinsi marehemu baba yako alivyosihi tusije
pokea mahari ya mwingine maana ameshamchukua Pam na kumfanya ni Mgini? Au
umesahau?” “Hapana mama. Ila kwa sababu niliishia katikati, nilidhania natakiwa
kuanza upya.” “Si kwa huku nyumbani. Si eti baba?” Akamsikia akimuliza babu yake Pam.
“Ni vile na sisi
ni wakristo. Ila kimila huyo Pam ni mkewe kabisa. Ile harusi alifanyiwa siku
ile, ndio ilikuwa imekamilisha kila kitu huku nyumbani.” Mill na Pam walifurahi
hao. “Nashukuru sana wazee wangu. Acha nianze utaratibu wa kumalizia
kanisani. Nitawajulisha hivi karibuni.” Wakamshuru huyo
baba Shema kama mungu vile.
~~~~~~~~~~~~~~~
Mpaka Mill
anakata simu, Pam hana nguo hata moja. Acha Mill arushe simu mbali na kuvua kwa
haraka. “Ningekuvua Pam wangu.” “Nimekusaidia kwa hatua uliyochukua.
Nakushukuru Mill.” “Nakupenda Pam. Na sikuwa nimekusudia eti tuendelee kuishi
hivi! Hapana. Lazima nikuoe ili niweze pia kurudi kwa wadogo zangu kwa heshima.
Nimeshindwa kabisa kuwatafuta. Nimejiona kama msaliti wa baba. Aliniacha
kuwa kiongozi, nimeharibu.” “Anza kutengeneza hapa kitandani, halafu
tujipange huko nje.” Mill alicheka sana na kuanza penzi.
~~~~~~~~~~~~~~~
Kwa haraka sana
Sonia akapata neno la maarifa baada ya kugundua hofu ya Pius. “Usikubali
akuingie akilini Pius. Kama kweli yeye anao uwezo wa kukufanikisha, kwa nini asijifanyie
yeye huo uchawi ndio akashika nyadhifa zako hizo anazokwambia amekufanikisha?”
Akamfanya Pius atoe macho kwa Raza na kumgeukia yeye.
“Kwa nini aloge
ili wewe ufanikiwe hivyo na si yeye ambaye pia amesoma!? Si angeloga
yeye ndio ayapate hayo yote anayokwambia amekufanyia ili wewe ndio uwe ukimuomba
pesa?” “Lakini kweli!” “Ona anapoishi huyo mganga wake! Kama kweli wananguvu
hiyo si hata yeye angekuwa na maisha mazuri?” Kidogo Pius akaanza kutulia.
“Huo ni uongo
na usikubali. Upo ulipo kwa akili zako na kufanikiwa kwasababu umefuata kanuni
za kawaida tu alizoweka Mungu. Amebariki kazi ya mikono yako wala si kwa
uchawi wake. Shetani HANA zawadi kwa mwanadamu zaidi ya uharibifu tu. Anachoweza ni kuharibu si kubariki. Asikuogopeshe.”
“Na sikwambii
ufanye nini na mkeo. Ila jua mimi nitaendelea. Sitishwi na uchawi mimi. Nitamuwajibisha
mkeo bila hofu pamoja na mganga wake. Umesikia Raza?”
“Hivi mumeo
ameniwahi tu. Ilikuwa nikutafute leo, nikupe onyo bila kujua umbali
ambao umeshakwenda. Maana mawasiliano niliyokuwa nayo si ya undani
hivi kama ya mumeo. Ni malalamiko yako na vitisho ulivyotuma kwa
ndugu wa Mina, basi. Nikijua ni vitisho tu, nikataka na wewe upewe onyo
kisheria. Ila kwa hapa ulipofika, kukupa onyo ni kutotimiza wajibu
wangu, na mimi naishi kwa neno langu.”
“Hili
nilimwambia mumeo. Hata akiamua kukusamehe kwa udanganyifu wowote
utakaochagua wewe kumdanganya ili akuhurumie, akaamua yaishe, sio
kwangu. Kwa msaada wake au la, wewe nitakuwajibisha. Hutauwa
mtoto wa Mina kwa uonevu. Na kuwasaidia tu wewe na mganga wako, jua Mina
anaomba sana. Na mama yake haachi kumuombea mwanae mchana na usiku tena
kwa kufunga na kuomba. Hata muhangaike vipi, hamuwezi kumpata Mina. Ana ulinzi
wa kimungu na hii nimesikia kutoka kwa Mina mwenyewe na kutoka kwenye jumbe za
ndugu zao. Yule mama ni muombaji, hamuwezi pata binti yake. Haya,
wachukueni nawafuata kituo cha polisi, kesi yao inaanza ramsi leo.”
Akamgeukia Zilo.
“Twende.” Raza na Katibu wakatiwa pingu, wakaingizwa ndani ya gari ya wale
askari kanzu, wakaondoka. Akafuata Sonia na Zilo, Pius naye ikabidi ajikusanye
awafuate akiwa anahofu ya kupita kiasi. “Mpaka watoto wangu!?” Aliendelea
kujiuliza bila jibu.
~~~~~~~~~~~~~~
Hofu ya kurudi
kwake ikamuingia. Hajui analalaje pale kwenye kitanda alichokuwa akilalia na
Raza, alichogundua alikuwa akilalia hirizi. Hofu akihisi nyumba
nzima imejaa majini. Akampigia simu mama yake. “Kwema?” “Naomba tuhamie
hapo kwako kwa muda.” “Wewe na nani, na kwa nini?” “Mimi na Polla! Sababu
nitakuja kukueleza nikifika, ila kama unakubali, namtuma dereva amlete hapo,
ila hatakuwa na nguo mama. Naomba nenda ukamnunulie nguo aina zote unazojua
atahitaji kuanzia usiku huu mpaka kesho akiamka. Nataka awe hata na begi la
shule jipya. Sitaki atumie alilokuwa nalo.”
“Ni nini kinaendelea Pius? Raza
yuko wapi?” Pius akajikuta machozi yakimtoka. Alilia,
mpaka akaegesha gari pembeni na kuzidi kulia. Alilia sana mama yake
akimsikiliza huku akiingiwa hofu.
“Tafadhali tulia ili tuweze
kuzungumza Pius. Unamtia hofu mama yako.” Akasikia sauti
ya baba yake. Akajaribu kutulia na kuondoa tena gari. “Pius? Raza
yuko wapi na kwa nini muhamie hapa na mtoto?” “Acha kwanza nimtume dereva
amlete Polla hapo. Kisha nitawapigia.” Akaagana na
baba yake na kumtafuta dereva wa Polla.
Upandacho Ndicho
Uvunacho.
Alishaacha gari
nyumbani kwani siku yake ya kazi huisha huyo mtoto anaporudishwa nyumbani.
Akamuomba arudi akamchukue na kumpeleka kwa bibi yake. “Utamkuta
yupo tayari.” Kisha akakata simu na kumpigia simu binti
yake.
“Ungependa kwenda kulala kwa bibi?”
Polla hujua ratiba yake na jinsi inavyosimamiwa,
haijawahi badilika. “Kesho shule dad na nina mtihani! Hapa nilikuwa sijalala,
namsubiria mama. Hajarudi nyumbani mpaka sasahivi, na simpati kwa simu. Nina wasiwasi,
siwezi kulala bila ya kuzungumza naye.” Ndipo akili
ikamjia Pius, huyo ni kiziwanda kweli wa Raza, alimdekeza kupita kiasi.
Raza na ukorofi wake
wote lakini kwa huyo mtoto hajiwezi. Na huyo mtoto anazungumza na mama yake
kuliko mtu mwingine yeyote. Wakati mwingine Raza huenda kukaa naye chumbani usiku
mpaka apitiwe na usingizi. Na huyo mtoto humwambia mama yake kila kitu. Ndiye msiri
wake.
“Sijamsikia mama, dad! Nashindwa kulala.” “Simu
yake itakuwa imeishiwa tu na chaji. Yupo safarini.” “Amekwenda wapi!?” “Safari
ya kikazi.” Polla akashangaa sana. “Mama hana
safari za kikazi. Kwanza hawezi kusafiri bila ya kuniambia mimi.” Ni kweli. Pius aliropoka tu. Raza hanaga safari za kikazi. Pius ndio huwa
anasafiri, si Raza.
“Beba madaftari yako tu. Utakuta
bibi amekununulia vitu vingine, na mimi nitakuja kwa bibi. Umesikia?” “Leo!?” Akamuuliza kwa kushangaa sana. “Dereva
anakuja kukuchukua muda si mrefu. Nitakwambia kila kitu tukikutana kwa bibi.” “Mwambie
bibi nitalala kwake siku nyingine. Leo nalala nyumbani, namsubiria mama.” “Polla,
mama yako hatarudi nyumbani leo.” “Kwa nini na yupo wapi? Mbona mimi
hajaniambia! Mama hawezi niacha nikalala bila kuzungumza na mimi hata kama
anachelewa kurudi nyumbani, lazima anazungumza na mimi. Haijawahi tokea
akaacha kuzungumza na mimi.”
“Kwanza hata hajanipigia kuniuliza maswala
ya shule na kuniandaa kwa mtihani kesho. Halafu kesho kutwa ni mashindano. Amesema
nitakuwa naye kuanzia asubuhi kwenye mazoezi kabla ya mashindano jioni, ambayo
ameshawaambia kila mtu awepo kwenye mashindano. Na bibi na babu walisema watakuja,
kwa kuwa hawatasafiri. Hata Poliny alimkubalia mama kuja kwenye mashindano
yangu. Kwanza leo aliniambia atanijia na swimming suits mpya. Za mazoezi
na za siku hiyo ya mashindano. Kuna mahali yeye ndio ananinunulia.”
“Mimi nitakununulia kesho.” “Kwa
nini sio mama?! Wewe hujui. Kwanza hujawahi hata mara moja kuninunulia swimming
suits zangu! Hujui zinapouzwa, na hujui aina ninazopenda. Mama yeye anajua.
Na huwa kwenye mazoezi yote ya siku ya jumamosi au wakati mwingine ijumaa jioni
anakwenda na mimi, sio dereva.” Pius akajua kwa Polla kazi
atakua nayo. Maisha yake yamezungukwa sana na mama yake.
“Mimi namsubiria mama. Kwaheri.” “Usikate
simu Polla.” “Mimi leo siendi kulala kwa
bibi, kwanza silali. Namsubiria mama. Mpaka aje, tupange mipango ya kesho. Ndio
nalala. Kwanza nasoma. Kesho asubuhi nina mtihani. Mama ananisaidia kupitia
maswali kabla sijalala. Namalizia kusoma, akija akiniuliza maswali, akaridhika,
ndio nalala.”
“Mimi nitakusaidia.” “Namtaka mama.
Mama ndiye anayejua kuniandaa kwenye kila mtihani wangu. Sio mkali
kwangu kama wewe na Poliny. Nyinyi mnataka nielewe harakaharaka, ila
mama yeye ananichukulia taratibu. Nyinyi mnanipanikisha. Mama ananifanya
natulia, naweza kufikiria.” Pius akakwama.
“Mama akikupigia, mkumbushe mtihani
wangu wa kesho. Mwambie namsubiria. Silali mpaka aje.” “Nisikilize Polla. Mama yako
hatarudi leo. Lazima ujifunze kusoma peke yako. Unaweza. Acha uoga.” “Umeanza
kunigombesha dad! Na ndio unazidi kunitia hofu.”
“Sijagomba Polla. Ila nakwambia
unaweza.” “Kwani kuna tatizo gani kumsubiria mama?! Mbona kila siku namsubiria
yeye?” “Nimekwambia mama yako amesafiri.” “Mimi nina uhakika mama hajasafiri. Mimi
najua anarudi. Asubuhi alinisaidia kujitayarisha kwenda shule. Akaniaga. Na aliniahidi
atarudi na vitu vyangu vyote na atanisaidia kujiandaa na mtihani wangu. Angekuwa
anasafiri, angeniambia mimi. Pengine amechelewa tu. Ila atakuja. Mama
hanidanganyi. Na kama kuna dharula, angeniambia. Mimi najua na nina uhakika.” Pius akakwama.
Ukweli Raza
aliwekeza kwenye mambo ya nyumbani. Japokuwa Pius alipenda sana binti zake na
walijua, lakini yeye Raza ndiye aliyekuwa mtekelezaji wa kila kitu na alikuwa
na hao watoto bila kuzembea. Uzima wao na ugonjwa wao, baba yao anapokuwa
safarini, ni Raza. Wakilazwa mahospitalini walikuwa na mama yao mchana na
usiku.
Kwa ukweli, yeye
ndio alikuwa karibu na watoto wake. Ratiba ya huyo mtoto aliiweza. Kila mashindano
ya huyo mtoto yeye ndio alikuwa mstari wa kwanza kuhamasisha watu wa familia,
popote anapokwenda kushindana, wahudhurie. Pius angeweza kukosa sababu
ya safari za kikazi, lakini si Raza.
Na Polla ameanza
kuogelea tokea mtoto mdogo sana, akiwa na mama yake. Raza alijua walimu wake
wote waliokuwa wakimfundisha kuogelea, na kuulizia njia za kumsaidia kuwa mzuri
majini. Huyo Polla huwa siku za weekend anapelekwa na mama yake
viwanjani kukimbia angalau kwa masaa mawili. Raza alisimamia mambo ya watoto
wake bila kuchoka wala kuzembea. Ilimradi kuwafanya bora hata kama si wakiume.
Huyo Polla akiwa
majini, unaweza sema samaki. Hakuna aliyewahi mpita kwenye kuogelea. Akiingia uwanjani
kukimbia, utatamani kumwambia ashindane mbio za riadha, lakini ilibidi kukimbia
ili kumsaidia pumzi majini. Yote hayo ni juhudi za Raza, kuwekeza kwake
tokea mdogo.
Ni hivyo tu Poliny
anakichwa kama cha baba yake. Lakini hata yeye anajua jinsi mama yao
anavyohangaika nao tokea wadogo. Tena peke yake bila kulalamika kwa sababu baba
yao alikuwa mtu wa kusafiri safiri sana. Raza akakwepa kabisa safari za kikazi
hata kama zina pesa, ilimradi tu aweze kuwepo nyumbani na binti zake.
Alijaliwa roho ya
umama, na kuishilia hiyo familia kwa mikono yake yote miwili bila kutaka
chochote kiingilie. Mambo ya nyumbani kama mama, alikuwa makini mno kiasi ya
kwamba hata Pius mwenyewe hapo mwanzoni alipokuwa akisikia alimloga ili
amuoe, aliona hajapoteza. Raza ni mke kwa yeyote aliyehitaji wife material.
Hapajaonekana tatizo kwake mpaka ya sirini yalipowekwa mwangani au pale Mina
alipoingia pichani ndio akawekwa mwangani.
Hata Pius
alipokuwa akishindwa mambo ya unyumba, Raza hakuonyesha tatizo kitu
kilichomsaidia Puis na kutomtoa ujasiri kama mwanamme. Wakati mwingine alipokuwa
akishindwa, basi Raza alikuwa akimtuliza na kumwambia pengine amechoka
sana, wajaribu tena kesho yake. Tena kwa upendo tu, kitu kilichokuwa kikimuacha
Pius salama. Na anapofanikisha penzi kitandani, basi huyo Raza
huwa anamsifia mumewe! Utafikiri mchepuko kapewa penzi la mume wa mtu! Atampamba
hapo weee, nakumfanya Pius ajisikie vizuri, asijue kumbe Raza ndiye ameshika
makali. “Namalizia kusoma dad, baadaye.” Simu ikakatwa.
~~~~~~~~~~~~~~~
Pius akabaki
amesimama njia panda, moyo unavutwa pande zote mbili. Hatua ni nzito kama
kufunga jiwe shingoni. Akili ikabaki ikipima faida na hasara, moyo ukilia
maumivu.
Njia ya kulia ni salama,
lakini baridi; ya kushoto ni hatari, lakini ipo historia NZITO.
Kilio cha nafsi
kinagongana na sauti ya UHALISIA.
Raza ni mke
wa miaka kibao! Si hawara. Amezaa watoto, na amepanda vilivyo. Huyo Polla ni mavuno
ya Raza aliyewekeza kwa jasho
lake, bila kuzembea. Hawezi kuepuka HILO. Polyin yupo chuo kikuu kwa juhudi za mama yake, hata kwenye sherehe ya mahafali
yake alikiri wazi mbele za watu kuwa mama yake alihangaika kumtafutia walimu wa ziada kuhakikisha masomo
yanayomsumbua anafanya vizuri, ndio maana amefaulu vizuri sana kumaliza
kidato cha 6.
Gari alinunuliwa
na baba yake, lakini mwalimu alikuwa
Raza mwenyewe mpaka Polyin aliyekuwa muoga barabarani akaweza kuendesha vizuri.
Japokuwa hupishana,
lakini mama ni mama. Akisikia baba
yake amemfunga jela!?
“Nifanye nini, nipoteze nini?” Pius
akabaki akijiuliza.
“Maamuzi ni
kivuli cha hatima, nami natega sikio kwa sauti ya ndani.” Akabaki akiwaza barabarani, hajui chakufanya tena
Anamlinda Ayvin au Polla na dada yake?
Pam
analilia ndoa ya kanisani.
INAENDELEA…
0 Comments:
Post a Comment