Ila kwa kuwa
alikuwa amekasirika akamjibu, “Sisi tutakuwa sawa.” Akaendelea kusaka
sufuria. Akagundua hata jiko hana. Mill amesimama anaangalia. Akageuka.
“Naomba nikalie na Shema mara moja naenda kutafuta jiko.” “Sasa kwa nini
tusiongozane wote tukaenda kula na kufanya manunuzi mengine?” Akaondoka kurudi
chumbani bila ya kumjibu. Akamfuata.
“Unanichukia
bure mimi, malaika wa Mungu. Shida yangu ilikuwa kupendwa tu. Lakini
sasahivi lawama zote ni mimi! Lakini mkubwa jalala, nakubali
makosa. Naomba weka hasira zote pembeni, tufanye mambo ya msingi.”
“Nataka kubadili nguo.” “Nakuahidi sitakuangalia.” “Mill! Toka bwana!” “Hakuna
pakwenda kukaa!” “Huna lolote, wewe unataka kuchungulia tu. Toka bwana!”
Akaanza kucheka.
“Hakika
kungekuwa na makochi, ningetoka.” “Basi nenda chumbani kwa Shema.” “Pam amekosa
imani na mimi! Mbona mwanzo umevaa hapa kila kitu na nilikuwepo?” “Ulikuwa
kwenye simu, na nikajua mawazo yamezama huko. Hapa sasahivi umenisimamia
na unajua kabisa nabadili nguo, macho yatashindwa kujizuia.”
“Nitayakataza.” “Hapana. Ondoka. Wewe unataka kuchungulia wanawake
wangapi kwa wakati mmoja? Toka.” Hapo akatoka kimyakimya.
~~~~~~~~~~~~~~
Baada ya muda
akarudi na vyakula. “Muwe na siku njema.” Akatilisha huruma mpaka
kumshangaza Pam. Ile jeuri wanayowekeana ni kama ilipungua. “Wewe
umeshakula?” “Mimi kula wimawima siwezi. Acha niwaache tu.” Pam
hakumjibu, kweli akaondoka. Akala na mwanae, wakajikuta wamelala kitandani
kwake mpaka jioni, aliporudi.
Pam akatoka
kitandani na kwenda kumfungulia. “Nimewaletea tv na meza ya kulia chakula.” Pam
hakuamini. “Pole Mill! Mimi nilijua umekwenda kupumzika!” “Acha waingize ndani
na kukupangia kabisa. Hii tv naiweka chumbani kwako mpaka utakapoenda kuchagua
makochi unayopenda. Sikutaka kukuchagulia kitu ambacho hutapenda.” “Nakushukuru
sana.” Wakawawekea kila kitu. Hakukaa, maana hapo alikuwa akitokwa na jasho haswa.
Hata hivyo Pam alijua anajikaza tu. Mill hapendi joto kabisa.
Akaaga bila
maneno mengi. “Dereva atakuja kumchukua huyu asubuhi. Muwe na usiku mwema.” “Na
wewe.” Akaondoka. Hakumsikia tena siku hiyo hata kwa ujumbe wa usiku mwema.
Akajua yupo na Brenda akaona ajinyamazie tu.
Jumatatu Baada
ya Kuhama.
Kama kawaida
akaamka kumsaidia mwanae kujiandaa, alipokuja kuchukuliwa, na yeye akaondoka
kwenda kazini. Siku ikaanza kama kawaida. Upande walipo wao sio wa wagonjwa.
Kumetulia. Kila mtu na kazi yake. Hakuwa amemuona Mill tangia amefika. Ila ni
kawaida. Mill huwa ofisini kwake muda wote ni mpaka awe anatoka au akuite
ofisini kwake ndio kumuona. Sasa aliyemkuta hapo huyo muhasibu ndiye aliyekuwa
akizungumza na Mill mara kwa mara na kumpa maagiza Pam, kwa hiyo hawakuwa na
sababu ya kuonana hapo kazini. Kwanza ni kama hawakuwa wakifahamiana wanapokuwa
hapo kazini.
~~~~~~~~~~~~~~
Muda wake wa
kwenda benki ulipofika, akatoka. Alipofika huko akamtumia ujumbe Mbise, muhasibu
wa hapo kazini, ambaye ndio kama bosi wake. ‘Nitarudi baada ya muda wa chakula,
kuna mtu nakutana naye kwa chakula cha mchana, ila sitachelewa.’ ‘Leo naona
mambo yako si mabaya.’ Akamtania kwa sababu hakuwahi kutoka kwenda
kula, hula hapohapo. ‘Acha hizo.’ Akamalizia hivyo, akaendelea na yake.
~~~~~~~~~~~~~~
Sasa huku nyuma
ikawa hekaheka. Pam harudi. Kumbe yeye Mill anamfuatilia. Anajua
anatoka muda gani na anao rudi. Akaanza kuangalia saa, Pam harudi.
Uzalendo ukamshinda. Akamfuata Mbise. “Umemtuma wapi Pam?” “Benki tu.”
Akaangalia saa hapohapo mbele yake. “Benki mpaka sasa?!” Mbise akakumbuka.
“Aaah! Nimekumbuka. Aliniambia atapitia kula kabisa.” Akaangalia muda
unakaribia wa chakula cha mchana. Akatoka.
Baada ya dakika
tano akarudi ofisini kwa Mbise. “Amesharudi?” “Bado.” Akaangalia tena
saa yake ya mkononi, hapohapo mbele yake, akatoka. Akaenda kukaa ofisini kwake
kama dakika 10 nyingine, akarudi tena. “Amesharudi?” “Hapana Kiongozi.”
“Kwani huko benki ulimtambulisha kwa watu wa namna gani? Isije kuwa ni wahuniwahuni
wakaanza mambo yao ya ajabuajabu!” Wivu.
“Ni walewale wa
siku zote. Tunaheshimiana sana. Labda atarudi baada ya muda wa chakula. Maana
huu ndio muda wenyewe wa chakula.” Akaangalia tena saa, na kuondoka. Mbise
akaangaliana na mfanyakazi mwingine.
“Kwema!?” “Naona
Pam ana bahati mbaya! Siku ya kwanza kutoka ndio anahitajika kweli!”
“Labda umpigie umshitue.” “Kama yupo na mtu wake je? Mimi
niingilie, si nitaonekana hovyo!” Kama aliyekuwa mlangoni, akarudi.
“Mtu wake! Mtu gani?! Maana Pam ni mama watoto wangu!” Ndio kila
mtu akashangaa mpaka Fatma aliyekuwa mapokezi alisikia. Wote wakatega sikio vizuri.
“Kwa hiyo kama
kuna linalo endelea, ningependa kufahamu. Unanisikia Mbise?” Akamjia juu
Mbise. “Maana wewe ndio upo naye ofisi moja. Na ndiye uliyekwenda kumtambulisha
huko. Isijekuwa umemtambulisha kwa watu walio anzisha jambo la tofauti
kwake badala ya maswala ya kazi tu.” Mzee akang’aka. “Kwakweli sifahamu
Kiongozi. Kwanza hajawahi toka kwa chakula cha mchana, yaani leo
ndio kwa mara ya kwanza ametoka!” “Ndio amekuaga anakutana na mtu
muda huu?” Hapo Mbise akaona atakuwa amezua janga.
“Pengine sikuwa nimemuelewa
vizuri. Ila nina uhakika alisema leo atakula kabisa hukohuko ndipo arudi.”
“Alikwambia kwa njia ya simu au ujumbe?” Mbise akajua amekamatwa. Kabla
hajajibu akaongeza. “Naomba kuona huo ujumbe.” “Labda akirudi
nitakujulisha Mkuu.” “Screen short mazungumzo yenu juu ya kuchelewa
kwake, unitumie sasahivi.” Akatoka amepaniki kwelikweli.
~~~~~~~~~~~~~~
Wasijue huwa ana
udhaifu wa miguu ya Pam na ile rangi yake. Sasa huwa anajua muda wa Pam
kufika kazini. Hufungua pazia za ofisini kwake kusudi ili kumuona
anapopita akiingia hapo kazini na muda anaotoka hapo ofisini. Sasa siku
hiyo Pam alivaa gauni jeusi, fupi mpaka katikati ya magoti, halafu
likamshika. Ni la kiofisi na alimnunuliaga yeye mwenyewe Mill, zamani akifanya
kazi kwa Sandra. Lina zipu nyekundu moja mgongoni, ndefu kuanzia juu mpaka
chini kabisa kama ndilo linalounganisha hilo gauni.
Akitembea kiungo
cha mguu, gotini mpaka chini vinaonekana. Mill huupenda SANA mguu wa Pam.
Hata kwenye romance ilikuwa lazima aushike kwa kupapasa, humpa mzuka
zaidi na hapo atafanya naye mapenzi kwa kufurahi mwanzo mwisho. Mguu wa
Pam!
~~~~~~~~~~~~~~
Sasa kile
kigauni na ile rangi, Pam aliwaka haswa halafu kilimkamata vizuri, umbile lake
ambalo ndio udhaifu zaidi wa Mill, ikawa bayana mpaka kina Mbise
walipiga miluzi alipoingia asubuhi hiyo. Na kwa sababu hutembea kutoka kituoni
mpaka ofisini na nyumbani mpaka kwenye daladala basi huvaa viatu vya chini, ila
akifika ofisini hubadili na kuvaa vya juu.
Sasa siku hiyo
akavalia kiatu cha juu chekundu kama hiyo zipu huko mgongoni. Bwana Pam
alipendeza! Napo pia Mill alimchungulia alipokuwa akienda benki. Hapo alikuwa
amepandwa na mzuka, hawezi kukaa chini.
Halafu mbaya
zaidi, huyu Pam alishaacha kujali maswala yake na Brenda. Akamuonyesha hajali tena
na kwake hataki tena kuhamia. “Ukute alishaniona mimi si kitu, kashamkubali jamaa
mwingine huko, anaona kuhamia kwangu atakosa uhuru na mtu wake!” Akazidi
kuwaza Mill akili zikienda kasi.
Akakumbuka vile
Pam alivyomwambia hata Brenda anaweza tu kuja kwenye shuguli ya mtoto wao. “Yaani
anikatalie, halafu baadaye akubali aje! Hapana, ipo namna. Huyu Pam ananitega
tu. Alitaka Shema anione mimi na Brenda, mwanamke mwingine, halafu ili yeye
akija sasa kumtambulisha mtu wake, iwe sawa!” Mill akazidi kuvurugwa mawazoni.
~~~~~~~~~~~~~~
Ikabidi Mbise
apige picha ule ujumbe na kumtumia bosi wake kitu ambacho si kawaida na ndio
wamejua yule mtoto anayekuja pale, akizunguka na Mill, ule weupe ni wa Pam.
Maana hakuwa mgeni hapo. Mill alishamzungusha Shema kila mahali. Wanamfahamu
Shema. Mbali na hapo, picha zake zimejaa ofisini kwa baba yake kama raisi wa
nchi. Ofisi nzima kimya, wakiingiza taarifa za Pam, mama
watoto wa bosi wao.
“Sasa na Brenda
naye vipi?!” Fatma maneno mengi, sekretari wa ofisi, akawafuata na kuwauliza
kimbea. “Hapo ndipo kitendawili!” “Sasa mbona Pam naye hata kutukonyeza!”
“Kama hujamgundua Pam ni msiri sana.” “Lakini si kwa jambo zito
hivyo bwana! Hata kujishaua kama na yeye mama bosi!” “Sasa leo hapa, pashawaka,
Fatma. Utakutwa humu ndani, utamtibua zaidi.” Vile Fatma anarudi
mapokezi, Mill naye anarudi kwa Mbise akiwa amemchanganya zaidi.
~~~~~~~~~~~~~~
“Kwamba Pam
anakutana na mtu kwa chakula cha mchana! Kwamba ndio wamefika mbali hivyo! Ukute
inabidi kukutana mchana na kufanya mambo yao, kwa sababu nishapajua walipohamia,
na nilishamkataza asilete mtu alipo Shema. Mwanaume gani tena huyu, au ukute
wamerudiana na Mgaya nini!” Ndipo kiti
kikazidi kuwa cha moto na kumfuata tena Mbise.
~~~~~~~~~~~~~~
“Amerudi?” “Au
labda nimpigie simu, nimwambie arudi.” Akamuona kama amesita. Halafu
tena kama aliyeogopa! Mbise hakuelewa. Maana alifanya ikawa kama kosa,
gafla akanywea kusikia apigiwe! Akaweka msisitizo. “Naweza mwambia arudi
sasahivi.” “Hapana! Hapana! Huu ni muda wake wa chakula.” “Basi akirudi
nitamwambia kama ulikuwa ukimtafuta.” Akamuona ameshituka tena.
“Hamna haja!”
Akaondoka akiwa ametulia kabisa. Wakaangaliana na wenzie. “Ni nini
kinaendelea!?” Wakanong’ona. Na wao wakaona watoke, wakatete vizuri huko kwenye
mgahawa wa hospitali.
~~~~~~~~~~~~~~
Wakaanza
kucheka. “Ni kile kigauni tu, kampagawisha.” “Lakini hajamuona!” “Sasa
wewe uwe na mali kama ile, usichunge? Atakua ashazoea hatoki,
anayetoka ni yeye tu. Sasa leo mwenzie katoka, ndio wivu.” Wakaanza
kucheka. “Sasa mtoto mtamu vile, anahangaika na makapi
kina Brenda wa nini?” “Kwani na wewe Mbise unamuona Brenda ni makapi!?
Bosi wa viwango!” “Huwezi mfananisha na Pam bwana!” Wakaanza kumchambua
Brenda na Pam, wanacheka mbavu hawana.
Kuliko Ungua Mpini,
Likabaki Shoka
Andy waliondoka
na familia yake jijini wakiwa kitu kimoja na mipango ya KUANZA upya.
Kulijawa na tumaini kwa wawili hao! Kitu kipya kikajengeka. Tena safari
hii wakiwa makini wakijua hakuna kitu cha kudumu, wakati wowote walichonacho
wanaweza poteza. Kukawepo na heshima na umakinifu
ukajengeka kwa wote wawili.
~~~~~~~~~~~~~~
Haikuwa hivyo
kwa Pius. Moyo wake ulikuwa umejuruhiwa vibaya sana na Raza mkewe.
Kitendo cha kumfunga yeye nguvu za kiume halafu yeye ana mahusiano
nje! Halafu mbaya zaidi kuhalalisha alichokifanya hadharani mpaka ndugu
kujua na kuaibishwa kwa kiasi kile!
Alinyanyuka pale
alipokuwa wameachwa wamekaa na mama yake. Akatoka kimyakimya na kwenda kuegesha
gari Shoppers plazza. Akabaki garini akiwaza anayofanyiwa na mkewe. Na nini
afanye. Alijua akimuuliza, asingekubali. Akabaki garini muda ukienda mpaka
kwenye majira ya saa nne na nusu usiku binti yake alipomtumia ujumbe wakumtakia
usiku mwema na kuwa anampenda sana. Akajua ndio anataka kulala. Akamjibu
na kurudi nyumbani.
Isivyo kawaida,
chakula alichokuta pale nyumbani kilimshinda kabisa kula. Alikaa mezani
akikiangalia akishindwa hata kuweka mdomoni. Raza alikuwa sebuleni kwenye
luninga akimsubiria ale. Huwa ni lazima chakula cha usiku awe anakula
nyumbani na Raza alishazoea hivyo. Lakini siku hiyo alishindwa kabisa.
Hakumsemesha sana Raza, akaenda kuoga na kulala.
~~~~~~~~~~~~~~
Kesho yake
alitoka nyumbani akawahi ofisini kama kuripoti tu. Kisha akatafuta mawasiliano
ya Raza. Akaomba kupakuliwa ya miezi sita nyuma. Jumbe na simu zake. Akapata
na kwenda kukaa nayo sehemu na kuanza kusoma jumbe kuanzia za asubuhi hiyo
kurudi nyuma.
Jasho lilikuwa likimtoka Pius kadiri alivyokuwa akisoma zile jumbe.
Zilizomuuma zaidi ni zile za vitisho kwa kijana wake, na mipango
aliyokuwa akifanya kwa siri juu ya huyo mtoto. Ni kweli Raza alikusudia kumuangamiza
Ayvin. Bado Sonia alionekana hakuwa amemtafuta. Akajua Mina hakukosea.
Akarudi kwa
upende wa mahusino ya siri aliyokuwa nayo. Walionekana ni wapenzi wa
muda mrefu na walichofanya ni kubadili tu muda. Kutoka kukutana jioni
mara tu baada ya kazi mpaka usiku, wafanyakazi hao waajiriwa, walikuwa wakikutana
muda wa chakula cha mchana. Pius alikuwa akitetemeka mpaka baridi.
~~~~~~~~~~~~~~
Akafikiria
chakufanya, akamtumia ujumbe Raza. ‘Leo badala ya kukutana na Chezo
mida yenu ya mchana, tafadhali naomba tukutane.’ Raza
alipopata huo ujumbe kutoka kwa mumewe, alikaribia kurusha simu. Alishituka, hakutegemea.
Kisha akaongeza ujumbe wa pili. ‘Nitakutumia sehemu utakayo nifuata.
Na Raza, nakuonya. Kutofika kwako kwa wakati, sehemu nitakayokwambia,
kwa sababu yeyote ile utakayochagua wewe kuja nidanganya nayo baadaye, hutapenda
matokeo yake. Itakuwa ni kunikaidi vibaya sana, maana ikiwa ni miahadi
yako na Chezo huwa huchelewi. Sasa kwangu USITHUBUTU kufanya kinyume.’ Raza alikuwa na hali mbaya, alishindwa hata kujibu.
Kwa Sonia.
Wakati
akisubiria muda wa mkewe kupata mapumziko ya chakula cha mchana akaamua
kumtafuta Sonia ili azungumze naye. Sonia akawa muungwana kumsikiliza
kwa upande wake. Akamkaribisha ofisini kwake. Alifika bila ya kuchelewa. Kwa
Sonia alikiri kosa la kusababisha karaha kwa Mina ila hakukiri
kosa la ubakaji wala hakuweka mazingira ya kutaka kuzungumzia hilo.
“Ukiniuliza kwa
nini, sitakuwa na jibu zuri. Ila nakiri sikuweka mazingira mazuri tokea Mina
anarudi na mtoto. Nilimpokea nikiwa na paniki huku na furaha ya kumuona
mtoto ambaye kwanza sikujua kama alizaliwa au la. Kisha kuletwa akiwa
mgonjwa. Wasiwasi wangu mpaka sasa ni kule kujiona ni kama nipo ndotoni,
nahisi naweza kuamka na kujiona nilikuwa nikiota. Ndio kutapatapa
kwangu.”
“Ila naahidi kubadilika.
Nimefanya kosa, ila nakuahidi kuanzia sasa, nitakuwa makini kwa
kila nitakachofanya ili kumfanya Mina na mtoto wangu watulie. Mimi mwenyewe
nitaweka ulinzi kwao, nikitambua uwepo wa Andy.” “Hili ndilo
nataka kulisikia.” Sonia akaonekana kuridhika.
“Sasa basi, NAANZA
na Raza. Nimeona jumbe zake mbaya sana. Nimeweza pata mawasiliano
yake yote mpaka na ya huyo mganga wake.” Sonia akashituka sana. “Kwamba
ameshaanza kufanyia kazi!” “Kabisa. Hivi ninapozungumza na wewe, ninazo jumbe
zake au mawasiliano yake ya mpaka jana usiku. Ameshamtumia mganga wake mpaka
picha ya kijana wangu.” “Haiwezekani! Huyu aliyerudi na Mina juzi tu!?” “Nina
mtoto mmoja tu wa kiume ambaye nimezaa na Mina. Kwa hiyo kujibu swali
lako ni huyohuyo.”
“Tena simu
yake ya mwisho kwa huyo mganga wake, japo sijui alizungumza naye nini ni
usiku wa kuamkia leo. Jana niliwahi kulala kabla yake, na kwa mara ya
kwanza sikula nyumbani. Pengine hilo lilimshitua.”
“Kwani yeye alishakutana
na Ayvin? Namaanisha alipata wapi picha ya kumtumia mganga wapi au ndio kutoka
kwa dada yako?” “Nina uhakika ni hivyo. Na yeye amepokea onyo lako, mbele
yangu na wazazi. Sidhani kama atakuja rudia tena.” “Au wote wana njama
ya kumuua kijana wako?” “Paulina yeye ni mchonganishi tu. Furaha yake
ni hii hali iliopo sasa. Lakini si kuua kama Raza. Raza amefika mbali
sana.”
“Turudi nyuma
taratibu. Yeye aliyachukuliaje mahusiano yako na Mina? Nikimaanisha tokea
mwanzo, hayohayo ya kishemeji! Maana Mina amekiri kwangu hapakuwa na
mahusiano ya kimapenzi kati yenu. Ila ni jambo lililotokea katikati ya ulevi.
Ila amekiri mlikuwa karibu sana, hata mida mwingine mlijikuta usiku peke
yenu, na likawa jambo la kawaida hata kwenye familia yenu, watu wakijua
ulikuwa ukiwasaidia familia ya mdogo wako!”
“Ni kweli hapakuwa
na mahusiano mengine ila hayohayo yakatuweka karibu kwa muda mwingi.” “Hilo
ndilo likaibua maswali kwangu. Mkeo alichukuliaje hilo? Kurudi
kwako usiku, ukisema unatokea kwa Mina! Nikahisi pengine hilo ndilo lililo
ibua chuki kwake tokea mwanzo. Lakini katika upelelezi wangi, ndipo
nikaja kugundua kuwa na yeye anayo mahusiano yaliyokuwa
yakimuweka nje mpaka usiku mwingi, kiasi cha kumfanya mke wa huyo jamaa,
niliyetajiwa kwa jina la Chezo.” “Sawasawa.” Pius akaafiki.
“Alikuwa
akilalamika kuwa mkeo, yaani Raza, anamchelewesha mumewe nyumbani.”
Ndipo akagundua kuwa yeye ndiye aliyemwambia Mina habari za mahusiano ya nje ya
Raza. “Cha kwanza, sikuwa nikikaa usiku mwingi hivyo kwa Mina. Nilikuwa nikijitahidi
kurudi nyumbani muda mzuri tu, maana chakula cha usiku mara zote inakuwa ni lazima
nile nyumbani, na Raza ndiye aliyekuwa akindaa mara anapotoka kazini.”
“Huwa akitoka
kazini lazima arudi nyumbani. Tuna binti bado anaishi nyumbani. Lazima kuzungumza
naye na kuangalia kazi zake za shule. Na yeye lazima kusimamia chakula
cha usiku. Ndipo anatoka sasa kwa starehe. Na mara nyingi ilijulikana anakuwa
na hao rafiki zake. Ni kama wana kikundi chao. Basi hukutana sehemu, au
niseme club kwa kula na kunywa. Huna muda ukampigia akashindwa
kupokea.”
“Nawafahamu hao
watu niliodhania anakuwa nao muda wote akiwa kwenye starehe na mimi
wananifahamu, wote ni watu na kazi za maana tu. Wamejitengenezea kundi lao. Sikuona
tatizo maana mimi sinywi pombe ile ya kukaa baa. Ni wine tu. Raza ni mnywaji. Sikutaka
kumfunga kwa starehe ambayo alichagua mwenyewe na sikuona madhara
yake.”
“Sikuwa nikiyajua
hayo mahusiano hata kuyahisi kwa sababu hakuna cha ajabu
kutoka kwa Raza kilichobadilika na kuibua maswali kwangu. Kama ni kuchelewa
kurudi nyumbani lilikuwa jambo la kawaida. Na hakuwa akichelewa sana, sababu ya
kazi siku inayofuata. Hatazidisha saa tano usiku. Sasa kwa mtu aliyetoka
nyumbani tuseme saa moja usiku au 12:30 jioni. Akafanya majukumu yake
kama mama. Anaporudi nyumbani saa 4 usiku au tano, sio jambo la kuibua maswali.
Au tuseme binafsi sikujali kwa sababu na mimi swala la kusafiri nje ya
nchi kikazi ni kawaida sana. Sipo nyumbani, na yeye akajitengenezea marafiki
zake, sikuona ajabu.”
“Ila ni kama akabadili
ratiba. Si siku zote anakuwa club na hao marafiki zake. Akitoka kazini akirudi
nyumbani, hatatoka tena labda siku za ijumaa, ndipo atafanya hivyo na atarudi
usiku mwingi tu kwa sababu siku inayofuata jumamosi haendi kazini. Sasa kwa mtu
ambaye hatoki siku za katikati ya juma, mpaka ijumaa na anakuwa na watu unao wafahamu,
binafsi sikuona tatizo. Ni maisha aliyochagua, nikamuacha.”
“Kumbe walichofanya
baada ya mke wa Chezo kugundua, na kumsemelea kwa Paulina akimtisha
atakuja kumsemea kwa mzee wangu, walibadilisha tu sehemu wanayokutania
na MUDA. Ndio maana kumbe siku hizi Raza anawahi nyumbani na Chezo hivyohivyo. Wote
waliogundua hayo mahusiano yao ndio wanadhania wameachana,
kumbe la. Hawakuwahi kuachana.”
“Jinsi yao ya
kuwasiliana ni Whatsapp na wameweka Disappearing messages.
Kwamba hata wakisahau kufuta jumbe zao, basi system inawasaidia
kufuta. Huwezi kukuta jumbe zao hata kwa bahati mbaya. Mimi mwenyewe imenibidi KULIPIA
pesa nyingi tu ili kuweza kufufuliwa jumbe zao.” Sonia akachoka
kabisa.
“Utafanyaje
Pius, na huyu ni mkeo?” “Mke anayenifunga mimi, akinitesa halafu yeye
anastarehe na wanaume wengine! Anafurahia kuteseka kwangu, tena akiniona!
Ananifanyia kusudi tu! Halafu anataka kuua kijana wangu asiye na
hatia! Kweli Sonia?” “MmmH! Nionyeshe kile ulichonacho Pius. Maana mimi
nilichonacho ni vitisho tu. Sikujua kama atafanya kweli!” Ndipo
wakalinganisha alichonacho Sonia na yale aliyoyakamata Pius juu ya mkewe
kwa mtoto wake, yaani Ayvin na mengineyo. Mpaka Sonia akaingiwa hofu.
“Pius!” “Ni hatari
sana. Mpaka najiuliza huyu ni kiumbe gani mwenye roho ya kikatili
hivi!” “Bado narudia swali langu, Pius. Utafanyaje? Maana mimi nilitaka
kumtafuta ili kumtisha tu. Lakini hivi ilivyo, si kutishana tena! Mkeo
ameshafika mbali na maangamizi yake yameshaanza.”
~~~~~~~~~~~~~~
Kama swali la
Sonia, Je kwa Yote aliyofanya, nini Pius atafanya kwa Raza.
Ni Umbali gani
Raza amekwenda kumuangamiza Ayvin?
Pam&Mill nao? Pam yuko wapi mchana huo? Ni kweli ameamua kuendelea na yake?
Nani anakutana
na Pam mchana huo?
0 Comments:
Post a Comment