Mpaka Mill
alipoamua kuweka kikomo na kujishusha ndipo alipoweza kunasa samaki wake
kwa utulivu. Ilikuwa usiku mwingi tu pale walinzi walipokuwa wakimfungulia geti
nyumbani kwake. Akavuta gari mpaka kwenye hiyo nyumba ndogo. Akaanza mwenyewe
kuwashushia vitu hata kabla hawajaamka. Aliacha gari ikiwaka.
Akiwa anamalizia
ndio Pam akashituka. “Tumefika?” “Karibuni sanaaa.” “Hiyo sanaaa
yako iishie hapohapo Mill. Mimi nina usingizi.” Mill alicheka sana.
“Hakuna kukukaribisha
nyumbani?” “Hapana. Leo tulale, kesho ndio tutakaribishana. Mwenzio nimechoka.
Wewe umeshalala.” Akatoka garini na kukutana na nyumba hizo! Akatulia.
“Hapa sijui
nianzie wapi? Kote hapa unaishi peke yako?” “Ndio na nyinyi.” “Mill! Hii nyumba
umeijenga kwa muda gani?!” “Sio muda mrefu, ila niamini nikikwambia imechukua pesa
yakutosha. Nyingi MNO. Hapa hutasikia shida ya umeme wala maji.
Matatizo yenu yale ya mgao si hapa. Nilihakikisha katika hilo eneo
Mike anasimamia kwa makini. Wakati jua likiwachoma huko nje, mimi
natengeneza umeme hapa. Utawasha taa hapa, masaa 24, hakuna
wakukuuliza. Hata ukitaka kufua kila baada ya lisaa! Huna atakaye kubugudhi.
Mashine zinafanya kazi utakavyo. Nimechimba kisima cha maji, hata ukiamka usiku
wa saa ngapi, maji yanatoka ndani. Jumatatu mpaka jumatatu. Moto
na baridi, kila bomba. Ushindwe wewe tu.”
“Mmmh! Na hii
ulioyosema ndogo, mbona hivyo!?” “Hiyo ni vyumba viwili tu, lakini nilihakikisha
ina kila kitu ndani. Kila chumba kina jitegemea na choo chake pamoja na bafu, closet
na sehemu ndogo ya sebule yenye tv. Ila kuna choo cha wageni, hakina bafu.
Jiko, sebule kubwa ya wote na sehemu ya kulia. Twende ukaone.” “Na kwenyewe
kuna maji na umeme kama
huko kwako?” Mill akaanza kucheka.
“Maana unaweza jipendelea,
halafu wapangaji wako tukawa tukiishi kwa shida huku.” “Mfumo wa
umeme kote ni sawa. Nakwambia nimeingiza vifaa vya solor power kutoka
nje ya nchi. Sikutaka kutapeliwa. Twende ukaone.” Wakaingia ndani na
Shema aliyekuwa na usingizi hajali alipo ilimradi alishajihakikishia mama yake
yupo.
~~~~~~~~~~~~~~
Pam alifikiri
Mill angelala kwake, ila alichofanya ni kuhakikisha mwanae amelala chumbani
kwake. Kila kitu kilikuwa kipo sehemu yake. Alichofanya Pam ni kutoa mashuka yaliyokuwepo kabatini na
kutandika vitanda, ndio mwanae akalala. Palikuwa pazuri, pakuvutia mno.
Zaidi hata ya hoteli ya kitalii.
Wakati
anamalizia kujipanga alale, Mill akamwambia yupo mlangoni, amfungulie. “Ni nini
Mill usiku huu, kwa nini hutulii kwako?!” “Nimekuleta hapa karibu na
mimi ili nikufaidi. Unafikiri utakuwa hapa halafu mimi
nilale kule! Hata kidogo.” Akajikaribisha mpaka chumbani kwa Pam, akajirusha
kitandani na PJ zake. Pam akamfuata.
“Njoo kwanza nikulambe
mwili mzima, ninyonye nitakapo ndio nitaweza kulala.” Pam alifurahi
huyo, hata hakujivunga, akakimbilia kitandani. “Muone! Si ulikuwa unajidai hunitaki
wewe?” “Nilivyokuwa na hamu na mapenzi yako! Acha Mill! Unanifanya nifurahie nilivyo.
Hakuna kiungo mwilini mwangu hukithamini! Unajua kunishika.” Mill
akamsogelea na kuanza kumvua nguo taratibu huku akimbusu kila anaposogeza nguo.
Akaanza kumsisimua. “Endelea nakusikiliza.” Maneno yakaanza kuwa mazito,
hayatoki. Walikesha hapo.
Mpaka kwenye
majira ya saa kumi ndipo Pam akazima kabisa kama mshumaa. Mill akategesha saa ili
imsaidie kumuamsha, kisha amuamshe na Shema. Na kumtumia ujumbe dereva afike
hapo kwake kumchukua Shema kumpeleka shule. Akambadilishia na muda.
Siku ya Kwanza
nyumbani kwa Mill
Bado ilikuwa
kama ndoto kwa Mill, haamini kama yupo nao hapo. Aliamka pembeni mwa Pam! Kwa
dakika kadhaa alibaki akimwangalia kama sungura na ndizi mbivu mtini. Akili
ikataka kumrudisha kwenye asubuhi alizokuwa akimka kwenye nyumba aliyokuwa
akiishi na Kisha pamoja na wanae, akagoma kujiharibia siku yake. “Mungu
amenitoa huko.” Akavuta pumzi kwa nguvu na kutoka kitandani kwenda
kumuamsha Shema, mama yake akiwa amelala hana habari.
Walisumbuana na
Shema, maana alishazoea kuandaliwa na mama yake. Hajui jinsi nyingine ila vile
anavyoandaliwa na mama yake. Mpaka Mill anafanikiwa kumpandisha ndani ya gari, hawazungumzi.
~~~~~~~~~~~~~~
Kwenye majira ya
saa tatu na nusu ndio Pam anaamka kwa kukurupuka. Akakimbilia chumbani kwa
Shema, hakumkuta ndipo akaangalia muda. Akatulia. Akaingia kuoga na kujisafi
haswa, Mill hakuwepo. Akajua yupo kwake.
Wakati
anatandika kitanda akagundua Mill aliacha ujumbe juu ya mto aliokuwa amelalia
hapo. ‘Ukiamka, nipigie.’ Akampigia. “Nakuja twende
tukapate kifungua kinywa kizuru ndipo tuanze fungate ya pili kabla ya kubwa
ninayo kuandalia.” Pam akacheka na kuanza kubadili sasa ili
apendeze.
~~~~~~~~~~~~~~
Baada ya muda
akaingia. “Naanza upya na wewe. Nahisi niliruka hatua moja. Nataka kuanza
kukutoa kama wasichana wengine. Date. Tunaanza upya. Nakutoa kwa chakula, movie
na mambo mengine mengi ndio tufikie pale tulipoachia.” Hatimaye kungojangoja
kwa Pam kunazaa tunda zuri lenye ladha tamu isiyofifia. Alifurahi
huyo mpaka usoni akaonyesha.
Mill alimvuta kupata
kiss isiyo haraka. Pam akatulia akisikilizia ladha yake. Ni Mill. Akimuweka
mikononi, hajiwezi. Alikuwa akisikia raha! Hajui afanyaje, maana alikuwa
akimnyonya ulimi na midomo kwa huba! Kama amvue chupi, lakini akamuachia. “Nakupenda
Pam, na hakika utajua nakupenda.” “Na mimi nakupenda Mill.” Akampa kiss
ya juu ya mdomo. “Halafu umependeza sana.” Akamsifia akimkiss tena juu ya
midomo, Pam akajua hapo njaa inamuuma, hakuna penzi mpaka ale. “Na wewe
umependeza. Nisubiri nimalizie tutoke.”
Mill akamfuata
chumbani. “Nashukuru kunisaidia Shema.” “Ahaaaa! Hakika naomba badilika
jinsi unavyomkuza aisee!” Pam akakunja uso na kugeuka. “Atakuja kukwambia.
Ameondoka amekasirika, na ameniambia eti yeye kesho anataka aandaliwe na
mama yake.” Pam akaanza kucheka.
“Kwa nini?!”
“Eti yule baba mtu mzima, anataka kwanza eti yeye wakati akioga, akute
nguo zake kitandani! Safi, zimenyooshwa, zinamsubiria yeye mpaka boksa!”
“Sasa, kumbe!?” Pam akashangaa. “Kwani yeye hana mikono! Yaani eti nimemkuta
ametoka kuoga amesimama chumbani, ananiuliza, ‘mbona hakuna nguo kitandani!’
Namuelekeza zilipo, ananiambia, ‘Mama anahakikisha kila kitu kipo kitandani.
Nikitoka kuoga, nikuvaa tu.’ Nikamwambia sasa nishamuonyesha, achukue avae,
akaanza kulalamika. Eti yeye mama yake huwa hamfanyii hivyo.” Pam akazidi
kucheka.
“Tena anasema, ‘mama
yangu.’ Yaani kama mimi simfahamu huyo mama yake. Haya, hapo tukasumbuana,
tukamaliza. Tukaja kwenye chai. Nimemuwekea mezani, namwambia mbona
hali, anasema sijampoozeshea!” Pam alicheka mpaka machozi. “Nikafikiri sijamsikia
vizuri. Nikamuuliza. Akasema yeye mama yake anampoozeshea kwanza,
ndio anampa. Yeye hawezi kunywa, anaogopa kuungua! Nikampa kikombe cha
pili. Maana hapo alikuwa kashanikera. Ananiambia, mama yake
hataki ajipoozeshee. Namuuliza kwa nini, anasema ndio mwanzo wa kujiunguza,
ampe huyo mama yake majonzi. Halafu eti, anaweza jichafua, ikaanza
kazi ya kutafuta shati jingine!” Pam alikuwa akicheka mpaka akakaa.
“Namwambia mimi namuamini
kuwa ni mkubwa, hatajiunguza. Eti ananiuliza na akijiunguza nitamwambia nini mama
yake. Aisee aligoma kunywa chai. Akasema ni bora aende shule bila
kula, asije akampa mama yake majonzi. Namwambia mimi nitamuelekeza, akakataa.
Halafu ananiuliza sasa nitamwambia nini mama yake, akijua amekwenda
shule bila kula! Maana mama yake anamwambia akiwa na njaa, hawezi
kujifunza vizuri. Haya nikapoozesha nikampa, akala.”
“Namwambia
aharakishe dereva ashafika, ananiambia yeye mama yake huwa anawahi
kumuamsha, ili apate muda wa kutosha wa kula, na hajawahi chelewa shule.
Nikanyamaza maana alishanikera. Ananitishia mama, wakati mwenzie yatima.
Haya, tukaja kwenye kuvaa viatu. Bwana yule mtoto hajui kufunga kamba za
viatu kabisa! Nikaanza kumgomea. Namwambia aende hivyohivyo. Akaniambia
kuna hatari ya kukanyaga zile kamba na kuanguka. Eti sasa mimi
nitamwambia nini mama yake akiumia!” Pam alikuwa akicheka mpaka
machozi.
“Ukamfunga?”
“Nifanyaje? Nikamfunga huku namwambia akirudi lazima ajifunze. Ndio
akaniambia yeye kesho anataka kuandaliwa na mama yake. Na mimi
nikamwambia hakuna tena kuandaliwa na mtu. Nitakuwa namsimamia ajiandae
mwenyewe, yeye mkubwa. Ndio kaondoka amenuna. Sasa akirudi hapa, na wewe
usianze kumbembeleza. Mwambie kuanzia leo mimi nitakuwa nikimuandaa.
Lazima akue.” “Acha kumpania bwana! Taratibu, hatua kwa hatua. Hutaki
wewe ndio akufanye adui. Tufanye kwamba mimi na wewe tunasimama sehemu moja.
Hata kama na mimi namwandaa, nianze kumfundisha kujitegemea ili msitengeneze
uadui.”
“Adhabu
yeyote kutoka kwangu, ataichukulia kwa upendo. Lakini ikitokea
kwako mtatengeneza uadui. Wewe niambie vile unavyotaka, halafu
mimi nitaanza kumnyoosha taratibu. Tusimfanyie mabadiliko mengi, kwa
wakati mmoja.”
“Tumemuhamisha
kule kwenye ule mtaa ambao ndio amekulia kule. Wale watoto wa pale
mtaani wamemzoea na yeye anawapenda kama moja ya familia. Najua
itakuja kumuumiza tu akitulia na kujua hawezi rudi tena kule. Halafu tumehamia
huku kwako ambako tena mnakwaruzana! Tukimfanyia mabadiliko mengi
kwa wakati mmoja, tutamuumiza na wewe atakuona adui wakati najua
unakusudia mazuri kwake.” Hapo Mill akatulia akijua ni kweli.
“Nakushukuru kunifikiria
Pam. Kweli sitaki mwanzo mbaya na yeye. Asijeona mimi ni tatizo. Ila lazima
tutekeleze bila kuzembea. Ndio mzaliwa wangu wa kwanza huyo! Sitaki akue
kizembe.” “Atabadilika tu wala usijali. Si mkorofi hivyo, ila hajui maisha
mengine ila hayo tumeishi naye. Na wakati mwingine nilikuwa nikifanya kuokoa
muda au kuepusha garama za hospitali kwa ajali zisizo lazima au ninazoweza
epuka, lakini si kumdekeza.”
Kifuniko
Kinapopasuka, Kweli Yabaki Wazi
Ndiyo yaliyokuwa yamempata Pius. Ilikuwa
kama anaondolewa ukungu machoni nakuona yote ya mkewe kwa wazi
kabisa bila kificho. Alikuwa kwenye hali ambayo hawezi mueleza mtu akaelewa. Ila
kwa kuwa hakuwa amekula tokea jana yake usiku, na Pius ni kama huyo mwanae
Ayvin, hawajiwezi kwa njaa. Alipofika tu hapo mgahawani akaagiza chakula
kizuri tu akabaki akiwaza akiwa anasubiria chakula, mpaka kikaletwa. Akamuona
Sonia na watu watatu wanakaa meza ya pembeni yake wala si mbali na yeye. Na wao
wakaagiza chakula. Hawakusemeshana. Ila yeye Sonia na hao askari kanzu
waliendelea kuzungumza yao kama wanao fahamiana kwa karibu tu.
Chakula chake
kikaletwa, akaanza kula taratibu tu akiangalia muda. Bila ya kuchelewa, Raza
akawasili akionekana na hali mbaya mpaka usoni. Pius akamtizama wakati akivuta
kiti akikaa mbele yake.
Akamwangalia
alipokaa huku akiendelea kutafuna. Raza akameza mate na kuanza. “Kuhusu swala
la Chezo…” Pius akamtizama na kumuwahi. “Najua umejiandaa kwa UONGO mwingi tu. Ushajipanga na kujua nini chakuniambia.
Usipoteze muda na usiniudhi zaidi. Nyamaza kabisa, mimi ndiye niliyekuita
hapa.” Raza akatulia.
Pius akaendelea
kula. Kimya. Raza akitetemeka mpaka tumbo lake lilikuwa likisikika likiunguruma
kama mvuvi kwenye mtumbwi, katikati ya bahari, dhoruba ikipiga chombo chake,
hajui anatoka vipi.
Baada ya muda
akamwangalia. “Bila maneno mengi, nataka unijibu, ni umbali gani kutoka hapa,
mpaka kwa Katibu, mganga wako.” Mwisho wa uwongo ni kilio cha
moyo, kwani ukweli unaibuka kama jua kuteketeza giza la udanganyifu.
Raza alitamani ardhi ipasuke aingie humo ndani. Akabaki ameganda, kama sanamu.
Maana lilikuwa swali la moja kwa moja, hakuna kuzunguka.
“Nakuuliza Raza,
kutoka hapa, mida hii, mpaka kwa mganga wako, itachukua muda gani? Na uongo
si muda wake. Zaidi sasahivi. Hutafurahia endapo utanidanganya
kwa lolote lile, maana tunakwenda wote sasahivi.” “Inategemea.” Ndilo aliloweza
kujibu Raza. Pius akabaki akimtizama huku akitafuna. Kimya.
“RAZA?” Akamuita
kwa ukali mpaka Raza akashituka na watu kuwageukia. Na hapo ndipo alipoiona
hasira ya mumewe. Chuki iliweza kuchomoza kutoka kwenye vipande vya moyo
uliovunjika, kama mchanga mkali unaotoka kwenye glasi
iliyopondeka. Hapo Raza aliogopa zaidi. “Inategemeana na foleni.” Akajibu
kwa haraka. Pius akaendelea kula mpaka akamaliza, Raza amekaa mbele yake
akishindwa hata kujisogeza hapo kitini.
Kifo Cha Kivuli
Kibaya
Alikula na
kunywa kinywaji chake mpaka akamaliza. “Mwaga kila kitu kilichopo kwenye pochi
yako, hapo mezani.” Raza akabaki akitetemeka, pochi bado ipo kwapani
amening’iniza begani. “Namaanisha sasahivi. Na utoe vitu vyote mpaka kwenye
zipu za pembeni ya hiyo pochi. Weka hapo mezani.” Akaanza kutoa simu. “Unanichelewesha
Raza. Nimekwambia mwaga na kung’uta. Au unataka nimuite mtu akusaidie?” Kwa
hakika Raza alishindwa. Ndipo akaamini kweli kuna anavyoweka humo
ndani na kutembea navyo kama ulinzi.
“Nipe hiyo
pochi.” Raza akabaki ameshikilia pochi yake. Pochi yenyewe ilionekana ya thamani
SANA. Nzuri, classic.
“Raza? Sitajirudia tena. Nipe hiyo pochi. Maana sitaondoa gari yangu hapa
kuongozana na wewe ukiwa unazungukwa na madudu uliyopewa na
mganga wako.” Akabaki akimtizama Pius akitetemeka. Pius akasimama na kuivuta
kwa nguvu, kisha akamwaga mezani.
Yaliyotoka humo, usingedhania kama yanatoka kwa mrembo kama Raza. Maana
hapo kwenyewe Raza alikuwa amependeza! Nadhifu! Anavutia kwelikweli.
Hapakuwa na ubishi kama ni mke wa Pius Ruhinda. Yeye mwenyewe ni msomi anafanya
kazi ya maana, mshahara mzuri. Halafu alijiweka kisomi haswa. Amejipangilia juu
mpaka chini. Gari aliyeegesha hapo nje, ilitangaza utajiri usio kificho. Kwa kumwangalia
tu, usingedhania vilivyopo mezani ni vyake. Pius mwenyewe alishituka
mpaka akaruka pembeni akibaki akikodolea macho kwa hofu.
Sonia akasimama.
“Naomba kijana wangu achuchukue picha na video, nataka ushahidi
wakueleweka.” Raza akageuka asielewe. Walishavuta macho na masikio ya watu hapo
kwenye huo mgahawa wa maana haswa. Kijana wa Sonia akapiga picha na kuchukua
video mpaka akaridhika, Raza akiwa amekaa vilevile.
“Naona kwa hapa,
kwangu inatosha. Anaweza tu rudisha kwenye pochi.” “Rudisha madudu yako.” Mumewe
akamuamuru akiwa amesimama pembeni kabisa akiogopa hata kusogea. “Na
akimaliza naomba mimi nitunze hiyo pochi kama ushahidi mbali na hizo picha.”
Sonia akaongeza na kumshangaza Pius.
“Kwamba ukae
nayo hayo madudu!?” “Oooh yeah! Itanisaidia ushahidi huko
polisi.” “Huogopi!?” Sonia akacheka. “Hakuna silaha itainuka kinyume
nami ikafanikiwa, Pius. Mimi nalindwa eti.” Sonia akajibu kwa
kujiamini, Pius amesimama pembeni kwa hofu. “Na kama anashindwa, naweza
kumsaidia kukusanya.” Sonia akaongeza. Raza akakusanya kwa haraka na kurudisha
ndani ya pochi yake.
“Huwezi chukua
pochi yangu.” “Usinitanie Raza. Mpe hiyo pochi.” “Sasa yeye inamuhusu nini?”
“Nitakwambia tutakapotoka nje. Lakini hutashikilia tena hiyo pochi.” Sonia akamjibu.
“Na wala simu. Vyote vitabakia ndani ya hiyo pochi.” Akaongeza Pius hapo kwa
Sonia.
Mmoja wa wale
askari kanzu akachukua pochi kwa Raza na kumtaka asimame. Wakatoka hapo kwenye
eneo la watu la bishara huku Pius akiomba radhi kwa wateja wengine kwa
kuwabugudhi.
~~~~~~~~~~~~~~
“Sasa, utaongoza
njia mpaka kwa mganga wako. Na nakuonya Raza, usifanye mchezo wowote huko
barabara. Hakikisha hupotei njia. Wote hao wanamajukumu yao, hakuna
mwenye muda wa kupoteza. Fanya ili kufupisha hii safari. Na mkifika mimi ndio
nitazungumza na mganga wako si wewe.” Hakujibu.
Wakamuingiza kwenye
gari yao wake askari kanzu, safari ikaanza. Wao wapo mbele, Pius kwenye gari
yake, na Sonia akiwa na kijana wake kwenye gari ingine wanafuata nyuma.
Mganga wa Raza
alikuwa akiishi mbali na jiji. Mkadini, panapakana na Chalinze na
Bagamoyo. Mpaka Pius akashangaa. Walikaza mwendo wakifuatana hayo magari matatu
bila kuruhusu gari yeyote katikati yao. Waliacha lami na kuanza kufuata
barabara ya vumbi. “Mbali kote hivi, huyu alikuwa akija muda gani!?”
Pius akajiuliza akiendelea kufuata nyuma ya gari iliyombeba mkewe, mpaka kwa
huyo mganga. Ilishakuwa saa kumi jioni.
Walipofika Pius
hakuamini. Kijumba chenyewe kimechoka! “Unauhakika ni hapa?” Kabla Raza
hajajibu Katibu mwenyewe akatoka. “Kwema Raza?” Akamuuliza kwa kumtambua
kabisa, Pius akamuwahi kabla hajajibu.
Machozi ya
Mwisho ya Shetani
“Mpaka
mawasiliano yako ya mwisho na Raza ya jana usiku, akikulalamikia juu ya dawa
zako kutofanya kazi kwangu, maana nimempokea mtoto wangu, na
naonekana kumkubali si kama ulivyomuahidi. Na akikuuliza njia
gani nyingine atumie maana kwa mara ya kwanza nimekataa kula chakula alichoniwekea
ambacho kilikuwa na dawa ulizompa WEWE, na mengineyo ambayo najua unayajua
nazungumzia nini, sitaki kujirudia na kupoteza muda, mawasiliano yenu NINAYO.”
Katibu alishituka sana.
“Sasa nakuonya
kama nilivyomuonya mteja wako hapa, usinidanganye na kunipotezea
muda. NATAKA upindue yale YOTE uliyoyafanya kwangu, tokea mwanzo
wako na Raza na..” “Kwamba unataka kuanzia tokea hujamuoa?! Maana hapo
itakugarimu sana.” Pius akazidi kushituka.
“Kwamba huyu
ameanza kunileta hapa KWAKO kabla sijamuoa!?” Hapo Katibu akajua
ameshamwaga mchele kwenye kuku wengi. Alidhania Pius anajua yote, kumbe ya
nyuma yeye hakuwa akiyafahamu ndio anatoa siri.
“Wewe Katibu?
Inamaana huyu ananifanyia haya mambo tokea sijamuoa?” “Wala si
tokea zamani, ni kipindi hicho nilipokuwa tukitafuta mtoto wa kiume,
ndio nikaelekezwa kwake kuwa atanisaidia kupata mtoto wa kiume. Ndio…”
“Unaanza kudanganya Raza, na nitakuumiza hapahapa. Nilikwambia
nini?” Pius akamuuliza kwa ukali.
“Hapa nazungumza
na yeye, kwa nini wewe unaingilia? Hicho unachozungumza sasahivi
najua ni sababu uliyotengeneza ukiwa njiani tukija hapa maana hukuwa ukijua kama
nakuleta hapa mpaka tulipokutana pale mgahawani. Sasa nakuonya Raza. Nyamaza.”
“Aisee kweli! Kumbe wewe unamjua mkeo. Maana Katibu amesema kwa wazi kabisa ni
tokea hujamuoa, yeye ashatengeneza uongo unaofanana na kweli!”
“Na kwa taarifa yako, nilishajua kama ulinifanyia mauchawi yako
ili nikuoe. Nilinyamaza, sikukuuliza kwa kuwa kwa wakati huo sikuona ubaya
kwako. Kwangu ulijionyesha ni mwanamke wa kawaida tu. Nikajiambia
japokuwa ulinifanyia mambo yako, sina nilichopoteza. Nilitaka mke, nikakupata
wewe!”
“Sasa badala utulie
ukiwa ni mke wangu. Sina ubaya na wewe Raza. Nakutunza bila hata
kukuuliza pesa yako. Nakupa unachokitaka na bad…” “Unajuaje kama na hayo yote
unayomfanyia ni moja ya uchawi wake ili umpe anachotaka?” Mmoja
wa askari kanzu akamfanya Pius azidi kuogopa.
“Wala
sijamfanyia hivyo. Amekuwa akinipa kwa ridhaa yake.” Raza akakanusha.
“Tutajuaje kama ni kweli kwa mtu uliyemloga mpaka akakuoa? Kama umeweza
kumfanya akuoe kwa sababu zako, utashindwa vipi kuhakikisha hizo sababu
zinatimia?” Mwingine tena kamuuliza. Pius alishajisogeza mbali kidogo ya Raza
kama aliyeingiwa hofu naye.
“Mimi napenda
jinsi Pius anavyoendesha haya mambo. Tafadhali usipotee kwenye Lengo Pius.
Rudisha akili kwa Katibu.” Sonia akaweka msisitizo. Yupo kikazi. Anachotaka ni
ushahidi. Na kijana wake aliendelea kuwachukua video bila kuwafanya wakajua.
Pius akajaribu
kutulia, nakuendelea. “Sitajali unarudia umbali gani. Nataka kuanzia ananileta
hapa kwako unifanyie anachokitaka mpaka jana usiku. Yote uliyoyafanya, nataka
tuingie wote humo ndani, uyapindue. Na ndipo uje kwenye swala la kijana
yangu. Hayo majini mliyoyatuma kwake, yakamuharibu sijui kumuangamiza,
uyaite mbele yangu, yarudi na kumuacha mwanangu huru. Unanielewa
Katibu?”
“Sasa yote hayo
unayotaka nikufanyie ni lazima kuwe na damu. Siwaoni hapa hata na jogoo!” Mpaka
hapo Sonia akawa amepata UKIRI wa Katibu. “Maana kwenye kila jambo ninalofanya
lazima agano la damu. Na Raza anajua kabisa. Iweje leo aje mikono
mitupu? Makubaliano yetu ni afike hapa siku ya jumamosi na kila nilichomuagiza.”
Sonia akatoa zile karatasi za jumbe za Raza.
“Ulimuagiza
lini?” “Jana. Na akaahidi ataleta kila kitu siku ya jumamosi bila
kukosekana kitu. Sasa kwa kuwa tunaanzia mbali, na ni kama tunatengua
kila kitu, lazima kutuliza mizimu. Hivyo nilivyomuagiza hapo
lazima kuongeza na mbuzi, tena beberu.” Sonia akarudisha macho kwenye
mawasiliano yao. Akasoma na kumuonyesha Pius na yeye akasoma na kutingisha
kichwa kwa masikitiko.
“Yote hii ni
pesa yangu unachukua na kutumia kunifanyia mimi mwenyewe uchawi! Yaani
unatumia pesa yangu kwa kuniangamiza mimi na kijana wangu!” Pius
akaongea kwa uchungu sana akilalamika. Raza kimya.
“Huwezi pokea
pesa, taslimu?” “Beberu ni lazima ili mizimu inywe damu kuituliza.
Ukishafanya nao agano, huwezi badilisha hivihivi.” “Naomba tuzungumze hapo
pembeni, Pius.” Sonia akamgusa Pius.
~~~~~~~~~~~~~~
Akajivuta
pembeni kabisa na Pius. Akaridhika hawatasikika. “Nisikilize Pius. Sijui unapotaka
kuelekea, lakini agano la damu ni halisi. Utakapotoa tu
hivyo vitu ili wafanye kafara, yakubatilisha hayo mambo yao, jua
wazi umejiingiza kwenye mkataba nao, hutatoka.
Huwezi jua na Raza naye alianzia wapi mpaka kujikuta anaendelea naye.
Sijui kama unanielewa?”
“Hawa watu
wamefanya mambo mengi sana kwangu, Sonia! Na umeona ahadi aliyompa Raza.
Kwamba wameshatuma mashambulizi kwa kijana wangu. Wanasubiri tu
kukutana, aletewe hivyo vitu wahitimishe.” “Naelewa. Ila nataka na wewe
uelewe hivi, kamwe hutamshinda shetani kwa kutumia nguvu zake.
Huwezi na hakuna aliyeweza mshinda shetani kwa nguvu za giza maana ni zake.”
“Ninapokwambia
Mungu ni muweza, nina uhakika naye kwa KUMTHIBITISHA mimi mwenyewe kwa
kuona si kusimuliwa. Hayo yote uliyofanyiwa wewe na kijana wako, anaweza
kukurejeshea tena maradufu, halafu bila DENI.” Sonia akaendelea.
“Yule binti niliyekwambia
alimloga dada yake na shemeji yake, alianza kwa kusaidiwa hivyohivyo na mganga,
lakini na yeye alimuendesha haswa. Akamlazimisha kuja kulala naye.” Pius
akashituka na kumgeukia Raza kwa sekunde kadhaa.
“Na dada mwenyewe
ni mzuri haswa, msomi anayejielewa. Lakini mganga akawa akimtaka kimapenzi huku
akimtisha. Yakaendelea hayo mpaka akaja kumpa mimba.” Pius akazidi kuingiwa
hofu.
“Shetani hana
zawadi ya bure Pius. Ila Yesu ninayekwambia atakupa uzima.
Atakuweka huru na kukurejeshea uliyopeteza bila kukudai
ila kukutaka tu mahusiano naye tena bila kukulazimisha! Achana na
haya. Yatakurudia na kukutesa sana.” “Sasa tutafanyaje? Natamani walipe
kwa waliyonifanyia.”
“Sasa wewe
endelea na msimamo huuhuu. Nenda naye hivyohivyo kama unataka akufanyie.
Mwambie upo tayari kumlipa pesa yeyote ile, na tutawatuma wale askari wakalete
huyo beberu. Atakubali kwa haraka na kukutajia pesa anayotaka yeye. Lakini wewe
mwambie hutalipia hiyo pesa mpaka ujue anakuagua kwenye lipi. Kwa kuwa
anajua unayo pesa, na Raza anaonekana alikuwa akimlipa bila shida, atataja kwa
haraka. Akishataja ndipo tutamuweka chini ya ulinzi. Tunaondoka naye hapa ili
asirudie kudhuru wengine.” Hapo Pius akakubali. Wakarudi.
~~~~~~~~~~~~~~
“Sasa Sonia
amekubali kutuma vijana wake wakaniletee huyo beberu. Vingine umekubali iwe kwa
pesa. Si ndivyo?” “Kabisa. Ila ujue itakuwa garama maana tunaanzia tokea
mwanzo.” “Hamna shida. Ilimradi tu mimi na kijana wangu tupone.” Pius
alionekana ametulia kabisa na anataka kufanyiwa na yeye.
“Kiasi gani?” Akamtajia
mamilioni ya pesa akijua anayo tu, maana alimjua huyo Pius hata kabla hajafika
hapo. Yeye mwenyewe tu na gari yake alitangaza utajiri. “Yote hiyo! Kwani unaniagua
nini na nini?” Akaanza kumtajia kishawishi. “Tokea hamjaona, alitaka
umpende yeye tu. Hapo kuna maagano yake. Kukurudishia fikra
zako, hapo kuna maagano yake.” Pius akakumbuka dawa
alizojuwa amewekewa chini ya mto anao lalia kila siku usiku. Akahisi pengine
ndio kazi yake. Akazidi kuogopa.
“Kukurudishia
nguvu zako za kiume, ili urudi kuwa kama zamani. Sio mpaka Raza
akufungue. Hapo napo kuna agano lake.” Pius akamtizama Raza, akainama.
Akaendelea kumtajia mwanzo mpaka hapo kwa Ayvin akitaka kiwe kifo cha
usingizini. Pius alikuwa akitetemeka baridi kama yupo kwenye friza.
“Na usifikiri
hilo la mtoto kwa sababu hakuna kilichotokea ndio udhanie hakuna
kilichofanyika! Nishatuma jeshi, tulikuwa tumalizie akija hiyo
jumamosi. Kwa hiyo hapo nataka pesa kutuliza mizimu na kurudisha
jeshi zima. Tena ujue hivyo nakupunguzia. Na Raza anajua bei zangu. Sifanyagi
kwa pesa hizo. Nafanya kwa bei hii kwa kuwa nabadilisha alichokianzisha
mkeo ndio maana unaona sianzii mbali na kuna punguzo la bei.” Akaongea mengi
akijisifia asijue anamfunga Raza na kujifunga mwenyewe.
Mpaka hapo Raza
hakujua kwa hakika kinachoendelea kati ya Sonia na Pius. Alijua ni kweli mumewe
anataka kuaguliwa, afute aliyoanzisha. Alikuwa amenyamaza muda
mwingi akishindwa hata kumtizama mumewe.
“Mimi naona
nimetosheka Pius. Nipo sawa kabisa.” Sonia akafanya wamuangalie. “Unauhakika?”
“Kabisa. Au unasemaje Zilo.” “Aisee nimewapata wote, tena vizuri kabisa.
Kila mmoja na UKIRI wake. Hapa hutapata shida. Sasa tunaweza kwenda tu, ukaanze
kazi.” Ndipo wote wakamgeukia huyo Zilo aliyekuwa akichukua video. Moja kwa
moja Raza akajua amejifunga.
“Sasa mnaweza
kuwachukua. Wote wawili.” Raza alishituka, asiamini kama mumewe anataka
akafungwe. “Kwamba Pius unataka kunipeleka polisi kwa kuilinda familia yetu?!”
Pius akashangaa sana.
“Umechanganyikiwa
Raza au na wewe haya madudu ya mganga wako yanakufanya hujielewi!
Kwa haya uliyofanya mpaka sasa, unalinda familia ipi?!” “Mina amekuloga
Pius. Ona ulipo, na vile anavyotufanyia kutusambaratisha. Muulize Katibu
mambo anayoyaona kwa Mina, kila akiita jina lake!” “Sina muda huo.” “Kwa kuwa
amefanikiwa kukufunga Pius! Mina ni mshirikina sana ndio maana unaona
napambana naye.” “Unazungumza ni nini Raza wewe!? Kwani Mina amekuja
kwenye maisha yetu lini na wewe umeanza kunifanyia haya mambo lini?”
Kabla hajajibu akaendelea.
“Kwani Mina alikuwepo
wakati ukitaka nikuoe?” Kabla hajajibu akaongeza. “Kwani Mina alikuwepo
wakati unakuja hapa kunifunga nguvu za kiume?” “Hiyo ni kwa nia nzuri
tu ulipokuwa ukienda huko kwenye safari zako za kikazi ili kukunusuru
Pius. Watu wanatembea na vijidudu vya UKIMWI, kazi yao kusambaza.” “Kwa hiyo
wewe kufanya umalaya ni ruksa, ila si mimi?” Hapo Raza akakwama.
“Unataka kuja
kuwa mama wa namna gani kwa binti zangu wewe?” “Mimi napenda wanangu
Pius. Na wewe ni shahidi.” “Kwa hiyo hizi ndio njia ulizokuwa ukiwafundisha
wanangu muda wote?” “Sijawahi leta wanangu kwa mganga hata mara moja.” “Raza!?”
Katibu akamuita kwa kumsuta.
“Sasa kuwazindika
ndio…” Pius alishituka sana. “Kwamba hata watoto wangu umewafanyia haya mambo,
Raza!?” “Ni kwa nia nzuri ili mtu asiwadhuru! Huoni walivyotulia,
hawana hata mambo ya wanaume? Na darasani wanafanya vizuri.” “Naombeni mumtoe
hapa haraka sana kabla sijamjeruhi vibaya
sana. Mimi nilikuwa nikifanya vizuri mpaka kwenye shahada zangu zote, mbona
mama yangu hajawahi nipeleka kwa mganga?” “Nakuonya Pius, usiende kinyume na
mimi. Utajuta.” Raza akamtisha. “Na kweli!” Katibu akaongeza kitisho. “Haya
mambo hayaendi hivihivi! Unajidhuru zaidi, wewe mwenyewe.”
“Mtanifanya
nini? Mtaniloga zaidi?” Pius akauliza kwa kuwadhihaki. “Upo chini ya maagano
makali sana. Unaudhi mizimu na hawatakuacha hivihivi. Hakika utajuta.”
Katibu akaongeza kama akimsihi kwa kitisho. Mkewe akaongeza kwa Katibu. “Wewe
unafikiri umefika hapo ulipo hivihivi? Kwa kipi mno? Mimi ndiye
niliyekuwa nikikusaidia ufike hapo. Bila mimi hata biashara zako zisingekuwa
hivyo. Sasa usije fikiria umefika hapo hunihitaji mimi! Utarudi kuwa
chini kabisa. Muulize Katibu jinsi anavyokusaidia. Maana wewe
umeshikilia upande mmoja tu, wa huyo Mina, hujui upande mwingine.” Pius alibaki
akimwangalia mkewe kama ameona msukule.
“Nafasi ZOTE huko
ofisini ulizokuwa ukishika ni juhudi yangu na Katibu. Kila mafanikio
uliyo nayo usifikiri ni hilo jina lako la Ruhinda, ni mimi kuhangaika
sana mpaka watu wanaona nyota yako. Lasivyo ungeishia vilevile kawaida.
Na jua wazi, wewe si kitu bila MIMI. Sasa wewe kubali Mina akupotoshe uone
yatakayo kutokea.”
~~~~~~~~~~~~~~
Nguvu ya mke aliyeishi
naye kwa muda mrefu.
Alimjulia
mumewe, alijua wapi pakumpata. Akatumia uzoefu wake kwake mpaka
akafanikiwa kumuweka mumewe njia panda, kiasi cha
kuona kila upande una kiza.
Kwa mara ya
kwanza akaanza kutilia shaka juhudi zilizomfikisha hapo alipo na mafanikio
yake yote anayosifiwa nayo.
Ni kweli mafanikio
yake yote yameshiliwa na Raza?
Akimuweka jela
na KUHARIBIKIWA kikazi na kibiashara je?
“Kweli nianze moja!?” Pius akabaki akijiuliza akiwa njia
panda amejawa hofu.
0 Comments:
Post a Comment